Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Elibariki Emmanuel Kingu (4 total)

MHE. ELIBARIKI E. KINGU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya kaka yangu Mheshimiwa Jafo, nilikuwa nataka nipate hakikisho kwa sababu hivi tunavyozungumza mimi na wananchi tumeanzisha ujenzi wa zahanati katika vijiji 19 kwa nguvu zetu.
Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atanihakikishia kwamba zahanati hizi za Nkunikana, Puma, Msambu, Unyangwe, Chungu, Kinyampembee, Mpetu, Mayaha, Misake, Maswea, Nsogandogo, Kipunda, German, Mahonda, Iyumbu, Mlandala, Kaugeri, Mduguyu, Mpugizi na Namnang’ana ambazo tumezianzisha kuzijenga ndani ya kipindi cha miaka miwili katika huu mgao, Mheshimiwa Naibu Waziri ananihakikishia kwamba na zenyewe zinakwenda kukamilishwa? Hizi ambazo tumezianzisha sisi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza kama nilivyosema pale awali, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Kingu kwa kazi kubwa anayofanya katika ile Wilaya yote ya Ikungi kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa bajeti wa mwaka huu tumetenga karibuni shilingi bilioni 251 katika Local Government Development Grants, lakini katika hizo karibu shilingi bilioni 68 kwa ajili ya kuboresha vituo vya afya na zahanati, yaani yale maboma yaliyojengwa. Katika hizo nilisema pale awali 1.4 billion ni kwa ajili ya Halmashauri ya Ikungi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tu Kamati ya Fedha itakapokaa pale, katika vipaumbele vya umaliziaji wa maboma, haya maeneo ambayo tumesema tutawaletea fedha, basi ni vyema katika ule mpango ni lazima tuhakikishe maboma haya yamekamilika kwa sababu Serikali ndiyo imeshafanya jambo lake hilo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Mheshimiwa Kingu alileta concern kubwa ya Halmashauri yake kuhusu changamoto ya afya. Ndiyo maana kama Serikali kwa ujumla, hivi sasa tunawapelekea fedha za kwanza, karibu shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya pale Ihanja ambapo tunajua pale kutakuwa na theater kubwa na maabara. Kwa hiyo, eneo lile litabadilika.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutakuwa na fedha nyingine kwa ajili ya ununuzi wa vifaa. Kwa hiyo, Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba wananchi wa Halmashauri yote ya Ikungi inapata huduma nzuri kama tunavyotarajia.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nina nyongeza ndogo. Kwanza kabisa kwa kifupi sana na mimi nimpongeze sana dada yangu Juliana na nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuona vijana wanaweza kumsaidia. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa je, Serikali ipo tayari kuweza kuitumia Miji aidha Mji wa Dodoma au Singida kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, inajulikana kabisa kwamba Singida sasa hivi tayari tuna kiwanja cha kisasa kabisa cha Namfua ambacho kimeshafanyiwa miundombinu ya kisasa na Singida tunaendelea tuna hoteli za kisasa ambazo zimejengwa na wazalendo.
Mheshimiwa Spika, Dodoma pia tunaona Serikali yetu imehamia hapa na Mheshimiwa Rais anakuja hapa, Waziri Mkuu tayari tunae hapa na Makamu wa Rais anakuja. Sasa kwa nini Serikali isiamue tu kwa makusudi kuchagua mikoa hii miwili kati ya Singida au Dodoma kufanyika mashindano ya AFCON 2019? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuweza kuwapongeza Wabunge wote wa Mkoa wa Singida kwa jitihada zao nzuri ambazo wamezifanya katika kurekebisha Uwanja wa Namfua. Nichukue nafasi hii kuomba Wabunge wote lakini vilevile mikoa yote ya Tanzania kuweza kuiga mfano huu mzuri ambao umeoneshwa na Wabunge wa Singida lakini vilevile wananchi wa Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikienda sasa kwenye swali lake la msingi ambapo amependekeza kwamba nini Uwanja wa Namfua, Singida usitumike katika mashindano haya. Niseme kwamba moja ya vigezo ambavyo huwa vinazingatiwa katika kuchagua haya maeneo. Jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba huo mji ambao unapendekezwa uweze kuwa na viwanja ambavyo vinakidhi ubora wa Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kigezo cha pili ni lazima kwamba mji huo uweze kuwa na hoteli ambazo zitaweza ku- accommodate wageni wote ambao watakuja katika mashindano hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme kwamba kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, Mheshimiwa Kingu kwamba sasa hivi kuna Kamati ambayo imeundwa na Mwenyekiti wa hiyo Kamati ni Waziri wangu Dkt. Mwakyembe.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme kwamba nimtoe hofu mimi kama Naibu Waziri nitamshauri Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe sasa aangalie namna gani kwamba ile Kamati ambayo imeundwa ifike Singida ili kuweza kukagua ile miundombinu ya michezo ambayo ipo katika Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili ametaka kujua kwamba kwa nini Dodoma isitumike katika mashindano haya. Kwanza napenda nichukue nafasi hii kuweza kumpongeza sana kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa sababu kwa jitihada zake yeye binafsi sasa hivi Dodoma tunajengewa uwanja mkubwa kabisa wa Kimataifa wa michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba hii inaonesha kabisa kwamba Rais wetu ni Rais ambaye ana ushawishi mkubwa sana kwa Mataifa ya nje lakini inadhihirisha kwamba Rais wetu ni mwanadiplomasia na ni Rais ambaye anapenda michezo ndio maana ameweza kumshawishi Mfalme wa Morocco kuja kutujengea kiwanja hapa katika Mkoa wa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba wazo lake ni zuri na niseme sisi kama Wizara tunachukua hilo wazo lakini kama ambavyo nimesema awali, kwamba uwanja huo unajengwa kwa msaada wa Mfalme wa Morroco. Kwa hiyo, sisi kama nchi hatuwezi kumpa deadline kwamba uwanja huo ukamilike ndani ya muda gani.
Mheshimiwa Spika, tunachokifanya na nimwombe kabisa Mheshimiwa Kingu kwamba endapo uwanja huo utakamilika kabla ya hayo mashindano kufanyika mwaka 2019, basi tutaangalia ni namna gani ambavyo uwanja huo unaweza kutumika katika mashindano hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba na mimi niulize swali moja tu, ni lini Serikali ya Chama cha Mapinduzi itakwenda kutekeleza miradi ya visima 10 vilivyochimbwa Jimbo la Singida Magharibi katika vijiji vya Minyuge, Mpetu, Kaugeri, Mduguyu pamoja na Vijiji vya Mnang’ana, Munyu na Irisya ukizingatia Jimbo la Singida Magharibi ni miongoni mwa Majimbo ambayo yana changamoto kubwa sana ya maji? Naomba nipate jibu serious kutoka kwenye Serikali serious. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kingu kutoka Singida Magharibi, kama ifuatavyo:-

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Siyo daktari.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Nimekutunuku au siyo. Wanasema dalili nje huonekana asubuhi, daktari rudi shule ukapate hiyo profession. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni maeneo yote ambayo yalishafanyiwa usanifu tunakuja kuhakikisha kazi zinafanyika ndani ya wakati. Hivyo visima vyote vitachimbwa kadiri ambavyo vipo kwenye bajeti na maji tutahakikisha hayaishii kwenye kisima bali yanatembea kwenye bomba kuu na kuwafikia wananchi kwenye mabomba yao katika makazi lakini vilevile katika vituo vya kuchotea maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanakwenda kutekelezwa kwa kipindi hiki kilichobaki cha mwaka wa fedha na mwaka wa fedha 2021/2022. Isitoshe nitafika kuona eneo husika na kuleta chachu zaidi kwa watendaji wetu, japo tayari tuna watendaji wazuri katika Wizara na wanafanya kazi vizuri sana. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nilikuwa nina swali dogo moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tathmini inaonesha zaidi ya tani 200 za mazao aina ya alizeti zimeteketezwa na ndege hawa. Je, Mheshimiwa Waziri na Serikali wako tayari kupeleka mitego hii haraka kwenye Kata za Mwalu, katika Vijiji vya Mwalu, Minyuve, Mayaha, Ifyamahumbi, Kipunda, Maswea, Igombwe, Ihanja, Mahonda, Mtunduru, Songandogo pamoja na Gerumani ili kuweza kuwasaidia wakulima wetu kwa sababu, kwa kweli jambo hili liko very serious kwa wakulima wa alizeti katika Jimbo la Singida Magharibi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kingu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri Mheshimiwa Kingu amekuwa akifuatilia jambo hili kwa muda mrefu kwa ajili ya wananchi wake na yeye ndio aliyesababisha Wizara ya Kilimo mwaka jana mwezi Mei tukapeleka wataalamu kwa ajili ya kufanya tathmini na kuweza kutambua katika central corridor maeneo yenye maotea ya mazalia ya ndege hawa. Nataka tu nimwambie na nimpe commitment na kuwapa commitment wananchi wake na wananchi wa mkoa wa Singida kwamba Wizara kuanzia mwezi Mei itapeleka wataalamu na vitendea kazi kwa ajili ya kuanza kushughulika na wadudu hawa, ahsante.