Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mussa Ramadhani Sima (24 total)

MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Malengo ya Dira ya Taifa 2025, inaeleza kwamba ifikapo mwaka 2025 Tanzania itakuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda.
(a) Je, Serikali imeweka mkakati gani wa kuinua wananchi wa tabaka la kati (middle class) kuweza kujitegemea?
(b) Je, ni kampuni ngapi zilizowekeza nchini na Serikali ina hisa kiasi gani kwenye kampuni hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkakati Unganishi wa Maendeleo ya Viwanda yaani Integrated Industrial Development Strategy 2020 unahimiza ushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo malighafi zake zinapatikana hapa nchini. Mikakati mingine ni pamoja na mkakati wa pamba mpaka mavazi, mafuta yatokanayo na alizeti lakini ngozi bidhaa pamoja na ngozi yenyewe pamoja na mkakati wa mazao ya jamii ya kunde.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hiyo ni utekelezaji wa mpango elekezi wa miaka 15 wa Dira ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2025 unaolenga kutanzua vikwazo vya uchumi hapa nchini. Mpango wa pili una dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Mpango wa tatu unalenga kuimarisha ubunifu na ushindani wa Kimataifa. Msukumo wa mipango hii ni kuhakikisha kuwa na rasilimali za fursa za nchi zinatumika vizuri katika uchumi wa viwanda vya kati hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Taarifa za Ofisi ya Msajili wa Hazina kuna jumla ya makampuni 61 yaliyowekeza katika sekta mbalimbali za uzalishaji na utoaji wa huduma hapa nchini. Ukitoa makampuni 21 ambayo Serikali inamiliki asilimia 100; lakini makampuni mengine manne Serikali inamiliki hisa asilimia 50, na makampuni meninge manne pia asilimia 50 pamoja na makampuni asilimia 32 yanayomilikiwa asilimia 50.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Kumekuwa na mlundikano wa madeni ya watumishi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuyalipa madeni hayo?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa hakuna madeni tena?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kupokea na kuhakiki madai ya watumishi wa umma yanayohusu mishahara na kuyalipa kwa kadri ya uwezo wake wa kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 Serikali ililipa madai ya malimbikizo ya mshahara ya shilingi 56,293,372,627.37 ambayo yalilipwa kwa watumishi 55,688 waliokuwa na madai yaliyotokana na kupandishwa vyeo, ajira mpya na sababu nyinginezo.
Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Serikali imeendelea kulipa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma ambapo hadi kufikia mwezi Juni, 2016 watumishi 31,032 walilipwa jumla ya shilingi 28,929,095,373.89.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 7,871 yenye jumla ya shilingi 13,754,462,429.29 tayari yamehakikiwa na yameshaingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara na yanasubiri kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya watumishi 8,776 yenye jumla ya shilingi 15,590,586,474.69 yanaendelea kuhakikiwa ili yaweze kuingizwa kwenye mfumo tayari kwa kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika shughuli za kila siku madeni huzalishwa, lakini ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba madeni haya yanalipwa mara yanapojitokeza.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Miradi ya kuboresha huduma ya maji inayofadhiliwa na Benki ya Kiarabu (BADEA), Shirika la Mafuta Ulimwenguni (OFID) na Serikali ya Tanzania katika Kijiji cha Mwankoko na Kisaki katika eneo la Irao inaleta changamoto kubwa.
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kulipa fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo ambapo tayari uthamini ulishafanyika kwa mara ya pili ambapo Mwankoko wanadai shilingi 1,510,427,634 na uthamini ulifanyika tarehe 13 Machi, 2014 na mradi wa Irao shilingi 2,932,001,058/=?
(b) Mradi wa maji wa Irao katika visima vyake vyote viwili vinapoteza uwezo wa kutoa maji kutoka Q250-170 kwa saa na kisima cha pili ni Q150-70 kwa saa. Je, Serikali ina mpango gani juu ya kukabiliana na tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha uhakiki wa fidia kwa eneo la Mwankoko na imetuma kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kulipa fidia ya eneo hilo. Kwa upande wa Irao inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 2.9 zitahitajika kulipia fidia katika eneo hilo. Serikali inaendelea na tathmini ya uhakiki wa gharama za fidia hiyo na uhakiki huo ukikamilika fidia hizo zitalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika kwa mradi wa maji safi Mjini Singida, kumejitokeza tatizo la kushuka kwa viwango vya uzalishaji maji katika visima viwili vya Irao. Kutokana na tatizo hilo, Serikali imechukua hatua za haraka ikiwemo kusafisha visima hivyo, kushusha pampu za visima vyote ili kuongeza kina cha kuchota maji. Baada ya jitihada hizo, imeonekana uwezo wa visima kutoa maji uliongezeka kwa kiasi. Aidha, Serikali imepanga kubadilisha pampu hizo ili kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendelea kuboresha huduma ya maji, Serikali imepanga kufunga pampu kwenye visima vitatu vya akiba vilivyochimbwa awali wakati wa utekelezaji wa mradi mkubwa katika Manispaa ya Singida. Kazi hii itatekelezwa pamoja na shughuli ya ulazaji wa mabomba kutoka kwenye visima hivyo vitatu hadi kwenye tanki dogo la kukusanya maji yanayovutwa na kusukumwa kwenda kwenye matenki makubwa katika eneo la karakana.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Kuna mahitaji makubwa ya umeme katika Jimbo la Singida Mjini hususani katika kata za pembezoni kama vile Kisaki, Mtama, Mtipa, Mwankoko, Uhamaka, Unyambwa, Unyamikombi na Unyianga.
(a) Je, Serikali ina mpango gani kuvipatia umeme vijiji katika mwaka huu wa fedha?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia rasilimali ya nguvu ya upepo iliyopo Singida ili kuongeza nishati ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Kisaki, Mtama pamoja na Mtipa pamoja na Mwankoko zimejumuishwa katika mradi kabambe wa REA III unaoanza mwezi Machi, 2017. Katika kazi hizi, maeneo haya yatapelekewa mradi kupitia desification, grid extension pamoja na renewable utakaoanza mwezi huo nilioutaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji hivyo inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 105, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 126.9, ufungaji wa transfoma 31, pamoja na kuwaunganishia wateja wa awali 1,111. Kazi hii itagharimu shilingi bilioni 8.15.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa muda mrefu wa Serikali ni kutumia vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ikijumuisha upepo uliopo katika eneo la Singida ambapo katika mpango kabambe wa kuendeleza sekta ya umeme wa mwaka 2016, mradi huu umepangwa kuanza kuzalisha megawati 50 za awamu ya kwanza mwaka 2018. Mradi huu unakadiriwa kugharimu dola za Marekani 136 na utatekelezwa katika maeneo ya Kisasida, Ipungi, Mughamo na Unyankhyanya. Kampuni ya Geo Wind pamoja na Acciona wameingia exclusive agreement kwa ajili ya kipindi cha miezi minne ambayo itaishia mwezi Februari mwaka huu kwa ajili ya kujiridhisha kwa wananchi kama watakubaliana na utekelezaji wa mradi huu ili waweze kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni mbalimbali binafsi zimeonesha nia ya kuzalisha umeme kwa kutumia upepo katika Mkoa wa Singida ikiwa ni pamoja na Kampuni ya Wind East-Africa iliyojitokeza kuzalisha umeme wa megawati 50 kwa awamu ya kwanza na baadae kufikisha megawati 100. Mradi huu utatekelezwa katika eneo la Kititimo. Gharama ya mradi huu ni dola za Marekani milioni 264.77.
MHE. MUSSA R. SIMA Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uwanja wa ndege katika eneo lililotengwa katika Kijiji cha Manga kwa msaada wa Benki ya Dunia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipata mkopo kutoka Benki ya Dunia ambapo sehemu ya mkopo huo imetumika kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa viwanja 11 vya ndege vya Iringa, Njombe, Songea, Lindi, Kilwa Msoko, Tanga, Moshi, Lake Manyara, Musoma, kiwanja kipya katika Mkoa wa Simiyu na Singida kwa ajili ya ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja hivyo kwa kiwango cha lami.
Ninapenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kiwanja cha Singida unafanyika katika eneo la kiwanja cha sasa na si katika eneo jipya la Manga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafutaji wa fedha za kazi za ukarabati, upanuzi na ujenzi kutoka vyanzo mbalimbali utaanza baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao kwa sasa upo katika hatua za mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kazi hii ya usanifu ikiendelea, Wizara yangu ilipata maombi ya Mkoa wa Singida ya kutaka wataalam kwenda kufanya tathmini ya awali ya eneo jipya linalopendekezwa katika eneo la Uhamaka karibu na kijiji cha Manga kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo la Uhamaka limependekezwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha Mkoa wa Singida katika mpango kabambe wa uendelezaji wa Manispaa ya Singida kwa mwaka 2015 – 2035. Tathmini ya awali iliyofanywa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mnamo Februari, 2016 kuhusu eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2400 (kilometa sita kwa kilometa nne) imeonesha kuwa eneo pendekezwa linafaa kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia matokeo ya tathmini, hatua zitakazofuata ni utwaaji rasmi wa eneo hilo unaohusisha ulipaji fidia ya mali za wananchi waliomo ndani upimaji wa eneo kwa ajili ya hatimiliki, usanifu wa miundombinu ya kiwanja, utafutaji wa fedha za ujenzi wa kiwanja na hatimaye ujenzi wenyewe.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Singida Mjini ni Mji unaokuwa kwa kasi sana na tumetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji:-
Je, Serikali iko tayari kuleta wawekezaji?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhamasishaji wa uvutiaji wa uwekezaji ni jukumu la msingi la Serikali. Katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2016/2017 –2020/2021 imeelezwa wazi kwamba malengo ya Serikali ni kuongeza kasi ya kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje katika sekta zenye tija kwa Taifa. Hivyo, Wizara yangu imekuwa ikihamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza nchini ikijumuisha Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya kivutio cha msingi
cha uwekezaji ni uwepo wa maeneo ya uwekezaji. Hivyo, Serikali imeendelea kuhamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Mikoa na Wilaya kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji. Kutokana na juhudi hizo, hadi kufikia Aprili, 2017, jumla ya Mikoa 13 imewasilisha taarifa ya utengaji wa maeneo katika mikoa yao. Napenda kuchukua fursa hii kuupongeza Mkoa wa Singida kwa kuitikia wito huo na tayari wametenga hekta 6,595.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na jitihada hizo, katika kipindi cha kuanzia mwaka 1996 hadi Aprili, 2017, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania, imefanikiwa kuandikisha miradi 33 kwa ajili ya Mkoa wa Singida yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 997.879. Kwa muhtasari huo, kazi iliyofanyika katika uhamasishaji uwekezaji Mkoani Singida, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Singida kuwa Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji kuwekeza katika Mkoa wa Singida. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Serikali imekuwa na dhamira ya dhati ya kuboresha maslahi ya Watumishi hususan Walimu kwa kutoa nyaraka mbalimbali ikiwemo Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa tarehe 20/10/2014 unaohusu mishahara na Posho ya Madaraka kwa Viongozi wa elimu (Responsibility Allowance):-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kutekeleza waraka huo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa Posho ya Kufundishia (Teaching Allowance) ili kuleta ufanisi wa kazi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Serikali ilianza kutekeleza Waraka Na. 3 wa mwaka 2014 tangu tarehe 1 Julai, 2016 kuhusu Posho ya Madaraka kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu Kata. Walimu Wakuu wanalipwa sh.200,000/= kila mwezi na Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata wanalipwa sh.250,000/= kila mwezi. Kwa mwezi mmoja, Serikali inatumia takriban shilingi bilioni 5.01 kwa ajili ya kulipa Posho za Madaraka kwa viongozi hao kwa ajili ya kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, posho ya kufundishia ilijumuishwa katika Mshahara wa Walimu ili kuboresha maslahi ya Walimu wanapostaafu. Hata hivyo, Serikali hivi sasa kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora inafanya mapitio ya kazi kwa watumishi wote nchini ili kuboresha maslahi kwa kuzingatia uzito wa kazi.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa vifaa tiba kwenye Hospitali ya Wilaya ya Singida Mjini au kituo cha afya Sokoine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sima, Mbunge kutoka Singida, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanikiwa kununua vifaa tiba vyenye thamani ya Sh.102,939,700.00 kwa kutumia fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Vifaa vilivyonunuliwa ni vitanda vitatu
(a) vya kujifungulia, mitungi mitano (5) ya kuhifadhia gesi, vitanda ishirini (20) vya hospitali na mashine tatu (3) za kutakasia vyombo vya hospitali. Vifaa vingine vilivyonunuliwa ni pamoja na mashine moja (1) ya kutolea dawa ya usingizi (anaestheric machine), kitanda kimoja (1) cha upasuaji (operation table) na mashine ya kutakasia vifaa tiba vyenye ujazo wa lita 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya Sh.160,866.466.01 kwa ajili ya kununua vifaa tiba kwenye kituo cha afya cha Sokoine. Kati ya fedha hizo, Sh.41,451,400 zimeshalipwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD)kwa ajili ya vifaa tiba. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Serikali imekuwa na dhamira ya dhati ya kuboresha maslahi ya Watumishi hususan Walimu kwa kutoa nyaraka mbalimbali ikiwemo Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa tarehe 20/10/2014 unaohusu mishahara na Posho ya Madaraka kwa Viongozi wa elimu (Responsibility Allowance):-
• Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kutekeleza waraka huo?
• Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa Posho ya Kufundishia (Teaching Allowance) ili kuleta ufanisi wa kazi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Serikali ilianza kutekeleza Waraka Na. 3 wa mwaka 2014 tangu tarehe 1 Julai, 2016 kuhusu Posho ya Madaraka kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu Kata. Walimu Wakuu wanalipwa sh.200,000/= kila mwezi na Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata wanalipwa sh.250,000/= kila mwezi. Kwa mwezi mmoja, Serikali inatumia takriban shilingi bilioni 5.01 kwa ajili ya kulipa Posho za Madaraka kwa viongozi hao kwa ajili ya kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, posho ya kufundishia ilijumuishwa katika Mshahara wa Walimu ili kuboresha maslahi ya Walimu wanapostaafu. Hata hivyo, Serikali hivi sasa kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora inafanya mapitio ya kazi kwa watumishi wote nchini ili kuboresha maslahi kwa kuzingatia uzito wa kazi.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Tunatambua kuwa michezo duniani kote imekuwa chanzo cha mapato na kuinua uchumi wa Taifa husika, lakini nchini Tanzania michezo hususan soka imebaki kuwa burudani tu.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuinua Soka la Tanzania?
(b) Je, kuna mahusiano gani kati ya Serikali na TFF
katika kuimarisha soka la Tanzania kuanzia ngazi ya Wilaya?
(c) Je, Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF) linapata fedha za ruzuku kiasi gani toka FIFA na Wadhamini kama TBL na Serengeti Breweries?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuhakikisha kuwa michezo ikiwepo soka inaimarika nchini, imeendelea kuendesha mashindano mbalimbali ya michezo mashuleni kitaifa ikiwepo UMISETA pamoja na UMITASHUMTA ili kuibua vipaji mapema na imeteua shule 56, mbili kwa kila mkoa hadi tatu kwa kila mkoa ili ziwe shule za michezo kwa ajili ya kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo ikiwepo mchezo wa soka.
Aidha, Serikali kupitia Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, imeendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na mafunzo ya muda mrefu kwa wakufunzi wa michezo mbalimbali ukiwepo mchezo wa mpira wa miguu.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, TFF, vyama vya michezo pamoja na mashirikisho mengine ya michezo vimesajiliwa na kufanya kazi chini ya Sheria ya Baraza la Michezo (BMT) Na. 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya mwaka 1971. Aidha, TFF inaendelea na uboreshaji wa viwanja vya soka nchini, mfano ni viwanja vya Kaitaba na Nyamagana mkoani Mwanza. Vilevile TFF inatoa msaada wa kiufundi katika viwanja mbalimbali ili kuhakikisha kwamba viwanja vinakuwa katika ubora unaotakiwa. Wizara yangu inaunga mkono programu mbalimbai za TFF katika kukuza mchezo wa mpira wa miguu wilayani na mikoani zikiwemo programu mpya kabisa za grass root pamoja na programu ya live your goals kwa wanawake ambazo zilizinduliwa Mkoani Kigoma Februari, 2018. BMT nayo inaendelea kusimamia utekelezaji wa Katiba, Kanuni na Sheria zinazosimamia michezo mbalimbali nchini.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mapato ya TFF; kwanza TFF ina udhamini wa miaka minne (2015-2018) kutoka FIFA kwenye programu ya FIFA Forward ambayo hutoa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1.25 kwa mwaka ambapo kati ya hizo dola za Kimarekani 750,000 hutumika kwa ajili miradi ya maendeleo na dola za Kimarekani 500,000 hutumika kwa ajili ya gharama za kuendeshea ofisi, timu za Taifa pamoja na ligi. Fedha hizi za maendeleo hazikuwahi kutolewa na FIFA tangu mwaka 2015, hivyo, TFF wanatarajia kupokea kiasi fedha cha dola za Kimarekani milioni tatu kwa ajili ya kutekeleza miradi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, TFF iliingia mkataba na Kampuni ya Bia ya TBL mwaka 2013-2017 kwa thamani ya Dola za Kimarekani milioni 10 kwa ajili ya Timu ya Taifa ambap kwa sasa mkataba huo umeshamalizika. Hivyo, TFF imeingia mkataba wa ufadhili na Kampuni ya Bia ya Serengeti wa miaka mitatu (2017-2019) wenye thamani ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya timu ya Taifa ya wanaume na shilingi milioni 450 kwa ajili ya ligi kuu ya wanawake nchini.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja sasa ya kuziagiza rasmi Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwezesha Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kutekeleza baadhi ya majukumu yake ili walimu wapate huduma stahiki kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Utumishi wa Walimu ilianzishwa kwa Sheria Na. 25 ya mwaka 2015 ili kuwahudumia walimu wa shule za msingi na sekondari za umma Tanzania Bara. Aidha, Tume ya Walimu ina fungu lake (Fungu 2) linalojitegemea na watumishi wake kupitia wasimamizi wao huripoti moja kwa moja kwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Makao Makuu ya Tume. Hivyo Mamlaka za Serikali za Mitaa hazina bajeti za kuwawezesha uendeshaji wa siku kwa siku wa kazi za TSC zilizoainishwa na sheria kwa kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ziko chini ya mafungu mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Bunge limeiidhinishia Tume ya Utumishi wa Walimu jumla ya shilingi bilioni 12.515; kati ya hizo shilingi bilioni 4.622 ni matumizi mengineyo ili tume ipate vitendea kazi kama magari, samani za ofisi na pia kugharamia vikao vya mashauri ya nidhamu na rufaa. Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu wa Tume, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimewapatia Makatibu Wasaidizi wa Tume katika Wilaya zote nchini Ofisi na baadhi ya vitendea kazi. Serikali itaendelea kuiimarisha Tume ya Utumishi wa Walimu ikiwemo kutatua changamoto za kiutendaji ndani ya wigo wake wa kisheria ili itekeleze majukumu yake vizuri zaidi.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Je, ni vigezo vipi ambavyo Serikali imeviweka juu ya kampuni zinazowekeza kwenye michezo nchini kuruhusiwa Ligi husika kubeba majina ya kampuni hizo kama vile Vodacom Premier League badala ya Tanzania Premier League?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kuongezeka kwa gharama za mfumo wa uendeshaji wa Mpira wa Miguu Duniani, Shirikishao la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limelazimika kutafuta wadhamini au wafadhili wa kusaidia kuendesha shughuli za mpira wa miguu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya makubaliano yanayofikiwa kati ya Shirikisho na Wadhamini ni mdhamini kujitangaza kupitia mchezo wenyewe. Kwa mfano, ligi kuu ya Uingereza wakati ikifadhiliwa na Benki ya Backlays, ligi ilijulikana kwa jina la Backlays English Premier League. Hapa Afrika Mashariki kuna mashindano ya Kagame Cup ambayo mfadhili wake ni Rais wa Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame na yanajulikana kama CECAFA Kagame Cup.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo suala la ligi kuu ya Tanzania kutumia jina la Mdhamini wa ligi hiyo, Kampuni ya Vodacom, linatokana na makubaliano ya kimkataba baina ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania na mdhamini wa ligi hiyo ambayo ni kampuni ya Vodacom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkataba huo, miongoni mwa masuala waliyokubaliana ni pamoja na mdhamini kuwa na haki ya kutumia jina lake (Naming Right) katika uendeshaji wa ligi hiyo.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-

Je, Serikali imeweka mkakati gani wa kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini ili kuacha na kuagiza vifaa hivyo nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba ina jumla ya viwanda 14 ambapo viwanda 12 vinatengeneza dawa za binadamu viwanda viwili dawa za mifugo; na kiwanda kimoja kinatengeneza Vifaa Tiba. Wizara imeendelea kuchukua hatua za makusudi ili kuhakikisha Sekta hiyo inaongeza uwekezaji kwenye Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hiyo inakwenda sambamba na kuongeza ufanisi wa viwanda vilivyopo ili kufikia asilimia 60 ya uwezo wa uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini ifikapo mwaka 2025. Hatua hizo ni pamoja na kuunda Kamati ya Kitaifa inayoshughulikia Sekta ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba (National Pharmaceutical Coordination Committee - NPCC); na kuweka vivutio vya uwekezaji kwa lengo la kuhamasisha wawekezaji wa ndani na Nje ya Nchi ili kuwekeza katika sekta hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ili kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo, Serikali imeondoa VAT kwenye vifungashio vya dawa zinazozalishwa nje na ndani ya nchi; imeshusha kodi ya mapato kwa asilimia 30 ambayo imesaidia kuhamasisha uwekezaji mpya na upanuzi wa viwanda kwa muda wa miaka miwili kwa miradi mipya ya viwanda vya dawa na kuweka upendeleo maalum kwa ununuzi wa dawa zinazozalishwa na viwanda vya ndani kupitia MSD.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeendelea kufuatilia uwekezaji na ambapo sasa hivi kuna viwanda 11 vinavyoendelea na ujenzi wa Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba na ujenzi umefikia katika hatua mbalimbali. Lengo la Serikali ni kuokoa fedha zinazotumika kuagiza dawa na vifaa tiba hivyo kutoka nje ya nchi kwa kuzalisha na kuwezesha upatikanaji wa uhakika wa dawa hizo nchini na hivyo kuendelea kutengeneza ajira hapa nchini. Aidha, lengo hilo linakusudia kuhakikisha afya za Watanzania zinakuwa ni suala la kipaumbele wakati wowote.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanya Lugha ya Kiswahili kuwa bidhaa ya kimataifa ili kuendeleza na kukuza utamaduni wetu Duniani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuwa, Serikali imeanzisha mipango kadhaa ya kimkakati ya kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa ya Kimataifa. Tayari kanzidata ya wataalam wa Kiswahili imeanzishwa na wataalam 1318 wamesajaliwa. Pamoja na hayo, Serikali imenunua vifaa vya kisasa vya mafunzo ya ukalimani kwa vitendo na matumizi ya TEHAMA katika ukuzaji wa Kiswahili ambayo yametumia zaidi ya milioni 181.8.

Mheshimiwa Spika, tayari tunao mpango wa kufundisha Kiswahili kwa wageni kupitia balozi zetu nje ya nchi. Vile vile, Serikali imeboresha na kuimarisha mafunzo ya stadi za kufundisha Kiswahili kwa wageni. Pamoja na kutoa machapisho ya Kiswahili rahisi kwa wataalam wetu, na pia kwa lengo la kusaidia nchi zilizoonesha nia ya kuingiza Kiswahili katika mitaala yao ya Elimu mfano Afrika Kusini, Namibia, Rwanda na Uganda.

Mheshimiwa Spika, afua ya hayo, mwaka 2019; wakati wa Mkutano wa 39 wa Wakuu na Viongozi wa Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika-SADC Serikali ilifanikiwa kukifanya Kiswahili kuwa moja ya Lugha nne rasmi zinazotumiwa wakati wa vikao na mikutano ya nchi hizo. Naombwa kuwasilisha.
MHE. FRANCIS I. MTINGA K.n.y. MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha kilimo cha mkataba kwa njia ya outgrower scheme ili kupanua wigo wa upatikanaji wa soko kwa wakulima wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha mkataba kinawezesha wakulima kuwa na soko la uhakika na wanunuzi kununua kuwa na mazao yenye ubora kulingana na mahitaji. Aidha, kilimo cha mkataba kinachangia kutatua changamoto za upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kuimarisha upatikanaji wa mitaji kutokana na makubaliano baina ya mkulima, taasisi za fedha na wanunuzi wa mazao husika kulingana na mahitaji ya soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 kilimo cha alizeti kitakuwa cha mkataba na mpaka sasa Wizara imewasiliana na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji ili kusimamia kilimo cha mkataba. Kilimo cha mkataba kimeleta matokeo mazuri katika zao la ngano katika Mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha.

Aidha, tayari Serikali imekutana na makampuni ya Pyxus Tanzania Agriculture Limited, Mount Meru, Mwenge Sunflowers na makampuni mengine yanayozalisha mazao ya alizeti kama Jackma CO. Ltd. yamefanya vizuri katika mikoa ya Manyara katika kilimo cha mkataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutumia kilimo cha mkataba Wizara kwa kushirikiana na Sekta binafsi inaendelea kuhamasisha wakulima kushiriki katika kilimo cha mkataba ambacho kimeonesha mwelekeo mpya katika kuhakikisha masoko ya uhakika, bei nzuri na viwango bora vya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatekeleza haya kwa kuzingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 na maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa sekta ya kilimo ijitegemee.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kulifanya somo la kilimo kuwa la lazima kuanzia ngazi ya elimu msingi mpaka chuo kikuu kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu na mchango mkubwa wa Kilimo katika maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, somo la kilimo linafundishwa katika ngazi zote za elimu hapa nchini. Kwa mfano, katika ngazi ya mtaala wa ngazi ya elimu ya msingi maarifa na stadi za kilimo zinafundishwa katika somo la stadi za kazi. Kwa upande wa Sekondari, somo la kilimo ni somo chaguzi na linasomwa na wanafunzi kuanzia kidato cha Kwanza hadi cha Sita.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inahuisha miongozo ya eimu ya kujitegemea kuanzia shule za msingi hadi vyuo vya ualimu. Miongozo hiyo imelenga kuziwezesha shule na vyuo vya ualimu kuanzisha na kusimamia kwa ufanisi miradi ya uzalishaji mali ikiwemo shughuli za kilimo na biashara. Elimu hiyo itamsaidia mwanafunzi kujifunza kwa vitendo stadi mbalimbali za maisha ikiwa ni pamoja na kilimo kwa lengo la kuwajengea misingi imara ya kujitegemea na kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa Wizara kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania inafanya mapitio ya mitaala ya ngazi zote za elimu msingi, suala hili litajadiliwa na kufanyiwa maamuzi stahiki. Ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa muongozo kwa Vyama vya Wafanyakazi hasa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na kupunguza ada ya uanachama au kuondoa kabisa mfumo wa asilimia ili kuweka kiwango kitakachokubaliwa na wanachama wenyewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Vyama vya Wafanyakazi kikiwemo Chama cha Walimu Tanzania (CWT) vimeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo ndiyo inayoongoza vyama vya wafanyakazi, vyama vya waajiri na mashirikisho vikiwa na lengo la kusimamia haki na maslahi ya wanachama wake ambao ni wafanyakazi walio katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu 47(c) cha sheria hiyo kimetoa sharti kwamba katiba za vyama lazima zieleze kuhusu ada ya uanachama au njia yoyote ya kuamua ada hiyo. Kwa mantiki hiyo, chama kupitia katiba yake na wanachama ndio wenye mamlaka ya kujadili na kukubaliana masuala ya ada za uanachama katika chama husika na siyo Serikali.

Mheshimiwa Spika, katiba ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kupitia kifungu cha 23.1(c) kimetoa mamlaka kwa Mkutano Mkuu kufanya mabadiliko ya katiba kwa uamuzi wa theluthi mbili za wajumbe walio na haki ya kupiga kura. Hivyo kupitia mkutano huo, wanachama ndiyo walioamua kuhusu njia ya ukataji wa ada kwa asilimia mbili. Hivyo, kwa kutumia chombo hicho hicho wanachama wanaweza kuamua kuweka utaratibu mwingine wa ukataji wa ada husika bila kuvunja sheria. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SHEKIBOKO K.n.y. MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kurasimisha vijana waliopata ujuzi nje ya mfumo rasmi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PATROBAS P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao mkakati kupitia Mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano wa kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo kwa vijana 100,000 ifikapo mwaka 2025/2026. Aidha, katika utekelezaji wake hadi kufikia Juni, 2022 kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi jumla ya vijana wapatao 22,296 (kike 3,349 na kiume 18,947) kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara wamerasimishwa ujuzi ikiwemo Singida zaidi ya watu 1,138.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo fani kumi zinazohusika katika urasimishaji ambazo ni uashi, useremala, ufundi magari (makenika), upishi na uhudumu wa hoteli, baa na migahawa, ufundi bomba, unyooshaji bodi za magari, umeme wa majumbani; ushonaji nguona uchomeleaji vyuma. Aidha, kutokana na manufaa wanayoyapata vijana, katika mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya vijana 18,445 (wa kiume 13,873 na wa kike 4,572) wamejitokeza na kukuziwa uchuzi na kuchukua fomu kwa ajili ya kurasimishwa ujuzi wao kupitia programu hii ambapo taratibu zinakamilishwa ili waweze kupatiwa fursa hiyo. Ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Kiwanja cha Ndege Singida Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanja cha Ndege cha Singida kilifanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mwaka 2017 kupitia mradi wa Transport Sector Support Project (TSSP) kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Kiwanja hiki cha Ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo vya Ndani na Washirika wa Maendeleo ili kuanza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Singida.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya Singida Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa fedha Shilingi Bilioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ambapo itakapokamilika Hospitali inayotumika sasa itabaki kuwa Hospitali ya Manispaa.

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali mpya katika Manispaa ya Singida, ambapo fedha hiyo sasa itatumika kukarabati majengo katika Hospitali ya Mkoa ya sasa ambayo itabadilishwa hadhi kuwa Hospitali ya Manispaa ya Singida. Ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA K.n.y. MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya mchepuko kutoka Kisaki – Unyamikumbi - Unyambwa hadi Mtipa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imekamilisha Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa kina wa barabara ya mchepuko katika Mji wa Singida (Singida Bypass) kutoka Kisaki – Unyamikumbi – Unyambwa hadi Mtipa yenye urefu wa kilometa 46. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha maslahi ya Wathibiti Ubora wa Walimu nchini ili kuinua ubora wa elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza Muundo mpya wa Utumishi wa Maafisa Udhibiti Ubora wa Shule kuanzia Julai, 2023 ambao unatoa maslahi na motisha kwa Maafisa Udhibiti Ubora wa Shule kwa kuwaongezea Mishahara na kuwabadilishia ngazi ya mishahara kutoka TGTS kuwa TGQS. Hii ina maana kuwa kwa sasa mwalimu atakayeteuliwa kuwa Mdhibiti Ubora lazima awe amefikia ngazi ya mshahara ya TGTS G pamoja na sifa nyingine za uteuzi wa viongozi wa elimu kwa kuzingatia mwongozo wa uteuzi. Aidha, maslahi mengine ni kuongeza ukomo wa ngazi ya mshahara toka TGTS I hadi TGQS J yenye maslahi makubwa kuliko awali. Muundo huo umetambua majukumu makubwa ya Wadhibiti Ubora wa Shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi ya Wadhibiti Ubora wa Shule, Serikali imefanikiwa kutoa vifaa mbalimbali vya TEHAMA kwa Wadhibiti Ubora wa Shule Tanzania Bara, ambapo vishikwambi 1,680 vilitolewa kwa Maafisa Udhibiti Ubora wa Shule, photocopia 234, kompyuta za mezani 769, printer 450 na kompyuta mpakato (laptops) 1,002.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imefanikiwa kujenga ofisi tano za Wadhibiti Ubora wa Shule katika Halmashauri za Wilaya ya Njombe, Tarime, Bunda, Ubungo, na Nyasa na hivyo kufanya au kuwezesha halmashauri 181 kuwa na ofisi. Lengo ni kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi, nakushukuru.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE K.n.y. MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-

Je, lini Mradi wa TACTIC utaanza Singida Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Singida ni miongoni mwa Miji 45 ambayo imepewa kipaumbele cha kupata ufadhili wa Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji, Manispaa na Majiji ya Tanzania ambao unaitwa Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness (TACTIC) Project. Ufadhili huu ni wa Serikali Kuu kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia ambapo unaratibiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Mradi huu unatekelezwa katika Miji ya Tanzania kwa awamu tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili ina Miji 15 ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Singida. Serikali inatarajia kutangaza zabuni za kuwatafuta wasanifu (Design Consultants) mwishoni mwa mwezi Mei, 2023 ambapo wasanifu watakapopatikana wataanza kazi ya usanifu mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2023/2024 na ujenzi utaanza mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA K.n.y MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu, madarasa, samani na miundombinu mingine inayochagizwa na utekelezaji wa Sera ya Elimu bila Malipo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua kukabiliana na upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari nchini kwa kuajiri walimu na kuwapanga katika maeneo yenye uhaba, kufanya msawazo wa walimu katika maeneo yasiyo na walimu wa kutosha

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kukabiliana na changamoto ya miundombinu ya elimu inaendelea kujenga shule mpya, madarasa yenye samani ndani yake na kuboresha miundombinu chakavu kupitia bajeti ya Serikali na miradi ya kuboresha elimu kama vile BOOST, SEQUIP, EP4R na GPE LANES II.