Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. John Peter Kadutu (21 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo imesheheni kila kitu, matatizo yetu yote yako pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa maneno ya shukrani. Kwanza niishukuru Serikali, tumekuwa tukipiga kelele juu ya uanzishwaji wa Jimbo jipya la Ulyankulu pamoja na Halmashauri na Wilaya ya Ulyankulu. Tunaishukuru sana Serikali, niombe Serikali ikubali shukrani zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Ulyankulu kwa kuniamini. Hawa jamaa kule kwangu wanajua, Mheshimiwa Rais alipata 81% na mimi kwa sababu nilimpigia kelele sana yeye nikapata 75%. Kwa hiyo, hawa jamaa wacha watoke sisi tuendelee na kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru familia ya Mtemi Mirambo. Mwenyekiti wewe ni Mtemi na mimi nikuarifu tarehe 28 Novemba, nimepewa Utemi kwa maana ya kuongoza jamii ya Wanyamwezi wote wa Ulyankulu. Kule kwetu ukipewa Utemi unapewa na jina lingine. Sasa jina nililopewa linatuletea taabu, nimepewa jina la Mbula maana yake mvua, toka siku naapishwa kupewa Utemi mvua zinanyesha siyo kawaida. Itabidi nirudi kwa familia ya Mirambo inioneshe namna ya kuipunguza mvua. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa na mambo mbalimbali yanayotukabili ndani ya Jimbo letu jipya la Ulyankulu. La kwanza, inawezekana watu mkashangaa, bado uchaguzi wa kata tatu haujafanyika ndani ya Jimbo kwa maana ya Kata ya Milambo, Kanindo na Igombe Mkulu. Eneo hili lilikuwa la wakimbizi waliokuja mwaka 1972. Tulikuwa nayo makambi matatu makubwa kwa maana ya Ulyankulu, Mishamo na Katumba. Wenzetu wa Mishamo na Katumba baada ya kupewa uraia wamefanya uchaguzi wa Rais, wa Mbunge pamoja na Madiwani lakini eneo hili la kata hizi tatu wameweza kuchagua Mbunge pamoja na Rais. Niiombe tu Serikali na hasa kwa kuzingatia ahadi za Mheshimiwa Rais alipokuja, kata hizi zifanye uchaguzi haraka iwezekanavyo ili kazi za maendeleo ziweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko tatizo la uanzishwaji wa mamlaka ndani ya eneo lililokuwa Kambi ya Wakimbizi. Kwa hiyo, Serikali tuiombe iharakishe lakini pia Wizara ya Mambo ya Ndani iharakishe kwa sababu ndani ya kambi kwa maana ndani ya eneo hili wapo wakimbizi ambao walikubali kuwa raia, wapo wakimbizi waliokubali kurudi Burundi lakini wapo wakimbizi ambao hawakutaka lolote. Serikali iwaamulie mapema ili jambo hili likae vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko shida ndani ya mambo haya, wapo viongozi wa Wizara na hasa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Kitwanga nadhani utanisikia vizuri, leo anakuja Naibu Katibu Mkuu labda, siwezi kujua kama ni huyu wa sasa, anasema marufuku kujenga, kesho anakuja mwingine anasema pako vizuri. Ifike mahali Serikali inyooshe maneno kwamba lipi linafanyika. Kwa hiyo, nadhani hilo ni vyema tuliweke sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe tu ahadi ya Rais, pamoja na azma hii ya kubana matumizi, bado iko haja ya kuanzisha Wilaya ya Ulyankulu na Halmashauri yake ili kusogeza huduma. Kutoka Ulyankulu kwenda Kaliua ni mbali, kutoka pale kwenda Kahama kuna kilometa kama 80 lakini kutoka Ulyankulu kwenda Makao Makuu ya Mkoa kuna kilometa 90. Kwa hiyo, niombe tuharakishe uanzishwaji wa Wilaya pamoja na Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya ujumla, liko tatizo la maji na Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema. Upo mradi unataka kutoa maji kutoka Ziwa Viktoria kupeleka Tabora, Sikonge na Igunga. Kutoka Tabora Mjini kwenda Ulyankulu ni kilometa 90. Niombe sana Serikali ituongezee sisi ili tuwe sehemu ya mradi wa maji ya Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini upo mradi wa maji kutoka Malagarasi kuja Kaliua na Urambo. Kutoka Kaliua kwenda Ulyankulu kilometa 60, sidhani kama Serikali inaweza kushindwa kuunganisha wapiga kura wangu hawa wanaotaabika na shida ya maji. Iko option nyingine, sasa hivi Mto Igombe umejaa kweli kweli mpaka kuna mafuriko, kwa nini Serikali isivune maji yale ambayo yanaweza kutosheleza Jimbo zima na tuka-supply maeneo mengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la barabara. Tunayo matatizo, barabara kutoka Tabora kwenda Ulyankulu, kama nilivyosema kilometa 90, ndiyo inayotegemewa kuleta tumbaku Tabora kabla haijapelekwa Morogoro. Niombe sana, barabara zote zinazoingia Mji wa Tabora zina lami na kama hazina lami ziko kwenye mpango, Serikali iingize kwenye Mpango huu barabara ya kutoka Tabora kwenda Ulyankulu kujengwa kwa kiwango cha lami. Tutafurahi sana watu wa Ulyankulu, tumechelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini iko barabara inatoka Ulyankulu kwenda Kahama, kwenye Ilani ya Chama chetu barabara kutoka Mpanda - Kaliua, Ulyankulu - Kahama kilometa 428 iko kwenye Mpango. Mimi niombe sana haya mambo ya kuweka upembuzi yakinifu basi ifike mwisho barabara ianze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la tumbaku, tutapiga kelele sana na Mheshimiwa Mwigulu umetuahidi tunaotoka kwenye maeneo yenye kilimo cha tumbaku tukutane. Ninachotaka kusema kila Serikali imekuwa inajaribu lakini haifanikiwi. Wakulima wetu wanadhani tunaogopa wazungu wa makampuni kwani watu hawa wanaungana kuwanyonya wakulima wetu. Iko mianya mingi zao la tumbaku linanyonywa. Kwa hiyo, Serikali ifike mahali tukae vizuri turekebishe jambo hili na mambo yaende vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme vijijini, Mheshimiwa Muhongo, umeme unaotoka Tabora kwenda Ulyankulu mradi huu unasuasua. Wenzetu wa Upinzani wakati wa kampeni walisema zile nguzo tutatengeneza mkaa. Sasa zimelala chini, sehemu kubwa kazi ile haijafanyika. Niombe tuongeze speed ili wananchi waamini kweli kuna umeme unakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo la maslahi ya Madiwani. Waheshimiwa Wabunge, tunapokuwa kwenye kampeni Madiwani wanatupigania sana na mara nyingi tunasema mafiga matatu, hakuna maslahi mazuri kwa Waheshimiwa Madiwani, watu ambao wanafanya kazi kwa niaba yetu. Madiwani wanalipwa kidogo lakini pia hawaheshimiwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumzie kipindi ambacho Madiwani wanakuwa hawapo wamekwenda kwenye uchaguzi, kazi zile hufanywa na watendaji wa Halmashauri kwa maana ya Wakuu wa Idara. Mwezi Novemba, Katibu Mkuu TAMISEMI, najua ameshaondoka lakini Serikali ipo, alitoa Waraka wa ajabu sana. Naomba nisome kipengele kimoja kwa ruhusa yako halafu uone jinsi gani tunawanyima Waheshimiwa Madiwani kazi.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mtemi.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii Wizara yetu ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ambayo mimi ni mdau mkubwa kwenye sekta hii. Nianze kwanza kwa kumpongeza Waziri Mheshimiwa Nape pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Anastazia Wambura kwa kuteuliwa kushika nafasi hii, sisi wanamichezo tuna imani nao, najua bado muda ni mapema tuwape muda ili waoneshe njia na nina uhakika tutafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na jambo ambalo wenzangu wamelipitia pitia ni hili la Sheria ya Bahati Nasibu. Kwanza, lazima tuelewe Shirika hili la Bahati Nasibu limekuwepo kwa muda mrefu, na sidhani kama ile bahati nasibu tuliyokuwa tunaifahamu mpaka sasa ipo. Ni vema sasa Serikali ikabadilisha sheria, Sheria ya Bahati Nasibu ya Taifa ihamishiwe Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Nasema hivi kwa sababu sheria haisemi mapato ya bahati nasibu yanaenda wapi lakini tunaelewa kabisa kwamba bahati nasibu ni michezo ya kubahatisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye michezo ya kubahatisha kuna michezo mingi tu ya kubahatisha, kuna casino, kuna betting, kuna mapato pia yatokanayo na michezo mbalimbali yanayofanywa na makampuni ya simu. Tuna imani sana pesa nyingi zinapatikana kule na zinatosha kabisa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo (Sports Development Fund). Mfuko huu ndiyo unaweza ukafanyakazi ya kuendeleza michezo badala ya kuhangaika, ni fedha nyingi sana na hata nchi zingine zina mfuko kama huu. Hakuna haja ya kuhangaika kupitisha kikombe kwa ajili ya kuchangia, lakini muda mwingi hii bahati nasibu ya Taifa na kwa vijana wa sasa hata hawaelewi kazi gani hasa inafanya.
Kwa hiyo ushauri wangu Mheshimiwa Nape ukae na viongozi wengine, mlete sheria hapa Bungeni tubadilishe, Sheria ya Bahati Nasibu ibadilishwe. Bahati nasibu kwa sasa iko chini ya Wizara ya Fedha, bahati nasibu inapaswa kuwa chini ya Wizara ya Michezo, maana yake hii ni michezo ya kubahatisha, hii ni kekundu na keusi umeliwa ndiyo maana yake hii. Kwa hiyo ni vizuri ikaletwa kwenye Wizara yako ili mapato haya na uanzishwe mfuko huu nimesema Sports Development Fund, mfuko huu ndiyo unaweza kuwa mkombozi wa kazi mbalimbali za michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwanja wa Taifa, kama ilivyo jina ni Uwanja wa Taifa. Tumekuwa na uwanja wa Taifa sasa na Uwanja wa Uhuru, huu uwanja wa uhuru ndiyo tulizoea kuuita Uwanja wa Taifa au shamba la bibi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ku-declare mimi ni kati ya wale tunaoleta timu za nje kucheza Tanzania, kwa hiyo ninayoyaeleza ni ya ukweli na hakika. Viwango au tozo kwenye uwanja wa Taifa ni vingi mno, tunanyonya jasho la wachezaji na viongozi wanaotengeneza timu hizi, ukicheza Uwanja wa Taifa iko VAT asilimia 18, iko gharama ya mchezo asilimia 15, lakini iko asilimia tano kama ni CRDB asilimia tano lakini kama hii Max Malipo ambayo inazungumzwa kuletwa sasa ni asailimia tisa. Kwa hiyo, utaona kabisa kuna karibu asilimia 42 ya mapato yote yanapotea kwenda kwenye vyanzo hivi. Uwanja wa Taifa umejengwa na Serikali kama ambavyo tunapita kwenye madaraja na kutumia barabara hizi ni huduma, Serikali haifanyi biashara na hata kama ikifanya biashara haiwezi kufanyia biashara jasho la wachezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima sasa wakati umefika tozo hizi zipungue, ukiwa Uwanja wa Taifa mbali na hizi nilizosema yako makato mengine ya umeme, usafi sasa vyote hivi kama mmekata asilimia 15 ya mchezo kwa nini mkate tena umeme, kwa ni mkate usafi, wapo Wachina pale na wenyewe wanalipwa kiajabu ajabu, ukienda pale yaani kama na wewe ni mshiriki wa kuagiza timu, unaweza ukatoka pale hata senti tano hujapata kwa sababu ya tozo hizi, yaani zile asilimia 58 zinazobaki, baadaye zinapotea hapo bado timu hazijagawana, hazijafanya nini. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali iangalie tozo za Uwanja wa Taifa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la TFF na TRA. Mheshimiwa Waziri nimwombe sana sakata hili limekuwa linazungumzwa tu, hebu wakati wa majumuisho njoo na taarifa tujue nani mwenye tatizo kati ya TRA, TFF na Hazina kwa sababu deni hili siyo deni halisi la TFF, deni hili ni la Serikali ukishasema nitamlipa mshahara huyu maana yeke ni pamoja na kodi yake kwa maana ya PAYE. Sasa utasemaje unalipa mshahara unalipa net pay kwa nini usilipe na kodi na Serikali iliji-commit kulipa mshahara ya hawa makocha kutoka nje, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri njoo na majibu hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mechi ya Brazil limezungumzwa hapa, mechi ya Brazil na Taifa Stars, mechi hiyo jamani haikuwa chini ya TFF ilikuwa chini ya Kamati iliyoundwa na Serikali na fedha zote walichukua, wao ndiyo wenye wajibu sasa makato ya VAT tena yanaongeza deni ambalo TRA inakuja kuchukua.
Mimi nadhani mnawaonea TFF, akaunti tunaambiwa zimefunguliwa lakini fedha imechukuliwa, kwa nini fedha zichukuliwe na kama akaunti imefunguliwa iko vizuri, lakini je, TRA ina maana wameona hela tu za TFF zinaweza kumaliza matatizo tuliyonayo ya maji, umeme na nini? Nadhani Waziri njoo hapa utuambie nini kimetokea kwenye fedha za mechi ya Brazil pamoja na Taifa Stars mpaka kufikia TFF inafungiwa tunapata taabu, mpira sasa tunaendesha kwa madeni, haifai. Mimi ni Mjumbe wa TFF kwa hiyo ninayoyasema ni mambo ambayo nayajua vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo la nyasi bandia uwanja wa Nyamagana, nyasi bandia za uwanja wa Nyamagana Halmashauri ya Jiji la Mwanza ililipa kiasi chake ambacho kilitakiwa kabla ya FIFA kuleta msaada ule tukalipa, nyasi bandia hizi sasa imekuwa kama story, lini zitafika Mwanza na lini kazi ile itakwisha maana yake sasa uwanja ule umegeuka kuwa gofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine mwaka 2014 mimi niliongozana na timu ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwenda Brazili kwenye Kombe la Dunia, timu ile ikashinda ikaja hapa Bungeni mkaishangilia sana, zikatoka ahadi za Serikali nyingi sana. Mojawapo ni uwanja, Serikali iliahidi kutupatia uwanja kwa ajili ya watoto hawa ambao ni mabingwa wa dunia, hapa hakuna bingwa wa dunia mwingine, ni wale watoto wa Mwanza ambao mwaka kesho kutwa tunaenda Urusi kutetea kombe la dunia.
Mheshimiwa Nape najua utakuwa bado upo tusaidieni nauli za kwenda kwenye kombe la dunia, mashindano yale hufanyika kila kabla ya world cup mtusaidie kama Serikali kwenda kule, pia tunataka ahadi ya Serikali ya kutupatia uwanja.
MHE. JOHN P. KADUTU: Nakushukuru naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. JOHN P. KIDUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kukushukuru wewe mwenyewe kunipa nafasi hii kuchangia mchana huu hoja mbili zilizopo ya TAMISEMI pamoja na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijachangia nichukue fursa hii kuipongeza timu yetu ya Bunge kwa ziara nzuri kule Zanzibar, ni katika kuuimarisha Muungano wetu. Nitoe wito kwa niaba ya uongozi wa timu ya Bunge, Wabunge pamoja na Mawaziri tuungane kufanya mazoezi kila asubuhi pale uwanja wa Jamhuri. Mfano mzuri ni wewe Mheshimiwa Naibu Spika umekuwa unatutia moyo kuwepo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niwapongeze Mawaziri wawili hawa, Ndugu yangu Mheshimiwa Simbachawene pamoja na dada yangu Mheshimiwa Angellah.
Mheshimiwa Naibu Spika, TAMISEMI ni dude kubwa, ukishakabidhiwa Wizara ya TAMISEMI lazima utambue ni dude kubwa na bahati nzuri Mheshimiwa Simbachawene unalijua hilo kwamba TAMISEMI ni dude.
Kwa hiyo, niwapongeze sana kwa hotuba zenu nzuri. Pia nichukue fursa hii kuwapongeza wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kwa kazi nzuri iliyofanyika mpaka tumepata hati nzuri ndani ya miaka miwili na hasa kwa sababu mimi ndiye nilikuwa naongoza Halmashauri ile kama Mwenyekiti wa Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa Waziri wangu Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Waziri Mkuu wanisikilize kwa makini, iko hoja nilianza kuizungumza wakati nachangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, bahati mbaya muda haukuwa rafiki, nayo inahusu waraka aliokuwa ametoa Katibu Mkuu, TAMISEMI wa wakati ule akikataza Mabaraza ya Madiwani kuhoji yale yaliyokuwa yamefanyika wakati Mabaraza yakiwa yamevunjwa. Tarehe 10 Novemba alitoa waraka wa kukataza jambo hilo wakati akielezea taratibu za kuitisha mikutano ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako naomba nisome kipengele (g) cha waraka aliokuwa ametoa Katibu Mkuu, TAMISEMI na bahati nzuri mimi niseme ni bahati nzuri kumuondoa pale kunatusaidia kwenye TAMISEMI kukaa vizuri maana makatazo mengine haya hayafai.
Anasema, moja ya kazi za mkutano ule wa kwanza, kipengele (g) anasema; “Kupokea taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri kuhusu kumbukumbu ya maamuzi ya utekelezaji wa shughuli za Halmashauri zilizofanyika katika kipindi ambacho Baraza la Madiwani lilivunjwa.” Akaweka msisitizo kwenye maandishi; “Wajumbe wa Baraza watapokea taarifa hiyo ya utekelezaji na kuijadili bila kubatilisha maamuzi yaliyofikiwa.” Maneno haya siyo mazuri kwa kazi nzuri inayofanywa na Halmashauri. Tukiwa na watendaji ambayo si wazuri maneno haya wanaweza kuyatumia kufanya wanalotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa nini Baraza la Madiwani lizuiwe kuhoji yale yaliyofanyika? Tunao ushahidi kesho yake Madiwani wanarudi yamefanyika jana yake. Sasa kama umewakataza wasijadili maana yake unawakataza haki yao. Kwani kuna ubaya gani Bunge hili likajadili kazi ya Bunge iliyofanyika huko nyuma? Kwa hiyo, kazi kubwa lazima ifanyike hapa. Niombe Mheshimiwa Waziri toa tu tamko ili kufuta Waraka huu nadhani watu wengine huwa wanalewa madaraka, hilo lilikuwa la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuna ahadi ya Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za mwaka 2010, eneo letu lilikumbwa na mtafaruku katika kulizimazima jambo lile, Mheshimiwa Kikwete akaahidi Ulyankulu kuwapatia Wilaya pamoja na Halmashauri. Bahati mbaya mtani wangu huyu Mkwere kaondoka hatujapata Halmashauri kule na wala Wilaya haijapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati Mheshimiwa Rais anapita kwenye kampeni za uchaguzi uliopita na yeye akasisitiza jambo hili kuwapatia wananchi wa Ulyankulu Wilaya pamoja na Halmashauri. Kwa kweli wananchi wana imani hiyo kwamba upo utaratibu wa kuhakikisha jambo hili linakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe basi Serikali ije na majibu wakati wa kujibu suala hili limefikia wapi ikizingatiwa kwamba ahadi zimetolewa toka mwaka 2010. Wapo watu hapa wanasema tuzuie kuanzisha maeneo mapya ya utawala. Zinaweza zikawepo sababu kule unapotoka wewe kuna kaeneo kadogo, ukitembea saa tatu umemaliza jimbo lako lakini kutembea Jimbo la Ulyakulu Mheshimiwa Waziri Mkuu unajua ni kati ya majimbo makubwa na lenye watu wengi. Kwa hiyo, tunahitaji jambo hili likamilike ili wananchi wawe na imani, tupate wilaya na Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maslahi kwa Madiwani. Jamani zile pesa Wabunge mnazopata mwishoni Madiwani wanapata shilingi milioni 11, ni kiasi kidogo mno, hebu tuwasaidie. Kama hatuwapi hizi stahili zao za kila siku, zile za mwisho basi wapate. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la magari, yapo magari yamekwishakuwa allocated, tulizungumza nina imani utakuja na majibu hapa. Watu wanashindwa kukagua miradi kwa sababu magari hakuna lakini magari yameshakuwa allocated muda mrefu yapo yard kwa nini yasiende site yakafanye kazi? Bila shaka jambo hili litakaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni juu ya fedha za Serikali Kuu kwenda kwenye Wilaya, speed ya pesa kwa maana ya bajeti ni ndogo sana. Kufikia Machi Halmashauri ya Kaliua ilikuwa imepelekewa asilimia 62 tu lakini kwa mwaka jana pesa zilizoletwa kwa ajili ya maendeleo ziliishia asilimia 30 asilimia 70 hazikuletwa. Kwa hiyo, jambo hili linafanya miradi mingine iende kwa kusuasua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala lingine la hizi Sekretarieti za Mikoa kuingilia kazi za Halmashauri. Ni sehemu yao ya kazi lakini mara nyingine wanaingilia shughuli za Halmashauri katika hali ambayo inafanya hata ikosekane maana ya kuwepo Madiwani. Baraza linaamua hivi lakini Sekretarieti za Mikoa zinaingilia kati na maamuzi mengine yanakuwa ya hasara kwa Halmashauri. Kwa hiyo, niombe basi Mheshimiwa Waziri utupe mwelekeo mzuri lakini hizi Sekretarieti za Mkoa ziweze kuzuiwa na ziache mambo mengine ambayo yanaamuliwa na Halmashauri kwa maana ya Madiwani na Baraza lao waweze kutekeleza mambo yao yaende vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, michezo kwa shule za msingi na sekondari. Nimekuwa nikisema yupo mzee wetu mmoja nadhani alilewa au uzee au vipi alikataza michezo kwenye mashule. Nishukuru Serikali sasa michezo inachezwa, lakini iko haja ya kuongeza nguvu kwa maana ya bajeti ya ile michezo ya shule za msingi pamoja na sekondari kwa maana ya UMISETA. Pesa inayopelekwa kwa ajili ya michezo hii ni ndogo mno kiasi kwamba michezo haina tija yaani mafanikio ya michezo hii yanakuwa madogo kuliko kawaida. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri ulitolee ufafanuzi jambo hili ili mambo yaende vizuri.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii, niseme tu naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia kwenye bajeti yetu ya kwanza kabisa ya Serikali ya Awamu hii ya Tano. Nakushukuru sana kwa sababu nafasi hizi ni adimu na Wabunge ni wengi na tuna hamu sana ya kuishauri Serikali. Niiambie tu Serikali kuanzia kwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango, fungueni masikio msikie Waheshimiwa Wabunge wanasema nini, msizibe masikio. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la ku-withdraw benefits. Mimi niseme nimefanya kazi mining, najua shida za waajiri wa aina ile na makampuni yanayofanana nayo. Naishangaa sana Serikali kukazia hapo, kutaka watu wakae mpaka miaka 55, wakati Serikali hii inayaruhusu makampuni mbalimbali kuingia mikataba ya mwaka mmoja mmoja. Sasa kama mtu anafanya kazi mwaka mmoja anaingia mkataba mwingine na mwingine, stability ya ajira yake haipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri hebu watu hawa waachwe; mtu akimaliza kazi yake achukue chake. Hakuna haja ya kuwazuia. Labda kwa sababu Serikali inakopakopa hizi fedha za wafanyakazi, kwa hiyo, naona ili kuzifanya ziwepo, ni kuwazuia watu kuchukua. Kazi za sasa huwezi kuwapata watu wenye umri zaidi ya miaka 50, kama akina Mheshimiwa Kadutu. Vijana wengi wako chini ya miaka 20, 28 au 30, anafanya kazi mwaka mmoja, mwaka wa pili kaenda kwingine; lakini kuna uwezekano wa kukosa kazi kwa miaka hata sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, aendelee kusubiri miaka 55? Nadhani siyo jambo jema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, migodini kule ziko kampuni ambazo zina mikataba na makampuni mama kwa maana ya yanayoendesha migodi, lakini zile kampuni kwenye Mikataba ya Wafanyakazi zimeweka sharti kwamba pindi mkataba wa kampuni mama na kampuni hiyo nyingine ndogo utakapokwisha au utakapositishwa, automatic na wewe mfanyakazi mkataba umekwisha. Sasa mtu huyu unataka abaki aje kuwa mzee, ni nani atakayekubali kufanya kazi katika mazingira hayo?
Kwa hiyo, nilikuwa nadhani muda umefika, itatamkwe tu; Serikali itamke, mtu akiachana na mwajiri wake, kwa nini iwe kikwazo? Kwanza siku hizi mmetoa ruhusa ya kuchangia mfuko wowote unaotaka, kwa nini iwe kikwazo mtu kuchukua amana zako? Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni hili ambalo kila Mbunge analisema, nami nadhani Dkt. Mpango utakuwa umesikia vizuri. Kila Mbunge anaposimama anasema hapana. Basi hapana hii iwe maana yake hapana. Hivi unataka kutoza kodi kwa Mbunge; nawaambieni Waheshimiwa Wabunge sisi tuko tofauti na wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wako Wabunge hapa wanachangia maendeleo ya majimbo yao kwa shilingi milioni 500 mpaka shilingi bilioni moja. Je, na sisi tuanze kuandika invoice kuidai Serikali? Yako maeneo yamepangiwa pesa hayakupelekewa pesa hata senti tano, lakini shughuli za maendeleo zinakwenda. Sasa je, na sisi tuanze kuidai Serikali? Kwa sababu wajibu wa kufanya kazi hiyo ni wa Serikali. Kwa nini Serikali inataka kutugombanisha? Baadaye mtatuona sisi wakorofi, haiwezekani. Lazima mtambue shida ambazo tunazitatua kwa Majimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Doctor labda niseme, kama watu hawakwambii, watu wanasema labda kwa sababu Dkt. Mpango hana Jimbo. Watu wandahani hivyo. Iko shida Jimboni ambayo Mbunge anatumia pesa hizi hizi kupata nguvu ya kuendesha shughuli za Majimbo, lakini hili tuko wenyewe. Tunapunguziana nguvu za mwisho za kupambana kwenye uchaguzi. Ukikata shilingi milioni sitini au ngapi, maana yake umedhoofisha Mbunge huyu anayetaka kurudi tena kuwatumikia wananchi, hana nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Uchaguzi umekuwa ghali, sasa na nyie mnataka kunyofoa shilingi milioni 60, 70, za nini? Serikali ina wasomi wengi, tafuteni mbadala. Tafuteni njia nyingine za kutoza kodi, kwani lazima mwangalie tu mafao ya Mbunge? Sasa mkikata zetu, Madiwani je? Maana mtafanya siasa iwe kazi. Kuna siku mtatutoza fedha kuingia hapa. Badala ya ku-punch finger print, tutakuwa tunalipia hapa, kwa sababu hamtaki kutafuta kodi nyingine. Jamani tafuteni kodi nyingine. Hivi imefika wakati mtukamue sisi mpaka damu? Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili mpaka mwisho mimi sikubali. Kama ni hivi, hii kazi ya Ubunge ni kazi ya hasara. Tutashindwa kuwahudumia wananchi kwa sababu kila kukicha kale kadogo alikopewa Mbunge mnataka kukachukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali isikie vizuri, kelele zote hizi haziwezi kuwa kama jogoo. Kule Unyamwezini tunasema jogoo anaweza akapiga kelele usiku mmelala ili muamke; lakini yeye hawezi kujifungulia mlango. Sasa tusipige kelele kama vile jogoo. Sisi mlango tunao, wenyewe ndio tunasema hii bajeti sawa au haipo. Sasa isije kuwa mambo yamekwama mkimbilie caucus. Tumalizane tu humu jamani, mtusikilize na sisi.
Kuhusu pesa za maendeleo kwenye Halmashauri, hazipelekwi kwa wakati katika Halmashauri zetu. Hazipelekwi! Mwaka uliopita 30% tu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kaliuwa ilipelekwa, 70% yote haikupelekwa. Unategemea nini sasa? Maana yake kazi haziendi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tusichomeke. Nami naishauri Serikali, kama ina mambo yoyote muhimu, sijui madawati, maabara, itakuja na nyingine sijui itatengeneza jina gani, yaleteni mapema kwenye bajeti, siyo kuyachomeka wakati hayana mafungu. Matokeo yake Halmashauri zinaparaganyika. Zinakusanya, haziwezi kutumia kwa sababu tayari kuna maagizo. Tafuteni pesa kokote mlipo, eeh, maabara, eeh sijui madawati. Kazi ya Serikali, leteni mpango kama sasa, badala ya kuchomeka chomeka. Kwa nini tuchomeke wakati ninyi wataalam mpo na bajeti mnatengeneza? Naiomba sana Serikali isitengeneze utaratibu wa kuchomeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, madeni ya wazabuni. Mheshimiwa Waziri hebu tujaribu kuyaondoa madeni, ni aibu. Tunakazana, lakini huko madeni ni mengi, wazabuni walio-supply shuleni, kwenye hospitali, Halmashauri, Magereza, watu wanaidai Serikali, ni aibu! Tudaiwe basi na mashirika makubwa na nchi nyingine, lakini humu humu ndani mtu deni lake halali, anadai hata shilingi milioni mbili; hivi kuhakiki shilingi milioni mbili mnataka tena mtafute wataalam kutoka nje waje wahakiki deni? Haiko vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, CAG report kule kwenye Halmashauri Mheshimiwa Waziri tafuteni mzungumze na TAMISEMI. CAG report ni serious report, haiwezi kuwa inajadiliwa haraka haraka halafu inafunikwa tunaondoka. CAG report inaonesha kama kuna madudu, kama kuna mafanikio, lakini eti kwa kubana matumizi, tunaziambia Halmashauri zijadili siku moja au masaa, haiwezekani. Mbona wenyewe CAG report anakuwa amekagua karibu mwezi mzima amepiga kambi; lakini kujadiliwa na Madiwani, inajadiliwa kwa nusu saa au kwa masaa mawili. Mheshimiwa Waziri tengenezeni utaratibu CAG report ipate muda mzuri wa kujadiliwa kama ambavyo tunaweza kujadili hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imechangiwa kwa utaalam na Waheshimiwa Wabunge wengi, nisingependa kusubiri kengele, lakini mtusikie, kodi kwa Waheshimiwa Wabunge, achaneni na mpango huo, tafuteni mbadala. Withdraw benefit, waacheni watu wachukue mali zao kama ambavyo na sisi Wabunge tunachukua mali zetu. Kwa nini muwakabe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia taarifa hizi za Kamati mbili kutokana na ukaguzi wa CAG.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niiambie Serikali kwamba eneo hili ni muhimu kuliangalia na kusikiliza kwa makini lakini tupate matokeo mazuri. Kwenye ripoti hizi hakuna siasa, hili ni jicho la tatu la kuona utendaji wa Serikali yetu kupitia Halmashauri na Serikali kwa ujumla na kwa sababu nia yetu ni kutengeneza na siyo kuharibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la uteuzi wa Wakurugenzi. Kwa upande wangu sina tatizo na mamlaka ya uteuzi kwani inafanya kazi yake vizuri, lakini sisi kama Kamati ya LAAC tumeona upungufu mwingi siyo kidogo ya utendaji ya Wakurugenzi wetu. Wapo Wakurugenzi ambao hawajawahi kufanya kazi kabisa kwenye mfumo wa Serikali hata kwenye mashirika ya Serikali kiasi kwamba hata hawajui uendeshaji wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali kwa nia njema tu, tusibane sana matumizi, tuwafanyie mafunzo kidogo. Kuna Wakurugenzi walikuja mbele ya Kamati hawajui hata itifaki ya vikao. Sasa ukiwa na Mkurugenzi wa aina hiyo, unajua maneno wanayotumia wengi wanasema mimi nimeteuliwa na Rais, wanadhani uteuzi wa Rais unaweza kumfanya akaendelea kudumu pale, mimi sikubaliani nao. Bahati nzuri mimi nimetokea kwenye Halmashauri, kwa hiyo najua vizuri mno shughuli za Halmashauri, lakini kwa uelewa wangu mdogo wa hesabu Wakurugenzi wengi kwa kweli hawana uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, wapo ma-DT kwa maana ya Watunza Hazina wetu pamoja na kuwa na vyeti hawana uwezo wa kazi. Wapo ma-DT ambao wana CPA, lakini uwezo wao wa kufanya kazi ni mdogo sana. Kwa hiyo, niiombe Serikali tutupie macho utendaji wa watu hawa hasa Wakurugenzi na Watunza Hazina. Kule kwenye uteuzi kama nilivyosema hatuna mamlaka nako, lakini basi wapewe mafunzo kuwapa uwezo wa kufanya kazi na kuzielewa kazi. Wenzangu wamesema kuna watu wametoka kwenye NGOs, mashirika, VETA na sehemu mbalimbali, kwa idadi kubwa wachache sana waliotoka kwenye Local Government. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie kidogo suala hili la UDA. Tumepata taarifa Kamati mbalimbali zimekuwa zinashughulika na jambo hili la UDA. Niiombe Serikali ifike mahali tumalizane na UDA. UDA kila siku inatajwa Bungeni, kila siku haina mwenyewe, tumehoji nani mmiliki wa UDA mpaka tunamaliza vikao hatujapata majibu nani wamiliki wa UDA. Ifike mahali sasa tupate majibu nani wanamiliki na ilikuwaje alipatikana Simon Group.
Mheshimiwa Naibu Spika, Simon Group kwenye ripoti mbalimbali ameibuka tu kwamba huyu kapatikana anauziwa hisa, sasa amepatikana vipi hapaonyeshi mchakato ulioendeshwa kumpata Simon Group. Hili ni jambo la hatari kama kampuni inakuja tu ghafla, Serikali inakubali inaipa kazi. Tumempa umiliki mtu ambaye hajashindanishwa, hili ni jambo la hatari sana. Sasa tunataka tumjue mmiliki kwa sababu kumekuwa na shida ya kujua nani na nani anamiliki UDA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema mwenzangu pale Mheshimiwa Msuha zipo hisa zilipouzwa ilikubalika ziende kwenye shughuli za maendeleo, kwa muda wote hizi pesa zimetunzwa pale BOT. Kwa nini sasa muda usifike uamuzi upite zile fedha ziende kwenye shughuli za maendeleo. Ni fedha ndefu hizi, barabara, huduma za hospitali na shughuli mbalimbali za maendeleo zinahitajika kwa nini pesa ikae tu BOT ambapo yenyewe inatunza pesa tu ambazo kumbe zingekwenda kwenye shughuli za maendeleo. Zile hisa nyingine zilizobaki zigawanywe kwenye Manispaa nyingine ili Manispaa zote ziweze kumiliki UDA kwa pamoja. Hata hivyo, kama Serikali inaamua iachane nayo basi tujue imefika mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipendekeze sasa labda Kamati ya PAC, LAAC zikutane kwa pamoja kulimaliza jambo hili. Kwa sababu kila Kamati ina uamuzi wake, ina uchunguzi wake, ina mapendekezo yake ambayo hayaishi. Kwa nini sasa sisi kama Bunge tusiungane pamoja tukamaliza jambo hili. Sasa UDA tunaona imeingia kwenye kazi nyingine mradi unazidi kuwa mkubwa halafu tunamuacha mwekezaji huyu ambaye hatujui wenzake ni akina nani na kazi gani anafanya, lakini baadaye hata huu mradi wa DART utatuingiza kwenye shida. Nina imani Serikali ni sikivu na Mawaziri wapo wanasikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni uhai wa Halmashauri. Kwa wale ambao hamfahamu hizi Halmashauri zilikuwepo zikafa kama ushirika lazima tuangalie nini kiliua Halmashauri zetu. Sasa hivi toka tulipokwenda kwenye uchaguzi mwezi Juni, 2015 pesa ya maendeleo haijaenda na hii quarter ndiyo kabisa pesa ya maendeleo haijaenda, kule kwenye Halmashauri zimelala hakuna kazi inayoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Serikali pamoja na Waheshimiwa Wabunge tutaua hizi Halmashauri kwa mara nyingine tena kama hatukuwa makini. Tuliua Halmashauri hizi zamani, tukaua ushirika baadaye tumevirudisha vyama vya ushirika pamoja na Halmashauri, kutozipelekea pesa kunaua kila kitu. Athari zake ni nini? Toka tumemaliza uchaguzi wananchi wanadhani Serikali ipo likizo kwa sababu hakuna kazi inayoendelea kwenye Halamshauri zetu, Halmashauri zimelala, ofisi za Serikali za Vijiji hazichangamki. Siku zote kukiwa na pesa vijijini wanachangamka na utaratibu wetu ule wa kupeleka watu sita kwenda kusaini hata kama shilingi 200,000 hakuna sasa. Kwa hiyo, lazima tuhakikishe Serikali lazima ipeleke pesa kule. Pesa haziendi, tunasema madawati, tunasema hiki, sasa hivi kuna maboma mengi, litakuja agizo maboma yaishe, wanatoa wapi pesa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zipo Halmashauri zinaishi kwa ubuyu. Samahani watani zangu Wagogo, zipo Halmashauri zipo hoi bin taabani lazima tuziwezeshe. Zipo Halmashauri mpya ambazo zinahitaji kuongezewa nguvu ili ziweze kusogea. Halmashauri hizi nyingine hazina mapato. Kulishawahi kutoka tishio hapa kwamba Halmashauri kama haikusanyi itajifuta, sasa mbona Serikali yenyewe haipeleki pesa na yenyewe itajifuta? Jambo hili haliwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwasihi sana Serikali tupeleke pesa za maendeleo ili maendeleo yaonekane. Pia ni namna gani tunatimiza ahadi au Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni lazima pesa ziende kama haziendi tutakuwa tunarudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la madeni. Halmashauri hizi pamoja na mambo mengine kuna Halmashauri zinadaiwa mpaka shilingi bilioni 16 na wadau mbalimbali, watoa huduma, tender, Halmashauri zitalipa lini. Kama Serikali tunalipa madeni ya nje sasa wakati muafaka umefika tulipe madeni ya ndani ili huduma ziendelee. Shule na vyuo wataanza kufunga kwa sababu hakuna mtu ataendelea kutoa huduma wakati halipwi. Kwa hiyo, Serikali tupelekeni pesa tulipe madeni ya ndani ili Halmashauri zetu zifanye kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi sana yametokea huko lakini kikubwa kingine tumeshindwa kuelewa Wakurugenzi wanatoa wapi kiburi cha kutokujibu hoja za CAG. Siyo hoja tu za CAG hata maagizo ya Kamati yaliyopita, Wakurugenzi wanakuwa na kiburi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri Mheshimiwa Waziri ajaribu kuliona hili kama CAG anadharauliwa, kama Kamati ya Bunge inatoa maagizo hayajibiwi maana yake ni dharau. Hebu tulirekebishe hili ili Bunge kama Bunge maana yake Kamati ni Bunge lichukue nafasi yake tukiwa tunatoa maelekezo na maagizo yajibiwe. CAG anatoa maelezo yake yajibiwe, kama yanakaliwa kwa kweli tunakuwa hatuitendei haki ripoti ya CAG. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, CAG hapiwi pesa za kutosha na kuna tishio mwaka huu CAG anaweza asikague Halmashauri hata kumi. Kwa hiyo, kama pesa haziendi kwa CAG ambaye ndiyo jicho letu sisi hatuna uwezo wa kwenda kwenye Halmashauri kugundua tunaletewa kitu kilichofanyiwa kazi. Niiombe Serikali pamoja na mwaka huu tulipiga kelele wakati wa bajeti hebu mchakato wa bajeti unaokuja tumuangalie kwa karibu sana CAG ili apewe pesa za kutosha kufanya kazi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo vizuri kupigiwa kengele la pili na mimi ni Chifu nisingependa kupewa adhabu, nakushukuru.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa fursa hii ya kuchangia jioni hii kwa ajili ya ripoti ya Kamati zetu hizi mbili, Kamati ya Kudumu ya masuala ya UKIMWI pamoja na Huduma na Maendeleo ya Jamii. Nizipongeze sana Kamati hizi mbili kwa kuja na taarifa ambayo inatupa mwanga nini kinaendelea kwenye Kamati hizi lakini ndani ya Serikali pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mimi nichangie eneo ambalo nadhani ndani ya Bunge humu leo au siku mbili, tatu halijazungumzwa. Kwa niaba ya wanamichezo wote tuipongeze timu ya Serengeti Boys kwa kufaulu rufaa yake na sasa itashiriki fainali za under 17 kule Cameroon. Fainali hizi zilikuwa zifanyike Madagascar na sasa zitafanyika Cameroon. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa ushauri kwa Serikali na bahati nzuri mdogo wangu Mheshimiwa Nape yupo, ni vyema yakafanyiwa kazi haya tunayosema. Tumekuwa watu wa kufurahia matokeo. Tunapokuwa na matokeo mazuri kila mmoja anafurahia. Juzi tulipopata taarifa ya Serengeti Boys kufaulu kwenda kucheza fainali tumepongezana sana, lakini hatufikirii maandalizi sasa ya michuano hii. Ni juu ya Serikali kuanza kuona ni namna gani inaweza kuweka mkono wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1980 kwa wale mliokuwepo, Serikali yetu ilikuwa bado ina matatizo ya uchumi. Tutakumbuka tulikuwa tumetoka kwenye vita ya Uganda ya Nduli Iddi Amin, uchumi wetu ulikuwa umeparaganyika sana na Mwalimu alikuwa ametupa miezi 18 ya kufunga mkanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali ya Mwalimu ambaye tulidhani labda hapendi michezo, ilitia mkono wake tukafika Lagos kwa ajili ya AFCON, wakati ule tunaita fainali za nchi huru za Afrika. Hata matokeo tunayoyaona ya Cameroon, Ghana na nchi nyingine hazipati matokeo mazuri tu kwa kuachia vyama vya mpira, Serikali lazima iweke mkono wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nashauri, tuanze sasa. Mheshimiwa Nape wakati wa bajeti lete mapendekezo hapa tuone kama yatakwama. Tupo Wabunge tuta-support ili Serikali itie mkono wake isiwe Serikali ya kusubiri matokeo mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawapa mfano, mwaka 2014 mimi niliongoza msafara kwenda Brazil na kikosi cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwenye World Cup. Mashindano hayo huwa yanatangulia World Cup yenyewe. Tulikwenda na tukachukua ubingwa wa dunia na tukakaribishwa hapa Bungeni, Waziri Mkuu wakati ule alikuwa Mzee Pinda, Serikali ikatoa ahadi nyingi tu mpaka leo hata ahadi moja haijatekelezwa. Sasa tunaanza kujiandaa kwa kombe la dunia lingine mwaka kesho. Mwaka kesho ni World Cup, sisi tutatangulia kwenda Urusi na timu ile kwenda kutetea ubingwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe Serikali basi itie mkono pale tutakapohitaji msaada hata nauli. Maana yake tunagharamia wenyewe, tunakuja na kikombe tunafurahia wote kwa pamoja. Iko haja ya Serikai kuliona hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kushinda, tunataka kwenda kufanya vizuri kule Cameroon na watoto hawa wa under 17…..
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niseme kidogo, leo sina maneno mengi wala mapepo hatuyatoi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utangulizi ninaotaka kusema nataka kuhubiri juu ya amani. Amani ni kitu muhimu ambacho hakuna mwenye dhamana zaidi ya Watanzania wote. Viongozi wa kisiasa, mwananchi mmoja mmoja tunapaswa kuilinda amani bila kujali itikadi zetu na bila
misimamo ya kimihemuko na ushabiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika siku za karibuni na hasa wanasiasa tumekuwa na matamko mbalimbali yanayoashiria kupoteza amani, vitisho mbalimbali vinatokea na matukio mbalimbali kama haya ya utekaji na mambo kadha wa kadha ambayo lazima kama Wabunge humu ndani tuyakemee kwa nguvu zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwa miaka miwili na nusu iliyobaki, nasema iliyobaki kwa sababu mwaka 2020 sitagombea Ubunge, nitaendelea kuhubiri amani na baada ya kumaliza Ubunge nitaendelea na kazi ya kuhakikisha amani inaendelea kupatikana, hiyo ni njia sahihi ya kuwakumbusha Watanzania wote juu ya amani. Watu mbalimbali tumekuwa na matamko ambayo napata taabu sana. Kwa hiyo, nilitaka kuwakumbusha wenzangu juu ya umuhimu wa amani, kila mmoja anatamka anavyoweza na kila mmoja ana uhuru wa kutamka anayoweza lakini lazima tuwe na akiba ya maneno, tuwe na vifua vipana vya kuhifadhi maneno, lakini kutafakari athari za maneno tunayoyatamka.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sasa nichangie kidogo juu ya hotuba ya Waziri Mkuu. Watu wa Tabora na Jimboni kwangu Ulyankulu, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakupongeza sana kwa kazi nzuri ambayo umeifanya juu ya zao letu la tumbaku, Bodi ya Tumbaku, Bodi ya WETCU na kwa sababu umeahidi kwamba utakuja sasa kumalizia kazi hizo tunakukaribisha kwa niaba ya wenzangu wote tunakuunga mkono kwa hatua mbalimbali unazozichukua. Huu ushirika umekuwa na shida, ushirika ulivunjwa, ukarudi lazima sasa Serikali iwe karibu sana na ushirika na hasa hawa Warajisi wa Ushirika Mikoani, ni watu ambao wakati mwingine wanasaidia kuharibu nia njema ya ushirika na tukukaribishe tena Tabora na utusimamie vizuri hasa uanzishwaji wa vyama vyetu vya ushirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani nyingine ni kwa niaba ya Wabunge wenzangu wenye ulemavu, nitoe shukrani kwa Katibu wetu wa Bunge na Sekretarieti yake kwa kuwa karibu na sisi Wabunge wenye ulemavu. Ofisi ya Katibu wa Bunge imekuwa ikiratibu mambo mbalimbali toka tukiwa na Mheshimiwa Possi na sasa tunakwenda vizuri, lakini tuombe tu Ofisi ya Katibu waweze kutekeleza ombi ambalo tulitoa kwamba Ofisi ya Utawala itengenezewe lift kuwawezesha Wabunge wenye ulemavu kuweza kufika kule juu kuliko na ofisi mbalimbali za Utawala, tuna imani Katibu wa Bunge atakuwa amelisikia, tunafanya kumkumbusha jambo ambalo tulilizungumza huko mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine Mheshimiwa Waziri Mkuu ni juu ya uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala. Ukiuchukua Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Tabora eneo lote lile lilikuwa Mkoa wa Tabora limeendelea kukatwa polepole na sasa bado Mkoa wa
Tabora ni Mkoa mkubwa kulikuwa Mikoa yote Tanzania. Lakini hapa katikati Serikali imekuwa inatoa maeneo sisi kazi yetu tunasikiliza tu, mara mmekata Mkoa gani mmewapa, lakini
Tabora hamtaki kuugawa Mkoa, kwa sababu ni Mkoa mkubwa bado tunahitaji Mkoa ugawanywe hata kama tuna azma ya kupunguza matumizi, Wilaya zetu ni kubwa, ukiichukua Wilaya ya Uyui peke yake inaweza ikakusanya Mkoa wa Kilimanjaro na Mkoa wa Tanga ikawa sawa na Wilaya ya Uyui. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua Wilaya ya Kaliua inaweza kuwa sawa na Mkoa pia wa Kilimanjaro na Tanga kwa pamoja. Kwa nini sasa tukazingatia tu kwamba tunataka kubana matumizi. Mheshimiwa Waziri Mkuu tuombe sana, Ulyankulu tumeomba Wilaya, tumeomba Halmashauri na jambo hili Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliahidi kwamba siku tatu tu zingemtosha kutoa uamuzi sasa tuna mwaka mmoja na nusu bado tu hamjatafakari kutupa
Wilaya? Bila shaka ujumbe umefika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu nimalizie sitaki kuwa na maneno mengi na sitaki kumaliza dakika zangu zote, kwa niaba ya TFF nitoe shukrani kwa Serikali pamoja na TRA kwa kumaliza mgogoro ambao umekuwepo hata kama haujaisha moja kwa moja lakini
hatua iliyofikia kati ya Shirikisho la Soka nchini pamoja na TRA liko vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa katikati tuliona na kusikia kwamba TRA iliweza kuwateremsha vijana wetu mashujaa wetu wa Serengeti Boys kwenye basi kisa deni, mpaka pale mamlaka zingine zilipoingilia kati. Mchana huu nilikuwa nawasiliana na Ndugu Malinzi, Rais wa TFF ameniambia kwamba tuko vizuri pamoja na Serikali pamoja na TRA juu ya jambo hili. Kwa niaba ya wadau wote wa mpira na michezo kwa ujumla Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakushukuru kuweza kulirahisisha jambo hili ili watu wafanye kazi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kumaliza dakika zangu na inanitosha. Wengine kwenye Wizara na Taasisi nyingine tutakutana mbele ya safari. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya yangu kuendelea kuimarika. Nitumie fursa hii kuwatoa wasiwasi wapiga kura wa Ulyankulu, nina imani Mwenyezi Mungu atanilinda mpaka 2020 tukamalizana salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kuwapongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake Kwa hotuba iliyoletwa mbele yetu na kwa sababu Mheshimiwa Mwakyembe hana muda mrefu pale, pamoja na kwamba yeye ni mtu wa habari, lakini tumkaribishe na tuna imani naye, kazi itakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza mtangulizi, Mheshimiwa Nape. Sisi wanamichezo tulifarijika sana naye na niseme tu alifanya kazi nzuri, haya mengine ni ajali za siasa. Nimtie moyo Mheshimiwa Nape, asikate tamaa na kwa sababu yeye ni msanii, basi aendelee kuwepo kwenye vuguvugu letu hili la michezo na usanii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tunafahamu sasa timu yetu ya Serengeti Boys kama siyo jana basi watakuwa wameshafika Gabon. Ni juu ya sisi sote kuonyesha mshikamano juu ya timu hii. Kuzijenga timu, hazijengwi kwa maneno. Kuzitengeneza timu zipate mafanikio, hazitengenezwi kwa maneno. Kwa sasa nchi nzima na familia ya wanamichezo tunachangia mafanikio na gharama mbalimbali za Serengeti Boys. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, tushiriki basi kwa dhati badala ya kushiriki kwa maneno tu na kuwalaumu wenzetu wa Wizara kana kwamba kila jambo wanafanya wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata huko Hispania, Madrid, Barcelona wapo watu wanahangaika nazo. Ukienda Uingereza, Liverpool, Manchester United au timu ya wenzangu wale ambao wanaishi kwa wasiwasi Arsenal, zote hizi zinatengenezwa na watu. Tusiishie tu kusema maneno na kulaumu, tujaribu kushiriki na sisi katika kuhakikisha maendeleo haya tunayoyasema yanafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, liko jambo ambalo kila mwaka mimi nalisema, hata kabla sijaingia Bungeni nimekuwa nikilisema. Mimi kama mwanamichezo ni juu ya michezo mashuleni. Hiyo Taifa Star tunayoizungumza ya mwaka 1980 iliyocheza mpira kule Nigeria, sehemu kubwa ya waliocheza kule walitoka mashuleni, walitengenezwa.

Mheshimiwa Spika, michezo ya shule za msingi, michezo ya sekondari, michezo ya vyuo ilikuwa ni chachu ya kutengeneza wachezaji kwenye michezo yote. Iwe riadha, iwe mpira wa miguu, iwe netball ambayo sasa sijui inaelekea kufa, itabaki Bungeni tu sijui! Yote ilitengenezwa kutoka mashuleni. Sasa hatutaki kusema juu ya waliotangulia wakafuta michezo ile mashuleni adha yake tunaiona.

Mheshimiwa Spika, sasa michezo imebaki kwenye shule mbalimbali chache ambazo siyo za Serikali, wanatusaidia sana kuhakikisha michezo inakwenda vizuri. Je, Serikali, TAMISEMI, Wizara ya Habari na Wizara ya Elimu kwa nini sasa isishirikiane kuhakikisha michezo mashuleni inarudi kama zamani na iwe ndiyo jiko letu la kupika wachezaji na wanamichezo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, hebu utakapokuwa unakuja kuhitimisha, hebu ingia kidogo pale utufafanulie mambo yalivyojipanga kwa ajili ya michezo mashuleni. Bahati mbaya simuoni Mheshimiwa Profesa Ndalichako, angekuwepo na yeye ni pamoja na Mheshimiwa Simbachawene, hizi Wizara zote tatu zishirikiane…

SPIKA: Mheshimiwa Ndalichako yuko Arusha, kutuwakilisha kwenye lile jambo la msiba ule mkubwa.

MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Spika, ahaa basi.

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu na mimi sikuwepo.

Mheshimiwa Spika, maana yangu ni kwamba Serikali iko hapa, ione umuhimu huo. Badala ya kuwa tunasubiri mafanikio tu kama alivyosema Mheshimiwa Mtolea, kwamba tunasubiri mtu ameshinda huko, tunamleta hapa Bungeni na kupiga naye picha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikizungumzia juu ya Watoto, mabingwa wa Dunia wa michezo ya Watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Timu yetu ya Mwanza na mwaka kesho tunakwenda Kombe la Dunia; je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuisaidia hiyo timu ikafanye vizuri? Hivi karibuni timu ya walemavu ilikuwa inashiriki mashindano pale Uingereza; je, inasaidia nini kutaka kwa watoto hawa?

Mheshimiwa Spika, suala nyingine ni juu ya viwanja. Bahati mbaya sana Serikali yetu haina viwanja vya kutosha. Tunavyo viwanja hivyo; Kiwanja cha Uhuru pamoja na Uwanja wa Taifa, lakini muda sasa umefika Serikali itengeneze viwanja vyake yenyewe, kuliko kutegemea viwanja ambavyo sasa ni mali ya taasisi nyingine.

Mheshimiwa Spika, pia viwanja hivyo visitengenezwe Dar es Salaam tu. Dodoma hapa tunahitaji kiwanja, tunahitaji kiwanja Mwanza, tunahitaji Arusha, viwanja vya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni juu ya makato. Mimi nashiriki sana michezo hii, makato ni makubwa sana kwenye viwanja. Watu wanakusanya pesa lakini pesa hizi zinakusanywa na wachezaji. Wachezaji wanachapa kazi ndiyo maana pesa inapatikana, lakini makato ni makubwa kiasi kwamba yaani faida inayobaki iwe kwa TFF, iwe kwa Chama cha Mpira cha Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira Mkoa wa Tabora. Nafahamu, yaani kinachokuja kubaki ni kitu kidogo sana. Serikali basi iangalie; je, inajenga viwanja hivi kuwakomoa wanamichezo? Je, inajenga viwanja hivi ili shughuli ibaki ya matamasha au ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, tuna michezo ya Afrika Mashariki ya Bunge. BungeSports Club imesajiliwa kwa kanuni zile zile kama za Simba, kama za Azam kama za Yanga. Tuna michezo hii lazima Wizara ioneshe kutuunga mkono kama Bunge Sports Club. Tumekuwa ni watu ambao kama vile sisi tunacheza michezo mingine tu ambayo haitambuliki. Bunge Sports Club na ninyi Mawaziri mko humu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, BungeSports Club ni club ya Wabunge wote na wafanyakazi wote. Nawaomba Mawaziri kutumia jukwaa hili; Mawaziri fikeni basi mje mfanye mazoezi na sisi. Pia mshiriki, muwepo kutuhamasisha kuona kwamba michezo ya Afrika Mashariki inayokuja tunaweza kushinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ninaunga mkono hoja ya Waziri.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipatia fursa hii ili na mimi niweze kuchangia machache juu ya mpango huu. Kwanza kabisa nimshukuru Spika, kwa asubuhi ya leo amefungua milango ya namna ya uchangiaji na kututoa hofu. Wapo watu wamekuwa na hofu namna ya kuchangia wakihofia labda mtu anaweza kutumia maneno yakasababisha kupelekwa kwenye Kamati ya Maadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ndivyo, ushauri wangu sasa kwa Wabunge wote lakini zaidi kwa vijana wasomi, mnayo nafasi ya kuisaidia Serikali, kuishauri kwa uwazi na kwa haki ili mawazo yenu na ushauri uweze kupokelewa. Hatuna haja ya kuwa na wasiwasi na bahati nzuri uteuzi umepita mpaka 2020 naamini tusiwe na hoja ya kufikiri kwamba, kuna uteuzi au mambo gani. Kwa hiyo, tujikite kuishauri Serikali kwa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwapongeza Mawaziri, kwanza wale waliobaki kwenye Baraza la Mawaziri, lakini pili ni wale ambao wamepata fursa ya kuingia kwenye Baraza la Mawaziri, ni imani yangu nafasi hiyo wataitumia vizuri kutusaidia kusonga mbele kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia liko jambo ambalo ni vizuri nikalisema ambalo ni tatizo lililoko jimboni kwangu, lakini kwa maana ya kitaifa juu ya hifadhi. Wananchi wetu sasa wanateswa. Tunazungumzia mipango ya maendeleo, wakati huo huo kuna watu wanapitisha mabango kusema shughuli za kibinadamu zisifanyike, watu baada ya wiki mbili wahame, unazungumzia Wilaya ambayo
asilimia 90 ni hifadhi, lakini ndani ya hifadhi kuna vijiji ambavyo vimesajiliwa, kuna shule ambazo zimesajiliwa, tunaenda wapi? Unapowaambia watu eneo lote la Ulyankulu ni hifadhi, halafu watu wako mle kabla, si ajabu hata ya Sheria ya Hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuiombe sana Serikali kama kweli tunazungumzia maendeleo hebu tusiwabughudhi watu wetu, tusiwaone watu bora wakati wa kufikia uchaguzi. Wakati tunapo-approach uchaguzi mambo yote haya tunaambiwa kaeni, chapa kazi muishi kwa amani, lakini hapa katikati anakuja mtu wa TFS anavuruga kila kitu, unataka watu waishi wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani jimbo zima, wilaya nzima tunatunza miti, ifike mahali tujue nani bora, bora msitu au bora binadamu? Itatusaidia sana badala ya kuwa tunawavuruga wananchi wetu, wanapanga na wao mipango yao ya maendeleo, leo unawaambia kuanzia sasa shughuli za kibinadamu zisimame, maana yake maendeleo yasimame. Maeneo hayo yanayoambiwa hivyo, labda wiki moja u mwezi mmoja nyuma Waziri Mkuu amepita na hata yeye kuchangia.

Kwa hiyo, Serikali hii iangalie huyu anasema hivi, kesho mwingine anasema hivi na mwingine atakuja weka ndani. Imefikia hatua Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya anawekwa ndani kwa jambo kama hili. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali itusaidie kutuliza hali hiyo na ninajua mdogo wangu Mheshimiwa Kigwangalla atalirekebisha pamoja na Mheshimiwa Hasunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa twende kwenye kilimo. Kilimo ndio uti wa mgongo tunavyozungumza kila siku na kilimo ndicho kinachotuletea pesa nyingi za nje, hapo tunakuwa tunazungumza habari ya mahindi. Nawashangaa sana watu wanaotetea wakulima wasiuze mahindi, sisi mishahara yetu hakuna anayetupangia matumizi. Iweje mkulima ambaye kalima bila mkopo, kwa fedha zake, halafu apangiwe namna ya matumizi ya mahindi yake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Ulyankulu tunalisha Mwanza, tunalisha Shinyanga kwa mahindi yanayotoka Ulyankulu. Ni kwa vile tu mnaowataja hamuitaji Tabora, lakini kumbuka kwamba watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga, Kahama, mahindi wanayokula yanatoka Ulyankulu na sisi tuko tayari kuuza. Kama ni hivyo mimi siko tayari kuhimiza kilimo kwa sababu watu wanafanya juhudi, wanalima chakula kipatikane, lakini tunaanza kuweka vikwazo kwa mkulima kutumia rasilimali zake. Mbolea amenunua mwenyewe kwa pesa zake, kila aina ya pembejeo amenunua, lakini inafika amevuna anapatikana mtu wa kumpangia, haijapata tokea, hayo ni mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumbaku hii ya sasa imekuja mwaka 1967, na mimi mkubwa tu mwaka 1967, sasa tumbaku hiyo huko nyuma tarehe 5 au 6 Julai, kabla ya Sikukuu ya TANU ilikuwa ni lazima wakulima wote wawe wameshapata pesa; haijapata tokea safari hii masika mvua inanyesha tumbaku bado iko kwenye ma-godowns, tumeweza kwenye makinikia eti tunashindwa kwenye tumbaku, haiwezekani. Nini kipo hawa wazungu wa tumbaku wawe na kiburi kuliko wa makinikia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi tena siko tayari, nasema kabisa, yaani siwezi kusimama jukwaani kuhimiza kilimo ambacho watu wanateseka, tumbaku limekuwa zao la kuleta umaskini sasa. Hiyo korosho ya wenzetu Mtwara huko, Lindi zamani isingesikika, lakini kwa sababu nia ya Serikali ilikuwa kuhakikisha kuwakomboa wenzetu wakulima wa korosho, leo hii wanafurahia. Lakini tumbaku tunahangaika. Tumbaku iko kwenye ma-godown, mvua zinanyesha, lakini utashangaa tunasema tumbaku hii ni zao linaloleta pesa kuliko mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kampuni ile iliyochukua mali za TAT inauza mpaka ma-godown, itauza kwa tender ma-godown yote nchi nzima yametangazwa yanauzwa, hiyo tumbaku itakuwepo, haitakuwepo. Na leo hii tunazungumza hivi kama mzaha, watu wameuza tumbaku wale ambao hawakuwa kwenye mpango kwa maana ya bajeti ile ya tumbaku wameuza mpaka ile bajeti ime-burst, wale wakulima sasa waliochelewa wanaambiwa mna tumbaku ambayo hamkupangiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaleta taabu. Sisi wanasiasa wa Tabora na hasa Wabunge tunapata kigugumizi, iko shida lazima, iko shida hapa katikati. Tumesafisha WETCU, lakini iko shida hiyo shida huko mbele najua itakuja kuumbua watu, hatuwezi kukaa jambo moja tu tunarudia, Waziri Mkuu amekuja karibu mara nne, lakini hakuna ufumbuzi. Wazungu wameona kwamba, wao ni zaidi ya Serikali, lakini tunaambiwa watu tutafute masoko wenyewe, hivi mkulima mmoja mmoja aanze kwenda Uchina, Indonesia, wapi, kutafuta soko, haiwezekani, maendeleo gani hayo tunayataka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa muda si mrefu tutaanza kusimama majukwaani kuwaambia acha kulima tumbaku. Nitawaambia watani zangu Wasambaa na Wadigo leteni katani tuanze kulima katani kwa sababu sasa tumbaku haitusaidii. Watu wetu wamekuwa maskini, sio vizuri na Serikali muangalie kule ambako Serikali inapata mapato, nayasema haya kwa uchungu. Jimbo la Ulyankulu ndio linalotoa mahindi kwa wingi, tumbaku kwa wingi. Aah, hii kengele tayari? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maji, tumesema hapa leteni mpango kuhakikisha nchi nzima inapata maji kama ilivyo REA I, REA II na sasa tunakwenda kwenye REA III, shida gani ipo? Maji yakipatikana hayo mambo mengine yanakwenda vizuri, lakini maji haya imekuwa tatizo, maji ya Ziwa Viktoria wanatumia wenzetu kule Misri, wanatumia Ethiopia, wanatumia sijui Sudan, wapi, sisi eti tukitaka kutumia, tayari kaja mtu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tu miradi hiyo amekuja mtu kutembelea Tanzania, hatujui walichonong’ona, lakini tetesi ni kwamba wanapata hofu. Maji tunayo tele yanaweza yakasambaa nchi nzima, kwa nini tusifanye hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Malagarasi pale kuna maji, ingawa yana shida, lakini maji ya Ziwa Victoria ni maji mengi sana, leteni huku. Tunakaa tunahangaika ooh, mvua, kwa nini tusipate maji kutoka Ziwa Victoria?

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara. Barabara tumekuwa na mipango. Ukiangalia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ziko barabara nyingi sana, acha mbali ahadi za Mheshimiwa Rais, lakini je, utekelezaji wake uko kwa kiwango gani? Leo tuna miaka miwili tunazo barabara nyingi, mojawapo barabara kutoka Mpanda – Ulyankulu mpaka Kahama, tunazungumzia ujenzi wa lami, barabara ni pori, hata upembuzi yakinifu hatuoni, mipango gani hii sasa?

Kama hatuna barabara zinazopita kwenye maeneo ya uzalishaji tunajidanganya. Ndio hii sasa mazao yanabaki sehemu yana bei ndogo, tunapiga kelele. Mheshimiwa Mpango jaribuni kuliangalia hilo barabara zetu zikae vizuri. Kuwe na nia ya dhati kwamba, sasa tunataka kutengeneza barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini reli hiyo standard gauge sina hakika tutachukua miaka mingapi, hapajaelezwa, lakini lazima kama ni hivyo reli zetu tuziimarishe. Tunayo reli ya kati, tunayo reli ya Singida, tunayo reli ya Moshi – Tanga, hebu tuingize nguvu zaidi kule wakati tunaendelea na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Umeme REA III. Aah, speed imekuwa ndogo kabisa, Mheshimiwa Kalemani sijui speed yake imeshia wapi. Sijui baada ya kufika huko aliko, speed ya REA III ni ndogo sana. Tuiombe Serikali iongeze speed kwenye huu mradi, lakini kuhakikisha vijiji vyote ambavyo havikupitiwa, lakini taasisi zote, lakini na sisi wanasiasa tusiweke fitina maeneo mengine. Huko kuna uhakika kwamba, wanasiasa wakati mwingine tunapindisha maeneo mengine yasipate umeme kwa sababu za kisiasa, hebu tuache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za maendeleo kwenda kwenye Halmashauri bado ni tatizo. Iko Halmashauri moja ilipangiwa kupelekewa bilioni 11 imepelekewa bilioni moja, hebu tuone hivi kweli kuna jambo litaendelea? Kutoka shilingi bilioni 11 inapelekewa shilingi bilioni moja, shilingi bilioni nyingine shilingi bilioni 10 hazijaenda, unategemea nini katika eneo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zetu bado ziko tete haziwezi kujiendesha. Ziko Halmashauri hata kulipa posho ya Madiwani haziwezi kumudu, ningeomba sana uwepo utaratibu wa kuwahisha pesa. Mbona tunazungumza tunakusanya sana, sasa kama tunakusanya pesa inaenda wapi? Kama pesa kila siku tunasema makusanyo yamepanda, eeh, mbona pesa haziendi Halmaashauri? Iko nini? Iko shida gani? Pelekeni hela kule tuone tutakachokwama, bahati nzuri Wabunge wote sisi ni sehemu ya Halmashauri. Bila shaka Mheshimiwa Mpango utakuwa umenipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari? Aah, bado bwana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwe na upendeleo kwa machifu.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii kuchangia hoja iliyoko mbele yetu, hoja muhimu kwa maisha ya Serikali yetu pamoja na wananchi wetu, wakati huu tunapohangaika na maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nachukua fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na timu ya uongozi wote wa Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko tofauti ya bajeti ya mwaka unaokwisha na hii iliyoletwa mwaka 2016 na mwaka huu wa 2017 kuna tofauti kubwa, kuna maboresho, lakini bado yapo mambo ambayo tunapaswa kuyatilia mkazo ili maisha ya wananchi wetu yaende vizuri na yawe bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo huduma tunazozingumzia hasa barabara. Toka mwaka 2016 tumekuwa tunazungumzia barabara inayotoka Mpanda kupitia Kaliua, Uliyankulu hadi Kahama. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu itakuwa inaunganisha mikoa karibu mitatu au minne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama azma ya Serikali yetu kuunganisha mikoa kwa lami, basi baada ya kipande cha Chaya na Nyahuwa kupata pesa, basi naomba Wizara ya Fedha na Wizara ya Ujenzi mwelekeze sasa nguvu zote kwenye barabara hii inayotoka Mpanda kupitia Uliyankulu mpaka Kahama. Ni kilomita 428 na nina imani wakipatiwa Wakandarasi kama watatu, kazi inaweza kwenda vizuri, badala ya kila mwaka kuizungumza kwenye Ilani lakini utekelezaji wake hakuna. Tunataka pia tupate performance ya utekelezaji wa mradi huu umefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo tunalizungumza hapa, lakini Serikali bado inakuwa ipo kimya. Suala la Mfuko wa Maji; tumezungumza sana lakini Serikali ije basi na kauli, tunakubaliana au hatukubaliani? Maana unapozungumza halafu mwenzako kakaa kimya, maana yake labda unachozungumza ni msamiati wa Kichina au Kijapani, maneno ambayo ni michoro michoro ambayo huwezi kuielewa. Serikali ije hapa na majibu: Je, tumekubaliana juu ya mfuko wa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, tatizo la maji vijijini ni kubwa kuliko tunavyodhani. Mpo wengine hapa ndani mkienda vijijini kwenu mnabeba maboksi ya maji. Hakuna mtu anayekwenda kunywa maji ya kijijini. Yawezekana mkaona hakuna haja kwa sababu huku ndani mjini mnaoga vizuri, mnakunywa vizuri, maji ya kupikia mazuri, hakuna anayejali. Kwa nini Serikali isije na majibu basi! Toka mwaka 2016 tunazungumzia Mfuko wa Maji, lakini tunaona kama vile mmeziba masikio. Njooni na ufumbuzi wa tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wiki nzima nilikuwa Jimboni, kila eneo ukienda ni shida ya maji, lakini humu Bungeni kila mmoja akiulizwa swali la maji, maswali ya nyongeza Bunge zima linasimama, hata wewe Mwenyekiti unapata tabu sasa nani aulize na nani aache kuuliza? Hiyo ni kuonesha ni jinsi gani ambavyo suala la maji lina umuhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukamilishaji wa mradi wa umeme; tunakwenda tumeshaanzisha REA III. Naiomba sana Serikali, sasa tusiichie njiani, maana yake shida ni kwamba watu wote tunaelekea kenye madini; wote mazungumzo yamekuwa ni madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukamilisha REA III liende kweli likatatue matatizo yaishe. Siyo tena tuje tuambiwe kuna REA IV na V. Itafika wakati hata pesa hatutapeleka kwenye umeme, kwa sababu umeme utaonekana siyo tena jambo la umuhimu. Kwa hiyo, nashauri hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala lingine juu ya suala la ujenzi wa Zahanati pamoja Vituo vya Afya. Jambo hili kama tunawaachia wananchi zaidi, hatuwezi kulikamilisha. Lazima Serikali ielekeze nguvu huko. Sasa tulisema kila Kata ijenge Kituo cha Afya; mabadiliko yamekuja, kila Kata mbili zijenge Kituo cha Afya; tunaanzisha tena migogoro kituo hicho kijengwe wapi? Kila Kata inapiga chepuo kujenga eneo lake. Kwa hiyo, nadhani Serikali kwa makusudi kabisa tuelekeze nguvu huko kwenye ujenzi wa Vituo vya Afya pamoja na Dispensary.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningumzie hili suala la madini, migodi na kodi; mimi kabla ya kuingia hapa Bungeni, nimekuwa mfanyakazi huko kwenye migodi. Mwaka 2008 wakati issue ya Buzwagi inaletwa hapa, mimi nilikuwa mgodini. Sisi wafanyakazi wa kule tumekuwa tukipaza sauti sana juu ya matatizo haya ya uibiwaji wa mali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaziona ndege, tunasema, lakini watu walikuwa hawasikii. Tumezungumza sana juu ya mambo haya! Kule mgodini pia kuna mambo ya unyanyasaji, kuna ubaguzi mkubwa na hasa raia hawa wa Kizungu wanaotoka South Africa, wananyanyasa. Sasa wakati wafanyakazi mgodini wanaponyanyaswa, wanapaza sauti juu ya wizi wa mali hii, lakini hakuna aliyesikia. Leo hata tukisema, hao wanaokuja kufanya kazi migodini, hawana elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule nimeshuhudia watu wana vyeti vya semina ya siku tatu; na wenzetu wapo makini sana. Ukipiga semina hata ya siku moja, unapata cheti. Ukipiga semina ya siku mbili, unapata cheti; ndizo CV walizonazo. Ukienda Idara ya kazi, vibali vinatoka kila siku watu wafanye kazi, ambapo masharti yanataka mtu mwenye elimu zaidi, lakini awe na mpango wa kufundisha wazawa. Hakuna anayejali. Watu wapo migodini wanakamatwa na bangi, wanafikishwa Mahakamani, lakini kesho yake mtu huyo huyo anaomba kibali anaruhusiwa kufanya kazi ndani ya ardhi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie ukwepaji kodi. Wote hapa akili sasa ipo kwenye Barrick na Acacia, lakini migodini, Mheshimiwa Waziri wa Fedha anisikie vizuri, zipo Kampuni nyingi zaidi kuliko kampuni tunayoizungumza, lakini hawa watu wanaiba, wanakwepa kodi kwa njia mbalimbali. Pesa zao wao wanalipana juu kwa juu, hakuna malipo ya moja kwa moja. Maana yake hata kodi haijulikani ni kiasi gani. Hata mifuko ya jamii hii hawachangii, kwa sababu wao wanarekodi mishahara midogo kuliko mishahara wanayolipwa kule nje. Mimi ni shahidi na niko tayari kueleza jinsi kodi inavyoibiwa kwa sababu nimekuwepo kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ajaribu kuangalia sana, tusijikite kwenye Kampuni moja tu kubwa, wakati mle mgodini kuna kampuni nyingi zinafanya shughuli hiyo. Kwa hiyo, nashauri, kuchunguza kwa makini zaidi wizi au ukwepaji wa kodi wa kampuni zile ndogo ndogo ambazo zimepewa kazi na makampuni ya migodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la shilingi milioni 50. Imekuwa ni msumari huu, kila ukizunguka kwenye majimbo swali kubwa ni shilingi milioni 50, hatuna majibu! Serikali ije na majibu hapa. Siyo dhambi kusema kwamba tumeahirisha au tutafanya mara nyingine. Tuondokane na jambo hili au liletwe katika mpango mwingine kuliko kung’anga’na tutatoa shilingi milioni 50; huu ni mwaka wa pili sasa hatujatekeleza. Hatujafanya hata majaribio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabla hata kengele haijanililia kama kawaida yangu, fedha za maendeleo zinazopelekwa kwenye Halmashauri zetu, hata mwaka 2016 nilisema, lazima tuhakikishe fedha zinazokwenda kwenye Halmashauri ziende kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama fedha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chifu wetu nikushukuru kwa kunipa fursa hii ambayo naitafuta muda mrefu, mambo yanakuwa magumu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile sikuwahi kuzungumza toka tumeanza Bunge hili la bajeti, naomba nitoe maneno ya utangulizi juu ya amani kwa Watanzania wote. Suala la amani Waheshimiwa Wabunge si jambo la kikundi fulani au si jambo la Wabunge peke yake amani, dhamana ya amani ni ya wananchi na Watanzania wote. Tunafanya makosa sana kudhani sisi wanasiasa ndiyo wenye dhamana ya amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi niseme wazi mimi sikufurahishwa na mjadala wa kuwajadili viongozi wa dini. Sisi ni sehemu yake na wao ni sehemu yetu. Kila wakati viongozi wa dini wanatuhubiri tuache mambo mabaya, mnaambiwa muache kuzini, wizi, rushwa mnashangilia lakini mkiambiwa jambo linalogusa mambo yenu mengine mnakuja juu. Tumerogwa na nani Watanzania kudhani kwamba viongozi wa dini wanachokisema ni cha uongo? Leo hii unakwenda unanyenyekea kwa jina la Baba, la Mwana na la Roho Mtakatifu, lakini ukiambiwa jambo hili halifai, unakuja juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tuache kwani wao ni sehemu yetu. Mbona sisi tukifanya humu tunakuwa wakali na kupelekana Kamati ya Maadili, wapi sasa wao watajadili, wao hawana Kamati ya Maadili, wao kupitia majukwaa ya Makanisa na Misikiti ndiyo uongozi tulionao. Kila siku tukipata mafanikio tunakwenda kunyenyekea kuombewa. Hakuna mtu humu hajaombewa baada ya kupata Ubunge hapa, lakini leo viongozi wetu wa dini tunawabeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili sijalifurahia kabisa na mimi niko tayari kutokuelewana na wengine. Najua 2020 tutakutana huko tukiwaombeeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, kwanza hii habari ya dakika tano mimi niseme tu sikubaliani nayo, muda mdogo sana huu kueleza mambo mbalimbali ya majimbo yetu na nianze na ujenzi wa barabara ya Urambo – Kaliua. Barabara hii ina kilomita 28 na inajengwa na mkandarasi mzalendo. Mimi nasema huyu mkandarasi mzalendo hana uzalendo. Haiwezekani karibu miezi nane anashughulika na usafi tu kama wa kilomita mbili. Mimi ningekuwa mwamuzi leo tunamnyanga’anya kazi hii. Hatuwezi kukaa na mtu ambaye uzalendo wake una mashaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina nia njema tu kwamba kilomita chini ya 30 tuwape wazawa wafanye kazi lakini kazi zenyewe hawafanyi. Magari kutoka Kigoma na sehemu nyingine yanazama eneo la tukio mkandarasi yupo pale wala hajali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi gani hana uwezo hata wa kujenga kambi? Mvua zinanyesha za kwao, kila jambo baya wao, wapo pale. Mheshimiwa Waziri alikuja hawajali kabisa habari ya Waziri, wana kiburi kutoka wapi? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri, wananchi wa Wilaya ya Kaliua wamechoshwa na jambo hili. Hatuwezi kukubali, tutafanya utaratibu tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema tofauti mnanielewa, kama hawezi sisi tutatafuta njia ya kumfanya asifanye kazi na tuko tayari kwa lolote hatuwezi kuvumilia. Kwa hiyo, tunataka sasa baada ya bajeti hii tuone mabadiliko pale na mimi kila siku napita pale pamoja na kwamba njia siyo nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani suala la amani kila mmoja alizingatie, wote tuwe na dhamana ya amani. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE.JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata fursa hii. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri na Watendaji wa Taasisi zote zinazoshughulika na michezo na bila shaka wanajua mimi ni mwanamichezo niliyekubuhu na nashughulika na michezo zaidi ya miaka 40 sasa. Kwa hiyo, najua kila kitu kilichoko ndani ya Wizara hii na ndani ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii na sehemu kubwa, maoni yetu ni yale ambayo tuliyajadili kule, nami nikiwa mdau pia, maoni yetu tuliyatoa kwenye Kamati na Serikali tuliieleza kila kitu, kwa hiyo, hapa nitakuwa na mchango mdogo tu wa kusisitiza. La kwanza ni juu ya michezo mashuleni. Kwa hulka Watanzania hatuna Academy za michezo nyingi kwa sababu ya gharama za uendeshaji. Sasa vituo vyetu hivi kwa maana ya Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo ndiyo Academy zetu zinazoweza kutoa wanamichezo wazuri na hasa kwa kuzingatia historia huko nyuma, UMISETA tulikuwa na wachezaji wazuri waliotutetea vizuri kwenye timu za Taifa na pia UMITASHUTA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maoni yangu ni kwamba Serikali hebu ijaribu kurejea huko nyuma tulifanyaje kwenye michezo shuleni pamoja na kwamba hapa katikati kuna watu walilewa madaraka wakafuta, nadhani tuwaache tu na mambo yao, lakini turudi nyuma kabla ya kufutwa, nini kilifanyika na nini tulifanikiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni juu ya ruzuku kwa Vyama vya Michezo. Huko nyuma Serikali ilikuwa na mkono wake kwenye Vyama vya Michezo na tuliona faida zake, lakini sasahivi imebaki tunasifia tu, timu ikifanya vizuri tunasifia lakini kwa sasa naona msaada wa Serikali au mkono wa Serikali uko mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iweke mkono kwenye Vyama vya Michezo ili iwe na power ya kuwaambia no, hiki wanachokifanya siyo. Kama tunasubiri tu mafanikio, mtu tukafanikiwa huko anakuja hapa Bungeni tunapiga makofi na nini, mkono wa Serikali kama haupo, maana yake ni kwamba hata kuwagusa watu hawa hatutaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chumi amezungumzia ushiriki wa timu zetu za Taifa, siyo kwa maana ya mpira wa miguu tu peke yake. Juzi tumeona kwenye madola, tunaondoka kwa mbwembwe lakini tunarudi hata haijulikani timu imerudi au haijarudi. Maana yake hatuna
maandizi. Ikifika mahali tunashindwa, turudi kwenye ushauri ule, tuache kwenda kucheza ili tujitengeneze vizuri tukaporejea, turudi na nguvu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya mapato ya Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru. Kamati imetoa maoni yake, lakini mimi nakuja na kitu kingine kabisa. Mapato ya Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru, Baraza la Michezo linachukua asilimia 15, TFF inaambulia asilimia tano. Nadhani jambo hili siyo sawa. Tutoe asilimia tano ya wenye uwanja, tuwape TFF kwa maana ya kuimarisha Mfuko wa Timu ya Taifa, angalau watakuwa na pesa nyingi za kuweza kuhudumia. Vinginevyo, Timu ya Taifa ni mzigo mkubwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unajua Timu ya Taifa ni mzigo. Tunaweza kufikiri kwamba mapato yapo ni mengi ya kuweza kuhudumia, lakini wakati mwingine hata kucheza mechi za Kimataifa timu inashindwa kwa sababu ya gharama. Kwa hiyo, wazo langu, tuangalie, ukiacha viwanja vingine hatuwezi kuvisemea viwanja vile vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi mimi siwezi kuwasemea, lakini nazungumzia viwanja vinavyomilikiwa na Serikali; asilimia tano tuitoe kule ili iende kwenye asilimia za TFF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, sitaki kutumia dakika nyingi. Nimekuwa nasema hapa toka 2010 tunayo Timu ya Vijana Wanaoishi katika Mazingira Magumu kule Mwanza. Timu hii 2010 ilikwenda kushiriki Kombe la Dunia la Watoto Wanaoishi katika Mazingira Magumu kule South Afrika. Tumetoka kule tukawa washindi wa pili. Mwaka 2014 tumekwenda Brazil, tukawa mabingwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupata ubingwa, watu wakafurahi, wakaja hapa wakatupokea Bungeni, tukaona raha na ahadi nyingi, mpaka leo hakuna jambo lililotekelezwa. Serikali ijaribu kurudi wapi imejikwaa, kwa nini itoe ahadi ya zawadi hewa? Mpaka leo vijana hawajapewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wiki ijayo tunakwenda Urusi kama mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia la Watoto Wanaoishi katika Mazingira Magumu. Nini msaada wa Serikali juu ya timu hii? Wakati mwingine hapa Tanzania hakuna bingwa wa dunia isipokuwa wale watoto, hatuoni fahari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia, tukipata ubingwa kama hamtusaidii ni afadhali msituite Bungeni. Bungeni hapa tutakuja kwa utartaibu mwingine. Habari ya kuahidi hapa kila siku, watoto tunawaahidi wanatoka hapa wanasema tumeahidiwa moja, mbili, tatu, sijui viwanja, sijui maisha bora kule kwenye kambi yetu; kama hamtusaidii, wala msianze kufurahia tutakacholeta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kawaida, maneno yangu huwa hayapasi papasi. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Hizi dakika tano inabidi uwe na speed kama ya Profesa J kwa sababu inahitaji uwe na speed kubwa sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie fursa hii kuwapongeza Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wake kwa kazi ambayo ina changamoto nyingi lakini ni kazi ambayo inataka uvumilivu wa hali ya juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja moja tu na ndiyo maana nimekubali kuchangia dakika tano au dakika mbili zinaweza kunitosha. Jimbo lote la Ulyankulu ni hifadhi, toka tumeanza kuambiwa Kamati ya Wizara mbalimbali itakutana kuliamulia jambo hili bado hatujapata suluhisho. Mwaka 1972 msitu ulikuwa mkubwa waliletwa wakimbizi ndugu zetu kutoka Burundi lakini kama kuna sheria za kikoloni sheria hizi zilimkuta Mtemi Mirambo na mpaka leo Mtemi Kadutu yupo. Kwa hiyo, hakuna suala la kusema kwamba wananchi waliwakuta wakoloni maana wakoloni hawawezi kufika sehemu ambayo haina watu. Kwa hiyo, jambo hili ni kama vile artificial ifike


mahali sasa Serikali itueleze wananchi wa Ulyankulu wapi tutakwenda kama bado wameng’ang’nia hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati wa uchaguzi, wenzangu mtanisamehe kidogo kwa maneno yangu wakati mwingine. Wakati wa uchaguzi tuliambiwa baada ya siku tatu tutapata wilaya, tutapata halmashauri lakini mpaka sasa hakuna. Kila tukikumbusha habari ya halmashuri, tukikumbusha kupewa wilaya tunaambiwa hifadhi. Kwa hiyo, hili neno hifadhi ni msamiati wa Kijapan au Kinyamwezi au wa wapi. Tunataka Serikali ituamulie inatupeleka wapi basi? Kama sisi tulikuwepo kabla ya hizo sheria za hifadhi, leo hii watu tumeenea jimbo zima halafu unatuambia hii ni hifadhi jimbo zima ni jambo la ajabu kabisa, yaani bora msitu kuliko wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unatufahamu sisi Wanyamwezi tunaweza kubadilika na tukaanza mapambano, hilo linajukana tutazuia kila kitu kisifanyike kila siku nasema hapa. Mheshimiwa Waziri mdogo wangu HK tuletee taarifa hapa wananchi wa Ulyankulu wapate imani vinginevyo wazee wenzangu huku 2020 ni kiboko. Suala hili la kuwahamisha watu halitakubalika, hatuwezi kuwa tunawaahidi watu wakati wa uchaguzi halafu tukishashinda tunawatelekeza, haiwezekani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hebu tusaidie hiyo Kamati ya Wizara mbalimbali lini itakuja na maneno hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ndiyo maana nimesema sina maneno mengi, Mheshimiwa Waziri alikuja Ulyankulu akiwa Naibu Waziri wa Afya. Kwa kidogo sana aliona changamoto zilivyo, niwaalike sasa Waziri pamoja na Naibu Waziri njooni Ulyankulu mjionee wenyewe, je bado kuna haja ya kusema hifadhi maana eneo lote lina watu na linatumika. Sasa njooni wenyewe badala ya kupata taarifa tu kutoka kwa wataalam na ambao hawajafika mjione Ulyankulu je bado inaendelea kuitwa hifadhi au ni makazi ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana lakini naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa hii ili nitoe mchango wangu kidogo kwa bajeti Kuu ya Serikali. La kwanza nizungumzie mambo ya jumla, kwenye jimbo letu kuna mambo hayajanyooka. Kumekuwa na shida, uchaguzi kila siku napiga kelele uchaguzi wa kata zetu tatu haukufanyika na mpaka sasa Serikali haijatoa maelezo yoyote kwamba nini kitafanyika, lakini watu hawa wamemchagua Rais, wamemchagua Mbunge, lakini kama tuliwapa uraia hawa kwa masharti ni vizuri tukaondoa masharti. Nchi yetu kama ilitoa uraia kwa nia njema, lakini tunaanza kuwabagua na jambo hili sio zuri sana kwa mustakabali wa maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niseme Waheshimiwa Mawaziri waache kubagua, watembelee na majimbo mengine hata kama, niishie tu kusema hata kama. Mawaziri kuna maeneo wanapishana Mawaziri wanne wanakwenda sehemu moja, tunashuhudia lakini kuna maeneo kama Uliyankulu hawataki kabisa kuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka afike Waziri Mkuu na Waziri Mkuu alikuja kutusalimia kwa sababu alikuwa DC wetu, lakini wengine kila siku hapa tunapigizana kelele, lakini mtu akiuliza hapa, hii nazungumzia mimi Waziri atakwambia tu niko tayari kuambatana na wewe, lakini muda ukifika ziara inapeperuka. Wananchi wetu wanakata tamaa kwamba hili eneo lilitengwa toka miaka yote toka enzi za Mzee Maswanywa, Mzee Sitta, Mzee Kapuya watu hawaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Uliyankulu linataka dhamira ya dhati, kama hawatupendi sisi tutajua namna ya kupendwa. Nawasihi sana waje bwana, basi waje waangalie tu hata kaburi la Mirambo, hawataki na yenyewe, nadhani wamenisikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kumaliza habari ya wakimbizi na kambi za wakimbizi ni jambo muhimu likaisha kama kuna sheria tunaziona ngumu, kama tunaona uamuzi wetu wa kuwapa uraia ulikuwa na shida tutamke, watu hawa sasa hawawezi kujenga kwa sababu kambi haijafungwa lakini ndani ya kambi kuna watu hawataki uraia wa Tanzania na hawataki kurudi Burundi, tunafanya nini? Najua mdogo wangu Mheshimiwa Mwigulu ananisikia vizuri na anajua vizuri. Kama Serikali walimalize hili kwa hiyo, watu wamekaa pale stranded hawajui kama watahamishwa au kama wataendelea kukaa hapo, matokeo yake wanatufikiria tofauti hasa wakati wa uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema wakati mwingine wanasema nasema sana, nimechaguliwa asilimia 70 ya raia wake wamenichagua, sasa piga hesabu wakigeuka? Ndio hofu lazima tuambizane, wakigeuka ni matatizo. Haya mara waseme hifadhi, kwa hiyo sisi watu wa Ulyankulu tupo tu kwa sababu watapita watatoka Tabora, wataenda Kaliua, Urambo, wataenda Kigoma lakini Ulyankulu lazima aje Ulyankulu awe na dhamira kweli leo nakwenda kwa Mheshimiwa Kadutu, hivi hivi hatuwezi kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuliwahi kusema hapa suala la kugawa maeneo, lakini sasa hivi Serikali inasema wanabana matumizi hawataki kugawa maeneo. Jamani Tabora ilivyo, hiyo sehemu ya Sumbawanga ilikuwa Tabora, Katavi yote ni Tabora, mkoa bado ni mkubwa kuliko kawaida, wataugawa lini, mpaka watakapotaka kuwagawia wengine ndio na sisi watupitishie humo, hiyo sio haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua ipo siku hapa tutasimangana hapa, kuna eneo watatoa eneo jipya la utawala ndio watakumbuka sasa na Ulyankulu. Tunataka sisi Ulyankulu iwe Wilaya, iwe halmashauri na uwezo huo tunao own source ya Wilaya ya Kaliua ndio inayoongoza kwa Mkoa wa Tabora kuliko hao wengine, sisi tunaweza kuleta hapa own source Bahi, nani wote hawa tukawasaidia, lakini hawataki kutupa eneo, sijui mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema ahadi za Rais zitatekelezwa, sasa hii ni ahadi ya Rais wakati wa uchaguzi. Wakati wa uchaguzi kulikuwa na mambo mawili, kuna ahadi za Rais, lakini kuna Ilani ya Uchaguzi. Sasa hizi ni ahadi za Rais alituambia siku tatu akiingia ofisini tunapata Wilaya na tunapata halmashauri, lakini mpaka leo! Sasa wameleta habari kwamba gharama kubwa na nini, lakini yako maeneo madogo wamewapa mkoa, wengine wilaya, watukumbuke basi na sisi Mkoa wa Tabora. Upo mkoa tulishapendekeza Mkoa wa Nzega na Mkoa wa Urambo ambao JK aliacha amependekeza. Sasa yale yaliyotendwa na wazee wetu walioondoka tuyatekeleze basi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi zile zilizomo ndani ya ilani lazima tujipime, sasa tumebakiza labda mwaka mmoja tu na nusu, je, tumetekeleza kwa kiwango gani? Yako mambo mengi hivi hakuna hata uratibu wa kuyaondoa moja baada ya lingine, wametuahidi lami, wametuahidi hiki tena ndogo ndogo tu kilomita tatu, kilomita ngapi, hakuna hata dalili. Hata hivyo, tunakuwa tunaona yapo mambo ambayo hayamo kwenye ahadi, hayapo kwenye ilani yanatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatupendi kwa kweli kuyasema lakini wakati mwingine hivi watu wa Ulyankulu huko wamenituma, halafu nakaa napiga makofi tu hapa mimi siwezi bwana. Tusaidieni ili hata uchaguzi wa 2020 watu mpete, hata tukisimama pale tunapiga kampeni wakati huo mimi mstaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze sasa juu ya fedha za maendeleo, hapa juzi wenzangu wamezungumza wengi tu hapa juzi wakaitwa Wenyeviti na Wakurugenzi hapa, tumewaita wapangue mpango huu, tunataka miradi ya mkakati tutatoa huko miradi midogo midogo achaneni nayo, wakaja hapa wakamaliza wakarudi kwenye halmashauri wakaitisha Finance pamoja na Baraza, watu wakalamba posho. Leo hii ni tarehe 20 maana yake zimebaki siku 10 tu, watuambie Serikali wanao uwezo kweli wa kuleta pesa kule? Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Waziri ni kwamba halmashauri zile ambazo hazina own source zitakufa kifo cha kimya kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nimetoka huko kwenye halmashauri, nazijua vizuri kweli, lakini wakati mwingine tarehe 28 wataingiza pesa ambayo haitatumika mwisho wa mwaka na CAG atahoji kwamba hizi pesa vipi mbona hawakuzitumia tutaleta maswali mengine. Mheshimiwa Dkt. Mpango ajaribu katika hali ya kibinadamu sasa juu ya madeni ya mawakala wa pembejeo na wazabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi uhakiki wa mawakala ambao hawafiki 1,000 unaweza kufanana na wafanyakazi zaidi ya 800,000. Wafanyakazi mnahakiki na imejulikana huyu tupa kule huyu huku, tupa huku, kazi imekwisha. Hivi uhakiki wa madeni ya wazabuni pamoja na mawakala wa pembejeo hivi kweli hawaoni ni tatizo. Mawakala sasa hao kila Bunge wapo hapa na wakati mwingine wanaishiwa hata pesa ya kula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tunahangaika kuwalisha, siku moja Mheshimiwa Jacqueline hapa mpaka analia, hivi kweli wanataka watu tuanze kulia wote huko haifai. Kazi leo Mheshimiwa Waziri waifanye tu kwa nia ya kibinadamu kwamba watu wamekopa maeneo, sasa hata mali zao watafilisiwa. Kama mtu alidanganya watoe basi orodha, hawa wafuatao ndio wako halali, hawa wengine utapeli jazz band. Watu watajua ili jambo hili lifike mwisho kwa sababu sasa kwa mfano sisi wengine vijijini huko na kilimo kwa mfano cha tumbaku, yaani bila mbolea huwezi kufanikiwa, bila mtu kukusaidia wakulima wetu wamezoea hiyo, hawana nguvu za kununua pembejeo wenyewe, tusaidieni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuje suala la kilimo; kwenye vitabu vya Mheshimiwa Waziri amesema kweli kwamba pato la Serikali asilimia 30 linatokana na kilimo, lakini hebu atafakari mwenyewe, kilimo wameipa asilimia ngapi basi ya pesa hizi?

Maana kilimo hatukizingatii. Mwaka jana hapa zao letu la tumbaku maana yake sisi ukizungumza siasa lazima uzungumzie tumbaku hata kama huipendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Serikali ika-delay kutoa uamuzi, niseme tu natoka kwenye eneo linalolimwa tumbaku nyingi Tanzania, kwa hiyo, najua vizuri. Matokeo yake hapa tukajichanganya Serikali imechelewa kutoa maamuzi wakulima wetu wamekwenda kuuza tumbaku kwa bei ya chini zero point. Wamepata hasara, mtu alikuwa ame-plan kupata milioni ishirini, anaishia milioni mbili laki tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali lazima iangalie, hili zao tunasema asilimia thelathini ya pesa inakwenda Serikalini inazalisha mazao ya kilimo, lakini sisi hatutaki kuhudumia kilimo. Unasikia korosho wanalalamika, kahawa wanalalamika, ndugu zangu kule Kanda ya Ziwa pamba wanalalamika, kilimo kipi sasa ambacho tumefanikiwa matikiti? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda matikiti yamekuwa mengi, mtu anaweza akasimama hapa akasema tumefanikiwa, lakini kila eneo la kilimo, kelele hata kwa ndugu zangu kule Wanging’ombe maua sijui nini, wote kule ni malalamiko. Hakuna yaani sijui lumbesa sasa haitajwi yaani shida tupu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, wajaribu kukaa, kweli wote humu hatuwezi kuwa wachumi, lakini tuna macho na akili. Tunaona, mambo haya wayarekebishe twende mbele, tumebakiza mwaka mmoja tu, yaani bajeti yenye kuweza kujadili kwa utulivu imebaki moja, ile nyingine watu wote humu watakuwa akili kwenye uchaguzi. Hakuna tena majimboni, watu wanatafakari nani ananifuatafuata huku, hakutakuwa na mjadala mzuri, umebaki mmoja, hebu wajaribu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lingine tumeshafanya Serikali imefanya mambo hayo makubwa ya ununuzi wa ndege, sijui ujenzi wa reli, hebu sasa twende kwa wananchi wa kawaida, yale mapato ya pesa, watu wapate wananchi wa kawaida wazione. Unajua ukimweleza mwingine, kwa mfano, kule Ulyankulu ukimweleza habari ya bombadier mimi nasema ukweli tu, wakinichukia na wanichukie, bombadier mfano Ulyankulu wao wanaamini hizi hela za Serikali zinatokana na tumbaku. Sasa ukiwaeleza habari za bombardier, barabara mbovu, hospitali mbovu hawaelewi wapeleke sasa huduma hizi ziende kwa wananchi, barabara kule vijijini ziboreshwe, hao TARURA wapewe pesa, tutakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapa..
Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtemi Chenge nakushukuru kwa kunipa hizo dakika tano niweze kusema machache, japo nilikuwa na mlolongo mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mwaka jana nilipiga kelele juu ya Maziri kutofika Jimboni Ulyankulu, lakini leo napenda kuwashukuru Mawaziri karibu watano, sita, wamefika Jimboni Ulyankulu nawashukuru sana wamekuja kunitutia moyo kwa kazi zetu hizi za maendeleo, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa usimamizi wa shughuli za Serikali lakini kubwa zaidi ni lile la kuwa karibu sana na timu yetu ya Taifa. Kupitia yeye na Serikali niipongeze TTF ambayo nami ni sehemu yake. Tutaendelea kujipanga kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri na niwaalike Waheshimiwa Wabunge mwezi Juni twende Misri kwenda kushangilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo kwa haraka haraka ni suala la umeme, ile spidi ya umeme vijiji inaelekea imepungua kabisa. Sasa niwaombe wenzetu wa Nishati wajaribu kuihuisha tena, kazi hizi za umeme zinaleta maendeleo makubwa sana kwenye vijiji vyetu, basi haraka uwepo na utekelezaji maana yake yawezekana Mawaziri wakasema, wakiondoka huku nyuma watendaji wakawa si watu wazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mzuri wa uchimbaji bwawa pale kwenye Kijiji ya Ichemba, niombe sana Wizara inayohusika kumekuwepo na upembuzi, lakini toka wameondoka hatujui kinachoendea

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la barabara, kwa nafasi hii nimshukuru Mheshimiwa Kwandikwa, jirani yangu huyu, anapita kila wakati kuzikagua hizi barabara, Jimbo la Ulyankulu lina barabara kama tatu. Barabara ya Tabora Mjini kuja Ulyankulu; halafu barabara ya kutoka Kahama kwenda Ulyankulu mpaka Kaliua. Barabara hizi zinatusaidia kwa matatizo mbalimbali, jiografia ya jimbo la Ulyankulu si rafiki, nitatoa mfano, Kaliua tunajenga Hospitali ya Wilaya, tunajenga ofisi mbalimbali lakini wananchi wa jimbo la Ulyankulu hawapati huduma kule, wanapata Kahama pamoja na Tabora Mjini. Kwa hiyo, tunaposema maeneo ya utawala, najua hilo tumeshamwelewa Mheshimwa Rais, lakini najua mbele ya safari litakuja kukubalika tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uchaguzi kwenye kata tatu bado nitaendelea kulisemea. Inakuwaje hawa watu wametupigia kura na Mheshimiwa Rais, lakini Serilkali imewazuia kupiga kura kwa ajili ya Madiwani, jambo hili sidhani kama lina majibu yaliyonyooka na Serikali inapindisha pindisha. Hebu Serikali ije na ufumbuzi wa haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Afya pamoja na TAMISEMI kwa kutupatia shilingi milioni mia nne, tumeweza kutengeneza kituo vizuri cha pale Ulyankulu. Lakini imetuhamasisha na sisi kama wananchi kujenga vituo viwili vya afya vingine kwa nguvu zetu. Bahati nzuri Wilaya ya Kaliua ni Wilaya inayoongoza kwa mapato ya ndani kwenye Mkoa wetu wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tumeweza kujenga shule za sekondari na shule za msingi, sasa tuombe tu Serikali iharakishe hasa kwenye shule ya msingi vile vikwazo vikwazo vya ubora na nini, watusaidie kuvipunguza ili watoto waweze kuendelea na masomo vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kuendelea na mambo mengi, nisingependa kengele inikute. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Chief nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, leo nina jambo moja mahususi. Bahati nzuri mapacha wa wakimbizi tupo watatu hapa, mwenzangu amekwishaanza kuligusia. La kwanza nimpongeza rafiki yangu Mheshimiwa Kangi Lugola kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hii. Ni Wizara kubwa yenye changamoto nyingi, panataka utulize kichwa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe darasa kidogo, mwaka 1972 kulitokea vita kwa wenzetu Burundi, enzi za utawala wa Mchombelo, kundi kubwa likakimbilia Tanzania wakati ule Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa mzee Maswanya, wakaangalia maeneo ambayo yana nafasi kwa hiyo wakaamua wakimbizi kundi kubwa liletwe Ulyankulu, Mishamo na Katumba, nasi tukasema njoo tuwasaidie katika hali ya kibinadamu, sasa tumekaa nao miaka 44.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014, Serikali ya Awamu ya Nne ikatoa uraia ikiwa tarehe 14 Oktoba, nami nikiwa Mwenyekiti wa Halmashauri, lakini kwa ahadi, wale waliokuwa wakimbizi wakaahidi kuwa watiifu kwa Serikali mbele ya Mheshimiwa Kikwete, kwa hiyo walipata uraia. Baada ya hapo kumekuwa na mazungumzo je, zifungwe kambi hizi zote tatu au ziendelee kuwepo? Bahati nzuri Kamati ya Ulinzi na Mambo ya Nje imejadili sana jambo hili. Mabunge yaliyopita ilifika hatua, kuna Wabunge humu walikuwa wanasimama humu kukataa watu hawa wasipelekwe katika maeneo yao, kwa sababu mkishawapa uraia ile sio kambi tena ya wakimbizi, ni sehemu halali ya kuishi au kambi ifungwe na watu wahame. Analosema Mheshimiwa Kakoso, wapo watu walikataa Utanzania, walikataa kurudi Burundi, wanataka nchi ya tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya kwa taarifa yenu wakimbizi wa uraia wa Ulyankulu wanazaliana sana kuliko eneo lolote Tanzania. Kwa maana hiyo tunapongea hapa ile idadi ya wakimbizi waliokuwa wamebaki hawana uraia imekwishaongezeka, lakini Serikali yetu inapata kigugumizi kila wakati, ukiwagusa ndugu zangu wa TAMISEMI ndio kabisa hawataki kuleta majibu ya kueleweka, bado unamfuata Kadutu kagombee, utagombeaje kama watu hawahudumii watu wako. Watu wale wananipenda sana, lakini hawajatekelezewa, huduma za Serikali hazifiki kule. Sasa kwa nini Serikali isiwe na kigugumzi juu ya jambo hili, kwani wakisema kambi imefungwa, bahati mbaya kwenye kitabu cha hotuba ya Waziri eneo lile la Idara ya Wakimbizi limeguswa kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu 70% ndio wapigakura wa Ulyankulu, ndio wapigakura waliomchagua Kadutu na Magufuli, lakini wakakataliwa kuchagua Madiwani, lakini ajabu kwa Kakoso kule na kwa Mbogo wamechagua Madiwani. Hebu waniambie hasira waliyonayo itakuwaje? Hivi viongozi hawalioni hili? Serikali hawaoni? Tunaenda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, mle ndani kuna Serikali mbili; kuna mkuu wa makazi ana mamlaka yake, halafu TAMISEMI inaingia kwa kuviziavizia, Serikali yetu halafu tunaingia kwa kuviziavizia, ya wapi hiyo? Kwa nini tusiwe na mamlaka kabisa tunaviziavizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa lakini mle ndani kuna Serikali mbili. Kuna Mkuu wa Makazi ambaye ana mamlaka yake halafu TAMISEMI inaingia kwa kuviziavizia. Serikali yetu tunaingia kwa kuviziavizia, kwa nini tusiwe na mamlaka kabisa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme Serikali ifike mahali ieleze, kama tunadhani Mheshimiwa Kikwete alikosea, tu-review uamuzi kwa sababu wapo watu walikuwa tayari kurudi Burundi lakini walipopata fursa ya kuchagua kurudi Burundi au Tanzania wakasema sisi ni Watanzania. Hata hivyo, kuna jambo ninyi hamlijui, hawa wenzetu tayari wamo kwenye Wizara zenu, iwe Wizara ya Fedha, Mambo ya Ndani, TAMISEMI na ninyi mnakaa nao hamjui kumbe huyu Mrundi, huyu hivi, huyu hivi, wamo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mnasema mna Idara nzuri ya Usalama wa Taifa, Polisi lakini mnakaa nao. Pakitokea jambo Ulyankulu tayari, ndiyo watu wanasema huku bado hapajakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimesema nitachangia suala hilo hilo tu, niwasihi sana Serikali, Kamati ya Ulinzi na Mambo ya Nje mbona imesema na imeshauri muda mrefu, kwa nini tusiwe na uamuzi? Tunafunga kambi ili wale ambao wamejidai kutafuta nchi ya tatu waondoke tubaki na wale walio tayari basi! Baada ya hapo tutakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwani ukiwaambia chagueni Diwani kuna tatizo gani? Mbona Kadutu wamemchagua? Mbona Mheshimiwa Rais Magufuli wamemchagua? Kuna shida gani wao wasichaguane? Zamani watu walikuwa wanasema, ooh, misitu, sasa misitu kwenye kura, ni jambo la ajabu hili. Jamani tutafute sababu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa fursa ya kuchangia jioni hii juu ya jambo muhimu sana kuliko mambo mengine, maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasema maneno yangu, Mheshimiwa Waziri, Profesa, pamoja na mdogo wagu Mheshimiwa Aweso, mimi sina matatizo na ninyi bali Serikali. Kwa sababu hapa ndani wakati mwingine Wabunge tunazungumza inaweza ikaonekana kama tuna matatizo na Mawaziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema maji ni uhai. Mawaziri mnisikilize vizuri, maji ni uhai. Waheshimiwa Wabunge, hebu tujaribu wiki yote moja hii tule bila kunywa maji tuone itakuwaje, hapo ndiyo tutakapojua maji ni uhai. Sasa ukishakuona ndugu na jamaa zako wanakutenga na maji, hawa wana mawasiliano na Mwenyezi Mungu afungue lango la mbinguni ili wewe uende kule maana yake hawataki upate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Ulyankulu tumetengwa na nitaendelea kusema mpaka siku ya mwisho. Alikuja Makamu wa Rais, unajua wanasiasa unaweza ukaanza kusema lolote, mtu mmoja akasema Ulyankulu ni mbali kwa hiyo maji yasiende, ajabu kabisa hii. Sasa kutoka Tabora kwenda Ulyankulu yaani kuingia kwenye Kijiji cha Kadutu kilometa 60…

MBUNGE FULANI: Ni mbali sana.

MHE. JOHN P. KADUTU: Ni mbali hiyo? Kutoka Tabora kwenda Urambo kwa Mheshimiwa Mama Sitta ni kilometa 94; kutoka Tabora mpaka Kaliua ni kilometa 120, hapo ni karibu sana; kutoka Kahama kwa ndugu yangu Mheshimiwa Kishimba pamoja na Mheshimiwa Kwandikwa kuingia kwenye Jimbo langu la Ulyankulu ni kilometa 80, bado watu wanasema Ulyankulu ni mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna miradi miwili, mradi wa kwanza unatoa maji Ziwa Victoria, hawataki ufike Ulyankulu. Kwa sababu maji Kahama yapo yangeweza kuletwa Ulyankulu watu wakatulia, Tabora yatafika lakini hata maandishi tu ya kupeleka maji Ulyankulu hayapo. Tuna mradi wa maji Malagarasi, hapo sasa nadhani ndipo hatutaelewana, maji ya Malagarasi yanatoka Ulyankulu lakini mradi huu umeandikwa maji yatakwenda Kaliua na Urambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku tulikuwa tunakutana Kaliua na Profesa akija kwenye ujenzi. Kuna picha moja ya Chuck Norris walikuwa na kamanda mwingine hivi wakapotezana kwenye ile filamu. Siku ya mwisho kamanda yule anamwambia Chuck Norris we meet again, sasa Mheshimiwa Profesa tumekutana tena. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa alikuwa anakuja nakupokea Kaliua nikakwambia Ulyankulu mpaka uwe na dhamira ya kwenda Ulyankulu, sasa maji mimi sina. Sasa huu mradi wa Malagarasi maji yanatoka Mto Igombe Ulyankulu, sasa niwaambie tu, kama hamtatupatia maji watu wa Ulyankulu tunakwenda kuziba mto halafu mje mniweke ndani mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila jambo Ulyankulu inatengwa. Sijui na kwenye maji mtasema wakimbizi. Jamani hebu kuweni na huruma wakati mwingine. Hatupendi kusema Mheshimiwa Profesa, hebu tupeni maji muone, tutatulia. Maji yanawezekana, kilometa hizo nimesema lakini kama nilivyosema, mtu anasimama kwa Makamu wa Rais unadanganya yaani ili kuhakikisha tu watu wa Ulyankulu hatupati maji. Mheshimiwa Profesa na Naibu wako fanyeni mnaloweza tupate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tutatengwa kwa kila jambo? Tuna mradi wa bwawa pale Kijiji cha Ichemba, wameshakuja wametembeatembea sijui ndiyo upembuzi, lakini wamekwenda moja kwa moja hatujui itakuwaje, wananchi bado wana taharuki kwa sababu hawajajua mradi ule utapita kwenye mashamba gani ya watu. Kwa hiyo, hatuna shida nyingine zaidi, kama kila huduma ya Serikali hailetwi Ulyankulu mimi siwezi kujua, sijui tatizo ni Kadutu, sijui kama kweli ni wakimbizi au ni nini, hata maji? Hivi mtu anaweza kuja nyumbani kwako akakuomba maji kikombe kimoja, utamnyima? Huwezi kumnyima, tupeni basi maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hamtaki kutupa tawala za mikoa tupeni maji tu tutaishi. Kama hamtupi maji hatuwezi kuishi. Maana ninyi mna mawasiliano na Mwenyezi Mungu, tutaona sasa nani mwenye mawasiliano na Mwenyezi Mungu na lango halitafunguliwa, hatutakufa sisi, tutakuwepo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilisema last week na kama alivyosema Mheshimiwa Ndassa, tunakuwa na hoja mahsusi moja, tusipende kuchanganya na mimi sijapenda kuchanganya. Bahati nzuri wataalam wako hapa nyuma yangu, wajue tu tutaleta vagi hata wenyewe hawatakanyaga huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa John Kadutu, tunaendelea na Mheshimiwa Lucia Mlowe.

MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Kabla sijachangia niombe niseme maneno mawili, matatu, hasa ni shukurani. Nakushukuru wewe, Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Katibu wa Bunge na Wakurugenzi wote pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote, kwa upendo ambao mlionesha wakati nikiwa hospitali ICU. Ni jambo kubwa sana limefanyika kuokoa maisha yangu. Kwa hiyo nawashukuruni sana kwa moyo wa ukunjufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mawili tu, la kwanza hili lililotokea na kukaa ICU. Tunazungumzia mipango hapa ukiniuliza sana nitakueleza labda ukiacha mkono wa Mungu ni vifaa pamoja na mabingwa walioweza kuokoa maisha yangu, sasa ni wakati muafaka Serikali imeshafanya mambo mengi sitaki kuyataja, imeshafanya mambo mengi, lakini sasa tujikite kuhakikisha watu wetu wanapata uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema, ukipelekwa Muhimbili ndugu zangu umepona. Muhimbili ya sasa sio kama zamani, wewe omba ufike emergency utaona jinsi gani madaktari mabingwa tena vijana watakapokufanyia kazi hapo mpaka ukafikishwa kama ni wa ICU au wa wodini unajua kabisa kwamba hiyo hospitali ina vifaa na ina wataalam, hivyo vitu ndio tunakosa mikoani. Badala ya kudhani kwamba kila siku… naogopa kidogo kuyataja mengine, tupeleke sasa pesa kwenye hospitali za mikoa ziwe na vifaa, ziwe na wataalamu ili watu waokolewe huko huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba mimi ningeweza kupona nikiwa Tabora lakini kama tutategemea tu hospitali moja ya Muhimbili maana yake maeneo mengine yote kwa sababu ukiacha bima nani atakuwa na uwezo wa kusafiri mpaka Muhimbili ni tatizo, nadhani hata wanaotibiwa nje watapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nadhani Serikali sasa iwe na uwamuzi tu wa makusudi, hizi MRI zikipelekwa kila mkoa watamalizana huko CT-Scan nini watu watapona. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali na bwana Mipango jaribuni kuliona hilo ili kuokoa maisha ya watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kuchukua muda mrefu, la pili ni maji. Maji limekuwa tatizo na haya maji tunazungumzia maji ya Ziwa Victoria tu. Hivi wataalam wana mipango, wanashindwa kutupatia mbinu mbadala au vyanzo vya maji vingine, hivi kama tunaweza kukinga Rufiji tukapata umeme huku mikoa mingine hatuwezi kukinga maji. Kwa mfano Mkoa wa Tabora maji yako mbali sana chini, ndio maana shida ya maji ipo kila siku, matokeo yake tutazozana mimi hamjanipangia sijui lakini maji ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumeweza kwenye umeme kwa nini maji tusiweze lakini shughuli ya maji inakwenda polepole sana. Kwa hiyo, nilikuwa nawashauri hebu na kwenye maji tujaribu kupaona pakoje ili watu wetu waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho tunapanga mipango hapa huku tukijua mapato yetu yatakuwaje. Leo hii tumbaku makampuni yanaondoka na kwa utaratibu wa kilimo cha tumbaku mpaka upewe makisio usipopewa makisio huruhusiwi kulima. Eneo kubwa kwa mfano tunakolima tumbaku Lyakulu wapi na wapi hawajapewa makisio na makampuni yanaondoka maana yake hiyo mipango tuliyopanga kama kulikuwa na pesa ya tumbaku hatutaipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nafikiri Serikali hivi imeshindwa na hawa wazungu wa tumbaku mbona wa korosho wanaweza. Tumbaku tu ndio imekuwa shida, hiyo mipango kama imepangwa na hela ya tumbaku imo nataka nikwambie kwamba tumbaku itakuwa kidogo sana na maeneo ambayo yanalima tumbaku sana hayatakuwa na tumbaku. Mojawapo huko Lyankulu kampuni zinaondoka lakini Serikali imeshindwa majadiliano na hawa watu! Lakini unasikia kabisa wanaenda jirani, wanaenda Zimbabwe manake sisi mipango yetu kwenye kilimo hiki cha tumbaku haiku vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie tena nakushukuru sana na uongozi mzima kwa yale mliyonifanyia na nina imani kabisa nisingeweza kutoka ICU kurudi Bungeni, ningekuja hapa nikiwa ndani ya sanduku ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi lakini nianze kukupongeza wewe mwenyewe kwa miaka mitano hii umetuvumilia sehemu kubwa ni kipindi chetu cha kwanza yawezekana mara moja mara mbili labda tulikosea hata kanuni umeendelea kutuvumilia, kwa kweli nafikiria namna ya kuja kukusaidia kampeni kule Kongwa. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuiongoza Serikali hapa Bungeni lakini kwa kuja kututembelea Ulyankulu. Wewe kule ni kwako na tuendelee kukuomba ukipata nafasi uje, bado watu wanakukumbuka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo nianze na Tume ya Uchaguzi na jambo hili nitaendelea kulisema hata nje ya Bunge mpaka pale tutakapopata ufumbuzi. Mwaka 2015 wakati wa uchaguzi kundi kubwa la watu wetu kule Ulyankulu hawakupiga kura za madiwani na kwa kweli ilileta sintofahamu sana mpaka leo hawajapiga kura kisingizio ni raia wapya lakini kule Katumba na Mishamo ni raia wapya lakini waliweza kupiga kura. Tumefatilia jambo hili kila wakati hatupati majibu na kila wakati nasema hapa na inawezekana Waheshimiwa Wabunge wakawa wanashangaa Kadutu alishang’ang’ania hiyo hoja hapana karibu asilimia 70 ya wapiga kura wa Ulyakulu wanatoka kwenye eneo hili ambalo halikuruhusiwa kupiga kura ya madiwani.

Mheshimiwa Spika, lakini mwaka huu watu hawa hawakuruhusiwa kupiga kura ya Serikali za Mitaa kwa maana ya mwaka jana Novemba hata kuandikishwa na sasa haijajulikana kama watapiga kura au wataendelea tu kukaa kimya au wataendelea kutupigia kura Wabunge na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nadhani jambo hili lifikie mwisho Kamati yetu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Usalama imekuwa inajadili TAMISEMI inajadili na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu unalifahamu jambo hili hebu huko Serikalini limalizeni ili na wengine tupate hoja zingine kwa sababu kila ukifika kule swali ni hilo, Mheshimiwa Kadutu tutapiga kura au hatupigi kura hawana maswali mengine, je tutaendelea kuishi hapa au tutahamishwa, je wale ambao hawataki uraia wa Tanzania na hawataki kurudi Burundi wataondoka lini? Je, kambi ya wakimbizi na hizo zingine zitafungwa lini? Ni jambo ambalo linawapa shida sana ndugu zangu hawa. Lakini ni lazima tufikirie kama tumewapa narudia tena tuliwapa uraia kwa roho safi basi tuwaruhusu na kama kuna uamuzi tofauti wa Serikali uje badala ya watu kukaa hawajui kinachoendelea hawajengi hawafanyi shughuli kubwa za kiuchumi na mnajua wenzetu wale na sisi wenyewe ni wazalishaji wazuri wa mazao. Tunalisha Kahama, Shinyanga, Mwanza kama mtu anabisha asimame hapa.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie habari ya kilimo, kwenye kilimo nimshukuru tena Waziri Mkuu kwa kushughulikia kero za mazao na hasa tumbaku. Waziri Mkuu alijikita sana kuhakikisha tumbaku inasimama inakaa vizuri, vyama vya ushirika vinakaa vizuri lakini yawezekana Serikalini hamfahamu wiki iliyopita nilikuwepo jimboni nashuhudia kwa macho tumbaku inanunuliwa shilingi 100 mpaka 300 kutoka maalfu ya pesa sasa tumbaku inanunuliwa kwa dharau ile ni dharau. Huwezi kununua tumbaku kwa shilingi 100 kwa shilingi 300 na kama hutaki watu wanasema toa tumbaku ichomwe moto. Hivi kweli mtu msimu mzima masika yote ameshughulika na zao leo anakuja kuwaambiwa shilingi 100 au anaambiwa 300. 300 mtu ana kilo 1000 hakuna kitu pale niiombe sana Serikali isimame iongee nao hawa wenye makampuni wasifanye dharau na ni dhuluma, hii ni dhuluma. Mtu anachukua tumbaku kwa shilingi 300 kwa kweli ni dhuluma.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu mimi nikuombe urejee tena uangalie namna ya kuwasaidia wakulima wa tumbaku vinginevyo kilimo cha tumbaku kitakufa na watu wataangalia tena habari ya mazao mengine. Lakini huko nyumba tumbaku ndio ilikuwa zao linaloongoza kwa kuingiza pesa nyingi za kigeni. Leo hii sio kama ilivyokuwa zamani.

Mheshimiwa Spika, linalofanana nalo liko suala la mawakala wa mbolea limechukua muda mrefu toka tumeingia hapa Bungeni mawakala wa Mbolea wamejikusanya wanakuja Dodoma hawajapatiwa majibu. Yaliwahi kutoka majibu kwamba baadhi yao walifanya udanganyifu tukasema sawa lakini wapeni majibu wajue kwamba jambo hili liko mwisho na nani amekosema atolewe ambao hawana makosa wafanye kazi hizo. Kero kama alivyosema mtani wangu mgosi Shangazi suala la NIDA, NIDA hasa vijijini ni tatizo hata huo usajili wa laini za simu umesumbua. Hebu Serikali ihakikishe ifanye tathmini watu wameandikisha na wapya hawajaandikisha waandikishwe lakini Serikali itengeneze mpango mtoto anazaliwa apate usajili wa moja kwa moja tuepukane na jambo hili.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa kwa sababu mengine tutakutana nayo kwenye Wizara wapo watu wanashangilia ligi ya mpira wetu kusimama. Niwaambie wenzetu wale watoto wa mama mdogo, ligi hata ikisimama bingwa ni Simba.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kunipa nafasi hii kuchangia jioni ya leo juu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ambayo imekuwa ni tatizo. Leo niipongeze Serikali kwa kuleta mabadiliko haya na kwa kusikia kilio cha Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla, Serikali imekuwa na speed nzuri na mimi nimeshawishika kuipongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuingia hapa mjengoni nilikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa hiyo najua madhara na madhira ambayo halmashauri zinapitia. Ni shida sana kuitekeleza lakini mkafanikiwa, muda mwingi mnatekeleza sheria lakini upande wa pili mnaingia gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni lile alilosema Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Hawa Ghasia, sina hakika kama ni kanuni au ni waraka lakini mimi nadhani ni waraka. Serikali iufute ule waraka uliokataza Waheshimiwa Madiwani kujadili mambo yaliyokuwa yamefanyika wakati Waheshimiwa Madiwani wako kwenye mchakato wa uchaguzi, kwa nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mabaraza mengi yamepitisha mambo haraka haraka hasa ya manunuzi haya kwa kujua Waheshimiwa Madiwani wangekuja na kuchambuachambua. Kwa hiyo, jambo hili lazima Serikali iwe inasikia kama ilivyosikia kuleta mabadiliko, sioni tatizo kama Serikali inaweza kufuta waraka uliotolewa na Katibu Mkuu wa TAMISEMI wakati huo. Jambo hili litaturahisishia sana kuondoa ugomvi kati ya Madiwani na Watendaji wetu wa Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la Bodi za Zabuni. Mimi niishauri sana Serikali na hasa viongozi wa Serikali Mikoani kutokuziingilia Bodi za Zabuni. Mara nyingi bodi hizi ni za wafanyakazi ambao ni Wakuu wa Idara, zinaundwa pale kwenye halmashauri lakini viongozi wa mikoa wengi wanaziingilia, wanaingilia maamuzi, sana tu, jambo ambalo linasababisha shida lakini inapokuja habari ya TAKUKURU watu wanaruka. Watu wakisikia tu kuna kubanwa na TAKUKURU wanasema hapana ulipaswa kutekeleza yale ambayo unapaswa kutekeleza. Kwa hiyo, nadhani Serikali iko hapa viongozi wa mikoa na sekretarieti za mikoa waambiwe waziache Bodi za Zabuni ziwe huru kufanya mambo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la ucheleweshaji wa michakato ya manunuzi. Sheria hii inasaidia, itapunguza muda kwa sababu muda ulikuwa mrefu na matokeo yake gharama ilikuwa inaongezeka. Ni wakati sasa Serikali ihakikishe sheria hii inasaidia kupunguza huo mchakato na watu wajikite kwenye manunuzi kwa speed na kazi ifanyike bila kuchelewesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la wataalam amelizungumzia Mheshimiwa Dkt. Kamala. Maafisa Ugavi ni wachache sana. Pamoja na uchache wao lakini taaluma hii inaoonekana kama kutokuheshimika kama ambavyo Mheshimiwa Dkt. Kamala amesema ukilnganisha na fani zingine za uhasibu, udaktari na uanasheria kwani bodi au taaluma hizo zinaheshimika sana tofauti kabisa na hawa. Maafisa Ugavi hawaheshimiki na wanasakamwa sana kwa kudhani kwamba wao ndiyo sehemu ya ulaji wa rushwa kumbe wanahitaji na wenyewe waheshimike na labda chombo chao kiweze kuwa strong kuweza kusimamia mambo haya ya manunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la madeni, nililizungumza wakati wa mjadala wa bajeti kuu. Madeni ni mengi mno katika magereza, hospitalini, kwenye shule, watu wametoa huduma kwa nini Serikali inasuasua kuwalipa watu hawa? Maana yake ku-supply ni kuisaidia Serikali, ni kwamba wameikopesha Serikali, Serikali ifanye kila inaloweza kulipa madeni haya tuondokane na shida zilizoko. Maana kila siku Mbunge ukifika au Mwenyekiti wa Halmashauri ukifika lazima watu wanakufuata kwa ajili kukusisitiza madeni yao yaweze kulipwa. Siyo wao tu, wakandarasi hawalipwi kwa wakati na matokeo yake miradi hii inakwenda kwa kusuasua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sikuwa na mengi sana kwa sababu kama nilivyosema leo niko sambamba na Serikali, ingekuwa tofauti mimi napasua pale pale. Leo naipongeza Serikali, Mheshimiwa Waziri hongera sana kwa kuwasikia Waheshimiwa Wabunge na kwa ku-react kwa speed na Serikali nzima ahsante sana.