Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla (98 total)

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-

Serikali kwa miaka mingi imekuwa na mpango wa kujenga Hospitali za Rufaa za Kanda; na tayari Kanda zote zina hospitali hizo isipokuwa Kanda ya Kusini tu:-

(a) Je, ni lini Serikali itaanza kujenga hospitali hiyo ya Kanda ya Kusini ambapo tayari eneo la Mitengo Mikindani limetengwa kwa zaidi ya miaka saba na hakuna kinachoendelea?

(b) Je, ni Serikali haioni kama hawatendei haki wananchi wa maeneo ya Kanda ya Kusini kama wananchi wa maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini ningependa kutoa maelezo ya awali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mpango wa Serikali kila Kanda inatakiwa kuwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda, katika Kanda saba zilizopo ni Kanda nne tu ambazo zina hospitali za Rufaa za Kanda.

Kwa Kanda ya Mashariki Serikali iliipandisha hadhi Hospitali ya Lugalo ya Jeshi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda. Kanda ya Ziwa kuna Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando ambayo ilijengwa na taasisi ya hiari. Kanda ya Kaskazini kuna Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC inayomilikiwa na Taasisi ya hiari. Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuna Hospitali ya Rufaa ya Mbeya inayomilikiwa na Serikali. Kanda tatu ndizo bado hazijapata Hospitali za Rufaa za Kanda ambazo ikijumuisha kanda ya Kati yenye Mikoa ya Dodoma Singida ambapo ni Makao Mkuu ya Serikali. Kanda ya Magharibi ikijumuisha Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi na Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Mtwara na Lindi.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya awali sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha A. Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali tayari ilikwishaanza ujenzi wa hospitali ya Kanda ya Kusini katika eneo la Mitengo Mikindani na hatua zifuatazo zimetekelezwa na zinaendelea kutekelezwa kwa awamu. Maandalizi ya mpango kamambe yaani masterplan na michoro pamoja na makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi yalikamilika tangu mwaka 2009. Awamu ya kwanza ya utekelezaji ilikuwa kujenga uzio kuzunguka eneo lote la hospitali na tayari ujenzi wake umekamilika. Awamu ya pili ilikuwa kujenga jengo la wagonjwa wa nje ambalo hadi Disemba, 2015 ujenzi wake ulikuwa umefikia asilimia 85. Serikali inatoa kipaumbele cha kipekee katika ujenzi wa hospitali hiyo na uongozi wa juu wa Wizara umekuwa ukitembelea na kukagua maendeleo yake mara kwa mara.
(b) Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa si kweli kwamba Serikali haiwatendei haki wananchi wa maeneo ya Kanda ya Kusini na pia Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo haibagui Kanda au eneo lolote. Vilevile usanifu wa hospitali hii ya Kanda ya Kusini ulizingatia mahitaji ya sasa katika hospitali ya ngazi ya Kanda. Hospitali hii itakapokamilika itakuwa ya kisasa zaidi ikilinganishwa na Hospitali za Kanda zilizopo, na itakuwa ni ya pili ya Kanda kujengwa na Serikali yetu. Ya kwanza ikiwa ni ile ya nyanda za Juu Kusini ya Mbeya.

Aidha, napenda kutumia fursa hii kuyapongeza mashirika ya dini na taasisi binafsi kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuanzisha Hospitali za Rufaa za Kanda.
MHE. CECILIA D. PARESSO (k.n.y. MHE. MARYAM SALUM MSABAHA) aliuliza:-

Kumekuwa na ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Dodoma, Mwanza na kadhalika. Watoto hawa wengi wao hawaendi shule na kazi yao ni kuomba omba barabarani:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha watoto hao wanarudishwa shuleni kusoma?

(b) Je, ni lini Serikali itawachukulia hatua wale wote wanaowatumia watoto hao kuombaomba?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango Kazi wa II wa Taifa wa huduma kwa watoto walio katika Mazingira hatarishi wa mwaka 2013/2017, ambao umeainishwa majukumu ya Serikali Kuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na wadau wengine.

Mnamo mwaka 2011, Wizara yetu ilifanya utafiti ili kubaini ukubwa wa tatizo la watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani, katika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo watoto wapatao 5,600 walibainishwa. Baada ya utafiti huu uliandaliwa mradi wa majaribio wa namna ya kuwaondoa watoto hao mitaani kati ya mwaka 2011 hadi 2014 ambapo watoto wapatao 226 waliweza kuunganishwa na familia zao.

Mheshimiwa Spika, watoto 179 waliweza kurudishwa mashuleni, watoto 196 walipatiwa huduma za afya na 1,000 walipatiwa unasihi. Aidha, mradi huu ulibainisha Mikoa tisa (9) ambayo inaongoza kwa kuleta watoto katika jiji la Dar es Salaam. Mikoa hii ni Pwani, Iringa, Lindi, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Kilimanjaro, Tanga na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, baada ya utafiti, Wizara yetu iliandaa mpango kazi unaolenga kuzuia watoto kuingia mitaani, kuwarejesha na kuwaunganisha na familia zao na kufanya ufuatiliaji.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuondoa ombaomba mijini wakiwemo wanaowatumia watoto kwa mfano, kwa Mkoa wa Dar es salaam mwezi Septemba, 2013 ombaomba 253 na watoto 135 walirejeshwa makwao kati ya watoto 33 walirejeshwa shuleni katika Mikoa walikotoka. Zoezi hili linaendelea katika mwaka huu wa fedha 2015/2016 ambapo watoto 47 wameunganishwa na familia zo na kati yao 35 wamerejeshwa shuleni.

Mheshimiwa Spika, suala la ombaomba ni mtambuka, linazihusisha mamlaka za Serikali Kuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zisizo za Kiserikali, jamii na familia. Nachukua fursa hii kutoa wito kwa kila mdau kutekeleza wajibu wake katika suala hili.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Je, ni lini Benki ya Wanawake itaanza kutoa huduma zake Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Faida kwa kufuatilia na kuuliza swali hili kwa mara ya tatu sasa. Hii inaonesha dhamira ya dhati aliyonayo kwa wanawake na wananchi wa Zanzibar. Mheshimiwa Faida aliuliza swali hili mara mbili katika Bunge la Kumi na aliendelea kuuliza swali hilo kwenye vikao mbalimbali vya iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii katika kipindi kilichopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Wanawake ilianzishwa kwa mtaji wa shilingi bilioni 2.8 ambao ni kiasi kidogo sana. Ili Benki iweze kutimiza kigezo cha kuwa Benki ya Biashara kamili na kuweza kupata kibali cha Benki Kuu cha kufungua Matawi nchi nzima, inahitaji mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 15. Hivi sasa benki hiyo ina mtaji wa shilingi bilioni 8.5.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi za kuanzisha shughuli za kibenki Zanzibar zilianza tangu mwaka 2013, kwa Menejimenti kutembelea Zanzibar katika lengo lake la kupata jengo zuri kwa shughuli za kibenki. Hata hivyo, juhudi hizi hazikuzaa matunda na ndipo Makamu wa Rais wa sasa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliporidhia kutoa Ofisi yake ndogo iliyokuwa katika Hoteli ya Bwawani ili kuanzisha huduma hiyo na kuwanufaisha wananchi wa Zanzibar, hususan wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, benki ipo katika hatua za mwisho za kupata kibali cha Benki Kuu ili kuanzisha rasmi Kituo cha Mafunzo na Mikopo kwa Wajasiriamali wa Zanzibar na tunategemea kitaanza shughuli zake kabla ya mwezi Juni mwaka huu yaani mwaka 2016 na kama nilivyoeleza awali mtaji wa benki hii ukiimarika benki itafungua tawi kamili Zanzibar.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR aliuliza:-
Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa huduma za afya na haki za uzazi katika baadhi ya sehemu jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya wanawake:-
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali namba 54 la Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nasikitika kuwa bado kuna ukiukwaji wa huduma za afya, haki za afya na haki za uzazi katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Tafiti zinaonyesha kuwa suala hili linadumaza matumizi ya huduma na kuhatarisha maisha ya wanawake. Serikali inajukumu la kutoa na kusimamia na kutoa utoaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto na jukumu hili linatekelezwa kwa kutumia vituo vya kutolea huduma za afya ya uzazi na mtoto vya umma na binafsi kote nchini. Huduma hizi hutolewa kwa kuzingatia haki za wateja kama ilivyoainishwa kwenye miongozo ya utoaji wa huduma hizi. Haki hizi ni pamoja na upatikanaji wa taarifa sahihi, ubora na usalama wa huduma, usiri na ufaragha katika utoaji wa huduma, haki ya kusikilizwa, haki ya kuheshimiwa na haki ya kutumia huduma kwa hiari pasipo shuruti.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa haki hizi zinapatikana, Serikali kwa kupitia mifumo yake ikiwa ni pamoja na Mabaraza ya weledi kwa maana ya Mabaraza ya Wauguzi, Madaktari, Wafamasia, Wataalam wa Radiolojia na kadhalika, Kurugenzi ya Uhakiki na Ubora wa Huduma za Afya na idara mbalimbali zilizo chini ya Wizara zinatoa mafunzo kwa watoa huduma za afya kuhusiana na haki za wateja na mahitaji muhimu ya mtoa huduma ili waweze kutekeleza haki hizo. Aidha, wateja wanaotumia huduma mbalimbali za afya uzazi na mtoto hupewa elimu kuhusu haki zao ili kuzifahamu na kuchukua hatua pindi wanapoona haki zao zinakiukwa.
Katika kutekeleza hili, vituo vyetu vya kutolea huduma za afya vina masanduku ya maoni na ofisi za malalamiko ambazo ni sehemu muhimu ambapo wateja wanaweza kupeleka malalamiko yao ili hatua zaidi zichukuliwe kukomesha na kutokomeza ukiukwaji wowote wa haki za mteja.
Mheshimiwa Spika, Serikali hufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa kushtukiza katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na binafsi kwa lengo la kutambua malalamiko yaliyofumbiwa macho na kujiridhisha na ubora wa huduma zinazotolewa. Ukaguzi huu wa kushtukiza hufanywa na Kiongozi yeyote wa Serikali mwenye dhamana ya kusimamia huduma za jamii. Ukaguzi huu wa kushtukiza huleta matunda katika uboreshaji wa huduma na haki kwa wateja. Kwa mikakati hii, nina imani kuwa tatizo hili litapungua kama siyo kumalizika kabisa.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Hospitali ya Mji wa Tarime hutoa huduma kwa wananchi wa Wilaya za Tarime, Rorya, Serengeti na nchi jirani ya Kenya na kwamba hospitali hii ina ukosefu mkubwa wa madawa na vifaa tiba:-
Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha hospitali hii inakuwa na madawa pamoja na vifaa tiba vya kutosha kutoka MSD?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali namba 55 la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma na vifaa katika vituo vya kutolea huduma za afya ni mojawapo ya vipaumbele vya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali ilipeleka kiasi cha shilingi bilioni 37.2 Bohari ya Dawa yaani MSD ili kuboresha uwezo wa Bohari ya Dawa kuhudumia vituo vya kutolea huduma za afya ambapo hospitali ya mji wa Tarime ilipata shilingi milioni 76.5.
Mheshimiwa Spika, aidha, katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 51 kwa ajili ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa ajili ya hospitali ya Mji wa Tarime. Hadi sasa hospitali hii imeshapelekwa kiasi cha shilingi milioni 35.8.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutenga bajeti kwa ajili ya kununulia dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. Serikali imejipanga kuimarisha ukusanyaji na udhibiti wa mapato yatokanayo na uchangiaji huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo hospitali ya Mji wa Tarime.
Mapato hayo yataelekezwa katika kuhakikisha dawa na vifaa vinapatikana muda wote vinapohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya. Mapato hayo ni kama ifuatavyo; uchangiaji wa papo kwa papo, mapato yatokanayo na Mfuko wa Taifa na Bima ya Afya na fedha zitokanazo na Mfuko wa Afya ya Jamii. Aidha, Serikali imeandaa Mpango wa Afya kwa wote na italeta Bungeni Rasimu ya Sheria ya Mpango huo ili kila mwananchi apate Bima ya Afya itakayosaidia kuondokana na changamoto ya kukosa dawa na huduma nyingine za matibabu.
MHE. ESTER A. BULAYA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-
Mabaraza ya makundi maalum ya kijamii kama wanawake, vijana, wazee, watoto na walemavu ni vyombo muhimu katika kuwaunganisha kimaendeleo:-
(a) Je, ni lini Serikali itawasilisha taarifa ya tathmini ya utendaji wa Mabaraza ya Watoto na Walemavu?
(b) Je, Serikali imefikia hatua gani katika kuwezesha kufanya kazi kwa Baraza la Vijana la Taifa baada ya sheria yake kupitishwa?
(c) Je, ni lini Serikali itawezesha kuundwa kwa Baraza la Wanawake la Taifa ili kuwaunganisha katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali namba 87 la Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu imeanza kufanya tathmini ya utendaji wa Mabaraza ya Watoto ngazi za Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa katika mikoa sita ya Tanzania bara. Lengo kuu la tathmini hii ni kubaini hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa malengo ya Mabaraza kama ilivyokusudiwa katika uanzishwaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili litakamilika mwezi Mei, 2016. Mara baada ya kukamilika kwa zoezi hili, Wizara itaandaa ripoti ambayo itaonesha matokeo ya tathmini ya utendaji wa Mabaraza hayo katika ngazi zote na kuiwasilisha kwa wadau kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wa Baraza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Taifa la Ushauri la Watu Wenye Ulemavu lilizinduliwa tarehe 1 Novemba, 2014. Kutokana na ufinyu wa bajeti, Baraza hili lilifanya kikao chake cha kwanza tarehe 14 na 15 Januari, 2016.
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, yenye dhamana ya kushughulikia watu wenye ulemavu itafanya tathmini na kutoa taarifa baada ya kumalizika kipindi cha mwaka mmoja baada ya Baraza hili kuanza kufanya kazi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lilipitisha rasmi Sheria Na. 12 ya uundwaji wa Baraza la Vijana la Taifa yaani The National Youth Council, 2015 na kusainiwa na Mheshimiwa Rais tarehe 22 Mei, 2015. Hivi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu ipo katika hatua ya kutunga kanuni za utekelezaji wa sheria hii kwa mujibu wa kifungu Na. 27 cha Sheria, ili kuwezesha uundwaji wa Baraza kuanzia ngazi ya Kata hadi Taifa. Aidha, Wizara inatarajia kanuni hizi kukamilika mwaka huu wa 2016 ili Baraza lianze kufanya kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo na vijana.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwepo kwa jitihada za wanaharakati, wanazuoni na watafiti katika kusaidia kuundwa kwa chombo cha kuwaunganisha wanawake kwa lengo la kuimarisha juhudi zao katika mapambano ya kulinda haki zao na kuleta usawa wa kijinsia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa kutambua jitihada hizo Serikali imepanga kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kujadili na kutoa maoni kuhusu haja ya kuwepo kwa Baraza la Wanawake Tanzania ambalo litasaidia kulinda maslahi na haki zao kwa mujibu wa sheria na kuleta usawa wa kijinsia.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED aliuliza:-
Takwimu zinaonyesha kuwa kuna kasi kubwa ya ongezeko la wagonjwa wa maradhi ya moyo, kisukari na vidonda vya tumbo (ulcers):-
Je, Serikali ina mkakati gani kukabiliana na tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imeshuhudia kasi kubwa ya ongezeko la magonjwa ya moyo, magonjwa ya kisukari na magonjwa ya vidonga vya tumbo, ambayo ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Hii imechangiwa na mabadiliko ya mfumo wa maisha kama ulaji usiyo sahihi, kutokufanya mazoezi, kutokula matunda na mboga mboga kwa wingi, uvutaji wa sigara na tumbaku na unywaji wa pombe uliyokithiri. Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo ya utafiti wa STEPS uliyofanyika mwaka 2012 yalionesha kuongezeka kwa viashiria yaani indicators vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Aidha, utafiti pia ulionesha karibu asilimia 9 ya Watanzania, wanaugua ugonjwa wa kisukari na wengi wao kwa bahati mbaya hawajijui. Kwa kutambua ongezeko hili Wizara yetu imeanzisha sehemu ya kushughulikia huduma ya magonjwa haya yaani kitengo cha Non Communicable Diseases, Mental Health and Substance Abuse chini ya Kurugenzi ya Tiba pale Wizarani. Miongozo na mikakati mbalimbali imekwisha kutengezezwa ikiwa ni pamoja na mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yaani magonjwa ya kisukari, moyo na mengineyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu kwa jamii ni kubadili mtindo wa maisha yaani life style kwa kula vyakula vinavyofaa, kupunguza unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara na tumbaku na kuwa na tabia ya kufanya mazoezi ili kuepuka uwezekano wa kupata maradhi haya.
MHE. FATUMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Ujenzi wa Maternity Complex katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ulianza tangu mwaka 2009 ambapo majengo hayo yana uwezo wa kuweka vitanda 180, lakini hadi leo jengo hilo halijakamilika kutokana na Serikali kuamua kuimarisha huduma ya afya ya mama na mtoto kwa kuzingatia vipaumbele vya Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati wa kutekeleza Matokeo Makubwa Sasa kwa kuiangalia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa jicho la pekee kwa kuipatia fedha ili jengo hilo likamilike haraka ili kuwaondolea adha kubwa wanayopata akinamama wakati wa uzazi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imelipa kipaumbele suala la kupunguza vifo vya akina mama na watoto vinavyotokana na uzazi kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za uzazi salama katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Wizara ilifanya tathmini na kubaini mikoa ambayo ina idadi kubwa ya vifo vya akinamama na watoto vinavyotokana na uzazi na kuanza kutekeleza Mradi wa Kuharakisha Kupunguza Kasi ya Vifo vya Akinamama Wajawazito Vinavyotokana na Uzazi (Strenthening Maternal Mortality Reduction Program (SMMRP). Mikoa hiyo ni Mtwara, Tabora na Mara. Serikali imefanya jitihada kubwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za uzazi salama katika mikoa hiyo kwa kujenga na kukarabati vyumba vya upasuaji, majengo ya huduma za afya ya mama na mtoto na nyumba za watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mkoa wa Dodoma, Serikali kupitia Ofisi ya Rais (TAMISEMI), inakamilisha ujenzi wa Martenity Complex katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Kazi hii iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mifumo ya maji yaani plumbing system, kupaka rangi kuta na kazi ndogo za nje ya jengo hilo yaani external works na ununuzi wa samani. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, itashirikiana na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati ili kuwawezesha wananchi wa Mkoa wa Dodoma na maeneo ya jirani kupata huduma bora za uzazi salama.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kununua mashine mpya za CT-Scan kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Jimbo la Chemba, napenda kuwakumbusha Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kwamba leo ni Siku ya Saratani Duniani. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Tunaweza, ninaweza kwa pamoja tuwajibike kupunguza janga la Saratani duniani”. Ili kupambana na ugonjwa wa saratani inabidi kuepuka matumizi ya tumbaku, ulaji usiofaa na utumiaji wa pombe kupita kiasi. Nawaasa mfanye mazoezi ili kuzuia kwa kiasi kikubwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefuatilia mwenendo wa huduma ya vipimo vya radiolojia inayotolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kubaini baadhi ya upungufu. Miongoni mwa upungufu huo ni kuharibika mara kwa mara kwa CT-Scan na kupelekea usumbufu kwa baadhi ya wagonjwa kutopata huduma ya kipimo hicho kwa wakati muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na sababu mbalimbali, Serikali katika mwezi wa Desemba, 2015, ilifanya maamuzi na kupeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mashine mpya ya CT-Scan ambayo inatumia teknolojia ya kisasa yenye X-ray tube mbili na uwezo wa kupiga picha ya 128 Slice mara mbili.
Faida ya mashine hii ni pamoja na kuhudumia mgonjwa kwa haraka na kutoa nafasi kwa mgonjwa mwingine hali ambayo inatoa nafasi kwa wagojwa wengi zaidi kwa maana ya zaidi ya 40 kupata kipimo hicho ndani ya siku moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida nyingine ni kwamba mgonjwa anapata mionzi michache, karibu nusu ya ile anayoweza kupata kutokana na mashine yenye tube moja. Aidha, mashine hii ina uwezo wa kuchunguza magonjwa yanayohusu moyo, mishipa ya damu, mishipa ya fahamu na ubongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ununuzi na usimikaji wa mashine hii, imefanya sasa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwa na mashine mbili za CT-Scan. Kwa hali hiyo, hatutegemei kusimama kwa utoaji wa huduma ya vipimo vya CT-Scan. Aidha, Serikali pia imefunga X-ray mpya ya digitali na Ultra-Sound mpya ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kuboresha huduma za vipimo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH aliuliza:-
Ni jambo la kusikitisha sana kwa wananchi wanaosumbuliwa na saratani kuchelewa kupatiwa huduma katika Hospitali ya Ocean Road:-
Je, Serikali inalifahamu jambo hilo na inachukua hatua gani dhidi ya tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inalitambua sana tatizo la upatikanaji huduma za matibabu katika taasisi ya Saratani ya Ocean Road na inafanya juhudi za ziada katika kuhakikisha changamoto hizi zinatatuliwa kwa kiasi kikubwa, kama siyo kwisha kabisa. Serikali pia hugharamia matibabu ya saratani kwa wananchi wake wanaobainika kuwa na ugonjwa huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya dawa za chemotherapy za kutibu saratani kwa mwaka 2015/2016 ilikuwa ni shilingi bilioni 7.2. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara imekuwa ikiongeza bajeti kwa ajili ya kununua dawa za saratani kupitia MSD na kuzisambaza kupitia hospitali husika, hususan Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2011 Serikali kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa ya Bugando ilianza ujenzi wa Taasisi ya Saratani katika Hospitali hiyo. Taasisi hiyo itaongeza uwezo kukabiliana na ugonjwa wa saratani ambao hapo awali umekuwa ukitibiwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road pekee.
Mradi huo wa ujenzi wa jengo hilo lenye vyumba maalum sita (bunkers) kwa ajili ya kusimika vifaa, mitambo na mashine kubwa za mionzi (LINAC) umeshakamilika. Hatua inayofuata ni kusimika vifaa hivyo ambavyo tayari vimeshapokelewa hospitalini hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mojawapo ya bunkers hizo ndiyo itaweka mashine hiyo ya LINAC ambayo ni mara ya kwanza kufungwa Tanzania.
Aidha, huduma za kutibu saratani kwa njia ya dawa za chemotherapy imeanza na hivyo wagonjwa wanaohitaji tiba ya aina hiyo hupewa.
MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:-
Tanzania kuna mashirika makubwa yasiyo ya Kiserikali ambayo yanaisaidia sana Serikali katika kuwahudumia wananchi hasa wanawake misaada ya Kisheria. Mfano wa Mashirika haya ni TGNP, LHRC, WILDAF, TAWLA, lakini yanafanya kazi kwa kutegemea ufadhili wa wahisani kutoka nchi za nje:-
(a) Je, ni lini Serikali itatenga asilimia kidogo ya pato lake kuyapatia ruzuku mashirika haya kama Serikali inavyotoa kwa vyama vya siasa?
(b) Je, ni lini Serikali itayahamasisha mashirika na makampuni ya ndani nayo kuona umuhimu wa kuingia nayo mikataba ya ushirikiano ili kutoa huduma kwa kiwango kikubwa zaidi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndila Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua haja ya kufanya kazi kwa ubia na mashirika yasiyo ya Kiserikali na pia kuyapatia ruzuku kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Kwa kuzingatia azma hiyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia mikutano mbalimbali ya wadau imekuwa ikihamasisha Taasisi za Serikali kufanya kazi kwa ubia na mashirika haya, kama inavyoainishwa katika Sera ya Taifa ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali. Kutokana na jitihada hizo, baadhi ya Taasisi za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wizara, Idara na Wakala za Serikali zimeanza kutoa ruzuku kwa mashirika haya.
Kwa mfano, katika miaka ya hivi karibuni Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Kimataifa na Halmashauri mbalimbali zimekuwa zikitoa ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayojishughulisha na masuala ya VVU na UKIMWI, Maadili na Mazingira. Mfano mwingine ni Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ambayo katika mwaka 2015 ililiwezesha Shirika la Mbozi Society for HIV/AIDS Campaign and Social Economic Development kwenda vijijini kutoa elimu ya VVU na UKIMWI.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Serikali kuhamasisha mashirika na makampuni ya ndani kuingia mikataba ya ushirikiano na Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kupitia mikutano baina ya Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali na wadau mbalimbali iliyofanyika katika mikoa 22 ya Tanzania Bara, imekuwa ikihamasisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuanzisha ushirikiano na ubia na Serikali pamoja na sekta binafsi, ikiwemo makampuni.
Kutokana na jitihada hizi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yameanza kufanya kazi kwa ubia na makampuni mbalimbali hapa nchini. Mfano mzuri ni Shirika lisilo la Kiserikali la Mbalawala Women Organisation (MWO) linalofanya kazi kwa ubia na Kampuni ya Tancoal Energy Limited katika kukuza ajira ya wanawake kwenye vya Ntunduwaro na Ruanda, Wilayani Mbinga, Mkoani Ruvuma.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Ugonjwa wa myoma ni moja kati ya matatizo makubwa yanayoathiri akinamama kuzuia uzazi na kusababisha kansa ya kizazi pamoja na kupoteza maisha:-
Je, ni kwa kiasi gani Serikali imefanikiwa katika kuwasaidia akinamama wanaoteseka na matatizo hayo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, myoma au kwa jina la kitaalam unajulikana kama uterine fibroid au leiomyoma ama kwa Kilatini leiomyomata uteri, ni uvimbe unaoota kwenye misuli ya tumbo la uzazi la mwanamke. Chanzo halisi cha ugonjwa huu hakijulikani ila kila myoma huanza kwa ukuaji hovyo wa seli moja ambayo hutoa protini kwa wingi. Tafiti pia zimeonesha kwamba ugonjwa wa myoma ama fibroid hutokana na mabadiliko ya vinasaba kwenye seli za myoma ambazo hubadilisha ukuaji wa seli hizo. Aidha, mazingira pia huchangia ukuaji wa myoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema ni kuwa, myoma ni uvimbe ambao siyo saratani na narudia, myoma ni uvimbe ambao siyo saratani na hauna tabia ya kubadilika kuwa saratani. Myoma ikiwa kubwa sana huweza kuonesha dalili kama vile kuvimba tumbo, kuvuja damu kwa wingi na maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu. Uvujaji wa damu kwa wingi huweza kupelekea mama kupoteza maisha.
kabla ya kushika ujauzito, wakati wakiwa wajawazito au wakati wa kujifungua. Serikali kupitia Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, huwahamasisha akinamama kupima afya zao kabla ya kushika ujauzito, wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama wanaogundulika na matatizo haya hufanyiwa upasuaji, aidha wa kutoa uvimbe au kutoa kizazi kama uvimbe huo umekuwa mkubwa na unaambatana na matatizo mengine kama ya kuvuja sana damu. Wataalam huamua kuondoa uvimbe peke yake au kuondoa uvimbe na kizazi. Hata hivyo, siku hizi kuna dawa ambazo Daktari anaweza kumpatia mama kabla ya uvimbe kuwa mkubwa na dawa hiyo kusaidia kupunguza uvimbe. Aidha, kama uvimbe umekaa sehemu ambayo haufai kutolewa wenyewe na mama amekwishamaliza kuzaa, basi hushauriwa kutoa mfuko wote wa kizazi (uterus).
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko mengi ya wananchi kutopata huduma nzuri katika hospitali za umma, vituo vya afya pamoja na zahanati:-
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kusimamia Madaktari na Wahudumu wa Afya ili kuweza kuwapatia wananchi huduma bora na kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatib, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
kuhusu huduma zinazotolewa na vituo vya huduma za afya vya ngazi zote hapa nchini. Katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinazotolewa zina ubora unaotakiwa na zinawafikia wananchi…
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge upande wa Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba utulivu tafadhali, tumsikilize Naibu Waziri.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo malalamiko ya wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na vituo vya huduma za afya vya ngazi zote hapa nchini. Katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinazotolewa zina ubora unaotakiwa na zinawafikia wananchi, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeweka utaratibu wa kusimamia utoaji wa huduma hizo. Utaratibu huu ni pamoja ni:-
(1) Kuwepo kwa Mabaraza ya Taaluma yenye nguvu za kisheria ambayo husimamia wataalam katika taaluma husika. Kila taaluma ya afya, ikiwemo ya udaktari ina Baraza linalosimamia wanataaluma wake;
(2) Kuwepo kwa miongozo inayosimamia utoaji wa huduma za afya zenye ubora unaotakiwa; na
(3) Kuwepo kwa uongozi katika kila kituo cha kutolea huduma za afya ambao husimamia utoaji wa huduma katika kituo husika kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imebaini udhaifu wa utekelezaji wa utaratibu uliowekwa. Hii imedhihirishwa na ukweli kwamba hata katika vituo vyenye dawa za kutosha na watumishi wa kutosha pamoja na vitendea kazi vingine bado malalamiko yamekuwepo. Tofauti kati ya halmashauri zinazofanya vizuri na zile zinazofanya vibaya ni uongozi madhubuti katika ngazi mbalimbali za usimamizi. Kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara inaendelea kuboresha utekelezaji wa taratibu zote zilizowekwa ikiwa ni pamoja na kuboresha usimamizi wa utoaji wa huduma bora za afya katika vituo vyote nchini.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Sekta ya Afya hutenga fedha za Mfuko wa Pamoja (HSBF) kwa ajili ya kununua dawa, vifaa tiba na kadhalika:-
(a) Je, Serikali imejipanga vipi kuboresha mfumo wa manunuzi ili kupunguza mlolongo mrefu wa manunuzi uliopo sasa wa Halmashauri kutoa fedha, kisha kusubiri mpaka MSD itafute mzabuni mwingine?
(b) Mgao unaotolewa kutoka MSD kwenda vituoni ni kwa vituo vyenye fedha tu; Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa vituo vyote vinapata dawa kwa wakati ili kuhudumia wananchi wake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali, naomba nitumie nafasi hii kwa heshima na taadhima kuwashukuru Wabunge wenzangu wote wa CCM kwa kunipa kura nyingi, nami nawaahidi sitowaangusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha mfumo wa ununuzi wa dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi, Wizara inaomba Halmashauri kuwasilisha mapema maombi ya kununuliwa dawa na vifaa hivyo, ili MSD iweke kwenye mpango wake wa mwaka mzima wa manunuzi. Pia MSD imeingia mkataba, yaani frame work contracts na washitiri ili kupunguza mlolongo mrefu wa manunuzi ya dawa kwa sasa, mikataba hii, itasaidia Halmashauri kupata dawa katika muda mfupi zaidi.
Pia, MSD imeingia mkataba na washitiri wa ndani, yaani prime venders ili waweze kusambaza dawa pale ambapo zitakosekana katika maghala ya bohari ya dawa MSD. Idadi ya washitiri wa ndani kwa sasa imefikia 13 na juhudi zinafanyika kuongeza idadi hiyo ili kuimarisha utoaji wa huduma za dawa nchini. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pia imewasilisha mapendekezo ya kufanya mapitio ya Sheria ya Manunuzi, ili dawa ziweze kununuliwa kwa muda mfupi zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mgao wa dawa unaotolewa kutoka MSD kwenda vituoni, Serikali imetoa maelekezo kwamba, vituo vyote vya umma vipatiwe dawa bila kujali kama vina deni MSD. Pale Wizara inapopata mgao wa fedha kutoka Hazina madeni hayo hulipwa, pia Wizara yangu imeagiza Halmashauri kutumia vyanzo mbadala vya mapato kama vile Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) makusanyo ya papo kwa papo na fedha toka Bima ya Afya (NHIF), zitumike kununulia dawa ili kuziba pengo la bajeti toka Serikali Kuu. Fedha zingine ni za Mfuko wa Pamoja, (Health Basket Fund), ambapo asilimia 67 inatakiwa itumike katika kununulia dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi. Vyanzo vyote hivyo vikitumika na kusimamiwa vizuri, vitapunguza sana pengo la bajeti kutoka Serikali Kuu.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Serikali kupitia mfumo wa Bima ya Taifa ilitoa tenda kwa kampuni moja binafsi kwa ajili ya kufunga mfumo wa kielektroniki wa kutunza kumbukumbu za wagonjwa na taarifa za Bima:-
(a) Je, ni fedha kiasi gani ilitumika kwa hospitali hizo kufunga mfumo huo?
(b) Je, ni kwa kiasi gani Serikali ilizingatia thamani halisi ya fedha (value for money) ukilinganisha na mahitaji makubwa katika sekta ya afya kama madawa, vifaatiba na watumishi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwaniaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Zabuni hii ilitangazwa Kimataifa ambapo kampuni za ndani na za nje ziliruhusiwa kushiriki. Na jumla ya kampuni 17 ziliwasilisha zabuni zao. Baada ya mchakato wa uhakiki, kampuni ya Maxcom Africa Limited ya hapa nchini ikishirikiana na kampuni ya Sevenhills E-Health PVT LTD ya nchini India zilishinda zabuni hii. Thamani ya zabuni hiyo ni shilingi 5,887,079,539 ikijumuisha kodi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini zabuni hii ilizingatia thamani halisi ya fedha kutokana na uzoefu ambao Wizara yangu imeupata kwa kuimarisha mifumo ya habari na mawasiliano, ambao ni pamoja na vituo kuongeza mapato ambayo yamepelekea kuongezeka kwa ari na tija katika vituo vyetu. Vile vile, zabuni imewezesha upatikanaji wa taarifa na takwimu za uhakika kuhusu huduma za afya nchini. Taarifa hizi zinasaidia katika mipango mbalimbali na utoaji taarifa mbalimbali kwa wadau wa sekta ya afya pamoja na tafiti mbalimbali zinazohusu sekta hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani ya Wizara yangu kuwa, kwa kuwa na mifumo madhubuti ya kielektroniki katika taasisi hii, tutaweza kuongeza tija katika utoaji huduma za afya kwa wananchi wetu hasa tunapoelekea kuwa na Bima ya Afya ya lazima kwa kila mwananchi. Aidha, kwa kupitia zabuni hii sasa Taasisi yetu ya NHIF (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya) imeweza kupata mfumo halisi (source code) inayoumiliki na kuwezesha mfumo huu kuwekwa katika vituo vingine nchini katika siku za usoni.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR (K.n.y. MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR) aliuliza:-
Vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia unaendelea kushamiri Tanzania hususan Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Visiwa vya Zanzibar, watoto wengi wanakataa kwenda shule kutokana na udhalilishaji huo. Aidha, wengi wao wanaogopa kunyanyapaliwa ama kuona haya au aibu juu ya vitendo wanavyofanyiwa watoto wa kiume na wa kike:-
(a) Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha suala hilo linapungua au linaondoka kabisa?
(b) Je, Serikali ya Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Zanzibar inawasaidiaje watoto hawa ili waendelee na masomo bila kunyanyapaliwa?
(c) Je, Serikali haioni kuwa haiwatendei haki watoto hawa kwa kuonekana watuhumiwa nje wakati wamewavunjia utu na maisha yao kwa kisingizio cha ushahidi haujakamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Mussa Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Taifa wa kudhibiti ukatili dhidi ya watoto wa mwaka 2013 - 2016, malengo ya mpango huu yakiwa ni pamoja na kuanzisha na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto, kuanzisha na kuimarisha Dawati la Jinsia na Watoto katika vituo vyote vya Polisi nchini, kuendelea kutoa mafunzo ya elimu ya malezi chanya kwa wazazi, Walimu na wanajamii, kuendesha mafunzo kuhusu Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 kwa wasimamizi wote wa sheria na kusimamia utekelezaji wake na kuhamasisha utumiaji wa huduma ya mtandao wa simu ya kusaidia kutoa taarifa za ukatili dhidi ya mtoto kwa kutumia Child Help Line Number 116.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo Serikali za Mitaa inaziwezesha Kamati za Ulinzi na Usalama wa Mtoto kutambua na kutatua matatizo ya watoto yakiwemo ya kisheria, kisaikolojia na kielimu.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendeshwa kwa mujibu wa sheria ambapo haki za raia wote ikiwemo haki za watoto zinalindwa na kusimamiwa kikamilifu. Mtuhumiwa wa vitendo vya ukatili anapokamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, taratibu za uendeshaji kesi hufuatwa ikiwa ni pamoja na kuithibitishia Mahakama kuwa kweli mtuhumiwa katenda kosa ua la. Hivyo, Serikali haipendi kuwaachia watuhumiwa wa vitendo vya ukatili punde wanapokamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, bali mara nyingi kunakosekana ushirikiano wa jamii katika kutoa ushahidi wa kumtia hatiani mtuhumiwa.
MHE. ANNA R. LUPEMBE (K.n.y. MHE. HALIMA ALI MOHAMED) aliuliza:-
Serikali imedhamiria kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga wakati wa kujifungua:-
Je, Serikali ina mikakati gani kufanikisha dhamira hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohamed, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kupunguza vifo vya wanawake wajawazito, pamoja na watoto wachanga kwa kuweka mipango na mikakati mbalimbali ikiwemo; kwanza, kupandisha hadhi Vituo vya Afya na kuviwezesha kufanya huduma za upasuaji wa dharura wa kutoa mtoto karibu zaidi na wananchi. Hadi sasa vituo 189 vimeshakamilika na vinafanya kazi hiyo.
Pili, kuanzisha Benki ya Damu kwa kila Mkoa ili kuimarisha upatikanaji wa damu; tatu, kugawa kwa wajawazito vifaa muhimu vinavyotumika wakati wa kujifungua; nne, kutoa kutoa huduma majumbani kwa wajawazito hadi wiki sita baada ya kujifungua; na watoto chini ya miaka mitano kwa kuwatumia Wahudumu wa Afya katika Jamii; na tano, kuendelea kutekeleza Sera ya Afya ya kutoa huduma bila malipo kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, lengo likiwa kuhakikisha kwamba makundi haya maalumu yanapata huduma muda wote bila kuchelewa. Ili kuhakikisha kwamba haya yanatekelezwa, Serikali kwa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, imeandaa mpango mkakati wa mwaka 2016 hadi 2020, wenye mikakati ifuatayo:-
(1) Kuboresha huduma zinazotolewa kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga, ikiwa ni pamoja na kuwapatia watoa huduma ya afya elimu kazini, kuongeza dawa, vifaa tiba na vitendea kazi;
(2) Kutoa elimu kwa jamii na hasa vijana kuhusu afya ya uzazi, pamoja na kutilia mkazo juu ya lishe bora;
(3) Kushirikisha jamii katika mambo yanayohusu afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja na kuwahimiza wanawake wajawazito wajifungulie katika vituo vya kutolea huduma ya afya; na
(4) Kushirikisha wadau mbalimbali na kufanya kazi kwa pamoja, kwa kutekeleza afua zenye matokeo makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutekeleza haya, tunaamini kwamba vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga vitaendelea kushuka kwa kasi siku hata siku.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR (K.n.y. MHE. KHATIB SAID HAJI) aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitoa huduma za dawa bila malipo kwa baadhi ya maradhi kama vile UKIMWI, TB na kadhalika:-
(a) Je, ni maradhi ya aina gani yaliyo katika orodha ya kupatiwa dawa bila malipo?
(b) Je, ni kwa kiasi gani Serikali imefanikiwa kufikia malengo katika mpango huo wa kusaidia wananchi kupata dawa hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Jimbo la Konde, lenye Sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 kifungu cha 5.4.8 (3) kuhusu msamaha wa uchangiaji wa gharama za huduma za afya kwa makundi maalum ambayo yanapatikana (uk.29) wa Sera ya Afya, inayataja maradhi ambayo yatatibiwa bure kuwa ni Saratani, UKIMWI, Kisukari, magonjwa ya Moyo, Pumu, Seli Mundu (Sickle cell), Kifua Kikuu, Ukoma na magonjwa ya akili.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha wagonjwa wote walioandikishwa na wenye vigezo vya kupata dawa zinazotolewa bure wanapata dawa hizo.
Kwa mfano, kwa magonjwa ya UKIMWI na Kifua Kikuu, aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge kwenye swali lake, wagonjwa wote kwa asilimia 100, walioandikishwa na wenye vigezo wanapata dawa hizo bila malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mara chache sana hutokea wagonjwa wakakosa dawa. Serikali inaendelea kuongeza fedha za bajeti ya dawa pamoja na kutumia asilimia 50 ya mapato ya vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya manunuzi ya dawa na vifaa tiba ili kuhakikisha pale penye upungufu wa dawa zinakuwepo kwa ajili ya kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
MHE. ASHA A. JUMA aliuliza:-
Kumekuwa na muingiliano wa wananchi kuishi karibu, ndani au pembezoni mwa maeneo ya Kambi za Jeshi kama ilivyo kwenye Kambi ya Chukwani.
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenganisha maeneo hayo na makazi ya wananchi kwa kuweka mipaka madhubuti?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia suala hili mapema ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea baina ya Jeshi na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (Kn.y WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Jeshi, yale ya makambi, ya mafunzo au vikosi yana mwingiliano mkubwa na wananchi au taasisi zingine. Mwingiliano huu husababishwa na wananchi wenyewe kutoelewa mipaka vizuri, lakini walio wengi huingia kwa kujua na wakati mwingine husaidiwa na wataalam wa Ardhi wa Manispaa na Halmshauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili linashughulikiwa kupitia marekebisho ya sheria ili kuimaliza migororo hiyo.
(a) Serikali inaona umuhimu mkubwa kuyatenganisha maeneo hayo yasiwe na mwingiliano na wananchi au taasisi zingiene. Hatua zinazochukuliwa ni kujenga kuta au uzio wa waya kwenye maeneo madogo lakini kuna mpango wa kupanda miti kwenye maeneo makubwa sambamba na kuweka mabango makubwa ya tahadhari.
(b) Serikali kupitia Jeshi, tayari imeanza mikakati ya kupanda miti kwenye maeneo ya kambi. Hivi sasa upo mkakati kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 wa kuanzisha vitalu vya miti kwenye baadhi ya kambi kwa ajili hiyo.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR (K.n.y. MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR) aliuliza:-
Suala la Madaktari feki limezoeleka nchini Tanzania na linazidi kuendelea siku hadi siku katika hospitali zetu:-
(a) Je, Serikali haioni kuwa suala hili ni kuhatarisha maisha ya Watanzania kutokana na uzembe na usimamizi mbovu wa hospitali zetu?
(b) Je, Serikali imechukua hatua gani kuondoa kadhia/ kero hii isiendelee?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainabu Mussa Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa suala hili la madaktari feki linahatarisha afya na maisha ya Watanzania. Mara nyingi tatizo hili linatokea katika hospitali zenye idadi kubwa ya Madaktari, hali inayowapa urahisi Madaktari feki kutotambulika upesi. Kwa kutambua hali hii Serikali imeweka utaratibu wa kudhibiti uwezekano wa kuwepo kwa Madaktari feki kwa kufanya mambo yafuatayo:-
(1) Kuimarisha utendaji wa Baraza la Madaktari na Madaktari wa Meno linalosajili na kusimamia utendaji kazi wa Madaktari na Madaktari wa Meno. Baraza hili linahakikisha kuwa Madaktari na Madaktari wa Meno wenye sifa zinazostahili ndio wanasajiliwa na kuruhusiwa kutoa huduma. (Makofi)
(2) Kuimarisha usimamizi wa watumishi ikiwa ni pamoja na Madaktari katika vituo. Utekelezaji wake unajumuisha kuvaa vitambulisho vinavyoonesha majina ya watumishi na kwamba Daktari ambaye ni feki itamuwia vigumu sana kuvaa kitambulisho feki na hivyo kumfanya aonekane kwa haraka.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ambazo Serikali imechukua kuondoa kadhia/ kero hiyo ni pamoja na kuhakikisha kuwa:-
(1) Madaktari wote walio kazini wanavaa vitambulisho vinavyoonesha majina yao.
(2) Viongozi wote wanaosimamia sehemu za kutolea huduma wanawafahamu vyema watumishi walio chini yao ikiwa ni pamoja na Madaktari.
(3) Viongozi wa vituo vya kutolea huduma (hospitali za ngazi zote, vituo vya afya na zahanati) wanahakiki kila mtumishi anayefika kituoni kuanza kazi baada ya kuajiriwa au kuhamishiwa katika kituo husika kutoka sehemu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hizi zinachukuliwa ili kudhibiti hali hiyo kwa sababu kila siku Madaktari feki hawa wanakuja na mbinu mpya za kujificha wakati wakifanya vitendo vyao viovu.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Nachingwea ni miongoni mwa Wilaya chache zilizo na historia ndefu katika kusaidia nchi nyingi za Afrika kupata uhuru; kwani wapiganaji wengi wa nchi hizo walihifadhiwa kwenye Kambi ya Ukombozi Farm 17 iliyopo Nachingwea:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhifadhi na kuendeleza maeneo ya Kambi ya Farm 17 hata kama yamegeuzwa kuwa Sekondari ili kuwa maeneo ya kihistoria na kuweza kuwavutia watalii?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzishawishi nchi zilizonufaika na Kambi ya Farm 17 kama Msumbiji na Zimbabwe ili ziangalie kwa karibu kambi hiyo kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu muhimu zilizopo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO – (K.n.y WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala Mbunge wa Jimbo la Nachingwea kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Farm17 ni miongoni mwa maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika katika harakati za ukombozi. Serikali kwa kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo Sanaa na Vijana imeanzisha mradi ujulikanao kama Road to Independence kwa lengo la kutunza kumbukumbu za historia ya ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo Farm 17. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itashirikiana na Wizara hiyo katika kuhakikisha kuwa eneo hili linatunzwa ipasavyo ili kuvutia watalii wakaolitembelea. Aidha, tunapenda kuushauri uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kusaidia shule ya sekondari Farm 17 kuendeleza uhifadhi wa miundombinu ya kihistoria iliyopo shuleni hapo ili kutunza historia hiyo muhimu ya ukombozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina mpango wa kuzishawishi nchi zilizopata hifadhi ya wapigania uhuru hapa nchini, kusaidia juhudi za uhifadhi wa maeneo hayo kwani nchi zenyewe zina hiari ya kuona umuhimu huo kwani lengo la Serikali ilikuwa ni kusaidia harakati za ukombozi kwa nchi husika.
MHE. RUTH H. MOLLEL aliuliza:-
Kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikipeleka viongozi na wananchi wengine nje ya nchi kwa matibabu yanayohitaji utaalam wa hali ya juu:-
(a) Je, Serikali imetumia kiasi gani cha fedha kwa matibabu nje ya nchi kuanzia mwaka 2011 – 2015?
(b) Je, Serikali imetumia kiasi gani cha fedha kununua vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya Hospitali za Mikoa ambazo kwa sasa zimepandishwa hadhi na kuwa za rufaa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Hiyob Mollel, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu sahihi zilizopo za fedha iliyotumika kwa matibabu ya nje ya nchi kuanzia mwaka 2012 ni Sh.32,856,890,858.90. Takwimu za miaka ya nyuma ya hapo zilizopo hazina usahihi wa kutosha na zinaendelea kufanyiwa kazi na pindi zitakapokaa sawa tutamkabidhi Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya rejea yake.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kiasi cha fedha zilizotumika kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya Hospitali za Rufaa za Mikoa zilizopandishwa hadhi ni sh. 4,128,262,150/=. Mchanganuo wa fedha hii ni kama ifuatavyo:-
(i) Mgao wa kawaida wa fedha za kununulia vifaa ulikuwa ni sh. 2,292,187,500.
(ii) Mkopo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa ajili ya kununulia vifaa uliotolewa kwa Hospitali za Rufaa ngazi ya Mkoa ni sh.1,836,074,650.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Hivi sasa kumeibuka wimbi kubwa la wagonjwa wa kisukari na miongoni mwa waathirika ni wanawake wenye kipato cha chini:-
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kisukari katika zahanati na vituo vya afya vya Serikali ili kusaidia watu wasio na uwezo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa ugonjwa wa kisukari ni moja ya magonjwa yasiyoambukizwa yanayoongezeka kwa kasi hapa nchini. Kitaalam imethibitika kuwa moja ya sababu kubwa ya ongezeko la ugonjwa wa kisukari hasa kwa watu wazima linatokana na mtindo wa maisha kama vile kutokufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika,ugonjwa wa kisukari unahitaji wataalam wenye ujuzi wa kumchunguza mgonjwa na kuhakikisha maendeleo yake ya kiafya yanakuwa mazuri na pia kubaini magonjwa yatokanayo na kisukari na kuyadhibiti mapema kabla hayajaleta madhara kwa mgonjwa. Madhara yake mara nyingi ni kama vile kukatwa mguu, athari kwenye macho, figo na moyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu sasa huduma za matibabu ya kisukari zimekuwa zikipatikana katika ngazi ya Hospitali ya Wilaya. Hii imetokana na ukosefu wa watumishi wenye ujuzi na weledi wa kuhudumia wagonjwa wa kisukari katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya. Pia mwongozo wa matibabu yaani standard treatment guidelines umeelekeza dawa za kisukari kupatikana kuanzia ngazi ya Hospitali ya Wilaya na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho yanayoendelea katika sekta ya afya ikiwemo kutoa mafunzo kwa watoa huduma katika ngazi za zahanati na vituo vya afya, Serikali itaanza kutoa huduma za matibabu ya kisukari katika ngazi hizo kwa awamu kuanzia kwenye vituo ambavyo watoa huduma wamepata mafunzo. Mpaka sasa watumishi wapatao 150 wamepewa mafunzo kuhusu matibabu ya akinamama wajawazito wenye matatizo ya ugonjwa wa kisukari. Pia mwongozo wa matibabu utafanyiwa mapitio na Wizara yangu ili uendane na mahitaji ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwapima wagonjwa wa kisukari zinakuwepo katika vituo vyote vya huduma za afya zenye kliniki za wagonjwa wa kisukari katika halmashauri zote zilizopo hapa nchini. Pia utoaji wa Huduma za Mkoba (Outreach clinics) utaimarishwa katika maeneo yasiyo na kliniki.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa IV wa Afya wa mwaka 2015 – 2020, mwelekeo ni kuongeza kasi ya kuzuia kuongezeka kwa wagonjwa wa kisukari kupitia uelimishaji kwenye jamii na mashuleni. Pia uhamasishaji wa kula vyakula visivyoongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari na kufanya mazoezi. Vilevile utambuzi wa mapema wa ugonjwa na kupata matibabu mapema kupitia mifumo iliyopo ni mambo ya kipaumbele katika miaka mitano ya kutekeleza mpango mkakati wa sekta ya afya.
Watoto wengi nchini wameendelea kudhalilishwa kwa kukosa malezi bora ya wazazi wao hali inayosababisha waishi maisha ya kuombaomba na kwa kuwa baadhi ya wazazi wanaosababisha hali hiyo ni wanaume wanaoharibu maisha ya wasichana kwa kuwapa mimba na kukwepa jukumu la kulea watoto wanapozaliwa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwabaini wanaume hawa na kuwafikisha mahakamani kwa kosa la kuwatelekeza watoto na kuwasababishia mateso na kuwanyima haki zao za msingi?
(b) Je, ni lini Serikali italeta Bungeni muswada wa kufanya marekebisho katika sheria husika ili kuwashughulikia wazazi wanaowatelekeza watoto wao kwa kutowahudumia ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mipango mbalimbali ya kuwababini wanaume wanaotelekeza familia na vitendo vingine vya unyanyasaji. Mipango hiyo ni pamoja na Mpango wa Muitikio wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili Dhidi ya Watoto wa mwaka 2013 hadi 2016 na Mpango wa Kuzuia Ukatili Dhidi ya Wanawake wa mwaka 2005 – 2015. Mipango hiyo hivi sasa inaunganishwa kuwa mpango mmoja wa Kitaifa ili uweze kukidhi haja za upatikanaji wa taarifa zinazohusu ukatili dhidi ya watoto na wanawake ikiwemo utelekezaji wa familia. Kupitia mpango huu, Serikali itahamasisha jamii kuibua vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kuwabaini wahusika na vitendo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara yangu imeanzisha mtandao maalum wa mawasiliano kwa ajili ya kutoa taarifa mbalimbali za ukatili dhidi ya watoto (the child helpline number 116) ambapo mtoto mwenyewe au mtu mwingine kwa niaba ya mtoto huweza kuripoti tukio lolote la ukatili dhidi ya watoto. Vilevile, Wizara inatekeleza Mpango wa Ulinzi na Usalama wa Mtoto wa mwaka 2013 – 2017 na kupitia mipango hii jamii zimekuwa zikielimishwa masuala mbalimbali yanayohusu ukatili, unyanyasaji na mazingira hatarishi kwa watoto na wanawake ili waweze kutoa taarifa ya matukio hayo yanapotokea na kuwabaini wahusika ili kuchukuliwa hatua stahiki.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 imezingatia suala zima la utoaji wa malezi, matunzo na ulinzi kwa kutoa majukumu kwa wazazi, walezi, jamii pamoja na Serikali. Aidha, kifungu cha 14 cha sheria hiyo kimeweka adhabu kwa wazazi au walezi watakaokiuka kutoa malezi bora kwa kulipa faini ya shilingi milioni tano za kitanzania au kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijapokea changamoto yoyote inayohitaji marekebisho kuhusu utekelezaji wa kifungu hiki cha sheria.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Bei ya dawa za binadamu imekuwa ikipanda kila wakati na Serikali imekaa kimya wakati wananchi wake wanaumia:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha chombo maalum cha kudhibiti bei ya dawa za binadamu hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Seleman Nkamia, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli dawa za binadamu huwa zinapanda mara kwa mara kutokana na ukweli kwamba asilimia 80 ya mahitaji ya dawa yananunuliwa kutoka nje ya nchi. Pale ambapo sarafu yetu inaposhuka thamani, au sarafu ya dola inapopanda, basi bidhaa mbalimbali toka nje ya nchi zikiwemo dawa hupanda bei. Ili kudhibiti upandaji wa bei za dawa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara na Viwanda, tunaandaa mkakati wa kuongeza uzalishaji wa dawa ndani ya nchi ili angalau kukidhi asilimia 60 ya mahitaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pia inaangalia uwezekano wa kuunda chombo cha kusimamia gharama na bei zinazotozwa na vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na bei za dawa na vifaa tiba. Vile vile bohari ya dawa imeandaa mipango ya kuanza kununua dawa moja kwa moja, toka kwa wazalishaji ili kudhibiti bei za dawa na kuongeza upatikanaji wake, kwa bei nafuu. Naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati mikakati hii ya kudhibiti bei za dawa inaendelea kutekelezwa.
MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza:-
Benki nyingi nchini zimekuwa na Riba kubwa, hali ambayo inafanya wanawake washindwe kukopa kujiinua kiuchumi. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Benki ya Wanawake Mkoa wa Songwe ili wanawake wajasiriamali wanufaike na mikopo hii ya riba nafuu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Benki ya Wanawake Tanzania ni kusambaza huduma zake katika maeneo yote ya Tanzania ikiwemo Mkoa wa Songwe. Hata hivyo, azma hii inakwamishwa na mtaji mdogo wa benki hii, ndiyo maana kwa sasa imejikita zaidi katika kutoa huduma zake kwa kutumia vituo vya mikopo ambapo hadi sasa benki ina vituo 89 katika mikoa saba ukiwemo Mkoa wa Mbeya ambao hadi mwaka 2015 ulikuwa sehemu ya Mkoa huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango mkakati wa Benki ya Wanawake wa mwaka 2014/2017 ni kufungua angalau matawi matatu kila mwaka. Hii itawezekana tu endapo mtaji wa benki utakuwa kama inavyotegemewa. Hivyo benki itauingiza Mkoa mpya wa Songwe kwenye mipango yake ya upanuzi wa huduma kwa mwaka 2017/2018.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Kumekuwepo malalamiko kwa upande wa huduma za afya kwa wanajeshi wetu ambao kimsingi hawana Bima ya Afya kwa sababu Jeshi lina zahanati na hospitali.
Je, Serikali haioni haja ya kuwapatia wanajeshi Bima ya Afya?
SPIKA: Naomba tuendelee kwa sababu kwa kweli Mheshimiwa Naibu Waziri ameshajibu na swali hili pia katika majibu yake swali la 10 limeshapata majibu. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi.
Kuanzisha Mfuko wa Kulinda Ustawi wa Watoto Nchini

Ni wajibu wa Serikali kulinda na kuhakikisha ustawi wa watoto katika nchi;
Je, ni lini Serikali itatenga asilimia ya mapato yake katika bajeti ili kuwepo na Mfuko wa Kulinda Ustawi wa Watoto wa nchi hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ina wajibu kulinda na kuhakikisha ustawi na maendeleo ya watoto nchini, wajibu huu umeainishwa katika Katiba, Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali kuhakikisha kuwa watoto wote nchini wanapata haki zao za msingi. Baadhi ya jitihada hizo ni pamoja na kutoa msamaha wa huduma za afya kwa wototo wenye umri chini ya miaka mitano na akina mama wajawazito, kutoa elimu bure kwa watoto kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali kupitia Wizara yangu na wadau mbalimbali wa watoto imekuwa ikitoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa wazazi, walezi, familia na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa matunzo na ulinzi wa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa haijaona umuhimu wa kuanzisha Mfuko Malaam wa Watoto kwa kuwa, afua zilizopo zinakidhi mahitaji. Hata hivyo, nachukua fursa hii kutoa wito kwa wazazi, walezi, familia na jamii kwa ujumla kutekeleza wajibu wao katika makuzi na maendeleo ya watoto kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ni wajibu wa Serikali ambazo ziko katika mamlaka za Serikali za Mitaa, kuhakikisha kuwa mamlaka zenyewe zinaweka mipango madhubuti ya kulinda ustawi na maendeleo ya watoto katika maeneo yao. Wakati huo Serikali itaendelea kusimamia na kuratibu huduma zinazotolewa kwa watoto ili kuhakikisha kuwa haki na ustawi wao unazingatiwa ipasavyo kama ilivyoainishwa katika Katiba, Sheria na Mikataba mbalimbali ya Kimataifa iliyoridhiwa na nchi yetu.
Mheshimiwa Niabu Spika, suala la ulinzi, ustawi na maendeleo ya watoto ni mtambuka, hivyo, naomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kuwa Halmashauri zetu zinatenga bajeti katika maeneo haya yanayohusu ustawi wa watoto.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Mwongozo wa fedha za wafadhili wanaochangia katika Sekta ya Afya (Health Basket Fund) katika Halmashauri zetu unaelekeza asilimia 33 ya fedha hizo zitumike kwa manunuzi ya dawa na asilimia 67 zitumike katika shughuli za utawala, uaimamizi na ufuatiliaji;
(a) Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kubadili mongozo huu?
(b) Je, ni lini Serikali taacha kutegemea fedha za wafadhili na hasa katika Sekta ya Afya.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsate. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso Mbunge wa Viti maalum lenye sehemu A na B kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haiwezi kubadili mwongozo wa mgao huo kwasababu unalindwa na makubaliano baina yake na wadau wa mfuko wa pamoja wa Afya (Health Basket Fund). Hata hivyo, kwa kuzingatia mahitaji ya sasa Serikali inaangalia uwezekano wa kufanya mapitio ya makubaliano hayo na wadau wa Health Basket Fund.
(b) Mheshimwa MWenyekiti, Serikali haitegemei fedha za wafadhili kuendesha huduma za Afya kwa asilimia 100. Wafadhili wanachangia tu gharama za baadhi ya huduma. Uchumi wa nchi yetu utakaporuhusu utegemezi utapungua kama siyo kwisha kabisa. Hata hivyo, katika kuelekea kujitegemea, Serikali imetengeneza mkakati wa ugharamiaji huduma za afya na imeandaa mapendekezo ya Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ambayo yatawasilishwa hapa Bungeni pindi mchakato wa ndani ya Serikali utakapokamilika. Mheshimiwa Mwenyekiti, inatarajiwa Sheria hii kama itapitishwa na Bunge lako tukufu kila Mtanzania atapata huduma za Afya kwa kadi yake bila kiwazo cha kifedha.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vituo vya kulelea watoto wasio na makazi katika kila kanda nchini na kuwjajengea stadi za kazi na ujasiriamali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima, Abdallah Bulembo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua haki ya msingi ya mtoto ya kulelewa katika familia Serikali kwa sasa haina mpango wa kuanzisha vituo vya kulelea watoto wasio na makazi katika kila kanda nchini kwa sababu jukumu la kutoa malezi kwa watoto ni la wazazi ama walezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, pale ambapo wazazi ama walezi wamefariki au kwa sababu moja au nyingine wameshindwa kuwalea watoto, jukumu hio linapaswa kuchukuliwa na ndugu ama jamaa au wana jamii wengine. Lakini pale inaposhindikana watoto hao hulazimika kulelewa katika makao kwa ajili ya malezi ikiwa ni hatua ya mwisho baada ya njia nyingine kushindikana. Na wanapokuwa makaoni hupatiwa huduma zote za msingi kama chakula, malazi, matibabu, elimu ya msingi na sekondari, msaada wa kisaikolojia na kijamii na stadi za maisha, ufundi na ukasiriamali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kutekeleza Mpango wa Ulinzi na Usalama wa Mtoto kwa Mwaka 2013/2017 katika jitihada za kuboresha malezi ya watoto kwa kuimarisha mfumo wa malezi, matunzo na ulinzi wa watoto katika ngazi ya familia na jamii. Kupitia mpango huo Wizara kwa kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa, pamoja na wadau wa maendeleo imeanzisha timu za ulinzi na usalama wa mtoto katika ngazi ya halmashauri, kata na vijiji ama mitaa katika halmashauri 38 nchini. Zoezi la uanzishwaji wa timu hizi linaendelea ili kufikia halmasahuri zote nchini.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) aliuliza:-
Katika Jimbo la Muhambwe kuna Chuo cha Wauguzi (MCH) ambacho ni muhimu sana katika sekta ya afya, lakini hakiko katika hali nzuri.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukiboresha chuo hicho na vingine vya aina hiyo ili viweze kujiendesha na kulipa wazabuni wengi ambao wanawadai?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Uuguzi na Ukunga Kibondo kilichopo Jimbo ka Muhambwe, ni kati ya vyuo sabini na saba ambavyo vinamilikiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Vyuo hivi vilijengwa kwa nguvu ya Serikali na wadau wa maendeleo miaka michache baada ya uhuru, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa watumishi wa afya na kipaumbele ikiwa ni afya ya msingi kwa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Wizara kujikita katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) mwaka 2007, tumekuwa tukitenga fedha za maendeleo kwa ajili ya kufanya ukarabati na upanuzi ili kukidhi ongezeko la udahili wa wanafunzi kwa lengo la kufikia udahili wa wanafunzi 10,000 kwa mwaka na pia kushirikisha sekta binafsi katika kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hili la udahili limeongeza mahitaji ya kupanua miundombinu na pia kufanya ukarabati wa mara kwa mara kukidhi ongezeko hilo. Wizara imekuwa ikitenga fedha za ukarabati kupitia Mfuko wa Fadhili wa Pamoja yaani Basket Fund hadi mwaka 2006/2007. Kutokana na kusitishwa kwa fedha za basket mwaka 2006, majengo mengi ya Wizara hayakukamilishwa na kubakia magofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali imejikita katika kutenga fedha zake za ndani kukamilisha majengo hayo kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa mwaka wa 2016/2017, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni nane kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Vyuo vya Afya vya Serikali, ambapo Chuo cha Uuguzi na Ukunga Kibondo kimetengewa Sh. 630,000,000)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya wazabuni, ni kweli Wizara inadaiwa na wazabuni mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa huduma za vyakula vibichi, vya kupikwa na huduma zinazoendana na ukamilishaji wa huduma hiyo, ambapo malimbikizo ya madeni kuanzia mwaka 2009 hadi 2015 yalifikia jumla ya sh. 6,859,299,159.05. Madeni yote hayo yamehakikiwa na yanasubiri upatikanaji wa fedha toka Serikalini ili yaweze kulipwa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kuanzia mwaka wa masomo 2015, huduma hii haigharamiwi na Serikali tena bali sekta binafsi imepewa fursa kutoa huduma kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE (K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO) aliuliza:-
Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inaainisha kuwa, mtu akifika umri wa miaka 18 huyo ni mtu mzima na Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, Ibara ya 13 inasema umri wa msichana kuolewa ni miaka 15 na mvulana kuoa ni miaka 18:-
Je, ni lini Serikali itaifanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa, ili watoto wa kike wasiolewe na umri mdogo kama ilivyo sasa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa, kumekuwa na mkanganyiko kati ya Sheria hizo mbili, hususan kuhusu umri wa kuolewa, kwani Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 katika Kifungu cha nne imetafsiri mtoto kuwa ni mwenye umri chini ya miaka 18, ingawa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, Kifungu cha 13, kinaruhusu mtoto wa chini ya miaka 15 kuolewa. Serikali ilishaanza kufanyia kazi marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 baada ya kupokea taarifa ya Tume ya Kurekebisha Sheria ya mwaka 1996 kuhusu sheria kandamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya kazi zilizofanyika ni pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria kuandaa Waraka Maalum wa Serikali (White Paper) kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi kuhusu marekebisho ya Sheria hiyo. Kwa sasa Waraka huo Maalum upo katika ngazi ya Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kutolewa maamuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hii, Serikali pia, imefanya juhudi nyingine, kama vile kutungwa kwa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009, iliyofuta vipengele vya 161 mpaka 166 vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971. Ili kuweka tafsiri moja ya mtoto kuwa ni chini ya umri wa miaka 18. Hatua hii inaifanya sasa Sheria ya Mtoto kutumika katika mashauri mengi yanayohusu haki za mtoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kutambua thamani na haki za makundi yote katika jamii Serikali imeweka Ibara Maalum ya 57 inayohusu Haki za Watoto katika Katiba inayopendekezwa. Hivyo, endapo Katiba inayopendekezwa itapitishwa basi taratibu zitafuata za kufanyia marekebisho Sheria zote kandamizi kwa wanawake na watoto.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-
Kituo cha Utafiti wa Malaria kilichopo Kata ya Vuje, Tarafa ya Gonja, Jimbo la Same Mashariki kimejengwa miaka ya 1960 na kina majengo ya kisasa kumi na kwamba Serikali ilikifanyia ukarabati mkubwa mwaka 2007, lakini mpaka sasa hakifanyi kazi badala yake kimegeuzwa kuwa nyumba za kulala wageni na pesa zinaingia mfukoni mwa watu.
Je, Serikali inafahamu jambo hilo na kama inafahamu inatoa kauli gani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki kuwa ni kweli Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) inamiliki maabara, jengo la utawala na nyumba ya wageni (rest house) katika kituo chake cha Gonja Maore, Wilayani Same. Kulingana na jiografia ya Gonja, rest house hiyo ilijengwa kwa madhumuni ya kufikia wafanyakazi wa taasisi kutoka vituo vyake vingine wanaokwenda pale Gonja katika maeneo hayo kwa malengo ya kikazi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa rest house, licha ya kuhudumia wafanyakazi wa taasisi pia inatoa huduma kwa wananchi ikiwa pia ni mojawapo ya vyanzo vya mapato kwa taasisi. Taasisi imeweka taratibu na miongozo mahsusi inayoongoza utoaji wa huduma katika rest house zake zote ikiwemo ile ya Gonja, katika utaratibu huo wageni wote wanaohitaji huduma katika rest house huwajibika kujisajili katika register ya wageni ya rest house na stakabadhi hutolewa kwa malipo yoyote yatakayofanyika. Hivyo, majengo yote ya kituo yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, iliagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuanzisha maduka ya dawa kwenye hospitali kubwa nchini.
(a) Je, ni lini Serikali itaagiza MSD kufungua duka la dawa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida ili kuwasaidia wananchi kununua dawa kwa bei nafuu tofauti na zile zinazouzwa kwenye maduka ya mitaani?
(b) Je, lini Serikali itasambaza vifaa tiba vya kutosha kama vitanda vya wajawazito katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Hospitali za Wilaya za Mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali zetu, Serikali iliangiza maduka ya dawa yafunguliwe kwenye Hospitali za Kanda na Taifa nchini. Aidha, ikumbukwe kwamba siyo jukumu la Bohari ya Dawa kuuza dawa kwa rejareja moja kwa moja kwa wateja, kuruhusu hili litokee ni kujaribu kunyakuwa fursa ya hospitali husika kupata mapato kwa kuuza dawa kwa wateja hivyo kuzichelewesha kuanza kujitegemea. Ili kutekeleza agizo hilo kwa Tanzania nzima ilionekana itahitajika rasilimali watu na fedha nyingi sana ambapo Bohari ya Dawa peke yake isingeweza kumudu. Kwa hiyo basi, Bohari ya Dawa ilikubaliana na TAMISEMI kuwa hospitali zilizo chini yake basi zifungue maduka yao wenyewe na MSD itakuwa tayari kutoa ushauri wa kitaalam pamoja na kuziuzia dawa na vifaa tiba.
(b) Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Singida inashauriwa kutenga fedha kwenye mgao unaoletwa na Wizara kila robo mwaka pamoja na makusanyo kutoka vyanzo vingine kama Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili iweze kununua vifaa, vitendea kazi pamoja na vitanda vya wajawazito.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Benki ya Wanawake ni chombo muhimu sana hasa kwa wanawake wa Tanzania:-
(a) Je, ni lini litaanzishwa tawi la Benki ya Wanawake katika Mkoa wa Morogoro ili wanawake wa Morogoro wapate kunufaika na benki yao?
(b) Je, kuna mkakati gani wa kuanzisha matawi ya Benki ya Wanawake katika Mikoa yote ya Tanzania ili wanawake waweze kukopa kwa urahisi?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Wanawake Tanzania ilianzishwa mwaka 2009 kwa lengo kuwawezesha wanawake kiuchumi hasa kupata mikopo ya fedha yenye masharti nafuu. Hadi sasa benki hii ina matawi mawili katika Mkoa wa Dar es Salaam.
minne wa 2014-2017, benki imepanga kufungua matawi angalau matatu kwa mwaka kama mtaji utakua kama inavyotegemewa. Hata hivyo, hadi sasa benki haijaweza kufungua matawi katika mikoa mingine kwa sababu haijawa na mtaji wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hii, benki ina mkakati wa kuuza hisa katika soko la hisa mwaka huu 2016 kwa lengo la kupata mtaji wa kutosha ili kutimiza kigezo muhimu cha kupata kibali toka Benki Kuu cha kuanzisha matawi sehemu nyingine hapa nchini ikiwemo Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika kuhakikisha kwamba Benki inasogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi hususan wanawake, kuanzia mwaka 2012 benki imeshafungua vituo 89 vya kutolea mikopo na mafunzo kwa wajasiriamali katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa, Ruvuma na Njombe.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD (K.n.y. MHE. NAJMA MURTAZA GIGA) aliuliza:-
Licha ya kuwa na sheria kali kuhusu udhalilishaji wa wanawake na watoto, bado watoto wadogo wa kike na wa kiume chini ya miaka 10 wameendelea kudhalilishwa, baadhi ya watu wanaowafanyia udhalilishaji ni baba wazazi wa watoto hao:-
(a) Je, Serikali haioni haja ya kuweka adhabu tofauti kwa wazazi wanaobainika kuwaharibu kwa kuwabaka watoto wao wenyewe;
(b) Je, Serikali haioni haja ya kuongeza adhabu kwa kuwahasi wanaume wanaopatikana na tabia hii chafu na ya kikatili, licha ya kuwafunga kifungo cha miaka 30?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009, imeelekeza adhabu kali kwa yeyote atakayebainika kutenda kosa la kumdhalilisha mtoto au kumbaka mtoto ikiwemo kifungo cha miaka 30. Hata hivyo, imekuwa vigumu kuwatia hatiani wakosaji hasa wa ndani ya familia kwa kukosekana kwa ushahidi. Wengi wao wanaogopa kutoa ushahidi kutokana na hofu ya kupoteza moja ya wanafamilia kutokana na adhabu ya kifungo cha maisha. Aidha, kutokana na mtazamo hasi wa jamii, familia nyingi huhofia kudhalilika au kunyanyapaliwa baada ya kubainika mkosaji.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatunga sheria kwa kuzingatia Katiba ya nchi na Mikataba ya Haki za Binadamu, hivyo haitakuwa busara kuwahasi wanaume wanaopatikana na makosa ya aina hii kwa kuwa kumhasi binadamu siyo tu ni ukatili bali pia ni kinyume cha haki za msingi za binadamu.
Serikali pia inaandaa Mpango wa Taifa wa kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Mpango huu utachangia kutoa elimu kwa familia na jamii na kuhakikisha kuwa sheria zinatumika inavyotakiwa ili wahusika wa matukio haya wapewe adhabu wanayostahili na kuwalinda watakaotoa ushahidi wa matukio ya vitendo vya ukatili vinavyofanywa dhidi ya watoto na wanawake. (Makofi)
MHE. JOSEPHINA T. CHAGULA aliuliza:-
Hivi sasa kumeibuka wimbi kubwa la wagonjwa wa kisukari na miongoni mwa waathirika ni wanawake na watoto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kisukari katika Zahanati na Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephina Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, dawa za ugonjwa wa kisukari zinapatikana katika ngazi zote za huduma za afya kwa kupitia utaratibu wa Bohari ya Dawa (MSD). Kwa wananchi walio kwenye Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) wanapata dawa hizo kwa kupitia bima zao. Watoto chini ya umri wa miaka mitano wao wanapata dawa hizi bila malipo yoyote kupitia Mpango wa Taifa wa Kisukari. Kwa wale watu wazima ambao hawamo kwenye NHIF, wao wanazipata kupitia utaratibu wa kuchangia huduma za afya (cost sharing).
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeongeza bajeti ya fedha za kununulia dawa kutoka shilingi bilioni 33 mwaka 2015 hadi 2016 hadi kufikia shilingi bilioni 251.5 kwa mwaka wa Fedha 2016/2017. Hivyo ni matarajio yetu kuwa upatikanaji wa dawa utaongezeka ikiwa ni pamoja na dawa za kutibu magonjwa ya kisukari.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Serikali imekuwa na azma nzuri kujenga zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata nchi nzima:-
(a) Je, ni lini Serikali itapanua Chuo cha MCH Mbulu kinachotoa cheti kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Binadamu kwa kuwa tayari Baraza la Madiwani limekubali kutumia ardhi yake ya akiba?
(b) Je, kwa nini Serikali isitembelee chuo hicho ili kujionea fursa zilizopo?
(c) Je, ni kwa nini pia Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tango FDC kisitumike kama chuo cha VETA kwa sababu kwa sasa hakina taaluma nzuri katika fani mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Uuguzi na Ukunga Mbulu kiliandaliwa kwa ajili ya kukidhi mafunzo kwa ngazi ya cheti kutokana na miundombinu iliyokuwa nayo pamoja na uwezo wa hospitali inayotumika kama sehemu ya mafunzo. Upanuzi wa vyuo kudahili wanafunzi wa kada za juu kwa kawaida huwa unaendeana sambamba na upanuzi wa miundombinu na upatikanaji wa wataalam kwenye hospitali iliyoridhiwa kuwa ni hospitali ya mafunzo. Wizara ya Afya inaishukuru Halmashauri ya Mbulu kwa kuanzisha mchakato wa kukitengea eneo zaidi chuo hiki ili kijipanue zaidi. Wizara itashirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI juu ya upatikanaji wa ardhi hiyo kabla ya kuingiza suala la upanuzi wa chuo hiki katika mipango yetu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imekuwa ikitembelea Chuo cha Mbulu katika taratibu zake za kawaida za kiutendaji. Mwaka 2015/2016, timu za Wizara zimefanya ziara za ufuatiliaji kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya ukusanyaji taarifa na pia katika kukagua miradi ya maendeleo na ukaguzi wa hesabu za mapato na matumizi ya fedha. Kwa mwaka 2016/2017, Wizara itafanya ufuatiliaji kwenye chuo hiki na lengo kuu litakuwa ni kuona utekelezaji wa ahadi hii ya Halmashauri kuhusu upatikanaji wa ardhi.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi – Tango kinatoa mafunzo ya maarifa na stadi katika fani za kilimo na mifugo, ushonaji, useremala, uashi na umeme wa majumbani. Aidha, hutoa pia mafunzo ya udereva kwa muda mfupi wa miezi mitatu. Chuo hiki kina watumishi wapatao 21 na wakufunzi 10. Kwa sasa chuo kina wanachuo 98 ambapo 59 wanachukua mafunzo ya ufundi stadi kwa kufuata mtaala wa Mamlaka ya Ufundi Stadi yaani VETA Level I - III na 39 wanachukua mafunzo ya muda mfupi ya udereva.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vina makubaliano maalum na VETA yaani MOU (Memorandum of Undestanding) ya kutoa mafunzo ya ufundi stadi sanjari na yale ya elimu ya wananchi ambayo yalikuwa yakitolewa tangu awali. Kufuatia makubaliano hayo, vyuo 25 viliboreshwa na kuanza kutoa mafunzo ya ufundi stadi sanjari na mafunzo ya elimu ya wananchi kuanzia mwezi Januari, 2013. Lengo likiwa ni kuhakikisha Vyuo vyote 55 vya Maendeleo ya Wananchi vinatoa mafunzo kwa mifumo yote miwili yaani mafunzo ya elimu ya wananchi na yale ya ufundi stadi (VETA).
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tango kimewekwa katika awamu ya pili ya maboresho hayo.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Je, Serikali imeweka mikakati gani ili kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini inayojengwa Mikindani Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini, Wizara inaendelea kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo katika sekta ya afya ili waweze kuchangia gharama za kukamilisha mradi huu. Vilevile Wizara inaendelea kufanya majadiliano na taasisi mbalimbali za Serikali ambazo zinaweza kutoa mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi huu.
Hata hivyo, katika Bajeti ya mwaka 2016/2017, Wizara imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza kwa awamu nyingine ya ujenzi wa majengo mengine ya kutolea huduma baada ya kukamilika kwa jengo la matibabu ya magonjwa ya nje (Out Patient Department) na mapokezi.
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA aliuliza:-
Hospitali nyingi nchini ikiwemo zilizo katika mji wa Kahama zina upungufu mkubwa wa vifaa tiba kama x-ray na ultra-sound. Nchi ya Kenya baada ya kutambua changamoto ya upungufu wa vifaa tiba ilitunga sera kuhusu kampuni binafsi kuingia ubia na hospitali kununua vifaa tiba na kugawana mapato yanayotokana na vifaa hivyo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuiga mfano huo mzuri wa Kenya ili kunusuru maisha ya wagonjwa wetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumanne Kibera Kishimba, Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya inatambua modules mbalimbali na Serikali inaendelea kuangalia ni kwa jinsi gani inaweza kuzitumia katika eneo hilo. Aidha, Serikali inaendelea kununua vifaa na vifaa tiba na kusambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya kulingana na uhitaji wa eneo husika. Sanjari na hilo, tunaendelea kuangalia mikataba hii ya kampuni binafsi ni kwa jinsi gani tunaweza kuichukua na kuitekeleza katika kusaidia upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba katika hospitali na vituo vyetu vya kutolea huduma za afya hapa nchini.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Hospitali ya KKKT Hydom ilipanda hadhi kuwa Hospitali ya Mkoa muda mrefu, sasa inahudumia Mikoa ya Manyara, Shinyanga, Singida, Arusha na Simiyu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuipandisha hadhi ili iwe Hospitali ya Kanda kuiwezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Hospitali ya KKKT Haydom ilipandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa mwaka 2010. Aidha, hospitali hii haikupandishwa hadhi ili iwe Hospitali ya Mkoa. Mkoa wa Manyara una Hospitali yake ya Rufaa ya Mkoa. Madhumuni ya kuipandisha hadhi Hospitali hiyo yalikuwa ni kuifanya itoe huduma za ngazi ya rufaa ya Mkoa ikisaidiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara. Ili hospitali iwe ya rufaa ngazi ya Kanda, ni lazima iwe na miundombinu bora tofauti na iliyopo sasa, pamoja na watumishi waliopata mafunzo yanayohitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kanda ya Kaskazini tayari kuna hospitali zinazotoa huduma za kibingwa kama KCMC ila kwa vigezo vingine Hospitali hii imeshakaguliwa na imeonekana ina upungufu kadhaa, pale utakapokamilika itatoa huduma hizo. Aidha, hosptiali ya KKKT Hyadom toka awali ilikuwa inahudumia wananchi wa mikoa iliyotajwa. Hali hii inachangiwa na sehemu ya kijiografia iliyopo hospitali hiyo kwani inafikika kirahisi na wananchi wa mikoa hiyo.
MHE. MUNIRA MUSTAFA KHATIBU aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vituo maalum vya kulelea watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kuliko ilivyo sasa ambapo huchanganywa na watoto wenye matatizo mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustafa Khatibu, Mbunge wa Viti Maalum, kwa niaba wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati wanayo mahitaji maalum ukilinganisha na watoto wengine. Matatizo yanayoambatana na kuzaliwa kabla ya wakati au uzito pungufu yaani chini ya kilo 2.5 yanachangia kwa asilimia ishirini na tano ya vifo vya watoto wachanga nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kwamba Serikali wameshindwa kuweka sehemu yao ila imeonekana kuwa ni msaada kuwafanya waweze kupona na kukua katika uhalisia na mazingira bora kama watapewa huduma na wazazi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ilianzisha huduma ya matunzo ya mtoto mchanga aliyezaliwa kabla ya wakati kwa kumbeba kifuani ngozi-kwa-ngozi yaani Kangaroo method na huduma hii ilianzishwa katika hospitali zote za mikoa na baadhi ya hospitali za wilaya na hivi sasa tuna vituo vipatavyo sabini vinavyota huduma hii muhimu hapa nchini. Wizara inaendelea na kazi hii ya kuanzisha vituo hivi kwa kasi zaidi na tunategemea kuanzisha vituo vingine zaidi katika hospitali za wilaya nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa mwaka wa fedha 2016/2017, kwa ufadhili wa fedha za RMNCH Trust Fund, Wizara imenunua vifaa mbalimbali ili kurahisisha uanzishaji wa huduma hii. Vifaa hivyo ni pamoja na vitanda maalum vya kutolea huduma hii, vikombe vidogo vya kulishia watoto hawa ambao mara nyingi hushindwa kunyonya ipasavyo, vipima joto maalum (low reading thermometers), mizani ya kupima uzito na watoto wachanga na mablanketi.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Benki ya wanawake nchini ilianzishwa kwa nia ya kuwasaidia wanawake kupata mikopo kwa haraka na kwa riba nafuu.
Je, ni wanawake wangapi wameshanufaika na mikopo ya benki hiyo kwa Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) ilianzishwa mwaka 2009 katika misingi ya kujiendesha kibiashara ikiwa na jukumu mahsusi la kuwapatia wanawake mikopo yenye masharti nafuu na kwa haraka. Kimsingi benki hii inatoa huduma zake kwa wananchi wote bila ubaguzi na ndiyo maana tunasema hii ni benki pekee kwa wote. Benki ya Wanawake kwa Mkoa wa Dodoma ilianza kutoa huduma zake Disemba, 2012 ikiwa na vituo vinne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Septemba, 2016 benki kwa Mkoa wa Dodoma ilikuwa jumla ya vituo 18. Walionufaika na mikopo katika Benki ya Wanawake katika Mkoa wa Dodoma ni watu 19,740 kwa kipindi cha kuanzia Disemba, 2012 hadi Septemba, 2016; mikopo hii ina thamani ya shilingi 6,231,891,236. Kati ya hao wanawake waliopata mikopo hiyo ni 16,676 yenye thamani ya shilingi 5,063,765,641 sawa na asilimia 81 ya mikopo yote na wanaume wakiwa 3,064 ambao wamepata mikopo yenye thamani ya shilingi 1,168,125,595 sawa na asilimia 19.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Wananchi wamehamasika kujenga zahanati kwenye vijiji vyao lakini baadhi hazijakamilika na hata zile zilizokamilika hazijafunguliwa bado na watumishi nao hawatoshelezi mahitaji; hali hii inasababisha hospitali za mkoa ambazo ndizo za rufaa kuwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya Wilaya hazina Hospitali za Wilaya.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani ya utekelezaji wa kutoa unafuu wa uchangiaji huduma kwa akina mama wajawazito wanaoenda katika Hospitali za Rufaa?
(b) Je, ni lini Serikali itachukulia afya kuwa ni kipaumbele cha nchi hasa ikizingatiwa kuwa afya ni kila kitu katika maisha ya mwanadamu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu (a); Sera ya Afya ya mwaka 2007 inaeleza kuwa huduma za akina mama wajawazito katika vituo vya ngazi zote ni bure na hazipaswi kuchangiwa. Aidha, mwongozo wa uchangiaji pia umesisitiza utekelezaji wa sera hii. Ili kuhakikisha akina mama wajawazito wanapata huduma wanazozihitaji Wizara inahakikisha wanakuwa na vifaa muhimu vya kujifungulia, ambapo vifuko maalum vyenye vifaa vya kujifungulia (delivery packs) vitasambazwa kwa wanawake 500,000 nchi nzima kulingana na uhitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu (b); siku zote Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele kwa sekta ya afya katika nyanja zote na ndiyo maana Serikali inatoa huduma ya afya bure kwa watu wasiojiweza na kwa usawa kwa wote. Sekta ya afya imeendelea kuwa ya kipaumbele kwa Serikali kwani katika mgao wa bajeti ya mwaka 2016/2017 imekuwa ya tatu kwa kutengewa asilimia 9.2 ya bajeti yote.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali ya Watu wa Jamhuri ya China wasichangie huduma za afya kwa wananchi wanaopata ajali zinazotokana na waendesha bodaboda?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO ajilibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Kikwembe, Mbunge wa Jimbo la Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa sasa kumekuwepo na ongezeko la ajali nyingi za bodoboda ambazo zinaongeza gharama za matibabu. Ongezeko la ajali hizi limekuwa likichangiwa na sababu mbali mbali ikiwemo vifaa hivi kutofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara, madereva kukosa umakini, ulevi, uzoefu na miundombinu chakavu.
Mheshimiwa Spika, vyombo hivi vinapoingia nchini kuna mamlaka mbalimbali ambazo zinasimamia uingiaji wake. Mamlaka hizi ni pamoja na ile ya udhibiti wa ubora yaani TBS na Mamlaka ya Mapato (TRA) ambapo hulipiwa ushuru kabla havijaingia sokoni.
Aidha, kabla mtumiaji hajaanza kutumia kwa biashara inamlazimu kukata leseni ambayo pia hukusanywa na Serikali. Sanjari na hilo ni vyema kufahamu kwamba pikipiki zinazoingizwa nchini zinatoka nchi mbalimbali na si China peke yake.
Mheshimiwa Spika, katika Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo ninatarajia kuiwasilisha hapa Bungeni, nimependekeza kuwa kila mwananchi awe na kadi ya bima ya afya ili e ndapo atapata ajali aweze kupata matibabu bila kiwazo chochote.
Mheshimiwa Spika, hata kama watu wote watakuwa na bima, suala hili la ajali za bodaboda halikubaliki na halivumiliki. Ninaomba wote tukemee vitendo vya uendeshaji mbaya wa bodaboda ili kulinda uhai wa wananchi wetu. Aidha, ninaliomba Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani kuendelea kulisimamia suala hili ili kupunguza ajali za barabarani zinazoweza kuepukika.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Tatizo la ukeketaji katika jamii nyingi nchini bado ni kubwa na sasa ukeketaji huo unafanywa kwa usiri mkubwa hasa baada ya jamii hizo kugundua kuwa ipo sheria dhidi ya ukeketaji.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kufuatilia ukatili huu wanaofanyiwa watoto wachanga na kuhatarisha maisha yao?
(b)Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanusuru watoto wachanga dhidi ya ukatili huu wa ukeketaji unaofanywa na baadhi ya jamii nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, (a) Serikali katika kufuatilia ukatili wa watoto wachanga imekuwa na mikakati mbalimbali ikiwa ni pamona na kuwa na vikundi vya uelimishaji kupitia mangariba, kuanzisha madawati zaidi ya 417 ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi, kuanzisha mtandao wa huduma ya mawasiliano ya kusaidia watoto namba 116 (child helpline) pamoja na uanzishwaji wa timu za ulinzi wa mtoto katika Halmashauri mbalimbali ili kukabili tatizo la ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuongeza msukumo zadi katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuachana na mila zilizopitwa na wakati pamoja na ufuatiliaji kupitia wauguzi toka mtoto alipozaliwa hadi anapotoka hospitalini.
Mheshimiwa Spika, (b), Serikali inaendelea na mkakati wa kutoa elimu ya uzazi salama kwa wakunga wa jadi, akina mama na wauguzi katika zahanati na vituo vya afya kubaini na kutoa taarifa kuhusu mtoto aliyekeketwa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya mzazi huyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, mikataba ya kimataifa na ya kanda kuhusu haki na ustawi wa mtoto na Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009; na pia kutekeleza Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012, kifungu cha 169(1)(a) pamoja na Mpango wa Taifa wa Mwitikio na Kuzuia Ukatili Dhidi ya Watoto wa mwaka 2013 hadi 2016.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeandaa mpango kazi wa Taifa wa kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaoanza mwaka 2017 hadi mwaka 2022 utakaozinduliwa Novemba, 2016, ambapo masuala ya ukatili hasa utokomezaji wa mila na desturi zinazopelekea ukeketaji zitashughulikiwa ipasavyo.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Tanzania ina upungufu mkubwa wa huduma ya tiba shufaa (Palliative Care Services) ukilinganisha na majirani zetu wa Kenya, Uganda na Rwanda. Hali hii inapelekea wagonjwa wengi walio katika hatua za mwisho za maisha yao kuwa na maumivu na mateso makali sana:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha tiba shufaa inaboreshwa hapa nchini?
(b) Kwa kuwa, kuna upungufu mkubwa wa watoa huduma hii, Je, Serikali inatoa tamko gani au ina mkakati gani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi kama Balozi wa wanawake nina masikitiko makubwa sana kwa ndugu Hillary Clinton kupoteza uchaguzi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha huduma za tiba shufaa zinapatikana hapa nchini, Hospitali takriban 35 zikiwemo Hospitali za Rufaa za Kanda za Bugando, KCMC na Mbeya, Hospitali za Mikoa na Wilaya za Mwanza, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro, Kagera, Kigoma, Mtwara, Pwani, Mara na Tanga zinatoa huduma hii. Aidha, Hospitali za dini zilizopo chini ya ELCT kama Hospitali ya Seliani na zingine pia zinatoa huduma hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, huduma za tiba shufaa kwa majumbani zimekuwa zikitolewa sambamba kwenye maeneo yenye hospitali zinazotoa huduma hizo, hii ikimaanisha kwamba, watoa huduma za majumbani husaidia kumfikia mgonjwa nyumbani na kumpatia huduma. Kama tatizo litaonekana ni kubwa, hushauri mgonjwa apelekwe hospitali.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu uhaba wa watumishi katika Sekta ya Afya, hivyo Serikali katika Sera ya Kitaifa ya Tiba Shufaa (National Polliative Care Policy Guideline) iliyotolewa mwezi Juni, 2016, imeagiza mafunzo yafanyike kuwajengea uwezo watumishi waliopo katika vituo vya afya na hospitali ili watoe huduma hii ya tiba shufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Chama cha Tiba Shufaa hapa nchini (The Tanzania Palliative Care Association) na wadau wengine wameanza kusimamia utekelezaji wa sera hii ya tiba shufaa ili kuhakikisha huduma hii inapatikana kwa wagonjwa wanaohitaji na inapatikana kwa wakati wote. Lengo kuu likiwa ni kuwepo na watumishi watano katika kila kituo cha afya wenye uwezo wa kutoa tiba shufaa wakimemo Madaktari, Wauguzi, Wafamasia na Maafisa Ustawi wa Jamii.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA aliuliza:-
Huduma za afya bila malipo kwa wamama wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka mitano ni Sera ya Afya ya Taifa lakini utekelezaji wake umegubikwa na rushwa na urasimu mkubwa.
(a) Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha utekelezaji wa sera hiyo ili kupunguza vifo kwa makundi hayo mijini na vijijini?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za upasuaji wa kupanga na ule wa dharura kwa akina mama wajawazito hasa wa vijijini ili kupunguza vifo vya mama na mtoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutumia Sera ya Afya ya mwaka 2007 iliyoainisha makundi maalum ya watu, (wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee wanaozidi miaka 60, watu wenye ulemavu na wasiojiweza) kwa kuzingatia sheria zilizopo ili kutekeleza mikakati ya kuleta unafuu kwa huduma za afya kwa watu wote wanaotakiwa kupewa huduma za afya bila malipo. Aidha, Wizara inaendelea na maandalizi ya utaratibu ambao utawafanya wananchi wote wawe wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Hatua hii ikifikiwa, changamoto nyingi zinazowapata watu walio katika makundi maalum wanaotakiwa kupewa huduma za afya bila malipo zitakuwa historia. Vilevile Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, inaendelea na kuimarisha uongozi katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuhakikisha kuwa watoaji wa huduma kwa makundi haya wanazingatia sera, sheria, mikakati, miongozo na maelekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi kwa ujumla wake.
(b) Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa wananchi, hasa wanaoishi vijijini, wanapata huduma za upasuaji za kupanga na zile za dharura, Wizara inaendelea kutekeleza mkakati wa kuvijengea uwezo vituo vya afya, hasa vilivyopo vijijini ili viweze kutoa huduma za upasuaji hasa wa dharura. Vituo hivyo vimeonesha kuwa na uwezo huo na vinaokoa maisha ya wananchi, hasa wanawake wanaohitaji upasuaji wa dharura. Katika kuvijengea uwezo vituo hivyo, Wizara ikishirikiana na wadau mbalimbali inaboresha miundombinu, watumishi, upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA aliuliza:-
Ugonjwa wa sickle cell umejitokeza kwa wingi hapa nchini na watu wengi hawajui sababu zinazosababisha ugonjwa huo, huku wengine wakiamini kuwa unasababishwa na kurogwa au imani za kishirikina.
(a) Je, ugonjwa huo unasababishwa na nini?
(b) Je, dalili zake ni zipi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsantem kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanne Ismail Mchemba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, naomba kuuhakikishia umma kwamba ugonjwa huu ni wa kibaiolojia na hauna mahusiano yoyote na imani za kishirikina. Ugonjwa wa sickle cell ambao kwa lugha ya kiswahili huitwa ugonjwa wa selimundu ni ugonjwa wa kurithi wa kupungukiwa na damu, ambapo mgonjwa huwa hana damu ya kutosha kwa sababu ya seli zake za mwili sio imara kiasi cha kubeba hewa ya oxygen kwenda sehemu mbalimbali za mwili wa binadamu.
Mheshimiwa Spika, ili mtoto aweze kupata ugonjwa huu ni lazima wazazi wawe na vimelea vya ugonjwa huo. Chanzo halisi cha ugonjwa huu ni kubadilika kwa mfumo wa mwili wa kutengeneza vimelea vya kutengenezea damu yaani haemoglobin. Hii husababisha seli zinazotengenezwa kuwa na shape ya seli kujikunja mithili ya mundu ambayo siyo ya kawaida. Mgonjwa hupata vimelea vya ugonjwa huu kutoka kwa wazazi wote yaani baba na mama kitaalamu tunaita carriers. Mama na baba wanaweza kuwa hawana dalili yoyote lakini wamebeba vimelea vya ugonjwa huo kwenye damu zao na kumzaa mtoto ambaye ana ugonjwa huu.
(b) Mheshimiwa Spika, mgonjwa wa selimundu yaani sickle cell haonyeshi dalili yoyote mpaka afikishe miezi minne ya umri tangu kuzaliwa na huanza na dalili zifuatazo; Kuishiwa damu, kuvimba vidole, kuchelewa kukua kwa watoto, kutoona vizuri na kusumbuliwa na mashambulio ya maumivu mara kwa mara sababu ya kukwama kwa seli hizo na kuzuia oxygen kwenda sehemu ya viungo vya mwili.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru kulikuwa na Chuo cha MCH kilichokuwa kikitoa mafunzo ya taaluma mbalimbali za afya kwa vijana wengi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru lakini mwaka 1980 chuo hicho kiliungua moto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukikarabati chuo hicho ili kiweze kuendelea kutoa wataalam wa afya kama hapo awali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Tunduru ni mojawapo wa vyuo vilivyokuwa vimefungwa baada ya kusitisha mafunzo ya Martenal and Child Health Aider mwaka 1998. Chuo hiki ambacho kipo katika eneo la Hospitali ya Tunduru kiliungua moto sehemu ya bweni na bwalo la chakula. Katika utekelezaji wa mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) vyuo vinne vya aina hii ambavyo vilikuwa vimefungwa vilifanyiwa tathmini mwezi Agosti 2008 kwa nia ya kuvifufua kuanza kutoa mafunzo kwa wauguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika tathmini hiyo ilipendekezwa Vyuo vya Nzega, Nachingwea na Kibondo vifufuliwe na kuanza kutoa mafunzo ili kuchangia kuongeza idadi ya wataalam kutokana na mahitaji ya Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya Chuo cha Tunduru hakikukidhi vigezo vya kufufuliwa kutokana na gharama kubwa iliyohitajika kufanya ukarabati. Aidha, nafasi ya upanuzi wa chuo ilikuwa ndogo hivyo kupendekeza sehemu hiyo ya chuo kujumuishwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Tunduru.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Mgonjwa anapotoka Zanzibar na kupelekwa kwa matibabu nje ya nchi analazimika kupata rufaa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili licha ya kuwepo kwa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Zanzibar ambayo ina madaktari wenye uwezo kama wale wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
(a) Je, kwa nini Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja haijapewa uwezo wa kutoa rufaa ya matibabu nje ya nchi?
(b) Je, kuinyima uwezo huo Hospitali ya Mnazi Mmoja ni kutoiamini hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, sio kweli kwamba Hospitali ya Mnazi Mmoja haina uwezo wa kutoa rufaa kwa wagonjwa wanaohitaji kupelekewa nje ya nchi kwa huduma za afya ambazo hazipatikani katika hospitali hiyo. Hospitali ya Mnazi Mmoja ina uwezo na ina utaratibu wake wa kutoa rufaa kwa wagonjwa wanaolazimika kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Hospitali ya Mnazi Mmoja inaweza kutoa rufaa kwa wagonjwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili au hospitali nyingine yoyote watakayoona inafaa. Aidha, wagonjwa wengine kutoka Zanzibar huwa wanakuja Tanzania Bara kupata huduma za hospitali zilizopo bara bila kupata rufaa ya Hospitali ya Mnazi Mmoja. Wagonjwa hawa wanapohitaji kupelekwa nje ya nchi watapewa rufaa na hospitali ya mwisho inayowapa huduma kwa wakati huo. Hospitali hiyo inaweza kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili au nyingine yoyote ile ya ngazi ya Kitaifa. Wagonjwa hawa hawawezi kurudishwa Zanzibar kwenda kupewa rufaa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kuwa hospitali ya Mnazi Mmoja imenyimwa uwezo wa kutoa rufaa kwa wagonjwa wanaotakiwa kupelekwa nje ya nchi kwa uchunguzi na matibabu. Hospitali ya Mnazi Mmoja ina uwezo kamili wa kutoa rufaa kwa wagonjwa wanaotakiwa kupelekwa nje ya nchi na imejiwekea utaratibu wake wa kufanya hivyo.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Ni azma ya Serikali ya CCM kumuinua mwanamke kiuchumi na azma hiyo ilipelekea Serikali kuanzisha Benki ya Wanawake.
Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka kufungua madirisha ya benki hiyo mikoani hasa Mkoa wa Iringa ambapo kuna Community Bank (MUCOB) iliyopo Wilayani Mufindi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Desemba, 2016 Benki ya Wanawake imefanya kazi katika mikoa saba ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma. Mwaka 2014 madirisha mawili yalifunguliwa Iringa Mjini na Makambako na hadi kufikia Desemba, 2016 jumla ya wajasiriamali 6,850; wanawake wakiwa 5,350 na wanaume wakiwa ni 1,500 walipata mikopo kupitia madirisha hayo ambayo wajasiriamali wa Mufindi nao wamefaidika. Aidha, benki imefungua vituo vya kutolea mikopo 252 kufikia Desemba, 2016 na Mufindi kuna kituo kimoja kilichopo Mafinga ambacho kimetoa mikopo ya jumla ya shilingi milioni 120 kwa wateja 146, wanawake wakiwa 117 na wanaume wakiwa 32.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake Tanzania imeingiza suala la kufungua dirisha katika Benki ya Wananchi ya Mufindi (MUCOB) kwenye mpango mkakati wa mwaka 2012 mpaka 2017. Tunatarajia dirisha hili litafunguliwa mara tu tutakapopata fedha za kutekeleza mpango huu. Benki ya Wanawake ina mkakati wa kuenea nchi nzima, lakini kikwazo kikubwa ni ukosefu wa mtaji. Endapo benki itafanikiwa kupata mtaji wa kutosheleza itaweza kufungua ofisi zaidi mikoani ili kuwahudumia wananchi wengi zaidi na kwa ukaribu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Jukumu la MSD ni kununua na kusambaza dawa na vifaa tiba; na MSD
inakabiliwa na tatizo kubwa la fedha za kununua dawa na vifaa tiba:-
Je, Serikali itakubaliana nami kwamba ipo haja kubwa ya MSD
kuwezeshwa kuwa na Fungu (Vote) maalum kutoka Hazina?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George
Malima Lubeleje, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la MSD kuwa na Fungu (Vote) lilishaanza
kushughulikiwa tangu mwezi Desemba, 2015. Hatua hii ilichukuliwa kufuatia
ushauri uliotolewa na iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za
Jamii. Wizara iliwasilisha ombi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora ambayo ndio yenye mamlaka na majukumu ya utoaji wa mafungu
(Votes).
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupitia maombi hayo walishauri
kwamba, MSD ipewe line item ndani ya kifungu (sub vote) chini ya Fungu la
Wizara yaani Fungu Na. 52. Ushauri huu ulitolewa kwa kuzingatia utaratibu uliopo
Serikalini kwamba, Fungu hutolewa kwa taasisi za Serikali Kuu peke yake ikiwa ni
maana ya Wizara na Ofisi za Wakuu wa Mikoa. Baada ya kupokea ushauri huu,
Wizara iliwasilisha ombi kwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya MSD
kupatiwa line item.
Mheshimiwa Naibu Spika, MSD wameshapatiwa line item ndani ya
Kifungu 2005 chini ya kitengo cha Huduma za Dawa (Pharmaceutical Services
Unit) pale Wizara ya Afya. Baada ya kupatiwa line item ndani ya kifungu hicho
yaani kifungu 2005 itahitajika kutenga bajeti, mwaka ujao wa fedha 2017/2018
inayokidhi mahitaji ya msingi kwa ajili ya MSD kutekeleza majukumu yake.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha SUZA wa Sayansi ya Afya na Mazingira (Bachelor of Science in Environmental Health) ambao wanafanya internship ya mwaka mmoja Tanzania Bara sambamba na wale wanaomaliza Vyuo vya Tanzania Bara, hawalipwi posho yoyote ya internship wakati wenzao wanaomaliza Tanzania Bara wanalipwa posho hizo:-
Je, ni kwa nini wanafunzi hao hawalipwi posho hizo kama ambavyo wenzao wa Tanzania Bara wanalipwa ili kuwaondolea maisha magumu waliyonayo wakati wa internship ambayo yanaweza kusababisha kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Baraza la Kusajili Wataalam wa Afya ya Mazingira, huratibu zoezi la internship na hutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Sheria ya Kusajili Wataalam wa Afya ya Mazingira ya mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, Sheria hii, inawataka wataalam wa Afya ya Mazingira wote wanaomaliza Shahada ya Afya ya Mazingira Tanzania Bara, washiriki mafunzo ya kazi kwa vitendo (internship) kwa kipindi cha miezi 12 kabla ya kuajiriwa. Hivyo basi, Serikali hulazimika kuwalipa posho ya kujikimu wakati wa mafunzo kwa vitendo ili kukidhi matakwa ya sheria hii.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itashauriana na Wizara ya Afya Zanzibar ili nao waangalie uwezekano wa kuwalipa wahitimu kutoka Chuo Cha SUZA, waweze kutekeleza vyema mafunzo ya kazi kwa vitendo (internship) kwa kipindi cha miezi 12 kabla hawajasajiliwa ili kuwaondolea maisha magumu waliyonayo wakati wa mafunzo haya, ambayo yanaweza kusababisha kushindwa kutekeleza wajibu yao kwa ufanisi.
MHE. LEONIDAS T. GAMA aliuliza:-
Zahanati zetu zilizopo vijijini ambako ndiko walipo wazee walio wengi wakiwemo wastaafu ambao mara kwa mara hukabiliwa na magonjwa yanayotokana na utu uzima ikiwemo shinikizo la damu zinazokabiliwa na ukosefu wa dawa za magonjwa hayo na inasemekana pia zahanati hazitakiwi kuwa na dawa za shinikizo la damu hivyo wazee kutakiwa kwenda ngazi za vituo vya afya na au hospitali hali inayopelekea wazee hao kupewa dawa za kukojoa tu (Lasix) badala ya dawa za shinikizo la damu kwa ajili ya matibabu. (a) Je, Serikali haijui kuwa wazee wengi wanaosumbuliwa na magonjwa hayo wanaishi vijijini ambako kuna zahanati pekee na siyo hospitali? (b) Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha dawa za aina mbalimbali za shinikizo la damu zinazowekwa katika zahanati zetu zilizoko vijijini ambako ndiko wazee wengi walipo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa wazee wengi sehemu za vijijini ambao wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya utu uzima ikiwemo shinikizo la damu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imeboresha mgao wa fedha utakaowezesha upatikanaji wa dawa zikiwemo za shinikizo la damu katika ngazi zote za kutolea huduma za afya kuanzia hospitali hadi vituo vya afya na zahanati kulingana na miongozo iliyopo ya utoaji huduma za afya nchini. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inao mwongozo wa utoaji tiba za dawa unaojulikana kama Standard Treatment Guideline ya mwaka 2014 ambao umeambatanishwa na orodha ya taifa ya dawa muhimu (National EssentialMedicines List of Tanzania). Orodha hiyo imebainisha dawa mbalimbali ambazo zinatumika katika ngazi mbalimbali za vituo vya kutolea huduma za afya, ikiwemo vituo vya afya na zahanati. Dawa za shinikizo la damu zilizopo kwenye orodha hiyo ni kama Propranolol,Methyledopa, Frusemide, Hydrochlorthiazide na Bendrofuazide. Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vituo vya kutolea huduma za afya vinayo mamlaka ya kuagiza dawa nyingine za kutibu shinikizo la damu nje ya hizi tulizozitaja hapo juu kulingana na uwezo na kiwango cha elimu cha wataalam waliopo kwenye kituo husika. Hii ina maana kuwa Wizara hauizuii kituo chochote kuagiza dawa mahali popote za kutibu shinikizo la damu ikiwa kituo husika kitaona kina uwezo wa kufanya hivyo kwa kutoa huduma kwa viwango vinavyostahili. Sanjari na hilo, kulingana na mfumo uliopo wa ugavi na usambazaji wa dawa za Serikali, ni jukumu la watendaji wa vituo husika kuainisha mahitaji ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi na kuagiza mahitaji yao kutoka Bohari ya Dawa (MSD) kwa kutumia fomu maalum ya taarifa na maombi (Report and Request – R&R).
MHE. COSATO D. CHUMI Aliuliza:-
Serikali katika mwaka huu 2016 imeelekeza wazi kuwa haina mpango wa kununua magari ya wagonjwa na kwamba jukumu la kununua magari hayo limeachiwa Halmashauri za Wilaya ambazo hazimudu kununua magari hayo hali inayowafanya baadhi ya wahisani kujitolea kununua magari hayo.
Je, ni lini Serikali italeta mapendekezo ya kubadilisha sheria hiyo ili magari hayo yaingie kwenye Jedwali la Saba na hivyo kupata msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa haina mpango wa kuleta mapendekezo ya kubadilisha Sheria ya Ununuzi wa Magari ya Kubebea Wagonjwa. Jukumu la kununua magari hayo ni la Halmashauri husika ambao wanatakiwa kutenga fedha na kuhakikisha kuwa wananunua magari hayo kulingana na mahitaji. Wizara pindi inapopata misaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo imekuwa ikigawa magari hayo katika Halmashauri mbalimbali nchini kwa kuzingatia mahitaji.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Kodi ya mwaka 2014, Jedwali la Saba imeeleza kuwa ununuzi wa vifaa tiba utapatiwa msamaha baada ya kuridhiwa na Waziri mwenye dhamana ya afya. Magari ya kubebea wagonjwa ambayo yana vigezo ambavyo vimewekwa, huombewa msamaha wa kodi na Waziri wa Afya ambapo hupatiwa exemption certificate yaani hati ya msamaha na Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kujiridhisha kuwa yana vigezo stahiki. Niwasihi Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote wenye nia ya kusaidia kukabiliana na changamoto hii kwa kununua magari, kuwasiliana na Wizara ya Afya kuhusu vigezo
vinavyotakiwa kabla ya kuagiza magari hayo ili yaweze kustahili kupatiwa msamaha wa kodi.
Mheshimiwa Spika, sanjari na hilo, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuzihimiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga fedha za ununuzi wa magari haya kulingana na uhitaji halisi katika Halmashauri husika.
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA aliuliza:-
Inapotokea wazazi wametengana na mama akaondoka na mtoto na kwenda kuishi naye, lakini tangu wazazi hao watengane mama hatoi nafasi kwa baba kwenda kumtembelea mtoto:-
Je, baba ataipata wapi haki hiyo ya kumwona mtoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bhagwanji Maganlal Meisuria, Mbunge wa Jimbo la Chwaka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 imezingatia suala zima la utoaji wa malezi, matunzo na ulinzi wa mtoto kwa kutoa majukumu kwa wazazi, walezi pamoja na Serikali. Kifungu cha 7(1) cha sheria hii kimempa mtoto haki ya kuishi na wazazi wake au kuishi na mlezi. Aidha, kifungu cha 26(1) kimeeleza haki za mtoto endapo wazazi watakuwa wametengana. Haki hizo ni pamoja na kuendelea kupewa matunzo pamoja na elimu kama ilivyokuwa kabla ya wazazi kutengana, kuishi na mzazi mmojawapo baada ya mahakama kujiridhisha kuwa mzazi huyo anao uwezo wa kumlea mtoto. Pia mtoto kuwa na haki ya kumtembelea na kukaa na mzazi wake mwingine pale atakapotaka kufanya hivyo isipokuwa kama itabainika kuwa kumtembelea mzazi mwingine kutaathiri masomo na ustawi wa mtoto.
Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa zipo taratibu za kufuata endapo mzazi mmoja (baba au mama) atakosa haki ya kumwona mtoto wake ambaye anaishi na mzazi mwingine. Kwa mujibu wa taratibu, mlalamikaji atatakiwa kuripoti ofisi za Ustawi wa
Jamii za Halmashauri pale ambapo mzazi mwenza anaishi na mtoto ili waweze kukutanishwa na kufanyiwa unasihi ili hatimaye waweze kufikia makubaliano ya pamoja ya kumlea mtoto.
Mheshimiwa Spika, aidha, pale inaposhindikana, mashauri haya huelekezwa kwenye Baraza la Usuluhishi lililoko chini ya Kamishna wa Ustawi wa Jamii na pindi wasipofikia makubaliano kwenye Baraza la Usuluhishi, shauri hupelekwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:-
Ndoa za utotoni kwa sasa zimekithiri sana na ndoa hizi zina athari kubwa ndani ya jamii:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutokomeza ndoa hizi za utotoni?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua athari kubwa zanazosababishwa na ndoa za utotoni katika jamii yetu ya Tanzania. Ndoa za utotoni zinawanyima watoto wa kike fursa ya kupata elimu na hivyo kusababisha umaskini miongoni mwao punde wanapokuwa watu wazima kwa kuwa wanakosa mbinu mbadala za kujikwamua kiuchumi kutokana na kukosa elimu. Aidha, mimba za utotoni ni hatari kwa afya ya mama na mtoto kwa kuwa maumbile ya kibaiolojia ya mtoto hayawezi kuhimili mchakato wa uzazi na mara nyingi mimba hizi zimesababisha vifo.
Mheshimiwa Spika, kulingana na takwimu za afya na idadi ya watu nchini za mwaka 2016, ndoa za utotoni zimeshamiri katika Mikoa ya Shinyanga kwa kiwango cha asilimia 59, Tabora kwa kiwango cha asilimia 58, Mara asilimia 55 na Dodoma asilimia 51.
Mheshimiwa Spika, kwa kukabiliana na changamoto hii, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya malezi chanya kwa wazazi na walezi ili waweze kutambua umuhimu wa kumwendeleza mtoto wa kike. Elimu hii imetolewa katika Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Miji 72 nchini. Msukumo umeongezwa zaidi katika kuelimisha familia, wazee wa mila na jamii kuachana na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati za kuoza watoto wa kike. Mwaka 2015, Serikali ilizindua rasmi kampeni ya Kitaifa ya kutokomeza ndoa za utotoni ambayo iliwataka wadau wote zikiwemo familia kushirikiana kutokomeza kabisa ndoa za utotoni hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa muundo wa kisera na kisheria, Serikali imezifanyia maboresho sera na sheria ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa na mimba za utotoni mfano Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inaelekeza kutolewa kwa elimu bure na ya msingi kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha nne pamoja na marekebisho ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353 yaliyopitishwa na Bunge la 11 ambayo inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa mtu yeyote atakayempa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari.
Mheshimiwa Spika, tarehe 13 Desemba, 2016, Serikali ilizindua mpangokazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto uliojumuisha sekta zote zinazohusu wanawake na watoto kwa lengo la kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Mpangokazi huu ambao utaanza kutekelezwa mwezi Julai, 2017, umelenga zaidi kuzuia na kupunguza vitendo vyote vya ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia 50 na umeweka lengo la kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 47 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2022.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-
Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa ulianzishwa kwa ajili ya kuratibu na kusimamia matibabu kwa watumishi wa Serikali, taasisi na mashirika ya umma nchini:-
(a) Je, hadi sasa ni Taasisi na Mashirika ya umma mangapi yamejiunga na mfuko huo?
(b) Je, ni Taasisi na mashirika ya umma mangapi hayajajiunga na mfuko huo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Asaph Mlinga, Mbunge wa Ulanga lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulianzishwa kwa ajili ya kuratibu na kusimamia matibabu kwa watumishi wa Serikali, taasisi na mashirika ya umma nchini. Hadi kufikia mwezi Machi, 2017 idadi ya wanachama katika mfuko ni 792,987 kutoka
wanachama 474,760 mwaka 2012. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, mfuko umefanya maboresho mbalimbali ya vitita vya mafao na namna ya kuchangia kwa makundi mbalimbali ya jamii. Maboresho haya yamewezesha kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wanachama walio katika mfumo huu wa bima ya afya nchini na kufanya wanufaika kufikia asilimia nane. Aidha, hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2016
idara za Serikali, taasisi na mashirika ya umma zilizotumia huduma za bima ya afya za NHIF zimefika 307. Idadi hii imetokana na jitihada za makusudi za kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na Bima kwa watumishi wa umma.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mashirika, taasisi na idara za Serikali ambayo hayajajiunga na mfuko yapo 23 yakiwemo TRA, BOT, TANESCO, NHC, TPA, PSPF, LAPF, PPF, EWURA, NCA na GEPF. Mfuko unaendelea na jitihada za kukutana na uongozi wa mashirika haya ya umma kwa lengo la kutoa elimu na kuwahimiza juu ya umuhimu wa kujiunga kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Mfuko.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Katika Mkutano wa SADC uliofanyika Nchini Swaziland pamoja na mambo mengine suala zima la kupambana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu na Silicosis lilijadiliwa. Ugonjwa huo unaathiri sana watu wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini na wale wanaoishi kandokando na maeneo ya uchimbaji:-
(a) Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi wanachama wa SADC; je, inalifahamu tatizo hilo?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kupambana na Ugonjwa huo wa Kifua Kikuu na Silicosis, hasa katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Jimbo la Busanda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania inafahamu changamoto ya uwepo wa Magonjwa ya Kifua Kikuu na Silicosis katika maeneo ya wachimbaji. Kwa upande wa Kifua Kikuu inakadiriwa kuwa ukubwa wa tatizo hili ni kubwa zaidi ikilinganishwa na hali halisi katika maeneo mengine na kwa upande wa Silicosis kumekuwepo na ripoti za wagonjwa wachache katika hospitali za Serikali ikiwemo Kibong’oto
kuhusu wachimbaji wadogowadogo kutoka maeneo ya migodi. Kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund to Fight AIDS, Tuberculosis and Malaria), nchi kumi wanachama wa Jumuiya ya SADC ikiwemo Tanzania zipo katika utekelezaji wa mpango wa kudhibiti kifua kikuu na magonjwa ya mfumo wa hewa yatokanayo na uchimbaji madini ikiwemo Silicosis.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia halmashauri zilizo katika maeneo ya migodi imeanza kuweka mikakati ya kudhibiti magonjwa haya kama vile kutoa elimu kwa wachimbaji ya namna ya kujikinga na vumbi na kutumia njia sahihi za uchimbaji. Vilevile, katika mpango huu wa
Global Fund to Fight HIV AIDS, Malaria and Tuberculosis kuna afua (intervention) itakayoshughulika na Sera za Udhibiti wa Vumbi katika Maeneo ya Wachimbaji (The Dust Control Policy) ambayo itawabana wachimbaji kudhibiti vumbi wakati wa shughuli za uchimbaji. Aidha, Serikali itaongeza wigo wa huduma katika vituo vya afya kwenye maeneo yaliyoathirika ikiwemo Mkoa wa Geita ili vituo viwe na uwezo wa
kuchunguza na kutibu magonjwa hayo na kuwajengea uwezo wataalam wa afya katika kuhudumia wagonjwa katika maeneo ya migodi.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE (K.n.y. MHE. HAWA
M. CHAKOMA) Aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali haitumii mfumo wa Ubia na Sekta Binafsi (PPP) kwenye mipango yake ya ununuzi wa vifaa tiba vya bei kubwa kama MRI, CT-Scan na X-Ray?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kukua kwa kasi ya sayansi na teknolojia ya uchunguzi wa magonjwa, Wizara inakubaliana kabisa na wazo la Mheshimiwa Mbunge juu ya kuangalia namna nzuri ya kushirikiana na Sekta Binafsi (PPP) katika utoaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara imeanza hatua za awali za uainishaji wa gharama, uandaaji wa mfumo mbadala (Option Development) na upembuzi wa kina wa aina ya ubia ambapo Wizara kwa kuanzia inafikiria ushirikiano kwa kupitia ukodishaji wa vifaa (lease agreement) ambapo Serikali itakodisha mashine hizo ambazo zitakuwa za mbia na Serikali haitahusika na ununuzi, ufungaji na matengenezo kinga ya mashine hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mfumo huu, Wizara itakuwa na jukumu la kusimamia utoaji wa huduma na itapata gawio lake kutokana na makusanyo yatokanayo na uchangiaji wa huduma kulingana na mkataba. Ni imani ya Wizara kuwa kutumia mfumo wa Ubia na Sekta Binafsi (PPP) huduma za uchunguzi wa
magonjwa zitaimarika na kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama.
MHE. MARTHA J. UMBULLA Aliuliza:-
Kulingana na takwimu za mwaka 2010 Mkoa wa Manyara unaongoza kwa mila potofu ya ukeketaji wa wanawake kwa asilimia 71 hapa nchini hali inayotisha na kuhatarisha maisha ya wanawake.
(a) Je, Serikali katika kufanya utafiti imebaini ni Wilaya zipi na vijiji vipi vinaongoza?
(b) Je, hali hii na mila hii potofu imesababisha athari na vifo kiasi gani mkoani Manyara?
(c) Je, Serikali ina mikakati gani ya dharura ya kukabiliana na mila hii potofu ili kuondoa kabisa athari za ukeketaji?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII JINSIA NA WAZEE NA WATOTO Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, lenye vipengele (a),(b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utafiti uliofanya na Serikali katika Mkoa wa Manyara, imebainika kuwa ukeketaji upo vijijini kwa asilimia 100. Wilaya karibu zote zinajihusisha na vitendo hivi hasa Wilaya ya Hanang. Makabila yanayofanya ukeketaji katika wilaya hiyo ni Wairak, Wabarbaig na Wanyaturu hasa katika maeneo ya Kata za Balanglalu na Basutu.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, athari zinazotokana mila hizi potovu ni kubwa sana kwa wanawake hususan wakatiwa kujifungua. Kwani huweza kusababisha ulemavu wa kudumu; vifo kutokana na kutokwana damu nyingi; maumivu makali kupatwa na ugonjwa wa fistula na wakati mwingine kupata madhara ya kisaikolojia. Ni vigumu kutambua vifo vinavyotokana na ukeketaji kwani hufanyika kwa siri katika jamii hiyo.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetunga sheria mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hili. Hata hivyo, tunaamini kuwa sheria peke yake bila elimu kwa Umma haziwezi kumaliza tatizo hili. Ndiyo maana tunawawatumia Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii ili kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuondokana na mila za tamaduni hizi.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:-
Asilimia kubwa ya watu wenye ulemavu wana vipato duni sana kiasi cha kushindwa kumudu ghamara za matibabu.
Je, Serikali haioni kuwa ni muda muafaka sasa wa kuwajumuisha Watanzania hawa wenye kipato duni na wenye ulemavu kwenye sera ya msamaha wa uchangiaji huduma za afya kama ilivyo kwa wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimwia Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Sera ya Afya ya mwaka 2007 imeainisha makundi yanayostahili kupata msamaha wa kulipia huduma za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma.
Kulingana na Sera hiyo, Serikali inatambua kuwepo kwa wananchi wasio na uwezo wa kuchangia gharama za huduma za afya, ikiwa ni pamoja na wale walio katika makundi maalum ya kijamii, mathalan Wazee walio na umri zaidi ya miaka 60 ambao hawana uwezo wa kipato, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, watoto walio katika mazingira hatarishi, wanawake wajawazito na watu wasiojiweza kiuchumi. Pia watu wenye magonjwa sugu kama saratani, UKIMWI, kisukari, magonjwa ya moyo, pumu, sickle cell, kifua kikuu, ukoma na magonjwa ya akili. Madhumuni ya sera hii ni kuwezesha makundi maalum kupata huduma bora za afya sawa na wananchi wengine.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kuwa watu wenye ulemavu wamezingatiwa katika makundi ya watu wanaostahili msamaha.
Mheshimiwa Spika, aidha, msamaha kwa kundi hili utatolewa kwa kuzingatia kama mlemavu huyo atabainika kuwa hana uwezo wa kulipia huduma au kuwa katika moja ya makundi yanayostahili msamaha niliyoyataja.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-
Upungufu wa dawa katika Hospitali mbalimbali za Serikali nchini umeleta athari kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera na Wilaya zake zote:-
Je, Serikali inakiri uwepo wa upungufu wa dawa nchini? Kama inakiri hivyo, inawaambia nini wananchi kuhusu tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulitaarifu Bunge
lako Tukufu kuwa mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kuboresha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa umma hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azma hii, Serikali ya Awamu ya Tano ilichukua juhudi za makusudi kwa kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 251.5 katika mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa hadi kufikia mwezi Aprili, 2017 jumla ya sh. 112,198,920,456/= zilishatolewa na kupelekwa Bohari ya Dawa ili kuviwezesha vituo vya kutolea huduma za afya vya umma kupata mahitaji yake ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia ongezeko hilo la fedha, hali ya upatikanaji wa dawa nchini imeimarika na kumbukumbu zilizopo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinaonesha kuwa hali ya upatikanaji wa dawa nchini imeimarika kwa kufikia asilimia 83. Kadhalika, hadi kufikia tarehe 15 mwezi Januari, 2017 Mkoa wa Kagera pekee umepokea kiasi cha sh. 4,150,767,216/= kupitia Fungu Namba 52, yaani Wizara ya Afya, kwa ajili ya kununulia dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-
Moja kati ya maeneo yaliyomo kwenye mkataba wa ushirikiano baina ya Tanzania na Cuba (1986) ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya.
Je, ni kwa kiasi gani Tanzania imefaidika na utekelezaji wa mkataba huo katika sekta ya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Jimbo la Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Cuba katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya afya tangu 1986, ambapo mkataba ulisainiwa kati ya Serikali hizi mbili. Kupitia mkataba huo, Serikali ya Tanzania imekuwa ikipokea Madaktari Bingwa kutoka Cuba ambao wamekuwa wakifanyakazi katika hospitali za Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Hospitali ya Tumbi na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Madaktari hawa wamekuwa wakitoa huduma mbalimbali za Kibingwa kwa wananchi na kuwajengea uwezo madaktari wanaofanya nao kazi katika hospitali hizo. Aidha, kwa kushirikiana na kampuni ya Labiofarm ya Cuba, Serikali imeweza kujenga kiwanda cha kutengeneza viuadudu vya kibaiolojia yaani biolarvicides kwa ajili ya kuua viluilui vya mbu waenezao malaria. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iligharamia ujenzi wa kiwanda hicho na Serikali ya Cuba ilitoa msaada wa wataalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, matarajio yetu ni kuwa, wataalamu hao watawajengea uwezo Watanzania ili waweze kutengeneza bidhaa hizo bila kutegemea wataalam kutoka nje ya nchi kwa siku zijazo. Viuadudu hivyo vimeanza kutengenezwa kuanzia mwezi Disemba 2016, na kwa sasa uhamasishaji wa Halmashauri mbalimbali nchini kununua bidhaa hizo umeanza. Endapo viuadudu hivyo vitatumiwa vizuri vitasaidia kupunguza mbu waenezao malaria na hivyo kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria nchini.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufuta tozo na gharama za vifaa vya kujifungulia na upasuaji kama ilivyofuta za matibabu ya wazee na wagonjwa wa kisukari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatibu, Mbunge wa Viti Malaam kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Afya ya mwaka 2007 inaeleza kuwa huduma za kina mama wajawazito katika vituo vya ngazi zote zinapaswa kutolewa bila malipo. Serikali haijawahi kuweka tozo na gharama za vifaa vya kujifungulia na wala vya upasuaji. Huduma hizo zinatolewa katika ngazi zote katika vituo vya umma vya kutolea huduma kwa gharama za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha sera hii inatekelezwa kwa vitendo, Wizara inahakikisha akina mama wanakuwa na vifaa muhimu vya kujifungulia, ambapo vifuko maalum vyenye vifaa vya kujifungulia (delivery packs) kwa wanawake 500,000 vitasambazwa nchi nzima kulingana na uhitaji. Kwa wastani nchini Tanzania jumla ya akina mama 1,900,000 wanajifungua kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwa tusaidiane kusimamia utekelezaji wa sera tulizokubaliana katika maeneo yetu kwa kuhakikisha huduma hizi za akina mama zinapatikana kwa gharama za Serikali ili azma ya Serikali ya kuhakikisha akina mama wajawazito wanapata huduma nzuri na lengo la kupunguza vifo vya Mama na watoto hapa nchini lifikiwe. (Makofi)
MHE. WILFRED M. LWAKATARE (K.n.y. MHE. LUCY F. OWENYA) aliuliza:-
Je, Moshi wa bangi una madhara gani kwa binadamu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya Mbunge wa Viti Maalum, kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali hili naomba niungane na wewe kumpa pole Mheshimiwa Lucy Owenya na watu wote walioguswa na msiba huu wa baba yake mzazi.
Mheshimiwa Spika, bangi ni mmea ambao huota sehemu nyingi duniani. Mara nyingi watu huvuta bangi kama sigara. Kemikali inayoleta ulevi na madhara mwilini kwa mtumiaji wa bangi inaitwa tetrahydrocannabinol (THC) ambayo hutoka kwenye moshi wa bangi inayochomwa au kuvutwa, hivyo moshi ambao unatokana na kemikali hiyo humletea mtu mwingine madhara sawasawa na ya mvutaji. Madhara hayo ni pamoja na akili kushindwa kuzingatia mambo kwa wepesi wake, huweza pia kuathiri vichocheo vya kike na vya kiume, kufanya mishipa ya kusafirishia damu kutokuwa na mnyumbuko halisi yaani kusababisha hardening of arteries na kuchanganyikiwa.
Mheshimiwa Spika, madhara ya kuvuta bangi hadharani ni makubwa hususani kwa vijana kwani madhara yake kwa mtu asiyevuta ni sawa na kwa ambaye anavuta. Ukweli wa madhara haya hudhihirika pale unapochukua sampuli ya damu na mkojo kwa mtu ambaye havuti bangi kwani utaikuta kemikali hii, hivyo kuonyesha uwezekano wa madhara ya moshi kwa mtu ambaye hatumii (passive cannabis smoker). Serikali inaendelea kutoa ushauri kwa vijana kuacha tabia ya uvutaji bangi na kushauri pia kwa wale ambao hawajaanza kuvuta kutojihusisha kabisa na uvutaji.
Mheshimiwa Spika, tunawashauri wale ambao wanavuta kutembelea vituo vya kutolea huduma kote nchini ili waweze kusaidiwa namna ya kuacha matumizi ya bangi.(Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. RAPHAEL J. MICHAEL) aliuliza:-
Hospitali ya KCMC inamilikiwa na taasisi ya kidini ikishirikiana na Serikali na imekuwa ikitoa huduma bora zinazofanya wagonjwa wengi kutoka ndani na nje ya nchi kukimbilia hospitali hiyo hivyo kuifanya hospitali hiyo izidiwe na uwezo wake wa kuhudumia wagonjwa hususani miundombinu na samani za hospitali.
(a) Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuisaidia hospitali hiyo ili iweze kutoa huduma bora zaidi kulingana na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaokwenda kutibiwa hapo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kiasi cha pesa inachopeleka katika hospitali hiyo na kuhakikisha kuwa kile kiwango kilichotengwa kwa sasa kinapelekwa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaipa uzito mkubwa Hospitali ya KCMC na inaipongeza kwa huduma bora za afya inazozitoa kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini na wengine kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Spika, Wizara inafanya jitihada za makusudi za kuiwezesha Hospitali hii kuendelea kutoa huduma bora, ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara ilitenga kiasi cha shilingi 12,202,942,000 kwa ajili ya hospitali hii. Kati ya fedh hizo, shilingi 11,275,224,000 zilikuwa nikwa ajili ya Mishahara ya watumishi, na shilingi 427,718,000 zilikuwa kwa ajili ya matumizi mengineyo (Other Charges) na kiasi cha shilingi 500,000,000 zilikuwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwenye wodi ya dharura kupitia bajeti ya Miradi ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, ili kuzipunguzia mzigo wa wagonjwa hospitali za rufaa za Kanda ikiwemo KCMC Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaboresha huduma katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, hospitali za Wilaya pamoja na vituo vya afya na zahanati ili kupeleka huduma bora karibu zaidi na wananchi ili wale wachache tu wenye kuhitaji huduma za rufaa basi wafike katika Hospitali za Rufaa za Kanda, hospitali maalum pamoja na hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mheshimiwa Spika, ili kuziwezesha hospitali na taasisi nyingine zote zilizo chini ya Wizara kujiendesha kiuendelevu, Wizara inatekeleza mkakati wa kuhakikisha hospitali na taasisi zote zilizo chini yake zinafunga na kutumia mifumo ya kielektroniki ili hospitali hizo ziweze kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma. Vilevile katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 Wizara imetenga kiasi cha shilingi 11,004,329,000 kwa ajili ya matumizi mengineyo na mishahara, lakini pia shilingi 500,000,000 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
MHE. MAULID S.A. MTULIA aliuliza:-
Sera yetu ya Afya ni kuchangia gharama ili kupata huduma ya afya isipokuwa kwa wazee, mama na mtoto:-
Je, ni fedha kiasi gani zimekusanywa kutokana na tozo za uchangiaji gharama ndani ya miaka mitano na ni nini matumizi ya fedha hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kulingana na Mwongozo, fedha za uchangiaji zinakusanywa katika vituo vya kutolea huduma na zinatumika mahali zilipokusanywa kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma. Katika kipindi cha miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015, jumla ya Sh.62,244,000,000 zimekusanywa kutoka katika vituo vyote vya kutolea huduma nchini.
Mheshimiwa Spika, kulingana na mwongozo huo, fedha hizi zinapaswa kutumika kwa kuweka kipaumbele katika ununuzi wa dawa, vitendanishi, vifaa na vifaa tiba lakini pia ukarabati mdogo, kulipia maji, umeme na matengenezo ya magari ya kubebea wagonjwa.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Vifo vya akinamama na watoto kwa takwimu za hivi karibuni Mkoani Manyara vinatisha:-
Je, Serikali inatoa kauli gani ya mwisho ili kukabiliana na janga hili ikiwepo kuimarisha Vituo vyote vya Huduma ya Mama na Mtoto Vijijini bila kujali uwezo wa wanawake kulipia au kutolipia huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha kwanza cha Wizara ni kuhakikisha afya ya Watanzania wakiwemo akinamama na watoto inaboreshwa. Hivyo basi, ili kukabiliana na janga hili, Serikali imeweka mikakati ifuatayo kama ilivyoanishwa kwenye Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya wa Nne, Mpango Mkakati wa Pili wa Kuongeza Kasi ya Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, kama ifuatavyo:-
(i) Kufuatilia vifo vyote vitokanavyo na uzazi na kuvitolea taarifa kila robo mwaka ili kuongeza uwajibikaji na kugundua ukubwa wa tatizo katika kila Halmashauri nchini;
(ii) Kupandisha hadhi asilimia 50 ya vituo vya afya
na kuviwezesha kufanya upasuaji wa kutoa mtoto tumboni. Hadi sasa vituo 159 vinatoa huduma ya upasuaji wa matatizo yatokanayo na uzazi pingamizi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa damu. Kati ya hivi, vituo 106 ni vya Serikali hii ni sawa na asilimia 21 ya vituo vya afya vya Serikali 484;
(iii) Kuanzisha Benki za Damu katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi yenye idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi. Hadi sasa benki zimeanzishwa katika Mikoa ya Mara, Kigoma, Simiyu na Geita. Hii ni katika kuimarisha upatikanaji wa damu kwenye vituo vya kutolea huduma ya upasuaji;
(iv) Kuanzisha Mpango wa Kifuko chenye Vifaa Maalum kinachohitajika wakati wa kujifungua ambacho mama mjamzito atapewa kuanzia wiki ya 28 ya ujauzito anapohudhuria kliniki;
(v) Kutoa huduma ya Mkoba kwa wajawazito hadi wiki sita baada ya kujifungua na kwa watoto chini ya miaka mitano kwa kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii;
(vi) Kuwajengea uwezo watoa huduma wa afya kwa kuwapatia mafunzo ya huduma muhimu wakati wa ujauzito, stadi za kuokoa maisha kwa matatizo ya dharura yatokanayo na uzazi;
(vii) Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itashirikiana na wadau kuboresha upatikanaji wa vifaa, vifaa tiba na vitendanishi;
(viii) Kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kwa mwaka 2015/2016 watoa huduma 917 walipatiwa mafunzo jumuishi ya afya ya uzazi na mtoto. Hii ni katika kuhakikisha huduma ya afya ya uzazi inakuwa endelevu ili kuifikia jamii; na
(ix) Kuendelea kuelimisha jamii na hasa vijana kuhusu afya ya uzazi na kutilia mkazo juu ya lishe bora kwa kutumia vyombo mbalimbali vikiwemo redio, luninga na simu za kiganjani.
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuomba ufadhili wa wadau mbalimbali ili kusaidia kujaza pengo la uhitaji wa ambulance. Kwa kutekeleza haya, tunaamini kwamba vifo vya wanawake wajawazito, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano vitaendelea kushuka kwa kasi.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete, aliahidi kupandishwa hadhi Kituo cha Afya Kibiti kuwa Hospitali ya Wilaya:-
Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya ni Kituo kinachotoa huduma za afya ndani ya wilaya na ambacho hupokea wagonjwa kutoka zahanati na vituo vya afya ili kuwapatia huduma ambazo hazipatikani kutokana na uwezo mdogo uliopo katika vituo vidogo, yaani zahanati na vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwamba Kituo cha Afya Kibiti kipandishwe hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya, Wizara ilituma wataalam wake kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambao walifanya ukaguzi mnamo tarehe 13 – 16 Novemba, 2015 na kuwasilisha taarifa kwetu iliyotoa ushauri na maelezo pamoja na maelekezo ya kufanyiwa kazi ili kukiwezesha Kituo cha Afya Kibiti kumudu vema majukumu yake ya kutoa huduma katika ngazi ya hospitali ya wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla taarifa ilionesha kuwa, mazingira ya kituo yalihitaji maboresho kadhaa ili kituo hiki kifikie uwezo wa kutoa huduma za hospitali ya wilaya. Wizara inajiandaa kwenda kufanya ufuatiliaji ifikapo Oktoba, 2017 endapo itahakikishiwa kuwa upungufu uliobainishwa na ukaguzi ule utakuwa umefanyiwa kazi ili kituo hicho sasa kiweze kutangazwa rasmi kuwa Hospitali ya Wilaya.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la tatizo la Wanaume kupungukiwa nguvu za kiume, jambo ambalo linaleta tafrani kubwa na kusababisha ndoa nyingi kuvunjika na zilizobakia kuwa katika hali ya mashaka:-
(a) Je, Serikali inalijua tatizo hilo?
(b) Kama inalijua, je, inachukua hatua gani kukabiliana na tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, nijibu swali hili muhimu la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Jimbo la Konde, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa tatizo hili japokuwa hakuna jibu la moja kwa moja la kufahamisha umma ukubwa wa tatizo hili, kwa sababu tendo la ndoa ni tendo ambalo hufanyika katika mazingira ya usiri kati ya wanandoa wenyewe.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuelezea kwa kifupi ni jinsi gani mwanaume hupungukiwa na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili kwa kawaida huwapata kwa kiasi kikubwa watu wenye umri mkubwa, hasa kuanzia umri wa miaka 60 na wagonjwa wenye magonjwa sugu mbalimbali kama vile shinikizo la damu, kisukari, kifua kikuu, kansa, UKIMWI na wale wanaotumia dawa kwa muda mrefu. Hata hivyo, mwenendo wa tatizo hili kwa sasa umekuwa hauzingatii umri kuwa mkubwa, linawapata watu wa rika zote, vijana na hata watu wazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wazee tatizo la nguvu kupungua kwa mara nyingi ni jambo la kawaida na naomba ieleweke kwamba, kwa wanaume kadri umri unavyozidi kuongezeka uwezo wa kufanya tendo la ndoa unapungua taratibu. Pia, huchangiwa na ukosefu wa afya njema.
MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-
Mkoa wa Manyara ni mojawapo ya mikoa inayoongoza kwa ukeketaji wa watoto wa kike; takwimu za mwaka 2017 zinaonesha kuwa Mkoa wa Manyara unaongoza Kitaifa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kukomesha ukatili huo wa kijinsia pamoja na kutoa semina elekezi kuhusu madhara yatokanayo na ukeketaji wa mtoto wa kike hususan Wilaya ya Hanang, Simanjiro, Kiteto na Mbulu?
(b) Kwa kuwa, Ngariba sasa wanatumia mbinu mbadala za kuwakeketa watoto wa kike wa kuanzia miezi sita (6) hadi mwaka mmoja na miezi sita. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwakamata Ngariba wote wanaofanya ukatili huo na kuwachukulia hatua za kinidhamu, hatua za kibinadamu ili wawe sehemu na fundisho la kukomesha ukatili huo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango madhubuti wa miaka mitano wa kutokomeza vitendo vya ukatili ujulikanao kama Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/2018 – 2021/2022) ulioandaliwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na asasi mbalimbali za kiraia. Kupitia mpango kazi huu, Serikali imedhamiria kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji wa watoto wa kike kutoka asilimia 32 ya mwaka 2016 mpaka kufikia asilimia 11 ifikapo 2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mpango kazi huu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, iliwapatia mafunzo Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mikoa yote 26 na baadhi ya asasi za kiraia yaliyolenga kuwajengea uwezo wa namna bora ya kutekeleza mpango kazi huu. Aidha, kuanzishwa kwa madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya Polisi ambapo hadi sasa kuna jumla ya madawati 516 kumeongeza mwamko wa wananchi kujiamini na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ikiwemo ukeketaji wa watoto wa kike katika maeneo yao.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na watoa huduma wa afya ya mama na mtoto, Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa iliyoshamiri vitendo vya ukeketaji ikiwemo Mikoa ya Manyara na Dodoma imeweza kusambaza dodoso ili kuwatambua wale watoto waliofanyiwa kitendo cha ukeketaji pale wanapopelekwa kliniki. Katika zoezi zima la upimwaji wa maendeleo ya mtoto watoa huduma hao huwachunguza watoto kama wamekeketwa. Aidha, zoezi hili pia hufanyika kipindi mtoto anapoenda kuanzishwa darasa la kwanza, ikitokea mtoto amekeketwa wazazi/walezi huchukuliwa hatua kali za kisheria.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaboresha MSD ili dawa zifike kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya mabadiliko makubwa katika utendaji wa MSD. Kutokana na malalamiko mengi juu ya utendaji wa MSD siku za nyuma, katika mwaka wa fedha 2015/2016 Serikali iliajiri Kampuni ya Ushauri wa Kitaalam ya Deloitte ili kupitia mfumo wa utendaji kazi wa MSD kwa minajili ya kuuboresha. Deloitte walitengeneza ripoti ya utendaji wa MSD na kuleta mapendekezo ya maboresho ambayo iliwasilishwa Wizarani mnamo mwezi Januari, 2016. Taarifa hiyo ilikuwa na mapendekezo 21 ya utekelezaji ili kuiboresha MSD na kuhakikisha dawa zinafika vituo vya afya kwa wakati kulingana na mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo hayo yalikuwa pamoja na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ya MSD, kuongeza mtaji wa usambazaji dawa, kulipwa kwa deni la MSD, kuboresha mifumo ya kusimamia rasilimali watu, kuupitia mnyororo wa ugavi wa dawa nchi nzima na kuondoa kero ya uhaba wa dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupokea ripoti hiyo, Wizara iliunda timu maalum ya kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Deloitte kuhusu uboreshaji wa MSD ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali. Napenda kukujulisha kuwa hadi kufikia tarehe 31/7/2017 MSD ilikuwa imetekeleza mapendekezo 19 kati ya 21 ya Deloitte. Mapendekezo mawili yaliyosalia ya kuongeza upatikanaji wa dawa na kufuta deni la MSD yanaendeea kufanyiwa kazi na yanatarajiwa kukamilika kabla ya Juni, 2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho hayo ndani ya MSD, kwa sasa hali ya upatikanaji wa dawa muhimu imeendelea kuimarika hadi kufikia wastani wa asilimia 80. Aidha, ununuaji wa dawa kutoka moja kwa moja kwa wazalishaji kumepunguza gharama za ununuzi wa dawa kwa wastani wa asilimia 40 na hivyo kuwawezesha wananchi wengi kupata dawa nyingi zaidi kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kukujulisha kuwa ili kuhakikisha dawa zinafika kwa wakati, Wizara kupitia msaada wa Mfuko wa Dunia (Global Fund to Fights Aids, Malaria and Tuberculosis) inatarajia kuipatia MSD magari ya usambazaji 181 kwa ajili ya usambazaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba ili ufanyike kila baada ya miezi miwili badala ya miezi mitatu ya sasa. Utaratibu huu utaongeza upatikanaji wa dawa kuanzia mwezi Januari, 2018.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga makazi bora katika Kituo cha Wazee cha Kolandoto kwa kuwa makazi haya yamekuwa ya muda mrefu na yamechakaa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Makazi ya Wazee ya Kolandoto yaliyopo Manispaa ya Shinyanga yalianzishwa mwaka 1917 kwa lengo la kutoa huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa ukoma ambao walikuwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kolandoto. Aidha, baada ya kupona maradhi hayo waliendelea kubaki eneo la Kolandoto kwa sababu ya kuepuka unyanyapaa uliokithiri katika jamii zao. Tangu kipindi hicho, Serikali ilichukua jukumu la kuwatunza wananchi hao na kuwapokea wazee wengine wasiojiweza ambao walihitaji huduma za ustawi wa jamii.
Mheshimiwa Spika, napenda nikiri kuwa makazi haya ni miongoni mwa makazi ambayo yanahitaji ukarabati kutokana na uchakavu wa nyumba za makazi ambazo zilijengwa miaka mingi iliyopita.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hali hiyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa kipaumbele cha kuboresha hali ya Makazi ya Wazee wa Kolandoto kwa kujenga bweni lenye uwezo wa kuchukua wazee 20, wa kiume 10 na wa kike 10. Ujenzi huo utakamilika ifikapo Oktoba mwaka 2017.
Mheshimiwa Spika, pia Wizara imejenga jiko ambalo limefungwa majiko yanayotumia nishati ya gesi. Majiko hayo yameanza kutumika kupikia chakula cha wazee badala ya kutumia kuni.
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJAD aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko ya matokeo ya uchunguzi yanayofanywa kwa kutumia mashine ya kutambua vinasaba (DNA) kutoka Zanzibar kutopatikana kwa wakati na kusababisha kesi mbalimbali kushindwa kusikilizwa kwa wakati muafaka zikiwemo za jinai kama ubakaji.
(a) Je, kwa nini matokeo ya uchunguzi yamekuwa yakichukua muda mrefu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakati uchunguzi huo una umuhimu mkubwa katika kupambana na vitendo vya uhalifu?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mashine za kutosha ili uchunguzi ufanyike kwa wakati kutokana na vitendo vya udhalilishaji wanawake na watoto kuendelea kuongezeka baina ya pande mbili za Muungano?
(c) Je, ni lini Hospitali ya Taifa Muhimbili itaweka utaratibu wa kuchunguza sampuli za Zanzibar kwa wakati kwa kutumia mashine ya kuchunguza vinasaba (DNA)?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, sampuli za uhalali wa watoto kwa wazazi (paternity case samples) zinafanyika kwa wepesi zaidi kuliko sampuli za makosa ya jinai (criminal case samples) kwa sababu sampuli za paternity zinachukuliwa moja kwa moja toka kwa wahusika (direct samples) na hivyo kurahisisha uchunguzi wake endapo wahusika wa uchukuaji watachukua kwa umahiri na uhifadhi utafanyika kwa namna stahili. Aidha, sampuli za uchunguzi wa makosa ya jinai (criminal case files) zinachukuliwa toka maeneo ya matukio, kwenye crime scene, hivyo, uchunguzi wake unaweza kuchukua muda zaidi kutegemeana na aina ya sampuli na eneo zilipotoka.
(b) Mheshimiwa Spika, mikakati ya Serikali katika kuongeza mashine za kutosha ili kuwezesha uchunguzi ufanyike kwa wakati kwa vielelezo vya makosa ya jinai, ikiwa ni pamoja na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, Serikali imedhamiria kununua mashine tatu za vipimo vya vinasaba (DNA) ili vitumike katika maabara za kanda, na hivyo kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018.
(c) Mheshimiwa Spika, vipimo vya vinasaba (DNA) kwa ajili ya uhalali wa watoto kwa wazazi (paternity) na kesi za jinai (criminal case) vinafanywa na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na sio Hospitali ya Muhimbili.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Tohara kwa wanaume imethibitika kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kiasi kikubwa.
(a) Je, kwa nini Serikali isiagize tohara kuwa ya lazima kwa wanaume wote?
(b) Je, elimu kuhusu tohara imefikishwa kwa wananchi kwa kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, si rahisi kwa Serikali kuagiza tohara kuwa lazima kwa wanaume wote nchini japokuwa tohara ina faida kubwa sana kiafya kwa wananchi wetu. Wizara iliweka mikakati ya kubaini mikoa ya kipaumbele ambayo haina utamaduni wa kutahiri na ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na kutoa huduma ya tohara kama afua rasmi. Mikoa hiyo ni 14 ambayo ni Iringa, Njombe, Tabora, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera na Musoma. Itakapofika mwezi Oktoba, 2017 mikoa mipya minne ambayo ni Singida, Kigoma, Mara na Morogoro itaongezwa na hivyo kufikisha idadi ya mikoa 17. (Makofi)
(b) Mheshimiwa Spika, elimu kuhusu tohara imefikishwa kwa wananchi kwa kiasi kikubwa ambapo Serikali kwa kushirikiana na wadau wake katika mikoa ya kipaumbele imekuwa ikitoa elimu kabla na baada ya huduma ya tohara katika vituo vya kutolea huduma za afya na wakati wa huduma mkoba zinazotolewa ngazi ya jamii kupitia kampeni mbalimbali. Serikali iliendesha Kampeni kubwa ya Tohara maarufu kama Dondosha Mkono Sweta ambapo elimu kuhusu tohara ilitolewa kupitia matangazo na vipindi vya redio na televisheni, mabango, machapisho, vijarida mbalimbali, filamu na waelimisha rika.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ujuzi wa kufanyia matengenezo vifaa tiba kutokana na ukosefu wa watu wenye utaalam huo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwa na chuo maalum kwa ajili ya kufundisha wataalam wa vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mafunzo ya wataalam wa matengenezo ya vifaa tiba yanatolewa kwenye Vyuo viwili ambavyo ni Dar es Salaam Institute of Technology (DIT) pamoja na Arusha Technical College (ATC). Mafunzo haya yalianza hapa nchini mwaka 2011 kwa kufundisha Stashahada (Diploma) za matengenezo ya vifaa tiba kwa miaka mitatu, jumla ya wanafunzi 32 walihitimu mwaka 2014 ambapo wahitimu 17 walitoka DIT na 15 walitoka ATC. Wahitimu wote hao walipata ajira sehemu mbalimbali nchini. Mwaka 2015, jumla ya wataalam wengine 32 walimaliza mafunzo yao na sasa wanasubiri ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya wahitimu wa fani ya ufundi wa vifaa tiba kuanzia mwaka 2016 ni 60. Idadi hii itaongezeka na kufikia wahitimu 85 mwaka 2019. Idadi ya wahitimu wote ifikapo mwaka 2025 inakadiriwa kuwa 1,107 ambayo ni sawa na asilimia 24 ya mahitaji yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho ya utoaji wa huduma za kibingwa hapa nchini kufanywa na sekta ya umma lakini pia na sekta binafsi, hasa katika kuongeza vituo vya utambuzi wa magonjwa ni dhahiri kuwa mahitaji ya wataalam hawa yataongezeka maradufu na hivyo uzalishaji wa wataalam hawa ni kipaumbele kwa Serikali na hivyo, mipango ya kuongeza vyuo vya mafunzo iko bayana.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Mwaka 2007 Serikali ilianzisha rasmi Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) kwa lengo la kuwawezesha wanawake wajasiriamali kupata huduma za kibenki ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, lakini mpaka sasa benki hiyo ina matawi manne tu, mawili yakiwa Dar es Salaam na mengine Mikoa ya Mwanza na Dodoma wakati wanawake wenye uhitaji wa huduma hiyo wako nchi nzima.
Je, Serikali, ambayo inamiliki TWB kwa zaidi ya asilimia 90 inakwama wapi kuiwezesha benki hii ili kufungua matawi kote nchini ili wanawake waweze kunufaika na huduma hizo na hatimaye kujikwamua kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Wanawake Tanzania ilianzishwa mwaka 2009. Tangu kuanzishwa kwake benki imefanikiwa kuwa na matawi mawili katika Mkoa wa Dar es Salaam na mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa huduma za Benki ya Wanawake Tanzania zinawafikia wanawake waliopo katika mikoa yote hapa nchini. Utekelezaji wa mpango huo unakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa mtaji wa benki. Hivyo, katika kuhakikisha azma hii inafanikiwa, benki imekuwa ikipanua huduma zake katika Mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa awamu kwa kufungua vituo vya kutolea mafunzo na mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa benki imeanzisha jumla ya vituo 252 katika Mikoa saba ya Dar es Salaam, Mbeya, Njombe, Iringa, Mwanza, Ruvuma na Dodoma. Kwa mwaka 2017/2018, benki inatarajia kufungua vituo vipya vya kutolea mafunzo na mikopo katika Mikoa ya Singida, Arusha na Zanzibar. Aidha, katika kipindi husika, kituo cha Dodoma kitaboreshwa na kupandishwa hadhi na kuwa tawi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali itaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa mtaji wa benki hii unaimarika ili huduma za Benki ya Wanawake Tanzania ziweze kupatikana katika mikoa yote ya Tanzania. Jitihada hizo ni pamoja na:-
Kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wakopaji; kuongeza amana kutoka kwa wateja na wawekezaji binafsi; kuimarisha ubia wa kimkakati na wadau, mfano African Development Bank pamoja na kuendelea kuajiri wafanyakazi wenye weledi na walio waadilifu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. CONSTANTINE J. KANYASU) aliuliza:-
Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hivi karibuni alitoa agizo la kuwakamata wanawake wanaojiuza:-
Je, zoezi hili limefanikiwa kwa kiasi gani nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa kumekuwa na vitendo vya wanawake kujiuza katika sehemu mbalimbali nchini, hasa maeneo ya mijini. Tatizo hili limekuwa kubwa zaidi katika Mikoa na Miji mikubwa kama vile Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa vifungu vya Sheria Na. 146A, 176(a) na 176A vya Sheria ya Makosa ya Jinai, (Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002), kitendo cha mwanamke kuishi akitegemea kipato chake au sehemu ya kipato chake kutokana na ukahaba ni kosa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, katika kuhakikisha kuwa sheria hii inatekelezwa ipasavyo, viongozi katika mikoa mbalimbali ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria wanawake wanaojiuza.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inaendelea kufanya operesheni ya kuwabaini na kuwakamata wamiliki wenye madanguro yanayotumiwa na makahaba hao. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la Polisi na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutahakikisha wanawake wanaojihusisha na biashara hii wanaendelea kukamatwa ili kulinda heshima, utu na hadhi ya wanawake wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nitumie fursa hii kuwataka wanawake wanaofanya biashara hii kuacha mara moja na kutafuta shughuli nyingine ya kujipatia kipato cha halali. Pia napenda kuwaasa wanaume kuacha kujihusisha katika biashara hii yenye madhara kwa familia zao kiuchumi na kijamii, kwani wao wakiacha wanawake hawa watakosa soko. Aidha, kwa mwanaume kuwa mteja wa biashara hii nalo pia ni kosa kisheria. (Makofi)
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI ya Februari, 2017 fedha za wafadhili zinaendelea kupungua na baadhi yake kuwa na masharti yasiyoendana na mila na desturi za Kitanzania.
Je, Serikali imejipangaje kuendeleza huduma zilizokuwa zikitolewa na wafadhili, hususan dawa za kurefusha maisha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie kwamba Wadau wa Maendeleo wameendelea kutoa msaada wa dawa za kurefusha maisha (Antiretroviral Drugs - ARVs) mbali na kwamba Serikali imeendelea kupinga maadili mbalimbali yasiyoendana na mila na desturi za Kitanzania kwa kutoa miongozo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha tunajipanga vyema na upatikanaji, hususan wa dawa za kurefusha maisha (ARVs), Serikali kwa sasa imeanzisha Mfuko Maalum wa UKIMWI unaojulikana kama AIDS Trust Fund (ATF). Mfuko huu utachangiwa na Serikali, mashirika, sekta binafsi pamoja na wahisani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kuu la mfuko huu ni kuchangia upatikanaji wa dawa za kurefusha maisha hapa nchini.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
• Ni vifaa gani muhimu vimewekwa kwenye vifungashio vya akinamama wakati wa kujifungua (delivery kit) takribani 500,000 zinavyokusudiwa kusambazwa na Serikali?
• Je, ni kwa nini Serikali inasuasua kwenye usambazaji wa delivery kits kama mkakati ulivyo?
• Je, ni kwa kiasi gani agizo la Mwandoya la Serikali la kuanzisha huduma za upasuaji kwenye vituo vyote vya afya nchini limetekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kuna tofauti ya matumizi ya maneno delivery kits ambayo humaanisha vifaa vyote vinavyopaswa kuwepo kituoni katika chumba cha kujifungulia na delivery Packs ambavyo, ni kifurushi muhimu anachotakiwa kupewa mama mjamzito akija kliniki kitakachomsaidia wakati wa kujifungua, kwa maana ya vifungashio (delivery packs). Vifungashio hivi vina vifaa vifuatavyo; pamba, pedi, kifungia kitovu cha mtoto, kitambaa cha kumfutia mtoto, sindano, mipira ya kuvaa mikononi (surgical gloves), mpira wa kulalia wakati wa kujifungua, uzi (chronic cutgut 2”), vidonge vya kuzuia umwagikaji wa damu na wembe. Na gharama ya vifungashio hivi ni shilingi 25,000 kwa kila kifurushi.
(b) Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, hadi sasa imesambaza vifungashio (delivery packs) 60,000 kwa mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ambayo vifo vingi vya wamama wajawazito na watoto vinatokea huko. Aidha, ni jukumu la kila halmashauri kuweka mahitaji ya vifungashio kwenye mpango kabambe wa afya wa Halmashauri, yaani Comprehensive Council Health Plan (CCHP).
(c) Mheshimiwa Spika, agizo la Mwandoya lilitaka kila Halmashauri nchini kwa kutumia pesa zao za ndani kuhakikisha wamejenga au kukarabati vyumba vya upasuaji katika vituo vya afya kwa kipindi cha miezi sita, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto na kupeleka huduma karibu zaidi kwa wananchi. Baada ya muda huo kumalizika Wizara imeongeza miezi mitatu kukamilisha agizo hilo. Wataalam wa Wizara kwa sasa wanatembelea vituo katika Halmashauri nchi nzima kufanya tathmini kubaini waliotekeleza na ambao hawajatekeleza, ili hatua za kinidhamu zifuate mkondo wake.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imepata ufadhili wa shilingi bilioni 66 kutoka Benki ya Dunia na imeshirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kubainisha vituo 100 vitakavyoboreshwa, ili kutoa huduma za dharura za upasuaji wa kutoa mtoto tumboni. Taya ri fedha za utekelzaji zimeanza kupelekwa katika Halmashauri mbalimbali husika hapa nchini.
STELLA I. ALEX aliuliza:-
Kwa kuzingatia umuhimu wa taulo za kike nchini. Je, Serikali inaonaje ikiondoa kodi kwenye taulo hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maombi ya kuondoa kodi kwenye taulo za kike yamewahi kuwasilishwa na watumiaji pamoja na wauzaji wa bidhaa hiyo.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo na maazimio yametolewa katika vikao mbalimbali vya wadau na Serikali. Maamuzi ya suala hili yamechelewa baada ya kubaini kuwa bidhaa hii haikuwa miongoni mwa orodha ya vifaa vya matibabu (vifaa tiba) ambavyo huondolewa kodi isipokuwa zimeondolewa ushuru wa uingizaji (import duty) na aina nyingine za kodi zinalipiwa kama bidhaa nyingine zote.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewaandikia barua Wizara ya Fedha na Mipango kuona namna ya kuondoa kodi katika bidhaa hii. Majadiliano yanaendelea kuwezesha bidhaa hii iunganishwe katika orodha ya vifaa tiba ili viweze kupata msamaha wa kodi sambamba na vifaa vingine vya tiba. Hii itapunguza gharama za upatikanaji wake kwa kuziondolea baadhi ya kodi zenye kuongeza bei kwa kiwango kikubwa mfano kodi ya ongezeko la thamani (Value Added Tax).
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-
Hospitali za Serikali zimeandaliwa kupata huduma za dawa MSD lakini wakati mwingine baadhi ya dawa zimekuwa hazipatikani MSD na hospitali haziruhusiwi kununua dawa nje ya MSD.
Je, Serikali imetoa maelekezo gani pale ambapo MSD wamekuwa hawana baadhi ya dawa hizo zinazohitajika kwa wagonjwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 na Kanuni zake za mwaka 2013 kifungu cha 140, inavitaka vituo vyote vya kutolea huduma za afya kuleta MSD (Medical Stores Department) maoteo ya mahitaji ya mwaka mwezi Januari ya kila mwaka ili kuiwezesha MSD kuyaingiza kwenye mpango wake wa manunuzi. Vituo vya kutolea huduma za afya vinatakiwa kununua mahitaji yake kutoka MSD na pale ambapo madawa hayo yatakosekana katika maghala ya MSD yaliyopo kwenye Kanda na Makao Makuu ya MSD, MSD anapaswa kumtaarifu mteja ndani ya siku moja ya kazi ili akanunue kwa watu binafsi.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Nne ilianza ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini katika eneo la Mitengo Mikindani – Mtwara.
• Je, kuna mikakati gani ya kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa hospitali hiyo?
• Je, ni lini wananchi wategemee kuanza kutumia hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Wizara ipo kwenye hatua ya kuandaa awamu nyingine ya kumalizia sehemu iliyokwishaanzishwa ya jengo la mapokezi ya wagonjwa wa nje yaani Out Partient Department (OPD) pamoja na kukamilisha majengo mengine kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, ambapo kiwango cha kazi kilichoingiwa mkataba kwa awamu ya kwanza kimekamilika na kukabidhiwa kwa Wizara. Mwaka 2011 Wizara ilijenga uzio wa ukuta wenye kilometa 2.7 kwa ajili ya usalama na uhifadhi wa eneo la hospitali. Sanjari na hilo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wamekubali kutoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la Wagonjwa wa nje OPD na ujenzi huo utaanza mapema pindi taratibu za ndani zitakapokamilika.
(b) Mheshimiwa Spika, matarajio ya Wizara kwamba kipindi cha mwaka mmoja baada ya kumpata mkandarasi wa awamu ya pili sambamba na upatikanaji wa fedha za kuendelea na ujenzi, jengo la wagonjwa wa nje litakamilika na kuweza kuanza kutumika wakati majengo mengine yanaendelea kukamilishwa.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Sheria nyingi nchini hususan zile zinazohusu haki na stahili za wanawake zimepitwa na wakati na hivyo kuwanyima haki wanazostahili makundi hayo.
Je, ni sheria zipi zinazowanyima haki wanawake na watoto nchini?
Je, ni lini Serikali italeta miswada ili kuboresha au kubadilisha sheria hizo ili ziendane na wakati na kuwapatia haki zao wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
– Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria za Mirathi za Kimila (Customary Declaration Orders, GN. No. 279 na 436 za mwaka 1963 zimekuwa zikiwanyima haki za urithi na umiliki wa ardhi wanawake na watoto.
Vilevile Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 katika Kifungu cha 13 na 17 vinaruhusu mtoto wa kike kuolewa katika umri mdogo wa miaka 14 au 15 kwa ridhaa ya wazazi au uamuzi wa mahakama. Vifungu hivi humnyima mtoto haki zake za msingi.
– Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mirathi tayari yamewasilishwa Wizara ya Sheria na Katiba pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi. Taratibu zote zitakapokamilika muswada utawasilishwa Bungeni.
Aidha, katika jitihada za kukomesha ndoa za utotoni, mwaka 2016 Serikali ilifanyia marekebisho Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 ili kuzuia watoto wa shule wasiolewe. Kwa mujibu wa Sheria hii Na. 4 ya mwaka 2016 Kifungu cha 60A hairuhusiwi mtu yeyote kuoa au kumpa ujauzito mwanafunzi wa Shule ya Msingi au Sekondari. Kwa kuwa sheria hii inalenga zaidi ulinzi kwa watoto walio mashuleni, bado ipo haja ya kuviondoa kabisa vifungu vinavyoruhusu ndoa za utotoni kwenye Sheria ya Ndoa kama ilivyofanyika kwa nchi nyingine kama vile Bangladesh, Yemen, Kenya na Malawi ili kuondoa mkanganyiko wowote unaoweza kujitokeza.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA aliuliza:-
Je ni lini Serikali itaanza ujenzi wa duka la dawa la MSD kwenye Hospitali Teule ya Sengerema?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemirembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali za umma, Serikali iliagiza maduka ya dawa yafunguliwe kwenye hospitali za umma. Kama sehemu ya utekelezaji wa agizo hilo, bohari ya dawa imeshafungua maduka katika hospitali za Muhimbili, Mount Meru, Ruangwa, Sekou Toure, Mbeya, Katavi na Chato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa kuanzisha duka la dawa katika hospitali una faida kubwa ambazo ni pamoja na kuunga mkono dhamira ya kuleta dawa na vifaa tiba karibu na wananchi; kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa bei nafuu na kwa ubora kwa Watanzania; kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na TAMISEMI katika kudhibiti kuongezeka kwa gharama za huduma za afya; kuondoa utegemezi wa fedha kutoka Serikali Kuu na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa na vifaa tiba kwa wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza agizo hilo kwa Tanzania nzima, inaonekana itahitajika rasilimali watu na rasilimali fedha nyingi sana ambapo bohari ya dawa ilikubaliana na TAMISEMI kuwa hospitali zilizo chini yake zifungue maduka yao zenyewe na MSD itatoa ushauri wa kitaalamu pamoja na kuziuzia dawa na vifaa tiba.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Kutokana na msongamano mkubwa wa wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Ocean Road pamoja na gharama kwa ndugu wa wagonjwa ya kuwaleta na kuwauguza ndugu zao.
Je, Serikali haioni haja ya kuanza kutoa huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII (K.n.y WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza leo nasimama hapa toka niteuliwe na Mheshimiwa Rais, naomba na mimi nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini na kunipa majukumu zaidi kwenye Serikali yake, pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Nzega Vijijini, Wilaya ya Nzega na Mkoa wetu wa Tabora kwa ujumla kwa ushirikiano ambao wameendelea kunipa. Napenda kusema tu kwa wote kwamba kwa hakika sitowaangusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa wenye Saratani ili kusogeza huduma hizi karibu zaidi na wananchi na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Ocean Road, pia kupunguza gharama kwa wagonjwa na ndugu. Kwa sasa Serikali inakamilisha maandalizi ya kuanzisha matibabu ya saratani kwa mionzi katika Hospitali ya Bugando ambapo baadhi ya majengo kwa ajili ya huduma husika yamekamilika, yakiwemo jengo maalum ambalo ni kwa ajili ya kudhibiti mionzi, ambapo ukuta wake umejengwa kwa zege nene la mita moja (bunkers), jengo la kutolea huduma za mionzi, baadhi ya wataalam wapo na baadhi ya mashine za matibabu kwa mionzi zimeshanunuliwa zikiwemo Cobalt 60 na CT Simulator.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha brachytherapy na immobilization devices zinatarajiwa kuwasili mwezi Disemba, 2017. Kwa sasa huduma za tiba ya saratani zinazopatikana Bungando ni zile za matibabu yasiyo ya mionzi (chemotherapy) na zilianza mwezi Januari mwaka 2009, kufuatia sera ya Serikali ya kutoa huduma hizo kikanda. Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa kipindi cha mwaka 2009 - 2017 hospitali imetoa matibabu kwa wagonjwa 39,300 kati yao 12,200 wakiwa ni wapya, sawa na wastani wa waginjwa 1,500 kwa mwaka.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. SAVELINA S. MWIJAGE) aliuliza:-
Serikali ilitoa tamko kuwa watoto chini ya miaka mitano, wazee pamoja na wagonjwa wa UKIMWI na TB watibiwe bure.
(a) Je, Serikali imetekelezaje mpango huo?
(b) Je, makundi hayo yameshaanza kupata matibabu bure kama ilivyopangwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri makini, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Savelina Silvanus Mwijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Sera ya Afya ya mwaka 2007 ya kutoa huduma bila malipo kwa watoto chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito na wazee wasio na uwezo ambapo sera na mwongozo wa uchangiaji unaelekeza wazi kuwa makundi haya hayapaswi kugharamia huduma za afya pale wanapohitaji. Pia wagonjwa wa UKIMWI na TB wamekuwa wakipata matibabu bure pale wanapohudhuria kliniki kupata dawa na ushauri nasaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha mwezi Julai, 2015 hadi Juni, 2016 jumla ya watu 839,574 waliopatikana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI wamepatiwa huduma za dawa za kupunguza makali ya VVU. Kuanzia mwezi Oktoba, 2016 Wizara imeanza kutoa dawa za ARV kwa watu wote wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI bila kujali kiwango cha CD4 badala ya kuanzia CD4-500 kama ilivyokuwa hapo awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile huduma hii hailipiwi. Huduma zote ni kwa gharama za Serikali. Takribani watu 1,200,000 wanatarajiwa kuhudumiwa katika mpango huo. Tutahakikisha kila mtu anayepima virusi vya UKIMWI na kugundulika na maambukizi, anapatiwa dawa ikiwemo wazee na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wameendelea kupata huduma za matibabu bila malipo katika vituo vyote vya Umma vya kutolea huduma. Huduma hizo ni pamoja na chanjo zote zinazotolewa kwa watoto pamoja na huduma nyingine zote bila malipo yoyote. Kutokana na juhudi hizo, tumeweza kufikia wastani wa asilimia 97 ya kiwango cha chanjo nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tiba kwa wazee, Serikali imekuwa pia ikitekeleza mpango wa huduma ya matibabu bila malipo kwa wazee wasio na uwezo nchini kote. Aidha, wazee katika maeneo mengi wametengewa maeneo ama madirisha maalum ya kuwapatia huduma kwa haraka bila bughudha. Ninaendelea kuwataka watumishi katika sekta ya afya nchini kuhakikisha wanatekeleza sera hiyo ya kutoa huduma kwa wazee wasio na uwezo bila malipo kwa umakini mkubwa zaidi.
ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. PAULINE P. GEKUL) aliuliza:-
Kuna mkanganyiko wa kutoza ada ya ukaguzi kati ya TFDA na Halmashauri kwa wafanyabiashara wale wale.
Je, ni kwa nini chanzo hiki cha mapato kisiachwe kwa Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, majukumu ya TFDA yanatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura ya 219. Kutokana na uhaba wa rasilimali watu na ili kusongeza huduma karibu zaidi na wananchi, baadhi ya majukumu ya TFDA yamekasimishwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kwa mujibu wa Kanuni za Kukasimu Madaraka na Majukumu (The Tanzania Food, Drugs and Cosmetics (The Delegation for Powers and Functions) Order (GN No. 476) za mwaka 2015. Kwa mujibu wa Kanuni hizi, ada zote za udhibiti zinazotozwa kwa majukumu yaliyokasimiwa kwa Halmashauri hutumiwa na Halmashauri zenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusisitiza kuwa ada zinazotozwa na Halmashauri kutokana na udhibiti wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha kuwa watumiaji bidhaa hizo wanalindwa afya zao ipasavyo.
MHE. LUCIA M. MLOWE (K.n.y MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko ya kupokea dawa za ARV zilizokwisha muda wa matumizi (expired) kwenye vituo vya afya katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla:-
Je, ni lini Serikali itafanya ukaguzi katika Manispaa ya Ujiji na Mkoa wa Kigoma ili kubaini ukweli wa malalamiko hayo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ina utaratibu mahususi wa kuangalia dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kabla ya kuvitoa katika Bohari ya Dawa na kuvisambaza kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya nchi. Kwa kutambua unyeti na umuhimu wa kutoa dawa salama zenye ubora kwa wananchi, Bohari ya Dawa yenye jukumu la kununua, kutunza na kusambaza dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi hutumia utaratibu ufuatao:-
• Mfumo wa ukusanyaji na utengenezaji wa nyaraka za ugavi una uwezo wa kuona kuwa dawa inayotakiwa kutolewa kuwa imebakisha muda gani kabla ya kwisha muda wake wa matumizi. Iwapo dawa hizo zitakuwa zimebakisha muda wa miezi sita mfumo huo hutoa tahadhari kwa afisa na kusitisha taarifa hiyo kutumwa kwa ajili ya kutoa dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi husika.
• Kamati ya Dawa ya Kituo husika hupokea dawa hizo na kufanya ukaguzi kabla ya kusaini form mahususi ya kupokelea dawa na kujiridhisha kuwa dawa hizo zimekabidhiwa na kupokelewa kama ilivyoainishwa katika nyaraka za manunuzi kwa idadi baada ya kuhesabu na kuangalia kama zina ubora unaotakiwa. Iwapo kamati ama anayepokea dawa hizo ataridhika basi atasaini katika nyaraka hizo na anayekabidhi dawa huondoka na nakala. Iwapo Kituo hakitaridhishwa na dawa zilizofika, hulazimika kuzikataa na kujaza form maalum inayoitwa Discrepancy form.
Mheshimiwa Spika, tunaomba vituo au Halmahsauri hizo kuwasiliana moja kwa moja na taasisi za Serikali zinazohusika na usambazaji wa dawa katika Bohari za Dawa za Kanda au Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi ili yaweze kufanyiwa kazi mara moja pindi yanapotokea ili kwa pamoja tulinde afya za wananchi tunaowatumikia.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Wataalam wa Afya wanaeleza kuwa mtu anaweza kuwa na virusi vya UKIMWI lakini hana ugonjwa wa UKIMWI:-
Je, nini maana ya maelezo haya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Jimbo la Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mtu anaweza kuwa na virusi vya UKIMWI lakini hana ugonjwa wa UKIMWI. Maana yake ni kuwa, mtu atakuwa na ugonjwa wa UKIMWI pale ambapo kinga zake zinapokuwa zimeshuka sana na hivyo kuanza kupata magonjwa nyemelezi ya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha kuwa na virusi vya UKIMWI bila kuonyesha dalili za ugonjwa wa UKIMWI kawaida kinaweza kuchukua muda mrefu kuanzia miaka mitano hadi kumi zaidi tangu mtu apate maambukizi ya virusi vya UKIMWI. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Kituo cha Afya cha Mji Mwema katika Manispaa ya Songea kinahudumia watu zaidi ya laki mbili lakini kinapata mgao wa dawa sawa na vituo vingine vya afya:-
(a) Je, Serikali ina mpango wa kukiongezea dawa kituo hiki ili kipate mgao wa dawa na vifaa tiba kama Hospitali ya Wilaya?
(b) Je, ni lini Serikali itakamilisha vifaa vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mji Mwema?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafanya mgawanyo wa fedha za dawa kulingana na idadi ya watu wanaopata huduma katika kituo husika. Takwimu za Wizara za mwaka 2015 zinaonesha kituo hicho kinahudumia wananchi 20,000. Kama kuna mabadiliko ya idadi ya wananchi wanaopata huduma katika kituo hiki ni vyema takwimu hizo ziletwe Wizarani na Mganga Mkuu wa Wilaya husika ili marekebisho yaweze kufanyika. Kwa kuwa hiki ni Kituo cha Afya, hakitapata mgao kama Hospitali ya Wilaya mpaka pale ambapo kitapandishwa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kukamilisha upatikanaji wa vifaa vya upasuaji wa Vituo vya Afya nchini kikiwemo cha Mji Mwema chini ya mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Mpango huu ni wa miaka mitatu na umelenga kupunguza vifo vya akinamama kwa asilimia 20. Katika kipindi hicho cha 2015 – 2018, Vituo vya Afya nchini vitaboreshwa ili kutoa huduma za upasuaji hasa kwa akina mama ambao wameshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida. Serikali pia itaboresha idadi ya wataalam na upatikanaji wa dawa hasa za mpango wa mama na mtoto.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Mgogoro wa mipaka kati ya Kijiji cha Kikulyungu na Hifadhi ya Selous ni wa muda mrefu:-

Je, Serikali itamaliza lini mgogoro huo?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa mgogoro wa mpaka kati cha kikulyungu na poro la Akiba Selous umekuwepo kwa muda mrefu. Chanzo cha mgogoro huo ni wananchi wa kijiji hicho kufutiwa kibali cha kuvua samaki katika bwawa la kihurumila ambalo limo ndani ya Pori la Akiba Selous baada ya wananchi wa kijiji hicho uanza kuvua kwa njia zisizo endelevu au haribifu ikiwemo kutumia sumu. Baada ya kufutiwa kibali wananchi wa Kikulyungu walianza kulalamika na kudai kuwa mpaka wa Selous na kijiji hicho upo mto Matandu jambo ambalo ni kinyume na Tangazo la Seriklai Na.475 la Mwaka 1974.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya uhakika wa mipaka imekamika na taarifa imewasilishwa Wizarani kwangu. Aidha, zoezi la kuhakika mipaka hiyo lilienda sambamba na uwekaji wa alama za kudumu baada ya maridhiano ya pande zote kwa kuzingatiwa tangazo la Serikali kuanzishwa kijiji cha Likulyungu, Tanganzo la Serikali kuanzishwa pori la Akiba la Selous GN. Na. 275 la 1974 na Tanganzo la Serikali la kuanzishwa pori tengefu Kihurumila Na.269 ambalo pia ni la mwaka 1974 lililopo kati ya kijiji cha Likulyungu na pori la Akiba Selous.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa uhakiki huo umefanywa na wataalam kutoka Wizara yenye dhamana ya ardhi na kushirikisha pande zote zilizohusika katika mgogoro huo, ni imani kuwa mgogoro huo umemalizika.
MHE. GODFREY W. MGIMWA aliuliza:-

Jimbo la Kalenga lina vivutio vya utalii vinavyoweza kuingiza nchi yetu pesa za kigeni kama vile Isimila Stone Age na Makumbusho na Mtwa Mkwawa Mkwavinyika:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kushirikiana na Halmashauri ya Iringa Vijijini kuimarisha na kujenga mazingira na kuvitumia vivutio hivyo ili kuongeza Pato la Taifa?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Isimila Stone Age na Makumbusho ya Mtwa Mkwawa yanasimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambapo Shirika lina jukumu la kuhifadhi na kuendeleza vituo hivi. Aidha, kwa kuzingatia changamoto zilizopo katika vituo tajwa, Wizara kupitia Mradi wa Kusimamia Maliasili na Kuendeleza Utalii, Nyanda za Juu Kusini yaani (Resilient Natural Resources for Tourism and Growth - REGROW) na kwa kushirikiana na Halmashauri za Mkoa wa Iringa, itaimarisha miundombinu hiyo. Kwa kupitia mradi wa REGROW maeneo haya yataboreshwa ikiwa ni pamoja na kujenga ituo cha Kumbukumbu na Taarifa ili uhifadhi Kumbukumbu ya Mtwa Mkwawa na utamaduni wa Wahehe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na hatua hiyo, Wizara kwa kushirikiana na Mkoa wa Iringa pamoja na Chuo Kikuu cha Iringa imekarabati boma la Mjerumani na kulifanya kuwa Makumbusho ya Mkoa. Aidha, Wizara ilitoa wataalam wa ujenzi kuandaa na kupanga vioneshwa ndani ya makumbusho ya jengo hilo, duka la zawadi, mgahawa na studio ya kurekodi nyimbo za asili. Mapato yatokanayo na jengo hilo yanaingia katika Mkoa wa Iringa.
MHE. AIDA J. KHENAN aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha kwenye kivutio cha maporomoko ya Kalambo?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maporomoko ya Mto Kalambo yapo katika Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Kalambo yenye ukubwa wa hekta 41,958. Hifadhi hii ni muunganiko wa misitu miwili; Msitu wa Mto Kalambo na Msitu wa Hifadhi wa Maporomoko ya Mto Kalambo. Kutokana na kuwepo kwa maporomoko hayo, eneo hili lina bioanuai nyingi. Kwa kuzingatia umuhimu wa eneo hilo, mwaka 2019, Serikali ilipandisha hadhi msitu huo kwa Tangazo Na. 127 kuwa Msitu wa Mazingira Asilia.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), mwaka 2016 ilianza kuboresha miundombinu katika Maporomoko ya Kalambo ili kuwezesha watalii kuvifikia kivutio husika kwa urahisi, ikiwa ni pamoja na kujenga ofisi sita, kutengeneza njia za kutembelea wageni (walk trail) na kujenga ngazi katika maporomoko ya Mto Kalambo ambapo hadi sasa takribani ngazi zenye urefu wa mita 450 zimekamilika.

Mheshimiwa Spika, aidha, kazi ya ujenzi iliyoanza mwaka 2018 ambayo inahusisha ujenzi wa jengo la ofisi, ngazi zenye urefu wa mita 514, vyoo na geti inayofanywa na kampuni iitwayo Green Construction Limited inaendelea kufanyika katika maporomoko hayo na kazi hii inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu wa 2020.

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha mazingira ya utalii katika eneo hilo, Serikali itahamasisha sekta binafsi ili zijengwe nyumba za kulala wageni, kumbi za mikutano na eneo la kuhifadhi wanyamapori hai (zoo) ili kuweka mazingira rafiki kwa watalii.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-

Je, Tanzania ina Mabwana na Mabibi Misitu wangapi wenye elimu ya Cheti na Diploma?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, taaluma ya Misitu kwa ngazi ya cheti na diploma hapa Tanzania hutolewa na Chuo cha Misitu Olmotonyi kilichopo Arusha. Baada ya uhuru mwaka 1961 hadi 2019, Serikali kupitia Chuo cha Misitu, Olmotonyi imetoa jumla ya wataalam 4,063 wa misitu. Kati ya hao, ngazi ya diploma ni 1,788 wanaume 1,239 na wanawake 549 na katika ngazi ya cheti wataalam ni 2,275 wanaume 1,544 na wanawake 731.

Mheshimiwa Spika, aidha, Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) kilichopo Mjini Moshi hutoa wataalam wa kusimamia viwanda vya mazao ya misitu katika ngazi ya cheti (astashahada) na diploma (stashahada). Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975, Chuo kimetoa jumla ya wataalam 627, kati ya hao, wangazi ya astashahada ni 510 na stashahada ni 117.

Mheshimiwa Spika, baada ya wahitimu kumaliza masomo yao huajiriwa ama na sekta binafsi, Serikali Kuu, mathalani Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake zikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Serikali za Mitaa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI).

Mheshimiwa Spika, kwa sasa jumla ya Mabwana na Mabibi Misitu 1,227 wenye diploma na cheti wameajiriwa ambapo 770 wapo katika taasisi za Wizara (Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) 748, Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) 16, Chuo cha Misitu Olmotonyi wanne na Chuo cha Viwanda vya Misitu wawili) na 457 wameajiriwa na Serikali za Mitaa. Hata hivyo, ni vigumu kujua kwa usahihi ni wangapi kati ya waliokwishahitimu mafunzo wanaitumikia taaluma yao katika maeneo mbalimbali kutokana na ukweli kwamba baadhi yao wameshastaafu na wengine huenda wanafanya kazi tofauti na taaluma waliyosomea.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Mwaka 2000 Serikali kupitia Mradi wa Msitu wa Nishati Ruvu ilitoa leseni ya wakulima zaidi ya 300 kutoka katika Kata za Msangani, Kongowe na Mkuza kulima kwenye hifadhi hiyo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwamilikisha wakulima hao walioendeleza kilimo kwa takribani miaka 19?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Msitu wa Hifadhi wa Ruvu Kaskazini umehifadhiwa kisheria kwa Tangazo la Serikali Na. 309 la mwaka 1957. Mwaka 1999/2000 Serikali ikishirikiana na Norwegian Agency for Development Cooperation (NORAD) ilibuni mradi wa kuinua kipato cha wananchi wanaozunguka eneo la Hifadhi ya Msitu wa Ruvu Kaskazini kwa kupitia kilimo mseto ambapo mazao ya chakula pamoja na miti yalipandwa katika eneo moja. Katika kufanikisha hilo, jumla ya wakulima takribani 300 kutoka Kata za Msangani, Mwendapole, Mkuza na Kongowe walipewa eneo la ekari saba kila mmoja kufanya shughuli za kilimo kwa masharti maalum ikiwa ni pamoja na utunzaji misitu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uharibifu uliokithiri pamoja na wakulima wengi kushindwa kutimiza masharti ya leseni walizopewa, mwaka 2015, Serikali iliamua kuachana na utaratibu huo na kuamua kuanzisha mradi mkubwa wa upandaji miti katika eneo husika.

Mheshimiwa Spika, Serikali haina mpango wa kumilikisha sehemu ya msitu huo kwa mtu au taasisi yeyote. Kwa sasa, umefanyika uwekezaji mkubwa wa kupanda miti mbalimbali kibiashara. Kupitia uwekezaji huo, ajira takribani 2,000 zimezalishwa na zinaendelea kuongezeka kufuatia kuanzishwa pia viwanda vya kuchakata mazao ya misitu, hususan bidhaa za mimea ya bamboo.

Aidha, ili kukabiliana na mahitaji ya ardhi kwa wale wenye uhitaji, Serikali inatoa fursa ya kulima kwa mfumo wa kilimo mseto (taungya system), ambapo wakulima wataruhusiwa kulima mazao kwenye maeneo yanayolimwa au kuvunwa miti kwa kibali maalum.