Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka (38 total)

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mamlaka ya Maji ya Tabora Mjini (TUWASA) ina matatizo makubwa ya malimbikizo ya madeni zaidi ya bilioni mbili ambayo inawadai Taasisi za Serikali na hasa majeshi yetu na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema katika majibu yake ya msingi kuna pesa zimetengwa kulipa katika miradi mbalimbali. Je, ni lini Mamlaka ya Maji Tabora watalipwa pesa zao ambazo zinawafanya sasa wasifanye kazi kwa ufanisi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, madeni ya maji ambayo Taasisi za Serikali zinadaiwa katika mwaka wa fedha zitalipwa moja kwa moja kwenye Fungu la Hazina. Kwa hiyo, tutakapoanza kutekeleza Bajeti hii ambayo mmeipitisha tutaangalia tuweze ku-manage fedha zile, tuweze kulipa kwenye mamlaka husika ili waweze kuendelea kutoa huduma za maji.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Pamoja na majibu mazuri ya Waziri, ninaomba kumuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa kwenye bajeti ya Serikali mwaka huu moja ya vitu vilivyoainishwa mle ni pamoja na kufanya review ya mikataba mingi kwa hawa waliobinafsishiwa viwanda. Sasa ni lini Serikali itafanya review ya kujua uwezo wa huyo mwekezaji kuhusu kuwekeza Tabora Mjini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna tuhuma zinazomuhusu mwekezaji huyo wa kiwanda cha Nyuzi kwamba kuna mashine mbalimbali ambazo aliziuza kama vyuma chakavu, ambazo zilikuwa mle kwenye kiwanda na kwamba kuna mashine nyingine ambazo tayari zilishasafirishwa, hazipo kabisa pale;
Je, ni lini Serikali itafanya ukaguzi ili kujiridhisha kwamba mwekezaji yule kweli hajaziuza mashine hizo au kuzihamisha nje ya nchi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu review, sina sababu ya kukuficha, review ilishaanza kuhusu Tabotex, nimeshakwenda kumuona hata aliyekuwa Meneja, ambaye sasa hivi ni Meneja Mwatex. Aliyekuwa Meneja wa kiwanda hiki sasa yuko Mwatex Mwanza, nimemfuata nikamuhoji. Ngoja nikueleze, kuna mambo mengine anapoteza muda, kuna majibu amenipa anapoteza muda na iko kwa Msajili wa Hazina na atamshughulikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu namba mbili, kwamba kuna mashine zimeuzwa, ile tathmini nzima ndiyo itakuja kuhitimisha kwamba alipotoa mashine hii na kuleta mashine nyingine aliitoa kwa misingi gani. Niwaeleze ukweli ambao nimeushuhudia, mitambo ya viwanda vyetu vya nguo, viwanda vingine vilikuwa na mitambo ya mwaka 1963, kwa hiyo mwekezaji makini anapoingia ile mitambo ya mwaka 1963 ataiondoa. Nimeona mashine moja imeagizwa kutoka Swiss, kwenye kiwanda kimojawapo, mashine moja ina uwezo wa kufanya kazi kuliko mitambo 10 ya zamani ukiunganisha. Kama amefanya kwa nia hiyo tutamhukumu kwa alivyotekeleza, lakini kama nilivyosema maslahi yetu ni kwamba kiwanda kifanye kazi, kitoe ajira, kizalishe bidha na hatimaye alipe kodi, akitimiza hayo sina tatizo naye.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa mazungumzo na hawa wawekezaji mahiri wa kusindika tumbaku na mambo ya sigara yanaendelea. Je, mazungumzo hayo yakifanikiwa, ana uthibitishia Mkoa wa Tabora kwamba utapata upendeleo kwa kujengwa Kiwanda cha Tumbaku? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameonesha nia ya Serikali kuwashirikisha mashirika ya kijamii kama NSSF kushiriki kwenye ujenzi wa viwanda na biashara, je, ni lini mazungumzo hayo, Serikali itaanza na haya mashirika ya kijamii?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ujenzi wa Kiwanda cha Tumbaku Tabora ni la wadau wa Tabora ambao walikaa pamoja na ninyi Wabunge. Nimewaeleza kwamba tunahangaika kutafuta wawekezaji, siku ya Jumapili mwekezaji kutoka China atafika Tabora. Kwa hiyo, Wabunge wa Tabora tukimaliza kikao tukutane kusudi ninyi mtangulie kumpokea Jumamosi halafu tujadiliane. Masharti ni yale yale, kama mtatoa eneo bila kuweka vikwazo vya fidia za ajabu mtapata upendeleo, hali ndivyo ilivyo, utakavyotoa vivutio utapata upendeleo. Ujumbe wa China unakwenda Tabora na Precision Jumapili, tangulieni, Jumamosi tukakutane kule tuweze kuwakaribisha wawekezaji. Kwa hiyo, Tabora nimewafanyia kazi, ni jukumu langu pia ni jukumu lenu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, uwekezaji wa hizi Social Securities, maelekezo ya Mheshimiwa Rais nimeyasikia, nilichofanya nimemwagiza Katibu Mkuu anayeshughulikia biashara na uwekezaji Wizarani kwangu, akutane na Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kazi inayosimamia haya mashirika, akutane na Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo, wote wakae, wabainishe ni wapi kwenye shughuli zenye tija ambako hizi Social Securities zinaweza kuwekeza na kuweza kurudisha pato lake. Kwa hiyo ,watalaam watafanya kazi hiyo na nimewaambia kabla ya tarehe 26 waniletee orodha na nitaitangaza hapa Bungeni kwako.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, tatizo linalowakabili wananchi wa Maswa Magharibi kuhusu bwawa lao, linafanana kabisa na tatizo la bwawa la Kazima Mjini Tabora ambalo maji yake yanapungua mara kwa mara hasa wakati wa kiangazi, kutokana na tope pamoja na mchanga uliojaa pale. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha lile tope pamoja na mchanga linaweza kuondolewa ili wananchi wa maeneo yale waweze kupata maji ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri bwawa la Kazima nimelitembelea ni bwawa kubwa na kweli nimelikuta lina matatizo. Moja, kipindi cha kiangazi kutokana na miti mingi iliyoko kwenye lile bwawa maji yanabadilika rangi, lakini pia bwawa lile linajaa tope kutokana na shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumeshaongea na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji wa Tabora, kuhakikisha kwamba tunashirikisha jamii. Nimwombe pia Mheshimiwa Mwakasaka, shida kubwa inayojitokeza ni kwamba wananchi wanalima sehemu ambayo maji yanatoka; baada ya kulima mvua zikinyesha zinabeba zile tope kuleta kwenye bwawa. Kwa hiyo, suala la msingi ni kwamba kwa kushirikiana na Halmashauri, tujaribu kuhakikisha kwamba tunaacha eneo la kutosha kuja kwenye bwawa, wananchi wasifanye shughuli za kilimo pamoja na ufugaji ili tuweze kulilinda bwawa letu lisijae mchanga.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wakulima wa tumbaku wamekuwa wakikopwa na pesa zao zinachukua muda mrefu sana kuja kulipwa, Serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia wananchi hawa wanaolima tumbaku hasa Mkoa wa Tabora kuhakikisha kwamba wanalipwa pesa yao na riba kama wanavyofanya mabenki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa utaratibu wa tumbaku kuchukuliwa na baadaye ndipo wakulima hulipwa kumesababisha matatizo makubwa sana na ndicho hasa chanzo cha kurundikana kwa madeni mengi ya wakulima kutoka kwenye Vyama vya Ushirika. Tunafahamu kwamba mfumo mzima wa ushirika siyo kwenye tumbaku tu lakini katika mazao mengi una changamoto na ndiyo maana Bunge hili lilifanya uamuzi mzuri sana wa kuleta Sheria mpya ya Tumbaku, Sheria Na.6, 2013 ili kuondokana na changamoto hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kuimarisha ushirika ili isitokee tena kwamba wakulima wanachukuliwa tumbaku yao na wanakaa miaka mingi bila kulipwa. Kwa hiyo, tunaamini kwamba kwa mfumo huu wa ushirika ambao tunauleta sasa haitawezekana tena wananchi kukopwa lakini tunahakikisha kwamba tumbaku ya wananchi inakuwa inalipwa moja kwa moja. Badala ya kuchukua kwanza na kulipa baadaye ni kwamba tutakuwa tunatumia mfumo kama ule wa korosho ambapo tumbaku ikishakusanywa kwenye Vyama vya Msingi wanunuzi wanakuja kununua pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafahamu changamoto hii, inafanyiwa kazi na tunaamini katika mfumo uliokuja wa Vyama vya Ushirika utarekebisha matatizo makubwa ambayo yametokea. Vilevile sheria hii imeweka mazingira mazuri sana ya kuwabana na kuwafikisha katika vyombo vya sheria si tu wafanyakazi wa Vyama vya Ushirika lakini vilevile hata Maafisa Ushirika ambao wanashirikiana katika kuwahujumu wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilieleze tu Bunge lako Tukufu kwamba changamoto kubwa iliyoletwa na mfumo wa ushirika ambao tunauondoa ni kwamba kumejengeka utatu usio mtakatifu kati ya viongozi wa Vyama vya Ushirika, mabenki na watendaji wa Serikali. Kwa hiyo, tunahakikisha kwamba utatu huu ambao umeleta matatizo kwa wananchi unavunjwa ili wananchi waweze kupata haki yao na kusiendelee kutokea changamoto katika zao la tumbaku.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Raphael Michael, Mbunge wa Moshi Mjini ametoka nje, naomba nitumie nafasi hii kwa sababu swali alilouliza linafanana kabisa na suala ambalo liko Tabora katika Hospitali yetu ya Mkoa ya Kitete, naomba niulize swali kwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Hospitali yetu ya Mkoa wa Tabora ya Kitete ina tatizo lile lile la mlundikano wa wagonjwa kama ambavyo iko Moshi Mjini. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Hospitali ya Wilaya inajengwa Tabora ili kuweza kupunguza huu mlundikano wa wagonjwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete ina upungufu mkubwa sana wa Madaktari, tuna Daktari Bingwa mmoja tu. Serikali inajipanga vipi kuhakikisha Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete inapata Madaktari Bingwa wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanasema hata katika mpira vilevile, ikitokea mpira unapigwa golini halafu mtu kaondoka wewe piga goli tu. Kwa hiyo, naomba nimpongeze kwa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Tabora ya Kitete aliyoizungumzia kwamba kwa sababu changamoto ni nyingi tuna mpango gani wa kuanzisha Hospitali ya Wilaya. Katika hili naomba nielekeze, tuweke vipaumbele katika Manispaa zetu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Serikali iko tayari kabisa kushirikiana na wananchi wa Tabora ili kuhakikisha wananchi wa Tabora wanapata afya njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, napenda kuwashukuru wana Tabora kwa ujumla wao, kwa sababu nilipopita kule Tabora nimeona shughuli mbalimbali za kusimamia miradi. Nilitembelea Kituo cha Afya cha Itobo na kile kingine cha Bukene nimeona vifaa vya upasuaji vimewekwa kwa ajili ya akinamama. Kwa hiyo, juhudi zile wakati tukifanya mpango wa pamoja sasa kuimarisha Mkoa wa Tabora, kwa sababu tukiangalia sehemu ile hata watu kutoka Kigoma watakaopata matatizo wanaweza wakaja pale, ni vema kabisa tukaendelea kuweka nguvu. Katika mpango wetu mkakati wa Serikali kuimarisha Hospitali za Mikoa kupitia ule mradi mkubwa, nadhani tutaelekezana hapo baadaye jinsi gani tutafanya na Tabora ipewe kipaumbele kikubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la watumishi kwamba hatuna Madaktari Bingwa, bahati nzuri katika mchakato tutakaoufanya ni pamoja na kuhakikisha Madaktari Bingwa wanafika katika kanda mbalimbali. Imeonekana mara nyingi sana Madaktari Bingwa wanaishia katika maeneo ya miji mikubwa sana hasa Dar es Salaam. Katika maeneo ya pembezoni Madaktari Bingwa hasa madaktari wa magonjwa ya akinamama (gyno) wanakosekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili nililigundua hata nilipofika katika Mkoa wa Singida, kuna hospitali nzuri lakini Madaktari Bingwa wamekosekana na hata nilivyofika Songea jambo hili nililiona. Mpango wetu ni kwamba kupitia Wizara ya Afya vilevile tutafanya mkakati sasa kuweka mipango vizuri ili Madaktari Bingwa waweze kufika maeneo mbalimbali ikiwemo na Tabora, lengo kubwa wananchi wetu wapate huduma bora.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI, napenda kumthibitishia Mheshimiwa Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini kwamba, Tabora ni mojawapo ya mikoa tisa ambayo Wizara ya Afya imeifanyia tathmini kwamba inayo uhaba mkubwa wa Madaktari Bingwa pamoja na Mikoa ya Kigoma, Mara, Katavi, Rukwa na Simiyu. Kwa hiyo, tutakapopanga Madaktari kwa mwaka huu wa fedha, tutatoa kipaumbele kwa Mkoa wa Tabora na mikoa mingine nane.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe Madaktari wote na wataalamu wa afya ambao mnatarajia kuomba kazi Serikalini kwamba tutawapanga katika mikoa hiyo tisa ndiyo kipaumbele chetu. Kwa hiyo, kama wanataka kukaa Dar es Salaam wajue hatutachukua daktari ambaye anataka kukaa Dar es Salaam. Nakushukuru.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kutokana na msongamano huo wa magereza na mahabusu ambao hata Mheshimiwa Waziri ameukiri hapa, kunasababisha magonjwa mengi hasa ya mlipuko; nimewahi kutembelea Gereza la Uyui pale Tabora, kulikuwa na wagonjwa wengi wa upele; na sasa hivi kuna tatizo kubwa sana la upatikanaji wa madawa sijui Serikali ina mkakati gani wa kufanya upendeleo kuhakikisha wale mahabusu na wale ambao ni wafungwa wanapata dawa za kutosha?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge Mwakasaka amefuatilia mara nyingi sana jambo hili na hata kuna kipindi tumekaa, yeye pamoja na wenzangu wa Wizara ya Afya. Jambo lake tulishalipokea, kadri mtiririko wa fedha unavyokuja tutalifanyia kazi kwa sababu ni jambo ambalo alishalifuatilia hata kwa ngazi ya Wizara na tulimuahidi kwamba tunalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, naomba uendelee kuvuta subira na niwapongeze wana Tabora kwa kukuamini kwa sababu kwa kweli umeendelea kulifuatilia hilo pamoja na mambo ya uhalifu ambao mara nyingi mmekuwa mkiusemea na sisi tunachukua hatua.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo lililopo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, linafanana kabisa na tatizo ambalo lipo kwenye Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Rufaa ya Kitete. Kuna tatizo kubwa sana la wagonjwa na hasa akinamama wanapoenda kujifungua, wodi ile ni ndogo na wengi wanalala chini wakiwa hata wale wachache wanakuwa wana-share kitanda kimoja:-
Je, Serikali inajipanga vipi kutatua hili tatizo la muda mrefu la msongamano wa akinamama wanapojifungua pale Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Hospitali ya Kitete pale Tabora ina changamoto kubwa na ndiyo maana ukifanya rejea ya majibu yangu mbalimbali niliyoyatoa hapa Bungeni, tumesema kwamba catchment area ya Mkoa wa Tabora, ukubwa wake na jiografia yake ilivyo ina kila sababu tuweke nguvu. Ndiyo maana katika bajeti ya mwaka huu sitaki kutaja figure hapa exactly, tuna fungu ambalo tumelitenga kwa ajili ya suala zima la ukarabati pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaangalia ni kipi kilichotengwa katika mwaka huu. Lengo ni kwamba ile fedha ipatikane tu ikafanye kazi na value for money ionekane. Naamini ule ukarabati utaanza mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nikuhakikishie kwamba katika majibu yangu ambayo nayakukumbuka hapa Bungeni niliyoyatoa ni suala zima la Hospitali ya Kitete; naomba tuwasiliane kwa karibu zaidi ili tujue ni fungu kiasi gani limetengwa, lakini tuhimize sasa ile fedha ili iweze kufanya kazi vizuri.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mkoa wa Tabora hususani Tabora Mjini tuna mabwawa makubwa mawili, Bwawa la Igombe na Bwawa la Kazima, pia tuna mradi wa bwawa ambalo lipo Kata ya Ndevelwa ambalo limeigharimu Serikali zaidi ya shilingi bilioni moja ambalo mpaka sasa hivi halifanyi kazi kwa sababu linavuja.
Mheshimiwa Spika, sijui Serikali ina mkakati gani wa kufanya mradi huu ambao kwanza umekwama, lakini pamoja na haya mabwawa mengine yaweze kutumika katika kilimo cha umwagiliaji ili wananchi kwa ujumla waweze kupata ajira pamoja na kuweza kupata mazao kwa ajili ya kujikimu kutokana na hali mbaya ya chakula ambayo inaikabili nchi yetu kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, mabwawa mawili ya Igombe na Kazima yanatumika kwa ajili ya maji ya matumizi ya binadamu na Bwawa la Igombe limeshaboreshwa tayari lina maji ya kutosha, sasa kuangalia uwezekano kwamba yanaweza yakatumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji basi tunalichukua tuweze kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu bwawa hili ambalo limebomoka, hili kwa sasa tayari tumejikita kuhakiksha kwamba mabwawa yote ya zamani yanaboreshwa ili yaweze kufanya kazi zilizotarajiwa.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa
kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu
Waziri, nauliza swali ambalo kama ilivyo Rungwe ule mradi wa Masoko, Tabora
Mjini ule mradi wa Ziwa Victoria, kuna vijiji ambavyo niliviorodhesha kwenye swali
Na. 57 lililojibiwa hapa Bungeni ambavyo ni Vijiji vya Itetemla, Uyui, Ntalikwa,
Kabila, Mtendeni, Itonjanda na baadhi ya maeneo ambayo ni ya Kata za Tumbi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji hivi na hizi Kata havijaorodheshwa kwenye
huu mradi wa Ziwa Victoria na vina shida sana ya maji. Sijui vitapitiwa lini na
mradi huu wa Ziwa Victoria? Naomba swali langu lipatiwe majibu. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,
kwanza kabisa Tabora Mjini kuna mradi mkubwa wa maji ambao umekamilika
kutoka bwawa la Igombe na kwamba maji yanayozalishwa ni lita milioni 30 kwa
siku wakati mahitaji ni lita milioni 24. Kwa hiyo, kwa maana ya Tabora Mjini tayari
imeshakamilisha huduma maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tupo na mradi ambao sasa hivi upo kwenye
zabuni ambao utatoa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Nzega, Tabora na Igunga. Kwa hiyo, nina hakika kabisa kwamba sasa Tabora itakuwa na maji
mengi na ndiyo maana tunataka hayo maji yakishafika tuyaelekeze yaende
mpaka eneo la Sikonge. Kwa hiyo, Vijiji vyote Mheshimiwa Mbunge ambavyo
havina maji nje ya Manispaa ya Tabora kupitia mradi huo tutakuwa na maji ya
uhakika kuhakikisha sasa kata na vijiji vyote vinapata maji ikiwemo na sehemu ya
eneo la Uyui.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kwa kuwa huu mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria unaonekana unaendelea kusuasua na hauna uhakika exactly lini utaanza na wananchi wa Tabora wanaendelea kuteseka kwa shida ya maji na sisi pale Tabora Mjini tuna bwawa kubwa la Igombe ambalo lina-access ya maji kwa maana ya lita za ujazo ambazo Serikali kama itaweka mpango mkakati wa kusambaza maji yale ya Igombe na kwa unafuu, Wananchi wa Tabora Mjini watapata nafuu ya tatizo la maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba yale maji ya Igombe yaweze kusambazwa kwa bei nafuu kuliko kusubiri huo mradi wa Ziwa victoria ambao haujulikani utaanza lini? Hilo la kwanza
Swali la pili, moja ya tatizo lingine linalosababisha ile Mamlaka ya Maji (TUWASA) Tabora inapata matatizo katika uendeshaji wake ni pamoja na kutolipa deni ambalo Mamlaka ya Uendeshaji ya Maji - TUWASA pale Tabora inaidai Serikali kwa muda mrefu zaidi ya shilingi bilioni 2.3 ambazo zinadaiwa hasa kwenye taasisi zetu za majeshi pamoja na taasisi zingine za Serikali.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha TUWASAwanalipwa pesa hizo ili Tabora iweze kupata maji ambayo yatakuwa ni ya uhakika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka tuweke kumbukumbu sawa. Katika mradi huu wa Tabora-Sikonge ambao katika bajeti yetu mwaka huu nadhani tulipitisha pamoja hapa. Tulitenga takribani shilingi bilioni 29 ukiangalia kitabu cha maendeleo lakini kwa juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali kupitia ufadhili kutoka India ndiyo maana nimesema ile figure zaidi ya shilingi bilioni 500 ambayo Serikali imeshaweka commitment hiyo. Hivi sasa mchakato wa manunuzi upo katika hatua mbalimbali na lengo la mradi huu kati ya mwezi Aprili mpaka mwezi Mei mradi huu utakuwa umeanza, kwa hiyo, ndugu yangu, mtani wangu, Mnyamwezi wa Tabora naomba ondoa hofu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala zima la jinsi gani tutumie bwawa la Igombe, wataalam wetu wameshaanza kufanya tathmini pale. Takribani ule mradi utagharimu shilingi bilioni 1.5 na hili ndiyo maana tumeona kwamba jambo hili kama Ofisi ya Rais - TAMISEMI lakini na kushirikiana na wenzetu ambao ni Wizara mama wa Wizara hiyo tutaangalia jinsi gani tutafanya kwa pamoja katika mchakato wa pamoja wakati tunasubiri mradi mkubwa wa maji wa hizo shilingi bilioni 500, jinsi gani tutafanya hizo back up strategy ya mradi mwingine huu mdogo katika bwawa la Igombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo lengo letu kama Serikali ni kuweza kutatua shida ya maji katika Mkoa wa Tabora na ndiyo maana nimesema mradi huu siyo Tabora peke yake, kuna watu wa Tinde pale, kuna watu wa Kahama, kuna watu wa Shinyanga mradi huu utakuja kujibu matatizo ya watu wote wa ukanda ule. Niseme, Wasukuma na Wanyamwezi wa eneo hilo mmepata bahati kubwa sana kwa Serikali kuwaona kwa jicho la karibu kuwatengea takribani shilingi bilioni 580.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo, suala zima la bili ya maji; suala la bili ya maji ni kwamba tumetoa maelekezo mbalimbali hapa kwamba bili ya maji kupitia Waziri wa Maji ameshatoa maelezo mbalimbali, sasa naomba niziase taasisi mbalimbali; kila taasisi inayodaiwa deni la maji liweze kulipa deni la maji siyo Tabora peke yake lakini katika maeneo yote ya nchi hii, kama taasisi inayodaiwa na maji, miradi hii ya maji au hizi mamlaka za maji zitashindwa kutupatia maji kwasababu watu wanashindwa kulipa bili za maji.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa hii biashara ya vyuma chakavu inavikumba pia viwanda vilivyobinafsishwa kwa muda mrefu sasa kikiwemo Kiwanda cha Nyuzi Tabora, na kwa kuwa kuna taarifa kwamba mashine nyingi mle ndani zimeuzwa kama chuma chakavu na kimefungwa kile kiwanda, je, Mheshimiwa Waziri, kwa sababu nimewahi kulalamika hapa Bungeni na kutoa taarifa kuhusu kufanyika kwa vyuma
chakavu, ni lini tunaweza tukaenda tukakagua kile kiwanda kwa sababu sasa hivi umetoka kusema utakula nao sahani moja, tuweze kujua kama vile zile mashine hazijauzwa kama vyuma chakavu?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora kina mwenye nacho (owner) kwa hiyo, mwenye mali anapoibiwa mimi siwezi kwenda kuangalia mali yake yule, lakini taarifa nilizonazo kutoka kwa mwenye kiwanda ameniambia amepata soko la nyuzi na kiwanda hicho kitaanza kazi. Kwa hiyo, mimi naweza kumbana yule kwa kupitia msajili wa hazina kwamba aanze kazi na ndio wajibu wangu. Sasa kama alizembea, mali ikaibiwa mle hilo nadhani ni suala la kila abiria achunge mzigo wake.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongezana ninaomba kuiuliza Serikali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba hii migogoro kweli ipo na ni ya muda mrefu, Jimbo la Tabora Mjini linazungukwa na kambi nyingi za Jeshi ambazo migogoro mingi inapelekea kuhatarisha amani miongoni mwa wanajeshi pamoja na raia. Ni lini sasa Serikali au Serikali ina mpango gani wa kuwakutanisha wanajeshi wahusika ili waweze kukaa na wananchi kuweza kutatua migogoro hiyo ya ardhi iliypo Tabora Mjini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali inafanya uhakiki mbalimbali kuanzia watumishi wa Serikali na mpaka leo tumeona wale wa vyeti, lakini ni lini Serikali itafanya uhakiki wa hawa Maafisa wa Ardhi ambao wanaingiza migogoro kwa makusudi kati ya wananchi pamoja na Serikali kwa kufanya mpango wa kugawa viwanja; kwa mfano kiwanja kimoja kutolewa zaidi ya mtu mmoja (double allocation). Maafisa hao wapo na hawajafanyiwa uhakiki ili wachukuliwe hatua. Ni lini Serikali itafanya uhakiki wa hawa maafisa wanaoleta migogoro ili na wao wachukuliwe hatua?
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA, MAENDELEO NA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu ni kweli alichokisema kwamba maeneo mengi ambayo yamezungukwa na Majeshi na wala si majeshi tu hata watu wengine wa kawaida, kumekuwa na migogoro baina ya wananchi na pande ya pili inayomiliki wakiwemo Jeshi. Kuhusu zoezi alilouliza, mimi nimwambie tu kwamba naomba wananchi wa Tabora wawe na subira kwa sababu tayari zoezi la kuhakiki maeneo ambayo yana migogoro na yale ambayo yanamilikiwa na Jeshi limeshaanza. Upande wa wenzetu Wizara ya Ulinzi wameshaunda kamati ambayo imeanza kupitia katika maeneo na mimi nikiri tu wazi na ni-declare interest kwamba hata kwenye Wilaya yangu pia kulikuwa na tatizo hilo lakini tayari Kamati ile imeanza kupita na wanafanya uhakiki wa mipaka.
Mheshimiwa Spika, na wanapofika katika maeneo
yale wanahusisha uongozi wa eneo husika. Kwa hiyo, wakifika pale lazima uongozi wa Wilaya na uongozi wa Mitaa au Vijiji vinavyohusika watahusishwa ili kuweza kubaini ile mipaka iliyokuwepo toka mwanzo. Wenzetu Jeshi wameenda mbali zaidi, kwa yale maeneo ambayo watakuwa hawayahitaji baadae watasema nini cha kufanya katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuyarejesha pia kwa wananchi; lakini ni baada ya uhakiki kwasababu mengine yako strategically huwezi kuyaondoa leo na kuwapa wananchi. Kwa hiyo, uhakiki huo Mheshimiwa nikuhakikishie umeshaanza, unafanyika na Tabora watafika na tatizo litakuwa solved.
Mheshimiwa Spika, swali la pili amezungumzia suala la uhakiki wa maafisa ambao wanaingiza mgogoro kati ya Serikali na wananchi. Mimi niseme tu kwamba katika ziara ambazo tunafanya mimi pamoja na Mheshimiwa Waziri kila tunapopita tukikuta kuna tatizo hatua zinachukuliwa palepale. Ni juzi tu hapa alikuwa Lindi ambako tumekuta kuna mtu kamilikishwa eneo kubwa la wananchi zaidi ya ekari 4,000 lakini Mheshimiwa Waziri ame-declare pale pale kwamba ardhi ile irudi kwa wananchi na yule mtumishi amesimamishwa. Hata hivyo mimi pia nilipopita katika maeneo yale kuna wafanyakazi idara hiyo tumewatoa katika eneo lile na kuweza kutafuta wale wengine wanaohusika.
Mheshimiwa Spika, niseme kwa upande wa Maafisa Ardhi wale ambao ni wateule ni jukumu la Halmashauri, tukiona kwamba huyu mtu hafanyi kazi yake vizuri ni lazima tumuondoe na tunaleta jina lingine kwa maana ya ku-propose ateuliwe kuwa Afisa Ardhi Mteule; kwa sababu wale nao wasipofanya kazi yao vizuri hawa wadogo wa chini wanaharibu kazi zaidi. Kwa hiyo, ni jukumu letu sote katika maeneo yetu kuona wasiofanya kazi vizuri wachukuliwe hatua kwa sababu mamlaka ya ajira yako pale pale katika maeneo yao, kwa maana ya Mkurugenzi. (Makofi)
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Matatizo yaliyopo Kwera yako sawasawa kabisa na matatizo ambayo yapo kwenye Manispaa ya Tabora kwenye barabara ile ya Mambali ambayo inapita Misha, Kata ya Kabila, Kata ya Ikomwa mpaka kutokea Bukene. Barabara hii kwa kiwango kikubwa eneo kubwa lipo eneo la halmashauri na haijapandishwa daraja pamoja na maombi ya muda mrefu. Hata hivyo, kwa kuwa Halmashauri ya Tabora uwezo wa kuitengeneza barabara hii kwa lami unaonekana haupo kabisa, Serikali ina mpango gani kuhakikisha barabara hii inawekwa kiwango cha lami ili iweze kuwa endelevu katika uchumi wa Mkoa wa Tabora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwakasaka ni mjumbe wa Kamati yangu ya Miundombinu. Tumeliongea sana hili katika Kamati na naomba tu nirudie kumhakikishia, kama ambavyo tulikuwa tumeongea katika Kamati, kwamba Serikali muda si mrefu itakamilisha kupitia maombi yote ya barabara ambazo zimeombwa kupandishwa hadhi na matokeo ya maombi hayo yatatangazwa kwenye Gazeti la Serikali hivi karibuni.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali inakiri kwamba ujenzi wa bwawa hili ulikamilika mwaka 1958, kwa maana hiyo ujenzi huu uliwakuta wananchi wengi ambao walikuwepo pale kwa miaka mingi kabla ya hapo na kwa kuwa wananchi wanaendelea kunyanyasika maeneo yale na hasa kwa kukosa sehemu ya kilimo; na kwa kuwa kuna wananchi ambao wao ni waaminifu na hawaharibu mazingira.
Je, Serikali iko tayari angalau kuwapa wananchi maeneo mbadala ya kuweza kufanya shughuli zao za kilimo maeneo yale?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa maeneo yale kumekuwa na matatizo ambayo yanahusiana pia na mifugo ya wananchi hao hao wamekuwa wakikamatiwa mifugo yao na maafisa wa wanyamapori na wengine wala siyo maafisa wa wanyamapori wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi, wakikamata ng’ombe zao na wengine kuwapiga fine ambazo hazina hata receipt.
Nini tamko la Serikali kuhusu hawa maafisa wa wanaymapori hewa ambao wanakuwa wanafanya uhalifu ndani ya maeneo yale?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, mwaka 1958 eneo la Hifadhi ya Igombe halikuwa na wati wowote waliokuwa wanaishi pale katika kipindi hicho, kwa hiyo wote wameingia baada ya huo mwaka kwahiyo hakuna uhalali wowote kusema kwamba wananchi wameingiliwa na Mkoa wa Tabora bado ni mkubwa kwa hiyo watu wanaweza wakatafuta maeneo mengine kwenda kuendeleza maisha yao.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la unyanyasaji, ni kwamba mifugo na wewe Mheshimiwa Mbunge unafahamu kwamba sasa hivi Serikali inajitahidi. Tumekuwa kwamba watu hawakuwa na maeneo kwa ajili ya mifugo yao, lakini tumeendeleza kuongeza mifugo bila kutafakari ni jinsi gani ambavyo tunaweza tukamiliki maeneo yetu kwa ajili ya mifugo, kwa hiyo, ni kwamba mifugo imeingia katika lile eneo. Hata hivyo ni lazima tu-balance, ni kwamba lile bwawa likipotea, Tabora haina chanzo kingine cha maji.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi angalau tunatoa maji kutoka Ziwa Victoria lakini kabla ya hapo hatukuwa na chanzo kingine. Hebu tujionee huruma sisi kam binadamu. Mifugo imeingia pale, tuache lile bwawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu watu wa mifugo watafute eneo lingine. Mimi niseme hakuna unyanyasaji wa aina yoyote lakini mnyanyasaji ni yule mfugaji ambae anaingia katika lile eno halafu anasingizia watu wa Serikali.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la kutolipa wakandarasi au wazabuni katika sehemu mbalimbali za nchi hasa wale ambao wanatoa huduma kwenye vituo vya polisi limekuwa ni kubwa kwa muda mrefu. Kwa mfano, mkoani Tabora kuna wazabuni wengi ambao wanaidai polisi malimbikizo ya muda mrefu ya huduma wanazotoa na hasa utengenezaji wa magari.
Kwa mfano Tabora yapo malalamiko ya muda mrefu ya mzabuni ambaye anatengeneza magari ya polisi hajalipwa sasa hivi ni zaidi ya miaka mitatu, anadai zaidi ya shilingi milioni 222. Sijui Mheshimiwa Waziri anazo taarifa hizi na kama hana, atasaidiaje mkandarasi huyu ambaye ndiye anatengeneza magari ya polisi pale Tabora Mjini alipwe fedha zake?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazo taarifa anazozisemea Mheshimiwa Mbunge. Nakumbuka nilivyotembelea Mkoa wa Tabora nililetewa jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, ni utaratibu wa Serikali tulioweka wa kuhakiki kwanza madeni yote. Baada ya kuwa tumeshafanya uhakiki, yale madeni ambayo yamehakikiwa ndiyo yanalipwa kukiwa na kumbukumbu sawa za kazi iliyofanyika na fedha zinazodaiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, kwa jambo hili ulilolileta Mheshimiwa Mbunge, mhakikishie mtoa huduma huyo kwamba baada ya uhakiki huo ambao ulishafanyika nitawaelekeza watu wangu waweke kipaumbele katika kulipa madeni hayo ili kutokuwakwamisha wazabuni wetu kuweza kuendelea na shughuli zao na kutoa huduma hizo ambazo wametoa hata huko kwetu.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tabora Manispaa tuna tatizo kubwa la msongamano wa wagonjwa katika Hospitali Teule ya Kitete na kwa kuzingatia hilo, Tabora Halmashauri kwa kushirikiana na Madiwani pamoja na wananchi wengine tumetenga eneo kwa ajili ya kujengwa Hospitali ya Wilaya ambayo mpaka sasa hivi ujenzi wake unasuasua kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Je, Serikali inajipanga vipi katika kusaidia uwezeshaji wa kuweza kujenga hospitali hiyo ya wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Mwakasaka pamoja na Waheshimiwa Madiwani katika Manispaa ya Tabora kwa kutenga eneo la kujenga Hospitali mpya kwenye Manispaa ya Tabora ambayo itakuwa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huohuo, kwa kuzingatia kwamba Hospitali ya Kitete ni kweli imezidiwa na mzigo maana yake ndiyo hospitali pekee ya rufaa ya mkoa, Serikali inaahidi na namwomba ushirikiano wake, wakati tutakapokuwa tunaweka kwenye bajeti tushirikiane ili tuweze kupitisha kwa pamoja. Ahsante sana.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nukipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Tabora una vivutio vingi vya utalii ukiwemo uwandaji. Ni lini Serikali itafanya uhakiki wa vitalu vya uwindaji vilivypo Tabora? Kwa sababu kuna taarifa kwamba vitalu vya uwaindaji vilivyopo vinasomeka ni vichache kuliko uhalisia wa vitalu vilivyopo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kuna vitalu viko vingi katika nchi yetu na kazi yetu kubwa ambayo tunaifanya sasa hivi, tunapitia upya vitalu vyote ili tuweze kuvibaini na kuona vipi vinafaa na vipi havifai. Kwa hiyo badaa ya kukamilisha hilo zoezi ni wazi kabisa Mheshimiwa Mbunge atafahamu ni vitalu vingapi ambavyo vinapatikana katika Mkoa wa Tabora.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Tabora Manispaa imeathirika sana na migogoro ya ardhi. Kuna kata ambazo zinapakana na maeneo ya jeshi, ambazo ni Kata za Cheyo, Mbugani, Tambuka Reli, Uyui na Micha. Maeneo yale yamekuwa na migogoro ya mipaka ya muda mrefu. Je, Wizara ya Ardhi imejipangaje kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi ili waweze kuoanisha sasa mipaka halisi ili kuweza kutatua migogoro hii ya mipaka katika kata hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Tabora kama nilivyosema manispaa imekuwa na migogoro mikubwa ya ardhi na hasa bomoa bomoa. Tabora imeathiriwa sana na zoezi la bomoa bomoa; si maeneo ya reli tu lakini hata maeneo mengine yanayopaka na mashule kama Tabora Girls…
Wananchi wale na maafisa kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri wengine si waaminifu. Je, Serikali kwa kuwa hawa wananchi wengi waliobomolewa hayakuwa makosa yao, inawachukulia hatua gani hawa ambao wamesababisha wananchi wamepata hasara kubwa na sasa hawana hata amani na wamekuwa katika hali isiyoeleweka?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza amezungumza habari ya mipaka kuathiri maeneo yaliyopakana na Jeshi na ametaja kata ya Cheyo, Tambuka Reli na nyingine. Naomba tu nimthibitishie Mheshimiwa Mwakasaka kwamba Wizara ya Ulinzi ilishachukua hatua ya kuunda Kamati ambayo imepitia katika maeneo yote ambayo yana migogoro ya Jeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo walikuwa wakifika wanaongea na watu wa eneo lile na kuweza kubainisha mipaka; kwa sababu kuna mengine ambayo wananchi lakini maeneo mengine Jeshi liliingia ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kabla ya kuanza kuweka mipaka upya au kuipitia kwanza wanachambua yale maeneo. Wakishamaliza shughuli hiyo ndiyo Wizara itaingilia kati katika suala la kupanga. Hata hivyo, kwanza tuitambue tuibaini ili kuondoa ile migogoro. Zoezi limeshaanza katika baadhi ya wilaya na Kamati ile inafanya kazi vizuri kwa sababu inashirikisha uongozi wa maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la bomoa bomoa katika maeneo ambayo yamevamiwa au watu wamebomolewa pengine hawakuwa na tahadhari; kwanza naomba nitoe tahadhari kwa wananchi wengi, kwamba maeneo mengi ya taasisi za umma yamevamiwa sana na wananchi na wengine wamejenga nyumba za kudumu kwa muda mrefu. Hata hivyo, unapoangalia kisheria na taratibu na ukubwa wa shule yanayotakiwa kuwa unakuta sehemu nyingi yamevamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa makosa ya watendaji wetu kuna wengine pia walithubutu kutoa hati katika maeneo ambayo ni ya shule. Kwa hiyo zoezi hili linafanyika ili kuhakikisha kwamba maeneo yote yanapimwa na yanatambulika na wale wote walioingia ndani basi sheria inachukua mkondo, wake kwa maana ikiwa ni pamoja na kuvunjiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale ambao watakuwa wamevunjiwa kimakosa ni lazima uhakiki ufanyike tuweze kujua pengine hata ile hati aliyonayo si sahihi. Kwa hiyo kama tukikuta mtu amevunjiwa katika utaratibu ambao ni wa kimakosa basi tutaona namna ya kuweza kumpatia kiwanja mbadala. Nitoe rai tu kwamba wale wote walioko kwenye maeneo ya umma ni vizuri wakayaachia.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, tatizo la akina mama kujifungua mara nyingi wakati mwingine linaletwa pia na matatizo ya baadhi ya ma-nurse ambao huwa wanawanyanyapaa akina mama wenzao wanapotaka kujifungua.
Sasa sijui Serikali ina mpango gani au huwa inachukua hatua gani kuwadhibiti hawa akinamama ambao wana tabia za kuwanyanyasa akina mama wenzao wanapotaka kujifungua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na tatizo la baadhi ya watoa huduma kutoa lugha zisizokuwa sahihi kwa wagonjwa ambao wanafika katika hospitali, na hili ni jambo ambalo ni kinyume kabisa na maadili na taaluma za afya ikiwa ni pamoja na ma-nurse.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeendelea kuimarisha mabaraza yetu na hivi karibuni, wiki iliyopita tu, Mheshimiwa Waziri alitoa kauli ya kuhakikisha kwamba watoa huduma wote, ikiwa ni pamoja na madaktari na ma-nurse, wanakuwa wanatoa huduma nzuri ambayo inazingatia maadili na miiko ya kazi ambayo wanayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naendelea kulisisitiza hilo, na tumeendelea kuimarisha mabaraza yetu na tumeanza kuchukua hatua kwa wale ambao wanakiuka taratibu hizo.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza mradi mkubwa sana wa maji wa kutoka Ziwa Victoria kwenda Tabora na mradi huo kuna kipindi vifaa vya ujenzi vilikuwa vina mikwamo kwamo. Swali langu ni dogo tu, je, mradi huo umefikia kwenye hatua gani ya utekelezaji na wananchi wa Tabora wategemee kupata maji hayo lini? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji unaendelea vizuri sana, tulikuwa na matatizo machache ya kuhusu masuala ya msamaha wa kodi lakini tumeshayamaliza, na Mheshimiwa Mbunge wewe mwenyewe ni shahidi; wakandarasi wote watatu wameshaanza kazi, mabomba wanaendelea kuleta na sasa hivi kama unaenda barabara ya kwenda Dar es Salaam utakutana na malori yanabeba mabomba kupeleka Tabora; kwa hiyo mradi unaendelea vizuri. (Makofi)

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo Chamwino ndiyo tatizo lililopo Manispaa ya Tabora. Ofisi mpya ya Halmashauri imekwama kwa muda mrefu sasa kukamilika kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Kwa kuwa ombi maalum kupitia Hazina Serikali iliahidi kutoa shilingi bilioni mbili ili kuweza kukamilisha ujenzi huo pamoja na kumlipa mkandarasi anayedai karibu shilingi bilioni moja Masasi Construction.
Je, Serikali ni lini italeta pesa hiyo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ili jengo hili liweze kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli lilikuwa ombi maalum, lakini tutaenda kulifanyia kazi. Siwezi kutoa commitment hapa lakini tutaenda kulifanyia kazi tuangalie kwamba lile ombi la awali limefikia wapi halafu tutapeana mrejesho nzuri na Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu najua ni kweli Manispaa ya Tabora wanapata shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutakwenda kuangalia jinsi gani tutafanya.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo la Tabora Mjini, Kata ya Ikomwa maeneo ya Kapunze; Kata ya Kabila, maeneo ya Igosha; Kata ya Ndevelwa, maeneo ya Ibasa; na mengine ambayo kwa muda mrefu hayana mawasilino, Halotel inaonekana inasuasua hata kwenda kufanya survey tu maeneo yale. Sijui Serikali ina mkakati gani kuhakikisha hawa Mameneja wa Mikoa wa Halotel wanafanya kazi ipasavyo ili maeneo hayo yapatiwe huduma ya mawasiliano? Serikali ina mkakati gani kwa kuwa hiyo pesa inalipwa na Serikali kuhakikisha hawa Mameneja wa Mikoa wa Halotel wanafanya kazi yao kwa ufanisi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa taarifa hiyo, lakin nataka tu niweke record sawa, Kampuni ya Halotel haijengi kwenye vijiji kwa kutumia fedha za Serikali ni fedha zao ila tumekubaliana na Serikali kwamba tuwape unafuu fulani wa kupata wayleave bila kulipa fidia ili waweze kufikisha mawasiliano katika vijiji vingi zaidi Tanzania, tuliwapa vijiji 4,000. Kwa hiyo ni fedha zao siyo hela za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu nimhakikishie kwamba tutaliangalia na hilo eneo, tuone kama Halotel wataweza kufikisha mawasiliano mapema au tuviingize hivi vijiji katika mpango wa Mawasiliano kwa Wote, ambapo hapo ndiyo tunatoa fedha za Serikali kwa makampuni ambayo yanashinda tenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana kwa juhudi zake za kufuatilia masuala ya wananchi wake na mkutano wetu uliotukutanisha mimi na Waziri wangu kuyaongelea haya masuala, nimhakikishie kwamba tutatekeleza yale ambayo tulikubaliana kwenye kikao pamoja na kwamba leo amerudia kuliuliza hilo, labda kwa sababu ni muda mzuri wananchi wasikie. Hata hivyo, tunatambua juhudi zake na kwa namna ambavyo amelifuatilia sana suala hilo ofisini kwetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Walimu ndiyo wanaowalea watoto wetu shuleni na ndiyo wanaotegemewa zaidi kuwa walinzi wa watoto hawa wanapokuwa shuleni. Hata hivyo, baadhi ya Walimu ndiyo wamekuwa na tabia za kuwadhalilisha watoto kwa vitendo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa kuna suala la elimu, mtoto yule anakuwa mwoga kutoa taarifa pale anapodhalilishwa na Mwalimu. Serikali ina mkakati gani wa kuwapa watoto elimu ili wawe na ujasiri wa kuripoti vile vitendo ambavyo wanafanyiwa na baadhi ya Walimu? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali imeweka utaratibu shuleni wa kuwawezesha watoto wa kike kuwa na ujasiri wa kuripoti matukio ya udhalilishaji ambayo yanafanyika yaani life skills na pia tumeanzisha club mbalimbali za kuwawezesha watoto kuwa na ujasiri wa kuweza kuripoti matukio hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kuomba na kuwasihi watoto wasiwe na uwoga wowote kwa sababu Serikali yao inawalinda. Pale ambapo anafanyiwa vitendo ambavyo ni kinyume na matakwa ya Serikali, watoe taarifa na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote wanaodhalilisha watoto na kuwasababishia wasisome shuleni kwa amani. (Makofi)
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa hawa baadhi ya maaskari wetu ambao wamekuwa wakiwakamata hawa bodaboda wakiwa kwenye mwendo na kuwasababishia ajali ambapo wengine wamepata ulemavu mkubwa na hata kusababisha kifo. Sijui Serikali pale inapokuwa imethibitisha kwamba uzembe ulikuwa ni wa askari na yakatokea madhara kwa muendesha bodaboda, sijui huwa wanakuwa na mpango gani wa kuwapa fidia hawa waendesha bodaboda? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, kuna malalamiko mengi ya waendesha bodaboda kwamba mara nyingi wanapokuwa wamekamatwa huwa wanabadilishiwa mashtaka wanapofika kituoni. Sasa kwa kuwa hatuna CCTV camera za kuangalia hasa yule wa bodaboda alikamatwa kwa kosa gani, je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba kosa lile alilokamatiwa yule mhusika ndilo analoshtakiwa nalo? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuleta swali hili kwa sababu ni kweli ni jambo ambalo linajitokeza katika baadhi ya maeneo na linaleta malalamiko.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba maisha ya vijana wetu yakipotea hayana fidia ya kusema umeweza kufidia maisha. Kwa hiyo, jambo ambalo tunafanya kama Wizara kwa kweli sisi kiutawala tunaelekeza utaratibu wa kiustaarabu wa ukamataji wa vijana hawa ili isisababishe ajali ambazo zinapoteza maisha kwa vijana wetu. Pia, tumeendelea kuwaelezea vijana wetu kwa sababu wamekuwa na uongozi kwenye vituo vyao kuhakikisha kwamba nao wanatoa ushirikiano, kwa wale ambao wamefanya makosa ni haki yao kufika kwenye adhabu ili kuweza kupunguza makosa hayo yanayojitokeza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu yale ya kubambika kesi hilo ni kosa la kimaadili na sisi kama Wizara wale wote wanaofanya haya kwa wananchi wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa utaratibu wa ufanyaji kazi wa Jeshi la Polisi.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na taarifa mbalimbali kuhusu baadhi ya halmashauri kutoa mikopo hii ya vijana na akina mama kwa upendeleo. Serikali imewahi kulifanyia uchunguzi jambo hili na inasema nini kuhusu suala hili kama kweli lipo katika baadhi ya halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ngazi yetu sisi ya Wizara hivi karibuni hatujawahi kupokea malalamiko ambayo ni ya msingi kabisa kutoka katika halmashauri yoyote, kwamba kuna upendeleo katika utoaji wa mikopo. Kwa sababu utaratibu uliopo kila halmashauri inatakiwa iwe na Kamati ya Mikopo ambayo ndiyo hupitisha mikopo ile na miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya Mikopo ni Waheshimiwa Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nijibu tu kwamba, kwa kweli utaratibu uliopo inawezekana kuna baadhi ya vikundi vikawa havijaguswa kwa mwaka ule husika kwa sababu fedha zenyewe zinakuwa hazitoshi, ni kidogo. Kwa mfano, unaweza ukawa na shilingi bilioni moja ukataka kutoa mikopo kwa vikundi 80 katika halmashauri, lakini halmashauri ina vikundi 600 kwa hiyo ni wazi kwamba kuna baadhi ya vikundi vitakosa. Kwa hiyo, jambo la msingi ambalo nataka nishauri halmashauri ni kwamba wasirudie kuvipa mikopo vikundi ambavyo vilipata mikopo mwaka jana na mwaka huu vikapata, bali vipate ambavyo mwaka jana havikupata. Huo ndiyo utaratibu mzuri zaidi na hiyo ni kupitia Kamati ya Mikopo ya Halmashauri.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri nyingi ikiwemo ya Tabora Manispaa uwezo sasa wa kifedha hasa zile zinazotokana na own source umepungua kutokana na baadhi ya mapato ya Halmashauri kwenda kwenye Serikali Kuu na hii imesababisha huduma nyingine kama za afya na hasa vituo vya afya Halmashauri kushindwa kupeleka fedha kule kutokana na upungufu huo. Serikali ina mpango gani wa kuziba pengo hilo ili zile Halmashauri ambazo hazina uwezo ziweze kupata fedha ambazo zinaweza kusaidia vituo vya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakasaka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata fursa ya kutembelea Manispaa ya Tabora na katika nafasi ile tulitembelea na kuona vyanzo vya mapato vya Manispaa ya Tabora. Nilikuwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge na tukawashauri, vile vyanzo vilivyopo kwanza ni vizuri wakavisimamia wakahakikisha kwamba hakuna hata senti tano ambayo inapotea. Tulitembelea eneo la stendi, jinsi ambavyo wanakusanya hatukuridhika na jitihada ambazo zinatumika katika kukusanya, lakini pia kuna vyoo pale na maeneo mengi ambayo hakika wakisimamia vizuri, bado ni maeneo oevu ambayo pesa zinaweza zikakusanywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kushirikiana na Halmashauri pamoja na TAMISEMI, nguvu yetu tukiweka pamoja hakika huduma katika vituo vya afya na hospitali zitaweza kuboreshwa. Naye mwenyewe ni shuhuda, ameona jinsi ambavyo bajeti ya afya imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mpaka shilingi bilioni 269. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ni azma na nia ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaboresha vituo vya afya.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, nianze kwa kuishukuru hii Wizara ya Nishati chini ya Dkt. Kalemani pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Subira kwa kazi nzuri mnayofanya, hongereni sana. Ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Tabora kwa kuitamka inaonekana kama hata vile vijiji vinavyozunguka ni kama vipo karibu sana, lakini vijiji vingi vipo mbali na maeneo ya mjini. Huu mradi ambao unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kusambaza umeme unaonekana unasuasua maeneo mengi ya vijiji hivi ambavyo vimetajwa. Kama kuna uwezekano naomba Serikali iangalie uwezekano wa kuingiza vijiji hivyo kwenye mradi huu wa REA III ili viweze kupatiwa umeme haraka, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nilipata taarifa kwamba Mheshimiwa Waziri anaweza kufanya ziara Tabora wiki ijayo sehemu za Urambo, kwa kuwa Tumbi hii ninayoizungumzia ipo njiani, anapokuwa Mheshimiwa Waziri anaelekea Urambo lazima atapita Tumbi pale. Je, Waziri yupo tayari kusimama maeneo yale hata kwa dakika chache ili asikilize kero za wananchi pale zinazohusiana na hilo suala la usambazaji umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mwakasaka, kwanza hilo la pili nipo tayari kusimama, nitasimama na nitafanya kazi pale, Mheshimiwa Mbunge nakupongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vijiji kweli kabisa Jimbo la Tabora kwanza lina kata 29 na kata 15 zipo mjini na kata 14 kimsingi zipo vijijini ingawa ni za Manispaa. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya wananchi wake zile kata 14 ambazo kimsingi zipo vijijini tumezipelekea kwenye miradi ya REA kwenye mpango wa Peri-Urban. Kwa hiyo, wananchi wake wataendelea kupata umeme kama kawaida. (Makofi)
MHE. ADAMSON E. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika hii Mifuko ambayo wanakopeshwa vijana, kumekuwa na tatizo kubwa la wale wanaokopeshwa kurudisha mikopo hiyo ili na wengine waweze kukopa. Je, Serikali ina mpango gani mahsusi kuhakisha wale wanaokopeshwa wanarudisha ile mikopo ili na wengine waweze kukopeshwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunao Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao umekuwa ukitoa fedha za mikopo kwa makundi mengi ya vijana na kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge wapo baadhi ya vijana kupitia makundi hayo wameshindwa kurejesha fedha hizi kwa wakati. Tunachokifanya ni kuwasiliana na Halmashauri husika ambao tunafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba wanaendelea kutoa elimu kwa makundi haya ya vijana kwa sababu fedha ile si fedha ambayo inatakiwa tu watu wapewe na ibaki hivyo hivyo, ni pesa ambayo ni revolving. Kwa hiyo, tunaendelea kutoa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumekuwa tukifanya kaguzi za mara kwa mara kuwahimiza vijana hawa kuendelea kurejesha fedha, mpaka ninavyozungumza hivi sasa makundi makubwa ya vijana wameelewa na wameanza kurudisha fedha hii kwa ajili ya kuwafanya vijana wengine waweze kukopeshwa pia.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA. Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Tabora hasa Manispaa imezungukwa na kambi za jeshi kwa eneo kubwa. Kutokana na hali hiyo kumekuwa na migogoro mikubwa ambayo inapelekea wananchi ambao wamekuwa wakitumia maeneo kwa muda mrefu kufikia hata kupigwa wanapokuwa wanafanya shughuli zao. Kwa mfano, kuna eneo ambalo kuna barabara inapita katika kata nne eneo la Uyui, kuna eneo la Rada, barabara hii ni ya miaka mingi na ni hiyo tu ambayo wananchi wa kata hizo nne wanaitumia, ikifika saa moja na nusu mpaka saa mbili usiku, wananchi wakipita maeneo maeneo yale wamekuwa wakipigwa na wakati mwingine hata kunyanganywa vifaa vyao vya usafiri zikiwemo baskeli. Je, Serikali ina mpango gani kuhusiana na eneo hilo ambalo wananchi wamekuwa wakitumia kama barabara?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa shughuli nyingi zimesimama katika maeneo hayo hasa za wananchi ambao walikuwa wakitumia maeneo hayo kwa kulima ambayo wamekuwa wakilima muda mrefu, lakini wengine na shughuli zao za kiutamaduni kwenye mapori ambayo wamekuwa hata hawayapi athari yoyote. Je, kutokana na hali hiyo ambayo ni ya muda mrefu Mheshimiwa Waziri yupo tayari sasa kuja Tabora ili tuweze mimi na yeye kwenda kukagua maeneo haya na kuyapatia utatuzi ambao ni mgogoro wa muda mrefu? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara inayopita kuelekea eneo la Rada la jeshi na kwamba wananchi wanapopita hapo wanapigwa, suala hili nitalifuatilia ili niweze kupata taarifa rasmi ya nini hasa kinachoendelea. Hakuna sheria inayoruhusu wananchi kupigwa, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge nitakuwa tayari kwenda kufanya ziara katika eneo hili la Tabora Mjini ili nijionee mimi mwenyewe hali ilivyo pale na tutafute ufumbuzi, suluhu kwa ajili ya maslahi ya pande zote. Ni vema wananchi watambue kwamba, yale mapori yanayoonekana kama hayana kazi, ni maeneo ambayo wanajeshi wanafanya mazoezi, kwa hiyo yana kazi maalum. Tukifanya hii ziara, tutaweza kuambatana na viongozi wa jeshi ili tuone ni ufumbuzi gani ambao unaweza ukapatikana.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa vijana wengi hasa wa kizazi hiki kipya hawaelewi vizuri umuhimu wa kuuenzi Muungano, Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ya kutosha hasa kwa vijana wa sasa na hata wale wa zamani ili kujua umuhimu wa kuuenzi Muungano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakasaka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimdhihirishie tu kwamba Serikali inaendelea na mchakato na imeendelea kutoa elimu juu ya faida za Muungano na labda kama bado ziko changamoto ambazo elimu hii haiwafikii vijana walio wengi, nadhani ni wakati muafaka sasa wa kuendelea kuhimiza kuhakikisha kwamba elimu hii inawafikia vijana wote.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa, hili swali limekuwa la muda mrefu na maeneo mengi ya Tabora Mjini zikiwemo Kata za Itetemya maeneo ya Kipalapala, lakini pia maeneo ya Ndevelwa, Ikomwa, Kakola, Uyui na mengine bado yana matatizo mengi sana ya mawasiliano ya simu. Namuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa hili Bunge lina muda mrefu na tutakuwa na siku za katikati za mapumziko ya wiki, ni lini atakuwa tayari kuongozana na mimi angalau tukakague pamoja miradi hii aweze kuona shida ya wananchi wa sehemu hizo kwenye mambo ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Adam Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwakasaka kwa juhudi nyingi sana anazozifanya katika kushughulikia kero za wananchi katika Jimbo la Tabora Mjini. Mwenyewe nimekwishafika pale, Mheshimiwa Mwakasaka na unakumbuka tulikuwa wote tukazungukia baadhi ya maeneo niliyozungumza yamefungiwa minara na nakuhakikishia kwamba niko tayari wakati wowote twende kutembelea maeneo mengine na nitaambatana na timu ya watalaam kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, ahsante.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Shule ya wasichana ya Tabora (Tabora Girls) ni shule kongwe sana hapa nchini ambayo pia ina vipaji maalumu. Shule hii kwa muda mrefu imetelekezwa kuhusu uzio. Ile shule haina uzio kabisa kwa miaka mingi na tayari juhudi za viongozi mbalimbali nikiwemo mimi mwenyewe tumeshaanza mkakati wa kujenga uzio huo.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutusaidia katika kukamilisha uzio huo wa Shule ya Wasichana Tabora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, nakushukuru. Namwomba Mheshimiwa Mbunge tuonane tuone. Kama wananchi wameanza kujitolea na wadau mbalimbali akiwepo Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ya wananchi wake anaowawakilisha hapa Bungeni, basi tuonane tuone ni changamoto gani zilizopo na sehemu gani ya kuweza kusaidia kumalizia uzio huo.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, kwa kuwa madeni haya ni ya muda mrefu na imetokea mara nyingi Serikali imekuwa ikilipa madeni yaliyokuja baadaye wanaacha yale ya nyuma. Sijui ni vigezo gani vinatumika kuacha madeni yale ya muda mrefu na kulipa yale ambayo yamekuja baadaye?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wazabuni wengi wanaodai magereza kwa maana wale wanaofanya zabuni ya chakula wengi sasa wana hatari ya kuuziwa nyumba zao hasa wale ambao wamekopa katika taasisi mbalimbali za fedha. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha hawa wazabuni mbalimbali inawakomboa wasiweze kuuziwa nyumba zao na taasisi za kifedha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, madeni ambayo yanalipwa ni miongoni mwa madeni ambayo tumeshalipa kama ambavyo nimeeleza katika jibu la msingi pia yako madeni ya zamani na nilieleza kwamba madeni mengine ambayo hayajalipwa ni kutokana na kwamba mengine yameshahakikiwa na hivyo basi pale fedha ambapo zitapatikana yatalipwa. Naamini kabisa yatakapokuwa yamekamilika madeni hayo kulipwa kama ambavyo nia ya Serikali ilivyo basi yale matatizo ambayo yanakabiliwa na hawa wazabuni yataweza kupatiwa ufumbuzi. Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha madeni haya yanalipwa ili kuepusha usumbufu wowote kwa wazabuni wetu.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nilikuwa na swali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Tabora mjini pamoja na kwamba liko mjini lina Vijiji vipatavyo 41 ambavyo mawasiliano yake si mazuri na Mheshimiwa Naibu Waziri Nditiye hivi karibuni tulitembea wote baadhi ya sehemu.

Swali kwa kuwa tayari andiko lilishaandikwa la kuomba minara ya simu kwa TTCL sijui zoezi hilo limefikia wapi kuhakikisha Vijiji hivyo vinapata mawasiliano ikiwepo eneo tulilokwenda pamoja Mheshimiwa Waziri linaloitwa Iteteme?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Mwakasaka kama ifuatavyo. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake kuhusiana na masuala ya tenda, lakini kwa nyongeza ni kwamba nchi yetu kwa sasa ina usikivu wa asilimia 94, imebakiza asilimia 6, na kama alivyozungumza kwamba tumetangaza tender nyingine ambayo Vijiji 1222 sasa vitapata minara.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwakasaka na ndugu zangu majirani zangu wana Tabora baada ya hii tenda tunakamilisha minara kwenye maeno yote usikivu utakuwepo maeneo yote pamoja na eneo la delta.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wazabuni wengi na nina imani hii ni kwa nchi nzima lakini hapa niwe specific kwa Tabora, ni wafanyabiashara wadogowadogo na wengi wapo sokoni wamekuwa waki-supply vyakula mbalimbali Serikalini kwa maana ya magereza na hata shuleni. Wengi wa wazabuni hao pamoja na kuhakikiwa madeni yao, hawajalipwa kuanzia mwaka 2013, inafika miaka sita (6) sasa na wazabuni hawa wengi wamekopa kwenye mabenki. Leo hii wengine wameuziwa nyumba zao na wengine wana kesi mbalimbali mahakamani. Serikali inasemaje kuhusu suala hili la kuwalipa wazabuni hawa kwa sababu madeni yao ni ya muda mrefu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwa na mtindo wa walipaji ambao wapo kwenye malipo mbalimbali hayo ya wazabuni kulipa madeni ya karibuni yaani wao kwa mfano deni ni la mwaka huu au la mwaka jana wanalipa hayo kwanza, yale ya miaka mingi ambayo watu wamekuwa na madeni haya ambayo yamepelekea mpaka kuuza nyumba zao hawalipi. Serikali inasemaje kuhusu hilo suala hilo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwakasaka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza kwamba wapo wazabuni tangu 2013 hawajalipwa. Naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu kama nilivyosema kwenye jibu la msingi imekuwa ikilipa madeni haya kila mwaka. Kuanzia mwaka 2016/2017 tulitenga bajeti ya shilingi bilioni 625 na tukalipa shilingi bilioni 746. Mwaka 2017/2018 tulitenga shilingi trilioni 1 kwa ajili ya ulipaji wa madeni na tukalipa shilingi trilioni 1.096. Mwaka 2018/2019 tumetenga shilingi bilioni 600 na tukalipa shilingi bilioni 600.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeendelea kulipa madeni haya. Sasa linalonishangaza ni kusema kuna wazabuni wadogowadogo wa tangu mwaka 2013. Naomba nitoe wito wangu kwa Makatibu Tawala wa Mikoa wote waweze kuwasiliana na wazabuni kwenye mikoa yao ili wahakikishe kama madeni yao bado ni halali kwa sababu madeni yote ambayo ni halali tumekuwa tukiyalipa mpaka mwaka 2020/2021 tutakuwa tumekamilisha kulipa madeni yote na deni lililopo sasa ni shilingi bilioni 325 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili ni kwa nini wanalipa madeni ya karibuni. Tuna vigezo vya ulipaji wa madeni haya, kigezo kimojawapo ni kuhakikisha kuwa madeni ya zamani yanapewa kipaumbele kwenye kulipwa. Kwa hiyo, nitoe wito wangu kwa Maafisa Masuuli wote wanapopelekewa fedha za kulipa madeni wafuate vigezo walivyopewa na Mlipaji Mkuu wa Serikali ili tuweze kuwasaidia wazabuni wetu.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kumekuwa na vitendo vingi vya unyanyasaji na hasa kwa watoto wadogo ambavyo haviripotiwi kabisa na akina mama kwa sababu ya kuogopa wakati mwingine usalama wao, lakini wengine pia kwa sababu ya kutojua haki zao za Kisheria. Sijui Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha akina mama wanapata elimu hiyo ili watoto wanapopata matatizo ya kudhalilishwa waweze kuwa na ujasiri wa kuripoti vitendo hivyo?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Emmanuel Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini kwa swali lake la nyongeza kuhusu uwepo wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Swali lake kwa ujumla anasema tuna mkakati gani wa kutoa elimu, nimetoa maelezo wakati najibu swali la Mheshimiwa Sonia Magogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kubwa tutaendelea na jitihada za kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari hata ukiangalia TV, ukisikiliza radio na vipeperushi mbalimbali, tumekuwa tukichapisha juu ya suala hili la vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Mkakati mwingine Mheshimiwa Mwakasaka ambao tunautumia, tuna namba ya simu bure 116 ambayo inatoa fursa kwa mtu yeyote na nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba mwananchi yeyote ambaye ana tatizo la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto mnaweza mkajaribu hata sasa hivi kupiga namba 116 itapokelewa na taarifa dhidi ya vitendo hivyo inafika katika mahala, vyombo vya Serikali na kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuameanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika Jeshi la Polisi. Tuna madawati zaidi ya 350 ambayo kazi yake pia ni kutaka kutoa uhuru kwa wanawake na watoto kwenda kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto bila vikwazo vyovyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema suala hili kwa kweli tutaendelea kulifanyia kazi, nikiwa kama Waziri ninahusika na masuala ya haki na ustawi wa mtoto. Kwa kweli kuna ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, ubakaji na ulawiti umeendelea kuongezeka katika jitihada zetu. Kwa hiyo, tuanze sisi ndani ya familia, kwa sababu vitendo hivi vinatokea pia katika familia husika, watu wa karibu ndiyo wanajihusisha kwa kiasi kikubwa na vitendo hivi vya ukatili dhidi ya watoto.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nilikuwa naangalia kwenye haya majibu ya Serikali naona wametenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali, lakini pamoja na vituo vya afya, lakini kwenye majibu haya sijaona pesa ambayo imetengwa kwa mwaka 2019/2020 kwa ajili ya maboma ambayo yako mengi sana sehemu mbalimbali ambayo wananchi wamejitolea nguvu zao kwa ajili ya kukamilisha maboma hayo hasa ya zahanati, ujenzi wa zahanati.

Mheshimiwa Spika, sijui Serikali ina mpango gani wa kusaidia kukamilisha ujenzi wa maboma mbalimbali ambayo yamo katika sehemu mbalimbali za majimbo yetu? Swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Tabora Manispaa jengo la Halmashauri limechakaa sana mpaka linavuja, sehemu nyingi zinavuja, lakini Halmashauri kwa mapato yake ya ndani imejitahidi kuligharamia jengo hilo na imelipa mpaka sasa hivi zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwa mapato ya ndani na toka ujenzi umeanza mwaka 2014 Serikali imewahi kutoa shilingi milioni 450 tu katika kusaidia ujenzi wa jengo hilo. Sasa sijui Serikali ina mkakati gani wa kusaidia ujenzi wa jengo hilo ambalo ujenzi wake unafikia shilingi bilioni tano ambayo kwa mapato ya Halmashauri kama ya Tabora Mjini si rahisi kukamilisha, Serikali ina mkakati gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, katika swali lake la mwanzo anauliza haoni fedha ambazo Serikali imetenga kwa ajili ya kumalizia maboma ambayo wananchi wametumia nguvu katika kuyajenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, msingi wa majibu katika majibu yangu ya msingi yametokana na swali alilouliza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu katika swali lake la msingi ni kama vile hakuona jitihada ambazo zinafanywa na Serikali katika kuhakikisha ujenzi wa vituo vya afya, hospitali pamoja na zahanati na ndiyo maana katika majibu ambayo nimempa nimeonesha idadi ya fedha ambazo zimetolewa na Serikali na nia njema ya Serikali ambayo inaongozwa na CCM na sisi katika Ilani yetu tumeahidi pale ambapo wananchi wanatoa nguvu yao na Serikali tunapeleka mkono kusaidiana na wananchi ili kuhakikisha nguvu ya wananchi haipotei na yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge ni shuhuda nguvu kubwa ambayo inapelekwa na Serikali kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika swali lake la pili kuhusiana na ujenzi pale Manispaa ya Tabora ambao unatakiwa ugharimu kama kiasi cha bilioni tano ni ukweli jengo limeanzishwa ni kubwa kweli kweli na katika hali ya kawaida kwa bajeti ya Serikali inavyotengwa si rahisi kwamba jengo hili litakamilika lote kwa mara moja na ndiyo maana tumekuwa tukiwashauri ni vizuri tukaanza upande ambao tunaweza tukaukamilisha ukaanza kutumika wakati ujenzi mwingine unaendelea kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu. (Makofi)