Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Yahaya Omary Massare (34 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na taasisi inayoshughulika na kutoa asilimia 25 zinazotokana na fedha za wawindaji katika vitalu vya utalii katika maeneo yetu. Wilaya ya Manyoni tuna vitalu vya utalii lakini Manyoni kuna Halmashauri za Wilaya mbili, kuna Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vitalu 11 katika Wilaya yetu lakini vitalu saba vipo katika Halmashauri ya Itigi na vitalu vinne tunashirikiana pamoja na Halmashauri Mama ya Wilaya ya Manyoni. TAWA tumewapelekea taarifa siku nyingi na mipaka wanaijua, wamekuwa wakipeleka pesa za mgao zile asilimia 25 moja kwa moja kwa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni wakati Halmashauri ya Itigi ipo na akaunti zilishapelekwa kwao, lakini kumekuwa na kizungumkuti hatuelewi. Mpaka sasa hivi Halmashauri yangu ya Wilaya Itigi inaonekana inasuasua katika makusanyo ya ndani kwa sababu tu ya uzembe wa watu ambao hawataki kuwajibika katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri awasiliane na hawa watu na anipe majibu mazuri, kwa nini watu wenye maeneo hawapelekewi pesa katika eneo lao. Tuna Halmashauri kamili na tunatakiwa pesa zile ziende kwetu. Hivi tunavyozungumza pesa za mwezi huu ambao umekwisha hawajapeleka, lakini miezi ile iliyokwisha walipeleka milioni 128 katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na pesa za Itigi zikiwemo. Sasa ni kitu gani hawajui au hawataki, kama hawataki kutupa waseme tu basi ninyi mkae kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki na usawa huu Halmashauri kama ile tuanze kuhangaika wakati tuna kitu chetu pale. Naomba hawa wataalam, sasa sijui ni Mkurugenzi au ni nani kwenye hicho kitengo amweleze Mheshimiwa Waziri. Mimi nitalia na Mheshimiwa Waziri kwa nini sisi hatupati hizi pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tuna vitalu vya utalii, tuna mbuga ya Rungwa, Muhesi lakini na mbuga ya Kizigo. Rungwa, Muhesi iko katika Jimbo langu na kuna changamoto kadhaa zinazotokana na wanyama hawa kuwemo katika maeneo yetu, wamekuwa wakivuka mipaka yao na kwa sababu wanyama hawana akili wanaingia maeneo ya watu na wanafika mahali wanaua watu wetu, lakini wanakula mazao ya wananchi ambayo wameyalima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukitoa taarifa hapa katika Bunge hili, wapiga kura wangu wawili wamepotea, kwa hiyo nimepoteza kura za watu waaminifu kabisa, lakini wakati huo huo sasa tulitoa taarifa kwa Mheshimiwa Naibu Waziri hatua zilichukuliwa kidogo hazikuwa na uzito naomba mara nyingine tukiwapa taarifa kuna watu wa Rungwa pale, kuna kikosi kikubwa kabisa cha KDU pale Manyoni, hawachukui hatua hata kufika kwenye eneo la tukio kuwafukuza wale wanyama warudi katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara hii wazingatie kuwa karibu na wananchi ambao wanawachunga wale wanyama lakini wanapodhuriwa basi wafike haraka na tutoe kifuta machozi hicho ambacho wamekianisha japo ni kidogo sana, lakini kifike kwa wakati, ili watu kabla hawajaanza kuchoka na kujisika huzuni kwamba Serikali yao inawatelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika Sekta ya Misitu. Wizara hii niipongeze kwa kazi nzuri ilizofanya lakini kuna upungufu kadha wa kadha. kuna baadhi ya Maofisa wao ni wala rushwa sana. Suala hili tumelisemea sana na Mheshimiwa Waziri anajua, nilishamwona na nikamwambia, walishafikishwa hadi Mahakamani, wamekamatwa na rushwa katika check point, lakini viongozi wa pale TFS pale Makao Makuu waliamua kumtoa yule mtu pale. Badala ya kumtoa Mheshimiwa Waziri kamrudisha matokeo yake sasa lile eneo lote linanuka rushwa. Ni vizuri mtu anayetuhumiwa kwa rushwa akakaa nje ya mfumo wa makusanyo kodi au maduhuli kwa sababu tu atasababisha na ataambukiza, samaki akioza Mheshimiwa Waziri ataambukiza na yeye atanuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote samaki akioza katika tenga, anaweza akasababisha ukatupa tenga zima. Sasa ni vizuri ukawahi kutoa ili wale samaki wengine wazuri tuwapeleke katika masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kumekuwa na matukio machache ambayo Wizara hii lakini hasa wadau hawa wa TFS wamekuwa wakiyafanya, mengi ni ya kupongeza lakini kuna changamoto kadha kidogo. Bei ya TIKI katika minada kama hivi hapa majuzi juzi, katika mnada wa Mtibwa kulikuwa na shida lakini bahati nzuri Lunguza niwapongeze wamefanya vizuri, wameuza vizuri na wamepata bei nzuri, kwa hiyo wanaisaidia Serikali yetu katika kukusanya maduhuli, kuna changamoto kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnategemea viwanda vya misitu vifanye kazi kwa maana viwanda vile vina matatizo sana ya Saw Doctor, hapa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 85 Chuo cha FITI hajakipa uzito, hatuna Saw-Doctor kabisa nchi hii na wachache wale mnaozalisha wengi wanachukuliwa na Serikali. Sekta binafsi hii ambayo inategemewa ndiyo watakaokuwa wana- process haya mazao ambayo mnayauza, hawana Ma- Saw Doctor. Je ni utaratibu gani mtatumia hao watu mnaowazalisha pale FITI japo ni wachache, kwa sababu katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri, ameonyesha ni watu 80 tu na kitu hawafiki hata 100 kwa mwaka ambao anawazalisha katika soko la ajira, Serikali hao hao inawahitaji, na wengi wanapotoka FITI hawaajiriwi kama wataalam wa misumeno matokeo yake wanarudi kuwa Forester na kazi kubwa wanapewa ya kukusanya maduhuli. Mheshimiwa Waziri ajitahidi kutuonyesha na wale wadau wa misitu wanapataje wataalam wanaozalishwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa hivi hakuna chuo kingine mbadala cha kuzalisha Saw Doctor, katika nchi hii. Inafika mahali makampuni mengi wanaanza kuajiri wageni kwa sababu upande wa Serikali ikishawazalisha inawaajiri wao, lakini upande wa sekta binafsi hamna. Hatukatazi ajira kwa vijana wetu tunafurahia sana, wanapoajiriwa na soko kuu ambalo ni rasmi, lakini watoe basi fursa kwa watu ambao wanahitaji kupeleka vijana wao pale FITI basi gharama ziwe rafiki ili Saw Doctor kutoka katika viwanda binafsi nao waweze kuhudumiwa na chuo hiki ambacho ni cha umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya mkaa, Serikali imekuwa ikizuia mkaa kutoka eneo moja kwenda lingine, wameanzisha magulio kama walivyosema, lakini haiwawezeshi wadau ambao wanataka kutengeneza hata mkaa mbadala. Mkaa mbadala unaotokana na nyasi, mkaa mbadala unaotokana na vumbi la mbao, yote hii Serikali haijaonesha dhamira ya dhati, inapozuia mkaa unaotokana na miti. Ni vizuri sasa basi tutafute katika Mfuko wa Misitu au mahali unapoona.

Mheshimiwa Waziri hata mimi akiniwezesha nitazalisha mkaa, mimi ni mdau wa mazao ya misitu najua vizuri. Sasa watuwezeshe sisi wadau tuweze kuzalisha mkaa tuondokane na kukata miti. Wakati huu hakuna mbadala unaooneshwa, hata bei ya gesi bado siyo rafiki sana kwa wananchi wetu, wakulima wa vijijini. Watanzania walio wengi wanatumia mkaa tukiacha wale wa miji mikubwa tunatumia sisi wa vijijini pia. Sasa siyo rafiki, mtungi wa gesi unakaribia laki moja, Sh. 65,000 - 70,000 mpaka 90,000 ule mtungi mkubwa, sasa ni vigumu sana kwa mtu wa kawaida uweze kutumia. Tusaidieni sisi tuweze kusaidia hilo ambalo litatufika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ufugaji nyuki halijatiliwa maanani kabisa, Mheshimiwa Waziri amelizungumza juu juu, hakuna mizinga angalau anaweza akatupa; kila Mbunge akapata hata mizinga 100 tu akapeleka katika maeneo yake. Maeneo ya misitu tunayo mengi, ili tuondokane na umaskini huu. Katika Tanzania ya viwanda ameonesha kiasi kidogo cha nta kilichouzwa katika soko la nje, lakini Serikali inaweza ikawekeza na namna ya kuwekeza ni kidogo tu, ana wadau wengi, asaidie wananchi... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Na mimi kwa kuwa ni mara ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, namshukuru Mwenyezi Mungu, nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kuniteua kuwa mgombea wa chama hiki katika Jimbo la Manyoni Magharibi pia nawashukuru wananchi wakazi wa Jimbo la Manyoni Magharibi kwa kuniamini na kunipa nafsi hii na leo nasimama mbele yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza tu moja kwa moja kwa sababu muda huu siyo rafiki sana, nianze na suala zima la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo haya ya Mpango yameonesha maeneo ambayo wataelekeza katika jamii yetu kusaidia maji. Jimbo langu ni miongoni mwa Majimbo machache sana ambayo maji hayapatikani kwa asilimia ya kutosha; ni chini ya asilimia 10.
Naomba sasa kwa Waziri husika kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi walimpa kura nyingi, zaidi ya asilimia 80 na alipokuja pale aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi na Mji wa Itigi kwamba atasaidia maji katika kipindi kifupi kijacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Waziri mhusika alione hili ili kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa mpango wa elimu bure. Mpango huu una tija na wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi wamenituma niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kufanya mpango huu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo langu wana tatizo kubwa sana la afya. Tuna Kata 13 lakini Kata zenye vituo vya afya ni mbili. Tunategemea sana Wamisionari; na bila Wamisionari, wananchi wa Jimbo langu wasingekuwa wanaongezeka kwa kiasi hiki ambacho wanaongezeka kwa sababu hata watoto wangekuwa wanakufa mapema. Jiografia yake ni ngumu, lakini vituo vya afya hakuna, zahanati zipo chache; kwa kushirikiana na TASAF zilijengwa lakini hazina matabibu. Naomba sana, Mheshimiwa Waziri yuko hapa, alifanyie kazi hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ahadi pia ya Mheshimiwa Rais. Tunaitegemea sana hospitali ya Wamisionari ya Mtakatifu Gaspar. Hospitali ile ina gharama kubwa sana. Wakati alipokuja katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka wa 2015 aliwaahidi wananchi wa Jimbo langu kwamba atalipa mishahara yote ya watumishi wa hospitali ile, atatoa ruzuku kwa ajili ya vifaa tiba na ataleta Madaktari Bingwa. Pia atafanya mgao kutoka MSD ili tu kusaidia wananchi wa Jimbo lile ambao hawana hospitali mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya iko mbali; naomba sana ahadi ya Mheshimiwa Rais itekelezwe, tena katika kipindi kifupi. Wananchi tuna taabu na tunakufa kwa sababu ya gharama ni juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuunganisha mikoa kwa barabara za lami; Mkoa wa Singida umeunganishwa na mikoa mingine; lakini Mkoa wa Singida kuunganisha na Mkoa wa Mbeya, ni kitu ambacho kinashangaza. Mimi kama kiongozi ambaye nimetokana na wananchi wale, leo hii nimepokea message nyingi kwamba barabara baina ya Itigi na Rungwa, imekatika, hakuna barabara. Kikosi kazi kiko pale lakini hakuna kinachofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii jana amenipa barua kwamba wanatafuta fedha katika barabara hii ya Mkiwa – Rungwa hadi Makongorosi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe kwamba barabara hii amekuwa akiisemea toka Mbunge wa wakati ule Mheshimiwa Iwvata. Mheshimiwa Lwanji katoka hapa miaka kumi, bado ni ahadi zile zile. Naomba sasa mtekeleze ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyowaambia wananchi wa Itigi na Jimbo la Manyoni Magharibi kwamba katika utawala wake, atajenga barabara ile kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atakapokuwa una-wind-up hapa atuambie ni lini barabara ya kutoka Mkiwa – Itigi – Rungwa itajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Wabunge walioongelea kuhusu reli ya kati, nami Jimbo langu reli inapita pale na wananchi wangu wananufaika sana na reli inapopita pale. Sisi tunatumia usafiri ule wa reli kwa ajili ya kwenda maeneo jirani, lakini pia hata kwenda Kigoma. Mji wa Itigi ni mji ambao tumechanganyika, kwa hiyo, tunatumia sana reli kwa maslahi ya jamii yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la kilimo, tufike mahali sasa tuondokane na kilimo hiki cha mvua. Wakati mwingine mvua zinakuja kidogo wakati mwingine zinazidi. Maeneo ya Itigi ni mazuri, tukiweka miundombinu tu ya Irrigation Schemes yoyote, deepwell ikifanyika pale, maji yatapatikana ya kutosha na tunaweza tukaanzisha irrigation scheme, tukaondokana na utaratibu huu wa kutegemea mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mpango wa matreka ambao ulikuwepo katika awamu iliyokwisha. Wananchi wa Jimbo langu hakuna hata mmoja aliyefaidika na manufaa ya Serikali yao; na wao ni waaminifu na ni watiifu, hawajawahi kufikiria kuchagua chama kingine zaidi ya CCM. Hivi tunavyozungumza Halmashauri ya Itigi ni mpya, lakini Madiwani wote ni wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi walione hili kuwasaidia wananchi. hawa ambao ni waaminifu! Waswahili wanasema, chanda chema huvikwa pete. Sasa tunavikaje pete ambacho siyo chanda chema? Tuwaone hawa wananchi ambao ni waaminifu kwa Serikali hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifugo; kuna changamoto kubwa sana kwa bei ya mitamba katika mashamba ya Serikali. Bei ya mitamba ni kubwa kuliko bei ya ng’ombe ambaye unamuuza mnadani. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alifuatilie hili ili mitamba ishuke bei, watoe ruzuku ili wananchi tununue, lakini pia madume ya kuhamilisha mifugo ili tutoke katika…
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Hii ya kwanza eh!
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu lina ofisi ndogo ya TANESCO ambayo inahudumia kutoka Itigi hadi Mitundu, kilometa 70; na REA II umeme unakwenda hadi Mwamagembe, kilometa 63 toka Mitundu. Ofisi hii pia inahudumia toka Mkiwa hadi Itigi kilometa 30. Kwa maana hiyo ukianzia kilometa 30 ongeza 70 ongeza 63; na ukiongeza REA III mtandao unaongezeka. Jimbo langu kwa sasa lina Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kwa maana karibuni kutakuwa na Wilaya ya Itigi, hivyo noamba ofisi yenye hadhi ya Wilaya ili kuendana na mtandao mzuri wa Wizara hii ambayo nami naipongeza. Ahsante.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipia nafasi hii kwa asubuhi ya leo na mimi niweze kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Mheshimimwa Naibu Spika, nianze tu kwa kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri iliyofanya katika masuala mazima ya huduma za jamii lakini suala la miundombinu, kilimo na mengine mengi likiwemo kubwa la umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu ambao umewasilishwa tulipokuwa Dar es Salaam na leo Mheshimiwa Waziri hapa, maeneo mengi yameguswa lakini barabara nyingi zilishatengenezwa na sasa ni wakati mzuri katika miaka mitano hii kuangalia maeneo yale machache ambayo bado Serikali haijayafikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kukumbusha kwamba kuna barabara ambazo zimekuwa zikisemewa sana na viongozi wetu wakuu, Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, lakini Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na hadi sasa Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli wa hapa kazi na juhudi zake zimeonekana katika barabara ya kutoka Mkiwa, Rungwa hadi Makongorosi. Serikali katika Mpango wa mwaka huu imeonyesha kwamba inajenga barabara kutoka Chunya hadi Makongolosi lakini niombe sana katika mipango endelevu barabara hii katika kipindi hiki cha miaka mitano ionwe na ikiwezekana iishe. wananchi wa Majimbo yanayopitiwa na hii barabara likiwemo la Mheshimiwa Kakunda na Jimbo langu mimi lakini ni barabara kubwa inayounganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Mbeya kupitia Mkoa wa Tabora. Kumekuwa na ahadi nyingi, sasa si vibaya safari hii basi na sisi tukaonwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ahadi nyingine ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alikuwa afungue barabara ya kutoka Mkoa wa Singida inapita katika Wilaya ya Chemba inakwenda Kiteto na hadi Handeni. Barabara hii ina fursa nyingi za wajasiriamali, maeneo ya wakulima wakubwa wa nchi hii wanaolisha Mikoa ya Dar es Salaam na hata Tanga wapo maeneo yale lakini sisi wakulima wa Mkoa wa Singida barabara ile kama itafunguliwa itakuwa na tija sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo, nimpongeze sana Waziri wa Kilimo, kijana wetu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alipiga kazi sana wakati wa uchaguzi, alitembea nchi nzima na sasa juhudi zake zinaonekana. Nataka nimkumbushe tu kitu kidogo kwamba wafugaji wa maeneo yetu hususan katika Jimbo la Manyoni Magharibi wana shida kidogo ya maeneo ya malisho. Jimbo langu sehemu kubwa ni Hifadhi ya Rungwa Muhesi Game Reserve ambayo ina eneo kubwa. Kuna wafugaji wanaopakana na maeneo yale na kwa sababu maeneo yale sasa hivi wafugaji wanaotoka Mkoa wa Shinyanga wamekuwa rafiki zetu na wamekuwa wengi pale na mifugo imekuwa mingi, si vibaya tukaliona hili katika mipango yetu ijayo tukawapa fursa nao malisho kidogo yakawa yamekaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati na timu yake, Mheshimiwa Kalemani yuko hapa, amekuwa msikivu sana. Amenipa maeneo mengi, anafanya jitihada za kunipatia za umeme lakini naomba utekelezaji uwe wa haraka. Wataalam wamefika ila sijaona vizuri kwenye randama ya bajeti ya Mpango huu kama wamelizingatia hilo lakini naamini ananisikia na atalifanyia kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizopo katika Jimbo langu ni pamoja na shida kubwa ya maji. Sisi mikoa ya katikati hatuna mito lazima tuchimbe maji. Katika Mji Mdogo wa Itigi kuna visima vikubwa sana vya maji na vizuri vimechimbwa na Serikali katika bajeti hii inayoisha. Niombe katika Mpango ujao wa Miaka Mitano basi tuwekewe miuondombinu ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la afya, tunazo changamoto, kuna zahanati zilijengwa na TASAF ambazo zina shida ya Waganga Wasaidizi ambazo ni pamoja na Gurungu, Njirii, Ipande, Kitopeni, Ukimbu na Kintanula. Sasa wakiziangalia hizi kwa macho mawili naamini Serikali ya hapa kazi hawa wanaolaumu baadaye wataacha kulaumu kwa sababu Serikali imefika kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze juhudi za Mheshimiwa Waziri wa Viwanda aliposema kwamba nchi hii itakuwa ya viwanda. Moja ya eneo ambalo nitapenda kuona juhudi za Serikali zinachukuliwa ni pamoja na kuwa na kiwanda kwa Mkoa wa Singida na mikoa yote ya katikati. Jimbo langu lina malighafi nyingi ya gypsum itakuwa vizuri kutengeneza ajira kwa ajili ya vijana wetu kwa sisi kupatiwa kiwanda cha malighafi inayopatikana pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maliasili, kumekuwa na changamoto nyingi, hatujafika mahali pazuri kuvuna maliasili zetu. Tumekuwa tunaweka vikwazo matokeo yake kunakuwa na wezi wa mbao misituni kwa sababu hatuko rafiki sana katika kuhakikisha zile mali ambazo zime-mature kwa ajili ya uvunaji. Tumekuwa tuna-ban sana lakini pia tumekuwa na tatizo kubwa la uwekezaji katika kuhakikisha kwamba kuni hazitumiki nyumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaiomba Serikali ije na mpango mzuri wa gesi. Nchi yetu imegundua gesi, sasa gesi imefika Dar es Salaam si vibaya kukawa na mpango wa gesi ile iende Mwanza ipite Mkoa wa Singida na sisi tunufaike kama wananchi ambao ni walipa kodi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mitamba alizungumza Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado hata mimi nasema bei zile ni kubwa si vibaya zikaboreshwa ili baadaye na wafugaji wetu nao wakanufaika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona jioni hii, nami nitumie fursa hii kumpongeza tena Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nimpongeze kipekee Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uwasilishaji wake mzuri wa hotuba iliyogusa maeneo mengi ambayo kwa nchi hii tunahitaji viongozi kama hawa ambao walithubutu kutumbua jipu ambalo lilikaa muda mrefu la watu ku-bypass bomba la kushusha mafuta bandarini, lakini kuzima mita kupima kiwango cha mafuta kinachoingia nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imegusa maeneo yote muhimu ikiwemo elimu, afya, maji, miundombinu na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kipekee Waheshimiwa Mawaziri wanaomsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu; Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Abdallah Possi. Ni watu ambao wamekuwa na ushirikiano mkubwa, mimi niko katika Kamati ambayo ipo chini ya Wizara yake; Kamati ya UKIMWI na Masuala ya Madawa ya Kulevya. Wamekuwa karibu sana nasi pale tulipowahitaji na wamekuwa wakitushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa kuchangia kwa kuomba mambo machache yaweze kufanyiwa jitihada za makusudi. Suala zima la ajira kwa vijana wetu, lakini na akinamama ambao nchi hii ndiyo inawategemea sana katika suala zima la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema sasa tukaelekeza mawazo yetu katika kubadilisha kilimo hiki cha kutegemea mvua; tukatoka hapo tukaanzisha kilimo cha umwagiliaji; kilimo ambacho kama kitatiliwa mkazo, nchi hii tutatoka kule ambako tuko na tutakwenda kule ambako tunatolea mifano nchi za wenzetu; Malaysia, Vietnam na nchi nyingine ambazo tulikuwa nazo level sawa ya uchumi. Lazima tuthubutu kidogo, tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu kuna bwawa la Itagata, zuri tu, Serikali imewekeza pesa za kutosha, lakini lile bwawa linavuja. Naomba sasa ifanyike juhudi za makusudi liweze kuzibwa ili wananchi; vijana wa pale wapate ajira, wajiajiri wenyewe kwa kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuajiri vijana wengi, ni lazima pia tufungue miundombinu ya barabara; waweze kujiajiri kwa kununua mazao na kuuza. Pia katika maeneo mengi ni wakulima wazuri, waweze kutoka na kufika haraka katika masoko ambayo yako katika maeneo ya miji likiwemo Soko la Kimataifa la Kibaigwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hili suala la elimu bure. Naipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kuliona hili. Kuna changamoto kadhaa ambazo naamini zikifanyiwa kazi zitakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika milioni 50 kwa kila kijiji. Kabla ya hizi shilingi milioni 50, kulikuwa na mabilioni ya Mheshimiwa Kikwete katika Serikali iliyopita. Kulikuwa na changamoto kadhaa. Sasa tujifunze kutokana na changamoto zile! Mabilioni yale hayakufika katika vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmojawapo katika Jimbo langu, watu wangu hawakupata kukopeshwa hata kikundi kimoja. Kwa bahati nzuri hili linalenga vijiji na mitaa yetu. Kwa maana sasa utengenezwe utaratibu mzuri wa namna gani na watu gani watakopeshwa na urejeshaji utakuwa katika utaratibu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikishauri mara nyingi vijana wangu wa maeneo yetu kwamba mabenki siyo rafiki sana hasa kwa vikundi vya vijana kwa sababu riba, mara nyingi ndiyo inakuwa faida ya wale ambao ni wajasiriamali. Kwa hili, naipongeza sana Serikali lakini iangalie tu changamoto ambazo zitajitokeza ili lisijekuwa gumu kama lile ambalo limepita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilo hilo la ajira kwa vijana, napenda sana nizungumzie suala la mbolea. Tumekuwa tukizungumzia ruzuku ya vocha za mbolea katika baadhi ya maeneo. Napendekeza kwamba, ni vizuri sasa tukabadilisha mtazamo, badala ya kutoa vocha ya mbolea, sasa Serikali iwekeze moja kwa moja katika mbolea yoyote ambayo itauzwa nchini iwe imepewa ruzuku. Tutaondoka mahali hapa pa kuweza kusukumana; huyu kaiba, hapa halikutekelezwa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nzima ikauza mbolea ya ruzuku, itaondoa gharama hizi za kusafirisha mbolea kwa Sh. 3,000/= kutoka Dar es Salaam mpaka Tabora. Itaondoa msukumano ambao upo, watu badala ya kufanya kazi nyingine, tunafutilia nani alipewa vocha na hakuifikisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa mbolea wa kilo 50 au 25, ni sawasawa na mfuko wa cement. Mfuko wa cement kuutoa Dar es Salaam mpaka Tabora, unapita pale kwangu Itigi, unapelekwa kwa Sh. 500/= tu, lakini ulizia mfuko wa mbolea, utafikiri umebeba tani; mifuko sita ya cement inasafirishwa sawa na mfuko mmoja wa mbolea kwenda katika mikoa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatokana na udhaifu wa sera. Naomba tubadilishe, hakuna haja ya kuweka vocha, mbolea yote iwekewe ruzuku, ndiyo mahali ambapo Serikali itawekeza, kila mkulima anayetaka kununua mbolea, akute bei iko pale. Tutaondoka katika hili wazo la kuanza kusukumana na kutafuta nani kala na nani kafanya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la ulinzi na usalama, Jimbo langu ni Jimbo ambalo lina jiografia ngumu kidogo. Kutoka Makao Makuu ya Jimbo mpaka mwisho pale Rungwa kuna kilomita 190 karibu 200, Kituo cha Polisi kipo Itigi, hakina gari. Naomba sasa, Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo ina Serikali, Mawaziri wake wasikie, watuletee gari mpya. Mara nyingi wamekuwa wakiwapa vijana wale magari makuukuu. Njia ni mbaya, barabara mbaya, gari bovu; huwezi kufika mahali popote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali yangu hii ni sikivu, naamini wamesikia. Vile vile kuna jambo dogo tu la usikivu wa redio ya Taifa katika maeneo ambapo mimi natoka. TBC haisikiki katika masafa ya FM. Kuna redio ambayo imeweka busta yake pale; Redio Mwangaza, ni redio ambayo inasikika vizuri sana. Sasa wakati mwingine mtu anahitaji kusikia habari kama hizi za Bunge.
Pale kwangu hawasikilizi, labda itokee mtu ana runinga kwa ule muda ambao umeamuliwa. Naomba sasa Serikali ilifanyie kazi hili la masafa ya Redio ya Taifa. Hizi nyingine tutaachia wawekezaji wenyewe, wataangalia namna gani ambayo watatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Mawaziri wote wa Serikali hii ya Ma-Doctor na Maprofesa ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri wanayofanya, inapelekea hata rafiki zetu, watani zetu sasa wanafika mahali wanakuwa hawana cha kusema, wananyamaza tu na matokeo yake sasa tunawasemea sisi kuwaombea katika Majimbo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uteuzi mzuri wa Baraza la Mawaziri, wameteuliwa majembe ambayo kwa hakika tunaamini yatatufikisha katika safari yetu hii ambayo tunayo. Niwashukuru tena kwa mara nyingine wananchi wangu wa Jimbo la Manyoni Magharibi kwa kuniamini na kunileta humu na mimi ninaamini kwamba sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kazi nzuri wanayofanya katika Wizara hii kwa kuimarisha hospitali yetu kubwa ya Taifa, Hospitali ya Muhimbili lakini Hospitali ya Saratani ya Ocean Road. Kuna changamoto kadhaa ambazo tunatakiwa tuzione na Serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha wagonjwa wote hawaendi katika hospitali hizi kubwa na ili wagonjwa wasiende katika hospitali hizi kubwa lazima tuimarishe hospitali za kanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 2011/2012 hivi, Serikali ya Awamu ya Nne kuna hospitali ilizipandisha hadhi kuwa Hospitali za Rufaa ikiwemo Hospitali ya Mtakatifu Gasper ya Itigi ambayo inatoa huduma kwa wananchi wa Itigi lakini kwa Kanda nzima ya Kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ile ina gharama kubwa sana kutokana na Serikali kuachia wananchi kuhudumiwa kwa gharama za Wamisionari wale ambao kwa wakati fulani kule nyuma walikuwa wakipata dawa kutoka kwa wahisani wao lakini baadaye Serikali iliwazuia wakawa wanatakiwa wachukue dawa kutoka MSD, ruzuku wanayopata ni kidogo, matokeo yake hospitali ile imekuwa na gharama kubwa sana sasa na itapelekea hospitali hizi kubwa za Muhimbili, KCMC na nyingine kupata mzigo mkubwa kwa sababu hizi Hospitali za Kanda na za Rufaa hazifanyi kazi vizuri. Gharama zile ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni katika uchaguzi uliokwisha. Wananchi wale ni waaminifu walikipa chetu Chama cha Mapinduzi kura nyingi sana na Mheshimiwa Rais walimpa kura nyingi lakini moja ya ahadi yake ilikuwa kwamba atatoa ruzuku ya Serikali kwa Hospitali ile ya Mission ili iwasaidie wananchi wa maeneo yale ikiwemo wananchi wa Jimbo langu la Manyoni Magharibi hususani wananchi wa Mji wa Itigi na vijiji ambavyo vinaizunguka takribani kata 13 ikiwemo Wilaya nzima ya Manyoni watu wanakimbilia pale wanaposhindwa katika Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Mheshimiwa Rais ilikuwa ni kupeleka Madaktari Bingwa pale lakini kuongeza ruzuku na kutoa mgao kutoka MSD. Tukilifanya hili tutakuwa tumewasaidia wananchi wa Jimbo langu na watakuwa wameendelea kumuamini Mheshimiwa Rais wetu na ahadi zake zitakuwa endelevu kwa sababu aliyasema haya katika mkutano wa hadhara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wagonjwa wafike katika hospitali hizi kubwa wanatokea katika vituo vya afya. Katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi kuna kata 13 lakini tuna vituo vya afya viwili na kimoja ndiyo tuko katika kuhangaika kujenga na mafungu yenyewe ndiyo haya ya taabu. Kwa hiyo, niombe sasa Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Mawaziri hawa, madaktari na maprofesa watusaidie sasa wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi kwa kuhakikisha tunajenga kituo cha afya kwa kila kata lakini na hospitali kila kijiji na sisi tutasaidia pale ambapo tutapaswa kuwajibika katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna janga kidogo hapa katika vituo vidogo hivi vya zahanati za vijiji hazina matabibu wale kwa maana ya Clinical Officers hawapo kabisa. Baadhi ya zahanati kama Gurungu, Njirii, Ipande, Kitopeni, Ukimbu na hata Kintanula. Kuna nesi mmoja huyo huyo ndiye anaenda kukuandikia dawa, anakupatia tiba na baadaye anakutolea dawa. Sasa ni wakati muafaka wa kutekeleza Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kuyafanya haya yawe mepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya ahadi zetu katika chaguzi ilikuwa ni pamoja na kusogeza huduma hizi lakini kusaidia wazee na kwamba watapata matibabu haya bila usumbufu, lakini bure. Hii imekuwa changamoto kubwa, matibabu ya bure yamekuwa na udhia sana kwa wazee hasa wanapofika hospitali. Kama nilivyokwishatangulia kusema mimi katika Jimbo langu watu wangu wanatibiwa katika Hospitali ya Wamisionari. Jambo hili wamekuwa hawalitambui sana, sasa si vibaya Serikali ikaingilia kati iwasaidie wananchi wale ili wazee nao wanufaike na mpango huo wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni bima ya afya, kuna huu Mfuko wa CHF umekuwa na changamoto nyingi. Wakati mwingine watu wanachangia zile fedha lakini anapofika katika kituo cha afya au zahanati anakuta dawa hazipo. Niombe sasa juhudi za makusudi kwa Serikali hii kushirikiana na TAMISEMI, Wizara ya Afya wayafanye haya yawe mepesi ili wananchi wetu kule vijijini waendelee kuwa na imani hii ambayo wanayo sasa ya kutuchagua sisi viongozi tunaotokana na Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo nimetaka kulizungumzia kidogo, tumeweka nguvu sana kwenye matibabu ya moyo katika hospitali hizi kubwa. Niipongeze Serikali kwa juhudi hizi ilizochukua kuhakikisha sasa magonjwa haya makubwa yatatibiwa katika Hospitali yetu ya Taifa. Hata hivyo, kuna janga lingine la magonjwa haya yasiyoambukiza ukiwemo ugonjwa wa kisukari, tumekuwa hatuchukui hatua za kutosha na sasa watu wengi wakiwemo Waheshimiwa Wabunge ni wagonjwa wa ugonjwa huu wa kisukari. Ni vyema sasa Serikali nayo ikatafuta matabibu wazuri, Madaktari Bingwa aidha watu wetu wakaenda kusoma kwa nchi ambazo tayari zinaonyesha kwamba zina maendeleo mazuri juu ya tafiti na kugundua tiba nzuri ya magonjwa ya kisukari. Watu wetu wamekuwa wakifa kwa kupewa dawa ambazo pengine si sahihi au utaalamu ambao hautoshi. Niiombe Serikali yangu Mawaziri hawa ambao mimi nawaamini kwa asilimia mia moja kutokana na ushirikiano wanaotupa sisi Wabunge basi na hili jambo walichukue, walifanyie kazi ili baadaye ugonjwa huu usiwe tatizo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitaki kupigiwa kengele, naomba kumalizia hapa na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nichangie katika mjadala huu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara nyeti, Wizara ambayo ndiyo moyo wa uchumi wa nchi yoyote duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako naomba nisome tu Ilani ya Chama chetu Chama cha Mapinduzi, kipande kidogo tu, paragraph moja. “Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, 2015, kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wabunge wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani, imeandaliwa ikiwa ni mkataba kati ya CCM na wananchi.” Niishie hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma ilani hii kuweka msisitizo jinsi tulivyoji-commit tukiwemo sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwa wananchi wetu waliotuamini hususan katika suala hili la miundombinu. Katika ilani hii, ukurasa wa 57 umetaja kwa msisitizo mkubwa sana, barabara ya kutoka Mkiwa, Itigi, Rungwa hadi Makongorosi, kilomita 413 ikiamini na kuwatilia uzito wananchi waamini kwamba wakichagua Chama cha Mapinduzi, barabara hii itajengwa katika kipindi cha ilani hii cha miaka mitano; yaani 2015 - 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii imekuwa ikizungumziwa na Wabunge wanaotoka katika Jimbo ninalotoka mimi sasa na Wabunge hawa wakitokana na hiki Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Ismail Iwvata lakini Mheshimiwa John Paul Lwanji ambaye nimempokea kijiti. Inawezekana ikawa sababu ya yeye kutokurudi humu barabara hii ikawa na mchango mkubwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu sasa kidogo inaonekana Serikali hii sikivu ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais ambaye alikuwa ametokana na Wizara hii, Waziri aliyempokea ameonesha alama ndogo kuonesha kwamba sasa barabara hii itajengwa kwa kilomita 35 kutoka Mkiwa hadi Itigi na kupita kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ilani hii, miaka mitano imesema kwamba barabara hii itakuwa imejengwa kwa kiwango cha lami. Kilomita 413, Jimbo langu peke yake kuna kilomita 200. Barabara hii imekuwa ikijengwa miaka ya nyuma kutokea Mkoa wa Mbeya, kuna kilomita 36 zimejengwa kilomita 36 tena na mwaka huu zinajengwa kilomita 43. Upande wa Mkoa wa Singida ambapo Jimbo langu limo, ndiyo kwanza wameanza na kilomita 35. Nakushukuru sana Profesa Mbarawa kwa kuanza hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hesabu ndogo tu ambayo haihitaji sana kwenda kwenye vyuo kusomea hesabu hii kwamba 200 ukigawa kwa 35 unapata ngapi? Kwa maana kwa mpango huu wa 35, barabara hii itajengwa kwa zaidi ya miaka saba na kama kila mwaka watajenga kilomita 35, ilani hii itakuwa imeleta shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuona na kuanza kujenga barabara hii lakini niombe sasa; kama tuna dhamira ya kweli ya kutekeleleza ilani tuliyoiahidi, Mheshimiwa Rais wetu wakati akiwa katika ziara yake ya kutafuta kura katika Jimbo langu, moja ya sehemu ya hotuba yake ambapo wananchi walipiga makofi ni pale alipozungumzia kwamba sasa anajenga barabara hii katika kipindi chake cha miaka mitano ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilomita 35 mara tano maana yake, hataweza kufika hata nusu ya hii barabara. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri, aoneshe msisitizo kwamba ile ahadi ya Mheshimiwa Rais, basi anaitimiza, aongeze japo 35 nyingine, ikifika mara tano at least tutakuwa tumesogea kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni ndefu na inapita katika Vijiji vya Gurungu, Sanjaranda, Songambele, Majengo, Itigi Mjini, Doroto, Lulanga, Itagata, Ukimbwi, Chabutwa, Mtakuja, Mitundu na Kalangali. Katika Wilaya ya Sikonge kuna Vijiji vya Kiyombo, Kirumbi na Mwamaluku; wakati inakuja tena katika Jimbo langu, Vijiji vya Mwamagembe, Kintanula na Rungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri atuongezee, awape thamani wananchi ambao wamekuwa wakikichagua chama hiki toka uhuru, hawana mpango wa kubadilisha mawazo, tusiwape fikra mbaya wananchi waaminifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naombe sasa niongelee barabara nyingine ambayo tumejengewa pale kutoka Manyoni, kupita Itigi, hadi Chaya. Naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kujenga barabara hii ya kilomita 89.3; imekwisha lakini kuna shida pembeni mitaro ya kupitisha maji ya mvua haiko vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema ikamaliziwa barabara hii kutoka Chaya kwenda Nyahuwa ili tuwaunganishe wananchi wa Mkoa wa Singida na Mkoa wa Tabora. Tukiijenga barabara hii itakuwa na tija sana kiuchumi kwa wananchi wa Mikoa ya Kati lakini Mkoa wa Tabora kusafirisha mazao yao kuleta katika masoko ya Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la shida kidogo ya mitandao katika baadhi ya maeneo yangu katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi; katika vijiji vichache tu, Mheshimiwa Waziri akitusaidia watu wa mitandao wakatufikia katika Kijiji cha Idodiyandole na Kijiji cha Mbugani na Ipanga Masasi, tutakuwa tumemaliza tatizo hili la mawasiliano na wananchi wangu watakuwa katika dunia ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna shida kidogo ya usikivu wa redio katika masafa ya FM katika maeneo yale. Hawa watu wa mawasiliano kila nikiwasiliana nao wanasukumiana; huyu wa Habari, huyu wa Mawasiliano. Serikali ni moja naomba tusaidiwe kama ni busta, pale kuna redio yetu ya Wamisionari ya St. Gaspar pale wanaitwa Redio Mwangaza wameweka busta yao, sasa redio kubwa kama ya Taifa bado haisikiki. Tunaomba Serikali itusaidie hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la service levy pia za minara zimekuwa ni shida zimekuwa kidogo kidogo sana; minara hii ambayo inajengwa hasa na hallotel. Makampuni yale mengine wanatulipa vizuri, kuna shida tu katika jinsi ya kupata malipo, lakini ukipata malipo yao yanatosheleza. Naomba sasa Serikali itusaidie, vijiji ambavyo minara ya Hallotel imewekwa na tunatumia simu zao na tumekuwa ni wateja wakubwa, basi nao walipe levy vizuri, vijiji vyetu navyo vinufaike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kupigiwa kengele, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, basi Waheshimiwa Mawaziri watuangalie, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii mchana huu ili nami nichangie kidogo katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ambayo inagusa karibu kila jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchagua majembe haya mawili ambayo yanapiga kazi katika Chama hiki na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali hususan ya awamu iliyopita, Waziri aliyekuwa na dhamana katika Wizara hii alitusaidia watu wa Wilaya ya Manyoni. Tulikuwa na mgogoro wa muda mrefu sana na Wilaya ya Sikonge, Mkoani Tabora. Kwa sasa mgogoro ule umekwisha na ulitatuliwa baada ya wataalam wa ardhi kuja kufufua mipaka ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nina machache ambayo nitapenda kuyagusia. Katika Jimbo langu tuna mgogoro mdogo lakini una kero kubwa baina ya Kijiji cha Lulanga ambacho zamani kilikuwa Itagata na hifadhi yetu ya Muhesi na Rungwa Game Reserve. Najua jambo hili pengine lina-interfere Wizara hizi mbili ikiwemo Wizara ya Maliasili lakini mtu wa ardhi naomba naye alichukue hili kwa upande wake ili aone jinsi ya kusaidia wananchi hawa wa Kijiji cha Lulanga katika Jimbo la Manyoni Magharibi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba pia Waziri atuletee wataalam katika kufufua mipaka ya Vijiji vya iliyokuwa Majengo zamani na sasa Sanjaranda. Kuna mgogoro mdogo pale lakini Vijiji vya sasa ni Kihanju, Songambele na hiyo Sanjaranda ambavyo vinasuguana, kwa hiyo tunashindwa kuelewa kipi ni kipi hata tunapotaka kufanya maendeleo ikiwemo kujenga shule tunasukumana kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda nipongeze jitihada za Serikali kupitia Shirika hili la National Housing kwa uwekezaji wake mkubwa katika nchi hii. Japo nyumba hizi kuna changamoto zina bei kubwa, lakini ni watu ambao tunapaswa tuwasifie sasa na tuwatie moyo ili waendelee na juhudi hizi ila changamoto hizi ziangaliwe. Hapa kuna changamoto kubwa ya kodi ya VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani), kama ingeondolewa basi wananchi wetu wangeweza kumudu gharama za manunuzi lakini pia katika vifaa vya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza mji huu wa Kigamboni kuna kitu kimeanzishwa pale kinaitwa KDA ambayo haitofautiani sana na CDA ambayo iko hapa Dodoma. CDA wamepoka mamlaka ya Manispaa ya Dodoma, matokeo yake kuna migogoro mikubwa sana baina ya Halmashauri ya Manispaa na wao CDA. Kipindi cha nyuma Serikali ilikuwa imetia mkono, imetia nguvu kubwa ikawepo hadi Wizara inayoshughulikia Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu lakini leo CDA wamebaki wanajiendesha kwa makusanyo ya kodi, matokeo yake wanatoza watu wa Dodoma kodi kubwa ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu yangu ni kwamba inawezekana na hii KDA ikaja katika mpango ule. Kama Serikali katika ukurasa wa 47 inaonyesha barabara elekezi kilomita 71, lakini hakuna mafungu yanayoelekea pale, naamini tunapoelekea Kigamboni napo tutakuja kama CDA ilivyo sasa kwamba imeachwa pale kama mamlaka inafanya kazi za Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Tusije tukazua mgogoro baina ya Halmashauri ya Temeke au Halmashauri ya Wilaya mpya ya Kigamboni pamoja na hii KDA. Niombe sasa juhudi za makusudi zichukuliwe ili wahusika wajitambue na kila mmoja awe na mipaka yake mapema kuondoa hii changamoto ambazo zimejitokeza na uzoefu unatuonyesha kwa CDA ya Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitabu hivi tulivyopewa leo katika mabegi haya nilikuwa napitiapitia nimeona shamba moja ambalo na mimi pale ni mfugaji labda, niombe ku-declare interest nafuga katika Kijiji cha Magodani katika Wilaya ya Rufiji. Mwekezaji mwenye shamba hili lililotajwa katika ukurasa huu wa 122 sehemu ya kwanza ya kitabu hiki ni mtu ambaye kwa hakika amewanyanyasa sana wananchi wa maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuliona hili na kuliweka katika kitabu hiki kwani wananchi wa Vijiji hivi vya Magodani, Kazore pamoja na Lugwadu wamefikia mahali hata kuuawa katika msitu ambao umefugwa na mwekezaji huyu lakini amekuwa anafanya patrol na bunduki na kutishia kuwapiga risasi wananchi wale. Hata wananchi waliovamia ni watu majasiri tu kuingia katika eneo lile lakini kama ingekuwa siyo juhudi kubwa za Mwenyekiti wa Kijiji kile Adam John, basi leo ungekuta maiti nyingi sana katika eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameonesha hapa katika kitabu hiki kwamba mamlaka ya utatuzi ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga. Halmashauri ile ndiyo iliyopelekea mgogoro huu kuwepo hadi leo. Kile Kijiji cha Vikindu ambacho kilitoa muhstasari ule wa heka 1,000 baadaye mwekezaji kapimiwa zaidi ekari 3,000. Kama mipaka ile itafufuliwa itaonekana ni zaidi ya ekari 3,000 lakini zimeonyeshwa pia ekari 1,700 katika nyaraka zake. Kwa hiyo, ni kwamba kuna udanganyifu mkubwa baina ya maafisa wetu hawa wa Halmashauri ambao wanashiriki katika haya mambo. Niombe sasa Mheshimiwa Waziri achukue juhudi za makusudi kusaidia wananchi hawa wa vijiji hivi ili waondokane na hii hali ya kunyanyasika na mwekezaji ambaye hana tija katika eneo lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niipongeze Wizara kwa kujali, katika ukurasa wake wa 71 katika afua za UKIMWI wameonesha kuwajali wafanyakazi wao ambao wanafanya kazi katika Wizara hii. Mimi nikiwa mjumbe wa Kamati ile niipongeze Serikali na hasa Wizara hii, nimeona katika ukurasa wa 71 katika hotuba ya kitabu cha Mheshimiwa Waziri ameonesha Wizara yake inajali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami nichangie katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Niungane na wenzangu kupongeza uteuzi wa Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe katika nafasi hii nyeti na ngumu kidogo ya Uwaziri pamoja na Naibu Waziri. Niwapongeze kwa kuteuliwa lakini niwapongeze kwa kazi yenu nzuri mlizozionyesha toka mmeteuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni miongoni mwa Wabunge ambao majimbo yao yanapakana na mapori ya akiba. Napakana na pori la Rungwa Game Reserve na Muhesi, liko katika Halmashauri yangu mpya ya Itigi lakini Jimbo la Manyoni Magharibi. Ni miongoni mwa wanufaika wazuri sana na mapori haya na mchango wao mkubwa umekuwa ukisaidia vijiji vyetu katika maendeleo mbalimbali kutokana na mgawanyo ule unaotokana na asilimia ile ambayo inapelekwa katika vijiji na pia katika Halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki cha madawati na sisi ni miongoni mwa watu ambao tumenufaika kwa pesa zile lakini hatujajua tu hizi zilizotolewa na Wizara ni kiasi gani tutapata. Sasa si vibaya Mheshimiwa Waziri akatuonesha Halmashauri yangu ya Itigi imepatiwa nini kwa sababu nasi tunapakana na Game Reserve hizi za Rungwa na Muhesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matukio na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa kazi za kila siku za Wizara hii hususani katika vijiji vinavyopakana na hifadhi hizi. Kumekuwa na tatizo ambalo sijui ni la watumishi, sijui ndiyo sera ya Wizara, lakini dhana yangu nadhani ni kwamba baadhi ya watumishi wanapelekea sasa Wizara hii iendelee kulaumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la watumishi hawa ambao wamekuwa wanajihusisha sana na rushwa ndio wanaofanya leo Mawaziri toka mwaka 2010 waliopita katika Wizara hii wamekuwa na hesabu kubwa na wengine wakiwa wanatoka kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi hawa wameendelea kuwepo pale na watumishi wa juu sana ni watumishi wa kati kati wakiwemo Maafisa hawa wa Wanyamapori tuseme Maaskari wa Ma-game hao wanachukua pesa kidogo wanawaweka watu katika hifadhi wanaposhindana ndipo migogoro inapokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu miaka miwili iliyopita kulitokea tatizo kama hili, walishindana na kijana mmoja katika Kitongoji cha Matumaini katika Kijiji cha Kintanula, yule Bwana aliuwawa kwa kutofautiana tu lakini hadi leo hamna taarifa nzuri iliyotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi majuzi tu hata mwezi bado katika Kijiji cha Mwamagembe Maaskari wa reserve walimuua kijana mmoja. Walikwenda kijijini akawasaidie kwenda nao porini kutafuta majangili kwa sababu wanakuwa na knowledge ya kujua ni nani na nani wanaojishughulisha; walipofika yule kijana mmoja walimuua wao wakasema kauawa na majangili. Lakini wale watatu wengine ambao walikwenda nao walikuja kuonekana baadaye. Bahati mbaya au nzuri shauri hii tumeliachia vyombo vya usalama vishughulike nalo pamoja na Diwani wa Mwamagembe ambaye alifichwa juu ya tukio hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na-declare interest, mimi ni mdau katika uvunaji wa mazao ya misitu katika nchi hii lakini pia nashughulika na usafirishaji wa mazao haya ya misitu nje, sasa nihamie katika sekta ambayo naijua vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna jambo hili la recovery rate ya mbao ambayo ni asilimia 30. Recovery hii iliwekwa wakati ule mashine zilipokuwa za kizamani, misumeno ilikuwa na milimita zaidi ya tano, sita; sasa hivi taaluma imeongezeka, teknolojia imepanda bado tuna-recovery rate ya asilimia 30 ambayo inapelekea kuchonganisha wadau wavunaji wa mazao ya misitu pamoja na Maafisa ambao wanakagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka porini kupata 70 percent ni sawa, recovery ya asilimia 60 ya slipper ni sawa, kunakuja shida hapa tunapokuja katika recovery ya asilimia 30 ya mbao. Ukitumia mashine nzuri recovery ni kubwa sasa unapoonyesha kiwango kikubwa basi inakuwa tatizo linahamia hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Wizara ichukue juhudi za makusudi kabisa kupitia Taasisi zake za FIT lakini na Taasisi zingine ikiwepo TAFORI kufanya tafiti za sasa recover rate iliyo nzuri kwa mbao ni ipi ili kuondoa mgogoro huu ambao unatengeneza rushwa kwa sababu wale wakaguzi wanatumia fursa hii ya wavunaji wengi wasiojua hesabu za kutafuta volume hii ya cubic meter kuwasulubu kwa kutumia Sheria namba 14 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utendaji mbovu wa baadhi ya maafisa hawa ambao tumesema katika Wanyamapori lakini huku upande wa misitu ndio umekithiri sana. Kamati ya TFS tangu imeundwa imekua ni taasisi iliyofanya kazi vizuri sana kuanzia juu mpaka katikati; lakini kule chini bado ni kuzuri, hapa katikati ndiyo kuna shida kama nilivyokwisha kusema. Kuna Maafisa ambao wanafanya kazi kwa kutegemea sana kupata kipato nje ya mishahara yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ndio wanaopelekea leo Mawaziri wengi wanasulubiwa. Hapa katikati Mheshimiwa tunavyovizuia ambavyo ukaguzi wake haueleweki, ni vigumu sana kukagua mzigo ukiwa ndani ya gari, lakini kuna checkpoint ya mwisho, Mbezi pale ambayo nayo wanakagua, bandarini ambapo mizigo ya export inapelekwa nayo ina ukaguzi; kuna Maafisa zaidi ya saba pale, lakini hawaaminiani, hakuna Afisa mmoja anayekuwa na maamuzi mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe Wizara hii, ni wakati umefika wa kufanya kama walivyofanya TRA. TRA wao walikuwa wanakimbizana hivi hivi na wadau wao, lakini mwisho wa siku walipoamua kuwa waaminifu, wakweli kwamba wewe unatakiwa kulipia kodi ya asilimia ya pesa hizi, basi watu wote walipe asilimia hizo. Yule mwingine anayekuja ana-verify kwamba wewe ulistahili kulipa hiki. Na kama hukustahili kulipa anafanya maamuzi ya papo kwa hapo na ni maamuzi ambayo yana tija na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye TFS watumishi wao wamekuwa na shida. Kuna miongoni mwao Mheshimiwa Waziri nilishampa na taarifa na anajua, jinsi wanavyotumia udhaifu huu wa watu hawa ambao hawajui kutengeneza volume hii ya cubic meter, wanavyosulubiwa na Maafisa hawa. Anatumia kutokujua kwa yule mtu anam-sue mara mbili na anam-compensate mara nne zaidi ambacho hawakupaswa kukilipia. Sasa shida ni pale anapokutana na watu kidogo wanaojua ndipo linakuwa tatizo. Tuliwaambia huyu mtu amekuwa akitajwa mara nyingi, amekuwa akizungumzwa na watu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri sasa asiingie katika mtego ambao wamekuwa wakiingia Mawaziri wengi, wa kukumbatia watu na taasisi za rushwa zilishawakamata, lakini kwa sababu ushahidi wa moja kwa moja unakuwa ni mgumu kumtia hatiani mtu wa namna ile, ni vizuri akaondoka katika lile eneo ambalo nadhani kwamba atatengeneza mazingira ya kupata rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nataka nizungumzie leo kinachoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam. Inapofika mwezi wa Saba, Wizara hii huwa inatoa kitu kinachoitwa approval, yaani nikibali cha mtu kusafirisha mazao ya misitu nje ya nchi. Kile kibali kinampelekea mtu aingie mikataba na mabenki na wadau mbalimbali….
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie katika mjadala huu wa bajeti ya Serikali. Nikupongeze sana wewe, kama walivyokupongeza wajumbe wenzangu wa Baraza hili la Kutunga Sheria kwa maana ya Bunge, kwa ujasiri wako na weledi mkubwa wa kuliongoza Bunge hili Tukufu kwa kufuata Kanuni ambazo Bunge hili limejitungia ili kujiendesha. Kwa mwanamke kijana kama wewe umeonesha umahiri mkubwa na ni mfano mzuri wa kuigwa kwa viongozi waandamizi wa nchi hii, nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri wa Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Mpango kuanzia kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge lakini kuwa Waziri wa Wizara nyeti, Wizara ambayo ndiyo mhimili wa Serikali. Pia nimpongeze mdogo wangu Mheshimiwa Dokta Kijaji naye kwa kupata fursa hii adhimu ya kulitumikia Taifa hili kwa nafasi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa utendaji mzuri. Mheshimiwa Rais amekuwa akifanya kazi nzuri sana pamoja na changamoto za hapa na pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze kwa kuchangia kuhusu Wizara yenyewe ya fedha, lakini bajeti nzima ya Serikali. Waziri amekuja na mpango mzuri sana hapa, suala la kutokupandisha bei katika tozo za mafuta, niipongeze sana Serikali kwa kuliona hili kwa sababu impact yake huwa ni kubwa na inapelekea mfumuko mkubwa wa bei. Kwa kufanya hivi, maana yake sasa tutabaki katika mpango ule ule, kwa hiyo tutakuwa na changamoto chache.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nikumbushe Waziri au Serikali iangalie sana maduhuli ambayo yanakusanywa na Serikali hii kupitia maeneo mbalimbali (mapato yasiyokuwa ya kodi). Kuna eneo ambalo tukiliangalia kwa makini sana linaweza likachangia sana, eneo la misitu ya asili lakini eneo hili la misitu ya kupandwa na Serikali. Kuna mashamba makubwa ya Serikali, utaratibu mzuri ukitumika na kuhakikisha wazawa wananufaika na mashamba yale, basi yana mchango mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka mitano iliyopita miongoni mwa maeneo ambayo yalichangia katika Wizara ya Maliasili ni pamoja na sekta hii ya misitu. Mashamba ya Lunguza, Mashamba ya Mtibwa lakini misitu ya asili kama itavunwa kwa utaratibu mzuri bila uharibifu wa mazingira, Serikali ina chanzo kizuri sana cha mapato. Niiombe sasa Serikali napo hapo ipaangalie kwa macho mawili, ipatendee haki ili Serikali inufaike na rasilimali zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika huduma za jamii Serikali imekuwa ikifanya vyema sana. Katika afya kuna mpango wa kujenga zahanati kila kijiji, lakini kuna kujenga kituo cha afya kwa kila kata, mpango huu umekuwepo kinadharia sana. Wakati umefika na wakati muafaka, kwa sababu ahadi yetu sisi Wabunge, Mheshimiwa Rais wetu wa Chama cha Mapinduzi tulikuwa tukimuunga mkono kwa kuwaambia wananchi kwamba sasa Serikali inayokuja itakuwa na mpango wa kujenga zahanati kila kijiji lakini kila kata kitajengewa kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji tuone hapa na Serikali ije itueleze sisi Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwamba inajipangaje kuhusu kutekeleza ahadi hizi ambazo humu katika makabrasha ya bajeti haionekani vizuri, sijui wana mpango gani. Tusije tukaenda kwa mpango ule tulikuwa na dhamira ya kujenga maabara kila shule ya sekondari matokeo yake zile nguvu zikasukumwa kwa wananchi moja kwa moja. Ni jambo la hatari na mpaka leo kuna baadhi ya maabara hazijakwisha kwa sababu kulikuwa hakuna mafungu isipokuwa mkoa mmoja tu wa Dar es Salaam ambapo Serikali ilitenga bajeti na ika-facilitate ule mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye elimu, tumeliona hili la elimu bure. Niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa utekelezaji wa jambo hili ambalo maswali kwetu sisi kama wawakilishi wa wananchi yamepungua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa sana katika suala hili la huduma za jamii ikiwemo maji. Wabunge wengi wamezungumzia maji ni tatizo katika maeneo yao lakini na mimi niseme wazi kwamba miongoni mwa majimbo ambayo maji ni tatizo Jimbo langu la Manyoni Magharibi maji ni tatizo kubwa. Ile mita 400 kule kwetu hata ukifanya mkutano ukiwaambia mita 400 watakushangaa sana labda useme angalau tupunguze kutoka kilomita saba, nane zilizopo sasa kufuata maji mpaka angalau kilomita mbili, sasa tunafanyaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri sasa Serikali ikajipanga isaidie Wabunge ambao majimbo yao ni magumu, tuongeze mafungu pale ili maji yaweze kupatikana na tutakapofika katika chaguzi zingine tuweze kuwa na kauli nzuri na kuhakikisha chama hiki ambacho ndiyo chenye Serikali kinarudi na Wabunge wengi zaidi kuliko tuliopo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa mikoa maskini ni Mkoa wetu wa Singida. Mkoa wa Singida na mikoa ya katikati kwa ujumla, Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine ambayo tunapakana nayo watu wake ni hodari sana katika kilimo lakini tumekuwa na changamoto ya kilimo hiki cha kutegemea mvua. Niiombe sasa Serikali ifike mahali tuwe na mpango madhubuti, tutoke katika kilimo hiki cha kutegemea mvua ili tuweze kutengeneza miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, water table ya maji ipo karibu tukiyachimba na kuyapandisha yale maji kwa miundombinu safi na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji, haya majanga yanayotukabili watu wa mikoa ya katikati likiwemo baa la njaa yataondoka kabisa. Niiombe sasa Serikali ije na mpango wa kuondokana na kilimo hiki cha mvua tuweze kutegemea kilimo cha umwagiliaji ambacho kitakuwa na tija kwa nchi yetu na jamii yetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali yangu pia kwa kuondoa mageti haya ambayo yalikuwa yana shida kwa wakulima wetu. Pia nizungumzie hili pia la ujenzi wa reli ya kati pamoja na matawi yake. Jambo hili ni jema na likienda na mpango huu kwa hakika uchumi utaendelea kwa sababu miundombinu ikiwa mizuri basi uchumi unakuwa ni rahisi na unakuwa mwepesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wamezungumzia sana kuunganisha RAHCO na TRL, RAHCO ni mmiliki wa miundombinu, TRL aendeshe reli. Ikiwa mwendesha reli akamiliki miundombinu ni hatari sana. Tuendelee kubaki na utaratibu tulionao leo, RAHCO aendelee kumiliki miundombinu kwa niaba ya Serikali, lakini TRL libaki kama shirika linaloendesha miundombinu ambayo ni mali ya Serikali. Ni jambo la hatari kama tutafika mahali tutabinafsisha Shirika la Reli na miundombinu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri na pili, naunga mkono hoja. Napenda kujielekeza katika ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo hasa katika halmashauri mpya kama ilivyo Halmashauri yangu ya Itigi. Pia, kuna upungufu mkubwa wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na hata watumishi katika mahakama hizi. Nashauri Wizara yake iajiri Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na hasa vijijini, kama ilivyo Jimbo langu la Manyoni Magharibi. Halmashauri za Wilaya zina hadhi sawa na wilaya ya kiserikali, hivyo zipewe hadhi ya kuwa na Mahakama za Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri alitazame Jimbo langu la Manyoni Magharibi kwa jicho la kipekee katika ujenzi wa Mahakama za Mwanzo kwani, zilizopo ni chakavu na hazina hadhi, kama ilivyo Wizara yako ilivyo na heshima kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na narudia tena naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie katika Wizara hii ambayo kwa hakika sasa inatenda haki na inafanya kazi ambazo zinaonekana kwa kila mtu ikiwemo katika Jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 164 wameonesha barabara hii ya Makongorosi hadi Mkiwa kipande cha Nolanga – Itigi – Mkiwa kilomita 56.9 zitajenga kwa kiwango cha lami. Shida kubwa iliyopo pale tayari ujenzi unakaribia kuanza, lakini mpaka sasa hivi hakuna ufidiaji kwa maana ya compensation kwa wale ambao wanafuatwa na barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri sasa azingatie kwamba wanapokwenda kujenga barabara, kuna wananchi wa Itigi ambao wamefuatwa na barabara hii ambayo ni kubwa inayojengwa mwaka huu, waweze kulipwa mapema kuondoa usumbufu ambao utajitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara hii kwa kazi nyingi ilizofanya, lakini katika Jimbo langu kuna changamoto kidogo. Mheshimiwa Waziri, Profesa Mbarawa wakati anatembelea barabara hii kutoka Mbeya hadi Itigi alikutana na changamoto kubwa sana ya mawasiliano. Kuna shida, hakuna minara ya mawasiliano maeneo mengi, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri akumbuke maeneo yale aliyopita kutokea kule Rungwa, Mwamagembe, Kintanula na maeneo ya Vijiji vya Mkoa wa Tabora ambavyo katikati yake vinaingiliana na eneo hili hadi kufika Kalangali. Maeneo haya mwenyewe aliona mawasiliano ni shida. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuwakumbusha waweze kuliona Jimbo la Manyoni Magharibi, kwa kweli mtandao wa barabara utasaidia lakini pia mawasiliano ni shida, hilo tu nilitaka kukumbusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia Serikali yangu kwa kuamua kujenga reli ya kiwango cha standard gauge, pale walipoanzia lakini naomba sasa wafanye jitihada wasogee ifike hadi Itigi kwa kipindi kijacho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante sana.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niseme kwamba naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Simbachawene kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangazo la Mheshimiwa Rais siku ile ya sherehe za Muungano kwamba sasa Dodoma limekuwa Jiji, limewafarijisha pia wananchi wa mikoa ya jirani ukiwepo Mkoa wa Singida kwamba Jiji litakapokuwepo Dodoma nao watapata fursa mbalimbali zikiwemo za kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutangaza, lakini kabla hajatangaza, alifanya kazi moja kubwa ambayo ilikuwa ni kero iliyopelekea wananchi wa Dodoma kuwa na mtafaruku, mamlaka mbili zilikuwa zinausimamia Mji huu; Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma lakini wakati huo huo kulikuwa na Mamlaka ya CDA. Kwa kuivunja Mamlaka ile ya CDA kumetoa fursa sasa kwa Jiji la Dodoma kusimamiwa na mamlaka moja ambayo itaupanga Mji, lakini kuhakikisha inafanya maendeleo kwa ajili ya wananchi wa Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii lakini nikiiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano isaidie Jiji la Dodoma kuhakikisha kama ilivyofanya Jiji la Dar es Salaam, kitengo cha Wizara ya Ardhi kiondoke katika Jiji kiende Wizara ya Ardhi ili kuondoa mtafaruku ambao utakuja kupelelekea squatters tena zianze kuwepo Dodoma. Viwanja vipimwe vya kutosha, miuondombinu ipelekwe, lakini wakati huo huo Halmashauri ya Jiji ishughulikie na ukusanyaji na mapato yake ili kuboresha Jiji ili tuweze kufanya Jiji hili liwe la mfano lakini Jiji la kielelezo kama yalivyo Majiji mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Majiji yetu mengi katika nchi hii yamepangwa vibaya. Jiji hili la Dodoma ikiwa Manispaa, lilikuwa limepangwa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naiomba Serikali ije na mchakato katika Bunge hili kuleta sheria ya kutangaza sasa Jiji hili la Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie Wizara hii ya Fedha na Mipango katika kufanya nchi yetu iende. Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waisalam wenzangu wanaoendelea na mfungo huu wa mwezi Mtukufu mwezi wa Radhamani, nawaombea Ramadhani Mubarak. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara hii ya Fedha kwa juhudi na kazi nzuri ilizoonesha hasa katika suala zima la kusimamia kulipa deni letu la nje. Wizara ya Fedha imesimamia kwa ukamilifu kwa mwaka uliokwisha na naomba sasa waendelee kusimama imara kuhakikisha nchi hii inaaminika baadaye ili tuweze kufanya maendeleo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Wizara ya Fedha kwa usimamizi wao madhubuti sana ambao ulikutana na changamoto mbalimbali katika kusimamia mashine hizi za elektroniki (EFDs) kwa wajasiriamali wahakikishe wanazitumia ili kurahisisha makusanyo ya kodi za Serikali. Ni ukweli usiopingika kwamba Wizara hii ina mafanikio kiasi kikubwa na niwapongeze sana. Nataka kushauri Serikali yangu na Wizara hii tujaribu kuweka sera ambayo itaeleweka juu ya watu wetu, Serikali tusiwe na sera za mlipuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo nataka kulisemea na hata Mheshimiwa Waziri amelionyesha katika ukurasa wa 41 kwamba sasa tunatoa nafasi kubwa kwa sekta binafsi kusaidia katika uchumi na hasa kuweza katika maeneo mbalimbali. Tukikumbuka kule nyuma Serikali ilikuwa ikifanya biashara kupitia mashika yake ikiwemo RTC, NMC na hata mashirika kama GAPEX, badala ya mashirika haya kulipa kodi yalikuwa yanachukua ruzuku kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipoondoka kule nilitegemea kwamba sasa Serikali haitajiingiza tena katika biashara, kuna viashiria vidogo vidogo vinaoonesha kwamba Serikali inataka ijaribu kuingilia katika biashara. Niombe sana Mheshimiwa Waziri ang’ang’ane hapo alipoonesha ukurasa wa 41 kwamba sasa sekta binafsi itawekeza maeneo mbalimbali na ametolea mifano ambayo iko hai, gari za mwendo kasi pale Dar es Salaam lakini barabara ya Dar es Salaam Chalinze ambayo inategemea iwe ya kutoza toll kwa maana ya road toll.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejifunza kutoka nchi mbalimbali walioendelea waliachia sekta binafsi, Serikali kwa uwezo wake haiwezi kufanya kila kitu, lakini sekta binafsi inashindwa kuja katika nchi hii kwa sababu ya kutokuwa na uwazi katika sera za nchi. Hatuna sera, akija Waziri huyu ana tamko lake, akija huyu ana tamko lake. Tukiweka hilo itatusaida na wadau mbalimbali kutoka nchi mbalimbali miongoni mwetu Wabunge na hata wananchi na wafanyabiashara mbalimbali wanaweza kuleta watu wa kuwekeza katika maeneo mbalimbali kama tu tutakuwa na Sera ambayo itaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu vya kuimarisha ili sekta hii binafsi ambayo tunaitegemea isaidiane na Serikali katika kuboresha maendeleo ya nchi yetu ikiwemo miundombinu, maeneo mbalimbali ni lazima tuboreshe, Benki ya TIB. Mheshimiwa Waziri ameonesha kwa vipengele vifupi tu ukurasa wa 49 na ukurasa wa 90. Naomba sasa juhudi za makusudi benki hii ya TIB ndiyo mkombozi wa sekta binafsi, kwa sababu benki hii itahusisha mwekezaji yeyote anaweza kwenda pale na akapewa mkopo ambao ataulipa kwa kile alichowekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, benki hii inasuasua, mtu akihitaji mkopo mkubwa Waziri mwenyewe ni shahidi na ameonesha katika kurasa hizi kwanza benki haijawa sawasawa. Kwa hiyo tumwombe sana Mheshimiwa Waziri asimame imara kuisaidia nchi yako. Tuna mategemeo mkubwa na yeye lakini safu yake na Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara yake, tunaamini kwamba wataisaidia Serikali hii ya Awamu ya Tano kwenda na fikira ambazo Mheshimiwa Rais anadhani na anafikiri ni vizuri kwamba siku moja baada ya kipindi chake nchi hii itakuwa imesimama yenyewe kwa miguu yake, lakini inasimamaje kwa miguu yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tuondokane na fikra za kwamba Serikali inaweza kufanya biashara, Serikali kazi yake ni kusaidia miundombinu, kurahisisha mambo yaende ili sasa sekta binafsi nayo ichukue nafasi. Mfano ni huo kama nilivyotolea pale Dar es Salaam. Tulivyojenga miundombinu ya barabara. Leo mtu kutoka Kimara mpaka posta haizidi dakika 40. Ni mfano kama huo na iko mifano mingi ambayo itawekezwa. Hata Mheshimiwa Mwijage anapokuja na viwanda vyake vile vya mwendo kasi kama Serikali tutaifanya benki hii ya TIB iweze kuwa na nguvu basi wale wajasiriamali tukiwemo Wabunge kama anavyosema viwanda vidogo tunaweza tukawekeza, kupitia benki hii tunaweza kwa mawazo yake Mheshimiwa Mwijage. Mheshimiwa Waziri wa Fedha akisaidiana kama Serikali na Mheshimiwa Mwijage naamini hili linawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Wizara hii, mashirika wanayoyasimamia yakiwemo mashirika ya hifadhi ya jamii, yameonesha mfano nzuri sana katika kuwekeza. Nimwombe Mheshimiwa Waziri asimamie hilo, sekta binafsi na sekta ya umma lakini wanawekeza katika sekta binafsi naamini siku moja yatakuja kuwa mwarobani wa shida zetu na ajira za vijana wetu ambao wako na wanaosoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo katika huduma ya mfuko wa huduma ndogo za fedha, ukurasa 202, Mheshimiwa Waziri ameonesha kwamba watakopesha wajasiriamali vikundi vidogo vidogo vile bilioni 20, sijui wamefikia wapi, sijui wanakwenda kweli, au ndiyo tunakwenda kisiasa. Niwaombe sana wale watu wetu wa SACCOS za vijijini wana dhamira njema na kama tutawawezesha tutaondokana na mpango huu wa kuitegemea Serikali ituletee viwanda vya kutengeneza chaki kule katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Mipango ndiyo kitu ambacho naamini kama kitaweka mipango iliyo sawasawa, chuo hiki kinatengeneza wataalam ambao wanaamini wao wataenda kufanya kazi tu Serikalini. Ni vizuri tukabadilisha mfumo na mawazo ya watu wanaotokana na chuo hiki waweze kuangalia na sekta binafsi ili waweze kutoa utaalam wanaoupata. Nchi hii ili iweze kwenda mbele kama nilivyosema ni lazima sekta binafsi kwa asilimia kubwa nayo ihusishwe. Mifano kwa nchi zote ambazo zimeendelea, leo tunalitolea mfano Taifa la India, wamehusishwa sana wananchi pia watu ambao wako nje ya nchi ile ambao wana nguvu ya kiuchumi wameitwa, wamekuja kuwekeza maeneo mbalimbali na sisi tunayo fursa hii, lakini Chuo cha Mipango kikifanya kazi hii kwa weledi naamini hili linawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu pia kwa jitihada zinazosimamiwa na Wizara hii hasa katika suala la kulipa wazabuni ambao walikuwa wanahudumia katika taasisi za Kiserikali kama Magereza na maeneo mengine, leo wameanza kulipa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri waongeze juhudi kuhakikisha wale watu ambao walikuwa wanadai, wana madeni mbalimbali katika mabenki, wengine nyumba zao zimetaka kuuzwa na nyingine zimeuzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili watu hao waondokane na hali hii, kwa sababu walikuwa wanaisaidia Serikali yetu, wakisaidia watu wetu, wakisaidia wafungwa wetu na pia Majeshi yetu, leo kwa kuwa wameonesha dalili ya kuwajali naomba tu waongeze nguvu ili watu hawa nao waweze kulipwa kwa wakati ili kesho na kesho kutwa mpango uende vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nashukuru kwa nafasi hii ambayo umenipa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie katika Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2018/2019 pamoja na Mwongozo wake wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yangu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika jitihada zake za kuhakikisha rasilimali za nchi hii zinanufaisha wananchi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niipongeze Serikali kwa jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi ikiwemo hili kubwa la Serikali kuhamia Dodoma ambapo ni katikati na Makao Makuu ya nchi hii. Kuna kazi nyingi zinazofanywa na Serikali ni njema kabisa, lakini pia kuna changamoto kadhaa. Sasa mimi nijielekeze sasa hivi katika changamoto, lakini pia katika kupongeza yale ambayo yamefanywa mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais na Serikali yake na Mawaziri wake ambao tuko nao hapa wamejitahidi na wameonesha dhamira ya kweli katika ujenzi wa reli katika kiwango cha standard gauge ambacho leo mkandarasi wa pili ameshasaini mkataba, reli hii itasogea hadi karibu na Mkoa wa Singida, kule Makutupora. Mimi nikiwa Mbunge wa Mkoa wa Singida, mikoa ya katikati ni mikoa ambayo inanufaika sana na itanufaika na ujenzi wa reli hii ya kati kwa kiwango ambacho ni cha standard gauge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunazo changamoto pamoja na jitihada kubwa sana za Serikali kutaka kuunganisha mikoa yake ifikike kwa njia ya barabara. Mkoa wa Singida ukiwa mmojawapo kuunganishwa na Mkoa wa Mbeya, lakini pia na Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango nimeona jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha miundombinu hii inafanyika, lakini niombe jicho la tatu katika barabara za Mkoa wa Singida kuunganishwa na Mkoa wa Mbeya. Barabara inayotokea Mkoa wa Singida kuunganishwa na Mkoa wa Simiyu kupitia Daraja la Sibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, njia kuu na uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yoyote duniani miundombinu ikiwa rafiki ni rahisi mwananchi kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine, itarahisisha ulipaji wa kodi na hata kuirahisishia Serikali kukusanya maduhuli na kodi mbalimbali kupitia wananchi hawa wanapowezeshwa katika kuhakikisha wanasafiri na kupeleka mazao yao katika masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kufanya Makao Makuu Dodoma ningeomba sana Serikali iangalie barabara inayotoka Mkiwa kwenda Rungwa hadi Makongolosi. Kuna ahadi ya Serikali ya kuijenga barabara ile katika kipindi hiki, lakini kumekuwa na ukimya ambao hatuuelewi. Sisi Wabunge ambao tulienda kuwaambia wananchi kule kwamba Serikali yenu sikivu ya Chama cha Mapinduzi, mimi nikiwa Mbunge wake, tumeiomba na imekubali kujenga barabara na hata Mheshimiwa Rais alipokuja pale aliendelea kutoa ahadi hii, lakini kumekuwa na ukimya ambacho tunapata kidogo mashaka, tunaomba basi mje mtuambie mmefikia wapi katika kujenga barabara ile kutoka Mkiwa kuelekea Rungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni kipande pekee ambacho kimebaki kikubwa chenye urefu mkubwa, barabara hii ambayo leo bado ni kilometa 413. Ni barabara pekee ambayo ni ndefu, lakini barabara ya zamani, barabara ambayo ina uchumi mkubwa sana katikati yake kuna reserve za wanyama na maeneo mbalimbali, lakini na wakulima wengi wazuri wako maeneo haya ambayo tunatarajia kuleta na kuuza mazao hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo tunahitaji tuiombe Serikali yetu ilifanyie kazi kwa bidii sana ni suala la umeme vijijini. Kuna maeneo mengine kazi imefanyika vizuri na nipongeze jitihada za Mawaziri husika kwa kazi wanazozifanya, hasa Mheshimiwa Kalemani, lakini na Naibu ambaye ameteuliwa hivi karibuni, naona jitihada zake zinaweza zikatupeleka pazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umeme vijijini Mkoa wa Singida, mkandarasi alitangazwa, lakini baadaye akapotea. Tulipofuatilia tukaambiwa kwamba, yule mkandarasi kuna sifa zilipungua, walishindwana naye, kwa lugha ya sasa tunasema alitumbuliwa. Sasa alipotumbuliwa ndiyo wamepata mkandarasi mwingine, leo wananchi wa Mkoa wa Singida hatujafika popote, hakuna hata kijiji kimoja ambacho unaweza ukasema REA Awamu ya Tatu nayo imeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe basi Serikali yangu ya chama changu basi iwaangalie wananchi waaminifu wa Mkoa wa Singida katika umeme vijijini. Ni eneo pekee ambalo lina tatizo sana vijiji, vingi havijafikiwa na umeme na mimi naamini mkifanya hivi itatusababisha sasa na wananchi wa Singida, maeneo yote ya Mkoa wa Singida na hata Mkoa wa Dodoma bado wakandarasi hawa wanaonekana hawajafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ahadi zetu kwa wananchi wetu kuhakikisha tunaboresha huduma za afya katika vijiji vyetu kwamba tujenge zahanati kila kijiji. Wananchi wameanza kujenga kwa juhudi, Serikali zao za vijiji na wakati mwingine tunaiomba Halmashauri au Serikali itusaidie kufunika yale maboma, lakini tuliahidi kila kata kujenga kituo cha afya. Hili naomba sana katika mipango tunayokwendanayo nalo tulizingatie, ni miongoni mwa mambo ambayo ninaamini yatatufanya tuwe na jambo zuri la kufanya huko mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji vijijini ni changamoto kubwa sana. Vijiji vyetu vingi na hasa mikoa kame hii ya Dodoma na Singida hatuna mabwawa, basi tufanye juhudi za makusudi angalao basi malambo madogo madogo katika maeneo mbalimbali. Tumekuwa tukisema hapa Wabunge tunaotoka katika mikoa hii kwamba, kungekuwa na mito basi angalau, hatuna mito, mito ile ni ya msimu mvua ikinyesha baadae jioni imekauka, njia rahisi ya kusaidia wananchi ni kuchimba visima. Halmashauri zetu tunajitahidi, Serikali basi ituunge mkono katika hili ili wananchi wetu wengi nao wapate huduma hii. Ninaiomba Serikali mlitolee jicho la tatu kuona vijiji vyetu vingi vinapata huduma hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu katika kuona kwamba, sasa gesi hii ambayo ipo kwenye Mikoa ya Kusini imefika Dar es Salaam. Ni wakati sasa wa kuona na kujipanga na kuona tunafanyaje ili gesi hii ipite mikoani ikiwezekana ifike hadi Mwanza kwa kupita Dodoma, ikija Morogoro – Dodoma – Singida pengine Simiyu au Shinyanga ikafika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo kuna viwanda vingi. Naamini watu wanashindwa kujenga viwanda maeneo mengine kwa sababu tu pengine ya miundombinu, likipita bomba la gesi tukawekeza katika gesi, nchi hii ninaamini kule mbele hatutakuwa na changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wawekezaji wako wengi wana nia ya kuwekeza, lakini changamoto hizi za miundombinu ikiwemo matatizo ya umeme, kukatika-katika kwa umeme kunasababisha watu wapate uwoga wa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango basi muangalie mipango madhubuti ya kuhakikisha bomba la gesi linakwenda hadi Mwanza pengine na Mikoa ya Kaskazini na hata Mikoa ya Kusini kama Mbeya na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilikuwa na haya machache yanatosha. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwa muhtasari tu hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada kubwa na za dhati na za makusudi katika kuhakikisha nchi hii inafikia malengo yake ya kujitegemea kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuomeona hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ilivyoainisha na kuonesha makusudio mazima na dhamira nzuri ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutaka kufanya nchi hii wananchi wake waendelee kukiamini Chama kinachotawala sasa, Chama cha Mapinduzi kwa maana ya CCM. Ndiyo chama ambacho huwezi kuacha kuihusisha nchi hii na chama hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake ya Wizara ya Fedha kwa kuona na kutambua wananchi wanyonge ambao walikuwa wananyanyasika kwa kusumbuliwa sana na hususan katika kodi mbalimbali hizi ndogo ndogo, ikiwemo ya kusafirisha mazao kidogo chini ya tani moja, kutoka Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine, lakini kutambua sekta isiyo rasmi ya akinamama Lishe na wajasiriamali wadogo wadogo ili nao wawe na mchango katika uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kuishauri Serikali kidogo hasa katika kuhakikisha nchi inajitegemea katika suala zima la chakula. Ni vizuri sasa tukaanza kufikiria na kuondokana na utegemezi huu wa kilimo kinachotegemea mvua. Nchi hii tumekuwa tunategemea sana kilimo kinachotegemea mvua. Skimu za Umwagiliaji ziko kidogo sana na ziko maeneo ambayo yana uasilia wa mito labda na maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa tukatengeneza miundombinu ya makusudi, yakiwemo mabwawa madogo madogo kwa maana ya malambo, kuhakikisha wananchi sasa wanalima kilimo cha umwagiliaji kutokana na hali ya hewa ambayo inabadilika badilika. Kumekuwa na changamoto ya tabia ya nchi, wananchi wetu na maeneo yetu mengi, ikiwemo mwaka huu maeneo mengi ya hali ya chakula siyo nzuri sana, ikiwemo Mikoa ya Kati, hata Mikoa ya Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja ya juhudi za makusudi za Serikali kuwekeza katika kilimo hiki cha umwagiliaji. Ni vizuri sasa na sisi tutoke tukajifunze kwa baadhi ya nchi zilizofanikiwa nchi ambazo zilikuwa maskini wenzetu lakini sasa wametoka kabisa huku ambako tupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kusaidia wakulima ambao ndio wengi katika nchi hii, lazima tuhakikishe mbolea yetu inawekewa ruzuku. Kulikuwa na mpango hapa wa Waziri wa Kilimo aliyekuwa ametoka kwenye nafasi yake sasa amepewa Wizara nyingine ya kulinda watu wetu na mali zao; ni kwamba kulikuwa na mpango wa kuhakikisha mbolea yote ambayo inaingia katika soko inawekewa ruzuku. Hii itaondoa kufuatanafuatana; kazi kubwa itakuwa ya kudhibiti kwamba hii mbolea sasa badala ya kutumika ndani isitoke tu nje ya mipaka yetu, iuzwe kama bidhaa nyingine ambazo mkulima anaweza kununua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwe na ruzuku ya mbegu iwe wazi iingie masokoni ili mkulima akienda kwenye duka, mbegu iwe tayari ina ruzuku. Kama Serikali haitathubutu bado wakulima wa nchi hii wataendelea kusumbuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nchi hii tuna tatizo la maji. Naomba Serikali ifanye juhudi za makusudi mazima kuhakikisha upatikanaji wa maji vijijini. Tumediriki sana katika miji yetu mingi, tumeona juhudi kubwa za Serikali kupitia Wizara ya Maji kuhakikisha miji inapata maji, lakini vijiji vingi vina tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sasa Serikali ifike mahali ione na ichukue mawazo ya Waheshimiwa Wabunge. Wameongeza Sh.40/= katika kuhakikisha tunaziba mapengo ambayo yatatokana na misamaha ambayo wametoa. Naomba basi iongezeke hata Sh.10/= tu ambayo itasaidia kuongeza katika Mfuko wa Maji ili miaka hii iliyobaki tuweze kutekeleza vizuri ilani ya chama chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina dhamira njema ya kuunganisha Mikoa yote kwa lami, ukiwemo Mkoa wa Singida ambao natoka mimi. Tuna nia ya kuunganisha Mkoa wa Singida na Mbeya, kunabaki kilomita 413. Kilomita hizi ni nyingi. Naishukuru Serikali kwa kuanza kutaka kujenga sasa kilomita 56.9 kutoka Mkiwa, Itigi hadi Noranga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara hii ya Ujenzi, kwamba ukijenga kilomita 57 hizi takriban, bado utakuwa umebakiza kilomita 300 na zaidi. Ikiwezekana, ni vizuri basi speed ikaongezeka, lakini Waziri wa Fedha aone, awasaidie. Ule Mradi Mkandarasi hadi sasa hajafika, hatumjui mpaka sasa hivi, lakini tunaambiwa tunajengewa kilomita 56.9 takriban kilomita 57.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu kupitia daraja la Simbiti ni jambo ambalo tunataka tuone sasa wananchi wa Mikoa hii wanasafiri lakini wanapita katika barabara kama wenzao wanaotoka maeneo mengine. Napongeza kwa sasa kumalizia kipande cha barabara ya kutoka pale Chaya mpakani kwenye Mkoa wa Tabora maeneo ya Nyahuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeze Serikali pia kwa kusimamia kutaka kujenga reli hii ya Kati, kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, lakini dhamira ni kufika Makutupora katika Mkoa wetu wa Singida. Vile vile kuna reli hii ya Kati ambayo ni kutoka Dar es Salaam, Kigoma na Mwanza, ina tawi lililoanzishwa na Mheshimiwa Mwalimu Nyerere Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa hili kutoka Manyoni kwenda Singida, haizungumzwi hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli hii ilikuwa na msaada mkubwa katika uchumi wa nchi hii. Sisi ni wakulima na kulikuwa na mashamba ya NAFCO. Kule Basutu yalikuwa yakipita pale inarahisisha kufika kwa walaji wengi ambao ni miji mikubwa lakini kwenye viwanda kule Dar es Salaam. Ni vizuri sasa mkaanza kufikiria reli hii ya Manyoni – Singida nayo iwe katika kiwango kizuri; lakini wameanza kung’oa hadi mataruma. Sasa sijui uwekezaji ule nchi inaenda namna gani? Naiomba Serikali iangalie kipande hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kidogo kuhusu suala zima la hifadhi ya chakula. NFRA wametengewa hela mwaka huu, lakini hapa nyuma tumeshuhudia maeneo mengi yanapata upungufu wa chakula lakini msaada na namna ya kuwahami wananchi wetu unachelewa sana. Leo hii tumeanza kutoa eti chakula cha bei nafuu wakati tayari watu wameshavuna. Naiomba Serikali kwa makusudi mazima, panapokuwa na upungufu wa chakula, basi zichukuliwe hatua za makusudi kusaidia watu wetu waweze kulima na kurudi tena mwaka mwingine usiwe na njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapokutana na hali ya uhaba wa chakula, hawezi hata kufanya kazi zake za kila siku. Kwa hiyo, tunatengeneza mazingira ya janga kubwa zaidi kama hatutaweza kutumia akiba ya chakula ya Taifa kuwanusuru wananchi wanaokutana na tatizo hili. Hii imetokea sana miaka hii miwili ambapo nami nimeona nikiwa Mbunge kwamba hazichukuliwi hatua za haraka, wanaposaidia wananchi, wanapewa chakula kile wakati tayari wameshaumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka nisemee kuhusu ujenzi wa Zahanati kila kijiji na ujenzi wa Kituo cha Afya kila Kata; ni ahadi yetu ya uchaguzi. Sasa sijui tukirudi tutakuja kusema nini? Naomba sasa juhudi za makusudi angalau tufikie nusu ya yale ambayo tuliahidi.

(Hapa kengele ilia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nichangie katika Wizara hii ambayo nayo ni mhimili wa uchumi katika nchi yoyote duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa jitihada zake za kujenga miundombinu ya reli lakini kutaka kuunganisha mikoa yote kwa njia ya barabara za lami. Dhamira hii ya Serikali ya kuunganisha mikoa kwa kiwango cha lami imekuwa ya siku nyingi lakini barabara ambazo hata Mheshimiwa Waziri ameionesha katika kitabu chake, barabara ya kutoka Makongolosi hadi Mkiwa, kuna kilometa 413, katika Jimbo ambalo mimi ndio mwakilishi wake ziko kilometa 219.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inajengwa kutoka Mbeya, Mbeya – Lwanjilo - Chunya, sasa wanajenga Chunya hadi Makongolosi katikati pale kilometa 43. Upande wa Singida barabara hii sijui kuna makosa gani ambayo watu wa Singida wamefanya hadi hii leo, mwaka jana katika kitabu cha Waziri alionesha dhamira kwamba barabara hii inajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati Naibu Waziri aliyekuwepo yeye mwenyewe Waziri amefika Itigi kuzungumza na wananchi kwamba barabara hii itajengwa na tukawaaminisha wananchi barabara hii sasa inajengwa. Ikatengwa pesa, ikatangazwa barabara na mkandarasi akapatikana. Hata hivyo, baada ya muda sijui kilizuka kitu gani barabara hii nayo mwaka huu imewekwa katika mpango vilevile, mkandarasi alipatikana Sinohydro lakini sasa sijui wamemwondoa sijui wamemfanyaje, tunapata taarifa kwamba watatangaza lakini sio rasmi, hizi ni redio mbao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri kwa kuwa mwenyewe yupo hapa hebu atuambie na awaambie wapiga kura waaminifu kwa chama hiki ambacho Serikali yake na yeye ndio anatoka wamenichagua mimi kwa ajili ya kuhakikisha barabara hii sasa inajengwa. Atawaambiaje wananchi wa Itigi, mwaka huu tunaanza kujenga barabara au tutabaki na zile story za miaka nenda, miaka rudi toka enzi ya Baba wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ina kilometa mia nne na kumi na, ni barabara pekee inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Singida, hakuna barabara mbadala na ukitoka Singida kwenda Mbeya lazima uje tena Dodoma – Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi Profesa Mbarawa yeye ni mwaminifu, ni mtu kweli; hebu sasa awaoneshe watu wa Itigi ukweli wake kwamba barabara hii mwaka huu wanaijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,nifurahie na niseme kwamba Serikali hii imeonesha usikivu kwa kuonesha kuunganisha Mkoa wa Singida na mikoa mingine kupitia barabara hii ambayo ameitaja katika kurasa zake wakati anazungumza katika ukurasa huo wa 147 amezungumzia barabara ya Handeni – Kiblashi – Kibaya, ni kilometa 460 ukitokea Singida mpaka pale Handeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali kweli imedhamiria kuijenga barabara ile kwa kiwango cha lami ina maana inaungana na mpango ule wa East Africa wa Serikali ya Uganda kupitisha bomba lile katika ukanda huu wa kwetu. Kwa hiyo, wananchi wanaotoka na mizigo yao katika Bandari ya Tanga na bandari ambayo tunaamini Wizara hii inahusika itakuwa ni miongoni mwa bandari ambazo zitaihudumia sana nchi hii kuisaidia mzigo uliopo katika bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, barabara hii ikijengwa itasadia mizigo ambayo inakwenda nchi jirani pamoja na nchi ya Kongo, watu hawatapita tena Dodoma na hapa makao makuu patapunguziwa mzigo, wajasiliamali hizi by pass tunazozijenga za mji zitapunguziwa mzigo, watu watatoka Bandari ya Tanga, watapita Handeni pale moja kwa moja wanatokea Singida, tayari tunaboresha uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la mawasiliano, baadhi ya maeneo ya Jimbo langu yana shida ya mawasiliano ya simu. Maeneo ya Mbugani, Kintanula, Gulungu nilishaandika barua, lakini na Wizara ilishatambua maeneo ya Lulanga na Itagata kuwa yana shida hii ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara hii sasa basi waweke mkazo katika suala hili ili wananchi ambao nao ni wa nchi hii wanufaike na rasilimali za nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niisemee Serikali niipongeze kwenye suala la kuimarisha na kuhakikisha TTCL inasimama imara, lakini kuna tatizo ambalo TTCL wanalo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuishukuru Wizara hii kwa kuniteua kuwa Balozi wa Utalii wa Ndani, lakini pia nipongeze utendaji mzuri wa Waziri Mwalimu wangu Ndumbaro na Naibu wake kwa utendaji mzuri sana katika Wizara hii. Vile vile niwapongeze zaidi kwa hili ambalo wameliona juzi tarehe 2 kwa kuruhusu export ya mti wa mkurungu ambao ulikuwa barned pasipo sababu ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya maamuzi haya mazuri, lakini baada ya maamuzi haya kuna changamoto ambazo mimi naziona na naomba niishauri Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi, lakini bahati nzuri zaidi kwa TFS ambao wapo hapa chini ya Wizara hii, kuna jambo ambalo sidhani kama wanaliona; tunapoamua sasa kufanya export ya mbao ngumu tunahitaji ma-saw doctors. Vyuo vyetu vya FITI bado havijatengeneza ma-saw doctors ambao wanafaa kufanya kazi maeneo yetu. Viwanda vilivyopo maeneo ya Mufindi na maeneo mengine ya mbao laini bado wanatumia ma-saw doctor ambao hawana elimu ya kutosha, ndio maana uchakataji wa magogo umekuwa na tatizo kubwa kwa maana mbao hazinyooki sababu ya kufanya hata export hizi zinakuwa na shida katika masoko ya dunia ni kwa sababu mbao zetu hazinyooki kwa sababu hatuna ma-saw doctors.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Serikali ni moja, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu ikubali wanapowadau wa misitu hasa wawekezaji wanapowekeza katika mazao ya misitu kwenye viwanda vya misitu, Serikali ikubali kuajiri ma-saw doctor wa kigeni ili kusaidia ku-train watu wetu baada ya muda nao wataweza kuchukua nafasi zile ambazo zinafaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo ambalo hapa limekuwa na changamoto kubwa sana, wananchi wengi hasa sisi wawakilishi wao wametutuma tuwazungumzie kuhusu sakata hili la mkaa. Gunia moja mtu anatakiwa kulipia sh.12,000, bado nchi hii hatujawa na mbadala wa nishati, sasa ni namna gani tunajipanga. Kwa kuwa Serikali ni moja labda ingefanya utaratibu basi gesi hii ambayo tunayo itapakae nchi nzima mabomba ya gesi yatoke kule Dar es Salaam yaje mpaka Mwanza, yaende mpaka Tanga na Mbeya kwako kule ili wananchi waweze kutumia hii gesi ya asili lakini matumizi mbadala leo ya mkaa hatuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali iangalie namna bora hasa TFS watafute species za miti ambazo ni nyepesi kama alivyosema jana ndugu yangu hapa Mheshimiwa Profesa Kishimba, miti ambayo inaweza kupandwa kwa haraka na ikaota kwa ajili ya kupata mkaa kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie bajeti hii Kuu ya Serikali kwa mwaka huu 2018/2019. Nitangulie kwa kuunga mkono hoja, lakini pia nitoe pongezi zangu za dhati kwa Mawaziri, Waziri wa Fedha na Naibu wake, kwa hotuba yao nzuri, yenye nia njema kwa nchi hii na kuifanya nchi hii ijitegemee kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia juhudi kubwa za Serikali katika kujitegemea katika umeme kwa kujenga sasa Stiegler’s Gorge. Vile vile nipongeze juhudi za Serikali za kujenga Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mawazo yangu kidogo ya kuishauri Serikali, kwamba sasa ione sekta ya kilimo inaweza ikawa na mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi hii, lakini ni sekta iliyoajiri zaidi ya asilimia 66 ya Watanzania lakini haija-reflect vizuri katika bajeti hii ni namna gani tunawabeba wakulima wetu ambao baadaye tunatarajia kwamba sasa sekta hii iendelee kuajiri hata wasomi ambao wanatoka katika vyuo vikuu ambao ajira katika sekta iliyo rasmi imekuwa hamna kama inavyoonekana. Sasa nia yangu ni kuishauri Serikali tuone namna gani sasa tutawezesha kilimo hiki. Tukiendelea kutegemea kilimo hiki cha mvua bado hatutaweza kufika popote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa Serikali ikatoa mwelekeo wa namna gani tutaweza kuwa na kilimo cha umwagiliaji maeneo mengi, ni namna gani tutawezesha miundombinu ya kufanya kilimo cha umwagiliaji kiwezekane hususani katika mikoa kame Mikoa ya Kanda ya kati ya Dodoma na Singida. Katika mpango wake kuna bwawa hili la hapa Farkwa ambalo kama litajengwa kwa wakati lina msaada mkubwa sana kwa wakulima wa Kanda ya Kati, Skimu za umwagiliaji ambayo ipo ya Bahi na maeneo mengine ya mkoa wa Singida yatanufaika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Serikali ione ni namna bora ya kufanya sasa hata deep well za kutosha ambazo zitafanya maeneo mengi ya umwagiliaji. Tukitegemea kilimo hiki cha mvua ambacho tumekizoea mwaka ambao mvua itakuwa kidogo itakuwa ni namna ngumu sana ya kujitegemea hata kwa chakula ambacho kwa miaka hii mingi sasa tumeanza kujitegemea. Ni vizuri sasa Serikali ikawekeza pahali hapo ili wananchi wetu na nchi kwa ujumla iweze kunufaika. Hata hivyo, niipongeze Serikali kwa kutenge pesa kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima hususani mahindi ya kupitia NFRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sekta pia ambayo imesahauliwa. Sekta ya misitu ilikuwa na mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi hii lakini hapa katikati kumeyumba, tumekuwa tunagemea export za species chache sana kama mitiki, lakini wakati huo wanunuzi wa tiki na wachakataji wa tiki wamekuwa na usumbufu lakini bei za mazao yale katika mashamba ya Serikali zimekuwa ni kubwa zaidi kuliko hata bei za masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna uwezo sasa kuiambia Serikali ifanye machakato wa kutosha kuona specie nyingine ambazo ziko kwa wingi katika nchi yetu. Na-declare interest mimi ni mdau katika sekta hiyo, zinaweza kutuondoa katika changamoto hii ya maduhuli ya Serikali kwa kiwango kikubwa sana. Miaka 2011, 2012 hadi 2013 ukiangalia katika mchakato mzima wa export ya nchi hii sekta ya misitu ilikuwa na mchango mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea hapa katikati kumekuwa na ban za ajabu ajabu, zinafika mahali wananchi wajasiriamali na wenye viwanda sasa wanakosa malighafi katika viwanda ambavyo Serikali iliwashauri wananchi watoke kule ambako walikuwa wana export mazao ghafi. Sasa wamewekeza kwenye viwanda sasa hivi tena viwanda vile vile vimekosa malighafi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya misitu kama itasimamiwa vizuri itakuwa na mchango mkubwa sana kama zilivyo sekta za utalii na wanyamapori katika uwindaji wa kitalii; lakini sekta hii ya misitu nayo naamini kwa weledi ambao kama watasimama vizuri Wizara ya Maliasili wataisaidia Serikali kama Wizara ambayo ina mchango mkubwa kwenye kukusanya maduhuli ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu na kuunganisha mikoa ya nchi hii kwa kiwango cha lami bado ni changamoto. Suala la Mkoa wa Singida kuunganishwa na Mkoa wa Mbeya limekuwa likizungumziwa kwa muda mrefu. Wabunge wote wa miaka mingi ya nyuma, hata mwaka juzi mimi nilisimama na ilani hapa kuonesha, mwaka jana wakaonesha nia ya kutaka kujenga Barabara ya Mkiwa hadi Rungwa, kilomita angalau 56.9, ikawekwa kwenye bajeti ikatangazwa kazi mkandarasi akapatikana na Mheshimiwa Rais akaja pale akazungumza na wananchi akaonesha dhamira yake ya kujenga barabara lakini mchakato ule ukafa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi hivi tunavyozungumza tumeona tu katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2018/ 2019 barabara hii imeonesha ukurasa wa 49 kilomita 56.9, lakini mpaka hivi wananchi wale wa jimbo ambalo mimi ni mwakilishi wao hawajui barabara hii itaanza kujengwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa Serikali ioneshe dhamira ya kweli ya kuunganisha mikoa kwa njia ya lami, ndiyo itakayofanya wananchi wakimbie. Walipa kodi wa maeneo ya pembezoni watalipa kodi kwa sababu watakuwa wanafanya biashara zenye tija kwa kufuata biashara maeneo makubwa. Leo mji wa Dodoma ndio Makao Makuu ya nchi Dodoma imetangazwa kuwa jiji mikoa ya jirani kama mikoa na majimbo ambayo mimi natoka yatakuwa na manufaa sana kama yataunganishwa kwa kiwango cha lami na mikoa jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia niiombe Serikali iendelee kutia mkazo barabara hii ya kutoka Handeni, Kiberashi, Kijungu, Kibaya, Njoro, Olboroti, Mrijo Chini, Dalai Bicha, Chambalo, Chemba kwa Mtoro hadi Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuchumi barabara hii ina manufaa makubwa sana, ni njia ya mkato kabisa ya watu watakaokwenda Bandari ya Tanga; na tuna matarajio yetu kwamba tunajenga bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Chongoleani Tanga. Kwa maana hiyo barabara hii kama itajengwa kwa kiwango cha lami itasaidia sana hata nchi jirani ya Rwanda, Uganda, Burundi kama watatumia Bandari ya Tanga kuondoa msongamano katika bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafsi na pia naomba niunge mkono hoja hii ya Waziri wa Fedha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami nichangie Wizara hii ambayo kama itasimamiwa vizuri inaweza kuwa mhimili mmojawapo ambao utachangia katika uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi za dhati sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kuona kwamba Wizara hii sasa iwe Wizara kamili na kama ilivyoundwa na Naibu Mawaziri wawili kaipa thamani kubwa. Niwaombe viongozi walioteuliwa katika nafasi hii, Waziri na Naibu Mawaziri waione thamani ya Wizara hii na waitendee haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na jambo moja ambalo hatulioni sana. Wabunge wenzangu wamezungumza mambo mengi lakini na Wizara wenyewe katika kitabu chao wamejielekeza katika mambo mengi na Kamati pia. Wizara hii inaweza ikafanya kitu kimoja ambacho mimi nakiona ni bora sana. Tumekuwa tunakwenda nchi kama Dubai tunaona uhuria uliopo wa biashara lakini Singapore na maeneo mengine ambayo wamekuwa katika uhuria wa biashara kwa maana ya kwamba unaweza kwenda na mzigo wako pale lakini usiulizwe ili mradi tu unalipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri Wizara hii waanzishe soko huria la dhahabu kwa maana wananchi wa ukanda huu wa nchi 10, 13 za nchi hizi za Afrika Mashariki na Kati zina dhahabu nyingi sana na wananchi wanatafuta mahali pa kuuza dhahabu lakini hawana. Matokeo yake sasa watu wamekuwa wanapitisha dhahabu kinyemela na kwenda kuuza Kenya kwa sababu ya ile fursa iliyopo ya kuuza dhahabu Kenya kuliko ukionekana na dhahabu Tanzania. Nashauri Wizara ije na mkakati ambao utakuwa na soko ambapo Tanzania itakuwa sehemu ambayo itapelekea watu wa nchi jirani kuleta dhahabu yao hapa na kufanya wananchi wa nchi mbalimbali za huko waje wanunue lakini pia itaongeza kwa upande mwingine suala la utalii. Kwa hiyo, itachochea biashara na utalii pia katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo taarifa mbalimbali katika Wizara ya Madini zikiwepo zile quarter degree sheet ambazo zipo zenye taarifa za madini, zile zina taarifa za muda mrefu sana. Naomba Wizara hii kwa kuwa sasa imekuwa Wizara kamili wajikite kuboresha taarifa ili tuwe na latest kiasi kwamba mtu ukichukua ile taarifa ya pale uweze kuiuza kwenye maeneo mengine na kufanya wawekezaji waje. Sisi tunakosa wawekezaji mpaka mtu awe na shimo, anatoa dhahabu au aina nyingine ya madini, hatuna taarifa kama zilizofanywa na geo-survey wakati ule na zilizofanywa na taasisi zingine. Tumefika mahali tumesahau kabisa kazi ya kuhuisha taarifa za maeneo ambayo madini yapo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na masuala ambayo yalikuwepo hapo nyuma, nashukuru sana sasa hivi Serikali imeliona kwamba gemstone ni madini ambayo yanatakiwa yachimbwe na wazalendo tu kwa maana wananchi wa Tanzania. Suala hili lilikuwa linaleta kero kubwa hasa tanzanite pale walipoingia ubia na hawa watu wa Afrika Kusini. Hii ilituletea shida kwa sababu ni miongoni mwa rasilimali chache sana ambazo tunazo nchi ya Tanzania na zinapatikana Tanzania lakini nchi za India, Afrika Kusini na Kenya ndiyo walikuwa wanaongoza kuuza tanzanite katika masoko ya dunia. Kwa mpango huu ambao umefanywa na Serikali na hili pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake mkubwa na wa makusudi kabisa kujenga ukuta pale, kwa maana hiyo sasa kama nchi tutanufaika na rasilimali hii ambayo ipo hapa Tanzania pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo nataka niombe Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wake walione, suala la masoko ya madini haya. Ni vizuri basi kama Serikali ikatangaza madini ambayo yapo katika maeneo yetu, hata hizo tanzanite na rubi na madini ambayo yalisemwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge masoko yake ni mpaka mtu tu a-penetrate mwenyewe kwenda kutafutia soko. Hatuna latest taarifa kama nilivyosema kwenye maeneo haya lakini pia ni kwa kiwango gani wazalishaji wetu wa migodi midogo wanatambuliwa na kujengewa uwezo wa kuuza katika soko la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri walio chini ya ofisi yake kwa utendaji wao uliotukuka. Pia nipongeze hotuba yake nzuri na bora yenye dhamira ya kuifanya nchi hii ijitegemee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 42 ameonesha nia na dhamira ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya nchi yetu. Ipo dhamira ya Serikali ya kuunganisha mikoa yote kwa kiwango cha lami. Mkoa wa Singida unaungana na Mkoa wa Mbeya kwa njia ya barabara. Barabara hii imejengwa toka Mkoa wa Mbeya, Serikali ilionesha nia ya kuanza kujenga kutokea Mkoa wa Singida kutoka Mkiwa Itigi hadi Moranga kilometa 56.9 na mkandarasi alipatikana ambaye ni SIMOHYDRO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuwa anafungua barabara ya Manyoni – Chaya kilometa 89 tarehe 25 Julai, 2017 alibaini mchakato wa zabuni ulikuwa na harufu mbaya na akatoa maelekezo yaliyosababisha barabara hii kutokujengwa au kuanza kujengwa hadi hivi leo. Je, ni lini sasa Serikali itaona ni vyema kuwatendea vyema wananchi wa jimbo langu kwa kuanza kuijenga barabara hii.

Naomba sasa mwaka huu basi Serikali ianze ujenzi wa barabara hii ambayo ni muhimu sana katika kuunganisha Mkoa wetu wa Singida na Mkoa wa Mbeya. Barabara hii ndiyo pekee iliyobaki ya kuunganisha mkoa na mkoa ambayo ni ndefu kuliko zote Tanzania kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii tena kuipongeza Serikali na pia nimpongeze kipekee Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa utendaji wake na juhudi nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa na ununuzi wa ndege na hata vivuko katika maziwa yetu.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie mapendekezo haya ya Mpango ya mwaka 2019/2020.

Mimi nataka nianze na suala la umaskini ambalo limeoneshwa katika ukurasa wa nane. Jambo hili lina dhamira njema nimeona dhamira ya Serikali katika mapendekezo haya. Lakini kuna taatizo kubwa hapa riba ya mikopo hasa kwa taasisi ambazo hizi mabenki yetu imekuwa si rafiki kwa watu wetu wengi. Ni namna ngumu sana wananchiili waweze kujiwezesha hususani wajasiliamali wadogo wadogo, taasisi hizi za fedha lazima ziwe rafiki na ili uchumi wa nchi hii uweze kwenda mbele, wananchi hawa wakiweza kukopeshwa lakini tuweze ku-increase export katika mazao yetu ikiwemo mazao ya misitu, asali na mazao mengine ya kilimo ambayo yamekuwa na matatizo makubwa tumeshuhudia kuona leo mazao kama ya mbaazi yamekuwa hayauziki katika mikoa ambayo inalima mazao haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napendekeza Serikali tuishauri ione namna bora ya kuwezesha wananchi wakulima hasa wadogo wadogo wa vijijini ili waweze nao kushiriki katika kujenga uchumi wa nchi hii. katika suala la kilimo limeonyeshwa ukurasa wa 17 lakini ni namna gani tunawezesha wakulima tumeshuhudia kuona matrekta yako pale Kibaha yanaunganishwa, ni kwa nini basi sasa tusijikite namna bora kama iliyofanya ile kilimo kwanza ambayo imepelekea nchi hii leo tunajitegemeakwa kiasi kikubwa sana katika uchumi hasa kilimo tumekuwa ukanda huu wa Afrika tumekuwa tunauza mazao kwa nchi za ambazo tumepatakana nazo kwa sababu mpango wa kilimo kwanza ulikuwa na tija matrekta yalikuwa vijijini na wananchi walikuwa wanalima.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mikopo ambayo ilikuwa ni rafiki japo wengine changamoto zilijitokeza wengine hawakuweza kulipa lakini sio iwe ndoo tatizo tu-deal na issue ya mtu ya mmoja mmoja, mpango ule wa kilimo kwanza ulifaulu sana na matrekta yanapokaa pale Kibaha sioni kama itakuwa ni faida kwa Serikali hata huyu muwekezaji tunamvunja moyo kuona matrekta badala ya kwenda kwa wakulima kule vijijini ili yaendelee kuleta mengine basi anakuwa hawezi kufanya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza katika kuboresha uchumi suala zima la gesi nalo tulione gesi iko Dar es Salaam leo makazi ya watu wa Dar es Salaam nimeona majaribio yanataka kufanyika kwa maeneo machache tu yakiwemo kwenye maeneo makazi ya watu wanene kule Masaki na maeneo mengine. Lakini maeneo ya makazi ya watu wadogo kama sisi tunaokaa pembezoni basi isaidie gesi hii iwe sehemu kubwa ya kupikia kuondokana na ukataji wa miti ambao si rafiki kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifugo tumelina ukurasa wa 18, lakini hakuna mikakati kabisa inayoonesha kwa makusudi mazima kuona sasa mifugo hii yetu inatoka katika utaratibu ule wa kuchunga na sasa waweze kufuga. Ni vizuri tumeona kwamba mna mpango wa madume bora, lakini naona ni machache ambayo yako kwenye taasisi tu kubwa kubwa, wafugaji wadogo wadogo bado hatujawaweka wala hatujawa-accommodate kama nao wawe sehemu ya kunufaika na mapendekezo haya ambayo yanaletwa mbele ya Bunge hili tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika ukurasa wa 27 na 28 barabara nyingi zinaonekana zinataka kujengwa, lakini bado barabara zinazounganisha mikoa hazijamalizika. Mikoa ya Singida kuunganisha na Mkoa wa Mbeya ambako na mimi jimbo langu limo humo, barabara yake haionekani humu katika mapendekezo ya mpango huu. Ni mpango gani upo na Serikali kwamba tunauunga Mkoa wa Mbeya kupitia Itigi? Lini sasa wataanza kuonesha katika mapendekezo yajayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri uje na mapendekezo yanayoonesha utakapokuja kwenye mpango tuone ni nini dhamira ya Serikali ya kuunganisha wananchi wa mkoa mmoja na mkoa mwingine, ukiwemo Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu. Daraja la Sibiti tumeliona kwa hili nipongeze sana na juhudi za Serikali ziko wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 30 wa mapendekezo haya, nimeona nishati vijijini (REA). Bado wakandarasi wengi hawajaanza kufanya kazi, hatujui tatizo ni nini. Sasa kwenye mapendekezo haya hatuoni dhamira gani ya Serikali Mkoa wetu wa Singida mojawapo ni miongoni mwa mkoa ambao REA wamefika, lakini hawajaanza kazi, basi tunataka tuone maboresho katika sula hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona suala la afya umelionesha katika ukurasa wa 38, lakini bado Hospitali za Rufaa ni changamoto, tumeona hospitali moja tu mmeitaja, Hospitali ya Benjamin Mkapa, lakini mikoa mingine hospitali zao za rufaa hazijaoneshwa kwamba hamjazizingatia katika mapendekezo ya mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mengi ambayo tunatakiwa kuona, lakini Wabunge wanataka kuona mchakato huu wa reli unafika basi Kigoma, unakwenda hadi Mwanza, umeoneshwa tu kwa kifupi. Nichukue nafasi hii kumshauri Mheshimiwa Waziri azingatie hilo nalo na kwenda makutupora basi na kule mbele tuone basi juhudi hizi ambazo zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa na haya machache tu ya kuchangia mpango huu wa mapendekezo ambayo nimeona kwa kweli, dhamira njema ya Serikali ya kufanya maendeleo katika nchi hii. Ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie katika Wizara hii ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Niendelee kupongeza kama walivyopongeza Wabunge wenzangu kwa utendaji mzuri wa Mawaziri, Mheshimiwa Waziri Kamwelwe, wasaidizi wake, Manaibu Waziri wote wawili, Katibu Mkuu wa Wizara hii na Watendaji wote katika Wizara hiyo. Wamekuwa wakifanya kazi nzuri, lakini zipo changamoto ambazo tunatakiwa tuwasaidie na kuendelea kuishauri Serikali kuona namna iliyo bora ya kufanya sasa nchi hii iweze kukaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inasimamia suala zima la barabara. Suala la barabara, dhamira ya Serikai na Ilani ya chama cha Mapinduzi ni kuunganisha Mikoa yote kwa njia ya barabara za kiwango cha lami. Tunayo barabara moja katika Mkoa wa Singida inayounganisha Mkoa huu wa Singida na Mkoa wa Mbeya. Ametoka kuzungumza sasa hivi mwenzangu hapa ambaye nimepakana naye, Mheshimiwa Mwambalaswa, kule kwake wanajenga barabara hiyo hiyo kwa kiwango cha lami. Awamu ya kwanza walianza Mbeya kwenda Rwanjilo, ya pili Rwanjilo kwenda Chunya, sasa wanajenga kutoka Chunya kwenda Makongorosi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Mkoa ambao tunapakana nao mwaka 2017 barabara hii ilipata mkandarasi, ilitangazwa mchakato ukaisha. Mheshimiwa Rais alipokuja Itigi mwezi wa Saba tarehe 25 alikuta tatizo katika barabara hii. Mchakato ulionekana una harufu ambayo siyo nzuri, akazuia, akasema kwamba kwa pesa ambazo zinatolewa, aidha, mkandarasi afanye negotiation na TANROADS waongeze kilometa au kilometa zipunguzwe kulingana pesa na mchakato ambao ulikuwa umeingia katika mkataba ule,

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia 2017 mpaka leo hii waliposhindana kwenye mazungumzo mkandarasi mwaka 2018 aliondoka. Mwaka 2018 katika bajeti iliyokwisha ikaoneshwa kwamba barabara hii iko katika mpango wa kujengwa. Katika kitabu hiki ukurasa wa 181 barabara hii imeoneshwa kwa pesa kiduchu ambazo zimeoneshwa katika jedwali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu yangu, wananchi wa Mkoa wa Singida Jimbo la Manyoni Magharibi, aidha watanichukua mimi Mbunge wao au wataichukia Serikali yao, kwa sababu hawajaambiwa neno la ukweli toka mwaka 2017. Naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, Mawaziri mlioteuliwa, Mheshimiwa Waziri Kamwelwe, mnaaminiwa na Mheshimiwa Rais, barabara hii hata wewe Mheshimiwa Waziri inakufaa sana. Kwenda kwako kule badala ya kupita Tabora utapitia Itigi, utakwenda Rungwa, Rungwa - Ipole, Ipole unakwenda Mpanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kama hutaijenga Mheshimiwa Waziri maana yake unataka nami mwakani nisiende kuomba kura; au nikiomba kura nitapata taabu sana namna ya kuwaeleza wananchi waelewe. Namwomba Mheshimiwa Waziri barabara hii niliiona humu basi mwaka huu tuone mkandarasi anapatikana na ujenzi unaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri wataalam wote wako hapa, Katibu Mkuu yuko hapa. Eng. Nyamwanga alishafikisha pazuri sana barabara hii katika kutaka kuijenga, lakini Katibu Mkuu mpya naamini ni msikivu, Eng. Mfugale uko hapa, mimi ndiyo natoka Itigi, siku ile ulikuwepo pale. Naomba sasa masikio yako yarudi yafunguke yaone ahadi ya Mheshimiwa Rais kwa wananchi wale. Tunawategemea ninyi, 2015 tunakwenda katika Uchaguzi wa Vijiji mwaka huu, tunataka tushinde vijiji vyote. Nami naahidi nitasimama imara CCM itashinda vijiji vyote, lakini hili litaweza kuja kutugharimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Mheshimiwa Waziri ananiangalia, naamini hili limeingia. Naomba tu mnisaidie, nami sitaongea tena suala la barabara. Tusaidiane, barabara hii ina maslahi mapana na watu wa Mkoa wa Singida, Katavi na Mbeya. Makao Makuu ya Serikali yako Dodoma. Mtu wa Katavi anapokuja Dodoma, akipita Tabora anaongeza urefu wa safari, lakini ukipitia Rungwa - Itigi ni kwepesi, hata Mheshimiwa Mwambalaswa atakuwa hawezi kuzungukia tena Makao Makuu yake ya Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niendelee kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya ya ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge. Sisi watu wa Mkoa wa Singida reli inapita Itigi katika eneo langu. Naomba tu juhudi ziendelee, lakini kwa hakika tunafarijika sana na kazi inayofanywa na Serikali hii kupitia Wizara yenu hii. Hayo mengine tunasema ili nanyi mtuone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la minara ya simu. Suala hili linaonesha kuna shida kidogo. Mwaka 2018 karibu na bajeti tulipitishiwa makaratasi hapa ya kuonesha mnara utajengwa mahali kadhaa, mahali kadhaa; na mwaka huu umekuja mpango ule ule. Ile ya mwaka 2018 haujajengwa, lakini mwaka huu umekuja utaraibu ule ule. Sasa naomba sana Waheshimiwa Mawaziri mnapokuja na yale makaratasi na kuchukua majina, basi tuone yana-reflect kwa wananchi wetu. Ukishaniambia mimi, nami nikifanya mikutano, nawaambia wananchi hapa Serikali inaleta hiki. Sasa ninapokwenda kwa mara nyingine tena nakuja na story inakuwa haipendezi na hasa sisi wenzenu wa upande huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya, lakini niunge mkono hoja hii kwa asilimia mia moja ili mkipata pesa mkatekeleze miradi hii ambayo mmeiomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja hii. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie mawazo kidogo katika rasimu hii ya mpango 2021/2022 – 2025/2026, hasa katika suala zima la kilimo.

Mheshimiwa Spika, wananchi wetu wanategemea sana kilimo, lakini hata makusanyo ya serikali kupitia viwanda vyetu ambavyo vinatoa kodi kubwa ambayo tunategemea kwenda kukusanya mazao, kwa maana ya malighafi itategemea kilimo.

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali kuhusu suala la mbegu ambalo limekuwa nichangamoto kubwa na ni kubwa kweli kweli. Sisi Mkoa wa Singida ni wakulima wazuri wa alizeti, lakini mbegu nzuri ili mwananchi avune na apate kile ambacho anategemea, kulingana na mwaka mzuri wa mvua nzuri inauzwa Shilingi 35,000 kwa kilo moja. Lakini akishavuna gunia zima anauza Shilingi 60,000 na si Zaidi ya Shilingi 70,000. Maana yake ni kwamba, ataweza kununua kilo mbili kwa kuuza gunia moja ili aje alime.

Mheshimiwa Spika, Serikali iliangalie hili kwa macho mawili . Unapomuuzia mkulima mbegu kwa bei kubwa hauchechemui uchumi hasa kilimo. Sasa, ni namna gani mpango huu utaenda kuangalia, kwa hii miaka iliyobaki, kuona sasa Serikali inaweka mkono wake kwa maana ya ruzuku katika mbegu ili wananchi wanunue mbegu kwa bei nafuu, uzalishaji uwe wa kutosha na mazao yawe bora?

Mheshimiwa Spika, kuchechemua uchumi ni pamoja na miundombinu. Barabara zetu za vijijini, barabara zinazounganisha mkoa na mkoa bado kunachangamoto kubwa kabisa tunapoenda katika mpango huu wa miaka hii ya kumalizia mpango huu ambao umebaki.

Mheshimiwa Spika, sisi wa Mkoa wa Singida ni miongoni wa watu wanaosononeka kwa kutounganishwa na mikoa mingine. Ni kweli tumeunganishwa na Mikoa ya Dodoma na Tabora lakini hatujaunganishwa na Mikoa ta Mbeya na Simiyu mpaka hivi tunavyoongea. Tumeshamaliza daraja ambalo ndilo lilikuwa kikwazo, Daraja la Sibiti, na leo limemalizika, lakini hatua mipango ambayo Serikali inaenda kuchechemua uchumi kwa wananchi hawa ambao ni wazalishaji wakubwa. Hebu tuje sasa na plan ambayo barabara hizi; barabara ya Mkiwa kwenda Makongorosi ambapo barabara kubwa iliyobaki ina kilomita 412 kutoka Mkiwa mpaka ilipoishia kandarasi inapoendelea sasa. Sasa, hawa wananchi unategemea nao washindane na wenzao? Hawawezi kwa sababu mahali pa kutembea masaa matatu unatembea masaa kumi na tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali ije na mpango mahsusi. Tunapokwenda kwenda na standard gauge, tunapokwenda kutengeneza Bwawa la Nyerere. Tuna vijana wasomi wanaotolewa na vyuo vikuu vyetu, sasa wanakwendaje kuingia katika ajira hasa hii ambayo tunaitegemea wakajiajiri. Kilimo ukishalima, ukishavuna unaingia barabarani unatembea masaa mengi barabarani ili ufikishe mazao hayo sokoni.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali yangu hii sikivu chini ya Mheshimiwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha dhamira njema kabisa kwa maneno yake na sisi Watanzania tuko nyuma yake tunaamini si miongoni wa wale watakaotia ulimi puani, kufata nyayo za aliyekuwa Rais wetu, Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa haya ambayo aliyaanzisha hasa suala zima la miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba sasa mawaziri ambao wako humu wamsaidie Mheshimiwa Rais kuona zile changamoto kubwa ambazo ndio kero ya wananchi zinatatuliwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote na changamoto lakini na pongezi zipo, Serikali hii imejenga miundombinu mizuri sana hasa katika vituo vya afya, katika huduma zote za afya na elimu. Bado suala hili tu, kidogo maji, lakini na miundombinu ya barabara zinazounganisha mikoa na mikoa. pia barabara zetu za vijijini ni za kutolea macho mawili. Kama Waheshimiwa Wabunge wengi walivyoshauri namna ya kuiongezea TARURA pesa; ni namna gani tuongeze na ni wapi muangalie ambako hakuna shida, wengine wameshauri kwenye mafuta. Busara itumike na TARURA waongezewe pesa ili barabara nyingi za vijijini ziweze kufanya kazi vizuri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Massare.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, nimeona ni vema nami nikachangia mchango wangu mdogo katika Wizara hii ambayo inasimamia utamaduni wetu, sanaa na michezo.

Mheshimiwa Spika, napenda kuipongeza Wizara hii kwa kazi nzuri inayofanywa na Waheshimiwa Mawaziri wakiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe na Naibu wake, Mheshimiwa Juliana Shoza, Katibu Mkuu na uongozi mzima wa Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, pamoja na sifa hizi nzuri kwa Wizara hii bado kuna changamoto ya usikivu wa TBC Taifa, hususani katika Jimbo langu la Itigi na hasa katika Mji wa Itigi. Itigi kuna redio ya Kanisa Katoliki (Redio Mwangaza) ambao wamefunga mtambo wao ambapo umezuia kabisa matangazo ya TBC Taifa. Je, ni lini sasa TBC itasikika Itigi?

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na majibu ya Serikali mara kwa mara kuwa katika bajeti ya nyuma yaani miaka iliyopita kuwa Serikali itafunga mtambo Itigi ili kuifanya TBC Taifa isikike. Naomba sasa katika bajeti hii Serikali kwa maana ya Wizara hii sasa ifunge mtambo Itigi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia 100.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Mimi ni muhanga wa barabara, ninyi ni mashahidi, nikisimama hapa ni kulalamika. Pamoja na kuanza hivi vibaya, lakini nataka niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa utendaji mzuri sana wa kazi ambazo zinaonekana na wananchi wanaziona. Miundombinu inayojengwa na Serikali iko bora na kwa kiwango kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze sana Engineer Chamuriho kwa kupata nafasi hii ya Uwaziri katika Wizara hii. Hata hivyo, nataka nimtahadharishe kwamba amekalia kaa ambalo kidogo lina moto mkali, akifanya vizuri kama Wizara ya Maji inawezekana mwakani bajeti yake nayo ikawa nafuu. Watu wa maji wewe ni shahidi umekuwepo hapa toka 2015, bajeti ya maji, ilikuwa ni miongoni mwa bajeti ngumu kupitisha ukikaa kwenye hicho kiti. Leo bajeti iliyopita ya maji imejipambanua na watu wa nishati wamefanya kazi ambazo zinaonekana. Niombe sana Mawaziri hawa walioko hapa Mheshimiwa Chamuriho na Manaibu Waziri wawili, waone mifano ya Wizara nyingine, walisimama katika kuhakikisha kazi zinafanyika na zinafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kwangu ambayo nataka niizungumzie ni Barabara ya Mkiwa – Itigi - Noranga inaenda mpaka Mitundu hadi Rungwa. Upande wa Singida ziko kilomita 219, lakini ukiiunga barabara hii kwenda Makongorosi ambako ndio mkandarasi anaishia kuna kilomita 412 kama si 413, ndio barabara pekee iliyobaki nchi hii ya kuunganisha mkoa na mkoa ambayo ni ndefu kuliko zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi barabara hii imefumbiwa macho. Barabara hii mwaka 2017 ilitangazwa na ikapata mkandarasi na mkandarasi alishafika site akataka kuanza ujenzi. Bahati nzuri…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Massare kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hussein Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba si barabara hiyo tu katika nchi hii, hata Mkoa wa Geita, Mwanza na Shinyanga kupitia Wilaya ya Nyangh’wale hakuna lami kabisa. (Makofi)

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa yake, lakini kilomita nyingi…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Yahaya Massare unaipokea taarifa hiyo?

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa yake, lakini kilomita nyingi za barabara za kuunganisha mkoa mmoja na mkoa mwingine ziko katika barabara hii. Barabara hii kutoka Mbeya kwenda Arusha kama mtu anasafiri kama ingekuwa lami huwezi kupita Dodoma ni barabara fupi na ambayo kiuchumi itainua uchumi wa nchi hii. Barabara hii ilipotangazwa mwaka 2017 na ikapata mkandarasi, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alikuja pale akagundua kwamba, katika mchakato ule wa zabuni kulikuwa na upigaji, akazuia barabara hii isiendelee kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hayati Magufuli akataka wakae wazungumze TANROADS na mkandarasi kilomita ziongezeke kwa pesa ile au pesa zipunguzwe kwa kilomita zilizopo. Mwisho walishindana sijui walifikia wapi, inawezekana watu walishachukua chao hakukuwa na namna, ile tender ikafutwa. Mwaka 2020 Mheshimiwa Rais alipokuja kuomba kura pale kwa niaba ya chama chetu na kuniombea kura mimi na Wabunge wa Mkoa wa Singida, Itigi alizungumzia barabara hii kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami lakini ataweka wakandarasi wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunavyozungumza hapa imeonyeshwa ukurasa wa 36, lakini ukurasa wa 171 katika hotuba ya kitabu cha Waziri, lakini kilomita zinazoenda kujengwa inaonekana ni zile 56.9, lakini kwenye kutangazwa nina mashaka zinaweza zikatangazwa chini ya hapo. Niwaombe sana Wizara hii ili na sisi tusije kuwa wapiga kelele na kushika shilingi ya mshahara wa Mheshimiwa Waziri, atoe nafasi ya kutangaza kilomita za kutosha. Barabara ina kilomita 412 kutoka Makongorosi, akitangaza kilomita 20 au 25 ni miaka mingapi atajenga barabara hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana katika vitu ambavyo Waziri azingatie, Mtendaji Mkuu wa TANROADS yuko hapa, anaijua ile barabara, aone namna ya kufanya barabara ya Makongorosi kuja Mkiwa kuunga Mkoa wa Singida na Mkoa wa Mbeya, inawekewa lami. Angalau kilomita zitoshetoshe hamsini hizi na zingine hamsini hata zikianzia kule kufika Rungwa itaonyesha kwamba Wizara ina dhamira njema ya kutenda haki. Wananchi wa mikoa mingine wasije wakasononeka kwamba wengine wanapendelewa na wengine hawapendelewi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapopiga kura tunapigia kura Wabunge wa CCM, mimi nimetumwa hapa, lakini walituma Wabunge wengi kama mimi kwenye Bunge hili na waliondolewa na sababu kubwa walinyimwa kura kwa sababu ya barabara hii. Naomba sasa Mheshimiwa Chamuriho alinde kura zangu za mwaka 2025. Kama asipojenga barabara hii maana yake sasa yeye ndio atakuwa sababu ya mimi kutoka katika Bunge hili na sitokubali katika bajeti ijayo, hii nitakuwa mpole kidogo, nitashika shilingi tu kidogo, lakini ijayo sijui kama tutapita na bajeti ya Waziri hapa, naamini ataendelea kuwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sasa Mheshimiwa Waziri ukaangalie barabara hii lakini kuna barabara ambazo zinaanzia Handeni, Kibalashi, Kiteto, Chemba, Kwamtoro hadi Singida. Barabara hii ambayo inaambatana na lile bomba la mafuta nayo ni barabara muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni barabara ambayo itakuja kuchechemea uchumi kwa sababu ya mahusiano yatakayokuwepo baina ya mikoa hii mitatu. Mkoa wa Singida, Mkoa wa Dodoma na Manyara lakini na Mkoa wa Tanga mikoa minne ambayo inapitiwa na hili bomba la mafuta. Na ile mikoa ya kule Geita, Shinyanga na Mwanza kule ambayo ukijumlisha inakuwa mikoa kama nane au tisa ambayo uchumi wa Nchi hii utaenda kuongezeka na hata makusanyo ya kodi yatapatikana lakini kama barabara ni mbaya mtu badala ya kulipa kodi kubwa atalipa kidogo kwasababu anachelewa kufika mahali ambako anatakiwa afike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja ambalo nitalichangia haraka haraka la ving’amuzi vya mabasi. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nitangulie kwa kuunga mkono hoja hii ya Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, bila kumsahau Katibu Mkuu wa Wizara hii, Mheshimiwa Dkt. Zainab Chaula kwa kazi nzuri wanayoifanya katika nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizi, naomba kukukumbushia ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alipokuja Itigi katika Hospitali ya Rufaa ya St.Gaspar katika Siku ya Wauguzi 2017 na kuahidi kutoa gari kwa Kituo cha Afya Mitundu ambacho kipo zaidi ya kilometa 100 toka Hospitali yetu ya Wilaya ya Manyoni. Nia yangu ni kukukumbusha tu ahadi hii aliyoitoa kwa wananchi wa Halmashauri ya Itigi, Jimbo la Manyoni Magharibi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie kuunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada huu wa Tamko la Makao Makuu ya Nchi kuhamia Dodoma rasmi lakini upitishwe na Bunge lako hili Tukufu siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitangulie kwa kuunga mkono hoja hii ya Serikali yenye dhamira njema kabisa ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma, lakini wananchi wote wa Tanzania Mikoa yote 26 na mingine mitano ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni zuri tena zuri sana toka ilivyotamkwa mwaka 1973 ilifuatia utekelezaji wa Serikali kuhamia Dodoma. Waziri Mkuu wa pili wa Tazania Mheshimiwa Rashid Mfaume Kawawa alihamia Dodoma miaka ile ya 1975/1976 na hata Waziri Mkuu aliyemfuatia Edward Sokoine alifanya kazi Dodoma na Dar es Salaam. Salim Mohamed Salim alifanya kazi Dodoma na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuletwa Muswada huu leo miaka mingi baadaye ni tija kubwa kabisa kwa Serikali ya CCM ambaye sasa inaongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa dhamira njema kabisa yakuifanya nchi hii sasa pia tupunguze msongamano mkubwa ulioko katika Jiji kubwa la Tanzania hii Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira hii na sifa kubwa za mji wa Dodoma kwamba upo katikati, lakini mimi ni Mbunge ninaye toka katika Mkoa wa Singida Mkoa ambao ni jirani na Mkoa huu wa Dodoma jirani na Makao Makuu ya Nchi lakini Singida ilikuwa sehemu ya Dodoma kipindi cha nyuma. Hivyo, dhamira hii inapaswa kuungwa mkono na wananchi wa mikoa jirani ukiwemo mkoa wangu ambao nawakilisha wananchi wa Manyoni Magharibi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faraja ya mji huu wa Dodoma kuwa Jiji, kuwa Makao Makuu ya Nchi kutapelekea sasa mji huu ambao ni miongoni mwa miji michache kabisa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao umejengwa kwa mpangilio mzuri. Ilipotangazwa mwaka 1973 ilifuatia kuundwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu. Mamlaka hii ilifanya kazi nzuri sana ambayo iliupanga mji huu na leo ni miongoni mwa mji ambao ukiwa angani unaouona kweli mji huu unastahili kuwa Makao Makuu ya Nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto ambazo zipo nakubaliana kabisa kwamba sasa ni wakati muafaka wa Serikali kuhamia Dodoma na kufanya kazi kama inavyofanya sasa. Itarahisisha mikoa ya pembezoni kufika Dodoma kwenda kuona Viongozi wa Serikali. Hapa tunapozungumza Waziri Mkuu yupo Dodoma, Bunge lako Tukufu liko Dodoma, lakini Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo Dodoma, Wizara zote, Mawaziri wako Dodoma.

Mheshimiwa Spika, ni jambo la kujivunia lakini katika kutekeleza Ilani ambayo tuliwauzia wananchi na wakaamini kuchagua chama hiki kwamba kinatekeleza yale ambayo tuliwaambia kwamba tunakwenda kutekeleza Ilani yetu kwa kufanya haya yafuatayo likiwemo hili la kuifanya Dodoma sasa iwe Makao Makuu ya Nchi. Hivi juzi juzi tu Mheshimiwa Rais alisaidia sana Mji huu wa Dodoma ulipotangazwa kuwa Jiji kwa hiyo umeendelea kuboreshwa na utaendelea kuboreshwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona jinsi Serikali inavyochukua juhudi za kujenga barabara za pembezoni lakini Mji wa Dodoma sasa unaboreshwa. Niombe sasa labda Serikali iangalie suala zima la Miundombinu ya maji kuwahakikishia bwawa lile la Farkwa nalo linawekewa mkazo ili baada ya population kuongezeka basi Dodoma kusijekuwa na tatizo la miundombinu hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na machache haya ya kuchangia katika jambo hili la kufanya Mji huu wa Dodoma kuwa Makao ya nchi na naunga mkono hoja hii ya Serikali kuleta Muswada huu mwaka huu wa 2018 tarehe 04 Septemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii nichangie katika bajeti hii kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassana aliyepokea kijiti kwa Dkt. John Pombe Magufuli, Hayati mpendwa wetu ambaye alitutoka pasipo sisi kutaka lakini kazi ya Mungu huwa haina makosa mara zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa sana, sana kabisa mama yetu ambaye juzi tu ameonesha namna gani wanawake kuwa ni tea bags ambazo lakini bila maji ya moto haziwezi kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa jinsi ilivyotufanyia vizuri katika Majimbo yetu. Jimbo langu ambalo nimekuwa mwakilishi kwa vipindi viwili, limefanyiwa mambo mengi sana na Seriakli yake chini ya Dkt. John Pombe Magufuli lakini sasa mama Samia Suluhu Hassan ameenda kuongezea kutuletea shilingi 500,000,000 kwa ajii ya kuboresha miundombinu iliyokuwa imechakaa katika barabara zetu za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye ni kiranja wa Serikali na kiongozi wa Serikali katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano kwa jinsi alivyopokea mawazo ya Wabunge hususan katika kilimo cha alizeti na hivi juzi tu alikuwa Singida akizungumza na wadau mbalimbali juu ya kilimo cha alizeti ili kuondoa pungufu hili la mafuta ya chakula ambayo tunaagiza kutoka nje kupitia alizeti naamini kwa mikakati ambayo inapangwa sasa inaweza ikasaidia sana mikoa hii mitatu ambayo imewekwa kimkakati kuweza kulima alizeti zenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii haija-reflect sana kwenye kilimo lakini tafiti za mbegi ambazo zinatakiwa ziende zikalimwe katika mikoa hii mitatu ya Simiyu, Singida na Dodoma zinafanyika katika mikoa ambayo ina mvua nyingi. Niombe Wizara ya Kilimo ikiwezekana, tafiti za mbegu za alizeti ambazo zitalimwa katika mikoa hii mitatu zikafanyike katika miongoni mwa mikoa hii mitatu. Mkoa wa SIngida uwe kielelezo kwa sababu ndiyo waanzilishi wa zao hili na mbegu za kulima alizeti zizalishwe katika Mkoa wa Singida ili kuonesha matokeo chanya ya alizeti ambayo yatakuwa bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa katika kilimo hapo hapo, Serikali inatakiwa iongeze nguvu kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji. Tutengeneze mabwawa kukinga mito ambayo inapeleka maji katika mito, maziwa, mito inayopeleka maji katika mabwawa kama hili hapa Suruingai – Bahi na mito mingine ambayo iko katika mikoa hii ya katikati ambayo ni mikoa kame tuweze kupata kilimo cha umwagiliaji scheme nzuri kama iliyopo scheme ya Bahi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Singida nasi tunayo mito hata katika Jimbo langu. Niombe watu wa kilimo waje wafanye tafiti tuone ni eneo gani tunaweza tukaongezea hasa upande wa Jimbo ambalo natoka. Tuna scheme moja tu ya umwagiliaji ambayo ni scheme ya Itagata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mifugo, mikoa hii ambayo inaenda kulima alizeti, mashudu ya alizeti baada ya kukamuliwa ni chakula bora sana kwa mifugo. Wizara ya Mifugo nayo ije na mkakati wa kuhakikisha tunapata malambo ya kunyweshea mifugo yetu hasa katika Jimbo ambalo natoka limekuwa na wafugaji wengi, wengi wametoka kanda ya ziwa kwa sababu sisi tulikuwa tuna nafasi kubwa wamekuja kupata fursa ile ya majani na eneo pana la kuchungia mifugo. Tuna tatizo kubwa la malambo, lakini na majosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hiyo ya Waziri Mkuu, nimpongeze sana Mheshimiwa jenista Mhagama kwa kazi nyingi na nzuri sana ambazo amekuwa akifanya katika Wizara hii ya Sera, Bunge, Vijana na watu wenye Ulemavu. Taasisi zilizo katika Wizara hii, mfano Taasisi ya OSHA ilikuwa ni kero kubwa sana kwa watu wenye viwanda, kulikuwa na tozo nyingi hasa unapoanza ujenzi wa jambo lako lolote OSHA walikuwa ni kikwazo. Leo wamepunguza tozo nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii ya Bunge lako tukufu kuwapongeza OSHA lakini na kumpongeza sana Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kazi nzuri aliyofanya na kufanya sasa zile kero nyingi ambazo zilikuwa zinatokana na Taasisi hizi sasa ziweze kuwa ni changamoto ambazo zimeanza kuisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini taasisi nyingine iko chini ya Wizara hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi ya WCF, miongoni mwa Wabunge ni mashahidi jinsi walivyopata kupata compensation kwa matukio mbalimbali yaliyowapata ni mmojawao ambao nilifidiwa baada ya kupata ajali mbaya ya gari kupitia Taasisi hii ya WCF. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jenista Mhagama na Wizara yake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Naibu mawaziri waliopo katika Wizara hiyo kwa kazi nzuri ambazo tumeendelea kuziona zikionekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu huwezi kuzungumzia jambo lolote bila kuzungumza barabara. Sisi watu wa Mkoa wa Singida tunaunganishwa na Mkoa wa Mbeya kupitia barabara ambayo inapita katika Jimbo langu na ni barabara pekee ambayo imebaki ina urefu mkubwa. Ina kilometa 412. Katika kilometa 412, kilometa 219 ziko ndani ya Jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kwa kuonesha nia ya kujenga kilometa 56.9 japo zimetangazwa kilometa 25 lakini kwa kilometa 25 maana yake itatuchukua zaidi ya miaka 20 kumaliza hizo kilometa 412. Niombe sasa Serikali ichukue juhudi za maksudi kuongeza kipande cha barabara cha kutoka Mkiwa – Rungwe, zile kilometa angalau zifikie kilometa 100 tunazozijenga kipindi hiki ili wananchi hawa nao waunganishwe na mtandao wa barabara, waweze kukimbizana na hali hii ya uchumi, waweze kuwa walipakodi wazuri lakini mazao yao yafike katika masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida pia unaunganishwa na Mkoa wa Simiyu kupitia daraja la Sibiti. Haijaonekana popote katika Bajeti ya Serikali, Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwamba mnaenda kuanzia wapi. Niombe sana Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi, Waziri wa Fedha unatoka Singida, uone watu wa Singida wanavyoweza kuunganishwa na mikoa mingine. Usije kuwa mpishi alilia kwenye… itoshe hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo moja mahsusi ambalo nilikuwa nataka nizungumzie. Hapa katikati kulikuwa na ugaidi mkubwa katika hifadhi zetu na mapori tengefu. Watu wanaomiliki silaha hasa bunduki aina ya rifle walifika mahali ukisalimisha silaha ile unasafiri basi huwezi kuichukua tena lakini ukiuza silaha yako au ukinunua silaha kwa mtu mwingine au mtu aliyekuwa anamiliki silaha akafariki, warithi wake sasa hawapati vibali vya kumiliki silaha. Ni nini tatizo? Mtuambie zimepigwa marufuku? Silaha hazihamishwi? Hasa rifle, zote kuanzia 22 mpaka 458.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali basi ije na matamko ya kuonesha kwamba hwa watu wanaotaka kumiliki silaha kwa njia nzuri wanapata kumiliki silaha. Ahsante sana. Naunga mkono hoja ya Serikali. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii nami nichangie katika hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nami nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Chama change, Chama cha Mapinduzi, hususan Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anafanya hasa sisi Wabunge ambao tunatoka Majimbo ya vijijini. Ametupa heshima kubwa sana, kwa fedha nyingi ambazo zimeelekezwa katika shule zetu, hasa shule chipukizi. Mimi ni miongoni mwa jimbo ambalo ni Halmashauri na limenufaika sana kwa fedha za Mheshimiwa Rais hizi alizoenda kututafutia huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama kiranja wa Serikali. Amefanya kazi iliyotukuka na anakisaidia sana Chama chetu, Chama cha Mapinduzi kutekeleza Ilani yetu ya mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa spika, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, wanashughulika na vijana ambao ndio waathirika wakubwa sana wa ajira za nchi hii. Tunategemea vijana hawa waajiriwe katika Sekta ya Kilimo. Ofisi hii ya Waziri Mkuu imekuwa inashughulika pia na vitalunyumba, wakitoa mafunzo kwa vijana ili waweze kujiajiri katika kilimo hiki cha umwagiliaji wa njia ya matone kupitia vitalunyumba.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo ambalo naomba niishauri Serikali kupitia Ofisi hii ya Waziri Mkuu. Vitalunyumba hivi vinauzwa ghali sana. Vifaa peke yake inafikia takribani shilingi milioni 14 kujenga kitalunyumba ambacho ni cha kawaida. Kwa wananchi wetu masikini na hasa wa vijijini ambao wamekosa ajira; na vijana hawa wamepata elimu lakini ajira hakuna, wana nia ya kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, naishauri Ofisi ya Waziri Mkuu itenge fedha kiasi kuweka ruzuku katika vitalunyumba ili vishuke bei na wananchi, wale vijana wanaopata mafunzo; ambapo wanatoa mafunzo kwa vijana 100 kwa kitalu nyumba kimoja ambacho kinajengwa katika Halmashauri moja. Sasa kitalunyumba kimoja kinaweza kuendeshwa na vijana watatu mpaka watano. Sasa wale vijana wanaobaki 97 wanakuwa wamepata elimu, lakini hakuna cha kufanya. Naishauri Serikali iweke ruzuku katika vitalunyumba, kwani itaongeza wigo wa ajira katika sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, tumeona juzi Mheshimiwa Rais akitoa vitendea kazi zikiwemo pikipiki kwa Maafisa Ugani wetu, lakini tunashuhudia kuona nia ya kuongeza bajeti ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, tunapokwenda kuongeza bajeti ya kilimo, tuhakikishe basi kunakuwepo na matrekta na pembejeo nyingine zikiwemo power tiller, plau za kukokotwa na ng’ombe, lakini mbolea. Serikali inatumia fursa hii kuweka ruzuku. Juzi tumeona baadhi ya Wabunge wakichangia na kulalamika, matrekta yaliyoletwa yanakatika kwa sababu hayana ubora. Huko nyuma Serikali yetu ilikuwa na sera mbalimbali za kilimo ikiwemo siasa ni kilimo, hapa tulimsikia Mheshimiwa hapa mwandishi wa vitabu Shigongo akisema. Pia kulikuwa na kilimo cha kufa na kupona na mwisho hapa juzi juzi tulikuwa na kilimo kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule nyuma tulikuwa na matrekta bora sana. Yalikuwepo matrekta ya Ford, Massey Ferguson, John Deere lakini kuanzia kilimo kwanza tumeanza kuleta matrekta ya ajabu. Kulikuwa na matrekta ya Farm Truck mtu anakopeshwa trekta kabla hajalipa deni, trekta limeshaharibika na ndio maana umeona taasisi ile ambayo ilikuwa inakopesha matrekta SUMA JKT walipotea hapa. Kwa sababu, hasara ile ilikuwa huwezi kuikamata, trekta imeshakuwa scraper na mtu bado ana deni. Baadhi ya vijiji vingi na wakulima wengi waliathirika, lakini hii Ursus ambayo imeletwa miaka hii ya karibuni ni ya hatari kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini tusirudi tukaleta matrekta ambayo yanafaa kwa kilimo cha ardhi ya Tanzania? Matrekta ya Ford, Massey Ferguson, John Deere, matrekta imara ambayo mtu alinunua akiwa kijana na mpaka anafikia miaka 60 kama mimi anaweza kulitumia. Leo trekta zinauzwa mpaka shilingi milioni 50, shilingi milioni 60. Kama tunataka kwenda kufanya kilimo kama ilivyo kilimo ni uti wa mgongo basi tuhakikishe Serikali inaweka nguvu kubwa katika kuleta trekta, ambazo ni imara lakini ruzuku ya Serikali iwepo ili ziuzwe kwa bei ambayo mwananchi anaona anaweza kununua. Mwananchi mmoja akinunua trekta watakaolima ni zaidi ya familia 10, kwa sababu akishamaliza kulima shamba lake atamkodisha mwingine, akimaliza atamkodisha mwingine. Hii maana yake ni nini? Tunaongeza kilimo katika fursa ambayo tunaitarajia kwamba iajiri wananchi walio wengi katika Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini Serikali kwa ujumla imeifanya Mkoa wa Singida, Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Simiyu kuwa mikoa ya kielelezo, katika kuhakikisha kupunguza deficit hii ya mafutam ambayo tunaagiza mafuta ghafi kule nje ili yaje yachakatwe hapa ili tutengeneze mafuta ambayo hayana cholesterol yanayotokana na mbegu za alizeti. Serikali ilifanya jitihada sana za kusambaza mbegu japo hazikuwa bora. Dhamira yetu ni kuona sasa basi Serikali inaingia katika kusambaza mbegu bora kabisa za Hysun za alizeti ambazo zitakuwa na tija kubwa katika kuzalisha mazao ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kuishauri Serikali iongeze na iendelee katika kilimo cha umwagiliaji. Kilimo ambacho kitatoa ajira na ambacho kina uhakika sana na uvunaji, ukiacha kilimo cha mvua ni kilimo cha umwagiliaji. Tuna namna nyingi ambazo baadhi ya mito inapotea, inakwenda kumwaga maji katika bahari na maziwa, tungeitumia ile kukinga mabwawa ya kutosha ili tuweze kupata kilimo cha umwagiliaji. Pia maji ya chini ya ardhi yakitumika yatatusaidia sana kuongeza kilimo, kama njia mojawapo ya kusaidia kilimo cha nchi hii.

Mheshimiwa Spika, ninalo jambo lingine ambalo naishauri Serikali, irudishe Tume ya Mipango ili ibuni vyanzo vingi vya mapato. Tumezoea kujikita katika vyanzo ambavyo ni vile vile miaka nenda, miaka rudi. Kama tusipoirudisha Tume ya Mipango, isaidie kuchakata namna bora ya vyanzo vipya vya mapato, tutaendelea kubaki hapa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sidhani tunapokwenda tunaongeza shilingi trilioni tatu kwa kila mwaka au shilingi trilioni mbili kutoka 36 kuja 39 bila vyanzo vipya vya mapato, tutaendelea kuikaba sekta ya mafuta ya petroli, ndio chanzo chetu kikubwa cha mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo hili ambalo limeanza mchakato siku nyingi, naiomba sana Serikali yangu, iikubali na imalize mchakato wa kuchakata LNG, gesi yetu ije katika kimiminika iweze kutumika kama mbadala wa mafuta. Magari mengi madogo yaweze kutumia LNG ili tutoke katika utegemezi wa kuagiza mafuta. Tumeshuhudia mafuta yalivyopanda kutokana na vita ya nchi jirani zinazosakamana na kusukumana za Ukraine na Urusi. Leo dunia inahamanika kwa sababu hii. Kama tungekuwa tumeanza kuichakata gesi yetu na ikatumika kama kimiminika, leo baadhi ya magari mengi yangeanza kutumia LNG na tungetokana na tungepunguza kiasi kikubwa cha utegemezi wa mafuta ya petroli katika uendeshaji magari na mitambo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 4) ACT, 2021
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii nichangie kidogo katika Muswada huu wa Sheria Mbalimbali Na. 4 wa Mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi kusimama hapa mbele yako na kuujadili Muswada huu wa Serikali ambao uliletwa mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Spika, mambo mengi yamejadiliwa na wenzangu lakini Mheshimiwa AG amechukua mambo mengi ambayo tulikuwa nayo katika Kamati. Kuna machache ambayo nataka labda kuyatolea tu ufafanuzi kidogo.

Mheshimiwa Spika, Muswada huu ulipokuja ukiwa na Sheria 13 nyingi zilikuwa katika kiwango kizuri na bora sana na hasa katika uandishi wa sheria. Tunaipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu lakini Mwandishi wa Sheria (CPD) amekuwa na weledi wa kutosha sana. Umeona hata wanasheria nguli kama Mheshimiwa Balozi Pindi Chana amejaribu kurekebisha maeneo machache tu ambayo ameyaona.

Mheshimiwa Spika, lakini, Kamati pia ilifanya mengi ambayo tumeona kwamba sasa Serikali imeweka dhamira nzuri na hasa katika suala zima la uwekezaji ambalo nchi yetu inakwenda kushindana na nchi nyingine. Lakini, sheria zile ambazo kidogo zilikuwa zinaleta ukakasi zimeoneshwa na katika sheria hii ambayo ilikuja katika Kamati hii tumeitendea haki na tumebadilisha mambo ambayo yanaleta ukakasi hasa katika ajira za wageni.

Mheshimiwa Spika, nataka tu nilipongeze Bunge lako tukufu kwa kipindi hiki cha miaka michache hapa nyuma tumetunga sheria ambazo ni nzuri sana zinazosababisha wawekezaji kuendelea kushawishika kuwekeza katika nchi yetu. Lakini changamoto hii ya uchache wa watu kuchaguliwa aina kwamba lazima wahakikiwe na taasisi zetu na wakati mtu ambaye ana mitaji yake alikuwa anakuja kuwekeza katika eneo letu ambalo sisi kama nchi lakini kama wawekezaji wa ndani tulikuwa hatuwezi kuwekeza kutokana na wingi wa pesa zile au utaalam.

Sasa Serikali na Kamati ilikubaliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ilimshauri kwamba atoke katika uhiari wa kuleta makaratasi kama ilivyokuwa TIC.

Mheshimiwa Spika, hapa nyuma tumeona TIC jinsi watu walivyosongamana…

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Massare. Twende kwenye maeneo ambayo bado unadani mna tofauti.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, tofauti ipo kidogo tu hapa katika suala la ufifilishaji. Sheria hii ilivyokuja haioneshi ni namna gani sasa mnapokubaliana yule mtu aliyekuwa…

SPIKA: Ibara ya ngapi?

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, Ibara ya 123. Katika Sheria ambayo jana ilikuja kwako Sheria ya NEMC ilikuwa imetaja kwamba…

SPIKA: 123? Nadhani unaongelea 28.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ndiyo, 28 Sheria ya Madini Sura ya 123.

SPIKA: Eeeh! Sasa hii 28 Kamati imeshawasilisha rasmi kwa hiyo tutaipitia wakati wa vifungu.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Basi niipongeze sana ofisi ya AG kwa kuondoa ile Sura ya 422 nayo ilikuwa na ukakasi mkubwa. Basi kwa haya machache naunga mkono hoja za Kamati. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) wa Mwaka 2021
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) ambao uliletwa katika Kamati yetu ya Katiba na Sheria na kwa hakika umechakatwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kukupongeza wewe kwa kupata nafasi hii kubwa katika Bunge letu hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee pia nampongeza sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye aliwasilisha hoja hii ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali katika Kamati. Kwa mara ya kwanza nimeshuhudia Mwanasheria ambaye ni msikivu sana. Kwa bahati, mimi nimekuwa katika Kamati hizi kwa muda mrefu kidogo, lakini Mwanasheria huyu amekuwa ni mtu ambaye ameitendea haki jamii ya Watanzania, kwa sababu marekebisho aliyoyaleta yanakwenda kuondoa ukakasi mwingi katika maeneo mengi ambayo yamerekebishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo ambayo yalikuwa na ukakasi sana na hata Kamati ikajadili sana, lakini wewe mwenyewe ni shahidi na amekuja kusema mbele yako kwamba hili ameliondoa. Hata Mheshimiwa Makamba alipotaka kupata hoja pale, bahati nzuri na wewe ulishaiona, ukamfafanulia mapema kwamba hii imeondolewa. Ni kichaka kibaya sana ambacho kilikuwa kinakuja.

Mheshimiwa Spika, Mwanasheria huyu ambaye sasa kwa kweli nasi tunamkubali kwa asilimia kubwa ni kwa jinsi alivyoweza kuishauri Kamati ilete hapa katika Bunge lako hili Tukufu ili sheria ipite ambayo haina ukakasi na haitakinzana na katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nitajadili kidogo katika sheria hii ambayo imerekebishwa Na. 40, Sehemu ya Nne, kipengele ambacho kinatokana na Finance Bill ambayo tuliipitisha katika Bunge lililopita katika bajeti ambayo tunaendelea nayo, inaleta sababu ya Serikali kuleta mabadiliko haya ili tuweze kukusanya hizi pesa zinazotokana na Sports Betting na ziweze kuwa na mfuko maalum.

Mheshimiwa Spika, nataka tu niwashauri Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba jambo hili ni jema kwa sababu watu wengi na hasa vijana wanashiriki katika michezo hii ya kubahatisha; na michezo hii itakuwa na tija pale ambapo kumekuwa na migogoro mbalimbali katika michezo. Hata timu zetu za Taifa zimekuwa hazina fungu maalum. Kwa hiyo, tukianzia hapa tutapata sababu mojawapo ya timu za Taifa kwenda kuiwakilisha nchi zikiwa angalau na kafungu kazuri kidogo.

Mheshimiwa Spika, napenda pia nichangie kidogo na kutoa ufahamu kwa wenzetu ambao hawakuweza kushiriki katika Kamati yetu katika Bunge hili kuhusu sheria hii ambayo Ibara 49 ambayo inakuja kurekebisha mtu ambaye anatoa mafunzo ya kijeshi na anayepewa mafunzo ya kijeshi, wote wawe na adhabu sawa na wote wawe ni wakosefu mbele ya sheria.

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia ugaidi ukiwepo katika nchi yetu. Tulikuwa tunajiona kisiwa, lakini matokeo yaliyotokea Rufiji, Ikwiriri kule na maeneo mengine na hadi Mtwara; na leo nchini Msumbiji wametokana na upungufu huu wa sheria. Kwa hiyo, Mwanasheria huyu, Mheshimiwa Dkt. Feleshi amekuja kutusaidia sana. Katika marekebisho haya atatibu ugonjwa ambao tulikuwa tunauona ni mdogo na ni ugonjwa mkubwa kweli kweli wa watu kutoa mafunzo ya kijeshi na tukawachukulia tu wale watoaji mafunzo kwamba ndio wakosaji, wale ambao wanapewa mafunzo siyo wakosefu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninafurahi sana kwa nafasi hii ya kuchangia hapa na kutoa ufafanuzi huu mdogo. Nashukuru, ninapongeza sana na ninaunga mkono hoja hii ili nishawishi pia Wabunge wenzangu waweze kukubali kupitisha hoja zilizopitishwa na Kamati kwamba zina maslahi mapana na nchi yetu. Ahsante sana. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 2) Act, 2022
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nami nimshukuru Mungu kwa kuniwezesha leo kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kuchangia katika Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 wa mwaka huu 2022.

Mheshimiwa Spika, mimi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ambao tulichakata Muswada huu kwa weledi mkubwa na niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge kupitia wewe mwenyewe Spika wetu, muweze kuupitisha Muswada huu kwa sababu umezingatia maslahi mapana ya nchi yetu na watu wetu.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia, naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anazozifanya, hasa katika Majimbo yetu huku. Wabunge hawa ni mashahidi wa jinsi Serikali inavyoelekeza pesa kule kwa wananchi wetu ambao wametuleta katika nyumba hii, anatutendea vizuri sana. Naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikupongeze pia wewe mwenyewe kwa jinsi unavyoliendesha Bunge letu hili Tukufu kwa weledi mkubwa sana, na umekuwa ukifanya kazi ambazo kwa hakika unatosha kwa kiwango cha kutosha.

Mheshimiwa Spika, marekebisho haya yamekuja yakiwa katika sehemu tatu kama alivyosema, upande wa biashara haramu ya binadamu. Nianzie hapo tu kwa kifupi. Tumekuwa mashahidi hapo nyuma, watu wetu wanaovuka mipaka ya nchi yetu bila kutumia utaratibu, kuna mawakala ambao wanawavusha. Hao ndiyo waliokusudiwa humu hasa vijana wa kike ambao wanakwenda kufanya kazi ambazo hazina utu katika baadhi ya nchi, hasa nchi za Asia.

Mheshimiwa Spika, watu hawa wamekuwa wakitumia namna nzuri na urafiki wa mipaka yetu ambayo imepakana na nchi nyingi kupitia bahari zetu, maziwa na kuwavusha katika nchi nyingine hatimae wanaondoka kwa njia ambazo siyo sahihi. Ndiyo maana sheria hii inakuja kuweka adhabu kali sana, na hasa wale wanaorudia makosa yale.

Mheshimiwa Spika, wengine wamekuwa wakikamatwa lakini kumekuwa na tabia za kurudiarudia, wanakuwa ni wazoefu. Adhabu zimekuwa kali, kama alivyosema Makamu Mwenyekiti wetu wakati anasoma hapa, ni adhabu kubwa kwelikweli na lengo hasa ni kuhakikisha matukio haya hayatokei.

Mheshimiwa Spika, wewe ulikuwa shahidi, Bunge la Kumi na Moja kulikuwa na malalamiko makubwa sana ya watu wetu wanaopelekwa nchi za Kiarabu kufanya kazi wakidhani wanakwenda kufanya kazi kumbe wameuzwa. Sasa yule aliyenunua anajua amenunua mtu kumbe yule aliyepelekwa anajua amekwenda kufanya kazi. Ule utu wake unapotwezwa anafika mahali anajitupa hadi kwenye maghorofa.

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia watu wetu na hasa mikoa hii ya katikati, Mkoa wa Singida ukiwa kati ya Mikoa iliyoathirika, Mkoa wa Dodoma, kuna mabinti walijirusha huko nchi za Kiarabu, hatuwezi kuzitaja kwa sababu ni marafiki zetu. Lakini sheria hii inakwenda kupunguza kama siyo kutibu kabisa changamoto hii ambayo imekuwepo.

Mheshimiwa Spika, hapahapa tumeona watu wanaotoka nje wanapita hapa kwetu, wanaipa gharama kubwa Serikali yetu kwenye magereza yetu. Wale hawapiti peke yao, kuna watu ambao wanawavusha kutoka mpaka mmoja wa nchi kupitia nchi yetu na kwenda nchi nyingine. Adhabu hizi zitakwenda kuwafanya na kuwatia hofu wale ambao ni mawakala wa hii kazi waweze kuacha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba Bunge lako likubaliane na kupitisha Muswada huu wa Marekebisho haya kwa maslahi mapana sana ya nchi yetu kwa sababu AG ambaye ni mtu msikivu sana kwa kipindi hiki tumefanya naye kazi kwa takribani mwaka mmoja, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana, nasi kama Kamati anatupa ushirikiano mzuri na pale ambapo anaona pana ugumu na Kamati inaona ugumu hasiti kukubali na kuondoa hiyo hoja ambayo alikuja nayo.

Mheshimiwa Spika, katika Sheria ya Dawa za Kulevya, mamlaka imetaka tuingize kemikali bashirifu miongoni mwa vitu hatari. Kemikali bashirifu ni dawa za kawaida ambazo baada ya kushepushwa kwa matumizi ambayo siyo ya kawaida ambayo yalitegemewa kupelekwa katika hospitali zetu, hasa hizi hospitali kubwa ambazo zinafanya operesheni kutumia dawa fulani za kupumbaza na kufanya ili mtu aweze kufanyiwa matibabu mengine, sasa watu huzitumia hizi kuzitengenezea pia dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, ni kitu ambacho ni muhimu sana sisi kama Kamati tumeona madhara yake. Bahati nzuri mimi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ile ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya, kule pia tunakutana na hali hii. Kwa hiyo ilipokuja kwenye Kamati ya Katiba na Sheria kwa kweli tumeshiriki kwa kiasi cha kutosha na kulishawishi Bunge lako Tukufu likubaliane na hii hali.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu nafasi hii ya kukamata na hasa kutoa hati ya ku-search ambayo mamlaka inakwenda kupewa lilikuwa ni gumu na kabla haijatoka ile hati tayari watu walikuwa wanapata taarifa. Kwa sababu mtandao wa hawa watu, kama alivyosema mchangiaji aliyepita ambaye ni Mwenyekiti wetu wa Kamati, ni kwamba wana nguvu sana za kiuchumi na kwa kuwa wana nguvu za kiuchumi wana ushawishi kwa Watumishi wa Umma wakiwemo Polisi na Taasisi nyingine ambao wanaweza kutoa hivi vibali vya upekuzi, inapofika mezani kwake anaweza aka-delay kwa dakika chache tu na taarifa hii ikawa imefika kwa wale ambao wanakusudiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wakipewa mamlaka maana yake sasa suala hili linakwenda kufanyika kwa usiri mkubwa kiasi kwamba tunaweza tukakamata mapapa wengine wengi zaidi kama ilivyotokea hapa nyuma.

Mheshimiwa Spika, niipongeze mamlaka hii, Mkuu wa hiki kitengo alipoteuliwa tu kwa kweli kazi yake ni kubwa sana na ni nzuri. Kuna mapapa hawakuwa wanakamatika lakini sasa wako ndani na kwa kiasi kikubwa sisi kama Wabunge tunashuhudia na wananchi wanashuhudia mitaani wale mateja walikuwa wamezidi kupita kiasi, wamepungua sana. Kwa hiyo, ninaomba niendelee kuwashawishi Wabunge wenzangu kukubaliana na sheria hii.

Mheshimiwa Spika, hata uanzishaji wa mahabusu kwa kweli ni jambo ambalo tunaliona lina tija kubwa, kule mbele litaisaidia sana Serikali, litaisaidia nchi na wananchi kuondokana na hali ya nguvukazi kupotea kwa kiasi kikubwa kupitia dawa za kulevya kwa sababu ya watu wachache ambao wanataka kujinufaisha kupata pesa ambazo ni haramu na hatimaye huingiza pesa hizi katika mzunguko kwa njia halali.

Mheshimiwa Spika, wanaingia katika biashara ambazo watu wanafanya na wanafanya biashara kwa ushindani ambao siyo ili yeye mwezetu ana nia ya kutakatisha pesa zile alizopata kwa dawa za kulevya, sasa mnapofanya biashara unakuta mwenzio anauza rahisi, wewe umenunua ghali, sababu ni hizi.

Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa nafasi hii, ahsante sana. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2022
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya leo, na mimi nichangie kwemye Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ambao uko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, viko vipengele vingi ambavyo tunatakiwa tuvichangie na tuvisemee sisi ambao tuko kwenye Kamati ya Katiba na Sheria. Nianze na sehemu ya tano, na kama muda utakuwepo nitaangalia sehemu nyingine. Sehemu hii ina upande ambao Serikali inaenda kutoa kama kitu kipya hivi. Tulikuwa na leseni za uchenjuaji kwa kampuni kubwa, zile smelter; lakini sasa tunaenda kutoa leseni za uchenjuaji kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo. Ilikuwa ukitaka kuchenjua lazima uwe na leseni ya uchimbaji. Fursa hii itasaidia wawekezaji wa ndani na hasa wananchi ambao mitaji yao ni midogo ambao hawana nguvu ya kununua mashine zile za kuchenjua. Ilikuwa mtu anaweza akaleta pale na akajiegemeza kwa mchimbaji mdogo na akawa anachenjua na kutoza tozo ambzo Serikali pia haipati makusanyo ya maduhuri yake au kodi kwa namna moja au nyingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo marekebisho haya yanakuja kutengeneza na kuongeza ajira kwa watu wetu katika sehemu hii ya uchimbaji. Wachimbaji wadogo hata kwetu Mkoa wa Singida tunao pale Sambalu na maeneo mengine ya Geita kule, wale wanaochenjua ni watu ambao hawalipi kodi kabisa. Kwahiyo, Sheria hii inakwenda kutibu na kuongeza kiwango na wigo wa maduhuri ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, katika sehemu ya tano, Ibara ya 29 inarekebishwa ili kumpa mamlaka Mheshimiwa Waziri kuchukua maeneo ya uchimbaji na maeneo ya utafiti ambayo yamekuwa na mtu kwa muda mrefu. Kwa kawaida sheria iliyopo inamruhusu mtu kupata leseni, lakini wakati akitafiti baada ya muda fulani ana-renew ya kwanza, ana-renew ya pili na renew ya mwisho ni ya tatu. Hivyo, kama lessen ni kubwa (PL) huwa anatumika kama miaka tisa hivi anaendelea kumiliki.

Mheshimiwa Spika, sheria iliyokuwepo ilikuwa inampa fursa mtu yule yule kujibadilisha na kuomba leseni upya kwa sura nyingine. Sasa Serikali inakwenda kuona kama uwezekano wa kuirudisha ile ardhi kwa Msajili wa Hazina, kwa maana Serikali inaweza ikaingia ubia na mtu mwenye nguvu kuliko aliyekuwepo. Maana yake tunaweza kwenda kuongeza migodi mingine mipya kwa marekebisho haya. Migodi iliyopo ni ile ambayo Serikali ilikuwa na hisa kwa maana ya STAMICO au MEREMETA kwa makampuni yake ambayo yalikuwepo, lakini migodi ambayo imeanzishwa upya kabisa ni michache sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunakwenda kutengeneza kitu ambacho ni fursa kwa nchi pengine kuja na uwezeshaji wa kupata ajira kwa watu wetu, makusanyo ya mirabaha na maduhuli ya Serikali kupitia sekta hii ya madini.

Mheshimiwa Spika, jambo hili ambalo linampa mamlaka Waziri kuchukua ardhi hiyo ambayo ni ya utafiti au uchimbaji, tumeitaka Serikali ilete na iweke ushindani, isiwe tu kwamba ikifika mahali imekwisha, basi inabeba, inakunyakua. Lazima iweke ushindani, itangaze tenda. Kama hakuna mtu anaonesha nia, hapo ndiyo Serikali iweze kuchukua na kumpa Msajili wa Hazina. Maana yake tutaendelea kuweka ushindani ulio wazi lakini kuhakikisha kwamba wawekezaji wa mitaji ambao wanakuja kuwekeza katika sekta hii, kuwapa security ya fedha watakazowekeza katika utafiti.

Mheshimiwa Spika, katika sekta hii, sehemu kubwa ni Kamari, utafiti wa madini, hususan madini yenye thamani kama dhahabu. Ndiyo maana hata GST wanaenda kupewa mamlaka ya kutafiti kwa kina zaidi. Utafiti unatumia gharama kubwa, ndiyo maana watu wetu namna ya kuchimba unapoanza wakati mwingine inachukua mitaji mikubwa sana. Mtu anawekeza pesa, inafika mahali sasa mamlaka ya Waziri yanampoka, ndiyo maana tuna tumeiambia Serikali na bahati nzuri Mwanasheria Mkuu huyu ni mtu msikivu sana, na hata Waziri aliyepo, Mheshimiwa Dotto Biteko alipokuja kwenye kamati, wameridhia kwamba lazima wataweka kwanza ushindani kabla ya kuirudisha kwa Msajili wa Hazina ili kulinda wale watakaokuja kwenye sura ya uwekezaji wenye tija na nchi hii na watu wetu.

Mheshimiwa Spika, ibara ya 30 ya sehemu hii ya tano, inampa mamlaka GST kutafiti kwa kina zaidi. Mwanzo alikuwa anafanya mapping na kutambua maeneo yenye mashapo ya dhahabu, lakini hakuwa na mamlaka ya kuchimba; kufanya drilling na kujua kiasi ambacho anaweza akahodhi zile leseni zilizokuwa kwa Msajili wa Hazina, akawa na taarifa ambazo anaweza akaziweka sokoni. Siku moja mwekezaji mwenye dhamira na nia nzuri ya kuwekeza katika eneo hili, akaja kutokana na taarifa za GST, zikamshawishi sasa kuweka mtaji. Ilivyo kwa sasa, anakupa tu taarifa za juu juu, ili wewe ndio uende na mtaji wako ukafanye drilling na exploration ya kina.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa mabadiliko haya, yanaenda kumpa mamlaka GST kufanya kazi ya kitafiti ya kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, ibara ya 34 inazungumzia habari ya local content. kizungumkuti kikubwa katika eneo la uwekezaji, na katika eneo ambalo lina kandarasi kubwa ni hiki kipande cha local content. Wakandarasi au wale wachimbaji wenyewe, makampuni makubwa hatuwezi kuyataja hapa kwa sababu ni watu wetu, makampuni makubwa yanayochimba, huwa wanaunda vikampuni vidogo vidogo miongoni mwao na wanaagiza bidhaa na wanafanya manunuzi wakijifanya ni watu ambao ni Watanzania. Wanawekwa watu boshen, Yahaya Massare anaingizwa pale kwamba ni mbia wa kampuni, kumbe hana chochote, anapewa tu kamshahara.

Mheshimiwa Spika, adhabu kubwa inakuja katika kipande hiki ili kuifanya nchi na watu wetu, wananchi wa Tanzania waweze kunufaika na uwekezaji huu mkubwa ambao unakuja katika marekebisho haya. Kipande hiki nimeona nikisemee na ndiyo maana leo Mwanasheria Mkuu yupo, kaja na sheria hii, nami nakubali na ninaunga mkono. Naomba nishawishi Bunge lako Tukufu, likubali marekebisho haya kwa sababu ya manufaa makubwa sana kwa nchi.

Mheshimiwa Spika, sehemu ndogo ya tatu ambayo nitaitolea maelezo kwa kiasi kidogo ni Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha. Sheria hii ilikuwa imeweka kiwango maalum cha mtaji wa benki. Kulingana na namna uchumi uavyokwenda na mabadiliko ya dunia, unapoweka kiwango kwenye sheria, unamnyima fursa Governor wa Benki Kuu kuamua kutokana na upepo uliopo huko duniani, lakini kutokana na ukwasi na namna ambavyo Taasisi za Fedha zinavyojiendesha kulingana na dunia inavyokwenda, kwa hiyo, marekebisho haya, yanampa mamlaka Governor wa Benki Kuu kupitia kanuni, kuweka kanuni na kwa kipindi fulani, kwamba sasa tutakwenda kuweka benki katika nchi hii, uje na mtaji wa kiasi hiki.

Mheshimiwa Spika, kuna namna nyingi ambazo zina ufafanuzi, sitaki kwenda sana huko.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja hii ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, na nishawishi Bunge lako likubali kupitisha Marekebisho haya kwa nia njema na dhamira njema kabisa ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.