Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Daniel Edward Mtuka (9 total)

MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imepata USD 17 milioni katika mgao wa USD 500 milioni zilizotolewa na Serikali ya India kusaidia miradi ya maji kwa bajeti ya 2016/2017.
Je, ni lini fedha hizo zitaanza kupelekwa katika Halmashauri husika ikizingatiwa kuwa shida ya maji imezidi kuwatesa wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kwingineko katika nchi yetu kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwezi Julai, 2016, Serikali ya Tanzania na Serikali ya India zilifikia makubaliano ambapo Serikali ya India imekubali kuikopesha Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya miradi ya maji. Mkopo huu utatekeleza miradi katika Miji 17 ikiwemo Mji wa Manyoni.
Mheshimiwa Spika, Miji mingine itakayofaidika na mkopo huu ni pamoja na Muheza, Mradi wa Maji wa Kitaifa wa Wanging‟ombe, Makambako, Kayanga, Karagwe, Songea, Zanzibar, Mradi wa Maji wa Kitaifa wa HTM, Njombe, Mugumu, Kilwa Masoko, Geita, Chunya, Mradi wa Maji wa Kitaifa wa Makonde, Sikonge, Kasulu na Rujewa.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi ya maji chini ya mkopo huu itaanza mara baada ya kukamilisha taratibu za mkopo. Aidha, miradi hii itatekelezwa moja kwa moja na Wizara hivyo fedha hazitatumwa kwenye Miji au Halmashauri husika.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-
Watanzania wengi wanahitaji umeme mjini na vijijini lakini wanashindwa kuvuta umeme kutokana na gharama kubwa ambapo service line ni shilingi 177,000 na zaidi na gharama ya nguzo ni shilingi 337,740 na zaidi:-
(a) Kwa kuwa nguzo ni mali ya TANESCO, je, kwa nini nguzo hizi zisilipiwe na Serikali?
(b) Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka wa kupunguza service line costs kuwa shilingi 27,000 kama ilivyo kwa mradi wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, TANESCO hugharamia miundombinu ya umeme ikiwemo nguzo na vifaa vingine ili kupeleka umeme kwa wateja. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa bajeti si rahisi kupeleka miundombinu ya umeme maeneo yote kwa wakati mmoja. Kwa maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya umeme wananchi kwa hiari ya kuchangia gharama husogeza miundombinu hiyo katika maeneo ili kuharakisha huduma hiyo. Aidha, kulingana na Kanuni za Sheria ya Umeme ya mwaka 2011, wateja wanaruhusiwa kugharamia miundombinu hiyo kisha kukubaliana na TANESCO namna ya kurejeshewa malipo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa maeneo ambayo tayari yamefikiwa na huduma ya umeme, wananchi huchangia kwa kulipia vifaa muhimu ikiwemo nguzo, mita pamoja na gharama nyingine.
Mheshimiwa Spika, Serikali inagharamia Miradi ya Umeme Vijijini (REA) kwa asilimia 100 na kiasi cha shilingi 27,000 wanacholipa wananchi ili kuunganishiwa umeme katika miradi hii ni kwa ajili ya gharama ya VAT tu. Lengo ni kuhamasisha na kuwawezesha wananchi wa vijijini ili wapate huduma hiyo kwa gharama nafuu. Baada ya miradi ya REA kukamilika, wateja huunganishiwa umeme kwa kufuata taratibu za TANESCO ambapo gharama yake ni shilingi 177,000 kwa umbali usiohitaji nguzo.
Mheshimiwa Spika, gharama za kuunganisha umeme kwa wateja wa majumbani maeneo ya mijini ni shilingi 320,960 kwa umbali usiohitaji nguzo ambapo wateja hufungiwa waya na mita. Gharama za maombi ya services charge ziliondolewa tangu tarehe 01 Aprili, 2016 lengo likiwa ni kupunguza gharama kwa wateja.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-
Eneo la Muhalala katika Wilaya ya Manyoni ni moja ya maeneo matatu yaliyoteuliwa na Serikali kujenga vituo vya ukaguzi wa mizigo katika barabara ya kati; maeneo mengine ni Vigwaza Pwani na maeneo mawili yameshajengwa kimebaki kituo cha Muhalala tu:-
(a) Je, ni lini wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa tangu mwaka 2012 watalipwa fidia?
(b) Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Ukaguzi wa Mizigo Muhalala baada ya kituo cha Vigwaza kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali imeamua kujenga vituo vya pamoja vya ukaguzi wa mizigo inayokwenda nje ya nchi katika barabara ya Ukanda wa Kati na Ukanda wa Dar es Salaam. Katika Ukanda wa Kati vituo vitajengwa Muhalala, Mkoani Singida na Nyakanazi Mkoani Kagera chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya. Aidha, katika Ukanda wa Dar-es Salaam, vituo vitajengwa Vigwaza, Mkoani Pwani, Ruaha-Mbuyuni, Mkoani Morogoro, Makambako, Mkoani Njombe na Iboya - Mpemba Mkoani Mbeya chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 5.86 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa watu watakaoathirika na ujenzi wa vituo hivyo. Tathmini ya maeneo ya watu walioathirika na ujenzi huo katika Ukanda wa Kati yaani (Muhalala - Manyoni na Nyakanazi - Kagera) imefanyika na malipo kwa waadhirika wa ujenzi wa vituo hivyo yamefanyika na kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mkataba wa ujenzi wa vituo vilivyopo Ukanda wa Kati ulisainiwa tarehe 16 Disemba, 2016 kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mkandarasi M/s IMPRESA DI CONSTRUZIONI ING E. MANTOVANI wa Italia. Mpaka sasa mkandarasi yupo katika eneo la kazi na yupo katika hatua za awali za ujenzi wa vituo hivyo. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Septemba, 2018.
Mwasa MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-
Kwa kuwa bwawa linalotarajiwa kuchimbwa katika Kijiji cha Mbwasa, Tarafa ya Kintinku ni bwawa la kimkakati kwa wakazi wa Tarafa nzima ya Kintinku.
Je, ni lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa bwawa hilo baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ilipanga kujenga Bwawa la Mbwasa kwa kupitia Mto wa Msimu wa Luwila ikiwa ni hitaji la wananchi wa Kijiji cha Mbwasa kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo na matumizi ya nyumbani. Ujenzi wa Bwawa la Mbwasa ulikusudiwa kunufaisha pia wananchi wa vijiji vya jirani vya Mwiboo, Mtiwe na Chikuyu, lengo kuu ikiwa ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji wa zao la mpunga. Hali hii inatokana na maeneo hayo kutokuwa na uhakika wa mvua za kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, upembuzi yakinifu na usanifu wa Bwawa la Mbwasa ulifanyika kupitia Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Dodoma. Aidha, matokeo ya upembuzi huo yalibaini kuwa jumla ya shilingi 2,500,000,000 zingehitajika kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo. Hata hivyo, bajeti za maendeleo za fedha za ndani iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji ikiwemo Bwawa la Mbwasa haikutolewa na hivyo kusababisha ujenzi wa bwawa hili kutotekelezwa.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilianza kufanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa Mwaka 2002. Kwa kutambua umuhimu wa ujenzi wa mabwawa kama hatua ya kimkakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Bwawa la Mbwasa limepewa kipaumbele na litaingizwa katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza utekelezaji ili hatimaye lengo la Serikali na wananchi wa Kijiji cha Mbwasa pamoja na vijiji vya jirani kuwa na kilimo cha uhakika.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-
Bwawa linalotarajiwa kuchimbwa katika Kijiji cha Mbwasa, Tarafa ya Kitinku ni la kimkakati kwa wakazi wa Tarafa nzima ya Kintinku.
Je, ni lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa bwawa hilo baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2012/2013 Halmashauri ya Manyoni ilipanga kujenga Bwawa la Mbwasa kwa kupitia Mto wa Msimu wa Liula ikiwa ni hitaji la wananchi wa Kijiji cha Mbwasa kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo na matumizi ya nyumbani. Ujenzi wa Bwawa la Mbwasa ulikusudiwa kunufaisha pia wananchi wa vijiji jirani vya Mwiboo, Mtuwe na Chikuyu, lengo kuu likiwa na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji wa zao la mpunga. Hali hii inatokana na maeneo hayo kutokuwa na uhakika wa mvua za kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2012/2013 upembuzi yakinifu na usanifu wa Bwawa la Mbwasa ulifanyika kupitia Ofisi ya Umwagiliaji wa Kanda ya Dodoma. Aidha, matokeo ya upembuzi huo yalibaini kuwa jumla ya shilingi bilioni 2.5 zingehitajika kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.
Mheshimiwa Mwenyiti, katika mwaka wa fedha 2016/ 2017 Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilianza kufanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 kwa kutambua umuhimu wa ujenzi wa mabwawa kama hatua ya kimkakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Katika kuwezesha kilimo cha uhakika katika maeneo kame, Bwawa la Mbwasa litapewa kipaumbele katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza utekelezaji.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-
Taarifa ya Idara ya Upimaji wa Ramani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inalitaja eneo la Chisinjisa lililopo Wilaya ya Manyoni kuwa ndipo alama pekee ya katikati (center point) ya Tanzania inapatikana.
• Je, ni lini Serikali italitambua rasmi eneo hili na kulitangaza katika Gazeti la Serikali?
• Je, Serikali haioni umuhimu wa kuendeleza na kulitangaza eneo hili ili kuvutia utalii wa ndani na nje kama chanzo cha mapato?
NAIBU WAZIRI WA ARIDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali namba 474 kutoka kwa Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hakuna taarifa rasmi za kitaalam zilizobainisha kwamba Kijiji cha Chisinjisa ndipo alama pekee ya katikati (center point) ya Tanzania pamoja na wenyeji wa eneo hilo kudai kuwepo kwa alama hiyo eneo la Sukamahela.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Idara ya Upimaji na Ramani inakusudia kufanya utafiti wa kina kwa kutumia elimu ya jiometriki (geometics) ili kubaini eneo rasmi ambalo alama ya katikati (center point) ya Tanzania inapatikana.
Mheshimiwa Spika, baada ya utafiti huo kukamilika eneo la katikati ya Tanzania litatangazwa katika Gazeti la Serikali. Aidha, mamlaka zinazohusika na masuala ya utalii zitaliendeleza eneo husika ilikuvutia utalii wa ndani na nje kama zinavyofanya nchi nyingine duniani na kuongeza mapato ya Serikali.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-
Kampuni ya Simu ya Viettel (Halotel) imepewa zabuni ya kusimika minara ya mtandao wa simu katika Jimbo la Manyoni Mashariki. Kasi ya usimikaji wa minara hiyo ni ndogo; mfano Vijiji vya Hika – Sanza hakina mawasiliano ya simu kabisa:-
Je, Serikali ina mkakati gani thabiti wa kuibana kampuni hiyo ili kutekeleza mkataba wake kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Mtandao ya Viettel kuhusu utekelezaji wa mpango wa mawasiliano. Mkataba huo ulisainiwa tarehe 16 Julai, 2014 ukiwa na mpango wa kukamilisha utekelezaji wake ndani ya miaka mitatu hadi kufikia tarehe 30 Novemba, 2017. Katika mkataba huo makubaliano ya kufikisha mtandao wa mawasiliano ya simu kwenye vijiji 4,000 yalitakiwa kufanyika katika awamu tatu. Awamu ya kwanza ni kufikisha mtandao wa mawasiliano ya simu kwenye vijiji 1,800 ifikapo Novemba, 2015; awamu ya pili ni kufikisha mtandao wa mawasiliano ya simu kwenye vijiji 1,200 kwa kipindi cha Novemba, 2015 hadi Novemba, 2016 na awamu ya tatu kufikisha mtandao wa mawasiliano ya simu kwenye vijiji 1,000 kwa kipindi cha Novemba, 2016 hadi Novemba 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia tarehe 30 Julai, 2018, jumla ya vijiji 3,712 vilikuwa vimefikiwa na mtandao wa mawasiliano ya simu. Aidha, ucheleweshwaji na utekelezaji wa mradi huu umechangiwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upatikanaji wa vibali vya ujenzi wa minara hususani kwenye maeneo ya hifadhi za Serikali, mbuga za wanyama na kadhalika ambapo vibali vimekuwa havipatikani kwa wakati. Vilevile taratibu za masuala ya mazingira zinazoratibiwa na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zinachukua muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali kupitia ukaguzi wa mradi na vikao mbalimbali inaendelea kusimamia utekelezaji wa mkataba wa Kampuni ya Simu ya Viettel ili kuhakikisha kwamba makubaliano yaliyowekwa yanakamilishwa. Aidha, usimikaji wa minara kwa ajili ya mtandao wa simu katika Vijiji vya Hika, Igwamadete, Isimbanguru, Mangoli na Mafulungu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Septemba, 2018. Hivyo, baada ya kukamilika kwa minara itakayosimikwa katika maeneo hayo kipande cha barabara ya Manyoni – Hika – Sanza kitakuwa na mawasiliano ya simu.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-

Barabara ya Surungaji inayoanzia Chikuyu - Chibumagwa - Majiri – Ikasi (Kilomita 76.2) ni barabara muhimu sana inayohudumia wakazi wa bonde la ufa katika Jimbo la Manyoni Mashariki kwa kusafirisha chumvi, samaki, ufuta na alizeti:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii pamoja na daraja katika Mto Nkonjigwe.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Chikuyu- Chibumagwa –Majiri-Ikasi yenye urefu wa Kilomita 76.2 inahudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni. Katika kilomita 76.2 ni kilomita 32 tu zinazopitika majira yote ya mwaka (kilomita 14.8 ni za changarawe na kilomita 18.8 ni za udongo), kilomita 4.2 ambazo ni kutoka majirimpaka Ikasi hupitika wakati wa kiangazi pekee.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Chibumagwa-Majiri- Ikasi ilitengewa kiasi cha Sh.29,500,000.00 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo jumla ya kilomita tisa zilifanyiwa matengeneza (sehemu korofi kilomita saba na ya kawaida kilomita mbili) kuanzia Chikuyu-Chibumagwa na kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kiasi cha Sh.11,600,000.00 kimetumika kujenga makalavati (line culvert)mbili katika eneo la Mpandagani kwenye barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/20 TARURA inatarajia kufanya usanifu wa Daraja la Mto Nkonjigwe lenye urefu wa mita 35 na kina cha mita sita lililopo barabara ya Chikuyu-Chibumagwa-Majiri-Ikasi. Fedha za ujenzi zitatengwa kwenye bajeti baada ya usanifu ili tuweze kujuwa gharama halisi.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-

Kumekuwa na ajali za barabarani za kutisha katika Milima ya Sukamahela eneo la Mbwasa, Manyoni na Sekenke Shelui:-

(a) Je kwa kipindi cha miaka miwili yaani 2016 na 2017, ni ajali ngapi zimetokea katika milima tajwa?

(b) Je, ni watu wangapi wamepoteza maisha na wangapi walijeruhiwa katika kipindi hicho?

(c) Je, Serikali inatoa tamko gani ili kupunguza au kukomesha kabisa ajali katika maeneo haya ndani ya Mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya ajali 28 zimetokea katika kipindi cha miaka miwili yaani tarehe 1 Januari, 2016 mpaka tarehe 31 Disemba, 2017 katika sehemu hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya watu 33 wamepoteza maisha na jumla ya watu 26 walijeruhiwa katika kipindi tajwa.

(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inawataka madereva kuwa makini wanapoendesha vyombo vya moto barabarani na wazingatie sharia, kanuni, taratibu na alama na michoro ya barabarani. Pia waendeshe kwa kuzingatia udereva wa kujihami (defensive driving) ili kuepusha ajali, kwani ajali nyingi zinazotokea katika maeneo haya zinasababishwa na uzembe wa madereva, ubovu wa magari, uchovu wa madereva hususani kwenye uwepo wa kona kali, milima na miteremko mikali.