Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Mashimba Mashauri Ndaki (7 total)

MHE. SHALLY J. RAYMOND Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzalisha mbegu bora za kuku wa kienyeji na kuhakikisha zinawafikia wafugaji wa kuku katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa bei nafuu ya ruzuku na kwa wakati?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza nimshukuru Mungu sana kwa kutupa uzima sisi wote na kutulinda, lakini kwa vile ni mara ya kwanza na mimi nasimama mbele ya Bunge lako tukufu, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kunipa nafasi ya kuweza kuendelea kuhudumu kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuku wa asili ambao yeye ameita kuku wa kienyeji, hususan katika uzalishaji na lishe bora kwa watumiaji. Wizara kupitia taasisi yake ya utafiti TALIRI Kituo cha Naliendele, Mtwara inaendelea kufanya utafiti wa aina ipi ya kuku wazazi wa asili watakaotumika kuzalisha vifaranga hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa imesajili makampuni mawili ya AKM Glitters Company, Dar es Salaam na Silverland Poultry Company iliyoko Iringa, kuanzisha mashamba ya kuku wazazi ili kuzalisha vifaranga vya kuku chotara aina ya kuroila na sasso, ambao wanauzwa kwa bei ya ruzuku ya shilingi 1,400 kwa kifaranga cha sasso na shilingi 1,500 kwa kifaranga cha kuroila.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge tunamshauri, kama Wizara, awasiliane na mawakala zaidi ya 15 waliopo mkoani kwake ili waweze kumhudumia pale inapohitajika.
MHE. YAHAYA O. MASSARE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga malambo katika Halmashauri ya Itigi kwa ajili ya wafugaji kunyweshea maji mifugo yao?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inategemea ifikapo mwaka 2025, tutaongeza idadi ya malambo na mabwawa ya maji ya mifugo kutoka 1,384 hadi 1,842 na visima virefu kutoka 103 hadi 225. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara inakamilisha ujenzi wa mabwawa matatu ya Chamakweza kule Chalinze, Kimokouwa, Longido na Narakauo, Simanjiro pamoja na ujenzi wa visima virefu viwili cha Usolanga, Iringa na Mpapa, Manyoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa 2021/2022 Wizara imepanga kutekeleza ujenzi wa mabwawa matano yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 na visima virefu sita vyenye thamani ya shilingi milioni 560 kwa maeneo yenye changamoto ya ukame na uhitaji mkubwa wa maji hapa nchini. Wizara itaangalia uwezekano wa kuingiza Halmashauri ya Itigi katika mpango kutegemeana na bajeti tutakayokuwa tumeipata kwa mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge, Madiwani na Wakurugenzi katika Halmashauri zetu, ikiwemo Halmashauri ya Itigi, kutenga na kutumia asilimia 15 ya mapato ya ndani yatokanayo na mifugo kujenga miundombinu muhimu kwa mifugo, ikiwa ni pamoja na mabwawa, majosho, malambo, visima, minada na kadhalika.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itabadili utaratibu kuwataka wavuvi wanaotumia ring net kutoruhusiwa kuvua mchana na kuvua chini ya mita 50?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya wavu wa ring net wakati wa usiku yanawezesha kuvua samaki wanaolengwa yaani dagaa pekee na kupunguza uwezekano wa kukamata samaki wasiolengwa yaani by-catch. Aidha, matumizi ya wavu wa ring net kwenye kina cha mita 50 wakati wa maji kupwa kwa upande wa baharini na katika umbali wa mita 1,000 kutoka ufukweni kwenye visiwa na rasi kwa upande wa Ziwa Tanganyika yanawezesha kuwa na uvuvi endelevu kwa kutovua samaki wachanga na kutosababisha uharibifu wa maeneo ya mazalia, makulia na malisho ya samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wavuvi pamoja na wadau wa uvuvi kudhibiti matumizi ya zana haramu katika shughuli za uvuvi ikiwemo matumizi ya ring net kwenye kina cha maji chini ya mita 50 na wakati wa mchana ili kuwa na uvuvi endelevu. Hivyo, kupitia Bunge lako tukufu; Serikali inatoa wito kwa jamii za wavuvi kuendelea kuzingatia sheria za nchi katika kulinda rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya sasa na ya kizazi kijacho.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA K.n.y. MHE. JULIANA D. MASABURI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa Vichanja vya kuanikia dagaa Wanawake Wajasiriamali wa Mkoa wa Mara?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kukuza na kuendeleza zao la dagaa na kuliongeza thamani ili liwe moja ya zao kuu la kimkakati litakalochangia katika kuongeza fursa za ajira, usalama wa chakula na lishe na kukuza uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutimiza azma hiyo, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara inatekeleza programu maalum kwa kutumia fedha za mkopo uliotolewa kupitia dirisha la Extended Credit Facility kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa; ambapo shilingi bilioni 1.25 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya ubaridi na mitambo ya kuzalisha barafu kwenye masoko saba ya mazao ya uvuvi na ujenzi wa vichanja vya kukaushia dagaa katika mialo mitatu ya kupokelea samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaangalia uwezekano wa kuwajengea vichanja vya kuanikia dagaa wanawake wajasiriamali wa Mkoa wa Mara katika awamu ya pili ya utekelezaji wa programu hiyo.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga majosho ya mifugo katika Kata za Makilawa, Igelansoni, Iyumbu, Ighombwe, Mgungira na Mwaru Wilayani Ikungi?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu Mbunge wa Singida Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, Wizara inakamilisha ujenzi wa majosho 168 katika Halmashauri 80 kwa gharama ya shilingi bilioni 3.033. Aidha, kati ya majosho hayo, majosho mawili yanajengwa katika Kata za Mgungira na Siuyu katika Halmashauri ya Ikungi.

Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua uhitaji mkubwa wa majosho katika maeneo mbalimbali nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara itaendelea na ujenzi wa majosho katika maeneo yenye uhitaji yakiwemo ya Jimbo la Ikungi. Ahsante.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi wa madarasa katika Kampasi ya Chuo cha Uvuvi Kibirizi utaanza?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kupitia kampasi ya Kibirizi ulianza kutoa mafunzo ya muda mrefu ya tasnia ya uvuvi mwaka 2013/2014 kwa kutumia majengo ya kilichokuwa Kiwanda cha Mashua Kigoma ambacho kilikuwa katika eneo la Kibirizi. Hivyo, kwa sasa kampasi ya Kibirizi inatoa mafunzo ya teknolojia ya ukuzaji viumbe maji (aquaculture technology) katika ngazi za Astashahada na Stashahada kwa kutumia madarasa yaliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuimarisha Kampasi ya Kibirizi kwa kujenga madarasa mapya na kuipatia vitendea kazi ili iweze kutoa mafunzo zaidi ikiwemo masomo ya sayansi na teknolojia ya uvuvi (fisheries science and technology) na usimamizi wa uvuvi (fisheries management) ngazi za Astashahada na Stashahada, ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwezesha ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki katika Wilaya ya Ukerewe?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika uchumi unaozingatia misingi ya Sera ya soko huria ujenzi wa viwanda mbalimbali vikiwemo viwanda vya kuchakata samaki unafanywa na sekta binafsi. Jukumu la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda. Kwa kuzingatia sera hiyo Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuhamasisha wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje kuja kujenga viwanda vya kuchakata samaki katika Wilaya ya Ukerewe pamoja na maghala ya kuhifadhia na kugandisha mazao ya uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuhamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi, maghala ya kuhifadhia na kugandishia mazao ya uvuvi katika maeneo ya uvuvi yenye mavuno mengi hapa nchini ikiwemo Wilaya ya Ukerewe. (Makofi)