Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Selemani Jumanne Zedi (20 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri na moja kwa moja nitaanza na mitandao ya simu katika maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kubaini kwamba, makampuni ya simu za mikononi yamekuwa reluctant kujenga minara katika maeneo ya vijijini kwa sababu maeneo hayo hayana mvuto wa kibiashara Serikali kwa nia njema kabisa iliamua kuanzisha Mfuko Maalum wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili uweze kutumia fedha za mfuko huo kujenga minara katika maeneo ya vijijini. Lakini mpaka sasa nimeona kuna jitihada fulani zimefanyika, lakini bado maeneo mengi ya vijijini hayana huduma hii muhimu ya simu za mikononi. Mimi mwenyewe kwenye jimbo langu katika huu mfumo wa UCSAF ni kata za Isagehe na Semembela na Kamahalanga ndizo ambazo ujenzi wa minara ya simu umeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ombi langu kwa Serikali ni kwamba, kwa kuwa bado makampuni haya ya simu ya Airtel, Vodacom na Tigo tukiyaachia yenyewe yajenge minara kwenye maeneo ya vijijini hayataweza kufanya hivyo kwa sababu, hakuna mvuto wa kibishara. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwenye maeneo mengi ya Vijijini bado mfuko huu wa UCSAF utalazimika kujena minara hata kwa kutoa ruzuku kwa asilimia mia moja. Tukiyaachia haya makampuni ya simu hayataweza kujenga kwa sababu maeneo hayo mengi hayana mvuto wa kibiashara na makampuni haya motive yake kubwa ni faida tu hayataweza kwenda huko. Kwa hiyo, tunahitaji mfuko wa UCSAF ujenge minara maeneo ya vijijini, maeneo mengine uwe tayari kujenga hata kwa asilimia mia moja kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu tatizo la upelekaji wa fedha katika Halmashauri zetu za Wilaya hasa Mfuko wa Barabara na fedha za ruzuku (LGCDD), ili kuhudumia barabara ambazo zinahudumiwa na Halmashauri za Wilaya. Kuna tatizo kubwa sana la kwamba fedha tunazopanga kwenda kuhudumia barabara zetu za Halmashauri mwisho wa mwaka unapofika ni asilimia ndogo mno ya fedha inakuwa imekwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano wa Halmashauri yangu ya Wilaya ya Nzega, mwaka 2014/2015 kwenye Mfuko wa Barabara tulitenga takribani milioni 700 kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Nzega inamtandao wa barabara wa karibu kilometa mia sita na kitu. Kwa hiyo, tulitenga na tulipanga shilingi milioni 700 ziende kuhudumia barabara za Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, lakini mpaka mwisho wa mwaka unafika ni shilingi milioni 300 tu zilikuwa zimekwenda na hivyo kufanya barabara nyingi kukosa huduma. Lakini hali ilikuwa mbaya sana kwenye mfuko wa LGCDD ambako tulipanga zipelekwe shilingi milioni 700, lakini mpaka mwaka unaisha ni shilingi milioni 49 tu zilikuwa zimekwenda kwa hiyo…
MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono hoja na tulikubaliana na Mheshimiwa Mwakasaka atamalizia dakika tano nyingine, asante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kilometa 149 iliyomo kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 inayoanzia Tabora – Mambali – Bukene – Kagongwa haimo kabisa katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha bajeti ya 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ilishindikana kufanyiwa upembuzi yakinifu mwaka wa jana kwa kuwa fedha iliyokuwepo kwa kazi hii milioni 400 haikutosha. Nilitarajia kuwa mwaka ujao wa fedha wa 2017/2018 barabara hii ingeongezewa fedha shilingi milioni 400 zingine ili zifike milioni 800 ambazo zingetosha kwa ajili ya kufanyia upembuzi yakinifu. Nimepitia kitabu chote na nimepitia miradi yote ya barabara kwa mwaka 2017/2018 lakini sijaona barabara hii ya Tabora – Mambali – Bukene – Kagogwa kilometa 149.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwasilisha jambo hili kwa Naibu Waziri Mheshimiwa Edwin Ngonyani ambaye aliongea na Meneja na TANROADS wa Tabora Ndugu Ndabalinze, lakini sijapata mrejesho wowote. Naomba barabara hii ipate fedha za kufanya upembuzi yakinifu ili tutimize ahadi ya CCM kama ilivyo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi jioni ya leo niweze kuchangia mjadala huu ambao uko mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza kwenye maeneo kadhaa ambayo ningependa nitoe mchango kuhusu hotuba ya mapendekezo ya bajeti iliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango. Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua vizuri sana kwa kuja na nguvu sana katika eneo la kudhibiti ubadhirifu katika matumizi ya fedha za umma na mimi naunga mkono kabisa kwa sababu ni jambo jema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya kupitia hotuba ya mapendekezo ya Waziri wa Fedha nimeona kuna contradiction ya ajabu. Kwa sababu huwezi kupambana na ubadhirifu wa matumizi ya fedha za umma kwa kauli tu za kisiasa. Ni lazima uwe na vitendo ambavyo kweli vitapelekea kupambana na ubadhirifu huu wa fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna taasisi muhimu ya kimkakati katika kupambana na ubadhirifu wa fedha za umma basi taasisi hiyo ni Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yaani CAG. Contradiction ninayoisema ni kwamba kwa upande mwingine Serikali inasema tumedhamiria kupambana na ubadhirifu wa matumizi ya fedha za umma, lakini kwa upande mwingine taasisi ambayo ndiyo taasisi ya mkakati, ndiyo hasa kiini, ndiyo key institute katika kupambana na ubadhirifu ambayo ni CAG imepangiwa fedha ambayo kwa kweli haiwezi kabisa kutimiza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii tunayokwenda nayo ambayo inakwisha mwezi huu wa Sita ni bajeti ya shilingi trilioni 22. Katika bajeti hii CAG tumemtengea shilingi bilioni 74 ili kukagua shilingi trilioni 22. Bajeti hii ambayo tunaijadili sasa ni ya shilingi trilioni 29 lakini CAG tumempangia shilingi bilioni 44 tu. Huu ndiyo nauita mkanganyiko na contradiction ya ajabu kwa sababu kwenye bajeti ya shilingi trilioni 22 CAG tumempa shilingi bilioni 74 kwa ajili ya kukagua lakini kwenye bajeti ya shilingi trilioni 29 ambapo kuna ongezeko la shilingi trilioni saba tumepunguza hela ya kumwezesha kukagua sasa tunategemea nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwangu mimi hii ni contradiction na naona kabisa kama hatutafanya chochote, basi kauli za kusema tumejipanga kupambana na ubadhirifu ni kauli tu za kisiasa na ambazo hatutafikia matokeo tunayotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuchangia, nimeangalia katika hotuba Mheshimiwa Waziri wa Fedha amependekeza kufuta utaratibu wa retention kwenye taasisi za Serikali ambazo kimsingi zilikuwa zinaruhusiwa kubakiza fedha ambazo zinakusanywa ili ziweze kutekeleza majukumu yake. Mojawapo kati ya taasisi hizo ni Shirika la Maendeleo la Petrol (TPDC).
Mheshimiwa Naibu Spika, sipingani na wazo la kufuta retention, lakini angalizo ninalolitoa ni kwamba, kuna taasisi nyingine muhimu, ni taasisi za kimkakati kwa mfano TPDC. Najaribu ku-imagine endapo Wizara ya Fedha kupitia Hazina itakapotekeleza agizo la kutoruhusu TPDC kuwa na retention ikachukua fedha zote ambazo TPDC inakusanya ikazipeleka Mfuko Mkuu wa Serikali halafu ikashindwa au ikachelewesha kupeleka fedha TPDC kwa mujibu wa bajeti yake na ikaifanya TPDC ikashindwa kufanya baadhi ya majukumu, nakuhakikishia tutapoteza fedha nyingi kuliko ambazo tunadhani tutaziokoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TPDC ndiyo jicho la Serikali kwenye shughuli zote za gesi. Sasa hivi tumefanikiwa kugundua kiasi kikubwa sana cha gesi lakini walio kwenye biashara ya gesi wote ni wawekezaji binafsi na TPDC ndiyo mbia ambaye anasimamia kwa upande wa Serikali. Moja kati ya kazi zake ni kufanya ukaguzi wa shughuli zinazofanywa na wawekezaji wa gesi ili kujua mapato wanayopata na kujua mgao wa Serikali kama ni sahihi. Kwa hiyo, TPDC wasipokuwa na fedha za kufanya kazi hii, nakuhakikishia tutapigwa bao na hao wawekezaji wa gesi, fedha nyingi sana zitachukuliwa na lile lengo letu la kusema kwamba eti wasibaki na retention ili Serikali iweze kupata fedha nyingi halitafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuwe makini na angalizo langu hapa ni kwamba, tuhakikishe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kupitia Hazina upelekaji (disbursement) wa fedha kwenye taasisi kwa kweli ni jambo ambalo lisije likawa kama utaratibu ulivyo sasa kwa sababu tutaingia kwenye athari kubwa kuliko ambavyo tunatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda nichangie ni suala la value for money kwa miradi ambayo imekamilika. Kuna miradi mingi nchini kwetu ambayo imekamilika lakini haijaweza kuleta manufaa kwa wananchi kama ambavyo imetarajiwa. Kuna maeneo mengi utakuta madaraja, miradi ya umwagiliaji mabilioni yametumika lakini haifanyi kazi kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jimboni kwangu mimi Serikali imetumia fedha nyingi sana kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika wameweza kujenga zahanati za kisasa katika Kata ya Itobo na Tarafa ya Bukene na wameweza kufunga vifaa vya kisasa vya upasuaji. Hata hivyo, sasa hivi ni karibu mwaka mzima umepita majengo ya kisasa yamekamilika, vifaa vya kisasa vya upasuaji vimefungwa huduma za upasuaji hazijaweza kuanza kufanyika. Kwa hiyo, mabilioni yametumika lakini wananchi hawanufaiki chochote na mabilioni hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna haja ya Serikali kujipanga kupitia Wizara ya Fedha na Wizara husika kuhakikisha kwamba pale ambako tumewekeza fedha nyingi na miradi imekamilika, ifanye kazi sasa wananchi waweze ku-enjoy matunda hayo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kushirikiana na Mheshimiwa Waziri wa Afya na TAMISEMI, naomba kabisa kupata suluhisho kuhusu huduma za upasuaji katika vituo vya afya vya Itobo na Bukene ambapo fedha nyingi zimetumika, huduma hii ianze kutolewa, ni mwaka sasa. Vifaa vilivyofungwa vinakaribia kuanza kuota kutu na mabilioni ya fedha yametumika, hatuwezi kukubali hali kama hiyo. Hivyo, nashauri huduma ya upasuaji iweze kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa niliwekee mkazo ni suala la upelekaji wa umeme REA III. Hili ni muhimu sana, nimeona Serikali imetenga fedha za kutosha na nina imani kwa namna ambavyo Wizara ya Nishati na Madini imejipanga na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara kule maeneo ya kwetu na aliongozana na mkandarasi na kuhimiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika baadhi ya maeneo matunda yameanza kuonekana na nina uhakika miradi ambayo iko katika REA awamu ya III itatekelezeka na wananchi waweze kupata manufaa. Kama tunataka kukuza ajira hasa maeneo ya vijijini basi umeme vijijini ni lazima uwepo kwa ajili ya shughuli za kusindika mazao ya kilimo ili yaweze kuongezewa thamani na yaweze kuuzwa sokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii ili jioni hii name niweze kuchangia taarifa hii ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na kwa hiyo mchango wangu kwa kiasi kikubwa utajikita kwenye mapendekezo ya Kamati yangu ya LAAC kama ambavyo yalivyo kwenye kitabu cha taarifa ya Kamati tulichokiwasilisha hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu ya LAAC imependekeza mambo kadha lakini mojawapo ambalo nitaelezea kwa kwa kifupi kwanini tumependekeza ni kwamba katika kamati ya LAAC baada ya kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali tumependekeza kuhusu Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, kwamba yale malimbikizo ya nyuma ya michango ambayo halmashuri zilipaswa kuchangia kwenye Mfuko huo kabla ya sheria mpya ya kufanya jambo hili kuwa sharia, malimbikizo yale kwa hali ya halisi kwa sababu hayawezi kulipika, tumeomba Serikali ianze mchakato wa kuangalia namna ya kuyafuta yale malimbilikizo ya nyuma kabla ya Sheria ya Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu kuwa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumependekeza jambo hili baada ya kuangalia kwa kina karibu halmashauri zote zilizokuwa zikija mbele ya Kamati yetu ukiangalia malimbikizo ya fedha ambazo halmashauri hazikuweza kuchangia kwenye Mifuko hii miaka ya nyuma kabla ya mwaka jana kabla hatujaweka sharia, utakuta halmashauri zina madeni makubwa ambayo kwa hali halisi hayawezi kulipika. Kwa hiyo tukaona kwamba hata kama tukilazimisha halmashauri zilipe malimbikizo hayo ambayo hawakuchangia itakuwa ni kazi bure kwa sababu ni figure kubwa ambazo hakuna halmashauri hizi za kawaida zinazoweza kulipa, kwa sababu kutokana na analysis imeonekana kwamba halmashauri nyingi haya malimbikizo ni makubwa kulingana na mapato yao ya ndani ya mwaka .

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo unakuta halmashuri mapato ya ni bilioni moja, lakini malimbikizo ambayo hawajayapeleka kwenye Mfuko ni zaidi ya bilioni moja, kwa hiyo hakuna namna halmashauri hii inaweza kulipa. Kwa hiyo tumependekeza kwamba yale malimbikizo ya nyuma, jambo la kukusisitiza hapo ni kwamba kabla ya mwaka jana tulipoamua kwamba jambo hili liwe sharia, huko nyuma ambako halmshauri zili-relax na kutengeneza malimbikizo mengi Serikali iangalie namna ya haya malimbikizo kuyafuta, tuanze upya kwa sababu nina uhakika Halmashauri zitaweza kulipa current figure, lakini huo mzigo wa nyuma tusaidie namna ya kuondoa, kwa hiyo hilo ni pendekezo letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tumependekeza baada ya kuangalia taarifa ya Mkaguzi ni kwamba, bado kuna tatizo kubwa la upelekaji wa fedha za maendeleo kwenye halmashauri zetu ambazo zimeidhinishwa kwenye bajeti. Taarifa ya Mkaguzi kwamba bado halmashauri zinakuwa na bajeti za maendeleo ambazo zinaidhinishwa na Bunge lakini mwaka unaisha Hazina haijapeleka fedha za maendeleo kwenye halmashauri na miradi mingi inashindwa kufanyika.

Mheshimiwa naibu Spika, jambo hili limevunja moyo hasa katika maeneo ambayo miradi kwa hatua ya kwanza ilichangiwa na nguvu za wananchi. Leo hii ukipita kwenye majimbo yetu utakuta kuna maboma ya madarasa, nyumba za Walimu, zahanati, vituo vya afya ambavyo wananchi walichangia kwa fedha zao na ilikuwa kazi ya Serikali kukamilisha na halmashauri nyingi zimekuwa zikipitisha fedha hizi kwenye bajeti ili Hazina itoe ili kwenda kumaliziai kazi hizo ambazo zilianzwa na wananchi, lakini miaka yote fedha zimekuwa haziji pamoja na kwamba zipo kwenye bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jambo hili limekuwa likivunja morali ya wananchi kuchangia kwa sababu wamechangia sana lakini maboma yamebaki maboma tu. Kuna maboma mengine yana miaka mitano, sita, saba mpaka 10 hayajaweza kumaliziwa na Serikali. Kwa hiyo tumeiomba Serikali kwamba miradi ya maendeleo ambayo fedha zake zinapitishwa na Bunge, Hazina iweze serious kuhakikisha angalau kwa 90% fedha zinakwenda kwa sababu jambo hili limekuwa likifunja moyo wananchi ambao wanachangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo Kamati imeliona na kupendekeza ni kuhusu udhaifu katika mfumo wa udhibiti wa ndani katika halmashauri nyingi. Taarifa ya Mkaguzi imebaini kwamba kumekuwa na miamala isiyofuata taratibu mingi katika miamala inayofanywa na halmashuri na sisi Kamati tumeona hili jambo linasababishwa na ubovu wa mifumo ya udhibiti wa ndani. Katika dunia ya leo unaweza ukadhibiti kiasi kikubwa miamala ambayo inafanywa kinyume cha taratibu kwa kuwa na mifumo ya kisasa inayozuia.

Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo kama unakuta halmashauri inahamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya amana, fedha ambazo labda zilikuwa kwa ajili ya malipo ya Walimu au mitihani, halmashauri inazihamisha na kuzipeleka kununua mafuta au kufanya jambo ambalo halijakusudiwa. Jambo hili unaweza ukalizuia kama una mfumo wa kisasa wa kudhibiti kwa sababu unatakiwa mfumo ndio ukatae. Ukitaka kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya amana kwenda kwenye jambo lingine ambalo halikubaliki inatakiwa mfumo ukukatalie, yaani inatakiwa jambo hili lizuiwe na mfumo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Kamati tumebaini kwamba mifumo na accounting package ambazo zinatumika kwenye halmashauri bado kuna haja zikaboreshwa zikawa za kisasa na zikaweza kuzuia irregularity mbalimbali ambazo kwa sasa zinafanyika kwa sababu mifumo inaruhusu. Ushauri mkubwa wa Kamati hapa ni kwamba TAMISEMI ijaribu kuja na mifumo ya kisasa ya udhibiti wa ndani wa namna hesabu zinafanyika ili kuzuia irregularity na miamala ambayo inakwenda kinyume cha taratibu. Haya mambo kwa dunia ya kileo yanatakiwa kuzuiwa na mifumo. Ukiwa na mfumo wa kisasa, wenyewe ndio unakuzuia. Ni kama vile sasa hivi ukitaka ku-raise purchase order ya kununua bidhaa fulani, kama kwenye bajeti hela hiyo haipo kwenye maana yake purchase order haitoki, huwezi kui- process ikatoka. Kwa hiyo tunataka mifumo ya namna hiyo kwa dunia ya kisasa ili kuweza kuzuia mambo ambayo hayatakiwi yafanyike. Kwa hiyo kuna kila haja ya TAMISEMI kuja na accounting package ya kisasa ili kuweza kuzuia mambo mengi ambayo yanaweza yakazuilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumegundua ukosefu wa ujuzi wa kutumia mifumo kwa watumishi wengi wa halmashauri zetu. Kumekuwa na matatizo ya miamala mingi kushindwa kufanyika, ripoti kushindwa kuchapishwa katika halmashauri zetu kwa sababu mifumo iliyopo ya TAMISEMI watu walipo kwenye halmashauri nyingi wamekuwa hawana ujuzi na utalaam mzuri wa kuitumia. Kwa hiyo mambo mengi yanashindikana na sababu unaambiwa mfumo haufanyi kazi, lakini kumbe ni utaalam. Kwa hiyo tumependekeza kwamba TAMISEMI iwe na progamu za kutoa mafunzo kwa ajili ya watumishi wa halmashauri mbalimbali ili waweze ku-master hii mifumo ya kisasa iliyopo ili shughuli nyingi za halmashauri ziweze kufanyika kwa mifumo na taratibu za kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa jumla taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa ambapo sisi kama Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa wajibu wetu ni kuangalia maeneo sugu katika taarifa ya Serikali za Mitaa ukilinganisha na miaka ya nyuma, ukiangalia trend utaona kwamba pamoja na kwamba matatizo bado yapo, lakini kwa kiasi kikubwa kadri tunavyokwenda matatizo katika maeneo yote yanapungua; maeneo ya malipo yasiyo na nyaraka, maeneo ya ukiukwaji wa taratibu za manunuzi na maeneo mengi yenye matatizo, ukingalia trend mtiririko ni kwamba kuna improvement kubwa na kwamba matatizo hayo yanaenda yakipungua kadri siku zinavyokwenda. Kwa hiyo ni imani ya Kamati kwamba jitihada zinazofanywa na TAMISEMI zikiendelea tunakwenda mahali ambapo kutaleta picha nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono taarifa yangu ya Kamati ya LAAC kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha. Ahsante. (Makofi)
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na afya njema ili na mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia hoja muhimu sana ya Wizara ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa uwasilishaji mzuri sana na hotuba nzuri sana ambayo imewasilishwa kwa weledi wa hali ya juu, hongera sana Mheshimiwa Ummy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kwa kusema kwamba naunga mkono hoja hii asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene, kwa dhati kabisa ya moyo wangu niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha kwamba Jimbo langu la Bukene kwa mara ya kwanza linapata huduma ya upasuaji kwa vituo viwili vya afya. Huduma ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nichukue fursa hii nimpongeze Naibu Waziri ya Afya Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye alifunga safari baada ya kufanya ufuatiliaji wa muda mrefu na kuja hadi kituo cha afya cha Itobo kufanya uzinduzi kwa niaba pia ya kituo cha afya cha Bukene, hongera sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri hiyo uliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo hivi vya upasuaji ni azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kupunguza vifo visivyo vya lazima vya akina mama na watoto. Kabla ya vituo hivi akina mama waliokuwa wakihitaji huduma za upasuaji katika Jimbo la Bukene walikuwa wakilazimika kusafiri zaidi ya kilometa 80 kutoka maeneo mengine hadi hospitali ya Wilaya ili kupata huduma hii. Lakini sasa huduma hii imesogezwa karibu sana na niseme tu kwamba katika muda wa hii miezi miwili ambayo upasuaji umeanza muitikio ni mzuri sana na tumeweza kufanya operesheni za kutosha na kuokoa maisha ya akina mama na watoto wa ndani ya Jimbo la Bukene.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni moja tu, pamoja na kwamba huduma hii imeanza, lakini kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi. Katika kituo cha afya cha Bukene mganga anayeweza kufanya upasuaji yuko mmoja tu na huyu anaifanya shughuli hiyo kwa muda wa saa 24. Kwa hiyo, inapotokea kwamba anakuwa kwenye majukumu yasiyoweza kuzuilika mgonjwa akifika pale kama anahitaji upasuaji anakosa hiyo huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hivyo hivyo kwenye kituo cha afya cha Itobo, mganga anayeweza kufanya upasuaji kwa sasa tunaye mmoja tu na kwa Itobo ni mbaya zaidi kwa sababu mganga huyu bado ana miezi michache tu ili astaafu. Kwa hiyo, kama hakutakuwa na jitihada za ziada ili kupata mganga basi huenda kituo hiki kikashindwa kutoa huduma ya upasuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Halmashauri ya Nzega tumejaribu kufanya re-allocation ya kuwatoa waganga kutoka Hospitali ya Wilaya kuwapeleka kwenye hivi vituo vya afya lakini re-allocation hii sasa imefika mwisho kwa sababu hata Hospitali ya Wilaya nao wana upungufu. Hata hao wawili huyu aliyeko Bukene na aliyeko Itobo tumewatoa pale Hospitali ya Wilaya ya Nzega. Kwa hiyo, re-allocation ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imefika mwisho haiwezekani tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Wizara itufikirie kama ombi maalum ili tuweze kupata madaktari wanaoweza kupasua wapangwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega na mmoja hususan apelekwe kituo cha afya cha Itobo na mmoja hususan apelekwe kwenye kituo cha afya cha Bukene ili huduma hizi muhimu na nzuri za upasuaji ziendelee kupatikana ili wananchi wetu, na hasa akina mama na watoto waweze kuepukana na vifo ambavyo kimsingi vinaweza kuzuilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni huduma za x-ray katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega. Leo hii tunapozungumza hapa ni miezi mitano sasa x-ray ya Hospitali ya Wilaya ya Nzega imekufa haifanyi, kazi. Hoja yangu hapa ni kwamba tatizo sio kufa kwa x-ray; x-ray ni kifaa ambacho kinafanya kazi kwa hiyo kinaweza kufa. Lakini hoja yangu hapa ni uharaka wa namna ambavyo x-ray iliyokufa inaweza kushughulikiwa ikapona na ikaendelea kutoa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, x-ray ya Hospitali ya Wilaya ya Nzega imekufa tangu tarehe 13 Desemba, 2016 na baada ya kufa tu Mkurugenzi wa Halmasauri ya Nzega aliandika barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ili Wizara wai-engage kampuni ambayo ina mkataba wa kutengeneza hizi x-ray za Phillips ili iweze kuja Nzega na kutengeneza. Lakini speed imekuwa ndogo mno, mpaka leo tunaongelea mwezi wa tano ni danadana tu. Hao mafundi walikuja mara moja wakaangalia vifaa, wakatoweka mpaka sasa hawajaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho tutataka tujue utaratibu au mkataba uliopo kati ya Wizara na hawa watoa huduma wa ku -service hizi x-ray aina ya Phillips ukoje na umekaa vipi kwasababu kama utaratibu ni mbaya basi tupendekeza kwamba Hospitali za Wilaya zenyewe zitafute mafundi au service provider wenye uwezo ili waweze kutengeneza x-ray. Kwa sababu ni jambo ambalo halikubaliki x-ray kukaa miezi mitano imekufa na wagonjwa wanakwenda pale wanakosa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaleta usumbufu mkubwa sana kwa wagonjwa wanaofika Hospitali ya Wilaya ya Nzega na ambao matatizo yao yanahitaji huduma za x- ray wanapata taabu sana. Kwa hiyo, niombe kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majumuisho atoe ufumbuzi, kwamba x-ray ya Hospitali ya Wilaya ya Nzega ambayo miezi mitano sasa imekufa ni lini itaweza kushughulikiwa ili wananchi waweze kupata huduma hiyo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nizungumzie upatikanaji wa dawa katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Kwanza niipongeze Serikali kwa dhati kabisa kwa kutenga hela nyingi za kutosha kununua dawa. Hili kwa kweli ni jambo la kupongezwa, haijawahi kutokea kiwango cha bajeti kilichokwenda kwenye dawa mwaka huu ukilinganisha na miaka ya nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hoja hapa ni sasa madawa yapatikane, kwa sababu kupatikana kwa fedha za kununua dawa ni jambo moja lakini kupatikana kwa dawa pia ni jambo linguine. Kwa sababu utaona kwamba fedha za dawa ambazo zinapelekwa kwenye akaunti za vituo vya afya au zahanati kule MSD kwa hiyo, unakuta vituo vya afya au zahanati vikiomba dawa MSD kunakuwa na out of stock nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega. Taarifa za tarehe 28 mwezi uliopita, ukijumlisha vituo vya afya na zahanati zote tuliomba dawa za shilingi milioni 126 lakini tukapata dawa za shilingi milioni 24 tu, ambayo ni kama asilimia 20 tu. Kwa hiyo, utakuta kwamba sasa hivi tuna balance ya fedha za dawa ambazo ziko MSD, karibu shilingi 503,000,000. Hata hivyo ukiomba dawa sasa upatikanaji wa dawa unakuwa mdogo. Kwa hiyo upatikanaji wa fedha uendane sambamba na upatikanaji wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia 100 na Wizara ya Afya wanafanya kazi nzuri sana. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa Mwaka 2016
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Muswada huu muhimu sana ambao ni Muswada wa huduma ya msaada wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme naunga mkono Serikali kuleta Muswada huu kwa asilimia mia moja na kwa mtazamo wangu ni kwamba Muswada huu umechelewa sana kuletwa. Ulipaswa kwamba uwe umeshaletwa siku nyingi sana, kwa sababu ni Muswada muhimu sana sana kwa watu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono Muswada huu, kwa sababu ni Muswada unaokwenda kusaidia wananchi wetu ambao kimsingi hawana uwezo wa kulipa gharama za mawakili na wanahitaji kupata huduma za kisheria. Pia wote tunafahamu kwamba matatizo ya kisheria ambayo yanaweza kumfanya mtu ajikute yupo mahakamani kwenye mkondo wa kisheria yanaweza kumkuta mtu yeyote yule, bila kujali hali ya kiuchumi, au hali yoyote ile. Pia kuna ushahidi wa kutosha kwamba kuna wananchi wetu wengi tu ambao wamejikuta wanapata matatizo ikiwemo hata kuhukumiwa kufungwa, lakini kimsingi ni kwa sababu tu hawakupata msaada huu muhimu wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kutoa mchango wangu kwa baadhi ya vifungu vya Muswada huu, ambavyo naona inabidi viboreshwe. Muswada huu unakwenda kuwatambua kisheria taasisi ambazo zitakuwa zinatoa huduma za kisheria na ndani ya taasisi hizi kutakuwa na mawakili kutakuwa na wanasheria na kutakuwa na wasaidizi wa kisheria ambao wanaitwa paralegals.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa paralegals wasaidizi wa kisheria sasa hivi tunao lakini Muswada huu ndio unakwenda sasa kuwatambua kisheria na hawa wako maeneo karibu yote ya vijijini, wilaya zote kwenye kata mpaka vijijini, sasa hivi wapo lakini Muswada huu unakwenda kuwatambua kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo naomba liboreshwe kwenye kifungu cha 19 ni sifa za hawa ma-paralegal (wasaidizi wa kisheria) ambao kimsingi wako maeneo yetu ya kata na vijijini kule. Muswada unasema kwamba hawa wasaidizi wa kisheria watakaokuwa wanakaa na wananchi huko vijijini na kimsingi watakuwa wanatoa usaidizi huu wa kisheria bila kuwatoza gharama wale wateja wao wanaohitaji msaada kisheria, sheria inataka wawe na sifa zifuatazo; wawe na degree ya sheria, wawe na diploma ya sheria, wawe na certificate ya sheria.
Mheshimiwa Spika, sipingi vigezo hivi, sipingi wawe na degree, diploma au certificate lakini nilikuwa naomba tuboreshe, kwamba tusibague wale ambao wana elimu chini ya hapo. Kwa mfano watu ambao wana elimu ya kidato cha nne na darasa la saba; kwa sababu katika Kamati tuliita wadau mbalimbali na baadhi ya wadau hawa zilikuwa ni taasisi ambazo tayari sasa hivi zina ma-paralegal, zina hawa wasaidizi wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulipata ushuhuda kwamba sasa hivi nchi yetu tuna wasaidizi wa kisheria, hawa ma-paralegal, waonaweza wakafika takribani 9,000 nchi nzima wamesambaa kwenye kata na vijiji, na walio wengi elimu yao ni kidato cha nne na darasa la saba, na kuna maeneo mengine wengine hawakumaliza hata darasa la saba, ilimradi wanajua kusoma na kuandika, lakini pia wamepata mafunzo ya kisheria ya kuwa paralegal.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliweza kupata mfano wa paralegal mmoja, (msaidizi wa kisheria) ambaye alikuwa maeneo ya watu wa kabila la Wahadzabe ambaye aliweza kuwasaidia Wahadzabe wenzake wasiweze kudhulumiwa ardhi na mwekezaji, wakati huyu ni paralegal ambaye amepewa mafunzo na hajakwenda shule hata darasa la saba na kimsingi anajua tu kusoma na kuandika na amepewa mafunzo ya u-paralegal.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mapendekezo yangu hapa ni kwamba sawa wawe na degree, wawe na diploma, wawe na certificate, lakini tusibague wale wa kidato cha nne, wale wa darasa la saba, hata wale wanaojua tu kusoma na kuandika ilimradi katika maeneo yao wanaweza wakapata mafunzo ya kisheria na wakatoa huduma za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukizingatia hawa ma-paralegal (wasaidizi wa kisheria) ni watu ambao wanaishi vijijini na jamii kule kule. Kwa hiyo, tuki-restrict sana, degree na diploma, tunaweza tukawaengua watu muhimu sana ambao wangeweza kusaidia wananchi wetu katika maeneo ya vijijini na maeneo ya kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu kingine ambacho napendekeza mabadiliko ni kifungu cha 27(b). Kifungu hiki kinawapa mamlaka Majaji na Mahakimu kuamua kesi inapokuja mbele yao kuweza kufanya analysis na kuona kwamba huyu mtu anahitaji msaada wa kisheria na kuagiza Msajili amtafutie usaidizi wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napendekeza haki hii ifikishwe pia kwa Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Kata. Kwa sababu watu wetu wa vijijini kule wana mashauri mengi, mengine yanahusu ardhi, migogoro ya ardhi, ambayo hawaendi mahakamani kwanza, wanaenda kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Kata. Kwa hiyo, wale Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi za Vijiji na Kata hata Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya pia sheria hii iwape uwezo wa kuona kwamba shauri hili linahitaji msaada wa kisheria au shauri hili halihitaji msaada wa kisheria. Kwa hiyo, isiishie kwa Majaji na Mahakimu peke yao, bali uwezo huu upelekwe mpaka kwa Wenyaviti wa Mabaraza ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu kingine ambacho napendekeza maboresho ni kifungu cha 49(2). Kama kilivyo sasa kwenye muswada kinasema kwamba baada ya sheria hii kupitishwa na kuwa sheria, wale wote ambao sasa hivi wanatoa huduma ya msaada wa kisheria baada ya miezi 12 wanatakiwa wasimamishe huduma zao waombe upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ikibaki kama ilivyo kuna hatari ya wananchi ambao sasa hivi wanahudumiwa na ambao baada ya miezi 12 kesi zao zitakuwa hazijaisha kukosa haki ya kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu ni kwamba muswada huu wa sheria utambue kwamba wale wote ambao ni taasisi halali zinazotoa legal aid sasa hivi sheria hii mpya izitambue automatically, kwamba waendelee kutambulika na sheria mpya kuwa ni watoa huduma halali wa msaada wa kisheria badala ya kuwaambia kwamba baada ya miezi 12 wajisajili upya kwa sababu kitendo cha kujisajili upya kinaweza kikafanya shughuli zao zisimame na zile kesi walizokuwa wanaendelea nazo ziishie hapo; italeta usumbufu na kukosesha haki wananchi wetu ambao tayari walikuwa na mashauri ambayo yanaendelea kuhudumiwa.
Kwa hiyo, sheria hii mpya iwatambue automatically na waendelee kutoa hizo huduma muhimu za kisheria ambazo wananchi wetu kwa kweli wanazihitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu kingine ambacho napendekeza kifanyiwe maboresho ni kifungu cha 16(3), ambacho kama kilivyo sasa kwenye muswada kinasema kwamba hii taasisi inayotoa msaada wa kisheria ambayo ndani yake kuna Mawakili, kuna Wanasheria, kuna Paralegal ni kwamba mmojawapo kati ya hawa watu, hawa office bearer, aidha awe wakili au mwanasheria au paralegal akifanya kitendo chochote kinachokiuka maadili ya taaluma basi taasisi nzima inafungiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maboresho yangu hapo ni kwamba tuweze kutenganisha makosa ambayo yamefanywa na individual wakili au mwanasheria au Paralegal yasiiadhibu taasisi nzima ikafungiwa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja. Unaweza kukuta taasisi ina mawakili saba, ina wanasheria kumi, ina paralegal 20, kwa hiyo mwanasheria mmoja akifanya kitendo cha kukiuka maadili basi, eti taasisi nzima ifungiwe. Naona halijakaa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maboresho yangu hapa ni kwamba, taasisi isifungiwe kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa sababu tu eti wakili mmoja au mwanasheria mmoja au paralegal wa ndani ya taasisi hiyo amefanya kitendo cha kukiuka. Badala yake huyo mtu mmoja ambaye amefanya kitendo hicho yeye ndiye aadhibiwe, kama ni kufukuzwa kazi na hiyo taasisi yake basi yambo hilo lifanyike, lakini taasisi nzima isiadhibiwe kwa kosa la mtu mmoja na tukiruhusu jambo hili litasababisha watu wetu kukosa haki muhimu ambayo tunaihitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla niseme kwamba, sisi ni wawakilishi wa wananchi wa hali zote na tuna wananchi wengi kimsingi ambao kiukweli kabisa hali zao haziwawezeshi kumudu kulipia mawakili na kumudu huduma za kisheria ambazo zinalipiwa kwa gharama. Kwa hiyo, muswada huu lengo lake kubwa ni ku-enhance access to justice kwa watu wasio na uwezo wa kifedha wa kuwalipia mawakili na gharama nyingine za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa vyovyote vile mwakilishi yeyote yule ambaye anawakilisha watu wa aina hii hawezi kupinga muswada huu, atauunga mkono kwa sababu unakwenda kutoa suluhisho la wananchi wake anaowawakilisha ambao kimsingi hawana uwezo wa kulipia mawakili; na sasa hivi Serikali inakuja na programu ambayo watu hawa sasa wataweza kupata huduma hiyo bila kulipia, bila gharama yoyote. Kwa hiyo ni muswada ambao kimsingi unapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote na wawakilishi wote wa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema naunga mkono kwa asilimia mia moja muswada huu, na ninasema muswada huu umechelewa sana, ulipaswa uje siku nyingi sana. Nashukuru sana kwa nafasi hii.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi kupata nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia bajeti hii ambayo mimi naiita ni bajeti sikivu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niungane na Waheshimiwa Wabunge wote ambao kwa dhati kabisa wametoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua za dhati anazochukua kulinda raslimali za Nchi yetu ya Tanzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba ujasiri na uthubutu wa Dkt. John Pombe Magufuli haupo tu ndani ya Tanzania bali umevuka mipaka ya Tanzania. Mimi mlinipa heshima mlinichagua kuwa Mbunge kuwakilisha Tanzania kwenye Bunge la nchi za SADC mara zote hivi karibuni nilipokuwa nikienda kwenye vikao vya Bunge la SADC, Wabunge wote wa nchi za SADC ambazo ni nchi kama 14 wakiwemo na Maspika wa nchi zao, tunapokutana, tulikuwa South Africa, tulikuwa Namibia, kila unapojitambulisha kama ni Mbunge umetoka Tanzania baada ya salamu tu, suala linalofuatia ni kuuliza how is Magufuli doing? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wana shauku ya kujua wengine wanauliza huyu mtu kabla hajawa Rais alikuwa nani, wanataka kujua ni kwa sababu ya uthubutu na ujasiri ambao kwa kweli umevuka kiwango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo naipongeza bajeti hii kwa sababu ni bajeti sikivu kwa maana ya kwamba imezingatia maoni ambayo kwa muda mrefu Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukiyatoa na tumekuwa tukitaka yatekelezwe, sasa yamekubalika na ndiyo maana naiita bajeti sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba ukiacha Madini eneo lingine ambalo kuna potential kubwa ya kupata mapato ni eneo la gesi asili. Ushauri wangu hapa ni kwamba Bunge lililopita Bunge la Kumi, mimi nilikuwa kwenye Kamati ya Nishati na Madini tuliunda Kamati Ndogo ambayo tulipitia mikataba ya gesi na kuona loophole na mianya ambayo inaleta upotevu wa fedha kwenye sekta ya gesi asilia. Nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Mipango atafute report ya Kamati Ndogo ya Nishati na Madini iliyoshughulika na gesi ya mwezi Novemba, 2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mapendekezo mengi na ushauri ambao tumetoa ya namna ambayo Serikali inaweza kupata mapato mengi tu ya kutosha kutoka kwenye sekta asilia ya gesi, pamoja na kwamba gesi kubwa ambayo tumevumbua sasa hivi haijaanza kuzalishwa, lakini hiyo hiyo ya Songosongo kuna potential kubwa sana ya kupata mapato ambayo sasa hivi hatuyapati. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha tafuta hiyo report upitie mapendekezo na ushauri nina uhakika utapata mambo mazuri tu hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti hii kwa sababu Jimboni kwangu kuna kero nyingi ambazo nataka zitatuliwe na mambo yote tunayoyahitaji, tunasema watu wetu wanahitaji umeme, wanahitaji maji, wanahitaji barabara, haya yote hayawezekani bila kupata rasilimali fedha na bajeti hii kwa kiwango kikubwa imekuwa very smart, imeainisha namna ambavyo wananchi watalipa kodi na watalipa kodi bila maumivu makubwa jambo ambalo litafanya tupate fedha za kutosha ili tuweze kushughulikia matatizo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu kuna mradi mkubwa wa REA Phase III ambao zaidi ya vijiji 40 kwa mara ya kwanza haijawahi kutokea vinakwenda kupata umeme, lakini kuna vijiji ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikisubiri umeme vijiji vya Mwamala, Igusule, Lububu, Kasela, Kayombo, Karitu na Isagehe kwa kipindi kirefu mno, kila ninapokwenda kule kero yao ni nishati muhimu ya umeme na sasa hili linakwenda kutokea kwa vitendo. Kwa hiyo, ninaipongeza sana bajeti hii kwa kuzingatia hilo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalonifanya kifua mbele kabisa kupongeza bajeti hii ni namna ambavyo bajeti hii imepunguza ushuru wa mazao. Jimbo langu la Bukene asilimia 90 ni vijiji na shughuli kubwa ya wananchi kule ni kilimo cha mpunga, kilimo cha mahindi na hii hii mpunga na mahindi ni mazao ambayo kwetu sisi ni ya biashara, lakini hayo hayo pia ni mazao ya chakula. Kwa hiyo, wananchi wengi wamekuwa wakisafirisha mazao yao kwa ajili ya kuuza, lakini kulikuwa na kero hiyo ya kwamba hata gunia tano/sita chini ya gunia kumi watu walikuwa wanatozwa kwenye vivuko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bajeti imezingatia hilo na kuanzia sasa chini ya tani moja ambayo kama ni magunia ya kilo mia mia magunia kumi hayatatozwa chochote kwenye mageti kwa hiyo nia jambo ambalo wapiga kura wangu wamekuwa wakinipigia simu wakifurahia na kusema kweli kwamba hii Serikali ya Awamu ya Tano kweli ni Serikali kwa ajili ya wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kodi ya majengo na tunafahamu Urban Authority Rating Act inazipa Halmashauri uwezo wa kutoza kodi za majengo, lakini ushauri wangu hapa ni kwamba namna ya utekelezaji ambao unafanyika huko ngazi za chini na niseme hapa kwamba ninafahamu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano siyo kuwanyanyasa au kuwasumbua wananchi na sisi Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kwenye ngazi za Halmashauri ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba Wakurugenzi na wataalam hawakiuki au hawatekelezi jambo hili kwa namna ambayo inaleta madhara, ninafahamu maeneo mengine kwa mfano Nzega, tumeanza kuweka alama kwenye nyumba kwa ajili ya maandalizi ya kwenda kwenye zoezi hilo, lakini maeneo mengine Watendaji wamekuwa wanakwenda kinyume wanaweka alama kwa ajili ya kutoza hadi kwenye nyumba ambazo zimeezekwa kwa nyasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba ambazo zimejengwa kwa matope ambazo sio nyumba za kudumu, na tunajua utaratibu na muongozo ni kwamba kodi ya majengo ilipwe kwenye nyumba za kudumu na nyumba ya kudumu ni nyumba ambayo imejengwa kwa matofali ya saruji au matofari kuchomwa na imeezekwa kwa bati. Lakini sasa maeneo mengine kwa makosa ambayo haya ni makosa ya Watendaji, siyo sera, siyo sheria, ni watendaji maeneo mengine ambako unakuta hata nyumba za nyasi, nyumba za matope ambazo sio za kudumu nazo wanazitosa kodi ya majengo. (Makofi)

Lakini hili ni jambo la sisi hatuwezi kutegemea Mheshimiwa Mpango aende kijijini kwangu kule Semembela akaseme hii nyumba inafaa ni sisi sasa Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kwenye ngazi za Halmashauri tusimamie hilo ili kodi hii isiwe kero kwa wananchi. Lakin nishauri Halmashauri pia zianzishe mfumo wa kuzitambua hizi nyumba, ili uwe na uhalali wa kuitoza nyumba ushuru wa majengo ni lazima uitambue. Kwa hiyo maeneo ambayo nyumba zimeishajengwa na hauwezi kutoa hati basi angalua mfumo wa kutoa leseni za makazi, kama ambavyo Halmashauri nyingine zinafanya basi ufanyike ili nyumba itambulike na baada ya hapo ikionekana ina sifa za kuanza kutozwa kodi iweze kutozwa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nipongeze Serikali kwa uamuzi wa kufanya majadiriano na kukubaliana na Serikali ya Uganda ili bomba la mafuta lipite kwetu, kutoka Uganda mpaka Tanga na hili bomba Jimboni kwangu litapita kwenye Kata kama tano; Kata ya Igusule, Kata ya Mwamala, Kata ya Kasela na Kata Mwangoye. Ushauri wangu yule Mkandarasi Mkuu atakayepewa kazi ya kujenga bomba, basi kazi ndogo ndogo atoe, agawe kwa wakandarasi wa ndani lakini maeneo ambayo bomba la mafuta litapita wale vibarua ambao wanatakiwa kufanya kazi zisizohitaji ufundi basi watoke maeneo hayo hayo ya vijiji, ambalo bomba linaweza kupita ili angalau wananchi waweze kunufaika na bomba hilo kupita kwenye maeneo yao. Naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara muhimu sana, Wizara ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, kwa dhati ya moyo wangu, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za dhati za kuzuia wizi kwenye rasilimali za nchi yetu na hasa rasilimali katika sekta ya madini. Jambo ambalo tunatakiwa wote tuwe clear ni kwamba hakuna anayepinga au anayekataa uwekezaji. Mheshimiwa Rais hapingi wala hakatai uwekezaji na siku zote Mheshimiwa Rais amekuwa akihimiza wawekezaji wa ndani na wa nje waje kwa wingi kadri iwezekanavyo. Mheshimiwa Rais anachochukia ni wizi wa rasilimali zetu na ambao tukiuacha uendelee utaturudisha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bashe asubuhi wakati anatoa taarifa kwa Mheshimiwa Sixtus aligusia kidogo, sisi Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ni wahanga wa kudhulumiwa na haya makampuni ambayo wakati mwingine hayafuati taratibu na sheria zinazotakiwa. Resolute Tanzania Limited wamechimba dhahabu pale Nzega tangu mwaka 1999 na sasa hivi wamesimamisha uchimbaji lakini navyoongea sasa hivi Resolute wameondoka na service levy zaidi ya shilingi bilioni kumi ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega. Mara zote tukifuatilia wanatoa visingizio vya kisheria, by-laws lakini kimsingi wanapaswa watulipe fedha hizi. Nina imani kubwa Serikali hii ya Awamu ya Tano itaingilia kati kutusaidia ili Halmashauri ya Wilaya ya Nzega tusiweze kudhulumiwa shilingi bilioni kumi zetu za service levy ambazo kimsingi ni haki yetu tulipaswa tupate kama sehemu ya ushuru wa huduma kutoka kwa Kampuni hii ya Resolute. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kampuni hii imesimamisha uzaliashaji na haina mfanyakazi hata mmoja lakini tunajua ma-directors wapo na tunajua director mmoja ni Mtanzania na wengine wa nje. Tunajua bado wapo wana issue zao zingine za kikodi na mambo mengine wanaendelea ku-sort out lakini kampuni ipo. Kwa hiyo, bado kuna uhalali wa sisi kuendelea kudai na wao kutulipa stahili yetu kama ambavyo inastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kushauri ni kwamba Mheshimiwa Rais ameonesha mfano kwenye eneo la madini lakini naomba jitihada hizo za Mheshimiwa Rais ziende sasa mpaka kwenye rasilimali ya gesi. Bahati nzuri gesi ambayo tumeigundua kwa kiwango kikubwa hatujaanza kuichimba nako huku kuna dalili kwamba tusipokuwa makini pia kuna uwezekano mkubwa wa wawekezaji kwa maeneo haya wakaendelea kutunyonya au kutudanganya na hatimaye tukajikuta kwamba hatupati stahili zetu kama ambavyo tunatakiwa. Kwa hiyo, jitihada hizi ziende hata kwenye eneo la gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie eneo la wachimbaji wadogo. Napongeza jitihada za Wizara, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Kalemani tumekuwa tukiwasiliana lakini na watendaji wake wa madini, Ofisi ya Tabora na ya Kanda nipongeze kwa jitihada ambazo sasa hivi wanazifanya katika kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogowadogo maeneo ya Nzega na yanayozunguka wanapata leseni na shughuli zao zinarasimishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Nzega kuna maeneo mengi tu ambayo leseni zilizokuwa zinamilikiwa na hii Kampuni ya Resolute ambayo imeondoka na kimsingi walisha-surrender leseni zao. Wananchi wengi ambao sasa wameamua kuondokana na umaskini kwa kufanya shughuli hizi za uchimbaji mdogo mdogo wamekuwa wakiomba leseni ili waweze kuchimba kihalali lakini kutokana na mfumo wa kuomba leseni, mfumo bado unaonesha leseni hizi zinamilikiwa na hawa Resolute, kwa hiyo wananchi kila wakiomba mfumo unawakatalia lakini maeneo hayo yako wazi, Resolute walishaondoka hawafanyi chochote. Kwa hiyo, naomba Wizara ifanye utaratibu ili maeneo haya sasa ndani ya mfumo yafunguliwe ili wananchi na vikundi ambavyo vimejihamasisha, vimeji-organize, wameamua kuondokana na umaskini kwa kuanzisha ajira katika shughuli za uchimbaji mdogomdogo mfumo uweze kuwakubaliana kuomba leseni hizi na kuweza kupata hatimaye wafanye shughuli zao kihalali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya yamezunguka eneo lililokuwa la Mgodi wa Resolute lakini hata maeneo ya Mwangoye ambayo yako ndani ya Jimbo la Bukene pia yanakabiliwa na tatizo hili. Nina imani kubwa sana na Naibu Waziri, Mheshimiwa Kalemani na wafanyakazi wa Ofisi ya Madini Tabora na Kanda, nina uhakika jambo hili liko ndani ya uwezo wao na watalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni bomba la kutoa mafuta Uganda mpaka Tanga. Jimbo langu la Bukene na Wilaya ya Nzega ni moja ya maeneo ambayo yatanufaika na kupitiwa na bomba hili. Juzi Jumatatu nilikuwa Jimboni na kuna Kampuni ya GSB ambayo ndiyo wamepewa kazi ya kufanya tathmini ya mazingira na athari za kijamii, walituita pale ili kutu-sensitize kuhusu bomba hili. Niseme kwamba wananchi wa Jimbo la Bukene na Wilaya ya Nzega wako tayari, wanalisubiri bomba kwa mikono miwili na habari njema tulizopata ni kwamba maeneo yote ambayo bomba litapita kutakuwa na fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ushauri wangu ni kwamba yule mkandarasi mkuu wa bomba ahakikishe kazi zile ndogo ndogo ana-subcontract kwa makampuni ya wazawa ili na wenyewe waweze kufaidi. Pia kazi za vibarua zisizohitaji utaalamu wa juu basi wapewe vibarua ambao wanatoka katika maeneo ya vijiji husika ambapo bomba litapita. Nimeambiwa kwangu pale katika Kata ya Igusule ndipo kutakuwa na kituo kikubwa ambacho kutakuwa na wafanyakazi zaidi ya 1,000. Kwa hiyo, sisi tunalichukulia hili kama ni fursa ya ajira, kupata uzoefu na kuinua hali ya maisha ya wananchi wetu wa Jimbo la Bukene. Kwa hiyo, wananchi wa Igusule, Mwamala, Kasela, Mwangoe na Lusu wako tayari wanalisubiri bomba hili kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu umeme wa REA Awamu ya Tatu. Nichukue fursa kwa dhati kabisa niipongeze Wizara na hasa Naibu Waziri Mheshimiwa Kalemani ambaye alikuja Jimboni kwangu na kuhamasisha umaliziaji wa umeme wa REA Awamu ya Pili. Sasa hivi maeneo yote ambayo umeme umeweza kufanikiwa kumetokea mabadiliko makubwa kabisa kwa hali za maisha na hali za kiuchumi za wananchi. Kwa hiyo, Jimbo langu la Bukene ni mfano wa namna ambavyo nishati ya umeme inaweza kubadilisha maisha ya mahali fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja na nawapongeza sana watendaji wote wa Wizara hii, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niwe mchangiaji katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai; pili, kwa dhati ya moyo wangu kabisa namshukuru sana Rais wetu wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kuleta maendeleo katika Taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kazi kubwa anayoifanya na ambayo inaonekana dhahiri ya kuleta maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ambalo inabidi nichangie ni eneo la afya. Kwanza kabisa naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, kwa taarifa sahihi zilizopo ni kwamba Halmashauri yangu ya Nzega DC ni mojawapo ya Halmashauri 67 ambazo zimepewa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga hospitali mpya. Napongeza sana hatua hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ni matumaini yangu, kama ambavyo tumeelezwa kwamba fedha hizi zinakuja na ramani maalum kutoka Wizarani; na kwamba kwa kuzingatia matumizi ya force account katika ujenzi wa miradi sasa hivi, ni matumaini yangu kwamba shilingi 1,500,000,000 zitatosha kabisa kujenga hospitali hii mpya kwa kutumia force account na ramani maalum ambayo imekuwa tested kwenye ngazi ya Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo liko dhahiri ambalo ni lazima nipongeze ni hali ya upatikanaji wa dawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za Wilaya. Tunafahamu kwamba Kitaifa Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza bajeti ya dawa kutoka bajeti iliyokuwa awali, mwaka 2015 ambayo ilikuwa around shilingi bilioni 31 kwa mwaka, imeongezwa mpaka shilingi bilioni 269 kwa mwaka. Hili ni ongezeko kubwa sana na kwa Halmashauri yangu ya Nzega DC pekee ongezeko hilo limetoka shilingi milioni 300 kwa mwaka 2015 mpaka shilingi milioni 700 mwaka huu. Hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100 na ushee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni jambo ambalo liko dhahiri sana na kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene na Halmashauri ya Nzega DC kwa ujumla, ninapongeza kwa dhati, kwa sababu hali ya upatikanaji wa dawa kwa kweli ime-improve, imeongezeka kwa sababu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo sasa inabidi lifanyike na huu ni ushauri wangu, baada ya kuhakikisha sasa tunapata dawa za kutosha kwa kuwa na bajeti ya kutosha, jambo kubwa ambalo inabidi lifanyike sasa ni ku-address tatizo la uhaba mkubwa wa waganga na madaktari katika vituo vyetu vya afya, hili bado ni tatizo. Mimi katika kituo changu cha afya cha Itobo na Bukene ambavyo ni vituo ambavyo vimejengwa kwa hadhi ya kisasa, vina vifaa vizuri vya kufanyia upasuaji, lakini katika vituo vyote hivi viwili mganga anayeweza kufanya upasuaji ni mmoja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Itobo kuna mganga mmoja tu anayeweza kufanya upasuaji na hata Kituo cha Afya cha Bukene pia kina mganga mmoja tu anayeweza kufanya upasuaji. Sasa kutokana na workload, idadi ya wagonjwa wanaokuja kupata huduma pale, huyu mganga mmoja kwa kweli ameelemewa, hawezi kutoa huduma stahiki inavyotakiwa.

Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba tumeweza ku- address tatizo la access to health services, sasa twende hatua nyingine ya ku-address tatizo la quality (ubora wa huduma za afya) kwa maana ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na Waganga na Madaktari na vifaatiba vya kutosha ili huduma hii muhimu iweze kupatikana kwa wananchi wetu ambao wanaihitaji sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni eneo la miradi ya maji. Kwanza nitumie fursa hii, kama Mbunge wa Jimbo la Bukene, lakini Mbunge katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, kuipongeza Serikali kwa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria. Tunafahamu kwamba Serikali imewekeza shilingi bilioni 600 ili kuhakikisha maji yanatoka Kahama na kufika Tabora Mjini. Kutokana na zoezi hilo, sisi watu wa Nzega tunanufaika; tuna vijiji vingi sana ambavyo vitapitiwa na maji na kufanya wananchi wetu wapate maji salama ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya mradi huo mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria, Serikali kwa kutumia Mfuko wa Maji wa WSDP (Water Sector Development Programme) imetupatia shilingi bilioni tatu kwa ajili ya miradi ya bomba yanayotokana na visima virefu. Katika Jimbo langu la Bukene pekee tunakwenda kupata visima virefu katika Vijiji vya Mambali, Lugulu Lwanzungu, Luhumbo, Bukene yenyewe, Kabanga, Itunda, Kasela, Isagehe, Ilagaja, Lyamalagwa, Mwamala na Kayombo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni vijiji 12 ambavyo shilingi bilioni tatu itatumika kutafuta maji chini ya ardhi na kujenga miradi mikubwa ya kusambaza maji ya bomba. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo liko wazi. Kama mwakilishi wa wananchi, naipongeza Serikali kwa juhudi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kuwe na flexibility katika matumizi ya fedha hizi, kwa sababu eneo letu la Nzega na Mkoa mzima wa Tabora kuna tatizo la kupata maji chini ya ardhi. Sasa hivi mkandarasi yuko site, lakini visima vingi anavyochimba anakwenda mpaka mita 150, 200, lakini anakosa maji. Kwa hiyo, kuwe na flexibility kwamba endapo tutakosa maji chini ya ardhi, fedha hizi ziruhusiwe kutumika katika vyanzo vingine ambavyo siyo lazima iwe chini ya ardhi, kuna vyanzo vya mabwawa, kuna vyanzo kwa mfano maji ya Ziwa Victoria yakifika Nzega yenyewe pia yatakuwa chanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, fedha hizi zitumike kwenye usambazaji kwa sababu kuna uwezekano tukakosa kupata maji chini ya ardhi kwa visima vyote ambavyo tumepanga kupata. Kwa hiyo, ushauri wangu hapa ni flexibility ya matumizi ya fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni la barabara; ninafahamu kwamba sasa hivi mkandarasi yuko site kwa maana ya kufanya upembuzi wa kina kwa barabara ya kilometa 189 ambayo inatoka Tabora kupitia Mambali – Bukene – Itobo – Mwamala – Kagongwa na hatimaye kuunganisha na Mkoa wa Shinyanga. Hii ni barabara muhimu sana kwa sababu itaunganisha Mikoa ya Tabora na Shinyanga kwa kupitia maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa sana wa mpunga, alizeti na mazao mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba Serikali ifanye usimamizi wa karibu sana kwa huyu Mkandarasi anayefanya usanifu wa kina, kwa sababu mkataba unasema, anapaswa kukabidhi kazi hii mwisho wa mwezi wa Kumi na Mbili mwaka huu. Kwa mujibu wa makubaliano ya awali ni kwamba barabara hii katika Miji ya Bukene na Itobo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hoja hii muhimu sana ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati Dkt. Kalemani na Naibu wake Mheshimiwa Subira Mgalu kwa utayari wao wakati wote kuwasikiliza Wabunge na kupokea ushauri wao na kuufanyia kazi. Kiukweli Mheshimiwa Dkt. Kalemani na Mheshimiwa Subira Mgalu ni mfano mzuri wa Mawaziri ambao wanasikiliza Wabunge na kufanyia kazi kero za Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati REA awamu ya III inaanza, Waheshimiwa Wabunge tuliombwa tutoe mapendekezo katika maeneo yetu kwamba ni vijiji gani ambavyo tunadhani ni muhimu vipatiwe umeme. Waheshimiwa wote tulitoa mapendekezo yetu lakini orodha ya REA awamu ya III ilipokuja kulikuwa na mkanganyiko mkubwa sana, vijiji vingi vilikuwa vimerukwa, vimeachwa na vingine ambavyo siyo muhimu ndiyo vilikuwa vimewekwa. Niwapongeze tena Mheshimiwa Dkt. Kalemani alikuwa very flexible, alizingatia kwa umakini hoja za Wabunge na marekebisho makubwa yalifanyika karibu Wabunge wengi maeneo mengi ya vijiji ambayo yalikuwa yamerukwa au yameachwa yakawa incorporated kwenye REA awamu ya III.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu kwa mfano vijiji muhimu kama Vijiji vya Mwamala, Lububu, Kayombo, Sekondari ya Kili, Karitu na vingine vilikuwa vimeachwa kimakosa lakini baada ya kumfuata Mheshimiwa Waziri na kumuelezea umuhimu wa vijiji hivi alikuwa very flexible, aliwasiliana na REA na pia niwapongeze REA kwa sababu nao waliitikia kwa uharaka na sasa hivi tunavyoongea vijiji hivi vimo kwenye REA awamu ya III na kazi nzuri inaendelea. Mheshimiwa Dkt. Kalemani na Mheshimiwa Subira Mgalu hongera sana na naomba muendelee na ari hiyo hiyo ya kusikiliza Wabunge na kufanyia kazi hoja zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea suala la uwezo mdogo wa TANESCO kukidhi mahitaji. Hili jambo ni very serious, inabidi jitihada za makusudi zifanyike ili kuisaidia TANESCO iweze kukidhi mahitaji ya wateja. Hali ilivyo sasa hivi kwa TANESCO kwa kweli siyo ya kuridhisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ya Nzega, Ofisi ya TANESCO Nzega, leo hii kuna malalamiko makubwa sana. Wateja ambao wamelipia ili wapatiwe umeme tangu mwezi Januari mpaka leo hawajaweza kupatiwa umeme, tunakaribia miezi sita (6) sasa. Speed hii ni ndogo mno na kwa standard na level yoyote ile haikubaliki. Haiwezekani mteja alipie kupata huduma tangu Januari mpaka leo tunakaribia Juni hajaweza kupata huduma. Ni kipindi kirefu sana na wananchi wanakata tamaa na huduma ya namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba hiki kilio cha uwezo wa TANESCO, Serikali ikifanyie kazi. Kwa kweli TANESCO wamechoka na uwezo wao ni mdogo sana. Nitakupa mfano, Jimbo langu kuna Kata inaitwa Mambali ni kilometa 40 kutoka Nzega Mjini kina huduma ya umeme, ikitokea technical fault pale TANESCO Mjini Nzega hawana hata uwezo wa kufika kilometa 40, hawana hata gari lolote la kubeba nguzo, kubeba vifaa vya kujengea, hivyo, hawawezi ku-attend technical fault yoyote ambayo iko nje ya Mji wa Nzega na TANESCO Nzega inahudumia radius kama ya kilometa 40 ama 60 hivi. Kwa hiyo, hali TANESCO ni mbaya, hawawezi kukidhi mahitaji ya wateja. Haiwezekani mtu asubiri nguzo miezi sita wakati ameshalipia, hili kwa kweli lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema REA awamu ya III, tatizo ninaloliona hapa ni speed ndogo sana. Nikubaliane kwa sababu REA inachofanya ni kusambaza umeme, kinachotakiwa sasa hizi jitihada kubwa za kusambaza umeme vijijini lazima ziendane na ongezeko la uzalishaji wa umeme kwa sababu huwezi kusambaza bidhaa ambayo hujaizalisha, huwezi kusambaza kitu ambacho huna. Kwa hiyo, niunge mkono hoja aliyozungumza Mheshimiwa Simbachawene kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa na uzalishaji wa uhakika wa umeme wa kutosha ndipo tuusambaze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu REA wanachofanya ni kusambaza lakini huwezi kusambaza kitu ambacho hakijazalishwa. Kwa hiyo, jitihada kubwa bado nashauri kwamba Serikali iendelee na miradi yake ya kuzalisha umeme kwa wingi ikiwemo Stiegler’s Gorge ili tupate umeme wa kutosha ambao ndiyo sasa utasambazwa kwenye vijiji. Hatuwezi kukazania usambazaji wakati hatujui sasa utasambaza nini kama umeme huo haujazalishwa. Kwa hiyo hilo, naomba lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie bomba la mafuta…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara kwa jitihada kubwa inazofanya kuhakikisha kwamba tatizo la maji katika nchi yetu linapatiwa ufumbuzi na kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata maji safi na salama kama ambavyo tumeahidi kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa maji, hasa maeneo ya vijijini bado siyo nzuri na hairidhishi. Nashauri kwamba namna ambavyo tunapima upatikanaji wa maji kuna haja ya kuangalia kama upimaji huu unatupa figures ambazo ni sahihi. Tunasema kwamba upatikanaji wa maji sasa hivi maeneo ya vijijini ni asilimia 58 lakini ukienda maeneo ya vijijini kwenye majimbo yetu jinsi hali ya upatikanaji wa maji ilivyo ukiwaambia wananchi upatikanaji wa maji ni asilimia 58, wananchi wanakushangaa. Hali haiko vizuri kabisa na nadhani kuna haja ya kupima kupata hali halisi badala ya hizi takwimu ambazo kimsingi hazioneshi picha halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani namna wanavyopima hii percentage ya upatikanaji wa maji wanaangalia tu fedha zilizotumika kujenga miradi ya maji na kwamba miradi hiyo ingehudumia wananchi wangapi lakini kimsingi kuna miradi mingi fedha zimetumika, imejengwa imefika mwisho lakini haitoi maji na haimnufaishi yeyote.

Mimi Jimboni kwangu kuna miradi miwili ya tangu wakati ile ya Benki ya Dunia, miradi kumi kila Wilaya, kuna miradi mikubwa zaidi ya milioni 400/400 karibu shilingi bilioni moja imetumika lakini mpaka leo miradi ile haitoi maji, wananchi hawanufaiki. Kwa hiyo, katika mahesabu ya wananchi wangapi wamenufaika na yenyewe utakuta inahesabiwa. Kwa hiyo, nadhani kuna haja ya kuwa na hesabu za uhakika kuliko kuwa na figure ambayo ina-mislead; tunasema asilimia 58 maeneo ya vijijini, lakini kimsingi maeneo hayo bado yako chini sana kwa upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Spika, nimeangalia ukurasa wa 130, Halmashauri yangu ya Nzega imepatiwa shilingi milioni 884 kama fedha za ndani kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji vijijini, lakini kama Halmashauri nzima ni shilingi bilioni 2.6 nyingi ni fedha za nje, za ndani ni shilingi milioni 884. Kwa hali halisi ilivyo ya tatizo la maji fedha hizi ni ndogo mno na najua bila fedha hakuna chochote unachoweza kufanya. Kwa hiyo, nashawishika kuunga mkono pendekezo la kuongeza shilingi 50 kwenye bei ya lita moja ya dizeli na petroli ili tupate fedha za kutosha na Halmashauri zetu zipangiwe fedha za kutosha. Hii shilingi milioni 884 kwa mwaka mzima kwa Halmashauri kubwa kama ya Nzega yenye vijiji zaidi ya 167 ambavyo vyote vina hali ngumu ya upatikanaji wa maji, kwa kweli mimi naona hazitatufikisha popote pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuipongeza Wizara na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kuyafikisha Tabora Mjini ambayo yanapita pia Wilaya ya Nzega na baadae yata- branch kwenda Igunga. Huu ni mradi mkubwa, zaidi ya shilingi bilioni 600 zitatumika, siyo jambo dogo, ni jambo kubwa sana. Rai yangu hapa tu ni kwamba usimamizi wa makini unahitajika ili ujenzi wa mradi huu uende kwa spidi ambayo inatakiwa na muda ambao tumewaahidi wananchi kupata maji waweze kupata maji. Kwa sababu zaidi ya vijiji 110 na wananchi zaidi ya milioni 1.1 ndani ya Mkoa wa Tabora watafaidika na maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kwamba sisi watu wa Nzega na hasa Mkoa wa Tabora kwa ujumla tunaangalia maji haya yanayotoka Ziwa Victoria yatakapofika Tabora; Nzega – Tabora – Igunga, sisi haya ndiyo yatakuwa chanzo sasa cha maji kuyatoa yalipofika kuanza kusambaza maeneo mengine. Kwa sababu Mkoa wa Tabora na hasa Wilaya ya Nzega, tuna tatizo la kupata maji chini ya ardhi, visima vingi vinachimbwa hata ukipata maji lakini ni machache ambayo kiangazi visima karibu vyote vinakauka.

Kwa hiyo, tuna shida ya maji chini ya ardhi, sasa maji ya Ziwa Victoria yakishafika Nzega tunayachukulia kama ndiyo chanzo sasa, kuanzia pale tutaanza kuyasambaza kuingiza ndani na kwenye vijiji vingine. Kwa hiyo, tunachukulia maji ya Ziwa Victoria kama kitakuwa chanzo muhimu cha kutupatia maji sasa na kuyasambaza kuelekea maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, niombe Wizara hapa kuwe na flexibility kidogo. Sasa hivi Halmashauri ya Wilaya ya Nzega tuna shilingi bilioni tatu za miradi mikubwa ya visima vya maji, lakini mkandarasi tuliyempa kazi amechimba visima karibu 26 lakini visima ambavyo vimepata maji ya wingi wa lita 4,000 kwa saa ni visima vitatu tu kwa sababu ni shida sana kupata maji chini ya ardhi. Kwa hiyo, kuna hofu kubwa tarehe 30 Juni itafika hela hazijatumika na zitapaswa kurudi na zinarudi siyo kwa sababu ya uzembe wa Halmashauri kutozitumia lakini kwa hali halisi na nature ya Nzega maji chini visima vimechimbwa vya kutosha lakini vyote hakuna maji.

Mheshimwa Spika, kwa hiyo, naomba hapa flexibility ya Wizara kwamba fedha hizi sasa badala ya kutumika kutafuta maji chini ambayo hayapo zitumike kwa usambazaji (distribution) kutoka kwenye vyanzo vya mabwawa na hapo ambako maji ya Ziwa Victoria yatafika. Kwa hiyo, naomba flexibility hiyo Wizara ijaribu kuiangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo kuhusu skimu za umwagiliaji. Kwangu mimi naona hii ni solution ambayo itafanya wananchi wetu ambao hawana uhakika wa maji wawe na kilimo cha uhakika kwa kuwa na mabwawa ya umwagiliaji. Halmashauri ya Wilaya ya Nzega tumepata mabwawa mawili ya Kahama Nhalanga na Lusu, kazi imekamilika, wananchi wameanza kunufaika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ni kubwa mno, vijiji 167, vijiji viwili tu kupata mabwawa haitoshi. Tunapenda mabwawa haya watu wa Mambali ambako tathmini ilifanyika kuna uwezekano wa bwawa kubwa kujengwa lijengwe; watu wa Kasela ambako tathmini imefanyika kuna uwezekano wa bwawa kujengwa, lijengwe; watu wa Mwangoye na vijiji vingine vingi tu ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ambavyo tathmini za mabwawa makubwa ya umwagiliaji zilifanyika na zinasubiri tu pesa ni vema mabwabwa yakajengwe. Kwa hiyo, naiomba Wizara ijaribu kufanya upendeleo maalum kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kwa sababu ni halmashauri kubwa, ina vijiji vingi na mtawanyiko wa mvua siyo mzuri, haya mabwawa yatatusaidia katika kuhakikisha kwamba tunapata kilimo cha uhakika.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, nisisitize tu kwamba Serikali ikubali ombi la Waheshimiwa Wabunge la kuongeza hiyo shilingi 50 kwenye bei ya lita ya petroli na bei ya lita ya dizeli. Tuumie sasa lakini tunaumia kwa ajili ya manufaa ya kupata fedha ziende kwenye miradi ya maji ili wananchi wetu waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la msingi tu hapa ni kwamba fedha hizi kweli ziende kwenye miradi ya maji na iwe maji vijijini. Tunafahamu kwamba miradi mikubwa ya maji maeneo ya mijini hasa miji mikubwa ya Dar es Salaam, Arusha na miji mingine ina vyanzo vingine vya fedha, kwa hiyo, hizi fedha za tozo ya mafuta ziwe ni za maji vijijini siyo maji mijini...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nami kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia kwenye taarifa hii muhimu sana inayohusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa pamoja na Mwongozo wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nichukue fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kazi kubwa anayofanya. Takwimu rasmi ziko wazi kwamba uchumi wa Tanzania ndiyo uchumi unaokua kwa kasi kuliko chumi zote za nchi za Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeupitia Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa na kwa mujibu wa mpango huu, Serikali imepanga kukusanya na kutumia takribani shilingi trilioni 33 na kati ya hizi takribani shilingi trilioni 23 ambayo ni sawa na asilimia 69 ni fedha ambazo zinatokana na mapato yetu ya ndani. Naipongeza Serikali na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuja na mpango ambao hatimaye tutatengeneza bajeti ambapo asilimia 69 karibu asilimia 70 ya fedha zote zitagharamiwa kutokana na fedha zetu wenyewe za ndani. Natoa pongezi sana kwa hatua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia vipaumbele vilivyoorodheshwa kwenye mpango huu lakini nina ushauri kwamba kipaumbele namba moja ambacho tunatakiwa kupambana na kuhangaika nacho ni kukuza uwezo wa kukusanya mapato. Katika bajeti siku zote tunazungumza namna tunavyotumia fedha lakini bajeti na mpango siku zote vina pande mbili; kwanza inabidi uwe nazo ndiyo unaweza kuzitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kipaumbele changu cha kwanza nadhani Serikali itumie nguvu, itumie mikakati na ubunifu na wataalam wote ilionao ili kuhakikisha kwamba tunapata mapato kwanza kabla ya kuona kwamba tutayatumiaje. Hii itawezekana tu pale ambako tutaweza kuwa wabunifu na kuja na vyanzo vipya vya mapato. Tupanue wigo na tuondokane na zile njia za kiasili (traditional ways) za kupata fedha ambazo kila mwaka ndiyo tunazo hizo hizo. Kwa hiyo, lazima tuumize vichwa tuje na vyanzo vipya. Mazingira yetu ya kiuchumi na kijamii yanawezesha jambo hiki kuwezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni lazima tuwe na namna ambayo tutaweza kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato. Kwa sababu kuwa na vyanzo vya mapato ni jambo moja lakini kuweza kukusanya na kudhibiti mianya ya upotevu wa hayo makusanyo ni jambo lingine. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba ni lazima Serikali kwa kupitia Wizara ya Fedha iimarishe namna ambavyo mapato yatakusanywa lakini yatadhibitiwa ili yasiweze kuponyoka na kwenda kwenye vyanzo vingine ambavyo havitarajiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa kuwa na mapato unajionyesha kutokana na mwenendo wa namna ambavyo tumekuwa tukipanga bajeti lakini namna ambavyo tumekuwa tukitoa fedha kwenda kutekeleza bajeti hizo. Taarifa ya Kamati ya Bajeti ukurasa wa 16 umebaini kwamba kumekuwa na mwenendo usioridhisha wa utoaji wa fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka 2016/ 2017 bajeti ya fedha za maendeleo ilikuwa ni shilingi trilioni 11 lakini zilizopelekwa zilikuwa ni shilingi trilioni 6.4 tu ambayo ni asilimia 55 tu ya fedha zilizopaswa kupelekwa. Mwaka 2017/2018 bajeti iliyotengwa ili kwenda kugharamia miradi ya maendeleo ilikuwa shilingi trilioni 11.4, lakini fedha zilizoweza kupatikana na kwenda zilikuwa shilingi trilioni 6.5, hii ni sawa na asilimia 57 tu. Ndipo hapo umuhimu wa kuwa na fedha unakuja kabla ya kufikiria kutumia. Kwa sababu kupanga bajeti ni jambo lingine lakini kuzipata fedha ili ziende zikagharamie ni jambo lingine. Ndiyo maana unakuta bajeti ni kubwa lakini fedha zinazokwenda ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nadhani ni kipaumbele, nikubaliane na maoni ya Kamati ya Bajeti ukurasa wa 24 ambapo imependekeza Serikali ione kwamba ni jambo la kipaumbele kutenga na kupeleka fedha kwa ajili ya kuezeka na kukamilisha maboma ya zahanati na shule yaliyopo nchi nzima. Ukipita kwenye Majimbo ya Wabunge wengi utakuta kuna maboma mengi ya zahanati, madarasa ya shule ambayo wananchi walitumia nguvu zao lakini Serikali iliahidi ingekamilisha lakini haikukamilisha. Jambo hili linavunja moyo wananchi. Nakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti yaliyoko ukurasa wa 24 kwamba Serikali itafute fedha, itenge na ipeleke fedha ili maboma ya zahanati na shule yakakamilishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye maji. Kuna matatizo kwenye sekta ya maji. Wakandarasi wengi wamefanya kazi lakini hawajalipwa mpaka leo. Katika Halmashauri yangu ya Nzega kuna wakandarasi wanadai zaidi ya shilingi milioni 560 tangu mwezi Juni. Wamekamilisha miradi ya maji, wametengeneza performance certificate lakini hawajalipwa. Kwa hiyo, jambo hili linadhoofisha ukamilishaji wa miradi ya maji na baadaye linaleta malalamiko kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ni kwamba miradi hii kama ya maji ambayo ina vyanzo vya fedha mahsusi, Serikali ihakikishe kwamba miradi hii inakamilika. Kwa hiyo, hawa wakandarasi wa maji ambao naamini wako nchi nzima, fedha zao zitengwe, zipelekwe na wakalipwe ili miradi ya maji iweze kukamilishwa na wananchi wetu waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni miradi ya umeme, REA III kasi ni ndogo. Natambua dhamira ya dhati ya Serikali lakini kuna haja ya kuongeza kasi na hii maana yake ni kuongeza fedha ili wakandarasi hawa waweze kutandaza na kusambaza umeme kwa kasi ambayo inatarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia kwenye hotuba hii muhimu sana ya jambo muhimu sana la maji.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuipongeza Wizara; Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Makatibu na wataalam wote wa Wizara kwamba pamoja na kwamba bado changamoto ya maji ni kubwa, lakini kuna kazi kubwa ambayo inaonekana inafanyika kwa hiyo nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha uliopita kwa maana ya 2017/2018, Halmashauri yangu ya Nzega DC kupitia Mpango wa Water Sector Development Programme (WSDP) ilipata karibu one billion ya kutekeleza miradi ya maji. Kwa hiyo, pale halmashauri sisi tulifanya usanifu tuka-engage wakandarasi wa miradi mikubwa mitatu ya visima virefu, lakini tangu wakati huo tulikuwa hatujapata go ahead ya Wizara ya kuwaruhusu wakandarasi wale waanze sasa kufanya kazi. Tulifuatilia, niliwasiliana na Mheshimiwa Naibu Waziri na naipongeza Wizara kwamba sasa hivi, muda mfupi tu, kama mwezi mmoja uliopita, Wizara imetoa go-ahead ili wakandarasi wale sasa waanze kutekeleza ile miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilichotokea hapa ni kwamba wakandarasi wale tuliwa-engage mwaka wa fedha uliopita mwezi Juni, 2018 na karibu mwaka sasa umekaribia kuisha, kwa hiyo wakandarasi wale sasa hivi wanaomba review ya mikataba kwa sababu wanadai kwamba bei za vitu zitakuwa zimebadilika na vitu kama hivyo. Sasa rai yangu kwa Wizara ni kwamba kwa sababu Wizara wamechelewesha huo mchakato, kwamba badiliko lolote ambalo litatokea kwa maana ya bei basi Wizara iwe tayari kuli-accommodate ili fedha ziweze kutosha na miradi ile ifanyike. Kwa sababu ni kweli tuliwa-engage mwaka sasa umepita na huenda kweli baadhi ya bei zimebadilika.

Mheshimiwa Spika, angalizo lingine ni kwamba kwenye kitabu cha Wizara ya Maji mwaka huu halmashauri yangu imepangiwa shilingi milioni 620 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya maji. Kwa hiyo, hofu yangu ni kwamba isije ikawa hizi milioni 620 za mwaka huu zikatumika kulipia ujenzi wa miundombinu ya hii miradi ya mwaka wa fedha uliopita. Ninaomba Wizara wawe makini kwamba hizi milioni 620 zilizopangwa zilizo kwenye kitabu hiki zitumike kwa ajili ya miradi mipya, miundombinu mipya itakayojengwa na wala zisije zikatumika tena kwa miradi hii ya mwaka wa fedha uliopita kwa sababu hii ilikuwa na fedha zake na hizo fedha zake ndiyo zitumike.

Mheshimiwa Spika, kama ni kuchelewesha ni Wizara ilichelewesha na ninaamini kwa sababu fedha zilikuwa zinatoka Wizarani basi wanazo kule na zilezile ndiyo zitekeleze hii miradi ya nyuma na hizi milioni 620 zitekeleze miradi mipya ambayo tutaisanifu kwa ajili ya mwaka huu wa fedha unaoanza mwezi Julai unaokuja.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu mradi wa Ziwa Victoria; nimeona kwenye kitabu cha bajeti zimetengwa milioni 500 za ndani lakini na bilioni 23 za nje kwa ajili ya kutekeleza mradi huu wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyafikisha Tabora Mjini na Igunga kupitia Nzega. Tulilalamika kwamba usanifu wa mwanzo wa mradi huu uliruka baadhi vijiji lakini naipongeza Wizara kwa sababu imelizingatia hili, vile vijiji vilivyorukwa vimeingizwa kwenye usanifu lakini tatizo ni kwamba baada ya kuingizwa vijiji hivi vingi vimepewa gati moja tu au magati mawili.

Mheshimiwa Spika, vile vijiji vya zamani vilivyokuwemo kwenye usanifu wa zamani unakuta kijiji kama kina vitongoji saba kimepewa magati saba, kama kijiji kina vitongoji nane kimepewa magati nane, lakini hivi vilivyorukwa ambavyo sasa vimeingizwa unakuta kijiji kimepewa gati moja, sasa unakuta kijiji kina vitongoji nane lakini kimepewa gati moja tu, maana yake ni kitongoji kimoja tu ndiyo kitapata maji. Kwa hiyo hofu yangu ni kwamba tukiacha hivi ilivyo badala ya kuona kwamba wananchi wamepelekewa maji kitakachotokea ni malalamiko makubwa kwa sababu vile vitongoji vingine vyote vitakuwa havijapata maji na tutakuwa hatujafikia lengo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ushauri au ombi langu hapa ni kwamba hivi vijiji ambavyo vilikuwa vimerukwa na sasa vimeingizwa na vyenyewe vipatiwe idadi ya magati kama vile vijiji vya mwanzo kulingana na vitongoji ambavyo viko kwenye vijiji husika. Vijiji ambavyo vilikuwa vimerukwa ni Ilagaja, Bulambuka, Isalalo, Mizibaziba, Mwamalulu, Mabisilo, Mihama, Ilela Mhina, Kiloleni na Kipugala. Vijiji hivi vipatiwe magati ya kutosha ili kwa kweli waweze kufurahia na wao maji ya kutoka Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, tulifanya ziara na katika ziara yetu tulifanya ukaguzi wa miradi ya maji, miradi mingi ilikuwa ni ya maji, hasa ya vijijini. Nashauri maeneo ya vijijini Wizara ije na mwongozo kwamba usanifu wa miradi ya maji ya vijijini basi usanifiwe kwa namna ambayo utaendeshwa kwa pampu zitakazotumia umeme wa jua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo ya vijijini hizi pampu za dizeli zina gharama kubwa na unakuta watumia maji wa vijijini wameshindwa kabisa kuendesha miradi hii na hata kunufaika na hayo maji kwa sababu maji yamewafikia, wameyapata, lakini gharama zinakuwa kubwa na kuna vijiji vingine mradi hautumiki kabisa kwa sababu wananchi wameshindwa. Mimi kwangu kule nina Miradi wa Mahene, Nawa, Buhondo, Sojo, Ikindwa, ni miradi mikubwa, mirefu, inafanya kazi lakini hata bei ya shilingi 100, 200 kwa ndoo wananchi kule vijijini bado wanasuasua kuweza kuimudu. Kwa hiyo napendekeza kwamba usanifu wa miradi ya maji ya vijijini usanifiwe kwa namna ambavyo itaendeshwa kwa pampu za umeme wa jua badala ya dizeli, dizeli bado ni gharama na wananchi wanashindwa kuimudu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu mwingine ni kwamba maeneo mengi ya vijijini tu-focus kwenye visima vifupi badala ya virefu kwa sababu kisima kirefu kimoja ambacho kinagharimu milioni 300, 400 unaweza ukapata visima zaidi ya kumi, 15 vifupi. Kwa hiyo katika maeneo mengi ya vijijini, kwa mfano kule kwangu nime-experience, ukijenga kisima kirefu unanufaisha kijiji kimoja unatumia milioni 400, milioni 400 hizo hizo ukisanifu visima vifupi vya pampu ya mkono unapata visima kumi mpaka 15 na eneo ambalo unahudumia linakuwa pana kwa maana ya vitongoji na vijiji vingi.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile gharama ya kuendesha pampu ya mkono kwa wananchi wetu wa vijijini ni nafuu haihitaji fedha kulikoni kisima kirefu ambacho kinahitaji fedha za dizeli na kuendesha. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba visima vya vijijini visanifiwe kwa…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia katika Wizara ya Afya ambayo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza kwa dhati Waziri wa Afya, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kwa kazi kubwa anayofanya na hakuna mtu yeyote ambaye ana mashaka na uchapakazi wao. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka miwili iliyopita, nilisimama hapa Bungeni nikalalamika sana kuhusu ubovu wa X-Ray katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega ambapo kuna wakati fulani ilikuwa inachukua mpaka miezi sita X-Ray haifanyi kazi. Leo hii nasimama hapa kutoa pongezi za dhati kwa niaba ya wananchi wote wa Wilaya ya Nzega kwamba Serikali sasa imesikia kilio hicho na imetupatia X-Ray mpya kabisa ya kidigitali ambayo inafanya kazi kwa ufanisi na inatoa picha za ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya aananchi wa Nzega lazima niishukuru Serikali kwa kutupatia X-Ray hiyo mpya kabisa. Kwa hiyo, sasa hivi uchunguzi wa magonjwa unafanyika kwa usahihi na maana yake ni kwamba tiba itapatikana kwa usahihi. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Serikali. Nimeangalia ukurasa wa 54, kwa kweli kuna mambo makubwa ambayo sisi kama wawakilishi wa wananchi ni lazima tuipongeze. Kabla ya mwaka 2017, kuna matibabu makubwa ya kibingwa yalikuwa hayawezi kufanyika hapa nchini, lakini sasa yanafanyika. Kwa mfano, kupandikiza figo, jambo hili limeokoa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa kipindi hiki tu ambapo wagonjwa 38 wameweza kupandikizwa figo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna mambo makubwa yamefanyika. Kwa mfano, kabla ya mwaka 2017, hatukuwa na uwezo wa kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto wadogo. Hili ni jambo kubwa ambalo sisi wawakilishi wa wananchi tunatakiwa kutoa pongezi za dhati. Fikiria mtoto anazaliwa hawezi kusikia, lakini anafanyiwa operesheni, anawekewa vifaa vya usikivu, anaweza kusikia. Kwa hiyo, anaweza kufanya mambo yote ya kupata elimu na haki nyingine zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni jambo ambalo siyo dogo, ni kubwa na ninachukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa kufanikisha jambo kama hili. Pia jambo kama hili linaokoa fedha nyingi ambazo zinatumika katika mambo mengine muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaungana na mapendekezo ya Kamati ya Huduma za Jamii. Ukiangalia ukurasa wa 20 mpaka 21, Kamati imeitaka Wizara ya Afya kuwaangalia kwa makini wahudumu wa afya katika ngazi ya jamii kwa sababu hawa wanasaidia sana katika kuhakikisha kwamba tunapata kinga na kila mmoja anajua kwamba kinga ni bora kuliko tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mapendekezo yote ya Kamati ya Huduma za Jamii yaliyo katika ukurasa wa 20 mpaka 21 ninakubaliana nayo kwamba Wizara ya Afya iangalie namna ambavyo itaweza kuwa-accommodate hawa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili tuweze kuhamasisha akina mama wakajifungulie kwenye zahanati, tuweze kuhamasisha matumizi bora ya vyoo, tuhamasishe unywaji wa majisafi na salama ili kuepuka magonjwa ambayo yanaweza yakasumbua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kuongelea ni uhaba wa watumishi hasa Waganga katika zahanati zetu. Ningependa Wizara ingetoa mwongozo wa kuhakikisha kwamba angalau katika kila zahanati kunakuwa na Mganga.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ilivyo sasa hivi, kwa mfano katika Halmashauri yangu ya Nzega Vijijini, katika zahanati 39 tulizonazo, zahanati 12 hazina kabisa Waganga, zinaendeshwa na Ma-nurse. Jambo hili siyo jema kwa sababu tunapaswa tuwe na Waganga ambao mgonjwa akifika anahudumiwa, anakuwa prescribed na Mganga halafu ndiyo wanahudumiwa na Nurse.

Mheshimiwa Naibu Spika. Zahanati 12; Zahanati ya Mboga, Zahanati ya Semembela, Zahanati ya Nkindu, Ikindwa, Lakui, Mwangoye, Mwasala, Malilita, Uhemeli, Mirambo Itobo, Magengati na Shila; hizi zahanati hazina kabisa Waganga. Kwa hiyo, ombi na ushauri wangu kwa Wizara ni kwamba tuhakikishe kwamba zahanati hizi ambazo tayari zipo angalau zinakuwa na Waganga ili wagonjwa wakifika pale waweze kupata huduma za tiba za uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili litakwenda sambamba na Ilani yetu ya uchaguzi ambayo tunahimiza kwamba kila Kijiji kiwe na zahanati. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba tunakwenda kujenga zahanati za kutosha nyingi. Sasa zahanati ili ziweze kufanya kazi, ni lazima ziwe na Waganga na Ma-nurse. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nawapongeza Wizara kwa kazi kubwa wanayofanya kuimarisha afya katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kwanza, nianze kwa kuwapongeza Waziri na Naibu Mawaziri wawili wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi uliopita niliuliza swali hapa Bungeni kuhusu barabara ya kilometa 149 inayoanzia Tabora kupitia Mambali – Bukene- Itobo na hatimaye Kagongwa. Barabara hii ndiyo barabara pekee iliyo bado kwenye hali ya changarawe inayotoka Tabora mpaka Kahama na barabara hii kwanza ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na pili, imo kwenye Ilani yetu ya uchaguzi. Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kutupatia milioni 789 ambazo zimekamilisha usanifu wa awali na mwezi uliopita Waziri alijibu swali langu kwamba mwezi wa sita ule usanifu wa kina unakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwamba Wizara ijitahidi kwamba kama ilivyoahidi (commit) kwamba ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza kabla ya 2020 wakati ambako tutaingia kwenye uchaguzi. Kwa hiyo, nina imani na Serikali yangu najua hili litafanyika lakini ni wajibu wangu kulikumbushia.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii wakati tunasubiri iweze kujengwa kwa kiwango cha lami, inapaswa iwe inapitika wakati wote. Ninaipongeza Wizara kwamba nimeangalia kwenye kitabu cha hotuba ya Waziri kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya kuhakikisha barabara hii wakati wote inapitika. Fedha hizo zipo kwenye mafungu mawili; fungu la kwanza ni fedha zinazotoka Mfuko wa Barabara na fungu la pili ni fedha zinazotoka Mfuko wa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa Mfuko wa Barabara, barabara hii imepangiwa milioni 332 na upande wa fedha zinazotoka Serikali Kuu, barabara hii pia imepangiwa milioni 330. Ni rai yangu kwa Wizara kwamba fedha hizi zilizotengwa zipatikane na zipelekwe ili barabara hii iweze kuwa inatengenezwa kila wakati na hasa yale matengenezo ya muda maalum (periodic maintenance) wakati wa mvua barabara hii huwa inaharibika vibaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fedha ambazo zimepangwa kwa ajili ya Mkoa mzima wa Tabora kama bilioni 2.4 kwa ajili ya kutengeneza kilometa 1180. Sasa hoja yangu hapo ni kwamba fedha hizi zimepelekwa kwa ujumla, zinasema tu ni za Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kutengeneza kilometa 1180 lakini Mkoa wa Tabora una Wilaya 7 na zote zina barabara hizi za changarawe. Kwa hiyo, hotuba ya Waziri haijaainisha kwamba ni kiasi gani kitatengeneza barabara zilizopo Nzega, kiasi gani Sikonge, Kaliua au Urambo. Kwa hiyo, imewekwa jumla na hatari yake ni kwamba fedha zote zinaweza zikaelekezwa Wilaya 1 au 2 halafu zingine zikakosa. Kwa hiyo, tuainishiwe kabisa hizi bilioni 2 ni kiasi gani kitakwenda kila Wilaya ili angalau tuwe tunajua ufuatiliaji utakuwaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Miaka miwili nyuma hapa niliomba minara ya simu ya Kata 4; Kata ya Kahamahalanga, Kata ya Karitu, Isagehe na Semembela lakini ni kata mbili tu ambazo zimepata hiyo minara ya simu; Kata ya semehembela na Kata ya Karitu bado hazijapata ingawa zilikuwa kwenye orodha ambayo Mheshimiwa Waziri aliitoa ya kata ambazo zitapatiwa minara ya simu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunajua kwamba sasa hivi maisha ya sasa ni mawasiliano ya simu, kwa hiyo, kunapokuwa na maeneo tunayaacha bila kuyapatia mawasiliano ya simu za mkononi kama ilivyo Semembela na Karitu, maana yake ni kwamba tunawaacha nyuma ya ulimwengu wa kisasa. Sasa hivi maisha ya kisasa kwa sehemu kubwa simu za mkononi zinachangia, ukiwa na simu za mkononi utaweza kulipa ada za watoto, ankara au madai mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunapeleka umeme vijijini, tunataka wananchi wetu wa vijijini waweze kulipia LUKU na bili za umeme huko huko wakiwa vijijini. Kwa hiyo, kuna umuhimu sana wa maeneo ambayo hayana minara ya simu yaweze kupatiwa minara ya simu. Nitumie nafasi hii kuikumbusha Wizara kwamba Kata ya Semembela na Kata ya Karitu ambayo tangu miaka miwili nyuma ipo kwenye orodha, safari hii na yenyewe kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iweze kupata mawasiliano hayo muhimu sana ya simu za mkononi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja asilimia mia moja, asante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia taarifa hizi mbili ambazo zimewasilishwa leo hapa Bungeni. Kwa kuanzia naunga mkono taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambayo mimi pia ni Mjumbe kama ambavyo imewasilishwa na Mwenyekiti wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mojawapo ya kazi za Kamati ya LAAC kikanuni ni kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu katika matumizi ya fedha za umma zinazopelekwa kwenye Serikali za Mitaa. Sasa mimi nilipata bahati ya kuwa pia kwenye Kamati hii ya LAAC kwenye Bunge la Kumi na sasa hivi pia niko kwenye Kamati hii ya LAAC.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema katika eneo hili la maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi ya fedha za umma zinazopelekwa kwenye Serikali za Mitaa ni kwamba, pamoja na kwamba maeneo haya yenye matatizo sugu hajashughulikiwa kikamilifu yote, lakini kuna improvement kubwa sana ukilinganisha hali ilivyokuwa miaka mitatu, minne nyuma kwenye maeneo haya haya na hali ilivyo sasa pamoja na kwamba hayajakwisha kabisa lakini improvement kubwa sana ambayo inatia moyo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia eneo moja la mapato ya ndani, kama ambavyo tunafahamu vyanzo vikubwa viwili vya fedha kwenye Serikali za Mitaa ni fedha zinazotoka Serikali Kuu na fedha ambazo ni makusanyo ya ndani ya halmashauri yenyewe. Sasa Kamati yetu baada ya kupitia halmashauri kadhaa na kufanya mahojiano jambo ambalo limebainika wazi ni kwamba halmashauri zilizo nyingi karibu zote zina tatizo kubwa sana la kushindwa kukusanya mapato yao ya ndani kwa mujibu wa bajei zao ambazo zilikuwa zimepangwa. Ukisikia tunasema halmashauri haikuweza kukusannya mapato ya ndani maana yake ni kwamba kuna kazi ambazo zilipaswa zifanywe hazikufanywa, ndiyo maana yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, huu mwaka wa fedha ambao tunauhoji ambao taarifa yake imewasilishwa ni mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambako miongozo ya kibajeti ilikuwa inazitaka halmashauri zichangie kutoka mapato yake ya ndani, zichangie asilimia 60 kwenda kwenye miradi ya maendeleo. Kwa hiyo ukisikia tunasema halmashauri haikukusanya mapato yake ya ndani kwa mujibu wa bajeti maana yake ni kwamba hizi fedha zitakazopelekwa kwenye maendeleo hazikupelekwa na kama hazikupelekwa maana yake kuna kazi za maendeleo zilizokuwa zinapaswa zifanywe hazikufanyika, kuna madarasa yalikuwa yajengwe hayakujengwa, kuna zahanati zilizokuwa zijengwe hazikujengwa na shughuli nyingine mbalimbali za kimaendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo impact ni hiyo, tunaposema halmashauri zinashindwa kukusanya mapato yake ya ndani haiishi hapo maana yake tunasema kuna shughuli za kimaendeleo zilizotakiwa zifanywe hazikufanyika na hii ndiyo inafika wakati wanafunzi wanamaliza darasa la saba wamefaulu kwenda kidato cha kwanza, tunajikuta madawati hakuna, vyumba vya madarasa hakuna, ni kwamba hayo yote yaliyokuwa yafanywe hayakufanywa kwa sababu halmashauri hazikukusanya mapato ya ndani na ile asilimia iliyopaswa kwenda kwenye miradi ya maendeleo haikuweza kwenda na hili haliathiri tu miradi ya maendeleo, lakini hata matumizi ya kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na halmashauri kushindwa kukusanya ndiyo maana karibu halmashauri zote sasa hivi zina tatizo kubwa, Madiwani hawalipwi kwenye vikao vyao vya Kisheria na unakuta kwa mfano pale Nzega halmashauri ya Nzega DC sasa hivi hata Madiwani wanashindwa hata kupita hesabu wanadai halmashauri kiasi gani kwa sababu wakati mwingine wakienda kwenye kikao wanalipwa posho ya kikao night hawalipwi, wakati mwingi wanalipwa night posho ya kikao hawalipwi, wakati mwingine hawalipwi posho ya kikao wala hawalipwi night na wakati mwingine unakuta halmashauri ya Nzega DC ina Madiwani 52 wamefanya kikao wamemaliza wanakwenda kwenye foleni ya kulipwa posho wanalipwa mpaka Diwani wa 23 hela zinakwisha, waliobaki wengine hawalipwi, kwa hiyo ni vurugu tupu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaposema kwamba halmashauri inashindwa kukusanya maana yake ni kwamba kuna madhara makubwa sana na hili kwa kweli ushauri wangu ni kwamba; TAMISEMI itoe maagizo mahususi kwa Wakurugenzi wa halmashauri ili kabla mabaraza hayavunjwa mwezi wa Sita hawa Madiwani wawe wamepata stahiki zao zote wanazodai ili mabaraza yanapovunjwa wawe hawadai, hata ikiwezekana kwa halmashauri kukopeshwa na TAMISEMI na watajua namna ambavyo watafidiana wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo Kamati imebaini baada ya kuhoji halmashauri ni eneo la miradi inayotekelezwa kwa force account. Kwa ujumla wake imethibitika bila shaka yoyote kwamba miradi inayotekelezwa kwa force account inashia kuwa ni miradi yenye gharama nafuu ukilinganisha na ile miradi ambayo ilikuwa inatekelezwa na ma- Contractor. Hata hivyo, issue iko kwenye quality (ubora) na hii inatokana na halmashauri nyingi kutokuwa na Wahandisi wa kutosha wa kwenda kuzikagua kazi kadri zinavyojengwa kwa sababu force account huko vijijini kwenye kata wanaajiri ma-local Fundi, Mafundi wanaopatikana kulekule. Kwa mfano wanajenga darasa, wakijenga msingi ni lazima Mhandisi wa Wilaya aende akaukague aone uko sawa atoe go ahead, ndiyo waendelee. Sasa unakuta Wilaya kama ya Nzega vijiji 167Mhandisi mmoja vijiji vyote vinamuhitaji unakuta kijiji kinahitaji Mhandisi aje aangalie kazi atoe go ahead kina msubiri miezi mitatu, minne wamekaa hawaendelei.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mwisho wa siku unakuta kazi iliyokuwa ifanywe kwa miezi mitatu inafanywa kwa mwaka. Kwa hiyo maana yake ni kwamba gharama inakuwa kubwa na ubora unakuwa ni compromise. Kwa hiyo eneo hili ushauri wangu ni kwamba pamoja na kwamba Mainjinia wengi walikwenda TARURA, lakini halmashauri kwa maana ya majengo na usimamizi wa hii miradi ya force account ni lazime iwezeshwe kwa kuwa na Wahandisi wa kutosha ili waweze kuzikagua kazi na kutoa go ahead na kuhakikisha miradi ya force account siyo tu kwamba inapunguza gharama, lakini inahakikisha ubora wa miradi unakuwepo kadri ambavyo tunatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tumebaini baada ya kuhoji halmashauri ni kwamba, halmashauri zina tatizo la kutowasilisha michango ya akiba ya uzeeni ya wafanyakazi wake kwenye mifuko husika. Hili ni hatari, sasa hivi unaweza usilione kama hatari, lakini baadaye mfanyakazi anapostaafu, akifika kule fedha zake hazipo hapati, anateseka na inakuwa kero kubwa. Kwa hiyo ushauri wangu hapa ni kwamba iwe ni kipaumbele kwa Wakurugenzi kuhakikisha kwamba makato ya akiba za uzeeni kwa wafanyakazi yanawasilishwa kwenye mifuko husika kuliko ilivyo sasa ambavyo yanakatwa lakini hayapelekwi yanatumika pale halmashauri na baadae inakuwa kero kubwa kwa wahusika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba hii ya Wizara ya Nishati. Kwanza kabisa nichukue fursa hii niungane na Waheshimiwa Wabunge kuwapongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati Mheshimiwa Kalemani na Naibu wake Mheshimiwa Subira Mgalu, kwa sababu hawa ni Mawaziri ambao wanasikiliza Wabunge na wanachukua hatua kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia bomba la mafuta ambalo linalotoka Uganda mpaka Tanga. Katika bomba lote hili la mafuta jimboni kwangu Kata ya Igusule, Kijiji cha Sojo ndipo itajengwa kambi na kituo kikubwa cha kuyafunika mabomba ili yasipate kutu na kuweza kuzuia joto mabomba yote ya njia nzima coating itafanyika pale Igusule ambapo ndio kijiji kwangu.

Mheshimiwa Spika, shughuli ya kujenga hiki kituo pale kijijini itaingiza bilioni 600. Ni shughuli kubwa sana bilioni 600 zitaingia pale. Sasa hoja yangu hapa ni local content, ni namna gani wananchi, Watanzania wa Kijiji cha Igusule, Jimbo la Bukene na Wilaya ya Nzega na Watanzania wote watanufaika na huu uwekezaji wa hizi bilioni 600.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Wizara tuna Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 ambayo ina kipengele cha ushirikishwaji wa wananchi, ningeomba Wizara ijipange kutumia sheria hii ili kwa makusudi kuwa na mpango wa makusudi wa kusaidia Watanzania hasa wa Jimbo la Bukene pale Igusule kuhakikisha kwamba wananufaika na hizi bilioni 600. Hivyo, lazima kuwa na mpango wa makusudi, kwa hivyo watu wa maeneo yale lazima tujue kazi zitafanyika pale, kazi za ujuzi, kazi za ujuzi wa kawaida, vibarua, huduma mbalimbali ambazo zitatolewa pale na Serikali imejipangaje ili kuwasaidia kwa makusudi watu wa maeneo yale waweze kufaidika na uwekezaji wa bilioni 600.

Mheshimiwa Spika, hili jambo tukiliacha hivi hivi, Watanzania wananchi wa Nzega, wananchi wa Jimbo la Bukene tukiacha hivi hivi bila hatua za makusudi, tunaweza tukajikuta bilioni 600 zimewekezwa pale mradi ukaisha, lakini ukipima manufaa ya wananchi wa pale utakuta kwamba hawajanufaika chochote. Tunachohitaji watu wa pale ni kwamba, hali za maisha za wananchi wa maeneo yale ambapo bilioni 600 zitawekezwa Igusule, Jimbo zima la Bukene na Wilaya nzima ya Nzega hali zao za maisha baada ya uwekezaji wa bilioni 600 ni lazima zibadilike zi-reflect kweli kuna bilioni 600 ziliingia, otherwise kutakuwa hakuna manufaa yoyote ya bilioni 600. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ushauri wangu kwa Wizara hapa ni kwamba, lazima kuwe na mpango wa makusudi, hapa na-underline neno makusudi; mpango wa makusudi, ukiacha kama ilivyo wananchi kwa kweli bila kusaidiwa, bila kuwa na mpango maalum, tutashangaa bilioni 600 zimewekezwa, lakini wanaweza wakaja watu ambao sio Watanzania, wajanja wengine ndio wakanufaika zao. Kwa hiyo lazima tulindwe, tuwe protected ili tuweze kunufaika na hizi.

Mheshimiwa Spika, hili la Miradi ya REA limeongelewa na Wabunge wengi, kwa hiyo ushauri wangu ni kwamba natambua jitihada za Mheshimiwa Waziri Dkt. Kalemani na Naibu wake katika kuwasukuma wakandarasi ili waweze kutimiza majukumu yao lakini pamoja na jitihada hizi bado wakandarasi wanasuasua katika maeneo mengi kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamesema.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwamba mwishoni wakati Mheshimiwa Waziri ana-wind-up atueleze ili tujue tatizo ni wakandarasi au tatizo ni Wizara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuwa na afya njema ili nami nipate nafasi ya kuchangia Muswada huu muhimu sana wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa (The Access to Information Act) ya 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo imeshasemwa Ibara ya 18(d) ya Katiba yetu inatoa haki ya wananchi wote wa Tanzania kupata taarifa. Haki hii imekuwa haitekelezeki au haipatikani vizuri kwa sababu tumekuwa hatuna sheria ambayo kimsingi ndiyo inapaswa sasa kuwalazimisha watoa taarifa kuweza kutoa taarifa hizo kwa wananchi. Jamii yetu tumedhamiria kutengeneza jamii na nchi ambayo inaheshimu misingi ya uwazi na uwajibikaji.
Mheshimiwa mwenyekiti, huwezi kuwa na jamii inayoheshimu misingi ya uwazi na uwajibikaji kama ndani ya jamii hiyo upatikanaji wa taarifa unakuwa haupo. Kwa hiyo, muswada huu wa sheria ni muafaka kabisa, umekuja kwa wakati unaohitajika kabisa ili sasa upatikanaji wa taarifa uwe ni jambo ambalo ni la lazima. Kwa hiyo, itatupelekea sasa kutimiza azma yetu ya kujenga jamii na nchi ambayo inaheshimu misingi ya uwazi na uwajibikaji.Ukiangalia muswada huu katika kifungu cha 9(1)(b) ndiyo kifungu ambacho sasa kinatoa namna ambavyo sasa sheria hii itaanza kutekelezwa. Kifungu hiki kimetoa utaratibu ambao unamtaka mmiliki wa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu kwamba tuna taasisi za umma nyingi; kuna Wizara, Mashirika, Halmashauri na hata taasisi binafsi ambazo zina maslahi ya umma. Tunafahamu kwamba majukumu ya taasisi hizi yamepishana na kwa hiyo, taarifa zitazopatikana kutoka kwenye taasisi moja na taasisi nyingine kwa vyovyote vile lazima zitatofautiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kifungu hiki cha muswada huu wa sheria kinamtaka mmiliki wa taarifa ambaye ni Mkuu wa Taasisi au Wizara au Shirika au Taasisi yoyote ndani ya miezi 36 baada ya kupitishwa kwa sheria hii kuandaa orodha ya taarifa ambazo zinaweza kupatikana ndani ya Taasisi zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano zuri ni TAMISEMI - Makao Makuu ambao wameandaa Client Service Charter ambayo inaonyesha taarifa zote ambazo unaweza ukazipata ukienda kuziomba kutoka TAMISEMI - Makao Makuu na wamekwenda zaidi mpaka kutoa muda ambao taarifa fulani unaweza kuipata ndani ya wiki mbili, taarifa fulani ndani ya wiki moja, taarifa fulani ndani siku mbili na taarifa fulani ndani ya siku moja. Kwa hiyo, kifungu cha 9 cha muswada huu ndicho hasa kimetoa wajibu kwa wamiliki wa taarifa wote ndani ya miezi 36 tangu sheria kupitishwa kuandaa orodha ya taarifa zote zinazoweza kupatikana ndani ya taasisi zao ili mwomba taarifa sasa anapokwenda kwenye taasisi aweze clearly kabisa kusema nataka taarifa hii na hivyo atajua kwamba ataweza kuipata kwa muda gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kifungu cha 6, kimeorodhesha taarifa ambazo haziruhusiwi kutolewa. Mimi naungana kabisa na kifungu hiki kwa sababu haiwezekani tukaruhusu taarifa zote za aina yoyote ziweze kutolewa, litakuwa ni jambo ambalo ni hatarishi na hatuwezi kulikubalia. Kifungu hiki kimetoa orodha ya taarifa ambazo zinazuilika na zina mantiki. Kwa mfano, taarifa zote ambazo zikitoka zinapelekea kuhatarisha Usalama wa Taifa, hatuwezi kukubali taarifa hizi zitolewe.
Vilevile kuna taarifa ambazo kama zitatolewa, basi zitapelekea uchumi wa nchi yetu kuhujumiwa. Taarifa hizi zimezuiliwa na hatuwezi kukubali taarifa zinazohujumu uchumi ziweze kuruhusiwa kutolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kifungu hiki kimezuia taarifa ambazo zina mgongano wa kimaslahi wa kibiashara. Kwa hiyo, tunajua madhara yanayoweza kupatikana kama taarifa zenye mgongano mkubwa wa kibiashara kuruhusiwa kutoka. Kwa hiyo, kifungu hiki pia kimezuia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia kifungu hiki cha muswada utaona orodha ndefu ya taarifa ambazo zimezuiliwa zisitoke. Mwisho kifungu hiki cha 6(6) kimetoa adhabu ya mtoa taarifa kama atabainika ametoa taarifa ambayo imezuiliwa kutoka na nakubaliana na kifungu hiki lakini napendekeza marekebisho kidogo kwa sababu kifungu hiki kimetoa adhabu moja ya jumla kwa makosa yote yaliyoorodheshwa, wakati ukiangalia makosa haya yanapishana uzito. Kwa mfano, makosa ya mtu aliyetoa taarifa inayopelekea kuhatarisha usalama wa Taifa na makosa ambayo yanatoa adhabu kwa mtu ambaye ametoa taarifa inayopelekea kuhujumu uchumi wa nchi, ni tofauti kabisa na makosa ya mtu ambaye ametoa taarifa ambayo pengine imeleta tu mgongano wa kibiashara kwa washindani wawili wa kibiashara. Kwa hiyo, Kifungu cha 6(6) kimetoa adhabu moja tu, kwamba wote hawa wakipatikana wataadhibiwa kwenda jela kipindi kisichopungua miaka 15 na kisichozidi miaka 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naona hapa tufanye marekebisho kwamba yale makosa ya mtoa taarifa ambaye anatoa taarifa zinazohatarisha usalama wa Taifa na yule anayetoa taarifa zinazohujumu uchumi, hao wapewe adhabu hiyo ya miaka 15 mpaka 20; lakini wale wengine wanaotoa taarifa zinazopelekea matatizo madogo tu kama mgongano wa kibiashara, kwamba mtu ametoa taarifa ambayo imefanya mshindani wake ajue labda yeye raw material ananunua wapi au analipaje wafanyakazi, kwa hiyo, ameleta mgongano wa kibiashara, kwa hiyo, watu kama hawa adhabu yao napendekeza angalau iwe kifungo kisichopungua miaka mitatu na kisichozidi miaka mitano. Naona siyo sahihi sana hawa nao kuwafunga miaka 20 sawasawa na mtu ambaye ametoa taarifa za kuhujumu uchumi. Kwa hiyo, pendekezo langu hapa ni kwamba adhabu zitofautiane kutokana na uzito wa kosa na siyo kwamba makosa yote yawe na adhabu moja, jambo ambalo naliona kama haliko sahihi.
Kifungu cha 18 cha muswada kinakataza upotoshaji na kimetoa adhabu kwa mtu yeyote atakayepata taarifa halafu akazitumia taarifa hizo kupotosha, basi akibainika afungwe kifungo kisichopungua miaka mitano. Mimi nakubaliana na pendekezo la Muswada huu kwa sababu tukiacha hivi hivi kuna baadhi ya watu ambao watatumia hii kama loophole, hasa baadhi ya waandishi wa habari ambao wanataka kuuza kwenye vyombo vyao, wanaweza wakaenda mahali fulani kuchukua taarifa ambayo ina mlengo fulani lakini wao wakaipotosha ili tu kuuza gazeti au kufanya biashara yoyote. Kwa hiyo, pendekezo la kifungu hiki la kutoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka mitano kwa mtu anayepotosha taarifa, nakiunga mkono kwamba kiendelee kama hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 19 kinatoa fursa kwa mtu aliyeomba taarifa kama amekataliwa kupewa taarifa na haridhiki na sababu za kukataliwa anaruhusiwa kukata rufaa kwa Mkuu wa ile Taasisi ambayo amekwenda kuomba taarifa na pale ambapo bado haridhiki na sababu za huyo Mkuu wa Taasisi kumkatalia kumpa taarifa, basi kifungu hiki kimesema anaweza akakata rufaa kwa Waziri na uamuzi wa Waziri utakuwa wa mwisho.
Napenda hapa tufanye mabadiliko kwamba baada ya huyu mtu kukataliwa kupewa taarifa na Afisa Habari akakata rufaa kwa Mkuu wa Taasisi bado akakataliwa, basi aruhusiwe kwenda mahakamani kupata haki yake ya kupata taarifa kwa sababu tukisema uamuzi wa Waziri utakuwa wa mwisho, inawezekana pengine Waziri akawa na msimamo mmoja na Mkuu wa Taasisi, kwa hiyo, ukakuta mwomba taarifa akakosa haki ya kupata taarifa ambazo anazihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza kifungu hiki kitoe ruhusa, kisiishie kwamba Waziri ndio ana mamlaka ya mwisho kumkatalia mtu kupata taarifa. Kifungu hiki kitoe ruhusa kwa mtu ambaye amekataliwa na watu wote hao watatu aweze kwenda mahakamani ili kupata haki yake ya kupata taarifa ambayo yeye anaona ni muhimu na anastahili kuipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyeiti, hayo ndiyo yalikuwa mapendekezo yangu, naunga mkono sana muswada huu, umekuja kwa wakati muafaka na utasaidia sana katika kujenga jamii na nchi ambayo inathamini misingi ya uwazi na uwajibikaji. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, 2017
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kukushukuru sana kunipa nafasi hii, ili na mimi niweze kuchangia kwenye Muswada huu muhmu sana wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2017 ambao kimsingi unafanya marekebisho kwenye Sheria ya Bajeti na kwenye Sheria ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme nakubaliana kabisa na mapendekezo ambayo yameletwa na Serikali kweny Muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba sikubaliani kabisa na mawazo yaliyomo kwenye taarifa ya Kambi ya Upinzani ambayo yanasema Muswada huu unakwenda kunyang’anya mamlaka ya Bunge, sikubaliani kabisa na hilo na badala yake mimi naona kwamba Muswada huu unakwenda kuhakikisha kwamba, sasa Bunge linapoletewa taarifa, linaletewa taarifa ambayo ni rasmi na hivyo linafanya maamuzi based on taarifa ambayo ni rasmi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Serikali kwenye mambo ya muhimu kama Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, Taarifa ya Uhamisho wa Fedha, Taarifa ya Matumizi ya Kila Kasma, Compliance Report, Taarifa ya Misamaha ya Kodi, hizi ni taarifa rasmi za Kiserikali ambazo ili iitwe taarifa rasmi ya Kiserikali ni lazima iwe imepita kwenye process kadhaa. Wizara ya Fedha kazi yake ni ku-compile taarifa hizi zote nilizozisema kutoka kwenye taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Halmashauri na Mashirika mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ku-compile, Wizara ya Fedha inapitisha kwenye hatua nyingine ikiwepo Inter-Ministerial Technical Committee ambayo na yenyewe inapitia taarifa hizi na kuzihakiki na baadaye kuzithibitisha na badaye taarifa hizi zinakwenda mpaka kwenye Cabinet na kwenye Cabinet nako inahakikiwa na kupitishwa. Sasa
process hii ya taratibu zote hizi za Kiserikali hufanyika kila baada ya miezi sita ndio maana kuna mid year review.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mapendekezo haya yanataka kuhakikisha kwamba taarifa zitazokuwa zinaletwa hapa na Serikali zitakuwa ni taarifa ambazo zimepita process zote hizi za Serikali mpaka approval ya Cabinet na hivyo kuwa taarifa ambazo ni rasmi na ambazo taasisi nyeti kama Bunge inafaa kuletewa na kufanya maamuzi. Ni kwamba sitegemei kama kuliletea Bunge taarifa ambazo ni interim, taarifa ambazo ni awali, taarifa ambazo hazijapita process hizi, eti ndio kulipa Bunge mamlaka. Kwa hiyo, sikubaliani kabisa na hoja iliyoletwa na Upinzani kwamba jambo hili litapunguza mamlaka ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mhagama, amesema wakati anachangia, ni kwamba Muswada huu hauzuii Kamati ya Bajeti au Bunge wakati wowote ule litakapoona inafaa kuitisha taarifa yoyote kutoka Serikalini ambayo itakuwa ni taarifa ya awali kwa ajili ya kufanya mapitio au kufanya maamuzi yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mahali popote kwenye Muswada huu ambapo Muswada umesema Kamati ya Bajeti imezuiliwa kabisa au Bunge limezuiliwa kabisa kuitisha taarifa ambayo Bunge litaonakwamba, inafaa kuitisha kwa wakati huo, hata kama iko kwenye hatua za awali, ili kufanya baadhi ya maamuzi ambayo yataonekena yanafaa kwa hiyo, Muswada huu hauzuii kwa hiyo, hakuna hofu yoyote ya kusema kwamba eti mamlaka ya Bunge yanapunguzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikubaliane na mapendekezo ambayo tumetoa kwenye Kamati ambayo yanataka kwamba, mtumishi yeyote wa umma atakayepatikana kwamba, amekiuka Masharti ya Sheria ya Bajeti, basi aweze kupewa adhabu. Muswada umependekeza kukatwa mishahara ya miezi sita, lakini kuwa subjected na hatua za kinidhamu za Sheria ya Utumishi wa Umma, lakini sisi tumependekeza kwamba, mtumishi wa namna hii aongezewe pia tuhuma za kijinai kwamba kwa kukiuka masharti ya bajeti basi haitoshi tu kumkata mshahara wa miezi sita, bali akatwe mshahara wa miezi sita, awe subjected kwenye Sheria ya Utumishi wa Umma, lakini in addition to that vile vile apelekwe kwenye tuhuma za kijinai. Hili ni pendekezo ambalo tumelipendekeza kwenye Kamati yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba Muswada huu maudhui yake makuu ni kuongeza ufanisi wa Serikali lakini kuhakikisha kwamba Bunge linaletewa taarifa za Serikali ambazo ni rasmi ambazo zimepita hatua zote za uandaaji wa taarifa hiyo na zimepata approval zote kutoka za Wizara Interministerial Technical Committee mpaka na Cabinet yenyewe. Kwa hiyo, taarifa itakayokuwa inakuja kila baada ya miezi sita ni taarifa ambayo ni complete, imejaa facts, ni taarifa rasmi na ambayo itafanya unyeti wa Bunge sasa uonekane kwamba ni chombo ambacho kinaletewa taarifa ambayo kwa kweli ni taarifa ambayo tunaweza kuiita taarifa kamili ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii na nashukuru sana kwa nafasi hii.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye Muswada huu wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2017 ambao kimsingi ni mapendekezo ya marekebisho ya Sheria Mbalimbali ambazo zitawezesha sasa Bajeti Kuu ambayo tumeipitisha iweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza kwa dhati Waziri wa Fedha na Mipango kwa bajeti nzuri ambayo imepita kwa kishindo, kwa vyovyote vile haya marekebisho ambayo sasa yatasababisha bajeti hiyo itekelezeke, tutayapitisha kwa kishindo kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kukubaliana na mapendekezo ya kubadilisha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ambayo sasa yanakwenda kupunguza ushuru wa mazao. Wabunge ambao Majimbo yetu eneo kubwa ni vijiji hii maana yake tunaifahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Bukene asilimia 99 ni vijiji na shughuli kuu ya watu wangu ni kilimo, ili waweze kunufaika na kilimo, sehemu ya mazao haya ni lazima wayauze. Kwa hiyo, ilikuwa ni kero kubwa wakulima wangu wanapokuwa wana gunia saba, nane au tisa wanapotaka kuzihamisha kutoka kwenye eneo la uzalishaji kupeleka kwenye eneo la soko walikuwa wakisumbuliwa na kero ya vizuizi vya ushuru huu. Sasa mapendekezo ya sheria hii yanakwenda kuondoa ushuru huu kwa mazao yote ambayo yatakuwa ni chini ya tani moja. Hili ni jambo ambalo nalikubali na litaondoa kero kwa wananchi wangu wengi wa Jimbo la Bukene ambao ni wakulima wadogo wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii pia inapunguza ushuru wa mazao kutoka kiwango cha sasa cha asilimia tano mpaka asilimia tatu kwa mazao ya biashara na asilimia mbili kwa mazao ya chakula. Hapa ningeshauri tu tafsiri nzuri ipatikane kwa sababu kuna mazao mengine, kwa mfano, zao kama tumbaku au ambalo moja kwa moja linajulikana ni zao la biashara kwa sababu pamba huwezi kuila, lakini kuna mazao kwetu tunalima kule kama mpunga au mahindi ambayo ni mazao ya chakula lakini pia ni mazao ya biashara. Kwa hiyo sasa inapotokea kwa mfano mpunga ama mchele ambao kwetu ni zao la biashara lakini mpunga/mchele huo ni zao la chakula. Kwa hiyo, tunataka tafsiri sahihi kwamba utatozwa asilimia ngapi kwa sababu uko kote, ni zao la biashara vilevile ni zao la chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho mengine ambayo nayaunga mkono ni hii sheria ambayo inakwenda kurekebisha Sheria ya Kodi ya Majengo. Hii inakwenda kuwa mkombozi hasa kwa wamiliki wa nyumba wote ambao wana umri kuanzia miaka 60 na kuendelea. Tunajua miaka 60 watu wamestaafu hata kama siyo mfanyakazi kama ni mkulima nguvu zimekwisha, hana kipato, kwa hiyo kuna logic ya kumwondolea kodi ya majengo. Hivyo, suala hili la kuwaondolea, kuwasamehe kodi ya majengo wazee wote kuanzia miaka 60 naliunga mkono kwa asilimia mia moja kwa sababu linakwenda kuwapa nafuu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono pia sheria hii inakwenda kutoa tafsiri sahihi ya nyumba zipi zitozwe kodi ya majengo. Nimeona kwamba kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mipango ameainisha kwamba nyumba zote zilizojenga kwa miti, kwa tope zilizoezekwa kwa nyasi zote hizi zitaondolewa, hazitahusika na kulipa kodi ya majengo. Kwa hiyo, hii inadhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujali watu ambao wana hali za maisha ya chini. Kwa hiyo, hili nalipongeza sana.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia kupata tafsiri kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri, yale maeneo ambayo yanastahili kutozwa kodi ya majengo, yametajwa kwamba ni Majiji, Manispaa, Miji na Miji Midogo. Kuna Halmshauri, kwa mfano pale Wilaya ya Nzega tuna Halmashauri mbili. Kuna Halmashauri ya Mji wa Nzega ambayo inajumuisha pale Nzega Mjini, lakini kuna Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ambayo asilimia mia moja ni vijiji tupu hakuna Mji wala hakuna hata mamlaka ya Mji Mdogo. Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ni vijiji tupu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tafsiri sahihi kwamba Halmashauri kama hii ya kwetu ya Nzega Vijijini ambayo asilimia moja ni vijiji tupu, je na yenyewe inakuwemo katika kuondolewa kabisa kulipa kodi ya majengo kwa sababu haina hata kamji kamoja kalikofikia hadhi ya kuitwa Mamlaka ya Mji Mdogo, ni vijiji tupu, kwa hiyo tupate tafsiri kwa sababu as we speak now Halmashauri hii ya Nzega Vijijini watu wanatozwa, wanalipa kodi ya majengo wakati ni vijiji tupu. Tunaomba Mheshimiwa Waziri tupate clearance nzuri ili tuweze kuwa na uelewa wa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho mengine ambayo nayaunga mkono ni hii asilimia moja kwenye madini kama clearance fee ambako Serikali itaanzisha utaratibu wa kuweka maeneo maalum kwenye migodi, kwenye viwanja vya ndege ili madini yanayopatikana yaweze kuhakikiwa. Kwa hiyo wafanyabiashara ambao wana malengo ya kuyauza iwe ndani ya nchi au nje ya nchi, waweze kulipa asilimia moja ya thamani ya hayo madini. Hili litatuongezea mapato ya kutosha ambayo kwa sasa hivi tulikuwa hatuyapati. Kwa hiyo naunga mkono hili kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naliunga mkono ni kuondoa ada ya kibali cha kufungua maduka ya madawa. Hapa naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada kubwa za kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kununua madawa. Hii ni dhamira tosha ya Serikali ya Awamu ya Tano kwamba inajali afya za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tunafahamu kwamba juhudi za Serikali lazima ziungwe mkono na sekta binafsi, hivyo pale ambapo watu wanajitokeza ili kuanzisha maduka ya madawa, ni mantiki na ni hoja sahihi kwamba waondolewe hii ada ya vibali iwarahisishie kufungua maduka ya madawa ili upatikanaji wa madawa kwa wananchi wetu uweze kuongezeka. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo naliunga mkono kwa sababu lengo lake ni kuimarisha afya ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naliunga mkono ni uamuzi wa kufanya marekebisho ya sheria ili kuondoa VAT kwenye magari ya wagonjwa. Hili ni jambo jema kwa sababu tunajua huko tuliko kwenye Majimbo vituo vya afya, hospitali za Wilaya, magari ya wagonjwa hayatoshi na tunahitaji tupate mengi zaidi lakini VAT ilikuwa moja ya kikwazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu uamuzi wa kuondoa kodi hii ya VAT kwenye magari ya wagonjwa nauunga mkono kwa sababu ni uamuzi ambao unakwenda kuimarisha afya za Watanzania na kimsingi unakwenda kuokoa maisha ya Watanzania ambao wangeshindwa kuwahishwa kwenye huduma za afya, lakini sasa upatikanaji wa haya magari ya wagonjwa utawafanya waweze kufikishwa kwenye vituo vya afya ili waweze kupata huduma muhimu ambazo wanazihitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba, kimsingi marekebisho ya sheria hizi ambazo yatafanya sasa utekelezaji wa bajeti tuliyoipitisha uweze kufanyika, nayaunga mkono kwa asilimia mia moja, kwa sababu yamekaa vizuri, nina uhakika sasa tunakwenda kuwa na bajeti ambayo itatekelezeka na ambayo kwa kweli inakwenda kujibu kero za wananchi wetu ambazo tumekuwa tukizisemea ziku zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nimpongeze Waziri wa Fedha kwa safari hii kuleta bajeti ambayo ni sikivu, bajeti ambayo imezingatia maoni na ushauri kwa kiwango kikubwa sana ya Waheshimiwa Wabunge ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiyatoa. Kwa hiyo, niwapongeze sana kwa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.