Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Athumani Almas Maige (71 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilipata mtihani mkubwa sana wa kukuamini kama ni mtemi au siyo. Lakini ulilolifanya Mheshimiwa ndani ya Bunge lako hili kama Mwenyekiti umeonyesha kweli wewe ni mtemi. Fujo iliyotokea hapa hakuhitaji busara, ilihitaji nguvu na uwezo mkubwa sana nakushukuru sana na pole sana. (Makofi)
Mwishoni katika shukrani zangu nimshukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutusaidia chakula cha njaa. Tulipata matatizo sana sisi mwaka huu na nilipokwenda kuwaona nashukuru sana tulipata msaada huo, haukutosha lakini si haba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo chache naomba sasa nijadili hotuba ya Mheshimiwa Rais kuanzia ukurasa wa 16 mpaka 22. Mheshimiwa Rais ameongelea kuwaanda vijana kielimu, na mimi ningependa tukazanie hasa shule za ufundi (Technical Schools) na VETA.
Mimi ni zao la shule ya ufundi ya Moshi Technical na nipokwenda kuitembelea mwaka huu nikataka kulia. Shule hizi zimetoa watu wenye uwezo mkubwa sana, ma-engineer wengi waliopo sasa na wataalam wengi walipita katika vyuo hivi na shule hizi za ufundi lakini sasa hali yake imekuwa mbaya sana. Ningeomba Mheshimiwa Rais aelewe kwamba tunamuunga mkono sana katika hotuba hii, lakini vilevile ajue kwamba kuna vitu vya kufanya na shule za ufundi zipewe umuhimu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa unaofuata, Mheshimiwa Rais ameongelea kuwaandaa pia vijana kimtaji, akaongelea SACCOS vikundi vya kiuchumi vidogo vidogo lakini vyenye uwezo wa kuwezeshwa na mimi namuunga mkono kwa sababu mimi mpaka sasa ni Trustee wa NSSF kutokana na madaraka niliyonayo katika Chama cha Waajiri.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshaachia lakini naongelea nilivyokuwa kwamba ni muhimu sana Mheshimiwa Rais aungwe mkono na mifuko hii yote ya hifadhi ya jamii iweze kuwasaidia hawa vijana ambao Mheshimiwa Rais ametaka kuwasaidia kwa mpango ambao mifuko hii inao na ningependa tu kuitaja ni NSSF, PPF, PSPF na LAPF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais ameongelea katika hotuba yake gap linaloonekana sasa kati ya walionacho na wasionacho, maskini na wenye nacho. Wako watu ni kweli wametoka shuleni juzi au wamefanya mchezo fulani kwa kuacha kulipa kodi au kwa njia nyingine ya udanganyifu wamekuwa matajiri sana, kwa kufanya hivyo wamefanya watu wengine wawe maskini sana. Mheshimiwa Rais limemuuma sana hilo. Kwa hiyo, anafanya kazi kubwa ya kukusanya hela na kuzipeleka Hazina ili sasa aweze kuzigawa kwa wananchi wote. Suala hili mimi naliunga mkono na ninaomba watu wote tumpongeze Mheshimiwa Rais katika suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira katika ukurasa wa 16 Mheshimiwa Rais ameongelea kukuza ajira nchini ili vijana wenye uwezo wa kuajirika na uwezo wa kufanya kazi waweze kufanya kazi na hapa alikuwa anailenga sekta binafsi. Narudia tena sekta binafsi ndiyo engine au mhimili mkubwa sana wa kutoa ajira hapa nchini. (Makofi)
Lakini nao pia wamekuwa na malalamiko ya hapa na pale kwamba ziko tozo nyingi sana ambazo si za lazima ambazo pia Mheshimiwa Rais ameziongelea ziondolewe katika sheria ya 21 alizizozitaja kwamba kero kwa wananchi. Tozo moja kubwa iliongelewa leo asubuhi hapa ya Pay As You Earn, lakini pia ningependa kuitaja kero moja ya SDL. Sasa hivi Tanzania inafanya tozo la asilimia tano ambalo ni kubwa sana duniani, katika nchi zinazozunguka zote tozo kubwa kabisa katika nchi za jirani hapa ni asilimia 1.2. Sisi waajiri wanatozwa kila kichwa cha mwajiriwa asilimia tano, hicho ni kiasi kikubwa sana na imefanya tusiwe competitive katika nchi jirani tunapoajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Rais katika hotuba yake amegusa mambo ya maji, na Kanuni zinanikataza kurudia mambo yaliyoongelewa lakini ningependa kuchangia kidogo tu kwamba ule mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kupitia Shinyanga na Kahama unapita Makao Makuu ya Wilaya ya Uyui pale Isikizya ambako wafanyakazi wameshindwa kuhamia kwa sababu hakuna maji. Lakini vilevile mradi huu utagawa maji kilomita sita kushoto na kulia kwa barabara, tungependa mradi huu upanuliwe kuenda kilomita 25 ili kupeleka maji kwenye kituo cha afya cha Uyui Jimbo la Tabora Kaskazini na kituo kimoja tu cha afya Uyui na ambacho akifanyi kazi kwa sababu hakuna umeme na hakuna maji. (Makofi)
Katika suala hilo pia itasaidia kupeleka maji katika zahanati ya Ikongolo pale, kijiji cha Majengo na Kijiji cha Kanyenye. Vilevile umeme limekuwa tatizo kubwa sana katika Jimbo langu la Uyui mimi ningeomba wapiga kura wangu walionichagua walikuwa wanajua kwamba najuana na Mawaziri wengi na ni kweli hakuna Waziri humu ndani ambaye hanijui, tunajuana sana lakini hatupeani kazi kwa kujuana tunapeana kazi kwa mahitaji. Naomba Mheshimiwa Profesa Muhongo aangalie sana kupeleka umeme katika hiyo zahanati na kituo pekee cha afya pale Upuge.
Mwisho, ili niwaachie wenzangu waongee wananchi wa Uyui wanapata taabu sana na ikumbukwe kwamba Uyui ndiyo mkulima wa tatu wa tumbaku, lakini bahati mbaya sana tumbuka na sheria ile ya ushirika, ndiyo maana asubuhi nilitaka kuchangia hapa bahati mbaya sikupata nafasi. Ile Sheria ya Ushirika imetoa fursa kwa watu fulani kuwaibia wanyonge inaumiza sana, kwamba mkulima anayelima tumbaku analazimika akauze kwenye Chama cha Ushirika ambacho hakikopesheki na kama kinakopesheka kina madeni makubwa, anakatwa hela ambazo hajakopa. Mwaka jana amekatwa na mwaka huu amekatwa au wengine wamepeleka tumbaku hawalipwi chochote kwa sababu sasa wanadaiwa tumbaku ya miaka mitatu iliyopita kama vile hawana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linaumiza sana na wananchi wamekata tamaa kabisa, nafurahi nafurahi Waziri wa Kilimo anakutana na sisi kesho, mimi nimeandika paper ambayo inaeleza matatizo yote na itakuwa jambo la kuongelea kwenye mkutano wa kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala dogo sana lililobakia naomba Serikali ifanye juhudi kubwa kutambua au kutumbua majibu katika Vyama vya Ushirika ili vyama hivi viweze kuwatambua wafanyakazi wabaya ili wananchi waweze kuuza tumbaku na waweze kulipwa tumbaku imetusomesha sisi lakini sasa leo tumbaku imetia umaskini wazee wangu wote katika vijiji vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru niwaachie wenzangu waongee. ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu na mimi nichangie Mpango huu wa Maendeleo unaopendekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa vile natoka Mkoa wa Tabora siwezi kuanza vyovyote kwa sababu siasa ya Tabora ni tumbaku. Ndiyo maana kila Mbunge aliyesimama leo hapa ameongelea tumbaku. Kilimo cha tumbaku kimetulea Tabora kwa miaka 50 iliyopita lakini tukio la sasa la tumbaku kutonunuliwa limekuwa tatizo. Wakulima wa tumbaku ambao walitakiwa wauze tumbaku miezi sita iliyopita leo wanayo tumbaku ndani ya maghala na matokeo yake hawana chakula wala mavazi, watoto wa shule wamefaulu, wengine wamepewa ufadhili wa kulipiwa vyuo vikuu, wameshindwa kulipia ile registration fee lakini pia hata kuwasafirisha wameshindwa, pia kuna wagonjwa wameshindwa kutibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatusaidia sana, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja mara mbili ameongea na wakulima, ameongea na wanunuzi wa tumbaku. Mimi nimefanya kazi ya kukutana na wanunuzi wote watatu wa tumbaku, TLTC, Aliance One na GTI. Wote hawakuwa na bajeti ya tumbaku iliyolimwa kwa mwongozo wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo Morogoro wakati Serikali iliposema wakulima limeni tumbaku, itanunuliwa. Wamelima tumbaku nje ya makubaliano ya makampuni yale ya ununuzi, tumbaku ile ndiyo ilikuwa tegemeo la wakulima ambao wengine walikuwa hawajalima, wanakopeshwa mbolea na vyama vya ushirika vikuu WETCO, sasa hawawezi kuuza tumbaku, walikopa mabenki, wanauziwa mali zao, hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, Makampuni haya hayakuwa na bajeti ya tumbaku ya ziada, yamejikunakuna, yamejivuta, mimi sitetei makampuni lakini nasema kama biashara, wametafuta hela za ziada, wako tayari kununua tumbaku kwa dola 1.25, Serikali imewapangia bei ya dola 1.75, hawana hela hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoka kutembea kwenye Jimbo langu lote la Tabora Kaskazini wananchi wako tayari kuuza tumbaku hata kwa dola 1 ambayo ni sawasawa na Sh.2,250 kwa kilo, Serikali imekataa. Sasa wananchi hawataki hata kumwona Waziri wa Kilimo kwa sababu ameleta chuki kubwa sana. Kwa nini Serikali isiruhusu wananchi hawa wauze tumbaku kwa sababu tumbaku sasa baada ya mwezi mmoja itakuwa haina thamani tena. Tumbaku itakuwa imeoza, itakuwa imeharibika na imekuwa nyepesi, haina thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili la tumbaku Serikali imeona kila Mbunge wa Tabora akisimama anaongelea tumbaku, sisi sio wajinga, tuna uchungu, tunahurumia wananchi. Mimi nikienda jimboni nafukuzwa, simu yangu imejaa maswali tumbaku inanunuliwa lini na sina majibu. Serikali kama ina huruma kweli kwa wakulima tofauti ya bei ambayo Serikali inataka wanunuzi wanunue dola 1.75 na wanunuzi wako tayari kununua kwa dola 1.25, Serikali itoe ruzuku ya senti 50 kwa tumbaku iliyopo ya kilo milioni 14.7, thamani yake ni shilingi bilioni 15. Basi itoe ruzuku hiyo kwa wakulima ili waweze kuuza tumbaku iliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumbaku imekuwa tatizo kubwa sana na Serikali ndiyo imekamata kwenye mpini. Wananchi wanasikitika sana, wanailaumu Serikali kwa nini imezuia. Kwanza tumbaku wameilima wao wenyewe, wamekopa mikopo wao wenyewe, wanataka kuuza hata kwa dola moja, makampuni yametoa dola 1.25 kwa nini Serikali inakataa? Maana kuna mwaka wa hasara na faida, tukubali wakulima wa tumbaku safari hii tupate hasara lakini itakuwa hasara zaidi kama mwezi mmoja utapita bila kununua tumbaku hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tumbaku, lipo suala ambalo tunafikiri ni zuri sana. Serikali imefanya kazi nzuri sana ya kujenga reli ya standard gauge, lakini bajeti inayowekwa kwenye standard gauge ni ndogo, itachukua muda mrefu sana kuja kufika Tabora. Tuna habari kwamba imefika mpaka Morogoro, inawezekana ikafika mpaka Dodoma lakini kuja kufika Tabora kwa bajeti hii ya kusuasua hatuwezi kumaliza hiyo standard gauge. Ni wazo zuri, ni mpango mzuri lakini tufanye mpango wa kumalizia, siyo mpango wa kwenye makaratasi halafu hauishi. Nakumbuka tulipanga mwaka mmoja uliopita na leo reli haipo hata kilometa 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala zuri pia la anga. Tabora tunajengewa kiwanja kipya cha ndege lakini vilevile tunajengewa na jengo la wageni, hii ni hatua nzuri sana. Hata hivyo, lipo tatizo, uendeshaji wa Shirika hili la Ndege mimi sidhani kama tuko kibiashara zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo pia tatizo la ndege zetu kukamatwa huko nje. Mimi nalijua suala hili kwamba Shirika la Ndege halikuweza kununua ndege zake kwa sababu ndege yetu yoyote ambayo ingeruka nje ingekamatwa. Tunapenda kujua, ndege ambayo imekamatwa huko nje inakuja? Serikali iwe wazi iseme ndege inakuja lini ili wananchi tuendelee kushangilia mafanikio ya anga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa bomba la kutoka Uganda kuja Tanzania, ni mradi mzuri ambao Serikali na wananchi wote tunashangilia kwa sababu bomba hili lilikuwa na ushindani na jirani zetu. Kwa hiyo, mafanikio haya tunayapongeza, ni jambo zuri, Serikali imepambana na kupata mradi huu ambao utaleta faida. Kwanza kupitisha mafuta tutapata hela lakini italeta ajira kubwa kwa wananchi ambao watajenga bomba hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu, nashukuru sana pia kwamba barabara sasa zitajengwa lakini katika barabara za mikoa ipo barabara ya kutoka Tabora kwenda Mambali inaunganisha Shinyanga, ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini sioni utekelezaji wake ukitokea, hata upembuzi wake hakuna. Ilikuwa ni hadithi tu au kweli barabara hii itajengwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ikijengwa itasaidia kuunganisha Mikoa ya Tabora na Shinyanga. Pia ipo kwenye corridor ya mazao, kwa hiyo barabara hii kwetu ni muhimu sana kwa watu wa Tabora, Bukene na Shinyanga. Katika Mpango huu siioni barabara hii. Naomba Serikali itakapojibu ituambie barabara hii ya Tabora – Mambali imo au haimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la REA, nimeshangaa sana, nimetembea jimbo zima siioni REA na REA III tumezindua Sikonge kule, kwenye jimbo langu mbona simwoni mkandarasi, yuko wapi, kimetokea nini, kiini macho gani? Wananchi wananiuliza REA vipi Mheshimiwa Mbunge wetu, sina jibu. Serikali ituambie hatua kwa hatua utekelezaji wa kuweka umeme vijijini, ni muhimu. Sisi kule tumbaku tunalima halafu tunakausha kwa kukata miti, ili kulikimbia jangwa tukaushe tumbaku kwa umeme.

Mheshimiwa Spika, tunaomba REA iwe na mpango ambao unaeleweka sasa hatuelewi REA inaenea kweli vijijini au ilikuwa hadithi? Mbona imekuwa tofauti sana na ilivyoanza REA I na II, REA III imetokea nini, limetokea jini limemeza umeme, mbona hatuoni maendeleo ya umeme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la elimu, licha ya kizungumkuti ambacho Mheshimiwa Waziri wa Elimu leo amekielezea hapa kuhusu jinsi ya kuwa-sponsor wanafunzi lakini mimi nina wanafunzi baba zao walifariki, nimeiandikia Bodi ya Mikopo, mwaka jana wamekosa na mwaka huu pia wamekosa. Vigezo nimesikia hapa anasema moja ni kutokuwa na wazazi au uwe mwenye ulemavu, mimi nina wanafunzi wawili ambao nimechukua jukumu la kuwaandikia barua na kumwandikia Mkurugenzi wa Bodi ya Mfuko wa Elimu lakini wamekosa tena na hawana baba, mama hawana mtu yeyote wataenda wapi na wamefaulu division one wote lakini wamekosa, sasa mfumo ukoje?

Mheshimiwa Spika, kama kigezo ni kuwa yatima na hawa ni yatima wamekosa, kama kigezo ni kufaulu vizuri wamefaulu, kama kigezo ni masomo ya sayansi wamechukua sayansi tena mmoja alikuwa Chuo cha Sokoine akaondolewa. Nataka Serikali iniambie nikiwapa majina ya hawa wanafunzi wawili ambao wamefaulu vizuri na mmoja alikuwa anaendelea na masomo watampa mkopo na kwa nini walimpa mara ya kwanza halafu wamemkata na hana baba wala mama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ndiyo inayosomesha wataalam watakaofanya kazi viwandani. Kwa sababu ambayo siijui Waziri aliyepita na bahati mbaya alishafariki aliondoa elimu ya ufundi ambayo ilikuwa na mfumo wa kupata watu wenye Full Technician Certificate (FTC). Kwa mfano, mtu alikuwa anatoka Ifunda Technical, Dar Technical, Moshi Technical au Tanga Technical kwenda Chuo cha Ufundi, miaka minne amechagua kozi ya umeme kwa mfano, anakwenda Technical College miaka mitatu anapata cheti cha FTC, lakini baadaye akirudi miaka mitatu anakuwa na miaka 10 katika field ile, kwa hiyo akienda kufanya kazi ni mtaalam aliyefaulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi bahati mbaya sana mfumo huo umevurugika wala hakuna anayejali. Matokeo yake ni nini? Hakuna mafundi viwandani, mafundi sanifu wenye FTC hawapo lakini Kanuni za Mainjinia wanasema kila Mhandisi mmoja katika kiwanda anatakiwa asimamie technicians 25 sasa hao technicians hawapo na mainjinia tunatoa wa white colour. Mimi watu wa Engineering wa University wanapochora maboksi (Geometrical and Techninical Drawing) niliifanya form one na form two lakini sasa wanayafanya chuo kikuu wanatoka pale white colour hawana wa kuwasimamia, FTC tumeifuta.

Mheshimiwa Spika, napenda vyuo vya ufundi virudishwe lakini pia chuo cha ufundi kiendeleze kozi ya FTC inayotoa mtaalam wa fundi sanifu. Nashukuru Serikali imenisaidia hela jimboni kwa ajili ya high school ya Ndono na shule ya msingi lakini pia naomba kabisa kabisa mjaribu kurudisha mfumo ule wa Ujerumani wa Technical Engineers na Academic Engineers, hiyo peke yake ndiyo mkombozi wa watumishi viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora. Nililalamika humu ndani ya Bunge lako kwamba jamani kama Mahakama inaongelea kuweka Mahakama nyingi kila Kata au katika Kila Wilaya kule Upuge kwangu Mahakama imetelekezwa. Mahakama ya mwaka 1954 imefanya kazi mpaka baada ya uhuru na kuendelea lakini sasa imetelekezwa, majengo yake mazuri yako wazi, panya na nyoka wameingia, mwisho wakulima wamevamia wanakaa mle mwenye majengo mazuri.

Mheshimiwa Spika, palepale mbele yake kuna kituo cha afya hakuna Madaktari kwa sababu hakuna nyumba. Nikasema kama kulikuwa na sababu nzuri basi ya kuiacha hiyo Mahakama zile nyumba zitumiwe na Idara nyingine za Serikali na nillikuwa nalenga kituo cha afya.

Mheshimwa Mwenyekiti, kituo cha afya tunajenga vizuri, tumepata shilingi milioni 500 kukiboresha kwa kujenga wodi za wagonjwa lakini sasa Madaktari hakuna, hakuna nyumba na mita 500 kuna majengo ya Mahakama ambayo hayana kazi. Kwa bahati mbaya Mheshimiwa mmoja alijibu humu ndani kwamba Mahakama inafanya kazi jambo ambalo si kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikishaji wa sekta binafsi. Waziri Mpango amesimama juzi hapa akasema sisi tunajua injini ya uchumi ni sekta binafsi, injini gani haina mafuta? Mnasema ndiyo uti wa mgongo, uti wa mgongo hauna mfupa, hamuisaidii, sisi tumekuwa tunalalamika hapa ndani kwamba sheria zilizopo hazitupi competitiveness na jirani zetu, tukishindana tunashindwa katika ushindani, tender wanapata wenzetu, makampuni ya hapa yaki-bid yanashindwa kwa sababu ndani yake kuna kitu kwa mfano kinaitwa SDL. Sisi hapa Tanzania tunalipa SDL ya 4.5% ndiyo ya highest duniani.

Mheshimiwa Spika, muda wote waajiri tumeomba mtupunguzie highest ya SDL iko Kenya 1.2% lakini kwa ajili ya Idara moja tu ya Utalii kwingine kote hakuna, Uganda, Rwanda na Burundi hakuna, sisi tuki-bid tender za international maana lazima tuweke SDL tunakosa hizo tender competitiveness hakuna Tanzania. Sasa mnasema private sector ndiyo injini, injini gani bila mafuta?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Serikali haiko tayari kufanya PPP, nina mfano mzuri sana. Mimi baada ya kwenda Jimboni kwangu nikagundua kwamba watu hawana elimu kubwa sana kuhusu mambo yanayotokea duniani nikaamua kufungua kituo cha redio na kwa sababu Halmashauri ndiyo nailenga itumie kituo hicho nikaipa 30% kama PPP.

Lakini tangu tumeingia ubia huo Halmashauri imeshindwa kupata kibali cha kuwaruhusu tufanye PPP. Kwa sababu lazima tupitie Kamati ya Fedha na Uongozi, Baraza la Wilaya, Baraza la Mkoa, Mkuu wa Mkoa, Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Fedha, Kamishna wa Bajeti ndiyo wapate kibali kwamba ingieni, imeshindikana, mwaka mzima sasa mradi umesimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru sana kuniruhusu na mimi nichangie hotuba hii ya ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango kuhusu Mapendekezo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi wa Bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kuanza kutoa maoni yangu kabla ya kusema ukweli wa utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Magufuli, mimi naamini sasa masia nyumbani haaminiki, upande wa pili kule wanasema maneno mabaya ambayo hatuelewi kuhusu utendaji mzuri wa Serikali ya Awamu ya Tano. Sisi huku tunapongeza mambo mazuri yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano lakini sio sisi tu, hata nchi za nje wanapa taabu kujua lugha gani watumie neno gani watumie wamesema magufulification na sisi tunasema kazi tu maana yake kazi nzuri imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nitaje mafanikio yaliyotajwa hapa kweye kitabu cha Mheshimiwa Mpango pamoja na kukusifia wewe na taaluma yako wewe na dada yangu Kijaji, Naibu Waziri lakini pia watendaji wa kazi ya Wizara yako ambao wameleta mpango mzuri sana katika mapendekezo yenu ya maendeleo ya huu mwaka moja na mpango wa bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na ukuwaji wa uchumi. Uchumi wa Tanzania hakuwi wenyewe unakuzwa ina maana kuna watu wanafanya kazi ili uchumi wetu ukuwe, lakini mapato ya kodi za pamoja na mapato yasiyokuwa ya kodi yamekuwa sana kulinganisha miaka mitatu iliyopita, lakini vilevile ulipaji wa madeni na mimi naomba niseme hapa ni declaire interest, Wizara hii imenilipa madeni kama mkandarasi, wakandarasi walipolipwa na mimi naipongeza Wizara hiyo kwa sababu nilikuwa mtu ambaye niliyolipwa madeni hayo ya wakandarasi, lakini pia barabara pia mimi ni moja watu walio benefit na barabara inayojengwa kutoka hapa kwenda Tabora imebakia karibu kilometa 65 tu ili barabara yote iliyojengwa pale ikamilike tuwe tunatoka hapa kwenda tabora kwa muda masaa mawili/matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna reli ya standard gauge sitaki kuisema sana imetajwa mpaka imekuwa tunu ya Tanzania, lakini pia kuboresha shirika la ndege, mimi niseme nini. Kila mtu mwenye macho ahambiwi tanzama ndege zote zile tangu lini sisi tungeweza kupanda dream line ndani hapa hapa ndani lakini kila mtu ana panda dream line kwa faida kubwa tunaipata, lakini viwanja vya ndege pamoja na kiwanja cha Tabora kimekarabatiwa vizuri, lakini bandari imejengwa vizuri, imefungwa mitambo ya kuona vitu vya kuona mitambo ya kuona vitu vinavyopita kwenye makontena yale na kazi kubwa imefanyika ya kukamata watu wanaojaribu kuiba nyara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo mimi sisemi, kazi kubwa ya kilimo imefanyika lakini hapa nitakuwa na mapendekezo yangu baadae, lakini huduma ya afya katika Jimbo langu pamoja na zile vituo vya afya 295 vimetolewa mimi nimepata kituo kimoja ambacho kimejengwa na kila kitu sasa kipo ndani kazi ndogo iliyobakia tunaomba gari la wagonjwa ili tuweze kuwakimbiza wale wangonjwa wanaozidiwa kwenda Hospitali ya Rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nishati tumesikia miradi mipya ya Kinyerezi, miradi mpya ya umeme na umeme wa REA ambao sasa utaleta maendeleo vijijini. Lakini huduma ya maji sisi upande wa Tabora tumepata mpaka maji kutoka Ziwa Victoria mradi mkubwa na mabomba yamekaribia kabisa jimboni kwangu na kwenda Tabora Mjini, lakini pia kuamasisha makao makuu kutoka Dar es Salaam kuja hapa lilikuwa jambo lisilowezekana mbona hamshangili? Mbona hamuoneni ukweli huo kwamba tupo hapa Dodoma pamoja na kila mtu isipokuwa Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais yupo hapa, Waziri Mkuu yupo hapa, Mawaziri wote wako hapa. Jambo limekaa miaka 43 karibu hawashangai upande wa pili na hili pia hamlioni wakati mnajua tupo hapa? Lakini pia mambo ya madini mwaka huu tumepata bilioni 301 faida au mapato kutokana na madini, ilikuwaje miaka iliyopita hayakupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maoni yangu kuhusu elimu lakini tunasoma elimu ya msingi bure jambo hili haliwezekani na halikuwezekana miaka iliyopita tunatumia zaidi ya bilioni 20 kwa mwezi kulipia watoto wetu waende shule, lakini pia usafiri wa majini, meli zimejengwa pamoja na ajali iliyotokea tunaomba Mungu awarehemu marehemu waliofariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sasa ni change mimi mambo gani ingefaa Wizara yako Mheshimiwa Mpango ifikirie mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafute mahusiano kati ya sekta binafsi na Serikali; kuiwezesha sekta binafsi Mheshimiwa Dkt. Mpango itazalisha na kuuza uchumi wa nchi hii, duniani kote Tanzania tu ndio tunasema kwamba labda Serikali peke yake itafanya, lakini sekta binafsi ina mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi.

Kwa hiyo, mimi napendekeza Serikali itafute jinsi ya ku-engage private sector tuweze kuitumia ikuze uchumi na kuongeza ajira. Lakini pia Serikali itoe kipaumbele kwa katika kurasimisha baadhi ya kazi, shughuli nyingi hapa Tanzania za wananchi hazijawa rasmi na hiyo sekta na hiyo isiyo rasmi hailipi kodi, lakini inapata mgao mkubwa wa maendeleo wa fedha za maendeleo lakini kama ingerasimishwa basi tungeweza kupata mapato makubwa kuongeza kwenye kapu la mapato ya Serikali pamoja na kuwatengea vijana na akinamama katika Halmashauri zetu lakini hela hizo haziendi, kwa mfano katika Halmashauri ya Uyui hela zote zaidi ya milioni 400; milioni 500 zilizogaiwa hazifiki milioni 46 kwa mwaka mzima. Hili ni tatizo. Kwa hiyo, Serikali itafute njia ya kuweza kurasimisha upatikanaji wa hela za wale akina mama na vijana huko vijiji ili waweze kuleta maendeleo na kujibudu huko.

Mheshimiwa Mwenyeikiti, lakini pia Serikali ifanye kazi ya kurejesha elimu ya ufundi hapa nchini na hili ni jambo la muhimu kabisa, viwanda haviwezi kwenda bila mafundi sadifu na mafundi mchundo, ninamaanisha artisans na full technician certificate people, bila hiyo viwanda haviwezi kwenda hali hii ilikuwepo miaka iliyopita ikatokea bahati mbaya sana elimu ya ufundi imedhalilishwa, imeteremshwa mimi nafikiri ni muhimu sasa kila shule za kata ipewe somo moja la ufundi labda umeme, labda ujenzi wa mabomba na kadhalika ili tuwe na mafundi kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyetiki, mwisho jambo muhimu sana ni kuweza kutumia kukuza uchumi wetu ni kutumia taasisi za majeshi, katika nchi zingine kwa mfano Vietnam na sio Vietnam peke yake kwa sehemu kubwa ya maendeleo katika nchi imetumika majeshini aidha katika kufanya research au kuzalisha mali ambao ilikuza uchumi, sisi tuna mashirika matatu hapa makubwa sana. Shirika la Mzinga pale Morogoro lingeweza kufanya kazi kubwa sana ya kukuza uchumi wakiwezeshwa, lakini pale Kibaha kuna Shirika la Nyumbu ambapo wanayo Research and Development Unit (R&D) wangeweza kufanya kazi kubwa sana za kiuchumi na kuwa chanzo cha kukuza uchumi na kuongeza ajira. Lakini mashirika yale mawili yametelekezwa na yanahangaika peke yake na yanatumia bajeti ya Ngome ambayo hakuna hela, Serikali ichukue jukumu muhimu la kuwezesha maeneo haya mawili tunaweza kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango lakini lipo Shirika la SUMA JKT ambayo pia unaweza kuwa uzalishaji mkubwa sana na jua chakula kina-stabilize mfumo wa bei, Magereza wakiwezeshwa wanaweza kulima chakula cha kutosha kula watu wote lakini pia wanaweza kuleta chakula cha kutosha kuziba nafasi ya mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Mwenyekit, mimi nafikiri nilitaka kusema hayo, lakini la mwisho kabisa niongelee kuhusu lugha ya kufindishia. Elimu ni ufunguo wa kila kitu, hakuna maendeleo bila elimu, lakini elimu yetu inawapa watoto mzigo kweli kweli. Watoto wanasoma darasa la kwanza mpaka la saba kwa kiswahili na mwaka huu watoto wamefeli sana kiingereza halafu wakifika darasa la saba wakienda form one wana switch frequency, wanasoma kiingereza kwanza wanapata tabu yakuelewa kiingeraza, lakini wanapata tabu ya kuelewa masoma kuna tatizo gani hapa la watu wasisome kiswahili, kwanini watoto wetu wasome kiswahili zipo nchi nyingi wanasoma lugha za kwao na hata nikizitaja Ufaransa, Uingereza, Marekani, Ujerumani Urusi, China kote wanasoma lugha zao na watoto wanaelewa, mimi nilikuwa kwenye mahafali mbili kwenye shule za sekondari jimboni kwangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kuunga hoja mkono hii asante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALMASI A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana kwa kuniruhusu kuchangia hoja hii ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza naomba nitoe shukurani na najua wewe mara nyingi unasahau kwa sababu unawahudumia wengi, unawasaidia wengi. Mimi umenisaidia sana kufika hapa nilipo, ulikuwa chachu ya mimi kugombea Ubunge kutoka katika Bunge la Katiba.

Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Katiba nikukumbushe wakati Wapinzani walipokataa hati ya Muungano na wakawa tatizo kubwa sana na hata mlipotupa Hati ya Muungano, Wapinzani wakasema imefojiwa, mimi nilishawishi nichangie kutoka katika lile kundi la 221 na nikasema mimi na mtu mmoja wa upinzani wanipe hiyo hati tuipeleke Ubalozi wa Marekani tukaangalie tu wino kwa sababu walikuwa na uwezo wa kusoma wino wa miaka kabla ya kuzaliwa Nabii Issa, watuambie tu huo wino umeandikwa lini wakati marehemu Karume yupo au baada ya kufariki marehemu na ikawa ndiyo maziko ya suala la Hati ya Muungano iliyofojiwa, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika,tangu nimeingia hapa Bungeni huu ni mwaka wa nne, umenisaidia mambo makubwa mawili. Kwanza nilileta Muswada Binafsi wa Sheria ya Sekta ya Ulinzi. Kwa kweli ulinisaidia sana, uliupokea Muswada ule ukafanyiwa kazi na Bunge na mapendekezo yakaenda Serikalini, Serikali wakauchukua Muswada huo watauleta kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani. Hiyo ni kumbukumbu ya mambo uliyonisaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hivi karibuni nimekuletea Hoja Binafsi ya kutaka lugha ya Kiswahili itumike kama lugha ya kufundishia. Bunge limeifanyia kazi na kuniandikia mimi tena nilipeleke suala hilo au hoja hiyo kwanza ipate maoni ya Chama change. Chama changu wanalifanyia mchakato hoja hii na baadaye wataniarifu itakuwaje. Haya ni mambo makubwa sana kwangu mimi na nitakuwa nimeweka alama kubwa katika Bunge lako kwa msaada wako. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,pia naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na hasa kwa matendo yake makubwa ya kusaidia nchi hii kuipeleka mbele katika miaka mitano ambayo amekuwa Rais na kitaifa lakini pia katika Jimbo langu amefanya mambo makubwa sana. Ameniletea maji kwenye vijiji vyangu vyote karibu asilimia 48, umeme wa REA, kituo cha afya, hospitali ya Wilaya, kituo cha VETA shilingi bilioni 5 na ananijengea Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi katika Kata yangu ya Magiri, Kijiji cha Malampaka. Mambo haya siyo madogo, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kitendo chake cha kuishi ndani ya mambo aliyoyafikiria Mheshimiwa Marehemu Baba wa Taifa hasahasa misingi ya Azimio la Arusha na mimi ninalo. Hili hapa ndiyo Azimio la Arusha ambalo lipo na kila nikilisoma hili linanikumbusha mambo yangu ya miaka 1965 nilipotembea kilometa 50 kuunga mkono Azimio hili. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuliamsha dudu hili la Azimio la Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niende kwenye mambo muhimu ya kuchangia katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza nimshukuru Waziri Mkuu kwani yeye ni tofauti na Mawaziri Wakuu wote niliowafahamu. Nakiri kwamba nimefanya kazi na Mawaziri Wakuu waliopita lakini Waziri Mkuu huyu ni muungwana, mpole lakini anayependa watu.

Mheshimiwa Spika, hata nilipokuwa nalalamikia tumbaku ndani ya jengo hili na hata nilivyofanya kosa la kwenda kumshtaki kwake Waziri wa Kilimo hakuchukua hatua yoyote mpaka alipokwenda Tabora kuthibitisha niliyoyasema na baadaye akachukua hatua nzuri sana na tukauza tumbaku. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni mtu wa watu, anapenda wanyonge, amefanana sana na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,pia nimshukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama, huyu binti wa Kingoni, mweupe maana sisi Wanyamwezi watu weupe, mara anikatishe tamaa aniite baba, mara aniite kaka, akikumbuka mambo yangu ya zamani kwamba nilikuwa Rais wa Afrika ananiita bosi, mara aniite mzee hata sijui ananiita nani sasa. Namshukuru sana kazi maana zake ni nzuri sana na ameongoza Wizara hii kwa nguvu sana. Mimi jina langu kwake na roho yangu nyeupe ni mtani wangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika,lakini pia ana Mawaziri wadogo wawili…

SPIKA: Nataka kumwambia tu Mheshimiwa Jenista, Wanyamwezi hawazeeki.

MHE. ALMASI A. MAIGE: Ni kweli kabisa. (Kicheko)

SPIKA: Endelea Mheshimiwa Maige. (Kicheko)

MHE. ALMASI A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniongezea hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niwashukuru Mawaziri wadogo wawili, ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Ikupa. Hawa nimewajua mimi nikiwa Mwenyekiti wa Waajiri Tanzania.

Mheshimiwa Spika,katika mchango wangu nitachangia mambo ya kazi na ajira lakini pia mambo yanayohusu tozo zile za SDL. Nianze na suala la kazi na ajira. Sisi waajiri na naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mwajiri na ni Mkandarasi Daraja la Kwaza, bado tunategemea kwamba Serikali itafanya mpango wa kupunguza SDL kutoka asilimia 4.5 iliyopo sasa mpaka asilimia 2 kulingana na watu wengine walioko huko Duniani hasa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana tulikuwa tumepanga kwenye bajeti hii ya Wizara ya Kazi na Ajira kurekebisha sheria za kazi ambazo zimepitwa na wakati. Sheria hizo hazikurekebishwa na mapungufu yake tunayaona sasa. Wakati huu imetokea Corona tunafunga biashara, tunafanya watu wasiende makazini lakini hakuna nafuu kwa mwajiri, tunaendelea kulipa mishahara na hii tunaona kwamba siyo sahihi. Kama ingekuwa sahihi basi kwenye hili la force majeure kwa maana ya jambo lililotokea nje ya waajiri na wafanyakazi ilitakiwa tupewe nafuu wote wawili.

Mheshimiwa Spika, lipo suala la Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), mimi na wenzangu waajiri tunaamini kwamba bado Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) kuendelea kuwa chini ya Wizara ya Elimu ni makosa. Mwanzo iliwekwa vile kwa sababu tulikuwa tunatafuta hela za mikopo ya wanafunzi sasa hivi tunakusanya hela zinakwenda kwenye central account, kwa hiyo sababu ile imekufa, siyo muhimu tena. Tunaomba VETA kwa sababu ni Vyuo vya Ufundi Stadi vinafundisha wafanyakazi wetu ambao wako chini ya Wizara ya Kazi na Ajira virudishwe tena chini ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa maana hakuna sababu ile kubwa iliyokuwepo ya kukusanya hela kwa ajili ya mikopo kwani hela zinakwenda kwenye central account.

Mheshimiwa Spika, sasa niongelee Mfuko wa Fidia. Mfuko wa Fidia ulipoanzishwa tuliunga mkono na ulikuwa na wigo wa matawi mawili tu kwamba utakusanya tozo kwa waajiri wa umma yaani public na sekta binafsi. Sasa sisi tukawashauri kwamba hapana wapanue wigo ili waajiri wenye kazi za hatari na zenye madhara walipe zaidi halafu waajiri wenye kazi salama na hazina madhara walipe kidogo kwa mfumo huo huo kwamba wale wa public na wale wa binafsi.

Mheshimiwa Spika, tulifanya stadi Waziri aje na matokeo ya stadi hiyo ilisemaje. Sisi Waajiri tunaamini kwamba ni muhimu sana sana kuwe na sababu ya kupanua wigo ili hela nyingi zikusanywe kwa sababu ya kufidia wafanyakazi wetu watakaoumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwishoni nina ukakasi. Uwakilishi ndani ya Bunge letu katika muktadha wa ajira na kazi ni wa utatu na utatu huu unasajiliwa na kusimamiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambao ni wa Serikali, Waajiri na Wafanyakazi. Nauona huu uwakilishi katika Bunge lako kwa theluthi mbili. Naiona Serikali chini ya Waziri Mkuu na Mawaziri wake, nawaona wafanyakazi, Majimbo mawili ina maana Wabunge wawili walioingia humu Bungeni kupitia wafanyakazi lakini siwaoni waajiri.

Mheshimiwa Spika,najua tulipotokea siku za nyuma ilitakiwa iwe hivi kwa sababu waajiri ndiyo waliokuwa mabepari na makabaila na tulitaifisha mali zao lakini yameshapita hayo, tusiendelee kuganga yaliyopita. Hivi kwa nini hivi sasa kusiwe na uwakilishi wa waajiri humu ndani? Kasoro itakuwa nini? Iam thinking loudly, tatizo ni nini kuweka uwakilishi wa waajiri?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii na kwa kweli naunga mkono mambo yote yatakayoongelewa katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara ya Kazi na Ajira.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu na mimi nichangie kwenye Bunge hili la Bajeti na hasa katika Wizara hii ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo. Kwa vile hii ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili, kwanza napenda kusema machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mambo haya anayofanya. Mimi namchukulia Mheshimiwa Rais kama captain wa meli ambayo ilitaka kuzama. Tanzania kama meli ilikuwa na abiria wa aina mbili, wale ambao walikuwa juu na wale walioko chini. Kawaida daraja la kwanza katika meli wanakuwa juu na daraja la chini wanakuwa chini sasa chakula chote kilikuwa kinakwenda juu. Kwa bahati nzuri walioko chini wakaona matatizo ya njaa wakatoboa meli kwa hiyo meli ingezama, waliokuwa juu ambao ndiyo mafisadi na waliokuwa chini masikini wote wangezama. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais ameliona hilo kwa hivyo anakusanya hela zote na kuzipelekea Hazina halafu azigawe kwa wananchi wote wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichangie machache, juzi niliwaona wenzetu wa UKAWA, katika hotuba yote aliyosema Mheshimiwa Rais pale, pamoja na kupunguza ile Pay As You Earn kidogo wakacheka lakini muda mrefu walikuwa wameangalia luninga iliyokuwa live kwa hiyo kila ilivyopita kamera pale kwao wakajikumbusha wapo Bungeni wakashangilia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye suala hili kuhusu bajeti ya Wizara ya Kilimo. Mimi nina imani sana na viongozi hawa aliowateua Mheshimiwa Rais katika Wizara hii hasa Mheshimiwa Mwigulu na Naibu Waziri. Pia nina imani na Baraza zima la Mawaziri ambao watasaidiana kwa pamoja na Mheshimiwa Rais kuendesha Serikali. Kuhusu mambo ya kilimo sasa, nina imani Mheshimiwa Mwigulu atakuja na majibu mazuri kuhusiana na matatizo makubwa waliyonayo wakulima. Napenda sana Mheshimiwa atakapokuja kuhitimisha anieleze upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima wetu wote lakini vilevile matatizo makubwa ya wakulima wa tumbaku. Zao la tumbaku Tabora limekuwa na matatizo makubwa na halina mafanikio hata kidogo kwa wakulima wa tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kabisa Serikali itambue kwamba kazi ya kulima tumbaku ni kazi ngumu (hard labour). Kwa hiyo, napenda Serikali itambue kulima tumbaku ni kazi ngumu kwa hivyo wakulima walipwe mara mbili, kwanza kwa kulima tu tumbaku halafu pia wakiuza tumbaku walipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningeshauri Waziri wa Kilimo atakaporudi kujumuisha masuala haya ya Wizara ya Kilimo aongelee kilimo cha mazao mengine katika eneo langu la Tabora Kaskazini. Miaka yote wakulima wa Tabora Kaskazini wanalima tumbaku tu kama zao la biashara lakini inavyoelekea tumbaku inazidi kwenda chini na ukiangalia kwenye jedwali lake Mheshimiwa Waziri ameeleza jinsi kilimo cha tumbaku kinavyokwenda chini, lakini vilevile wavutaji wa tumbaku wanapungua kwa hivyo siyo zao linaloweza ku-sustain baada ya miaka 10 ijayo.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Serikali ipendekeze zao lingine kule Tabora lakini wakulima wanaogopa kulima zao lingine la biashara kwa mfano ufuta, karanga na alizeti kwa sababu mazao haya hayana soko la uhakika. Nina hakika Mheshimiwa Waziri akija na majumuisho yake awashawishi wakulima wa Jimbo langu kulima mazao mengine waepukane na tumbaku ili waweze kuwa na mazao ambayo yatawapa faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kujua msimamo wa Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo kuhusu ujenzi wa Kiwanda cha Tumbaku pale Tabora. Kiwanda cha Tumbaku kilikuwa na uwezo mkubwa wa kusaidia kama kitajengwa Tabora na kupunguza gharama kubwa kwa wakulima. Sasa hivi wakulima wanalipia pia gharama ya kuhamisha tumbaku kutoka Tabora kuja Morogoro ambako tumbaku hailimwi. Vilevile tumegundua makampuni yanayonunua tumbaku ambayo ni matatu tu yamejenga makao makuu yao Morogoro ingawa wananunua tumbaku kutoka Tabora na wakulima wanagharamia kuleta tumbaku Morogoro. Napenda kupata tamko la Serikali inafikiria nini kuanzisha Kiwanda cha Tumbaku pale Tabora?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Kiwanda cha Nyuzi ambacho sasa kinafugiwa mbuzi mule ndani. Kiwanda kile kina uhusiano wa karibu sana na walimaji wa pamba. Kwa hiyo, napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha aelezee hatma ya kiwanda kile ambacho kilikuwa ndiyo ukombozi wa wakulima wa pamba katika Mikoa ya Shinyanga na Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri au Waziri aje na majibu kwa nini mali za Bodi ya Tumbaku ziliuzwa na zikanunuliwa na moja ya kampuni inayonunua tumbaku na bado usimamizi wa zao la tumbaku likabaki mikononi kwa Bodi ya Tumbaku ambayo sasa haina meno? Usimamizi wa zao la tumbaku hauna mwenyewe, matatizo yote yanayotokea kwenye zao la tumbaku hilo ambalo nalisemea muda wote ni kwa sababu halina msimamizi.
Napenda kujua kwa nini Bodi ya Tumbaku imepewa jukumu la kusimamia tumbaku na wakati haina uwezo wowote kwa sababu mali zake zote zimeuzwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni vituo vya utafiti. Hatuwezi kuendesha kilimo hapa Tanzania bila utafiti. Nimeangalia kwenye jedwali la Mheshimiwa Wiziri ya Kilimo, utafiti umepewa hela ndogo sana na kwa sababu hiyo tunaendesha kilimo ambacho hakina utafiti wa kutosha. Napenda Serikali iongeze fedha kwenye utafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee mambo ya ruzuku. Fedha zinazoletwa kwa ajili ya pembejeo na mbegu wafikiriwe kwanza makampuni yanayotengeneza mbegu na mbolea hapa Tanzania kwa sababu tunayalipa makampuni yanayotoka nje na yakiharibu hatuwezi kuyakamata. Hivi karibuni Kanda ya Ziwa waliuziwa mbegu ya pamba ambayo haikuota na hili katika nchi nyingine unaweza kushtakiwa ulipe gharama ya wakulima kwa mazao waliotegemea kuvuna. Mbegu za pamba zimeuzwa, wananchi wamepanda, wakaweka na mbolea na mbegu hazikuota. Hili ni jambo baya sana na limefanya wananchi wawe na chuki kwa Serikali yetu. Tungependa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu maswali haya aongelee vizuri sana jinsi ya kusimamia ruzuku inayotolewa na Serikali kwenda kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko pia suala la pembejeo, pembejeo imekuwa kiini macho inatajwa hapa na kwenye bajeti hela nyingi, lakini gharama ya pembejeo inayofikishwa kwa wakulima kule Jimbo la Tabora Kaskazini ni kubwa mara tatu, nne ya bei ya mbolea hiyo Dar es Salaam. Mbaya zaidi mbolea ya ruzuku kwa mfano ya kupandia inafika katikati ya kilimo yaani kilimo kimeshaisha ndipo mbolea ya ruzuku inafika, mbolea ya kupandia imekuwa ya kuvunia. Vilevile mbolea ile inayotolewa kama ruzuku haiwafikii wananchi inafikia kwa madalali jambo hili limekuwa baya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mheshimiwa Waziri wa Kilimo atakapokuja aje na majumuisho mazuri kuhusu upatikanaji wa pembejeo na hasa mbolea ya ruzuku kwa wakati ili wananchi waiamini Serikali yao. Sasa hivi watu wote ukisema ruzuku ni kama vile wanabeza kwa sababu kwa kweli mbolea ya ruzuku haifiki na mbaya zaidi wakulima hawa maskini wanapata tabu sana kwa sababu mtu aliyetakiwa kupeleka mbolea kwa mfano tani 10, anapelekea tani moja na baadaye anaenda kusainisha vocha kwa watu maskini kwa kuwahonga hela ndogo ndogo halafu yeye analipwa hela nyingi sana, Serikali lazima ihurumie watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile yako mambo ya ushirika. Vyama vya Ushirika na Sheria ya Ushirika ni mbaya sana kwa wakulima. Viongozi wa Chama cha Ushirika ingawa wametokana na wakulima wenyewe hakuna anayewasimamia. Vyama vya Ushirika havikaguliwi, vinaiba, vina madeni makubwa wanalipa wakulima. Mbaya zaidi wakulima waaminifu …
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kama makelele yangekuwa yanashinda kesi basi upande wa Upinzani wangeshinda sana, lakini ndiyo wamepoteza kesi zote ambazo walishtaki kwa sababu ya kushindwa kura, licha ya makelele yote ambayo wanafanya humu ndani, mahakamani hatushindi kura kwa kupiga makelele. Pia niungane na mwenzangu Mheshimiwa Tundu Lissu, aliposema asubuhi kwamba tunaposema sisi sikilizeni msiumie, tuseme mtusikilize.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu hawa hawajielewi kwa nini hawapewi Serikali, hawapewi Serikali kwa sababu wananchi hawawaamini, hawa ni ving‘ang‘anizi hawa kwenye madaraka. Tawi lao la CUF la UKAWA la CUF, Kiongozi wake ana miaka 20 anagombea yeye peke yake, vilevile hawajielewi wenzetu hawa kwa nini hawapewi madaraka.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema tukiumia tuvumiliane, neno la ufisadi lilikuwa ndiyo ajenda ya Upinzani kwa mwaka mzima mmetangaza ufisadi kwamba haufai. Imetokea nini?
Mimi nina orodha ya mafisadi ambayo mliitangaza ninyi UKAWA, lakini shemeji yangu huko umemchukua namba moja fisadi unaye wewe huko na jambo hili linafanya wananchi wasiwaamini. Mnawafanya watu waamini kwamba ninyi ni vinyonga, mnabadilika badilika, hatutaki sera ya namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uchaguzi wa Zanzibar. Hakuna mtu aliyewakataza kushiriki uchaguzi uliorudiwa na hasa tawi lenu hilo la CUF, siyo kosa la Chama cha Mapinduzi kushinda kura zote kwa sababu ninyi mlitia mpira kwapani.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, hawa UKAWA wanajua siri kwa nini hawakushiriki uchaguzi mbona hamuendi mahakamani? Mbona hamsemi kwa nini hamkushiriki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mapinduzi ya Zanzibar ni kweli kwamba Tanzania Bara ilishiriki na kusaidia mapinduzi kwa nguvu yote na sababu kubwa tulijua kwamba mapinduzi yale ni haki, yanaleta uhuru kwa Wanzanzibar. Wale ambao wanapinga Mapinduzi sasa ni mikia au vitukuu vya wale watawala waliotawala Zanzibar. Najua inawauma sana na itawauma sana, lakini tunaendelea kusema Mapinduzi daima. (Makofi)
Mheshimwa Naibu Spika, nirejee katika hoja iliyopo mbele yetu ya Katiba na Sheria na kwanza nianze kwa ku-declare interest kwamba mwaka 2014 Shirika la Kazi Duniani liliipa fursa Tanzania kuwa Kiongozi wa Vyama vya Waajiri Afrika na huyo Mtanzania ni mimi Mbunge mwenzenu. Vilevile mimi ni Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri hapa Tanzania na mwishoni Serikali ya Jamhuri ya Muungano inafanya kazi vizuri katika kujenga barabara na kujenga majumba mazuri kama hili tulilomo ndani kwa kutumia wakandarasi. Naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mkandarasi daraja la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba nirejee kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais alipohutubia humu ndani, kwamba kulikuwa na sheria anazozifahamu yeye na wanasheria wote wanazifahamu ni mbaya kwa Watanzania na angependa sheria zifanyiwe marekebisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na Sheria ya Manunuzi ya Umma. Sheria hii ina kasoro haitoi upendeleo kwa wazawa wale wanunuzi wanapofanya manunuzi kwa mali na kazi inayopatikana pia kwa Watanzania. Ninashauri Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie lini sheria hii italetwa hapa kwa marekebisho ili iweze kutoa fursa kwa Watanzania. Vilevile inatoa uhuru mkubwa kwa wanunuzi kuchagua mzabuni wanayemtaka na hiyo inasababisha mirejesho ya rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ina mapungufu pia na ningependa Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria anapokuja kuleta majumuisho yake hapa atuambie lini Serikali italeta sheria hiyo hapa kurekebisha mambo yafuatayo; moja ni likizo ya uzazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la likizo ya uzazi limekuwa kero kubwa kwa waajiri. Waajiri wanapata taabu sana kuwahudumia akina mama wanaorudi baada ya kujifungua, kuna watu wanaenda kunyonyesha kwa muda wa masaa mawili, kwa mwaka mmoja, miaka mitatu mpaka miaka mitano, sheria haisemi mpaka wa muda wa kunyonyesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile sheria hii inaleta machungu makubwa wakati wa kuachana na wafanyakazi wabaya, wafanyakazi wakikaribia kutimiza muda wa kustaafu wanafanya makosa makusudi, aidha wanaiba na ukiwapeleka mahakamani kesi ikianzishwa mahakamani mwajiri hawezi kumfukuza huyu mfanyakazi na kesi itaendelea na kama alikuwa anapata marupurupu ya nyumba, gari na wafanyakazi nyumbani ataendelea kulipwa na mnavyojua sheria humu ndani na mahakama inachukua muda mrefu, mwajiri ataendelea kumlipa mfanyakazi huyu hata kama kesi itachukua miaka kumi. Tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria utakapokuja ujaribu kutusaidia suala hili pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia lipo suala lingine ambalo ni sekta ya ulinzi binafsi, sekta hii haina sheria huu mwaka wa 36 tangu ianzishe hapa na matokeo yake sekta hii inajiendesha hovyo hovyo tu, na kuleta matatizo kwa watu ambao wanaendesha biashara hii. Sheria hii ikitungwa italeta udhibiti wa sekta ya ulinzi binafsi na kuwafanya watu hawa waweze kufanya kazi kama ambavyo Serikali itataka na kwa manufaa ya Watanzania. Watu wengi wameumizwa na makampuni ya ulinzi binafsi lakini hakuna sehemu ya kuyashitaki, napendekeza atakapokuja Mheshimiwa Waziri aje na majibu kwa nini asilete Bungeni humu Muswada wa kuanzisha sekta ya ulinzi binafsi, Sheria ya Ulinzi Binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, anisaidie pia kule kwetu Upuge iko Mahakama ya Msingi ambayo ni nzuri ina majengo yote, mahakama yenyewe lakini na majengo ya kukaa wafanyakazi imetelekezwa huu mwaka wa 12, majengo yale sasa wanakaa panya, wanakaa wanyama hovyo. Ningependa pia anieleze itakuwaje kuhusu majengo yale yaliyopo kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapo na naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Miaka Mitano ya nchi yetu. Na nitajikita katika maeneo matatu, maji, kilimo, uvuvi na la nne elimu kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji tumeiona kwenye taarifa hapa kwenye Mpango mzima kwamba imekamilika mingi lakini mingi bado haijakamilika. Lipo tatizo kubwa, miradi mikubwa imefanywa lakini baadaye inaharibika, hali hii ni kwasababu kubwa moja tu, mradi kwa mfano wa Ziwa Victoria umegharibu karibu shilingi bilioni 617 halafu baadaye umekabidhiwa kwa CBOs wa uendeshe. Hauna fundi, hauna mtaalam yeyote na miradi mingine kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na Chuo cha Ufundi wa Maji pale Dar es Salaam, lakini bahati mbaya chuo kile kimetelekezwa na ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Serikali na Wizara ya Maji, Chuo kile kifufuliwe ili kifanye kazi iliyokusudiwa. Kutengeneza mitambo ya maji, tumeshaacha mambo ya visima sana lakini miradi mikubwa ya maji haiwezi kukabidhiwa kwa watu ambao hawajui ufundi wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani tukajenga shule, tukawakabidhi watu ambao sio walimu, haiwezekani tukajenga zahanati tusiwakabidhi madaktari n.k. Hata barabara tunajenga tunawakabidhi wahandisi kuitengeneza. Miradi mikubwa ya maji iliyokamilika mingi yake haifanyi kazi kwasababu haina wataalam wakuendesha mitambo ile ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kumekuwa na matatizo makubwa sana, tunasema maji yako vijijini asilimia 85 lakini sijui wanapima pimaje kwasababu kuna sehemu nyingine maji hakuna kabisa, hakuna, wanasema asilimia 85 au 75. Nafikiri upimaji wa upatikanaji wa maji wa vijijini na mijini pia uangaliwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la kilimo ambalo nilisema nitaligusia. Tanzania nzima tunalima kilimo cha kudra ya Mwenyezi Mungu, yaani mvua inyeshe na isiponyesha hatupati; ukame ukija hatupati. tuachane na suaLa hilo la kizamani. Duniani kilimo kikubwa kinachokusudiwa kuleta tija ni kilimo cha umwagiliaji. Pale kwetu Tabora kuna mbuga kubwa na maji mengi, mvua ikinyesha tunakazana kujenga madaraja maji yapite. Hatuyazuii yale maji yakawa mabwawa ya kumwagilia, tumekazana kufungua madaraja makubwa maji yapite, yaende wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hapa Dar es Salaam, tunafungua daraja lile la Magomeni pale maji yapite yaende baharini. Maji yale yangeweza kutumika kwa umwagiliaji mkubwa sana. Kwa hiyo, kilimo hiki cha kudra ya Mwenyezi Mungu hakiwezi kutuvusha. Tunataka kilimo kile ambacho kitaleta tija kwa kupima. Tuna maji haya, ekari hizi tutazalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara ya Kilimo sasa ijikite katika umwagiliaji. Mbuga kubwa kubwa zilizopo hapa zimejaa maji, baadaye maji yanakauka na jua, yanapotea wakati tungeweza kuzalishia chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uvuvi. Nchi yetu imezungukwa na mabwawa, maziwa na bahari, lakini hatupati chochote kikubwa kinachoweza kuingizwa kwenye uchumi wa nchi kutokana na samaki. Pia, ufugaji wa Samaki; nimetembea, nimeangalia huko na huko, tunajaribu hapa na pale, lakini pia hata wavuvi wenyewe wanaotakiwa kuvua samaki wanatungiwa sheria ngumu sana, wavue samaki usiku tu, wasivue samaki mchana, wavue samaki kwenye maji machache yenye mita fulani mengi na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia liko tatizo la kuwekeza katika uvuvi wa samaki. Tulikuwa na meli na Shirika letu la TAFICO, likauzwa na bahati mbaya sana likauzwa kwa watu ambao hawakuwa na tija na nchi yetu hii na hilo Shirika likafa. Wakati linakufa lilikuwa linaingiza mabilioni. Sasa ndilo kiungo peke yake; katika bajeti hii nimeona kwamba kuna meli zinanunuliwa kwa ajili ya kufufua uvuvi. Meli tano zitakuwa Tanzania Bara na nne zitakwenda Tanzania Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, meli hizi kiungo chake kiwe Shirika la TAFICO ambalo lilikuwa na wataalam wazuri, lilikuwa na taaluma na mitambo mizuri, yaani majengo yake. Majengo yameshaoza na kadhalika. Naomba sana Serikali ionyeshe umuhimu wa uvuvi ili tupate hela kutokana na uvuvi unaoitwa uchumi wa bluu. La sivyo, tunakuwa tunasema, wenzetu wanafaidika. Meli kubwa kubwa zinavua tu na kule, zinaondoka nao. Sisi tumekalia; tutauza hili, tutauza hili. Naomba sana ndugu zangu, Waziri wa Uvuvi na Mifugo ajitahidi sana kuleta tija katika uvuvi ili Serikali ipate mapato ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu. Waziri wa Elimu naona atanichoka maana nimekuwa nasema. Elimu yetu iendane na Sera yetu ya Viwanda na Biashara. Tunataka kukuza viwanda; viwanda haviwezi kuendelea bila kuwa na mafundi. Mtu ananunua mashine mpya analeta hapa nchini, halafu baadaye zinakufa, hakuna mafundi. Zamani tulikuwa tukileta mafundi kutoka nje. Sasa kila mtu anashangaa, shule zote hizi, vyuo vyote hivi, kimetokea nini? Limetokea tatizo dogo tu, tumejenga gap kati ya Wahandisi ambao ni white colors na wale walioko chini ma-artisan. Wanaofanya kazi ni hawa FTC technicians. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu iandae upya sera itakayowarudisha Mafundi Sanifu au Fundi Sadifu ili waunganishwe na mafundi Artisan au Fundi Mchundo na Wahandisi. Sasa hivi nchi hii inazalisha Wahandisi wengi ambao sio Watendaji kazi, ni wafikiriaji, wanataaluma kuliko watendaji kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niko kwenye sekta binafsi na ninaajiri mafundi. Ukichukua mafundi kutoka Chuo Kikuu na Vyuo vingine, wako juu, lazima umpe na Idara maana ni Mkuu wa Idara. Watu gani watafanya kazi viwandani huku chini? Utamtuma nani? Ukimtuma mtu wa chini kabisa, vitu havielewi. FTC hapa hawapo. Chuo cha Ufundi (Technical College) kilikuwa ni branch ya TFC. Rudisheni hiyo ndiyo itatupeleka kwenye viwanda. La sivyo, viwanda vitazorota vile vile. (Makofi)

(Hapa kengele ililiakuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, najua kengele ya kwanza hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo haya nayasema yananisumbua sana. Sisi huko, waajiri tunapata taabu kuajiri watoto wanaotoka shuleni hapa Tanzania. Unamweka wapi? Matokeo yake tumekuwa tunafungua kampuni tunaleta maombi ya kuajiri skilled people kutoka nje. Wenzetu kule nje wameendeleza polytechnic ambayo inasuka watoto wote kuanzia engineer, FTC na artisans. Sasa hili linatupa taabu sana. Nawaombeni sana, niseme namna gani sijui mnielewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri wa Elimu nifikirie. Usifikirie ulikotoka wewe, form one, form five, form six, chuo kikuu. Hiyo ni linIe moja tu. Kuna line nyingine inaanzia Technical School, Technical Secondary School, Technical College, ina-produce engineers, watendaji kazi. Mwifikirie hiyo ambayo ilifutwa, irudishwe tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala lingine muhimu sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia, juzi ameligusa, anasema Kiswahili tunafundisha kama lugha. Mimi nilimwelewa sana. Lugha ya kufundishia iwe Kiswahili, kwa sababu watoto tunafundisha darasa la kwanza mpaka la saba, Kiswahili; halafu tunabadilisha kinakuwa Kiingereza, lakini kuna kitengo fulani cha Walimu wanafundishwa Kiswahili Chuoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mchanganyiko wa kufundisha watoto wetu haueleweki. Wanafika vyuoni kule wanaanza kujifunza lugha kwanza Kiingereza ndipo waanze kujifunza masomo. Tunawakata elimu mara mbili; kujifunza lugha na kujifunza taaluma. Tunapoteza muda nusu nusu, kama wamekaa miaka mitano au minne shuleni, walikuwa miaka miwili wanajifunza lugha. Wote duniani hakuna mtu aliyeendelea kwa kutumia lugha ya mwenzake. Lugha ya mama ndiyo inayomfanya mtoto aelewe. Vinginevyo watoto hawaelewi shule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshatoa mifano mingi sana hapa kwamba, elimu na lugha ni vitu viwili tofauti. Tunasema, mtoto anaongea Kiingereza kama maji, kasoma sana yule! Hajui hata mbili kuongeza mbili, ila anaongea Kiingereza kama maji. Ni tofauti na mtoto ambaye hajui chochote katika lugha; anajua kujumlisha hesabu, anajua maarifa. Tutofautishe kati ya maarifa na lugha. Bado naahidi na bado nina nia ya kuleta hoja yangu binafsi Bungeni humu ya kutaka Kiswahili iwe lugha ya kufundishia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, ni lini Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi italeta Bungeni Sheria ya Sekta Binafsi ya Ulinzi? Miaka minne mimi nilileta Bungeni Muswada wa Sheria hii na Serikali iliuchukua Muswada ule kwa ahadi kuwa kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wangeleta Bungeni muswada ulioboreshwa wa sekta binafsi ya ulinzi. Leo ni mwaka wa tano na Serikali haijaleta muswada huo.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali itoe tamko lini muswada wa The Private Security Industry Bill Bungeni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mhehimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa fursa ya mimi kuchangia Wizara hii muhimu sana ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na data za Wilaya yangu ya Uyui kwamba kuna kata 30, vijiji 156, vitongoji 688. Data za afya ni Hospitali ya Wilaya inatakiwa iwepo moja hakuna, vituo vya afya vinatakiwa 30 kipo kimoja na zahanati mbovu mbovu zipo 45. Eneo hili lina ukubwa wa kilometa za mraba 11,804 na wakazi 404,900. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti kabla ya yote, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Afya amenisaidia sana kunipitishia zahanati moja kuwa kituo cha afya, kwa hiyo, theoretically nina viwili. Pia nitoe pongezi kwa kijiji kimoja kinaitwa Chambola ambacho kimepigana na kuondoa kabisa vifo vya akina mama, kwa muda wa miaka kumi sasa hakuna mama hata mmoja aliyekufa akijifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kituo cha Afya cha Upuge, kituo hiki kimejengwa kwa mkopo wa hela za ADB. Kituo hiki kina mitambo yote ya kisasa, kuna mitambo ya kutengeneza oxygen inaweza kujaza hospitali zote za Kanda ya Magharibi, kuna seti ya kisasa kabisa ya vitanda viwili wanaweza kufanyiwa operesheni akina mama wawili. Mitambo hii ina miaka miwili tangu ilipokamilika na kufungwa lakini haijafanya kazi hata siku moja. Mheshimiwa Waziri naomba aje na jibu zuri la suala hilo kwa sababu wananchi wote na hata ADB waliotupa hizo hela wakija leo watatushangaa sana. Tulienda kuomba mkopo kwamba ni jambo muhimu sana lakini mpaka sasa mitambo mwaka wa pili haijafanya kazi. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri aje na mambo mazuri kuhusu suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati nyingine, kule kwetu Unyamwezini, kule Uyui hakuna dawa. Zahanati kilometa 50, 100 mtu anakwenda hakuna dawa. Matokeo yake waganga wa kienyeji kina Maji Marefu wangekuja kule wangetengeneza hospitali. Hakuna hospitali kule, kuna majengo mabovu mabovu ya zahanati hakuna dawa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata taabu sana ninaposikia hapa kuna bajeti imeandaliwa ya Wizara ya Afya, nimepitia hii bajeti sioni utashi wa Serikali kunijengea vituo hivi ninavyovidai. Kama Uyui nzima ina kituo kimoja cha afya vinatakiwa 30 ningeona kwenye bajeti hapa Uyui tumeongeza vituo hata viwili, bora kuanza kuliko kukaa pale pale. Mimi ningeshukuru sana kama Mheshimiwa Waziri atakuja na majibu kwamba katika Wilaya ya Uyui hii mpya inakusudiwa kujengewa kituo. Bahati nzuri Naibu Waziri wa Afya anatoka vilevile Tabora na anajua hii hali. Kwa hiyo, ningetegemea kwamba nitapata upendeleo maalum lakini mambo haya yananipa taabu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maradhi kuondolewa ilikuwa ni ajenda ya kwanza tulivyopata uhuru kwa maana ya maadui wale watatu ilikuwa maradhi, umaskini na ujinga. Kule kwetu Jimbo la Uyui Kaskazini na Wilaya nzima ya Uyui sioni kama kweli ipo kisiasa nia ya kuondoa umaskini pale au nia ya kuondoa maradhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ndugu yangu Waziri, kwanza ni mtani wangu namshukuru sana ananisaidia lakini aje na dawa ya H5 yaani aje aseme natibu, hakuna maji H ya kwanza, H ya pili hakuna umeme kwenye kituo changu cha Upuge hicho, H ya tatu hakuna wataalam, atibu na H ya nne hakuna gari la wagonjwa, atibu na H ya tano hakuna vifaa vya tiba katika zahanati nyingine zote. Mimi nitamshukuru sana Mheshimiwa Waziri akija na mambo hayo ambayo nimeyataja hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ajaribu kutatua tatizo la dawa. Kila siku nasikia Medical Store au MSD tunavyoiita wanachoma tani 30, 40 za dawa ambazo zimepitwa na wakati, zime-expire. Dawa hizi wakiona kama bado miaka miwili zigawanywe bure badala ya kuzichoma zitumike kwa sababu kuna watu wanataka dawa leo hawangoji za mwaka kesho. Kama Medical Store wanachoma tani tatu au 10 za dawa, inagharimu kuchoma dawa lakini dawa zimenunuliwa na mahitaji ya dawa katika nchi hayajapungua hata siku moja. Uwepo mpango mzuri Mheshimiwa Waziri wa kuzuia kuchoma dawa badala yake zigaiwe bure maana kama mnazichoma wapeni watu bure hizo dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la Community Health Fund. Huu mfuko ulikuwa kimbilio yaani kule kwetu waliposikia kuna huu mfuko wamepapatikia kweli kweli lakini badala yake mzee mwenye nyumba anafariki amekamata kadi, ameenda hospitali hakuna dawa au kafiwa mama na kadi yake mkononi ya CHF hakuna dawa. Kadi zile watu walifikiri labda watapata dawa, lakini kadi zile hazitumiki na zikitumika hakuna dawa Mheshimiwa Waziri. Hii ni reality tuje tuangalie, unajua leo naongelea serious issues hapa hakuna kipepeo wala kupeperushana nasema ukweli kwamba CHF imekuwa kama mchezo fulani. Nakushukuru sana kwenye hotuba yako hii Mheshimiwa Waziri umesema utaileta iwe sheria na mimi naahidi nitawanunulia kadi kaya 2,000 ili mradi kuwepo na dawa, watu wapate kadi ambazo watapatia dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kata moja inaitwa Igulungu ilijengwa zahanati kwa mchango maalum ikafikia mpaka linta, ikaambiwa zahanati hiyo imejengwa karibu na hifadhi ikatelekezwa, huu mwaka wa 15 jengo lipo vilevile. Mimi wakati napiga kampeni nikasema nitalimalizia wakasema huwezi. Mimi nina uwezo wa kulimalizia jengo hilo lakini kuna stop order kwamba lipo karibu na Hifadhi ya Wanyama sasa nini bora wanyama au watu? Naomba Serikali itoe mwongozo kuhusu zahanati hii iliyojengwa karibu na wanyama. Watu hawatakwenda kwenye wanyama, kwanza wagonjwa watakimbizaje wanyama, hawawezi kukimbiza wanyama, watakuja kununua dawa au kutibiwa pale kwenye zahanati. Serikali iingilie kati ili tumalizie hiyo hospitali kwani hatutakwenda kukamata wanyama au kuingia kukata misitu, watu wagonjwa hata shoka hawana wanasogeleaje misitu! Hawa watu wana hatari gani, hawana hatari yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda sana kuwa mkweli, naipenda Serikali yangu, nampenda Waziri na Waziri mdogo ni ndugu yangu, mwanangu lakini katika suala hili wamenituma wananchi nije nidai hospitali na zahanati zijengwe. Tumepiga kura kumpa Mheshimiwa Rais kwa ahadi hiyo kwenye Ilani na mimi nimetangaza na mtu mzima kama mimi kuonekana muongo kwa wapiga kura hairuhusiwi. Nimewaambia tutaleta zahanati na kutakuwa na dawa sasa naonekana mimi muongo. Mimi sipendi naomba Mheshimiwa Waziri aje na dawa yangu ile ya H5. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana niachie wengine, naunga mkono hoja hii, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwanza nitoe pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu Waziri, lakini vile vile naipongeza Idara ya Magereza na Idara ya Uhamiaji kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalipongeza Jeshi la Polisi kwa ujumla kwa kulinda amani na kulinda raia na mali zao hasa wakati wa uchaguzi uliopita huku Bara na uchaguzi ule wa marudio wa Zanzibar baada ya Mheshimiwa Jecha kuufutilia mbali uchaguzi wa awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba niongelee suala la kurasimisha Sekta ya Ulinzi binafsi. Sekta hii ya Ulinzi inafanya kazi nzuri sana sambamba na Jeshi la Polisi. Wako Askari wengi sana, lakini naiomba Serikali ilete mchakato wa kuanzisha Sheria ya Ulinzi Binafsi (Private Security Industry Act) pamoja na Sheria ya Kuanzisha Mamlaka ya Sekta ya Ulinzi Binafsi (Private Security Industry Authority)
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni haya yalianzishwa mwaka 1980 yakiwa mawili tu, lakini makampuni haya yamekua na kuwa makampuni 850 yakiajiri watu zaidi ya milioni moja na nusu kama Askari; lakini yanafanya huduma zifuatazo: ulinzi wa watu (Man Guarding) wanafunga mitambo kama hiyo tunayoiona hapo nje tunapoingilia, vilevile wanafanya upelelezi binafsi na wanafanya kazi ya ushauri (Security Consultancy).
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu makazi yao yanaonekana, iko haja ya kuwatungia sheria. Sasa hivi hakuna sheria yoyote ya Sekta ya Ulinzi Binafsi na kwa bahati mbaya zaidi hata GN ya kuonyesha hii Sekta haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kutaja matukio ambayo yametokea kwa sababu hakukuwa na sheria. Liko tukio la Temeke pale NMB, ambapo walinzi binafsi waliuawa na majambazi na pia Polisi wakauawa. Sekta ya Ulinzi Binafsi ilipata tabu kujiamini kwa sababu Polisi walisimamia marehemu, yule wa Polisi na kumhudumia na kusahau yule Polisi au Askari wa Ulinzi Binafsi, jambo ambalo lilileta kidogo mkanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mnakumbuka kesi ya Kasusura, ambapo walinzi walitumwa kwenda kuchukuwa fedha Dar es Salaam, Airport wakaondoka na hizo fedha. Kulikuwa na kesi ya NMB wakati walinzi walitumwa kugawa mishahara, wakaondoka wakawavua nguo wakaacha na masanduku wakachukuwa fedha zao. Kwa hiyo, pangekuwa na sheria wangekamatwa wenye kampuni, siyo wale walinzi walioshitakiwa kwa sababu ya jinai!
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko kesi ya Shule ya Upili ya Tabora Girls, ambapo walinzi waliokuwa wanalinda lindo hilo mchana, usiku wakarudi wakaja wakaiba na bahati mbaya mlinzi mmoja akapigwa na kuuawa pale. Pangekuwa na sheria, mambo haya yasingetokea. Pia walinzi wanashtakiwa wanapoua, wanapopiga majambazi, lakini Polisi wakiua majambazi wanapongezwa. Hawa nao wanafanya kazi ile ile, kwa hiyo, kungekuwa na sheria, wangetambuliwa hao kwamba walikuwa nao wanapigana wakati wanalinda mali za raia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala lingine baya; makampuni haya yalianzishwa mwaka 1980 kwa kupewa vibali, lakini bahati mbaya vibali vile sasa vinakaribia miaka 36 na waliopewa vibali hivyo wameshafariki, wamekufa, hawapo. Watu walioyarithi makampuni yale hawana taaluma kabisa ya Sekta ya Ulinzi Binafsi, lakini bado wanatumia vibali vile kuendesha Sekta ya Ulinzi Binafsi na mbaya zaidi, wana silaha. Kuna kampuni za silaha, mpaka 50, bunduki mpaka 100, mpaka 200 na hawa hawana taaluma yoyote ya ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kuongelea kwamba kuna dhana tu kwamba inawezekana ziko sheria ambazo zinatumika kulinda au kuendesha Sekta ya Ulinzi Binafsi. Sheria hizi hazipo na imethibishwa kwamba sheria zote ambazo zipo hapa nchini hazikutungwa wala hazikuandaliwa kwa ajili ya kuendesha Sekta ya Ulinzi Binafsi, kwa sababu Sekta hii imeanza mwaka 1980 na Sheria nyingi zimetungwa kabla ya hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizitaje Sheria hizo: Criminal Procedure Act ya Mwaka 1985; Penal Code Cap 16; Law of Contract Ordinance; The Evidence Act ya 1967; Civil Procedure Code ya Mwaka 1966 na; Police Force Ordinance Cap 322.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zote hizi zinaanza kutumika baada ya sheria inayofikiriwa ipo, kufeli, yaani Sekta ya Ulinzi wanalinda raia na mali zao, likitokea tukio, mali ikapotea au maisha yakapotea ndipo sheria hizi zinakuja kuchukua nafasi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza, kwa kuwa makampuni ya ulinzi binafsi yanafanya kazi nzuri sana na kwa upande mwingine yametoa ajira zaidi ya milioni moja na nusu, lakini vilevile kila mahali penye uwekezaji kuna Sekta ya Ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndani mkishafunga Bunge kuna kampuni za ulinzi zinalinda hapa nje, Wizara zinalindwa, lakini vilevile kila mahali ambako sasa hivi kuna gesi, kuna makampuni ya ulinzi binafsi. Makampuni haya hatuwezi kuyaondoa sasa, lakini tunaweza kuyatungia sheria tuweze kuyadhibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho yake, aje na mpango au mchakato wa kuanzisha Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi. Sekta hii ya Kampuni binafsi na kampuni za ulinzi, tunaweza kuitungia sheria na kuiwekea mamlaka ya kuziongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sielewi tatizo ni nini, lakini miaka 25 ambayo nimefanya katika Sekta hii sikuona tatizo. Liko tatizo dogo tu kwamba, baadhi ya Polisi wana makampuni ya ulinzi na hiyo imekuwa inaleta hali ya migongano ya maslahi na wanashindwa kuishauri Serikali kwa sababu na wao ni wadau wa Sekta ya Ulinzi Binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wengine wa Polisi wanaendesha kampuni za ulinzi na Ma-IGP karibu wote waliopita wana kampuni za ulinzi. Pia wana kampuni za ulinzi, yaani Polisi wengine wapo kazini na mchana ni Maafisa wa Polisi lakini jioni wana kampuni za ulinzi binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wamekuwa kikwazo kutunga sheria na kuanzishwa mamlaka, kila mara wanajitetea kuwa eti Ibara 147 ya Katiba, ibara ya (1) inazuia kutungwa kwa Sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunatunga Katiba inayopendekezwa, tulitafsiriwa nini maana ya majeshi yanayoelezwa katika Ibara ile ya 147 kwamba, majeshi haya maana yake ni majeshi ya JWTZ, Majeshi ya Anga, Majeshi ya Ardhi na Majeshi ya Maji. Siyo idara ndogo ndogo hizi za Sekta ya Ulinzi Binafsi na ndiyo maana Sekta hii imeendelea kuwepo kwa muda wa miaka 36 na hakuna mgongano kati ya yenyewe na Jeshi la Wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni la maslahi binafsi ya viongozi wa Jeshi la Polisi wenye Kampuni za ulinzi; tuseme sasa basi, miaka 36 inatosha kuendesha nchi na Sekta hii bila Sheria, yaani Private Security Industry Authority pamoja na mamlaka ya kuendesha sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niachie wenzangu waongee, naunga mkono hoja hii moja kwa moja, lakini pia naomba kurasimishwa kwa Sekta ya Ulinzi Binafsi. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nilishakupongeza sana, nilishasema sana kuhusu sifa zako, leo sirudii, lakini pia kabla ya kuendelea niwasaidie Waheshimiwa Wabunge wanaom-judge Mheshimiwa Mlinga haraka haraka. Wakati wa kipindi cha vitendawili, Mwalimu aliwauliza wanafunzi, haya vitendawili; mmoja akasema mimi. Akamwambia, Mariam, sema. Akasema, nivue nguo nikupe utamu. Mwalimu akaja juu sana, kaa chini wewe, tabia yako mbaya, lakini basi haya toa jibu, akasema ndizi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napata tabu watu ambao hawamwelewi Mheshimiwa Mlinga. Naomba wamwelewe Mheshimiwa Mlinga, dogo yule kama alivyo Mheshimiwa Mlinga ana mambo mengi ya kusema, lakini tumwelewe. Mwalimu yule alijielekeza kubaya, aliposema mwanafunzi nivue nguo nikupe utamu, akamtukana, lakini baadaye akasema toa jibu akasema ndizi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo sasa nije kwenye mjadala huu wa hoja ambayo iko mezani kwetu. Kwanza nifafanue mambo mawili, matatu ambayo wananchi na pia Wabunge hawa wanataka kujua, nayo ni mimi kwenda Geneva mwaka huu nikipeleka kijiti cha Uongozi wa Bara la Afrika, Urais; na kama mnavyojua, Tanzania ilikuwa Rais wa Waajiri Afrika kwa muda wa miaka miwili na mwaka huu tulikuwa tumemaliza, lakini tulipofika kule Geneva, wenzetu ambao walitakiwa kupokea kijiti hicho DRC Congo wakasema hawakuwa tayari kwa hiyo, Mkutano Mkuu wa Waajiri Afrika ulimteua tena Mtanzania wa nchi ya Tanzania. Mtanzania huyo ni Mbunge mwenzenu, aendelee kuwa Rais wa Waajiri Bara la Afrika. Nawashukuru sana na Mtanzania huyo ni Almasi Maige, Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye bajeti ambayo tunaiongelea leo. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wamesema mambo mengi katika bajeti yao hii waliyoipendekeza katika mwaka huu wa 2016/2017. Nami nawapongeza kwenye maeneo ambayo yananihusu sana; maeneo ya Pay As You Earn, kupunguzwa kutoka ile 11% mpaka single digit ya 9%. Pia, niwashukuru kwa kupunguza SDL kutoka 5% mpaka 4.5%. Nafikiri Serikali ingeenda mbele zaidi, ingetupa 1% na mwelekeo wa kuteremka uendelee kwa kupanua wigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliwaambia yako makampuni mengi hayalipi kodi na biashara ambazo siyo rasmi zingelipa kodi, mngepunguza asilimia hizi za kutuwezesha sisi waajiri na hasa wawekezaji waweze kuwa na mazingira safi, mazingira bora ya kuanzisha biashara hapa nchini kwa kupunguza SDL. Bado SDL hii ya 4.5% ni kubwa kuliko zote duniani, inayofuatia ni 1.2%. Sasa katika ushindani wa kibiashara Payroll ni moja ya cost za mwajiri anapopiga hesabu zake na anapolipa kodi. Kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa 0.5 waliyotupa, lakini tulitegemea wangetupa at least 1% na wakusanye kodi kutoka katika maeneo mengine kufidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, niongelee sasa mambo ambayo ni mtambuka. Bajeti hii inaongelea kununua ndege tatu za ATCL; Shirika la Ndege Tanzania. Mimi nasafiri sana, nimesafiri na ATC kabla haijafa mpaka nikaacha kwa sababu mimi ni mzalendo na baadaye nikapanda ndege hizi za mashirika mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania haiko tayari kuendesha Shirika la Ndege yenyewe. Ningefurahi sana kama wangesema sisi tununue ndege tatu tutafute na mbia mwingine naye anunue ndege tatu au hata ndege tano, tufanye ubia, lakini anayekuja awe na taaluma na uwezo wa kuendesha biashara ya abiria wa ndege au mashirika ya ndege. Sisi wenyewe hizi ndege, wanasena Wanyamwezi “zitahomba,” zitalala pia! Hatuwezi kuendesha shirika la ndege sisi wenyewe. Tiketi nyingi watu walikuwa wame-book wakati ule shirika la ndege, wameandika majina yao, watu wamejua ndege imejaa, inaenda na watu nusu. Wameyafuta wapi hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndege yetu imekwenda ikapasuka matairi kule Zimbabwe haikuridi tena, matairi ya spare hakuna. Mafuta tumekopa, madeni mpaka leo hatujalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko haja ya ku-call spade a spade! Koleo, koleo! Ninavyoamini, Shirika la Ndege la Tanzania haiwezekani tukaendesha Watanzania peke yetu. Kwa hiyo, bajeti hii ingekuja na sisi tukanunua ndege tatu, lakini vilevile tuwe na mpango wa kupata wenzetu wa kutuunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nimekuwa naliongelea sana ni Sheria ya Manunuzi. Namwamini sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango kwamba kabla ya kufunga Mkutano huu wa Tatu wa Bunge la 11, Sheria ya Manunuzi marekebisho yake yataletwa humu Bungeni, sina matatizo na hayo. Ni muhimu sana; asilimia kubwa ya bajeti hii ni manunuzi. Kama Sheria hii ya Manunuzi haikurekebishwa, tutapoteza hela nyingi hizi, badala ya kufanikisha, tutafeli kama ilivyokuwa miaka iliyopita. Nina imani Wabunge wengi humu ndani wanajua kwamba hii Sheria ya Manunuzi ni tatizo kubwa sana. Sijui kwa nini hailetwi humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwamini sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, atakuja sasa na utekelezaji wake wa yale mambo niliyoyalalamikia kuhusu Benki Kuu kwa sababu ushahidi nimeshampelekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni suala la maji. Kule kwangu Jimbo la Tabora Kaskazini, Uyui, hakuna maji chini. Sijui Mungu aliumba hivyo kuwa maji yapite tu mvua zikinyesha yanaenda kujaza Wembele na maeneo mengine ambayo yako chini; lakini Jimbo langu lote halina maji chini. Kwa hiyo, mpango wa kuchimba visima kuwapatia maji wananchi wa Tabora Kaskazini imeshindikana. Kwa hiyo, kipekee mradi ambao unawezekana ni wa kuchimba malambo ili yajae maji na wananchi watumie. Naomba katika bajeti hii, Mheshimiwa Waziri wa Fedha aangalie kutekeleza mawazo aliyoyatoa humu Bungeni kwamba Serikali itachimba malambo kama mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia liko suala la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Fund). Mfuko huu malengo yake ni mazuri sana, lakini Mfuko huu malengo yake hayo yanagongana na mafao ya mifuko mingine. Kwa mfano, Mfuko ule wa NSSF unao pia fao la bima; lakini pia wako waajiri ambao wamewawekea bima wafanyakazi wao, nzuri sana ya Kimataifa. Hawa wafanyakazi watapoteza mafao mazuri haya ambayo waajiri wao wa makampuni ya kigeni na kadhalika wamewawekea. Kwa hiyo, tungependa Mfuko huu ujaribu kuongea na waajiri hawa ambao wana bima zao au ulinganishe mafao ya Mifuko mingine yasigongane ili kuleta harmonization ya Mifuko yote hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Mfuko huu una mafao mazuri sana, lakini hauzidi baadhi ya mafao ambayo waajiri tumewawekea wafanyakazi wetu. Kwa kutekeleza mafao ya Mfuko huu, wafanyakazi watapoteza zaidi kuliko kupata. Hatuombi mtu apate ajali, lakini tumeweka mambo mazuri sana kwa wafanyakazi wetu, hasa makampuni haya ambayo yamewawekea bima.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa fursa ya kuchangia Wizara yetu hii ya Fedha. Kabla ya kuchangia mimi niseme maneno machache sana, jambo usilolijua ni kama usiku wa giza. Watu ambao wanakukimbia wewe, wanatoka nje wanakuacha wewe hawakujui. Wewe unajua mimi nakujua sana kabla hujawa Naibu Spika, utendaji wako ulikotoka, chuoni, maisha yako yote, mwadilifu, mpole, msikivu, mtoto wa maskini, umesoma shule za kawaida, unajua mila za Kitanzania, wewe ni mzalendo, hawakuwa na sababu ya kutoka, wametoka hawa ni kama usiku wa giza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwe na moyo, wale wote wanaokufahamu kule nje, wanayokwenda kuyasema watawazomea. Sisi tuliobaki humu ndani tunakufahamu fanya kazi, tuamini, tuko nyuma yako. Mimi nakupongeza sana, nampongeza pia Mheshimiwa Rais aliyekuteua kuwa Mbunge na baadaye ukagombea nafasi ya Naibu Spika. Nafasi ya Naibu Spika hajakupa Mheshimiwa Rais tumekupa sisi Wabunge kwa kukupigia kura. (Makofi)
Mhehimiwa Naibu Spika, kila jambo lina mwanzo wake, mwanzo wa wewe kuwa Naibu Spika ni sisi Wabunge humu ndani, walielewe hilo. Tunataka ufanye kazi na tunakuunga mkono sisi. Wote tuliobakia na walioko nje, raia, wananchi wa Tanzania wanakupenda, wanakuamini, fanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo sasa nichangie hoja iliyopo mezani na nitajikita katika mambo matatu.
La kwanza ningependa kuongelea ushiriki wa sekta binafsi hapa nchini na naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mdau wa sekta binafsi. Serikali hii inaongelea kwamba uchumi huu injini yake ni sekta binafsi lakini Serikali hii haioneshi utatu ule unaotakiwa kwamba Serikali isaidie kuikuza kwanza na kuimarisha sekta binafsi ili yenyewe iwe injini kweli ya uchumi. Yapo mambo mengi, Serikali hii inaitoza kodi nyingi sana sekta binafsi, lakini ziko tozo ambazo hazina lazima kabisa. SDL tumeilalamikia kwa muda wa miaka mitano sasa kwamba ni kubwa kuliko kokote duniani. Asilimia 5 ya tozo ya SDL haina tija kwa waajiri ambao ndiyo waanzishaji wa ajira ambazo zitakuza uchumi. SDL wanasema inaenda kwenye VETA, kuna makampuni mengi hayana interest kabisa na VETA, hayatumii mafunzo ya VETA. Sekta ya ulinzi binafsi kwa mfano, hakuna kwata kule kwenye kozi ya VETA, u-nurse wanalipa hakuna kwata kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile yapo mambo mengine ambayo tunaona kwamba yanatubana sisi sekta binafsi. Ukitaka kuanzisha shughuli hapa Tanzania, utaenda nenda rudi, yanayosemwa kwamba BRELA wamepunguza ukiritimba si kweli. Wewe leo andika kwamba unataka kujua status ya kampuni yako, miezi sita na ukawaone watu mikononi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee Sheria ya Kazi. Najua sana watu wengi tukiongelea Sheria ya Kazi wanaona kama ni jambo la Wizara ya Sheria lakini ndani ya Sheria ya Kazi yako mambo ambayo yanaleta chokochoko ya watu kudharau kuajiriwa. Watu wanafanya mpango wa kutokwenda kazini na huwezi kuwafukuza kazi kwa sababu sheria inakubana na ukimfukuza utaanza mambo mengi na Serikali. Tumeomba sisi waajiri tuweze kuruhusiwa kubadilisha sheria ile lakini lazima tupite kwenye ukiritimba wa Wizara ya Kazi na kule kuna Baraza la LESCO halikutani, kwa hiyo sekta binafsi inadumaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la kutokusikilizwa. Serikali inaamua mambo yake bila kufikiria utatu uliopo na ushoroba uliopo. Juzi hapa tumeshuhudia ndani ya Bunge lako sekta binafsi ya elimu imejieleza mpaka watu karibu walie humu ndani, Serikali imekaa na kujaribu kupanga ada elekezi bila kuwahusisha wahusika. Tunashukuru sana Serikali hii sikivu suala hilo limesitishwa na nafikiri watakapoanza kulifikiria tena wadau wote wa sekta ya elimu watakutana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka niliongelee ni Sheria ya sasa ya Manunuzi. Hapa pia naomba ni-declare interest kwa sababu ni Mkandarasi Daraja la Kwanza. Sheria hii ya Manunuzi imeanzisha vitengo vinaitwa PMU katika kila mnunuzi wa umma. Mashirika haya baada ya kuanzishwa vitengo hivi yamekuwa na mpango wa kutengeneza bei wao wenyewe. Kwa hiyo, badala ya kufanya kazi vizuri na sheria hii imekuwa chanzo cha rushwa katika makampuni ya umma yanayonunua manunuzi ya umma, lakini vilevile yametajirisha watu binafsi badala ya Serikali kupata manufaa ambayo yalikusudiwa na sheria hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii imekuwa chanzo cha watu fulani kuingiza makandarasi kutoka nje kwa sababu wanataka kuhongwa dola. Pia wanataka safari za nje makampuni haya yakipewa tender wanataka kwenda kuangalia, wanasema wanafanya due diligence na huko ndiko wanapewa hela chungu mzima na imekuwa ndiyo kanuni. Kwa bahati mbaya sana nina mfano mzuri sana wa Shirika la Umma kubwa kabisa na naomba nilitaje kwa sababu nina ushahidi nalo. Benki Kuu ya Tanzania ndiyo shirika kubwa sana la umma linalovunja Sheria ya Manunuzi hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki hii au taasisi hii ya umma Mkurungenzi wake amefungwa jela miaka mitatu kuthibitisha kwamba kuna uvunjifu mkubwa wa Sheria ya Manunizi ya Umma. Pia hapa mkononi nina hukumu ya PPRA ambako Benki Kuu wameshindwa kesi miaka kumi iliyopita na bado wanataka kumpa yule yule aliyefutiwa tender na PPRA na wamefanya hivyo na wamempa. Mbaya zaidi wako wafanyakazi wa Benki Kuu wamefungua kampuni zao wenyewe na wanachukua zabuni za mwajiri wao Benki Kuu. Nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aniambie wafanyakazi hawa ambao wamefungua makampuni wanachukua zabuni za Benki Kuu na wao ni waajiriwa wa Benki Kuu amechukua hatua gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo haya kwa watu wasiojua yanaonekana kama ni mzaha mzaha, hela nyingi sana Benki Kuu zinatoka nje ya nchi kwa sababu makandarasi walioletwa pale wanatoka nje ya nchi na ingawa sheria inasema kama hela ya Tanzania zinatumika zote 100%, ifanyike local bidding. Benki Kuu wameweza kutengeneza njama ya kumtafuta mtaalam kutoka nje aka-specify mitambo inayofanya kazi pale kwamba lazima itoke kwenye kampuni moja fulani. Kampuni hii ndiyo ilishtakiwa miaka kumi iliyopita na kufungiwa na tender ikarudiwa lakini sasa huyo ndiye msemaji mkuu wa zabuni tena za usalama wa Benki Kuu. Mimi naomba atakapokuja Mheshimiwa Waziri alieleze suala hili la Benki Kuu na zabuni kupewa wafanyakazi wa Benki Kuu pamoja na watu waliochongwa kwa ajili ya kufanya kazi za siri za Benki Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie na naunga mkono hoja hii asilimia mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda huu nami niweze kuchangia hotuba ya Mawaziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais; Waziri wa Nchi wa TAMISEMI na Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi yake nzuri anayoifanya katika kutekeleza wajibu wake na katika kuendesha nchi yetu ili wananchi tuweze kuwa na amani na tuweze kukuza uchumi wetu. Sisi Wanyamwezi tunapenda sana kupongeza jambo kwa kushangaa na maneno yetu ya kushangaa ni mawili tu, yaani ‘ish!’ na ‘jamani!’
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ametushangaza sana na tunamwona wa ajabu. Kwa mfano, Mheshimiwa Rais kanunua ndege mbili, sisi tukashangaa, ish! Pia, Mheshimiwa Rais amegundua wafanyakazi hewa wengi, tukasema, jamani! Mara tumesikia Mheshimiwa Rais huyu huyu anajenga reli ya standard gauge, tukasema, ish! Kapata wapi hela? Hatujakaa vizuri, Mheshimiwa Rais huyu huyu akasema tunahamia Dodoma, jamani! Wote tuko Dodoma!
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa UKAWA kule wamekosa maneno mazuri ya kumpongeza, lakini na wao pia wanashangaa. Wanamshangaa kwa mazuri anayoyafanya katika kutekeleza majukumu, wanabaki kusema Rais wa ajabu, kama ambavyo sisi tunasema Rais
wa ajabu kwa mambo mazuri anayoyafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko fujo zinazolalamikiwa na dawa hiyo ya kulalamikiwa fujo hizo, mimi niliileta katika Mkutano wetu wa Pili wa Bunge hili la Kumi na Moja. Nilileta kwa Mheshimiwa Spika Muswada wa Sheria wa Sekta ya Ulinzi Binafsi. Sheria ile ingeweza sana kutibu mambo ambayo tunayaona sasa. Vikundi mbalimbali vinavyojitokeza sasa ni kwa sababu hakuna sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alete sheria hiyo haraka ili tuweze kudhibiti vikundi ambavyo vinafanya fujo kwa wananchi, vinapiga na kukaba watu. Serikali na Waziri wa Mambo ya Ndani, kama nilivyosema, ni budi alete sheria hiyo ili tuweze kudhibiti matukio ambayo yanatokea sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nichagie ukurasa wa 65 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, kuhusu TAMISEMI. Katika DCC ya Wilaya ya Uyui pamoja na Halmashauri na Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC) tuliomba jina la Halmashauri ya Uyui libadilishwe kutoka Tabora District Council liwe Uyui District Council. Jambo hili linachanganya wakati wa maagizo ya kiserikali kutoka Serikali
Kuu, lakini pia tumeshuhudia fedha za Wilaya ya Uyui, Halmashauri ya Uyui, zikienda Manispaa ya Tabora. Kwa hiyo, mikutano yote miwili ya Wilaya pamoja na ya mkoa ilileta maombi kwa Waziri anayehusika na TAMISEMI ya kubadilisha jina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba atakapokuja Mheshimiwa Waziri hapa kujadili kufikia mwisho wa majumuisho yake, asiache kueleza kwa nini Halmashauri ya Uyui isiitwe Halmashauri ya Uyui badala ya Halmashauri ya Tabora? Kwa sababu hatuhitaji bajeti ya hela. Ni maombi yetu sisi wananchi wa Uyui na yeye ni kutoa kibali tu. Kwa hiyo, sidhani kama itakuwa tatizo kwa Mheshimiwa Waziri wa
TAMISEMI kutukubalia ombi letu hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nichangie kwenye Kifungu cha 33 kuhusu uboreshaji wa huduma za afya. Halmashauri ya Uyui na Wilaya nzima ya Uyui haina Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, tunategemea kituo kimoja cha afya ambacho hakifanyi kazi vizuri na hakiwezi kufanya upasuaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Naibu Waziri wa Nishati ambaye amenisaidia kupeleka umeme pale; umeme tunao sasa, lakini hatuwezi kufanya upasuaji kwa sababu ya matatizo makubwa. Hicho ndicho kituo pekee cha afya katika Jimbo langu na katika Wilaya nzima ya Uyui. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aje na msaada wa kusaidia kituo kile na hatimaye kusaidia majengo
yanayojengwa na Halmashauri ambayo yamejengwa kwa hela ya ndani ili tuweze kuyamalizia na tupate Kituo cha Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali, hasa Wizara ya TAMISEMI kuanzisha Mfuko au kuanzisha Kitengo cha Barabara, Uwakala wa Barabara Vijijini. Wilaya yangu ni mpya na Jimbo langu ni jipya, hatuna barabara za ndani kabisa. Tuna barabara ambayo ni lazima utoke barabara kubwa uende mjini, huwezi kwenda katika kijiji kingine. Hakuna barabara! Kwa hiyo, tumefurahi sana kusikia kwamba mwezi wa saba Serikali itaanzisha Wakala wa Barabara Vijijini. Tuna imani kwamba wakala huyu atafanya kazi sawasawa na Wakala wa TANROADS ambaye anafanya kazi nzuri. Wakiiga hivyo, basi Jimboni kwangu kutakuwa na barabara za kutosha ili kusafirisha mazao na kuweza
kuwasiliana. Nina imani kwamba wakala huyu atakuwa ndiye kichocheo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niongelee mambo ya utawala bora. Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais kuhusu mambo ya Utawala Bora, watu wengi, Wabunge wengi humu ndani na wananchi kule nje, wanalalamika sana kuhusu mpango mzuri ulioanzishwa wa TASAF. Kwetu umesaidia sana. Tulipoanza mpango huo ulifanya kazi nzuri sana, lakini baadaye mpango umekuja kuwafuta watu waliokuwa wamepewa hela; wanatakiwa wazirudishe kwa madai kwamba wamekosewa kupewa hizo hela, hawamo tena katika sifa za wanaopokea hela.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili limeleta mgongano mkubwa sana. Wengine wameomba Wabunge tuwasaidie, nasi hatuna hizo hela, lakini pia wananchi hawana hizo hela kuzirudisha tena. Kosa lililofanywa na TASAF lisahahihishwe kwa Maafisa wa TASAF na siyo kusahihisha kwa wazee. Wazee wengine wanaotaka kurudisha hela, kwa kweli, ukimwangalia hivi ni maskini na hawana uwezo kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri mhusika mwenye jukumu hilo atakapokuja kufanya majumuisho yake, aeleze tutafanyaje kuondoa matatizo ya wazee kuwaomba hela ambayo tuliwapa sisi wenyewe?
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono na nakushukuru sana kwa kuniruhusu kuchangia katika Wizara hizi mbili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia Wizara hii ya Sheria na Katiba. Kabla ya kuanza kuchangia, naomba ku-declare interest kwamba mimi taaluma yangu ni ya ulinzi na usalama katika sekta binafsi lakini vilevile nina kampuni kubwa ya ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipeleka kwa Katibu wa Bunge Muswada Binafsi kama ilivyo katika Kanuni yetu ya 81(1)(2) na (3), Toleo la 2016. Baada ya kupeleka Muswada wangu binafsi katika Ofisi ya Katibu wa Bunge alinijibu rasmi kwamba Muswada ule ulikuwa ni mzuri na Serikali iliuchukua Muswada huo kwa nia ya kuuleta tena Bungeni baada ya kutimiza kanuni za kuleta Muswada Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni binafsi ya ulinzi yalianza mawili tu mwaka 1980 lakini leo yapo makampuni karibu 850, yameajiri askari walinzi wengi zaidi ya mara tano au mara sita ya Jeshi la Polisi. Makampuni haya yanafanya kazi nzuri sana ya kulinda raia na mali zao lakini hayana miongozo, kanuni, sheria na wala hayana mamlaka binafsi ya kuongoza makampuni haya kama ilivyo kule nje yalikotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifungua milango ya sekta ya ulinzi binafsi hapa nchini na ikafungia nje sheria za kuyaongoza makampuni haya. Suala hili limekuwa ni tatizo kwani makampuni haya yana silaha, yanavaa sare kama za jeshi, yanacheza gwaride, yanafuata kanuni za kijeshi na yameajiri wataalam kutoka nje ya nchi wenye taaluma kubwa ya kijeshi. Hatuwezi kuyazuia tena makampuni haya hapa nchini yasifanye kazi kwa sababu kila kwenye uwekezaji mkubwa makampuni haya yapo na yanafanya kazi nzuri sana, tunachoweza kufanya ni kuyadhibiti makampuni haya binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni haya hayawezi kudhibitiwa bila sheria. Ni lazima Sheria inayoitwa Private Security Industry Act or Bill iletwe Bungeni ipitishwe. Huko yalikotokea makampuni haya kote, wenzetu Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Uingereza, Marekani, Ulaya ziko sheria na mamlaka ya sekta ya ulinzi binafsi. Sheria ile niliyoleta mimi kama Muswada Binafsi ilizingatia kuanzishwa kwa mamlaka ya sekta binafsi ya ulinzi. Nia ile na sababu hiyo haijafutika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, ajaribu kulieleza Bunge lako kama maslahi na madhumuni ya kuwepo sheria sasa yamefutika au mchakato wake umefikia wapi ili tujue tuweze kudhibiti makampuni haya ya ulinzi binafsi yaweze kulipa kodi na vilevile yanaajiri watu kinyume na kanuni. Kule kwenye Mahakama ya Kazi, robo tatu ya kesi zote ni za makampuni ya ulinzi, inakuwa kama ile Mahakama ya Kazi imeandaliwa kwa sababu ya makampuni ya ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile makampuni haya yanatumia sheria ya kiraia, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004. Sheria hii ni ya kiraia na imepigwa marufuku majeshini kote. Hairuhusiwi kutumika Polisi, JWTZ, Magereza wala Immigration. Sheria hii kutumika katika sekta ya ulinzi binafsi inaenda kinyume na inashindwa kuyadhibiti makampuni hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inaruhusu migomo. Hebu tufikirie ikatokea siku makampuni ya ulinzi yamegoma au wafanyakazi wa kampuni za ulinzi wamegoma, wakaacha malindo wazi na wana silaha mikononi, itakuwaje? Naomba Waziri atakapokuja hapa aeleze Bunge lako hili amefika wapi na Sheria hiyo niliyoipendekeza ya Sekta ya Ulinzi Binafsi yaani Private Security Industry Act or Bill pamoja na pendekezo la kuanzishwa Private Security Industry Authority.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo niende kwenye Idara ya Mahakama. Waziri wa Sheria hapa mwanzoni alisema kwamba wangependa kila Kata iwe na Mahakama. Kule kwetu Tabora Kaskazini (Uyui) kuna Mahakama ya Mwanzo ina kila kitu, Mahakama ipo, ina mabenchi, jengo zuri la Mahakama, nyumba nane za wafanyakazi wa Mahakama lakini imetelekezwa, huu ni mwaka wa 10 haifanyi kazi. Watu wameiba milango na madirisha yaliyojengwa kwa thamani kubwa na mpaka sasa sijui sababu ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu nimekuwa Mbunge, wananchi wananiuliza imetokea nini Mahakama ikatelekezwa na kuna kesi nyingi. Juzi juzi kumetokea kesi ya mauaji kule Tabora, Uyui ndiyo inaongoza kwa kesi mbaya za mauaji, wizi na kadhalika lakini Mahakama ya Mwanzo imefungwa. Nimeona katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri anaongelea kujenga Mahakama za Mwanzo katika maeneo mbalimbali, lakini Mahakama ya Mwanzo katika Kata ya Upuge, Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora imesimama na haifanyi kazi na majengo yanabomolewa tu wananchi wanachukua kama shamba la bibi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba atakapokuja Mheshimiwa Waziri kuhitimisha hoja yake ya bajeti, anieleze kimetokea nini mpaka Mahakama ya Mwanzo inayotakiwa sana kutelekezwa. Pia anieleze majengo yale yafanyweje sasa, maana watu wanaingia na kuiba milango kama haina mwenyewe. Mimi ningeshukuru Mahakama ile ingeanzishwa tena kwa sababu kesi za kutosha zipo, lakini kama kuna sababu iliyofanya Mahakama ile ifungwe naomba nielezwe ili nikawaambie wananchi wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuniruhusu kwa heshima kubwa, nakushukuru sana na niwaachie wenzangu wachangie.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi pia naomba nikushukuru sana kuniruhusu nichangie bajeti hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote humu ndani, naomba niwashauri tu kwamba wampe pongezi Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na Mawaziri hawa ambao ni vigogo. Siyo kweli kwamba Mawaziri hawafanyi kazi, lakini Wabunge wote imekuwa tunataka maji hata kama tungepewa ng’ombe tugawane hatoshi, kinachotolewa sasa kinatosha sana. Mimi naomba niwashukuru sana Mawaziri ninyi wawili na hasa mpelekeeni salaam Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa miradi mitatu ambayo iko Jimboni kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, mradi ule wa umwagiliaji katika kata ya Shitage, unaenda vizuri lakini naomba muusimamie vizuri umalizike. Vilevile hivi karibuni tumesaini mkataba wa bomba la maji kutoka Ziwa Victoria kuleta maji Uyui na kupeleka Tabora. Mabilioni ya fedha yamewekwa pale, tungepata wapi kama siyo Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli? Pia tume-comission mradi mkubwa wa maji pale Mabama kwa niaba ya Mkoa mzima wa Tabora uliosaidiwa na Japan, mradi mkubwa vijiji 31 katika kata zangu vinapata maji, tungepata wapi mtu kama Mheshimiwaw Dkt. Magufuli? Aidha, uko mradi nimeuona umeanzishwa kutoka Malagarasi kuleta maji Urambo na Kaliua unapita pia mpaka kata zangu za Ndono pale Ilolangulu. Mradi huu mmeutengea shilingi bilioni mbili, naona Mheshimiwa Mama Sitta hakuwa ameiona hiyo lakini naomba muuanze ili tuweze kuufanikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako matatizo katika Wizara hii ambayo kwa kweli mimi sidhani kama yanatokana na wao wenyewe. Tumeona bajeti haitoshi, tunawashauri wakachukue shilingi 50 za mafuta waziweke kwenye mradi wa Mfuko wa Maji ili akina mama hawa wapumzike. Ni kweli akina baba wanawakosa akina mama asubuhi, hii hairuhusiwi. Nashauri tuimarishe suala hili ili watoto waende shule wameoga na akina mama wateke maji maeneo ya karibu. Wabunge wote tumeomba humu ndani ya Bunge Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kubalini hilo tupate hela za mfuko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mnisikilize vizuri sana Mawaziri, katika Jimbo langu katika kijiji cha Majengo lilijengwa bwawa, wananchi wakafurahi, wakaanza kuvua samaki, wakamwagilia, bwawa likapasuka baada ya miaka miwili; huu ni mwaka wa tano hamjarudi tena kurekebisha bwawa lile. Mheshimiwa Waziri kama husemi vizuri kuhusu bwawa hili na mimi nitatoa shilingi. Bwawa la Majengo katika kata ya Ikongolo mlijenga limefanya kazi vizuri miaka mitatu limepasuka, mwaka wa tano hamjarudi wala hamjasema sababu kuwaambia wananchi kwa nini hamrudi, naomba mrudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu wanakesha wanatafuta maji, nimelipa Serikalini hela nyingi kuwaita Wakala wa Maji na Mabwawa na Wachimba Visima wakapima maji yapo chini, cha kusikitisha, huu ni mwezi wa tano nakutafuta Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, Halmashauri wameleta ripoti maji yapo chini tena ya kutosha kwenye vijiji viwili vile vya Inonelwa pamoja na Ikongolo ambako ndiyo hakuna maji, maji yapo chini mengi. Mimi Mbunge nimelipia hela zangu, nataka mje mchimbe kwa sababu maji yapo. Namuomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri mnipe majibu kwa nini hamji kuchimba maji ambayo nimegharamia kuyatafuta na yapo chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, mmeutaja mradi huu wa Shitage mwaka wa tatu huu eti wamefanya mita 170, mradi hauendi. Wananchi wanategemea kumwagilia mpunga tupate mpunga pale kwa nini hauendi? Naomba mtakapokuja tena mniambie kwa nini mradi huu wa Shitage umekwama?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunagombania muda hapa, mimi naunga mkono hoja na nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya Wizara ya Maji, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. ALMAS A. MAIGE – MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HAKI, MAADILI NA
MADARAKA YA BUNGE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kufanya majumuisho ya taarifa ya utekelezaji wa majukumu na shughuli za Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kipindi cha Januari 2017 mpaka 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi mengi yameongelewa na mimi nilibakiza na kipande kidogo tu katika kumaliza kuhitimisha hii taarifa yangu.

La kwanza, nataka Wabunge wenzangu humu ndani na wananchi waelewe kwamba kimsingi kazi ya Kamati yangu sio kutoa adhabu kwa Waheshimiwa Wabunge na kwa raia yeyote bali ni kuhakikisha kuwa nidhamu, ustahimilivu, heshima, utulivu na uzingatiaji wa kanuni za majadiliano ndani ya Bunge unazingatiwa kwa ukamilifu ili kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake kikatiba kwa manufaa ya wananchi tunaowawakilisha na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo haki na madaraka ya Bunge, Kiti cha Spika, shughuli za Bunge ni lazima vilindwe kwa mujibu wa sheria na kanuni dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoweza kupotosha, kudhalilisha, kuingilia na kushusha hadhi ya mhimili wa Bunge. Lakini pia watu na raia na Waheshimiwa Wabunge mjue kwamba mhimili huu ni moja ya mihimili mitatu ya dola hapa nchini kama inavyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimepokea kwa maandishi michango ya Waheshimiwa Wabunge, naomba niwataje Mheshimiwa Mary Muro, Mheshimiwa Rhoda Kunchela na Mheshimiwa Lucia Mlowe. Lakini pia nimepokea mchango wa Mheshimiwa Mwakasaka na Mheshimiwa Dkt. Ishengoma wote wameongelea maboresho ya kanuni, lakini pia wameomba uwepo usawa katika maamuzi hasa tunaposhauri Bunge. Na mimi nawaambia kwa sababu Kamati hii inafanya kazi chini ya maelekezo ya Mheshimiwa Spika nitafikisha yote niliyoyapokea kwa maandishi kama ambavyo mmetaka.

Waheshimiwa Wabunge wenzangu na jamii kwa ujumla nasema asanteni sana kwa ushirikiano mlionipa mimi na wajumbe wote wa Kamati ya Haki na Madaraka ya Bunge. Ushirikiano huo ulitupa hamasa na nguvu ya utekelezaji hasa jinsi ya kutekeleza majukumu na shughuli za Kamati kwa ufanisi mkubwa. Nasema ahsanteni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wajumbe wa Kamati hii wamepata taabu kwa baadhi ya Wabunge wameacha kutusalimia, tukiwasalimu hawajibu na wengine wanaona kama sisi tunafurahi sana tunapofanya maamuzi. Naomba nikiri kwamba hatuko hapa kwa sababu ya kuwakomoa Wabunge; hapana, hatuko hapa kwa sababu ya kuwakomoa raia hapana, tuko hapa kulinda maslahi ya muhimili wa Bunge kama ambavyo ipo katika Katiba na kama hivi ilivyo katika Kanuni ya Bunge za mwaka za 2016.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa hoja kwa Bunge lako, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja sasa Bunge lako lipitishe taarifa yangu hii ya mwaka ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, asante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo kwa kweli ndiyo msingi wa maisha ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuendelea kuchangia napenda pia nitoe shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Rais na Mawaziri wote wa Wizara hii ya Elimu. Vile vile nijikite kwenye mambo haya manne ambayo nitayaongelea, moja shule za ufundi lakini mambo ya VETA, tozo ya SDL na mimba za utotoni. Naomba nianze na suala hili la mimba za utotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili limekuwa linaomba tuletewe sheria itakayozuia watoto kuolewa wakiwa wadogo. Bunge hili limepitisha sheria kali sana kwamba mtu ambaye atampachika mimba mtoto wa shule, afungwe miaka 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa, watu wanachangia tena Bunge hili linaruhusu watoto kupata mimba wakiwa mashuleni. Hii ni kinyume! Bunge linaomba tulete Sheria ya Kuzuia Watoto Kupata Mimba lakini Bunge hili hili leo linataka tupitishe kanuni au ruhusa watoto wapate mimba shuleni. Tunajikanyaga! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ku-declare interest kwamba mimi ni Muislamu na niko wazi kabisa na nina hakika dini zote zinakataza mambo ya zinaa kabla ya ndoa. Kwa hiyo, ni vigumu sana mimi kwa imani yangu ya dini kuruhusu watoto hawa watiwe mimba halafu warudi shuleni. Ina maana niwaruhusu wapate mimba kabla ya kuolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaunga mkono kama Bunge hili litaruhusu watoto wa shule waolewe, wazae ndipo warudi shuleni. Kinyume chake ni kosa kubwa sana. Pia nimepitia takwimu; wanasema kama huku-research usiseme; tatizo la mimba shuleni mwaka 2015 jumla ya watoto wote wa primary and secondary school 3,937 ndio waoliacha shule kwa sababu ya kupata mimba, lakini watoto walioacha shule kwa makosa mengine ya utoro 139,866. Hili ndiyo tatizo kubwa sana, siyo la mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuruhusu watoto wapate mimba warudi shuleni, itaharibu nidhamu ya shule kabisa. Watoto sasa hivi wanaogopa kupata mimba kwa sababu wanajua watafukuzwa shule, sasa tukiruhusu wapate mimba wakasome, itakuwaje? Serikali imeshaweka muundo wa watoto wanaopata mimba wakarudi nyumbani kama mama watoto, wasome elimu ya watu wazima ambayo inaanzia Shule ya Msingi mpaka Chuo Kikuu, wanakosa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuruhusu watoto walioitwa mama, wanajua mambo yote ya kulea mtoto wakakae darasa la saba tena, haiwezekani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kidini nakataa, lakini Bunge hili limelaumiwa kutunga sheria zinazokanganyana zenyewe; huku tunakataza watoto wasifanyiwe zinaa wakiwa wadogo chini ya miaka 18 na mtu akifanya kosa afungwe miaka 30. Huku tunaruhusu hiyo tena ifanyike kuwa watoto wapate mimba warudi shuleni. Hii sheria itatukanyaga wenyewe, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa maoni yangu ni kwamba watoto hao wanaoacha shule kwa kupata mimba wafukuzwe kabisa. Waliowatia mimba wafungwe miaka 30 na watoto wasirudi shuleni kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni la kwanza. Naomba sasa niongelee mambo ya Elimu ya Ufundi. Mfumo wa elimu unaotolewa sasa hauwezi kulingana na matakwa ya Mheshimiwa Rais ya kujenga nchi ya viwanda na hili naomba lisikilizwe vizuri sana. Mimi ni zao la Elimu ya Ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka iliyopita kulikuwa na Shule ya Ufundi, Moshi; kulikuwa na Shule ya Ufundi, Ifunda. Shule zote zilikuwa zikipeleka wanafunzi waliotoka Form Four kwenda Chuo cha Ufundi (Technical College) na hao walichagua ufundi tangu mwanzo, walikuwa kama Fundi Umeme miaka minne ya Sekondari, inaitwa Trade School, baadaye kama wewe ni Civil Engineer, utaanzia mambo ya engineering kuanzia form one.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michoro wanayochora Chuo Kikuu leo ya technical drawing niliichora nikiwa Form One. Tulikwenda pia Chuo Kikuu cha Ufundi (Technical College) tukachukua miaka mitatu, tukajaliwa watoto wanaoitwa Mafundi Sadifu (Technicians).

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, tumefanya kazi nje, tukarudi tena Chuoni, tukasoma Diploma ya Engineering. Kwa hiyo, tuna miaka 10 katika ufundi uliochagua ukiwa form one. Kama ni electrical, ni miaka minne form one mpaka form four, kama ni Civil, ni miaka minne form one mpaka form four, lakini miaka mitatu ya ufundi inakuwa jumla saba. Ukirudi kuchukua Diploma, una miaka kumi katika ufundi. Tulizalisha mafundi kama mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mifumo miwili ambayo ilikuwa inajulikana waziwazi. Mfumo wa Academicians form one mpaka form four, form five, form six na Chuo Kikuu cha Engineering au cha Udaktari. Ufundi tulianzia Sekondari ya Ufundi, Chuo cha Ufundi, unarudi unapata fundi anaitwa Diploma Engineer, hawa ndio ambao wanaendesha kampuni nyingi mnazoziona leo, ndiyo wako viwandani. Mfumo huu ulifutika kwenye Awamu ya Pili ya Uongozi wakati Mheshimiwa Mungai (Marehemu) alipofuta shule za ufundi zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi suala hili haliwezekani tena. Tuna Artisan kutoka VETA. Hawa watu wa VETA ni wa chini kabisa katika Elimu ya Ufundi, lakini baadaye kutoka hapa mpaka hapa, hakuna ma-technician, mafundi sadifu hawapo.

Mheshimiwa Rais anaongelea ufundi, viwanda vya ufundi, viwanda vya kuzalisha mali; wanaoendesha viwanda hivi ni mafundi sadifu. Mafundi VETA wana-repair mashine zikiharibika na kadhalika. Namwomba Mheshimiwa Rais afikirie kuendeleza elimu ya viwanda, afikirie kurudisha mfumo wa zamani wa Diploma Engineers ambao walifanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, sisi waajiri tunaona kwamba VETA kuwekwa chini ya Wizara ya Elimu ni kosa. Kufanya kosa siyo kosa, kujisahihisha ni bora. Tunapenda VETA iwe chini ya Wizara ya Kazi na Ajira ambako ndiko tunafanya uendelezaji wa stadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Kenya Polytechnic walilinda mambo hayo na matokeo yake, hela tunayochanga sisi kama SDL inakwenda kusomesha watoto High Learning Institution, tungependa sisi hela yote iende VETA, lakini vile vile tungeomba pia VETA yote katika mfumo mpya wa kuanzisha Mfumo wa Elimu ya Ufundi irudi tena katika Wizara ya Kazi ambako ndiko tunaendeleza stadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi waajiri tunapata taabu sana katika suala hili, tunaona kwamba VETA imewekwa sehemu ambayo labda kwa makosa ambayo hatuyajui, lakini tunaomba sasa VETA irudishwe tena Wizara Kazi ili iweze kuendeleza ujuzi wa wafanyakazi lakini vile vile ujuzi wa wanafunzi wapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, mimi bado naumia na tozo. Najua tunaongelea tozo ya SDL ambayo iko chini ya Wizara ya Elimu. Napata ukakasi! Ningependa kuongelea tozo ikiwa chini ya Wizara ya Kazi, lakini iko Wizara ya Elimu. Hii inatupa tabu sisi waajiri kuchangia kwa sababu tunaona tozo hii inakwenda kwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini vile vile naomba sana Serikali ichukue ushauri ambao nimeutoa. Ahsante sana kwa kuniruhusu niongee.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu na mimi nichangie bajeti hii ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Msemaji aliyenitangulia mimi amesema sana, lakini mimi naomba niseme ukweli kwamba Wizara hii inafanya kazi sana. Tuseme ukweli Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inachukua asilimia 75 ya Watanzania wote, lakini bajeti yao si asilimia 75 ya bajeti yote, hili lieleweke hivyo pia. (Makofi)

Kwa hiyo kidogo ambacho wanapata kinatufikia vijijini lakini hakitoshi, si mapungufu ya Wizara hii, ni mapungufu ya hali halisi ya uchumi wa nchi. Nina uhakika Mheshimiwa Rais akifanikiwa katika malengo ambayo anataka kutupeleka tukapata hela za kutosha ataangalia kundi kubwa hili la asilimia 75 ya Watanzania wanaoishi vijijini. Kwa sasa twende kama tulivyo. Hata hivyo tusahihishe makosa ambayo tunafikiri tunayoweza tukayasahihisha ili kuweza kuleta ufanisi zaidi kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze na kero za asilimia 75 ya Watanzania wote wanaoishi vijijini ambayo ni mbolea au pembejeo za wakulima, lakini pia vyama vya ushirika na tozo kwenye mazao ya wakulima. Nimesoma sana hotuba hii na yote nimemaliza. Ingawa tumeipata leo lakini sikupumzika mchana. Yako mambo ambayo tunaweza tukayasahihisha, yako mambo tunaweza kusema okay,
twende nayo mpaka hali itapopendeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la mbolea. Mimi nimegombana, nimepigana sana kupata zile vocha za ruzuku lakini hazisaidii, mbolea haifiki kule, vocha zinafika, wazee wale wasiojua kusoma wanasainishwa vocha lakini mbolea hawakupata, wanapewa hela kidogo na wanaosambaza hizi mbolea za ruzuku wanachukua hela. Lakini nimeona leo Serikali inakuja na mfumo mzuri ambao nillikuwa sikuutegemea kabisa. Mfumo huu tuliutumia kwa ubunifu mkubwa kwenye ununuzi wa mafuta kwa pamoja na EWURA wakasimamia. Sasa naambiwa tutanunua mbolea kwa pamoja (bulk procurement) halafu Shirika la Mamlaka ya Uboreshaji wa Ubora wa Mbolea lisimamie ununuzi huu. Hii pekeyake ndiye mkombozi wa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila treni bora ina kasoro yake isije ikatokea usimamizi ukalegalega na hili shirika la usimamizi wa ubora wa mbolea sasa lisimamie usimamizi wa ununuzi wa mbolea bora. Neno ununuzi liongezeke pale ili tuweze kupata bei nzuri na wakulima waweze kununua mbolea kwa hela yao. Sasa hivi haiwezekani mbolea mimi nimekwenda Ulaya kufuatilia bei za mbolea mfuko mmoja wa mbolea dola 25 na hapa tunasema imepunguzwa bei dola 42, 43 mara mbili/mara tatu zaidi. Lakini mbaya zaidi kampuni inayoagiza mbolea iko moja tu, kwa mfano NPK na sitaki kuitaja kampuni hiyo. Hiyo ndiyo inayogawa mbolea kwa wauzaji wengine halafu nayo ina-bid kwenye tender hiyo. Cha kushangaza wale walionunua mbolea kutoka kwake wanakwenda kuuza, yeye anauza ghali ana-bid bei ya juu, haiwezekani. Mimi nauza vitu nawagawia wenzangu wanakwenda ku-bid, mimi na-bid bei ya juu kuliko ninaowauzia mimi, haiwezekani lazima kunaujanja fulani sasa hii itakoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahi sana, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kubuni mfumo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la tozo, tozo imekuwa ndiyo sumu kubwa sana ya kuchukua mapato ya wakulima. Niongelee wakulima wa tumbaku, ambako ndiko natoka. Tozo imekuwa kubwa kiasi kwamba wakulima hawaoni faida yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ku- declare interest, nimetembea nchi tano za Ulaya kutafuta wanunuzi wa tumbaku kwa gharama yangu. Nimekwenda Uturuki, Greece, nimekutana na Wakorea kutafuta wanunuzi wa tumbaku. Kwa gharama yangu! Nimeshindwa kupata mnunuzi hata mmoja! Sababu ni nini? Bei ya tumbaku ya Tanzania ni ghali sana kuliko bei zote duniani; na matokeo yake mimi nina bei ya wakulima waliouza Uturuki mwaka 2016. Ubelgiji imeuza Uturuki kilo 34,967,318, kilo milioni na kitu, wakati Tanzania imeuza Uturuki kilo 32,000. Mnaweza mkaona tofauti yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewauliza kwa nini hamnunui kutoka Tanzania? Sababu kubwa wanasema bei iko juu sana. Bei iko juu kwa sababu ya tozo hizi! Tozo ambazo nimeziona katika hiki kitabu cha Mheshimiwa Waziri, itatusaidia kupunguza bei ya tumbaku ya Tanzania nje. Kwa hiyo, wanunuzi hawa watauza tumbaku nyingi na hivyo watanunua tumbaku nyingi kwa wakulima. Naomba, imesahaulika tozo moja muhimu sana; tozo ya unyaufu, ambayo ndiyo peke yake inayowasaidia wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale ambao hamjui maana ya unyaufu ni kwamba, wakulima wakiuza tumbaku leo, aliyenunua haji kuichukua. Akija kuichukua kutoka kwenye ghala anaipima tena, anakuta imepungua kilo 400, mia ngapi, wanamkata mkulima. Kwa nini wasinunue na kuichukua tumbaku yao ile? Wanasema kama tungeweza kuiuza kwenye center moja, basi gharama ya center watalipa wao. Gharama ya kuibeba watabeba wao wenyewe lakini suala la unyaufu halitakuwepo tena. Naomba Mheshimiwa Waziri afute tozo ya unyaufu na atusaidie kuanzisha masoko ya pamoja. Hii itasaidia moja kwa moja kupunguza gharama na kuongeza bei ya mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala lingine ambalo linanisumbua sana, nalo ni ushirika. Vyama vya Ushirika Mheshimiwa Waziri anisaidie sana. Nimemwomba mara nyingi sana kwamba Sheria ya Ushirika ina kasoro nyingi sana; ilitungwa ile Sheria na Wanunuzi. Sheria inasema, bei ya tumbaku itapangwa na wanunuzi na wakulima. Wakulima darasa la saba, wanunuzi wana degree tatu. Kutakuwa na ukweli hapo? Matokeo yake wamekuwa wakulima wanaitwa kwenye mikutano mikubwa, wanapewa posho, halafu bei wanapanga wanunuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kusema hapa, alete sheria hii. Bunge linatengeneza sheria hapa, turekebishe kipengele kinachosema Serikali hairuhusiwi kabisa ku-discuss bei, bei itapangwa na wakulima na wanunuzi. Wanunuzi wana degree tatu, wakulima darasa la nne. Inawezekana kweli! Nyie Wanasheria humu ndani mnaona balance iko kweli pale! Wala haruhusiwi hata mtu mmoja nje ya mkulima na mnunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Waziri Mkuu. Waziri Mkuu amesikia maneno mabaya na mambo mabaya, madudu ya Tabora kule kuhusu tumbaku. Waziri Mkuu amevunja Bodi ya Tumbaku jambo ambalo nimekuwa nikimwambia kila siku kwenye mikutano ya mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwambia Waziri wa Kilimo vunja Bodi ya Tumbaku, ilikuwa ngumu, lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu amevunja Bodi ya WETCU, Chama Kikuu cha Ushirika, ambacho wamekuwa wanaogelea kwenye mihela kama vile baharini. Zitakuja na mfumo mzuri wa ununuzi wa tumbaku pamoja na bulk procurement ya mbolea, kwa sababu hawa ndio wanaotangaza tenda ya kununua mbolea. Nafikiri atawashirikisha kwenye bodi mpya, wapate Bodi nzuri ambayo itawasaidia wakulima wangu kule Uyui. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa, kuna kituo kinaitwa OXEN Training Center kituo cha ku-train Maksai pale Upuge kilifunguliwa na Mwalimu Nyerere. Mwalimu amefariki amekwenda mara mbili kuangalia kituo kile. Baada ya kufariki Mwalimu, kituo kimekufa. Hamna aibu! Land Mark ya Mwalimu mmeiua! Mile Stone ya Mwalimu mmeiua! Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja aniambie future ya kituo cha kufundishia wanyama kazi pale Upuge.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote nawaachia wenzangu waongee. Naunga mkono hoja hii na kabisa kabisa namuunga mkono Mheshimiwa Rais. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii iliyoko Mezani kuhusu Bajeti na hasa mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kwenye madini. Madini popote duniani ndiyo inayotoa tathmini ya utajiri wa nchi. Kwa hiyo, kabla ya mafuta, madini yalikuwa ndiyo kipimo cha utajiri wa nchi. Kwa hiyo, matapeli na waaminifu wamejikita kwenye madini. Kwa hiyo, Serikali yetu ijue kwamba kwenye migodi yetu hapa kuna makundi ya aina mbili; wako watu waaminifu sana na wako wahalifu. Hawa wahalifu wanangojea fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uelewa wangu mdogo, biashara hii ya madini, hasa kwa wenye migodi, wana malengo yao na malengo yao ni kuwa matajiri. Utajiri huo wanaupata kwa aina mbili. Kwanza kwa kuuza madini yenyewe, lakini pia kufanya biashara na migodi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa makampuni haya, aidha yananunua mitambo kutoka kwenye kampuni tanzu au kampuni mama, kwa hiyo, matumizi ya mitambo ambayo kwa mfano mgodi ulianza kuchimba uwekezaji mkubwa wakapata na holiday ya kutolipa kodi, lakini wakanunua mitambo ya kuchimba labda mita 100; kwa kipindi chote hicho watapata hasara. Gharama ya mitambo na dhahabu wanayoitoa, hawalipi kodi. Baada ya mita 100 watawekeza tena kutoka mita 100 na kuendelea na hivyo hivyo hawatapata faida, watapata hasara. Kwa hiyo, kodi haiwezi kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo matatu ambayo ni muhimu sana ili nchi iweze kufaidika na madini, la sivyo itabaki na mashimo ya madini. Madini yote yataondoka. Mambo haya matatu, la kwanza, ni lazima Serikali iwe na hisa kwa niaba ya wananchi wake katika kila mgodi ambao unafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kuwa na hisa, Serikali itakuwa na Wajumbe wake wa Bodi, lakini pia itakuwa na wafanyakazi wa Bodi, kwa hiyo, watajua kiasi gani madini yanachimbuliwa na kiasi gani yanauzwa nje. Kwa sisi kuwa nje, tunawaachia wale wote madini ya kwetu na wachimbe wapeleke nje, hatujui kiasi gani cha madini kinachimbuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la pili, nalo ni ulinzi. Sasa hivi migodi yetu yote ina viwanja vya ndege na ndege zinatua pale na kuondoka na madini na haziji Dar es Sa- laam wala haziendi Mwanza wala Tabora, zinakwenda nje ya nchi. Matokeo yake tunabaki na mashimo makubwa ya madini kule, lakini hatuyaoni madini yale.

Katika taarifa ya Tume iliyotolewa leo na tunashukuru leo karibu Watanzania wote tuna msiba baada ya kujua kiasi gani tumeibiwa, hata furaha ya kuchangia inakuwa taabu kidogo. Madini yote yameenda nje, tumebakia na mashimo, lakini hatuna chochote tulicholipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya tatu ambayo ni mbaya zaidi ni hii ya kutofuata local content. Makampuni haya yote yanakuja kutoka nje, yanakuja na makampuni ya ulinzi, kazi ambayo ingefanywa na makampuni ya nchini hapa. Wanakuja na makampuni ya ulinzi kwa sababu hawataki Watanzania tujue ulinzi ule, kiasi gani mali inatoka? Kwa kufanya hivyo, miaka yote hii ambayo makampuni haya yamechimba yamekuwa na makampuni yao ya ulinzi na kwa hiyo, mali iliyotoka nje hatujui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ni manunuzi. Manunuzi imekuwa ndiyo unapofanya mizania ya kulipa kodi ili uonekane kama unapata faida, wanajaribu kupanga kiasi gani tumepata na kiasi gani tumetumia na miaka yote miradi mingi ya migodi imeonesha kwamba wamepata hasara badala ya faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kungojea sisi tupate mapato, kampuni zioneshe mapato, ndipo tudai kodi TRA waende, tumekuwa tunapata hasara badala ya kupata faida. Manunuzi haya kama sisi tungekuwa na nafuu ya kujua kiasi gani gari moja la kuchimbia mgodini linauzwa; na je, dumper lile shilingi ngapi? Tungeweza kujua kwamba tunadanganywa. Kwa vile tuko nje, hatuwezi kujua kiasi gani tunadanganywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la ulinzi wa mali migodini lipo kisheria. Makampuni haya na siyo haya tu, hata ya gesi na mafuta yamekataa katakata kutumia makampuni ya Tanzania na wWanazo sababu. Mimi nimekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya Ulinzi kwa miaka 15 na nimejitahidi sana kupata makampuni ya Tanzania yakalinde kwenye migodi, imeshindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa ni kwamba wanasema Kampuni za Tanzania hazina viwango, hazina sheria, hazina kanuni na hazina miongozo. Ndiyo maana nilipokuja Bungeni humu jambo la kwanza nililolifanya ni kuleta Muswada Binafsi wa Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi ili hiyo Sheria iunde Mamlaka ya Kampuni za Ulinzi Binafsi, ambapo mamlaka hiyo ndiyo itakayodhibiti uwezo wa kampuni. Kampuni ambazo zinalinda migodini, nyingine hazina uwezo kuliko kampuni za Tanzania, lakini hatuna mizania ya kupimia kwa sababu hatuna Mamlaka ya Kampuni za Ulinzi Binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, ni lazima tusonge mbele. Serikali iliniomba mimi rasmi kwamba, tunaomba Muswada wako huo tuulete sisi, lakini huu ni mwaka wa pili, na mimi naona kama tunachelewa. Yaliyosemwa leo katika taarifa ile ya Tume ya Pili ya Mheshimiwa Rais inasikitisha, ni kama vile mali imechukuliwa wenyewe wamelala au hawapo. Tungekuwa na macho yetu kule, tungekuwa na Sheria ya Ulinzi ya Binafsi, maana haiwezekani tukapeleka majeshi kwenda kulinda migodi ya watu binafsi au polisi kulinda migodi ya watu binafsi. Duniani kote migodi hii inalindwa na kampuni za Sekta ya Ulinzi Binafsi, lakini kwa kufuata sheria iliyopo na mamlaka iliyopo. Umefika muda sasa Serikali ilete Muswada hapa utakaosaidia sisi kuweza kudhibiti migodi yetu kwa macho ambayo tunayaamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi Jimboni kwangu. Tunayo matatizo makuwa sana Jimboni kwangu, hakuna maji. Tunakubali kwamba kutakuwa na Mradi wa kutoka Ziwa Victoria, lakini nikisemea Mkoa mzima, huo mradi haufiki Urambo, haufiki Kaliua, haufiki maeneo yote ya Jimbo langu; na chini ya ardhi ya Jimbo langu kuna mwamba. Kwa hiyo, visima vingi vilivyochimbwa vimekufa, zimebakia sehemu chache zenye chemchem kama vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu, nimegharamia kwenda kuchunguza wapi maji yapo? Pale maeneo machache ambayo tumepata maji, Serikali iniunge mkono ije ichimbe maji kwa faida ya wananchi wangu. Tuna taabu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kusimama hapa kila siku nagombana na Waziri wa Maji, nagombana na kaka yangu Mheshimiwa Kamwelwe. Naomba nipate ahadi sasa kwamba watakuja kuchimba vile visima hata vitatu, vinne kwa faida ya Jimbo langu. Wananchi wangu wananishangaa sana, kama nimegharimia mamilioni kuwaleta watu wapime maji, maji yakapatikana, kuchimba imekuwa taabu! Mimi napata taabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni upande wa mawasiliano. Wilaya yangu ni mpya, haina barabara za ndani. Ili uje Tabora Mjini lazima uende Nzega ukapite kule kwenye barabara ya lami ndiyo uje mjini. Imekuwa gharama kubwa; watu wanapanda baiskeli, halafu wanaacha baiskeli wapande magari kwenda mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili suala la barabara za ndani liangaliwe sana katika bajeti. Ipo barabara moja tu ya Tabora - Mambali ambayo ilikuwa iwekewe lami kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, sasa imewekewa iwe TANROADS, lakini barabara zote ndani hakuna. Tunatembea kwa miguu kama mwaka BC huko!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu inisikie na haya ambayo nimeyasema kuhusu madini, yachukuliwe kwamba ni mambo muhimu sana. Mambo matatu; manunuzi, ulinzi, kwamba ije Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi, lakini pia mambo yanayohusu hisa za Watanzania ndani ya migodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeki, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niongee au nichangie katika Wizara hii ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuwapongeza sana Wizara hii ya Nishati na Madini na niwakumbushe wananchi na Wabunge wenzangu humu jinsi gani tulikuwa miaka mitatu, mitano, sita iliyopita wakati ambapo tulikuwa na mgawo, siku mbili au siku tatu hakuna umeme na hatukulalamika; leo mgawo umekuwa historia hakuna mtu anayepongeza? Si tuwapongeze hawa wenzetu kwamba, wamefanya kazi kubwa sana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, nyuma ya mafanikio yote haya yupo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye amekuwa anatoa miongozo ya kulipa hela chungu nzima kwa mfano Kinyerezi Phase II ilisimama kwa sababu haikuwa na hela. Hela nyingi zimeingizwa pale ili mradi ule uanze, haya ni mafanikio makubwa sana. Vile vile iko miradi ya Rusumo huko, miradi mingine ya gesi inayoleta umeme ambao tunautumia majumbani na viwandani; haya ni mafanikio ambayo Wizara hii inatakiwa ipongezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, niseme ukweli kwamba mwenzangu, rafiki yangu Mheshimiwa Profesa Muhongo amepata ajali ya kisiasa na amemwacha hapa Mheshimiwa Engineer Merdad. Bado Wizara hii imewasilishwa vizuri na mwenzangu Mheshimiwa Mwijage hapa leo, tumefurahi kwa yote aliyoyasema na kama alivyosema yeye Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Merdad ameziba pengo, amevaa viatu vya Mheshimiwa Profesa Muhongo. Naipongeza Wizara hii kwa mambo hayo makubwa iliyoyafanya, lakini hasa kusimamia miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuongea kwangu leo nitaongelea pia, suala la REA ambao ni mradi mkubwa unaoendelea, lakini vile vile ningependa nichukue nafasi hii kuongelea mambo ambayo yametokea hivi karibuni ingawa yameongelewa pia, lakini suala la makinikia haliwezi kupitwa bila kusemewa kwa undani na kwa ukweli wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunapenda ku-quote au kunukuu maneno katika lugha nyingine, mimi ningependa kunukuu leo maneno kutoka lugha yetu ya Kinyamwezi na maneno hayo ni kwamba, “Mradi Kuyile” yaani mradi tunakwenda, “Nabhagemanyile” nilikuwa najua na kudharau yani “Kubyeda”.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo fulani akifanya kiongozi wa nje ya nchi, hasa kutoka kwa wakubwa hawa, kama container hili moja lingekamatwa kule Malaysia au Singapore au Marekani, basi watu hapo wangeandika na kusifia sana. Tumekamata makontena 277 watu wanaona business as usual, mradi kuyile, mradi tunakwenda, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, madini haya yaliyokuwemo katika mchanga huu wa makinikia umetia hasara sawasawa na bajeti ya nchi hii kwa miaka mitano. Si chini ya miaka mitano, makontena haya kwa miaka 17, tungeweza kupata mali iliyotoka mle ndani tungeweza kuendesha nchi hii kwa miaka mitano, bajeti ya nchi nzima. Sasa Mheshimiwa Rais amefanya juhudi kubwa sana, ametimiza wajibu wake wa kukamata makontena haya, lakini bado naona tayari kunakuwa na watu ambao wameanza kudharau suala hili, jambo hili si sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna juhudi kubwa sana ya waliokamatwa sasa kujaribu kufunika jambo hili na kuna watu wanasema tutashitakiwa, mimi nashindwa kuelewa! Umuibie mtu na ushahidi upo halafu ukamshtaki! Sielewi kama kutakuwa na sheria, au sijui watatumia njia gani ya kutushitaki sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napata tabu sana ninapoona wenzetu wanaanza kuongelea, kwamba ni tatizo la mikataba, kwa hiyo mikataba hii ingeanza kwanza kuchanganuliwa kabla ya kushughulikia makontena. Hata hivyo, ijulikane kwamba ili uuchambue upya mkataba lazima mkataba uwe na makosa, sasa makosa yameonekana, kumbe katika mkataba huu watu wanaiba, sasa huu wizi ndio ushahidi wa kuweza kuchambua mikataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani kwamba, sisi wote humu ndani ya Bunge hili tunao wajibu wa kutetea maslahi ya watu waliotuleta humu ndani, nao ni wananchi, ili wananchi hawa wasiibiwe, lakini vile vile wananchi hawa wasidhulumiwe na wananchi hawa wajione wako salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilinukuu maneno ya Kinyamwezi, lakini sasa ninukuu maneno ya Kiyunani, “Delegatus Non Protest Delegae”; mtu aliyepewa jukumu, wajibu wa dhamana hana haki ya kumkabidhi mtu mwingine tena wajibu huo aliokabidhiwa. Wajibu wetu sote humu ndani ni kuungana kwa pamoja kutetea wananchi waliotuleta humu ndani; leo inakuwaje sisi Wabunge tunaanza kubadilika na kutetea mambo ambayo hayana ukweli ndani yake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameunda Tume ya Wataalam, wamechambua mchanga ule na kutoa majibu; je, hatuaminiani? Wabunge humu ndani wanaanza kuongelea kwamba, inawezekana ule mchanga ni hadithi ambayo wanaicheza ngoma ya walioibiwa. Ukweli ni kwamba kuhusu mchanga ule tufuate maelekezo na taarifa iliyotolewa na wataalam wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye miradi ya REA. Pamoja na mafanikio makubwa katika awamu ya kwanza na ya pili ya REA kumekuwa na udhaifu mdogo mdogo uliotokana na utendaji, hasa uwajibikaji wa watu fulani katika mradi ule, wameruka vijiji fulani. Kwa mfano jimboni kwangu vijiji vikubwa ambavyo vina shule, vina zahanati, vina vituo vya afya vimerukwa! Bahati nzuri nilimwona Mheshimiwa Muhongo kabla hajaacha kuwa Waziri na tukakutana pia na mkandarasi huyu, nina imani tuliyoongea yatakuwa sahihi kwamba, watafanya variance ya mabadiliko kidogo ya mkataba kwa aslimia 15 ambapo Vijiji vya Majengo, Ikongolo, Kanyenye, Nzubuka na Kituo cha Upuge vitapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa anithibitishie kwamba, waliyoniambia viongozi wa REA kwamba, maeneo haya yatapata umeme, yapate umeme. Maana itakuwa jambo la ajabu bahati nzuri au mbaya katika vijiji hivyo ndiko mimi natoka, sasa watu wamekuwa wanasema ahaa, Mbunge huyu mnaona hafai, hata umeme kwake hakuna! Hayumo kwenye REA Phase Two na Phase Three.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo litaleta matatizo makubwa sana ya kisiasa, nawaombeni sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha awe ameongea na watu wa REA ili waingize Vijiji vya Upuge kwenye kituo kimoja cha afya kiko pekee, Vijiji vya Majengo, Kanyenye, Ikongolo, Nzubuka na Kiwembe.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengine katika Wizara hii ambayo ni mazuri sana, lakini mambo madogomadogo haya yanaipaka matope Wizara na ionekane kama haifanyi kazi. La sivyo, Wizara hii imefanya kazi kubwa sana kutafuta gesi, kusimamia upatikanaji wa gesi, kusimamia uunganishaji wa bomba kutoka Uganda kuja Tanga, kusimamia mambo mengi, gesi kutoka kule Mtwara kuja Dar-es-Salaam na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema sana, naomba niwaachie na wenzangu. Naunga mkono hoja moja kwa moja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya Kamati ya Kudumu za Bunge na hasa Kamati hii ya Kilimo, Mifugo na Maji. Maji limekuwa tatizo kubwa sana katika maeneo yetu hasa Majimbo ya vijijini kuliko mijini ambako maji hayapatikani kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nianze kuishukuru Serikali kwa kubuni Mradi huu wa Ziwa Victoria ambao unakuja kuleta maji katika Jimbo langu la Uyui-Tabora Kaskazini na Tabora Mjini. Ukitoa mradi huu pekee, Jimbo langu la Tabora Kaskazini hakuna maji chini, yako katika maeneo machache tu na ningeomba Serikali itumie uonekanaji wa vyanzo hivi vya maji kuwagawia maji wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limekuwa tatizo kubwa sana wakati Wizara ya Maji inazo fedha na Halmashauri kupitia Wizara ya TAMISEMI ndiyo nao wanatafuta wakandarasi au wazabuni wa kuchimba maji. Tunaye Wakala wa Maji kama alivyo Wakala wa TBA huyu ni DDCA. Hawa ni wataalam wazuri sana na wana bei chini kabisa lakini Halmashauri nyingi ikiwemo ya kwangu hawawatumii watu hawa, hawatumii wakala huu wa Serikali ambao wangeweza kuchimba maji kwa bei rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mifano miwili. Hivi karibuni wananchi wa Kata ya Ikongolo ambayo ina vijiji vinne vya Majengo, Kanyenye, Ikongolo yenyewe na Kiwembe walitafuta eneo ambalo kiangazi chote wanateka maji pale kama chanzo kikubwa cha maji lakini kukawa na kutoelewana na Halmashauri kwamba watafute mzabuni apime maji pale ikashindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge nalijitolea kutafuta hawa watalaam wa DDCA wakaenda wakathibitisha maji yako pale na vilevile wakatoa na ankara za uchimbaji wa visima vitatu. Bahati mbaya sana mwaka huu wa 2016 wakasema Halmashauri haina fedha, lakini baadaye ilipopatikana fedha kwa kutumia nafasi hiyo wakatangaza zabuni wakati mkandarasi DDCA ameshapeleka bei ya shilingi milioni 15 kwa kisima. Wakatangaza zabuni na wakachimba visima kwingine kabisa kwa bei ya milioni 27 karibu milioni 30 kwa kisima karibu mara mbili ya bei ambayo DDCA alisema, sasa mimi naona hili ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshamwona Mheshimiwa Waziri wa Maji, nimeshamwona Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na nafikiri kama walivyoniahidi watalifuatilia suala hili. Sioni kama ni halali tunaye Wakala wa Serikali na anaweza kuchimba maji kwa bei nafuu kama ambavyo Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliamua kuwapa kazi TBA ilitokana na matatizo ya wakandarasi wababaishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Waheshimiwa Mawaziri wote wawili watakapokuja kufanya majumuisho, waniambie tatizo hili la maji kwa nini hawakutumia DDCA wakatafuta wakandarasi wengine ambao watachimba kisima kimoja kwa bei ya visima viwili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika vijiji vyote vinne vile kisima kimoja hakitoshi. Kwa hiyo, bado tu wataendelea kuchimba kisima cha pili au cha tatu au vinne kwenye vijiji vyote vinne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie kilimo. Kila mtu akisimama humu ndani anajua kwamba asilimia 75 mpaka 80 ya wananchi wanakaa vijijini na kilimo ndiyo msingi wa maisha kule na ndiyo wanaolima tunakula sisi tunaokaa mijini. Hata hivyo, kilimo hakipewi thamani kama vile ambavyo afya ikikosekana mahali tunapiga kelele wote, maji yakikosekana mahali tunapiga kelele wote, usafiri ukikosekana mahali tunapiga kelele wote, hawa watu asilimia 75 hatupigi kelele sana na kuwasaidia wakulima wetu hawa ili Maafisa Ugani wafanye kazi sawasawa na Madaktari wanaotoka kwenye sekta ya afya au wanaofanya kazi kwenye sekta ya barabara yaani sekta hii ya kilimo haiangaliwi na matokeo yake haikui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kauli mbili leo asubuhi hapa, kuna kauli iliyosema sekta inakua kwa asilimia 1.2 nafikiri mwaka jana, mwaka huu sekta ya kilimo ambayo ndiyo sekta muhimu sana kinakua kwa asilimia tano, haisadiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kilimo kimekuwa cha kizamani. Siku za nyuma kulikuwa na vituo vya kufundishia mifugo kufanya kazi ya wanyamakazi, lakini vimetelekezwa. Pale kwangu Upuge kuna kituo kizuri sana alifungua Marehemu Mwalimu Nyerere kimetelekezwa na nimekuwa napiga kelele humu ndani kwa sababu mashine nyingine bado nzima zingeweza kusaidia kufufua utengenezaji wa mikokoteni au vifaa vya kilimo na ufundishaji wa maksai ili kilimo kiwe rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mazao ya biashara. Tumbaku imekuwa issue pale kwetu, sasa hivi kuna mpango wa korosho na sasa hivi korosho imetuaibisha huko nje, watu wasiojulikana wamepakia nusu ya gunia vitu vingine siyo korosho na nusu korosho. Mambo haya yametutia aibu kwenye soko ambalo tulilipata huko Vietnam lakini pia hapa waliopakia mizigo ile wamechukuliwa hatua gani? Serikali lazima ijisafishe iseme kwamba tatizo hilo ni watu wachache siyo Serikali nzima, siyo Tanzania yote tumefanya kosa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupata soko ni kazi kweli kweli lakini siyo kazi kama kulitunza. Sasa kama kuna watu walifanya hivyo miaka iliyopita kwenye pamba, pamba ilituharibikia kweli kweli mikononi mwetu, soko la pamba lilipotea kabisa lakini baadaye limerudi na kwa vile limerudi kwa matatizo makubwa namna hii sasa litunzwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani ni muhimu sana wasimamie pamba itoke safi, zamani sisi kule Usukumani na Unyamwezini pamba tuliita dhahabu nyeupe lakini baadaye ikawa takataka, ikatuangukia mikononi. Tunaomba sana sana Serikali itakapokuja hapa ituambie mikakati ya kutunza pamba itoke safi na mikakati ya kutunza korosho zitoke safi ili masoko tuliyoyapata tuweze kuwa nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sipendi kupigiwa kengele mara mbili, naomba niseme hayo ndiyo nilitaka kuwasilisha. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, marejesho ya mkopo; suala la fedha zinazotengwa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri hukopeshwa vijana na akinamama. Fedha hizo zinaporudishwa hazifuatiliwi na nyingi hutumika katika mafungu mengine katika halmashauri husika. Wabunge tumekuwa tukidai zitolewe lakini hatudai marejesho ya mikopo hiyo. Namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitia Waziri anayehusika na Uwezeshaji wa Vijana kutoa maelekezo ya fedha zinazorudishwa na waliokopeshwa ambao ni vijana na akinamama, fedha hizi za marejesho hazisimamiwi kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi katika utekelezaji uliotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa, Naibu wake Mheshimiwa Kwandikwa na Mheshimiwa Nditiye kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017/2018 tulipitisha shilingi bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kahama – Bulyanhulu – Geita kwa kiwango cha lami. Hata hivyo, hadi leo Aprili, 2018 taratibu za kupata mkandarasi hazijakamilika na kazi hazijaanza. Mwaka huu 2018/2019 Serikali imependekeza bajeti ya shilingi bilioni 18 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kufahamu lini hasa mkandarasi atapatikana na kazi kuanza? Shilingi bilioni 12 za mwaka 2017/2018, kiasi gani kimetolewa na kimefanya kazi gani? Lini hasa mradi huu utakamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana mimi kuniruhusu nichangie hoja hii ya Hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwa muda huu mfupi niliopewa nitachangia mambo machache lakini muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa muhimu ni kuipongeza Wizara hii niliyofanya kazi nyingi sana kukuza elimu yetu nchini. Nampongeza sana Mheshimiwa Ndalichako na timu yake pia silisahau Baraza la Mitihani. Mimi nimefanya kazi Baraza la Mitihani kwa miaka 15 na naelewa kiasi gani tulipata taabu, miaka minne imepita hatujasikia mitihani imevuja. Jambo hili ni muhimu sana lieleweke kwamba Baraza limefanya kazi nzuri sana chini ya Mheshimiwa Waziri Ndalichako pamoja na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo ningependa kuchangia changamoto, mimi kwangu naona changamoto kubwa sana kwenye wizara hii ni lugha ya kufundishia. Mimi naelewa ziko nchi ambazo zimeendelea sana kwa sababu ya kutumia lugha ya kufundishia ambayo watoto wanaelewa. Kusema kiingereza sio elimu ni lugha tu. Mimi nimekaa Uingereza kuna watu hata kuandika hawajui wanajua kiingereza sana. Mfumo wetu wa elimu wa kufundisha darasa la kwanza mpaka la saba kiswahili halafu watoto wakahamia kiingereza secondary school au shule ya upili unaleta matatizo makubwa sana, wanafunzi hawaelewi masomo na hii ni kikwazo kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua sana kwamba kuendeleza kiingereza ni kuendeleza mambo ya kutawaliwa, kutumia lugha ya watu wengine. Sisi tumeweza kufanya vizuri sana kutumia kiswahili chetu pia tunasema kiswahili ni tunu ya Tanzania. Ningependa tunu hii ipewe heshima yake, ningependa mimi kuona watoto wanafundishwa kiswahili, wanaelewa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko nchi ambazo zimeendelea sana kwa mfano Uingereza wanatumia kiingereza, vile vile Uturiki wanatumia kituruki, Ufaransa wanatumia kifaransa, Ujerumani wanatumia kijerumani na wengine Waarabu wanatumia kiarabu na watoto wao wanaelewa vizuri sana. Lugha hii ni kikwazo kikubwa sana kwa kufundishia watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi hata kama tungepiga kura leo wangapi wangependa kusoma kiswahili. Watoto wanasoma kiingereza, shule ya upili na kuendelea huku chini msingi ni kiswahili wakimaliza shule na chuo kikuu, Bunge tunaongea kiswahili, Serikali inatumia kiswahili tunawaacha watoto hawa hawaelewi la kufanya. Pia liko tatizo na Mheshimiwa Ndalichako nimekuwa nasema mara kwa mara la kuondoa shule za ufundi. Tunaongelea Serikali ya viwanda hatuna mafundi, hatuna mfumo mzima mafundi sanifu na mafundi mchundo haupo. Watu wale wanaotoka VETA hawatoshelezi kufanya kazi ya ufundi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ndalichako nimekuwa nasema mimi ni zao la Chuo cha Ufundi Moshi (Moshi Technical College), Ifunda Technical College pamoja na Tanga Technical College.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ndilo jopo ambalo linafanya kazi viwandani. Itatupa taabu sana baada ya kuwaacha muda mrefu; fikirieni sasa hapa shule za kata na za sekondari, kila halmashauri itenge shule fulani zifundishe ufundi kwenye level ya form four itasaidia kupata mafundi vijijini hata wa kutengeneza mikokoteni ya ng’ombe na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya ufundi ndiyo key issue ya development ya nchi zote, hata Ujerumani wako vizuri kwa sababu wana mfumo huo wa ufundi ambao wanaweza kuongoza shuleni zao, sisi hapa tumepoteza nafasi hiyo. Mfumo uliokuwa unatumika zamani wa diploma engineers na engineers umekuwa ni kitu muhimu sana kwa Ujerumani, sisi tumeupoteza. Nimekuwa nikisema hapa, ilikuwepo system nzuri, imepotelea wapi? Naomba Serikali irejeshe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua ni jambo gumu kuishauri Serikali wewe mtu mmoja ikatekeleza lakini naongelea ndani ya Ukumbi wa Bunge hili, naomba Bunge lichukue umuhimu wake wa kuishauri Serikali. Serikali tafadhalini sana, nasema kwa uhakika, kwamba watu wote wanaofanya kazi viwandani sasa walitokea shule za ufundi ambazo sasa hazipo, imebakia Moshi Technical, Ifunda na nyingine zina masomo ya kawaida. Tumekwama hapo Mheshimiwa Ndalichako, naomba unisaidie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mimi napata taabu sana sana, nimetokea sekta binafsi, waajiri tumekuwa tunalalamika sana. Skill development training inatokana na uendelezaji wa ujuzi wa wafanyakazi. Kuiweka VETA chini ya Wizara ya Elimu ni misplacement, imepotoshwa kidogo, lakini najua inaingiza mapato Serikalini. Si vibaya hata kama VETA itabakia Wizara ya Kazi na Ajira, lakini hela ikaenda inapotakiwa kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi inakuwa vigumu sana sisi waajiri kufanya kazi ya kuchangia mfuko wa elimu ya juu ambao si hata tulilolenga ilipoanzishwa hii VETA. VETA ilianzishwa ku-develop skill za wafanyakazi wetu sisi tuliowaajiri si wanafunzi wenye elimu ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua tunasaidia lakini tume- misplace kitu kikubwa sana pamekuwa na ombwe kubwa ya tulichokitaka sisi. Mimi ningeshauri sana mjadili huko kwenye Serikali rudisheni hii VETA pale pale ilipokuwa zamani lakini hela kama zinatakiwa kwa ajili ya elimu ya juu ziende, lakini sisi tupeleke wafanyakazi wetu sehemu ambayo ni ya kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tungependa waajiri tupeleke wafanyakazi wetu VETA ambayo iko chini ya Wizara ya Kazi na Ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa muda huu siwezi kufanya jambo lingine tena. Nashukuru sana na ninaunga mkono hoja mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa fursa hii nichangie hoja iliyopo mezani inayohusu Wizara hizi mbili, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli siyo kujipendekeza, sitaki kusema najipendekeza, nataka kusema kweli kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano imefanya mambo makubwa sana na kwa vile Wizara hii inayohusika ni Waziri ambaye ni Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, sifa nyingi zinazokwenda kwenye Wizara hii zinakwenda kwa Mheshimiwa Rais, Mawaziri wote wawili na Naibu Mawaziri wote wawili na watendaji wote wa Wizara hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na afya; Serikali imefanya kazi kubwa sana hasa kwenye Jimbo langu licha ya mambo makubwa kwenye Mkoa mzima lakini Jimbo langu limepata milioni 500 za kusaidia kituo cha afya, ime-upgrade vituo vitatu vya afya, lakini vilevile imetoa fedha za kukarabati zahanati zote katika Jimbo langu, kwa nini nisiseme ukweli kwamba wamefanya kazi, siyo kujipendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie hata wale ambao wanasema tunajipendekeza wangepata fursa hii ya kupata hivi vitu ambavyo tumepata na roho nzuri kama za kwetu wangeshukuru. Hawa watu wana roho mbaya, wamepewa vitu, wamepelekewa maendeleo katika maeneo yao hawashukuru, wamekalia kusema mabaya. Serikali hii hakuna nafasi ya kuilaumu, iko nafasi ya kuipongeza tu basi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema mambo yanayohusu afya kwamba Serikali wamefanya nzuri sana Serikali, lipo jambo ambalo ndiyo sehemu kubwa ya uchangiaji leo. Suala la elimu; TAMISEMI imefanya kazi kubwa sana, wametoa elimu ya msingi mpaka sekondari bure nchi nzima, haijapata kutokea, kama ilitokea ni katika nchi nyingine siyo hapa kwetu. Sasa huku nako siyo kusema ukweli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama meli imeenda Zanzibar inafika na mawimbi yapo lakini inafika, sasa kama kuna mawimbi kwenye suala la kusomesha watoto bure, yapo matatizo sijui ya walinzi, imepungua sijui kufyeka majani, hayo ni mawimbi lakini hatuwezi kutoa meli kwenda Zanzibar kwa sababu tu kuna mawimbi. Iko haja ya kusimamia mfumo huu wa elimu bure katika kiwango ambacho kinatakiwa na mapungufu madogo haya yanaweza kusahihishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo moja kubwa ambalo nataka kuliongelea kuhusu elimu. Wapo wataalam wa lugha wanaweza kunisahihisha na kunisaidia, nchi yetu inasomesha watoto wetu kwa lugha ya kiingereza, kutoka shule ya msingi darasa la kwanza mpaka la saba wanasoma kiswahili, wakifika darasa la saba watoto wetu hawa wanabadilisha elimu kama mawimbi ya redio kutoka TBC 1 kwenda TBC 2, vilevile wanabadilisha mawimbi kutoka labda ZBC 1 kwenda ZBC 2, kutoka kiswahili kwenda kiingereza. Ulipoanza mfumo huu kulikuwa na kipindi cha watoto wa form one kukaa wiki nne shuleni, shule ya upili kabla ya kuanza masomo wakisoma lugha ya kiingereza, siku hizi mfumo huo haupo. Kwa hiyo, wanatoka shule ya msingi wanakwenda kusoma kiingereza, hawaelewi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumewapa watoto hawa mizigo miwili; kwanza wajifunze lugha ya kufundishiwa, vilevile wajifunze masomo yale ambayo wanatakiwa wayasome kwa kiingereza. Tatizo hili limekuwa kubwa sana, lakini bila kujua kwamba tumeingizwa kwenye vita vya ukoloni mambo leo. Wapo watu na zipo nchi ambazo hazitaki tuwafundishe watoto wetu kwa lugha ya kiswahili ambapo wataelewa zaidi kuliko kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mfumo miaka iliyopita kwamba tutafundisha watoto wetu kwa lugha ya kiswahili na wataalam wakaandika vitabu. Mimi nilikuwa mmoja kati ya watu walioandika vitabu, niliandika vitabu viwili kwa ajili ya somo la umeme, nina kitabu kinaitwa Mwandani wa Fundi Umeme (Pocket Book for Electrical), nina kitabu kinaitwa Misingi ya Umeme na Sumaku (Basic Principles of Electronic and Magnetism). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitabu hivi vipo vya kiswahili, watoto wanapenda kuvitumia, lakini mitihani inakuja kwa kiingereza, matokeo yake vitabu hivi havitumiki. Wapo wataalam walioandika vitabu vya kemia na fizikia lakini vitabu vile watu wanakata tamaa, mimi mpaka nimezeeka nimakata tamaa sasa vitabu vyangu haviwezi kutumika na nimekuwa kama niliota na baadae nikaamka asubuhi hakuna kilichofanyika. Lugha ya kiswahili ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matumizi ya lugha ya kiswahili ni muhimu ili kuendeleza elimu yetu, na kwa kuwa kukandamizwa kwa matumizi ya kiswahili katika shule zetu sasa umefikia mwisho, na kwa kuwa sasa umefika muda nchi yetu itumie kiswahili ili kunyanyua elimu yetu, na kwa kuwa tunae Mheshimiwa Rais ambaye amekuwa anatoa maamuzi magumu kwa faida ya nchi yetu na kwa faida ya wananchi wa Tanzania; kwa mfano reli ya standard gauge aliisema imetekelezwa, amesema mambo ya ununuzi wa ndege imetekelezwa, amesema mradi wa umeme wa Rufiji, tumeambiwa tusiseme Stieglers Gorge tuseme Rufiji limetekelezwa, amesema ujenzi wa ukuta kule Mererani limetekelezwa na amesema tuhamie Dodoma limetekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Rais ambaye ndiyo Waziri wa Wizara ya TAMISEMI atolee uamuzi suala la kusomesha watoto kwa lugha ya kiswahili. Suala hili linahitahitaji utafiti na utafiti umefanyika, nimesikia kwenye redio wameongea wataalam wa kiswahili kwamba walikuwa tayari lakini kwa vile Serikali haikuonesha nia ya kwenda kwenye lugha ya kiswahili suala hili likawekwa kabatini. Nina hakika mambo yalikuwa madogo kuliko kujenga reli ya kati ya standard gauge, kujenga ukuta wa Mererani na kununua ndege cash. Mheshimiwa Rais ambaye ni Waziri wa Wizara hii akitamka tutumie kiswahili nina hakika litakuwa jambo dogo kuliko kuhamia Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende upande wa Wizara hii ya Mheshimiwa Mkuchika ya Utumishi na Utawala Bora. Kila mtu akisimama hasa upande wa pili kule kumekuwa na maoni ya kutokuwa na utawala bora hapa nchini, nawashangaa sana. Wamekuwa pia wanaisakama Idara ya Usalama wa Taifa wanasema Idara ya Usalama wa CCM, jambo hili ni baya sana. Kila mtu anaamka hapa na kufanya kazi vizuri kwa sababu kuna utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lawama hizi zinatokana na watu kujua na Mheshimiwa Mkuchika anielewe vizuri, kujua kazi za Idara ya Usalama wa Taifa. Siku moja amezisema humu ndani, huenda haitoshi ni bora ifanyike elimu ya semina kwa Wabunge wote juu ya kazi ya Idara ya Usalama wa Taifa, itasaidia kwa sababu tunawakilisha watu wote nchi nzima, watu wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamewakilishwa humu. Tukipata elimu ya Idara ya Usalama wa Taifa tutaenda kuisema kule na wananchi wote wataelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Usalama wa Taifa ni kuleta amani hapa nchini, umoja na mshikamano, haya yote tunayoyaona, utulivu huu umeletwa na Idara ya Usalama wa Taifa. Kwa hiyo, ni muhimu sana wale wote wanaolaumu wakauliza vilevile Mheshimiwa George Mkuchika, Waziri wa Utawala Bora ni bora ukaandaa semina, tulifanyiwa wakati wa Bunge la Katiba, tulifanyiwa semina tukaelewa sana na haikutupa taabu kuendeleza, kutunga ile Katiba Inayopendekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwanza nianze kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwa maana ya Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Masauni, pia Katibu Mkuu wao na viongozi wote wa Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Vilevile niwapongeze Wakuu wa Idara wote, Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza na Zimamoto. Nawapongeza sana kwa kazi nzuri wanayofanya pamoja na matatizo madogo madogo yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko changamoto ambazo hatuwezi kunyamaza tusiseme. Changamoto hizo nimezipanga kwa idara, nianze na Jeshi la Polisi, huu ndiyo mhimili mkuu unaotegemewa na raia hapa kwa sababu wao ndiyo wamepewa kazi ya ndani ya ulinzi wa raia na mali zao, lakini Jeshi hili la Polisi halitoshi, kwani askari ni wachache kuliko raia wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi nyingine kampuni za sekta binafsi za ulinzi zinafanya kazi pamoja na Jeshi la Polisi kuendeleza ulinzi wa raia na mali zao. Hapa kwetu tuna makampuni mengi sana ya ulinzi, lakini kwa bahati mbaya sana makampuni haya hayana sharia. Nimekuwa nasimama mara kwa mara nikidai sheria, lakini kumekuwa na dalili ya kupindisha hiyo sheria kama ilivyo katika nchi nyingine, nchi nyingine kote kuna sekta za ulinzi binafsi na kuna sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sielewi kwa nini tatizo limetokea hapa la kutoleta sheria hiyo hapa Bungeni. Naambiwa sheria hiyo inaweza ikapinda ikawa ni uendelezaji wa maboresho ya Sheria ya Polisi. Mimi nasema kote duniani yalikotoka makampuni haya ya ulinzi au idea ya sekta ya ulinzi binafsi kuna sheria yake ya kuyaongoza makampuni haya na Tanzania hatuwezi tukawa na kisiwa. Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi ni lazima ije ili makampuni haya yanayoajiri mara tano, mara sita wingi wa Jeshi la Polisi yatusaidie kulinda raia na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nikiongelea sasa hali halisi ya utendaji wa Jeshi la Polisi. Kumekuwepo na suala linalosemekana watu wasiojulikana na wenzetu wa upande wa Upinzani kule wamekuwa wanadai kwamba huenda watu wasiojulikana wanafanya matukio upande wa Upinzani tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina orodha ya maafisa na viongozi wa CCM waliofanyiwa matukio na watu wasiojulikana. Badala ya kulaumu kwamba watu wasiojulikana wanakuja upande wenu, nikiandika orodha ya watu waliofanyiwa matukio upande wa Upinzani hawafiki hata robo ya watu waliofanyiwa matukio upande wa CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichukua tu watu wa CCM waliofanyiwa matukio upande wa Rufiji kule lakini hata jana Katibu Mwenezi…

T A A R I F A . . .

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ndiyo tatizo la watu kuwa na mawazo kichwani badala ya kusikiliza anachosema mtu. Mimi siongelei Jeshi la Polisi kukamata watu au kuua watu, naongelea watu wasiojulikana kufanya matukio. Mimi siongelei Jeshi la Polisi kufanya lolote, naongelea matukio yanayofanywa na watu wasiojulikana kwamba matukio hayo ni machache kwa upande wa Upinzani kuliko yaliyofanywa upande wa CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko haja sasa ya Serikali kuiongezea nguvu na uwezo Idara ya Upelelezi.

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sijaongelea uraia wa mtu, wala chama naongelea watu wasiojulikana kufanya matukio. Watu wanaofanya matukio na hawakamatwi ndiyo ninachoongelea. Nasema Serikali ifanye juhudi kubwa ya kuiongezea nguvu Idara ya Upelelezi ili watu hawa wanaofanya matukio kwa pande zote mbili waweze kukamatwa. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongelea ombi langu kwa Serikali kuiboresha Idara ya Upelelezi ya Polisi ili iweze kuwakamata watu wasiojulikana wanaofanya matukio. Hiyo ndio message yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie upande wa magereza. Sisi tumetembelea magereza na mambo makubwa yanayotokea kule yanahitaji msaada wa Serikali. Changamoto kubwa tuliyoikuta kule kwanza ni makazi yao na vilevile wafungwa wengi wamerundikana katika magereza. Kwa hiyo, programu hii ya adhabu mbadala ni muhimu sana ikachukuliwa umuhimu wake ili kupunguza mrundikano magereza. Vilevile ni bora magereza wawe na kiwanda chao cha kutengeneza sare ili waweze kuwa na sare za wafungwa na sare zao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumekuta upungufu wa chakula na yako madeni makubwa sana ya wazabuni wa chakula kwenye magereza yetu ambayo hayajalipwa na mbadala wake ingefaa kama magereza ingerudia mfumo wa zamani wakati sisi wadogo magereza walikuwa wakilima mashamba makubwa wakijilisha wao na kuuza chakula kwenye idara nyingine za Serikali. Kwa hiyo, napendekeza magereza wapewe uwezo wa matrekta ili waweze kufungua mashamba makubwa waweze kujilisha wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la zima moto. Zima Moto wana kazi kubwa kabisa ya kuokoa maisha ya raia na mali zao lakini hali ya jeshi hilo kwa sasa ni mbaya. Kwanza hawana vifaa vya kufanyia kazi lakini pia madawa ya kuzima moto hawana. Kwa hiyo, ningependa Serikali inapopanga bajeti yake iiangalie idara hii kwa macho mawili ili waweze kupewa kile ambacho kimepangwa katika bajeti ya kila mwaka. Kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza ukali wa upungufu wa Idara ya Zima Moto ili waweze kutusaidia yanapotokea majanga ya moto hasa mijini na maeneo ambayo ni sensitive sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la Idara ya Uhamiaji. Hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya kukamatwa wahamiaji haramu hapa nchini lakini wahamiaji hawa wanapita katika nchi jirani. Mimi sielewi huko nchi jirani wanawaruhusu waje kwetu hapa kwa sababu sisi tunapata gharama kubwa sana kuwatunza hawa wahamiaji kwa maelfu halafu kuwasafirisha walikotoka na tukiwafunga magereza yetu yanafurika, lakini wanapita katika nchi jirani kule bila kusimamishwa. Inawezekana ni mkakati waende Tanzania kama ngao tu, ni gharama kubwa sana, kwa nini nchi jirani hawawazuii hawa wahamiaji mpaka waje wakamatwe hapa kwetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza sasa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi jirani wakutane wajadiliane suala hili la wahamiaji. Haiwezekani kila mwaka tukamate maelfu ya watu wanaopita katika nchi jirani wanakuja kukamatwa hapa kwetu, ni gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia Idara ya Uhamiaji wanatumia hela nyingi sana kuwatunza lakini mahakama pia inachukua muda mrefu kujadili kesi ambazo sio za lazima. Kama kuna uwezekano wa kuongea na nchi jirani kwamba wazuiwe kule wanapoingia mpakani badala ya kuvuka nchi tatu waje wakamatwe hapa, ikiwa na sisi tutawaruhusu wapite itakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa kuwa wanasema hawaji Tanzania wanaenda nchi fulani, wanapita transit hapa, kama hatusaidiani ujirani huu mwema basi na sisi tufunge mikono piteni, si wanapita tu bwana ila watakaobaki hapa tuwakamate. Kama wanapita waacheni wapite waende zao huko wanakotaka kwenda maana hakuna ushirikiano kati ya nchi na nchi. Hili ni tatizo kubwa sana na ni lazima Idara ya Uhamiaji isaidiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Idara ya Uhamiaji pia kwa hizi passport ambazo tulikuwa tunaziona kama ndoto ziko mikononi mwa wananchi wa Tanzania. Hili ni jambo zuri sana, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii moja kwa moja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nami nichangie hii Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwanza leo nina furaha sana pale kwenye nafasi ya Wageni wa Mheshimiwa Spika, wako watu muhimu sana. Walikuwepo watu muhimu sana, Jenerali Sarakikya, alikuwepo Jenerali Mbona, Jenerali Waitara, Jenerali Mwamunyange na Mheshimiwa Jenerali Mabeyo. Katika nchi nyingine huwezi kupata mfumo wa namna hii wa kukaribishana majeshini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila kiongozi wa jeshi aliyeondoka, ameondoka na mgogoro mkubwa sana. Ni Tanzania tu ndipo unaweza kuona mfumo huu na hii inaashiria nini? Maana yake ni amani na usalama. Jambo hili ni geni katika nchi nyingine, limejengwa, halikuja tu Tanzania, maana yake kuna viongozi wamefanya kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Zungu amenifilisi, lakini yako machache ambayo ni muhimu nami niyachangie, mojawapo likiwa la pongezi kwa majeshi yetu. Majeshi yetu yanafanya kazi kubwa sana huko nje, yanasifiwa sana. Ila kama wanavyosema watu kwamba Masihi hasifiwi kwao, sisi hapa kwetu tunasahau Vita ya Kagera. Leo mtu anasimama hapa anaongelea negative ya Vita vya Kagera. Kaenda kutembelea makumbusho ya Vita ya Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ku-declare interest, mimi nilikuwa Operation Kagera na nina medali ya Vita vya Kagera, mimi na mke wangu. Ukienda pale siyo mahali pa kuangalia negative, ni mahali pa kusifia. Vita ile ni sifa kubwa ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, siyo la kubeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo ambalo limejitokeza hapa la kuwekewa ceiling jeshi katika matumizi yake. Jeshi lisiwekewe ceiling na wanasiasa au Waziri wa Fedha aweke ceiling ya matumizi ya Jeshi. Ni vigumu sana kutambua matumizi ya Jeshi. Jeshi linabadilika na hali ya dunia, teknolojia, electronic warfare ndiyo inayochukua nafasi. Tanzania hatukuwa na miundombinu ya electronic warfare, maana ndiyo kwanza inakuja. Lazima Serikali ijiandae kutoa hela nyingi kujenga miundombinu ya electronic warfare. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ulinzi katika dunia yote unahusu mambo ya defence, siyo kupigana physically. Hakuna mtu anayetaka kwenda vitani, ila kila mtu anataka kuzuia vita. Huwezi kuzuia vita kwa maneno ya bajeti ya shilingi mbili tatu. Jeshi linahitaji hela na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali nzima tujue kwamba tunataka Jeshi imara lenye weledi na usasa, haliwezi kuwa hivyo bila kupewa hela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali hii itoe hela kuyasema yote, kuyatekeleza yote ambayo Mheshimiwa Zungu ameyataja, yanahitaji hela. Mkono mtupu haulambwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo issue mbaya sana. Sera ya Sheria ya Ulinzi wa Taifa, imekaa miaka chungu nzima Zanzibar, wenzetu waipitie tu kwa nini hairudi hapa, kwa nini haiji Bungeni ikajadiliwa hiyo sera? Naomba Kiti hicho kitumike, kwamba Bunge liiombe Serikali ilete sera hiyo hapa tuijadili ili kuboresha Sheria ya Ulinzi wa Taifa, ni muhimu sana na tukichelewa ni adhabu mbaya tutawapa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangependa sera hii ijadiliwe upungufu wote ambao umetajwa kwamba Majenerali wanaostaafu, mishahara tofauti imo ndani ya Sera ya Ulinzi wa Taifa ambayo imekwama Zanzibar. Zanzibar kuna nini, huo Muungano una nini, hawataki ulinzi Zanzibar? Hebu Bunge liisimamie Serikali kuleta hiyo sera humu ndani haraka iwezekanavyo.
kutoka SUMA JKT wakidhani wamepewa bure, imetimia bilioni 40 ni hela nyingi sana. Wakilipwa kidogo hata nusu wao pia matrekta hayo wameyakopa huko yalikotoka hawakupewa bure. Naomba Serikali isimamie suala hili, kuna Halmashauri zimetajwa pale, Geita na wapi warudishe hizo hela walizokopa kwenye matrekta, najua wameyauza lakini hela hawakurudisha, walete hela za SUMA JKT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala dogo la SUMA Guards. SUMA Guards ni walinzi, lakini hapa nchini kuna sekta ya ulinzi binafsi inafanya kazi hizo zinazofanywa na SUMA Guards. Tatizo la SUMA Guards ambalo limejitokeza ni kwamba watu wanaopewa huduma ya SUMA Guards wanafikiri Serikali inatoa bure kama vile inavyofanya walivyokuwa wanalinda Mgambo au Jeshi la Polisi, hawawalipi SUMA Guards. Matokeo yake madeni yamekuwa makubwa na SUMA inachelewa kupanuka. SUMA Guards kingekuwa chombo kizuri cha kutegemewa hapa nchini, lakini wanabanwa kwa sababu hawalipwi wanafanya kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati tumesema sana, wamejitahidi kukusanya hela kidogo, lakini wangeweza kupanuka zaidi kama wangekuwa wanalipwa madeni yao. Kwa hiyo, ushauri ni kwamba wapate zabuni, wasiitwe njooni mlinde hapa, wasiende, kwa sababu mtu anawaita hivyo hana bajeti, lakini anayetangaza zabuni ana bajeti ya zabuni hiyo kama ambavyo makampuni mengine ya ulinzi yanapata zabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na malalamiko ya chini chini na hili tuliseme wazi. Makampuni ya sekta ya ulinzi binafsi yanalalamika kwamba SUMA Guard wanapendelewa. Kwa vile wataomba zabuni watapata zabuni kwa ushindani, suala hili la kupendelewa litakufa, itakuwa jiwe moja ndege wawili. Kwanza watapata hela lakini kwamba wanapata kazi bure itafutika vilevile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwamba Mheshimiwa Zungu alinifilisi....

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono. Ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee yako madeni ya SUMA JKT ya matrekta, watu wamekopa matrekta
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuendeleza suala la kuomba matumizi ya lugha ya kufundishia katika shule za msingi na shule za upili kuwa Kiswahili. Naelewa kuwa suala hili ni la kisera chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia lakini niliomba uamuzi wa Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ndiyo sababu ya kuleta suala hili kupitia Hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atakapokuja kutoa majumuisho yake alisemee suala hili la kufundisha shule za msingi na shule za upili kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. GODBLESS JONATHAN LEMA (MB)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja hii iliyoko mezani inayomhusu Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Godbless Lema.

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge ipo kisheria ndani ya Bunge na ipo kikanuni. Kabla ya kuanza kazi ya Kamati hii tulipewa instruments; tulipewa Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2016, tulipewa Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge, lakini pia tulipewa Katiba ya nchi hii ili Kamati hii itende haki.

Mheshimiwa Spika, Kamati hii inafanya kazi kwa kanuni ya Nyongeza ya Nane, kanuni ya 4 inayotaka; na naomba kwa faida ya Bunge hili ninukuu, inasema: “Kamati ya Haki na Maadili ya Madaraka ya Bunge itatekeleza majukumu yafuatayo:-

(a) Kuchunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala yote ya haki, kinga na Madaraka ya Bunge, yatakayopelekwa kwake kwenye Kamati hii na Spika.

(b) Kushughulikia mambo yanayohusu maadili ya Wabunge yatakayopelekwa na Spika.”

Mheshimiwa Spika, suala la Mheshimiwa Godbless Lema chimbuko lake lilitokana na kesi ya Mheshimiwa Profesa Assad aliyetamka maneno kuhusu dharau na kuliteremsha hadhi Bunge, akisema Bunge hili ni dhaifu. Suala hilo lilishadidiwa na Mheshimiwa Halima Mdee aliyasema pia yeye ni Mbunge mzoefu na ana hakika Bunge hili ni dhaifu. Mheshimiwa Godbless Lema alishadidia zaidi naye akasema kwamba yeye ni Mbunge mwenye vipindi viwili, naye anashadidia kwamba Bunge hii ni dhaifu.

Mheshimiwa Spika, kisheria Mheshimiwa Godbless Lema aliunganishwa na kesi ambayo aliikuta. Kwa hiyo, akathibitisha kwamba naye pia anafanya kosa hilo hilo kwa ushahidi alionao yeye mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, ulimleta Mheshimiwa Godbless Lema aje athibitishe kwenye Kamati kwamba anao ushahidi wa kutosha kwamba Bunge hili ni dhaifu.

Mheshimiwa Spika, neno “shahidi” linatumika kwa ajili ya Wabunge wanaokuja kwenye Kamati. Shahidi huyu alipofika kwetu alithibitisha kwamba naye bado anaamini kwamba Bunge ni dhaifu. Kwa hiyo, anakiri kwamba alifanya kosa hilo na alithibitisha na bado aling’ang’ania kwamba ni kosa hilo.

Mheshimiwa Spika, msemaji aliyetangulia hapa, ndugu yangu Mheshimiwa Mnyika, ame-quote kifungu cha sheria ambacho hajui kwamba tulikitumia au hatukukitumia. Tunatumia sheria mara nyingi kwa watu ambao hawahusiki. Ali-quote kifungu cha 33 na ange-quote na cha 26 pia cha Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge, lakini sisi tunatumia sana kanuni hizi kwa ajili ya Wabunge ambao ni wanachama wa Bunge hili na angekwenda kwenye kifungu cha 74 kingemsaidia zaidi kupata majibu, kwa nini Mheshimiwa Lema amechukuliwa hatua.

Mheshimiwa Spika, nami kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge wengine, ningependa kusoma kanuni ya 74 (4) wale wenye kanuni za Kudumu za Bunge, inasema hivi: “Bunge linaweza kuzingatia ushauri mwingine wowote utakaotolewa na Kamati ya Haki Maadili ya Madaraka ya Bunge kuhusu adhabu anayostahili kupewa Mbunge aliyekiuka masharti ya kanuni hii.

Mheshimiwa Spika, vile vile kanuni ya 74 kifungu kidogo cha (5) inasema: “bila ya kujali masharti ya fasili ya (4) ya kanuni hii, Bunge linaweza kumchukulia hatua nyingine za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kazi Mbunge yeyote atakayetenda kosa chini ya kanuni hii.” Kwa hiyo, kanuni aliyojielekeza Mheshimiwa Mnyika sidhani kama aliamini kwamba tuliitumia sisi.

Mheshimiwa Spika, nini maana ya kazi ya Kamati hii? Sisi katika Kamati ya Maadili, tuko pale kwa ajili ya kutumia Kanuni, kusahihishana Wabunge, kwa Wabunge ambao umewaleta wewe kwenye Kamati yetu. Hata hivyo, huyu Mheshimiwa Lema ambaye ni shahidi wa mwisho kwa suala hili, alipokuja kwetu hakuonesha hata kidogo kujutia kosa alilolifanya alithibitisha kwamba amelifanya na tulipompa nafasi ya mwisho aseme, akasema moja nawaombeni kabisa kabisa msinihurumie. Narudia, tulipompa ruhusa aseme chochote kwamba sisi tunataka kumtia katika hatia kwa sababu amevunja kanuni kwa kulidhalilisha Bunge kwamba Bunge hili ni dhaifu, akasema, naiomba Kamati hii isinionee huruma na wala isinipe msamaha. Sasa sisi tulibaki na jambo la kushangaa sana Mheshimiwa Lema tulipotaka, unamwambia Hakimu wewe Hakimu usinihurumie mimi na wala usinisamehe, wewe hukumu.

Mheshimiwa Spika, imetupa tabu sana, tukafikiria makosa ya nyuma ya Mheshimiwa Lema. Mheshimiwa Lema huyu alipoitwa mara ya kwanza kwa kudharau Bunge kule Dar es Salaam alisema naomba nikatafute Wakili na alipopewa fursa hiyo hakurudi tena. Kwa hiyo jana alipokuja alikuwa na wazo hilo kwamba naomba mnisamehe nikatafute Wakili, lakini tulipomwambia wewe unaweza kujitetea, akaongea mambo mengi sana ya kujitetea, lakini sio kujitetea ili asamehewe, ya kusema mambo mabaya kuhusu Bunge ili Bunge halina uwezo na uwezo wa Spika si, alisema maneno mengi kwenye Kamati ile na akatuma salamu tukwambie Mheshimiwa Spika kwamba unavyoendesha Bunge sio vizuri na tulivyomwambia aeleze hasemi lolote la maana akijaribu kusema kwamba mimi nathibitisha kwamba Bunge hili ni dhaifu.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilimtia hatiani kwa adhabu ambayo azimio limeomba na mimi naunga mkono adhabu hii ya mikutano mitatu na kwa kweli Kamati ingeomba zaidi mikutano zaidi ya mitatu iliyoombwa sababu kubwa ya kumpa mikutano mitatu ni kwamba Bunge linakaribia mwisho, tumetaka awepo kwenye Mkutano wa mwisho wa Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waheshimiwa Mawaziri na watendaji wote katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri na hasa usimamizi wa Serikali na miradi mikubwa ya maendeleo. Hata hivyo ninayo mambo yafuatayo kama ushauri:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya ufundi, kwa kuwa Serikali imejikita katika uchumi wa viwanda ni lazima irejeshe elimu ya ufundi ya mafundi sadifu (technicians), sasa hivi Serikali inajikita kuandaa mafundi mchundo (artizans) kutoka VETA. Mfumo huu wa elimu unaacha ombwe kati ya mfumo wa utendaji kazi za ufundi, Mhandisi mmoja kutoka vyuo vikuu, Mafundi Sadifu 25 kutoka vyuo vya ufundi na Mafundi Mchundo 15 kutoka VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waajiri sekta binafsi wanalipa tozo ya SDL ya 4.5% iliyolengwa kupelekwa VETA kuongeza ujuzi wa wafanyakazi, lakini fedha hizo hazipelekwi zote, sehemu kubwa inapelekwa vyuo vya elimu ya juu kwa wanafunzi, siyo wafanyakazi, waajiri wanaona kuwa hii si sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waajiri wanaamini kuwa lilikuwa kosa la kiufundi kuiweka VETA chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, VETA ilistahili kuwa chini ya Wizara ya Kazi na Ajira, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa sababu VETA ililenga kuongeza ujuzi wa wafanyakazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nami kuniruhusu nichangie hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani vifungu 28, 29, 51 na 93.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kutoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais Joseph Pombe Magufuli kwa kuliwezesha Jeshi la Polisi kufanya kazi kubwa ambayo linafanya. Pia pongezi kwa Wizara nzima ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi hasa kwa kuendeleza amani na utulivu hapa nchini, kwa kulinda raia na mali zao Ila nina jambo la kusema leo ambalo limenisumbua sana.. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, upande wa pili kule wanaye Mnadhimu Mkuu au Msemaji wa Kambi ya Upinzani. Mnadhimu huyu, Mheshimiwa Tundu Lissu amekuwa anasema maneno mabaya kuhusu nchi hii, kuhusu Serikali, kuhusu Mheshimiwa Rais na wenzetu hawa wamekaa kimya. Huyu ndiye Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni. Kwa hiyo, anayoyasema kule ndiyo haya haya ambayo hawa wanayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka hawa waseme leo: Je, ni kweli mnamuunga mkono Tundu Lissu au mko tofauti? Mseme ili wananchi wajue mko upande wa watu wanaochukia Tanzania, wanaomchukia Mheshimiwa Rais, wanaochukia Serikali, wanaochukia maendeleo yote; wanachukia miradi ya nchi hii inayoletwa na Serikali ya Awamu ya Tano. Mseme wananchi wawajue ili wasiwape kura kwenye uchaguzi unaokuja. Hamfai kuongoza nchi. haiwezekani muishi kama popo upande huu mko ndani ya Bunge mnasema mnaipenda Serikali ya Jamhuri ya Muungano, mnachangia mtu anayekosoa Serikali. Sasa hivi mnawasema vibaya hawa hawa. Haiwezekani mkia uwe tofauti na kichwa kiseme tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii wakati ilipofika Wizara ya Sheria na Katiba, wamesoma hotuba ya Mheshimiwa Tundu Lissu. Kwa hiyo, wanamuunga mkono yote anayoyasema, lakini nje hamwambii wananchi kwamba ninyi hamuipendi nchi hii, semeni. Msiendelee kukaa kimya, upande wa pili mnasema watu, nchi za nje ziinyime misaada Serikali yetu, lakini vilevile hamtaki misaada yoyote ije kwa watu ambao wanawasaidia, Serikali inayowasaidia dada zetu, mama zetu na kaka zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana upande wa Upinzani leo useme kwamba anayoyasema Mheshimiwa Tundu Lissu ni ya kwao au ni ya kwake? Ili wananchi wajue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sasa naomba nichangie. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani anipelekee salamu zangu kwa Mheshimiwa Rais za kuwapa pole familia za Askari waliofariki wakitetea amani na usalama wa nchi yetu. Askari hawa ambao wanabezwa na upinzani wamefanya kazi kubwa sana. Hakuna mtu kati yetu Bungeni humu aliyejitolea kufa ili jirani yake aishi. Askari wetu wamekufa. Wamekufa Rufiji, hata juzi wamekufa, wanapambana na majambazi ili kuleta usalama wa raia na mali zao. Iko haja ya kuwasifia sana lakini kutoa pole kwa familia zinazobaki, waliokuwa wanawategemea Askari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu ya NUU imefanya kazi ya kukagua miradi yote muhimu ya Jeshi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwemo miradi muhimu, lakini kote kumekuwa na kilio, hakuna fedha iliyopelekwa kwenye maendeleo hata kidogo. Fedha iliyopelekwa ni kidogo, haiwezi kumalizia miradi ambayo ipo. Naiomba Serikali, Wizara ya Fedha iwapatie fedha miradi hii katika Jeshi la Polisi, Idara ya Zimamoto, Idara ya Magereza na Uhamiaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la Sheria ya Sekta Binafsi ya Ulinzi. Sheria hii niliileta nikaipeleka kwa Mheshimiwa Spika na baadaye Serikali ikaiomba kwamba yenyewe itaileta kwa sababu ilikuwa inahusishwa kuanzishwa chanzo cha kupata kodi na Mamlaka ya Sekta ya Ulinzi Binafsi, (Private Security and Authority). Sasa zilikuwa siku, ikawa wiki, ikawa miezi, mwisho imekuwa ni miaka mitatu tangu sheria imechukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mheshimiwa Waziri atapokuja alieleze Bunge hili, ni lini sheria hii italetwa? Sheria hii ni muhimu sana kwani italeta win win situation kwa makampuni yanayoendesha biashara hii ya ulinzi binafsi lakini pia Serikali itapata kodi kwa kudhibiti mapato yanayotengenezwa na makampuni ya ulinzi binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo iwapo sitasemea suala linalompata mwenzetu Mheshimiwa Kadutu katika makazi ya wakimbizi kule Ulyankulu. Sisi tumekuwa na makambi ya wakimbizi kule Ulyankulu, Mishamo, Katumba na kwingineko. Wakimbizi hawa wanavyoishi na wanavyotenda ni kama vile wameanzisha nchi nyingine ndani ya nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakimbizi hawa wamefikia kiwango cha kuchagua nani awe kiongozi wao wa kisiasa kwa nafasi zote; Diwani, Katibu nani, hata Mbunge wanayemtaka wao. Vilevile bahati mbaya Mwenyekiti iko haja kubwa ya kuangalia maslahi wanayopata hawa wakimbizi ambayo sasa wako kama raia wa Tanzania; na hawa wanapata elimu bure, wanapata maji bure, wanapata chochote ambacho Watanzania wanapata. Imekuwa mbaya zaidi, inahofiwa kwamba hawa wanaongezeka kwa wingi sana lakini pia wanasoma sana wanapata hata mikopo ya elimu ya juu na vilevile kuingia katika nafasi za kazi muhimu sana kwa ajili ya Tanzania. Hii ni hatari kwa usalama wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo ya kuchangia. Nakushukuru sana kwa muda ulionipa. Ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nami nichangie hoja hii ya hotuba ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia. Nami nitachangia mambo mawili tu. La kwanza, nitatoa shukurani kwa ajili ya kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, lakini nitachangia sana kwenye sera ambayo itakuwa na vijpengele viwili; kipengele cha Elimu ya Fundi kama ilivyo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri lakini pia kipengele cha lugha ya kufundishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi kubwa kwa Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa fedha nyingi ambazo amezitenga kwa ajili ya Wizara hii. Fedha nyingi ambazo zimefika ni pamoja na elimu bure na ujenzi wa shule, ujenzi wa madarasa na kwangu katika Jimbo langu la Tabora Kaskazini Uyui, tumepata fedha za kutosha karibu shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi ya shule za high school na shule za msingi na shule za sekondari. Kwa hilo nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na watendaji wote katika Wizara hii Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye sera. Nianze kwa ufafanuzi wa maneno ambayo yamekuwa hayaeleweki; na katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna baadhi ya ufundi hakuutaja kabisa; na ndiyo ilivyo katika Wizara ya Sayansi na Teknolojia. Kwa hiyo, nianze na Technical Colleges (Vyuo vya Ufundi). Hivi vinazalisha mafundi wanaitwa technicians au kwa Kiswahili ni Fundi Sadifu; na hili Mheshimiwa Waziri hakulitaja kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna vituo vya ufundi vinaitwa VETA kwa Kiingereza. Hivi vinazalisha Artsans ambao ni Fundi Mchundo. Sasa taaluma nzima ya fundi inafanya kazi hivi: Juu tuna engineer, wanatafuata technician halafu Artsans. Ni kama vile madaktari, ukiwatoa ma-nurse pale hawafanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka wataalam wa elimu wamweleweshe vizuri Waziri wangu. Waziri ametoka kwenye ule mfumo wa kuanzia form one, form five, form six, university. Na sisi tumetokea shule za ufundi miaka minne ya ufundi uliochagua kama ni umeme au Civil Engineering halafu unaenda Technical College miaka mitatu unachukuwa FTC, unatoka kwenda kufanya kazi, unarudi unachukua Diploma in Engineering (DE) miaka mitatu, unakuwa na miaka kumi katika ufundi ambao umeusomea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, field hii ikifa tutafanya jambo ambalo haliwezekani. Wahandisi hawawezi kufanya kazi na Artsans. Kwa hiyo, kunakuwa na engineer huku kichwani, kiwiliwili hakuna, kuna miguu (Artsan) kule chini. Kwa hili lazima lisahihishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba nzima Mheshimiwa Waziri ameongelea mambo ya vyuo. Neno “vyuo” akiwa na maana ya vituo vya VETA. Tunajenga vyuo vingi; hatujengi vyuo vingi, tunajenga vituo vya VETA. Vyuo vya ufundi ni Dar Tech. ilivyokuwa nao wakapelekwa watu pale wakajaribu kuifanya iwe University College au University. Ikaacha mfumo mzima wa ufundi ikaenda kwenye mambo ya academicians. Halafu kimebakia chuo kimoja Arusha Technical College, maana yake hata Mbeya mmebadilisha, siyo college ya ufundi, imekuwa University. Matokeo yake tunakuwa na white collars hatuna Blue collars katika engineering na jambo hilo haliwezi kufanikiwa hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba, kwangu nina shule 22 za secondary school na nina shule za msingi 222, hatuna chuo cha VETA. Vyuo vya Ufundi nafikiri nisimseme sana Mheshimiwa Waziri wangu, amenielewa; ni kwamba hakuna vyuo vya ufundi vinavyozalisha technicians wanaoitwa Fundi Sadifu. Fundi Sadifu ni tofauti na Fundi Mchundo. Serikali inajenga Vyuo vya Ufundi Mchundo ambapo katika elimu tunakokwenda huko kwenye Sera ya Uchumi na Viwanda hawatatusaidia Artsans, tunahitaji Fundi Sadifu (Technicians) hili lisahihishwe mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaotuna wengi hapa, humu tuna mafundi; mimi ni fundi tena mkongwe. Wamo mafundi wengine kumi humu ndani tumetokea Ifunda au Moshi Technical, au Tanga Technical au Mtwara Technical College, tukasoma FTC halafu tena tukarudi, tukachukuwa Diploma…

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa. Nataka nimpe taarifa muongeaji.

MWENYEKITI: Unataka umpe taarifa eeh! Mheshimiwa Maige, mnakutana mafundi mchundo.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba ameitaja Arusha Technical. Hiyo Arusha Technical College sasa hivi kuna kozi ya kusuka nywele. Kwa hiyo, tunakwenda kuharibu utamaduni ule wa ufundi. Kuna kozi za kusuka nywele, kuna shule upishi. Wakati mimi nipo pale Arusha Techn. Zile kozi hazikuwepo. Sasa hivi tunaanza kuwachanganya, hatuwezi kupata mafundi kwenye style hiyo. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Almasi.

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni sawa kabisa, nakubali, huyo ni Fundi Sadifu mwenzangu (technician).

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niendelee kwenye suala la lugha ya kufundishia. Nimesema naongelea mambo mawili tu; kwa ufundi nafikiri niishia hapo, lakini nijikite hasa katika suala la lugha ya kufundishia. Suala hili limo katika Sera ya Elimu na limeelezwa vizuri sana katika sura ya tatu ambayo inahusu mambo ya maazimio na malengo na lugha ya kufundishia. Ninayo Sera ya Elimu hapa ya mwaka 2014 ukurasa wa 38 inasema: “lengo ni kutumia lugha ya Kiswahili katika kufundishia.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maelezo, lakini muda sina, ila wenye sera hii wakasome sura tatu ukurasa wa 37 mpaka 38. Sasa naomba ni nukuu: “lengo la kutumia lugha ya Kiswahili katika kufundishia.” Tamko, nasoma kipengele cha 3, 2 na 19. “Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumiwa kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu na mafunzo na Serikali itaweka utaratibu wa kuwezesha matumizi ya lugha hii kuwa endelevu na yenye ufanisi katika kuwapatia walengwa elimu na mafunzo yenye tija Kitaifa na Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo tafiti zaidi ya 30 kwa muda wa miaka 45, zote zinasema: “mtoto yeyote ataelewa masomo vizuri kama atafundishwa kwa lugha ya kwanza au ya pili ya mtoto huyo.” Tafiti zote zimesema Kiswahili ndiyo lugha ya kwanza au ya pili kwa Watanzania wote. Kwa hiyo Kiswahili ndiyo lugha pekee inayofaa kufundishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hilo, kipo kipengele kidogo cha mistari mitatu kimechomekwa hapa, naomba nikisome. Ni kipengele cha 3.2.20: “Serikali itaendelea na utaratibu wa kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiingereza katika kufundishia na kujifunzia, tena katika ngazi zote za elimu na Mafunzo.” Hivi vipengele viwili vinagongana na matokeo yake, imeacha nchi nzima isieleweke tunatumia lugha gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hilo, napenda kusema yafuatayo: kwa kuwa tafiti zimeonyesha kuwa Kiswahili ndiyo lugha ya kwanza na inazungumzwa na Watanzania wote ikitumika kufundishia, kujifunzia elimu na maarifa mafunzo, yataeleweka zaidi kwa walengwa; kwa kuwa Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa na Tunu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo haya ya kwenda kutumia Kiswahili; na tatu, kwa kuwa tafiti zaidi ya 30 zilizofanyika katika miaka zaidi ya 40 zimeonyesha kuwa Kiswahili ndiyo lugha inayofaa kwa Tanzania kufundishia na kujifunzia; na kwa kuwa nia ya mabadiliko ya lugha ya kufundishia na kujifunzia ni pamoja na kuimarisha mbinu za kufundishia Kiingereza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie; na kwakuwa muda sasa wa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi zake kubwa za kukithamini na kukikuza Kiswahili. Hivyo, kitumike Serikalini, Bungeni na kuwa lugha ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu na mafunzo nchini. Serikali ilete Bungeni hoja…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maige.

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tabora Kaskazini lina kituo kimoja tu cha afya. Namwomba sana Waziri tuipandishe hadhi Zahanati ya Ilolangulu iwe kituo cha afya ili kwa jumla tuwe na vituo viwili vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya, hongereni sana. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwajali wanyonge, Wilaya ya Uyui tumepewa Hospitali ya Wilaya inayojengwa kwa shilingi bilioni 1.5 pia Kituo cha Afya cha Upuge kwa shilingi milioni 500. Namkaribisha Mheshimiwa Waziri atembelee Jimbo langu na Kituo cha Afya cha Upuge lakini pia Zahanati ya Ilolangulu ili ajionee mwenyewe ujenzi uliofanyika hasa katika zahanati na akiridhia kiwe kituo cha afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba gari la wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Upuge.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, kwanza nawapongeza Mheshimiwa Waziri Kamwelwe na Naibu Mawaziri; Mheshimiwa Kwandikwa na Mheshimiwa Nditiye kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, kuna shida kubwa ya kukosa minara ya mawasiliano Kata za Shitage, Igulungu na Makazi. Naomba minara katika kata hizo.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Tabora – Mrambali – Ishitimulwa - Mhulidede ni muhimu kuwa na lami. Barabara hii muhimu kwani inaunganisha Mikoa ya Shinyanga na Tabora.

Mheshimiwa Spika, pongezi kwa Mamlaka ya Mawasiliano TCRA. TCRA wamefanya kazi kubwa ya kubadili mawasiliano na matangazo ya TV kutoka analojia na kuwa digitali na kuwa moja ya nchi za kwanza Barani Afrika na ya kwanza EAC. Vilevile wanasimamia mgawanyo wa masafa (frequency monitoring) na ugawaji bora wa leseni za redio na televisheni. TCRA wamefanya kazi kwa weledi sana kusimamia mashirika ya huduma za simu na kuhakikisha wanalipa kodi za Serikali kwa kutumia mtambo wa TTMS.

Mheshimiwa Spika, natanguliza shukrani.
Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kinga na Maslahi ya Kidiplomasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (The East Africa Community Protocol on Information and Communication Technology)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kinga Maslahi ya Kidiplomasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tukumbuke ilitokea nini mwaka 1977 wakati hapakuwepo Itifaki kama hii kwa ajili ya Kinga ya mali za Jumuiya, Watumishi wa Jumuiya na maslahi mengine ya Kijumuiya zikiwemo fedha nakadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ilikuwa mbaya Jumuiya ilipovunjika nchi wanachama ambao walikuwa na mali nyingi au chache walizuiwa zile ambazo walizokuwa nazo, kwa hiyom nchi nyingine zilipata hasara ikiwemo Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Itifaki hii nianze na Ibara ya 4 ambayo inaongelea kulinda mali za Jumuiya na Ibara ya 5 kulinda fedha za Jumuiya kutonyang’anywa fedha na kutotaifishwa mali lakini pia Ibara ya 8 inaongelea kulinda maslahi ya Watumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao jambo hili lilitokea bahati mbaya mwaka ule ilipovunjika 1977 hapakuwa na Itifaki ya hivi Watanzania ambao walikuwa wanafanya kazi kwenye Jumuiya mpaka leo hawajalipwa hela zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hizo ambazo zimezitaja na Ibara hizo ambazo nimetaja katika Itifaki hii naunga mkono Bunge lako kuridhia Itifaki hii ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Kalemani na Naibu Waziri Mheshimiwa Mgalu, wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia kuhusu mradi wa REA. Liko tatizo eneo langu la Tabora Kaskazini. Mkandarasi hafanyi vizuri, kasi yake ni ndogo sana. Niliomba kipaumbele eneo la vijiji anavyotoka Mbunge ambako kuna vijii barabarani; Vijiji vya Kasenga, Majengo, Kanyenye, Ikongolo, Nzubuka na Izugawima. Vijiji hivi vyote viko barabarani na ndiko Mbunge anakotoka.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri rafiki yangu, ndugu yangu niletee umeme katika vijiji hivyo ni muhimu sana. Kuna shule za msingi tano na shule za secondari mbili na zahanati pekee katika kata hiyo ya Ikongolo. Nakushukuru sana sana Mheshimiwa Waziri tafadhali sana; vijiji vya Kasenga, Majengo, Ikongolo, Kanyenye na Nzubuka ni muhimu sana. nakuomba Mheshimiwa Waziri Kalemani. Natanguliza shukrani.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hoja iliyopo, hoja ya Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Kwanza niwashukuru sana vingozi wote wa Wizara ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuleta mpango huu wa kujivunia, Mpango ambao unasomeka na kueleweka vizuri, lakini Mpango ambao umebeba matakwa yetu Wabunge kama ambavyo tulipendekeza kwenye pendekezo la awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango umegusa maeneo mbalimbali na miradi ya kimkakati. Miradi ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa reli ya kati, ujenzi wa mradi wa umeme, mradi wa Mwalimu Julius Nyerere huko Rufiji utakaozalisha umeme wa megawati 2015. Pia ufufuzi wa ndege za Shirika la Ndege, ununuzi wa ndege mpya, mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ambao limepitia kwetu likitokea Uganda na vilevile kuendelea na kutoa elimu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo pia ujenzi wa barabara na miradi ambayo imekusudiwa kumaliziwa katika mpango huu. Sisi Tabora tunajivunia Mradi wanaomalizia sasa wa Maji ya Ziwa Victoria, maji yanayochukuliwa kutoka Ziwa Victoria kuja Tabora imekuwa jambo kubwa sana kwetu na ningependa sana kuipongeza Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mpango huu umelenga kuendeleza na kukuza uchumi wa nchi yetu na kuwa kinara katika Afrika Mashariki na kwa kweli katika Afrika kwa kukuza uchumi wa asilimia 7.1, jambo hili sio rahisi na lilikuwa kama njozi tulipolifikiria hapo mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii imefanya mengi katika mpango huu uwezo wa kiuchumi na mimi nasema anayemulika nyoka anaanza miguuni mwake, sisi tumeguswa sana katika ukuzaji wa uchumi katika jimbo letu. Jimbo la Tabora Kaskazini limepata moja ya vituo vya afya na pia tumepata hospitali ya wilaya, vilevile hivi karibuni naipongezza Serikali kwa kunipa Chuo cha VETA na hili ni muhimu sana kwetu sisi kwa sababu jimboni kwangu kuna shule za sekondari nyingi na kuna shule za msingi nyingi lakini kuna high school moja tu ya Ndono, kwa hiyo vijana hawa watakaosoma VETA watatusaidia sana kukuza uchumi katika maeneo ya vijijini ambako ningependa pia kuipongeza Serikali kuleta mpango wa umeme wa REA. Umeme wa REA, ambao utakuza uchumi katika vijiji vyetu na wale vijana ambao tutawaandaa katika vituo vya VETA wanaweza kusaidia kukuza uchumi vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 16 naipongeza Serikali kupanga kipaumbele cha hela za maendeleo na hela zimepangwa katika miradi ambayo itakuza uchumi. Katika ukurasa huu wameelezea vizuri sana jinsi ambavyo hela zitapelekwa kwenye miradi ya kimkakati kama reli, barabara, viwanja vya ndege na hivi karibuni tumemalizia terminal III. Naipongeza Serikali kwa sababu katika mradi huo walifikiriwa pia makandarasi wa nchini hapa, naomba ku-declare interest kwamba nilikuwa mmoja wa makandarasi waliojenga terminal III Kiwanja cha Ndege Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii inatoa ajira kwa wananchi Watanzania vilevile inaweka miundombinu ambayo itadumu pia inakuwa chanzo cha mapato ya Serikali. Kumekuwa na maneno kuhusu ilipotolewa taarifa kwamba kwa kipindi fulani Shirika la Ndege uwekezaji mkubwa ule tulipata bilioni chache, lakini napenda kusema kwamba aliyetoa maneno hayo kwamba ndege imeingiza hela kidogo hakuwa na uga mpana wa busara yake kwa sababu ndege inafikiriwa yenyewe, sisi tulipokuwa tunawekeza kwenye ndege ilikuwa na maana ya ndege iwe chanzo cha mapato mengine. Kwa mfano kuleta watalii, kubeba mizigo vilevile kuonyesha kwamba sisi Tanzania tuna uwezo, wanasema watu the bigger the castle the stronger the can, kuonekana kwamba tuna ndege zetu pia thamani yake ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali katika Mpango huu imeelezea kuendelea kujenga na kumalizia hospitali za wilaya na vituo vya afya. Pia ukurasa wa 74, Mpango huu umeeleza jinsi ya kushirikisha sekta binafsi na hapo ndipo nami na-declare interest kwamba mimi pia ni mwajiri na katika Mpango huu Serikali imesema itawahusisha sekta binafsi katika kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kusema kwamba jambo kubwa linalotusumbua Mheshimiwa Waziri afikirie jinsi ya kurahisisha ufanyaji wa kazi yaani easy of doing business. Hii itatusaidia sana sisi waajiri wa Tanzania, tunalo tatizo kubwa la SDL kwamba kila mwajiri anamlipia kila mfanyakazi kiwango cha asilimia 4.5 cha mshahara wake kama tozo ya ujuzi na hii inatusumbua sana kwa sababu ni moja ya mambo yanayofanya sisi Tanzania tusiwe na ile fursa ya easy of doing business na kila mwaka tunaporomoka, kwa hiyo hatuwezi kushindanishwa katika ajira za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunaomba sisi waajiri kwamba ni bora SDL hii, tozo hii ya ujuzi ipunguzwe kutoka asilimia 4.5 ikaribie asilimia 2.0 na hii itatusaidia sisi kupata kazi katika maeneo mengine, lakini ni vigumu kupeleka wafanyakazi wako kutoka hapa kwenda kufanya kazi Uganda au kufanya kazi Kenya kwa sababu wage bill yako itakuwa kubwa kuliko wenzetu kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tumelilalamikia sisi waajiri ni Worker’s Compensation Fund. Tungependa tozo hii ya malipo ya mfanyakazi kuumia kazini ikadiriwe au ifikiriwe kutoka na uwezo wa shirika au mwajiri kwa mfano kama mwajiri anafanya kazi za hatari na likely hood uwezekano wa mfanyakazi kuathirika atozwe tozo kubwa kwa sababu ya kuweka akiba baadaye. Pia kuna kazi za salama kabisa na hazina tatizo na kwa kweli historia ya kazi hizo haijapata kuleta matatizo kwa wafanyakazi wake, kwa nini atozwe sawasawa tozo ya worker’s compensation. Wakati Mfuko huu umeanzishwa kulikuwa na utafiti unaofanywa ili kuweza kugawa madaraja ya Worker’s Compensation Fund, tozo ile ya asilimia 1.0 mpaka asilimia 2.0 kutegemea shughuli na utendaji wa mwajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mpango huu umeendelea kufikiria kukuza kuendelea kulipia shule bure, elimu bure ya msingi yaani darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Hili ni jambo muhimu, lilipoanzishwa lilionekana kama haliwezekani, lakini Mpango huu unathibitisha kwamba jambo hili litaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia hayo tu. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuwa mtu wa kwanza kabisa kuchangia Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa kipindi cha Februari, 2019 mpaka Januari, 2020.

Mheshimiwa Spika, acha nijikite kwenye Wizara zote tatu kwenye mambo muhimu ambayo nilifikiri kwamba yanahitaji kusukumwa ili kuleta ufanisi katika Wizara hizo. Naomba nianze na Wizara ya Mambo ya Ndani na nianze na kipengele kile cha Sekta ya Ulinzi Binafsi.

Mheshimiwa Spika, Makampuni ya Ulinzi Binafsi yalianza hapa nchini mwaka 1980 yakiwa na makampuni mawili tu; Ultimate Security na Group Four. Makampuni hayo yamezidi, leo hii yako 2,000 na zaidi, yakiajiri askari walinzi wanaozidi 200,000, karibu 250,000.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sekta hii ilianza miaka 40 iliyopita na haina sheria yoyote, haina miongozo yoyote, haina kanuni yoyote, wala ilipoanzishwa haikuwa hata na GN. Kwa hiyo, ilianzishwa tu na matakwa ya aliyekuwa IGP Philemon Mgaya kutokana na ombwe la kuhitaji ulinzi baada ya Serikali kubadilisha Sera ya Mali kutoka mali za Serikali na kuwa mali za watu binafsi zilizokuwa zimetaifishwa wakati ule na mashirika mapya yaliyoanzishwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa muda wa miaka yote hii makampuni haya yaliyoanzishwa kwa kanuni kwamba walioanzisha walikuwa ni Askari wastaafu wakiwa na miaka 60 na leo kama bado wapo wana miaka 100; kwa hiyo, makampuni haya yameendeshwa kwa kurithiana.

Mheshimiwa Spika, waliorithi makampuni haya huenda hawana hata ujuzi kabisa wa Sekta ya Ulinzi Binafsi, kwa hiyo, wanakamata silaha, wana bunduki, na kadhalika, lakini vibali vilivyokuwa vinatoka havikuwa na kanuni yoyote ya kusema kampuni, mwenye kampuni, mradi yeye alikuwa Askari. Bahati mbaya walipofariki, wamerithi watoto, wamerithi wake zao na ndugu wengine ambao hawana taaluma ya ulinzi. Kwa hiyo, uko umuhimu sasa wa kuanzisha au Bunge lako litunge sheria ya sekta ya ulinzi binafsi.

Mheshimiwa Spika, nilifanya juhudi kubwa ya kuleta Sheria ya sekta ya Ulinzi Binafsi hapa Bungeni; nikaleta Ofisini kwako na baadaye Serikali wakaichukua wakasema wangeileta hapa Bungeni kwa sababu ni muhimu sana na imetokea hivi karibuni mali nyingi za binafsi na miradi inahitaji ulinzi na makampuni yamejiimarisha kuleta wataalam wengine kutoka nje wenye uwezo mkubwa, makomandoo, wengine wakiwa ni Askari wenye rank za juu.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri makampuni yameanzishwa na wataalam waliokuwepo wakati ule, ma-IGP wote waliostaafu wameanzisha makampuni ya ulinzi, viongozi wengi wa majeshi wameanzisha kampuni za ulinzi, lakini hakuna sheria ya kuya-control makampuni haya jinsi ya kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri na Kamati ilishauri kwamba sasa umefika wakati Serikali ilete sheria ile ambayo inaishikilia mpaka sasa. Kwa hiyo, nategemea Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa ajaribu kutueleza sheria hii muhimu ya Sekta ya Ulinzi Binafsi inakuja lini Bungeni ili tuweze kuipitisha na baadaye itumike kwa ajili ya kuyaongoza makampuni? Hatuwezi kuyafukuza makampuni ya ulinzi, hatuwezi kuifunga Sekta ya Ulinzi Binafsi, ila tunaweza kui- control kwa kutumia sheria.

Mheshimiwa Spika, liko suala la NIDA. Katika Wizara ya Mambo ya Ndani, Taasisi ya NIDA imepewa jukumu la kugawa vitambulisho katika nchi yetu kwa wananchi wote nchini, lakini nasikitika sana NIDA imekuwa tatizo kubwa sana ambalo ni kichomi ambacho kimeshindwa kutatulika. Serikali imesaidia sana kuwapa fedha, lakini hatuelewi!

Mheshimiwa Spika, NIDA au Kitambulisho cha Taifa vijijini, nafikiri mpaka tutazeeka, tutaondoka wananchi wa Tanzania nzima hawatapata vitambulisho kwa sababu, hakuna msimamo au mkakati maalum wa kwenda vijijini kama ambavyo daftari la kupiga kura limeenda. Wananchi wote wanaotaka kupiga kura wamepata kadi za kupigia kura.

Mheshimiwa Spika, ulikuwa ni mpango mzuri wa NEC uliofanyika kufika vijijini. NIDA kijijini kwangu katika Jimbo langu sijawaona, hawajaenda, lakini wameenda sehemu ndogo tu, yaani sehemu za miji, basi. Hili limekuwa tatizo kubwa, limejitokeza hata wakati wa kusajili simu kwa vidole ambapo ilikuwa ni lazima NIDA uwenayo, imeonesha ni kiasi gani tatizo ni kubwa. Tusingejua kama tatizo ni kubwa kama kusingekuwa na kusajili line za simu. Kwa hiyo, nashauri na Kamati yetu imeshauri kwamba NIDA waje na mkakati mpya wa kufikia sehemu zote za vijiji.

Mheshimiwa Spika, liko suala lingine la wakimbizi. Wakimbizi kwa uungwana wetu Serikali iliwapa uraia, lakini bahati mbaya sana ikawaacha kwenye makambi yale yale waliyopatia uraia na wameanza kujiunda na kuunda na kuelewana wenyewe kwa wenyewe na wana mpango hata wa kuwa na Serikali yao ndani ya eneo lile walilomo; na kumekuwa na utata mkubwa sana, wakimbizi hawa sasa wanaishi kama raia wa Tanzania wa kawaida na wanasoma sana, wanajiingiza kwenye sehemu nyingine za kazi, sehemu za majeshi na sehemu za elimu ya juu.

Mheshimiwa Spika, tatizo linaonekana kwamba kwa vile wanakaa pamoja pale pale, mkakati wa kuwasambaza wakimbizi hawa ni suala la muhimu sasa ili wasije wakakaa na kuunda mkakati ambao utakuja kuleta hasara kwenye Serikali yetu na wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwenye shughuli za kazi za Wizara ya Mambo ya Nje tuliongelea mambo ya mipaka yetu na tuligusa mpaka wa Uganda ambako kumekuwa na utata wa nyuzi ngapi mpaka wa Tanzania unapita, lakini pia suala la mpaka wa Malawi, iko haja sasa Wizara ya Mambo ya Nje ione umuhimu wa kuweka mipaka katika maeneo ambayo tunafikiri kwamba yana utata katika Ziwa Nyasa na kule Uganda.

Mheshimiwa Spika, mwishoni nitoe shukrani kubwa, sikupata nafasi ya kuongea wakati wa sekta hizi nyingine. Nitoe shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Joseph John Pombe Magufuli pamoja na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambayo imeleta maendeleo makubwa katika Jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu tumepata Kituo cha Afya kimoja kwa gharama ya shilingi milioni 850; pia, tumepata Hospitali ya Wilaya kwa shilingi bilioni mbili. Vile vile tumepata mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria ambao utakuwa kwenye vijiji 40, kwenye 500 vijiji 80. Pia mradi wa REA una vijiji 18 katika vijiji vile 82. Tunaomba basi tuongezewe idadi ya vijiji ambavyo vitapata umeme wa REA.

Mheshimiwa Spika, pia tumepata mradi wa Kituo cha VETA kwa shilingi bilioni tano na sasa hivi kuna mpango wa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi ambayo itagharimu mabilioni mengi. Yote haya kwa kweli yamekuwa njozi tulikuwa tunaota, lakini kwa kipindi cha miaka minne Mheshimiwa Rais ametuletea mambo haya yote. Wananchi wangu wanafurahi sana, wanamshukuru sana na wanamwombea maisha marefu Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya Wizara ya Nishati iliyoko mezani kwetu sasa hivi. Kwanza natoa shukrani sana kwa Wizara hii na watendaji wa Wizara, Mheshimiwa Waziri Kalemani, Mheshimiwa Mgalu na Mheshimiwa Mwinyimvua kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya katika kazi kubwa ya kueneza umeme na kuondoa blanketi la giza katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii imeondoa mgawo ambao ulikuwa tatizo kubwa sana miaka iliyopita na kwa kweli, wanastahili sifa kubwa, lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuthubutu kujenga Kituo Kikubwa cha Umeme pale Mto Rufiji. Suala hili litatatua matatizo yote na itakuwa mfano katika nchi za Afrika Mashariki, nchi yetu itakuwa na umeme wa kutosha kwa hiyo, kwa uwekezaji wa viwanda na kukidhi haja ya kuwa na siasa ya viwanda mwaka 2025 na kuwa siasa ya nchi ya kati kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wameongelea Wabunge wengu kuhusu suala hili la kinu cha umeme huko Rufiji, leo nijikite katika kituo katika Mradi wa REA. mradi wa REA ambao Wizara hii inausimamia ni kichocheo kikubwa sana cha maendeleo vijijini, laki I mradi huu hauendi vizuri, mradi huu sasa umekuwa ni tatizo la Waziri, Waziri amekuja kwangu ameubeba mradi huu kama wa kwake mara tatu, lakini akiondoka Mheshimiwa Waziri huyu namshukuru sana, wakandarasi wanalala. Hatuoni maendeleo ya mradi huu vijijini kwetu, sehemu kubwa ya vijiji vyangu vyote havina umeme na sehemu ndogo iliyotiwa umeme haujawashwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na nguvu za Mheshimiwa Waziri kuja kwetu, lakini wakandarasi wanamuangusha na ningependa atakapokuja Mheshimiwa Waziri kufanya majumuisho aje anieleze katika Jimbo la Tabora Kaskazini au Wilaya ya Uyui vijiji gani vina umeme au vina mpango wa kuviwekea umeme kwa sabbu, imekuwa kero tunausikia umeme wa REA kwa wenzetu sisi kwetu hatuuoni umeme huu, hata nguzo haziji. Nimeshaongea na mkandarasi ananiambia tatizo kubwa ni nguzo, lakini nguzo zimeshapatikana, tatizo ni nini katika kuendeleza mradi wa umeme katika eneo langu?

Mheshimiwa Spika, wananchi wanalalamika sana, wanafurahi wanapomuona Mheshimiwa Dkt. Kalemani amekuja, tunamshangilia, karibu tumpe na mke na mbuzi tumpe, akiondoka umeme unapotea. Tunaomba Mheshimiwa Dkt. Kalemani utakapokuja kuongelea mwisho wa majumuisho yako utuambie Umeme wa REA katika Wilaya ya Uyui na hasa Jimbo la Tabora Kaskazini mpango ukoje? Mbona hatuoni unaendelea?

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali yetu ina mipango mizuri na kama ilivyoweka kipaumbele katika kitabu hiki cha bajeti. Mipango yote ikikamilika nchi hii itakuwa mfano mkubwa wa kuwa na kiasi kikubwa cha umeme nchini, lakini pia tutapata faida kubwa kuuza umeme huu nchi za nje, jirani zetu, lakini vilevile sehemu kubwa ya umeme huu utachochea maendeleo ya viwanda ambapo Serikali itapata mapato, lakini utaleta maendeleo kwa wananchi wote.

Mheshimiwa Spika, sikuwa na mambo mengi zaidi ya malalamiko hayo ya REA, lakini kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa mpango mzuri wa kuleta umeme katika nchi yetu. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri wa Fedha na Mipango wakati wa majumuisho afikirie mambo yafuatayo:-

(a) Kupunguza SDL ili kurahisisha ufanyaji wa biashara nchini;

(b) Kupunguza matumizi ya Wizara Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuleta mpango wa kujenga nyumba za Ofisi za Balozi zetu kwa mkopo na benki kwa dhamana. Nyumba zitakazojengwa ndani ya miaka 10 tutamaliza madeni na kuwa na nyumba zetu;

(c) Serikali ifikirie kuirudisha VETA kuwa chini ya Wizara ya Kazi na Ajira katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili waajiri wanaochangia zaidi ya shilingi bilioni tisa kwa mwezi waone faida yake iliyokusudiwa hapo awali ya kuongeza ujuzi wa wafanyakazi. Waajiri hawaoni mantiki ya VETA kuwa chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; na

(d) Suala la REA haliendeshwi vizuri katika vijiji vya Jimbo langu la Tabora Kaskazini lenye vijiji 87 na REA III (I) nimepangiwa vijiji 18. Mpaka sasa ni vijiji vitatu tu ndiyo vimewashwa, Waziri wa Nishati aje na maelezo kwa nini mradi huu unaendeshwa bila uwiano katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha pamoja na kielelezo cha nafuu ya SDL kwa nia ya kuongeza mapato kwa Serikali.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kuniruhusu na mimi pia nichangie Bajeti Kuu ya Serikali yaani mapato na matumizi kwa mwaka 2019/ 2020.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kutoa pongezi sana kwa Wizara hii, hasa kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango, dada yangu, Mheshimiwa Dkt. Kijaji na Katibu Mkuu - Ndugu Doto James, na wengine wote wataalam wa Wizara hii ambao wamekaa na kuandaa bajeti hii ambayo kwa kweli imekidhi viwango, lakini pia imekidhi matakwa ya wananchi wa Tanzania na vilevile itatuvusha hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeshuhudia upande wa pili kule wanaongea mambo mengi sana. Jana mtu mmoja alijikita katika kusema kwamba Mheshimiwa Dkt. Mpango na mama yangu, Mheshimiwa Dkt. Ashatu hawafai na waondolewe katika nafasi hizo. Lakini hiyo ni dalili ya rangi mbili waliyonayo hawa wenzetu, wamesema sana, lakini mimi nashuhudia kwamba Mheshimiwa Dkt. Mpango na wenzake, timu hii ndiyo bora kabisa katika utawala wa Tanzania, na ninawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile wenzetu hawa kwanza wanasema bajeti hii imepangwa vibaya na Mheshimiwa Dkt. Mpango hafai, lakini ukikutana nao kule nje wanaungana na wananchi ambao wanasema bajeti hii ni nzuri sana. Kwa hiyo, wao wanashindwa kujifaragua peke yao wanajiunga na wananchi ambao wanasema bajeti hii ni nzuri na hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mpango na hasa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alimteua Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu wake kufanya kazi hii ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna sungura mdogo hatuwezi kumgawa watu wote sawasawa akatuenea na kushiba, lakini tukubali kwamba kazi hii siyo rahisi, mtu yeyote akivaa viatu vya Mheshimiwa Dkt. Mpango na mwenzake Mheshimiwa Dkt. Ashatu, atapata tatizo hili ambalo tunalipata kwamba hela hii haitoshi na kinachopatikana tunakigawa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye kuchangia bajeti hii na nianze na umuhimu wa sekta binafsi hapa nchini. Sekta binafsi nchini hapa ndiyo inayojenga vitega uchumi vikubwa, kwa mfano barabara na hivi karibuni viwanja vya ndege, na mfano Terminal III ambayo inakusudiwa kuingiza hela nyingi sana kutokana na ndege zitakazotua pale, watalii na abiria ambao watalipia gharama za kiwanja hicho. Na mimi ni--declare interest kwamba katika local content ya kiwanja hicho, Kampuni ya Ulinzi na Usalama iliyofunga mitambo pale ni SSTL Group ambayo ni kampuni yangu.

Mheshimiwa Spika, sekta binafsi pia inajenga vitega uchumi vingine kwa mfano reli inayojengwa na Yapi Merkezi ni kampuni binafsi, lakini vilevile umeme wa Rufiji unajengwa na sekta binafsi; lakini pia umeme wa REA nchini hapa unajengwa na sekta binafsi. Kwa hiyo sekta binafsi hii ina miradi mingine kadhaa. Namuomba Mheshimiwa Dkt. Mpango aipe umuhimu wake kama uti wa mgongo kama ambavyo katika nchi nyingine imepewa. Sisi hapa uti wa mgongo huu wa sekta binafsi umepinda na hauna nguvu yoyote na sasa unalegealegea sana. Mheshimiwa Dkt. Mpango, uimarishe sekta binafsi ya ulinzi ili iweze kuchangia barabara katika kukuza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu sana tumelisema sana na ni-declare pia mimi ni mwajiri vilevile ni suala la SDL. Mheshimiwa Dkt. Mpango hili tumelisema sana. Sisi tunashindwa kufanya biashara hapa kwa sababu ya kitu kinachoitwa ease of doing business; asilimia 4.5 ni kubwa kuliko SDLs zote duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa Afrika Mashariki ni Kenya tu wana-charge sekta ya utalii asilimia 1.2, kwingine kote Uganda hakuna, Rwanda hakuna, Burundi hakuna, kote na dunia nzima Tanzania ina-charge asilimia 4.5, ni kubwa sana. Tunaomba utakapokuja kufanya majumuisho yako, hebu fikiria upunguze hata kidogo. Tumetoka mbali, tulikuwa na asilimia sita, lakini tunakuomba uipunguze taratibu, hatusemi mara moja, lakini fikiria hata kupunguza kiasi kidogo, sisi waajiri na wafanyabiashara tutafurahi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala hili limeletwa pia Serikalini, katika mambo ambayo Mheshimiwa Rais alitaka yaletwe Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) na waajiri tumekuletea hili suala la SDL, lipunguzwe hata kidogo. Tafadhali utakapokuja kufanya majumuisho yako tupunguzie SDL kutoka asilimia nne kwa kiasi chochote kile ambacho utaona kwamba hakitaumiza bajeti.

Mheshimiwa Spika, lipo suala la VETA; VETA ilipobuniwa ilikuwa katika Wizara ya Kazi na madhumuni yake ni kufundisha wafanyakazi skills. Lakini sasa VETA imehamishiwa kwenye Wizara ya Elimu ambayo inafundisha elimu. Sisi waajiri ambao tunachangia mfuko huo kwa zaidi ya shilingi bilioni tisa kwa mwezi tunaona kama zile hela zinapotea. Lakini pia imekuwa inachukua watoto badala ya wafanyakazi ambao walikusudiwa kwenda kuongeza ubunifu na ujuzi.

Mheshimiwa Spika, lipo suala la REA; REA hii haiendi vizuri kwenye jimbo langu. Mimi nina vijiji 87, katika REA III(i) nilipewa vijiji 18 mpaka leo hii vijiji vitatu tu, Mheshimiwa Dkt. Kalemani vijiji vitatu tu ndiyo vimewashwa katika 18, asilimia 16, basi na muda unakwenda. Lakini mbaya zaidi hata nyumbani kwa Mbunge umeme hakuna, nimesema, nisemeje sasa ili mnielewe?

Mheshimiwa Spika, lipo suala la mwihso ambalo pia namuomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango alifikirie kupunguza matumizi. Balozi zetu kule nje tunapanga nyumba na nyumba hizi ni ghali sana. Asilimia zaidi ya 60 ya matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje inakwenda kupanga majengo na tunadaiwa hatupeleki hela kule, tujenge majengo yetu kwa njia ya mortgage. Tukianza kujenga majengo kwa muda wa miaka kumi kwa mkopo na tuna-mortgage majumba yaleyale, baada ya miaka kumi tutakuwa na nyumba zetu.

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri hapa Tanzania, Mabalozi wangapi wamepanga? Wamejenga nyumba zao na sisi tuone mbali, Mheshimiwa Dkt. Mpango, punguza matumizi ya Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kujenga nyumba zetu. Mimi nilikwenda kuangalia kiwanja ambacho tulipewa Muscat, kwa gharama yangu, nimefika kule Muscat jiwe la msingi limewekwa na Mheshimiwa Dkt. Kikwete. Leo huu mwaka wa ngapi tangu Mheshimiwa Dkt. Kikwete aondoke. Mpaka tunaona aibu tumekwenda kuondoa kile kibao limekuwa pori.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tulipopewa kiwanja cha Kenya tulibadilisha kiwanja cha Kenya Ubalozi hapa, wenzetu wamejenga Ubalozi wa Kenya wanafanya matengenezo ya kawaida. Sisi kile kiwanja cha kwetu Kenya mara kitakiwe kuuzwa, Mzanzibari mmoja akaenda kukichukua akapeleka mahakamani; kwa nini tusijenge nyumba zetu kwa mkopo kutumia mortgage system? Jambo hili litatusaidia sana kuondoa madeni yaliyopo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie bajeti hii. Naunga mkono hoja mia kwa mia. Ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hotuba hizi mbili za Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, lakini leo naziite alama za Mheshimiwa Dkt. Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amechora ramani ya maendeleo ya nchi yetu na katika ramani hiyo, ameweka alama na alama hizi ndizo tunazozifuata sisi. Alama ya kwanza ni umeme wa REA. Anasema ameweka umeme katika vijiji 9,884 na vimebakia vijiji 2,000 tu. Alama ya pili pia anajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere kule Rufiji; pia ameweka miradi ya maji 1,422 na vijijini asilimia 70 na mijini asilimia 80. Mfano huu ni Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria katika Mji wa Tabora, Igunga na Nzega na mradi huu umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, alama nyingine ni elimu bure kwa Watanzania. Watoto wote wa Kitanzania, darasa la kwanza mpaka form four. Pia anajenga vituo vya VETA na hivi vinakuza uchumi. Zamani ilikuwa ukiharibikiwa na gari vijijini unamtafuta fundi kutoka mjini aje atengeneze gari, lakini anaondoka na hela, vituo hivi sasa vinajenga mafundi vijijini. Majokofu, vitu vya umeme, wanachomelea ma-grill na fedha zinabaki kule, kwa hiyo, zinazunguka badala ya kurudi mjini. Kwa hiyo, tunakuza umeme vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, alama nyingine kubwa ni ununuzi wa ndege 11 kwa ajili ya Shirika la Air Tanzania. Pia kuhusu alama ya huduma ya afya, amesema katika hotuba zake hizi, Mheshimiwa Rais amejenga vituo vya kutolea huduma za afya 1,887; zahanati 1,198, Vituo vya Afya 487, Hospitali za Wilaya 99, Hospitali za Rufaa 10, Hospitali za Kanda tatu na wagonjwa kwenda nje wamepungua na kufikia asilimia 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, Jimboni kwangu kuna changamoto. Kwa mfano, Jimbo zima lina Kituo kimoja tu cha Afya na tungependa viongezwe. Kuna vituo vile tunajenga sisi wenyewe, tunaomba vituo hivi visaidiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kitaifa liko suala la Kiswahili. Wiki hii Kiswahili kimepandishwa hadhi kabisa kwamba Wizara moja tu Tanzania ilikuwa inatumia lugha ya Kiingereza katika maandishi yake, Mahakama. Juzi umetoka Mwongozo kwamba Mahakama sasa zitumie lugha ya Kiswahili kwa ajili ya kutoa hukumu zake. Naona haitoshi tu hiyo, kwa sababu Kiswahili kitaanzia juu tena. Waswahili wanasema mtaka unda haneni, lakini mimi leo nanena hata kama litaharibika, watu wenye roho mbaya, ndiyo maana methali hii ipo. Nina nia ya kuleta tena hoja ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika shule zetu za msingi na sekondari. Hili litakuwa jambo zuri kwa sababu sasa hivi tutajenga Kiswahili kuanzia shule za msingi, sekondari na matumizi yake yatadumu vizuri katika taasisi zote katika mihimili yote mitatu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitasema hayo tu, nilikuwa nimekusudia kutaja hizo alama za Mheshimiwa Rais. Nakushukuru sana kwa kuniruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie katika Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria wa mwaka 2017. Nilitegemea Wabunge wote kuanzia jana na leo tungekuwa na furaha kubwa kwa sababu tunajaribu kusaidia Serikali kupitisha Muswada wa Sheria ambayo imeokoa na kutupa nguvu sana Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kifungu cha tano (5) cha Muswada huu Serikali imetuletea mapendekezo ya kuchukua uwezo wa madini ya uchumi wetu wote kuuweka mikononi mwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukiondoa Sehemu ya Kwanza ambayo ina tafsiri ya madini na maliasili ni nini na utendaji, Sehemu ya Pili ya Muswada huu imeleta marekebisho ambayo yatasaidia sana kumiliki madini haya. vilevile kuwa watu wa kwanza katika bara letu ambao tunajitetea kwa sheria yetu wenyewe kuweza kumiliki madini haya na kuweza kuyazuia yasitoke nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sehemu ya Tatu inaanzisha pia Kamisheni ya Madini na Kamisheni hii imepewa kazi maalum na kuondoa jukumu lote lililokuwa la mtu mmoja mmoja, Waziri na sasa utendaji na usimamizi wa madini haya utakuwa chini ya Kamisheni na chini ya mwongozo utakaotolewa na Baraza la Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzishwa kwa hifadhi ya madini na kuanzishwa pia clearing houses itasaidia sana kuweza kuyaona madini tangu yanapotoka mpaka yanapowekwa na kuyazuia yasitoke nje bila kujulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 20 na Ibara ya 21 imeanzisha Kamisheni ambayo itakuwa na msimamo na uongozaji wa madini, pia itaanzishwa kwa watu ambao wana uwezo. Atakuwepo Katibu wa Hazina, Katibu wa Ardhi, Katibu wa Wizara ya Ulinzi na TAMISEMI, watu hawa wamewekwa pale kimkakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nijikite sana kwenye sehemu ya local content. Kwa miaka mingi hawa watu wa
madini wamekuwa wakitumia huduma kutoka nje na imekuwa ndiyo sehemu kubwa sana iliyofanya sisi tushindwe kupata mapato ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, local content inayoongelewa hapa sasa ni huduma zote ambazo zinatoka nje zipatikane hapa ndani, zikiwemo huduma za ulinzi, insurance, financial, mambo ya sheria, mambo ya fedha pia mambo ya huduma za chakula (catering), mambo hayo yote yamekuwa yanatumika kama sehemu ya kutorosha mapato au ya ulinganifu mizania kati ya mapato na faida ili watu wenye migodi wasilipe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, limejitokeza suala la kutoiheshimu au kutoiamini Taasisi ya Mheshimiwa Rais. Naomba niwaambie wananchi na Wabunge wenzangu kwamba hatuwezi kuanzisha kitu kwa kupapasa tena. Kwa miaka yote karibu 57 na 60 ya uhuru wetu tumekabidhi ardhi yetu na vitu vyote kwa Taasisi ya Rais na hatujapata matatizo katika kukabidhi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya mpango na kwa sababu muda ni mchache nitajikita kwenye mambo mawili tu, nayo ni elimu na lugha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni zao la shule ya ufundi, tulisoma sisi kutoka Moshi Technical, kutoka Ifunda tukaenda technical college, tukatengeneza watu wanaoitwa FTC (Full Technician Certificate) na hawa ndio waliojenga viwanda, waliofanya kazi kwenye viwanda mpaka vilipokufa, lakini sasa elimu ya ufundi imekuwa hadithi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea uchumi wa viwanda, kama hakuna mafundi wa kutengeneza mitambo ndani ya viwanda hivyo, vitakufa. Ni sawa na magari yetu haya, kama hatuna garage ya kupeleka na mafundi wakawepo huko, magari hayawezi kuwa magari. Tulikuwa na mfumo mzuri sana wa elimu, kutoka shule za sekondari ufundi, form one mpaka form four unasoma umeme, unaenda technical college unasoma umeme, unamaliza FTC unarudi tena kusoma engineering, umeme miaka kumi mtu huyo anafanya kazi kiwandani kwa kujiamini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili limekufa toka marehemu Mungai alipofuta vyuo vya kati hapa akafuta na FTC, sasa tunafanya nini tunaendelea kukuza VETA na nashukuru sana VETA zinatengeneza mafundi wa vijijini, kwa hiyo uchumi utakwenda vijijini watatengeneza magari kule, watatengeneza mavitu ya umeme na kadhalika, kwa hiyo, watapata hela vijijini na uchumi utakua vijijini. Hata hivyo, hawa hawatafaa kiwandani, wako chini au ni wa ngazi ya chini ya ufundi unaoitwa artsan. Baada ya artsan kuna FTC halafu ndio kuna engineer pale juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa kazi ndiyo huwa unafanyika hivyo, engineer anafanya kazi na watu technicians 25, technician mmoja na Artsans 25, ndipo unakuwa mfano wa ufundi. Sasa viwanda hivi ambavyo tunakusudia vikuze uchumi, lazima tuwe na elimu ya ufundi ambayo itaendana sawasawa na uchumi tunaoutaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba chuo cha ufundi kianzishwe upya, DIT, sio chuo cha ufundi sio technical college imekuwa academic institute, Dar es Salaam Institute of Technology haitengenezi watu wa FTC blue color tunatengeneza white color. Kwa hiyo, degree, narudia tena degree, hazitatusaidia kukuza uchumi na ndio maana ziko nyingi mtaani zinatafuta kazi. Tunataka technicians, fundi sadifu na fundi mchundo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hatua ya pili, lugha ya kufundishia, kote duniani, hakuna nchi iliyoendelea kwa kutumia lugha ya watu wengine. Tunataka Kiswahili kitumike kwenye lugha ya kufundishia, shule ya msingi mpaka secondary school. Hivyo wanafunzi watakuwa na fursa ya kujifunza taaluma, sio kujifunza lugha. Tunataka Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kichina vifundishwe kama lugha katika shule zetu, lakini lugha ya kufundishia elimu iwe Kiswahili. Na- declare interest nitaleta katika Bunge lako hoja ya…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maige, ku-declare interest ni nini kwa Kiswahili? (Kicheko)

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena, nataka kuelezea maslahi yangu ya hapo baadaye kwamba, nitaleta hoja binafsi kama Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia elimu yetu. Nilifanya research ndogo au tafiti mdogo tu utafiti mdogo wa Kiswahili kinafaa kufundishia au hakifai, watoto wanielezee jinsi ya kupanda muhogo, darasa la saba wote wakapata, lakini wote nikawaambia andikeni sasa Kiingereza, wakaandika wote wakakosa, hakuna hata mmoja aliyepata hata chini ya 20 hawakupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ya mama ndiyo inayomfundisha mtoto, tafiti nyingi zimefanyika, watu wengi wanapinga Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia, hawasomi tafiti zilizofanyika, lakini pia wanakumbuka mambo ya nyuma. Nimekaa Uingereza miaka saba, watu wote mtaani kwangu wanaongea Kiingereza lakini hawajui kusoma wala kuandika. Hapa ndivyo ilivyo, watu wengi wanasema huyu mtoto anaongea Kiingereza kama maji kasoma, kumbe hajui chochote, lazima Kiswahili kitumike kama lugha ya kufundishia. Sasa hivi limekuwa jambo gumu sana, tunasoma darasa la kwanza mpaka la saba Kiswahili, halafu tunabadilisha kama masafa ya redio kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza. Watoto wakifika kidato cha kwanza, wanaanza kujifunza Kiingereza kwanza na wakati huo wanasoma masomo, wanafeli, watoto wengi tumewaacha nyuma sio kwamba hawana elimu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kuniruhusu kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu yenye mambo ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpenda sana Marehemu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na kumchukua. Mungu aiweke roho ya Marehemu Magufuli mahali pema peponi.

WABUNGE FULANI: Amen.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni siku ya 29 tangu ametutoka na kumpoteza mpendwa wetu huyu. Kwa hiyo, msiba huu kwetu sisi bado ni mbichi. Kwa mila zetu za Kitanzania ni mwiko au taboo kumwongelea Marehemu kwa mabaya, bali kumwombea ili Mungu ampokee na aiweke roho yake mahali pema Peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami niendelee kukemea wale watu wenye hulka ya kubadilika kama kinyonga, waache kumsema kwa mabaya Marehemu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, bali waendelee kumwombea na waone aibu na wamwogope Mungu. Kwangu mimi, Marehemu Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli anaishi bado kwa alama kubwa alizotuwekea ambayo ni pamoja na reli, vituo vya afya, bwawa la umeme, hospitali, barabara, ndege, kuhamia Dodoma, madaraja, vituo vya VETA, elimu bure na miradi mengine mingi kama maji na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, alama hizi zote sasa ziko mikononi kwa Mama shupavu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Tunamwomba Mungu ampe nguvu mama huyu, achukue jahazi hili na kulibeba kama ambavyo walilibeba wakiwa na Marehemu Mheshimiwa Dkt. Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu, ametaja mambo mengi, lakini mimi nijikite kwenye sekta binafsi ambayo ina sheria za kazi. Sheria hizi zilizopo katika matumizi kwa sasa zimepitwa na wakati. Kwa mfano, Baraza la Usuluhishi la RESCO halijakutana kwa muda mrefu sana na hili ndiyo lingekuwa nafasi ya kujadili matatizo ya waajiri na wafanyakazi. Tungependa Ofisi ya Waziri Mkuu inayohusika na sera na kazi na ajira iziboreshe sheria hizi. Kwa mfano, sasa hivi tulipata tatizo kubwa sana tulipozuiwa mambo ya Covid; waajiri walipata taabu sana kuendelea kulipa mishahara kama tungelifunga hata pale ambapo wafanyakazi hawafanyi kazi. Sheria za sasa zingeweza kuchukua nafasi hiyo na kulisahihisha tatizo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la umeme wa REA ambapo vijiji vyote vya Tanzania vitakuwa na umeme ifikapo mwaka 2022/2025 lakini pia umeme huo utakuwa na matumizi makubwa, kwa hiyo, kuna umuhimu wa kulipa nguvu wazo au mradi ule wa Bwawa la Nyerere likamilike ili kuleta umeme katika maeneo ambayo yatapatiwa umeme wa REA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la reli ya SGR ukurasa wa 50, kuna mtu amesema mradi huo utakamilika mwaka 2102, yaani miaka 81 kuanzia leo. Nimemshangaa sana kwa sababu, kanuni za miradi ni kuwa na tarehe ya kuanza na tarehe ya kumalizia. Kwa hiyo, miradi yote ya reli hii ya SGR inajengwa kwa awamu na vipande kutoka Dar es Salaam – Morogoro na Morogoro - Dodoma na baadaye Mwanza - Isaka na miradi hii yote ina tarehe ya kuanza na kwisha…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, haitafika muda mrefu huo.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maige, kuna kanuni inavunjwa. Mheshimiwa Halima Mdee.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 67(8), Mbunge hatasoma maelezo isipokuwa kwa madhumuni ya kutilia nguvu maelezo yake, anaweza kusoma dondoo kutoka kwenye kumbukumbu zilizoandikwa au kuchapishwa na anaweza pia kujikumbusha kwa kuangalia kwenye kumbukumbu alizoziandika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa mkongwe mwenzangu nimekuwa namvumilia, naona anasoma tu, sasa naomba umshauri mkongwe a-note tu, halafu atiririke. Kwa hiyo, naona hii Kanuni inavunjwa. (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Almas Maige nadhani ulikuwa unakumbushwa. Unajua pale hasomi maelezo anayosema, isipokuwa ameamua kuinamia kwenye mic yake. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Maige, hicho kisemeo hata ukitazama pembeni kinashika mawimbi, kwa hiyo, usiwe na wasiwasi. Karibu umalizie mchango wako. (Makofi/Kicheko)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mkongwe mwenzangu nakushukuru sana, lakini sikuwa nasoma, maana nilikuwa nimefanya notification, lakini mambo niliyoyaongea kabla ya kuanza kuongea haya, nilifikiri kwamba ningepotea. Nimeongea mambo mazito ndiyo maana ikanilazimu niwe na kumbukumbu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, afya. Jimbo la Tabora Kaskazini lina Kata 19 na Kituo kimoja tu cha Afya. Mimi nafikiri kwamba ipo haja ya Serikali kufikiria Jimbo la Tabora Kaskazini ambalo lina Kituo cha Afya kimoja tu, liweze kupata vituo vingine na hasa kusaidia vituo ambavyo vimejengwa kwa nguvu ya wananchi katika Kata ya Mabama, Kata ya Usagari na Kata ya Shitaghe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Leo nifuate mwongozo wako au ushauri wako kwamba uongee jambo moja linaloeleweka. Leo nataka kuongelea sekta ya ulinzi binafsi. Sekta ya ulinzi binafsi hapa imeanza mwaka 1980 na kampuni mbili na ilianzishwa na Mheshimiwa Rais aliyekuwepo madarakani kwa kumwita IGP kwamba sasa tunarudisha makampuni yote na mali zote za wenyewe hatuwezi kuendelea kuzilinda na mgambo, Jeshi la Polisi. Kwa hiyo yakaanzishwa makampuni mawili Group Four na bahati nzuri sana IGP aliyekuwepo akaomba share kwenye Group Four lakini pia Ultimate Security nayo pia Kamishna wa Polisi Rashid akaomba nae awe kwenye group hilo.

Mheshimiwa Spika, leo tuna makampuni 3,500 yameajiri askari walinzi laki tano, Jeshi la Polisi hawazidi elfu 60. Kwa hiyo sehemu kubwa ya ulinzi nchi hii inafanyika na sekta ya ulinzi binafsi. Hata hivyo, hakuna GN wala sheria wala mwongozo wowote ulioanzisha sekta hii nchi. Sekta hii imeendelea kukua, matokeo yake mambo mabaya sana yanafanywa kwenye sekta hii, lakini pia Serikali inakosa kodi, haina idadi kamili ya makampuni kwa sababu hakuna mwongozo wowote.

Mheshimiwa Spika, duniani, mimi nina sheria tatu hapa za sekta ya ulinzi binafsi, tulikoiga sisi; Private Security Services Act, lakini tuna Sheria ya Common Wealth, hii ni ya Jumuiya ya Madola, Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi, lakini kuna sheria nyingine muhimu sana inaitwa Data Protection Act ya sekta ya ulinzi binafsi, lakini pia kuna sheria nyingine Regulatory of Investigatory Power Act. Zote sheria tatu zinadhibiti makampuni ya ulinzi kwa sababu yanalinda raia na mali zao lakini wana silaha.

Mheshimiwa Spika, sekta ya ulinzi binafsi hapa nchini imesaidia kueneza silaha nchi nzima shotgun na udhibiti hakuna kwa sababu makampuni haya yalipoanzishwa mwaka 1980 na Jeshi la Polisi, viongozi wote wa Polisi wana makampuni ya ulinzi. Asilimia 75 makampuni ya ulinzi nchi yanaongozwa au yanadhibitiwa na polisi. Matokeo yake Polisi hawa viongozi waliokuwa na uwezo mwaka 1980, miaka 40 baadaye wamezeeka au wamefariki.

Mheshimiwa Spika, sasa makampuni haya yanaendeshwa na watu ambao hawana uwezo wowote, yamerithiwa kama mali ya mtu binafsi, watoto wamerithi, wake zao wamerithi na ndugu zao wamerithi. Mabunduki yako uvunguni, hivi karibuni naomba nitaje maslahi yangu, nilikuwa Mwenyekiti wa Sekta ya Ulinzi Binafsi, tulianzisha chama ili kuweza kuji-control sisi wenyewe. Nikamsaidia Mheshimiwa IGP Mwema kuanzisha at least kanuni ndogondogo ambazo sio sheria wala haziko kwenye sheria yoyote.

Mheshimiwa Spika, leo hii makamppuni yana hasara huku na huku. Kwanza makampuni yenyewe haya baada ya miaka 40 na kurithiwa na watu ambao hawana taaluma, yanaendeshwa yanapata mambo yafuatayo kama changamoto:-

Mheshimiwa Spika, Askari wanaiba mali za watu ambao wanawalinda, mnakumbuka kesi ya Kasusura aliyetumwa kwenda kuchukua milioni mbili dola akatoweka nazo; Wizi wa mishahara ya benki ya NMB, walitumwa wagawe hela, walinzi wakavua nguo pale Kawe wakachukua hela, wakaacha silaha na kila kitu; Wizi wa CRDB Azikiwe mabilioni; Wizi wa kule Moshi mabilioni pia; na Walinzi wanakufa na hakuna uhakika na hawapati haki zao.

Mheshimiwa Spika, Temeke NMB ilivamiwa, kulikuwa na Polisi na kampuni za ulinzi binafsi, walinzi wote wakafa, huyu Polisi wa cheo cha chini akazikwa na bendera ya Taifa na huyu mlinzi aliyekuwa Sergent wakati anastaafu akazikwa kawaida kabisa, hii sio haki. Vilevile walinzi wote waliopiga risasi majambazi wameshtakiwa kwa mauaji. Pale Tabora majambazi yanataka yambake mtoto, samahani lugha chafu, wanataka kumbaka mtoto wa kike, yule mlinzi amekamata silaha wanamsukuma mwisho akafyatua risasi, baadae amekamatwa kwa mauaji. Naye yupo kazini, hii ni kwa sababu hakuna sheria.

Mheshimiwa Spika, haya naweza kuyasema kwa uchungu sana. Mimi nilipoingia madarakani nilitoka sekta ya ulinzi binafsi, nimeleta mfano wa sheria, Serikali ikasema itaileta. Leo hii hakuna chochote kilichokuja humu Bungeni. Sheria itaanzisha mamlaka inaitwa Public Security Authority kama EWURA, TCRA, TRA na kadhalika, ndivyo ilivyotoka duniani kule, hiyo mamlaka itakuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani sio Jeshi la Polisi, lakini polisi hawa wanashindwa kuleta sheria hiyo kwa sababu sasa wenyewe ni wenyewe, wanajisimamia wenyewe.

Mheshimiwa Spika, limezuka jambo lingine ambalo linasikitisha sana, kutokuwa na mamlaka yoyote tunakosa local content kwenye migodi au kwenye mashirika makubwa ya kidunia, kwa sababu hatuna viwango. Makampuni ya Tanzania hayana viwango, hayana cheti wala hayajapangiwa kiwango gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuchukulie zabuni itangazwe ya kujenga barabara, si lazima mtu wa civil ndio afanye quotation kule na ufundi umeme naye ana-quote kwenye barabara; tunatangaza zabuni ya ulinzi wana-quote makampuni yote, kumbe kwenye sekta hii kuna man guarding, kuna mitambo, lakini kuna upelelezi na vilevile kuna wanaosindikiza mali wanajiita CIT. Sasa inatangazwa zabuni vurugu tupu, ni ya nani hiyo zabuni. Kungekuwa na mamlaka itapanga kwanza kazi hii daraja la ngapi.

Mheshimiwa Spika, tunapotangaza kazi ya ujenzi wa jengo hili tunasema mkandarasi daraja kadhaa, makampuni hayo huko yalikotokea yana madaraja la kwanza mpaka la saba, lakini pia yana taaluma hapa tunaenda fujo tu. Hivi karibuni kumekuwa na usemi wa Auxiliary Police wanasema haya makampuni yote ni Auxiliary Police, sio kweli, Auxiliary Police ni watu wengine na sekta ya ulinzi…..loh!

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti naunga mkono hoja hii nitaandika (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa kweli lazima nikiri kwamba Wizara hii imefanya kazi kubwa sana jimboni kwangu na nchi nzima. Mimi kwangu nawapongeza sana kwa kunijengea shule za upili wa juu. Tulipoingia madarakani hatukuwa na hata shule moja ya upili wa juu yaani high school tunazo mbili sasa. Pia wananijengea VETA na hii itasaidia sana kupeleka fedha vijijini kwani mafunzo yatakayopatikana watafanya kazi vijijini. Vilevile tumepata fedha za maboma na tumejenga nyumba za walimu na madarasa na tumepata madawati. Hapa pia nilishurukuru Bunge letu, Bunge lilitupa madawati ambayo yamekwenda kuwekwa kwenye shule zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo siongelei ufundi kwa sababu Mheshimiwa Manyanya amenigusa sana kwamba ilikuwa hujuma kuua shule za ufundi. Hili lichukuliwe kama ni sababu kubwa sana ya kulegalega kwa elimu ya ufundi hapa nchini, hujuma hii ilitupata sisi Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitaongelea suala la lugha ya kufundishia na VETA kuwa chini ya Wizara ya Elimu na Sayansi. Kiswahili mmekigusa kidogo mimi safari hii naomba Serikali ianzishe shule ya mfano itakayoanza kufundisha kwa Kiswahili kuanzia darasa la kwanza mpaka chuo kikuu. Wazo hili lilikuwepo sijui kwa nini Serikali haikuanzisha shule ya mfano. Ichukue shule yoyote ambayo watoto wapo darasa saba waendelee form one Kiswahili, shule moja tu tuone matokeo yake. Maana tunabishana wataalam hawataki kusoma tafiti ambazo zipo pale TATAC na BAKITA. Watu wote waliofanya utafiti kwa miaka 40 wamesema Kiswahili ni lugha mama Tanzania ifundishwe, bado watu hawataki kutofautisha kati ya elimu, maarifa na lugha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri akija hapa na nitazuia shilingi atuambie tatizo gani lilizuia Serikali kuanzisha shule ya itakayotumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia. Tunaandikia mate na wino upo, si tuanzishe tu shule leo iende mpaka form four, form five Kiswahili. Vitabu vyote TATAC vipo, wameshaandaa kitabu cha kwanza mpaka cha pili, wakianzisha shule hii wale watamalizia kidato cha nne na cha tano na watakuwa mbele hivyo wale wataalam wa TATAC na BAKITA kutafsiri kwa lugha la Kiswahili vitabu vyote vya kufundishia. Nawaombe sana tujaribu mfano huo kama itashindikana ndipo wazo la lugha litakufa kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri watu wana mawazo ya nyuma kwamba Kiingereza au Kifaransa ndiyo elimu. Mimi nashauri tuanzishe shule itakayotumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia darasa la kwanza mpaka chuo kikuu. Sasa hivi Chuma chetu Marehemu Magufuli, Rais wetu, alisema tu historia la kwanza mpaka chuo kikuu Kiswahili, asubuhi tumefanya hivyo mbona hawakukataa? Leo tunafundisha historia darasa la kwanza mpaka chuo kikuu kwa kutumia Kiswahili mbona imewezekana, kwa nini masomo mengine ishindikane, tena masomo sasa yamepungua yamebakia machache imebaki historia na kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako linaongea Kiswahili, Serikali inatumia Kiswahili, Mahakama inatumia Kiswahili, mnawachanganya watu, hao waliosoma Kiingereza wanatumiaje Kiswahili huku Mahamani au Serikalini, kumekuwa na mambo ambayo hayaeleweki. Naomba sana Kiswahili kipewe umuhimu na mimi hili kama Mheshimiwa Rais anasikia aliingilie kati, kabisa kabisa. Nashauri hili liamuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la VETA. Waajiri wanachangia Mfuko wa Elimu ya Ujuzi kupitia tozo ya SDL kwa asilimia 4 lakini fedha zile haziendi VETA zote. Sababu kubwa ilijulikana siku za nyuma kwamba fedha zilikuwa hazitoshi ndipo Mheshimiwa Kikwete akahamishia VETA Wizara ya Elimu ili ipatikane fedha ya kwenda Bodi ya Mikopo na ndivyo ilivyo sasa. Sasa hivi mantiki hiyo haipo kwa sababu fedha zote zinakwenda Akaunti ya Pamoja ya Hazina. Kwa hiyo, ile mantiki kwamba fedha za SDL ziende Wizara ya Elimu haipo tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, VETA maana yake ni kazi ndiyo maana sisi waajiri tunachangia. Tunachangia fedha zinapatikana lakini sasa VETA badala ya kusimamiwa na Wizara ya Kazi na Ajira ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Mheshimiwa Mama Jenista Mhagama sasa anasimamia Waziri wa Elimu, ni vitu tofauti. Sisi huku tunashangaa sana hii Serikali vipi? Mbona sasa ajira inasimamiwa na Wizara ya Elimu na wakati Wizara ya Ajira ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaombeni sana, waajiri huku wanashangaa. Hatukatai kuchangia na tunawashukuru sana Serikali tulikuwa tunachangia asilimia 6 mpaka imefika asilimia nne tunaomba sasa hii VETA irudi kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye ndiye anayesimamia ajira na kazi na ndiyo kuna mikataba ya kazi, tunataka wafanyakazi wapate ujuzi. Sasa tunasimamiwa na Wizara ya Elimu siyo shule ile; kile ni Chuo cha Ufundi Stadi ya wafanyakazi na ndiyo maana sehemu kubwa ya fedha yake inatoka kwa sisi waajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu na mchango huo naomba safari hii ufanyiwe kazi. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru sana kuniruhusu nichangie wa mwisho.

Kwanza nianze na pongezi, naipongeza sana Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa lakini pia niwapongeze viongozi wa Jeshi. Nianze na ndugu yangu Jenerali Mabeyo, lakini pia Mnadhimu Mkuu Jenerali Yacoub Mohamed, Makammanda wote wa Jeshi letu. Wamefanya kazi kubwa kuituliza nchi baada ya tukio kubwa hili la kupotelewa na Mheshimiwa Rais Marehemu Magufuli.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Almas Maige, huyu Mnadhimu Mkuu wa Jeshi ni Luteni Jenerali maana nafikiri nchi inakuwa na Jenerali mmoja halafu wengine wanakuwa ni Majenerali wastaafu.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunisahihisha. Luteni Jerenali Yacoub Mohamed. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo mimi nimejielekeza kwenye malengo ya Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na nianze na lengo la kwanza, kuwa Jeshi dogo lenye ufanisi mkubwa. Jeshi hili litakuwa na ufanisi mkubwa kama litapewa vifaa na zana hasa zana za EW (electronic warfare). Vita imeacha kupiganwa sana sana kwa mizinga na bunduki, lakini electronic warfare au vita vya elektroniki vinafanya kazi imara. Jeshi letu litakuwa na nguvu sana sana kama litapewa hela za kutosha kununua vifaa na zana hizi za EW. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye utafiti ambao ni lengo la Wizara lengo la tatu (c ). Hapa ndipo tunapata taabu sana na Jeshi letu, hawana hela za kufanyia utafiti. Jeshi litakuwa la kisasa, usasa ule na weledi utatokana na tafiti ambazo wanazifanya wao wenyewe. Huko tulikopita Jeshi lilitakiwa liandike andiko lipeleke COSTECH likasome, ndiko hela zipo, halafu wazipe Jeshi. Andiko la Jeshi ni la siri, haiwezekani raia wasome andiko la Jeshi wafanya maamuzi ya kuwapa hela. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iweke hela za utafiti wa Jeshi kama kweli tunataka amani ya nchi hii na utendaji wa Jeshi ufanyike. Wapeleke hela Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa au moja kwa moja Ngome. Wafanye utafiti wa silaha, utafiti wa maisha ya watu ili waweze kuwalinda. Utafiti haufanyiki na matokeo yake Jeshi hili haliwezi kuwa dogo likawa na nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niongelee eneo (d) kuimarisha Jeshi la akiba. Jeshi la akiba zamani tuliliita mgambo lilifanya kazi kubwa sana wakati wa vita vya Kagera, mimi nilikuwepo. Jeshi la akiba ni jeshi muhimu sana. Sasa hivi Wizara haina hela ya kuendeshea au kulifanya Jeshi hili liendelee kuwepo. Mafunzo na mazoezi ya jeshi la akiba ni muhimu sana, hela hakuna. Mimi nashauri Serikali iipe Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi lenyewe hasa ili waweze kuendeleza uwepo wa jeshi la akiba. Wamelitaja kama ni lengo la tatu katika malengo ya Wizara. Napendekeza, ni muhimu sana jeshi la akiba liendelee kuwa imara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la JKT; JKT imefanya kazi kubwa sana ya kuwafanya Watanzania wawe wazalendo. Suala hili naona kama lililegalega huko nyuma mpaka Jeshi lenyewe la JKT likaacha kuchukua vijana. Limeanza kuchukua vijana sasa hivi, lakini hawatoshi. Wafanyakazi, Mawaziri walioko leo madarakani ni watendaji wazuri wa Serikali, wana uzalendo kwa sababu walipita JKT. Katikati hapa vijana walianza kutawanyika bila kueleweka wewe ni Mtanzania au sio Mtanzania kwa sababu hawakuwa na uzalendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Kujenga Taifa ndicho chombo pekee kinachojenga uzalendo kwa Watanzania. Naomba hela zipelekwe ili watu wanaotakiwa kwenda kupita JKT wapiti, wale wa kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea. Mimi nasema uzalendo ndiyo chombo muhimu sana. Leo hii tungesema tupigane vita vya Kagera tungepata taabu sana. Mwaka ule wa 1978 wanajeshi wanasimamisha magari wanapeleka front line, mstari wa mbele. Leo mtu atasema nilipeni kwanza hela zangu ndipo niwapeni gari langu, uzalendo umepungua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chombo pekee cha uzalendo ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Naomba sana Serikali ifikirie kurudisha hela nyingi kwenye chombo hiki ambachi kimetusaidia sana kuleta amani na utulivu nchini. Watu wakiwa wazalendo hawawezi kutoa maneno ya misonge misonge kwa sababu watasema sisi ni Watanzania. Tunasema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee. Inaendelea kwa sababu kuna uzalendo rohoni, hawasemi tu mdomoni, kazi iendelee, hapana! Tunasema kwa sababu tunasema kweli na tumefundishwa na JKT. Kwa hiyo, Jeshi la Kujenga Taifa ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee sasa eneo la mwisho kuhusu SUMA guard, wanafanya kazi nzuri sana lakini ni sehemu ya sekta ya ulinzi binafsi, ni wanachama pia wa Chama cha Sekta Ulinzi Binafsi (TSIA). Liko tatizo, SUMA guards leo wanapewa kazi bila zabuni. Ni sehemu ya kazi za makampuni ya ulinzi binafsi pia, lakini wao wanapewa kazi bila zabuni. Lakini pia wanaomba zabuni kwenye kazi nyingine hizi. Kumekuwa na utata kidogo, kuna kusukumana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya ulinzi binafsi inazimika kwa sababu kazi zote za Serikali ambazo walikuwa wanalinda na wao pia wanapewa JKT, lakini na wao pia ni kampuni za ulinzi. Sasa hivi kumekuwa na mkorogano zaidi, hata Jeshi la Magereza nao wameanzisha, wanaita SHIMA. Mkorogano huu unaleta migongano na kuua ufanisi hasa wa sekta ya ulinzi binafsi.

Mimi nashauri SUMA guards washiriki zabuni, lakini pia waoneshe kwamba wanafanya kazi kweli sehemu ya ulinzi binafsi. Sasa ilivyo kuna upendeleo mkubwa huu ambao unavuruga mfumo mzima wa sekta ya ulinzi binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Nimemaliza.

NAIBU SPIKA: Ameshamaliza muda wake. (Kicheko/ Makofi)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kupata fursa hii ndogo, tuko wengi tunagombania muda huu. Mimi nitajikita kwanza kutoa shukrani kwa Wizara hii na Serikali yetu lakini pia malalamiko kidogo kwenye jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita kwa mradi huu mkubwa wa REA na hasa hasa kueneza umeme nchi nzima. Vilevile kujiandaa kuwa na umeme wa kutosha kwa kuleta miradi mingi ya kuzalisha umeme na baba yao ni Mradi mkubwa wa Mwalimu Julius Nyerere kule Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Wizara hii si kwamba ameivaa Mheshimiwa Kalemani, Mheshimiwa Kalemani amevaliwa na Wizara hii. Mheshimiwa Kalemani Wizara hii anaichukua kama familia yake. Mimi kwangu tulipoanza uongozi hapa mwaka 2015 hapakuwa hata na kijiji kimoja chenye umeme jimboni kwangu. Kwa kujua hilo, huyu Waziri amekuja jimboni kwangu mara nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna wilaya saba Mkoani Tabora. Kote mradi ulikuwa unaenda vizuri lakini Jimbo la Tabora Kaskazini halikuwa hata na kijiji kimoja chenye umeme, leo tuna vijiji 32 vina umeme. Alikuwa anasikiliza maoni ya wananchi wangu anatoka machozi, hili si jambo la kawaida kwa Waziri kuumia kama vile wale ni familia yake yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaambieni alipita jimboni kwangu kuzindua umeme REA III sehemu ya pili siku saba kabla ya kumpoteza Mheshimiwa Rais aliyetangulia mbele za haki. Hii ni kuonyesha kiasi gani alikuwa na uchungu wa kufanya kazi akijua kwamba ana matatizo ya familia yake, lakini akaweka familia ya Watanzania wote mbele. Huyu ndio Waziri Kalemani nayetaka kumtaja leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matokeo yake vijiji 12,000 vimepata umeme kutoka vijiji vichache vilivyokuwepo mwaka 2015 bado vijiji 1,900 na kitu basi nchi nzima iwe ya umeme. Ameitoa nchi hii kule chini kwa umeme leo ni nchi ya kwanza katika Afrika kuwa na umeme. Huyu ndiyo Waziri ninayesema Wizara imemvaa naye kaivaa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu tuna vijiji 96 Jimbo zima, 32 vina umeme na 64 havina umeme. Hata hivyo, kwa imani kubwa niliyonayo kwa Mheshimiwa Waziri ameshakuja na kuzindua REA III round II pale kijijini kwetu Kanyenye na kutoa ahadi kwamba vijiji vyote vilivyobakia vimo katika REA III round II na wilaya yote ya Uyui imepewa vijiji 100 vitakavyopatiwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, licha ya hivyo tulikuwa tumebakiwa na vijiji vitatu kujumuisha vijiji vyote vya Wilaya ya Uyui. Alipokuja tumeongea naye na wakandarasi wote tumekubaliana vijiji vile vitano vilivyobakia vimo pia katika mpango huu wa REA III round II. Kwa hiyo, mimi nina imani kwamba baada ya mwaka 2022 kama tunavyosema miezi 18 Jimbo langu na Wilaya yote ya Uyui itakuwa na umeme. Hili si jambo dogo, nimesimama hapa kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano na Awamu ya Sita kwa kazi nzuri inayofanya. Tusingoje mtu fulani afariki ndipo tumpongeze tunampongeza Mheshimiwa Kalemani yuko hai na anatusikia amefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la usalama wa mitambo inayoitwa Business Continuity Planning. Mitambo hii inafanya kazi kila siku lakini lazima kuwe na mbadala wake. Tumepata tatizo sana la LUKU wiki tatu zilizopita ilipoanguka awamu moja waliyonayo ya kuendesha mitambo hawakuwa na awamu ya pili jambo hilo limeleta mushkeli. Naomba waangalia kuwa na mitambo mbadala.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa kuchangia bajeti hii ya mwaka 2021/2022. Kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa kukamata usukani wa nchi yetu na kututembeza mpaka hapa tulipofika, nchi imetulia na nchi imekuwa na maelewano mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Waziri wa fedha na mipango, ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara hii kwa kuleta bajeti nzuri ambayo imekuwa ni ya kupigiwa mfano, kwa sababu hii ni bajeti ya kwanza kwa Mheshimiwa Rais Samia, lakini watu wameikubali. Mimi ni mmoja wa watu wanaounga mkono bajeti hii,na nina ushahidi wa kutosha kwamba bajeti hii imekuwa na kiasi kikubwa sana cha mambo ambayo Wabunge waliyaomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na ukweli kwamba bajeti hii itamalizia miradi ambayo ilikuwa ya kimkakati kama reli ya SGR, mradi wa umeme kule Mto Rufiji na mradi wa REA wa kupeleka umeme vijiji vyote. Vile vile bajeti hii imetafuta fedha kwa ajili ya TARURA ambazo Wabunge tumekuwa tunalia humu kwamba TARURA iwezeshwe na tumetafuta fedha kwenye vyanzo vya uhakika ambavyo tutawapa TARURA ifanye kazi ya kutengeneza barabara kwenye vijiji ambavyo hakuna barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia miradi mbalimbali ya kufua umeme, ambao umeme huo utatumika kwenye Mradi wa REA. Sasa hivi Mradi wa REA hata ukikamilika umeme utakatika kwa sababu uliopo sasa hivi hautoshi, pia miradi mbalimbali ya maji itakamilika. Kuhusu afya bajeti hii imelenga kumalizia majengo na kupeleka vifaa tiba kwenye majengo ya hospitali ambayo sasa yapo, lakini hayana vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fedha za majimbo. Hii ni bajeti ya kwanza ambayo imetupa hela mkononi Wabunge. Kwanza milioni 500 za kujengea barabara, vile vile milioni 600 za kujengea shule katika kata ambazo hakuna shule. Hapa nina maboresho kidogo, fedha hizi milioni 600 kuna majimbo mengine tayari yana shule na watapata hizo hela na kuna majimbo mengine yana kata zaidi ya tano katika kata 20 hazina shule, inakuwa tabu sana. Kwa mfano, jimboni kwangu nina kata mbili, hazina shule za sekondari. Hata hivyo, wenyewe tumeaanza kufurukuta, tumejenga kwa kutumia Mfuko wa Jimbo na michango ya wananchi. Kwa hiyo ningeomba kabisa mimi hizi hela milioni 600 nizigawe miloni 300 kila kata na tunaweza kumalizia shule ya sekondanri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala lingine ambalo bajeti hii imeligusa, nalo ni kuwagusa waajiri na wafanya kazi. Katika nyanja hiyo, bajeti hii Serikali imependekeza kupunguza PAYE kutoka asilimia tisa mpaka nane. Kwa hili tunaipongeza sana Serikali yetu. Pia Serikali imependekeza kwamba waajiri wenye wafanyakazi mmoja mpaka wanne sasa wasilipe tena SDL kama ilivyokuwa zamani, tumesogeza ile idadi ya chini ya wafanyakazi kuwa 10. Sasa hii imesaidia sana na waajiri wengi watalipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna huu Mfuko wa Matibabu au Malipo kwa Wafanyakazi Wanaoumia Kazini, yaani Workers Compensation Fund, tumekubaliana kwamba na bajeti imeonyesha kwamba sasa waajiri wa sekta binafsi walikuwa wanalipa asilimia moja watalipa asilimia 0.6. Sisi tuna maoni kwamba ingefaa hizi asilimia 0.5 kwa ajili ya wafanyakazi wa Serikali au public, iwe sawa na kwa ajili ya wafanyakazi binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kabisa nina maoni machache, kuboresha tu bajeti hii ambayo nimeisifia kwa ajili ya watu wote. Maoni yangu kwanza. Ni kweli kabisa naamini kwamba VETA ingefanya kazi vizuri sana kama ingekuwa chini ya Wizara ya Kazi chini ya Waziri Mkuu, kwa sababu VETA maana yake ni kuhudumia watumishi kwa wafanyakazi wa waajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napendekeza sasa Serikali ijiingize kabisa kabisa kwa ajili ya blue prints, tutekeleze mpango wa blue prints ambao ungerahisisha kufanya kazi kwa kufanya biashara yaani easy doing business hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu tozo za wafanyakazi nimeisemea, kuhusu tozo ya SDL. leo tumesimama katika asilimia nne ya mshahara wa mfanyakazi, nchi zote za Afrika Mashariki na SADC tozo hii ni ndogo sana. Kwa hiyo hii inatuongezea kuwa na gharama za ufanyaji biashara hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niongelee posho ya Madiwani ambayo Serikali inalipa, itawalipia moja kwa moja Madiwani wetu badala ya kulipwa na Halmashauri. Hii imeleta na imeibua wazo la utawala bora, maana wanaesema mtu anayemlipa mpuliza zumari, anachagua na wimbo wake. Sasa hii watalipwa Madiwani hao kwa hiyo watasimamia Halmashauri zetu vizuri. Naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina matatizo madogo jimboni, lakini sugu kabisa ni vituo vya afya. Jimbo zima lina kata 19, lina kituo kimoja tu cha afya. Nimelisema sana hili mpaka naona aibu kulirudia rudia, kama Waziri wa Afya yupo, Waziri wa TAMISEMI yupo, watusaidie kumalizia majengo kwenye kata ambazo nimezitaja; Shitage, Mabama, Ilolanguru na Usagari ambako tunajenga wenyewe kwa hela zetu za Mfuko wa Jimbo na nguvu za wananchi. Tuna shida kweli ya hospitali, tungependa sana kama Serikali itaingilia kati suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado naendelea na pongezi kwa Wizara ya Maji, imefanya kazi nzuri sana ya kugawa maji jimboni kwangu na nchi nzima. Hata juzi tumekwenda kufungua mradi huko Misungwi na Mheshimiwa Rais. Wizara hii imefanya kazi nzuri sana nawapongeza sana Mheshimiwa Aweso na timu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala muhimu sana la kilimo. Kilimo ndio uti wa mgongo katika nchi hii, lakini kilimo hakithaminiwi na Serikali kabisa. Wamesema Wabunge wengi hapa kwamba tunapata bajeti nzima ya Serikali kilimo kinachangia asilimia 27. Matokeo yake Serikali inawekeza 1.8 ya bajeti kwenye kilimo na tumesahau kitu kimoja kikubwa sana, nchi hii itatokea vita au ugomvi mkubwa sana kwa sababu Serikali haijaweka ardhi ya kilimo kama ambavyo tumeweka ardhi ya wanyama yaani hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, akishawekwa mwekezaji hapa anataka ekari 200 ziko wapi, hakuna. Anataka hekari 500, hakuna, anataka hekari 10,000 aweze kuweka shamba kubwa na uzalishaji wa tija, hakuna. Matokeo yake wananyang’anywa watu wenye mashamba yao kama vile sijui wamenyang’anywa na matumbo, kwa sababu hawa watu wenye mashamba yao watakula wapi, walikuwa wanalima, inachukuliwa ardhi anapewa mwekezaji. Iko haja ya Serikali sasa kuweka ardhi ya kilimo, demarcated kabisa kwamba ardhi ya kilimo ni hii, kama ambavyo tumeweka ardhi ya wanyama ni hii, itatusaidia sana kuondoa migogoro huko mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala hili la kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu limepitwa na wakati. Tunangoja mvua zinyeshe ndipo tuvune, kama hazikunyesha hatuvuni na hatuna simu sisi na Mwenyezi Mungu kwamba tuletee maji, tuletee mvua mwaka huu, hatujui, hata Waziri wa kilimo leo hajui kama kesho mvua itanyesha, imekuwa tu utabiri wa hali ya hewa ambao wanaona mawingu na kadhalika, hakina uwezekano wa kutoboa sisi kilimo bila ya kuwa na kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri, Serikali ibadilike itoke nje ya box, ising’ang’anie kusukuma wakulima na pembejeo tu kwenye maji ambayo hawayajui yako wapi, wakati kila mwaka mvua inanyesha maji mengi yanapita kwenye madaraja na tunakazana kujenga madaraja tu ili maji yapite, tuzuie sasa hayo maji tufanye umwagiliaji wa kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu kuchangia bajeti hii. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunruhusu na mimi nichangie hoja hii kuhusu Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Kuhusu Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kuunga mkono hoja hii; na kwa kweli Tanzania imechelewa sana karibu miaka nane imepita tangu wenzetu waliposaini Azimio hili na Itifaki hii kusainiwa na viongozi wa nchi zote za Afrika Mashariki ikabakia Tanzania. Tumepewa sasa mpaka mwezi wa 12 mwisho tuwe tumesaini Itifaki hii. Leo, ni siku ambayo tutajitahidi sana katika kupitisha Azimio hili. Naomba Bunge hili lipitishe Azimio hili kwa sababu lina manufaa sana kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kawaida, huwezi kuongea itu ambacho uko nje. Tulipata matatizo, mahindi yetu yalikwama pale mpakana na tumepata taabu kujadili na wenzetu kwa sababu sisi hatujasaini Itifaki. Lakini, Itifaki hii inapendekezwa na kuridhiwa na Bunge lako Tukufu, na kwa kweli ni muhimu, na tafadhali, Itifaki hii ina maana kubwa sana kwetu sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimejipanga kuongelea sehemu mbili. Ibara mbili tu muhimu katika Itifaki hii na ni Ibara ya 6 inayohusu usalama wa chakula na jinsi ya kudhibiti usalama huo hasa udhibiti wa chakula kinachotokana na mazao ya GMO.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia Serikali ikionge mara nyingi kwamba Tanzania haitaki GMO lakini hatuna sera hiyo. Sera inayoeleza kwamba Serikali haitaki au sheria inayosema Serikali haitaki GMO. Katika Itifaki hii GMO ni sehemu itakayodhibitiwa na Itifaki hii lakini sasa kama sisi huku hatuna instrument inayoweza kutusaidia kwenda kujadiliana kule itatupa taabu. Kwa hiyo, naiomba Serikali sasa ije na sheria au sera au kanuni instrument bora ya kupeleka kule kwenye usajili wa itifaki hii kwa katibu Mkuu wa Afrika Mashariki ili mazao ya chakula yanayotokana na Genetic Modified Organisms (GMO’s) yaweze kudhibitiwa kuingia nchini kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara nyingine ambayo ningependa kuiongelea ni ile Ibara ya 17 kuhusu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweza kutunza na kuhifadhi certified ya nyaraka na sheria na Kanuni ambazo Tanzania inaziwasilisha kule. Hili ni jambo muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona sababu ya Serikali iliyotoa kwanini kwa miaka nane hatukusaini Itifaki. Sababu kubwa ilikuwa ni kujiandaa, na tumeona maandalizi mazuri sana. Zimetungwa sheria na zimewekwa mamlaka mbali mbali kuhusu usalama wa chakula, mazao ya wanyama pia kuhusu mimea. Upande wa mimea, sheria kadhaa zimewekwa na mpaka mamlaka imewekwa lakini pia upande wa wanyama na mazao yake tumeweka sheria hizo na kuweka vile vile mamlaka au taasisi za kusimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hizi ndizo instrument zinazosemwa katika Azimio na zinasemwa katika article ya 17 ya itifaki hii inayosema na naomba noisome, ya kiingereza kifupi tu, mstari mmoja. Inasema “The Secretary General shall register the protocol with all Regional and International Organizations responsible for the implication of this” lakini pia inasema, “this protocol and all instruments of rectified shall be deposited with the Secretary General who shall transmit certified true copies of the protocol and instruments of the rectification to all partner states”.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu Serikali sasa ijiandae na instrument hizi, vitendea kazi hivi ambavyo vitatusaidia kwenda kujadili kule wakati tunapoona kwamba Serikali sasa imesimama na msimamo wake kwamba jamani tuli-rectify/kukubaliana/ridhia mkataba/Itifaki hii tulikuja na vitu hivi. Hizo ndizo nyaraka muhimu ambazo Serikali inapaswa kuziunganisha nazo wakati wa kupeleka itifaki hii ambayo sisi tumeridhia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kuchangia hilo tu. Kuitaka Serikali iwe Imara katika kuandaa nyaraka hizi na instrument za kufanyia kazi. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie Mapendekezo hayo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa ajili ya Mwaka 2021/2022 - 2025/2026. Kwanza nitoe shukrani, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha nyingi sana jimboni kwetu za madarasa, barabara lakini pia za hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mpango sasa, ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage amesema vizuri na Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Kilimo, sisi tunachangia kilimo. Sekta ya Kilimo ndiyo inayofanya tuseme, tuongee hapa. Kilimo kimekuwa na kauli nyingi sana; Kilimo cha Kufa na Kupona, Siasa ni Kilimo na Kilimo ni Uti wa Mgongo, lakini leo naona uti wa mgongo hauna mfupa, huu kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisemee mambo machache ambayo ni muhimu sana. Kilimo cha kwetu kinadumaa na kama kilimo kinadumaa na kinaajiri zaidi ya watu asilimia 75. Kwa hiyo watu wote huko vijijini hali siyo nzuri. Sababu kubwa ni uhaba wa mbegu, ukosefu wa mbolea, lakini vile vile bei kubwa ya mbolea na bajeti ndogo ya Serikali kwenye kilimo. Niwakumbushe tu kwamba bajeti ya mwaka jana ilikuwa asilimia 0.8 ya bejeti ndiyo kilimo, lakini pia tumetekeleza skimu zote za umwagiliaji lakini pia ukosefu wa watalaam wa kilimo, Maafisa Ugani Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kina mchango mkubwa sana kitaifa. Moja, kilimo kinatoa ajira kwa wananchi zaidi ya asilimia 75, lakini kinachangia bajeti asilimia karibu 27, lakini pia malighafi viwandani na chakula kwa Watanzania wote, kilimo ni kitu muhimu sana. Ili niweze kuchangia na niwe mkweli ningependa kupendekeza yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Fedha na Mipango ije na Mpango mzuri wa kujenga Viwanda vya Mbolea. Ili tuweze kupunguza bei kubwa ya mbolea lazima tuwe na Viwanda vya Mbolea hapa nchini, tulikuwa nacho kimoja huko Tanga kimekufa, Kampuni ile TFC haina kazi yoyote. Kwa hiyo, tunahitaji viwanda vya mbolea nchini, sisi tuna malighafi zote za kujenga viwanda vya mbolea hapa, gesi tunayo, lakini pia malighafi nyingine zinapatikana. Ndiyo maana watu kutoka Burundi wanakuja kujenga Kiwanda cha Mbolea hapa na hawaleti malighafi kutoka nje. Malighafi ipo hapa, tujenge Kiwanda cha Mbolea ambacho kitafanya mbolea ipatikane. Kwa wale ambao hawafahamu mbolea iliyopo nchini sasa ni asilimia 35 haizidi 40, lakini pia bei zake wananchi hawawezi kununua mbolea kwa bei ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, umefika wakati ni lazima tupange ardhi ya kilimo. Sasa hivi ardhi haijulikani ipi ni ya kilimo, tumepanga ardhi ya wanyama, National Games, maeneo oevu, lakini kwa kilimo, haiwezekani akaja mkulima mkubwa sana anataka Tanzania tumpe ardhi iko wapi? Haijawa demarcated.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda basi, kama inashindwa kuwa demarcated, Serikali irasimishe mashamba ya wakulima wadogo wadogo kama ardhi ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni kilimo cha umwagiliaji. Hatuwezi kutoka kwenye kilimo cha kutegemea mvua? Sasa hivi tunaambiwa mvua haitoshi, lakini mabwawa yapo yamejaa maji. Tungekuwa na skimu za kumwagilia zinazojulikana, siyo kumwagilia kwa mitaro, mashine kubwa zimwagilie mashamba ya kisasa. Tunaweza tukapanga kiasi gani tutavuna kwa mwaka kwa kutumia umwagiliaji. Siyo mvua hainyeshi, mwaka huu hatupati. Nashauri kilimo cha umwagiliaji ni jambo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ni kuongeza bajeti. Bajeti ya Serikali ya 0.8 kwa mwaka kusaidia sekta ya kilimo haitoshi kabisa. Napendekeza na watu wote duniani wanasema lile Azimio la Maputo, lilisema Serikali iweke asilimia 10, iwe ndiyo kwa ajili ya kilimo. Sasa mimi napendekeza hata twende 5% siyo 0.8%, hatuwezi kuwa na kilimo bora.

La mwisho ni Benki ya Kilimo. Tunayo Benki ya Kilimo hapa nchini. Hii benki haifanyi kazi yoyote kusaidia kilimo, haionekani popote katika ushiriki wake wa kujenga au kuongeza tija ya kilimo. Inakopesha watu na imekuwa tu ni wakala wa mabenki ya biashara na ili wananchi wachache wajanja wajanja waweze kukopa, lakini wakulima wadogo wadogo ambao benki hii ilikuwa imekusudiwa kwenda kuwasaidia, haionekani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nchi nzima hii ina ofisi moja tu kwenye hii benki ya kilimo. Haionekani mikoani kote wala kwa wakulima. Imekuwa tu Wakala kwamba unataka kwenda kukopa CRDB, unataka kwenda kukopa benki yoyote ile, sijui NMB, wao ndiyo wanakuwa brokers, wanasema wanaweka dhamana. Benki ya Kilimo ichukue jukumu lake na Serikali isaidie kuipa fedha nyingi Benki ya Kilimo ili iwakopeshe wakulima wadogo wadogo kuongeza tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo suala lingine dogo nje ya kilimo ambalo ni REA. Mradi wa REA ni muhimu sana, unaleta maendeleo makubwa vijijini, lakini utekelezaji wake umeanza kuwa na matatizo. Wanajenga halafu vijiji vingine wanaruka. Wale wananchi ambao wanarukwa vijiji vyao wanakuwa wanyonge sana. Wanakosa raha, wanakuwa kama siyo Watanzania. Tumefanya mikutano na watu wa REA, wale Wakandarasi wanasema wao wamepewa BOQ ya nguzo 20 kwa kijiji kimoja. Sasa kuna kijiji cha pili yake labda nusu kilomita wanakiruka, waya za umeme zinapita kwenda kuweka umeme kijiji kingine kinachofuatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imekuwa kasoro kubwa sana ambayo inaleta chuki kwa wananchi wetu na viongozi. Vile vile, suala hili linafanya wananchi wengine wawe na matabaka kati ya wananchi wengine; hapa pana umeme, umeme huo unaruka mahali fulani. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Nishati... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu Mpango wa Maendeleo lakini pia Mpango wa Bajeti 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye miradi ambayo ninafikiri ni ya kimkakati na nianze na Reli ya Kati - SGR. Reli hii inakusudiwa kuunganisha Tanzania na nchi jirani, ibebe mizigo ya nchi jirani ili tupate uchumi kwa nchi yetu lakini lazima reli hii ikamilike. Mimi nimeona mpango unavyoendelea kwamba Reli hii ya Kati itajengwa na tayari sehemu ya kwanza ile ya Dar es Salaam - Morogoro imekamilika na Morogoro - Makutopora iko asilimia Fulani lakini ninaomba Serikali iweke nia sana. Hatuwezi kuwa na mpango wa ujenzi wa reli ambayo hatujui itakamilika lini. Tungependa kujiwekea mpango kwamba reli hii itaisha lini ili ilete faida nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ningependa kuongelea ni ukamilishaji na ununuzi wa ndege Tano, ni wazo zuri sana kuiongezea uwezo ATCL na hasa ile ndege ya mizigo ambayo itabeba mizigo yetu kupeleka nje ya nchi moja kwa moja. Sasa hivi tunapata taabu ya kupeleka mizigo yetu kupitia nchi za Jirani, ni wazo zuri lakini Serikali isimame na tuipongeze iweze kukamilisha mradi huu wa ATCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa kufua umeme kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere kule Rufiji, napata kidogo matatizo, kila siku ng’ombe wanakamatwa kwenye vyanzo vya maji na ule mradi unatumia maji, maji yasipopatikana ya kutosha kujaza Bwawa lile kule kwa sababu yoyote ile, mradi ule utakuwa ‘White Elephant’. Yapo Mabwawa ya namna hiyo yalijengwa katika nchi zetu za Afrika mfano kule Ghana na lile Bwawa halina maji mpaka leo. Mimi sitaki kuona uchungu wa tunavyojibana kuitafuta hela ya kujengea Bwawa hilo halafu watu wanakwenda kwenye vyanzo vya maji yanayokwenda Rufiji wanaharibu! Iko haja ya Serikali kujikita kindakindaki kuzuia kabisa uharibifu wa vyanzo vya maji yanayokwenda Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa REA, mradi huu utafanya kazi vizuri sana kama Bwawa wa Mwalimu Nyerere litazalisha umeme wa kutosha lasivyo vijini umeme hautatosha. Tulionao sasa hivi hautoshi kuendesha vijiji vyote Tanzania nzima. Chanzo cha Mwalimu Nyerere ni muhimu sana kutunzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niwambie tu Waheshimiwa Wabunge, umeme vijijini huleta maendeleo makubwa sana. Badala ya watu kulala mapema na kuogopa giza, sasa kuna vituo wanaangalia centers nyingi za television, vile vile umeme wanachomeleaji grill wanazalisha kutokana na umemea ambao umewekwa vijijini. Kwa hiyo mradi huu ambao unaanza kusuasua tena, sehemu yangu katika vijiji vingi Wakandarasi wamedolora. Iko haja ya kuwasimamia ili ahadi ya Serikali kama ilivyo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba vijiji vyote vitapata umeme mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashuhudia pia mpango huu unaelezea ujenzi wa barabara na madaraja makubwa ambayo yataleta mhemuko wa kukua kwa uchumi kwa kusafirisha mizigo na watu. Madaraja mengine yanaunga nchi jirani na kadhalika. Kwa hiyo Serikali ikazane kumalizia madaraja na meli ambazo zinajengwa sasa hivi kwenye maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo, kila mtu anajua kwamba kulima kama biashara au kulima kama shughuli unagusa asilimia 67, kwa sababu kila mtu hapa anakula, na tunamalizia mkutano hapa tukale, kwa hiyo kilimo ni jambo muhimu sana. Serikali katika mpango wake huu imekuja na wazo zuri sana la kutoa ruzuku kwa ajili ya wakulima wote na kusajili wakulima wako wangapi; na sasa tumeshapata wakulima 2,118,911 mwanzo. Hata hivyo mbolea ya ruzuku imeshaagizwa ya kutosha na inagawiwa. Jambo hili litakuza uchumi na litakuza tija ya mazao shambani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo kadhaa ambayo mengine yameelezwa katika mpango huu hasa maji. Maji ni kikwazo kikubwa sana cha maisha vijijini. Hata hivyo mpango unaelekezea kukuza mpango wa maji mpaka asilimia 74.5, vile vile asilimia 86.5 mijini. Jambo hili si dogo ni jambo kubwa sana. Tunaishukuru pia Serikali imejiandaa kununua mitambo kwa ajili ya kuchimba malambo, Mabwawa na vile vile kuchimba visima. Jambo hili linastahili pongezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, mpango unaelezea kuendelea kupata elimu msingi bure, vile vile pamoja na elimu msingi hii tumejenga madarasa, tumejaribu kujenga maabara katika sekondari zetu. Kwa hiyo mpango uko vizuri kwa njia hiyo na elimu ndio ufunguo wa Maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchumi wa bluu yako mambo mengi ambayo yameelezwa kwenye uchumi wa bluu. Hapa Tanzania bara kulikuwa na shirika kubwa sana linaitwa TAFICO, lilikuwa shirika ambalo linajiendesha vizuri na ambalo lilikuwa ndilo chanzo cha mlango wa boiashara ya uchumi wa bluu. TAFICO ikauzwa, baadaye ikarudhishwa sasa hivi inajikongoja, hamna chchote. Naomba Serikali katika mpango wake isisahau uchumi wa bluu ili tuweze kuvua samaki. Pia tutumie mpango huo kwa ajili ya kupata fedha na kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi huko Lindi. Hivi karibuni tulipata meli kubwa ya kwetu, kibiashara tumeipeperusha bendera ya Tanzania. Ile meli haiwezi kuteremsha Samaki hapa Tanzania, na tulikuwa na mgao wa Samaki karibia tani 300, sasa inaenda kuteremsha Samaki seashells zitiwe kwenye kontena ndio zije hapa Dar es salaam. Jambo hili linawashangaza hata tuliowapa hiyo meli, kwamba hatuna pakuteremshia Samaki wala hatuna bandari. Kwa hiyo katika mpango huo wa maendeleo nimeona tuna mpango wa kuendeleza ile Bandari ya Uvuvi Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulikuwa na mpango wa kununua meli nane; lakini siuoni ule mpango na kulikuwa na meli moja kwa ajili ya TAFICO, meli nne ilitakiwa ziende Zanzibar na meli nne zibaki Tanzania Bara kwa ajili ya kukuza uchumi wa bluu, lakini sizioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la mradi wa gesi asilia. Mimi sitaki mambo ya kujifikirisha Mwenyewe kwamba tutapata. Tunataka kujenga LNG pale Lindi, mimi nilikwenda kutembelea mradi wa LNG ughaibuni kule, na jana tulikuwa na wenzetu wa Mozambique hapa tukawauliza wenzetu vipi LNG? Majibu niliyoyapata kule nje yalikuwa ni kwamba wananchi hawanufaiki na LNG. Kama ambavyo watu walivyochimba malori na malori ya dhahabu hapa hatukupata hata senti tano mpaka tulipobadilisha sheria. Naogopa Mradi wa LNG huu, kama hatutakuwa na sheria ambazo zitatulinda, watu watachimba gesi na kuzipeleka nje. Kama vilivyo vitalu vya gesi huko high seas hatufaidiki sisi. Naogopa sana kuutia mpango wa LNG kwenye mpango wa Serikali bila kuwa na uhakika kwamba utatuingizia hela au la.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kengele ya mwisho hiyo naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kuniruhusu nichangie hii hoja yetu ya Taarifa ya Mwaka ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na Wizara ya Maji. Kamati yangu ilitembelea miradi mbalimbali inayofanywa na Wizara ya Maji, lakini pia Kamati yangu ilitembelea miradi mikubwa ya DAWASA huko Kimbiji, Dar es Salaam; mradi wa maji kule Mlandizi, lakini pia tulitembelea miradi mingine kule Mwanza, Butimba na kule Musoma, Kiabakari ya Bugingo na Butiama.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa miradi mikubwa hii iliyolenga kauli ya mama Samia Suluhu Hassan ya kumtoa mama ndoo kichwani. Na Serikali imetoa hela nyingi sana na miradi hii inakwenda vizuri. Mpaka tulipokuwa tumetembelea miradi hii ya maji ilikua imepata asilimia 70 hela za ndani na asilimia 81 hela za nje. Serikali imetekeleza miradi hii mikubwa ya Mwanza na Musoma.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na ule mradi wa miji 28 katika nchi nzima kama ambavyo tumeisikia huko nyuma, lakini tumeona kwamba miradi hii imekwenda na upanuzi wa mradi ule wa Ziwa Victoria. Katika Jimbo langu kwa mfano, nitapata vijiji 58 na kwa kweli mradi unakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, tulipata tatizo dogo, mkandarasi mmoja hayupo site licha ya kupewa site miezi minne iliyopita, hapo ndipo ninaomba nipate maelezo kwa nini. Lakini miradi mingine jimboni kwangu inakwenda vizuri na ninaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi; Kamati yangu ilitembelea miradi kadhaa na miradi hiyo, kwanza niipongeze Serikali kwa kuanza mradi ule mkubwa wa bandari ya uvuvi kule Lindi. Lakini tuliona bandari ile badala ya kuwa bandari peke yake ambako meli zitakuwa zinashushiwa samaki, Serikali ifanye mpango wa kubuni industrial park pale ili samaki watakaoletwa na meli zile za uvuvi wachakatwe palepale na kutoa mazao ya samaki badala ya kuwasafirisha samaki waende wapi. Kwa sababu Bandari ya Dar es Salaam haina eneo la kuweka samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika suala hilo tumeona kwamba Serikali haikuwa na uwazi viwanda gani vitakuwa pale. Na tungependa meli zote zipeleke samaki pale watoke pale kama mazao ya samaki.

Mheshimiwa Spika, liko suala la mpango mzima wa kutumia fursa ya uchumi wa blue. Sisi tulikuwa tumejipanga huko nyuma – bajeti ya mwaka jana – kununua meli za uvuvi na kufufua ile Kampuni yetu ya TAFICO. Lakini hela inayopelekwa kule tumeona ni ndogo sana, haiwezi kulifufua Shirika la TAFICO likarudi kama lilivyokuwa zamani. Kamati yangu inaishauri Serikali iweke hela za kutosha kuifufua TAFICO ili tuweze kufaidi fursa hizi za uvuvi na uchumi wa blue.

Mheshimiwa Spika, liko pia suala la kufufua, nimesema kwa kifupi TAFICO, lakini tulipotembelea pale TAFICO hali haikuwa nzuri sana, niseme tu ukweli. Na hata juzi nilijitembeza mwenyewe pale, bado hali iko vilevile. Kwa hiyo ninaomba Serikali yetu iupe nguvu mradi huu wa kufufua TAFICO, utakuwa na faida kubwa sana kuliko hali ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie sasa suala la kilimo. Kilimo mwaka huu kwenye bajeti hii na Serikali ya Awamu ya Sita inahitaji kuchezewa ngoma tukafurahia. Kilimo, Waziri, Mheshimiwa Hussein Bashe, amevaa viatu vya kilimo, na kama anavyotaka mama Samia Suluhu Hassan, wanafanya mambo makubwa mapya, wana maingizo mapya kwa mfano kilimo cha block farms, kilimo kile cha mashamba makubwa ambayo yataajiri vijana wengi sana. Lakini pia Wizara hii imejikitika katika kupatisha mbegu wakulima na kuongeza bajeti mpaka tukapata ruzuku ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri Serikali ijenge viwanda vyake vya mbolea ili kuondoa matatizo ya utegemezi wa mbolea kutoka nje ambayo kwanza inachelewa kuja na inakosana na vipindi au ratiba ya kilimo. Kwa kuwa na viwanda hapa kwetu tutakuwa na faida kubwa sana. Tumeshuhudia kiwanda kimoja kimejengwa hapa lakini hakitoshelezi kupeleka mbolea nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana mama Samia Suluhu Hassan kwa kuona lengo la kilimo kwa maono mapya, kwa matoleo mapya, na matokeo yake kilimo kimekuwa cha kibiashara na kimevutia vijana wengi kwenda kuchangia kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo mipango mizuri kabisa ya kupata mbegu kutoka kwenye Shirika letu la ASA, lakini pia tafiti mbalimbali zinaendelea katika mashirika yetu. Tatizo ni hela kuchelewa kwenda au kutokwenda kabisa. Tunashauri Serikali ipeleke hela hizo ambazo sisi tumeziomba kwa ajili ya kuleta mafanikio ya kilimo cha kisasa na kuleta uwezekano wa kuongeza tija zaidi na zaidi kwa kuwa na mbolea itakayopatikana hapa kwetu.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kuchangia hayo; ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana lakini niwie radhi leo sauti yangu sijui nani watani zangu wa Tanga wameniroga lakini nasikika. Nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie lakini kwanza nianze shukurani kwa Wizara hii ya Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Bashungwa, Mheshimiwa Silinde, Mheshimiwa Festo na Watendaji wote wa Wizara hii wamefanya kazi kubwa sana, mambo yameonekana Jimboni kwangu tumepata fedha za kujenga kituo cha afya lakini nimepata fedha za TARURA. Pia upande wa elimu kuna madarasa mengi yamejengwa hii ni juhudi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niwaunge mkono wenzangu wanaosema Waziri huyu ni mtiifu, Waziri hana mabega ya juu, ni Waziri mzuri kijana mzuri na ataipeleka mbali sana Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze suala la Mfuko wa Jimbo. Mfuko huu umewekwa kwa ajili ya kuchangia au kuchochea maendeleo ya Jimbo na bahati nzuri sana, nimpongeze Waziri huyu pia ameongeza Mfuko huu kutoka shilingi bilioni 11 mpaka shilingi bilioni 15.9 karibu shilingi bilioni 6 ameongeza. Ameona umuhimu wa kuendeleza Majimbo na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuunga mkono suala hili na kuruhusu fedha zitoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo la ugawaji wa Mfuko huu, Kitaifa Mfuko huu unagaiwa kutokana na mahitaji ya kuchochea maendeleo ya Jimbo, lakini kuna Majimbo tofauti. Majimbo mengine yana maji, yana umeme, yana barabara, yana kila kitu na Majimbo mengine hayana chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Jimbo ndiyo umejenga maboma ya zahanati, maboma ya vituo vya afya, lakini maeneo ambayo kuna maendeleo tayari fedha hizi ziangaliwe kwamba zigawiwe kwenye sehemu ambayo kuna mahitaji. Haina haja ya kugawa Mfuko wa Jimbo sawasawa kwa Majimbo yenye uwezo mkubwa na Majimbo ambayo ni masikini kabisa, ningependa sana Wizara ifikirie kuugawa Mfuko huu kwa mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia liko suala la Halmashauri zenye Majimbo zaidi ya moja lakini tofauti ya Majimbo hayo katika Jiografia. Kwa mfano Jimbo lina Kata 19 na Jimbo lina Kata 11, Kata 10 au Kata Tano lakini Mfuko unagawiwa nusu kwa nusu, sidhani kama ni sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni Jimbo langu la Tabora Kaskazini katika Halmashauri ya Uyui, Jimbo la Igalula lina Kata 11 na Jimbo la Tabora Kaskazini lina Kata 19, Mfuko unagawiwa sawa sawa. Kwa hiyo, maendeleo yanadumaa kwenye Jimbo kubwa imekuwa haraka namna hiyo? Ningeomba Mheshimiwa Waziri Bashungwa ufikirie upya vigezo vya kugawa Mfuko huu ili haki itendeke katika Majimbo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la elimu ya kufundishia na hili nalisema hapa kwenye Wizara hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sababu ni suala mtambuka kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara hii ya TAMISEMI. Kumefanyika tafiti nyingi sana kutambua kwamba je, Kiswahili kinafaa kufundishia masomo hapa Tanzania kwa elimu yetu darasa la kwanza mpaka darasa la saba na sekondari? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba nalisemea hapa kwa sababu ni muhimu ieleweke kwamba sera ya elimu ndio inayoamua lugha gani itumike. Lugha ya kufundishia duniani kote hakuna nchi iliyoendelea kwa kutumia lugha ya watu wengine. Hakuna kokote duniani ambako watu wameendelea kwa sababu wanatumia lugha ya watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uingereza wanatumia Kiingereza, Wafaransa Kifaransa, Wachina Kichina, Warusi Kirusi, Wajerumani Kijerumani, lakini Tanzania tunatumia lugha ya kufundishia Kiingereza watoto wanasoma Kiswahili Darasa la Kwanza mpaka Darasa la Saba, halafu wanabadilisha mawimbi wanaanza kutumia Kiingereza. Nusu ya elimu yao wanajifunza lugha badala ya kujifunza elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ifanye tena utafiti ziko tafiti zaidi ya 40 kwa miaka 46 imefanyika na zote zinasema lugha inayofaa kufundishia Tanzania ni Kiswahili. Sasa naomba Serikali ifanye utafiti mahsusi kwa ajili ya lugha ya kufundishia iwe lugha gani Tanzania. Mimi nina imani nilileta katika Bunge hili Muswada wa kutaka Serikali ilete mabadiliko ya sera ili Kiswahili kitumike kama lugha ya kufundishia. Katibu wa Bunge alinirudishia Muswada huo akaniambia kwamba Serikali inafanya mchakato na katika mchakato wa kuchambua sera lugha itafikiriwa pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina habari kwamba tumerudia pale pale kwamba lugha ziwe mbili Kiswahili na Kiingereza. Kwa hiyo, nina nia tena ya kuleta tena Muswada huo binafsi wa kuomba Serikali ilete Sheria ya Sera ya Elimu hapa kubadilisha lugha ya kufundishia iwe Kiswahili. Nitatumia Kanuni yetu ya kawaida Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka, 2020 Kanuni ya 94 na Kanuni ya 95. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hotuba hii ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na leo nina machache sana dakika tano zinanitosha. La kwanza, ni ombi, kumekuwa na maombi kwa wale wanaopenda kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia lakini pia lugha ya kujifunzia. Serikali ianzishe shule ya mfano ambayo itafundisha Kiswahili darasa la kwanza mpaka Chuo Kikuu, ili kufuta kabisa wazo kwamba Kiswahili kinafaa au hakifai kufundishia. Suala hili litaonesha mfano mzuri, nimekuwa nikisema hivi watu wanaleta hoja yangu mimi binafsi badala ya kuchangia hoja, wanasema wewe wanao wamesoma Ulaya au wamesoma nje ya nchi, wanangu wamesoma hapa hapa Tanzania. Watu wachangie hoja na kama hawakufanya research, hawakufanya utafiti, basi hawana haja ya kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la pili ambalo pia ni ombi, naomba Serikali ifanye utafiti mahususi je, lugha ya Kiswahili inafaa kufundishia au haifai kufundishia inafaa kujifunzia au haifai kujifunzia? Kumekuwa na tafiti kwa miaka 45 zote zinasema lugha ya Kiswahili ndio lugha mama kwa Tanzania inafaa kufundishia. Naomba Waziri Mheshimiwa Profesa Mkenda hebu, wafanye tena utafiti ili suala hili tulisahau kabisa, utafiti utoe jibu je, lugha ya Kiswahili inafaa kufundishia au haifai kufundishia? Watu waache kusema, watu wanaoomba Kiswahili sasa watoto wao walisoma nje ya nchi, watoto wetu wamesoma hapa hapa nchini na kwa kweli suala hili litakuwa la maana sana sana kama utafanyika utafiti leo ili kupata jibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Watanzania wajiamini kwamba Kiswahili ndio lugha inayofaa kufundishia lakini pia kuwe na utashi, kinachokosekana hapa naona ni utashi. Watu hawana utashi wa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia. Utashi wa kisiasa, nina imani iwapo kutakuwa na utashi wa kisiasa lakini uwepo utafiti wa kutosha kabisa kwamba Kiswahili hakifai au kinafaa. Utafiti wangu mimi mtu mmoja mmoja nimefanya, Kiswahili kinafaa kufundishia. Utafiti wa kina Profesa Mlama waliokuwa hapa jana, BAKITA, lakini pia TATAKI (Taasisi ya Taaluma za Kiswahili) pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamefanya utafiti na kuthibitisha kabisa kwamba Kiswahili kinafaa kufundishia. Wameandaa vitabu, vyote vipo lakini hatuna utashi wa kisiasa wa kukipenda Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna uthibitisho wa kutosha kwamba duniani kote hakuna nchi iliyoendelea kisayansi kwa kutumia lugha ya mtu mwingine lugha ya kuazima. Kote tulikokwenda kusoma nje ya nchi tumejifunza kwanza lugha ya nchi ile ndipo ufundishwe masomo ambayo umeenda kusoma. Uchina, Ufaransa, Uingereza, Urusi, Denmark, Sweden kote waliokwenda kusoma nchi za nje, watu wamejifunza kwanza lugha ya nchi ile kabla ya kujifunza masomo yale yaliyompeleka mtu kwenda kusoma. Nina Imani, leo naonekana kama nasema peke yangu, lakini baada ya miaka mitano, sita, kumi mtakuja kuniunga mkono lakini tusiache suala hili likapita kienyeji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana mimi kuniruhusu nichangie hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi naunga mkono pongezi zinazotolewa na Wabunge wenzangu kwa Wizara hii kwa ndugu yangu/mdogo wangu, Jumaa Aweso na Naibu Waziri Maryprisca Mahundi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii kwa kushirikiana na wenzao Mheshimiwa Katibu Mkuu Engineer Sanga na watumishi wengine wenye nidhamu nzuri sana katika Wizara hii hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha muda mfupi sana Wizara hii, Waziri huyu na wenzie wameokoa mamilioni ya fedha kutoka kwenye miradi iliyokuwa chechefu na hii haijapata kutokea kwa sababu miradi hii mingine imekaa miaka nenda rudi. Lakini pia nimehudhuria uzinduzi na Mheshimiwa Rais wa miradi mbalimbali kule Simanjiro Mugango, Kiabakari, Butiama na Misungwi. Miradi hii ilikuwa mikubwa sana na imepewa fedha na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na umeisimamia vizuri sana. Wizara hii haiwezi kupita bila hongera kubwa kutoka kwa Wabunge wote kwa sababu kila mahali Wizara hii imegusa tuwapongeze na hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia kwa kazi nzuri ya kuyavuta maji kutoka Ziwa Victoria na kuyapeleka kwa babu zao Wanyamwezi Tabora, Igunga, Nzega na Uyui; maji yenye thamani ya Shilingi Bilioni 615 na mradi ule umesimamiwa na unafanyakazi vizuri hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia sisi Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji tulitembelea miradi ya Kimbiji pamoja na Kisarawe II, ambayo ni miradi mikubwa imekaa muda mrefu sasa wameikwamua na inaendelea vizuri hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la upatikanaji wa fedha, ni lazima tuipongeze Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapa fedha Wizara hii kwa kiwango cha asilimia 95 cha mahitaji yao ya fedha zilizokuwa zimepangwa. Hongera sana mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto katika Wizara hii ambazo hatuwezi kukaa kimya kwa sababu tunataka tuwasaidie na wao waweze kutusaidia. Kwanza, ukosefu wa mafundi, fundi mchundo na fundi sanifu. Miradi hii mikubwa ya maji ambayo tumeongelea hapa imefanikiwa kujengwa vizuri itahitaji matengenezo. Mimi ninashauri Wizara hii ifanyekazi karibu sana na Chuo chao cha Maji na wakiwezeshe, ili hatimaye wapate mafundi wa kutengeneza miradi hii itakapoharibika. Pia liko suala la kupungua kwa maji.

Wizara na Mamlaka zake zote za maji na RUWASA waanze sasa kufikiria jinsi ya kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji hasa Mito na ardhi oevu, kuvuna maji ya mvua, na ikiwezekana kuhifadhi maji hayo katika mabwawa makubwa badala ya kuacha yakapotea. Maji haya yanaweza kutokana na madaraja ya kwenye reli lakini pia na madaraja ya barabarani badala ya kuachwa yakafanye mafuriko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, suala la kumalizia miradi ambayo imeanzishwa mikubwa lakini bahati mbaya sana haikamiliki. Mfano mzuri, tulikuwa na mradi wa Ziwa Victoria kuleta maji Uyui, Tabora, Nzega na Igunga. Katika Jimbo langu la Tabora Kaskazini kulikuwa na vijiji kadhaa ambavyo vimeorodheshwa; na Wizara hii ilibakisha fedha (bakaa) Shilingi Bilioni 25 na miradi hii kwenye vijiji hivyo ninavyovitaja vijiji vya Ikongoro, Kanyenye, Kiwembe, Mbiti na Mogwe gharama ya miradi ile yote kwenye vijiji hivyo ni kama Shilingi Bilioni 5 hivi. Walikuwa na Shilingi Bilioni 25 lakini vijiji vile mpaka leo havijapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina hakika hii hali ya kuacha miradi na fedha zipo inatuletea kasoro katika Wizara hii na mimi ninafikiri, Mheshimiwa Aweso na wenzake watarekebisha mara moja ili miradi itakayoanza na ambayo ina fedha ikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo pia suala la makusanyo ya masurufu au fedha kwa ajili ya mamlaka zao za maji na RUWASA. Sasa hivi tunakusanya fedha hizi kwa kutumia dira au mita za maji, na kuna wasomaji. Sio vibaya ndugu yangu Mheshimiwa Waziri Aweso, Naibu Waziri na Katibu Mkuu mkaiga wenzenu wa TANESCO ambao waliiga mita za LUKU kutoka Afrika Kusini. Si vibaya na ninyi mkaiga hizi mita za LUKU; na tena niwapeni njia rahisi, mkaziita Lipia Maji Kadri unavyotumia (LUMAKU) na watu watakuwa tayari kulipia hayo maji kabla ya kuyatumia. Hii itaingiza mapato ya kutosha kwenye mamlaka za maji lakini pia RUWASA. Pia itaondoa gharama za udanganyifu wa watu wanaokwenda kusoma mita ambao ni chechefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mradi wa Miji 28, tumeusikia; mimi naunga mkono, kwamba Waziri amesema kabla ya bajeti hii kabla ya mwezi Juni, mradi huu utaanza na kwamba Mheshimiwa Rais ameunga mkono na ameridhia mradi huu uanze. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nautaja mradi huu kwa sababu nami utanipitia utakapopita kwenda Sikonge. Utakapokwenda Urambo vijiji vyangu kadhaa vitapata maji na kutimiza jumla ya vijiji 58 katika Jimbo langu. Ukipita kwenda Urambo Vijiji vya Kata za Ndono, Ufuluma, Makazi, Mabama, Lakasisi A, Kalola na Isila vitapata maji kwa sababu viko ndani ya ile kilometer 12 za bomba la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, Mungu awatangulie na awape afya njema Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Jumaa Aweso, ndugu yangu Maryprisca Mahundi, Engineer Sanga na watumishi wote wa Wizara hii ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo imetandawaa kwenye bajeti yote, lakini pia imekuwa mtambuka kwa maoteo ya bajeti yote ya Serikali kwa mwaka huu unaokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo niko hapa kuipongeza Serikali. Pamoja na upungufu ambao umetajwa na CAG, nimeweka kiporo kwa sababu kwa kweli siyo muda wa kujadili hotuba ile, hotuba ile itakuja baadaye baada ya kuangaliwa vizuri kwenye Kamati yetu ya PAC. Najua taarifa ile imeonesha uchafu, lakini kuifua nguo inaruhusiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kuipongeza Serikali kwa mambo makubwa; miradi mikubwa ya kiuchumi ambayo imefanya hata ikasababisha uchumi wa nchi hii kubaki kama ulivyo na pia bila kukua kwa bei za vitu. Japo bei zimepanda, lakini kiujumla, nitamke wazi wazi kwamba, sisi hapa tumefanya huu mfumuko wa bei ubakie chini kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mikubwa ambayo imejengwa na Serikali ambayo inajengwa sasa hatuioni kwamba muhimu, lakini ni muhimu sana. Nikiitaja kwa mfano Bwawa la Umeme la Rufiji, Reli ya SGR, ujenzi wa madaraja, ujenzi wa meli kadhaa maziwani, ujenzi wa barabara za kisasa, ununuzi wa ndege, miradi ya afya, miradi ya maji, miradi ya elimu, na kadhalika, mambo haya yakikamilika, nchi hii itapaa na watu wengi watakuja kushangaa kwa nini tulifanya hali ngumu hii na tukamwona Mheshimiwa Mama Samia anahangaika, lakini badaye watu watafaidi na watafaidika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo langu tumefanyiwa miradi mingi sana. Alama ambazo ziko kwenye jimbo langu ni mfano wa kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. Kwanza elimu; bado wanafunzi wanasoma bure, vile vile tumejenga madarasa, nyumba za walimu na kituo kikubwa kabisa cha VETA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maji, jimboni kwangu kuna mwamba chini ukichimba visima maji yanakauka. Leo tumetandaza maji ya Ziwa Viktoria, tunafungua maji kwenye mashamba na chini ya miti. Leo kuna vijiji 64 vina maji ya bomba kutoka Ziwa Viktoria. Hili siyo jambo dogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umeme, tulipoanza hapakuwa hata na Kijiji kimoja chanye umeme. Leo kuna vijiji 51 vina umeme katika jimbo langu. Hili siyo jambo rahisi. Pia barabara za ndani, tumekuwa na barabara kila mahali ambako kulikuwa hakuna barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya afya. Sisi jimbo lile ni jipya na Wilaya yetu ni mpya, ilikuwa haina hospitali ya Wilaya. Tumejengewa hospitali ya Wilaya nzuri kabisa, lakini vituo vya afya katika jimbo langu, vinne vinajengwa, vilevile tumejenga zahanati katika jimbo langu na kule kulikokuwa hakuna huduma ya afya, sasa inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utawala bora. Serikali ya Awamu ya Sita haikutusahau. Halmashauri ya Uyui haikuwa na majengo kabisa. Naipongeza sana Serikali, sasa tuna majengo mapya ya Halmashauri. Hili limetufanya sisi wana-Uyui tujisikie kwamba ni sehemu ya utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili ambayo ninadhani ni muhimu sana niyachangie leo. Katika Jimbo langu na Wilaya yangu ya Uyui tunaishi na ahadi za Marais watatu kuhusu kujenga Kituo cha Afya. Huu ni mwaka karibu wa tatu, wa nne, au wa tano umepita, lakini Marais wote; Marehemu Benjamin Mkapa, Marehemu John Pombe Magufuli na Rais wa sasa waliahidi kujenga kituo. Ilitokea historia ya kituo hiki kujengwa na Marehemu Benjamin Mkapa. Alikwenda kufungua kituo kidogo cha afya, lakini alipokwenda akasema kituo hiki ni kidogo, mimi nina miaka 97, naahidi kwamba, nitajenga hospitali kubwa hapa. Akamaliza muda wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoingia madarakani tumeenda kuanzisha mradi wa kituo kile, alipokuja marehemu Magufuli, Rais wangu aliyetangulia, nikamwambia kuna ahadi ya Mheshimiwa Benjamin Mkapa, akasema anzeni, nami nakuja kuchangia, tutamaliza, na nitakuja kufungua mimi. Bahati mbaya amefariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia alikuja Tabora Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wangu mpendwa, mama mwenye maono makubwa, nikasimama tena nikamwambia, kuna ahadi ya Marais wawili. Akasema hili jambo litafanyika mara moja. Wakati huo Mheshimiwa Silinde alikuwa Naibu Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Akamwambia hili tafuteni hela mara moja, hili limeisha. Sasa kumekuwa na kuhamishwa Mawaziri huku na huku, suala lile la hospitali ile ya ahadi ya viongozi watatu, limekuwa mwiba kwa wananchi, hawaelewi kwa nini hospitali ile haijengwi,
tumejenga sasa mpaka imefikia wodi ya mama na watoto, lakini bado ahadi hiyo haijatekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia liko suala la pili ambalo linanisumbua mimi. Tumekuwa tunashauri humu ndani kwamba ni muhimu sana kupanua wigo wa kodi. Mimi nimetoka katika sekta ya ulinzi binafsi na kule kuna hali nzuri sana ya kukusanya kodi, lakini kampuni zile karibu 1,200 sasa hakuna GN wala sheria ya kuiziongoza. Kwa hiyo, zinajiendea tu. Tumejaribu kuzikusanya huku na huku sisi wenyewe tumekusanyana na kuanzisha sekta ya ulinzi binafsi. Chama chetu kinaitwa Tanzania Security Association lakini ni vigumu sana kusema wanalipaje kodi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunagombania kodi. Nilileta Muswada Binafsi hapa mwaka 2017, na Muswada ule ulinigharimu sana kwenda nchi za nje kutafuta input za Muswada ule. Nilipouleta hapa, Muswada ulipelekwa Bungeni kwa Katibu wa Bunge, lakini Mheshimiwa Spika na wataalamu wote wa Bunge wakapitia Muswada ule wakasema unafaa, Serikali ikauchukua ikasema itauleta hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutumia Kanuni ya 94 ambayo inaruhusu Mbunge kuleta Muswada Binafsi Bungeni, na kanuni hizi ndiyo zinatulinda sisi hapa tuweze kufanya kazi kama Wabunge, mpaka leo Serikali haijaleta Muswada huu. Licha ya kuahidi na kuuliza maswali ya kibunge, lakini Muswada huu utasaidia kodi, utasaidia mapato ya Serikali, utaanzisha mamlaka kama vile EWURA, mamlaka kama vile ya kusimamia sekta hii ya ulinzi binafsi ifanye vizuri. Tangu mwaka 1980 zikiwa kampuni mbili, zimekua mpaka kuwa kampuni 1,200, lakini hakuna sheria, hakuna kanuni, wala miongozo ya kampuni hizi. Serikali inapoteza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulisema juzi juzi hapa, tozo, tozo! Leo tozo tunafaidika, tunajenga barabara, tunajenga shule na kadhalika. Tozo au kodi itakayotokana na uendeshaji bora wa kampuni za ulinzi zitafaidisha wananchi na zitafaidisha Serikali. Kwa hiyo, nilikuwa naomba, ili kuweza kupanua wigo wa kodi, basi Serikali ilete ule Muswada wa Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu waajiri; kumekuwa na matatizo sana huko kwa waajiri, lakini mjue waajiri tumefanya kazi kubwa sana ya kuzuia migomo hapa nchini, kwa kuongea vizuri na wenzetu wa TUCTA na wafanyakazi wenzetu. Sisi tunalalamika; nina maana waajiri wanalalamika, sheria ile ya Na. 6 ya Mwaka 2004 imepitwa na wakati, inatakiwa ifanyiwe mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baraza linasaidia kutunga sheria za kazi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Maige, kengele ya pili.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana namimi kunipa fursa hii ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka huu wa 2023/2024. Kwanza naipongeza Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kuongeza Bajeti hii ya Kilimo tena mwaka huu kwa asilimia 29, ni pongezi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia maeneo mawili tu. Nitachangia zao la tumbaku lakini pia kilimo cha umwagiliaji. Kuhusu zao la tumbaku, kwa kipindi cha miaka minne zao la tumbaku lilikaribia kufa kabisa. Mimi humu ndani Bunge lililopita walikuwa wananiita mzee wa matumbaku, kwa sababu nilikuwa napambana kweli kweli kuleta kilimo cha tumbaku juu lakini bahati nzuri sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alisikia kilio hicho vilevile akafanya hatua kubwa sana, leo anastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ule tunapambana kulikuwa hakuna ununuzi wa tumbaku na wakulima walikuwa tumbaku yao hainunuliwi na wakati fulani ikiitwa makinikia, lakini hivi sasa tunaongelea masoko ya tumbaku yanarindima huko Tabora na maeneo mengine ya tumbaku. Hili siyo jambo rahisi, tulikuwa na wanunuzi watatu na mmoja akaondoka akiwa TLTC lakini tumepata sasa wanunuzi wa tumbaku sita kutoka wawili. Hongera sana Serikali na Mheshimiwa Bashe hatua kubwa waliyochukua ya kutafuta wanunuzi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haitoshi Mheshimiwa Rais ametuteulia Waziri wa Kilimo ambaye ni mtoto wa matumbaku. Mheshimiwa Bashe siyo kwamba tu anayasikia matumbaku, kaona tumbaku inavyolimwa na alishuhudia jinsi ilivyokuwa tabu wakulima wakivaa ukosi wa shati kwa sababu tumbaku wanayo, wamelima na hawana pa kuiuza. Leo tumbaku imepanda bei kutoka senti 65 ya dola mpaka dola 3.2 kwa soko la leo. Hii ni hatua kubwa sana na mapato makubwa kwa wakulima wangu wa tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haikutosha hiyo, Mheshimiwa Rais ametuteulia mtu mmoja muhimu sana. Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Mwambalaswa ambaye alikuwa Mbunge humu ndani kabla ya kutoka kwenye tumbaku amekulia kwenye zao la tumbaku. Matokeo haya chanya yanayotokea yanatokana na malengo ya Mheshimiwa Rais kumteua pia Mheshimiwa Bashe lakini pia kumteua Mheshimiwa Mwambalaswa. Tunampongeza sana sisi wakulima wa Tabora Mheshimiwa Rais kwa mambo hayo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo matatizo ya tumbaku yaliyokuwa yanatukabili miaka iliyopita sisi tumekulia tumbaku, tulipoona inazama tukaona kama nchi hii imetutupa. Imekuwa historia, tunachekelea, lakini pia juhudi kubwa sana imewekwa. Wabunge humu ndani tumepambana sana kutetea zao letu la tumbaku lakini Waziri Bashe amekuja ametetea sana, Serikali Mama Samia imetetea sana, mpaka kuliweka sawa zao la tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mnunuzi mmoja anasema yeye yuko tayari kununua tani 90 za tumbaku, ambazo ni sawa sawa na kilo milioni 90 za tumbaku kwa mwaka yeye pekeyake. Pia anajenga kiwanda cha tumbaku cha kutengeneza sigara hapa Morogoro. Hii ni hatua kubwa sana na hili zao linaingiza fedha nyingi sana. Kama nimesema tunalima kilo hizo nilizozitaja 120 milioni, kwa kila kilo ikiuzwa kwa shilingi dola 3.2 ni mapato mengi ya fedha za kigeni katika zao la mkakati la tumbaku. Tuipongeze sana Serikali kugundua hilo na kuitendea haki tumabku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusemea pia mambo mengine katika kilimo, hasa kilimo cha umwagiliaji. Hatuwezi kuendelea na kutoboa au vijana wanasema na kutoka kwa kutegemea kilimo cha kudra za Mwenyezi Mungu cha mvua. Mvua na hali hii ya tabianchi inaanza kunyesha, wakulima wakianza kulima inanyesha katikati ya mazao kutaka kukua, mvua imekatika. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, ameweka fedha nyingi sana kwenye umwagiliaji na ndiYo njia pekee itakayotutoa sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawapati mvua, hakuna mvua kabisa. Wanaishi, wanalima kwa sababu ya kumwagilia. Sisi hapa tuna nchi kubwa sana, tuna maji mengi sana chini, tuna mvua zinanyesha, maji yanapita madarajani. Maji haya yakusanywe kama ambavyo imeonyeshwa katika mradi unaokuja sasa hivi wa kilimo cha umwagiliaji. Tukifanya hatua kubwa mbili tu; moja, kilimo kiwe cha mashamba makubwa na tunakwenda huko, BBT; mashamba ya block farms; lakini yawe mechanized, yawe ya ulimaji na umwagiliaji wa mitambo kwa maji kutoka kwenye mabwawa. Hii ndiyo njia peke yake naiona ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imeiona itatutoa. Hatuwezi kunyamaza Wabunge bila kuipongeza Serikali. Hongera sana Mama Samia, hongera sana Mheshimiwa Bashe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni muhimu sana kukumbuka kwamba kilimo hiki kimebadilishwa sasa kimekuwa cha kibiashara. Kwa hiyo, vijana wanaofundishwa kilimo, watakaolima sasa, licha ya kuwa na kilimo cha kujikimu tu pekee, sasa kitakuwa kilimo cha kibiashara, watu watapata hela mashambani na watapata hela za kula. Hili ni wazo kubwa ambalo tumechelewa kulipata, lakini kwa bahati nzuri, Wizara hii ya Kilimo imechukua suala hili la kilimo cha biashara na kilimo cha mashamba makubwa kuwa mfano katika nchi ya Afrika Mashariki. Hili litatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tupongeze kwamba hela zipo katika bajeti hii ya sasa za kufanya mabadiiliko haya makubwa ambayo tunayasema. Hili likibadilishwa kama tunavyoliona kwenye maandishi haya ya Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, basi kilimo cha nchi hii kitabadilika na baadaye tutakuwa katika hali ya kujilisha, na pia uchumi wa nchi utakua na kilimo sasa kitachagia kiasi kikubwa katika mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina suala lingine dogo. Wakulima wa tumbaku baada ya kuamka sasa, wana mamilioni ya fedha, wanauliza kwa nini wasilipwe kwa Dola? Wana sababu. Wakulima hawa wanakopesha pembejeo kwa Dola, mabenki yanalipa vyama vya ushirika kwa Dola, lakini vyama vya ushirika vinawalipa wakulima kwa Shilingi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Almas.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kukushukuru sana, lakini naomba sasa vyama vya ushirika viwalipe wananchi, wakulima kwa Dola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na mimi kuniruhusu nichangie hii hoja ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa bajeti yao ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitachangia mambo mawili tu, la kwanza, litakuwa lugha ya kufundishia na la pili, elimu ya ufundi. Mambo haya mawili sio mageni humu Bungeni na wala sio mageni Serikali na hasa mimi pia sio mgeni kwenye mambo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nijiunge na watu wote Wabunge waliochangia kuishukuru Serikali yetu. Serikali hii ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya mambo makubwa sana katika kukuza elimu na hasa bajeti pia. Pia tunapata elimu bure, ujenzi wa miundombinu, madarasa, maabara, nyumba za walimu lakini mabweni. Hii inatupunguzia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Pofresa Mkenda na Wizara yake kwa kujituma sana na kuonesha haya, kuyatekeleza maoni ya Mheshimiwa Rais, kwa vitendo, wote Wizarani nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la lugha kufundishia elimu yetu, najua liko tatizo la watu kupenda mambo ya kigeni, kupenda mambo ya kizungu. Moja kwa lugha lakini pia hata kwa mavazi na kusema mtoto huyu amesoma sana anaongea kingereza kama maji au anaongea kifaransa kama maji. Kwa hiyo, amesoma sana, wanalinganisha elimu na lugha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hapa Tanzania, Serikali ilikuwa na mpango mzuri wa kuendelea kutumia kiswahili kama lugha ya kufundishia na ikachukua muda mrefu, Serikali iligharamia gharama kubwa sana kuandaa vitabu vya kufundishia baada ya Elimu ya darasa la saba Kidato cha kwanza na chapili na wataalamu kule TATAKI Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliandaa vitabu hivyo wakiwa tayari sasa baada ya tafiti nyingi kuonyesha kwamba mtoto ili aelewe maarifa lazima afundishwe kwa lugha ya mama yake, na lugha ya mama hapa Tanzania asilimia 85 ni kiswahili kwa hiyo Serikali ilijikita kufanya tafiti na kupata majibu hayo wakaamua sasa watafute vitabu vya kufundishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iligharamia gharama kubwa sana kuandaa vitabu vya kufundishia baada ya elimu ya darasa la saba Kidato cha kwanza na chapili na wataalamu kule TATAKI Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliandaa vitabu hivyo ikiwa tayari sasa baada ya tafiti nyingi kuonyesha kwamba mtoto ili aelewe maarifa lazima afundishwe kwa lugha ya mama yake, na lugha ya mama hapa Tanzania asilimia 85 ni Kiswahili. Kwa hiyo Serikali ilijikita kufanya tafiti na kupata majibu hayo wakaamua sasa watafute vitabu vya kufundishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi hapa leo nimesikitika sana matokeo ya Tume ya mapitio ya Sera pamoja na Mitaala kupendekeza kwamba nyuma tutakuwa na lugha mbili za kufundishia kama ilivyokuwa zamani kiingereza na Kiswahili. Hii mimi ninaona kwamba tunarudi hatua kubwa sana nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spoika, mimi hapa nina vitabu. Jiografia kidato cha pili na mwandishi, ni Makunda lakini pia hiostoria kidato cha kwanza na Mwandishi Sago na Jiografia kidata cha kwanza, mwandishisi Makunda huyo. Pia nina kitabu Misingi ya Umeme na Sumaku, mwandishi Almasi Maige. Pia nina kitabu hapa kidato cha kwanza baiolojia mwandishi Isack na mwenzie Mustapha, nina kitabu hapa cha kidato cha kwanza Jifunze Kemia mwandishi Lema na Kimbi, nina kitabu hapa Uraia Kidato cha Kwanza mwandishi Kajigiri lakini nina kitabu hapa Mwandani wa Fundi Umeme mwandishi Almasi Maige, nina kitabu hapa cha Hisabati Kidato cha Kwanza mwandishi Saidi Sima, na nina kitabu hapa cha Fizikia Kidato cha Kwanza mwandishi Thadei na mwenzie Kiiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini kimetokea kupiga gia ya kinyume Serikali bila kutoa sababu. Mimi ningefurahi sana Waziri akisimama hapa atoe sababu kwa nini wameamua kurudi nyuma baada ya gharama kubwa hii iliyofanywa na Serikali ya vitabu vyote kidato cha kwanza na cha pili na kuwa tayari nani amesema turudi nyuma?

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna nchi yoyote iliyoendelea kisayansi kwa kutumia lugha ya watu wengine. Wafaransa Kifaransa, Waingereza Kiingereza, Warusi Kirusi, Wajerumani Kijerumani, Wachina Kachina, na kadhalika. Zipo nchi pia za wenzetu, Misri katika Afrika na nchi nyingine kadhaa sisi nini kinatushinda?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Kiswahili kimekua na kutumiwa kote, lakini kinachoendelea kule wanasoma kama somo. Mapendekezo ya mapitio ya sera pamoja na elimu wanasema na sisi Tanzania tunatumia Kiswahili kama somo. Ndio wenye Kiswahili lakini tunatumia Kiswahili kama somo. Sisi tulitaka, mimi na wenzangu ambao ni wazalendo, wanapenda lugha ya Kiswahili, tuna uthibitisho kwamba mtoto akifundishwa Kiswahili ataelewa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejivua, inasema kwamba wanaotaka sasa kutumia Kiswahili waanzishe shule zao na wanaotaka Kiingereza waanzishe shule zao. Inawezekana, watu hao watakaoanzisha shule zao watapata wapi gharama za kutafsiri vitabu kama hivi vyote viwe vya Kiswahili, watapata wapi walimu hawa wa kufundisha? Hili ni jukumu la Serikali. Serikali inashindwa, Serikali sasa ituambie kwamba sasa jukumu la elimu liwe kwa watu binafsi. Kwa sababu ni nani mtu binafsi ataanzisha shule ya Kiswahili? Haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kukwepa, wanafanya mchepuko kwa sababu ambazo sisi hatuzijui. Mimi sijaelewa kwa nini Serikali isije na msimamo wa kusema hatutaki elimu hii ifundishwe Kiswahili. Na mimi nimekuwa nasema, kwa nini Serikali isianzishe shule ya mfano watoto wakasoma darasa la kwanza mpaka la sita Kiswahili, wakaendelea mpaka sekondari school Kiswahili? Labda hadi kidato cha pili cha tatu na cha nne tukaona matokeo yake? Kwa sababu watakuwa wanasoma Kiingereza kuanzia darasa la kwanza watakuwa pia wanajua Kiingereza. Kwa hiyo ikionekana elimu haifundishiki Kiswahili huko mbele hii shule watajiunga Kiingereza. Kwanini Serikali haitaki kufanya hivyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi wanatushangaa sana Watanzania, sana, nawaambieni. Mimi nasafirisha rangi nchi za nje kule, nikiwaulizia taaluma yetu ifundishweje wanasema kwa nini msitumie Kiswahili kama vile Wachina, Wafaransa, Waingereza na kadhalika? Kwetu ni nini kimetokea? Mimi ninapendekeza Serikali isijivue jukumu la kuendesha shule ya mfano ya Kiingereza, lakini pia nashauri vilevile pamoja na kuanzisha shule hiyo Serikali ianzishe shule hiyo ya mfano na shule hiyo iangaliwe, ichague wanafunzi wazuri kuanzia darasa la kwanza mpaka shule ya sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naiongelea Elimu ya ufundi. Ninaipongeza sana Serikali kwa kuja na mfumo ule na kubainisha kwamba kunatakiwa kuwe na mitaala miwili, mmoja unaitwa huu elimu amali au elimu ya ufundi. Wako watu humu ndani tulisoma elimu hiyo ya ufundi, akina engineer manyanya. Tuliicha baadaye kwa sababu ilionekana kwamba huko mkimaliza wote mna-degree sawa huyo aliyesoma mtaala wa ufundi na aliyesoma mtaala wa kawaida tunapata mishahara tofauti. Mtu aliyesoma kutoka Dar es Salaam Technical College akarudi kuwa mhandisi pale anapata mshahara kima cha chini ya mhandisi aliyesoma chuo kikuu, kwa hiyo Elimu hiyo ikafa. Leo tumeona, ninawapongeza sana. Kwamba mitaala yote miwili itaenda sawa na mtu wa mwisho kule, mhandisi wa mwisho kutoka taaluma hii ya amali na ya kawaida wote watakuwa na thamani sawa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu na mimi nichangie hoja hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo mawili ya kuchangia katika Wizara hii. Kwanza ni shukrani; na ninaipongeza sana Serikali kwa kazi nyingi na miradi mikubwa inayofanya na kwa kipindi hiki chote ambacho tumepita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mikubwa imefanyika ikiwemo viwanja vya ndege, barabara, madaraja, meli zinazojengwa huko, vivuko na baba lao kabisa SGR. Baada ya miradi hii kukamilika Serikali itakuwa bingwa wa usafirishaji wa nchi kavu, pia usafiri wa baharini na katika maziwa kote nchini; lakini bila kusahau maombi ya wenzetu wana Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema hongera sana kwa Mama Samia Suluhu Hassan na Wizara hii na hasa Profesa Mbarawa na wenzake wamefanya kazi kubwa sana. Sisi kule kwetu Unyamwezini tuna msemo unasema “hapana kujidharau” au kinyamwezi “yaya kuibyeda.” Hili ni jambo kubwa sana sana, hela za ndani na za nje lakini tumejenga barabara zetu madaraja na yale niliyoyasema yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni kuhusu suala la bandari ya Dar es salaam. Kwanza nikiri kwamba mimi ni mkandarasi daraja la kwanza, kwa hiyo naitumia sana bandari hii kuagizia vitu kutoka nje. Bandari ilivyo sasa ilifika wakati mimi nilipata hasara kandarasi tatu; mradi mkubwa wa STR pale Arusha na mradi wa ZBC kule Zanzibar na mradi wa Bunge hili. Wakati tukiagiza mitambo kupitia bandari palikuwa na matatizo makubwa sana, meli zilikuwa zinakaa nje muda mrefu mpaka leo zinakaa nje muda mrefu lakini vilevile kulikuwa na ukiritimba ambao ulifanya mimi nicheleweshe mizigo kuleta kwenye miradi kwa hiyo nikapigwa adhabu kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za bandari si huduma, ni biashara, na wafanyabiashara wanafanya biashara ili wapate faida, hakuna mfanya biashara anayependa kupata hasara; na bandari ina kipimo au KPI, na KPI kubwa ya bandari ni kutoa mizigo. Kama bandari haitoi mizigo inakuwa hasara kubwa sana. Lakini nimejifunza kwenye bandari nyingine, kwa sababu wakati fulani tuliacha kupitisha mizigo, nikiwemo mimi mwenyewe, kupitisha mizigo Bandari ya Dar es salaam tukapitisha Mombasa.

Muda wa kupeleka mizigo kule na kupeleka magari kuleta mizigo tena Dar es salaam au Arusha ilikuwa muda mfupi kuliko meli iliyokaa muda mrefu pale bandarini, kwa siku 21. Asubuhi unaambiwa meli yako imefika lakini bahati mbaya unaambiwa rudini meli iko nje siku 21na mzigo unatakiwa uje kwenye site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hiyo ni bahati kama mzigo umefika moja kwa moja, lakini bahati mbaya zaidi ukifanyiwa Tran sequent, yaani mzigo unaokuja Dar es salaam meli inaona kwamba hautoshi mzigo kuja Dar es salaam inaancha mzigo Durban halafu meli nyingine ifuate kule inayokuja huku ikae wiki tatu inangojea mzigo kuja hapa, matokeo yake mzigo unachelewa sana, sababu ni nini uwezo wa bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu tusiangalie hapa usoni tuangalie huko mbele tunakokwenda. Ndani ya miaka mitano sita Bandari ya Dar es salaam haitafaa tena kufanyia kazi kubwa kwa sababu meli kubwa zinazoitwa kizazi cha nne na tano au fourth and fifth generation, hazitaweza kuweka nanga Bandari ya Dar es salaam mbili tatu au nne kwa pamoja kwa sababu bandari ni ndogo sana. Inatakiwa bandari hii ipanuliwe na iwe kubwa, lakini mpango mzurini kujenga Bandari kubwa ya Bagamoyo. Tunataka tufanye hivyo sisi, hatuna uwezo, hatuna hela za kujenga Bandari ya Dar es salaam, kuipanua kuweka vifaa vya kisas.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bandari nyingine kila dakika kumi contena tatu nne tano zinatoka sisi hapa kontena ngapi kwa siku? kontena ngapi kwa wiki? Meli zimepiga foleni kule nje tunataka aje mwekezaji ambaye atakuwa na nia ya kuendesha bandari kama ilivyo kule duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishasema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haifanyi biashara, bandari siyo huduma ni biashara, kujitoa Serikali na kuweka mkandarasi, kuweka mwekezaji ambaye atakuwa na malengo mawili kwanza a- operate aendeshe bandari lakini licha ya kuendehs bandari ile awe na lengo la uwekezaji kuipanua bandari lakini bandari imefika kikomo haiwezi kupanuka ni ghali sana. Njia rahisi mwekezaji huyo anayekuja awe na wazo la kujenga Bandari kubwa ya Bagamoyo ili tuweze kufanya biashara ya usafiri wa meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napata tabu sana watu ambao hawaoni umuhimu wa kuipanua bandari, kuikuza bandari, ni sawa na kuwa na ng’ombe mzuri mmoja au wawili umewakamata unasema wa kwangu. Watu wanakwambia ngoja tuwalishe hao ng’ombe wewe unasema a’ a’ ng’ombe ng’ombe wangu. Ndivyo ilivyo Bandari ya Dar es salaam tutaendelea kuikamata sisi bandari ile haitatusaidia baada ya miaka kumi, itakuwa absolute, haitafanya kazi na fedha hatuna, tuna miradi mikubwa sana ya kufanya huku bara kwenye maeneo mengine kuliko bandarini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashauri na ninashauri kabisa, aje mkandarasi, lakini hatutaki mkandarasi aliyekuwa mbaya kama TICTS, tunataka mkandarasi ambaye atakuja na malengo yanayojulikana na Serikali ituhusushe wadau wote tuone atafanya nini, na tukubaliane mkandarasi atapata hiki na wananchi au Serikali ya Tanzania watapa hiki ili tuweze kuleta ufanisi wa bandari yetu. Sasa hivi bandari hii itatudodea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina uhakika baada ya makubaliano mazuri ya mwekezaji mzuri, aje na malengo mazuri na Serikali ikubali, bandari itakuja kuwa eneo la biashara kubwa na kuingiza hela kwenye Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nakushukuru sana kuniruhusu kuchangia, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita kwenye jambo moja tu la kujaribu kuelezea Sekta ya Ulinzi Binafsi (Private Security Industry). Sekta hii ilianzishwa huko Ulaya miaka mingi iliyopita, lakini ilianzishwa baada ya kuwa na sheria zake zote na kanuni zake ndipo wenzetu wale wakaanzisha hii sheria. Sekta hii ya ulinzi binafsi hapa kwetu Tanzania imeanza mwaka 1980 yaani miaka 43 iliyopita na hapakuwa na sera wala sheria wala GN.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii inafanya kazi chini ya mwamvuli wa ulinzi wa raia na mali zao na wakishirikiana na Jeshi la Polisi, lakini sekta hii inafanya kazi zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ulinzi wa watu (man guarding), kusindikiza hela (cash in transit), ulinzi wa mitambo (security installation) kama tunayoiona hapa Bungeni, huduma za zimamoto (fire rescue), upelelezi binafsi (private investigation), lakini na ulinzi wa watu binafsi ambao unaitwa bodyguard au kifupi bouncers.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta sasa imeajiri ajira karibu 450,000 nchi nzima na hili ni jeshi kubwa sana. Linasaidia sana kupata kodi, lakini pia limesaidia ajira kwa vijana wetu. Sasa yako makampuni elfu mbili na zaidi, wakati ilipoanza mwaka 1980 ilikuwa na kampuni mbili tu, lakini sheria inazotumia ni za kiraia yaani sheria ile ya BRELA ya Usajili wa Makampuni, lakini Sheria ile ya Ajira na Mahusiano Kazini ya Mwaka 2004.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zote hizi mbili ni za kiraia na hazifai kutumia kwenye sekta ya ulinzi binafsi kwa sababu sekta ya ulinzi binafsi ni karibu jeshi. Kwanza wanavaa kijeshi, lakini vile vile wanafanya kazi zile zile kama za polisi yaani kulinda raia na mali zao, lakini wanavaa sare za kijeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilianzia wapi hii sekta ya ulinzi binafsi? Ilitokana na ombwe mwaka 1980 wakati Mheshimiwa aliyekuwepo, IGP Philemon Mgaya alipomwomba Mheshimiwa Rais wakati ule Mheshimiwa Mwinyi, ili wapate fursa ya kulinda mali ambazo zilikuwa zimetaifishwa na Azimio la Arusha, wakarudishiwa wenyewe mwaka 1980 na kuondoa mgambo au polisi waliokuwa wanalinda mali hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pakawa na ombwe kubwa sana hakuna sasa walinzi na kwa vile ilikuwa haraka haraka Mheshimiwa Rais Mwinyi akatoa ruhusa ya kuanzisha sekta ya ulinzi na ndipo yakaja makampuni mawili la Group Four na Ultimate Security. Tangu hapo makampuni yamekua na kuendelea kufanya kazi ambazo nimezitaja hapo juu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa limejitokeza, yako mapungufu makubwa na mengi kwa sekta hii binafsi kuendeshwa bila sheria, kanuni wala miongozo. Kwa hiyo hatuna sheria wala mamlaka, kule nje kuna mamlaka (Private Security Industry Authority) kama vile EWURA au TCRA na kadhalika. Kwa kukosekana mamlaka hizo Private Security Industry Authority (PSIA), kampuni za ulinzi hazina madaraja. Ukitangaza kazi kampuni yoyote inaomba kazi bila madaraja. Tofauti na wakandarasi. Wakandarasi lazima uwe daraja la kwanza mpaka la saba, lakini makampuni haya hayana madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni haya ya ulinzi hayatambuliwi na mashirika ya kigeni yanayokuja hapa kwa sababu hayana certification, hayana uthibiti. Kwa hiyo makampuni haya yanazurura tu na yanapata tabu sana ikitokea kazi, kwa mfano, kwenye gesi kwenye oil, lakini pia kwenye migodi, lazima yajiunge na kampuni nyingine ya nje ili yapate kazi huko na imekuwa hasara kubwa sana na huduma kwa kampuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako matukio mengine mabaya sana katika sekta hii kutokana na kutokuwepo kwa sheria, kwa mfano, walinzi kushtakiwa kwa mauaji. Watu wamevamia lindo na askari ana bunduki, akipiga akaua jambazi anashtakiwa kwa mauaji, wakati polisi wakipiga jambazi wanapongezwa na kupewa vyeo, lakini wote wanafanya kazi zile zile. Hili ni pungufu moja kubwa sana. Bahati nyingine wakati fulani hawa askari walinzi binafsi walitoka kwenye Jeshi la Polisi au Jeshi la Wananchi. Wana vyeo vikubwa wale walinzi kuliko wale walinzi ambao wako pale pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wateja wa sekta kuumizwa na kukosa pa kukimbilia. Kwa hiyo wako watu sana waliajiri walinzi, lakini wakaumizwa. Walinzi kugeuka majambazi, wakawaibia wateja wao, lakini pia walinzi kuwadhulumu wateja kwa mfano, wizi wa Tawi la CRDB Azikiwe, mabilioni yalichukuliwa kwa mpango wa kupanga, lakini pia kesi ya Kasusula mnaifahamu, alitumwa kwenda kuchukua dola 2,000,000 akaondoka nazo kutokea Airport.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wizi wa NBC Moshi mabilioni yalichukuliwa. Walinzi wa shule ya sekondari ya wasichana huko Tabora mchana wanalinda, usiku wanaenda wanawaibia wasichana, wakampiga mlinzi akafa, lakini walinzi kuuawa malindoni huko Temeke, walinzi waliuawa pamoja na mlinzi mmoja wa polisi na mlinzi mmoja aliyekuwa Sajenti Mstaafu wa sekta ya ulinzi binafsi. Mambo mabaya yalitokea pale. Yule Polisi aliyekuwa junior staff akazikwa kwa bendera ya Serikali huyu wa sekta binafsi akatupwa kama maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tiba ya kasoro hizi ni kuwezesha sekta ya ulinzi binafsi iwe na sheria yake. Iwe na mamlaka yake Private Security National Authority na hii itatokea tu kwa kuleta sheria ndani ya Bunge lako. Nilileta sheria ya sekta hii hapa mwaka 2016 na Serikali iliipenda sana ikaichukua sheria hiyo kwa mategemeo kwamba wangeiletea haraka iwezekanavyo lakini nashangaa mpaka leo haijaja. Kwa hiyo nimwambie Waziri nina mpango wa kukamata shilingi niende nayo Uyui aifutae huko Tabora Uyui ili atueleze, nataka tu commitment ya Serikali, Serikali itoe ahadi lini sheria hii itakuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nakushukuru sana kwa muda wako. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nami nichangie hoja hii ya hotuba ya Wizara ya Fedha na Mipango, lakini pia mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii yenye mapato na matumizi ya mwaka 2023/24 ni bajeti ya wananchi. Na hii tumpongeze sana Mheshimiwa Rais, bajeti imebeba unafuu wa maeneo kadhaa muhimu kwa ajili ya wananchi. Mimi nampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan lakini pia kwa kuweka vipaumbekle vya sekta zifuatazo; elimu, maji, barabara, nishati na afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hizi ndiyo zinazongoza kwa maendeleo ya wananchi. Wananchi wakipata mafanikio katika haya mambo matano, ndiyo watakuwa wamesema tumepata maendeleo. Maeneo haya matano yanagusa wananchi wote Tanzania na ndiyo maana nasema kwa kweli bajeti ya mwaka huu ya mama Samia Suluhu Hassan na ndugu yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Wizara yake, ni ya wananchi. Hongereni sana Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wataalam wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa mliyoifanya kuandaa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitaje maeneo ambayo yametugusa sisi wananchi, na haya ni baadhi tu; moja, tozo ya SDL au ujuzi wa elimu. Tozo hii nilipoingia Bungeni hapa ilikuwa ni asilimia sita ya kila mfanyakazi wa sekta binafsi mshahara wake analipiwa na mwajiri asilimia sita. Na hii ilikuwa taabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya kuomba kazi katika Nchi za Afrika Mashariki, ile gharama ya ajira kwetu ilikuwa iko juu sana. Hii tozo haipo Uganda, haipo Rwanda wala Burundi, Kenya ipo asilimia ndogo tu kwenye sehemu ya utalii. Lakini Tanzania ilikuwa asilimia sita. Leo nasimama hapa – na ninaomba nitoe taarifa kwamba ni mwajiri imepunguzwa kutoka asilimia sita mpaka asilimia tatu; sisi waajiri tunampongeza sana mama. Na hili hakika hatutamsahau. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, kuondoa ada za vyuo vya kati. Nimesoma vyuo vya kati hivyo, vinaitwa elimu ya ufundi ama elimu ya amali, kutokea shule ya msingi na kwenda shule ya upili (sekondari) form one mpaka form four (kidato cha kwanza mpaka cha nne) unachagua masomo ya kiufundi, halafu unakwenda chuo cha ufundi. Wakati huo zilikuwa shule mbili tu, Shule ya Sekondari ya Ufundi Ifunda na Moshi Technical. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunalipwa hela na Serikali sisi kusoma pale. Sijui ilitokea nini wakaondoa ikalazimu wanafunzi walipe ada pale, wazazi wenye uwezo wa chini walishindwa kupata wataalamu wa ufundi kwa sababu hatukuweza kulipa tena ada; tunamshukuru sana mama Samia na kwa hilo mama Samia hatuwezi kukusahau kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni Serikali kutofunga biashara kwa sababu ya migogoro ya kodi kati ya wafanyabiashara na Serikali. Suala la kufunga biashara ilikuwa inafunga mapato ya Serikali, ilikuwa inafunga kodI za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ndugu yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, umepiga ndipo. Kwa kuondoa hizo gharama za kuwafungia watu, wengine wamepoteza roho zao, wengine wamekufa, ilikuwa taabu sana. Hebu fikiria una biashara yako unakula na unaishi halafu imefungwa kwa sababu ulikosea kidogo mahesabu na siyo watu wote ni wataalamu; umefanya jambo zuri sana, Mungu akuongoze na hatutakusahau. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne; mapendekezo ya Serikali yanalenga kuendeleza miradi iliyopo. Nimepitia bajeti yote hii, inalenga matrilioni ya fedha ili kumaliza miradi inayoendelea kimkakati. Niitaje hapa; Bwawa la Mwalimu Nyerere, SGR, Daraja la Magufuli, ununuzi wa ndege, ujenzi wa meli, ujenzi wa barabara, kuendeleza REA (umeme), ujenzi wa viwanja vya ndege, ujenzi wa vituo vya afya, elimu bure, kuongeza bajeti ya kilimo. Haya siyo mambo madogo. Ndiyo maana nasema leo hii, na ninaweza kusema kifua mbele kwamba bajeti hii ni ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kulijali sana jimbo langu. Jimbo la Tabora Kaskazini ukifumba macho ukaangalia mambo yaliyopita lilikuwa la ajabu ajabu sana. Leo tumepata hela nyingi sana kupitia Halmashauri ya Uyui, tumepata fedha nyingi sana kutekeleza miradi ya elimu, maji, umeme, barabara, afya na utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Uyui ilikuwa hana majengo, tulikuwa chini ya mti tumejishikiza kwa DC. Tumepata majengo ya shilingi bilioni nne, majengo mazuri ya kisasa. Tena ndiyo ghorofa la kwanza kijijini kule lipo; tunamshukuru sana mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaka unda haneni, maana yake akinena kishapata, naogopa kuyasema mambo mazuri yanayokuja kwangu, lakini wacha niwatajieni machache, hamtayaondoa. Kwa ufupi, bajeti hii iliyomalizika imefanya mambo yafuatayo katika Jimbo langu, na nimesema niyataje; tumejenga kituo cha VETA, tumejenga madarasa mengi ya shule za sekondari na msingi, tumejenga mradi wa BOOST, tumepewa shule mpya ya msingi (milioni 500), mpya kabisa tujenge; tumepewa shule ya sekondari mpya tujenge (milioni 470). Na kuhusu afya tumepewa vituo vya afya vitatu tumejenga na vimekamilika. Lakini pia tumepewa zahanati mbili na zahanati nyingi tumekarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya siyo madogo ya kuacha kupongeza. Ni lazima tumpongeze mama huyu ambaye ana utu, ana mapenzi na wananchi wake, lakini ni mlezi wa wananchi wake, ametuona sisi Uyui. Nani kama mama? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Hakuna.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji, nikwambie, ndiyo nimesema mtaka hunda haleni msione wivu kidogo. Jimbo la Tabora Kaskazini lina vijiji 68 tunafungua maji ya bomba chini ya miti kutoka Mwanza Ziwa Victoria na haya hayakuwepo kabisa. Leo tuna maji ya bomba ya Ziwa Victoria lakini pia mradi wa ile miji 28 katika vijiji vyangu 82 utaongeza vijiji vinavyopata maji mpaka vifike 72. Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Mwigulu na Wizara yako, mmetutendea mambo mazuri sana Jimbo la Tabora Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na umeme, umeme tulipoingia madarakani sisi hata Kijiji kimoja hapakuwa na umeme. Leo hii nasimama hapa nasema vijiji 58 tunawasha umeme, bado vijiji 24, na ambavyo mpaka mwezi wa nane unakamilika. Hii ni bajeti ambayo sisi wana Uyui tunaiona kama ni ndoto vile lakini ni bajeti ambayo tunafikiria kwamba imetubeba vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara, Jimbo langu ni jipya, Wilaya yangu ni mpya tulikuwa hatuwezi kutembeleana barabara hakuna tumejenga barabara. Mama ametupa ela nyingi karibu bilioni tatu tujenge barabara na barabara zimekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeitaja miradi hii ambayo ni alama za utu, upendo na ulezi wa Mama Samia Suluhu Hassan jimboni kwangu. Pongezi nyingi kutoka kwa wana Uyuwi Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge hoja mkono, Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya Wizara ya Nishati kuhusu bajeti yao kwa mwaka 2022/2023. Kwanza nijiunge na Wabunge wote wanaotoa pongezi kwa Wizara hii. Nimefurahi sana Mheshimiwa Rais kumteua mwanangu Makamba kwa sababu baba January tunajuana sana mimi na yeye, ni marafiki. Wamefanya kazi nzuri sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele hivi walivyoviweka hapa vikitekelezwa nchi hii haitaingia tena gizani, tuwapongeze sana. Unajua ukisema juu juu bila kuzama chini huwezi kufanikiwa, ukitaka kuijua Wizara hii, uende ukaone mitambo yao, ukaone station zao, ukaone wanakozalisha umeme na kazi ngumu. Wizara hii peke yake ndiyo umeme ukikatika unarudi baada ya muda mfupi. Zamani tulikuwa na simu unaripoti simu mbovu, wiki nne, wiki tano haijatengenezwa. Umeme unaripoti na mjue Waheshimiwa Wabunge kila mtu anayewasha umeme haukuja kwa rimoti kama microwave, umeungwa na waya mpaka Kidatu mpaka unaposindikwa umeme huu, ni jambo gumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema katika Jimbo langu tulipoingia madarakani Awamu hii ya Sita na Awamu ya Tano kulikuwa hamna hata kijiji kimoja chenye umeme leo nina Vijiji 41 vina umeme na unawake. Hata juzi wamewasha umeme katika vijiji vyangu vinne Kinyamwe, Ibelamirundi, Ikongolo, Utemini na Ndono na kule ni msituni, sisi Tabora tuna misitu, lakini wanapitisha umeme katikati ya msitu na unakwenda katika vijiji. Hili si jambo la kubeza, ni jambo la kuwapongeza sana, hongereni sana Wizara ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mama Samia Suluhu Hassan kurithi mradi ule mkubwa wa umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere, ni fedha nyingi sana linajengwa lile bwawa, amejikita na Mawaziri wake Waziri Makamba na mwenzie Naibu Waziri kumalizia mradi huu, siyo jambo rahisi tumpongeze Mama Samia Suluhu Hassan sana. Ni moja ya miradi waliyosema itatelekezwa mbona inaenda sana! lakini panapokwenda meli Zanzibar na mawimbi yapo tutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa mpango wa kuwa na miradi mingi ya kuzalisha umeme nchini, inalenga kutatua matatizo ya umeme kabisa. Zamani tulikuwa na mradi mmoja na mashine za kukodisha, lakini leo kuna mkakati wa kujenga mitambo yetu wenyewe ya kufua umeme. Mimi nina hofu ndogo sana, nina hofu ambayo sijui naogopa nini? Kituo cha Umeme cha Msamvu (Vital Installation) kimeungua mara mbili, unajua kwa nini naogopa? Kituo hiki kinaunganisha umeme unaotumika kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere na kila kinapoungua mradi kule unasimama, ni moja ya sababu ya kuchelewesha mradi ndiyo maana naogopa hii Vital Installation itaunguaje mara mbili pale pale? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kujiuliza ni hujuma au ni uzembe, ni nini sasa? Mheshimiwa Makamba tafadhali sana, naomba sana muweke kitengo cha uchunguzi, hii Vital Installation kuungua mara mbili kwa muda mfupi isiungue tena mara ya tatu inatuchelewesha. Nashauri sana hebu fungueni macho muangalie kuna nini huko? Zamani TANESCO walikuwa na kitengo kile cha Business Intelligence na kulikuwa na watu kutoka TISS wanafanya kazi huko, Mheshimiwa marehemu Kasanzu na Mheshimiwa Kiza walitoka TISS kwenda kusimamia ulinzi na usalama wa vituo Vital Installation ya TANESCO. Sijui kama imerithiwa au inaendelea sina hakika, naomba sana Mheshimiwa Makamba usimamie ulinzi wa vituo vyako vya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utafutaji wa mafuta, mimi sijui kwa nini Tanzania hatujapata mafuta, sina sababu inayoniweza nikawaza nikajua kwa nini hatuna mafuta Tanzania? Kwa sababu wenzetu walivyopata mafuta ni ushoroba ule ule wa Bonde la Ufa na sisi linaanzia kwetu hapa kwanini sisi hatuna mafuta? Najiuliza ni teknolojia tu tunayotumia kutafuta mafuta au utaalam ni mdogo au uwekezaji mdogo au hakuna utashi ni hujuma ni ukosefu wa uzalendo na nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Makamba hili mimi nitakukamata wewe, kwa sababu wewe ni kijana unayejua sana mambo haya, hivi kweli kwa nini hatupati mafuta? Huko Uwembele Tabora huko kuna mahali wanasema hapo panafaa mafuta yapo, uchunguzi ni mdogo sana unaokwenda kufanya kazi kule, wataalam wanaokwenda kule hatuwaoni wakabeba vitu vikubwa vya kutafutia mafuta, hamtaki kupata mafuta hapa? Kipaumbele cha kutafuta mafuta na gesi mmekiweka Namba 11 kwa nini kisiwekwe cha kwanza? Maana yake mafuta tunahangaika hovyo hata hatujui tufanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia gesi kule wenzetu Ruvuma kule wale watu wa Mozambique kwenye Jimbo lao wanaloungana na Ruvuma ndiyo wamepata gesi, trillion na trillions za cubic, sisi bahati mbaya hata hatujaanza kutafuta kule. Tafuteni gesi kule la sivyo gesi inatembea kama mkondo kule chini wakitoboa kule gesi itahamia kule yote, naombeni sana jaribuni kutafuta mafuta Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja ahsanteni sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kutamka rasmi kwamba naunga mkono hoja hii ya bajeti ya kufurahisha.

Nakushukruu sana kuniruhusu na mimi nichangie hoja hii ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023. Nianze kwanza na pongezi na shukrani. Mimi nampongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan kwa alama nyingi alizotuwekea katika Jimbo langu la Tabora Kaskazini. Niruhusu nizitaje baadhi ya alama ambazo kila mtu anaziona na ndiyo maana ninasema Mama Samia tunamuona kila siku Jimbo la Tabora Kaskazini. Mama Samia hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna miradi ya maji Ziwa Victoria Vijiji 58 vitapata maji kutoka Ziwa Victoria kutoka kule Mwanza hadi Tabora Vijijini tuna maji, pia umeme tulikuwa hatuna sasa tunavyo vijiji 41 umeme unawaka tunamshukuru Mama Samia. Kuhusu afya tulipewa fedha za kujenga zahanati Nne tumejenga tatu na moja inaendelea kujengwa, pia vituo vya afya vitano tayari vitatu, bado viwili vinaendelea kujengwa kikiwemo kile cha Marehemu Benjamini Mkapa pale Usagali. Tunampongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan, pia tumejenga hospitali kubwa ya Wilaya hongera sana Mama tunakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhsuu elimu, sawa tuna elimu ya bure kuanzia darasa la kwanza hadi Form Six, tuna kuunga mkono na tunampongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan, lakini pia tumejenga madarasa 17 ya shule za Sekondari na shule mbili shikizi, tunampongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan. Pia tunayo shule mpya inayojengwa tumepewa Milioni Mia Nne itakayoitwa Almas Maige kule Gilimba tunampongeza sana Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. Pia kipo kituo cha VETA ambacho kimegharimu karibu Bilioni Mbili kinakaribia kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niende kwenye bajeti, kabla ya bajeti kuna barabara sita zinajengwa kwa fedha ya bajeti iliyopita, kuhusu bajeti ya sasa tunao pia utawala bora ambao tumejengewa jengo la Halmashauri ya Wilaya jipya kabisa Shilingi 1,750,000,000.

Mheshimiwa Spika, kuhusu bajeti ya sasa Serikali inatakiwa ipongezwe sana na wananchi, tumeona kwamba bajeti ni ya wananchi kwa sababu imeongeza fedha za sekta ya kilimo kutoka Milioni 254 mpaka Milioni 954 hii haijapata kutokea, na sisi tumeona kwa sababu asilimia 75 karibu ya Watanzania wote ni wakulima bajeti hii imewagusa wakulima moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa nina ushauri wangu ninaomba Serikali ifanye jukumu kubwa sana la kufanya kilimo cha umwagiliaji na siyo kilimo cha mitaro, ni kilimo cha kumwagilia kwa mashine na ichimbe mabwawa au ipate maji kwa kukinga kwenye mabwawa ya mito wakati wa mvua au mito ya msimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa mbolea nashauri kwakweli turudi kama tulivyokuwa kule nyuma, tujenge viwanda vyetu vya mbolea ambavyo itafanya mbolea ipatikane kwa urahisi na kuwafikia wananchi na hasa wananchi wa Uyui.

Mheshimiwa Spika, lipo suala la ruzuku nchi zote duniani inatoa ruzuku kwa wakulima wao, tungependa pembejeo za wakulima wa Tanzania zipatikane kwa ruzuku na kwa mtandao wa nchi nzima kwa hiyo tutaongeza tija ya kilimo nchini kote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu kukuza bajeti ya kilimo hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2030, jambo hili ni la kupongezwa na Serikali itilie mkazo, isiwe porojo ya bajeti hii tulione linakua kila mwaka hadi mwaka 2030 tupate asilimia 10 ya Bajeti ya Kilimo iwe sawa na asilimia 10 ya bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu uchumi wa Bluu, tuna bahati kubwa ya kuwa na mito na maziwa mengi sana lakini bahati mbaya sana hatupati faida ya uchumi wa bluu na hapa ninapendekeza kuwa moja, tumekuwa tunaongelea bandari ya Bagamoyo ipo haja ya kusema sasa tunaijenga hiyo bandari ili iweze kuwa kitega uchumi chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono mawazo ya Serikali katika bajeti hii ya kujenga Bandari ya Bagamoyo, lakini pia tunaomba uendelee ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kule Lindi ili tuweze kupata mazao ya uvuvi kutoka meli mbalimbali ambazo zitatua pale.

Mheshimiwa Spika, lipo pia suala la kufufua TAFICO, TAFICO lilikuwa ndiyo shirika kubwa linalotengeneza faida hapa Tanzania tukaliuza, sasa nimeenda kutembelea juzi TAFICO unaweza ukalia hakuna chochote, lakini Serikali ina nia ya kufufua TAFICO ninaiomba Serikali yangu iweke nia ya kuweka fedha za kutosha ili TAFICO ilete faida hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika bajeti iliyopita tulikusudia kununua meli nane lakini mwaka huu bajeti imepungua kutoka meli nane hadi meli mbili, hata hivyo ninaipongeza sana Serikali kuwa na wazo la kununua meli za uvuvi mbili. Ahsante sana naipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Spika, suala kubwa la mwisho niliongee kwa kituo ni kuhusu kodi, wigo wa kodi ni mdogo sana, watu Milioni Tatu tu ndiyo wanaolipa kodi nchi hii katika watu Milioni Sitini, wigo huo hautoshi! Yapo maeneo mengi ambayo najua kwamba yakifanyiwa kazi yanaweza kuingiza fedha na wananchi wakalipa kodi. Kwa mfano, Sekta ya ulinzi binafsi hapa nchini ilianza na makampuni mawili sasa ina makampuni 3,500, imeajiri watu chungu mzima askari, kama ingesimamiwa vizuri kama ambavyo Serikali inasimamia SUMA guard wanapatiwa kazi lakini pia wanalipa kodi na kwa kufanya hivyo kama sekta ingesimamia Makampuni yote 3,500 tungepata fedha nyingi sana lakini hatuwezi kusimamia sekta ya ulinzi binafsi kama hakuna sheria wala GN ya kuanzishwa kwa sekta ya ulinzi binafsi. (Makofi)

Kwa hiyo, nashauri Serikali sasa ije na nia bora ya kuleta Muswada wa Sekta ya Ulinzi Binafsi hapa Bungeni ili iweze kuundwa mamlaka ya kusimamia makampuni haya ya ulinzi ya sekta binafsi ambayo itazaa hela nyingi na itakuwa chanzo rasmi cha mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nikushukuru tena na naunga mkono hoja kwa mara ya pili. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mimi kuniruhusu nichangie hii hoja ya Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Mimi nitaongelea mambo matatu, jambo la kwanza ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, pili ni programu ya kukuza ujuzi na Sheria ya Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Mfuko huu wa Maendelo ya Vijana. Mfuko huu ulianzishwa mwaka 1993 na mpaka mwaka 2023 ulikuwa umekopesha vijana wetu jumla ya shilingi bilioni 8.9 hongera sana Serikali. Mfuko huu una mapungufu makubwa mawili, kwanza Serikali imekuwa ikitenga shilingi bilioni moja kila mwaka tangu mwaka ule wa 1993 lakini hasa hasa kuanzia mwaka 2015 mpaka 2022. Kwa hiyo ukipiga hesabu jumla ya hela zote ilikuwa bilioni tisa lakini mpaka 2020/2021, 2021/2022 ilikuwa imekusanya bilioni moja tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali imeufelisha Mfuko huu kwa sababu mwaka 2022/2023 kulikuwa na maombi ya shilingi bilioni 6.7 ya mikopo lakini mfuko ulikuwa na shiling bilioni tatu tu, kwa hiyo ukashindwa kabisa kufanya wajibu wake. Mfuko pia umekuwa na utata wa pili wa kukusanya madeni ambapo mwaka 2022/2023 Mfuko ulipata marejeshio ya shilingi bilioni 2.6 lakini ulikuwa unadai jumla ya shilingi bilioni 4.6, kwa hiyo hela nyingi haijakusanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayochangiwa na theluthi moja ya Tozo ya CBL kutoka kwa waajiri wote Tanzania, Kamati ilibaini kuwa mgao huo umekuwa ukipungua kila mwaka. Mfano, kutoka bilioni 18 mwaka 2019/2020 mpaka bilioni tisa tu mwaka 2023/2024, upungufu huo umefanya idadi ya vijana waliotakiwa kuwasomesha kupata ujuzi kupungua kutoka 42,000 kwa mwaka mpaka 12,000. Jambo hili limeangusha programu nzima. Kwa hiyo, Serikali imepunguza idadi ya wanaotakiwa kupokea mafunzo hayo kutoka wale watu iliyokusidia kuwafundisha kwa mwaka 136,000 mpaka 12,000 haya ni mapungufu makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu nataka niongelee mahusiano yetu waajiri, Serikali na wafanyakazi, utatu ambao unasimamiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO). Tunaunganishwa na Sheria ya Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Sheria hii imepitwa na wakati, inashindwa kufanya kazi ya kutibu kasoro ya ajira na kazi na mahusiano kazini kama ilivyokusudiwa. Mfano mzuri tulipatwa na COVID hapa, COVID-19 matokeo yake nchi ilipokuwamba na COVID wafanyakazi fulani walizuiwa majumbani, wengine waliwekwa karantini hospitali lakini waajiri wengine walifunga, lakini muda wote huu waajiri walitakiwa kuwalipa wafanyakazi mishahara yao, hii haikuwa sahihi kwa sababu waajiri hawakuleta COVID hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wao kuendelea kuwalipa wakati hawazalishiwi mali yoyote na wafanyakazi ambao walikuwa wanafanya kazi kwa muda wa kulipwa kila siku wakang’ang’ania kwenda kazini ambako hakuna kazi na mwajiri amefunga mlango. Kwa hiyo, wafanyakazi waliokuwa wanapata hela kwa wiki hawakupata hela, waajiri mali haikuzalishwa lakini vilevile waliofungiwa ndani kwa sababu ya COVID hawakufanya kazi, lakini waajiri walitakiwa kuendelea kuwalipa. Tuona kwamba sheria hii sasa Serikali iilete kupia Baraza la Sheria za Kazi (LESCO) ili iweze kurekebishwa iweze kutibu kasoro au mapungufu haya ambayo tumeyaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia pia sekta ya ulinzi binafsi ambayo inafanya kazi kwa kutumia sheria hii ya kiraia ipo katika matatizo makubwa sana na haitendewi haki. Moja, hawa wa sekta ya ulinzi binafsi wanabeba silaha, wanavaa sare, wanafanya kazi kama askari lakini wanatumia Sheria hii ya Kiraia na sheria hii itakuwa sawa tu kama sheria hii ya Labour Relations Act ya mwaka 2004 itarekebishwa. Sasa hivi wafanyakazi hawa askari, walinzi wanalazimishwa kufanya kazi masaa mengi zaidi kuliko saa ambazo zimetajwa katika Sheria hii ya Labor ya sasa. Kwa hiyo, tungependekeza sheria mpya itakayokuja itibu pia tatizo la askari binafsi wa ulinzi ambao wanafanya kazi kama askari lakini wanatumia Sheria ya Kiraia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni nini? Wakati huo wote ambao askari hawa, walinzi hawa binafsi wanafanya kazi wanasukumwa na sheria hii ya sekta ya ulinzi binafsi ambayo haipo, lakini wanasukumwa sasa na sheria hii ya kiraia, matokeo yake waajiri wengi wako mahakamani - CMA kwa ajili ya kudai overtime au kwa ajili ya kutumikishwa masaa ya ziada kuliko ambavyo sheria inataka. Dawa yake ni kuleta Sheria mpya ya Ajira, Kazi na Maelewano kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa ruhusa, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Muswada huu naona kama umechelewa lakini ni muhimu sana. Kama tunavyosema, sekta binafsi ni uti wa mgongo au injini ya maendeleo ya uchumi, basi Muswada huu unakuwa kama mafuta kwenye injini hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu unafupisha muda wa kuangaliwa mradi ambao unatakiwa uwe wa PPP. Mradi huo unaopendekezwa sasa utapitia hatua nne tu badala ya hatua nyingi ambazo zilikuwepo kwenye sheria iliyopita au sheria inayorekebishwa leo. Mradi huu unaandaliwa na aidha Idara ya Serikali, Wizara au TAMISEMI unapelekwa sasa kwenye kituo cha ubia yaani PPP Center, pia mradi huu utapelekwa sasa kwenye Kamati uidhinishaji baada ya kuangaliwa pale chini, juu yake uidhinishaji na baadaye kwa Waziri wa Fedha na mradi pale unakuwa umetekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni njia ya mkato sana na njia ambayo itaeleweka kwa watu wote wanaotaka kuwekeza. Hapo zamani kwenye sheria iliyopo, haikuwa inajulikana mradi utauanzisha upeleke wapi yaani umeanzisha mwenyewe binafsi au Serikali imeuanzisha, hujui yule mbia wa sekta binafsi ataingilia wapi, lakini hata akiiingia itakuwaje baadaye? Tafsiri ya marekebisho haya yanaweka njia bayana kwa watu wote wawili yule wa sekta ya umma na sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu pia unayo malengo mazuri sana na kwanza ni kuweka masharti kwamba taarifa sasa ziripotiwe kila nusu mwaka yaani compliance ya reporting kutoka wanaotekeleza mradi. Vilevile marekebisho haya yanaruhusu miradi midogo midogo. Zamani ilikuwa ni vigumu sana mradi mdogo unatupiwa usoni, haufai kabisa, ilikuwa inachukuliwa miradi mikubwa ambayo ilionekana kwamba Serikali inaipenda, lakini pia itakuwa na faida kubwa badala ya miradi midogo ambao wananchi wa Tanzania tulikuwa hatuwezi kushirikiana nao. Sasa kwa kuweka nafasi ya miradi midogo midogo tutaruhusiwa pia watu binafsi kushirikiana na Serikali au sekta za umma na sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti imependekeza mambo fulani muhimu sana. La kwanza, inasema kuwepo na mfuko wa uwezeshaji wa miradi ya PPP. Hili halikuwepo huku mwanzoni. Vilevile imependekeza uazishwaji wa benki ambayo itasimamia au itatoa mikopo kwa ajili ya miradi hii ya PPP kwa sababu benki za biashara haziwezi kukopesha miradi ya PPP ambayo inachukua muda mrefu kuanza kupata faida na benki zinataka kupata faida hiyo haraka haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imependekeza pia mafunzo kwa watu watakaoandika mikata hii. Tumeshuhudia mikataba mingi mibovu imetutia hasara nchi yetu, hatutaki tena kuanza na bahati mbaya ya kubahatisha. Tunataka miradi iandikwe vizuri mikataba yake kusiwe na migongano huko baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuongelea hali halisi ilivyokuwa huko nyuma. Nina mifano ya miradi ambayo ilianzishwa kwa nia nzuri kabisa iwe PPP. Kwa kuchelesha miaka mitano au sita Serikali ikapata hasara ya mabilioni. Mradi mmojawapo ni wa daraja Kigamboni. NSSF walipoanzisha daraja lile na kuomba tuwe PPP na Serikali, na wale ambao, naomba radhi nilikuwa na conflict of interest, nilikuwa Mwenyekiti wa Waajiri Tanzania na nilikuwa mdau kwenye daraja lile, Serikali ilijivuta miguu mpaka wafadhili waliokuwepo wakajitoa na baadaye NSSF ikatumia nguvu yake kubwa kujenga daraja lile kwa hasara. Bei tuliyopewa mara ya kwanza na mjengaji wa daraja lile ikawa imezidi kwa karibu shilingi bilioni 10, hiyo ni hasara kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ambao umeshindwa kutekelezeka kabisa ulikuwa NSSF ingejenga line sita za barabara kutoka Chalinze kwenda Dar es Salaam. Tumeandaa upembuzi yakinifu na wataalamu wetu tukaiomba Serikali, Serikali ikasema itangaze mradi ile halafu na wengine wagombee kwa kutumia document ambayo sisi tumeiandaa, tukabaki nyuma. Matokeo yake mradi ule haujatekelezwa mpaka leo. Sasa Serikali inajaribu kuutekeleza pamoja na NSSF lakini kwa hasara kubwa kwa sababu bei miaka kumi iliyopita na leo ni tofauti sana. Hii ni mifano ya miradi ambayo Marekebisho ya Sheria ya PPP inajaribu kuondoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine mkubwa ambao ulishindikana ni wa kujenga Ubalozi wetu huko Nairobi. NSSF walitaka pia kujenga Ubalozi wa Nairobi kama mtakumbuka, wakati Mheshimiwa Rais wetu alipopewa hati ya kiwanja kule Nairobi, nasi tuliwapa hati ya kiwanja cha Dar es Salaam. Wenzetu wa Kenya wameshajenga nyumba yao, sasa wanafanya ukarabati sisi kiwanja kinagombewa Nairobi, kwa sababu tunavutana, PPP ilikuwa haieleweki. Sasa baada ya marekebisho haya kupita tunajua hatua ya kwanza ni upembuzi, hatua ya pili ni kupokea mradi, utatoka hapo mpaka hatua nne, tunajua mradi unashindikana au unakubalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuchangia hayo kwamba sasa marekebisho haya ni kama yamechelewa, lakini tushukuru Mungu yamekuja na tuyapitishie ili yatusaidie. Kama tunavyojua sekta binafsi ndiyo uti wa mgongo wa uchumi, lakini pia ndiyo injini ya uchumi kwa kuunganisha na Serikali tutakwenda mbele haraka na uchumi wetu utakua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia kwa mia. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia Muswada huu ulioko mezani leo, Muswada wa kutunga Sheria ya Kuanzisha Bodi ya Kitaaluma ya Walimu. Kwanza nami namshukuru sana Waziri wa Elimu na wadau wote ambao kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana kuuleta Muswada kama ulivyo. Pia ninayo machache ya kuchangia vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ualimu ni taaluma kama ilivyo taaluma ya uhandishi, udaktari, ukandarasi, sheria na kadhalika. Kinyume cha Bodi zote ambazo zinaongoza taaluma zetu hapa nchini, ualimu unaonekana kwamba siyo chochote na haukuwa na Bodi yoyote ya kitaaluma kuweza kuuongoza na kuusimamia. Matokeo yake watu wengi ambao hawana taaluma ya ualimu wameenda kufanya kazi ya ualimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sawasawa na watu fulani wajitolee kwamba wanajua udaktari waanze kutibu watu, hao waandisi bila kuzuiliwa chochote mtu ajitangaze yeye ni mhandisi aanze kujenga majengo kama hili Bunge letu. Kazi ya kuingiliwa namna hiyo ilitokea katika kazi ya ualimu tu. Kwa hiyo, kwa muda mrefu taaluma hii ya ualimu ambayo ni muhimu sana kwa kweli ndiyo mlango pekee kwa mtu yeyote anayetaka elimu kinyume chake ni kuingia ule mlango wa wajinga. Leo Bunge lako linajadili Muswada muhimu sana ambao utaunda Bodi itakayolinda elimu yetu. Mlango huu wa elimu utalindwa sasa kwa Bodi ya kitaaluma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ualimu ni taaluma, kwa hiyo matokeo ya watu kuingia katika taaluma hii na kufanya kazi, walifanya iporomoke. Matokeo yake walimu wakaanza kujitetea tu kwamba taaluma ya ualimu ni wito na wamedumu kwa njia hiyo kwamba ukiingia huku, basi ni wito usifanye mabaya. Matokeo yake ni nini? Baadaye maneno ualimu ni wito yakashindwa kubeba taaluma ya ualimu na tumeanza kuona kuporomoka kwa taaluma, walimu ambao hawakuwa walimu sasa wakaanza kufanya matendo mabaya, walimu ambao ni bandia wameanza kulala na wanafunzi wao; wameanza kuiba mitihani; wakaanza kuwasaidia wanafunzi kufanya mitihani; wakaanza kuwapiga wanafunzi bila mpangilio; na wengine wakawapiga mpaka wakawaua. Maneno kwamba ualimu ni wito hayakuweza kuhimili kishindo cha taaluma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunajaribu kuandaa tiba ambayo walimu waliingoja kwa muda mrefu sana. Kwa hiyo, Muswada huu uliopo mbele ya Bunge lako, utaleta taaluma ya ualimu kuwa sambamba na taaluma nyingine nilizozitaja hapo nyuma. Kwa kifupi, utasimamia taaluma ya ualimu na kuwa tiba ya matatizo yote ya walimu hapa nchini na hivyo kuleta jambo ambalo walimu wamekuwa wanalidai la usalama wa taaluma ya ualimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Muswada huu, kifungu cha 6(1)(a) mpaka (j) kimeweka majukumu ya Bodi ambayo tunaipendekeza. Bodi itafanya kazi ya kuweka viwango vya utaalamu wa ualimu; kusajili walimu wote nchini; kutakuwa na leseni ya kufundishia walimu; itasimamia uwezeshaji na kusimamia utoaji wa mafunzo kwa walimu; itafanya kazi ya kusimamia maadili na utaalamu wa walimu; itafanya kazi ya utafiti hususan kuhusiana na utaalamu wa ualimu nini kifanyike ili kuboresha tasnia hii; itafanya kazi ya kusikiliza mashauri dhidi ya walimu waliofanya makosa na kuvuruga au kwenda kinyume na maadili na taaluma ya Ualimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya siyo madogo. Mambo haya ndiyo walimu wamekuwa wakilia miaka yote kwamba tungefanyiwa hivi msingetulaumu kwa sababu wanaofanya makosa siyo wanataaluma ya ualimu ambao sisi tumesomea. Leo Serikali ya Awamu ya Tano imesikiliza. Najua Bodi hii au Muswada huu umekaa miaka mingi ukijadiliwa na walimu pamoja na wataalamu wa elimu na kufikia hapa tulipofikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo tunajaribu kutoa tiba ya matatizo ya walimu nchini. Kwa hiyo, ni lazima tunapokwenda, mambo ambayo yalikuwepo yatafutika kama mtu aliyefua nguo iliyokuwa chafu na kuwa safi. Bodi hii imeliliwa na walimu kwa sababu walitaka kuthaminiwa, kuheshimiwa na kutambuliwa kitaaluma. Kwa hiyo, kutungwa kwa Sheria ya Kuanzisha Bodi ya Kitaalam ya Walimu ni jambo muhimu sana kwa faida ya maendeleo ya elimu nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuchangia hivyo. Naunga mkono hoja, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nami kuniruhusu nichangie Muswada huu wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2021/2022. Muswada huu umelenga kukusanya fedha ambazo zitatumika katika Mpango wa Bajeti ambayo tumeipitisha hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Orodha ya Sheria ambazo zitarekebishwa ipo katika ukurasa wa pili na wa tatu wa Muswada wenyewe huu. Naomba nijikite katika maeneo yafuatayo; nianze kwanza kuishukuru sana Serikali. Kwa mara ya kwanza Serikali imefanya jambo kubwa sana la kusaidia kutuletea bajeti ambayo itasaidia wananchi wa chini kabisa wa nchi yetu na kila mwananchi atafaidi kutokana na bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite kwenye mambo yafuatayo; kwanza Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Sura ya 82. Idadi ya chini kabisa ya wafanyakazi watakaolipiwa SDL kutoka wanne waliokuwepo kwanza mpaka 10. Hii imetusaidia sana, lakini SDL tunayolipa hapa nchini ni kubwa sana, asilimia nne. Katika nchi zote za East Africa; hizi za Afrika Mashariki na SADC, ya juu kabisa ni 2%. Tunaomba kwenye bajeti ijayo, mwaka unaofuata, basi SDL tena iteremke kidogo baada ya kuongeza maeneo fulani ya kodi. Nami nashauri Serikali ijikite kwenye kupanua wigo wa kodi na eneo moja ambalo lina kodi kubwa ambayo haijulikani sana sana ni sekta ya ulinzi binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Serikali hebu ilete Sheria ya Sekta ya Ulinzi hapa Bungeni tuweze kuyatambua Makampuni yapo mangapi; yana wafanyakazi wangapi? Watalipwa SDL kubwa na kodi itapatikana badala ya kung’ang’ani kiwango kikubwa cha SDL kipungue kutokana na uwingi wa watu watakaolipa SDL. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Muswada huu utarekebisha Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta Sura ya 220 ili kupata fedha za TARURA. Suala hili ni zuri sana. Tumeweka kiwango kidogo sana, shilingi 100/= kwa aina yote ya mafuta kwa lita, lakini fedha hizi zitakuwa nyingi sana. Wabunge humu tunatumia lita ngapi kwa siku? Wananchi wa Tanzania nzima wanatumia lita ngapi kwa siku?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sio mtaalam wa mafuta, lakini nafiriki nikifumba macho naota mahela mengi yatakayopatikana. Sitaki tuje tuone aibu hapa. Waziri wa Fedha awe na fedha nyingi ambazo hajui pa kuzipeleka. Tuzipeleke kwenye Mfuko wa TARURA ili tuone kweli barabara zinajengwa kutokana na mfuko huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Muswada wake amesema kutakuwa na Mfuko Maalum wa TARURA ambapo fedha zitakwenda siyo kwenye Central Account halafu zianze kuchukuliwa moja moja. Jambo hili likitekelezwa, wananchi hawatakuwa na kilio cha kupandishiwa nauli kidogo, wataona barabara hii haikuwepo imejengwa, pale palikuwa hakuna barabara, pamejengwa; itasaidia kuzima kelele za lawama kwa Waziri kwa bajeti hii iliyoleta fedha za TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sehemu ya Nane inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Kodi Na. 332; Sehemu ya Nne, kupunguza Payee as You Earn. Jambo hili watu ambao sio waajiri kama vile halina mhemko, halina impact. Kwa kweli limetusaidia sana na wafanyakazi wenyewe pia kutoka asilimia 11 tuliyokuwa nayo wakati tunaanza Bunge hili mwaka 2015 mpaka 8%, ni fedha nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua tu Wage Bill, yaani gharama ya mishahara kwa mwezi kwa Serikali, shilingi bilioni 600, hebu toa 1% ile, ni fedha nyingi sana. Hata sekta binafsi inaajiri wafanyakazi wengi sana. Kwa hiyo, asilimia hii ndogo imetupa nafuu na Serikali tunaipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sehemu ya Tisa; marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Majengo. Hapa kuna utata. Maelezo ya Mheshimiwa Waziri juzi, Sura 289, jana yamekuja maswali sana. Wanasema sasa kodi italipwa kwenye Luku. Ghorofa 28 zipo na watu wa kazi kwenye sehemu mbalimbali ya jengo hilo kuna Luku. Sasa hivi tunalipa kodi hii mara moja kwa mwaka, sisi wenye majengo. Tunalipa kodi mara moja kwa mwaka ya jengo, mwezi Julai.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sijui Mheshimiwa Waziri alikuwa na maana gani kwamba kila tunaponunua umeme tutalipa kodi, itakuwa kila unaponunua umeme unalipa kodi, hakutoa maelezo ya kutosha. Je, hao wananchi au watu wanaokaa kwenye jengo la fulani ambao wapo 300 kwenye Luku 100; watakatwa fedha ambayo watampelekea tena Ankara huyu mwenye jengo?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri hakutoa maelezo, atueleze hilo, kwamba hawa wapangaji wangu mimi wataniletea hiyo bill waliyokatwa niwarudishie wao? Kwa sababu ninayetaka kulipa kodi ni mimi mwenye jengo. Haya ni masuala ambayo hayakueleweka vizuri. Ni jambo zuri sana kwamba kodi kweli italipwa, lakini kiwango kikubwa cha majengo hapa pia hayatumii umeme; ni asilimia ndogo sana umeme upo katika majengo ya mjini, lakini kuna majengo mazuri ukipita barabarani hapa Kibaigwa, sijui wapi, ukienda Chalinze kuna majengo mazuri sana yanatakiwa yalipe kodi. Mengine hayana umeme na mengine yana umeme, itakuwa tunapata taabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maoni yangu nafikiri kwamba, huu uchukuaji wa kodi ni mzuri sana, lakini yanatakiwa maelezo zaidi, nani atalipa mwishoni? Mwenye jengo au hao wenye Luku wamekuwa wachangiaji wa kodi ya jengo?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na huo ndiyo mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Tume ya Mipango wa Mwaka 2023.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nami nichangie Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, lakini mimi nitajikita zaidi kwenye ule Muswada wa Mapendekezo ya Sheria ya Usalama wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nakushukuru sana na kukupongeza kwa kusudio la kugombea nafasi ya Rais wa IPU. Mimi nafikiri utashinda, nina hakika kwa kaliba yako, taaluma yako na uwezo wako unaojionesha, Mungu atakutangulia na utashinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kweli kwa kuleta Muswada huu ambao utasaidia sana Idara ya Usalama wa Taifa kufanya kazi zake kikamilifu. Muswada huu ukipitishwa na Bunge lako Tukufu utaleta maboresho makubwa ya kiutendaji kwa Idara ya Usalama wa Taifa lakini pia Sheria inayopendekezwa italeta tija kwa wafanyakazi Maafisa wa Idara ua Usalama wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, majukumu makubwa na muhimu ya Idara ya Usalama wa Taifa yameendelea kulifanya Taifa hili liwe na amani na utulivu lakini kukuza uchumi kwa miaka mingi hawa watu.

Mheshimiwa Spika, Idara imezuia matukio makubwa ambayo yamezima chini kwa chini kama ilivyo kazi yao ya secret na sisi raia hatukujua matukio gani yametokea lakini mengine yalikuwa bayana kama Mapinduzi na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, Sheria inayopendekezwa itaziba mapungufu hayo yaliyokuwepo katika Sheria ya sasa. Hata hivyo naomba nipendekeze na mimi niweze kuchangia marekebisho ya vifungu vifuatavyo;- kifungu namba 24(1) kinachoweka zuio la watu walistaafu kuongelea mambo ya Idara kutoa taarifa za Idara kifungu hiki kitaimarisha sana usiri wa Idara lakini pia kuficha na kuwazuia watu wanaojifanya watu wa idara walifanya kazi zamani kusema mambo ya Idara na sasa Mkurugenzi Mkuu atakuwa na udhibiti huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina maoni mengine pia katika maboresho ya Kifungu cha 25 kinachozuia kuweka zuio la kuingia katika maeneo ya Idara ya Usalama wa Taifa. Maoni yangu ni kwamba masharti hayo ya kifungu hicho yangeongezwa kujumuisha pia mazuio ya kupiga picha au kuchora maeneo hayo kwa mkono au kwa njia yoyote ile kijiti au kifaa kingine chochote.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono pia malengo ya marekebisho ya Muswada huu kwamba ni kuleta usawa wa mifumo ya kiutendaji sawa na Idara za Kimataifa Duniani lakini kuboresha na kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika Sheria iliyopo sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono pia Idara hii kuwa chini ya Rais kwa sababu hii itampa nguvu Mheshimiwa Rais kuisimamia vizuri Idara hii lakini Mkurugenzi Mkuu atakuwa na nguvu zaidi kuliko ilivyo sasa kupitia kwa Waziri anayehusika.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono pia marekekbisho ya kifungu cha 10 ili kumtambua Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kwamba ndiye mtaalam anayeweza kumshauri Mheshimiwa Rais na kuishauri Serikali kuhusu masuala ya Usalama wa Taifa na huyu actually ndiye mtaalamu namba moja wa masuala hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono pia mapendekezo ya kuwalinda Maafisa wa Idara wanaofanya kazi baada ya kustaafu na wakiwa ndani katika madaraka yao kwa kazi wanaiyoifanya au kwa makosa yatakayotokana na utendaji wao wa kazi. Hii itawapa nguvu Maafisa hawa kufanya kazi kwa nguvu wakiwa na imani kwamba hawatadhurika baada ya matendo yao mazuri yaliyofanywa kwa uaminifu mkubwa kulinda nchi hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache nakushukuru sana kuniruhusu. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Yatokanayo na Urekebu wa Sheria wa Mwaka 2023 .
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nami nichangie Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, lakini mimi nitajikita zaidi kwenye ule Muswada wa Mapendekezo ya Sheria ya Usalama wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nakushukuru sana na kukupongeza kwa kusudio la kugombea nafasi ya Rais wa IPU. Mimi nafikiri utashinda, nina hakika kwa kaliba yako, taaluma yako na uwezo wako unaojionesha, Mungu atakutangulia na utashinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kweli kwa kuleta Muswada huu ambao utasaidia sana Idara ya Usalama wa Taifa kufanya kazi zake kikamilifu. Muswada huu ukipitishwa na Bunge lako Tukufu utaleta maboresho makubwa ya kiutendaji kwa Idara ya Usalama wa Taifa lakini pia Sheria inayopendekezwa italeta tija kwa wafanyakazi Maafisa wa Idara ua Usalama wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, majukumu makubwa na muhimu ya Idara ya Usalama wa Taifa yameendelea kulifanya Taifa hili liwe na amani na utulivu lakini kukuza uchumi kwa miaka mingi hawa watu.

Mheshimiwa Spika, Idara imezuia matukio makubwa ambayo yamezima chini kwa chini kama ilivyo kazi yao ya secret na sisi raia hatukujua matukio gani yametokea lakini mengine yalikuwa bayana kama Mapinduzi na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, Sheria inayopendekezwa itaziba mapungufu hayo yaliyokuwepo katika Sheria ya sasa. Hata hivyo naomba nipendekeze na mimi niweze kuchangia marekebisho ya vifungu vifuatavyo;- kifungu namba 24(1) kinachoweka zuio la watu walistaafu kuongelea mambo ya Idara kutoa taarifa za Idara kifungu hiki kitaimarisha sana usiri wa Idara lakini pia kuficha na kuwazuia watu wanaojifanya watu wa idara walifanya kazi zamani kusema mambo ya Idara na sasa Mkurugenzi Mkuu atakuwa na udhibiti huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina maoni mengine pia katika maboresho ya Kifungu cha 25 kinachozuia kuweka zuio la kuingia katika maeneo ya Idara ya Usalama wa Taifa. Maoni yangu ni kwamba masharti hayo ya kifungu hicho yangeongezwa kujumuisha pia mazuio ya kupiga picha au kuchora maeneo hayo kwa mkono au kwa njia yoyote ile kijiti au kifaa kingine chochote.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono pia malengo ya marekebisho ya Muswada huu kwamba ni kuleta usawa wa mifumo ya kiutendaji sawa na Idara za Kimataifa Duniani lakini kuboresha na kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika Sheria iliyopo sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono pia Idara hii kuwa chini ya Rais kwa sababu hii itampa nguvu Mheshimiwa Rais kuisimamia vizuri Idara hii lakini Mkurugenzi Mkuu atakuwa na nguvu zaidi kuliko ilivyo sasa kupitia kwa Waziri anayehusika.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono pia marekekbisho ya kifungu cha 10 ili kumtambua Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kwamba ndiye mtaalam anayeweza kumshauri Mheshimiwa Rais na kuishauri Serikali kuhusu masuala ya Usalama wa Taifa na huyu actually ndiye mtaalamu namba moja wa masuala hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono pia mapendekezo ya kuwalinda Maafisa wa Idara wanaofanya kazi baada ya kustaafu na wakiwa ndani katika madaraka yao kwa kazi wanaiyoifanya au kwa makosa yatakayotokana na utendaji wao wa kazi. Hii itawapa nguvu Maafisa hawa kufanya kazi kwa nguvu wakiwa na imani kwamba hawatadhurika baada ya matendo yao mazuri yaliyofanywa kwa uaminifu mkubwa kulinda nchi hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache nakushukuru sana kuniruhusu. Naunga mkono hoja. (Makofi)