Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwantakaje Haji Juma (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kuhusu suala la utalii wa Zanzibar. Utalii wa Zanzibar wageni wengi wamepungua kwa sababu mbalimbali za kisiasa na mengineyo. Sasa naomba Serikali ya Tanzania Bara iweze kusukuma utalii huu wa Zanzibar ili kupata nguvu kama utalii wa Tanzania Bara na wananchi wengi wanategemea utalii hususan vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mapato. Hii tozo inayotokana na utalii ikusanywe vizuri ili Zanzibar iweze kupata mapato vizuri. Kama ilivyoelezwa katika ukurasa wa 88 kuwa tufahamu wageni wanaingia na kutoka. Hiyo tozo inayopatikana ni kiasi gani ili wananchi wa Zanzibar waweze kufahamu, kwa mwaka mapato yanayopatikana, ili kusukuma maendeleo ya Zanzibar yatokanayo na utalii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa ruhusa hii nami kuchangia Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Nichangie kwenye kituo changu cha Bububu.Kituo cha Bububu hakina Kompyuta, hakina photocopy machine, copy wanakwenda kutoa nje ya kituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu matundu ya choo. Matundu ya choo hali ni mbaya katika kituo changu cha Bububu. Askari wanawake wanatoka nje wanakwenda kujisaidia na wao hawako salama, kwa sababu tunaijua Bububu ilivyo ni hatari. Tunamwomba Waziri kile kituo akitendee haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la watani zangu. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya, katika Jimbo langu kulikuwa na uhalifu mkubwa sana, amejitahidi uhalifu ule umepungua kwa asilimia mia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi kule sasa hivi wameanza kujikusanya vikundi wakiwa wanazungumza tunaita Zanzibar drip, wanasema uchaguzi upo kesho Maalim Seif anapewa nchi kesho. Tena niwahakikishieni kama ni uchaguzi umemalizika na tusubiri mwaka 2020, baada ya miezi mitatu, minne tutakuwa na wagonjwa wa hali nyingi, wagonjwa wa wasiwasi na wagonjwa wa presha kwa sababu akikaa tu Maalim Seif kesho anapewa nchi. Uchaguzi umemalizika tufanyeni kazi kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye kituo changu cha Polisi Bububu. Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri alijitahidi sana kwa sababu pale palikuwa na Mwekezaji, wameondoka na kituo kipo salama kwa sababu sisi wenyewe wananchi tulikuwa hatuko salama kwenye kituo kile. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Naibu Waziri kwa hali aliyoichukua pale kwenye kituo akamwondoa yule mwekezaji na sasa hayupo, nashukuru kituo kimebakia salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia juu ya mia.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia natoa pongezi kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Hussem Ali Mwinyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kuhusu uvuvi wa bahari kuu. Mnamo mwaka 1980 kilikuwepo chuo kinachofundisha somo la fisheries, hili somo ni zuri sana kwa sababu wananchi wetu itapelekea kupata ajira na kupelekea kupunguza umaskini na kuwezesha viwanda katika uchumi wa bluu. Wananchi wa Tanzania ni wavuvi ambao wamekulia katika mazingira ya uvuvi ipo haja Tanzania kuwa na wataalamu wa uvuvi. Naomba kuishauri Serikali ya Tanzania kushiriki katika uchumi wa bluu kwa kufanya yafuatayo; kwanza kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha kupata vibali vya ajira ili itusaidie kupunguza umaskini kwa namna moja au nyingine. Pia naishauri Serikali iweze kuweka njia ya kuwafundisha vijana wetu na kufufua rasilimali zetu na kutumika. Kwa mfano kuweka ufugaji wa kaa/majongoo/samaki na kadhalika na pia tuweke vizimba kwa wingi vya mazao ya baharini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunanunua meli za uvuvi lakini hatujajiandaa na wataalamu wa uvuvi wa bluu. Pia kwa sasa naomba kuishauri Serikali kwamba Chuo cha Uvuvi kijengwe Zanzibar kwa sababu Zanzibar imezungukwa na bahari na mikoa yake yote ina pwani na mikoa ya nyanda za juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali inawasaidiaje vijana ili kuwawezesha na kuwashirikisha katika uchumi wa bluu? Naomba kuiomba Serikali tuweke mazingira mazuri ili kuwezesha wananchi kupata mitaji ili waweze kushiriki katika uchumi wa bluu na pia kupata pesa za kigeni, kupunguza umaskini na kukuza utalii wetu. Ahsante.