Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. John Peter Kadutu (14 total)

MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninamuomba awahakikishie wananchi wa Kata hizo kwa sababu siyo wote ni wakimbizi, ni lini zoezi hilo la naturalization litakamilika ili kusudi nao wapate kutimiza haki yao ya kidemokrasia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, mchakato pale ulikuwa ni mpana sana, kama alivyosema pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba zoezi lile lilikamilika na kuhakikisha Kata zinapatikana lakini ilikuwa ni baada ya uchaguzi, baada ya hapo kuna zoezi kubwa la integration ambalo linafanyika ambalo lina-involve pesa na awali mchakato uliokuwa unaendelea ni suala zima la kupata fedha kutoka Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa sababu Serikali ime-invest vya kutosha kuhakikisha wakimbizi hawa wanakuwepo maeneo haya kipindi chote, maana yake Serikali ya Tanzania ilitumia jukumu kubwa la kiutu na kiubinadamu na resources nyingi sana kuhakikisha wakimbizi hawa wanakuwepo, lakini suala la kuhakikisha unajenga miundombinu ni jambo lina-involve pesa.
Kwa hiyo, Serikali iko katika mchakato kuangalia jinsi gani tutafanya, suala la kujenga structure zikamilike baadaye basi uchaguzi uweze kufanyika, kwamba sasa eneo lile uchaguzi ufanyike rasmi baada ya kuwa na muundo rasmi wa Serikali za Mitaa. Ahsante.
SPIKA: Ahsante sana, tunaendelea na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, swali linaulizwa na Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kwa niaba yake tafadhali endelea.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza, je, Serikali iko tayari kuwahakikishia wananchi hawa ni lini wale ambao hawajaamua kubaki au kuondoka na kurudi Burundi? Kwa sababu siyo kweli kwamba watu wote wameshapata uraia; wako ambao hawajapata na hawajasema wanataka nini. Je, Serikali iko tayari kutoa tamko nini kifanyike?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna takribani wakimbizi 8,800 ambao hawajapatiwa uraia kati ya wale 162,000 na zaidi ya wale ambao walipatiwa uraia, lakini kulikuwa na sababu kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa sababu hizo ni kwamba wengine ni watoto wa wakimbizi ambao walizaliwa baada ya wazee wao kupata uraia, lakini wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa hajaidhinisha bado uraia. Wapo wengine ambao hawakupewa uraia; walinyimwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo hali zao za uhalifu na mambo mengine ambayo hayakuweza kukidhi vigezo na sifa za kupata uraia nchini kwetu.
Mheshimiwa Spika, sasa ninachoweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwa wale ambao hawakupata uraia na wamekidhi vigezo na wameomba uraia, maombi yao yanashughulikiwa na yatakapokuwa yamekamilika watapewa uraia kwa wale ambao watakuwa wamekidhi vigezo.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Waziri wa Wiwanda, ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka ya karibuni viwanda vingi vilibinafsishwa na kuuzwa, vikiwemo viwanda vya mazao ya kilimo na mifugo na kubadilishwa matumizi yake.
Je, Serikali iko tayari kuhakikisha madhumuni ya awali yanatekelezwa kama ilivyoainishwa uko mwanzo?
Swali la pili, kwa vile suala la vipimo vya kienyeji, kama rumbesa na ndoo, maarufu kama Msumbiji limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu; Je, Serikali haioni kuna haja ya kutoa tamko ni lini hasa wakala wa vipimo na mamlaka za Serikali za Mitaa zitaanzisha hivyo vituo? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya kujenga uchumi wa viwanda, inaendana na utaratibu wa kuhakikisha viwanda vyote vile vilivyobinaifishwa vinarudi kufanya kazi. Wale ambao walipewa viwanda hawakuuziwa walipewa, kwa sababu walilipa kishika uchumba tu, hawakulipa fedha kamili ya kununua kiwanda, ni kwamba wanapaswa wavirudishe. Na napenda nitoe taarifa kwa Bunge lako Tukufu kwamba wanaitikia vizuri na wote watakuja kuendesha viwanda kwa misingi ambayo walikusudia. Atakayeshindwa atanyang‟anywa na atapewa Mtanzania mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mkapa, alikuwa na dhamira safi ya kuwapa Watanzania ili kusudi watoke, wajijenge kiuchumi lakini dhamira yake watu wakaitumia vibaya ndiyo hayo wakaenda kutumia viwanda ambavyo havikukusudiwa.
Mhesheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, vipimo aina ya rumbesa, Msumbiji, na wengine wanaita badimanyaira. Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, wameshatoa maelekezo na mtakuta hata njiani, mimi napokea simu nyingi, watu wengi wanakamatwa. Uuzaji wa mazao unakuwa na vituo maalum na Maafisa Ugavi na Watendaji wa Kata, ni moja ya jukumu lao kufika maeneo yale na mnunuzi yeyote hakikisha unapima kilo zisizidi 100. Nitafanya jitihada zaidi kuhakikisha kwamba tunawapelekea mizani kadri tutakapopata uwezo wa kuweza kununua mizani hiyo ili kusudi wananchi pamoja na kupima usawa wa gunia lakini wawe na uhakika kwamba ni kilo 100 tu, wasiwanyonye wauzaji.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu yenye kukatisha tamaa, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa mpango wa kujenga kwa lami inaonekana haupo kwa sasa na kwa kuwa barabara hizi mbili zinatengenezwa vipande vipande kila wakati na kuleta usumbufu kwa wananchi wetu: Je, sasa Serikali iko tayari kujenga kwa kiwango cha changarawe barabara nzima badala ya vipande vipande?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Kadutu kwa uamuzi huo ambao naweza kuuita wa kihistoria wa kurudi nyuma. Ila namwomba sana Mheshimiwa Kadutu, tunapojenga vipande vipande, hatimaye tutakamilisha.
Nami siamini kama wananchi wa Ulyankulu watapenda barabara hii ibakie katika kiwango cha changarawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwa namna anavyotusumbua ofisini, maana yake nimeambiwa na Waziri wangu jinsi alivyokuwa anapoteza muda wake pale Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia ujenzi wa barabara hii. Namhakikishia kile ambacho tulimwambia ofisini tutakitekeleza. Atupe fursa ya kujenga vipande vipande hadi itakapokamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hii barabara ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 na namhakikishia katika kipindi hicho tutatekeleza ahadi hiyo ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoahidiwa.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nimuulize Waziri swali dogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Bodi ya Tumbaku inafanya kazi ndani ya Serikali na kwa maagizo ya Serikali; na kwa kuwa Bodi ina upungufu wa fedha unaosababisha kutokupatikana wanunuzi wengi wa kutosha, je, Serikali iko tayari kuwaongezea Bodi ya Tumbaku pesa ili waongeze wanunuzi wa tumbaku na kuongeza masoko? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Bodi ya Tumbaku inakabiliwa na changamoto za fedha. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikijaribu kuangalia uwezekano wa Bodi za Mazao kujitegemea zaidi badala ya kutegemea ruzuku ya Serikali. Kwa hiyo, utaratibu ambao unatumika ni kuhakikisha kwamba Bodi ya Tumbaku inaweza ikapata fedha za kujiendesha yenyewe bila kupata ruzuku kubwa kutoka Serikalini. Ndiyo maana tunafikiria kuwa na Mfuko wa Bodi ya Tumbaku kama ilivyo kwenye korosho na kahawa ili wadau wenyewe waweze kujiendesha bila kuingiliwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimueleze vilevile Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la soko la tumbaku ni zaidi ya ukosefu wa fedha kwa Bodi ya Tumbaku. Soko la tumbaku linaathirika na namna zao linavyochukuliwa duniani. Wote mnafahamu kwamba tumbaku ndiyo zao la pekee ambapo kunakuwa na vita sana kwa hiyo inafanya wanunuzi wengi mara nyingine wasijiingize kwenye tumbaku. Hata hivyo, tunaendelea kutafuta aina zingine za tumbaku ambazo zinawavutia watumiaji wengi hasa Wachina.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumiaji wa China wanapendelea tumbaku inayozalishwa Zimbabwe. Kwa hiyo, tumeongea na Bodi ya Tumbaku wajaribu kuangalia ni namna gani tumbaku ambayo inazalishwa katika maeneo mengine kama Zimbabwe na ambayo inapendwa na watumiaji wengi wa China inaweza ikaoteshwa nchini. Kwa hiyo, jitihada zinaendelea kwa ajili ya kuweza kuimarisha bei ya tumbaku.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa vile Mradi huu wa REA katika Jimbo la Ulyankulu umekuwa ukisuasua na wakati mwingine unatia hofu kwa wananchi kwa sababu maeneo muhimu ya taasisi, zahanati na vituo vya afya mfano, kama Barabara ya Kumi pamoja na Shule ya Sekondari Mkindo na maeneo mengi tu yamekuwa yakirukwa. Serikali ituambie ni lini mradi huu utakamilika na umeme kuwashwa katika Jimbo la Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli umeme umekuwa ukirukaruka kama ambavyo wananchi wanasema na kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema. Hata hivyo, kama nilivyokwishaeleza, maeneo yote ambayo yamekuwa yakirukwarukwa, siyo kwamba yalirukwa, kulikuwa na mpango madhubuti kwamba umeme mwingine utakuja chini kupita kwenye vitongoji vyote. Kwa hiyo, vitongoji vyote vya Mheshimiwa wa Ulyankulu vitapitiwa na umeme katika Awamu hii ya II.
Mheshimiwa Naibu Spika, Awamu ya II inakamilika mwezi Juni, 2016 kama ambavyo nimekuwa nikieleza na Awamu ya III inaanza mwezi Julai, 2016 na itakamilika baada ya miaka mitatu hadi minne. Kwa hiyo, vijiji vyote vya Ulyankulu vya Mheshimiwa Mbunge, ikiwa ni pamoja na eneo la Barabara ya Kumi, vituo vya afya, zahanati pamoja na shule zitapatiwa umeme chini ya mradi wa Underline Transformer na chini ya Mradi wa REA Awamu ya III unaoanza mwezi Julai, 2016.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza; kumekuwa na taarifa kwamba asali yetu ya Tabora ina chembechembe za sumu, lakini je, Serikali imewahi kufanya utafiti wa kisayansi na kuja na majibu ambayo yataleta ukweli wa jambo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali sasa iko tayari kuwasaidia wanaoshughulika na zao la asali kuwapatia masoko yenye uhakika, kwa sababu mara nyingi wanakuja watu kutoka nchi za Uarabuni na kununua asali katika njia za panya.
Je, sasa Serikali inao mkakati gani mahususi kuwasaidia wananchi hawa ili asali yao iweze kupata soko la uhakika bila kunyonywa?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asali ya Tabora na asali ya Tanzania haina chembechembe yoyote ya sumu, ni asali safi na world demand (mahitaji ya dunia) kwa asali ya Tanzania ni tani 5,000 kwa wiki, tani 260,000 kwa mwaka, kiasi kinachoweza kuingiza trilioni nane kwa asali ni kwamba sisi tumebaki kuchangamka. Kwa hiyo, wanaosema ina sumu hawatutakii mema tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko ya uhakika kwa kushirikiana na UNDP, TAN TRADE na Wizara yangu tunaandaa mfumo wa soko na mfumo wa soko unaanza kwa kuchakata asali. Nilijibu swali la kwanza la msingi, kimsingi ni-declare interest, kuna mwenzetu tunahangaika kupeleka kiwanda cha kwanza cha asali Tabora. Kiwanda cha asali ni dola 50,000 kwa hiyo, wenzetu wanaotupiga madongo toka nchi jirani wamekuwa wakichukua ile raw honey ambayo haijachakatwa na kuchakata nchini kwao na ku-pack kupeleka. TANTRADE na Wizara yangu, tunalishughulikia na nichukue fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, tuelekezane, nunua viwanda, mtaweza kuona faida, faida iko kwenye asali. Trilioni nane ni mara mbili ya pesa tunazotumia kununua mafuta jamii ya petroli ambayo inatu-cost trilioni nne kwa mwaka.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu. Swali langu la kwanza la nyongeza ni kwamba, katika ajali hizi mbalimbali zinazowapata wafanyakazi kazini, wapo wanaopoteza viungo vya mwili kwa maana wanapata ulemavu; kwa hiyo, inabidi wapate viungo bandia ili maisha yaweze kwenda. Je, Serikali sasa iko tayari kuweka sheria ili waathirika wa ajali hizi wapatiwe viungo bandia bure?
Pili, kumekuwa na usumbufu mkubwa sana katika malipo haya ya wafanyakazi wanaoumia kazini: Je, Serikali sasa iko tayari kuweka utaratibu mzuri ili wanaopata ajali kazini na kupoteza viungo na uwezo wa kazi waweze kupata malipo yao haya ambayo ni sehemu ya faraja katika maisha yao? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la msingi ameulizia kama tunaweza tukatunga sheria ambayo itawarahisishia hawa wanaopata matatizo wakiwa kazini kupata viungo bandia vya bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, kwa sasa hakuna haja ya kutunga sheria nyingine kwa sababu sheria iliyopo ndicho ambacho imekuja kuki-address. Sheria yetu ya sasa ya Workers Compensation Act, kazi yake kubwa ni pamoja na ku-cure mischief ambayo ilikuwa inatokana na sheria iliyopita, ambapo katika sheria ile iliyopita, fidia yoyote ambayo ilikuwa inalipwa, maximum payment ilikuwa ni sh. 108,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho ya sheria hii sasa, inakuja kuyajibu hayo matatizo ambayo yalikuwa yakisababishwa na sheria iliyopita kiasi kwamba wafanyakazi wengi walikuwa wanaumia, lakini malipo yao yalikuwa siyo stahili na yalikuwa hayaendani na lile jeraha ambalo amelipata. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge tu kwamba, sheria ipo na itaendelea kutekelezwa na kwa sababu ndiyo kazi imeanza hii, WCF ndiyo wenye jukumu la kufanya hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Mheshimiwa Mbunge, ameuliza kuhusu usumbufu wa malipo. Nimwondoe hofu pia kwamba Mfuko huu ambao umeanzishwa kwa mujibu wa sheria Na. 5 ya mwaka 2008 umeweka utaratibu mzuri wa malipo ya namna gani malipo yatafanyika ikitokea mtu amepata matatizo akiwa kazini. Kwa hiyo, kwa sababu Mfuko umeanza kazi tarehe 1 Julai, 2016 kwa maana ya kuanza kulipa fidia, nimwondoe hofu tu kwamba wenzetu wa Mfuko wamejipanga vizuri kuondoa usumbufu na kuhakikisha kila mtu ambaye amepata majeraha akiwa kazini anashughulikiwa ipasavyo.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nataka kujua kwa nini hasa Jimbo la Ulyankulu lilitengwa kwa miradi hii mikubwa kwa sababu kutoka Tabora Mjini kwenda Ulyankulu centre ni kilometa 90, kutoka Kaliua kwenda Ulyankulu ni kilometa 90, kutoka Kahama kwenda Ulyankulu ni kilometa 90…
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini Serikali isi-plan kuhakikisha mradi mmojawapo unapeleka maji Ulyankulu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Naibu Waziri yuko tayari sasa kuambatana na mimi baada ya Bunge hili akaone mwenyewe vyanzo vya maji badala ya kusubiri taarifa za maandishi za wataalam wake ambao mimi naamini kabisa taarifa wanazoleta siyo sahihi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge niseme Jimbo la Ulyankulu halijatengwa, ni jimbo jipya, limetangazwa juzi juzi. Nafahamu Ulyankulu ina miradi ya maji ambayo kidogo haina hali nzuri, inatakiwa tuifanyie ukarabati kwa sababu kuna mabwawa ambayo muda mrefu yanatumika na mabomba yapo. Kwa hiyo, tutayafanyia kazi ili kuhakikisha yanaimarika na wananchi wanapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tutafanya utafiti na kufanya ulinganisho ama kutoa maji Kahama au kutoa maji upande wa bomba hili litakalotoka Malagarasi sehemu ya Kaliua. Pale patakapokuwa pako cost effective, tutahakikisha kwamba maji yanatoka ama Ziwa Victoria au kutoka Malagarasi na kuhakikisha wananchi wanapata maji yenye uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameomba kufuatana na mimi. Mheshimiwa Mbunge niko tayari tukimaliza Bunge tufuatane ili na mimi niende nikajionee huko na tushauriane pamoja na Halmashauri ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na salama kwa haraka.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa fursa ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwanza, ni vigezo gani viliifanya Serikali kurudisha mali za madhehebu mengine kama hospitali ya KCMC, Bugando na mashule na kwa nini isirudishwe mali za Kanisa hili la Moravian?
Swali la pili, kwa kuwa mgogoro huu na utata huu umechukua zaidi ya miaka 44, je, sasa Serikali ipo tayari kukaa katika meza ya majadiliano na Kanisa kumaliza utata huu uliodumu kwa miaka hiyo 44? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba baada ya zoezi lilioendelea baada ya miaka ya 1960 ya shule nyingi zilizokuwa chini ya mashirika ya dini kupelekwa Serikalini kwa makubaliano maalum, lakini baadaye kuna baadhi ya huduma kama za hospitali ambazo zilirudishwa.
Naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba urudishwaji wa hospitali zile na baadhi ya huduma imefanywa kwa makubaliano maalum na madhehebu ya dini, vivyo hivyo hata shule ambazo zimeendelea kubakia Serikalini ambazo zamani zilikuwa ni shule za taasisi za kidini, kubakia Serikaini vilevile ni suala la makubaliano. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kusaidia na madhehebu ya dini na mashirika mbalimbali na sekta binafsi katika kuendeleza elimu ikiwa ni pamoja na kuendelea kuzihudumia shule hizo kwa sababu inafanyika kwa maslahi mapana ya Taifa. Ifahamike kwamba miaka ya 63 zoezi hilo lilivyochukuliwa kulikuwa na makubaliano kama njia mojawapo ya kuhakikisha kwamba kunakuwa na usawa wa utoaji huduma na hususani elimu Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili kwamba ni lini majadiliano yatafanyika na Kanisa la Moravian kuhusu eneo la Chuo cha VETA tunachokizungumzia, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa hakuna mgogoro wowote uliopo katika umilikaji wa eneo hilo kwa sababu tokea lilipotolewa mwaka 1973 ilifanyika kwa makubaliano na makubaliano hayo bado yanafanya kazi, changamoto kidogo ambayo imetokea ni kuhusu chuo kuendelea kutumika kwa malengo yale ambayo ilianzishwa nayo na malengo yenyewe ilikuwa ni kuwasaidia wanafunzi ambao wamekosa fursa ya kwenda katika elimu ya sekondari sasa hili linaweza likajadiliwa lakini mgogoro haupo kwenye umiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu kwamba, Wizara yangu na Serikali iko tayari kuendelea kushirikiana na Kanisa la Moravian, ni washirika wetu tokea siku nyingi sana tokea miaka ya 1970, tunawashukuru sana, tutaendelea kujadiliana nao namna bora ya kutumia chuo hiki kwa maendeleo ya Taifa.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Serikali iliahidi kupeleka fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati na kuviwezesha vituo vya afya karibu sehemu yote ya nchi. Mojawapo ni kituo cha afya cha Ulyankulu. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutupa status ya utumaji wa fedha hizo kwenye vituo vya afya kote nchini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS – TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri wangu kwa ufafanuzi mzuri wa swali la awali. Hata hivyo, napenda kutoa status ya suala la ujenzi wa vituo vya afya ambavyo tumesema ni ukarabati mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulifanikiwa kupata fedha kutoka mifuko miwili. Fedha kutoka World Bank ambapo lengo letu ni kukarabati vituo vya afya 100, lakini nyingine tulipata fedha kutoka Ubalozi wa Canada tumeshazipeleka katika kila kituo takriban shilingi milioni 500. Hali ya ujenzi mpaka sasa, wengine wako katika stage ya lenta na wengine wanapauwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zilizotoka Mfuko wa World Bank, fedha zile zilichelewa kidogo ambapo ndani ya wiki hii fedha hizo ndio zitafika vituoni, japokuwa tulitoa deadline kwamba, tarehe 30 mwezi wa 12 vituo vyote viwe vimeweza kukamilika, kwa sababu hizi fedha kutoka Mfuko wa World Bank zilichelewa kufika vituoni tuta-extend huo muda angalau tufike mwishoni mwa mwezi Januari. Hali halisi hivi sasa fedha za Canada zimeshafika, lakini za World Bank ndiyo wiki hii zinafika vituoni. (Makofi)
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza, naomba tufanye marekebisho kidogo kwenye majina ya vijiji, kijiji kinaitwa Ichemba na wala siyo Lihemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile minara hii inajengwa kwa umbali mrefu karibu kilometa 30 kwenda mnara mwingine, je, Serikali kwa kushirikiana na makampuni haya iko tayari kuongeza minara mingine katikati ili kuongeza upatikanaji wa mawasiliano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwenye jibu ametaja mchakato wa ujenzi au kutengeneza minara katika Vijiji vya Ichemba, Kanoge, Busanda na Igombemkulu utafanyika siku za usoni. Kwa Kiswahili rahisi ukisema siku za usoni maana yake haijulikani ni hata baada ya miaka 10, 15 ni siku za usoni. Je, Serikali sasa iko tayari kueleza muda maalum badala ya kutuambia habari za siku za usoni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Kadutu kwa sababu pamoja na mambo mengine tumekwishawasiliana kuhusu masuala ya mawasiliano kwenye jimbo lake na nilimweleza vizuri tu hatua mbalimbali ambazo Serikali imeendelea kuzichukua. Kawaida umbali kati ya mnara na mnara katika eneo ambalo halina milima mingi sana ni radiance ya kilometa 80.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imeendelea kuweka umbali wa radiance ya kilometa 60 kwa sababu umbali huo unarahisisha kuweka mnara mwingine umbali wa kilometa hata 60 kama hakuna milima. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Kadutu kwamba umbali wa minara kama yeye anapata kwa kilometa 30 ni kwa sababu maeneo yaliyopo yana milima milima na tutajitahidi kuangalia sehemu zote ambazo hazipati mawasiliano tusogeze minara mingine ili wananchi waweze kupatiwa mawasiliano kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini miradi kwenye vijiji vilivyotajwa pale itapatiwa mawasiliano. Kwa sasa hivi tunaorodhesha vijiji na kata mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya nchini mwetu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Hivi ninavyoongea tumepanga tufanye ratiba ndefu ya miezi miwili baada ya Bunge la Bajeti kwa ajili ya kupima kwa kutumia GPS na kuweka alama ni wapi tutaweka minara kwa ajili ya kuwezesha wananchi wa Tanzania wote waweze kupata mawasiliano.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Kwa vile Naibu Waziri ameona aondoe sentensi moja, mimi nasema paragraph yote majibu hayafanani na swali nililouliza. Mimi sitaki kuuliza maswali mengi, nimwombe tu Mheshimiwa Naibu Waziri au Mawaziri wote watatu wa TAMISEMI wafike Ulyankulu kujionea haya yaliyoandikwa, je ni kweli? Kwa sababu haya yote yaliyoandikwa si kweli.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nimwombe Naibu Waziri au wenzake waweze kufika Ulyankulu na kujionea kile wanachopewa na wataalam na je, ndicho kilichoko site? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, naomba sana nimwombe Mheshimiwa John Kadutu, awepo Jimboni tarehe 10 Julai, ili tuweze kutembelea shule hizo kwa pamoja.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kabla sijauliza maswali ya nyongeza, nitumie fursa hii kuwashukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kuja kutembelea Jimbo la Ulyankulu na kuona changamoto zetu. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, katika vijiji ambavyo vimeshapitiwa na umeme, kumekuwa na upungufu mkubwa sana wa nguzo kiasi kwamba maeneo mengi hayatapata umeme. Je, Serikali inasema nini kuhusu suala hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, umeme kuupeleka kwenye Mgodi wa Silambo, kuna njia mbili. Je, mkandarasi anaweza kuelekezwa umeme kuelekea katika Mgodi wa Silambo ukapitia eneo la Ikonongo badala ya kupita Uyoa kutoka Kaliua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kadutu. Nami nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Kadutu na Wabunge wote wa Mkoa wa Tabora kwa kazi nzuri zinazoendelea katika majimbo yao, hususani katika kufuatilia Mradi wa REA Awamu ya Tatu unaoendelea. Nawashukuru kwa ushirikiano wao kupitia ziara zetu tunazofanya katika majimbo yao, mara zote tunawakuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika maswali yake ya nyongeza, swali lake la kwanza ameeleza kuhusu vijiji ambavyo vinapatiwa umeme na akasema nguzo ni chache, nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu kupitia swali hili la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Kadutu kwamba kwa kweli hii miradi ya umeme kwa kila kijiji inapokwenda kunakuwa na wigo, kilometa na wateja wa awali lakini kazi ya kuunganisha inaendelea. Ndiyo maana kwa kurahisisha zoezi hilo, tumeielekeza TANESCO na wao wataendelea kusambaza kwa bei ileile ya REA ya Sh.27,000. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge Kadutu kwamba kazi hiyo itaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nimtaarifu tu Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa tisa ya awali ambayo Mradi wa Awamu ya Pili ya Ujazilizi unatarajiwa kuanza hivi karibuni na taratibu za manunuzi zinaendelea na kiasi cha shilingi bilioni 169 zimetengwa na Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kazi ya ujazilizi. Kwa hiyo, maeneo ya vijiji ambapo kuna vitongoji havikufikiwa vitafikiwa kupitia Mradi huu wa Ujazilizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Kadutu ameulizia kama tunaweza tukatoa maelekezo ya kupeleka umeme kwenye Mgodi wa Silambo kupitia njia ya kutoka Ikonongo. Nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa ametoa wazo hilo nilichukue na baada ya kipindi cha maswali na majibu tukutane na tuweze kufanya mawasiliano na TANESCO na REA tuone uwezekano huo ambao pengine hautaathiri kilometa ambazo zimetajwa katika mradi wa kupeleka umeme katika mgodi alioutaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)