Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Musa Rashid Ntimizi (20 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza kabisa nikupe pole kwa yaliyotokea leo lakini umeonesha ujasiri mkubwa na sisi tupo pamoja na wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba nzuri aliyoitoa hapa wakati analizindua Bunge hili. Hotuba ambayo ilionesha mwelekeo wa Serikali yetu kwa miaka mitano inayokuja. Hotuba ambayo ina matumaini makubwa kwa Watanzania kutoka hapa tulipo kuelekea kwenye maendeleo zaidi. Pia ameonesha kwa vitendo kwamba sasa tunaelekea kuzuri, ametenda alichonena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru pia kwa kifupi wananchi wa Igalula kwa imani kubwa waliyonionesha mimi kwa kunileta katika Bunge hili, nawaahidi sintowaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka na mimi nijikite katika maeneo mbalimbali ambayo Mheshimiwa Rais ameyagusia wakati wa hotuba yake. Nianze na eneo alilolizungumzia kuhusu tatizo la maji. Katika kitabu chake cha hotuba ukurasa wa 6 na 22, Mheshimiwa Rais amezungumzia shida ya maji kubwa tuliyonayo katika maeneo mbalimbali aliyopita. Inawezekana kila eneo lina shida kubwa ya maji lakini sisi katika Mkoa wetu wa Tabora tuna shida sana ya maji. Tumekuwa tunaahadi ya kupata maji kutoka Ziwa Victoria. Mradi huu ni mkubwa na inawezekana ikachukua muda mrefu mpaka kufikia kukamilika na wananchi Mkoa wa Tabora kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi huu ni mkubwa, tunatarajia Serikali yetu itautekeleza lakini kwa sasa katika Mkoa wetu wa Tabora mvua nyingi zinanyesha, maeneo mengi yamepata mafuriko kwa sababu yale maji hayakingwi vizuri kwa matumizi ya binadamu na matumizi mengine. Mimi nataka kuishauri Serikali ione umuhimu wa kutega mabwawa kwenye maeneo mbalimbali ili kuondoa shida kubwa ya maji tuliyonayo katika Mkoa wa Tabora. Maeneo mazuri yapo ya kutega mabwawa haya na baadhi yameshategwa kwenye maeneo machache, yameonesha kusaidia sana kupunguza kero ya maji katika eneo letu la Mkoa wa Tabora. Niombe sana Wizara ya Maji iliangalie hili badala ya maji haya kupotea bure basi yaweze kutegwa na kuweza kutusaidia kwa matumizi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa 11 amezungumzia hali ya barabara katika maeneo yetu. Amesema kuna haja ya kukamilisha barabara zinazotengenezwa na kuziimarisha zile ambazo zimeharibika. Naomba niizungumzie barabara ya kutoka Tabora - Nyahua - Chaya - Itigi. Barabara hii kwa asilimia zaidi ya 65 inapita kwenye Jimbo langu la Igalula lakini mpaka sasa imekamilika kipande cha Tabora – Nyahua, kilometa 89 kutoka Nyahua - Chaya hazijashugulikiwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuja hapa nilikwenda TANROADS kuongea na Meneja, anasema shida kubwa ni consultant anashindwa kukamilisha haraka kazi yake ili tender itangazwe. Designing zinatofautiana na watu wa TANROADS. Niiombe Serikali, kwa sasa ninavyozungumza barabrara ya Itigi - Chaya inapitika, ukifika Chaya - Nyahua imekatika na mvua mara nane. Haipitiki, imesababisha matatizo makubwa, mabasi yaliyokuwa yanapita njia ile sasa yanazungukia Singida – Nzega, wanaongeza zaidi ya kilometa 180 kwa kuzunguka na siyo mabasi tu hata wananchi wa kawaida waliokuwa wanatumia njia hii sasa haipitiki. Hata mimi kwenda Jimboni kwangu inabidi nikitoka Tabora nipite Singida kuingia tena Jimboni kwangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hatua za haraka zichukuliwe ili kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika. Vilevile tuombe Serikali iweke nguvu ya kutosha kwa sababu tumehakikishiwa pesa zipo, huyu consultant amalize kazi haraka ili mchakato wa kumpata mkandarasi na kuanza kujengwa barabara hii uanze kufanyika haraka sana. Kiuchumi tunaitegemea sana barabara hii, kuna haja itengenezwe haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala la viwanda. Katika ukurasa wa 11 Mheshimiwa Rais amesema viwanda tutakavyowekeza ni vile ambavyo malighafi yake inapatikana hapa hapa nchini. Ukizungumzia Mkoa wetu wa Tabora, kuna uwezekano wa kujenga viwanda zaidi ya viwili au vitatu. Zaidi ya asilimia 75 ya tumbaku inayolimwa katika nchi yetu ya Tanzania inatoka Tabora lakini cha ajabu Kiwanda cha Tumbaku kimejengwa Morogoro.
Niiombe Serikali, kwa kuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais ni kwamba tutajenga viwanda katika maeneo ambapo mazao yanapatikana, sisi tunalima tumbaku, tunaomba kiwanda cha tumbaku kijengwe katika Mkoa wetu wa Tabora. Itasaidia ajira, itasaidia kukuza uchumi wa mkoa wetu na itasaidia pia ubora wa zao letu la tumbaku kwani kusafirishwa kutoka Tabora kuja Morogoro linazidi kuharibika kwa hiyo ni vema tukatengenezewa kiwanda pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunarina asali nyingi katika Mkoa wetu wa Tabora. Tunaomba tutengenezewe kiwanda cha kusindika asali katika Mkoa wetu wa Tabora. Nisikitike tulikuwa tuna Kiwanda cha Nyuzi sasa kimekufa. Tunaomba pia Kiwanda cha Nyuzi katika Mkoa wetu wa Tabora kiweze kushughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kilimo kwa sababu muda unakwenda haraka na hasa nitazungumzia tumbaku. Mkulima wa tumbaku bado hajasaidiwa vya kutosha, kero zake zimekuwa nyingi na utatuzi wake umekuwa wa taratibu sana. Tunaomba Serikali itatue haraka kero za mkulima wa tumbaku ili kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja katika Mkoa wetu wa Tabora. Wananchi wengi wanalima tumbaku na wanaitegemea sana kwa uchumi wao na kuendesha maisha yao. Vilevile Serikali inaweza kukusanya kodi ya kutosha kutokana na zao la tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunalima mpunga mwingi Tabora. Tunaomba tutengenezewe miundombinu ya kuweza kufanya kilimo cha mpunga kisaidie wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wetu wanahangaika, hawana maeneo ya kufugia. Tunaomba Serikali ichukue hatua kuwasaidia wafugaji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, suala la umaskini ambalo Mheshimiwa Rais amelizungumza. Kuna programu ya kupeleka shilingi milioni 50 katika kila kijiji. Tunaipongeza Serikali yetu kwa wazo hili. Tunachoshauri ni kwamba utengenezwe utaratibu mzuri wa kusimamia fedha hizi zisije zikawa kama zile za Mfuko wa Jakaya, zilipotea bila ya maelezo mazuri. Serikali ina nia nzuri itengeneze utaratibu mzuri ambao utasaidia pesa hizi zije kuonekana zinasaidia vijana wetu katika kufanya shughuli zao mbalimbali. Wataalamu waende wakawafundishe vijana wetu kule vijijini namna ya kuendesha biashara ndogo ndogo, lakini na menejimenti pia ya pesa hizi ili zitumike kusaidia vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda ningeweza kuzungumza mengi lakini kwa leo naomba niishie hapa, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya, nampongeza Mheshimiwa Waziri Jenista na mdogo wangu Mheshimiwa Mavunde kwa kazi nzuri wanayomsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu, mambo
yanakwenda vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi zangu naomba nianze kuchangia katika kilimo cha tumbaku ambacho wakazi wa Mkoa wa Tabora ndiyo zao la kiuchumi kubwa tunalolitegemea katika mkoa wetu. Baada ya malalamiko mengi ya Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa
Waziri Mkuu kwa usikivu mkubwa sana ameanza sasa kufuatilia kero mbalimbali na kutatua changamoto zilizopo katika zao letu la tumbaku.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, hongera kwa kazi kubwa unayoifanya sasa wananchi wa Tabora, kwa kuwa walikuwa wanahisi kwamba korosho na wewe unatoka huko sasa tunaamini ni mchapakazi na kero za tumbaku zitakwisha na sasa tunakoelekea mkulima wa tumbaku atapata faida ya zao hili la tumbaku ambalo analilima. Mheshimiwa Waziri Mkuu unajua tumbaku ikisimaiwa sawasawa ni zao ambalo linaingiza pato kubwa kwa nchi yetu, itasaidia katika maeneo mbalimbali ya kutatua kero za wananchi wetu kwa ujumla katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo machache ambayo tunataka Mheshimiwa Waziri Mkuu utusaidie ili zao hili liendelee kumnufaisha mkulima wetu. Zipo tozo mbalimbali ambazo mkulima anakuwa-charged zinapunguza faida yake katika zao zima la tumbaku. Tunaomba tozo hizi zipungue zibakie tozo za msingi ili kumwondolea mkulima mzigo mzito aliokuwa nao. Tunataka tupate bei nzuri na ili kupata bei nzuri ni lazima sasa tuangalie pia masoko mengine ya kuweza kupata wanunuzi wa tumbaku ili zao hili sasa liweze kuleta tija kwa mwananchi wa Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala dogo pia kuhusu hawa wakulima (independent farmers) ambao tuliwaambia warudi kujiunga na ushirika, wamekubaliana na wazo hili wameshajiunga na vyama vya ushirika, tunaomba sasa na wenyewe wasaidiwe ili kuwasaidia katika kilimo chao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia wakati tunaangalia zao la tumbaku, sisi Tabora tunarina asali nzuri sana, tunarima asali nyingi, juhudi hizo zinazoelekezwa katika kutatua changamoto za mazao mengine naomba tuliangalie zao la asali pia katika kuboresha mazingira yake,
kwanza katika kuliandaa zao lenyewe na kurina asali hiyo mwisho wa siku kuitafutia soko litakalomsaidia mkulima wa asali katika Mkoa wa Tabora. Asali ni dawa, asali ni kitu ambacho kinasaidia katika maeneo mengi na vilevile inaongeza mapato kwa wananchi wetu wa Mkoa wa
Tabora na maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee tatizo la maji lililopo katika Mkoa wa Tabora sana katika Jimbo langu la Igalula. Tunapongeza juhudi za Serikali katika kutatua changamoto za maji katika Mkoa wetu wa Tabora, kwa sasa tunatarajia kupata maji kutoka Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema huko nyuma, mradi huu wa kuleta maji toka Ziwa Victoria katika Jimbo langu la Igalula hatumo katika programu ya kuleta maji ya Ziwa Victoria, baadhi ya maeneo mengine wanapata maji hayo sisi tumekubaliana na hilo, tunajua Serikali itatuangalia baadae, kwa sasa tunaomba Serikali iangalie njia mbadala za kutatua kero za kupata maji katika Jimbo letu la Igalula ikiwemo kuchimbiwa visima, kuchimbiwa malambo kwa sababu mazingira yanaruhusu kuweza kuchimba mabwawa na kuweza kutatua kero za maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tuliambiwa tutafanyiwa usanifu katika Kata ya Goweko tuna bwawa moja kubwa na Kata ya Loya, lakini sijaona chochote ambacho kimefanyika, tunaomba Serikali iangalie. Tumekosa mradi wa maji ya Ziwa Victoria basi tuweze kuangaliwa
kupata maji katika maeneo mengine.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua bajeti mwaka huu sio nzuri sana kuweza kutekeleza miradi yote ya maji lakini nakumbuka tulijaribu kuishauri Serikali namna ya kupata pesa za kugharamia miradi ya maji katika vijiji vyetu. Tulishauri hapa kwamba tuongeze hata shilingi 100 katika bei ya petroli ili hela hizo ziende kwenye mfuko wa maji ziweze kutatua kero za maji katika vijiji vyetu, Serikali haijakubaliana na wazo hilo. Naomba sasa Serikali ikubali tuongeze shilingi 100 katika
bei ya mafuta ili tuweze kutengeneza mfuko wa maji utakaosaidia kutatua kero za maji katika maeneo yetu, tumtue mama ndoo kijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mama anateseka kupata maji kilometa zaidi ya 10 hadi 15, mwisho wa siku mama huyu anarudi apike chakula, mama huyu tunashindwa kumsaidia. Tunaomba tuweze kufanya hili ili kuweza kusaidia kutatua kero ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisemee kidogo suala la barabara. Wakati nataka kuchangia katika barabara naomba nitoe pongezi kwa Serikali kusikia kilio chetu cha
barabara ya Itigi – Tabora, kipande cha Chaya – Nyahua cha kilometa 85 ambacho kimekuwa ni kero kubwa sana kwa wasafiri wanaokwenda Kigoma, Mpanda na Katavi, pamoja na wasafiri wanaokwenda Tabora. Kipande kile kikitengenezwa wasafiri wa Kigoma badala ya kuzungukia Nzega na Igunga watapunguza kilometa zisizopungua 140 kufika Tabora na maeneo mengine. Tumepata pesa toka Kuwait Fund nina hakika kabisa tutatengenezewa barabara hii, tunashukuru sana kwa kusikia kilio cha Wanatabora na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliomba kipande changu cha barabara kipandishwe hadhi kutoka Buhekela kuja Miswaki kuja Loya kwenda Iyumbu. Barabara hii ni muhimu sana inaunganisha majimbo manne ya uchaguzi, Jimbo la Igunga, Jimbo la Manonga, Jimbo la Igalula na Jimbo la
Singida Vijijini, inaunganisha Wilaya tatu, Wilaya ya Igunga, Wilaya ya Uyui na Wilaya ya Singida Vijijini. Pia inaunganisha mikoa miwili ya Tabora na Singida. Kuna kilimo kikubwa sana cha mpunga kule, barabara hiyo mvua ikinyesha katika kipindi cha miezi minne haipitiki, tunaomba Serikali itusaidie katika hili kama walivyosikia barabara ya Chaya nina hakika na barabara hii tutasaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la elimu. Ninaipongeze Serikali kwa namna inavyoboresha upatikanaji wa elimu sasa, elimu bure baadhi ya watu wanasema haijaleta mafanikio makubwa, lakini kila jambo lazima liwe na mwanzo, mwanzo lazima kuna changamoto nyingi, tumekutana na changamoto nyingi Serikali itazifanyia kazi. Kiukweli wananchi wetu waliokuwa wanashindwa kupeleka watoto wao shule sasa wanapeleka watoto shule na ushahidi ni kwamba shule hizo madarasa yamejaa tunaelekea kupata changamoto ya kujenga vyumba vya madarasa. Kwa hiyo, Serikali ijipange kuboresha kupata madarasa pia napongeza tumetengeneza madawati ya kutosha, mpaka sasa madawati yanawekwa nje, hili lazima tupongeze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuboreshe mazingira ya ufundishaji, maslahi ya walimu ni lazima tuyaboreshe, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge pale madai ya walimu ni lazima tuyaangalie. Tunapoboresha maslahi yao, mazingira ya kufundishia pia lazima tuyaboreshe kwa maana ya kujenga nyumba za kuishi walimu katika maeneo yetu, walimu wanapata taabu pa kukaa, wanaondoka kufundisha vijijini kwa sababu hakuna nyumba za kuishi. Lazima tutengeneze mkakati mzuri wa kuhakikisha kwamba katika kuboresha elimu na nyumba na maslahi ya walimu ni jambo la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika elimu pia naomba niseme jambo moja, vijijini kuna maeneo ni mbali zinapopatikana shule za msingi. Tumeanza kuhamasisha kujenga satellite schools ambazo zinasaidia watoto badala ya kutembea kilometa zaidi ya 20 kwenda kufuata shule
mama tumeamua kuzijenga ili ziweze kutatua changamoto ya elimu, lakini bahati mbaya sana Wizara ya Elimu haitusaidii, wananchi wanajenga shule hizi katika wakati mgumu sana, nyingine zimetimiza vigezo zaidi ya asilimia 70 lakini kigezo kikubwa sana ni umbali kutoka katika satellite kwenda kwenye shule ile mama, zaidi ya kilometa 20 mtoto anatembea, hii inasababisha mtoto anakataa tamaa ya kwenda shule, wasichana wadogo wanabakwa njiani wanakatishwa masomo, tunasema tunataka kuzuia mimba za utotoni lakini kwa kuzuia kusajili satellite schools hizi tunaweza tukasababisha pia mimba za utotoni kwa hawa watoto kubakwa njiani wakati wanakwenda kutafuta shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba zile shule ambazo tumesema zisajiliwe Mheshimiwa Waziri, tunatoka huko mazingira ni magumu, wananchi kutokana na hali ngumu hii tunawachangisha pesa tunajenga shule zile, zingine zimefikisha vigezo at least aslimia 70 na kuendelea, tunaomba zisajiliwe. Kikubwa ni kusaidia nguvu za wananchi ambazo wanazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya yetu ya Uyui ni Wilaya mpya, tunajenga…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nianze kwa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya. Amefika Jimboni kwangu Igalula, ametatua kero za tumbaku katika Jimbo langu la Igalula sasa wakulima wa tumbaku wanaanza kupata kile ambacho wanategemea kutokana na zao lao la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri, MheshimiwaJenista na Naibu Waziri mdogo wangu Mheshimiwa Anthony Mavunde na Dada yangu Stella Alex Ikupa kwa kazi kubwa wanayomsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu, mambo yanakwenda vema na sisi tunaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati alivyokuja Jimboni kwangu hakuondoka hivi hivi, aliniachia mchango katika kituo changu cha afya na sasa tunakwenda vizuri. Namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe shukrani zangu kwa Serikali hasa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alivyokuja Jimboni kwangu Igalula nilimweleza matatizo ya miundombinu katika Jimbo letu la Igalula, barabara yangu ya Chaya – Nyahua na aliniahidi baada ya mwezi mmoja Mkandarasi atakuwa site na hivi ninavyozungumza Mkandarasi yupo site na barabara imeanza kutengenezwa. Nashukuru sana kwa kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Igalula unapozungumzia reli ya kati, ujenzi unaofanyika sasa wa standard gauge unatugusa sisi kwa asilimia 100. Wananchi wetu kusafiri wanategemea sana reli katika Mkoa wa Tabora na kusafirisha mazao yetu kutoka Tabora kwenda sokoni kunategemea sana usafiri wa reli. Kwa hiyo, ujenzi wa standard gauge kwa sisi wananchi wa Tabora tunapongeza kwa kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunamwomba aendelee kuwa na afya njema ili ujenzi huu uweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kidogo suala la Watendaji wa Vijiji na Kata. Nashukuru baadhi ya Wabunge wamelizungumzia, kuna waraka umetoka Watendaji wetu wa Vijiji na Kata ambao wana elimu ya darasa la saba ambao wengi wao wameajiriwa takribani miaka 20 iliyopita leo wanatakiwa waondoke kwenye ajira, wanapoteza mafao yao na kazi zao. Baadhi yao wana takribani miaka miwili wanaelekea kwenye kustaafu, mtu aliyefanya kazi kwa miaka 20, leo anaambiwa anaondoka kwenye kazi hana mafao na hajui ataenda kuishi vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watendaji hawa ndio tuliwatumia kujenga shule zetu za msingi, tuliwatumia kujenga shule za sekondari, kujenga nyumba za Walimu, tumewatumia kusimamia ulinzi na usalama katika maeneo yao, wamefanya mambo mengi kwa miaka 20, leo malipo yake ni haya! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu na namuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu waliangalie hili kwa macho mawili ili tuwasaidie watendaji hawa ambao wengi wao baada ya miaka miwili mitatu wanaondoka kwenye utumishi, tusubiri waweze kumaliza muda wao tuanze upya utaratibu wa kuajiri watu wengine baada ya hawa kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la afya. Ilani yetu inazungumzia kila Kijiji kiwe na zahanati lakini kila Kata iwe na kituo cha afya. Haya yote tunataka kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma bora na salama za afya. Tunataka kuhakikisha kwamba mama na mtoto wanajifungua salama, wanapata huduma zilizo bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Igalula hatuna kituo hata kimoja cha afya katika Jimbo zima. Tunazo zahanati lakini referral ya kutoka kwenye zahanati ni hospitali yetu ya Kitete iliyopo Tabora Mjini takribani kilomta 100 toka Jimboni Igalula. Mama mjamzito anapopata tatizo la kujifungua kutoka Igalula kwenda kwenye Hospitali ya Serikali ya Kitete takribani kilomita 100, asiyekuwa na uwezo wa kusafiri wanapata matatizo, wengine wanapoteza maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuingia madarakani sisi tuliliona tatizo hili, tumeanza kujenga vituo vya afya katika kila Kata, lakini Kata zetu tano za Jimbo la Igalula tumeshafika katika eneo la lenta tunasubiri sasa Serikali iweze kutusaidia. Tunaomba waliopata milioni 500 na sisi tuangaliwe tuweze kusaidiwa kupata fedha hizo kujenga vituo vya afya katika Jimbo la Igalula ili kuondokana na tatizo la vifo vya mama na mtoto kama Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la maji na umwagiliaji ambalo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ipo katika ukurasa wa 27 ikiambatana na upatikanaji wa chakula kwa wananchi wetu. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya kuondoa kero ya maji katika maeneo yetu. Wamefanya haya kwa bajeti tuliyowapitishia mwaka jana ya Sh.50 tuliyoiongeza katika lita moja ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nnaomba kama waliweza kufanya mambo makubwa haya kwa Sh.50 tulizoziweka kwenye bajeti iliyopita, kama kuna uwezekano tuwaongezee Sh.50 tena katika lita ya mafuta iwe Sh. 100 iingie katika Mfuko wa Maji, nina hakika kero kubwa ya maji katika maeneo yetu itakwisha. Niombe Waheshimiwa Wabunge tusimamie hili sisi tunaotoka vijijini tunaiona kero kubwa ya maji. Tulisema tutamtua mama ndoo kichwani, tutekeleze kwa vitendo kwa kumwongezea bajeti ili aweze kutekeleza. Tusipoweka bajeti ya kutosha haya yote hayawezi kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la upatikanaji wa chakula linaendana na kuboresha miradi ya umwagiliaji katika maeneo yetu. Tukitengeneza miradi mizuri ya umwagiliaji suala la upatikanaji wa chakula katika maeneo mengi halitakuwa tatizo. Tunapowaambia wananchi wasiseme kama kuna njaa wakati hatutengenezi mazingira bora ya umwagiliaji tunakuwa hatutendi haki, lakini yapo maeneo mengi ambayo miradi hii ipo inaweza ikafanyika na ikasaidia upatikanaji wa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu kuna miradi miwili mikubwa, Goweko kuna mradi wa umwagiliaji umeshatengenezewa feasibility study, umeshafanyiwa usanifu na imeshapatikana hati ya mazingira. Katika Kata ya Loya tumeshapata hati ya mazingira na usanifu umefanyika. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, iliwekwa miradi hii iweze kutekelezeka, lakini mpaka leo haijaweza kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu ili wananchi wetu wasiwe na shida ya chakula, miradi hii iweze kuangaliwa kwa makini iweze kutengewa fedha, ikiweza kutekelezeka hatutakuwa na shida ya chakula. Wananchi wetu watapata fedha za kuchangia miradi ya maendeleo, Halmashauri zetu zitapata kodi na mwisho wa siku hata uchumi wa viwanda tutakwenda nao vizuri huko tunapokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la barabara. Nilipoanza kushukuru barabara yangu ya Chaya – Nyahua nilizungumzia umuhimu wa barabara hii. Barabara hii inaunganisha Mikoa ya Katavi, Mkoa wa Kigoma lakini pia ni njia rahisi kufika Bukoba, Kahama na Mwanza. Inapotengenezwa barabara hii maana yake tunawasaidia hata ndugu zetu wa mikoa ya jirani kuunganisha safari zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika barabara hii kuna kipande ambacho naomba kifanyiwe kazi, kifanyiwe upembuzi kuanzia pale Chaya kuja Lutende kutokea Ndala kwenda kutokea Puge na Nzega. Barabara hii kama itatengenezwa itapunguza tena siyo chini ya kilometa 120 kutoka Dodoma – Tabora – Mwanza na maeneo mengine badala ya kupitia Singida na Nzega. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niliomba barabara yangu ya Miswaki – Loya – Iyumbu kilometa 75 iweze kutengenezwa. Kwa nini niliomba barabara hii iweze kutengenezwa? Kuna kilimo kikubwa cha mpunga tunalima mpunga mwingi sana kule, barabara hazipitiki wakati wa mvua. Kupitia TARURA tuliomba fedha ili iweze kufunguliwa barabara hii. Kuna uchumi mkubwa wa Wilaya yetu ya Uyui, Halmashauri inakusanya zaidi ya milioni 200 kutokana na kodi kwa sababu ya mpunga unaolimwa kule. Barabara hii ikitengenezwa itasaidia wananchi wetu kuweza kujikwamua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu. Nipongeze elimu bila ada. Wananchi wetu wanapata fursa kubwa ya kupata elimu, wale ambao walikuwa hawapati elimu lakini changamoto zilizojitokeza, kwanza vyumba vya madarasa vimepungua, nyumba za Walimu zimepungua, Walimu wamekuwa wachache na matundu ya vyoo pia yamekuwa machache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosahuri ni kwamba Serikali sasa ije na mkakati maalum kama ilivyofanya kwenye madawati, tuwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba tunajenga sasa nyumba za Walimu za kutosha, tuongeze Walimu, tujenge matundu ya vyoo lakini pia tuweze kupata nyumba za Walimu na madarasa pia yaongezeke ili kutatua changamoto hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani yake hapo wananchi wetu wamejenga majengo haya mengi ambayo maboma hayajakwisha kwa ahadi kwamba wakifikisha kwenye lenta Serikali itakuja kuwasaidia. Katika maeneo mengi majengo haya yapo, siyo katika Jimbo la Igalula tu, ni nchi nzima. Serikali sasa lazima ije na utaratibu wa kuhakikisha kwamba na haya maboma yote yanaisha ili nguvu za wananchi zisipotee bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie ofisi za Wabunge. Suala hili naomba lichukuliwe katika uzito mkubwa sana. Waheshimiwa Wabunge kuendelea kupewa ofisi kwenye ofisi za ma-DC siyo sawasawa. Waheshimiwa Wabunge kwenda kukodisha ofisi mitaani siyo sawasawa. Ninachoomba Bunge lije na mkakati maalum kusaidia upatikanaji wa ofisi za Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ahsate sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kupata muda wa kuchangia kidogo katika Wizara hii ya Afya. Kwanza kabisa, kwa haraka nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri sana wanayoifanya, tunaahidi tupo nyuma yeo, tunawaunga mkono kwa kazi nzuri wanayoifanya. Tunajua wana jukumu zito mbele yenu, lakini Mungu atawasaidia, watafanya kazi nzuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri, Wilaya yetu ya Uyui tulileta maombi ya zahanati zetu mbili kuona uwezekano wa kupandishiwa hadhi kuwa vituo vya afya, nashukuru sasa mchakato umekamilika, zahanati ya Ilolangulu na Malongwe zinapandishwa hadhi kuwa vituo vya afya. Tunaomba mchakato wa kupata barua na kuingizwa kwenye bajeti ufanyike ili vianze kufanya kazi. Nashukuru sana kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie mambo mawili au matatu kuhusu uhaba wa dawa kwenye zahanati zetu. Uhaba wa dawa ni mkubwa sana, tunaomba juhudi zinazofanyika zizidi kufanyika sawasawa ili zahanati zetu zipate dawa za kutosha ili wananchi wetu wanapokwenda kupata matibabu waweze kutibiwa na kupata dawa katika zahanati zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua juhudi kubwa inafanyika sasa lakini pamoja na dawa muda mwingine kufika kwenye maeneo yetu, udhibiti wake unakuwa ni mdogo, wajanja wanazitumia vibaya tofauti na matarajio. Tunaomba pia udhibiti wa dawa hizi zinapokuja kule ufanyike sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami kama walivyoomba wenzangu, kwanza naipongeze MSD, tunatarajia kutenga pesa kulipa deni lao kubwa ili kuwawezesha kufanya kazi zao vizuri sana. Naomba tuweke pesa zaidi kulipa deni lote ili kuwafanya waweze kutoa huduma ya dawa vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia maduka ya MSD ambayo yanafunguliwa katika Hospitali za Mikoa, ni wazo zuri na tunalipongeza, lakini sasa Wizara ifikirie kuona namna MSD itakavyofungua maduka haya kwenye Wilaya zetu. Kwenye Hospitali za Wilaya ambapo ndiko kuna wagonjwa wengi na wananchi wengi wanatibiwa katika hospitali zetu za Wilaya, yakifunguliwa maduka huko, itasaidia huduma hii kuwafikia wananchi wetu wengi tofauti na maduka haya kuishia kwenye hospitali za mikoa peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie huduma za wazee. Sera ya Huduma kwa Wazee Kutibiwa Bure, inatakiwa itengenezewe utaratibu mzuri zaidi. Hii sera ipo, lakini practically haifanyiki hivyo, wazee wetu wanateseka, wakienda hospitali zaidi ya kuandikiwa panadol hakuna dawa wanazopata.
Wakati mwingine kwa sababu hawatoi pesa, hata huduma wanazopata zinakuwa za kusuasua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara isimamie hili, kwa sababu kama Mheshimiwa Waziri alipokuwa anazungumza katika hotuba yake anasema mzee alikuwa kama sisi na sisi tutakuwa kama yeye hapo baadaye, kuna haja ya kuangalia wazee wetu kwa macho mawili zaidi ili wapate huduma ambayo inastahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, huduma za mama na mtoto, kwa asilimia kubwa wanaokwenda kupata matibabu katika zahanati zetu ni wazee, akinamama na watoto. Sera inasema watapata matibabu ya bure, lakini naomba tena hapa, Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze ni mkakati gani anataka kuuweka sasa ili kusaidia huduma ya mama na mtoto katika zahanati zetu huko chini, ikiwemo pia na upatikanaji wa dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, nizungumze la mwisho. Tumepata hamasa ya kuwaambia wananchi wetu wajenge zahanati katika maeneo yetu. Tumejenga zahanati za kutosha lakini hatuna wauguzi katika zahanati nyingi. Kwa sasa vijana wetu wengi wanahitimu Udaktari na Shahada mbalimbali katika fani ya Udaktari na utabibu, lakini hawaajiriwi na Serikali yetu ili kufanya kazi…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwa kupata nafasi ya kuchangia Hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utawala Bora. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa kazi nzuri wanayoifanya, Watanzania tuko nyuma yenu, tunawaunga mkono na Mheshimiwa Rais, Wabunge wa CCM tunakuunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mawili, matatu ya kuchangia kama ushauri, lakini mwisho kuna haja ya kuendelea kuwaeleza ndugu zetu namna ya kuendesha nchi yetu tofauti na wanavyozungumza wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Halmashauri yangu ya Uyui ni Halmashauri mpya, ambayo tumekuwa tukiomba pesa kwa sababu ya ujenzi wa Halmashauri yetu, tuna miaka mingi pesa hazijafika, tunaomba Serikali ituangalie tuweze kumaliza ujenzi wa Halmashauri yetu. Kujenga jengo la utawala, tuna ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, tunaomba Serikali katika bajeti ya mwaka huu ituangalie tuweze kukamilisha hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna maombi ya kupata Halmashauri mpya ya Igalula, kutoka katika Halmashauri yetu iliyopo ya sasa, haya ni maombi ya muda mrefu, tunaomba pia liangaliwe tuweze kupata Halmashauri yetu ya Igalula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Vitongoji. Wenyeviti hawa wanafanya kazi kubwa sana, ni kiungo muhimu sana katika utendaji wa shughuli zetu katika maeneo yetu. Ni wasimamizi wa maendeleo katika maeneo yetu. Miaka mingi wemekuwa wanasahaulika hawa pamoja na kazi kubwa wanayoifanya, tunaomba Halmashauri zetu ziangalie namna ya kuwalipa posho zao. Vilevile posho zenyewe ni ndogo, tunaomba tuangalie uwezekano wa kuziagiza Halmashauri zitenge hizi pesa, na ziwafikie Wenyeviti wetu wa vitongoji na vijiji. Posho zenyewe ni shilingi 10,000, naomba ikiwezekana tuwaongeze posho hizo, ikiwezekana tutengeneze utaratibu pia wa kuwapatia posho Wajumbe wa Serikali za Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia maendeleo katika maeneo yetu, pesa kubwa, pesa nyingi zinakwenda kwenye Serikali za Vijiji, utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo unafanyika katika Serikali zetu za Vijiji. Hawa watu wasipoangaliwa, wasipojaliwa maslahi yao, utendaji wao wa kazi utakuwa ni mdogo, na uwajibikaji utakuwa ni mdogo, tunaomba tuliangalie sana hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata, watendaji wa vijiji na Kata hatujaangalia maslahi yao vizuri, Watendaji wa Vijiji wa Kata wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. Hawana usafiri, maeneo yao ya kazi ni makubwa, wanapata taabu sana kufanya kazi hizo katika maeneo ya vijijini. Ushauri wangu Serikali iangalie uwezekano wa kuwapatia usafiri hata wa pikipiki, ili waweze kutimiza wajibu wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watendaji wa Vijiji ndiyo wanajenga sekondari, ndiyo wanajenga zahanati, wanajenga nyumba za walimu, lakini Watendaji wa Vijiji wanakaa nyumba za kupanga. Tuone uwezekano pia wa Serikali kupata kuwajengea nyumba Watendaji wa Vijiji, na Watendaji wa Kata. Maslahi yao pia bado ni madogo, Serikali ione uwezekano wa kuwaongezea maslahi yao watendaji wetu wa Vijiji na wa Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia suala la Halmashauri yetu ya sasa ya Uyui kwa maana Iskizia, tulikuwa tunapata pesa kwa sababu ya kuendeleza Halmashauri yetu mpya. Lakini mpaka sasa hatuna nyumba za wafanyakazi pale Isikizya kiasi kinawafanya wafanyakazi wetu waishi mbali na makao makuu ya Halmashauri yetu. Tumejengewa nyumba za shirika la nyumba pale wanaziita nyumba za low cost housing, lakini ukiziangalia nyumba zile gharama yake moja ni shilingi milioni 52, wafanyakazi wetu hawana uwezo wa kuzinunua. Halmashauri yetu haina uwezo wa kuzinunua. Tunaomba Serikali ione namna ya kutusaidia ili wafanyakazi wetu wa Halmashauri ya Tabora kwa maana ya Uyui, waweze kukaa karibu na eneo la kazi ili waweze kuwa na ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Kizengi ilitangazwa muda mrefu, karibu miaka mitatu, minne iliyopita. Pamoja na kutangaza Tarafa yetu ya Kizengi mpaka sasa haijaanza kazi rasmi, hatuna Afisa Tarafa na hili naomba liangaliwe sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamezungumzia kuhusu asilimia kumi inayotengwa kwa sababu ya vijana na akina mama. Tunaomba kujua hili suala ni la kisheria au ni kwamba Halmashauri ikiamua inatenga au laa. Maeneo mengi hizi pesa hazitengwi, maeneo mengi vijana hawanufaiki na hizi asilimia tano na akina mama katika maeneo yetu. Tunaomba Halmashauri zote ziagizwe ni lazima zitenge hizi asilimia tano kwa sababu ya kuwasaidia vijana na asilimia tano kuwasaidia akina mama na ufuatiliaji wake uwekewe utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengi lakini kwa sababu ya muda, nijikite kwenye masuala mawili, matatu ya mwisho. Unapozungumzia demokrasia kuna mambo mengi ndani yake, Wazungu wanasema charity begins at home. Kuna msemo mmoja sungura alikuwa na hamu ya ndizi, alivyozikosa zile ndizi akaanza kuimba sizitaki mbichi hizi, wenzetu wanazungumzia demokrasia kwamba katika chama chetu hakuna demokrasia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotaka kutoa uchafu kwenye jicho la mwenzako angalia uchafu kwenye jicho lako kwanza. Kuna Wabunge wamepata Ubunge wakiwa wako CCM, lakini leo wapo CHADEMA; wapo watu ambao wamekitumikia chama kile kwa muda mrefu, wamekuja kuingia kwenye dirisha dogo juzi. Sasa demokrasia hiyo, ukiangalia wao na sisi nani ana demokrasia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusiana na TAMISEMI; amezunguzia suala la kuonekana kwenye tv, anayezungumza anazungumza kuhusu kuonekana kwenye tv. Mimi nataka niseme, unaposema kwamba wananchi hawapati fursa lakini…
TAARIFA...
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakataa taarifa yake. Yeye amelelewa ndani ya Chama cha Mapinduzi ndiyo maana leo tuko naye hapa. Mimi nimechaguliwa na wananchi kwa kura za kutosha.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilinde muda wangu. Mimi nimechaguliwa na wapigakura kwa kura zaidi ya 38,000, mgombea wa CHADEMA alipata kura 4,000. Kwa hiyo nimekuja Bungeni kwa nguvu ya wapigakura wangu na mtoto wa simba ni simba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Utawala Bora na amezungumzia kuhusu watumishi hewa. Naomba ni-quote ukurasa wa tisa, anasema; “Mheshimiwa Spika, sababu kubwa ya kushindwa kutatuliwa kwa tatizo la watumishi hewa ni kukosekana kwa uadilifu katika mfumo mzima wa utumishi wa umma. Watumishi hewa ni tatizo la kutengenezwa kwa makusudi.”
Mheshimiwa Mwenyekit, kwa bahati mbaya sana aliyekuwa Katibu Mkuu wa Utumishi ndiye alikuwa anasoma hotuba ya Upinzani. Nadhani anajua siri kubwa sana ya watumishi hewa. Mheshimiwa Magufuli atusaidie kuangalia namna ya waliotengeneza watumishi hewa, inawezekana na wengine tuko nao humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni la kuliangalia sana maana unapomnyooshea mwenzako kidole kimoja vitatu vinaweza vikawa vinakuangalia wewe mwenyewe. Kuna haja kabisa Mheshimiwa Rais aangalie namna anavyotumbua majipu haya na macho mengine yaangalie humu ndani, inawezekana kabisa wakatusaidia katika kuweka mambo haya sawa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka niseme haya kwa kifupi, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata muda wa kuchangia kidogo katika bajeti ya Wizara hii muhimu kwa uchumi wa nchi yetu na wananchi wake. Kwa sababu ya muda mchache nitazungumzia maeneo mawili kwa haraka haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie barabara yetu ya Itigi – Chaya – Nyahuwa - Tabora. Barabara hii kipande cha Itigi - Chaya kimekamilika kwa asilimia zaidi ya 90; kutoka Nyahuwa - Tabora imekamilika kwa zaidi ya 90% lakini katikati kipande cha Chaya - Nyahuwa bado hakijaanza kushughulikiwa. Niiombe Serikali na Mheshimiwa Waziri kwa kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kipande hiki kukamilika na kutumika, kwa kweli tuiangalie kwa macho mengi barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapotoka Manyoni kuja Tabora kwa kupitia Singida - Nzega unatumia kilometa 460 kufika Tabora. Unapotoka Manyoni kuja Itigi kupitia Chaya mpaka Tabora ni kilometa 254, kwa kuzunguka unaongeza kilometa 206. Wanaokwenda Kigoma wakipitia Chaya maana yake watapunguza zaidi ya kilometa zaidi ya 206 kwa safari yao. Wanaokwenda Mwanza wakipitia njia ya Chaya - Tabora - Nzega watapunguza kilometa zisizopungua 110 kufika Mwanza badala ya kupitia Singida na Igunga. Barabara hii ni muhimu sana, tunaomba Serikali sasa ifike wakati watuambie mkandarasi anaanza lini ujenzi kipande kile cha Chaya - Nyahuwa.
Mheshimiwa Naibu spika, kwa kweli Mheshimiwa Waziri anajua 100% ya kipande hiki kimepita kwenye jimbo langu, atakapokuja kuhitimisha hapa basi atueleze imefikia wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna maombi ya kupandisha hadhi barabara, maombi yako mengi Mheshimiwa Waziri alituambia lakini basi tuone taratibu maombi yale yanaanza kupunguzwa. Mimi nina kipande cha barabara ya Bwekela - Miswaki - Loya - Iyumbu ambacho kinaunganisha majimbo ya Igunga, Manonga, Igalula na Singida Vijijini. Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wetu kwa sababu kuna kilimo kikubwa cha mpunga kule, kuna haja barabara hii itengenezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisipozungumzia reli wananchi wangu hawatanielewa. Ukianzia Kalangasi mpaka Igalula reli inapita katika jimbo letu na ni muhimu sana. Juhudi zinazofanyika kuimarisha reli yetu zinaonekana tunaipongeza Serikali. Napenda nimpongeze Mkurugenzi wa TRL kwa kufanya sasa TRL ianze kujiendesha kiuchumi kwa mipango mbalimbali ambayo inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Wabunge waliosema kuna haja ya kuunganisha TRL na RAHCO kwa sababu ya kuisaidia TRL kujiendesha. TRL ili ijiendeshe inahitaji kutengeneza pesa za ndani lakini vilevile iweze kukopa. TRL haina assets za kukopea ili iweze kufanya mipango yake ya kimaendeleo. Assets ziko RAHCO, TRL hawana assets, wanashindwa kufanya mipango mizuri ya kimaendeleo mwisho wa siku wanaitegemea Serikali kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, ukiangalia RAHCO hawajaiangalia vizuri miundombinu ya reli ambapo ili TRL ifanye vizuri lazima miundombinu ya reli iwe imara. RAHCO hawana wafanyakazi wengi, hawana wataalamu wa kutosha kuweza kui-service reli yetu ikawa inapitika kwa muda wote. Kuna haja kabisa Serikali kuleta sheria hii Bungeni tuiangalie upya, tuunganishe sasa RAHCO na TRL zifanye kazi ambayo italisaidia Shirika letu la Reli kuweza kufanya kazi vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli ni kiungo muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Barabara zinaharibika kwa sababu mizigo mingi inasafirishwa kwenye barabara zetu. Kuna haja kabisa ya kutengeneza mazingira yaliyo bora zaidi ili reli yetu ilete tija na faida katika uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, utunzaji wa misitu na maliasili yetu ni jambo la msingi sana. Kila Mtanzania ana wajibu wa kutunza na kuhifadhi mazingira. Wafugaji wapo ambao wanafuata sheria za nchi za uhifadhi wa mazingira yetu na wapo ambao ni waharibifu wa mazingira. Kuna haja Serikali kusimamia sheria katika kuhakikisha ufugaji hauathiri mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wafugaji ambao hawafuati sheria za uhifadhi wasisababishe wafugaji wote wakaonekana ni adui mkubwa wa hifadhi ya nchi. Lazima pia tujiulize ni kwa nini wapo baadhi wanafuata sheria na wengine wanakiuka sheria? Je, Serikali yetu imetimiza wajibu wake katika kuwasaidia wafugaji wetu? Sheria za nchi zinaangalia vipi hifadhi zetu za mapori zilizotengwa miaka hiyo, idadi ya watu waliokuwepo miaka hiyo na mahitaji yao ya ardhi, ikiwepo mahitaji ya ardhi kwa ajili ya makazi, mahitaji ya ardhi na idadi ya mifugo yetu iliyopo kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja ya kujiangalia upya kisheria kuweza kupata ardhi kulingana na mahitaji ili kuepusha mauaji, mapigano na kugombea ardhi katika maeneo mbalimbali. Wafugaji wasibezwe na kuonekana wao ni tatizo kubwa katika kuharibu mazingira. Naomba niulize, je, wafugaji na wakata mkaa nani anaharibu mazingira?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwahukumu wafugaji kwa kigezo cha kwamba wao wanaharibu mazingira. Tuwatengee maeneo kisheria, tuwamilikishe tuone kama kweli watakiuka utaratibu na wataharibu mazingira. Nakubali wapo wafugaji wanaingilia maeneo ya wakulima na kusababisha uharibifu. Narudia, haiwezi kuwa wafugaji wote wapo hivyo. Isituondoe katika kutetea wafugaji wetu kupatiwa haki zao na wajibu wetu wa kuwapatia mazingira bora ya ufugaji wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wangu katika Jimbo la Igalula, Kata ya Goweka Miyenze, Intende na Kigwa wanateseka sana na wanateswa na kusumbuliwa sana na askari wa maliasili, wakati mwingine ng‟ombe wanakua nje ya reserve sisi tunaita ujije, wanaswaga mifugo hiyo na kuiingiza reserve na kuwakamata na kuwatoza fedha nyingi au kutaifisha mifugo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lote la Jimbo la Igalula halina eneo rasmi la wafugaji, lakini kuna mifugo mingi na pia wakulima wapo wengi lakini pia maeneo makubwa ya Jimbo yamo ndani ya hifadhi. Mgogoro wa eneo la kulimia, kufugia na makazi ni tatizo kubwa sana. Tunaomba wakulima wetu wapewe eneo la kufugia na kulimia ili kuondoa tatizo hili. Tulishaomba kumegewa eneo la kilometa nne katika eneo lililohifadhiwa katika Kata ya Lutende na Miyenze ili wapewe wafugaji na wakulima ili kuondoa adha hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwabeze wafugaji wetu, ndiyo wapiga kura wetu, leo tusiwadharau na kuwabeza. Watengenezewe mazingira rafiki ili wasiwe tatizo katika uharibifu wa mazingira. Tuangalie wakata mkaa na mbao kama waharibifu wakubwa wa mazingira na si wafugaji wetu ambao wana haki pia katika nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wafugaji wangu wa Kata za Lutende, Miyenze, Kigwa na Goweko wapewe maeneo na wamilikishwe ili wapate eneo la kufugia mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kama wafugaji wetu wataheshimiwa na kuthaminiwa na si kuonekana wahalifu na watu wabaya kwa mazingira.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia mawazo na kutoa ushauri wangu katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017. Nashukuru na kuipongeza Serikali kwa kuleta bajeti nzuri ambayo inajali maslahi ya Watanzania wote kwa ujumla wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo kama sitakupongeza kwa ujasiri uliokuwa nao katika kipindi hiki kigumu ambacho umepitia lakini nakuamini wewe ni mwanamke jasiri na unaendelea kutuongoza vizuri bila kutetereka. Sisi tuko pamoja na wewe katika kuhakikisha kwamba kanuni na taratibu za Bunge zinafuatwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa bajeti nzuri lakini kuna haja ya baadhi ya maeneo tukayasemea na kuyaboresa. Cha msingi tunachomuomba Mheshimiwa Waziri asikilize mawazo ya Wabunge na kuyafanyia kazi, penye wengi pana mengi.
Mengi yaliyosemwa na Wabunge ni kwa niaba ya wananchi wengi walioko huko nje. Tunaomba Mheshimiwa Waziri ayafanyie kazi ili kuleta ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nigusie baadhi ya mambo ambayo yanagusa jimbo langu nikianza na suala la maji. Niungane na Wabunge wenzangu waliounga mkono na waliotoa wazo la kuongeza pesa katika Mfuko wa Maji kutoka Sh.50 kwenda Sh.100. Tunahitaji tupate pesa za kutosha katika Mfuko wa Maji ili kutatua kero kubwa ya maji iliyopo katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali isiwe na kigugumizi katika hili, Wabunge wengi wanahitaji kutatuliwa kero za maji katika maeneo yao, akina mama wanapata taabu kubwa ya maji katika maeneo yetu tunakotoka. Tunahitaji miradi mingi ya maji itekelezeke katika maeneo yetu ndiyo maana tunashauri Sh.50 iongezwe kuwa Sh.100 ili pesa nyingi ziende zikatatue kero za maji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeamua kuanza na hili kwa sababu mimi na wananchi wa Jimbo la Igalula tuna masikitiko makubwa sana. Katika mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria Jimbo la Igalula lililopo katika Mkoa wa Tabora hatumo katika mradi huu. Majimbo yote maji ya kutoka Ziwa Victoria yatafika lakini Jimbo la Igalula tumesahaulika. Napenda kujua wananchi wa Igalula wameikosea nini Serikali hii mpaka kutusahau kutuingiza katika mradi wa maji wa Ziwa Victoria wakati tuna shida kubwa ya maji? Katika kuchangia Hotuba ya Rais nilisema tuna shida ya wafugaji wanahitaji maji kwa ajili ya mifugo yao kwa maana ya malambo, tunahitaji mabwawa ya maji kwa sababu ya kutatua kero kubwa ya maji iliyopo katika Jimbo la Igalula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejaribu kuchimba visima vifupi na virefu havitoi maji kwa sababu eneo kubwa la Mkoa wa Tabora hakuna maji chini. Nilishauri, katika Jimbo letu la Igalula kuna maeneo mengi ambayo tunaweza tukatega mabwawa ya maji na watu wakapata maji lakini Serikali mabwawa imetunyima, malambo imetunyima, maji ya kutoka Ziwa Victoria hatuna, tunaambiwa tutapata maji ya kutoka Mto Malagarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Malagarasi ni zaidi ya kilometa 150, lakini maji yanayotoka Ziwa Victoria yanapopita Uyui kwenye Jimbo la Tabora Kaskazini ni chini ya kilometa 30 kufika katika Jimbo letu la Igalula. Ni rahisi zaidi kuyatoa maji ya Ziwa Victoria kutoka Uyui kwa maana ya Makao Makuu yetu ya Wilaya kuyaleta katika Jimbo la Igalula kuliko kuyatoa katika maeneo mengine. Niombe Serikali itueleze, Waswahili wanasema awali kuu, sasa Ziwa Victoria tunakosa tunaahidiwa ya baadaye. Sisi tunahitaji kuwepo katika mradi wa maji wa Ziwa Victoria ili kuondoa tatizo la maji katika Jimbo letu la Igalula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie kidogo kuhusu afya, tulipitia bajeti ya Wizara ya Afya na Wizara ya TAMISEMI. Lakini katika ilani ya Chama cha Mapinduzi ya miaka kuanzia ya 2000 mpaka sasa tulizungumzia ujenzi wa zahanati katika kila kijiji, lakini pia tulizungumzia vituo vya afya katika kila kata. Nataka nisikitike, sioni ilani hii inatekelezwa namna gani kwa sababu Serikali katika bajeti zote za Wizara ya Afya, TAMISEMI na hii bajeti kubwa haijazungumza kwa uzito mkubwa kuhusiana na tatizo kubwa la afya vijijini kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati nyingi zimejengwa hazijakwisha, zilizokwisha kwa nguvu za wananchi hazina wataalam. Katika Jimbo la Igalula tumeanzisha kujenga vituo vya afya katika kila kata, lakini mpaka leo hatujui Serikali itakuja kukamata namna gani miradi ile ambayo wananchi wanawekeza pesa nyingi kuondoa tatizo la afya katika maeneo yetu. This is very serious. Tuiombe Serikali iangalie, ione umuhimu wa ku-implement upatikanaji wa vituo vya afya na zahanati katika kila kijiji na katika kila kata ili kuondoa tatizo la afya katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye reli, unapozungumzia reli umuhimu wake kila mmoja anajua. Kwa sisi wana Igalula ni usafiri unaoturahisishia kufika maeneo mbalimbali. Wananchi wangu wanafanya biashara katika maeneo ya reli zile, lakini reli katika uchumi wa nchi unasaidia sana katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoa ushauri mara nyingi, umuhimu wa reli kuunganishwa na RAHCO. TRL inategemea kwa kiasi kikubwa ruzuku kutoka Serikalini kwa sasa, RAHCO wanategemea ruzuku kutoka Serikalini. RAHCO tegemezi, TRL tegemezi, lakini kuna uwezekano wa TRL ikiunganishwa na RAHCO, TRL ikaweza kujiendesha kiuchumi, ikaweza kukopa na ikaweza kulifanya Shirika hili likajiendesha bila hata wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliomba Serikali ilete sheria ya kubadilisha ili tuunganishe tena RAHCO na TRL ili kuleta ufanisi wa haya mashirika mawili; lakini mpaka sasa Serikali imekuwa kimya. Tunaomba Serikali ifanye umuhimu katika kuunganisha mashirika haya mawili ili kuleta ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nisemee zao la tumbaku. Tumbaku ni nguzo ya uchumi wa Wilaya yetu ya Uyui na Mkoa wa Tabora. Mapato makubwa ya Wanatabora yanategemea sana zao la tumbaku. Serikali kila siku inasema inazijua changamoto za mkulima wa tumbaku, utatuzi wake, kila siku tutatatua kesho lakini kero za mkulima zinazidi kuongezeka, mkulima anazidi kunyonywa, masoko yanakuwa shida. Nataka niiombe Serikali sasa, badala ya Waziri kuahidi kuja Tabora kuzungumza na wakulima kero hizi tumezileta sisi wawakilishi wao, kero hizi wanazijua, sasa Serikali tunataka majibu ni lini mkulima wa tumbaku atapata afueni na zao lake la tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kodi nyingi, makato mengi, bei ndogo, soko tabu, wanadhulumiwa. Mfano mdogo, Mheshimiwa Waziri, CRDB waliingia mkataba na Vyama vya Msingi kujenga magodauni katika maeneo yetu mbalimbali. Mkandarasi walimtafuta wao, wakaingia mkataba, wakajenga magodauni yale, mwisho wa siku magodauni yale hajakwisha, yamedondoka, hayasaidii mkulima, lakini mpaka kesho mkulima anakatwa pesa kulipia magodauni yale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kero ya mkulima wa tumbaku sasa iweze kwisha. Mkulima…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hata hizi dakika tano. Kwanza kabisa, kwa haraka haraka, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri kwa namna wanavyoshughulikia zao la tumbaku katika Mkoa wetu wa Tabora. Zao la tumbaku lilikuwa na changamoto nyingi sana, tumekuwa tunalalamika sana, lakini sasa tunakoelekea zao la tumbaku litamnufaisha mkulima wetu wa tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipongeze kwa hizi tozo ambazo zimepunguzwa katika zao letu la tumbaku. Baadhi ya watu wanasema hizi tozo hazimsaidii mkulima, lakini tozo hizi zimemgusa mkulima, zimemgusa mnunuzi, mwisho wa siku inagusa bei ya mkulima. Nina uhakika kabisa tunakokwenda, bei ya tumbaku itakuwa inamnufaisha mkulima wetu kwa sababu tozo nyingi zitakuwa zimepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba watusaidie kitu kimoja, tuna grades za tumbaku kama 67, hatujamsikia Mheshimiwa Waziri akilizungumzia hili kwa mapana ili kuondoa grades zilizopo kumsaidia mkulima wetu wa tumbaku auze katika grades ambazo zitamsaidia mkulima wetu wa tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba nigusie pia suala la mbolea kwenye tumbaku na mahindi. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa wazo la bulk procurement, itasaidia sana. Ilikuwa vichekesho, mbolea ya kupandia ilikuwa inakuja wakati wa kukuzia, mbolea ya kukuzia ilikuwa inakuja wakati tunavuna. Kwa hiyo, ilikuwa haitusaidii sisi kama wakulima wa mazao ya tumbaku na mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kidogo nimwombe Mheshimiwa Waziri anieleze, asali ni zao linalofahamika au halifahamiki na Serikali yetu? Kwa sababu nimejaribu kupitia kitabu chake sijakuta sehemu hata moja ameizungumzia asali, asali ni zao ambalo linasaidia kipato cha mkulima katika maeneo yetu. Igalula na Urambo tunarina asali nyingi sana na ni asali bora kabisa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atueleze ana mkakati gani na wakulima wa asali ambao hawajatengenezewa mazingira yoyote ya kufanya asali yao iweze kuwasaidia kuongeza kipato. Vilevile Mheshimiwa Waziri, asali hii ikisimamiwa vizuri inaweza ikaongeza pato la nchi. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie kama anafahamu kuna sehemu wanarina asali na asali hii inaweza kusaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie wafugaji kwa haraka haraka. Sisi katika Jimbo la Igalula tuna wakulima na wafugaji lakini hata siku moja hujawahi kusikia tuna migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Ninachotaka nishauri, wafugaji wetu tusiwaone kwamba ni tatizo katika maeneo yote ya nchi, wafugaji wetu wana haki kama watu wengine katika nchi hii. Bahati mbaya sana hatujawa na mkakati mzuri wa kuwasaidia wafugaji wetu, hatujawatengenezea mazingira ya kufugia, maeneo ya kwenda kufugia, leo lazima tutamlaumu mfugaji kwamba ni mkorofi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna maeneo mengi ya reserve lakini labda tufanye tathmini, hayo maeneo yanastahili kuendelea kuwa reserve mpaka sasa? Maeneo mengi ya reserve watu wa maliasili wamekuwa wakiyatumia kama maeneo ya kupatia kipato. Wafugaji wetu wakienda kule wanakamatwa, wanatozwa faini kubwa bila sababu lakini ukiangalia Serikali haijatenga mazingira mazuri ya kumwezesha mfugaji huyu akafuga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niulize, hivi mkata mkaa na mfugaji wa ng’ombe, nani anaharibu sana mazingira? Inaonekana sana mfugaji akipeleka mifugo kwenye maeneo ya reserve anaharibu mazingira lakini magunia ya mikaa yanayoondoka kila siku katika maeneo yetu ni mengi sana. Naomba Serikali imwangalie sasa mfugaji, akitengewa maeneo mazuri, nina uhakika hatutakuwa na migogoro hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi katika Jimbo la Igalula tuna maeneo ambayo tulishatoa mapendekezo tuwaongezee wafugaji kilometa tano ili waweze kufanya shughuli zao za ufugaji. Mheshimiwa Waziri, sisi katika Jimbo letu hatuna migogoro lakini kama hatutatengeneza mipango mizuri ya wafugaji wetu migogoro itakuja na Waziri ndiyo atakuwa amesababisha migogoro hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Tizeba, tunamwambia mambo mengi hayafanyiki, lakini niombe Wizara ya Fedha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia mawazo ya Wanaigalula katika bajeti hii ambayo ni nzuri, ambayo Wanaigalula wanaiunga mkono kwa sababu kwa asilimia kubwa inatatua matatizo na mambo ambayo wanadhani ni shida kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika bajeti ya mwaka huu. Yako mambo ambayo tuliyashauri mwaka jana tulidhani hayajafanyiwa kazi kumbe walikuwa wanajipa muda wa kutafakari na sasa wameyaweka na kuyafanyia kazi katika bajeti ya mwaka huu. Mimi nataka niungane na wale wote wanaoipongeza bajeti hii kwa sababu yale yote yaliyozungumzwa katika bajeti ya mwaka huu mengi tuliyashauri katika bajeti ya mwaka jana na mengi tumekuwa tukiyashauri siku hadi siku. Nina hakika kwa asilimia kubwa yamefanyiwa kazi na yamewekwa katika bajeti ya mwaka huu. Natoa pongezi kubwa sana kwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mwizi wa fadhila nisipompongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni Rais msikivu. Wamekaa pamoja na Waziri wa Fedha wamekubaliana na wametuletea bajeti ambayo nina uhakika kama itatekelezwa vizuri itakwenda kutatua kero na changamoto nyingi tulizonazo katika majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ni nzuri lakini yapo mambo ambayo tunaendelea kuishauri Serikali yetu iyafanyie kazi ili kuendelea kuiboresha zaidi bajeti yetu iwe nzuri zaidi. Kwanza kabisa nianze kuzungumzia reli. Naipongeza Serikali kwa uamuzi wa kujenga standard gauge, reli ambayo itatusaidia sisi wana-Igalula na mikoa mingine katika usafiri na usafirishaji wa mazao yetu. Tulikuwa tunasafirisha tumbaku
yetu kwa malori kwa gharama kubwa, sasa nina uhakika standard gauge ikikamilika usafiri wa tumbaku yetu toka Tabora kuja sokoni utakuwa ni wa rahisi na kutusaidia kuongeza faida katika zao letu la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maendeleo yoyote changamoto lazima ziwepo. Wakati tunaanza kujenga standard gauge, kuna wananchi maeneo mengi wanalalamika wanaanza kuvunjiwa nyumba zao bila utaratibu. Niombe Wizara husika ikakae na wananchi wetu katika maeneo itakapopita reli hii ambapo wananchi wote wanakubali ujenzi wake ili waelimishwe wafanye uhakiki mzuri ili wale wanaostahili kuvunjiwa maeneo wavunjiwe wakiwa wanajua taratibu zimekamilika na ziko sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu barabara. Naomba niipongeze Serikali baada ya kusikia kilio chetu sisi wana-Igalula cha barabara ya Chaya - Nyahua, tumepata shilingi bilioni 110 kutoka Kuwait Fund itakayoenda kujenga barabara ile. Barabara hii kwa asilimia 100 inapita katika Jimbo la Igalula lakini inaunganisha Mikoa ya Tabora na Singida, Tabora na Kigoma na Tabora na Katavi, barabara hii ni muhimu sana. Unapozungumzia kipande hiki cha barabara cha kilometa 89 kitasaidia sana usafiri na usafirishaji katika maeneo ya mikoa hii niliyoitaja lakini sisi wana-Igalula tutanufaika kwa asilimia kubwa kwa sababu asilimia 100 barabara hii inapita katika Jimbo la Igalula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukipata kikubwa na kidogo pia unaomba, tuna barabara tuliomba ipandishwe hadhi ya kutoka Buhekela - Miswaki - Loya ambapo tuna kilimo kikubwa cha mpunga. Tunaposema wananchi wetu wawe wakulima wazuri, tusipowatengenezea miundombinu iliyo bora ya kufanya wapate faida ya mazao yao tunakuwa hatujawasaidia. Barabara hii haipitiki kipindi kikubwa kwa sababu ni mbovu. Tuliomba ipandishwe hadhi ili wananchi wa kule wanaolima mpunga waweze kupata faida kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la maji. Sisi Mkoa wa Tabora tunaipongeza tena Serikali kwa uamuzi wake wa kuyatoa maji toka Ziwa Victoria kuyaleta katika Mkoa wetu wa Tabora. Najua kuna baadhi ya maeneo mradi huu wa Ziwa Victoria hautafika ikiwemo Urambo, Kaliua, Ulyankulu na sisi Igalula. Najua ipo mipango inafanyika kupata maji ya uhakika katika maeneo haya lakini kipindi hiki ambacho tunasubiri mipango hiyo, tunaomba taratibu za kupata maji ikiwemo kuchimbiwa visima virefu, mabwawa ili tuweze kupata maji ya uhakika katika baadhi ya maeneo yetu ifanyike. Sisi Igalula tuliahidiwa kujengewa bwawa kubwa katika Kata ya Goweko na Loya lakini mwaka wa fedha uliopita havikutekelezeka. Naomba katika mwaka huu wa fedha tuweze kusaidiwa kupata maji katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na mawazo ya Mheshimiwa Ndassa aliyesema zile shilingi 40 ziongezwe na shilingi 50 ya mwaka jana ziwe shilingi 90 zikatatue kero ya maji katika maeneo yetu. Bajeti kubwa ya mwaka jana ya Wizara ya Maji ya kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ilitokana na shilingi 50 tuliyoipitisha sisi hapa ndani. Kama ikiongezwa shilingi 40 ile, nina uhakika miradi mingi ya maji katika maeneo yetu itakwenda kutekelezeka. Wale wanaopinga kuongezeka shilingi 40 nadhani hawawatakii mema wananchi wetu wanaopata taabu ya maji katika maeneo yetu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nizungumzie kidogo suala la kilimo cha tumbaku, tunashukuru juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yetu katika kutatua kero za tumbaku katika maeneo yetu. Unapozungumzia tumbaku ni uchumi wa wananchi wetu wa Igalula na Mkoa wa Tabora. Unapozungumzia tumbaku, ni uchumi wa nchi kwa sababu nchi inapata kodi kubwa katika zao la tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo yanatakiwa yaendelee kufanyiwa kazi ikiwemo soko la tumbaku na tuondolewe grades mbalimbali katika zao la tumbaku ili iweze kupata bei nzuri, lakini kikubwa Serikali sasa ifikirie kujenga kiwanda cha tumbaku katika Mkoa wa Tabora linapozalishwa zao hili la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hotuba ni nzuri, naomba na mimi niungane na wale wote wanaosema bajeti hii ni nzuri. Tunachoshauri sasa yakatekelezwe yale yote ambayo yameahidiwa katika bajeti hii ikiwemo na mawazo sasa ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wanaongezea katika kuiboresha zaidi bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Nashukuru kwa kupata nafasi na mimi pamoja kwamba ni dakika tano at least nichangie katika Mpango huu ulio mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuleta Mpango huu mzuri ambao na sisi kama Waheshimiwa Wabunge tunatimiza wajibu wetu katika kuongeza yale ambayo tunadhani yanaweza kusaidia katika kuleta maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu wa Taifa unajumuisha mipango midogo midogo tuliyokuwa nayo katika maeneo yetu, katika wilaya zetu, katika majimbo yetu ndio wanatengeneza mpango mkubwa wa Taifa letu. Mengi yameshazungumzwa lakini na mimi nilitaka niseme mambo machache kwa haraka haraka kwa sababu ya muda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumzia eneo la kilimo. Eneo la kilimo likitengenezewa mkakati mkubwa linaweza kusidia mapato ya nchi yetu, linaweza kusaidia wakulima wetu, linaweza kusaidia wakulima wetu, wakapata mapato yaliyo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najikita katika zao la tumbaku. Serikali lazima, lazima, lazima iangalie Mpango ulio bora wa kuliimarisha zao la tumbaku. Zipo changamoto nyingi; lakini nataka niseme pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali yetu bado zao la tumbaku halijamkomboa mkulima na halijachangia vizuri Pato la Taifa. Kama zao la tumbaku likisimamiwa vizuri linaweza likachinga katika Pato la Taifa kwa kiasi kukubwa sana. Niombe sana Mheshimiwa Waziri katika Mpango wako tuangalie namna ya kupata soko zuri la tumbaku nina hakika kabisa wakulima wetu kule tuna wahamasisha wafanye kilimo ili waondokane na umaskini, wanaweza kuondokana na umaskini kwa kiasi kikubwa kama zao hili la tumbaku litasimamiwa viilivyo vizuri zaidi.

Halmashauri zetu zinategemea sana sana mapato yanayotokana na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundominu. Nipongeze kwa kuanzisha TARURA, lakini kama walivyosema watu wengine TARURA inahitaji iwezeshwe kifedha ili kusaidia ujenzi wa barabara katika maeneo yetu. Unapohamasisha viwanda, viwanda hivi vinatakiwa vipate pembejeo kutokana na mazao ya wakulima wetu. Wakulima wanalima vijijini barabara ni mbovu, kutoa mazao toka vijijini kuleta katika soko ni tatizo kubwa sana. Tukiimarisha TARURA, malengo yake yakatimizwa sawa sawa, mipango yake ikawa mizuri nina hakika kabisa itatusaidia sana katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la afya, hili tunalizungumza kila siku. Tuweke mpango uliothabiti wa kujenga vituo vya afya katika kila kata katika nchi yetu ya Tanzania. Tunapoimarisha Hospitali za Wilaya na za Mikoa hazitosaidia sana kama hatutoimarisha vituo vya afya katika kila kata, vituo vya afya vitasaidia kupunguza msongamano katika Hospitali za Wilaya na katika Hospitali zetu za Mikoa, hili ni jambo la msingi sana. Katika mpango nimeona tunaimarisha sana Hospitali za Rufaa na za Mikoa. Lakini hazitosaidia sana kama wananchi wengi watakuwa wanatoka katika zahanati zetu wanaenda moja kwa moja kutibiwa kwenye Hospitali za Rufaa. Wanatakiwa wakitoka kwenye zahanati waende kwenye vituo vya afya ili kupunguza msongamano katika Hospitali zetu za Wilaya na za Mikoa; hili ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kuhusu wafugaji wetu. Wafugaji wakitengenezewa mpango ulio bora wataleta pato kwa taifa, viwanda vyetu vitapata bidhaa za maziwa, ngozi na tutapata viwanda vya kutengeneza viatu. Hata hivyo leo wafugaji wanaonekana ni adui katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji hawa ndio wapiga kura wetu, lakini kama nilivyosema tukiangalia vizuri na tukawatengenezea mazingira yaliyo bora wafugaji hawa wataleta pato kubwa sana katika nchi yetu na kuchangia katika kuboresha uchumi wetu. Tuwatengenezee mazingira bora ya kufugia badala ya kuendelea kuangaika nao. Kama hawajatengewa mazingira yaliyo bora tutaendelea kusumbuana naona haitotusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani nimetumia muda wangu vizuri nashukuru kwa kupata muda huo, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya, Naibu Waziri na Katibu Mkuu. Vile vile nawapongeza Wakuu wa vyombo vilivyo chini ya Wizara hii. Nampongeza IGP kwa kazi nzuri anayoifanya, Mkuu wa Magereza, Kamishna wa Zimamoto na Kamishna wa Uhamiaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hapa upo upungufu katika Majeshi yetu, lakini yako mambo mazuri yanayofanyika katika Majeshi yetu. Ni vizuri kueleza upungufu uliopo ili uweze kurekebishwa, lakini wakati tunaeleza upungufu huo tusisahau wajibu wetu kama viongozi pia kupongeza pale ambapo mazuri yanafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko humu ndani kushauri na tusijiondoe katika utaratibu huo. Tuna nafasi ya kuendelea kushauri pale ambapo upungufu unatokea. Sasa namna gani tunashauri, ni jambo la msingi sana sisi kama viongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia ni zao la Polisi. Baba yangu alikuwa Polisi na mama yangu alikuwa Polisi. Najua changamoto za Polisi. Ninapozungumza hapa leo, nazungumza nikijua kabisa shida za Polisi ziko wapi, ndiyo maana nataka leo niwapongeze kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi tunaotoka vijijini, Jimbo langu ni la kijijini, Makao Makuu ya Polisi yalipo na maeneo yangu ni takriban kilometa 120, maeneo mengine kilometa 150. Wananchi tunapopata matatizo, kama Polisi hawapo katika maeneo yetu, shida tunazozipata, ndiyo maana tunajua umuhimu wa Polisi katika maeneo yetu. Usipopata Polisi katika maeneo yako huwezi kuona faida na hasara zake Polisi asipokuwepo katika maeneo yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja. Kata yangu moja ya Loya siku moja majambazi waliingia kwenye Kata yetu moja ya Loya, walivamia wakaiba pesa, wakafanya wanachotaka. Waliomba mpaka kupikiwa ugali, wakala. Tulipiga simu Polisi, walifika baada ya masaa mawili. Maeneo ambayo Polisi wapo, ujambazi au wizi hauwezi kufanyika katika maeneo hayo. Kwa hiyo, umuhimu wa Polisi katika maeneo yetu sisi tunaojua, tunapongeza kazi kubwa wanayofanya pamoja na changamoto zilizokuwepo katika maeneo yao ya utekelezaji wa kazi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka pia napongeza kazi nzuri wanayofanya Askari wetu wa kawaida.

Askari hao wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, lakini hawajaacha wajibu wao wa kusimamia ulinzi na usalama katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie baadhi ya changamoto ambazo zipo, nami najielekeza katika Wilaya yangu ya Uyui na Jimbo langu la Igalula. Wilaya yetu ya Uyui Makao Makuu yetu yapo Isikizya, ni Makao Makuu mapya lakini mpaka sasa tuna takriban mwaka mmoja Askari wetu wamehamia pale, hakuna nyumba za kuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hakuna nyumba za kuishi Askari wetu, Askari wetu wamekubali kwenda kupanga nyumba mitaani, wanalipa gharama hizo wenyewe. Niombe sasa Wizara hii ya Mambo ya Ndani ione umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za Askari wetu pale Isikizya Makao Makuu ya Wilaya yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Serikali lazima iangalie sasa wale Askari wanaoishi katika nyumba za kupanga, wanaojilipia fedha kutoka katika mishahara yao, waone namna ya kuwapa posho ya kujikimu, kuweza kulipia makazi yao wanapokaa huko uraiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Makilagi, wanakaa katika mazingira magumu. Wale ambao sisi wahalifu tunakaa nao mitaani mle, lakini Mwenyezi Mungu anaendelea kuwalinda Askari wetu, tuone umuhimu kwa kweli kabisa wa kutenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za Askari wetu katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Igalula kama nilivyosema ni kubwa sana, takriban kilometa 150 toka Makao Makuu ya Isikizya, lakini Wilaya yetu ya Uyui ina upungufu wa magari ya Askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza, tukio likitokea Kata moja mpaka Askari waweze kufika, kwanza wana upungufu wa magari, lakini wakitaka kufika huko magari saa nyingine mabovu au hayana mafuta. Naomba Wizara iangalie utoaji wa magari kwa Wilaya ambazo zina changamoto ya umbali. Tukipata magari ya kutosha maana yake hata kama kuna matatizo Askari wetu wanaweza kufika katika maeneo mbalimbali kwa haraka na wananchi wetu wakaweza kupata huduma za kipolisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara iangalie kwa ujumla wake nchi nzima uhitaji wa Vituo vya Polisi katika nchi yetu yote, ije na mpango mahususi wa kujenga Vituo vya Polisi katika maeneo yetu. Tumewahamasisha wananchi wetu na maeneo mengi wamekubali kujenga Vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, katika Kata yangu ya Loya ambayo iko takriban kilometa 120 toka Makao Makuu ya Isikizya, Halmashauri yetu ilitenga shilingi milioni 200, tumejenga Kituo cha Polisi pale. Wananchi wamechangia takriban shilingi milioni 50, mimi Mbunge wao nimechangia takriban shilingi milioni 10. Mpaka sasa kituo kile kimefikia asilimia zaidi ya 95, kimekwisha, lakini mpaka leo kituo kile hakijafunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba waangalie mazingira, kilometa 150 toka Makao Makuu ya Wilaya ambako ndiyo Polisi ipo, mpaka kufika Loya, tuliamua kujenga kwa sababu ya umuhimu wake na sababu za kiusalama kutokana na maeneo yenyewe yaliyokuwa kule. Naomba Kituo hiki cha Polisi kiweze kukamilishwa, kifunguliwe na kiweze kupatiwa nyenzo za usafiri ili kuweza kusaidia usalama katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shida kubwa ya mafuta ya kusaidia magari ya Polisi wetu kufika maeneo mbalimbali. Kama nilivyoeleza ukubwa wa Jimbo langu, saa nyingine Polisi wana magari, wanapigiwa simu kwenda kwenye maeneo mbalimbali kunakuwa na shida kubwa ya mafuta. Mgao wa mafuta uangalie na jiografia ya Majimbo yetu. Jiografia ya maeneo mengine trip moja ya gari kwenda Kata moja mpaka nyingine ni takriban lita 150 mpaka lita 200, lakini mgao wa mafuta kwa mwezi unaweza ukakuta OCD anapewa lita 200 au lita 300. Naomba hili liangaliwe ili tuweze kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Maji ambayo ni Wizara muhimu sana katika maisha yetu na ya wananchi wetu, hasa sisi watu wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza na mimi nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Injinia Kamwele, mdogo wangu Naibu Waziri na Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Pamoja na changamoto nyingi za maji tulizonazo katika maeneo yetu na nchi yetu lakini kwa kweli wanajitahidi kutimiza wajibu wao. Pamoja na bejeti ndogo wanayopata lakini maeneo mengi wanajitahidi kufika na kutatua kero zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo naomba nitoe shukrani kwa Mheshimiwa Waziri na watendaji wake, bajeti zilizopita nilikuwa nazungumzia sana shida ya maji katika Jimbo langu la Igalula, ukizingatia mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Viktoria unaokuja katika Mkoa wetu wa Tabora, Jimbo langu la Igalula lilikuwa halimo katika maeneo yanayopata maji kutoka Ziwa Victoria. Nilijaribu kuomba mara mbili, tatu kwamba, kama kuna uwezekano tuone uwezekano wa kupata maji mbadala wakati maji ya Ziwa Viktoria tunategemea yatakuja hapo baadae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sasa miradi imeanza kuja jimboni kwangu, mradi wa Igalula tumepata zaidi ya shilingi milioni 380, tumekarabati bwawa kubwa la maji lilipo pale Igalula na sasa tunaelekea kupata maji ya uhakika katika Jimbo letu la Igalula hasa katika Kata ya Igalula. Pia upembuzi yakinifu unaendelea kufanyika katika mradi wa Kata ya Nsololo na Goweko, wataalam wameshakwenda, nina hakika maji yatapatikana muda si mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Loya na Tura tuna bwawa kubwa sana kuliko Bwawa la Kazima lililo katika Manispaa ya Tabora Serikali kupitia Wizara ya Maji imekubali sasa kuuwekea miundombinu mradi ule mkubwa wa maji wa Tura, nina hakika sasa wananchi wangu wa Jimbo la Igalula tutapunguza kero kubwa ya maji tuliyokuwanayo, nashukuru kwa kazi kubwa inayofanyika.

Naomba pia nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa TRL kwa kukubali lile bwawa walilochimba TRL liweze kutumiwa na wananchi wangu wa Tura kwa kuwekewa miundombinu na Wizara baada ya Mheshimiwa Waziri wa Maji kukubali kuweka miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya yote niliyoyaeleza, nilitaka nitoe ushauri kidogo ili tuendelee kutatua changamoto ya maji, najua hatuwezi kumaliza matatizo ya maji kwa mara moja, lakini kuna namna ambayo tunaweza tukafanya tukaendelea kupunguza matatizo ya maji katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusema maeneo yangu ya Jimbo la Igalula tumejaribu kuchimba visima vingi virefu na vifupi, upatikanaji wa maji umekuwa ni mdogo sana na siyo katika Jimbo la Igalula tu maeneo mengi ya Mkoa wetu wa Tabora visima vinachimbwa lakini baada ya mwezi mmoja visima hivyo vinakuwa havitoi maji. Ushauri wangu ni kwamba Serikali sasa iwekeze kwenye uchimbaji na utegaji wa mabwawa ambayo mara nyingi yanasaidia sana upatikanaji wa maji ya uhakika. Zile fedha nyingi tunazozipoteza katika kuchimba visima nadhani sasa Serikali ijipange na mradi mkubwa wa kuangalia maeneo yanayoweza kuchimbwa mabwawa yakachimbwa mabwawa na yakawekewa miundombinu inasaidia sana kupunguza kero ya maji kuliko hizi fedha zinazoendelea kupotea katika visima tunavyovijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mimi kwangu Igalula tuna bwawa lilichimbwa mwaka 1970, mwaka huu zimetolewa shilingi milioni 380 tumelirekebisha lile bwawa, tumeliwekea miundombinu, watu takribani 20,000 wanapata maji kupitia mradi ule wa bwawa lakini tungechimba kisima cha shilingi milioni 40 kisingeweza kutoa maji ya kutosha watu takribani 40,000 wa Kata ya Igalula. Kwa hiyo, Wizara ije na mpango mahsusi katika maeneo yetu nchi nzima, hata kama tutapata kidogo kidogo, lakini tuanze kufikiria sasa kuchimba na kutega mabwawa ili wananchi wetu waweze kupata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la miradi ya umwagiliaji. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa, na mimi nataka miradi hii haijapewa umuhimu wa kutosha. Naomba Wizara iangalie umuhimu wa miradi hii ya umwagiliaji. Miradi hii ya umwagiliaji ina faida zake, kwanza wananchi wetu wanapata maji ya uhakika, lakini wananchi wetu watasaidiwa upatikanaji wa chakula; wananchi wetu watapata kipato kutokana na mazao yatakayopatikana katika ule mradi wa umwagiliaji, lakini pia halmashauri zetu zitakusanya kodi kwa sababu uzalishaji utakuwa mkubwa, watapata kodi ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine wananchi wetu wataondokana na umaskini. Wanapokuwa na uhakika wa chakula maana yake wananchi wetu hawatakuwa ombaomba na wananchi wetu wataweza kusomesha watoto wao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ya umwagiliaji iwekewe fedha na sio itengewe tu fedha, fedha ziende kwenye miradi hii. Tusipofanya hivi wananchi wetu watakosa faida kwa sababu miradi mingi ya umwagiliaji inatengewa fedha, inafanyiwa feasibility study, inafanyiwa kila kitu, lakini mwisho wa siku haitengewi fedha na kwenda kutekelezwa, hili ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa maji, kuna miradi wamezungumza Waheshimiwa Wabunge haitekelezeki kutokana na kutopelekwa fedha. Niiombe Wizara ijipange miradi yote ambayo ilitengewa fedha na haijakamilika ipelekewe fedha ikakamilike nchi nzima. Tunapoteza fedha za walipa kodi na mwisho wa siku wananchi wanakuwa hawatuelewi, shida ya maji inaendelea kuwepo na fedha zimepelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna maeneo mkandarasi amekimbia site, aidha, kwa kutolipwa fedha au mwingine ameshindwa kuiendeleza ile miradi. Wale ambao wameshalipwa fedha, kama walivyosema wenzangu, Wizara lazima iwachukulie hatua hawa wakandarasi, aidha kuwashitaki au kuhakikisha wanarudi site kuikamilisha miradi iliyoanzishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho Wizara hii imepumulia zile shilingi 50 tulizowawekea kwenye tozo ya petroli, Mawaziri wanajua bila fedha hii miradi yote ambayo imetekelezwa isingeweza kutekelezeka. Kwa hiyo, kwa sababu tumeweza kupumulia shilingi 50 na miradi mingi imeonekana katika katika maeneo yetu, wazo langu nataka Bunge hili liungane tuhakikishe safari hii kieleweke, shilingi 50 lazima iongezwe kwenye bei ya petroli na fedha hiyo iende kwenye miradi ya maji. Kwa sababu sisi ni waathirika hasa sisi tunaotoka vijijini, safari hii hakitaeleweka hapa kama shilingi 50 itakataliwa kuongezwa, tunataka ifike shilingi 100. Kama kwa shilingi 50 tumeweza kufanya miradi mikubwa mingi kiasi hiki na sisi tuliahidi kumtua mama ndoo kichwani kijijini, miaka inazidi kwisha, tunataka shilingi 50 iongezwe ili twende tukatekeleze miradi iliyopo katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kuishukuru sana Wizara hii. Changamoto wanazokutana nazo ni kwa sababu ya shida kubwa ya maji tuliyonayo katika maeneo yetu. Tunaomba wasikate tama, waendelee kufanya kazi, sisi tuko pamoja nao na Mungu atawabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia mawazo yangu na ya Wana-Igalula katika mpango na bajeti ya Serikali ambayo imesomwa na Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nitoe pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia uchumi wetu na kumshauri Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi hii unakwenda vema na mwisho wa siku maisha ya wananchi wetu yanakwenda sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ya Mipango na Bajeti amezungumzia mambo mengi, lakini nataka nimpongeze ameondoa baadhi ya kodi na tozo ndogo ndogo ambazo zilikuwa kero kubwa kwa wananchi wetu huko vijijini. Naomba nipongeze kazi kubwa ambayo inafanyika, tulishauri katika bajeti zilizopita kwamba uchumi wa nchi yetu unachangiwa sana na ubora na utendaji kazi wa bandari yetu. Sasa tunaona bandari yetu inaboreshwa, ni moja ya sababu itakayosababisha uchumi wa nchi yetu uende sawasawa. Napongeza sana kwa kazi kubwa inayofanyika pale katika bandari yetu ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uanzishaji wa blue print, wafanyabiashara walikuwa wanalalamika taasisi nyingi za kutoza kodi lakini leo tunaenda kuzikusanya katika sehemu moja. Jambo hili litawarahisishia wafanyabiashara wetu kufanya biashara katika maeneo yao mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia ununuzi wa ndege. Tunataka kuimarisha uchumi wetu, tunataka tukusanye fedha za kutosha katika eneo la utalii, ni lazima tufanye maamuzi mengine ambayo baadhi ya watu wanayaona ni matatizo lakini huko tunakokwenda yataleta manufaa makubwa sana kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi wakazi wa Mkoa wa Tabora ujenzi wa reli ya standard gauge ilikuwa ni kilio chetu kikubwa sana. Kwa sasa usafiri wa reli siyo madhubuti sana, lakini kwa ujenzi wa standard gauge tunaelekea kwenye usafiri wa uhakika sana kwa sisi wakazi wa Mkoa wa Tabora. Hata tumbaku yetu inaposafirishwa kutoka Tabora kwenda sokoni, inatumia barabara na gharama zake zinakuwa kubwa. Kwa hiyo, ujenzi wa standard gauge utatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitoe mawazo haraka haraka kwa sababu najua muda ni mdogo, nianze na nukuu ya Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 79. Wakati anafanya hitimisho alisema, kujenga uchumi wa viwanda utachochea ajira na ustawi endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie sana hapa hasa kwa sisi tunaotoka vijijini, unapozungumzia uchumi wa viwanda na maisha ya wananchi wetu asilimia kubwa unazungumzia raw material. Raw material za viwanda hivi zinatokana na kilimo na asilimia 85 ya wananchi wetu wanategemea kilimo sasa kisipoboreshwa hata hili suala la kusema kwamba tunataka kukuza uchumi wa viwanda itakuwa ni tatizo. Viwanda vyetu vinategemea tumbaku, katani, mpunga na nyanya. Je, bajeti yetu inasema nini katika kuwawezesha hawa wananchi wetu kuweza kuendesha kilimo cha kisasa ambacho ni kilimo cha umwagiliaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia bajeti tunayoimaliza sasa, kwa kweli katika eneo la umwagiliaji ni sawasawa na zero, hatujafanya kwa kiasi kikubwa sana. Naomba Mheshimiwa Waziri, tukitaka kuzungumzia uchumi wa viwanda tusiache suala la kusaidia kilimo cha kisasa hasa katika eneo hili la umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya sisi kuzalisha raw material tunatakiwa tusafirishe mazao yetu kwenda sokoni. Ni jambo la msingi sana kuiwezesha TARURA. TARURA inatengeneza barabara zetu za vijijini. Kama barabara za vijijini zitakuwa mbovu, usafirishaji wa mazao kutoka vijijini kuja kwenye soko pia ni tatizo, utaongeza gharama za raw materials hizo na mwisho wa siku itakuja ku-affect viwanda vyetu huko tunakokwenda. Tuiangalie TARURA na tuipatie fedha za kutosha ili iweze kutatua kero ya barabara zetu huko vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia uchumi wa viwanda, uchumi wa vidogo vidogo unaajiri kwa asilimia kubwa sana watu ambao wako katika maeneo yetu ya vijijini. Viwanda vidogo visipowezeshwa na hapa nataka nizunguzie SIDO, SIDO inatengeneza zana ambazo nyingi kati ya hizo zinatumika vijijini kwetu. Kama nilivyosema, viwanda vidogo vingi ndiyo vinatoa ajira ya kutosha. SIDO haijawekewa fedha za kutosha, naomba tuiangalie ili iweze kusaidia viwanda vidogo vidogo katika maeneo yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la umeme. Unapozungumzia uchumi wa nchi kama suala la umeme litakuwa ni tatizo, bado tutakuwa tunapiga mark time. Shida moja iliyopo pale ni bajeti tuliyoipitisha kupelekwa ili kutekeleza miradi iliyopo. Miradi mingi ya umeme vijijini kwetu kwa sasa inasuasua kwa sababu Wizara haijawezeshwa fedha za kutosha ili kutekeleza miradi hii. Hapa nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya lakini tuwawezeshe fedha ili waweze kutekeleza miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la maji. Unapozungumzia uchumi maji ni jambo la msingi sana. Mwaka jana tulitenga shilingi bilioni 673 walipelekewa shilingi bilioni 347 tu. Tuli-survive na ile Sh.50 tuliyoipitisha hapa ya tozo ya mafuta, Wabunge wengi walishauri tuongeze Sh.50, hebu naomba tukubali tuongeze ile Sh.50 ili tupate Sh.100 tukatatue tatizo la maji. Tunahitaji tutengeneze miradi mikubwa ya umwagiliaji, tujenge mabwawa ya maji na kulipa wakandarasi wanaofanya kazi kule. Tukiongeza ile Sh.50 nina hakika kabisa miradi mingi ya maji itatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sana kwamba tunapopitisha bajeti kupanga ni jambo moja na sisi tunatimiza wajibu wetu wa kushauri. Mambo mengi yanashindwa kutekelezeka kwa sababu bajeti tuliyoipanga na kuipitisha mara nyingi haiendi katika zile sekta husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara ya Fedha ijitahidi kupeleka fedha zile ambazo tumezipitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika mpango. Kwanza kabisa nianze kwa pongezi. Naipongeza Serikali kwa kutekeleza mpango ambao tuliupitisha hapa mwaka 2017, leo tunaona uanzishwaji wa ujenzi wa Standard Gauge unaendelea, napongeza sana, pamoja na kwamba kuna baadhi ya watu wanasema Standard Gauge tunaizungumzia kwenye muda wa kusafiri tu. Sisi watu wa Tabora na mikoa mingine tunarajia Standard Gauge itakuja kutusaidia katika usafirishaji wa haraka na bei nafuu wa mazao yetu, mfano tumbaku na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia ununuaji wa ndege unaofanyika. Tulikuwa tunasema ni tatizo kubwa sana, lakini sasa Shirika letu la Ndege linaelekea kuja kuchangia katika uchumi wa nchi yetu, lazima nipongeze hili. Tuna ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya nchi nzima. Limekuwa ni kelele sana na tumekuwa tunalizungumzia sana hili, lakini Serikali yetu sikivu imeanza kukarabati vituo vya afya takriban 200 sasa katika maeneo yetu. Vilevile kuna ujenzi wa Hositali za Wilaya, zimetoka takribani shilingi bilioni moja na nusu katika Wilaya zetu na ujenzi wa Hospitali za Wilaya unaendelea. Ni utekelezaji wa mipango mizuri ambayo tuliipanga mwaka uliopita na sasa inaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miundombimu tumeshuhudia ujenzi wa barabara kubwa nchi nzima. Pia flyover za Dar es Salaam, zinasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamo. Kuna ujenzi unafanyika Mkoa wa Tabora, tulikuwa tunasema sana barabara kubwa ya Chaya
- Nyahua ambayo inaunganisha karibu mikoa mitano ya Kanda yetu huku, ujenzi wake umefikia asilimia 30. Mipango yote hii ilikuwa mizuri na sasa inatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri, nilikuwa na machache ya kushauri. Nikianza na eneo la utangulizi la Mheshimiwa Waziri, nina maeneo matatu ya kuzungumzia. La kwanza ni vipaumbele ambavyo vimewekwa katika hii miaka mitatu ya mpango wetu. Moja la vipaumbele ni suala la viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda vyetu. Hapa nilitaka nizungumzie maeneo mawili tu kwa kifupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni SIDO. Unapozungumzia SIDO ni eneo ambalo linasaidia uchumi mdogo wa maeneo yetu ya vijijini. Katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Mipango, amezungumzia kilimo kilivyokua kwa 7% na kusaidia usalama wa chakula, kupunguza mfumuko wa bei, ku-stabilize uchumi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kilimo kiende vizuri pamoja na upelekaji wa mbolea na upatikanaji wa masoko na kadhalika, lakini kilimo chenyewe kinahitaji zana za kilimo. SIDO wanatengeneza majembe ya ng’ombe ambayo tunayatumia sana vijijini, wanatengeneza mashine za bei rahisi za kusagia na kukamulia mafuta na kadhalika. Nina hakika SIDO ikiwezeshwa, wananchi wetu watanufaika sana na uchumi utazidi kukua katika maeneo yetu ya vijijini ambao unakuja kuchangia katika uchumi mkubwa wa nchi hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka Serikali iliangalie sana ni CAMARTEC. CAMARTEC ni Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini ambacho kipo Arusha. Watu wengi hawaifahamu CAMARTEC lakini wanatengeneza zana za kilimo na teknolojia za vijijini, ni sawasawa na SIDO. Hawa wanatengeneza mashine za kupandia mbegu za mazao mbalimbali ikiwemo tumbaku, korosho na kadhalika. Pia wanatengeneza kwa bei nafuu mashine za kusagia karanga na nafaka nyingine. Nasisitiza kwamba mpango huu uangalie sana haya maeneo mawili kwa maana ya SIDO na CAMARTEC ili kusaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo limepewa kipaumbele katika mpango ni kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu. Hapa naomba nipongeze upatikanaji wa huduma bora za afya vijijini kwetu. Kama nilivyosema ili wananchi waone ukuaji wa uchumi wao, zile huduma mbalimbali lazima zionekane zinapatikana katika maeneo yetu. Siyo tu kupata fedha mfukoni, lakini unapozungumzia huduma za afya, leo upatikanaji wa dawa ni asilimia takribani 80 katika maeneo yetu. Tumeongeza bajeti ya dawa na dawa zinapatikana. Mheshimiwa Dkt. Mpango katika hili nakupongeza. Pia naipongeza Serikali kama nilivyosema katika suala la ujenzi wa vituo vya afya na hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia ujenzi wa barabara kuu zinazosaidia usafirishaji na ufanyaji wa biashara kwa gharama nafuu. Nimesema barabara zinatengenezwa, lakini hapa naomba nizungumzie suala la TARURA. TARURA inatengeneza barabara zetu ndogo kuja katika barabara kuu. Ili mkulima asafirishe mazao yake kwa gharama nafuu ni lazima barabara zetu za vijijini ziwe nzuri. Leo tusipoiwezesha TARURA hata hizi barabara kubwa tunazozijenga zitakuwa hazina manufaa makubwa sana kwa wananchi wetu. Naomba tuiwezeshe TARURA ili barabara zetu zipitike vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilo hilo, kuna suala la upatikanaji wa maji safi na salama. Nimeona tunachimba visima katika maeneo mengi, lakini nashauri tuangalie uchimbaji wa mabwawa makubwa yatakayosaidia upatikanaji mkubwa wa maji tukiyawekea miundombinu. Yako maeneo yanayowezekana kuwekewa miundombinu hiyo, tuwekeze katika uchimbaji wa mabwawa makubwa na kuyawekea miundombinu ili kusaidia wananchi wetu katika maeneo mbalimbali. Mpango pia uangalie kwenda kukamilisha miradi ya maji ambayo imeanzishwa vijijini na imekwama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka nishauri, kama kweli kilimo kinasaidia katika uchumi wetu, tuwekeze katika mpango wa kilimo cha umwagiliaji. Tukiwekeza katika kilimo cha umwagiliaji tuna uhakika wa kupata mazao mengi zaidi, maana tutapa fedha zaidi kwa wakulima wetu, kodi tutapata nyingi na vilevile usalama wa chakula utaongezeka na uchumi wa nchi yetu utaongezeka. Sijaona mpango uliozungumzia kilimo cha umwagiliaji, mwaka jana nilisema na mwaka huu narudia kusema, tunayo maeneo mazuri ambayo yakitengenezewa miradi ya umwagiliaji itatusaidia sana. Kwa hiyo, nashauri mpango uangalie eneo la umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, REA ni sehemu ambayo inahitajika sana kuwekeza. Naomba tuongeze fedha katika miradi ya REA, pamoja na juhudi zinazofanyika za kuongeza upatikanaji wa umeme kwa miradi, mfano Stiegler’s Gauge. Tukiwekeza katika REA maeneo yetu ya vijijini yakapata umeme wa uhakika, tutakuwa na teknolojia ya kisasa ya gharama nafuu ya kusaidia uzalishaji kwenye maeneo yetu. Kwa kweli miradi ya REA bado inasuasua kwa sababu ya kukosekana kwa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la tatu la uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji. Kwanza naipongeza Serikali, tulishauri uboreshaji wa bandari zetu ikiwemo ya Dar es Salam. Sasa hivi Bandari ya Dar es Salaam inaboreshwa, inaongezwa kina, maana yake ufanyaji wa biashara katika eneo lile unaweza ukasaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo moja la blue print. Tumeandaa blue print ili kusaidia mazingira ya uwekezaji katika nchi yetu ya Tanzania...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya na Watanzania wanaiona. Anafanya kazi anajitoa sana, anatembelea kwenye majimbo yetu, anahakikisha kabisa kwamba utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi inakwenda sawasawa. Hata hivyo, kwa kufanya kwake kazi vizuri ana wasaidizi wake lazima na wenyewe tuwapongeze, hawalali usiku na mchana kuhakikisha kwamba kazi zinakwenda sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mhagama, dada yangu anafanya kazi nzuri sana; Mheshimiwa Kairuki, anafanya kazi nzuri sana; Mheshimiwa mdogo wangu Mavunde, big up anafanya kazi nzuri sana, hatuangushi vijana wenzake; Mheshimiwa Stella Ikupa anafanya kazi nzuri nzuri sana. Kwa ujumla Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu mambo vizuri na mambo yanakwenda sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka minne iliyopita tulikuwa tunaiomba Serikali kutekeleza ahadi ambazo tuliziahidi wakati wa uchaguzi. Leo katika kipindi cha miaka minne tuna haki leo Wabunge kusimama hapa na kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa iliyoifanya kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ambayo tulikuwa tumeahidi. Kwa hiyo sisi Wabunge wa CCM tunajivunia, tunakwenda kwenye uchaguzi mambo yetu yakiwa yako juu sana na kazi hii imefanywa vizuri kwa uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tunasema kwamba tunakwenda vizuri. Naomba niseme maneno machache, hasa mimi natoa mfano kwenye Jimbo langu la Igalula na nchi yetu kwa ujumla, kuna watu wanazungumza ujenzi wa standard gauge hauna faida kwa nchi yetu. Tulikuwa tunalalamika mizigo, sisi ambao tunatoa mikoa ambayo reli ya kati inapita, reli iliyokuwepo ilikuwa ni tatizo kubwa kwa usafiri wa wananchi wa mikoa hiyo, usafirishaji wa mizigo ulishuka kwa asilimia kubwa sana kwa sababu ya reli yenyewe kutobudu uzito wa mizigo inayosafirishwa kwa reli hiyo, leo tunajenga reli ambayo itabeba mizigo mizito na mizigo mingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, pia tunazungumzia muda wa usafiri utakuwa mchache, maana yake kutoka Dar es Salaam kwenda Tabora unakwenda kwa saa tano, wakati tulikuwa tunakwenda kwa siku tatu, tunaadhirika sana njia. Kwa hiyo sisi tunaotoka katika maeneo yale tunaona umuhimu wa standard gauge kwa maana reli ya kisasa inayokuja, tutakuwa na uhakika wa gharama za usafiri zitakuwa ndogo, tutakuwa na uhakika wa safari yetu kwa sababu zamani treni ilikuwa inadondoka sana, sasa hivi tutakuwa uhakika wa usalama wa safari yetu. Kwa hiyo unapozungumzia standard gauge kwa wananchi wa Igalula tunatarajia itasafirisha tumbaku yetu toka Igalula kwenda sokoni kwa gharama nzuri na kwa muda ambao unategemewa kuwa mdogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi katika Igalula tunashukuru, tulikuja tukazungumza kwamba kuna maboma mengi wananchi wamejenga kwa nguvu zao yanatakiwa Serikali itenge fedha kuyakamilisha. Nataka kusema tumepekea milioni 500 kukamilisha ujenzi wa madarasa ya shule za misingi na shule za sekondari katika Jimbo la Igalula ambazo zilianzishwa na nguvu za wananchi. Kwa hiyo katika bajeti hii ya Waziri Mkuu, naomba nifikishe salamu za wananchi wa Igalula zile nguvu zao walizoziweka katika kujenga maboma yale Serikali imeona uwezekano wa kuwasaidia na imetuletea zaidi ya shilingi milioni 500. Ambacho tunakiomba, tuna maboma mengi zaidi, tunaomba tuendelee kuangaliwa ili tuweze kusaidia nguvu za wananchi ambazo wameziwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo pia kwenye eneo la afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, upo upungufu mchache ambao tunaomba Serikali iendelee kuuangalia ili wananchi wa Igalula waendelee kuwa juu kama vile ambavyo Serikali yetu ipo juu katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Katika Mkoa wetu wa Tabora tuna takribani kilomita 8,000 za barabara, lakini tunaletewa shilingi bilioni nane kutengeneza zile kilomita 8,000, hazitoshi, mtandao wa barabara ni mkubwa na fedha tunazoletewa ni ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Serikali iungalie Mkoa wetu wa Tabora, tuongezewe fedha ili ziweze kusaidia huu mtandao mkubwa wa barabara uliopo katika Mkoa wetu wa Tabora. Hata hivyo, nishauri katika eneo letu la kilimo, miaka yote tunashauri kilimo cha umwagiliaji ndio kitakuwa mkombozi wa wananchi wetu ambao wanalima huko vijijini, tusipowekeza katika kilimo cha umwagiliaji, hatutowasaidia wananchi wetu. Naomba Serikali iliangalie hili ili tuongeze tija katika kilimo, tuweze kupata pato la wananchi wetu na tuweze kupata pato la nchi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nataka niishukuru sana Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya, lakini niombe katika Mkoa wetu wa Tabora, Wilaya yetu ya Uyui ni Wilaya kubwa sana, DC wetu aangaliwe sana. Mwaka wa nne sasa hana gari na wilaya ni kubwa, anahitaji kufanya kazi ya ziada kusimamia miradi mingi ambayo inakuja katika Mkoa wetu wa Tabara. Niombe sana tuweze kuangalia namna ya kusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado inahitajika nguvu kubwa katika eneo la afya. Sisi katika Jimbo la Igalula tumejenga vituo zaidi ya vitano lakini tumepata fedha za kituo kimoja cha afya. Nina hakika katika bajeti hii inayokuja tutaendelea kuangalia nguvu hizi za wananchi na kuongeza fedha na zaidi ili ziweze kusaidia kuondoa tatizo la afya kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimalizie, kwa miradi ambayo inafanyika katika maeneo yetu, mimi nitoe mfano wa mwisho, katika barabara tumepokea zaidi ya bilioni mbili za barabara zetu za ndani katika Jimbo la Igalula, kwa nini tusiishukuru Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa ambayo inaifanya. Tumepata zaidi ya bilioni 149 za kujenga barabara ya lami ya Chaya - Nyahua ya kilomita 189 ambayo inakaribia kwisha, ni lazima tuendelee kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri ambayo inaifanya na tunazidi kuwapa moyo kwamba Wabunge wenu wa CCM tunaona kazi ambayo inafanyika na tunazidi kuwatia moyo kwamba wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Maji, Wizara Muhimu sana katika maisha ya wananchi wenzetu na sisi wenyewe hapa tulipo. Nianze kwa kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Waziri kaka yangu Mheshimiwa Profesa. Mbarawa, mdogo wangu Mheshimiwa Aweso na Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara pamoja na changamoto nyingi zilizopo za upatikanaji wa maji nchini, ikiwemo pia na changamoto ya kibajeti.

Mheshimiwa Spika, nami nianze kwa kushukuru kwa mradi wa maji wa Kijiji cha Igalula, nimeona imetengwa shilingi milioni 76 hapa za kwenda kumalizia kumlipa mkandarasi aliyefanya kazi katika Kijiji cha Igalula. Kwa kweli nashukuru sana Wizara kwa kazi kubwa iliyofanyika pale.

Mheshimiwa Spika, nina masikitiko, lakini mwishoni nitachangia. La kwanza, mradi wa Ziwa Victoria unakuja katika Mkoa wa Tabora, unakwenda katika Majimbo yote ya Mkoa wa Tabora kasoro Jimbo la Igalula. Hili nimekuwa nalisema sana na nimekuwa nikiahidiwa kwamba kuna miradi mingine mbadala itakuja lakini pia nimeahidiwa kwamba Jimbo la Igalula itaingizwa katika awamu ya pili ya mradi wa maji wa Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na subira hiyo, lakini pia Mheshimiwa Rais amekuja Igalula katika Kata ya Kigwa akaahidi kwamba maji ya Ziwa Victoria yatakuja. Nasikitika kwamba nimeona pia kuna mradi tena wa miji 29 na bado Jimbo la Igalula halijaangaliwa. Miji ambayo tayari inapelekewa maji ya Ziwa Victoria tena karibu na Jimbo langu imewekwa tena katika miji 29 kwenda kuwekewa miradi mingine ya maji.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Igalula nimejaribu kupitia sijaona mradi hata mmoja ambao unakuja kusaidia kutatua kero ya maji katika Jimbo la Igalula. Bado katika mgao wa fedha za Halmashauri kwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo yetu, ukiangalia Wilaya yetu ya Uyui, tuna Majimbo mawili; Tabora Kaskazini kwa Mheshimiwa Almasi Maige na Jimboni kwangu; tumepata fedha takribani shilingi milioni 500 tu, lakini kuna Majimbo ambayo yanapita maji ya Ziwa Victoria, yana Jimbo moja, wanapata zaidi ya shilingi milioni 800. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisemi kwamba yamefanyika makosa, lakini tuangalie, Jimbo la Igalula maji hayaendi, fedha tunazotengewa ni ndogo, miradi hii itatekelezwa namna gani? Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Tabora, Igalula tukamweleza, kuna vyanzo vya maji viwili vimepatikana katika Kata ya Loya na Tura. Usanifu umefanyika, namshukuru Katibu Mkuu alinisaidia; katika Kata ya Loya usanifu ulishafanyika, documents ziko Wizarani kwenu, lakini hakuna chochote kilichoandikwa katika kitabu cha bajeti kuhusiana na mradi wa maji wa Loya na kuhususiana na mradi wa maji wa Tura.

Mheshimiwa Spika, nataka nikwambie, tanki kubwa la maji linalopeleka maji Manispaa, linalopeleka maji Sikonge na Urambo linajengwa kilomita 15 toka Jimboni kwangu Igalula. Wananchi wanaona tenki linatengenezwa pale, maji Igalula hayaji, this is not fair at all. Wananchi wanasikitika lakini kabisa hatutendewi haki. Kilomita chini ya 15 tenki kubwa linajengwa lakini wananchi hawapati maji. Mheshimiwa Waziri, naomba hili tuliangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka pia nizungumzie mgawanyo wa fedha hizi ndogo ambazo nimejaribu kusema hapa; ukiangalia ukurasa wa 129, ukurasa wa 148, tazama na ukurasa wa 147, kuna maeneo wanafaidika na maji ya Ziwa Victoria yanakwenda. Miradi zaidi ya mitatu inazungumzwa katika kitabu hiki inakwenda Jimbo jirani na kwangu, wananchi wangu wanapata taarifa hizi. Inaonekana sisi hatufanyi kazi. Inaonekana wananchi wangu wamesahaulika kwenye suala la maji. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tuangalie maeneo ambayo yana matatizo ya maji tuweze kupeleka hizo fedha.

Mheshimiwa Spika, nami nizungumzie suala la kuongeza fedha katika Mfuko wa Maji ili miradi hii iende. Nimeanza kuzungumzia changamoto za Igalula kwa kifupi tu; lakini miaka yote mitatu tuko hapa, nimekuwa nazungumzia uwezekano wa Serikali kuongeza shilingi 50/= ili ziende kwenye Mfuko wa Maji ziweze kutusaidia sisi wenye matatizo ya maji katika maeneo yetu. Utamu wa ngoma uingie ucheze. Kwa sisi tunaotoka vijijini, unapozungumzia suala la maji, ukamwambia mwananchi eti tukiongeza shilingi 50/= kutakuwa kuna inflation, hawezi kukuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi effect za inflation kwa wananchi wetu wa Igalula na effect za kukosa maji, zipi tatizo ni kubwa sana kwa wananchi wetu? Kukosa maji ni tatizo kubwa sana. Ikiongezwa shilingi 50/= shida yake watakayopata wananchi wetu ni ndogo kuliko wananchi kuendelea kukosa maji kwa sababu eti ya shilingi 50/=. Kama alivyosema Mheshimiwa Chenge, nami nataka nimuunge mkono Mheshimiwa Chenge. Alichosema ndugu yetu Musukuma ni cha msingi, Mheshimiwa Waziri safisha Wizara yako, miradi inaonekana ina thamani kubwa haiishi, lakini haina manufaa kwa wananchi wetu. Kisima kimoja kinachimbwa kwa shilingi milioni 45, lakini utafiti tulioufanya kisima kinachimbwa kwa shilingi milioni 20 na wananchi wanaweza kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yapo matatizo katika Wizara, tunaomba Mheshimiwa Waziri asafishe Wizara yake ili hizi fedha tunazomwidhinishia hapa, ziende zikalete matokeo kwa wananchi wetu ambao wana matatizo makubwa sana. Pamoja na matatizo yaliyopo katika Wizara yake, sisi Wabunge kazi yetu ni kumpitishia fedha, kumpatia fedha ili miradi iende. Hatuwezi kuacha kumwongezea fedha eti kwa sababu kuna ubadhirifu katika Wizara yake. Wizara yake ikisafishwa, hizi fedha zikienda wananchi wetu watanufaika kwa njia moja au nyingine.

Mheshimiwa Spika, hili suala la kusafisha Wizara halihitaji kuchukua miezi miwili au mitatu. Tunajua Mheshimiwa Waziri amezianza juhudi, lakini zifanyike haraka sana ili mwisho wa siku hizi fedha tunazozipitisha hapa zikalete matokeo chanya kwa wananchi wetu na siyo kingine ni kupata maji kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaweza kuona hapa Wabunge wote watakaosimama, wanachokihitaji wao ni maji. Suala la kwamba unapata wapi fedha, tuachie sisi. Tutasimamia Azimio letu la shilingi 50/= ili uweze kuongezewa fedha za Mfuko wa Maji. Nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote, shida ya maji inatukuta sisi sote, kwa hili tusimamie Azimio letu, ule upungufu tumwachie Mheshimiwa Waziri akayafanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, hapa Jumatatu hakitaeleweka mpaka shilingi 50/= iongezwe. Wananchi wa Igalula wanataka maji, tunajua hatuwezi kuzungumza kupata maji bila kupata rasilimali fedha. Hii fedha tutasimamia aipate, lakini tukiipata maji yasipopatikana, sasa Mheshimiwa Waziri huo mzigo utakuwa ni wa kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nilitaka niseme hayo, lakini naomba Mheshimiwa Waziri aangalie mgao wa fedha unaokuja katika mikoa yetu, aangalie changamoto zilizopo. Kwa sababu Igalula tuna changamoto tofauti na Sikonge na maeneo mengine. Mgao wa fedha uje, miradi ambayo tumeshaifanyia usanifu iletewe fedha ili iweze kutusaidia kutekeleza miradi tuliyokuwa nayo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, lakini Jumatatu hakieleweki hapa mpaka shilingi 50/= iweze kupitishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia katika Mpango huu ambao umewasilishwa na Serikali.Kwanza kabisa niungane na wale wote ambao wametoa pongezi za dhati kabisa kwa Mawaziri hawa kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutengeneza Mpango mzuri, lakini Mpango huu ni mwendelezo wa mipango ambayo tumekuwa tunaizungumzia miaka yote toka tumeingia hapa Bungeni. Kwa kweli nataka niwapongeze sana, Mipango ambayo wanaileta inatekelezeka na tumeiona katika maeneo yetu mengi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia tulivyofika hapa tulisema tutarekebisha reli yetu ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Leo hii tunakwenda vizuri na tunakaribia kufika Dodoma. Sisi watu wa Tabora kama siku zote tunavyosema ni waathirika wakubwa sana wa reli hii ya kati kwa usafiri na usafirishaji wa mazao yetu, mfano, tumbaku, pamba na kadhalika. Kwahiyo, mpango unakwenda vizuri kwa kweli sisi tunapongeza sana kwa kazi nzuri inayofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia maeneo ya kufungua barabara zetu; mimi nina mfano mmoja; tulikuwa tuna mpango wa kuifungua barabara yetu ya Tabora – Itigi, kilikuwa kipande cha Chanya hajikamilika lakini leo zimetolewa zaidi ya bilioni 141, kipande kile kinakwenda kukamilika kwa asilimia zaidi ya 60 na wananchi watapata faida ya mipango mizuri tuliyokuwa tunaipanga huko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia katika eneo la maji; katika Ilani yetu tulisema kwamba tutamtua Mama ndoo kichwani lakini kwa mipango mizuri ya Serikali hii na mipango mizuri ambayo inaendelea kutekelezeka, Mkoa wetu wa Tabora sasa unapata maji ya Ziwa Victoria, tuna asilimia zaidi ya 70 mradi ule unakaribia kufika sasa Tabora. Ni mipango mizuri ambayo inatekelezwa na Serikali yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda na mimi nichangie kidogo pale ambapo wenzangu wamegusiagusia sana; ukiangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 14 inaeleza upatikanaji wa chakula. Ukichukua mwaka 2018/ 2019 ilikuwa asilimia 129, lakini mwaka 2019/2020 imekuja asilimia takribani 124 lakini sasa imekuwa asilimia 119. Ukiangalia uzalishaji wa chakula umepungua na ukiangalia upatikanaji wa chakula una athari kubwa sana katika uchumi wetu, unaathari kubwa sana kwa wananchi wetu na kadhalika. Kwahiyo ukiangalia kwamba kama chakula kinakuwa kinashuka, hapa tulishauri jambo moja; suala la kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji katika kilimo chetu ni jambo la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo mengi ambayo katika maeneo yetu yanaweza yakatengenezewa miundombinu ya umwagiliaji na kuongeza upatikanaji wa chakula. Nashauri; katika kitabu chote nimejaribu kuangalia, hatujazungumzia sana uwekezaji katika umwagiliaji na hakika maeneo yapo, tukiwekeza katika umwagiliaji upatikanaji wa chakula utakuwa mzuri na utakwenda kuleta athari nzuri kwa uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze eneo hili la TASAF kusaidia kaya maskini; nimeona zimetoka takribani bilioni 118 mwaka uliopita kusaidia kaya zile maskini. Nazungumzia hapa kwamba pamoja na kwamba tunawapa zile fedha kusaidia kusomesha watoto wetu na kupata mahitaji mbalimbali, ni jambo la msingi, lakini kule vijijini ili kumsaidia mtu ambaye ana kaya maskini ni kuwekeza vyema katika kilimo. Hizi fedha pamoja na kusomesha watoto wetu lakini wangetumia sehemu ya fedha hizi katika kufanya kilimo ambacho kimeboreshwa nina uhakika kabisa suala la chakula na hata huu mpango mzuri wa kusaida kaya maskini ungekuwa na maana zaidi na mwisho wa siku ungesaidia katika uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie pia katika eneo la upaitikanaji wa maji; kwa sasa Serikali kutokana na mipango mizuri tuliyoipanga huko nyuma, hali ya upatikanaji wa maji vijijini inaongezeka siku hadi siku na hali inazidi kuwa nzuri kwa sasa. Ilani yetu ilisema inataka kumtua mama ndoo kichwani, tunaelekea kutimia kwa asilimia kubwa sana katika maeneo yetu. Nimezungumzia upatikanajiwa maji ya Ziwa Victoria kutoka Mwanza kuja Mkoani Tabora, lakini kuna uchimbaji mkubwa wa visima katika maeneo yetu mbalimbali. Ninachotaka kushauri hapani nini? Maeneo mengi tumechimba visima havitoi maji ya kutosha baada ya muda mchache. Serikali inatumia fedha nyingi na upatikanaji wa maji baadhi ya maeneo hayo unakuwa siyo mzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kushauri hapa ni nini? Yako maeneo ambayo tunaweza tukatega maji kwa maana ya kujenga mabwawa ambayo yale mabwawa yakija yakijengewa miundombinu kwanza yatakuwa ni chanzo cha uhakika, lakini pili, itazuia upotevu wa fedha mkubwa ambao unapotea katika uchimbaji wa visima hivi katika maeneo mengi ya vijijini na hausaidii wananchi wetu. Tukijenga mabwawa na haya maeneo yapo, kwanza mabwawa haya yatakuwa yana uwezo wa kuhifadhi maji ya kutosha, gharama zake ndogo lakini yatasaidia maeneo mengi hata kwenye eneo la umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la miundombinu; mipango yetu pia ijielekeze kwenye miundombinu. Hapa nazungumzia miundombinu ya simu kwa maana ya mawasiliano lakini bado pia nataka nisemee suala la barabara. Unapozungumzia mawasiliano sasa hivi ni Benki unatembea nayo mkononi, ni kifaa kichokusaidia kufanya biashara zako kwa urahisi. Tukitengeneza mazingira ya kufanya wananchi wetu wakafanya biashara kwa urahisi kwasababu kutumia simu sasa unawezaukanunua bidhaa, unaweza ukatuma fedha, unaweza ukahifadhi fedha kwa usalama zaidi. Wananchi wetu wanaokaa vijijini Benki ziko mbali. Kwenda kutembea zaidi ya kilometa 100 kufuta benki wakati mwingine inakuwa ni gharama kubwa kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, wanapokuwa na simu siyo tu kwa mawasiliano, inawasaidia kufanya biasharazao kwa urahisi. Kwahiyo nishauri Mpango wetu uangalie pia katika kuboresha upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo yetu mbalimbali hasa vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo pia nataka nizungumzie barabara; unaporekebisha miundombinu ya barabara unasaidia hata kilimo chetu kupata soko kutoa mazao kule kijijini kupeleka kwenye soko, barabara zikiwa nzuri tunatumia gharama ndogo, mwisho wa siku tija inaonekana kwa mkulima na mwisho wa siku Serikali inaweza kupata mapato.TARURA wawezeshwe wapate bajeti ya kutosha.

Mheshimwa Mwenyekiti, nimalizie la mwisho kwenye eneo la afya; Ilani yetu inasema kila kijiji kiwe na zahanati, kila kata iwe na kituo cha afya. Tunakwenda vizuri kwa sasa, lakini nataka niiombe tu Serikali, mipango mizuri ya kujenga hospitali za wilaya sawa, lakini katika maeneo mengi bado vituo vya afya havijakamilika. Niombe mipango sasa ielekezwe katika kukamilisha baadhi ya maeneo ambayo hayana vituo vya afya ili kusaidia mrundikano utakaokuwa unakwenda kwenye hospitali zetu za Wilaya kwasababu rufaa ya zahanati unakwenda kwenye kata kwa maana ya kituo cha afya, ukitoka kwenye kituo cha afya unakwenda kwenye hospitali ya wilaya na ya mkoa. Sasa kwasababu ya kukosekana vituo vya afya katika baadhi ya maeneo, watu wanatoka kwenye zahanati wanakwenda kwenye hospitali za mikoa na kuzifanya zinashindwa kutoa huduma iliyo bora zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi tu nataka nipongeze kwa mipango mizuri inayotekelezeka ambayo tunakwenda nayo sasa kwa miaka minne inaonekana, Mheshimiwa Waziri wa Mipango hongera sana, Mheshimiwa Naibu Waziri hongera kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, naashukuru mimi Musa Rashid Ntimizi huyu Ahangazi wa Tanga huko. Nashukuru kwa kupata nafasi niweze kutao mchango wangu kidogo, katika hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa pongezi za dhati kwa hotuba nzuri na kazi nzuri ambazo zinafanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Nimpongee dada Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kuwa kiungo kizuri sana kati serikali na Bunge letu tukufu kwa kazi zuri ambazo zinafanyika pale. Waziri wa Uwekezaji, dada yangu Mheshimiwa Ikupa na mdogo wangu Mheshimiwa Mavunde kwa kazi nzuri ambazo anafanya kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kutekeleza majukumu yake mazuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba na mimi nichukue nafasi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Igalula kupongeza kazi nzuri ya Serikali hii ya Awamu ya Tano waliyoifanya katika kipindi chote na sasa wanaelekea kumaliza na sasa tunaelekea kumaliaz miaka mitano. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Rais amesimamia kauli zake, Mheshimiwa Rais amesimamia ahadi zake ambazo alituahidi wana Igalula ambacho kipindi chote ambacho amekuwa katika uongozi wake.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii fupi nikupongeze wewe na Bunge lako tukufu kwa kazi kubwa ambazo umezifanya mafanikio mazuri ya serikali yetu ya Awamu ya Tano yanatokana na kuungwa mkono na Bunge lako na kutekeleza na yanastahili kulifanya. Nakuongeza sana na pia nawapongeza Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia miradi iliyotekelezwa kimkakati katika nchi yetu katika kipindi cha miaka mitano, ikiwemo bwawa na ufuaji la umeme la Mwalimu Nyerere Mradi mkubwa wa Standard Gauge, mradi wa REA, ununuzi wa ndege sisi kwa tabora maji ya kutoka Ziwa Victoria, ujenzi wa wilaya na vituo vya afya, elimu bure na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, naomba hii miradi yote ambayo imezungumzwa hapa imeleta impart katika uchumi wetu na kuongeza ajira kubwa sana rasmi na zisizo rasmi kwa nchi yetu, watu wengi wanasema Serikali haitakangazi ajira lakini miradi hii katika utekelezaji wake kama alivyosema Mheshimiwa Waziri Mkuu imeleta ajira nyingi sana zilizo rasmi na zisizo rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nigusie miradi ambayo ni ya kimkakati aliyozungumzia Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kutoa ushauri ili iweze kuboresha huko tunakokwenda mbele. Nikianzia katika eneo la kilimo kwa haraka haraka pamoja na kwamba tunaporesha miundombinu yote hii yote ambayo tumeitaja ya reli, kutengeneza mradi wa umeme, REA na kadhalika inaenda ku-effect kwenye kilimo chetu. Lakini yapo mambo ambayo tunatakiwa tuyafanya ili kusaidia kilimo ambacho kinachangia wa asilimia 29 ya GDP ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia suala la miundombinu la umwagiliaji ni eneo ambalo hatujaliwekea msisitizo sana.

Niombe Wizara ya Kilimo iliangalie hili eneo ili tutakapoboresha miradi hii ya umwagiliaji itaenda kusaidia uchumi kama onavyoona eneo hili la kilimo linasaidia katika asimilia 29 katika GDP. Tukirekebisha miundombinu ya uwagiliaji na hakika tutaongeza upatikanaji wa chakula na mwisho wa siku wananchi wetu wakulima tutawasaidia.

Mheshimiwa Spika, lakini hapo hapo tuangalie masoko ya mazao yetu ya kimkakati ikiwepo Tumbaku, Kahawa, Korosho, na Pamba. Tuangalie bei ya mazao haya, tuangalie soko la mazao haya tuangalie upatikanaji wa pembejeo ya mazao haya hapa nazungumizia tupate mbolea kwa wakati mbolea ya kupandia ije wakati wa kupanda, mbolea ya kukuzia ije wakati wa kukuzia. Lakini pia tuongeze ruzuku kwenye mbolea ili kushusha bei ya mbolea iweze kumsaidia mkulima. Lakini vile vile usimamizi wa vyama vya msingi ushirika ili mwisho wa siku mkulima aweze kupata tija.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la miundombinu ya barabara, unapozungumzia ukuaji wa kilimo unazungumizia masoko yake unazungumzia na bei yake. Kama barabara zetu za kijiji hazipitiki mwisho wa siku bei ya mazao haya bei inakuwa ndogo au itakuwa kubwa mwisho wa siku mkulima hatopata faidi. Gharama za usafirishaji zitaongeza na mwisho wa siku hata mazao yanaweza fika sokoni yakiwa yameharibika. Niombe tuiongezee TARURA uwezo wa kifedha ili mwisho wa siku tuweze kutengeneza barabara hizi zisaidie mkulima huko kijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba naomba kidogo nizungumzie kidogo REA, REA inafanya vizuri nipongeze kwa kazi nzuri inayofanyika. Maeneo yetu ni makubwa changamoto zake ni nyingi lakini wanajitahidi wanafika maeneo mengi kwa hili kabisa naomba nitoe shukrani za dhati kwa miradi ya rea inayofanyika. Lakini ninachotaka ni shauri hapa zipo changamoto ndogo ndogo. Vipo baadhi ya vijiji ambavyo vinarukwa, vipo baadhi ya vitongoji ambavyo vinarukwa basi haya mapungufu yaweze kufanyiwa kazi, na serikali iweze kutoa fedha kwa REA kutekeleza miradi yake.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la afya nipongeze kazi kubwa ya ujenzi wa hospitali za wilaya nipongeze kazi kubwa ya ujenzi wa vituo vya afya, nipongeze kazi kubwa inayofanya ya kuleta madawa n.k. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili eneo nataka nishauri kitu kimoja tusisahau ujenzi wa zahanati, wananchi wamechangia kujenga zahanati lakini mwisho wa siku hatujawasidia vya kutosha. Rufaa yakutoka zahanati inaenda kituo cha afya, kituo cha afya inayo hospitali ya wilaya then hospitali ya mkoa. Tusiporekebisha huku kwenye zahanati tunakapatikana zahanati za kutosha na huduma zikawa nzuri tutakuwa tuna mapungufu kidogo katika utoaji wa huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengine nitazungumza kwenye sekta husika lakini nataka nimalizie moja, la watendaji wetu wa vijiji na kata. Hawa ndio wasimamizi wakubwa wa maeneo yetu ya maendeleo katika maeneo ya vijiji. Nilikuwa nashauri la kwanza tuwatafutie usafiri wa ukakika wa kufanya shughuli zao ikiwe hata pikipiki. Lakini na pili watendaji wa vijiji wanajenga nyumba za waganga lakini wao hawana nyumba za kuishi. Watendaji wa kata wanajenga nyumba za waganga lakini wao hawana nyumba za kuishi. Tujenge nyumba za watendaji hawa tuwapatie usafiri mwisho siku wasimamie vizuri miradi katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka nichangie hayo naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Reli wa Mwaka 2017
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kidogo katika Muswada huu wa Reli.

Kwanza kabisa binafsi nina furaha leo kuiona Serikali imepokea mawazo na ushauri wetu tuliokuwa tunatoa siku nyingi kuhusiana na kuunganisha RAHCO na TRL. Tulikuwa tunatoa mawazo hayo kwa sababu tulikuwa tunahitaji tupate shirika ambalo litaisaidia nchi na litasaidia wananchi wetu katika kupata huduma za usafiri. Leo tunashuhudia
Serikali imekubali wazo letu na sasa tunaelekea kuyaunganisha mashirika mawili ya TRL na RAHCO kuunda shirika jipya la TRC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya watu wanasema tunarudi kule kule lakini kwa muswada ulivyo, tunaunda shirika jipya la TRC baada ya kuunganisha TRL na RAHCO. Naunga mkono muswada huu kwa asilimia mia moja, lakini mimi pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu. Tumeishauri Serikali kwa kiwango kikubwa sana lakini yapo ambayo pia ningeongezea kama mchango kwa niaba ya wananchi wa Igalula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema tunaunda sasa Shirika la TRC lakini pia Serikali yetu sasa iko katika mkakati mkubwa wa kujenga reli ya standard gauge kuanzia Dar es Salaam kuelekea Tabora. Na mimi kabla sijafika mbali niungane na wazo la Mheshimiwa Hussein Bashe la kuangalia faida ya standard gauge kuipeleka Kigoma kabla ya kuipeleka Mwanza, kiuchumi itatusaidia zaidi kuliko hili wazo la sasa la kuipeleka kwanza Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, reli inapoboreshwa, tutakapojengewa standard gauge sisi kama nchi tutapata faida kwa maana ya kwanza tutasafirisha mizigo yetu mingi na mizito kupitia reli yetu. Tutatunza barabara zetu ambazo tunatumia gharama kubwa sana kuzijenga kwa kodi ya wananchi, nina hakika kabisa tukiitengeneza reli ikawa bora ikasafirisha mizigo mingi hela zile tunazotengeneza barabara zitaenda kwenye maeneo mengine ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tutachangia Pato la Taifa, Tutasafirisha mizigo mingi, maana yake sasa Serikali itapata kodi nyingi, itapata pesa nyingi shirika letu la reli sasa litaweza kuchangia katika Pato la Taifa badala ya sasa Shirika la Reli linaendeshwa na ruzuku kutoka Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Igalula reli ni usafiri tunaoutegemea sana. Kata ya Tura, Kizengi, Kata ya
Goweko na Kata ya Igalula kwa asilimia mia moja wanategemea usafiri wa reli. Kuimarika kwa shirika hili kutasaidia usafiri wa mazao yao, kutasafirisha asali yao, kutasafirisha wananchi wao na vilevile kupunguza shida kubwa ya usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada unaanzisha Shirika jipya la TRC na Bodi ya Wakurugenzi, kifungu namba nne cha muswada, tunaitaka bodi sasa iwe na muono wa kibiashara wa shirika hili. Tuondokane na kule ambako tulikuwa tunaliendesha shirika hili kama kutoa huduma ya usafiri tu, lakini sasa shirika na bodi inayoundwa ikaangalie namna ya shirika hili kujiendesha kibiashara. Tuondokane na mazoea. Shirika hili lilivyokuwa mwanzo lilikuwa linaendeshwa kwa mazoea, lakini sasa tunataka kwa sababu tunaanzisha shirika jipya, liwe jipya sio kwa kubadilisha jina lakini liwe jipya kwa huduma zitakazotolewa, tuwe na mabehewa ya kutosha ya kusafirisha mizigo na abiria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani kulikuwa na wizi mkubwa wa mafuta na vipuri udhibitiwe, pia huduma za ndani ya treni zilikuwa haziridhishi. Mabehewa mengine yalikuwa mpaka yana kunguni na chawa ndani. Hatuwezi kufanya biashara kwa mazoea. Vilevile tuboreshe mtandao wa reli, reli ilikuwa inapata ajali mara kwa mara kwa sababu mtandao wa reli ulikuwa umeshachoka kwa kiasi kikubwa sana. Pia tujali muda, muda wa safari treli mara nyingi ukikata tiketi, unaweza ukakata tiketi kuondoka saa 12 lakini ukakaa stesheni mpaka saa 12 kesho yake safari bado haijaanza. Tunaomba sasa shirika hili linalokuja liangalie yote haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotaka kuanzisha shirika hili jipya tuangalie maslahi ya wafanyakazi wetu. Tuliingia mgogoro mkubwa sana wakati tunaanzisha RITES na RAHCO, wafanyakazi wakaenda Mahakamani wanadai haki zao. Kudai haki zao wafanyakazi wetu wana nafasi ya kuhujumu shirika kwa namna moja au nyingine. Mimi nashauri wakati tunaanzisha mchakato huu maslahi ya wafanyakazi yashughulikiwe kwanza, walipwe madai yao kwanza ndiyo sasa tuhame a fresh kwenye shirika jipya la TRC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu namba tano cha Muswada kinazungumzia majukumu ya shirika. Kinazungumzia uendeshaji wa reli ndani ya mtandao na miundombinu yake. Kuhakikisha ulinzi na usalama wa mazingira ya reli. Hapa nataka nisemee suala ambalo Wabunge wamelisemea sana, kuhusiana na bomoabomoa sasa. Kama shirika hili lingeendelea kutunza mipaka na maeneo yake kwa muda mrefu, haya matatizo ambayo tumeingia sasa yasingekuweko. Wananchi wamejenga kwa zaidi ya miaka 40 katika maeneo haya, leo wanakuja kuambiwa wanavunjiwa. Shirika lilikuwa wapi? Mamlaka zilikuwa wapi? Lakini tunachokiomba sasa wananchi wetu wanataka standard gauge, wanataka reli iliyo bora. Wale waliokuwa katika zile mita za reli wako radhi kuondoka, lakini kuna mgogoro mkubwa wa wananchi wetu ambao walijenga yanayosemekana ni maeneo ya reli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba wananchi hawa Serikali iwaangalie na ikiwezekana mamlaka zilizohusika katika kufanya haya waweze kuchukuliwa hatua ili wananchi wetu waweze kupata haki yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.