Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mussa Hassan Mussa (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MUSSA HASSAN MUSSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ambayo imewasilishwa asubuhi hii. Kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama Samia Suluhu Hassan, kwa namna ya maoni yake na uoni wake na maneno yake. Mheshimiwa Samia amenikosha sana kusema kwamba yeye na Hayati Dkt. Magufuli ni kitu kimoja. Hii ni kuonesha kwamba ile shughuli ambayo alikuwa anaifanya basi yeye ataiendeleza na kwa kweli yote ni mema.

Mheshimiwa Spika, jana tu nimemsikia Makamu wa Rais anasema kwamba hana msamaha na mtu yeyote ambaye atachezea Muungano wa Jamhuri ya Muungano. Sasa nataka nimseme Waziri, namsema kwa nia njema kabisa; muda mfupi tu kuteuliwa Waziri, Mheshimiwa Jafo, tayari amefanya ziara Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, sisi tulikuwa tuna kitu choyo tunapoambiwa huyu ni Mbunge, pia ni Diwani katika halmashauri yake, kitu hiki kwetu hakipo. Athari yake ni nini? Mbunge anashindwa kushiriki kuona miradi ya maendeleo ndani ya jimbo lake, ile iko kwenye halmashauri na anayeshiriki pale ni Diwani, basi.

Mheshimiwa Spika, sasa katika kuweka mambo haya kuwa mema, tulitazame hilo. Kwa upande wa kwetu kule tutafanya hivyo lakini kwa sababu itakuwa ni sheria basi na hapa najaribu kuwachombeza Waheshimiwa Wabunge tufanye hivyo.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, kama hilo halitoshi, tunapozungumza suala la Muungano tumekubaliana wote kwamba Muungano ni Tunu ya Nchi yetu na Muungano huu tunapoita Tanzania chanzo chake ni Tanganyika na Zanzibar, bila Zanzibar kulikuwa hakuna neno Tanzania. Sasa neno Tanzania ni tunu na lazima tulidumishe lidumu.

Mheshimiwa Spika, cha msingi, Zanzibar imetoka wapi? Zanzibar huru imetoka kwenye Mapinduzi ya tarehe 12, Januari, 1964. Ukienda ndani, Zanzibar imetokana na nani? Wazanzibari watatu; Karume, Thabit Kombo, Hamid Ameir na mwingine anatiliwa kwamba yuko upande mmoja Bara, mmoja Zanzibar, lakini waliobakia wote ni watu kutoka Bara. Hizi tofauti zinatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waliofanya mapinduzi pale, kuna mtu anaitwa Edington Kisasi, Mchaga; Hamis Daruweshi, mtu wa Songea; Natepe, mtu wa Kusini Lindi; hao ndio waliofanya Mapinduzi ya Zanzibar na ikawa Zanzibar huru na Muungano umekuja kwa Zanzibar ambayo imeshakuwa huru na Tanganyika, ndiyo tukapata neno Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa vijana wenzangu, maana mimi bado kijana, nataka niwaambie; kama wazee wetu walifanya jitihada hiyo na nilikwishasema kwenye Bunge hili, kwamba barua imetoka tarehe 22, Aprili kwa marehemu mzee Lusinde ambaye yuko Dodoma, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema na mzee Moyo, wote wameshatangulia, wale kama ndio wameanzisha huu Muungano, sisi kwetu ni kuuendeleza. Sasa hii tofauti, huyu Mzanzibari, huyu nani, sasa sote hapa tuna jina moja, Watanzania. Mzanzibari au Muunguja na Mpemba ilikuwa pale miaka ya nyuma ya 1964, sasa sote ni Watanzania, tumeungana tuko katika nchi moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kumwambia Ndugu yangu, Mheshimiwa Jafo; hebu atufanyie utaratibu katika uratibu wake wa Mfuko wa Jimbo. Wenzetu Bara wameshamaliza kutumia hela ya Mfuko wa Jimbo, sisi Zanzibar imetoka juzi baada ya yeye kwenda. Inazunguka sana. Hebu tuandae utaratibu wa kwamba ule Mfuko unapotoka sisi tuwe Zanzibar pale tuufanyie kazi, lakini umetoka juzi sisi tuko Bungeni, miezi mitatu.

Mheshimiwa Spika, ukimuuliza Mbunge wa Mainland huku atakwambia tayari amemaliza miradi yake. Sisi tuko hapa shughuli yenyewe bado, wengi wetu hatujaipokea.

Mheshimiwa Spika, huu muda wa leo, ni sawa. Nakushukuru sana na naunga mkono hoja; ahsante. (Makofi)