Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. John Peter Kadutu (10 total)

MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Katika Jimbo la Ulyankulu, Kata za Milambo, Igombemkulu na Kamindo bado hazijafanya uchaguzi:-
Je, ni lini Kata hizo zitafanya uchaguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia Tangazo la Serikali Na. 295 la Tarehe 23 Julai, 2015 ilitangaza jumla ya Kata 3,946 kwamba ndizo zitakazoshiriki uchaguzi wa Madiwani kwa Tanzania Bara katika uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba, 2015. Kata za Kamindo, Igombemkulu na Milambo hazikujumuishwa katika orodha hiyo kwa kuwa ni maeneo mapya yaliyowasilishwa na Serikali baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa imekamilisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba 2015.
Vilevile zoezi la utoaji uraia (naturalization) na utangamanisho (intergration) kwa baadhi ya wakimbizi bado linaendelea katika maeneo hayo. Zoezi hilo litakapokamilika taratibu za kisheria zilizopo zitazingatiwa kabla ya kufanya uchaguzi katika maeneo husika.

MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Ulyankulu kwa muda mrefu wamekuwa wakipata tabu ya usafiri kutokana na barabara zake kuwa mbovu kwa muda wote:-
(a) Je, ni lini barabara ya kutoka Tabora hadi Ulyankulu itajengwa kwa kiwango cha lami ili kuondoa kero hiyo?
(b) Je, ni lini barabara ya kutoka Ulyankulu hadi mpakani mwa Kahama itaimarishwa zaidi hata kwa kiwango cha moramu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Tabora – Ulyankulu yenye urefu wa kilometa 79 ni barabara ya Mkoa na inahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS). Kwa sasa kipaumbele ni kuunganisha Mkoa wa Tabora na Mikoa ya Mwanza, Kigoma, Singida na Katavi kwa barabara za lami. Hatua hii ikikamilika Serikali itaanza kujenga barabara za mikoa kwa kiwango cha lami kwa vipaumbele kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Ulyankulu – Kashihi - Nyandeka hadi Kahama yenye urefu wa kilometa 344 ni sehemu ya barabara ya mkoa kutoka Mpanda – Ugala – Lumbe – Kaliua - Ulyankulu hadi Kahama yenye urefu wa kilometa 428 ambayo ipo katika mpango wa kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utakapokamilika, barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji na fedha. Ujenzi huo utajumuisha madaraja yaliyopo katika barabara hii. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha katika bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara hii kwa kiwango cha changarawe.
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Kwa miaka mingi kumekuwa na Sheria mbaya za fidia kwa wafanyakazi wapatao ajali:-
Je, ni lini Serikali italeta Muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Workmen’s Compensation ili kwenda na wakati kwa vile Sheria iliyopo haiwasaidii waathirika wa ajali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya mwaka 2008, fidia kwa wafanyakazi zilikuwa zikilipwa kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya zamani ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura 263 na Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2003. Sheria hizi za fidia kwa wafanyakazi zilitumika kulipa fidia kwa watumishi wote kutoka sekta binafsi na umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya Sheria ya Workmen’s Compensation, Sura ya 263 yalifanyika mwaka 2008 ambapo Bunge lilitunga Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Act) Na. 20 ya mwaka 2008 ili kuondoa upungufu kadhaa ulioonekana katika sheria zilizotangulia ikiwa ni pamoja na kiwango kidogo cha fidia kwa mfanyakazi aliyeumia au kupata maradhi akiwa kazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii imeanzisha Mfuko wa Fidia ambao unashughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika Sekta ya Umma na Binafsi Tanzania Bara ambao wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi wanazofanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko huo umeanza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2016 ambapo waajiri katika sekta binafsi wanachangia 1% na Sekta ya Umma 0.5%. Mfuko huu umeanza rasmi kulipa mafao ya fidia kwa wafanyakazi wanaoumia au kupata maradhi wakiwa kazini kuanzia tarehe 1 Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia Mfuko huu, utaratibu wa kupata huduma za fidia umerahisishwa sambamba na mafao kuboreshwa kwa kiwango kikubwa.
MHE. CONSTATINE J. KANYASU (K.n.y JOHN P. KADUTU) Aliuliza:-
Kampuni binafsi ya migodi zimekuwa zikikiuka mikataba ya kazi na pia zikikandamiza na kuwanyanyasa wafanyakazi:-
(a) Je, ni lini Serikali itafanya ukaguzi wa mikataba kwa kampuni zinazofamya kazi migodini?
(b) Je, kwa nini Serikali isiamue kuwaondoa nchini waajiri wakorofi kwa unyanyasaji wanaoufanya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, waajiri wote nchini yakiwemo na makampuni ya madini wanapaswa kutekeleza matakwa ya Sheria za Kazi kwa lengo la kulinda haki za wafanyakazi, kupunguza migogoro isiyo ya lazima sehemu za kazi na kuongeza tija na uzalishaji mahala pa kazi. Ofisi yangu imeendelea kutekeleza majukumu yake ya usimamizi wa sheria kwa kufanya kaguzi sehemu za kazi kwa lengo la kuhakikisha kuwa waajiri wanazingatia matakwa ya sheria. Pia elimu ya sheria za kazi zinatolewa kwa waajiri, wafanyakazi na vyama vyao ili kuongeza uelewa wao katika kutekeleza sheria. Aidha, hatua zinachukuliwa kwa kuwafikisha Mahakamani waajiri wanaokiuka masharti ya sheria za kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ukaguzi wa mikataba wa kampuni zinazofanya kazi migodini, Serikali iliunda kikosi kazi ambacho kilishirikisha Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, NSSF, SSRA, OSHA, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Wakala wa Ukaguzi wa Madini. Kikosi hiki kilipewa jukumu la kufanya ukaguzi wa kina kwenye migodi iliyopo kanda ya Ziwa na Kaskazini kwa lengo la kuangalia hali halisi ya utekelezaji wa sheria za kazi, afya na usalama mahali pa kazi, masuala ya hifadhi ya jamii, fedha na kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha Serikali inatambua umuhimu wa uwekezaji katika kukuza fursa za ajira kwa Watanzania na kuchangia kukua kwa uchumi. Serikali itaendelea kusimamia sheria za kazi ili kuhakikisha kuwa waajiri wote nchini wanatimiza wajibu wao na wawekezaji wanapata nafasi ya kuwekezana kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi yetu kwa kufuata sheria zilizoko nchini.
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itaunganisha Jimbo la Ulyankulu katika miradi ya maji toka Ziwa Victoria na maji toka Mto Malagarasi?
(b) Je, Serikali iko tayari kuyakinga maji ya Mto Igombe ili kuwa na bwawa kubwa ambalo litapunguza shida ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshaanza utekelezaji wa mradi kutoa maji kutoka Mto Malagarasi kwa ajili ya kuleta maji katika Miji ya Urambo, Kaliua, Nguruka na Usoke. Mradi huu pia utahudumia baadhi ya vijiji vilivyopo Wilayani Uvinza na maeneo mengine ya Wilaya ya Uyui, Manispaa ya Tabora na vijiji vitakavyokuwa umbali wa kilometa 12 kandokando ya bomba kuu. Mradi huu utasaidia kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wengi zaidi kwa kuwa Mto Malagarasi unayo maji mengi yanayotiririka wakati wote wa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jimbo la Ulyankulu, Serikali imemuagiza Mhandisi Mshauri katika usanifu unaoendelea kuweka matoleo kwa ajili ya upanuzi wa mradi kwa awamu zitakazofuata ili wananchi wengi zaidi wakiwemo wa Ulyankulu waweze kufaidika na mradi huo. Usanifu wa mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Juni, 2017.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la kukinga maji ya Mto Igombe kwa ajili ya kujenga bwawa kubwa linahitaji kufanyiwa utafiti na usanifu wa kina ii kulinganisha gharama za uwekezaji na manufaa ya mradi huo. Mipango ya Serikali katika kuendeleza hifadhi ya vyanzo vya maji ni pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa mabwawa makubwa. Aidha, kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji Serikali imetoa wito katika Halmashauri zote nchini kuanza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa madogo ambayo yatasaidia kutatua shida ya maji kwa wananchi, mifugo pamoja na umwagiliaji. Kwa sasa Ulyankulu inapata maji kutoka kwenye visima virefu.
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Miaka mingi iliyopita Serikali iliwahi kuzichukua hospitali, shule na huduma nyingine nyingi kutoka katika mashirika ya dini na baadae Serikali ilirudisha huduma hizo kwa wamiliki wake, Kanisa la Moravian Tabora lilikuwa na eneo la VETA, Serikali wakati wa kurudisha haikurudisha eneo hilo kwa Kanisa hilo.
(a) Je, ni lini Serikali itarudisha eneo hilo kwa wamiliki wake?
(b) Je, Serikali ipo tayari kulipa fidia kwa kuwa na eneo ambalo siyo lake?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo mwaka 1973, Kanisa la Moravian Tanzania Magharibi lilikabidhi eneo, majengo na mali inayohamishika na isiyohamishika kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara. Misingi na sababu maalum ambazo zilikubaliwa na pande zote mbili ilikuwa ni kwamba eneo hilo litumike kama chuo cha kufundishia mafunzo mbalimbali ya ufundi. Walengwa walikuwa ni vijana ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari baada ya kuhitimu elimu ya msingi na lengo ilikuwa ni kwamba ni kuwapa stadi mbalimbali za ufundi kwa ajili ya kuweza kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kukabidhiwa eneo hilo, lilikabidhi kwa Shirika la SIDO lililokuwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwama 1974 ili eneo hilo litumike kuendesha mafunzo ya ufundi. Hata hivyo, mwaka 2002 eneno hilo lilikabidhiwa kwa VETA kwa lengo la kuendelea kutoa mafunzo ya ufundi stadi. Aidha, VETA imeendelea na majuku hayo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa mwenyekiti, napenda kukifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Serikali haijarudisha maeneo yote ya kielimu ambayo awali yalikuwa yanamilikiwa na mashirika ya dini bali kuna baadhi ya maeneo ambayo yalirudishwa kwa makubaliano ya pande zote mbili. Aidha, kwa ajili ya manufaa mapana ya Taifa kwa sasa Serikali haina mpango wa kurudisha maeneo mengine kama hayo.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE ( K.n.y MHE. JOHN P. KADUTU) aliuliza:-
Kumekuwa na maombi ya kupata Wilaya na Halmashauri ya Ulyankulu kwa muda mrefu sasa. Pia zimetolewa ahadi za kuunda Wilaya na Halmashauri tangu mwaka 2010.
(a) Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi Wilaya na Halmashauri kwani vigezo vya kuwa Wilaya/Halmashauri ni kama vile vya Jimbo ambavyo tayari vimetimia?
(b) Je, ni kikwazo gani kimesababisha kutopata Wilaya/Halmashauri mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi ya kuanzisha Wilaya ya Ulyankulu ya mwaka 2010 hayakufanikiwa kutokana na kutokidhi vigezo vikiwemo idadi ya watu pamoja na sehemu kubwa ya eneo hilo kuwa ni hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maombi ya mwaka 2010 hayakukidhi vigezo na kwa sasa kama Halmashuari inaona eneo hilo limekidhi vigezo hivyo, tunashauri Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kuanzisha mchakato wa kujadili mapendekezo hayo upya na kuyapitisha katika Baraza la Madiwani na Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa na hatimaye kuwasilisha Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ili yaweze kufanyiwa kazi. Serikali haitasita kuridhia pendekezo hilo endapo litakuwa limekidhi vigezo na taratibu zilizokuwa zimewekwa kwa mujibu wa Sheria.
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Jimbo la Ulyankulu linakabiliwa na tatizo la mawasiliano ya simu hasa katika Vijiji vya Ibambo, Mwongozo, Ichemba, Kanoge, Ilege, Busanda, Bulela, Ikonongo, Igombemkulu na maeneo mengine mengi:-
Je, ni lini kampuni za simu zitamaliza tatizo la mawasiliano katika Jimbo la Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliingia Makubaliano na Kampuni ya Mawasiliano ya Vietel ya Vietnam (Halotel) kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara ikiwa ni pamoja na maeneo ya Vijiji vya Ibambo, Mwongozo, Ilege, Bulela na Ikonongo. Utekelezaji wa kuleta mawasiliano ya simu kwa miradi hiyo umekamilika ambapo minara imejengwa katika Vijiji vya Ibambo, Keza na King’wangoko. Hata hivyo, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itahakikisha maeneo yote yanapata huduma hiyo muhimu kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Lihemba, Kanoge, Busanda na Igombemkulu vitaainishwa na kuingizwa katika orodha ya miradi ya kuwapatia mawasiliano inayosimamiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itakayotekelezwa siku za usoni kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Kabla ya kuanzishwa Shule za Kata, kulikuwa na mpango wa kujenga shule katika tarafa. Kwenye Jimbo la Ulyankulu kulijengwa shule tatu ambazo ni Kashishi, Ulyankulu na Mkindo; Shule ya Kashishi hivi sasa ina kidato cha tano na sita:-
Je, ni lini Shule za Mkindo na Ulyankulu zitapewa hadhi ya kuwa na kidato cha tano na sita ili kuwapunguzia wanafunzi gharama za kufuata mbali masomo ya kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naomba kwa ruhusa yako niondoe sentensi moja tu inayoanza na neno Tarafa mpaka pale mwisho na sita.
Mheshimiwa Spika, malengo ya Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa, kila Tarafa angalau ina shule moja yenye kidato cha tano na sita. Mkakati uliopo kwenye maeneo ambayo tayari kuna shule zinazotoa elimu ya kidato cha tano na sita ni kuziimarisha kwa kuziwekea miundombinu, kuzipatia vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuzipatia Walimu wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, ili shule iweze kupandishwa hadhi na hatimaye kusajiliwa kama Shule ya Kidato cha Tano na Sita ni lazima itimize vigezo vifuatavyo:-
(a) Iwe na miundombinu inayojitosheleza kama mabweni, madarasa, bwalo, jiko na maktaba;
(b) Iwe na huduma muhimu na za uhakika za maji na umeme; na
(c) Iwe na Walimu wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Shule za Sekondari Ulyankulu na Mkindo bado zina changamoto ya miundombinu isiyojitosheleza kama mabweni, madarasa, bwalo, jiko na maktaba. Hivyo, naishauri Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua ifanye jitihada za makusudi kuwezesha shule hizo mbili kufikia vigezo vinavyohitajika ili ziweze kusajiliwa. Aidha, kwa kuwa bajeti ya Wizara ya Elimu pamoja na ile Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka 2018/2019 zimeshapitishwa na Bunge, itakuwa vigumu shule hizo kusajiliwa na kuanza kuchukua wanafunzi wa mwaka huo.
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-

Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) unaendelea kote nchini. Katika Jimbo la Ulyankulu bado umeme haujafika katika maeneo mengi:-

(a) Je, ni lini sasa umeme utasambazwa katika Kata za Uyowa, Silambo, Igombe Mkulu, Seleli, Nhwande na Kanoge?

(b) Hivi karibuni Wilaya ya Kaliua imesajili Shule za Sekondari tano (5) na Vituo vya Afya pamoja na Sekondari ya Mkondo; je, ni lini sasa umeme utafikishwa katika taasisi hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo vijiji 49 vya Jimbo la Ulyankulu kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza unaoendelea. Jumla ya Vijiji 19 vinatarajiwa kupatiwa umeme ambavyo ni Mwongozo, Mapigano, Mwanduti, Kanoge, Utamtamke, Iyombo, Ikonongo, Mbeta, Kagera, Ulanga, Imara, Kanindo, Nhwande, Keza, Mkiligi, Ilege, Konane, Busondi na Seleli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 127.96; njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 76; ufungaji wa transfoma 38 za KVA 50 na KVA 100 pamoja na kuunganishia umeme wateja wa awali 1,246. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 6.8 na kwa sasa mkandarasi JV Pomy Octopus na Intercity anaendelea na kazi mbalimbali za miundombinu ya umeme katika kata 12 zikiwemo Kata za Kanoge, Nhwande, Seleli na Igombe Mkulu. Kazi za kufikisha umeme katika vijiji hivyo itakamilika ifikapo mwezi Juni, 2020.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza, taasisi zote za huduma za kijamii zikiwemo afya, elimu na maji zinapewa kipaumbele. Kwa sasa mkandarasi anaendelea na kazi ya kupeleka umeme katika Kituo cha Afya cha Mkondo na Shule ya Sekondari Mkondo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.