Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Daniel Edward Mtuka (20 total)

MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona, naomba na mimi niulize swali dogo la nyongeza;
Kwa kuwa, Mji wa Manyoni ni mkongwe ni sawa na ule wa Mpwapwa na matatizo ni makubwa, mitambo ya maji iliyopo sasa hivi imezeeka sana. Sasa hivi inakisiwa kwamba asilimia 35 tu ya wananchi wa Manyoni ndiyo wanapata maji na asilimia 65 hawapati maji;
Je, Serikali inatoa kauli gani ya matumaini kwa wananchi wa ule Mji wa Manyoni Mjini, kwa sababu shida ya maji ni kubwa. Maeneo ya Sayuni, Mwanzi, Kipondoda, Mgulang‟ombe, Mwembeni, Manyoni Mjini, Majengo hali ni mbaya akina mama wanapata shida sana, Serikali ina kauli gani kuhusu shida hii ya maji katika Mji wa Manyoni. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIJAI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumeishaelekeza kwamba sasa hivi katika awamu ya pili ya program ya maendeleo ya maji, tutahakikisha kwamba miundombinu ya zamani inafanyiwa utafiti, tunatoa fedha na tunakarabati ili mfumo wa maji ule uweze kuendelea. Pamoja na kukarabati tutapanua kwa sababu katika hayo maeneo kwa mfano, kama mtambo ulijengwa muda mrefu miaka ya 1960 au 1970 wakati ule wananchi walikuwa ni wachache, sasa hivi wananchi wameongezeka, huduma za binadamu vilevile zimeongezeka kwa hiyo mahitaji ya maji yameongezeka. Hivyo, pamoja na kukarabati hiyo mifumo tutahakikisha tunaipanua ili kuhakikisha kwamba huduma ya maji inakuwa ya kutosheleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane pamoja na Halmashauri yako, ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti wa kuchimba mabwawa. Kama vile Itigi Serikali imekamilisha bwawa na ninayo taarifa bwawa hilo linavuja na nimeishaelekeza kwamba wataalam waende kuhakikisha wanaziba ili tuwe na maji ya kutosha.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa muda niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa hali ya maji Manyoni ni tete kwa watu na kwa mifugo. Tunajua bado taratibu za mkopo zinaendelea. Wakati wa Mkutano wa Tatu, aliyekuwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba wakati anawasilisha hotuba yake ya bajeti alisema analitambua suala la ukame na hasa kwenye maeneo yale kame na kuna utaratibu Wizara ya Kilimo itawasiliana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa waweze kupata kibali…
MHE. DANIEL E. MTUKA: Nakuja kwenye swali. Barua ile ilikuwa imeshaandikwa kwa maana ya mawasiliano ya Wizara mbili ya Kilimo na Wizara ya Ulinzi. Sasa swali, Wizara ya Ulinzi au Serikali inatoa majibu gani kuhusiana na mawasiliano ya Wizara ya Kilimo ili kuweza kuruhusu yale magreda kwenda kutuchimbia mabwawa kwa ajili ya watu na mifugo kwa ajili ya umwagiliaji? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, naona Mheshimiwa Mbunge pamoja na kuuliza swali la nyongeza anajaribu kutushauri Serikali kutumia Wizara na taasisi zilizopo ndani ya Serikali kushughulika tatizo hilo. Ningeshauri tu tuwasiliane naye halafu tuweze kujua tunaweza kuunganishaje hizo taasisi katika kutatua tatizo lake. (Makofi)
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Manyoni kuna barabara ya kutoka Manyoni kwenda Sanza. Tatizo la Mto Sanza ni sawa kabisa na tatizo lililoko kule Morogoro Kusini. Daraja hili ni kubwa, linaunganisha Manyoni na Dodoma kwa jirani yangu Mheshimwa Badwel. Daraja hili lilijengwa mwaka 2014 na kukamilika lakini mwaka 2015 mvua iliponyesha likabomoka na sina mawasiliano na jirani yangu hasa wakati mvua zikinyesha:-
Je, ni lini Serikali itatujengea daraja hili?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge ambaye ni kati ya Wabunge wa Mkoa wa Singida walio…
MHE. DANIEL E. MTUKA: Manyoni Mashariki.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Wa Mkoa wa Singida, Jimbo la Manyoni Mashariki ambaye ni makini kama walivyo Wabunge wengine katika kufuatilia masuala ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami kwa kweli nichukue nafasi hii kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufuatilia mahitaji ya wananchi wa Manyoni Mashariki. Kwa kweli huwa anaenda mbali zaidi, anafika hata maeneo ya Bahi yale ambayo yanaungana na maeneo yake na Manyoni Magharibi, yeye pamoja na Mheshimiwa Mama Mlata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana na kwa kweli nawapongeza sana kwa juhudi hizi zote wanazozifanya. Nawaombeni muendelee kutuunga mkono katika dhamira yetu ya kuwajengea Watanzania miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, hivi ninavyoongea CEO wa TANROADS Taifa, Ndugu Patrick Mfugale, ananisikia na atahakikisha anawasiliana na wasaidizi wake wa mikoa hii miwili; Dodoma na Singida ili waweze kuangalia hili eneo ambalo kwa taarifa ya Mheshimiwa Mbunge mawasiliano yamekatika. Nilisema kwamba baada ya mvua kukatika, mkazo wetu mkubwa kwa sasa ni kurudisha mawasiliano katika maeneo yale yaliyokatika. Kwa hiyo, eneo hili ni mojawapo kama ambavyo amelisema; hao viongozi wa TANROADS nawataka walishughulikie haraka sana ili warudishe mawasiliano na wananchi waendelee kupata huduma za usafiri.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba na mimi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa wakulima wa eneo langu Manyoni Mashariki eneo la Makuru, Heka na Mkwese wana kilio kikubwa sana cha mapunjo ya bei ya tumbaku kutokana na hawa wapangaji wa madaraja (classifiers) kutokuwa waaminifu na pia kutokana na utitiri/wingi wa madaraja ya tumbaku, yapo 72. Waziri anatoa tamko gani kusimamia hawa classifiers vizuri kwa maana ya kutoa elimu kwa wakulima?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, ni lini Serikali…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtuka swali la nyongeza huwa ni moja, Mheshimiwa Waziri.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Naomba majibu tafadhali.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wako classifiers ambao siyo waaminifu, lakini katika kumwajiri mtu huwezi ukajua mara moja kwamba huyu siyo mwaminifu ni mpaka pale anapoingia kazini ndiyo tabia zake za hovyo hovyo zinaanza kuonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na Wizara ilichokifanya sasa hivi ipo katika utaratibu na imekwishatoa idhini au kibali cha ajira kwa Bodi ya Tumbaku iajiri classifiers wengine 35 katika mwaka huu wa fedha unaokwisha ili kuongeza idadi ya classifiers hawa wafike kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya jambo ambalo limekuwa linasababisha kufanya vitu ambavyo siyo vya kiadilifu katika kukagua madaraja ya tumbaku ni kwa sababu classifier wanakuwa wachache, anahitajika maeneo mengi kwa hivyo anaanza kutumia ule uhaba wao kufanya mambo ya kuomba kitu hiki au kingine. Kwa maana hiyo, hawa watakapokuwa wameajiriwa tunatarajia kwamba angalau hilo zoezi la kutambua madaraja ya tumbaku litakwenda bila vikwazo au tabia hizo za kuomba rushwa kwa wenye tumbaku.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni ombi, baadhi ya vitongoji ndani ya Mji wangu wa Manyoni havijapata umeme mpaka sasa hivi ninavyozungumza, ukitembea usiku utakuta pale umeme unawaka, pale umeme hauwaki, karibu nusu ya Mji wa Manyoni upo gizani na tatizo kubwa ni gharama za nguzo kuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kwa bajeti ya kuanzia mwaka huu imtengee fedha Meneja wa TANESCO wa Wilaya ya Manyoni angalau aweze kununua nguzo na sisi tutaweza kuchangia gharama nyingine ndogo ndogo, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mkandarasi anayetekeleza Mradi wa REA II katika Tarafa ya Nkonko yenye vijiji 25 hajakamilisha mradi huu mpaka sasa hivi ambapo ilitakiwa aukamilishe Septemba, 2015. Pamoja na juhudi za Mbunge, Naibu na Waziri kufuatilia zimegonga mwamba, mkandarasi huyu anaonekana ni mzembe na mvivu. Wananchi wa Manyoni wamenituma, wanasema hawataki kumuona hata kwa sura yule mkandarasi, Kampuni ya Spencon.
Je, ni lini Serikali itatuletea mkandarasi mwingine kwa sababu yule hatumtaki tena, hatufai kabisa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mtuka kwa jinsi anavyofuatilia maslahi ya wananchi kwa upande wa umeme. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Manyoni Mashariki kwamba ni kweli kabisa vile vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme, kulikuwa na shida ya nguzo kwa mkandarasi lakini nimhakikishie kwamba tumeanza kutekeleza Mradi wa REA III kuanzia tarehe 6 Januari, 2017. Nitumie nafasi hii kuwaarifu Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na wananchi kwamba utekelezaji wa REA III umeanza tangu tarehe 6 Januari, 2017 na utaendelea kutekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo.
Mheshimiwa Spika, tumeanza kutekeleza Mradi wa REA katika mikoa sita ikiwemo Mikoa ya Pwani, Tanga, Mara, Iringa, Arusha pamoja na Mbeya. Kadhalika tumeanza kutekeleza mradi huo katika mikoa mingine ambayo ilikuwa kwenye mikoa mama hapo awali ikiwemo Mkoa ya Songwe pamoja na Njombe.
Mheshimiwa Spika, sasa ili nijielekeze kwa swali la Mheshimiwa Mtuka, nimhakikishie vile vijiji 75 ambavyo havijapata umeme kikiwemo Kijiji chake cha Simbangulu, Makutupora, Mwembela na London vitapata umeme. Kwa hiyo, namhakikishie Mheshimiwa Mtuka kwamba vijiji vyake 75 vilivyobaki vitapata umeme bila mashaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na mkandarasi Spencon, nichukue nafasi hii kusema rasmi kwamba yule mkandarasi amesimama kazi tangu mwezi Novemba. Ni kweli kati ya wakandarasi tuliokuwa nao hakufanya kazi kwa ufanisi na kama Serikali tumeshachukua hatua. Hatua ya kwanza tuliyochukua tumeshikilia mshahara wake wa mwezi Novemba. Hatua ya pili, tumepeleka shtaka rasmi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tumshtaki mahakamani na hatua ya tatu hatumpi kazi tena kwenye kandarasi zinazofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatua nyingine tuliyochukua ni kuanza majadiliano na kumpeleka mkandarasi Octopus katika Mkoa wa Singida ili ianze kutekeleza mradi huu mara moja. Kwa hiyo, wananchi wa Singida watapata umeme haraka iwezekanavyo.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuunganisha mikoa miwili ni jambo kubwa sana; na kwa kuwa barabara ya Manyoni - Sanza pamoja na ile ya Chali - Igongo zote zina hadhi ya TANROADS, na tatizo kubwa ni Daraja la Mto Sanza; daraja hili muda mrefu limekuwa ni wimbo. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa daraja hili ili sasa kuunganisha mikoa miwili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kufuatilia suala hili, kwa sababu sio mara ya kwanza kulisema hapa. Amemuona Waziri wangu kwa ajili ya utekelezaji wa suala hili. Utakumbuka tulikuambia na ninaomba kupitia nafasi hii wananchi wako wajue kwamba daraja hili ni kipaumbele katika Wizara yetu katika bajeti itakayofuata, labda kama vyanzo vya fedha mtavipunguza, lakini kama hamtavipunguza tuna uhakika tutapata fedha za kutosha kwenye bajeti ya Wizara kuhakikisha na Daraja hili la Mto Sanza tunaliingiza kwenye bajeti.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la gari la wagonjwa Jimbo la Nsimbo ni sawasawa kabisa na tatizo hili linalotukabili Wilaya ya Manyoni. Tunayo Hospitali kubwa ya Wilaya pamoja na vituo viwili vya afya vya Nkonko pamoja na Kintinku. Magari tuliyonayo ni chakavu sana na kumekuwa na matukio mengi ya kubeba wagonjwa na magari yanaharibika njiani mpaka kulala njiani, inabidi utoe gari sasa kutoka Manyoni Mjini kwenda kufaulisha wale wagonjwa.
Je, ni lini Serikali sasa itatupatia nasi angalau gari la wagonjwa kwa Wilaya ya Manyoni ukizingatia hali halisi ya Manyoni pale, kuna ajali nyingi zinatokea kwenye ule mlima wa Saranda Sukamahela?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lugha ya kwetu sisi, ndiyo maana mwanzo nilianza na kile kitu kinaitwa kingilambago. Nilieleza pale awali kwamba, lazima hili jambo tuliainishe katika suala zima la mpango wetu wa bajeti. Mheshimiwa Mtuka naomba nikuhakikishie kwa sababu nami nilifika pale Manyoni, kwanza nilitoa maelekezo katika hospitali yako kwa sababu, hata hili suala la referral ni lazima maeneo yetu watu wafanye kazi vizuri, niligundua baadhi ya uzembe pale katika watalaamu wetu, nikatoa maelekezo. Jambo hili naomba nikuhakikishie katika mpango wako wa bajeti 2018/2019 naomba liainishwe wazi na likifika kwetu katika Ofisi ya TAMISEMI tutalipa nguvu ili kwamba eneo la Manyoni pale tupate gari la wagonjwa.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Niipongeze pia Serikali ni kweli majuzi tumepokea ugeni na shughuli hiyo imeanza mara moja. Hiyo ndiyo Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kuna nyumba zinatakiwa kubomolewa maeneo ya Kintinku, Chikuyu, Maweni barabara kuu zimewekewa alama ya kijani tangu 2013 na kijani maana yake ni kwamba kuna malipo ya fidia, lakini hawajalipwa fidia, Serikali inasema nini? Ni lini wananchi hawa watalipwa?
Samahani Mwenyekiti, swali la pili. Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu 2013 tuliomba barabara inayoanzia Chikuyu – Chibumagwa - Mpandagani - Ikasi ambayo ina urefu wa kilomita 84 ipandishwe daraja lakini tangu kipindi hicho naona ni kimya Serikali haijaleta majibu. Hata hivyo, tarehe 17/3/2015 wataalam kutoka Wizara husika walikuja kukagua barabara hii. Tulitegemea majibu yatoke lakini mpaka sasa hivi ni kimya. Ni lini sasa Serikali itapandisha hadhi barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Kintinku - Chikuyu na Maweni ambayo yapo katika barabara kuu yamewekewa alama ya ‘X’ ya kijani kama ambavyo tumeweka alama za ‘X’ za kijani na nyekundu katika barabara nyingi sana humu Tanzania tokea Sheria ile ya 2007 ilipopitishwa na Kanuni ya 2013 ilipopitishwa. Maana ya zile ‘X’ ni kwamba tunakujulisha eneo hilo liko ndani ya hifadhi ya barabara kwa mujibu wa Sheria mpya ya mwaka 2007 lakini eneo lako liko kati ya mita 22.5 ambayo ni hifadhi ya barabara kwa sheria ya zamani na mita 30 kwa sheria ya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu upanuzi huu umefanyika wakati wewe tayari ulishajenga unastahili kulipwa fidia lakini unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kwamba huongezi maendeleo yoyote katika eneo hilo, hiyo ndiyo maana yake. Sasa fidia inakuja wakati eneo hilo linapohitajika. Eneo hilo linapohitajika kupanua barabara tunawalipa fidia kabla hatujaanza kazi ya upanuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama ambavyo yeye alisimama na mimi nikasimama, barabara inayoanzia Chikuyu - Chibumagwa na kuendelea ombi la kwamba ipandishwe hadhi nimwombe tu avute subira majibu yatolewa. Tuna maombi mengi tu yamekuja na mara yatakapokamilika tutatoa taarifa barabara zipi zimepandishwa hadhi na zipi hazikupandishwa hadhi kutokana na vigezo ambavyo tumejiwekea wenyewe kwa mujibu wa sheria.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nina maswali mawili ya ngongeza. Hali ya upatikanaji wa maji hasa katika eneo la Bonde la Ufa katika Jimbo la Manyoni Mashariki ni ngumu sana, hivi ninavyozungumza mifugo inahangaika, watu wanahangaika, akinamama wanalala kwenye visima ambavyo havina uhakika wa kupatikana kwa maji, hali ni ngumu sana kwa kweli. Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba litawekwa katika kipaumbele cha bajeti inayokuja, ninaomba tu ni ombi, kwa emergency, kwa hali ambayo nimeielezea hii, hali ni ngumu, naomba liingizwe kwenye bajeti ya mwaka unaofuata.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Kata ya Sorya Wilayani Manyoni, kwenye Jimbo langu katika harakati za kuhangaika kuwatafutia ajira vijana na akina mama tumetenga eneo, zaidi ya eka 400 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na tumechimba visima vitatu kwa fedha yetu wenyewe. Tuna shida ya umeme kwa ajili ya kufunga pampu za kutoa maji ili tuweze kumwagilia.
Je, Serikali inaweza kutusaidia sasa kupeleka umeme kwenye visima vile ili kunusuru wananchi hawa wanaohangaika, hasa vijana, tuweze kumwagilia maeneo haya na tuweze kujinusuru kwa suala la njaa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie kama tulivyoji-commit kwenye jibu la msingi, kwamba tutaweka kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa hiyo naomba nimhakikishie kwamba tutafanya hivyo kwa sababu tumeshatoa jibu la namna hiyo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu ekari 400 ambazo mmepanga kuendeleza kilimo cha umwagiliaji; nilipokee ombi lake lakini tutaangalia uwezo wa bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu wa fedha, kama itawezekana tutasaidia, lakini vinginevyo tutaangalia katika bajeti ya mwaka utakaofuata.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nina maswali mawili ya ngongeza. Hali ya upatikanaji wa maji hasa katika eneo la Bonde la Ufa katika Jimbo la Manyoni Mashariki ni ngumu sana, hivi ninavyozungumza mifugo inahangaika, watu wanahangaika, akinamama wanalala kwenye visima ambavyo havina uhakika wa kupatikana kwa maji, hali ni ngumu sana kwa kweli. Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba litawekwa katika kipaumbele cha bajeti inayokuja, ninaomba tu ni ombi, kwa emergency, kwa hali ambayo nimeielezea hii, hali ni ngumu, naomba liingizwe kwenye bajeti ya mwaka unaofuata.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Kata ya Sorya Wilayani Manyoni, kwenye Jimbo langu katika harakati za kuhangaika kuwatafutia ajira vijana na akina mama tumetenga eneo, zaidi ya eka 400 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na tumechimba visima vitatu kwa fedha yetu wenyewe. Tuna shida ya umeme kwa ajili ya kufunga pampu za kutoa maji ili tuweze kumwagilia.
Je, Serikali inaweza kutusaidia sasa kupeleka umeme kwenye visima vile ili kunusuru wananchi hawa wanaohangaika, hasa vijana, tuweze kumwagilia maeneo haya na tuweze kujinusuru kwa suala la njaa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie kama tulivyoji-commit kwenye jibu la msingi, kwamba tutaweka kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa hiyo naomba nimhakikishie kwamba tutafanya hivyo kwa sababu tumeshatoa jibu la namna hiyo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu ekari 400 ambazo mmepanga kuendeleza kilimo cha umwagiliaji; nilipokee ombi lake lakini tutaangalia uwezo wa bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu wa fedha, kama itawezekana tutasaidia, lakini vinginevyo tutaangalia katika bajeti ya mwaka utakaofuata.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Niipongeze tu Serikali kwa jibu zuri lenye matumaini hasa kwa wananchi wa Manyoni wanaoishi katika Bonde la Ufa katika maeneo ya Unyambwa, Unyangwila na Mgunduko. Hata hivyo, nina swali dogo la nyongeza pamoja naombi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ombi, naomba katika bajeti hii inayofuata ya 2018/2019 nione bajeti ya uchimbaji wa bwawa hili imetengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza ni kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imebainisha maeneo katika vijiji vitatu kwa ajili ya kuchimba mabwawa madogo. Vijiji hivi ni Makutupora, Winamila pamoja na Igwamadete. Je, Serikali itakuwa tayari kutuuunga mkono kama Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya kuwatetea wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa napenda nimueleze Mheshimiwa Mbunge, sisi ni Wizara ya Maji na jukumu letu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji. Nimhakikishie katika Bwawa lile la Mbwasa tutawaweka katika bajeti 2018/2019 ili kuhakikisha wananchi wake wanapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa lingine pamoja na jitihada ya kuainisha maeneo kwa ajili ya mabwawa, nataka nimhakikishie Serikali na Wizara yetu pamoja na wadau wa maendeleo tumekuwa tukishirikiana katika kuhakikisha tunachimba mabwawa maeneo yenye ukame. Sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo, tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge katika kuhakikisha maeneo yenye uhitaji wa mabwawa wanapata mabwabwa ili waondokane na ukame kwa kupata maji. (Makofi)
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo kubwa sana katika nchi hii hasa katika utekelezaji wa miradi mikubwa, mkandarasi kupewa Mikoa zaidi ya miwili ama mitatu. Jambo hili limekuwa likiifanya miradi kuchukua muda mrefu, kwa mfano miradi ya REA.
Je, hatuna wakandarasi wa kutosha kwa mfano katika miradi ya REA ili kila mkoa uwe na mkandarasi mmoja kuokoa muda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miradi ya REA kuna sababu maalum ya kufanya hivyo na imetokana na uzoefu wa nyuma. Lakini kimsingi katika miradi ya masuala ya ujenzi iwe majengo, barabara au reli tunafuata qualificatio/sifa ambazo huyu mkandarasi amefuata na kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi inavyotuongoza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tufuate hivyo, inawezekana kabisa mkandarasi wa Mkoa mwingine akapata kazi mkoa mwingine ni kitu cha kawaida kabisa kama ilivyo mkandarasi wa nje ya nchi anapopata ndani ya nchi yetu ni kitu cha kawaida kinachoangaliwa ni sifa ya mkandarasi aliyeomba hiyo kazi na kwa mujibu wa taratibu za zabuni.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Huu ni ubunifu mkubwa na wa kupongezwa kwa wananchi wa Manyoni Mashariki kwamba tuwe na eneo sasa litambuliwe la katikati ya nchi, na kwa sababu taarifa za awali zinaonyesha kwamba eneo hili liko kwenye Manyoni Mashariki. Nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa Serikali imeona umuhimu wa kulitambua, kulipima na kulitangaza eneo la katikati ya nchi kwa lengo la kukuza utalii; na kwa kuwa wananchi wa Manyoni wako tayari kushirikiana na Serikali katika kuliendeleza eneo hilo pamoja na kujenga mnara mrefu ambao utawekwa taa au bendera ya Taifa.
Je, Waziri anaweza kutoa maelekezo sasa hivi hapa ndani amuagize Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani aanze kazi hiyo mara moja ya kulitambua eneo hili? (Makofi)
(b) Kwa kuwa lengo kubwa hapa ni kukuza utalii na kuongeza vivutio vya watalii, tunayo hazina ya mali kale, kubwa eneo la Kilimatinde pale Manyoni.
Je, Waziri na Maliasili na Utalii atakuwa tayari kufuatana na Mbunge kwenda kuona eneo hilo ambalo ni hazina kubwa ya kumbukumbu za biashara ya utumwa pamoja na ngome za wakoloni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza amesema je, niko tayari pengine kutoa tamko hapa, ili Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani aende aanze kufanya kazi hiyo; nadhani katika jibu langu la msingi nimesema kwamba Wizara sasa tayari inaweka mikakati ya kuweza kufanya ufatiliaji wa karibu, kwa sababu tumeona kuwa na eneo ambalo linatambulika kama ndilo center (katikati) ya nchi si tu kwamba tutatambua eneo hilo na kuliacha kama lilivyo, lakini bado ni sehemu ambayo inaweza ikatumika pia kama utalii. Ndiyo maana nimesema uendelezaji wa eneo hilo, unaweza ukafanyika katika mustakabali wa kutaka patambulike.
Mheshimiwa Spika, na kwa sababu wananchi wa Manyoni Mashariki wanasema wako tayari kushirikiana mara zoezi hilo litakapoanza tutawashirikisha kwa pamoja ili tuweze kuona suala lile linafanyika katika umakini zaidi ili kuweza kupafanya pawe kivutio cha kweli.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili la kuweza kutambua vivutio vilivyoko katika maeneo ya Kilimatinde, nadhani hili ni la Wizara ya Utalii, lakini kwa sababu wote tunajenga taifa moja, tutashirikiana na wenzetu kuweze kuona maeneo hayo yanatambulika na yanaingia katika historia, lakini pia kuweka kama vivutio vya utalii ili paweze kufikika pia na patakuza soko la utalii kwa nchi yetu.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII:
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Manyoni.
Mheshimiwa Spika, Mbunge wa Manyoni tunamshukuru sana kwa kutupa taarifa ya malikale hizo ambazo ziko katika eneo hilo na ninataka nimhakikishie kwamba tuko tayari kutembelea eneo hilo na kufanyia kazi vivutio hivyo, ahsante. (Makofi)
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nami niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kushirikiana na Mbunge mwenzangu wa Bahi, Mheshimiwa Badwel, tumeweza kuchonga mfereji kutoka Mto Bubu kwenda kwenye vijiji vyetu kwenye skimu za umwagiliaji kwa kushirikiana na wananchi na Mfuko wangu wa Jimbo. Je, Serikali itakuwa tayari kutusaidia kuboresha miundombinu kwa maana ya mifereji midogo pamoja na mabanio katika Vijiji vyangu vya Lusilule, Udimaa, Ndamloi na Igose?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mtuka pamoja na Mheshimiwa Badwel wa Bahi kwa mapenzi ya dhati kwa wananchi wao katika kuhakikisha wanawasaidia. Sisi kama Wizara ya Maji katika kuwaunga mkono, hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha tunawasaidia ili wananchi wao waweze kupata miundombinu mizuri.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nampongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, utetezi wa mkandarasi kwamba kulikuwa na changamoto za kupata vibali vya ujenzi kwa kweli haina mashiko kabisa kwa sababu mimi kama Mbunge na Mkurugenzi wangu tulishirikiana na mkandarasi huyu vibali vikapatikana kwa muda mwafaka na akajenga minara miwili ikakamilika pamoja na kujenga msingi wa mnara mmoja wa tatu. Ni muda wa mwaka mmoja na nusu sasa minara hiyo haijawashwa. Ni lini atakamilisha kazi hii kwa sababu tunahitaji mawasiliano Manyoni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, utoaji wa huduma za mawasiliano umeligawa jimbo langu, kwa mfano, Kata ya Makulu na hasa Kijiji cha Hika hakina mawasiliano kabisa hata upande juu ya mti huwezi kuwasiliana na watu na unakuwa umeshajitenga na dunia kabisa.
Je, ni lini Serikali italeta huduma hii ya mawasiliano katika kata hii, hasa katika Kijiji cha Hika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inazo taarifa za kuchelewa kuwashwa kwa minara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja katika eneo hili la Sanza na Sasilo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi unaokuja hii minara hii itawashwa. Kwa hiyo nakuhakikisha Mheshimiwa na nikupongeze sana kwa kufuatilia juu ya suala hili na niwahakikishie wananchi kwamba sasa watapata mawasiliano muda siyo mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, niseme tu kwamba eneo hili la Makulu Mheshimiwa Mbunge amelitaja kwamba tunayo orodha ya vijiji vingi ambavyo tayari viko kwenye hatua sasa ya kuweka minara tunavyo vijiji 369 orodha ninayo hapa Mheshimiwa Mbunge. Lakini pia tunakamilisha hatua za manunuzi mwanzoni mwa mwezi ujao tutakuwa na orodha nyingine mpya ya vijiji vingi tu ambavyo tutaenda kujenga minara.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha maeneo ambayo yana shida ya minara na mawasiliano hafifu tunaendelea kuyaboresha ili wananchi Watanzania kwa ujumla waweze kupata mawasiliano ambayo ni muhimu katika harakati za maendeleo.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niulize swali la nyongeza. Kampuni ya East Africa Fossils Limited inakamilisha kazi ambayo iliachwa na Spencon ya kupeleka umeme awamu ya pili katika Tarafa ya Nkoko, Jimbo langu la Manyoni Mashariki. Kutokana na kasi kubwa ya kampuni hii kumekuwa na uhaba mkubwa sana wa nguzo za umeme. Mpaka navyozungumza hapa wameshachimbia mashimo karibu kilomita 10 nguzo hamna, kila wanapoulizwa wanasema Mufindi imezidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini nguzo zitapelekwa katika kampuni hii ili tuweze kukamilisha suala la umeme katika Tarafa ya Nkoko?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampa pole kwa msiba alioupata hivi karibuni lakini tunafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa sana na Mheshimiwa Mtuka na ana kata nne ambazo hatujazigusa. Mkandarasi ameagiza nguzo 2,278 na amenipa taarifa kwamba kuanzia wiki ijayo nguzo zitaanza kwenda site. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mtuka kwamba maeneo yote ya kata zake 12 na hizi nne tulizoongeza yatapelekewa umeme kwa sababu sasa nguzo zinapatikana. (Makofi)
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kw akunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Manyoni hususan Jimbo la Manyoni Mashariki tunavyo vivutio vingi sana vya utalii. Kwa mfano, tunazo kumbukumbu ya kituo kikubwa cha msafara wa watumwa wa njia ya kati kuanzia Ujiji, Unyanyembe kwenda Bagamoyo, lakini pia tunayo kumbukumbu ya ngome kuu ya Wajerumani iliyotumika kupambana na Mtemi Mkwawa wa huko Uheheni; lakini pia tuna jiwe la picha ya Bikira Maria kule Iseke. Je, Serikali iko tayari kusaidia kutangaza vivutio hivi ili kuinua kiwango cha ajira? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, mimi mwenyewe juzi Jumamosi nilikuwa kule Wilaya ya Manyoni na nimetembelea katika maeneo yote aliyoyataja na kuona utajiri mkubwa ambao Wilaya ya Manyoni inao hasa katika haya maeneo ambayo ameyataja.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ambazo tunategemea kuchukua kama Wizara ni kwamba tutakwenda tutatangaza sasa vivutio vyote vile pamoja na historia nzuri ambayo ipo pale. Kuna jiwe moja ambali linajulikana kama jiwe la mjusi lakini zaidi ya hapo tumefika sehemu ambayo tunaita ndipo kitovu cha nchi hii yaani katikati ya Tanzania. Kuna maeneo mengi sana yenye vivutio vizuri sana kule Manyoni ambayo tutayatangaza sanjari na hatua ambazo tunazichukua katika kutangaza utalii katika maeneo yote nchini. (Makofi)
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nami niulize swali moja dogo la nyongeza. Hospitali ya Wilaya ya Manyoni pamoja na kuhudumia Wilaya ya Manyoni lakini inahudumia Wilaya ya Ikungi, Sikonge, Wilaya ya Bahi, Wilaya ya Chemba imezidiwa sana na haina kabisa gari la wagonjwa. Je, ni lini sasa Serikali itaipatia hospitali hii ya Wilaya gari la wagonjwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakubaliana Wabunge wote kwamba, nia ya Serikali na jinsi ambavyo inatenda katika kupunguza adha ya wagonjwa kwa maana ya uwepo wa magari sote ni mashuhuda tumeliona. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pale ambapo nafasi ya kifedha itaruhusu tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba maeneo yale yote ambayo yanahitaji kupelekewa gari za wagonjwa tunapeleka na kwa kufuata vigezo kama ambavyo nilivyotangulia kujibu katika swali langu la msingi.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika,ahsante kwa kunipa muda niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza niipongeze sana Serikali na majibu imejibu vizuri, imepeleka faraja kwa wananchi wa Jimbo la Manyoni hasa Manyoni Mashariki, niombe kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara hii tunayoizungumzia ya Chikuyu Majiri-Ikasi, kipande kile cha mwisho kabisa cha kilometa 40kwa maana ya Majiri kwenda Ikasi, ni miaka zaidi ya 40 hakijapata fedha ya matengenezo ya mara kwa mara.

Naomba tu kuhakikishiwa na kuwahakikishia wananchi wangu wa Manyoni ni lini au ni bajeti ya mwaka huu watatoa fedha ya kutengeneza barabara hii maana ni miaka zaidi ya 40? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtuka Motokari kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la nyongeza anasema miaka zaidi ya 40 barabara hii haijatengewa fedha yoyote, wakati mwingine mipango ya Mwenyezi Mungu inakuwepo ili mtu fulani aweke alama, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mtuka laiti barabara hiyo ingekuwa imetengenezwa isingekuwa kwake yeye rahisi kuacha alama, naomba nimhakikishie ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa na hasa baada ya kujua gharama ya daraja ambalo ndiyo kubwa zaidi na yeye atakuwa ameacha alama muhimu sana kwa wananchi ambao miaka zaidi ya 40 ilikuwa haipitiki.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, uzembe na uchovu wa madereva, ubovu wa barabara, hii ni kampeni ya kila siku ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuzuia ajali lakini katika eneo hili bado ajali zinaendelea kutokea. Nilidhani labda Wizara ya Ujenzi itoe jibu la kiufundi zaidi kwa maana ya kurekebisha eneo hilo. Je, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi iko tayari kufanya usanifu upya katika eneo hilo na kufanya marekebisho ili kupunguza ajali?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ajali zimekuwa nyingi sana katika eneo hilo, kwa mfano magari ya mafuta yamekuwa yakidondoka pale na moto unalipuka, majeruhi ni wengi lakini tumekuwa na tatizo la magari ya zimamoto pamoja na ambulance.

Je, Serikali iko tayari kutuletea magari ya zimamoto pamoja ambulance katika Wilaya ya Manyoni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kujibu swali la nyongeza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba kabla ya ujenzi wa barabara katika eneo ambalo analitaja, ajali zilikuwa nyingi sana kuliko ilivyo sasa. Pamoja na ajali kuendelea kutokea, sisi Wizara ya Ujenzi baada ya ujenzi mara zote huwa tunaendelea kufanya tafiti ili kuona changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge eneo ambalo analitaja tutaweka msukumo mkubwa tuone kwa nini hizi ajali zinaendelea kutokea kutokana na hali ilivyo pale ili tuweze kuchukua hatua muafaka. Ni muhimu tu niendelee kusisitiza kama ilivyo kwenye jibu la msingi watumiaji wa barabara maeneo yote wazingatie alama za barabarani zinazowekwa kwa sababu maeneo ambayo ni hatari, sisi Wizara ya Ujenzi tumejitahidi kuweka alama kutoa tahadhali kwa watumiaji wa barabara ili muda wote tuwe salama tukiwa barabani.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Mtuka kwamba eneo hilo tutaliangalia kwa macho mawili ili tuone nini la kufanya. Hata hivyo, jambo hili lazima tushirikiane na watumiaji wengine wa barabara. Ahsante sana.