Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. George Malima Lubeleje (87 total)

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali ya nyongeza.
Kwa kuwa barabara ya barabara ya Mbande - Kongwa – Mpwapwa mpaka Kibakwe ni muhimu sana kwa maendeleo na uchumi wa Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa; na kwa kuwa barabara hii inaunganisha Majimbo matatu; Jimbo la Kongwa, Mpwapwa pamoja na Kibakwe; na kwa kuwa ni ahadi ya Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Kikwete na ahadi ya Mheshimiwa Rais John Magufuli ambaye ni Rais wetu sasa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba ipo haja sasa ya kukamilisha barabara hii kwa kujengwa kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa barabara ya kutoka Mpwapwa – Gulwe kwenda Berege – Mima mpaka Iwondo haipitiki, ni mbaya sana kwa sababu ya mvua zinazonyesha. Je, Mheshimiwa Waziri ana maelezo gani kuhusu wananchi wa Jimbo la Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la kwanza ni kama nilivyojibu katika swali la msingi. Sana sana ninachoomba kuongezea ni kwamba dhamira yetu kama Serikali ni kubwa sana. Tuna nia ya kutekeleza ahadi za Marais hao; na kwa kweli mara fedha zitakapopatikana tutaendelea na kipande hiki kilichobakia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili, Wabunge wengi ni mashahidi kwamba maeneo mengi yaliyoharibiwa na mvua zinazoendelea, vijana wetu wa TANROAD wanafanya kazi kubwa. Naomba kwa upande wa TANROAD Dodoma waliangalie eneo hili ili kile wanachokifanya katika maeneo mengine na hapa wakifanye kwa ukamilifu ili wananchi waweze kupata mawasiliano ya uhakika.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa barabara hii ya kwenda Kondoa – Babati inafanana kabisa na ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais Mstaafu na Rais huyu wa sasa, Mheshimiwa Magufuli, kwamba barabara ya kutoka Mbande – Kongwa – Mpwapwa mpaka Kibakwe itajengwa kwa kiwango cha lami; na ahadi hii ni ya miaka nane: sasa namwuliza Mheshimiwa Waziri, je, katika bajeti ya mwaka huu barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa lubeleje pamoja na Wabunge wengine wa maeneo husika kwamba barabara inayoongelewa ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa kipindi cha mwaka 2015/2020, kwamba itakamilishwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, naomba tusubiri tarehe 17, bajeti ya Mheshimiwa Waziri itasomwa ambayo itatoa majibu yote kwa undani zaidi na nisingependa kueleza sasa nikagusa hotuba yake.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, nimeleta maombi yangu Wizarani kwa sababu Halmashauri ya Wilaya haina uwezo wa kukarabati barabara hii ya Gulwe - Berege - Chitemo - Mima - Sazima - Igoji Kaskazini - Fufu na Iwondo, sasa hivi haipitiki wananchi wanapata taabu hasa abiria kufika Makao Makuu ya Wilaya na ndiyo maana nimeleta. Tayari tulikuwa na kikao cha Bodi ya Barabara tarehe 29 mwezi wa Februari nilipeleka ombi hili. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri muifikirie barabara hii kuipandisha hadhi ili TANROADS waweze kuitengeneza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya kutoka Mbande - Kongwa kwa Mheshimiwa Spika, Mpwapwa na Kibakwe kwa Mheshimiwa Simbachawene Waziri wa TAMISEMI, hii barabara imeahidiwa kutengenezwa kwa kiwango cha lami na ahadi hiyo ni ahadi ya Rais Mstaafu Mheshimiwa Kikwete mwaka juzi na mwaka jana wakati wa kampeni za CCM Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wetu aliahidi kuitengeneza barabara hii ya Mbande - Kongwa - Mpwapwa mpaka Kibakwe kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Waziri huoni kwamba kuna umuhimu wa kutengeneza barabara hii ambayo ni kiungo kikubwa cha Majimbo matatu Kongwa, Mpwapwa na Kibakwe?(
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, barabara hii kama ambavyo tumejibu hapo nyuma kwamba Serikali imedhamiria kuijenga na imeanza kuijenga na itaikamilisha mapema kwa kiwango cha lami kutokea Mbande - Kongwa - Mpwapwa hadi Kibakwe kama ambavyo Mheshimiwa Lubeleje, Mheshimiwa Job Ndugai pamoja na Mheshimiwa Simbachawene walivyokuwa wakitusukuma katika kuhakikisha hii barabara inakamilika kwa haraka.
Mheshimiwa Spika, ninawahakikishia mtapata majibu mazuri zaidi wakati wa bajeti kuhakikisha kwamba ninachokisema hapa na kwa kweli hatutarajii kitu ambacho Mheshimiwa Lubeleje mnamfahamu ni mtu wa siku nyingi sana na hatungependa aendelee kufika mara zote ofisini kwetu kufuatilia barabara hii mara kwa mara ni lazima tuifikishe mwisho.
Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Gulwe - Berege - Mima hadi Fufu pamoja na nilivyojibu katika jibu langu la msingi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Lubeleje kwamba Mfuko wa Barabara utaangalia kwa makini na hasa kwa kuzingatia kwamba mwaka huu mvua imekuwa nyingi sana na zimeharibu barabara nyingi sana uwezo wa Halmashauri wa kuzirudisha hizi barabara ni mdogo.
Mheshimiwa Spika, tutaomba Mfuko wa Barabara na TANROADS wajaribu kusaidia maeneo mbalimbali katika kurudisha mawasiliano katika barabara zote zilizokatika nchini ikiwa ni pamoja na hii ya Gulwe - Berege - Mima hadi Fufu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nina swali dogo la nyongeza;
Kwa kuwa, wananchi wa Kijiji cha Majami, Kibolianana, Mlembule na Mgoma tayari wameshaonesha juhudi ya kujenga majengo ya zahanati, kilichobaki ni Serikali kusadia. Lakini Igodi Kusini, Isalanza jengo lipo tayari limekamilika pamoja na Igodi Kaskazini.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri utakuwa tayari kuwapelekea watu wa Igoji Kaskazini na Kusini huduma ya madawa na kusaidia hawa ambao tayari wameonesha nguvu za kujenga zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia kilio hiki na bahati nzuri Mheshimiwa Lubeleje kama ukifanya reference mwenyewe hili ni miongoni mwa maswali mengi sana aliyouliza katika sekta ya afya, Mheshimiwa Lubeleje nikuhakikishie kwamba katika eneo hilo kwanza ahadi zetu zile za kwanza ni lazima tutazitembelea zahanati hizi kuziangalia kama kuna changamoto tuweze kuzitatua; hali kadhalika tutafanya utaratibu jinsi ya upatikanaji wa dawa, kwa sababu nikijia Jimbo lako ni kubwa, maeneo yako ni makubwa. Nimefika katika sehemu wanaita Makutupa, kutoka Makutupa mpaka mtu anaenda kufuata huduma ya afya ni mbali sana. Kwa hiyo Mheshimiwa Lubeleje juhudi unayoenda kufanya endelea kuifanya, tutaunga mkono lakini lazima tu-visit tuangalie kama kuna changamoto nyingine tuweze kurekebisha, tuwaambie wataalamu wetu tuweze kufanya hata allocation ya wataalamu wa ndani na madawa tutafanya ili vituo hivi viweze kufanya kazi na wananchi waweze kupata huduma.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE:Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ya Maji.
Kwa kuwa tatizo la maji ni kubwa sana karibu nchi nzima na Majimbo matatu haya ya Kibakwe, Mpwapwa na Kongwa ni tatizo kubwa. Kuna visima ambavyo vilianzishwa kuchimbwa vya Benki ya Dunia mpaka sasa havijakamilika. Mpaka sasa hivi Mjini Kongwa, dumu moja la maji wananchi wananunua shilingi 1,000;
Je, Mheshimiwa Waziri, utakuwa tayari kutembelea maeneo hayo kuhakikisha kwamba miradi hii ya Benki ya Dunia ambayo haijakamika sasa ikamilishwe?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo maeneo ambayo tunayo hii miradi ya vijiji kumi ambayo haijakamilika na tumesema tu katika Awamu hii ya Pili kwanza tunakaribisha miradi ambayo imeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo suala la kutembelea kuangalia hiyo miradi ambayo inasuasua, kwa sababu kusuasua inawezekana ikawa tatizo ni mkandarasi ambaye amewekwa. Sasa kama itaonekana ni tatizo la mkandarasi tutachukua hatua kulingana na mkataba wenyewe.
Kwa hiyo, kama tatizo ni fedha nimeshasema fedha sasa hivi Awamu ya Tano imeshajipanga vizuri, fedha zipo za kuweza kukamilisha miradi hii ambayo tayari iweze kupata huduma ya maji kwa wananchi wetu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize
maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza
napenda niishukuru sana Serikali kwa kutupatia kiasi kidogo cha chakula katika Wilaya ya
Mpwapwa.
Kwa kuwa, Wilaya ya Mpwapwa ina Majimbo mawili, Jimbo la Mpwapwa na Jimbo la
Kibakwe, na kwa kuwa chakula hicho ambacho tumepatiwa ni kidogo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutuongezea chakula cha njaa Wilaya ya Mpwapwa?
Swali la pili, kwa kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wameacha kulima mashamba yao
wanalima vibarua ili wapate hela ya kununua chakula. Je, utakubaliana na mimi kwamba iko
haja sasa ulete chakula hicho haraka kwa Wilaya ya Mpwapwa na Wilaya ya Kongwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU -
(MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mbunge wa Jimbo
la Mpwapwa Mheshimiwa George Malima Lubeleje, kwamba Serikali inatambua jukumu lake la
kuwalinda na kuwasaidia wananchi wote wanaopatwa na matatizo mbali mbali, ikiwemo baa
la chakula.
Kuhusu swali lake la pili, tunafahamu umuhimu hiyo na tathmini itafanywa ili kuwezesha
upatikanaji wa chakula hicho kwa haraka.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo la Chilonwa na Jimbo la Mpwapwa yanapakana, na kwa kuwa matatizo ya barabara ya Jimbo la Chilonwa ni sawa kabisa na matatizo ya Jimbo la Mpwapwa, Kibakwe na Kongwa.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri utatusaidiaje wananchi wa Jimbo la Mpwapwa kuhusu barabara ya kutoka Lupeta - Bumila - Makutupa kwenda Mbori - Mang‟weta - Mlali mpaka Pandambili. Barabara hii iko chini ya TANROADS, lakini ni muda mrefu sasa haijatengenezwa, pamoja na barabara ya Mkanana – Majami pamoja na Nana. Nakuomba Mheshimiwa Naibu Waziri Serikali itoe tamko kuhusu barabara hii, ni lini itaanza kuzikarabati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema wiki iliyopita kwamba greda ni la zamani lakini makali yale yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii anayosemea Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ukitoka huku baada ya kuvuka Kibaigwa unafika sehemu inaitwa Pandambili, unapita ile barabara ambayo ni ndefu sana, inapita Mlali, inapita Cha Mkoroma, inapita Makutupa, katikati inapitia Mang‟weta mpaka unafika pale Mpwapwa Mjini ni barabara ndefu kwa kweli. Kijiografia ni barabara ambayo watu hawa zamani walikuwa wakipitia barabara ya Kibaigwa kuzunguka huku walikuwa na tatizo kubwa sana, kufunguka kwa barabara ile kwa kiwango kikubwa imesaidia sana watu wa eneo hilo. Barabara ile takribani mwezi uliopita niliipita mimi mwenyewe kwa gari yangu, nimeiona na kiufasaha ni kwamba ukiangalia katika vitabu yenyewe imejiainisha katika barabara za TANROADS kwamba ni miongoni mwa barabara zitakazofanyiwa matengenezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu kubwa ni kwamba Mheshimiwa Lubeleje, barabara hiyo itaendelea kutengezwa ili watu wa maeneo yale ambao najua suala zima la uchumi wa eneo lile unakua kutokana na ujenzi wa barabara ile, basi naamini kabisa Serikali kwa sababu imetenga katika bajeti ya mwaka huu wa fedha ukarabati wa barabara ile, ukarabati huo utaendelea kufanyika kama ilivyokusudiwa.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
25
Kwa kuwa Serikali ilikuwa imeniahidi kupandisha barabara ya Gulwe, Berege, Chitemo, Mima, Chazima, Igoji mpaka Seluka Ufufu. Barabara hii ni mbaya, Halmashauri haina uwezo. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini sasa mtapandisha hadhi barabara hii pamoja na kuweka lami barabara ya Mbande - Kongwa - Mpwapwa na Kibakwe?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumemuahidi na tunalifanyia kazi mara tutakapopata fedha za kutosha barabara hiyo tutaipandisha kama nilivyosema mwanzo nia ya Serikali hii ni kuhakikisha kwamba barabara zote zinakuwa nzuri na zinapitika wakati wote na pale tunapokuwa na fedha za kutosha tutahakikisha kwamba barabara zote tunazijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali ya nyongeza. Kwa kuwa katika kipindi hiki cha mvua barabara nyingi sana zimeharibika, mfano, Wilaya ya Mpwapwa; Kata za Matomondo, Lembule, Mlima, Bereje, Mkanana, Londo, Chamanda, Majami mpaka Nana kule. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kutenga fungu la kutosha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo kwa sababu zinapitika kwa shida?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAMISEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi na Mheshimiwa Lubeleje hivi karibuni tumekwenda Wilaya ya Mpwapwa pale kutembelea kuangalia baadhi ya huduma zikiwemo huduma za afya, huduma ya shule, takribani wiki mbili na nusu zilizopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nimeona changamoto ya barabara katika maeneo yale, lakini nimesema katika kila mgawanyo wa halmashauri una fungu lake. Jukumu letu kubwa ni hii bajeti iliyotengwa, ikishapatikana basi iende kuweka miundombinu, kwa sababu utengaji wa bajeti ni jambo moja na utekelezaji wa bajeti ni jambo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutajielekeza kuhakikisha pesa yote iliyotengwa angalau iweze kufika katika maeneo kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu inarekebishwa. Kwa hiyo, Mheshimwa Lubeleje kwa sababu na mimi nilifika kule nimeona hali jinsi gani ilivyo naomba tushirikiane kwa pamoja kuangalia kile kitakachowezekana tuweze kukifanya ili mradi wananchi wa Mpwapwa waweze kupata huduma ya miundombinu ya barabara.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, na mimi niulize swali moja dogo tu. Kwa kuwa vijiji vya Chipogolo, Mima, Pwaga, Kibakwe, Berege, Mbori na Chunyu vina idadi ya watu wengi sana, ni trading centers ambazo ni kubwa sana na kuna wafanyabiashara wengi.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, atakubaliana nami kwamba sasa ipo haja kwenda kufanya utafiti kuona kwamba vinaweza kupewa hadhi ya kuwa Miji Midogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri wazi kuwa juzi nilikwenda pale Mpwapwa, katika kuangalia ule mfumo wa maji kama vijana wa sekondari ya Mpwapwa wanapata maji na kuangalia huduma ya afya kama wanatumia mifumo ya electronic katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Wilaya ile ina Majimbo mawili, Jimbo la Kibakwe na Jimbo la Mpwapwa, lakini jiografia yake ni kubwa zaidi; na kwa sababu najua utaratibu wa kuomba maeneo hayo sasa kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo, maana yake mchakato wake unaanza katika ngazi za chini, kuanzia ngazi za vijiji, katika mikutano ya Baraza la Madiwani, halikadhalika katika WDC na Baraza la Madiwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakavyoona kuwa hiyo nafasi inatosha, basi nadhani michakato hiyo itaanza na Ofisi ya Rais, TAMISEMI itafanya tathmini kuangalia kwamba, basi kama kuna hadhi ya kuipa mamlaka ya Miji Midogo hatutasita kufanya hivyo. Kuhusu kuangalia kama vile vigezo vitakuwa vimefikiwa.
Kwa hiyo, kwa kushirikiana na Mheshimiwa George Simbachawene ambaye ni Waziri wa Nchi yuko eneo hilo, halikadhalika Mheshimiwa Lubeleje ambaye ni Mbunge wa Mpwapwa aliyeleta concern hii, nadhani tunaweza kufanya mchakato huo, basi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, haitasita ikiona kwamba pale mahitaji yanayotakiwa yaweze kufanyiwa hivyo.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mpango wa REA umesaidia sana kusambaza umeme katika vijiji vyetu, je, SIDO haiwezi kuwasaidia vijana wetu vijijini kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kukamua karanga, ufuta ili tuweze kupata mafuta kwa ajili ya kuwauzia wananchi wetu likiwemo Jimbo la Mpwapwa
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ya Serikali ni kwamba, kupitia kata na wilaya watenge maeneo ambapo miundombinu wezeshi ya umeme na maji itapelekwa pale. Pia Mamlaka ya Wilaya ibuni ni kiwanda gani kitengenezwe kwa kuangalia malighafi, nguvukazi, soko na teknolojia rahisi. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itawapa elimu na utaalam na inapobidi Ofisi ya Waziri Mkuu inayohusika na Uwezeshaji itaweza kuwawezesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee majibu ya swali la Mheshimiwa Mchafu. Mkoa wa Pwani kuna viwanda vikubwa vingi vitajengwa, hilo sina tatizo nalo. Kuna viwanda vikubwa vitajengwa Mkuranga mfano kiwanda cha kutengeneza tires na vigae, hiyo sina shida nayo. Kama nilivyomjibu Mheshimiwa Lubeleje, mtengeneze maeneo kwenye kata, muangalie rasilimali zinazopatikana, tuwapelekee umeme, tuwapelekee maji halafu wataalam watawaonesha kitu gani mtafanya kulingana na hulka zenu na ubunifu mlio nao.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi; na kwa kuwa Manispaa ya Dodoma imekamilisha vigezo vyote vya kupata hadhi ya kuwa Jiji; na kwa kuwa majengo ya Manispaa ya Dodoma yamejengwa kitaalam, yamefuata master plan, hakuna squatters. Ni lini Serikali sasa itatangaza Mji wa Dodoma kuwa Halmashauri ya Jiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Mheshimiwa Lubeleje anafanya rejea ya siku alipokuwa akiniambia suala la Jiji la Dodoma; lakini nadhani ombi lake alivyokuwa anazungumza vile tukiwa barabarani, Mungu amelitilia tunu juu yake kiasi kwamba sasa hivi naona Serikali yote kiukubwa wake yote inahamia Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili nadhani halina mashaka, ni taratibu tu zitakamilika hapa na kwa sababu michakato mipana inakwenda na Serikali yote inahamia Dodoma, uwanja wa ndege unaimarishwa, basi nadhani vikao sahihi vitakaa na kufanya mapendekezo haya. Ofisi ya Rais - TAMISEMI haitasita kwa sababu nchi kwa ujumla wake sasa, Serikali yote inahamia Dodoma.
Kwa hiyo, ni mambo ya kimchakato tu, Mheshimiwa Lubeleje avute subira na tunavyoendelea kuliimarisha Jiji letu la Dodoma, nadhani itakuwa ni sehemu ya fahari ya Tanzania. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nataka kuongezea kwenye swali lililouliza kwamba je, ni lini Dodoma itatangazwa kuwa Jiji?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tu Dodoma sasa ndiyo tunafanya jitihada za kuhamia kwa sababu tayari imeshaamuliwa kuwa ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu, kwa kawaida na kwa utaratibu ni lazima iwe Mamlaka ya Jiji. Kwa hiyo, utaratibu huu utakwenda sambamba na hii jitihada inayofanyika, lakini pia Dodoma ina faida kubwa kwamba walipokuwa wanatenga na kuitengenezea ramani yake, walitenga mipaka mikubwa, ina square kilometer zaidi ya 250,000. Kwa hiyo, ni eneo kubwa sana na linafaa na lina sifa zote kuwa Jiji. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa Naibu Waziri umeshatembelea Wilaya ya Mpwapwa na Wilaya ya Mpwapwa kuna vijiji ambavyo vina matatizo makubwa sana ya maji; kwa mfano Kijiji cha Tibwetangula, Lupeta, Bumila, Makutupa, Nana, Chimai, Salaza, Iyoma, Ngalamilo, Chamanga na Majami.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri utatembelea maeneo hayo, ili uone shida ya maji wanayopata wananchi wa Jimbo la Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimshukuru Mbunge huyu, tulifanya ziara ya pamoja pale katika sekondari yetu ya Mpwapwa tukabaini wanafunzi wanashindwa hata kufanya mitihani vizuri kwa sababu, maji hawapati. Reason behind kuna connection ya maji ya shilingi milioni nne tu! Tumeshirikiananae kwa pamoja, juzi hapa nimekwenda, sasa vijana wa sekondari ya Mpwapwa wanapata maji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lubeleje nakushukuru kwa uongozi wako mzuri, mradi ule umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo kweli, ukiangalia katika jimbo lake lile, ni pana! Jimbo lile sasa hivi na Jimbo la Kibwakwe lote linafanya Halmashauri ya Mpwapwa. Na nilipotembelea nikuhakikishie Mheshimiwa Lubeleje, nilifika mpaka katika Kijiji cha Makutupa, pale hata ukitokea msiba pale kupata maji maana yake wananchi wanaenda kuyapata maji mbali zaidi. Lakini Jimbo lako Mheshimiwa Lubeleje ni kwamba ukiliangalia jiografia yake lina tatizo kubwa sana, lakini hata nikapita maeneo mengine ya Chamkoroma kule watu msitu wamekata wote, maana yake hata vyanzo vya maji vya mtiririko maana yake vimepotea. Sasa nini tutafanya? Ulichoniomba nitembelee kule, lakini nakwambia nimeshatembelea in advance mpaka maeneo ya kambi kule ndani nikavuka na ule mto! Tutaendelea kufanya hivyo tena, lengo kubwa ni kubaini hizo changamoto kwa pamoja, tujadili kwa pamoja, tuondoe matatizo ya wananchi wetu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, matatizo ya Jimbo la Tarime Vijijini yanafanana na matatizo ya Jimbo la Mpwapwa. Kwa kuwa barabara ya kutoka Mbande - Kongwa - Mpwawa - Kibakwe tayari ilishafanyiwa upembuzi yanikifu na detailed design na ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya 2015 mpaka 2020 na ni ahadi ya Rais mstaafu pamoja na Rais wa sasa. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini sasa mtaanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali pili, unakumbuka Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu swali langu nilitoa ombi kwamba barabara ya kutoka Gulwe, kwenda Berege, Chitemo, Mima, Chazima, Igoji mpaka Ihondo na Fufu kwamba barabara hii iko chini ya Halmashauri ya Wilaya, lakini Halmashauri ya Wilaya haina uwezo wa kutengeneza kwa sababu haina fedha na imeharibika sana, mvua zimeharibu sana. Je, Mheshimiwa Waziri anawaambia nini wananchi wa kata hizo kwa sababu barabara hiyo inapitika kwa shida sana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoiongelea ya kutoka Mbande, Kongwa, Mpwawa hadi Kibakwe kama alivyosema ni barabara ambayo imeahidiwa na viongozi wetu wa Kitaifa, lakini vilevile ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 ya Chama Tawala cha CCM. Naomba nimwahidi na nilishaongea naye pamoja na Mheshimiwa Job Ndugai, Mbunge wa Kongwa pamoja na Mheshimiwa George Simbachawene, Mbunge wa Kibakwe wote tuliongea kwa undani kuhusu barabara hii na bahati nzuri tuliwasiliana vilevile na viongozi wenzangu Wizarani ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu. Kwamba barabara hii pamoja na kwamba kwenye bajeti iliyopitisha hatujaitengea fedha nyingi lakini ni lazima ianze kujengwa kuanzia mwaka huu wa 2016/2017 kama tulivyoahidi. Namhakikishia nitalisimamia hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili kuhusu barabara ya kutoka Gulwe, Berege, Kitemo, Uhondo na kuendelea, naomba naye nimhakikishie kwamba barabara hii iko chini ya halmashauri, tutawasiliana na wenzetu wa TAMISEMI, tuone ni namna gani tunaweza tukaitendea haki hii barabara ili ipitike siyo kwa tabu kama ilivyo sasa bali ipitike kwa mwaka mzima bila matatizo yoyote.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na kutenga shilingi milioni 15 kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Mima na shilingi milioni 35 kwa ajili ya kukamilisha Kituo cha Afya cha Mbori, je, Mheshimiwa Waziri haoni fedha hizi zilizotengwa ni kidogo kiasi kwamba vituo hivi vitachukua zaidi ya miaka mitano kukamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna majengo ya zahanati ya Kijiji cha Igoji Kaskazini na Igoji Kusini Salaze yamekamilika na kinachohitajika sasa ni huduma za dawa.
Je, yuko tayari sasa majengo haya yakaanza kutumika kwa ajili ya huduma za dawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Lubeleje, kama nilivyosema wiki iliyopita kwamba yeye ni greda za zamani lakini makali yale yale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Mima kimetengewa shilingi milioni 15 na Mbori shilingi milioni 35, Mbunge anasema fedha hizi hazitoshi. Hata hivyo, katika mchakato wa bajeti tulikuwa tunapokea mapendekezo mbalimbali ambapo wahandisi wetu walifanya analysis ya kila jengo linahitaji kiasi gani ili liweze kukamilika. Kama fedha hizi hazitoshi basi tutaangalia nini cha kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika jibu langu la swali la msingi la wiki iliyopita nilisema, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Afya na Kamati ya Bunge tulifanya zoezi moja ambalo tunaendelea kulifanya mpaka hivi sasa na tumeshapeleka maelekezo mbalimbali kwa Wakurugenzi wetu wa Halmashauri, wabainishe miradi yote ambayo haijakamilika halafu tuifanyie analysis tuone ni jinsi gani tutafanya ili mradi miradi hiyo yote iweze kukamilika. Kwa sababu ukiachia kwa Mheshimiwa Lubeleje sambamba na hilo kuna maeneo mbalimbali miradi mingi sana iliyojengwa miaka ya nyuma bado haijakamilika. Kwa hiyo, ndiyo maana Ofisi yetu ikaamua ni vyema tubainishe miradi yote na tuifanyie tathmini ya kina ili tujue tunahitaji pesa kiasi gani ili iweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuahidi Mheshimiwa Lubeleje kwamba lengo letu ni kukamilisha maeneo haya nikijua wazi kwamba Halmashauri ya Mpwapwa na Jimbo lake la Mpwapwa na Kibakwe ambapo kijiografia ni eneo kubwa sana, wananchi wake lazima wapatiwe huduma. Kwa hiyo, tuna kila sababu kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhakikisha huduma za wananchi hasa huduma za afya zinapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwamba vituo vya afya vimekamilika lakini kuna tatizo kubwa la ukosefu wa dawa na vifaa tiba, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyofanya siku chache zilizopita kutembelea Jimbo lake na kubaini huduma na changamoto mbalimbali, tutajitahidi kadiri iwezekanavyo vituo hivi viweze kufanya kazi ili wananchi wapate huduma.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, vilevile katika Jimbo langu la Mpwapwa kuna matatizo makubwa sana ya maji katika Vijiji vya Mima, Chitemo, Berega, Nzase, Lupeta, Bumila na Makutupa na kulikuwa na mradi mkubwa sana wa maji na mpaka sasa umechakaa. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuusaidia ule mradi uanze kuhudumia wananchi wa vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari na ndiyo maana inatenga bajeti na imetenga bajeti kwenye Wilaya zote ikiwemo pamoja na Wilaya ya Mheshimiwa Lubeleje. Katika malengo yetu tunakamilisha miradi inayoendelea, lakini pia, tunaomba Halmashauri mtuletee maombi ya fedha kwa ajili ya ukarabati wa miradi ya zamani ili iendelee kufanya kazi kama ambavyo nilijibu katika swali la msingi la Mheshimiwa Abood kule Morogoro kwamba, tunataka tuhakikishe kwamba, miradi yote inayoendelea inakarabatiwa, ili kuondoa matatizo ya uvujaji wa yale mabomba unaosababisha maji kupotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa tu kwamba, tuko pamoja na yeye na Serikali iko pamoja na Halmashauri yake. Kinachotakiwa watumie fedha tuliyowapa, lakini mwaka wa fedha utakaokuja basi walete maombi tena ili tuweze kutoa hiyo fedha.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa niliwahi kumlalamikia Mheshimiwa Naibu Waziri wakati tunakwenda Mpwapwa kwamba kuna vituo viwili vya afya ambavyo havijakamilika sasa ni miaka 10, Kituo cha Afya cha Mima na Kituo cha Afya cha Mbori na bajeti haijatengwa zaidi ya miaka 10. Je, unawaeleza nini wananchi wa maeneo hayo ya Mima na Mbori na kwamba vituo hivyo vitakamilika lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, siku tulipokwenda pale Mpwapwa nilipokuwa na Mzee Lubeleje nikawaambia watu wa Mpwapwa, Mzee Lubeleje huyu nimemwita kama greda la zamani lakini makali yaleyale, alikuwepo na sasa amerudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nlipofika pale Mpwapwa tulitoa maelekezo kwamba licha ya hivyo vituo anavyozungumza lakini Hospitali yao ya Wilaya walikuwa hawajaanza kutumia mifumo ya electronic. Siku nne zilizopita nimekwenda Hospitali ya Mpwapwa na mimi mwenyewe nilikuwa mteja wa kwanza kukata risiti ya mfumo wa electronic. Kwa hiyo, Mzee Lubeleje namuunga mkono kwanza katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nini tumefanya? Ndiyo maana nimeeleza toka mwanzo tuna maboma mengi yamekaa muda mrefu, mengine yamekaa miaka saba, mengine miaka nane, wananchi wameshafanya juhudi ya awali, ndiyo maana nimesema hapa jana Kamati ya Bajeti ya Bunge hili ilikaa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Afya na jana tumeshatoa maelekezo kwenda kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri 181 waainishe maboma yote yamefikia hatua kiasi gani na yanahitaji fedha kiasi gani, lengo ni maboma yote haya yaweze kwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukimaliza maboma yote tutakuwa tumepiga hatua moja kubwa sana. Imani yangu ni kwamba, haya maeneo mawili ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyasema ni miongoni mwa mambo ambayo tunaenda kuyafanyia kazi katika ule mpango mkakati mkubwa. Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imejipanga katika hili na tunajipanga siyo Wizara ya Afya peke yake, siyo TAMISEMI peke yake halikadhalika Kamati ya Bunge ya Bajeti jana kikao hicho kilifanyika.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni muda mrefu Wabunge tumekuwa tukiishauri Serikali kuwalipa wazee kiinua mgongo. Mimi tangu nimeanza Ubunge zaidi ya miaka 20 nadai hivyo na leo Serikali inasema wapo katika mipango, sasa mipango hii ni lini itaisha? Sisi tunaomba kama inawezekana katika bajeti hii wazee waanze kulipwa kiinua mgongo
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia majibu yale yale tu ya kwamba suala la kuwalipa pensheni wazee kama ambavyo imesemwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM Serikali itatekeleza, kilichobaki hivi sasa ni kwamba mpango huu mwanzoni ulikuwa umeshakamilika katika awamu lakini baadaye likaingizwa pia suala la watu wenye ulemavu, kwa hiyo, ikabidi tuanze kuangalia na mazingira mengine ya watu wenye ulemavu. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu hizi ziko ukingoni kukamilika na Serikali itaanza kuwalipa pensheni wazee. Kwa sababu katika utaratibu wa jambo lenyewe jinsi lilivyo upo muundo wake ambao ni kuanzisha kamati mbalimbali kuanzia chini mpaka Taifa ambazo nazo pia zimeanza kufanyiwa kazi na zitakamilika muda siyo mrefu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge mtuamini kwamba siyo maneno tu, lakini mikakati hii imeshakamilika Serikali itawalipa pensheni wazee kama ambavyo nimesema hapo awali.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa, Wilaya ya Mpwapa na Kongwa kuna mabonde mazuri sana ya maji na yanatiririsha maji mwaka mzima. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga scheme ya umwagiliaji katika vijiji vya Godegode, Nzovu, Bori, Msagali, Tambi, Mang’weta, Chamkoroma, Mseta na maeneo mengine ili scheme hii iweze kusaidia kilimo cha umwagiliaji na kusaidia kuondoa tatizo la njaa, katika maeneo hayo?(Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, mapendekezo yake ya kutaka scheme hizo za Godegode na zingine mara nyingi tunaziandaa wakati tunatayarisha bajeti, kwa mwaka huu katika mapendekezo ambayo tulikuwa tumeyapitisha kwenye bajeti kwanza ni kuendeleza na kukamilisha scheme ambazo tayari zilikuwa zinaendelea na zina makandarasi, tukasema awamu hii tutaendelea kwanza tufanye usanifu katika miradi mingine itakayofuata baada ya kukamilisha hii ambayo inaendelea. Kwa hiyo Mheshimiwa, Godegode kwanza tuangalie zile scheme ambazo tayari tunazikamilisha halafu tutaanzisha na hizo zingine mpya. Tutazifanyia usanifu Tume ya Umwagiliaji ndiyo kazi kubwa itakayofanya mwaka huu wa fedha katika kuhakikisha maeneo mengi ambayo yanaweza kufanyiwa umwagiliaji tuweze kuyafanyia kazi.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa maeneo ambayo ameyataja, kwa mfano Iyoma, Mzase na Bumila kwamba kazi inaendelea. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kufuatana na mimi kuona kama kazi hiyo imeanza? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mji wa Mpwapwa ni mji wa zamani sana, una zaidi ya miaka 100 sasa tangu mwaka 1905 lakini vyanzo vya maji ni vilevile, kuna maji baridi na kuna maji ya chumvi, na kuna maeneo ambayo wanaweza wakachimba visima vya maji tukapata maji baridi ili wananchi wa Mpwapwa waweze kupata maji baridi. Je, Serikali iko tayari kutuma watafiti waende waanze kufanya utafiti ili kuongezea visima vya maji kwa Mji wa Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Lubeleje, ambaye mimi namwita greda la zamani lakini makali yale yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niko tayari, tena hata kipindi hiki cha Bunge tunaweza tukatoka Mpwapwa ni karibu hapa tukaenda kutembelea hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, katika suala zima la kufanya utafiti, ni kweli, ukiangalia Mji wa Mpwapwa siku ile tumekwenda pamoja Mheshimiwa Mbunge, chanzo cha maji sasa hivi kimeelemewa na hata ile changamoto kubwa ni kwamba uharibifu wa mazingira ndiyo umekuwa ukiathiri sana suala zima la maji yanayopatikana katika Mji wa Mpwapwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hivi sasa kuna watu wako site wanafanya utafiti maeneo mbalimbali lakini kwa uzoefu wako uliokuwa nao na kwa kushirikiana na watafiti hawa kuangalia jinsi gani tutafanya kwa pamoja kama Serikali, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Lubeleje, katika safari yetu ya pamoja tutaangalia, tutaonana na wataalam wa maji katika ofisi yangu kama sehemu ya awali. Mwisho wa siku ni kwamba watu wa Jimbo lako la Mpwapwa, lakini Halmashauri yote ya Mpwapwa kwa ujumla waweze kupata fursa ya maji kama Mbunge wao anavyowapigania.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa REA inafanya kazi nzuri sana na imesambaza umeme karibu nchi nzima na Mpwapwa kuna vijiji ambavyo havijapata umeme, kijiji cha Kibojani, Mgoma, Mzogole, Viberewele, Sazima, Mkanana, Igoji Kaskazini na Igoji Kusini pamoja na Iwondo.
Je, Mheshimiwa Waziri, utakuwa tayari kupeleka umeme katika vijiji hivi kwa sababu umeme ndio uchumi wetu na ndio maendeleo yetu katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa tuko tayari kupeleka umeme kwenye vijiji vyote vya Mheshimiwa Lubeleje. Mheshimiwa Lubeleje ni Mbunge mkongwe, nadhani kati ya Wabunge wote ambao tuko hapa Mheshimiwa Lubeleje ni wa zamani sana kwa hiyo, hatuwezi kumuangusha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lubeleje nikuhakikishie vijiji vyako vyote vya Lugoma na Kiwelewele vitapelekewa umeme kupitia REA Awamu ya Tatu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza. Kabla ya kuuliza swali, naomba niwape pole wananchi wa Kitongoji cha Chinyika na Kwamshango kwa maafa waliyopata ambapo watu watano wamefariki kwa kusombwa na maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize swali. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa na anajua vijana wengi sana katika Wilaya ya Mpwapwa hawana ajira na hizo fedha zinazotolewa ni kidogo sana. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuongeza fungu la fedha hizo ili vijana wengi waweze kupata ajira pamoja na wa Wilaya ya Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna changamoto ya Mifuko hii ya Uwezeshaji ya Mitaji na Mikopo kwa vijana hasa kwa kushindwa kukidhi mahitaji ya vikundi vingi ambavyo vimekuwa vikiomba mikopo hii. Tunachokifanya kama Serikali ni nini? Sisi kazi yetu kubwa tunayoifanya kwanza kabisa ni kuwatambua vijana nchi nzima kutokana na mahitaji yao na kazi, pili ni kuwarasimisha na tatu ni kuwajengea uwezo wa kifedha kupitia mifuko mbalimbali ya Serikali lakini na kushirikiana na wadau mbalimbali. Nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na jitihada za kuwa-invite wadau wengi zaidi wa maendeleo ya vijana ili watusaidie katika eneo hili la uwezeshaji na kuongeza mfuko wetu ili tuweze kuwafikia vijana wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho, Bunge hili ndilo ambalo tunapanga bajeti, muone pia haja ya kutuongezea fedha kwa ajili ya Mfuko wa Mendeleo ya Vijana ili tuwafikie vijana wengi zaidi nchi nzima.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru
sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali hayo. Sasa nina maswali
mawili.
Kwa kuwa, MSD imetengewa fedha shilingi bilioni 251 kwa ajili ya kununua
madawa, kwa kuwa kuna upungufu mkubwa sana wa madawa katika hospitali
zetu wagonjwa wakienda hospitalini wanaandikiwa vyeti na Madaktari
wanawaambiwa mkanunue dawa maduka binafsi. Je, kwa nini hizo fedha bilioni
251 zisipelekwe moja kwa moja MSD badala ya kukaa Hazina na wanapelekewa
kidogo kidogo?
Swali la pili, kwa kuwa, katika Jimbo langu la Mpwapwa kuna Vituo vya
Afya, vya Mima, Mbori, Berege, Mkanana pamoja na Zahanati za Chamanda,
Igoji Kusini, Kibojane Lupeta, Makutupa, Majami, Nana, Mgoma havijakamilika
hadi sasa na ujenzi huu sasa umechukua zaidi ya miaka kumi. Je, Serikali ina
maelezo gani kwa wanachi wa vijiji hivyo, kwa sababu wananchi wa vijiji hivyo
hufuata tiba zaidi ya kilomita 15?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA
WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa fursa hii. Swali lake la kwanza
kuhusu kwa nini Serikali isipeleke pesa moja kwa moja kutoka Hazina kwenda
MSD moja kwa moja tayari nilikwishatoa maelezo ya msingi, kwenye jibu la
msingi; kwamba Idara za Serikali zinazopewa vifungu ni Serikali Kuu tu na Ofisi za
Wakuu wa Mikoa na pamoja na Wizara. Kwa hivyo, MSD hawezi kupewa pesa
moja kwa moja kutoka Hazina ambapo ni Serikali Kuu na bila kupitia Wizara ya
Afya, kwenye kifungu kile ambacho sasa tumepewa kinaitwa kifungu 2005 chini
ya Mfamasia Mkuu wa Serikali. Kwa hivyo, utaratibu huo ni lazima uzingatiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii pia kukanusha kauli
yake ya kwanza aliyoisema kwamba kuna upungufu mkubwa wa dawa,
hapana, hakuna upungufu mkubwa wa dawa nchini. Kwa taarifa tulizonazo sisi
na ukweli ni kwamba upatikanaji wa dawa (Drug availability) kwa sasa ni wa
kiwango cha asilimia 84 kwa mujibu wa taarifa za wiki iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili lina maelezo yake sipendi kupoteza muda
wako, naomba nisiyatoe hapa lakini huo ndiyo ukweli. Serikali katika Awamu hii
ya Tano imewekeza sana kwenye dawa na ndiyo maana tumepewa bilioni 251.5
ukilinganisha na bilioni 31 kwenye mwaka wa fedha kabla ya huu. Bilioni hizo
mpaka sasa tunavyozungumza kufikia Desemba tulikuwa tumeshapokea bilioni
84 kutoka Hazina kwa ajili ya manunuzi ya dawa. Kwa hivyo upatikanaji wa dawa
ni wa kutosha pengine hizo anazozisema Mheshimiwa George Malima Lubeleje ni
hadithi za zamani kidogo anapaswa kufanya utafiti wa kina.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu kukamilisha zahanati na
vituo vya afya kwenye jimbo lake, naomba nitoe rai kwake yeye mwenyewe,
Halmshauri yake pamoja na kwa Wabunge wengine wote na Halmashauri zote
nchini kuzingatia ukweli kwamba, ukamilishaji wa majengo ya zahanati na vituo
vya afya inapaswa kuwa kipaumbele cha Halmashauri husika. Kwa sababu miradi hii ya maendeleo kama ambavyo imewekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi
kwamba tutajenga zahanati kila kijiji, kituo cha afya, kila kata hatuwezi kusema
sasa tunapewa pesa na Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ili tujenge hapana. Sisi
sote tuna wajibu wa kutimiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima katika Halmashauri zetu tuweke
kipaumbele kwenye kukamilisha miradi ya zahanati ambayo imeanzishwa na
wananchi kwa kujitoa sana kwenye Halmashauri tukakamilishe zahanati hizo ili
ziweze kuanza kufanya kazi. Wala tusitarajie kwamba sasa Wizara ya Afya
itatuletea pesa ili tukamilishe. Pesa ile inapaswa kutoka kwenye ownsources za
Halmashauri na maamuzi ya kufanya hivyo wanayo Waheshimiwa Wabunge na
Waheshimiwa Madiwani kwenye Halmashauri zao.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ina upungufu mkubwa sana wa chakula pamoja na Wilaya za Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida; na kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna Halmashauri za Wilaya 55 ambazo zina upungufu mkubwa sana wa chakula na Serikali ina chakula cha kutosha kwenye maghala. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali itaanza kusambaza chakula cha bei nafuu kwasababu hivi sasa debe la mahindi ni shilingi 20,000 na mfuko wa sembe ni shilingi 40,000 ni lini Serikali itaanza kusambaza chakula cha bei nafuu Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa pamoja na hizi Halmashauri 55?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Waheshimiwa Wabunge, kama mnavyokumbuka tulishakuja kwenye Bunge hili mapema kueleza na kutoa taarifa ya tathmini ya kina ambayo Wizara imefanya kuhusiana na usalama wa chakula na katika taarifa ile kama mlivyosikia Waheshimiwa Wabunge tuliweza kuainisha maeneo ambayo yana upungufu mkubwa, lakini vilevile katika taarifa ile tulieleza kwamba Serikali imejidhatiti vilivyo kuhakikisha kwamba upungufu ambao unaelekea kutokea kati ya mwezi Januari na Aprili kwamba utashughulikiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, nimahakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zinaendelea ili kuhakikisha maeneo yale ambayo yana upungufu kwamba wananchi wanapata chakula cha bei, nafuu kwa hiyo, naomba uvute subira taratibu zinaendelea.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kila Halmashauri ya Wilaya ina Mratibu wa TASAF na waratibu ndiyo wameandikisha kaya
maskini, walijua kabisa kwamba kaya hii ni maskini. Hivi
karibuni kuna kaya ambazo zimeondolewa kwamba hazina sifa na wanaambiwa warejeshe fedha, wengine ni wazee kabisa. Mheshimiwa Waziri nani mwenye makosa, ni mratibu aliyeorodhesha au ni yule ambaye ameambiwa kwamba alipe hizo fedha?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia utekelezaji mzima wa mpango huu, lakini zaidi namna ambavyo amekuwa akifuatilia kaya zile ambazo zimeondolewa. Mpaka sasa tumeshaondoa kaya 63,819 katika maeneo 162 ya utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, napenda tu
kusema kwamba, wale ambao wamelengwa kuondolewa katika uhakiki huu ni zile kaya ambazo hazikustahili kuingizwa katika mpango. Tumekuwa tukishuhudia pia katika zoezi hili, kama mnavyotambua wakati wa utambuzi na uandikishaji, chombo kikuu kinachoshiriki ni mkutano wetu mkuu wa kijiji au katika shehia lakini unakuta wengine waliwaingiza wenye uwezo matokeo yake baadaye wanajikuta wanakuja kuondolewa tunakuja tunasikia maneno kama hayo.
Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba,
kama kweli kaya ilikuwa ni maskini, ikawa imejiboreshea maisha haikutakiwa kuondolewa bila kufuata vigezo vya msingi. Tumeanza kufanya zoezi hili, tumeshawaandikia Wakurugenzi wote tangu mwezi Februari waweze kupitia
kwa kina. Napenda tu kusema kwamba waratibu wengi pia walishiriki, hawakuwa makini katika ufuatiliaji na katika tathmini zao na ndiyo maana tayari tumeshawachukulia hatua waratibu zaidi ya 91 na tutaendelea kufanya hivyo kila ikibidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile napenda tu kusema
kwamba, wale ambao tunawalenga ni wafanyabiashara, unakuta kuna mtu alikuwa ana bucha na mambo mengine ameingizwa, haiwezekani! Vilevile unakuta wengine ni watumishi wa umma wameingizwa katika mpango hawastahili kuanzia siku ya kwanza, hao ndio ambao tunawalenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda tu
kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa namna ambavyo wamekuwa wakifuatilia suala hili. Tutaendelea kuwafuatilia na tutaendelea kuchukua hatua. Kwa wale ambao ni maskini kweli kwanza wanatakiwa warudi kwenye mpango na si kumfuatilia aweze kurudisha fedha.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa kuchimba visima vya maji katika kijiji cha Bumila, Iyoma na Mima. Hata hivyo, sasa ni miezi nane tangu visima vimechimbwa, hakuna pampu zilizowekwa, hakuna mabomba ya kusambaza maji wala matenki. Je, Serikali inasemaje kwa wananchi wa vijiji hivi ambao wana shida kubwa sana ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 na bajeti hiyo bado inaendelea. Kwa kutumia nafasi hii nimuagize Mkurugenzi wa Mheshimiwa Lubeleje, suala la pampu ni rahisi sana, maeneo yote ambayo visima vimeshachimbwa tunahitaji quotation ambayo tunaiweka kama ni certificate, ukiileta tunatoa hela ili uweze kununua pampu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kama inahitajika miundombinu ya ujenzi wa tenki na mabomba ya kusambaza maji na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, Mheshimiwa Lubeleje Mkurugenzi wako afanye usanifu wa haraka, atangaze tender. Kama ana upungufu wa wataalam Wizara ya Maji tuko tayari, atuandikie barua ili tuweze kumpa support ya kumpelekea wataalam ili kazi hiyo ifanyike haraka wananchi wa Jimbo lako Mheshimiwa Lubeleje waweze kupata maji kwa haraka.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Meneja wa TANROADS wa Mkoa ameshaikagua barabara ya kutoka Gulwe – Berege –Chitemo – Mima – Chazima - Igodi Moja – Igodi Mbili mpaka Seluka; na kinachosubiri sasa hivi ni barabara hii ipandishwe hadhi ili iwe barabara ya Mkoa.
Je, Mheshimiwa Waziri anasemaje na kwa ombi hilo Serikali inawaambiaje wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lubeleje, grader la zamani, makali yale yale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Lubeleje swali hili alikuwa akiliuliza mara kadhaa na hapa umesema kwamba ni kweli. Kwa sababu naamini wenzetu wa Wizara ya Ujenzi jambo hili walishalisikia na ninakumbuka Naibu Waziri wa Ujenzi siku ile alikuwa analizungumza suala hili kwamba jambo hili linafanyiwa kazi. Imani yangu ni kwamba kwa sababu barabara hii ni ya kimkakati nami nakiri wazi kwamba na wewe barabara hii inakuhusu katika eneo lako. Basi naamini Wizara ya Ujenzi itafanya kila liwezekanavyo barabara hii kuipa kipaumbele katika yale matakwa ya wananchi wa eneo hilo.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kuna miradi imeshaanza kutekelezwa, kwa mfano, Wilaya ya Mpwapwa tulikuwa na matarajio ya kujenga barabara za lami, Mpwapwa Mjini kilometa 10; na kwa kuwa fedha iliyoletwa ni kidogo sana na ni karibu Majimbo yote kuna viporo; je, fedha iliyobaki Serikali italeta fedha zote kwa Wilaya zote? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya kujenga Vituo vya Afya Mima na Mbori ni kidogo sana na ndiyo maana havijakamilika sasa zaidi ya miaka kumi; je, Serikali itaongeza fedha ili tukamilishe vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Lubeleje kwa jitihada zake za kufuatilia maendeleo ndani ya Mpwapwa na ndani ya Wilaya nzima ya Mpwapwa, wananchi wako wanakutegemea sana kaka yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni kupelekwa fedha zote. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, upelekaji wa fedha hutegemea mapato ya Serikali na hivyo fedha hizi zinapopatikana, lengo la Serikali ni kuhakikisha bajeti yetu inatekelezeka kwa asilimia 100. Kwa hiyo, fedha hizi tutakapokuwa tumezipata fedha zote zitapelekwa na miradi yote tuliyopanga itatekelezwa kama ambavyo tulipitisha bajeti yetu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la Vituo vya Afya kuongeza bajeti, ni imani yangu Wizara ya Afya watakapoleta bajeti yao hapa tutaiona na tumelizingatia hilo, vituo vyote vya afya ambavyo vimejengwa miaka mingi havijakamilika tumevizingatia katika bajeti yetu ya mwaka huu 2017/2018.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijiji vya Makutupa, Mlembule, Tambi, Bolisazima na Mgoma tayari nyaya na nguzo zimeshawekwa bado transfoma. Sasa namuuliza Naibu Waziri, vijiji hivi vitapata lini transfoma ili waweze kuanza kupata huduma ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Lubeleje, Mbunge Mkongwe katika Bunge hili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kulikuwa na transfoma mbili mbovu katika Jimbo lake na jana tulikuwa tunawasiliana na Meneja na amenihakikishia kwamba mwisho wa wiki hii transfoma mbili zitapatikana. Nimpongeze sana Mheshimiwa Lubeleje kwa niaba ya wananchi wake na nimwambie kwamba transfoma hizi mbili zitapatikana Ijumaa (kesho kutwa) mwezi huu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wazabuni wanaohudumia chakula Mpwapwa High School, Mazai Girls’ School pamoja na Berege Secondary School form five na six sasa ni zaidi ya miaka miwili hawajalipwa na bado wanahudumia na wamekopa benki. Mheshimiwa Naibu Waziri amefika Mpwapwa sekondari na ameona hali ilivyo na wanataka kukamatiwa nyumba, je, hawa wazabuni watalipwa lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lubeleje, Senior MP wa Bunge hili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na kwa bahati mbaya kwa Halmashauri ya Mpwapwa siyo kesi ya wazabuni wa chakula peke yake isipokuwa kuna kesi ya wakandarasi mbalimbali ambao wamefanya kazi pale Mpwapwa lakini bado hawajalipwa. Hili napenda hasa nimuelekeze Mkurugenzi wetu wa Halmashauri ya Mpwapwa kwamba madeni mengine ambayo hayajalipwa ni suala la kuangalia Menejimenti ya Kurugenzi yake jinsi gani itafanya kuweza kuyalipa.
Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Lubeleje kwamba Mpwapwa ndiyo maeneo ya priority kwa sababu ofisini kwangu hata watu wa CRDB walifika kulalamikia Halmashauri ya Mpwapwa. Hata hivyo, ukiachia hizo fedha kutoenda lakini kuna mambo mengine ya ziada lazima tuyasimamie. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba tutafanya kila liwezekanalo hasa kwa wazabuni wa Mpwapwa na maeneo mengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuweze kuwalipa fedha hizi ili wasije wakataifishiwa mali zao na mabenki ambazo ziliwekwa kama dhamana wakati wanachukua mikopo. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa magari ya kunyonya maji machafu na kuzoa taka siyo lazima tu iwe kwenye Manispaa au Majiji, hata Wilaya zetu tunahitaji magari ya kunyonya maji machafu na magari ya kuzoa taka. Je, Serikali ina mpango gani kupeleka gari la kunyonya maji machafu pamoja na kuzoa taka katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI naomba kujibu swali la Mzee wangu Lubeleje, mimi namuita greda la zamani makali yale yale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mzee Lubeleje naomba tuiweke katika vipaumbele vyetu vya Halmashauri, naomba nikusihi Mheshimiwa Lubeleje katika mpango wenu wa Halmashauri hilo jambo mkiliainisha, na sisi katika kupitisha bajeti tutalipa kipaumbele. Ninajua kwamba kweli ni jambo la msingi kufanya usafi na kuwa na mitambo hii ya kuzolea taka na kunyonyea maji, kwa hiyo mkiweka katika kipaumbele, mchakato wa bajeti ujao kama Mpwapwa mtaweka kipaumbele basi sisi hatutasita kuhakikisha jambo hilo tunaliwekea kipaumbele hilo ili Mpwapwa mpate gari la kunyonyea maji taka.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwanza napenda niipongeze sana Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kuanza kujenga barabara ya lami kuanzia Mbande kwenda Kongwa - Mpwapwa mpaka Kibakwe. Sasa swali langu ni hivi, je, hii barabara ikishafika Njia Panda ya Kongwa inaendelea moja kwa moja mpaka Mpwapwa? Hilo ndiyo swali langu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, barabara ya Mbande –Kongwa – Mpwapwa mpaka Kibakwe ni barabara moja. Tumeianza na tutahakikisha tunaikamilisha kama ambavyo imeandikwa katika Kitabu cha Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 hadi 2020.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatuishii Kongwa, tutaendelea na ujenzi wa hiyo barabara kama ambavyo kwenye Ilani tumeahidi.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii nisema kwamba wakati nikitembelea barabara hii, wananchi wa Kongwa walikusifu sana. Na mimi niombe nichukue fursa hii, pamoja na kwamba pengine siyo sahihi, lakini ni muhimu nizifikishe zile sifa za wananchi wa Kongwa ambao walikuwa hawategemei kama hiyo barabara tutaijenga. Na mimi niliwahakikishia hii barabara iko katika ilani na ahadi zote tulizoweka katika ilani tutazikamilisha pamoja na barabara hii ya kutoka Mbande – Kongwa – Mpwapwa hadi Kibakwe kwa Mheshimiwa Simbachawene.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, nilishamwomba Mheshimiwa Waziri kwamba, wataalam wa utafiti wa visima vya maji, visima ambavyo vitatoa maji baridi wafike na kufanya utafiti wa visima hivyo. Kwa sasa wananchi wa Mji wa Mpwapwa wanatumia maji ya chumvi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu ombi langu hilo la kutafiti visima vingine vya maji baridi, ni lini atalitekeleza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, ameomba kupata watafiti wa kuweza kugundua maji yaliyoko chini ya ardhi kama yana chumvi au hayana chumvi. Utaalam wa namna hiyo, kwanza haupo. Ni kwamba, lazima kwanza tuchimbe, tuyapate yale maji tukayapime ndipo tutajua yana chumvi na chumvi kiasi gani na kama inahimilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tutakachofanya ni kwamba, tunakwenda kufanya tu tafiti kuona kwamba maji yapo mahali fulani, yatachimbwa halafu tutayapima na kuweza kuona. Kwa hiyo, wataalam hawa tutawapeleka kama anavyoomba, lakini kwa maana ya kujua maji yaliyopo pale, ni lazima kwanza tuyachimbe ndiyo tuweze kujua kama yana chumvi au hayana chumvi.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza utaratibu wote umeshafuatwa, vijijji vimekaa, Kamati ya Maendeleo ya Kata imekaa, Full Council imekaa na mpaka kwenye Kamati ya Ushauri ya Mkoa na ni ombi la muda mrefu sana. Wananchi wa Mkanana wanapata shida, kwanza hakuna mawasiliano ya barabara kabisa na ninakuomba tukimaliza Bunge tuende kule upite ile njia uone kama inapitika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, kwa kuwa kwenye swali langu limetaja kuna umbali kutoka Mkanana, Chibwegele mpaka Chitemo ni kilometa 45 ndipo wananchi wanafuata usafiri. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, utakuwa tayari kukubali ombi langu tufuatane na wewe sasa baada ya Bunge hili, ukawaone watu wa Mkanana, Chibwegele, wanavyopata shida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri nipokee kama taratibu zote mpaka katika ngazi ya mkoa zimekamilika tutafanya ufuatiliaji kuangalia utaratibu umefanyika lini. Kama sio yale maombi ya zamani ambayo mwanzo yalikuwa hayakukizi vigezo, kama haya mapya, ofisi yangu nadhani inafanya uchambuzi wa maeneo mbalimbali katika maeneo haya mapya.
Mheshimiwa Spika, lakini katika jambo lingine la pili, Mheshimiwa mbunge ameomba ikiwezekana twende pamoja, naomba nikueleze wazi na mimi niko pamoja kwa sababu, najua Mheshimiwa Mzee Lubeleje watu, wanahistoria hawafahamu kwamba Mpwapwa yote ilikuwa Jimbo moja wakati huo, baadaye ikagawanyika na Jimbo lingine la Kongwa. Kwa hiyo, alifanya juhudi hizi miaka mingi sana katika michakato mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niwahakikishie Wana-Mpwapwa, Wana-Kongwa na sehemu uliyosema, tutafika pale tutabaini miongoni mwa mambo hayo, lakini hasahasa tatizo la barabara katika Wilaya ya Kongwa na Wilaya ya Mpwapwa, nini tufanye kwa pamoja kuwasaidia wananchi hawa ambao kwa kiwango kikubwa wameisaidia sana Serikali hii katika mambo mbalimbali.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri, niipongeze sana TASAF kwa kazi nzuri, sasa nina maswali mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kwamba kazi hii kweli imeanza Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado haijakamilika katika vijiji ulivyotaja. Ni lini kazi hii itakamilika ili maeneo haya yaweze kupata huduma ya maji kwa sababu kuna shida kubwa sana ya maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ina mpango gani wa kuongeza vijiji katika mpango wa kuchimbiwa mabwawa, katika vijiji vya Kisisi, Ngalamilo, Iwondo pamoja na Nana kwa sababu hawa nao wana matatizo makubwa sana ya maji. Ni lini wataanza shughuli hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lubeleje, Senior MP kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lini miradi hii itakamilika na kuweza kutoa huduma ya maji, kwanza naomba nimuahidi katika Bunge hili la bajeti linaloendelea nitaomba mimi na Mheshimiwa Lubeleje twende katika miradi hii tukaiangalie kwanza halafu tushauriane vizuri tukiwa site kwa sababu najua Wilaya ya Mpwapwa ina tatizo kubwa sana la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vijiji vingine ambavyo ameviorodhesha ni kweli, nafahamu maeneo kwa mfano hata kule Tambi hali ya maji ni mbaya mpaka wanakuja huku Chamkoroma kutafuta maji. Kwa hiyo, tuna kila sababu kuhakikisha kwamba Wilaya ya Mpwapwa tunaipa kipaumbele. Pia katika ziara yangu hii nikiwa na Mheshimiwa Mbunge tutaambatana na wataalam kutoka kwenye Halmashauri tuweze kufika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Makutupa ambako Mheshimiwa alikuwa anapigia kelele sana muda mrefu jinsi gani tutafanya kuweka mipango sahihi kusaidia shida ya maji katika Wilaya yetu ya Mpwapwa.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa mwaka 2015 wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais alituahidi kilomita10 Mpwapwa Mjini na kwa kuwa bajeti iliyopita tumepewa kilomita moja tu, hata Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo analifahau hilo. Je, Mheshimiwa Waziri ataahidi wananchi wa Mji wa Mpwapwa kwamba hizo kilomita 10 zitakamilika?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Naibu wangu kwa ufafanuzi mzuri wa maswali ya awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika swali la Mheshimiwa Lubeleje, ni kweli anachozungumza na mimi na yeye tulikuwa pamoja pale Mpwapwa Mjini kukagua barabara na ndiyo maana tumempelekea injinia mzuri sana kupitia TARURA na injinia yule wakati tunafanya ukaguzi wa Shule ya Sekondari ya Mpwapwa nilimpa maelekezo maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimtoe hofu Mheshimiwa Lubeleje ule ujenzi wa lami unaoendelea pale Mpwapwa Mjini tutaukamilisha na itakapofika 2020 Mheshimiwa Lubeleje awe na uhakika kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais itakuwa imekamilika na kuthibitisha kwamba Mbunge wao amefanya vyema kusimamia eneo hilo. Ahsante sana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa lengo la Serikali kuchukua vyanzo vingi vya Halmashauri za Wilaya ilikuwa ni kusaidia ruzuku ya kutosha kwenye Halmashauri hizi. Lakini kwa kuwa ruzuku inayotolewa haitoshelezi kabisa kwa Halmashauri hizi kujiendesha.
Sasa swali langu, naishauri Serikali kwamba je, Serikali inaweza kurudisha baadhi ya vyanzo vya mapato kwa Halmashauri ili nazo ziweze kujiendesha badala ya kusubiri ruzuku na ruzuku yenyewe inachelewa sana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu wangu katika swali la msingi nilipenda kujibu swali la Mheshimiwa Lubeleje ambapo mimi ninamuita greda la zamani makali ya yale yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna vyanzo mbalimbali vilichuliwa na Serilkali Kuu. Hata hivyo, kwa mamlaka tuliyopewa tutafanya namna ili kuhakikisha kwamba mapato, hata hayo ya vyanzo vilivyobaki yaweze kukusanywa vizuri.
Mheshimiwa Spika, ilikuwa kwamba hata miongoni mwa vyanzo tulivyokuwa navyo ukusanyaji ulikuwa na changamoto kubwa na ndiyo maana katika program zetu hivi sasa tunafanya namna ili tuweze kutumia mifomu ya electronic kwa ajili ya uongezaji wa mapato.
Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishieni kwamba sasa hivi Wizara ya Fedha imefanya commitment kwamba fedha zote zilizokusanywa zipelekwe na ndiyo maana mpaka leo hii ninavyozungumza katika quarter ya kwanza zaidi ya shilingi trilioni moja imechukuliwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika OC na miradi ya maendeleo.
Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba kutokana commitment ya Serikali katika ukusanyaji wa mapato jambo hili litakwenda vizuri; na hatimaye Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaweza kutimiza wajibu wake kama inavyokusudiwa.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, nina maswali mawili.
Swali la kwanza, kwa kuwa MKURABITA katika Wilaya ya Mpwapwa walichagua vijiji viwili; Kijiji cha Inzomvu na Kijiji cha Pwaga, lakini kwa upande wa Kijiji cha Pwaga mambo ni mazuri, mradi ulitekelezwa, masijala ilijengwa na wananchi walipewa Hati za Kimila. Lakini katika Kijiji cha Inzomvu hakuna kilichofanyika, baada ya kupima mashamba wananchi walipewa mafaili tu wakaenda nayo majumbani, hakuna chochote na ofisi ya masijala haipo.
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi kwamba ipo haja sasa ya Serikali kuleta muswada hapa ili tubadilishe chombo hiki MKURABITA ambao unategemea zaidi fedha za mfadhili na fedha za Serikali ni kidogo sana ili tubadilishe uwe mfuko wa urasimishaji ili wadau wengi waweze kuchangia na chombo hiki kiwe na fedha za kutosha ili wananchi wengi waweze kunufaika?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi kusikia kwamba Mpwapwa iliingia katika majaribio, walipata vijiji viwili, kijiji kimoja kinafanya vizuri kingine hakijafanya vizuri. Nimuombe tu ndugu yangu, Mheshimiwa George Malima Lubeleje apange muda anaoona yeye inafaa ili mimi na yeye twende katika kijiji hicho ambacho kimesahauliwa na mimi nikajifunze nikajue kimetokea nini, nichukue hatua ili vijiji hivyo pacha viweze kufanana katika utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kwamba kuletwe muswada utakaobadilisha chombo hiki, Serikali inapokea rai hii, lakini nataka nieleze kwamba kama nilivyosema tangu mwanzo tunakusudia kuanzisha Mfuko Maalum wa Urasimishaji, wakati wa kuanzisha mfuko maalum wa urasimishaji ikionekana haja iko ya kubadili sheria, suala hilo litazingatiwa na taratibu za kubadilisha sheria zinafuata ngazi kwa ngazi, itatekelezwa kadri Serikali itakapoona inafaa.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Swali langu ni kwamba, kwa kuwa kuna waajiri ambao wanakata mshahara lakini hawapeleki fedha hizi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Je, Serikali inawachukulia hatua gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria kila mfanyakazi aliyeandikishwa na anayekatwa makato yake kwa ajili ya hifadhi ya jamii yanapaswa kuwasilishwa katika mfuko husika. Kinyume na kufanya hivyo ni kukiuka taratibu za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana baada ya kuziangalia sheria zetu tukafanya marekebisho ya mwaka 2016 katika Sheria Na. 7 ya Mwaka 2004 ambayo inashughulikia masuala ya Taasisi za Kazi ambapo lengo lake ni ku-compound hizo fences na inapotokea mwajiri amekiuka taratibu hizi tutakachokifanya ni kwenda kumpiga faini ya papo kwa papo ili kufanya deterrence na kumpunguzia mzigo mfanyakazi lakini kumfanya mwajiri awe ana-comply na sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba jambo hili linafanyika kwa mwajiri kuwasilisha mchango wa mwajiriwa wake ikiwa ni haki yake ya mchango ambao ni sehemu ya mshahara wake.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa mgao wa Road Fund Serikali Kuu wanachukua asilimia 70 na Serikali za Mitaa asilimia 30 na kwa kuwa Serikali imeunda chombo cha TARURA na kama mgao utakuwa asilimia 30 zile zile na barabara zetu ni mbaya sana vijijini kule hasa Wilaya ya Mpwapwa.
Je, sasa mgao utaongezeka iwe asilimia 50 kwa 50?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi asilimia 70 na asilimia 30 ni kwa mujibu wa Sheria na Sheria hii ilitungwa na Bunge lako Tukufu. Kama haja itakuwepo kwa wakati huo tutakubaliana kiasi gani ambacho kitafaa na lengo ni kuhakikisha kwamba chombo hiki ambacho tumekianzisha TARURA kinakuwa na uwezo ili kiweze kukidhi haja iliyoanzishwa.
Kwanza ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ni kweli mitambo imekarabatiwa, lakini bado huduma ya maji haiwafikii wananchi wa vijiji vya Ving‟awe namba 30, Mbuyuni, Ving‟awe Juu, Ilolo, Kwa Mshangu, Mahang‟u na Ising‟u; kwa hiyo nilikuwa nakupa taarifa tu kwamba maji hayafiki kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kwamba kuna vijiji ambavyo hakuna uwezekano mwingine wa kupata chanzo cha maji ni kuchimba visima. Sasa naiomba Serikali, kwa vijiji nitakavyovitaja iwachimbie visima ili waweze kupata huduma ya maji. Kwanza Ngalamilo, Mgoma, Mzogole, Kisisi, Godegode, Mkanana, Chamanda, Lupeta, Makutupa, Nana, Simai, Isalaza, Nzonvu pamoja na Iwondo. Naomba sana wananchi hawa wana shida kubwa sana ya maji Serikali iwasaidie. Je, Waziri unasemaje kuhusu hilo.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lubeleje babu yangu gereda la zamani huyu, lakini makali ni yale yale, anafanya kazi nzuri sana kwa wananchi wa Jimbo la Mpwapwa.
Mheshimiwa Naibu Spika nikupe taarifa tu kwamba, wiki mbili zilizopita Mheshimiwa Lubeleje, aliondoka na Waziri wangu kwenda Mpwapwa kwenda kuangalia ukarabati wa hizo starter na sasa hivi kwa kweli Mpwapwa maji yanapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji bado havifikiwi na hayo maji, katika jibu langu la msingi nimesema kwamba Serikali itaendelea kufanya matengenezo na nimuahidi kwenye awamu ya pili ya program ya maendeleo ya maji, tutahakikisha kwamba Mpwapwa tunahakikisha vijiji vyote vinafikiwa na maji. Swali hapa muhimu ilikuwa ni kuna vijiji kwa sababu Mpwapwa ni kubwa, kuna vijiji ambavyo bado havijapata huduma ya maji yenye mfumo na ameomba kwamba tuchimbe visima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu na Babu yangu Mheshimiwa Lubeleje katika Bajeti ya mwaka huu, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.58 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kipaumbele. Kwa hiyo, nikuombe ushirikiane na Halmashauri yako kuhakikisha hivi vijiji, basi mnafanya study na mnachimba visima ili mwaka wa fedha utakaofuata, tuendelee kutoa hela kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata huduma ya maji, kwa maana ya kuchimba visima; lakini ikiwa ni pamoja na kujenga mabwawa ili tuwe na uhakika wa maji katika maeneo ya Mpwapwa.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika mipango yote ya kujenga shule za sekondari, shule za msingi, zahanati, vituo vya afya tunasahau sana huduma za maji, umeme pamoja na afya. Sasa nataka niulize swali kwa Mheshimiwa Waziri na bahati nzuri sana Mheshimiwa Jafo, Waziri wa TAMISEMI Mpwapwa anaifahamu vizuri sana. Katika bajeti ya mwaka 2018/2019; je, Serikali itakuwa tayari kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vituo vya afya, zahanati, shule za msingi, sekondari zote Jimbo la Mpwapwa zinapata huduma ya maji, umeme na afya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri wangu kwa majibu mazuri sana aliyoyatoa hapo awali. Pia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lubeleje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ukiangalia hali halisi ya Jimbo la Mpwapwa changamoto hizo alizozungumza Mheshimiwa Mbunge ni kweli, lakini hata hivyo tunachokifanya ni kuhakikisha kwamba tunawapatia huduma ya maji. Nafahamu kwamba Jimbo la Mpwapwa, Wilaya ya Mpwapwa ina changamoto kubwa. Tumeweza kuhakikisha kwamba; kwa mfano ile miradi sita na Mzee Lubeleje anafahamu tulivyokuwa kule Mima pamoja katika ujenzi wa Kituo cha Afya, mtandao wa maji ambao kwa muda mrefu wakandarasi walikuwa mradi huo walikuwa hawajaanza sasa wakandarasi wote sita wako site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu letu kubwa ni kwamba maji yale yatakapotoka katika jamii kuna water points tutazipeleka katika taasisi hizi za Umma kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango wa REA mnafahamu kwamba Wizara ya Nishati imezungumza wazi katika mpango wa REA Awamu ya Tatu kwamba itahakikisha katika sehemu zote za umma hasa vituo vya afya, shule pamoja na taasisi za dini zote zitapatiwa umeme kupitia katika mpango wa REA III. Isipokuwa katika hili niwaombe Waheshimiwa Wabunge katika ajenda hiyo lazima tuanze maandalizi ya awali ya kuweka wiring katika maeneo hayo, kwa sababu umeme ukishafika hapo ni lazima taasisi yenyewe iwe imeshafanya wiring ili kuhakikisha kwamba huduma hiyo inapatikana vizuri. Ahsante sana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Kadutu la Ulyankulu linafanana kabisa na Tarafa ya Mima ambayo imeshatangazwa kwamba imeanzishwa kuwa Tarafa ya Mima, lakini mpaka sasa hakuna majengo, hakuna watumishi. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini mtajenga majengo, mtaleta watumishi ili kweli ile Tarafa ya Mima ianze kufanya kazi mara moja maana sasa inatamkwa tu Tarafa ya Mima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Kata za Matomondo pamoja na Mlembule ni kata kubwa sana na zina vigezo vyote kuwa tarafa, je, Mheshimiwa Naibu Waziri, unasemaje kuhusu hili? Ni lini mtaanzisha Tarafa hizi Kata mbili, Mlembule na Matomonda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Senior MP Mheshimiwa Lubeleje ambaye mimi namuita grader la zamani makali yale yale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika Tarafa ya Mima ambayo kwa mujibu wa utaratibu Mheshimiwa amesema kwamba imeshaanzishwa lakini majengo ni bado. Basi mimi naomba nielekeze katika Halmashauri husika kwa sababu nadhani wakati tunafanya mchakato wa kuanzisha tarafa hizi ni lazima tutakuwa tumejipanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nafahamu kwamba unafanya juhudi kubwa, lakini niwasihi wenzetu kule, kwa sasa hivi iangalie namna ya kufanya katika mipango ile ikiwezekana ya Kihalmashauri na Kiwilaya. Katika maana hiyo tuanze michakato ya kuanzisha majengo kwa kuangalia suala zima la ki-bajeti. Jambo hili linaanzia kule kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wakati wa mchakato wa bajeti na sisi tutaunga mkono suala la watumishi; ambayo ndiyo mamlaka yetu kupeleka watumishi kama Serikali. Nikuhakikishie Mheshimiwa Lubeleje kwamba jambo hili tutalifanya kwa kadiri taratibu za Serikali zinavyokwenda sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuanzishwa tarafa mpya katika Kata ya Matomondo na. Najua kwamba michakato hii iko vile vile kwa mujibu wa Sheria za uanzishwaji wake. Kwa sababu hiyo basi nishauri Baraza la Madiwani kwamba jambo hili likionekana linakidhi sasa katika Halmashauri yetu ya Mpwapwa basi liweze kufanyika katika ile michakato ya kimsingi ambayo inaanzia katika vijiji inakuja katika vikao vya Ward C, na Halmashauri ya Wilaya then DCC ya wilaya na Mkoa, baadaye inakuja Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kwa maamuzi zaidi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Lubeleje naomba nikuhakikishie kwamba mkianza mchakato huo Ofisi ya Rais TAMISEMI itasikiliza kilio chenu na kuweza kukifanyia kazi kwa kadri inavyoona inafaa.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwaka 1998/1999, mimi nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Katiba ya Sheria na Utawala, Serikali iliamua TRA ijaribu kukusanya kodi ya majengo na walianzia na Halmashauri za Manispaa tatu za Ilala, Temeke na Kinondoni. Baadaye walishindwa, Serikali ikarudisha tena kodi hizo zikusanywe na Manispaa hizo. Sasa ni sababu gani za msingi tena Serikali imeamua kodi ya majengo ikusanywe na TRA na siyo Halmashauri zenyewe? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Sababu ya msingi kwa nini Serikali ilifanya maamuzi kwamba sasa kodi hii ianze kukusanywa na Mamlaka ya Mapato, kwanza, niseme Mamlaka ya Mapato kazi yake ni kukusanya mapato yote wala siyo ya kodi peke yake.
Pili, tuliona udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato katika ngazi ile na ndiyo maana lengo la Serikali ni kusema tutumie chombo ambacho kina wataalam waliobobea kwa ajili ya kukusanya mapato haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili la kusema huko nyuma walishindwa kwani ukishindwa maana yake ndiyo basi tena. Mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje tumepata uzoefu, tumejifunza kutokana na uzoefu, tumefanya maandalizi ya kutosha na tuna hakika awamu hii tutaikusanya kodi hii ipasavyo. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mimi nina swali moja tu; kwa kuwa Serikali imerejesha Kambi ya JKT Mpwapwa na kwa kuwa vijana wengi wa Wilaya ya Mpwapwa wanataka kujiunga na JKT Mpwapwa, je, ni taratibu gani watumie ili waweze kujiunga na ile kambi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba JKT ina azma ya kufungua makambi mapya katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mpwapwa, na utaratibu utakaotumika wa kujiunga ni ule ule ambao unatumia sasa kwamba wakati ukifika JKT itatoa nafasi za vijana wa kujitolea kuomba ili kuingia katika makambi haya mapya. Kwa pale Mpwapwa haitokuwa vijana wa Mpwapwa peke yao, itakuwa kwa nchi nzima, tutazigawa nafasi kama tunavyozigawa sasa kupitia Wilayani na Mikoani na hatimaye vijana watajiunga na Kambi hiyo ya Mpwapwa itakapokuwa tayari kutoa mafunzo. Vile vile kwa siku zijazo tukiwa tayari kambi hiyo pia itatumika kwa vijana kwa mujibu wa sheria.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa magari ya kunyonya maji machafu na kuzoa taka siyo lazima tu iwe kwenye Manispaa au Majiji, hata Wilaya zetu tunahitaji magari ya kunyonya maji machafu na magari ya kuzoa taka. Je, Serikali ina mpango gani kupeleka gari la kunyonya maji machafu pamoja na kuzoa taka katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI naomba kujibu swali la Mzee wangu Lubeleje, mimi namuita greda la zamani makali yale yale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mzee Lubeleje naomba tuiweke katika vipaumbele vyetu vya Halmashauri, naomba nikusihi Mheshimiwa Lubeleje katika mpango wenu wa Halmashauri hilo jambo mkiliainisha, na sisi katika kupitisha bajeti tutalipa kipaumbele. Ninajua kwamba kweli ni jambo la msingi kufanya usafi na kuwa na mitambo hii ya kuzolea taka na kunyonyea maji, kwa hiyo mkiweka katika kipaumbele, mchakato wa bajeti ujao kama Mpwapwa mtaweka kipaumbele basi sisi hatutasita kuhakikisha jambo hilo tunaliwekea kipaumbele hilo ili Mpwapwa mpate gari la kunyonyea maji taka.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja dogo. Bahati nzuri mimi nimekuwa Diwani kwa miaka kumi na tano na Mwenyekiti wa Halmashauri. Kazi ya Udiwani zamani ilikuwa mikutano tu, unakuja kuitwa kwenye kikao unarudi nyumbani; lakini kwa kuwa sasa hivi Udiwani ni kusimamia miradi, ikianza kujengwa darasa mpaka jioni uko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana nami kwamba mtekeleze yale maagizo au maelekezo ya Tume ya Lubeleje ya kushughulikia maslahi ya Madiwani, muwalipe Madiwani posho ya kutosha ili nao waweze kumudu maisha kwa sababu wanashinda kwenye miradi mpaka jioni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mbunge wa siku nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri wazi kwamba kuna Tume iliundwa ambayo Mheshimiwa Lubeleje ambaye ni Mbunge; ndiyo maana namwita Senior MP alikuwa ndiye Mwenyekiti wa Tume ile. Tume ile ilitoa mapendekezo mbalimbali na miongoni mwa mapendekezo hayo yaliyotolewa katika Tume ya Lubeleje ndiyo haya yaliyosababisha kufanya maboresho ya hata hivi viwango tunavyoviona hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kikubwa zaidi na tukiri wazi kwamba Madiwani ndio wenye jukumu kubwa sana la kusimamia kazi za kule site. Ndiyo maana nimesema kwamba Serikali inalitazama hili kwa upana wa hali ya juu; kwamba nini tufanye. Kwa hiyo, hali itakapokuwa imeridhisha na maamuzi yakifanyika naamini kwamba posho ya Madiwani itaongezeka. Lengo ni kuwawezesha kufanya vizuri katika usimamizi wao wa kazi kwani wanafanya kazi kubwa na hakuna mtu anayebeza katika hili.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali hili linafanana kabisa na vituo vya afya vya Mima na Mbori ambavyo havijakamilika sasa ni zaidi ya miaka 10 lakini naishukuru Serikali kwamba mmetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha vituo hivyo. Sasa Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari kutembelea kuona ujenzi wa kituo cha afya - Mima na kituo cha afya cha Mbori?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa kuna mpango wa kujenga kituo cha afya Chunyu na eneo la Chunyu lina idadi ya watu wengi, je, mpango huu umefikia wapi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lubeleje, greda la zamani makali ya yale yale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kutembelea kituo cha afya Mima na Mbori, tumekubaliana na Mheshimiwa Mbunge licha ya vituo hivi vya afya, tutakwenda kutembelea na miundombinu ya barabara katika Jimbo lake ambalo kwa kweli lina mtandao mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika kituo cha afya hicho ambacho ameuliza kwamba mpango ukoje, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tukishafika site sasa japo tutatembelea vituo hivi vya afya viwili, lakini ni vema tutembelee na kituo cha afya hiki kipya ambacho kiko katika mpango wa ujenzi halafu pale tutajadiliana kwa pamoja nini tufanye ili wananchi wa kituo hiki kiweze kujengwa na wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Katika Wilaya ya Mpwapwa, Vijiji vya Bumila, Mima na Iyoma vilichimbwa visima vya maji na maji yalipatikana, sasa ni miezi nane hakuna cha bomba, hakuna cha pampu. Sasa nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri vile visima vilichimbwa kwa ajili ya mapambo kuonyesha wananchi tu au ni lini wataweka pampu na mabomba wananchi wanapata tabu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulishazungumza naye na nimeshazungumza ndani ya Bunge lako hili Tukufu, ukishachimba kisima maji yakapatikana Mkurugenzi unatakiwa utengeneze quotation ya kununua pampu. Ukishatuletea quotation sisi hiyo tunaiweka kama ni certificate tunakupa hela ili uende ukanunue pampu na pampu hizi zifungwe wananchi wapate maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kama tulivyoongea nje kwamba amwambie Mkurugenzi wake wa Halmashauri atengeneze quotation na kama hana huo utaalam basi tuwasiliane ili Wizara ya Maji na Umwagiliaji, tutume mtaalam wetu akamsaidie Mkurugenzi wake wananchi wapate maji.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, tarehe 30 Desemba, 2017, Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo alitembelea Kijiji cha Mima na kuona barabara ya Mima ilivyo mbaya na nilimwonyesha ni barabara ya kwenda Mkanana, ile barabara kilometa 26 zote ni mawe matupu wala hakuna udongo kule, yote ni mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri anaposema anatengeneza eneo korofi, hili eneo lote kubwa linalobaki atatengeneza nani na wananchi wa Mkanana, Kibwegele wana shida? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alipotembelea Mpwapwa tarehe 30 Desemba alikakuga barabara ya lami kilometa moja Mjini Mpwapwa na aliwaahidi wananchi wa Mji wa Mpwapwa kwamba kilometa zote 10 watazijenga kwa kiwango cha lami. Mbona sijaiona bajeti hii ya kujenga barabara za lami Mpwapwa Mjini kilometa 10? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lubeleje, senior MP, ambaye mimi huwa napenda kumuita greda la zamani makali yaleyale kutokana na kazi yake kubwa anayoifanya kule Mpwapwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nikiri wazi kwamba nilikuwa na Mheshimiwa Lubeleje katika Jimbo lake na ni kweli barabara ile ina changamoto kubwa na hata siku ile tulivyoenda kukagua kituo cha afya cha Mima tulitumia muda mrefu sana kutokana na changamoto za barabara ile. Hata hivyo, niliwaagiza wataalam kwamba wafanye uchambuzi wa kutosha nini kifanyike katika barabara ile, maana ukiangalia wigo wake, siyo hiyo peke yake, barabara hizo zote ambazo anazizungumzia Mzee Lubeleje ziko katika hali mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa bajeti iliyokuwepo hapa ni ndogo lakini kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) tunaziweka katika mpango wa utekelezaji maalum kwa kuzitafutia fedha kwa sababu eneo lile lina changamoto kubwa. Kwa hiyo, naomba nimwombe Mheshimiwa Lubeleje avute subira kwani ofisi yetu inafanya kazi kwa sababu wataalam nimewatuma kufuatilia kazi ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara za Mji wa Mpwapwa, ni kweli, mpango uliokuwepo pale ni takribani kilometa tano lakini mtandao wote wa barabara ya lami ni karibu kilometa 10 Mjini Mpwapwa. Hivi sasa wakandarasi wanaendelea na kazi na katika mpango wa bajeti ya mwaka huu, majibu ya Naibu Waziri alipokuwa anazungumza hapa ambayo ni mazuri sana yalikuwa yakijibu suala zima la Mtanana lakini suala la mtandao wa barabara za lami katika mpango wa bajeti ya mwaka huu Mheshimiwa Lubeleje ataona jinsi gani Serikali imejipanga kutekeleza mpango ule wala asiwe na hofu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze vijana wetu wa Timu ya Simba, wamefanya kazi nzuri sana ya kutwaa ubingwa kabla ya mechi zingine hawajacheza, hongereni sana. (Makofi/ vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili; mwaka 2011 aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Mizengo Pinda alitangaza kwamba Mima sasa ni Tarafa itakayokuwa na Kata za Berege, Kitemo, Mima, Ihondwe na Mkanana. Sasa ni miaka 11 hakuna hata jengo; na hizo Sh.50,000,000 sijaziona. Sasa nataka nimuulize swali Mheshimiwa Naibu Waziri, haya yalikuwa ni matamshi ya mdomo tu au hiyo tarafa ipo kwenye Gazeti la Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Tarafa hii ya Mima ina miundombinu mibovu sana; barabara zote hazipitiki, kuanzia Gulwe kuja Berege, Chitemo, hapa Mima Sazima, Igweji Moja, Igweji Mbili mpaka Seruka na kutoka Igweji moja kwenda Ihondwe njia ya mkato hazipitiki. Je, Mheshimiwa Waziri ana maelezo gani kwa wananchi wa Jimbo la Mpwapwa na hasa Tarafa ya Mima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia angalia labda kuna Waziri amesimama lakini basi nitaendelea kulijibu mimi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lubeleje ni maswali magumu, na mimi napenda kuyajibu kama ifuatavyo. Ni kweli kwamba Mheshimiwa Mizengo Pinda alitangaza Tarafa ya Mima kuwa Tarafa mwaka 2011, wakati huo alikuwa Waziri Mkuu lakini ndiye alikuwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba Tarafa ya Mima sawasawa na Tarafa nyingine imetangazwa kwenye Gazeti la Serikali na ndiyo maana akateuliwa Afisa Tarafa Maalum kwa ajili ya tarafa hiyo, kwa hiyo tunaitambua. Hizi Sh.50,000,000 amesema hajaziona, ni kweli hajaziona kwa sababu bado hazijapelekwa. Tunajiandaa kuzipeleka hivi karibuni na tumemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri kwamba atakapopata hizi fedha azi-commit haraka kwenye kazi ili kusudi kazi iweze kufanyika ya kujenga Ofisi ya Afisa Tarafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kuhusu miundombinu; nchi yetu imekumbwa na matatizo makubwa sana hivi karibuni baada ya mvua kubwa kunyesha, maeneo mengi sana miundombinu imeharibika. Kwa hiyo hili najua ni swali la Wabunge wengi, lakini kwa Mima anaulizia kwa sababu kwa kweli kuna barabara huko hazijawahi kutobolewa na mambo mengine mengi na kazi ya kutoboa barabara ni kazi ya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana nikitoka hapa Bungeni niweze kumtuma Mkurugenzi wetu wa Miundombinu atembelee Tarafa ya Mima. Baada ya hapo tutapata majibu mazuri zaidi.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Halmashauri tano za Mkoa wa Dodoma zilipata fedha za kujenga barabara za mijini, lakini halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa hatukupata na nimezungumza na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa kwamba Mpwapwa na Kongwa hatukupata barabara za kujenga mjini na ilikuwa ni ahadi ya Waziri wa TAMISEMI, tarehe 30 Desemba, Mheshimiwa Jafo.
Naomba maelezo ya Waziri kwa nini, Kongwa na Mpwapwa hatukupata hizi hela katika hiyo bajeti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yale yote na hasa kwa sababu na yeye amesema kwamba ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri, naomba nimhakikishie dhamira ya dhati ipo, lakini ni ukweli usiopingika kwamba miji mingine yote kwa Mkoa wa Dodoma imepata. Maana yake katika hatua inayofuata lazima tuhakikishe kwamba na maeneo hayo mawili ikiwepo eneo la kwako Mheshimiwa Spika yanatiliwa mkazo, ili barabara zijengwe kwa kiwango cha lami na kwa Mheshimiwa Lubeleje. Naomba nilichukue kwa mikono miwili kwa dhati kabisa kuhakikisha kwamba, na hasa kwa kuanzia kwa Mheshimiwa Spika hatukusahau hata kidogo. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya Vituo vya Afya vimepewa shilingi milioni 500 ili vikamilishe ujenzi wake; na kwa kuwa ujenzi wa Kituo cha Afya Mbori, Wilayani Mpwapwa sasa ni miaka 10 haujakamilika. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Afya Mbori ili waweze kukamilisha ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, ni azma ya Serikali kuhakikisha Vituo vya Afya 513 vinafanyiwa ukarabati ili ziweze kutoa huduma tunayokusudia. Namwomba Mheshimiwa Mbunge aridhike na kasi ya Serikali kwamba tumeanza na vituo 208 na juzi vimeongezeka viwili ikiwa ni Kituo cha Afya cha Kibondo na kingine Nsimbo. Baada ya wafadhili kuona kasi nzuri ya Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli kuhusiana na suala zima la afya, nao wameamua kuweka nguvu katika maeneo ambayo yanahudumia wakimbizi. Kwa hiyo, badala ya vituo 208 sasa tuna vituo 210.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii asilimia 10 ya vijana na akina mama hii ni revolving fund, mtu anakopa, anarejesha. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, hawa tunaowakopesha, je, wanarejesha na kama hawarejeshi, wanachukuliwa hatua gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba fedha hizi wanapokopeshwa vikundi vya vijana na wanawake wanatakiwa kurejesha na mratibu mkuu wa marejesho ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika halmashauri husika. Kwa hiyo, kama kuna sehemu hawarejeshi kabisa, huo utakuwa ni udhaifu mkubwa sana wa kikazi wa huyo Afisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati yake ya Mikopo ya Halmashauri. Wito ambao tunautoa ni kwamba ni lazima wanaokopeshwa warejeshe, vinginevyo hatua zitachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo zuri kabisa ambalo amelifanya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI wakati anawasilisha hotuba ya bajeti ni kutoa tangazo kwamba kuanzia mwakani atafuta au amefuta riba kwenye mikopo ya wanawake na vijana. Kwa hiyo, hiyo iwe kichocheo cha mwananchi yeyote atakayekopeshwa mikopo hiyo arudishe fedha kama alizokopa bila riba. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa daraja la Gwedegwede lilisombwa na maji wakati wa masika; na kwa kuwa wananchi wa Kata wa Zagaligali, Mbuga, Lumuma, Pwaga na Godegode wanazunguka mpaka Kibakwe, zaidi ya kilomita 75 ndipo wafike Mpwapwa Mjini. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja la Godegode ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja ambalo Mheshimiwa analitaja ana uelewa mzuri na daraja hilo. Naomba baada ya kumaliza kipindi hiki cha Bunge tuwasiliane ili tujue; kabla ya kuanza kujenga daraja hilo lazima tufanye tathimini tujue gharama kiasi gani cha fedha inahitajika ili tuhakikishe kwamba daraja hilo linajengwa ili kuondoa adha kwa wananchi ambao wanalazimika kuzunguka umbali mrefu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza katika majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba watajitahidi kukwepa hii reli mpya watakwepa Mto Mkondoa na Mto Kinyasungwi na hii mito ndiyo yenye maji mengi yanayosababisha mafuriko maeneo ya Gulwe mpaka Godegode.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, kwa kuwa maji haya huwa yanasambaa kilometa tatu na yeye anasema atajenga kukwepa kilometa mbili, Je, itawezekana? Mafuriko siyataendelea na reli itaharibika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili; eneo la Gulwe kuna makorongo makubwa sana. Mwaka 1996 tulipata mtaalam Johnson kutoka Marekani alijenga ma- gabion makubwa sana lakini mvua moja tu ma-gabion yote yalikwenda. Sasa una maelezo gani Mheshimiwa Naibu Waziri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana kwa jinsi anavyofuatilia na mara kadhaa amekuwa akifika hata ofisini kwa ajili ya kuangalia kwamba eneo lenye matatizo ya mafuriko ya mara kwa mara linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumtaarifu tu kwamba ni kweli maji huwa yanasambaa mpaka kilometa moja, lakini kama atavuta kumbukumbu vizuri mwezi wa pili mwishoni nilitembelea eneo la mafuriko na nikatoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya wa eneo hilo pamoja na kuwasihi wananchi kwamba eneo la reli kwa upande ule ni mita 60 kwa upande wa kushoto na mita 60 upande wa kulia, hawatakiwi wafanye shughuli zozote za kibinadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za kibinadamu ni moja kati ya sababu kubwa zinzosababisha reli yetu kufurikishwa na maji kwa sababu ukishaanza kulima kando kando ya reli unasababisha ule udongo unakuwa tifutifu, ukisababisha udongo kuwa tifutifu maji yakija ni lazima yatabomoa ile reli, lakini kama hakuna shughuli za kibinadamu maana yake ile miti itaendelea kuota na kuzuia. Ile reli haikujengwa kwa bahati mbaya, ilifanyika utafiti ndiyo ikajengwa maeneo yale, lakini niendele kutoa msisitizo kwa wananchi kwamba wasivamie maeneo ya reli na wakae mbali mita 60 kutoka kwenye reli ilipo upande wa kushoto na kulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili; ni kweli kwamba hiyo gabion ilijengwa kubwa na kutatua hilo ni ile njia yetu ya pili kwamba reli itajengwa ndani ya mahandaki mbali kilometa mbili kutoka reli ilipo. Tutajenga meter gauge pamoja na standard gauge ili kuhakikisha kwamba hayo maji sasa hayaji na wananchi tuna uhakika hawatakuja kutuvamia kule kwenye milima ambapo tunajenga reli yetu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imesitisha ugawaji wa maeneo makubwa yakiwemo Majimbo pamoja na Wilaya, lakini kuna Kata moja iko mlimani inaitwa Kata ya Mkanana, hata Mheshimiwa Spika unaifahamu ni milimani hasa. Makao Makuu ya Kata yako kilometa 50 wanateremka kusikiliza mikutano. Je, Serikali inasemaje kuhusu Kata hii ya Mkanana na Chibwegere ili wazigawe? Wananchi wanapata shida sana kusafiri.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyosema, tumesitisha, lakini kulingana na umuhimu na mahitaji ya muda maalum, kama ambavyo tumepitisha uanzishwaji wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuutangaza Mji wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi kwa sababu ni mahitaji maalum kwa muda maalum, kwa suala hili la Kata ya Mtanana kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amelieleza vizuri sana hapa Bungeni na kwa sababu anawawakilisha wananchi wake ambao anaamini wanapata shida kwenda kwenye Makao Makuu ya Kata kilometa 50, namuagiza Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa kesho aende Mtanana na timu yake ya wataalam ili watuletee mapendekezo yao.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja. Kwa kuwa tayari Serikali imeshakubali kujenga barabara ya lami kutoka Mpwapwa kwenda Kongwa, ninachotaka Mheshimiwa Naibu Waziri awathibitishie wana Mpwapwa ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa na kiasi gani kimetengwa kwa sababu ni muda mrefu, sasa ni mwezi wa Tisa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO – (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi barabara hii ya kutoka Mpwapwa kuja Kongwa ni sehemu hii ya barabara ambayo inakuja mpaka eneo la Mbande na kwa kiasi kikubwa barabara hii inaendelea na ujenzi. Najua concern ya Mheshimiwa Mbunge ni ule ujenzi wa barabara hii sasa kuwa na kasi kubwa kutokea Mpwapwa kuja Kongwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kiasi cha fedha ambacho kimetengwa, najua tumetenga fedha, tuwasiliane tu na Mheshimiwa Mbunge ili angalau basi tuone kwa undani kwamba ni kiasi gani kimetengwa. Nimhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mpwapwa eneo la Mpwapwa nimelitembelea tumejipanga ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Mpwapwa wanaunganika vizuri na Makao Makuu ya Nchi hapa Dodoma.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Nina swali moja tu la nyongeza; kwa kuwa maji ni siasa, maji ni uchumi, na maji ni maendeleo; na kwa kuwa Serikali ilikuwa na mipango ya kuchimba visima vya maji katika Kijiji cha Majami, Nana, Mafuto, Lupeta 30, Makutupa pamoja na Ngalamilo na walielezwa kabisa fedha zilizotengwa kwa ajili ya visima hivyo.
Je, ni lini sasa Serikali watakwenda kuanza kuchimba visima vya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Wizara yetu ya Maji ni katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi, salama. Nimuombe sana Mheshimiwa Mbunge mimi kama Naibu Waziri wa Maji nipo tayari kufanya cross check na watu wa DDCA waende mara moja katika kuhakikisha wananchi wake wa Mpwapwa wanapata safi, salama na yenye kuwatosheleza, ahsante sana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa elimu ya bure ni kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la kumi na mbili, lakini kidato tano na sita hawamo. Hawa wote ni watoto wa mtu mmoja, kuna sababu gani za msingi form five na six wakaachwa kusamehewa karo? Naomba Waziri atoe maelezo kwa sababu wote ni watoto wake, kwa nini hawa waachwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema kwamba watoto wote ni watoto wa Taifa hili kwa hiyo haitakiwi kuwa na ubaguzi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali siku zijazo kadri uwezo utavyoruhusu tutatoa elimu bure ikiwezekana mpaka chuo kikuu bure. Kwa sasa, kutegemeana na hali halisi ya kifedha, tutaendelea kwanza kuimarisha miundombinu na mazingira katika shule za ngazi ya elimu msingi, kuanzia shule za awali mpaka kidato cha nne na kuendelea kutoa elimu bure na uwezo ukiongezeka hatuna shida kuongeza kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kama mnavyofahamu Serikali inatoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu. Tunatoa shilingi bilioni 427 kila mwaka kwa sasa. Kwa hiyo, anachosema ni kitu cha kweli. Kwa kweli siku zijazo uwezo utakapoongezeka hata kidato cha tano na sita nayo itakuwa ni elimu bure.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa katika Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa kuna skimu za umwagiliaji ambazo zilijengwa sasa ni miaka 10 hazijafanyiwa ukarabati, katika Kijiji cha Chamkoroma, Mseta, Tumbugwe, Mlembule, Boli na Injovu. Hakuna hata mtaalam mmoja ambaye amepitia kuziona skimu zile. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kwenda kukagua skimu za umwagiliaji katika maeneo haya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwa kutambua sasa hivi tunaelekea katika uchumi wa viwanda na uchumi wa viwanda unategemeana kabisa na kilimo cha umwagiliaji. Nipo tayari Mheshimiwa Mbunge kuongozana na yeye katika kuhakikisha tunakwenda kuziangalia skimu zile zake za umwagiliaji.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, shule za sekondari za kidato cha kwanza mpaka cha nne Serikali imezipandisha hadhi baadhi yake kuwa shule za kidato cha tano na cha sita, kwa mfano, Kibakwe, Berege, Mazae na Kongwa Mjini. Hata hivyo, watoto katika shule hizi wanasoma katika mazingira magumu sana kwanza madarasa, hosteli pamoja na mabweni lakini hata chakula wanachopewa hela ni kidogo sana. Mheshimiwa Naibu Waziri anasemaje kuhusu suala la kuboresha shule za form five na six katika kata hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nichukue nafasi hii kumpongeza, yeye ni Mbunge mzoefu wa siku nyingi na kutokana na Ubunge wake ndiyo maana ameweza kupata maendeleo makubwa katika Jimbo lake hadi shule hizo alizozitaja zimesajiliwa kuwa katika hadhi ya kidato cha tano na sita. Kuwa na shule tatu au nne kwenye Jimbo moja za kidato cha tano na sita siyo kazi ndogo, ni kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika jibu hili, napenda kujibu kwa ujumla kwamba shule zote za kidato cha tano na sita na hata za kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, zote zinapewa fedha sawasawa kwa nchi nzima. Kwa hiyo, haiwezekani kwa mfano tukasema kwamba, kwa sababu shule hizi sasa Mheshimiwa Mbunge amesema zina matatizo makubwa, basi tuziongezee shule zile za Jimbo lake tu, ni kitu ambacho hakiwezekani. Kwa hiyo, nakaribisha maoni kama haya ili tuweze kuyajadili kwa pamoja kwa ajili ya shule zote nchini badala ya shule moja moja. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa barabara kutoka Mpwapwa – Lupeta kwenda Matomondo – Mlali mpaka Pandambili ni barabara ya mkoa. Namshukuru sana Meneja wa Mkoa anajitahidi lakini kwa kuwa kuna daraja la Matomondo la Tambi linashindikana kujengwa kwa sababu ya gharama kubwa. Je, Waziri anasemaje kuhusu daraja hilo na yuko tayari kutembelea hiyo barabara? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli mara kwa mara nimetembelea eneo hili la Mpwapwa ili kuweza kujionea hali ya uharibifu kwa sababu tuko karibu hapa na nimeweza kuona kwamba ziko changamoto. Ni kweli daraja ambalo Mheshimiwa Mbunge anazungumza ni daraja kubwa, iko nafasi ya kuweza kuhamisha ili daraja liwekwe sehemu ambapo gharama za ujenzi zitakuwa ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nia ya Serikali tuweze kujenga kwa tija lakini pia kupunguza gharama, gharama zikipunguza zitatuwezesha kutoa huduma maeneo mengine. Kwa hiyo, namwambia Mheshimiwa Mbunge, nitakuwa tayari kutembelea eneo hili ili wakati mwingine mimi na yeye tukiwa na wataalam tuweze kuona kwamba ni wapi tunaweza tukahamishia daraja hili ili tusaidiane pale itakapohitajika saa nyingine wananchi kuachia maeneo haya. Lengo tuweze kupata daraja ambalo linawapa huduma wananchi hawa wa maeneo haya. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Chombo cha TARURA ni kipya na kilipoandaliwa kilipewa fedha ndogo; na kwa kuwa fedha iliyotengwa na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, anazifahamu sana barabara za Mpwapwa, barabara za mjini na barabara za Mima; je, TARURA iko tayari kuongezwa fedha ili zile barabara za Mpwapwa Mjini na Mima ziweze kutengenezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kwanza katika sehemu ya kwanza ya swali lake, maana kauliza kama maswali mawili; ni kwamba TARURA iko tayari kuongezwa fedha, hiyo, niseme wazi. Pia jambo la msingi la pili ni kwamba tunajua mazingira yote katika Tarafa ya Mpwapwa na Tarafa ya Mima kwa sababu, aliuliza swali la msingi hapa na katika swali la msingi tukamuahidi kwamba, tutatuma wataalam. Wataalam wamekwenda kule wakiwemo Wahandisi walioko kwenye jimbo lake, wamefanya tathmini na wametuletea ofisini, hivyo, tutaifanyia kazi katika mwaka ujao wa fedha.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anaifahamu vizuri sana Mpwapwa na barabara ya kutoka Kongwa - Mpwapwa anaifahamu vizuri sana; na kwa kuwa Serikali imekubali kujenga barabara ya lami kutoka Kongwa - Mpwapwa, je, barabara hii kama nilivyoomba itaanzia Mpwapwa - Kongwa? Naomba Waziri awathibitishie hilo wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa au yeye anasemaje?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwei Mheshimiwa Lubeleje amekuwa akifuatilia sana barabara hii. Wiki kama nne zimepita baada ya mvua kupungua nilitembelea eneo la Mpwapwa nimeenda kuona hata eneo la Godegode ambalo amekuwa akipigia kelele sana ili tuje na utaratibu wa kuhakikisha turekebisha barabara iweze kupitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu barabara hii ya lami inayotokea barabara kuu kwenda Kongwa ujenzi unaendelea vizuri, hii ndiyo sehemu ya barabara ambayo Mheshimiwa Mbunge anazungumza. Nafahamu concern yake ni kuhakikisha tunajenga ile barabara ya kutoka Mpwapwa Mjini ili ije ikutane na hii barabara inayotoka Kongwa na tumetenga fedha. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Lubeleje juhudi zake zinazaa matunda na anafanya kazi nzuri na wananchi wa Mpwapwa watambue hivyo kwamba tutaendelea kujenga barabara hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata jana tulipiga hesabu kidogo kuona kwamba kwa kiasi cha fedha ambacho tumetenga tunaweza sasa tukawa na utaratibu wa mkataba wa kilometa karibu 7 hivi tukaanza kujenga kutoka Mpwapwa Mjini. Kwa hiyo, tutakwenda hatua kwa hatua kadiri fedha zinavyopatikana kuhakikisha eneo lake lote hili linapata barabara ya lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lubeleje asiwe na wasiwasi.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, Kituo cha Afya cha Mbori kinachojengwa kinakaribia kukamilika pamoja na kwamba hakijapata milioni 500, lakini kwa kuwa kituo hiki kitahudumia Kata ya Lupeta, Kimagai, Godegode, Mlembule na Matomondo. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kuwapeleka gari la wagonjwa kwa sababu litahudumia watu zaidi ya laki moja.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kwa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Lubeleje jinsi ambavyo amekuwa akiwapigania wananchi wake na hasa kuhusiana na suala zima la afya. Baada ya kupongeza ni vizuri Mheshimiwa Lubeleje kwa kushirikiana na wananchi na Halmashauri yake wakahakikisha hicho kituo cha afya ambacho anakisema hakijamalizika jitihada ziongezwe ili kiweze kukamilika kwa wakati. Pia nimhakikishie kwamba ni azma ya Serikali pale ambapo uwezo unaruhusu kupeleka gari za ambulance maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami naomba niulize swali moja tu. Kwa kuwa benki zote ziko chini ya Wizara ya Fedha na kwa kuwa CRDB wameanza kupunguza riba, je, kwa nini benki nyingine zisipunguze riba ili wananchi na wafanyabiashara waweze kupata mikopo kuliko hali ilivyo sasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la nyongeza la kaka yangu Mheshimiwa George Lubeleje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwenye jibu langu la msingi na nizipongeze Benki ya CRDB, NMB na ABC, benki zote hizi zimeshusha riba yao kutoka zaidi ya asilimia 20 mpaka asilimia 17. Ni imani ya Serikali kwamba benki zote zitafuata mwanzo huu mzuri ulioanzwa na benki hizi tatu nilizozitaja kama njia mojawapo ya kuakisi jitihada njema za Serikali ya Awamu ya Awamu ya Tano na Mheshimiwa Rais wetu dhamira yake ya kuhakikisha Watanzania wanapata fedha za mitaji kwa bei iliyo chini kabisa.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa niko kwenye Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na ndiyo tunayekagua miradi hii; na kwa kuwa tulishatoa maelekezo kwa Serikali kwamba wale wote walioandikishwa na kupata msaada wa TASAF na siyo kaya maskini wafutwe kwenye orodha lakini mpaka sasa bado wanapata zile fedha. Je, sasa Serikali imeshawafuta wale ambao wana uwezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yeye mwenyewe alivyosema ni Mjumbe wa Kamati yetu inayosimamia Utawala pamoja na Serikali za Mitaa na sisi kama Serikali mara nyingi huwa tunazingatia sana ushauri wa Kamati. Naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba ni kweli siku za nyuma kulikuwa na makosa ambayo sisi kama Serikali tumeshayarekebisha na ndiyo maana nimesema sasa tunaendelea kuboresha mfumo na tutaanza kutumia mfumo wa kielektroniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja.Kwa kuwa ujenzi wa Kituo cha Afya Mboli ambapo hata Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI Jafo anakifahamu maana ndiyo barabara yake ya kwenda Chamkoroma kule. Na kwa kuwa kituo hiki hakijakamilika wamejenga wananchi, nilikwishawaomba shilingi milioni 500 TAMISEMI ili wakamilishe kituo kile.
Je, Serikali inasemaje kuhusu kutoa shilingi milioni 500 ili tuweze kukamilisha kituo kile ili wananchi wa Kata ya Matomondo, Kata ya Mlembule, Kata ya Chamkoroma na Kata ya Tubugwe waweze kupata huduma?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikiri wazi kwamba nishukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri kwa maeneo yale ya Mheshimiwa Mgimwa ambayo ndiyo Serikali imejipanga katika utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti,kwa swali la Mheshimiwa Lubeleje ambaye mimi namwita greda la zamani makali yale yale, si muda mrefu nilikuwa naye kule Wilayani Mpwapwa takribani wiki tatu zilizopita tulikuwa Mpwapwa. Hata hivyo kutokana na mchango mkubwa wa Mzee Lubeleje sasa hivi tunakamilisha Kituo cha Afya cha Mima na ndiyo maana siku ile alitoa hoja ya Kituo cha Afya cha Mboli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jukumu la Serikali kuhakikisha wananchi wa maeneo mbalimbali watapata huduma. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lubeleje uwe na amani kwamba ni mpango wa Serikali kuboresha vituo vya afya na miongoni mwa vituo vya afya tutakavyoviimarisha ni Kituo cha Afya cha Mboli. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, anasema kwamba halmashauri waongeze makusanyo ya mapato ya ndani (own source) na kwa kuwa Serikali ilichukua vyanzo vingi vya mapato ambavyo vilikuwa vinaipatia halmashauri mapato, sasa Serikali inasema halmashauri ziongeze makusanyo ya mapato ya ndani, hayo makusanyo ya ndani yatatoka wapi na kwa nini Serikali isiongeze ruzuku ili Madiwani waongozwe posho? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Madiwani ni viongozi kama sisi Wabunge; na kwa kuwa viongozi wa kisiasa wengi wamewekwa kwenye Sheria ya Mafao ya Viongozi wa Kisiasa, kwa nini hawa Madiwani nao wasiwekwe kwenye sheria hii ili waweze kutambulika kisheria kwa sababu ni viongozi muhimu? Katika Uchaguzi Mkuu ni mafiga matatu, baada ya uchaguzi figa la tatu linameguka wanakuwa viongozi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa George Malima Lubeleje kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Mbunge anauliza kwamba kwa sababu kuna vyanzo vimechukuliwa na Serikali Kuu na kwa hiyo mapato ya halmashauri yamepungua ni kwa nini tusitoe ruzuku. Kwanza naomba ieleweke kwamba vyanzo vilivyochukuliwa ikiwemo kodi ya majengo inakusanywa na TRA kwa niaba ya Serikali nzima lakini fedha hizi zinarudishwa kwenye halmashauri kwa ujumla wake kwenda kufanyia kazi shughuli za maendeleo katika halmashauri zetu hizo hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa sasa hili jambo la ruzuku halijafanyiwa kazi, naomba tulipokee tulifanyie kazi, kadri uwezo utakavyoruhusu basi tutaona kama kuna uwezekano wa kupeleka ruzuku. Kwa sasa kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi ni kwamba posho za Madiwani na malipo mbalimbali zinatokana na vyanzo vya ndani na sasa tupo kwenye mchakato wa kuandaa bajeti ya 2019/2020, naomba halmashauri zetu ziangalie uwezekano wa kuongeza posho na mapato ili waweze kujilipa wenyewe kwa sababu ndipo msingi wa malipo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili anazungumza habari ya sheria kuweza kuwatambua; hili ni jambo jema, lakini kwa sheria iliyopo huu ndiyo utaratibu wa kawaida, sasa kama kuna maoni mengine kama alivyopendekeza tupo tayari kuyapokea, tuyafanyie kazi na hatimaye kuyaingiza kwenye sheria ili waweze kulipwa kama watumishi.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa miradi mingi ya maji imesimama katika Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa na hivi sasa wananchi wanakosa huduma ya maji; makandarasi hawajalipwa fedha:-

Je, Mheshimiwa Waziri anasemaje kuhusu hili? Ni lini makandarasi watalipwa miradi ikamilike na wananchi waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ukimwona mtu mzima analia ujue kuna jambo. Nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha. Kiukweli tulikuwa na madai ya makandarasi takribani zaidi ya shilingi bilioni 104.5. Tunashukuru sana Wizara ya Fedha, baada ya kufanya ukaguzi imeonekana makandarasi ambao wanatakiwa kulipwa, wanadai zaidi ya shilingi bilioni 88. Wameshatupa fedha zaidi ya shilingi bilioni 44 mwezi huu Machi na wametupa commitment ndani ya mwezi huu wa Nne watatupa tena shilingi bilioni 44 katika kuhakikisha makandarasi wote fedha zao zinalipwa.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama kuna certificate yake hajalipwa, tuwasiliane tumlipe. Nataka nimhakikishie, baada ya kumlipa, ataendelea kuwa juu juu kileleni katika Jimbo lake la Mpwapwa. Ahsante sana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hivi karibuni Serikali imefanya ukarabati mkubwa wa shule za sekondari kongwe ikiwemo Shule ya sekondari ya Mpwapwa lakini mimi nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri mnafanya ukarabati wa shule tu lakini nyumba za walimu zimechakaa kweli kweli. Je, mna mpango gani wa kukarabati shule na nyumba ya walimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa George Malima Lubeleje (Senator), kama lifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba tunakarabati shule tu ukweli ni kwamba tumekarabati shule nyingi zaidi kuliko nyumba za walimu. Hata kwenye kitabu cha bajeti tunachojadili sasa ambapo Mungu akipenda tutahitimisha Jumatatu tarehe 15 akipitia kwenye majimbo mbalimbali ataona fedha zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za walimu. Uwezo wa Serikali siyo mkubwa sana, tunaomba Mheshimiwa Mbunge na wadau mbalimbali tushirikiane katika jambo hili kupunguza shida ya walimu katika nchi hii. Ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa line inayopeleka umeme Wilaya ya Mpwapwa inahudumia pia Wilaya za Chamwino, Kongwa, Gairo na Mpwapwa yenyewe na hivi karibuni line hiyo imeongezwa Tarafa ya Mwitikila, Mpwayungu na Nagulo. Kwa hiyo, line hii imekuwa overloaded na kusababisha kukatikakatika kwa umeme katika Mji wa Mpwapwa. Je, mko tayari kujenga line mpya ya umeme kuanzia Zuzu Main Station itakayopita Kikombo Station, Kiegea mpaka Mbande ambako mtajenga substation na pale ijengwe line moja kwa moja kuelekea Mpwapwa itakayojulikana kama Mpwapwa fider?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa vijiji vya Mima, Sazima, Igoji Mbili, Isalaza, Chamanda na Iwondo tayari vinapata huduma ya umeme lakini mkandarasi aliruka Kijiji cha Igoji Moja na tatizo la sasa ni transfoma. Je, uko tayari kupeleka transfoma katika Kijiji cha Igoji Moja ili wananchi wa pale waweze kupata huduma ya umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Lubeleje kwa kufuatilia masuala ya nishati kwa wananchi wa Mpwapwa, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lubeleje la kwanza, ni kweli umeme unaokwenda Mpwapwa unatoka Zuzu ambapo ni umbali wa kilomita 120 ni mbali sana. Mpango uliopo ni kwamba sasa hivi Serikali kupitia TANESCO tumeanza utekelezaji wa kujenga line mpya ya kutoka Zuzu kupita Kikombo ambapo ni kilomita takribani 42 na kutoka Kikomo mpaka Msalato kilomita 45 lakini kwenda Mpwapwa tutatoa sasa Kikombo kupita Kiegea kutoka Kiegea tunajenga substation Mbande na pale Mbande kwenda mpaka Mpwapwa itakuwa takribani kilomita 70. Kwa hiyo, wananchi wa Mpwapwa sasa wataanza kupata umeme kutoka Mbande ambao utakuwa ni mkubwa kuweza kuwahudumia wananchi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili, ni kweli tumepeleka umeme kwenye vijiji takribani 32 Mpwapwa lakini viko vijiji vya Mkanana, Mbande pamoja na maeneo aliyoyataja kama Igoji Moja au Igoji Kaskazini, nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge Igoji Kaskazini au Igoji Moja wakandarasi wameanza kazi tangu juzi na kufikia Jumapili ijayo watawasha umeme na watafunga transfoma nne za kilovoti 50 na kilomita zingine mbili wataweka na kufunga transfoma mbili za kilovoti 120 na wataunganisha wateja wa awali 78 wa phase one na wateja 9 wa phase three. Kwa hiyo, Igoji itakwenda kuwashwa umeme Jumapili ijayo. Nashukuru sana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spoika, kwa kuwa barabara ya kutoka Gulwe – Berege – Mima - Sazima - Seruka na barabara hiyo Spika unaifahamu kwa sababu umeishi Mima. Barabara hii TARURA hawawezi kuitengeneza kwa sababu hawana fedha za kutosha na Serikali ilikubali kuichukua barabara hii ili ifanyiwe matengenezo makubwa. Je, Mheshimiwa Waziri unasemaje kuhusu suala hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli eneo alilotaja Mheshimiwa Mbunge la Gulwe – Berege – Mima - Seruka ni eneo ambalo lina changamoto zake kwa sababu linapitiwa na maji mengi wakati wa mvua na kumekuwa na uharibifu mara kwa mara. Kikubwa tu Mheshimiwa Lubeleje nikuondoe hofu usubirie ni wiki ijayo tu Jumanne utaona namna tulivyojipanga kurekebisha barabara hii ikiwa ni pamoja na eneo la Godegode.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Bunge lako likitupitishia fedha tunakwenda kufanya usanifu na kufanya ujenzi kwenye eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi eneo hili na mimi nililitembelea na yako maeneo mengine pia Mheshimiwa Lubeleje atayaona kwa maana ya Mpwapwa kwa ujumla wake tumeitazama kwa macho mawili kwa sababu tunajua changamoto za barabara katika maeneo yake.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, lengo la kujenga vituo vya afya na zahanati ni kupunguza vifo vya akinamama wajawazito pamoja na watoto, lakini kwa kuwa, tatizo la upungufu wa madaktari ni kubwa sana. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri unasemaje kuhusu hilo, kuongeza madaktari katika vituo vya afya na hospitali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakiri kwamba, tuna changamoto ya rasilimali watu, lakini Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba, tunakabiliana na changamoto hii. Na katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19 Serikali iliajiri watumishi wa afya takribani 11000 na tunaendelea sasa hivi mkakati tuliokuwanao ni kuziba mapengo ya hawa ambao wamestaafu, waliofariki na katika kipindi cha mpito. Lakini Serikali inaendelea kuweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba, katika vibali vya ajira mpya na watumishi wa afya wanakuwemo.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa madawa yaliyokwisha muda wake (expired drugs) ni hatari sana katika maisha ya binadamu; na kwa kuwa baadhi ya maduka hayakaguliwi vizuri kuhakikisha kwamba madawa yaliyokwisha muda hayapo.

Je, Mheshimiwa Waziri anasemaje kuhusu ukaguzi wa maduka yote ambayo yana madawa hayo yaliyokwisha muda wake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taratibu zetu za afya, dawa zilizoisha muda au matumizi hazipaswi kutumika kwa matumizi ya binadamu. Mahospitali pamoja na wauzaji wa maduka binafsi wanatakiwa wazitenge tofauti na dawa ambazo zinaendelea kutumika ndani ya vituo vyetu vya kutolea huduma za afya lakini vilevile katika matumizi ya dawa za kuuzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utaratibu maalum ambao umewekwa ambapo dawa na vifaa vya hospitali havichomwi tu kama takataka nyingine, vina utaratibu wake na utaratibu huu upo. Nitoe rai tu kuhakikisha kwamba mamlaka ambazo zinasimamia ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya TFDA na Baraza la Famasia, basi wapite kuhakikisha kwamba wanatoa elimu hiyo na kuweka utaratibu mzuri wa uteketezaji wa hizi dawa ili zisije zikaingia katika mikono isiyo salama.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ujenzi wa Kituo cha Afya Mbori ambacho hata wewe unakifahamu, Waziri wa TAMISEMI anakifahamu, sasa ni zaidi ya miaka kumi kinajengwa kwa nguvu za wananchi na Halmashauri ambayo haina fedha; na kwa kuwa nimeomba shilingi milioni 500 TAMISEMI wasaidie kukamilisha jengo lile:-

Je, TAMISEMI au Serikali inasemaje kuhusu kukamilisha Kituo cha Afya Mbori?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kama kuna Waheshimiwa Wabunge ambao wamekuwa wakiongelea kituo cha afya kwa kurudia mara nyingi ni pamoja na Mheshimiwa Lubeleje; na hivi karibuni alipata fursa ya kuonana na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na akamhakikishia.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumepata fedha kiasi, tumepeleka kwenye hospitali na vituo vya afya ikiwa ni pamoja na Kongwa shilingi milioni 400. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Lubeleje, ahadi ya Mheshimiwa Waziri hakika atatekeleza kama alivyomwahidi. Naomba avute subira fedha yoyote ikipatikana hatumsahau Mheshimiwa Lubeleje.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja na nyongeza. Kwa kuwa Serikali ilikuwa na mpango wa kuchimba visima vya maji katika Vijiji vya Ng’hambi, Kiegea, Kazania na Chimaligo; na fedha zilitengwa, visima havijachimbwa? Mheshimiwa Waziri unaweza kuwaeleza wananchi wa vijiji hivyo fedha hizo zilikwenda wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Kiukweli amekuwa mfuatiliaji mkubwa sana katika suala zima la maji. Ukimwona mtu mzima analia, ujue kuna jambo Mpwapwa. Sasa nataka nimhakikishie, kwanza nipo tayari kwenda Mpwapwa, lakini kuzifuatilia hizi fedha katika kuhakikisha zinafanya kazi na wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili. Kwa kuwa daraja lililosombwa na maji lilijengwa kwa gharama ya shilingi milioni 500 na limesombwa na maji, leo mnajenga daraja la shilingi milioni 325 hilo si ndiyo litachukuliwa mapema. Kwanini msiongeze fedha Mheshimiwa Naibu Waziri?

Swali la pili kwa kuwa barabara ya kutoka Mpwapwa, Lupeta, Mbori, Makutupa, Chamkoroma, Mlali mpaka Pandambili ni barabara muhimu sana kwa Majimbo mawili. Jimbo la Mheshimiwa Spika Mheshimiwa Ndugai Kongwa na Mpwapwa. Na kwa kuwa barabara hili huwa linatengewa fedha kidogo sana kwa ajili ya ukarabati.

Je, ni lini mtatenga fedha za kutosha ili barabara hii iweze kutengenezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Lubeleje, mimi siku hizi namuita mzee wa Godegode, anafuatilia sana ujenzi wa daraja hili na Godegode na maeneo mengine. Nikiri kwamba ni kweli, kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema, kwamba daraja hili lililokuwepo lilijengwa muda mrefu na lilijengwa kwa gharama alizozitaja Mheshimiwa Mbunge, kwa milioni 500. Katika jibu langu la msingi nimezungumza juu ya kutenga milioni 325 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuhakikishie kwanza Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii itafanyika vizuri tunafanya shughuli ya ujenzi kwa kutumia utaratibu wa design and construction. Kwa maana hiyo niseme tu kwamba tumetenga milioni 325 kwa ajili ya ule usanifu ambao utachukua muda mfupi sana kwasababu tutafanyakazi wenyewe kupitia wakala halafu baadaye tutaanza kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nikuhakikishie Mheshimiwa Lubeleje ukiangali kwenye kitabu chetu cha bajeti ukurasa 323 utaona kwamba pamoja na fedha hizi nilizozitaja kwamba baada ya design tutaanza kujenga na tumetenga milioni 180 ili sasa approach ya Kilomita 6 kwenye daraja la Godegode ili ujenzi uende sambamba kwa hiyo kuna fedha zingine milioni 180 tumezitenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalenga kwamba katika ujenzi wetu maeneo haya Godegode na maeneo mengine kusimamia vizuri ili gharama za ujenzi ziende chini huu ni mkakati wetu kama Wizara sio kama kujenga kwa fedha nyingi tumejipanga ili kusimamia vizuri gharama za ujezi ziweze kupungua. Mheshimiwa Lubereje utakubaliana na mimi kwamba sehemu ambapo daraja hili lipo ni sehemu ambayo imejengwa muda mrefu na mmomonyoko ni mkubwa na urefu wa daraja lile ni kubwa sana. Sasa tumejipanga kwamba kwenye daraja na godegode upande wa kulia kwake kama unaelekea kibakwe kwa maana kwamba tutalijenga upande kulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalenga kwamba span ya daraja lile itakuwa fupi, sasa span ikiwa fupi gharama ya ujenzi zitapungua, span ikiwa fupi pia tutatumia muda ili wananchi haya waweze kupata huduma za kupita katika maeneo haya. Na kwa maana hiyo pia tumejipanga ndio maana nikasema tutakuwa na approach tutaboresha ili ku- control mmomonyoko ili daraja hili liwe bora. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lubereje nikutoe wasiwasi kwamba tumajipanga vizuri kwamba tumejipanga vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu B Mheshimiwa Lubereje anasema kumekuwa bajeti ndogo katika eneo la mpwapwa, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mpwapwa ni kati ya Wilaya zilizokuwa katika Mkoa wa Dodoma ambayo ni Makao Makuu na Mpwapwa ndio wilaya pekee ambayo haijaunganishwa vizuri na mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumejipanga kama Serikali kufanya Mpwapwa iwe na barabara nzuri ili sasa iweze ku-support kazi nyingi ambazo zinafanyika katika Makao Makuu. Na kwa ushahidi tu Mheshimiwa Mbunge anafahamu tutaanza ujenzi wa lami kuanzia Mpwapwa kilometa kadhaa kuja kongwa. Lakini Mheshimiwa Lubereje nikuhakikishie kwamba kutoka Mpwapwa kwenda Gulwe kwenda Rudi, Chipogolo na penyewe tunasanifu kwa ajili ya ujenzi wa lami. Na barabara uliyo itaja barabara ya pandambili, Mlali Nghambi yapo kama maeneo manne matano ambayo tumeyatengea fedha za kutosha eeh…

MWENYEKITI: Ahsante

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): …sehemu korofi tumetengea milioni 120 kuna daraja pia milioni 150, tatu kuna zaidi ya milioni 600 ambazo tumezipanga katika mwaka huu wa fedha unaokuja ili kuifanya mpwapwa nao iweze kupata huduma za barabara.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuuliza swali moja la nyongeza:-

Kwa kuwa hospitali ya Wilaya Mpwapwa ilijengwa Mwaka 1975 na kwa kuwa wodi ya Wakina Mama wanaojifungua ni ndogo. Kama walivyosema wenzangu akina mama wanalala wawili, wanalala watatu ambapo ni hatari kaisa kuambukizana magonjwa.

Je, Mheshimiwa Waziri katika bajeti inayokuja, utatenga fedha kwa ajili ya kujenga jengo kubwa la wodi ya akina mama katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Seneta Lubeleje kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba hospitali za wilaya zilizojengwa miaka ya zamani ukilinganisha na uhalisia wa sasa hivi kumekuwa na upungufu wa baadhi ya majengo au msongamano umekuwepo kwasababu idadi ya watu inaongezeka. Naomba Mheshimiwa Mbunge akubaliane na kazi nzuri ambayo inafanya na Serikali. Tumeanza na hizo hospitali 67; kwa kadri Bajeti itakavyoruhusu na uhalisia na kwake pia tutatazama nini cha kufanya.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Kamati yetu ya Utawala na Serikali za Mitaa tulipotembelea Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu, tulikuta madaftari mengi wameorodheshwa watu ambao siyo walengwa, ni vijana ambao ni matajiri, wana mali na nyumba nzuri. Tulikwishatoa ushauri kwenye Wizara hii hawa vijana wote waondolewe. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, orodha ile mlihakiki na kuondoa majina hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba nimjibu swali dogo la nyongeza Mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli siku za nyuma kulikuwa na walengwa wengine ambao wana uwezo lakini walikuwa kwenye mpango. Serikali ya Awamu ya Tano hilo tumelidhibiti na hao wote tuliwaondoa. Ndiyo maana pia katika jibu langu la nyongeza nimesema katika sehemu yetu hii ya pili tunakwenda kielektroniki kudhibiti wale wote ambao wanasema wanatokana na kaya maskini lakini kumbe ni kaya maskini hewa. Hilo tumelidhibiti na tumeboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini ahadi hizi ni za muda mrefu kwamba Serikali ina mpango na mkakati wa kujenga daraja hili la Manamba kwenda Kijiji cha Tambi. Hapa anazungumzia kuhusu usanifu, je, ni lini sasa daraja hili litajengwa? Daraja hili ni upana wa mita 100 na wanafunzi wanashindwa kuvuka, ni lini sasa atajenga daraja hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari wanashindwa kuvuka mto huu kwenda shule ya sekondari na kwenda shule ya msingi na ni kero kubwa sana. Ni lini sasa pamoja na kutathmini mtajenga daraja hilo? Hata Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI analifahamu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Seneta wetu Mheshimiwa Mzee Lubeleje ambapo mimi huwa napenda kumuita grader la zamani makali yale yale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anayosema Mheshimiwa Lubeleje. Daraja lenyewe linaunganisha maeneo ya Mseta na Nambi lakini daraja lile ni kubwa kidogo na sasa hivi kuna korongo hata Mheshimiwa Mbunge anafahamu juzi juzi nilikuwa pamoja naye kule, ukiangalia tuna kazi kubwa ya kufanya. Tulikuwa na fedha kutoka DFID ambapo tulianza katika maeneo ili kuondoa vikwazo, tumekamilisha katika baadhi ya maeneo lakini pale lazima iwe fedha ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika tathmini inayofanyika lengo ni kutafuta fedha kwa sababu daraja lile siyo la shilingi millioni 300 au 4000, ni daraja kubwa linalotaka zaidi ya bilioni 2. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalifahamu daraja hilo na nimuagize Mtendaji wetu Mkuu, watu wameshafanya design pale afike yeye mwenyewe Mhandisi Seif akaangalie ili katika mpango wa bajeti tuweke vipaumbele kwa sababu eneo lile lina watu wengi lazima tuweze kuwaokoa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Lubeleje kwamba jambo lile tunalifanyia kazi kwa nguvu zote.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwaka 2000 mpaka 2010 Serikali iliunda Tume ya Kushughilikia maslahi ya Madiwani na tume hii iliongozwa nami na iliitwa Tume ya Lubeleje kwa ajili ya maslahi ya Madiwani, kwamba Madiwani waongezwe posho kulingana na majukumu yao:-

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri unasema nini kuhusu kuongeza posho ya Madiwani pamoja na kuwalipa Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni nia na lengo kubwa la Serikali ikiwa na uwezo mkubwa unaotosha tungependa kuongeza posho hii ya Waheshimiwa Madiwani ili waweze kujikimu kulingana na kazi wanazofanya katika Halmashauri zetu ambazo ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, swali la msingi hapo mwenyewe umeshuhudia, Mheshimiwa Mbunge anauliza, ni lini Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji wataongezwa posho?

Mheshimiwa Spika, nchi hii tuna mitaa zaidi ya 4,200 na kitu hivi; tuna vijiji zaidi ya 12,000; tuna vitongoji zaidi ya 64,000; na kila mtaa una Wajumbe sita, Kijiji kina Wajumbe 25. Ukipiga hesabu kwa ujumla wake, ni watu wengi kwelikweli; ongeza Madiwani wa Kata na Madiwani wa Viti Maalum.

Mheshimiwa Spika, naomba Waheshimiwa Madiwani waendelee kuchapa kazi, Serikali ya CCM inawaheshimu sana. Uwezo ukipatikana watapata posho, lakini tumeelekeza Halmashauri, wale Madiwani ambao wanadai posho zao na kukopwa, wasikopwe, walipwe kile ambacho kinawezekana kupatikana ili wachape kazi yao. Nakushukuru sana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ilichukua vyanzo vingi vya mapato katika Halmashauri zetu, kwa hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa haina mapato ya kutosha ya kuweza kujenga soko; je, kwa nini Serikali isitoe fedha kwa ajili ya kujenga soko la Mpwapwa kama vile inavyotoa fedha kujenga majengo mengine kama vile Vituo vya Afya na majengo mengine?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa mimi niliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa na kwa kuwa jukumu la Mikopo ya Serikali za Mitaa ni kukopesha Halmashauri ili ziweze kujenga masoko, kujenga Vituo vya Mabasi; je, huo mpango umeishia wapi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa George Malima Lubeleje, kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba kuna vyanzo vingine vilichukuliwa na Serikali Kuu kutoka Serikali za Mitaa kwa maana ya Halmashauri, lakini hizi fedha ambazo zilichukuliwa kuletwa Serikali Kuu, kwa maana Mfuko Mkuu wa Serikali ni fedha ambazo zinatumika kujenga miradi mikubwa ya Kitaifa ambayo inanufaisha maeneo yote ya nchi. Zingeachwa kama ilivyokuwa maana yake kuna Halmashauri zingine zingepata miradi zingine zingekosa miradi, kitendo cha kupelekwa Hazina maana yake fedha hizi zinasimamiwa na Serikali na inapeleka miradi mikubwa ambayo kila Mtanzania mahali popote alipo wananufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niliweke sawa jambo hilo, lakini jibu langu la swali la pili ni kwamba, ni kweli kwa sasa kuna miradi ambayo Halmashauri Kuu inapewa fedha kutoka pengine kwa Wafadhili wa nje, kadri muda ulivyokuwa unaenda miradi hii ilikuwa unapanga mipango ambayo huna uhakika nayo. Sasa Serikali imeleta Mpango Mkakati ambayo ina uhakika hata mikopo kutoka Mfuko wa Serikali za Mitaa ilikuwa ni fedha ambayo ina riba na wakati mwingine haina uhakika sana na kuna Halmashauri zingine zimekopa fedha zinadaiwa mpaka leo hawajawahi kurejesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo Serikalia imetengeneza Mkakati pamoja na Wizara ya Fedha, fedha zipo Halmashauri inaandika andiko na Mheshimiwa Mbunge ni Mjumbe katika Halmashauri yake vikao vya Kamati ya Fedha wanaainisha mradi ambao wanadhani wao utakuwa ni mkakati wao kupata fedha nyingi, wanaleta Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa unaenda Hazina unapitiwa na Wataalam, wakipata fedha hizo wataanzisha mradi mkubwa kama hilo soko Mbunge alivyosema hiyo, hiyo fedha ikipatikana watafanya miradi ambayo wana uhakika nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo juzi nilikuwa Manispaa ya Moshi, wana Mradi wa zaidi ya shilingi bilioni ishirini na nane, Jiji la Dar es Salaam wana bilioni hamsini na nane, maeneo mengine bilioni kumi na sita, kumi na saba, kumi na nane, kwa hiyo fedha zipo Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri husika waandae Andiko la Kimkakati, tufanye tathmini wapate fedha wajenge mradi ambao utapata fedha za uhakika ili waweze kufanya miradi ya maendeleo katika eneo lao. Ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa katika Jimbo la Mpwapwa, ni vijiji nane tu ambavyo havijapatiwa huduma ya umeme, na Vijiji hivyo ni Kiyegea, Kazania, Tumaligo, Mkanana, Ngaramiro, Nana, Mafuto, Kiboriani, Majani na Namba 30.

Je, Mheshimiwa Waziri ni lini vijiji hivi vitapatiwa huduma ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi katika mzunguko wa tatu, katika REA phase lll, mzunguko wa kwanza, ni kwamba tunatarajia kufikia mwezi wa sita, vijiji vilivyokuwa katika mzunguko huo viwe vimekamilika kupewa umeme na vijiji vingine vyote vinavyofuata tunatarajia kwamba vitaingia katika mzunguko wa pili ambao unategemewa kukamilika ndani ya miaka hii kufikia mwaka 2021. Kwa hiyo, vijiji hivyo kama havikuwemo katika mzunguko huo wa kwanza, basi naamini kwamba vitaingia katika huu mzunguko wa pili.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri mimi nimekuwa niliwahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya wakati ule Halmashauri zote vyanzo vyote vilikuwa pale, lakini kwa kuwa Serikali imechukua vyanzo vyote na tulikubaliana mpeleke ruzuku ya kutosha kwenye Halmashauri ili viongozi hawa Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Madiwani walipwe. Kwa nini hamuongezi ruzuku kwenye Halmashauri za Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Senator Mzee Lubeleje kama ifuatavyo:-

Ni kweli ni Mwenyekiti wa Halmashauri Mstaafu na alivyozungumza ni kweli wakati huo, lakini sasa hivi ni kweli kwamba baadhi ya vyanzo vimechukuliwa ili viweze kuratibu kwa sababu kuna Halmashauri ambazo zilikuwa na majengo mengi na mabango mengi na walikuwa wanaweza kupata fedha nyingi kwa wakati mmoja tofauti na maeneo mengine, Serikali imetumia busara kwamba fedha hizi zikusanywe centrally, lakini zipelekwe kwenye miradi ya wananchi ambayo ni nchi nzima hata Halmashauri ambayo ilikuwa na mapato machache ya mabango au na majengo inapata miradi mikubwa ya kimkakati ili maendeleo yaende katika msambao unaofanana katika nchi yetu.

Lakini hoja yake ya kuongeza posho na kupeleke ruzuku, miradi mingi ya ruzuku ilikuwa inategemea pia na wafadhili kutoka nje, sasa hivi ndiyo tukasema fedha zipo za kuanzisha miradi ya kimkakati na maelekezo yameenda kwenye Mikoa yote na Halmashauri zote. Ni wataalamu wa Halmashauri yako Mheshimiwa Lubeleje wanakaa, wanaandaa andiko, wanakaa na watu wa Wizara za Fedha na TAMISEMI, miradi inapelekwa ndiyo maana nikasema ukipata miradi ya kimkakati, masoko, stand kubwa kubwa zile mapato yataongezeka na kwa hiyo Halmashauri itaweza kulipa posho za Wenyeviti wa Mitaa.

Mheshimiwa Spika, niseme maneno ya nyongeza wenyeviti wa mitaa tunatambua kazi kubwa sana ambayo wanafanya na ndiyo maana miradi yote mikubwa ya kimkakati ipo kule wanaisimamia kwa kushirikiana na viongozi wa Kata na Madiwani na wengine, uwezo wetu wa Serikali ukiwa mkubwa tungeweza kulipa mishahara na posho kubwa kubwa, kwa sasa hatujafikia huko.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Wenyeviti wa Mitaa waendelee kufanya kazi kwa sababu wameaminiwa na watu wao, uwezo wa Serikali …, lakini Halmashauri zetu wajipange kila kinachopatikana wasiwasahau Wenyeviti wa Mitaa, wawawezeshe ili waweze kufanya kazi zao vizuri. Ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, barabara hii ninayoizungumzia kutoka Mima – Nkanana – Chibwegele eneo korofi siyo kilomita 5 ni zaidi ya hapo. Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha za kutosha kwa sababu shilingi milioni 42 hazitoshi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutambua kwamba barabara ya kutoka Gulwe – Berege - Mima - Chitope inahitaji shilingi bilioni 1.6 ili ipate matengenezo makubwa. Sasa ni lini fedha hizi zitatafutwa ili barabara hiyo iweze kufanyiwa ukarabati? Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ameshapita barabara hiyo. Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze Naibu Mawaziri wawili kwa majibu mazuri kwa maswali ya awali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lubeleje ambaye mimi namwita greda la zamani makali yaleyale siku zote ni Mbunge ambaye anafuatilia jimbo lake, ni kweli tulipokwenda ziarani jimboni kwake tumebaini changamoto kubwa, si barabara hiyo tu hata kwenda Nambi, Tubugwe na maeneo mbalimbali kuna changamoto kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana ukiangalia katika bajeti ya mwaka huu na Mheshimiwa Lubeleje anafahamu kwamba kwa kuwepo na kipaumbele kwanza, sababu changamoto yake kubwa hata pale mjini tumeamua mwaka huu tutaenda kuwawekea barabara za lami lakini ile barabara ambayo ina changamoto kubwa, siku ile tulipita katika mazingira magumu sana, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba awe na amani kwamba tutafanya kila liwezekanalo barabara hii ambayo kwa kweli haipitiki na shilingi milioni 42 ili kuifanya marekebisho makubwa. Hata hivyo, nimhakikishie kwamba ni commitment ya Serikali na hasa katika Jimbo la Mpwapwa na Wilaya nzima ya Mpwapwa tutafanya kila liwezekanalo ili wananchi wa Mpwapwa wafaidi matunda mazuri ya Mbunge wao ambaye ni senior MP katika Bunge hili.