Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka (15 total)

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza.
Kiwanda cha Nyuzi Tabora hakiendelezwi kwa muda mrefu sasa:-
Je, Serikali itasaidia vipi kumwajibisha mwekezaji wa kiwanda hicho kwa kushindwa kukiendeleza?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Tabotex kilichopo Mkoani Tabora kilikuwa kikifanya shughuli ya usokotaji nyuzi tangu mwaka 1978 chini ya umiliki wa Serikali. Ilipofika mwezi Aprili, 2004. Serikali ilikibinafsisha kiwanda hicho kwa Kampuni za Noble Azania Investments Ltd na Rajani Industries ltd.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa wamiliki, kiwanda hicho kimesimamisha uzalishaji mwaka 2015 kutokana na changamoto ya soko la uzi ndani na nje ya nchi. Aidha, kiwanda bado kina akiba (stock) kubwa ya uzi uliozalishwa mwaka 2013, ambao hadi sasa bado unaendelea kuuzwa. Kawaida wanunuzi wakubwa wa uzi ni viwanda vinavyofanya shughuli ya ufumaji vitambaa, lakini viwanda vyote inavyofanya kazi ya ufumaji vitambaa (weaving) nchini vikiwemo 21st Century, Sunflag (T) Ltd, Urafiki, NIDA, na Musoma Textile vina mitambo yake ya usokotaji nyuzi, hivyo soko la ndani la Tabotex limekuwa likitegemea wafumaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hilo, kiwanda hicho hivi sasa kinatafuta mwekezaji ambaye atakuwa tayari kuingia nacho ubia kwa kupanua wigo wa uzalishaji na kufanya shughuli za ufumaji vitambaa (weaving) hadi ushonaji (finishing). Wakati huo huo, kwa kuwa kiwanda hicho ni moja viwanda vilivyobinafsishwa, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na tathmini ya kiwanda hicho na pindi tathmini hiyo itakapokamilika na tukajiridhisha kuwa mwekezaji huyo hajatimiza matakwa ya mkataba wa Serikali, Serikali itachukua hatua stahiki ambayo itakuwa na faidia kwa Serikali na wananchi kwa ujumla.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Mkoa wa Tabora hauna viwanda kabisa na kwa sababu mkoa huu hulima tumbaku kwa wingi:-
Je, Serikali inasaidiaje kupata Kiwanda cha Tumbaku mkoani humo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kupitia TAMISEMI na hata kwenye Bunge lako Tukufu, Serikali imetoa mwongozo juu ya uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda na bayana tumeeleza wajibu wa kila mdau. Nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mkoa una viwanda. Mkakati wa Serikali ni kuhamasisha uwekezaji katika viwanda kwa nia ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo yanayopatikana katika maeneo husika. Lengo ni kuongeza tija kwenye shughuli za wakulima ili kuongeza ajira na kipato.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Mkoa wa Tabora hulima tumbaku na msimu wa mwaka 2015 Tabora ilizalisha tumbaku tani 39,502 ambayo yote ilipelekwa Mkoani Morogoro kwa ajili ya kusindikwa. Tumbaku hiyo pamoja na nyingine kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu husindikwa katika Viwanda vya Tanzania Tobacco Processing Limited- TTPL kinachosindika tumbaku asilimia 50 na Alliance One Tanzania Tobacco-AOTT asilimia 40 ya tumbaku inayolimwa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na mazungumzo na wawekezaji mahiri katika sekta ya kusindika tumbaku na kuzalisha sigara. Nirudie kueleza kuwa mpaka sasa tunaendelea kufuatilia wawekezaji kutoka Vietnam na China ambao tutawashawishi waje kusindika tumbaku na au kutengeneza sigara. Lengo letu ni kupata mwekezaji anayeweza kutengeneza sigara Tabora kwa “brand maalum” duniani na kwenda kuuza sigara hizo nje ya nchi yetu.
MHE. JOHN P. KADUTU (K.n.y. MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA) aliuliza:-
Serikali ina mpango wa kujenga maabara ya kupima ubora na kiwango cha asali inayozalishwa hapa nchini.
Je, ni kwa nini Serikali isijenge maabara hiyo mkoani Tabora ambako ndipo kunazalishwa asali nyingi kuliko mkoa wowote nchini?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali namba 84, kwa ruhusa yako nilikuwa naomba uniruhusu niseme kidogo juu ya janga lililowapata wananchi wa Tanzania, hususan Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Kamati ya Uongozi ya Bunge na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa namna ambavyo kipekee mliguswa na tatizo la wananchi wenzetu wa Tanzania walioko mkoani Kagera. Lakini nichukue fursa hii kuwashukuru wananchi na wadau ambao waliitikia wito wa Mheshimiwa Waziri Mkuu jana na kufika kumuunga mkono na kuweza kukusanya bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.369.
Nichukue fursa hii Waheshimiwa Wabunge, tusaidiane na Serikali kuhamasisha njia hii. Kiasi kilichokusanywa jana tulijiandaa kwa saa 30, tukijiandaa wote kwa pamoja tutatunisha Mfuko wa Maafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nichukue fursa hii kuwapa pole wananchi wa Mkoa wa Kagera, hasa Wilaya za Muleba, Karagwe, Kyerwa, Bukoba Vijijini, Bukoba Mjini na Misenyi, watulie Serikali ipo na Serikali itahakikisha hali inarudi katika hali ya kawaida na kimsingi baada ya kujibu swali hili itabidi niondoke mwenyewe niende site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijibu swali namba 84. Upimaji wa ubora na viwango vya bidhaa aina ya asali unafuata kiwango chenye namba 851 cha mwaka 2006. Chini ya kiwango hiki maelezo na vigezo vimetolewa ambavyo mzalishaji, mtunzaji, muuzaji na mpimaji wanapaswa kuzingatia ili asali iwe katika ubora unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wadau wote kwa kufuata vigezo na maelezo katika kiwango namba 851 wanaweza kupima asali; hata hivyo, maabara kuu inayopaswa kutoa uthibitisho ipo TBS Dar es Salaam. TBS Makao Makuu ndio wanaopaswa kisheria kutoa hati ya ubora chini ya utaratibu maalum. Tunapoendelea kuhimiza ujenzi wa viwanda, ikiwemo viwanda vya asali, tutahakikisha viwanda hivyo vinakuwa na maabara zinazoweza kupima viwango vya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa maabara Tabora, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, wawekezaji ambao wanafuatilia ujenzi wa viwanda vya asali mkoani Tabora, Wizara yetu itahakikisha wanakuwa na maabara za kupima viwango vya msingi na kuiachia TBS kuweka Viwango vya Kitaifa na kudhibiti viwango hivyo.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Jimbo la Tabora Mjini katika maeneo ya Kata za Uyui, Misha, Itetemia, Ntalikwa, Kabila, Mtendeni, Ifucha, Itonjanda na baadhi ya vijiji vya Kata ya Tumbi vina shida sana ya upatikanaji wa maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson, Mbunge wa Tabora Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua tatizo la maji Tabora Mjini, Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao utahudumia kata na vijiji vya Tabora Mjini. Mradi huo utahudumia vijiji na miji ya Nzega, Igunga, Isikizya yaani Uyui na vijiji vyote vilivyomo ndani ya kilometa 12 kila upande kutoka linapopita bomba kuu la kupeleka maji katika miji hiyo. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 589.6 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi huu utahusisha ujenzi wa mifumo ya maji katika Kata za Uyui, Misha, Itetemia, Ntalikwa, Kabila, Mtendeni, Ifucha, Itonjanda na Tumbi. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuanza kati ya mwezi Aprili na Mei 2017.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Jimbo la Tabora Mjini hususan katika Kata za Mpera, Malolo, Mbugani na Ng’ambo (Kidongo Chekundu) kuna migogoro ya muda mrefu ya ardhi na bomoa bomoa ya nyumba za wananchi.
Je, Serikali inafanya juhudi gani kuhakikisha inamaliza migogoro hiyo ya ardhi ambayo ni kero ya muda mrefu kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA, MAENDELEO NA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama Ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwepo na migogoro ya ardhi mingi baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi katika Jimbo la Tabora Mjini hususani katika kata za Mpera, Malolo, Mbugani, Ng’ambo na Kidongo Chekundu. Migogoro mingi inahusiana na madai ya fidia, kuingiliana kwa mipaka, kutozingatiwa kwa taratibu za uendelezaji, uvamizi wa maeneo yaliyopangwa kupimwa na kumilikishwa na miliki pandikizi.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na migogoro hiyo Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya urasimishaji wa maeneo yote ambayo yalikuwa yamevamiwa na kujengwa kiholela ili kuweka miundombinu ya huduma muhimu katika maeneo hayo. Vilevile Serikali imeimarisha ushirikishaji wa sekta binafsi katika kuanga na kupima viwanja kwa kushirikiana na wananchi ambapo makampuni binafsi ya upangaji na upimaji yaliyosajiliwa yameshaanza kufanya kazi ya kupanga na kupima katika maeneo ya Uledi, Kariakoo na Inala. Aidha, Mpango Kabambe wa Mji wa Tabora, (Tabora Master Plan 2015 - 2035) utatoa dira ya upangaji usimamizi na uendelezaji wa ardhi katika mji wa Tabora.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu pia imekuwa ikisisitiza Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha uwepo wa fedha kwa ajili ya kulipia fidia kabla ya kufanya zoezi la uthamini wa mali kwa ajili ya utoaji wa ardhi ili kuzuia uwezekano wa kuibuka kwa migogoro ya ardhi inayohusiana na fidia. Aidha, wamiliki wa ardhi wamekuwa wakishirikiana na makampuni binafsi ya upangaji na upimaji katika hatua zote za upangaji na upimaji wa viwanja katika maeneo yao ili kuhakikisha kuwa maslahi ya pande zote yanalindwa.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Matatizo ya mipaka kati ya hifadhi na wanakijiji wanaopakana na maeneo ya Hifadhi ya Bwawa la Igombe katika Jimbo la Tabora Mjini ni ya muda mrefu hususani katika Kata za Kabila, Ikomwa na Misha.
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro huo wa mipaka ambao ni wa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Bwawa la Igombe ambalo ni chanzo cha sasa cha maji katika Mji wa Tabora lilijengwa na kukamilika mwaka 1958 chini ya Serikali mkoloni Mwingereza. Bwawa hilo lina eneo la hifadhi lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 12,000. Sehemu ya eneo hilo linalohifadhi maji ni Kilometa za mraba 4,144 ndani ya hifadhi ya msitu wa Igombe, hivyo sehemu ya bwawa inazungukwa na hifadhi msitu wa Igombe na mipaka yake ipo kisheria na imekuwa ikilindwa na kuheshimiwa hata wakati wa operation vijiji ya mwaka 1974.
Mheshimiwa Spika, tatizo la msingi lililopo hapa ni kwamba baadhi ya wananchi wanaozungula Msitu wa Bwawa la Igombe wanataka uhalali wa kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ikiwa ni pamoja na kutumia kama malisho ya mifugo, kukata miti kwa ajili ya mbao na nishati ya mkaa, kulima bustani kando kando ya bwawa kwa kutumia maji ya bwawa hususani nyakati za kiangazi, utafutaji wa madini na baadhi ya wananchi kudiriki hata kuanzisha makazi ndani ya ene hilo.
Mheshimiwa Spika, mipaka ya Hifadhi ya Msitu wa Igombe iliainishwa vizuri na Ofisi ya Bonde la Ziwa Tanganyika na Wizara ya Maliasili na Utalii hivyo Serikali itaendelea kulinda mipaka hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa kata zinazoizunguka hifadhi hiyo ili kuhakikisha kuwa bwawa hilo na hifadhi yote inakuwa endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA,aliuliza:-
Kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi nchini inayosababisha uvunjifu wa amani miongoni mwa wananchi na hata katika baadhi ya maeneo migogoro hiyo imesababisha vifo;
(a) Je, Serikali imechukua hatua gani kutatua migogoro hiyo?
(b) Kwa kuwa Maafisa Ardhi wengi ndiyo chanzo cha migogoro hiyo, je, ni Maafisa Ardhi wangapi wamechukuliwa hatua kwa kusababisha migogoro hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu kwanza kwa sababu ni mara ya kwanza mwaka huu niwatake heri ya mwaka mpya wote na tumshukuru Mungu kwamba tunaendelea kulijenga Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa migogoro ya ardhi nchini na tayari imeweka mikakati mbalimbali ya kuitatua na kuzuia uwezekano wa kuibuka migogoro mipya. Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na:-
(i) Kutoa elimu kwa watendaji wanaohusika na utatuzi wa migogoro ya ardhi kuanzia ngazi za Serikali za Mitaa hadi Serikali Kuu na kuzifanyia marekebisho sera na sheria mbalimbali zinazosimamia sekta ya ardhi;
(ii) Kuboresha Mabaraza ya Ardhi na kuyaongezea watumishi pamoja na vitendea kazi;
(iii) Kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ya wilaya na vijiji; na
(iv) Kutekeleza mkakati wa kupima kila kipande cha ardhi nchini na kuboresha mifumo ya kutunza kumbukumbu za ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara imeanzisha utaratibu wa kushughulikia migogoro ya ardhi ambapo Mheshimiwa Waziri akiambatana na wataalam wa sekta ya ardhi amekuwa akikutana na wananchi papo kwa papo na kutatua migogoro na changamoto zinazowakabili kwa mfumo ambao tunaita Funguka na Waziri wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi kwa namna moja ama nyingine husababisha pia na watendaji wa sekta ya ardhi wasio waaminifu; lakini Serikali imeendelea kuwachukulia hatua maofisa hao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2014/2015 na 2016/2017, watumishi wanne wamesimamishwa kazi baada ya kufikishwa Mahakamani kutokana na ukiukwaji wa maadili ya Utumishi wa Umma; watumishi 16 walifukuzwa kazi kwa makosa mbalimbali ya kiutendaji; na watumishi 19 waliandikiwa barua za onyo na kutakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa watendaji wa sekta ya ardhi walio chini ya usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Wizara imekuwa ikishirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika kuhakikisha kuwa hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya watendaji hao ambao wamekuwa wakisababisha migogoro kutokana na kutowajibika au kukiuka masharti ya ajira zao.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Kumekuwa na ajali nyingi zinazotokana na vitendo vya baadhi ya Askari Polisi maarufu kama PT kuwakamata waendesha bodaboda wakiwa kwenye mwendo huku wakiwa wamebeba abiria. Hali hiyo hupelekea waendesha bodaboda na abiria kupata ajali mara kwa mara:-
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kuwa ajali za kizembe zinazosababishwa na baadhi ya Askari Polisi zinakomeshwa?
WAZIRI WA MAMBO NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa na Jeshi la Polisi, ajali za barabarani husababishwa na vyanzo vikuu vitatu ambavyo ni vyanzo vya kibinadamu ambavyo husababisha ajali kwa asilimia 76, vyanzo vya kiufundi ambavyo vinasababisha ajali kwa asilimia 16 na vyanzo vya kimazingira ambavyo vinasababisha ajali kwa asilimia 8. Ni katika vyanzo vya kibinadamu ndivyo tunakuta kuna uzembe ambao pia uko wa namna nyingi.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya vijana wetu waendesha pikipiki bado wana uelewa mdogo kuhusu sharia za usalama barabarani na wengine pikipiki zao zina mapungufu mengi ambayo huwafanya kutokujiamini wanapoendesha. Kutokana na sababu hizi na nyinginezo, waendesha pikipiki hujihisi wana makosa wakati wote wawapo barabarani na hivyo huwa na hofu ya kukamatwa na Askari Polisi.
Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa Askari Polisi kuhakikisha kuwa sheria zinafuatwa na si kuvunjwa. Waendesha pikipiki wanapaswa kutambua hilo na wao kutimiza wajibu wao wa kufuata sheria. Hali ya kutambua kuwa wana makosa ndiyo huwafanya kukimbia askari hata kama askari hana lengo la kuwakamata, hivyo husababisha ajali za kizembe bila sababu.
Mheshimiwa Spika, ili kuepukana na ajali za kizembe, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kutoa elimu kwa waendesha pikipiki ili kuwajengea uelewa wa sheria za usalama barabarani. Elimu hii itasaidia kuondokana na dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa waendesha pikipiki na wapanda pikipiki kutokutii sheria ama kusababisha vyanzo vya ajali barabarani kwa kuwakimbia Askari Polisi kwa hofu ya kukamatwa, hata kama hawana makosa.
Mheshimiwa Spika, aidha, natumia fursa hii pia kulielekeza Jeshi la Polisi nchini kutumia muda wao vizuri katika kuwaelimisha waendesha pikipiki kufuata sheria za usalama barabarani kwa ajili ya usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Katika Jimbo la Tabora Mjini hasa vijiji na kata zilizopo nje ya Manispaa ikiwemo Kata ya Tumbi na vijiji vinavyoizunguka kata hiyo havijajumuishwa katika Mpango wa REA Awamu ya Tatu.
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA katika kata na vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli vijiji vilivyopo nje ya Manispaa ya Tabora ikiwemo Kata ya Tumbi havikujumuishwa katika utekelezaji wa mradi wa REA III mzunguko wa kwanza. Sehemu ya vijiji katika Kata ya Tumbi ilipatiwa umeme mwaka 2006 kupitia mradi wa umeme chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden. Kwa kuwa baadhi ya vijiji vya Jimbo la Tabora Mjini viko ndani ya Manispaa ya Tabora, Serikali kupitia mradi wa Urban Electrification itaendelea kuyapelekea umeme maeneo yaliyomo katika Mamlaka za Miji, Manispaa na Majiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya Serikali ni kuipatia umeme Kata ya Tumbi na Vijiji vilivyoizunguka Kata hiyo katika Manispaa ya Tabora kupitia mradi wa Urban Electrification. Aidha, mradi wa Urban Electrification unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika utepeleka umeme katika vijiji na shule za Makunga, Mkinga, Mayeye, Shalua, Mtakuja, Chang’ombe, Itetemia, Itaga na Umanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine unaotarajiwa kutekelezwa ni densification kwa nia ya kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji ambavyo vimefikiwa na miundombinu ya umeme. Maandalizi ya awamu ya pili ya mradi huu yanaendelea na unatarajiwa kutekelezwa kwatika mwaka wa fedha 2018/2019. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Kwa muda mrefu kumekuwa na migogoro ya mipaka baina ya wananchi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika maeneo ya Mkonkole Kata ya Tambuka Reli, Usule Kata ya Mbungani na Kata ya Cheyo Tabora Mjini:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kutatua mgogoro huo ambao ni wa muda mrefu?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Mji wa Tabora, JWTZ lina Kambi kwenye maeneo ya Airport, Cheyo, Bomani, Mirambo, Usule na Kalunde. Maeneo yote hayo yalipimwa na ramani zake kusajiliwa. Wakati wa upimaji maeneo mawili walikutwa watu wachache. Eneo la Airport alikutwa mwananchi mmoja aliyekuwa anaishi hapo. Mwananchi huyo alishafanyiwa uthamini na ameshalipwa fidia yake. Katika eneo la Usale zilikutwa familia tatu. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa limefanya mawasiliano na familia hizi kwa ajili ya kufanyiwa uthamini na hatua ya kulipwa fidia kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuendeleza makazi katika Mji wa Tabora, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ilianza kupima viwanda ndani ya eneo la Kambi ya Mirambo ambalo tayari lilikuwa limepimwa. JWTZ ilichukua hatua ya kulifikisha suala hilo katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora ambayo ilisimamisha zoezi hilo. Wakati zoezi linasimamishwa, tayari wananchi wengine wameshagawiwa viwanja. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inaendelea kuwasiliana na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ili kuwaondoa wananchi hao ambao walipimiwa viwanja ndani ya eneo hilo likiwemo eneo la Tambuka Reli. Uondoshaji wa wananchi hawa utawezesha eneo hilo kuwa huu kwa matumizi ya kijeshi pekee.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Maeneo mengi katika Jimbo la Tabora Mjini na Iramba Mashariki hayana mawasiliano ya simu:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga minara ya simu katika maeneo hayo ili wananchi wa maeneo hayo wapate mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote inasimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 inayoelekeza kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo yote, yakiwemo maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa hivi jumla ya kata 703 katika mikoa yote Tanzania zimefikiwa na huduma za mawasiliano kwa jitihada za Mfuko, ambapo Watanzania zaidi ya milioni nne wanapata huduma za mawasiliano. Tabora Mjini zaidi ya wakazi 12,992 wamefikishiwa huduma za mawasiliano katika Kata za Kabila na Kampuni ya Halotel, Kalunde na Kampuni ya Vodacom na Uyui na Kampuni ya Vodacom vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada za Serikali zinazoleta mafanikio hayo bado kuna maeneo nchini yakiwemo baadhi ya maeneo ya Jimbo la Tabora Mjini ambayo hayajafikiwa na huduma za mawasiliano. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itafanya tathmini kamili ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika vijiji vyote vya kata za majimbo ya Tabora Mjini na vijiji vitakavyobainika kukosa mawasiliano au kuwa na mawasiliano hafifu vitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa hivi karibuni.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya malimbikizo ya madeni mbalimbali ya wazabuni wanaotoa huduma mbalimbali ikiwepo huduma ya kupeleka chakula kwa wanafunzi magerezani na matengenezo ya magari.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kulipa madeni hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali katika nyakati tofauti imekuwa na mkakati wa kulipa madeni yake ya ndani ikiwemo madeni ya watoa huduma, chakula cha wafungwa na matengenezo ya magari katika magereza yote nchini.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 hadi mwaka wa fedha 2018/2019 jumla ya kiasi cha fedha shilingi 23,563,630,710.61 zimelipwa kwa ajili ya watoa huduma za uendeshaji, chakula cha wafungwa na matengenezo ya magari yakiwa ni madeni ya mwaka wa fedha 2014/2015 hadi 2016/2017.

Mheshimiwa Spika, madeni ya mwaka 2012/2013 mpaka mwaka 2013/2014 na 2017/2018 tayari yameshahakikiwa, kinachosubiriwa ni fedha kutoka Hazina kwa ajili ya kulipa. Hata hivyo, madeni ya mwaka wa fedha 2018/2019 tayari yameandaliwa yanasubiri uhakiki kutoka Hazina ili kuhakiki madeni hayo na baadaye kuyalipa.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kulipa madeni ya wazabuni wanaotoa huduma mbalimbali ikiwemo chakula cha wafungwa na matengenezo ya magari kadri ya fedha itakavyopatikana.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya madeni mbalimbali ya wazabuni wanaoidai Serikali:-

Je, Serikali imefikia hatua zipi katika kuhakikisha inalipa madeni ya wazabuni nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kulipa madeni yaliyohakikiwa na kukubaliwa kupitia bajeti inayoidhinishwa na Bunge lako tukufu. Kati ya mwaka 2016/ 2017 na robo ya kwanza ya mwaka 2019/2020, Serikali imetoa jumla ya shilingi 2,528,619,142,345.21 kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, wazabuni, wakandarasi/wahandisi washauri, watoa huduma na madeni mengineyo. Kati ya kiasi hicho, jumla ya shilingi 379,072,545,151.14 zimetolewa kulipa madeni ya wazabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kupunguza madeni, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwenye bajeti kila mwaka kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa na kukubaliwa, kuweka sheria na kanuni zake kama vile Sheria ya Bajeti Sura 439 na Kanuni zake; Sheria ya Manunuzi, Sura 410; Sheria ya Fedha, Sura 348 na kutoa miongozo na maelekezo mbalimbali ikiwemo Waraka Na.1 wa Mlipaji Mkuu wa Serikali unaotolewa kila mwaka kuhusu utekelezaji wa bajeti na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti unaotolewa kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa, Serikali imeandaa mkakati wa kulipa madeni yaliyohakikiwa na kuzuia ulimbikizaji wa madeni. Madeni yanayohusika kwenye mkakati huo ni yaliyozalishwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea na Sekretarieti za Mikoa yakiwemo madeni ya watumishi, wazabuni na watoa huduma, pamoja na madeni ya wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto ya madeni, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa kwa kuzingatia mwelekeo ulioandaliwa wa kulipa madeni hayo kulingana na upatikanaji wa mapato.

Aidha, lengo la Waraka Na.1 wa Mlipaji Mkuu unaotolewa kila mwaka ni kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kudhibiti madeni na kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati ikiwemo kuzuia uzalishaji na ulimbikizaji wa madeni.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA) aliuliza:-

Waendesha pikipiki (bodaboda) nchini wamekuwa wakikamatwa na Askari wa Usalama Barabarani mara kwa mara kwa tuhuma za makosa mbalimbali:-

Je, zoezi hili la ukamataji wa waendesha pikipiki limefanikiwa kwa kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Mwakasaka, Mbunge wa Tabora kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja ya chanzo cha ajali za barabarani huchangiwa na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda. Mathalan mwaka 2016 nchini kote kulitokea jumla ya ajali za pikipiki 2,544 zilizosababisha vifo vya watu 890 na majeruhi 2,128. Mwaka 2017 zilitokea ajali za pikipiki 1,459 zilizosababisha vifo vya watu 728 na majeruhi 1,090. Mwaka 2018 zilitokea ajali za pikipiki 876 ambazo zilisababisha vifo vya watu 366 na majeruhi 694.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Januari hadi Juni, 2019 kumetokea ajali za pikipiki 334 zilizosababisha vifo 176 na majeruhi 289. Ukilinganisha na kipindi kama hicho cha Januari hadi Juni, 2018 ambapo ajali zilitokea 408 zikasababisha vifo 165 na majeruhi 344, utaona kuwa ajali za pikipiki zimepungua sawa na asilimia 18 ingawa vifo viliongezeka kwa idadi ya 11 ambayo ni sawa na asilimia 6.6 na majeruhi kupungua kwa idadi ya 55 ambayo ni sawa na asilimia 16. Kwa ujumla takwimu hizi zinathibitsha kupungua kwa ajali za bodaboda barabarani ambazo zinatokana na waendesha pikipiki kutozingatia sheria.

Mheshimiwa Spika, kupungua kwa ajilia hizi ni mafanikio yanayopatikana kutokana na usimamizi wa Sheria za Usalama Barabarani kwa kuwachukulia hatua waendesha bodaboda ambao wanakiuka sheria na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha Mahakamani.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Halmashauri nyingi zina uwezo mdogo wa kujiendesha kwa kutumia mapato yake ya ndani.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutenga fedha katika bajeti ili kuzisaidia Halmashauri kujenga hospitali na vituo vya afya badala ya kuziachia jukumu hilo Halmashauri pekee?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitekeleza mkakati wa ujenzi, upanuzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya kwenye Halmashauri mbalimbali nchini. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 na mwaka 2018/2019 Serikali imejenga, imekarabati na kupanua vituo 352 ikiwa hospitali tisa, vituo vya afya 304 na zahanati 39 vya kutolea huduma za afya nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 184.67.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 100.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali 67 za Halmashauri. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 10.4 kwa ajili ya ujenzi wa vituo 52 vya afya na shilingi bilioni 46.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali 27 za Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha na kujenga vituo vya afya vya kutolea huduma kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.