Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Allan Joseph Kiula (30 total)

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa, swali hili linafanana kabisa hali ilivyo na katika Wilaya ya Mkalama, mkandarasi yuko site lakini aliondoka kwa muda mrefu sasa ndiyo amerudi je, mradi huu utakamilika lini wa usambazaji umeme?
Pia kuna kata nyingi ambazo hazikupitiwa na mradi huu, Kata ya Kikonda, Kinankundu, Msingi, Pambala na Mwanga, je, lini vijiji vilivyopo kwenye Kata hizi vitajumuishwa katika mradi huu?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, mbali na majibu mazuri ya Naibu Waziri naomba nitoe ufafanuzi ufuatao, tarehe 6 na tarehe 7 mwezi huu tunafanya tathmini ya REA Awamu ya Pili, kwa hiyo, REA watakuja na orodha ya miradi iliyokamilika REA Awamu ya Kwanza, REA Awamu ya Pili tunataka na Wakandarasi tujue waliopewa kazi, malipo waliyopewa na kazi inakamilika lini. Kwa hiyo, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania vuteni subira baada ya hiyo tathmini mimi na Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Wakuu tutasambaa nchi nzima kwenda kuthibitisha tuliyoambiwa kwenye kikao chetu ambacho tutakifanyia Mtera.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo REA awamu ya tatu inatayarishwa, lakini REA awamu ya tatu haitaanza wala orodha haitakamilika mpaka kwanza REA awamu ya pili ikamilike na turidhike kwamba imekamilika. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tukiwa huko naomba ushirikiano wenu na ambaye anaona REA awamu ya pili haijaenda vizuri ni vizuri sana anipatie orodha kabla ya kikao chetu cha tarehe 6 na tarehe 7. (Makofi)
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi kuuliza swali la nyongeza. Ili misamaha ya kodi iweze kupungua kufikia asilimia moja ni pamoja na kuhakikisha kwamba sheria zilizopitishwa na Bunge hili zinatekelezwa kikamilifu. Kumekuwa na parallel system, mfano TIC kumekuwa na kikao cha TIC na TRA ambapo TIC ikipokea maombi ya wale wanaoitwa
Strategic Investors wanakaa kikao na wanachagua baadhi ya bidhaa wanazipa msamaha wa kodi. Jambo hili litakoma lini kufanyika? Kwa sababu, pia, linawaweka katika mtego wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato ambao wakishiriki kikao hicho ambacho kinatoa msamaha…
Mheshimiwa Naibu Spika, lini Serikali itahakikisha kwamba, Sheria za Kodi zinatekelezwa kama zilivyopitishwa na Bunge? Kusiwe kuna parallel system?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia kwamba, sheria hizi zinatekelezwa kama ambavyo zimepitishwa na vikao hivi huwa vinafanywa kwa pamoja kati ya wataalam wetu waliopo kwenye TIC na wale wa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Inapofikia sehemu ya discussion kuhusu kodi wataalam hawa hukaa pamoja kuona ni jinsi gani ya kutoa misamaha hii ya kodi. Hakuna sehemu ambako Wataalam wa upande mmoja hukaa peke yao katika kufikia maamuzi haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nalithibitishia Bunge lako sheria zetu kama zinavyopitishwa na Bunge zinatekelezwa kama tulivyopitisha.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo. Kwa sababu Mkalama kuna wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya shaba, ni lini Wizara itawasaidia wachimbaji wadogowadogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba eneo la Mkalama lina madini na siyo shaba tu, yapo madini ya shaba, madini ya ujenzi na madini mengine ya viwandani. Huduma ambazo zitatolewa na Serikali kwa wachimbaji wadogo ni kote nchini ikiwemo pia wachimbaji wadogowadogo wa Mkalama, ni kama ifuatavyo. Hatua ya kwanza kama tulivyosema kwenye bajeti yetu, Waheshimiwa Wabunge niwapongeze sana kwa sababu mmepitisha shilingi bilioni 6.68 kwa ajili ya ruzuku ya wachimbaji wadogo wadogo na ruzuku hiyo itatumika pia kwa wananchi wa Mkalama Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini manufaa mengine ambayo pia Serikali imejizatiti ni pamoja na kuyafanyia utafiti maeneo yote. Sasa hivi Wakala wa Jiolojia Tanzania anapita maeneo yote na kuyafanyia utafiti ili kubaini maeneo ambayo yanaweza kuchimbwa na wachimbaji wadogo kwa tija. Jambo lingine tunalofanya kama Serikali kusaidiwa wachimbaji wadogowadogo ni pamoja na kutoa elimu wezeshi na ushauri kwa ajili ya kuufanya uchimbaji mdogo uwe wa tija zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi tumesogeza sasa huduma zote za ugani huko wachimbaji wadogo waliko. Tumefungua ofisi za madini karibu kila mkoa ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata ushauri nasaha kwa masuala ya afya migodini pamoja na mazingira. Kwa hiyo, huduma za wafanyakazi, huduma za wachimbaji wadogo, zitaendelea kama kawaida na kama ambavyo nimeeleza.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru kwa kunipatia nafasi hii.
Kwa kuwa Wilaya ya Mkalama ni miongoni mwa Wilaya mpya ambazo hazina Mahakama ya Ardhi na huduma hiyo inapatikana Kiomboi.
Je, ni lini Wizara itaona umuhimu wa kutupatia Mahakama ya Ardhi na kuteua Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika majibu ya swali la msingi, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunasogeza huduma hizi kwa wananchi kwa kufungua Mabaraza mengi kama ambavyo tumeyataja namna ambavyo nilisema kwamba tayari Mabaraza 47 Gazeti la Serikali lilikwisha yatangaza. Kwa hiyo kwenye suala la kufungua Baraza la Ardhi katika Wilaya ya Mkalama, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo tutakuwa tumehakikishiwa eneo kwa ajili ya Mahakama, ambapo tumeomba pia Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya katika yale maeneo yenye uhitaji mkubwa waweze kutupa maeneo hayo ili kuweza kufanya. Hivyo, tutaweza kuangalia tukiona kama eneo lipo zuri la kuweza kutosha basi tutaweza kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa tuliyonayo pia, hawa Wenyeviti wa Halmashauri bado ni wachache ukilinganisha na Mabaraza tunayotaka kufungua. Kwa hiyo bado tutakuwa na Wenyeviti ambao watakuwa wanahudumia pengine zaidi ya Baraza moja kulingana na uchache wao. Pale ambapo tutapata ajira mpya basi tutaweza kuwaeneza katika maeneo yao, kwa sasa naomba tu Waheshimiwa Wabunge tuvumiliane katika hilo kwa sababu lengo ni zuri, ni jema lakini bado uhitaji ni mkubwa kwa maana ya Wenyeviti wa kuweza kufanya kazi hiyo. Pale tutakapokuwa tumewapata basi tutafanya kazi hiyo.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.
Kwa kuwa, katika Wilaya ya Mkalama wako wafadhili wa Marekani wanaitwa Family Community Connection wana pesa takribani zinazozidi shilingi bilioni moja, wamejitokeza kujenga kituo cha VETA Nkungi kwa masharti kwamba Halmashauri ipeleke maji na umeme, na Halmashauri haina pesa. Je, Wizara inasema nini, katika mazingira kama hayo na pesa ziko mkononi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ningemwomba kama fedha ziko mkononi anikabidhi basi niwe nazo mfukoni, zisiishie kuwa mkononi ziingie mfukoni kwangu. Lakini ningependa tu kusema kwamba kama suala ni upatikanaji wa maji na miundombinu, nadhani hayo ni mambo ambayo yanazungumzika na Wizara yangu haikuwa na taarifa na hili jambo basi atuletee tu rasmi tutalifanyia kazi, lakini naomba hiyo hela ije iingine mfukoni kwa Waziri wa Elimu ili tuweze kufanyia kazi.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutuahidi kwamba mwaka wa fedha 2017/2018 tutaanza kujengewa mahakama, lakini cha pili nimhakikishie kwamba kiwanja atapata, kiwanja kipo. Sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wananchi wa Mkalama wanapata adha kubwa na wanakwenda kilometa zaidi ya 100 kupata huduma hiyo Kiomboi, katika kipindi hiki cha mpito haoni umuhimu wa kuanzisha mahakama ya Wilaya ya mpito kwa maana kwamba hiyo mahakama ya Wilaya iliyopo inaweza kuhamishiwa katika mahakama iliyopo Gumanga au Iyambi, takribani kilometa 15, ambazo kilometa 15 ni ndani ya kilometa zinazokubalika ili wananchi waanze kupata huduma hiyo wakati wakisubiri hilo jengo jipya na la kisasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Waziri atakuwa tayari kutembelea Wilaya ya Mkalama katika kipindi hiki cha Bunge, maana tukitawanyika hapa tunakuwa hatuonani tena, ili aweze kujionea uhitaji wa Mahakama ya Wilaya na aone viwanja vilivyopo kwa wingi na huduma nyingine za Mahakama za Mwanzo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze na suala la kutembelea MkaLama, Mheshimiwa Kiula nakuhakikishia mkipata kiwanja, kama unavyosema mmepata, lakini chenye nyaraka zote, hata kesho mimi nakuja na nitajitahidi nije na viongozi wa Mahakama kuwathibitishia wananchi kuwa tumedhamiria kuwamalizia tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naelewa pressure aliyonayo Mheshimiwa Kiula kuwapunguzia adha wananchi wa Wilaya mpya ya Mkalama. Namuomba Mheshimiwa avute subira, hiyo mikakati ya mpito haitakuwa na tija sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili yasijitokeze maswali mengine ya nyongeza, nimeona Wabunge wengi wamesimama, naomba niwatulize Waheshimiwa Wabunge wote kuwa katika mwaka huu wa fedha Mfuko wa Mahakama umetengewa jumla ya shilingi bilioni 46.76 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini katika fedha hiyo ujenzi wa mahakama ni shilingi bilioni 36; kwa hiyo ukiunganisha na pesa tuliyokuwa nayo mwaka 2015/2016 ya shilingi bilioni 12.3 tuna shilingi bilioni 48.3 kwa ujenzi wa mahakama. Fedha hizi zitatumika kujenga mahakama 40 nchini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya ujenzi kwa mwaka 2015/2016 na 2016/2017 kwa fedha hii niliyoitamka itakuwa kama ifuatavyo ili Waheshimiwa Wabunge msisumbuke kusimama tena. Tunajenga Mahakama Kuu mpya nne katika Mikoa ya Mara, Kigoma, Dar es Salaam na Arusha.
Tunajenga Mahakama za Mikoa sita za Hakimu Mkazi, katika Mikoa ya Simiyu, Geita, Katavi, Njombe, Songwe na Lindi. Makakama za Wilaya tunajenga 14 ambazo ni Bunda, Kilindi, Bukombe, Chato, Makete, Ruangwa, Kondoa, Kasulu, Nkasi, Sikonge, Chamwino, Namtumbo, Nyasa na Hanang. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama za Mwanzo vilevile tunajenga mpya 16, tena katika kipindi kifupi. Tunajenga Mwanga, Makuyuni (Arusha), Ludewa Mjini, Longido, Lukuledi (Mtwara), Gairo (Morogoro), Nangaka (Nanyumbu), Makongorosi sasa hivi iko Mbeya, Ulyankulu (Tabora), Sangabuye (Nyamagana), Telati (Simanjiro), Mtowisa (Sumbawanga), Uyole (Mbeya), Kibaya (Kiteto), Mgandu (Wanging‟ombe) na Chanika (Dar es Salaam). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwamba katika ujenzi wa mahakama hizi, Mahakama kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi na Baraza la Taifa la Ujenzi watatumia ujenzi wa gharama nafuu, lakini majengo yatakuwa bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetumia teknolojia hii mpya kujenga Mahakama ya Wilaya ya Kibaha ambayo wengi mmeiona tena kwa gharama ndogo ya asilimia 40 chini ya bei ya kawaida ya hizi conventional methods tena kwa kipindi kifupi cha miezi mitatu tu na kwa kiwango kikubwa cha ubora wa jengo.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri yalitolewa na Naibu Waziri, lakini
ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Ulansoni, Nyalelembo Mkalama ambayo yanazalisha sana chakula, yameathirika sana na mmomonyoko wa ardhi. Je, Serikali ipo tayari kupeleka wataalamu kutoka Wizarani na kutoa ushauri namna ya kudhibiti hali hayo kupitia program maalum ya upandaji miti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa tupo katika mkakati wa upandaji miti kama ilivyoelezwa na Wilaya
ya Mkalama imeathiriwa na ukame, kutokana na kutokuwa na miti na mvua kutokunyesha, maeneo kama ya
Mwangeza, Ibada na Mpambala yatapata uhaba mkubwa wa chakula.
Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi hao ambao baadhi yao leo wamefika Bungeni kuweza kufuatilia
suala hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti,
kuhusu swali lake la kwanza la nyongeza ambalo anaomba kupeleka wataalamu katika maeneo hayo, namhakikishia kwamba kama Mheshimiwa alivyoomba, tutapeleka wataalam waliobobea katika mazingira, wataalam waliobobea katika masuala ya misitu kwa maana ya waliopo ofisi yetu na wengine walioko Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la kusema kuwasaidia kuhusu suala zima ambalo linajitokeza sasa hivi
la mmomonyoko mkubwa wa udongo, lakini ukame kutokana na miti imekatwa na uharibifu wa mazingira, hilo
kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi, kama kuna ombi mahususi, basi atuletee tutalishughulikia.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuweza kunipatia nafasi ya kuuliza swali.
Kufuatia majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, je, ni lini Wizara itashuka chini kwenye Halmashauri mpya kama
vile Mkalama, ikarasimisha maeneo ya wananchi kwa sababu kuna miji midogo inayochipua ambapo wananchi wanahitaji maeneo yao yarasimishwe ili waweze kupata mikopo na ardhi yao iwe na thamani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, mimi ningependa kushauri halmashauri mpya zinazoanzishwa, tusikimbilie kwenye suala la urasimishaji, kwa sababu urasimishaji si suluhu ya kupanga miji yetu. Mimi ninachomshauri Mheshimiwa waingie katika maandalizi ya kuwa na mpango kabambe wa kupanga mji wao, ili miji hii yote mipya inayoanza ianze katika mpangilio mzuri wa mipango miji na si kuanza zoezi la kurasimisha. Lakini kwa maeneo ambayo tayari yameshaendelezwa bila kufuata taratibu za mipango miji tutakuwa tayari kushiriki pamoja nao katika kuhakikisha kwamba tunafanya zoezi la urasimishaji, lakini wakati huo huo waingie katika mpango wa maandalisi ya mpango kabambe.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kwa sababu katika Wilaya ya Mkalama ziko shule shikizi ndio hizo satellite schools za Ilangida, Songambele, Ilama pamoja na Mkola ambazo zinafanya kazi lakini hazijasajiliwa. Na TAMISEMI tuliona udahili au uandikishaji unakuwa ni wa kiasi kidogo kwa sababu wanafunzi wengine wadogo wanashindwa kwenda mbali.
Je, Waziri yuko tayari kuingilia suala hili na kuhakikisha shule hizo nne zimesajiliwa, ambapo zimeshajengwa na miundombinu ipo kwa asilimia 80 kama alivyosema muuliza swali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi kama nilivyosema hapo awali kama shule inakidhi vigezo na inastahili kupata usajili basi ni suala la kuwasiliana tuweze kufanya hivyo.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza naomba niweke rekodi sawasawa. Cha kwanza, Wilaya ya Mkalama haina Hospitali ya Wilaya, pili mapato ya ndani ni kidogo ukilinganisha na mahitaji ya Wilaya mpya zote Tanzania na tatu ni kwamba gari lililopo lilirithiwa kutoka Wilaya ya Iramba na uzoefu unaonyesha mgawanyo wa mali unapofanyika Wilaya mpya zinapata yale magari mabovu mabovu, hilo gari lipo tu kwenye vitabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni lini Serikali itatoa magari mapya na ya uhakika kwa Wilaya zote mpya Tanzania ikiwepo Mkalama? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali pamoja na kujenga Kituo cha Afya ina mpango gani wa kunusuru vifo hasa vya akina mama na watoto katika mazingira ya kutokuwepo na gari la wagonjwa? Mheshimiwa Naibu Waziri ameshafika Mkalama na Naibu Waziri wa Afya naye alishafika Mkalama na kuona jiografia ile, hapa nilipo wananchi wangu wanalia kila siku msiba.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Mbunge Jimbo lake limegawanyika kutokana na lile Jimbo alilokuwa Mheshimiwa Mwigulu Mchemba. Tulivyofika pale miongoni mwa changamoto kubwa sana katika Jimbo lake, kwanza kweli hawana Hospitali ya Wilaya lakini ndiyo maana jambo kubwa tulilolifanya kutokana na shida kubwa iliyopatikana pale, Mheshimiwa Mbunge alinipeleka pale na tukaweza kuangalia kwa pamoja tukaweka katika mpango wao wa sasa kuhakikisha kwamba tunakikarabati kile Kituo cha Afya ili waweze kuwa na theater kabisa ya upasuaji wa watoto na Mungu akijalia tutapeleka mradi wa takribani shilingi milioni 700.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la lini gari la wagonjwa litapatikana, naomba nisitoe commitment ni lini litapatikana. Kama nilivyosema awali katika majibu yangu ya msingi kwamba jambo kubwa hili tuanzie katika needs assement ya Halmashauri yetu. Naomba niseme kwamba Serikali imesikia kilio cha Mheshimiwa Allan na tutaangalia uwezekano wowote utakaowezekana, tukipata fursa tutatoa kipaumbele kwa Jimbo la Mkalama kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya kutosha.
Mheshimiwa Mweyekiti, hata hivyo, niseme kwamba kama Serikali kwa umoja wake inajua kwamba wananchi wa Mkalama wana shida kubwa sana, tutajadiliana kwa pamoja kwa mawazo mapana zaidi. Kwa sababu licha ya kutokuwa na vituo vya afya…
Hata miundombinu ya barabara kuwasaidia wagonjwa kufika hospitalini ni shida tutalifanyia kazi.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa sababu kampeni ilizinduliwa tangu mwaka 2016 mpaka leo ni mikoa mitano tu na maeneo mengi yaliyofikiwa yana hospitali kubwa kama Muhimbili, KCMC, sasa ni lini kampeni hiyo itafika katika Mkoa kama wa Singida, Wilaya ya Mkalama na mikoa mingine maeneo ya vijijini kwa sababu vifo vinaendelea kutokea kwa kasi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali itawathibitishia vipi Watanzania, wakiwemo wananchi wa Mkalama, kwamba Serikali inagharamia matibabu kufuatia jibu la Waziri, kwa sababu mimi ni mhanga, mwananchi…
Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itawathibitishia wananchi kugharamia matibabu ya kansa? Mkalama kuna mwananchi amepoteza maisha kwa kukosa dawa.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, ni kwamba tumetengeneza ratiba. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira, muda utakapofika kwa Mkoa wa Singida nimwombe atoe ushirikiano ili zoezi hili liwe la mafanikio.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili ambalo lilikuwa linauliza Serikali imejipangaje kuhusiana na masuala ya upatikanaji wa dawa; napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali katika mwaka huu wa fedha imeongeza bajeti ya dawa kutoka bilioni 30 mpaka zaidi ya bilioni 260.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia, hadi hivi sasa, hali ya upatikanaji wa dawa za kansa ni zaidi ya asilimia 80 na vilevile, hospitali kama ya Ocean Road imefungua dirisha la dawa ambapo dawa nyingine ambazo hazipatikani pale zinapatikana kwa gharama nafuu kuliko katika maduka mengine ya dawa.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza kabisa namshukuru Waziri wa Wizara hiyo kwa sababu alifika na alifanya kazi mpaka saa mbili usiku na akanyeshewa na mvua alifika Ibaga. Pia Waziri aliacha maagizo ya kwamba umeme uende nyumba kwa nyumba usivuke na nguzo ziletwe zaidi ya 20. Nguzo zilizokuja ni 20 na umeme umekwishawaka lakini umetengeneza ubaguzi kwa sababu ziko taasisi za dini hazijapata, misikiti na baadhi ya wananchi. Kwa hiyo, umeme umewaka lakini bado umeleta matatizo. Je, ni lini agizo la Waziri litatekelezwa la kuongeza nguzo, umeme uwake katika maeneo hayo ili tatizo hilo liwe limekwisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wa Mkalama wako tayari kutekeleza sera ya viwanda inayoasisiwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Je, yupo tayari baada ya Bunge kutembelea na kuwathibitishia wananchi kuwaka kwa umeme kupitia REA III kwa Vijiji vya Mwanga, Kidarafa, Kikonda, Ipuli, Isanzu na maeneo mengine ya Mkalama ambayo yana uzalishaji mkubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Allan Kiula kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia utekelezaji wa miradi hii, nimepokea shukrani za Mheshimiwa Waziri wangu kwa ziara yake. Napenda nisisitize agizo lake la Mheshimiwa Waziri la kuagiza kwamba, zifike nguzo za kutosha katika maeneo ambayo miradi Awamu ya Pili haikukamilika katika Mkoa wa Singida litekelezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu kwamba, katika utaratibu huo mkandarasi mpya ambaye amepewa kazi ya kukamilisha miradi ambayo iliachwa na Mkandarasi wa awali Spencon, tumemwelekeza kwamba, maeneo yote nguzo zifike kwa wakati na ni nyingi na wananchi wote wa maeneo yale ambao wamekaa muda mrefu kusubiria umeme wa REA Awamu ya Pili wapatiwe huduma na pasiwepo kitongoji ambacho kimerukwa wala taasisi za jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili; umekuwa utaratibu wa Wizara yetu kwa kuwa, tunatambua miradi hii inatekelezwa vijijini kufanya ziara, wilaya kwa wilaya, kata kwa kata na kijiji kwa kijiji ambako miradi inatekelezwa. Kwa hiyo, nimuahidi kwamba, ziara katika Mkoa wa Singida katika maeneo aliyoyataja ikiwemo Ipali, Mwanga na Isanzu itafanyika kama ambavyo ilivyokuwa kawaida ya Wizara yetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, pia nishukuru kwa kutembelea Singida, tulikuwa pamoja Singida, ninakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la vitunguu maji ambalo linapatikana sana katika Mkoa wa Singida na hasa Mkalama nalo lina changamoto hiyo ya soko. Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuratibu uuzaji wa zao hilo la vitunguu ambapo naona sasa wananchi wanahangaika?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ninayoweza kumuahidi ni kwamba tutawafundisha zaidi wafanyabiashara namna ya kutafuta masoko, na watu wa Serikali ya Sudan Kusini wameonesha nia ya kununua bidhaa direct kutoka Tanzania. Vitunguu vyetu vilikuwa vinatoka hapa vinakwenda nchi nyingine, nchi nyingine inauza Sudan, kwa hiyo tutasaidiana kutafuta masoko, humu ndani na nchi kama nilivyoitaja hii ya Sudan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuratibu hatutaweka mikono kwenye shughuli is a free market tutaliacha soko liende lenyewe lakini mimi na wewe tutawafundisha watu wetu mbinu za kuweza kutafuta masoko ya nje, kuna soko kubwa. Vilevile nichukue muda huu kuwaomba wafanyabiashara wote wa Tanzania, kuna soko la vitunguu na viazi mbatata mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwenye Kisiwa cha Pemba. Wajaze majahazi na vyombo vyote wapeleke, soko liko Pemba kule.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza Wizara swali lifuatalo; kwa kuwa mradi wa vijiji kumi vya maji umefika mpaka Nduguti ambako ndio Makao Makuu ya Wilaya ya Mkalama na chanzo cha maji kimepatikana. Sasa ni lini Wizara itajenga miundombinu ili watu waweze kunywa maji na hiyo ni Wilaya kamili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kwanza ya sekta ya maji ni kutafuta chanzo. Chanzo kikishapatikana kinachofuata sasa ni kuyasambaza maji kuyapeleka kwa wananchi na ndio maana kama nilivyosema kwamba tunatenga fedha. Kwa hiyo, baada ya chanzo kupatikana tayari tumetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri na kwa sababu fedha iko kwenye Halmashauri na wewe ni Diwani katika hiyo Halmashauri basi tushirikiane kuyatoa maji pale yalipopatikana tuwapelekee wananchi. (Makofi)
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa Yulansori, Lelembo wanapata shida kubwa ya barabara na Halmashauri haina uwezo kama ilivyo kwa wananchi wa Mpwapwa na kwa bahati nzuri Waziri wa TAMISEMI alishatembelea maeneo hayo, je, Serikali ina kauli gani kuwasaidia wananchi hawa ambao ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya mahindi, alizeti na vitunguu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilifika maeneo yale mimi na Mbunge tumetembelea barabara ile yenye kilometa 25.2. Kwa sababu changamoto za barabara ile ni kubwa kwani mmomonyoko umekuwa mkubwa kwa bajeti ya kawaida imekuwa ni jambo kubwa sana. Tuliwaelekeza wataalam wafanye upembuzi yakinifu wa barabara ile na inaonekana kuna madaraja na ukibadilisha kuweka tabaka la kifusi, bahati nzuri taarifa hizo zipo katika Ofisi yetu na katika mpango wa bajeti wa mwaka 208/2019 barabara ile ni miongoni mwa barabara za kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwaka huu unaokuja barabara ile tunaenda kuishughulikia. (Makofi)
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza mafupi sana.
Kwa kuwa Serikali imetoa takwimu za mikopo inavyotolewa, lakini uhalisia wenyewe mikopo imekuwa haiwafikii wananchi wa vijijini ikiwemo Mkalama na Wilaya ya Dodoma ambako wanalima sana alizeti.
Je, Serikali iko tayari kuzielekeza benki hizo kwenda kwenye maeneo hayo mahsusi ili kununua zao la alizeti na vitunguu.
Swali la pili, swali la pili, je, Waziri yuko tayari kufuatana na mimi kwenda kuona wakulima wa vitunguu ambao sasa wanavuna ili aweze kutoa maelekezo ya upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo kwa haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nikianza na lile swali lake la nyongeza la (b) kwanza niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda katika Jimbo lake la Iramba Mashariki ili kujionea hilo.
Vilevile ni kwamba Serikali sasa hivi tunaimarisha tafiti zetu kuhakikisha kwamba tunapata mbegu ambazo zitakuwa bora na za uhakika na za bei nafuu tukishirikiana na wakala wetu wa mbolea.
Mheshimiwa Spika, pia tuko katika awamu ya mwisho ya kufanya tafiti ya mbegu tatu za alizeti na zenyewe hizo tafiti hatua ya mwisho tunategemea mwakani tutaanza kutumia.
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye swali lake la (a) ni kwamba lengo la Benki ya Kilimo ni kuhakikisha kabisa kwamba Wilaya zote za Tanzania wanapata mikopo kupitia Benki hii ya Kilimo na kama nilivyosema kwa kujibu katika swali langu la msingi Benki ya Kilimo riba yake ni asilimia nane mpaka 14 kitu ambacho ni masharti nafuu. Vilevile unalipa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, pia Benki ya Kilimo tumeigawa au imegawa kwa Kanda Nane na Mkalama iko katika Mkoa wa Singida na Mkoa wa Singida uko katika Kanda ya Kati kwa maana hiyo na yenyewe iko katika huo mpangilio.
Mheshimiwa Spika na vile vile Benki ya Kilimo ni kwamba inawafuata wakulima kule waliko. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru. (Makofi)
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Barabara ya kutoka Iguguno mpaka Bukundi ambayo ni Mkoa wa Simiyu inaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu, na tunaona sasa daraja la Sibiti linaendelea vizuri kwa ujenzi wake. Ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza kwa jitihada zake mbalimbali anazozifanya katika kuhakikisha kwamba barabara za Jimboni kwake zinapitika muda wote. Na kwa kweli hata wananchi ambao anawawakilisha wanakiri hilo kwa sababu nilipotembelea kule mara ya mwisho waliniambia jitihada zake anazozifanya na nikawaeleza wananchi wa pale jinsi ambavyo anafika ofisini mara kwa mara kuhakikisha kwamba barabara zinapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namshukuru vilevile kwa jinsi alivyotambua jitihada za Serikali za kuhakikisha lile daraja sasa limekwisha kuwa tayari na linapitika. Lakini wale wakandarasi waliotengeneza lile daraja bado wapo eneo la site na ni hao ambao tutawatumia kuhakikisha hicho kipande alichokitaja Mheshimiwa Mbunge kinatengenezwa na kipitike kwa kiwango cha lami.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji wa soko ni kitu muhimu sana hasa ukizingatia eneo hili vijiji vinavyozunguka Miganga, Mwanga na Nkalakala vinalima sana vitunguu na kilimo ni uti wa mgongo, na tunakwenda kwenye uchumi wa kati na uchumi huo lazima uwe supported (to be supported) na kilimo. Je, Serikali lini itatoa uwekezaji wa kutosha kuweza kujenga soko kubwa na la kisasa maana hapa tumeanza tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; upangaji wa madaraja na ufungashaji wa vitunguu unakwenda sambamba na utangazaji wa bidhaa hiyo ambayo ni vitunguu. Serikali inachukua hatua gani kutangaza bidhaa hii ambayo tunatambua kwamba inakwenda katika nchi jirani za Kenya, Mauritius na Sudan Kusini. Ni lini Serikali itachukua hatua za kutangaza bidhaa hii?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Allan Kiula ambavyo tumekuwa tukishrikiana katika suala hili. Niseme tu kwamba naishauri Halmashauri wakati wa bajeti itakapokuja tutenge fedha za kutosha na sisi kwa upande wetu Wizara tutaangalia kila uwezekano unapojitikeza kuweza kusaidia soko hili liweze kupata fedha za kutosha na kulifikisha katika kiwango cha kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusu kutangaza vitunguu vya maeneo hayo, niseme tu kwamba ni kweli vitunguu vinavyotoka kwa ujumla wake katika Mkoa wa Singida ni vizuri sana. Niwaombe Watanzania wote kutumia vitunguu hivyo, lakini pia tutaendelea kutangaza kimataifa na wakati wa shughuli za Sabasaba zinapojitokeza waje pia katika maonesho ili kutangaza vitunguu hivyo.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa sababu yapo maeneo mengine ambayo yanaweza na yenyewe kuwa ni urithi wa dunia, kama vile magofu ya Mjerumani ya Mkalama. Wizara inafanya juhudi gani kuyaweka katika orodha hiyo na kuona namna ya kuyaboresha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Allan Kiula, Mbunge wa Mkalama, rafiki na kaka yangu ambaye tunalingana urefu, hongera sana. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa katika maeneo yale kuna magofu yaliyoachwa na Mjerumani. Katika utaratibu ambao Wizara sasa imeamua kuchukua, tumeamua kuangalia mali kale zote zilizopo na kuziboresha. Ili tuweze kuziboresha, hatua ambazo tumechukua, tumeamua kushirikisha hizi taasisi zilizo chini ya Wizara zenye uwezo kidogo wa kifedha na kuwakabidhi hayo maeneo ili waweze kutengeneza miundombinu mizuri iweze kusaidia katika kuboresha na kuyatangaza na kuvutia watalii katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada hizi, nina imani kabisa yale maeneo ya magofu yatapata ufadhili mzuri sana na hivyo yataimarika vizuri sana na kuweza kuvutia watalii.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, wananchi wa Yulansoni, Lelembo hadi Kitumbili ni wazalishaji wakubwa na barabara hiyo haimo kabisa kwenye mtandao na TARURA haiwezi kutengeneza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI alishatembelea huko na kutoa ahadi ya kutafuta pesa ili barabara hiyo itengenezwe. Je, ni lini barabara hiyo itatengenezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki ambako tunaita maarufu Mkalama, lakini wenyewe tu hawajaleta ombi la kubadilisha jina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba, kuna changamoto kubwa sana katika eneo hilo lote la Mkalama. Wiki mbili zijazo nitatembelea Mkalama, tutapita mpaka hiyo barabara anayoitaja. Hata hivyo kwa hali halisi nitoe tu comfort kwa Bunge lako Tukufu na Wabunge wote, kwamba wenzetu Wahandisi, taaluma yao ni ya kuaminika kwa sababu wanajenga vitu vya kuonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa si kwamba tunadharau taaluma nyingine, ila ni kwa sababu wanajenga vitu ambavyo vinaonekana. Kwa hiyo ili kusudi wafanye kazi zao vizuri, mazingira ambayo tunayaandaa kupitia tathmini ambayo tumeifanya ni kuhakikisha kwamba, tunaweka mazingira mazuri ili kazi zao watakazozifanya ziweze kuonekana vizuri zaidi kwa wananchi.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuweza kunipatia nafasi hii. Umuhimu wa barabara ambayo imeulizwa katika swali hili inafanana kabisa na umuhimu wa barabara ya kutoka Haydom - Kidarafa - Mwanga - Nkhungi - Nduguti mpaka kwenye Daraja la Sibiti kwenda Simiyu. Ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiula, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu Mheshimiwa Kiula anafahamu kwa sababu muda si mrefu tulitembelea barabara hii kutoka Iguguno kupitia Gumanga, tukaenda mpaka Sibiti kuona maendeleo ya ujenzi wa daraja ambalo muda si mrefu litakamilika. Cha msingi niseme tu kwamba barabari hii ya Haydom – Kidarafa hatua zake za kuanza ujenzi ni nzuri na kama nilivyojibu siku chache zilizopita sasa tutakwenda kufanya mkutano wa wadau ikiwemo Waheshimiwa Wabunge na viongozi mbalimbali wa mikoa ambayo barabara hii itapita kwa sababu itaunganisha Mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Simiyu na mikoa mingine ile ya Kanda ya Ziwa. Kwa upande wa Serikali tuko katika hatua nzuri na wakati wowote tutaweza kuanza kujenga barabara hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Kiula asiwe na wasiwasi. Najua tu barabara hii ikikamilika hiki kiungo cha hii barabara tena kutoka Singida kwenda Sibiti nayo ni muhimu ili kufupisha gharama za usafiri kutoka Singida kwenda kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa sababu catch line ni kwamba Halmashauri haina uwezo wa kujenga mabwawa, Serikali ipo tayari kutoa pesa hata bwawa moja moja kujenga mabwawa Mkalama katika maeneo yaliyotajwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa sababu ni ukweli usiopingika kwamba Halmashauri hazina uwezo wa kufanya utafiti, Serikali iko tayari kunipa watafiti nikaondoka nao kwenda kufanya utafiti na mimi nitakuwa nao huko?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyowapigania wananchi wake. Kwa kutambua changamoto kubwa sana ya maji katika Jimbo la Mkalama, Mheshimiwa Waziri wangu aliona haja ya kumsaidia Mheshimiwa Mbunge, akaagiza Mamlaka kwa Wakala wa Uchimbaji Visima (DCCA) kumchimbia visima 20 katika Jimbo lake katika kutatua tatizo la maji. Namwomba Mheshimiwa Mbunge wakati Serikali ikiangalia namna ya kumchimbia mabwawa, asimamie visima hivi ili wananchi wake wapunguze adha ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kumpatia watalaam, sisi kama Wizara ya Maji hatutokuwa na kikwazo chochote kumpatia watalaam aende nao katika kuhakikisha wanafanya utafiti, wananchi wake waendele kupata maji. (Makofi)
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuweza kujenga hiyo Mahakama ya Mwanzo, ni Mahakama nzuri na ya kisasa. Swali la nyongeza, kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri amesema Mahakama ya muda itaanza kabla ya mwisho wa mwezi Juni. Je, ni lini maandalizi ya kuhamisha mafaili ya kesi zilizopo Kiomboi kwenda Iguguno yataanza ili wakati wa uzinduzi na mafaili yawepo? Tusije tukapeleka wafanyakazi halafu kukawa hamna mashauri ya kusikiliza?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeyapokea mapendekezo yake ya kuhakikisha kuwa kabla ya mwezi Juni, 2019 mafaili yawe yamehama kutoka Mahakama ya Kiomboi kwenda Iguguno. Nami nimhakikishie kuwa, ushauri huo tumeuchukua, tutaufanyia kazi na tutahakikisha kabla ya tarehe hiyo, mafaili hayo yatakuwa yamekwishahamia katika Mahakama ambayo imepangwa.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa tena nafasi. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza ikiwemo kushukuru ziara ya Makamu wa Rais ambaye alibaini ubadhirifu wa mradi wa Nyahaa, natumaini Wizara inaendelea kulifanyia kazi suala hilo. Swali la kwanza, je, Serikali iko tayari kuongeza fedha za utafiti hususan katika maeneo yasiyo na miradi mikubwa kama ile iliyopitiwa na maji ya Ziwa Victoria au mkopo wa India ikiwemo Mkalama ili kuweza kupata vyanzo vya uhakika vya maji?

Mheshimiwa Spika, swali la pili je, ni kweli Serikali inatekeleza miradi hiyo na pesa hizo zilitengwa, je ni lini certificate za wakandarasi zitalipwa ili kazi iweze kuendelea kwa sababu kazi kule imesimama kutokana na wakandarasi kutokulipwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Allan Kiula Mbunge wa Jimbo la Mkalama kwa kazi nzuri sana anayoifanya katika jimbo lake. Kubwa ni kuhusu suala zima la utafiti, sisi kama Serikali tunautambua umuhimu wa suala zima la utafiti hasa katika sekta ya maji kwa sababu italeta mapinduzi makubwa. Nataka nimhakikishie sisi kama Serikali hatutokuwa kikwazo kuongeza fedha za utafiti kadiri bajeti itakavyokuwa imeruhusu katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na tafiti ambazo zitaruhusu kufanya mapinduzi katika sekta ya maji.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu suala zima la madai ya wakandarasi hususan katika miradi ya jimbo lake. Utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha, tukubali tulikuwa na madai zaidi ya bilioni 88 ya wakandarasi lakini tunashukuru Wizara ya Fedha ijumaa imetupa zaidi ya bilioni 44 kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi certificate zao na wametupa commitment ndani ya mwezi huu wa nne watatupa bilioni 44 zingine kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi fedha zao.

Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge apate nafasi ya kuwasiliana na sisi katika kuhakikisha tunamlipa mkandarasi wake ili aweze kuendeleza miradi ya maji katika Jimbo lake la Mkalama.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa daraja Sibiti sasa limekamika kwa maana magari yanapita pale juu na Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya ile lami, sasa tungependa kujua kwamba ujenzi wa hizo kilomita 25 za lami umefikia wapi?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kiula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Daraja la Sibiti limekamilika na tayari tumesaini mkataba na mkandarasi yule yule ili aweze kujenga zile kilomita 25 za lami. Kwa hiyo, fedha ipo na mkandarasi yupo na mkataba umesainiwa, anaendelea kujenga kwa kiwango cha lami hizo kilomita 25.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa tena nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Namshukuru Naibu Waziri alishafika maeneo hayo na kesho Mheshimiwa Waziri atakuwa yuko Mkalama kwa suala hili hili.

Maswali mawili ya nyongeza; katika suala zima la mradi wa ujazilizi hasa katika vijiji vya Iguguno, Kinyangiri, Nduguti, Gumanga, Iyambi, Nkalakala, wananchi wameshaelimishwa? Kwa sababu wananchi wanalalamika. Sasa REA wamechukua hatua gani kuwaelimisha wananchi kwamba ujazilizi unakuja?

Swali la pili. Ziko sehemu ambazo umeme umeshawaka, lakini kumekuwa na maeneo ambayo yamerukwa na Naibu Waziri anafahamu na alifika. Ni lini umeme utawaka kwenye Kanisa la TAG Ibaga, Mkalama Kituo cha Afya, Matongo, Kijiji cha Kidi na Kitongoji kimoja cha Gumanga?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana kwa kazi nzuri anayoifanya. Ni kweli tuliambatana pamoja katika maeneo ya Nkito kama ambavyo nimeyataja katika swali langu la msingi, Ibaga na tukawasha umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maswali yake mawili, ameulizia mradi wa ujazilizi. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, ni kwamba Mradi wa Ujasilizi awamu ya pili unaanza Julai, 2019 kwa gharama za shilingi bilioni 197 kwa mikoa tisa ikiwemo Singida Tabora, Shinyanga, Dodoma, Kilimanjaro, Tanga, Pwani na maeneo mengine.

Kwa hiyo nataka nimthibitishie katika huu ujazilizi ya awamu ya pili katika Vijiji alivyovitaja ikiwemo cha Iguguno na Ibagala vitapatiwa umeme na nataka niielekeze REA pamoja na TANESCO ifanye uhamasishaji katika maeneo haya na kwamba TANESCO Mkoa wa Singida ijipange sasa kwa ajili ya vitongoji vyote ambavyo vinatakiwa viingie katika mradi wa ujazilizi, awamu ya pili, mzunguko wa kwanza na mikoa mingine 16 itapatiwa mradi wa ujazilizi, awamu ya pili, mzunguko wa pili, ambao utagharimu zaidi ya bilioni 460 na mazungumzo yanaendelea na Serikali ya Ufarasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza katika maeneo Mbaga na Mkalama kikiwemo na kituo cha afya, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa katika Wilaya ya Mkalama kwa mradi wa REA awamu ya tatu imegusa vijiji 30 na mradi wa REA awamu ya kwanza vilikuwa vijiji 14 na kwa kuwa wilaya yake ina vijiji takribani 70, ni wazi vijiji 26 vitaingia katika rea awamu ya tatu, mzunguko wa pili ambao pia unaanza sambamba mwezi Julai, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inayoendelea sasa hivi katika Wakala wa Nishati Vijijini ni kuandaa makabrasha kwa ajili ya kutangaza zabuni na kuwapata wakandarasi wa kuanza mradi huu ili iwezeshe nchi yetu ifikapo 2020/2021 Juni, tuwe tumemaliza vijiji vyote nchini ambavyo havikuwa na umeme. Ahsante sana.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, naishukuru tena Wizara kwa kazi kubwa inayofanyika hasa kwa kukamilisha Daraja la Sibiti. Napenda kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, Wizara ipo tayari kujenga kilometa 40 kutoka Iguguno mpaka Nduguti kabla ya barabara yoyote ile kukamilika kwa sababu shughuli nyingi zinafanyika sasa pale makao makuu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu barabara hiyo sasa ni barabara ya kiuchumi na magari mengi yanapita huko. Je, Naibu Waziri yuko tayari kufuatana na mimi baada ya Bunge hili ili akaone umuhimu wa uwekaji wa lami katika barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika jibu la msingi kwamba juhudi kubwa zinafanyika kuunganisha mikoa. Hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Kiula tumefanya juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba barabara hii aliyoitaja kutoka Iguguno – Nduguti - Igumanga kwenda mpaka Sibiti imekuwa bora na hata kufanya ujenzi wa madaraja makubwa.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Kiula kwa sababu tumejenga daraja kubwa pale Mnolo ni kwa sababu ya juhudi zake pia na ushirikiano anaoutoa. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo kuhakikisha maeneo mengi yamekuwa bora na yanapitika halafu kidogokidogo mbele ya safari tutakuwa na harakati ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu kuambatana na Mheshimiwa Kiula, Mheshimiwa Kiula anafahamu ipo miradi mingi inayofanyika katika eneo lake ikiwepo kwenye Daraja la Msingi kuna ujenzi mkubwa unaendelea vizuri na miradi mingine mingi ipo na ipo sababu pia ya kutembelea Mkalama. Nitatembelea huko ili tuweze kuona pia miradi mingine inakamilishwa kwa ubora mkubwa. Ahsante sana.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa vile Serikali ikishawekeza pesa nyingi kujenga Kituo cha Polisi cha Mkalama; na kwa vile Naibu Waziri alishafika na akakiona kituo hicho sasa kinaanza kuharibika, ni lini kituo hicho kitakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kituo hiki nakifahamu na tuliambatana na Mheshimiwa Kiula kukitembelea. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama ambavyo tulizungumza wakati wa ile ziara, nami nimeshawasilisha hiyo taarifa na hivi sasa Serikali ipo katika harakati za kutafuta fedha ili kituo hiki kiweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Kiula avute subira wakati Serikali inaendelea na jitihada hizo za kupata fedha za kumaliza Kituo hiki cha Polisi.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ya kukamilisha Daraja la Sibiti. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la pili, kwa sababu sasa Daraja hilo Sibiti limekamika na magari makubwa yanapita juu yakiwemo ma-semi trailer na makampuni mbalimbali ya mabasi yanayoonesha nia ya kupita huko ikiwemo Simiyu, Turu basi. Je, Serikali ipo tayari kuimarisha madaraja madogo madogo yanayokadiriwa kufikia nane ambayo yapo hatarini kuvunjika kutokana na uzito wa magari yanayopita kwenye daraja hilo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; barabara hiyo kwa sababu tumeelezwa kwamba itajengwa, Serikali ina kauli ipi kwa wananchi ambao wamewekewa alama ya X kwenye Vijiji vya Chemchem, Ibaga, Gumanga, Kisuluiga, Nduguti, Ishenga, Kinyangiri na Iguguno? Wangependa kupata kauli kuhusu hatima yao ya maeneo ambayo walikuwa wanayamiliki.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiula, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kiula namna anavyopigania maeneo ya Mkalama na Mkalama inafanya uzalishaji mkubwa sana wa mazao ikiwemo vitunguu na mahindi. Mheshimiwa Kiula mwenyewe ni mkulima kwa hiyo anafahamu mahitaji muhimu ya barabara katika maeneo yake. Niseme tu kweli barabara hii kutoka Iguguno Shamba kwenda Sibiti kilomita 103, iko kwenye utaratibu mzuri wa kuiboresha sana na Mheshimiwa Kiula atakubalina nami kwamba yale madaraja makubwa tumeshaanza kuyafanyia ujenzi na kuna miradi ya ujenzi inaendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Kiula kwamba, yale makalavati madogo madogo ambayo sehemu nyingi yanaonesha kuwa yana usumbufu tunaendelea kuyashughulikia ili yakae vizuri ikiwa ni pamoja na kuondoa zile kona, kwa sababu sasa hivi baada ya kukamilika Daraja la Sibiti magari makubwa nafahamu kwamba yanapita katika barabara hii kwenda kwenye mikoa hiyo ya Simiyu pamoja na Mwanza. Kwa hiyo tunaendelea kufanya marekebisho makubwa ili kusiwe na usumbufu, lakini pia kuepusha ajali ambazo zinaweza kutokana na barabara jinsi ilivyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu wananchi waliowekewa alama ya X niwahahakikishie wananchi hawa, kwanza niwapongeze na kuwashukuru kwa kutoa ushirikiano kwa kuwa na utayari wa kupisha eneo la mradi wa barabara hii muhimu na wananchi hawa wanafahamu kwamba barabara ni kwa ajili ya maendeleo yao. Kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba tumeweka alama za X ili kuwatahadharisha wananchi wasifanye maendelezo makubwa katika maeneo haya. Baada ya kumaliza usanifu wa awali na upembuzi yakinifu, tutajua gharama za kuwafidia wananchi hawa. Niwahakikishie wananchi hawa kwamba tutawafidia ili kupisha mradi ili tuweze kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Waziri ametoa maelezo mazuri sana kuhusu utafutaji wa masoko ambao unafanywa na TanTrade, lakini inaonesha kwamba hizo taarifa TanTrade wanakaa nazo. Na nafikiri kwamba TanTrade wanatakiwa wazipeleke hizo taarifa kwa wahusika, kwa maana watu wetu wa vijijini ambao ndio wakulima.

Je, TanTrade wana mkakati gani wa taarifa hizo kufika zinakohitajika badala ya Wizara kujibu hapa kwa sababu hii ni Wizara sasa tunataka TanTrade ifikishe taarifa kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza nimpongeze yeye pamoja na waliouliza maswali ya awali kwa jinsi ambavyo wanafuatilia suala la mazao haya na kwa manufaa ya wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba TanTrade kama Taasisi tunawataka kutoa elimu mara kwa mara, na sasa hivi pia kupitia maonesho ambayo yanategema kufanyika katika viwanja vya Sabasaba pale Temeke ni fursa nzuri na kubwa kwa wakulima kuweza kujifunza na kupata taarifa mbalimbali kuhusiana na uongezaji wa thamani mazao, lakini pia kupata masoko yanayotakiwa. Kwa hiyo, nimuombe tu kwamba Mheshimiwa Mbunge na yeye mwenyewe akiwa ni sehemu yetu basi anapofanya mikutano yake aweze kuwafikishia wananchi taarifa hizi.