Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Allan Joseph Kiula (14 total)

MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya na kuteua Mahakimu wa Wilaya?
(b) Je, kwa nini Serikali isiridhie Mahakama ya Mwanzo iliyopo ifanywe kuwa Mahakama ya Wilaya?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila wilaya ya kiutawa nchini inatakiwa kuwa na Mahakama ya Wilaya. Kutokana na utaratibu huu Serikali imekuwa ikijitahidi kwa kushirikiana na mahakama kuhakikisha kuwa wilaya zinazoanzishwa zinakuwa pia na huduma ya mahakama. Vigezo vinavyotumika kuanzisha mahakama katika eneo lolote ni pamoja na:-
(i) Hati ya kisheria ya kuwepo kwa Wilaya, Mkoa au Kata;
(ii) Umbali wa upatikanaji wa huduma za mahakama;
(iii) Idadi ya wakazi wa eneo hilo;
(iv) Uwepo wa huduma nyingine za Kiserikali kama Polisi na Magereza;
(v)Upatikanaji wa rasilimali fedha, watu na miundombinu mingine kama viwanja na majengo; na
(vi) Aina ya shughuli za kiuchumi na kijamii za eneo hilo zinazovuta aina fulani ya mashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto ya kukidhi baadhi ya vigezo nilivyoainisha hususan miundombinu, bado kuna Wilaya ambazo zinapata huduma ya mahakama kupitia Wilaya nyingine. Kwa sasa jumla ya Wilaya 21 nchini zinapata huduma ya mahakama kupitia Wilaya nyingine ikiwemo Wilaya ya Mkalama inayohudumiwa na Wilaya ya Iramba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imepanga kujenga jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mkalama kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, Mahakama imeomba kupatiwa kiwanja katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, bado mipango ya upatikanaji wa kiwanja hicho haijakamilika. Tunaiomba Halmashauri kupitia kwa Mheshimiwa Mbunge waweze kutupatia kiwanja hicho mapema ili kutuwezesha kujenga mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila ngazi ya mahakama ina mipaka yake kwa mujibu wa sheria na kanuni na hivyo kila moja inahitajika. Hivyo, hatuwezi kubadilisha Mahakama ya Mwanzo kutumika kama ya Wilaya. Aidha, kutokana na udogo wa jengo la Mahakama ya Mwanzo iliyopo sio rahisi kwa jengo hilo kutumika kwa Mahakama ya Wilaya na ya Mwanzo. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mkalama kuwa wastahimilivu wakati tunasubiri kujenga mahakama yao ya Wilaya.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya Mkalama ni kame sana.
Je, Serikali ipo tayari kusaidia mradi wa upandaji miti katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau wengine ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Mkakati wa Taifa wa Miaka Mitano wa Kupanda Miti (2016/2017 hadi 2020/2021). Kiasi cha shilingi bilioni 105 zinahitajika ambapo kila mwaka imependekezwa zitengwe shilingi bilioni 20 kutoka vyanzo mbalimbali vya Serikali na wadau wa maendeleo kwa ajili ya kutekeleza mkakati huu ambao unaelekeza kila mwananchi, taasisi za Serikali, taasisi za madhehebu, asasi zisizokuwa za kiserikali, kambi za majeshi, magereza, shule, makampuni na kadhalika kupanda na kutunza miti katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na miaka mingine iliyopita, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini, itahakikisha kwamba miti inayopandwa inatunzwa na kukua. Aidha, visababishi vinavyochangia miti kutokuwa vimeainishwa na mikakati ya kudhibiti imeandaliwa ikiwa ni pamoja na upandaji wa aina ya miti kulingana na maeneo na utunzaji wa miti hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Allan Joseph Kiula kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza zoezi la upandaji miti kote nchini kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Wakala wa Misitu Tanzania na Halmashauri zote ikiwemo Halmashauri ya Mkalama ambapo kila Halmashauri
inatakiwa kupanda miti 1,500,000 kila mwaka na kuhakikisha inatunzwa. Aidha, pale itakapoonekana inafaa, Halmashauri zihakikishe maeneo ya wazi yanahifadhiwa ili kuruhusu uoto wa asili ulegee au kutumia mbinu zijulikanazo kama kisiki hai ambapo visiki vilivyo hai hutunzwa hadi kuwa miti mikubwa. Iwapo Mheshimiwa Mbunge ana maombi mahususi awasilishe Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ushauri na hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itasimamia utekelezaji wa mkakati wa taifa wa kupanda na kutunza miti na kuendeleza kuhimiza utekelezaji wa kampeni za upandaji miti na mikakati mingine inayolenga kupanda na kutunza miti nchini.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Wilaya ya Mkalama ni mpya na haina vitendea kazi kama vile magari katika katika Idara ya Afya na huduma za dharura zinapatikana makao makuu huku tarafa zikiwa zimetawanyika hivyo wananchi hasa wajawazito na watoto wamekuwa wakipoteza maisha kabla ya kufika hospitali kwa kukosa usafiri.
Je, ni lini Serikali itatoa gari la wagonjwa (ambulance) tatu kwa kila tarafa ikiwemo Makao Makuu ili kunusuru vifo hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Allan Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ina gari moja la kuhudumia wagonjwa lenye usajili wa namba SM 4263 ambalo lipo katika Kituo cha Afya Kinyangiri. Kwa sasa Halmashauri imeandaa mpango wa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kupata gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Nyamburi ambacho kimewekwa katika mpango wa kufanyiwa ukarabati mkubwa kuwezesha huduma za upasuaji kutolewa.
Aidha, Serikali imepanga kuimarisha vituo vya afya na zahanati ili ziwe na uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa wengi na kupunguza rufaa kwenda katika Hospitali ya Wilaya. Ofisi ya Rais, TAMISEMI itatoa ushirikiano wake pale Halmashauri hiyo itakapoweka kipaumbele katika kutenga fedha kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa gari la wagonjwa katika eneo hilo.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanasababisha vifo vingi, hasa kwa Watanzania wanaoishi vijijini ambako madaktari bingwa na huduma za vipimo vya maabara havipatikani:-
• Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha programu maalum ya kupeleka Madaktari Bingwa na maabara zinazotembea vijijini?
• Je, Serikali ina mpango wa kutoa ruzuku ya tiba kwa Watanzania wasio na uwezo wanaougua magonjwa yasiyoambukizwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza, iliunda kikosikazi ambacho kina wataalam na vifaa tiba vya kutosha ambacho hushirikiana na timu za mikoa kupima na kutibu magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Kwa kuzingatia kuwa wataalam ni wachache hapa nchini na huduma lazima ziwafikiwe wananchi, Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza kimetengeneza mpangokazi na ratiba ya kuzunguka mikoa yote ili kuelimisha na kutoa huduma hizo bila malipo.
Mheshimiwa Spika, kampeni ya kwanza ilizinduliwa tarehe 17 Desemba, 2016 na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwenye Viwanja vya Leaders Club, Mkoani Dar es Salaam. Kampeni kama hizi zimefanyika katika Mikoa ya Dodoma, Katavi, Kilimanjaro na Ruvuma. Hadi hivi sasa utaratibu huu umeweza kuwafikia wananchi takribani 14,896.
Mheshimiwa Spika, aidha, upimaji huambatana na wagonjwa kuchukuliwa vipimo vinavyotoa majibu kwa haraka (rapid test), teknolojia ambayo inaruhusu vipimo kufanyika na majibu kupatikana katika mazingira husika. Hivyo, Serikali haina mpango wa kuweka maabara zinazohamishika (mobile clinics) kwa sasa.
(b) Mheshimiwa Spika, Sera ya Serikali kwa magonjwa sugu, yakiwemo yasiyo ya kuambukiza, ni kwamba matibabu yanatolewa bila malipo kwa wagonjwa kama vile wa kisukari, kansa na shinikizo la damu. Hivyo, Serikali haitoi ruzuku kwa wagonjwa wasio na uwezo, bali inagharamia matibabu kwa wagonjwa wanaogundulika kuwa na magonjwa yasio ya kuambukiza bila malipo. Nashauri wananchi kufika katika vituo vyetu vya kutolea huduma ili kupima afya zao na kupata ushauri wa matibabu mapema.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Wilaya ya Mkalama ina shida kubwa ya Nishati ya Umeme licha ya mpango wa REA II na REA III kuwepo nchi nzima:-
(a) Je, ni lini miradi iliyokuwa chini ya REA II itakamilika baada ya kutekelezwa katika Kata ya Ibega, Mwangeza na Mpambala?
(b) Je, ni lini REA III itaanza Mkalama hasa ikizingatiwa mikoa yote imepata wakandarasi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi ya REA II haikukamilika katika Mkoa wa Singida ikiwemo Wilaya ya Mkalama baada ya Mkandarasi aliyekuwa akitekeleza miradi hiyo kampuni ya Spencon Services kushindwa kukamilisha kazi hiyo kama ilivyopangwa. Utekelezaji wa miradi hiyo ulifikia asilimia 65.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya Kampuni hiyo kushindwa kukamilisha kazi kwa asilimia 35 iliyobaki, vifaa kwa ajili ya kazi hizo vimehifadhiwa katika Ofisi ya TANESCO Mkoani Singida. Vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa Mkandarasi aliyepewa kazi hiyo Mwezi Januari, 2018. Kazi za miradi zilizobaki zinatarajiwa kukamilika ifikapo Mwezi Agosti, 2018
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi anayetekeleza miradi ya REA III Awamu ya kwanza katika Mkoa wa Singida ni Kampuni ya CCCE-ETERN-HEI Consortium ambapo mkataba wa kazi hiyo umesainiwa Mwezi Oktoba, 2017. Kazi za miradi zilianza Mwezi Oktoba, 2017 ambapo Mkandarasi amekamilisha kazi za upimaji na usanifu wa njia za kusambaza umeme pamoja na ununuzi wa vifaa. Mzunguko wa kwanza wa mradi huu Mkoani Singida unatarajwa kukamilika ifikapo Mwezi Juni, 2019, gharama ya mradi ni shilingi bilioni 41.5 wateja zaidi ya 2,997 wanatarajiwa kuunganishiwa umeme kupitia mradi huu.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itachukua hatua za makusudi kutenga mitaji kwa wakulima wadogo wadogo wa mazao ya vitunguu na alizeti katika Wilaya mpya ya Mkalama kupitia benki za mikopo au ruzuku toka Serikalini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa mikopo na mitaji kwa wakulima ni mhimili muhimu katika maendeleo ya kilimo. Hata hivyo upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wakulima unakabiliwa na changamoto kutokana na sekta ya kilimo kukabiliwa na majanga mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na milipuko ya wadudu waharibifu na magonjwa ya mimea. Aidha, kumekuwepo na changamoto ya kukosekana kwa hatimiliki zinazoweza kutumika kama dhamana (collateral) pamoja na riba kubwa isiyoendana na msimu wa uzalishaji mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali ilianzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo inayotoa mikopo ya riba nafuu kati ya asilimia 7-15 ambapo kwa Benki za Biashara riba ni kati ya asilimia 18 - 24. Aidha, masharti mengine kwa waombaji mkopo katika vikundi ni kutumia mashamba yao kama dhamana ya mikopo ambapo muda wa kuanza urejeshaji mikopo (grace period) hufika hadi miezi sita na kipindi cha kurejesha mkopo kufikia hadi miaka 15 kulingana na aina ya mkopo. Aidha, benki hiyo, hadi kufikia mwezi Machi 2018, imeidhinisha mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 38.79 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kilimo nchini, ambapo kwa Mkoa wa Singida peke yake, benki inatarajia kutoa mikopo kulingana na maombi yatakayowasilishwa na wakulima kwa kuzingatia vigezo na masharti.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea kutoa mikopo kupitia Mfuko wa Pembejeo (Agriculture Input Trust Fund – AGITF) ambao unalenga kukopesha wakulima pembejeo na zana za kilimo kwa gharama nafuu, ambapo riba ya mikopo ya AGITF ni kati ya asilimia sita hadi nane ambapo waombaji wa mikopo katika vikundi vilivyosajiliwa hawahitajiki kuwa na dhamana ya hati au mali isiyohamishika.
Katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018 Mfuko wa Pembejeo umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 789,650,000 kwa wakulima wa Mikoa ya Singida na Dodoma ambapo mikopo hiyo ilijumuisha matrekta, pembejeo za kilimo, nyenzo za umwagiliaji na usindikaji.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa mitaji kwa wakulima, Serikali imekuwa ikiimarisha Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kuhamasiasha benki za biashara na wadau mbalimbali ikiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka mikopo kwa wakulima nchini.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio ya Serikali kwamba mikakati hiyo itasaidia katika upatikanaji wa mikopo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kwa riba na masharti nafuu ili kuwawezesha wakulima wadogo kuendesha kilomo chenye tija. (Makofi)
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga soko la kimataifa katika Kata ya Mwangenza kwa ajili ya kuweka katika madaraja vitunguu vinavyolimwa maeneo hayo ili kuvisafirisha katika masoko ya ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimniwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wakulima wa zao la vitunguu katika Wilaya ya Mkalama na Iramba wanakabiliwa na ukosefu wa miundoimbinu rafiki ya soko. Katika hatua ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto hii, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imetenga eneo la ukubwa wa mita za mraba 19,600 kwa ajili ya kujenga soko maalum la vitunguu. Eneo hilo lipo katika Kijiji cha Dominic na linamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa bajeti wa mwaka 2017/2018 kupitia fedha za ruzuku ya maendeleo (Capital Development Grants), Halmashauri ilipewa jumla ya shilingi milioni 40 ambazo zimetumika kuanza ujenzi awamu ya kwanza kwa kujenga uzio wa soko, vyoo kwa ajili ya wafanyabiashara na sehemu maalum ya kuanikia vitunguu yaani vichanja kwenye soko hilo. Kwa sasa eneo hilo linaendelea kutumika kama soko la vitunguu na Halmashauri hiyo imenunua mzani mmoja kwa ajili ya kupima uzito wa bidhaa hizo hivyo kusaidia wakulima kuachana na vipimo vya lumbesa ambavyo vimekuwa vikiwakandamiza kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukidhi matakwa ya masoko makubwa na maalum ya ndani na nje ya nchi, Wizara yetu kupitia wakala wa vipimo imeshauri Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI wanapoanza ujenzi wa soko awamu ya pili uhusishe sehemu ya vifaa vya kuweka madaraja na kufungasha vitunguu kwa viwango vya kimataifa.
MHE. JUSTIN J. MONKO (K.n.y MHE. ALLAN J. KIULA) aliuliza:-
Wilaya ya Mkalama ina vituo vya afya vitatu ambavyo vinakabiliwa na changamoto za uhaba wa watumishi, vipimo, majengo huku idadi ya wakazi wanaohitaji huduma ikiongezeka:-
a) Je, ni lini Serikali itaongeza idadi ya watumishi wa kada zote za kitaaluma katika vituo hivyo?
b) Je, ni lini Serikali itazipandisha hadhi zahanati kubwa ziwe Vituo vya Afya ili kuhudumia wananchi wengi zaidi kutoka Iguguno, Ilanda Msiu na Mkiko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Allan Kiula, Mbunge wa Mkalama, lenye sehemu
(a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeajiri watumishi wa afya 2,534 kwenye hospitali za Wilaya, vituo vya afya na zahanati nchini. Kati ya hao, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ilipata watumishi 12. Vilevile Serikali inakamilisha ajira za watumishi wa afya 6,018 ambao wataajiriwa katika hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati. Maeneo yenye upungufu vikiwemo Vituo vya Afya vya Mkalama vitawekwa katika kipaumbele cha kupatiwa watumishi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuboresha vituo vya afya vilivyopo ili viweze kutoa huduma bora kwa wagonjwa badala ya kupandisha hadhi zahanati zilizopo. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Serikali imejenga Kituo cha Afya Kinyambuli kilichogharimu shilingi milioni 400 ili kuboresha huduma za dharura na upausuaji kwa mama wajawazito.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Wilaya ya Mkalama iliyoko Mkoani Singida hupata mvua chini ya wastani na maji yote ya mvua hutiririka na kupotea.
i. Je, Serikali inachukua hatua zipi kutoa kipaumbele kwa Wilaya ya Mkalama kujengewa mabwawa makubwa hasa ikizingatiwa kuwa fedha za ndani (own sorce) za Halmashauri haziwezi kutosheleza ujenzi wa huduma hii?
ii. Je, ni lini Serikali itafanya utafiti kuona kiwango cha maji kinachopotea wakati wa mvua na kutoa ushauri wenye tija?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeziagiza Halmashauri zote nchini kuainisha maeneo yanayoweza kujengwa mabwawa na kutenga fedha kwenye bajeti zao kwa ajili kujenga angalau bwawa moja kwa mwaka. Katika mwaka 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imeendelea na kazi ya kuainisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ambapo hadi sasa Vijiji vya Kitumbili, Nkito, Malaja, Nkalankala, Lyelembo na Nduguti kazi hii imekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa maji hufanyika linapofanyika zoezi la kuyatambua maeneo yanayofaa kujengwa mabwawa ili kujua kiasi cha maji kinachoweza kuhifadhiwa katika mabwawa hayo ikilinganishwa na mahitaji. Hivyo, kazi hii ya utafiti ya maji yanayopotea kipindi cha mvua yanaweza kufanyika sambamba na zoezi la kuainisha maeneo yanayofaa kwa kujengwa mabwawa. (Makofi)
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-

Wakazi wa Jimbo la Mkalama wanapata shida sana kufuata huduma za Mahakama katika Wilaya ya Iramba – Kiomboi, umbali mrefu kutoka Mkalama:-

(a) Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya yalipo Makao Makuu ya Wilaya ya Mkalama?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuanzisha Mahakama ya muda ya Wilaya katika majengo ya Mahakama ya Mwanzo Nduguti?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama imejiwekea mkakati wa kujenga na kukarabati majengo ya Mahakama kwa awamu, lengo likiwa ni kuwa na majengo katika wilaya zote ifikapo mwaka 2021. Katika mkakati huo, jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mkalama limepangwa kujengwa mwaka 2019 na 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge kuhusu kutumia jengo la Mahakama ya Mwanzo Nduguti kuanzisha huduma za Mahakama ya Wilaya. Hata hivyo, tumefanya tathmini na kubaini kuwa jengo linalotumika sasa kwa Mahakama ya Mwanzo ya Nduguti halitoshelezi kuendesha Mahakama ya Wilaya na ya Mwanzo kwa kuwa mahitaji ya huduma za Mahakama za Mwanzo bado ni makubwa. Mpango tulionao ni kuanzisha Mahakama ya Wilaya katika Mahakama ya Mwanzo Iguguno, ujenzi wa jengo jipya katika Mahakama ya Mwanzo Iguguno umekamilika na kwa tathmini iliyofanyika linaweza kutumika kwa Mahakama ya Wilaya ya Mkalama na Mahakama ya Mwanzo Iguguno kwa muda wakati mipango ya kujenga ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tunaendelea kukamilisha taratibu za upatikanaji wa vifaa, watumishi, pamoja na taratibu za kisheria ili kuweza kuanzisha Mahakama hiyo kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2019.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-

Pamoja na mambo mengine, Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano imelenga kuongeza asilimia za upatikanaji wa maji vijijini.

(a) Je, lini Serikali itafanya utafiti wa vyanzo vya maji katika Jimbo la Mkalama ili kuwa na uhakika wa rasilimali hiyo?

(b) Je, lini Serikali itatoa fedha za kutosha kuwapatia maji safi wananchi wa Jimbo la Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, lenye kipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali kupitia Wizara ya Maji imetenga kiasi cha shilingi milioni 450 kwa ajili ya kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi katika maeneo kame ya Mikoa ya Singida, Mwanza, Tabora na Shinyanga. Utafiti huo utahusisha pia Wilaya ya Mkalama ambapo shilingi milioni 50 zitatumia.

Mheshimiwa Spika, pamoja na utafiti unaotarajiwa kufanyika, Serikali imekua ikitekeleza miradi mbalimbali yamaji katika Vijiji vya Ndunguti, Kinyangiri, Ipuli na pia inatekeleza miradi ya uchimbaji wa visima 24 katika maeneo mengine tofauti. Ili kuhakikisha miradi hii inakamilika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.36 kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-

Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza mpango kabambe wa kusambaza umeme vijijini chini ya mpango wa REA:-

(a) Je, ni lini vijiji vyote 70 vya Wilaya ya Mkalama vitapata umeme wa REA II?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuweka umeme katika vitongoji vinavyopitiwa na njia ya umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza dhamira yake ya kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini ifikapo mwezi Juni, 2021 vikiwemo vijiji 70 vya Wilaya ya Mkalama. Katika Awamu ya Pili ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA II), jumla ya vijiji 14 vya Wilaya ya Mkalama viliwekwa katika mpango wa utekelezaji wa kupatiwa umeme kupitia Mkandarasi M/S JV EMEC & Dynamics.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Aprili, 2019 vijiji vinne vya Nkito Kinyantungu, Nkito Nkurui, Ibaga Sekondari na Ibaga Centre viliwashwa umeme na wateja zaidi ya 100 wameunganishwa umeme. Kwa sasa, Mkandarasi anaendelea na kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji 10 vilivyobaki ambapo kazi hiyo itakamilika ifikapo mwezi Juni, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji na vitongoji vilivyopitiwa na miundombinu ya umeme katika Wilaya ya Mkalama vimejumuisha katika mpango wa kupatiwa umeme kupitia Mradi wa Ujazilizi (densification) awamu ya pili unaotarajia kuanza mwezi Julai, 2019. Aidha, mradi huo utahusisha pia kuvipatia umeme vitongoji vyote vya Wilaya ya Mkalama vilivyopitiwa na njia za umeme kupitia utekelezaji wa mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea. Mradi huu utakamilika mwezi Juni, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-

Barabara itokayo Iguguno –Nduguti –Sibiti hadi Meatu ni kiungo muhimu cha Mikoa ya Singida na Simiyu:-

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara hiyo hasa ikizingatiwa kuwa kazi kubwa ya ujenzi wa Daraja la Sibiti imekamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Bariadi – Kisesa – Mwandoya – Ngoboko – Mwanhuzi – Sibiti – Mkalama hadi Iguguno Shamba yenye urefu wa kilometa 289 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Sehemu kubwa ya barabara hii ni ya changarawe na inapitika wakati wote wa mwaka.

Aidha, ujenzi wa Daraja la Sibiti na barabara unganishi kwa kiwango cha changarawe zenye urefu wa kilometa 25 umekamilika. Hata hivyo, taratibu za manunuzi ziko katika hatua ya mwisho kwa ajili ya kuzijenga kwa kiwango cha lami barabara hizo unganishi zenye jumla ya urefu wa kilometa 25.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi nilizotaja, mkakati wa Serikali kwa sasa ni kukamilisha kuunganisha makao makuu ya mikoa kwa barabara za lami na kujenga barabara kuu zote zinazounganisha Tanzania na nchi jirani kwa kiwango cha lami kama ilivyoainishwa kwenye Shoroba za Maendeleo (Development Corridors). Baada ya hapo, barabara nyingine ikiwempo ya Iguguno – Mkalama – Sibiti – Mwanhuzi – Ngoboko – Bariadi zitafuata kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-

Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuunganisha kwa barabara za lami:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya lami inayounganisha Mikoa ya Simiyu na Singida kupitia Daraja la Sibiti lililopo Wilaya ya Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mikoa ya Simiyu na Singida inaunganishwa na barabara yakutokea Bariadi kupitia Maswa – Lalago-Ng’hoboko- Mwanhuzi- Sibiti – Mkalama- Gumanga – Nduguti - Iguguno Shamba hadi Singida Mjini yenye urefu wa kilomita 341 na inaunganishwa pia na barabara ya kutoka Bariadi kupitia – Mwandoya – Ng’hoboko – Mwanhuzi – Sibiti – Mkalama – Gumanga – Nduguti – Iguguno Shamba – Singida Mjini yenye urefu wa kilomita 338 na barabara hizi zinahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mikoa ya Singida na Simiyu.

Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti lenye urefu wa mita 82 umekamika na ujenzi wa barabara unganishi zenye jumla ya urefu wa kilomita 25 umekamilika kwa kiwango cha changarawe na ambapo taratibu za manunuzi za kuzijenga kwa kiwango cha lami zinaendelea. Barabara ya Sibiti – Mkalama – Gumanga – Nduguti hadi Iguguno kilomita 106 ipo upande wa Mkoa wa Singida na sehemu ya barabara hii kuanzia Sibiti hadi Mkalama kilomita 27 inaendelea kufanyiwa usanifu wa awali kupitia Mradi wa Serengeti Southern Bypass sehemu iliyobaki ya barabara hii ni barabara ya kiwango cha changarawe na hupitika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mkoa wa Simiyu barabara ya kuaznia Sibiti- Mwanhuzi-Ng’hoboko kupitia Lalago- Maswa hadi Bariadi, sehemu ya kuanzia Bariadi - Maswa kilomita 49.5 inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na sehemu ya kuanzia Maswa – Lalago – Ng’hoboko – Mwanhuzi – Sibiti kilomita 146.83 inaendelea kufanyiwa usanifu wa awali kupitia mradi wa Serengeti Southern Bypass Kisesa hadi Bariadi ni bararaba ya changarawe na inapitika vizuri majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina kwa sehemu zilizobaki ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami.