Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (53 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nami nitoe shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kunipa fursa hii na kwa wananchi wangu kwa kunirejesha tena Bungeni tena kwa kura za kishindo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya muda, sitaenda kwa kina kati ya yale ambayo nilikuwa nimekusudia kuyasema kufuatana na mpango wa Wizara, lakini pia kufuatana na hoja zilizotolewa na Wabunge. Nitafanya hivyo wakati nitakapokuwa nachangia kwenye mpango tutakapojadili baada ya ajenda hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge, kama mnataka mali mtaipata shambani. Naawaambia Waheshimiwa, vijana wenzangu, wahitimu wa Vyuo pamoja na Watanzania kwa ujumla kama mnataka mali mtaipata shambani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka kumekuwa na wimbi kubwa la vijana kutoka vijijini kwenda mijini. Leo niwaambie, ni wakati wa vijana kutoka mijini kwenda vijijini. Huko ndiko utajiri uliko na huko ndiko mali iliko. Mashambani kuna ufugaji, kuna uvuvi na kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu katika miaka mitano ya Rais aliyepewa dhamana na Watanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kitakuwa ni kipindi cha kuweka mabadiliko katika sekta nzima ya kilimo na kuipa hadhi inayostahili ambayo kila wakati tumekuwa tukisema ndiyo uti wa mgongo na ndiyo inayotoa ajira kwa asilimia kubwa kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wameongelea matatizo mengi. Moja, wameongelea upande wa wafugaji. Nitaenda kwa undani, lakini tunalopanga kama Wizara, tunapanga ni kuondoa utaratibu wa wafugaji kuzunguka na mifugo na hivyo kuleta ugomvi kati ya wafugaji na wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, namna ambavyo tunapanga kwenda kulifanya jambo hili, tunataka kufanya kama ambavyo katika Taifa kuna Ranchi zilizobainishwa miaka na miaka, kuna hifadhi ya mapori yaliyobainishwa miaka na miaka, tunakwenda kubainisha na maeneo ya wafugaji katika maeneo hayo tutakwenda kuweka miundombinu inayostahili ya mahitaji ya huduma za mifugo ili kuondoa tatizo la wafugaji kuzunguka zunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jambo hili tunao uwezo wa kushirikiana hata na wafugaji wenyewe kuweka miundombinu, iwapo tu watakuwa wameambiwa kwamba hili ndilo eneo na wakagawiwa kama vitalu na kuweza kufanya shughuli hizo za kuweka miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua fedha wanazodaiwa bahati mbaya na baadhi ya watumishi ambao sio waaminifu, wakazitoa kwa namna ya rushwa, ni nyingi kuliko fedha ambazo zingeweza kutumika kuendeleza miundombinu na wafugaji wakawa katika eneo salama, la uhakika na ambalo hata lingeweza kutupa takwimu ambazo zingewezesha hata mwekezaji anayetaka kuwekeza kwenye maziwa akajua katika ukanda huu kuna mifugo ya aina hii na inaweza ikatoa maziwa kwa kiwango kile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa ni ngumu sana kwa Mheshimiwa Mwijage kumshawishi mtu kuweka kiwanda cha maziwa kwa watu wanaohama kwa sababu haijulikani kama mpaka wiki ijayo watakuwa katika eneo hilo. Nitaenda kwa undani wake tutakapokuwa tunajadili Mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa pembejeo, Waheshimiwa Wabunge wameongea kwa uchungu sana. Na mimi katika kuzunguka katika kipindi kifupi, nimegundua utoaji wa pembejeo, ruzuku ambayo Serikali imekuwa ikitoa, uwianio wa fedha ambayo imetumika kwa takwimu na faida ambayo imetokana na utoaji wa ruzuku wa aina hiyo, haviendani.
Kwa hiyo, fedha imekuwa ikipotea kwa namna mbili; moja, ni kwa baadhi ya Maafisa pamoja na Mawakala wasio waaminifu kucheza deal. Wanapeleka mbegu, wanapeleka mbolea, wanapeleka mifuko ya kuonesha tu, baada ya hapo wanawapatia wananchi wengine ambao wameshapanda, wanawapatia kama ni 2,000 au 5,000, wanaondoka na mifuko ya mbolea na mifuko ya mbegu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara na Serikali kwa ujumla tunaangalia uwezekano wa kuwa na utaratibu mpya ambao utatoa majawabu ya kudumu ya tatizo hilo la upotevu wa ruzuku inayotelewa na Serikali. Tunaangalia uwezekano wa kuangalia kwenye makato, kwenye vitu vinavyosababisha bei ya mbolea inakuwa ya juu, tuweze kushughulika na bei hiyo na mbolea inayopatika iwe ya bei sawasawa na ya ruzuku na iweze kupatikana kwa wakulima wote badala ya wachache ambao wamekuwa wakilengwa kwa aina hii ya ruzuku. Nitalifafanua kwa kirefu wakati wa Mpango. (Makofi)
Jambo lingine ambalo ambalo Waheshimiwa Wabunge wameliongelea na lilimkera sana Mheshimiwa Rais wakati anazunguka na aliwaahidi Watanzania kwamba litafanyiwa kazi, ni jambo la makato mengi kwenye mazao ya wakulima. Tutalifanyia kazi, na niwaahidi tutakapokuja kujadili Mpango, nitaleta hayo mapendekezo na hatua ambazo Wizara inapanga kuzichukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata wewe nikukumbushe, kama mnataka mali mtaipata shambani. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nina shukrani kubwa mbele za Mungu hasa kujibu hoja leo hii mbele ya Mwalimu wangu aliyenifundisha Kiswahili, baada ya kufika darasa la kwanza nikiwa sijui Kiswahili na leo atashuhudia kwamba mwanafunzi wake alifaulu. Maana yake siku ya kwanza niliporipoti niliambiwa tupa takataka, nikatupa madaftari; tupa madaftari, nikatupa vyote kwenye maua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mafanikio makubwa ya Mwalimu huyu, baada ya kujua Kiswahili, niliweza kupata mke mrembo Kilimanjaro na nikaoa. Imagine, nisingejua Kiswahili ningempata vipi binti huyu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye kujibu hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Katika mazingira ya kawaida, itakuwa vigumu sana kujibu hoja moja moja, lakini vile vile huenda nisiweze kuwataja Wabunge wote kwa majina kufuatana na wingi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hii imechangiwa na Wabunge zaidi ya 92. Kwa ujumla wenu Waheshimiwa Wabunge, tunashukuru sana kwa maoni yenu. Nami niseme, tutawajibu kwa maandishi, tunatambua umuhimu wa hoja zenu, lakini pia siyo tu kuishia kwenye majibu, niwaahidi tu baada ya Bunge nitapita eneo kwa eneo kufuatilia ufumbuzi wa hoja hizi mlizozitoa. Nitafika mpaka Mafia kwa Mheshimiwa Dau, ameongelea suala la wavuvi wake na hili tutalifanyia kazi na hatua hizo tutazichukua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo limeongelewa kwa kiwango kikubwa, linahusu pembejeo na hili limeongelewa na Wabunge wengi. Mambo mengine yanayohusiana na hili limehusishwa upande wa fedha. Niseme tu, tatizo kwenye Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, hasa katika mambo haya ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na Watanzania, siyo fedha peke yake, kuna matatizo ya kiusimamizi, kimfumo na yale yanayohusisha mambo ya fedha. Sisi kama Wizara tumeamua tuhakikishe kwanza tunashughulikia yale ambayo yanahusiana na mfumo, muundo na utaratibu ambao umekuwa ukitumika katika upatikanaji huo wa pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mifumo yote ambayo imekuwa ikutumiwa na Serikali, hakuna ambao haujapata upungufu na mara zote nia ya Serikali imekuwa kuhakikisha kwamba kama inatenga fedha, fedha zile ziwafikie walengwa ili kuweza kutimiza jukumu hilo. Kwa hiyo, sisi kama Wizara, tunavyoliangalia jambo hili tumekuwa tukiangalia utaratibu ambao pembejeo hizo zitaweza kupata mchango ule ambao ni wa ruzuku zinapoingia ili zinapokuwa zimeshaingia ziweze kusambaa zikiwa tayari zina ruzuku na kila mtu aweze kuzipokea.
Kwa hiyo, jambo hili linahusisha Wizara zaidi ya moja, nasi tuna- coordinate na wenzetu ili tuweze kuona namna ambavyo formula hii itaweza kukubalika ya kuweza kuweka ruzuku kwenye source wakati bidhaa hiyo inaingia na punde inapokuwa imeshaingia iweze kuwafikia wakulima wote.
Hiyo ndiyo ilikuwa dhana ya kusema pembejeo; zikiwemo mbolea, mbegu, madawa, yatawafikia wahitaji kama Coca-Cola inavyowafikia matajiri na maskini na kwa wakati, popote pale wanapohitaji kupata bidhaa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa tunachokiangalia ni namna ya kuiweka ile formula kwenye bidhaa inapoingia. Mathalan mbolea inapoingia, iwe imeshakuwa na ruzuku na tunapiga hesabu ambayo itasaidia kwamba bei iwe ile ile ambayo inakuwa sawa na iliyokuwa inatumia vocha, lakini iwe wazi kwa tani zote ambazo zinapatikana. Tuhangaike na namna ya kulinda mbolea yetu isiende katika Mataifa mengine kwa sababu itakuwa ya bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanikisha hili, tunawaza, pamoja na fedha zinazotengwa kwa ajili ya ruzuku, tunawaza makato yaliyokuwa yanaenda kutumika kwenye shughuli nyingine iweze kuelekezwa kwenye Mifuko ya kuendeleza mazao husika ili wakulima waweze kunufaika na fedha wanazokatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa bado kuna mjadala kuhusu makato yale yanayokatwa kwenye ngazi za Halmashauri kwamba ipunguzwe kutoka 5% kwenda 3% kama ambavyo sheria imekuwa ikisema. Tukasema kama haipunguzwi, basi tuikate asilimia nusu iende kwenye Halmashauri na nusu iende kwenye Mfuko wa Kuendeleza Mazao ili wakulima watakapokuwa wamekatwa, watambue kwamba watapata pembejeo katika bei nafuu ambazo zitakuwa zimeshapata fedha kutokana na fedha zile walizokatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni sawasawa na ile ambayo Waheshimiwa Wabunge waliisemea; alisema Mheshimiwa Njalu na Mheshimiwa Doto, kwamba kulikuwepo na utaratibu wa zamani uliokuwa unaitwa pass kwa ajili ya pamba na wakulima walikuwa wananufaika kutokana na fedha walizochangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Ushirika, Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea sana. Kama nilivyosema na yenyewe hii tuko kwenye kuiunda upya. Baada ya kuwa tumepata Tume, sasa tunaangalia uwezekano wa kusuka upya kikosi kwenye Tume ya Ushirika na Muundo wake ambao utasaidia usimamizi uwe makini na uweze kusaidia hawa watu kutimiza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wengine waliokuwa katika ngazi ya Halmashauri na Mikoa. Kimuundo, mapendekezo ya kutaka kuwapeleka katika Tume ya Ushirika; na tunasema kila mmoja ataonesha umuhimu wake wa kuwepo kwenye Tume hiyo kufuatana na majukumu anayoyatekeleza. Wengi wao ambao watakuwa walisahau majukumu yao, tunawapa fursa wahakikishe kwamba kila mmoja anafanya jukumu lake kuhakikisha kwamba anapata sifa ya kuwa katika Tume hiyo ya Ushirika. Hilo litatusaidia katika kuhakikisha Tume hii inatekeleza majukumu yake kama ilivyokuwa imekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wameuliza pia, tunatumia utaratibu gani katika kuhakikisha kwamba tunaondokana na zana duni? Waheshimiwa Wabunge, niseme jambo hili linawezekana na kwa kuwa tayari Sekta Binafsi na Serikali imekuwa na miradi ya aina hii ya usambazaji wa matrekta, hata hivi sasa tayari tumeshapiga hatua, lakini tunapoendelea pia tunapanga kuhakikisha kwamba tunaondokana na kilimo cha jembe la mkono kwa sababu mageuzi ya kilimo yanahitaji utaratibu wa kutumia zana za kisasa katika kulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata vijana hawa niliokuwa nahimiza kwamba tunataka kuwapeleka vijana kwenda kulima, siyo kwamba watakwenda kulima kwa kutumia jembe la mkono. Hakuna kijana atatoka Chuo Kikuu halafu akahamasika kulima ekari tano, kumi kwa kutumia jembe la mkono. Tunapoongelea tunataka kuwapeleka vijana kwenye kilimo, tunasemea kwamba tunakwenda kubadilisha kilimo kiwe cha matrekta.
Waheshimiwa Wabunge, pana jambo moja ambalo kama Taifa bado tunakosea namna ya kuliingilia kwenye suala hili la matrekta. Kwa Watanzania wa kawaida, sio kila Mtanzania lazima awe na trekta lake. Mtu mwenye ekari tano, 10, 50 au 70; mtu mwenye ekari 50 siyo lazima awe na trekta lake. Sisi kama Serikali jambo ambalo tunataka tuhangaike nalo ni upatikanaji wa matrekta pale punde mkulima anapotaka kupata trekta aweze kulimia. Tunafanyaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ya wenzetu ambao wamehama kutoka jembe la mkono kwenda kwenye kilimo cha matrekta, wana centre ambapo matrekta yanapatikana kwa ajili ya kukodisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ilivyo kwa sasa, siyo kila Mtanzania lazima awe na bodaboda yake kwa ajili ya kumwahisha anakotaka kwenda; siyo kila Mtanzania lazima awe na basi lake kwa ajili ya kumpeleka Mkoa hadi Mkoa. Isipokuwa kila wakati anapotaka kupanda basi, anakuta mabasi yapo; kila wakati anapotaka kupanda bodaboda, anakuta bodaboda ipo.
Kwa hiyo, tunataka katika kupiga hesabu katika Mkoa, mathalan Rukwa, ukishajua ekari zinazopaswa kulima ni kiasi kadhaa, tunatakiwa tuwe na matrekta yanayotosha kulima ekari hizo; ikiwezekana kila ngazi ya Tarafa, ili mkulima anapotaka kupata trekta aweze kuyapata. Hiyo ndiyo dhana tunayosema ya kulipeleka jembe la mkono kwenye makumbusho na vijana wa leo, watoto wanaozaliwa hizi siku za karibuni waweze kuliona jembe la mkono makumbusho au wanapokwenda makaburini pindi panapokuwepo na haja ya kuchimba kaburi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tunahangaika nalo ambalo lipo na kwenye bajeti, tunaangalia...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kabla hujaanza hili jambo lingine, naomba ukae kidogo.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kunipa fursa ya kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tunaendelea nalo kwa sasa ambalo tunategemea kulitekeleza ni jambo la maghala na kutakuwa na maghala nane katika Kanda za uzalishaji, lakini pia katika Kanda za Usambazaji ambako itatusaida kurahisisha upatikanaji wa mahindi ama nafaka hizo kufuatana na uhitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, alitoa ushauri Mheshimiwa Serukamba kuhusu kuhusisha pia na Sekta Binafsi katika ununuzi huu wa mahindi. Sisi tunaona hilo ni jambo jema. Ikumbukwe kwamba kwa kutumia NFRA peke yake kununua mahindi, ni kweli NFRA malengo yake ni kuweka mahindi ya akiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea, tumepata uhitaji wa mahindi kutoka nchi nyingize za jirani, mfano DRC walikuwa wanahitaji tani 60,000; South Africa walikuwa wanahitaji tani 30,000; Zambia walikuwa wanahitaji tani 10,000; Zimbabwe tani 10,000; Sudani ya Kusini walikuwa wanahitaji zaidi ya tani 30,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi walipokuja kutuomba ni kipindi ambacho na sisi tayari tulikuwa na mahitaji mengi ya mahindi katika mikoa tofauti tofauti ya njaa, hatukuweza kuwapatia. Kwa hiyo, uwepo wa Sekta Binafsi pamoja na Bodi yetu ya Mazao Mchanganyiko, tunataka ifanye kazi hiyo na tayari nilishaelekeza kwenye Bodi ya Mazao Mchanganyiko waangalie setup ambayo itatuwezesha kuwa na wazo la aina hiyo na Bodi ya Mazao Mchanganyiko waweze kuwa na nafasi yao kwa ajili ya mazao yale ambayo itakuwa kwa namna moja ni soko la wakulima wetu ili kuweza kupanua wigo wa ununuzi wa nafaka kutoka kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwa upande wa wafugaji, Waheshimiwa Wabunge wameongelea sana kuhusu migogoro. Namshukuru Naibu Waziri wa Ardhi kwa niaba ya Wizara ya Ardhi wamelisemea. Sisi kama Wizara, mambo tunayowaza kuhusu wafugaji yako ya aina hii: jambo la kwanza, tunagawa makundi ya ufugaji katika ngazi mbili.
Ngazi ya kwanza tunasemea wale wafugaji ambao wapo kwenye vijiji, wana ng‟ombe wanaotumika kwa kufuga na kwa kulimia na kwa diet kwa ajili ya vyakula vya familia. Tunasema hawa tutashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Ardhi kwa ajili ya kuangalia mpangilio wa matumizi bora ya ardhi ambayo upangaji wake unahusisha Kamati za Ardhi zilizoko katika ngazi za vijiji. Kwa maana hiyo, hili katika kila Kijiji tumesema pawe na Kamati, wajiwekee utaratibu wao kwamba kutoka eneo fulani mpaka eneo fulani itakuwa ni kwa ajili ya mifugo, kutoka eneo fulani mpaka eneo fulani itakuwa ni kwa ajili ya ufugaji.
Ngazi ya pili tunayohangaika nayo, ni ile ya makundi makubwa, wale ambao wana ng‟ombe 1000, 2,000, 3,000 na kuna wengine wamebarikiwa wana hata zaidi ya ng‟ombe 6,000 na wengine 9,000. Kwenye makundi haya, tunasema tutawageuza wenye mifugo ya aina hii kuwa ndio wawekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaopongelea wawekezaji, wawekezaji wa kwanza ambao tutawalenga ni hawa hawa ambao tayari wana mifugo hiyo. Kwa maana hiyo, wale wote ambao walikuwa na ranch wamechukua maeneo, wamesema wanahangaika kutafuta mifugo, tunawaambia wala wasihangaike kutafuta mifugo kwa sababu sisi tayari tuna wafugaji wenye mifugo na wana hobby ya kufuga.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakalofanya, timu tayari inafanyia tathmini ya maeneo ya aina hiyo yaliyokuwa yanakodishwa. Baada ya hapo, tutapiga hesabu ya mifugo iliyopo tena kwa uwiano wa kitaalam, wa kisasa kwamba mifugo mingapi inatakiwa ichunge eneo gani kwa ajili ya ufugaji endelevu (sustainability) ili tuweze kugawa mifugo ya aina hiyo katika maeneo hayo.
Baada ya kuwa tumeshatengeneza utaratibu wa aina hiyo, ndipo tutakapomshirikisha ndugu yangu, pacha wangu Mheshimiwa Mwijage ili kuweza kushawishi watu waweke viwanda kwa ajili ya ufugaji endelevu. Kwa mazingira yalivyo sasa, imekuwa vigumu sana kwa mtu yeyote kumshawishi aweke kiwanda cha maziwa, kwa sababu hajui wale wafugaji pale ndugu zangu na Mheshimiwa Naibu pale, haijulikani kama mpaka wiki ijayo watakuwa bado wako pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ukiweka kiwanda, kesho wakahama, maana yake ni kwamba kiwanda kile hakitaweza kufanya kazi. Hivyo hivyo na kwenye nyama na ngozi. Tukishamaliza kuwaweka kwenye utaratibu ule, maana yake haya mazao yanayotokana na mifugo yataweza kupata soko lake na yataweza kushawishi kuwepo kwa kiwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo na lile alilolisemea Mheshimiwa Serukamba, linalohusu machinjio, kwa sababu elimu ya kuhusu kupanda majani, kupunguza idadi wa mifugo ina uhusiano wa moja kwa moja na unapopunguza ile mifugo unaipeleka wapi? Kama pana soko, sasa hivi wafugaji wanaweka fedha kwa muundo wa mifugo, lakini pakiwa na soko maana yake kama kuna kiwanda, kama kuna machinjio wataweka mifugo in terms of fedha. Kwa hiyo, hilo ndilo ambao tunaliangalia kwa namna hiyo na baada ya Bunge la Bajeti tunategemea kuanza kuzunguka katika maeneo hayo kuhakikisha tunalifanya hilo jambo kwa namna hiyo.
Kwa hiyo Mheshimiwa Doto, Mheshimiwa Mukasa, Mheshimiwa Bashungwa, Bilakwate pamoja na Mheshimiwa Shangazi na wengine ambao mlilisemea Mbunge wa Arumeru Ole-Meiseyeki. Tunafanya kwa utaratibu huo na kabla hatuja maliza Bunge hili tutapata fursa ya kukaa na viongozi wa wafugaji watakuja kwa kanda na kwa Wilaya kwa ajili ya mapendekezo ya namna ambavyo tunafanya. Lakini kwa yale yanayohusisha Wizara zaidi ya moja tutapata fursa ya kukaa na Wizara nyingine, lakini kwa yale yanayohusu kilimo, ufugaji na uvuvi yale yapo ndani ya Wizara yetu na sisi tutafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine linalohusiana na eneo hili kuna malalamiko mengi yanatolewa kuhusu makato mengi kwenye sekta ya maziwa, zamani hatua ziliwahi kuchukuliwa, sasa tutaongea na wenzetu wa fedha na tutawaandikia rasmi, waangalie uwezekano wa zero rating kwenye maziwa na bidhaa zake. Waangalie pia kuondoa kodi kwenye vifungashio vya maziwa kwa sababu hizi sekta bado chaga sana vinginevyo tutaendelea kuona wafugaji wakimwaga maziwa, halafu na tukitumia maziwa yanayotoka katika viwanda vya kutoka nchi jirani.
Kwa hiyo, tutayaangalia hayo na kwa kadri ambavyo tumefuatilia tumeona hata kiwango ambacho kinatoka huko kwa sababu ya uchanga wa sekta wala hakijawa kikubwa kwa kiwango hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirejea tena kwenye jambo moja ambalo liliongelewa na Waheshimiwa Wabunge wengi, nimpongeze Mheshimiwa Kangi Lugola aliliongelea, Mheshimiwa Aeshi, Mheshimiwa Nsanzugwanko ni suala la mbolea. Mbolea ya Minjingu ni kweli kuna kipindi ilikuwa inalalamikiwa, mimi nimepata fursa ya kuongea na wataalam wangu, lakini nikaambiwa kwanza wamebadilisha formula, waliyokuwa wanatumia mwanzoni mchanganuo wake waliokuwa wanatengeneza mwanzoni wameubadilisha, wame-develop kufuatana na uhitaji wa maeneo yetu, kwa sasa ukienda Kenya wanatumia mbolea nyingi zaidi ya Minjingu kuliko mbolea wanayotoa maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hapa kwa sababu ya kampeni hiyo na formula ile iliyokuwepo kumekuwepo na watu kuaminishwa kutokana na watu ambao wamesema bila kuamini kutokana na fomula lakini pia na matokeo yaliyotokea katika mashamba yenyewe. Kwa hiyo, kwa sasa hivi niliwaambia hata wao wataalam wahakikishe wanaelezea watu vitu vya kitafiti wananchi wanatakiwa wavijue. Kwa hiyo, naamini hilo watalifanya lakini pia niliwaambia na wenye kiwanda na wenyewe waelezee kwamba hivi NPK ya Minjingu inatofauti gani kwa formula na NPK ambayo siyo ya Minjingu. Kwa sababu Mwalimu Nyerere aliwahi kusema jambo la kipuuzi likisemwa Kiingereza linaonekana ni zuri, kwa hiyo kuna watu tu inawezekana wanaona Minjingu ni la Kiswahili, wanaona labda mbolea hii ni ya kiswahili-kiswahili.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tumesema wataalam wasemee zile fomula kwa muundo wa fomula NPK ya minjingu na NPK nyingine tunazozileta, urea ya Minjingu na urea kutoka sehemu nyingine kitaalam kwa zile content zenyewe tofauti zake ni nini ili tuweze kujua na watu wetu wayajue hayo, ili wanapotumia watumie wakiwa wanajua lakini wafuatilie na formula zake zilivyokuwa zinatakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine ambayo tuliyasemea Wizara lilikuwa ni jambo la kuwapeleka vijana shambani, jambo hili tumeshaongea na Waziri wa Ardhi na baada ya Bajeti tutakaa pamoja katika kuweka mkakati. Lakini sisi Wizara tunaanzia na mashamba yale ambayo yamebaki kama mapori. Shida moja kijana anayoipata moja ukimwambia tu aende akalime anaweza akashiriki katika lile shamba tu la mzee akalima, akashiriki kama tulivyokuwa tunafanya, Kinyiramba tulikuwa tunaita Nsoza unalimalima pembeni lakini sehemu kubwa unalima ya mzee. Tukisema tunaenda kwenye kilimo cha kisasa kijana atapata shida ya shamba, shida ya mahitaji yale ya kilimo cha kisasa, atapata shida ya matrekta, atapata shida mambo ya umwagiliaji, tunategemea Wizara hizi tukae tuamua tuone namna ya kutatua moja baada ya lingine. Lakini Wizara tumesema tutaanza na mashamba yale yanayomilikiwa na Wizara ambayo yamekaa kama mapori kama ulivyosema lile la Bugagara ambalo lipo kule kwako.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakachofanya kwa sababu mbegu zinahitajika tunatafuta vijana waliopo kule wakae kwenye kikundi wanaotaka kulima mbegu na soko lake la uhakika, mbegu zile zinahitajika. Sasa hivi tunaagiza mbegu kwa zaidi ya asilimia 60 kwa hiyo kwa kuwa zinahitajika tuna uhakika kwa kuuzia mbegu zile, shamba lipo limekuwa pori, sisi ambacho tutasaidia ni namna ya kulima, mbegu ya kulima na namna ya kumwagilia ili tuweze kuhakikisha kwamba vijana wale wanaweza kufanya shughuli hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata la ndugu yangu alilolisemea rafiki yangu Mollel, jambo lile pia linafanyiwa kazi, lile shamba hata hivi tunavyoongea Waziri yupo kule linafanyiwa kazi patakuwepo na sehemu ambayo vijana wako watapata ardhi ya kuendelea kutumia na patakuwepo na sehemu ambayo ushirika utakuwa na sehemu yao katika program yao. Serikali marazote ina nia njema ya kuhakikisha kwamba ina-balance mambo haya ya uchumi ili shughuli za uzalishaji ziweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwa ndugu yangu Mheshimiwa Joseph Kakunda alisemea fedha zile ambazo zilishakusanywa, nimepokea hoja yako nitakaa na wataalam wangu ili tuweze kulimaliza jambo hilo vizuri na liweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwaka pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine walioongelea mazao ya kwetu kutumika, Mheshimiwa Ngonyani alisema kuhusu benki, kupelekwa sehemu kubwa ya uzalishaji ambayo ipo Ruvuma pamoja na wengine walioongelea Benki ya Kilimo. Tumepokea hoja zenu tunazipa uzito na tutahakikisha kwamba tunalifanyia kazi jambo hilo na liweze kuwafikia watu hawa waliopo maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ndassa ameongelea suala la mbegu za pamba, tumekaa juzi juzi nilienda Mwanza nilikaa na watu wetu wa Ukiriguru. Niliongelea suala la pamba kwamba wakati tuna watafiti wachache enzi zile pamba ilikuwa inafanya vizuri na mbegu zilikuwa zinaota, lakini sasa tuna watafiti wengi, tuna watalaam wengi, tunao wasomi wengi, tumesambaza Maafisa Ugani ndicho kipindi ambacho mbegu hazioti, Nikawaambia lazima tuangalie ni wapi ambapo tumefanya makosa, kwa hiyo sasa hivi baada ya bajeti nitakutana na timu ile niliyoiunda ya wataalam kutoka Ukiriguru pamoja na watu wanaofanya kazi hiyo waje watuambie bila kuwa na mtazamo wa kimaslahi binafsi ili tuweze kupata jawabu la kudumu na watu wetu wa Kanda ya Ziwa ambao nembo yao mara nyingi ilikuwa pamba iweze kurejea katika hali yao, hivyo tutafanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata taasisi za utafiti tutaongea ngazi ya Wizara tuone kama na wenyewe wanaweza wakawa na shamba darasa la mbegu ili kuweza kuonyesha tofauti ya wao na wale wengine wanaozalisha kwa maslahi binafsi ambao katika maeneo mengine kwa wale wasio waaminifu mbegu zinazotolewa zinakuwa zilishaathiriwa na maslahi binafsi ikiwemo kuweka mawe ama kuziwekea maji kwa ajili ya kutafuta namna ya kujipatia kipato zaidi.
Mheshimiwa Almas Maige, Mama Sitta pamoja na Wabunge wa Mkoa wa Tabora nimesikia hoja yenu na mimi sina namna tukishamaliza shughuli hizi za Wizara nitakuja Tabora siyo mbali. Nitaunganisha na Wabunge wa Singida ambao wameongelea kuhusu alizeti na mimi ni mdau mkubwa wa alizeti na huko tutatafuta muda tutakuwa tunakimbia kuweza kuona namna ambavyo tunahamasisha shughuli hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni sambamba na yale ambayo yaliongelewa na Mheshimiwa Juma Nkamia ambapo ameongelea kuhusu eneo lake la Jimbo lake pamoja na majimbo jirani ikiwemo kwa mtani wangu Naibu Waziri wa Fedha. Nitakuja huko lakini niwaombe tu msinilazimishe kuwaletea nyama ya punda kwa sababu tulikuwa tunataniwa zamani tu, siku hizi huwa hatuli tunajua punda ni kwa ajili ya kubebea mizigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo lilijitokeza kwa kiwango kikubwa ni majosho pamoja na mabwawa. Mheshimiwa Bobali alisema tunakusudia kutumia Jeshi kwenye uvuvi, ulinukuu vibaya. Tulisema tunapanga kuongea na wenzetu wa Wizara ya Ulinzi kutumia vifaa vya Jeshi kuchimba mabwawa. Kwenye uvuvi hatujaongelea kuhusu kutumia Jeshi, tunachosema ni kwamba, kama tumetenga fedha kidogo ambazo zinaweza kutumika kujaza mafuta, kila Wilaya ina ma-engineer wanaoweza kusema bwawa linatakiwa liweje, kila Wilaya wakajua sehemu ambazo zinaweza zikawa na bwawa na wenzetu wa Jeshi wana vifaa na Wizara ya Maji pia kuna vifaa walivyochukua kutoka Wizara ya Mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini fedha zile tulizotenga zisitumiike tu kwa ajili ya kuweka mafuta, lakini vifaa kwa sababu vipo tutumie vile vifaa vichimbe mabwawa. Babu zetu zamani walikuwa wanachimba mabwawa kwa mikono. Kwa hiyo tunaamini kwamba tunaweza tukaongea, tunaandaa utaratibu wa kuwasiliana Kiserikali lakini nimeshaongea na Mheshimiwa Waziri tuone namna ipi itakuwa rahisi kuliko utaratibu wa mabwawa ya zabuni ambayo yanachukua muda mrefu lakini pia yanatumia gharama kubwa na kuwafanya wafugaji wasiendelee kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niliyekulia jamii ya kifugaji ukiniambia bwawa mimi ninachojua ni kukinga maji yaliyokuwa yanapita yanazagaa, ukipeleka mitambo ile kama ya Kijeshi naamini itaweka mazuio na maji yatapatikana na wafugaji watapata mahali pa kunyweshea maji, hicho ndicho tulichokuwa tunasemea kuhusu matumizi ya Jeshi, tulikuwa tunaongelea vifaa vya Kijeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upande wa korosho, Mheshimiwa Mama Ghasia, Mheshimiwa Mwambe pamoja na ndugu yangu Mpakate na wengine Kaunje, Mheshimiwa Chikota na wengine wote wa ukanda wa maeneo yapotoka mazao ya korosho, kwanza nitakuja mwenyewe.
Mliniambia hata matatizo ya bodi niwaambie tu, nitoe siri Waheshimiwa Wabunge kuna bodi nyingi sana kwenye upande wa mazao ya kilimo mpaka sasa nilikuwa bado sijapeleka mapandekezo ya majina, sababu kubwa ni moja tu na niseme na wenye bodi zile wajitambue, nilikuwanafanya tathmini ya justification ya uwepo wa bodi hizo, na kwenye vyama vya ushirika hivyo hivyo, kwenye APEX nilikuwa nafanya tathmini kwamba hivi kuna mazao hayana bodi, hatuna ulalamishi wowote wa kuhusu makato, hatuna ulalamishi kuhusu kuibiwa, watu hawa wanazalisha hakuna kesi ya wizi, hakuna kesi ya makato, hakuna kesi ya unyonyaji, hakuna kesi ya madeni ya mikopo kwa ajili ya kutumia hivi vitu na yanafanya kazi vizuri tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mpunga sasa hivi ni wa tatu kwa uzalishaji wa mpunga na hatuna bodi ya mpunga. Halafu maeneo ambapo tuna bodi ndipo wizi upo mkubwa, unyonyaji mkubwa, nitoe rai kwa maeneo haya niliyoyataja wajitathmini, wa-justify uwepo wao, kama hawatakuwepo tutatengeneza kuwa na bodi ya mchanganyiko halafu na bodi ya mazao ya biashara halafu tutatumia watendaji kusimamia mambo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni fursa yao ya mwisho, kwa sababu hatuwezi tukawa na taasisi ambazo zinatumika kama vichaka vya kuwanyonya wale ambao wanavuja jasho katika kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu makato hatuwezi tukawa na taasisi ambazo zinafanya kazi ya kuwa kichaka cha kuwanyonya wale wanaovuja jasho katika kuzalisha mazao hayo. Tunahitaji taasisi zozote zinazokuwepo zioneshe uhalali wao wa kuwepo katika shughuli hizo ambazo zinafanya zenyewe ziwepo. Hivyo hivyo hata kwa wataalam wetu.
Kwa hiyo, kwa upande wa makato tumebainisha maeneo yote. Mheshimiwa Kiswaga, Mheshimiwa Mabula pamoja na wengine wote wanaotoka ukanda wa uvuvi, tumeyapitia makato ya leseni yote tumeorodhesha, tumepitia makato yote kwenye mazao yote yaliyokuwa yanakatwa. Sasa hivi tunachofanya tumeshayafanyia uamuzi, kuhusu makato yale yanayokatwa, kama Wizara tunayofanya ni mawasiliano ya Kiserikali tunavyoelekea kwenye Muswada wa Fedha ambao utakuja mwishoni ili tuone yapi ambayo tutataja kwamba tumeshayafuta kwa sababu yanatakiwa yaingie kwenye kufutwa kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wavuvi kwa mfano wanapata leseni ya uvuvi, Leseni ya Vibarua, SUMATRA, BMU, Zimamoto, sasa zimamoto kule kwenye kuvua, maji yenyewe si ndiyo zimamoto, kwa sababu magari yenyewe hayaji na maji. Kwa hiyo, tunaangalia yale ambayo kwa kweli uwepo wake imetumika kama kichaka, tunaenda kuyafuta na tunahakikisha watu wetu wanapata tija. Nasikia mambo ya aina hii aliyasema pia Mheshimiwa Kemirembe, Mheshimiwa Kiteto pamoja na ndugu yangu wa Jimbo la Rorya Mheshimiwa Airo.
Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, hoja ni nyingi lakini kwenye makato niwahakikishie kwamba yote tulishaorodhesha na tunategemea tu-share na wenzetu tunapotengeneza sheria ile ili tuweze kurekebisha. Hiyo ndiyo ilikuwa dhana halisi ya kutengeneza chombo cha aina moja kinachokusanya ili kuweza kuondoa mlolongo. Hivyo hivyo na kwenye mageti, watu wengine walikuwa wanasema Halmashauri zitakosa mapato, Waheshimiwa Wabunge ninawaambia tu kwa nia njema, katika mazingira tuliyo nayo tunatoza ushuru mara mbili kwa zao moja ama bidhaa moja mara nyingi mno, watu wetu mpaka wanatushangaa! kwa hiyo lazima tutafute formula kitu ambacho kimeshatozwa, tena ni mara mia ikatozwa kwa kiwango kikubwa lakini mtu akajua sina usumbufu nikishalipa kitu cha aina hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wetu wanasumbuliwa fedha nyingine zinapotea kwenye rushwa tu, watu wengine wanapata ajali ya kupita usiku wanakimbizana na wale walioweka mageti, ni lazima tukaweka utaratibu kama Halmashauri zetu ziseme kwenye mageti zilipata fedha kiasi gani halafu zipewe, fedha nyingi zinapotelea kwa wale wanaokaa kwenye mageti na kuwatoza rushwa wale watu. Tutengeneze utaratibu bidhaa ikishalipiwa kodi ikawa na risiti, ile risiti imtoshe mtu kutembea akiwa anajua kwamba nimeshalimaliza hili, sitabugudhiwa na mtu na nakwenda kufanya kitu chenye tija. Hiyo ndiyo dhana halisi ambayo tunaiangalia katika taswira hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua sokoni ndiko ushuru unapotolewa, ukishafika mtu akawa na leseni anajua ameshatoa na masoko haya tunajenga kila mahali watolee katika maeneo hayo. Hiyo ni sawa sawa na maeneo ya minada na kwenye minada hivyo hivyo, kama mtu atakuwa ameshatozwa leseni ama ameshatozwa ushuru basi ile risiti ambayo ametumia kutozwa iwe inatosha anapokuwa ameenda katika eneo lingine.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea yale ya ndugu yangu Airo mnada ya Kirumi pale tumesema utaendelea hivyo hivyo, tulipokea pia mnada wa Magena kutoka kwa bibi yangu pembeni kule Tarime. Sisi kama Wizara tumesema wenzetu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wamesema sababu zilizosababisha mwanzoni isiwe hatuoni ubaya kama kutakuwa na mnada ambao upo Kirumi siku yake na kukawa na mnada huko Magena siku yake na kuna mnada upo pale mpakani kidogo na Kenya na wenyewe upo siku yake. Kwa hiyo mambo ya aina hii tunayaangalia na tutaangalia financial implication zake, lakini siyo jambo la kufa na kupona tukigombana na watu wanaotaka wakusanye fedha na watupatie fedha kama Serikali.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ya kawaida mambo yale yanayohusisha Wizara yetu na Wizara nyingine Serikali ni moja, Mheshimiwa Mukasa waambie wananchi wako wala wasinoe mapanga, Serikali tutakaa tutaamua, tutatoa uongozi ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanafanya kazi katika mazingira yaliyo rafiki kwa wao kuweza kufanya kazi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya niendelee kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge michango yenu ni bora sana tumeshaipokea, siyo tu kwa ajili ya majibu tutaifanyia kazi na niendelee kusema kama mnataka mali mtazipata shambani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba sasa kutoa hoja!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, pacha wangu ambaye tunategemeana. Kwanza naunga mkono hoja hii kwa sababu watu wangu hata wakizalisha namna gani, kama bajeti ya pacha wangu haijapita watakosa mahali pa kupeleka bidhaa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niseme kwamba bajeti hii ya leo tunayoipitisha ni jambo jema sana kama Waheshimiwa Wabunge wote tutaelewa dhana yake halisi iliyomo kwenye bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, kwanza hii ni bajeti ya kwanza ikiwa imebeba dhana hii ya kwenda kwenye Tanzania ya Viwanda na hivi tunapopitisha tunatengeneza pamoja na miundombinu yake ambayo inahusiana na suala hili la kukuza viwanda.
Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wote tuelewe kwamba suala la viwanda siyo suala la Serikali peke yake wala si suala la Waziri wa Viwanda peke yake, ni suala ambalo linaanzia kuanzia uzalishaji, linakwenda mpaka kwenye kujituma kwa Watanzania na linakwenda mpaka kwenye uwekezaji ambao unatumia sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno mengi ambayo yamesemwa na Waheshimiwa Wabunge, Wizara imezingatia na mimi kwa sababu pacha wangu nakaa naye karibu hapa, kuna hatua ambazo ameendelea kuzichukua hapa ambazo ni maelekezo ya ufanyiaji kazi wa mawazo ya Wabunge hata kabla hajasimama kujibu hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nijibu baadhi ya hoja ambazo zimejitokeza ambazo zinalenga kwa pamoja kwenye Wizara yangu na pamoja na mwendelezo wa ushirikiano wa Wizara yangu pamoja na Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye jambo alilolisema Mheshimiwa Leonidas Gama, Mbunge wa Songea Mjini ambalo lilikuwa linahusisha kiwanda cha kuchakata mihogo kifanyikie hapa hapa Tanzania badala ya mihogo kusafirishwa. Wizara zetu tayari zimeshachukua hatua kwenye hilo kuanzia kwenye mahitaji ambayo yanahitajika katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa. Nimpongeze sana kwa hoja hiyo na kwa concern yake, lakini nimhakikishie kwamba hicho ndicho ambacho kitafanyika. Hivi tunavyoongea mwekezaji mmoja wa Tanzania Agricultural Export Processing tayari alishajenga kiwanda Pwani, na anategemea kujenga Lindi, Mtwara, lakini hivyohivyo ndivyo itakavyofanyika katika maeneo mengine ambayo yanalima muhogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge, tuwahamasishe wananchi wetu waweze kujikita katika kilimo hiki kwa ajili ya soko lililopatikana, lakini pia kwa mimi wa kilimo niseme kama moja ya chakula cha akiba ambacho kinastahimili katika maeneo mengi ambayo yana mtawanyo hafifu wa mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Mheshimiwa Mbunge Mukasa wa Biharamulo, Mheshimiwa Innocent Bashungwa Mbunge wa Jimbo la Karagwe na Mheshimiwa Mbunge wa Innocent Bilakatwe Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum mgeni kabisa hapa Mheshimiwa Oliver na yeye amesema, pamoja na hawa wanaotokea Ukanda wa Tabora pamoja na Shinyanga wameongelea zao hili la muhogo. Sisi kama Serikali tunawahakikishia uhakika wa soko, lakini pia maabara ambayo imeshapitishwa ya kisasa kabisa ya kuweza kufanyia tathmini zao hili, ili liweze kuuzwa popote pale duniani. Kwa maana hiyo, Waheshimiwa Wabunge, tunapoongelea viwanda Serikali tumedhamiria na tuna uhakika hatubahatishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania siyo mara ya kwanza kwa Serikali ya CCM kuamua jambo na likafanikiwa. Tuna mambo mengi ambayo yamefanikiwa na ninyi ni mashahidi. Niwaambieni siyo miaka mingi sana ilikuwa ukitaka kupiga simu inabidi uende kusubiria simu za kuzungusha zile. Hili sijasimuliwa nimeshuhudia mwenyewe, lakini kwa sasa hivi hata wanafunzi wa shule za msingi wana simu za mkononi, hiyo ndiyo CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo siku nyingi ilikuwa mtu akitaka kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo lingine inabidi apange safari ya wiki nzima kwa hiyo, kama ana bidhaa zake atazipata baada ya mwezi mmoja. Lakini tuliposema tutaunganisha nchi hii Mikoa kwa Mikoa ili watu waweze kuwekeza na kusafirisha bidhaa, sasa hivi unaweza ukatoka na taxi Mtwara na taxi na ukaenda mpaka Mtukula kule kwa taxi. Ama ukatoka mpaka wa Zambia ukaenda Holili kwa taxi. Kwa hiyo, tunaposema tunaenda kwenye Tanzania ya viwanda tuna uzoefu wa kuamua jambo na tukatekeleza likafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaanza kuhamasisha uzalishaji kwa sababu, viwanda tunavyotaka kujenga siyo viwanda vya kuzalisha kwa wiki moja, tunataka viwanda ambavyo vitazalisha katika msimu wa uzalishaji na vizalishe katika msimu ambapo vina akiba ya malighafi. Kwa maana hiyo, jambo hili ni vema Watanzania wote tukaiitikia kauli ya Mheshimiwa Rais ambaye ameshatoa dira kwamba tunaenda kwenye Tanzania ya viwanda badala ya kuanza kauli za kukatishana tamaa ambazo zinaweza zikawaacha wengine wasijue ni lipi la kufanya. Ni vema tukawa na kauli moja kwa sababu nchi hii ni yetu sote na mafanikio haya yakiwa ya Taifa itakuwa ni heshima kwetu sisi sote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hili tulilosema la jembe la mkono kupelekwa makumbusho, jamani ni jambo ambalo linawezekana. Hatuwezi tukaendelea kujilaani kila leo kwamba sisi tutakuwa watu wa jembe la mkono. Tumedhamiria, tutatumia sekta binafsi, tutatumia jitihada za Serikali, tunaunganisha zote za sekta binafsi pamoja na jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba, tunaenda kwenye kilimo cha kisasa kwa sababu hatuwezi tukazalisha bidhaa za kutosha viwanda kwa kutumia jembe la mkono. Jambo hili lazima liwe na mwanzo na sisi tumepanga mwanzo ni sekta binafsi pamoja na sisi wenyewe Serikali, tayari tunakaa pamoja na Wizara ya Viwanda kwa ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba tunaweka mikakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayasema haya kwa sababu ndiyo tunaanza. Huu ndiyo wakati wenyewe wa kusema tumepanga nini na baada ya hapo tunaenda kwenye kutekeleza. Watu ambao mnakuwa na mashaka niwaambieni hiyo hairuhusiwi hata kwenye vitabu vya Mungu maana Mungu mwenyewe anasema mwenye hofu hatapokea kitu kwangu; and a person who is incapable of even trying, is incapable of everything. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie, nimeshuhudia nikiwa mdogo Mkoa wa Singida watu walikuwa wanaenda kusaga unga wa kula mara moja katika miezi sita, lakini sasa hivi lile jiwe la kusagia lilishapotea. Kwa hiyo, hata jembe la mkono nina uhakika litabaki maeneo matatu; eneo la kwanza kwenye makumbusho, eneo la pili makaburini kwenye kuchimba makaburi na eneo la tatu kwa ajili ya kumbukumbu litabaki kwenye bendera ya CCM, ili itukumbushe tulitoka wapi.! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nitumie fursa hii tunapochangia bajeti ya Viwanda na niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote tuzingatie, tuwahamasishe wananchi wetu waepuke kuibiwa, wanaibiwa kwenye uuzaji wa mazao kwa lumbesa. Nimesikia malalamiko hayo kwa Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, kwa Mheshimiwa Bosnia kule, nimesikia malalamiko kwa Jah People kutoka kule Njombe, kwa Mheshimiwa Hongoli pamoja na ndugu zangu wa Ludewa na maeneo mengine ambako wanazalisha mazao hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaelimishe wananchi wote watumie vipimo rasmi. Hii wanayouza kwa lumbesa ni namna ambayo wanunuzi wasio waaminifu wanawadanganya kwamba hii ni namna ya kupakia lakini ndivyo ambavyo wanawaibia wakulima wetu. Baada ya kuwa tumeshaanza mwaka mpya wa fedha, vyombo vya dola visimamie ili wakulima wetu waache kuibiwa, likienda sambamba na wale wanaonunua mazao mashambani wakiita wanachumbia, kwamba kama ni migomba inakuwa bado ndizi hazijawa tayari kwa ajili ya kuuza, wao wanawekeza fedha kwa bei ndogo wanaita kuchumbia na baadaye soko likiwa zuri wanakuwa tayari walishazinunua zikiwa bado ziko mashambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine limesemwa na shangazi yangu, Mheshimiwa Hawa Ghasia, la kuhusu kiwanda cha mbolea. Katika ukurasa wa 24 wa hotuba ya Waziri limeongelewa na hii ndiyo connection ambayo Mheshimiwa Zitto alikuwa anaitafuta. Niseme tu kwamba kwenye kitabu kuna maeneo ambayo yameongelewa connection ya uzalishaji pamoja na viwanda, mojawapo ni hili la kiwanda cha mbolea ambacho sisi tunakitegemea sana na liko katika ngazi ya Serikali pamoja na wawekezaji na Mheshimiwa Waziri atalielezea pia, atakaposimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utitiri wa tozo, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha ameliweka vizuri na niseme tu tayari Waziri mwenye dhamana alishaelekeza kupitia kwa Katibu Mkuu anayeshughulikia mambo ya uwekezaji kwamba ataratibu ile timu ya Makatibu Wakuu, ili kuweza kujua tozo gani za kuondoa, lakini pia na kuweza kuunganisha zile ambazo zitaonekana zinatakiwa ziwepo ijulikane ni nani anatoza ili pasiwepo na huu utaratibu wa kila mmoja kwenda kwa wakati wake na kuleta usumbufu kwa wanaochangia ili waweze kufanya shughuli zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili litaenda sambamba hata katika utaratibu wa kupata leseni ama vibali vya kufanyia kazi. Mtu akishamaliza eneo moja ajue kwamba tayari ameshamaliza katika utaratibu wa kupata vibali ili aweze kufanya shughuli zake za kibiashara. Serikali inalifanyiakazi kuweza kutengeneza mazingira ya kufanyia biashara katika nchi yetu ambayo ina fursa kubwa kuliko nchi nyingi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Ukanda wa Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limeongelewa, amelisemea sasa hivi Mheshimiwa Mwamwindi linalohusu kinu cha Iringa. Vinu vingi vya Serikali vilikabidhiwa kwa Bodi ya Mazao Mchanganyiko na utaratibu huu tuliona pamoja na kwamba tuna NFRA ambayo yenyewe ni Hifadhi ya Chakula, tuliona tuwe na chombo kingine ambacho kinashughulika na mambo ambayo yanaweza yakawa ya kibiashara zaidi na hapo ndipo ambapo ilianzishwa hii Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Katika jambo hili tumesema hawa wakiwa sehemu ya ununuzi na tukachukua na lile wazo alilolisemea Mheshimiwa Serukamba la kuunganisha na sekta binafsi wanaotaka kufanyakazi katika maeneo haya ya kununua mazao, tuna uhakika kwamba wakulima wetu watakuwa wamepata soko pia, watu hawa wataweza kuweka uwiano wa bei, wakati bei ziko chini waweze wao kujitokeza na wakati bei ziko juu waweze wao kujitokeza ili wakulima wetu wasipate hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wazo lake tunalipokea na wafikishie wana-Iringa kwamba, hoja yako uliyoitoa Mawaziri wote wawili mapacha wamelipokea kwa nguvu zote na watalifanyia kazi na waendelee kukupa heshima ya kukuchagua kwa sababu umewasemea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo lilisemewa na Mheshimiwa Sabreena, amelisemea suala la zao la mchikichi kwamba halina Bodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, sisi kama Serikali jambo pekee ambalo tunaungana naye, Mheshimiwa Zitto Kabwe na yeye amelisemea mara nyingi kuhusu zao la michikichi ni kwamba tunahitaji kuimarisha uzalishaji wa mazao haya ambayo bidhaa zake tunaagiza kutoka nje. Jambo la kusema tuanze na Bodi kabla ya zao lenyewe halijaanza kuzalishwa ama halijaanza kuwa na tija, tutaleta mgogoro na tutaleta gharama ambazo hazihitajiki. Kwa hiyo, jambo ambalo tunalifanya kama Wizara ni kuhamasisha wakulima waone kwamba pana fursa katika jambo hilo. Sisi kama Serikali kuweka kila jitihada kusaidia pale ambapo patahitaji msaada kuhakikisha kwamba wakulima hawa wanasaidiwa, lakini tukianza kusema kila zao tuliwekee bodi hata ambayo hayajaanza kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema hata juzi wakati nahitimisha hotuba yangu, nikasema ni lazima tufanye tathmini, kila taasisi tunayoiunda uhalali wake uonekane kutokana na kazi unazozifanya. Leo hii kwenye mpunga hatuna bodi, lakini nchi yetu inapiga hatua, inajulikana hapa Afrika na inajulikana hapa duniani, kwenye mahindi hivyohivyo tunafanya vizuri, hatuna kesi ya kuibiwa, hatuna kesi ya wizi, hatuna kesi ya utapeli. Leo hii tukiwaza kwamba uwepo wa Bodi ndiyo utaibua mchikichi au utaibua alizeti, hili ni jambo ambalo mimi mwenye sekta nawashawishi lazima tutathmini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema kwenye mpunga, kwenye mahindi, wanayo tu bodi inaitwa Bodi ya Mazao Mchanganyiko, tunasema bodi zisipoweza kuondoa uozo unaojitokeza kwenye mazao haya yenye bodi na kwamba kama uwepo wao haujaweza kusaidia, tutawaza uwepo wa chombo kimoja ambacho kitaitwa Bodi ya Mazao Mchanganyiko ili kuweza kuhakikisha kwamba tunaondokana na haya ambayo yanawakera watu wanaovuja jasho kila leo huku wakitozwa makato mengi kwa ajili ya uwepo wa taasisi nyingi ambazo tukienda kwenye uhalali haziwasaidii ama zimepunguza uhalali wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameongelea kuhusu kushuka kwa uzalishaji wa pamba. Mheshimiwa Ndassa, Mheshimiwa Kiswaga, Mheshimiwa Kemirembe, Mheshimiwa Njalu pamoja na Mheshimiwa Nyongo na Wabunge wengine wanaotoka maeneo yanayolima pamba akiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Kalemani ambaye nimemuona ameongelea vizuri sana suala la umeme, akanikumbusha enzi za Mheshimiwa Rais akiwa Waziri, jinsi alivyoweza kutaja maeneo yale anayoyasimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameliongelea kwa machungu suala hili la zao la pamba akiwemo ndugu yangu Mheshimiwa Kangi Lugola kutoka kule Mwibara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tunarejea katika misingi tujue kitu gani kimepotea hapa hata uzalishaji ukashuka. Tumeshaweka timu yetu na tunategemea baada ya kuwa tumeshamaliza bajeti na pacha wangu hapa akamaliza ya kwake tunaenda sasa kwenye utekelezaji ili kuhakikisha kwamba tunatengeneza hii chain kuanzia kwenye uzalishaji tunaenda kwenye kutunza iliyozalishwa, tunaenda kwenye ku-process ambayo ndiyo inayoangukia kwenye Wizara yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Wabunge tumpitishie Mheshimiwa Waziri bajeti yake, tumpe kazi, ili tuweze kuanza hii ramani ya kwenda kwenye Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja mia kwa mia na niendelee kusema kama mnaitaka mali mtaipata shambani na mali yenye tija inapatikana kwenye viwanda.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia hoja hii iliyopo Mezani. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniongezea timu katika Wizara yangu. Katika wiki hizi mbili ameteua Kamishna Mkuu mpya wa Magereza, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji aliyeteuliwa leo, Kamishna Mkuu wa Kupambana na Madawa ya Kulevya na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai. Hawa ni watu wa muhimu sana katika kazi hii. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwaambie, ndiyo kwanza kazi inaanza. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, niwashukuru sana Kamati kwa ushauri ambao wamekuwa wakitupatia Wizara. Niwaambie tu kwa ujumla wao mapendekezo na ushauri wote ambao wametupatia tutaufanyia kazi na hasa tunapoelekea katika maandalizi ya bajeti ya mwaka unaofuata. Nakushukuru sana Mwenyekiti wa Kamati, wewe umekuwa dictionary yetu nzuri katika Wizara hii ukizingatia institutional memory uliyonayo ya kufanya kazi katika Wizara hii pamoja na timu yako. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo tumelipokea, mmeongelea sana suala la vitendeakazi pamoja na maslahi ya askari wetu wa vyombo vyote ambavyo viko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Wenzetu wa Wizara ya Fedha tayari wameshatusaidia baadhi ya vitu ambavyo vilikuwa vinadaiwa na askari wetu. Kuna baadhi ambavyo tayari wameshaanza kutoa na tunaamini kwa kadri ambavyo wamekuwa wakijitahidi wataendelea kutoa na vingine. Kwa hiyo, jambo hilo linafanyiwa kazi na stahili hizo zimekuwa zikitolewa na hivyo kupandisha morali ya kazi ya vijana wetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunasubiria magari, Waheshimiwa Wabunge wengi katika maeneo yenu mmeongelea suala la magari. Ni kweli nimepita katika maeneo mengi ambako nimeona umbali na uhitaji wa magari kwa ajili ya operesheni pamoja na mambo mengine ni mkubwa. Niwaahidi, tutatoa vipaumbele kwa kadri ya maeneo yalivyo kadri tutakavyokuwa tumepata magari hayo ili kuweza kuongeza tija ya usalama wa raia pamoja na mali zao katika maeneo yenu, tutalifanyia kazi hilo. Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea pia maombi ya vituo, tutaendelea kushirikiana nanyi na hamasa mnazozifanya katika maeneo yenu ili hili nalo liweze kupewa uzito unaostahili. Sisi tutajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kuweza kuhakikisha tunatengeneza mazingira hayo. Nia yetu ni moja ya kuweza kuhakikisha mazingira ya askari yanaendana na kazi wanayofanya ili raia waweze kujizalishia mali katika mazingira ambayo ni salama na wao waweze kufanya kazi wakiwa salama. Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo limeongelewa na Kamati pamoja na Waheshimiwa Wabunge ni lile linalohusu wakimbizi pamoja na makazi ya wale raia ambao walipewa uraia baada ya kukaa kwa muda mrefu. Jambo hili tunaendelea kulijadili na wiki ijayo tutakaa kikao cha pamoja kuweza kujadiliana. Mambo ambayo tunategemea kuyajadili ni pamoja na njia nzuri. Wazo hili lilipoahirishwa mwanzoni ilikuwa hawa watu wapewe fedha za kwenda kuanzia maisha sehemu nyingine. Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara mtazamo wetu uko sawasawa na mtazamo wa Kamati kwamba hatuwezi tukawapa watu uraia halafu wakatengeneza kanchi kao ndani ya nchi yetu kwa kukaa eneo lao, kwa kuwa na uongozi wao, wana lugha yao moja na tabia zao moja. Watu wakishapewa uraia wa Tanzania wanakuwa Watanzania na wanatakiwa waishi kwa desturi na Katiba ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo tutajadiliana na development partners pamoja na sisi wenyewe kuweka huo msimamo na tutalitolea uamuzi katika Serikali. Tutawajulisha Kamati pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa kadri tutakavyopata muda na forum zetu hizi ambazo ni za Kibunge za kupeana taarifa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa wakimbizi tulifuta utaratibu wa wakimbizi kuingia kwa ujumla kwa sababu hali ya mara baada ya tension za kisiasa na kabla na sasa ilivyo ni tofauti. Kwa hiyo, tunatengeneza utaratibu ule ikiwa ni pamoja na udhibiti ili kuweza kudhibiti uhalifu kwani kuna wengine wanaweza wakaingia kwa gia ya ukimbizi na wakafanya vitu ambavyo ni vya kihalifu. Hii inadhihirika katika ukanda ambako wakimbizi wapo jinsi ambavyo matukio ya uhalifu yamekuwa yakizidi maeneo mengine na upatikanaji wa silaha ambazo si za Tanzania ukizidi katika maeneo hayo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine na Mheshimiwa Naibu Waziri alilisemea kwa kiwango kikubwa nampongeza kwa hilo linahusu namna ya kuifanya Magereza ijitegemee. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu tayari ameshaitisha kikao ambacho kitafanyika Jumatatu lakini lengo lake ni namna ya kutumia fursa tulizonazo katika Magereza kwenda kwenye uzalishaji. Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilipokuwa najibu swali nililisemea kwamba tunataka Magereza ambayo yana maeneo ya uzalishaji tuyatumie kwenye uzalishaji. Tutatoka kwenye uzalishaji wa kizamani kwenda kwenye uzalishaji wa kisasa ili maeneo yote yale yazalishwe kwa zaidi ya asilimia 85. Tukifanya hivyo tuna uhakika Magereza yatajitegemea kwa chakula lakini hata kwa fedha kwa sababu tunaamini uzalishaji huo ukishazidi kuna baadhi ya mazao ambayo tutauza NFRA pamoja na maeneo mengine na vilevile tunaweza hata tukapeleka kwenye shule za bweni ili watu wetu waweze kupata chakula hicho. Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho lililoongelewa sana ni hili la madawa ya kulevya. Vita hii ya madawa ya kulevya ni vita ya kila Mtanzania na vita hii haijaanza sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi tangu nilipofika nilikuta tayari Mheshimiwa Kitwanga ameshakamata mapapa wakubwa tu na tulivyotoka pale tumeendeleza. Ninachowaambia Waheshimiwa Wabunge tunaweza tukatofautiana mtazamo kwenye approach na ninyi kama Wabunge na kama washauri wetu mkitushauri njia nzuri ya kufanikisha jambo hili sisi mara zote tutakuwa tunapokea ushauri huo. Kwa sababu vita hii si ya mtu mmoja, mkituambia tukifanya hivi tutafanikiwa zaidi maana yake vita ni yetu sote, sisi tutaendelea kupokea ushauri. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja tu ambalo nawahakikishia na ambalo nawaomba wote tuwe nalo, tusibadili lengo la kuhakikisha tunapambana na vita ya madawa ya kulevya, tuendelee nalo. Mheshimiwa Rais alishatoa dira hiyo na sisi wasaidizi wake tunatembea katika nyayo zile kuweza kuhakikisha tunafanikiwa hilo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wengine walikuwa wanasema mbona Waziri hujasema, nimeshazunguka mikoa yote kasoro Njombe, Ruvuma, Singida na Songwe. Kwenye mikoa yote huko nilikopita nimetoa maelekezo ya makosa ambayo ni ya kipaumbele ya kufanyiwa kazi:- Moja, ni madawa ya kulevya, kila mkoa nimeelekeza, si jambo la mjadala. Mbili, ni uhalifu wa kutumia silaha, nimesema si jambo la mjadala. Tatu, nimesema ni ubakaji, si jambo la mjadala. Nne, nimesema ni ujangili, si jambo la mjadala. Tano, nimesema yale masuala yanayohusisha ugaidi, si mambo ya mjadala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikishatoa maelekezo kama hayo sibinafsishi tena hiyo shughuli…
Mtanzania ambaye linamhusu jambo hili popote pale alipo na mkiwepo Waheshimiwa Wabunge lazima tusimamie mambo haya kwa upana wake kwa maslahi ya Taifa letu. Jambo likishakuwa la aina hii kila mmoja anatakiwa atimize wajibu wake. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge katika masuala haya ambayo ni ya Kitaifa tushirikiane wote, tusaidiane wote. Watu huwa hawagombani kwa ajili ya kazi, watu wanasaidiana kazi, tusaidiane kazi kuweza kuhakikisha kwamba inapofanikiwa inakuwa yetu sote na inaposhindikana tunakuwa tumeshindwa wote kama Taifa. Taifa letu likipata hasara, Taifa letu likipata aibu tunakuwa tumepata aibu wote. United we stand divided we fall, twende pamoja tuweze kuhakikisha kwamba tunafanikiwa katika mambo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuhitimisha hoja baada ya kuwa tumepata michango toka kwa Kamati, kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani na kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niwashukuru wote waliochangia, tukianza na maoni ya Kamati, maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na Waheshimiwa Wabunge ambao ndiyo mmetoka kuchangia hivi punde. Wizara tumeyapokea maoni yenu, tutayafanyia kazi na tutayachambua yale ambayo yanahitaji ufafanuzi wa kina zaidi, tuweze kuyajibu kwa maandishi. Kwa yale ambayo mmetupa ushauri ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kwa ujumla wake kwa sababu hoja ni nyingi, niwaambie tu kwamba tumeyapokea na tutayafanyia kazi, kama ambavyo tumekuwa tukipokea ushauri kutoka kwenu mnapokuwa mmetimiza wajibu wenu wa kikanuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na hoja za jumla kabla sijaenda kwenye hoja mojamoja kati ya hoja ambazo zilijitokeza. Hoja ya kwanza ambayo imeongelewa kwa upana ni hii ambayo ilikuwa inahusisha mambo ya Vyama vya Siasa pamoja na Wabunge na ndugu yangu Mheshimiwa Lijualikali akasemea kwamba labda haya yanafanyika kwa Wabunge wa Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niweke kumbukumbu sawa; moja, vyama vingi vya siasa kwenye nchi yetu viko kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa sababu viko kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kila Mtanzania kuwa kwenye chama anachokitaka si kosa. Mtu anapokuwa kwenye Chama chake siyo kosa. Ikumbukwe tu kwamba wakati vyama vingi vya siasa vinaanzishwa kilikuwepo chama kimoja tu, Chama cha Mapinduzi na kwa aina ya watu waliokuwepo na maoni yaliyotolewa kulikuwepo na fursa pana zaidi ya kuwa na chama kimoja kuliko kuwa na vyama vingi, kwa maana hiyo Chama cha Mapinduzi kwa ridhaa yake ndiyo kilianzisha vyama vingi na kama Chama cha Mapinduzi kilianzisha vyama vingi na tangu vyama vingi vianzishwe Chama cha Mapinduzi hakijawahi kuyumba kuhusu ushindi wake, kuanzia ngazi ya vijiji mpaka ngazi ya Urais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, panatokea kamsukosuko kadogo mnaanza kutafuta mchawi, mara wanasema wanatumiwa mara wanasema wanatumwa na juzi nilimsikiliza Kiongozi wenu Mkuu akisema hao wanatumwa. Niwatoe hofu, Serikali pamoja na Chama haiwezi ikaanzisha yenyewe vyama vingi na yenyewe ikaanza kushiriki kuviondoa vyama hivyo, kwa sababu hata hivyo haijawahi kupata tishio lolote na uwepo wa vyama vingi bali imepata faida na uwepo wa vyama vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, katika mazingira haya, niwashauri kitu kimoja, ndugu yangu Mheshimiwa Khatib Said Haji, ndugu yangu Mheshimiwa Katani walioongea, panapokuwepo na misukosuko ni wakati wa kutulia, huu nimewapa tu ushauri kwa kifupi ni wakati wa kutulia. Pia panapokuwepo na mizozo inayotishia usalama wa raia litakuwa jambo la kushangaza kama watu ambao wana jukumu la kusimamia usalama wa raia wasipoingilia kati, wakiingilia kati hilo ndilo jukumu lao, kwa sababu leo hii kukitokea jambo ambalo linatishia watu kupigana halafu Polisi kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Ndani wakawa wameshapewa taarifa wasiende watakuwa hawajatimiza wajibu wa kulinda usalama wa raia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pande zozote zile, hata mechi tu za mchezo wa ndondo, wakiona pana tishio la usalama wanaita Polisi wanaenda kuwasaidia. Kwa hiyo, ndugu zangu pande zote zinazoona mnatofautiana mkiona mna shida toeni taarifa ili polisi iweze kuingilia kati. Sisi tusipoingilia kati tutakuwa hatujatenda haki ya kuwahakikishia raia wa Tanzania usalama wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira kama hayo, mambo ya aina hii, niwaombe msitafute mchawi nje yenu, tumieni Katiba yenu, tumieni taratibu zenu ili muweze kulimaliza jambo hilo na nchi yetu inufaike na malengo yaliyokusudiwa kwa ajili ya uwepo wa vyama vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu, Mheshimiwa Katani ndiyo amenichekesha zaidi, anasema kulikuwepo na mkutano wa ndani kule kwao, mkutano wa ndani tu, halafu ndiyo anatolea mfano kwamba Waziri ulitamani mpaka Urais halafu hukuingilia kati ume-prove failure. Unajua kwa mtu anayetamani mpaka Urais kuingilia kitu ambacho OCD tu kinamtosha na yenyewe haijakaa sawa. Jambo ambalo lilikuwa la mkutano wa ndani la kibali cha mkutano wa ndani, hilo ni jambo ambalo Mkuu wa Polisi wa ngazi ya Kata ile anaweza kulimaliza na inapotokea limeshapita ngazi zote zile, basi utaratibu unaelekeza kukata rufaa kwa maandishi kwenda kwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijawahi kupata rufaa hiyo ambayo inaelezea kwamba kuna jambo mahali fulani limeshindikana, mara zote inapotokea jambo limetokea la aina hiyo niwashauri kwamba tumieni taratibu, tumieni ofisi. Mara zote Polisi hawatungi sheria, Polisi wanasimamia sheria na pale ambapo sheria sisi wenyewe ndiyo tumepitisha, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wala tusiwalaumu Polisi na kama tunaona zina kasoro basi tuzirekebishe ili wao wasimamie kwa urahisi bila kupata shaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge, baada ya kukaa kwenye Wizara hii nimekuja kuona kwamba lawama nyingi sana wanazopelekewa polisi hazitokani na polisi wenyewe. Kwa mfano, hata mambo haya yanayoongelewa sana ya kubambika kesi, mimi naweza nikawambia kwa kiwango kikubwa kesi za kubambikwa hazibambikwi na polisi ila wananchi wenyewe kwa kuhasimiana ndiyo wanaobambikiana kesi hizo. (Makofi)

Kuna Wilaya nilienda, tulijaribisha hata kufanya kura ya maoni, tulifanya kura ya maoni ya wazi ya kutafuta wahalifu; ili muweze kuona makundi yanayohasimiana yanavyoweza kubambikiana kesi. Baada ya kura ya maoni ile kupigwa kutafuta wahalifu wa CCM wote waliandika wahalifu ni wale wa CHADEMA, halafu wale wa CHADEMA waliandika wahalifu wote ni wale wa CCM. Leo hii ukienda Pemba ukiitisha kura ya maoni kutafuta wahalifu itakuja kwa muundo huo huo; na hata ukienda kwenye kesi nyingine kubwa, ndiyo maana wakati mwingine uchunguzi unachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda ukakuta msikiti ambao hauna ugomvi, umetulia kabisa ibada zinaenda vizuri hamna kesi ya ugaidi, ukienda kwa wale waliogombana zinatokea kesi za ugaidi. Sasa polisi ambaye hasali pale amejuaje huyu ana kasoro hii na hii? Wengine ni wacha Mungu tu wanatumia muda mwingi sana kutimiza ibada zile lakini ndiyo hivyo kwa sababu ya maslahi mengine ya kiuongozi wala siyo ya kiibada yanatokea hivyo.

Kwa hiyo, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tunapokuwa tunaongelea mambo ya polisi tuweke akiba tukizingatia kwamba wao wanatimiza sheria, lakini pia taarifa nyingi wanazozitumia kuchukua hatua zinatoka kwa wananchi na tukishalijua hilo tutawasaidia waweze kutimiza wajibu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokutana na ma-RPC niliwaambia wasitumie taarifa za mahasimu wanaohasimiana kuwa ndiyo taarifa pekee za kujenga hoja katika kuandaa mashitaka hayo. (Makofi)

Tutaendelea kulifanyia kazi, lakini makundi yanayohasimiana hayajengi hoja ya kuweza kujitosheleza. Hatutapuuza kitu lakini ile siyo njia pekee ya kuweza kujengea hoja na kumtia mtu hatiani. Hata tu ukimuuliza Ndassa kwenye michezo ni nani wanaocheza rafu yeye atakutajia wale tu anaohasimiana nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye hoja moja moja, nikianza na zile zilizotolewa kwenye Kamati. Serikali imepokea ushauri wa Kamati na utazingatiwa; na kama ambavyo tumekuwa tukifanyia kazi na tutaendelea kushauriana nanyi kuweza kuhakikisha kwamba yale yaliyotolewa na Kamati tunayafanyia kazi na majawabu yake mnayaona.

Kwa upande wa Zimamoto, hoja iliyotolea na Mheshimiwa Mkuchika tumeipokea, lakini si kwamba hatukuweka uzito, tuna mipango ambayo inaenda sambamba na hii ambayo imeonekena kwenye bajeti. Bajeti kubwa ya Serikali kuu itakapokuja itakuwa na dirisha ambalo Serikali inategemea kukopa fedha; na sisi tumeshafanya mazungumzo kama nilivyosema na wenzetu wa Ubelgiji pamoja na Australia ambapo tunategemea kupata zaidi ya Euro 22,000 kwa ajili ya manunuzi ya magari ya zimamoto na uokoaji. Kwa hiyo, pamoja na bajeti iliyotengwa, kuna njia zingine ambazo zinaenda sambamba ambazo ndizo tunategemea zituongezee nguvu za kupata magari hayo ambayo tunayahitaji.

Waheshimiwa Wabunge wengine waliochangia kwenye upande wa zimamoto, Mheshimiwa Juliana Shonza, Mheshimiwa Shabani Shekilindi, Mheshimiwa Sophia Mwakagenda pamoja na Mheshimiwa Japhet Hasunga tumepokea hoja zenu, hoja zenu ni za msingi na niwahakikishie kwamba Serikali inazifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa hoja zingine za mtu mmoja mmoja zilizotolewa, zimetoka hoja za masuala ya umeme aliyotoa Mheshimiwa Lucy, kuna hoja ilitolewa na Mheshimiwa Mtumwa kwa ajili ya kituo cha polisi, Mheshimiwa Raza na ndugu yangu Kangi Lugola; tumeyapokea na katika bajeti hii ni moja ya mambo ambayo tumeyazingatia sana haya yanayohusu maslahi ya askari wetu pamoja na haya ya vituo vya polisi na masuala ya umeme kama ambavyo Mheshimiwa Kiwelu aliulizia pamoja na Mheshimiwa Kangi Lugola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetolea ufafanuzi zaidi na tutawapa kwa maandishi kwa namba na kwa maelezo jinsi mafunzo ambavyo yameweza kufanyika kwa vikosi vyetu vyote ambavyo viko ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Jambo lingine ambalo liliongelewa ni lile linalohusu package kwa vikosi vingine vilivyosalia. Ameisema kwa kirefu Mheshimiwa Gekul na mara kwa mara amekuwa akiisemea Mheshimiwa Esther Matiko pamoja na ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa.

Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba ilikuwa ni utaratibu wa utoaji wa fedha kwa vipaumbele, haikuwa kuweka madaraja, ilikuwa ni utaratibu wa utoaji wa fedha kufuatana na upatikanaji wa fedha na mahitaji kwa sekta nzima kwa maeneo yote katika nchi yetu. Kwa mfano, fedha zinapopatikana kipaumbele cha kwanza kinakuwa ni mishahara ya watumishi wote kwa ujumla wao, ukishatoka hapo kunakuwepo na suala la Deni la Taifa na ukishatoka hapo kunakuwepo na mafungu madogo madogo kulingana na bakaa inayosalia.

Kwa hiyo, kwa utaratibu ule, ili na shughuli zingine ziweze kuendelea ilionekana ni vyema tuanze na kikosi kimoja kimoja kwa maana ya taasisi moja moja zilizoko kwenye vikosi, hivyo ndivyo ilivyotokea wakapata wa kwanza wakaja wakapata Polisi na kwa sasa tunavyoongea mwezi huu watapata Magereza na baada ya hapo watapata na wengine. Niwatoe hofu jambo hili kila askari ana fedha yake; kwa hiyo hakuna wa kusema huyu aliyechelewa labda atakuwa amekosa, watapata kama wenzao waliokuwa wamepata na watapata arrears zao kama ambavyo ilitakiwa waweze kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hili la Magereza alilisemea nadhani na mmoja wa wachangiaji kwamba nitembelee Magereza. Mimi nimeshatembelea Magereza mengi sana, yamebaki machache sana ambako sijaenda, na kote nilikopita nimeziona hizo hali zote. Ndiyo maana tunapotengeneza utaratibu wa utekelezaji wa mpango wetu tunazingatia yale ambayo tumeyakuta katika hali halisi za Magereza yale. Hata lile la Hanang nilifika na nimeona ujenzi ambao ulishaendelea lakini halijaanza kutumika kwa sababu sehemu ya jengo la utawala lilikuwa bado halijakamilika, na hicho ndicho ambacho tunaweka uzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaitambua hiyo hoja ya kwamba mahabusu wanakuwa hawaendi kusikiliza kesi zao kwa sababu kwanza, panakosekana magari, lakini pili wakati mwingine mafuta yanakosekana; pia na ule umbali unasababisha hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mary Nagu amelisema sana na amelililia sana na hata alishachangia sehemu ya ukamilishaji wa jengo hilo na mimi niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tunatoa vipaumbele kwenye maeneo hayo. Hoja yako tumeipokea, kwamba watu hawa wanakosa haki zao, lakini niseme kwamba ni jambo ambalo tulishalipokea na mimi nilishafika katika ene hilo, na hiyo hoja ya kutokutumia angalau yale majengo ambayo yalishajengwa nilishaiona na niwahakikishie kwamba tutalipa uzito unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye maoni ya Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani; Mheshimiwa Lema ameulizia kwa nini Jeshi la Polisi linazuia mikusanyiko ya kisiasa kwa sababu za kiintelijensia. Jeshi la Polisi halizuii mikutano ya kisiasa iwapo muhusika atafuata taratibu na kwa upande wa Waheshimiwa Wabunge nilishalielezea kwenye briefing na nilishaelezea siku nilipokuwa najibu maswali hapa.

Waheshimiwa Wabunge, baadhi yenu mmoja mmoja tulishaongea, kwenye hili la mikutano ya hadhara hatujataka utaratibu ambao uko duniani kote ila tumetaka utaratibu wa kimazoea na kwa sababu tunabeba utaratibu wa kimazoea tunasababisha jambo zima lionekane liko tofauti. Utaratibu uliopo kama taasisi zile za vyama vya siasa zingekuwa zinaangalia hata mataifa mengine yanafanyaje kile ambacho kingekuwa kinadaiwa hakikupaswa kiwe hiki ambacho kinadaiwa kwa sasa hivi. Kwa sababu hiki ambacho kinatokea ndiyo common practice katika mataifa yote ambako tunajifunza demokrasia ya vyama vingi. Naiunga mkono hiyo kwa sehemu hiyo ya kuhakikisha kwamba kila mtu kwenye anuani yake aende akafanye shughuli zake za kazi za watu wake ambako wanaweza wakamhoji na akafanya kazi za kwake za kisiasa.

Kwa maana hiyo kama jambo hili lingekuwa linajadiliwa kwa sehemu ya wale ambao jukumu lake si sehemu ile aliyochaguliwa ile ingekuwa ni mada nyingine, lakini ule utaratibu uliokuwa unatumika wa kiholela hata Watanzania wenyewe walikuwa hawaridhiki nao na ni utaratibu ambao umewagharimu sana Watanzania katika baadhi ya maeneo na ninyi ni mashahidi. Hata hivyo utaratibu huu ambao umekuwa ukitumika katika maeneo mengine umesababisha mpaka vifo. Kwa maana hiyo hili ni jambo ambalo Mheshimiwa Rais alilitolea dira, ndio utaratibu ambao na maeneo mengine unatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mheshimiwa Lema alisema kwa nini Jeshi la Polisi linafanya kazi ya kukusanya mapato na tozo wakati hiyo ni kazi ya TRA. Tuna mapato ambayo yanakusanywa na TRA, lakini vile vile kuna sehemu ya mapato ya Serikali yanayojulikana kama maduhuli yanakusanywa na taasisi mbalimbali za Kiserikali kufuatana na convenience ya kuweza kukusanya mapato hayo. kwa

mfano mapato kidogo yanayoweza kukusanywa na Jeshi la Polisi ni convenience kwamba hawa watu wametapakaa maeneo mengi wanaweza wakaifanya kazi hiyo kwa ufanisi kuliko kutumia TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameelezea suala la Wakili Mwale ambalo amesema kwamba kesi yake imechukua muda mrefu. Niseme tu kwamba nimelipokea na kwa sababu ni eneo ambalo na mimi napanga kuzungukia, ni maeneo ambayo tumekuwa tukizungukia kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Katiba na Sheria, ni jambo ambalo tunalipokea, tutafuatilia undani wake tujue imefika wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka hata DPP amezunguka maeneo tofauti tofauti akiwa na Dkt. Mwakyembe, na wakati mwingine tumezunguka tukiwa wote watatu kama Wizara, kuna baadhi ya maeneo ambayo tuliyatolea ufafanuzi na kuna baadhi ya maeneo ambayo tulichukua hatua kwa watu ambao walikuwa na matatizo ya aina hiyo..

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni hoja ambayo tumeipokea, tutakaa na kaka yangu tulione na tufuatilie, tujue undani wake umefikia wapi; lakini na kile ulichosema kwa huyu tuweze kuangalia na wengine ambao wanaangukia kwenye mkumbo huo ili waweze kupata haki zao na waweze kuendelea na maisha yao, tumeipokea na tutaifanyia kazi. Kwa Wabunge wengine ambao mmepokea hoja za aina hiyo, tunaweza tukapenyezeana lakini na sisi tutazungukia katika maeneo tofauti tofauti ili tuweze kuchukua hatua na watu hawa waweze kupata haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la askari wa usalama barabarani (traffic) kupata mafunzo na wengine elimu ya usalama barabarani tumeshalisema na kuna hatua ambazo tumesema tutazichukua ili kuweza kuhakikisha kwamba watu wetu wanaendelea kuwa na mafunzo na wanafanya kazi kwa weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine lilisemwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwamba Jeshi la Polisi nchini litahakikisha kwamba amani na utulivu vinakuwepo. Hili ni jambo la kipaumbele kwa Wizara yetu na tumesema hata katika haya maeneo ambayo katika siku za hivi karibuni kumetokea na rabsha za hapa na pale, niwahakikishie kwamba kazi inaendelea kwa ufanisi mkubwa sana, kazi inayoendelea ni kubwa sana na kwa sababu ya mazingira ya kiusalama hatusemi mipango tunayoifanya na hatusemi hatua tunazochukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo miwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mnaotokea katika maeneo hayo na maeneo mengine kuweni na uhakika kwamba Serikali iko kazini, Wizara ya Mambo ya Ndani iko kazini, Jeshi la Polisi liko kazini na niwahakikishie kwamba ni suala la muda tu. Wale ambao wameamua kujipima kwenye hilo, mimi niwatangazie kwamba wameshindwa kabla hata hawajaanza na tutashughulika na mmoja mmoja mpaka tutampata wa mwisho anayeshughulika na mambo hayo. Mpaka sasa zoezi hilo linaendelea vizuri na watakuwa wanajihesabu na wengine wanawaona wakiwa huko magerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutamvumilia hata mmoja asababishe maisha ya wananchi wetu yawe ya hekaheka. Kwa hiyo, tutashughulika na mmoja mmoja lakini na yoyote yule ambaye atashirikiana na wahalifu na yeye tutamuunganisha na wahalifu. Hatutaruhusu watu wetu washindwe kufanya shughuli za uzalishaji kwa sababu ya watu ambao hawataki amani katika suala la aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa hoja za maandishi, Mheshimiwa Mwikabe alisema askari wana madai mengi ya likizo, safari na kuistaafu. Nilielezea kwenye hotuba, kazi kubwa sana imefanyika ya malipo, na ukiangalia malipo ya madai ndiyo utaona kwamba Magereza hatuwabagui, kwenye madai yale tuliyolipa, Magereza tumewalipa fedha nyingi kulikoa hizi taasisi nyingine ambazo ziko Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwa hiyo, tunatoa tu vipaumbele vinavyolingana lakini panapotokea pana mtiririko wa fedha ambao hautoshi kuwalipa wote kwa pamoja tunafanya kwa namna hiyo.

Ndugu yangu Mheshimiwa Njalu alisemea kuhusu malalamikoa ya askari kuhusu nyongeza ya mishahara na posho; tumeweka yale mapendekezo niliyoyasoma wakati nawasilisha bajeti leo hii mapema.

Waheshimiwa Wabunge wengine wameelezea kwa kirefu, Mheshimiwa Mponda, Mheshimiwa Mtulia, mama yangu wa Iringa, ndugu yangu Mheshimiwa Kakoso wa Mpanda na ndugu yangu Mheshimiwa Shangazi tumepokea hoja zenu. Hii aliyoisemea Mheshimiwa Kakoso aliisema pia Mheshimiwa Kadutu, ameisema pia ndugu yangu Mheshimiwa Mbogo wa Nsimbo, jambo hilo kwa ngazi ya Serikali tumelipokea kuhusu uamuzi uliofanyika siku zilizopita wa kuwapa uraia ndugu zetu wapendwa wa kutoka Burundi na nchi nyingine, lakini baada ya kuwapa wakaendelea kukaa wamoja katika eneo lao moja ambalo baadhi yao wasiojua vizuri misingi ya nchi yetu, wanatengeneza kanchi ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelipokea, tunaendelea kujadili kwa ngazi ya Serikali kuangalia utaratibu ni upi mzuri ambao utawafanya baada ya kuwa wameshakuwa Watanzania wasichukue hata kimoja kilicho kibaya kutoka katika Mataifa yao yaliyosababisha hata wakatoka kule walikokuwa.

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tumelipokea na baada ya kuwa tumeshamaliza bajeti kwa ngazi ya Serikali tutajadiliana na ninyi tutawahusisha na Kamati tutaihusisha kwa sababu ilishatembelea hata hayo maeneo ili tuweze kuona njia muafaka na ya kudumu ya watu hawa ambao walipata uraia. Kwa sababu hawatakuwa watu wa makazi yenye taswira ya kiukimbizi lakini wakiwa ndani ya nchi. Hivi ilivyo sasa, sheria wanazozitumia wanazitumia ambazo ni za makazi ilhali walishakuwa raia kwa kupewa uraia. Kwa hiyo, hilo tumelipokea na niwahakikishie kwamba tutalifanyia kazi. (Makofi)

Ndugu yangu Mnyika ameongelea kuhusu vituo vya polisi katika Wilaya yake; nilisemee tu kwamba tayari tuna hatua ambazo tunazichukua. Maeneo yale ya mji ni moja ya maeneo ambayo tunaweka vipaumbele kwa sababu uhalifu unapotokea katikati ya Jiji unahamia pembeni. Kwa hiyo, hivi tunavyoongea pale Madale kuna kituo kimekamilishwa cha Daraja B, Kiluvya pana kituo kimekamilishwa na Mburahati ambacho ni cha Class A.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya aina hiyo pia ameisemea Mheshimiwa Bonnah kwa upande wa Segerea; tumeipokea na yenyewe tutaipa uzito unaostahili na baada ya Bunge kuwa limeisha tunategemea kufanya tathmini kujua hayo maeneo ambayo yameshauwa na watu wengi yanastahili kuwa na vituo lakini kwa mazingira yalivyo yanaendelea kutokuwa na vituo na hivyo kusababisha matatizo.

Ndugu yangu Mheshimiwa Dau ametoa hoja yake na ndugu yetu Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ametoa na yeye maoni yake kwa maandishi. Mheshimiwa Adadi nikuhakikishie tu kwa kuwa wewe ni dictionary inayotusaidia kwenye taasisi hii na kumbukumbu nzuri kwenye taasisi hii, hoja yako ambayo umeitoa tumeipokea. Tunawapongeza sana wananchi wa Muheza kwa kukuchangua kwa kweli umekuwa dictionary inayotusaidia katika Wizara yetu, tutaifanyia kazi hoja yako kwa uzito unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Faida Bakar ulipewa dakika chache sana lakini mambo uliyoyaongea yamekuwa na msingi sana na yatatusaidia sana, tumeyapokea. Ni kweli Jeshi la Polisi katika maeneo ya Pemba wanafanya kazi kwa mazingira magumu sana na mimi nilishafika huko, tumeyazingatia yote uliyasema, tunayapa uzito. Juu ya hoja yako uliyotoa katika eneo lake itatupa fursa ya kuifanyia kazi na kuwapa faida na maeneo mengine. Kwa sababu kuna maeneo mengine yanayofanana na huko ulikotolea mfano na mimi nilijionea nilipofika katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa uhamiaji hoja zilizotolewa zilikuwa ni Serikali iendelee kutekeleza mpango wa kuwarudisha makwao wahamiaji haramu walioko magerezani ili kupunguza gharama za kuwahudumia na kupunguza msongamano. Jambo hili lina matatizo lakini tumeendelea kulijadili. Waheshimiwa Wabunge hata ninyi mtakubaliana nami kwamba lina matatizo. Moja wengi wa wahamiaji haramu tulionao kwenye magereza yetu kimsingi ni wapitaji haramu, kwa sababu wengi wao nia yao huwa si kukaa Tanzania; ndiyo maana unakuta wengine walishapita, wanakaribia kupita wanakamatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tatizo lake ni kwamba tumeingia kwenye mikataba ya kimataifa ya kutokufanya biashara ya usafirishaji wa binadamu. Kwa hiyo, hilo ambalo linatokea, linatupa shida ya namna ya ku- facilitate upitaji wao kwa sababu ya mikataba hiyo kwamba tupo kwenye mstari mwembamba sana wa kuonekana tumewasaidia wapite kwa sababu hawakai kwetu, lakini vilevile kwa wakati ule ule iwe hatujavunja hilo sharti la kuwa tumeshiriki kurahisisha usafirishaji wa binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa mazingira kama hayo tunajadiliana tuone ipi ni njia muafaka na hili litajadiliwa kwa ngazi ya nchi wanakotoka hawa watu ili kuweze kuonekana ni namna gani ambavyo tunaweza tukalifanya. Lakini sasa hivi Serikali inaendelea na juhudi za kuwaondosha nchini kwa taratibu zilizopo. Zoezi hili limekuwa likitekelezwa punde fedha zinapopatikana kwa sababu linahitaji fedha kuweza kuwasafirisha watu hawa. Kwa hiyo, juhudi hizo za kuwaondoa kwa utaratibu huu ambao hautatufanya tuonekane tumevunja mikataba hiyo na tuonekane ni sehemu ya nchi inayofanya biashara za kusafirisha wanadamu tuwe tumelikwepa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ilikuwa kwamba Serikali iwezeshe bajeti ya Fungu 93 kwa kufanya makisio ya doria ili kubaini na kuwaondosha wahamiaji haramu, jambo hilo limezingatiwa na bajeti imeongezewa. Lingine ilikuwa kuhusu hati za kusafiria; Serikali ipo katika mpango wa kutoa passport mpya za kielektroniki ambapo kwa mujibu wa makubaliano ya Wakuu wa Nchi wa Jumuiya za Afrika Mashariki, passport za ki-diplomasia zitakuwa na rangi nyekundu kwa nchi zote za Afrika ya Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ndugu yangu Mheshimiwa Hamidu na ndugu yangu Mheshimiwa Zainab waliongelea kuhusu masuala ya Msumbiji na Mtwara. Raia wa Msumbiji wanaoishi katika Mkoa wa Lindi na Mtwara ni wahamiaji walowezi na hivyo kisheria hawana haki ya kupiga kura. Aidha, katika Katiba yetu pamoja na sheria haviruhusu uraia wa nchi mbili, kwa maana hiyo ili kuondoa utata walowezi wote hao wanaoishi bila vibali hawatambuliki. Hata hivyo Serikali inaendelea na zoezi la kuwatambua ili kuweza kuwapatia kibali kinachoitwa Settled Migrants Spars ambapo kitawawezesha kisheria kwa mujibu wa marekebisho ya Kanuni za Sheria ya Uhamiaji ya mwaka 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirudi kwa upande wa NIDA, alisema kwa kuandika Mheshimiwa Upendo Peneza pamoja na ndugu yangu Mheshimiwa Pondeza. NIDA anasema iliandaliwa shilingi bilioni 172 kwa upande wa JKU Zanzibar na Serikali ielezee hili deni litalipwa lini, nimelipokea.

Mheshimwia Mwenyekiti, jambo lingine alilolisema ndugu yangu Jaku, nimuombe wala asishike shilingi, jambo lake tulishalipokea, tumelifanyia kazi kwa kiwango kikubwa. Isipokuwa ni kwamba kiserikali kuna procedure ambazo ni lazima zifuatwe hasa mambo yanapokuwa ya kimalipo. Lazima uhakiki ufanyike na uhakiki ukishafanyika kuna taratibu za kuweza kuanza kulipa. Kwa maana hiyo taratibu ambazo zinahusisha fedha pamoja na kuielewa vizuri hoja yake, lakini lazima taratibu zingine za uhakiki ilikuwa ni lazima zifanyike ndipo taratibu hizo za malipo ziweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuhakikishie kwamba baada ya kuwa taratibu za uhakiki wa malipo, uhalali wa deni zitakapokuywa zimeshafanyika malipo yatafanyika. Yeye nimpongeze kwa kufuatilia kwa umakini na kwa ukaribu hoja zinazohusu wapiga kura wake; na siku akiwa na uchaguzi aniambie tu nitawasemea wapiga kura wake kwamba Jaku anapokuwa Bungeni hana mchezo na akipewa hoja za wapiga kura wake huhakikisha kwamba anazifanyia kazi kwa uzito unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi kama nilivyosema wameandika hoja zao kwa maandishi na hapa tulipo tunazo nyingi sana ambapo ni wengi sana. Kwa mujibu wa kanuni zetu nisingeweza kuwataja mmoja mmoja, lakini niwahakikishie kwamba hoja zenu kwa ujumla wake tumezipokea, tunawashukuru na tunazifanyia kazi na nyingine tutazitolea ufafanuzi kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea pia hoja alizotoa Janet Mbene, tutazifanyia kazi na kuhakikisha kwamba tunatoa majibu. Amesemea ndugu yangu Ritta Kabati suala la gereza nililielezea na wakati ule wala asishike shilingi. Huo ndio uamuzi wa Serikali, mapendekezo hayo aliyoyatoa ndicho tutakachofanya na ameyasema. Ameandika ndugu yangu Oliver tutayafanyia kazi yale yote na wengine wote ambao sijataja ambao wako kwenye orodha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa ufafanuzi wa hoja hizi, naomba kutoa hoja, ahsante sana kwa kunipa fursa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa nami nichangie hoja iliyoko mezani. Kimsingi hoja hii ni ajenda ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tunapojadili hoja hii, tunapaswa kuwa Watanzania ili tuunge mkono jitihada anazofanya Mheshimiwa Rais, kiu ambayo Watanzania wamekuwa nayo kwa siku nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mjadala huu tunaojadili, ukiangalia haraka haraka, unaweza tu ukaingalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, lakini ukaacha kuangalia uamuzi wa makusudi ambao Serikali imeufanya kwa nia njema ya kutekeleza Sera yake ya Tanzania ya Viwanda. Ni bahati mbaya sana Watanzania tulio wengi huwa tunapenda matokeo ya haraka haraka kama ya kamari vile, kwamba unacheza halafu unapata matokeo; kama umepatia, umepatia; kama umekosea, umekosea.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo tunalolizungumzia leo, siyo jambo linaloota kama uyoga, ni jambo ambalo linahitaji utengenezaji wa vitu vingi sana ndiyo matokeo yake uweze kuyaona. Kwa mfano, leo hii tunavyoongea, tangu muda mwingi sana Serikali iliondoka kwenye sera ya kujenga viwanda, lakini leo tunapoongea kwenye Awamu ya Tano, Serikali imeweka mkono wake kwenye kujenga viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatua kubwa na ni utekelezaji wa vitendo wa dira ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati wa Kampeni, wakati wa kuzindua Bunge, lakini pia na kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengine mnasema Waziri anahamasisha, anahamasisha, lakini Serikali ilisema itajenga viwanda; mimi niwakumbushe, Serikali imetafuta dirisha ambalo itaweka mkono wake wa kujengea viwanda. Hivi leo tunavyoongea, Taasisi ama Mashirika ambayo yako chini ya Serikali kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, kwa Dira ya Mheshimiwa Rais, yamebadili mwelekeo ambao yalikuwa yakifanya kwa muda mrefu ambao haijafanyiwa tathmini na ikaingia kwenye utekelezaji wa ujenzi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyoongea, PPF walishaingia mkataba na Magereza wa kufufua kiwanda cha viatu kule Karanga na mwelekeo na maelekezo tuliyoyapata na ambayo tumekubaliana kama Wizara, wateja wa kwanza tutakuwa watumishi wenyewe wanaopatikana kwenye vyombo vyetu vilivyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na tutakwenda na kwenye Taasisi nyingine ambazo wanahitaji viatu hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kwa tathmini ya haraka ni kwamba soko la bidhaa hizo zitakuwepo na hivyo itawezesha kiwanda kuwa endelevu. Maana yake lilikuwepo swali lingine kwamba ni namna gani mtahakikisha kwamba viwanda mnavyovijenga havitakufa? Kwa hiyo, moja ya sifa, utakuwepo upatikanaji wa soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tumeongelea hiki alichotoka kukielezea Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu mambo ya sukari. Ni kweli sukari bei yake imepanda ukilinganisha na miaka kadhaa iliyopita. Hata hivyo, Tanzania siyo kisiwa; panapokuwepo na bei za juu sana kwenye nchi zinazotuzunguka, ni kanuni za kiuchumi kwamba lazima na sisi tutaathirika na bei zitapanda. Ukiangalia kwa mfano, Uganda kwa bei ya Kitanzania sukari inakaribia Sh.5,000/=, ukienda Kenya inacheza kwenye Sh.4,300/= hadi Sh.5,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, kama tuna sukari kwetu huku na wao bei yao iko juu namna hiyo, ni lazima itaathiri bei kwa sababu watu watatorosha. Hatua za muda mfupi na za muda mrefu tunazochukua, kwanza tunakataza utoroshaji wa sukari na nimeelekeza taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani kuchukua hatua kwa wale wote watakaofanya zoezi la kutorosha sukari na kusababisha upungufu na kusababisha madhara ya bei katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijaishia kuchukua hatua za mpito hizo za kuzuia za kuweka doria, Mheshimiwa Rais ameelekeza na dira hiyo inafuatwa na Wizara zinazohusika ikiwepo kinara Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kazi, Wizara ya Mambo ya Ndani; hivi tunavyoongea, ndani ya wiki chache utekelezaji kwa maana ya kupata mtengenezaji wa kiwanda katika Gereza la Mbigili utakuwa umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua za awali sasa hivi za utengenezaji wa mradi huo zilishatekelezwa na kiwanda hicho kitaweza kuzalisha sukari kati ya tani 30,000 mpaka 50,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maelekezo ya Mheshimiwa Rais, haijaishia hapo; kutakuwepo na mradi mkubwa wa Mkulazi ambao tuliuweka kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais na kwenye Hotuba ya Waziri wa Fedha na kwenye Hotuba ya Waziri mwenye dhamana ya Viwanda, katika vipindi vyote ambavyo amekuwa akisemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili unaona kwamba litaenda kutuondolea kabisa upungufu uliokuwa unajitokeza katika eneo hilo na liko katika hatua za mwisho za kwenda kwenye utekelezaji. Maandalizi ya eneo katika utekelezaji huo uko katika hatua za juu kama ambavyo atabainisha Mheshimiwa Waziri mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ambayo ni tathmini ya jumla ya ajenda ya viwanda, wengine walikuwa wanasema kwamba mwekezaji atawekezaje wakati vivutio tumeviondoa?

Waheshimiwa Wabunge, siyo siku nyingi sana kwenye mijadala yetu, ukichukua Hansard za Bunge lililopita, mijadala yetu ilikuwa inajikita kwamba vivutio tunavyovitoa siyo vyenyewe. Kwa kuwa tulikuwa tunasema vivutio tunavyovitoa siyo vyenyewe, sababu tulizokuwa tunatoa ni kwamba baadhi ya nchi bado zinatuzidi kwenye wawekezaji ilikuwa ni aina ya vivutio. Sasa Mheshimiwa Rais amelenga kwenye vivutio vyenyewe ambavyo vinatumika Kimataifa, vinavyoondoa vikwazo kwenye uwekezaji na kuleta sifa halisi ya mwekezaji kuweza kuvutiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya vitu ambavyo vinavutia kwa kiwango kikubwa na Serikali imechukua hatua kubwa, Mawaziri wenye Sekta watasema kwa kirefu, mojawapo ni kasi kubwa inayofanyika kwenye umeme. Mojawapo ni kasi kubwa inayofanyika kwenye barabara; mojawapo ni kasi kubwa ya ujenzi inayofanyika kwenye reli na nyingine ni vita kubwa inayopiganwa ambayo Mheshimiwa Rais ameiishi kwenye maneno na kwenye vitendo ya mambo ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye nchi nyingine utasifia kwamba wamefanikisha mradi kwa haraka, lakini utakuta wametumia vibaya fedha za walipa kodi wa nchi zao. Sisi tunaenda katika utaratibu ambao tunapata mradi ukiwa umejumlishwa na matumizi bora ya fedha za walipa kodi. Kwa mwekezaji yeyote asiye mbabaishaji, atapenda sifa hizo kwamba pana umeme, pana amani, pana muunganiko wa kusafirisha bidhaa, lakini pia pana matumizi bora ya fedha za walipa kodi katika nchi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vyote lazima vitaongeza ufanisi, vivutio vingine ambavyo tulikuwa tunavisema vya rejareja vinatumiwa zaidi na wawekezaji wababaishaji, lakini katika nchi zao ambako na nchi ambako tunatumia kama mifano walikowekeza vivutio vikubwa ambavyo ni standard katika uwekezaji, huwa ni vya aina hiyo na ndivyo ambavyo mwekezaji asiye mbabaishaji angependa avikute katika Taifa husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa dira yake hii na kwenye historia za nchi yetu Marais hukumbukwa watakapokuwa wameshaweka alama. Kwa hiyo, hizi kelele nyingi, miezi mitatu tu baada ya kumaliza awamu zake mbili, watakuwa wakiona mwekezaji mbabaishaji amepewa fursa, wanasema enzi za Mheshimiwa Magufuli hili lisingetokea. Watakuwa wakiona rushwa imetokea mahali wanasema enzi ya Magufuli hili lisingetokea hili, watakuwa wakiona viwanda vinaanza kufa, ama ndege zilizokuwa tano zinaanza kurudi kuwa nne, watasema enzi ya Magufuli hili lisingetokea. Sasa kwa sababu Tanzania itaendelea kuwa chini ya CCM, tuna hakika haya anayoyafanya Mheshimiwa Magufuli yanatengeneza viwanja kwa ajili ya nchi yetu kuweza ku- take off.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Watanzania wote wafunge mikanda, tuiandae nchi yetu, kwa dira ya Mheshimiwa Rais ili tuweze kuiona Tanzania ya viwanda na hiyo ndiyo itakayotengeneza ajira nyingi na sisi tutakuwa wauzaji wa bidhaa na sio waagizaji wa bidhaa kama ambavyo kwa kipindi kirefu tumeishi katika mazingira hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya pacha wangu na huku nikimshukuru kwa kuwekeza kwenye Gereza la Karanga ambako ukiondoa viatu vyako na vya Mheshimiwa Waziri Mkuu, basi humu Bungeni mimi ndio nimependeza zaidi viatu vilivyotoka Gereza la Karanga, vimetengenezwa hapa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kusema machache kwenye hoja zilizojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zimejitokeza hoja takribani tatu ambazo zinahitaji kutolewa ufafanuzi, na mimi nitaenda moja baada ya nyingine. Nikianza na hoja iliyojitokeza kuhusu ununuzi wa magari ya polisi.

Kwanza nishukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kusema hoja hiyo lakini nitoe majibu ya Serikali kwamba jambo hili Serikali inalijua na limeshafanyiwa kazi kwa kiwango kikubwa sana. Niwakumbushie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba kabla jambo hili hata halijatoka kwenye
ripoti hii Mheshimiwa Rais ameshafanya ziara bandarini alishatoa maelekezo na baadhi ya vyombo vinaenedelea kufanyia kazi, kila chombo na nafasi yake ya utaalamu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna timu zinazofanyia kazi upande mmoja tu wa ubora wa magari na hilo ni jambo ambalo na Waheshimiwa Wabunge wamelisemea, hakuna gari bovu litakalopokelewa. Kuna timu inayofanyia kazi kuhusu ubora wa magari, lakini kuna timu ambazo zinafanyia kazi kuhusu masuala ya kiujumla ya kimkataba. Nimpongeze pia Mheshimiwa Naibu wangu Engineer Masauni baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwenye Wizara na yeye alishaenda akiwa na Katibu Mkuu pamoja na IGP. Kuna timu ambayo inaundwa na watu wa kutoka ofisi tofauti tofauti ambao nao wanafanyia kazi jambo hili hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna vyombo vingine ambavyo vinafanyia kazi upande wa kimaadili kama kuna maeneo kama ambavyo Kamati iliweza kusema yanayohusisha mambo ya kimaadili, kuanzia mchakato wa kwanza mpaka ukamilishwaji wake. Jambo moja tu ambalo Kamati ilisema kwamba magari yamelipiwa cash, si cash. Utaratibu unaotumika wa credit export guarantee ni kwamba nchi na nchi zinaingia mkataba, zikishaingia mkataba malipo yanakuwa yanafanywa na yule aliye guarantee mkopo ule, pale ambapo recipient atakuwa amepokea na kukiri kupokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo baada ya units za kwanza kuwa zilipokelewa, mnakumbuka yalikuwa magari takribani 77, ndipo malipo yakafanyika kwa zile units ambazo zilikuwa zimepokelewa. Kwa hiyo si kwamba fedha zote zimelipwa kabla ya magari kupokelewa, si hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kwa ujumla wake kwa hoja zilizojitokeza yale yote ambayo yana makandokando yanafanyiwa kazi na Serikali kwa hatua ya mbele kabisa kabisa katika kuhakikisha hatua hizo zinachukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wabunge mimi niwaombe muendelee kuiamini Serikali, muendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na hakuna kitu ambacho kina ukakasi kitakachofanyika, Serikali iko macho na iko mbele ya matukio kuhakikisha kwamba hatua zinachukuliwa haraka iwezekanavyo pale ambapo panatokea kuna jambo lisilo la kimaadili limefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili limesemwa ni hili la upande wa mkataba wa Vitambulisho vya Taifa, amelisemea babu yangu Mheshimiwa Heche. Niseme tu kwamba taarifa alizozisema si sahihi na kile ambacho kimefanyika. Moja, amesema kwamba mkataba ulibadilishwa na bei ya kitambulisho ikabadilishwa.

Waheshimiwa Wabunge, jambo lilofanyika liko namna hii; ni kweli Serikali ilikuwa na mkataba na kampuni ile ya kutengeneza vitambulisho vya uraia na kulikuwepo na makubaliano ya kimkataba ya malipo pamoja na urefu wa mkataba. Hata hivyo kwa kuwa kuna baadhi ya vitu vilikuwa bado havijakamilika havikukamilika vyote kwa mfano mambo kama ya connectivity mambo ya server, mambo ya integration mmeona mengine yamekuja kuanza kukamilika wakati printing zikiwa zimeshaanza kufanyika, yakiwemo na mambo ya malipo pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kilichofanyika muda wa utekelezaji wa mkataba ulikuwa unafika, mwisho muda wa utekelezaji ulikuwa unafika mwisho. Mathalani tukienda kwa uhalisia wenyewe ulikuwa unatakiwa uishie Septemba 2016. Sasa mwaka 2016 imefika server hazijakamilika zile ID zenyewe raw card hazijakamilika, malipo hayajakamilika. Kilichotakiwa na ambacho kimefanyika ilikuwa ni kuwapa ruhusa ya kuendelea kufanya kazi lakini kwa fedha ile ile kwa makubaliano yale yale kwa gharama zilezile hakukwepo na makubaliano mapya ya bei za vitambulisho wala fedha zingine zaidi ya zile ambazo zilitakiwa zifanyike katika mkataba huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, kama ambavyo nimesema tangu mwanzo na namjua babu yangu Mheshimiwa Heche, tangu akiwa kwenye BAVICHA kule haka kawimbo ka ufisadi kalikuwa kananoga sana majukwaani. Hata hivyo nikuhakikishie tu si kwa awamu hii, Serikali iko macho na inachukua hatua mara panapokuwepo na jambo lenye harufu za aina hiyo na kama kuna mtu anadhani haya ninayosema siyo atasubiri sana. Mimi niwahakikishie Serikali iko macho na wala hairuhusu harufu za aina hiyo ziweze kujitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la mwisho lililoongelewa lilikuwa la passport. Hili na lenyewe taarifa alizozisema sio hizo na mimi niwaaambie kwamba mwanzo upembuzi uliokuwa unafanyika na hatua ambazo zinachukuliwa kabla ya Serikali haijaingilia kati, ukubwa wa mradi ni ule ule na fedha zilizokuwa zinatarajiwa kutumika ilikuwa dola takribani milioni 192; ukiweka na VAT zilikuwa zinaenda kwenye mia mbili plus. Component zile kama ulizosema zilikuwa zile nne.

Sasa hivi tunachotofautisha sasa babu yangu anasema imekuja kufanyika component moja kwa dola milioni 50 si hivyo component ni zilezile nne na kinachofanyika na kilichofanyika jana ni kwamba tunaanza na component ya kwanza, lakini mkataba ambao umesainiwa una component zote nne na ni sharti uanze na kimojawapo ambacho kina uharaka ni dola milioni 57.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatumika kwa component zote. Tunaanza na e-passport tutaenda e-gates, tutaenda e-permit na tutaenda la mwisho ambalo kwa mfululizo ambao sio huu nilioutaja tunatoka e-passport, tunaenda e-visa, tunaenda e-gates, tunaenda e-permit ni dola milioni 57.8. Hii ndiyo tumeshaanza na hicho ndicho kitakachofanyika. Sasa mimi ninayesema ndio Waziri wa Wizara ninyi kama mna retire imprest hapa rudisheni hizo taarifa hizo mnazozitoa si sahihi, hizi ninazosema ndio taarifa sahihi za jambo linaloenda kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Waheshimiwa Wabunge wengine ambao mnajua kazi inayofanyika nitoe wito kwamba sasa mnaweza mkafanya application online mkapata e-passport mtakapoenda Dar es Salaam mtaenda kupiga picha. Hapo hapo unapomaliza kupiga picha ukimaliza kupanda juu unaenda kuchuka passport yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tuko online hapa ulipo unaweza ukaingia kwenye mtandao ukafanya application, ukatuma picha halafu utakapozungukia Dar es Salaam ukapate passport.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wabunge na kwa Mtanzania yeyote ambaye anataka apate passport ya kisasa ambayo inatumika duniani si lazima kusubiri kwanza kile kitabu kingine kiishe hata sasa unaweza ukapata hiyo nyingine na ukaendelea kuitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limefanyika kwa uangalifu mkubwa. Mimi nimpongeze na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha pia kwa kutoa dira nzuri sana ambayo imetuweka kwenye historia nzuri, na jambo hili limezingatia matumizi bora ya fedha za walipa kodi watanzania na si vinginevyo kama ambavyo ndugu yangu alitaka kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge kwenye hizi hoja zilizojitokeza niwahakikishie kwamba hatua thabiti zitachukuliwa pale ambapo Serikali imeshaona kuna jambo la kuchukua hatua, lakini kwa hizi zingine Serikali imezingatia matumizi bora ya fedha za walipa kodi na miradi ambayo imetekelezwa inatekelezwa kwa umakini mkubwa tena kwa ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, passport yetu hii ambayo imeshatoka mtachukua hata nninyi na mtakayechukua Yule atakayesafiri aende aifananishe na ya Marekani, aende aifananishe na ya Uingereza, yetu itakuwa ya kisasa kuliko ya Uingereza naitakuwa ya kisasa kuliko ya Marekani ya sasa.

Ninaamini na wao watataka kufanya za kisasa baada ya kuwa tumeshaenda kwenye teknolojia ya kisasa zaidi na kampuni iliyofanya kazi hii ilishashinda kwenye European union ilikuwa na passport za kisasa kuliko zote kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni kitu ambacho nakisema na ni kitu ambacho ni cha uhakika nakushukuru sana na naunga mkono maelezo yaliyotolewa na Waheshimiwa Mawaziri katika hoja zingine zote, Serikali iko macho, iko macho, iko macho kupindukia na imebeba dhamana ya kuhakikisha kwamba inawafikisha Watanzania kwenye matarajio yao nakushukuru sana asante sana kwa kunipa fursa hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuhitimisha hoja kwa kusemea hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge walizitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme kwamba hatutaweza kuzijibu hoja zote kwa muda huu, lakini Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla wao wametoa hoja nzuri, hoja nzito na sisi kama Wizara zile ambazo zimekaa kwa muundo wa ushauri tumezichukua tutazifanyia kazi na zile ambazo zipo kwa maandishi tutaweza kujibu kwa maandishi. Nia yetu sote ni ya kujenga na tunakubali sana hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na suala la hoja zilizotolewa kwenye upande wa Jeshi la Zimamoto, kimsingi zilikuwa linaongelea kuhusu vitendea kazi na umuhimu wa Jeshi letu hili la Zimamoto. Tumepokea jambo hili na bahati nzuri umelikazia sana jambo hili tungali kwenye Kamati na tumelipokea ndani ya Serikali na tunaendelea kufanya mawasiliano kuweza kuhakikisha kwamba tunakamilisha viporo vile ambavyo ni vya ununuzi wa magari lakini pamoja na maeneo mahsusi yakiwemo ya majengo na kama ambavyo umetoka kusema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale yanayohusu sare za Askari wetu Waheshimiwa Wabunge wamesema kwa hisia tumepokea na tunaendelea kuyafanyia kazi na hatua za mwanzo zimeshaanza zinazohusisha sare ili Askari wetu waweze kupata sare na waweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale yanayohusu kuweka miundombinu ya kisasa ili Jeshi la Zimamoto liweze kufanya kazi hizo na yenyewe tumeendelea kufanya mawasiliano ndani ya Serikali na kuwezesha mazingira yawe rafiki ili Jeshi la Zimamoto liweze kufanya kazi vizuri. Mambo haya yanahusiasha masuala ya ujenzi, masuala ya ujenzi wa miundombinu kama maji pamoja na vitendea kazi vingine ambavyo vinatumika katika masuala mazima ya kazi kuhusu Jeshi letu la Zimamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kutoa elimu na wananchi waweze kutambua kwamba pana mambo ambayo ni ya msingi ya kuzingatia kabla moto haujatokea ama kabla janga halijatokea ambayo yanafanya ufanisi uwe mkubwa punde janga linapotokea tofauti na ilivyo sasa ambapo mambo hayo yasipozingatiwa huwa yanakuja kuleta upungufu katika utekelezaji wake punde janga linapotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili si tu la Wizara wala si tu Jeshi la Zimamoto na wala siyo tu la Wabunge ni jambo la nchi nzima, kuzingatia masuala ya tahadhari kwenye masuala ya moto kabla moto haujatokea ama kabla janga hilo halijatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwa upande uhamiaji jambo hili limesemewa sana na Waheshimiwa Wabunge, tunawapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kutambua kwamba kwanza kazi nzuri inayofanywa na Jeshi letu la Uhamiaji, lakini na kazi nzuri ambazo zinafanywa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma na kila mmoja amekiri kwamba kazi hizo zinafanyika vizuri na niendelee kusisitiza hata Wabunge tusiondoke hapa Dodoma kabla hatujapata passport zetu za kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Waheshimiwa Wabunge ambao tayari wameshapata passport zao, zoezi hili ni jepesi tu ukichukua zile alama asubuhi baada ya nusu saa ama dakika 40 taarifa zote zinakuwa zimeshaingia kwenye mfumo na order ya ku-print inafanyika na kwa mazingira maalum tumeshaliongelea kwa wale ambao watahitaji mazingira maalumu tutayafanya kwa umaalum huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja ambalo niliona nilisisite sana na nilifafanue na nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tuelewane vizuri kwa sababu sisi ndiyoi tunakaa na wananchi ni hili suala la uraia na watu kuhojiwa panapotokea masuala ya passport, licha ya kwamba wapo ambao walishapata passport zilizopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imepita katika hatua tofauti kuhusu utambuzi wa uraia, jambo hili la uraia ni jambo la kisheria siyo jambo la jiografia wala siyo jambo la hisia ni jambo la kisheria. Hata hivyo, kwa wananchi wetu wengi wengi bado tunaenda na jambo la historia pamoja na jambo la jiografia. Hata wengine wapo ambao nimeongea nao mimi mwenyewe wakisema wazazi wangu walizaliwa Tanzania ama wazazi wangu walikuja wakati wa uhuru na wengine wa rika letu wakisema mimi nimezaliwa Tanzania nitakuwaje siyo Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili wala siyo la ugomvi na nitoe rai kwa Watanzania tuelewane kwamba, ni jambo la kisheria na panapotokea mambo yanayohusu sheria ni vema tukafanya marekebisho yake. Jambo hili liko namna hii, mwanzoni tulikuwa na sheria iliyokuwa inatambua mtu aliyezaliwa ndani ya Tanzania kuwa raia wa Tanzania na nadhani kuna nchi ambazo zina utaratibu huo kwamba raia yeyote aliyezaliwa ndani ya jiografia ya eneo husika la nchi hiyo anakuwa raia wa nchi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwenye nchi yetu tulienda hatua zaidi za kisheria ambazo zinamtambua raia wa Tanzania si tu kwa kuwa alizaliwa ndani ya eneo la Tanzania bali awe amezaliwa na mzazi mmoja aliye raia wa Tanzania. Yule aliyezaliwa na mzazi mmoja aliye raia wa Tanzania analazimika na yeye atapofika miaka 18 aweke wazi kama anataka kuwa raia wa Tanzania ama anafuata uraia mwingine ambao ni wa mzazi asiye Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, tuna idadi ya Watanzania ambao katika kipindi fulani waliwahi kuwa na passport za Tanzania. Hata hivyo, sheria ilipokuja kutambua kwamba raia wa Tanzania lazima awe amezaliwa ama na mzazi mmoja wa Tanzania ama wazazi wote wote wa Tanzania wale ambao walishapata hata hizo passport wanalazimika kurekebisha uraia wao ili waweze kuendana na masharti ya kisheria. Ni masharti ya kisheria na sheria tumetunga wenyewe wala Idara ya Uhamiaji siyo iliyotunga na masharti ya sheria ambazo zimetungwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa wale ambao ama wazazi wake walikuja Tanzania na yeye akazaliwa na wazazi wakiwa bado hawajawa Watanzania ana wajibu wa kurekebisha status yake ya uraia ili aweze kuwa raia wa Tanzania wa kisheria. Watu wa aina hii hawana masharti magumu kwa sababu tunatambua kwamba hawana nchi nyingine, nchi yao ni hii kwa maana ya kwamba wamezaliwa hapa hawana nchi nyingine. Tunachofanya ni kuweza kurebisha status zao za kisheri na hata gharama zao ni tofauti na wale watu wanaokuja kuomba uraia wa Tanzania kwa kutokea Mataifa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitoe rai watu wanapoona kwamba kuna jambo la kosoro kwa upande wa masharti haya ya kiuraia wasichukulie kama ni jambo la ugomvi, wachukulie ni jambo la kisheria na wanachotakiwa kufanya ni kupewa ushauri, kupewa mwongozo na wao wafuate mwongozo huo ili kuweza kurekebisha matatizo ya aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo liliongelewa amelisema sana Mheshimiwa Mwilima na ameliongea kwa hisia sana kuhusu masuala ya watu kuhojiwa masuala ya uraia na akasemea sana kuhusu watu wa mipakani. Serikali kwa sasa inafanya zoezi kubwa sana ambalo litaenda kumaliza matatizo hayo ambayo yamekuwa yakiwapata wananchi wa mipakani kwa kutokutambulika ama kwa kupata kashikashi za kutiliwa mashaka. Zoezi la vitambulisho vya Taifa linaloendelea litakapokuwa limemalizika na kila Watanzania wakatambulika tutakuwa tumeshapata jawabu la nani si Mtanzania na nani ni Mtanzania, kwa hiyo na hiyo itaenda kuondoa bughudha hizo ambazo zimekuwa zikijitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge ameileta hoja kwa uzito mkubwa na alishaileta hata Ofisi tumeipokea na tutayafanyia kazi na hasa haya ambayo aliyoyasemea ambayo yanahusu utendaji kazi hasa aliposemea kuwa kuna watu wanadaiwa fedha ili waweze kuandikishwa vitambulisho hivyo vya Taifa. Jambo hilo ambalo halijatolewa maelekezo kwamba wafanye hivyo tunachukulia kama masuala ya kimaadili na tutafuatia nimeshaelekeza timu ya Wataalam, nimeshaelekeza idara inayohusika waweze kufuatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili alilileta Mheshimiwa Mbogo pia kutoa Mkoa wa Katavi pamoja na Wabunge wengine ambao jambo hili lilijitokeza katika mazingira ya aina hii. Ikitokea mmoja mmoja akafanya hivyo siyo maelekezo ya Wizara na wala siyo mpango wa Wizara kufanya hivyo, atakuwa ametokea mtu mmoja akapotoka na sisi wakitokea watu wa aina hiyo tutachukua hatua zinazostahili. Kwa hiyo, tuendelee kuwasiliana, kupeana maendeleo ya jinsi zoezi hili linavyoendelea ili tuweze kulifanya zoezi la ufanisi mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lililojitokeza linalohusiana na masuala ya uraia pamoja masuala ya vitambulisho vya Taifa alilisemea ndugu yangu Mattar Ali Salum, aliposemea kuhusu kitambulisho cha Mzanzibari vis- a-vis kitambulisho cha NIDA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba kitambulisho cha Mzanzibari kinatambulika ni kitambulisho halali kimetumia gharama za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweza kutengenezwa. Wizara idara hizi ambazo ziko ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinafanya kazi kwa pamoja, lakini maelekezo tuliyoyatoa ilikuwa tu ni kwamba maadam kwa Zanzibar uandikishaji wa kitambulisho cha NIDA umeshafanyika kwa zaidi ya asilimia 90 na kwa kuwa taarifa hizo zinasoma upande NIDA pamoja na Idara yetu ya Uhamiaji tuliona tuwapunguzie Watanzania usumbufu wa kutoa taarifa kama tayari walishatoa taarifa, waweze kutumia taarifa hizo ambazo tayari zimeshapatikana ili kuweza kuwapunguzia mlolongo wa kuendelea kuulizwa taarifa zilezile ambazo wameshatoka kuzifanya huku database zetu zikiwa zinasomana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haikuwa nia mbaya ya kutaka kutokutambua kitambulisho cha mkazi ama kutokutambua juhudi ambazo zimefanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, lakini ilikuwa ni kuweza kutumia data ambazo zimeshafanyika. Kwa Zanzibar zoezi la utambuzi na uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa limeshafanyika kwa kiwango kikubwa mno na ndiyo maana tuliona tuanze zoezi hilo la kuanza kuoanisha data ambazo tumeshazipata kwa ajili ya Watanzania wetu, kuliko kila wakati kuwa tunatumia utaratibu wa kuanza kumhoji Mtanzania upya ilihali akiwa ameshatoa taarifa hizo katika ofisi ya Serikali ile iliyo moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Magereza zilijitokeza hoja nyingi, moja zinazohusu mambo ya sare, tayari zabuni ya upatikanaji wa sare imeshafikia hatua za mwisho na inafanyika ndani ya nchi hapa kwenye viwanda vinavyotengeneza majora hapa na hatua zitakazofuata sasa itakuwa ni ushonaji, vijana wetu wataenda kupata sare na baada ya vijana wetu kupata sare tutazingatia pia na suala la wafungwa ambalo na lenyewe lilisemewa kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo niliona niliweke sawa, Mheshimiwa Mbunge nadhani Mheshimiwa Mary Deo Muro wakati anachangia alisemea masuala ya watoto. Ni kweli kuna watoto ambao wazazi wao wanatumikia vifungo mbalimbali, kwa sasa watoto ambao walishachukuliwa na ndugu zao kwa takwimu zilizopo sasa ni sita, watoto walioko magerezani ni kama 45 na wafungwa wajawazito ni 37.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja tu naomba Bunge lako Tukufu lipate kumbukumbu zilizo sawa, hakuna mimba zinazopatikana gerezani. Narejea tena hakuna mimba zinazopatikana magerezani, kuna akinamama wajawazito ambao wamepata ujauzito kabla hawajaanza
kutumikia vifungo, kwa maana hiyo zinafuata taratibu za kisheria, kwanza mtoto akiwa bado mdogo kwa umri ambao akina mama mnajua, analazimika kuwa na mama yake. Akiwa katika umri ambao unamruhusu mtoto kutenganishwa na mama inafuata tu utaratibu kama ndugu atawepo atakayejitokeza kumpokea mtoto yule wanampokea, lakini kama ni upande wa Ustawi wa Jamii na yenyewe anaenda kupokelewa kufuatana na makubaliano yanayokubalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilijitokeza, lilikuwa la masuala ya kulifanya Jeshi la Magereza kujitegemea. Jambo hili Wizara tumepokea ushauri huu na jambo hili tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu alishalitolea maelekezo, tulishakaa tutaanza kwa mfano, kwa Magereza yaliyo na maeneo makubwa kuweza kufanya utaratibu wa kulima kwa kisasa na tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu alishaelekeza utaratibu wa kuyaunganisha matreka utakapokamilika tutaanza na 50 kwa upande wa Jeshi la Magereza ili kuweza kuhakikisha kwamba tunalima kwa kisasa na tunalifanya Jeshi la Magereza liweze kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo haya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyaelekeza kwa uzito mkubwa na mara kadhaa Mheshimiwa Rais ameelekeza kuhakikisha kwamba hatuchukui fedha ambazo zingetumika katika maeneo mengine kwenda kulisha wafungwa na badala yake Jeshi la Magereza lijitegemee na ikiwezekana hata likatoa huduma zinazotokana na uzalishaji wake katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara tumezingatia na tumeshaanza miundombinu kama hii niliyoisemea, tukianza na tunalenga Gereza la Songwe, Kitengule, upande wa Ludewa, Isapilo pamoja na maeneo mengine ambayo ipo miundombinu ya asili ama miundombinu ya awali ambayo italiwezesha Jeshi la Magereza kuweza kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazingatia ushauri ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge kwenye upande wa kuboresha masuala mazima yanayohusu magereza ili tuweze kuhakikisha kwamba tunavuka hatua hii tuliyonayo tuweze kwenda ngazi zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazingatia masuala ambayo yamesemewa ya kiutumishi ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema masuala yanayohusu masuala ya kiutumishi, masuala ya maslahi kwa vijana wetu, tunaendelea kuyafanyia kazi na hii kwa sababu tuna mambo tunaendelea kuyafanyia kazi yatakopokuwa yamekamilika, tutafanya utaratibu rasmi wa kuweza kuliarifu Bunge lako ama kupitia Kamati ili tuweze kuwa na uwelewa wa pamoja kwa jinsi ambavyo tutakuwa tumeshafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni jambo ambalo lina umuhimu mkubwa sana ukizingatia kazi wanazofanya vijana wetu na tunaheshimu kazi wanazofanya, tunaheshimu mchango wanaoufanya na tunaheshimu moyo wao wa kujitoa kwa uadilifu na kwa uaminifu mkubwa katika kulitumikia Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala yaliyoongelewa yanahusu maslahi ya askari wetu haya ni mengi, tutakapokuwa tumeyashughulikia tutaendelea kupeana taarifa ili tuweze kuhakikisha kwamba Waheshimiwa Wabunge hoja zao wanaona kuwa tumezifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilijitokeza Mheshimiwa Maige alisemea kuhusu Muswada wa Ulinzi wa Sekta Binafsi. Jambo hili tumeshalipokea na Serikali imeshafanya nalo kazi kubwa, tayari Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kushirikiana na wadau ilishaandaa rasimu ya mapendekezo ya kutunga sheria na hatua kubwa zilishafanywa kuhusu utaratibu wa rasimu wa kutunga sheria, kwa Tanzania Bara tayari yalishakamilika na maoni ya kutoka Zanzibar yalishakusanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatarajia mpaka ifikapo mwisho wa mwaka huu tutakuwa tumeshafika hatua nyingine ambayo inaelekea kwenye utungwaji wa sheria hiyo ikiwepo kupitia Cabinets Secretariat pamoja na Baraza la Mawaziri ili jambo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amekuwa mdau mkubwa na amekuwa akitoa maoni mazuri liweze kutimia na hatimaye liweze kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka michango mizuri iliyotolewa na Wabunge kuhusu masuala ya magereza Mheshimiwa Omari Kigua, Mheshimiwa Deogratius Ngalawa, Mheshimiwa Maige mwenyewe, Mheshimiwa Maryam Msabaha, Mheshimiwa Rhoda Kunchela, Mheshimiwa Shekilindi, Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko pamoja na wengine wote ambao wameongelea masuala haya yanayohusu masuala ya magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, orodha ninayo ndefu sana ikiwemo Mheshimiwa Amina Makilagi, Mheshimiwa Magdalena Sakaya, Mheshimiwa Zacharia Issaay ndugu yangu wa kutoka Mbulu na Mheshimiwa Zuberi pamoja na wengine, tumepokea hoja zenu zote tutazifanyia kazi, tutachambua moja baada ya nyingine, yale ya kiushauri tutayafanyia kazi na yale ambayo ni maelekezo tutapokea tuweze kuyafanyia kazi kwa sababu ni maoni mazuri na tunaamini yatatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge walilizungumzia sana ni hili la vijana wa bodaboda. Kwanza kuna mambo ambayo sote tunakubaliana. Moja ni kweli, matumizi haya ya bodaboda ama usafiri huu wa bodaboda umetengeneza ajira nyingi sana kwa vijana wetu, hakuna Jimbo hata moja ambalo hawana bodaboda. Katika kuzunguka kwangu kila eneo kuna bodaboda. Kwa maana hiyo ni kweli jambo hili limetengeneza ajira kwa vijana wetu wengi sana hili hatubishani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kweli kwamba jambo hili la usafiri wa bodaboda linaajiri vijana wengi sana na wengine wanafanya shughuli hizi za bodaboda wakiwa wamepata uelewa mdogo sana kuhusu matumizi ya vyombo vya moto. Hili wala hatubishani nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tumeelekeza maeneo yote, mikoa yote kuwapa elimu vijana hawa wanaofanya shughuli hizi za bodaboda, lakini changamoto tunayokutana nayo kwa sababu ni wengi na wanaoingia kwenye sekta hiyo wanaingia karibu kila siku, kwa hiyo hakuna mkoa ambao unaweza ukasema umefanya mafundisho hayo na kuyamaliza kwa sababu wanaingia kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wengine ambao wanaazimana pikipiki ndani ya muda mfupi Wizara tunaendelea kulikazia kwamba jambo hili ni la kijamii wala siyo jambo tu la Wizara na hata Waheshimiwa Wabunge ni vema tukawaambia wananchi wetu kwamba hili ni jambo la kijamii na tukaliongea kama mambo mengine ambayo huwa yana athari kubwa katika jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema yanaathari kubwa kwa sababu ukienda kwenye takwimu ni kweli kwamba vijana hawa wengi wanaumia, wengi wanapata ulemavu wa kudumu, wengi wanapoteza maisha, wengi wanapoteza maisha ya abiria waliokuwa wamewabeba kwa sababu ya haya niliyoyasema ya kujifunza muda mdogo, kutokuwa na uelewa wa matumizi ya vyombo vya moto, kutokuwa na matumizi ya barabara ambapo kuna vyombo vingine vya moto na mambo haya yanasababisha hasara kubwa kwa Taifa letu kwa sababu yanapunguza nguvu kazi za vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja ambalo nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge, kwa yale ambayo yanafanyika kwa utaratibu wa ukamataji ambao unasababisha ajali zingine au unaleta madhara hiyo tutaelekezana ndani ya Ofisi kuweza kuzingatia utaratibu bora wa ukamataji ili kuweza kuwalinda vijana wetu hawa wakati tukiendelea kuwafundisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitoa maelekezo hata nilipokuwa Tanga naendelea kusisitiza pia kwamba vijana hawa wengine wamepata mikopo, lakini pia wanatengeneza ajira. Tumesema kwa wale ambao tunafahamu walipo tusichukue njia ya kuona ni vema pikipiki hiyo ikaozea kituoni kwetu badala ya kuwapa na kuwataka walipe gharama zile ambazo wanatakiwa walipe. Huu ni utaratibu ambao unatumika hata katika nchi zilizoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizoendelea mtu akifanya kosa kama ana gari halazimiki ku-park gari ile mpaka alipe gharama ile anayodaiwa. Anapewa kwamba unatakiwa ulipe gharama hii na anapewa muda kwa hiyo hata upande wa bodaboda nimeelekeza wakishamtambua na kituo chake kinatambulika na kosa ameshaelezwa alilokosea apewe pikipiki yake, aendelee na kazi lakini aelekezwe kwamba unatakiwa ulipe, pia unatakiwa usifanye makosa ya aina hiyo ili kuepuka kugeuza ofisi zetu kuwa ni karakana ama kuona ni vema pikipiki yake ikaozea pale kwa sababu hajaleta Sh.60,000 pikipiki ambayo ilinunuliwa kwa zaidi ya milioni mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunaendelea kuongea na wenzetu wa Wizara ya Fedha kutofautisha faini kwa pikipiki hizi ukilinganisha na magari, kwa sababu kwa kweli kuweka faini ile ile kwa Basi ama Coaster iliyobeba watu 20 ama 30 inavyopita kwenye kosa moja la barabarani utoze faini sawa sawa na pikipiki iliyobeba mtu mmoja ndiyo tunawafanya wale vijana wanashindwa kuzikomboa pikipiki zao na kuzifanya ziendelee kubaki katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja tu ambalo ni vema tu likawa wazi, kuna makosa ambayo pikipiki zile zimebaki kama ushahidi. Kwa mfano, kama pikipiki mtu alibeba watu wa madawa ya kulevya ama watu waliofanya uhalifu wa matumizi ya silaha, ama watu waliofanya ubakaji na makosa mengine makubwa makubwa, ambapo pikipiki hizo zinatakiwa ziende kama ushahidi kwenye taratibu zingine za kisheria, hayo yanatakiwa yaendelee kubaki hivyo hivyo ya ukubwa wa makosa na uhitaji wa pikipiki hizo katika kesi ambazo zinatakiwa zisonge mbele. Kwa yale ambayo tunaweza tukayamaliza kwa kuonyana na masuala ambayo hayakuwa na athari ndiyo hayo ninayosemea, akishajulikana na kituo chake kinajulikana waruhusiwe kuendelea na kazi huku wakiwa wamepewa lini wanatakiwa wamalize kufanya malipo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda upande wa Jeshi la Polisi. Moja ya mambo ambayo yamejitokeza kwa kiwango kikubwa, nikianza na suala la watu kupotea, suala la mauaji, Waheshimiwa Wabunge wameongea kwa hisia kubwa sana. Nikianza na matatizo haya yaliyojitokeza kwa siku za hivi karibuni, nianze kwa kumpa pole sana Mheshimiwa Heche kwa kuondokewa na Ndugu yake na kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wametolea mfano, hatua zimeshachukuliwa kwenye jambo hilo na taratibu za kisheria zitafuata mkondo wake. Nitoe pole pia kwa familia na jamaa wengine ambao wamepatwa ama wameguswa na matatizo ya aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilihakikishie tu Bunge lako Tukufu kwamba panapotokea matatizo ya kiutendaji ya aina hiyo, hayo siyo maagizo na wala siyo maadili ya Jeshi la Polisi, inakuwa imetokea mtu mmoja katika upungufu wake wa kibinadamu anafanya hivyo na akishafanya mmoja siyo maelekezo ya Wizara wala siyo maelekezo ya Jeshi la Polisi na kwa maana hiyo yanapofanyika hiyo ambayo yanakiuka maadili, mara zote sisi kama Wizara na kama Jeshi la Polisi tunachukua hatua kwa wale wanaofanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za aina hiyo kwa watu wanaofanya makosa hilo ni kosa kubwa lililopitiliza, lakini yapo na mengine yanayofanyika ambayo yanatambulika kwamba yanakiuka maadili namiiko ya utendaji wa kazi kila wakati taratibu za kisheria na taratibu za kijeshi zimekuwa zikichukuliwa ili kuweza kauhakikisa kwamba wananchi wananufaika na uwepo wa Jeshi la Polisi na wanafurahia uwepo wa Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mambo mengine yaliyoongelewa, tulitaka kuingia kwenye mtego wa kuona kama vile tuna madaraja ya Watanzania. Ni vema sana Bunge lako Tukufu likaelewa vizuri sana kwamba hapa Tanzania wananchi wote walioko ndani ya mipaka ya Tanzania, kwanza ambalo ni kubwa kuliko yote, tulipozaliwa tulizaliwa wanadamu hilo ni la kwanza. La pili ikafuatia kwamba atakuwa amezaliwa mwanadamu amezaliwa Mtanzania baadae anatambulika anatokea eneo (a), baadae anatambulika anatokea imani (a), baadaye anatokea anatambulika imani ya Chama (a), lakini la kwanza ambalo ni kubwa kuliko yote tumezaliwa wanadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukishazaliwa mwanadamu, damu ya mwanadamu haiwezi ikalinganishwa na gharama ama na thamani ya Chama chochote cha Siasa, haiwezi ikalinganishwa na thamani ya imani yoyote wala haiwezi ikalinganishwa na thamani ya kabila lolote. Kwa maana hiyo, hii dhana ya kwamba labda kuna utaratibu wa watu kutokupewa uzito ulio sawa kutokana na ama vyama vya siasa, ama kabila, ama dini, hiyo dhana siyo njema ikawepo katika nchi yetu. Ni dhana potofu na Serikali tunalinda usalama wa raia wote wa nchi yetu na hivyo ndivyo ambavyo tumekuwa tukifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea haya masuala na huku tukiwa tunaongelea katika kipindi ambacho kuna watu wengine wameguswa na matatizo kama hili tulilosema, ni vema sana tukahifadhi utu ambao unawahusu watu ambao wamepatwa na matatizo ya aina hiyo. Tukijumuisha tu kwamba kuna watu wamepotea, wameuawa, moja siyo dhana sahihi nitawapa sababu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, katika kipindi hiki kuna mambo mengi ya kimaadili ambayo tumeyafanyia msako. Kuna watu wengine hawako kwenye familia zao kwa kukimbia misako ya ushiriki kwenye madawa ya kulevya, wapo ambao tunaendelea kuwatafuta mpaka sasa ambao wapo kwenye orodha ya watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya na wengine tumeambiwa hata wameshavuka mipaka ya nchi yetu. Sasa mtu wa aina hiyo ambaye ameshiriki kwenye madawa ya kulevya, tunamtafuta, amekimbia familia yake, akitokea mtu akisema mtu huyu haonekani kwamba ameuawa na mtu huyu kwamba haonekani kwamba anatafutwa, ukituuliza yuko wapi nasi tunakuuliza yuko wapi tunamtafuta, kwa sababu tunaendelea kufanya msako wa watu wote wanaofanya vitu vya aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, tumefanya msako ya watu ambao wamefanya uhalifu kwa kutumia silaha maeneo tofauti tofauti, tumefanya mapambano hayo. Kuna wengine ambao tuliwakamata wanaendelea kuwataja wenzao waliokuwa wanafanyakazi hizo pamoja wakiwa wanatumia silaha, tumewasaka watu wa aina hiyo na watu wa aina hiyo wengine tunaambiwa wameshavuka hata mipaka ya nchi yetu, wapo watu wa aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama watu wanatumia silaha na wenzao tumeshawakamata na wamekimbia, wametorokea mipaka ya mbali ama wako nje ya mipaka ama popote pale walikojificha, kama tunaendelea kuwatafuta kwa uhalifu huo, ukituuliza kwamba kwenye familia hii huyu mtu yuko wapi nasi tutakuuliza yuko wapi tunamtafuta, kwa sababu wale wote wanaofanya uhalifu nasi tunaendelea kuwatafuta watu wa aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, ukijumuisha tu watu wote wambao hawako kwenye familia zao ukasema wamekufa that is totally wrong over generalization. Kwa sababu hata sasa hivi, Watanzania ambao wako wanashikiliwa nchi zingine kwa kushiriki kwa madawa ya kulevya wako kwenye magereza ni zaidi ya 1,000. Hivi sasa watu wa aina hiyo, familia za aina hiyo, hao watu wao hawapo, wewe ukisema tu kwamba watu wa aina hiyo wameuawa, that is wrong kwa sababu kuna watu wako na makosa mbalimbali, lakini hata ondoka zao wanaondoka kwa njia ambazo ziko tofauti tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, kuna kijana mmoja siku moja nilitembelea gerezani nikaenda kuongea naye akakiri kufanya matukio ya uhalifu, alitaja zaidi ya matukio matano ya uhalifu. Walipochukua silaha Bukombe akasema na mimi nilikuwepo, walipoua Askari pale Sitakishari akasema na mimi nilikuwepo, waliposhiriki matukio ya Mbagala pale akasema na mimi nilikuwepo, akasema lakini naomba kama utanihakikishia niendelee kukwambia, nikamwambia nimekuhakikishia sema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akasema Mheshimiwa mimi nimeshiriki sana haya matukio hata kwenye utekaji wa basi kutoka Itigi kuelekea Makongorosi hadi Mbeya mimi nilikuwepo. Akasema tuliteka Sekenke nilikuwepo lakini akasema Mheshimiwa Waziri jambo moja tu, katika hizi kazi tulizofanya, ilikuwa kila tukifanya shughuli hizo, katika mapambano wengine wanauawa. Akasema mimi mnihakikishie kwamba mtanisamehe, nimeshaacha kufanya hivyo, yuko gerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama watu wengine ambao wako gerezani wanasema mwingine huyu tumefanya naye tukio hapa akauawa, mkija mkauliza tu kwamba kuna watu hawa hawapo, mmeshachukua takwimu za wahalifu? Mmeshachukua takwimu za madawa ya kulevya? Mmeshachukua takwimu za wale ambao tunawatafuta mpaka sasa ambao wameshiriki kwenye uhalifu wa silaha? Mmeshachukua takwimu za wale wengine ambao wamekimbia tu wako kwenye mafunzo ya mambo ya uhalifu katika maeneo mengine? Waheshimiwa Wabunge, ni vema sana jambo ambalo linahusu masuala ya usalama tukayabeba kwa umakini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, IGP, kama tunasema kuna watu tunawatafuta, tunasema kuna watu wamekimbia na tunasema kuna watu wameshiriki kwenye uhalifu na tunasema hakuna mtu ambaye ameuawa, kama kuna mtu anayesema kuna mtu ameuawa ni vema sana akajitokeza akaenda akasaidia jambo hilo kwa sababu mambo ambayo yanatokea ya kiuhalifu tunahitaji kuyashughulikia, kwa sababu kuua mtu asiye na hatia ni uhalifu na kama kuna mtu amefanya hivyo ili tuweze kufanyia kazi mambo ambayo yanahusu uhalifu wa aina hiyo, kuliko kuwa watu wana majonzi halafu sisi tunafanya ni jambo ambalo tunaweza tukajibizana. Hii haiwezi ikajenga jamii yetu, inaweza ikatengeneza uhasama ambao hautalifaa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wengine tukiongelea hawa watu ambao wamekuwa wakitupwa na hawa watu wanaosafirisha watu kwa njia haramu, kuna wengine wana- challenge. Ndugu zangu mnapo-challenge basi muwe na takwimu rasmi. Tumekamata kule watu wakiwa wamebebwa pamoja na mkaa, wame-faint, wakapoteza maisha kule Lituhi na Kitahi, tumekamata watu huku Handeni wakiwa wamechanganywa na cement wame-faint wakapoteza maisha. Tumekamata watu 80 wakiwa wametupwa, actually tumewaokota wakiwa wametupwa kwenye hifadhi kule mpakani mwa Tanga na Bagamoyo. Polisi na Magereza wamelazimika kuwatengenezea uji mwepesi ili wapate fahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu kwa sababu wakichoka wengine wanawatupa ili safari iendelee. Kama wanaweza kutupa watu 80, hivi mpaka watu 80 wa-faint kwa nini huwezi ku-suspect kwamba inawezekana walishatupa wengine ambao walipoteza maisha? Kwa nini sisi tunafurahia sana kujengea taswira nchi yetu kwamba kuna mambo mabaya yanafanyika kuliko kuona na tunabisha ambayo yanaonekana, interest yetu ni ipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani haya yote yanayotokea Waheshimiwa Wabunge hatuoni kwamba inaweza ikawa moja ya jambo na tuhamasishe ama tuhimize jambo hili udhibiti ufanyike kwa kiwango kikubwa zaidi kwa sababu unachafua taswira ya nchi yetu, sisi tunatamani yale ambayo yana taswira kwamba yanaweza yakawa yana reason kwamba siyo hayo, tunatamani yale yanayochafua nchi yetu, tunanufaika na nini ikiwa hivyo? Hivi nani ananufaika ama nani anafurahia ikionekana kuna Watanzania wanauawa, Watanzania wauawe ili tunufaike na nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, Waheshimiwa Wabunge ni vema sana na ni afya sana kwa Taifa letu tunapoongelea mambo haya makubwa tuwe na vivid evidence na kama tuna vivid evidence tu-report kwenye chombo kilicho rasmi ili taratibu ziweze kufanyika. Sasa mtu akikataa akasema wale waliookotwa walikuwa ndugu wa hawa watu, tunawaambia basi kama kuna ndugu wanahisi wale walikuwa ndugu zao kila mwili uliookotwa tunachukua DNA ili kama kuna mtu atajitokeza afananishwe na yule mtu aende kwenye DNA ili afananishwe hivyo ndivyo tunavyofanya. Sasa wewe kama watu wanaelekea kuharibika unataka tufanyeje? Tuwahifadhi Ofisini? Tunachukua DNA halafu ndiyo tunawazika hivyo ndivyo duniani kote wanavyofanya ili ikitokea mtu akafanya claim iweze kufananishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, niwaambie tu jambo moja, siyo jambo zuri sana kujadiliana ama kutolea mfano watu ambao wako kwenye majonzi lakini ilishatokea mifano ya watu ambao wametaka kufananisha DNA na jambo hilo likafanyika na vipimo vikaonesha, sasa kwa nini tunang’anga’na tu kutaka kulazimisha yale ambayo kuna Mataifa wangetamani anyway iwe hivyo nasi tunatamani yawe yale, tuna interest gani kwenye hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge kwanza tunapojadili jambo la aina hii twende kwa tahadhari lakini kama tuna mtu ambaye ana taarifa za mambo haya specific issues tusaidiane ili tuweze kuisaidia jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa sababu kengele ilishagongwa, lilijitokeza suala la maagizo. Kama kuna mtu ana maelekezo yaliyo tofauti atayafikisha kama Waziri wa Nchi alivyosema, lakini mambo yanayohusu Wizara ya Mambo ya Ndani kama kuna Mbunge hajapata kibali, alitoa taarifa ya kufanya jambo lake hakupata kibali, taratibu zinasema ana-appeal kwa Waziri. Kama kuna jambo linahusu uraia wa mtu yeyote ama jambo lolote linalohusiana na uraia anayetoa uraia ni Waziri. Kama kuna jambo la mtu kuondoshwa nchini anayeondosha watu hao ni Waziri, sasa mnatafuta juu ipi? Juu yenyewe ndiyo hii!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna jambo unakutana nalo ukiona OCD akasema limetoka juu na yuko Wizara ya Mambo ya Ndani, RPC akasema limetoka juu na yuko Wizara ya Mambo ya Ndani wewe tuko wote hapa mara zote, Mbunge mwenzangu na mimi ndiyo niko juu sasa si useme kuna jambo liko hapa. Nimeshafanya mambo ya aina hiyo ambayo yalijitokeza katika maeneo husika nimeshafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja nitoe mfano tu, kuna siku moja Mbunge wa Viti Maalum, Njombe, Diwani wake alikuwa na mkutano pale yeye wakamwambia hatakiwi kuhutubia, Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge anayetambua juu akaniambia Mheshimiwa Waziri, mimi ni Diwani katika Manispaa hii kuna mkutano wa Diwani mwenzangu hapa na niko Mkutanoni nimezuiwa kuongea. Nikawaambia mkutano ule ni wa nani? wa Diwani wa CHADEMA na yule Mbunge ni wa Chama gani? Ni Mbunge wa CHADEMA, kuna jambo lolote la kiusalama hakuna! Nikawaambia basi mwacheni aongee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine lilitokea la misinterpretation mkoa mmoja, Maaskofu waliandaa kongamano lao, wanafanya kongamano lao wameshaweka vyombo pale wameshaweka maturubai, wameshaita wahubiri wao kikatoka kibali wasifanye mikutano, nauliza kwa nini, yule mmojawao pale akaja juu kwangu, nilivyouliza kwa nini mmewazuia, wakasema unajua Mheshimiwa Rais amezuia mikutano, nikawauliza amezuia lini? Kwa hiyo nikawaambia waruhusuni waendelee na mikutano yao. Sasa wewe ukishapata jambo hilo ukatulia tu na huku tuko wote siku zote hapa, unatafuta kutengeneza taswira ya juu yako unayoielewa, huo siyo utaratibu wa Kiserikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twendeni kama tuna hoja tusaidiane, wala msitafute juu wala msitafute taswira, hapa tuliko hapa juu zote ziko hapa, mbona mambo mengine mkiyapata hapa mkitoka kwa Waziri mnaenda juu nyingine iko hapa hapa? Kwa nini tunataka kutengeneza na yenyewe iwe story. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge hoja nyingine mlizosema za ufanyaji wa kazi za Kibunge Wabunge wote ni daraja moja, kazi za kibunge Wabunge mnatakiwa kufanya kazi za Kibunge, tusichanganye taratibu, tufanye kazi za Kibunge kwa taratibu na wala tusitengeneze ajenda ambazo zinatugawanya badala ya kutuunganisha kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii naomba sasa kutoa hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kuhitimisha Hoja niliyoitoa hapo tarehe 8 Februari, 2021. Awali ya yote, nikupe pole wewe mwenyewe pamoja na Mheshimiwa Spika na sote hapa Bungeni kwa ajili ya kuondokewa na mpendwa wetu ambaye tumekuwa naye muda wote hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kusema hapo tarehe 8 Februari, 2021 niliwasilisha katika Bunge lako Tukufu Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 hadi 2025/ 2026, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa ya Mwaka 2021/2022 na Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti kwa Mwaka 2021/2022 ambapo Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuyajadili kwa siku takribani tano na kuiwezesha Serikali kupata maoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru sana wewe binafsi pamoja na Mheshimiwa Spika kwa kuendesha mjadala huu kwa ustadi mkubwa ambao tunauhitimisha hii leo. Aidha, napenda kuchukua fursa hii pia, kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini, kwa maoni na ushauri mzuri walioutoa kwa ajili ya kuboresha mapendekezo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa ufafanuzi walioutoa pamoja na michango ambayo wametupenyezea ya kuendelea kuboresha mpango huu, nikitambua mchango wa Naibu Waziri aliyeleta mapendekezo kuongeza masuala yanayoongelea upande wa watu wenye ulemavu. Aidha, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango waliyochangia na hadi sasa imefikia Wabunge 164 waliochangia; kati yao 153 wakiwa wamechangia kwa kuzungumza na 11 wakiwa wamechangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba, kusudi la mjadala huu ilikuwa ni Wabunge waweze kutoa maoni yao, ili tuweze kuboresha mapendekezo haya na sisi kwa niaba ya Wizara tuseme tumeyapokea, kwa niaba ya Serikali tuseme tumeyapokea. Yale ambayo moja kwa moja yataenda kuboresha Mpango tutayafanyia kazi kwa namna hiyo na yale ambayo yanahitaji ufafanuzi mengine tutafafanua hapa na mengine tutaleta kwa maandishi kwa kuzingatia kwamba, michango imekuwa mingi san ana michango mingi imekuwa na manufaa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie kwa kufafanua michache tu ile ambayo inahitaji ufafanuzi na ile yote ambayo inaboresha Mpango na mapendekezo haya tutaenda kuitumia kwenye kupendekeza, ili tuweze kuleta tena, kama taratibu za kibunge zinavyosema. Moja ya hoja ambayo ningependa sana kuitolea ufafanuzi ili kuweka kumbukumbu sawa ni ule mjadala uliokuwa unahusisha masuala ya tafsiri ya uchumi wa kati, maana yake na kwa mwananchi mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ilikuwa inatolewa hoja kana kwamba, kipato kile kilichopimwa ni kidogo sana, lakini lingine ilikuwa inatiliwa mashaka tu dhana yenyewe ya kwamba, tuko uchumi wa kati. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, kwanza utaratibu wa kuingia uchumi wa kati ni utaratibu ambao unazingatia vigezo. Tanzania kuingia uchumi wa kati haikutuma maombi kwamba, tunaomba na sisi tuingie tuwe nchi ya kipato cha kati. Hatukufanya application na wala Tanzania kuingia kipato cha kati haikulipia, ni tofauti na utafiti unaweza uka-commission team kwamba, nifanyieni utafiti huu mniletee ripoti; hatukulipia kwamba, tunalipia ili mtufanyie utafiti mtuambie kama tumeshafika uchumi wa kati ama la. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ni jambo linalozingatia vigezo tena vigezo vyenyewe vimezingatiwa na taasisi kubwa zinazoheshimika duniani, World Bank, IMF na wachumi wote ambao wameitangaza Tanzania kwamba, ni ya uchumi wa kati wala sio washabiki wa CCM. Ni taasisi za wasomi waliobobea na hawajaanza kwa kuitangaza Tanzania, zipo nchi ambazo ziliwahi kufika kule na zimefika kule kwa kuzingatia vigezo. Vigezo vyenyewe hata hapa sisi ukianza kuangalia tangu tumeanza kutekeleza Mpango mpaka tumefika hapa ni vigezo ambavyo tofauti zinaonekana na vigezo hivyo kwa yule ambaye ataifanyia tathmini Tanzania yetu kiungwana, lazima atafikia katika majawabu ya aina hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale waliokuwa wanasema kiwango chenyewe kile tulichofika ni kidogo sana, kwanza hawaitendei haki nchi yetu na pili hawamtendei haki Rais wetu, kwa sababu, tulitarajiwa tufike by 2025 tumefika mapema kabla ya muda ule. Tumefika mapema kabla ya muda ule kwa sababu ya ujasiri na uthabiti wa Rais wetu kwamba, kuna mambo ambayo yametekelezwa kwa kasi kubwa na kwa kiwango kikubwa kuliko ambavyo yalikuwa yakitekelezwa kwa muda mrefu tangu tumeweka mpango ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ukiangalia vigezo ambavyo huwa vinatumika, pato la mtu mmoja mmoja kufikia wastani wa dola za Kimarekani 1,036; la pili, kupungua kwa utegemezi wa bajeti na kuongeza fedha kwenye matumizi ya huduma za kijamii. Mengine ni kuboreshwa kwa miundombinu katika nchi husika. Ukienda kwenye wastani ambao waliutumia na ndio wakatoa majawabu yale, utaona kwamba, wastani wa pato la mtu mmoja mmoja GNI per capita uliongezeka kutoka Sh.990,462 sawa na dola za kimarekani 980 kwa mwaka 2015 hadi kufikia Sh. 2,577,967 sawa na dola za kimarekani 1,000,080 kwa mwaka 2019, hivyo, kuvuka kigezo kile kilichowekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kupungua kwa utegemezi wa kibajeti. Ninyi wenyewe ni mashahidi, kama ninyi mnasema wale watu wamesema tu kama na Benki ya Dunia na IMF imeshakuwa umoja wa vijana na wengine UWT, angalieni ninyi wenyewe utegemezi wa bajeti ulivyopungua. Mwaka 2015/2016 bajeti yetu tuliyokuwanayo ilikuwa takribani trilioni kama 22 hivi, hivi tunavyoongea tumeshavuka trilioni 34 na utegemezi umepungua zaidi, lakini si hayo tu ambayo tunayataja kwa bajeti kwa ujumla wake, nendeni mkaangalie sasa kwenye huduma ambazo wao ndio wanapima ambazo zimetuvusha kwa kiwango kikubwa, nendeni mkaangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye afya, katika miaka mitano takribani trilioni moja imeenda kujenga vituo vya afya vile na imetengeneza wastani wa kila tarafa ina kituo cha afya ambacho kinaweza kikatoa huduma kwa akinamama, kwa watoto, theatre, maabara, pamoja na vitu vingine vyote vya muhimu vinavyotakiwa. Ukienda kwenye umeme zaidi ya vijiji 10,000 vimewaka, ndani ya miaka mitano na zaidi ya trilioni tatu zimekwenda tena ni fedha za bajeti yetu. Ukienda kwenye miundombinu ambayo na yenyewe ni msingi mkubwa wa kujenga uchumi unaojitegemea, zaidi ya trilioni 8.6 zimekwenda kutengeneza miundombinu ya aina hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye utawala bora karibu trilioni moja. Ukienda kwenye usafiri wa majini karibu trilioni moja. Wewe unayepinga kwa nini unaona sifa kuitwa maskini? Yaani wenzako wamekuangalia wakaona wewe umeshaondoka kwenye umaskini, wewe unajisikia bora zaidi wakuone wewe ni maskini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, angalia nchi inayoweza kutoa bilioni 24 kila mwezi kupeleka elimu kwa watoto wake na haijakwama. Angalia nchi inayoweza kutoa takribani bilioni 700 kulipia watoto kwenye elimu ya juu, tunaita mikopo, lakini kimsingi ni bajeti ya Serikali kwa sababu, hawakopi benki hawa ni bajeti ya Serikali. Mambo mengi yamebadilika, hata jana tu simba kushinda kule ni uchumi wa kati, ndio maana hawakuwahi kushinda siku zilizopita, viwango vyao vilikuwa vya kiuchumi wa kati. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokisisitiza kwamba, vigezo vyote ambavyo nchi ya uchumi wa kipato cha kati inatakiwa kufika, Tanzania imevifikia na tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ya uthabiti wake tumeweza kuyafikia haya na wale wapiga ramli wanaosema hatutaweza, niwaambieni tunasonga mbele haturudi nyuma, tunakwenda Kaanani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni mazoea, mtu aliyezoea sana kuitwa maskini, aliyezoea, bado anahitaji tiba kwenye mindset kuona kwamba, yeye hayuko kwenye umaskini. Ni kama kuku aliyefungwa miguuni muda mrefu, kuku aliyefungwa miguuni muda mrefu hata ukimwondolea kamba anaendelea kuegama hivyohivyo akidhania bado amefungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wengine wakiambiwa ni wastani wa pato la Taifa limegawanywa kwa uwiano wa wananchi waliopo wanadhani pakigawanywa hivyo kila mtu anapelekewa fedha nyumbani; kwa sababu, tunasema tunagawanya pato, wanadhania wataletewa kila mmoja nyumbani. Si hivyo, huu ni wastani na kama wewe hautashiriki kwenye kuzalisha, kama wewe hautafanya kazi ni dhahiri hautapata hela, kwa sababu, haujazalisha. Wewe ambaye hufanyi kazi na hupati hela ndiye unayetuchelewesha tusiende kwenye takwimu kubwa zaidi ile ambayo tunatakiwa tuifikie. Huo ndio utaratibu na hivyo ndivyo uchumi unavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wengine wanawaza changamoto tu za maisha kwamba, sasa hivi mambo mengi ambayo ni ya kimaendeleo ndio yanatufanya tuwe na matumizi mengi, ndio inafanya wachukulie kwamba, huo ndio ugumu wa maisha. Hebu fikirieni zamani kabla ya changamoto za maendeleo bajeti zilikuwa zinaenda wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hatukuwa na simu, kwa hiyo, hakukuwepo na mambo ya simu yenyewe, air time, wala MB. Tulikuwa tunakula chakula kilichosagwa kwenye jiwe na mama zetu na dada zetu waliokuwa wanasaga tulikuwa hatuwalipi, tulikuwa hatutumii gharama ya kwenda kulipia mashineni. Tulikuwa hatuna umeme kwa hiyo, tulikuwa hatuunganishi hatuna gharama ya umeme, tulikuwa hatuna TV, hatuna ving’amuzi. Tulikuwa tunachota maji kwenye madimbwi, tulikuwa hatulipii, sasa unatakiwa ulipie na bili ya maji na umeme. Tulikuwa tunalima tu ardhi ina rutuba kwa hiyo, tulikuwa hatutumii mbolea tunatumia samadi, hatutumii mbegu tunaanika tu mbegu zile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, sasa hivi hizi changamoto zote ambazo ndio maendeleo yenyewe zimesababisha bajeti constraint, yaani fedha yako ile igawanyike kwenye matumizi mengi, hiyo ndio tunaenda kusema hakuna maendeleo ni maisha mabaya. Ni tafsiri mbaya na wengine waliokuwa wanatafsiri walikiri wenyewe, nilimsikia Mheshimiwa Halima akisema kama bajeti hii imeandikwa na Dkt. Mpango Gwiji wa Uchumi ambaye anatambulika na Benki ya Dunia na IMF na vyuo vyote vya duniani, yeye ni nani hata aseme lingine?

Mheshimiwa Naibu Spika, alikuwa anawaambia kwa lugha nyingine kwamba, yale anayoyasema yeye kwenye area hii yapuuzeni haelewi kitu. Ukweli ni haya ambayo yameandikwa kitaalam na ninyi mnatakiwa mwelekee katika mwelekeo wa aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hii ya Stieglers Gorge kule ambayo ilikuwa inasemwa, Mwalimu Nyerere Power Station; watu wanaenda kusema tu kwenye asilimia eti ni asilimia 25 tu, hata reli ya kati wanasema eti imeshajengwa tu ni kiwango hiki hapa tu. Fuatilieni hata historia, reli ya kati hii hapa ilijengwa kwa takribani miaka 10. Tena kipindi hicho hakukuwepo na fedha zinazokwenda kwenye elimu bure, hakukuwepo na fedha zinazojenga hospitali nyingi hivi, hakukuwepo na fedha zinazojenga lami kilometa 13,000, hakukuwepo, hata population yenyewe iliyokuwa inahudumiwa na Serikali ilikuwa ndogo tu, lakini leo hii ukianzia kule kilometa 300 za kwanza ni aslimia 90. Hata kile ambacho kinachelewesha ni utaratibu wa kujenga kwa uimara zaidi, lakini mambo yote yameshakamilika mpaka mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Stieglers Gorge hivyo hivyo, Mwalimu Nyerere Power Station ile, wanasema ni asilimia 25 tu, lakini nendeni mkaangalie fedha iliyowekwa pale ni trilioni 1.9. Kwa hiyo, vingine ni kiutaratibu kwa sababu, hatupimi kwa kumwaga tu fedha, kuna shughuli zinafanywa tena kwa uthabiti mkubwa. Haya ni mambo ambayo napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na wale wasioyapongeza haya, watoto wao watakuja kuwasuta kwamba, aliwahi kupita Rais mmoja akiitwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alifanya mambo makubwa haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo liliongelewa sana lilikuwa hili jambo la matumizi ya kutumia task force kwenye makusanyo ya mapato. Kwanza Waheshimiwa Wabunge niwaombe sana kwenye hili jambo tunapoliongelea hili la makusanyo tunatakiwa twende kwa tahadhari sana. Mwenzenu nina kumbukumbu nzuri kabisa kwa sababu, niliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha wakati awamu inapita inamalizikia na Awamu hii ya Tano inaingia; natambua kazi kubwa waliyofanya Serikali ya Awamu ya Tano kwenye mambo ya makusanyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kipindi tumekipita ambacho ulipa kodi, elimu ya mlipa kodi, uhiari na uzalendo, lilikuwa jambo kubwa na gumu sana kwa watu wetu, kwa walio wengi, hasa wafanyabiashara wakubwa, hasa walipakodi wakubwa. Ukwepaji wa kodi, nendeni mkafuatile Hansard za Bunge lile lililopita, fuatilieni Hansard muone kilio kikubwa kilikuwa wapi? Kilio kikubwa kilikuwa walipa kodi hasa wakubwa hawalipi kodi ipasavyo; walipakodi waliokuwa wanabeba nchi ni watumishi wa umma kwa kiwango kikubwa na walipakodi wadogowadogo na baadhi yao walipa kodi wakubwa waliokuwa waaminifu, kulikuwepo na kiwango kikubwa sana cha ukwepaji wa kodi, kikubwa mno na kulikuwepo na Serikali bubu, Serikali ikipanga namna ya kukusanya kodi kulikuwa na reaction ya Serikali moja bubu; ipo kule tu yenyewe ipo tu, mkipanga bajeti ina-hire ndege inakuja, hii haitatekelezeka, ilikuwa namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujasiri wa Rais wetu pamoja na ubunifu wa Waziri wetu katika kumsaidia Rais pamoja na timu yake ya wataalam wakiwepo TRA wamepiga hatua kubwa sana. Sasa, sasa hivi hili jambo linaloanza kujitokeza la kwamba, task force ndio zinakusanya na TRA imeacha majukumu yake, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba, TRA bado wanaendelea kukusanya mapato wao wenyewe. Pale ambapo inatokea task force inakusanya kunakuwepo na hatua zinazofuatwa. Moja, kunakuwa na taarifa kwamba, kwa mlipakodi huyu kuna viashiria vya kutokulipa kodi ipasavyo. Baada ya hapo kunatumwa timu ya kwenda kukagua, timu ya kawaida tu ya kwenda kukagua ambayo ni Mamlaka ya Mapato, ni wataalam wao. Wakishakagua wanaambizana, wanaelekezana kwa mujibu wa sheria, sheria zetu mlipakodi mnajadiliana katika yale makadirio, wanakubaliana na wakati mwingine wanasainiana, inatokea hataki kulipa ama inatokea amekata rufaa. Hili lilikuwa linatumika sana miaka kadhaa ile iliyopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwa mtu akiona anataka kudaiwa kodi anaenda anai-park mahali pale panaitwa appeal, ana-park mahali hapo halafu maisha yanaendelea. Akitoka hapo anaipeleka tribunal ana-park hapo maisha yanaendelea. Sasa inatokea uamuzi umeshafanyika kwamba, anatakiwa alipe ama inatokea pana taarifa zinazoonesha kuna ukwepaji mkubwa, hapo ndipo kwa kukwepa, kwa kuondokana na uwezekano wa kufanya kazi kwa mazoea, kwa kukwepa na kuondokana kwa uwezekano wa vitendo vya rushwa kuweza kutumika katika masuala haya ya ku-bargain rushwa, ya ku-bargain fedha za kodi, timu maalum inapelekwa na Kiingereza chake ndio hiyo inaitwa task force ambayo kiongozi wao anazingatia ile miiko ambayo inatakiwa itumike katika kukusanya kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata Bunge lako tukufu lilikuwa likisisitiza panapokuwepo na operation isiende taasisi moja wala asiende mtu mmoja, ndio tunavyotumia hata kwenye operation zingine, tunatengeneza team ambazo ni multidisplinary ili kuweza kuchangia uzoefu, lakini pia na kuzingatia maadili ya kwenda kufanya jukumu lile pasiwepo na rushwa, pasiwepo na uonevu, lakini pia pawepo umakini mkubwa zaidi katika jambo lile. Hicho ndicho ambacho kimekuwa kikifanyika katika jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amelisisitiza sana jambo hili kwamba mara zote mfanyabiashara anayefanya kazi zake ama biashara zake ambazo zimenyooka asibughudhiwe, ameshawaambia hata wafanyabiashara wenyewe kwenye vikao vile, ameishaielekeza Wizara, ameshawaelekeza Mamlaka ya Mapato, wazingatie miiko hiyo. Kinachofanyika ni pale panapotokea sasa kuna watu wasiozingatia taratibu wa kulipa kodi, panapotokea watu wanakwepa kodi, panapotokea watu wanafanya njama na njama ziko nyingi sana za kukwepa kodi. Ndio Kamishna wa Mamlaka ya Mapato kwa kutumia sheria inayomruhusu kutengeneza kikosi kazi kama ambayo mnajua, Sura ya 348 ya Sheria ya Utawala wa Kodi inampa mamlaka Kamishna kuunda vikosi na kushirikisha taasisi zingine za umma, Kifungu cha 64 vifungu vidogo mpaka 67 vinampa mamlaka ya kutengeneza vikosi kazi ambavyo vinaweza kwenda kusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge kwa mazingira haya kwamba tuna miradi tunatekeleza, kuna wengine wasiotutakia mema hata wasingependa tutekeleze, hatuwezi kutekeleza kwa kuomba hela, hatuwezi kuitekeleza kwa kukopa mikopo ya kibiashara halafu tukatekeleza miradi mikubwa ya kiwango hicho, lakini pia hatuwezi tukatekeleza hata hii miradi mingine yote hii tunayoitekeleza bila kuzingatia suala la kulipa kodi. Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania wote tuendelee kujenga uzalendo kwa Taifa letu, maendeleo yetu yatakuja kwa sisi kulipa kodi. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na timu yake pamoja na TRA waendelee kufanya kazi kwa kuzingatia maadili pamoja na miongozo ambayo inawaongoza katika kutekeleza majukumu yao hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutoa rai kwa Watanzania tulipe kodi na kwa wale ambao walizoea kukwepa kodi kuwaachia mzigo watu wengine na kupata mapato hayo ambayo yalitakiwa yakasaidie huduma za jamii wakayageuza yawe ya kwao, niwahakikishie mazingira ya yao kufanya ukwepaji wa aina hiyo yataendelea kuwa magumu tu, kwa mtu anayepanga kufanya biashara kwa kukwepa kodi mazingira hayo yataendelea kuwa magumu tu kwa sababu haturudi tena kule, tunataka tujenge utamaduni wa watu kulipa kodi kwa sababu hiyo ndiyo inayotufanya nchi yetu iweze kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Wabunge wenzangu wa CCM Watanzania wengi hawakumchagua Rais kwa sababu ya rangi ya nguo aliyovaa, walimchagua kwa sababu wameona miradi hii iliyotekelezwa haijawahi kutekelezwa kwa kiwango kikubwa cha kiasi hiki. Mtu yeyote akitushauri tuache kujitegemea, mtu yeyote akitushauri tuache kutekeleza miradi, tunatakiwa tuchukulie huyu mtu anataka kutukwamisha kwenye nia yetu hii ya kuwatumikia Watanzania na Ilani yetu tuliyoitengeneza ya mwaka huu ni kubwa kuliko ile ambayo tuliitengeneza kwa wakati ule. Nini kinachowauma wengine huku ni uchache wenu, mmejua tumefanya makubwa tumeingia wengi kwa sababu ya ushindi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo ningependa nilifafanue kuna hoja ilitolewa kuhusu mfumuko wa bei hii na yenyewe niliona ilikuwa ina misinterpretation ina tafsiri ambazo zinakinzana. La kwanza, mfumuko wa bei siyo bei, inflation rate is just a rate is percentage rate showing how quickly the prices are changing.

WABUNGE FULANI: Kwa Kiswahili.

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mfumuko wa bei ni kile ile kasi ya kile kiwango cha bei zinavyobadilika, siyo bei zenyewe. Ukienda tu ukasema mimi jana nimeenda nikakuta bei imeshakuwa hivi, bei iko hivi, ukilinganisha na ya mwaka jana ama ya mwaka juzi, sijui wengine wanachukuliwa ya mwaka gani, ule si mfumuko wa bei, zile ni bei na bei zingine zinatokana na seasonalities, ni kubadilika kwa majira. Kwa mfano bei ya alizeti wakati wa mavuno na bei ya alizeti wakati ambao siyo wa mavuno, ni vitu tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo unailinganisha tu mavuno ya mwaka jana na mavuno ya mwaka huu yalikuwaje na mmevuna kwa kiwango gani. Kwa mfano mwaka ule uliokuwa na mafuriko makubwa sana umeathiri kilimo, kwa hiyo kuna baadhi ya mazao yanayotokana na kilimo cha aina hiyo kama dengu, maeneo yale yaliyokuwa yanalimwa ikitokea pamekuwa na mafuriko kote hayajatoka vizuri, definitely mwaka kama ule karibu na kilimo kingine kutakuwepo na tofauti ya bei. Ttunachokisemea kama Serikali ni kwamba ile kasi ya kubadilika kwa bei kwa mazao yaliyo mengi na kwa bidhaa zilizo nyingi zinazotumika kwenye viashiria, kwa kipindi chote hicho imekuwa imara. Hicho ndicho tunachopima kwenye mfumuko wa bei na hatufanyi mfumuko wa bei uwe imara kwa kutumia Jeshi wala Polisi, tumetengeneza miundombinu ambayo inafanya ule uimara wa bei katika bidhaa hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, wale waliokuwa wanabeba vitunguu kutoka Manyara kuleta Dodoma kabla ya miaka mitano walikuwa lazima wazungukie Singida waje hapa. Wale waliokuwa wanabeba bidhaa kutoka Mbeya, Njombe, Iringa kuleta Dodoma ilikuwa lazima waende Morogoro ndiyo walete hapa. Kwa kutengeneza miundombinu inayopunguza gharama za uzalishaji na gharama za usafirishaji, kunatengeneza bei ziwe imara, zikishakuwa imara hicho ndicho tunachokipima kwa sababu zinasawazisha kutoka kwenye wingi kwenda kwenye upungufu, hiyo ndiyo mikakati na ndiyo maana tunasema miundombinu hii inaenda kumsaidia mwananchi moja kwa moja kwenye maisha yake. Hili limekuwa likifanyika, kwa hiyo tusije tukachukulia kwa dhana finyu ambayo inawaletea hamaki wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nimeisikia kengele imegonga, niende hoja moja ya mwisho wakati namalizia malizia. Lingine ambalo lilijitokeza kwa kiwango kikubwa lilikuwa suala la deni la Taifa. Nishukuru na nipongeze hoja ya Kamati wameleta kiashiria kile walichokisema cha kuangalia mapato, hicho huwa kinatumika tunapoangalia masuala ya ndani, lakini kwenye vigezo vile vinavyotumika ambavyo ni standard na vimewekwa standard ili uweze kulinganisha na maeneo mengine, niwatoe hofu kwamba uchambuzi wa deni la Taifa unatumia model ambayo ni ya Shirika la Fedha la Dunia na viashiria vyote vinaonesha deni ni himilivu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, deni la nje kwa pato la Taifa ukomo wake huwa ni 55%, sisi tuko 17.3%. Thamani ya deni la nje kwa mauzo ya bidhaa na huduma za nje ya nchi ukomo wake huwa ni 240%, sisi tuko 113.2% tu. Uwiano wa malipo ya madeni ya nje kwa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ukomo wake huwa ni 21%, sisi tuko 14% tu na uwiano wa malipo ya madeni ya nje na mapato ya ndani ambapo kwa mwaka huwa ni 23% sisi tuko 13.7%. Kwa hiyo haya mambo yote yanafanyiwa tathmini na pale tunapokwenda kwenye masuala yanayohusu mikopo ya ndani ambapo soko la fedha la ndani bado lina ukwasi wa kutosha huwa tunazingatia kile kigezo ambacho kimewekwa cha ukomo katika masuala haya ya kukopa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja zenu zote mlizozitoa tunazizingatia, tumezipokea na majina yenu yote yameingia kwenye hansard (Kumbukumbu Rasmi za Bunge) na sisi tumepokea na zile hoja zenu zitachambuliwa moja baada ya nyingine na zingine zitakwenda kuboresha Mpango na zingine ambazo zinahitaji ufafanuzi ambazo nitakuwa kwa ajili ya muda sijagusa, mtaletewa kwa maandishi ili muweze kuona ni kitu gani ambacho Serikali imekieleza kwenye jambo mlihitaji ufafanuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hili ndiyo Bunge la kwanza kwa Mpango huu tunaoupanga na kwa awamu hii, niwaombe tuendelee kutoa uongozi, tumsaidie Mheshimiwa Rais. Kwa sisi ambao tumefanya naye kazi, Mheshimiwa Rais wetu uzalendo wake kwa Taifa hili ni wa kiwango cha juu sana na Watanzania wanakiona. Nia yake kwa maisha ya Watanzania ni ya kiwango cha juu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefuatilia sana hizi siasa, nilikuwa napenda siasa tangu niko shule ya msingi. Afrika hapa kupata Rais ambaye 24 hours na kwa mwaka mzima na kwa awamu nzima anashughulika na maisha ya watu wake tu, tuwe wa kweli its very rare, ni ngumu kupata kitu cha aina hiyo. Kuna marais wako, sitaji nchi hizo, Afrika hapa hapa, wanaongoza nchi wakiwa hoteli huko nchi za Ulaya, yuko hoteli na mke wake huko wanaongoza, wako nje, wa kwetu hata akipata likizo unamwona yuko Chato tu na anaendelea kufanya kazi hapo hapo anashughulika na maisha ya Watanzania. Fedha zote zinakwenda kwenye mambo ya maendeleo.

Kwa hiyo hata hapa ambapo unaona namna hii tulivyofanya hapa, mlivyoona hii miradi na miaka mitano hiyo mpaka tukaweza kuingia kwenye kipato cha kati na tukaweza kutengeneza maendeleo kwa kiwango kikubwa hivyo unaweza ukaona ni commitment ambayo imetokea kwa maaana hiyo na sisi kama viongozi tuendelee kuunga mkono shughuli hizi maendeleo yanapotokea ni yetu sisi sote na sisi tutaingia kwenye record ya kuwa tulichangia pale ambapo tulikuwa na nafasi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa, nimetoa ufafanuzi huu naomba sasa kutoa hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niseme tu kwamba mimi na timu yangu ya wataalam pamoja na Naibu wangu, tumepokea maoni yote ya Waheshimiwa Wabunge waliyoyatoa kuhusu Wizara yetu ambayo wangependelea yaonekane kwenye Mpango na tutakaa na wenzetu wapokee Mpango wetu kama Wizara waweze kushirikisha kwenye Mpango mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba pia tutatumia mawazo ambayo tumeendelea kukusanya kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na leo hii tunakutana na Wabunge karibu wa sekta zote, nadhani Bunge litahamia pale Msekwa. Lengo letu tunapotoka hapa, tunavyokwenda sasa kukamilisha jambo zima la Mpango tuwe na mawazo kwa upana yanayotokana na uwakilishi wa wananchi ambao ni Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee tu kusema kama mnataka mali mtaipata shambani na leo hii niende kwa kusema kwamba tunavyotawanyika hapa katika maeneo ambayo yanahusu sekta yangu, wale ambao wanatusaidia walioko mikoani na wenyewe watusaidie na nitazungukia katika maeneo hayo kuweza kuona utekelezaji wake.
Jambo la kwanza, tunajua utaratibu wa mgawanyo bora wa ardhi unaanzia ngazi ya kijiji, unakwenda mpaka ngazi za mikoa na baadaye unaenda ngazi ya Mheshimiwa Waziri kwenye Wizara yake ambako kuna timu ya mpango bora wa matumizi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekeze ofisi zetu za Wakuu wa Mikoa wachukue hatua ya kuzungukia kila eneo, wapange maeneo ambayo wanayabainisha kwa ajili ya ardhi ya mifugo na kwa ajili ya ardhi ya kilimo na nitapita kuzungukia maeneo hayo ili tukishayatenga tuweze kuwa na maeneo ambayo yanajulikana matumizi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti mpaka sasa nchi yetu ina hekta zaidi ya milioni 60 ambazo zinafaa kwa mifugo, lakini eneo ambalo linahusika kwamba hili limepimwa na linalindwa kwa ajili ya mifugo ni 2% tu. Kwa hiyo, tunahitaji maeneo haya yapimwe na yabainishwe matumizi yake na kama shida ni gharama tutaweka hata beacon za asili. Nakumbuka vijijini tulikuwa tunapanda hata minyaa, inajulikana kwamba huu ni mpaka. Tutaweka hivyo ili wakulima na wafugaji wasiendelee kuuana katika nchi ambayo ina wingi wa ardhi ambayo inaweza ikapangiwa matumizi na ikapata matumizi bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme, mwenzangu wa Wizara ya Viwanda, kama tutakuwa tumeweka vizuri kwenye upande wa mifugo, pakajulikana wapi pana mifugo kiasi gani, itakuwa rahisi yeye kushawishi mtu aweke kiwanda cha maziwa, kiwanda cha nyama au kiwanda cha ngozi. Hili linawezekana kwa sababu katika mazingira ya kawaida, Wizara inawaza kutumia wafugaji wetu hawa hawa kuwa chanzo cha kwanza cha watu wa kufikiriwa kuwa wawekezaji kwenye mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ambaye ameweza kufuga kwa shida akapata mifugo 2,000, nina uhakika akitengewa eneo na likawa na miundombinu na huduma za ugani, ni mmoja anayeweza kuwa mwekezaji mkubwa, lakini wakati ule ule wafugaji wetu wakawa wamehama kutoka katika ufugaji wa kuzungukazunguka na kwenda kwenye ufugaji wa kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo nilishasema kwamba, tumekusanya mawazo ambayo tutayatumia katika kuondoa zile ambazo ni kero, ambazo Mheshimiwa Rais alishawaahidi Watanzania kwamba atazifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine ambayo yamekuwa yakiwasumbua wananchi ni upande wa masoko. Tutaimarisha kuanzia upande wa ubora katika uzalishaji ili kuweza kujihakikishia ubora wa masoko na niwahakikishie kwamba, katika mazao mengi yanayopatikana hapa Tanzania soko lake bado kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo, zamani tulikuwa tunajua mahindi ni zao la chakula au mchele ni zao la chakula, lakini niwaambie Waheshimiwa Wabunge, hivi tunavyoongea, zaidi ya watu bilioni 7.3 wanaoishi hapa duniani, nusu yao wanategemea mchele kama chakula na 40% wanategemea kula ngano kama chakula na zaidi ya bilioni moja wanategemea mahindi kama chakula. Kwa maana hiyo, hilo soko ku-saturate bado sana. Tuna mahali pa kuuzia mchele wetu, licha ya sisi wenyewe kwanza bado tunahitaji kwa ajili ya chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu jambo moja kwenye mazao. Kumekuwepo na unyonyaji mkubwa ukifanywa kwa wananchi wangu, wa upande wa sheria atasema anayehusika na sheria hizo na usimamizi wake, wa upande wa Viwanda pamoja na upande wa TAMISEMI. Wanunuzi wanapokwenda kununua wananunua kwa hivi…..
ili wananchi wauze kwa vipimo vinavyojulikana. Zimeshakwisha?
MWENYEKITI: Ndiyo, muda umekwisha.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Mpango na naunga mkono hoja iliyoko mezani kwetu. Ahsante sana.
Hoja Kuhusu Bei ya Kuuza na Kununulia Mahindi
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii ili niweze kuchangia. Nitanukuu maneno ya Waziri wa Sekta. Ukifuatilia mjadala niliona kuna maeneo hivi ambayo yalikuwa yanaleta confusion kidogo. Kwa hiyo, naomba nisisitize ambayo Mheshimiwa Waziri wa Kisekta alisema, Serikali haijafunga mipaka.

Mheshimiwa Spika, nadhani tukiongelea kufunga mipaka, tukiongelea NFRA tunaleta mkanganyiko. Serikali haijafunga mipaka na hili Waziri wa kisekta alilisisitiza sana. Serikali imetoa utaratibu wa namna ya kuvuka hiyo mipaka. Vile vile, Waziri wa Viwanda hapa amesisitiza na ameonesha jinsi ambavyo masharti yale yamepunguzwa. Waheshimiwa Wabunge, kwa maana hiyo na jana Mheshimiwa Spika alitoa maelekezo, nadhani tungejikita sana kwenye kuhamasisha hawa wenzetu ambao wanauza hayo mahindi, wawahi wachukue hizo leseni na wapeleke hayo mahindi nje. Wanunue, kila mtu aende anunue, wala hatujafunga soko, wala hatujapunguza hiyo competition.

Mheshimiwa Spika, kila mtu aende achukue leseni, anunue na apeleke anakotaka kupeleka. Pia, tukishafanya hivyo ingekuwa ni vema sana tungekuwa tunajadili kama upatikanaji wa leseni ni mgumu, hilo ndilo lingetakiwa liwe jambo la mjadala na sio kuhusu mipaka kwa sababu mipaka iko wazi, lakini kuhusu leseni watu wachukue leseni.

Mheshimiwa Spika, niombe Waheshimiwa Wabunge tuelewane vizuri kwenye hilo. Serikali imekwenda kuwekeza na kuona kwamba potential ya nchi yetu iko kwenye kilimo. Nikiongea kilimo naongea kwa dhana pana ambapo kuna kilimo, mifugo na uvuvi. Kama huo ndio mwelekeo, ni vizuri sana tuendelee kuweka misingi ya kufanya urasimishaji kwenye eneo hili, vinginevyo tutawafanya watu wetu waumie, halafu hiyo nguvu yote, watu watakuwa wanajiingilia tu kama matunda ya mti wa barabarani, kila mtu anachuma na kuondoka ambacho sio kitu kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu NFRA hiyo tumeongezea ushindani tu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde thelathini, malizia Mheshimiwa Waziri, kengele imeshagonga.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, tuimeongezea fedha NFRA ili na yeye aweze kununua. Ndio maana mwaka 2022 ilikuwa Sh.100,000 tu sasa hivi tumeenda Sh.400,000 na fedha hiyo imekwishapatikana. Kwa maana hiyo itakwenda kuongeza bei kwa mkulima na kuweka uhakika.

Mheshimiwa Spika, nadhani tuwaelimishe watu wetu, wawahi wakate hivyo vibali na waweze kuuza mazao wanakotaka kuuza.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
WAZIRI WA KILIMO, MIFUNGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia katika Mpango wa Maendeleo ambao umewekwa mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme tu kwamba sisi kama Wizara tumepokea michango na maoni ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu Mpango, na tumepokea maoni na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge yanayolenga katika Wizara yetu, yote tumeyapokea na tutayafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii huenda nisijibu yote kwa ajili ya muda, lakini niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mambo mawili kwamba la kwanza tumepokea maoni yao, na pili tutaendelea kujibu kwa sababu bado tutakuwa na fursa ya kufanya hivyo katika majibu ya bajeti za kisekta ambapo Waheshimiwa Wabunge watachangia tena katika bajeti ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea wachangiaji wote ambao waliigusa katika Wizara ya Kilimo, lakini pia walipogusa katika Mpango kwa ujumla. Niseme tu kwamba Mpango wa Maendeleo ambao umewekwa mbele yetu umeipa nafasi kubwa sekta ya kilimo, na umeipa nafasi kubwa pale ulipoongelea kwamba mpango unalenga kunufaisha viwanda na kuinua viwanda hasa vinavyotokana na mazao ya kilimo.
Jambo la pili Mpango huu umeipa fursa kubwa sekta ya kilimo, kilimo kwa dhana pana, kwa maana ya kilimo, mifugo na uvuvi pale ulipoongelea kwamba unapanga kuhuianisha maendeleo ya viwanda pamoja na maisha ama maendeleo ya watu. Ikumbukwe kwamba katika nchi yetu kilimo kinaajiri asilimia kubwa ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hata katika maeneo ambayo Mpango huu umeongelea neno kilimo ni kwa maana pana ambapo unaongelea mazao, unaongelea mifugo na unaongelea uvuvi.
Nikienda katika eneo moja moja, machache, Mheshimiwa Ally Saleh alisema kwamba ianzishwe na Benki ya Uvuvi. Katika Benki ya Kilimo inatamkwa kilimo lakini ni kwa dhana pana ambapo uendelezaji wa mazao ya kilimo, kwa maana ya mazao yanayotokana na kilimo mikopo yake inapatikana katika Benki ya Kilimo, lakini pia kwa wale ambao wanaendeleza mazao ya mifugo na wenyewe wanapata fursa hiyo sawa na upande wa mazao, lakini vivyo hivyo kwa upande wa uvuvi. Jambo hili tulilisemea hata tulipokuwa tunajibu swali la jana ambalo lilikuwa linahusisha mambo ya ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Yahaya Massare aliongelea kuhusu malisho pamoja na Waheshimiwa wengine ambao waliongelea kuhusu malisho ya Mifugo akiwemo ndugu yangu wa Jimbo la Kilindi na ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, pamoja na ndugu yangu Mheshimiwa Kakunda na wengine wote ambao waliongelea kuhusu malisho. Jambo hili la malisho kwa mifugo siyo jambo la siku moja, sisi kama Serikali tunaendelea kulifanyia kazi kwa sababu linahusisha Wizara zaidi ya moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Lukuvi ambaye tumekuwa tukishirikiana naye mara kwa mara yanapotokea matatizo ya migogoro yanayohusisha matumizi ya bora ya ardhi. Waheshimiwa Wabunge, jambo la matumizi bora ya ardhi halianzii kwenye ngazi ya Wizara bali linaanzia katika Kamati zetu za matumizi bora ya ardhi ambazo ziko katika ngazi ya vijiji. Wabunge kama wawakilishi tushiriki katika kutoa maoni na katika kutenga maeneo katika matumizi bora ya ardhi pale Kamati zetu zinazotenga matumizi bora ya ardhi zinapokutana. Mimi kama Waziri ni dhahiri kwamba naunga mkono jitihada za Kamati zetu zinapokuwa zinakutana kwa ajili ya kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo liliongelewa na Waheshimiwa Wabunge wengi lilikuwa jambo linalohusu makato katika mazao. Jambo hili pia kwa sababu linahusisha Wizara zaidi ya moja tumeendelea kuyafanyia kazi na tunaamini tunavyoenda katika Bunge hili la Bajeti ambapo mwishoni kabisa tutatengeneza Finance Bill, tunategemea yale ambayo yanahusisha tozo ama makato ambayo yanaangukia katika sheria zinazopita katika Bunge letu tutapata fursa ya kuyangalia, lakini Wizara ya Kilimo pamoja na TAMISEMI pamoja na Wizara ya Fedha tumeendelea kuyafanyia kazi haya kwa sababu tayari uamuzi wa Serikali ulishatoka kuhakikisha kwamba tunawatengenezea mazingira bora wakulima, wafugaji na wavuvi ili waweze kufanya kazi zao na kuweza kujiletea tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tunalifanyia kazi, Waheshimiwa Wabunge ambao wengi wenu mmeliongelea ni kuhusu pembejeo. Jambo la pembejeo linalohusisha ruzuku, Serikali tunaendelea kulifanyia kazi kuangalia utaratibu mzuri ambao utakuwa endelevu na ambao hautaruhusu mianya ya matumizi mabaya ya fedha za umma ambayo yanatokana na baadhi ya mifumo ambayo tumekuwa tukiitumia ya ugawaji wa ruzuku. Kwa hiyo, katika jambo hili, kwanza tunaangalia utaratibu ambao utakuwa endelevu, lakini vilevile tunaangalia utaratibu ambao utagusa watu waliowengi wanaohusika katika sekta hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili tuliangalia uwezekano wa kuangalia kwanza fedha ambazo zinapatika katika kila sekta, tuliangalia hata katika mazoa utaona makato mengi yaliyokuwa yanalalamikiwa ni makato ambayo hayaendi kuendeleza sekta husika, tunaangalia uwezekano wa makato hayo yaweze kunufaisha sekta na ambayo hayanufaishi sekta yasiwekwe kwenya sekta hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia100 kwa 100, na niendelee kusema kwamba kama mnataka mali mtazipata shambani!
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante!
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja, nikushukuru wewe mwenyewe kwa fursa hii pamoja na Naibu Spika kwa kuendesha vizuri mjadala huu na niishukuru Kamati ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini pamoja na wajumbe wake kwa michango waliyoitoa kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa mpango huu.

Mheshimiwa Spika, jumla ya Wabunge waliochangia ni 111 wakiwemo 94 waliochangia kwa kuongea na 17 waliochangia kwa kuandika. Na niseme michango ya Wabunge wote kwa kweli imekuwa ya Kibunge kwelikweli na ninaamini itatusaidia katika kutekeleza mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya muda, kabla sijaenda kwenye hoja moja moja, nianze kwanza kwa kuisemea hoja ya jumla ile ambayo ilikuwa inahusisha kama wasiwasi kidogo hivi kuhusu utekelezaji wa mpango huu.

Mheshimiwa Spika, dira aliyoitoa Mheshimiwa Rais tangia ameapishwa na ambayo ameendelea kutoa katika maelekezo mbalimbali, katika matukio mbalimbali ya kitaifa ni dira tosha ambayo inatutosha kutupa uhakika wa utekelezaji wa mpango huu unaofuata, Mpango wa Tatu.

Mheshimiwa Spika, niwakumbushie tu Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania ni maelekezo yapi yale yanayotoa dira ambayo yanatosha kutupa matumaini makubwa kwamba mpango huu tunakwenda kuutekeleza ili wote tuyazingatie.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, kauli moja tu ya kwanza Mheshimiwa Rais aliyoitoa ni ile iliyokuwa inahimiza mshikamano katika Taifa letu. Alisema huu ni wakati wa kushikamana kuliko wakati mwingine wowote ule, tukishikamana mtu mmoja mmoja, viongozi, Serikali, sekta binafsi, ni dhahiri kwamba tunakwenda kuutekeleza mpango hii kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Mheshimiwa Rais alisema atasimama imara kwenye masuala ya mapato na matumizi. Na sisi viongozi tukiondoka na dira hiyo, sisi kwenye ngazi ya Wizara tumeshajipanga kwenda kuhakikisha kwamba tunatekeleza maelekezo hayo ya kusimama imara kwenye masuala ya mapato na matumizi. Tukisimama imara kwenye masuala ya mapato na matumizi ni dhahiri kwamba tunakwenda kutekeleza mpango huu kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Rais alisema atasimama imara, alisema atasimama imara kwenye masuala ya rushwa, zero tolerance on corruption. Jambo hili tukitembea nalo Watanzania wote kama dira ni dhahiri kwamba tunakwenda kuutekeleza mpango huu kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Rais alilisema kwa nguvu kubwa, tena waziwazi, ni kwamba kodi za dhuluma, no! Akasema nendeni mkakusanye kodi kwa kutumia akili zaidi badala ya nguvu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni nadra sana kusikia kauli za aina hiyo katika viongozi wengi sana wa Kiafrika. Dhamira ya aina hiyo ni jambo ambalo litafungua ushiriki wa hiari na wa kizalendo wa Watanzania wote kwenda kutekeleza mpango huu wa maendeleo. Na ni sifa moja ambayo naamini itatusaidia pia kwenda kuhakikisha kwamba tunatekeleza mpango huu kwa uhakika.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, alisema Mkaguzi Mkuu (CAG) usiwe na kigugumizi. Maana yake ni nini; maana yake anachofanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kujenga taasisi katika utendaji wa kazi. Ameelekeza hilo na maana yake kila sekta na kila taasisi ziwajibike katika kufanya kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo na Mawaziri wengine wamelisemea ni miradi mikubwa yakielelezo yote iendelee. Na tumeona hatua ambazo zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, mengine ni masuala ya haki. Amesema kesi za uonevu zote zifutwe, zile ambazo hazina base, zile ambazo hazina msingi, zifutwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hakuishia hapo, akasema wananchi hawana fedha mifukoni, madeni yalipwe na vitu vingine ambavyo vinaweza kuchochea mzunguko wa fedha kwenye uchumi, na punde mzunguko wa fedha unapokuwa mkubwa maana yake tutakuwa na makusanyo na tunapopata makusanyo maana yake tunakwenda kutekeleza miradi hii ambayo tumeiainisha katika Mpango huu wa Maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania, kwa hiyo dira ya aina hii sote tunatakiwa tuiunge mkono, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais ili tuweze kutekeleza mpango huu. Na naamini ni jambo ambalo litaleta tija.

Mheshimiwa Spika, tuache chachandu chachandu zingine. Maana yake kauli zenye dira zimetolewa halafu kunatoa vimaneno vimaneno vingine; tuache chachandu chachandu zingine, kauli aliyoitoa Mheshimiwa Rais na maelekezo aliyoyatoa yanatutosha kutupeleka kutupeleka mbele, yanatosha kutupeleka mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wengine wanasema tumesikia kauli lakini hatuna imani, tunataka tuone vitendo. Kazi ya Urais si kama tofali useme utamuona siku moja anabeba tofali hivi uone ndiyo kitendo kile pale amekifanya; haya maelekezo aliyoyatoa ndiyo yameshaanza kufanyiwa kazi na wengine wameshaanza kutoa ushahidi kwamba akaunti zimefunguliwa, wengine wameshatoa ushahidi kwamba kesi imefutwa, kati ya yale ambayo alikuwa ameyatolea maelekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na sisi wasaidizi wake tayari tunaendelea kuyafanyia kazi na kila taasisi ambayo inaguswa na maelekeo imeingia kazini kuyafanyia kazi. Mheshimiwa Askofu Gwajima yuko hapa angeweza kutuambia, walikuwepo wale waliokuwa na mashaka, wasaidizi wa Yohana, akawatuma, nendeni mkamuulize hivi yule ni yule tuliyekuwa tunamngojea au tuendelee kumngojea mwingine? Wala hakuwajibu kuwa ni mimi, akawaambia tu vipofu wanaona, viwete wanatembea, wakoma wanatakaswa na akasema heri mtu yule ambaye hana mashaka nami. Sasa na wale ambao wana mashaka tuwaambie ni huyu huyu, hakuna tunayemngojea. 2025 tunaweka comma tu lakini safari inaendelea, nukta ni mpaka 2030. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wengine wanadiriki kuruisha mishale mpaka kwa Hayati. Nilisikia mahali hivi wengine wanarusha mishale; mwacheni mzee apumzike. (Makofi)

(Hapa Waheshimiwa Wabunge walishangalia sana)

SPIKA: Nakuongezea Mheshimiwa Waziri wa Fedha; tena apumzike kwa amani. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru; tena apumzike kwa amani. Amemaliza kazi yake Serikalini, amemaliza kazi yake duniani, tuliosalia ndio tuna kazi, tuna wajibu sisi tunalifanyia nini Taifa letu. Si utaratibu wa Kiuchamungu kumrushia mishale mtu ambaye ametangulia mbele za haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa dira hii ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa, nitoe rai na nirudie tena; twendeni, tuchape kazi, kazi iendelee na twendeni kila mmoja awajibike katika eneo lake ambalo anawajibika kufanya kazi ili tuweze kuutekeleza ipasavyo mpango wetu.

Mheshimiwa Spika, tukienda kwenye hoja moja moja; Kamati ilikuwa inapendekeza kwamba tuone umuhimu wa mikopo yote kuelekezwa katika kukamilisha miradi ya maendeleo, hasa ile ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo haya yamezingatiwa na yanakwenda sambamba kabisa na sheria, sura ya 5 kipengele Na. 5.7 na sehemu ya vipaumbele vya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa pamoja na kifungu cha tathmini na uhimilivu wa deni la Taifa katika Knauni ya 38 ya Sheria ya Mikopo, Dhamana pamoja na Misaada. Kwa hiyo, haya yamezingatiwa kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao walilisemea.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo kamati ilitolea maoni, iliona kuna umuhimu wa malengo kwenda sanjari na hatua stahiki zinazochukuliwa katika mpango wa utekelezaji ukiwa umekwenda sambamba na mikakati ya utekelezaji wa mpango, mkakati wa ugharamiaji wa mpango, mkakati wa ufuatiliaji pamoja na tathmini wa mpango pamoja na mapitio na mikakati ya mawasiliano ndani ya Wizara zetu.

Mheshimiwa Spika, Kamati pia ilitoa maoni kuhusu wakandarasi wa ndani, jambo hili pia limezingatiwa na matumizi mbalimbali ya fursa pamoja na ugharamiaji wa mpango; jambo hili pia limezingatiwa. Jambo lingine ambalo limeongelewa na Wabunge wengi kuhusu tathimini pamoja na ufuatiliaji, jambo hili tumezingatia taratibu ambazo zinatumika katika nchi nyingi, lakini pia zinazotumia utaratibu wa tathimini ambao wametungua sheria na zile ambazo wanatumia utaratibu wa ufuatiliaji wa ndani ya taasisi husika. Kwa msingi huo na kwa kutambua umuhimu wa kuwa na nyenzo za ufuatiliaji na tathimini Serikali imechukua hatua ya kuandaa mwongozo na ufuatilaji wa tathimini ili kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zinajitokeza kuhusiana na masuala haya ya ufuatiliaji.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelisemea kwa kiwango kikubwa ni lile lililokuwa linasema bajeti za maendeleo zitekelezwe kama ambavyo zilikuwa zimepangwa na kupitishwa na Bunge; jambo hili linazingatiwa. Jambo lingine ni uwepo wa uwajibikaji wa kina katika matumizi ya fedha; jambo hili litazingatiwa na Mheshimiwa Rais tayari alishalitolea kauli na kauli hiyo ni mwongozo kwa taasisi zote, Wizara pamoja na idara zote huku Serikalini.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo lilitolewa maoni na Wabunge wengi ni kuongeza wigo wa kodi na mahsusi ilikuwa Serikali ipunguze kiwango cha kodi ya makampuni ili kuvutia uwekezaji wa ndani na kampuni za nje ili kuongeza multiplier effect katika kuimarisha ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, jambo hili limekuwa likifanyiwa kazi. Ukiangalia katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilipunguza kiwango cha kodi hiyo kutoka asilimia 30 hadi 20 kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2018/2019 hadi 2022/2023 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya madawa ya binadamu pamoja na viwanda vinavyotengeneza bidhaa za ngozi. Sambamba na hilo mwaka 2019/2020 Serikali ilipunguza kiwango cha kodi ya mapato ya kampuni kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2020/2021 kwa wawekezaji wapya wanaotengeneza taulo za kike.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo makampuni mapya yaliyosajiliwa na Soko la Hisa la Dar es Salaam yalitozwa kodi ya mapato ya kampuni ya asilimia 25 kwa kipindi miaka mitatu mfululizo kuanzia tarehe iliposajiliwa. Kwa maana hiyo Serikali itaendelea kuyaangalia masuala ya haya ambayo yalitolewa hoja na Waheshimiwa Wabunge kama ambavyo nimesema. Yale masuala mengine ambayo yametolewa na Wabunge yanayoashiria, ambayo yamebeba maudhui ya kikodi tutayaelezea kwa kina tutakapokuja kwenye Bajeti Kuu pamoja na Muswada ule wa sheria, yaani Finance Bill. Yale mengine ambayo yanawahusu sekta, sekta zinazohusika zitaendelea kuyaelezea punde tu tutakapokuwa tunaenda kwenye mawasilisho yale ya kisekta.

Mheshimiwa Spika, concern nyingine ya Wabunge wengi ilikuwa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo pamoja na kutekeleza masuala mengine. Ni vyema ukaweka viwango vya maisha tofauti ikiwa ni busara mpango huu uweze…

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana nitalisemea hili kwa kuwa naelekea dakika za mwisho za wasilisho.

Kwa kuhitimisha nirudie tena kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya mapendekezo wa Mpango huu wa Taifa. Nichukue fursa hii kuzitakia Wizara, Idara zinazojitegemea Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza ipasavyo falsala yetu ya kazi iendelee, na hivyo wajielekeze katika kusimamia utekelezaji wa mpango huu ili tuweze kufikia azma yetu ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuhitimisha hoja. Kwa kuanzia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii, imechangiwa na zaidi ya Wabunge 23 kwa kuongea na Wabunge watatu wamechangia kwa maandishi. Niwahakikishie tu kwamba hoja ambazo huenda hatutazitolea majibu hapa zingine tutazitolea kwenye hotuba kuu ya Serikali na zingine tutazitolea kupitia Finance Bill zile ambazo zimekaa kwa muundo wa masuala ya kisheria na zingine tutaendelea kuzitolea majibu kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Spika, la pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutoa ufafanuzi wa kina wa hoja. Navyomuona Mheshimiwa Naibu Waziri wangu kadri tunavyoenda na yeye atapata ubatizo kama ule aliopewa Waziri wa Ulinzi ambaye ni Mhasibu lakini alishabatizwa na alishapewa degree kwamba yeye ni engineer, namuona Naibu Waziri wangu akiwa mchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianzie pale alipoishia Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa King aliuliza ile asilimia tatu ya VAT ambayo inatofautiana kati ya asilimia 18 ya Mainland na ile ya 15 ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa zile bidhaa ambazo haziko kwenye kodi ya Muungano na zile ambazo ziko kwenye masuala ya VAT kwa ngazi ya bidhaa za viwandani ambazo kwa sheria ambayo ilikuwa inatumika mpaka hivi sasa ziko zero rated. Kwa maana hiyo, mwananchi anaponunua hizo bidhaa ambako zipo zero rated hatozwi kodi huko anakonunulia anakwenda kutozwa kodi ya VAT kule kwa mtumiaji. Kwa maana hiyo ile tofauti ya VAT hiyo asilimia 18 na 15 inakuwa haimgusi kwa sababu anakuwa hakutozwa kule wanakotoza 18 anakwenda kutozwa kule wanakotozwa 15, kwa hiyo, anakuwa ametoa tu ile ile ambayo inastahili.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa bidhaa zile ambazo bei zake ama utozwaji wake unatozwa maeneo tofauti, hilo ni jambo ambalo kama alivyoelezea Mheshimiwa Naibu Waziri limefanyiwa kazi na tuko kwenye hatua za mwisho za kulimalizia. Tunaamini ndani ya hizi siku mbili tutakavyokuja kwenye hatua zinazofuata tutakuwa tumeshakamilisha utekelezaji wake utakavyokuwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa King na nimpongeze kwa uchangiaji wake. Nimhakikishie kwamba kipengele cha kwanza ambacho tumekielezea kipo vile lakini kile ambacho kilikuwa na matatizo kidogo kwa zile bidhaa ambazo hazikuwa zero rated tutakipatia majibu tunavyokuja kwenye hizo hoja kubwa zinazokuja hapo baadaye.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa King aliongelea pia zile fedha na alitaja kiwango kama shilingi bilioni 28, kama nimempata vizuri, ambazo zilitakiwa zirudishwe Zanzibar. Ni kweli kulikwepo na jambo la aina ile na kama alivyoeleza mawasiliano kati ya Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato yamefanyika na kiasi cha fedha tayari kilishapelekwa Zanzibar ambacho kilikuwa kinatokana na Excise Duty. Kwa upande wa kiwango kikubwa kile ambacho kilikuwa bado hakijapelekwa lilikuwa jambo la mawasiliano na mimi nielekeze leo hii Kamishna wa Mapato Tanzania pamoja na pacha wake wa Zanzibar wakae wamalize usuluhishi wa takwimu zile ambazo zilikuwa zinawakwamisha ili waweze kutatua tatizo hilo. (Makofi)

Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar ni Muungano wa kindugu, hatuwezi tukatofautiana kwa kushindwa tu kuzioanisha takwimu hata tukaenda kwenye manung’uniko. Huu siyo Muungano wa Amri ya Mahakama, ni Muungano wa kindugu, kwa hiyo, takwimu haziwezi zikatupa hiyo shida na hata tukashindwa kuziweka sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilitolewa na Mheshimiwa Mpina kuhusu ukusanyaji na akaelezea kuhusu hizo taasisi alizozitaja TANAPA, Ngorongoro, TAWA na kama je, kushuka kwa makusanyo kwa kiwango hicho ni Covid peke yake? Ni kweli kunaweza kukatokea matatizo mengine hasa katika taasisi zingine lakini kwa kesi ya TAWA, Ngorongoro pamoja na TANAPA hizi ni moja ya taasisi ambazo ziko kwenye sekta ambayo iliathirika kwa kiwango kikubwa zaidi na masuala haya ya Covid. Hii inatokana na idadi ya watalii waliotembelea katika hifadhi hizo, baadhi ya nchi mliona zilifungia wananchi wao kutoka. Kwa hiyo, ni dhahiri kwenye eneo hilo kidogo tunaweza tukapata matatizo ya aina hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini hoja zingine zilizotolewa, kulikuwepo na hoja kama misaada ambayo inaenda Zanzibar ni lazima ipokelewe na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Ndugu yangu mpaka alianza kusema Waziri wa Fedha wa Tanzania Bara. Kwenye hili sheria imeshaweka wazi na utaratibu ule ndivyo unavyotumika. Waziri wa Fedha wa Zanzibar sheria imempa nafasi ya kukasimiwa kupokea misaada pamoja na taasisi nyingine ambazo zimeelekezwa kwenye sheria ambazo zenyewe si lazima Waziri wa Fedha aweze kupokea.

Mheshimiwa Spika, maeneo pekee ambayo Waziri wa Fedha anahusika ni yale ambayo yanatumia Kamati ya Madeni kama ambavyo Kamati ya Bajeti ilisema, yale ambayo Kamati ya Madeni ni lazima ishauri kuna umuhimu wake. Maana hoja ilikuwa inatolewa kwamba kwa nini hata misaada ipitie kwenye Kamati ya Ushauri. Jambo hili liliwekwa kwa makusudi kwa sababu kuna mazingira ambapo misaada inaweza ikawa na masharti ndani yake ambayo kwa ukubwa wake ama kwa ugumu wa masharti yale yasipofanyiwa tathmini ya kina yanaweza yakawa na athari kwenye Taifa. Vilevile kuna baadhi ya misaada katika utekelezaji wake kwa sheria zilizokuwepo ina masharti ya kikodi ndani yake kwa maana hiyo na yenyewe lazima implication zote ziwe zimepitiwa na zimeridhiwa kuweza kuona namna ya kutumia.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kipengele hiki kinachohusisha masuala ya misaada kinafanyiwa kazi kwa kina na ndani ya siku hizi mbili tutakuwa na majibu kuhusu baadhi ya maeneo. Pia baadhi ya misaada inaweza ikawa na masuala ya kiusalama ambayo lazima yawe yamezingatiwa ili kuweza kuhakikisha kuwa inaenda kutumika huku tukiwa na uhakika na matumizi yake.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo liliongelewa, Kamati imeshauri Serikali kuhamasisha Serikali za Mitaa kuwa na mabadiliko na maandiko ya miradi ambayo ina sura ya kibiashara itekelezwe kwa mfumo wa PPP. Siku hizi mbili, tatu tumekaa na mabenki yote yaliyoko hapa na tume-share nao utaratibu huu unaopendekezwa na Kamati na tumeshirikiana nao na tumegawanya miradi ambayo ni zaidi ya miradi 75 wameichukuwa na baadhi yao wameshafika hatua ambazo ni za juu tunategemea baada ya hapo watasema kila mmoja ambao wameona wanaweza wakatekeleza. Hili ni wazo jema tu ambalo linaweza likafanyika, miradi ile ambayo ni ya kibiashara kama masoko, stendi pamoja na vitu vingine ambavyo vinaweza vikawa vya kisasa vinaweza vikanyiwa tathmini za kina na vikafanywa kwa utaratibu huu wa PPP. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri mwingine ambao umetolewa ni mtizamo hasi kuhusu miradi ya PPP ni changamoto kubwa kwa Serikali katika kutekeleza miradi ya PPP, Serikali itatue changamoto hii. Hili suala la mtazamo hasi kwenye miradi ya PPP si jambo la Serikali peke yake, hii ni mindset ya nchi nzima, ni mindset ya wananchi. Kwa hiyo, upande wa Serikali, Serikali inaundwa na wananchi, viongozi walioko Serikalini wote wanatokana na wananchi, viongozi wanatokana na Watanzania, hili suala la mindset kuhusu PPP ni jambo kubwa ambalo na lenyewe lazima tuanze kupeana elimu kuhusu utekelezaji huu.

Mheshimiwa Spika, mwanzoni wakati tunapata Uhuru ni dhahiri kwamba Serikali ingeweza kutelekeza miradi yote na wakati uleule ikatoa huduma za jamii, kwa sababu idadi ya wale ambao walikuwa wanatakiwa kupewa huduma chukulia mathalani elimu walikuwa wachache tu, ngazi zote unazozitaja walikuwa wachache tu, ukienda kwenye afya hivyo hivyo walikuwa wachache. Pia hata kwenye huduma zingine kama za maji, katika enzi ile maji yalikuwa yanapatikana tu kila eneo. Kwa maana hiyo Serikali ingeweza kutekeleza vizuri miradi yote ya maendeleo kwa kutumia mkono wa Serikali na wakati uleule ikatoa huduma. Sasa kwa mabadiliko haya niliyoyasema ni dhahiri kwamba uhitaji wa kutekeleza miradi kwa kutumia PPP ni mkubwa zaidi ili Serikali iweze kutekeleza majukumu ya kutoa huduma za jamii ambayo ni ya msingi na ni majukumu ya lazima kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, hili la mindset ni jambo ambalo linatakiwa lianze kidogokidogo kueleweka kwa Watanzania. Kwa sasa hivi Tanzania akitokea mwekezaji yuko na mtaji kamili, tutolee mfano tu, anataka kuleta meli ya uvuvi kwenye kina kirefu (deep sea fishing), ana mtaji kamili wa kuleta meli. Wale samaki wapo pale msipowavua wanaweza wakatembea wakavuliwa kwingine na anapanga aweke hiyo meli. Akitoka kwenye meli, natoa mfano, ajenge na bandari ya uvuvi kwa ajili ya lile limeli likubwa la kwenda kuweka nanga pale na kupakua. Akitoka pale aweke na kiwanda cha kuchakata samaki; awe na mtaji wote ule uko kamili. Kwa mindset ya Kitanzania tulio wengi, swali la kwanza utakuwa unasikia; hivi huyu ana mtaji kweli huyu, siyo tapele kweli huyu?

Mheshimiwa Spika, wakijiridhisha siyo tapeli, swali la pili, hivi huyu hatatuibia kweli? Wakijiridhisha na hilo, kwamba hivi huyu hatatuibia, maswali yakiwa mengi akitokea mmoja akasema nadhani hili wazo ni zuri, swali la tatu kwa Watanzania walio wengi litakuwa hivi huyu anayesema hivi hajala chochote kweli?

Kwa hiyo ni mlolongo wa maswali matatu ndiyo unaoua PPP. Moja, je, siyo tapeli? Wakigundua siyo tapeli, la pili; hatatuibia? Wakibishana akatokea mmoja akasema nadhani hatatuibia; hivi huyu anayesema hatatuibia hajala chochote kweli huyu? Hii ndiyo inayoua PPP. Haya masuala ya PPP ni lazima yaendeshwe kwa kuaminiana.

SPIKA: Hata Spika akisema wanasema inaelekea kahongwa huyu. Ndipo tatizo letu lilipo hapo. (Kicheko)

Mheshimiwa Waziri, endelea tafadhali.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utaratibu wa PPP kwenye miradi ambayo inaweza ikawa ya kibiashara ni jambo ambalo linatakiwa litolewe elimu na watu waelewe na ni utaratibu ambao unaweza ukaipa nafasi Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo. Kwa hiyo hata waandaaji pia wa kwenye miradi bado iko vile. Hata Serikalini hilo bado lipo pia; kukiwa na line moja inahusisha PPP na kukawa na line nyingine kwamba inaweza ikatumia bajeti ya Serikali, itakayochangamkiwa ni ile ya bajeti ya Serikali. Hayo ndiyo mazoea. Hata kama itasuasua itakuwa tu hiyo ndiyo ambayo inapewa kipaumbele kikubwa kwa sababu ni mazoea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili ni jambo ambalo linatakiwa liangaliwe na sisi huku tutaendelea kuwasisitizia wataalam wetu wafuate vile vigezo ambavyo vinatakiwa, wafanye miradi ambayo inaweza ikawa ya mfano, lakini pia waendelee kutoa elimu kwa kutumia miradi ambayo ni ya mfano ili watu waone kwamba ni jambo ambalo linawezekana.

Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri Serikali kuacha utaratibu wa kutenga fedha Fungu 21 zinazohusu watumishi kwa ajili ya kupandisha madaraja; utaratibu uliopo sasa hivi ni kwamba, fedha za kupandisha madaraja zinatengwa kwenye Mafungu husika. Hata hivi sasa katika mwaka huu wa fedha, zaidi ya bilioni 209 zimetengwa katika Mafungu husika, isipokuwa fedha ambazo zinawekwa kwenye Fungu 21 ni zile tu ambazo watu wake hawajajulikana watakaopandishwa.

Mheshimiwa Spika, kama haijajulikana ni akina nani watakaopata uteuzi, ni akina nani watakaokuwa katika fungu hilo mahususi; zile fedha ndiyo zinawekwa pale kwa ajili ya kusubiria hitaji kamili litakavyokuwa wakati utakapofika.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limeongelewa kwa kiwango kikubwa ni hili la kwamba Kamati inashauri Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba inapitia kanuni na taratibu za utolewaji wa misamaha ya kodi, ifanyike haraka kuepuka ucheleweshaji. Jambo hili linaendelea kufanyiwa kazi, liko hatua za mwisho. Kama nilivyosema, tutakavyokuja katika siku hizi mbili zijazo tutakuja na jambo hilo tukiwa tumelisemea.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wameliongelea kwa kiwango kikubwa, lilikuwa ni ile miradi ambayo ni pamoja na wa Mara, wa Zanzibar na wa Dodoma. Nitoe tu taarifa kwamba hatua ambazo Wizara ya Fedha ilitakiwa kuzifanya ilishafanya. Wizara ya Fedha ilishafanya mapitio na kuona umuhimu wa miradi hiyo katika kukabiliana na athari za tabianchi. Tarehe 12, Aprili, ilitoa vibali vyote kwa NEMC kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo. Kwa sasa NEMC wanaendelea kukamilisha taratibu zake za ndani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatoka BOT na kuendelea katika utekelezaji wa miradi husika. Hata hivyo, tunaendelea kutafuta jawabu la kudumu ili kuondoa huo ukiritimba ambao umejitokeza katika jambo hili na siku si nyingi tutatolea kauli jambo la aina hiyo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwepo pia na ushauri uliotolewa ambao ulikuwa unahusu michango ya watumishi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ipelekwe kwa wakati. Huu ushauri tumeupokea na tutatoa majibu tutakapokuja kwenye hotuba hizi za siku mbili ili tuweze kutafuta jawabu la kudumu kwenye tatizo hilo lililotajwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wameshauri kuhusu Wakaguzi kuhamia kwa CAG na wengine wamesema kuhamia kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani. Kuna umuhimu wa Wakaguzi wa Ndani kuwa huru na kutoingiliwa na mamlaka wanazozikagua. Kwa mujibu wa muundo, Wakaguzi wa Ndani wote wapo chini ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali. Hata hivyo, utaratibu wa shughuli za utendaji na utawala za kila siku za Wakaguzi wa Ndani zipo chini ya mamlaka ya Maafisa Masuuli ili kusaidia kudhibiti mifumo ya mapato na matumizi ya taasisi husika.

Mheshimiwa Spika, aidha, taarifa za ukaguzi zinazoandaliwa na Wakaguzi wa Ndani kwenda kwa Maafisa Masuuli hunakiliwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali. Hivyo, Wakaguzi wa Ndani ni sehemu ya muundo wa Mkaguzi Mkuu wa Ndani.

Mheshimiwa Spika, tumepokea ushauri na mapendekezo yaliyotolewa. Kilichokuwa kinatumika kwa sasa hivi, kuwapeleka moja kwa moja kwenda kwa CAG ingetengeneza line nyingine ya Wakaguzi wa Nje, kwa sababu tayari tuna safu ya Wakaguzi wa Nje na tuna safu ya Wakaguzi wa Ndani na kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alifafanua hapa, Wakaguzi wa Ndani kimsingi walitakiwa wawe jicho la kuonesha mambo yanavyokwenda na wawasaidie Maafisa Masuuli.

Mheshimiwa Spika, tukiwa hatuna pia Wakaguzi wa aina yoyote mule ndani kwenye ofisi zetu, kuna tatizo lingine litajitokeza, watakuwa wanafanya makosa yote yale wanasubiri mpaka waje wale wanaotoka nje kuja kuwaambia mmefanya makosa moja, mbili, tatu, nne. Kwa maana hiyo, kilichokuwa kinatakiwa, na hivyo ndivyo ambavyo inatakiwa na ndivyo ilivyokusudiwa, hawa wakaguzi ambao wako ndani mle wanapaswa kushauri na ku-control, lakini pia taarifa zao wanazipeleka katika line ile nyingine.

Mheshimiwa Spika, ni ajabu kwa wale ambao watakuwepo palepale ndani halafu waka-compromise taaluma zao wakashiriki katika uovu ambao utakuwa umejitokeza na kusubiri yule mwenzake ambaye ana taaluma sawa na yeye aje amwambie kwamba hapa mlikuwa mmekosea.

Mheshimiwa Spika, ikitokea Maafisa Masuuli wakafanya makusudi kwa kuwahamisha wale Wakaguzi wa Ndani ambao kimsingi wanatakiwa wawasaidie, nisitumie neno lingine, nitumie lilelile ambalo Mheshimiwa Kilumbe ametumia, itakuwa ni kukosa busara ama itakuwa ni bahati mbaya sana. Kwa sababu Serikali ni moja na Serikali ndiyo iliyoanzisha idara hizi zote na Serikali ina uchungu na fedha za walipakodi, kwa hiyo isingeweza kuogopa kukaguliwa, Serikali inahitaji kuona fedha zake zinatumika kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, hili la upande wa watumishi wa TRA, tumepokea ushauri huo na Naibu Waziri amelisemea vizuri, ni suala la kiutawala tutalifanyia kazi. Ni jambo ambalo kwa kweli lina umuhimu huo kwa sababu tunahitaji kuimarisha utaratibu vizuri sana kule kwenye upande wa mapato. Kwa sababu hatuwezi tukatekeleza miradi ya maendeleo bila kupata mapato.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo liliongelewa na Waheshimiwa Wabunge kuhusu kuweka ukomo wa uhakiki wa malimbikizo ya madeni. Tumelipokea hili la masuala ya madeni na lenyewe kama ambavyo unaweza ukaona, Serikali imeendelea kuweka uzito mkubwa unaostahili kwenye masuala ya madeni.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha huu unaomalizikia, Serikali ilitenga zaidi ya bilioni 600 ambazo zimekwenda kwenye kulipa madeni ya watoa huduma wa ndani. Hata katika bajeti hii inayokuja tumetenga fedha za kutosha ambazo zitakuwa zaidi ya bilioni 600 kwa ajili ya masuala ya madeni ya watoa huduma wa ndani. Hata hivyo, tunapanga kuharakisha utaratibu ule wa uhakiki ili kuweza kuhakikisha kwamba watu wetu hawakwamishwi na hawacheleweshewi malipo yao ama madeni yao wanayodai Serikalini kwa sababu tu ya suala zima la uhakiki.

Mheshimiwa Spika, Kamati pamoja na Waheshimiwa Wabunge wameongelea kuhusu utaratibu wa hatua za kuchukua kukabiliana na masuala ya COVID-19, hasa kwa taasisi ambazo zimeathirika pakubwa zaidi. Serikali imeendelea na utaratibu huo ikiwepo kushusha viwango vya riba vinavyotozwa na Benki Kuu wakati mabenki yanapokopa kutoka asilimia saba kwenda hadi asilimia tano, kushusha viwango vya chini vya kisheria ambavyo ni sehemu ya amana ambapo benki zingine zinatakiwa ziweke Benki Kuu kutoka asilimia saba kwenda asilimia sita.

Mheshimiwa Spika, pia hatua nyingine ambazo zimechukuliwa ni zile za kuendelea kugharamia mahitaji ya taasisi za utalii pamoja na TANAPA, TAWA na Ngorongoro, kuongeza kasi ya kulipa madeni kama nilivyosema, ili kuweza kuwawezesha wale ambao walikopa na wameshatoa huduma na wanatakiwa waweze kuendelea na shughuli zao ambazo walikuwa wanazifanya.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuongeza wigo wa kaya zinazonufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kama ambavyo mliona katika hotuba ya Waziri mwenye sekta; Lingine ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo ya gharama nafuu kwa wajasiriamali wadogowadogo na wa kati; na Lingine ni kuendelea kuhakikisha halmashauri zinatenga fedha za asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, haya yote ni hatua ambazo zinalenga kupunguza yale makali na kuweza kuchochea uchumi wetu kwa kuongeza ukwasi kwenye mzunguko wa uchumi ili shughuli za uzalishaji ziweze kuendelea na kuweza kulinda ajira za watu wetu katika kipindi hiki ambacho chumi zimepitia misukosuko kutokana na jambo hili ambalo lilikuwa linaendelea duniani kote.

Mheshimiwa Spika, kulikuwepo na ushauri uliotolewa kuhusu masuala ya watu wenye bureau de change na Mheshimiwa Mbunge alisema nitafute muda tukutane nao; bureau de change wale wa Arusha tulishakutana nao na tumeongea, tumewasikiliza, walikuja ofisini, tumeongea na tumewaelewa.

Mheshimiwa Spika, tutachukua hatua na tulishaelekeza timu ndogo inafanyia uchambuzi wa namna ya kuweza kushughulikia jambo hilo. Nakumbuka Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, alikuwa anakwenda mguu kwa mguu na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Arusha Mjini; alikuwa anakwenda mguu kwa mguu na leo hii Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum amelileta hapa; tulishakutana nao.

Mheshimiwa Spika, nimesikia hata Mbunge wa Iringa Mjini alikuja nalo pia; ni jambo kubwa, linahitaji katahadhari katika kulibeba. Mheshimiwa Paresso, tumelibeba jambo hilo, tutalifanyia kazi kiutawala, pamoja na maeneo mengine ambayo yanahusiana na jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Tarimba aliniambia nimpe na dondoo kuhusu tarehe 3. Mheshimiwa Tarimba hilo ni dogo tu; tarehe 3 wale wakija na paka, wananchi ninyi nendeni na mbwa tu, paka wote wataondoka halafu muweze kufanya shughuli kama mnavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nikushukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kuhitimisha hoja niliyoitoa mnamo tarehe 10 Juni mwaka huu na kabla sijaanza kuhitimisha nianze kwanza kwa kutoa shukrani na pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa anayoijenga kwa wananchi wa Tanzania pamoja na Jumuiya za Kimataifa, pamoja na maelekezo yake ya mara kwa mara yanayotuwezesha tutekeleza majukumu yetu kikamilifu, hakika kazi zake anazozifanya zinafanya kazi yetu pia iwe nyepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili nitumie fursa hii pia kukushukuru wewe mwenyewe Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson - Naibu Spika pamoja na Wenyeviti kwa kuendesha kwa weledi mkubwa mjadala huu muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nitoe pongezi na shukrani kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu Bunge ya Bajeti Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini; Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi pamoja na Kamati nzima ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ambayo wametupa ushirikiano mzuri na wa hali ya juu ambao umewezesha kazi yetu hii kuwa ya ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia nitoe shukrani zangu kwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania waliochangia kwa maandishi, kwa kuongea na wale waliotoa ushauri wao katika kuonana na sisi ana kwa ana, kwani wamewezesha sana shughuli hii iweze kukamilika kikamilifu na niwaombe wananchi wa Tanzania watambue tu kwamba Wabunge wao wametoa michango yenye maana kubwa sana kwa Taifa letu pamoja na kwamba huenda nikawataja wachache, lakini wapiga kura wao wote watambue kwamba Wabunge wao wamechangia kwa hoja za msingi na zenye tija kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vile tu kwa wingi wao sitaweza kumtaja mmoja mmoja, kwa hiyo hata kama Mbunge wao hatatajwa watambue kwamba wamechangia kwa hoja makini sana ni wingi wao tu hatuwezi kuwataja wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jumla ya Wabunge 209 wamechangia na kati ya hao 206 wamechangia kwa kuongea na Wabunge watatu wamechangia kwa maandishi na kama nilivyotangulia kusema wengine wametupa ushauri wao kwa kuongea/kwa kujadiliana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kutoa ufafanuzi wa hoja zilizojitokeza; kati ya hoja ambazo kwenye mjadala zimejitokeza kwa kiwango kikubwa zilikuwa zinahusisha maeneo yale ambayo tuliweka tozo mpya.

Mheshimiwa Spika, la kwanza niwapongeze Wabunge kwa kuelewa hoja ya Serikali na umuhimu wa jambo lile ambalo tulikuwa tunaongea lugha moja ambalo kwa kiwango kikubwa Wabunge wenyewe walikuwa wameibua kwamba tunahitaji tuangalie kwa jicho la tofauti katika matatizo yanayojitokeza katika sekta zetu za muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sekta ya kwanza ambayo tuliangalia kwa umakini mkubwa ilikuwa ni sehemu ya TARURA, barabara zetu na pili tulikuwa tumeangalia kuhusu upande wa maji, la tatu tulikuwa tumeangalia kuhusu upande wa elimu, la nne tulikuwa tumeangalia upande wa afya, miundombinu yake pamoja na mwelekeo wa kwenda kwenye universal health care na kipengele cha mwisho tulikuwa tumeongelea kuhusu miradi ya kimkakati ambayo ni miradi urithi kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo tulikuwa tumependekeza ambayo kwa kiwango kikubwa Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania walitamani kupata ufafanuzi, moja ya eneo ilikuwa kuhusu makato ya kwenye simu upande wa muda wa maongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili kwa kiwango fulani lilikuwa halijaeleweka kile ambacho tulikuwa tunakimaanisha, kuna wale ambao walikuwa wanadhania makato haya yanaenda kukatwa kwa idadi ya siku kwenye mwezi, kwa maana kwamba itahesabiwa kuanzia tarehe ya kwanza ya mwezi mpaka tarehe ya mwisho na kama hukuweka salio siku ukiweka unahesabiwa siku zote katika mwezi husika.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo ilikuwa inafananishwa kama ile ya nipige tafu ambayo kama jana hukuweka ama jana ulitumia kwa kukopa basi siku ukiweka inatakiwa ikatwe kwanza ile ambayo siku hiyo ilishapita. La hasha, sisi tulichopendekeza ni kwamba tumechukua takwimu za watumiaji wa simu, tukaweka makundi yao, kuna watumiaji wasiopungua milioni nane kwa viwango vya mwanzo ambao wana matumizi yao yasiozidi shilingi 1,000 inaenda inakuwa mpaka inafika wale wanaotumia shilingi 100,000 na kuendelea ambao wenyewe si wengi sana wako kwenye 60,000 naa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tulichoweka kwa wale watumiaji wanaotumia viwango vya chini kwa mfano anayetumia shilingi 1,000 na kwenda chini yeye atakatwa shilingi tano, na hiyo shilingi tano atakatwa pale alipoweka tu, kwa wale wanaotumia shilingi 7,500 hadi shilingi 10,000 atakatwa shilingi 76. Kwa wale wanaotumia shilingi 10,000 hadi shilingi 25,000 maana yake huyu inaweza ikawa ni mtu anayejiunga muda wa maongezi wa mwezi mzima kwamba ameweka kifurushi chake cha mwezi mzima kina range shilingi 10,000 mpaka shilingi 25,000; chukulia ni shilingi 25,000 kwamba ndicho anachojiunga nacho anakatwa shilingi 112; maana yake ni kwamba mwezi mzima amekatwa shilingi 112. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama anajiunga kwa shilingi 50,000 kwa mfano nani Halotel wana bundle linaitwa Tanzanite ambalo ukijiunga unaongea kwa mwezi mzima, chukulia ni shilingi 50,000; kwa hiyo kwa mwezi mzima anakuwa amekatwa shilingi 186; ni tofauti na ile hesabu tuliyokuwa tunapiga kwamba ni 200 kwa siku maana yake kwa mwezi ni shilingi 6,000 unaona hiyo tofauti kati ya shilingi 6,000 ambayo ilikuwa inatisha na shilingi 186 kwa mtu anayetumia shilingi 50,000.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema siku naweka hoja hapa mezani kwamba kwa kweli nachukia kuwapa Watanzania mzigo na kwa kweli nawahurumia Watanzania, lakini nikasema nawahurumia zaidi wanaojifungulia vichakani, kwa mtu anayeweza kutumia shilingi 50,000 kwa mazungumzo akichangia shilingi 180 ili kuokoa maisha ya mama zetu kuna shida gani kwa mwezi mzima! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mtu ambaye anaweza kutumia shilingi 25,000 ndio ni Mtanzania wa kawaida, akatumia shilingi 25,000 kwenye mazungumzo ndio ni Mtanzania na shilingi 100 ni kubwa, tukimuongezea kwenye matumizi yake ndio ni kubwa, mzigo, tunamhurumia, lakini shilingi 100 hiyo ikasaidia kupatikana vifaa tiba hospitalini, shilingi mia hiyo kwa mtu anayeweza kuongea kwa shilingi 25,000 kwa mwezi kwenye simu akasaidia tukapeleka vijana 21,000 waliokosa mkopo wa familia za kimaskini kuna shida gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo niendelee kutoa rai kwamba nchi hii itajengwa na Watanzania wenyewe, ni lazima tubebe majukumu hayo kama wazazi, lazima tubebe majukumu hayo kama Watanzania kwa sababu majukumu hayo ni yetu. Hata anayetumia shilingi 1,000 mpaka shilingi 5,000 katikati mle kuna shilingi 1,000 mpaka shilingi 2,500 anapoweka akichangia shilingi 10 halafu fedha ile ikaenda ikatusaidia upatikaji wa maji, kuna watoto wadogo wanabakwa wakiwa wanatafuta maji usiku ipo hiyo na sasa hivi imeongezeka na shida ya corona inayotuhitaji tuwane kwa hiyo kuna maisha yatapotea tusipokuwa na maji kwa jambo dogo tu la kunawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nakumbuka vizuri haya matatizo ya maji tulipokuwa kule vijijini ilikuwa ikifika mwezi wa sita na kuendelea mpaka Krismas mnaanza kusoma nusu siku tu ili muende kutafuta maji. Sasa kwa umri wa nchi yetu hivi si vitu vya kuviruhusu viendelee, vitakuwa vinapingana na hatua ya maendeleo tuliyoyafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niliwahi kuumia hiki kidole tukiwa tunachimba maji, hakijawahi kupata shape, hakijawahi kurudi kwenye hali yake ya kawaida, shida ya maji bado ni tatizo katika kila eneo. Kwa hiyo, hili na lenyewe tuliona tuifanye hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo huu ndio mtiririko, tutaanza na shilingi tano na pale ni mtu anapoweka na itaenda inakuwa kufuatana na matumizi yake na mpaka inaenda hiyo shilingi 222 kwa wale ambao watatumia shilingi 100,000 na kuendelea na hili si jambo la kila siku, ni pale mtu anapotumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukirudi upande wa miamala; kwenye miamala tulienda kuzingatia hivyo hivyo kwamba nchi yetu ina matatizo, pamoja na jitihada kubwa ambazo zimefanyika, lakini kila hatua ya maendeleo unayoifanya itakuletea changamoto zaidi; ndio utaratibu wa maendeleo ulivyo, kila hatua ya maendeleo unayoifanya ndio inakuletea changamoto zaidi, kwa mfano, tunapoongelea kila kijiji kiwe na umeme, kila mtaa uwe na umeme, kila familia iwe na umeme, umeme ule sio nguzo na nyaya za umeme, tunahitaji chanzo cha kufua umeme kitakachotosheleza mahitaji ya nyumba kwa nyumba kwa nchi nzima kuwa na umeme. Vinginevyo tukiwekeza tu kwenye kusambaza nguzo yatakuwa makao ya kunguru tu wanapandapanda mmewaongezea miti, lazima tuwe na chanzo cha uhakika kitakachofua umeme kiweze kusambaza umeme katika maeneo hayo ndio maana tunasema kila familia lazima iwe na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo tuna miradi ya kimkakati ambayo na yenyewe tukasema lazima tupate fedha na tukasema kama tutatafuta fedha kwa njia ya mikopo tu, tuna mzigo mkubwa Waheshimiwa Wabunge kwenye bwawa la umeme peke yake kwa muda huu ili likamilike mpaka mwisho zimeshatumika trilioni kama mbili hivi bado tuna mzigo karibu trilioni nne.

Mheshimiwa Spika, ukitoka hapo ukiweka na reli, reli sio njia moja tu tunataka kuijenga, hii njia ambayo tunaondoka nayo, huu ni mwanzo kama alivyosema Waziri mwenye sekta, tuna na reli zingine Kusini, Kaskazini pamoja na yale matawi tukishafika Tabora mtawanyiko wake ule, ukipiga hesabu yake yote hiyo ni karibu dola bilioni 10 ambayo ni zaidi ya shilingi trilioni 22.

Mheshimiwa Spika, sasa fedha za aina hiyo ukisema tu uende ukakope zote tena uikamilishe kwa muda mfupi maana yake ni kwamba kwanza masharti tutakayopata hayatakuwa rafiki, lakini mbili mzigo utakalolibebesha Taifa utakuwa ni mzigo wa roho mbaya kwamba sisi tukope tu watakuja kulipa ambao hawajazaliwa, tutakuwa tunafanya kitendo ambacho vizazi vijavyo vitalaumu kizazi cha leo kwamba kama hawakutaka kujenga reli kwa nini wasingeacha tu tuje tujenge wenyewe uende tungekuja kukopa kwa masharti ambayo ni nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sisi tumeona ni vyema tukafanya utaratibu wa kupata fedha kiasi tutapeleka kule wakati tunasubiri credit rating pamoja na taratibu zingine, lakini kwa wakati huo huo tuwe tunatafuta mikopo yenye masharti nafuu ambayo haitaipa mzigo mkubwa wa deni kwa Taifa letu ambao pia unaweza ukatusababisha tukaingia kwenye sifa mbaya za nchi zilizokopa kupita uwezo wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hicho ndicho ambacho tulikizingatia kwa upande huo wa miamala na mimi niwaombe Watanzania kama nilivyosema tunazingatia mambo yanayotukabili mbele yetu na ndicho tulichofanya kuamua tukasema ni vyema tukafanya hivyo. Na kwa nini tuliona tufanye hivyo; mfumo wa kodi wa kwetu ulivyo ile tax base ilivyo mpaka hivi tunavyopanga bajeti ya leo ukiiondoa indirect taxes zile kodi ambazo kila mtu anaguswa kwa matumizi ya bidhaa wale ambao wameandikishwa huo mzigo unaangukia kwa watu wachache.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano mpaka sasa tunavyoonge walipa kodi wakubwa ni 504; ukienda walipa kodi walioandikishwa ni 3,162,000; sasa kama una walipakodi wakubwa 504 na walioandikishwa milioni tatu; una miradi inayohitaji shilingi trilioni 20 na kuendelea; karibu shilingi trilioni 24 hiyo hatujataja miradi mingine ambayo na yenyewe ni mikubwa, miradi kama ya madaraja, barabara za kuunganisha, hapo hatujaenda kwenye hizi za kimkakati tunazosema za kwenye vijiji vyetu ambavyo ni za muhimu sana, unawezaje kupeleka malipo haya yote yaangukie kwa hawa watu niliowataja hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukasema kazi kujenga nchi yetu lazima ifanywe na Watanzania wote na Watanzania wajivunie kuijenga nchi yao. Kila Mtanzania anapoona jambo la maendeleo limefanyika ajivunie kwamba na mimi nimeshiriki, tukasema hii na yenyewe tushirikishe kwa upana wao, ndipo tulipoona tuanze kugusa awepo wa shilingi 10, shilingi 16, yupo wa shilingi 50, yupo wa shilingi 25, yupo wa shilingi 125, ukienda wa shilingi 30,000 ni shilingi 1,000 ukiienda shilingi 40,000 ni shilingi 1,500; ikaenda mpaka yule wa shilingi milioni tatu na kuendelea milioni tano, milioni 20, milioni 15 na kuendelea tukasema kwa kazi tuliyonayo kama Taifa kama unaweza ukawa na ukwasi wa milioni 15 tukichukua shilingi 10,000 kwako halafu ukajivunia kujenga nchi yako, kuna ubaya gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaingia kwenye rekodi ya kujenga nchi yako, unaingia kwenye rekodi ya kujenga nchi yako, sisi wengine huwa tunajivunia sana lift hizi kwamba inapojengwa reli unaingia kwenye kumbukumbu kwamba reli inajengwa ilikuwa umri wetu kama wazee wanavyotuambia kwamba wakati vita vya Kagera vinapigana mimi nilipeleka ng’ombe, wanajivunia wakati wa vita vya Iddi Amini mimi nilipeleka ng’ombe, mwingine anasema mimi nilipeleka mbuzi, wanajivunia wazee wetu,

hawakuwa matajiri wakubwa kihivyo, walikuwa matajiri wa moyo kwamba mimi nilipeleka mbuzi wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wengine walikuwa na mabasi yalikuwa yanashusha abiria wa biashara wanabeba wanajeshi waende kupigana, ana-sacrifice fedha ambayo angeipata kwa biashara yake anapeleka basi liende kwenye ile vita. Sasa hivi hatuna vita za kiuvamizi, vita zilizosalia kwenye nchi zinazoendelea ni vita za kiuchumi kujenga mataifa yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tuwe na moyo wa aina hiyo kwa sababu hii nchi lazima iende na sisi tujivunie kwamba hapa lilifanyika hili tukiwepo, lilifanyika na hili tukiwepo, hebu fikirieni vijana wa rika langu, wakubwa zetu na wadogo zetu mnaofuatia, siku ikitokea katika kizazi chetu tukajenga reli zote za Kusini huku Mtwara kwenda kwenye maeneo ya uzalishaji, tukajenga Kaskazini huku kote, tukajenga na hizi kubwa tukasema hizi zilijengwa katika kizazi hiki, na Rais aliyekuwepo alikuwa Mama yetu Samia Suluhu, hili ni jambo la heri kwa kila Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo ndivyo tulivyowaza wenzenu, tukasema hii kazi lazima tuibebe wote, hivyo ndivyo tulivyofikia katika uamuzi huo na mimi naamini Watanzania tukikubaliana na mwenendo huu tutapiga hatua ambayo Tanzania itarudisha ile sifa iliyokuwa mbele inatajwa na kila mtu wakati wa ukombozi wa Kusini mwa Afrika. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, makofi hayo hayatoshi kwa kweli, kabisa. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, sasa tunachopendekeza, baada ya kuwa tumepata yale mapato nini tunapendekeza; tunapendekeza tupeleke shilingi bilioni 322 ziende kwenye maeneo yetu ambayo hayapitiki, hayana barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulishapitisha bajeti ya TARURA karibu shilingi bilioni 400 na sehemu, kama mnavyokumbuka. Zile zitafanya ile kazi ya kawaida ya spotting na periodic maintenance kama ambavyo zilikuwa zinafanyika na zingine mgao ulishapita. Tunapendekeza tuongeze ziada ya zile shilingi bilioni 400 na bahati nzuri hiki chanzo kinakwenda moja kwa moja kwenye mfuko. Kwa hiyo, tutakapotumia zaidi maana yake makadirio haya yanaweza yakazidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, twende tukafungue maeneo ambayo hayapitiki. Mijini na vijijini tuna maeneo mpaka karne hii, nilisema na siku ile tuna eneo unakuta kijiji kina shule ya msingi, taasisi ya Serikali, ina zahanati, lakini hakuna gari inaweza ikafika pale. Hali ya aina hiyo haiendani na umri wa nchi yetu na heshima ya kiuchumi ambayo nchi yetu imetambulika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata Jiji kubwa kama Dar es Salaam, nilikuwa naongea na Mbunge wa Kibamba akasema hata kwake kuna maeneo ambayo kwenye ramani yanaonekana kabisa yana mitaa, lakini hayapitiki. Sasa mtu anaishi Dar es Salaam, jiji kubwa ambalo linatambulika, lina mpaka flyovers halafu eneo lingine mlemle hata pikipiki haipiti, haya hayaendani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alisema jana kwamba tunaondoa miradi ile ya DMDP pamoja na TACTIC, muielewe vizuri. Tulichokuwa tunasema fedha hizi siyo za kwenda kwenye mapambo yale, kwamba wengine waendelee kubandika na kubandua halafu kwenye eneo lilelile pawe pana watu ambao hawajawahi kupata kitu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ile miradi itakuja, kama alivyosema Waziri, lakini alichomaanisha kwamba kuna maeneo yapo hayajafunguka kabisa, yapewe kipaumbele na haya yanakwenda kwenye majimbo yenu huko huko; awe Mbunge wa Dar es Salaam ana maeneo ya pale mjini na pembezoni; awe Mbunge wa kwenye miji ile 45, ana maeneo ya mjini na mle pembezoni. Kwa hiyo, hiki ndicho alichosema Waziri wa TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tunakwenda kupata, ukiangalia kwenye hesabu, Wabunge na hapo ndiyo wapiga kura wenu waone kwamba walileta majembe kweli kweli; mnavyoondoka hapa kila mmoja ataondoka na siyo chini ya shilingi bilioni moja, inakwenda kwenye barabara hizo. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, mkifuatilia hapa mtakuta kuna wakati TARURA ilikuwa inapata shilingi milioni 30, majimbo mengine yalikuwa yanapita kapa, mwaka mzima unapita. Sasa waambie wananchi wako kwa jinsi Mbunge ulivyo mjanja sasa hivi, umeishauri Serikali sikivu na ulivyopaza sauti mama yetu akasikia kilio chenu, na akasikia kilio cha wananchi wote, unakwenda kuondoka na siyo chini ya shilingi bilioni moja, iende kwenye kufungua barabara ambazo hazijawahi kupitika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tukienda na utaratibu huu mwaka wa kwanza, wa pili, wa tatu tukaendelea nao kama walivyoanza TANROADS, walianza na kufungua mkoa mmoja mmoja na sisi tukianza hivyo hivyo tukafungua kijiji kwa kijiji, mtaa kwa mtaa, tutafika wakati hatutaongelea changarawe mitaa yote, tutaanza sasa kuwaza makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vijana wengine wanadhani zile barabara kubwa za TANROADS za lami zinazounganisha mikoa zilikuwa hivyo hivyo, hawakusafiria yale mabasi yenye carrier juu. Mkipita mnavyofika mkishuka abiria na kondakta wote mko sawa, lakini tulianza na utaratibu huu huu na ndiyo maana tunasema Mheshimiwa Dkt. Magufuli, Mungu amrehemu kule aliko, wakiwa wanakwenda na utaratibu huo wa mfuko na kuanza hatua kwa hata wakaenda, sasa hivi tunaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa nchi ni kama ujenzi wa nyumba, kuna anayejenga msingi, kuna anayejenga kuta, kuta anayepaua, kuna anayeweka marumaru. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapendekeza na tumeongea na wenzetu wa Wizara ya Elimu, Mheshimiwa Profesa Ndalichako, tumeongea naye na wataalam wake na wametuambia wanafunzi 11,000 waliokosa mikopo mwaka jana na wa mwaka huu walikadiriwa kama 10,000; ni kama 21,000 plus, mahitaji ya fedha ni shilingi bilioni 70. Kwenye shilingi bilioni 500 ambayo tulishapeleka tunaongeza shilingi bilioni 70 ziende ziwapeleke watoto wa mwaka jana…(Makofi)

MBUNGE FULANI: Haleluya!

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hapa hujaeleweka, hebu rudia kidogo, maana yake Wabunge wengine naona kama hawajaipata hii vizuri. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, mwaka jana walikosa mikopo takribani watoto 11,000 wale ambao wana admission, wamepokelewa na vyuo kwamba wana sifa za kuingia vyuoni, lakini walikosa masomo kwa sababu walikosa mkopo na wazazi wao hawana uwezo, wengine hawana wazazi na wakabaki majumbani 11,000. Na wanakadiriwa mwaka huu tena wangekosa 10,000 na kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kwenye familia zetu mtoto ambaye amefaulu mtihani huwa inakuwa faraja ya familia na ukoo mzima. Ikitokea amekosa mkopo, siyo fedha ya msaada, mkopo, inaleta majonzi kwenye familia na ukoo mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapendekeza kuongeza kwenye bilioni tulizopitisha kwenye Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, shilingi bilioni takribani 500, tunaongeza shilingi bilioni 70 ambazo zinakwenda sambamba kuwapeleka watoto wote. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Haleluya!

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ummy Nderiananga aliongelea upande wa wanafunzi wenye ulemavu; tumepokea mapendekezo yako na tunaendelea kuyafanyia kazi Kiserikali, tutajua kwenye utekelezaji wake kuhusu wanafunzi wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapendekeza kwa upande wa maboma ya elimu, kama tusipopanga kuanzia sasa kule tunakokwenda watoto wetu watapata sifa za kuingia shuleni, lakini hawatakwenda kwa sababu kuanzia mwaka kesho tunakwenda kupata toleo la kwanza la wale wanafunzi walioandikishwa kwa elimu bila malipo shule ya msingi, darasa la kwanza, ndiyo wanakwenda kumaliza darasa la saba na wanatakiwa waanze kidato cha kwanza.

Mheshimiwa Spika, tusipojipanga kwenye miundombinu kuanzia sasa takwimu zinaonesha tutakuwa na uhitaji wa vyumba vya madarasa wa kiwango cha juu sana na hatutaweza kufanya kwa muda mfupi.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka, bahati nzuri wewe ni kaka yetu tulio wengi hapa, utakumbuka zamani kwa ajili tu ya kukosekana miundombinu watu ni hawa hawa, Watanzania ni hawahawa na akili zao ni hizihizi, lakini ilikuwa inatokea kijiji kizima, darasa lenye watu sitini, mia, inatoka kapa. Mnaambiwa tu wamefaulu 50 lakini hawakuchaguliwa, maana yake wakichaguliwa wanakwenda wapi, ndivyo ilivyokuwa. Mimi nakumbuka hata Mazengo tulikwenda watano.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi tulivyojenga shule kwenye kila kata mmeona wanaobaki wameendelea kuwa kidogo sana. Maana yake nini; wana pa kwenda na kule kule wanakokwenda ili muone kwamba akili wanazo, wanapata division one kule kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuna rika hapa la enzi ya wamefaulu ila hawakuchaguliwa, kuna rika la watu wana akili sana na wangelitumikia Taifa, hawakwenda kwa sababu ya nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hata sasa kuna baadhi ya mikoa kwa sababu bado tunagawanya chumba kimoja tunaweka ubao katikati, watoto wengine waangalie ubao mmoja wengine waangalie mwingine; kwa hiyo, mikoa ile ikitokea ametokea mtoro amekwenda kuchunga kama tulivyokuwa tunachunga wengine, hata hawahangaiki kumtafuta kwa sababu wanajua ametupunguzia na kero ya madawati huyu, ametupunguzia na mbanano. Tumefanya suala la elimu liwe la kuviziana kwa sababu miundombinu haitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara tunaoshughulika na mipango tunaona hili jambo tunaweza tusilimalize mara moja, lakini ni vyema tukaanza kupanga haya mambo tunakokwenda. Uamuzi wa maeneo mengi tunaufanya kwa kuviziana kufuatana na miundombinu iliyopo na ndiyo maana familia tulizokuwa tumezaliwa watoto kumi au 11 hatukuwa tunafanya birthday, utakumbuka birthdays ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hata kwenye masuala ya miundombinu, uamuzi wa kupeleka watoto shuleni miundombinu inachangia. Hata haya mambo tumebishana ya waliopata ujauzito warudi ama wasirudi, unaweza ukakuta uamuzi unakuwa shaped na wakirudi wanakwenda wapi. Tunafanya kuviziana kwa sababu ya miundombinu.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la elimu linatakiwa liwe wazi tu, hata ukitaka kusoma lini wewe soma, si tunataka upate akili, upate uelewa? Mbona elimu ya watu wazima tuliwasomesha wazee, tulisomesha na wana wajukuu. Kwa hiyo, tumeona lazima tushughulike na miundombinu.

Mheshimiwa Spika, nini tunachopendekeza; tunapendekeza tuanze na maboma 10,000 ambapo tunapendekeza tupeleke shilingi bilioni 125 kwenye upande wa maboma na hapa kila Halmashauri mtaondoka na maboma yasiyopungua kumi kwenye maeneo yenu ili kila mmoja aweze kwenda nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tutakapoenda kwa mwaka hadi mwaka tunakwenda kuyamaliza na yenyewe na hapo yatakwenda juu zaidi kufuatana na mchanganuo wa gharama halisi utakavyoonekana kwenye fedha hizi ambazo tumeweka za nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye maboma ya afya; tuna maboma tulikuwa tumetengeneza, kuna zahanati na kuna zahanati zile zilizoko kwenye kata. Tuna zahanati ziko kwenye kila kijiji na tuna zingine tumeziweka kwenye kata, hii ni tofauti na vile vituo vikubwa ambavyo tunaviweka vina facilities nyingi. Vilishajengwa vingine vina miaka kumi, vingine 15 na hii ilikuwa nguvu ya wananchi. Tunapendekeza tupeleke shilingi bilioni 100 kwa ajili ya eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye haya maboma ya afya tunapendekeza tuyafanyie kazi kwa sababu hiki tunachoendea mbele cha bima ya afya kwa wote, hiyo bima ya afya kwa wote siyo ile kadi, ni facilities (vitendea kazi) ambapo inaanza na hospitali zenyewe, lakini pia dawa pamoja na vifaa tiba ambavyo vinatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ni lazima tukamilishe kwanza haya yapatikane kila eneo na tunaendelea kufanya tathmini, wenzetu wa TAMISEMI wanaendelea kufanya tathmini na maeneo yale ambayo ni ya tarafa ama maeneo ya kimkakati ambayo hayajapata vituo vya aina hiyo. Lakini sambamba na yale ambayo yanahitaji ukamilishwaji ambayo tayari kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu aliposema kazi iendelee na kazi inaendelea, alikuwa anamaanisha hivyo. Hapatakuwepo na sehemu pana gap ya kazi inayotakiwa kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hilo hilo la afya kwenye bima ya afya kwa wote na hospitali hizi ambazo zinaangukia Wizara ya Afya, tunapendekeza tupeleke shilingi bilioni 50 kwa ajili ya vifaa tiba pamoja na dawa, na hii ni nyongeza ya fedha ambazo zilishatolewa kwenye bajeti mama ya sekta ambayo tuliipitisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hoja za Wabunge, jambo moja ambalo lilisemewa kwa sauti kubwa sana na kwa msisitizo sana, lilikuwa jambo la ring fencing ya fedha hizi. Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanataka kujiridhisha kwamba fedha hizi zitatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja, niwahakikishie Wabunge kwamba Mheshimiwa Rais yuko makini sana kwenye masuala haya ya fedha, sana. Sisi tulioko kwenye Wizara ya Fedha anatuelekeza kila wakati kuhakikisha fedha zinakwenda kwenye maeneo yaliyokusudiwa na maeneo yenye tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaifafanua zaidi tutakapokuwa tunaongelea masuala ya siku 100; lakini niwaelezee tu kwamba Serikali iko makini kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwenye hili ambalo Waheshimiwa Wabunge mmelisema kwa nguvu sana, nilikuwa nawaona Mheshimiwa Munde, Mheshimiwa Lucy, Mheshimiwa Jesca, Mheshimiwa Matiko, Mheshimiwa Nape pamoja Wabunge wengine wengi, ni vile tu siwezi kumtaja kila mmoja, mlisema sana tuwahakikishie kwamba fedha hizi zitakuwa ring fenced. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi niseme mbele yako, kwa sababu sekta hizi tunazozipelekea fedha nyingi zina mfuko, wala hatukuona sababu ya kuanzisha mfuko kwa sababu tumekitaja chanzo na tukataja zinapokwenda. Maana yake zinatoka kwenye chanzo, zinakwenda moja kwa moja kwenye mfuko ule ambao upo.

Mheshimiwa Spika, nimeshaeleza maeneo mengine, nilikuwa bado sijaelezea upande wa maji. Maji tulishapeleka bajeti. Muda huu ambapo tumeweka nyongeza hii tuliyoomba kwa Bunge lako Tukufu, tunapendekeza tuwapelekee Wizara ya Maji shilingi bilioni 207 za nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kama alivyosema Mheshimiwa Maganga jana, kwamba yeye ile fedha ya TARURA anatamani anunue greda; na mimi naendelea kuungana naye na ninamshauri Waziri wa Maji, fedha nyingine wanunue magari ya kuchimba visima, nyingine wanunue magreda ya kuchimba mabwawa, halafu fedha nyingine twende kwenye utaratibu wa kisima kila kijiji. Kama umeme upo kila kijiji tunakosaje kisima kila kijiji? Hili ni jambo ambalo litaweza kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo Mfuko wa TARURA upo kisheria, hivi tunavyoongea, na chanzo tumekitaja. Maana yake fedha itatoka kwenye chanzo inakwenda kwenye Mfuko wa TARURA kama ambavyo fedha zile zilizokuwa zinakwenda kwenye TARURA zimetumika zilivyokusudiwa kwa sababu kuna Mfuko wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna Mfuko wa Maji; fedha tulizotaja kutoka kwenye chanzo zinakwenda kwenye Mfuko wa Maji. Tuna Mfuko wa Elimu ya Juu, Bodi ya Mikopo, fedha iliyotajwa inakwenda moja kwa moja kwenye Mfuko wa Elimu ya Juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa bima ya afya kwa wote sheria inakuja siyo siku nyingi, kwa hiyo, hatukuona kutengeneza sheria inayohusu tu huo mfuko wakati kuna jambo linakuja kubwa linalohusisha bima ya afya kwa wote. Kwa maana hiyo na mfuko wake utatajwa na sheria ambayo itakuja kufuatana na mpangilio unavyopangwa wa shughuli zetu za Kibunge (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upande wa maboma, hiyo kwa sababu ni maboma, ni kitu endelevu, tumeona yenyewe itakuwa fedha ambayo inakwenda kwenye Wizara husika kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, SGR pamoja na reli, Mfuko wa Reli upo, kwenye SGR ni mradi wa kimkakati ambao wote tunautolea macho kwamba ni lazima ukamilike. Kwa hiyo, tumeona kwa kweli Wabunge pamoja na Watanzania mtuamini kwenye hili, tunakwenda kulifanyia kazi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa TARURA tunarekebisha kipengele kile ambacho kilikuwa kinazuia Halmashauri, Majiji na Manispaa kutengeneza barabara. Kama tumeshachukua baadhi ya mzigo wa kuwalipa Madiwani kwenye makusanyo yao ya ndani tunafungulia kanuni ile na wenyewe waweze kufanya periodic maintenance ya barabara zao. Kwa hiyo hilo tutalifanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ninaamini tuna majiji ambayo wana uwezo mkubwa kabisa wa kuweza kuzitengeneza barabara zao na tukaunganisha nguvu hii ambayo tumeisema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo lilichangiwa kwa hisia na Waheshimiwa Wabunge na kule kwa wananchi wetu lilikuwa na hisia, ni jambo la kodi ya majengo kwa kutumia LUKU. Kati ya maswali yaliyokuwa yanaulizwa ni inakuaje mpangaji ndio awe mlipaji? Je, nyumba zenye mita nyingi? Nyumba kubwa zenye mita moja? Itakuaje kwa nyumba ya nyasi? Itakuaje kwa nyumba za vijijini; itakuaje kwa nyumba zisizo na umeme; taasisi pamoja na rika lililosamehewa itakuaje?

Mheshimiwa Spika, moja niwaombe Watanzania tusiigope teknolojia, teknolojia imekuja ili itusaidie, duniani kote teknolojia imeletwa ili kurahisha ufanyaji wa mambo, ndiyo kazi moja kubwa ambayo unaweza ukaitaja kwa sentensi ya ujumla, imekuja kurahisisha kazi. Sasa wenzetu ambao wanashughulika na masuala ya umeme pamoja na wale wanaoshughulika na IT wametuhakikisha kwamba mambo haya yote yanakwenda kwa programming.

Mheshimiwa Spika, leo hii hata tulivyoongea na Waziri wa Nishati walituhakikishia kwamba wanao uwezo wa kuitisha LUKU zote, wanao uwezo wa kuitisha mita zote, wakajua na mtumiaji anatumia kiwango gani, wanajua, wanajua hata trend ya matumizi wanajua, wanajua na nyumba zenye mita zaidi ya moja, hazikujibandika zile mita zimeenda kuwekwa.

Mheshimiwa Spika, takwimu zake zote zipo na zipo namna ya kuitisha, tulivyohakikishiwa hayo tukaona ni jambo ambalo tutafanya programming na wenzetu hivi wapo busy wanafanya programming. Watafanya programming tunaitoa sheria nzima ile iliyokuwa inatumika kukusanya manually tunaipeleka tukusanye kiteknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuendi kuvunja Torati, tunaenda kuimarisha Torati, vilevile ilivyokuwa inafanyika manually tunaipeleka tunaikusanya kiteknolojia, kwa mfano, kama jengo moja ambalo linastahili kuwa la mita moja lina mita 12 tunaenda kuzi-program kwamba zipo 12; kwa hiyo, kwenye 12,000 tunagawanya kwa 12 tunazi-program kwa hiyo kwa mwezi atakuwa analipa mia, mia badala ya 1000 ni 12 gawanya kwa watu 12. Tunagawanya kwa idadi ya mita tupate ka kiwango ambacho kwenye kila kijimita tutapata.

Mheshimiwa Spika, wengine walikuwa wanasema je, wale ambao hawatumiagi hata shilingi 1,000 hiyo kwa mwezi, wenzetu kimtandao unaitisha wale ambao hawatumiagi hata hiyo maana yake unawatoa kiurahisi kuliko kutembea siku nzima unawatafuta. Unaitisha tu au una blacklist hawapo na wale waliosamehewa hivyo hivyo una program unawatoa, hivyo hivyo na kwenye nyumba ambayo ina mita zaidi ya moja na kwenye eneo lilitakiwa kuwa na mita zaidi moja mathalani ghorofa lilitakiwa kuwa na malipo yanayoendana na flats zile ilivyokuwa imebainishwa kwenye sheria tuna program hivyo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi tuliona hii imerahisisha utaratibu kwa wananchi wetu ni wao tu kukubaliana na hali hiyo na waweze kujua kwamba teknolojia imekuja iturahisishie. Hebu fikiria uwezekano katika karne hii eti watu wanatangaziwa deadline ya kulipa mita unakuta wamepangana mstari kama hapa na Dodoma Sekondari kule, wanaenda kulipa shilingi 10,000; mwingine ametoka sijui wapi anapanda gari, mwingine anatumia nauli, mwingine anaendesha gari, mwingine anapoteza na muda anaenda kulipa shilingi 10,000, anaenda kulipa shilingi 50,000 tumezigawanya kama tulivyozigawanya, tuna program, zitakuwa programmed hivyo ndivyo ambavyo itafanyika, hivi vitu vinawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa wale waliokuwa wanapata msamaha kama ni wazee, kama ni Taasisi za Kidini tunaenda kufanya hivyo hivyo, tuna program kwenye vitendea kazi vyetu hawatakuwepo na tunaenda kutekeleza sheria vilevile. (Makofi)

Kwa nyumba zile ambazo zipo vijijini wengine walikuwa wanabandika tu kanyumba kapo kijijini hapana, hii hatutaenda kutoza kwenye kila mwenye umeme na wala hatutaenda kutoza kwa matumizi ya umeme kwa sababu tukitoza kwa matumizi ya umeme tutaongeza gharama za uzalishaji, tunaenda ku-program kodi inayotakiwa kutozwa ya jengo kwenye eneo husika.

Mheshimiwa Spika, nchi zote zilizoendelea hawatozi kwa kupanga mistari, wanatoza kieletroniki hiyo ndiyo faida ya teknolojia. Hata hapa Afrika, Namibia kuanzia kodi ya ardhi wanatoza kwa utaratibu wa LUKU, kodi ya jengo wanatoza kwa utaratibu wa LUKU, kwa hiyo mtu anakuwa anajua kwamba nina commitment zangu hizi hapa anazitoa kwa kutumia simu yake akiwa yupo nyumbani kwake, akiwa yupo ofisini kwake bila kusumbuana kupanga foleni kwa njia zile za kienyeji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hata maeneo ambayo yatatozwa ni yaleyale yaliyoanishwa yenye sifa siyo kila kijiji, siyo kila nyasi, siyo kila mwenye umeme ni yule ambaye anaangukia kwenye sifa zile ambazo tulishakubaliana kisheria. (Makofi)

Kwa wale wachache ambao wanatumia solar hili eneo tumesema ni wachache wale wataendelea ku- graduate kuungana na wale wenye umeme, tumewaachia TAMISEMI watafanya hiyo na kitakuwa moja ya chanzo ambacho na wenyewe watatumia kwenye haya maeneo mengine ambayo tunawakabidhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine lilikuwa linasemwa kwamba sasa je, kwa nini itozwe kwa mpangaji? Nasema na nasisitiza kodi hii si ya mpangaji, hii ni kodi ya mmiliki, hii si kodi ya mpangaji ni kodi ya mmiliki, utaratibu huu tunaotumia ni utaratibu ambao hata kwa karatasi alikuwa akikutwa yule ambaye anaishi kwenye ile nyumba anasaini kwa niaba ya mwenye nyumba, wakionana kwa taratibu wanazozijua wana-offset hiyo difference hata kwa karatasi ndivyo walivyokuwa wanafanya, ndiyo utaratibu uliokuwa unafanyika, hakuna nyumba ambayo ina mita ambayo haihusiani kabisa na mwenye nyumba na hakuna nyumba ambayo mtu anaishi hausiani kabisa yaani hawajuani wala hawajahi kuwasiliana hata kwa kutumia mtu wa kati kama dalali kwamba wewe basi kaa hapa, hakuna mtu anayeenda kuingia tu kwenye nyumba isimekane kwamba hata muona wala hawatakuwepo na hata third ya part wa kuonesha huyu anakutana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hoja ya kwamba akitokea mwenye nyumba asiye na busara au akatokea aliyemkorofi, niwatangazie wenye nyumba wote hili si jambo la mahusiano, hili si jambo la mahusiano ya mpangaji na mwenye nyumba wala hili si jambo la kirafiki hili ni jambo la nchi, jambo la sheria, akitokea mkorofi nchi hii haijawahi kushindwa kushughulika na wakorofi, akitokea asiye na busara pia na yenyewe tutafundishana busara hili ni jambo la nchi ni jambo la sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo wapangaji wala wasipate shida, kama una mwenye nyumba ambaye atakiuka sheria za nchi zinazohusu masuala ya kodi sheria zetu zipo wazi kwa watu wa aina hiyo ni kitu gani kinafanyika kwa maana hiyo hatua za kisheria kwa watu wa aina hiyo zitafuata tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliona hili na lenyewe nilisisitize na niwaombe Watanzania tusiogope teknolojia, tutumie teknolojia itusaidie kuendesha mambo yetu kwa urahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa hapa kwenye hilo la upande wa kukusanya; watu wameanza kuchanganya hii habari ya kulipa kodi. Tunaposema kulipa kodi kwa hiari watu wameanza kuchanganya wanadhania kodi ni hiari, tunaposema tutoe elimu watu walipe kodi kwa hiari watu wameshaanza kuchanganya wakidhani kodi ni hiari na wengine wanachanganya halali na hiari, kana kwamba sasa mtu atakuwa na uamuzi wa kulipa ama kutokulipa kwamba anaweza kupanga tu kwamba yaani anaambiwa kabisa kodi yake stahiki ni hii ila anapanga kama alipe au asilipe, that is a gross mistake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kodi yoyote anayostahili mtu kulipa ni kitu cha lazima, lazima alipe. Tunachosema kwa hiari tunasema usisubiri kusukumwa, tunaongelea wajibu kwamba watu wawajibike kulipa, watu wanataka kuchanganya hiari aone kama vile anaweza akawa na uamuzi wa kulipa ama kutokulipa. Si jambo la kuamua ama ulipe ama kutokulipa, kodi stahiki kwa mtu yeyote kodi stahiki lazima alipe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachosema tutatoa elimu tunasema usisubiri kusukumwa na wala usiingie kwenye mitego ya kukwepa kulipa unatafuta matatizo, hivi tunavyoongea tunapoanza Julai, tutafuatilia utaratibu wa matumizi ya EFD, tutayafuatlia sana lakini pia tutafuatilia watu walipe kodi stahiki, tutafuatilia sana watu walipe kodi stahiki, tutalifuatilia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa wale ambao wanapenda kuamua kwamba nipewe bei isiyo na risiti au yenye risiti twendeni tutoke kwenye kupeana bei yenye risiti au isiyo na risiti twendeni bei ni moja yenye risiti lipa kodi ya Serikali. Tutaelimishana kwenye hili na wakati ule nilimteua unajua kuteua ni kuzuri, nilimteua Subira natamani kulirudia hili neno nilimteua Balozi wa Kutoa Elimu ya Kulipa Kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafanya na teuzi zingine namteua na Zulfa Omary kutoka Pemba na yeye atatusaidia…(Makofi)

SPIKA: Yupo wapi Mheshimiwa Zulfa. (Kicheko)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, namteua na Ndugu yangu Ameir Abdalla Ameir yule shabiki mpya wa Yanga ambaye aliguswa na bajeti hii, haukuwepo siku ile kwenye kiti, Mheshimiwa Ameir alisema tangu ujana wake, tangu mtoto kwa takribani zaidi ya miaka 12 iliyopita alikuwa shabiki wa Simba ila anasema kwa bajeti hii ameamua kuingia Yanga. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hii elimu pia ya mlipa kodi, si elimu ya darasani tu, kule tunapata elimu ya darasani, lakini pia tunataka tufanye elimu ya hamasa ya kuhamasishana, taasisi yangu ya Mamlaka ya Mapato watafundisha kitaalamu technical issues pamoja na faida zile, wataonesha na kinachofanikiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini, vijana wetu pia wana lugha wanazoelewana wao wenyewe, kwa hiyo na kule nateua kwenye kundi hilo, nateua mabalozi wa kuhamasisha kulipa kodi kwa hiari, namteua mwana kabumbu mashuhuri Mbwana Samatta na yeye awepo kwenye Mabalozi ya Kulipa Kodi, namteua Ndugu Edo Kumwembe na yeye awepo kwenye Mabalozi ya Kulipa Kodi na kwa wanawake namteua Ndugu Hamisa Mobetto na yeye atatusaidia kuhamasisha kwenye walipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo tulikuwa tunapata shida nalo ambalo na lenyewe tunalifanyia kazi kama Serikali na kama Wizara, tuna tatizo kwenye masuala ya ukadiriaji, tunashida kubwa kwenye masuala ya ukadiriaji, ndiyo maana tuna mrundikano mkubwa sana wa kesi kwenye vyombo vyetu.

Mheshimiwa Spika, wanauliza huku hamna balozi? Subirini nimemteua Matiko kuwa Balozi wa Usemaji upande wa Magereza. (Kicheko/Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri bado sijaisikia vizuri hii. (Kicheko)

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nimemteua Esther Matiko Msemaji wa upande wa Magereza. (Kicheko)

SPIKA: Ana uzoefu wa kutosha. (Kicheko)

WAZIRI WA FEDHA NA MAPINGO: Mheshimiwa Spika, na nimemteua Mheshimiwa Ester Bulaya upande wa masuala ya wastaafu, amelisemea sana hilo pamoja na wenzake na Mheshimiwa Cecilia upande wa mfumuko wa bei, hizo hoja zilikuwa zinakuja huku mbele. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo, kwenye upande wa ukadiriaji kuna shida moja tu sisi kama Serikali tumeiona. Moja; ukadiriaji ile ya kwamba mimi nakukadiria, usiporidhika kesho uje tuongee na mimi mwenyewe na usiporidhika nenda kwenye hatua nyingine, lakini ili usikilizwe huko unapokwenda ulipe kwanza theluthi moja ya kile ambacho umekikataa.

Mheshimiwa Spika, hivi theluthi moja ya bilioni 150 ni ngapi? Theluthi moja ya bilioni 90 ni ngapi? Sasa tunapendekeza tunapokwenda tutaanzisha chombo cha Msuluhishi wa Masuala ya Kikodi ili kuwatengenezea watu wetu badala ya kutumia njia moja ya kupeleka kwenye Mahakama ya Kikodi pamoja na bureau za kikodi wawe na fursa ya kusemea mambo yao, lakini pia tunaendelea kuimarisha ile mifumo ya ndani ili pasiwe na uonevu kwenye ukadiriaji wa kodi mtu akadiriwe kodi anayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuanzia tarehe 1 Julai hili na lenyewe tutalifuatilia kwa karibu sana. Kwa mfano nilipata kesi moja hivi juzi, kuna mtu mmoja alienda akakadiriwa shilingi milioni 400, alivyokadiriwa shilingi milioni 400 yule aliyemkadiria akamwambia alete shilingi milioni 200 za kwao wale wakadiriaji, akakataa, alivyokataa hiyo ilikuwa tarehe 23 Novemba, akakataa kutoa shilingi milioni 200 hiyo alivyokataa, tarehe 23 Novemba alivyokadiriwa kwa barua kwamba makadirio yako ni shilingi milioni 400, lakini akaambiwa lete shilingi milioni 200 alivyosumbuka sumbuka akaambiwa wewe unajifanya mjanja. Tarehe 27 kutoka tarehe 23 Novemba siku nne baadaye akakadiriwa shilingi bilioni 2.5, hiyo ni tarehe 27 Novemba 2020, alivyokadiriwa hii sasa kaenda akaongea nao kwamba ule mpango basi nimeshakubali akatanguliza shilingi milioni 100, alivyotanguliza shilingi milioni 100 tarehe 3 Disemba ikashushwa ile kutoka shilingi bilioni 2.5 ikarudi shilingi milioni 320. Maana yake nini? Maana yake hii ni rushwa, haya hayawezi yakawa makosa ya kawaida. Nimepeleka kumbukumbu hii vyombo vya dola vitachukua kazi yake na wale watu nimemuelekeza Kamshina achukue hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dakika zangu zimekwenda, nilipokea jambo lile alilisemea Mheshimiwa Nape la kule TIPER, nimeelekeza zoezi lile liendelee, waendelee na utaratibu, kulikuwepo na shida ya taratibu zetu za kindani ya kiofisi nimeshaelekeza waendelee hizo hatua zingine ambazo zilikuwa zinakwamisha zitakuta wale kule wanaendelea pasiwe na gap pale.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Wenyeviti wa Vijiji pamoja na Ma-VEO, pamoja na posho mlizotaka za Madiwani ziongezeke za Watendaji niwaombe mridhie tumeanza na hatua hii, na kama ambavyo Mheshimiwa Rais alisema kwa wafanyakazi wote, alisema tunaanza na hatua hizi mwaka kesho tutaangalia zaidi na mimi nitumie kauli ile ile aliyoisema Mheshimiwa Rais tuanze na hatua hizo halafu mwaka kesho tutaangalia zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mifugo, kilimo na uvuvi, tumeshaongea na Wizara zinazohusika na mimi natoa ridhaa ya yale maeneo ambayo yanataka kufanya financing za kisasa wafanye hivyo kwa upande wa mifugo, kilimo na uvuvi na sisi kama Wizara tutafanya nao karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata kwa upande wa Zimamoto, upande wa Zimamoto tumeongea na Waziri anayehusika natoa ridhaa arekebishe kanuni kwenye upande wa makato yale ya tozo zile ambazo zinakuwa ngumu kukusanyika kwa upande wa Zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Askari Magereza pamoja na wa Zimamoto na yenyewe tunaoanisha, tumeongea na Waziri mwenye sekta, Mheshimiwa Simbachawene, tumeoanisha na wenyewe kwenda miaka sita kama tulivyosema kwa polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye mambo ya sensa ya mwaka huu inayokuja tunapanga tuimarishe na kile kipengele cha makazi, tulikuwa tunaangalia zaidi upande wa idadi ya watu, tutaweka mkazo kwenye upande wa makazi ili hivi vitu vingine ambavyo vinahusiana na mambo ya makazi na vyenyewe viweze kuzingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa miradi ya kimikakati, Mheshimiwa Asenga amesema sana kule kwake, nimemuelekeza Katibu Mkuu ashungulikie yale maoni yako, asimamishe lile jambo ambalo lililokuwa linafanyika ambalo umelisema kwa nguvu sana ili waweze kuingia kwenye mkataba ambao utakuwa na manufaa kwa wananchi siyo ule ambao unaleta fedha, unatumia fedha nyingi kuliko maeneo mengine yote ambayo yaliwahi kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa Covid tunaenda na utaratibu ambao Mheshimiwa Rais aliunda Kamati na kamati ile ilishatoa taarifa na sisi tutaendelea kufanya kama ambavyo imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mengine tutaendelea kufafanua tunapokuja kwenye Finance Bill, lakini nililisikia jambo la Mheshimiwa Festo Sanga la nyasi wamesema na Wabunge wengine wengi ambao wamesema kwa kweli isiishie tu majiji na sisi tunakubaliana, tutaenda mpaka Manispaa na kwa maeneo mahususi ambayo hayako Manispaa wala hayako, lakini yanauwitaji huo tutaweka kipengele ambacho itahiji ruhusa maalumu mbali na ile ya BMT ambayo mlipendekeza tuipeleke ya kutolea ridhaa ili iweze kuombewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutaenda mpaka Manispaa, lakini kama kuna eneo mahususi litaombewa tutaweka kwenye kipengele tunavyokuja kwenye Finance Bill kwa yale ambayo hayako pale, tumeona tuanze na hivyo kwa ajili ya control, hilo lilikuwa na nyasi bandia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona kengele imeshagongwa kwa kumalizia, tumeongelea hii sekta ya michezo, lakini lazima kwenye michezo mimi ninavyoangalia hii naongea tu kiuanamichezo, siyo kama shabiki na uniazime dakika zingine mbili za nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwenye michezo bado tunakosea kwenye mipangilio/mipango yetu, vitu vyetu vingi bado vinakuja kwa dharura. Ninaposema haya kwanza niipongeze kabisa Simba imefanya hatua kubwa sana mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mimi nilivyokuwa naiangalia Simba ya mwaka huu, Simba ya mwaka huu ilikuwa ya kwenda kuchukua ubingwa. Kuna mahali tumekosea na tunakosea pale ambapo hatuweki vipaumbele, yaani sisi kwetu mambo yote yako sawa tu, kwamba mtu anaenda kucheza mchezo ambao unaweza kuleta kombe Tanzania kwa mara ya kwanza, anaenda kucheza nusu fainali, maana yake ili ucheze fainali lazima ucheze nusu fainali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anaenda kucheza mchezo mkubwa wa kuleta kombe mathalani, ukishinda nusu fainali na kiwango nilichokuwa nakiona wangeweza kuleta kombe. Huku una mchezo wa nusu fainali wa muhimu kwenye historia, katikati yake unaweka mechi ya watani. (Kicheko)

Sasa mimi nilivyoona Simba walivyofungwa kule Afrika Kusini, wao na wengine wanaaminishwa kama wamehujumiwa na nani yule/anaitwa nani yule, Senzo, wengine wanaaminishwa kwamba wamehujumiwa na watani mnawalaumu watani bure. Kiuanamichezo kabisa tunakosa mpango, Simba imeenda kucheza South Africa bila game plan, yenyewe ilijiandaa na mechi ya mtani na mimi niwapongeze Yanga, walivyoenda uwanjani wakakaa dakika kadhaa wakaona Simba hawapo, wakajua wanajiandaa na mchezo hawa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, on a serious note timu zinazokwenda kwenye mashindano ya Kimataifa, zinaleta sifa ya Taifa. Lazima bodi hizi zinazosimamia wawe wanawapa kakipaumbele wawape, waangalie wangeweza kupeleka mchezo huko. Kwa sababu leo hii, kwenye timu zetu hata kama ni fainali ukiweka mtani hapa akili zote na miundombinu yote inaelekea hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Simba hii ilivyokuwa imempiga Al- Ahly ingehujumiwa na Senzo kweli! Eti ihujumiwe na mashabiki! Hapa walienda bila game plan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, la mwisho niwapongeze sana wana Yanga ambao wamewaunga mkono Simba. Wamewaunga mkono Simba, wana Yanga wamewaunga mkono Simba kwa kuwapa Morrison, licha ya wana Simba kuwa na mashabiki wenye heshima wengine tunao humu humu, hawakuwahi kurudisha hata tiketi tu ambayo Yanga walimletea Morrison hapa. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, nakukumbusha baada ya hapa kuna kura zinapigwa! (Makofi/Kicheko)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wana Yanga muendelee na upendo huo huo na wala waachieni tu Morrison anakuja Makambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa nimewasilisha na kufafanua baadhi ya hoja, msingi wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2021/2022, 2025/2026, wenye dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu, kwa mara nyingine tena nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge wote, wananchi na wadau wote kwa kuendelea kushirikiana pamoja katika kutekeleza mpango huo. Na niwaombe Watanzania wote tujitoe tumuunge mkono Rais wetu katika kutekeleza dira hii twende naye bega kwa bega nchi hii itajengwa na Watanzania wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru tena, Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuiunga mkono Serikali na kabla sijahitimisha maelezo yangu, nichukue fursa hii pia niwashukuru watumishi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango, nikianza na Naibu Waziri - Mheshimiwa Mhandisi Hamad Masauni, Mbunge na Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu Emmanuel Mpawe Tutuba, Naibu Makatibu Wakuu - Ndugu Amina Shaban, Dkt. Hatibu Kazungu na Ndugu yangu Adolf Ndunguru kwa kutupa ushirikiano mkubwa katika kuandaa na kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Niishukuru tena Kamati yako ya Bajeti nimeenda mle hii Kamati inafanya mambo very professional, tulifanya uchambuzi ulio bora sana na ndio maana kazi yetu inakuwa rahisi. Naamini tutatekeleza pakubwa zaidi na hata zile hoja walizotoa za kutengeneza utaratibu wa monitoring and evaluation, unaweza pia ukaendelea kuzitumia Kamati hizi. Kamati ya Bajeti, ya LAAC pamoja na ya TAMISEMI kwenye haya maeneo ambayo tunaelekeza fedha nyingi wakaweza kufanya ufuatiliaji sambamba na taasisi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa nimetoa ufafanuzi huu naomba sasa, Bunge lako liridhie bajeti hii na nawaomba Wabunge wote na naamini Halima Mdee kwa mara ya kwanza utapiga kura ya ndiyo. Wote tuipigie bajeti hii kura ya ndio kwa sababu inakwenda kufanya mapinduzi. Wote na wenzako, hii ni bajeti yetu, tumeshiriki kuitengeneza na angalieni vitita tunavyoondoka navyo kwa ajili ya miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waheshimiwa wananchi nifafanue tu hilo sio kila Mbunge atabeba kwenye pickup hizo fedha, bali zitakwenda kwenye Halmashauri zetu Wabunge wenu wameziomba tu, ila wasije wakafika kule wakasema Waziri aliwaambia mtakuja na hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitumie fursa hii kukushukuru wewe mwenyewe, Naibu Spika, Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Bunge ya Bajeti pamoja na wajumbe wa Kamati lakini pamoja na Wabunge wote waliochangia katika hoja hii ya leo ambayo nahitimisha muda huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote baada ya hayo nitamke kwamba hoja zote zilizotolewa kuanzia hoja zilizotolewa na Kamati, hoja zilizotolewa na Wabunge, hoja zilizotolewa na Mawaziri, tumezipokea sisi kama Wizara na tuwaahidi kwamba zitafanyiwa kazi na tutakapokuja na draft nyingine ya Mpango ambao utakuja kwa hatua nyingine tutakuwa tumejumuisha na maoni hayo ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo nikuombe na Waheshimiwa Wabunge watuamini na hatutaweza kuiongelea hoja moja baada nyingine kwa sababu hoja hizo zilizotolewa ni nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo machache tu ambayo nitaomba uridhie niyagusie ni yale ambayo yanahitaji ufafanuzi yale ambayo tumepewa maoni na tumepewa ushauri tutachukua na kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na eneo hili hili ambalo limejadiliwa muda siyo mrefu ambalo lilikuwa linaongelea masuala ya madeni kwa wastaafu. Kwanza kwa mtu akisema Serikali haina nia njema na madeni haya ya wastaafu itakuwa ni bahati mbaya sana na atakuwa hata hajazingatia kwamba hata hilo deni kiini chake kilitoka wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madeni haya ambayo tunaongelea leo mengine ilikuwa ni hiyari ya Serikali tu kwamba tunaenda kuwalipia watumishi wetu na yalichukuliwa Serikali ilikubali kubeba mzigo ili iwalipie watumishi wake. Katika hilo si kwamba tangu muda ule hamna kinachofanyika Serikali imeshafanya ni vile kwamba kulikuwepo na accumulation kubwa lakini Serikali imeshafanya na imefanya kwa kiwango kikubwa tu ambacho kinastahili kupongezwa na ukichukuliwa jinsi ambavyo Serikali inafanya inatakiwa iweke matumaini kwamba hili ni jambo ambalo linaenda kukamilika na katika suala la muda tutaweza kufika katika hatua nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika siku ambazo si nyingi sana tayari PSSF walishapewa bilioni 500 kwa ajili ya jambo hilo hilo na NSSF walishapewa bilioni 100 na katika kipindi cha ndani ya miezi mitatu kwenda minne iliyopita tuliongezea bilioni 50 nyingine kwa ajili ya masuala hayo hayo ya kuwalipa wazee. Na hata hii tuliyosema tunafanya noncash bond labda hii taaluma na yenyewe labda iwe na shida watu hawajui hii ni float ya kwanza tume-float ya kwanza kwa kiwango hicho na siyo ya mwisho tuna float ya kwanza kwa kiwango hicho na siyo ya mwisho. Tuna float ya kwanza tunaitekeleza halafu tuna-assess imefanyikaje tuna-assess deni halafu baada ya hapo tunaendelea na utekelezaji ule ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wengine wanaolalamika sana ni vile tu Bunge lako si kiwanja cha utani ingekuwa kiwanja cha utani hawa wangekuwa watani zangu ningeweza kukwambia wao wanadaiwa nini hata wao binafsi waone suala la madeni huwa likoje na hata sasa wanatamani uwaruhusu hata gratuity. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapoongelea haya mambo kwa mwingine ambaye anafanya jukumu kubwa tusiwe tunasahau undani wa mzigo wenyewe unavyokuwa Serikali imeshafanya jambo kubwa na itaendelea kufanya jambo kubwa na katika kipindi ambacho tayari Serikali imechukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hatua ambazo zimewabadilishia maisha wazee hao ni jambo kubwa ambalo limefanyika ambalo halipaswi kubezwa ilikuwa ikitokea Bunge inaendelea kama hivi unakuta wazee wengine wako misikitini wengine wako makanisani wengine wako tu wamehifadhiwa mahali hivi. Lakini baada ya utaratibu huu wa kuanza kutoa hizo fedha tena kwa mtiririko tena kwa ukaribu karibu jambo hili limeanza kubadilika pakubwa na tunaamini baada ya hatua hii kubwa ambayo Mheshimiwa Waziri anaifanya kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kukamilisha masuala ya kikokotoo tutaongeza zaidi kasi na tutaenda kulifanyia jambo hili ambalo lilikuwa tatizo kuwa ni historia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine hiki kinatajwa tu kwamba CAG amesema deni ni trilioni 19 hii ni namba na watu wale wale CAG yule yule aliposema madeni yanayodaiwa na TRA ni trilioni 360 walisema hii haiwezekani kwamba hizi ni namba tu CAG kazitaja tu kwenye hii hapa namba hii hii wanaona hiyo ndiyo namba tu. Lakini niwaambieni kila kitu kinachoitwa deni yanafanyika verification na yale ambayo yameshakuwa verified yanafanywa malipo na hilo ni jambo ambalo litafanyika na litakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningeomba nilisemee kwa uzito mkubwa unaostahili ni hili ambalo na Mheshimiwa Naibu Waziri ameshalielezea, sitaelezea katika angle ambayo tayari ameshafafanua hili jambo la deni la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la deni la Taifa tuna orodha ndefu sana ya miradi ambayo imeshafanyika na niwaombe watanzania hasa hasa sisi Wabunge ambao ni viongozi tusianzie mbali sana twendeni tu tuanzie wakati deni la Taifa liko katika kiwango tuseme cha trilioni 10 tuanzie hapo hapo halafu tuanze kuangalia katika mwaka 1995 tuseme tuangalie katika mwaka 1995 deni lilikuwaje halafu tuangalie pia na miradi ambayo ililetwa na fedha zilizokopwa kipi tulitakiwa tukifanyie uamuzi katika mwaka huo ambapo tunaongelea deni la Taifa likiwa dogo, hatukuwa na mikoa ambayo imeunganishwa kwa barabara za lami yaani kutoka Singida kuja Dodoma hapa tulikuwa tunahitaji siku nzima. Kutoka Singida kwenda Arusha tulikuwa tunahitaji siku nzima, kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam tulikuwa na option ya kupita nchi mbili kutoka Kagera kwenda Dar es Salaam tupite nchi mbili, kutoka Dar es Salaam kwenda Lindi tulikuwa tunahitaji wiki kabisa. Kutoka Dodoma hapa walioingia vipindi viwili vitatu kutoka Dodoma hapa kwenda Isimani hapa ilikuwa lazima uende kwanza Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengine ni wadogo sana hawajui haya yaani ukitaka kusafiri begi kwanza mabasi yenyewe begi lilikuwa linakaa kwenye carrier halafu mnapofika yeye aliyemsafiri na yule utingo wote hamtofautiani ndivyo ilivyokuwa sasa analysis iliyofanyika ni je, tuchukue makusanyo ya fedha tujenge barabara zetu tufungue uchumi halafu tukishafungua uchumi ule utuletee fedha tuendelee kulipa madeni ndiyo uamuzi uliofanyika. (Makofi)

MWENYEKITI: Halafu Mheshimiwa Waziri yale mabasi yalikuwa yameandikwa ukiingia mle ndani kwamba kila abiria tunza mzigo wako wa ndani ule wa kwenye carrier utingo atajua endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndivyo ilivyokuwa kwa hiyo ukatakiwa ufanyike uamuzi wa makusudi tu kwamba je tuendelee na hali kama hii hii halafu na deni letu liwe dogo au tuchukue fedha tutengeneze miundombinu tufungue nchi yetu halafu miundombinu hiyo ituletee fedha tulipe deni tunalokopa. Ndiyo uamuzi uliofanyika sasa hivi baada ya njia kuwa zimeshafunguliwa sana karibu kila eneo na hii nimeongelea tu barabara lakini ni maeneo mengine mengi kwenye umeme hivyo hivyo sehemu ya robo ya nchi ndiyo ilikuwa na umeme kwingine kote ilikuwa giza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo kwenye umeme hivyo hivyo na sekta zingine taja na sekta taja kwenye afya taja kwingine kote uamuzi ukafanywa kwamba je, tubakie na deni dogo halafu na miundombinu yetu yote hafifu au tukope tufungue miundombinu halafu baada ya hapo tulipe? Ndicho kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna orodha ya miradi inaelekea karibu 1000 ambayo imejengwa siwezi hata kuanza kuutaja mmoja mmoja lakini kwa sababu sisi ni viongozi kila mmoja aanze kupekua mmoja mmoja ambao ana maslahi ya kutaka kufahamu aone umejengwa kwa kiwango gani umejengwa kwa financing gani? Imefungua nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata masuala tu ya umeme wenyewe umeme si nguzo za umeme, umeme ni uzalishaji wenyewe wa umeme imefanyika njia hizo hizo mpaka sasa hivi watu karibu nchi nzima walishazoea masuala ya umeme watu karibu nchi nzima walishazoea masuala ya mawasiliano ya simu hayo yote ni analysis za kufanya uamuzi halafu likafanyika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani wakati tunasoma ilikuwa umeme unakatika ukiwaka mnashangilia kama goli la simba maana yake simba siku hizi ikifunga dakika zimeshaenda watu wanashangilia mpaka nyumbani. Watu wanashangilia kumbe umeme tu umerudi umeme. Kwa hiyo, tathmini ikafanyika uamuzi ukafanyika na madeni haya yameongezeka lakini pia miundombinu iliyojengwa na fedha hizo imeongezeka tusifanye tathmini ya deni tu kama vile tumebambikwa tufanyeni tathmini ya deni huku tukifanya na tathmini ya miradi ya fedha hizo ambazo zimefanywa kutokana na deni hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wengine wanaenda mbali zaidi hizo ndiyo cheap politics wanaenda wanasema Serikali ya Awamu ya Sita imeingia tu kwa miezi sita imeshakopa zaidi ya bilioni tisa. Jamani ndugu zangu hivi hata ibada hamfanyagi, hamuogopi hata Mungu? Mkopo wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Sita mkopo wa kwanza wa mama ni hii trilioni 1.3 ambayo imetoka IMF na kwa mazungumzo yanayoendelea utakuwa mkopo ambao una masharti nafuu kuliko mikopo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo mkopo wa kwanza na mpaka sasa Serikali ya Awamu ya Sita haijakopa mkopo wowote wenye masharti ya kibiashara bado haujakopa labda mkopo wa kwanza utakuwa wa kukamilisha loot ya tatu ya nne na ya tano. Sasa hata hilo ni jambo ambalo tunatakiwa tufanye tathmini tu je, tuache tu kufunga hiyo loot three, loot four na loot five? Kwa kuogopa deni? Au tupitishe bakuli maana yake hata Yanga tulishaacha kupitisha bakuli tunachukua mzigo mkubwa tunamalizia loot hiyo hapo tunaanza inayoenda Kigoma tunaanza inayoenda Kalemi tunakamilisha zote tunafungua fursa za biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni miradi ya msingi ambayo unafanya analysis kama uchukue deni au uache ubaki umeufunga uchumi wako haya ni mambo ya msingi Serikali yetu haijawahi kukopa kwa ajiili ya kulipa mishahara wala kwa ajili ya kujaza mafuta kwenye magari inakopa kuweka miradi ya wananchi ambao wananchi wenyewe tumeshawatengenezea kiu kila mwananchi anataka jambo lifanyike zuri zaidi katika eneo lake na hii niwahakikishie watanzania tuko kwenye mwelekeo ambao ni sahihi na wengine walikuwa wanasema hata kwamba Serikali imetumia reserve zilizoachwa. Reserve zilizoachwa hazijaguswa na zimeongezeka sana sasa hivi tunaumiza vichwa ku-control mfumko wa bei kwa sababu pia fedha zinapokuwa nyingi sana inabidi muangalie na kwenye policy aspects za kuangalia mfumko wa bei ukoje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda mwaka 2015 reserve zilikuwa dollar bilioni 4.3 wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia wakati Serikali ya Awamu ya Tano inamaliza ilishaongeza reserve kutoka bilioni 4.3 kwenda bilioni 5.04. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Machi 2021 wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia, tayari imeshapandisha kutoka bilioni 5.03 kwenda bilioni 6.4 hizo ndiyo reserve zetu tulizonazo ni zaidi ya miezi sita ya uagizaji wa bidhaa tuko juu kabisa mbali na kiwango kinachotakiwa katika standard za kimataifa. Na ukienda kwenye tathmini angalieni IMF wanatutathmini vipi, angalieni Benki ya Dunia inatutathmini vipi halafu ndiyo hapo muweze kuangalia ni kitu gani ambacho kinaweza kikaangaliwa ili uweze kutoa hoja kama mtu unataka kutoa hoja katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya ni mambo ambayo watu wanatakiwa wayafanyie tathmini fedha zingine za miradi mikubwa hii zingine zimetoka Awamu ya Tano zimeingia Awamu ya Sita zingine zilitoka Awamu ya Nne zikaingia Awamu ya Tano hatupaswi sana kuangalia tu mambo ya fedha tunatakiwa tuangalie fedha hizi zimefanya nini unajua ingekuwa jambo la msingi sana watu wangekuwa wanasema hii fedha hamjaitumia katika eneo ambalo linaleta manufaa. Hilo ndiyo jambo la msingi kuongelea ongelea fedha tu hii watani zangu hapa sijui ni akina nani unakuwa kama Wanyaturu wanaogopa kupanda karanga kwamba nalalaje ndani halafu karanga ilale nje kumbe unavyopanda karanga ndiyo utavuna nyingi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwekeze tunatakiwa tujadiliane kuhusu tumewekeza sahihi au si sahihi hiyo ndiyo itakuwa akili ya watu wenye maarifa ya kuwaza nchi inaelekea upande gani. Siyo kila siku watu wanawaza wanaangalia namba tu halafu na wengine wanawatisha wananchi wetu kwamba unajua zitaanza kugawanywa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat anatoa macho hapa, ahsante endelea Mheshimiwa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie fedha zilikowekezwa, na jambo lingine zuri zaidi na hata Mbunge wa Mtama Mheshimiwa Nape alitoa pendekezo, pendekezo hilo sisi tunachukua kama Wizara tutafanya tathmini halafu tuangalie kama tunaweza tukaongea na taasisi halafu tufanye refinancing tuangalie tufanye refinancing ni kitu ambacho watu huwa wanafanya. Unaweza ukakopa ulikuwa na mradi una uharaka ukakopa halafu masharti yakawa yako juu sana unaangalia kama unaweza ukapata refinancing kwa mfano kama hivi tunasema tumepata fedha hizi trilioni moja na zaidi zikawa hazina riba halafu grace period miaka 10 ukiwa na fedha nyingi za aina hiyo unaondoa zile ambazo ulikuwa na grace period ya miaka miwili na riba ya asilimia 9 halafu unakuwa na fiscal space ambayo unaweza ukatekeleza shughuli zingine za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ambayo yanaweza yakaweka ahueni kwenye upande wa deni lakini pia ikatusaidia kuendelea ku-finance miradi ya maendeleo ambayo wananchi wetu wanahitaji kuendelea kuona maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amesema tutafungua mikoa yote ambayo bado haijamaliziwa kufunguka wapi huko Mpanda kwenda Kigoma kwenda Rukwa kwenda Tabora wapi huku Lindi maeneo yale ambayo yanauzalishaji mkubwa Mtwara yanauzalishaji mkubwa wa korosho lakini barabara hazifikiki wapi huku kwenye mbao na maeneo mengine huku Ruvuma maeneo mengine kule Manyara na mikoa mingine mingi kwenda Simiyu huko na maeneo mengine mengi Ifakara huku maeneo mengine yote yale ambayo yanatuletea uzalishaji mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amesema yaangaliwe yawekwe kwenye mpango ili tuweze kufungua uchumi unajua tunapofungua uchumi tunagusa mpaka kwenye kilimo, tukifungua barabara tunagusa mpaka kwenye uzalishaji upande wa kilimo haya yote tunaenda kuyaangalia ili yaweze kufanyika kuleta tija kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwa ajili ya muda niweze kuliongea na lenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri ameshaliongelea upande mmoja nitaongelea upande mwingine ni upande wa kilimo. Eneo hili la kilimo na Waheshimiwa Wabunge tunakubaliana wote sisi hatupingani na mawazo ya Wabunge, lakini kitu kimoja tu tunachosema ambacho tumekuwa tukijadili sana na Wizara ya Kilimo na tunaendelea kuwa na uelewa wa pamoja ili tuweze kusonga mbele na tunaongelea kilimo kwa ile dhana pana ambayo inaweka na mifugo inaweka na uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, safari ya sekta hizi siyo fupi ni safari ndefu tu ambayo tumekubaliana tu kwamba tunaanza wapi katika huo mwelekeo wetu. Kati ya maeneo haya ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kesho ama keshokutwa nadhani hata sasa hivi tunavyoongea Mheshimiwa Naibu Waziri ameniambia kuna kazi ambazo zinaendelea lakini na Waziri tulikuwa tumekaa meza pale akasema anashughuli nyingine ambayo anatakiwa aifanye inayohusiana na masuala ya kilimo, lakini akasema angekuwepo humu Bungeni angetamani aseme neno moja tu ahaa amesharudi huyu hapa Waziri wa Kilimo. Aliniambia neno moja analotamani kusema yaani tofauti ya sasa na muda mwingine Wizara ya Kilimo, Wizara ya Kilimo sasa haijaomba fedha ikakosa na anatarajia kwamba mpaka anamaliza mwaka huenda akawa amepata asilimia 100 ya bajeti huyu hapa yupo amesema hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba inawezekana kwa mwaka huu sasa Wizara ya Kilimo ikawa na asilimia 100 ya bajeti tofauti na ilivyokuwa 12, 20, 13, 20. Hiyo ni hatua ya kwanza tumewapatia fedha hata kama ni kidogo zile walizoomba, lakini hatua ya pili tumesema tutatenga fedha kwa ajili ya mbegu. Maana yake Mheshimiwa Waziri amesema transformation anayotaka kufanya siyo tu ya kiutawala kwenye Wizara ya Kilimo anataka hasa kwenye sekta yenyewe. Kwa hiyo la kwanza ni mbegu na sisi tumesema tunavyoanza kutengeneza bajeti hii tuta- accommodate bajeti ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu tumeongea na Mheshimiwa Waziri tukasema kwenye umwagiliaji kuna angle mbili, angle ya kwanza tunaweza tukavuna maji, duniani kwote wanatumia pia umwagiliaji wa kuvuna maji. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ameshanunua mitambo kwa ajili ya kuchimba mabwawa. Tumeongea na Waziri na ile Idara ya Umwagiliaji wafanye tathmini kwenye mitambo ile ya kuchimba mabwawa je, kwa bwawa la umwagiliaji ni mitambo gani bado inakosekana? Walete tathmini tuiongeze na hiyo, kwa sababu wakulima wetu wengine siyo wakulima wa ma-estate makubwa ni wakulima wa mashamba ya kawaida ambayo yanaweza wakatengeneza mabwawa ya umwagiliaji wakamwagalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mifano ya maeneo ambayo watu wameweza kumwagilia na wakaweza kubadilisha maisha yao. Kwa hiyo hili ni jambo lingine ambalo Rais wetu ametuelekeza tukae na wenzetu tufanye tathimini na yale ambayo yatahitajika tutafanya hivyo ili umwagiliaji uweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umwagiliaji mwingine ni ule umwagiliaji mkubwa wa kuweka mabomba ya kutoa maji kutoka eneo la mbali kupeleka eneo lingine la umwagiliaji. Haya tumesema taasisi ile ya umwagiliaji wakae na Wizara ya Maji tutakapokuwa tunafanya miradi mingine mikubwa ya maji, tutakapokuwa tunatekeleza miradi mingine mikubwa ya maji labda kutoka Mto Ruvuma kwenda Ruvuma yenyewe kwenda mpaka Lindi na Mtwara au kutoka Tanganyika kwenda Katavi, kwenda mpaka Rukwa waangalie teknolojia za kisasa za kutengeneza miundombinu hiyo pawepo na lane zinazopeleka maji ya matumizi ya nyumbani, pawepo la lane zinazopeleka maji ya umwagiliaji. Tuone kama kuna namna ya engineering hiyo ambayo inaweza ikafanyika ambayo inaweza ikawa cost effective na ikatusaidia kuweza kutekeleza hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumesema tutayaangalia haya mazao ambayo ni mazao makubwa katika nchi yetu kuna mazao yalishawahi ku- peak mpaka worldwide yakawa yanajulikana ikafika mahali yakawa yameshukashuka tumesema tutayaangalia, tutaangalia pia refinancing yake, mifano imeshapatikana katika maeneo ambapo pembejeo zimeweza kuwa refinanced kutoka katika utaratibu wa ndani ya mazao yenyewe. Tumesema hayo yote tutayaangalia tuone ni namna gani tunaweza tukaweka utaratibu ambao utatusaidia katika uhakika wa masuala haya ya pembejeo na jambo hili ni jambo ambalo linawezekana na litawezekana kwa mazao yote hayo na tunatambua Bodi hizi zimekuwa na viporo viporo vingi hivyo hivyo na TFC yote haya tutakaa na wenzetu tuone ni namna gani tutafufua haya maeneo ili tuweze kuendelea na yaweze kupiga hatua kubwa zaidi na wakulima wetu na wananchi wetu waweze kupiga hatua kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya tunayoyasema kwenye upande wa kilimo nimesema ni hivyohivyo na sub- sectors zingine ambazo zinaangukia katika eneo hilo, tutafanya hivyo kwa mifugo, tutafanya hivyo kwa uvuvi kwa sababu ni sekta hizo kubwa ambazo zinabeba eneo kubwa la wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kufanya hii transformation kwenye hii sekta ya kilimo tutakuwa na risk mbili; risk ya kwanza sustaining kuendelea kupanda kwenye rating hizi za kipato cha kati, kipato cha kati cha chini, kipato cha kati cha juu itakuwa ni ngumu sana kwa sababu watu wenye eneo kubwa ambao wanatakiwa wafanyiwe hiyo tathimini ya kipato kwa mtu mmoja watakuwa bado wapo mbali na utaratibu wa kuweza kupata kipato kikubwa kwenye shughuli ambazo zinawaingizia kipato. Kwa hiyo tunalenga kufanikisha hili ili kipato cha mtu mmoja mmoja kiweze kupanda kwa sababu population iliyokubwa ipo eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tunalolenga katika eneo hili la kukuza hizi sekta tulizozitaja ni ili tuweze kukipeleka kizazi cha leo katika shughuli za uzalishaji. Kuna Mbunge mmoja alisema hamna utafiti ambao umeshafanyika kwenye hili eneo, niwahakikishie utafiti umeshafanyika majibu tunayo na siku si nyingi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ama Waziri Mkuu mwenyewe atatoa tamko linalohusiana na matokeo ya utafiti wa eneo hilo. Kati ya maeneo ambayo yamekuwa na yanaajiri watu wengi tena ngazi hii ya vijana ni eneo hilo hilo ambalo mmoja wa msemaji alisema halijafanyiwa tathmini nani hilo hilo ambao linahusisha mpaka upande wa kilimo, upande wa vijana wanaojiajiri wamachinga na hilo ni eneo ambalo tutaliangalia vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo kitu kingine ambacho tunakilenga kwenye upande wa kilimo ni kwa ajili ya ajira, tunataka tupeleke hii generation ya kileo iweze kufanya shughuli hizo za kilimo, mifugo pamoja na uvuvi. Tusipo-transform hizi sekta hii generation ya kisasa haitaweza kufanya hizo shughuli. Katika maeneo mengi ambayo kilimo ama mifugo ama uvuvi unafanywa kwa zile traditional ways katika maeneo ambayo kilimo kinafanywa kwa njia ya zamani sana kizazi cha leo hakishiriki kwa asilimia kubwa katika hicho kilimo. Kwa hiyo, inabakia kama ngoma ya kienyeji hivi inafanywa na wazee wa zamani ndiyo wanaweza wakakuimbia ukaona kumbe hii ndiyo ngoma ya kabila letu. Kwa maana hiyo tuta-transform ili tupeleke kizazi cha leo hii shughuli ili tuweze kuwa World’s largest exporter wa zao fulani tunahitaji na kizazi cha leo kishiriki katika uzalishaji wa shughuli hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo na kwa upande wa machinga taarifa njema inakuja hii ya utangulizi mmeshaipata na Mheshimiwa Rais anania njema sana kwenye jambo hili na yeyote ambaye atalifuatilia kwa umakini na baada ya muda fulani ataona kwamba Mheshimiwa Rais anataka awabadilishe wamachinga kutoka kwenye kutumikishwa wao wenyewe wapate mtaji waweze kusimama wafanye hizo shughuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ya sasa hivi walichokuwa wanafanya anatembea na bidhaa za watu kwa sababu hatuwezi tukawafikia hata tukitenga hizo asilimia ngapi ngapi hizo hatuwezi kuwafikia. Sasa tukiwa na uwezo wa kuwafikia, mmeona Dar es Salaam wameshaanza, maeneo mengine wameshaanza wanatengeneza SACCOS zao tunaamini wakishakuwa katika maeneo ambayo yatafikiwa wataweza kupata fedha kwenye SACCOS zao, wataweza kutembea na bidhaa zao, wataweza kuuza bidhaa zao na tunaendelea kuangalia na Waziri wa Ardhi yupo hapa, eneo moja ambalo tutaliangalia kwa umakini na Mheshimwa Rais ndivyo alivyoelekeza ni kuwaweka katika maeneo ambayo ni very strategic ili yule mtu aliyekuwa anaenda kwenye eneo lile ambalo ana-first target yake anavyomaliza hiyo first target yake asitake kusafiri kwenda mbali sana kwenda kumtafuta huyo mtu mwingine mwenye bidhaa ndogo aweze kumfikia na yeye hapo hapo, lakini kwenye utaratibu ambao umepangiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivi vitu vingine watu wengine unaweza ukadhania kwamba wao ndiyo wanawahurumia lakini kumbe wao ndiyo hawawahurumii hawa vijana wetu kuna maeneo mengine wanafanya hata katika mazingira sana lazima tuyabadilishe. Mimi nilipita eneo lingine mvua ikija yao, jua likija lao, lakini kama tunaenda tunaendelea tuwabadilishe kuzingatia tu wawe katika eneo ambalo haliathiri wao kufikika kwa wateja wao ambao wanawategemea katika kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kutambua michango ambayo Waheshimiwa Wabunge wameisema eneo lingine ambalo lilitajwa kwa kiwango kikubwa lilikuwa la riba ufafanuzi wake ni mrefu na niendelee kusema kwamba hayo ni maoni yametolewa sisi tutaendelea kukaa na wataalam wetu kuyafanyia kazi, lakini pia tutaendelea kuchukua hatua ambazo zitatupeleka kwenda kufanikisha riba hizo kuwa rafiki ili ziweze kuleta tija. Eneo hili la riba na lenyewe lipo trick kidogo, lakini kama ambavyo Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo akiwa Mwanza na ameendelea kutoa maelekezo akiwa ndani ya Serikali tunaamini kwamba tutalifanyia kazi na litaweza kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge kazi hii inayofanyika na kule tunakoelekea huu ni mpango ambao tunajadiliana, lakini pia tunajadiliana maeneo ambayo tumeyafanyia kazi. Hata hapa tulipotaja tumetaja machache tu, yale yote ninyi mlioyataja yapo na mengine sisi tumeyataja kwa maandishi yote tutaendelea kuyafanyia kazi na tutayaweka kwenye utaratibu wa kuyaboresha kwa maana ya kwenye Mpango, lakini pia tutaboresha kwa maana ya utekelezaji wake ili tuweze kuhakikisha kwamba mpango unaofuata unafanya kazi kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda pia kutekeleza miradi mikubwa moja mmetoka kumsikia Waziri wa Nishati, lakini ipo pia miradi mingine mikubwa ambayo tunategemea itaweza kutengeneza impact kubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii mikubwa itakavyotekelezwa bomba la mafuta, LNG pamoja na miradi mingine hii ambayo ni mikubwa na ya kimkakati inayoendelea, yote hii itaendelea ku- inject fedha kwenye uchumi wetu na hata hilo alilosema mdogo wangu wananchi wanataka fedha mfukoni, yaani hata hii fedha tu ambayo mkienda huko Majimboni watendaji wetu watawaambia kwamba katika kipindi cha muda mrefu hawajawahi kupokea fedha nyingi hivi kwa wakati kwa mara moja kwenye miradi mingi hivi, mwisho wa siku fedha hizo zitakwenda kwa wananchi, kwa sababu ndiyo watakaojenga madarasa, ndiyo watakaojenga vituo vya afya, hata wale wakandarasi watakaochukua kazi hizo watatengeneza ajira za watu watakao ingia katika kutengeneza iwe darasa, iwe kituo cha afya au iwe madarasa ya shule zile za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni awamu ya kwanza tunaendelea nayo, tuna maliza hii tunaenda majengo mengine hiyo yote ndiyo itakayokuwa njia ya fedha kuendelea kuzipeleka kwa wananchi. Sasa hivi kila Wilaya hawataazimana mafundi yaani kila fundi aliyepo kwenye Wilaya yake atabaki pale pale kwa sababu shughuli zinaendelea kila Kata. Trilioni moja na zaidi inaenda kwenye kila Kata, kila eneo, kila Wilaya ya nchi hii na fedha hizo zitakuwa zinazunguka kwa wananchi mle mle na hayo yote yanaendelea kuchochea fedha ziwepo nyingi kwenye mzunguko kwa sababu hatutoi mkandarasi kutoka nje ya nchi kujenga darasa maana yake atakuwa wa humo humo, maana yake hiyo fedha itakuwepo humu hiyo itaongeza fedha katika mzunguko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, in long run pia tutaendelea kutengeneza ajira za kudumu kwa sababu hatuwezi tukajenga madarasa elfu 15 halafu Walimu wakawa wale wale, tutaongeza walimu hatuwezi tukajenga vituo vya hivyo vya afya vyote hivyo kila tarafa halafu yakawepo majengo tu, hatuwezi tukashusha X-Ray hizi zote kila wilaya CT scan kila Mkoa halafu pasiwepo na ajira ya kudumu, ajira za kudumu na zenyewe zinaenda kutengenezwa tutaongeza na wataalamu katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hili jambo siyo la mara moja yaani hii maana ya ‘Kazi Iendelee’ hii siyo jambo la mara moja maana yake linaendelea, watu wengine baada hizi fedha kushuka nyingi hivi walidhani ni bajeti ya miaka mitano, yaani hii hapa ni bajeti inayoenda mpaka mwezi wa sita tu, na mama akasema ule mwaka mwingi unaofuata utakuwa kiboko zaidi na hivi tunavyoongea kuna fedha zingine zipo kwenye reserve. Kwa hiyo inayokuja itakuwa kiboko zaidi, sasa wewe chukulia madarasa ya mara hii ongeza ya mwaka kesho unakuja, ongeza vituo vya afya mwaka kesho nenda kwenye barabara hivyo hivyo fedha zinakwenda kwenye ofisi ya TARURA katika kiwango hicho, ongeza na mwaka mwingine, ongeza na mwaka mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi tu hapa mlioko hapa Waheshimiwa Wabunge niwaambie neno moja tu hili la kindugu kabisa, msingekuwa wakinamama mngepata kazi sana kwenye kugombea, lakini kwa kuwa ni wakinamama mkifika maeneo hayo mtakuwa mnasema mimi ndiyo Samia wa eneo hili mtapata kura, lakini ukweli wa mambo mtu yeyote asiyeona kazi anayofanya Mheshimiwa Rais, kwa sababu mlikuwa mnabishabisha atakuwa haitendei haki nafsi yake na atakuwa pia haitendei haki nchi hii. Kazi hii inayofanyika ni kazi ya kihistoria ni kazi ambayo inabadilisha maisha ya wananchi wetu. Kazi ya kihistoria ni kazi inayobadilisha maisha ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tukisharudi Majimboni kazi hii anayoifanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kazi ya kihistoria na nikazi inayokwenda kubadilisha maisha ya Watanzania. Waheshimiwa Wabunge tukisharudi Majimboni kwa sababu madarasa yatakuwepo yakutosha, madawati zaidi ya laki sita halafu na Walimu tunaenda kuongeza nendeni muwashawishi hata wale ambao walishaacha masomo, wanafunzi wale ambao wengine wanatokea jamii za kifugaji kama zetu, waambieni warudi shuleni elimu yenyewe bila ada, madarasa hamna kubanana kwenye madawati, halafu hamna hata yule ambaye hajaelewaelewa hamna kukaa kwenye mawe maana yake zamani ilikuwa usipo fanyafanya vizuri hesabu wewe ndiyo unakosa nafasi ya kukaa, hii na Walimu tumesema wanaenda sambamba na majengo haya, hatutajenga majengo tu na Walimu katika kipindi hiki kifupi na Walimu wanakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya aina hiyo siyo kazi ya kuibeza na kazi ya aina hiyo haijasimamisha miradi mikubwa na miradi mikubwa na yenyewe inaendelea, miradi mikubwa ya kimkakati inaendelea na kwenye shughuli za uzalishaji kama mpango tulioutoa na tumesema tutaunyumbulisha kwa sababu kwa wakati huu tulileta ili tupate maoni tumeshapata, tumepata maoni mengi sana na baada ya hapa tumeyapokea na timu ya wataalam tutaendelea kukaa, lakini pia Kamati yetu na yenyewe itaendelea kuchambua, tutaendelea kupata maoni zaidi tutakapokutana tunaamini tutatengeneza jambo lililo bora sana ambalo litatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ninalowaomba twendeni tukamsaidie Mheshimiwa Rais kusimamia fedha hizi kule zilipokwenda. Upande wa wizara tumesema tutaituma Idara yetu ya Ukaguzi wa Ndani ambao wapo kila eneo wasimamie effectively na siyo fedha hizi tu na fedha zingine zote ambazo zinahusu maisha ya Watanzania ambazo zinaenda katika miradi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini haya yote yatafanyika na yataweza kubadilisha maisha ya Watanzania na Watanzania watafurahia vizuri sana kazi anayofanya Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake anayoiongoza pamoja na ushauri mzuri ambao Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu wanatupatia ili kuweza kuboresha mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa nimeyasema hayo nakushukuru sana. Naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Utakumbuka tarehe 7/11/2022 niliwasilisha katika Bunge lako tukufu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti pamoja na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe mwenyewe pamoja, Naibu Spika, Wenyeviti wote wa Bunge, Kamati ya Bunge, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa maoni ambayo wameyatoa. Nasi kama Wizara tumeyapokea. Kama ilivyo kwenye kanuni, lengo la wasilisho hili ni ili tuweze kupokea maoni na kuendelea kuboresha document hii ambayo tutaiwasilisha tena na hatua nyingine ziweze kufuata mpaka ambapo tutakuja kwenye bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeyapokea maoni haya na Waheshimiwa Wabunge zaidi ya 90 wamechangia katika mjadala huu. Nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri ambao wamekwisha kupokea mapendekezo ambayo yanaangukia katika sekta zao na kufafanua katika baadhi ya maeneo ambayo yalihitaji ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba kanuni za Bunge hili ni kupokea maoni na kama ambavyo wenzangu wametangulia kufafanua katika baadhi ya maeneo, naomba nami nifafanue katika baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kubwa ambalo nahitaji kulifafanua ni ile hoja ambayo ilitolewa kuwa Tanzania imeshuka toka uchumi wa kati wa chini na kwenda kwenye kundi la zile nchi masikini. Napenda nitoe ufafanuzi huu kwa sababu hoja hii imekuwa ikipotoshwa mara kwa mara. Kwanza tuna mambo mawili ambayo yanafanana ambayo tunapojadiliana lazima tuwe makini tunapoyaongelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kuna nchi inapokuwa imepangwa kwenye kundi fulani la kukua kwa uchumi na kipato cha watu wake; pili, kuna ule uwiano wenyewe wa kukua kwa uchumi katika nchi. Yaani hapa tunaongelea ile growth rate na kundi ambako nchi yetu imepangwa. Namaanisha nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipopata COVID katika nchi nyingi takwimu ndogo ndogo ambazo tunazipima kwa majira mafupi mafupi, wengine wanapima kwa muda mfupi zaidi, sisi tunapima kwa robo mwaka. Takwimu ya growth rate ndiyo takwimu ambayo imekuwa na namba tofauti tofauti tunazozitoa kwa kila wakati. Yaani kabla ya COVID tulikuwa around 7%, baada ya hapo tukashuka mpaka 8%. Tulipoenda kwenye utekelezaji wa mpango wa kuondokana na UVIKO tumepanda tukaenda 9%; tuliweka projection za kurudi tena zaidi ya 5% kabla ya vita vya Ukraine, baada ya athari za vita vya Ukraine, tukarudi kwenye projection ya 4.7%. Baada ya kuweka mpango mkakati na bajeti hii tuliyoiweka, matarajio yetu tunaenda kupanda tena kuzidi 5%. Hiyo ni growth rate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nchi iko kundi gani la kipato, ambayo ndiyo hoja aliyoisema juzi Mheshimiwa Profesa Muhongo, kuna namna mbili za kupima na kupanga nchi katika makundi kulingana na pato la Taifa. Yaani the key measures for income per capita. Ya kwanza ni GDP per capita na ya pili ni GNI per capita ambayo zinaongelea pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Dunia (World Bank) haitumii GDP per capita kupima kundi nchi ilipo, inatumia GNI. Katika taarifa zake zote ambazo imekuwa ikitumia Benki ya Dunia huwa inatoa takwimu hizo za GNI per capita kwa nchi kila Julai mosi, kila mwezi wa Saba wa mwaka na takwimu zinazokuwa zimetolewa ni zile za mwaka uliopita. Kwa maana Julai Mosi, 2022 ilitoa makundi ya nchi kwa mwaka 2021, tarehe Julai Mosi, 2021 ilitoa makundi ya mwaka 2020 na tarehe Julai Mosi, 2020 ilitoa makundi ya nchi kwenye vipato vyao kwa mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hiki alichokisema Profesa Muhongo kwamba tumeshuka mwaka 2022, tathmini hiyo hata haijafanyika, takwimu hiyo itatolewa Julai Mosi, 2023. Kwa maana hiyo zile takwimu alizozitoa sizo na zile ambazo zilishatolewa mpaka sasa ambazo zinaongelea kwa mwaka uliopita, zilizotolewa kwa mwaka huu zinaonesha Tanzania bado tuko kwenye dola 1,140 ambayo tumeshapiga hatua kubwa sana tangu pale tulipokuwa tumepanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho niliona nikiseme, ni kwamba ile nukuu aliyosema imetoka Benki ya Dunia, mimi kwa kuwa Waziri wa Fedha nakuwa Gavana wa Benki ya Dunia. Kwenye internal memo ya Benki ya Dunia waliandika kusikitishwa nanukuu ile ambayo ilinukuliwa ikionesha imetoka Benki ya Dunia kama ninavyoweza kusoma hapa. Alisema:

“Honorable Minister we have learned with a shock that it was said Tanzanians GDP per Capita is now 990, trying to make the public of Tanzania to believe that Tanzania has slipped to lower income countries. That was refered that Tanzania is now GDP per Capita range to 990 USD.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakaitaja ile website ambayo ni trading economies.com wameiweka hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema; “It appears to be incorrect as the figures does not confirm. In any case GDP per Capita is not what we use in income classification. Besides the number they have given does not appear to be consistence. This is not from the World Bank. Please note that, some countries have slipped from middle income to lower income but Tanzania has maintained its status since becoming lower middle-income country in 2020. Please note World Bank does not GDP per Capita for income classification and this articles which was refereed is incorrect and is not from the World Bank. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi kwa mujibu wa taarifa hizo Benki ya Dunia haijatoa hizo takwimu na Benki ya Dunia wakati tuko kwenye vikao vilivyoisha tu vya juzi mwezi huu uliopita. Benki ya Dunia wakati wanahutubia Mawaziri wa Caucus ya huko Afrika, waliwatuma Mawaziri wengine waulize Tanzania imefanyaje kuweza ku-maintain status na kuendelea kukua zaidi na kauli hiyo ilitolewa na Rais wa Benki ya Dunia na ikatolewa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia. Ni siku hizo hizo tu wasingeweza kuipongeza Tanzania na wakasema tumfikishie salamu hizo Mheshimiwa Rais na wakati ule ule pato la Tanzania liwe limeshuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama kuna watu ambao wanasubiri sana Tanzania ishuke kutoka uchumi wa kati kwenda wa chini, niwahakikishie wanapoteza muda wao, Tanzania haitashuka kwenda kwenye kipato cha chini, inasonga mbele. Itatoka kwenye uchumi wa kipato cha chini kwenda kipato cha kati cha juu. Hii si kwa maneno ni kwa hatua ambazo Mheshimiwa Rais na Serikali anayoongoza inachukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba zinaongea, huwezi kwenye nchi ambayo unajenga bwawa kubwa la umeme kwa ajili ya grid stabilization utegemee ukishamaliza mradi huo eti ushuke kutoka pale ulipokuwa uende chini. Huwezi kwenye nchi ambayo unaboresha bandari kwa ajili ya kufungua shughuli kubwa kubwa kwenye lango la nchi ambazo hazina huduma ya maji, ukishamaliza miradi hiyo eti uchumi wako ushuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kwenye nchi ambayo imeweka bajeti kubwa kwenye historia inayokwenda kwenye shughuli za uzalishaji, bajeti ya kilimo inaenda kwenye umwagiliaji, haya si maneno ni scheme ambazo zitaonekana na watu watazalisha na ambao ndio wengi katika Taifa hili. Huwezi ukamaliza kujenga irrigation schemes ukaondoka kwenye kutegemea mvua ukaenda kulima kwenye uhakika kwa kutumia mbegu bora, halafu ukishamaliza hapo GNI yako na kipato na position ya nchi yako iweze kushuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi hiyo hiyo, huwezi ukaendelea kuboresha viwanda, mashamba kama ya Mkulazi, Mbigili, Bagamoyo Sugar ambayo na sukari za kwanza zimeshaanza kutokea ni miradi mikubwa mikubwa, ujenzi wa reli ya kisasa ambayo itafungua uchumi na ni uti wa mgongo wa uchumi, halafu ukishamaliza kuijenga tu nchi ishuke pale ilipokuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukatekeleza mradi mkubwa kama wa LNG injection yake ni ya billions, trillions, halafu ukishamaliza kuutekeleza na uka-take off ajira zitakazotengenezwa pia na production zitakazofanyika halafu baada ya hapo nchi hiyo ishuke kwenye nafasi ilipokuwa iende upande wa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji unaofanyika kwenye elimu, miundombinu ya barabara kutoka kwenye uzalishaji, nyie Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwa Wabunge ambao wameshakaa zaidi ya kipindi kimoja watasema. Fedha zilizokwenda kwenye TARURA kufungua barabara kutoka kwenye uzalishaji kwenda kwenye feeder roads ni nyingi kuliko katika kipindi chochote kile cha historia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji katika sekta nyingine, kwa mfano, imenunuliwa mitambo kwa ajili ya kuchimba mabwawa. Mabwawa yale yatanusuru mifugo iliyokuwa inakufa. Watu mifugo yao ikanusuriwa wakaanza kufuga kisasa, hawawezi wakarudi nyuma, wale watu watasonga mbele. Hivyo hivyo mitambo ile itaenda kutengeneza schemes ndogo ndogo ambazo zitaenda kuongeza uzalishaji katika maeneo husika. mazingira bora ya uwekezaji na kuvutia mitaji kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya na wawekezaji wanatiririka, yatatengeneza ajira, tutapunguza unemployment, hao watu wote wataenda kuwa na vipato vyao. Watu wengi wa aina hiyo wakishakuwa na vipato vyao nchi haiwezi ikashuka ilipokuwa kwenye daraja lile kwenda chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona nilisemee lile na niwaombe Watanzania kama ambavyo Chief Whip amesema hapa. Ni vyema tukaipenda nchi yetu na wala tusichanganye, mambo mengine ni ya kitaalam. Kwa mfano, kuna watu wana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri dakika tatu, malizia kengele ya pili imeshagonga.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati watu wanachanganya cost of living na standard of living na kipato nchi ilipo. Haya mambo ukilinganisha nchi na nchi utaweka phenomenon nyingi za kiuchumi, ni lazima ukitaka kulinganisha sawasawa uweke na purchasing power kwa sababu zile exchange rate za nchi na nchi zinatofautiana. Mtu anaweza akawa analipwa vizuri sana, ana kipato kizuri sana, kama eneo alipo na yule mwingine aliko bei za bidhaa zinaenda tofauti yule pamoja na kuwa kipato kikubwa yeye atakuwa na maisha magumu kuliko yule mwingine ambaye huenda ana kipato kidogo, lakini bei zake ziko tofauti. Kwa hiyo haya mambo lazima mara zote tuwe tunafahamu undani wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine walisema ukomo wa deni la Taifa. Wanasema Bunge labda liwe linaweka ukomo wa kukopa. Hata sasa Bunge limeweka ukomo wa kukopa, kwa sababu nchi yetu kila mkopo tunakopa kwa mradi na kila mradi tunapitisha kwa bajeti. Hakuna sehemu ambako tunakopa bila mradi na hakuna sehemu tunakopa bila bajeti. Tumeweka kwenye kila mwaka ukomo wa kukopa ndani, kukopa nje, misaada, makusanyo, hivyo ndivyo bajeti inavyokuwa. Kwa maana hiyo hakuna siku ambako inaenda inakopwa holela tu kwamba ni open cheque, haijawahi kutokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo yote inakopwa kwa mradi, na busara inayotumika ni kupeleka kwenye miradi ambayo italeta tija kubwa, itafungua uchumi. Fedha zote hizo zinazokopwa zinakwenda kwenye uwekezaji. Wengine wakiona mkopo umetajwa labda dola bilioni mbili labda trilioni nne inakuwa program labda na multilateral ambayo inachukua si mwaka mmoja na fedha hizo huwa zinakwenda kwenye mradi mahususi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wengine wanaangalia mradi ni endelevu, wanadhani kama mradi ni endelevu deni litabaki lilelile. Hebu niambieni kama fedha ya kwanza iliyoingia ilikuwa ya lot one hivi tunaweza; lot one imeishia Morogoro, hivi tunaweza tukafika mpaka Mwanza sasa deni likabaki lilelile la lot iliyokuwa imeishia Morogoro? Haiwezekani! You can’t eat the cake and have it.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema unataka ukusanye kamoja kamoja ndio upeleke kwenye lot ukaimalizie utachukua miaka 100 mpaka 120, ni mkandarasi gani atakayekusubiria tu ukusanye kila mwezi umpelekee? Tunachukua cha jumla tunatekeleza mradi uishe haraka ili tuweze kurejesha pale tulipochukua na hizo ndizo tathmini za kitaalam zinazofanywa kuweza kupima kwamba huyu anaweza akakopesheka. Nchi zozote ambazo zinakua ndizo ambazo madeni yao yanakua. Chukueni tathmini si vizuri kutaja sana nchi, chukueni nchi zile mnazozifahamu ambazo hazina uchumi kabisa muangalie kama zina deni. Maskini yeyote hadaiwi, anadaiwa atalipa kitu gani? Ukiona nchi inayodaiwa sana ni nchi inayokua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi mwekezaji yeyote, mtoa fedha yeyote anaiangalia Tanzania kwa sababu wale wengine hawana cha kuwalipa, ndio maana unaweza ukaona hata miradi inagombaniwa. Hiyo tunatakiwa tuone kwamba tuna fursa kubwa na hizi fursa zitafungua uchumi, zitafungua ajira ili tuweze kuhakikisha kwamba tunajenga nchi yetu na Watanzania wanapata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa tunawaza kila wakati, kuangalia na hilo ndio tatizo kubwa sana…

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa leo tulikuwa tunapokea tu maoni, niwahakikishie yote tumeyapokea, Dira ya Taifa mpya, kazi inaendelea kuiandaa na inaandaliwa ikiwa na mwendelezo wa hii itakayokuwa imeisha. Miradi ya EPC+F imefanyiwa tathmini na tunaelekeza nguvu kubwa kwenye PPP kama nilivyosema kuweza kuhakikisha kwamba maeneo ambayo Private Sector inaweza ikashiriki kikamilifu Private Sector ipewe fursa ishiriki kikamilifu ili iweze kutengeneza ajira kwa vijana wetu na kuweza kuongeza kipato kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naomba sasa kutoa hoja na nirejee kauli ya mwanzo ambayo niliwasilisha kwamba nimewasilisha maandalizi ya Mpango wa Bajeti kwa Mwaka 2023/2024 na Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti pamoja na Mpango wa Maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepokea Maoni na Ushauri wa Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 113(5)(c).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia. La kwanza niseme kwamba yale yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wametupatia kama ushauri na yale ambayo wametupatia kama maelekezo tumeyapokea. Tutaenda kuyafanyia kazi; na yale ambayo yanaangukia kwenye Sekta yetu, tumeyapokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niweke kumbukumbu sawa katika baadhi ya mambo ili Hansard zako ziweze kupata vizuri. Nikianza na jambo moja ambalo ameliongelea Mheshimiwa Mpina; katika mchango wake amechangia mengi, lakini eneo mojawapo amesema tunapata mfumuko wa bei kwa sababu ya mismanagement ya Sera za Fedha. Akaelezea kwamba tumefanya malipo nje ya bajeti. Kwa maana hiyo, yeye akakichukulia hicho kama kitu ambacho ni mismanagement ya Sera za Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niweke kumbukumbu sawa. Moja, fedha hizo anazosema zimelipwa, siyo zilizolipwa. Ni vizuri sana Waheshimiwa Wabunge, tunaitwa Waheshimiwa, tunapotoa taarifa kwenye chombo hiki kikubwa tuwe tunatoa taarifa ambazo tuna uhakika nazo. Fedha ambazo tumelipa nje ya bajeti, yako mafungu kama matatu hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fungu la kwanza tumelipa fedha nje ya bajeti baada ya kugundulika kuna wanafunzi 29,000 wamekosa mikopo ya elimu ya juu. Tukaja hapa Bungeni, Waheshimiwa Wabunge mkasema tena kwa azimio, kwamba tafuteni fedha kokote watoto hawa wote wawe wameenda vyuoni; na walikuwa wanatangatanga, wanazagaa zagaa. Wameshapata admission, lakini hawana fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda kuchukua Shilingi bilioni 86 ambazo hazikuwepo kwenye bajeti, na watoto wetu wako Vyuo Vikuu hivi tunavyoongea. Tusingeweza kuwaacha wanafunzi 89,000 kisa eti hazikuwepo kwenye bajeti ilhali Bunge liliopitisha bajeti limeshatoa maelekezo hayo ya kuwapeleka watoto hawa vyuoni. Hilo lilikuwa eneo la kwanza ambalo tumetoa fedha ambazo hazikuwepo kwenye bajeti. Wanafunzi 29,000 wanapata mikopo na sasa wapo mashuleni na wiki ile ile Bunge lilipotoa maelekezo, kulitulia, hamkusikia tena kelele inayohusu mikopo ya elimu ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo tumetoa fedha ambazo hazikuwepo kwenye bajeti, tulitoa Shilingi bilioni 160 kwa ajili ya kujenga madarasa 8,000 ili mwaka huu wanafunzi wote waliotakiwa kwenda Form One, waende Form One. Ninyi mmetokea majimboni kule, mmeyaona hayo madarasa, na ninyi wenyewe ndio mmeshawishi fedha hizo za madarasa zipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anapotokea Mbunge anasema tumetoa fedha hizo nje ya bajeti na kuishambulia Serikali kama vile imefanya uamuzi mbaya, nadhani lazima kuwe na kasoro katika thinking. Kama mzazi huwezi ukachukia wanafunzi masikini kupewa mkopo; kama mzazi huwezi ukachukia fedha zinazotolewa kwenda kwenye madarasa. Nilitamani na nilidhani Wabunge makini wangemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuchukua uamuzi huo wa kutoa fedha na watoto wote wakapata mikopo. Nilidhani Mbunge yeyote aliye makini atampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutoa Fedha zikajenga madarasa 8,000 mpaka na second selection watoto wale wakaenda shuleni… (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niliona hiyo niiweke sawa. Bunge lilitoa maelekezo kwamba watoto hawa waende shule na Serikali ikaitikia, tukatoa shilingi bilioni 86 za mikopo ya elimu ya juu, tukatoa shilingi bilioni 160 kwa ajili ya madarasa 8,000 ambayo yamejengwa katika majimbo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo tusiwe tu tunatamani kushambulia Serikali hata kama haijafanya makosa. Serikali ikifanya makosa ikosoeni, lakini ikifanya jema, iambieni. Hizi ndizo fedha ambazo zimetoka nje ya bajeti. Hizi fedha ninazosema zimetoka nje ya bajeti, wala haziwezi zikasababisha mfumuko wa bei. Sijui ni uchumi wa wapi huo ambao ukijenga madarasa yanaleta mfumuko wa bei wakuweza kuleta matatizo hayo. Niliona niliseme vizuri hili ili liweze kueleweka. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine limeongelewa kwamba tunasamehe wawekezaji na tunatoza masikini. Nchi hii imetoka mbali sana mpaka kufika hapa; nchi hii imetoka katika miaka ambapo ilikuwa na mainjinia wawili na madaktari wawili; nchi hii imetoka katika eneo ambalo wanafunzi wa elimu ya juu ilikuwa nao saba ikaenda kumi ikaenda ishirini, ikaenda thelathini. Hivi tunavyoongea kila mwaka ukijumlisha wanafunzi waliotoka Darasa la Saba na hawakwenda Kidato cha Kwanza, ukajumlisha waliotoka Kidato cha Nne na hawakwenda Kidato cha Tano, ukijumlisha waliotoka Kidato cha Sita na hawakwenda Vyuo Vikuu na ukajumlisha Vyuo vya Kati wamemaliza, na ukajumlisha waliotoka Vyuo Vikuu wamemaliza, utakuwa na idadi isiyopungua wanafunzi milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kama kuna wanafunzi zaidi ya milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira, lazima ubadili utaratibu wa kuwaza kuhusu utengenezaji wa ajira hizo.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kutengeneza ajira hizo ni kuvutia uwekezaji. Hawa wote hawawezi wakaingia kwenye Halmashauri. Huwezi ukawa na wanafunzi milioni moja kila mwaka wanatafuta soko wakaingia kwenye Halmashauri, wakaingia Serikalini. Lazima utengeneze uwekezaji unaostahili kuajiri hawa, lazima utengeneze viwanda, lazima utengeneze uzalishaji.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu. Utaratibu!

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mawazo ya kudhania unasamehe mwekezaji kwamba unamsamehe mtu tajiri na unamtoza masikini, ni utaratibu ule ule wa baba asiye na hekima ambaye anaonea wivu kupanda mbegu kwa kudhania kwamba anatakiwa apike ile mbegu ili wale kama familia. Ukitaka kuvuna lazima upande ndiyo utaratibu wa kiuchumi. Ukitaka kuvuna, lazima upande. Huwezi ukavuna bila kupanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapowekeza, tutatoza watakapoanza uzalishaji. Huwezi ukaendelea kuwazia kutoza watu ambao hawajaja. Umewasamehe wapi ambao hawajaja? Tunatengeneza vivutio waje ili tuwatoze. Unahesabu kumtoza mtu ambaye hajaja! Yaani unahesabu watoto walioko tumboni mwa mama zao kwamba hawafanyi kazi! Watafanya kazi gani nyingine? Unatakiwa ulee mimba, wakizaliwa uwalee, uwatunze, wakishakua ndiyo uwatume kazi. Mnataka kuwatuma kazi watu ambao bado wako kwenye mataifa yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavutia wawekezaji, tunaweka na vivutio waje wawekeze. Wakishawekeza, Watanzania watapata ajira, na waliowekeza watalipa kodi. Ninyi mtaka kuhesabu kodi ya watu ambao hawajaja! Uchumi wa wapi huo? That is vicious cycle, kuwaza kwamba unamhurumia masikini kwa kuzuia uwekezaji, that is vicious cycle. Unawasababisha masikini waendelee kuwa masikini. Wekeza wapate kazi ili watoke kwenye umasikini. Wekeza wapate ajira ili watoke kwenye umasikini. Wekeza ili upate sekta binafsi kubwa ili sekta binafsi ilipe kodi uwatoe masikini kwenye kulipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masikini wakibaki peke yao utaendelea kuwatoza wao wenyewe. Masikini wakibaki wao watupu, utaendelea kuwatoza wao watupu. Tunaleta wapya, tunaleta makampuni mapya yawekeze, tunaleta sekta binafsi ikue ili tuweze kuitoza hiyo sekta binafsi tuwahurumie masikini. That is how to broke the vicious cycle.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tujadilini mambo mengine mengine huko yanayohusu uganga wa kienyeji na vitu vingine, kwenye uchumi, this is my profession. Tunajadilije hivi vitu ambavyo vipo clear? (Makofi)[Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tusimvunje moyo Mheshimiwa Rais anavyo…

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: …anavyohurumia masikini, anataka Sekta iendeshe uchumi…

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumebakiza Watumishi wa Umma ndio walipakodi wa nchi hii. Watumishi wa Umma ndio tunaotoza kodi kwa sababu hata hawawezi kukwepa. Walipa kodi wakubwa…

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe na Sekta binafsi imara ndiyo tunaweza kuongeza…

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilidhani niyaseme hayo. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu. Awali ya yote, nitamke rasmi kwamba naunga mkono hoja. Nina imani kubwa na Mheshimiwa Waziri wa Elimu. Naomba Bunge lako Tukufu, Waheshimiwa Wabunge tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri, kwa nia yake na kwa jitihada anazozifanya kuhakikisha kwamba anarekebisha Sekta hii ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania watakubaliana na mimi kwamba kama Taifa tuna safari ndefu kwenye Sekta hii ya Elimu.
Naweza kusema kwamba baada ya kuwa tulishapiga hatua kubwa, tulipofanya uamuzi wa kuwa na sekondari kila Kata, pamoja na kuwa na ongezeko kubwa katika Shule za Msingi, jambo hili la kuwa pia na vyuo vingi limepelekea nchi yetu kuwa katika hatua ya mpito kwenye elimu. Kwa hiyo, tutakuwa na mambo mengi ya kurekebisha mambo ambayo siyo ya siku moja, mwezi mmoja, wala miezi sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie tu, kwa kutambua hilo, ndiyo maana Mheshimiwa Rais, alitafuta mtu mahsusi, akamteua na kumleta katika sekta hii kwa kuzingatia weledi wake, na kwa kuzingatia uzoefu wake katika sekta hii. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, tumpe muda Mheshimiwa Waziri, tumuunge mkono na Watanzania wote tumuunge mkono. Mimi naamini tunakokwenda ni kuzuri na wote tutakuja kutambua kwamba kweli Mheshimiwa Rais, alifanya jambo jema kwa kutafuta mtu mahsusi katika sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirejea kwenye historia, leo hii tunaongele kuhusu shule binafsi, shule za Serikali, ni dhahiri kwamba kinachotambulisha kwenye shule binafsi, ni dhamira ya mzazi. Kile kinachotambulisha kwenye shule ya Serikali, ni uwezo wa mwanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wazi tu kwamba Ubunge wangu niliupata kuanzia nilipofaulu kwenda sekondari. Yaani kile kitendo cha kutangazwa kwamba nimefaulu na kwenda shule ya vipaji maalum ya Ilboru, Tarafa mbili tayari zilitambua kwamba huyu ni mtu wa tofauti na tangu namaliza walikuwa wanasema ukimaliza kusoma, chagua Ubunge. Kwa hiyo, kiwango na ubora wa shule una umuhimu mkubwa sana katika kutengeneza jamii yetu na mchango wao katika maisha ya kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, sisi kama Wabunge, ni vyema sana tukaunga mkono jitihada za Serikali; na kwakuwa ni mambo mengi ya kurekebisha, tukatoa fursa kwa Mheshimiwa Waziri na timu yake, wayafanyie kazi moja baada ya lingine. Nia ya Serikali na nia ya Mheshimiwa Rais mara zote anaposimama na anapotuelekeza, imekuwa ya dhati ya kuhakikisha kwamba heshima ya elimu inarudi kwenye mstari wake kama ambavyo amekuwa akifanya katika sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge pamoja na Kamati na Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Kuna hoja ambayo ilitolewa kuhusu uchelewezwahji wa fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu wa juu, lakini taarifa zilizoko ambazo ni taarifa rasmi ni kutoka Wizara ya Fedha, zinasema, hadi Machi, 2016 kama ambavyo tunajua kwamba mikopo huwa inaenda kwa quarter, Serikali imetoa mikopo ya elimu ya juu yenye thamani ya shilingi bilioni 331.9 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2015/2016, mikopo ya elimu ya juu Bodi ilitarajiwa kukusanya shilingi bilioni 34.7 na hadi kufikia Machi, Bodi ilikuwa imekusanya bilioni 22.9. Kwa hiyo, ukichukua na zile ambazo Serikali imetoa, utaona kwamba tayari shilingi bilioni 354 zilikuwa zimekwisha kutolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati hapa na pale kunatokea ucheleweshwaji ambao ni wa kiutendaji zaidi katika masuala ya mgawanyo wa fedha, hayo ni ya kiutendaji ambayo mara zote yamekuwa yakirekebishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge, hali ilivyokuwa siku za nyuma na sasa iko tofauti. Zamani ilikuwa kawaida; na ilikuwa jambo la kawaida mpaka wanafunzi wagome ndiyo mikopo itoke, lakini mtakumbuka kwamba katika miaka ya hivi karibuni na siku za hivi karibuni, jambo hilo linaenda likirekebishwa, hasa hasa yamekuwa tu yakitokea yale ambayo ni ya kiutendaji ya ndani ya usambazaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilijitokeza lilikuwa ni fedha za mchango wa Serikali, Mradi wa Mlonganzila, ambao kwa bajeti ilikuwa inatarajiwa zitumike dola milioni 755. Tayari Serikali ilishachangia shilingi bilioni 18 na tayari zilishalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelisema, ni lile ambalo linahusu pendekezo la bajeti ya Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI angalau kuongezeka kutoka asilimia 11 kwenda 15 hadi 20. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwa hesabu zetu tulizozipiga; na hii ni taarifa rasmi kutoka Wizara ya Fedha, kwamba tayari tumeshavuka hiyo asilimia inayopendekezwa na Waheshimiwa Wabunge na sasa tuko asilimia 22 ambayo ni shilingi bilioni 4,777 za bajeti yote. Kwa hiyo, tayari Serikali imeshavuka lengo hilo ambalo Waheshimiwa Wabunge wanapendekeza la kufika asilimia 20, sasa tuko asilimia 22.1. (Makofi)
Jambo lingine ambalo liliongelewa ni kuhusu madai ya Walimu yasiyo ya mishahara. Serikali imechukua hatua, tayari imetenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 626 kwa ajili ya kushughulikia madeni ambayo yamehakikiwa. Kingine kikubwa ambacho Serikali imefanya ni kuhangaika na mianya iliyokuwa inasababisha malimbikizo ya aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu uliopita, ilikuwa inatokea Waalimu wakitaka kufanyiwa promotion, kubandishwa madaraja, walikuwa wanaulizwa. Kwa hiyo, ilikuwa inatokea Mwalimu ambaye amesoma Chuo kimoja na mwenzake, wamepangiwa vituo kwa wakati mmoja; lakini ikitokea yeye akachelewa kupokea barua ambayo inaelezea kuhusu kupandishwa kwake, ilikuwa inatokea Waalimu waliosoma pamoja, wamepangiwa kazi pamoja, wanapandishwa madaraja tofauti kufuatana na kupokea taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali itaenda moja kwa moja kuwapandisha watu ambao wana sifa bila kuwauliza kwa sababu ni dhahiri kwamba hakuna mtu atakataa kupandishwa daraja kama amefuzu sifa zile ambazo zinatakiwa, atapandishwa. Hiyo itaondoa Walimu ambao wamemaliza pamoja na wamepangiwa pamoja kazini, wameanza kazi pamoja kuwa na madaraja tofauti kama walivyopandishwa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote nipokee maoni ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge, tumeyapokea, tutayafanyia kazi na mengine tutaendelea kupeana mrejesho kwa sababu, tukimaliza Bunge hili litakuja Bunge lingine ambalo litakuwa linahusisha bajeti, panapo Mungu akitujalia afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mambo ambayo niliona pamoja na kupokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge waliyoyatoa, ningependa nitolee ufafanuzi hoja chache. Hoja ya kwanza ambayo Waheshimiwa Wabunge wameongelea kwa sauti kubwa ni kuhusu uchache wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA). Kwanza kabisa niliombe Bunge lako tukufu liridhie tumpongeze Mheshimiwa Rais kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa TRA walikuwa hawajaajiriwa katika kipindi cha muda mrefu kidogo, miaka yapata mitano sita saba hivi, lakini tulipokuja kwenye mwaka wa fedha uliopita hapa Bunge lako lilielekeza Serikali kuweka uzito kwenye uajiri wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato - TRA, hivi tunavyoongea ndani ya mwaka huu mmoja, kibali kilitolewa na Mheshimiwa Rais kuajiri watumishi kwa mpigo 2,100 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Kwa taratibu za kiutumishi, sekta moja kupata watumishi 2,100 kwa mpigo siyo jambo dogo na hivi tunavyoongea 1,500 tayari walishaajiriwa na wengine 500 wako hatua za mwisho za taratibu za kiuajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii ni namna gani unaweza tukawaambia jinsi Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inavyopokea na kuyafanyia kazi mapendekezo ya Bunge. Ni ndani ya mwaka huu wa fedha tupo nusu mwaka tu, wafanyakazi 2000 wameshaajiriwa na 170 wako hatua za mwisho kwenye taratibu za masuala ya vibali wakati wanakamilisha usaili wa hao wengine. Kwa hiyo, maoni yenu Serikali inayapokea na inayafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia kama mwaka mmoja wameajiriwa 2100 kama wangekuwa wanaajiriwa hivyo hivyo kwa miaka kumi tungekuwa na watumishi wangapi. Sasa pengo la Watumishi wa Umma wakiwa hawajaajiriwa kwa muda mrefu huwezi ukaliziba kwa mara moja, ukiajiri wengi kwa mara moja pia, kwa sababu watakuwa bado hawajazalisha utatengeneza tatizo tena kwenye upande wa mishahara, kwa sababu utakuwa umeajiri wengi ambao bado hawazalishi. Kwa hiyo, ninawaomba mridhie Serikali hatua hizi inazochukua, iwaajiri hawa waingie kazini waendelee kuzalisha, wakati huo tutakuwa tunaendelea pia kutekeleza masuala ya kimfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aliongea Mheshimiwa Esther Matiko nami nakubaliana naye, tatizo siyo watumishi peke yake, siyo idadi peke yake, tunayo maeneo mengine ambayo tunaendelea kuyafanyia kazi, masuala ya uadilifu, masuala ya matumizi ya EFD na masuala ya hamasa tu ya wananchi wenyewe kuwianisha kodi na maendeleo yao. Kwamba kila mmoja awiwe kulipa kodi anapo nunua bidhaa na anapofanya biashara nyingine yoyote ile. Kwa hiyo, hili tunaenda nalo lakini kama nilivyosema ni jambo ambalo linatakiwa liende hatua kwa hatua, niliona nilisemee hilo kwa sababu lilijitokeza lakini tunaendelea kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi ni mashahidi mtaona kwamba makusanyo yameongezeka siyo tu kwa kuwianisha malengo na makusanyo lakini hata kwa namba, Machi 2021 makusanyo ya mwezi yalikuwa trilioni 1.2 lakini Disemba hii tumepiga zaidi ya trilioni 2.7, kwa hiyo mnaweza mkaona kwamba hata kwa real terms makusanyo yameendelea kuongezeka. Niliona nilisemee hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili na ninaomba hapa tuelewane vizuri sana Waheshimiwa Wabunge, vinginevyo tutabadilisha Bunge hili kuwa platform ya kujadili matukio. Hiki chombo ni kikubwa sana siyo chombo cha kujadili matukio tu. Kinatakiwa kiishauri pia Serikali ni namna gani inaweza ikaweka mipango yake ya kuwatoa Watanzania kwenye umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninasema hivi, ukiangalia Hansard za Bunge letu hili, utaweza kuona michango ya Wabunge inavyokuwa tofauti Bunge moja na Bunge lingine linalofatia. Leo hii kwa sababu inasikika vizuri kwa watu ikionekana unasemea bei, kila mmoja anaongelea bei lakini twendeni katika hali ya uhalisia. Nchi hii ina wazalishaji na ina walaji lazima mara zote tukumbuke hilo. Nchi hii ina wazalishaji na walaji, na hivyo vyakula vinavyozalishwa havizalishwi kwa mashamba ya Vijiji vya Ujamaa ni watu binafsi wanaingia gharama zao kuzalisha, ni mtu binafsi anajipinda anahangaika anazalisha, kuna upande mmoja unazalisha kuna upande mmoja unatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama watunga sera kama watunga sheria ni lazima tuwe makini sana ku-balance haya maeneo mawili. Tujiulize kwa nini nchi hii ina wakulima wengi sana halafu inakuwa ni nchi maskini na ardhi inayo! Tujiulize jibu sahihi utakalolipata ni kwa sababu wamekuwa wakizalisha wanapata hasara katika uzalishaji wao, ndiyo jibu sahihi hilo. Wanafanya kazi kwa bidii anazalisha magunia 400 anaambiwa usiuze popote halafu yanakutwa na mvua yananyeshewa yako hadharani. Wakati huo yananyeshewa yule aliyeelekeza kwamba usiuze popote hayupo kwenda kuyafidia yanakutana na mazao mengine, hii inatengeneza umaskini kwa wakulima wetu.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachokifanya ni kipi, leo hii imetokea, mazao tunayotumia sasa hivi kama alivyosema Waziri wa Kilimo ni yale mazao ambayo uzalishaji wake mbolea ilikuwa zaidi ya shilingi 120,000. Bunge hili lilipiga kelele kubwa sana kuhusu bei ya juu sana ya mbolea mwaka jana! Haya ndiyo mazao yanayotumika sasa hivi, yamezalishwa kwa gharama za juu sana. Mafuta yalikuwa juu ilikuwa kabla ya ruzuku, mbolea ilikuwa juu ilikuwa kabla ya ruzuku, ndiyo yaliyozalishwa sasa hivi. Itakuwa ni ukatili sana kwa Serikali ukienda tu uweke maelekezo tu ya moja kwa moja kwamba wewe uza shilingi 100 debe hili hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya nini kwa kutambua hivyo? Serikali ndiyo hicho alichofanya Mheshimiwa Samia katika mwaka huu wa Fedha, katika haya mazao ambayo ndiyo tunatarajia kuyavuna, ameweka nusu bei ya mbolea kwenye kila mfuko Serikali ibebe, impunguzie gharama mzalishaji kwenye mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikaweka ruzuku kwenye mafuta Bilioni 100 kila mwezi ili kupunguza gharama ya usafirishaji na gharama ya uzalishaji. Sasa mazao yatakayovunwa yaliyotumia ruzuku tunayatarajia yawe na bei ya chini. Hivyo ndivyo uchumi unavyopaswa kwenda lakini leo hii tukisema tu kwamba, mtu yuko pale kwenye uzalishaji anasema Serikali inajificha tu kwenye Ukraine, Sisi tumezalisha hapa hapa kwa nini bei iko juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmezalisha hapo kwenu ndiyo mmezalisha Mwanzugi lakini Mwanzugi hamtengenezi Mbolea. Mbolea mliyotumia kuzalishia ni ya bei ya juu, ndiyo hiyo iliyosababisha yale yatakayozalishwa kama mfuko ulitumia wa shilingi 140,000 au shilingi 120,000 ni lazima yale mazao hata kama umeyazalisha kijijini kwako yatakuwa ya bei ya juu. Bado usafiri, kama mafuta unayotumia kusafirisha yako juu utazalisha nyumbani kwako pale pale lakini bado yatakuwa na bei ya juu! Ndiyo maana Mheshimiwa Rais akasema tuweke ruzuku ili kupunguza pale mtu alipozalishia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu Serikali haijaishia hapo kushughulika na suala la mfumuko wa bei. Baada ya kuwa imefanya hivyo imetoa akiba yake kwenye maghala ya chakula kwenda kupeleka kwenye soko na kuwapelekea wale ambao ni kaya zenye uwezo mdogo kukabiliana na jambo la aina hii. Ni lazima tunapoelezea matatizo yaliyopo tuelezee na hatua zinazochukuliwa, tusioneshe ufahari katika kuwatajia Watanzania matatizo. Unawatajia tu bei kwamba kuna bei hii, bei hii iko juu wanazijua kila siku wananunua hivyo vitu. Taja kama unaona hatua zilizochukuliwa na Serikali hazitoshi taja za kwako mbadala kwamba Serikali iongeze hatua hii, hatua hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipokuwa makini tutafanya kila kitu kwa kuhemka, leo hii tunavyoongea ninyi Wabunge mmetoka wiki moja kule Majimboni, mkirudi wengine wanakaribia kuanza kuvuna mazao yao, sasa mnataka leo tuagize mahindi ya Pakistan, tuagize mchele wa Pakistan uje ukutane na uzalishaji wa wazalishaji wetu, Bunge lijalo usimamishe shughuli za Bunge tujadili mazao ya wakulima hayana bei yatakuwa yamekutana flooding.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara zote ukiona kelele zinapigwa kwenye haya mambo ya dharura kuwa makini sana, wakati mwingine unaweza ukabeba na deal za watu humo humo, lazima tuwalinde wakulima wetu na lazima tuwalinde walaji wetu, ni lazima tu-balance. Wananchi wengi wanaona umachinga unaweza ukalipa kuliko kilimo, kwa sababu gani? Kwa sababu tunaki-mistreat kilimo. Mimi nimekulia huko najua jinsi ilivyo kazi kulima asubuhi mpaka jioni halafu uhangaike kutunza yale mazao, halafu uvune. Lazima tuwalinde hao watu, halafu ushuhudie yananyeshewa mvua hayana pa kupeleka. Tulinganishe hata hizo bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie lingine ameongea tena Ndugu yangu na jirani yangu kwamba reserve zinashuka sana, akilinganisha kwamba mwaka juzi reserve zilikuwa Dola bilioni 6,000 sasa zimesharudi bilioni 4,500. Jamani haya masomo ya uchumi ni sayansi, narudia tena, twendeni tufuatilie kwa makini reserve zina-build vipi, reserve zinaongezeka vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilipokuwa 6,300 tulikuwa na Trilioni Moja tumeitoa IMF ndiyo ikaongeza ile reserve, sasa tumeichukua ile tumejengea madarasa yote unategemeaje reserve iwe ile ile? Iliongezeka kwa sababu tulipokea kwa mkupuo trilioni 1.3, tulipoitoa tukajengea madarasa ni kweli itashuka, sasa shida iko wapi? Haya ndiyo matatizo ya kutaka kuonea huruma mbegu, unaogopa kupanda mbegu kwa sababu ghala litapungua, panda ili uvune zaidi, ndicho tulichofanya!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulileta kwa ajili ya madarasa na vitu vingine, baada ya hapo tumeitoa, ni kweli reserve zitashuka! Lakini siyo hilo tu, reserve pia ni function ya import na export, uwiano au mizania yetu ya importation ni kubwa kuliko exportation, sababu moja ya msingi ni kwamba tunayo miradi mikubwa kuliko nchi zote za SADC, vitendea kazi vyote tunavyojengea miradi hii tuna-import. Uki-import kilo moja ya tumbaku na vyuma vilivyoenda kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere mizania yake hailingani. Uki-export kilo kadhaa za mafuta ya alizeti hapa, galoni kadhaa za mafuta ya alizeti ya Singida, mizania yake na importation ya material tunayotumia kwenye reli, mizania ya reli ni kubwa, kwa maana hiyo mizania ya export na import, import ziko juu kwa sababu ya miradi mikubwa. Tuna daraja la Busisi unategemeaje reserve ziwe zile zile tu. You can’t have your cak and eat it too!

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kazi sana kutumia Bunge lako kufundisha mtu yule yule ambae ametaka kwa maksudi kutokuelewa! Haiwezekani tukawa tunatumia muda wa Bunge kujadili kitu kile kile tunataka ku-achieve kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna mashaka kuhusu reserve nchi yetu iko na zaidi ya miezi ya 4.7 ya importation. Wastani ni miezi Minne tu, tuko makini kwenye hilo. Hata ya Deni la Taifa tuna asilimia 73 ya mikopo yetu tangu uhuru imekopwa kwa consessional miaka 40 kipindi cha malipo na grace period miaka 10, interest rate 0.75, asilimia 73 ya mikopo ni consessional.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia hii 26 inayosalia ni commercial ambayo tumeamua kukopa kwa sababu miradi hiyo isingeungwa mkono. Jamani, tumesahau sasa hivi tu vita ya kiuchumi tumeimba muda siyo mrefu. Ulikuwa na option moja tu ama uache miradi hiyo, ama tukope commercial, tukasema tukope commercial tuweke back born ya uchumi wetu na backbone ya uchumi wetu tunao uhakika italipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna uhakika reli italipa, bwawa la Mwalimu Nyerere litalipa, sasa hapa unatishatisha watu kwa ajili ya nini? Ni wahakikishie na wala hata siyo mbaya kwa sababu hii siyo Honorary Doctorate nimeingia darasani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Samia mbinu alizochukua na vision aliyoiweka kwenye masuala ya kiuchumi siyo ya kutiliwa mashaka. Wafuatilieni wabobezi wa IMF, World Bank, wafuatilieni Wachumi wote wanao-classify kuhusu uchumi, wanasema uchumi wa Tanzania unaelekea pazuri, uko pazuri na unaelekea pazuri. Haya siyo maneno ya Mwigulu! IMF wamesema hivyo, World Bank wamesema hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache kujidharau dharau, Watanzania tumezoea sana kujidharau. Hata juzi imetoka classification kwamba league ya Tanzania ni ya Tano, jamaa mmoja anasema haiwezekani league yetu haiwezekani league yetu ikawa ya tano. Sasa wewe unaumwa nini Tanzania ikiwa inafanya vizuri! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, majirani wote wanasema Mheshimiwa Rais Samia unaupiga mwingi majirani wote, kote juzi tulikuwa kwenye jukwaa la uchumi la Dunia, (World Economic Forum), miadi ya watu kumuona Mheshimiwa Rais ilikuwa haina hata nafasi, wanaona uchumi wa Tanzania ulivyo imara na matarajio yake yalivyo imara. Halafu sisi kutwa tunaona hatuendi vizuri!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutofautishe mfumuko wa bei na bei, mfumuko wa bei ambacho ndiyo Wachumi huwa wanapambana nacho kila wakati ni kiwango cha kubadilika kwa bei siyo bei! Inflation is the rate of average change of prices, not prices. Bei ni function ya cost of production na cost of transportation. Kama mtu kanenepesha ng’ombe wake kwa Milioni Moja huwezi kumwambia bei yake iwe Laki Mbili, hiyo ni kuu sekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumuko wa bei wa Tanzania siyo kama nchi zile ambazo asubuhi unabadilika, saa nne unabadilika, saa tano unabadilika, saa sita unabadilika, huo ndiyo mfumuko wa bei ambao it is a problem kwenye uchumi. Kama tatizo ni bei zinashughulikiwa kwa hatua hizi ambazo Mheshimiwa Rais amezichukua za kuongeza uzalishaji. Hatuwezi kuwa unatumia udikteta kwenye shughuli ambazo watu wamewekeza nguvu, wamewekeza fedha, wamewekeza muda. Kwa hiyo, hii hatua ambayo Mheshimiwa Rais ameIchukua actually ni long-term na itaenda kuhamisha watu kutoka mijini kwenda vijijini siyo siku nyingi. Tukifanya kilimo kikawa kinalipa tutaondoa rate hii ya unemployment na hii misongamano ya mjini lakini pia GDP itaongezeka. siyo hilo tu, per capital income itaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijasema mwenyewe tu leo, Mzee Kimei kasema, Balozi wa Kodi Mheshimiwa Subira Mgalu pia kasema, na wengine nao humu wameyaona kwa namna hiyo. Ningeshauri sana Bunge lako Tukufu liwe linatoa ushauri kwenye jambo la dharura, tulenge hilo la dharura halafu tumalize tuendelee na mambo mengine tusiwafanye wananchi wa-panic wananchi. Tunawapanikisha wananchi. Uchumi ni basi tu stock exchange hai-determine sana maisha mengine, nchi zingine ukitoa kauli moja tu unashusha uchumi chini kabisa, kwa hiyo tusiwe tunatoa toa kauli za unazuiwa hapa unapita hii, unazuiwa hapa unapita hii! Tuna-hinder investment, Rais anafanya kazi kubwa ya kuita investment sisi tumekazana kusema hii mbaya hii mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niliseme hili kwa msisitizo kwamba unaenda vizuri, yale yaliyo maoni tumeyapokea tutayaboresha, bahati nzuri sana maoni haya mengi tunatumia tunapokea kwenye Kamati lakini pia na Bunge zima hili. Kwa hiyo, tutaendelea kuyafanyia kazi yale lakini nitahadharishe tena, tusije tukawa tunajipaka taswira ambayo hatuna. Hali ya Dunia nzima wameongea pia Wabunge wengine, ina madhara kwa namna moja ama nyingine ndiyo maana tunachukua hatua za ndani kuweza kukabiliana nayo, Mheshimiwa Rais jitihada alizofanya ndiyo zinazotofautisha na maeneo mengine, tunakoenda tutakuwa hata imara zaidi kuliko hata hivi tulivyo. Nakushukuru sana Mwenyekiti. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja zetu zilizoko mezani. Awali ya yote nikiri kwamba tumepokea maeneo ambayo yanahusu ushauri, tutayafanyia kazi ili kuweza kuboresha kama Waheshimiwa Wabunge walivyoshauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hoja zilizojitokeza nifafanue hoja mbili/tatu. Hoja ya kwanza, limejitokeza jambo la Taarifa ya CAG.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri sana kwenye hili pia tukazingatia taratibu zinazotumika. Utaratibu unaotumika ambao tulijiwekea wenyewe kwenye sheria ni kwamba baada ya CAG kufanya ukaguzi wake, cha kwanza anachotoa ni hii taarifa yake, na baada ya hapo kutakuwepo na utaratibu wa Serikali kujibu. Lakini kwa taratibu zilivyo akishatoa taarifa ile Waziri wa Fedha anaipeleka Bungeni. Sasa zikishapita taratibu hizo itachambuliwa, ikiwa kwenye hatua za kwanza inapokuwa imekamilika kunakuwepo na hoja za ukaguzi na baada ya uchambuzi kutakuwepo na wizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa hoja za kiukaguzi kuna vitu vingine vinakuwa vya kiuhasibu. Hata hapa tu sasa hivi ukituuliza tutoe risiti mara moja kwa watu wengi namna hii, tutoe risiti mara moja ya mafuta ya kujia hapa, hauwezi ukapata risiti hizo kwa mara moja. Kwa hiyo, aliyekagua mara ya kwanza anaweza akaona risiti aliyotumia Mheshimiwa Dotto haipo. Huu hautakuwa wizi mpaka pale ambapo itajulikana kwamba Mheshimiwa Dotto hakwenda Dodoma lakini mafuta yake yametoka. Kwa hiyo, kunakuwepo na hoja za ukaguzi ambazo Serikali itafanya reconciliation, ikishafanya reconciliation hatua inayofuata tunabainisha yale ambayo yanahusu criminality, yale ambayo ni ya wizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na utakumbuka kauli ya Mheshimiwa Rais; mara ya kwanza tu alipokuwa anapokea Ripoti ya CAG, alimwambia CAG usipepese macho, usifanye kuficha. Kauli ya aina hiyo ni mwongozo mkubwa ambao Waheshimiwa Wabunge hampaswi kutilia shaka utayari wa Serikali kuchukulia hatua masuala yanayohusu rasilimali za nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, sisi tumepokea taarifa ya CAG kama Serikali na hatua zinazofuata itafuata taratibu hizo za kiutawala bora kama inavyotaka, kukagua wapi pana hoja ya kiuhasibu na wapi pana upotevu. Pale ambapo pana upotevu hatua stahiki zitachukuliwa, wale waliohusika watafika kwenye mkono wa sheria na watawajibika kwa makosa ambayo wameyafanya.

Kwa hiyo, kwenu ninyi Waheshimiwa Wabunge tumepokea maelekezo yenu na Serikali itachukua hatua kwa yote yale ambayo yanahitaji hatua za kisheria kuchukuliwa; na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ameongelea kwa upande wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, na si tu taarifa ya CAG, makosa yote yanayohusisha ukosefu wa maadili kazini yamekuwa yakichukuliwa hatua hata kabla ya Taarifa ya CAG kutolewa. Kuna watu wanafukuzwa kazi, kuna watu wanapelekwa mahakamani, kuna watu wako TAKUKURU, kuna watu wameshahukumiwa. Tuna kesi za kutosha, na ndiyo maana tukienda kwenye utawala bora tunakuwa kwenye rank za nchi ambazo zinafanya vizuri, ni kwa sababu tunafuata utaratibu wa utawala bora. Utaratibu wa utawala bora una gharama yake, gharama yake ni ufuate taratibu na wakati ule ule wakithibitika wanachukuliwa hatua. Kwa wale Wanasheria watasema kwamba ni namna gani ambavyo kwao kisheria ni kosa kubwa sana kumwonea ambaye hana hatia kuliko hata kuswaga wale ambao wana hatia ukaunganisha na wale wasio na hatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la mwisho lilikuwa linahusu suala la mfumo, Mheshimiwa Mbunge ame- generalize sana, anasema muda wote mnatudanganya, mnasema mifumo, mifumo, mifumo. Ndiyo haya ninayoyasema tuongee kama viongozi, panapokuwepo na tatizo tuliseme lile tatizo tu tusi-over generalize, unavyo-over generalize hivi tunaipaka matope nchi yetu, pia tunamvunja moyo Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge hawa wanatoka majimboni, katika kipindi ambacho fedha zimemiminika mikoani kuliko kipindi chochote ni wakati huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zilizokwenda TARURA ni nyingi kuliko kipindi chochote tangu TARURA ianzishwe, namba hazidanganyi, ndivyo ilivyo. Ukienda kwenye Elimu hakuna mwaka tumewahi kujenga madarasa mengi kwa mpigo kuliko hii miaka miwili iliyopita, hizo ni fedha zinakwenda kwenye halmashauri zetu. Sio hivyo tu, ukienda kwenye elimu bure ambako na kwenyewe wanapokea watoto wetu, hakuna mwezi umepita kwamba fedha hazikwenda. Kwa hiyo, ikitokea mfumo umeleta hitilafu either kwenye mwezi, either kwenye halmashauri, either katika baadhi ya maeneo...

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba anavyosema Waziri wa Fedha hakuna wakati kama sasa fedha nyingi zimetengwa kwenda kwenye halmashauri. Shida kubwa iliyokuwepo kuanzia mwezi Oktoba mpaka Januari pamoja na uwepo wa hizo fedha nyingi, lakini fedha zilikuwa hazitoki. Kwa hiyo hazitoki kwa nini? Mfumo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani zipo nyingi na kwa kweli tunamshukuru kwa kutenga fedha hizo nyingi, lakini zilikuwa hazifanyi nini? Hazitoki, ndio shida iliyokuwepo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, taarifa hiyo.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge ameongea Kibunge ili na Watanzania waweze kuelewa nampongeza sana Mheshimiwa Kanyasu. Hilo likoje? Liko hivi unapokuwa na utekelezaji wa miradi mingi kwa wakati mmoja. Zimeiva certificate mathalani imeiva Busisi ina deadline, imeiva Bwawa la Mwalimu Nyerere ina deadline, imeiva ya reli lot mbili, tatu, nne, kwa utaratibu wowote ule imeangukia pamoja na mishahara, imeangukia pamoja na Deni la Taifa. Utaratibu wa malipo unaanza na first charge, baada ya hapo unaenda kwenye vyombo, baada ya hapo unaenda kwenye mikataba ambayo ukichelewa ina riba, baada ya hapo tunaendelea kutiririka na zingine, hivyo ndivyo tunavyofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwenye kipindi ambacho hutekelezi miradi mingi ni kawaida kwamba kila unachokipeleka kitakuwa kinatoka tu. Kwa mfano, sisi tu hapa tukiambiwa tutoke kwa mara moja hapa, siku zingine tunavyotoka kwa utaratibu huu mlango ni mkubwa, lakini tukiambiwa tutoke kwa mara moja hapa hatutaweza kutoka kwa wote kwa mara moja. Sio kwamba humu ndani kutakuwa hakuna watu, tupo wengi wa kutosha, lakini hatuwezi tukatoka mara moja mlango ule pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, fikirieni Mheshimiwa Rais wakati anaingia Bwawa la Mwalimu Nyerere lilikuwa kama asilimia 34, 35 au 37 Wizara ya Kisekta inaweza ikaniweka sawa, lakini ndani ya miaka miwili tumeshapiga tunaitafuta asilimia 90; hebu waniambie mtiririko wa certificates ukoje, kuna wakati certificate zinaingia kwa mara moja. Kwa mfano mwezi ule uliopita aliotolea mfano hapa, certificate ya bwawa peke yake ilikuwa dola milioni 137, dola milioni 137 kwa mradi mmoja weka Busisi, weka reli, lot moja unakuta dola milioni 49 au 50 ukiziweka zote ni dola milioni 150 haya weka ya elimu bila malipo kuanzia chekechea mpaka form six. Ukishachanganya haya yote kuanzia tarehe 20 mpaka tarehe 24 au 25 kuna mishahara, baada ya hapo kuna deni la Taifa, ndugu yangu ni lazima tu mtiririko wa malipo lazima uwe na namna ya kuwa na utaratibu kwenye miradi ile mingine midogo tofauti na utaratibu ulivyokuwa mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu huo, ushahidi ndio huo sasa, hakuna mradi wowote ambao umekosa malipo, yaani hakuna mradi ambao umekwama mikubwa kwa midogo. Kwa hiyo, ule utaratibu wa mtiririko kama alivyosema Mheshimiwa Kanyasu nadhani ni vizuri kuelewa majira ya utekelezaji wa miradi na kuweza kwenda sambamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lile lingine alilosema Mheshimiwa Mbunge kama fedha zipo toeni. Narudia tena utaratibu wa utoaji wa fedha tunautoa kwa certificate na huu utaratibu umewekwa na Bunge, hatugawanyi fedha kufuatana na bajeti kwamba kwa sababu huyu ana bajeti ya kiwango hiki tunampatia akae nazo, hapana. Tunatoa kufuatana na certificate, tunatoa kufuatana na utekelezaji wa mradi, kazi zilizofanyika. Fedha ambazo tunazitoa ifikapo muda ni mishahara, ukifika muda wa mishahara tunatoa, lakini utekelezaji wa mradi, kama mradi wa ni trilioni 20, hatutoi trilioni 20 hizo zote zisubirie utekelezaji wake, tunatoa kufuatana na certificate, kwamba wametekeleza hapa, pameshakaguliwa na pameonekana panafaa kulipwa, ndio tunalipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na miradi hii yote kama ambavyo nimekuwa nikisema na huu ni ukweli...

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Hakuna nchi inatekeleza miradi mikubwa mingi kwa wakati mmoja kama Tanzania, kwa Afrika Mashariki na SADC, hakuna mradi ambao umelala kwa sababu tumeshindwa kuulipia hivyo hivyo na kwa miradi mingine…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwigulu kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kinachozungumzwa na Mheshimiwa Kanyasu labda pengine hakukipata vizuri. Ni kwamba kule kwenye halmashauri zetu tunakuwa na pesa na zimeshaingia kwenye vitabu vyetu, sasa certificate inaletwa, lakini pesa haitoki kwenye mfumo, ndio hilo tu labda angetusaidia kufafanua, haviingiliani kabisa taarifa za Nzega Vijijini haziwezi kuingiliana na miradi mikubwa ya kimkakati kama Daraja la Kigongo - Busisi haviwezi kuingiliana, hiyo ni project tofauti na Nzega ni project tofauti. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, mtoa ruhusa wa malipo yoyote ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, kama hilo litaingilia katika kipindi ambacho ni cha malipo ya mishahara definitely itasubiri, kitakachokuwa kimesubirisha ndio hicho kule mfumo utakuwa down kwa sababu mlipaji mkuu haja authorize, first charge lazima itoke kwanza ndio utaratibu ulivyo. (Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi niongelee vitu vilivyojitokeza kwenye eneo linaloangukia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiwango kikubwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inahusisha Ofisi ya Vitambulisho vya Taifa, Zima Moto, Uhamiaji, Polisi na Magereza. Hata hivyo, kwa kiwango kikubwa masuala yaliyojitokeza zaidi yanahusisha, Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, sitasema kwa kirefu kwa sababu tutakuwa na fursa katika Wizara yangu tutakapoongelea suala la bajeti yetu na utekelezaji wa bajeti katika kipindi kilichopita lakini kwa utangulizi tu kati ya yale yaliyojitokeza toka kwa Wabunge wengi, moja ya hoja ilikuwa ni malipo yanayotakiwa kwenda kwa Askari wa Magereza, Zima Moto pamoja na Uhamiaji ambao bado hawajapata package yao kama wanavyoita wenyewe wakijilinganisha na wenzao ambao tayari walishapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge pamoja na vijana wetu kwamba jambo hilo linafanyiwa kazi na watapata kama ambavyo wamepata wenzao na kama ambavyo ilikuwa ahadi ya Serikali. Ni kwamba tu kwa utaratibu wa Wizara yetu ya Fedha na kwa utaratibu wa hali halisi, wanapofanya malipo kuna vitu walivyoviweka kama first charge. Wanatoa kwanza mshahara wa watumishi, deni la Taifa na baada ya hapo kinachobaki wanaangalia namna wanavyoweza kugawa katika matumizi mengine haya ambayo tumeyasema. Kwa
maana hiyo, ndicho kilichosababisha wagawe kwa mafungu fedha hizo ambazo zilikuwa zinaenda kwenye vyombo vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwahakikishie vijana wetu walioko kazini wala wasivunjike moyo na wala wasiwe na hofu. Wale ambao walishapata na wenyewe watapata na mwisho wa siku wote watakuwa wamepata.
Ni ahadi ya Serikali na ni jambo ambalo litatekelezwa na ni jambo ambalo ni endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimelisikia sana kwa Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mchengerwa alilisema, ndugu yangu Mheshimiwa Ridhiwani alilisema, Mheshimiwa Matiko amelisema na wengine waliochangia. Ni jambo ambalo kama Serikali tunalifanyia kazi kwa ukaribu na
tunashirikiana na wenzetu na niwaombe vijana wetu in particular askari wetu watambue ni kautaratibu tu wala hatuna maana ya kuweka madaraja, lakini ni utaratibu tu wa utoaji wa fedha kufuatana na upatikanaji wa dirisha la kulipia fedha hizo zinazokwenda kwenye matumizi haya tuliyoyataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo liliongelewa sana na Waheshimiwa Wabunge na lilijitokeza kwa kiwango kikubwa ni suala la treatment ya Wabunge wanapokuwa hapa Dodoma na wanapokuwa kwenye maeneo yao ya kazi. Waheshimiwa Wabunge, nimelielezea
na kama nilivyosema kwenye briefing, tuna mambo mawili lazima tukubaliane nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kwamba nchi yetu inaendeshwa kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, yale yaliyo ya sheria ni lazima sheria iongoze na ndivyo tulivyokubaliana na sisi ndiyo tuliotunga sheria. Hata hivyo, kuna mistreatment inayotokana na mtu mmoja mmoja, tumeyatolea maelekezo ili haki ya Wabunge na ya wananchi wengine iendelee kuzingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba kwa umaskini wetu tulionao tungetamani tuwape watu vitu vingi sana lakini hatuwezi tukawapa kila kitu wananchi wetu. Hata hivyo, kitu kimoja pekee ambacho tunaweza tukawapa wananchi wetu ni haki yao ya msingi, haki ambayo wanastahili na hicho ndicho ambacho na sisi tunakisemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukirejea kwa Waheshimiwa Wabunge, nimetolea maelekezo na linapotokea suala la aina hiyo Mheshimiwa Mbunge uko maeneo fulani, uko kazini au hata kwenye mikutano, kwa wale walio wapya ni vizuri tukatambulika na tukajitambulisha
na ni vizuri tukatoa hizo taarifa kwamba kutakuwepo na shughuli A, B, C, D kama ni ya mikutano na tukaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wengine wameendelea kuelezea kuhusu mikutano. Tulishasema, Waheshimiwa Wabunge wanaruhusiwa kufanya mikutano yao kwenye majimbo yao. Nilirejee moja ambalo limeelezewa sana kuhusu Wabunge wa Viti Maalum. Wabunge wa Viti
Maalum majimbo yao ni kwenye mikoa yao na wenyewe watoe taarifa ili kuondoa usumbufu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine lililojitokeza ambalo na lenyewe nimeona nilitolee taarifa hapa leo, Waheshimiwa Wabunge na hasa katika kipindi hiki ambacho tuko Bungeni, Mheshimiwa Spika alishalisemea alipokuwa akitoa mwongozo kuhusu namna ya ukamatwaji
au kufanyiwa mahojiano kwa Waheshimiwa Wabunge, mimi nasisitiza kile kile alichosema Mheshimiwa Spika. Ni mamlaka yake, ameelekeza kama Mheshimiwa Mbunge atatakiwa kwa mahojiano, taarifa itatolewa kwa Mheshimiwa Spika. Hilo lilishasemwa na hivyo ndivyo itakavyokuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wangu kwenye ile inayoangukia kwenye mamlaka yangu, naelekeza, kama suala ni mahojiano angalau kwa kipindi hiki ambacho Wabunge wako Bungeni hapa na wanafanya kazi ya kitaifa, waliyotumwa na wananchi waliowachagua, basi wale watakaokuwa wanataka mahojiano waje wawahojie Wabunge hawa hapa hapa Dodoma. Wachukue hayo maelezo hapa hapa Dodoma na wao warejee katika ofisi zao na yale maelezo waliyowahojia hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sababu kubwa tatu. Moja, kazi wanayofanya Waheshimiwa Wabunge hapa Dodoma ni ya kitaifa lakini pili unapunguza risk ya kumsafirisha Mbunge umbali mrefu huku unaenda tu kule kuchukua maelezo na tayari ulishafika pale pale na yeye
alikuwepo pale pale ungeweza kumhoji kile unachotaka kumhoji na ukaondoka na hayo maelezo. Kama ni vitu vingine ambavyo viko nje ya mhimili wangu kama ni vya kimahakama kwa maana kwamba viko nje ya Wizara yangu, basi hilo litaelekezwa na mamlaka husika kama ni la eneo ambapo anatakiwa akafanyie sio hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mahojiano, yule anayetaka kumhoji Mbunge aje na kumbukumbu zote, aje yule yule ambaye anataka kumhoji. Bahati nzuri Idara yetu imekamilika kila mkoa, kwa hiyo, hata kwa kutuma tu kwamba mhoji kwenye hili na hili inawezekana. Pia yule ambaye ana maelezo aliyetaka kuhoji na yeye anaweza akaja akamhoji Mbunge hapa hapa na hilo likaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini usalama wa raia kwa ujumla wake, naendelea kurudia kusema kwamba, hatutaruhusu na hatutakubali uhalifu uendelee katika nchi yetu. Tunaendelea kupambana kama Serikali, kipaumbele kikubwa ni usalama wa raia wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapooongelea usalama wa raia wetu tunaongelea maisha ya watu wetu. Waheshimiwa Wabunge wengine mlikuwa mnauliza Waziri wa Mambo ya Ndani mbona husemi? Niwaambie kitu kimoja, hii sio Wizara ambayo kila kitu ni habari. Siyo kila habari kwenye Wizara hii ni habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani siwezi kusema kabla vyombo vyangu havijanipa cha kusema na ni utaratibu wa utendaji kazi katika vyombo hivi. Waziri ukiwa mstari wa mbele kutenda kazi kwenye Wizara ambazo ni za vyombo lazima utoe fursa; moja, ya vyombo kufanya kazi; lakini mbili watu kutendewa haki ili vyombo vifanye kazi kwa mujibu wa sheria, siyo kwa mujibu wa macho ya Waziri yanavyoona kwa sababu taasisi hii inatakiwa ifanye kazi kwa mujibu wa sheria na kwa maslahi ya Taifa na siyo kwa maslahi ya Waziri au vitu binafsi vya Waziri. Ndiyo maana tunatoa fursa ya vyombo vyetu kufanya kazi na Wizara, ndiyo maana tunatoa fursa hii ya kuweka ushirikiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mengine tutaendelea kuyapata kwenye Wizara yetu na kwa kuwa hotuba hii ni kubwa basi tutapokea maelekezo kutoka kwa viongozi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu. Kwanza niunge mkono hoja na niwapongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri wake kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu vingi ambavyo Waheshimiwa Wabunge wanavisema ndiyo vitu ambavyo Profesa na Injinia huyu wanahangaikia kila leo, katika kazi waliyotumwa na Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba wanarekebisha baadhi ya maeneo ambayo kama Watanzania tunayaona yakiwa na kasolo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wangu baadhi ya mambo yaliyogusa Wizara yangu niongelee moja, Mheshimiwa Mahawe pamoja na Wabunge wengine waliongelea jambo lililohusu masuala ya usafiri hasa wakigusia usafiri wa wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nilivyosema wakati wa bajeti yangu nitoe pole kwa familia pamoja na Watanzania wote tuliokubwa na tatizo hilo. Sasa nitoe maelekezo kwamba baada ya jambo hili kutokea, askari wetu wasifanye kwa zimamoto jambo hili.

Katika wiki mbili hizi ambazo shule nyingi zinaelekea likizo, wawaandalie vitu vinavyotakiwa kuwa kwenye magari yanayobeba wanafunzi. Wawaandalie masharti yanayotakiwa kuwa kwenye magari na shule zitakapofungwa wamiliki wote wa magari hayo, pamoja na wamiliki wa shule wanaotumia magari hayo waweze kufanyia kazi mambo hayo na kabla ya shule kufunguliwa watoe taarifa ni namna gani wametekeleza masuala hayo ambayo yatakuwa yameainishwa yanayohitajika katika shule hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishughulikia tunayemkamata peke yake, yule ambaye tutakuwa hatujaweza kumkamata ataendelea kuwa na gari bovu na tutamtambua siku ambapo litakuwa Limeshaleta matatizo, hiki ndicho kilichojitokeza katika siku hizi zilizopita.

Kwa hiyo, Idara zinazoshughulikia masuala ya usafiri likiwepo hili la mashuleni pamoja na maeneo mengine yanayobeba abiria, wabainishe vitu ambavyo vinatakiwa, wawapatie wamiliki na kwa shule wiki hizi mbili, zinatosha kuwaandalia masharti hayo. Kipindi cha likizo kinatosha kwa wamiliki wa magari pamoja na wamiliki wa shule kutimiza masharti hayo, lakini shule zitakapofunguliwa watoe taarifa, ukaguzi ufanyike na masharti kwa wanafunzi wanaosafiri mwendo mrefu lazima magari yale yawe yamepitishwa kwamba yanaweza yakabeba abiria kama ambavyo tunafanya kwa mabasi. Tusikamate moja moja kwa rejareja halafu tukaacha wale ambao hatukuweza kuwaona ama kuwakamata na tukaacha kuwapa masharti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili lililosemwa kwa kirefu ni hili jambo la mimba kwa wanafunzi/mimba za utotoni. Waheshimiwa Wabunge, niwaombe kwenye jambo hili tuelewane vizuri na niwaombe tusikilizane vizuri. Moja sisi ni viongozi, na siyo tu viongozi, tena watunga sheria, ni lazima jambo hili tulibebe kwa upana wake, tusilibebe kwa kipengele kimoja kimoja ambapo tutajikuta tunatunga sheria zinazokinzana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, siku tulipokuwa tunapitisha bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, mjadala mzito ilikuwa kuhakikisha tunatimiza sheria inayotaka ndoa zifanyike baada ya miaka 18 na kuendelea. Bunge hili na Wabunge hawa pia, Bunge ni Taasisi tulitunga sheria inayosema mtu akibaka ama akampa mimba mwanafunzi anatakiwa kufungwa miaka isiyopungua 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo tukisema hilo ni kosa, lakini leo hii tukichukua kipengele kimoja kimoja tena kwa kutumia kigezo cha huruma, tukahalalisha makosa hayo kuna sheria zingine tutashindwa kuzitunga na tutashindwa kuzitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu tu jambo ambapo huwa likitokea baya, tunatafuta namna ya kulihalilisha, watu wakipata njaa hatuhangaika kujiuliza kwa nini watu wanapata njaa, tunataka wapewe chakula kama vile kitashuka toka mbinguni. Watoto waki-fail sana mtihani hatuhangaiki kwa nini wana-fail tunabadilisha fail grade ili wafaulu vilevile, leo hii watoto wengi wakipata mimba hatuhangaiki ku-protect kwa nini wanapata mimba, kwa nini tuzuie wasipate mimba utotoni, tunahangaika kutaka kunahalisha wapate mimba. Hatuwenzi tukaipa dhambi jina zuri na baadae tukaitukuza, dhambi ni dhambi itabakia kuwa dhambi, hatuwezi tukaipa jina zuri na hatimaye tukaitukuza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi atakaye mpa mimba mwanafunzi tutamkamata, atafika kwenye mikono ya sheria na mzazi atakayeshabikia mwanafunzi kupewa mimba na yeye atakuwa ameshiriki kwenye uovu wa aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto mdogo aliyeko shuleni atakayeruhusu masuala ya kupata mimba ajue anakiuka maadili ya elimu, anakiuka maadili ya mila, anakiuka maadili ya imani na anakiuka maadili ya kisheria za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, mimi naijua vizuri Tanzania hii, kuna watu wanaijua Tanzania hii kwa vipande vipande. Kwa mfano, katika nchi yetu hata ukiruhusu watoto kurudi shuleni wanaopata mimba, watoto wa Kilimanjaro uwezekano wa kuwepo wanaopata mimba ni mdogo sana. Kwa sababu Kilimanjaro level yake civililazition, level yake ya sensitization ya elimu ilishafika juu…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango chake ni kikubwa, lakini leo hii ukiruhusu watoto kupata mimba na kuendelea na shule, halafu ulishaondoa viboko mashuleni, ulishaondoa adhabu mashuleni, huku Bara kwetu wanapomaliza mtihani wa kidato cha nne nusu yao ama wote wa kike watakuwa walishaolewa wana mimba wanasuburi wazae warudi mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme moja kubwa la ngazi ya watunga sheria kama Wabunge, tuangalie, tusichukue sheria moja tuangalie kwa ukubwa wake. Jimboni kwangu hivi nilivyoongea siyo kwamba natukuza watoto kupata mimba, lakini kama Kiongozi nimefanya hamasa Umoja wa Vijana wa CCM wote wafyatue tofali, nimetoa Mfuko wa Jimbo nikapeleka cement, nimepeleka nondo, nikatafuta na wadau tumeanzisha ujenzi wa hostel kwa shule zote 20 za kata kwenye Jimbo letu, ili kuwatengenezea watoto mazingira yatakayowaondoa kwenye mazingira ya kupata mimba.

Hatuwezi viongozi leo hii tukasema kwa sababu wanapata mimba basi turuhusu waendelee kupata mimba halafu waendelee na shule. Utaratibu gani huu wa nchi gani hii ambao watu wanarahisisha mambo kwa namna hiyo? Hatuwezi tukaruhusu vitu vya aina hiyo, halafu leo hii tukiruhusu aliyepewa mimba akaonekana hana kosa kwa neno lolote zuri tutakaloliweka, yule tunayemshtaki tunamshtaki kwa kosa gani? (Makofi)

Mambo makubwa matatu ninayoyasisitiza, moja Wabunge ni watunga sheria, tuangalie sheria hizi zinazokizana kwa mapana yake. Pili, tusiangalie sana suala la mimba hata tukaacha vigezo vingine, manaa yake tunaongelea mimba kama vile mimba inaweza ikaingia halafu mtoto asipate UKIMWI. Tunawasisitizia watoto wakafanye mambo hayo kama vile watapata mimba waendelee na shule, kama vile mimba itaingia halafu asipate UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge na Watanzania ni vema tukaweka uzito kwenye suala la maadili, kwenye suala la malezi, tukaweka na mazingira bora ya watoto kukaa bila kupata mimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi wakati naenda kuanza form one baba yangu aliniambia ukipata mjukuu mjini usimuache kule, lakini mama yangu akaniambia unavyoenda kule mjini uwe makini kuna UKIMWI kuna mtu tumemzika juzi. Hata kwenda disco sikuenda nikidhania wote wanaocheza disco wana UKIMWI, lazima tuwasisitizie watoto wetu madhara ya matatizo wanayoweza kuyapata wakifanya ngono katika umri mdogo na siyo kuwaambia fanyeni ngono mtarudi muendelee na masomo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo Serikali imeendelea kuweka mazingira ambao yanawa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji )

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri ahsante.
Itifaki ya Nagoya ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo Sahihi wa Faida zitokanazo na Matumizi ya Rasilimali za Kijenetiki.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa na niwashukuru Wabunge wote kwa umoja wao kwa kuridhia mapendekezo haya ya maazimio pamoja na itifaki tuliyoweka mezani. Kwa kuwa wameridhia kama ulivyosema sitakuwa na mengi ya kusema, niseme mawali tu ambayo yameleta sura za tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Serikali strong, yenye nguvu ni Serikali inayochukua hatua, inatenda na siyo Serikali inayosema na hiki ndicho kinachoendelea. Mheshimiwa Mnyika anaposema tumeongea sana kwenye mikataba na anajua ukubwa wa mambo yale, lakini Serikali jasiri na yenye nguvu imeenda kwenye kutenda, hicho ndicho ambacho Wabunge na Watanzania wote wametamani muda mwingi sana kukiona na ndicho ambacho Mheshimiwa Rais anakwenda kukitenda na analiomba Bunge lione umuhimu huo kwa ukubwa wa rasilimali za nchi yetu na ukubwa wa jambo lenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ukigeugeu ndiyo ambao huwa unaweka mashaka kwamba mtu ambaye ameliongea kwa muda mrefu sana jambo, linapoletwa anageuka inaleta maswali kwamba huyu mtu amegeukaje. Nimemshukuru sana ndugu zangu hapa walipokuja kuongelea kwamba siyo kila kitu kupinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili jambo ambalo lina maslahi ya Taifa, niwaambie Waheshimiwa Wabunge hata kama ataunga mkono mtu mmoja tu, Serikali hatuwezi tukarudi nyuma maadam tumepewa dhamana ya rasilimali za nchi yetu. Wabunge na kama Serikali na Wasaidizi wa Rais tunawahakikishia kwamba nia na dira aliyonayo Rais ni njema sana kwenye rasilimali za nchi yetu. Nawaombeni twende tuunge mkono wala tusipepesuke kwa kuzingatia vitu vingine ambavyo haviko kwenye dira yetu visije vikatutoa kwenye dira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi sana ambayo yamo kwenye itifaki hizi yalishaletwa mbele ya Wabunge na Wabunge wameshafuatilia na yamefanyiwa kazi na watalaam ambao wana dhamana na wenyewe kwenye Taifa letu, hatuna haja ya kuwa na mashaka, niwaombe tuende turidhie ili yaweze kwenda kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine Waheshimiwa Wabunge tunapoongelea ameongea Mheshimiwa Lema na Mheshimiwa Mnyika, ni vema sana tukawa makini sana tunapoongea. Nimemsikia akiongelea suala la Kibiti, lakini ningekuwa nakuuliza maswali mengi, najua usingepata majibu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kama una uhusiano na wale wahalifu hata ukadhani wameshinda, hebu waulize walianza wangapi na sasa wapo wangapi. Mwenzio Lema kwa sababu alikuwa kule gerezani anaweza akawaona wengine kule, wewe Mheshimiwa Mnyika ambaye hujaenda unaweza ukatusaidia, wewe unayedhani wameshinda wapo wangapi na wapo wapi? Lakini nikuhakikishie kwamba sisi kama Serikali hatutaacha eneo hata moja la nchi yetu hii likatawaliwa na uhalifu. Tutashughulika na mmoja mmoja na lazima haki ya watu wetu itasimama katika eneo lote la nchi yetu watasimama wakiwa wanafanya kazi kwa mazingira yaliyo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaongea kimzaha mzaha, lakini taswira iliyopo ndani kabisa na niliisema mahali pengine, ina taswira hiyo ya siasa siasa. Leo hii ukituambia kwamba yale yanayoendelea Kibiti yataenda na maeneo mengine, tunaendelea tu kutafuta connection unajuaje kwamba yanaendelea na maeneo mengine. Kwa sababu kama anauawa Mwenyekiti wa CCM, anauawa wa CCM, wanaruka nyumba ya yule asiye wa CCM na wewe unasema yataendelea na maeneo mengine, una haja ya kutusaidia kujua kwa nini yataendelea na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini unadhani kwamba wanashinda,kwa sababu sisi kwenye mpango kazi wetu tuliopanga, tunaenda hatua kwa hatua kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo yote ya nchi yetu wanakuwa katika mazingira salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sentensi kama hizi pamoja na kwamba zimesemewa Bungeni nadhani kuna umuhimu sana ndugu zetu hawa watasaidia kujua kwamba kumbe sisi tunavyotafuta sana kumbe kiini ama kinatoka Bungeni au Serikalini, lakini sasa wanaenda kuhangaika na wananchi ambao ni very innocent, ndiyo maana sisi tunakuwa very responsible.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu kwenye mambo ya siasa tunatakiwa tupambane sisi wanasiasa na siyo wananchi wengine ambao wanashughulika na shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda umeisha, ninaomba tu kutoa hoja kwamba Bunge lako sasa katika Mkutano wake wa Saba liridhie Maazimio tuliyoyaleta pamoja na marekebisho na Itifaki tuliyoleta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2023
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kutoa machache katika kuihitimisha hoja hii. Awali ya yote niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja hii ambayo tumeiweka ya PPP, natambua mchango wa Mwenyekiti wetu wa Kamati, maoni ya Kamati yenyewe, maoni ya Wabunge wengine waliochangia akiwemo Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Katimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeyapokea maoni hayo na yanaenda sambamba na hatuna haja ya kubishana nao kwa sababu hoja hizo zote ambazo wamezitaja zina mantiki na kwa kweli hilo ndio lengo mahususi ambalo Mheshimiwa Rais ameliona katika kuifanya Sheria yetu hii ya PPP iweze kufanya kazi kwa urahisi. Mheshimiwa Kandege ameelezea kuhusu barabara pamoja na bandari lakini na barabara ya upande wa pili kwenda DRC, haya ndio hasa maengo mahususi ya sheria hii kwamba tuweze kuongeza wigo wa kufanya shughuli za maendeleo kwa njia hii ya ushirikishaji wa Sekta Binafsi ikishirikiana na Sekta ya Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu hii imetoka mbali sana, ukichukua ulinganifu wa hata upande wa makusanyo tu kabla ya ushiriki mpana wa Sekta Binafsi na sasa pana utofauti mkubwa sana. Ukichukua wakati tuko Sekta ya Umma kufanya kazi kwa asilimia zote, chukulia mfano wakati Awamu ya Pili inaingia makusanyo kwa mwezi yalikuwa takribani bilioni 30. Bilioni 30 kwa mwezi makusanyo hayo leo hii tunaongelea ni fedha iliyo chini hata ya mgao wa Wizara moja katika fedha ambazo zinakwenda kwenye Wizara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unaweza ukaona kwamba ushiriki wa Sekta Binafsi ambapo unaenda kuongeza shughuli za uzalishaji, leo hii umeweza kuongeza makusanyo kwa kiwango kikubwa na ushiriki wa wananchi ambao wanashiriki katika shughuli za maendeleo kupitia Sekta Binafsi. Kwa hiyo Sheria hii ambayo tumeileta inaenda kupunguza kama tulivyoelezea wakati wa kutoa maelezo kupunguza yale yaliyokuwa yanakwamisha miradi kuweza kutekelezwa kwa namna hiyo. Hivyohivyo na kile ambacho Kamati imetushauri na kile ambacho Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Sillo ameelezea ni yale ambayo yanaenda kuboresha kuanzia mchakato wa ushiriki wa Sekta Binafsi lakini pia na baada ya kuwa mradi umeshaanza kutekelezwa kwa njia hizo za ubia.

Mheshimiwa Naibu Spika, yale yote ambayo yameelezewa ambayo yanaenda kuboresha zaidi utendaji, tumeyapokea na tutakapoenda kwenye utungaji wa kanuni tutazingatia ili kuweza kuleta ufanisi wa Sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Sapika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hiyo na kwa ajili ya muda niende kwenye mambo makubwa tu yanayohitaji ufafanuzi, yale mengine yaliyo ya maoni niseme tu tumeshapokea maoni hayo tutayafanyia kazi kiutawala kwa ukubwa wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na hoja hii ambayo ilikuja kama swali anayoisemea Mheshimiwa Msigwa kama Mheshimiwa Rais alichozindua ni e-passport ana ni e- immigration.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lilirudiwa kukosewa hata siku ile Mwenyekiti wa Kamati husika aliposema na niliona Wabunge wakishangilia wakisema kwamba tungeanzia kuzindua e-immigration ndio tuzindue e-passport.

Mheshimiwa Naibu Spika, e-immigration ni set na hivi vingine tunavyoendelea navyo ni subset za e-immigration, so the whole system ni e-immigration ndani yake kuna e- passport, kuna e-visa, kuna e-permit, kuna e-gate kwa maana hiyo Mbunge, Mwenyekiti wa Kamati ile aliyosema anashangaa kwa nini tumezindua e-passport badala ya e- immigration ni confusion, is a total confusion kwa sababu e-immigration hamna sehemu utaenda kuishika kwamba hii ndio e-immigration. Lakini tunachosema…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri naomba utusaidie kwa sababu jambo hili limesha pelekwa kwenye Kamati ili nyaraka zipelekwe huko, mimi ningeomba ujielekeze kwenye mambo mengine kwa sababu hili tayari tutaletewa ufafanuzi na kamati mahsusi.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, lakini kuna mambo ambayo yalikuwa ya Wizara kwa mfano anaposemea hii ilikuwa inauzwa pound nane hii ni dola 68. Dola 68 hii siyo arrangement ya supplier, hii ni bei ya immigration ambayo sisi kama waendesha mradi tuna amri ya kutoa passport bure kama tunavyotoa kitambulisho cha Taifa ama kuuza, kwa hiyo tumepiga hesabu tukaona hii tunatakiwa tuuze ili kuweza kutengeneza maduhuli lakini pia na ku-cover gharama za mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa umetolea maelekezo na mimi wakati wa kusimama nilikuwa natamani nimwambie Mheshimiwa Msigwa aweke hizo nyaraka leo leo lakini mmempa muda mrefu zaidi basi ngoja aende kwenye hiyo ya muda mrefu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kwenye hili la ulinzi wa Waheshimiwa Wabunge, hoja ya viongozi kupewa ulinzi ni hoja ya msingi na sisi kama Serikali hatuwezi tukapingana na hoja ya ulinzi kwa viongozi na hoja ya ulinzi kwa wananchi ni hoja ya msingi ambayo sisi kama viongozi hatuwezi tukapinga hoja ya ulinzi kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini jambo moja tu ambalo naomba nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge ni kwamba kuna miundombinu ambayo lazima iwe imefanyika katika nchi ili uweze kufanya ulinzi wa Mbunge mmoja mmoja. Kwa mfano kwa hapa Dodoma sisi tayari tulisha kubaliana na Kamati na tulikubaliana na tulitoa taarifa kwamba maeneo wanapokaa Wabunge tutaimarisha doria punde Wabunge wako hapa, na maeneo ambako kuna Wabunge wengi wanakaa kwa pamoja tutaweza kutengeneza utaratibu wa askari ambao watakuwa katika maeneo hayo ama kwa njia ya doria ama kwa kuwaweka katika station hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini utaratibu wa kuwa na ulinzi kwa Mbunge mathalani kwa kila jimbo ni jambo ambalo linahitaji miundombinu kwanza kabla hujaweka utaratibu huo. Lakini hata hapa kuna maeneo mengine ambako Wabunge wanakaa. Kwa taratibu za kiusalama lazima utengeneze miundombinu kwanza kwa sababu si kila eneo unaweza ukam–station askari, unaweza ukamuweka kwenye risk ya kushambuliwa hasa katika maeneo ambayo watu wangeweza kutaka hata kuchukua silaha hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo wazo kama hilo kufika Serikalini ni jambo jema, ni wazo ambalo ni la kitaifa na sisi tungeomba Wabunge waelewe kwamba jambo hilo linahitaji miundombinu kwanza kabla hujaweza kupeleka ulinzi katika eneo hilo. Kwa mfano nchi zingine ambako wanafanya ulinzi wa aina hiyo, Mbunge akishachaguliwa kuwa Mbunge hakai eneo alikokuwa anakaa, anakaa wilayani kama mkuu wa wilaya anavyokaa na kwa namna hiyo unaweza ukasema hili ni eneo la viongozi unaweza kupeleka ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwetu sisi katika nchi yetu utaratibu huo haupo na hata sheria yake haipo kwa maana hiyo kama jambo hilo litakubalika kama Taifa kuna miundombinu mingi sana ambayo inatakiwa ifanyike na hiyo ndiyo ingeweza kuwa njia njema ya kulifanyia jambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nizitakie kila la heri timu zinazocheza weekend hii hasa Simba kwasababu mara ya mwisho Simba kushiriki mashindano haya Zitto Kabwe alikuwa bado yuko CHADEMA.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika eneo hili la uwekezaji pamoja na viwanda. Nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kazi kubwa anayofanya ya kutekeleza maono ya Mheshimiwa Rais katika sekta hii.

Mheshimiwa Spika, mtaweza kuona kwamba uwekezaji ambao umeishaingia ndani ya nchi yetu, pia na performance za viwanda ambapo sisi ni wadau wakubwa sana kwenye masuala ya performance za viwanda na uwekezaji katika eneo la kupata kodi pamoja na kukuza GDP, tunaiona wazi wazi. Hongera sana Mheshimiwa Waziri na hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kuchangia nianzie kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na kukiri kwamba hoja zile ambazo wamezileta zinazo angukia upande wa Wizara yetu tumezipokea na tutazifanyia kazi na bahati nzuri sana wametoa maoni haya katika kipindi ambacho tunaendelea kukamilisha nyaraka ambazo tutazileta kwa ajili ya mjadala mpana wakati wa Hotuba ya Bajeti ya Serikali lakini pia na katika Finance Bill ambayo itajadiliwa mara tu baada ya bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, nikianza na yale masuala ambayo wameyaongea ya kikodi nitaomba uridhie na Waheshimiwa Wabunge niwaombe waridhie nisipitie kamoja kamoja kwa sababu ndiyo tunaendelea kukamilisha waraka huo. Tumepokea maoni yenu na niwaahidi kwamba tutakuja na hatua za kikodi ambazo ni rafiki kwa sekta binafsi kwa sababu huo ndiyo muelekeo wa nchi yetu na ndiyo muelekeo wa Mheshimiwa Rais kwa kutengeneza sheria za kodi ambazo ni rafiki kwa sekta binafsi na ni rafiki kwa uwekezaji, rafiki kwa mazingira ya biashara ili kuweza kutengeneza ajira na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja pamoja na uchumi wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, liliongelewa kwa sauti kubwa suala la Kariakoo na lenyewe tumelizingatia tumepokea na yenyewe tutakapo kuja kwenye mjadala tutakuwa tumezingatia maoni yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye masuala mahususi yaliyoongelewa, jambo moja ambalo limeongelewa lilikuwa la ETS yale masuala ya Electronic Tax Stamp.

Mheshimiwa Spika, jambo hili utakumbuka lina maelekezo ya Bunge katika kipindi kilichopita mwaka mmoja ama miwili Bunge lilielekeza Waheshimiwa wabunge kwa kauli moja walielekeza kwamba Serikali iangalie upya jambo hili kwa sababu bei zinazotolewa na mtoa huduma ni kubwa. Serikali ilichukua hatua kwa kutangaza hili jambo hili lifate taratibu za International Tendering ili kuweza kualika wadau wengi wanaofanya kazi hiyo tukiwa tunashirikiana na sekta binafsi kuweza kupata mdau ambaye ataweza kutoa huduma hiyo kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Spika, mchakato uliendelea na wakati mchakato unaendela, nilisikia kauli moja anasema mbona akapewa sasa yule aliyekuwepo. Kwa sababu utaratibu wake unachukua takribani miezi sita na kuendelea, tuliona lazima utaratibu wa makusanyo uendelee katika kipindi hicho cha mpito ambacho ni cha mwaka mmoja, kwa hiyo utaratibu umeenda mpaka mwisho na nitawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa umahsusi wa jambo hili katika hatua fulani hivi waridhie kwamba tutalielezea kwa kina katika ngazi ya kamati na kamati inawakilisha Bunge lakini wapokee maelezo haya ninayoyatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipofikia katika hatua ya kufanya uchambuzi. Uchambuzi ukafanyika mpaka mwisho na timu iliyokuwa inafanya uchambuzi ilikuwa imekusanya wazoefu wa utaratibu hizi za kimanunuzi kutoka taasisi zetu zote muhimu tunazozifahamu zote za vyombo pamoja na zile ambazo ni za kimanunuzi.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho wa siku taarifa ile ya mwisho ilionesha kwamba bei zilizokuja hazitofautiani sana na zile zilizokuwepo na wahusika ambao wameenda kwenye hatua hizo wanaeleka kwenye utaratibu ule ambao bei ziko zile zile ambazo zilikuwa zimeamsha hisia hizi za wabunge na kuleta hoja ya kutaka tupate mtoa huduma mpya.

Mheshimiwa Spika, sasa ilivyofika mpaka mwisho pale sifa zile zilizokuwa zinatakiwa zilionekana hazijafuzu kwa sababu kile kilichokuwa kinatafutwa kuanzia maoni ambayo yalitolewa na wabunge ya bei hayakuwa yametimia. Kwa hiyo, kile ambacho kilikuwa kimefikia kwa hatua hii ilikuwa ni mchakato ule ufanyike upya na mchakato wenyewe unafanyika kwa hatua zote ikiwepo ya Window Shopping, ikiwepo ya National Shopping, kwa hiyo timu mbalimbali zimeenda katika maeneo ambako wananweza wakapata teknolojia mpya, teknolojia rafiki, teknolojia ambayo ina gharama nafuu lakini pia ikizingatia uwezekano wa kuihamishia teknolojia hiyo katika mamlaka zetu za usimamizi ili hitimisho wa siku jambo hili liweze kufanywa na watanzania wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ombi langu kwa waheshimiwa wabunge, kama kuna Mbunge ambaye ana mtu ama kampuni, ama taasisi ama teknolojia ama anajua mahali ambako teknolojia tunaweza tukaipata ambayo inaweza ikatoa huduma hiyo hata kwa nusu ya ile ambayo ipo, nimkaribishe aje ofisini aonane na mamlaka yetu inayosimamia jambo hilo Mamlaka ya Mapato Tanzania, halafu aweze kuunganisha timu ile inayofanya hiyo shopping pamoja na hiyo taasisi ambayo inaweza ikatoa huduma hiyo ili tuweze kukamilisha mchakato huo kwa ufanisi na tuweze kupata kile ambacho sekta binafsi yetu itanufaika na Watanzania watanufaika lakini na Serikali iweze kupata kodi katika gharama ambazo zinahilimika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo hilo liko hatua hiyo na tunaamini si muda mrefu sana tutaenda kwenye hatua ya mwisho na tutaendelea kulitolea taarifa jambo hili katika Kamati ya Bunge pamoja na Bunge lenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikihamia katika hoja ya pili ambayo ni mahsusi ni jambo lile la kiwanda cha Twiga, jambo hili ni jambo nyeti sana. Moja, sisi kama Serikali tuna interest kubwa sana kwenye jambo hilo kwa sababu kati ya wale wawekezaji kwenye kiwanda hiki ambacho tunakiongelea asilimia takribani sitini na nane ni hawa ndugu zetu wa AfriSam lakini asilimia zinazosalia mnajua kwamba upo mkono wa Serikali kupitia mifuko yetu ya hifadhi ya jamii ambalo ni jambo nyeti sana kwetu sisi kama Serikali. Kwa maana hiyo niwahakikishie Wabunge Serikali inapeleka macho yake yote mawili kuhakikisha kwamba jambo hili halifi bali linaendelea na hiyo ndiyo ambayo imekuwa concern ya wabunge kwamba labda kiwanda hiki kinaweza ikafanyika janja janja kwamba kikanunuliwa halafu kikafungwa. Hakiwezi kufungwa kwa sababu kimebeba maslahi ya nchi, kimebeba maslahi ya Serikali na kimebeba maslahi ya watanzania, hakiwezi kikafungwa. Mbali na habari ya ajira lakini ile tu yenyewe kwamba kwenye umiliki tuna taasisi zetu ambazo zina mkono mle hatuwezi tukaruhusu kikafa na hatuwezi tukaruhusu wale watakaofanya merging wakakipeleka kwenye kufa hilo halitatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili tukiacha utaratibu ukaendela hivi ilivyo sasa mwisho wa siku Serikali itaenda kubeba mzigo ule wote kwa sababu nimewatajia aina ya wamiliki walioko mle. Kiwanda hiki kikifa maana yake wale watu hawawezi wakapata hiyo hasara hii hasara itahamishiwa Serikalini. Kwa maana hiyo kwa hali waliyonayo ya sasa hivi kwa takribani cash flow zao ziko negative zaidi ya bilioni kumi na moja, hivi tunavyo ongea hawawezi wakastahimili kuendelea wao wenyewe tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye upande wa madeni wana deni kubwa ambalo linazidi bilioni mia mbili na tatu. Mnaweza mkaona kwamba hata wa kuwafufua tu anatakiwa awe na muscle kwelikweli. Wana 203 deni na wana overdraft ya zaidi ya bilioni 19 wanapumulia mashine hao walipo hapo wanahitaji wa kuwainua mwenyewe awe very strong. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa taratibu hizo zimeshafanyika zimeenda hatua nyingi. Mheshimiwa Naibu Waziri ameshaelezea vizuri masuala ya kisheria mimi naomba Waheshimiwa Wabunge muiamini kamati yenu Serikali tutaenda kuelezea kwa kina na niwaombe tusije tukalipazia sauti sana hili jambo, kwa sababu ukiondoa uwekezaji huu peke yake masuala ya kiuwekezaji ni very sensitive. Hizi back and forth tunaweza tukashughulika na mwekezaji mmoja lakini tukakimbiza wengine 50 kwa sababu tu ya back and forth ambazo tunazifanya.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri tukaenda kwenye hatua kama nchi tukaendelea kupunguza yale ambayo kwenye rating tunakuwa rated chini kwa kuchelewesha uwekezaji na kuwa na milolongo mingi ambayo ina mikono mingi kwenye taratibu ambazo zinahitaji jambo liishe halafu tuweze kuendelea na uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema na nimeshaona kengele ya pili imeshagongwa niwaombe Waheshimiwa Wabunge waiamini Serikali, lakini pia waiamini Wizara, lakini pia waiamini Kamati. Tutaenda kutoa maelezo ya kina Kamati ya Bajeti na tutatoa maelezo ya kina kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara kwa niaba ya Bunge zima ili tuweze kuelewana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ili kuweza kuhitimisha hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote niwapongeze Waheshimiwa Wabunge kwa hoja ambazo wamezitoa na nianzie ufafanuzi wangu kwenye eneo hilo la jumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili na Watanzania wajue, leo hii tunayoijadili ni Wizara ya Fedha, Bajeti ya Serikali itakuja wiki ijayo. Kwa hiyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge tumepokea hoja zote, na waridhie zile zinazoangukia kwenye hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali, kwa sababu matayarisho yake bado yanakamilika kamilika zikiwepo zile za hatua za kikodi, waridhie kwamba tumezipokea na tutakuwa na mjadala mpana tutakapokuwa tumewasilisha yale ambayo tumeyaweka maoni yao na yale ambayo watatamani tuyabadilishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo yale masuala yote ambayo yamejitokeza yanayohusisha masuala ya kikodi niwaombe waridhie kwamba tutayajadili kwa upana baada ya kuwa tumeshawasilisha kile ambacho tumekiandaa katika kauli ya Serikali, ambayo tutaiotoa tarehe 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, pia kwa manufaa ya ufafanuzi ili na wananchi waelewe; bajeti ya maendeleo ambayo tunaiongelea kwenye muktadha huu hapa ni bajeti ya maendeleo kwa Wizara ya Fedha na taasisi zake. Huwa inatokea tukisema bajeti ya kawaida ni mathalan hapa shilingi trilioni 15, wanatokea wengine wanasema bajeti ya maendeleo ni kidogo, kama hivi iko shilingi bilioni karibu 500, inazidiwa na bajeti ya matumizi ya kawaida. Kwa leo hii hapa tunapoongea bajeti ya matumizi ya kawaida ndani yake ina takribani shilingi trilioni 10 ambazo zinaangukuia kwenye Deni la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Deni la Taifa kama tulivyotoa kwenye ufafanuzi wa majukumu ya Wizara linasimamiwa na Wizara ya Fedha. Kwa hiyo tuna trilioni 10 ambazo zenyewe ni Deni la Taifa kwa mwaka, na bilioni 500 wanayoiona hiyo ni bajeti ya maendeleo kwa Wizara ya Fedha na taasisi zake. Bajeti ya Maendeleo ya Nchi nzima tutaitaja tutakapotoa Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, na Deni la Taifa wanaloliona, hizo shilingi trilioni ni Deni la Taifa kuanzia awamu ya kwanza. Awamu ya kwanza, awamu ya pili, awamu ya tatu, awamu ya nne, awamu ya tano na kwa awamu ya sita kwa mikopo hii ya roll over pamoja na ya ndani kwa sababu za mikopo ya nje bado hazijaiva ndiyo inayoleta jumla ya deni la hilo la shilingi trilioni 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Fedha pia ndani yake pia kuna Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ambapo na yenyewe fungu lake tunaliomba pamoja na mafungu haya mengine, na tuna ofisi zingine kama tulivyoziorodhesha wakati wa kuwasilisha taarifa hii rasmi ya leo. Kwa hiyo uwiano ule wa fedha za matumizi ya Kawaida kuwa kubwa na uwiano wa matumizi ya maendeleo kuwa ndogo ni kwa sababu matumizi ya kawaida yanahusisha Deni la Taifa ambalo ni la awamu zote. Na matumizi ya maendeleo namba yake ni ndogo kwa sababu tu inahusisha matumizi ya Wizara ya Fedha na taasisi zake na matumizi ya maendeleo ya jumla yatakuja kwenye Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea ushauri wa kamati, na maeneo yale kama nilivyosema mengine yamejikita kwenye sera za masuala ya kikodi kwa hiyo tutatoa tamko tutakapokuja wakati wa tamko la Bajeti ya Serikali. Tumepokea hoja kubwa ambayo imejadiliwa kwa mapana na Wabunge wengi kuhusu ukaguzi wa ndani. Wabunge watakumbuka mwaka jana walitupitishia mabadiliko ya kimuundo ya Ofisi ya Ukaguzi wa Ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilichokuwa kinatokea kabla ya huo muundo wa mwaka jana ambao tulipitishiwa mapendekezo na Bunge, Wakaguzi wengi wa Ndani walikuwa ni sehemu ya management. Kwa sababu Fungu lao, vote yao ilikuwa inaangukia kwa wale wanaowasimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufikia mwaka jana tulibadilishiwa muundo, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani ilipewa vote yake na mtiririko wake. Sasa baada ya Bunge kupitisha, ilienda kwenye hatua za kutengeneza muundo wake ambao wanaweza wakaona labda haijaweza kuwa na kiwango kikubwa. Kwa sababu ndiyo kwanza mwaka huu ambao tumeumaliza ndiyo tumepata ridhaa ya Bunge baada ya kupitishiwa mapendekezo na tukaenda kwenye kutengeneza muundo na muundo ambao umefanyiwa kazi ni kwamba taarifa zote zile sasa hazitakuwa zinapelekwa kwa yule anayekaguliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyokuwa mwanzo ilikuwa ukimkagua yule unayemkagua ndiyo unampatia ile taarifa ya ukaguzi, lakini kwa sasa watatoa ushauri kwa wale wanaofanya nao kazi. Kama ni halmashauri watatoa ushauri kwa Mkurugenzi, kama ni ofisi yeyote ile watoa ushauri kwa mkurugenzi. Lakini taarifa itaenda kwenye ofisi ya juu ya yule aliyekaguliwa, za halmashauri zinaenda mkoani na siyo kwa Mkaguzi Mkuu wa upande wa mkoa lakini ni kwa mkoani kwa maana kama Mbunge alivyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa zile ambazo zinakwenda juu kwa maana ya ngazi ya Taifa, tulizipeleka ziende kwa Mkaguzi Mkuu wa Taifa ili baadaye yeye ndiye anayehusika kwenda kuwasilisha kwa Kamati ya Baraza la Mawaziri la kazi, ambalo linaongozwa na Waziri Mkuu ambaye ndiyo coordinator wa Shughuli za Serikali. Hapo ndipo ambapo tuliona yule Mkaguzi Mkuu wa Ndani anatakiwa aende kuziwasilisha. Hii tumeiweka pale kwa sababu tuna taarifa za halmashauri, tuna taarifa za local government, tuna taarifa za Serikali Kuu na tuna taarifa za Mashirika ya Umma, kama ambavyo zinaweza kuwasilishwa kwa upande wa CAG.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imeongelea upande wa nyongeza ya fedha kwa upande wa CAG. Tukishamaliza bajeti hii tutakuwa na mashauriano ya Serikali na Kamati, kwa hiyo yale yote yanayohusisha nyongeza tumeyapokea na tutaenda kuyaandalia majibu kupitia mashauriano ambayo yatafanyika kati ya Kamati na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea ushauri kuhusu masuala ya fedha haramu, tumepokea ushauri kuhusu kufanya marejeo masuala ya pensheni, yote yale tumeyapokea na Naibu Waziri amejibu. Tumepokea maoni ya Mheshimiwa King yanayohusisha masuala ya mgao pamoja na mahusiano. Yote hayo yanafanyiwa kazi na yako hatua nzuri yatakapokuwa yamekamilika tutatoa kauli na yataenda moja kwa moja kwenye utekelezaji ambao utakuwa umeshafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya kimfumo, kazi kubwa inaendelea kwa upande wa mifumo ya TRA na kwa upande huu ambao Waheshimiwa Wabunge wameongea ETS na yenyewe yanafanyiwa kazi. Tunajua mifumo na yenyewe hawafanywi mara moja, kujenga mfumo si jambo la mara moja. Unatakiwa kutathimini aina ya mifumo, kusimika mifumo, kuweka mifumo iweze kusomana na hilo ndiyo jambo kubwa ambalo linafanyika hata lile alilosema Mheshimiwa Kishimba la dola tutalitolea kauli tunaposoma Hotuba kubwa, kwa sababu kazi yake kubwa imeendelea kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, alilolisema Mheshimiwa Katimba la suala la manunuzi, Sheria ya Manunuzi tunaileta upya, imeshasomwa kwa mara ya kwanza. Itakuja hapa na itajadiliwa kwa mapana yake na tunaamini kwamba itakuwa na ushauri wote ule ambao Mheshimiwa Mbunge amesema.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameongelea Mheshimiwa Nusrat, masuala ya kodi na yenyewe nimeishasema tutayaongelea kwa mapana tutakapoleta kodi na lile alilosema kuhusu kutoa elimu. Tunatarajia tufanye semina kwanza kwa Waheshimiwa Wabunge, tuwaelezee haya masuala ya kodi na jinsi ambavyo yanawiana na maendeleo yetu na jinsi ambavyo inawiana, kwamba watu wengi sana wakilipa kodi itatuwezesha kupunguza ukubwa wa kodi. Kwa kadri wanavyolipa kodi watu wachache ndivyo tunavyofanya mzigo ule uwe mkubwa zaidi, kwa sababu unabebwa na wachache.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa tumeshafanya semina Waheshimiwa Wabunge wakaelewa, tutaomba ninyi wenyewe ndiyo mkawe mabalozi kila mtu kwenye Jimbo lake kama tulivyofanya kwenye Sensa na tukaona mafanikio makubwa, yakajitokeza katika Sensa ile tuliyoifanya mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea yale ya Mheshimiwa Hasunga. Tumepokea yale ya real time ya Mheshimiwa Songe, Mbunge makini, tumepokea yale ya Mheshimiwa Swai, ya Mheshimiwa Kwagilwa nimeshajibu, ya Mheshimiwa Sillo Mwenyekiti wangu kabambe kabisa nimeshajibu, ya Mheshimiwa Hassan king nimeshajibu. Tumepokea yale ya Hotel Levy Mheshimiwa Kilumbe na tulikuwa kwenye zana na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI. Kwa sababu tutakuwa na mashauriano na tutaangalia upya haya masuala ya kikodi, niombe Wabunge waridhie kwamba yote hayo tutayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea hoja za Wabunge wote waliochangia kwa kuongea na wale waliochangia kwa maandishi na yote yale tutayafanyia kazi, kwa sababu bado tutakuwa na muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kuhitimisha hoja ambayo niliiweka mezani mnamo tarehe 15 Juni, 2023 ambapo niliwasilisha katika Bunge lako Tukufu Hali ya Uchumi kwa mwaka 2022, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2023/2024 na Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe mwenyewe pamoja na Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge, kwa kuendesha mjadala huu kwa umakini mkubwa.

Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu hoja mbalimbali za Wabunge, napenda kutumia fursa hii kupaza sauti tena kwamba Mama apewe maua yake kwa sababu ya kazi nzuri anazowafanyia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale ambao hawajazoea kufuatilia mambo yanavyofanyika wanaona Waheshimiwa Wabunge wanaposimama kusifia kazi nzuri, wanafanya tu hivyo kama ni utamaduni. Hata hivyo, naomba dakika chache tu niseme baadhi ya mambo kwa ufupi.

Mheshimiwa Spika, fedha zinazokwenda kwenye shughuli za maendeleo kwenye Wizara zetu, mikoa yetu, wilaya zetu, majimbo yetu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, ni kiwango kikubwa cha fedha ambacho hakijawahi kutokea tangu uhuru.

Mheshimiwa Spika, fedha zilizokwenda TARURA kutengeneza barabara za mijini na vijijini ili wakulima waweze kupitisha mazao yao, watoto wanaokwenda shule wasisombwe na maji mvua zinaponyesha, akinamama wajawazito wasifariki njiani kwa sababu ya kukosa barabara za kuwafikisha kwenye vituo vya afya ni fedha nyingi kuliko zilizowahi kutokea tangu TARURA ianzishwe. Hivyo ndivyo Mama anavyowajali Watanzania na anavyowajali wananchi wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha zilizokwenda kutengeneza barabara zinazosimamiwa na TANROADS na hivi juzi tumesaini mikataba ya barabara zile saba pamoja na ya nane ikiwa imekaribia kukamilika, ni barabara zenye urefu mkubwa kuliko barabara zilizowahi kusainiwa Afrika kwa mara moja tangu Nchi zote za Afrika zipate uhuru. Hivyo ndivyo Mama anavyowatumikia Watanzania. Mama apewe maua yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha zinazokwenda kwenye Elimu bila Malipo, Mikopo ya Elimu ya Juu, Miundombinu kuanzia Shule ya Msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu, ni fedha nyingi ambazo zimewahi kwenda kwa mara moja katika mwaka wa fedha tangu nchi hii ipate uhuru. Hivyo ndivyo Mama anavyowajali watoto wa Watanzania maskini.

Mheshimiwa Spika, fedha zinazokwenda kwenye afya, kwenye kazi za Sekta ya Afya, Miundombinu ya Sekta ya Afya, vitendea kazi kwenye Sekta ya Afya ni fedha nyingi Kwenda katika mwaka wa fedha kuliko kipindi chochote kile.

Mheshimiwa Spika, fedha zinazokwenda kwenye kilimo. Fedha zinazokwenda kwenye miundombinu ya umwagiliaji, mbegu bora, maghala ya uhifadhi wa chakula, fedha zinazokwenda kwenye kuendeleza vijana katika ku–modernize kilimo, ni fedha nyingi zilizowahi kutolewa katika Sekta ya Kilimo kwenye mwaka wa fedha kuliko kipindi chochote tangu tupate uhuru. Hivyo hivyo, katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi na hivyo hivyo katika sekta nyingine.

Mheshimiwa Spika, hata fedha ambazo zimekwenda kwenye Sekta ya Maji. Usambazaji wa maji, magari ya kuchimba visima, mitambo ya kuchimba mabwawa, fedha zilizokwenda kwenye kujenga miundombinu ni fedha nyingi zilizowahi kwenda katika mwaka wa fedha kwa mara moja kuliko kipindi chochote tangu tupate uhuru. Hivyo ndivyo Mama anavyowajali Watanzania. Mama yuko kazini, Mama apewe maua yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha zinazokwenda kwenye utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati. Reli, Bwawa la Mwalimu Nyerere, fedha zinazokwenda kwenye kutekeleza miradi mingine kama mafao ya wastaafu, mtakumbuka mwaka 2022 tuliweka hati fungani zaidi ya trilioni mbili. Maslahi ya watumishi wa umma, kukuza sekta binafsi, kuvutia uwekezaji pamoja na uboreshaji wa vyombo vya ulinzi na usalama, ni fedha nyingi kuliko kipindi chochote katika mwaka wa fedha wowote utakaoutaja.

Mheshimiwa Spika, nimetaja tu sekta chache, lakini kuna sekta nyingine huu ndio utaratibu na hivyo ndivyo fedha zilivyokwenda. Pia, hapa ndipo Watanzania wajiulize, kuna Watanzania wengi sana ambao wamekuwa wakiwaaminisha watu wengine kana kwamba kumekuwa na wizi mwingi wa fedha za umma.

Mheshimiwa Spika, hivi fedha kama zimwekwenda nyingi hivyo kwenye miradi ya maendeleo na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kila jimbo limepata fedha nyingi kuliko kipindi chochote kile. Hivi kama wizi umeongezeka, katika kipindi ambacho wizi haukuwepo hizo fedha zilikuwa zinakwenda wapi? Kama sasa zimekwenda nyingi kuliko kipindi chochote, katika kipindi ambacho wizi haukuwepo hizo fedha zilikuwa zinakwenda wapi?

Mheshimiwa Spika, Watanzania watofautishe na tusichanganye uwazi katika matumizi ya Serikali kuongezeka, ni tofauti na wizi kuongezeka. Nirudie tena kusema kwamba, haya niliyoyasema ni kwenye baadhi ya sekta tu, lakini maendeleo yametokea katika sekta nyingi na Watanzania wote ni mashahidi. Hata Yanga kufika fainali na kuchukua vikombe vyote ni hatua ya maendeleo ambayo haijawahi kufikiwa. Hata lile la mataifa walilichukua kwa sababu chanya moja na chanya moja ziko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru tena wewe pamoja na Naibu Spika wako kwa jinsi ambavyo mmendesha vikao vizuri. Vile vile, niwashukuru Wenyeviti na nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mheshimiwa Daniel Baran pamoja na Mheshimiwa Omari Kigua ambaye ni Makamu Mwenyekiti pamoja na Kamati nzima ya Bajeti. Pia, napenda kuwashukuru Mawaziri wote ambao walitoa ufafanuzi wa hoja za kisekta siku ya Ijumaa.

Mheshimiwa Spika, pia, napenda kumshukuru Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande, Naibu Waziri wa viwango kabisa na ananisaidia vema katika kutekeleza majukumu haya. Vile vile, nawashukuru watendaji wote wa Wizara ya Fedha wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Natu Mwamba, Daktari Bingwa kabisa wa masuala ya uchumi pamoja na timu yote ya wataalam ambao wanasaidia katika shughuli hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imeanzisha Mafungu mapya matatu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mipango, uwekezaji na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Mafungu hayo ni :-

(i) Ofisi ya Rais Uwekezaji;

(ii) Tume ya Mipango; pamoja na

(iii) Kituo cha Ubia kati ya Serikali na sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, hivyo, napenda kutoa taarifa kwamba bajeti za mafungu haya zimetengwa kupitia kasma ya Matumizi ya Kitaifa (National Expense) iliyopo Fungu 21 Hazina. Kwa muktadha huo Sheria ya Matumizi ya mwaka 2023 (Appropriation Bill, 2023) itajumuisha bajeti za mafungu haya baada ya Serikali kukamilisha taratibu zote.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye ufafanuzi wa mafungu nitaomba uridhie niende kwa hoja kwa sababu ya wingi wa hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Waheshimiwa Wabunge wengi wameongea kuhusu masuala ya maendeleo kwenye Majimbo yao yanayohusisha sekta zao, wameongelea kwenye maji, wameongelea kwenye elimu, wameongelea kwenye afya, wameongelea kwenye miundombinu.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge hoja zenu zote hizo tumezipokea na mara tutakapoenda kuna zile ambazo mmeziwasilisha kwa maana ya udharura na ulazima katika maeneo hayo. Wizara ya Fedha tutakaa na Wizara za Kisekta ili tuweze kuona utekelezaji wake tunaweza tukaufanya namna gani. Liliongelewa kwa sauti kubwa suala la Uwanja wa Ndege wa Mwanza Ndugu yetu Musukuma alilisema na bahati nzuri Uwanja wa Ndege wa Mwanza hiyo center wote tunaijua.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge tumelipokea tutakaa na Wizara ya Kisekta taratibu za kutafuta fedha ni taratibu endelevu tutaendelea na tutaweka uzito unaostahili katika jambo hilo na Mheshimiwa Mbunge uliongelea kushika shilingi hata usishike shilingi, Uwanja wa Ndege wa Mwanza hata mimi naupenda na ni nyumbani kwetu, kwa hiyo tutakaa na Wizara za Kisekta tuweze kuangalia ili tuweze kuona namna ya kulitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili Mheshimiwa Rais alishalielekeza siku nyingi, nakumbuka alipokuwa ziara kule katika Nchi za Umoja wa Ulaya ni moja ya maeneo ambayo alikuwa anayasisitiza kila wakati sisi Wizara ya Fedha tuweze kukaa na wenzetu tuweze kuyafanyia kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, yaliongelewa masuala barabara Ndugu yangu Mheshimiwa Taletale, Mheshimiwa Mwenyekti Kihenzile, Mheshimiwa Bilakwate, Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri mwenzangu Jafo, Ndugu yangu Mheshimiwa Asenga, Ndugu yangu Mheshimiwa Kamamba tumepokea barabara zote ambazo waheshimiwa Wabunge mmeziwasilisha. Waheshimiwa Wabunge barabara zingine mlisema zimetengewa fedha kidogo, tunapoweka fedha kidogo hatuna maana kwamba katika mwaka huo tutatekeleza mradi wa barabara kwa kutumia fedha hizo, fedha zingine ni kwa ajili ya upembuzi lakini maeneo ambako upembuzi ulishafanyika kama kule Nyororo tumeweka fedha kwa sababu zoezi la kutafuta fedha ni endelevu, tunaendelea kukamilisha masuala ya fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuliweka fedha kwa ajili ya kushikilia kifungu ili wakati wa kutekeleza kuwe na kifungu ambacho kilipitishwa kwenye bajeti. Kwa maana, hiyo barabara zote ambazo zitatekelezwa kwa P4R ni kwamba fedha zitakapatikana zitaendelea kutoka kadri utekelezaji unavyoendelea. Kwa hiyo, hatuna maana kwamba tutatekeleza kwa kiasi kidogo kile ambacho kimewekwa, kile kinashikilia kifungu ili tutakapokwenda kutekeleza tuweze kutekeleza kwa kutumia kifungu ambacho kilipitishwa na kwa utaratibu wa P4R ambapo fedha inaendelea kutoka kufuatana na utekelezaji wa mradi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge miradi yote ile mliyoitaja ya barabara, miradi ya maji, miradi ya afya tumeipokea tutakaa na Wizara za Kisekta kama ambavyo Mawaziri wa Kisekta walizisema siku ile wakati wanahitimisha.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee niwapongeze Wabunge wote ambao walihimiza wananchi pamoja na viongozi kwenye suala la kulipa kodi. Suala hili la kulipa kodi ndilo linalotutambulisha kuhusu kujitegemea, ndilo linalojitambulisha kuhusu uhuru wetu, ndilo linalotutambulisha sisi kuhusu uwezo wetu wa kutekeleza miradi ya maendeleo. Mheshimiwa Bilakwate ulisema kabisa ulikpokuwa unaomba ilikuja hiyo kama ndoto na ilikuja ikakuelekeza hivyo nilimsikia Mheshimiwa Kwagilwa, Mheshimiwa Matiko, Mheshimiwa Mnzava, Mheshimiwa Subira, Mheshimiwa Riziki Mama yangu na Wabunge wote ambao mmeongelea kuhusu hamasa hii.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge, twendeni tukawaelimishe wananchi wetu, tukawahamasishe kwamba jambo la kulipa kodi ni jambo letu sisi sote, ni jambo la Watanzania, ndiyo maendeleo yetu na jambo hilo kama wananchi wote wataitikia mwito huo nchi yetu itashusha viwango vya kodi.

Mheshimiwa Spika, leo hii viwango vya kodi ni vikubwa kwa sababu wanaolipa kodi ni wachache, maana yake mzigo wa maendeleo, mzigo wa huduma za jamii unabebwa na wachache. Kwa maana hiyo twendeni tukawahamasishe na kama kila mmoja atalipa kodi, kila mmoja atatumia mashine za kilektroniki, kila mmoja atadai risiti, kila mmoja atatoa risiti, anapouza maana yake tunaianza safari ya kupunguza viwango vya kodi. Leo hii kila mfanyabiashara anaona viwango vya kodi ni vikubwa lakini hii vicious cycle inatakiwa kukatwa kwa kuanzia kila mmoja alipe kodi ndipo tutakapoweza kupunguza viwango hivyo vya kodi.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye hoja nyingine ambayo iliongelewa kwa kiwango kikubwa na Waheshimiwa Wabunge ilikuwa ni hoja ya ngano. Na nilimsikia Mheshimiwa Mbunge wa Makete akiongea kwa sauti kubwa sana pamoja na Wabunge wengine wote ambao waliongelea suala la ngano. Waliona kama vile Wizara ya Fedha imeshusha kiwango cha kutoka asilimia 35 kwenda asilimia kumi.

Mheshimiwa Spika, nikuambe kwamba jambo hili tumekaa na Wizara ya Kisekta tuko na sauti moja kwenye jambo hili, kinachotokea hiyo ni terminology ambayo inatumika kwenye masuala hayo ya kikodi. Kama ambavyo huwa tunafanya kwenye sukari, ile sukari ya gap sugar inapoagizwa, pale ambapo huwa tuna upungufu ama wazalishaji au waagizaji huwa wanapewa nafuu kwa hiyo hata hii duty remission ni lugha ya kitaalamu inayomaanisha kwamba wale wote ambao watanunua ngano ya ndani. Ngano ya ndani ikishaisha anapewa ruhusa ya kuagiza Ngano ya nje kwa bei iliyo nafuu.

Mheshimiwa Spika, hicho ndicho kilichofanyika hakijapunguzwa ili aagize nje aache ngano ya ndani, ila anapewa nafuu pale atakapokuwa amenunua. Kwa hiyo, anapewa motisha ya kununua ngano ya ndani, kwa maana hiyo atakapokuwa amenunua ngano ya ndani ikaisha anapewa ruhusa ya kuagiza Ngano ya nje kwa kiwango ambacho kiko chini ya kile cha kawaida, mtu mwingine yeyote yule ambaye hanunui ngano ya ndani hanufaiki na hiyo duty remission. Kwa maana hiyo, hii ni motisha ambayo sisi Wizara ya Fedha pamoja na wenzetu wa Wizara ya Kilimo tuko na sauti moja na uagizaji wake utaratibiwa na Wizara ya Kisekta ya Kilimo kwamba yule ambaye amemaliza kununua ngano ndiye ambaye atapewa hiyo duty remission kama motisha ya wale ambao wananunua ngano ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge kwa hiyo niwaombe mkubali hilo pendekezo liko sawa na huo ndiyo utaratibu ambao ni standard na ile ni lugha ya kitaalam ambayo imetumika. Hatujapunguza ili tuue wakulima wa ndani, tumepunguza kumpa motisha yule atakayenunua ngano yote ya ndani, ile iilikuwa ilitolewa kwa sababu kuna wakati watu walikuwa wanapendelea kununua ngano za nje ngano za nje, kwa hiyo, ikaleta unafuu kama motisha kwa yule ambaye atanunua ngano ya ndani, hiyo ndiyo maana ya duty remission

Mheshimiwa Spika, kuna Wabunge wengine waliongea kwa sauti kubwa kuhusu upande wa mafuta ya kula. Tumeliangalia jambo hili na kwa jinsi ambavyo tumeliangalia tumeenda kutoa unafuu kwa wale wazalishaji wa ndani ili mafuta ya ndani yasije yakazidiwa na yale mafuta ya nje, kwa hiyo tutaleta kwenye schedule of amendment nafuu ambayo tumeitoa kwa wazalishaji wa ndani kama motisha ya kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekubaliana ndani ya Serikali kwamba jambo hili tutaendelea kulifuatilia kwa ukaribu, lakini kingine ambacho ndani ya Serikali tunakubaliana tukasema tuanze nalo hilo kwa uzito mkubwa ni kudhibiti uingiaji wa mafuta kwa njia ambazo siyo rasmi, ambao ndiyo ambao unaleta hiyo flooding ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeiongea kwa sauti kubwa. Tumepokea nakumbuka ndugu yangu Mheshimiwa William aliongea na Mheshimiwa Kunti na wengine wote akina Mheshimiwa Musa na wengine wote wanaotokea katika maeneo ya wakulima wa alizeti, tumeyapokea na tutakaa na wazalishaji tutakaa na vyombo kuhakikisha kwamba uingiaji wa mafuta kiholela unadhibitiwa ili kuondoa hiyo flooding ambayo ndiyo inaleta tatizo kubwa la bei ya mafuta ya kula. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge mkubali mapendekezo hayo na Mheshimiwa Rais anawajali wakulima ndiyo maana anaweka uwekezaji mkubwa katika sekta hizo za kiliomo.

Mheshimiwa Spika, kuna Waheshimiwa Wabunge wengine waliongelea kuhusu kuboresha kuboresha mazingira ya kufanyia biashara, tumeyapokea ninayo orodha ndefu ya wale Wabunge ambao walisema mazingira yawe rafiki, tunaendelea na hayo ndio maana hata katika mapendekezo yetu kuna maeneo ambayo tumeyaboresha zaidi na tunaenda full swing kwenye utekelezaji wa blue print. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Wabunge ambao waliongelea kuhusu Wakandarasi kulipwa, kuna walioongelea kuhusu makundi maalum, Sheria ile ya Manunuzi kutekelezwa, kuna wale walioongelea kuhusu kuwianisha mapato na matumizi. Tumeyapokea hayo na nadhani katika Bunge lijalo kama itakupendeza tunaleta Sheria ile ya Manunuzi ambayo itaangalia hivi vitu vyote, pia Serikali ya Mheshimiwa Samia iliona hilo tatizo ambalo linajitokeza kwenye upande wa riba zinazojitokeza kufatana na wakandarasi kutokulipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, chimbuko la tatizo hilo ni pale ambapo miradi mingi inaingiwa mikataba kwa mara moja kwenda kwenye utekelezaji ambayo haioani, haiwiani na fedha ambazo zinapatikana za kulipa hiyo. Kwa hiyo, kama madai ni makubwa kuliko fedha zilizopo ni dhahiri kwamba watalipwa wachache na wengine ambao hawajalipwa watenda kwenye kudai riba. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais ameona afufue Tume ya Mipango na ijitegemee ili utekelezaji wa miradi uwiane na mipango iliyopo, kama utekelezaji wa miradi utawiana na mipango iliyopo ni dhahiri kwamba miradi inayotekelezwa itakuwa inawiana na uwezo wa Serikali wa kuilipia miradi ile na kama uwezo wa kuilipia miradi ile utaweza kuendana na miradi inayotekelezwa ni dhahiri patakuwa hapana riba.

Mheshimiwa Spika, kinachojitokeza ni kama miradi inayotekelezwa kama certificate zilizoiva ni nyingi kuliko fedha zilizopo, ni dhahiri huwezi ukazilipia zote na wale ambao hawajalipwa ni dhahiri watadai riba. Kwa hiyo, hicho ni kitu ambacho Serikali imeenda kwenye utekelezaji wake lakini ndiyo maana pia Mheshimiwa Samia akaona aweke utekelezaji wa miradi ya barabara kwa EPC+F ambapo baada ya kukamilika kwa maridhiano ya Serikali na Benki inayotoa fedha hizo, fedha zitaanza kutolewa moja kwa moja kwenda kwenye mradi kwa hiyo hapatakuwepo na utaratibu wa fedha ambazo zilipangwa ziende kwenye mradi, kuweza kutumika labda katika maeneo mengine ambayo yanapunguza uwezo wa Serikali labda kulipa katika miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo ambalo tumekaa ndani ya Serikali tunaliangalia kwa ukaribu ni vile tuna madeni ya ambayo yalishazalishwa siku nyingi hatuwezi tukayaacha wala hatuwezi kuyakana tunaendelea kulipa mafungu kwa mafungu na tutaendelea kutoa taarifa hiyo kwenye Kamati ya Kisekta, Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Spika, kuna mambo mengine aliyasema Mheshimiwa Mpina akiwa anapinga hatua ambazo Serikali inazichukua. Napenda kumshauri rafiki yangu jirani yangu maana Iramba na Meatu zinapakana. Si ubingwa na wala si ustaarabu kusema na kupinga kila kitu hata ambacho hakistahili kupingwa.

Mheshimiwa Spika, namuelewa sana Rais Samia anapoleta hatua hizi za kikodi namuelewa sana, mwenzangu asipokuwa anaelewa haya si mbaya pia ukimuona Mbunge mwenzako Kibunge tu ukamuuliza hili linamaana gani? kuliko aibu ya kusema jambo, unapinga jambo ambalo lina maana kubwa sana kwa mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Spika, Rais Samia anapendekeza kwamba tuache utaratibu wa kufunga biashara ama shughuli ya uzalishaji, kwa sababu shughuli ya uzalishaji mle ndani kwenye shughuli za uzalishaji kuna watu ambao hata siyo wamiliki lakini maisha yao yanategemea hiyo shughuli ya uzalishaji. Tuache kufunga biashara kwa sababu huyo ni mtu anayeendesha biashara ni mtu ambaye ameamua kuisaidia Serikali, badala ya kukaa kutafuta ajira yeye ameamua kujiajiri na ameamua kuwatafutia ajira na Watanzania wengine.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais anasema badala ya kufunga biashara, kama kuna makosa yapo tukae na yule anayetakiwa kutatua yale makosa na penalty imewekwa kwa mtu ambaye hatasikia taratibu za kisheria zichukue mkondo wake, lakini Mheshimiwa Mpina anaona jambo hilo halina maana anasema tuendelee kufunga biashara kwa sababu yeye kwa hulka yake anafurahia watu wakiumia.

Mheshimiwa Spika, tunakumbuka jinsi alivyokuwa anafanya sherehe kwa kuchoma nyavu bila kudhibiti nyavu zile kuingia, tunatambua jinsi alivyokuwa anafurahia kwenda kufunga viwanda anafika tu anakuta mchirizi hivi anasema hiki nimeshafunga mpaka mwezi ujao. Kwa nchi ambayo ina tatizo kubwa la ajira ambalo tunataka sekta binafsi ikue ili tupate kodi huo siyo utaratibu ambao mtu yeyote mwenye hekima anatakiwa kuupigia debe. Angalieni nchi ambazo zimeendelea zilizokuza sekta binafsi zinaishi vipi, ni watu ambao wana adabu kwenye sekta binafsi, watu wanaheshima kwenye sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, Rais Samia anachotufundisha, anatufundisha kwamba sekta ya umma na sekta binafsi siyo maadui, hawa ni wabia wa kuendesha nchi. Hawa ni wabia siyo maadui, lazima tufanye mtu kufanya shughuli ya kujiajiri aione ni shughuli yenye heshima. Sasa hivi nchi nzima watu wanataka tu watoto wao waende kufanya kazi Serikali, kila mtu anataka watoto wake waende Serikalini na wengine wanakuwa specific zaidi wanataka tu watoto wao waende TRA kwa sababu gani? ukiwa Serikalini ndiyo shughuli pekee ambayo ina heshima, watu wote wanaheshimu hiyo peke yake, lakini Mheshimiwa Rais Samia anachotaka kutufundisha anataka kutufundisha shughuli yoyote ya uzalishaji iheshimiwe na yule anayefanya hiyo shughuli aheshimiwe, hata pale ambapo panapoonekana pana matatizo pawe na utaratibu wa kiungwana wa kurekebisha.

Mheshimiwa Spika, sasa unafunga shughuli ya uzalishaji kuonesha tu ubosi unafika tu unafunga na kuondoka, umevaaa zako tai, hautambui hata kwamba hiyo tai uliyovaa pamoja na suti hiyo na mshahara unaopokea unaupokea kwa sababu ya huyo huyo uliyemfungia biashara yake. Mheshimiwa Mpina kwa uelewa wake hilo halioni kabisa, hajui kabisa kama Serikali hata Bunge tulipokaa hapa mchango wa sekta binafsi upo. Mchango wa sekta binafsi ili Bunge likae upo, hayajui haya.

Mheshimiwa Spika, mimi naunga mkono kama Waziri niliyepewa dhamana ya kusimamia uchumi, maoni haya ambayo Mheshimiwa Rais anataka kuyaweka ni maoni ya msingi yataikuza sekta binafsi yatakuza tax base na yataongeza ajira pamoja na hamu ya watu kujiajiri, lazima mtu ambaye hatma ya wenzake aheshimiwe na apewe jina lililojema ili aweze kuvutia na wengine waweze kujiandaa nalo kwenda na hilo wazo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili tunasema tuache kukamata mizigo, tuache kushikilia mizigo na vitendeakazi vya watu. Mheshimiwa Mpina anasema na hilo ni baya tukamate tu anasema taasisi hizo zinafanya vizuri sana. Hebu niambieni Waheshimiwa Wabunge ninyi ni wawakilishi wa wananchi hebu fikiria mzigo ambao siyo mali haramu, eti tumetofautiana kodi siyo sumu, eti tumetofautiana kodi badala yake tunakaa nayo mwezi wa kwanza, wa pili, wa tatu, wa nne, wa tano, wa sita, mwaka wa kwanza, mwaka, wa pili, hebu niambieni. Je hivi tungepokea kodi ile ambayo hatubishani nayo halafu tuandikishiane ile ambayo tunatofautiana, halafu huyu mtu bidhaa yake apewe aendelee na biashara, niambieni kwa miaka mitatu ambayo tumeshikilia mzigo tungeshapokea kodi ngapi? Mheshimiwa Mpina anasema wakamatiwe tu huo utaratibu Serikali mnaotaka kuufanya ni mbaya. Ni lazima tuheshimu mitaji ya watu!

Mheshimiwa Spika, niambieni ni wafanyakazi wangapi unaweza ukashikilia mishahara yao kwa miaka miwili halafu wasilalamike ukae tu? Kwa sababu yule mwenye mtaji wake ile biashara ndiyo mshahara wake. Ili tuweze kukuza sekta binafsi kama wapo ambao hawajaelewa maoni, mawazo ya Mheshimiwa Rais kama Mheshimiwa Mpina tunawakosea sana watoto wa Kitanzania ambao hatma yao inategemea sekta binafsi kukua.

Mheshimiwa Spika, ni lazima nchi hii na viongozi wote wa Serikalini walitambue hilo, lazima tuheshimu mitaji ya watu, huwezi ukakaa na mtaji wa mtu umeushikilia tu, wewe fikiria mtu amekopa amekopa akaenda kufuata bidhaa hiyo, bidhaa imefika wewe unaishikilia yeye amekopa ameweka rehani nyumba, nyumba inaenda kuuzwa wewe umeshikilia bidhaa yake. Umeshikilia tu kwa sababu unayomamlaka na uko ofisini na unalipwa mshahara halafu Rais anasema tuondoe huo utaratibu tutafute njia mbadala ya kushughulikia matatizo ambayo hayajakubalika, Mbunge anayelipwa kwa kodi ya sekta sinafsi anasema hili jambo siyo zuri, ninyi endeleeni kukamata tu. Sasa Mheshimiwa Mpina kwa sababu ni jirani yangu usikute yale mambo kaambiwa kule wanakoamini sana mambo yale kwambe wewe pinga kila kitu tu. Si kila kitu kinafaa kupingwa mambo mengine ni lazima tutumie logic ilipo.

Mheshimiwa Spika, tumeondoa pia utaratibu na tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge, Wabunge walikuwa wanasema kule kwenye Halmashauri kwa nini kila taasisi ya Serikali inakwenda yenyewe kudai? Tumeandaa blueprint imeeleza kwamba tukitaka kukuza sekta binafsi tuondoe ule utaratibu wa kuwafanya watu wa sekta binafsi siku nzima kusikiliza ama kuhudumia Serikalini tu. Anatoka wa fire anaenda wa OSHA, anatoka wa OSHA anaenda wa TFDA, anatoka wa TFDA anaenda wa TBS, anatoka wa TBS anaenda…, utitiri wa watu wote wanaotoka Serikalini. Tukasema tutengeneze dirisha moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunayo mifano ambayo tumefanikiwa kwenye hilo, tumeweza kufanikiwa kwenye upande wa mafuta, tunakusanya mara moja, tukishakusanya kuna fedha inaenda REA, kuna fedha inaenda reli, kuna fedha inaenda TANROADS, tuna fedha inaenda maji, tuna fedha inaenda TARURA lakini imekusanywa mara moja. Sio kila taasisi inaenda kukusanya maana yake na katika dunia hii ya kidijitali inawezekana. Hata zile kaguzi zilizo rasmi si vyema kila mtu anaenda kwa wakati wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wengine hawajaona sana tatizo tulilonalo kwenye nchi hii. Mimi namwelewa sana Rais Samia, watu wengine wanataka tuishi kama ile enzi niliielezea sana kwenye hotuba siku ile. Mheshimiwa Rais alitupa dira tatizo anavyoliona na jinsi anavyoona tunaweza kulitatua.

Mheshimiwa Spika, pale zamani Watanzania walikuwa wachache tuko milioni tisa, vyuo vikuu una wataalam 12; una wataalam wawili, una wanafunzi 42. Hao wanafunzi huna kuumiza kichwa kuhusu ajira zao, lakini mazingira ya sasa eneo pekee ambalo linaweza likaajiri Watanzania wengi ni sekta binafsi. Sasa tuna kazi, tuna kazi ya kuifanya sekta binafsi ikue, tuna kazi ya kuwafanya watu waone ni heshima kufanya kazi kwenye sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ilivyo sasa kuna watu ambao hata wako sekta binafsi hawaoni kama wako kazini, kwa sababu ya jinsi ambavyo tunai–treat sekta binafsi na kwa jinsi ambavyo tunaweka majina kwa watu wa sekta binafsi, lakini kama wote tutaipa heshima sekta binafsi, kama wote tutakuwa na lengo la kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika kukuza sekta binafsi, naamini watu watakuwa wanaona ni heshima kwenda kufanya sekta binafsi na tutakuza tax base.

Mheshimiwa Spika, tusipokuza sekta binafsi kodi zote zitabebwa na wanyonge, kwa sababu hauwezi ukaleta kodi mpya bila shughuli mpya ya uzalishaji, maana yake kama hatutakuza sekta binafsi tax base yetu itaendelea kubakia wafanyakazi wataendelea kubakia wachache ambao wanalipa kodi. Niliona niseme na hiyo ili tuweze kuelewana.

Mheshimiwa Spika, kuna Wabunge ambao waliongelea kuhusu taasisi zetu za Maliasili, Wizara ya Kisekta ilishafafanua na kama walivyosema Wizara ya Kisekta tumekaa nao na kwa kweli kuna mapendekezo ambayo tumeyaweka ambayo yataenda kutusaidia tuweze kupiga hatua kubwa kuliko pale ambapo tulikuwa.

Mheshimiwa Kakoso hewa ya ukaa pamoja na wenzake tumelipokea, tutakaa na Ofisi ya Makamu wa Rais kuweza kukimbizana na hili ili liweze kuwahi kufika hatima njema.

Mheshimiwa Spika, jambo la ETS limeongelewa sana na lenyewe tulikubaliana kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi na kikao ambacho Serikali ilikuwa inafanya mashauriano na Bunge, tumekubaliana tunapokuja Bunge lile lingine tunatarajia na Mungu atusaidie tutakuja na utaratibu ambao tunaamini itakuwa hatua nzuri ambayo itatutoa hapa tulipo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwepo na maeneo mawili yaliongelewa kwa nguvu; eneo moja lilikuwa la mafuta, tozo ya shilingi 100 kwenye mafuta; mimi niwaombe Wabunge na Waheshimiwa Watanzania, Serikali inafanya simulation/inafanya ufuatiliaji wa ndani kuhusu Soko la Dunia kwenye masuala ya mafuta (fuel), kwenye suala la mafuta ya kutumia nishati ile ya mafuta. Tena Watanzania hata msiwe na hofu na hii shilingi 100; kwa sababu gani? Kuna wakati ambapo mafuta yalipanda kwenye Soko la Dunia sio hata kwa ajili ya shilingi 100, Serikali ikaweka ruzuku ili mwananchi asipate shida. Sasa ikitokea mafuta yanashuka kwenye Soko la Dunia, si mbaya Serikali ikikusanya fedha hizo na ikapeleka kwenye miradi ya kimkakati, kwa sababu hata ikipanda kwa sababu nyingine ambayo sio hii ya shilingi 100 Rais Samia amekuwa akiwapa nafuu wananchi. Kwa nini upate shida? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna wakati mafuta yamepanda hata sio kwa ajili ya shilingi 100 na Rais akatoa unafuu. Sasa kama Soko la Dunia mafuta yanashuka ile difference Serikali ikikusanya ikatekeleza kwenye miradi kuna shida gani. Wanasema huenda yakapanda kule mbele, sasa kama mafuta yakipanda na Rais amekuwa anatoa unafuu kwa wananchi wake, hofu yako ni nini? Angalieni kwa nchi zote za SADC na EAC muone jinsi tofauti ya Rais Samia na maeneo mengine ambavyo walifanya. Kwa hapa aliweza kuweka ruzuku shilingi bilioni 100 kila mwezi na hapo sio kwamba Serikali ilikuwa imepandisha, yalipanda kwenye Soko la Dunia kule. Maana yake kama sio mtu anayejali wananchi wake angekuwa na sababu ya kutosha kabisa kusema yamepanda kwenye Soko la Dunia, kwa hiyo tupambane na hizo hali, lakini yeyye akasema wananchi wasipambane na hali zao, akawapambania kwa kuweka shilingi bilioni 100 kila mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo niwasihii wananchi wenzangu wa Tanzania kwamba hii ni jambo jema kwa maana linataka kutunisha mifuko ya Serikali katika kutekeleza miradi ya kimkakati. Niwakumbushe Watanzania na Waheshimiwa Wabunge miradi ambayo Tanzania inatekeleza, miradi ya maendeleo ambayo Tanzania inatekeleza, hakuna nchi nyingine yoyote, majirani zetu na ukanda wote huu wa Afrika wanaotekeleza miradi mikubwa kwa mara moja kama Tanzania inavyotekeleza, hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo wala tusitoetoe sana mifano mingine mingine, tunaweza tukawa tunatolea mfano kwa watu ambao hawa mradi hata mmoja mkubwa. Unaweza ukasema mbona hawa wanaishi hivi, unaweza ukawa wale unaowatolea huo mfano hawana hata mradi mmoja wa maendeleo, lakini sisi tuna miradi mikubwa ambayo tunatakiwa tujionee heshima kutekeleza miradi ya aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ukubwa wa miradi hiyo unatuonesha sisi ni nchi ya aina gani na vision ile ya viongozi wetu katika kutekeleza shughuli zinazolenga kuwakwamua wananchi kimaendeleo na Waheshimiwa Wabunge miradi hii mtaiona faida yake ikikamilika. Tunapojenga barabara za lami hatuna maana kwamba barabara hiyo tutaenda kukusanya hela, lakini shughuli zile zinazorahisisha katika kutembeza zile shughuli za kimaendeleo ndizo ambazo zinatuletea tija kubwa.

Kwa hiyo, hata hii miradi yote, bandari, reli madaraja, linalolengwa ni hilo, twendeni tuunge mkono wala tusirudi nyuma ndio patakuwepo na mzigo mzigo hivi lakini tuubebe tunaubeba kwa ajili ya nchi yetu na maendeleo yetu.

Mheshimiwa Spika, niwaombe Watanzania haya ni mambo mema yanatutofautisha na watu wengine. Tunataka tunapomaliza dira ile nyingine inayofuata nchi yetu iwe imeshatoka kwenye zile nchi zinazokuwa kwenye lile kundi la nchi maskini zaidi.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo ilitokea kwenye upande cement; Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote naomba watuelewa Serikali kwenye jambo hili, iko namna hii, nchi yetu ilijengwa kwenye misingi ya ujamaa na kujitegemea, watu wengi hizi concept mbili huwa hawazielewi sawa sawa. Ujamaa ni undugu kwamba usifurahie tu wewe pekee yako kufanikiwa huku wengine wakiwa wanapata shida. Sisi tuliokulia kwenye maji, Mheshimiwa Doto anafahamu ile mkijifunika nguo mmoja ilikuwa inaitwa Japan ukiigusa tu hivi inafyatuka inawakimbia wote, kipande kimoja cha Japan mnajifunika watu watano. Kwa hiyo, hapo anapata faida ni yule wa katikati wanakuwa wanapambana hawa wa pembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajua usifurahie wewe kufanikiwa pekee yako, lazima umbebe na mwingine wa chini ni jukumu lako, hivyo ndivyo ilivyo. (Makofi)

Sasa niambieni Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukilia dakika zote hapa kuna watoto wanapangwa elimu ya kati pale, wanapangwa waende vyuo vya kati pale, niambieni ninyi wenyewe anapangwa mtoto wa maskini aende vyuo vya kati pale. Vyuo vingine vyote tumewapa waweze kupata mikopo wote, lakini kwa idadi tu ya wingi wa watoto wa Kitanzania kwamba hawawezi wote tena wakaenda kidato cha tano na sita, haujafikiwa huo uwezo labda kwa sababu ya ongezeko linaloongezeka. Hivi tunavyoanza hivi kutoka mwezi wa tano mpaka sasa hivi tangia matokeo yametokea tumelazimika kujenga madarasa ya kuweza kukidhi lile ongezeko, ongezeko la watoto waliofaulu wametoka 75,000 mpaka 192,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tuna maeneo mengine kama hivyo vyuo vya kati hivyo MUST, Arusha Technical pamoja na DIT vipo ni vyuo vinavyozalisha wataalam tena wanaotakiwa na uelekeo wa nchi yetu katika kukuza sekta ya ualishaji, lakini watoto wa kimaskini wakienda kule wanakutana na ada. Mheshimiwa Samia akasemaje tutafute kwa yeyote aliye na kaunafuu unafuu atoe shilingi 20 kwa kilo, atoe shilingi 20 tupeleke elimu bure kwenye vyuo vyetu vya kati na tupeleke tuanze kutoa mkopo kwenye vyuo vya kati kwa sababu hata wanaokwenda kwenye vyuo vya kati ni watoto wa Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutatoa wapi fedha ya kusomesha watoto wetu wa Kitanzania wanaokwenda vyuo vya kati. Ni lazima Watanzania tutagusana tu, ni lazima tutagusana, ndio tutagusana tu. Ndio inaweza ikakuongezea ka gharama, lakini ni lazima tumjali mtoto huyo. (Makofi)

Mimi baba yangu alikuwa na uwezo wa kuuza ng’ombe mmoja naenda sekondari, lakini nilipofika Chuo Kikuu kama nisingepata dirisha lile la grant, nisingeweza kufika kule Chuo Kikuu. Familia za aina hiyo bado zipo, mzazi wa mtoto maskini wa kijijini akiambiwa atoe shilingi milioni tatu, shilingi milioni nne, milioni ngapi, tena wengine wanasomea masomo ambayo tunayahitaji sana, sekta za afya, sekta hizi za uzalishaji. Watanzania tutakuwa tumeonesha mfano mbaya sana wa kizazi hiki cha leo tukishindwa kuwalipia watoto hao kwa sababu tu tunataka tujilimbikizie sisi ambao tumeshapata nafasi hiyo, kwamba wewe uwe hata na nyumba tano, uwe na nyumba kadhaa, lakini wale pale uwaache kabisa kwa sababu tu tunaogopa kubeba mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watoto wa Watanzania ni watoto wetu ni lazima tubebe huo mzigo, nawaomba Watanzania wote tukubaliane na maoni hayo hata kama yanatuongezea mzigo, inatuongezea mzigo kwa ajili ya watoto wetu. Hizo ni fedha ambazo zinakwenda kwenye kutengeneza Taifa lililo bora katika sasa na miaka inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe Watanzania urithi tuliopewa wa kuthaminiana ni urithi mkubwa sana katika Taifa letu. Hicho ndicho Rais Samia anachokisisitizia kwamba kama una unafuu, haujenda mbali sana, lakini una unafuu wasaidie na wengine walioko chini waweze kupanda, hicho ndicho anachojaribu kutuelekeza kwa kutumia taritibu hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunatambua tunapoenda kuongeza tozo mahali ama kuongeza kodi mahali, ni kweli tunatambua kiwango kile kinaweza kisibaki kile kile. Tunaomba Watanzania wote tuelewane, ni lazima tutekeleze miradi ya kimaendeleo na ni lazima watoto wetu waweze kupata fursa hiyo.

Mheshimiwa Spika, nchi hii imewahi kupita kipindi ambacho watoto walikuwa wanafaulu vizuri halafu wanaambiwa hawajachaguliwa. Wengi wa rika letu hili watafuteni rafiki zetu, wengi walikuwa na akili na walifaulu, lakini waliambiwa hawajachaguliwa kana kwamba kwenda kidato cha kwanza ama kidato cha tano ni uchaguzi, unaambiwa huyu hajachaguliwa.

Mheshimiwa Spika, watoto wameongezeka sana baada ya elimu bila malipo. Tusiirudishe nchi yetu kwenye upungufu wa miundombinu ama upungufu wa uwezo wa kuweza kuwasaidia watoto wanaokwenda elimu ya juu, ama vyuo vya kati, ama sekondari kwa sababu za kibajeti. Ni lazima tuwabebe watoto wetu wote wapate elimu, tena elimu inayolingana, hiyo ndio future ya Taifa letu, ndio maana Rais Samia akaongeza boom elimu ya juu, boom sio lilelile ameongeza, ameongeza elimu bila ada kidato cha tano na sita, ameongeza elimu bila ada kwenye vyuo vile vya sayansi na ameongeza vyuo vya kati viingie hatua kwa hatua kwenye mikopo. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, hata hilo la hatua kwa hatua wala msilichukulie kwa negative na Watanzania wala msilichukulie kama wazo hasi, ni wazo chanya hata sasa kwenye elimu ya juu, sasa hivi kwenye elimu ya juu tulianza kwanza na watoto waliopangiwa vyuo vya Serikali, ndivyo tulivyoanza. Hatukuanza anza tu siku ya kwanza tukaanza vyuo vyote, tulianza na wachache, lakini tukawatumeanza, ikapiga hatua tukaongeza idadi, ikafika hatua tukaongeza vyuo, ikafika hatua tukaenda vyuo vya sekta binafsi ndio wabia wetu hao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivi sasa tukianza na wachache hii ni bajeti moja ya mwaka huu, mwaka unaofuata ndio na hii hamasa tunayoijenga na hii kukuza sekta binafsi na miradi mingine itakuwa imeisha, miaka miwili ijayo hatutakuwa na commitment za Bwawa la Mwalimu Nyerere. Tutakuwa tumemaliza, uzalishaji utaongezeka, ile saving ambayo tunapeleka trilioni 1.6 kila mwaka haitakwenda tena kwenye bwawa, maana yake tutaongeza uwezo wa kuwapeleka watoto walioko vyuo vya kati vya Serikali na visiovyo vya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais Samia aliona tuwe na mahali pa kuanzia, fikirieni lipi ni jema je, angesema uwezo hauruhusu tukaacha kabisa vile vyuo vyote vya sayansi tukaacha kabisa, vile vya kati tukaacha kabisa, ili tusibiri uwezo utakaporuhusu, la hasha! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yeye akaona twendeni tuanze kidogo kilichopo tuanze hatua kwa hatua kama tulivyoanza zamani. Zamani mikopo ilikuwa inapatikana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Allied Universities, nadhani Muhimbili pamoja na UCLAS baadaye baadaye ikaja na Mzumbe, baadaye baadaye ikaja UCLAS. Ikaenda ikiwa inakuwa mpaka ikaenda na vyuo vya sekta binafsi. Niwaombe mridhie huu ni utaratibu mzuri utaenda kuwagusa watoto wa Watanzania. Tusiridhike tukiwa tumekosa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo hiyo concept na inatumika sana hata kwenye masuala ya uwekezaji. Siku moja niliona kikatuni cha Kipanya kile, nilikiona kikatuni kile ni kama vile kuna mama mmoja alikuwa anaulizwa, Kipanya anamuuliza hivi katika nchi hii kuna matajiri na kuna maskini, wewe unapendaje, upandishwe uwe tajiri au matajiri washushwe wote wawe maskini? Yule akawaza it’s sadistic mind akasema, kwa kuwa kutajirika ni kugumu mimi naomba washushwe wote tuwe maskini tu. Hilo si wazo jema, kama wanaweza wakapata wachache waanze, tutaenda tukikuwa waanze tunaenda tukikuwa yule ambaye haukuguswa mwaka huu ama kile chuo ambacho hakikuguswa kwa maana labda ni cha sekta binafsi wajue ndivyo tulivyoanza hata vile vyuo vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaenda na miradi fulani fulani tunaimaliza kama nilivyosema Daraja la Busisi linaelekea kuisha na Bwawa la Mwalimu Nyerere linaelekea kuisha. Kwa hiyo, tutaenda tukimaliza miradi hiyo na tutakapokuwa tumemaliza maana yake uwezo wa Serikali utaongezeka. Yule ambaye anakuwa na mashaka kuhusu utekelezaji wa mambo haya ya Rais Samia anajipa mashaka yeye mwenyewe tu. Miaka miwili tu aliyoingia Rais Samia mikopo ya elimu ya juu ilikuwa chini ya shilingi bilioni 500 ilikuwa bilioni mia nne naa, hivyo tunavyoongea imeshafika shilingi bilioni mia saba naa, hilo ni ongezeko kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tunavyoongeza na hii ya vyuo vya kati hii inaenda kwenye shilingi bilioni 800 maana yake anavyomaliza miradi ile mama ni mama mpeni maua yake. Hatuna haja ya kuwa na mashaka. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, Chief Whip amesema nirudie. Mama ni mama, mama yuko kazini mama apewe maua yake. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, kwenye Biblia wale walienda wakamtembelea Yohana Mbatizaji alipokuwa amefungwa kule wakaenda wakamuelezea kwamba amepita Yesu amefanya hivi na hivi halafu yeye akawatuma, nendeni mkamuulize; je, wewe ni yule tuliyekuwa tunakusubiri au tuendelee kumsubiri mwingine? Yesu hata hakupata shida kuwaelezea zaidi akasema tu, “Wagonjwa wanapona, viwete wanatembea; nendeni mkawaambie heri wale wasio na mashaka na mimi.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa wale wengine wote, wale wengine wote wanaojadili kuhusu 2025. Ndugu zangu nimewatajia miradi yote hii na mambo ambavyo yameongezeka kwa kiwango cha mvua ile ambayo hamuwezi mkaonana nae, kwa kiwango cha mafuriko, unajadilije kuhusu uchaguzi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mengine niliyoyataja hapa kuna mengine hata sikuyataja ambayo Rais anafanya. Unajua mzigo mzito ukibebwa na mwenye nguvu kuna wakati huwa unaweza kuanza kuonekana ni mwepesi. Mambo anayofanya Rais Samia siyo kila mtu anaweza kuyafanya, siyo kila mtu anaweza kuyafanya. Kuna mengine siyo fedha, siyo fedha, siyo fedha lakini kama Kiongozi wa Nchi amesimamia tu mtu apatae haki yake lakini faraja anayoitengeneza kwa watu hao ni kubwa sana na inawaongezea umri wa kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, demokrasia ndani ya nchi kwa sababu ni jambo la kikatiba na kwa sababu imeonekana wazi ni jambo linaloleta maendeleo, jinsi ambavyo Rais amewaunganisha Watanzania ni mtaji mkubwa sana wa maendeleo kwenye nchi yetu na hili watu wote wanapaswa kuliheshimu. Mambo mengine Mheshimiwa Rais anafanya kwa hekima yake yeye kama yeye. anafanya yeye kama yeye na Mungu alivyomjalia anafanya kama kiongozi lakini anasaidia kuiunganisha nchi, anasaidia kuvutia uwekezaji lakini pia anaisaidia nchi kueleweka hata kwenye taasisi za kifedha sisi tukienda kule tunasikilizwa na fedha zinakwenda kwenye majimbo yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo anafanya kwa hulka yake. Ni mengi tu hata sitaweza kuyataja kwa hiyo ni vyema tukamuheshimu na ni vyema tukamuunga mkono tusije tukafanya kama majuzi ambavyo ilianza kuonekana watu wanaweka weka vimaneno maneno. Mheshimiwa Rais ameonesha mfano ambao ni wa kiongozi na ni wa upekee hata hapa kwenye ukanda achilia mbali Tanzania, hata kwenye ukanda tu wa nchi majirani hakuna ambaye amefanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata Katiba ya Nchi iliyoweka vyama vingi hakuna sehemu iliposema Mwenyekiti wa chama tawala aende kwenye chama kingine kwenye shughuli ya chama kingine, ni hulka yake na upendo wake amefanya hivyo. Hata kiwango cha uhuru wa kutoa maoni alichokitoa na hata wengine wakaamua kumsema yeye mwenyewe ni hulka yake na mimi niwakumbushe Watanzania tusije tukafanya kazi ya kuwatengenezea viongozi roho mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapohama kwenye hoja, Mheshimiwa Rais anakaribisha sana hoja lakini unapoondoka kwenye hoja za maendeleo ukaenda kwenye personalities hizo ni jitihada za kutengeneza roho mbaya kwa kiongozi. Tunasahau mapema sana, tunasahau mapema sana kwamba Katiba hii haijabadilika ni hii hii kama kuna wakati umenyimwa uhuru ni Katiba hii hii na kama kuna wakati umepewa uhuru wa kuweza hata kunyoosha kidole namna hiyo na kusema chochote namna hiyo na kubeza namna hiyo na kubagua namna hiyo na kutumia lugha ya kibaguzi namna hiyo ni Katiba ni hii kwenye Lugha ya Kiswahili. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, ni kwamba pamoja na Katiba kuwepo unatakiwa utambue kuwa kiongozi pia amekufanyia uungwana kwamba angeweza kufanya kingine lakini kakufanyia uungwana. Kwa hiyo, Lugha ya Kiswahili inasema, “Usitukane mamba kabla ya kuvuka mto.” Tusifanye jitihada, tusifanye jitihada za kutengeneza roho mbaya kwa viongozi wetu, tuwalipe uungwana. Tuwalipe uungwana, inapokuwepo hoja tujadili hoja kwa Lugha ya Wanairamba tunasema usimfuate mamba kwenye kina kirefu cha maji. Twendeni tuwe tunajikita kwenye hoja tumepewa fursa ya kujadili hoja tuwe tunajikita kwenye hoja. Tuache kuongelea, tuache kuvuka mipaka, tuache kuongelea hoja zinazoweza kuligawa Taifa letu. (MakofiVigelegele)

Mheshimiwa Spika, niliona nilipazie sauti hilo kwa sababu sisi wengine wa rika lako na wadogo zako hatujawahi kuijua nchi nyingine tunaijua Tanzania tu na Mtanzania wa kona yoyote ya nchi ni Mtanzania hakuna nusu Mtanzania na hakuna Mtanzania na nusu. Mtanzania aliyeko kona yeyote ya nchi hii ni Mtanzania. Twendeni tuwe tunajadili hoja zinazoweza kuboresha utekelezaji wa masuala ya maendeleo badala ya kujadili watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa sababu nimesikia kengele. Tumezipokea hoja zote, hoja za kisekta zingine zimejadiliwa na Mawaziri wa Kisekta. Hoja zingine Waheshimiwa Wabunge mmezitoa moja moja, sisi Wizara tutakaa na Wizara za wenzetu za kisekta tutajadili hoja moja moja na zingine Waheshimiwa Wabunge mmekuwa mkifanya kazi nzuri sana na Wapigakura wenu watambue mmekuwa mkifanya kazi nzuri sana za kwenda kwenye Wizara moja kwa moja, mmekuwa mkifanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna Mbunge ambaye hajaenda kumwona Waziri wote mmekuwa mkifanya hivyo mnaenda kufuatilia hoja moja kwa moja kwenye Wizara za kisekta. Kwa hiyo, hata zingine ambazo hatujazijibu ninawatangazia wananchi wenu kwamba Wabunge tutaendelea kukaa kwenye sectors na zile ambazo zinahusu Wizara ya Fedha tutakutana Wizara pamoja na Mbunge kwa eneo mahususi, mradi mahususi ili tuweze kutekeleza na hayo ndiyo ambayo Mheshimiwa Rais amekuwa akitutuma na mengine Mawaziri wa kisekta pamoja na watendaji watakuja kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisisitize moja la mwisho, twendeni tuendelee kuhamasishana kwa ajili ya kulipa kodi na kule watendaji tuendelee kusimamia miradi kwa ukaribu ili fedha hizi ambazo zinakwenda kule ziweze kutimiza malengo yaliyokusudiwa. Watendaji wote wa Serikali mnapopokea kule kwenye wilaya zetu, mnapopokea fedha watendaji wote mnapopokea fedha wajulisheni Wabunge hawa ambao wanafuatilia fedha huku kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haikupi gharama kumwambia Mbunge fedha zile ulizokuwa unafuatilia zimeshakuja na tunaanza utekelezaji haina gharama. Ni uungwana, yeye kafuatilia, yeye kafikisha mpaka kwa Rais, Rais amemjibu, fedha zimekuja kwenye jimbo lake ni jambo dogo tu mjulishe kwa sababu fedha zinaweza zikaja kabla ya vikao vile rasmi ambavyo vinakaa, mjulishe. Mimi ndivyo ambavyo wenzangu kule Iramba wamekuwa wakiniambia, wanawaambia madiwani, wanawaambia Mwenyekiti wa halmashauri, wananijulisha na mimi nashiriki na nikifika kwenye vikao tunaenda sambamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, watendaji wote, wakurugenzi wote wajulisheni Wabunge fedha zinapofika. Mama amewasikiliza Wabunge ameleta fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo, wajulisheni kama zimekuja kabla ya kikao, msisubiri kuja kusema wakati wa vikao ili waendelee kutafuta fedha zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge mpokee salamu za Mheshimiwa Rais, yuko nanyi bega kwa bega tulipokuwa tunapitisha, tulipokuwa tunatoa briefing ya kikao hiki alisema yuko nanyi bega kwa bega na anawaomba mkitoka hapa mpeleke salamu kwa wananchi wote na yeye anawatakia kila la kheri. Anawaunga mkono, mko naye pamoja mtakapokuwa mnaelekea majimboni mwenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika na baada ya kusema hayo sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Awali ya yote niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na niwaambie kwamba michango yao tumeipokea baadhi nitaisemea hapa, lakini nitawaomba waridhie mingine tutaitoa kwa maandishi na kwa hotuba tutakapokuwa tunawasilisha Bajeti Kuu ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wangu Mheshimiwa Chande kwa ufafanuzi wa hoja ambazo amezitoa na kwa ushirikiano ambao amekuwa akinipatia katika kutekeleza majukumu yangu.

Mheshimiwa Spika, la tatu, niwapongeze Kamati ya Bunge wakiongozwa na Mwenyekiti pamoja na Makamu wake, Kamati nzima pamoja na wataalam wa Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi zake kwa kweli kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakinipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaelezea hoja zilizotolewa na Wabunge naomba mambo haya nitakayosema yaingie kwenye kumbukumbu. Jambo la kwanza naomba Bunge lako tukufu litambue ukubwa wa kazi aliyonayo Mheshimiwa Rais ya kuwezesha miradi ya maendeleo iweze kufanyika katika nchi yetu. Hili jambo baadhi ya watu ambao hawajaangalia takwimu za nchi yetu zinasemaje wanaweza wasijue kazi aliyonayo Mheshimiwa Rais japo wanaona mambo yanakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu karibu kila kitu ni cha lazima, karibu kila kipengele cha matumizi ni kipengele usichoweza kukiahirisha, kipengele hicho ndicho kinachofanyakazi iwe ngumu sana kwa sababu karibu kila expenditure item, kila kipengele cha matumizi unachokigusa ni kipengele usichoweza kukiahirisha. Kwa mfano tumetoa kwenye taarifa yetu kwamba makusanyo yetu ya ndani yalikuwa shilingi trilioni 19.99 ukienda kwenye mchanganuo wa haraka Deni la Taifa kwa mwaka linachukua karibu shilingi trilioni 6.9 ni kama shilingi trilioni saba hivi, mishahara ukiweka na tunakoelekea itachukua zaidi ya shilingi trilioni sita na sehemu ukiweka na mahitaji mengine ambayo ni ya lazima.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye miradi mikubwa reli peke yake tuna zaidi ya shilingi trilioni 1.45 kwa miradi ambayo kwa lot ambazo zilikuwa zinaendelea. Ukienda kwenye barabara tuna zaidi ya shilingi bilioni 579 ambazo hizi zinapitia kwenye TANROADS, ukienda kwenye TARURA barabara za vijijini ambazo fedha hizo ziko kwenye mifuko hugusi gusi tu ni zaidi ya shilingi bilioni 414 kwa mwaka, ukienda kwenye elimu ya juu peke yake ni zaidi ya shilingi bilioni 423.5, ukienda kwenye REA ni zaidi ya shilingi bilioni 367, ukienda kwenye maji ni zaidi ya shilingi bilioni 346, ukienda kwenye elimu bila malipo ni zaidi ya shilingi bilioni 202. Hapa unaongelea kwenye mahitaji yale usiyoweza kuyaahirisha ni shilingi trilioni 16.5 kati ya shilingi trilioni 19 hayo ni yale mahitaji usiyoweza kuyaahirisha, yale ambayo fedha zake zimehifadhiwa mahsusi kwa matumizi yale.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake afya peke yake inachukua zaidi ya shilingi trilioni 2.5, elimu inachukua zaidi ya shilingi trilioni 5.6, maji yanachukua zaidi ya shilingi bilioni mia nane na nusu na social production inachukua zaidi ya shilingi trilioni 1.8. Unaweza ukaona ni space kiasi gani inayosalia kwenye matumizi ya shughuli zingine, ni kiasi gani kinachosalia kwenye shughuli zingine haya ni matumizi mengine ambayo hauwezi ukarudi nyuma pawe na UVIKO, pawe na vita Ukraine, pawe na ukame, haya ni matumizi ambayo huwezi ukayaahirisha.

Mheshimiwa Spika, kazi hii yote ndiyo inayomfanya Mheshimiwa Rais asilale, ndiyo maana utaona leo yuko huku, leo yuko huku na wengine wanadhani haya mambo yanaweza yakaenda hata pasipokuwa na mwanga, hata pasipokuwa na jua limewaka. Mimi nawaulizeni swali dogo tu ni Waziri gani wa Fedha wa nchi za kiafrika anaweza akafanya appointment ndani ya wiki moja akaonana na Rais wa Benki ya Dunia? Ni Waziri gani wa nchi za Kiafrika anaweza akafanya appointment ndani ya siku tatu akaonana na Rais wa IMF? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ni mambo ambayo yanafanyika kwa uzito wake na Mheshimiwa Rais anaona ayaongezee nguvu na ndiyo maana unaona alipoenda kwenye nchi za Ulaya alionana na taasisi zote zile za muhimu kwa shughuli za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alipoenda Marekani alionana na taasisi zote hizi za muhimu kwa wiki moja ameonana na Rais wa Benki ya Dunia, Rais wa IMF na ameonana na Makamu wa Rais wa nchi kubwa kama ya Marekani na mimi namshukuru sana alinifanya niwe Mnyiramba wa kwanza kuingia Ikulu ya Marekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ni sehemu tu ya kazi kubwa ambazo zinalazimika Rais aingie mstari wa mbele ili kazi hizi ziweze kwenda. Hivyo hivyo na alivyokuwa Falme za Kiarabu kule alionana na viongozi wakuu wote wale na maeneo mengine yapo ambayo yanakuja ambako yatatusaidia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa hiyo, nimshukuru sana na nimpongeze na niwaombe watanzania waielewe kazi hiyo ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alisemea Mheshimiwa Mbunda pamoja na Wabunge wengine waliochangia kuhusu jambo la ukaguzi wa ndani, tumepokea hoja hiyo tutaitolea ufafanuzi tutakapokuja kwenye Bajeti Kuu.

Kuhusu Ofisi za Mamlaka ya Mapato tumepokea hilo nilishapokea na baadhi ya Wabunge wengine ambao wameongelea katika Bunge hili wakiwa wanaongea wengine kupitia maswali pamoja na hawa ambao ameongelea tumelipokea na hilo tutabainisha na mipaka mingine tutatembelea na tutachukua uamuzi baada ya tathmini ili tuweze kuwarahisishia wananchi utaratibu wa kupata huduma hiyo.

Mheshimiwa Spika, tumepokea suala la chuma chakavu na Naibu Waziri ameliongelea vizuri. Tumepokea hoja pia aliyoisemea ndugu yangu Tarimba mwananchi bingwa mtarajiwa ambaye amelielezea sana katika eneo hili la kutumia mifumo ni njia ambayo itatupa ufanisi na Mheshimiwa Rais amelisisitiza sana hili na sisi ndani ya Wizara tunaendelea kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ameongelea Mwenyekiti wangu wa Kamati Mheshimiwa Sillo mazingira ya kufanyia biashara hii ni kazi kubwa tunaendelea nayo namna ya kutekeleza blue print yetu ambayo imebainisha maeneo mengi sana ambayo yatatupa mazingira mazuri ya kufanyia biashara zikiwemo biashara kubwa pamoja na biashara ndogo ndogo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine ambayo ameongelea yanayohusiana na mikataba ya double taxation. Mafunzo tumepokea na hilo ni jambo ambalo tunatoa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mama yangu Leah pamoja na Wabunge wengine wameongelea fedha za miradi na kwa kweli kazi kubwa sana imefanyika kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea karibu mikoa yote ya nchi yetu imepata zaidi ya asilimia 100 ya fedha za maendeleo walizokuwa wanatarajia kuzipata katika mwaka huu wa fedha na ndiyo maana mnaona miradi ya maendeleo inaenda kwa kasi ambayo inastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimemsikia ndugu yangu Mtemvu, nimemsikia rafiki yangu Maganga Ofisi ya TRA nitatembelea, tutaenda kuifungua na Maganga wewe ni kichwa ulitoa wazo la kununua mitambo ya kutengenezea barabara wazo lako tulilitekeleza katika Wizara ya Maji na tutaangalia na katika maeneo mengine na kuhusu masuala ya riba tunaendelea kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachotumia kwenye riba ni utaratibu kwamba soko letu tunatumia nguvu ya soko katika kuamua masuala haya ya kiuchumi. Majirani zetu waliwahi kujaribu kutumia nguvu ya dola kuweka ukomo kwamba asubuhi tu tunaamka tunasema leo riba itakuwa asilimia tano, ilileta madhara kiuchumi kwa sababu hivi viashiria vya kiuchumi mpana huwa vinategemeana, unaweza ukakiathiri kimoja ikaleta tatizo kwenye viashiria vingine. Kwa hiyo, tutaendelea kutumia nguvu ya soko lakini pia na ya kisera kuweza kuhakikisha kwamba tunafika katika hatua hiyo hili linakwenda likitekelezeka na tunaamini itaenda kufanyika na kukamilika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jerry nimesikia haya masuala ya Bodi tutayajibu katika hotuba kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu nani atatumika kwenye sensa, sasa hivi vijana hata ukiondoa walimu tuna vijana ambao ni wasomi ambao na wenyewe ni walimu kimsingi wengine ni walimu, wengine ni walimu wa akiba, kwa hiyo, tuliona kwa sababu zoezi hili linahitaji watu wengi sana, walimu watatumika kufundisha, watatumika kusimamia, lakini na hawa vijana ambao wengi wao wameshasoma, ni wasomi wazuri na wenyewe watafanya hiyo kazi huku wakishirikiana na walimu ili tuweze kuleta ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kubwa tulilolifanya tumefanya hawa vijana watoke katika maeneo yale yale ambayo watayasimamia ili kupunguza gharama kwa sababu kwa sasa hivi hakuna kata isiyo na wasomi. Kwa hiyo, tuliona watumike kule kule waliko ili waweze kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.

Mheshimiwa Cecilia pamoja na mama mkwe wangu pale Mama Kaboyoka nimepokea jambo hilo tutalisemea kwenye hotuba kubwa, lakini hili la maduka ni jambo ambalo tunaendelea kulifanyia kazi, hatujamaliza idadi yote, lakini tunaendelea kulifanyia kazi na Mheshimiwa Cecilia mtani wangu, ukihitaji takwimu pia nitakupatia, lakini hatujafika mwisho kwa sababu tunafanya kwa umakini, lakini nikuhakikishie ni zoezi ambalo linaendelea kufanyiwa kazi na wewe ukitafiti zaidi utapata taarifa kama hizi ninazokwambia na baadhi ya watu wameshapata utekelezaji wa jambo hili.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu wale walioomba leseni mpya pamoja na yale masharti hilo ni jambo kubwa la kisera nitaomba uridhie ili tulitolee tamko baada ya kuwa tumeshakamilisha hotuba yetu kubwa tunayoiandaa ili tuweze kutoa tamko ambalo litahusika na watu wengine wote waweze kufuata muongozo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hiyo kama nilivyosema mambo mengine tutayajibu kwenye hotuba kubwa ya bajeti, nakushukuru na nakupongeza kwa kuendesha kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya kusema maneno hayo naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
WAZIRI WA FEDFHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote na mimi nipongeze Taarifa za Kamati na nimpongeze CAG kwa kazi kubwa ambayo ameifanya.

Mheshimiwa Spika, ninapoanza, niwaombe Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania tukubaliane yalikoanzia mafanikio haya makubwa ya leo yameanzia mpaka yamefika hapa, maana naona tulianza pamoja lakini kwenye kuvuna naona kama tunatawanyika.

Mheshimiwa Spika, taarifa hii na hata Watanzania watakuwa mashahidi, imewasilishwa kwa namna tofauti kuanzia kwa CAG na imejadiliwa na Bunge kwa namna ya tofauti.

Mheshimiwa Spika, wengine ambao tumekuwemo humu tumeanzia mbali, tulikuwa wote humu. Kuna mambo ambayo tulikuwa tunayalalamikia na Bunge limesema kwa miaka yote. Wabunge wamelalamika miaka yote na wananchi wamelalamika miaka yote na Serikali ilikuwa inaona lakini ilikuwa haijatoa majawabu ya matatizo yale yanayojitokeza.

Mheshimiwa Spika, mambo yale yalikuwa yapi? Nianze na la kwanza; na Mbunge mmoja alisema pale na wewe ukaunga mkono; kwa sheria tulizokuwa nazo na kwa aina ya ukaguzi tuliokuwa tunaufanya ilikuwa inawezekana kuanzia bajeti inavyopita, mradi unapobuniwa, taratibu za manunuzi zinavyofanyika; taratibu zote zinafanywa lakini mradi unakuwa hauna thamani ya fedha iliyotumika. Hivyo tukasema huku ni kuiba kwa mujibu wa sheria. Lilikuwa linafanyika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa miaka yote CAG alikuwa anakagua compliance, utaratibu wa kiuhasibu tu ndio aliokuwa anakagua CAG kwa miaka yote.

Mheshimiwa Spika, Wajumbe wa Kamati watakumbuka, nilipoteuliwa Waziri wa Fedha jambo la kwanza ambalo Mheshimiwa Rais alilonituma; na bajeti ikiwa imeshafungwa; Bajeti ya CAG inapitishwa na Kamati ya Bajeti, ilikuwa imeshafungwa, imepitishwa ya kutekeleza compliance. Mheshimiwa Rais akasema hapana, hatuwezi tukaendelea na utaratibu wa kukagua compliance, yaani kukagua na kubariki watu wanaoiba kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Rais, akasema nenda kaiombe Kamati, ifungue bajeti ambayo ilishapitisha tumuongezee CAG fedha anazotaka ili aanze kukagua real time, akague value for money. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilienda kuongea na Mwenyekiti wa Kamati nikamwambia hii bajeti mlishaipitisha lakini tunaomba tumwongezee CAG fedha. Nikaongea na CAG akaniambia fedha anazotaka.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, sahani…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Subiri kidogo Mheshimiwa Tabasamu. Mheshimiwa Waziri nikuombe, unapozungumza, ukigeuka nyuma maneno yale hayaingii kwenye Taarifa Rasmi za Bunge. Kwa hiyo jitahidi hapo hapo kwenye kisemeo ili tuyapate hayo maelezo kwenye Taarifa Rasmi za Bunge maana ukigeuka nyuma hatuyapati. (Kicheko)

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naomba wasinisemeshesemeshe maana nilishashika kasi hapa, waniache niseme ili tuelewane.

Mheshimiwa Spika, ninachosema ni nini; niliongea na CAG,

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA FEDHA: ...nikamwambia Mheshimiwa Rais anataka aongeze fedha ukague value for money, thamani ya fedha, real time audit, ukague kwa wakati.

SPIKA: Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, kuna taarifa.

WAZIRI WA FEDHA: Nikaongea na Kamati wakaongeza zaidi ya bilioni tano.

SPIKA: Mheshimiwa Nchemba, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anasema kwamba akaongeza pesa katika bajeti ya CAG. Bunge hili ni Bunge linaloendeshwa kwa tamaduni za Jumuiya ya Madola. Je, Jumuiya ya Madola tunatoa asilimia ngapi kuipa bajeti Ofisi ya CAG, aeleze umma wa Watanzania maana anapewa ela ndogo kiasi hicho wakati anatakiwa apewe asilimia kumi ya bajeti ili tukague miradi yote ya Serikali nchi nzima.

SPIKA: Haya, ahsante sana, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba.

WAZIRI WA FEDHA: Yeah, wang’wise huyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo baada ya hapo tukakubaliana na Kamati tuongeze fedha ya kwa ajili ya kuanza kukagua real time. Wengine labda wanaweza wakasema wang’wise ni jambo baya, Wang’wise ni kaka yangu, yaani nimesema huyu ni kaka yangu, sijampa jina hata la tuzengano ni kaka yangu, wang’wise ng’wanuyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tukaongeza bilioni tano kwa ajili ya kumwezesha CAG, aanze kufanya real time audit, na hiki, Mheshimiwa Rais ndiye aliyesema sitaki kuona watu wanaendelea kukagua compliance ambayo inawafanya watu waibe kwa utaratibu; hapo ndipo tulipoanzia. Kwa hiyo, bajeti ya mwaka ule uliotangulia ilikuwa takribani bilioni 78 tukaipeleka mpaka sasa imeshafika 97 kwa ajili ya CAG, na ndipo mwaka 2020/2021 akaanza na akakagua, alianza na technical audit nne. Mwaka uliofuata akapeleka nane na mwaka uliofuata 11.

Mheshimiwa Spika, jambo hilo limewezekana tu baada ya kuanza kukagua value for money halafu real time. Yaani mradi ukiwa unaendelea; na ndipo CAG anapofanya kazi yake ya udhibiti; anaendelea kukagua. Amefanya hivyo kwenye miradi mikubwa.

Mheshimiwa Spika, jamani Afrika yetu tunaijua, ni mara chache sana nchi za kiafrika zinakuwa na Rais anayeweza kumwambia CAG usipepese macho kwenye taarifa. Mbona tunataka kusahau mapema? Ni marachache sana Afrika Rais anamtuma CAG akakague miradi mikubwa ya kimkakati tena ikiwa inaendelea. Amekagua miradi ya barabara, amekagua miradi ya kilimo na miradi yenyewe sio ya kitoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye barabara ameenda kukagua Daraja la Busisi likiwa linaendelea, kwenye umeme amekagua bwawa likiwa linaendelea. Ameenda kukagua reli ikiwa inaendelea. Irrigation schemes zinaendelewa kujengwa na CAG yuko site kukagua na haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais na ameweka fedha mahususi kukagua value for money sio vitabu...

SPIKA: Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Anatropia.

WAZIRI WA FEDFHA: ... kama kweli wote tuna nia njema, Je, kuna mtu anaweza kuwa na nia njema zaidi ya aliyetoa fedha ziende kukagua….

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Haya, Mheshimiwa Nchemba, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Anatropia.

TAARIFA

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nashukuru, nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri, kaka yangu anayeongea. Itakuwa ni moja kati ya makosa makubwa kudhani kwamba Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kupewa fedha kiasi gani na kukagua ije kwa hisani. Kwanza anakagua kwa mujibu wa sheria na kuna kaguzi za aina tofauti tofauti. Ni wajibu wetu na wajibu wa Serikali kuhakikisha inamwezesha na si tu audit…
SPIKA: Haya, ngoja.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: ...tunayoifanya, tufanye forensic audit ili tuweze kuwakamata na hizo ndio ripoti zinazoweza kwenda mahakamani.

SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, unapokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, mimi sina hata haja ya kubishana na taarifa yake. Ninachomsisitizia ndicho na yeye anachosema. Tunachosema ni kwamba cha kwanza kilichotangulia ni political will.

Hivi mbona Watanzania tunasahau mapema sana, hivi Prof. Assad alishindwa kukagua, halafu aliondokaje? [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, kwa nchi za Kiafrika, political will ni jambo la msingi sana kufanya ukaguzi kwa uwazi, kwani jambo hili ni la kawaida?

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, ngoja, umeanza maneno political will yaliyoendelea hapo mbele, hebu yafute, halafu…

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, ili nisipoteze muda nayaondoa. Nasema nilichotaka kukwambia ni kwamba, Rais ameonesha political will na akaongeza fedha wala sio kwa hisani, ameongeza fedha kama ambavyo katiba inasema lakini kilichotangulia ni political will yake, kwa sababu hajabadili katiba ili kuongeza hizo fedha. Ameonesha tu political will na jinsi utayari wake wa kutaka majizi kuonekana ndio hicho ninachokisisitiza.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, dakika moja malizia.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwenye upande wa Mkaguzi wa ndani; Mkaguzi wa Ndani amepewa vote yake na Bunge lilipitisha hapa, ameitengenezea muundo mpya ambao Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanasema hapa, kwa hiyo na yenyewe ni kwa ajili ya kudhibiti fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi naomba tusitawanyike twendeni tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, ameshaonesha nia ya kushughulikia vitu hivi tena kwa njia ya kikatiba na Waheshimiwa Wabunge, nilimsikiliza ndugu yangu Mheshimiwa Mpina…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kengele ya pili imeshagonga.

WAZIRI WA FEDHA: ... sisi wote tunapo kuja hapa ni Wabunge, tena mimi ni Mbunge wa jimbo anayekubalika Jimboni kwake...

SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana.

WAZIRI WA FEDHA: ...kwa hiyo unapoongelea jambo…

SPIKA: Mheshimiwa Mwigulu Nchemba…

WAZIRI WA FEDHA: ...kitu ambacho hujathibitisha na hakipo kwenye taarifa ni vyema tukaheshimiana…

SPIKA: Mheshimiwa Mwigulu Nchemba…

WAZIRI WA FEDHA: ...maana mimi ninapotangazwa Jimbo zima huwa linashangilia, sio kama wewe tunajua unavyoshinda… (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Mwigulu Nchemba…

WAZIRI WA FEDHA: …lazima tu…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuturuhusu na sisi tuweze kuanza kutoa mchango kwenye baadhi ya maeneo yanayogusa sekta zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwanza naunga mkono hoja yake aliyoiweka mezani na maelezo ya kina kuhusu baadhi ya hoja zilizotolewa na Wabunge tutayatoa wakati wa bajeti yetu ya Wizara. Hapa niseme tu yale yaliyo ya jumla na nianze kwa haya ambayo yamesemewa kwenye michango na yamejitokeza kwenye baadhi ya maswali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na hili ambalo lilikuwa linaongelea kusuhu masuala ya upelelezi kuchukua muda, haki za watuhumiwa na watu kubambikwa kesi. Niseme kwenye jambo hili ambalo ni la msingi na linahusu haki za watu wala sisi Serikali hatuwezi tukatofautiana na ninyi Waheshimiwa Wabunge. Hata juzi Arusha kule Mheshimiwa Rais alituelekeza kati ya mambo ambayo tunatakiwa tuyafanyie marekebisho kwenye utendaji wetu wa kazi ni kuhusu masuala ya ubambikaji wa kesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme hili ni jambo ambalo tumelichukua na tumeshaanza kulifanyia kazi. Kama kuna baadhi ya maeneo ambako bado mambo hayo yanaendelea kujitokeza yatakuwepo makosa ya kibinadamu ambayo yanaweza kujitokeza katika utekelezaji wa kazi, lakini Serikali kama Serikali kusudi lake ni kuhakikisha inalinda haki za raia wake kwa sababu ni sehemu ya haki muhimu sana ambazo Watanzania wanatakiwa kuzipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upelelezi kuendelea kufanyika wakati mtu ameshafikishwa Mahakamani, hili nalo lipo kwenye utaratibu wa kisheria na si wote wanapokwenda Mahakamani wanakosa dhamana. Kwa hiyo, huwa tunaona ni vema mtu akapelekwa Mahakamani kwa sababu dhamana inakuwa wazi ili mtu aweze kupata dhamana hata kama upelelezi unaendelea. Kwa wale wanaokwama kupata dhamana yenyewe inakuwa inatokana kwa kiwango kikubwa na aina ya makosa pamoja masuala ya kiusalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge walilisemea kwa sauti kubwa suala hili linalohusiana na watu kulundikana magerezani huku wakiwa hawajapata ufafanuzi kuhusu makosa yao ama hatma ya makosa yao. Hata sisi kama Wizara ni jambo ambalo tunaliangalia kwa jicho la tofauti. Kwanza ni gharama kwa Serikali kuwa na watu ambao labda makosa yao yangeweza kumalizika haraka, lakini la pili ni jambo hatarishi kuwachukua watu ambao wana makosa madogo wakakaa pamoja na watu walio na makosa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewaambiwa hata wasaidizi wangu Jeshi la Polisi pamoja na wengine kwamba kama kuna watu ambao tunaweza tukatathmini tukajua yale waliyofanya na tukaangalia kama hayana matatizo ya kiusalama kwa wao kuwa nje, basi ni vema sana hao watu kutokuwachanganya na watu ambao wana makosa makubwa ambao wako magerezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu taarifa za kiuchunguzi tulizozipata kuna baadhi ya watu wanapokaa na wahalifu wazoefu ama na wahalifu wenye makosa makubwa ilhali wao wakiwa na makosa madogo, wengine wanapata mafunzo ya kufanya makosa makubwa na wengine watengeneza ushirika na wale ambao wanafanya makosa makubwa. Kwa maana hiyo, tunazipokea zile hoja na tutaendelea na kuzifanyika kazi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu sekta hizi zote zinapofanya kazi kwa pamoja zinaharakisha utoaji wa haki za watu ameziangalia kuanzia Mahakama hadi Magereza pamoja na Jeshi la polisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo ilizungumziwa ni kuhusu matumizi ya askari kwenye masuala ya chaguzi. Sisi kama Jeshi la Polisi na kama Wizara ya Mambo ya Ndani hatupendi kuona wananchi wetu wanaumizana kwenye masuala ya uchaguzi. Kwenye chaguzi nyingi tumeshuhudia na mara zote ninapopata fursa ya kuongea na wananchi naendelea kuwaambia ni aibu sana kwa nchi ambayo ina siasa za vyama vingi kwa zaidi ya miaka 20 lakini wananchi wake wanafanyiana fujo pale panapotokea pana uchaguzi katika eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba kama pana uchaguzi katika Kata A na vyama vyote vinashiriki maana yake vyama vyote vitakuwepo katika eneo hilo. Kwa hiyo, tulitarajia watu waheshimu taratibu na wanapoheshimu taratibu maana yake hapatakuwa na ugomvi katika maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani hatutavumilia kuona watu wanakatana mapanga halafu tukasema kwa sababu ni chaguzi ama ni siasa tukaacha kwa sababu tunawajibika kulinda usalama wa raia mara zote na kuwahakikishia usalama mara zote wanapotokea wana mikusanyiko ama wako katika maisha yao ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa sababu nimeisikia kengele, liliongelewa suala la kijana kule Mtwara pamoja na lile la Msikitini. Nimewaelekeza wafanye uchunguzi wa ndani ili tuweze kupata taarifa kamili na tutaendelea kuzitoa taarifa hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge pale panapokuwepo na jambo limempata mmoja wa Watanzania tuepuke sana kuliunganisha jambo hilo na dini yake kwa sababu yanapotokea masuala ya uhalifu mtu hakamatwi kutokana na dini yake, kabila au chama chake cha siasa alichonacho bali anakamatwa kutokana na kosa alilolifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tusije tukatumia utaratibu wa kuunganisha kosa mtu alilofanya pamoja na kabila lake, dini yake au chama chake cha siasa. Ingekuwa vitu hivi havifanywi na watu wa makabila haya haya, wa vyama hivi hivi, wa dini hizi hizi basi katika maeneo mengine ambapo tunapaamini kwamba ni mahali patakatifu tusingekuwa tunapata makosa ya aina hiyo. Kwa hiyo, watu wanakamatwa kutokana na makosa waliyofanya na wala kosa alilofanya mtu lisiunganishwe na imani yake, chama chake cha siasa ama kabila lake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kufafanua hivi vitu kwenye bajeti zetu za Wizara husika. Kwa muda huu, naomba kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu iliyowekwa mezani. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuhitimisha hoja ya upande wa Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema mtangulizi Kaka yangu Profesa Kitila, kama Serikali katika hatua hii na kama Kanuni zetu zinavyotutaka, tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge. Tumewasikiliza na tutakuwa na kazi katika ngazi ya Serikali kufanyia kazi maoni ya Waheshimiwa Wabunge katika maandalizi ya bajeti ambayo itakuja mapema mwakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hatua hii nikushukuru wewe pamoja na Kamati na Wabunge wote kwa maoni waliyoyatoa kwa wingi na uzito mkubwa. Waheshimiwa Wabunge, tumewasikilza, tumeyapokea na kwa kweli sisi tuliokuwa tunawasikiliza, tuwahakikishie wapiga kura wenu kwamba wana Wabunge makini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa tumepokea, katika kuhitimisha naomba niseme mambo machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jambo la kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, kwa kuwa amefanikiwa kubadilisha kwa kiwango kikubwa kubadilisha kumbukumbu za Bunge na michango ya Wabunge katika kipindi cha sasa katika Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne na nimekuwa kwenye Baraza Serikali ya Awamu ya Tano. Michango mingi ya Wabunge katika Bunge lako Tukufu yanapokuja masuala ya bajeti ilikuwa ni Wizara ya Fedha inakwamisha Wizara nyingine kwamba, fedha haziendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kila Mbunge anakiri kupokea fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo katika majimbo yenu. Kila mmoja, kila wilaya na hata panapokuwepo na mikutano ama vikao vya Wakuu wa mikoa ama Wakuu wa Wilaya, kila Mkuu wa Mkoa anakiri kupokea fedha nyingi katika maeneo yao ya utawala. Hizo ndizo kazi anazozifanya Mheshimiwa Rais anapokesha na anapozunguka huku na kule, nchi na nchi, bara na bara anatafuta fedha na zinamiminika katika miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo moja pekee kwenye upande wa bajeti ambalo limeongelewa na Waheshimiwa Wabunge ni kuhusu usimamizi wa fedha zinapokwenda kwenye miradi hii ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili Mheshimiwa Rais alilitambua mapema tu. Alipoapishwa na wakati anaapishwa na kwenye Baraza la Mawaziri mara nyingi amekuwa akielekeza kuhusu usimamizi wa fedha za umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hatua ambazo zimechukuliwa ambazo Waheshimiwa Wabunge wameziongelea kwa kiwango kikubwa ambazo zinahusisha namna bora ya kusimamia fedha za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ngazi ya Serikali na ngazi ya Wizara ya Fedha masuala haya ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasemea, sisi tutaendelea kuyazingatia. Mheshimiwa Rais alielekeza tuimarishe nguvu ya Wakaguzi wetu, CAG pamoja na Mkaguzi wa Ndani ili wakague thamani ya fedha katika miradi yetu. Jambo hilo linafanyika na fedha zimeendelea kuongezewa kwa ajili ya Wakaguzi wetu ili wakague miradi ya maendeleo. Nitoe rai kwa viongozi wote Serikalini wakiwemo Maafisa Masuuli tufuatilie kwa ukaribu na tuchukue hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ya utawala wa sheria ni kufuata utaratibu. Natamani hata mimi niende kama ambavyo maoni ya wananchi wengi na hata baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliliona kwamba lazima panapotokea jambo pachukuliwe hatua pale pale, lakini gharama ya utawala wa sheria ni lazima taratibu zifuatwe. Kwanza panafanyika ukaguzi, pili, panafanyika majibu kutoka kwa Maafisa Masuuli waelezee hoja zile zilizokuwa zimetolewa na hatua zinazofuata panatakiwa pafanyike uchunguzi na baada ya uchunguzi hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa. Hiyo ndio gharama ya utawala wa sheria. Rai yangu watendaji wote Serikalini katika ngazi zao wachukue hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muundo wa nchi yetu ni mzuri sana. Ukienda ngazi ya Wilaya ambako ndiko miradi inatekelezwa pana muundo mzima ule ambao uko katika ngazi ya Kitaifa, pale kwenye mradi pana Mkuu wa Wilaya kama ni ngazi ya Wilaya, pana Kamanda wa TAKUKURU, pana Kamanda wa Polisi, pana Idara, pana Upelelezi, pana Mahakama, pana wa kukamata na pana Magereza. Kila kitu kipo palepale mradi unapokamilikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hatuna haja ya kusubiri ziara za Viongozi Wakuu ili tuchukue hatua kwenye maeneo ambayo mradi haukutekelezwa vizuri. Kwa kweli kama darasa limejengwa vibaya, tukataka tusubiri Rais aje mpaka kwenye kijiji achukue hatua kwenye darasa ambalo lilijengwa vibaya, tutakuwa hatumtendei haki Rais ambaye ametutafutia fedha zimekuja na eneo ni letu na mradi ni wetu, lakini tumeshindwa kuusimamia na kuchukua hatua ama kuchukuliana hatua katika eneo husika. Kwa hiyo nitoe rai ngazi zote zinazosimamia miradi wasimamie ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hatua hii ya uandaaji wa Bajeti, hoja zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge tumewaelekeza Maafisa Masuuli wote wazingatie miradi inayoendelea, tuitengee fedha kama kipaumbele miradi inayoendelea ili tusiwe na matumizi mengi ya fedha zinazotumika nje ya bajeti au kuwa na miradi ambayo haina fedha katika bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wameongelea suala la fidia, tumelizingatia, maeneo yote ambayo hayana mizozo, tutaendelea kulipa fidia. Tumeelezea habari ya maeneo ambayo yamechukuliwa kwa ajili ya EPZA, tumeelezewa maeneo ambayo Serikali imeyachukua kwa matumizi tofautitofauti kwa miradi ya maendeleo. Tutaendelea kulipa fidia kwa maeneo hayo ili kuweza kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri. Haya ni maeneo ambayo Taasisi zetu za Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimechukua maeneo kwa ajili ya maendeleo, lakini kuna maeneo ambayo wananchi wanapisha miradi ya maendeleo ama kuna maeneo ambayo tunajenga miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo hayo ambayo tunajenga miradi ya maendeleo mathalani tumeenda tunajenga mradi wa umwagiliaji katika eneo lao, kama tumeondoa nyumba ya mwananchi atalipwa fidia lakini kama tunajenga Mradi wa Umwagiliaji katika eneo ambalo wananchi wale watalima kisasa wale ambao eneo lile unajengwa mradi wa umwagiliaji mathalani bwawa watapewa maeneo ya kulima. Watapewa maeneo ya kulima washiriki kwenye mradi ule wa umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusije tukakwamisha Miradi ya Umwagiliaji tukarudi kenye utaratibu wa kutegemea mvua kwa sababu ya kubishana kuhusu wapi tujenge mradi wa umwagiliaji. Hii ni teknolojia, ni ulimaji wa kisasa, unatuhitaji wote tujitoe kwa ajili ya kukamilisha hilo. Kwenye maeneo haya niliyoyasema ambayo yanachukuliwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo nilimsikia Mbunge wa Segerea akiongelea fidia yao ya eneo la Kipunguni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishafika eneo lile na tuliwatangazia wananchi kwamba tunataka tuanze kulipa mwezi Septemba. Kilichotuchelewesha kama ambavyo Mbunge ameongea kwa hisia si kwamba fedha ilikosekana ya kulipa fidia hiyo, isipokuwa ilipofanyika uhakiki iligundulika kati yao miongoni mwao kuna ambao tayari walishapewa maeneo mengine lakini majina yao yalikuwepo tena kwenye fidia kwa maana hiyo ingeweza kuwa kulipa fidia mara mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wengine tuliposema tunataka kuanza kulipa, wakawa hawajaridhika na fidia inayotakiwa kulipwa, kwa maana hiyo ilibidi ufanyike utaratibu wa kuweza kulimaliza hilo ili masuala ya kulipa yaweze kuendelea. Kwa hiyo tutaendelea kulipa, tunaamini kwamba baada ya kuwa tumeshamaliza mzozo huo ndani ya mwezi mmoja ama mwezi mmoja na sehemu hivi tutaenda kwenye utaratibu wa kulipa hili likiwa linahusisha Kipunguni pamoja na maeneo mengine ambayo yalikuwa na kesi ya aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liliongelewa pia jambo la masuala ya mifumo tumeshapokea, kazi inaendelea, sasa hivi tunaweka automation kwenye masuala ya mifumo ya upande wa Forodha, tutaendelea na mifumo kwenye upande wa kodi za ndani na tutaendelea na mifumo kwa upande wa makusanyo mengine ili maelekezo ya Mheshimiwa Rais yanayohusisha mifumo yaweze kutekelezwa kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumalizia, mwenzangu mtangulizi wangu ameongelea suala la kilimo na amegusia pia na masuala ya uhifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti pamoja na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote, kuna hili suala la suala la mifugo. Naomba tukubaliane kwamba mambo yamebadilika sana na jambo hili halihitaji taharuki katika kulishughulikia. Sote tunakubaliana kwamba hatuwezi kudiriki kutangaza kwamba ufugaji katika nchi yetu ni jambo la hatari, wote hatuwezi tukadiriki kufanya hivyo. Ufugaji na mifugo ni mali na ni utajiri wa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wengine sisi tuliotokana na jamii hizi za kifugaji tunajua, mifugo inakuwa sehemu ya familia na mifugo ina majina mengine yana majina ya mjomba, wengine shangazi ni sehemu ya familia na mtu akichukua mifugo ni kama vile ameteka watoto wako ni kama vile ameteke sehemu ya familia yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hatuwezi tukatangaza nchi hii kwamba itakuwa ya mifugo tu, utaratibu tuliokuwa tunatumia kufuga zamani, sasa hivi unaendelea kuwa mgumu na tunakokwenda utaendelea kuwa mgumu zaidi. Kwa hiyo ni lazima tukubaliane tena bila taharuki utaratibu mpya ambao tutatumia kulima, utaratibu mpya ambao tutatumia kufuga na utaratibu tutakaotumia kujenga. Hivi vitu vitatu kwa sababu uwingi wa watu unaongezeka, uwingi wa mifugo unaongezeka, mahitaji ya kulima yanaongezeka, hivi vitu vitatu kwa uchache wake lazima vyote viweze kubadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mimi nikichunga ilikuwa ukiamka ukishakula, wewe ni kupiga mluzi tu na kuwahimiza, tulikuwa tunaongea tunaelewana na mifugo, ukiamka tu hapa unasema wochage mapembe bije, ukishafungulia mlango unaachilia siku nzima mpaka mkishaona mmechoka jua linaelea, mnarudi tena lakini sasa hivi mazingira hayo yanaenda hayawezekani. Kwa hiyo ni lazima tuwekeze kwenye ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu vitu vingi vizuri tunavifanya kwa kuonesha. Ukienda kwenye Maonesho ya Nanenane ukaiona mifugo ile, ni mifugo ambayo inapatikana na kwingine kote duniani. Ukishamaliza maonesho imeisha hiyo, ukienda kwenye kilimo hivyohivyo, vitu unavyoviona kwenye maonesho ni bora sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuweze kukabiriana na huku kupungua ama kuongezeka kwa mpambano wa matumizi ya ardhi, ni lazima hivi vitu ambavyo huwa tunavionyesha kwenye Maonesho ya Nanenane ndiyo uwe mtindo wa maisha. Maana yake tutapata wingi uleule kwa ubora, tutapata mahitaji yaleyale kwa kiasi kidogo lakini kwa ubora mkubwa, hiyo itatusaifdia katika matumizi ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongea na wenzetu wa Wizara ya Mifugo na tumeongea na wenzetu wa Wizara ya Kilimo na Mheshimiwa Rais ametoa hayo maelekezo. Tuwawezeshe wenzetu hawa wa hizi sekta ili kuweza kufanya hizo transformation ambazo ndio itakayotoa majawabu ya moja kwa moja ya kupunguza huu ushindani wa matumizi ya ardhi. Hizi sekta zote ni za muhimu katika nchi yetu na ni sekta za kihistoria na vilevile tunaendelea kuongea na wenzetu wa Wizara ya Ardhi kuangalia pia mjengo wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaendelea kujenga huu mjengo tunaotumia kwa huu mtawanyiko mkubwa, sasa hivi kwa sensa hii tuliopewa ukiongeza miaka 20 miaka 30 ijayo tutaelekea milioni 200, kwa mjengo huu tunaoenda nao kwanza mkumbo singalila, kama majani yale yanayotambaa hayaendi juu. Hii nchi yote itakuwa na maeneo ya makazi. Tutakosa maeneo ya uzalishaji, hatutakuwa na eneo la kulima, hatutakuwa na eneo la kufugia. Kwa hiyo ni lazima na hilo na lenyewe tumeendelea kuongea huko tunakokwenda mbele tuendelee kuliwekea utaratibu ambao utasaidia kukidhi mahitaji makubwa yanayohitajika ya matumizi ya ardhi, huku ukiruhusu shughuli nyingine za kimaendeleo ziendelee kufanywa na wananchi wetu kujipatia kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Waheshimiwa Wabunge, tumepokea yale yaliyokuwa yanahusiana na Majimbo yenu, hatuwezi kutaja mmojammoja, kila Mbunge ametaja baadhi ya mambo ambayo yanahusu miradi inayoendelea na mahitaji ya fedha katika sekta za huduma za jamii, miundombinu pamoja na maeneo mengine. Mchango wa kila mbunge tumeuchukua na tulikuwa tunaongea hapo na Waziri wa TAMISEMI, tumeyachukua na tukishamaliza Bunge hili hiyo ndiyo itakayokuwa kazi tutakayoenda kuifanya ili kuweza kuhakikisha tunapokuja Bunge la Bajeti tuweze kutoa taarifa hiyo ya utekelezaji wa maeneo hayo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa mara nyingine na nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)
MUswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu wa mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kuweza kuhitimisha hoja hii na nianze kwanza kwa kukushukuru kwa kuendesha vizuri mjadala huu na niwashukuru Wajumbe wa Kamati wakiongozwa na Mwenyekiti ambapo wametoa maoni kuanzia kwenye Kamati na hapa ambapo Mwenyekiti amewasilisha vema na kuweka wazi kwamba kwa kiwango kikubwa karibu yote tulishakubaliana kati ya Serikali na Kamati na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwenye hii hoja na kuhitaji baadhi ya maeneo yawekewe ufafanuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikuombe niende moja kwa moja kwenye baadhi ya maeneo ambayo yangehitaji ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na haya machache aliyoyasema Dkt. Pindi Chana ambayo ndiyo yapo hapa mwishoni mwishoni, kwenye eneo lile ambalo anaongelea kuhusu terms and conditions as he may determine akiwa anaelezea kwa maana hiyo Waziri na sisi Serikali tulishaliona na kwa ajili ya muda tumeweka baadhi ya marekebisho. Kwa hiyo, tukubaliane na yeye marekebisho ambayo anayaandaa yaendane na ya kwetu ambayo tumeshayaandaa kwa mujibu wa Hansard iweze kusomeka subject to sub-section (2) the Minister shall appoint the Executive Director on the Board in accordance with the Public Service Act, on such terms and condition as provided for in the scheme of service; ambapo itakuwa imeshaondoa ile dhana ya kwamba atakavyoona inafaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kile kipengele cha pili ambacho kilikuwa kinaongelea which working experience, Mheshimiwa alichokuwa anakisema kina mantiki kwamba ni experience ipi, lakini Serikali tulikuwa tunaona iendelee kuwa vile kwa maana ya hii working experience ambayo tumeiandika hapa ni nyongeza ya zile sifa sasa ambazo Mheshimiwa Mbunge amezisema kwamba ni vizuri zikawepo. Kwa maana hiyo hii working experience tuliyoiweka ina- supplement zile sifa sasa za field yake kwa sababu hapo juu tumeshataja (a) awe holder of at least Master Degree in Accounting, Finance, Management and Economics; has an accountancy professional qualification obtained from recognized institution; is a registered hapo kwa mujibu wa gender sensitivity he or she is registered by the board as a Certified Public Accountant or Certified Public Accountant in Public and Practice. Sasa hii inaongezea hizi sifa kwa hiyo tukizichukua tena hizi sifa ziwe hapa tulikuwa tunaona inaweza ikawa ina repeat kwa sababu already huyu mtu tunayemuongelea tunasema awe na hizo sifa hapo juu. Halafu tukasema basi kwa sababu anaenda kwenye menejimenti awe pia sasa na nyongeza ya working experience katika level ya menejimenti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo alilisema Mheshimiwa Mbunge ndugu yangu aliyekuwa anaongelea kuhusu pande mbili hizi za Muungano, haya masuala ya pande mbili za Muungano yanakuwa guided na miongozo pamoja na sheria inayoongelewa kama ni ya Muungano au laa. Kama sheria si ya Muungano kwa vyovyote vile sheria itakayotawala utaratibu wa utungaji ama marekebisho lazima yafuate utaratibu huo.

Kwa maana hiyo jambo hili kwa kuwa si la Muungano tusingeweza kushirikisha upande mwingine kama ambavyo Mheshimiwa Hasunga ameliweka vizuri, taratibu zinazotegemewa hadi sasa ni kwamba wenzetu wa upande wa pili wa Zanzibar na wenyewe watapita hizi hatua, tunajua, lakini taratibu hizo zikiwa zimeshafanyika na ambavyo ilikuwa ikitumika kutakuwepo na kusaini MoU kwa ajili ya makubaliano ya namna ya kushirikiana ili watu ambao watakuwa certified upande wa huku ama certified upande wa pili wa Muungano ile certification iweze kutambulika katika hizo pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kabla ya sheria, administrative measure zitaendelea kufanyika za MoU za mashirikiano na kwa sababu hii nchi ni moja na Muungano wetu ni wa kindugu hili jambo mpaka sasa wameweza kuwa wanafanya hivyo na baada ya taratibu za aina hii kufanyika pia upande wa pili wa Muungano mashirikiano haya yataendelea kufanyika ili certification hizi ziweze kutambulika pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ilikuwa imetolewa ambayo ilikuwa inahusisha aliisema Mheshimiwa Salome iliyokuwa inahusisha wajumbe wale wawili kama Waziri asiwateue kutoka sehemu yoyote, jambo hili tulishakubaliana kwenye Kamati na kwenye marekebisho tumeweka na nadhani kile tulichokiweka tulishasema moja atoke kwenye higher learning institution na wale wawili watoke kwenye association hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge alikuwa anazisema na tukaongeza pia kwamba au kwenye private sector kwa sababu pia tunaweza tukapata experience hiyo ya wale ambao wameshafanya na kazi katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lile lingine ambalo alikuwa analisema Mheshimiwa Kigwangalla moja kama alivyosema Mheshimiwa Hasunga moja tayari tumeshakubaliana kwenye Kamati vile viwango tumeshaweka kwenye turnover milioni 500 na kwenye assets tulishaweka milioni 700.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisisitize kimoja tu, essence ya kuwa na wahasibu katika taasisi zetu hizi na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla anasema tusifungue chungu kilichokuwa kimefungwa zamani, kuna umuhimu mkubwa sana wa watu wetu kuanza kuwa oriented, kuelekezwa namna ya kuendesha hizi shughuli kwa njia za kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia kuna maeneo mengi watu wetu wanaumizwa katika hatua fulani, fulani hivi kutokana tu na kwamba hawatunzi kumbukumbu na wengine wengi kwa sababu hawakutunza kumbukumbu huwa wanaridhika tu kuumia na hatambui kama ameumia kwa sababu kumbukumbu hazikuwepo. Sana sana tu unakuta anaona kikubwa kile anachoona anakadiriwa kwa sababu hata hivyo hana cha kulinganisha nacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo tunakokwenda kama alivyosema Mheshimiwa Hasunga ni vizuri watu wetu wakaanza, kadri biashara zinavyoanza kutengemaa, zinavyoanza kuwa rasmi, ni vizuri sana wakaanza kutunza vizuri mahesabu yao kwa sababu itawaepusha kwenye kuonewa na itawaepusha kwenye kuumia na biashara nyingine unaweza ukakuta hazikui kwa sababu kile kinachokadiriwa huenda kikawa siyo sahihi kwa sababu kumbukumbu iliyo sahihi haipo. Kwa maana hiyo sisi bado tunaona ni vyema sana watu wetu wawe oriented kwenye kutunza kumbukumbu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakubaliana na Waheshimiwa Wabunge na tulikubaliana na Kamati kuhusu viwango vile kuwa vidogo sana kwamba tutakuwa tumewaweka kwenye gharama hata wale ambao biashara zao bado ni ndogo. Lakini biashara zikishakuwa rasmi, kama ambavyo Mheshimiwa Hasunga amesema ni vizuri sana watu wetu wakaenda kwenye utaratibu ulio rasmi ili kuweza kutunza kumbukumbu vizuri na pia kwenda kwenye ile essence ya hoja aliyoisema Mheshimiwa Rais ya watu kulipa kodi iliyo halali, mtu alipe kile anachostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kuna baadhi ya maeneo, siyo mengi lakini yapo, kuna baadhi ya maeneo, hata mwananchi anapolalamika kuna wakati unashindwa umsaidiaje kwa sababu hata yeye ukimuuliza kumbukumbu zake zinasemaje, anakuwa hana. Kwa hiyo, unakuta umetumika tu uzoefu, ama mtazamo, ama kumbukumbu za hisia kwamba mwaka fulani aliwahi kufanya hivi, mwaka fulani akafika hapa, basi ndiyo inajengwa trend ambayo huenda ikawa si sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nitoe rai watu wetu tukubali kwenda kwenye mifumo hii iliyo rasmi kwa sababu ndiyo tutakuwa tunakwenda kuwa rasmi na tutaweza kutunza kumbukumbu zilizo sahihi na si vyema sana na si uungwana kuwa na maisha ya kudanganya danganya kila wakati, yaani unapoulizwa na benki unatoa namna hii, unapokuja kukaguliwa na upande mwingine tena unatoa hesabu zilizo namna nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla alikuwa anasema kwamba wazee wetu waliyaona hayo na wakaacha hivyo hivyo, tunakokwenda ukiweka na kukua kwa teknolojia, mifumo mingi itakuwa inakwenda inasomana. Kwa hiyo, kuna watu siku zinazokuja kule mbele anaweza akakosa mkopo kwa vile tu kuonekana takwimu anazopeleka ni za kudanganya na moja kwa moja akaonekana huyu kumbe ana asili ya udanganyifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunakokwenda biashara zikiwa zinafanyika vizuri na mifumo hii inasomana, ni vizuri tuwe na kumbukumbu ambazo ziko sawa na ndiyo zitakuwa zinamtambulisha mtu huyo na zitakuwa zinaitambulisha biashara hiyo na hakuna ukaguzi unaoweza kumpeleka hatiani kama hizo ndiyo kumbukumbu zinazosomeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo hili nilikuwa nalisisitiza hata watu pia wanapofanya manunuzi, siyo busara, wala uungwana, wala uzalendo kwenda kuuliza bei mbili, kwamba kitu hikihiki nipe bei isiyo na risiti ya TRA au nipe yenye risiti. Bei iwe moja tu ile ile kwamba ina risiti ya Mamlaka ya Mapato ya EFD ambayo ina-include pamoja na kodi zinazostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo tukirasimisha haya masuala ya biashara na kumbukumbu zake zikawa zinatunzwa vizuri itatusaidia kuondokana na baadhi ya migogoro ambayo inajitokeza inayohusisha uonevu, lakini pia itatuweka mahali pazuri sisi pia hata kama Serikali kwenye upande wa kuweza kukadiria. Sasa hivi makadirio yanakwenda yakiwa hayatabiriki kwa sababu kumbukumbu katika baadhi ya maeneo zinaweza zisiwe zimenyooka.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru Wabunge wote waliochangia na niombe kama kuna eneo moja sijalitaja mridhie tu kwamba tumeshaweka kwenye mabadiliko, kwa hiyo, kuna baadhi ya maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge mmechangia, tumeshaya-include kwenye mabadiliko yetu haya ambapo mabadiliko mengi pia tulishakubaliana na Kamati ambao ni wawakilishi wa Bunge katika mjadala huu tuliokuwa tunaufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya na kwa sababu tutakwenda pia kupitia eneo moja baada ya lingine, kama kuna eneo nitakuwa pia nimeliacha pembeni basi tutapitia pia pale tukumbushane kile ambacho tutakuwa tulishakubaliana kwenye Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nitumie fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hoja hii. Pili, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao makini kabisa waliyoitoa. Tatu, niishukuru sana Kamati ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Daniel Silo Baran pamoja na Makamu wake Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi pamoja na wajumbe wote kwa ushirikiano, lakini pamoja na ushauri waliotupatia na uchambuzi ili kuweza kufanikisha kukamilisha jambo hili katika hatua hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli hii ambayo tuunaendelea nayo ni ya kutunga Sheria ya Fedha. Pamoja na kwamba tunatunga sheria lakini jambo la kwanza la msingi ambalo naendelea kulisisitiza ni wananchi wote kutambua umuhimu wa kutimiza wajibu. Sheria tunajiwekea tu kama kuwekeana miiko na mipaka, ili tuweze kuenenda tunawekeana miongozo lakini kubwa la kwanza ambapo ndiyo sheria iliyoandikwa kila mtu moyoni mwake ni yeye kujitambua kutimiza wajibu wake kwa Taifa lake. Hili ni jambo la msingi ambalo mara zote tutaendelea kulisema.

Nawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa sababu sisi ni viongozi tuendelee kutembea na kauli mbiu hiyo kwamba watu wetu lazima watembee kizalendo, watembee wakijua wanahitaji kutimiza wajibu kwa Taifa leo, mara zote walikumbuke jambo la aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii sio nchi ya viongozi na wala haitajengwa na viongozi tu, ni nchi ya Watanzania wote na inatakiwa kujengwa na Watanzania wote. Pamoja na kwamba tuna kitengo cha kutoa elimu pale Mamkala ya Mapato, kinawakumbushia watu, lakini sisi kama Wizara tumeendelea kuongea na wenzetu wa Wizara ya Elimu kuuona umuhimu kwamba tunakijenga vipi kizazi cha nchi yetu tangu wakiwa wadogo waelewe masuala haya ya wajibu, uzalendo na masuala ya kodi na masuala ya kupinga rushwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hapa ndani tunawapongeza Wabunge ambao wameona taswira ya aina hiyo, Kalumbu Suma nilikusikia ukisema tunaonaje jambo la kodi hili lingewekwa kwenye Shule ya Msingi? Nimemsikia na ndugu yangu Mheshimiwa Kiruswa na wengine walileta kwa maandishi, nilipokea ya Mheshimiwa Oliver. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo ni kubwa. Nilipokuwa mdogo; sasa hivi nimekua kidogo, nilipokuwa mdogo zaidi, wakati tunasoma vile vitabu na kuelezewa na tukiwa tunazisikia nyimbo za wapiganaji waliotoka Vita vya Kagera, walikuwa wanatuimbia, “mimi Amini akifa, siwezi kulia. Wakatuonesha na vile vitabu vya kwanza, tunajifunza kusoma, vinaonesha Amini amebeba vichwa vya watu hivi. Katika umri ule nilijua kabisa kwamba yule bwana alikuwa anabeba vichwa, kama tunavyobeba maji vijijini, kwamba unabeba begani, kibuyu kingine kipo mbele, kingine nyuma. Kwa hiyo, niliimeza kama ilivyo kwamba huyu alikuwa anabeba vichwa vya watu hivyo. Kwa hiyo, nikaichukia hivyo na nilikuwa nimehamasika hivyo, kwamba huyu akifa siwezi kulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, ninachomaanisha ni nini? Watoto wetu tukiwaambia tangu wadogo wakaanza kuona ni aibu kukamatwa kwenye masuala ya kukwepa kodi, tangu wapo shuleni kama alivyosema Mheshimiwa Suma na ndugu yangu Mheshimiwa Kiruswa hapa, tangu wapo shuleni wakaanza kuona kwamba ukionekana unakwepa kodi ni jambo la aibu, yaani ni jambo la aibu kwenye familia yenu; ama mambo ya rushwa ni jambo la aibu kwenye familia yenu, wakajua wangali wadogo, Taifa litakalojengwa na kikazi cha aina hiyo, litakuwa bora sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa hatujafikia sana hatua hiyo watu kuona kukwepa kodi kama ni jambo baya, wala hatujafikia hatua hiyo watu kushiriki kwenye mambo ya rushwa kuona kama ni jambo la aibu. Hata wengine wangali wadogo wanadhania ni jambo jema. Kuna rafiki yangu mmoja ningali ofisini alikuwa anasema Taifa letu lina safari ndefu sana kwenye mambo ya rushwa. Mwanae alifanya mtihani kwenye shule moja binafsi ya kutafuta nafasi ya kujiunga na chekechea, madarasa ya awali haya ya chini, akakosa. Akawa anamwambia mama yake, yaani tumekosa hii nafasi mama, yaani hata ukiwapa fedha hawataniruhusu! Yaani bado yupo ngazi ile, anamwambia mzazi wake, hivi hata ukiwapa fedha hawataniruhusu! Maana yake hivi vitu vinaanza kujengwa tangu mwanzo kwamba unaweza ukavifanya tu hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili jambo kulifundisha kuanzia watoto wangali wadogo ni jambo ambalo linaweza likasaidia sana. Hivyo hivyo na nyimbo tulizokuwa tunaimba za ukombozi wa Kusini mwa Afrika zilituhamasisha tukaona kwa kweli Tanzania haiwezi ikawa huru kabla ya Mataifa mengine haya kuwa huru; hatuwezi tukasema tuna uhuru kamili kama South Africa bado haijawa huru. Kwa hiyo, hiki ni kitu ambacho ninaamini tutaendelea kukifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nilikuwa nasema tuongeze pia na elimu ambayo siyo technical issues; hii dhana ya kuteua mabalozi ilikuwa ni kuweka watu wa kuhamasisha waongee lugha ambazo wanaweza wakaongea kwenye masuala mengine ili waweze kuelewana vizuri. Kwa hiyo, hii kwa kuwa na wenzetu wa Wizara ya Elimu wanaendelea kurejea rejea mitaala, naamini tutaendelea kuangalia. Mbona somo la Uraia liliweza kueleweka vizuri kwenye mambo ya Multipartism, ninaamini hata hilo litaendelea kueleweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo imetolewa na imetolewa kwa uzito ambayo napenda nianze nayo, tumechanganua sana hizi fedha za TARURA na katika maelezo, tulisema zinakwenda kwenye mfuko. Mfuko wa Maji uko moja kwa moja unatambulika na chanzo kile kitatoka kitakwenda moja kwa moja kwenye Mfuko wa Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye TARURA tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge na wameelezea kwa kirefu sana kuhusu set up ya mfuko huu. Ndugu yangu Mheshimiwa Tabasam, ndugu yangu Mheshimiwa Kandege, Ndugu yangu Mheshimiwa Kakunda, ndugu yangu Mheshimiwa Kasalali Mbunge wa Sumve na nilimsikia Mheshimiwa Kyombo na Mheshimiwa Mwijage na Wabunge wengine wengi. Kama nilivyosema ni ngumu tu kutaja kila mmoja; lakini mlioliongelea jambo hili, tumelipokea na sisi tulivyokaa tukatafakari tukaona ni kweli muundo ule wa mwanzo ulikuwa unatumika kwa sababu kwa kweli TARURA ilikuwa inapewa lift. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha ile Ilianza kama ya Mfuko wa Barabara lakini badaye tulivyoona huku nako kuna tatizo tukasema hawa wapate lift, lakini mapendekezo yanayosema sasa kama tumeweza kubaini chanzo kikubwa kinachotakiwa kwenda kwenye TARURA, TARURA sasa haipaswi kuendelea kuonekana inapewa lift, ilhali ina barabara nyingi kwa urefu inazotakiwa kuzihudumia. Kwa hiyo, tumekubaliana na pendekezo hilo la kuanzisha mfuko rasmi wa TARURA na wataalam wangu walishike vizuri, wafanye haraka maboresho hayo tutengeneze Mfuko wa TARURA.

Vyanzo vyake Waheshimiwa Wabunge mridhie wataalam wetu waviweke vizuri, ni shilingi 100 ambayo tumeipitisha hapa na asilimia 30 ile iliyokuwa inatoka kwenye mgawanyo ule uliopita; na vyanzo vingine ambavyo vilikuwa vimebainishwa awali kama vyanzo vya Mfuko wa TARURA viweze kuelekea pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwepo na matatizo madogo ya hapa na pale, nakumbuka kwa mfano kuna kipindi kimoja fedha ambayo ilitakiwa ipelekwe TARURA Agosti na Septemba ilikawia mpaka ikaja ikapelekwa mwezi Februari. Kwa hiyo, hoja za Wabunge walizotoa zina mashiko, nasi kama Wizara hatuwezi tukang’ang’ania jambo moja peke yake; hapa tunatengeneza mambo ya nchi, siyo mambo ya Wizara yetu, ni mambo ya nchi nzima na Waheshimiwa Wabunge mmekuja hapa kwa ajili ya kufanya jambo hili liweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini taratibu nyingine zitafuatia ambazo zitalifanya jambo hili liweze kukaa vizuri zaidi, lakini mantiki yake na uharaka ambao Mheshimiwa Rais anataka miradi iweze kutekelezwa, hatupaswi kuacha kitu chochote hapa kinachotuletea ukiritimba ambao unaweza ukatucheleweshea utekelezaji wa miradi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo Mheshimiwa Kunambi aliuliza kuhusu sheria ile tunaposema tutaweka utaratibu mwingine; akauliza utaratibu ule ni upi? Utaratibu ule, tuliosema tunataka kutengeneza Ofisi ya Msuluhishi wa masuala ya kikodi. Kwa hiyo, siyo utaratibu ambao utakuwa siyo rasmi. Tunataka tutengeneze Ofisi ya Msuluhisi wa Masuala ya Kikodi na huu ni utaratibu ambao upo common.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza siku ile ni kwamba itatutengenezea utaratibu kwa wale watu ambao wanataka tu masuala ya kueleweshana waende kwa mtu ambaye wanaweza wakaona kwamba kidogo ni independent. Ilivyokuwa sasa hivi ni kama tayari tulishatofautiana. Hata kama tungekaa tena sisi ambao tulishatofuatuana ni dhahiri kwamba kuelewana kwake kungeweza kuwa na ugumu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea maoni mengine likiwemo swali la itakuwaje pale bei ya mafuta itakaposhuka? Tumelipokea jambo hili na kwenye Bunge hili Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Tabasam, Mheshimiwa Abood na Mheshimiwa Shabiby wametusaidia sana kwenye eneo hili la mafuta. Nami nawateua wawe washauri binafsi kabisa wa Waziri kwenye masuala haya ya uchumi wa gesi na mafuta; na Mheshimiwa Tabasam ongeza kabisa kwenye CV yako hii, kuwa wewe ni Mshauri wa Waziri wa Fedha kwa Masuala ya Uchumi wa Gesi na Mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwa sababu utaratibu unaotumika sasa hivi ni wa bulk procurement ambapo tunaagiza mafuta kwa wingi kwa ujumla, lakini pia kuna administrative measures ambazo zinafanyika na EWURA. Tunaomba Wabunge waridhie hili jambo tulipokee kwanza, tulifanyie kazi ndani ya Serikali, halafu tuweze kuona kule mbele tunapokwenda. Tukiweka mabadiliko mengi kwa wakati mmoja na kwa wakati mfupi mfupi, alignment zake wakati wa utekelezaji inaweza ikatupatia shida kati kati yake. Waridhie, hii siyo bajeti ya mwisho, panapo uzima, Bunge litaendelea, tutakuja tena kushauriana yale ambayo tumeyapokea muda ukiwa umeshafika tuyafanyie kazi. Tujipe muda huu tuweze kuyarekebisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea hoja nyingi na nyingine tayari tulishaweka ile budget framework, tulishaweka mahesabu yetu na makadirio upande wa mapato na makadirio upande wa matumizi. Kwa maana hiyo, tukifumua tukaweka vyanzo vingine vya mapato na vikatuletea mapato mengi, tutakuwa tunalazimika turudi tena kule ambako utaratibu wetu wa kikanuni hata hauruhusu kwenda kufumua ambacho tulishapitisha kule. Kwa hiyo, nawaomba mridhie kwamba maoni mengine ni mazuri, tunayapokea, basi tutayafanyia kazi kwa sababu tayari tulishapitisha bajeti kuu ambayo tumeshapitisha na appropriation yake ambayo inatulazimu mambo mengine yakae ndani ya vile ambavyo tayari tulishavipitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo liliulizwa, ameuliza Mheshimiwa Maige pamoja na Wabunge wengine. Nimemsikia nadhani na Mheshimiwa Kunambi na wengine wengine wengi, naomba wananchi wenu waridhie tu kwamba ni ngumu kumtaja kila Mbunge, lakini mmechangia hoja za msingi kabisa kwamba tutafanyaje fedha ya Luku kwa mtu ambaye angetaka kulipa mara moja? Vile vile tutafanyaje kwa sehemu ambayo mmiliki anataka kulipa yeye mwenyewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, jibu lake kama nilivyosema awali, jambo hili tunalifanyia programming; kama ambavyo umeme huwa ukileta hitilafu, tunawaona wale wale TANESCO, umeme ukileta hitilafu nyumbani huwa tunawona, wapo miongoni mwetu, huwa tunawaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwa na jambo linahusu suala hili la utozaji wa property tax kwa njia hii ya Luku, ukaona kuja jambo unataka kulifanya, unawaona tu wana-program vile unavyotaka. Kwa maana hiyo, kama unataka iwe inalipwa mara moja, inakuwa programed kwamba inakatwa mara moja na haitakatwa tena. Kama unataka iwe programed mwanzo wa mwezi, itakuwa programed; kama unataka iwe programed kwa mgawanyo kufuatana na idadi ya hizo mita, hivyo ndivyo itakavyofanyika. Hivyo ndivyo teknolojia inavyorahisisha masuala ya utendaji wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo na kwa yule ambaye atataka alipe yeye mwenyewe, tumesema hawa watu hakuna mita ambayo haina mahusiano kabisa na mwenye nyumba, wala hakuna mita ambayo haitakuwa na uhusiano kabisa kabisa na wale waliopo, wala hakuna mita ambayo mtu atakuwa anaishi hana mahusiano kabisa. Hizi nyumba ni tofauti na vichuguu, wale wanaoishi mule anayetaka anaingia tu, kama kipo wazi unaingia. Hapa kuna arrangement nyingi tu. Kubwa ambalo kila mtu tumesema lazima alizingatie, ni kwamba hii ni sheria ya nchi. Hili ni jambo la kisheria. Kwa hiyo, maelezo yake hapo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwa maghorofa yaliyo mengi, utaratibu wake ni ule ule; na tukawepa pia kwa wale ambao hawatakuwemo kwenye huu mfumo wataendelea kutumia utaratibu ule ambao ni manual ambapo wataweza kukutana na wenzetu wa Serikali za Mitaa ambao tumewapa jukumu la periodic na sport maintenance ya barabara zetu ambapo tunaamini baadhi ya vyanzo vya mapato ambavyo wataendelea kuvipata wataongezea na hicho ili waweze kutekeleza utaratibu wetu wa kutengeneza hizo barabara kwa vipindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine ambalo lilitolewa upande wa masuala ya boda boda. Maoni mapya aliyoyatoa Mheshimiwa Lugangila tunapokea na hiyo tutaongea na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ambao ndiyo wenye sheria, kuangalia siyo tu kwa boda boda, ni kwa vyombo vyote vya moto. Hiyo ni standard ambayo inaweza ikatumika kwa dereva ambaye amesharudia makosa ya aina ile ile kwa kipindi kirefu, hivi ataendelea kutozwa faini tu? Hiyo tutaiangalia tuweze kuona utekelezaji wake hata huo utaratibu uliopendekezwa wa kutumia points. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo nchi ambazo zinatumia utaratibu wa aina hii, lakini hili la kusema faini ikipingua kwamba kutoka shilingi 30,000/= mpaka shilingi 10,000/= kwamba vifo vitaongezeka, Waheshimiwa Wabunge kwa mtu yeyote akitusikiliza kwenye hiyo hoja, lazima aone, basi kama Taifa tutakuwa na shida kubwa sana. Tukiwa na Watanzania wanaogopa faini kuliko kifo, basi tuna tatizo moja kubwa sana la msingi, kwamba yeye kinachoweza kumfanya awe mwangalifu ni faini peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema ajali zinaua au uzembe unaua kwake yeye haliingii sana akili, kwamba yeye busara hiyo haioni, anaona faini ndiyo inaweza ikamfanya akaogopa sana faini ikiwa kubwa kuliko kifo, kuliko maisha ya wale waliowabeba, akaithamanisha sana shilingi 20,000/ = ile kwamba ningelipa shilingi 20,000/= hawa ningewafikisha salama. Ningeongezewa na hii ikawa shilingi 30,000/= hawa ningewafikisha salama, kuliko thamani ya maisha yao wenyewe wale aliowabeba, basi kutakuwa na tatizo kubwa sana la msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoamini, kwanza ukifanya tathmini ya wakati boda boda zinaanza kuingia hapa Tanzania na sasa, pana tofauti kubwa sana. Tunakwenda tunabadilika. Mwanzoni ilikuwa kawaida sana, huyu kijana asubuhi tu hapo anakabidhiwa boda boda kwa mara ya kwanza, anapiga route moja mpaka getini pale na kurudi, anabeba abiria. Sasa hivi wameendelea kutengeneza vikundi vyao na uongozi wao na wanaendelea kuelimishana wao wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshiwima Wabunge, kwa sababu hawa boda boda wako majimboni kwetu, kila kijiwe tunao na wale viongozi wetu, hata sisi, hebu tutumieni muda kuwaita hata wasiwe wote, tuwaite hata wale viongozi tu wa boda boda kwenye maeneo yetu. Tuwaite na tuwaambie neno moja tu kwamba jambo hili mnalofanya siyo la kibiashara pale yake, mnabeba uhai wa watu. Mnabeba maisha ya watu, lakini hata ninyi mnategemewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja tumewahi kwenda pale Jimboni kwangu kuongea na baadhi ya vijana humo, wakasema tunaelewana. Nimewahi kuzungukia na maeneo mengine, wakasema tunaelewana. Wakati mwingine zile stress na zenyewe za kukimbizana kwa ajili ya faini hizo na zenyewe zilikuwa zinasababisha ajali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi ninaamini, twendeni tuongeze elimu ya kusisitiza; wapite kwanza mafunzo kwamba awe ameshakuwa dereva anayeweza kuendesha, lakini pia mafunzo ya uungwana tu yale ya ustaarabu kuweza kuona kwamba amebeba maisha ya watu. Hili na lenyewe lipo ndani ya uwezo wetu na tunaweza tukafanya, tusiwaachie Polisi peke yake, hata sisi tunao uongozi kwao tuwaambie.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwaelezee hata wenzetu wa Tawala za Mikoa kule kwenye vikao vyao upande wa Madiwani kila Kata, ni eneo dogo tu. Diwani akitaka kuongea na vijiwe vyote vya boda boda anaweza akaongea nao, awaambie na wenyewe waendelee kukumbushiana; na viongozi wengine waliopo ngazi hizo waendelee kuwakumbushia. Hili ni jambo ambalo tunaweza tukalifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilichokuwa kinasomeka, hakileti picha nzuri sana na ndiyo maana Mheshimiwa Rais aliona alisemee siku ile, kwamba hata tunapotoa makadirio ya mapato yetu, tunapotoa taarifa kwamba makusanyo yetu yalifanikiwa kwa kiwango gani, tunasema makosa yalipungua, kwa hiyo, hatukuweza kufikia lengo. Hii kiuchumi haileti taswira nzuri sana kuweka malengo kufuatana na makosa. Kwamba hawakukosa sana, kwa hiyo, hatukufikia malengo. Haisomeki vizuri sana hii. Pamoja na kwamba kifo kipo tu, ni sawasawa na biashara ya mtu alalamike kwamba siku nzima leo majeneza yangu hayakutoka. Haileti picha nzuri sana kwamba kusema majeneza yangu hayakutoka, kwa hiyo, leo biashara yangu haikuwa nzuri kabisa. Kwa hiyo, hivi ni vitu ambavyo tunaweza tukavifanya kwa kutumia elimu na bado tukaweza kupiga hatua nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii haisomeki vizuri sana, ni sawasawa na biashara pamoja na kifo kipo tu, ni sawasawa na biashara ya mtu alalamike kwamba siku nzima leo majeneza yangu hayakutoka, haileti picha nzuri sana kwamba majeneza yangu hayakutoka, kwa hiyo leo biashara yangu haikuwa nzuri kabisa. Kwa hiyo hivi ni vitu ambavyo tunaweza tukavifanya kwa kutumia elimu na bado tukaweza kupiga hatua nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kanyasu ameongelea suala la nyasi bandia; niwaelekeze tu wataalam wangu kwa sababu Mikoa isiyo Manispaa ni mitano nadhani Simiyu, Geita, Njombe, Katavi na Manyara. Nadhani ni mikoa mitano ndiyo ambayo ni mikoa mipya ambayo imeongezeka ambayo si Manispaa. Wakati nasoma hapa nilisema tutaweka provision kwa ruhusa maalum kwa maeneo mengine ambayo yako tofauti. Kwa ushauri wa Mheshimiwa Kanyasu tutaongezea tu na Makao Makuu ya Mikoa ambayo haijawa Manispaa ili iweze kusomeka hivyo ili iweze kujumuisha na mikoa ile ambayo siyo manispaa wala siyo majiji, lakini ilishafikia hatua ya kuwa mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni mengine tumeyapokea, kama hili alilolisema Mheshimiwa Kanyasu tumefanya kwa upande wa hospitali lakini bado kwenye shule, tunaomba mridhie na lenyewe tulipokee tuendelee kulifanyia kazi zaidi kwa sababu kwa sasa tumeshaweka fremu yetu ya mapato na tunaamini kwamba haitakuwa vizuri sana tukifanya muda huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Tadayo aliongelea kuhusu TRA kuendelea na masuala ya elimu ya mlipakodi tumepokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kigwangala aliongelea habari ya kodi ya majengo nimetoka kulifafanua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ali King pamoja na ndugu yangu ambaye ametoka kumalizia amesemea habari ya upande wa Zanzibar. Tulisema yale marekebisho tuliyoyafanya, yale marekebisho tumeyafanya, tena tumeyafanya kwa kushirikiana pande zote mbili. Nilikutana na Mheshimiwa Waziri wa Fedha wa Zanzibar akiwa na timu yake ya wataalam na mimi nikiwa na timu yangu ya wataalam, tukayarekebisha yale ambayo tuliyarekebisha na kwa mwaka huu tukakubaliana tuanzie hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka tumeanza kazi tukiwa tayari Mabunge ya Bajeti yanaendelea kwa maana hiyo kazi ya kwanza ambayo imebidi tuje tuifanye ilikuwa ni ya kuandaa nyaraka hizi za bajeti. Tumepanga kuendelea kukutana kuangalia mengine ambayo bado yanaleta manung’uniko, baada ya bajeti tutaendelea kufanyia kazi mengine. Inakuja sheria hii ambayo ilikuwa inaleta usumbufu wa vyombo vya moto kutoka upande mmoja kuja upande mwingine, tunalifanyia kazi na tutakuja na jawabu la kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaenda kwenye lile jambo kubwa zaidi la mambo ya Mfuko wa Pamoja, tunataka tujue kwanza numbers zinasemaje kwa sababu eneo moja la kuanzia nadhani ni pale kwenye numbers, zinasemaje kwenye yale mapendekezo ambayo mara zote yamekuwa yakiongelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu haya ya mapato ambayo pande zote ziko mbili; tunatumia sheria ile ile ambayo ipo, kwamba, kama ambavyo tunatumia kwenye exercise ya sasa hivi, kwamba fedha ambazo zinakatwa pale zilipotokea ndipo zinakotumika kama tulivyofanya kwenye masuala ya uhamiaji, pale zinapotokea ndipo zinapotumika. Hii ni rahisi tu, kama mtu anatuma M-pesa yuko Zanzibar na tukakata maana yake fedha ile iko pale pale. Kama aliyetoa yuko pale pale na tunakata fedha ya kutolea, maana yake iko pale pale. Kwa maana hiyo na mitambo ambavyo inarahisisha maana yake lile halina tatizo kabisa, fedha zile ambazo zimetumwa ama kutolewa kwa upande wa Zanzibar zitatumika pale Zanzibar na zile ambazo zimetolewa Bara ama kutumwa Bara zitatumika Bara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, kwa heshima na itifaki ya mamlaka, kitu pekee ambacho hatuwezi tukafanya ni kuzipangia fedha zile ambazo zimepatikana kwa upande wa Zanzibar zitumike wapi, ile ni mamlaka na wenyewe watapangia ziweze kutumika wapi. Hili ni jambo ambalo tunaweza kulifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Waheshimiwa Wabunge, nina matarajio kwamba tunaenda kukusanya fedha, tutapata fedha. Naendelea tu kulisisitiza hili jambo, ndiyo maana sikubishana sana na Waheshimiwa Wabunge wakati wanatoa maoni tuzitumieje hizi fedha, tuzilinde vipi hizi fedha na ndiyo maana niliona tutumie hayo mawazo kwa sababu fedha hizi ni za wananchi na uamuzi huu tumeufanya pamoja, kwa hiyo twendeni tukasimamie. Naamini tutakapokuwa tumefanya jambo hili, tutafungua uchumi na kadri tunavyofungua uchumi kwa kufungua barabara, kwa kufungua masuala ya huduma zingine za jamii, naamini uchumi wetu utaendelea kupanda na tukishatoka hapo tutaenda kuyafanyia kazi mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mawili ya mwisho kama utaridhia dakika mbili zako, jambo la kwanza ni hili ambalo lilijitokeza la upande wa hii transfer mispricing, ambayo tulikuwa tunaiongelea hii transfer pricing.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitoka kwa ajili ya kuwahi kuja kupokea hoja hapa, lakini Kamati pamoja na wajumbe waliokuwepo kule, makubaliano waliyofikia ni kufanya mabadiliko. Kwenye pendekezo tulilokuwa tunapendekeza kuweka asilimia 75, wanapendekeza iwe asilimia 100 ya kodi iliyotakiwa kutozwa. Kwa maana hiyo kodi itakuwa imezidishwa mara mbili ya ile ambayo ilitakiwa itozwe kama huyo mtu hakuikwepa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali kama nilivyosema, tunapokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge na Kamati ni mwakilishi wa Bunge, wamependekeza hilo pendekezo. Kwa hiyo hicho ndicho ambacho wataalam wangu watakiandika kama Kamati ya Bunge ilivyopendekeza, marekebisho hayo yaingie kama yalivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja la mwisho, imeongelewa hii habari ya Withholding kwenye kilimo na naomba na Waheshimiwa Wabunge tusikilizane vizuri sana kwenye jambo hili. Hiki ambacho tumekipendekeza hakiendi AMCOS wala hakiende kwa mkulima mdogo na withholding nature yake jinsi ilivyo, yule ambaye anatozwa hii kodi, huyu mtu wa kati anayeshughulika kwenye hiyo biashara, mwisho wa siku anai-recover ile fedha kama hakustahili kuilipa kupitia yale mapato yake, ana-offset, atakuwa tu ni yule ambaye atakuwa bahati mbaya sana akitaka kuipasisha iende kwa mkulima. Kwa sababu hii hapa ina kuwa sehemu wakati ana calculate yeye kodi zake za mwaka, inakuwepo, ndiyo nature ya withholding tax zinavyofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kitu tulichopendekeza NFRA na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wana withholding hiyo ya 2% hiyo hiyo. Tulisema kama hawa wanafanya biashara eneo lile lile na soko lile lile, kwa nini NFRA wanafanya na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wanafanya na hawajawahi kuathiri wakulima wetu na hata wakulima wote huwa wanapenda mazao yao wauze NFRA, tuliona tunaweza tukawianisha ili tuweze kuendelea nalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu ni vile muda huu ulikuwa mfupi sana, nikiri kwamba hatukufanya mengi zaidi kwenye sekta hii ya kilimo tumekaa na wenzetu wa Kilimo pamoja na Mifugo, tukasema kwa kuanzia tuanze na bajeti zilizokuwepo, lakini pia tuanze na maeneo tunayoweza kuchochea masuala haya ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, safari tuliyonayo kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni ndefu sana. Ni safari moja ndefu sana na siku tuki-mechanize production kwenye kilimo mifugo na uvuvi nchi yetu hii uchumi wake ukanda huu wa Afrika labda tutakuwa tunapambana na South Afrika sijui na nani mwingine, kuna kazi kubwa sana tunatakiwa kufanya. Kazi hii lazima tufanye tathmini ya measures tunazofanya kwenye kilimo, mifugo na uvuvi, zimesaidia kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, angalia tangu tuanze kukata hizi tozo, tufanye comparison tujue kwanza tozo hizi ambazo tumewahi kuziondoa hivi zina amount kiasi gani na je, zimesaidia kwa kiwango gani? Nilimsikia Mheshimiwa Spika siku moja akiwa amekaa pale nadhani siku ya Bajeti ya Kilimo, akawa anajiuliza tu swali fikirishi, hivi hii bajeti hata kama ingeenda yote hivi ingemfikiaje mkulima, alikuwa anajiuliza hivyo. Swali linabaki pale pale hizi measures tunazofanya kwenye hii Sekta kubwa hizi za Kilimo, Mifugo na Uvuvi hivi ni kweli zime-transform hizo sekta?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukirudi ukaangalia ni nini kinachotakiwa jibu linakuja siyo. Moja, ili kilimo chetu tuki-transform na tunakaa sana vikao vingi na Wizara ya Kilimo, Mwalimu wangu Prof. Mkenda pamoja na Mheshimiwa Bashe, tunawaza tukibadilishie wapi hiki kilimo. Maeneo ambayo tunatakiwa tuguse ili kiweze kubadilika kilimo, mifugo na uvuvi kwa kiwango kikubwa bado tunahangaikia huku kwenye administrative issues, kwa maana hiyo panakazi kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge waridhie, kwa sasa hivi na kwa muda tulionao tuendelee kwa sababu tumesha-fix tax measures zetu pamoja na makadirio, lakini waturuhusu sisi tumesema tukimaliza tu hivi tunaanza kujiandaa kuhusu hizi sekta. Siku tuki-transform, sasa hivi nikiwa namalizia tu neno la mwisho, ukienda kule vijijini kazi hii ya kilimo inafanywa tu na wazazi wetu na babu zetu, hiki kizazi cha leo hakifanyi kwa sababu uzalishaji unaotumika ni wa zamani. Graduates wengi hawawezi wakafanya shughuli ya uzalishaji uliokuwa unafanywa na bibi zetu, wanahitaji tutengeneze mechanization ambayo watazalisha kisasa na watakopesheka kwenye mabenki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuna kazi kubwa sana. Wabunge waridhie, tutakuja na mapendekezo huku tuki-implement kidogo kidogo haya ambayo tumeshaongea na wenzetu wa Wizara ya Kilimo pamoja na ile ya Mifugo na Uvuvi, kuna kazi kubwa sana tunatakiwa kufanya hapa. Tunaongea hata na Wizara ya Maji kwamba kuanzia sasa miradi mikubwa watakayo-design kama ni mradi wa kutoka Ruvuma kwenda baharini yaani miradi yote ya kwenye mito mikubwa inayomwaga maji baharini waki-design mradi mkubwa wa maji kwa matumizi ya nyumbani waweke na matoleo kwa ajili ya maji ya umwagiliaji, ili siku tukitaka kutengeneza umwagiliaji tusihitaji kulaza bomba lingine. Tuna kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu ambao wananchi kame wanamwagilia, lakini sisi bado tunahangaika na zile administrative. Ukiangalia hatua zilizokuwa zinatumika, kuna wakati tulikuwa tunasema watu wakikosa chakula tunawapelekea chakula cha msaada, hii haikuwa sustainable. Kuna muda tukasema watu wakikosa chakula hatutawapa, hii na yenyewe siyo sustainable, iliyo sustainable, kama wakilima mara moja wanakosa chakula tuwafanye walime mara mbili na wavune mara mbili ili waweze kupata kile chakula. Kwa hiyo haya ndiyo mambo ambayo tunataka tuangalie tunaweza tukayafikia kwa namna gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa, niwatakie kila la kheri Mheshimiwa Mwakasaka, Mheshimiwa Bashe na Mheshimiwa Gulamali, tuna jambo letu kule Tabora. Hebu waende wakafanye kazi ile ya ukombozi ambayo iliwahi kufanywa na Chama Cha Mapinduzi na TANU pamoja na timu ya Yanga ambao walishiriki kuikomboa Tanzania pamoja na Nchi za Kusini mwa Afrika. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa nimeyasema hayo, naomba sasa kutoa hoja ili shughuli zingine ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu wa Mwaka 2022
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kukushukuru wewe binafsi na Wenyeviti, kwa kuendesha mjadala huu kuhusu Muswada wa Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu kwa kiwango kizuri sana. Napenda kutambua michango iliyotolewa na Kamati ya Bajeti ambayo imewasilishwa hapa mbele yako, chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Daniel Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini. Michango ya Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza na kwa maandishi nawashukuruni sana. Kama alivyosema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tumefanya kazi vizuri ya Kibunge ya kutunga sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nichukue fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Jaji Eliezer Mbuki Feleshi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa kufafanua vizuri hoja mbalimbali zinazohusu Muswada huu. Aidha, nitumie fursa hii pia kumshukuru na kumpongeza Naibu Waziri wa Fedha Mheshimiwa Chande kwa ufafanuzi wake, lakini pia na yeye kwa ushiriki mkubwa katika utengenezaji wa Muswada huu. Aidha, nimshukuru sana Bwana Njole, Mwandishi Mkuu wa Sheria na wataalam walio chini yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na wataalam wengine wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri sana waliyoifanya usiku na mchana, kwa kushirikiana na wataalam wengine ambao wako chini ya Taasisi hii. Pamoja na kiongozi wa Taasisi hii kwa michango yao na kazi kubwa ambayo wameifanya, katika kupokea michango ya Waheshimiwa Wabunge na kutayarisha majedwali mbalimbali ya marekebisho na majibu mbalimbali ya hoja za Wabunge. Nawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza awali nafarijika sana kwa michango mizuri iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na nitaeleza tu kwa muhtasari, mengine tumechukua kwa sababu imetolewa kama ushauri. Nikianza na michango iliyotolewa na Kamati yetu; Kamati imeongelea suala la bajeti na suala la kuongeza nguvu kazi pamoja na masuala ya mafunzo. Tumepokea maoni hayo pamoja na mengine waliyoyatoa, tutaendelea kuyafanyia kazi, likiwepo suala hili la bajeti ambalo tayari Serikali ilishaanza kulifanyia kazi. Mfano, tayari Serikali iliongeza takriban Shilingi milioni 568 ili kuwezesha shughuli hizi ziweze kufanyika vizuri. Hivyo hivyo na suala la Taasisi kuongezewa watumishi tumelipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingine ilitolewa kuwa Taasisi hii ipewe hadhi ya Wakala. Tumepokea ushauri huu, lakini pamoja na hivyo nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba, pamoja na hali ilivyo sasa ya Taasisi hii, Taasisi hii inafanya kazi kikamilifu. Ukienda kwenye viwango vya ufanyaji wa kazi wetu sisi bado tuko vizuri ukilinganisha na nchi zingine zinazotuzunguka katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki pamoja na huku SADC. Hata kimuundo karibu nchi nyingi kama sio zote zinatumia utaratibu huu huu wa kuwa unit na tunatofautiana tu, kuna baadhi ya maeneo Taasisi hii inaripoti kwa Waziri wa Fedha na baadhi ya maeneo ni Taasisi ambayo inaripoti moja kwa moja Ofisi ya Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hoja nzuri hizi kuna hoja zingine ambazo ningetamani nifafanue hata kidogo tu. Kuna hoja moja aliitoa Mheshimiwa Halima Mdee wakati anachangia. Kwa kweli wakati namuona kwenye screen, niliona leo Halima Mdee amependeza kuliko siku zingine. Hata nilipomuuliza Naibu Waziri Mheshimiwa Geophrey Pinda akasema na yeye anamuona hivyo hivyo na Naibu wangu akasema hivyo hivyo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati anachangia aliweka neno kwamba, Serikali baada ya kutumwa na mabosi wao kwamba imetumwa na Wazungu. Kwanza niseme kwamba Tanzania ni nchi huru haina bosi. Hakuna mabosi wanaoituma Tanzania, wala hakuna Wazungu wanaoituma Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina wajibu na wajibu huo umetimizwa vizuri sana na kiongozi wetu, Rais wa nchi yetu mama yetu, mama Samia Suluhu Hassan kwa kutumia utashi wa kiuongozi na kutoa uongozi, kwamba, nchi yetu ina wajibu wa kulinda heshima yake, wala sio kwa kutumwa, ina wajibu wa kulinda heshima yake na hicho ndicho Rais alichokifanya. Kwa Rais wetu hili sio jambo la kwanza ambalo amelifanya ambalo linalinda heshima ya nchi yetu. Tayari ameshatimiza wajibu huo katika kuitengenezea Tanzania taswira njema sana, ya masuala ya kidiplomasia na masuala ya Kimataifa. Tayari ameshatengeneza ramani bora sana ya kuwahakikishia wawekezaji kwamba Tanzania ni destination bora sana kwa uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari ameshatengeneza taswira bora sana kwamba Tanzania ni nchi inayojali utu, Tanzania ni nchi inayojali demokrasia na Tanzania ni nchi ambayo inalinda watu wake na mali zao. Kwa hiyo, haya yote anayafanya kwa kutoa utashi wa kiuongozi na kutoa uongozi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wale ambao wamempongeza Mheshimiwa Rais wamefanya, jambo jema sana na Mheshimiwa Rais ameyafanya haya kwa maeneo mengi sana tofauti tofauti na wala sio hili tu. Jambo hili Mheshimiwa Rais ameona ni vyema likafanyika kwa sababu mambo haya ambayo yanahusisha utakatishaji wa fedha yanazingatia sana chanzo cha fedha hizo ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkifuatilia katika maeneo mengi vyanzo vya fedha zinazoweza kutakatishwa inaweza ikawa either fedha hizo zinatokana na biashara ya madawa ya kulevya. Sasa ubaya wa biashara ya madawa ya kulevya na athari za madawa ya kulevya wala huhitaji mzungu, wala bosi yeyote kukwambia ni utashi wa kiongozi ulio bora kama alivyofanya mama yetu, mama Samia Suluhu Hassan. Si hiyo tu fedha zinazoweza kutakatishwa zinaweza zikawa zimetokana na rushwa, ama matumizi mabaya ya madaraka. Hili nalo huhitaji mzungu yeyote kwa nchi kama Tanzania ambayo ina kiongozi anayesimamia maslahi ya wananchi wake, haihitaji bosi yeyote kukwambia. Yeye amefanya hivyo kwa sababu ana nia njema na nchi yetu na ameyafanya haya katika maeneo tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hayo tu, kuna maeneo mengine mengi ambayo Mheshimiwa Rais amefanya, ambayo yanalenga kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na heshima na inasimamia yale ambayo ni standard ambazo zimewekwa. Kwa hiyo, kuhusisha kwamba watu wa mataifa mengine wametoa neno, hizo ni standard tu ambazo ziko katika maeneo mengine mengi. Rais wetu ameona ni jambo jema kuzitimiza standards kama hizo, ili heshima ya nchi yetu iendelee kuwa katika nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania mara zote imekuwa nchi ambayo inaheshimika na nchi ambayo inatolewa mifano iliyo bora. Mama yetu, anaona mbali sana na ameshafanya mambo mengi ambayo yanaonyesha tofauti na mengine nyinyi wenyewe Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi. Hata katika masuala ya ndani ya nchi tu ambayo yanahusisha utekelezaji wa bajeti karibu mikoa yote sasa hivi tunavyoongea, mingine imeshapokea zaidi ya asilimia 100 ya fedha ambazo ilikuwa inazihitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,Nilikuwa naongea na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wakasema kwenye jimbo letu huku, kwenye wilaya yetu huku kwa kweli kuhusu masuala ya fedha hatuna hoja. Hayo ni mambo ambayo mama yetu anayafanya kwa kutoa uongozi katika Taifa letu. Tuendelee kumwombea na tuendelee kumuunga mkono ili aendelee kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania, kwa kuifanya nchi yetu ionekane kwenye ramani na isomeke kwenye heshima yake inayostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ilikuwa Serikali iandae sera ya kusimamia masuala ya fedha haramu. Kama ambavyo nimesema jambo hili halijafanywa kwa kukurupuka, ni jambo ambalo Serikali imelifanyia kazi na kwa kutambua umuhimu wake ndivyo maana umeona kwamba limeletwa kwa hati ya dharura. Kuletwa kwa hati ya dharura sio kwamba jambo hili limeletwa kwa kukurupuka, ni jambo ambalo limefanyiwa kazi ila uzito wake ndio uliosababisha lifanyiwe kazi kwa uharaka kwamba lipitishwe ili liweze kuanza kutekelezwa. Kwa hiyo, kwa upande wa sera ya kusimamia masuala ya fedha haramu Mheshimiwa Rais alishatuelekeza mapema sana kuanzia alipokuwa anatutuma haya majukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hilo la sera tayari linafanyiwa kazi na wadau mbalimbali wanaendelea kushirikishwa na tunaamini ifikapo Machi kwenda Juni, tutaliarifu Bunge lako Tukufu hatua ambayo itakuwa imekamilika na tunaamini kwamba tutakuwa tunakwenda kwenye kuwatangazia Watanzania kwamba hiyo sera sasa iko tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mafunzo kwa watoa taarifa kama nilivyosema, bajeti yake ipo jambo hilo litaendelea kutolewa taarifa hizo. Kadri ambavyo umuhimu huo utakuwa unafanyika mafunzo hayo yataendelea kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lilisema Serikali iboreshe mifumo ya taasisi zinazosaidiana na utambuzi, sambamba na yale masuala ambayo ameyasema kwa nguvu Mheshimiwa Kwagilwa, Mbunge makini wa Handeni pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine ambao nimewasikiliza wakisema jambo hili na wale wote ambao wamechangia kuhusu masuala ya vitambulisho kuwa vingi. Jambo hili pia Mheshimiwa Rais alilitolea maelekezo mahususi kabisa.

Sambamba na kuwa na mifumo inayosomana, sambamba na kuwa na mifumo ambayo ipo harmonized. Mifumo ambayo imewianishwa ili kuwa na mfumo mmoja ama mifumo inayosomana ambayo inaweza ikafanya kazi pamoja. Kwa hiyo, jambo hili na lenyewe linaendelea kufanyiwa kazi na tayari hivi tunavyoongea, kitambulisho cha Taifa kimeshaanza kutumika katika maeneo tofauti tofauti. Ili kuweza kupunguza mtu kuulizwa taarifa hizo hizo katika maeneo tofauti tofauti atakayokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili mifumo itakapokuwa inasomana maana yake rejea za taarifa zitakuwa rahisi sana na jambo hili linaendelea kufanyika, hata katika maeneo mengine ambayo yalikuwa yanahusisha mtu kwenda ofisi zaidi ya moja na kuweza kuulizwa taarifa zinazofanana. Hili na lenyewe Mheshimiwa Rais alilitolea maelekezo mahususi na sisi kama Wizara, pamoja na Wizara zingine zote ambazo zinahusishwa na jambo hili, tunaendelea kufanyia kazi na tunaamini litakamilika na litaweza kuwa na msaada kwa wananchi wetu kupunguza matatizo ambayo yanaweza kujitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya viashiria hatarishi na gharama zake amelisema Dkt. Kimei. Masuala haya yote yamefanyiwa consideration na viwango vyake na masuala ya mapitio yatakuwa yanafanyika kuhusu viashiria. Kwa upande wa Serikali imejipanga vizuri kuangalia masuala hayo ya assessment, itafanya mapitio kila baada ya miaka mitatu. Watoa taarifa wataandaliwa na kuweka taratibu, ambazo zitakuwa zimekuwa-shared nao kuhusu masuala haya ya mapitio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge kama ambavyo umekiri, nyingi tumekuwa tumeshakubaliana kati ya Serikali na Kamati kwa niaba ya Bunge. Kama ambavyo Mheshimiwa Rais ametoa muongozo wa namna ya kufanya kazi hizi kwa kushirikiana, Wizara imekuwa bega kwa bega ikishirikiana na Kamati. Ndio maana unaona katika vitu vyote vinavyohusisha Wizara na Kamati mara nyingi, tunafikia muafaka kwa sababu kazi hiyo ni moja na tunafanya kwa niaba ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru tena wewe mwenyewe, Waheshimiwa Wabunge wote waliotoa michango na kuboresha Muswada huu. Nawashukuru tena na wale wengine wote ambao walitoa michango ya kuandika na wale wote, ambao wamesisitiza maeneo ambayo tunatakiwa tuyafanyie kazi huko tunakokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameongea vizuri sana mwananchi mwenzangu Mheshimiwa Abbas Tarimba pamoja na wengine. Yale ambayo yatahitaji kufanyia kazi baada ya kuwa tumeshapitisha Muswada huu tutaendelea kuyafanyia kazi, ili kuweza kuhakikisha kwamba vipengele vingine ambavyo vitafanya Muswada huu ufanye kazi vizuri vinatimia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alishasema na leo Attorney General amerudia kwamba, Sheria nzuri sana ni ile iliyoandikwa moyoni. Ile iliyoandikwa moyoni ndio Sheria iliyo nzuri sana. Sheria pekee ikiwa nzuri kama wale watekelezaji hawatendi haki, Sheria ile haitakuwa na manufaa kwa wananchi. Kwa maana hiyo, hivi vingine vyote ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamevisema ambavyo vinahusu kutenda haki, kiongozi wetu ametoa dira na mmeona kwa vitendo vile vitu ambavyo anavifanya ambavyo vinazingatia ulinzi wa haki za watu. Kwa hiyo, Watanzania pamoja na Waheshimiwa Wabunge wasiwe na mashaka tuko katika mwelekeo sahihi, tuko katika kasi iliyo sahihi na tunaamini tutafika pazuri ili wananchi waweze kupata ustawi mzuri katika maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa nimeyasema haya, nakushukuru sana na naomba sasa kutoa hoja.

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2023.
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kuhitimisha hoja ambayo niliwasilisha leo asubuhi. Awali ya yote niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa hoja walizozitoa na niwahakikishie kwamba kwenye hoja hii hakuna pande mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hoja hii Serikali pamoja na Wabunge tunaongea lugha moja. Kuanzia tulivyoenda kwenye Kamati tuliwaambia position ya Serikali kwamba tunataka tutunge sheria itakayotibu matatizo yanayoikabili nchi hii kwenye masuala ya manunuzi.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Wabunge wametoka kuchangia na nikimnukuu Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni, jambo hili Mheshimiwa Rais aliahidi kwanzia kwenye hotuba yake kwamba atafanyia marekebisho sheria zozote zile ambazo zinatukwamisha kuweza kupiga hatua, kwenye hotuba ya Bajeti ya Serikali ya mwaka huu tulitoa ahadi hiyo kwamba tutarekebisha Sheria ya Manunuzi, tutarekebisha Sheria ya Ubia Kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma. Sheria ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma ilishapitishwa na Bunge na ilishasainiwa na leo hii tukaileta hii kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliahidi katika baadhi ya hotuba zake na ambavyo tulileta katika Bajeti Kuu ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yale ambayo Waheshimiwa Wabunge wamesema, naomba nitoe ufafanuzi moja baada ya lingine. Kama ambavyo nimesema hii si sheria ambayo tuna ubishani nayo kwa sababu lengo ni kuwawezesha Watanzania na lengo ni kuwezesha shughuli hizi za masuala ya manunuzi zifanyike kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikianza na hoja aliyoitoa Mheshimiwa Eric Shigongo, ameweka kwenye pendekezo lake na ameongea kwa hisia kuguswa kwake kuhusu suala la wazawa. Hii ni concern ya Serikali kuhakikisha kwamba wazawa, wananchi wa Tanzania wanawezeshwa, wanapata fursa na lengo la sheria hii ilikuwa kuweka masharti hayo ambayo yatawawezesha Watanzania waweze kupata fursa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali inakubaliana na hilo wazo la kupeleka kiwango cha tenda, zile zabuni ambazo zitakuwa za ndani ya nchi ambazo ni local sio international tender kufika hiyo bilioni 50. Sisi tulikuwa tumeweka bilioni 30, Mheshimiwa Shigongo amependekeza tuiongeze zaidi ifike bilioni 50 na sisi kama Serikali hatuna tatizo na kupeleka kiwango cha zabuni za ndani ya nchi kufika bilioni 50. Tunataka tuwajengee uwezo wazawa na tunataka tuwajengee Watanzania waweze kushiriki katika shughuli hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeongea hata ndani ya Kamati ambacho tulikuwa tumekibishania kwa sehemu ndogo ilikuwa ni kuhusu iandikwe wapi. Sisi tukasema kwa majira haya ambayo mabadiliko yanabadilika sana, yanaenda kwa kasi sana. Mabadiliko ya exchange rate pamoja na yale mengine, tulisema Waheshimiwa Wabunge waridhie kiwango kile, tuweke kwenye sheria, mkakati huu wa kuwawezesha wazawa, kiwango kile cha bilioni 50 kiwekwe kwenye kanuni. Tulisema kiwekwe kwenye kanuni kwa sababu kwa mabadiliko haya ya exchange rate, lakini pia na kukua kwa uchumi tunaweza tukakaa baada ya mwaka mmoja, watu wenye bilioni 50 wakawa wameshakuwa wengi, tukataka tuweke bilioni 100, ama tuweke bilioni 150, tukasema hii isitutake tuitishe Bunge zima kuweza kuibadilisha hiyo.

Mheshimiwa Spika, tunaweka bilioni 50 na inakaa kwenye Kanuni, tunaendelea kusonga mbele kwa sababu uchumi unakua na masuala ya kifedha yanabadilika. Tunaungana na Mheshimiwa Shigongo, tunaungana na Kamati ya Bajeti pamoja na Wabunge wengine kuweka international tender iwe kuanzia bilioni 50 kwenda juu na bilioni 50 yenyewe na 50 kuja chini ziwe ni local tendering. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Serikali tumeenda hatua zaidi kwenye lile jambo ambalo Mheshimiwa Shigongo ameliongea kwa uchungu sana, Serikali tumeenda hatua zaidi. Mheshimiwa Rais mara zote amesema anataka kutengeneza mabilionea wa Tanzania, Watanzania na wenyewe waheshimike kwenye nchi yao, wajengewe uwezo, sasa hatua nyingine ambayo tumeiweka mtaona kwenye sheria yenyewe ile ambayo tunapendekeza. Tunapendekeza kampuni ya Kitanzania yenye uwezo, ikieleza kwamba kwenye kazi kubwa ambayo inataka kufanya, kama itapata wabia, au mshirika wa makampuni makubwa kutoka nje na wao Watanzania waruhusiwe kupewa kazi kama ambavyo wageni wamekuwa wakipewa kazi na kuruhusiwa kuwashirikisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni hatua kubwa ambayo itaenda kujenga uwezo kwa makampuni ya Watanzania na hata siku nyingine yaweze kwenda kushindana nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuweka kwenye sheria moja kwa moja kwamba makampuni ya Kitanzania hayatakiwi kupata kazi kubwa ni sheria ambayo inawakandamiza Watanzania na ni sheria ambayo inawapimia Watanzania kwamba wao wanatakiwa wawe wadogo tu na isitokee siku wakakua. Ni sheria ambayo tunawafanya wale wenzetu wa mataifa mengine waendelee kuwa wakubwa na sisi Watanzania tuendelee kuwa wadogo. Sasa kwenye sheria hii tumeleta pendekezo ambalo linasema, kampuni ya Kitanzania ikitaka kutekeleza mradi mkubwa iweke sharti la kuwaleta wale wakubwa ambao watatekeleza nao na wakionesha hiyo capacity kwamba tutashirikiana na hawa wakubwa na wenyewe waruhusiwe kuweza kupata mradi mkubwa waweze kushirikiana nao.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa benki tumeweza kufanya hivyo. Tukitaka kufanya syndication ya kutafuta fedha nyingi, tunaruhusu benki ya Kitanzania hapa kuwa lead arranger, yeye ndiye anakuwa kiongozi halafu anatafuta benki zingine wamsaidie kuhamasisha kupata hizo fedha.

Mheshimiwa Spika, tumesema uwezo utaendelea kuamua lakini tusiweke sheria ambayo inawazima Watanzania wao waendelee kuwa vibarua, sub contract bila kujali kwamba kuna siku na sisi tunataka hawa wawe wakubwa waweze kufanana na wale wengine. Tunaamini tutapiga hatua.

Mheshimiwa Spika, tumeona tufanye hivi kwa sababu gani? Mara nyingi imekuwa ikitokea, haya makampuni makubwa tunayoyaamini, tena wasikie, kuna maeneo wanakuwa hawawatendei haki Watanzania. Tunasaini mikataba tena kwa dola na tunaweka kwamba kila ifikapo tarehe 31 fedha zao za certificate ziwe zimelipwa, halafu wakishalipwa wanapeleka fedha makwao, hawawalipi subcontractors wa ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nimesikia malalamiko baadhi ya maeneo, certificate zinalipwa kwa wakati lakini ukienda kwenye utekelezaji inatokea makampuni ya ndani yanawadai wao, sasa tutengeneze utaratibu na kampuni ya ndani ikipata hiyo kazi iwapimie wao kwa kufanya kazi na faida ibaki ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, tumeenda hatua nyingine kubwa zaidi. Tumependekeza tuzo ziruhusiwe kwa kampuni za ndani na kwa zile kampuni ambazo ziko ndani ya nchi, ambazo zinawekeza ndani ya nchi. Makampuni ya kigeni ambayo yanapata kazi ndani ya nchi na yanawekeza ndani ya nchi yaweze kupata upendeleo.

Mheshimiwa Spika, imekuwa ikitokea hasa kwenye hii miradi mikubwa mikubwa, watu wanatekeleza mradi wanapata fedha nyingi lakini wanawekeza nchi ya Jirani pale. Wanachukulia fedha kwetu wanawekeza nchi nyingine pale, sasa kwa sababu fursa za uwekezaji kwenye nchi yatu hazijajaa, tunapendekeza kampuni ile ambayo inawekeza ndani ya nchi na ile ambayo inaweka commitment kwamba ikipata mradi itawekeza ndani ya nchi, itapewa kipaumbele ili tuweze kuongeza uwekezaji ndani ya nchi. Haya ni mambo ambayo katika nchi za wenzetu yanawezekana.

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye jambo lingine moja. Mheshimiwa Halima Mdee aliongea kwamba Serikali tuliweka pendekezo la Sheria ya PPRA kuja ndani ya Bunge na baadae tukalitoa. Ndiyo, tuliahidi wakati tunasoma na matamanio yetu yalikuwa hivyo, tulitamani Sheria ya PPRA, tulitaka taarifa ya PPRA, Taarifa ya Mkaguzi wa Ndani, Taarifa ya TAKUKURU, Taarifa ya EWURA.

Mheshimiwa Spika, tulitaka taarifa za taasisi hizi ziende kwenye Bunge lakini tumeshauriwa kisheria na bahati nzuri Mheshimiwa Mdee ni Mwanasheria. Tumeshauriwa kisheria kwamba taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali iko Kikatiba. Ukienda kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 143 inataja kwamba kutakuwa na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali na baadae ikataja majukumu yake, ukienda Ibara ya 43(3) inasema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kila mtumishi wa Serikali anayeruhusiwa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ataruhusiwa kukagua vitabu, akaelezea vitabu atakavyokagua na majukumu mengine yote yakaelezewa.

Mheshimiwa Spika, lakini kipengele cha (4) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinasema; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa mujibu wa masharti ya Ibara ndogo ya (2) ya Ibara hii na baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais atawaagiza watu wanao husika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kinachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa ya CAG, hili ni takwa la Kikatiba.

Mheshimiwa Spika, tulipoona kuna taarifa ambayo ipo Kikatiba na inapitia taarifa hizi zingine zote, Taarifa ya TAKUKURU, Taarifa ya Mkaguzi wa Ndani, Taarifa ya PPRA, Taarifa ya PPA, tukasema hili la kikatiba libaki kama Katiba inavyoelekeza.

Mheshimiwa Spika, taarifa hizi zingine za PPRA, TAKUKURU na Taasisi zingine zote zimewekewa utaratibu wake wa kuingia Bungeni kwa sababu zile ni taarifa za kazi. Taarifa za kazi za mashirika yote ya umma zina Kamati zake ambazo zinazisimamia na zinakagua utendaji wake, na taarifa zile zinaingia Bungeni kwa kutumia mgongo ule wa Kamati inayosimamia majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, hivyo ndivyo ilivyo hata kwa taarifa zingine kwa taasisi zingine zilizosalia, kwa hiyo hata hii ya PPRA itaendelea kukabidhiwa kwa Rais, itakabidhiwa kwa sekta inayohusika, itaenda kwenye Kamati inayosimamia majukumu ya PPRA na Kamati hiyo italeta taarifa hiyo Bungeni ili iweze kusimamiwa kama vile ambavyo sheria zingine zinasema.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hatuna haja ya kuvutana kwenye hili kwa sababu ni taratibu za kisheria ambazo tumezitunga. Hivyo hivyo na hili ambalo umeshalifafanua, sihitaji kufafanua bahati nzuri wewe ni Mwanasheria, Mwalimu na umewafundisha wanafunzi wengi humu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, hata hili la kutunga kanuni na majukumu yaliyopo kwenye sekta hizi yapo kikatiba na yapo kisheria. Mheshimiwa Halima wakati anaongea alikuwa anasemea rafiki yangu, wakati mwingine urafiki ndiyo unatuponza inaonekana hivi viapo tulivyonavyo ni vidogo, majukumu haya tuliyonayo yapo Kikatiba.

Mheshimiwa Spika, kumeanza kuzuka utaratibu hivi wa mtaani mtaani na baadhi ya maeneo ya watu kut kuamini. Unaweza usimheshimu yeye kama mtu lakini heshimu jambo alilopewa na Katiba na unatakiwa uamini kwamba viongozi wote walioko Serikalini ni Watanzania, hakuna mtanzania na nusu kwa sababu hayupo Serikalini na yule aliyepo Serikalini ni nusu mtanzania kwamba anaweza akajali maslahi ya Tanzania nusu nusu. Mheshimiwa Halima angekuwepo ningemwambia, tumeibeba Tanzania mioyoni na wengine tumeibeba shingoni hapa. Tunajali maslahi ya Watanzania na hiki anachofanya Mheshimiwa Rais ni kwa ajili ya kuongeza ufanisi na kuongeza ustawi wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe utaona kasi ya kubadilisha hizi sheria ambazo zinalenga kukuza sekta binafsi, sheria zote hizi zinazolenga kukukuza sekta binafsi, zinalenga kuwaongezea Watanzania utajiri. Hii siyo sheria ya usimamizi, hii ni sheria inayolenga kuwawezesha Watanzania washiriki katika keki ya Taifa. Kwa maana hiyo ni sheria yenye malengo mazuri kwa Watanzania, Vivyo hivyo na zile zingine ambazo tumezitoa.

Mheshimiwa Spika, lilikuwepo jambo lingine kuhusu mchango alioutoa Mheshimiwa Mpina. Alisema kwenye force account tuongeze wigo. Sisi tulikuwa tumependekeza milioni 50, yeye anapendekeza ifike milioni mia moja.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema…

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, samahani, Mheshimiwa Mpina ameleta mchango kwa maandishi? Maana hapa sijamsikia akichangia na sina mchango wake hapa mbele.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nilipokea pendekezo, sijui kama limeingia ama halijaingia.

SPIKA: Hapana. Kama ni schedule of amendments utapata nafasi ya kuzungumza tutakapoanza kushughulika na amendments, kwa sababu hapo umesema mchango wa Mheshimiwa Mpina na Mheshimiwa Mpina hajachangia, labda kama ameleta mchango kwa maandishi.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, ninakubaliana na mapendekezo yako kwa sababu sisi kama Serikali tulikuwa tunajiandaa na sheria ambazo zinatakiwa zije, ndiyo maana nimechangia na ya Mheshimiwa Mpina. Tunakubaliana na maelekezo yako.

Mheshimiwa Spika, pendekezo lingine ambalo lilitolewa na Mheshimiwa Reuben kuhusu kuleta sheria. Ndani ya Serikali tutajiratibu sera ya masuala ya manunuzi na tutaileta, hilo halina pingamizi. Kama nilivyosema, maoni yote ya Wabunge yanayoboresha ufanisi unaowafanya Watanzania wafurahie matunda ya uhuru wa nchi yao, wafurahie keki ya Taifa lao ni jambo ambalo Serikali hatupingani nalo na hatutachelewa hata sekunde moja kuweza kutekeleza masuala ya aina hiyo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kimei pamoja na Mwenyekiti wamechangia na yale yaliyotolewa na Kamati, tumekubaliana mengi kwenye Kamati kasoro yale machache, kama lile ambalo umelitolea ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo haya ya kutunga Kanuni, Kanuni hizi zinatungwa kwa kuzingatia sheria ambazo zinakuwa zimeshawekwa, ambazo ndio muhimili unaotoa mwongozo kwenye upande wa zile Kanuni.

Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo mengine ambayo tumepokea kutoka kwa Mheshimiwa Zainabu Katimba pamoja na Mheshimiwa Elibariki Kingu, tumeyapokea na tutakapoenda kupitia sheria, vipengele kwa vipengele, ni maoni makini nani maoni ya Wanasheria na yanaendana na mapendekezo ambayo ndani ya Serikali tulikubaliana nayo.

Mheshimiwa Spika, kuna Mheshimiwa Mbunge alisema jambo moja la kuwekea sheria masuala yanayohusu madeni. Mheshimiwa Halima amesema kwamba TAMISEMI kuna bilioni mia moja, Mashirika kuna bilioni mia moja, Serikali Kuu kuna trilioni 83 pamoja na yale yanayohusisha mifumo tunaendelea nayo. Utekelezaji wa masuala ya mifumo tunaendelea nayo, kama nilivyosema Mheshimiwa Rais anachukua hatua za kutatua tatizo moja baada ya lingine. Kulikuwepo na matatizo ambayo yalikuwa yanatusababishia malimbikizo mengi ya madeni, na malimbikizo mengi yalikuwa yanatokana na mismatch ya mapato pamoja na matumizi tunayopeleka.

Mheshimiwa Spika, haya yalikuwa yanatokea kwa sababu kuna vitu vingi vilikuwa vinajitokeza wakati tunaendelea kutekeleza bajeti. Mheshimiwa Rais kwa kuona hilo akairejesha Tume ya Mipango ambapo vitu vingi vitakavyokuwa vinatekelezwa vitakuwa vimepata kwanza ridhaa kutoka katika Tume ya Mipango. Maana yake vitu vitatekelezwa ambavyo viko kwenye mipango, vitatuondolea hiyo imbalance ambayo Waheshimiwa Wabunge wameiongelea hapa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali ilishachukua hatua kwenye hilo na wala halihitaji Sheria ya Manunuzi kuweza kudhibiti masuala hayo ya upande wa madeni. Tunaamini tunakokwenda kutakuwa na huo mpango wa muda mrefu, kutakuwa na mipango ile ambayo ni ya muda mfupi, kutakuwa na ile mipango ya miaka mitano, na kwa sababu Tume ipo na hiyo ndiyo itakuwa inafanya kazi zake na Waziri makini Mheshimiwa Mkumbo yupo hapa, haya yataenda kutuondoa kwenye utaratibu ambao ulikuwa unazalisha hii mismatch ya matumizi pamoja na mapato ambayo ilikuwa inasababisha haya madeni.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali tumeleta sheria hii kwa nia njema ya kuhakikisha kwamba yale ambayo tumekuwa tukiyalalamikia kwa muda mrefu yapate suluhu. Hicho ndicho ambacho Mheshimiwa Rais amekuwa akikiona, siyo tu kwa sheria hii, mtakumbuka tumesharekebisha sheria nyingi, tumerekebisha Sheria ya Uwekezaji, Sheria ya Mawasiliano, Masuala ya Manunuzi, tumerekebisha hii ya Tume, Sheria ya Msajili wa Hazina, zote hizo zikiwa zinalenga kutengeneza mazingira wezeshi ya kumwezesha Mtanzania aweze kuwa na ustawi unaostahili na kunufaika na rasilimali zilizopo.

Mheshimiwa Spika, kwa sheria hii ilivyokuwa kuna mambo ambayo ilikuwa inakosea na ndiyo maana tumeileta hapa, hata kwenye mchango haijajionesha sana lakini kwenye hotuba yetu tumeiandika. Tumeweka ukomo katika manunuzi, hii ilikuwa inatumiwa vibaya, ule uwazi uliokuwepo ulikuwa unatumiwa vibaya, kwamba bidhaa ikienda tu kununuliwa na Serikali ghafla bei zake zinapenda ukienda kwenye soko bei ziko chini. Tukasema tukiweka tu bei elekezi ama bei kikomo au bei ya chini, bado haitoshi. Tukaongeza na ile bei kikomo, bei elekezi na tukaongeza bei ya chini kwa sababu kuna mazingira yalikuwa yanajitokeza katika sheria iliyokuwepo ya manunuzi kwamba, mtu anashindania kwa bei ya chini na akipewa zabuni, ile kwamba amepewa kwa kushindania bei ya chini lakini ukienda kwenye bei ya soko, gharama yake inakuwa ni mara tatu ya bei ya soko.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, anakuwa ameshinda kwa bei ya chini lakini ukienda kwenye thamani ya fedha, value for money anakuwa yupo mara nne, mara tatu au yuko mara tano na ukienda kwa baadhi ya Watanzania wasio waaminifu wanaweka njama tu. Wanakaa kwenye Halmshauri wanakuwepo watu wasio waaminifu watatu au wanne wanashirikiana na mmoja asiye mwaminifu ambaye yuko kwenye manunuzi wanakubaliana kwamba, wewe kwenye sekta ya afya uje tu kunitengenezea mimi kushinda, wewe kwenye sekta ya elimu mimi nitakuja nikutengenezee wewe kushinda.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwenye afya yote yeye anakuja, kama thamani ya bei ya mradi kwenye soko ni kama bilioni 20 yeye anaweka bilioni 80 halafu yule aliyeletwa tu wa kuharibu soko anaweka bilioni 120, kwa hiyo tunampatia wa bilioni 80 tena kwa kufuata taratibu zote za manunuzi, huku tukisema huyu ndiye kashinda na ameteuliwa kwa sababu ndiye aliyeweka zabuni kwa bei ya chini. Bei ya chini bilioni 80 lakini bei halisi ilitakiwa iwe bilioni 20. Tumesema Hapana! Tumwezeshe Afisa Masuuli muungwana, mzalendo akiona bei halisi ni bilioni 20 hata kama wa chini alikuwa amefikia bilioni 80 aseme bado hii haina thamani ya fedha katika project hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ilivyokuwa sasa, kama ameshinda kwa bilioni 80 hata kama project ile ni bilioni 15 akikataa ataonekana aliyetaka kumpa hajashinda kwa hiyo ameamua kuifuta. Itaonekana ameifuta kwa sababu kuna mtu alikuwa anamtafuta na ameshindwa na huyo aliyeweka bilioni 80. Tumesema hapana, tunataka manunuzi yaangalie thamani ya fedha, yasiangalie tu huyu kashindania bei ya chini bali yaangalie thamani, value for money, ili yeyote atakayetoa zabuni akampa aliyeshinda lakini ikienda kwenye soko ikaonekana amempa ya juu sana, naye awe kwenye hatia kwa sababu yamekuwa yakitokea haya ambayo hayalindi thamani ya fedha ya mlipa kodi wa Tanzania katika miradi hiyo. Kwa hiyo, hili na lenyewe tumeliweka na mengine mengi ambayo yanahusiana na kuboresha shughuli hizi.

Mheshimiwa Spika, pale kwenye bilioni 50 ambayo tulisema hatupingani na Waheshimiwa Wabunge tumeongeza. Tukasema tukiweka asilimia na Mheshimiwa Katimba ameiongelea kwenye upande wa makundi maalum, tunaendelea na lenyewe kulitafakari. Tuliweka asilimia hata kwenye sheria iliyopita, tukasema asilimia 30 iende kwenye makundi maalum, lakini kwa kuwa tu tumeweka asilimia iende kwenye makundi maalum ikawa kama tumeandika barua kwa yeyote anayehusika ambayo haijibiwi kwa sababu haina mtu wa kukujibu.

Mheshimiwa Spika, kila mtu anapopata fungu lake la kutekeleza miradi anaendelea kutekeleza tu, ukienda mwisho wa mwaka haipatikani ile asilimia 30 iliyoenda kwenye makundi maalum. Hivyo, tukasema hata wazawa tukiweka asilimia itakuwa inaenda hivyo hivyo inapita. Tukasema tutaje kiwango ili yeyote anayefanya manunuzi akikuta kiwango kile ajue hii inaenda huku, sasa tunaendelea kuangalia kuhusu ufatiliaji wa masuala ya makundi maalum kama alivyolisemea Mheshimiwa Katimba ili tuwe na utaratibu wa kuweza kuona kwamba hiki tulikiweka kwenye sheria na katika mwaka wa fedha ambao umefanyika utaratibu wake umetumika.

Kwa hiyo, tumesema tutaiweka kwenye kanuni ili kuweza kuweka enforcement ambayo itawawezesha Maafisa Masuuli na Kamati zetu za manunuzi ziweze kuzingatia kile kinachokwenda kwenye makundi maalum.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hoja ni nyingi, tumepokea na tumesema hatubishani. Mengine tutakwenda tunarekebisha kadiri tutakavyokuwa tunapitisha kipengele kwa kipengele.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
The Finance Bill, 2022
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimia Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuhitimisha hoja hii. Awali ya yote, namshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa mwongozo wake ambao ametupatia kuanzia kwenye mjadala wa Bajeti na kwenye mjadala huu wa kutunga sheria, ambapo ametupa fursa ya kuweza kuyasikiliza maoni ya Wabunge na kuyafanyia kazi. Narejea kauli yake, alisema, mtakapopokea mawazo haya, pamoja na kwamba mmeenda na mapendekezo yenu na mitizamo yenu, lakini lazima mwasilikize wawakilishi wa wananchi. (Makofi)

Mheshimia Spika, sisi tuliokulia vijijini, tuliolima na majembe yale ya kukokotwa na ng’ombe, speed ya wale ng’ombe wa nyuma, huwa inafuata speed ya ng’ombe wa mbele. Ninyi ndio mnaweza mkaona hicho kimesaidia sana Wizara ya Fedha kuwa flexible, kuweza kusikiliza maoni ya wawakilishi wa wananchi ambao kwa kweli nikiri kwamba mmewawakilisha vyema sana wananchi wa Majimbo yenu na wananchi wa maeneo yaliyowachagua. (Makofi)

Mheshimia Spika, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, pamoja na Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti, mtani wangu Ndugu Daniel Sillo kwa ushauri wao walioutoa wakati wa majadiliano ya Muswada ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa sana katika kuboresha Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kutambua michango ya Wabunge waliyoitoa hapa Bungeni, na niwaambie, kama ambavyo tulisema, kwa kiwango kikubwa tumeweza kutekeleza, kuyajumuisha maoni kama ambavyo mmetoa. Kamati ilipendekeza Serikali ianzishe tozo ya parking fee, carbon emission fee pamoja na tollgates kwa malori; Serikali imepokea mapendekezo hayo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu carbon emission, kwa upande wa Tanzania, mtakumbuka zamani tuliwahi kuwa na utaratibu huo, lakini kwa ajili ya kupunguza usumbufu, tulijumuisha kwenye tozo nyingine ambazo zinatozwa, kama tulivyofanya kwa upande wa road license, badala ya kutoza road license kama Kifungu kinachojitegemea, nakumbuka tulijumuisha kwenye mafuta ili kupunguza tu usumbufu. Kwa hiyo, hata kwenye carbonate emission tulishafanya hivyo tukaweka kwenye tozo nyingine ili kuondoa utozaji wa mara mbili.

Mheshimia Spika, kwenye upande wa tollgates ilikuwepo na yenyewe kwenye upande wa barabara kuu hizi, lakini na yenyewe tuliiondoa kwa sababu ya kuwa na vizuizi vingi sana njiani. Mtakumbuka kuna wakati ilikuwa inatokea gari inaweza ikatoka kwenye mpaka mmoja, mpaka ikakize katikati ya nchi ya Tanzania, unakuta ilishasimama mara nyingi kwa idadi ya Wilaya mathalani. Jambo la aina hii lilikuwa linafanya muda uwe mrefu sana wa magari kupita ndani ya nchi kwenda maeneo mengine na ilikuwa inasababisha usumbufu wa wasafirishaji na vikwazo visivyo vya kikodi, vya kibiashara. Kwa maana hiyo, na yenyewe tuliitengenezea utaratibu wake ambayo ipo kwenye sheria ile ambayo tulikuwa tunajadili inayohusisha magari ya kigeni yanayopita. Kwa hiyo, yenyewe ilishajumuishwa mle kwenye ulipiaji wa magari ya kigeni.

Mheshimia Spika, zile tozo tulizoziweka, nakumbuka na hiyo ilikuwemo kwenye uchangiaji, siyo tozo mpya. Tulichofanya kwenye Bunge hili la sasa, tumeshusha ile tozo tuliyokuwa tunatoza sisi kama nchi, tumeiwianisha na zile tozo zinazotozwa kwa upande wa COMESA, kwa upande wa EAC, ambapo sisi tulikuwa tunatumia SADC ambayo ilikuwa juu kuliko hizi. Tumerudisha ili iweze kuwiana na nchi nyingine. Kwa hiyo, hakuna athari ambayo itatufanya sisi tusiwe washindani tukilinganisha na nchi nyingine. Tumeishusha ili tuweze kulingana na wenzetu wa Kenya, Uganda na nchi nyingine ambazo ziko COMESA zinazotumia kiwango hicho ambacho mwanzoni sisi tulikuwa tunatumia kiwango kikubwa kuliko cha nchi wanachama tulionao kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimia Spika, Mheshimiwa Kandege, aliongelea kuhusu Serikali iwekeze kwenye matumizi ya mifumo. Ushauri wake ni mzuri tumeupokea. Mheshimiwa Halima Mdee, aliongelea kuhusu kuzingatia taratibu za urejeshwaji wa mikopo; ushauri huo ni mzuri, tumeuzingatia, tutateta na wenzetu wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Neema Lugangira, pamoja na Mheshimiwa Joseph Kakunda, waliongelea mapendekezo ya Serikali kuangalia utaratibu wa pump za maji. Tumepokea ushauri huo. Mheshimiwa Japhet Hasunga, aliongelea jambo lake lile na nilishalifafanua kwenye maeneo yale ambayo yalikuwa bado yanahitaji ufafanuzi tumeielezea kwa kirefu kwenye badiliko letu kwamba, siyo kodi mpya isipokuwa tumetengeneza utaratibu wa kuweza kutofautisha na kuweka ufanisi zaidi. Ila siyo kodi mpya, ni kodi ambayo ilikuwepo. Mheshimiwa Shamsi Vuai, ameelezea kuhusu upande wa masuala ya utalii, Serikali imepokea ushauri wake.

Mheshimia Spika, Engineer Mwanaisha aliongelea kuhusu suala la ukusanyaji wa tozo. Ni kweli, ushauri alioutoa ni wa msingi kabisa. Naomba niweke hilo pendekezo ambavyo inatakiwa kusomeka, nadhani tulikuwa tumeweka kwenye maelezo yetu. Wakati nasoma hotuba, ni kweli nilitaja hivi vitu vya tollgates. Tunatarajia kujenga expressway kutoka Kibaha kuja mpaka Morogoro. Tulikuwa tunaangalia pia expressway ya upande wa kwenda mpakani kule Mbeya kwenda Tunduma. Pia kwenye Hotuba ya Bajeti tuliongelea upande wa Tanzanite ambapo tathmini bado inafanywa na Wizara ya Kisekta kuona feasibility kama jambo hilo litakuwa feasible kwa kiwango gani?

Mheshimia Spika, napendekeza kurekebisha Sheria ya The Road and Fuel Tall Act ya Cap. No. 220 katika Kifungu cha 7(2) kwa kuongeza Kifungu kidogo cha 7(2)(d) ili viweze kusomeka kama ifuatavyo: Ile (d) isomeke: “The owner or the driver of the vehicle passing through the specific public road as may be specified by the Minister responsible.” Kifungu hiki kitampa Waziri wa Fedha kutangaza barabara ama madaraja yanayopaswa kulipiwa road tall. Aidha, napendekeza kurekebisha Kifungu cha 7 cha sheria hii na kuongeza kifungu kipya kidogo cha 7 kisomeke kama ifuatavyo: “the rate of the road tall and the public road in the respect of which such a tall shall be payable may be prescribed by the order in the gazette.” Kifungu hiki kitamwezesha Waziri wa Kisekta kubainisha kupitia hati itakayotolewa na Waziri wa Fedha.

Mheshimia Spika, Mheshimiwa Kunambi, ameongelea jambo linalohusisha misamaha ya miradi ya maendeleo. Tumepokea ushauri, tutaangalia kiutawala hili jambo linafanyikaje? Utaratibu Serikali iliokuwa inatumia, zamani miradi hiyo hati zake zilikuwa zinatolewa na Waziri. Kwa ajili ya kuweka ufanisi, tukaisogeza kwa Kamishna wa Mapato ili awasiliane na Mameneja wake wa Mikoa ili waweze kusaidiana katika kuharakisha jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kiutawala tutaliangalia hili ili kuweza kuweka ufanisi mkubwa zaidi ili miradi isichelewe kwa sababu ya jambo hilo, huku tukidhibiti. Tuliweka chini ya Mamlaka ya Kamishna Mkuu kwa ajili ya udhibiti ili kuweza kuhakikisha kwamba misamaha hiyo haichepushwi. Kwa sababu pakiwa na hatua kidogo za kiudhibiti miradi hiyo inaweza ikatumika kupitisha misamaha ambayo haiko kwenye miradi ile ambayo imekusudiwa.

Mheshimia Spika, kwa upande wa jambo la Mheshimiwa Mwambe, ameelezea kuwa fedha zile zielekezwe kwenye korosho. Jambo hili tumelizingatia sana na Wizara ya Kilimo iko makini kwenye jambo hili. Kwa sababu kuna taratibu ambazo zinaendelea kufanyika ambapo Wizara ya Kisekta inafanya mageuzi katika sekta mbalimbali ikiwemo hiyo ya upande wa zao la korosho, tuliona tupeleke kwenye Wizara ili usimamizi uweze kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba kuna wakati fedha zilikuwa zinaenda kwenye Bodi, kuna maeneo haikufanya vizuri sana. Ndizo sababu za kimatumizi zilizosababisha fedha hizo zikaamuliwa ziende kwenye Mfuko Mkuu. Kwa hiyo, bado tunaamini tuiachie Wizara ili iweze kuratibu na nia ni hiyo hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge amesema, ndicho ambacho na Wizara wanalenga kukifanya.

Mheshimiwa Spika, kwenye vipengele vile vingine alivyokuwa anapendekeza kutengeneza mgao zaidi, tulikuwa tunaomba Mheshimiwa Mbunge aridhie kwamba tuna masuala ya kibajeti ambayo yanatulazimisha kuendelea kutunisha Mfuko Mkuu. Kwa mwaka mmoja kupandisha bajeti kutoka Shilingi bilioni 200 kwenda zaidi ya Shilingi bilioni 900, na utakumbuka wakati ule nasema hapa, nilisema bado tunaendelea pia na mashauriano, ambapo kwenye Wizara ile ya Kilimo kuna component nyingine ambayo itahusisha private sector, kwa maana ya utoaji wa LC pamoja na mengine. Tunaendelea kuongea na benki za nje, huenda bajeti hii ya kilimo ikazidi shilingi trilioni moja kwa zaidi ya shilingi bilioni 100 nyingine, kwenye ile sehemu ambayo tutahusisha sekta binafsi na yenyewe itakapoingia kwenye eneo hilo la kilimo. (Makofi)

Mheshimia Spika, kwa hiyo, tunapopandisha bajeti hivi, kuna fedha tunazitoa katika maeneo mengine. Kwa mfano, fedha za ruzuku ya mbolea zitatoka kwenye Bajeti Kuu, lakini pia na fidia za maeneo mengine ambayo tumesamehe. Kwa hiyo, tuliomba hata Wizara ya Kisekta ilikuwa na kiu hiyo hiyo ya kuona tunapeleka fedha zaidi, lakini tuliwaomba waone kwamba tuna majukumu mengine ya kuweza kufidia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, hapa tutahitaji kuweka fidia kwenye kupoza gharama za maisha kwenye mafuta ya magari au mafuta haya ya nishati. Pia tumeongeza fedha ambazo zinatakiwa ziende kwenye elimu bure pamoja na maeneo mengine yale ambayo yameongeza fedha. Haya yote yatahitaji yafidiwe kwenye Mfuko Mkuu. Utaona kwamba pengo lile ambalo linatakiwa kuzibwa linahitaji tuokote fedha kutoka katika maeneo mengine na hicho ndicho ambacho tumekitumia.

Mheshimia Spika, Mheshimiwa Mpina ameongelea kuhusu miradi hii ya wawekezaji mashuhuri kwamba kuipeleka kwenye Baraza la Mawaziri itasababisha Serikali yote iingie. Tukiwaza katika sura ya kimakosa kwamba hivi vitu vinaweza vikapitishwa kimakosa, tunaweza tukapata picha hiyo anayoisema Mheshimiwa Mpina. Ila tukiwaza katika sura ya kuweka ufanisi, ukipeleka kwenye Baraza la Mawaziri ndipo ambapo utapata ufanisi mkubwa zaidi. Kwa sababu ili jambo liende kwenye Baraza la Mawaziri kwanza lazima litakuwa limetoka kwenye kikao hicho cha NISC ambacho Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu, lakini likienda kwenye Baraza la Mawaziri kabla halijaenda kwenye Baraza la Mawaziri, lazima lipite kwenye kikao cha Makatibu Wakuu wote wa Serikali ambako Mwenyekiti wake ni Katibu Mkuu Kiongozi.

Mheshimiwa Spika, vile vile kabla halijaenda kwenye Baraza la Mawaziri ambapo Mwenyekiti wake ni Rais, lazima vyombo vyake vyote vinavyomsaidia Rais viwe vimeshafanyia uchambuzi. Sisi tulidhani likifanyika hivyo, tunakuwa tumejihakikishia zaidi ufanisi katika Taifa kuliko kupeleka jambo hilo kwa Waziri peke yake ambaye hana vyombo kwa kiwango kile cha kuweza kumfanyia uchambuzi wa kiwango hicho. (Makofi)

Mheshimia Spika, Mheshimiwa Mpina anasema ikienda kwenye Baraza Waziri atapata mwamvuli, kwa hiyo, atakuwa amepata kinga, hiyo tutakuwa tunawaza katika namna ya kuacha jambo litokee, tupate kwanza hasara, halafu tuhangaike na kumwajibisha Waziri. Tukipeleka kwenye vyombo vya nchi nzima ambavyo vitafanyia tathmini, tutakuwa tumehangaika na kuzuia matatizo yasitokee, kuliko kusubiri matatizo yatokee ndiyo tuanze kuhangaika na matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kwamba mapendekezo haya Serikali iliyoleta yanalenga zaidi kulinda rasilimali za Watanzania, na hiyo ndiyo dira ya Mheshimiwa Rais. Anatamani rasilimali za Watanzania zilindwe. Tusihangaike na makovu, tusihangaike na hasara, tulinde hasara zisitokee, tulinde maovu yasitokee, tuhakikishe kwamba rasilimali za wananchi zinatumika katika matumizi yaliyokusudiwa.

Mheshimia Spika, nimalizie la mwisho. Mheshimiwa Mohamed Issa ameongelea jambo la ZRB pamoja na TRA. Mheshimiwa Mbunge ametoa hoja nzuri, isipokuwa namwomba aipitie kwa undani zaidi. Hicho alichokuwa anakisema, actually, mapendekezo haya yanalenga kuwasaidia wananchi wa Zanzibar. Kwa sababu walikuwa wanapata usumbufu. Hii haiendi kuongeza wala kupunguza. Ilikuwa mlipa kodi huyo huyo inabidi waje watu wa aina mbili ama tatu zaidi wanaotoka kwenye nchi hiyo hiyo. Tulichofanya, ametolea mfano, akasema, mbona mainland ZRB haiji? Hicho ndicho tunachofanya, kwamba hapa ingekuwa TRA inakusanya, halafu makusanyo ambayo ni ya upande wa Zanzibar kwamba ZRB ije kukusanya huku, tungekuwa tunatengeneza usumbufu.

Mheshimiwa Spika, kuna kodi ambazo zinahusu Zanzibar, lakini ZRB huwa haiji kukusanya, TRA ndiyo huwa inakusanya ina-remit kwa upande wa Zanzibar. Kwa mfano, mawasiliano; hata miamala inayotumwa upande mwingine, mkusanyaji anakuwa mmoja, mgawanyo unafanyika kufuatana na sheria inasemaje. Hata huko Zanzibar tumesema kwa sababu mifumo ilishakuja kurahisisha kazi si jambo la busara, nikope msemo wa Mheshimiwa Halima; “si busara mifumo, imeshakuja ya kurahisisha utaratibu huo sisi tuendelee kutuma watu kwenda kuwasumbua watu mara mbili mbili.”

Mheshimiwa Spika, tukasema yule aliyopo pale akusanye, halafu namba zinasema kipi ni kipi, tunakuwa tumeshawapunguzia usumbufu wa kufuatwa na watu mara nyingi nyingi. Kwa hiyo, ndicho tulichokifanya, hakiendi kuwaongezea mzigo Wazanzibar, actually kinakwenda kuwapunguzia usumbufu na jambo hili tumekaa vikao vingi vya Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara ya Fedha ya Zanzibar tukiishirikisha na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ili vitu vyote vinavyohusisha pia kisheria viweze kutengemaa. Lakini lengo ni kuongeza ufanisi katika ukusanyaji.

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini si mwisho kwa umuhimu, Waheshimiwa Wabunge tunakwenda majimboni, tunakwenda kwa wapiga kura wetu katika kipindi ambacho nchi iko kwenye zoezi la sensa. Rai yangu kwenu, nawaombeni twende tukatoe elimu kwenye masuala ya sensa, tuwahamasishe wananchi wajitokeze kwenye masuala ya sensa; tuwaelimishe wananchi sensa ni kwa ajili ya maendeleo yao; sensa ni kwa ajili ya mipango ya nchi yetu; sensa ni kwa ajili ya maisha yao wao wenyewe. Wasiendelee kupotoshwa na baadhi ya watu ambao bado wana mila zile potofu zinazopotosha masuala haya ya sensa.

Mheshimiwa Spika, misemo mingine ile ilikuwa misemo tu ambayo ilikuwa inanogesha, tumeambiwa maneno mengi sana, zamani tulikuwa tunaambiwa usile mayai utapata kipara, kumbe walikuwa wanataka tu wazazi wetu watakapokwenda kazini wasikute mayai yote pale nyumbani yameshafanyiwa kazi. Kwa hiyo, hata hii habari kwamba usihesabiwe sijui ukihesabiwa itakuwaje, hizo zilikuwa story za mijadala tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sensa ni kwa ajili ya maendeleo, duniani kote masuala ya sensa yanafanyika na Waheshimiwa Wabunge niwahakikishie kama kuna vipeperushi vinatakiwa ili mfanye semina vizuri; nitawaelekeza wataalam wetu wawapatie vipeperushi, kama mtatakiwa mpate tai kama ya Mheshimiwa Naibu Waziri pale na vilemba vya sensa kwa ajili ya hamasa, hivyo na vyenyewe tutatoa na maandiko yote ambayo yameshatolewa ambayo yanahusiana na sensa ili mkatoa elimu tutatengeneza utaratibu ili muweze kupata na hatimaye mkatoe elimu na wananchi wote washiriki kikamilifu zoezi hilo la sensa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya naomba sasa kutoa hoja.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia hoja iliyoko mezani na nianze kwa kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anazozifanya. Mheshimiwa Dkt. Hussein amekuwa mfano bora sana katika kazi anazozifanya na atakumbuka nilipoteuliwa kwenye nafasi ya Wizara ya Mambo ya Ndani nilimfuata kumwomba ushauri kwamba ni namna gani anaongoza Wizara hizi za vyombo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ushauri wake alionipa ndiyo maana nami leo nimeweza kuonekaonekana kufuata hekima anazotumia kuongoza Wizara hizi za vyombo ambazo kimsingi kwa kweli majukumu yao ni tofauti sana na Wizara za kiraia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia hapo hapo kwenye pongezi nilizozitoa, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara hizi za vyombo zikiongozwa na Wizara anayoiongoza Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi zina itifaki zake na majukumu yake yanafuata itifaki zao. Pamoja na kufanya kazi kwa kushirikiana lakini kila chombo kina kazi zake za kufanya. Ukihusisha Wizara kama ya Ulinzi na majukumu mengine ambayo yako kwenye idara zingine za vyombo utakuwa umekosea na utakuwa unakiuka itifaki hizo ambazo ziko katika vyombo vyetu vilivyoko katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kuwa vyombo hivi vinafanya kazi kwa kushirikiana yanapokuja masuala ya majukumu ya ulinzi wa nchi yetu, ni makosa makubwa kwa Mbunge kudhania kwamba kuna majukumu ambayo yanahusu masuala ya kiulinzi, kuna vyombo vya dola vinaweza vikaona uhalifu na vikavumilia. Vyombo vya dola viko kazini na hakuna siku utasema vyombo vya dola viko likizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu haya ambayo Mheshimiwa Mbunge alikuwa anayataja yakihusisha masuala ya intelijensia ya Jeshi la Polisi, niwahakikishie kwamba Jeshi la Polisi pamoja na idara zake halijashindwa kazi, zinafanya kazi nzuri, vinachapa kazi nzuri na hata kazi hizo zinazofanyika zinaonekana. Ndiyo maana Mbunge akisimama akisema intelijensia ya Jeshi la Polisi imeshindwa kazi yake na hata akataja uhalifu, huwa nataka kujua kama anajua idadi ya wahalifu na kama anawajua wale wahalifu na kama huwa wana vikao akutane nao awaulize wamebaki wangapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama havijashindwa kufanya kazi ya kukabiliana na uhalifu na wala hatuwaombi wahalifu kuacha kufanya uhalifu, tutakabiliana nao na tutashughulika na mmoja mmoja na tutahakikisha kwamba uhalifu hauwezi ukatawala hata kwenye mtaa mmoja katika nchi yetu. Sisi tuko kazini na kazi hiyo itafanyika kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambako uhalifu ulikuwa unajitokeza wanaweza wakasema mazingira ya kazi yakoje na sisi tuko kazini kuhakikisha kwamba tunashughulika na uhalifu na kuhakikisha kwamba hakuna eneo wahalifu watajitamba ama kujigamba kwamba wao wanaweza wakawa washindi. Hatuwezi tukaupa fursa uhalifu katika nchi yetu ukatamalaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo sisi kama Wizara ambazo zinahusu vyombo, tunaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana. Hata kwa upande wa mafunzo, tumeendelea kupokea vijana wanaotoka Wizara ya Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa ambao wametokea JKT. Vijana wale ambao wametokea JKT wanakuwa wameshapata mafunzo makubwa ya awali hivyo wanapochukuliwa kwenye vyombo vingine ambavyo viko Wizara ya Mambo ya Ndani inakuwa ni sehemu ama mwendelezo wa kuweza kupata tu specifications za mafunzo ya kikazi ambayo yana uhitaji mahsusi katika Wizara ama idara zilizoko ndani ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine lilijitokeza ambalo lilikuwa linaongelea vijana ambao wamehitimu JKT pamoja na wale ambao walijenga ukuta. Pamoja na kwamba hatuwezi tukaweka kauli ya kwamba vijana wote waliohitimu Jeshi la Kujenga Taifa watachukuliwa na vyombo ama idara hizi kwa sababu mafunzo wanayopewa yapo na mengine ambayo yanawaruhusu wao kujiajiri, lakini niseme hivi ambavyo tuko kwenye mchakato wa kupata vijana katika idara zetu, tunatarajia kwenda kuchukua vijana wengine ambao wamejenga ukuta na tunatarajia wengine tuwapate ambao wametoka kuhitimu katika kambi mbalimbali za Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa column tulizopewa, tutapata zaidi ya vijana kama 1,500 kwa upande wa Jeshi la Polisi, tuna vijana karibu 1,500 kwa upande wa Jeshi la Uhamiaji, hivyo hivyo na kwa Idara ya Magereza pamoja na upande wa Zimamoto. Hao wote kama ambavyo Mheshimiwa Rais alishaelekeza tunategemea kuwapata kutoka Jeshi la Kujenga Taifa. Vijana wote ambao watakuja kwenye idara zetu tunatarajia kuwapata kutoka Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile taasisi zetu hizi zinahitaji sana hawa vijana, tutaendelea kupokea hata wengine ambao watakuwa hawajaitwa kwenye awamu ya kwanza wajue tu ni suala la kimafunzo wataitwa tu kadri tutakavyoendelea kuita kwa ajili ya mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge kwa sababu najua na wao wana vijana wao ambao wanatoka Majimboni mwao wawaelekeze tu watume maombi kupitia kambi walizokuwa, kwa hivi tunavyoongea utaratibu wa awali unaendelea ili kuwapeleka kwenye upande wa Jeshi la Polisi na kidogo Uhamiaji na Zimamoto pamoja na Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilisemewa na Mheshimiwa Waziri atalisema ni kuhusu watu wanaova sare za kijeshi na kufanya uhalifu. Wahalifu wana mbinu tofauti tofauti za kufanya uhalifu, lakini kama tulivyosema, sisi tunachofanya ni kukabiliana na watu wanaofanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila leo umekuwa ukisikia watu ambao walikuwa wakijifanya maafisa wakikamatwa na siyo tu waliovaa nguo za Jeshi la Wananchi, kuna wengine wanajifanya Maafisa wa TAKUKURU, TRA na Ardhi, wote wanaofanya uhalifu wa aina hiyo tumeendelea kushughulika nao na tutaendelea kushughulika nao. Kuhusu upande wa mavazi nitamwachia kaka yangu atalisemea zaidi kwa upande wake na jinsi ambavyo sheria zinasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge na niwaombe tu waendelee kuvipa heshima vyombo hivi. Vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kubwa sana. Ndiyo maana leo hii ukienda duniani kote utaona Jeshi la Wananchi wa Tanzania linatambulika na linaheshimika na sisi tuwe wa kwanza kuenzi heshima hiyo ya jeshi letu na kazi kubwa ambazo zinafanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine kama mimi ambao nimeenda kuomba ushauri kwa Mheshimiwa Dkt. Hussein, hata wao kwenye vyombo wanasaidiana na wanapeana ushauri na ndiyo mnaona kazi zikiendelea. Mimi nimtakie tu kazi nzuri Mheshimiwa Dkt. Hussein na kwa kweli tunamtakia kila la kheri ili kazi nzuri hii iendelee kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nikupe pole, asubuhi niliona ulipata sekeseke, walistahili na kwa kweli nitumie fursa hii kuwapongeza Simba kwa kupata ubingwa. Mimi nilikuwa nawaombea tu wapate kwa sababu ilishaanza kuleta picha mbaya kwenye nchi jirani kwa timu kubwa kama hiyo kukaa zaidi ya misimu mitano hawajashiriki mpaka nchi jirani walishaanza kudhani labda wameshuka daraja, hii ilianza kuharibu utani wa jadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachowaambia, wanapojisifia sana watambue kwamba wakati Yanga wanapata ubingwa mara tatu mfululizo na wao walikuwepo kwenye ligi hiyo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mwanangu ana miaka 13, tangu azaliwe hajawahi kuona Simba imepata ubingwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. MWIGULU L. NCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia hoja zetu hizi ambazo ni muhimu sana zilizoko mezani. Jambo la kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazofanya yeye pamoja na wasaidizi wake, lakini pia niwapongeze Mawaziri walioko katika Wizara hizi ambazo leo ajenda hizo ziko mezani hapa Bungeni kwako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia nimesikiliza pia hata hoja za wachangiaji wengine. Tunapoongea masuala makubwa hasa ya kitaifa ni vizuri sana tukawa tunapata tafsiri zilizo sahihi, kwa sababu usipopata tafsiri zilizo sahihi zinaweza zikasababisha taharuki kwenye mambo ambayo hayapo. Nilikuwa namsikiliza shemeji yangu Mheshimiwa Komu pale ameongelea kipengele kimoja cha balance of payment (BoP).

Waheshimiwa Wabunge jambo alilokuwa analisemea Mheshimiwa Komu ni jambo la kiuchumi na unapoangalia performance ya uchumi katika Taifa huangalii kigezo kimoja na ambacho mabadiliko yake yanabadilika majira kwa majira, unaangalia vigezo ambavyo vinatokana na utekelezaji wa kisera per se. Kwa mfano, huwezi ukasema uchumi wetu umeyumba kwa kuangalia kigezo cha BoP kwamba imerekodi deficit katika majira ambayo katika Taifa letu si majira ya uvunaji, si majira ya mavuno, ni majira ambayo kwa vyovyote vile hata ukiangalia katika miaka mingine katika Taifa lolote katika majira ambayo si ya mavuno utakuta BoP ina-deteriorate kutokana na kwamba si majira ya kuuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia vigezo kama mfumuko wa bei ambacho ni kitu cha kisera, ukaangalia vigezo kama akiba ya fedha katika Taifa ambacho ni kigezo cha kisera Tanzania imevunja rekodi na tumepata taarifa kwamba zile minimum requirement…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Nimeshasema taarifa hamna tena kaa chini na Mheshimiwa Zitto, Mheshimiwa Zitto, rudi kwenye kiti chako

MBUNGE FULANI: Zitto ndiyo Mwalimu wenu.

MHE. MWIGULU L. NCHEMBA: Imezidi miezi mitatu, iko zaidi kwa mbali kabisa miezi mitatu ambayo huwa inapimika katika importation lakini na mfumuko uko chini kwa muda mrefu, yaani siyo mfumuko ambao unayumbayumba ambao mwekezaji yeyote angetakiwa kuangalia katika Taifa aone jinsi suala lilivyo. Hivi vigezo vingine ambavo amevisemea vinavyohusiana na indicators za ufanyaji wa biashara, labda nimwombe kwenye hili Mheshimiwa Waziri na Wizara yake watafute copy ya vitabu vile vya blue print ambayo ilishapitishwa na Serikali na ilishakuwa tayari kwa ajili ya utekelezaji na baadhi ya mambo tayari yameshaanza kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yale hata siku ambapo Mheshimiwa Rais alikutana na wafanyabiashara ni mambo yaliyotolewa ufafanuzi na wafanyabiashara waliondoka wakiwa wameridhika. Siku ile wao wenyewe ni mashahidi kwa sababu jambo hilo halikuwa kifichoni, lilikuwa live. Wafanyabiashara walipopewa mambo ambayo Serikali ya CCM imeshafanya, waliona kazi iliyofanyika. Hii blue printing ambayo tayari ilishapitishwa inatoa majibu mengi ya vitu hivi vilikuwa vinasema ranking yake ambavyo anavisemea vinashusha ranking ya nchi yetu katika ufanyaji wa biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni utamaduni hasa hasa wa kiafrika kupenda kusema mabaya ya kwako na kudhania kwingine kuko vizuri. Ukienda nchi nyingi za Afrika wao wanatolea mfano mambo mazuri ya Tanzania, ukienda kwenye SADC watatolea mfano Tanzania, ukienda EAC watatolea mfano Tanzania, ila ukirudi Tanzania watasema tume-stack. Sasa ni utaratibu wa kutokujisomea labda kujua wengine wanafanyaje? Haya ambayo tunaweza tukayasema ambayo Mheshimiwa Lema alisema purchasing power ni utaratibu wa kujua unaanzia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa ni lazima ufanye utaratibu wa kuondoka kwenye vicious circle lazima uvunje ile circle, ukiamua kutokuvunja vicious circle kutokutoka kwenye mduara ule wa umaskini utaendelea kuwa kwenye umaskini. Natoa huo mchango na kwa sababu tunaongelea mambo ya viwanda nasema lazima utoke kwenye vicious circle ili hili somo waweze kulielewa. Makofi

Mheshimiwa Mwenyekiti, unatokaje kwenye vicious circle ili uweze kwenda kwenye viwanda, lazima kwanza uweke miundombinu ambayo ni very solid na niipongeze Serikali kwenye hili, haisemei tu kwenye matamko ama kauli mbiu kama mchangiaji mmoja alivyosema, hatua tunaziona ambazo zinaenda kwenye miundombinu ambayo ni very solid kwenda kwenye viwanda. Moja ya kitu kinafanyika ni kuwa na umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni requirement ya msingi sana katika nchi yoyote inayotaka kwenda kwenye viwanda. Ukiamua kuwa na vile walivyokuwa wanafanya babu zetu kusaga kwa mawe au unaweza usihitaji umeme lakini kama unataka kwenda kwenye solid foundation ya viwanda lazima uwe na umeme wa uhakika. Jambo hili Serikali imefanya tena kwa makusudi na halijafanyika mafichoni, mnaona maeneo ambayo uwekezaji kwenye umeme unaenda na mambo haya yataenda mpaka vijijini. Kwa hiyo, kwenye hili la solid foundation kwenye miundombinu moja ni umeme; la pili ni maji; lakini la tatu hata hii miundombinu mikubwa ya usafirishaji, tumeona kwenye reli, lakini tumeona kwenye barabara na kwa sababu ili uchumi uwe inclusive inaenda mpaka kwenye barabara za vijijini na huko kuna TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo machache ambayo napenda kushauri; jambo la kwanza kwenye ushauri; kwa sababu tunatengeneza miundombinu ya miaka mingi itakayohimili uchumi wa viwanda, ni vizuri sana kwa sasa hivi kila mkoa jambo ambalo Mheshimiwa Raisi ameshalisisitiza mara nyingi likafanyiwa kazi la kuwa na industry tax, watu wanaotaka kuwekeza kwenye viwanda wasije wakawa wanaenda kuuziana maeneo na wenyeji, mwisho tunakuja kujikuta kuna kiwanda kipo kwenye makazi na hiyo inatokea utiririshaji maji machafu pamoja na vitu vingine katika makazi, jambo hili limesemwa sana kwa hiyo wenzetu waliopo kwenye kule mikoani lakini pia na Idara zinazohusika ni vyema sana wakalizingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni vizuri sana kufanya ile zoning nchi yetu ili kuondoa migogoro kwa sababu population inaongezeka na ardhi ni ile ile ni vizuri sana kama tunataka kulifanikisha jambo hili ambalo limeshaanza kufanyiwa kazi vizuri tukawa na zoning, lazima kuwa na maeneo ambayo yameshajitambulisha yenyewe ili yaweze kupewa kipaumbele katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kanda ya Kati kuna mambo ya alizeti, lilikuwepo hili jambo la cluster ambalo lilishaanzishwa, ni vema likatiliwa nguvu, kuwe na corridors ambazo ni mahususi kwa ajili ya mchele, hapo tutakapoweza kuwa wauzaji wakubwa wa mchele kidunia, maeneo mengine ya ng’ombe wa nyama, maeneo mengine ng’ombe wa maziwa ili kuondoa mwingiliano kwamba wale wengine wamepanda mchele wale wengine wamepitisha mifugo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa sababu nilishaona kingele imegonga na Watanzania kwa ujumla, ni vyema tukaendelea kutambua nguvu tuliyonayo kwenye upande wa soko la bidhaa zetu, matumizi ya bidhaa kwa maana ya kupenda bidhaa zetu. Hili ni jambo ambalo litatusaidia lakini kama tutategemea vya wenzetu na wenzetu wakategemea vya kwao ni dhahiri kwamba sisi vya kwetu vitakosa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata Bungeni kanuni zetu hizi tulizoweka kama sisi wanaume zinatutambua tu kwamba tunatakiwa tuje tumevaa hizi western suit, mngetafuta siku nyingine mseme Wabunge wa kiume tungeruhusiwa mashati ya vitenge yanayotokana na bidhaa za kwetu hapa, unakuwa nadhifu na shati la Kitanzania, lakini siyo hii ambayo ipo kikanuni kabisa kwamba, lazima uje na suti ya kimagharibi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MWIGULU L. NCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MWIGULU L. NCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. La kwanza, nitumie fursa hii kuwapa pole sana wananchi wangu wa Kata Tulya ambao wamepatwa na matatizo ya shule ya msingi kuharibiwa na mvua pamoja na zahanati yao. Niwaambie wawe watulivu, nami nitapata fursa weekend kwenda kuungana nao katika shida hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya yeye pamoja na wasaidizi wake kwenye Wizara hizi ambazo leo hii tuna mjadala mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, kwa sababu leo ni weekend na nchi yetu itakuwa na jambo kubwa upande wa michezo, nawatakia kila la heri vijana wetu wa umri wa chini ya miaka 17 na wapeperushe vizuri bendera yetu ya Taifa. Nawatakia kila heri pia club ya Simba ambao na wenyewe watakuwa wanapeperusha bendera ya nchi yetu kwa upande wa vilabu bingwa barani Afrika watakapopambana na wenzetu wa kule Kongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa nimeyasema hayo, niende moja kwa moja kwenye maombi. Jambo la kwanza ambalo ningependa kulileta mezani kwa Mheshimiwa Waziri ni hili ambalo moja kwa moja lina muunganiko na dhahama iliyowapata ndugu zetu wa Kata ya Tulya, kwamba kwa kuwa zahanati ile imeharibiwa na kwa kuwa ndugu yetu Mheshimiwa Jafo amekuwa mstari wa mbele sana katika kusaidia upande wa Sekta ya Afya, naomba apatapo nafasi tena ya kutupatia vituo vya afya, basi Kata ya Tulya ambayo zahanati yake imeharibika katika Kijiji cha Doromoni, iweze kupewa kipaumbele. Sambamba na hiyo, aikumbuke pia Kata ya Mtoa ambayo ni Kata ya Mbugani ambako upatikanaji wa huduma za afya umekuwa wa shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa nimeyasema hayo, naomba niende kuweka ushauri kwenye mambo mawili makubwa. Jambo la kwanza, nimefuatilia mijadala tangu Waziri alipotoa hoja hii. Ni vizuri sana niwashauri Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania, kuna mambo ambayo tunatakiwa tuwe tunayabeba kwa umakini mkubwa sana, hasa katika kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais wetu ametangaza vita ya kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wakati wa kubigania uhuru walikuwa na stahili zao za kupambana na walikuwa na namna ambazo wanakumbana nazo. Sasa hivi ambapo pana vita ya kiuchumi, hao watu tunaopambana nao kwenye vita za kiuchumi ni watu wenye akili, ni watu wenye fedha, na ni watu watu wenye uwezo wa kijasusi. Kwa maana hiyo, kila jambo linapotokea kwenye nchi yetu ni vyema sana tukawa tunalitafakari kwa uzito mkubwa badala ya kwenda kwenye uzito mwepesi kama sisi tunavyofanya mambo yanapotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tumeshuhudia katika nchi yetu yakitokea matukio ya kiuhalifu mengi mengi hivi, ambayo kwa bahati nzuri sana Serikali iliyadhibiti yote; moja ya matukio mabaya ni kama yale ya Kibiti; matukio mengine kama yale ya utekwaji wa watoto kule Arusha; matukio mengine ni kama yale ya utekwaji watoto kule Njombe; na mengine ya kiuhalifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya aina hii yote yamedhibitiwa na Serikali kupitia vyombo vya dola hivi hivi. Ni jambo la ajabu sana linapotokea tukio mojawapo la kiuharifu, badala ya watu kuona kwamba nchi yetu imekuwa na matukio ya kiuhalifu ambayo yanashughulikiwa na Serikali, kwa sababu za kisiasa na kutengeneza taswira chafu kwa Serikali, watu wanakimbilia kwenda kuhisi kwamba huenda matukio yanafanywa na vyombo vya dola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilimsikiliza mchangiaji mmoja, Mheshimiwa Mbunge wa kutoka Dar es Salaam akisema matukio ya aina hii kwa nini yasichukuliwe kwamba yamefanywa na Serikali au kupitia vyombo vyake? Akatolea mfano tukio la kutekwa kwa Mo. Hata mwizi tu ambaye ajaenda shule; mwizi wa mifugo aliyeko kijijini, hawezi kuiba mfugo, akaenda kuchinjia ng’ombe wake wa wizi mlangoni kwa nyumba yake. Sijui nimeongea Kiswahili cha Kikenya! Yaani mwizi hawezi kwenda kuiba ng’ombe, akamchukua ngo’ombe wa wizi akaenda kuchinjia nyumbani kwake ama mlangoni kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukianza kuwaza kwamba vyombo vya dola vinaweza vikawa vimeshiriki kwenye utekaji, halafu yule mtu akaokotwe, halafu vyombo hivi vikampeleke pale; ni kitu ambacho ni kuwaza kwa haraka haraka na kwa kutafuta kuaminisha watu jambo ambalo silo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa watu wanaofikiria, unaweza ukaona na ni muunganiko mkubwa kwamba hawa ni watu wanaotengeneza chuki dhidi ya Serikali na mambo mengine yanaweza yakawa yanafanyika ya muundo huu.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo niliona pia ni vyema nikalishauri, hiki ni chombo cha uongozi. Bunge ni chombo cha uongozi, ni chombo cha uamuzi, ni chombo cha sera. Kwa kuwa ni chombo cha viongozi, tunapokuwa tunajadili hapa, ingefaa miaka kadhaa itakayokuja watu wakipitia Hansard zeweze kuwapa dira kwamba katika kipindi hiki Taifa lilikuwa linatekeleza mambo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sote tunajua kwamba tunatekeleza miradi mikubwa itakayoiwezesha nchi kwenda uchumi wa kati. Kwa maana hiyo, kwa kila tunachokusanya kama Taifa na kwa kila Mtanzania siyo viongozi tu; kila mtanzania anatoa mchango wake katika kutekeleza masuala haya; ni vyema sisi tulio viongozi tukaweka kipaumbele kuwaelezea Watanzania kwamba kila jambo linalotokea halitokei kwa bahati mbaya, bali linatokea kwa mpangilio kwamba tuna ajenda tunayoitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, siyo halali kwa viongozi ambao wanajua kinachofanyika kuwa wa kwanza kulalamika kwamba hatuzioni fedha za matumizi mengineyo. Tunatekeleza miradi ambayo itafanya siku zijazo tupate fedha za matumizi mengineyo nyingi kuliko za sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, tunajenga vituo vya afya ambavyo havikujengwa kwa muda mrefu; siyo kwamba havijawahi kujengwa, vilishajengwa, lakini sasa hivi pia kuna vituo vituo vinajengwa maeneo ambayo hajawahi kuwa na kituo. Mfano kama Kinampanda pale hatukuwahi kuwa na kituo lakini kimejengwa. Sasa tunapokuwa tunatekeleza miradi ya aina hiyo tunatumia fedha hizo hizo ambazo tunajibana Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inapotokea kwamba tunajibana ili tutekeleze miradi ya maendeleo, wengine wasitumie kama fursa ya kutengeneza chuki dhidi ya kundi mojawapo kwamba halijatendewa haki. Mifano inayotolewa ya watumishi wa Umma; na wenyewe ni sehemu ya mpango mkakati huu tunaotekeleza wa kuweza kuhakikisha kwamba tutakapokuwa tumeshatengeneza miradi itakayotengeneza fedha nyingi, tutaweza kujipandishia mishahara tunavyotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuwapandishia watumishi wa umma…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mwigulu.

MHE. MWIGULU L. NCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MWIGULU L. N. MADELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia Wizara hii nyeti, Wizara iliyobeba msingi mkubwa kabisa wa Ilani ya Uchaguzi ya 2015/2020 chini ya Rais wetu na Mwenyekiti wetu wa CCM wa Tanzania ya viwanda ambao Mheshimiwa Rais ameusema na ameanza kuitekeleza kwa kiwango kikubwa tangu ameingia madarakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatofautina katika maeneo mengi sana tunapotazama jambo hili la viwanda, wapo wanaoona kazi haijafanyika, lakini na wapo wanaofanya uchunguzi wa kina kwenye mahitaji makubwa ya viwanda tunaoona kwamba kuna kazi kubwa sana imefanyika. Matatizo ya sekta hii ya viwanda na biashara yapo mengi lakini nitataja yaliyokuwepo kwenye ngazi nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, ngazi ya kwanza ilikuwa katika mazingira ya uzalishaji na mazingira ya kufanya biashara. Katika mazingira ya kufanya biashara, Serikali ilishatambua jambo hili na kuna kazi kubwa ambayo imeshafanya na jambo hilo ni kuandaa dira (blue print) ambayo imebainisha matatizo na imeweka mapendekezo ya namna ya kutatua matatizo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu kwa Wizara ni kwamba, kama ambavyo Serikali iliweza kuleta sheria tukarekebisha kwenye upande wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ilete sheria ambayo itafanya merging ya zile taasisi zote ambazo ndiyo zinaleta multiplicity ya duties pamoja tozo ambayo inaleta matatizo katika mazingira haya ya ufanyaji wa biashara katika nchi yetu. Hatutaweza kuondoa tu vile vitu ambavyo vinafanya wananchi wetu wananyanyasika na mazingira ya ufanyaji wa biashara yanakuwa mabaya kama hatutaanza kwanza kwa kuziunganisha taasisi hizo ambazo kuishi kwake zinategemea tozo zinazotolewa na wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, kwa sababu dira ile ilikuwa imebainisha maeneo ya taasisi ambazo majukumu yake yanafanana, iletwe sheria ile ambayo itaunganisha taasisi hizo zote na tukiunganisha taasisi hizo, zile tozo zinazoenda sambamba ambazo zinaleta matatizo kwa wananchi wetu, zitakuwa zimefutika. Hatutaweza kuzifuta tozo peke yake kwa sababu taasisi nyingi hizo zinaishi kwa kutegemea tozo hizo ambazo wananchi wetu wanatozwa na zinasababisha matatizo katika biashara za watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa tumeshatatua tatizo pia la muda mwingi kutumika kwa wananchi kusubiri vibali vya taasisi nyingi ambazo zina-justify kutoza tozo hizo kwa kujifanya kwamba zina majukumu japo majukumu yale yanafanana na yangeweza kufanywa na taasisi moja na ikaondoa gharama na muda ambao unatumika kwa watu wanaoshughulika na biashara kwenda katika madirisha mengi. Kwa hiyo, jambo hili kwa sababu Serikali tayari ilishatengeneza blue print ile, tunaweza kusema kwamba kuna hatua kubwa ambayo imeshafanyika sasa tufanye ile ya umaliziaji ili tatizo hilo liweze kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo lilikuwa tatizo na lilikuwa kigezo ambacho Serikali imeshalifanyia kazi kwa kiwango kikubwa na Waheshimiwa Wabunge wengine wameshaongelea ni suala la umeme. Suala hili la umeme ni jambo muhimu na kigezo muhimu sana kwenda kwenye viwanda serious katika nchi yoyote inayoenda kwenye viwanda vikubwa ambavyo vinaweza vikachukua vijana wengi wakapata ajira katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili wengi tunaweza tusitambue faida yake na kwa nini tunalisemea kwa kiwango kikubwa na kwa nini Rais aliamua kufanya uamuzi wa kijasiri kuweza kuhakikisha kwamba tunakuwa na uzalishaji mkubwa wa umeme ambao unaweza ukaendesha viwanda. Kwa umeme tuliokuwa nao, mtakumbuka hata matumizi ya majumbani tu tulikuwa na mgao wa umeme; tusingeweza kuwa na viwanda vingi serious kwa kiwango kile cha umeme tulichokuwa tunakuwa nacho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo limesalia ambapo Serikali na Wizara inatakiwa ilifanyie kazi ni kwenye ngazi ya uzalishaji. Kwa malighafi tulizonazo tukiweza kutengeneza viwanda vikubwa ambavyo vinatakiwa vitumie umeme mkubwa huu tunaotengeneza na picha kubwa aliyokuwa nayo Mheshimiwa Rais ya kutengeneza viwanda, tunahitaji tutengeneze zoning katika nchi yetu ili kuweza kutengeneza mazingira (mechanization) kwenye uzalishaji ili tuweze kuzalisha malighafi ambazo zinaweza zikatosha kuwa na viwanda vikubwa ambavyo vinaweza vikatufanya katika sekta ambazo tutakuwa tumezitaja tuweze kuwa wazalishaji wakubwa duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ilishagonga Mheshimiwa Mwigulu, ahsante sana.

MHE. MWIGULU L. N. MADELU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na kazi kubwa inayofanywa na Rais na Wizara hii. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2023
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuhitimisha hoja; na katika kuhitimisha hoja niseme tu mambo mawili.

Mheshimiwa Spika, nikianzia na hili ambalo amemalizia Mheshimiwa King, ni kwamba katika majadiliano tulipokaa na Kamati ni moja ya eneo ambalo ndani ya Serikali tulikuwa bado hatujalimaliza. Kwa maana hiyo lilikuwa na mapendekezo ambayo yalikuwa yanahusisha Wizara ya Kazi na kulikuwepo na yanayohusisha Wizara ya Elimu pamoja na eneo lingine lilikuwa linahusisha Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, busara ambayo tuliipata, tulisema tu maintain status quo ili tuweze kukubaliana ndani ya Serikali kuhusu ule mgao namna ya Kwenda; kwa sababu ikibaki namna ilivyokuwa bado kwenye utekelezaji fedha zitakwenda vile zile zinazotakiwa kwenda kwa vijana na zile zinazotakiwa kwenda elimu ya juu zitakwenda. Na hili tutakapokuwa tumekubaliana labda Bunge linalokuja lingine linaloshughulikia mambo ya finance bill kama muda huu, tuweze kutekeleza tukiwa tumekubaliana.

Mheshimiwa Spika, lakini lingine pia ambalo hatukuwa tumemaliza na Kamati lilikuwa ni lile la masuala ya software, kwa hiyo na yenyewe tumeshauriana ndani ya Serikali twende na position ya Kamati ili tuweze kuhitimisha jambo lenyewe vizuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya mengine yote, tumekubaliana na Kamati naomba sasa Bunge lako Tukufu likubaliane kupitisha Muswada huu pamoja na Marekebisho yake.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake
MHE. DKT. MWIGULU L. NCHEMBA: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza na mimi nikushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuwa sehemu ya wachangiaji wanaoweka kumbukumbu sawa ndani ya Bunge lako Tukufu, ubora wa kazi na kazi zinazoishi ambazo anazifanya Mheshimiwa Rais kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kazi anazofanya Rais Magufuli hata kama tungejifanya vipofu tukaamua kupofusha akili zetu ili tusiziseme lakini kazi zenyewe anazozifanya zingesema kwetu kwa watoto wetu, kwa wajukuu zetu na vitukuu vya taifa hili, Kwasababu kazi anazozifanya zitaishi muda mrefu kuliko umri wetu na watoto wetu na wajukuu zetu.

Mheshimiwa Spika, tukiangalia katika sura ya kiuchumi kazi moja kubwa inayojumuisha kazi zote zinazofanyika, ni kwamba Mheshimiwa Rais anatuondoa kwenye mnyonyoro wa umaskini ametutoa kwenye mzunguko wa umaskini; anakata ule mrija anakata ule mnyororo ambao kiuchumi tunaita vicious cycle of poverty ambayo ni lazima uwe na uwamuzi dhabiti na ujasiri dhabiti na udhubutu dhabiti ndipo unaweza kufanya kwa sababu cake ile ile ambayo unatakiwa uigawe ili uweze kuondoka kwenye mnyororo huu.

Mheshimiwa Spika, ni kitu gani kinatokea; Mheshimiwa Rais angekuwa na uamuzi wa kuamua kufanya jambo lolote lile ambalo lingehusisha matumizi na fedha hizi hizi ambazo zinajenga vituo vya afya, bwawa la umeme, barabara na zinasomesha watoto zikapita katika mianya ambayo haingeweka alama; lakini yeye ameamua kufanya udhubutu, uamuzi wa busara wa kutengeneza uridhi wa watanzania wa leo na Watanzania wajao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua ambazo tulikuwa tunaenda nazo kama taifa tungeweza kujipiga kifua, tungeweza kujivuna lakini tungeweza kujivuna kwa fedha za kukopa kwa fedha za kuazima na kwa fedha zenye masimango. Hiki anachokifanya leo anatengeneza miundombinu ya uchumi ambayo itatuondoa kwenye utegemezi na tukaenda kwenye kujitegemea na tukaweza kufanya maendeleo mengine makubwa na tukawa kuweka ustawi wa jamii yetu ya kitanzania inayojitegemea na ambayo ina maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kimojawapo ambacho tunaweza tukakisemea; anzia kama Mbunge aliyepita alivyotokea kusema ukitaka kuondoa umaskini kwa kaya moja moja unatakiwa uelimishe watoto wao kwa sababu vingine ambavyo unaweza ukavifanya, hata ungewagawia fedha wazazi wao bado zile fedha wangetumia zisingeweza kutengeneza uridhi kama wa elimu ambao unatengeneza, ambayo mtoto akishapata elimu hata kama mzazi usipomwandikia miradhi elimu yake aliyopata ni miradhi ambayo haina ugomvi na haina ndugu anayeweza kwenda kuilalamikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa wengine wanashindwa ku- connect hivi vitu ambavyo Mheshimiwa Rais anafanya, kila Mbunge akisimama atasemea kwamba angehitaji apate umeme kila kijiji, lakini baadhi yetu hapo hasa upande mwingine utakuta wanasema hakukuwa na ulazima wa kutengeneza bwawa kubwa la umeme litakalotengeneza megawatt nyingi kuliko zile ambazo ziliwahi kutengenezwa katika historia. Umeme siyo nguzo za umeme, unaanzia na chanzo cha kufua umeme ambao utasafirishwa ili wananchi waweze kupata umeme. Hilo ni moja kubwa ambalo linaingia kwenye historia ambalo hata tusingesema watoto wetu wangekuja kusema kwamba kuna bwawa kubwa la umeme ambalo ilikuwa maono ya Mwalimu Nyerere, akaja Rais moja anaitwa Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli akaja akalitimiza ndoto hiyo na watoto wa Tanzania wakapata urithi huu.

Mheshimiwa Spika, hili linabadilisha maisha ya kila mtu mmoja mmoja katika vijiji vyetu tulipo, vijiji ambavyo tulikuwa navyo kabla ya kuwa na maendeleo haya na tulivyokuwa navyo sasa ni vijiji tofauti. Si hilo tu, miundombinu hii mingine ambayo inatengenezwa ambayo italenga kuboresha kuanzia uzalishaji mpaka uchakataji, vyote vinahitaji miundombinu mikubwa hii ambayo inatengenezwa ambayo mwisho wa siku itaunganisha uchumi kuanzia uzalishaji mpaka uchakataji na baadaye kupeleka kwenye soko bidhaa ambazo zitakuwa zimezalishwa zikiwa za kisasa ambazo ni za kukidhi masoko ya kisasa, ambayo si lazima yawe ya ndani hata ya nje, zikaweza kukidhi viwango vinavyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kitendo cha Bunge lako kuridhia kutengeneza historia hii iingie kwenye hansard ni jambo ambalo na wewe umefanya kitu cha kiungwana ambacho kinastahili tukupongeze kwa sababu hii sasa Kumbukumbu Rasmi za Bunge liliweza kupongeza kazi kubwa anazozifanya Mheshimiwa Rais. Kwa maana hiyo hata wale ambao hawatasema kwa sababu wanatoka katika maeneo yaliyopo humu humu nchini kwetu, kazi anazozifanya Rais zitaendelea kusema na zitaendelea kuwakumbusha wawe na moyo wa kiungwana na moyo wa kizalendo wa kupenda nchi yao ili waweze kusema haya mambo makubwa yanayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nikiongea kama Naibu Katibu Mkuu mstaafu, Mheshimiwa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa chama chetu amekiheshimisha sana chama chetu. Kuna kipindi wanachama wetu walikuwa wanaogopa kutembea hata na uniform za chama kwa sababu ya mashambulizi waliokuwa wanapata yanayotoka kwa wapinzani wao wa kisiasa, lakini kwa sasa hivi hata wale wasio na CCM angalau wanababaisha kwa kuvaa jezi za Yanga, lakini kimsingi wanataka wavae za CCM na wenyewe wajifananishe na mafanikio makubwa yanayofanyika ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya. Kwa hiyo sisi kama wanachama wa CCM tunajivunia sana kwamba jemedari wetu tuliyemkabidhi Ilani ya Uchaguzi ameitendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amezidi sana, maana amezidi maeneo hata yale tuliyokuwa tumeandika kwenye ilani. Tukienda kwenye umeme amevuka, zaidi ya asilimia 10 zimevuka zile tulizozikadiria kwenye ilani, ukienda kwenye maji, ukienda kwenye barabara na mambo mengine ya maendeleo. Viva Magufuli na itakapofika 2020 itakuwa chagua Magufuli kazi iendelee.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Tumwombee Mheshimiwa Rais afya njema aendelee kudunda na sisi tuendelee kutembea kifua mbele. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Awali na yote na mimi nianze kwa kumshukuru Mungu kwa afya na kwa hatua hii.

Nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kunipa upendeleo huu tena wa kuendelea kumsaidia katika nafasi hii ya Waziri wa Katiba na Sheria. Pia niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Iramba kwa kunirejesha tena Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikirejea kwenye hoja zilizojitokeza hapa leo, hoja ambayo iko mbele yetu ni Hotuba ya Rais na sisi kwa upande wa Mawaziri Hotuba ya Rais ni maelekezo na ni dira na sisi tumepokea twende tukaifanyie kazi. Kwa hiyo, kitu pekee ambacho nitazungumzia hapa, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia katika mwelekeo huo wakitambua kwamba jambo hili ni la kisera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitafafanua tu mambo machache yale ambayo yaliguswa katika Wizara ya Katiba na Sheria. Kuna baadhi ya mambo ambayo yameongelewa, niongee huku nikiwa natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge sisi kama viongozi tuwe watu wa kwanza kuzingatia masuala yanayohusu sheria na katiba ya nchi yetu. Kuna hoja hapa zilizokuwa zinatolewa kwa muundo wa nchi yetu na mipaka ya kikatiba iliyowekwa kwenye taasisi zetu na hata kikanuni humu humu ndani ya Bunge hayapaswi kuongelewa. Sitataja moja baada ya lingine lakini kuna masuala ambayo yameongelea kesi ambazo ziko mahakamani ambazo ziko kwenye mhimili mwingine wa kutoa haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya aina hiyo Waheshimiwa Wabunge yanapokuwa yako kwenye mhimili ambao unasimamia masuala tena uliopewa mamlaka haya ya kikatiba ni masuala ambayo hayapaswi kuongelewa kwa hisia tu na hayapaswi kuongelewa tunapokuwa hapa kama kanuni zetu zinavyoelezea.

Kwa hiyo, kwa hoja zile zilizojitokeza zilizokuwa zinalenga masuala ambayo yako kwenye mahakama zetu tuache utaratibu wa kikatiba, sheria na kanuni tunazozitumia uweze kufanya kazi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kuna mambo mengine baadhi ya wachangiaji walitaka kuyajenga kama vile yanafanyika kwa hisia kama wao walivyobeba hisia. Wanasema kuna watu wetu wamewekwa ndani, kuna watu wetu wamebandikwa kesi, kuna watu wetu wamekamatwa na wengine wanafika hatua ya kusema tu Waziri anayeshughulikia awaachie. Tunawatengenezea Watanzania hisia kana kwamba kuna watu wanaweza wakawekwa ndani bila makosa na kana kwamba kuna watu wanaweza wakatolewa bila kufuata taratibu zetu za kikatiba na za kisheria tulizoziweka. Huu siyo utaratibu uliosawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengine wanasema ni kesi za uchaguzi, niwaambieni na sote tuwe na uelewa wa pamoja, kesi za uchaguzi ni zile zinazohusu rufaa zinazopinga matokeo ama zinazopinga mwenendo. Makosa yoyote ya jinai yanayotokea wakati wa uchaguzi hayafi kwa sababu ulikuwa ni wakati wa uchaguzi. Jinai si kesi ya uchaguzi ni kesi ya makosa ya jinai na taratibu zake za jinsi ya kufanyiwa kazi tumeweka kwenye Katiba na sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mengine yako kwenye mamlaka ambayo imepewa mamlaka yake ya kuchunguza kikatiba na kisheria, hatuyafuti kwa hisia. Mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka iko kikatiba na imepewa mamlaka ya kuangalia kesi ambazo hazifai kuendelea ikazifuta na kesi ambazo zinafaa kuendelea ziendelee. Hatuzifuti kwa hisia wala hatuzifuti kwa maelekezo, ni mamlaka inayojitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuyaelewe haya na tuwaelezee wananchi wetu ili waelewe mipaka ya utawala wa kisheria. Utawala wa kisheria unaendeshwa kwa sheria siyo kwa hisia. Tukiendelea na utaratibu huu wa kusema kwa hisia tunaichafua nchi yetu ambapo wengine sisi hatuna mbadala wa nchi, nchi yetu ni hiihii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliona mengine yanaibuka watu wanasema haki, haki, haki. Kati ya jambo ambalo nina uhakika nalo hata lisingeandikwa kwenye kakitabu kokote kale kwa Rais Magufuli limeandikwa moyoni ni jambo la haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengine wanasema Tume, Tume. Hivi kwa kazi zote hizi zilizoorodheshwa unaenda kushindana kwenye uchaguzi huu na Rais Magufuli utashindaje, unataka Tume ikusaidieje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote tushuhudieni tulipokuwa Majimboni walikuwa wanasema tushindane Udiwani na Ubunge kwa Rais tiki. Wewe unaenda kwanza huna agenda, pili huna mgombea, mgombea wako ana tiketi ya kuja na ya kuondokea, unategemea Tume ya Uchaguzi ikusaidie, inakusaidia wapi? Lazima uanze kuanzia mwanzo uangalie ulikuwa una agenda gani kwenye uchaguzi huo na ulikuwa na mgombea gani, mgombea anayeangalia tiketi, anaangalia nitawahi vipi ndege hii halafu unategemea umpambanishe na mtu ambaye usiku na mchana anashughulika na maisha ya Watanzania, hili haliko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mnaongelea uchumi wa kati eti tumeingizwa uchumi wa kati, ama tumedanganywa, sijui takwimu haziko sawa. Sikilizeni, uchumi wa kati hatuingii kwa kupigiwa kura, hii siyo Bongo Star Search, ni jambo la maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama miaka mitano zaidi ya vijiji 9,800 vimepata umeme na wananchi wake wameunganisha umeme ule. Kama ndani ya miaka mitano zaidi ya trilioni tatu zimekwenda kwenye elimu, zaidi ya trilioni mbili zimekwenda kwenye maji, zaidi ya trilioni moja imekwenda kwenye afya, zaidi ya trilioni moja imekwenda kwenye utawala bora, zaidi ya trilioni tisa zimekwenda kwenye miundombinu ya kuunganisha hawa watu wasafirishe mazao yao, wewe unashangaa kwamba eti tumeambiwa tumeingia, hujui hata kama umeshaingia! Wale ambao wanapata mashaka na jambo hili ombeni darasa muelezewe tu masuala ya uchumi wa kati yanaendaje ili tuache kuichafua nchi yetu wakati inapiga hatua. Hata wale wanaoweka vigezo hivi wanatuheshimu ndiyo maana hata kwa lugha yao kila wakipata tatizo wanasema we need a person like Magufuli ninyi mnakwama wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi, mengine tutaongea kwenye mpango wa maendeleo wiki inayofuata. Ahsante sana, naunga mkono hoja 100%. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi kuweza kuchangia mjadala huu. La kwanza, nitoe pole kwa Watanzania wote kwa msiba huu uliotupata; na nikiri kwamba naunga mkono hoja iliyotolewa na watoa hoja, na kwa kweli wamefafanua kwa kirefu na kwa kina na wameutendea haki mjadala wenyewe huu tunaoujadili, ambao utakaa kwenye kumbukumbu zetu rasmi za Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianzia hapo hapo; katika jambo hili lililotokea nitumie fursa hii kuwashukuru Watanzania. Watanzania wametendea haki uhuru wa nchi yetu, wameipa heshima nchi yetu kwa namna walivyomsindikiza kiongozi wetu, kwa namna walivyomuaga kiongozi wetu. Ni kiongozi aliyesimamia waziwazi uhuru wa nchi yetu, ni kiongozi aliyesimamia waziwazi maslahi ya Watanzania, ni kiongozi aliyesimamia waziwazi na aliyeyatoa maisha yake kwa ajili ya Watanzania. Heshima aliyopewa wakati wanamuaga katika maeneo alikopelekwa; mimi niliendelea kupata hata message maeneo mengine wakisema tunatamani na majiji mengine apite, tunatamani na huku apite; ni basi tu kwa ratiba ilivyokuwa tukafanya kwa uwakilishi. Ile ilikuwa heshima inayolinda na inayotambulisha uhuru wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na wakati anachaguliwa Mheshimiwa Rais wetu pamoja na Makamu wake, watanzania walipiga kura kwa siri. Zile zilikuwa kura za siri na asilimia ilizopatikana ile ilipatikana kwa kura za siri. Lakini namna walivomsindikiza wameitangazia dunia kwamba kwa kura ya wazi walikuwa wanamaanisha nini wakati wanapiga kura wakati wa Uchaguzi Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu neno la faraja kwa Watanzania, kwamba hili limeshatokea. Niwape neno la Faraja; wakati tunaingia kwenye uchaguzi mwaka 2015, Ilani ya Uchaguzi ambayo imetupa matokeo makubwa haya, ambayo ndiyo ilikuwa ahadi kwa Watanzania wabeba maono, kwenye Ilani alikuwa Dkt. Magufuli na Mama Samia Suluhu. Kwahiyo hakuna namna mafanikio yale tuliyoyapata kutoka 2015 - 2020 ukayaongelea bila kumtaja Mama Samia Suluhu. Ameshiriki kikamilifu na yeye ni sehemu ya mafanikio yale. Na katika mafanikio yale wakiwa wao wabeba maono msimamizi wa maono yale, msimamizi wa kazi alikuwa Waziri Mkuu ambaye yupo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo mmoja wa mbeba maono yupo, msimamizi wa mbeba maono yupo lakini wakati mbeba maono na msimamizi wa wapo, pia mbeba kikapu yule aliyekuwa anawezesha yale maono yatekelezwe Dkt. Mpango naye yupo. Kwa maana hiyo hatuna haja ya kuwa na hofu kwa sababu seti hiyo bado imekamilika, ambayo imetupa mafanikio makubwa haya ambayo tumeweza kuyasimulia leo hii. Tunachotakiwa ni kuendelea kwa wale ambao ni mihimili, Bunge na Mahakama kutoa ushirikiano. Kwetu sisi ambao ni wasaidizi wa Serikalini tumepokea maelekeo na tunasimama kuendelea kupokea maelekezo kama ambavyo tumekuwa tukifanya na kuyasimamia ili tuweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hata katika utekelezaji, kinachomfanya kiongozi aweze kusimama na kutekeleza wala si jinsia yake, kinachomfanya kiongozi akemee rushwa wala si jinsia yake, ni uadilifu wake; hata mwanaume akiwa mla rushwa hawezi kukemea rushwa; ni uadilifu wake. Sasa fuatilieni historia ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa sasa hivi, hana record yoyote ya kukosa uadilifu, ni muadilifu ambaye anaweza kwa namna yoyote bila uoga kukemea rushwa mahali popote pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ukiangalia ni mchapa kazi ambaye hapendi kazi ilale. Sisi ambao tumekuwa tukipokea maelekezo tangu muda wote ule tuna uhakika na haya tunayowaelezea. Hata juzi aliposema pale kwetu sisi tayari tumeshapokea yale ni maelekezo. Amesema atasimama imara kwenye mapato na matumizi na masuala ya rushwa. Sisi wasaidizi wake tayari tumeshapigia mstari, na mimi nilishawaelekeza wasaidizi wangu kuendelea kutafasiri yale waendelee kuyafatilia ili yale ambayo yataenda kinyume na maelekezo yake yaweze kuchukuliwa hatua. Maana yake hapo tayari ni zero tolerance of corruption no nonsense on public offices and public funds pamoja na kusimamia haki za watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa mwanamke katika jamii yoyote, mwanamke ni baraka, mwanamke ni kibali. Tanzania inaenda kupata kibali. Na hata ukienda tu kwenye mifano hata ya kawaida, kwasababu nimeshaona kengele imegongwa, hata kwenye mifano ya Maisha ya kawaida tu, yaani hata simba tu tangia wapate CO mwanamke mambo yao yamewanyookea kweli kweli siku hizi hawang’oi hata viti. Maana yake wanabaraka katika nafasi yao na wanafanya vizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliona niweke na hili kwa sababu tunaomboleza, watu wasitoke bado wananyong’onyea nyong’onyea ili tuendelee kuwatia moyo wananchi wetu na Taifa letu liweze kusonga mbele. Naunga mkono hoja na watoa hoja wameielezea vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili na mimi niweze kuchangia azimio hili, na kabla sijaongea niseme moja kwa moja kwamba naunga mkono azimio hili. Ni azimio ambalo limekuja kwa wakati na ni azimio ambalo limebeba uhalisia.

Mheshimiwa Spika, sisi kwa upande wa Wizara ya Fedha tunavitu vingi vya kusema ambavyo vimeshajitokeza katika kipindi cha miaka miwili ambavyo vina beba uzito wa azimio hili. Hivi tunavyoongea katika bajeti hii tunayoitekeleza kwa jitihada za Mheshimiwa Rais za kukuza Demokrasia pamoja na Diplomasia ya Uchumi Kwenye bajeti yetu tulipata dola 500, sawa na trilioni 1.2 katika mwaka wa fedha huu ambao tunaendelea kutekeleza; na hii ni kupitia dirisha la Development Policy Operation, DPO ambayo inatolewa na World Bank. Dirisha hili lilikuwa limefungwa kwa miaka Takribani saba, Tanzania ilikuwa imetolewa katika dirisha hili kwa sababu vigezo vyake vinapatikana kwa good governance, transparency na kwa juhudi za kupambana na masuala ya rushwa. Sasa hivi tuko kwenye programme hiyo ambayo jumla yake ni dola bilioni moja. Milioni 500 zimeingia katika mwaka huu wa fedha na milioni 500 zinaingia katika mwaka wa fedha unaokuja. Kwa hiyo hii ni jambo ambalo tayari limeshafanyika na dirisha ambalo lilikuwa limefungwa.

Mheshimiwa Spika, lakini sio hilo tu tuko kwenye programme mbili na IMF, mojawapo tulifanya ile ya RCF lakini ya pili tumefanya ile ya ECF ambayo ni takribani dola bilioni 1.1. Kwa mwaka wa fedha huu tayari tumeshapata dola milioni 152 quarter ya kwanza na quarter hii kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha tunaoendelea nao tutapata dola milioni 152 nyingine. Fedha hizi ni za recovery programme ndizo ambazo zinaenda kwenye kilimo, umwagiliaji, modernization kwenye mifugo na kwenye uvuvi, hili ni jambo ambalo limeshafanyika na ni programme ya takribani miezi 40. Kwa hiyo tutaendelea na programme hii ambayo ni ya recovery na zinakwenda kwenye sekta za uzalishaji. Na hii inapewa nchi ambayo inakidhi vigezo. Na vigezo vyenyewe vinahusiana na good governance pamoja na matumizi bora ya rasilimali.

Mheshimiwa Spika, kuna hatua zingine ambazo ni kubwa ambazo tunaziendea ambazo mataifa makubwa yamefanya. Moja, tuko kwenye hatua za mwisho za credit rating, tumeshaonana na magwiji wa kufanya credit rating kwenye mataifa, walikuja Mood’s na wengine tumemaliza nao wiki iliyopita. Credit rating inafanyika kwa Taifa ambalo linakidhi vigezo na vigezo vyenyewe ni vya demokrasia pamoja na good governance, na diplomasia ya kiuchumi ambayo hiyo Mheshimiwa Rais amefanya na kwenye ukanda wetu huu Tanzania ndiyo ilikuwa na score kubwa.

Mheshimiwa Spika, tunatarajia watakapotoa report tutakuwa tumepanda juu zaidi, na hii inafanyika na tayari tumeshamaliza tunajua tu report itatoka hivi karibuni. Lakini si hilo tuna lingine ambalo tuko hatua za mwisho ni kuweza kupata fedha za Climate Change RST. Si hilo tu tunatarajia tupate accreditation ya institution zetu. Hivi tunavyoenda accreditation ilikuwa kwenye baadhi ya sekta binafsi lakini sasa hivi tuko hatua za mwisho ili ofisi ya Rais TAMISEMI ipate accreditation na Wizara ya Fedha ipate accreditation,tutaweza kupata fedha ambazo zinatumika katika kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kuweka ustahimilivu wa uchumi pamoja na kuweka sawa kwenye masuala ya balance of payment.

Mheshimiwa Spika, lakini si hivyo tu tuko kwenye hatua za mwisho pia kuangalia na kukamilisha urejeshwaji wa MCC. MCC na yenyewe ilikuwa programme ambayo ilikuwa inatekelezwa na imesaidia sana katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Tuko hatua za mwisho naamini walivyotoa report iliyopita walitumia vigezo vya zamani, tunaamini sasa hivi wakirejea hivyo vigezo ambavyo tunaamini kila mwaka wanakuwa wanatoa hivyo vigezo, tunaamini Tanzania itakuwa imeshafuzu, na hii ni kwa sababu ya hatua kubwa ambazo zimeshafanyika. Vigezo vyenyewe ni vya mikutano ya hadhara ilisharuhusiwa, masuala ya uhuru wa habari ilisharuhusiwa, masuala ya data protection ilisharuhusiwa, protection of investment tulishafanya hivyo vitu.

Mheshimiwa Spika, sio hayo tu ni pamoja na masuala ya kupambana na matumizi bora ya rasilimali. Kuweka misingi bora ya matumizi ya rasilimali. Mheshimiwa Rais amepiga hatua kubwa, Mwaka jana tumeongeza fedha kwa CAG tumeongeza afanye late time audit. Tumeweka fedha kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani. Haya yote ambayo mnaweza mkaona ni kwa sababu ya Mheshimiwa Rais kuweka meno kwa CAG lakini pia na kuweka rasilimali kwa ajili ya ufatiliaji na ukaguzi ambao ndio unatoa majibu na kuweza kusaidia Bunge. Kwa hiyo, haya yote yanayofanywa yanaweka uzito kwamba tunatakiwa tumpongeze Mheshimiwa Rais, tumuunge mkono na kila mtu atimize wajibu wake. Sasa dada yangu, namshukuru Mheshimiwa Chumi amemjibu vizuri alipokuwa anasema kwamba watu wanauliza hii ilifikaje ilifikaje, hayo maswali ni ya kila mtu.

Mheshimiwa Spika, tumefika hapa baada ya Mheshimiwa Rais kwenda kwenye maridhiano na akaweka 4R hizo zote ni za kuweka misingi ya platform kwenye uwanja. Uwanja ukiwa rough lazima opponents awe tough, wewe unategemea watu wawe rough rough halafu umepewa jukumu la nchi uachie? Hamna nchi inayoweza ikaenda hivyo. Kwa hiyo, kwa kuwa Mheshimiwa Rais amekaa na pande zote, tukakubaliana tuendeshe vipi mambo ya nchi hii, hicho ndicho ambacho na CCM inaunga mkono kwa sababu CCM ndio kiongozi wa ustaarabu wa kuendesha nchi hii, ndio maana tangu uhuru mpaka sasa nchi hii haijawahi kupata dosari yoyote ya kukiuka masuala ya haki za binadamu wala hata yale ambayo yanasimuliwa kwenye hizo nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais na ameongea vizuri nadhani Mheshimiwa Ole-sendeka ama Mheshimiwa Mwakasaka kwamba haya tunayoyaweka na haya ambayo tunayokubaliana tuyaheshimu na twende nayo na hiyo ndiyo itakayokuwa dira na hiyo ndiyo itakayotupa sustainability. Maana yake aliuza kwamba kwa hiyo sasa baadaye itakuwaje? Baadaye itakuwa hivi hivi, tuyaheshimu tu haya ambayo tunakubaliana. Hiyo ndiyo misingi ya demokrasia na hiyo ndiyo misingi ya utawala bora na hiyo ndiyo misingi bora ya uendeshaji wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tukishaweka mifumo ikafanya kazi tutakuwa tumejihakikishia masuala ya uendeshaji wa nchi yetu na hivi tuko kwenye utengenezaji wa dira mpya na nawahakikishia kwa haya ambayo Mheshimiwa Rais anayajengea sasa hivi, tuna uhakika dira mpya itakapopinduka kwamba tumeshamaliza miaka mingine hiyo ambayo itakuwa ya utekelezaji wa dira, nchi yetu itakuwa imekwishaenda kwenye nchi zilizoendelea na Watanzania watapata manufaa makubwa ya kubadilisha maisha yao na haya ni mambo ambayo Mheshimiwa Rais anayapigania.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Engineer Chilewesa aliyeleta Azimio hili na Mheshimiwa Mbunge tunaliunga mkono mia kwa mia na tunamtakia kila la heri Mheshimiwa Rais katika kuendeleza haya mambo mazuri. Mengine tutaendelea kuyasema katika bajeti za kisekta na mengine tutayasema katika Bajeti Kuu ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba unipe ruhusa ya dakika moja niwatakie kila la kheri Timu ya Wanachi kesho wanapofanya kazi kubwa ya kupeperusha bendera ya nchi katika hatua kubwa hiyo ya nusu fainali, ambayo ni hatua kubwa sana kwenye mashindano hayo ya hapa Afrika. Niwape pole wenzetu juzi walipambana kule Mtwara lakini wamekufa kiume, mashindano ndivyo yalivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumepokea hoja zote ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezitoa. Hoja ambayo inaangukia katika upande wa Wizara yetu, ya kwanza illikuwa masuala ya kikodi. Kama nilivyosema wakati tunajadili Wizara zingine za Kisekta ambazo masuala ya kikodi yalijitokeza. Nilisema kwamba tunaendelea na mchakato wa kuandaa hatua za kikodi ambazo tutazileta hapa Bungeni na masuala ya Kilimo na yenyewe yapo ambayo yatafanyiwa rejea na kuweza kuboreshwa ili kuweza kutengeneza mazingira rafiki ya kuweza kukuza kilimo chetu. Wizara ya Kisekta inahusika pamoja na sekta binafsi wanahusika katika kuandaa hatua hizo mpya za kikodi ambazo zitakuwa rafiki katika kukuza kilimo chetu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo lilijitokeza pia suala la Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo, Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo tumezipokea hoja ikiwepo ushauri wa namna ya kutunisha mfuko huo kwa kuhusisha taasisi za kifedha za ndani ya nchi pamoja na nje ya nchi. Tumepokea ushauri huo na tutakuja na tamko la kisera tutakapoleta hotuba kuu ya Serikali mapema mwezi ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaahidi Waheshimiwa Wabunge Benki hii ya Kilimo ni Benki yetu na ni engine katika hatua za Mheshimiwa Rais za kuhakikisha tunakwenda kwenye kilimo cha kibiashara. Kwa hiyo tutakuja na tamko la kisera ambalo litakuwa linaendana na maono hayo ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, kwa maslahi ya muda, hoja ya tatu ambayo ilikuwa imetolewa imeongelewa na Waheshimiwa Wabunge na nimesikia Mheshimiwa Mpina akiliongelea na lilikuwa suala la fedha za maendeleo. Utaratibu wetu wa kibajeti tunaotumia hapa nchini ni cash bajeti. Tukishapata ridhaa ya Bunge hapa Bungeni tunapitishiwa makadirio ya mapato na matumizi, hatupitishiwi fedha kwamba ziko mahali hivi zianze kugawanywa kwenda kwenye kila Wizara. Tunapitishiwa makadirio ya mapato tunakwenda kukusanya na tunapitishiwa makadirio ya matumizi, tunapata ridhaa ya kwenda kutumia kwa kila miradi.

Mheshimiwa Spika, kwenye miradi ile ambayo wakati wake wa utekelezaji ni mfupi tunatumia force account. Pale kwenye force account tunatanguliza fedha tunawapatia wanaendelea kutekeleza, lakini kwenye miradi mikubwa kama ya barabara, miradi mikubwa kama ya umwagiliaji, tunachofanya tunafanya kwanza taratibu za mapitio ya taratibu za manunuzi kufuatana na bajeti iliyopitishwa. Tukishapitishiwa taratibu za kimanunuzi, mikataba inasainiwa, mikataba ikishasainiwa hatua ya kwanza ni kutekeleza taratibu za mkataba ambayo ni kulipa asilimia ya kwanza ya awali ambayo ni down payment kwa kila mradi.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo tunaanza kulipa certificate kufuatana na hatua za kiukaguzi wa utekelezaji wa mradi ambao umefikiwa. Hatuingii tu mkataba halafu tukampa fedha zote. Huu sio utaratibu kwamba kwa sababu bajeti ilipita ya bilioni 600 ama bilioni 300 basi baada ya kuingia mkataba tunaenda tunampatia bilioni 300. Huo utaratibu haupo na nimeshangaa sana kwa sababu aliyeongea Mheshimiwa Mpina ni Mbunge mzoefu na amekuwa kwenye Serikali. Ni Waziri mstaafu anajua kwamba tunapotekeleza mradi hata kama bajeti ilipitishwa hatuendi kumpatia yule mkandarasi fedha yote ili aanze kuchukua kutoka kwenye ghala lake.

Mheshimiwa Spika, tunamlipa down payment, tukishamaliza kumlipa down payment tunaanza kumlipa kwa certificate kufuatana na ngazi ya mradi alivyotekeleza na pale ambapo inatokea ngazi ya mradi ambayo ametekeleza haijafika asilimia 100 haina maana kwamba fedha ile imepelekwa kwenye matumizi mengine. Maana yake fedha hiyo inaenda hatua kwa hatua za utekelezaji kadri certificate inavyokuja. Hivyo hivyo hata Bwawa la Mwalimu Nyerere tunavyojenga hatuiingii mkataba wa trilioni sita halafu baada ya kuingia mkataba tukawapatia wakandarasi trilioni sita. Kwanza fedha zenyewe hizo haziko tu mahali zimerundikwa zisubiri kwamba unavyosaini mkataba umpatie yule anayetekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi ya umwagiliaji ni miradi kama ya barabara na hata hii ya sasa ambayo tunatekeleza, tunatekeleza si vimiradi vya mzaha mzaha hivi, tumeamua kutekeleza miradi seriously ya umwagiliaji. Miradi hii kiwango cha chini kabisa cha muda wa utekelezaji itakuwa kwenye miezi 24 hivi. Sasa kama ni miezi 24 mkandarasi unaingiaje naye mkataba halafu uende ukampatie fedha yote ya utekelezaji wa mradi. Unampatiaje fedha ya utekelezaji wa mradi wa miezi 24, siku moja? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatekeleza hivyo hivyo kwenye barabara, tunatoa kufuatana na certificate. Kwa jinsi Mheshimiwa Rais alivyodhamiria kwenye jambo hili la umwagiliaji, hatujakosa fedha ya kutekeleza miradi ya umwagiliaji na hii ni awamu ya kwanza na tutaendelea na awamu zingine na kwenye ile bajeti ambayo ameisoma Mheshimiwa Bashe bado tunamalizia majadiliano mengine na kuna miradi mingine mikubwa tunatarajia tuiseme wakati tunatoa tamko la kisera na tamko la bajeti tutakapoleta hapa kwa ajili ya kupata ridhaa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wananchi pamoja na Waheshimiwa Wabunge, huu ni utaratibu wa cash budget wala hamna fedha ambayo ina ukakasi wowote kuhusu utekelezaji huu wa miradi hii ya umwagiliaji. Kinachofanyika ni taratibu za kutekeleza miradi mikubwa na miradi ya kielelezo. Tumedhamiria kwenye hii miradi ya umwagiliaji na tutaenda kwenye hiyo hatua ambayo tunaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni jambo ambalo si jema sana ile ambapo kila mtu ukikaa unawaza tu kudhania wanaotekeleza wanakosea. Halafu na wengine walishawahi kuwa na fursa pia kama Mpina hivi, haangalii hata yale ambayo yeye aliwahi kutekeleza na watu walikua wanamuongelea namna gani. Yeye kila wakati kuwaza kila Wizara inachotekeleza inakosea. Hii si sahihi, nadhani Mheshimiwa Rais tumtie moyo. Fikirieni tuna miaka 60 tangu uhuru, hivi kwenye hekta zaidi ya milioni 29, ni hekta ngapi zimeshajengewa miradi serious ya umwagiliaji. Sasa mwaka mmoja tu ambao ameanza tunakuja na criticism kibao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. hapa ndio gari lilishaanza kushika gia, nimwachie Mheshimiwa Waziri wa Kisekta ila aendelee… (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi nichangie mambo machache.

Mheshimiwa Spika, kwanza naunga mkono hoja iliyowekwa mezani kwetu na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi pamoja na timu yake, ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta hii ya Ujenzi. Sekta ya Ujenzi ni moja ya sekta ambayo ina miradi mikubwa, miradi yote inaendelea kutekelezwa na tumeshapiga hatua kubwa sana katika utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu naomba nichangie mambo matatu. Jambo la kwanza ambalo ningependa kulichangia ujenzi kwenye sekta hii ya ujenzi, sekta zote ambazo zimetajwa na Mheshimiwa Waziri una bajeti takribani za aina tatu, nne hivi. Bajeti mojawapo ni bajeti hii ambayo tunapitisha, bajeti nyingine ni zile ambazo ziko kwenye mifuko mahsusi, bajeti nyingine ni zile barabara ambazo zinapata udhamini kutoka kwa wabia wetu wa maendeleo, bajeti nyingine ni hii ambayo tumeiongelea ya EPC+F.

Mheshimiwa Spika, niliona Waheshimiwa Wabunge baadhi katika kuchangia akiwepo Mheshimiwa Halima jana wakati anachangia alianza kupiga hesabu kana kwamba barabara zote tunazoenda kuzijenga zinajengwa kwa bajeti hii ambayo inapitishwa kwa maana ya kipengele kimoja kimoja kwa maana ya cash budget ambayo inapitishwa makusanyo ya kila mwezi.

Mheshimiwa Spika, nikaona nipate fursa ya kufafanua huu utaratibu tunaosema wa EPC + F maana yake nini na kwa nini tumebadili utaratibu tukasaini barabara yote kwa urefu wake.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara hizo hazitajengwa ndani ya mwezi mmoja na kwa kufatana na urefu zingine hata hazitajengwa ndani yam waka mmoja. Utaratibu wa EPC+F kwa jinsi ambavyo unatumika ni kwamba Wizara ya Ujenzi ikishafanya utaratibu wa kumpata mkandarasi na mkandarasi akaja na finance award Wizara ya Fedha inafanya terms zile, ina- negotiate zile terms inafanya majadiliano ya vile vigezo vya kupata mkopo wa kifedha ambavyo vinazingatia mambo ya riba pamoja na masuala mengine ya gharama za ukopaji, baada ya hapo kinachofata ni mkandarasi anaanza kulipwa kufatana na utekelezaji wa mradi na fedha zinatoka kwa yule ambaye ni financier wa mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo tulibadili utaratibu huu ili tuweze kupunguza utaratibu huu wa certificate kujazana. Maana yake natolea mfano, kama barabara ya Liwale – Nachingwe - Masasi labda financier wake ni Benki ya CRBD ama City Bank, ama itaje benki yoyote natolea mfano. Maana yake tukishakubaliana terms hiyo fedha itakuwa inatoka kadri anavyotekeleza mradi. Akishatekeleza hatua fulani Wizara inakagua inakubaliana kwamba hii imeshatekelezwa Wizara inatuarifu kwamba huyu hapa ameshatekeleza sisi tunawapa ruhusa benki wanalipa hiyo fedha ambayo imepitishwa kwa ajili ya mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo kwa mazingira hayo hatutarajii hiyo ya kusema kwamba zitatumika bilioni mbili, zitatumika kilometa 200, tutalipa kufuatana na kasi ya utekelezaji tu wa Mkandarasi anavyojenga hiyo ndiyo dhana ya EPC+F.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ziliongelewa barabara ambazo Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanafuatilia, barabara zipo ambazo tunaendelea na majadiliano tuko hatua za mwisho. Timu yangu iko Egypt kwenye annual meeting ya African Development Bank na barabara hizo tuna-conclude tunaamini kwamba zitafanyiwa marekebisho ziingie kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ili ziweze kutekelezwa. Tuna barabara ya Magu – Isandula - Bukwimba kwenda Hungumalwa, tuna barabara ya Kahama kwenda Geita ambayo tunaweka nyongeza kwenye ile fedha ambayo ilishatolewa na mgodi.

Mheshimiwa Spika, tuna barabara ya Iguguno -Nduguti kwenda Sibiti kwa jirani yangu Mheshimiwa Francis Isack naona ameamua kuwa jirani mpaka hapa. Tunayo barabara ya Singida - Ilongero - Haydom ambayo Mheshimiwa Mbunge aliongea kwa nguvu kubwa sana na tuna barabara ya Chunya - Makongorosi kwenda Itigi. Hizi ni barabara ambazo zilishafanyiwa mazungumzo kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na sasa hivi timu iko kule Egypt kukamilisha namna ya utekelezaji wa miradi mingi ikiwemo na hiyo ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho yamekuwa yakitokea pia maswali kuhusu certificate zinazoiva. Kwa utaratibu pale ambapo kasi ya utekelezaji wa mradi inakuwa kubwa sana kama hivi ilivyo sasa hivi, kasi ya utekelezaji wa miradi mingi ni kubwa, inatokea certificate zinakuja kwenye tarehe ambapo kuna commitment zile ambazo ni first charge, kwa hiyo ni kweli ikiangukia kwenye commitment ambayo ni first charge kunakuwepo na utaratibu wa kupitisha kwanza malipo yale yakiwemo ya mishahara ya watumishi wa umma, malipo ya Deni la Taifa, lakini mara zote tunaongeaga na Wizara kuangalia zile deadline ambazo zinajitokeza.

Mheshimiwa Spika, kuna mazingira ambapo mradi unafadhiliwa kwa mkopo ambao unaenda moja kwa moja kwenye utekelezaji wa mradi, mradi ule kama ni wa mkopo tutakuwa tunatekeleza mradi lakini mradi ule lazima utakuwa na riba kwa sababu mradi wenyewe ulikuwa unatekelezwa una mkopo kwa hiyo tunapotekeleza mradi panakuwepo pia na riba kwenye mradi huo.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge barabara hizi zitajengwa na zile ambazo zilikuwa zinaendelea kujengwa zitaendelea kujengwa na hata hivi sasa Mheshimiwa Rais pamoja na Wasaidizi wake anaendelea kututuma baadhi ya maeneo ili kuweza kuhakikisha tunatafuta fedha nyingi zaidi ili kuweza kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo. Tuna majadiliano tumeshafanya hatua ziko za kimikataba na wenzetu wa European Investment Bank, ambayo inahusisha viwanja vya ndege pamoja na baadhi ya barabara na yenyewe ikikamilika Waheshimiwa Wabunge mtaarifiwa miradi ambayo inapatikana katika Majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatekeleza mirdi hii ya barabara kwa sababu ni moja ya nguzo muhimu ambazo zinafungua uchumi wetu na wananchi waendelee kuiamini Serikali yao, waendelee kumwamini Mheshimiwa Rais, waendelee kuwaamini Waheshimiwa Wabunge ambao wao wenyewe wameshuhudia jinsi wanavyoisimamia Serikali na jinsi ambavyo wanasimama kidete kwa ajili ya kuomba barabara hizo ili ziweze kupitika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona kengele ya pili imeni-alert basi naunga mkono hoja na nawapogeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia katika mada ambayo iko mbele yetu. Kwanza naunga mkono hoja ya Waziri aliyoiweka hapa mezani. Pili, niseme tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwatoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, Wizara hii ya Michezo, Utamaduni pamoja na Sanaa ni Wizara mojawapo kati ya Wizara za kipaumbele. Niwaombe waendelee kuiona katika sura hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tuna Mheshimiwa Rais ambaye ni mwanamichezo kweli kweli, tena sio tu mwanamichezo ni mwanamichezo ambaye pia maono yake yana baraka, unaweza ukaona namna ambavyo timu zetu zilivyoweza kufanya vizuri. Taja timu zote ambazo umeona Mheshimiwa Rais ameweka mkono zimeweza kufanya vizuri sana ukianza na timu za wanawake, uje timu za vijana, uje timu za ngumi, taja kila aina ya mchezo unaweza ukaona ambavyo umefanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja tu ambalo linaweza likawa linatofautiana kwa nadharia halafu mpaka ikaonekana labda bajeti ya Wizara hii ni ndogo sana. Ni mategemeo ya Serikali na ni uelekeo wa Serikali ambapo tumeona vile vitu ambavyo vinaweza vikafanywa kwa ufanisi tuna Sekta binafsi, sio lazima Serikali iweke fungu kutoka kwenye Bajeti Kuu. Hii ni kwa sababu ya kukua kwa mahitaji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwambia experience nzuri tu ambayo Waheshimiwa Wabunge wametoa mifano hapa katika nchi zingine nyingi tu ambazo wamefanikiwa kwenye michezo, waliweka dirisha linalotoa fursa kwa sekta binafsi kwa makampuni yaweze kushiriki katika shughuli za michezo na kile watakachokuwa wamekitoa kwenye michezo kinakuwa deducted kwenye kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wenyewe walipitisha mwaka jana, jambo hilo lipo kwenye hatua zetu za kikodi. Kwa maana hiyo ni vile ambavyo labda hamasa haijaweza kukolea lakini jambo hili Bunge lako lilipitisha na huu ndio utaratibu mzuri ambao duniani kote sekta ya michezo inakuwa financed kwa namna hiyo, kwa hiyo nitoe rai kwa makampuni yashiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tutakuwa hatuitendei haki sekta binafsi, tukitaka hata magoli ya uwanja kwamba lazima yatengewe fedha kutoka Mfuko Mkuu. Kuna vitu vingi ambavyo tunaweza tukavifanya ambavyo sekta binafsi haiwezi ikafanya, lakini kwenye haya ya michezo tuna fursa nyingi ambapo sekta binafsi inaweza ikafanya na ika-complement bajeti ya sekta hii ikawa kubwa tu. Kwanza masuala ya michezo kwa jinsi yalivyo siyo mambo ambayo unaweza ukaya-streamline halafu ukaachia kila wakati yatoke Mfuko Mkuu. Kwa hiyo, nasema kwamba tunaendelea nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika pongezi hizi mnazoona mwaka jana, mwaka juzi hata hii five percent ambayo inaenda kwenye Sekta ya Michezo haikuwepo. Tumshukuru Mheshimiwa Rais mwaka jana akasema tutoe five percent ikaenda kule, lakini akaweka na ahadi nyingine kwamba tunapoenda kwenye Bahati Nasibu ya Taifa tutaweka kiwango kingine ni vile tu hatujapata total figure ni kiasi gani, lakini mchakato wa manunuzi utakapokamilika tutakaa na Wizara kwa sababu hilo linatarajiwa lianze tunapoenda mid-year review, tutakaa na Wizara tuwaongezee kiasi kingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hilo tu, tumekaa na Wizara tumewapa fursa EPC+ F kwenye ukarabati na ujenzi wa viwanja ambayo ni bajeti kubwa tutaisemea tunavyokuja kwenye bajeti kubwa ile inayokuja, lakini tulishatoa fursa kwenye bajeti hii inayomalizika wanayo hiyo commitment ili Wabunge waweze kuona ni kwa namna gani Serikali inaweka uzito kwenye jambo hili ambalo wameliongea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato wa bajeti ni mchakato, tumesikia maoni yote haya kwa ujumla wake, tunakokwenda mbele tutaendelea kuboresha ili tuweze kuya-incorporate haya maoni ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge katika kuboresha michezo. Mheshimiwa Rais ni mwanamichezo, mimi mwenyewe ulevi pekee nilionao ni huo wa michezo na nazitakia kila la heri timu zote, nikiipongeza Yanga, sisi ni Mabingwa na nitatoa mwondoko, mabingwa wanaondokaje, Mabingwa wa Afrika nitakapokuja kutoa Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa nafasi hii na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa hoja walizotoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni moja ya hoja ambayo kwa kweli hatukupaswa hapa Bungeni kugawanyika kwa sababu jambo tunaloongelea lina miongozo mikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Kiswahili ni lugha ya Taifa letu na Sheria Mama ya Nchi yetu ambayo ni Katiba imeliweka wazi kwamba lugha itakayotumika ni Kiswahili; na pale ambapo pana mzozo katika eneo ambalo lugha nyingine imetumika, itakayaoshika hatamu ni Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, baada ya kuwa Mheshimiwa Rais wetu, mbeba maono ameona kuna upungufu katika jambo hili la kutumia lugha ya Kiingereza katika uendeshaji wa shughuli zetu akaanza yeye mwenyewe kutolea mfano na hajakwama popote, sanasana amesaidia kunusuru hata fedha zilizokuwa zinapotea kwa watu kupata shida katika kuwasiliana wanapojadili mambo ya mikataba na hata kusaini mikataba. Akaanzisha yeye kuwa mfano kila anapokuwa na shughuli ya Kiserikali anatumia Kiswahili na hili jambo limewezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasi kama Wizara tukasema tutafuata nyendo hizo hizo, twende kwenye utaratibu wa kutumia Kiswahili. Itashangaza sana Mwakilishi wa Wananchi ambaye ametumwa na wananchi, anawajua wananchi walivyo, anakuja kusema kwamba “unajua tukitumia Kiswahili wale watu wa nje hawataelewa tulichokiongea.” Hivi sheria tunamtungia nani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wengi wanaumia, wanakosa haki kwa vile tu sheria na yale mambo wanayokatazwa yameandikwa kwa lugha wasiyoielewa na hata anapohukumiwa, anahukumiwa kwa lugha ambayo haielewi. Sasa wakija na wale wengine ambao wanatamani wapate biashara kwa ajili ya kumtetea mtu, yule ambaye hajasoma kile kilichoandikwa huenda angeridhia hata asingekata rufaa lakini anaambiwa tu unajua usipokata rufaa sasa kwa yule shughuli inaishia hapo, anaridhia tu kwamba basi endelea nalo lakini hajui wanachoendelea nacho ni kipi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge hata kabla hatujaanza mchakato huu, Mahakama walishaanza utaratibu huu. Mwenye mhimili (Jaji Mkuu) hata kabla hatujapitisha sheria alishasema mihutasari yote ya hukumu itaanza kutolewa kwa Kiswahili, maana yake ni kwamba hiki ni kitu kinachowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine sheria zote zitakwenda kutafsiriwa kwa lugha yetu. Tuna wataalam na tumeshajaribisha kwenye ngazi nyingine Serikali za Mitaa walishaanza uandishi huo hata Mahakama zingine zile za mwanzoni kule walishaanza kufanya namna hiyo, hili ni jambo ambalo linawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jaji Mkuu ambaye ni kiongozi wa mhimili alichokuwa anasema kifanyike ni kwanza tubadilishe sheria ambayo inasema lugha ya sheria na ya Mahakama itakuwa Kiswahili ili Hakimu yeyote yule anayetaka kuandika kwa Kiswahili asiwe anavunja sheria. Hawa ndiyo wanaofanya shughuli hizo wanasema jambo hili linawezekana, mwingine ambaye hafanyi shughuli hizo ambaye anatetea wale ambao hawako hapa anasema unajua tukifanya hivi tutawakwaza. Hatutungi sheria kwa ajili ya mataifa mengine wala wananchi wa mataifa mengine, tunatunga sheria kwa ajili ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata nilipoongea na marafiki wa Majaji walikuwa wananiambia, wakasema unajua Majaji tunawapa kazi kubwa sana. Wanawasikiliza watuhumiwa wanapofika pale wanapojieleza kwa Kiswahili, wanawahoji kwa Kiswahili, wanawasikiliza mashahidi na kuandika mashahidi walichokuwa wanasema kwa Kiswahili na mpaka wanafika hatua zile zingine zote kwa Kiswahili, wanaenda kupata shida kwa sababu unapotafsiri kile kinachoandikwa kwa Kiswahili ili wewe ukipeleke Kiingereza wanapata shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mmoja alikuwa ananiambia kwa mfano mtu yuko na kasi yake ya kuongea, wewe unatakiwa uibadilishe upeleke kwenye Kiingereza, anasema walinichoma singe, unaanza kutafuta hii walinichoma singe maana yake, inabidi tu uandike neno singe uende kuanza kutafuta kamusi ili uibadilishe uipeleke kwenye Kiingereza. Sasa utumwa wote huu wa nini yaani wewe mwenyewe Mswahili, unayemhoji ni kwa Kiswahili na makosa yake ni Kiswahili, hata unapolala unaota Kiswahili halafu unajifungia tu mahali ili umridhishe nani? Unaenda kuanza kuhangaika kujipa utumwa kuandika kwa Kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hili anatulindia uhuru wa Taifa letu. Tuache ule utumwa wa kuwaza kizamani. Lugha ya Kiswahili ililikomboa Taifa letu pamoja na mbinu zingine za kutumia kama timu ya Yanga hivi, lugha ya Kiswahili ndiyo iliyokuwa inawaunganisha Watanzania katika kupigania uhuru wakiongozwa na Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa nimetoa ufafanuzi huu, niwatoe hofu sisi Wizara tutaandaa utaratibu pamoja na kushirikiana na mhimili katika utekelezaji wa jambo hili. Hapatakuwepo na matatizo yoyote kwenye utekelezaji, tutaweka utaratibu mzuri. Mahakama wameshaanza tayari kubadilisha Kanuni zao, wataweka utaratibu mzuri. Tutaweka kipindi cha mpito ambacho ni kizuri wakati tunatafsiri sheria ambazo ni rejea katika majukumu haya yote. Hili jambo litafanyika kikamilifu na kwa sababu hatubadilishi hili kwa ajili ya wiki moja, ni jambo la kudumu, kule tunakokwenda baadaye hata hatutakuwa na matatizo ya aina hii lakini ilikuwa lazima tuwe na mahali pa kuanzia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilishawapongeza Simba basi niwatakie na Namungo ambao nao wanawakilisha Taifa wakacheze kwa viwango vya uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naomba kutoa hoja. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, sijaona wakisimama kuunga mkono hoja.

WABUNGE FULANI: Hajatoa hoja.

NAIBU SPIKA: Ametoa hoja.

Waheshimiwa Wabunge, tuwe tunasikilizana. Ukiongea sana unakuwa huna fursa ya kusikiliza wenzako.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 6) Bill, 2021
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa hoja hii imeungwa mkono na Waheshimiwa Wabunge, sitakuwa na mengi ya kusema. Labda moja tu ambalo nilitaka niwape assurance Waheshimiwa Wabunge ni hili ambalo wameulizia kuhusu uanzishwaji wa Ofisi ya Msuluhishi wa Masuala ya Kikodi.

Leo hii hivi tunavyoongea, Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye ndiye Mlipaji Mkuu, pamoja na timu ya ngazi ya Makatibu Wakuu, baadhi ambao walikuwa na masuala yanayohusu miundo kama hiyo, walikuwa na kikao ambacho bado kinaendelea kwa ajili ya kupitisha muundo ambao uta-fit in jambo hili ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelisemea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niliona nilisemee hili kuwapa assurance kwamba siyo jambo ambalo lilikuwa limesimama isipokuwa lilikuwa bado linafuata taratibu za kiutawala, baada ya kupitishwa sheria ingehitajika kutengenezwe muundo ili liweze ku-fit in kwenye muundo na hicho ndicho ambacho leo kikao hicho kilikuwa kinafanyika kwa ajili ya kupitisha muundo na baada ya muundo kupitishwa basi zitafuata taratibu za masuala mengine ya human resource ili ofisi iweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, lakni jambo lingine ambalo ningependa nilifafanue, alisema ndugu yangu kwamba tulitoza kwenye mazao halafu tukasamehe pombe. Hatujasamehe pombe, isipokuwa katika majira haya ya slow down ya kiuchumi, kuna maeneo kwenye sectors tulisema tu tusipandishe. Siyo kwamba tumesamehe, tulisema tusipandishe kwa ajili ya kuzingatia kwamba kama dunia nzima uchumi ulikuwa ume-slow down, ukiendelea kupandisha kodi unaweza uka-discourage zaidi production. Kwa hiyo, hayo ndiyo baadhi ya maeneo ambayo tulikuwa tumeyaangalia.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wote watashuhudia na lenyewe niliwekee tu kumbukumbu, Serikali inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan ni Serikali inayosikiliza sana. Hata Wizara tulipoenda kukaa na Kamati ukienda kwenye Hansard za Kamati wakati wa Bunge la Bajeti hata wenyewe walikiri kwamba kwa kweli tumesikilizwa na karibu kila hoja tulisikilizana. Kwa hiyo niliona na yenyewe hii niiweke sawa isije ikaonekana kama Serikali tunakuwa hatusikilizi.

Mheshimiwa Spika, tunapokea sana ushauri wa Kamati zetu na si kwa Wizara ya Fedha tu, bali kwa Wizara zote, tunapokea sana ushauri wa Kamati zetu na sisi tutaendelea kupokea na kufanyia kazi kama ambavyo matakwa ya sheria yanataka, lakini pia na ushirikiano ambao tunapata kutoka kwa Kamati zetu. Tunajenga nchi moja na hizi tulizonazo ni dhamana tu na kila mmoja hapa ana dhamana kufuatana na mipaka hiyo ya dhamana inavyosema . Kwa maana hiyo, ujenzi wa nchi unatutegemea tu sote na tutaendelea kuyapokea maoni na kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba pia Kamati imekuwa ya msaada sana katika masuala mengi tu. Ikitokea kuna jambo tumeliweka na ukahitajika ulazima wa kuliangalia hizo ni dynamics, unaweza ukaangalia sasa hivi mambo yanavyoenda yanabadilika kwa haraka haraka sana. Kwa hiyo, hizi dynamics ni sehemu ya kusikiliza ushauri na ni sehemu ya Serikali kuwa sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuhahakikishie kwamba kwa kwenda na usikivu huu huu, tutasababisha wananchi wetu kule wapige hatua kubwa sana za kimaendeleo kuliko kuwa rigid katika mambo ambayo uzito wa hoja umeshauona ila ukatae tu, kwa sababu utaonekana ume-create tatizo na kurudi kutafuta suluhisho. Nadhani kufanya uharaka huu ndiyo kupata suluhisho la haraka ambalo linaweza likatufanya tukatengeneza maendeleo na tukatengeneza fursa kwa ukubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, ilitolewa hoja ya kuhusu utekelezaji wa upande wa sheria ambao AG atajibu, lakini kwetu sisi utekelezaji wa hii ambayo itakuwa imepita, tutakaa na Wizara zote ambazo zimeguswa, tuone utekelezaji wake tunaenda nao namna gani. Tutakaa na Wizara zote zikiwemo Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Viwanda pamoja na Local Governments ambao kwa namna moja ama nyingine tutalazimika kushauriana katika baadhi ya maeneo kuhusu smooth transition ya utekelezaji wa jambo hili.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha wa Mwaka 2022
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Na mimi nianze kwa kuwashukuru na kuwapongeza Kamati kwa maoni yao ambayo yametolewa na Mwenyekiti mahiri kabisa wa Kamati ya Bajeti, ndugu yangu Daniel Sillo. Niwashukuru pia wajumbe wa kamati, nimshukuru Naibu Waziri na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao wametoa ushauri wao.

Mheshimiwa Spika, kabla sijafafanua chochote nianze kwanza kwa kuungana na Mheshimiwa Naibu Waziri kuyapokea yale ambayo tumepewa kama ushauri. Mojawapo ikiwa ni hilo la kusimamia kwa umakini maeneo yote yale ambayo yameombewa msamaha. Niseme tu, maeneo yote yale ambayo yatapewa msamaha baada ya idhini ya Baraza la Mawaziri, misamaha hiyo itakuwa inatangazwa kwenye gazeti; na endapo itakuwa misused kama ambavyo imewekwa kwenye sheria, basi itafutwa na ikishafutwa aliyetumia vibaya atalazimika kulipa fedha hiyo ambayo itakuwa aliikosesha Serikali.

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo linahusisha tathmini na lenyewe tumelipokea. Kimsingi tuna sura mbili kwenye masuala haya ya misamaha. Sura ya kwanza ukiiangalia kwenye eneo la papo kwa papo utaona masuala yanayohusu mapato, na ukiwa hujakusanya maana yake unakuwa umekosa mapato.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa sura ya muda mrefu na matatizo ya kiuchumi kwa ujumla, utaweza kuona kwamba tunahitaji uwekezaji kwa kiwango kikubwa zaidi ili kuweza kutengeneza ajira na kuweza kutatua tatizo la ajira na kuongeza mapato katika muda mrefu, kwa maana ya kutengeneza uwekezaji na kutengeneza fursa mpya za uzalishaji, kama ambavyo Mheshimiwa Dkt. Kimei alivyosema.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, sura hizi zote mbili ni lazima uzi- balance, lazima uziangalie kwa namna moja ili upande mmoja usielemewe, ukiuelemea upande mmoja tu wa kukusanya in the long run utakuwa hautengenezi maeneo mapya ya kuweza kukusanya. Kwa hiyo, hivi vyote ni vitu ambavyo vinafanyiwa balance na ndiyo maana unaweza ukaona kwamba maeneo yale ambayo ni ya umuhimu sana kuwekewa vivutio Serikali inaona umuhimu wa kuwekea vivutio.

Mheshimiwa Spika, jambo la tathmini na jambo la utafiti tumepokea, ni mambo ya msingi ambayo mara zote kwa ajili ya kuweza kwenda na mazingira sasa ni mambo ambavyo tunayafanyia kazi na leo tumepokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na tutaendelea kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, nisemee tu kwenye eneo hili la mvinyo. Hili jambo la mvinyo tumepata fursa ya kuwasikiliza hata wakulima wenyewe. Na ukienda kwenye maeneo kwa bahati nzuri zabibu inalimwa hapahapa Dodoma kwa hiyo hatuhitaji kusafiri mbali sana kuweza kupata maoni haya.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba wakulima wetu wamebaki na mvinyo kwa kiwango kikubwa sana, na ni uhalibifu pale ambapo anakosa soko la mvinyo wake. Na kama hatua zisingechukuliwa na Serikali, ni dhahiri kwamba tunakokwenda wakulima wetu wale wangehama kutoka kwenye kulima zabibu wangehamia labda mazao mengine, na hiyo ingeendelea kuturudisha nyuma katika hatua zetu za kulima mazao ambayo yanastawi katika maeneo husika kwa kiwango kikubwa ili tuweze kuuza katika soko la ndani pamoja na soko la nje.

Mheshimiwa Spika, habari iliyo njema, mara nyingi huwa tunakawaida Watanzania wakati mwingine kujikadiria kadirio la chini. Mvinyo wetu si mbaya na wala si kwamba hauna viwango vinavyotakiwa. Hivi tunavyoongea tuna mkulima mdogo tu ana kiwanda kidogo tu, lakini tayari amefikia masoko ya Zambia, Malawi, Uganda na Kenya. Kwa sasa hivi takriban kwa mwezi mmoja tuna-export zaidi ya makontena 10,000 yanakwenda China na makontena kadhaa ya mvinyo yanakwenda Italy. Sasa kama hata yanaweza kufika Italy, na China, na vilevile yameteka soko la ukanda wa kwetu hapa, nadhani si vyema kuendelea kutilia mashaka kwamba mvinyo wetu uko wa kiwango gani na uko wa kiwango gani.

Mheshimiwa Spika, na sasa hata vyuo vya VETA Mheshimiwa Rais alielekeza vianze kufundisha watu kazi wanazofanya katika maeneo husika. Kwa hiyo, tutaendelea hata kuboresha zaidi kuweza kuyafikia na masoko mengine.

Mheshimiwa Spika, na la mwisho Mheshimiwa Cecilia nilimsikia akisema kwamba yasiwe maneno tu iwe vitendo. Moja ya wakati ambapo tunaishara nyingi sana za vitu vinavyofanyika kuliko maneno nadhani ni wakati huu. Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha mwaka mmoja tu vitu ambavyo amevifanya vingekuwa vinapigiwa kelele nadhani vingekuwa vimevuta mipaka hata ya nchi yetu yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi ningeambiwa nimuelezee Rais Samia Suluhu Hassan kwa sentensi moja, kitu kimoja tu ambacho ningesema, sentensi hiyo ingekuwa nchi inasonga mbele kwa kasi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo si maneno ni vitendo. Yaani tunavyosema nchi inasonga hakuna mradi mmoja wowote mkubwa umesimama hata kwa wiki moja tu. Miradi yote mikubwa inaendelea. Lakini na nyongeza, katika kipindi cha mwaka mmoja tu, na ninyi ni Wabunge ndio wawakilishi, wa wananchi; barabara zimejengwa vijijini kuliko mwaka wowote ule katika record tangu uhuru. Tuna vijiji ambavyo tangu uhuru havikuwahi kupata barabara, lakini barabara hizo zimejengwa katika kipindi cha mwaka mmoja na zinapitika. Kwa hiyo, si maneno, ni vitu ambavyo wananchi wanaviona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si hivyo tu, tuna taraja ambazo hazikuwahi kuwa na vituo. Katika kipindi cha mwaka mmoja zimepata vituo na sasa hivi hatua inayofuata ni kwenda kuviwekea miundombinu ama vifaa tiba ili viweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si hayo tu, hata hii tuliyosema juzi kwamba tutabana matumizi si maneno ni jambo ambalo tunaenda kufanya. Tunamaliza makusanyo ndani ya mwisho wa mwezi huu, wiki ijayo tutatoa bilioni 160 kwaajili ya kupeleka ujenzi wa madarasa ambayo Mheshimiwa Rais amesema ifikapo Januari pasiwe na second selection. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka jana hapakuwa na second selection kwa vitendo watoto wote walienda shuleni shule zilipofunguliwa. Na mwaka huu Rais ameelekeza ifikapo Januari madarasa hayo yawe yameshajengwa, hapatakuwa na second selection. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeshaongea na Mheshimiwa Bashungwa, Waziri wa kisekta, wiki ijayo shughuli hiyo inaanza na fedha hizo sehemu zitakuwa zimetoka kwenye makusanyo, sehemu zinatoka kwenye kukata matumizi kufidia sehemu ile ambayo tumeisema katika kauli yetu. Kwa maana hiyo si maneno ni vitendo na vitendo hivyo vinaonekana na vinaongea kwa sauti kubwa kuliko maneno.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ufuatiliaji tutashirikiana na wenzetu wa mamlaka ya mapato pamoja na Wizara zingine za kisekta ili kuweza kuhakikisha tunafuatilia. Hata jana tulipokuwa kwenye Kamati tulikuwa na Wizara ya Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo pamoja na sekta zingine.

Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo ambayo yatahitaji performance agreement tutafanya hivyo ili kuweza kufanya ufuatiliaji unaopimika, na haya tayari tumeshaanza katika sekta zingine ambako maeneo yale tuliweza kuahidi hapa katika Bunge lako Tukufu wakati wa Bajeti Kuu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa nimeyasema hayo, nirejee tena kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.