Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Daniel Edward Mtuka (34 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii. Pia niwashukuru wananchi wa Manyoni Mashariki kwa kura zao nyingi, kwa imani yao kubwa kwangu mimi mpaka kuniingiza katika Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema, nimepitia mapendekezo ya mpango huu, nimeyapitia vizuri sana, nikiitazama nchi yangu Tanzania, nikiwatazama Wabunge wenzangu humu ndani kama Wawakilishi wa wananchi. Mpango huu nimeuelewa vizuri, sijaona mahali pabovu. Ni sisi tu Wabunge kujazia nyama ili Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake, waende sasa kuuandaa vizuri kwa ajili ya kuja kuuwasilisha kipindi kijacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kabla hata ya Mpango huu kuanza naona gari limeshaanza kuondoka na ninahisi gari hili kasi yake itakuwa kubwa. Nikimtazama dereva aliyepo ndani, Dkt John Pombe Magufuli ni dereva mahiri ametia imani Watanzania, gari litakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huu, naomba niende moja kwa moja kwenye mjadala. Baada ya kuupitia mpango huu, kuna vitu na mimi kama Mbunge ambaye ni moja ya kazi zangu naomba sasa nijazie. Mpango huu ni mzuri, utatuvusha kama tutayazingatia yote hayo. Kila mmoja kama akitimiza wajibu wake Waziri kwa maana ya Serikali watimize wajibu wao kwa kutenda na sisi tutimize wajibu wetu katika kushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kuna kipengele cha sheria, tukitazame kwa makini. Kuna sheria nyingi ambazo zinahitaji marekebisho, sheria zile ambazo zinagusa mpango huu. Sheria kwa maana ya sheria zile Principle Legislations, Sheria kubwa lakini pia sheria ndogo kwa maana Subsidiary Legislations, nikizitazama naona nyingi zina upungufu. Hazitakwenda na kasi ambayo Mheshimiwa Rais na Serikali yake ambayo naiona ni kubwa ni lazima kama Wabunge tuzitazame sheria hizi. Kuna Kamati zimeundwa, kuna Kamati ya Sheria na Katiba. Naomba wakae chini watizame sheria zote zinazogusa mpango huu, tafadhali sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sheria ya Manunuzi ya Umma namba Saba ya mwaka 2011, sheria hii imeijeruhi sana nchi yetu, sana tu. Naomba iangaliwe upya, Kamati hii ilete mapendekezo baadaye Waziri mhusika ailete, kama ni kurekebisha turekebishe, kama ni kufuta na kuandika nyingine ifutwe na tuandike nyingine, naomba tuiangalie ni sheria mbaya kabisa, sheria inayoruhusu kununua vifaa chakavu, sheria inayochukua mlolongo mrefu kwa muda kidogo tu. Kwa mfano, kujenga nyumba, jengo labda la ghorofa mbili, inachukua karibu miezi sita. Tunakwenda kwenye uwekezaji, tunakwenda kwenye kujenga viwanda, lazima sheria hizi ziwe rafiki, zichukue muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Mpango huu unatajwa kuinasua nchi kwenda kwenye kipato cha kati, bila kuja na sheria mahiri ya kuzuia na kupambana rushwa, tutakuwa tunatwanga maji na kuishia kulowa. Naomba sheria hii pia ibadilishwe, irekebishwe, hatuwezi kuendelea kuvumilia baada ya jalada la uchunguzi kukamilika, liende kwa DPP, ofisi inayojitegemea, Mkurugenzi wa TAKUKURU hawezi kumfuatilia huyu, kuhimiza kwamba muda ni mfupi, inachukua muda mrefu, hatuwezi kufika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama Maalum imetajwa, sheria hii itakapoundwa maana yake Mahakama Maalum kwa ajili ya makosa ya rushwa tu lazima iundwe. Nazigusa Sheria ziko sheria nyingi, Sheria za Uwekezaji, milolongo mirefu na regulations zake zina milolongo mirefu sana zinafukuza wawekezaji, lazima tuweke mazingira rafiki kwa wawekezaji wetu.
Niguse maeneo wezeshi kidogo tu angalau. Upimaji wa ardhi; hatuwezi kuzungumzia viwanda bila kupima ardhi zetu, hatuwezi! Tutumie wataalam tupime ardhi zetu. Tuainishe maeneo, maeneo ya makazi, maeneo ya viwanda, maeneo ya biashara, lazima tutenganishe. Huu ndugu zangu ndiyo ustarabu wa mwanadamu, planning. Tutumie wataalam wetu tu-plan, tu-plan Miji yetu, tuiangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa Mbeya, nilipita Kibaigwa hapa, kuna Mji mmoja unaitwa Tunduma, ka-centre kamoja kanakua kwa haraka sana. Ukiangalia nyumba zilivyomwagika kama takataka. Inaondoa ustaarabu wa mwanadamu. Tunao wataalam, tupime miji yetu. Msongamano wa Tunduma ule kama Mji ungekuwa umepimwa tusingekuwa na msongamano kama ule. Kibaigwa ule ni mji mmoja mzuri sana, lakini kama ungepimwa viruzi, ule mji ni ungekuwa ni mzuri sana. Tutumie wataalamu sasa wetu, kupima miji yetu. Pia kupima inasaidia kukusanya mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kushauri pia kwenye suala hili la mapato kwa maana ya kukusanya kodi. Hebu tuunganishe ukusanyaji wa kodi za majengo na ukusanyaji wa kodi za ardhi zilipwe katika eneo moja. Tutumie wataalam wetu wapo, GIS kwa maana Geo Information System nzuri kutambua maeneo na kuweza kukusanya kodi kwa urahisi kabisa. Tunayo deed capital kwenye majengo haya, kubwa mno kama tutatumia wataalam tutaweza ku-realise mapato makubwa sana ya kugharamia mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kidogo suala la utalii. Utalii pia ni chanzo kimoja kikubwa cha mapato yetu. Sisi Manyoni pale, Jimbo la Manyoni Mashariki tunalo eneo linaitwa Kilimatinde, eneo hili linavuma sana kwa umahiri kwa kumbukumbu nzuri ya mambo ya kale. Ukipita pale Manyoni kuna njia ya Watumwa ambao walipita karne ya 18. Tangu karne ya 18, pale alipokanyaga mtumwa mpaka leo hapaoti jani wala mti.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Daniel Mtuka muda wako tayari.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, TAKUKURU ni chombo ama Taasisi simamizi ambayo ikijengwa vizuri itasaidia sana kudhibiti rushwa, wizi, ubadhirifu na hivyo kupandisha GDP. OC haihusu mishahara bali ni kugharamia mafuta ya magari kuwapeleka Maafisa wa PCCB kufuatilia wahalifu, kutembelea miradi ambayo ipo chini ya viwango, rushwa katika idara mbalimbali, kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na kuendesha kesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nchi tumekubali kuwa rushwa ni adui namba moja Tanzania na hatuwezi kuistahimili (zero tolerance) ni lazima tupambane nayo. Hatukatai kwa Serikali kubana matumizi na kuzipeleka kwenye miradi ya maendeleo lakini hatuwezi kukwepa kuitengea fedha ya operesheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, udhibiti wa rushwa ni vita kubwa, tunahitaji kuwaweka na kuwapa kila aina ya support TAKUKURU ili wafanye kazi inavyotakiwa. Bajeti ya mwaka huu waliyotengewa kwa maana ya OC inanivunja moyo kwamba mapambano dhidi ya rushwa hayatakuwa precise.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, bajeti ya OC ya TAKUKURU kwa miaka mitano ni kama ifuatavyo:-
Mwaka 2012/2013 shilingi bilioni 15.5; mwaka 2013/2014 shilingi bilioni 15.5; mwaka 2014/2015 shilingi bilioni 16.5; mwaka 2015/2016 shilingi bilioni 14.2; na mwaka 2016/2017 shilingi bilioni 12.06.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali yangu iongeze OC kwa TAKUKURU ili ifanye kazi ya udhibiti. Sasa hivi mbinu za wala rushwa zimebadilika, idadi ya wahalifu imeongezeka kutokana na hali ya maendeleo ya nchi, watumishi wa TAKUKURU pia wameongezeka na thamani ya fedha imeshuka, hivyo kitendo cha mwaka 2012/2013, OC kupata fedha nyingi kuliko bajeti ya mwaka huu imeniogopesha sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuboresha bajeti hii ambayo imewasilishwa leo asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Wagogo tuna msemo unaosema, chigwie misi chiliwaone wenji maana yake tukio la mchana linaonekana na watu wengi. Kwa sasa Serikali inaonekana inavyofanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu wake ndugu yangu Ole-Nasha na timu nzima ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya na inaonekana tunawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye kuboresha maana naiunga mkono hoja hii ya bajeti kwa asilimia 120. Haya nitakayoyazungumza ni kuboresha tu na hasa jimboni kwangu. Katika mawasilisho ya Mheshimiwa Waziri asubuhi ametaja kitu kizuri sana, amesema anawasiliana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuweza kuazima magreda ili yakachimbe mabwawa kwenye maeneo yetu hasa vijijini ila wananchi tu watoe mchango wa mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hivyo ndivyo, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aiorodheshe Manyoni Mashariki namba moja, haya magreda tutaanza kuyatumia sisi. Tuko tayari kuchanga mafuta na Mbunge wao nasema niko tayari, natanguliza milioni tano kama mchango. Tunawajibika kuisaidia Serikali tusisubiri tu Serikali ihudumie kila kitu, sisi Manyoni tunataka tuanze. Tutaunda Kamati, mchango huu utaanza, mtuunge mkono mlete kweli magreda, tutasimamia fedha vizuri, mafuta yatajazwa kwenye magreda, tukachimbe mabwawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Manyoni hatuna mvua za kutosha, tuna msimu mmoja tu wa mvua hatuna vuli. Mito yetu inakauka na ukichimba maji chini ukiyakuta yana chumvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliposikia kuna magreda yanakuja kutusaidia kuchimba mabwawa nimefurahi sana. Hakika hili jambo naliunga mkono moja kwa moja; wa Manyoni mjipange magreda haya yaje kutuchimbia mabwawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mifugo kujaa Wilaya ya Manyoni. Wilaya hii imekuwa kimbilio la wenzetu kutoka Mikoa ya Magharibi, Kaskazini, kwa kweli mifugo imejaa kiasi cha kutosha. Naona kabisa mwelekeo sasa migogoro inakwenda kuzuka Manyoni. Mbaya zaidi wahamiaji hawa wa ndani, Mtanzania unaruhusiwa kuhamia au kuishi mahali popote lakini kwa utaratibu. Kuna wahamiaji wengine ni hatari sana wanakata miti sijapata kuona. Wanapoingia wanafyeka miti sijapata kuona. Silitaji hilo kabila lakini wanakata miti sana, wamehamia pale Manyoni. Wanakata miti, wanachimba visiki, wanalima miaka miwili, wanahama, wanafyeka pori, wanachoma, wanachimba visiki yaani miaka mitatu wakihamia unaangalia unakuta miti hamna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara isimamie jambo hili, jana bahati mbaya sikupata nafasi katika bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) lakini tuna tatizo kubwa sana la wahamiaji ambao wanafyeka misitu na kuharibu mazingira Wilayani Manyoni. Naomba mtusaidie sana, elimu itolewe na watu wa Mazingira na Kilimo ili muweze kuokoa misitu hii kwenye eneo la Manyoni Mashariki, Magharibi pamoja na sehemu ya Tabora, wanafyeka sana tena kwenye vyanzo vya maji, ni hatari sana. Naomba Wizara mtusaidie jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kukabiliana na majanga na naomba nizungumzie majanga mawili tu. Kuna suala la upungufu wa chakula, hili ni janga, Wizara naomba ijipange vizuri. Nawashukuru sana Wilaya ya Manyoni kwa maana ya Mkoa mzima wa Singida pamoja na Wilaya nyingine zote mwaka jana hatukupata mavuno ya kutosha. Tulilima vya kutosha lakini jua likawaka, mazao yakakauka, njaa ikatukabili lakini Wizara imesaidia ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, tunashukuru sana. Tulipata karibu tani 1,600 watu wetu wakapata ahueni lakini tulifanya kazi kubwa sana kwa sababu Wizara ilivyojipanga si sawasawa. Tulitumia msuli mkubwa sana mpaka watu wakaanza kuathirika. Naomba mjipange kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mjizatiti sana kwenye suala la kukabiliana na ndege waharibifu wanaoitwa quelea-quelea wanashambulia sana eneo la kati kwenye Bonde la Ufa. Tumeshambuliwa sana mwaka huu, tumetoka kwenye njaa, sasa ndege tena wakaanza kuharibu mazao, Tunapojaribu kufuatilia Wizarani inakuwa ngumu sana, tunaomba watendaji wa Wizarani mtusaidie sana. Mpaka sasa hivi navyozungumza ndege wanakula mtama na mpunga na hata mwaka huu nadhani mavuno hayatakuwa mazuri pale kwenye Bonde la Ufa, mtusaidie sana na mjipange. Kuweni na ndege ile ya ku-spray dawa za kuua ndege wale maana tunakodisha nchi nzima hatuna ndege kwa ajili shughuli hiyo, si jambo jema. Upatikanaji wa sumu pia siyo mzuri, naomba mtusaidie sana katika kushughulikia jambo hili. Naomba mjipange ili linapotokea janga kama hili muweze kulikabili mtunusuru tuweze kuvuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Wizara imetamka mpango wa kuondoa mageti ya ushuru kule vijijini, jambo hili tunalipokea kwa dhati. Suala hili la mageti ya ushuru imekuwa ni usumbufu mkubwa sana kwa wananchi wetu ni bora tukakutane kule kwenye soko kuliko kuweka mageti huku kusumbua wakulima. Manyoni kwa kweli tuna shida kubwa sana, gunia moja kupitisha kwenye geti pale ni shilingi 2,000 yaani unaweza ukalipia shilingi 2,000 zile karibu mara tatu. Nimefurahi haya mageti kuondolewa, ushuru utozwe sokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Manyoni tunaomba mbegu bora zilizofanyiwa utafiti za mazao ya biashara ya mpunga, ufuta na alizeti. Kuna mbegu moja ya ufuta inasemwa sana, nilienda siku moja Naliendele inaitwa Lindi 2002, naomba kwenye ruzuku mtukumbuke mbegu hizi zifike mapema lakini ziwe zimefanyiwa utafiti ili tukilima basi tuwe na kilimo cha tija kuwasaidia watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niishukuru Wizara hii naona sasa ina vijana ambao wamejipanga vizuri, wako kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja kwa mara nyingine na nakushukuru sana
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, private secondary schools wasifanye mchujo wa watoto kwa maana ya slow learners. Private schools wameweka pass mark yao tofauti na Serikali. Huanza mchujo kuanzia kidato cha pili hadi form IV terms za mwanzo. Hata kama watoto wakifikia kiwango cha “pass mark” ya Serikali kama hajavuka cha shule wanazosoma (private) huondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo lao matokeo ya mwisho final exams results wapate division I wengi na division II wachache basi, hawataki division III, IV na 0. Wanataka soko la shule zao liwe juu kwamba wanafaulisha sana. Huu ni unyanyasaji na ubaguzi wa hali ya juu, ukemewe kwa nguvu zote. Binadamu tumepishana, wengine fast learners na wengine slow learners lakini wote uelewa wao ni sawa. Ni mbaya sana inaleta pia usumbufu kwa wazazi, huitwa na kuambiwa mhamishe mtoto wako kwa vile hataweza ku-cope na wenzake. Hii ni mbaya, mbaya kabisa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hoja asilimia 100. Manyoni ni Wilaya ya zamani (kongwe) na Wilaya ya kwanza kuwa na Mkuu wa Wilaya Mwafirika. Tatizo kubwa Manyoni hasa Manyoni Mashariki hatuna kiwanda cha kati hata kimoja. Naipongeza Serikali imepata eneo kwa ajili ya Ukanda wa EPZ. Tunaomba tafadhali Serikali itenge fedha kwa ajili kuanza ujenzi wa viwanda ndani ya EPZ area.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ianze kutujengea kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti (sunflower) kwa kujenga kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti. kwa kufanya hili itakuwa imetoa hamasa kubwa kwa wakulima wetu wa alizeti katika Wilaya nzima ya Manyoni na hata Wilaya jirani za Chemba (Dodoma) na kadhalika. Aidha itatoa ajira kwa wingi kwa Wanamanyoni na maeneo mengine ya nchi. Mwisho viwanda hivi vitaongeza pato la Taifa kupitia kodi, nawasilisha na naunga mkono hoja.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuamsha leo salama na mimi kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme naipongeza hotuba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ni nzuri, iko vizuri na imekaa vizuri. Nimpongeze Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, anafanya kazi nzuri, yuko imara na jeshi liko imara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika niende moja kwa moja kwenye hoja yangu. Ukitazama Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa, Cap. Na. 193 ya mwaka 2010, (R.E), kifungu cha 6(2) kinataja umri wa mtu au umri wa Mtanzania kwenda Jeshi la Kujenga Taifa, ni kati ya miaka 16 – 35. Kwa nini nataja vifungu hivi? Nchi yetu zaidi ya 60% ni vijana na vijana ndiyo nguvu kazi ya kujenga nchi hii. Tusipowalea vijana vizuri, tusipowajenga vijana vizuri hakika mustakabali wa nchi yetu na hasa kwenda kwenye maendeleo na hasa kuipeleka nchi yetu katika uchumi wa kati itatuchukua muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji tuwajenge vijana katika uzalendo waipende nchi yao. Tuwajenge vijana katika utii na nidhamu, tuwape stadi za kazi, tuwape uaminifu ili wawe wanaitika kwa sauti moja ya kiongozi anaposema, nchi hii itakwenda vizuri, nilitaka nilisisitize hili. Hakuna chombo kingine kikubwa ambacho kinaweza kuwarekebisha vijana hawa, naliona Jeshi la Kujenga Taifa hata JKU – Zanzibar, ni vyombo vya muhimu sana katika kuandaa vijana wetu. Ni vya muhimu sana! Naomba tuwekeze vilivyo kwenye majeshi haya, Jeshi la Kujenga Taifa na JKU. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuwekeze kwa namna gani? Wengi wamechangia hapa, kuna chuo kikubwa cha VETA kinataka kujengwa Kongwa, naomba tuharakishe ujenzi huu, tuwapeleke vijana wetu huko VETA. Hata kwenye makambi, namkumbuka sana Mwalimu Nyerere, namkumbuka sana Mzee Karume, walipoanzisha majeshi haya waliainisha maeneo muhimu sana ambayo mpaka sasa hivi tunayatumia kwenye kambi za Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Kujenga Uchumi. Kuna maeneo mazuri ya kilimo, mimi nimepitia pia, tulikuwa Mgambo Tanga kule, tulikuwa tunalima mahindi Gendagenda, tulikuwa tunalima machungwa na maeneo mengine kama Itende na Chita, yamekaa vizuri kwa ajili ya uchumi. Tukiwekeza vizuri hawa hawa vijana watazalisha, watajilisha na watailisha nchi lakini tutakwenda kwa pamoja wakiwa watii ndani ya jeshi na kupitia Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme jambo moja la msingi sana. Nimesikia maneno ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani, amesema mambo mazuri, mimi ni muungwana, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Kwenye mazuri mtu nitampongeza, akikengeuka nitamwambia hapo hapana!
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja alilisema, sim-quote lakini najaribu kutoa tu ile maana kwamba anashangaa Mheshimiwa Rais anateua Wanajeshi wastaafu kuwa viongozi kwa mfano Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa kwamba hawa wasingekwenda huko kwa sababu ni Wanajeshi. Mimi nasema hapana! Hawa ni reserve army, reserve army ni yule mtu ambaye amekwenda jeshi either amepata kazi au hajapata lakini ni reserve army, lazima tumtumie. Amejifunza utii, anaweza kufanya kazi na ni mzalendo huyu na wamefanya kazi nzuri sana watu hawa. Tunawaona wanachapa kazi sana hawa Wanajeshi, kwa mfano Wakuu wa Mikoa tumeona wanafanya kazi nzuri sana, tuwatumie. Hiyo ndiyo maana ya jeshi la akiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nihame hapo niseme jambo moja kuhusu nafasi hizi za kwenda Jeshi la Kujenga Taifa. Vijana wako tayari kila mahali kwenda Jeshi la Kujenga Taifa lakini kumekuwa na ukiritimba kwenye nafasi hizi. Nadhani nafasi hizi zimegawanywa kimikoa na kiwilaya, kila wilaya na mikoa ina nafasi zake. Naomba tulisimamie vizuri suala hili kwa mfano Mkoa wa Singida wanatoa vijana kutoka Arusha wanawaleta Mkoa wa Singida. Wale viongozi, washauri wa Mgambo wanatawala zoezi hili, wanawanyima haki wale vijana wa kwenye maeneo yale. Naomba mlisimamie vizuri jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu. Tuliomba hapa wakati tunachangia Wizara ya Kilimo kwamba Wanajeshi wakati wa amani wasaidie maeneo mengine. Tuna vyombo hivi, wana ma-grader, vijiko, malori ya ujenzi, hebu vyombo hivi vitumike kutusaidia kwa mfano kuchimba labda mabwawa na kujenga barabara, wananchi tuko tayari kuchangia mafuta.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtuka muda wako umekwisha.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja hii mia kwa mia. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii na mimi nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye barabara zangu za hadhi ya mkoa, kwa maana ya jimboni kwangu Manyoni Mashariki. Ubora wa barabara hizi si wa kuridhisha, ninaomba sana Wizara husika, nadhani watu wa TANROADS Mkoa huwa hawaendi kusimamia ujenzi wa barabara hizi, kwanza upana hauko sawasawa, tuta linanyanyuliwa katikati, magari makubwa ya mizigo hayawezi kupishana na mpaka sasa hivi magari mawili yameanguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia madaraja; ukienda kwenye daraja lile la Mto wa Sanza, nilipita juzi pale! Nakuomba Mheshimiwa Waziri siku moja tupange safari twende kule ukaangalie tulinganishe BOQ na kitu ambacho kipo kule kwenye lile daraja lenye mita mia moja, ni refu. Nimekuta kitu cha ajabu sana kule, nondo milimita sita inajenga daraja! Milimita sita! Hii ni hujuma ya ajabu sana. Naomba tuangalie ubora katika ujenzi wa barabara na hasa katika usimamizi wa hizi barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja upande wa ujenzi wa kituo kinachoitwa One Stop Inspection Station pale Muhalala; hivi vituo ni vitatu katika hii central corridor, moja ni kule Muhalala. Sasa tatizo ni kwamba wale wananchi hawajalipwa fidia. Mwaka wa tatu sasa hawafanyi shughuli zao za kimaendeleo, hawalimi, hawajengi na ardhi imechukuliwa, lakini hawalipwi fidia. Naomba Waziri akijumuisha atoe majibu, lini watalipwa fidia watu hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye reli ya kati. Naomba niungane na Wabunge wenzangu, reli hii ni ya gharama kubwa sana standard gauge, nadhani katika historia ya nchi hii hatujawahi kuingia mradi mkubwa wenye thamani kubwa kama huu. Naomba tutafute mkandarasi…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kuna ujenzi wa One Stop Inspection Station (OSIS) karibu utaanza eneo la Muhalala, Wilayani Manyoni. Ombi langu ni kulipwa fidia wananchi wa Muhalala ambao walitii kutofanya shughuli zote za kilimo na ujenzi eneo hilo wakisubiri fidia tangu mwaka 2013. Malalamiko ya wananchi hawa wazalendo ni makubwa, tafadhali nipate majibu, ni lini fidia hii inalipwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; Manyoni Mashariki tuna barabara mbili za hadhi ya mkoa, kama vile Manyoni - Iteka - Sanza - Chali Igongo na Ikungi - Londoni - Kilimatinde (Solya). Tatizo langu ni kiwango cha ujenzi ni cha chini sana. Kiwango cha ujenzi hakitofautiani na barabara za Wilaya, wakati wa ujenzi hawamwagi maji ya kutosha, vifusi vinarashiwa sana, sehemu kubwa wanakwangua tu na graders, hawashindilii vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, culvets katika mapito ya maji ni vichekesho kwa baadhi ya maeneo, maji yanapita pembeni badala ya kupita ndani ya culvets. Upana wa barabara ni wa kuangalia upya, siyo rahisi kupishana mabasi au malori mawili yakiwa na mzigo kwani katikati pamenyanyuliwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja kubwa la mto mkubwa wa Sanza lililokamilika miaka miwili iliyopita limekatika. Kuna maajabu katika nchi hii, nashauri Waziri aidha, wewe mwenyewe au Afisa kutoka Wizarani nitampeleka akakague nondo zilizojengea daraja hili tulinganishe na BOQ, kuna hujuma mbaya sana. Tatizo kubwa ni usimamizi mbovu au wasimamizi Ofisi ya Meneja wa Mkoa wameungana na makandarasi kuwahujumu Wanamanyoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya Manyoni - Singida; tunaomba sana rejesheni huduma ya reli hii hata kama inashia Singida, ni sawa tu. Tuna vitunguu, viazi vitamu, kuku wa kienyeji, miwa, mbuzi, chumvi na mizigo mingine mizito kama mafuta kwenda na kutoka Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii kutoa mchango wangu mdogo. Niseme tu jambo moja kwamba nimepitia hotuba ya Bajeti ya Wizara hii, nimepitia hili begi ambalo tumepewa, nilikesha, nimesoma vizuri sana. Nimepata matumaini makubwa sana kama mtaalam wa ardhi tumetukanwa kwa miaka mingi kwamba hatufanyi chochote, kazi zetu ni kusababisha migogoro, kuuza viwanja na kadhalika, lakini nimepata matumaini makubwa niliposoma makabrasha haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kitu kimoja kwamba nimeridhika sana na kitabu hiki cha Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi. Hili ndilo suluhisho pekee, hiki kitabu ndilo suluhisho pekee la migogoro na kila mmoja sasa tukitekeleza hili tutaishi kwa amani katika nchi hii na kila mmoja atafaidi kipande cha Ardhi ambacho atapewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri yafuatayo ili kutekeleza mpango huu:-
Kwanza, naomba tutunge sheria moja tu inayo-govern suala la ardhi. Hatuhitaji Sheria ya Ardhi namba tano ya Vijiji, sheria namba tano ya vijiji tunaomba tuifute, inaleta migogoro mingi na ardhi ya vijiji ni sehemu kubwa kuliko hata ile nyingine iliyobaki. Hatuwezi kusema ardhi ya vijiji, ya mjini ardhi ni ardhi tu, tafadhali sana tukishatunga sheria hii utekelezaji wa sheria ufuatwe. Kila mmoja wetu, Mbunge, watendaji, wale watu wa vijijini naomba tutekeleze Sheria ya Ardhi, tusimamie utekelezaji wa ardhi. Sheria nyingi nzuri zimetungwa ziko kwenye makabrasha, sheria nyingi nzuri lakini bila utekelezaji, ni kazi bure, naomba hili mlishike sana wenzetu mliopewa dhamana hii kwa maana ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye mpango huu, tuajiri wataalam wa kutosha wanaoshughulikia mambo haya. Vyuo vyetu vimetoa watu wa kutosha, Chuo Kikuu cha Ardhi, Morogoro, Tabora wametoa wataalam wa kutosha, wako mitaani tunawaona. Ajirini wataalam hawa waje kusimamia mpango huu. Inatia mashaka na inasikitisha sana mnapounda mabaraza vijijini mnakamata tu wazee pale kwamba wewe mzee ndiyo utakuwa Mwenyekiti. Hivi unaweza ukaenda dispensary pale ukakuta tu mzee anatibu hajasomea uganga?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakwenda kule mahakamani unakuta tu mtu anatoa hukumu hajasoma mambo ya Sheria? Kwa nini tunakabidhi suala hili zito la ardhi watu ambao hawajasoma? Yaani ardhi tunaidharau kiasi hiki? Ardhi ambayo ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wataalam wa-play kila mahali kuanzia vijijini mpaka huku Taifa. Watu wamesoma, hii ardhi ni taaluma hatuwezi kucheza na ardhi, hatuwezi kukabidhi mtu ambaye hana ajira na hana liability yoyote yaani hatuwezi kumbana. Unapomwajiri mtu ambaye ni mtaalam atakuwa anasema mimi ni mtaalam, lakini pia nimeajiriwa, nalinda kibarua changu. Sasa unampa tu mtu unamkamata barabarani wewe utakuwa mshauri kwenye Baraza la Ardhi haiwezekani, liability iko wapi, lazima atavuruga tu ndiyo maana ya kwenda shule, naomba tulizingatie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishakwenda kwenye mpango huu maana yake ni kwamba, sasa tukapime ardhi ya nchi nzima. Nimepitia kwenye mpango huu nadhani kuna pilot project kwenye wilaya karibu 63, mmeweka mipango hii, lakini nasema hivi tukapime nchi nzima, siyo wilaya kadhaa, wala manispaa kadhaa , wala halmashauri kadhaa, twendeni tukapime nchi nzima, tutumie wataalam wetu kwenye halmashauri zetu, wapo wataalam, kama hawapo tuajiri kama nilivyosema tukaipime nchi nzima ipimwe sasa siyo kupima maeneo mengine na maeneo mengine kuachwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimefurahishwa kwenye mpango huu, jambo ambalo litatuondolea migogoro ni kwamba, tupime ardhi kwa uwiano hasa ardhi ya kilimo na ardhi ya ufugaji ipimwe kwa uwiano. Fanya sensa ya mifugo mahali, angalia ardhi iliyopo pima ile ardhi wagawiwe wafugaji kwa mujibu wa idadi yao na idadi ya mifugo na ardhi iliyopo. Hesabu wakulima wako wangapi, pima ardhi iliyopo kwa ajili ya kilimo kwenye eneo husika kama ni wilaya kama ni kijiji igawe ardhi kwa uwiano wa idadi ya wakulima waliopo hilo litaondoa migogoro, tugawe ardhi kwa uwiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo nadhani tukienda hivyo migogoro haitakuwepo na iwekwe kwenye sheria hii ambayo tunakwenda kuitunga hasa kwenye kilimo na ufugaji kumekuwa na mgogoro mkubwa sana, gaweni ardhi kwa uwiano. Siyo mfugaji mmoja anayemiliki maekari na maekari na wengine hawana ardhi. Mkulima mmoja anamiliki maekari na maekari wengine hawana ardhi katika kijiji, tugawe ardhi sasa kwa uwiano, kwa mujibu wa sheria na tusimamie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, change of land use, hasa nazungumzia eneo ambalo limepimwa. Suala hili limekuwa na mgogoro mkubwa sana, sheria zimetenga kabisa upimaji ule kwa mfano kwenye miji umetenga maeneo mazuri, maeneo ya makazi, ya biashara, ya viwanda na ya kumwaga takataka. Zile plan zinakuwa vizuri mnapoanza. Kwa mfano, mradi wa viwanja 20,000 ukiuangalia zile ramani ziko vizuri lakini ukienda sasa hivi kwenye utekelezaji yaani ile plan imeshavurugika tayari watu wanabadilisha matumizi ya ardhi bila utaratibu. Sheria ipo ya kubadilisha matumizi kwa kufuata sheria na kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nenda kwenye makazi ya watu miziki inadundwa mpaka saa nane, saa tisa za usiku kwenye maeneo ya makazi. Petrol station zinajengwa kwenye maeneo ya makazi kinyume na ile plan ya zamani. Watu wabadilishe matumizi ya ardhi kutokana na sheria na sheria ipo tulinde plan zetu maeneo ya wazi yameshajengwa, yanavamiwa hovyo. Eneo lilitengwa kwa ajili ya shule, watu wamejenga maeneo ya biashara tunakwenda wapi, mbona sheria zipo? Enforcement of laws ni jambo la muhimu sana katika ku-plan mambo ya ardhi, naomba sana tuzingatie.
Mheshimiwa Mwenyekitii, mwisho, kule kwangu Manyoni kuna mgogoro wa ardhi, kati ya wananchi na Hifadhi ya Muhesi-Kizigo, ndiyo haya mambo niliyokuwa nayazungumza. Mgogoro wetu ni tofauti kidogo na maeneo mengine, sisi tunagombana na hifadhi kwa sababu ile hifadhi walitunyanganya lile eneo wakapanua ule mpaka wakala kijiji, wakala maeneo ya malisho ya mifugo, wakala maeneo ya kilimo kule Manyoni. Huo ndiyo mgogoro wetu, sisi hatuombi kuongezewa kumega hifadhi hapana, tunaomba mpaka wetu ule wa zamani urudishwe, hilo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha huu mgogoro wa Muhesi Kizigo na wananchi wa Manyoni wanaoishi pembezoni mwa ule mpaka, wanaomba sana warudishieni ule mpaka wa zamani, yale mashamba yao yamebanwa, hawana pia maeneo ya kulisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna unyama mkubwa sana wa hawa wenzetu wanaolinda yale maeneo, nadhani hili linamhusu Profesa Maghembe, hili eneo Wizara ya Maliasili na Utalii kile kikosi wanaenda kinyume kabisa na sheria za kibinadamu. Unakuta mtu amejenga nyumba, ameweka makenchi yake, wanapanda juu wanashusha makenchi, hizo kenchi unajuaje kama mtu alinunua mbao zimegongwa mihuri wa kibali au hapana mtu amepandisha kenchi wewe unaenda unashusha, kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ameshachonga madirisha mnakwenda mnachukua yale madirisha mnapiga watu, mama tu ameingia kuchukua kuni pale anapigwa mpaka anazimia na anakwenda kufunguliwa kesi. Ninazo kesi nyingi pale Manyoni yaani kuna watu wamejaa pale kwenye mahabusu ya Manyoni. Hivi ni balaa kupakana na hifadhi? Naomba tafadhali sana hebu tufuate sheria na toeni pia elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ule mpaka haujulikani, yaani ukienda nionesheni mpaka hifadhi ni wapi inapoanzia na kile kijiji kinapoanzia hawawezi kuonesha. Kwa hiyo, naomba sana wana Manyoni wanasema rudisheni ule mpaka wa zamani kule ambako ulikuwepo, muwaachie mashamba yao na eneo lao la kulima. Pia wekeni ule mpaka unaoonekana, pandeni hata miti, kule Bukoba wanaita bilamla, kule Manyoni tunaita machito, weka mpaka hata chimbia hata miti, hata vile vinguzo, panda hata minyaa angalau kuwe na mpaka unaoonekana kwamba hapa ndiyo mwisho, hii itapunguza sana migogoro.
Mheshimiwa Mweyekiti, mwisho kabisa, nirudie kwa kutoa wito kwamba mpango huu ni mzuri tujipange vizuri kama nchi twendeni tukaipime Tanzania, tuiweke kwenye ramani, tuepushe migogoro, mpango huu unatekelezeka na ni mzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umbali wa mita 60 kutoka ufukwe wa bahari, kingo za mito, mialo ya maziwa, maeneo yote tengefu na maeneo hatarishi (hazardous land) yazingatiwe kama sheria zinavyotaka. Kwa mujibu wa section 7(1)(d) of Land Act No. 4 of 1999 au section 7 kwa ujumla wake inaelezea kwa kirefu namna ya kuyabaini na kuyatangaza katika Gazeti la Serikali. Naomba Wizara isiishie hapo, waweke alama inapoishia mita 60 kama walivyofanya TANROADS na TANESCO wameweka vigingi vya zege kuonyesha mwisho wa mipaka ya maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote ya wazi kwa mujibu wa cadastral surveys wapewe watu vibali siyo hatimiliki kama waangalizi. Kwa kibali maalum cha Wizara wataruhusiwa kufanya beautification kama kupanda maua (lawn grasses), kutengeneza miundombinu ya kuchezea watoto kama bembea na kadhalika. Tahadhari wasijenge majengo ya kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo yote yaliyotengwa kwa taasisi kama viwanja vya kujenga majengo ya shule, nyumba za ibada, mabenki, vituo vya polisi na huduma nyingine kama vituo vya mafuta, Wizara au Halmashauri zihakikishe unawekwa utaratibu kila mwananchi ayatambue maeneo haya na wawe walinzi wa maeneo haya yasivamiwe. Vichimbiwe vibao vikitaja maeneo haya ili ku-prohibit uvamizi wa maeneo haya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimwa Mwenyekii, nikushukuru kwa nafasi hii, na mimi niweze kutoa mchango kwenye Wizara hii ya maliasili na utalii. Niende moja kwa moja kwenye eneo la migogoro kati ya hifadhi na wananchi, lakini migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini chanzo cha migogoro hii? Iko mingi lakini mimi nimeona viko vyanzo vinne. Sababu ya kwanza ni ongezeko ya watu na mifugo wakati ardhi haiongezeki. Ni kweli wakati wa uhuru tulikuwa watu milioni tisa sasa hivi tunakwenda kwenye 50. Mifugo ilikuwa michache lakini sasa hivi mifugo ni mingi, lakini ardhi iko palepale. Pale kwangu Manyoni sasa hivi tumeongezeka sana lakini pia watu wanaohamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili ya migogoro hii, ni uharibifu wa mazingira, tunakata miti sana. Kwa mfano, kwangu pale Manyoni upande wa Mikoa ya Magharibi wamekata miti sana, mazingira yameharibika, sasa wanakuja wanasogea Mkoa wa Singida-Tabora wanavamia huko kuja mpaka Chunya na Mbeya. Watu wanakata miti watu wanachoma mikaa. Kaskazini huku, kuna shida pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hicho ni chanzo cha mgogoro cha nne kwamba, baada ya mwaka 2009 sheria ilibadilishwa mipaka ya hizi hifadhi ikafinywa ikala maeneo makubwa sana, Umasaini huku, Ugogoni huku, imekula sana Usukumani huku. Watu wanahama kutoka Umasaini, watu wanahama kutoka Usukumani magharibi wanakuja kuvamia Morogoro, Rukwa na maeneo mengine; huu ni mgogoro wa moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikia mchangiaji mmoja jana anachangia kwa nguvu sana kwamba sisi hatukuwahi kuona ng‟ombe wengi wa namna hiyo. Sasa hivi tunaona malaki ya ng‟ombe ni vitu vigeni kwetu lazima huo ni mgogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha mwisho nilichokiona mimi ni uvamizi wa mifugo kutoka majirani zetu, Rwanda, Kenya, wanaingia kwenye misitu, wanawasukuma wenyeji huku tunaanza kugombana nao, hicho ni chanzo pia cha migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini sasa kifanyike? naiomba Serikali yangu ambayo ni sikivu ya Chama cha Mapinduzi irejeshe mipaka ya zamani kwenye hifadhi. Zamani ile mipaka Mungu ameiweka ni ya asili, Wanyama wanakaa kule Binadamu anakaa huku tusilazimishe kuongeza mbuga zile, tusilazimishe kuongeza misitu wakati sisi tunaongezeka, mifugo inaongezeka. Naomba sheria hii ibadilishwe, mipaka hii irejeshwe ile ya zamani, eneo hili litatupa ardhi kubwa sana migogoro hii itapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, njia nyingine ya kupunguza migogoro ni wakati sasa wa kutekeleza ule mpango wa matumizi bora ya ardhi. Tutenge sasa matumizi bora ya ardhi. Kilimo tuwatengee eneo lao, wafugaji maeneo yao, makazi maeneo yake, viwanda maeneo yake, madini maeneo yake. Hebu tupange hii. Tuipime nchi tuweke mipaka ambayo iko clear, ugomvi huu utapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho kitasaidia, kuna dormant Ranches. Ranch ambazo hazitumiki, tuangalie uwezekano wa kubadilisha matumizi. Kuna maeneo ya hifadhi pia ambayo hayana tija, tuyabadilishe matumizi pia. Tugawe kwa wakulima, tugawe kwa wafugaji, itatuongezea ardhi na pia migogoro hii itapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine. Sisi wakulima na wafugaji, mimi ni mkulima pia na ni mfugaji. Namwomba hata Mzee Mtuka anisikilize kwenye jambo hili. Wafugaji tuwe tayari kupunguza idadi ya mifugo. Tupunguze idadi ya mifugo tumeongezeka na mifugo imeongezeka. Ardhi haiongezeki, sehemu za kuchungia haziongezeki, tuwe tayari kupunguza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ilisimamie hili, zile Wizara nne zile zisimamie, zikae na wakulima, zikae na wafugaji, waseme wao kiwango cha mwisho cha mfugaji kuwa na mifugo ni kiasi gani? Kama ni ng‟ombe mia moja tukubaliane iwekwe kwenye sheria, tukubaliane hilo. Haiwezekani mtu ana ng‟ombe 2,000 mwingine 5,000 haiwezekani ardhi haipo. Wafugaji wenzangu natoa wito, tukubaliane kiwango rasmi ambacho kila mfugaji ataishia kufuga. Huwezi kufuga tu yaani ng‟ombe unaotaka, haiwezekani, hili pia liwekwe kwenye sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti lakini kingine, baada ya kugawa yale maeneo, upande wa wafugaji nashauri sana wawekewe miundombinu. Hebu Serikali itusaidie, leteni hata yale magreda na vile vijiko vya Jeshi. Chimbeni mabwawa kule kwenye maeneo ya wafugaji ambayo yametengwa, chimba hata mabwawa maji yajae huko, weka majosho, weka majengo ambayo Wataalam wa Mifugo watakuwepo kule ili kuwa-control hawa wafugaji wasiweze kuhama hama. Ukiweka miundombinu hii, wafugaji hawatahama. Naliomba sana hilo, Serikali isaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nihame hapo, nizungumzie kidogo vivutio vya utalii. Sisi Manyoni kule tuna kivutio kipya ambacho tunataka tukitilie nguvu na tunaomba Serikali ituunge mkono. Ukiiweka Tanzania kwenye ramani, ukai-set kwenye mitambo ile, ukatafuta kile kitovu cha nchi kinatua Manyoni, kuna sehemu inaitwa Kisingisa. Hebu naomba mtusaidie Serikali eneo lile.
MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa muda huu kupewa na mimi nafasi ya kuchangia bajeti kuu. Nianze moja kwa moja kuchangia bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia bajeti iliyotengwa kwa vyombo ambavyo vinatakiwa kusimamia bajeti hii, taasisi simamizi, oversight institutions, kwa maana ya TAKUKURU na Ofisi ya CAG. Ni kweli wazungumzaji wengi wameongea, Ofisi ya CAG ni muhimu, ndiyo jicho, tunajua asilimia 40 imetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lazima kuwe na jicho hili, tumuongezee pesa huyu afuatilie fedha hizi, hii shilingi bilioni 44.7 haitoshi, tunaomba aongezewe fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini TAKUKURU pia, wengi walikuwa wanasema amewekewa hela nyingi, hakuna, hela imepungua. Naomba ku-declare interest kwamba mimi nimekuwa Kamanda wa TAKUKURU - Kanda Maalum mpaka nakuja hapa. Mkoa wa Dar es Salaam kwa muda wa miaka mitano, kwa mfano 2012/2013, OC ambayo ndiyo inayotumika kwa ajili ya mafuta watu waweze kwenda kufanya kazi, ndiyo kuna per diem za watu zipo hapo ili waende kufanya kazi, ndiyo kuna fedha za stationeries kwa ajili ya kwenda kufanya kazi ilikuwa shilingi bilioni 16, mwaka 2013/2014 ilikuwa shilingi bilioni 15.5, mwaka 2014/2015 ilikuwa shilingi bilioni 16.5, mwaka 2015/2016 ilikuwa shilingi bilioni 14.2 ikapungua, mwaka huu wa fedha 2016/2017 ni shilingi bilioni 12.03, imepungua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia hii 40 inakwenda kwenye miradi, watu mambo yameongezeka lakini pia taasisi hii watu wamekuwa wengi, wapo wafanyakazi karibu 2,001, magari yameongezeka, mafuta yanahitajika lakini tunayo shilingi bilioni 12 tu. Kipindi kile kabla sijastaafu kule tulikuwa tunajibana sana kwa hizi shilingi bilioni 16, 15, 16, 14, sasa mwaka huu hata fedha yenyewe imeshuka wanakuja kwenye shilingi bilioni 12 yaani hii hela ni ndogo mno, sijui, namhurumia sana huyu Mkuu wa TAKUKURU sijui atafanya kazi gani. Atafanya lakini kwa kujinyima na hali kwa kweli ni ngumu sana, wanategemea kufungua wilaya nyingine 25, wana-operate mikoa yote, wilaya zote za zamani, sijui watafanya nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, rushwa ndugu zangu ni adui wa haki, rushwa tunaona madhara yake ni makubwa mno, taasisi hii iko kila mahali. Rushwa imesababisha migogoro ya ardhi, ni kazi ya ofisi hii, rushwa imeingia michezoni watu wanapnga matokeo ni kazi ya taasisi hii, rushwa imeingia hospitalini, twende mahakamani watu wanabambikiwa kesi vituo vya polisi ni kazi ya ofisi hii, wakandarasi tunapata wabovu yaani kuna vurugu. Nenda sekta ya ardhi akina mama wanadhalilishwa, rushwa ya ngono, ajira, ni kazi ya TAKUKURU kwenda kule. CAG ni moja wa informers wa TAKUKURU, makabrasha yale yote yanashughulikiwa na ofisi moja tu. Bado nchi nzima wanapeleka taarifa TAKUKURU, atafanyaje kazi huyu?
Mheshimiwa Naibu Spika, najua hii haiwezi kubadilishwa lakini kipindi kijacho naomba suala hili litazamwe upya. Najua Watanzania wanajua hizi hela zilivyotajwa 72.3 labda ni nyingi, hapana, siyo nyingi, kuna mambo ya mishahara ile ni fixed, kuna ujenzi wa Ofisi ya Ushauri ya Afrika kule Arusha, ndiyo imeweka amount hii imekuwa kubwa lakini zile za kufanyia kazi ni ndogo mno na kwa kiasi ambacho kimepunguzwa sana mwaka huu, nawahurumia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba taasisi hii ndugu zangu hebu tuisemee, tuitetee, ndiyo mkombozi wetu huyu. Nchi imechanwachanwa vipandevipande kwa sababu ya rushwa. Tunasimika viongozi wabovu kwa sababu ya rushwa, tuimarishe hiki chombo kifanye kazi vizuri. Yapo mambo mengi ambayo chombo hiki kinafanya inabidi tukisemee, ndiyo mkombozi wetu katika nchi hii yaani chombo hiki kikilegalega ambacho ndiyo msimamizi wa mapambano haya hali itakuwa ngumu sana. Hata uchumi wa viwanda tunaouzungumzia sijui tutakwendaje kama hatujaimarisha taasisi hii. Kwa hiyo, tuzisemee taasisi mbili hizi simamizi CAG na TAKUKURU, hawa ni mapacha, lazima tuwatetee, wapewe fungu kubwa hawa ili wafanye kazi. Nilitaka niseme hilo kwa uchungu mkubwa kwa sababu naitazama Tanzania yangu nakata tamaa kwa sababu hivyo vyombo vimepewa hela kidogo sana vitasimamiaje majukumu yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo property tax, kuna ugomvi hapa kidogo, TRA ni wataalam wenyewe wa mambo ya kodi, ni mahiri kwenye mambo ya kodi lakini pia Halmashauri kuna wataalam wa mambo ya ardhi, wathamini wanaojua thamani za ardhi. Kodi hii huwa ina-base kwenye thamani ya jengo pamoja na ardhi, TRA siyo wataalam wa mambo ya ardhi, wataalam wako kwenye Halmashauri, kwa hiyo kuna mambo mawili hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashauri, acheni wataalam wa ardhi wafanye makadirio ya kodi hii, wakabidhini sasa hawa mahiri wa kukusanya kodi maana wao ni kukusanya tu siyo kukadiria. Ndiyo maana kuna mchangiaji mmoja amesema inafika mahali sasa mnatoza flat rate, kibanda cha jiko kinakuwa na kodi yake, nyumba kubwa inakuwa na kodi yake, kwenye evaluation hatufanyi hivyo wataalam wa ardhi. Jengo moja linakuwa na vijengo vidogovidogo, vinaitwa art building, ni sehemu ya jengo kubwa, wataalam wanajua, waachieni wataalam wakadirie kodi hii, TRA wenyewe ni wataalam wa kukusanya tu, basi. Naomba hili Mheshimiwa Waziri alizingatie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Singida, Mkoa wangu ninaoupenda. Nimesoma hiki kijitabu kidogo kinachozungumzia hali ya uchumi, ukurasa wa 10, Singida ni namba nne kwa umaskini katika nchi hii. Jamani hatukujitakia, tumejikuta tuko pale Singida, tumezaliwa pale, ndiyo mkoa wetu sisi. Ndiyo mkoa wetu ule…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante kwa nafasi hii nitoe mchango
wangu. Kwanza niwapongeze Kamati ya Miundombinu pamoja na Kamati ya Nishati na Madini.
Baada ya pongezi hizo niende moja kwa moja kwenye point.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu bado liko pale pale kwa REA II ambao ni mradi
ulikuwa umeanza tarehe 25 Novemba, 2013 na ulikuwa uishe tarehe 25 Novemba, 2015. Mpaka
hivi ninavyozungumza hata robo haijafikia mradi ule, mkandarasi yule ni mbabaishaji SPENCON
na nilishasema hapa huyo mtu hatumtaki. Tunaomba tubadilishiwe mkandarasi aletwe
mkandarasi mwingine ili aweze kukamilisha mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu umeme ni fursa, kuna mashine za kukoboa,
saluni vijana wafungue za kiume na za kike, welding, carpentry, tufunge pump za maji za
umeme pia, zahanati zetu, vituo vya afya, shule. Sasa mtu anacheza cheza na maisha ya watu,
hatumtaki huyu mkandarasi tunataka mkandarasi mwingine. Naomba mlisikie hilo Mawaziri
mtusaidie tunataka umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni REA III; tunaomba ianze. Tuliambiwa Desemba mwaka
uliopita lakini haikuanza, Februari haikuanza, tunaomba hii tarehe 15 Machi ambayo mmeisema
basi tunaomba ianze REA III. Kwangu kule Manyoni, vijiji ambavyo vina umeme ni vile ambavyo
vimepitiwa tu na njia kubwa ambavyo ni REA II, lakini kuingia ndani vijijini huko ambako ni mbali
na njia kuu hakuna umeme. Nikizungumzia Jimbo la Manyoni Mashariki, vijiji ambavyo vimepata
umeme kwa maana ya vile 58 ni karibu robo tu ndiyo vimepata umeme vingine vyote
havijapata umeme. Lakini pia REA III component ile ambayo mnasema kwa kijiji kimoja kwa
mfano, sasa hivi kwenye REA II ambavyo vilipata umeme ni robo tu ya kijiji lakini robo tatu ya kijiji
hakijawashwa umeme. Kwa hiyo, tunaomba ile 100 percent kijiji kiwashwe kwenye REA III.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, Mji wa Manyoni unapanuka, tumepima viwanja zaidi
ya 2000. Tunahitaji miradi ya umeme kwenye mji wa manyoni ili upanuzi wa mji uende pamoja
na huduma ya umeme. Nimeliongea hili, naomba tena nirudie mara ya pili, tafadhali sana
mtusaidie kwa sababu bei ya nguzo zile ni gharama kubwa, hatuwezi kumuuzia mtu kiwanja,
mnawaambia waungane wanunue nguzo wapeleke umeme haiwezekani hatuwezi kupanua
mji kwa namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa upande wa
miundombinu tunawashukuru tumepata ile…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa naunga hoja mkono, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii ya dakika tano, nitajitahidi kwenda kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sipingi kabisa kwamba ni lazima tuhifadhi misitu; huo ni utangulizi wangu, lakini haya yafuatayo naomba niyaseme kwa masikitiko. Tunayo migogoro ya mipaka baina ya hifadhi pamoja na wananchi kule Manyoni Mashariki. Nakumbuka tarehe 27 Mei, 2016 walikuja wawakilishi 18 walikutana na Mawaziri; Naibu Waziri Maliasili na Utalii na Naibu wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na walitoa malalamiko yao kuna tatizo la kusongeza mipaka. Kuna hifadhi inaitwa Muhesi Game Reserve hii ni hifadhi mpya, ilianzishwa mwaka 1991.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hapo wananchi hawa walikuwa wanaishi kwenye vitongoji salama lakini baada ya kuanzishwa hii Muhesi ambayo ilianzishwa na GN Namba 531 tarehe 4 Novemba, 1991 ndipo ikawahamisha wananchi karibu vingoji vinane.Vitongoji hivyo ni Chisola, Msisi, Itovelo, Machochoroni, Mkindiria, Chigugu, Ngongolelo pamoja na Chibwee. Haya maeneo yalikuwa ni potential kwa ajili ya kilimo; kwa mfano kulikuwa na eneo linaitwa Chiumbo ni eneo ambalo ni productive kwa kilimo cha mahindi, lakini pia kuna eneo linaitwa Iluma, eneo hili likuwa ni machimbo ya madini likiwa linatoa dhahabu ambayo haijawahi kushuhudiwa katika nchi hii, alluvial.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia taarifa za Benki Kuu za mwaka 1991 zinaeleza kwamba dhahabu inayotoka kwenye eneo hili hakuna katika nchi hii katika machimbo yote ambayo tumewahi kuyashuhudia, inaitwa alluvial.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya kutangazwa eneo hili pia likachukuliwa, ambapo ilikuwa ni kitegauchumi kizuri sana kwa wananchi wa Manyoni. Vilevile kwenye mito hii ya Muhesi na Kizigo ilikuwa ni source ya maji kwa ajili ya mifugo pamoja na wananchi. Baada ya hapo hatuna maji tena wala mifugo haiwezi kunywa maji pale. Pia tulikuwa tunafuga nyuki kwenye msitu ule wa Muhesi, sasa hivi hatufugi tena nyuki. Sasa ombi letu lilikuwa ni nini; ombi letu ni kwamba irudishwe ile mipaka ya zamani kwa sababu idadi ya watu imeongezeka, idadi ya mifugo imeongezeka pamoja na shughuli za kiuchumi zimeongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana Wizara ya Ardhi tulijadili sana mpango wa matumizi bora ya ardhi. Tunashindwa nini kugawa maeneo haya kwa kushirikisha wananchi kwamba wakulima kaeni huku na wafugaji kaeni huku, kitu gani kinashindikana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi ilipewa jukumu hilo, lakini nadhani sijui ndiyo ile Tume imeundwa lakini Manyoni kule hawajafika. Cha kusikitisha zaidi hawa wananchi walipozungumza na Waheshimiwa Mawaziri wetu hawajawahi kutoa taarifa juu ya maombi haya mpaka hivi ninavyozungumza, ili niwapelekee wananchi wa Manyoni. Hawajawahi kuniita hata mimi Mbunge wao kueleza hata kwamba tumejadili kitu gani hebu wapelekewe majibu haya wananchi wa Manyoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie jambo la Utalii. Tuna kivutio kipya kinaitwa Kisingisa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kuhusu migogoro ya mipaka baina ya hifadhi za wanyamapori au misitu na wananchi; katika Jimbo la Manyoni Mashariki jumla ya vijiji 12 vimepakana na hifadhi za misitu za Kizigo na Muhesi. Vijiji hivi ni Chikola, Chikombo, Mpola, Heka, Azimio, Nkonko, Chidamsulu, Iseke, Mpapa, Simbanguru, Sasilo, Chisinjisa na Imalampaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi katika vijiji tajwa wanalalamikia uhaba wa ardhi kwa ajili ya kilimo, malisho ya mifugo, uchimbaji wa madini na ufugaji wa nyuki. Aidha, wanalalamikia pia kuzuiwa kutumia maji ya mto uliopo mpakani kati ya hifadhi na vijiji. Uhaba wa ardhi umejitokeza badala ya ardhi yao kuchukuliwa na Serikali ulipofanyika upanuzi wa mipaka ya hifadhi za misitu tajwa mwaka 1994.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muhesi Game Reserve imeanzishwa rasmi kupitia GN. Na. 531 ya tarehe 04/11/1991 na kusainiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 09/03/1994. Muhesi ni hifadhi changa yenye kilometa za mraba 2,000, imesababisha machungu makubwa kwa wananchi katika maeneo haya. Tangazo la kuipandisha Muhesi kuwa Game Reserve mipaka yake mipya imeleta madhara makubwa kiuchumi, kwani imechukua maeneo muhimu kama eneo muhimu la kilimo cha mahindi liitwalo Chiumbo na eneo la Machimbo ya dhahabu aina ya Alluvial yaliyogunduliwa mwaka 1991. Hii ni dhahabu bora ambayo haijawahi kuonekana na kuchimbwa mahali
pengine katika nchi hii rejea Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya1992.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo au vitongoji vingine vilivyochukuliwa ni pamoja na Chosola, Msisi, Ilevelo, Machocholoni, Mkindilya, Chigugu, Ngongolelo na Chibwee. Aidha, maeneo haya yaliyochukuliwa yalitegemewa sana katika malisho ya mifugo, ufugaji wa nyuki na vyanzo vya maji safi ya kunywa binadamu na mifugo katika mito ya Muhesi na Kizigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko mengine ni unyanyasaji, utesaji na udhalilishaji unaofanywa na Askari Game Reserve dhidi ya wananchi. Naambatanisha na taarifa ya malalamiko ya wananchi yenye kichwa cha habari; “Yah: Malalamiko ya wanananchi kuhusu migogoro ya mipaka baina ya vijiji 12 na Hifadhi za Muhesi na Kizigo na manyayaso ya Askari wa hifadhi dhidi ya wananchi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko haya yaliwasilishwa na wananchi 18 kutoka Jimbo la Manyoni Mashariki wakiongozwa na Mbunge wao Mheshimiwa Daniel Mtuka walipokutana kwa mazungumzo ya ana kwa ana ofisini kwao Dodoma. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Engineer Ramo Makani tarehe 27/05/2016 mchana na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Tate Ole Nasha tarehe 27/05/2016 mchana. Tunasikitika hadi leo hatujajibiwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kwamba wananchi wangu bado wanasubiri majibu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi nichagie kidogo angalau kwa muda huu mchache. Kwanza nampongeza Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kazi anayoifanya inaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nizungumzie huduma ya maji katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki. Katika ukurasa wa saba Mheshimiwa Waziri mmesema kwamba hadi kufikia Machi, 2017 mmeweza kuwafikishia wananchi wale wanaoishi vijijini asilimia 72. Inawezekana ni sawa lakini si sawa katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki. Hali halisi ya Manyoni Mashariki ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyo vijiji 58, kati ya hivyo ni 19 tu vimepata maji. Vilevile nina vitongoji 248, kati ya hivyo 37 tu ndivyo vimepata maji, ambavyo ni sawasawa na asilimia 14.9. Ukijumlisha kwa maana ya Rural Manyoni ni asilimia 18.3 tu ya wananchi ndiyo wameweza kupata maji, hii 72 na 18 pengo ni kubwa mno na inasikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali halisi hii inaridhishwa na kilichopo ndani ya kitabu hiki cha bajeti. Ukiangalia jedwali namba 5(c) ukurasa wa 156 mpaka 157 item namba 10, orodha ya ile mikoa ambayo inatakiwa kujengewa miundombinu ya kusambaza maji ile mikoa kame ile, Manyoni Mashariki haipo, nimejaribu kuangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kama vile haitoshi, jedwali namba 8 ukurasa wa 174 mpaka 184, zile scheme za umwagiliaji, Manyoni Mashariki, pamoja na kwamba tuna Bwawa la Mbwasa, bwawa la kimakakati lile ambalo linatakiwa lichimbwe na upembuzi yakinifu ulishafanyika, inasikitisha halipo kwenye orodha hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi, jedwali namba 9(a) ukurasa wa 185 fedha za mfuko wa maji zilizopelekwa katika Halmashauri hadi Machi mwaka huu Manyoni Mashariki haipo inasikitisha. Kama vile haitoshi, jedwali namba 13 ukurasa wa 196, orodha ya visima vilivyochimbwa 272 katika nchi hii Manyoni Mashariki haipo; jambo hili linasikitisha sana ni lazima tulalamike. Kuna msemaji amesema huwezi kulalamika, lakini ni lazima mimi niseme kwa nini Manyoni Mashariki tu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilidhani Wizara kwa kuzingatia haya fedha ambayo imetolewa mwaka huu katika bajeti hii tumepewa shilingi milioni 611 tu. Tulidhani angalau tungepewa angalau shilingi bilioni nne Manyoni Mashariki lakini hii haitoshi pia nilidhani kwamba Wizara wangepanga mji wa Manyoni katika awamu ile ya kwanza, katika zile fedha za Mfuko wa India; zipo awamu tatu, Manyoni imepewa awamu ya tatu, kwa nini tusingepengiwa angalau awamu ya kwanza kwa sababu tuna kiu ya maji kwanini mnatuweka kwenye awamu ya tatu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuokoa muda nitoe ombi kwamba Kamati ya Bajeti mtakapokaa na Serikali hebu itazameni Manyoni Mashariki kwa jicho la peke yake, kwanini mnatubagua? Lazima nilalamike, hivi mimi ninakuja kuwapigia tu wenzangu makofi hapa, halafu narudi mikono mitupu kweli kabisa? Hapana, hebu itazameni Manyoni Mashariki tumekosa nini sisi? Sisi ni Watanzania wenzenu.

T A A R I F A . . .

MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba ulinde muda wangu, naikataa taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa, sijui kwanini kuna Waheshimiwa wengine hawasikilizi, hizi ni za mwaka wa jana, lakini pia nimeomba hizi pesa za India, nimesema nilidhani kwamba hizi fedha za India, Manyoni ingepewa awamu ya kwanza zipo awamu tatu hapo Mheshimiwa aliyenipa taarifa hebu apitie vizuri pale ziko awamu tatu wamegawanya Manyoni iko awamu ya tatu, tuna kiu, nimesema hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe na mimi nikubaliane na ile tozo ya shilingi 50 kwenye mafuta iongezwe ifike shilingi 100 mtusaidie na hii fedha ianzie Manyoni Mashariki jamani. Pia nakubaliana ya kwamba iundwe Wakala sasa wa Maji Vijijini kama ambavyo ilivyo REA, tusiiweke Seriakli kuu, Serikali Kuu tunaona pesa inapotea na usimamizi siyo mzuri naomba wakubaliane na hilo iundwe wakala kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa nafasi.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii adhimu ili nami nitoe mchango wangu. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais jinsi anavyokwenda, nasema mwenye macho haambiwi tazama, tunasonga mbele. Pili naipongeza Wizara ya Fedha kwa hotuba yake ya Bajeti Kuu ni bajeti nzuri ya kiwango. Nichangie kidogo tu kwa maana ya kufanya marekebisho madogo, lakini bajeti ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza bado Tanzania tunahitaji maji na hasa vijijini. Maeneo makubwa na mengi suala la maji ni shida kubwa. Niungane na ushauri wa Kamati ya Bajeti, moja ya vipengele ambavyo walikuwa wameshauri ni kwamba ile Sh.40/= tuongezee Sh.10/= ifike Sh.50/= ikaungane na ile tuipeleke kule kwenye Mfuko wa Maji. Tafadhali sana naomba ifanyike hivyo, vinginevyo hali ya maji bado ni tatizo kubwa sana hata katika uwekezaji huu bado itakuwa ni shida na hasa kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili lake la maji hilo hilo naomba sana Wizara inayohusika na maji igawe rasilimali maji kwa usawa. Kuna maeneo hasa ya vijijini asilimia zile, nimejaribu kuangalia bajeti ya maji ukurasa wa saba walipozungumzia kwamba asilimia 72.58 vijijini wanapata huduma ya maji ndani ya mita 400, inawezekana ni sawa, lakini baadhi ya maeneo, baadhi ya vijiji si sawa, Jimbo ninalotoka mimi la Manyoni Mashariki ni asilimia 18 tu, ndiyo wanaopata huduma ya maji vijijini. Ndio maana nimesema tugawe hizi rasilimali maji.

Mheshimiwa Spika, hii fedha iende sawa kama kuna maeneo yako chini, tuwanyanyue na wenyewe, wale ambao wamefikiwa hiyo asilimia 72 basi sawa, lakini hawa ambao wako chini, wanyanyueni na wenyewe twende kwa pamoja, nataka nilisisitize hilo kwa sababu Manyoni kule hali ni mbaya na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili bado nalalamika kwamba miji na vijiji naomba tuvipange kwa maana ya kupanga na kupima, bado hali ni mbaya,

kupanga miji na vijiji kwanza ukusanyaji wa mapato unakuwa rahisi sana, tunaimba property tax, tunaimba land rent, haitakuwa na ubishi inapokuwa tumepanga miji yetu, lakini pia huduma zingine zote. Unapokuwa umepanga mji wako au vijiji vyako huduma zote zinakwenda vizuri na ndio ustaarabu wa kibinadamu hatuwezi kukaa kama nyanya tumerundikana hivi, haiwezekani tupange miji yetu.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ardhi mimi nasema imeelemewa isaidiwe. Kusaidiwa kwake, tuwape Halmashauri nguvu za kupima vijiji na miji na unapowapa Halmashauri kazi hii maana yake ni kwamba uwawezeshe ile retention ya fedha, makusanyo ya kodi za viwanja zile ile asilimia 30 bado naihitaji ibaki kwenye Halmashauri tuwasaidie Wizara ya Ardhi kupima, wenyewe hawataweza. Kwa mfano, mwaka jana wamefanya kazi kwa asilimia 30 tu ile fedha imetoka asilimia 30 tu. Hawawezi kupanga na kupima miji wao wenyewe, haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, wamepeleka wataalam kule kuna Valuer kule kuna Surveyor kule, kuna Maafisa Mipango Miji kule Halmashauri, sasa kwa nini tusiwaachie hii asilimia 30 wapime huko wawasaidie. Wao wabaki tu ku–control? Kwa nini wang’ang’anie kukumbatia hii kazi na hawawezi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, naomba ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Fedha, ufafanuzi kwenye ukurasa 48 viwango vya kodi za majengo. Hapo kuna utata kidogo. Mimi ni mtaalam, unaposema flat rate kwa maeneo ambayo hayajafanyiwa valuation, sawa sikatai flat rate lakini flat rate ifanane fanane basi. Unaposema Sh.10,000/= kwa majengo ambayo yako chini, hujaweka pia categories ni ya aina gani, kuna watu wamejenga (massions) majumba makubwa lakini yapo chini, ukiangalia jumba kubwa zuri, hamjatenganisha ni biashara au ni ya makazi hii Sh.10,000/=, utakuta kuna gest houses sio za ghorofa lakini ni kubwa zina vyumba karibu 20 – 30 na wenyewe walipe hiyo property tax 10,000? Naomba waifafanue vizuri watumie wataalam wapo, tupo wataalam.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache, niongezee kwenye hiyo property tax. Property tax pia ninavyojua mtalaam inalipwa mijini sheria ile ipo, waitazame ile sheria. Sheria hii tunaiita Local Authority (Rating) Act, 1983 inasema ni mijini. Sasa mnaposema property tax iende mpaka vijijini sijaelewa na imetoa category ya nyumba sio ya tembe iwe nyumba ambayo angalau ya bati kwa mijini, sasa sijaelewa kama property tax tunaenda kuwatoza mpaka vijijini kule kwenye vijumba vya Wagogo vile vya tembe, sijafahamu.

Mheshimiwa Spika, naomba ufafanuzi na watumie wataalam zaidi pia, kwenye flat rate hiyo lakini na kwenye category ya majengo. Hata ghorofa nayo ina category zake, unakuta ghorofa ina vyumba vingi sana, kuna flat za kuishi kuna maghorofa ya biashara sasa ghorofa ipi ambayo itaingia kwenye flat rate kwamba ilipe 50,000; tutapoteza mapato mengi hapa lakini pia tutawaonea watu wengi hapa, naomba waifafanue sana watumie wataalam.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja na naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, asimame na msimamo ule ule, nchi hii sasa twende mbele.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DANIEL E. MTUKA: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi hii fupi nitazungumzia mambo mawili tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Wizara, nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, niseme tu kwamba Wizara hii mmeibadilisha mmeitoa mbali mmeibadilisha, wataalam wa ardhi tunajivunia sana kwa kweli kazi mnayoifanya mko aggressive, lakini pia mna- confidence na lakini la mwisho ni wachapakazi, tunawapongeza kwa hilo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maombi mawili mafupi, ombi la kwanza niunge mkono pia Wabunge wenzangu, retantion scheme ile asilimia 30 ya makusanyo ya kodi ya ardhi, naomba ibaki kwenye Halmashauri isiende huko Hazina, kwa sababu ikienda kule hairudi haraka mnatuchelewesha sisi tunataka tupime viwanja, squatter zinatusumbua, ninaomba sana hilo Mheshimiwa Waziri wakati una wind up hebu liweke vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unalia hapa kwamba malengo hayakutimia kwenye kupima viwanja na wataalam umeshawasambaza kwenye Kanda, acheni tupime ardhi Wilayani huku kwenye Halmashauri mnazipeleka hizo pesa za nini huko, nilikuwa nataka kulisisitiza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tuna ombi Manyoni, tunao upungufu wa watumishi. Wataalam wa ardhi tulionao pale Halmashauri wanatakiwa wawe 21 lakini wapo wa wanne tu, watafanya kazi gani? Squatter hizi zitaendelea pamoja na hayo tunajitahidi kweli tangu mwaka juzi mpaka sasa ninavyozungumza tumepima viwanja karibu 991 ambavyo tayari tunavigawa kule, kwa shida kwa kujibana bana lakini viwanja 1,400 tumevipima viko kwenye hatua za mwisho tunakamilisha cadastral survey kwa ajili ya kupata approve.

Mkeshimiwa Mwenyekiti, 220 tumefanya regulazation tunaanda hati tupo kwenye hatua za mwisho, watumishi wanne hawa tunajitahidi. Kama haitoshi tumejibana fedha kwa shida, tume-order GPS RTK sisi watu wa Manyoni inakuja na tumeshailipia, tunaomba basi mtusaidie mtuunge mkono, hatuna gari kwa hawa watalaam wa ardhi, Mheshimiwa Lukuvi tusaidie gari kama juhudi zote hizi tumejitahidi si mtuunge mkono jamani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tunayo Sheria Namba 8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007, tangu mwaka huo imetungwa lakini haina regulations hazijatungwa, inatekelezwaje hii sheria bila regulations? Naomba mjitahidi hii sheria itungiwe regulation zake. Tunasema kwamba planning ndiyo inayoanza, sasa mnafanyaje kazi bila regulations tangu muda wote ule?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni hili la ujumla, hebu tuitumie ardhi vizuri, ujezi wa horizontal ambao wa mtawanyiko siyo mzuri tunamaliza ardhi hii, ardhi itaisha Dar es Salaam kama tunge-opt vertical development tungekuwa tumeishia Magomeni tu pale. Ile population ya Dar es Salaam siyo watu wengi, lakini kila mmoja anataka amiliki kiwanja na eneo afuge mpaka kuku, siyo rahisi ardhi itaisha hii, tuende juu tusitawanyike tubakishe na maeneo ya kulima, tutalima wapi? Sasa kila mahali ni kujenga tu, haiwezekani lazima tu- plan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi National Housing wanavyojenga, kwa mfano nimeona ghorofa za Wanajeshi hapa Dodoma hapa, ziko vizuri, na scheme zingine za kujenga hebu waende ghorofa mbili tu juu watoe mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naunga mkono hoja, lakini retention scheme, ile fedha ibaki kwenye Halmashauri ili iwasaidie kupima viwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu katika mpango huu. Kwanza nitangulize tu kutoa shukrani zangu kwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli, amefanya mambo makubwa na kila mtu anaona. Kwa mfano, kwangu kule Manyoni hatukuwa na miradi ya maji, lakini sasa tuna miradi ya maji, fedha imeanza kutoka tunashukuru sana angalau mradi hata mkubwa wa wastani mmoja unaendelea. Sina budi kutoa shukrani zangu kwa niaba ya wananchi wa Manyoni Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nizungumzie jambo fupi tu. Tulikabidhiwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, lakini pia hata wenzetu wanatumia Ilani hiyo. Katika Ilani hiyo nimeigawa katika makundi makubwa mawili ya kusimamia. Eneo la kwanza ni la huduma za jamii, tunapozungumzia maji, afya, elimu, miundombinu, hizo ni huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti,eo nizungumzie suala la kuboresha uchumi kwa wananchi wetu, wamepata maji sawa, natoa mfano, lakini uchumi wao ukoje? Vile vikundi vyetu vya ujasiriamali vikoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na maoni ya Kamati katika ukurasa ule wa tano, kipengele cha pili kinasema, “Kuzingatia maeneo yanayogusa wananchi walio wengi kwa ajili ya kukuza kipato na kupunguza umaskini, hususan kilimo, uvuvi, upatikanaji wa pembejeo na mitaji.” Mimi nijikite kwenye eneo la kilimo. Manyoni kwa mfano, Mbunge pamoja na Madiwani wenzangu tunalala na kusugua vichwa ni namna gani tupate kuwawezesha wananchi wetu kupata ajira, tufanye nini, lakini tumekuja na tunayo mambo matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza; hivi ninavyozungumza Manyoni Mashariki eneo linaloitwa Masigati tumetenga ekari 3,200 kwa ajili ya kuanza ukulima wa korosho baada ya wataalam kutoka Naliendele kupima ule udongo na kutuambia mkilima korosho hapa mtapata korosho nyingi na bora kuliko zile za Lindi na Mtwara. Tumeshatenga ekari 3,000 hivi ninavyozungumza tunachangishana fedha kwa ajili ya kupata grader la kufyeka ule msitu, ili tuanze kupanda korosho na miche imeshaanza kuoteshwa kwenye vitalu, ekari 3,000. Tumeshachanga fedha shilingi milioni 36 mpaka sasa hivi kwa ajili ya mafuta, ila hatujui grader tulipate wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa bajeti hii inayokuja tukitenga fedha kidogo angalau kuwaunga mkono wananchi, Serikali tunaomba ipitishe ile bajeti ya watu wa Manyoni kwenye eneo hili la kilimo, ili tuweze kuajiri watu wengi zaidi pale Manyoni. Kama kiongozi, lazima tulale na kuota namna gani tutaweza kuongeza ajira kwa watu wetu. Manyoni tumeanza na tunaendelea, tunaomba Serikali ituunge mkono kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu huu sasa tungefurahi kusikia Serikali inasema angalau kuna kafedha ka dharura au kuna grader ambalo lipo mahali fulani kwenye Wizara labda ya Ujenzi, fedha tumeshakusanya ya mafuta, wakatusaidie kufyeka ule msitu tupande korosho, tutaajiri watu wengi sana kwenye eneo hilo, zaidi ya watu 3,000 watapata ajira Manyoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine hapo Manyoni kuna Kijiji kinaitwa Solya, ni katika kupambana tu kutafutia watu ajira, kuna eneo tumelitenga ni la mfano tunataka tuanze shamba darasa, tuna heka 10 pale. Tumeshachimba mabwawa ya urefu wa mita 10 kwa 20 yapo nane ya samaki. Pia tuna heka mbili tumeshaanza ni shamba darasa kwa ajili ya bustani, tunataka vijana wote ambao hawana ajira kwenye eneo lile waanze kupata ajira. Shamba darasa lile litasaidia sana kwa vijana wa Manyoni na maeneo mengine yote watakuwa wanajifunza pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo, maji yale ni ya kuchimba chini, tumechimba kisima kwenye shamba darasa pale na umeme tumevuta kwa nguvu zetu wenyewe. Hata hivyo, lakini kuna eneo ambalo tumelitenga ni kubwa pia la hekari 20, tunahitaji visima vitatu na wameshapima visima maji yapo lakini hatuna uwezo wa kuchimba vile visima. Kikubwa miundombinu ya umeme kwa sababu lile eneo ni nje kidogo ya kijiji. Tungeomba Serikali ituunge mkono, itusaidie zile nguzo zitoke pale, ni kama kilometa moja na nusu hivi zitoke kwenye sehemu ya umeme watupelekee umeme kwenye eneo hilo la shamba. Tunaomba sana Serikali itusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo ni mbinu ambazo Kiongozi yeyote ambaye anaweza kuona mbele, lazima afikirie kuongeza ajira na kutafuta ajira kwa watu wake na hasa vijana, akinamama na watu wote. Manyoni viongozi tunakosa usingizi kwa ajili ya kuongeza ajira, kumsaidia Mheshimiwa Rais anahangaika sana, Serikali mtuunge mkono, Manyoni tumeanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo eneo pia la machimbo ya chumvi, eneo linaitwa Kijiji cha Kinangali, tunayo chumvi nyingi sana, tunaomba sana msaada kwenye mambo ya kitaalam namna ya kuchakata ile chumvi, tunatumia mbinu za kizamani, tunakata miti sasa tunaharibu mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali mtusaidie utalaam, tumejaribu sana lakini tunaomba sana Serikali hasa sehemu ya Wizara inayohusika na mambo ya ajira na vijana, hebu watusaidie wataalam ile chumvi inavyochakatwa hasa kwa njia za kitaalam, tunayo chumvi nyingi sana. Tutasaidia ajira vijana wengi sana na akinamama kwenye lile eneo. Manyoni sisi tumeanza, tunaomba Serikali ituunge mkono kwenye maeneo haya ambayo nimeyataja hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikihama kwenye eneo hilo la kuongeza ajira kwa watu wetu, labda la mwisho tu. Jamani ndugu zangu haiwezekani katika nchi hii kila mahali ikawa ni sehemu ya kuishi, msitu mnene unakuta umefunga, mtu anatoka atokako anakaa katikati ya msitu. Kule Manyoni wanatuvamia watu wahamiaji, anakaa katikati ya msitu, miti minene ile imekua kwa miaka mingi, karne na karne mizuri katikati ya msitu anaanza kufyeka anajenga, anafyeka shamba na sehemu ya kulishia mifugo. Haiwezekani kila mahali pakawa pa kujenga tu, lazima tutunze mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia ule mpango wa matumizi ya ardhi ambao tumeusema tangu mwaka juzi, mpango huu unachelewa mno. Naomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mtusaidie kuharakisha huu mpango jamani, wakulima na wafugaji wapate maeneo yao, sehemu ya kujenga na viwanda pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuipime Tanzania, tuhifadhi mazingira jamani, ni sawa na mtu ambaye amepanda juu ya mti, amekalia tawi anafyeka kwenye shina kule, likidondoka lile tawi anatangulia yeye chini. Hawezi mtu kukaa katikati ya msitu anaanza kufyeka eti natafuta shamba ama anatafuta sehemu ya kujenga, haiwezekani. Anaacha vijiji vingi tu anaruka anakuja kujenga katikati ya msitu, haiwezekani! Tuipime Tanzania katika mpango huu wa matumizi bora ya ardhi, tuiokoe nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema hata mwaka jana nilisema hivi kwa mfano, hata hii migogoro ya mkulima na mfugaji tulisema tupime, sijui mpango umeishia wapi? Kwamba tupime, kuna maeneo mengi tu tunawanyanyasa wafugaji bure, kuna maeneo mengi ambayo tukijipanga vizuri tukayapima kila mmoja atakaa sehemu na mifugo yake kwa raha mustarehe wala haina shida, eneo tunalo kubwa tunakosa mpango tu. Ni mpango tu ndugu zangu tunaokosa ndio maana tunagombana, haiwezekani mfugaji au mkulima anakuja anachukua heka 1,000, wengine wanapata wapi? Ni lazima kila mmoja apate eneo ambalo atakaa nalo kwa kudumu pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo hifadhi za misitu au za wanyama ambazo zimekuwa redundant ambazo zimekosa sifa, zile tungezipima tukazigawa hata kwa wakulima na wafugaji. Tunazo ranchi zetu ambazo zimekuwa redundant tuzipime tuweke miundombinu, malambo, mabwawa na wataalam wa mifugo ili watu wafuge kule. Jenga hata viwanda vya kuchakata/kusindika nyama kule; tunayo maeneo makubwa tunakosa mpango tu, utaratibu mzuri wa kupima, tuipime Tanzania jamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mafupi, mimi sina cha zaidi, naunga mkono mpango huu, tuyazingatie haya mawili niliyoyazungumza, tulale na kufikiria kuwatafutia watu wetu ajira. Serikali ituunge mkono lakini tukaipime Tanzania kila mmoja apate mahali pa kufanyia kazi bila kugombana, kuharibu mazingira wala vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Niende moja kwa moja kwenye hoja kwanza niwapongeze wawasilishaji wetu Wenyeviti wa Kamati zote tatu kwa maana ya sheria ndogo, huduma za jamii pamoja na katiba na sheria. Niseme kidogo kuhusu kwa nini tunatunga sheria? Tunatunga sheria kwa ajili ya kuleta utengamano katika jamii pia kulinda haki za watu wote na hasa wanyonge. Hii ni tafsiri tu ya mtu ambaye yuko mtaani sio msomi lakini kwa ujumla hiyo ndio tafsiri ya sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Magufuli amekuwa makini sana katika kuzingatia utawala wa sheria, ni mwepesi sana. Tumeona hapa kila tunapopitisha sheria mara moja anazisaini kwa sababu anataka kwenda kuzifanyia kazi ili kuendeleza huu utawala wa sheria. Pia amekuwa mkali sana Mheshimiwa Rais hasa kwenye sheria hizi ndogo, ukichelewa kutunga kanuni ninyi watu ambao mmepewa mamlaka ya kutunga kanuni hizi Mheshimiwa Rais amekuwa mkali sana. Mmeshuhudia hivi karibuni sheria nyingi ambazo zimetungwa ambazo hazijawekewa kanuni Mheshimiwa Rais amekuwa mkali sana.

Mheshimiwa Mweyekiti, kwa utangulizi huo labda niseme tu mafupi kuhusu sheria ndogo. Nizungumzie tu umuhimu wa sheria ndogo. Sheria ngogo ni muhimu sana, ni sawasawa na sheria mama zile ambazo zinatungwa. Huwezi ku-apply sheria mama kama hujatunga kanuni, haiwezekani, itakuwa dormant ndio maana Mheshimiwa Rais amekuwa mkali kwamba tumetunga sheria hii mbona hamjaniwekea kanuni ili niweze kutekeleza sheria hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika uchambuzi wa mimi ni mmoja wa wajumbe wa Kamati hii ya Sheria Ndogo, katika uchambuzi wetu tumegundua mambo mengi sana ambayo tumesomewa hapa. Tathmini yangu karibu asilimia 50 ya sheria ndogo ambazo zimekuwa zikipita kwenye kamati yetu kwa kweli zina makosa. Sample hii naipeleka kwa nchi nzima kwa ninyi mliokasimiwa mamlaka haya ya kutunga kanuni kwa mujibu wa Ibara ya 97 naomba sana muwe makini kwa sababu mnapokuwa mnafanya makosa kwenye utungaji wa kanuni hizi zinakwenda kujeruhi wananchi, zinakwenda kuumiza watu. Kwa mfano tumeona ushuru wa mazao, kwa mfano mzuri hapa mwezi Julai wakati Waziri wa Fedha anasoma hotuba yake ya bajeti alisema mazao ya biashara ushuru utozwe asilimia tatu na ya chakula asilimia mbili lakini kuna Halmashauri bado zinatoza mpaka asilimia tano. Hii ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeletewa hapa tumejaribu kuangalia tumeshauri ikiwezekana wakati mwingine wapewe adhabu hawa wanaosimamia vitengo hivi vinavyotunga hizi kanuni zinaumiza wananchi wazingatie haya maoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizitake tu mamlaka kwa ujumla zote Wizara zote, agencies zote na mamlaka zote ambao wamekasimiwa mamlaka haya ya kutunga hizi kanuni wawe makini sana. Tumeona mfano wa hiyo Sheria ya Nzega ile ya Hifadhi ya Mazingira ni ya ajabu sana, unazungumzia Ziwa Tanganyika wewe upo Nzega. Mita 60 kwamba m-preserve mita 60 msilime ndani ya mita 60 kutoka ukingo wa ziwa, hii ni mbaya sana.

Mimi ningekuwa Mheshimiwa Waziri ningekuwa nimeshampa adhabu huyo ambaye alikuwa amesimamia kutunga hii sheria ndogo, hii ni mbaya sana inaonyesha watu wanaumia sana hasa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hii copy and paste watu hawasomi, hizi sheria zinapita maeneo mengi sana lakini mpaka waziri analetewa kusaini kitu kama hichi ni ajabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naunga mkono hoja zote tatu nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DANIEL E. MTUKA: Ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nashukuru kwa nafasi hii fupi, lakini nitajitahidi kujikita kwa harakaharaka kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya, Watanzania wote wanaona. Pia niwapongeze Mawaziri wanaohusika na Wizara hii, Mheshimiwa Profesa Mbarawa na ndugu yangu Mheshimiwa Kwandikwa, tunaona juhudi zao na wanavyochapa kazi kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe shukrani zangu baada ya kutizama kitabu hiki cha bajeti, Jimbo langu la Manyoni tumetengewa fedha katika barabara za Ikungi – Londoni – Kilimatinde; Manyoni – Heka – Ikasi; Heka – Iluma na pia Daraja kubwa la Sanza nalo limetengewa pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niombe ufafanuzi tu kidogo hapo kwenye barabara ya Ikungi – Londoni – Kilimatinde. Katika ukurasa wa 221, nimeona kuna barabara kama mbili tofauti, kuna moja imeandikwa Ikungi – Londoni – Kilimatinde na nyingine imeandikwa Ikungi – Kilimatinde. Mimi naona hicho ni kitu kimoja, lakini naona wametenganisha na fedha zimetengwa kwa kila kipande shilingi milioni 60. Kama ni kitu kimoja basi ile pesa msiitoe, iunganisheni tu basi nipate shilingi milioni 120. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mawasiliano ya simu. Wilaya ya Manyoni imekuwa na tatizo kubwa sana la mtandao wa simu, lakini naishukuru Serikali kwa kiasi imejitahidi sana kutujengea mitandao. Niombe kasi ya Kampuni ya Halotel ambao wamepewa tender hii hebu wafanye haraka, ni mwaka mzima sasa kwa mfano sehemu za Asasilo, Mpapa, Sanza na Nkonko minara wameweka tu misingi, hawaja-erect ile minara na kuwasha simu kwa mwaka mzima sasa. Naomba wahimizwe basi wajenge ile minara na kuwasha ili tuweze kuanza kuwasiliana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia maeneo ambayo hayasikiki kabisa katika jimbo langu ni vijiji vya Hika, Igwamadete, Mangoli, Mafurungu, Simbangulu, Imalampaka, havina kabisa mawasiliano. Ukifika katika eneo hili unakuwa kama uko katika kisiwa. Kampuni ya Halotel tunaomba sana Mheshimiwa Waziri awahimize kwa sababu ndiyo waliopata tender na wamezuia wengine, wafanye haraka basi sisi tunahitaji mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa reli, nizungumzie kidogo suala la reli ya Singida – Manyoni. Reli hii ilifunguliwa tarehe 24 Oktoba, 1985, ilikuwa kwa ajili ya kusafirisha mazao ya pamba na ngano kule Basuto pamoja na kuwasafirisha abiria na ilianza ku-operate vizuri sana ilikuwa na mabehewa matatu, mabehewa ya abiria mawili na la mizigo moja, ilitusaidia sana kipindi kile. Cha ajabu nilishuhudia tarehe 9 Septemba, 2009 ndiyo ilikuwa safari ya mwisho kusafiri lakini tarehe 12 Septemba, 2009 safari hizi zilisitishwa rasmi tukawa hatuna treni tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anayehusika tunaiomba treni yetu ya Singida kwa sababu mlisema kwamba tumesitisha safari eti kwa sababu ya ujio wa lami na pamba hailimwi tena. Sasa hivi sababu hizo hazina msingi wowote kwa sababu mtu anaposafiri analinganisha gharama za usafirishaji. Sasa hivi tunajenga Daraja la Sibiti, tutapata mizigo kutoka Simiyu na maeneo mengi ya Singida pale, tunalima vitunguu, tunao kuku, tunayo miwa, tuna viazi, tunaomba sana mturudishie treni ile, Mwalimu Nyerere hakukosea kutuletea treni ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika ujenzi wa standard gauge, msiisahau hii reli. Ifungueni ianze ku-operate sasa hivi, lakini standard gauge itakapoanza kujengwa reli hii pia ikumbukwe, mtujengee standard gauge, tunahitaji sana hii treni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie ajali zinazotokea sana kwenye mteremko wa Mbwasa pale Chikuyu. Kumekuwa na ajali nyingi sana pale Mbwasa na pale Sekenke. Mimi kama mtaalam wa mambo haya ya ujenzi wa barabara nilipoangalia pale kuna makosa ya design.

Naomba sana Mheshimiwa Waziri atume wataalam pale waende Mbwasa na Sekenke waka-design upya, wanyooshe zile kona maana kuna mteremko halafu kuna kona ghafla. Lori linapo-fail pale huwezi kukata kona ukikata kona ghafla unalipiga ngwala lile lori lazima litaanguka tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba waka-design upya ili wanyooshe zile barabara ziteremke pale chini halafu kona isiwe kali sana. Hili linawezekana mimi kama mtaalam nimepita, nimeona kuna uwezekano kabisa wa kufanya marekebisho kuepusha ajali hizi, tunapoteza maisha ya watu wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, ahsante.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DANIEL E. MTUKA: Ahsante Mheshimiwa Spika na mimi kupata nafasi hii kuchangia Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii, kwa kutupa uhai, lakini pia naipongeza Serikali yangu ya Jamhuri ya Tanzania hasa Mheshimiwa Rais anavyofanya kazi, wote tunaiona.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze pia Wizara hii ndugu yangu Kigwangalla, shemeji yangu, kwa maana ya Naibu Waziri Hasunga, nawaona ni vijana wanachapa kazi, wanazunguka huku na huku ukimuona Mheshimiwa Kigwangalla shemeji yangu amepiga buti zile za kijeshi ananikumbusha mbali sana wakati nikiwa kambi za jeshi huko. Kwa kweli nawapongeza sana wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hayo ninayo maoni machache, mchango wangu mdogo na nikianzia, ukifungua kwenye kitabu chako ukurasa wa 19 nimekuta kuna ulinzi wa wananchi na mali zao dhidi ya wanyama pori wakali na waharibifu. Nimejaribu kupitia Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori (Wildlife Conservation Act) Namba 5 ya mwaka 2009.

Mheshimiwa Spika, kwenye sheria hiyo nimeenda nimeangalia zile regulations zake, kwenye regulations hizo za mwaka 2011 nimekuta kuna jedwali namba nne ambalo linaonesha viwango vya fidia wanazolipwa watu ambao wanauawa na wanyama, wanaopata ulemavu wa kudumu, wanaojeruhiwa pamoja na uharibifu wa mazao.

Mheshimiwa Spika, viwango hivi ni vidogo na vinasikitisha sana. Ukiangalia kwa mfano binaadamu anapouawa na mnyama, ukiangalia kwenye lile jedwali inasikitisha sana.

Mheshimiwa Spika, binadamu anapouawa anasema fidia ni shilingi milioni moja lakini anapopata ulemavu wa kudumu, anapata shilingi 500,000 tu. Hapana, hiki kiwango ni kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naweza nikatoa mfano mdogo siwezi kulinganisha na mwanajeshi anapouawa anapokwenda kupigania kulinda amani, kwa mfano labda Darfur kwamba ameuawa kwa bahati mbaya. Tulijibiwa hapa na Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi kwamba fidia ya huyu mtu ni karibu milioni 150.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo hata wale waliouwawa kwenye vita vya Kagera wanalipwa pesa nyingi sana mamilioni ya fedha. Nimesema siwezi kulinganisha lakini angalau ukiangalia shilingi milioni moja dhidi ya milioni 150? Haya ni maisha wote wanakuwa wamepoteza maisha wanaacha familia zinahangaika lakini shilingi milioni moja ya fidia hii haitoshi hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara hii, shemeji yangu Kigwangalla naomba unisikilize, rudi, toeni mapendekezo, leteni hizi regulations, zibadilishwe viwango hivi viongezwe tafadhari; hiyo ni moja. Hata hivyo bei yake kwenye uharibifu wa mazao, nimejaribu kupekua sheria nimeangalia regulations na sheria zote zinazohusu wanyamapori kwenye fidia. Sasa hivi kwa mfano tumekuwa na shida sana manyoni sisi.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na shida sana, kwa mfano pale Manyoni. Manyoni tumepakana na Pori la…

T A A R I F A . . .

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwenye mazungumzo ya kawaida binadamu mnapokutana huwezi kuongea umekunja uso tu, unaongea maneno magumu, lazima uchombeze kidogo, naomba niendelee. Nimesema hiyo ni bei yake fidia hiyo ni ndogo. Nimesema fidia hiyo haitoshi, tafadhali sana leteni sheria zibadilishwe ili fidia hii iongezwe. Mnasema kifuta machozi, kwenye uhai sawa ni kifuta machozi, lakini famila inaachwa inaachwa hii. Shilingi milioni moja ndugu yangu ni kiwango kidogo sana hata hakiwezi kusemeka.

Mheshimiwa Spika, nimesema pia pili yake, mazao yanapoharibiwa ndani ya nyumba. Nimesema manyoni sisi kule unapakana na Mapori ya Mhesi na Kizigo, sasa wanyama wanahama, kiangazi mkulima amevuna mazao, ameweka ndani kwenye vihenge, amefungia ndani ya nyumba, tembo anatoka porini huko atokako anakuja anabomoa nyumba ananyanyua lile tembe la nyumba, anatafuta kihenge kiko wapi anakula mahindi yote kabisa yanaisha.

Mheshimiwa Spika, lakini nimeangalia sheria hakuna fidia. Ni bora hata yawe yameliwa porini, hiyo naweza nikasema sawa angalau, lakini mtu ameyavuna ameyaweka ndani tembo anakuja atokako anakula mahindi halafu hakuna fidia. Naomba pia turudi kwenye sheria, naomba turekebishe kipengele hicho. Kama mnyama ameingia, ameumiza mtu, amekula mazao pia hicho kipengele cha fidia kiwepo.

Mheshimiwa Spika, nisemee tatizo la mipaka kwa ufupi sana. Sisi Manyoni tumepakana na mapori mawili ya Hifadhi ya Mhesi na Kizigo kama nilivyosema. Mwaka 1994 Mhesi Game Reserve ilianzishwa, ni moja ya reserve changa kabisa ambayo ina ukubwa wa kilometa za mraba 2000. Ujio wa Mhesi imeleta kilio kikubwa sana kwa watu wa Manyoni kwa sababu kama ambavyo wenzangu wamelalamika, imeua vijiji na vitongoji vingi sana. Kwa mfano tulikuwa na vitongoji vya Chisola, Msisi, Ilowelo, Machochoroni, Mkindiria, chigugu, Ngongolelo, Chibwee na Iluma.

Mheshimiwa Spika, vijiji hivi tulikuwa tunavitumia kwa kilimo, machimbo ya dhahabu, kwa mfano Iluma pale. Ukichukua taarifa ya benki ya mwaka 1992 dhahabu inayotoka iluma ni dhahabu inayoitwa alluvial ambayo haijawahi kuchimbwa mahala popote duniani. Machimbo ya dhahabu tunajua huwa wanasaga kwenye mawe, wanatumia madawa makali, zebaki lakini ile unachimba tu unapuliza puliza lile vumbi basi unauza imeshajiunda tayari imeshaji-mould tayari, angalieni tarifa za benki za mwaka 92. Wameweka mipaka, wamezuia yale machimbo, ilikuwa ni neema kwa watu wa Manyoni. Jamani, hii mipaka hii, tuangalie upya mipaka hii ndugu zangu.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nizungumzie suala la uwekaji wa mipaka, wenzangu wamelalamika pia. Uwekaji wa mipaka tunaviziana, uwekaji wa mipaka si shirikishi kwa wananchi. Wanakuja huko watokako tunaona watu wanachimbia mambo wanaondoka, baadae inatolewa taarifa kwamba ninyi hapa mnatakiwa msiwepo maeneo haya. Jambo hili ni baya sana na limeleta mateso kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia pili, mipaka hii haionekani. Unaenda kuchunga ng’ombe hujui mpaka uko wapi, kumbe umeshavuka uko ndani ya hifadhi yao. Kipigo kinachofata hapo kwa wananchi wetu ni kikubwa mno ndugu zangu. Manyoni haisemwi sana sijui kwa nini, lakini Manyoni kuna watu wanateseka sana kwenye hii Mhesi na Kizigo.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2016 nakumbuka ulikuja msafara wa wananchi kutoka Manyoni. Nina vijiji 12 vinavyogusana na mpaka wa Manyoni kule Mhesi na Kizigo, nakumbuka sana, ilikuwa tarehe 25 Mei, na mimi mwenyewe niliwaongoza; walikutana na aliyekuwa Naibu Waziri kipindi kile Mheshimiwa Ramo Makani, kwenye Maliasili na Utalii. Vile vile walikutana na ndugu yangu Mheshimiwa William Tate Ole-Nasha akiwa Naibu Waziri wa Kilimo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, tuliongea kwa muda mrefu, tukapewa ahadi ndugu zangu mwaka 2016. Hata hivyo hata ile Kamati iliyoundwa kwenda kutatua migogoro ya kitaifa ile Manyoni hata hawakugusa, sijui ni dharau, sijui ni kitu gani? Watu wametekesa sana, wamekuja kwa utiifu wao, wamekutana na Mawaziri wametoa wito na wameahidiwa kwamba Wizara itakwenda. Kamati imeenda hata hawakupita Manyoni kwamba yaani wale hata hakuna kitu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja lakini tafadhali sana, naomba sana wananchi wangu wanapigwa sana kule Manyoni, njooni tutatue tatizo la mipaka. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii ili nami nitoe mchango wangu katika bajeti hii ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Niwapongeze sana Waheshimiwa Mawaziri hawa wawili, Waziri Lukuvi na Naibu wake, dada yangu Mabula, wanafanya kazi kubwa sana kwa sisi wataalam kwa kweli wanatufurahisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo, nina maombi mawili/matatu. Ombi la kwanza nianze na Wilaya yangu ya Manyoni. Nimejaribu kupekua kitabu hiki cha bajeti cha Mheshimiwa Waziri, nimefurahishwa sana na mipango hii kabambe ya uendelezaji wa miji na naziona juhudi katika wilaya nyingine. Hata hivyo, mara nyingine nimekuwa nikiimba sana na kuomba na kulia kwamba hebu itazameni na Manyoni katika mipango hii kabambe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalia kwa sababu Manyoni naitazama iko karibu na Dodoma, Manyoni pale ni kama hub ya mkakati wa maendeleo. Dodoma itakapojaa, mahali pazuri pa kupumulia ni pale Manyoni na si mahali pengine; kwa nini wanakuwa wanairukaruka? Nimechambua sana na naona Manyoni iko sidelined. Naomba sana wajaribu ku- concentrate Manyoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Manyoni pale tukiweka mipango kabambe tuna nafasi za viwanda, nimehangaika katika juhudi zangu binafsi, nimewasiliana na Walimu wa Morogoro, tumepatiwa wanafunzi pale, tunahangaika sana kuwalisha, kuwatunza kidogo angalau kwa bei nafuu, lakini bado tunazidiwa na juzi walikuwepo pale wameondoka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mkono wa Serikali basi, hebu tuipange Manyoni, kwani kuna shida gani Manyoni? Naona wanaruka tu, wakienda wanapita Manyoni kama vile hawaioni, wakati ile ni hub nzuri kwa maendeleo wapange ule mji, utatusaidia sana utasaidia maendeleo ya Dodoma hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliongea kwa uchungu kwa sababu nimekuwa nikifuatilia kwa muda mrefu na mimi ni mtaalam; sasa ninapoona maeneo mengine yanapewa huduma lakini Manyoni inarukwa na iko karibu na ni strategic position Manyoni pale, inaniumiza na inawaumiza watu wa Manyoni. Mheshimiwa Lukuvi, naomba hebu aikumbuke Manyoni, please.


Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nalo niseme, nimeona katika ukurasa wa 45 Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi, tumeona TANAPA walivyojitoa sasa kusaidia vijiji. Nikiona namba ya vijiji vile 392, sijajua, hakuna mchanganuo, sijui kama Manyoni pia ipo kwa sababu TANAPA inasaidia hivi vijiji ambavyo vimepakana na hifadhi za misitu, wanyama. Manyoni inavyo vijiji 12, sasa sijui kama Manyoni na vijiji ndani ya Manyoni ni miongoni mwa hivi vijiji 392.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, tafadhali, kama havipo hebu wavitazame waviweke, wasiipitepite Manyoni hivi hivi, Manyoni ni Mji mzuri mno, tunauita Ghana ndogo ile. Manyoni kwa wanahistoria ndiyo wilaya ya kwanza kuwa na Mkuu wa Wilaya Mwafrika, tuikumbuke Manyoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika Mpango huo huo ukurasa wa 45, hawa wenzetu wa misitu, pia nao wanasaidia katika upangaji wa matumizi bora ya ardhi. Naomba pia katika vijiji 50, sijajua kama Manyoni pia ipo, watusaidie kuipanga Manyoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niombe tu kwa ujumla kama ambavyo katika hotuba zote za bajeti za mwaka jana, mwaka juzi, mwaka huu, wanazungumza maneno mazuri sana, kwamba kupangwe matumizi bora ya ardhi katika nchi hii ili kupunguza migogoro; hebu wapunguze maneno sasa twende kwenye vitendo. Mimi napenda sana vitendo kuliko maneno, ndiyo maana huwa siongei sana, napenda sana kutenda, wakatende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo mafupi ambayo nilikuwa nataka kuchangia. Nashukuru sana kwa nafasi hii.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuwa kitinda mimba katika mjadala huu wa leo. Nami napongeza Kamati hizi tatu kwa taarifa zao nzuri. Pia nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesimama kidete sana katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na ndiyo maana tunaona matokeo haya sasa, tunazungumza ujenzi wa mambo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye Kamati, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI na Utawala. Kamati hii imetoa taarifa nzuri, nijazie tu kidogo kwa upande wa ukurasa wa 57 kuhusu ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya pamoja na zile hospitali 67 na vituo 350. Pale tumefanya ziara katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, lipo tatizo dogo kwamba katika utoaji wa fedha hatukuangalia sana, tumetoa ile flat rate, hatukuangalia utofauti wa maeneo. Maeneo yanatofautiana, kuna mengine yana udongo mbaya, topography nyingine ni mbaya.

Mheshimiwa Spika, tulienda Kituo cha Afya Mlali, walipewa shilingi milioni 400. Kuna maeneo kweli zimetosha, lakini Mlali hazikutosha. Ukiona kile kituo, wanasema kimekamilika lakini ukiangali ubora wa majengo, kwa kweli hauko sawa sawa. Majengo yameanza kupasuka kabla hata hayajakabidhiwa. Kwa hiyo, utoaji wa fedha uangalie maeneo na maeneo.

Mheshimiwa Spika, kuna vituo vingine wamejenga, lakini fedha zimeisha na vituo havijakamilika, kwa maana kwamba walizingatia ubora. Sasa katika kuzingatia ubora, zile fedha zikawa hazitoshi. Serikali itoe zile fedha iongeze vituo vile vikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la elimu kidogo. Tunao Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2016. Huu waraka unazungumzia ufaulu au kuruhusiwa Kidato cha Pili kurudia mwaka baada ya kufeli, kuvuka ile asilimia 30. Sasa hakuna waraka mwingine, ni huu katika private na shule za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kuna taarifa ambazo tumeletewa katika Kamati, kuna shule zinarudisha wanafunzi au zinahamisha wanafunzi ambao wameshavuka hizi asilimia 30, wameweka viwango vya kwao 45 na 50, wakishindwa kuvuka hiyo wanarudishwa na wengine wanahamishwa kabisa wanaondolewa. Anaitwa mzazi kimya kimya, anaambiwa mzazi huyu mtoto hakufaulu, hapa siyo mahali pake, mpeleke shule nyingine.

Mheshimiwa Spika, natoa masikitiko yangu, huu ubaguzi unatoka wapi? Hawa watoto ni wetu. Vidole hivi ni vitano lakini havilingani pia. Hawa watoto ni wetu, tunalilia kujenga umoja, leo tunataka shule zetu watoto cream, yaani tunataka wawe na akili tu! Wote wanaofanana ili wapate Division One wote! Hii haikubaliki. Unaposema ahamishwe, apelekwe wapi? Wewe humtaki, nani atampokea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba huu Waraka, atakaposimama kama atapata nafasi Waziri anayehusika, mwenye dhamana, Profesa wangu, hebu atoe msisitizo kwa hizi shule ambazo zinakataa hawa wanafunzi ambao wameshafaulu kwenye hii asilimia 30 lakini wanaondolewa ili tu kulinda hadhi ya shule waweze kuvutia biashara. Hii siyo biashara, hii ni huduma. Hudumieni hawa watoto, ni wa kwetu sote hawa watoto, ni wa Taifa hili. Sasa mnapoanza kuwabagua…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mtuka. Nakushukuru sana kwa mchango wako, dakika tano zimeisha.

MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hizi Kamati zote tatu kwa taarifa zao nzuri. Nakushukuru kwa nafasi hii, ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Mtuka, ile Mlali uliyokuwa unasema ni ya Kongwa au ya wapi?

MHE. DANIEL E. MTUKA: Ya Kongwa.

SPIKA: Nashukuru sana.

MHE. DANIEL E. MTUKA: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa zawadi ya uhai tumekutana tena safari hii, hii ni bajeti ya nne; tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya, kiongozi mahiri, wa kiwango na wa wakati huu. Nipongeze wizara hizi mbili hasa zikiongozwa na Mawaziri mahiri; Mheshimiwa Kapt. (MST) George Mkuchika pamoja na kaka yangu Mheshimiwa Jafo kwa kazi kubwa wanayoifanya pamoja na Naibu Mawaziri wao, Makatibu Wakuu, Naibu Katibu Wakuu na timu nzima katika idara zao katika wizara hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niungane na Mheshimiwa Mbatia leo ni tarehe 12 ni siku ambayo tulimpoteza kiongozi mahiri kabisa, Waziri Mkuu wa zamani Moringe Sokoine. Wote tunaungana naWatanzania wenzetu katika kukumbuka siku hii muhimu ambayo tulimpoteza shujaa wetu, aliweka alama katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huu, niseme tu kwamba kwa kuanzia Wizara ya TAMISEMI wanayo kazi kubwa kuwa na trilioni 6.2, asilimia 18 ya bajeti nzima; hili ni fungu kubwa sana. Mnayo kazi kubwa ya kufanya lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais, timu ambayo ameiweka nina uhakika wanafanya kazi vizuri na fungu hili najua litapita. Niwaombe Wabunge wenzangu tuwapitishie bajeti hii iliwaende wakafanye kazi. Naiona timu ni nzuri imehamasika watafanya kazi kama ambavyo inatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, niseme yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe timu hii ya Wizara na sisi tunawaunga, washughulikie jambo la udhibiti wa ubora hasa majengo na barabara, watusaidie sana. Mheshimiwa Katibu Mkuu yeye niengineer Ndugu Nyamhanga namfahamu, adhibiti sana ubora wa majengo pamoja na barabara. Hizi BOQ fedha hizi ni nyingi, ndipo tunapopigiwa hapa kwenye utaalam; mimi nipo very much concerned hapa kwenye BOQ. Wahandisi wa Wilaya kwenye Halmashauri zetu na Wakurugenzi wasimamie jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie na mimi kama wenzangu ambavyo wamesema natoa shukrani zangu nyingi/kubwa, wametutendea haki sisi Jimbo la Manyoni Mashariki kama Wizara, kabisa. Nimepokea Jimbo hili likiwa limechoka sana katika miundombinu ya elimu na afya lakini hivi ninavyozungumza auheni ni kubwa sana. Tumepokea milioni 900 katika vituo viwili vya afya, bilioni moja katika kuboresha huduma ya maji pale Manyoni Mjini, bilioni 2.2 katika mradi wa vijiji 10 wa maji, milioni zaidi ya 600 katika mradi wa ujenzi wa madarasa hizi fedha za EP4R pamoja na EQUIP na mambo mengi ambayo siwezi kuyataja. Kwa kweli sasa Manyoni naona inakwenda kinyume na zamani ambavyo niliikuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo tatizo dogo lakini ni kubwa la usimamizi wa fedha hizi, zinakuja nyingi lakini usimamizi bado mimi nauona haupo vizuri. Wanisaidie alizungumza Mheshimiwa Nkamia jana, lakini mwingine amezungumza leo suala la kozi ya viongozi ni muhimu sana na ni msingi kabisa, tunavurugana sana kule. Mbunge anasema hivi na Mkurugenzi anasema hivi badala ya kwenda kwa sauti moja kusimamia mambo haya na fedha hizi za Watanzania tunabaki kuvurugana na fedha na muda vinapotea. Kozi hizi ni muhimu sana, Manyoni tuna shida kidogo ndio maana hata tunadaiwa benki; Madiwani wanadai posho kwa sababu ya mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Mheshimiwa Jafo na timu yake hebu waitazame Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni watusaidie, ndiyo maana tupo hapa, hatuwezi kukaa kimya wala kulindana tunataka Watanzania wapate huduma sio kuzozana na kufukuzana na kukimbilia kwamba huyu ana cheo hiki au mimi ni mkubwa, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri, Mbunge anaweza akaenda kufanya mikutano kule kwa wananchi akapokea malalamiko, yale malalamiko Mbunge yeye kazi yake ni kuyapekela sasa kwa wenzake; la Mkuu wa Wilaya nalipeleka kwa Mkuu wa Wilaya na la Mkurugenzi nalipeleka kwa Mkurugenzi. Sasa nikimpeleka asiseme mimi namtuma kazi, ni katika utaratibu wa mgawanyo wa majukumu, mimi napokea kila kitu. Lazima hawa watusaidie sisi, ndio wenye vyombo na watekelezaji, sisi ni wasimamizi; kozi hizi ni muhimu jamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa ikama pia tuna shida, upungufu wa watumishi idara ya afya na idara ya elimu kwa kweli bado hali ni ngumu sana, watendaji ni wachache sana, watusaidie sana kwenye hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA fedha hii haitoshi, vijana wale wana moyo pamoja na kiongozi wao, wana moyo sana. Mimi wamenifungulia vibarabara vitatu pale wananchi wamefurahi sana, tumewaunganisha na vijana wana moyo wa kufanya kazi, lakini hawana fedha. Naungana na mimi na wenzangu waliotangulia angalau ile share ya 70/30 iwe 60/40. Najua TANROAD wana barabara chache lakini zina gharama kubwa sawa lakini ile share ikiwa 40/60 angalau tutapata fedha kule, ndio kwa wananchi kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kidogo kuhusu TAKUKURU, wawaongezee fedha, wawape nguvu, wanalinda heshima ya nchi hii.Hawa ndio ma-watchdog tunavyowaita. TAKUKURU bado ni chombo chenye heshima kubwa na nguvu, kama kuna watu wana matatizo wanashughulikiwa, lakini chombo chenyewe kama institution kinabaki bado kina nguvu, wawape hela wakafanye kazi. Naona vijana wale wana mori wa kazi, lakini hawana mafuta hata ya kufanyia kazi, hawana magari na ofisi bado ni chache kwenye Wilaya kule hebu tuwape nguvu walete heshima katika nchi hii. Mheshimiwa Rais tumsaidie analia sana, bado rushwa ipo, ndugu zangu naomba wanisikilizekwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, niseme tu kwamba naunga mkono hoja ya bajeti hizi mbilikwaasilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kutoa mchango wangu katika bajeti hii ya Afya. Kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai, kwa kutuwezesha leo kuwepo katika Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya. Tunaiona na kila mmoja anaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri, pamoja na Naibu Waziri, Makatibu Wakuu wale wawili na timu nzima ya Wizara hii kwa kubwa ambayo wanaifanya kutuhudumia hasa katika eneo la Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali kwamba katika Bajeti ya dawa imeongezeka sana kutoka shilingi bilioni 31 ambayo tulikuwa tunaizungumzia mwaka 2015/2016 sasa tunazungumzia shilingi bilioni 270 hivi sasa ninavyozungumza. Naipongeze sana Serikali kwa kweli kupitia Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Wizara na Serikali kwa Mkoa wangu wa Singida. Mkoa wangu umekuwa wa pili kwa kupata upatikanaji wa dawa zile 30 muhimu kwa Mkoa wa Singida. Mpaka sasa hivi tunapata asilimia 96.6, ni wa pili kutoka Mbeya ambao wanapata asilimia 97.1. Kiambatanisho Na. 5 cha Rejea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilete maombi machache sasa baada ya pongezi hizo. Ombi langu la kwanza, Mheshimiwa aliyemaliza kuzungumza dada yangu Mheshimiwa Sakaya amezungumzia Kituo cha Makazi ya Wazee wasiojiweza pale Sukamahela. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika tarehe 29 mwezi wa 10 mwaka 2018 pale akaongea na wale Wazee na pia alituahidi kwamba katika yale makazi 17, Mikoa 17 katika nchi nzima, akasema wana mpango sasa wa kuyapunguza na kuboresha yakawa machache kugawa katika Kanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walisema mojawapo ya Kanda nadhani Sukamahela itakuwa ni Kanda mojawapo. Nilisimama siku ile na kusema kwamba tunawakaribisha kwa sababu Sukamahela lile eneo ni kubwa, tunazo ekari 80 pale za kutosha kabisa, pia ni barabara kuu imepita pale, tunayo maji, tunao umeme, kwa hiyo, huduma zote zipo, tunawakaribisha sana; na wananchi wako tayari sana ili muweze kufanya eneo lile kwa kanda ya makazi kwa Kanda ya Kati. Tunaikaribisha sana Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la pili, ulipofika Mheshimiwa Naibu Waziri tarehe 29 hiyo mwezi wa 10 mwaka 2018, tulikuomba pamoja na mambo mengine ambulance. Mpaka sasa hivi bado hali ni ngumu, catchment population ya Hospitali ya Wilaya ya Manyoni kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 ni 250,000, lakini hivi ninavyozungumza nadhani sasa inakwenda kwenye 500,000 na zaidi kwa sababu maeneo mengi sana wanakuja; Sikonge wanakuja, maeneo ya jirani, Bahi huko wanakuja. Kwa hiyo, imesha-double ile catchment population.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kwa kweli pamoja na huduma nyingine, lakini ambulance tunaihitaji sana. Tulikuwa nayo lakini sasa imechakaa, iko kwenye mawe. Tufikirie sana kama Wizara, mgao utakaotokea wowote ule, Manyoni muifikirie sana kwa ile Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu lingine la tatu, Wilaya ya Manyoni sasa ni kubwa imekuwa, kile kilikuwa Kituo tu cha Afya, tukakikuza na tukakipandisha hadhi lakini majengo yale Mheshimwia Naibu Waziri amefika hata Mheshimiwa Waziri ameshafika pale. Ile siyo hadhi ya Wilaya kwa yale majengo. Mnapofikiria kujenga Hospitali za Wilaya katika nchi hii kwa mgao unaofuata, naomba sana muifikirie Wilaya ya Manyoni. Tunalo eneo tumelitenga, tumelipima, pana zuri, nasi mtupe huo mgao wa kujenga sasa Hospitali ya Wilaya, maana sasa Wilaya ya Manyoni imekua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu lingine la mwisho ni Ikama. Kama nilivyosema Wilaya ya Manyoni imekua sana, tunapokea wagonjwa wengi sana sasa hivi; pamoja na Vituo vya Afya vile viwili tulivyojengewa, tunashukuru, lakini bado ile Wilaya tunapokea wagonjwa wengi sana. Tunao Madaktari wanne tu. Watatu wanafanya kazi, lakini mmoja pia ni DMO, sasa ni watatu tu ambapo ilitakiwa wawe 14 mpaka 20, lakini ni wanne tu. Hebu fikiria hiyo situation, ni ngumu sana. Mtufikirie sana ikama kwa maana ya Madaktari pamoja na Wahudumu wengine kama Manesi. Kwa kweli hali ni ngumu, wamezidiwa sana kihuduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nashukuru sana, niachie na wengine wazungumze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja Wizara hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ili nami angalau kwa dakika chache hizi nitoe mchango wangu katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kwanza nimpongeze Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anachapa kazi. Ukiitazama nchi hii ya Tanzania ni kubwa, lakini ninavyozungumza kila mahali naona barabara zinajengwa; madaraja, flyovers zinajengwa; na mabwawa, visima, naona vinajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hospitali, vituo vya afya, zahanati naona zinajengwa; ukienda Kinyerezi Bonde la Mto Ruvu kule mitambo ya umeme inajengwa; REA nguzo naona zinatambaa kila mahali, kila kona ya nchi hii zinachimbiwa na umeme unakwenda; Viwanja vya ndege vinakarabatiwa, vingine vinajengwa vipya; lakini kuna ujenzi wa meli, vivuko, magati kwenye maziwa, bahari pamoja na mito yanajengwa; lakini kuna ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea; vyumba vya madarasa vinajengwa; matundu ya vyoo yanajengwa; ukarabati wa shule kongwe unaendelea; ujenzi wa vituo vya VETA unaendelea; ujenzi wa viwanda mbalimbali unaendelea; lakini bajeti ya dawa imepanda, kutoka bilioni 31 mpaka 270; lakini elimu bure pia shule ya msingi mpaka Form Four.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile amedhibiti matumzii ya fedha; kwa hiyo anapodhibiti matumizi ya fedha maana yake ni kwamba ameokoa fedha nyingi. Kwa mfano amedhibiti sana rushwa, amedhibiti wafanyakazi hewa, kwa hiyo pesa ile imeongezeka inakwenda kwenye kazi; naona kasi ya Mheshimiwa Rais ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi niwapongeze pia Waziri na Naibu Mawaziri pamoja na timu nzima ya Wizara. Nilete maombi machache kabla sijapigiwa kengele; kule Jimboni kwangu Manyoni kuna kituo kikubwa sana kile cha kati cha ukaguzi wa mizigo ya magari makubwa, pale Mhalala. Naona kwenye ukurasa wa 256 wametenga bilioni nne sawa, lakini ule ujenzi umesimama tangu Septemba, mwaka jana, naomba ile kasi iongezeke, tunataka kile kituo kikamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu Daraja la Sanza; nimeona kuna milioni 60 imetengwa hapa. Upembuzi yakinifu umeshafanyika, lakini imebakia tu ile process ya ujenzi ianze na mwaka huu tulitegemea kwamba fedha zile ziwekwe ujenzi uanze, lakini sioni fedha yoyote hapa, milioni 60 si kitu, yaani ni kama hakuna. Watutenge fedha watuongezee kwenye lile daraja, lile daraja ni muhimu kwa sababu ile barabara inayotoka kule Manyoni kwenda Sanza na kuvuka lile daraja kwenda Dodoma ni ya kiuchumi kwa Wilaya ya Manyoni kwa sababu lile eneo lote ndilo linalozalisha chakula kwa Mkoa wa Singida na Mkoa wa Dodoma sehemu pia wanapata. Kwa hiyo hilo daraja ni la msingi na la muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimeangalia barabara yetu ya Rungwa – Mkiwa; wenzetu kule wa Chunya tayari wameshapewa hela Chunya – Makongorosi, lakini Mbalizi – Makongorosi pia wameshapewa fedha nimeziona hapa, lakini sijaona Mkiwa kwenda Noranga, hakuna fedha pale, sijui kwa nini na ilikuwa tupewe fedha hizi tangu mwaka jana, hakuna fedha, hatuzioni. Kwa nini sisi hawajatenga ile fedha wanawatengea wenzetu wa upande ule? Nadhani utaratibu ulikuwa wakandarasi wakutane katikati, lakini wanatenga upande mmoja, watenge na huku basi ili wakutane katikati.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, minara ya simu; nimekuwa nikuliza mara nyingi sana, kuna Kata yangu moja inaitwa Makuru, hasa Kijiji kimoja kinaitwa Hika, kule tunahitaji minara. Njia ile ya kutoka Manyoni kwenda Sanza, mule njiani ukisafiri hakuna minara, kwa hiyo mawasiliano yanakatika, naomba sana Wizara hii iniangalie. Nimeshauliza mara nyingi sana hapa Bungeni, wameshajibu kwamba wataleta minara, lakini nimetazama sioni fedha yoyote iliyotengwa, naomba sana sehemu hii ya minara na mawasiliano ili tuweze kuwasiliana kwa sababu mawasiliano ni maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, nashukuru sana, naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru Mwenyezi Mungu kupata fursa hii kuchangia Mpango huu wa Maendeleo wa mwaka 2020/ 2021. Kwanza kabisa niipongeze Serikali yangu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mambo makubwa ambayo kipindi cha miaka minne tu tunaona mambo yamefanyika makubwa sana sina haja ya kuyataja wenzangu wameyataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende ukurasa wa 23 wa Mpango kwa maana ya mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo. Nizungumzie kidogo eneo la kilimo, niwapongeze sana Bodi ya Korosho kwa maana ndani ya Wizara ya Kilimo, wanajitahidi sana sana kusambaza mbegu, madawa pamoja na utaalam wote unaohusika katika uzalishaji wa korosho. Sisi Manyoni ni wachanga lakini wanaendelea kutusaidia sana lakini na maeneo mengine ambayo hasa wanalima korosho. Bado tatizo liko kwenye mazao mengine, nikizungumzia Mkoa wangu wa Singida sisi tunajulikana kwa kilimo cha alizeti kwa hiyo ni mkoa ambao ni giant kwa uzalishaji wa alizeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri sana Wizara ya Kilimo inapotokea kwamba mkoa ule ambao ni hasa chief producer wa zao fulani wapeleke nguvu basi kwenye mkoa huo, hasa kwenye mbegu, masoko tuna tatizo kubwa sana. Singida tunalia sana suala la mbegu sana tu tunachanganywa sana upande wa mbegu, kuna mbegu sijui zinaitwa Hyssun lakini bei ni kubwa sana zinauzwa kilo moja Sh.35,000, nilizungumza hata kipindi kilichopita. Kwa mkulima wa kawaida ambao tunategemea hawezi kumudu gharama hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye sekta ya elimu kwenye mapitio haya haya. Nijikite zaidi kwenye ukarabati wa shule kongwe za sekondari. Naipongeza sana Serikali yangu ya Awamu ya Tano imezikumbuka shule hizi zilikuwa zimeathirika sana lakini sasa ukienda kwenye shule nyingi hizi 87 zote zingine tayari ukarabati umeshakamilika, zingine ziko kwenye hatua za mwisho, naipongeza sana Serikali imefanya jambo kubwa sana pamoja na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu tu niongezee kidogo hapo, tunazo changamoto ndogo, kuna hawa jamaa wakala wa majengo ya Serikali TBA wanapewa tenda hizi za ukarabati za ujenzi, nadhani wajipange kwanza. Tusiwape tenda tena hapa kwa sababu wametuvurugia maeneo mengi sana kwenye ukarabati na kwenye ujenzi, wajipange vizuri, kwa sababu ni shirika la Serikali wanatuaibisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine niliyoiona kwenye maeneo haya, kwa mfano kwenye shule kongwe hizi, naomba sana shule hizi zinavamiwa Serikali ijitahidi kutenga fedha pia kupima maeneo haya, ni fedha ndogo tu. Kwa sababu tunao surveyors kwenye mikoa huko na halmashauri tuwatumie hao hao, wapime watoe hati na kuweka pia hata wigo ili lisivamiwe shule hizi. Tulipita siku moja shule ya Sekondari ya Mirambo kule hali ni mbaya sana uvamizi yaani usiku wanapita watu yaani ni vurumuai, hakuna utulivu wa masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa Mpango wenyewe ambao unatarajiwa twende ukurasa wa 66,snizungumzie kidogo suala la misitu na nyuki. Profesa mmoja anaitwa Dos Santos Silayo anasema ingeigharimu dunia trilioni 38 dola za Kimarekani kutengeneza oxygen ambayo ingewa-supply na kuwafaa binadamu kwa miezi sita kwa dunia nzima, ni gharama kubwa sana. Trilioni 38 karibu trilioni 40 USD dola kutengeneza oxygen, suppose kama miti ingekuwa haipo kwamba sasa oxygen inatengenezwa ni trilioni karibu 40 kwa miezi sita tu tena kwa binadamu tu sio wanyama wengine, fikiria hiyo gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna Dokta mmoja anaitwa Anne Marie anasema kuwa mtu mmoja huhitaji miti hai saba hadi nane imtolee oxygen kwa mwaka mzima. Nataka kuzungumzia umuhimu wa kutunza misitu yetu siyo oxygen tu na vyanzo vya maji. Manyoni kule sisi tuna Mto mmoja unaitwa Kizigo ambao unaungana na mito 18 ambayo inapeleka kwenye lile bwawa la Mwalimu Nyerere kule Rufiji. Sasa mazingira haya yanaanza kuharibiwa, Sheria ya Misitu, Na.14 ya mwaka 2002 na regulations zake za mwaka 2005 zinatoa asilimia 52 kwenye zile categories, maana kuna categories zimetajwa pale kwamba kuna misitu ya watu binafsi, kuna misitu ya vikundi, kuna misitu ya vijiji, kuna misitu ya Serikali Kuu, kuna misitu ya Serikali za Mitaa na kuna general land. Sasa misitu ya vijiji inachukua asilimia 52 kwenye sheria hii ina-provide na tunawaachia wanavijiji ndio watunze misitu hiyo. Hii ni hatari, wame-prove failure, misitu mingi inateketea kupitia kwenye vijiji, tuiangalie sheria hii upya vinginevyo tutajikuta tuna jangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu hawa wanavijiji hawana elimu yoyote, unamkabidhi asilimia 52 ya misitu yote ya nchi nzima, hapana. Mheshimiwa Dkt. Mpango kwenye vipaumbele waliangalie upya hili la misitu, sheria hii tuibadilishe, tujaribu kuangalia makundi mengine, nadhani Serikali Kuu iwe na dhamana ya kutunza misitu hii, hawa waombe tu kibali kwa sababu ni watumiaji washirikishwe, lakini waombe kibali ila mwangalizi awe Serikali Kuu na sheria iseme hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kusema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inakwenda vizuri naona kampeni kubwa kwenye uchaguzi ni kufanya kazi. Kwa hiyo kampeni kubwa ya Chama cha Mapinduzi imeshafanyika, tunasubiri tu tarehe 24 vijana wachukue nafasi zao, 2020 Mheshimiwa Rais na Serikali yake na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuchukue nafasi zetu kwa sababu tayari kampeni zimeshafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga mkono Mpango huu ni mzuri sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata fursa hii walau ya dakika tano. Ninayo tu mambo machache sana kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza, niende moja kwa moja kwenye hoja yangu, kaka yangu Mheshimiwa Mwaka, Mbunge wa Chilonwa, yeye alizungumzia hali ya hewa katika eneo la kati ya nchi hii ni kame. Naunga mkono hoja yake na mazungumzo yake, ni kweli kabisa tuko kwenye eneo kame, lakini kuwa na ukame maana yake sio kwamba hatuna udongo au hauna rutuba. Udongo wetu una rutuba ya kutosha, Mkoa wa Singida na Dodoma.

Mheshimiwa Spika, nikizungumzia hali ya Manyoni kwa mfano, bonde la ufa, limeimega Manyoni pamoja na Dodoma, kwa hiyo tumeshirikiana ule ukame. Kwa upande wangu bonde la ufa, hali ni ngumu sana kwa mfano kwa mwaka huu hatuna chakula, lakini nije na pendekezo la Mkakati kwa maana ya kupunguza sasa au kuondokana na hali ya njaa.

Mheshimiwa Spika, sisi Manyoni, tuna eneo linaitwa Bwawa la Tope la Bahi, Bwawa hili lina mito miwili mikubwa, ambayo inatoka ukanda wa Kaskazini, Manyara inamwaga maji kwenye lile bonde, ni bonde lina rutuba kubwa ya kutosha. Naomba Wizara hii ya Kilimo itusaidie, kukomesha njaa kwenye bonde hili, kwa upande Dodoma kwa maana ya Bahi na upande wa Manyoni. Tuwekeeni Bwawa kubwa la mkakati kwenye bonde hili, tunayo mito miwili mizuri inaleta udongo wenye rutuba ambao umetoka kule juu.

Mheshimiwa Spika, maji yapo ya kutosha na uwezekano ni mkubwa, hebu tusaidieni sana, walete wataalam, wafanye utafiti, watuchimbie bwawa la kutosha. Tunazo ekari zaidi ya 50,000 nzuri zenye rutuba tukaweka bwawa pale, watakuwa wametusaidia kabisa lakini tutalisha na sehemu zingine za nchi hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna kabwawa kamoja si ka mkakati ambako tayari andiko limeshakamilika liko Wizarani, mwaka jana ilikuwa iwekwe kwenye Bajeti ianze kwa sababu utafiti, upembuzi yakinifu ulishafanyika, usanifu wa kina umeshafanyika, kila kitu kiko tayari ni kujenga tu. Mwaka jana ilikuwa iingizwe kwenye bajeti wakasema tutaingiza mwaka huu, nimeuliza maswali karibu mara tatu katika Bunge hili, Bwawa la Mbwasa, lakini nimeangalia Bajeti tena halipo, sijui tatizo ni nini? Njaa itatuua jamani na mimi sioni aibu, nitaomba tu chakula kwa sababu lile bonde halina chakula sasa, lakini wakitujengea kabwawa haka, ile njaa nitakuwa nimeondokana nayo, hebu tusaidieni tuna maji ya kutosha, tusaidieni jamani.

Mheshimiwa Spika, naomba waangalie, Bajeti Kuu bado haijasomwa, waangalie bwawa hili, waliingize kwenye Bajeti ya mwaka huu, tuchimbiwe bwawa pale Mbwasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, Singida tumejinasibu kwamba tunalima alizeti na ndiyo brand yetu sisi, lakini bei ya mbegu iko juu sana hii ambayo imefanyiwa research kwa maana ya hybrid. Kwa mfano kilo moja tu ya mbegu inaitwa hysun F124 inauzwa kwa wastani wa shilingi 35,000 kilo moja. Wakulima wangu wale wa Manyoni wale, Singida yote ni wachovu, kilo moja shilingi 35,000 watalima wapi? Nani atanunua hiyo mbegu? Watuletee angalau ruzuku basi watunyanyue nyanyue ili tupandishe zao hili la alizeti, hii bei si rafiki kwa maana kwamba Singida tuwe ma-giant wa uzalishaji wa alizeti na mbegu hii, hapana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, malizia. (Makofi)

MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, baada ya machache hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DANIEL D. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii na mimi nitoe mchango wangu katika bajeti kuu pamoja na taarifa ya hali ya uchumi, pamoja na Taarifa ya Kamati ya Bajeti. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai ametukutanisha mpaka leo hii pia tunajadili tena bajeti kuu kama tulivyokuwa tumejadili miaka iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye majadala. Mimi nikupongeze Waziri Dkt. Mpango, uko kwenye njia sahihi, kelele nyingine hizi kila mmoja ana mdomo wake na ana uhuru wake, lakini angalia kwenye focus yako ndani ya miaka mitano uko kwenye right track na sisi Wabunge kazi yetu ni kuishauri Serikali. Naomba utege sikio sasa usikilize ushauri wa Mbunge anayeitwa Mtuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, twende ukurasa wa 80 wa hotuba yako, nikupongeze umetoa umeondoa ule ushuru wa uwindaji wa kitaalam kwa wazalendo pamoja na wageni, hii ni katika kuvutia na kukuza biashara ya utalii, sawa. Naomba nikuongezee na lingine, ukienda pale Wizara ya Mambo ya Ndani, Immigration pale, kuna kitu kinaitwa tozo ya kibiashara hii ambayo wanailipa wale wanaokuja kufanya mikutano ya kimataifa kwenye kumbi zetu, Mheshimiwa Kigwangalla amejinasibu vizuri kwamba sasa anakwenda kujenga kumbi kubwa na nzuri kwa mfano Bagamoyo, sasa muondolee hii tozo hii maana ndio wanayolipa hawa wanaokuja kufanya mikutano, huu ndio utalii wa mikutano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu mfano mfupi sana, Ethiopia wenzetu wanalipa dola 32, Kenya dola 40, Rwanda dola 50, South Africa dola 150, sisi tunatoza dola 250; ninashauri sana tutoze kama jirani zetu dola 40 vinginevyo Mheshimiwa Kigwangalla asije akajenga hizi matembo weupe hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee mbele zaidi, katika kukuza utalii hukohuko hebu pia tuangalie kutumia au kukarabati viwanja vyetu vya ndege, hasa ambavyo viko kwenye mbuga zile za wanyama, nasemea moja kwa moja Seronera. Juzi juzi Serengeti imetunukiwa kuwa mbuga bora kuliko zote Barani Afrika, kutakuwa na wimbi kubwa sana la watalii ambao watakuja, watakuja wengi sana, lakini pia tunataka kuanza safari za kufuata watalii Guangzhou, Mumbai, Johannesburg, tutakuja na watalii wengi sana na wengi wamesikia watakuja tu Serengeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serengeti lile ni likubwa sana, hebu chukulia ile 10 percent tu ya Serengeti ambayo inaitwa Masai Mara iko Kenya, wenzetu wanatengeneza fedha mara kumi zaidi ya sisi ambao tunamiliki asilimia 90, lakini wenzetu wametengeneza viwanja vya ndege, viwanja vizuri kabisa mle ndani. Kwa mfano wana kiwanja kinaitwa Kichwatembo; Masai Mara mle ndani, wana Kiwanja kinaitwa Masai, Alikiombo pia, viko mle ndani; hivi viwanja vimeunganishwa na viwanja vikubwa nikizungumzia Embakasi na Jomo Kenyatta.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndege kubwa ikitua pale inakuta tayari hizi Q400 iko tayari pale imeshawasha moto inasubiri wale watalii wanashuka comfortably wanaingia kwenye ndege zile wanaenda kutua Masai Mara kwenye vile viwanja, viwanja vile vimejengwa vina minara ya kuongozea ndege, taa za usiku, taa za kuongozea ndege, lami imewekwa. Sisi cha kwetu kile Seronera hakijawekwa, watalii watakuwa ni wengi mno tunawa-accommodate vipi wale? Tutakosa fedha hapa ambayo ni ya bure ni nje-nje hapa hii pesa, hii pesa tunaikosa hii. Naomba turekebishe kile kiwanja, chomoachomoa kwenye matengenezo ya viwanja vingine vya ndege hebu tuanze na Seronera tukitengeneze kile kiwanja zile ndege zitue kule zipeleke hawa watalii ni wengi mno, hii fedha sio ya kuiachia Mheshimiwa Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niende kwenye eneo lingine la kuboresha Shirika la Ndege; ndege hizi tumenunua za kutosha, tunaendelea kununua kama ambavyo tumejiwekea, ndio focus yetu. Mheshimiwa Rais ametusaidia tuna ndege sita na nyingine zinakuja, lakini pia mimi niseme tiketi peke yake kwenye ndege hizi hatutaweza kuendesha Shirika la Ndege. ziko shughuli nyingi ambazo tunaweza kuzifanya ATCL ikawa shirika tanzu kutoka kwenye ATCL tukawa na vikampuni vidogo vidogo vya kuendesha shughuli kama zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwanza; tuwe na shirika dogo ambalo linaendesha zile ground handling services ambazo Swissport wanafanya sasahivi. Hii itafanya huduma hizi kwa ndege zetu za ATCL, lakini pia na kwa makampuni mengine tutatengeneza fedha; tutaokoa fedha kwenye kampuni yetu, lakini pia tutafanya huduma kwenye ndege nyingine tutatengeneza fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tufanye shughuli nyingine inayoitwa in flight catering services, vyakula na vinywaji kwenye ndege ndani ya ndege zetu hizi. Tutengeneze ka-kampuni kadogo tanzu ka ATCL tuuze vyakula kwa kutumia kampuni hii, tuachane na mambo ya ku-hire ni gharama kubwa sana, tutauza vyakula, vitahudumia vyakula kwenye ndege zetu, lakini pia tutahudumia kwenye ndege nyingine, tutatengeneza fedha ya kutosha tu Mheshimiwa Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nyingine kuna tozo kama navigation charges; navigation charges ni kama zile ndege inapokuwa inatua lazima waelezwe hali ya hewa, sijui minara kwa mfano ya simu au umeme, zile tower kwa usiku zinakuwa zinachanganya. Kwa hiyo, kunakuwa na ile ramani ambayo inamwongoza rubani, hizo navigation fees.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fees zingine zinaitwa landing charges na parking charges. Mheshimiwa Mpango hizi gharama yake ni kubwa mno, inakaribia bilioni moja kwa mwezi ATCL inalipa, fikiria hii. Lakini nchi zingine kama kwa mfano Ethiopian Airlines, wale waaarabu kule Emirates kwa mfano Qatar Airways haya ni mashirika ya Serikali. Wamefanya exemption ya haya mashirika, hawalipi hizi charges tatu nilizozitaja, kwa hiyo wana-save. Kwa mfano, tuki-save bilioni moja kwa kila mwezi maana yake ni kwamba tunajiendesha hili shirika. Tuangalie hizi charges angalau tuwape hata muda mfupi wakati linakua tuziondoe hizi charges tatu, ni mwiba mkubwa mno, tufanye exemption, tutakuwa tumelisaidia sana shirika letu la ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunacho chuo kinaitwa ATC Cabin Crew School, hiki ni chuo kinachofundisha hawa ma- airhostess peke yake, hakiwafundishi marubani, marubani wanaenda kufundishwa maeneo mengine nchi za nje, hawa fresh kutoka shuleni. Tukisema hebu tuanzishe kozi sasa na kufundisha marubani pia tuwafundishe humu humu ndani. Kufundisha rubani mmoja kwa wastani ni shilingi milioni 80 kwa mwaka, ni hela nyingi sana, rubani mmoja huyu lakini tukiwa tunawafundisha humu ndani tutapunguza gharama, tuta-save, tutaokoa hii ATCL, tutakuwa tumeweza kulifufua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma nyingine, tunayo ma-godown. Kuna bidhaa zinaitwa sensitive goods; temperature ya sensitive goods. Kwa mfano mtu labda ametoka nje ametua hapa anaenda Malawi, ana goods zile ambazo ni sensitive na joto labda dawa zitaharibika, tutengeneze godowns, ni biashara nzuri mno, zile goods ambazo zipo on transit ni biashara nzuri mno; anasubiri ndege tunamtunzia bidhaa zake pale, unaona eeh baada ya kutimilika safari anachukua bidhaa zake anaondoka kwenda Malawi, ametuachia pesa. Tiketi peke yake si biashara ya ndege, ndiyo maana tunatoza labda kwa mfano tu Dodoma - Dar es Salaam hapa hela ni nyingi mno shilingi 400,000 mpaka shilingi 500,000 lakini tukizingatia haya Mheshimiwa Mpango na Wizara nyingine, unaweza ukaenda kata kwa 100,000 tu Dodoma – Dar es salaam… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, nianze kuhusu migogoro ya mipaka baina ya hifadhi za wanyamapori/misitu na wananchi. Katika ya Jimbo la Manyoni Mashariki jumla ya vijiji 12 vimepakana na Hifadhi za Kizigo na Muhesi. Vijiji hivi ni Chikola, Chikombo, Mpola,
Iteka Azimio, Nkonko, Chidamsulu, Iseke, Mpapa, Simbanguru, Sasilo, Chisinjisa na Imalampaka.

Mheshimiwa Spika, wananchi katika vijiji tajwa hapo juu wanalalamikia uhaba wa ardhi kwa ajili ya kilimo, malisho ya mifugo, uchimbaji wa madini pamoja na ufugaji wa nyuki. Aidha, wanalalamikia kitendo cha kuzuiwa kutumia maji ya mto uliopo mpakani kati ya hifadhi na vijiji. Uhaba wa ardhi umejitokeza baada ya ardhi yao kuchukuliwa na Serikali ulipofanyika upanuzi wa mipaka ya hifadhi za misitu tajwa mwaka 1994.

Mheshimiwa Spika, Muhesi Game Reserve imeanzishwa rasmi kupitia GN Na. 531 ya tarehe 04/11/1991 na kusainiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 09/03/1994. Muhesi ni hifadhi changa yenye kilometa za mraba 2000 na kwa hiyo imesababisha machungu makubwa kwa wananchi katika maeneo haya. Tangazo la kuipandisha Muhesi kuwa game reserve mipaka yake mipya imeleta madhara makubwa kiuchumi kwani imechukua maeneo muhimu kama eneo muhimu la kilimo cha mahindi liitwalo Chiumbo na eneo la machimbo ya dhahabu aina ya alluvial yaliyogunduliwa mwaka 1991. Hii ni dhahabu bora ambayo haijawahi kuonekana na kuchimbwa mahali pengine katika nchi hii (Ref: Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania, 1992).

Mheshimiwa Spika, maeneo au vitongoji vingine vilivyochukuliwa ni pamoja na Chosola, Msisi, Ilevelo, Machocholoni, Mkindilya, Chigugu, Ngongolelo pamoja na Chibwee. Aidha, maeneo haya yaliyochukuliwa yalitegemewa sana katika malisho ya mifugo, ufugaji wa nyuki na vyanzo vya maji safi ya kunywa binadamu na mifugo katika Mito ya Muhesi na Kizigo. Malalamiko mengine ni unyanyasaji utesaji na udhalilishaji vinavyofanywa na askari wa game reserve dhidi ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, naambatisha na taarifa ya malalamiko ya wananchi yenye kichwa cha habari; “Yah: Malalamiko ya Wananchi Kuhusu Migogoro ya Mipaka Baina ya Vijiji 12 na Hifadhi za Muhesi na Kizigo; na Manyanyaso ya Askari wa Hifadhi Dhidi ya Wananchi.”

Mheshimiwa Spika, malalamiko haya yaliwasilishwa na wananchi 18 kutoka Jimbo la Manyoni Mashariki wakiongozwa na Mbunge wao Daniel Mtuka walipokutana kwa mazungumzo ya ana kwa ana ofisini kwao (Dodoma) Naibu Mawaziri wawili; kwa wakati huo walikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Engineer Ramo Makani, tarehe 27/05/2016 (mchana) na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Tate Ole Nasha tarehe 27/05/2016 (mchana).

Mheshimiwa Spika, tunasikitika, hadi leo hatujibiwi (mwaka mzima)

Mheshimiwa Spika, ombi, wananchi wangu bado wanasubiri majibu.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami naomba nitoe mchango wangu kwenye huu Muswada ulio mbele yetu wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe furaha yangu kwa Muswada huu kwa sababu kwa muda wa miaka 22 ya taaluma yangu hii ya uthamini nimekuwa nikifanya kazi katika mazingira magumu sana. Hili ni wazo ambalo linawakilisha wathamini wote katika nchi nzima, nimekuwa nikipokea simu nyingi, wamefurahi sana, wanaomba tu jioni hii tuipitishe sheria hii ili na sisi tufanye kazi katika mazingira mazuri na tuweze kutoa mchango wetu katika Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza wenzangu ambao wametangulia wamesema karibu yote ambayo nilikuwa nafikiria lakini niguse kidogo maeneo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kifungu cha 28 ambacho kinazungumzia usajili kamili wa Mthamini. Naungana mkono na wenzangu kwani mapendekezo yangu na mimi ni hayohayo kwamba uwe mwaka mmoja huyu mtu au Mthamini aweze kupata usajili kamili kuwa mthamini. Ninazo sababu mbili, tatu. Hatuwezi kwenda miaka mitatu kwa sababu huyu anapokuwa mwaka wa kwanza mpaka anapomaliza kila mwisho wa mwaka anakuwa na practical training, anaenda field, tayari anaanza kupata uzoefu. Pia kutakuwa na mitihani ya usajili kama ambavyo tumeelezwa kwenye Muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi kutakuwa na continuing professional education, mafunzo ya kuendelea ambayo Mthamini Mkuu katika majukumu yake ya kazi anatakiwa aandae na haya tumekuwa tukiyafanya miaka yote. Pia hatuwezi ku-guarantee huu mwaka mmoja unaweza ukaongezeka, anaweza akafanya mitihani aka-fail, ni jambo la kawaida kwenye taaluma nyingine zote hata wahasibu wamekuwa wakirudiarudia, CPA mtu anaweza akafanya miaka zaidi ya mitano, sita hata kwenye uthamini ni hivyohivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anaweza asiende mwaka mmoja huu, anaweza akashindwa kwenye mitihani akarudia kwa hiyo miaka ile itaongezeka tu. Mtaani kuna vijana wengi sana tunataka wawe Wathamini kamili waweze kutoa mchango wao katika nchi hii lakini pia ni ajira. Kwa hiyo, naunga mkono usajili kamili uwe mwaka mmoja tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele kingine, nimejaribu kupitia makosa ambayo sisi Wathamini tunayatenda na ambayo tunatarajia labda yatakuwa yanatendeka. Section 67, nimeona mengi yameorodheshwa lakini kuna kipengele naomba kama ni kuongezwa kiongezwe au kama ni ku-rephrase tu-rephrase. Kuna kitu kinaitwa kula njama kutenda kosa (conspiracy).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uthamini, yamekuwa ni malalamiko ya muda mrefu.Unakwenda kufanya uthamini wa fidia, mwenye nyumba na mthamini wanakula njama kwa pamoja, bwana niongezee thamani ya hii nyumba yangu badala ya shilingi milioni 10 iwe shilingi milioni 20, tutagawana hapo katikati. Hili kosa limekuwa likitendeka, nadhani tungeongeza hii conspiracy iwe moja ya offence kwenye hili eneo kujaribu kudhibiti mtindo huu kwani Serikali inapoteza pesa nyingi sana, value zinakuwa juu sana, tudhibiti conspiracy.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele kingine ambacho pia naomba nikichangie ni kifungu cha 15 cha Muswada huu, uundwaji wa Kamati za Bodi. Sijajua hao wengine watatoka wapi kwenye hizi Kamati maana naona Wajumbe wa Bodi wako tisa lakini hizi Kamati ziko karibu nne au tano. Ukipiga hesabu unakuta kila Kamati itakuwa na wajumbe wawili. Napata mashaka kama Kamati itakuwa na wajumbe wawili. Kama kuna wengine wataongezeka nadhani ni vema isemwe wazi hao wengine watatoka wapi aidha kwenye regulations zitakapokuwa zinatengenezwa kwenye kifungu kile cha 70. Tunataka kukimbia kule ambako tumetoka kwa watu wengine ambao siyo professional hii kuingilia taaluma hii. Naomba suala hili lisemwe wazi kwenye regulations wanatoka wapi hawa wajumbe wengine kwa sababu naona ni wajumbe wawili tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa approval fee, unapokuwa umefanya kazi una-submit ile taarifa yako kwa Mthamini Mkuu kuna hela inalipwa Serikalini. Humu haijaoneshwa lakini najua ipo, naomba kwenye regulations ioneshwe na ikishaoneshwa naomba kuwe na exemption ya baadhi ya taasisi za Serikali ambazo zinafanya uthamini wa kazi hizi. Kwa mfano, taasisi mojawapo inayofanya valuation sana kwa wingi sana na inalipa approval fee fedha nyingi ni TAKUKURU. TAKUKURU ni chombo ambacho pia kina Wathamini ambao wanafanya valuation nyingi sana, kwa hiyo, kwa bajeti za kawaida kama watakuwa wanalipa approval fee watashindwa kufanya kazi yao na watashindwa kuwasaidia watu. Naomba ioneshwe kwenye regulations lakini kuwe na hiyo exemption ya approval fee kwa taasisi kama TAKUKURU. Approval fee ni fedha nyingi sana kwa taasisi hii kwa sababu wanafanya valuation nyingi sana. Nataka nishauri pia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uteuzi wa Assistant Chief Valuer, naomba niungane na wenzangu kusema uzoefu wa miaka mitano unatosha. Sitaki kuzungumza mengi, wenzangu wamezungumza, hatuwezi kusema uzoefu wa miaka 10, hii hapana! Kwa uzoefu wangu ninavyofahamu kwa sababu haya ninayoyasema tumekuwa tukiyatenda sijasoma tu kwenye document hii, ndio maisha yangu ya profession. Miaka mitano ni mingi inatosha kwa Assistant Chief Valuer.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho, kuna msemaji mmoja alitaka kutuchanganya kidogo, labda tu nimpe…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono sana na nawaomba Wabunge tuipitishe sheria hii ili na sisi tuwe miongoni mwa wataalam ambao wanaweza wakaisaidia nchi hii. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii angalau nitoe mchango wangu mfupi, mengi yameshazungumzwa na wenzangu sitataka kuyarudia sana. Niseme tu nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa maamuzi haya sasa ya kutushauri Wabunge kwa maana ya kuleta sheria hii sasa ya kubariki jambo hili sasa liwe rasmi maana limeanza tangu mwaka 1973.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo niseme tu kwa ufupi kwamba, naunga mkono hoja hii, mjadala ulioko wa kubariki hii declaration sasa ya kulitangaza jiji hili sasa kuwa Makao Makuu ya nchi. Kwa sababu zifuatazo chache tu wenzangu wamezigusia, niseme tu kwamba ndugu zangu, niwaombe na Watanzania wote, kwanza wamekuwa wakisubiri kwa hamu sana ujio wa jiji hili sasa kisheria. Tujiandae kisaikolojia, sasa Dodoma itakuwa makao makuu, najua Sheria hii inapita.

Mheshimiwa Spika, tunatamani sana Jiji hili kama ambavyo amesema dada yangu Mheshimiwa Bura, Jiji hili sasa tujiandae kisaikolojia kwamba tunataka tuandae jiji ambalo kwa kweli liwe miongoni ya majiji katika dunia hii ya kutolea mfano. Ibara ya tano (5) ya Muswada huu inasema kutakuwa na sheria itatungwa rasmi itakayoongoza namna ya kuendesha jiji hili. Naomba sana Sheria hii ikishapita hii isichelewe kutungwa kwa maana ya ku-manage namna ya kuliendeleza jiji. Sisi watu wa Mipango Miji tunatamani sana sheria ije hii jiji hili liandaliwe katika utaratibu unaotakiwa.

Mheshimiwa Spika, tumezungumzia, zipo sheria za mipango miji sawa zitatumika katika kuliendeleza jiji hili, ningetamani sana, kwa mfano master plan iliyopo au mpango kabambe wa kuendeleza jiji hili upo lakini ungehuishwa pia kidogo. Likae jopo la watalaam, watalaam wa Mipango miji na watalaam wa ardhi kwa pamoja wajadili na waweke utaratibu mzuri sasa wa kuhuisha mpango huu, uwe mzuri zaidi wauboreshe zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona maeneo mengine ya nchi nyingine duniani, kwa kweli wana mipango mizuri sana ya uendelezaji wa majiji kama haya. Tunatamani sasa kwa mfano maeneo ya makazi yawe ya makazi, lakini tunatamani maeneo ya kibiashara yawe ya biashara, tunatamani maeneo ya maofisi yawe ya maofisi, kuwe na mji wa viwanda. Mimi nilikuwa Rwanda juzi, nashukuru tulikuwa tumeenda kujifunza kule kwa wenzetu.

Mheshimiwa Spika,umetembezwa ule mji, kuna mtaa kabisa wa viwanda, unatembea huwezi kuona maeneo mengine, ni mji ule tu ndio viwanda. Kwa hiyo, natamani sana Dodoma tutengewe eneo kabisa sasa unaenda kutembea viwandani kule, hatutaki kuona mchanganyiko huo mara maji machafu hapa, harufu sijui nini, hapana tunataka tuwe na vitu hivi vitengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatamani kuwe na eneo la masoko mazuri, tunatamani tuwe na eneo la maegesho la magari makubwa na madogo, tunatamani tuwe na stendi kubwa imeshaanza kujengwa, stendi ndogo ya magari madogo, bandari kavu iwepo, tunatamani airport kubwa iwepo. Mji wa kielemu kwa mfano kama ambavyo tayari maeneo yameshapangwa uwepo, maeneo ya starehe, tuwe na bustani nzuri kama wenzetu walizonazo.

Mheshimiwa Spika, kwenye huduma za barabara tuwe na high ways, ring roads, tuwe na by pass, hatutaki magari makubwa hapa katikati ya mji. Tunataka mji ambao umetulia uko vizuri. Tuwe na flyovers, baadaye tuandae na zile provision za fly over, mji huu unakuwa. Tusianze tena baadaye kubomolea watu tunataka flyovers hapana ule mpango uonyeshe. Pia huduma tuwe nazo madhubuti, tuwe na vyanzo vya uhakika vya maji kwa mfano Mzakwe ile itazidiwa, Farukwa lile bwawa lile liharakishwe kujengwa ili tuwe na huduma nzuri ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tuwe na huduma ya umeme ambao ni wa uhakika, stable and reliance power, lakini tuwe na utaratibu mzuri wa waste management, takataka zinasumbua sana kwenye miji lakini kwenye plan ile ionyeshe s,torms water management tuwe na Dodoma hii ni plain area hii, ni bonde la ufa hili tuwe na utaratibu mzuri wa manage maji haya ya mvua yanasumbua kwenye mvua kubwa mafuriko Dar es Salaam imekuwa imetufundisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini natamani pia Dodoma tuwe na kasi ya upimaji wa viwanja na ugawaji wa viwanja hasa site and services. Pima kiwanja, peleka maji, peleka umeme, peleka huduma zote gawa kiwanja, watu wajenge. Vilevile Waziri wa Ardhi atusaidie sana na wote wanaosimamia mambo ya sheria, land speculation inatusumbua sana mtu ananunua kiwanja kwa ajili ya mjukuu?. Kinabaki kichaka katikati ya mji, hapana watu wajenge kwa muda unaotakiwa, tunataka jiji hili liwe limejengwa vizuri. Pia Dodoma tukubali kwamba ni eneo la mkondo wa matetemeko. Watalaam watushauri na wala sijengi hofu lakini tuwe na tahadhari hiyo kwamba, tuwe na nyumba za ghorofa zisiwe ndefu sana, ziwe standard. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ningependa mfano wa majengo kwenye majengo ya makazi, tunataka kwa mfano kama block nzima hivi iwe na ghorofa tatu iwe na rangi labda bati rangi nyekundu ziwe nyekundu, kama rangi nyeupe ziwe nyeupe na urefu uko sawa sawa, maeneo kama hayo, yaani ule mfanano wa uzuri ule inaleta picha nzuri ya mji.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho niseme tu kwamba wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla wanaojenga hapa tujiandae kisaikolojia kwamba, sasa tukubali huu ni mji sasa mambo ya kufuga sijui ng’ombe katikati ya mji sijui, usafi wa mazingira yaani tujiandae. Dada yangu Mheshimiwa Bura amesema kupanda miti, tupande miti tupendezeshe jiji letu hili tujiandae kisaikolojia kwamba sasa ni Jiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia maeneo ya jirani na Dodoma tujiandae pia, kwa mfano Manyoni pale mimi ni karibu. Manyoni na Bahi ni karibu lakini Manyoni ni nzuri zaidi kwa sisi kujiandaa zaidi kwa sababu Bahi kidogo haiko sawasawa, sisi pale tunalima, pamenyanyuka pale tunaweza tukapima pale watu wanakuja kupumzika pale. Manyoni ni juu ya Bonde la Ufa.

Mheshimiwa Spika, ukijenga hoteli pale juu ya bonde la ufa pale juu, unaliangalia bonde la ufa chini, watu wanaweza kuja kupata mahali pazuri sana pa kupumzika. Tuna eneo kwa mfano pale Kilimatinde, ukipanda pale Kilimatinde kuna sehemu inaitwa ukanda wa juu. Ukipiga mahoteli pale, ukiangalia lile bonde yaani mpaka maisha unaona yanaongezeka unapata burudani kuliona bonde, uwanda ule safi. Kwa hiyo, Manyoni tujiandae sisi pia maeneo ya karibu karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii hoja, huu kwamba sasa tunataka kuufanya declaration naiunga mkono sana. Naiunga mkono na kwa kweli na kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene amesema kwamba, ni baraka na ni ibada kubwa sana kubariki juhudi za Mwalimu Nyerere ambazo alizianzisha kwa kweli tunapata thawabu kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, naomba tu tuunge mkono Muswada huu Wabunge wote jambo hili ni jema, yametokea mambo, sisi sio malaika lakini jambo hili ni nzuri, hilo ndilo jambo la msingi. Hoja ya kusema Zanzibar haikushiriki tuna kamati, Kamati za Bunge za Kudumu tunao Wazanzibari, tumejadili kwenye kama lakini hapa Bungeni tuna Wazanzibari wenzetu.

Mheshimiwa Spika, sawa namalizia, tunao Wazanzibari wenzetu wameshiriki kwenye jambo hili. Kwa hiyo sio kwamba Wazanzibari hawakushirikishwa. Sisi ni watungaji wa sheria.

Mheshimiwa Spika, naomba sana kuunga mkono hoja. Nashukuru kwa nafasi hii.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii nami nitoe mchango wangu katika Muswada huu. Kwanza niipongeze sana Serikali kuleta marekebisho haya. Nitajikita zaidi katika ukurasa wa 21 wa Muswada, Part No. 9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ibara ya 29 ya Muswada huu inaleta marekebisho ya Sheria ya PCCB kwa maana ya PCCA. Ni-declare interest tu kwamba mimi nilifanya kazi kwenye ofisi hizi. Kwa hiyo, haya nitakayoyazungumza nimeyaishi na baadhi nimeyaishi na kuyafanya nikiwa katika utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali imeongeza sasa sub-section kwenye Kifungu cha 57 cha Sheria ya Makosa ya Rushwa kwa maana ya PCCA, zimekuwa sub- section tatu. Naomba ninukuu tu sasa itakavyokuwa inasomeka hasa ile Sub-Section (2) kwa maana ya 57(2) itasomeka kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unisikilize kwa makini. “Consent under Sub-Section (1) shall be obtained in accordance with the provisions of Section 9 of the National Prosecution Act, ile number (2), lakini ya mwisho ya tatu sasa itasomeka, “The DPP shall within 60 days,” hii sina tatizonayo. Tatizo langu kwenye Kifungu cha hiyo sub. (2).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeenda nimetazama hiyo NPSS ya mwaka 2008, pia nikaisoma kwamba sasa ule mfumo au mlolongo wa kupata kibali utafuata ile sheria ya Taifa, The National Prosecution Act. Nikaiendea nikaisoma inasema hivi, naomba ninukuu, “For the purpose of Sub-Section (6) The Director may by notice publish in the gazzete specify offences or threat a threshold of value involved in a case the prosecutions of which shall require the consent of the director in person and the power consenting the prosecution of which, may be exercised by such officer or officers subordinate to him as he may specify acting in accordance with his general or special instructions.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio changu hapa mamlaka sasa ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU hayapo. Mkurugenzi Mkuu kumbuka kwenye Sheria yake ya PCCA Section No. 5 PCCB ni Taasisi inayojitegemea, sasa iweje tena huyu Director wa PCCB aanze kupokea maelekezo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ni kitu ambacho sasa tunaiua TAKUKURU kabisa, nayasema haya nikiitaza nchi yangu siyo ushabiki wa mambo mengine yoyote yale adui rushwa ni mgogoro mkubwa sana katika nchi hii, hapa kwa kweli bado tunatwanga maji kwenye kinu tutaishia kuloa, hapa narudia kuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwenye kifungu hicho cha 57 (1) naomba sana viongezewe vifungu
kupanua wigo. Kifungu kinasema hivi except for the offences under section No. 16 tuongezee section zingine kwenye ile PCCA tupunguze sasa mlolongo wa makosa kwenda kwa DPP hawa wawe na uwezo wa ku-prosecute makosa mengi zaidi. Kwa mfano, ukiangalia Kanuni ya adhabu Penal Code Polisi wana uwezo wa kufanya prosecution makosa ya kwa mfano Kifungu cha 265 juu ya wizi, forgery, ubakaji, hawapiti kwa DPP, lakini makosa yanayofanana na haya ambayo yako kwenye Sheria ya PCCB kwanini waende kwa DPP?.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukienda kwenye Kifungu cha Na. 22 kutumia nyaraka ya kumdanganya Mwajiri si ndiyo ni sawa na kama forgery kule penal code, matumizi mabaya ya madaraka Na. 31 haihitaji kwenda kwa DPP. Rushwa za ngono haihitaji kwenda kwa DPP mbona Polisi wanaenda moja kwa moja kwenye mambo ya ubakaji. Kwa hiyo, haya makosa yote yarudishwe sasa yaongezewe hapa kwenye isiwe 15 peke yake, iwe 15, iwe 22, iwe 31 pamoja na 28 nadhani mambo ya ubakaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Traffic hapo hapo kwa mfano, makosa ya traffic yote unayoyajua Mheshimiwa Mwenyekiti hayaendi kwa DPP. Kwa nini sheria ya TAKUKURU inabanwa kiasi hiki, ninaomba sana baada ya mazungumzo haya mafupi niseme tu kwa ufupi sana tuitazame sana nchi yetu hii. Tukiibana hapa TAKUKURU juhudi za Mheshimiwa Rais na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano na zinazofuata itakuwa ni kazi bure.