Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Musa Rashid Ntimizi (12 total)

MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-
Wananchi wa Kata ya Loya katika Halmashauri ya Tabora (Uyui) wameitikia wito wa Serikali wa ulinzi kwa kujenga kituo kikubwa cha polisi katika kata yao:-
(a) Je, ni lini kituo hicho kitafunguliwa hasa ikizingatiwa kuwa Loya ni zaidi ya kilometa 120 kutoka Makao Mkuu ya Wilaya Isikizya ambako ndiko kwenye kituo cha polisi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea bajeti ya mafuta ili kuwarahisishia watendaji kazi maana maeneo ya Jimbo ni kubwa na yote yanahitaji huduma za kipolisi?
WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza kuwashukuru wananchi na wadau wote walihusika katika kuchangia ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Loya katika Halmashauri ya Tabora (Uyui). Pamoja na mwitikio huo bado kituo hiki hakijakamilika sehemu ya kuhifadhia silaha, huduma ya choo na makazi ya askari. Pindi vitu hivi vitakapokamilika kituo hiki kitafunguliwa na askari watapelekwa. Hivyo basi, namuomba Mheshimiwa Mbunge kuendelea na jitihada za kuwahamasisha wananchi wa Kata ya Loya ili kukamilisha ujenzi huo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kuongeza bajeti ya mafuta katika maeneo mbalimbali kulingana na upatikanaji wa fedha ili kukidhi mahitaji ya doria, misako na operesheni mbalimbali katika kutoa huduma ya ulinzi na usalama kwa wananchi.
MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-
Wilaya ya Uyui ni Wilaya mpya ambayo makao yako Isikizya na Jeshi la Polisi tayari limehamia yaliko Makao Makuu ya Wilaya, lakini mazingira ya hapo kwa askari polisi ni magumu sana kwa sababu hakuna maji, hakuna nyumba za kuishi askari hao ambao kwa sasa wanaishi kwenye nyumba za kupanga au kwenye mabanda ya mabati yaliyojengwa karibu na kituo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira hayo kwa askari wetu ili wafanye kazi katika mazingira bora zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Wizari ya Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa vituo vya polisi, majengo ya utawala na nyumba za kuishi askari ni suala ambalo linahitaji fedha nyingi kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na upungufu mkubwa kwenye Vituo vya Polisi Daraja la A na B ni vituo ambavyo vinatakiwa kujengwa katika Mikoa na Wilaya za Kipolisi na Miji inayokuwa. Vituo vya Daraja A vinavyotakiwa kujengwa nchi nzima ni 94 kwa wastani wa shilingi bilioni 94, Vituo vya Daraja B vinahitajika 382 kwa gharama ya shilingi bilioni 191 na Vituo Daraja C 4,043 kwa gharama ya shilingi bilioni 950.
Mheshimiwa Naibu Spika, majengo yanayotakiwa na Makamanda ni 15 wastani wa shilingi bilioni 15, nyumba za kuishi Askari ni zaidi ya 35,000 wastani wa shilingi trilioni mbili nukta nane.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kufanya yafuatayo, ili kukabiliana na tatizo hili la miundombinu ya Jeshi la Polisi:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba za kuishi askari Serikali ina mpango wa kujenga nyumba 3,500 kila mwaka kwa nchi nzima. Serikali kwa Awamu hii ya Tano ina mpango wa kujenga nyumba 4,136 za mkopo kutoka Serikali ya China na tayari mpango huo upo Wizara ya Fedha, mkopo utakaogharimu dola za Kimarekani zinazokisiwa kuwa milioni 500.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Vituo vya Polisi Daraja A, B na C na majengo ya makamanda, Serikali itaendelea kujenga vituo hivi kulingana na uwezo na upatikanaji wa fedha.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea kuwasiliana na Serikali za Mitaa, ili pale inapoanzishwa Wilaya au Mikoa mipya kuwepo na huduma zinazohusiana na masuala ya ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya polisi na nyumba za kuishi askari.
MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga viwanda mahali zinapopatikana malighafi.
(a)Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Tumbaku Mkoani Tabora?
(b)Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Kusindika Asali Mkoani Tabora?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-
(a)Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Tabora huzalisha tumbaku nyingi hapa nchini. Kwa mwaka 2015, Mkoa wa Tabora ulizalisha tumbaku tani 39,502. Pamoja na uzalishaji wa tumbaku hiyo, Mkoa wa Tabora hupokea tumbaku inayozalishwa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kigoma. Kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inalipa kipaumbele suala la ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani tumbaku mkoani Tabora. Serikali imefanya mawasiliano ya awali na wawekezaji nchini Vietnam na China ili kuvutia nchi hizi kuwekeza hapa nchini. Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kimepewa maelekezo maalum kunadi fursa hii kwa wawekezaji katika sekta ya tumbaku na sigara hapa nchini.
(b)Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Tabora unazalisha asali takribani lita 11,461,500 sawa na tani 11,500 kwa mwaka. Asali hiyo husindikwa na wajasiriamali wadogo kwa njia ya asili bila kutumia mitambo yenye teknolojia ya kisasa. Wajasiriamali hao wanasindika lita 4,126,140 sawa na tani 4,126 ikiwa ni wastani wa asilimia 36 kwa mwaka. Kiasi cha lita 7,335,360 kinabaki bila kusindikwa.
Mheshimiwa Spika, kulingana na maelezo hayo, Mkoa wa Tabora una fursa kubwa ya uwekezaji wa malighafi hiyo muhimu ambayo pia ina soko la kutosha ndani na nje ya nchi. Kinachotakiwa ni wananchi kutumia fursa hii kuanzisha viwanda vidogo na vya kati hapa nchini. Natoa wito kwa Halmashauri za Wilaya zitenge maeneo ya viwanda vidogo na vya kati na kuyajengea miundombinu wezeshi kisha kuchangamkia fursa kwa kufungua viwanda Tabora na maeneo yote inakopatikana asali kwa wingi.
MHE. ALMAS A. MAIGE (K.n.y. MHE. MUSA R. NTIMIZI) aliuliza:-
Eneo la kilometa 89 la kipande cha Barabara ya Chaya – Nyahua katika Barabara ya Itigi – Chaya – Nyahua -Tabora bado halijaanzwa kutengenezwa:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kujenga kipande hicho kwa sababu kwa sasa hakipitiki kabisa?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kipande hicho kinapitika wakati wote wakati mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo ukiendelea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Chaya hadi Nyahua yenye urefu wa kilometa 85.4 ni sehemu ya barabara kutoka Manyoni – Itigi – Chaya – Nyahua hadi Tabora yenye urefu wa kilometa 259.7. Zabuni za kumpata Mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara hii zilitangazwa tarehe 2, Februari, 2017 na ufunguzi ulifanyika tarehe 3, Aprili, 2017. Kwa sasa tathmini ya zabuni zilizopokelewa inaendelea. Mradi huu utagharamiwa kwa fedha za mkopo nafuu kutoka Kuwait Fund.
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018, jumla ya shilingi bilioni 15.73625 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Chaya – Nyahua kilometa 85.4. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka wakati kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami zikiendelea.
MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-
Serikali inahamasisha upatikanaji wa elimu kwa maana ya ujenzi wa shule nyingi zaidi karibu na makazi ya wananchi wetu yaani satellite schools na Waheshimiwa Wabunge na Madiwani wameitikia wito na viongozi tumezichangia sana.
Je, ni kwa nini Serikali haizisajili shule hizo na kupeleka walimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuanzishwa kwa satellite schools au shule shikizi ni kuwezesha watoto wadogo wa darasa la kwanza mpaka la tatu ambao hawana uwezo wa kutembea umbali mrefu kufuata shule mama kusoma karibu na makazi yao. Sababu nyingine za kuanzishwa shule hizi zinajumuisha kuwepo vituo vya msimu vya wavuvi, wafugaji wanaohamahama na kuwepo mazingira yanayosababisha maafa kama mafuriko na misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu za shule hizo kutosajiliwa na kupangiwa walimu ni kuwa ni za muda mfupi ambazo ziko chini ya shule mama husika. Kwa mfano, ikianzishwa kwa sababu ya mafuriko, mafuriko yakiisha na shule hiyo itakuwa imekufa. Vilevile shule hizi hazikidhi vigezo vya kusajiliwa ambavyo ni uwepo wa ofisi ya mwalimu mkuu, mwalimu mkuu msaidizi, ofisi za walimu, vyoo, vyumba vya madarasa, maktaba na store.
MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-
Serikali imeanza mchakato wa kutoa maji ya Ziwa Victoria kupeleka katika Mkoa wa Tabora:-
• Je, mradi huo utapita katika Wilaya ya Uyui?
• Je, ni vijiji gani katika Jimbo la Igalula vitanufaika na mradi huo hasa ukizingatiwa shida kubwa ya maji waliyonayo wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Jimbo la Igalula lenye vipengele (a) na kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeanza kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Uyui pamoja na Vijiji 89 vilivyopo umbali wa kilomita 12 kila upande kutoka bomba kuu. Katika mradi huo bomba la kupeleka maji katika Manispaa ya Tabora kutoka Mjini Nzega linapita katika Wilaya ya Uyui, ambapo jumla ya Vijiji 15 vitanufaika na mradi huo. Vijiji hivyo ni Upuge, Mhongwe, Lunguya, Kasenga, Magiri, Imalampaka, Kalemela, Ilalwasimba, Isikizya, Igoko, Ibushi, Ibelemailudi, Mtakuja, Itobela na Isenegeja.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jimbo la Igalula, Vijiji vyake vipo umbali unaozidi kilomita 12 kutoka bomba kuu. Vijiji hivyo vitaingizwa katika utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili iliyoanza kutekelezwa mwezi Julai, 2016.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU (K.n.y. MHE. MUSSA R. NTIMIZI) aliuliza:-
Barabara ya Buhekela-Miswaki-Loya-Iyumbu inaunganisha Majimbo ya Igunga, Manonga, Igagula na Singida Magharibi, pia inaunganisha Mikoa miwili ya Tabora na Singida, ina Mbuga kubwa ya Wembele ambapo wananchi wanalima mpunga na kulisha Mikoa ya Tabora, Shinyanga na Singida lakini ni mbovu sana:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuitengeneza barabara hiyo kwa umuhimu wake huo wa kiuchumi na kimawasiliano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Buhekela-Miswaki- Loya-Iyumbu inahudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), katika Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Igunga yenye kipande chenye urefu wa kilometa 102.79 ambayo ni barabara ya Igunga-Itumba-Simba na Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kwa maana ya Uyui yenye kipande chenye urefu wa kilometa 66.05 ambayo ni barabara ya Miswaki - Loya kilometa 28.68 na Loya-Nkongwa kilometa 37.37.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Igunga imepanga kufanya matengenezo ya muda maalum kilometa sita na matengenezo ya kawaida kilometa moja kwa gharama ya Sh.225,000,000. Mpaka sasa barabara zenye urefu wa kilometa sita zimeshachongwa na maandalizi ya kuziweka changarawe yanaendelea. Vilevile TARURA Halmashauri ya Igunga imepewa shilingi milioni 297 kwa ajili ya kujenga boksi kalvati tatu na kufanya matengenezo ya muda maalum kilometa 1.6.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa ujenzi wa boksi kalvati tatu umefikia asilimia 30. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Igunga imetengewa Sh.165,000,000 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi kilometa 23 na ujenzi wa boksi kalvati moja.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Tabora (Uyui) imeidhinishiwa Sh.400,000,000 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya kilometa 20 kwa kiwango cha changarawe pamoja na kujenga kalvati moja. Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MUSSA R. NTIMIZI aliuliza:-
Wananchi Halmashauri ya Wilaya ya Tabora kwa kushirikiana na Mbunge wamejenga kituo kikubwa cha Polisi katika Kata ya Loya kilichogharimu zaidi ya Sh.100,000,000/= lakini mpaka sasa hakijaanza kufanya kazi:-
• Je, Serikali ipo tayari kutenga bajeti kusaidia ujenzi wa nyumba za askari na kurekebisha upungufu mbalimbali uliopo?
• Je, Serikali ipo tayari kutoa gari jipya ili kusaidia kurahisisha kazi ya Ulinzi na Usalama katika eneo hilo kwani kituo hicho kipo kilomita 120 kutoka Makao Makuu ya Wilaya – Isikizya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itatenga fedha kwa ajili ya kumaliza Kituo cha Polisi cha Kata ya Loya ambapo nyumba, chumba cha kuhifadhi Mahabusu na chumba cha kuhifadhi silaha vitaimarishwa ili kituo hicho kianze kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, napenda kutoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Wananchi pamoja na Mheshimiwa Mbunge kwa kufanikisha ujenzi wa kituo hicho cha Polisi katika Kata ya Loya.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Uyui ambayo Makao Makuu yake yapo Kata ya Isikizya ina magari matatu na moja ni bovu ambalo linahitaji matengenezo. Serikali inaendelea na mchakato wa kutafuta magari kwa ajili ya Jeshi la Polisi na pindi yatakapopatikana yatagawiwa katika maeneo mbalimbali yenye mahitaji nchi nzima.
MHE. MUSA E. NTIMIZI aliuliza:-
Katika mradi wa kupeleka umeme vijijini, Jimbo la Igalula limepitiwa na umeme katika baadhi ya maeneo ya Kata za Kigwa, Igalula, Goweko na Nsolola tu kati ya Kata kumi na moja za Jimbo hilo:-
a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme katka Kata na Vijiji vya Jimbo la Igalula vilivyobaki?
b) Katika Kata ya Igalula, Kijiji cha Igalula ambapo kuna bwawa la maji kuna hitaji la nguzo kumi tu kwa ajili ya kusaidia kusukuma mitambo ya maji. Je, Serikali itasaidiaje kupeleka nguzo hizo ili kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Jimbo la Igalula, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme vijijini kupitia mradi wa REA III mzunguko wa kwanza. Katika Jimbo la Igalula lililopo Wilayani yui jumla ya vijiji 98 vitanufaika na Mradi wa REA III. Kupitia mradi huu jumla ya vijiji 25 vitaunganishiwa umeme. Aidha, vijiji 73 vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia REA III Mzunguko wa Pili utakaoanza kutekelezwa Mwezi Julai, 2019 na kukamilika Mwezi Juni, 2021.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa mkandarasi kampuni ya Intercity Builders Limited anaendelea na kazi za ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme katika vijiji vya Kata za Ibelamilundi, Ibiri, Kigwa, Goweko, Nsololo na Igalula. Aidha, vijiji vya Kigwa B, Goweko Market, Goweko Tambukareli, Goweko Juu, Imalakaseko, Igalula I na Igalula II vilipatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Pili uliokamilika mwezi Desemba, 2016.
Mheshimiwa Spika, kazi ya Mradi wa REA III unaondelea sasa katika Jimbo la Igalula zinajumuisha ujenzi wa njia ya msongo wa kilovott 33 yenye urefu wa kilometa 66.79; njia ya umeme wa msongo wa killovot 0.4 yenye urefu wa kilometa 102.242; ufungaji wa transforma 34; pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 2,235. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 6.62.
(b) Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Igalula ambako kuna bwawa la maji, TANESCO imeshakamilisha kazi na umeme umeshawashwa katika kituo cha pampu ya maji. Ahsante.
MHE. MUSA R. NTIMIZI alliuliza:-

Kata ya Mmale haina mawasiliano kabisa ya simu:-

Je ni lini Serikali itawapatia wananchi hao mawasiliano kwa kuweka minara ya mawasiliano katika kata hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Uyui, zaidi ya wakazi 66,056 wamefikishiwa huduma za mawasiliano katika Kata za Kizengi, Loya, Lutende, Mabama na Miswaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata ya Mmale. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itaviainisha vijiji vya Kata ya Mmale iliyopo katika Jimbo la Igalula kwa kufanya tathmini ya mahitaji kwa ajili ya kuvifikishia huduma ya mawasiliano na kuvijumuisha katika orodha ya miradi itakayoingia katika zabuni zinazotarajiwa kutangazwa ifikapo mwezi ujao wa tano.
MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-

Wananchi wa Kata ya Tura katika Vijiji vya Mwamlela, Mmunyu na Nkongwa hawana kabisa mawasiliano ya simu licha ya umuhimu wa mawasiliano kiusalama na kiuchumi:-

Je, Serikali inatoa ahadi gani ya kupatikana kwa mawasiliano katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Musa Ntimizi, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba uniruhusu nitoe ufafanuzi wa Serikali kuhusu hoja iliyojadiliwa jana na baadhi ya wajumbe kuhusu sifa za mtu kuajiriwa kufanya kazi katika Shirika letu la Ndege la ATCL. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika letu la Ndege la ATCL na Serikali kwa ujumla limeainisha sifa mbalimbali zinazomruhusu Mtanzania kuweza kuajiriwa na Shirika hilo la Ndege. Sifa yetu ya kwanza kabisa ni Mtanzania yeyote mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea ambaye anafahamu kwa ufasaha lugha mbili za Kiingereza na Kiswahili. Pia Mtanzania huyo anatakiwa awe na Cheti cha Kuongoza Ndege au Cheti cha Kufanya Kazi ndani ya Ndege (cabin crew) ambacho kitakuwa kina mafunzo maalum ya usalama ndani ya ndege lakini na huduma kwa abiria ambao wanatumia ndege ile. Sifa nyingine ya tatu na muhimu kabisa ni lazima awe na leseni ya kuruka inayotolewa na Mamlaka ya Anga au TCAA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa ya ziada ni lazima awe na uelewa mkubwa wa masuala ya kitaifa, kidunia, utalii hasa nchini kwetu lakini awe ni mtu awe na hekima, ana discipline na very ethical na tutamchunguza katika hayo kuhakikisha kwamba anaweza kuajiriwa ndani ya Shirika letu la Ndege. Sifa nyingine zote zilizozungumzwa siyo ambazo zinazingatiwa na ATCL wala zinazingatiwa na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, nijibu swali la Mheshimiwa Musa Ntimizi, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma za mawasiliano kote nchini. Mwezi Julai, 2019, Mfuko ulitangaza zabuni ya awamu ya nne kwa ajili ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata 521 zenye vijiji 1,222. Kata ya Tura ilijumuishwa kwenye zabuni hiyo ikiwa na vijiji vya Karangasi, Mmunyu na Mwamlela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zabuni hiyo ilifunguliwa na baada ya tathmini, tulipata wazabuni katika maeneo hayo. Utekelezaji utaanza baada ya mkataba kusainiwa mwezi Desemba, 2019.
MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-

Serikali ina mpango wa kuleta maji katika Mkoa wa Tabora toka Ziwa Victoria lakini Jimbo la Igalula halipo katika ratiba hiyo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza vijiji vya Jimbo la Igalula katika mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Tabora, Igunga na Nzega pamoja na vijiji zaidi ya 80 vilivyopo umbali wa kilometa 12 kila upande kutoka bomba kuu. Vijiji vilivyopo katika Jimbo la Igalula vipo umbali wa zaidi ya kilometa 30 toka linapopita bomba kuu, hivyo kushindwa kuingizwa kwenye mradi huu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali imeanza kutekeleza miradi mbalimbali katika Jimbo la Igalula kwa kutumia vyanzo vya maji vingine ambapo kwa sasa usanifu unaendelea katika Kata za Tura, Nsololo na Loya. Ujenzi wa miradi hii, inategemewa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2019/2020.