Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. George Malima Lubeleje (20 total)

MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa wanakabiliwa na tatizo kubwa la njaa, na katika msimu wa mwaka 2014/2015 mvua hazikunyesha kabisa na kusababisha wananchi wengi kukosa chakula kutokana na ukame; na Serikali imekwisha tamka kwamba hakuna mwananchi atakayekufa kwa njaa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kugawa chakula cha njaa Wilaya ya Mpwapwa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza napenda niishukuru sana Serikali kwa kutupatia kiasi kidogo cha chakula katika Wilaya ya Mpwapwa.

Kwa kuwa, Wilaya ya Mpwapwa ina Majimbo mawili, Jimbo la Mpwapwa na Jimbo la Kibakwe, na kwa kuwa chakula hicho ambacho tumepatiwa ni kidogo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutuongezea chakula cha njaa Wilaya ya Mpwapwa?

Swali la pili, kwa kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wameacha kulima mashamba yao wanalima vibarua ili wapate hela ya kununua chakula. Je, utakubaliana na mimi kwamba iko haja sasa ulete chakula hicho haraka kwa Wilaya ya Mpwapwa na Wilaya ya Kongwa?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU - (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi anayekufa kwa njaa kutokana na ukosefu wa chakula, Serikali imekuwa ikifanya tathmini ya hali ya chakula na lishe katika maeneo mbalimbali nchini na kutoa chakula cha msaada kwenye Halmashauri zilizoonekana kuwa na upungufu wa chakula ikiwemo Mpwapwa.
Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Disemba, 2015 Serikali ilitoa chakula cha msaada tani 200 za mahindi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. Aidha, kati ya tarehe 4 na 7 Januari, 2016 Serikali imepeleka Wilayani Mpwapwa chakula cha msaada tani 1,619 na shilingi milioni 35 kwa ajili ya kununua mbegu za mtama na mihogo. Hivyo jumla ya chakula cha msaada kilichopelekwa Wilayani Mpwapwa mwezi Disemba, 2015 na Januari, 2016 ni tani 1,819.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa chakula cha kupunguza makali ya bei ya soko tani 6,000 kwa Mkoa wa Dodoma kupitia wafanyabiashara wa Mkoa huo ili kuwezesha upatikanaji wa chakula chenye bei nafuu kwa wananchi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa wananchi waliopo kwenye maeneo yenye ukame wakiwemo wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha kuwa wanalima mazao yanayostahimili ukame na kufuata kanuni bora za kilimo ili kupunguza tatizo la upungufu wa chakula.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU - (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa Mheshimiwa George Malima Lubeleje, kwamba Serikali inatambua jukumu lake la kuwalinda na kuwasaidia wananchi wote wanaopatwa na matatizo mbali mbali, ikiwemo baa la chakula.
Kuhusu swali lake la pili, tunafahamu umuhimu hiyo na tathmini itafanywa ili kuwezesha upatikanaji wa chakula hicho kwa haraka.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliahidi kujenga barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa kwa kiwango cha lami; na barabara hiyo tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu.
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa yenye urefu wa kilometa 55 umeanza kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Ujenzi wa kiwango cha lami wa sehemu ya barabara hii ulianza katika mwaka wa fedha 2013/2014 ambapo jumla ya kilometa sita zilianza kujengwa na kukamilika kutoka Kongwa Junction hadi Kongwa, kilometa tano, pamoja na Mpwapwa mjini kilometa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya pili ya ujenzi wa barabara hii uliendelea katika mwaka wa fedha 2014/2015 ambapo kilometa moja ilijengwa kutoka Kongwa Mjini hadi Ugogoni; na kilometa moja inaendelea kujengwa Mjini Mpwapwa katika mwaka wa fedha 2015/2016.
Ujenzi wa barabara hii utaendelea kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 kulingana na upatikanaji wa fedha. Lengo likiwa ni kuikamilisha barabara ya Mbande - Kongwa Junction hadi Kongwa na Kongwa Junction – Mpwapwa – Gulwe hadi Kibakwe ambapo pana jumla ya kilometa 102.17 kwa kiwango cha lami.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Barabara kutoka Gulwe - Berege - Chitemo- Mima- Sazima - Igoji Kaskazini - Iwondo - Fufu inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ni mbaya sana na inapitika kwa shida sana hasa wakati wa mvua/masika.
Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba ipo haja kubwa ya barabara hiyo kuhudumiwa na Serikali Kuu (TANROADS) badala ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambayo uwezo wake kifedha ni mdogo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, baba yangu na Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kumshauri Mheshimiwa Mbunge na kama ambavyo tumeongea kwamba maombi hayo yaanzie katika Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dodoma na ninamhakikishia Mheshimiwa Lubeleje na kama ambavyo tumewasiliana maombi haya yatakapofika Wizarani tutayafikiria pamoja na maombi yale mengine yote na nina uhakika yatafika mahali pale ambapo yanatakiwa. Hayo yote ni kwa mujibu au matakwa ya Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na Kanuni ya 43(1) ya Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009.
Aidha, ninatoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara zinazotengwa kupitia bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ili iweze kupitika majira yote ya mwaka na kwa kweli tusiendelee kumpa kazi kubwa Mheshimiwa Lubeleje ya kuja Wizarani kwetu kama ambavyo anaifanya ili tuweze kuikamilisha hii barabara iweze kupitika na kusiwe tena na malalamiko makubwa kama yalivyo kwa sasa, kwa mujibu wa Mheshimiwa Lubeleje kadri anavyoyaleta Wizarani kwetu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Mji wa Mpwapwa wenye wakazi zaidi ya 41,000 unakabiliwa na tatizo kubwa sana la maji, ambapo wananchi wanapata shida kubwa sana kutembea mwendo mrefu zaidi ya kilometa tano kufuata huduma ya maji; na kuna baadhi ya mitambo imeharibika na Mamlaka ya Maji Safi na Salama hawana fedha za kukarabati mitambo hiyo. Je, Serikali haioni kwamba ipo haja kubwa ya kusaidia ukarabati wa mitambo hiyo ili wananchi wa Mji wa Mpwapwa na vitongoji vyake waweze kupata huduma ya maji karibu na makazi yao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya ukarabati wa mitambo ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ya Mpwapwa, kwa gharama ya kiasi cha shilingi milioni 24.5. Kazi zilizotekelezwa ni ununuzi na ufungaji wa mota mbili, pamoja na control panel ambazo zimebadili kutoka mfumo wa star delta starter, kwenda soft starter, kwa ajili ya kuendesha mota hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa kazi hiyo mwezi Aprili mwaka 2016, kumeongeza uzalishaji wa maji kutoka asilimia 59 hadi kufika asilimia 71, kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuondoa tatizo la kuungua mara kwa mara kwa mota za mitambo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kufanya matengenezo ya mara kwa mara, ili kuhakikisha huduma ya maji katika Mji wa Mpwapwa inakuwa endelevu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Serikali ilikwishaanza kujenga vituo vya afya katika vijiji vya Mima na Mbori na ujenzi huo umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo ili wananchi wa maeneo hayo wapate huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa jengo la Kituo cha Afya Mima ulianza mwaka 2008/2009 ambapo mpaka sasa umegharimu kiasi cha shilingi milioni 60. Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) liko katika hatua ya umaliziaji. Kazi ambazo hazijakamilika ni uwekaji wa dari, samani pamoja na vifaa tiba. Ili kumaliza kazi hiyo zimetengwa shilingi milioni 15 katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Aidha, imejengwa nyumba ya watumishi ambayo imekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 48.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo cha Afya Mbori ulianza katika mwaka wa fedha 2011/2012 ambapo mpaka sasa umegharimu kiasi cha shilingi milioni 82. Kazi zilizofanyika ni upauaji, upakaji rangi nje na ndani, uwekaji wa madirisha ya vioo pamoja na kupiga dari. Kazi zilizobaki ni pamoja na ufungaji wa umeme, ufungaji wa milango ya ndani 16, ufungaji wa taa na uwekaji wa mfumo wa maji safi na taka. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, kituo hiki kilitengewa shilingi milioni 15 ili kumalizia kazi zilizobaki na shilingi milioni 35 zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 ili kujenga nyumba ya watumishi (two in one).
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Vijiji vya Iyoma, Kisokwe, Idilo, Lukole, Lupeta, Bumila, Makutupa, Mkanana, Igoji Kaskazini (Isalaza), Nana, Kisisi, Ngalamilo, Godegoge, Mzogole, Mugoma, Kiegea, Kazania, Igoji Kusini, Chamanda, Simai, Makawila, Iwondo, Lupeta, Gulwe, Majami, Mwenzele na Mlembule katika Wilaya ya Mpwapwa vina matatizo makubwa sana ya maji na hivyo kusababisha wananchi wa vijiji hivyo kutembea umbali wa zaidi ya kilometa tano hadi kumi kutafuta maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima vya maji katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.58 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. Kazi zitakazofanyika ni uchimbaji wa visima pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ya maji iliyopo. Vijiji vilivyopo katika mpango ni Iyoma, Mzase, Mima, Bumila, Lukole, Kingiti, Kibakwe, Mbori, Mbuga, Iguluwi, Chogola, Kidenge, Iramba, Mlunduzi na Seluka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zinazoendelea kwa sasa katika uboreshaji wa huduma ya maji ni utafiti wa maji ardhini na uchimbaji visima virefu katika vijiji vya Mima, Mzase, Bumila na Iyoma. Uchimbaji wa visima virefu katika kijiji vya Mima na Mzase umekamilika. Kazi ya kuchimba visima virefu katika kijiji vya Bumila na Iyoma unaendelea na utakamilika mapema Novemba, 2016.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Jukumu la MSD ni kununua na kusambaza dawa na vifaa tiba; na MSD
inakabiliwa na tatizo kubwa la fedha za kununua dawa na vifaa tiba:-
Je, Serikali itakubaliana nami kwamba ipo haja kubwa ya MSD
kuwezeshwa kuwa na Fungu (Vote) maalum kutoka Hazina?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George
Malima Lubeleje, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la MSD kuwa na Fungu (Vote) lilishaanza
kushughulikiwa tangu mwezi Desemba, 2015. Hatua hii ilichukuliwa kufuatia
ushauri uliotolewa na iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za
Jamii. Wizara iliwasilisha ombi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora ambayo ndio yenye mamlaka na majukumu ya utoaji wa mafungu
(Votes).
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupitia maombi hayo walishauri
kwamba, MSD ipewe line item ndani ya kifungu (sub vote) chini ya Fungu la
Wizara yaani Fungu Na. 52. Ushauri huu ulitolewa kwa kuzingatia utaratibu uliopo
Serikalini kwamba, Fungu hutolewa kwa taasisi za Serikali Kuu peke yake ikiwa ni
maana ya Wizara na Ofisi za Wakuu wa Mikoa. Baada ya kupokea ushauri huu,
Wizara iliwasilisha ombi kwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya MSD
kupatiwa line item.
Mheshimiwa Naibu Spika, MSD wameshapatiwa line item ndani ya
Kifungu 2005 chini ya kitengo cha Huduma za Dawa (Pharmaceutical Services
Unit) pale Wizara ya Afya. Baada ya kupatiwa line item ndani ya kifungu hicho
yaani kifungu 2005 itahitajika kutenga bajeti, mwaka ujao wa fedha 2017/2018
inayokidhi mahitaji ya msingi kwa ajili ya MSD kutekeleza majukumu yake.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Kila mwaka Bunge limekuwa likipitisha Bajeti ya Serikali kuhusu Wizara, Mikoa na Wilaya lakini kumekuwa na ucheleweshwaji wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hususan katika Mikoa na Wilaya na kupelekea miradi mingi kutokamilika.
Je, ni sababu gani za msingi zinazofanya Serikali kuchelewa kuleta fedha za Miradi ya Maendeleo katika Mikoa na Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwenendo wa utaoji wa fedha
za utekelezaji wa Bajeti ya Serikali hutegemea mapato ya Serikali kupitia ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo vya kodi na visivyo vya kodi, mikopo pamoja na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo. Katika miaka ya hivi karibuni, mwenendo wa upatikanaji wa mapato ya Serikali umekuwa na changamoto nyingi katika miezi ya mwanzo wa mwaka wa fedha ambapo mikopo ya masharti ya biashara kutoka kwenye taasisi za fedha pamoja na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo imekuwa haipatikani kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, sababu kuu zinazochangia kutopatikana kwa wakati kwa fedha hizo ni pamoja na majadiliano na washirika wa maendeleo kuchukua muda mrefu, baadhi ya washirika wa maendeleo kutotimiza ahadi zao kutokana na sababu mbalimbali na kupanda kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la fedha la kimataifa.
Mheshimiwa Spika, fedha zinazokusanywa kutokana
na vyanzo vya mapato ya ndani zimekuwa zikielekezwa kugharamia matumizi mengine yasiyoepukika kama vile ulipaji wa mishahara, deni la taifa, ulipaji wa madeni ya watumishi, watoa huduma, wazabuni na wakandarasi pamoja na utekelezaji wa miradi yenye vyanzo mahususi kama vile Taasisi ya Umeme Vijijini, Mamlaka ya Elimu Tanzania, Mfuko wa Barabara, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Mfuko wa Maji na Mfuko wa Reli.
Mheshimiwa Spika, sehemu kubwa ya fedha za miradi
ya maendeleo katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa hutumia fedha za nje. Utoaji wa fedha hizo kutoka kwa washirika wa maendeleo huzingatia mpango kazi, masharti na vigezo mbalimbali vilivyowekwa ambavyo hupaswa kuzingatiwa na mamlaka zinazotekeleza miradi.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa miradi
ya maendeleo inatekelezwa badala ya kutegemea fedha za nje ambazo uhakika wake umekuwa hautabiriki, Serikali imeendelea kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hadi kufikia shilingi bilioni 8,702.7 kwa mwaka 2016/2017 ikilinganishwa na shilingi bilioni 1,366.1 mwaka 2010/2011. Aidha, Serikali yetu imeendelea kuboresha vyanzo vya ndani vya Halmashauri na kuzijengea uwezo zaidi kwa kukusanya mapato ili kutekeleza miradi mingi kwa fedha za ndani badala ya fedha za nje.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Serikali ilikuwa na mpango wa kuanzisha Kata mpya ya Mkanana ambayo ina vijiji vya Mkanana na Chibwegele na vipo mlimani ambapo hakuna huduma yoyote kama vile barabara ambayo ni mbaya sana na hupitika kwa shida wakati wote.
Je, mpango huo wa kuanzisha Kata mpya umefikia wapi?
Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba kuanzishwa kwa kata hiyo kutawezesha kuwasogezea karibu huduma mbalimbali wananchi wa kata hiyo kuliko ilivyo sasa ambapo Makao Makuu yapo Kijiji cha Chitemo, umbali wa kilometa 45?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Geogre Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kwa jitihada anazozifanya kupeleka maendeleo katika Jimbo lake. Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria maombi ya kugawa kata mpya yanaanzia katika Mikutano Mikuu ya Vijiji, Kamati ya Maendeleo ya Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa. Vikao hivyo vikikubali maombi hayo na endapo yataonekana yamekidhi vigezo, Serikali haitasita kuanzisha Kata hiyo ya Mkanana kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha maeneo mapya ya utawala zikiwemo kata, ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Hivyo, kama ilivyoelezwa katika sehemu
(a) ya jibu langu hapo juu, endapo Kata ya Mkanana itakidhi vigezo vya kuanzishwa, ili kurahisiaha upatikanaji wa huduma na kuchochea maendeleo katika kata hiyo, itafanyika.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Serikali ilikuwa na mpango wa kuchimba mabwawa katika vijiji vya Msagali, Bumila, Makutupa, Lupeta, Inzomvu, Vibelewele, Kimagai, Chunyu na Ng’ambi ambayo yatahudumia wananchi pamoja na mifugo na kilimo cha umwagiliaji.
Je, Serikali imefikia hatua gani ya utekelezaji wa mpango huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TASAF III imekamilisha uchimbaji wa malambo sita katika vijiji vya Bumila, Msagali, Lupeta, Chunyu, Kazania na Nzogole kwa gharama ya shilingi 83,194,200. Wananchi 19,304 watapata huduma ya maji kupitia vyanzo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu umefanyika katika kijiji cha Chunyu kwa ajili ya kujenga bwawa kubwa ambalo litahudumia vijiji vya Msagali, Berege, Kisokwe, Chunyu na Ng’ambi. Jumla ya shilingi bilioni 17 zitahitajika kukamilisha kazi hii. Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuanza ujenzi wa bwawa hilo.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Mpango wa MKURABITA ni muhimu katika kuwaletea wananchi maendeleo lakini unakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa fedha na hivyo kushindwa kuendesha shughuli za urasimishaji kwa ufanisi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mfuko wa urasimishaji utakaokuwa maalum katika Serikali za Mitaa ili kutatua tatizo la ukosefu wa fedha za kuendeleza shughuli za urasimishaji?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la ndugu yangu, mdogo wangu, somo yangu, Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa MKURABITA ni muhimu katika kuwaletea wananchi maendeleo, lakini mpango huu unakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa fedha na hivyo kushindwa kuendesha shughuli za urasimishaji kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania ulianzishwa na Serikali kwa lengo la kuwapa nguvu ya kiuchumi wananchi kwa kuwawezesha kumiliki ardhi na kuendesha biashara katika mfumo rasmi na wa kisasa unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa tatizo la upungufu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za urasimishaji na ndiyo maana Serikali imedhamiria kuanzisha Mfuko Maalum wa Urasimishaji utakaowezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yake ya urasimishaji bila vikwazo. Mfumo utakaotumika ni kwa Serikali kupitia MKURABITA kuweka fedha za dhamana katika taasisi za fedha zilizokubalika ili kuwezesha Halmashauri kukopa na hivyo kuendesha shughuli zake za urasimishaji. Kwa kutumia mfumo huu urasimishaji utakuwa nafuu, haraka na endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MKURABITA kwa kushirikiana na Benki ya NMB imekamilisha utaratibu wa utekelezaji wa miradi ya majaribio katika Manispaa ya Iringa na Halmashauri za Wilaya za Mbozi na Momba Mkoani Songwe. Baada ya majaribio haya ambayo yamepangwa kufanyika kwa miaka miwili, utekelezaji utaanza nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 243, fedha ambayo itatumika kama dhamana kwa ajili ya mikopo ambayo itakopwa na Halmashauri ambazo zitatekeleza miradi ya maendeleo. Aidha, urejeshwaji wa mikopo hii utatokana na michango ya wananchi wenyewe.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Barabara ya kutoka Mima hadi Mkanana ni mbaya sana na inapitika kwa shida sana wakati wote; na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa haina uwezo kifedha wa kuifanyia mategenezo makubwa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia matengenezo makubwa barabara hiyo ili iweze kupitika wakati wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mima hadi Mkanana ni barabara mlisho ya tabaka la udongo yenye urefu wa kilometa 26.5, inayounganisha barabara ya Kibakwe hadi Wotta yenye urefu wa kilometa 26 na barabara ya Gulwe hadi Seluka yenye urefu wa kilometa 64.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuifanyia matengenezo barabara hiyo ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Vijiji vya Mima na Mkanana. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 shilingi milioni 40.84 zilitumika kufanyia matengenezo ya sehemu korofi urefu wa kilometa nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha 2018/2019, TARURA imetenga shilingi milioni 57 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi urefu wa kilometa 6.5 na matengenezo ya kawaida urefu wa kilometa 10 ili iweze kupitika kwa wakati wote.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Jimbo la Mpwapwa lina tarafa mbili, yaani Tarafa ya Mpwapwa na Tarafa ya Mima, lakini tangu kuanzishwa kwa Tarafa ya Mima hakuna miundombinu yoyote iliyojengwa kama vile Ofisi ya Tarafa na vyumba vya watumishi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Ofisi ya Afisa Tarafa na za watendaji wengine wa ngazi ya tarafa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Afisa Tarafa wa Tarafa ya Mima hajajengewa ofisi, anatumia Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Mima kutekeleza majukumu yake. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga Sh.50,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Afisa Tarafa huyo itakayojengwa katika Kijiji cha Mima.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Stesheni ya treni ya Kidete - Godegode - Gulwe na Msagali treni hukwama mara kwa mara kutokana na mafuriko wakati wa mvua na Serikali ina mpango wa kujenga reli ya standard gauge kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamisha reli hiyo kuanzia Stesheni ya Kidete - Godegode - Gulwe mpaka Msagali na kupitisha eneo lingine ambalo hakuna mafuriko ili kuondoa usumbufu wa abiria ambao hukaa maeneo hayo treni inapokwama au reli inapochukuliwa na mafuriko?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seneta George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la mafuriko katika eneo hili ni la muda mrefu na Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi za kukabiliana na changamoto hii zikiwemo ujenzi wa mabwawa pamoja na kuendelea kutafuta fedha kutoka taasisi mbalimbali za kifedha kwa ajili ya ujenzi wa suluhisho la kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA tayari limekwishakamilisha upembuzi yakinifu kuhusu upatikanaji wa suluhisho la kudumu katika eneo hilo. Aidha, mazungumzo baina ya Serikali yetu na Serikali ya Japan yanaendelea ili kupata fedha kwa ajili ya kutatua tatizo hili la mafuriko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ili kuepukana na uharibifu unaojirudia kila mwaka kutokana na mafuriko, yafuatayo yanafanyika katika ujenzi wa reli mpya ya standard gauge:-
(a) Reli mpya haitokuwa karibu na mito na kuipitisha vilimani zaidi ya kingo za Mito ya Mkondoa na Chinyasungwi na kuna maeneo korofi ambapo reli itakuwa zaidi ya kilometa mbili kutoka reli ya sasa ilipo.
(b) Reli itajengwa ndani ya mahandaki yaani tunnels na madaraja yenye mihimili iliyoinuliwa juu zaidi. Kwa kuzingatia utatuzi huu, kutajengwa mahandaki manne yatakayokuwa na umbali wa jumla ya kilometa 2.75 pamoja na madaraja yenye uwazi yaani span ya mita 400.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kutoa wito kwa wnanachi wanaoishi jirani na reli zetu wazingatie na kuheshimu eneo la njia za reli kuepuka uharibifu wa reli zetu ambazo zinagharimu pesa nyingi kuzirekebisha.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Waheshimiwa Madiwani wana majukumu mengi ya kufanya katika kata zao; na posho wanayolipwa kwa mwezi hailingani kabisa na majukumu yao na ni ndogo sana:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza posho ya Waheshimiwa Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiongeza posho na maslahi ya Madiwani nchini kwa awamu kulingana na uwezo wa halmashauri kukusanya mapato ya ndani. Serikali ilipandisha posho za mwezi za Madiwani kutosha Sh.120,000 kwa mwaka 2012/2013 hadi shilingi 250,000 kupitia Waraka wa tarehe 16, Agosti, 2012 na posho za madaraka kwa Wenyeviti wa Halmashauri na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Halmashauri. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2014/2015 kupitia Waraka wa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa wa Tarehe 23, Desemba, 2014, Serikali ilipandisha posho za Madiwani kutoka Sh.250,000 hadi Sh.350,000 kwa mwezi kwa Madiwani na Sh.350,000 hadi Sh.400,000 kwa mwezi kwa Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya pamoja na posho nyingine kama ilivyoainishwa kwenye Waraka wa tarehe 26, Novemba, 2007.

Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko la posho na maslahi ya Madiwani inatokana na halmashauri kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani. Hivyo, natoa wito kwa halmashauri kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri ili kujenga uwezo wa ndani na kulipa posho hizo kwa Madiwani.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Katika Jimbo la Mpwapwa Vijiji vya Mkanana, Nalamilo, Kiboriani, Igoji Kaskazini, Mbori, Tambi, Nana, Majani (Mwenzele), Mafuto, Kiegea, Kazania, Chimaligo, Mbugani, Chilembe, Mazaza, Mwanjili, (Makutupora) na Chibwegele havina huduma ya umeme:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia huduma ya umeme vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya vijiji 31 katika Wilaya ya Mpwapwa vitapatiwa umeme kupitia Miradi ya Umeme Vijijini inayoendelea. Kupitia Mradi wa REA III Mzunguko wa Kwanza unaoendelea jumla ya vijiji 14 vitapatiwa umeme. Hadi sasa Vijiji vya Mbori, Tambi, Mnase, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mpwapwa, Kimangai na Chunyu Sekondari vimepatiwa umeme kupitia Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA III) Mzunguko wa Kwanza unaoendelea kutekelezwa hivi sasa na mkandarasi Kampuni ya A2Z Ifra Engineering Limited kutoka nchini India. Kazi za mradi katika Wilaya ya Mpwapwa zinahusisha ujenzi wa njia za umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 9.45, njia za umeme wa msongo kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 68, ufungaji wa transfoma 34 za kVA 50 na 100, pamoja na kuunganisha umeme kwa wateja wa awali 1,148 na gharama za mradi ni shilingi bilioni 2 na milioni 600.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vilivyosalia ikiwa ni pamoja na Mkanana, Ngalamilo, Kiboriani, Nana, Majami, Mafuto, Kiegea, Kazania, Chimaligo, Mbugani, chihembe, Mazaza, Mwanjiri na Chibwegerea vitapatiwa umeme katika Mzunguko wa Pili wa Mradi wa REA III unaotarajiwa kuanza Julai, 2019 na kukamilika Juni, 2021. Ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Daraja la Godegode limesombwa na maji wakati wa mvua za masika na daraja hilo ni kiungo kikubwa kati ya Jimbo la Kibakwe na Jimbo la Mpwapwa ambalo ndiyo Makao Makuu ya Wilaya Mpwapwa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja hilo ili kurudisha mawasiliano kati ya Wananchi na Kata za Godegode, Pwaga, Lumuma, Mbuga na Galigali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli daraja la Godegode lilisombwa na maji wakati wa mvua kubwa iliyonyesha kipindi ha masika mwaka 2018. Kwa kuzingatia umuhimu wa daraja hilo, Serikali ina mpango wa kurudisha mawasiliano kati ya Mpwapwa na Kata ya Godegode, Pwaga, Lumuma, Mbuga na Galigali kwa kujenga Daraja jipya. Ujenzi wa Daraja hilo utaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2019/20 ambapo jumla ya shilingi milioni 325 imetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Kati ya Kijiji cha Mbori na Kijiji cha Tambi upo mto ambao hujaa maji wakati wa mvua na kusababisha wananchi na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Tambi na Sekondari ya Matomondo kushindwa kuvuka:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja katika mto huo ili wananchi na wanafunzi waweze kuvuka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umepanga katika mwaka wa fedha 2019/2020 kufanya usanifu kwa ajili ya ujenzi wa daraja linalounganisha Vijiji vya Mbori na Tambi vilivyopo katika Wilaya ya Mpwapwa ili kurahisisha mawasiliano kati ya maeneo hayo. Kazi hiyo ya usanifu itakapokamilika itawezesha kujua gharama zinazohitajika ili kutafuta fedha za kuanza ujenzi wa daraja hilo.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Soko la Mji wa Mpwapwa, ni dogo, limechakaa na halifanani kabisa na hadhi ya Mji wa Mpwapwa ambao idadi ya watu ni zaidi ya laki moja?

Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ujenzi wa soko jipya na la kisasa katika mji huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa inafahamu changamoto ya udogo wa soko la Mji Mpwapwa na imekwishaandaa mikakati ya kujenga soko hilo la kisasa linaloendana na hadhi ya idadi ya watu katika eneo hilo. Halmashauri imetenga eneo katika Kiwanja Na. 61 Kitalu B Mazae chenye ukubwa wa mita za mraba 15,000 kilichopo katika Kata ya Mazae.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri inaendelea kuandaa Andiko la Mradi pamoja na kufanya usanifu ili iweze kuwasilisha andiko hilo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na hatimaye Wizara ya Fedha na Mipango kupitia utaratibu wa Miradi Mikakati, vilevile Halmashauri inaendelea na mazungumzo na uongozi wa Mradi wa Local Investmest Climate ili kupata fedha za ujenzi wa soko. Ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Serikali ilikuwa na Mpango wa kuifanyia matengenezo makubwa barabara ya kutoka Mima kwenda Mkanana hadi Chibwegele, Mpango huo haujatekelezwa mpaka sasa.

Je, ni lini Serikali itatekeleza Mpango huo ili barabara hiyo iweze kupitika wakati wote bila matatizo kuliko ilivyo sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mima hadi Mkanana yenye urefu wa kilomita 23 inaunganisha Kijiji cha Mkanana kilichopo Uwanda wa Mlimani na barabara ya Wilaya iitwayo Gulwe, Chitope inayoambaa uwanda wa chini wa safu za mlima. Barabara hii inahitaji matengenezo makubwa ya kuwekewa tabaka la zege katika sehemu yenye miamba na mlima kwa urefu wa kilomita tano, changarawe kwenye maeneo ya tambarare na ujenzi wa vivuko.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 99 kwa ajili ya kufanya matengenezo makubwa ya barabara ya Gulwe - Chitope yenye urefu wa kilomita 58.8 ambayo inaunganisha barabara ya Mima - Mkanana hadi Chibwegele, Makao Makuu ya Wilaya na Barabara kuu ya Iringa - Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa barabara ya Mima - Mkanana inafanyiwa matengenezo kwenye maeneo korofi kwa urefu wa kilomita tano kwa gharama ya shilingi milioni 42. TARURA imefanya tathmini ya kuikarabati barabara hiyo na kubaini kuwa kiasi cha shilingi bilioni 1.6 zinahitajika ili iweze kupitika katika nyakati zote. Hivyo, Serikali inaendelea kutafuta kiasi hicho cha fedha ili kuiwezesha TARURA kukamilisha kazi hiyo.