Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joseph George Kakunda (25 total)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa kulikuwa na maelekezo Serikalini kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya Wizara za Kisekta za SMT na zile za SMZ ambayo yalikuwa yanahimiza ushirikiano wa karibu wa kitaalamu na utafiti na pale Wizara ya Maji ilikuwa imepangwa, Waziri wa Sekta ya Maji Bara na Zanzibar tarehe 8 Juni, 2014; mkutano ule ukaahirishwa kusubiri Bunge la Katiba:-
Je, kwa sasa hivi maelewano hayo yanaendeleaje kuimarishwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya kazi ya Ofisi ya Makamu wa Rais ni kuratibu mahusiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mambo yasiyo ya Muungano. Mwezi wa kwanza tumetengeneza ratiba ya vile vikao ambavyo viliahirishwa na mambo ambayo yalibaki kufanyika katika kuhakikisha kwamba mahusiano hayo yanaimarishwa.
Kwa hiyo, moja ya kikao kilichopangwa kufanyika na ambacho tumeweka fedha kwenye bajeti ili kifanyike, ni pamoja na hicho unachoongelea Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kuwapa faraja na taarifa wenzetu wa Zanzibar kwamba tumedhamiria kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba Muungano wetu unaimarika katika mambo ya Muungano na yale yasiyo ya Muungano na kazi hiyo tutaifanya kwa nguvu ili kutimiza ahadi yetu kama tulivyowaahidi Watanzania. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Matatizo ya maji kwenye maeneo ya Shinyanga na Korogwe ni sawa na matatizo kwenye maeneo yetu. Naomba Serikali ituambie na iwape matumaini wananchi wa Tarafa za Sikonge, Kiwele, Inyonga mpaka Kwilunde ambako yeye Mheshimiwa Kamwelwe anawakilisha; ni lini sasa shida za maji za wananchi hao zitapungua au zitaisha kabisa? Ahsate sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Sikonge, niseme kwamba tulikuwa tumetoa nafasi kwamba kila halmashauri ilete vipaumbele ya vijiji ambavyo wataanza navyo katika kutekeleza programu ya maji. Kwa hiyo, hayo maeneo anayoyasema Mheshimiwa Mbunge naamini kabisa halmashauri yake imeweka ndivyo vipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema katika miaka mitano tunataka tupeleke miradi ya maji, kwa maana ya upatikanaji wa maji na ule mtawanyiko utakuwa kwa asilimia 85 ikifika mwaka 2020. Katika kutekeleza miradi hii ndiyo wao watachagua ni ipi tuanze na maeneo yale ambayo hayana maji kabisa wangeweka ndiyo kipaumbele ili kusudi tufikie asilimia hii tunayotaka kuifikia tukifika mwaka 2020. Kwa hiyo, yeye ndiye anajua vizuri zaidi majina ya vijiji na zile kata na wao ndiyo wanatakaoweka vipaumbele, Serikali tutaviwekea bajeti ili tuweze kufikia lengo na wananchi wetu waweze kupata maji.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa kuwa matengenezo aliyosema Mheshimiwa Naibu Waziri yalihusu kukwangua tu na kusawazisha barabara, badala ya kuweka kifusi na kushindilia, hali ambayo imesababisha mvua kidogo tu iliyonyesha, tatizo la mashimo kurudi pale pale. Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara hiyo, kwa kuweka kifusi na kushindilia ili iwe imara kabla hata ya lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti iliyosomwa jana, imepangiwa shilingi bilioni 120 kujengwa kwa lami kuanzia mwakani, ambayo ni asilimia 17 tu ya mahitaji yote ya fedha yanayohitajika. Pia Mheshimiwa Waziri hajajibu swali langu la mwisho sehemu (c); Je, ni lini barabara hiyo itakamilika kwa kiwango cha lami?
Naibu Spika, wakati mvua inanyesha, suala la kuweka kifusi nadhani lisingekuwa muafaka, kwa sababu ukiweka kifusi kitaharibu zaidi badala ya kujenga. Hivi sasa mvua kwa kuwa imekwisha suala sasa la kuimarisha kikamilifu hiyo barabara litafuatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka kwamba nilishatoa maelekezo kwa Mameneja wote wa Mikoa sasa kuelekeza nguvu zao kufungua barabara zote nchini ambazo zilijifunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, namwomba Mheshimiwa Mbunge akiri kwamba hiki kiasi ambacho amepangiwa, kinatosha ukilinganisha na mahitaji makubwa ya Waheshimiwa Wabunge wengi humu ndani.

WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami niongezee baada ya majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Barabara hii inafadhiliwa au inajengwa kutokana na pesa za Benki ya Afrika (ADB).
Kwa kawaida, barabara hii tutaigawa kwenye lots mbalimbali kwa sababu ni barabara ndefu sana. Kwa kawaida barabara hii kuanzia mwakani inaweza kuchukua baina ya miaka mitatu mpaka miaka minne, itakuwa imekamilika, itategemea hali ya hewa inavyokwenda.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
La kwanza, kabla ya kuvunjika kwa uhusiano wetu na nchi ya Israel kulikuwa na miradi mingi ya kimaendeleo inatekelezwa, mfano Hospitali ya Bugando, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Soko la Kariakoo na miradi mingine mingi. Je, baada ya sasa kuwa tumerudisha uhusiano hali ya ushirikiano wa miaradi ya maendeleo ikoje?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kufungua Ubalozi kwenye nchi fulani inahitajika fedha nyingi sana kuendesha. Na ndiyo hali hiyo husababisha nchi kuwa na Balozi chache au nyingi. Sasa kwa sababu, sasa hivi tuna mwendaokasi wa kufungua Balozi mpya, Israel, Kuwait, Qatar na kadhalika. Je, uwezo wetu kama nchi kwa sasa unakidhi kufungua Balozi mpya kwenye nchi nyingi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la kwanza, kwamba kabla ya mahusiano yetu kuvunjika na watu wa Israel tulikuwa na miradi mingi sana ya kimaendeleo na akihusisha mradi wa Bugando na anasema sasa baada ya kufungua hali itakuwa vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana nimesisitiza nimesema kutokana na kwamba sasa hivi Sera za Kimataifa zimebadilika na Tanzania imeamua kubadilika. Na kwa sababu tunasisitiza Sera ya Diplomasia ya Kiuchumi miradi hiyo ambayo ilikuwa imesimama wakati ule, ndiyo maana tunataka tuanzishe mahusiano haya kwa karibu ili kuweza kuendeleza miradi iliyokuwepo, lakini vilevile kufungua fursa mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika suala la pili ambalo Mheshimiwa Mbunge ana wasiwasi kwamba sasahivi kumekuwa na mazoea au mpango mkakati wa kufungua Balozi nyingi zaidi na ufunguzi wa Balozi unahitaji pesa nyingi. Na mimi nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyokuwa ninajibu wakati wa Bajeti kwamba Balozi hizi zitafunguliwa kutokana na uwepo wa pesa itakaokuwanao Serikali ya Tanzania. Sisi tunaelewa kwamba, ufunguzi wa Balozi ni gharama, lakini pia, gharama hiyo ya kufungua Balozi moja baada ya nyingine itategemea kwamba tutafaidika vipi katika ufunguzi wa Balozi hizo. Hatutafungua tu Balozi kwa sababu tunataka kufungua, lakini tutaangalia pia kwamba, tuna uwezo kiasi gani, kwa sababu pia ufunguzi wa Balozi unailetea faida Tanzania. Ahsante.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Nina swali dogo tu, nawaunga mkono wanaharakati wote kuhusu suala hili muhimu, sasa nauliza Serikali, je, itakuwa tayari kuingiza kipengele kwenye sheria ambacho kinazuia kuzaa kabla ya kufikisha miaka 18? Maana wapo watoto wanazaa wana miaka 13 au 14, lakini hawachukuliwi hatua yoyote. Je, Serikali itaweka kipengele kuzuia? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala lenye utata kidogo na katika hatua hii kwa kweli, hatujalifikiria hilo. Naomba tuchukue wazo lake tulifanyie kazi tuone kama ni jambo ambalo angalau linaweza hata likafikiriwa kwa sababu lina utata sana.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Uvuvi katika bahari na katika maziwa makubwa unafanyika usiku na mchana, lakini uvuvi katika Mto Koga kule Sikonge unafanyika mchana tu usiku Serikali inakataza. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, ni kwa nini Sikonge tu ndiko uvuvi unakatazwa usiku wakati ndiyo kuna samaki wengi? Ahsante sana.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Sikonge nimekaa miaka mitano kama Mkuu wa Wilaya na kwa hivyo hiki anachokisema nakifahamu vizuri sana. Ni kweli kwamba uvuvi katika mito na mto huo bahati mbaya eneo ambalo uvuvi unafanyika ni ndani ya hifadhi. Kwa hivyo, ili kuzuia shughuli ambazo si za kivuvi wakati wa usiku ndiyo maana imepigwa marufuku kufanya uvuvi usiku katika eneo hilo. Pia katika Mto huo Koga uvuvi pia unafanywa kwa msimu, wakati ule ambako shughuli za uwindaji katika hifadhi hiyo haziruhusiwi na uvuvi pia unazuiwa ili kutoa nafasi kwa samaki kuzaliana kwa ajili ya msimu unaofuata.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri kuhusu masuala ya ajali barabarani. Sasa nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, Tarafa ya Kitunda ambayo iko umbali wa kilometa 180 kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Sikonge ina Kituo cha Polisi kidogo ambacho kina polisi wanne ambao hawatoshi kuhudumia wakazi zaidi ya 80,000 kwenye Tarafa hiyo. Maana kuna majengo chakavu, polisi wenyewe ni wachache na hawana gari hata moja; lini Serikali itawasaidia polisi hao ili wafanye kazi yao vizuri? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mwezi Machi, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyahwa alichinjwa kama kuku na hadi leo wauaji wale hawajakamatwa. Ni lini Serikali itafanya kazi yake kikamilifu ili wauaji hao wakamatwe na kuondoa hofu Kijiji cha Nyahwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Kakunda kwamba concern yake ambayo amei-raise hapa tutaifanyia kazi ya kwa maana ya kwamba tutaongeza idadi ya askari katika kituo hicho. Kwa hiyo, nachukua fursa hii kuwaelekeza Jeshi la Polisi wale askari ambao wako depot, tunaotarajia kuwa-deploy karibuni, basi tuangalie uwezekano wa kuwapeleka Sikonge kuongeza ile idadi ya askari waliopungua pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia pale ambapo magari ambayo tunatarajia yataingia wakati wowote, nayo tuone uwezekano wa kufanya hivyo kwa kuzingatia changamoto eneo hilo baada ya kulifanyia utafiti wa kina pamoja na mahitaji ya nchi nzima.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara ya kutoka Mbeya hadi Mkiwa inaunganisha Mikoa mitatu ya Mbeya, Tabora na Singida na iliamuliwa kujengwa miaka 10 iliyopita. Sasa kipande cha kutoka Chunya hadi Itigi kitakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoingelea Mheshimiwa Mbunge imepangwa katika bajeti ya mwaka huu utakaoanza Julai. Kwa kweli nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wameipitisha bajeti. Hivyo, ni wajibu wetu kuhakikisha bajeti hiyo tunaisimamia ili itekelezwe kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema ni lini barabara hii itakamilika, namwomba sana Mheshimiwa Mbunge atupe subira kwa sababu hivi vitu ni vya kitaalam, vinatakiwa vifuatane na mikataba ilivyo. Namhakikishia kwamba barabara hii itakamilika – hilo ndilo la msingi. Lini hasa; nadhani tusiende sana kwa undani kiasi hicho ili baadaye tukaja kushikana uongo hapa.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza, wananchi wamekuwa wanalalamika sana kwamba vijiji ambavyo vimeshapatiwa umeme hadi sasa wanaopewa kipaumbele cha kuunganishiwa umeme ni wale tu wanaokaa kandokando ya barabara kuu. Je, ni lini wananchi wote ambao vijiji vyao vimeunganishiwa umeme watapatiwa umeme wanaohitaji?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri aliahirisha mwezi uliopita safari yake ya kuja Sikonge kujionea matatizo. Je, ni lini sasa atapanga ziara yake kuwatembelea wananchi wa Sikonge?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa REA Awamu ya II inayoendelea ambayo itakamilika mwezi huu, mpango wake mahsusi ulikuwa ni kupeleka umeme kwenye vituo vya vijiji na siyo kusambaza kwenye vitongoji. Sambamba na hilo, kabla hatujaanza Mradi wa REA Awamu ya III, kuna mradi mwingine unaosambaza umeme kutoka kwenye vituo na center mbalimbali na kuwapelekea wananchi kwenye vitongoji vyao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi huu nimekuwa nikiusema, unaitwa Underline Distribution Transformer ambao unaanza Julai, 2016 na utakamilika ndani ya miezi 18. Mradi huu utasambaza umeme kwenye vitongoji vyote ambapo umeme wa msongo wa kilovoti 33 umepita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge ni kweli tumekuwa tukiahidi kwamba tutapeleka umeme kwenye vitongoji. Nilimwomba Mheshimiwa Kakunda aniletee vitongoji vyake vyote, ameshaleta na namshukuru sana. Kwa hiyo, napenda kumwambia Mheshimiwa Kakunda vitongoji vyake ambavyo umeme umepita vitapatiwa umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ni lini tutatembelea, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge, kwa ridhaa yako nadhani tukishamaliza Bunge hili, niongozane na Mheshimiwa Kakunda na niwahakikishie Wabunge wa karibu na Sikonge nitawatembelea wote mara baada ya Bunge hili la bajeti.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini naomba niweze kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa amekiri kwamba wananchi wako tayari kupanda miti na kuna tatizo la vitalu vya miti, je, Serikali itaweka lini bajeti na utaalam ili kusudi vitalu vya miti viweze kuoteshwa katika kila Wilaya hapa nchini ili wananchi waweze kupanda miti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, miti mingi ambayo imekuwa inapandwa asili yake inatoka nje ya nchi siyo miti ya asili, je, ni lini sasa Serikali itaweka mkazo ili kusudi miti ambayo itaoteshwa kwenye vitalu ili wananchi waipande iwe ni miti ya asili ambayo ni rafiki wa mazingira na rafiki wa maji? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, suala la vitalu na Serikali kutenga bajeti, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya swali la msingi ni kwamba tayari tumeanza kutenga bajeti. Kwa mwaka huu kwa kuanzia tumetenga shilingi bilioni mbili na tunataka katika miaka ijayo ya fedha tuwe na wastani wa kutenga zaidi ya shilingi bilioni 20 kila mwaka ili kuweza kupanda miti inayostahili Kitaifa.
Vilevile tumesema kwamba Halmashauri zote zina jukumu pia la kutenga fedha kwa ajili ya shughuli hii na hivyo sasa katika mpango wa upandaji miti tuliouandaa wa mwaka 2016-2020 unabainisha haya na kwamba Halmashauri zote zitawajibika kuhakikisha tunakuwa na vitalu katika ngazi ya kata mpaka vijiji na kwenye taasisi kama shule ili wananchi waweze kupata miche na mbegu kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amesema kwamba miti mingi inayopandwa ni ya kutoka nje, suala hapa siyo miti kutoka nje bali tunapanda miti yenye faida na wananchi tunawasisitiza wapande miti yenye faida. Kwa hiyo, wataalam wetu wanaohusika na misitu pamoja na hawa wa mazingira wamefanya upembuzi wa kujua kila eneo linafaa kupandwa miti ya aina gani, linafaa kupelekewa miti ya aina gani ambayo inaweza kustawi lakini vilevile yenye faida kwa wananchi kwa mfano, miti ya matunda, mbao, dawa kikubwa tumewaelekeza wataalam wetu wapeleke miti yenye faida.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Sambamba na majibu aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri ninaomba awahakikishie wananchi wa Sikonge ambao wamekuwa hawaridhiki na matengenezo ya barabara ya Sikonge - Mibono hadi Kipili ambayo wakandarasi wamekuwa wakitengeneza kipande cha Sikonge hadi Mibono na kuacha kipande cha Mibono hadi Kipili bila matengenezoya aina yoyote kiasi ambacho haipitiki kila mwaka. Kwa sababu mwaka huu imepangiwa shilingi milioni 892 anawahakikishiaje wananchi wa Sikonge kwamba mwaka huu itatengenezwa kwa kiwango bora mpaka mwisho wa barabara ya Kipili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, pamoja na wananchi wa Sikonge kwamba fedha hizo zilizotengwa ni kwa ajili ya pamoja na kipande cha Mibono hadi Kipili na tutahakikisha tunasimamia ili barabara hiyo itengenezwe kwa kiwango kizuri kama ambavyo imetengenezwa eneo la Sikonge hadi Mibono.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Hapo kwenye hilo swali, napenda kuiuliza Serikali wapo wastaafu kule kwangu wengi zaidi ya 20 ambao wananifuata ofisini, ni wazee, wengine wameshafariki hawajalipwa waliokuwa watumishi wa Afrika Mashariki, waliokuwa watumishi kama Game Officers. Sasa kwa nini Serikali isiwe proactive kuwafuatilia hao wazee huko waliko ili waweze kulipwa mafao yao, badala ya kutusumbua Wabunge ambao tumeingia hivi karibuni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Watanzania wote ni mashahidi, Wizara ya Fedha na Mipango ina zaidi ya miezi mitatu sasa ikizunguka mikoa mbalimbali kufanya tathmini na kuhakiki wastaafu wote. Kwa hiyo, hilo alilolisema Mheshimiwa Kakunda, Wizara ya Fedha ilishafika Tabora na tayari imeshafika Sikonge. Kama wapo ambao hawakufikiwa tuna utaratibu zoezi hili ni endelevu waweze kufika na kuhakikiwa na haki yao watapata bila tatizo.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kunipa nafasi. Niseme wazi kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza kwamba wananchi wa Sikonge wemesikitishwa sana na majibu ya Serikali. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kutumia takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) za mwaka 2012 kama zilivyo ni sahihi, lakini je, Serikali haioni kuwa kutumia takwimu hizo bila kufanya projections kwa kutumia formular rasmi iliyo kwenye taarifa ya uchambuzi ya NBS inaweza kusababisha takwimu zisizo sahihi kwa mwaka 2017 na hivyo kusababisha Bunge hili pamoja na wananchi kuamini kuwa Serikali imelidanganya Bunge pamoja na wananchi? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kuwa takwimu rasmi zilizoko kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya ya Sikonge pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ambazo pia ndizo alizonazo Mkuu wa Idara ya Maliasili wa Halmashauri inaonyesha kwamba kati ya kilometa za mraba 27,873 za Wilaya ya Sikonge, kilometa za mraba 26,834 ambayo ni sawa sawa na asilimia 96.3 ni hifadhi za misitu, wanyamapori, mapori ya akiba na maeneo mengine ya hifadhi ambayo yote hayo yako chini ya udhibiti na dhamana ya Kisheria ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Je, wananchi tumebaki na kilometa za mraba elfu moja na thelathini na...
…hili la pili, Serikali itateua lini timu yake ije kufanya kazi na timu yetu Sikonge, ili kusudi tupate suluhisho la kudumu kuhusu takwimu hizo?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, takwimu huwa zina chanzo, na mara nyingi unapokuwa unataka kunukuu takwimu ni lazima useme chanzo cha takwimu hizo yaani hizo takwimu ni kwa mujibu wa nani aliyezifanya. Takwimu zina mwenyewe na mwenye takwimu ni lazima awe ni mtu mwenye mamlaka na kwa Taifa hili takwimu ni mali ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, takwimu nilizozitumia kwa kuwa ni za Mtakwimu Mkuu wa Serikali sina shaka kwamba takwimu hizi ni sahihi na hizi ndizo takwimu zinazotakiwa kutumika
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kufanya projections kwamba ilitakiwa kuzitoa kutoka mwaka 2012 kuzileta leo, hiyo inaweza kuwa ni hoja, lakini ingekuwa ni hoja tu kama kweli hoja ya takwimu ingekuwa ni ya msingi kutokana na swali la msingi lililoulizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ifahamike kabisa kwamba nchi yetu ndio nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na eneo kubwa lililotengwa kwa ajili ya uhifadhi kwa ajili ya wanyamapori, misitu na hifadhi nyingine. Sisi tumetenga asilimia 25 ya eneo zima la nchi yetu, hiyo inatosha kutuma ujumbe kwamba ni kweli tumehifadhi maeneo makubwa. Lakini hatukufanya hivyo kwa makosa, tulifanya hivyo kwa sababu za msingi ambazo ndio zimekuwa zikitupa faida nyingi sana zinazotokana na uhifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunapozungumzia uhifadhi kwenye eneo la Sikonge ifahamike kabisa kwamba uhifadhi huo sio kwa ajili ya Sikonge. Kila eneo lililohifadhiwa hapa nchini limehifadhiwa kwa maslahi ya Taifa. Eneo hilo litaweza kupitiwa pale ambapo kama Taifa tutaona kwamba kweli kuna haja ya kufanya mapitio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimuombe Mheshimiwa Mbunge, pamoja na kumpongeza kwamba yuko hodari wa kufuatilia masuala yanayohusu wananchi wake, na yeye atakumbuka vizuri kabisa kwamba mwanzoni mwa mwaka huu tulikuwa wote Sikonge, tumepita kwenye maeneo yake, nami napenda wananchi wa Sikonge wajue kabisa kwamba wanao jembe, Mbunge wao ni mfuatiliaji sana wa masuala yanayohusu wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huo huo nataka nimuombe kwamba atumie fursa hiyo ya kuwakilisha wananchi kwa kuwaambia ukweli kwamba akiba ni akiba na tunatakiwa kuyahifadhi maeneo yale kama akiba. Tutaweza kuyatumia pale tu itakapotokea kwamba kuna ulazima wa kuweza kufanya vinginevyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Serikali kuteua timu, nirudie tu kwamba tayari timu ipo na iko kazini na inaendelea na kazi hiyo, kinachosubiriwa sasa hivi ni wao na ile kazi yao kukamilika na kuweza kuleta mrejesho Serikalini kwa ajili ya kuweza kupiga hatua kutekeleza masuala haya yanayohusiana na upitiaji upya wa kile ambacho tunacho hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho kabisa niseme kwamba kamwe Serikali haitaweza kufikia mahali ikaamua tu haraka haraka kuweza kuyaondoa maeneo yaliyohifadhiwa kwa matumizi mengine bila kufanya tathmini ya kuangalia kwamba maeneo yasiyohifadhiwa yametumika kwa tija. Kwa hiyo, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba maeneo ambayo hatujahifadhi yanatumika kwa tija kwanza ndipo tuanze kugusa maeneo ambayo yamehifadhiwa kwa ajili ya akiba ya Taifa hili kwa ajili ya kizazi kijacho.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba barabara ya Sikonge – Mibono – Kipili ilipandishwa hadhi tangu mwaka 2009 na hadi leo imetobolewa kwa kiwango cha kilometa 42 tu kati ya 282 ambayo ni kama kilometa tano kwa mwaka; ina maana kwamba hadi itakapokamilika barabara hiyo tunahitaji miaka 44. Je, Serikali iko tayari kuwaambia wananchi wa Sikonge kwamba itajenga barabara hiyo kwa kipindi cha miaka 44 ijayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu wa fedha za Mfuko wa Barabara zinazogawiwa mikoani kwa ajili ya matengenezo, haturuhusiwi kutumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kutoboa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ombi lake tunalichukua na tutatafuta namna ya kuhakikisha barabara hii kipande hiki kipya cha kukitoboa tunakitoboa kwa haraka zaidi na naomba wananchi wote wa Sikonge wachukue hiyo ndiyo kama commitment ya Serikali.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha FDC Sikonge kinatakiwa kutoa mafunzo katika fani za useremala, uashi, uchomeleaji, ushonaji na ufundi umeme. Kutokana na upungufu wa walimu uliopo na uchakavu wa majengo, chuo kwa sasa kinatoa mafunzo kwenye fani ya umeme peke yake. Maswali yangu mawili, je, Serikali aione kuwa chuo hiki kinahitaji jicho la kimkakati ili kukiokoa?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika jibu la msingi ameahidi kwamba Chuo hiki kitatembelewa, kitatembelewa lini na nani? Ahsante sana.
NAIBU WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatambua umuhimu wa kuviimarisha vyuo hivi ili kuweza kuchukua wanafunzi wengi zaidi na kutoa mafunzo yaliyo bora zaidi kulingana na uhitaji wa soko, lakini vilevile kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi wanaweza kujiajiri wenyewe. Kwa upungufu alioainisha Mheshimiwa Mbunge tutatembelea chuo hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla wake Waheshimiwa Wabunge ili tu-save muda, kimsingi mkakati ni kutembelea vyuo vyote vya FDCs ili kuona namna bora zaidi ya kuviendesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la kwenda Sikonge nitakufahamisha Mheshimiwa, kimsingi tutaenda na kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ni muhimu kuwepo, tutakujulisha twende wote ikiwezekana katika kipindi hiki cha bajeti katika weekend mojawapo.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ninapenda niulize Serikali; kwa kuwa uwekezaji uliofanywa kwenye kituo hicho wa shilingi bilioni 1.8 ambao ulitumika kujenga majengo mbalimbali ikiwemo nyumba sita za kisasa kabisa ambazo hata Mheshimiwa Waziri Mkuu anaweza akakaa mule, na majengo mengine. Kwa nini Serikali isiharakishe usajili upya wa kituo hicho ndani ya mwezi huu wa Septemba ili tathmini ya kina ifanyike ndani ya mwaka huu wa fedha ili kituo hiki kianze kutoa manufaa kwa vijana walio wengi zaidi?
Mheshimiwa Spika, la pili, kwa kuwa kituo hicho kilizinduliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2014 na hakijaonesha sura iliyokusudiwa wakati kinazinduliwa.
Je, Serikali haioni kwamba upo umuhimu wa kuchukua hatua za makusudi za kiutawala, za kibajeti na kitaasisi ili kituo hicho kiwe na sura ile ambayo ilikusudiwa wakati kinazinduliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, katika swali la kwanza la kukamilisha usajili ndani ya Septemba hii, suala la usajili ni hatua na kama Serikali ambacho tutakifanya ni kuhakikisha tu kwamba tunahimiza kazi hii ifanyike mapema zaidi ili kituo hiki usajili wake ukamilike na baadaye sasa ifanyike tathmini ambayo itawezesha vijana wengi zaidi wa Sikonge waweze kunufaika. Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tutajitahidi kuhimiza taratibu hizi zikamilike kwa mujibu wa sheria ilivyowekwa ili zifanyike kwa wakati vijana wengi waweze kunufaika zaidi.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu bajeti na muundo wa utawala wa taasisi husika, na hasa ikizingatiwa kwamba kituo hiki kilijengwa kwa ajili ya kuwanufaisha vijana wa Sikonge, nichukue fursa hii tu kumuomba Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu kituo hiki kipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ambayo pia Mheshimiwa Mbunge ni Diwani katika eneo husika, wachukue fursa hii kwanza kabisa kuhakikisha kwamba katika ngazi ya halmashauri wanajitahidi kuweka mipango mizuri kufanya kituo hiki kiweze kufanya kazi ili kiwanufaishe vijana.
Mheshimiwa Spika, lakini pia na eneo lingine la masuala ya muundo wa kitaasisi na bajeti pia, nashauri katika mtazamo huu kwamba ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge waone namna bora ya kuweza kulifanya hilo pia. Na sisi katika upande wa Serikali Kuu kwa sababu tunashughulika na vituo vingi vya vijana, pia tutatoa msaada wowote ambao utahitajika hasa katika kuwawezesha na kuwajengea uwezo wataalam hawa ambao watashiriki katika kutoa elimu kwa vijana katika eneo husika.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Napenda kuikumbusha Serikali kwamba kwa barabara hii kama sehemu ya trunk road ya Tabora- Mbeya michakato ya upembuzi, upembuzi yakinifu, usanifu, usanifu wa kina ilianza mwaka 1974 sasa ni miaka 43 haijakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nipate majibu kwenye maswali mawili, la kwanza, je, Serikali iko tayari sasa kujibu swali langu la msingi lini itaijenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Serikali kama haitaji muda maalumu, je, haiashirii kwamba haiko tayari kuiweka kwenye mpango maalum barabara hii kuijenga kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Joseph George Kakunda kwamba Serikali mara itakapokamilisha upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni zoezi la kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii litafanyika kwa sababu wakati huo tutakuwa tumejua gharama za ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa George Kakunda tuwe wakweli na tuitendee haki sekta yetu ya ujenzi. Barabara hii ni sehemu ya barabara kuanzia Mbeya hadi Singida na tumekuwa tukifanya kipande baada ya kipande. Hivi tunavyoongea unafahamu kwamba sehemu kubwa imeshajengwa sasa tumebakiza kilometa hizi 172 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba Serikali iko makini inafuatilia ujenzi wa barabara hii na siyo kwamba hatuko tayari kama alivyosema kwenye swali lake la pili. Kama tungekosa kuwa tayari hatungekuwa tumeanza ujenzi katika maeneo hayo ambayo tumeshayajenga.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa Serikali kujibu swali langu Na. 22 vizuri. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; mnara wa Airtel uliojengwa kwenye Kata ya Kipili, Kitongoji cha Madoletisa ambao haujawashwa kwa miaka miwili sasa na mnara wa Vodacom kwenye Kata ya Kilumbi ambao nao haujawashwa kwa miaka miwili hadi sasa: Je, ni lini itawashwa ili wananchi waanze kufaidika na huduma za mawasiliano?

Mheshimiwa Spika, je, Miradi ya Mawasiliano Vijijini iliyomo kwenye Mpango wa Maendeleo wa 2019/2020 ambayo orodha yake ipo kwenye randama pia kwenye kijitabu cha taarifa ya Wizara ya Julai 2019, itatekelezwa lini?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, mnara uliojengwa katika Kitongoji cha Madoletisa ni kweli ni wa Kampuni ya Simu ya Airtel. Mnara huu ulijengwa kama mnara wa kupeleka mawimbi ya simu kwenda katika minara mingine ya mbali (Transmission Site). Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliliona tatizo la mnara huo ambapo unatumika kama transmission site bila kutoa huduma kwa wananchi waliopo Madoletisa na kuiagiza Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel wauwekee vifaa vya radio ili mnara huo pia utumike kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi. Tumewasiliana na Airtel ili wakamilishe kazi ya kuwapelekea wananchi mawasiliano mara moja ndani ya mwezi huu wa Aprili, 2020.

Mheshimiwa Spika, Miradi ya Mawasiliano Vijijini kwenye Vijiji vya Igigwa, Migumbu, Nyahua na Tumbili kutoka Kata ya Igigwa, Vijiji vya Ipole, Makazi, Udongo na Ugunda kutoka Kata ya Ipole, Vijiji vya Kanyamsenga, Kiloleli na Mtakuja katika Kata ya Kaloleli, Vijiji vya Imalampaka na Mibono katika Kata ya Kipanga pamoja na Kijiji cha Kiyombo kutoka Kata ya kipili, havikupata watoa huduma katika zabuni ya mwezi Julai, 2019. Miradi hiyo itatangazwa tena mwezi Juni, 2020.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, naomba niulize Serikali na wananchi wa Sikonge wanasikiliza na Mkoa wa Tabora; je, baada ya kuwa Serikali imekamilisha maandalizi yote ya ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Ipole - Lungwa yamekamilika usanifu kila kitu. Je, sasa bado fedha na mkandarasi Serikali itaanza lini kujenga barabara hiyo ili kuunganisha Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Tabora?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakunda, Mbunge wa Sikonge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Ipole - Lungwa ni kati ya barabara zinazounganisha Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Mbeya na kama alivyosema taratibu zote zimekamilika, kinachotegemewa tu ni lini itatangazwa kwa sababu sasa hivi tuko kwenye maandalizi ya manunuzi kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na kama alivyosema wananchi wake wanamsikia ni barabara muhimu inayounganisha na mkoa na mkoa, kwa hiyo ninahakika barabara hii itatengewa bajeti na taratibu za manunuzi once zikikamilika basi tutakuwa tumepata mkandarasi na itaanza kutekelezwa, ahsante.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali ambayo yametolewa vizuri kwa ufasaha, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; sina tatizo na risiti za MNRT Portal, tatizo langu ni kwa nini mtozaji wa faini asipewe post maalum ili atoe risiti halali badala ya zile za kuandikwa kwa mkono?

Mheshmiwa spika, swali la pili, kwa nini Serikali isitoe mwongozo kwa halmashauri na WMAs zote ili fedha zilipwe kwenye control number maalum benki badala ya kubeba kwenye mabegi na kwenda kulipia porini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kakunda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameongelea ni kwa nini tusitoe risiti za kielektroniki badala ya kutoa risiti za mkono. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi ni kwamba miongozo yote ya sasa tunayofanya ni kwamba Serikali inapokea mapato ya aina yeyote ile kutumia risiti za EFD na kwa upande wa Maliasili na Utalii tunatumia hiyo MNRT Portal ambayo ndio tunayopokelea fedha kwa kutumia control number.

Mheshimiwa Spika, suala analoliongelea Mheshimiwa Mbunge ni kwenye hizi Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori ambazo zinasimamiwa na Serikali za Mitaa kupitia halmashauri na tunazieleleza sasa halmashauri kwa kuwa fedha zake za jumuiya hizi zinakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali waangalie sasa utaratibu wa kuhakikisha kwamba malipo yote yanayotokana na faini yapitie kwenye utaratibu wa Serikali yaani EFD.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa mwongozo, mwongozo tulishautoa na utekelezaji wake unaendelea kufanyika isipokuwa usimamizi tu kama ambavyo amesema Mheshimiwa Mbunge kwamba imeonekana kuna wananchi wanabeba fedha kwenye mifuko. Tunatoa maelekezo sasa kwa halmashauri ambazo zinasimamia hizi jumuiya kuhakikisha kwamba usimamizi wa fedha za Serikali unapitia kwenye mifumo ya TEHAMA iliyoainishwa na Serikali, ambayo kwa Maliasili na Utalii tunatumia MNRT Portal ambayo inakusanya kwa kutoa control number na kwa wale wanaotumia EFD, basi Halmashauri zisimamie suala hilo ili fedha hizi sasa ziweze kufika kwenye Mifuko husika na ubadhilifu usiweze kujitokeza. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwanza naipongeza Serikali kwa majibu hayo na hasahasa kupima viwanja 56,792 katika kipindi kidogo cha miezi tisa, lakini Sikonge pale Mjini niao wananchi 2000 kwenye maeneo ya Ukanga wana viwanja 1400 na Majengo viwanja 6000 jumla viwanja 2000 kwa muda mrefu sana zaidi ya miaka 10 wanaomba hati hawajapatiwa.

Mheshimiwa Spika, sasa je, swali langu la kwanza wizara inawasaidieje wananchi wa Sikonge waweze kupata hati zao kwa haraka?

Mheshimiwa Spika, la pili je, Serikali haioni kwamba sasa hivi hapa nchini kuna uchumi mgumu kiasi ambacho wananchi wanapata shida kupata laki 150 kwenye miji ya vijiji kama Sikonge kupima kiwanja kimoja je, Serikali haioni kwamba hasa kuna wakati umefika wa kuwapa ruzuku ili waweze kupata hati zao za ardhi.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kakunda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kujua tu kwamba ni lini utoaji hati utafanyika katika maeneo hayo. Tayari tulishafungua ofisi za mikoa na katika kasi ya utoaji hati sasa hivi inakwenda kwa kasi kubwa naomba nimuhakikishie tu kwamba ofisi yetu ya Tabora Mjini itakwenda kukamilisha hiyo na kwa kupitia majibu ninayotoa sasa basi wafike katika hayo maeneo mawili ndani ya Sikonge yenye viwanja 2000 ambao nasema kwamba hawajapewa hati mpaka leo, iwapo watakuwa wamekamilisha taratibu zote za umilikishaji.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anazungumzia suala la ruzuku kwamba 150,000 katika suala zima la upimaji ni gharama kubwa. Naomba niseme tu kwamba gharama hii si kubwa kama tunavyofikiri lakini pia inategemea na eneo husika maana kuna maeneo mengine mpaka sasa wanalipa 60,000 wanalipa 90,000. Wakiwa watoaji ni wachache unakuta kwamba ile gharama hata ya yule anayeenda kupima inakuwa kidogo ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuwa na watu wengi kwa wakati mmoja wanayohitaji gharama zile zinashuka kwa hiyo gharama zinashuka kutegemeana na volume ya kazi ambayo mpimaji anakwenda kufanya pale. Niwaombe wananchi kwamba suala la urasimishaji linakwenda kuisha 2023 kama nilivyosema kwenye jibu la msingi kwa sababu ilikuwa programu ya miaka kumi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, waongeze kasi sasa hivi ili kazi ile iishe halafu tuendelee na upimaji wa kawaida ambao hautakuwa na zoezi la urasilimishaji ambao majengo yale yamekaa kiholela na upimaji wake unakuwa kidogo ni mgumu ahsante.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Naipongeza Serikali kwa majibu mazuri sana ambayo wameyatoa hapa mbele ya Bunge, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza; miti hii inapatikana kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na maeneo ambayo hayajahifadhiwa, yakiwemo mashamba ya watu binafsi na ardhi ambayo inamilikiwa na watu binafsi. Sasa swali langu; kwa nini Serikali isitoe ruhusa maalum itakayosimamiwa na Serikali za vijiji kwenye maeneo hayo ambayo hayajahifadhiwa ili watu waruhusiwe kuvuna miti wanayoimiliki kihalali kwa ajili ya matumizi ya ujenzi wa nyumba za asili pamoja na nyumba za kisasa bila kwanza kupata vibali vile vya maliasili kwa sababu maeneo hayo hayahusiani na maliasili? Kwa sababu matumizi yale siyo ya kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kuhusu uvunaji wa miti kwenye maeneo yaliyohifadhiwa; kwa nini Serikali isitoe elimu kwanza kupitia mikutano ya hadhara na njia nyingine za mawasiliano ili wananchi wapate ufahamu wa kutosha wa namna ya kuomba vibali ili wasiingie migogoro mara kwa mara ya kuvunja sheria za nchi? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali ipo kwa ngazi zote. Kuhusu swali lake linalosema kwa nini Serikali isitoe ruhusa kwenye maeneo yasiyohifadhiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yote ambayo yana rasilimali za misitu yanahifadhiwa na Serikali ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini kwenye ngazi za vijiji na maeneo ya wilaya, zinahifadhiwa na Serikali za Mitaa, zikiwemo halmashauri za wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maeneo haya ambayo vibali vyake vinatolewa na Maliasili ni yale maeneo ambayo yanahifadhiwa na Wizara. Hata hivyo, kuna yale ambayo yanahifadhiwa na Serikali za Mitaa, vibali vyote huwa vinatolewa kwenye level ya vijiji na wilaya. Kwa hiyo wale wote ambao wanahitaji kupata vibali basi wawe wanakwenda kwenye maeneo hayo na pia watapata hivyo vibali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe tu kwamba maeneo yote yanahifadhiwa, siyo kwa ajili ya kutunzwa peke yake, lakini pia na uhifadhi wa mazingira pamoja na utunzaji wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ameuliza kuhusu elimu; ni kweli kwamba Serikali imeendelea kutoa elimu mbalimbali kwa wananchi ili watambue umuhimu wa utunzaji wa miti. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango wa bajeti na fedha zilizoidhinishwa kipindi hiki tumeweka eneo la elimu ambalo tutapita kila maeneo ambayo yanazunguka hifadhi kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu ya kutosha na namna ya kuomba hivi vibali vya ukataji miti. Ahsante.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni pale ambapo Serikali imesema kwamba mwaka huu kulikuwa na kampuni nane za wazawa zimeingia mikataba na wakulima. Hadi ninaposimama hapa Bungeni mwaka huu kumekuwa na kuvunja rekodi ya kuwakopa wakulima maana yake wameuza tumbaku yao mwezi wa Tano, lakini hadi ninaposimama Bungeni hapa asilimia zaidi ya 50 ya wakulima hasa waliouza tumbaku yao kwenye kampuni hizo za wazawa hawajalipwa. Hawajalipwa kwa sababu kampuni hizo ndogo zimepata shida na changamoto katika kuuza tumbaku hiyo kwenye soko la dunia. Walikuwa wanauza kupitia Zambia, wamefungiwa huko. Walikuwa wanauza kupitia Malawi, wamefungiwa huko. Sasa je, Serikali haioni hasa kama Waziri, haioni umuhimu wa kukutana na hizo kampuni nane ili kuona namna ya kuwasaidia ili hatimaye nayo yawalipe wakulima haraka iwezekanavyo? Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, kwa mujibu wa sheria, zao la tumbaku linaendelezwa na kusimamiwa na Bodi ya Tumbaku. Tangu mwaka jana Bodi ya Tumbaku imemaliza muda wake, hadi sasa hivi inafanya kazi zake kinyume cha sheria. Hivi Serikali haioni kwamba inatakiwa iteue Bodi ya Tumbaku kesho? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kakunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza, Wizara ya Kilimo imeshakutana na kampuni zote nane za Kitanzania zinazonunua tumbaku na ningeomba tu-acknowledge kazi iliyofanywa na kampuni hizi za Kitanzania katika kununua tumbaku. Tumbaku yote iliyonunuliwa mpaka msimu unakwisha ni jumla ya bilioni 86. Fedha zilizolipwa mpaka sasa ni bilioni 82, kwa hiyo, sio sahihi kwamba zaidi ya asilimia 50 kwamba wakulima hawajalipwa. Tuna-acknowledge fedha ambayo haijalipwa ya wakulima mpaka sasa imebaki shilingi bilioni nne.

Mheshimiwa Spika, la pili, kwenye eneo hili tumbaku hii iliyonunuliwa na naomba Bunge lako Tukufu lifahamu kabla ya kuleta kampuni za Kitanzania katika mfumo wa ununuzi wa tumbaku pamoja na grade zaidi ya 60 za tumbaku, kulikuwa kuna tumbaku inaitwa reject inayotupwa ambayo mkulima anaitupa shambani. Ni kampuni hizi za Kitanzania ndiyo zimeenda kuinunua mpaka tumbaku inayoitwa reject na kwa mwaka huu hakuna tumbaku iliyobaki mikononi mwa wakulima. Kunapokuwa na success story, tu-acknowledge na hili ni jambo jema. Kwa miaka mingi sekta hii imekuwa kwenye dominance ya kampuni mbili tu. Tumeingiza kampuni za Kitanzania against all efforts za international market ambazo zilituzuia.

Mheshimiwa Spika, kuhusu malipo yaliyobaki na tumbaku iliyoko Malawi na Zambia, Balozi Simba aliyeko Zambia ameshafanya jitihada kwa sababu walio-block tumbaku yetu isinunuliwe Zambia ni hizi hizi kampuni kubwa zilizoko ndani ya nchi, zimetumia subsidiary companies zao kule nchi kuzuia tumbaku yetu isinunuliwe. Tatizo hili tumeli- resolve, tuko kwenye hatua za mwisho. Tumeongea na Benki ya CRDB na NMB watatoa fedha ili kampuni hizi zimalizie bilioni nne iliyobaki ambayo haijalipwa kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie Bunge lako Tukufu kusema tutaendelea ku-support kampuni za Watanzania kununua green tobacco na kui-export kwa sababu tumbaku haiwezi kugeuka kuwa chapati.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kuhusu suala la Bodi. Bodi ya Tumbaku imemaliza muda wake, ni kweli. Sisi kama Wizara tumeshapeleka mapendekezo vetting inaendelea na tumeshaomba kwa Mheshimiwa Rais ili aweze kumteua Mwenyekiti. Iko kwenye hatua za mwisho na ni interest yetu sisi kama Wizara kuhakikisha Bodi ya Tumbaku inafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria. Sasa hivi Bodi haipo, Mkurugenzi anafanya kazi chini ya Katibu Mkuu kwa mujibu wa sheria.

Kwa hiyo, Bodi ya Tumbaku inafanya kazi chini ya DG na anaripoti moja kwa moja kwa Katibu Mkuu. Tumeshapeleka mapendekezo na tunaendelea kufuatilia Serikalini.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa kuwa mitaala pamoja na mikopo huzalisha wahitimu na kwa sababu, Wizara hii ndio Wizara ya kisera. Kwa mujibu wa taarifa ambayo ilitolewa hapa Bungeni na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mwaka, kati ya ajira zilizoombwa za ualimu elfu 10, walioajiriwa kama elfu 10, lakini waombaji walikuwa zaidi ya laki moja. Maana yake ni kwamba, ukiangalia mpaka waliohitimu mwaka jana ukijumlisha pale ni zaidi ya laki moja wako mtaani hawajapata ajira. Sasa swali langu, ni kwa nini Serikali au Wizara hii wasijadili hili suala la ajira ili kuwasaidia, hasa Walimu ambao ni Walimu wa Kiswahili, waende kufundisha Kiswahili kwenye nchi za Afrika Mashariki pamoja na SADC?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Kakunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajira ni suala ambalo ni mtambuka na kwa vile Mheshimiwa Mbunge anatoa pendekezo kwamba, tuweze kuangalia namna gani tunaweza tukawasaidia Walimu kwenda kufundisha kwenye nchi hizi za Afrika Mashariki na Kati na Kusini mwa Afrika, tunaomba vilevile suala hili tulichukue, twende tukaangalie hizo fursa ambazo zinatokea kwenye nchi hizo na namna gani tunaweza tukakaa kitako na kuweza kushawishi namna gani Walimu wetu ambao wamehitimu kwenye shahada mbalimbali za ualimu, hasa hizi za Kiswahili kwenye vyuo vyetu, wanaweza kwenda kutumika kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunajua kwamba, masuala ya ajira mara nyingi sana yana-competition zake kwa sababu itakwenda kwenye usaili na watahitajika kwenda kwa ajili ya usaili huo. Kwa hiyo, hatuwezi kutoa guarantee moja kwa moja kwamba, tutafanya hivyo kwa asilimia 100, lakini nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, kwamba tunalichukua, tutaenda kulifanyia kazi na kuweza kuangalia namna gani nafasi hizo zinapatikana na tunaweza kunufaika sisi kama nchi.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza, napongeza majibu mazuri ya Serikali. Labda kabla sijauliza maswali ya nyongeza, nina maelezo ya ziada kwamba eneo la Uwanja wa Ndege wa Ipole liko chini ya Ofisi ya TAWA Kituo cha Ipole cha Pori la Akiba la Ugalla. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa kutoka Tabora mpaka Ipole ni kilomita 100; na kutoka Koga mpaka Ipole WMA ni kilomita 90: Je, Serikali haioni kwamba kujenga uwanja huo wa ndege pale Ipole kutakuwa na faida zaidi katika kuvutia watalii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: kwa kuwa huyu mwekezaji ameshajenga uwanja mdogo pale Koga na inaonekana kabisa Serikali haina nia ya kuendeleza ujenzi wa Uwanja wa Ndege pale Ipole: Je, Serikali iko tayari kuyarudisha mashamba na ardhi ya wananchi wa Ipole waliyoitoa mwaka 1996 kwa nia njema kwa Serikali kwa ajili ya kujenga Uwanja wa Ndege, kuwarudishia ili waendelee na shughuli zao za kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Kakunda kwa kuwa mhifadhi na pia ameendelea kuhamasisha utalii, ikiwemo maeneo haya yaliyopo katika Wilaya ya Sikonge hasa katika Pori la Akiba la Ugalla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kutoka Tabora mpaka Ipole ni kilomita 100 ambazo huwa zinasaidia watalii wanaofika Tabora kuelekea katika eneo hili la WMA. Sambamba na hilo, Mheshimiwa Kakunda ameomba Serikali iweze kujenga kiwanja katika eneo la Ipole ili kurahisisha watalii waweze kupita njia ambayo ameisema ya kilomita 90.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshauri tu kwamba maeneo yenye uhitaji ni mengi; na kwa kuwa kiwanja cha Tabora kinatosheleza maeneo haya kwa hizo kilomita alizozisema, basi naomba wananchi au wawekezaji waliopo katika maeneo hayo, waendelee kuvumilia wakati tunaangalia namna ya kuweza kuboresha, kiwanja kidogo kilichopo katika Kituo cha Ipole ili kuwawezesha wale watalii wanaotaka kuingia kwenye hiyo WMA ama kwenda kwenye Pori la Akiba la Ugalla waweze kufika kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba Pori la Akiba la Ugalla limeshapata mwekezaji na tayari huyo mwekezaji yupo tayari kuendelea kuboresha kiwanja hicho. Hata Serikali tutajipanga katika maeneo hayo kuhakikisha kwamba tunaboresha viwanja hivyo ili kurahisisha watalii waweze kufika katika maeneo hayo. Ahsante (Makofi)