Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Elibariki Emmanuel Kingu (11 total)

MHE. ELIBARIKI E. KINGU aliluliza:-
Wilaya ya Ikungi hasa Jimbo la Singida Magharibi inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vituo vya afya na zahanati. Aidha, umbali mrefu wa kutafuta matibabu umekuwa ukisababisha adha na taabu kwa wananchi wa kata za Lyandu, Igelansomi na vijiji vya Mduguya, Kaangeni, Chengu na Mayahu.
Je, Serikali ipo tayari kushirikiana na wananchi katika kukamilisha ujenzi wa zahanati mpya na vituo vya afya vilivyoanzishwa kwa ushirikiano wa wananchi na Mbunge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Emmanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza miradi ya vituo vya kutolea huduma za afya kwa kushirikisha nguvu za wananchi kupitia mpango wa fursa na vikwazo yaani O & OD. Serikali inampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi na wananchi wake kwa kuanza ujenzi wa vituo vya afya na zahanati.
Mheshimiwa Spika, katika kuunga mkono juhudi hizo, Serikali imetoa ruzuku ya maendeleo kwa Halmashauri hiyo, kiasi cha shilingi milioni 110 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati katika Wilaya ya Ikungi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.49 kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza:-
Uandaaji wa Mashindano ya Kimataifa ya Mpira wa Miguu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) unataka Miji miwili iteuliwe kuendesha mashindano hayo:-
Je, Serikali imeteua mji upi wa pili mbali na Dar es Salaam kuendeshea Mashindano ya AFCON ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya mwaka 2019 yatakayofanyika Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, naomba kwanza nichukue nafasi hii kuweza kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kwa kipekee kabisa nichukue nafasi hii kuweza kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani yake kubwa ambayo ameionesha kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kipekee kabisa nikushukuru wewe mwenyewe Naibu Spika pamoja na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango wenu na ushirikiano wote ambao mlikuwa mkinipa kipindi nikiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako pia naomba nichukue nafasi hii kuweza kuwapa pole wazazi, wanafunzi pamoja na Walimu wa Nduda iliyopo katika Mkoa wangu wa Songwe kwa kuondokewa na wanafunzi ambao walifariki baada ya kupigwa na radi wakiwa shuleni. Nawaombea Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uteuzi wa maeneo ya nchi yetu yatakayotumika kuendesha mashindano ya AFCON mwaka 2019 kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, utafanywa na Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya AFCON 2019 iliyotangazwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo siku ya Jumamosi tarehe 11/11/2017 Jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya mashindano haya ukiwemo uteuzi wa maeneo ya kuendeshea mashindano hayo, ni sehemu ya hadidu za rejea za Kamati hiyo ambayo Mwenyekiti wake ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Makamu wake ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ndugu Leodger Tenga na Mtendaji wake mkuu ni Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania, ndugu Henry Tandau.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kazi kubwa inayoikabili Kamati hii ni uboreshaji wa miundombinu kwa viwango vya Kimataifa, kazi ya uteuzi wa maeneo ya kuendeshea mashindano hayo itafanyika mapema iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima wa Jimbo la Singida Magharibi wanaoteswa na ndege aina ya selengwa kula mazao yao na kuwarudisha nyuma kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini vile vil ekumshukuru Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii ya utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi kwa niaba ya Waziri wa Kilimo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ndege aina ya selengwa ni moja ya aina ya kasuku wadogo waliopo nchini. Ndege hao wapo kwenye uhifadhi wa dunia kisheria kama ndege walio hatarini kutoweka toka mwaka 1985. Aidha, ndege hao wana tabia ya kuishi kwenye maeneo karibu na vyanzo vya maji na hula mbegu za nafaka zilizokomaa tofauti na ndege aina ya kwelea ambao hula nafaka zikiwa katika hatua ya maziwa. Ndege mmoja ana uweza wa kula kati ya gramu 45 – 60 kwa siku hivyo kundi lenye ndege wastani wa milioni moja linaweza kula kati ya tani 45 hadi 60 ya nafaka kwa siku moja. Kwa ulaji huu idadi ya ndege ya selengwa isipodhibitiwa inaweza kuleta madhara ya kiuchumi kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2004 idadi ya ndege hao imekua ikiongezeka na kuonekana katika maeneo ya mikoa ya Singida, Simiyu, Shinyanga na katika hifadhi za Taifa za Serengeti. Ili kudhibiti, Wizara ya Kilimo imeanza utaratibu wa kupata vibali ili tutumie mitego maalum kuanza kuwadhibiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia taarifa ya uwepo wa ndege aina ya selengwa katika Kata ya Minyuve, Mtunduru, Ihombwe na Makilawa za Jimbo la Singida Magharibi zilizotolewa taarifa na Mheshimiwa Mbunge mwezi Mei, 2020 Wizara ya Kilimo ilipeleka wataalam katika Mkoa wa Singida kwa ajili ya kutambua maeneo yenye mazalia ya ndege hao na kubaini kuwepo kwa mazalia ya ndege aina ya selengwa katika vijiji 12 ambapo yatakuwa yanafanyiwa tathmini kila mwaka kwa ajili ya kuchukua hatua za kuwadhibiti. Vijiji hivyo ni Pohama, Ngimu, Muhanga, Mguli, Mkola na Shahana katika Wilaya ya Singida, Ushora, Uruhu na Mlandala vilivyo katika Wilay aya Iramba na Iyumbu katika Wilaya ya Ikungi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbinu ya kuwadhibiti ndege aina ya selengwa ni tofauti na ile ya kudhibiti ndege aina ya kwelea kwelea wanaodhibitiwa kwa kutumia kiuatilifu kinachonyunyizwa kwa kutumia ndege. Kutokana na uwezo mkubwa wa ndege aina ya selengwa kusikia sauti ya ndege inayonyunyizia kiuatilifu na tabia yake ya kujificha, udhibiti kwa kutumia mitego umeonesha ufanisi zaidi. Hivyo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Halmashauri pamoja na wakulima, Wizara itapeleka wataalam kuwadhibiti ndege hao katika kipindi cha mwezi Mei na Julai, 2021 kwa kuwa ndicho kipindi ambacho ndege wanatarajiwa kuwa wamejikusanya kwa makundi kutokana na kuvutiwa mazao yaliyokomaa na vyanzo vya maji vilivyotuama katika kipindi cha kiangazi.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa kujenga miundombinu ya maji katika vijiji vya Kipunda, Minyughe, Ighombwe, Makungu, Mpetu, Magungumka na Mnang’ana?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Jimbo la Singida Magharibi. Ili kuendelea kutatua changamoto hiyo, Serikali imekamilisha upatikanaji wa vyanzo vya maji kwa kuchimba visima virefu katika Vijiji vya Kipunda, Minyughe, Ighombwe, Makungu, Mpetu, Magungumka na Mnang’ana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uendelezaji wa visima hivyo kwa kujenga miundombinu ya usambazaji utaanza mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja ununuzi na ufungaji wa pampu saba, ujenzi wa nyumba za mashine saba, matanki ya kuhifadhi maji saba yenye ukubwa lita 90,000 na 100,000 na ununuzi na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji umbali wa kilometa 85.9 na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 79. Pia, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imepanga kutekeleza miradi minne ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika vijiji vya Irisya, Iglansoni, Ihanja na Kaugeri vilivyopo katika Jimbo Singida Magharibi. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Singida ili ndege za ATCL zianze kutua na kurahisisha usafiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanja cha ndege cha Singida ni miongoni mwa viwanja 11 vilivyofanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina kwa ufadhili wa fedha kupitia mradi wa Benki ya Dunia. Viwanja hivyo 11 ni kama ifuatavyo; Lake Manyara, Musoma, Songea, Kilwa Masoko, Tanga, Iringa, Lindi, Moshi, Singida, Njombe na Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hatua ya awali ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina kukamilika, Serikali imejipanga kuanza hatua ya ujenzi kwa viwanja vyote vya ndege kwa awamu kwa kutumia fedha za ndani kutokana na ukweli kwamba gharama za ujenzi wa viwanja hivyo ni kubwa ukilinganisha na bajeti inayotolewa kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia bajeti, Serikali kupitia TANROADS imejipanga kuanza na ujenzi wa viwanja vya Iringa na Songea. Ujenzi wa viwanja vilivyobaki kikiwemo cha Singida utaanza mara Serikali itakapopata fedha. Aidha, kwa sasa Serikali inaendelea kuwasiliana na washirika wa maendeleo ili kuweza kupata fedha za kujenga viwanja hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo hayo hapo juu, namuomba Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu na wananchi wa Singida waendelee kuvuta subira kwani Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina nia ya dhati ya kujenga kiwanja hicho cha Singida. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO K.n.y. MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza maboma ya Zahanati ya Ufana, Kinyampembe, Mpeti, Misake, Mlandala, Kaugeri na Mtavira ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi kwa zaidi ya miaka mitano sasa katika Jimbo la Singida Magharibi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kujenga vituo vya kutolea huduma za afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha utoaji wa huduma za afya ya msingi kwa wananchi ikiwemo ukamilishaji wa maboma ya zahanati. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 28.2 za ruzuku kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 564 katika Halmashauri zote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Disemba, 2021 tayari Serikali imepeleka shilingi bilioni 15.4 katika Halmashauri nchini kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti iliyopangwa ambapo kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 200 kimepelekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kutekeleza ukamilishaji wa maboma ya zahanati nne za Ufana, Kinyampembe, Misule na Makotea. Aidha, Halmashauri kutumia mapato ya ndani imetenga shilingi milioni 50 kukamilisha boma la zahanati ya Kaugeri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka mpango wa kukamilisha ujenzi wa maboma ya zahanati yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi. Aidha, Serikali inazielekeza Halmashauri zote nchini kuendelea kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati hizo ili ziweze kutoa huduma tarajiwa kwa wananchi, ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Singida hadi Sepuka kuelekea Kizaga itajengwa kwa kiwango cha lami katika Wilaya ya Ikungi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa kina na maandalizi ya nyaraka za zabuni kwa barabara ya Sabasaba – Sepuka – Ndago hadi Kizaga yenye urefu wa kilometa 77.6 na inategemea kutangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami mwishoni mwa mwezi Novemba, 2022. Ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga majosho ya mifugo katika Kata za Makilawa, Igelansoni, Iyumbu, Ighombwe, Mgungira na Mwaru Wilayani Ikungi?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu Mbunge wa Singida Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, Wizara inakamilisha ujenzi wa majosho 168 katika Halmashauri 80 kwa gharama ya shilingi bilioni 3.033. Aidha, kati ya majosho hayo, majosho mawili yanajengwa katika Kata za Mgungira na Siuyu katika Halmashauri ya Ikungi.

Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua uhitaji mkubwa wa majosho katika maeneo mbalimbali nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara itaendelea na ujenzi wa majosho katika maeneo yenye uhitaji yakiwemo ya Jimbo la Ikungi. Ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaongeza madarasa katika Shule ya Msingi Puma kutokana na kuzidiwa na idadi ya wanafunzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa kutokana na utekelezaji wa sera ya elimu bila ada, kumepelekea ongezeko kubwa la wanafunzi na uhitaji wa miundombinu ya shule ikiwemo madarasa. Hatua mbalimbali za kukabiliana na uhitaji wa miundombinu ya shule zinaendelea kufanywa na Serikali katika halmashauri, manispaa na majiji hapa nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule ya Msingi Puma, Katika bajeti ya mwaka 2023/2024 shule hii imetengewa madarasa mawili sambamba na ufunguzi wa shule shikizi Isalanda ambayo itasaidia pia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya msingi Puma.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Singida – Sepuka - Ndago hadi Kizaga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandaasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Singida kuanzia Sabasaba – Sepuka – Ndago – Kizaga yenye urefu wa kilometa 77.6 amepatikana na mkataba wa ujenzi unatarajiwa kuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023, ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawasilisha Muswada wa Sheria unaozuia Polisi kukamata na kuwashikilia watuhumiwa kabla ya kukamilisha upelelezi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura Na. 20 kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 1 ya mwaka 2022 mwezi Machi, 2022, ambapo kwa sasa Sheria imeweka masharti ya kutofungua mashtaka mpaka upelelezi utakapokamilika, isipokuwa kwa makosa makubwa tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)