Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph George Kakunda (49 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mchango wangu ni katika maeneo matatu kwa kifupi kabisa ni kwamba nazipongeza sana Kamati zote kwa jinsi ambavyo wameandaa kazi zao na jinsi walivyowasilisha taarifa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa elimu ya msingi na sekondari hii changamoto ambayo imeletwa na elimu msingi bila malipo tunahitaji wote kushirikiana. Tunahitaji kuhamasisha wananchi waendelee kuchangia ujenzi wa madarasa, ujenzi wa nyumba za walimu, mabweni, mabwalo, maktaba pamoja maabara, Serikali peke yake haiwezi kuachiwa jukumu hilo maana mahitaji ni makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu agizo la Serikali kuzitaka Halmashauri kutenga …

(Hapa baadhi Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu agizo la Serikali kuzitaka Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na Vijana, imezungumzwa kwamba hakuna sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirejea chimbuko la Mfuko wa Vijana ulionzishwa mwaka 1993 ulianzishwa chini ya kifungu cha 17(1) cha Sheria ya Hati ya Idhini ya Malipo na Ukaguzi (Exchequer in Ordinance) Sura ya 439. Kwa hiyo, inatakiwa tu labda kama ni marekebisho tufanye marekebisho badala ya kusema kwamba hakuna kabisa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu maji vijijini. Ninaomba kuwasihi Waheshimiwa Wabunge, pamoja na utekelezaji unaoendelea ambao mzuri kasi zaidi itaongezeka kupitia Wakala wa Maji Vijiji, nadhani mambo hayo matatu yanatosha yawe mchango wangu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Ofisi yake ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniokoa kwenye ajali mbaya ya gari iliyotokea tarehe 6 Aprili, 2018 nikiwa katika utekelezaji wa mjukumu yangu, niliponea chupuchupu. Aidha, kwa mukhtadha huo naomba nimlilie kijana wangu Mhandisi Izengo Ngusa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, aliyefariki usiku wa kuamkia jana kwa ajali ya gari.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru familia yangu, hususan Mke wangu Bi Warda na watoto wetu wote nane, wakiwemo sita nilioachiwa na marehemu mke wangu kwa kunipa ushirikiano wa kifamilia.

Aidha, naomba sana niwashukuru wapiga kura wa Sikonge na Chama cha Mapinduzi kwa imani wanayoendelea kuwanayo kwangu pamoja na majukumu ya Kitaifa. Ninamshukuru Mheshimiwa Selemani Said Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa uongozi wake wenye nidhamu ya kazi, weledi, uaminifu na uadilifu. Sisi Naibu Mawaziri wake ametufunza mengi sana kuhusu namna bora ya kutimiza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati niwashukuru Watumishi wote katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kazi za kujituma katika kutimiza majukumu yao, kipekee naomba nimpongeze na kumtambulisha Bungeni Mwalimu Magreth Lubelege, kama yupo asimame ambaye licha ya kufundisha katika shule ya kawaida huko katika Manispaa ya Ilala, alikuwa pia akienda kuwafundisha watoto watukutu kwenye mahabusu yao, Upanga. Aliwawezesha wengi kufaulu mitihani ya darasa la saba kabla hajastaafu tarehe 30 Julai, 2017. Wengi wa watoto hao wako sekondari, wako vyuoni, wako vyuo vikuu na wengine tayari wameajiriwa. Mwalimu Magreth Lubelege ni shujaa kwani amewabadilisha watoto watukutu kuwa watoto wazuri. Maneno yake ni mafunzo kwa wengine, anasema alipouliza na waandishi wa habari na nanukuu’ “Mtoto kuwa gerezani si kwamba, hafai anafundishika ikiwa ataelekezwa na kufundishwa kwa upendo.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa walimu wote nchini kwamba, tumieni maneno ya Mwalimu Magreth Lubelege, waelekezeni watoto na kuwafundisha kwa upendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Mheshimiwa Waziri wetu alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imepata wachangiaji 71 waliozungumza Bungeni na wachangiaji 49 waliochangia kwa maandishi, nawashukuru sana Wabunge wote waliochangia. Wameonesha hisia zao za kutuunga mkono katika majukumu yetu yenye changamoto za mahitaji mengi yaliyopo kulinganisha na ukomo wa bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni na ushauri wote mlioutoa Waheshimiwa Wabunge tumeuchukua tukiamini kwamba, pale mlipokuwa wakali mlisukumwa na hisia za kutorodhishwa na utendaji wetu katika baadhi ya maeneo, tumewaelewa. Mnataka weledi, mnataka uaminifu, mnataka uadilifu, mnataka uzalendo na mnataka tuzingatie sheria, taratibu na kanuni za kazi, STK tutazingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika masuala mahsusi, ufafanuzi wangu katika masuala hayo utakuwa ni ufuatao:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Waheshimiwa Wabunge wengi ambao Mheshimiwa Waziri atakaposimama atawataja wamezungumza kuhusu umuhimu wa Serikali kujenga madarasa, vyoo, ofisi, nyumba za walimu, majengo ya utawala, mabweni, mabwalo, maktaba, maabara na kadhalika. Serikali ikiachiwa jukumu hilo peke yake tutachelewa mno, kwa mfano, kuanzia Julai, 2016 hadi Disemba, 2017 Serikali kupitia mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo pamoja na Mpango wa Equip, ilipeleka kwenye Halmashauri kiasi cha shilingi bilioni 106.5 mipango miwili kwa pamoja kukamilisha miundombinu iliyoanzishwa na wananchi kwa mwaka 2017/2018. Katika mwaka 2018/2019 tumetenga shilingi bilioni 8.7 kwa ajili hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ni makubwa mno wakati bajeti za Serikali zina ukomo. Hivyo, tunahitaji kuendelea kushirikiana na wananchi, wadau wa elimu wa ndani na nje ya nchi, huku mhimili mkubwa ukiwa ni wananchi wenyewe. Waraka Namba Tatu wa Elimu wa mwaka 2006 unaoainisha majukumu ya wazazi, jamii na wananchi wa maeneo husika bado uko hai, kilichokatazwa ni kuwatumia walimu kulazimisha michango kwa kuwapa adhabu wanafunzi, kuwatoa darasani ambao wazazi wao hawajachanga michango, hicho ndicho kilichokatazwa. Adhabu hiyo, haikuwa halali kwa mtoto kwa sababu hana kosa lolote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia siku ulipositishwa utaratibu huo michango yote ya wananchi kwa ajili ya miundombinu, chakula na hata kambi maalum za kimasomo inatakiwa iratibiwe na Serikali za Vijiji kupitia mikutano yao ya kisheria na taarifa lazima zitolewe kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, kuhusu viwango vya michango vilivyokubaliwa na kiasi kilichochangwa ili Halmashauri iratibu utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili na la muhimu sana, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia kuhusu tatizo la upungufu wa walimu kwenye shule za msingi, pamoja na shule za sekondari, hususan walimu wa masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukiri kwamba tatizo hilo lipo kama ifuatavyo; mahitaji katika shule za msingi ni walimu 273,454 waliopo 175,946, kwa hiyo, upungufu ni walimu 97,508. Mahitaji ya walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika shule za sekondari ni 35,136 waliopo ni 19,459, kwa hiyo, upungufu ni walimu 15,677. Tuna ziada ya walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari ambao ni walimu 21,165 ambapo wengi wao wana vipindi vichache sana vya kufundisha. Serikali inaendelea kuchukua hatua zifuatazo kurekebisha tatizo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya kwanza, kwa kuwa walimu wa masomo ya sanaa waliozidi katika shule za sekondari ni rasilimali watu ya Serikali, ili rasilimali watu hiyo itumike vizuri na kwa kuzingatia upungufu mkubwa wa walimu uliopo katika shule za msingi, imeamuliwa walimu hao 21,165 wahamishiwe kwenye shule za msingi. Huo ni uhamisho wa kawaida kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kituo kingine cha kazi, kazi hiyo ni hiyo hiyo ya ualimu. Mshahara ni ule ule haubadilishwi, daraja ni lile lile, kipaumbele cha juu katika uhamisho huo ni kuanza na walimu ambao zamani walikuwa katika shule za msingi wakajiendeleza kwa kusoma diploma au shahada ya kwanza ambao umahiri wa saikolojia ya watoto wa shule za msingi tayari wanao na wanayafahamu mazingira yaliyoko katika shule za msingi, wakiisha hao tunaenda kwa walimu wenye diploma na wakiisha tunaenda kwa walimu wenye shahada ya kwanza. Walimu wenye shahada ya uzamili hawahusiki na uhamisho huo isipokuwa kwa kibali maalum au maombi binafsi ya mwalimu mwenyewe na hayo ni maelekezo sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa agizo hili hadi ilipofika tarehe 31 Machi, 2018 jumla ya walimu 8,834 wamehamishiwa katika shule za msingi. Tumeyasikia malalamiko, tatizo kubwa lililopo ni utayari wa wanaohamishwa. Kuhamisha bila kuzingatia maelekezo tumeona katika baadhi ya maeneo na pia mazingira yale ya wanakopokelewa, jinsi ambavyo wale wanaotakiwa kuwapokea jinsi wanavyowapokea, hilo nalo limekuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaagiza Wakurugenzi na Maofisa Elimu katika Halmashauri zote kutengeneza mazingira bora ya utayari wa wanaohamishwa na pia wanaowapokea kwa kuanzia na wao wenyewe Maafisa Elimu wa Wilaya na Wakurugenzi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi zinazotakiwa kuzingatiwa pale anapohamishwa mtumishi, standing orders, lazima zifuatwe. Mfano, kama mtumishi anahamishiwa mbali na kituo chake cha kazi, lazima kumlipa posho stahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mukhtadha huo natoa wito kwa walimu wa sanaa waliozidi katika sekondari wakubali uhamisho ili waendelee na kazi hadi watakapostaafu kwa umri. Serikali inatambua kuwa licha ya tofauti ya lugha ya kufundishia mafunzo ya msingi kuhusu zana za kufundishia na saikolojia ni yale yale hakuna tofauti kubwa. Mukhtadha wa masomo ni ule ule, kama ni somo la historia ni lile lile, jiografia ni ile ile, kiswahili ni kilekile na kiingereza ni kile kile. Mwalimu anapofika kwenye kituo kipya cha kazi anachotakiwa kufanya ni kuchambua zana za kufundishia na ndani ya muda mfupi atajenga umahiri na weledi unaotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika baadhi ya masomo Maafisa Elimu wanaweza kuandaa mafunzo elekezi kwa njia ya mikutano ili kuelimishana vizuri zaidi kuhusu utekelezaji wa agizo hili la Serikali linalolenga kupunguza upungufu wa Walimu kwenye shule za msingi kwa asilimia 21.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine ni kuwa Serikali itaendelea kuajiri walimu kama hivi, tumepanga ifikapo Juni tuwe tumeajiri walimu 16,130, mwaka ujao tutaajiri walimu wengine 15,000 lengo ni kupunguza na kuondoa kabisa tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi katika shule za sekondari, ifikapo mwaka 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi wamelizungumzia ni umuhimu wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike. Suala hili ni muhimu sana, lakini linatakiwa kuandaliwa kwa umakini kwa kuzingatia sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kwanza ni tofauti zilizopo kati ya familia zinazoweza kuwanunulia watoto hao taulo hizo na familia maskini ambazo hazina uwezo huo.

Jambo la pili, ni tofauti za kimazingira zilizopo baina ya shule za mijini kwenye urahisi wa kupatikana taulo hizo na shule za vijijini hasa vijiji vya mbali sana na miji ambako hata kama mtu ana fedha anaweza asipate taulo hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya tatu, tofauti za ubora wa taulo zenyewe kutokana na viwanda zilikotengenezwa ili kuwa na uamuzi sahihi wa taulo zipi ni muafaka kutumika kwa wanafunzi wote wa kike katika shule zetu.

Nne, tofauti za bei ya taulo hizo kutoka eneo moja hadi lingine ambayo inaweza ikasababisha ugumu wa kupanga bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuzingatia sababu hizo, Serikali imeichukua hoja hiyo, ili mwaka 2018/2019 utumike kufanya uchambuzi na tathmini ya kina, ambayo hatimaye itatushauri kuhusu namna bora zaidi ya kutekeleza pendekezo hilo. Hatua ambazo tumeshaanza kutekeleza kwa sasa ni pamoja na kutoa maelekezo yafuatayo:-

(i) Kila shule iwe na mradi wa maji ikiwemo uvunaji wa maji ya mvua kwenye maeneo ya vijijini na shule za mijini waunganishe huduma za maji kutoka mamlaka za maji mijini.

(ii) Vilevile katika ujenzi wa vyoo vya shule wahakikishe chumba maalum kinatengwa mahsusi kwa ajili ya watoto wa kike kujihifadhi; na

(iii) Mwisho Wakuu wa Shule waendelee kuwatambua wanafunzi wanaotoka katika familia maskini zisizo na uwezo wa kuwanunulia watoto wao wa kike taulo za kike, ambao kwa kawaida huwa ni wachache. Kwa kutumia mwongozo wa ruzuku ya uendeshaji wa shule za sekondari wanaolekeza kutumia asilimia 10 ya ruzuku kwa ajili ya dawa na mahitaji maalum kwa wanafunzi wa kike, wawe na utaratibu wa kuwanunulia taulo hizo wanafunzi hao maalum kwa utaratibu utakaoratibiwa na Mkuu wa Shule husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo limezungumzwa na Wabunge ni wale ambao waliomba maombi maalum yanayohusu Majimbo yao, hususan kwa upande wa sekta za elimu na maji tumeyachukua kwa ajili ya kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na Wizara za sekta husika. Maombi hayo ni pamoja na usajili wa shule, kupandisha hadhi shule kuwa kidato cha tano na sita na wananchi kupatiwa huduma za maji na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi waliozungumzia ni kuhusu gharama ambazo hazimo katika fedha za elimu ya msingi bila malipo. Naomba kulihakikishia Bunge kuwa gharama za umeme na maji zimo ndani ya fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule. Suala la mahitaji ya walinzi wa shule, matron and patron, kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu na hata wale wa kike bado linafanyiwa uchambuzi wa kina ili hatimaye utekelezaji wake uwe mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ambalo Waheshimiwa Wabunge ningependa kufafanua hapa ni changamoto za miradi ya maji katika maeneo yao. Napenda nikiri kwamba zimekuwepo changamoto kadhaa ambazo tumekuwa tukizitatua kwa kusaidiana na Wizara ya Maji. Miradi ya maji ni miradi ya miundombinu ambayo kabla ya utekelezaji lazima kujua chanzo cha maji, uwezo wa chanzo cha maji, aina ya mradi utakayotumika kama ni kuchota maji kwa mashine ya kuendeshwa kwa mkono au kuendeshwa kwa nguvu za nishati ya jua au kwa umeme au kwa mafuta au maji yanayotiririshwa kwa mteremko na kadhalika. Hatua hii ni upembuzi yakinifu na hatua ya usanifu ndiyo huelekeza gharama zinazohitajika kutengeneza mradi. Tukishajua gharama za mradi fedha hutengwa kwenye bajeti na hatimaye mchakato wa kuwapata Wakandarasi wa ujenzi na wasimamizi wao hufanyika ambao hatimaye Mamlaka za Serikali za Mitaa husaini nao mikataba ya utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ipo miradi ambayo fedha nyingi zimetumika, miundombinu isiyozingatia viwango vilivyomo kwenye usanifu imejengwa chini ya kiwango, ikiwemo iliyojengwa bila ya kuzingatia uwezo wa chanzo, wakati mwingine wamefukuzwa wakandarasi katikati ya utekelezaji na hivyo miradi kuachwa bila kutimiza lengo lake la kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zilizopo zinaonesha moja kwa moja sababu ni Mkandarasi asiye na uwezo unaotakiwa ndiye aliyepewa mkataba. Kwa kuwa taratibu za kuingia mkataba na wakandarasi zinafahamika duniani kote, kwamba huwezi kuingia mkataba na Mkandarasi bila kwanza kumfania due diligence yaani upekuzi maalum ili kutathmini uwezo wake wa kutengeneza mradi kabla ya kusaini mkataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nihitimishe kwamba, tutaendelea kuwa wakali sana dhidi ya taratibu ambazo hazifuatwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kwanza naomba kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wa Maji; na kwa faida ya Bunge lako tukufu niseme tu kwamba sisi Watanzania ni ndugu. Maana yake ni kwamba Kamwelwe ni Kandege, Kakunda ni Kandege na Kandege ni Kandege kwa hiyo, tuko vizuri tunatumia jina moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitoe ufafanuzi kwa maeneo machache; kuna Waheshimiwa Wabunge ambao wamezungumza kwamba shule zote na taasisi zote za huduma za jamii zipatiwe huduma ya maji. Nitoe taarifa kwamba tumeshaziagiza Halmashauri zote kuweka kipaumbele cha kupeleka huduma za maji kwenye taasisi zote ikiwemo shule, zahanati, vituo vya afya na hospitali na tunalifuatilia sana kwa karibu agizo hilo kuhusu utekelezaji wake na tumewaambia Wakurugenzi wa Halmashauri tunawapima kwa kutekeleza vipaumbele hivi. Aidha, tumeagiza majengo yote ya shule na majengo ya taasisi yawekewe mifumo ya kuvuna maji mvua ili kusudi kupata maji ya uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; wako Wabunge ambao wamezungumzia umuhimu wa kuhamisha watumishi wetu mara kwa mara ili kuongeza ufanisi. Hilo ni wazo zuri, tumeshaanza kulifanyia kazi. Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita tu tumeshahamisha watumishi 26 na zoezi hili linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utekelezaji wetu, sisi katika serikali za mitaa, tunatekeleza kazi zetu kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 145 na Ibara ya 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Sheria Na. 7 kwa Halmashauri za Wilaya; Sheria Na. 8 kwa Halmashauri za Miji. Vilevile tunafuatilia sana utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Maji Na.12 ya mwaka 2009. Katika sheria zote hizo, kazi za Halmashauri na Serikali za Mitaa kwa ujumla ni utekelezaji wa miradi ikiwemo miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za Serikali Kuu kwa ngazi za Mikoa na Wilaya ni ufuatiliaji na usimamizi. Kazi ya Wizara ya Maji ni kubwa mno, kutunga sera, mikakati, sheria, kanuni, miongozo ya kitaalam, ufuatiliaji na tathimini. Miradi mikubwa inayohudumia wilaya zaidi ya moja, vilevile miradi mikubwa mikubwa ambayo inahudumia Mikoa zaidi ya mmoja. Lakini kubwa zaidi wanafanya kazi kubwa sana ya kutafuta fedha za kutekelezea miradi hiyo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ushirikiano wetu ni mkubwa sana sana. Na changamoto katika kazi hizi kubwa huwa hazikosi. Kwa hiyo tunaendelea kutatua changamoto kwa ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningesema mengi lakini mengi namuachia mwenyewe Mheshimiwa kaka yangu atayazungumza yanayohusu mambo yote ya kitaalamu kuhusu miradi ya maji atazungumza. Naomba sana kuunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kukupongeza kwa dhati wewe mwenyewe pamoja na Mheshimiwa Najma Giga ambaye alikuwa Mwenyekiti jana kwa jinsi mlivyotuongoza tangu nilipowasilisha hotuba yangu jana, mlivyosimamia mjadala na hadi kufikia muda huu nawapongeza sana na kuwashukuru sana.

Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge 40 ambao wamechangia kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge 37 ambao wamechangia kwa kusema moja kwa moja hapa Bungeni. Kwa ajili ya muda naomba majina ya Wabunge wote waliotoa ushauri, maoni, na mapendekezo yawe kwenye orodha ya hansard kwa ajili ya kumbukumbu, nawashukuru sana.

Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Naibu Mawaziri na Mawaziri waliopata nafasi ya kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyojadiliwa. Kwa namna ya kipekee namshukuru sana Naibu Waziri wangu Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya kwa jinsi alivyotoa ufafanuzi aliotoa hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikiri kwamba Wabunge wote waliochangia kwenye hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara wameipatia Serikali ushauri na maoni mazuri ambayo mengi tutayafanyia kazi na kutoa taarifa kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ufafanuzi wangu ninaotoa ni kwa maeneo machache yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa upande wa Kamati ni maeneo mawili tu ya kuzungumza. La kwanza niahidi kwamba mapendekezo ya Kamati tutayafanyia kazi, ingawa kuna baadhi ya mapendekezo yanagusa mikataba, kwa hiyo baadhi ya mapendekezo ambayo yanagusa mikataba itabidi yaingizwe kwenye mfumo wa majadiliano yanayoendelea. Kamati itapewa taarifa rasmi kupitia utaratibu wa ratiba zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kutopendwa sokoni kwa bidhaa zinazozalishwa nchini na ushauri wa Kamati wa kuhamasisha Watanzania kupenda kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya Tanzania. Tumeupokea ushauri huo kwa mikono miwili na moyo mkunjufu, kwa sababu mtu asiyependa chake ni sawa na kutojithamini mwenyewe. Viwanda vyetu vinazalisha vitenge vizuri sana, lakini vikiandikwa made in Tanzania baadhi ya Watanzania hawanunui mpaka baadhi ya viwanda vya nguo vinalazimika kuandika made in Nigeria ndiyo vipate soko. Sasa hii ni tatizo ambalo naomba Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane kuliondoa katika nyoyo za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ushauri huo wa Kamati ya Bunge letu tuanzie na Bunge, lionyeshe mfano kwa kupendekeza manunuzi ya bidhaa za Tanzania kwenye ofisi zote za umma, Ofisi za Bunge na hata Bunge hili likubali kubadilisha kanuni za mavazi ya Wabunge hasa Wabunge wanaume ikiwezekana waruhusiwe kuingia Bungeni wakiwa wamevaa mashati nadhifu ya vitenge vikiwa vya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba ya Upinzani niseme tu kwamba, mwaka wa fedha 2018/2019 haujakwisha, randama aliyoinukuu Mheshimiwa Waziri Kivuli ilikuwa na takwimu za hadi mwezi wa Tatu 2019, bado miezi minne hadi mwezi wa Nne takwimu zimebadilika na hadi wiki ijayo ninazo taarifa kwamba takwimu hazitakuwa zile zilizonukuliwa. Kwa maana hiyo kwa ajili ya kuweka kumbukumbu sawa, siyo sahihi kabisa na haitokuwa sahihi kabisa kusema kwamba eti bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ilikuwa ni bajeti hewa, isipokuwa kilicho sahihi ni kusema kwamba Serikali huwa ina umakini mkubwa katika kutoa fedha za utekelezaji hadi pale inapojiridhisha kwamba hatua stahiki za maandalizi ya utekelezaji zitakuwa zimekamilika. Mfano, baadhi ya maeneo yanayoendelea na ratiba ya mapitio ya mikataba na baadhi ya maeneo yanahitaji tafiti kwanza zifanyike na kukamilika kabla ya utekelezaji kuanza lazima fedha zake zitasubiri kutolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Viwanda na Biashara ina imani kwamba kwa maeneo na miradi ambayo taratibu za maandalizi zimekamilika mfano wa ulipaji wa fidia kwenye mradi wa Mchuchuma na Liganga fedha zitatolewa kabla ya kwisha kwa mwaka wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili katika hotuba ya Upinzani, ni lawama na kubeza utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa reli ya kati kwa viwango vya Kimataifa na mradi mkubwa wa kufufua umeme wa Stiegler’s. Napenda nisisitize pongezi zangu kwa Mheshimiwa Rais kwa maamuzi ya kihistoria aliyoyafanya kujenga miradi hiyo. Kwa mujibu wa Maazimio ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Dunia uliofanyika Rio de Janeiro, Brazil mwaka 1991, uchumi maana yake ni ardhi na anga kwa maana ya mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta za uchumi ambazo ni kilimo, mifugo, uvuvi, maji chini na juu ya ardhi, maliasili ikiwemo uoto wa asili na wanyamapori, madini na ujenzi kwa ujumla na sekta za uchumi anga ambazo ni pamoja na nguvu jua, mwanga, hewa na mvua ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yoyote ile ikiwemo Tanzania. Hata hivyo uzalishaji ghafi kwenye sekta hizo hauwezi kuwa na faida kubwa kiuchumi kama sekta ya viwanda haitachakata malighafi zinazozalishwa ili kupata bidhaa zenye thamani kubwa ambazo zitafikishwa kwenye maeneo mbalimbali zinakohitajika kwa matumizi ya binadamu na viumbe wengine kupitia mifumo wa biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili Sekta ya Viwanda na Biashara itimize jukumu lake hilo vizuri, inahitaji mazingira wezeshi yanayopunguza gharama za uzalishaji, gharama za hifadhi, gharama za usafiri na gharama za usafirishaji. Kwa maana rahisi mazingira wezeshi ni bandari inayofanya kazi vizuri, barabara nzuri za lami, madaraja makubwa, mfano, madaraja ya Mkapa, Kikwete na Magufuli, viwanja vya ndege, reli ya viwango vya Kimataifa, mradi mkubwa wa kufufua umeme wa uhakika kama Stiegler’s ambao utazalisha megawati 2,100 kuwa na uhakika wa kuhudumia viwanda. Miundombinu hiyo ndiyo chachu kubwa ya uwekezaji kwenye viwanda na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii itakapokamilisha miradi hiyo na miradi mingine ukiwemo ule ambao utatekelezwa baadaye wa reli ya Mtwara hadi Mbambabay, ambao baadaye itajengwa reli kupita kwenye maeneo ya miradi ya chuma ya makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma itachochea kwa kasi ya aina yake maendeleo ya ujenzi wa viwanda na biashara nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili limezungumzwa sana ni eneo la software kwenye biashara. Hoja hii imejitokeza kwa kuchangiwa na Wabunge wengi sana na ilionekana kama ndiyo pekee ambayo pengine inakwamisha maendeleo ya viwanda na biashara nchini. Serikali imedhamiria kutekeleza mapendekezo yaliyomo kwenye mfumo wa kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara, uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ambao utaboresha na kupunguza gharama za uwekezaji na ufanyaji biashara. Mfumo huo ambao ndiyo blue print utakaoanza kutekelezwa mwezi Julai ndiyo ambao utakuwa ni mwarobaini wa kuondoa malalamiko mengi sana ya sekta binafsi, sekta ya viwanda na sekta ya biashara hapa nchini. Tumejizatiti na naamini chini ya uratibu na usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, mambo mengi yatakaa vizuri na kuanzia mwaka ujao wa fedha malalamiko yatakuwa yamepungua sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, yamezungumzwa mengi sana na Waheshimiwa Wabunge kuhusu miradi ya kimkakati. Labda nikianza na Mradi wa Mchuchuma na Liganga, niseme tu kwamba Serikali imedhamiria kuanza uchimbaji wa makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga. Uendelezaji wa mradi huu utaanza mara tu baada ya mambo kadhaa kukamilika ikiwemo mchakato wa kurekebisha vipengele katika hati ya makubaliano kulingana na sheria mpya ya ulinzi wa maliasili, kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi watakaopisha utekelezaji wa mradi, kujenga miundombinu wezeshi kwenye eneo la mradi, hasa barabara, reli na njia ya msongo wa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kurekebisha vipengele vya mkataba ni kulinda maslahi ya nchi kufuatia Sheria mpya za Madini za mwaka 2017 na Sheria za kulinda maliasili zetu. Kwa hiyo majadiliano ya kina ni lazima yafanyike upya kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, vivutio vingi vilivyoombwa na mwekezaji vinapingana na sheria za nchi hivyo kufanya utekelezaji wake kuwa mgumu. Pili, mkataba uliosainiwa baina ya mwekezaji na Serikali una vipengele vingi vinavyomnufaisha zaidi mwekezaji kuliko Serikali. Tatu, kufanya tathmini upya juu ya kiwango na ubora wa madini ya chuma titanium, vanadium na aluminium katika mgodi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakumbuka kwamba wakati wa mkataba ule wa awali kilichokuwa kinatajwa ilikuwa ni chuma na makaa ya mawe peke yake ilidhaniwa kwamba titanium, vanadium na aluminium kwamba hiyo itakuwa na viwango kidogo sana ambavyo havitakuwa na maana katika mapato, kumbe hiyo tulikuwa tunaingizwa katika mkenge ambao Taifa hili kama mkataba ule ungesainiwa kama ulivyokuwa, inawezekana aliyesaini angebatizwa jina la Mangungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya jitihada za dhati kupunguza muda wa majadiliano ili kuhakikisha kwamba tunamaliza majadiliano ndani ya muda mfupi. Aidha, katika mradi huo Serikali inaangalia uwezekano wa kutenganisha mradi wa makaa ya mawe na ule wa kuzalisha umeme ili kurahisisha utekelezaji wake. Lengo ni kuwa na vyanzo vingi vya kuzalisha umeme wa uhakika ukiwepo uzalishaji wa umeme wa makaa ya mawe utakaotumika viwandani.

Mheshimiwa Naibu Spika, klatika mradi wa Liganga madhumuni ni kuchenjua na kuzalisha bidhaa mbalimbali za chuma ikiwemo vanadium na titanium ili kukidhi soko la ndani na nje ya nchi badala ya kuuza chuma ghafi. Kwa hiyo, kuuza bidhaa za chuma cha Liganga kwa wenye viwanda nchini ndiyo nia ya Serikali ili kuongeza mnyororo wa thamani na hivyo kukuza sekta ya chuma nchini. Azma hiyo itatekelezwa mara tu Mradi wa Liganga utakapoanza uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mwelekeo wa Serikali ni kutenganisha Mradi wa Chuma cha Liganga na ule wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma. Hata hivyo suala hili linahitaji majadiliano na wadau mbalimbali kwa kuwa mkataba wa awali ulikuwa unganishi kwa lengo la kuzalisha chuma na umeme kwa kutegemeana ambapo umeme unaotokana na makaa ya mawe ungetumika kuyeyusha chuma cha Liganga ili kupata bidhaa mbalimbali zitokanazo na chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tungetekeleza nina takwimu hapa, ule mkataba wa awali kama ungesainiwa ulivyokuwa, Serikali ingepoteza dola za Kimarekani bilioni kumi na tisa laki nane na milioni mia nane sitini kwa chuma na vile vile tungepoteza dola 23,342,200,000 kwa aluminium na dola milioni 450 kwa titanium. Hii ingekuwa ni hasara kubwa kwa Taifa na mikataba ya aina hii iliwahi kusainiwa huko nyuma na Bunge liliwahi kutangaza kwamba mikataba ile ilikuwa mibovu. Kwa hiyo, kwa sasa hivi tuko makini kuhakikisha kwamba tunalinda maslahi ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Soda Ash Engaruka; madhumuni ya Serikali katika Mradi wa Magadi soda wa Engaruka ambao utazalisha magadi soda kama msingi wa viwanda vya kemikali nchini yako wazi. Kwa sasa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu ambao inaitwa tekno economic study kama nilivyosema kwenye hotuba. Lengo la study hiyo ni kubaini faida na namna bora ya kutekeleza mradi huu. Kwa hiyo, upembuzi huu yakinifu utakapokamilika ndiyo utakaotushauri tutekeleze vipi mradi huu. Namwomba sana Mheshimiwa Mbunge Kalanga tushirikiane katika hili kwa sababu huwezi kuanza kujenga barabara ya lami leo kwenda kwenye eneo la mradi wakati upembuzi yakinifu haujatushauri je, tutajenga mabomba au tutajenga barabara ya lami au tutajenga barabara ya changarawe. Kwa hiyo naomba tuwe na subira, wananchi wawe na subira mradi huu utatekelezwa na tutakuwa na faida kubwa sana kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Matairi cha Arusha, napenda nirejee kama nilivyosema kwenye hotuba yangu Serikali imedhamiria kufufua kiwanda hiki, kile kiwanda cha Kenya wameshakifunga hakizalishi tena kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanasema hapa tunazidiwa na Kenya. Kenya watategemea matairi kutoka kwenye Kiwanda cha Matairi cha Arusha tutakapoanza uzalishaji. Kwa hiyo, hiyo ni fursa ambayo tutaitumia na hii kampuni ambayo tunaendelea na majadiliano nayo, majadiliano haya tutayakamilisha kwa haraka iwezekanavyo kama ambavyo Wabunge wameonesha ili tuhakikishe kwamba kiwanda kinaanza uzalishaji wa matairi. Tunawatafutia eneo lingine ili kuongeza eneo maana yake eneo hilo la Arusha limeonekana ni dogo, kwa hiyo tutawatafutia eneo la hekta 100 nje ya Arusha na litakapopatikana tu tayari tutaingia kwenye makubaliano rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Kiwanda cha Tabotex cha Tabora ni kweli kwamba kiwanda hiki hakifanyi kazi tumeshamwonya mwekezaji mara nyingi, ameandika barua kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu tangu mwezi wa 12 akiomba muda wa kufikiriwa kwa sababu alikuwa anatafuta mkopo TIB. Sasa mkopo wa TIB wa shilingi bilioni tano sisi hatujajua kama ameupata, lakini muda wake alioomba umepita. Kwa hiyo itakapofika tarehe 31 sawasawa na ambavyo tumezungumza kwenye viwanda vingine, kiwanda hiki itabidi kirejeshwe Serikalini kama hatakuja na concrete plan ya kuendeleza kiwanda hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kuhusu miradi ya mikakati, ni miradi ya EPZA. Miradi ambayo ni ya kujivunia sana hapa nchini ni miradi ya EPZA ingawa kuna changamoto katika baadhi ya maeneo machache, eneo la Tanga na maeneo mengine kwa ajili ya fidia, lakini miradi ambayo tayari inafanya kazi, inafanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Riziki Lulida alizungumzia mradi wa EPZA wa utengenezaji wa nguo pale Ubungo, akisema kwamba wafanyakazi pale ni kama vile wananyonywa, lakini nikwambie tu ukweli kwamba wafanyakazi walioajiriwa pale kiwandani kwenye kiwanda cha Took Garment Limited ni wafanyakazi 2,600 na idadi hii itaongezeka kufikia wafanyakazi 4,000 miezi michache ijayo. Wafanyakazi ukiwatembelea pale, nimetembelea pale nimeongea nao, wanaridhika na hali ya ajira kwenye kiwanda hicho na si kweli kwamba wanalipwa sh.100,000 au chini ya hapo, wafanyakazi wengi wanalipwa mishahara ambayo wamekubaliana. Kwa hiyo kazi inayoendelea pale inaendelea vizuri na kuna amani na utulivu na hakuna mgogoro wowote na endapo kutakuwa na mgogoro mimi nitakuwa wa kwanza kuusikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Indo Power nataka nirudie tena Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza, ile Kampuni ni Kampuni genuine kabisa iko Kenya imefanyiwa due diligence vizuri kabisa na Balozi wetu wa Tanzania nchini Kenya na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, tumepata taarifa za kutosha linafanya biashara hapo Kenya na ni Kampuni ambayo inastahili kufanya biashara ndani ya Kenya, Afrika Mashariki na Duniani kwa ujumla. Sasa mkataba ambao tuliingia na kampuni hiyo mkataba ule ulikuwa halali na ulikuwa na vipengele vya utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa bahati mbaya kampuni ile imechelewa kutekeleza baadhi ya vipengele, kiasi ambacho kikafikia tukaanza sasa kupata matatizo, baadhi ya watu wengine wa Tanzania hapa, kama benki inataka kulipa labda mtu fulani anataka kununua korosho Tanzania, wakaanza kupeleka taarifa kwamba mnalipa korosho, zimeshanunuliwa na kampuni fulani. Kwa hiyo ndiyo maana tumetangaza kwamba ile kampuni tumeamua kuachana nayo ili kusudi tuweze kuuza korosho na hizi korosho tutaziuza hivi karibuni tofauti na watu ambao wanafikiri kwamba hatutauza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kulinda viwanda vya ndani, naomba tushirikiane Bunge zima, Serikali nzima na wananchi tushirikiane kuhusu suala la kulinda viwanda vya ndani. Hatua ya kwanza ya kulinda viwanda vya ndani ni kuhakikisha kwamba wanapata raw materials kwenye viwanda. Kama kiwanda kinajengwa halafu hakipati raw materials kitakufa, kwa hiyo tusije kukamata koti la Mheshimiwa Kakunda, kwamba Kakunda hajasimamia vizuri viwanda vimekufa kama vimekosa raw materials itabidi wote tusimame tuulizane. Kwa hiyo jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, viwanda vinapata raw materials.

Mheshimimiwa Naibu Spika, mimi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tumeshazungumza tumekubaliana viwanda, kwa mfano, viwanda vya korosho tumekubaliana vitapata raw materials. Hata wale wanaotaka ku-invest kwenye viwanda vya korosho Tanzania tunawapa mkataba maalum kuwahakikishia watapata raw materials ili viwanda visife wala kuhamishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ngozi Serikali haijazui kuuza ngozi ghafi nje. Hadi sasa ngozi zinauzwa kwa wingi katika nchi za Ghana na Nigeria na vibali vinaendelea kutolewa kwa wale wanaohitaji. Hadi kufikia mwezi Machi, 2019 kilo za ngozi ghafi 3,636,700 za ng’ombe zenye thamani ya shilingi trilioni 4.6 na kilo 274,000 za mbuzi zenye thamani ya shilingi 320 zilisafirishwa nchi ya nje. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba tumezuia kusafirisha ngozi nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu miradi ya maendeleo kutumia vifaa vinavyopatikana nchini. Hili limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge, mambo mengine yanahusu mikataba, tunaendelea kuzungumza na Wizara ya Fedha na wadau wengine kuhakikisha kwamba sehemu kubwa ya matumizi kwenye miradi mikubwa ya maendeleo kwa mfano ujenzi wa barabara, reli na madaraja wanatumia vifaa ambavyo vinazalishwa ndani ya nchi ikiwemo bidhaa za chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani nitakuwa nimegusa maeneo maeneo muhimu sana ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge na mengine yote ambayo yamezungumzwa tumeyachukua na tutayatolewa taarifa wakati utakapofika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, ahsante sana.

WABUNGE FULANI: Toa hoja.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana ambaye ni Naibu Spika wetu; naomba awali ya yote kabisa nianze kwa niaba ya wananchi wa Sikonge kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuenzi maana halisi ya majina yake, maana Samia maana yake ni Msikivu, Suluhu maana yake ni Mpatanishi na Hassan maana yake ni Mzuri au mtu mwema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana, ndio maana mwezi uliopita kwa makusudi kabisa akaamua kuwaongezea Watanzania kwenye bajeti yao, zaidi ya Shilingi trilioni 1.3 ili zikapeleke rekodi ya maendeleo ambayo haijawahi kupatikana katika miaka ya hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza tena kwa kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango ambao Mheshimiwa Waziri aliuwasilisha kwa weledi mkubwa sana. Nimpongeze Waziri na timu yake yote kwamba, wameweza kuwasilisha kwa weledi mzuri sana Mapendekezo ya Mpango. Pia simsahau Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Daniel Sillo aliposimama kuwasilisha maoni ya Kamati aliwasilisha kwa ueledi mkubwa sana. Hongera sana Mheshimiwa Daniel Sillo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Spika Job Ndugai, siku ya Jumanne alitoa maelekezo muhimu sana kwa Serikali akiwa kwenye kiti kile pale. Akaiagiza Serikali kwamba, fanyieni kazi suala la upandaji wa bei ya mbolea kwa haraka iwezekanavyo. Hiyo kweli nampongeza sana Mheshimiwa Ndugai, kwa sababu, ni jukumu ambalo ni muhimu sana kwa Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maoni katika maeneo manne tu. Eneo la kwanza, naomba sana katika hatua hii ya mapendekezo ya Mpango naomba Serikali ikasisitize, Mpango utakaoletwa na bajeti yake itakayopendekezwa, ni muhimu sana Serikali itenge bajeti maalum kwa ajili ya vitu viwili; ruzuku ya pembejeo za wakulima na hii ni kwa nchi nzima. Pili, kupanga fedha za buffer stock kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima pale ambapo uzalishaji utakuwa mkubwa ukazidi soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kupendekeza katika maoni yangu, Mfuko wa Jimbo ni wa Sheria ya Mwaka 2009. Kwa sasa hivi una umri wa miaka 12, vigezo ni vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wakati Waziri atakapoleta Mpango azingatie vile vile, Serikali ilete marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Jimbo ili kuboresha zaidi malengo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, nilikuwa naangalia upandaji wa bidhaa muhimu nchini, hasa hasa bidhaa za ujenzi na nimeona kwamba kuna tatizo ambalo Serikali inabidi iweke mkakati maalum. Afrika Kusini mwaka uliopita 2019/2020, kwa sababu ya UVIKO walifunga viwanda 2,000. Mwaka jana na mwaka huu 2020/2021, wamefunga viwanda 1,000 kwa sababu ya mambo ya lock down. Sasa hii imesababisha demand ya bidhaa zinazotengenezwa Tanzania ivuke mipaka ya nchi kwa kasi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna demand kubwa ya bati, kuna demand kubwa ya cement, kuna demand kubwa ya bidhaa za chuma ikiwemo nondo katika nchi hizo za Kusini mwa Afrika - SADC kwa ujumla. Kwa hiyo, lazima Serikali itengeneze utaratibu/mkakati maalum wa namna ya kukabiliana na hiyo hali ya hiyo demand. Matokeo yake, uzalishaji wa Tanzania sasa umekuwa ni wa export zaidi, kwa hiyo demand ya ndani ya nchi nayo imeathirika matokeo yake bei zimepanda sana. Kwa hiyo, naomba Serikali ije na mkakati maalum wa namna ya kudhibiti hali hiyo ya biashara kuanzia sasa, sio kusubiri mwakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nitatumia muda kidogo hapa, kwa miaka mingi kumekuwa na udhaifu kwenye eneo la ufuatiliaji na tathmini na ndio maana akienda Mkuu wa Mkoa, anagundua matatizo, akienda Mkuu wa Wilaya kwenye miradi, anagundua matatizo, akienda mkimbiza Mwenge wa Kitaifa, anagundua matatizo, akienda CAG, ndio kabisa. Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuimarisha ufuatiliaji na tathmini (monitoring and evaluation). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana Kamati imekuwa inasisitiza mara kwa mara na Serikali imekiri Bungeni humu kwamba, upo umuhimu sasa wa Serikali kuja na sera na sheria maalum itakayo-guide M&E nchini. Nikisema hivi watu wengine watasema mbona sheria zipo tunazo, sawasawa ni kweli. Tuna Sheria 10 zinazo-guide M&E nchini na nitazitaja kwa kifupi kabisa. Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001, inayo-guide utunzaji wa nyaraka, matumizi na ukaguzi wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine ni Sheria ya Ununuzi wa Umma ina-guide M&E za mikataba, kukagua miradi na utunzaji wa nyaraka; Sheria ya Tawala za Mikoa, Sheria za Serikali za Mitaa, Sheria ya PCCB kuhusu masuala ya kudhibiti ubadhirifu, Sheria ya Polisi - Police Force Ordinance kuhusu ukaguzi wa sheria zote, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria ya Utumishi wa Umma kuhusu Strategic Plan na OPRAS, Sheria Kuu ya Jinai (Penal Code) kuhusu wajibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Sheria ya Kodi ya Mapato kuhusu kufuatilia ajira, biashara na uwekezaji. Halafu kuna Sheria nne kuhusu tathmini; Sheria ya Ukaguzi wa Umma ambayo anaitumia CAG; kuna Sheria ya Bajeti, halafu kuna Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana za Serikali ambao kwenye Financing Agreement inaweza ikatoa M&E framework, kwa ajili ya miradi na program fulani fulani. Halafu ya mwisho ni Sheria ya NBS – National Bureau of Statistics hii Sheria nayo ina-guide kuhusu evaluation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna Sheria 14 sasa kuna hapa na pale, kuna mambo fulani fulani ambayo inaonyesha kabisa kwamba hii M&E haipo streamlined. Kwa hiyo, ombi langu, Serikali mwaka ujao itunge Sera ya M&E halafu vile vile, ifuatiwe na Sheria ya M&E ambayo sasa hiyo ndio itatumia…

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya kufuatilia na ku-evaluate mambo ya Serikali yote kwa ujumla. Ahsante sana. Kuna taarifa hapa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome, naomba mchangiaji ameshasema ahsante sana. Umemaliza Mheshimiwa Kakunda?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Bado hajamaliza.

MWENYEKITI: Sawa, endelea Mheshimiwa Salome Makamba.

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Kakunda kwamba, tulishaleta mapendekezo ya kuunda sera ya monitoring and evaluation na Serikali ilishapokea na ikasema inaenda kulifanyia kazi. Kwa hiyo, labda tuombe Serikali walete kwenye commitment ya Mpango huu, sera hiyo, lakini tulishawapelekea. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome, unasema tulishaleta wewe na nani?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna-Caucus Maalum ya Monitoring and Evaluation, tulileta na Kamati ya Bajeti walileta lile pendekezo na walitoa Azimio la Bunge.

MWENYEKITI: Ngoja kwanza ngoja. Ukisema tulileta, maana yake ulileta kwa Spika, la sivyo useme tuliipelekea Serikali. Kama ukisema tulileta maana yake ulileta kwa Spika, ndio maana nakuuliza wewe na nani mlileta?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hicho Kiswahili chako hicho hicho ndio nachukua na mimi na-adopt, lakini point yangu ni kwamba suala hili Serikali ilishalipokea na ni Azimio rasmi la Bunge. Kwa hiyo, commitment ya Serikali wataleta lini sera hiyo ndio nafikiri alichotaka kukisema Mheshimiwa Kakunda. (Makofi/ Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kakunda unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge Wakereketwa wa ufuatiliaji na tathmini na naipokea taarifa ya Mheshimiwa ya Salome Makamba. Ndio maana mimi sikutaka kuisema hiyo, kwa sababu, ile ilipelekwa katika utaratibu ambao sio wa Bunge kwa maana kwamba, Kamati yetu sisi ya Wakereketwa mambo yetu humu Bungeni yanaletwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yalishaletwa humu na Waziri mwaka jana alisema kwamba suala hilo ni muhimu. Kwa hiyo, kama Serikali ilishakiri kwamba suala hilo ni muhimu ndio maana tunasisitiza kwamba, kwenye Mpango ujao walete sasa mchakato maalum ambao utatunga Sera ya M&E halafu itahitimishwa na utungaji wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie mchango wangu sasa kwamba lengo la pendekezo hili sio kuzifuta Sheria zile 14 nilizotaja, hapana. Lengo ni kunyoosha utaratibu wa usimamizi, ufuatiliaji na tathmini katika nchi yetu, ili uwe wa Kimataifa na kuhakikisha kwamba tunapunguza observations zile ambazo CAG ndio huwa anasubiri akienda anazikuta au mkimbiza mwenge akienda anazikuta, au Mkuu wa Mkoa akienda anazikuta, au Waziri au Waziri Mkuu au Rais akienda anazikuta yapunguzwe hayo kwa kufuatilia. Kuna maeneo 35 ya kufuatilia kwenye mchakato wote wa mradi. Maeneo hayo yakifuatiliwa vizuri, hizo observations za CAG na Wakaguzi wengine zitapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa heshima hii, nami niweze kuchangia uwasilishaji wa taarifa za kamati tatu za oversite. Nami nichukue nafasi hii kuanza kuzipongeza hizi Kamati zimefanya kazi zake vizuri kwa mujibu wa taarifa ambazo wamewaslisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ningependa kulizungumza, kabla ya kuanza kujadili taarifa ya CAG mimi binafsi nilikuwa natamani kamati zetu zingejadili taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa siku ya tarehe 30/03/2022 alipopokea taarifa ya CAG na taarifa ya TAKUKURU. Mheshimiwa Rais baada ya kupokea taarifa hizo, alibainisha na kutoa maagizo na maelekezo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza alisema, kupitia ripoti hizo mbili, kwamba kuna udhaifu katika uratibu wa Serikali kwa ujumla (Government coordination) ikiwemo kuchelewa kutoa maamuzi hasa kwenye miradi ya maendeleo. Kutokana na tatizo hilo, akaelekeza Katibu Mkuu Kiongozi achukue hatua mahususi kurekebisha udhaifu huo. Kwa hiyo, nilitegemea wapate taarifa ya utekelezaji kwa hii miezi tangu agizo hili litolewe. Hali ya utekelezaji wa agizo hili ikoje Serikalini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Mheshimiwa Rais alisema, kuna udhaifu kwenye ufuatiliaji wa tathmini ikiwemo utaalamu hafifu na nyenzo hafifu. Akaagiza Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) ifanye uchambuzi na kuishauri Serikali ipasavyo. Kwa hiyo, nilitegema Kamati zetu nazo zifuatilie status ya utekelezaji wa agizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, Mheshimiwa Rais akasema, kuna udhaifu Serikalini wa kuwa na mifumo mingi sana ya utoaji wa taarifa ambapo mifumo hiyo haiwasiliani, yaani haiongei. Akaagiza mifumo yote ya mawasiliano Serikalini na kupeana taarifa iangaliwe ili ikiwezekana kuwe na mfumo mkubwa mmoja unaoongea nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitegemea kwa sababu haya ni mambo ya msingi ambayo kama yatarekebishwa, yataweza kuondoa yale matatizo ambayo yanaonekana kwenye taarifa za CAG angalau kwa robo tatu yake. Sasa haya mambo ni muhimu sana. Nilikuwa napendelea sana hata kama hawakuyajadili, basi siku zijazo waweze kukaa na kupata status ya utekelezaji kwa sababu haya yalikuwa ni maelekezo ya kisera ambayo yana umuhimu wa kipekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye taarifa ya CAG. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 143 (1)(a) na (b) inampa mamlaka mdhibiti au CAG afanye kazi ya kudhibiti. Udhibiti (control); yaani controller anapewa mamlaka na hivyo vipengele viwili, (a) na (b). Sasa katika taarifa ya CAG mimi sijaiona taarifa ya CAG inayoelezea jinsi alivyotimiza jukumu lake la udhibiti kwenye taarifa hiyo. Nilitegemea aeleze. Tatizo ni nini? Tatizo kuu, usimamizi wa jukumu hilo umewekwa kwenye Mahakama, ndiyo maana amekuwa hatoi taarifa kuhusu udhibiti kwa Bunge au hata kwa Rais kwa sababu usimamizi wake umewekwa kwenye Mahakama, kupitia kipengele gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ibara ya 143 (6), nanukuu, inasema hivi: “Katika kutekeleza madaraka yake, kwa mujibu wa ibara ndogo za (2), (3) na (4) za ibara hii, CAG hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali, lakini maelezo haya ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili kuchunguza kama CAG ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo.” Mwisho wa kunukuu. Kwa hiyo, kama usimamizi wake umewekwa kwenye Mahakama, kwa hiyo, inategemea malalamiko. Ni nani alalamike Mahakamani ili CAG aweze kusimamia ipasavyo katika utelezaji wa jukumu hili la control?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitarajia CAG atueleze kwamba katika mwaka wa fedha huu alioukagua, yeye katika jukumu lake la udhibiti, tarehe fulani alitoa approval Serikali itumie kiasi kadhaa; tarehe nyingine akatoa approval Serikali itumie kiasi kadhaa; na tarehe nyingine akatoa approval Serikali itumie kiasi kadhaa. Hilo ni jukumu lake ambalo ni not delegated, yaani haliwezi kuwa delegated kwa mtu mwingine yeyote isipokuwa tu ni CAG mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu taarifa hizi huwa hatoi, nilikuwa napendekeza, utakapofika wakati wa kurekebisha Katiba, tuzingatie kwamba lazima CAG apewe chombo ambacho kitamsimamia kwenye jukumu hili la control kama siyo Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la tatu ambalo ningependa kulizungumzia kwa mujibu wa taarifa yake, huyu CAG amejipambanua kutekeleza vizuri sana jukumu lake la pili ambalo ni ukaguzi. Kafanya ukaguzi vizuri na taarifa yake imeeleza kwa asilimia 100 kuhusu jukumu lake hila la ukaguzi wa mahesabu. Amekagua vizuri na taarifa ziko vizuri. Tatizo lipo kwenye hatua za kuchukua baada ya taarifa zake. Hatua za kuchukua zimekuwa ndogo ndogo sana na kuoneana aibu, labda na kuheshimiana, vitu kama hivyo. Ndiyo maana kila mwaka amekuwa analeta kwenye taarifa zake matatizo yale yale yanayofanana, kwa sababu hatua hazichukuliwi. Matatizo gani ambayo yamekuwa yanaonekana kila mwaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kutokupatikana kwa nyaraka za mapato na matumizi ili azikague kwa wakati; la pili, nyaraka kutokuwa halali; la tatu, kutokutekelezwa kwa mikataba kwa wakati na mapungufu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokutekelezwa kwa mikataba ni tatizo kuu la msingi katika utekelezaji wa miradi. Kwa sababu utekelezaji wa mikatana ili uwe mzuri, kuna mambo mawili; sheria ya ununuzi imeelekeza kwamba kila Afisa Masuuli kule ambako mradi unatekelezwa, anatakiwa ateue wataalamu wawili, watatu au zaidi kadri atakavyoona yeye inafaa, wa kusimamia mradi siku kwa siku. Kwa hiyo, kila idara ya Serikali, kila Wizara, kila halmashauri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako ulikuwa umekwisha.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona nimetumia kama dakika tano hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila taasisi inatakiwa itekeleze hili jukumu, lakini wamekuwa wanalifanya nusunusu na ndiyo maana kunakuwa na matatizo. Sehemu nyingine hata hao wasimamizi hawateuliwi na hatua hazichukuliwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu lingine ili mradi utekelezwe vizuri, lazima kuwe na maafisa mahususi kwa ajili ya ufuatiliaji na tathmini. Nao vile vile wamekuwa hawatekelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ambalo limeonekana, ni kutokutekelezwa kwa ushauri na mapendekezo ya CAG kwa wakati. Hilo nalo ni tatizo. Sheria imeweka muda maalumu kwamba taarifa ya CAG baada ya kutoka, anatakiwa Afisa Masuuli aandae program au mpango mkakati wa namna atakavyotekeleza mapendekezo ya CAG. Wamekuwa hawafanyi hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mapendekezo yamekuwa yakijitokeza miaka yote na maafisa wetu wa Serikali wala hawaogopi chochote kwa sababu hatua zimekuwa hazichukuliwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na ushauri katika maeneo kama mawili au matatu hivi. La kwanza, sheria zipo na zinajitosheleza na zinaweza kutumika kuwachukulia hatua watu ambao wanakosea, lakini zimekuwa hazitumiki. Hawa watu siyo kwamba hawazijui sheria, wanazijua. Wanajua sheria ya ununuzi, wanajua Sheria ya Matumizi ya Fedha za Umma, wanazijua vizuri, lakini makosa mengi yanafanyika kwa makusudi. Naomba sana hatua zile zinazoeleweka ziwe zinachukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Kamati za Oversight naomba ziongeze ukali wa mapendekezo yao, ikiwa ni pamoja na kulishauri Bunge kuhusu maazimio ya kuchukua. Nimemsikia Mheshimiwa aliyekuwa anatoa mapendekezo ya maazimio ya Bunge, yeye mwenyewe, lakini yeye mwenyewe ni Mjumbe wa Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafikiri kule kwenye kamati ndiyo wangeshauri Bunge kwamba Bunge kwamba tunaazimia, ili Bunge liazimie kuchukua hatua moja, mbili, tatu. Hiyo ingelisaidia Bunge kufanya maazimio ambayo yangeisaidia Serikali kuweza kurekebisha maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu naona muda umekwisha, naomba niishie hapo. Naomba sana tujipambanue katika utekelezaji wetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Mheshimiwa Ole Nasha, Waziri na Naibu Waziri kwa kazi yao nzuri sana wanayoendelea kuifanya katika sekta ya elimu na sisi katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunaendelea kuwategemea sana katika utendaji wetu wa kila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naipongeza Kamati wametoa maoni, ushauri mzuri sana. Kwa kweli nakiri kwa mwaka huu wametoa ushauri ambao utatusaidia sana katika utendaji wetu wa kila siku. Ushauri kuhusu namna bora ya kuendesha sekta ya elimu, kuboresha ushirikiano wa wadau mbalimbali ikiwemo namna ya bora ya kutoa huduma za elimu kwa watoto wenye ulemavu, nasema tumeupokea na tunaufanyia kazi na tumeupokea kikazi zaidi. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametoa maoni na ushauri na ushauri wao tumeupokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wetu wa utekelezaji wa kazi za kila siku katika Halmashauri na mjadala wa kitaifa, Halmashauri zote hutekeleza kazi zao kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 145 na 146 na sheria mbalimbali za Serikali za Mitaa. Uwezeshaji wao unasimamiwa na Sheria Na.19 ya Tawala za Mikoa. Kwa hivyo, usimamizi kwa ujumla katika Serikali za Mitaa ni wa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wote tunaofanya katika sekta ya elimu tunaongozwa na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. Kwa muktadha huo, maoni na ushauri kuhusu kuwa na mjadala mpana wa kitaifa kuhusu mfumo wa elimu, majukumu ya wadau, uwajibikaji, tunajua pale wilayani kuna Idara tatu zote zinasimamia elimu: Kuna Afisa Elimu wa Wilaya, Mdhibiti wa Ubora na kuna Katibu wa TSC. Wote hawa wanahusika na maendeleo ya elimu kwa majukumu mbalimbali katika wilaya. Vilevile kuna masuala ya kuhusu ngazi za vidato, haki za watoto wa kike na watoto wenye ulemavu.

Kwa hiyo, suala la kuwa na mjadala mpana wa kitaifa kuhusu masuala mbalimbali kama hayo, sisi katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI hatuna tatizo nao kabisa na tumeupokea. Wiki ijayo tutakutana katika ngazi ya Naibu Mawaziri na mwenzangu wa Wizara ya Elimu, tutazungumzia namna ya kuuandaa huo mjadala pengine labda baada Bunge hili la Bajeti likikamilika basi tunaweza tukauitisha kama ambavyo tumeshauriwa na Waheshimiwa Marais Wastaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ya walimu, namshukuru Naibu Waziri wa Fedha amegusia, walimu 15,000 tayari wameshalipwa. Hata hivyo, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba tumekamilisha uhakiki wa madeni ya walimu 126,893 ambapo madai yao sasa yamepungua hadi shilingi 61,515,587,938 na haya tumewasilisha Hazina kwa ajili ya hatua zaidi. Serikali imeshaahidi madai yote yatakayothibitika kuwa halali yatalipwa. Kwa hiyo, tunaomba walimu wote wawe na subira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhamisho wa walimu wa masomo ya sanaa kutoka sekondari kwenda shule za msingi, tumesikia maoni lakini tunapenda kusisitiza kwamba uhamisho huu uliwahusu walimu 21,165 wa masomo ya sanaa ambao walikuwa wamezidi idadi kwenye shule za sekondari kwa maana kwamba walikuwa na vipindi vichache sana. Kwa hiyo, ili kusudi waendelee kuwa katika ajira ya utumishi wa umma kama walimu hadi watakapostaafu tuliona kwamba ni matumizi sahihi ya rasilimali za Serikali kuwahamishia kwenye shule za msingi ili wakaendelee na kazi kwa mshahara ule ule na kwa daraja lile lile. Serikali inaamini kwamba ukiacha wale ambao hawana uzoefu na zana za kufundishia shule za msingi ambao watahitaji mafunzo maalum elekezi ya muda mfupi, wale waliojiendeleza na wakahamia sekondari kutoka shule za msingi hawahitaji sana mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nakiri kwamba zimekuwepo changamoto kadhaa katika utekelezaji wa zoezi hilo ikiwemo baadhi ya waliostahiki kupata kulipwa posho hawakulipwa na hili natoa agizo kwamba pale ambapo Wakurugenzi wamekosea wafanye marekebisho haraka sana. Vilevile kulikuwa na malalamiko ya kuhamishwa wale wenye degree na wakaachwa wale wenye diploma, isipokuwa kama mwalimu mwenye diploma yuko peke yake anafundisha somo hilo ina maana kumhamisha mwalimu yule watoto wale watakosa somo hilo hata kama ni Historia au kiingereza, mwalimu huyo mwenye diploma anayefundisha somo hilo peke yake itabidi abaki wataondoka walimu wengine. Kwa hiyo, suala hili linahitaji umakini sana katika kulifuatilia. Waliokosea tumeshawaagiza warekebishe na naomba walimu wote wenye malalamiko watuandikie kupitia Katibu Mkuu, TAMISEMI ili hatua zichukuliwe haraka na hiyo ni pamoja na wale waliosimamia mitihani hadi sasa posho hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makato ya asilimia mbiliya CWT. CWT iliundwa kwa mujibu wa sheria sawa na vyama vingine vya wafanyakazi. Kwa hiyo, masuala ya kwamba wamekatwa asilimia mbili wanatakiwa wayajadili kwenye vikao vyao vya kisheria ili kusudi wakubaliane kama wataendelea kukatana au namna gani kwa sababu hatuwezi kuwaingilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira za walimu, sasa hivi tunaandaa mchakato wa kuajiri walimu 16,130; kati ya hao 10,130 ni wa shule za misingi na 6,000 wa sayansi katika sekondari kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madaraja, zoezi ambalo lilikuwa limesimama limeanzishwa tena tangu Novemba, 2017. Kwa sasa upandishaji wa madaraja unaendelea nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule ya sekondari ya Lindi, napenda kuwaondoa wasiwasi Wabunge wote kutoka Mkoa wa Lindi. Shule ile itajengwa na itakamilika mwaka 2018/2019 na wiki kesho itakuwa ni agenda mojawapo katika kikao chetu cha Naibu Mawaziri wanaoshughulikia elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ambayo ni ya ujumla makubwa napenda kuunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naomba nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuleta Muswada huu Bungeni na ninaamini Bunge lako Tukufu litaupitisha Muswada huu baada ya marekebisho machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya marekebisho ya mwisho ninaomba wataalamu wake warejee kupitia Taarifa ya Helena ya mwaka 1997/1998 ambayo ndiyo ilikuwa msingi wa Local Government Reform Programme. Vilevile warejee taarifa maarufu inaitwa ROSC au Report on Standard and Codes ambayo ilitolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) mwaka 1999 ambayo imekuwa msingi wa mabadiliko makubwa sana kifedha katika nchi yetu.
Vilevile warejee taarifa ya Benki ya Maendeleo ya Dunia (World Development Report) ya mwaka 2004 kuhusu kupeleka rasilimali kwa wananchi maskini. Taarifa hizo tatu zitawasaidia sana kuboresha baadhi ya vifungu kwenye huu Muswada, kama ambavyo na mimi nitavipitia vichache kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa muhimu sana ni zile zinazohusu maendeleo ya wananchi. Taarifa ya ROSC ilifanyiwa kazi na Serikali vizuri sana kuanzia mwaka 2001 mpaka mwaka 2007. Wizara ya Fedha kila ilipokuwa inatoa fedha kupeleka kwenye Halmashauri, ilikuwa inatoa matangazo katika magazeti kuonesha kila Halmashauri imepata kiasi gani kwa ajili ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za hivi karibuni utoaji wa taarifa kama huo umeminywa, umekuwa hauonekani kwenye vyombo vya habari kiasi hata Wabunge wamekuwa wanapata shida kufuatilia kupata taarifa ni fedha kiasi gani zimekwenda kwenye Halmashauri. Maelekezo yaliyokuwepo wakati ule, fedha zikifika kwenye Halmashauri taarifa ile inabandikwa kwenye mbao za matangazo za Halmashauri na zinabandikwa kwenye maeneo yenye watu wengi kama sokoni zinabandikwa. Tumepata fedha kwa ajili ya mradi huu kiasi kadhaa, inaonesha transparency ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri yenyewe inapopanga matumizi ya fedha zile kwenda kwenye kata na vijiji, vijiji na Kata nazo zinabandika taarifa zile kwenye shule za msingi na kwenye maeneo ambayo watu wanapita. Hiyo inaonesha uboreshaji wa hali ya juu wa upatikanaji wa taarifa za maendeleo kwa wananchi ili waweze kufuatilia maendeleo yao mahali ambapo wanaishi.
Kwa hiyo, ninaomba sana vipengele vitafutwe kwa sababu sheria hii imechelewa sana. Kwa maoni yangu ilitakiwa itoke mwaka 2001, sasa kwa sababu tuko mwaka 2016 ndiyo inatoka sheria hii basi naomba vipengele vile vya kutoa taarifa kwa wananchi viwekwe mahususi ili kusudi kuwalazimisha Mamlaka za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kutoa taarifa za maendeleo kama hizo kwa wananchi bila kizuizi chochote ili kuongeza transparent.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nizungumzie kuhusu sheria hii. Sheria hii haijagusa zile taarifa ambazo hasa hasa zinahusu moja kwa moja wananchi. Kwa mfano, taarifa za masoko, taarifa za wanunuzi wa mazao, taarifa za bei za mazao kabla mkulima hajaamua kuwekeza katika kilimo anatakiwa apate hizo taarifa, vipengele hivi ninaomba sana viwekwe. Vifungu vyote vilivyomo humu ni vya jumla tu vinahusu hasa Serikali Kuu lakini kule kwenye Serikali za Mitaa na hasa mambo yanayousu maendeleo ya wananchi bado hatujavigusa sana kwenye vifungu karibu vyote vya Muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo napenda kulizungumzia ni suala la kutunza taarifa kwa kipindi miaka 30. Katika baadhi ya taarifa, inawezekana muda huo ukawa hautoshi katika baadhi ya taarifa na katika baadhi ya taarifa unaweza ukawa unatosha. Nitatoa mfano, Afrika Kusini kwa kutumia sheria yao wametunza mahojiano ya kimahakama ambayo Mheshimiwa Nelson Mandela alishtakiwa na Serikali ya makaburu miaka ya 1960. Wameyatunza yale mahojiano kwenye vyombo ambavyo Mwafrika Kusini yeyote anayetaka kusikiliza mahojiano yale anaruhusiwa kwenda kusikiliza mahojiano yale na akajifunza na ikajenga uzalendo wa nchi ya Afrika Kusini.
Kwa hiyo, hata sisi kwa mfano kesi maarufu ambayo Mwalimu Nyerere alishtakiwa na wakoloni na akalipishwa faini, Mtanzania kwa sasa hivi akitaka taarifa hiyo aisikilize kwa kusikia kwa maneno maana yake najua ilirekodiwa wakati ule kwenye tape za wakati ule. Sasa imetunzwa wapi taarifa hii? Mtu au kikundi cha watu kikitaka kuisikiliza hiyo kesi kitaipata wapi? Ni tatizo! Najua kule Jeshini taarifa hizo zipo lakini inatakiwa iwekwe kwenye utaratibu huu.
Kwa hiyo, kumbukumbu kama hiyo kutunzwa kwa miaka 30 inaweza ikawa haitoshi, inawezekana tukaihitaji hata kwa miaka 100 ili iwepo vizazi na vizazi viweze kuitambua, kwa hiyo hiki kipengele cha miaka 30 ni lazima kuzingatia classification ya taarifa. Inawezekana taarifa zingine zikahitaji kipindi kirefu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusoma kwangu Muswada, sijakuta sehemu inaonesha uhusiano wa Muswada huu na kazi za Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu za Serikali pale Idara Kuu ya Utumishi. Ni vyema ikaainishwa wazi pamoja na kwamba tunataja kwa ujumla, lakini kwenye sheria ile iliyoweka utaratibu wa kazi za Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu za Serikali pale Idara Kuu ya Utumishi, ni vema kuainisha vizuri majukumu ili kusudi najua kwenye kifungu cha sita utaratibu umewekwa vizuri kuhusu taarifa ambazo ni classified, lakini ni vizuri kuweka utaratibu mzuri wa kimahusiano ili isije ikatokea mgongano kati ya idara moja na idara nyingine ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele kingine ambacho ninapenda kuzungumza, tumekuwa na clients service charter karibu katika kila idara ya Serikali ambazo hizo ilikuwa ni attempt ya Serikali kuji-commit kwa wananchi kama wateja namna ambavyo watawahudumia. Wakati ule inaanzishwa hii mikataba ya huduma kwa mteja kwenye kila idara ya Serikali na katika kila Halmashauri, wakati ule ilikuwa ni wazo tu la Utumishi kuhusu transparency. Namkumbuka Mheshimiwa Mary Nagu alikuwa anaongoza sana harakati hizo. Sasa kwa sababu sheria hii ndiyo inakuja, ninaomba kiwepo kipengele kinacholazimisha hii mikataba ya huduma kwa mteja ipitiwe upya ili kusudi kifungu hicho kiwalazimishe kila idara kuwahudumia vizuri wateja wao na hasa wananchi. Hayo ndiyo mambo ya msingi zaidi ambayo nimeona mimi yamesahaulika kwenye muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mawili ya mwisho ninayotaka nizungumzie ni kifungu cha 10. Kifungu cha 10 kinalazimisha kwamba taarifa lazima iombwe kwa maandishi; kidogo hapo tutakuwa tunaondoa uhuru wa muombaji wa taarifa.
Ninaomba taarifa inaweza ikaombwa kwa maandishi au ikaombwa kwa mdomo. Ninaposema haya najua kwamba kwenye kifungu cha 10(4) kuna maelezo yamewekwa pale kwamba kama mtu hajui kusoma na kuandika anaweza akaomba kwa mdomo halafu yule mwenye taarifa ndiyo akaweka maombi yale kwa maandishi halafu yule akaweka dole gumba. Lakini hiyo ni kulazimisha tu maandishi yawepo. Ninachosisitiza mimi ni kwamba tuweke uhuru kwa mwananchi, anaweza akaomba taarifa kwa maandishi au kwa mdomo. Hiyo kidogo itapunguza na kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi na hiyo itaongeza transparency ambayo kila mtu angependa aione transparency ina-prevail. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kwenye kifungu cha 11(1) hadi (3), vinaweka msisitizo wa siku 30 wa ombi kufikiriwa. Ninaomba taarifa hizi nyingi ziwe kwenye Wizara, ziwe kwenye Idara za Serikali, ziwe kwenye Mikoa, ziwe kwenye Halmashauri, ziko ndani ya taasisi. Kwa hiyo, zinaweza zikatafutwa na kutolewa ndani ya saa 24, kwa nini siku 30?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi siku 30 ni nyingi sana, kifungu hicho chote kifanyiwe marekebisho ili kupunguza muda wa kupewa taarifa, iwe aidha ndani ya saa 24 au ndani ya saa 48 ili kusudi kweli tuoneshe kwamba tuko serious kama nchi kuweka transparency katika jamii yetu ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa, kifungu kidogo cha sita na vifungu vingine vinavyozungumzia adhabu. Adhabu zilizomo ni kubwa mno! Hazitoi nafasi kwa wakosaji kupata adhabu na hapo hapo kujirekebisha ili warejee kuwa productive katika jamii. Kifungo cha miaka kumi gerezani, miaka 15 kwa kosa tu la kutotoa taarifa au kwa kosa la kuitumia vibaya taarifa, nadhani hizo adhabu ni kubwa sana zifikiriwe na kupunguzwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naipongeza Serikali kwa kufanya yote haya ni kutoa kwenye jamii ikiwemo Vyombo vya Habari na siyo kuzuia taarifa. Nashukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Ummy kwa kazi hii nzuri na Naibu wake Dkt. Kigwangalla, na naipongeza Serikali kwa ujumla kwa kuleta miswada hii miwili katika muda huu muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu ya kwanza kabisa ninaona kama vile hii tafsiri ya Kiswahili iliyo kwenye huu muswada inavyoonekana pengine ilifanywa haraka haraka. Ninaomba wataalam kabla hawajatoa nakala zingine huko baada ya kuwa tumepitisha, waiangalie hii tafsiri ya Kiwasahili kwa umakini zaidi. Kwa mfano, katika kifungu cha 4 hii tafsiri ya Kiswahili inaitaja mamlaka kama kampuni. Kwa hiyo, naomba sana wafanye mapitio ya kina kwenye tafisiri ili kusudi ilingane na zile maana iliyoko kwenye Kiingereza kule maana imekaa vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kifungu cha 3 chote sikuona tafsiri ya neno Waziri, iko tafsiri ya neno Wizara. Lakini iko tofauti kubwa kati ya neno Wizara na neno Waziri, kwa hiyo ninaomba sana Mheshimiwa Waziri azingatie kwamba wananchi watahitaji tafsiri ya nani Waziri katika sheria hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumza, katika kifungu cha 5(2) ziko (a) mpaka (i). Katika vipengele hivyo kipengele cha 5(b) kinasema; “Itasimamia Maabaraa za Kemia, Sayansi Jinai na Vinasaba ili kuhakikisha kuwa zinakidhi viwango vilivyowekwa.”
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kama kutakuwa na maabara yoyote ambayo imeachwa hapa itajwe, kuweka jumla jumla inaweza isieleweke. Kwa hiyo, ninaomba sana maabara zote za kisekta ambazo zitahusika kusajiliwa na hii Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, zitajwe kwa ufasaha katika kipengele hiki kifungu cha 5 vinginevyo inaweza ikaleta mkanganyiko baadaye. Kwahiyo kwenye ukurasa wa 44 pale kwenye tafsiri yangu ya Kiswashili ninaomba Mheshimiwa Waziri akubaliane na mimi kuhusu kutaja kwa ufasaha ni maabara zipi zitatakiwa kusajiliwa na kusimamiwa na Mamlaka hii ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwasababu ndani ya Muswada huu wote mzima haujataja maji. Mimi ningependa kuliuliza Bunge lako Tukufu, tangu asubuhi tulivyoamka leo ni nani hajashika maji humu ndani? Either kwa kuoga au kwa kufua au kwa kupikia au kwa kunywa, ni nani? Na maji yanaweza yakawa ni sumu mbaya sana katika afya ya binadamu, lakini muswada mzima huu hujataja maji. Ni ajabu ambayo nimeona mimi, hivyo ninaomba sana mapitio ya kina yafanywe ili kusudi maji ambayo hutibiwa na kemikali yatajwe humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu maoni yangu mengine yapo kwenye kifungu cha 6. Katika kifungu cha 6 imetajwa pale, mamlaka baada ya kushauriana na Waziri wa Fedha na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wataunda baadhi ya vitengo na kanda na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa naona kuna upungufu pale, kwamba mamlaka ikishashauriana na Waziri wa Fedha na Waziri wa Utumishi basi, wanaenda kutekeleza bila consultation au bila kupata approval ya Waziri. Mimi nadhani hapo kuna upungufu kidogo kwa hiyo nilikuwa napendekeza kwamba kibali cha Waziri mwenye dhamana ni muhimu sana kipatikane kabla hawajaenda kutekeleza yale ambayo wame-consult na Waziri wa Fedha na Waziri wa Utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kifungu 7(2) pale kuna Wajumbe wa Bodi na wameorodheshwa. Mimi pale nilikwa nina maoni sawasawa na maoni ya baadhi ya Wabunge ambayo wameyatoa humu ndani. Kuna mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi mwenye cheo cha ngazi ya Mkaguzi au zaidi, kuna mwakilishi kutoka Idara ya Utumishi wa Umma na kuna mwakilishi kutoka Wizara ya Fedha. Mimi nilikuwa nina mapendekezo tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka hii ambayo inaundwa ni mamlaka muhimu sana katika nchi hii. Katika mchango wangu wa awali ambao nimezungumza kuhusu maji, sekta ya maji mpaka sasa hivi ina maabara 16 hapa nchini ambazo ziko kwenye kanda mbalimbali. Pamoja na Makao Makuu ya Wizara ya Maji kuna maabara kubwa ya maji pale. Sasa maabara zote hizi zinafanya kazi kubwa sana kufuatilia na kushauri wadau wote kuhusu ubora wa maji hapa nchini, na majukumu ya kuchukua sampuli na kuzipima, kupima kibaiolojoia, kifizikia na mambo mengine yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa napendekeza, Jeshi la Polisi lipo na Wakaguzi wa Polisi wapo, tutawatumia tunapotaka; lakini japo nilikuwa naomba badala ya mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi awekwe mwakilishi kutoka Wizara ya Maji. Na pale kwenye uwakilishi kutoka Idara Kuu ya Utumishi nilikuwa naomba awekwe mwakilishi kutoka TBS. TBS ndiyo inahusika na viwango vya kila kitu tunachokitumia sisi kama binadamu hapa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri akubaliane na mimi kwamba mwakilishi kutoka TBS achukue ile nafasi ya mwakilishi kutoka Utumishi. Halafu wa tatu mwakilishi kutoka Wizara ya Fedha naye aondolewe, nafasi yake ichukuliwe na mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na nitazungumza, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ndiyo Wizara yenye dhamana ya maabara ya veterinary (maabara ya mifugo) na maabara za samaki. Tumeathirika sana sisi kama nchi kwa kusafirisha minofu ya samaki wabichi nje na kusafirisha nyama nje; tumeathiriwa sana na viwango, wanaita phytosanitary and sanitary standards. Hivi viwango vinadhibitiwa na kupimwa katika maabara.
Sasa ili kusudi tupate maendeleo katika Sekta hii, na kwa sababu hizo maabara zitasajiliwa na hii mamlaka ambayo tunaianzisha, ninaomba sana mwakilishi hasa hasa anayehusika na maabara hizi za veterinary na maabara za samaki awemo kwenye hiyo bodi ili kusudi kusaidia. Maana hii Bodi ni ya wataalam, wataalam wa maabara wakikaa, wakizungumza, wakielewana itakuwa vizuri sana kupeleka maendeleo mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hii ni pamoja na maabara za udongo ambazo zipo kwa ajili ya kubaini viwango vinavyohitajika vya ujenzi wa majengo, barabara, madaraja na miundombinu mingine na kubaini aina za mbolea ambazo zinahitajika katika maeneo mbalimbali nchini. Hayo ni miongoni mwa maeneo muhimu sana ya kuzingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ni katika eneo lingine la kifungu cha 8 ambacho kinahusu majukumu na mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, hasa vipengele (a), (b), (e), (f), (l) na (m). Vipengele hivyo ndiyo vinathibitisha uwakilishi unaohitajika wa kisekta kwenye hii mamlaka ambayo tunaianzisha. Vipengele hivyo sita ambavyo nimevitaja vinathibitisha kuhitajika kwa mwakilishi wa maji, kuhitajika kwa mwakilishi wa TBS na kuhitajika kwa mwakilishi kutoka Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nianze kumalizia mchango wangu kwa kuweka angalizo la jumla. Mimi nilipata bahati ya kutembelea maabara moja ya maji ambayo iko Ethiopia, na vile vile nimetembelea maabara ya maji ambayo iko Misri. Kabla hujaingia kwenye maabara unasafishwa viatu kwanza, unavalishwa vitu, wewe mwenyewe unajisikia kwamba unaingia kwenye maabara, ina viwango. Sasa tungetegemea maabara zetu ambazo baadaye zitakuwa accredited kimataifa nazo ziwe na viwango bora.
Kwa hiyo, naomba niweke angalizo kwamba humu kwenye sheria tumuwekee vipengele kumuongoza Mkemia Mkuu wa Serikali atakapokuwa anadhibiti maabara adhibiti na vigezo vya kuhakikisha kwamba maaba zetu nazo zinakuwa na viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sheria ya wataalam wa kemia. Sheria hiyo inawaweka wataalam wote wa kemia hasa watakaokuwa kwenye maabara chini ya Wizara ya Afya kama Wizara mama. Mimi naomba maeneo yote kuhusu ajira na usajili wa wataalam hao uwekwe utaratibu wa mawasiliano na Wizara na Taasisi nyingine za kisekta ili kuhakikisha kuwa wataalam watakaoajiriwa na kusajiliwa ni wale wanaokubalika kwenye sekta husika kwa viwango vinavyokubalika kwenye sekta hizo. Kwa sababu mazingira yanaweza kuwa tofauti na mazingira ya Wizara ya Afya, sasa akijifungia kule halafu wakaajiri wataalam wanaohitajika kwenye maabara ya sekta ya maji, wataalam wanaohitajika kwenye veterinary au wataalam wanaohitajika kwenye maabara ya samaki inawezekana ikawa tofauti na wale ambao kweli wanahitajika kwenye sekta hiyo hiyo halafu ikazua migogoro isiyo na sababu. Kwa hiyo viwepo vipengele vinavyoonesha mawasiliano yatakuwaje, na hilo ndilo la muhimu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mchango wangu ulikuwa ni huo. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makuzi yangu nimefundishwa lugha ya staha, uvumilivu na heshima kwa wakubwa na wadogo. Namwomba Mungu azidi kunidumisha katika hulka njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hatua hii nazipongeza sana Kamati zote, ikiwemo Kamati yetu ya Biashara na Mazingira, kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Wametoa maoni na ushauri mzuri na sasa sisi Serikali kazi yetu kubwa ni kuyachukua maoni na ushauri na kuufanyia kazi kwa manufaa ya Watanzania ambao wametutuma wote tuje kwenye Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojadili hoja humu Bungeni ni muhimu sana tukazingatia mambo muhimu ya msingi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Julai, 2017 Bunge hili lilipitisha sheria mbili kubwa, Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusu Umilikiwa Maliasili ya Mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio ya Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi Kwenye Mikataba Inayohusu Maliasili za Nchi ya Mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kipindi hicho hicho Bunge liliifanyia marekebisho makubwa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Lengo la hatua hizo lilikuwa ni kurejesha umiliki na udhibiti wa rasilimali zetu za Taifa kwa faida ya Watanzania walio wengi. Huo ndio msingi tulioutumia kufanya maamuzi ya kuifanyia mapitio ya kina baadhi ya mikataba, ikiwemo Mkataba wa Mradi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka na Mkataba wa Mradi wa Mchuchuma na Liganga na miradi mingine ya aina hiyo. Tutakapokamilisha mapitio hayo tutatoa taarifa kwa Watanzania kupitia Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ufafanuzi kuhusu eneo la biashara. Tunao mfumo uliopitishwa na Serikali wa kujenga mazingira rafiki ya kufanya biashara na katika maeneo kadhaa tumeanza kufanya utekelezaji hususani kwa mfano kwenye eneo la ushirikiano kati TFDA na TBS, hii ni mifano michache. Tunakamilisha mpango kazi utakaoanza rasmi utekelezaji wake 2019/2020 na kwa kufanya hivyo, tutapunguza sana gharama za ufanyaji wa biashara katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa Mheshimiwa S. H. Amon wa kukutana na wafanyabiashara au waagizaji wa bidhaa kutoka nje, tumeuchukua na tutaufanyia kazi mimi na Mheshimiwa Mpango, Waziri wa Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilipozungumzwa kuhusu uhasi wa balance of payments, nilisikitika kwa sababu ilihitajika sana uchambuzi wa kina. Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwezi Julai, 2018 imeonesha Tanzania imeuza zaidi katika soko la SADC na mauzo yameongezeka kutoka dollar milioni 397 mwaka 2017 hadi dollar 413 milioni ambayo ni ongezeko la asilimia 12; na wakati huohuo tumepunguza uagizaji kutoka SADC kwa asilimia 12. Maana yake ni kwamba tumepata mafanikio chanya kwenye soko la SADC. Sasa hizi hatua bado tunaziongeza kwenye masoko mengine. Dalili hiyo inaonesha kwamba Viwanda vya Tanzania vimeanza kufanya vizuri zaidi ukilinganisha na viwanda vya nchi nyingine hasa katika bidhaa kama unga wa ngano, sabuni, saruji, mabati na bidhaa nyingine.

Mheshimiwa Menyekiti, aidha, hatua ambazo Serikali inaendelea kuzichukua hususani katika ujenzi wa reli, barabara za lami za kitaifa na mikoa, viwanja vya ndege, bandari, umeme, mawasiliano ya simu, maji, huduma za afya, elimu hususani wahitimu wenye ujuzi mbalimbali (skills) ambao watakuwa na michango mikubwa kwenye viwanda, ni hatua ambazo zitaboresha sana mwelekeo wetu kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, kuhusu kuimarisha utendaji wa mashirika yetu kama SIDO, NDC, TEMDO, CAMARTEC, TIRDO, EPZA, TAN-TRADE, TBS na hata Wizara yetu ya Viwanda na Biashara, tutaufanyia kazi ushauri mzuri ambao Bunge limeutoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda, tunahamasisha viwanda na hata Waheshimiwa Wabunge tunawahamasisha wamiliki viwanda. Tumeweke vipaumbele vitatu muhimu; kipaumbele cha kwanza, ni viwanda vya kusindika au kuchakata mazao ya kilimo na mifugo; sekta ambazo zinategemewa na asilimia zaidi ya 75 ya Watanzania. Kipaumbele cha pili, ni viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumika zaidi majumbani na kwenye sekta ya ujenzi ili kulihudumia vizuri zaidi soko la ndani; na kipaumbele cha tatu, ni viwanda vinavyoajiri watu wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana tushirikiane kwa pamoja, sisi wote ni Watanzania, tukianza kutoleana maneno machafu hatutasonga mbele. Tushirikiane kama Watanzania kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania ili Taifa letu liweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo kuhusu viwanda vilivyobinafsishwa. Kati ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa, viwanda 88 vinafanya kazi, sawa na asilimia 56, viwanda 68 havifanyi kazi. Kati ya viwanda 88 vinavyofanya kazi viwanda 64 vinafanya kazi vizuri, tena kwa faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuonesha kwamba vinafanya kazi kwa faida kuanzia mwaka 2013 mpaka 2018 viwanda hivi hadi Oktoba, 2018 vimelipa kodi zaidi ya shilingi trilioni 4.6 TRA wanayo takwimu. Kati ya viwanda 64 visivyofanya kazi viwanda 20 vimefutwa kwenye orodha baada ya kubainika kwamba viliuzwa kwa rejareja; yaani viliuzwa mali mojamoja na vingine vimekosa sifa ya kuendelea kuitwa viwanda. Viwanda 14 tumeshavirejesha Serikalini baada ya wenye viwanda kutoonesha business plan ya kuvifufua na kuviendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tumevichukua Serikalini ili tuvitafutie wawekezaji wengine ambao watakuwa na nia ya kuwekeza mtaji ambao utavifufua viwanda hivyo na kuendelea na uzalishaji. Viwanda 34 vinafuatiliwa kwa karibu utendaji wake kwa mujibu wa ahadi zao za kufufua uzalishaji ambazo wametuahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu General Tyre; Serikali ilikamilisha tathmini ya kiwanda iliyoshauri kiwanda hicho cha General Tyre kifufuliwe kwa ubia na sekta binafsi kwa uwekezaji wa mitambo ya kisasa. Government Notice ya tarehe 11 Mei, 2018 ilikabidhiwa NDC na kiwanda rasmi kilikabidhiwa NDC tarehe 20 Disemba, 2018. Baada ya tathmini ya kina ya mali zote na madeni ambayo inaendelea NDC sasa itachukua hatua ya mwisho ambayo ni kualika makampuni yatakayokuwa tayari kwa ubia ili yalete maombi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Bunge lako Tukufu tuwe na subira wakati hatua muafaka hizi zinachukuliwa na hakuna haja ya kutoleana maneno ambayo yatafukuza hata wale ambao pengine wangeweza kuwa prospective kwenye uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mwelekeo mzuri kwa sekta zote. Sekta ya viwanda haiwezi kuendelea bila kuwa na uwekezaji kwenye sekta nyingine, huwezi kujenga viwanda bila kuwekeza kwenye sekta ya miundombinu. Hakuna eneo lolote la uwekezaji ambalo linaweza likavutia wawekezaji kama hakuna barabara inayofika kule, hakuna reli inayofika kule, hakuna umeme, hakuna maji, kwa hiyo hivi vitu vinategemeana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuwa na viwanda vya Agro processing kama kilimo hakifanyi kazi vizuri; na ndiyo maana katika mkakati maalum wa maendeleo ya viwanda katika nchi hii tumesema lazima uwe na mkakati wa pamba hadi nguo; yaani C to C (Cotton to Cloth). Ili uweze kufikia malengo mahususi ya kutumia malighafi ya pamba vizuri zaidi ndani ya nchi lazima uwe na viwanda ambavyo vitatengeneza nguo kutokana na pamba inayozalishwa ndani ya nchi. Lazima kama unataka kuwa na viwanda vya mafuta;

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Namalizia Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima uwe na uzalishaji mzuri wa alizeti ili uweze kukamua mafuta ya alizeti vizuri. Kwa hayo ndiyo mambo ambayo tunayafanya na mwelekeo ni mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kamati. Ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kabla sijachangia naomba niwashukuru sana wananchi wa Sikonge kwa kuniamini kuwa Mbunge wao kwa mara ya kwanza. Naomba niwatoe wasi wasi, wasiwe na wasiwasi wowote hapa kazi tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaingia katika hotuba, naomba nieleze kwamba nikiwa Mbunge nilifadhaika sana siku Mheshimiwa Rais alipotoa hotuba yake. Wakati Mheshimiwa Rais anaingia humu ndani, zilizuka fujo ambazo zilinifanya ninyong‟onyee kwa muda, nikishangaa
kwa sababu sikutegemea hadi wenzetu wakatoka wakisusia, hawakutaka kumsikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini leo...
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Leo nimefarijika kuona badala ya kumsikiliza siku ile Mheshimiwa Rais, leo wenzetu wamesoma vizuri hotuba yake na wakisimama wanamsifu bila vurugu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ustaarabu huu uliooneshwa leo Watanzania wanauona na sisi Wabunge wote kwa ujumla naomba tuuzingatie ustaarabu huu siku zote, ili kama kuna hoja ijibiwe kwa hoja badala ya vurugu ambazo zinatufanya sisi wote tupoteze heshima yetu nje ya
Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nije kwenye hotuba. Kiwango cha commitment kilichooneshwa na Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ni cha hali ya juu sana. Ni kiongozi ambaye yuko tayari kwa kauli na vitendo kupambana na vikwazo vyote ambavyo kwa muda mrefu vimekua vikimsababishia Mtanzania kero nyingi katika juhudi za kujikwamua kutoka kwenye umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matumaini ya sasa ya Watanzania ikiwemo Wanasikonge ni makubwa mno, kwamba, baada ya miaka 10 ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli akiwa Rais uwezekano wa kufikia malengo ya Dira ya Maen deleo ya Taifa ifikapo mwaka 2025 si wa kutilia
shaka tena, kinachotakiwa kila mtu kutimiza wajibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Rais ya tarehe 20/11/2015 na utendaji wake wa Rais na Serikali yake hadi sasa, umeongeza matarajio ya wananchi kuhusu kufanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kudhibiti
matumizi, kuimarisha uadilifu, uaminifu na uzalendo na vyote hivi vinaashiria matokeo makubwa katika kupunguza umaskini. Ili tufanikiwe katika yote hayo, yale majipu ambayo Mheshimiwa Rais aliyaahidi kuyatumbua, majipu makubwa, majipu madogo na hata vijipu uchungu, vyote lazima vitumbuliwe bila kuona huruma. Mheshimiwa Rais ameahidi na tayari utekelezaji unaendelea, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Sikonge walifurahishwa sana na hotuba ya Rais na wamekaa mkao wa hapa kazi tu, wanatimiza majukumu yao hususani katika sekta ya kilimo kwa kulima sana mashamba ya tumbaku na mazao ya chakula, kutengeneza mizinga kwa ajili
ya asali na nta na kutumia fursa nyingine zozote zilizopo kupambana na umaskini.
Wanakumbuka ahadi nzuri zinazojenga matumaini za Mheshimiwa Rais kwamba Serikali itawaboreshea zaidi mazingira ya kufaidika na jasho lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo ningependa kukumbusha kwa sababu yako katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, la kwanza, linalohusu eneo langu, kuondoa kero kwenye zao la tumbaku kwa kumwezesha mkulima apate pembejeo kwa urahisi na kwa muda muafaka
na kwa bei nafuu kwa kutumia mfumo rahisi ambapo mkulima kupitia Chama chake cha Msingi, akae kitako na mnunuzi ili waingie mktaba wa mnunuzi kukopeshwa pembejeo au pembejeo zitolewe kwa mkulima wakati wa msimu wa malipo kabla kilimo hakijaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mfumo wa malipo uboreshwe kuondoa malipo kuchelewa kwa zaidi ya miezi mitatu na Serikali imlinde mkulima asiibiwe wakati wa kubadilisha viwango vya fedha kutoka kwenye dola ya Kimarekani kwenda kwenye shilingi ya Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo kuna mambo mengi sana ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi. Watu wa Ushirika wanahitaji kuwasaidia wakulima katika maeneo mengi, COASCO ambao ni auditors wa ushirika ni tatizo kubwa, wamekuwa siyo wa kweli, ni bora tu
kuwaondoa ili mfumo wa ukaguzi ubaki chini ya ukaguzi wa ndani wa Halmashauri na CAG, hili litatusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mengi mno kwenye kilimo yatazungumzwa na wengine, naomba wakulima waonewe huruma, wasaidiwe na Serikali pamoja na wadau kuondokana na adha wanazozipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni kuboresha uhusiano kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi, kwa mfano, mfugaji wa nyuki ni rafiki mkubwa sana wa misitu kwa sababu yeye anategemea kuweka mizinga yake kwenye misitu, kwa nini mfuga nyuki aonekane adui kwenye hifadhi eti tu kwa sababu tu anatumia mzinga wa gome la mti! Kwa nini Serikali isitoe elimu na huu ni ushauri kwa wafuga nyuki, ili watumie mizinga ya kisasa itakayofanya hatimaye wawe na uhuru wa kuingia hifadhini kwa sababu watakuwa
wamesajiliwa, hata wavuvi wadogo wadogo nao wanahitaji kusaidiwa kwa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kuzungumzia kama kukumbusha kwa sababu liko kwenye hotuba, ni miundombinu. Barabara za lami na sisi tunahitaji kuunganishwa na Mikoa mingine kama Tabora - Katavi, Tabora – Mbeya - Singida, Tabora – Kigoma, kuboresha reli ya kati, miradi ya umeme vijijini na mitandao ya simu. Wilaya yangu ya Sikonge karibu 70% ya maeneo ya makazi hayajaunganishwa na mitandao ya simu. Ni muhimu sana kwenye awamu hii suala la mtandao lishughulikiwe kwa jicho kamilifu. Naomba maeneo yote yaliyo nyuma kwa miundombinu yapewe kipaumbele na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Serikali iendelee kuwekeza kwenye elimu. Katika Wilaya yangu kuna maeneo 49 ambayo yanahitaji shule mpya kabisa za msingi. Katika maeneo 19 wananchi wamejenga madarasa, Halmashauri haina fedha za kukamilisha, kwa hiyo, Serikali
Kuu bado tunaomba iendelee kuwekeza kwenye elimu ya msingi, siyo kwamba MMEM ilikwisha, basi hakuna uwekezaji mpya unao endelea, tunaomba tuendelee kuwekeza kwenye elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye afya tuna upungufu mkubwa sana wa zahanati, watumishi na dawa, vyote viendelee kuwa katika mipango ya Serikali. Kwenye maji tuna matumaini makubwa na mradi wa Ziwa Victoria, tunaomba ukamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naomba nimalizie kwa kusisitiza kuhusu barabara ya lami kutoka Tabora-Ipole-Mpanda. Tunaomba fidia ilipwe mapema, barabara ijengwe mapema kuondoa adha wanayoipata wananchi amabo ni watumiaji wa barabara hiyo.
Design yake ifanyiwe mapitio ili tuta la barabara ya lami liwe juu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kakunda muda wako umekwisha.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia, yaongezwe madaraja na makalvati…
NAIBU SPIKA: Naomba ukae tafadhali…
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: ...ili barabara itakayojengwa iwe ya kudumu. Naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nichukue nafasi hii kabla sijaanza kuchangia kumsifu sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuratibu kazi hii ya kuandaa Mpango wa Miaka Mitano na hatimaye ameuwasilisha leo mbele ya Bunge hili.
Natoa shukrani nyingi kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi ambazo imefanya mpaka sasa hivi. Ni kazi nyingi na nyingi zinaonekana kwa macho sio lazima kuambiwa.
Kwa hiyo, napongeza sana kazi ambazo zimefanyika mpaka sasa hivi. Kuanzia Awamu ya Kwanza, ya Pili, ya Tatu na sasa hii Awamu ya Tano ya hapa kazi tu naamini inajenga matumaini makubwa kwamba tuendako sasa kutakuwa na mafanikio na maendeleo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili viwanda vijengwe, viendeshwe kwa mafanikio na vistawi nchini, vinahitaji sana miundombinu ya barabara kuu za lami, za Mikoa, za Wilaya, za Kata hadi kwenye Kijiji ili malighafi iweze kufikishwa kiwandani au viwandani unahitaji miundombinu hiyo iweze kupitika muda wote wa mwaka. Kwa hiyo, kwenye Mpango nimesoma, nimeona kuna mipango mingi imepangwa mle, nachohitaji ni kuhakikisha kunakuwa na usimamizi madhubuti ili tuweze kufanikiwa. Kama usimamizi utalegalega itakuwa ni taabu, bidhaa haziwezi kufika sokoni vizuri na bei inaweza ikawa kubwa kama miundombinu hai-support bidhaa kufika sokoni kwa urahisi. (Makofi)
Nataka nikumbushe tu eneo moja ambalo liko kwenye Mpango ambalo linahitaji macho mengi kuangalia na kujua. Kati ya Chunya hadi Mkiwa, wapo takribani watu 1,500,000 ambao wanafanya shughuli nyingi sana za kiuchumi katika maeneo hayo. Ile barabara iliamuliwa tangu mwaka 2005 kwamba ijengwe kwa kiwango cha lami. Imechelewa na mimi nahitaji umadhubuti mkubwa katika kusimamia na kukumbuka. Nilikuwa nataka nipaze sauti kali ili Mheshimiwa Profesa Mbarawa huko aliko asikie lakini kwa sababu atakuja kusoma kwenye Hansard basi siwezi kupiga kelele hapa. Naomba sana hiyo barabara ikumbukwe kwa sababu kuna kazi nyingi sana za kilimo na maliasili nyingi sana katika maeneo hayo ambazo zikivunwa na zikafikishwa viwandani zinaweza kusaidia sana uchumi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa njia yoyote ile wataalam wa barabara wanatumia aina mbili za models kwa ajili ya kuamua barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami au isijengwe. Wanatumia HDM (Highway Development Model) au wanatumia RED (Road Economic Decision). Zote hizi ukizifanyia ukaguzi utagundua kwamba barabara hii inafaulu kwa model zote mbili.
Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Ujenzi mwongeze jicho lenu kwenye hii barabara ili kusudi watu wa maeneo hayo waweze kupata unafuu. Miundombinu mingine ambayo inahitajika kwa ajili ya viwanda na umeme mijini na vijijini; vijijini unahitajika zaidi umeme, tuwashukuru REA kwa kazi wanayoifanya. Awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu naomba ikamilike kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pesa ambazo zimepangwa kwenye Mpango ziwe zinafika kwa hawa watu wa REA ili kusudi utekelezaji ufanyike kwa wakati. Bila kufanya utekelezaji kwa wakati, hatutafanikiwa malengo yetu. Kwa sababu hata kama utajenga kiwanda halafu kikakosa umeme, hakitazalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana hiyo miundombinu wezeshi itiliwe mkazo kweli kweli katika kuisimamia na hii ni pamoja na mitandao ya simu. Katika maeneo yetu mengi hasa kwenye Wilaya yangu ya Sikonge, tuna-coverage ya asilimia 45 tu ya mitandao ya simu. Sasa watu watapashana vipi habari? Watapeana vipi habari za masoko? Watauza vipi bidhaa zao bila kuwasiliana? Kwa hiyo, hili la mitandao ya simu nalo naomba liwekewe mkazo sana katika usimamizi ili kusudi tuweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ambacho ndiyo kiwezeshi kikubwa kinachohitajika kwa ajili ya viwanda; kazi ya Serikali popote duniani huwa ni tatu. Kwanza, ni utafiti wa mbegu, miundombinu ya mazao na kadhalika; ya pili ni huduma za Ugani; na ya tatu ni kumlinda mkulima apate haki ya jasho lake. Hizo kazi ndiyo kazi za msingi za Serikali popote duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Mpango yameandikwa mengi, lakini naomba sana mkazo utiwe kwenye hayo maeneo matatu. Ni lazima utafiti ufanyike kuanzia Mtwara huko kwenye korosho mpaka kwenye tumbaku; kuna kilio kuhusu uwekezaji mdogo kwenye utafiti. Naomba sana Serikali ikumbuke suala la utafiti ni kazi yake ya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni huduma za ugani. Viko vijiji vingi havina Maafisa Kilimo ambao wanawajibika kuwashauri wakulima kuhusu kilimo bora. Sasa hili nalo linahitaji umakini wa hali ya juu wa Wizara ya Kilimo ili kusudi wananchi waweze kusaidiwa walime kilimo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, ni kumlinda mkulima apate haki ya jasho lake na hapo ndipo kuna matatizo makubwa. Mifumo ya pembejeo ina matatizo makubwa; wakulima wanapata madeni makubwa. Naomba sana Serikali ifanyie kazi suala la mifumo ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na kwa njia rahisi kusudi watu wetu waweze kulima bila usumbufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo ya masoko nayo ni tatizo kubwa ambalo linatakiwa lifanyiwe kazi. Wakulima wanapunjwa bei na kuchelewa kulipwa. Hayo inatakiwa yafanyike ili kusudi kilimo chetu kiweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa elimu kwa ajili ya kusaidia viwanda, tunahitaji shule maalum za kilimo na ufundi stadi zirejeshwe au zirejeshewe makali yake kama ilivyokuwa zamani. Zirejeshewe hadhi yake na zijengwe na nyingine mpya kwenye maeneo mbalimbali. Hii ni pamoja na kila Wilaya kuwa na VETA, hiyo itasaidia kupatikana nguvu kazi ambayo inahitajika viwandani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ambalo ningependa nizungumzie hapa, limetajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi, lakini kwenye Mpango sijaliona vizuri; suala la vikundi kazi vya kijamii vya vijana; vikundi kazi vya ujenzi, mafundi seremala na vya uzalishajimali. Tunajua Mipango ipo lakini ni muhimu sana tusisitize hili kusudi hivi vikundi kwanza vipate kazi kwenye Halmashauri zetu, vijiimarishe kiuchumi ili baadaye vyenyewe viweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo napenda kulizungumzia ni ufuatiliaji na tathmini. Ufuatiliaji na tathmini unaanzia kwenye mapato na matumizi. Naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano, inafanya kazi nzuri sana ya kufuatilia mapato ili kuhakikisha kwamba Serikali inapata kile ambacho inastahili kukipata kutoka kwenye kodi na vyanzo vingine ambavyo siyo vya kodi. Ni muhimu sana suala hili liendelee kutiliwa mkazo isijekuwa baada ya miaka mitatu tukarudi kule kule tulikotoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la kudhibiti matumizi; ilipoanzishwa MTEF mwaka 1999 ilikuwa matumizi yanaruhusiwa tu kwenye vile vipengele ambavyo vilipitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kadri ambavyo tumeendelea mpaka sasa hivi, matumizi yamekuwa yanabadilika, baada ya miezi sita watu wanaomba reallocation nyingi Wizara ya Fedha. Sasa matumizi lazima yadhibitiwe kwenye vifungu ambavyo vimepitishwa na Bunge kusudi baadaye tuboreshe mipango yetu ili izingatie uhalisia. Hapo tunaweza tukafanikiwa vizuri kutekeleza malengo yetu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mianya ya wizi, mikataba na usimamizi wake iendelee kudhibitiwa ili kusudi yale ambayo yamepangwa kwenye mkataba yaweze kutekelezwa kama yalivyopangwa. Vile vile flow ya fedha inatakiwa isimamiwe vizuri ili kusudi fedha ambayo imepangwa kwa ajili ya mkataba fulani ifike kutekeleza huo mkataba. Nadhani tukifanya hayo, huu Mpango wetu utatekelezeka vizuri na tutapata mafanikio makubwa na nchi yetu itafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, yangu yalikuwa ni hayo tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Napenda nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Sikonge kwa kunipa heshma ya kuwawakilisha kwenye chombo hiki muhimu sana katika nchi yetu.
Pili, napenda kumshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua ambazo anazichukua sasa hivi ambazo zimesaidia sana nchi yetu kuweza kurudi kwenye mstari. Naamini kwamba sasa hizi bajeti ambazo tunazipitisha hapa zote sasa zitakuwa zinafika kwenye utekelezaji. Kwa hiyo, naamini mambo mengi mazuri yanakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ambalo napenda nishukuru ni hatua ambazo Serikali na Menejimenti ya Bunge imezichukua hadi sasa ambazo zimezidi kuongeza heshima ya Bunge. Yale mambo ambayo yalikuwa yanatokea siku za nyuma yamepungua sana hata wewe mwenyewe ni shahidi. Michango ya Wabunge imezidi kuwa ni ile yenye maana kwa wananchi badala ya kuwa na mambo ambayo hayana maana yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake ameiwasilisha vizuri lakini nampongeza kwa kazi zake ambazo amekuwa akizifanya katika nchi yetu ya Tanzania kwa ajili ya kuinua na kuwasaidia wakulima na wafugaji. Nakupongeza sana Mheshimiwa Mwigulu, nakupa moyo endelea kuchapa kazi na Mungu atakulinda na sisi Watanzania tutakulinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kuhusu wakulima. Wakulima wa Tanzania hasa wa Sikonge wanajitahidi sana kulima zao la tumbaku, kilimo cha tumbaku ni cha jasho jingi lakini wamekuwa wakikatishwa tamaa na wajanja. Kama ambavyo utaona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 23 badala ya uzalishaji kuongezeka unapungua ni kwa sababu ya kukatishwa tamaa na wajanja. Naomba sana Mheshimiwa Waziri awadhibiti hawa ili wasiendelee kumnyanyasa na kumnyonya mkulima ili hatimaye uzalishaji uongezeke na Taifa lizidi kupata manufaa kupitia kilimo cha tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wajanja hao nitawataja wachache, kuna viongozi wa vyama vya msingi wasio makini na wasio waadilifu, kuna maafisa ushirika ambao sio waadilifu na kuna maofisa wa benki ambao sio waadilifu. Watu hawa wamekuwa wakishirikiana kwa utatu huo katika baadhi ya maeneo kuwadhulumu wakulima na kumsababishia mkulima madeni na mengine ni madeni hewa. Hadi sasa katika Mkoa wa Tabora asilimia 52 ya vyama vyetu vya msingi havikopesheki kwa sababu ya madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba niende moja kwa moja kwenye kupendekeza hatua au kushauri hatua za kuchukua. Pamoja na kwamba hotuba ya Mheshimiwa Waziri imetueleza hapa pembejeo sasa zitapatikana kama soda inavyopatikana dukani, lakini najua kwamba utaratibu huo utachukua muda mrefu, hautakuwa ni utaratibu wa kuja siku moja tu, hapana. Kwa hiyo, naomba sana hatua za makusudi zichukuliwe ili kusudi haya masuala ya kumfanya mkulima na chama chake cha msingi ndiyo kuwa mkopaji kwenye mabenki wakati mkulima elimu yake ni ndogo sana kuhusu masuala ya mikopo, naomba sana mkulima aondolewe huo mzingo wa kukopa badala yake kampuni ndiyo ikope halafu impatie pembejeo mkulima. Hiyo ndiyo itasaidia kuondoa mzigo kwa wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili naomba sana Serikali idhibiti wizi au udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wajanja kumuibia mkulima kupitia exchange rate. Leo dola inaweza ikawa shilingi 2,200 lakini mkulima ataambiwa ni shilingi 1,800, hapo anakuwa ameibiwa shilingi 400 au ataambiwa dola ni shilingi 2000 hapo atakuwa ameibiwa shilingi 200. Kwa sababu mkulima hana utaalamu anakuwa ameibiwa fedha nyingi sana kupitia njia hizi. Naomba sana Serikali ichukue hatua kudhibiti wizi unaofanyika kupitia thamani ya ubadilishaji wa fedha kutoka dola kwenda kwenye shilingi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, naomba sana Serikali isiendelee kujiweka pembeni kwenye suala la kupanga bei ya tumbaku. Najua Sheria ya Tumbaku imesema Serikali ijiweke pembeni iwaachie sijui Baraza la Tumbaku, kule kuna wajanja ambao ni makampuni, hao ndiyo ajenda yao wakiileta huwa inapitishwa vilevile kama ilivyoletwa. Bila Serikali kuingilia kati mkulima atabaki kunyanyasika kupitia bei ndogo sana ya tumbaku. Mbona kwenye sukari mnapanga bei? Kwenye sukari mbona mnajishirikisha kusema kilo ya sukari ni shilingi kadhaa, kwa nini kwenye bei ya tumbaku mnasema tunawaachia wakulima wenyewe matokeo yake wakulima hawawezi kupambana na wajanja. Naomba sana Serikali iwe makini katika suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ni kuhusu mbolea, ninapendekeza Serikali iongeze uratibu wake wa uingizaji wa mbolea kutoka nje. Utaratibu wa sasa wa kuingiza mbolea pale bandarini halafu ndiyo inaanza kusambazwa nchini kutoka bandarini pale unamsababishia mkulima gharama kubwa. Kwa sababu bei ambayo wana-charge wasafirishaji kutoka bandarini hadi mkulima anapoipata inakuwa kubwa mno badala yake napendekeza vianzishwe vituo maalum vya kupokeleana mbolea mikoani. Kwa mfano, Tabora pale unaweza ukajenga warehouse kubwa ikapokelewa mbolea yote ya Mikoa ya Tabora, Kahama na baadhi ya maeneo ya Kigoma halafu kutoka hapo kwenda kwa mkulima bei itakuwa ndogo kuliko kusafirisha mbolea kutoka Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tano ni makato kwenye sekta ya tumbaku yamekuwa makubwa mno na mengi hayakubaliki. Waziri Mkuu alipokuwa anatoa hotuba yake alizungumzia kuondoa au kupunguza makato kwenye zao la korosho. Naomba sana dhana aliyoitumia Mheshimiwa Waziri Mkuu kupunguza makato kwenye zao la korosho hiyo hiyo itumike kupunguza makato kwenye zao la tumbaku. (Makofi)
Mhesimiwa Mwenyekiti, kuna makato mengi, kwa mfano, mkulima ameuza tumbaku yake kwenye ghala lakini anakatwa fedha ya kusafirishia tumbaku kutoka kwenye ghala mpaka kwenye kiwanda Morogoro, ni kwa sababu gani? Kama mimi nikinunua cement Dar es Salaam hivi yule mwenye duka la cement niliponunua atalipia gharama za kusafirisha cement kwenda kwangu Tabora? Naomba hapo tubadilike na Serikali iwe makini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, makato ya APEX ambayo yalishafutwa bado mkulima anakatwa. Shilingi milioni 575 za mwaka jana zipo lakini sasa hivi wamezipangia matumizi kwamba hizo fedha badala ya kumrudishia mkulima wanataka wazitumie watu wa Wizara ya Kilimo eti kwa ajili ya kuja kutoa mafunzo. Kwa nini Serikali itumie fedha za mkulima kuja kutoa mafunzo, Serikali si imeweka bajeti na tulishawapa! Naomba sana fedha hizo warudishiwe wakulima wenyewe kama walivyokatwa. Pia kuna makato ya kuchangia union na kuchangia gharama za utafiti nayo yaondolewe kwa sababu utafiti ni kazi ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mawili kwa wakulima, naomba sana kilimo cha mkataba kirejeshwe, wakulima wanataka sana kilimo cha mkataba. Kama ni pembejeo wapewe na mnunuzi, hiyo itasaidia kuondoa mambo ya riba ambayo wanakabiliana nayo kwenye masuala ya kukopa benki.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wizara hii ya Sheria na Katiba ninayo machache sana. La kwanza imenipa faraja sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuonesha kwamba fedha za ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Sikonge zipo na akataja na kiwango kabisa. Mimi namuomba Mheshimiwa Waziri asimamie kwa sababu fedha hizo ni za mwaka huu wa fedha wa2015/2016 ili zifike haraka, ili kusudi hiyo Mahakama ianze kujengwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi nimejitolea kuruhusu ofisi ya zamani ya Mbunge iwe wazi kwa ajili ya matumizi ya Mahakama ya Wilaya ya dharura. Niliiachia hiyo ofisi tangu mwezi wa 11 mwaka jana, lakini mpaka sasa hivi Hakimu wa Wilaya hajahamia! Wakati anafanya majumuisho Mheshimiwa Waziri naomba aniambie kwamba Hakimu wa Wilaya atahamia lini? Labda wiki hii au wiki ijayo? Ili kusudi wananchi wasiendelee kutaabika! Wanatumia fedha nyingi kwenda Tabora kwa ajili ya kuhudhuria kesi zao au kesi za ndugu zao na hakuna sababu kwa nini waendelee kupata shida namna hiyo wakati ambapo Mbunge wao nimejitolea ofisi iliyokuwa ya zamani ya Mbunge, itumike kwa ajili ya Hakimu wa Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hata polisi wanatumia pesa nyingi sana, gharama kubwa kwenda kupeleka watuhumiwa Tabora wakati ambapo nimeachia ofisi! Ninaomba sana Wizara hii iweke msisitizo wa dharura kabisa ili Mahakama ya Wilaya ya Sikonge ianze kwa dharura hata wiki ijayo, wasisubiri mpaka majengo yakamilike! Najua majengo yatachukua muda mrefu, inawezekana wakianza ujenzi mwezi huu au mwezi ujao wanaweza wakachukua miaka miwili kukamilisha majengo, miaka miwili nadhani haitavumilika kuendelea kusubiri wakati maeneo ya kuanzia kwa dharura yapo, hilo lilikuwa jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili napenda kuzungumzia maeneo ambayo sheria zinakinzana. Ninajua sekta zinahusika lakini mratibu mkubwa wa sheria katika nchi yetu ni Wizara hii. Ninaomba sana ichukue uongozi wa kusoma sheria zote, ili kusudi maeneo yote ambayo yanakinzana, unakuta sheria hii inakinzana na sheria nyingine, zifanyiwe harmonization mapema iwezekanavyo ili kuondoa utata wa aina yoyote ambao unaweza ukajitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kuchangia ni masuala yanayohusiana na Sheria ya Ununuzi. Tuliahidiwa kwamba sheria ile itakuja ili kusudi tuifanyie marekebisho lakini bado mpaka sasa hivi naona haijaletwa! Sikuona vizuri kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri jambo hilo limeripotiwa! Kwa sababu sheria hiyo ni ya msingi sana na imekuwa ni sehemu kubwa ya malalamiko kwa watekelezaji wengi kuhusu kuchelewesha kazi na mambo mengine ninaomba sasa Wizara hii ichukue hatua za makusudi ili kusudi sheria hiyo ifanyiwe marekebisho haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya mambo ambayo kwenye sheria ile hayapo, kwa mfano, masuala yanayohusu miradi mikubwa ya miundombinu, turnkey projects. Kwa mfano, ujenzi wa Reli ya Kati, ujenzi wa barabara kuu kama kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma! Hizo ni turnkey projects ambazo unaweza ukakaribisha sekta binafsi zikaingia kwenye investiment.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya masuala yanayohusu turnkey projects hayamo kwenye hii sheria na yamekuwa yakisababisha utata mkubwa wakati mwingine Wizara zimekuwa zinaambiwa hazijafuata taratibu za manunuzi, lakini unakuta ule utaratibu haujaelezwa vizuri kwenye hiyo sheria
Mheshimiwa Naibu Spika, Kimataifa baadhi ya taratibu za turnkey projects zinapingana na Sheria ya Ununuzi ya kwetu hapa Tanzania! Nilikuwa naomba mambo kama hayo yafanyiwe haraka utaratibu ili kusudi tusiachwe kama kisiwa Tanzania twende pamoja na nchi za wenzetu ambazo zimeingiza taratibu za turnkey projects kwenye sheria zao za manunuzi ili tuweze kufaidika na uwekezaji mkubwa wa sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo napenda kulizungumzia kwenye sekta hii ya sheria ni idadi ya watumishi katika Idara ya Mahakama. Maeneo mengi sana hata Mahakimu tu wa Mahakama za Mwanzo ni shida! Kule kwetu Sikonge tumejitolea Kata tano zianzishwe Mahakama za Mwanzo, lakini wanatuambia sijui kama watapatikana Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo!
Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa tuna Tume ya Utumishi wa Mahakama na amepewa kazi bwana mkubwa mmoja ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI, yuko pale! Nilikuwa ninadhani labda hawana fedha, lakini sijaona humu kama fedha imeombwa kwa ajili ya watumishi! Naomba sana Serikali ichukue hatua za maksudi kuhakikisha kwamba Watumishi katika Idara ya Mahakama wanapatikana na wanakuwa wa kutosha. Hiyo ni pamoja na Majaji, pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Wilaya, Wasajili, ile schedule yote ya utumishi katika Mahakama ikamilike ipasavyo ili kusudi kama kesi kusikilizwa zichukue muda mfupi, kusiwe na muda mrefu wananchi wanasumbuliwa kusubiri kesi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hayo tu na mimi naunga mkono, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Haizuiliki kuzungumzia masuala ya kisera ya Wizara ya Afya ambayo wamesema kwamba kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya. Sera wanaimiliki wao, TAMISEMI kazi yao ni kusimamia na kuratibu utekelezaj wa sera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo langu kubwa ni ceiling ambazo Serikali huwa inailazimishia mikoa. Kwetu sisi Tabora kwenye ceiling ya TAMISEMI ambayo ndiyo tumepitisha bajeti, kwenye sekta yote ya afya ni shilingi bilioni 19 kwa mkoa mzima. Kama tunataka kutekeleza sera inavyotaka kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya, kwenye Wilaya ya Sikonge peke yake tunahitaji vituo vya afya 18 vipya na zahanati mpya 41. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo langu linakuja, nimewauliza watalaam wa afya kule kwangu, ili ujenge kituo cha afya kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Afya, majengo, vifaa, wataalam na kila kitu unahitaji zaidi ya shilingi bilioni mbili. Ili ujenge zahanati kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Afya kwa kila kitu unahitaji zaidi ya shilingi milioni 500. Ina maana kwa Sikonge tu tunahitaji zaidi ya shilingi bilioni 65, tutazipata wapi na tutakamilisha lini ikiwa Serikali inatupangia ceiling ya shilingi bilioni tatu kwenye wilaya yetu? Kwa hiyo, hilo ni tatizo kubwa na tusije tukaiacha hivyo hivyo, Serikali kwa ujumla wake inatakiwa ilifanyie kazi suala hili ili kusudi kweli sera hii iweze kutekelezeka, hilo lilikuwa la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu Maafisa wa Maendeleo ya Jamii. Zamani hawa tulikuwa tunawaita Mabwana na Mabibi Maendeleo. Taarifa ya Waziri kule mwisho kwenye majedwali inaonyesha kabisa kwamba Wilaya ya Sikonge tuna Maafisa Maendeleo ya Jamii 14 na wote wako Makao Makuu ya Wilaya. Katika kata zangu 20 hakuna Afisa Maendeleo ya Jamii ambaye yuko kwenye kata. Nashauri Serikali iachane na maneno, wakati wa utekelezaji ndiyo huu, hapa kazi tu, tuhakikishe kwamba hawa Mabibi na Mabwana Maendeleo wanafika kwenye kata ili kusudi waweze kuhamasisha maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ni kuhusu Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Wananchi hivi (FDCs). Tumeambiwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba tuna Vyuo tisa vya Maendeleo ya Jamii nchi nzima. Napendekeza vyuo hivyo viboreshwe zaidi ili vifikie hatua ya kutoa diploma na hata digrii ili kusudi tusomeshe watu wengi zaidi kwenye hii fani ya maendeleo ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu hivi Vyuo vya Wananchi (FDCs - Folk Development Colleges), kama tulivyokuwa tunazungumza siku tunajadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na hata siku ya kujadili Wizara ya Viwanda, tunahitaji watu wengi, tunahitaji staff, tunahitaji nguvu kazi ambayo itaajiriwa kwenye viwanda vidogo vidogo, kama hivi Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vitaendelea kufundisha elementary sijui kushona nguo, kitu ambacho hata fundi cherehani wa mtaani anaweza akakifanya, naomba hivi vyuo vibadilishwe viwe VETA za maendeleo ya jamii ili kusudi viweze kusaidia uchumi wetu na maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ambalo nataka kuchangia ni ukatili wa kijinsia. Kwa mwaka mmoja tu 2015, kwenye hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri aliyotupatia, inaonekana Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Pwani na Tanga imeongoza katika ukatiri wa ngono, hiyo mikoa mitano. Wana matukio zaidi ya 300 ya ukatili wa ngono, hii mikoa niliyoitaja. Mikoa ambayo ina matukio chini ya 100 ni Mkoa wa Simiyu peke yake, hii ni hatari!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nchi iwe na programu maalum ya elimu dhidi ya ukatili wa ngono, hilo ni suala la aibu sana, linatakiwa lipatiwe programu maalum kabisa. Sijaiona hiyo programu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, naomba sana suala hili lizingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwenye haya matukio ni mashambulio ya kudhuru mwili na matusi. Haya mambo ni mabaya na yanasababisha chuki katika jamii na familia nyingi. Imeonekana Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Morogoro tena na Rukwa ina matukio zaidi ya 1,000, hii ni hatari. Mikoa yenye matukio chini ya 100 ni Dodoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Mwanza, Mbeya, Pwani, Ruvuma na Simiyu tena. Hivi kule Mara walitumia mbinu gani kupunguza matatizo haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Mheshimiwa Waziri apeleke timu Mkoa wa Mara kuchunguza kuona hivi wale watu, kwa sababu wanaaminika wana hasira sana, wamepunguzaje haya matukio ya kushambuliana ili elimu ile iweze kutumika kwenye mikoa mingine hasa hii ambayo ina matukio mengi ili kupunguza matatizo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tano ambalo nataka kuchangia ni uchangiaji wa halmashauri kwenye Mfuko wa Wanawake - WDF. Katika halmashauri ambazo zimetajwa kwenye hotuba ya Waziri ni Halmashauri moja tu ya Iringa ndiyo imeonekana imechangia kwa asilimia 100. Kuna Halmashauri kama ya Kinondoni, Kigoma Ujiji, Sumbawanga, Tabora Manispaa, Misungwi, Mwanza na nyingine nyingi ziko chini ya asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hatua gani ambayo Serikali inachukua sasa kuhakikisha kwamba watu wanaboresha michango yao angalau inafika zaidi ya asilimia 50 na kuendelea. Kuna baadhi ya halmashauri mchango wao ni chini ya asilimia moja, hii ni serious. Naomba suala hili liweze kuchukuliwa kwa umakini wa hali ya juu kwa sababu hawa wanaotekeleza ni waajiriwa wa Serikali, wanatakiwa waheshimu miongozo inayotolewa na Serikali, wasiendelee kufanya kinyume na utaratibu ambao umeelekezwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nataka kuchangia ni suala la wazee. Naomba Serikali isimamie kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yake ya kisera. Kwa mfano, suala la huduma bure za afya kwenye hospitali za Serikali na vituo vya afya na zahanati kwa wazee lisibaki kwenye maneno wala kwenye makaratasi. Najua Waziri wa Afya alitoa Circular mwezi Februari lakini imeendelea kutoheshimika kwenye maeneo yaliyo mengi hapa nchini. Naomba sana ufuatiliaji wa karibu uwepo ili hiyo Circular iweze kutekelezwa isibaki kwenye karatasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati mgombea wetu wa Urais alizungumzia kuhusu pesheni ya wazee. Hili ni suala ambalo ukizunguka kwenye vijiji unaulizwa na wazee, bwana tuliambiwa kuhusu pesheni imefikia hatua gani? Naomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama aweze kulitolea maelezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kuna Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na Mfuko wa Vijana, sawa, lakini wazee wanauliza Mfuko wa Wazee vipi? Kwa maana ya hawa wazee waliostaafu, Mfuko wa Wazee Serikali inatufikiriaje sisi? Kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Afya ndiyo anahusika na masuala ya wazee, naomba wazee wangu wa kule Sikonge wasikie leo anazungumza kuhusu Mfuko wa Wazee atauanzisha lini? (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Wataona baadaye usiku. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwangu yalikuwa ni hayo lakini naomba nimalizie kwa vituko vya kisiasa. Ukistaajabu ya Mussa walisema utaona ya Firauni. Kule Uganda kilitokea kituko kimoja kikubwa sana jana lakini nisingependa kukieleza kwa kina kila mtu anajua. Kwa hiyo, kumbe Tanzania sisi tuna afadhali katika demokrasia na ni mfano wa kuigwa. Wenzetu wamefikia katika hali mbaya, naomba tuwaombee ili kusudi nchi ile iendelee kuwa na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naenda moja kwa moja kwenye hoja.
Naomba nimuunge mkono Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, lakini nimwambie kwamba Barabara ya Tabora - Itigi - Manyoni kilometa 260, ambayo ameipangia shilingi bilioni 79 hizi za Serikali hazitatosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo Kuwait wakati tunazungumza na Kuwait Fund kuhusu kupata fedha kwa ajili ya barabara hii na walisema ikikamilika barabara ya Kilwa the next road itakuwa ni hii barabara ya Tabora - Itigi - Manyoni. Kwenye hotuba yake amegusia kidogo tu kuhusu hayo mazungumzo, lakini hajasema commitment ya Kuwait Fund ikoje, naomba wakati ana-windup atupatie commitment ya Kuwait Fund ikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, barabara ya Makongorosi - Rungwa - Itigi hadi Mkiwa; hii barabara imeamuliwa kujengwa tangu miaka kumi iliyopita, ninaomba isifike miaka 20 barabara hii bado inajengwa, ninaomba sana. Hayo mawili yanamtosha Mheshimiwa Waziri kuyafuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu cha tatu kiwanja cha ndege cha Tabora, amepanga pale shilingi bilioni 7.8; kiwanja cha ndege cha Tabora kilianza kujengwa mwaka 1919, hadhi yake ya sasa hivi iko nyuma sana ukilinganisha kwamba pale Tabora ndiyo makao makuu ya Western Brigade ya Jeshi. Ninaomba sana Serikali iweke kipaumbele kwenye kiwanja cha ndege cha Tabora; kwanza, hizo fedha shilingi bilioni 7.8 zilizopangwa zionekane kwa macho zimetumika, kusiwe na uchakachuaji wa aina yoyote Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu reli ya kati. Reli ya kati madhara yake ni makubwa sana kama haitajengwa. Kusafirisha mafuta kwa njia ya barabara petrol, diesel, mafuta ya taa, ni gharama kubwa sana na hii ndiyo inasababisha bei ya vitu hivi kuwa kubwa, inaathiri sana maisha ya watu wetu. Naomba sana kipaumbele, kwa njia yoyote ile Serikali ifanye lolote inaloweza kufanya hii reli ya kati lazima ijengwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo napenda kuchangia ni kuhusu bandari. Upo mradi unaoendelea pale, ule mradi unaoendelea wa kuboresha bandari kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Serikali ya Uingereza ninaomba usimamiwe vizuri, ili hatimaye meli kubwa ziweze ku-dock pale na ziweze kushusha shehena kubwa sana, ili tusiathirike kibiashara. Bandari yetu ina potential kubwa sana ya kusaidia uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo napenda kuzungumzia ni mitandao. Kwetu kule tuna shida ya mitandao kwenye kata nyingi sana, lakini hasa kwenye kata za Kilori, Kipili, Kitunda na Majojoro, ninaomba sana wakati Waziri anaposimama aweze kuzungumza commitment ya Serikali kuhusu kuboresha mitandao kwenye Wilaya yangu ya Sikonge. Ahsante sana.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye mada ya leo. Nilipokuwa ninausoma mkataba hisia zikanipeleka kwenye historia. Miaka takribani mia moja iliyopita na zaidi walikuja wazungu na mikataba, lakini kabla ya kuja wazungu na mikataba wazungu walisitisha biashara ya utumwa na katika tangazo la kusitisha biashara ya utumwa ukisoma verses zilizokuwemo mle ni pamoja na kusema kwamba hii nguvu kazi ambayo tulikuwa tunaichukua tunaisafirisha ibaki kulekule ili izalishe kwa ajili ya viwanda vyetu. Baada ya hapo walifungua mashamba makubwa, mashamba yale yalikuwa ni kwa ajili ya kuzalisha malighafi zilizokuwa zinahitajika kwenye viwanda na wakati ule ndiyo ilikuwa mapinduzi ya viwanda yanafanyika Ulaya. Kwa hiyo, dalili zote za mfanano wa mikataba ya wakati ule imo kwenye huu mkataba, kwa hiyo mkataba huu una harufu ya ukoloni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yamezungumzwa mengi na wenzangu na mimi nirejee kwamba hakuna mkataba mbovu ambao nimewahi kuushuhudia kama huu kuanzia mwanzo tu. Pale kwenye kurasa za mwanzo kabisa ukisoma jinsi nchi zetu zilivyoorodheshwa, zimeorodheshwa kama block moja kwa moja, lakini walivyokuja kuorodhesha nchi zao wakaorodhesha moja moja halafu baadaye wakasema and the EU, hii aliisema mwanzoni kabisa Mheshimiwa Lugola. Mimi kuanzia hapo tu nilipata wasiwasi na nikapata wasiwasi zaidi hata wataalam wetu ambao walikuwa wanakwenda ku-negotiate tangu miaka ile ya 2007 mpaka juzi, nilipata wasiwasi kama kweli walikuwa wanajiandaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, viwango vilivyomo humu vya terms kwa asilimia zaidi ya 80 ni vya ukandamizaji, kutukandamiza sisi na mengine yamo humu yanalazimisha kwamba tukisaini mkataba huu ndiyo tutapata hata masuala ya development cooperation. Sasa suala hili limenisumbua sana kama ambavyo limewasumbua Wabunge wengine, ninaomba niunge mkono wale wote ambao wametoa wito, Serikali isikubali kusaini mkataba huu mpaka pale marekebisho makubwa yatakapokuwa yamefanyika ikiwemo kuruhusu nchi mojamoja kujitoa wakati wowote inapoona kuna hatari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ningezungumza mengi lakini mengi yameshazungumwa itakuwa ni kurudia, ninaomba niishie hapo, wote tuunge mkono kukataa kukataa mkataba huu. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.
Naomba niende moja kwa moja kwenye masuala machache, sasa hivi Wizara inafanya mapito makubwa ya sera ya ardhi na tunaona huko mikoani inaendelea. Naomba kwa hatua hii Wizara isifanye makosa waliyofanya mwanzoni pale. Baada ya sera ya mwaka 1995 waliandaa sheria halafu baadae ndiyo wakaja kuandaa mkakati wa kutekeleza sheria. Kilichokuwa kinatakiwa ni kwamba baada ya sera unaandaa mkakati wa Taifa ambao unakwenda sambamba na programu ya Kitaifa ya kutekeleza sera, halafu ndiyo unakuja unamalizia na sheria. Kwa hiyo, naomba safari hii wazingatie huo mfuatano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utekelezaji wa sera tunahitaji mambo mawili makubwa, kwanza awareness ya wadau wote waielewe sera, lakini pili tunahitaji rasilimali, rasilimali watu hiyo ni ya kwanza kabisa na rasilimali fedha. Kwa miaka mingi fedha ambayo imekuwa ikitengwa au inaombwa na Wizara hii imekuwa ni kidogo mno. Ndiyo maana Wizara hii ina upungufu mkubwa wa Maafisa Ardhi, Maafisa Mipango Miji, Wapima, Wathamini, Wachora Ramani, Wakadiriaji Majengo na kadhalika. Kwa kifupi ina nguvukazi kidogo sana, sidhani kama hiyo nguvukazi inaweza kutekeleza sera kama wanavyotaka. Vilevile rasilimali fedha imekuwa inapangwa kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukiangalia taarifa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri viwanja vilivyopimwa mwaka huu 2015/2016 ni 112,000 tu angalau wangepima 400,000 ingekuwa ni afadhali kwa nchi yetu. Kati ya hivyo viwanja 112,000 viwanja 38,700 vyote vimepimwa Dar es Salaam na Pwani ambayo ni asilimia 35, huu ni upungufu mkubwa sana. Hati miliki zilizosajiliwa 25,000 tu angalau wangekuwa na uwezo wa kusajili hati 100,000 kwa mwaka ingetusaidia kama nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama trend ni hii ina maana kwamba hata hii mipango kabambe ya majiji, manispaa na miji yetu inayoandaliwa haitaweza kutekelezeka kwa sababu ya ufinyu wa rasilimali fedha na upungufu wa rasilimali watu. Naomba sana Wizara ijipange ili kwenye mwaka mwingine unaokuja baada ya mwaka ujao (2017/2018), waje na mkakati wa maombi ya fedha za kutosha ili utekelezaji ufanyike vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu wa nguvu kazi au upungufu wa uwezo wa kutumia fedha. Katika mwaka huu wa fedha walipanga kutumia shilingi bilioni 3.45 kwa ajili ya miradi ya maendeleo wamepata shilingi bilioni 3.43 ambayo ni sawasawa na asilimia 99, lakini hotuba ya Waziri inatuambia wametumia milioni 745 tu ambayo ni asilimia 21. Ina maana hata kama tukiwapa pesa kumbe uwezo wa kutumia fedha yaani ile absorption capacity inavyoelekea kwa Wizara hii ni ndogo sana, sasa sijui watajipangaje. Mheshimiwa Waziri atakaposimama atueleze vizuri wamejipangaje, hivi uwezo wa kutumia fedha tufanyaje, sisi Wabunge tumsaidie vipi ili Wizara hii iwe na uwezo wa kutumia fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ni Shirika la Nyumba la Taifa, utekelezaji wake nao ni mdogo sana. Mahitaji ya nyumba kwa nchi yetu ni 200,000 kwa mwaka, lakini wao wamepanga kujenga nyumba 5,000 tu kwa mwaka ukilinganisha na nyumba 200,000 yaani ni upungufu mkubwa sana. Mahitaji ya jumla ya nchi yetu sisi tunahitaji nyumba 3,000,000, tutafikia lini malengo haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja zifuatazo katika Wizara hii kuhusu Jimbo la Sikonge:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha barabara kutoka Mibono hadi Kipili kwenye barabara ya Sikonge – Mibono – Kipili hakijatobolewa kwa muda mrefu, wakati inaunganisha Sikonge Makao Makuu ya Wilaya na Kata mbili za Kipili na Kilumbi ambako kuna zaidi ya wakazi 45,000. Kuna uchumi mkubwa sana, maelezo aliyonipa Naibu Waziri kuwa eti kutobolewa kwa barabara hiyo kunahitaji fedha nyingi sana sh. 12,000,000,000, sasa hoja yangu nauliza ni lini Serikalini sh. 12,000,000,000 zikawa nyingi? Au kwa sababu mzigo mzito mpe Mnyamwezi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua ingekuwa maeneo mengine ya nchi ingekuwa imeshatengenezwa japo kwa kiwango cha udongo/changarawe. Naomba Serikali ijipange ili barabara hiyo itobolewe ifike hadi Kipili kama siyo mwaka huu basi mwaka ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha barabara kutoka Ipole hadi Lungwa ni cha muhimu sana kama kweli tunataka kuunganisha Mikoa ya Mbeya na Tabora. Lini kipande hicho kitajengwa kwa kiwango cha lami? Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri namwambia kuwa Mbunge wa Sikonge ni mzigo mzito sana kulingana na jiografia yake na alijionea mwenyewe, mbona sijaona majibu yake kwenye hotuba yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano; nimeshaongea sana na Dkt. Sasabo ambaye ni Katibu Mkuu – Mawasiliano kuhusu kukosekana kabisa kwa mawasiliano ya simu katika Kata za Nyahua, Igigwa, Kiloleni na Ngoywa na pia mawasiliano hafifu kabisa kwenye Kata za Kipili, Kilumbi, Kiloli, Kitunda, Mole na Ipole. Fedha za mawasiliano vijijini zinatumika lakini Sikonge tuna njaa sana ya mawasiliano. Naomba sasa kwa maandishi haya Wizara hii itutendee haki na sisi tupate mawasiliano ya uhakika kama ilivyo kwa maeneo mengine ya nchi, watu wanatumia simu lakini hawana mawasiliano ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, lakini kwa masharti ya kusikilizwa kilio cha wananchi wa Sikonge.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naomba niseme kwamba wapinzani wamewasilisha malalamiko ya mtu mmoja bila ya kuleta bajeti mbadala ya upinzani. Hawa ni sawa sawa tu na Mbunge mmoja amesimama pale amechangia, lakini kusema hiyo ni hotuba ya upinzani kama bajeti mbadala hiyo ni bajeti hewa. Niliamini kama kweli ingekuwa ni Serikali kivuli basi ingewasilisha bajeti mbadala, mfano kama ameona shilingi trilioni 29.5 ni nyingi sana wao wanapendekeza trilioni ngapi? Tungesikia kutoka kwao, naamini Watanzania wamewaelewa hawa ndugu nadhani tuwaache kama walivyo na hawapo hapa Bungeni kwa sababu wamedharau. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kimkakati bajeti yetu ni nzuri sana, na vyanzo vya mapato vya bajeti hivi vinakusanyika vizuri. Kwa mfano kuondoa kodi ya majengo (property tax) kutoka kwenye Serikali za Mitaa ambazo kwa pamoja zilikuwa na uwezo wa kukusanya kati ya asilimia tano hadi 10 tu ya fedha ya kodi yote ambayo inaweza kukusanywa ni jambo la kupongeza sana. TRA kama watajitahidi, kama ninavyowafahamu mimi, wanao uwezo mkubwa wa kukusanya kati ya asilimia 50 hadi 70 ya potential. Ina maana wanaweza wakakusanya hadi trilioni 1.8 ambayo ukilinganisha na pato la zamani la shilingi bilioni 300 ina maana tutakuwa tumepiga maendeleo makubwa sana kwa hiyo naipongeza sana Serikali kwa uamuzi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa pili, makusanyo ambayo yalikuwa ya retention yalikuwa yanatumika vibaya sana kwa hiyo kwa sasa hivi itakuwa ni fursa ya mapato hayo kutumika vizuri.
Suala lingine zuri tumepunguza mikopo ya nje kwa trilioni 0.03 kulinganisha na mwaka jana kwa ajili ya kupunguza utegemezi, kwa hiyo, hilo ni jambo lingine la kupongeza sana Serikali. Angalizo pekee hapo ni kwamba tumeongeza mikopo ya ndani kwa trilioni 1.34 hatua hii ni nzuri, lakini Wizara ya Fedha itahitaji udhibiti na ufuatiliaji wa karibu sana, kwa sababu riba za mikopo ya ndani zipo juu sana Wizara ya Fedha na Benki Kuu wakizembea kidogo tu tutatumbukia kwenye mizozo isiyo na tija inayoweza kusababisha sintofahamu kupitia matokeo hasi kama mfumuko wa bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni ya upinzani dhidi ya bajeti ya Serikali yana ukakasi wa hasira ya kugomea Bunge bila sababu za msingi. Kwa nini tuandikie mate na wino upo? Wanazo Halmashauri kadhaa ambazo wanaziongoza hivi huko kwenye Halmashauri zao wamesamehe ushuru wote na tozo zote? Badala yake wameongeza ushuru na kodi kwa hiyo ina maana kwamba hapa wanakuja kufanya mchezo wa maigizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Watanzania waelewe kwamba sisi Wabunge wa CCM tuko hapa kuwawakilisha na tuko makini katika kazi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuweka vipaumbele vya kujenga uchumi wa viwanda kwenye bajeti hii mpya. Katika vipaumbele hivyo nashauri Serikali ikamilishe maandalizi muhimu yanayotakiwa kwenye sekta wezeshi ili kuhakikisha kwamba bajeti hiyo itatekelezeka vizuri sana. Kwa mfano kule kwetu kuna barabara ya kutoka Chunya hadi Itigi na barabara ya Ipole hadi Rungwa, barabara hizo mbili ni barabara muhimu sana kwa kwetu kwa uchumi wa viwanda, tunaomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Ziwa Victoria ni mradi mmoja wezeshi ambao ni muhimu sana. Miradi ya umeme vijijini, zahanati, vituo vya afya, shule ni miradi wezeshi ambayo tunaomba sana fedha ambazo zimepangwa kwa mwaka ujao ziweze kutolewa zote zitumike zote kwa ufanisi. Na vilevile pale ambapo kutakuwa na upungufu mwaka 2017/2018 tusisahaulike kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kusimamia utekelezaji wa mpango na bajeti napenda kujua ni shilingi ngapi zimewekwa kwa ajili ya monitoring and evaluation? Kwa sababu haiku wazi kwenye Bajeti hii. Bila monitoring and evaluation tutapata matatizo makubwa. Kwa mfano Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amepangiwa shilingi bilioni 34, kwa mtazamo wangu fedha hizo ni ndogo sana. Tunamtarajia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Ofisi yake iimarishwe zaidi ili afanye kazi vizuri zaidi. Tunahitaji awe na uwezo mkubwa wa kufanya ukaguzi wa kitaalamu au technical audit ambapo haiitaji wahasibu na wakaguzi wa ndani peke yake. Inahitaji wahandisi, wakadiriaji wa majengo, wachumi na wataalamu wengine wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunahitaji ofisi hii iweze kuimarishwa kwa nguvu kazi na uwezo wa kufanya kazi. Sasa hii pesa iliyowekwa hapa ni ndogo sana, kwa hiyo tunaomba sana ifikiriwe mara mbili ili kusudi bajeti hiyo iongezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kusisitiza ni bajeti ya utafiti. Kwenye sekta karibu zote ni bajeti ndogo sana imepangwa. Utafiti duniani kote ni jukumu la Serikali, kwa hiyo inatakiwa bajeti ya utafiti hasa kwenye mazao ya biashara na chakula iongezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuchangia ni kwamba, Serikali imekiri hapa kwamba kuna ugumu wa kukusanyaji wa mapato kwenye sekta isiyo rasmi. Sasa Serikali imejua tatizo inatakiwa ikamilishe sasa sehemu muhimu ya namna gani ya kutatua tatizo hili, kwa sababu tunahitaji kukusanya mapato kutoka kwenye sekta isiyo rasmi. Nashauri Serikali iweke kipaumbele cha kuisajili sekta yote isiyo rasmi ili kuijua vizuri na kurahisisha Serikali kukusanya mapato yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nafurahi kusikia kuwa deni letu la Taifa bado ni himilivu, na ili kudhibiti deni letu Wizara ya Fedha inatakiwa kuwa macho sana na madalali wa mikopo ya miradi mikubwa ambao hujiita transaction agents, ambao hujifanya wanasaidia nchi kupata mikopo mikubwa kutoka kwenye Serikali rafiki za nchi nyingine. Kama watu hao wasipodhibitiwa hatimaye tutakuwa na mikopo yenye gharama kubwa sana maana nao huwa wanatoza tozo.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yetu mikubwa kama ya reli, bwawa la Kidunda, bomba la mafuta, itaathirika kwa kuiingiza nchi kwenye gharama kubwa zaidi kama hatutawadhibiti hao transaction agents. Naomba sana Serikali iwe makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nina wasiwasi na bajeti ndogo sana kwenye sekta ya ardhi kukidhi kazi muhimu za kupima viwanja nchi nzima, lakini hasa hasa lile swala ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu alikubali hapa, kwamba inatakiwa iteuliwe Kamati ya Kitaifa ambayo itaunganisha Wizara zaidi ya nne kwa ajili ya kufanya kazi ya kubaini maeneo yote ambayo yanahitaji kuongezwa ili kusudi wakulima na wafugaji wapate maeneo mengi zaidi ya kufanya shughuli zao. Hii bajeti iliyoko kwenye sekta ya ardhi ambayo ndiyo ingegharamia kazi hiyo hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali ifikirie mara mbili, kazi hiyo ni ya muhimu sana kwa maendeleo ya taifa. Na kwa ajili ya kuliweka taifa letu katika amani na utulivu ni muhimu sana mapori ya akiba ambayo yamekosa sifa mpaka sasa hivi yako mengi sana hapa nchini hii timu inatakiwa iende ikafanye ukaguzi na kuleta mapendekezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kulitolea maoni yangu, ni kukata kodi gratuity ya Wabunge. Sidhani kama kulikuwa na ulazima wa kuleta suala hilo mwaka huu, lakini vilevile si dhani kama kuna ulazima wa kukata hiyo gratuity. Najua, inaletwa ili kusudi makato yaanze kufanyika kuanzia mwezi wa saba unaokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Ofisi ya Mbunge ni Taasisi inayojitegemea, na ina majukumu mengi sana kwenye jamii, na wananchi wanaitegemea, na fedha hizi nyingi huwa hazitumiwi na Mbunge binafsi, fedha nyingi huwa zinakwenda kwenye jamii, Mbunge huwa anachangia miradi mbalimbali. Kwa hiyo, mimi naomba sana...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kakunda muda wako umekwisha.
Naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.
Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwamba Bunge lako Tukufu liridhie mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumechelewa sana kama nchi na kwa kweli nchi yetu ya Tanzania kulinganisha na nchi ambazo zimetajwa kwenye hiyo orodha ya nchi saba ni kama aibu. Naomba sana leo hii turidhie na tuingie kwenye zile nchi ambazo zipo makini kwenye hili suala. Wanamichezo wengi wa Tanzania inawezekana wameathirika kutokana na matumizi ya hizi dawa. Ingawa mkataba huu una udhaifu wa kutokutoa viwango sawa vya udhibiti wa dawa kiasi ambacho kuna baadhi ya nchi wanaruhusu matumizi ya bangi, wanaona ni sawasawa tu, lakini kwa kweli tukiingia sisi inabidi tuwe na orodha ndefu zaidi kuliko ile orodha ambayo ipo kwenye huu mkataba ili kusudi Watanzania wote wanaoshiriki michezo na Watanzania ambao wako mitaani waweze kuishi wakiwa na afya njema; tuwalinde wote siyo tuwalinde wana michezo peke yao, Kwa sababu hata waliopo mitaani kesho wanaweza wakawa wanamichezo tukiwahamasisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko faida nyingi ambazo tutazipata kutokana na kutekeleza huu mkataba. Kwanza tutapata elimu; elimu ambayo kwa wana michezo na makocha wa michezo kuhusu makosa ya kutumia dawa hizo na madhara yake itasaidia sana kuweza kuokoa kundi na hasa la vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tutapunguza, tutazuia usafirishaji wa biashara ya vifaa na dawa ambazo zimezuiliwa, pia tutadhibiti matumizi kwa kuboresha njia mbalimbali za uchunguzi na vipimo kwenye maabara na inawezekana na sisi tukapata maabara yenye ithibati ya Kimataifa ya kuchunguza na kupima matumizi kama hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Kamati ambayo Mheshimiwa Hafidh ameipendekeza iwe inatoa adhabu kali sana kwa watakaogundulika kutumia hizo dawa, kwa sababu bila adhabu kali matumizi ya dawa hizo yataendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, ni wajibu wa Serikali na wadau kufadhili na kusimamia mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ambao utahakikisha utekelezaji sahihi wa kanuni zilizopo kwenye mkataba huo ili kuhakikisha kwamba matumizi ya dawa zote zilizoainishwa na ambazo sisi kama Taifa tutaziongeza yanadhibitiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Azimio hili la Bunge linaweza kusaidia nchi yetu kupata mafanikio kimichezo na kuondokana na sifa ya kuwa kichwa cha mwendawazimu, kwa sababu baadhi ya dawa kama bangi na mirungi na hata dawa za kusisimua misuli kwa wale ambao wanapenda sana kucheza michezo ile mingine ya usiku, nadhani zinaweza kusababisha afya kuathirika na nguvu zao kimichezo kupungua na viwango vyao vya michezo kupungua. Kwa hiyo, inabidi tuchukue hatua kali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nimalizie mchango wangu kwa kusema kwamba, kama nchi hizi hatua kali ambazo tutazichukua lazima ziandikwe kwenye sheria, kama hazijaandikwa kwenye sheria zikabaki tu kwenye kanuni ndogo ndogo sijui za Vyama vya Michezo tutakosa nguvu ya kuweza kutekeleza. Kwa hiyo, inatakiwa ziingie kwenye sheria zetu kama nchi, Mheshimiwa Waziri wa Sheria ashiriki kuhakikisha kwamba sheria inatungwa ambayo itatoa udhibiti na makosa ya matumizi ya hizo dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini nasema hivyo? Wapo wachezaji wengi sana wamecheza mpira kwa muda mfupi na wakaathirika; wamecheza mpira mwaka mmoja mtu anakuwa nyoronyoro kabisa. Nasikia pale Kariakoo kuna matatizo makubwa sana ndiyo maana wachezaji wengi wa Yanga huwa wanacheza kwa muda mfupi mpira, sasa hiyo inatakiwa ifuataliwe, siyo wote ni baadhi yao na hata wachezaji wa Simba!
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mchezaji mzuri anatoka mkoani akifika pale mjini mwaka mmoja, miwili tayari amepoteza kiwango chake, angalau wale ambao huwa wanatoka katika nchi za nje kidogo wanajua mantiki ya hizo dawa; huwa wanacheza kwa muda mrefu sana, kwa mfano yule Mkongo, anaitwa nani yule, yule wa Yanga ana umri wa miaka karibu 40 lakini anacheza mpira mpaka sasa hivi. Mwenzangu ameonesha wasiwasi kwamba huenda inawezekana labda anatumia lakini naamini yule hatumii ndiyo maana amecheza mpira kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mifano ya wachezaji kama Joseph Kaniki ambaye alikamatwa na dawa za kulevya kule Ethiopia na wachezaji ngumi ambao walisafirishwa na marehemu Shaban Mwintanga ambao walikamatwa kule Mauritius ni mifano ya aibu ambayo hatutegemei tuendelee kuipata katika nchi yetu ili kusudi hata sisi tujenge jina kwenye nchi nyingine kwamba sisi ni nchi ambayo ipo makini. Ni lazima uchunguzi wa kina uwe unafanywa kwa mfano kama timu inasafiri kwenda nje ya nchi, kabla hawajatoka nje ya nchi uchunguzi ufanywe wa kina kwamba hawana dawa na wanaporudi vile vile uchunguzi ufanyike wa kina kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango kwa uwasilishaji wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo. Nampongeza kwa kutuletea vipaumbele vilevile kama vilivyokuwa mwaka 2016/2017 kujenga msingi wa uchumi wa viwanda, kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara na usimamizi wa utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni commitment ya kuendelea kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo ya nchi na hii inaonesha kielelezo cha uendelevu wa mIpango yetu, kielelezo cha sera zinazotabirika na kielelezo cha mipango imara. Kwa hiyo, namshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi alipoonyesha katika kitabu hiki cha mapendekezo mkakati wa ufuatiliaji na tathmini chini ya uratibu wa Tume ya Mipango ambao umewekwa vizuri sana. Napongeza lakini natoa rai kwamba yale mazuri ambayo yalikuwa yanatekelezwa na ule Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, yaingizwe katika huu Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini ili kuboresha zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti nimeshituka kidogo niliposoma tathmini ndogo iliyoko kwenye kitabu cha mapendekezo hasa kuhusu hali ya viwanda ya sasa (status). Tuna viwanda vikubwa 1,322, tuna viwanda vidogo 47,921, takwimu ni nzuri. Hata hivyo tatizo nimeliona kwenye viwanda vikubwa vya uzalishaji yaani manufacturing industries viko 998; lakini kati ya hivyo 998 asilimia 53 ya viwanda hivyo viko katika mikoa mitatu tu ya Dar es Salaam, Arusha na Kagera. Sasa hii mimi nimeona kwamba kwa kweli uwiano wa uwekezaji katika viwanda vya uzalishaji nchini hauko vizuri. Naomba huko tuendako ili kusudi hii status iweze kubadilika, huko tuendako tuzingatie uwiano wa maendeleo ya nchi yetu kwa kuzingatia kwamba viwanda vya uzalishaji vinahitajika hata katika mikoa ambayo sasa hivi haina hivyo viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nije sasa kwenye miradi ya kipaumbele. Nimeisoma, ni mizuri na ninatoa maoni kidogo katika miradi ya kipaumbele kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa au standard gauge ni mradi muhimu sana. Juhudi ambazo zimeshaanza za kutafuta fedha kwa ajili ya mradi huu naomba zisilegezwe; zifuatiliwe kwa ukamilifu wake ili kusudi hii reli ijengwe kama ambavyo inaonekana katika mapendekezo. Umuhimu wake unaonekana kutokana na matokeo ya kiuchumi yatakayopatikana. Kwanza, ujenzi wa reli ya kati utashusha gharama za usafiri na usafirishaji ambazo ndizo kiini kikubwa cha kupanda gharama za maisha. Mfano, gharama za kusafirisha mbolea, gharama za kusafirisha mafuta ya petrol na diesel zitapungua kwa kiasi kikubwa na hivyo kupunguza bei ya petrol, bei ya diesel na bei ya pembejeo na hiyo itasababisha maisha yawe nafuu kwa wananchi. Kwa hiyo, mradi huo ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunahitaji barabara za lami, viwanja vya ndege, tunahitaji kuboresha barabara za changarawe na hili niliwekee msisitizo kwenya maeneo yangu ya Jimbo. Barabara ya Tabora – Ipole – Mpanda ambayo sasa hivi inajengwa, mkazo uwekwe, barabara ile ikamilike kwa ajili ya kunganisha Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Katavi. Barabara ya Ipole - Rungwa inaunganisha Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Mbeya. Naomba katika kipindi hiki cha mwaka 2017/2018 ianze kujengwa; na barabara ya kutoka Chunya – Itigi – Mkiwa, kipindi cha mwaka 2017/2018 barabara hii nayo ikamilike kwa sababu hapo kuna uchumi mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ni muhimu sana. Imetajwa miradi ya maji kwa ujumla jumla, sasa mimi nakwenda kwenye specific ili Mawaziri husika wa sekta husika wazingatie wakati watakapokuwa wanaweka maoteo ya bajeti rasmi kwa ajili ya kuingia kwenye rasimu ya mpango wenyewe, naomba sana mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ufike Sikonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, status ya sasa hivi wametangaza kandarasi tatu. Kuna lot inatoka Solwa mpaka Nzega; kuna lot inatoka Nzega mpaka Igunga; na kuna lot inatoka Nzega mpaka Tabora Mjini. Ile lot ya kutoka Tabora Mjini mpaka Sikonge haijatangazwa. Naomba wakati wa bajeti utakapofika, Waziri wa Maji asimamie hilo ili lot ya kutoka Tabora Mjini mpaka Sikonge ionekane kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018; vinginevyo kwa kweli tutakuwa hatuwatendei haki wananchi wa Sikonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mapendekezo ya jumla kuhusu afya; lakini nilitegemea kuona mkakati wa kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata, unakuwa wazi katika huu mpango. Nimesoma maelezo, yako jumla jumla sana, naomba tuwe specific; zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata ni sera ya Serikali na ni sera ya nchi yetu. Kwa hiyo, naomba sana iwe specific.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kuhusu mpango kwenye sekta ya kilimo. Sisi Sikonge hatuwezi kuzungumzia kilimo bila kuzungumzia tumbaku. Status ya sasa hivi kwa mwaka 2016/2017; hawa ndugu zetu makampuni yanayonunua tumbaku, yameshusha makisio kwa zaidi ya asilimia 50, maana yake nini? Maana yake ni kwamba kijiji ambacho kilikuwa na wakulima 300 wa Tumbaku mwaka huu hawataweza kulima wote 300, watalima labda wakulima 100. Ina maana wengine hata wakilima hawana pa kuuza.
Naomba sana Serikali kwanza kwa mwaka huu iwe macho kuhusu haya makampuni ili yafanyike marekebisho ya makusudi, lakini kwenye mpango wa 2017/2018 matatizo kama yaliyotokea mwaka huu naomba yasijitokeze kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mwongozo wa Uandaaji wa Bajeti ya mwaka 2017/2018, naunga mkono na ninaipongeza Serikali kwa kuendelea na vigezo vya asilimia 40 kwamba itumike kwa ajili ya miradi ya maendeleo na asilimia 60 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kwa kweli huo ndiyo msingi ambao utaendeleza pale ambapo tumeanza mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono vigezo hivyo vikuu vya ugawaji wa rasilimali kwa sababu nchi yetu itaendelea kuweka uzito unaostahili kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vigezo vikuu vya OC, napendekeza viwe ni pamoja na idadi ya miradi ya maendeleo inayosimamiwa na taasisi husika ili miradi hiyo utekelezaji wake usimamiwe vizuri na ulingane na thamani ya fedha itakayotumika. Kama idadi ya miradi ya maendeleo haitakuwa miongoni vya vigezo vya kugawa OC, basi tutakuwa tunatekeleza miradi ambayo haisimamiwi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile upo umuhimu wa kupitia upya vigezo vya kisekta ili kulingana na wakati uliopo ziandaliwe; maana yake hivi vigezo ambavyo viko kwenye hivi vitabu viliandaliwa kipindi kirefu sana, mwaka 2005/2006.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana vigezo hivyo vifanyiwe mapitio ili vilingane na wakati wa sasa. Mfano, ruzuku katika sekta ya maji kwa sasa inahitaji kigezo cha idadi ya watu tu wanaokaa vijijini, lakini kwa sasa hivi kuna wakazi wengi katika Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo ambayo ndiyo imejitokeza hivi karibuni. Mimi naomba vigezo hivi vifanyiwe mapitio ili kusudi vilingane na mahitaji ya wakati wa sasa maana yake ni vya muda mrafu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni machache tu, ni hayo, nawapongeza sana Serikali, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwenye Kamati
ya Miundombinu naunga mkono hoja, taarifa yao ilikuwa nzuri sana. Nakubaliana nao hoja
kwamba kuzorota kwa huduma za reli kumesababisha utegemezi kwenye barabara kwa
usafirishaji wa abiria na mizigo. Na hiyo ina matokeo mabaya sana kwa upande wa uchumi
wetu, kwa sababu barabara zetu zinaharibika kwa haraka, tunaongeza gharama za ukarabati,
uhimilivu wa barabara unapungua kutoka miaka 20 hadi miaka mitano na gharama za usafiri
na usafirishaji kwa ujumla zinaadhiri uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano lita moja ya petroli au dizeli kwa wastani inauzwa
kama shilingi 2,000; lakini kama mafuta yale yangekuwa yanasafirishwa kwa njia ya reli isingefika
bei hiyo ingekuwa labda shilingi 1000, shilingi 800 au shilingi 1200; na hiyo ingekuwa na matokeo
mazuri kwa uchumi. Kwa hiyo naomba kutoa wito Serikali isilale, ifanye mbinu zozote zile hata
kama gharama ni kubwa ijengwe reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa. Hiyo itakuwa ni
ukombozi mkubwa sana kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, wakati mbinu hizo za kujenga reli zinafanyika, wasiache
kuendelea kujenga barabara za lami na barabara za changarawe hasa vijijini ili kusudi
kuwezesha gharama zetu za usafiri na usafirishaji kupungua. Kwetu kule Sikonge kuna barabara
muhimu ambazo nataka nizitaje hapa, barabara ya changarawe ya Tutuo - Izimbili - Usoke,
barabara ya changarawe ya Sikonge - Mibono - Kipili naomba ziangaliwe kwa macho mawili.
Barabara hizi tunadhani huwa kuna mchezo unafanyika. Kwa mfano barabara ya Sikonge -
Mibono - Kipili kila mwaka hupangiwa fedha kwamba itatengenezwa kutoka Sikonge mpaka
Kipili, lakini wakifika Mibono wanaacha, kila mwaka. Naomba mwaka huu imepangiwa milioni
862 ifike Kipili.
Naomba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi aifikirie sana hiyo Wizara, na akubaliane na mimi
kwamba barabara ile itobolewe mwaka huu ifike Kipili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo napenda kulizungumzia, suala la kusema
Bandari ya Tanga na Mtwara zinajiendesha kwa hasara huo ni uongo uliopitiliza. Serikali ifanye
uchunguzi kubaini sababu kwa nini bandari hizi zijiendeshe kwa hasara wakati potential ni
kubwa? Kwa mfano wafanyabiashara wa pale Tanga Mjini kwa nini wapitishie mizigo
Mombasa? Ina maana kuna matatizo hapo kwenye bandari ya Tanga. Kwa hiyo, naomba sana
uchunguzi ufanyike ili watakaobainika hatua zichukuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la nne suala la mawasiliano. Zinatumika fedha nyingi za mfuko
wa mawasiliano vijijini, lakini kunakuwa na wababaishaji upande wa mitambo ambayo
inawekwa. Inakuwa wananchi hawapati coverage ambayo tunaitaka kwenye mawasiliano,
mtambo unawekwa lakini coverage inakuwa ndogo sana. Sasa mimi naomba Wizara
inayohusika; kule kwetu kuna kata za Kipili, Kirumbi, Kilori, Kitunda, Ngoywa, Ipole, Kiloleli, Igigwa,
Nyahuwa na Mole, hakuna mawasiliano ya uhakika licha ya kwamba kuna minara. Mimi
naomba sana Wizara inayohusika ifuatilie matumizi ya fedha za mfuko wa mawasiliano vijijini, je,
zilitumika kihalali au kulikuwa na ubabaishaji, ili kusudi hatua zichukuliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa kwenye umeme…
NAIBU SPIKA: Muda umekwisha Mheshimiwa.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi na taarifa yake kama ni sahihi kwa sababu mimi nimefanya kazi na Mheshimiwa Lowassa kwa karibu sana yeye labda hamjui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea, kutoka Pangale hadi Matagata kuna kilometa 416 sawasawa na kutoka Dodoma hadi Chalinze hivi ni Wilaya gani katika nchi hii unaipata ya namna hiyo, Wilaya gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaye Mkuu wa Wilaya mchapa kazi, tuna Mkurugenzi mchapa kazi safi kabisa, lakini kuna maeneo tangu waje hawajawahi kufika na huwezi kuwalaumu kwa sababu kwenda kama Matagata lazima ajaze full tank gari na bado kuna mafuta mengine yanatakiwa yawe kwenye dumu. Sasa gharama za uendeshaji wa namna hiyo nani ataziweza. Tumekubaliana kwamba tuanzishe ajenda ya kisheria iende kama sheria inavyotaka, kwamba tupitishe kwenye Kamati za Vijiji, kwenye Kata, iende Wilaya, iende Mkoani halafu ije kwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuwa Nzega alisema kwamba yeye hatarajii kuanzisha Wilaya mpya wala Mkoa mpya, kwa hiyo, hapo viongozi wanakuwa na kigugumizi kidogo namna ya kutekeleza hii.

Naomba kwa makusudi kabisa namuomba Mheshimiwa Rais huko aliko kwa makusudi kabisa, Sikonge tupate Wilaya mpya na ninajua hili Mkuu wangu wa Wilaya na Mkuu wangu wa Mkoa wananisikia hapa na nimeishazungumza na Mheshimiwa Waziri Mkuu suala hili ni muhimu sana, kama mwananchi wa Matagata anahitaji kumuona Mkuu wa Wilaya anatakiwa atumie siku tano, siku tatu za kusafiri, siku tatu za kurudi nyumbani, siku sita, kwa uchache kabisa siku nne, sasa kwa nini wananchi katika nchi hii moja wawe wanapata adhabu na wananchi wengine hawapata adhabu kama hizo. Kwa hiyo, tunaomba sisi Sikonge tupate Wilaya mpya, Mheshimiwa Rais akubali tupate Wilaya mpya. (Makofi)

La mwisho tuna sababu nyingi lakini sababu kubwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nianze kwa kupongeza kwa dhati kabisa Serikali kwa mambo manne makuu yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza, Serikali kutekeleza uamuzi wa miongo minne iliyopita wa kuhamia Dodoma, naipongeza sana. La pili, viongozi wa sekta za muungano na zisizo za muungano kuendeleza mashauriano chanya yenye nia ya kudumisha Muungano. Tatu, Serikali kukamilisha Kituo cha Kuhifadhi Taarifa na Takwimu za Serikali (Government Data Centre) ili kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa taarifa za Serikali. Hii ni pamoja na program ya kielektroniki ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na ahadi za Rais na viongozi wakuu wengine wa Kitaifa. La mwisho, hatua za kuboresha usimamizi kwenye sekta za mazao ya biashara ya korosho, pamba na tumbaku. Hili nampongeza kwa dhati sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kauli mbiu ya HAPA KAZI TU inaendelea kuthibitika, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina mchango katika maeneo machache, nikianza na afya. Uamuzi wa Serikali wa kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya ni wa takribani miaka 10 iliyopita. Kwenye hotuba ya Waziri Mkuu haijasisitizwa wito huo wa kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya. Nilitegemea Serikali ije na mkakati wa makusudi wa kusaidia Halmashauri angalau vijiji vitano kila mwaka viwe na zahanati na angalau kata tatu kila mwaka zipate kituo cha afya. Angalau hiyo inaweza ikaonesha utekelezaji lakini naamini hata kwenye bajeti ya Wizara ya Afya mkakati huo haupo. Naomba sana kama uwezekano upo wa kurekebisha hapo, tuweze kufanya marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, sekta ya kilimo. Sisi kule Sikonge tunalima sana tumbaku. Kitu ambacho nataka niongelee hapa pekee ni kiwanda cha kuchakata tumbaku cha Morogoro. Kiwanda hiki kilibinafsishwa na waliopewa kiwanda hiki na Serikali ni TLTC na Alliance One ambao kwa bahati mbaya sana hao nao ni wanunuzi wa tumbaku. Kwa hiyo, huwezi kupata good governance na fair competition ambapo wanunuzi hawa wawili wanamiliki kiwanda halafu kuna kipengele cha sheria ambacho kinawalazimisha wanunuzi wote, wao wenyewe pamoja na wengine kwamba hawaruhusiwi kusafirisha nje tumbaku hadi ipelekwe pale kwenye kiwanda cha Morogoro kuchakatwa. Kwa hiyo, ina maana kwamba, hiyo inazuia fair competition kwa wanunuzi wengine ambao sio wamiliki wa hicho kiwanda kwa sababu kuna uwezekano wakapewa rate ambazo ni tofauti na zile ambazo wanazitumia wao wenyewe ambao ni wamiliki wa kiwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suluhisho hapo kwa Serikali ni moja tu, aidha kukitaifisha kile kiwanda kirudi mikononi mwa Serikali au apatikane mtu mwingine akinunue tena kile kiwanda ambaye sio mnunuzi wa tumbaku au kufuta kile kipengele cha sheria ambacho kinalazimisha wanunuzi wote kuchakata tumbaku pale ili wengine wapate sehemu nyingine ya kupeleka kuchakata tumbaku badala ya pale. Hapo ndiyo wanunuzi wengi wa tumbaku watakuja Tanzania hapa na mkulima atanufaika kwa kuongeza ushindani kwenye zao la tumbaku, huo ni ushauri wa pili.
Mheshimiwa Spika, wa tatu ni kwenye eneo la utawala. Wilaya yangu ya Sikonge ina eneo kubwa sana. Kuna watu kule Matagata ili aweze kufika Sikonge Makao Makuu ya Wilaya analazimika kutembea kilometa 400. Ile Tarafa ya Kitunda ina wakazi 85,000 na wako mbali kwelikweli
na Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, mimi nilisoma Marekani, niliwauliza Abraham Lincoln alitumia kigezo gani kikubwa kuanzisha county ambayo ni sawasawa na wilaya zetu hapa? Alitumia uwezekano wa mtu kutembea na chombo cha usafiri cha kawaida cha wakati ule, farasi, atoke nyumbani kwake saa 12.00 asubuhi, aende Makao Makuu ya Wilaya amalize shida zake arudi nyumbani kabla jua halijatua, ndiyo kigezo ambacho alitumia. Mheshimiwa Spika, kama usafiri wetu wa kawaida ni baiskeli, tunamtegemea na mwananchi wa Matagata atoke Matagata aende kwa Mkuu wa Wilaya akamalize shughuli zake arudi nyumbani kabla jua halijatua. Ingawa kigezo kile hatuwezi kukifikia basi tumpunguzie mzigo huyu mwananchi. Kwa hiyo, ombi letu litakapokuja kwa Waziri Mkuu la kuanzisha Wilaya Mpya kwenye Tarafa ya Kitunda naomba lipate support ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la nne ambalo napenda nilizungumzie ni elimu. Tunaomba Serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha tunakuwa na usawa wa uwiano wa walimu na wanafunzi katika nchi nzima. Ipo mikoa hapa Tanzania ina ziada ya walimu, ipo mikoa kama Tabora ina upungufu mkubwa sana wa walimu. Kule ambako kuna ziada inatakiwa isawazishwe na kule ambako kuna upungufu ili ule uwiano wa 1:40 upatikane kwa mikoa yote badala ya mikoa mingine kuwa na walimu wengi mpaka na wa ziada ambao hawana kazi, wanasukana nywele tu kwenye shule na mikoa mingine ina upungufu mkubwa wa walimu. Naomba sana hili lisimamiwe na Waziri Mkuu, maana Wizara ya Elimu
wameshindwa kulitatua kwa miaka 10 iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nataka nilizungumzie ni eneo la barabara. Sisi kule kwetu tuna barabara mbili za kiwango cha changarawe ambazo ni muhimu sana. Barabara ya Ipole–Rungwa kilometa 182 na Sikonge–Mibono–Kipili kilometa 280. Barabara ya Ipole–Rungwa ilitengenezwa tu pale ambapo Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokuja Sikonge akatembelea Kitunda, tarehe 10/3/2010. Akatoa amri, nataka hii barabara itengenezwe kwa vyovyote vile. Wewe Regional Manager hakikisha unapata hela za kutengeneza hii barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba basi Rais apange safari ya kuja Sikonge ili aende Kipili ili na hiyo barabara ya Sikonge – Kipili nayo itengenezwe. Maana hao watu wa Wizara ya Ujenzi wanatwambia hakuna hela.
Mheshimiwa Spika, naomba niishie hapo. Ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii muhimu na adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai na uzima. Nikushukuru wewe kwa kuniruhusu na mimi nichangie ingawa kwa ufupi mapambano ya UKIMWI pamoja na kuendelea ndani ya nchi yetu lakini inaonekana bado UKIMWI unaongezeka pamoja na maambukizi mapya na kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa basi Taifa letu litafika pabaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa UKIMWI umekuwa uko sirini sana kiasi ambacho watu wengi wamekuwa na matumaini makubwa kwamba UKIMWI umepungua kwa style za watu zilivyo. Watu ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI si rahisi kuwatambua kama hajajieleza mwenyewe. Hii inatokana na kuitikia wito wa kujiunga na vituo vya dawa za ARV, kwa hiyo, watu wengi kwa kupungua athari za kuonekana moja kwa moja wanadhani UKIMWI umepungua. Kwa hiyo, ushauri wangu, mikakati na juhudi ziendelee kuelimisha Watanzania kwamba UKIMWI upo na bado unaua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wa UKIMWI wametoa taarifa kwamba Mkoa wa Njombe unaongoza kwa UKIMWI ambao una 14.8% hii ni asilimia kubwa na ya kutisha. Naomba Serikali ifanye utafiti ni jambo gani linalosababisha maambukizi makubwa kiasi hiki katika Mkoa huu, tatizo lijulikane, itolewe elimu ya uhakika kuondoa tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie kuhusu wazee. Tunafahamu fika kwamba wazee wa sasa ndio vijana wa juzi na jana ambao walijituma kwa utumishi uliotukuka na mafanikio ya utumishi wao mwema ndiyo uliolifikisha Taifa letu hapa lilipo. Hivyo, naishauri Serikali kutokuwasahau na kuwadharau wazee ambao ndiyo waliokuwa dira ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha ni kwamba, wazee hawapati huduma inavyopasa na badala yake wazee wanaonekana kama hawakuwa na mchango wowote katika Taifa hili. Mfano, katika huduma za matibabu, wazee wamekuwa wakisumbuka kana kwamba hawastahili kupatiwa huduma hii. Wamekuwa wakitozwa malipo makubwa ambayo hawayamudu lakini ni haki ambayo imeidhinishwa na Serikali kupatiwa. Naishauri Serikali kuweka kipaumbele juu ya kuwajali wazee kwa kuwapatia huduma wanazostahili. Serikali ina nia na dhamira thabiti juu ya wazee ila inaonekana changamoto hii inayowakumba ni utendaji mbovu usiojali mchango wa wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia hoja yangu, napenda kugusia angalau kidogo suala la mazoezi ya viungo kwa jamii. Mazoezi ni jambo muhimu sana kwa afya ya mwanadamu na michezo ni sehemu ya mazoezi. Kwa hivyo, michezo ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii na kiuchumi na hasa katika kuimarisha miili yetu kiafya na kuwa wakakamavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imekumbwa na magonjwa mengi sana ambayo kama tungekuwa makini na mazoezi tusingeathiriwa sana na magonjwa haya. Mfano wa magonjwa hayo ni kama vile kisukari, moyo na kadhalika. Magonjwa haya kwa ujumla wake yanaitwa magonjwa sugu yasiyoambukiza na yanayogharimu pesa nyingi za wananchi na Serikali. Naishauri Serikali na Wizara ya Afya kuhamasisha jamii kuhusu suala zima la kufanya mazoezi na kutoa misaada pale inapobidi ili kuendeleza mazoezi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo itaendelea kutekelezwa chini ya uratibu wa mipango shirikishi ya maendeleo ya sekta ya kilimo katika Halmashauri zetu n Na kwa kweli utaratibu huu utakuwa mzuri zaidi na utafanikiwa zaidi kama watu wetu watakuwa wamejitolea kusimamia vizuri kwa mujibu wa taratibu na sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo ndipo tunapoagiza na tayari Serikali imeshawaagiza watumishi hasa Maafisa Ugani na Maafisa Kilimo, wahakikishe kwamba mipango ya maendeleo ya sekta ya kilimo katika Halmashauri zetu lazima itekelezwe kwa umakini na weledi wa hali ya juu. Na tunawaamini, watumishi ambao walikuwa wamezoea kuweka kambi katika makao makuu ya Halmashauri hawawatembelei wakulima, Serikali imeshatoa maelekezo kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba lazima wawatembelee wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii kama tutaendelea kuona kwamba kuna uzembe kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi wamelalamika hapa, tutaanza kuchukua hatua kali, kwa sababu maelekezo haya ya Serikali ni halali. Lazima wakulima wapate haki yao ya kupata elimu ambayo inatoka kwa watu ambao wameajiriwa na Serikali, na hawa ni pamoja na maafisa walioko katika Halmashauri, Kata na katika Vijiji, lazima wafanye kazi zao. Utaratibu wa kusubiri posho, kwamba lazima kuwe na posho ndiyo mtu akafanye kazi yake ambayo ameajiriwa kuifanya, tumeshaupiga marufuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kupata kilimo bora kama hakuna elimu bora ya kilimo, na ndiyo maana tunawasisitiza hawa jamaa waweze kufanya kazi yao ambayo wameajiriwa kuifanya, hii ni pamoja na Maafisa Ushirika. Maafisa Ushirika wameshaelekezwa kwamba lazima Maafisa Ushirika wahakikishe wanafanya mapitio ya vyama vya ushirika vya msingi vilivyopo katika maeneo yao kuona utendaji wa vyama vya ushirika kama ni mzuri. Ili kama utendaji wao ni mbovu waweze kuvifuta na kuvisajili upya vyama ambavyo vitawasaidia wakulima. Hayo ni maelekezo halali ya Serikali na sisi tutaendelea kuyasimamia na kuyafuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani wameshaelekezwa wafanye mazoezi ya kuwatambua wakulima wote na mahitaji yao ya pembejeo ili Serikali ifanye maandalizi mazuri na mapema ya pembejeo, kwa hiyo hilo nalo tutaendelea kulifuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani nisiseme sana kwa sababu mwenye sekta mwenyewe yuko hapa, wale watu ambao wako chini ya TAMISEMI waipatepate huko waliko, wajue kwamba sisi tuko macho tutaendelea kuwafuatilia kuhakikisha kwamba uzembe wa aina yoyote hautavumiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, sana kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi swali langu la kwanza kwenye Wizara hii ningependa kuuliza, hivi nchi hii tuna Chuo cha Waamuzi wa Michezo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza hivi kwa sababu uamuzi ni tatizo kubwa sana. Waamuzi wamekuwa wakilalamikiwa sana mpaka wakati mwingine mtu unafikiria hivi hawa waamuzi au wanahongwa rushwa au wanapewa maelekezo na mtu fulani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati alilalamikiwa sana Waziri wa Mambo ya Ndani kwamba labda anatoa maelekezo, pengine labda kweli au wanamsingizia, lakini inawezekana. Sasa mambo kama haya naomba sana Wizara hii ituambie hivi tuna Chuo cha Waamuzi ambapo kuna curriculum inafundisha uamuzi wa mpira wa miguu, mpira wa pete, volleyball na michezo mingine kwa ujumla?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza kwa Mheshimiwa Waziri atakaposimama atueleze uamuzi wa michezo katika nchi hii curriculum yake iko wapi? Kama hakuna basi kama Taifa inatakiwa tuanzishe curriculum ya uamuzi michezo au chuo maalum cha watu kujifunza uamuzi badala ya kutegemea mafunzo ya muda mfupi kutoka kwa waamuzi ambao wana-experience na watu wengine wanatoka nje ya nchi wanakuja hapa wanafundisha brushing, hilo ni tatizo kubwa sana kwenye michezo.

Suala hili Mheshimiwa Waziri atakaposimama alieleze vizuri na hata Waziri wa Mambo ya Ndani naye kwa sababu anatajwatajwa asimame maana timu zinakwenda zinafungwa hovyo hovyo kwa sababu inaaminika bingwa huwa hapatikani kwa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu programu za michezo mashuleni na vyuoni ni jambo la muhimu sana Wizara hii kwa kushirikiana na Waziri wa Elimu na TAMISEMI wasimamie programu hizi. Nchi nyingi zimefanikiwa sana katika michezo kwa kupitia programu za michezo mashuleni na vyuoni. Kuna wakati zilifutwa, lakini nashukuru Serikali wamerudisha tena lakini uratibu wake hauendi vizuri sana kwa sababu gharama ni kubwa, wanaogopa gharama. Mimi naomba sana kwa kushirikana ndani ya Serikali Wizara kama mbili au tatu wahakikishe programu za michezo mashuleni na vyuoni zinafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ambalo napenda kuzungumzia ni academy za michezo au vyuo vya michezo. Nasikia kule Mwanza kuna Chuo cha Michezo lakini hicho chuo kimoja tu hakitoshi kwa nchi nzima hii. Nchi hii ni kubwa sana, mikoa yetu inahitaji angalau chuo kimoja kila mkoa, hicho kingefaa lakini sasa kwenye mpango wa maendeleo wa Wizara hii hakuna hata pendekezo. Mimi nadhani ili tuwe serious tutoe vijana ambao watashindana katika ngazi za kimataifa ni muhimu sana vyuo vya michezo vya watoto wadogo viwepo angalau kimoja kila mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuzungumzia ni suala la utamaduni, mwenzetu mmoja nimemsikia amezungumzia ngoma za asili. Hili suala la ngoma za asili limeachwa nyuma kabisa, sio kwenye television tu peke yake hata kwenye redio, zamani RTD ilikuwa kuna programu maalum kabisa ya ngoma za asili siku hizi hamna. Watu wanacheza miziki ya Marekani labda wataishia kucheza bongo fleva lakini ile tumbuizo asilia hakuna. Hilo ni tatizo kubwa sana. Wale wanaotoa leseni kwenye vipengele vya maelekezo ndani ya leseni wanatakiwa wawaambie na wafuatilie vituo vya television na redio lazima wazingatie kucheza ngoma zetu za asili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kuhusu ngoma za asili ni kuhakikisha kunakuwa na programu maalum hasa wakati ambao ni wa mapumziko vijijini. Kuna wakati ambao wakulima wameshavuna, zamani kulikuwa na matamasha ya ngoma za asili katika kila Wilaya, angalau wakati ule hasa hasa mwezi wa sita au wa saba wakati watu wamevuna hawana kazi nyingi za shamba, kipindi kile kingekuwa sasa kila Wilaya inaratibu tamasha la ngoma za asili ili kuhakikisha kwamba tunaendeleza utamaduni wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo naamini Mheshimiwa Waziri atatolea ufafanuzi na atazingatia kwenye kwenye hotuba yake.
The Finance Bill, 2016
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mimi niseme wazi kwamba naunga mkono sheria hii ipitishwe na Bunge ili Serikali iweze kukusanya mapato na bajeti yetu iweze kutekelezeka kwa sababu bila sheria bajeti haitatekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maoni machache tu kwenye sheria hii. Kwenye Sehemu ya Pili, inapendekezwa kwamba Bodi ya Bima ya Amana waongezewe muda kutoka miezi mitatu hadi miezi sita ili waweze kutayarisha ripoti yao. Napendekeza miezi iwe tisa au kumi kwa sababu CAG amepewa na sheria muda hadi tarehe 31 mwezi Machi kuweza kutoa ripoti zake za kila mwaka. Sasa kama ripoti ya CAG itachelewa na sisi tumewapa hawa miezi sita tu yaani kuanzia mwezi wa Julai hadi Desemba maana yake ni kwamba hawataweza kuandaa hiyo ripoti mapema na inaweza ikaathiri isipatikane hiyo ripoti. Kwa hiyo napendekeza miezi kumi badala ya miezi sita ambayo walikuwa wamepewa hapo awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sehemu ya Sita kwenye miamala ya simu, najua imeongezeka kodi ya asilimia 10. Najua kuna makampuni yameanza kutoa taarifa kwenye magazeti, napendekeza Benki Kuu, Wizara ya Fedha na TCRA washirikiane, wasimamie wananchi wasitozwe kodi au wasitozwe gharama zaidi kwenye suala hilo. Haya makampuni yanapata faida kubwa sana wananchi wasiongezewe gharama kwenye miamala badala yake makampuni yachajiwe kutokana na faida wanayopata wao wenyewe siyo kumuongezea mwananchi gharama kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo nataka niliseme, nchi yetu sasa inaingia kwenye hatari na ni hatari kubwa. Hawa wenzetu ambao wanapewa maelekezo na Kiongozi wao wa Upinzani Bungeni, sasa hivi hawatusalimii sisi Wabunge wa CCM. Hii ni chuki kubwa sana ikioteshwa katika nchi yetu inaweza ikasababisha Taifa letu hili liparaganyike. Wanafanya hivyo hata kabla hawajapata mamlaka, hivi watakapochaguliwa wao waongoze Serikali halafu sera zao ni hizo za kueneza chuki kwa wananchi, wananchi wasisalimiane, wananchi wasisali pamoja, wananchi wasiende pamoja kanisani, wasiende pamoja misikitini, wasipande mabasi pamoja, hivi itakuwaje, nchi hii itakuwa ni nchi ya aina gani na wao ndio wanatafuta kura kwa wananchi. Niliona niliseme hili ili kama huko waliko wanasikia au kama rafiki zao au watu wao au viongozi wao wanasikia wawakemee kwa sababu hilo taifa la chuki ya namna hiyo halitaweza kuendelea, tutaendelea kupata shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwangu yalikuwa ni hayo tu, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana ni vigumu sana mimi kuchangia vizuri sana kwenye hii Wizara kwa sababu kuna wakati Waziri Maghembe akiwa Waziri wa Maji nilikuwa mshauri wake, lakini kwa sababu mimi sasa hivi ni Mbunge wa Jimbo, inabidi nichangie vizuri kwa kutumia nukuu nyingi hasa za Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 8(1) ya Katiba inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya Kidemokrasia na haki ya kijamii na kwa hiyo (a) wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba; (b) Lengo kuu la Serikali litakuwa ustawi wa wananchi; (c) Serikali itawajibika kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 9 kuhusu mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha kuwa; (i) kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada za kuondosha umaskini, ujinga na maradhi.

Sasa kwenye wajibu wa kulinda maliasili, Ibara ya 27(1) kila mtu anawajibu wa kulinda Maliasilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi, na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi na pia kuheshimu mali ya mtu mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ndogo ya (2) watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali za mamlaka ya nchi ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu na kuendesha uchumi wa Taifa kwa umakini, kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haki ya kufanya kazi, Ibara ya 24(1) bila kuathiri masharti ya sheria za nchi, zinazohusika kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi kwa mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria. Sasa hapa kidogo nita-pause.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu ambao wananyang’nywa mali zao, mifugo, hasa ng’ombe bila fidia, hiyo inavunja Katiba, na wakati mwingine wanapigwa faini za mamilioni kwa risiti fake, hiyo ni kuvunja sheria za nchi na kuvunja Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na wakati mwingine katika risiti zile ambazo zingine mimi ninazo Mheshimiwa Profesa akizitaka mimi nitampatia, risiti imeandikwa hii umepigwa faini kwa ajili ya posho za viongozi, sasa kama posho ile huwa inakuja mpaka kwa Waziri mimi sijui, lakini risiti ninayo na imeandikwa faini hii umepigwa kwa ajili ya posho za viongozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Ibara 24(2) bila kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1) ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake, kwa madhumuni ya kutaifisha au madhumuni mengineyo bila idhini ya sheria ambayo imeweka masharti ya fidia inayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba, hii ambayo mimi ninainukuu hapa ambayo ndiyo Katiba yetu inakataza kutumia sheria ambazo zinanyang’anya mali ya wananchi bila fidia. Kwa hiyo mimi naomba sana tujitathimini kama Taifa, kama hatua zile kama zinaelekezwa na sheria hizo, basi sheria hiyo ni mbovu, na inatakiwa iletwe hapa tuirekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie masuala yanayohusu Jimbo langu la Sikonge. Jimbo la Sikonge au Wilaya ya Sikonge kwa asili yake hiyo Wilaya siyo ya wafugaji, lakini leo wafugaji wamekuja wengi sana kwa sababu ya makosa ya Serikali. Kosa la kwanza la Serikali, mwaka 1959 baada ya kuonekana kwamba kuna uharibifu wa mazingira katika maeneo ya wafugaji yaliyo mengi, Gavana alitoa order kwamba mifugo ipunguzwe hadi chini ya 100 kwa kila mfugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini order ile ilichelewa kutekelezwa mpaka tukapata uhuru, tulivyopata uhuru Mwalimu Nyerere akawatetea wafugaji kwamba hii mifugo sio mingi ukilinganisha na ukubwa wa nchi. Nchi bado tunayo kubwa sana, kwa hiyo, hawa wafugaji kama wanaharibu mazingira huko wanaweza wakasambazwa katika maeneo mengine ya nchi na wakapata huduma yao bila tatizo lolote la uharibifu wa mazingira. Na ndio maana Sikonge kukawa na wafugaji leo wengi na maeneo mengine wamekwenda mpaka Lindi kwa sababu ya order ya Mwalimu Nyerere ya mwaka 1961.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Mwalimu Nyerere aliwatetea, kwa nini sisi tumeweka sheria ambazo zinawanyanyasa? Kwa nini tumeweka Sheria ambazo zinakuja kuwabugudhi Watanzania hawa ambao walitetewa na Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa la pili la Serikali; mwaka 1968 – 1974 operation vijiji kule Sikonge vijiji vya zamani vilivyokuwepo wakati wanapima maeneo ya hifadhi, vilikuwa mbali na maeneo ya hifadhi, wakati wa vijiji vya ujamaa, vijiji vya ujamaa vikapelekwa mita 100 kutoka kwenye hifadhi, unategemea nini kama umemuweka mwananchi mita 100 kutoka kwenye hifadhi, lazima ataingia kwenye hifadhi, kule kwenye hifadhi kuna miti, asali, nta, na mazao mengine ya misitu, ataingia tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima kuwa na utaratibu ambao unalinda maslahi ya wananchi kwa sababu Serikali yenyewe ndiyo imechangia kufanya makosa mengi, nataja maeneo kama Ngoywa, Kipili, Kilumbi, Kiloleli, Usunga, Igigwa, Nyahwa, Mole, Ipole, Chabutwa, Kisanga, kata kumi kati ya kata 20 zote ziko karibu na hifadhi au ziko ndani ya hifadhi, viijiji 29 kati ya vijiji 71 vya Wilaya vyote viko karibu na hifadhi au ndani ya hifadhi. Sasa unategemea nini na Serikali yenyewe ndiyo imewapeleka karibu na hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanafaya uchaguzi, wana shule, umeme, kila huduma imepelekwa kule, leo hii unakuja unaweka beacon unasema hili ni eneo la hifadhi mhame. Karibu nusu ya watu wa Sikonge utawapeleka wapi, na ndiyo maana hoja ya Mheshimiwa Nape ya kusema Serikali iteue Kamati Maalum na kwa Sikonge iwe case study ninawaomba mje Sikonge mkae na DC, sisi tuna DC mzuri sana, kwanza hata kama mtakaa naye tu mimi sipo, mimi naunga mkono kila mtakachofanya kwa sababu yule DC yuko makini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nisisitize maeneo haya ya hifadhi yalipimwa mwaka 1954 na maeneo mengi upimaji ulikamilika mwaka 1956 wakati wanapima watu katika Wilaya ya Sikonge ya sasa watu walikuwa 16,000 leo hii kwa projection kwa kutumia formula ya NBS watu wanakaribia 300,000 katika Wilaya ya Sikonge. Sasa watu 16,000 wakati unapima, leo watu 300,000 eneo lako bado lilelile bado unadai kwamba watu waendelee kuishi kwenye eneo lile lile lenye ukubwa ule ule. Eneo la Wilaya ya Sikonge, kilometa za mraba 27,873 eneo ambalo watu wanaruhusiwa kuisha kisheria ni kilometa za mraba 1,049 asilimia 3.7; waende wapi hawa watu 300,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Kamati hiyo ije Sikonge tukae nayo na tuwaelekeze maeneo mengine ambayo yamekosa sifa za kuendelea kuwa hifadhi na mapori ya akiba yaondolewe kwenye utaratibu ili wananchi wapate kujitanua. Ng’ombe wakati wanapima walikuwa 2,500 leo tuna ng’ombe karibu 200,000 sasa tufanye nini katika hilo na kwa nini wananchi wamekuwa wanadhalilishwa na wanaonewa kwa sababu ya makosa ya Serikali kama nilivyoainisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwisho kabisa naomba sana njooni Sikonge, tukae kwa pamoja, sisi wote lengo letu moja, tunataka tulinde maliasili zetu, tunataka tulinde mazingira yetu na wananchi wako tayari, isipokuwa tu ramani zile zipimwe upya na wananchi tutaelimishana namna ya kulinda mazingira namna ya kulinda hifadhi zetu, zile ambazo zitakuwa zimepunguzwa ili kusudi kila mtu aweze kupata...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Suala hili linalozungumzwa hapa la sekta ya elimu ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yoyote ile, siyo Tanzania peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi hapa na Waheshimiwa Wabunge na mengine kwa kweli yanahusu masuala ya maadili. Na mimi nitapingana kidogo na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ambao ni wanaharakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo sheria nyingi sana hapa nchini nzuri sana, mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 ndipo yalipotokea mapinduzi makubwa sana ya sayansi na teknolojia, tukawa na tv na simu na hizi zimeleta matatizo makubwa sana kwenye mmomonyoko wa maadili ya vijana wetu. Kutokana na mmomonyoko wa maadili ulivyokuwa unatishia haki za wanawake na haki za watoto. Mwaka 1998 ilitungwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, Sura ya 101 ya Sheria za Tanzania. Sheria hiyo ni muhimu sana, isipokuwa tatizo letu sisi hapa Tanzania, tuna sera na sheria nzuri lakini zimekuwa hazitekelezwi. Matokeo yake tunakuwa tunapigia kelele jambo ambalo linaweza likadhibitiwa na sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ilirekebisha baadhi ya vifungu kwenye Penal Code (Sheria ya Kanuni ya Adhabu) na ikaweka utaratibu mzuri wa namna ya kushughulika na masuala ya maadili kwa ujumla. Makosa yanayofanywa na mwanaume, yanayofanywa na mwanamke, yamewekwa vizuri sana na adhabu zake zimewekwa vizuri sana, lakini utekelezaji hafifu wa sheria hiyo ndiyo maana unakuta baadhi ya Wabunge hapa wanasimama wanaanza kupiga kelele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tumepitisha sheria hapa ambayo inadhibiti mtu yeyote anayedunga (anayempa) mimba mwanafunzi, anayeozesha mwanafunzi, anayekwenda kwenye harusi ya mtoto mwanafunzi adhabu zake ni kifungo cha miaka 30. Sasa hata hatujasimamia utekelezaji wa sheria hiyo tunasimama hapa tunasema watoto wenye mimba waruhusiwe kusoma, sawa, lakini tukipitisha hapa sheria ikasema kwamba watoto wanaopata mimba shuleni waendelee kusoma maana yake ni kwamba wote watapata mimba...

Na hiyo itakuwa ni hatari, aidha, wote au walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifuatilia vizuri hizi sheria zenyewe zinadhibiti. Kwa mfano, kwenye Ilani ya Uchaguzi tumesema kwamba mtoto aanze kusoma darasa la kwanza mpaka amalize form four. Huyo mtoto ambaye atamaliza form four yuko chini ya miaka 18 ni yupi? Taratibu tukizifuatilia vizuri, anayedunga mimba miaka 30, ambaye anaacha shule naye vilevile atafutiwe adhabu kwa sababu tunapitisha sheria hapa tuwe na utaratibu mtu aanze darasa la kwanza hadi amalize form four. Akimaliza form four ameshafika miaka 18 basi hapo tutakuwa tumetatua tatizo la mimba mashuleni na kila kitu.

Kwa hiyo, naomba sana iwe tu kwa yule aliyebakwa, kama kuna ushahidi kwamba amebakwa, hapo kwa kweli inabidi tuwe na hatua zile za kuruhusu kwamba aendelee na shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie masuala ya Jimbo langu la Sikonge. Kule kwetu Sikonge, naomba Mheshimiwa Waziri asikie, bado tunahitaji shule mpya, zile shule ambazo zilijengwa kwa mpango wa MMEM zilitusaidia sana lakini bado tuna maeneo mengi yanahitaji shule mpya kabisa na sisi Halmashauri hatuna uwezo wa kujenga shule mpya na Serikali imeondoa utaratibu wa kujenga shule mpya, hapa ametamka shule sijui tatu au nne katika maeneo maalum. Mimi naomba aiweke Sikonge katika utaratibu wa Serikali kusaidiwa kujenga shule mpya, tuna maeneo takribani
30 ambayo yanahitaji shule mpya. Watoto wetu wanatembea kilometa tisa, kumi, kufuata shule na ni wengi. Kwa hiyo, naomba sana Serikali izingatie, iturudishie mpango wa MMEM maalum kwa ajili ya Wilaya yetu ya Sikonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mafunzo ya ufundi. Sisi Sikonge tuna maeneo mazuri mawili, naomba Wizara ya Elimu iwasiliane na Halmashauri yangu ili kusudi tuone potential hizo mbili, mojawapo kijengwe Chuo cha Ufundi cha VETA. Tayari tumeshawekeza baadhi ya fedha katika maeneo hayo, ni suala la kuendeleza tu, kuna chuo cha FDC pamoja na Kituo cha Vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo napenda kuongelea ni mgawanyo wa walimu. Baadhi ya maeneo hapa nchini yamekuwa yanaathirika sana katika matokeo kwa sababu ya mgawanyo wa walimu ambao hauko sawa. Kuna baadhi ya maeneo ya nchi hii yana ziada ya walimu na baadhi ya maeneo yana upungufu mkubwa wa walimu. Kwetu sisi Tabora tuna upungufu mkubwa sana wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana katika maeneo ambayo yana ziada ya walimu wapunguzwe waletwe Tabora na maeneo mengine ya nchi ambayo yana upungufu wa walimu yafanyiwe hivyo hivyo kama ambavyo napendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kusema mengi sana, haya yanatosha, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nipongeze kazi ya Kamati mbili na wachangiaji wote wamefanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, viwanda vyetu ya Agro-Processing ambavyo ni priority namba moja; viwanda vya kubangua korosho, vya kusindika alizeti, ufuta, pamba, kuzalisha mafuta ya kula, viwanda vya nguo, viwanda vya bidhaa za ngozi vinahitaji hatua madhubuti za kuvilinda dhidi ya ushindani wa aina mbili. Kwanza, ushindani wa bei ya malighafi kwenye soko unaosababisha viwanda vyetu kukosa malighafi na pili, bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda hivyo kushindwa kukabiliana na bidhaa za aina hiyo hiyo zinazoagizwa kutoka nje ambazo hata tukitoza kodi asilimia 35 bado bei ya bidhaa hizo sokoni inakuwa ndogo kwa sababu huko zilipotoka zilizalishwa kwa mamilioni ya tani kwa gharama ndogo ya jumla kwa ajili ya soko zima la dunia kulinganisha uzalishaji mdogo wa hapa nchini wa mia na maelfu ya tani ambayo yanalenga soko dogo la ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo, upo umuhimu mkubwa wa kuchukua hatua za lazima. Kwanza, kuhakikisha viwanda vyetu vinakuwa na uhakika wa kupata malighafi na hatua ambazo zitapendekezwa na wataalam zitatusaidia sana kupata maamuzi sahihi kwa ajili ya kulinda viwanda vyetu vya ndani. Pili, tunahitaji kutengeneza utaratibu wa makusudi wa kukabiliana na wimbi la waingizaji kutoka bidhaa kutoka nje kwa kutumia viwango maalum vya kikodi vitakavyotozwa kwa utaratibu wa kutoza kwa tani badala ya asilimia ambayo itasaidia kulinda viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Spika, kilimo chetu kinahitaji mbolea kama kweli tunataka kuongeza uzalishaji kwenye sekta ya kilimo. Uagizaji wa mbolea kutoka Ulaya hadi mbolea imfikie mkulima umekuwa ukigharimu fedha nyingi mno kwa mkulima. Serikali imeshawakaribisha wawekezaji kujenga viwanda vya mbolea hapa Tanzania, tunachotaka sisi ni ukweli na uwazi kwenye uwekezaji. Tunajua mwekezaji anahitaji mtaji ili awekeze lakini mtaji ule sisi tuna maslahi nao tunataka tujue, mtaji ule ndiyo unaotafsiri gharama za mitambo, majengo, teknolojia, uendeshaji ikiwepo kulipa wafanyakazi na usafiri na usafirishaji hadi kwenye soko. Pia ni lazima tujue tunamsaidiaje mwekezaji kupata malighafi anazohitaji kwenye kiwanda kutoka ndani ya nchi na kwa gharama gani?

Mheshimiwa Spika, ili tujue vizuri lazima tulinganishe model yake ya kifedha na ile model ya mfano ambayo imetengenezwa na wataalam wa Serikali ili tuweze kubaini hasa hasa je kuna udanganyifu au hakuna kwa sababu bila kufanya hivyo tutaingia kwenye machaka ambayo tuliwahi kuingia zamani. Kwa mfano, katika model moja ya kifedha iliyochambuliwa tulikuta gharama za wafanyakazi wote 1,000 ikiwemo wafagizi wote wamewekewa mshahara wa kila mfanyakazi dola 3,000 yaani Sh.6,430,000 jambo ambalo ni kinyume cha uhalisia kwenye ukweli na uwazi. Kwa hiyo, lazima tuwe makini mno ili kuhakikisha tunalinda maslahi ya Taifa kikamilifu, viwanda vya mbolea vinahitaji gesi asilia kwa mfano na mali ghafi nyingine lazima tujue gezi asilia ataipata kwa gharama gani na faida ya nchi itakuwa kiasi gani.

Mheshimiwa Spika, mwezi huu Februari tunaendeleza mazungumzo na wawekezaji kwenye eneo hili la viwanda vya mbolea na mwelekeo ni mzuri naamini tutafikia makubaliano mazuri. Haiwezekani tukubali kiwanda ambacho eti kitapata hasara kwa miaka zaidi ya 10 wakati ambako ile financial model inaonyesha kuna udanganyifu ambao utamfanya mwekezaji yeye aanze kwa kupata faida ya dola kama 600,000 kabla hata hajaanza uzalishaji halafu ile mizania yake itasoma hasara kwa zaidi ya miaka 10. Kwa hiyo, sasa hivi Serikali ya Awamu ya Tano ipo makini katika kujenga utaratibu wa win win situation ili tunapoingia kwenye kiwanda lazima tuhakikishe faida ya nchi inaonekana kwa wazi na uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.8) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, awali ya yote napenda kutangaza kwamba naunga mkono hoja hii ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini napenda nitoe maoni yangu kwenye maeneo mawili tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni eneo la kuweka utaratibu wa usuluhishi kwenye kesi za madai. Suala hili ni zuri sana kwa sababu kwanza litapunguza mlundikano wa kesi katika mahakama zetu, lakini wasiwasi wangu uko katika wakati Waziri atakapokuwa anatunga kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo Waziri atatunga kanuni inayoweka msuluhishi awe Jaji au Hakimu ambaye hajapangwa kusikiliza kesi hiyo bado huyo Jaji au Hakimu atakuwa hajatoka nje ya mfumo wa mahakama. Kwa hiyo, mimi nilikuwa napendekeza wakati Waziri anatunga kanuni asiweke msuluhishi ambaye hatoki ndani ya mfumo wa mahakama akawa huru kabisa anatoka ka wananchi maana yake anaweza akawa bias anaweza akawa anachukua upande kwa hiyo akaumiza upande fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napendekeza wakati Waziri atakapokuwa anatunga kanuni akumbuke kuweka mtu mwenye status ya ulinzi wa amani ambaye ana madaraka ambayo yanamfanya (yanam-pin) aweze kutenda haki katika usuluhishi huo, hilo ndio jambo la msingi ambalo nilikuwa napendekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kuweka utaratibu utakaomhusisha Mkurugenzi wa Halmashauri kwenye mashauri yanayohusu Serikali za Vijiji na maamuzi yake kisheria ikiwemo hitaji la notice ya siku 90; hili nalo ni zuri sana kwa sababu kwenye Serikali za Mitaa kuna ngazi mbili, kuna ngazi ya juu ya Serikali za Mitaa ambao ni Halmashauri ya Wilaya au ya Mji au ya Jiji. Wale wamekuwa wakilindwa sana kwenye kesi kwa kutetewa na wanasheria wa Halmashauri husika. Sasa hii Serikali ya chini kwa maana ya Serikali za Vijiji na maamuzi yake imekuwa mara nyingi wanaachwa nje kama kuna shauri lolote katika mahakama wanasheria wengi katika Halmashauri na wa Serikali wamekuwa wakisema hayo mashauri hayo kwa sababu yamefanyika kijijini yanawahusu wao wenyewe. Kwa hiyo, baadhi ya vijiji na baadhi ya Wenyeviti wa Vijiji na baadhi ya Wenyeviti wa Vitongoji wamekuwa wakishtakiwa mahakamani in person.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kweli naipongeza sana Serikali kwa kuchukua hatua hii ya kuhakikisha kwamba maamuzi ya kisheria, maamuzi yoyote yanayofanywa katika ngazi ya Serikali za chini za mitaa, nao walindwe na wanasheria wa Halmashauri na wanasheria wa Serikali Kuu. Hilo suala limekuwa ni zuri sana na litasaidia utendaji kwenye Halmashauri zetu nyingi za vijiji na vitongoji na watafanya kazi zao kwa kujiamini kwa sababu sasa watakuwa wanalindwa na sheria, lakini watakuwa wanalindwa na mfumo wetu wa sheria kwa kutetewa na wanasheria wa Serikali. Hili jambo kwa kweli ni zuri sana na naliunga mkono kwa asilimia 100 tumechelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naunga mkono hoja teba nashukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe pole kwa Wanzazibari kwa kufiwa, kwa kuondokewa na Viongozi wawili muhimu, Mheshimiwa Ally Juma Shemuhuna, na Mheshimiwa Ally Fereji Tamimu, Mwenyezi Mungu awaweke mahali pema.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri kwa hotuba nzuri na nizungumze machache tu katika hii Sekta ya Kilimo kwamba ukiacha malighafi ya mazao ambayo wenye viwanda pia wana mashamba kama viwanda vya sukari ambavyo kuna mashamba ya miwa, viwanda vya chai na mashamba makubwa ya mpunga ambayo yana viwanda vyake kama yale ya Kapunga kule Mbarali na viwanda vya maparachichi, tumekuwa tunapata matatizo makubwa kwenye mnyororo wa thamani kwenye viwanda vya mazao ambayo hayana mashamba kama korosho, viwanda vya nguo, viwanda vya kukamua mafuta, alizeti, pamba na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nizungumze machache tu katika hii sekta ya kilimo, kwamba ukiacha malighafi ya mazao ambayo wenye viwanda pia wana mashamba kama viwanda vya sukari ambavyo kuna mashamba ya miwa, viwanda vya chai, na mashamba makubwa ya mpunga ambayo yana viwanda vyake kama yale ya Kapunga kule Mbarali na viwanda vya maparachichi.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunapata matatizo makubwa kwenye mnyororo wa thamani kwenye viwanda vya mazao ambayo hayana mashamba kama korosh, viwanda vya nguo, viwanda vya kukamua mafuta, alizeti, pamba na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni kweli nikiri kwamba tunahitaji uchambuzi wa kina ambao utafanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wengine ili hatimaye tuweke mfumo wa uhakika wa kuhakikisha kwamba viwanda vyetu hivi, hasa ambavyo havina mashamba vinakuwa na uhakika wa kupata malighafi; na hiyo ndiyo itatupatia sustainability ya viwanda vyetu ambavyo vimekuwa vinaathiriwa sana.

Mheshimiwa Spika, ushindani wa bei kwenye soko umekuwa mkubwa kiasi ambacho viwanda vyetu vimekuwa vikipata shida kushindana bei na makampuni mengine ambayo yamekuwa yanatoa bei kubwa sana kwenye soko na matokeo yake viwanda vimekuwa vinakosa malighafi na hivyo kufa. Ukiangalia katika kipindi cha miaka mitano hadi 10 iliyopita viwanda vingi vya korosho vimekufa kwa sababu ya ushindani wa bei kwenye soko na hivyo kukosa maghafi.

Mheshimiwa Spika, kama nchi suala la kuendelea kuuza malighafi yetu kwenye nchi nyingine ni sawa na kuendeleza viwanda, ajira na faida kwenye nchi nyingine, kwa sababu bidhaa hizo a mbazo huzalishwa viwandani baadaye zitarudishwa tena kwenye nchi yetu na kuuzwa na kunuliwa na Mtanzania kwa bei ya juu zaidi. Endapo tutaendeleza mtindo huo hatutajikomboa kiuchumi. Watu wetu wataendelea kukosa ajira na hata faida za kiuchumi zitakuwa kidogo. Kwa hiyo Serikali inalichukulia suala hili kwa uzito mkubwa ili kuanzia mwaka ujao tuwe na mfumo mzuri utakaohakikisha viwanda vyetu vinapata malighafi ya kutosha kwa mwaka mzima na hivyo kulinda ajira na faida zaidi kwa Watanzania na wakati huo huo wakulima waendelee kupata bei nzuri.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la mapendekezo hapa. Wenzetu wamekuwa wanazungumzia mashtaka kwa wahujumu uchumi. Mimi niseme tu kwamba suala hilo ni suala la kisheria na sheria zina utaratibu wake ikiwemo kuwa na ushahidi wa kutosha kukamilisha taarifa za uendeshaji wa mashtaka. Sasa wakati tunamuachia Mwanasheria Mkuu wa Serikali mambo kama hayo tunatambua jambo moja la muhimu kwenye sekta ya korosho; kwamba kabla Mheshimiwa Rais hajachukua uamuzi wa Serikali kumkomboa mkulima kwa kumlipa shilingi 3,300 kwa kila kilo hakuna kampuni ya ununuzi hata moja ilikuwa imefikia offer ya bei hiyo ambayo Mheshimiwa Rais aliamua kuitoa kwa ajili ya kumkomboa mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ajabu ni kwamba mara baada ya Serikali kuanza kuwalipa wakulima shilingi 3,300 kila kilo baadhi ya makampuni yalijitokeza kusema kwamba sasa tupo tayari kulipa hiyo bei ya 3,300 au zaidi. Kwa hiyo hapo kama uchunguzi utaelekea kwenye mambo kama hayo mimi nadhani hapo tutaunga mkono wala hakutakuwa na shaka. Kwa hiyo kama tutachunguza kwa mwelekeo huo, si vibaya.

Mheshimiwa Spika, lakini si afya sana kuwekeza kwenye uchunguzi wa aina hiyo badala ya kuwekeza kwenye ufumbuzi wa kudumu wa matatizo yetu, hususan kuhakikisha viwanda vinapata malighafi na pia wakulima wanapata bei nzuri; kwa maana ya kuweka vizuri mfumo wa masoko ya mlighafi na mfumo wa masoko ya bidhaa za viwandani ili twende vizuri kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusu Indo Power…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa, dakika zimeisha.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, dakika moja tu. Indo Power ni kampuni halali ambayo imesajiliwa kwenye orodha ya makampuni ya Kenya, na hii ilithibitishwa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya na Balozi wa Kenya nchini Tanzania kwa barua rasmi ambazo zipo. Kwa hiyo kampuni hii inafanya kazi kihalali. Sasa kushindwa kuelewana na benki yake kwa ajili ya kutoa fedha za kununua korosho isitangazwe kwamba hiyo ni kampuni ya kitapeli. Ninataka kuthibitisha Bungeni hapa kwamba kampuni hiyo mpaka jana imeendelea kufanya biashara nchini Kenya, Afrika Mashariki na Dunia nzima. Kwa hiyo tumeachana na mkataba huo tunaendelea na kampuni nyingine, korosho zitauzwa na tutatangaza hapa Bungeni kabla Bunge halijaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchnago wangu wa maoni kwenye mapendekezo ya Mpango na muongozo wa Mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake yote kwa jinsi ambavyo wameleta mapendekezo haya na hasa hasa jinsi ambavyo amewasilisha kwa ufasaha mapendekezo haya na niseme tu kwamba bahati nzuri sisi katika Nchi yetu tumebahatika sana kuwa na nguli wa mipango tangu wakati wa uhuru mpaka leo. Nchi nyingine zimekuwa zinakuja kujifunza uandaaji wa mipango katika Nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka tangu enzi za wakina Dkt. Justina Rweyemamu, wakina Profesa Kigoma Malima na sasa Dkt. Mpango, mipango yote imekuwa ni mizuri, kwa kweli ni mizuri sana hata ukiitaza, ukisoma mpangilio wake, malengo, shabaha imekuwa ni mipango ambayo kwa kweli inalenga kumkwamua Mtanzania kutoka kwenye umasikini na kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mipango yetu kuanzia mwaka 2000 tulipoanza kutekeleza dira ya maendeleo ya Taifa, ule mpango wa kupunguza umasikini ambao ulilenga huduma za jamii, uje kwenye MKUKUTA wa kwanza, uje kwenye MKUKUTA wa pili ambao uliunganishwa na mpango wa kwanza wa miaka mitano kwa kweli mipango yote imekuwa ni mizuri sana na leo hii tunakaribia kuhitimisha Awamu ya II au mpango wa pili wa miaka mitano kuelekea kwenye mpango wa tatu wa miaka mitano ili tuendelee kusaidia uchumi wa Nchi hii ufike katika ngazi ya kati ya uchumi Kidunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuko katika mwaka wa nne wa utekelezaji na mpango ambao unapendekezwa leo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha unatupeleka kwenye maandalizi ya mpango wa mwisho wa miaka mitano. Kwa kweli hili ni jambo ambalo tunatakiwa tujipongeze kama Taifa, tunakwenda vizuri. Nchi nyingine huwa wanaishia katikati, wanakuwa na mpango wa miaka 15 (long term) wakifika baada ya miaka mitano wanaacha wanaingia katika kutatua mipango mingine lakini sisi tunakwneda sequentially. Baada ya miaka mitano tunaingia Awamu ya II tunaingia Awamu ya III. Hilo ni jambo ambalo tunatakiwa tujipongeze kama Taifa. Kwa kweli kama nilivyosema mwanzo mipango yetu ni mizuri sana na kazi zinazopangwa kwenye mipango ni nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo au maoteo ya makusanyo huwa ni mazuri sana yanalenga kuhakikisha wkamba mpango unatekelezwa, matarajio ya Watanzania ni mazuri tatizo ambalo ninaliona katika utekelezaji ni dogo sana. Kwa mfano, hadi sasa katika utekelezaji wetu tumekaribia kutekeleza malengo mengi kwenye mpango. Ukiangalia mipango mikubwa, ufufuaji wa Shirika la Ndege, ujenzi wa miundombinu, ukiangalia utekelezaji kwenye sekta ya umeme, ujenzi wa reli, ujenzi wa minara ya mawasiliano na maeneo mengi sana, vituo vya afya, hospitali mpya, ujenzi wa madarasa, mabwalo na mabweni kwenye shule za msingi na sekondari na kwa kweli katika maeneo mengi tumefanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji, jambo ambalo naipa heko serikali yetu ni jinsi ambavyo tumebadilika kutoka zamani ambako wenzetu walipokuwa wanatufanyia tathmini. Kwa mfano, nirejee taarifa ya maendeleo ya Dunia (World development report) ya mwaka 2004 ambayo ilisema kwa sababu ilifanyika Tanzania hapa, ilisema fedha haziendi kwa watu masikini lakini ukiangalia utekelezaji wetu wa leo chini hasa ya Awamu ya Tano hii, fedha nyingi zimekuwa zinakwenda kwa watu masikini katika sekta ambazo zimezitaja. Walisema kwamba kuna matatizo ya nidhamu makazini, kulikuwa na absenteeism leo hii nidhamu kazini kwa kweli imeongezeka na mambo mengi ambayo waliyaona kipindi kile yamebadilika. Kwa hiyo, kwa kweli napenda sana kuipongeza sana Serikali yetu kwa kufanya kazi kubwa sana ambayo inalenga kumkwamua Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto bado zipo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha amezitaja changamoto, kwa mfano, changamoto kwenye ukusanyaji wa mapato kwamba bado kuna mianya, mapato yanapotea na ndiyo maana hatujawahi kufikia asilimia 100 ya makadirio ya makusanyo na sababu zilizotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni pamoja na uwepo wa njia za panya yaani Bandari bubu, ukwepaji mwingine wa kodi, wahisani kutotimiza ahadi kwa kweli haya mimi nilikuwa naomba sana Serikali yetu iyavalie njuga kuhakikisha kwamba hizi changamoto zinaondoka. Tufanye kila mbinu kuhakikisha wkamba changamoto hizo zinaondoka ili tuendelee kufanya vizuri zaidi katika kumuhudumia Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine iko kwenye ufuatiliaji na tathimini, hapo nataka nisisitize kidogo; kuna tofauti kati ya kutembelea mradi na kufuatilia mradi hasa kwa wataalam. Kiongozi anaweza akatembelea mradi kwa maana ya kuona kama ni ujenzi unaondelea lakini mtaalam anapotembelea mradi hapo ndiyo naona ni kioja. Mtaalam hatakiwi kutembelea mradi, mtaalam anatakiwa afuatilie utekelezaji wa mradi, kwa maana gani?

Mradi wowote ambao kwa mfano, unajengwa na Mkandarasi una mkataba sasa mtalaam anapokwenda kufuatilia mradi mkataba hajausoma huu, hana mkataba hapo ndiyo unapoona kioja. Lazima wataalam wetu wabadilike, kazima wanapokwenda kukagua miradi au kufuatilia miradi wawe na nyenzo za ukaguzi au nyenzo za ufuatiliaji ambao ni pamoja na mkataba, ambao ni pamoja na makadirio ya ujenzi au BOQ, ambayo ni pamoja na michoro ili ajionee je, huu mradi unaotekelezwa unafuata makubaliano ambayo yako kwenye mkabata na yaliyopo kwenye michoro?

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu jambo la pili ni tathmini; tathmini ambayo tumeizoea sana Serikalini na nchini kwa ujumla ni tathmini ile ya kila mwaka ambayo inafanyika kupitia bajeti kila Wizara inafanya tathmini yake na Mheshimiwa Waziri wa Fedha akija hapa huwa anahitimisha ile inaitwa budget review au mapitio au tathmini ya Mwaka ya utekelezaji wa Mpango wa Mwaka wakati anasoma bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mipango hii lazima kuwe na tathmini ya nusu mwaka au medium review, tathmini ya nusu muhula au midterm review. Kama kuna mpango wa miaka mitano inapofika nusu lazima ifanyike tathmini ya nusu ya utekelezaji wa muda wa ule mpango halafu mwishoni mwa muhula yaani kama ni miaka mitano, mwishoni mwa miaka mitano ifanyike tathmini ya kina ambayo itasaidia sasa maandalizi ya mpango wa miaka mitano inayofuata. Kwa kweli hapa tumekuwa kidogo tunatatizo ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwasababu analifahamu ningependa alipe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa tumekuwa tukipata vipaumbele vingi, lakini nikitazama kwa undani, tumekuwa tuna upungufu kwenye eneo la ardhi. Sekta ya Ardhi kwa upande wangu ndiyo sekta mama ya uchumi. Hakuna mtu atafanya ujenzi wa aina yoyote bila kugusa Sekta ya Ardhi. Watu wa kilimo wanafanya shughuli zao kwenye ardhi, mifugo, uvuvi, maliasili na utalii ni kwenye ardhi; madini yako kwenye ardhi. Sasa Sekta ya Ardhi kama hatujaipa kipaumbele, kwa mfano kwenye eneo dogo tu la maeneo ya uwekezaji, hilo litakuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuipe kipaumbele Sekta ya Ardhi na Mheshimiwa Doctor, Mwalimu wangu anajua vizuri sana. Naomba sana, tunapoendelea kupanga vipaumbele vyetu tuikumbuke Sekta ya Ardhi. Huyu Waziri wa Ardhi tumsaidie aweze kutimiza matarajio ya Watanzania. Haiwezekani tuendelee kupima Dodoma na Dar es Salaam peke yake, lazima tupime miji yote ikae vizuri, makazi yakae vizuri. Halafu kule vijijini kuna miji ambayo inaibuka kwenye vijiji, ina ujenzi holela. Lazima tumsaidie Waziri wa Ardhi aweze kuratibu miji ambayo inaibuka vijijini iwe na makazi mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kila kipande cha ardhi Tanzania kikipimwa tutapata maendeleo ya kutosha kwa sababu ardhi itakuwa na thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani yangu ni hayo. Naunga mkono hoja, Ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana ahsante sana kwa nafasi hii kwanza nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja ya Kamati zote mbili, niipongeze sana Serikali kwa kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato pale TRA, mifumo ya disbursement ya fedha na mifumo ya ripoti ya fedha kweli imekaa vizuri sana kwa sasa hivi. Isipokuwa tatizo ambalo bado naliona ni mfumo wa uwajibikaji au accountability framework bado kidogo inahitaji kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si vizuri sana kusubiri mpaka CAG akague atoe ripoti ndio Watanzania wajue status ya thamani ya fedha kwenye miradi. Ingekuwa vizuri sana kama thamani ya fedha kwenye miradi ingekuwa inafatiliwa tangu fedha zinapopelekwa kwenye utekelezaji hadi utekelezaji unapofanyika mpaka miradi kukamilika. Kwa hiyo, nashauri tuboreshe mfumo mzima wa ufuatiliaji na tathmini ili tuweze kuboresha utekelezaji wetu. Taarifa ya utekelezaji wa bajeti nikiangalia ni nzuri sana lakini kipengele hiki cha ufatiliaji na tathmini kinachelewa kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mawili la kwanza ni muhimu sana tuwe na sera ya ufatiliaji na tathmini ya nchi, pili mikakati ya ufatiliaji na tathmini ambayo itaboresha mpaka idara zote ambazo zinahusika na mambo ya mipango, ununuzi, uhasibu, ukaguzi wa ndani na mambo yote yanahusiana na suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ushauri wa kuanzisha Ofisi ya Kamishna wa Mipango wa ufatiliaji na tathmini katika Wizara ya Fedha ni muhimu sana Serikali iutekeleze. Hapo mwanzo tulikuwa tunalalamikia wakandarasi sijui bei kubwa wakandarasi baadaye tukaagiza kwamba itumike force account lakini hata kwenye force account kumeanza kujitokeza matatizo ambayo yanapunguza ile thamani ya pesa kwenye mradi. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri tukiboresha eneo hili la ufatiliaji na tathmini tutakuwa tumeboresha sana matokeo bora ya miradi kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili fedha za mfuko wa jimbo kwa mfano mwaka jana zimetoka mwezi wa nane. Kamati za mfuko wa jimbo zimekaa kupanga matumizi ya hizo fedha lakini mpaka leo hii miradi mingi ya fedha hizi za mfuko wa jimbo haijatekelezwa kwa sababu tu fedha zilipokuja hazikuwa kwenye activity bajeti, kwa hiyo miradi yake ile mpaka iombewe kibali aidha kwa Wizara ya Fedha au TAMISEMI aidha reallocation. Nilikuwa nashauri ili kuondoa matatizo hayo Kamati za mfuko wa jimbo ziwe zinakaa mwezi Januari au Februari ili miradi ambayo imepangiwa matumizi iingie moja kwa moja kwenye activity budget wakati fedha zile zikitoka ziende kwenye utekelezaji na wakati ule Kamati za mfuko wa jimbo zifanye tu ufatiliaji na tathmini ya mradi unatekelezwa, hiyo itakuwa imeboresha kwa kiasi kikubwa sana utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho napenda kutoa pongezi kubwa kwa Serikali utekelezaji wa bajeti 2018/2019, 2019/2020 kwa kweli unaondelea ni mzuri na kazi kubwa sana zimefanyika hongera sana Serikali hasa kwenye miradi ya miundombinu, miradi ya afya, miradi ya elimu na kwa kweli naomba ndani ya Bunge hili nizungumze masikitiko yangu dhidi ya barua ambayo mwenzetu mmoja ameiandika kutaka kuzuia fedha za miradi ya elimu. Ni kituko na ni aibu sana kwetu sisi Wabunge kuona mwenzetu ameandika barua ile wangekuwa wameandika watu wa NGO huko nje mimi nisingeshtuka sana lakini mwenzetu kaandika barua ile katika jimbo lake Serikali imepeleka shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukarabati Sekondari ya Kigoma na sasa hivi sekondari ya Kigoma ni kama mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wamepeleka zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa ajili ya kuboresha elimu, sasa anazuia dola milioni 500 zisije kwa haraka kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kitanzania. Nadhani hilo kwa kweli nieleze masikitiko yangu makubwa sana, na nimuombe huko aliko amesoma vizuri tena amesoma hapa ndani akasoma nan je Ujerumani basi tuitumie elimu yetu kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa Tanzania hiyo ndio rai yangu badala ya kuwacheleweshea maendeleo. Unazuia shule 1000 zingeguswa na hizo fedha watoto zaidi ya 600,000 wangefaidika na zile fedha. Nadhani kwa kweli hilo mimi nasikitika sana sana na kama ananisikia huko aliko nilitamani nipaze sauti asikie huko aliko lakini kwa sababu yupo mbali basi naachia hapo lakini ataisikia kutoka kwenye Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii asante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kwa ushauri huo ambao umeutoa wa kitaalam kweli kweli kwa ajili ya kuepuka carbondioxide, hongera sana kwa utaalam huo na nitakufuata nije nijifunze funze kidogo mambo ya miti shamba.

Mheshimiwa Spika, watu wa Sikonge wamenituma kupitia mikutano ambayo niliifanya kwa kila kijiji mwaka jana, nije nitoe shukrani za dhati kabisa na pongezi nyingi kwa Serikali inaongozwa na Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa miradi mingi ambayo tumeipata Sikonge na imesimamiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu bila kumsahau Makamu wa Rais, Mawaziri wote, Watendaji Wakuu wa Serikali, kwa ujumla wao tunawapa pongezi kubwa sana kwa weledi ambao wameutumia katika kuiongoza nchi hii kwa viwango vya kihistoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nichukue nafasi hii kukupongeza wewe binafsi na uongozi mzima wa Bunge kwa kuendesha Bunge kwa weledi wa hali ya juu, lakini kwa kutuletea Bunge Mtandao imekuwa ni historia kubwa sana kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi kama Mbunge wa Sikonge, niliomba miradi mingi kwa niaba ya wananchi wa Sikonge, Serikali ilikubali na utekelezaji umekuwa mkubwa na nikwambie kwa mara ya kwanza tangu dunia iumbwe, wananchi wa Sikonge wameanza kuona lami ambayo inatoka Tabora, inapita Sikonge inakwenda mpaka Mpanda, hilo ni jambo la kihistoria kwao na kwa mara ya kwanza watu wa Sikonge watapata Mahakama ya Wilaya, ambayo ilikuwa ni shida kubwa, wengine walikuwa wanasafiri kilomita 500 kwenye Mahakama ya Wilaya, Tabora Mjini.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa mara ya kwanza tangu dunia iumbwe, wananchi wa Sikonge watapata Hospitali ya Wilaya ya Serikali. Kwa mara ya kwanza pia kumekuwa na ukarabati mkubwa sana kwenye Chuo cha Maendeleo ya Wananchi kimekuwa kipya cha kisasa. Kwa mara ya kwanza nyingine tumepata vituo vya afya viwili vikubwa Kituo cha Kipili na Kituo cha Nyahua; wananchi hao kutoka sehemu mbali kabisa kilomita 380 Kipili na kilomita 200 Nyahua wataanza kupata huduma vipimo na dawa huko huko waliko bada ya kwenda kusafiri kwenda Sikonge, Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, tangu dunia iumbwe, Jimbo langu la Sikonge na Wilaya ya Sikonge, tumepata shule mpya mbili za kidato cha tano na sita ambayo nayo ni historia. Niseme tu kwa mara ya kwanza shule zetu kongwe ambazo walisoma viongozi wetu wa juu kabisa wa nchi hii, akiwemo marehemu Mzee Sitta, zimekarabatiwa Shule ya Msingi Sikonge, Shule ya Msingi Chabutwa, imekarabatiwa sasa ni mpya kabisa. Kwa hiyo, kwa kweli mambo mengi yamefanyika Sikonge ambapo katika kipindi hiki cha miaka mitano imekuwa ni historia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maji kwa mara ya kwanza tumepata bwawa kubwa maana yake tulikuwa na Bwawa la Utiyati ambalo lilijengwa mwaka 1959. Kwa mara ya kwanza tumepata Bwawa lingine la Igumila ambalo ni kwa ajili ya matumizi ya wananchi. Ingawa huku mjini tutakuwa na maji kutoka Ziwa Victoria, ambayo sasa yamefika Tabora Mjini.

Mheshimiwa Spika, lazima nizidi kuipongeza Serikali kwamba yote haya yamefanyika chini ya usimamizi wa Chama cha Mapinduzi. Kamati ya Siasa ya Mkoa ilipotembelea Sikonge hivi karibuni ilitoa shukrani zake za dhati kwa Serikali kwa utekelezaji mzuri sana wa Ilani ya Uchaguzi katika Jimbo la Sikonge na kwa kweli kama Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya nizipokee hizo pongezi na naomba nizifikishe Serikalini kupitia kikao hiki cha Bunge ambayo ilipitia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, bado ziko changamoto chache ambazo ningependa kuziainisha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mafuriko, hii ni changamoto ni ya nchi nzima, lakini kwetu sisi katika jimbo imekuwa ni changamoto maalum kwa sababu mafuriko yametutenganisha na mawasiliano ya mikoa miwili. Hatuna mawasiliano na Mkoa wa Katavi na hatuna mawasiliano na Mkoa wa Mbeya kwa sababu ya mafuriko. Kwa hiyo, naomba hii changamoto Mheshimiwa Waziri Mkuu aipe kipaumbele cha juu kabisa kwa upande wetu katika Jimbo la Sikonge na Mkoa wa Tabora ili angalau tupate suluhisho la kipaumbele cha haraka sana ili tuweze kurudi katika mawasiliano na wenzetu wa Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Mbeya. Maeneo mengine yote ambayo yameharibiwa na mvua pia ni vizuri yakapatiwa mpango wa dharura wa utengenezaji ili wananchi warudi katika shughuli zao za kiuchumi za kawaida.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine bado tunaendelea na ufinyu wa ardhi ya kilimo na ufugaji katika Jimbo la Sikonge. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili alipotembelea Sikonge mwaka jana alituahidi kwamba Serikali itafanya utaratibu wa kuboresha na kuzipandisha hadhi hifadhi zetu na misitu iliyoko katika Wilaya ya Sikonge ili kupunguza maeneo yale ya misitu ambayo hasa ambayo hayatumiki sana ili kuwaongezea wananchi maeneo ya kulima na maeneo ya ufugaji. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili kupitia kwako, walikumbuke suala hilo hili mbunga zetu, hifadhi zetu na misitu yetu iboreshwe ipandishwe hadhi ili lipatikane eneo kubwa zaidi kwa ajili ya kilimo na ufugaji.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni tumbaku, kwetu sisi Sikonge au Mkoa wa Tabora Wilaya kama tatu au nne na baadhi ya wilaya nyingine nchini hapa tumbaku ni uchumi. Sisi ni wategemezi wakubwa sana wa tumbaku ili kupata fedha, wakulima wetu katika kipindi cha miaka mitatu minne iliyopita wamekuwa na changamoto kubwa sana ya soko, sehemu ya kuuzia tumbaku naamini hiyo ni kengele ya kwamba.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana TLTC waliondoka hapa Tanzania, kwa hiyo mnunuzi mmoja amepungua, hata kama hajaondoka TLTC bado tulikuwa na soko finyu la kuuzia tumbaku. Sasa ameondoka TLTC tangu mwaka jana British-American Tobacco wanaomba kuingia kwenye soko la Tanzania na tangu mwaka jana kumekuwa na majadiliano kati ya BAT, Wizara ya Kilimo, na Wizara ya Fedha kuhusiana na masuala ya kodi.

Naomba hiki kikosi kazi cha kodi kitilie maanani na wazingatie wakulima wa tumbaku ili kuhakikisha kwamba kama kuna vipengele vya kodi ambavyo vinahitaji marekebisho, basi vije kupitia Finance Bill ya mwaka huu mwezi sita ili mwezi wa Saba, BAT waingie kwenye soko la tumbaku ili kununua tumbaku.

Mheshimiwa Spika, hiyo itakuwa ni kazi kubwa sana na itakuwa ni mchango mkubwa sana kwa wakulima wetu kwa sababu BAT yeye kwanza kwa miaka miwili ya kwanza ataingia kununua tumbaku ambayo imekuwa inazalishwa kwa ziada na hii tumbaku ambayo imekuwa ikizalishwa kwa ziada, ndiyo tumbaku ambayo wakulima wamekuwa wananyonywa sana.

Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita kwa taarifa ambazo tunazo sisi kutoka Tabora, ni kwamba, wapo wakulima ambao walikuwa hawajauza, wameuza tumbaku kilo moja Sh.280 ambao ni unyonyaji wa hali ya juu sana kama anaingia BAT kununua tumbaku imezidi ziada ya mikataba maana yake ni kwamba atanunua kwa bei ambayo alinunua Alliance One ambayo alinunua mnunuzi mwingine itakuwa ni faraja kubwa sana kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali itilie maanani suala hili, vile vingezo ambao walikubaliana, najua Mheshimiwa Bashe ni mtu ambaye amelishughulikia sana suala hili na kwa kushirikikana na BAT na Wizara ya Fedha wamefanya vikao vingi sana tangu mwaka jana, lifikie hitimisho hili mapendekezo ambayo wamependekeza hapo awali yaweze kuingizwa kwenye sheria ili tuweze kupata mnunuzi mpya.

Mheshimiwa Spika, ya kwangu yalikuwa ni hayo kwa niaba ya watu wa Sikonge nashukuru sana. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba zake mbili nzuri ambazo zilinigusa mimi sana kama Mbunge wa Sikonge. Hotuba hizo mbili zimefanya mapitio ya nchi yetu, tulikotoka, tulipo na tunakoelekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili sisi Watanzania tuweze kujua tumetoka wapi na tunakoelekea ni wapi, jambo la kwanza kabisa ni kuangalia kwamba nchi yetu hii ilitawaliwa na wakoloni kwa muda wa miaka 74 na sisi tangu tujitawale kwa Tanzania Bara huu ni mwaka wa 60 na kwa Zanzibar ni mwaka wa 58. Utaona kwamba kipindi ambacho walikaa wakoloni katika nchi hii ni kirefu kuliko kipindi ambacho sisi tumekuwa huru. Katika kipindi ambacho tumekuwa huru, mambo ya maendeleo yaliyofanyika ni makubwa zaidi kuliko kipindi cha wakoloni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu tupate uhuru pia tumekuwa na vipindi vikuu vitano vya kiuchumi. Kipindi cha kwanza ni kipindi cha soko huria (1961 – 1967), kipindi cha pili cha uchumi hodhi miaka 18 kuanzia mwaka 1967 – 1985, kipindi cha tatu ni kipindi cha mpito cha marekebisho ya kufufua uchumi cha mwaka 1985 – 1995, kipindi cha nne ni cha mwaka 1995 – 2015 ambacho hicho ndiyo kiliweka prudent economic reforms ikiwemo ubinafsishaji, kurejesha baadhi ya njia ya kiuchumi kwenye sekta binafsi ikiwemo masuala ya ubi ana programs mbalimbali za maendeleo ikiwemo uandaaji wa dira na kuanza utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukirejea dira ina maeneo gani, maeneo makuu manne ya dira ambayo iliandaliwa na kuanza kutekelezwa mwaka 2000, eneo la kwanza ni huduma za jamii; eneo la pili ni amani, usalama na umoja wa Taifa; eneo la tatu utawala bora; na eneo la nne kukuza uchumi. Katika maeneo yote hayo manne hadi sasa tunavyozunguzma tumefanya vizuri zaidi na hasa kipindi hiki cha tano cha 2015 – 2025 tunakoelekea kumekuwa na uwekezaji kwenye maeneo karibu yote muhimu ya miundombinu na huduma za jamii, elimu, afya, maji, barabara, madaraja, viwanja vya ndege, bandari, reli na umeme mambo makubwa sana yanafanyika katika nchi hii hata watu wengine wanatuonea wivu. Juzi alikuja Mkongo mmoja akasema hebu tuazimeni Magufuli Congo angalau kwa muda mfupi aje kutawala huku. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais na kwa hotuba zake mbili muhimu sana. (Makofi)

Naomba sasa kupitia Bunge lako Tukufu niwasilishe changamoto kuu ambazo bado zinatukabili. Ya kwanza ni masoko ya mazao, bado wakulima katika maeneo mengi wana manung’uniko dhidi ya bei. Kwa Sikonge, tumbaku bado tuna manung’uniko makubwa lakini tunashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Bashe alivyokuwa Tabora juzi alitoa hotuba nzuri ambayo imetuletea matumaini, tunachoomba vision yake iweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili ni barabara vijijini. Ufinyu wa bajeti ya TARURA inatakiwa Serikali itafute chanzo chochote kile ili kuiongezea TARURA uwezo wake iweze kusaidia barabara vijijini. Hatuwezi kupata maendeleo ya kilimo kama TARURA hawezeshwi kutengeneza barabara za vijijini. Wanatengeneza barabara nyingi kwa udongo, ikija mvua kidogo tu inaosha na tunarudi kwenye matatizo yale yale. Changamoto kubwa ya tatu vijijini ni huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina maombi maalum kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Rais. Katika ukurasa wa 33 amesema: “Tunakusudia kujenga shule moja ya sekondari kila mkoa itakayofundisha masomo ya sayansi kwa wasichana”. Sikonge tunacho kituo cha vijana cha TULU ambacho kiliwekwa jiwe la msingi na Mheshimiwa Waziri Mkuu Pinda mwaka 2012 na kikazinduliwa na Mheshimiwa Rais Kikwete mwaka 2014. Hadi sasa waliofaidika pale hawazidi 100. Sasa kwa kuwa zilitumika shilingi bilioni 2.5 na zaidi za Serikali na kuna majengo pale Serikali iwekeze fedha kidogo tu ili tupate shule hii katika mkoa wa Tabora ambayo itakuwa Sikonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naomba Serikali ijenge barabara ya Ipole – Rungwe ili kuunganisha Tabora na Mbeya. Vilevile ijenge na ikamilishe barabara ya kutoka Chunya - Itigi - Mkiwa ili kuunganisha Mkoa wa Mbeya na Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nimesoma mapendekezo ya Mpango kwa makini na nimeona kwamba kuna maeneo mazuri kama kwa mfano maeneo ya malengo. Eneo la malengo limekaa vizuri; eneo la kazi za kufanya kufika malengo limekaa vizuri; eneo la mahitaji ya rasilimali watu na rasilimali fedha limekaa vizuri, lakini kuna tatizo kwenye maeneo mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo la mfumo wa ukusanyaji wa mapato, hili eneo inabidi Serikali iangalie kwa makini kwa sababu bado kuna vyanzo vingi havikusanywi. Vile vile Sheria ya TRA inaruhusu mapatano, yaani unakwenda kwa mtu unamkadiria alipe milioni mia nane, halafu akikaa kwenye mapatano unaweza ukashusha mpaka milioni mia nne. Hili ni tatizo kubwa. Hakuna utawala bora wa namna hiyo kwenye sheria. Kama sheria inaruhusu mapatano, hiyo sheria inakuwa haifai. Kwa hiyo, inatakiwa kwa kweli wafanye mapitio makubwa kwenye Sheria ya TRA ili sheria ikisema sharti hili kodi yake ni shilingi kumi na tano, iwe shilingi kumi na tano isiruhusu mapatano. Kuruhusu mapatano huo ni mwanya mbaya sana kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nimeona kwamba limefanyiwa mapitio ni mifumo ya udhibiti wa nje na ndani internal and external controls yaani ni muhimu sana kudhibiti matumizi ya fedha kama tunataka matokeo mazuri. Jambo la tatu eneo la ufuatiliaji na tadhimini, nalo halijakaa vizuri katika utekelezaji. Kwenye maandishi linaweza kukaa vizuri, lakini katika utekelezaji haijakaa vizuri, nani anawajibika pale ambapo kunakuwa na tatizo, anatakiwa a person, lazima mtu binafsi awajibike siyo taasisi kuwajibika. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo linatakiwa lifanyiwe mapitio ya kutosha ili tuwe na mpango mzuri hapa baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikipitia utekelezaji uliofanyika, umefanyika vizuri sana. Kwenye huduma za jamii, elimu, afya na maji, utekelezaji umefanyika vizuri sana kwa nchi nzima. Hata humu ndani walio wengi wa majimbo wamepita kwa sababu ya utekelezaji mzuri uliofanyika kwenye sekta za huduma za jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia utawala bora; sheria kama haitoi usawa, hiyo sheria ina matatizo. Kwenye eneo la utawala bora tulikuwa tunaathiriwa na upande wa sheria, sheria kwanza ni za zamani sana, zimepitwa na wakati, lakini kuna sheria hazitowi usawa. Kwa mfano, Sheria ya Trafiki, trafiki akikamata pikipiki anatoza shilingi 30,000 kwa kosa lolote lile; akikamata gari dogo shilingi 30,000; akikamata gari kubwa la mizigo shilingi 30,000. Hiyo sheria haitoi usawa, kwa mfano ingekuwa sawa pikipiki atoe shilingi 5,000; gari dogo atoe shilingi 10,000; gari nyingine yenye uzito fulani atoe shilingi 15,000 na gari kubwa atoe shilingi 30,000. Hapo ndio sasa Sheria ingetoa usawa kulingana na uzito wa matumizi ya vyombo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo ambalo limefanyika vizuri sana, nalo ni la amani, usalama na utulivu wa nchi. Kwenye eneo la kukuza uchumi, nina ushauri maeneo machache. Nchi hii haitaendelea bila ardhi kupimwa. Ardhi ndiyo uchumi, ardhi ndiyo itawafanya Watanzania wapate uchumi. Kama Wizara ya Ardhi itaendelea kushugulikia migogoro midogo midogo tu na kuwasubiri watu kwamba tunamsubiri mtu ambaye atakuja kuomba kupimiwa kieneo chake badala kupima ardhi yote, mtu kama anataka ardhi aende akachukue ardhi ambayo imepimwa, kitakuwa kitu kizuri sana kwa uchumi wa nchi hii. Kwa hiyo, Serikali lazima ioneshe kwenye Mpango namna ambavyo watapima ardhi yote katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kazi imefanyika vizuri sana kwenye maliasili, kwenye eneo la mawasiliano vijijini, barabara, madaraja makubwa, reli na bandari. Tatizo liko kwenye bajeti ya TARURA, namuunga mkono mzungumzaji, ndugu yangu Mheshimiwa Tabasamu, lazima TARURA waongezewe bajeti kama tunataka kusaidia uchumi wa nchi hii.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kakunda.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Fedha na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwa uwasilishaji wao mzuri leo asubuhi, kwa kweli mbinu waliyotumia kuwasilisha imefanya mpango wetu uweze kueleweka sio kwetu sisi Wabunge bali hata kwa wananchi, kwa hiyo, kwa niaba ya watu wa Sikonge nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme tu kwamba kwa niaba ya watu wa Sikonge nimeupokea Mpango uliowasilishwa leo asubuhi na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa mikono miwili na kwa matumaini makubwa. Thatimini ambayo ameitoa hapa ya utekelezaji wa mpango uliopita unatoa matumaini kwamba Mpango huu wa Tatu utakuwa na mafanikio makubwa zaidi na nina sababu mbili za kusema hivyo. Sababu yangu ya kwanza ni kwamba utekelezaji wa mpango uliopita katika maeneo mawili hasa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza, eneo la huduma za jamii, elimu, afya, maji kwa kweli tunahitaji kuipongeza sana Serikali na kuipa heko kubwa kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye eneo la huduma za jamii. Eneo la pili ambalo limetengezwa vizuri sana ni eneo la miundombinu kwa ajili ya kuhudumia uchumi, eneo la barabara, madaraja makubwa, vivuko, reli, umeme hasa umeme vijijini, maji, viwanja vya ndege na bandari.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo hayo yalionesha mfano mkubwa, safi kabisa na ni mfano wa kuigwa kwa Serikali nyingi katika Bara la Afrika kuhusu matumizi mazuri ya fedha za umma. Maendeleo tuliyoyapata kwenye eneo la miundombinu, kwenye maeneo hayo niliyoyataja yamefanya Tanzania iwe sehemu muhimu, nzuri ambayo inawavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Mazingira ni mazuri, kwa hiyo kutokana na mafanikio ya hivyo nashauri Serikali ni vema tuendelee kusimamia vizuri utekelezaji kwenye maeneo yote hayo ili tuendelee kuwa bora zaidi na hayo ni maeneo ya vipaumbele vya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya CAG ya juzi kwa kweli inanifanya niiombe Serikali kupitia Waziri Mkuu na viongozi wote wa Serikali kwenye Wizara mbalimbali naomba sana taarifa ya CAG muipitie kwa kina ninyi ndugu zetu mliopo Serikalini ili muweze kuchukua hatua stahiki, sio hatua za kukurupuka hapana, hatua stahiki kwa kila aliyehusika na ubadhirifu ili tunapoenda kwenye kutekeleza mpango mpya tupate mafanikio makubwa kwa niaba ya wananchi wetu na kila mwananchi aweze kufurahi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mimi natangaza rasmi kwamba Halmashauri yangu ya Wilaya ya Sikonge ni miongoni mwa Halmashauri ambazo zimepata Hati Chafu, hili mimi binafsi kama Mbunge wa Sikonge nawaambia wananchi wa Sikonge sijalifurahia na niomba mamlaka zinazohusika ziweze kufuatilia ili tusiwe na mambo kama hayo katika siku za usoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni na maeneo matano ya kushauri; eneo la kwanza, kwenye viashiria vya Taifa vya Uchumi kuna kitu kinaitwa mfumuko wa bei au inflation. Mimi ni mtaalam wa uchumi tena sio mtalaam wa hivi hivi, ni mbobezi kabisa kwenye eneo hilo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha anafahamu, hii habari ya kukaa tunatamba kama Taifa hapa unajua inflation yetu ni 3.5% sio kitu cha kujivunia sana, tunatakiwa kweli kuwa single digit, lakini ni single digit ambayo inasogelea 10% ili kuweza kuchochea faida za muda mfupi na faida za muda wa kati za wawekezaji na kwenye eneo la biashara, hii kuweka 3.5% na chini ya hapo ni kuufanya uchumi uwe dormant, sawa bei hazitabadilika sana, lakini je, uwekezaji? Je, biashara faida kwenye biashara itakuwaje? Kwa hiyo namshauri Waziri wa Fedha awaambie watalaam wasiwe waoga sana kwenye inflation hasa hii inflation ambayo iko chini ya 5% sio nzuri sana kwa Taifa ambalo tumeshatengeneza mfumo mzuri wa maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili; tunapozungumzia viwanda unataja maelfu ya viwanda, kweli na mimi nilikuwa Waziri wa Viwanda wakati fulani, nataja mafanikio, tumeanzisha viwanda 50,000; mimi kwangu binafsi mafanikio ni kwenye eneo la ajira, tume-create ajira kiasi kwenye sekta ya viwanda, sio kutaja viwanda 50,000 hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa viashiaria muhimu kabisa kwenye dira yetu ya Maendeleo ya Taifa tulisema kwamba ifikapo mwaka 2020 asilimia 40 ya ajira itatoka kwenye eneo la uzalishaji viwandani, kwa hiyo tunapotoa taarifa ya viwanda tulivyoanzisha lazima tuseme tumefikia hatua gani kwenye kufikia lengo la 40% ya ajira kwenye sekta ya viwanda, hilo ni la muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo na ningependa kulishauri maeneo ya utawala bora. Dira ya Maendeleo ya Taifa ina nguzo nne; nguzo ya kwanza huduma za jamii, nguzo ya pili umoja wa kitaifa, amani na usalama, eneo la nguzo ya tatu ni nguzo ya utawala bora halafu nguzo ya nne ni eneo la kukuza uchumi ambapo tunakuta na mambo ya infrastructure na nini. Hiyo ni kengele ya kwanza. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yote hayo manne lazima eneo la umoja wa kitaifa, eneo la usalama na amani ya nchi lazima tulihudumie vizuri, lakini vilevile eneo la utawala bora lazima nalo tulihudumie vizuri, kwenye eneo la utawala bora kuna vi-section kumi ambavyo nilikuwa nafikiria kwamba niwashauri wenzetu waweze kuviangalia na kuviongezea umuhimu katika bajeti na katika kuisimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni ukaguzi na urakibu wa polisi. Tunazungumzia hapo utekelezaji wa Sheria Kuu ya Jinai na hii ni muhimu sana katika kulinda mali na usalama wa wananchi. Polisi naamini katika eneo hilo hawana bajeti ya kutosha. Lakini eneo la pili ni Ukaguzi wa, Ukaguzi wa ndio risk manager wa fedha tunazopeleka kule kwenye Halmashauri na kwenye Wizara. Kwa hiyo, Ukaguzi wa Ndani unatakiwa upawe kipaumbele cha juu sana. Halafu cha tatu ni Ukaguzi wa Nje naye CAG wakati mwingine anakuwa na hela kidogo, eneo la nne, Tume ya Kudumu ya Uchunguzi, eneo la tano, Tume na Sekretariat ya Maadili ya Viongozi, eneo la sita Usalama wa Taifa, hawa watu wa Usalama wa Taifa wakati mwingine wanakuwa na informers wengi kuliko hata wao wenyewe ambao wameajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nashauri wale informers ambao wana uzoefu wawachukue waajiri ili kusudi Idara ya Usalama wa Taifa iweze kufanya kazi zake vizuri zaidi in a formalized manner.

Mheshimiwa Naibu Spika, la saba ni TAKUKURU hata Mheshimiwa Rais juzi aliwaambia TAKUKURU zingatieni sheria iliyoanzishwa TAKUKURU katika kufanya kazi zenu, sasa walikuwa wanaingilia na maeneo mengine ambayo wao hawahusiki. Lazima tuwajengee uwezo, tuwape watumishi wa kutosha ili waendelee kupambana na ufisadi na mambo mengine ya ubadhirifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la nane Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu hii inafahamika. Eneo la tisa vyombo vya kusimamia utoaji wa haki na eneo la mwisho kujenga umahiri wa viongozi kwenye ngazi za chini. Naomba nimalizie kwamba eneo hili la kujenga umahiri wa viongozi wa ngazi za chini kwa mfano Maafisa Watendaji wa Vijiji na Maafisa Watendaji wa Kata ni la muhimu zaidi kama tunataka tuendelee na vilevile kuwapa fedha TARURA nyingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kuunga mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote, akiwemo Naibu Waziri, kwa hotuba nzuri, fupi, ambayo inaeleweka; brief to the point. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. Kwa maana hiyo, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri kwa asilimia mia moja. Ndiyo maana nasimama hapa kuzungumzia suluhisho badala ya malalamiko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo nitakalolizungumzia ni la Jimbo langu la Sikonge. Jimbo la Sikonge au Wilaya ya Sikonge, ina eneo la kilometa za mraba 27,873. Eneo la Mkoa wa Kilimanjaro linaingia mara mbili na eneo la wilaya ni kubwa kuliko Mkoa wa Tanga. Kati ya kilometa hizo, eneo lililohifadhiwa ni kilometa za mraba 26,834, sawa sawa na asilimia 96.3 ya eneo lote la wilaya. Eneo ambalo wananchi wanaruhusiwa kuishi na kufanya shughuli zao za kiuchumi ni eneo la kilometa za mraba 1,039.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi takwimu hata kama mtu yeyote akiamua ku-google Sikonge District, atazikuta ziko hapo, Kimataifa, hata kama yuko Marekani. Hii ndiyo concern yangu kubwa na ni concern ya wakazi wa Sikonge kwa sababu moja kubwa. Wakati wa kupima eneo la kuhifadhi, mwaka 1954 mpaka 1956, wakazi wa Sikonge wakati huo ilikuwa kata tu, kwa ujumla wao hawakuvuka hata 30,000. Leo tuna wakazi wanaopindukia 350,000 katika eneo lile lile dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wanapima eneo hilo lililohifadhiwa mwaka 1954 hadi 1956, wakazi wa Sikonge wakati ule hawakuwa wafugaji wa asili. Kwa hiyo, ng’ombe kule hawakuzidi 2,500 kwa eneo lote. Leo tuna ng’ombe zaidi ya 400,000 kwa eneo lile lile dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema wakati mwingine lazima ndugu zetu walioko Serikalini tutumie busara katika kutekeleza sheria. Kwa sababu eneo hilo sasa lime-burst, hakuna sehemu tena ya makazi, hakuna sehemu ya ng’ombe, mtu yeyote anayefuga ng’ombe ataingiza kwenye hifadhi. Asipoingiza kwenye hifadhi atalisha mashamba, kwa sababu hakuna eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imesababishwa na makosa mawili makubwa ambayo yalifanywa na Serikali. Kosa la kwanza, mwaka 1959 Gavana wa kikoloni baada ya kuwa amepata taarifa ya uharibifu wa mazingira katika eneo la wafugaji kule Usukumani hasa, akatoa decree, inaitwa order, kwamba sasa kila mfugaji kwenye maeneo yale anatakiwa apunguze mifugo ibaki 100 au chini ya hapo kwa ajili ya kutunza mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana kipindi kile hakukuwa na Maafisa wa Serikali wa kuweza kutekeleza hiyo decree. Kwa hiyo, ikabidi isubiri decree kutotekelezwa mpaka tulipopata Uhuru mwaka 1961. Tulipopata Uhuru mwaka 1961, Mwalimu Nyerere akasema hii decree hatuwezi kuitekeleza katika nchi huru kwa sababu nchi hii Tanzania ina maeneo mengi ambayo bado wananchi wanaweza wakahamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo lilikuwa ni kosa la kwanza, kwa sababu uhamiaji ule sasa wa kutoka maeneo yale ya wafugaji, kuja kwenye maeneo ya Wilaya ya Sikonge, haukuratibiwa na Serikali. Hilo lilikuwa ni kosa. Kwa hiyo, matokeo yake, wameingia watu wengi sana Sikonge na hatuna eneo la kulima wala kufugia na mifugo ni mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa la pili la Serikali; ilikuwa ni wakati wa operesheni vijiji, walikwenda kuanzisha Vijiji vya Ujamaa karibu kabisa na hifadhi ndani ya mita 500 unaingia hifadhi. Nina kata 16, nina vijiji 40 viko ndani ya mita 500 unaingia kwenye hifadhi; kosa kubwa la Serikali hilo. Unategemea mtu ambaye yuko ndani ya kijiji mita 500, asiingie kwenye hifadhi? Kwa hiyo, hilo lilikuwa ni kosa. Ndiyo maana mimi niko hapa kwa sababu matokeo yake yamesababisha adha kubwa na usumbufu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono suluhisho ambalo linaletwa na Serikali la kuanzisha nature reserve kwenye maeneo yote haya. Nature reserve ambayo sasa itatoa nafuu kwa kupunguza eneo la hifadhi ili wananchi wabaki na eneo kubwa zaidi la kulima. Wananchi hao kupitia Halmashauri tumeshaanza kuzungumza nao namna ambavyo watashiriki kulinda ile nature reserve mpya ambayo itaanzishwa ambapo itaacha maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo ndilo suluhisho ambalo kwa kweli naomba kulileta mbele ya Bunge lako Tukufu ili Mheshimiwa Waziri na timu yake yote waje Sikonge, tukae pamoja tuweze ku-determine kwamba sasa eneo ambalo ni la nature reserve lianzie wapi? Lazima tulinde miti yetu mizuri kabisa; Mininga na miti mingine ya thamani tuilinde, lazima tulinde maeneo ya shoroba, lazima tulinde mbuga ambazo zina wanyama bado, tunazifahamu sisi. Kama hawafahamu wao, watuulize, sisi tunazifahamu zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimesimama hapa kuleta suluhisho la kudumu ambalo litaondoa malalamiko ya wananchi kutokana na yale makosa mawili makubwa ya Serikali ambayo yalifanyika ambayo yameifanya sasa Sikonge ime-burst, hakuna sehemu ya kuishi, hauna sehemu ya kulima wala kufanya shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya kuiwasilisha hoja hii hapa Bungeni na kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri; na ninamwamini huyu bwana kwa sababu tuliajiriwa siku moja Serikalini, mambo haya niliyowasilisha atayatilia mkazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nitoe mchango wangu kidogo kwenye Hotuba ya Bajeti iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kwanza nimpongeze yeye Waziri wa Fedha na pia Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Bajeti kwa uwasilishaji mzuri, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kuchangia maeneo ya uchumi machache, lakini mwishoni nitatoa pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze pale ambapo mwenzangu ameishia. Nimekuwa nikishangaa sana ninapoona Wachumi wa Benki Kuu, Wachumi wa Wizara ya Fedha na Wachumi wa Serikali wanatamba kwenye taarifa mbalimbali unajua Tanzania tuko imara, mfumuko wa bei uko asilimia 3 hadi 5 kwa miaka miwili mfululizo iliyopita na maoteo hivyohivyo mwaka ujao, halafu wanatamba kwamba, ni kitu kizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hilo sio zuri kwa sababu tuna uchumi imara. Tuna stable economy, ilitakiwa wacheze na buttons za kuweza kuruhusu inflations angalau isogee kwenye viwango vya SADC kati ya asilimia 5, asilimia 6, asilimia 7, asilimia 8, ili kuweza kuufumua uchumi usisimke watu wawekeze wapate faida za muda mfupi na muda wa kati, ili uchumi uweze kuwa stable zaidi na kutozalisha ajira kwa wingi na tuzalishe fedha kwa wingi ndani ya nchi, lakini iliyopo sasa hivi ni kwamba, uchumi ni kama vile uko- dormant. Kwa hiyo, suala hili la inflations asilimia 3 nikizungumzia kwa upande wa wakulima, wameathirika vibaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhamasishaji wa Serikali wakulima wamezalisha mazao ya chakula, wameongeza kwa zaidi ya tani milioni mbili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita; mwaka 2015 walizalisha tani milioni 15 mpaka ilipofika 2019 tulikuwa na tani milioni 17 za chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu ya inflation iko asilimia 3 matokeo yake ni nini, debe ambalo lilikuwa linauzwa shilingi 6,000, 8,000 mwaka 2015 leo linauzwa shilingi 3,000 hadi 5,000, ni kilio kikubwa sana kwa wakulima. Lakini suluhisho ambalo lingeweza kuchukuliwa na Serikali ambalo sijaliona kwenye hotuba ni kuwa na price stabilization fund ambayo ungeweka buffer stock wakulima wakizalisha zaidi ya mahitaji ya soko la ndani Serikali inanunua kilichoongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mwaka jana ingenunua tani milioni tatu ina maana kwamba, leo debe la mahindi lingeuzwa shilingi 6,000 na kuendelea, bado wakulima wasingekuwa kwenye kilio. Kwenye bajeti hii sijaona ile stabilization fund ya Serikali kwa sababu, Serikali lazima iongeze matumizi katika kuokoa uchumi wa nchi, hasa uchumi wa wakulima, lakini vilevile suala hilo lingeweza kuwapa nafuu wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano, mfano sera za fedha zinatwambia kwamba, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi umekuwa ukishuka. Mwaka 2019/2020 ulikuwa asilimia 13.5, mwaka 2020/2021 ulikuwa asilimia 11.6, maoteo ya mwakani 2021/2022 itakuwa asilimia 10.6 maana yake nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba, wafanyabiashara wanapunguza kukopa kwenye benki. Maana yake nini? Maana yake benki zinaatamia fedha. Fedha zinakuwepo, lakini hakuna mkopaji. Kwa sababu, gani hawakopi? Kwa sababu kuna masgarti ambayo sio rafiki ya riba ambayo yanaathiri faida. Mtu huwezi kukopa kwa sababu huwezi kupata faida na huo mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania pekee ndio utakuta tofauti ya riba ya mkopo na tofauti ya riba ya amana iko kati ya asilimia 7 mpaka asilimia 10. Hii ni mbaya sana na upunguaji wake umekuwa unapungua chini ya asilimia 1, sasa data hizo zipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili inatakiwa Serikali ifanye utaratibu mzuri wa kwanza kutokutafiti sababu ni nini? Sababu ni hiyo tu riba au kuna sababu nyingine ambazo zinasababisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo ningependa kulichangia; leo nimemtoa mtoto nenda dukani kanunue lita moja ya mafuta ya kula ya alizeti, kaambiwa dukani kwenye duka la jirani shilingi 9,000. Chupa hiyo hiyo ya lita moja ya alizeti mwaka jana nilikuwa nainunua shilingi 4,500 maana yake nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake kuna shida kubwa ya mafuta hapa nchini. Na viwanda vyetu ambavyo vilikuwa vinazalisha mafuta vimepunguza kuzalisha mafuta, ukiwauliza wanakwambia hatuna malighafi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali nimeona juzi Waziri Mkuu alikuwa Singida, hiyo mikakati ambayo wanaifanya kupitia mikutano ya wadau haitoshi. Inatakiwa ionekane kwenye Government expenditure wamechukua hatua gani za wazi za kuhakikisha kwamba, viwanda vyetu vinapata malighafi ya kuzalisha vitu ambavyo vinaumiza wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ningependa nitoe pongezi. Natoa pongezi bajeti kwa kweli, bajeti kwa ujumla katika maeneo fulani, fulani bajeti imekuwa nzuri sana, hongera sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hongera sana kwa mikakati ya kuongeza fedha kwa TARURA, kimekuwa kilio kikubwa kwa wananchi. Barabara za vijijini ni ukombozi mkubwa sana wa wananchi kuweza kusafiri wao wenyewe na kusafirisha mazao yao kwenda katika masoko, hilo ni jambo moja zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nime-calculate hapo mtaongeza karibu bilioni 400 kwa ajili ya TARURA, hicho ni kitu kimoja kizuri sana, lakini vilevile mtaongeza fedha kwa ajili ya maji, mtaongeza fedha kwa ajili ya umeme. Hiyo ni pongezi kubwa sana nawapa, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu utapata umaarufu mkubwa endapo masuala hayo matatu yatatekelezwa vizuri na kusimamiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pongezi kwangu kule mmeweka fedha shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuanza kujenga Barabara ya Ipole – Rungwa. Nawaombea mwakani muweke angalau bilioni 100 kwenye barabara hii kwa sababu, huwezi kuweka bilioni 5 kwenye barabara ya kilometa 172.

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu pongezi nyingine maji Ziwa Viktoria yatafika Sikonge, karibu zaidi ya bilioni 25 hongera sana, lakini Barabara ya Sikonge – Mbono – Kipili itakamilika. Barabara ya Tutui – Zimbili itaendelea kuwekwa changarawe, lakini vilevile tutaendelea kujenga Barabara ya Tabora – Sikonge – Mpanda ambayo nadhani ndani ya miaka miwili ijayo itakamilika. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna mpango mzuri wa kumalizia vijiji kuvipa umeme, lakini kuna kufikisha umeme kwenye Bwawa la Igumula. Kuna kufanya sensa mwaka 2022; hiyo sensa naipa kipaumbele cha juu sana na nitashiriki kwenye Jimbo langu la Sikonge siku zote za hiyo sensa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hongera sana kwa Serikali kupeleka mawasiliano ya simu kwenye kata zote za Jimbo la Sikonge ifikapo mwishoni mwa 2021/2022, lakini pongezi nyingine ni kwa Serikali kuanzisha nature reserve katika eneo la Sikonge ambayo itasaidia kupunguza eneo lililohifadhiwa na kuongeza eneo la wananchi kuishi na kufanya shughuli zao za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea utekelezaji wa mambo hayo uwe wa makini kwa sababu Serikali hii naiamini sana. Naamini hizi ahadi zote ambazo zimewekwa kwenye hotuba ya bajeti na hotuba za bajeti za kisekta naamini zitatekelezwa. Naomba sana niwashukuru sana Serikali, ahsanteni sana Serikali. Karibuni Sikonge tufanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Nyongeza ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. nakushukuru sana kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninaomba sana niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ya kuliomba Bunge liidhinishe shilingi trilioni 1.3 kwenye nyongeza ya bajeti yetu ya mwaka huu 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, waswahili walisema, usione vyaelea vimeundwa na mimi natumia nafasi hii kumsifu sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi yake na jitihada yake aliyoifanya hadi tukapata huu mkopo wa shilingi trilioni 1.3 ambao umekuwa na faida kubwa sana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jimboni kwangu peke yake nimepata madarasa 98, nimepata mashine ya x-ray, nimepata jengo la huduma za dharura na nyumba ya watumishi, na kwenye maji nimepata shilingi milioni 500. Hiyo kwa kweli ni boost kubwa sana kwa Watanzania na ni jambo ambalo linaonekana wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha na hata Waziri Mheshimiwa Masauni ambaye amewasilisha hapa, na watendaji wote wa Serikali waliohusika na hoja hii. Lakini nimpongeze Mwenyekiti wetu wa Kamati, Mheshimiwa Sillo na Makamu wake, Mheshimiwa Kigua, na Wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti kwa jinsi ambavyo wameichakata hoja hii kwa kina ndani ya vikao vya Kamati wakishirikiana na Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpango huu wa kukabiliana na athari za UVIKO Tanzania ulikuwa unahitaji shilingi trilioni 3.6, lakini zilizopatikana ni shilingi trilioni 1.3, kwa jinsi ambavyo hizo shilingi trilioni 1.3 zimekuwa na faida kwa Watanzania sipati picha tungepata hizo shilingi trilioni 3.6 hali ingekuaje. Kwa hiyo, naomba sana juhudi kama hizi ziendelee kwa sababu zina faida kubwa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiuangalia mgawanyo wa fedha hizi ambazo zinaombewa nyongeza nimeona kwamba shilingi bilioni 975.1 au asilimia 90 zimekwenda kwenye huduma muhimu za afya, elimu na maji ambayo lengo lake ni kuwakinga Watanzania wasipate maambukizi ya UVIKO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuwakinga kwa namna gani; mtu akielimika vizuri, atajikinga vizuri zaidi dhidi ya hatari za UVIKO. Kuongeza madarasa maana yake ni kupunguza msongamano kwenye madarasa ambayo hiyo ni kupunguza kitisho cha maambukizi dhidi ya UVIKO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye afya, kuboresha hizi huduma za dharura, huduma za wagonjwa mahututi, huduma za vifaatiba na vifaa vingine maana yake ni kumhudumia kwa haraka mgonjwa ili apate nafuu au apone kwa haraka. Hiyo ni kuwakinga wananchi na maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na maji hivyo hivyo; tunaambiwa kwamba ili mtu ajikinge vizuri na UVIKO anawe mikono kwa maji tiririka, sasa kama mtu hana maji atanawaje maji tiririka; maana yake ni kwamba kupeleka shilingi zote hizo kwenye maji inasaidia sana kupunguza hatari ya UVIKO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hizi shilingi bilioni 693 ambazo zinaongezwa kama mkopo kwenye SGR. Ni faraja kubwa sana kwa Watanzania kwani sasa tuna uhakika kwamba SGR inakwenda kukamilika. Kujengwa kwa kipande kutoka Makutupora mpaka Tabora ni dalili kwamba kumbe hata vipande vingine vya kutoka Tabora kwenda Mwanza, kutoka Isaka kwenda Keza, kutoka Tabora kwenda Kigoma, kutoka Uvinza mpaka Msongati, kutoka Tabora kwenda Mpanda mpaka Karema, vyote hivyo sasa hii ni dalilikwamba vinakwenda kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hii ni faida kubwa sana kwa nchi, na ninaomba sana Serikali iendelee kuhakikisha kwamba fedha zinatafutwa ili vipande vyote hivi vijengwe. Lego na faida ni nini; ya kwanza ni kusisimua ujenzi wa viwanda kwenye maeneo yote ya karibu na reli, lakini kushusha gharama za usafiri na usafirishaji, lakini tatu ni kupunguza kasi ya uharibifu wa barabara zetu; nne ni kusafirisha tani 10,000 kwa mkupuo mmoja. Hizi ni faida kubwa sana kwa uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake wote endeleeni kutafuta kila namna ili nchi hii iweze kupata maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami pia, nitoe pongezi nyingi sana kwa Serikali, hasa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Tizeba, kwa kuleta Muswada huu katika kipindi hiki muhimu kabisa. Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya mwaka 2016 pamoja na ile ya Uvuvi ni Miswada muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilikuwa nasema mara nyingi kwamba kazi za msingi za Serikali duniani kote kwenye Sekta ya Kilimo ni tatu kubwa; na katika kazi hizo tatu, ya kwanza kabisa ni utafiti; halafu ya pili ni kuwasaidia wakulima wapate mikopo, pembejeo, vifaa vya kilimo cha kisasa na ya tatu kuwalinda wakulima wapate jasho lao halali; wasinyonywe na wafanyabiashara wenye mbinu chafu ambao lengo lao ni kupata faida peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kazi hii ya msingi ambayo ni ya utafiti, naomba Serikali kama ambavyo imeleta Muswada huu, itoe kipaumbele cha kutosha kwa taasisi hii ya utafiti ili kusudi sheria hii ijitosheleze na taasisi ya utafiti itakapoanza kazi zake, ifanye kazi zake kwa ufanisi unaotegemewa. Kwanza, tafiti zifanyike; pili, taarifa za utafiti zitumike kwa ajili ya maendeleo; mafunzo kuhusu matumizi ya taarifa za utafiti yasiwe kwa wataalam peke yao, bali yafikishwe mpaka kwa wadau wakiwemo wakulima; masuala ya teknolojia yawekewe umuhimu wa kipekee na yasimamiwe vizuri ili teknolojia itumike kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii na teknolojia ni sehemu ya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wananchi wetu watabaki kutumia teknolojia zile zile za miaka yote; za tangu mwaka 1947 hatutafika popote. Vile vile bila utafiti kuhusisha masoko, mafanikio ya kilimo yatakuwa kidogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sina sababu ya kuchukua muda wako mrefu sana kujadili kitu ambacho ni kizuri sana. Nimepitia sheria yote, miundo ya usimamizi iko vizuri na mambo mengi sana yamewekwa vizuri na Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naipongeza vile vile Kamati kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kushauri. Pia naipongeza Serikali kwa mambo mengi ambayo Kamati imeshauri wameyaweka kwenye schedule of amendment. Kwa hiyo, kwa kweli, nawapongeza sana kwa hatua hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele kimoja ambacho ningependa kukitilia umuhimu wa kipekee ni source of financing. Vyanzo vya fedha vya taasisi hii ni kama vimefichwa. Naomba Serikali iweke wazi; kama nilivyosema, jukumu la kwanza kabisa la Serikali la msingi kwenye Sekta ya Kilimo ni Utafiti; ni lazima kuwe na Mfuko utakaosaidia tafiti za kilimo na Serikali itoe mchango mkubwa wa kibajeti kwenye Mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na taasisi huru kusiifanye taasisi hiyo iachwe kama yatima, iwe ndiyo kisingizio cha kutoipangia bajeti inayotosha kwa sababu wataachiwa wadau, wakiwemo wakulima kwamba sasa mazao yao yakatwe makato ili kusudi kuipa fedha Taasisi ya Utafiti. Naomba hili liwe wazi kabisa, Serikali ikubali kuweka Mfuko Maalum wa Utafiti na yenyewe ichangie zaidi ya asilimia 90 ya bajeti kwa ajili ya Mfuko huo na wadau wengine wataongeza pale ambapo patabaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu uwakilishi wa wakulima kwenye vyombo vya usimamizi, umetajwa vizuri, napongeza sana; lakini kama sifa za wale wakulima watakaowakilishwa hazitaainishwa vizuri kwenye sheria, basi unaweza ukawa na mwakilishi ambaye mchango wake ni hafifu. Kwanza, mwakilishi lazima ajue maana ya utafiti na awe na uzoefu nao ili kusudi mchango wake uwe mzuri kwenye vikao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda nizungumzie hapa ni uhusiano wa taasisi hii tunayoanzisha na taasisi nyingine zinazosimamia utafiti hapa nchini. Kamati ilizungumza sana kuhusu uhusiano na COSTECH, nami naongezea hapa, uhusiano kati ya taasisi hii tunayoanzisha na NIMR. Najua NIMR inasimamia tafiti za afya, lakini kuna baadhi ya mambo yanayohusu tafiti za afya yanahusu kilimo. Kwa mfano, kuenea kwa malaria inawezekana ikawa na uhusiano wa karibu sana na maendeleo ya kilimo, kwa sababu, malaria wale wakulima wanakolima ni kwenye maji na kwenye maji ndipo kunapozalishwa mbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo uwezekano tafiti zikagongana kati ya tafiti za afya na tafiti za kilimo. Kwa hiyo, uhusiano ni muhimu sana uwekwe vizuri kwenye hii sheria kwamba watahusianaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile COSTECH, ukisoma vizuri Sheria ya COSTECH, inaonesha kwamba, COSTECH ndiyo msimamizi mkuu wa tafiti zote, ukiacha zile za afya ambazo zinasimamiwa na NIMR. Kwa hiyo, mtafiti yeyote kwa mfano anayetoka nje akija Tanzania hapa kama anafanya utafiti; ukiwemo utafiti wa kilimo, lazima ajisajili COSTECH na afanye mtihani wa COSTECH, afaulu, ndiyo aruhusiwe kwenda kufanya utafiti wake. Kwa hiyo, ni muhimu sana uhusiano ukaelezwa vizuri kwenye sheria ili kusudi hapo baadaye kusiwe na mgongano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uzoefu wa kutosha katika hili kwa sababu nilifanya kazi Umoja wa Mataifa, UNDP na niliona kwamba COSTECH ndiyo msimamizi mkuu wa tafiti zote, ukiacha zile za afya ambazo zinasimamiwa na NIMR. Kwa hiyo, uhusiano wa taasisi hizi ambazo tunazianzisha, hii ya kilimo na ile ya uvuvi na COSTECH pamoja na NIMR ni muhimu sana ukaoneshwa vizuri kwenye sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu pili, la mwisho ni uhusiano wa taasisi hizi za Sekta ya Kilimo na Sekta nyingine wezeshi za kilimo. Mfano, huwezi kuendesha utafiti unaohusu kilimo cha umwagiliaji bila kuhusisha Sekta ya Maji. Sekta ya Maji ndiyo inabeba dhamana ya rasilimali za maji. Kwa hiyo, ni muhimu sana uhusiano ukawa vizuri kwenye sheria ili kusudi kusiwe na migongano na sekta nyingine wezeshi. Ushirikiano uwekwe vizuri na hasa kuwahusisha kwenye Kamati ndogo ndogo zitakazoundwa na kwenye Bodi na kwenye vyombo vingine vya usimamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mambo mengine, sheria imekaa vizuri. Natoa pongezi na naunga mkono Bunge hili lipitishe sheria ili zianze kutumika haraka iwezekanavyo. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2017
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Naomba nijielekeze kwenye kuchangia kuhusu DAWASA na RUBADA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilipoanzisha DAWASA ilianzisha kama mkakati wa kuhakikisha kwamba ile sheria ya zamani ya NUWA inaboreshwa na ikaanzishwa DAWASA- Dar es Salaam na katika miji mingine zikaanzishwa Mamlaka za Maji Mijini. Mamlaka za Maji Mijini kwa kweli nazipongeza zinafanya kazi nzuri sana, na hata DAWASA yenyewe nawapongeza. Isipokuwa miaka michache baada ya kuanzishwa DAWASA lilikuja wazo kwamba ni vizuri kukawa na DAWASA halafu kukawa na watu watoa huduma nyingine ambao watapangishwa miundombinu, kwa hiyo likaja wazo la kwamba tuwe na Kampuni binafsi ambayo itakuwa inatoa huduma za maji katika Jiji la Dar es salaam, na hapo ndiyo tuliingia mkataba na Dar es Salaam City Water Services

Mheshimiwa Naibu Spika, badaa ya City Water Services kukiuka mkataba ilibidi Serikali itangaze order ya kuanzisha DAWASCO ili kazi ambazo zilikuwa zinafanywa na City Water Services zifanywe na DAWASCO. Kwa hiyo DAWASCO ilianzishwa by order na kwa sheria hii marekebisho yaliyoko hapa yaliyowasilishwa leo maana yake ni kwamba DAWASCO inakufa na shughuli zake zote zinahamia DAWASA kama idara. Kwa hiyo, hilo kwa kweli napongeza sana Serikali kwa uamuzi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, uamuzi huu umechelewa kwa sababu kuwa na taasisi hizi mbili tumeingia gharama kubwa sana. Unajua pale DAWASA kwa kiasi kikubwa walikuwa wanafanya kazi kubwa ya kutafuta fedha tu kwa ajili ya miundombinu mikubwa, kwa hiyo kwa muda mwingi walikuwa wako ofisini pale kwenye viti vya kunesa nesa zaidi wakati kazi hasa ya kutoa huduma ilikuwa inafanywa na DAWASCO; kwa hiyo kwa sasa hivi watafanya kazi zote; kutafuta fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Maji kutoa huduma. Kwa uamuzi huu nawapongeza na itakuwa ni efficiency kubwa tunayoitegemea kutokana na maamuzi haya. Naipongeza sana Serikali kwa maamuzi haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wakati tulitembelea Durban kuangalia namna wanavyofanya kazi na tutakuta Durban pale ile Umgeni Water Resources inatoa maji kama bulk kwa Mamlaka tatu ambazo zinatoa huduma za maji pale Durban.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza, katika mpango huu ambao tunauanzisha leo tukipitisha hapa; kwamba Kanda za DAWASA zilizopo sasa hivi ambazo zilikuwa ni Kanda za DAWASCO ziimarishwe kama ambavyo TANESCO wameimarisha kanda zao ili kusudi maamuzi mengi na usimamizi mwingi ufanyike kule kwenye Kanda badala ya kufanyika Makao Makuu; hiyo itaboresha mawasiliano kati ya wateja na DAWASA.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia waanzishe vitengo vya dharura, kwa sababu wao ni kama vile hawana. Ningependa wajifunze zaidi TANESCO. TANESCO wana utaratibu mzuri sana wa kushughulikia mambo ya dharura, wana namba maalum wa kushughulikia wakati wa dharura sasa kuna wakati mabomba yanapasuka, kuna wakati wateja wazuri tu wanakosa maji kwa sababu bomba limepasuka. Naomba sana waimarishe kitengo cha dharura ili kuboresha response mara inapojitokeza dharura

Mheshimiwa Naibu Spika, nikichangia kuhusu RUBADA. RUBADA ilianzishwa kama taasisi baada ya uamuzi wa kutekeleza au uamuzi wa kujenga mradi wa Stiegler’s Gorge. Ule mradi wa Stiegler’s Gorge, kama project, ulipokubaliwa na Serikali miongoni mwa masharti yake ilikuwa ni kuanzisha RUBADA ili kusudi iwe Taasisi ya kusimamia utekelezaji wa ule mradi. Sasa bahati mbaya sana RUBADA ilipoanzishwa ikawekwa chini ya Wizara ya Kilimo na mradi wenyewe kitaalam ulitakiwa uwe chini ya Wizara ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri hiyo ni kengele ya kwanza. Kwa mujibu wa utaalam ulivyo ule mradi wa Stiegler’s Gorge ilitakiwa hata RUBADA ilivyoanzishwa iwe chini ya Wizara ya Nishati na Madini; tusingepata malalamiko na manung’uniko na kutokuelewana sana kwenye utekelezaji wa ule mradi. Hata hivyo, kwa kuwa sasa Serikali imeamua kuhamishia ule mradi wa Stiegler’s Gorge kwenye Wizara ya Nishati na Madini maana yake ni kwamba ile RUBADA inakuwa imekosa ile root of origin, kwa hiyo inakufa kifo cha kawaida

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu ya uamuzi huu naiomba Serikali ifikirie sana namna bora ya kuimarisha RUBABO; kwa sababu kualikuwa na RUBADA na RUBABO; RUBABO ni Rufiji Basin Water Board, ndiyo nimeiita mimi RUBABO. Sasa hii Rufiji Water Basin Board na RUBADA zilikuwa zinafanya kazi kwenye bonde lile lile na wakati mwingine walikuwa wanatekeleza majukumu yanayofanana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa sababu Rufiji Basin Water Board bado ipo, napendekeza Serikali ifikirie sana namna bora ya kuimarisha Rufiji Basin Water Board kwa sababu tayari Rufiji Basin Water Board wanao mkakati wa muda mrefu wa namna bora ya kusimamia matumizi ya maji katika bonde la Rufiji kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza sana, wakati watakapokuwa wanafanya mgawanyo wa mali na madeni ya RUBADA wazingatie sana namna ya kuimarisha Rifiji Basin Water Board au Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji ili kusudi bodi hii ya bonde la maji la Mto Rifiji iweze kufanya kazi yake vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu kwenye Sheria ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nitoe pongezi tatu. Pongezi ya kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwa uwasilishaji mzuri. Uwasilishaji wenu tumeuelewa, mlikuwa very eloquent lakini brief to the point. Hongereni sana, tumewaelewa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi za pili, naomba niipongeze nchi yangu Tanzania kwamba kama tulivyomsikiliza Mheshimiwa Mkuchika pale alipopewa nafasi siku ile alivyokuja mara ya kwanza Bungeni baada ya kuumwa alituambia kwamba akiwa India na baada ya kusikia habari ya ile transfer of power ambayo ilifanyika hapa Tanzania akapata furaha na amani kwamba sisi Tanzania tuna Katiba nzuri sana ambayo imetuvusha kwenye mawimbi makali. Tumepata msiba ambao Tanzania hapa haujawahi kutokea tangu uhuru wa kufiwa na Rais ambaye yuko madarakani lakini tumevuka salama kwa sababu tuna Katiba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tumepitisha bajeti hapa ambayo kwa kazi zake za awali za maandalizi ilisimamiwa na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa takriban asilimia 70. Baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais kuapishwa kuwa Rais alichukua kijiti kile kwa umakini mkubwa akaendeleza pale ambapo Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliishia na hakutaka kubadilisha vipaumbele bali akaja na
kaulimbiu ya Kazi Iendelee kumaanisha kwamba anaendelea na vipaumbele vilevile ambavyo vilikuwa vya Rais, Hayati Dkt. Magufuli. Jambo hilo ni la kujipongeza sana kama nchi, sio nchi zote zinaweza kufikia hatua kama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi za tatu, nimpongeze Waziri wa Fedha na timu yake yote ya Serikali chini ya usimamizi wa Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo wamekuwa wasikivu kwa hoja za Wabunge humu Bungeni lakini wamekuwa wasikivu kwa Kamati ya Bajeti na wadau mbalimbali ambao walikuja kuwafuata na kujadiliana nao. Hii ni hatua muhimu sana na ndiyo maana upitishaji wa bajeti wa jana umevunja rekodi ya miaka 25 iliyopita. Tangu mwaka 1995 Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi haijawahi kutokea bajeti ya nchi ikapita humu Bungeni bila kura ya ‘Hapana’ hata moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko hapa kwa ajili ya Sheria ya Bajeti na sheria hii ndiyo ambayo itahakikisha kwamba tunapata zile shilingi trilioni 36.3 kwamba tutazipata baada ya sheria hii kupita na itumike kuhakikisha kwamba tunapata hayo mapato ambayo tulilenga. Bila sheria hii kupata shilingi trilioni 36.3 itakuwa ndoto. Vipaumbele alivyotaja Mheshimiwa Waziri, elimu, afya, maji, barabara vijijini, miradi mikubwa na uendeshaji wa Serikali. Ni jambo ambalo inatakiwa tutafakari sana tunapozungumzia sheria hii kwa sababu tunahitaji kuzipata hizi shilingi trilioni 36.3. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana lugha ambayo Mheshimiwa Waziri aliitumia katika baadhi ya maeneo kwenye hotuba yake alizungumzia kuhusu kufunga mikanda. Lugha hii imetumika kututayarisha Watanzania kuwa Serikali inakuja na mbinu mbalimbali ambazo zitahakikisha kwamba tunatimiza matarajio yao ambayo walituchagua mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mbinu kadhaa ambazo zimeainishwa kwenye sheria hiyo. Mbinu ya kwanza kwa mfano kodi mpya kwenye baadhi ya maeneo, mfano, kodi ya kwenye muda wa maongezi, ukosaji wa kodi za majengo kupitia malipo ya umeme wa LUKU na maeneo mengine Serikali imeamua kutoa msamaha wa kodi kwa mfano, kuingiza simu janja kutoka nje, hili ni eneo ambalo limesamehewa kodi. Vilevile kuna baadhi ya maeneo kwenye sheria yamewekwa ili kuimarisha ukusanyaji na udhibiti wa mapato. Mfano, mapato ya bandari, TCRA na taasisi nyingine kama hizo kukusanywa kupitia akaunti moja, akaunti kuu. Hii itaongeza udhibiti wa mapato, hongera sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mikakati na mbinu hizo, naomba niishauri Serikali katika maeneo machache yafuatayo. Kwanza, fedha zote ambazo zitapangwa kwa ajili ya miradi ya kipaumbele, hiyo ya barabara vijijini, barabara za mitaa ambako hakuna barabara, maji na miradi ya afya na elimu ile ambayo iliongezwa, kama haitakuwa ring fenced itatumika kwa kazi nyingine. Hata kama fedha itaingizwa kwenye Mfuko wa Barabara maana hakuna sheria nyingine, ziende zikiwa ring fenced ili zisitumike kwa matumizi mengine bali kwa yale yaliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa pili kwa sababu Serikali iliahidi jana maeneo yanayokaribia shilingi trilioni moja na Mheshimiwa Waziri akasema tunawaongezea sekta. Mimi najua ni mchumi, mtaalam wa bajeti kabisa, kama Serikali haina mpango wa kuleta mini budget mwezi Desemba au Januari mwakani, maana yake ni kwamba kutakuwa na re-allocation ya kupunguza kwenye baadhi ya mafungu kupeleka kule ambako Mheshimiwa Waziri alitaja kama ni vipaumbele. Kwa hiyo, ni vyema Bunge lako Tukufu likapata angalau hint kwamba ni mafungu gani ambayo yatapunguziwa hizo fedha ili ziende kwenye yale ambayo Serikali sasa imekuja na zile ahadi ambazo Mheshimiwa Waziri jana alizitamka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli mimi baada ya kusema hayo, nisingependa niongeze maneno mengi yanaweza yakachafua utaratibu. Kwa hiyo, niseme tu naunga mkono hoja ya Waziri kuipitisha sheria hii, ahsante sana. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 6) Bill, 2021
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza napenda kupongeza sana sana Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali sana watanzania. Baada ya kuwa malalamiko yamekuwa mengi ndani ya Taifa letu malalamiko yamefika kwa Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais akaagiza kwamba sheria ambayo tulokuwa tumeipitisha mwezi wa 6 basi kile kifungu ambacho kilikuwa kinatoza asilimia mbili ya kodi ya zuio (withholding tax) kile kifungu kifutwe, kwa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni dalili moja wapo kwamba Serikali yetu inawajali wananchi pale ambapo zinatokeza changamoto Serikali inaitikia haraka kuweza kuondoa changamoto za aina kama hiyo. Mwanzoni wakati tunapitia sheria tulikuwa tumelenga kwamba watakaotozwa hiyo kodi yawe makampuni, lakini bahati mbaya sana sheria ile imepeleka mkono wake kutoza kodi kwa wananchi moja kwa moja, kwa wakulima moja kwa moja kwa hiyo kwa kweli ilikuwa ni usumbufu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii Bunge lako niliombe kwamba litoe shukrani kwa Serikali kwa hatua hii, maana yake Serikali ingeweza kukaa kimya na bado sisi tungeweza kulalamika na ingeweza kumaliza hata mwaka lakini haijamaliza hata miezi 6 tuemeweza kufuta hicho kipengela, kwa hiyo ni jambo la kushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha naye kwa kulichukua hilo na kulifanyia kazi, na nikupongeze na wewe kwa kulipokea hilo na kulifanyia kazi, na vile niwapongeze wajumbe wa kamati ya bajeti kwa kulifanyia kazi, hongera sana kwa kila Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna masuala yanayohusu miradi ya mikakati, na mradi mmoja wapo wa mkakati ambao tulisaini na wenzetu wa Uganda ni ule mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoyma, Uganda mpaka Chongeleani Tanga, huu ni mradi wa kimkakati na ni mradi ambao unabeba rasilimali yenye sifa za kidunia, na fadia zake kwa nchi yetu ni kubwa sana na hatua ambayo imechukuliwa ya kuleta marekebisho ambayo yanakwenda kuharakisha utekelezaji wa mradi huo ni ya manufaa makubwa sana kwa uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niipongeze Serikali kwa kukubaliana na kamati kufanya marekebisho ambayo yamefanywa ili kuweka jina halisi la mradi ule husika ambao baada ya mkataba ule kusainiwa na Serikali uliletwa hapa bungeni ukawa ratified na sisi kwa kweli imekuwa jukumu letu kama wabunge kuhakikisha tunaiunga mkono Serikali kwa ajili ya maslahi ya watanzania wote kwa ujumla, kuhakikisha vikwazo ambavyo vingeweza kufanya mradi ule uweze kuchelewa. Kwa upande wa Tanzania tunaviondoa kwa haraka kupitia marekebisho ambayo yamefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimpongeze kila aliyeshiriki, nimpongeze kila Mbunge nikupongeze Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali kwa hatua ambayo imefikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, isipokuwa maoni yangu ya nyongeza nilikuwa nafikiri kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali ananisikiliza hapa, nilikuwa nafikiri kwamba katika maandishi yale ya mwisho yaweke time frame kwamba yale tuliyoyaandika pale na kuyapitisha basi yaishie kwenye mwisho wa utekelezaji wa mradi isiwe kipengele kile kiachiwe tu kwa miaka 100 ijayo hapana, mradi utakapokamilika kutekelezwa basi iwe ndio mwisho wa kile kipengele ambacho tumekipitisha, zile incentive zote ambazo zinakuwa zimepitiswa. Nadhani hiyo ni kengele ya kwanza?

Mheshimiwa Spika, niipongeze pia kwamba katika majadiliano ambayo yamefanyika ya kuondoa yale mapendekezo maengine mawili, yalikuwa ya msingi kabisa…

SPIKA: Huko kwa sababu hilo jambo halijaletwa humu, sio sehemu ya mjadala huu sasa.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika nakushukuru sana, lakini nilikuwa napenda niseme kwamba mshikamano ambao umeonyeshwa kati ya…

SPIKA: Ahsante sana kama nia yako ni kujadili hilo…

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kuunga mkono hoja, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu wa Mwaka 2022
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami nianze kwa kumpongeza sana

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaendelea kuiweka nchi yetu katika ramani ya dunia; maana natambua kwamba vipengele hivi vya sheria ambavyo tunaenda kuvirekebisha leo, vinazidi kuiweka katika ramani nchi yetu kwamba inatekeleza good practices katika uga wa Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka kwamba chimbuko la Sheria hii na chimbuko la kazi hizi ilitokana na tangazo au taarifa juu ya uzingatiaji wa viwango na kanuni msimbo vya Kimataifa (Report on Observance of Standard and Codes) ya 1999 ambayo baadaye ndiyo ilipelekea tukatunga Sheria ya Uzuiaji wa Fedha Haramu, au ya kupambana dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu mwaka 2007.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo yanaletwa hapa marekebisho ya nane, lakini marekebisho haya yamekuwa comprehensive na yamegusa pia ugaidi; kuzuia ufadhili wa ugaidi na kuzuia ufadhili wa silaha za maangamizi. Kwa hiyo, hizi developments ni nzuri sana na inaifanya Tanzania ionekane kwenye Jumuiya ya Kimataifa kwamba na sisi ni mfano wa utekelezaji mzuri wa maazimio ya Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa hivi ni mengi, wanajua; lakini kazi ya sheria mpya inalenga kuweka misingi mizuri zaidi ikiwemo tathmini ya vihatarishi, kuwatambua wateja, utoaji wa taarifa kuhusu viashiria vya utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi. Kwa hiyo, majukumu yanaongezeka. Maana yake nini? Majikumu yakiongezeka hayaongezeki kwenye kitengo tu hiki cha Intelligence Unit, yanaongezeka na kwenye idara nyingine ambazo zinahusika katika utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nina maangalizo matatu tu. Angalizo la kwanza, uelewa wa Tanzania kuhusu mambo haya bado uko chini sana. Kuna watu wengi wanaweza wakawa convicted, wakashitakiwa Mahakamani kwa kufanya mambo kwa kutokujua. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iwekeze kiasi kikubwa cha fedha na watu kwa ajili ya kuendesha public campaign ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanaelewa sheria hii inahitaji nini kutoka kwao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kuwa sheria hii itawalazimisha watoa taarifa wawatambue wateja wao kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengine wamesema, ni muhimu sana kama Taifa tuimarishe mifumo ya utambuzi. Mifumo yetu ya utambuzi bado ni duni sana, hata ukichukua kitambulisho cha Taifa uka-click kwenye information ya mtu utakuta hapo cheti cha form four, tarehe ya kuzaliwa, basi. Yaani vitu ni vichache mno vinavyomhusu mtu. Hata kama alifungwa hizo taarifa haziko kwenye hiyo database.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunafanya nini; huyu mtu atatambuliwaje vizuri na huyu mtoa taarifa? Kwa hiyo naomba sana kama Taifa tuimarishe mifumo ya utambuzi. Sina wasiwasi na ndugu Ismail ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, lakini anatakiwa asaidiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwezekana mpaka mwakani mwezi Juni, Watanzania wote wawe wamepata personal identification number na Kitambulisho cha Taifa kipewe kipaumbele kwenye bajeti. Kama hawapewi kipaumbele kwenye bajeti wataendelea kutumia mifumo ya zamani ambayo haitawawezesha Watanzania kuwa bora kwenye mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ugaidi; naamini wasimamizi na watekelezaji wa sheria watakuwa makini kupima dhamira maana yake dhamira ndiyo ita-determine kama kosa lile lilikuwa la ugaidi au siyo. Kwa hiyo wasimamizi wawe makini kupima hiyo dhamira, kuiangalia kwanza, hiyo dhamira ndiyo ita-develop ushahidi ambao utam-convict mtuhumiwa mahakamani, lakini kama itakuwa ni kuchukua tu tukio juujuu hivi itakuwa ni kitu ambacho siyo kizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba Serikali ifikirie kuanzisha taasisi kubwa, kama sheria hii tutaipitisha, ikipita leo inaanzisha majukumu makubwa, kama kitengo ni kilekile hatutakuwa tunafanya chochote. Inawezekana mambo mengine yakaachwa bila kubadilika. Naomba Serikali ianzishe taasisi kubwa inayojitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha wa Mwaka 2022
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye huu Muswada. Jambo la kwanza niipongeze sana Serikali kwa kuja na mapendekezo ambayo yatakwenda kusaidia sana kuboresha maeneo ambayo kweli yalikuwa na matatizo. Hizi Sheria Tano zinazorekebishwa yale maeneo yanayorekebishwa yalikuwa yanaleta matatizo ya kuchelewesha hasa baadhi ya miradi na kuchelewesha uwekezaji na kuathiri hasa hasa eneo la wakulima.

Mheshimiwa Spika, tunayo miradi mikubwa ya kimkakati ya uwekezaji mahiri imechelewa kwa muda mrefu, mradi kama Liganga na Mchuchuma na miradi mingine ya aina hiyo, kama hii miradi ambayo tunaendelea kuzungumza kuhusu ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ina elements kama hizo. Nahisi kwamba sheria hii marekebisho haya hasa kwenye eneo hilo yamechelewa sana na yametuchelewesha kweli kupata faida kubwa kutokana na uwekezaji kwenye miradi hii mikubwa.

Mheshimiwa Spika, kuna sheria ya uwekezaji nzuri, imeweka utaratibu mzuri, tunakwenda kwenye Baraza la Ushauri la Uwekezaji chini ya Waziri Mkuu mwenyewe kabisa na Mawaziri ni Wajumbe, lakini wakitoa maamuzi au ushauri au mapendekezo, Waziri wa Fedha alikuwa anakosa power ya kuweza kutekeleza mapendekezo ambayo yametoka kwenye Baraza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo marekebisho ambayo yanakuja kupitia marekebisho haya, yanakwenda kumpa nguvu sasa Waziri wa Fedha baada ya approval ya Baraza ili aweze kutekeleza mapendekezo ya Baraza la Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, napenda kuwashawishi wenzangu kwamba tukubali, Bunge likubali marekebisho haya ili kuweza kuisaidia nchi kutekeleza miradi mikubwa ambayo inayo faida kubwa kwa nchi.

Mheshimiwa Spika, ninapongeza sana kile kipengele ambacho kimewekwa cha kuweka angalizo ili hawa watakaopewa misamaha wasiitumie vibaya, napenda kuiomba Serikali iwe macho ili hawa ndugu zetu ambao watakuwa wamepewa misamaha basi waitumie vizuri misamaha hiyo kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kumekuwa na kilio cha siku nyingi sana kuhusiana na togwa la zabibu au wengine wanaita mchuzi tulikuwa tunabishana ni mchuzi au togwa? Mimi nadhani mchuzi ni ule wa nyama sasa hii kuita mchuzi wa zabibu kidogo ilikuwa inaleta shida. Kwa hiyo, mimi napenda kutumia neno togwa la zabibu.

Mheshimiwa Spika, wakulima wengi wa Dodoma hapa walikuwa wanalalamika sana kwamba wanakosa soko na mambo kama hayo. Kwa hiyo, hii hatua inayo pendekezwa hapa ya kuongeza kodi kwenye uagizaji wa nje wa bidhaa hizi za togwa la zabibu na wines ni hatua ambayo itasaidia wakulima wetu wapate soko. Kwa hiyo, ni jambo ambalo sasa na Wagogo nao wataanza kupata uchumi kutoka kwenye kilimo, akina Mheshimiwa Simbachawene hawa. Kwa hiyo, wenzetu hapa sasa Wagogo wataanza kuongeza uzalishaji kwa sababu sasa watakuwa na soko la uhakika, hii ni hatua ambayo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ambalo ningependa nilizungumzie kutokana na marekebisho haya ni eneo la mbolea. Tangu tulipopata janga la UVICO-19 viwanda vilifungwa duniani, karibu viwanda 6,000 vilifungwa duniani vya kuzalisha mbolea, kukawa na uhaba mkubwa sana wa mbolea, sasa kwa sababu sisi hatuna kiwanda cha mbolea ndani ya nchi tunategemea kuagiza nje gharama za usafirishaji na ununuzi zilipandisha bei ya mbolea kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo hatua hapa ambayo kwanza naanza kuipongeza Serikali kwa hatua ambayo imechukua mwaka huu ya kuweka ruzuku kwenye mbolea ambayo imeshusha bei ya mbolea ni hatua muhimu sana hongera sana Mheshimiwa Rais, hongera sana Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha hiyo ni hatua muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni hatua ambayo sasa inakuja ku-target kupunguza gharama za uzalishaji kwa kupunguza mrabaha kutoka asilimia Tatu hadi asilimia Moja kwenye enforcement ambayo ni malighafi muhimu kwenye utengenezaji wa mbolea, hii ni jambo ambalo ni muhimu sana na kwa kweli limekuja katika wakati muafaka kwa nchi hii ambapo sasa tunaenda kuwa na kiwanda kitakachozalisha tani Laki Sita za mbolea hapa hapa Dodoma na tuna kiwanda kingine kule Manyara cha Minjingu kinazalisha nadhani karibu tani Elfu Thelathini sina takwimu sahihi. Kwa hiyo, ina maana kwamba katika muda mfupi ujao kupitia kipengele hiki tutaenda kushusha gharama za mbolea inayozalishwa nchini. Kwa hiyo, hii nayo ni hatua ambayo kwa kweli ni ya kupongeza sana Serikali na tukipitisha humu haya marekebisho ya sheria basi tunaenda kumsaidia mkulima wa nchi hii aweze kupata mbolea inayozalishwa ndani ya nchi kwa gharama nafuu. (Makofi)

Pili, ninaipongeza Serikali imekuwa sikivu sana kwenye majadiliano hasa hasa mwanzoni tulipokuwa tunapendekeza kwamba madini ya chokaa nayo ni muhimu sana katika utengenezaji wa mbolea. Kulikuwa na debate kubwa kulikuwa na mazungumzo marefu kwamba sasa tutadhibiti namna gani kwa sababu chokaa inayo matumizi mengi kwenye viwanda, kwenye ujenzi na kwenye maeneo mengine. Chokaa yenyewe ukimwaga kwenye ardhi inaongeza rutuba kwenye ardhi, chokaa yenyewe chokaa yenyewe ni mbolea vilevile chokaa yenyewe ni malighafi katika kutengeneza mbolea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hii hatua ya kukubali chokaa nayo iingizwe isipokuwa waongeze tu usimamizi na udhibiti ni jambo la kuipongeza sana Serikali, naomba sana Bunge lako Tukufu likubali marekebisho haya ili kumsaidia Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba sana niseme kwamba naunga hoja mkono. Ahsante sana. (Makofi)