Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Luhaga Joelson Mpina (11 total)

MHE. LUHAGA J. MPINA Aliuliza: -

(a) Je, ni sababu gani zilizopelekea kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere?

(b) Je, kwa nini Mkandarasi ameshindwa kujaza maji kwenye Bwawa kufikia tarehe 15 Novemba, 2021 kama ilivyokuwa imekubalika?

(c) Je, ni hatua gani zimechukuliwa kutokana na ucheleweshwaji huo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema wenzangu, nami kabla ya kujibu swali nimshukuru sana Mwenyekiti Mungu kwa afya na amani, lakini pia nimshukuru Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini kuhudumu katika nafasi hii ya Naibu Waziri wa Nishati. Pia niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kwa uchaguzi mkubwa, wa maajabu na wa furaha tulioufanya jana hapa Bungeni wa kumchagua Mheshimiwa Spika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wa kukamilika kwa mradi kimkataba ni tarehe 14 Juni, 2022. Tarehe hiyo bado haijafikiwa.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili bwawa la Mwalimu Julius Nyerere lianze kujazwa maji, ni sharti liwe limejengwa kufikia kimo cha mita 95 juu ya usawa wa bahari ambapo kazi hiyo imekamilika. Aidha, ilitakiwa handaki lililojengwa kuchepusha maji ya Mto Rufiji kuzibwa. Kazi ya kuziba au kufunika handaki kwa kutumia vyuma maalum vizito ilihitaji mfumo maalum ambao ni wa kudumu wa mitambo ya kubebea milango hiyo (Hoist Crane system) kuwepo katika eneo la mradi. Mfumo huo unatengenezwa mahsusi kwa ajili ya kazi hii na kazi hii inapoisha crane hizo huondolewa na hazitumiki kwa kazi nyingine. Mitambo hiyo ilichelewa kufika kwa wakati kutokana na viwanda kufungwa na safari za meli kuathiriwa kutokana na UVIKO 19. Milango na mtambo wa kubebea tayari imefika na kazi za kuifunga zinatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2022.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO inaendelea kumsimamia mkandarasi aongeze kasi ya utekelezaji wa ujenzi ili kufidia muda uliopotea kwa kuongeza wafanyakazi na muda wa kazi.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, ni nini kinachosababisha kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya shilingi trilioni 360 na dola za Marekani milioni 181.4 kutoamuliwa hadi sasa?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali haina kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya shilingi trilioni 360 na dola za Marekani milioni 181.4 ambazo hazijaamuliwa. Aidha, hadi Agosti, 2022 kulikuwa na mashauri 854 kwenye hatua mbalimbali za usikilizaji yenye kodi inayobishaniwa ya jumla ya shilingi 4,207,442,214,759.93 (trilioni 4.21) na dola za Marekani 3,480,867.96 (milioni 3.48) katika Bodi ya Rufaa za Kodi na Baraza la Rufaa za Kodi.

Hivyo, kwa sasa taasisi za rufaa za kodi zinaendelea kusikiliza mashauri hayo pamoja na mashauri mapya yanayoendelea kusajiliwa. Vilevile kwa nyakati tofauti, idadi ya mashauri ya kodi hupungua au kuongezeka kulingana na kasi ya usikilizaji na usajili.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, ni nini kinachosababisha kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya shilingi trilioni 360 na dola za Marekani milioni 181.4 kutoamuliwa hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hadi Agosti, 2022 kulikuwa na idadi ya mashauri 854 kwenye hatua mbalimbali za usikilizaji yenye kodi inayobishaniwa ya jumla ya Shilingi trilioni 4.21 na dola za Marekani milioni 3.48 katika Taasisi za Rufani za Kodi ambazo ni TRAB na TRAT. Hivyo, kwa sasa TRAB na TRAT zinaendelea kusikiliza mashauri hayo pamoja na mashauri mapya yanayoendelea kusajiliwa. Aidha, kwa nyakati tofauti idadi ya mashauri ya kodi hupungua au kuongezeka kulingana na kasi ya usikilizaji na usajili. Ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itarejesha kwa wafugaji mifugo iliyokamatwa na TAWA, TFS na WMA ambapo Mahakama ilitoa hukumu irejeshwe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ni kosa kuingiza na kuchunga mifugo ndani ya Hifadhi. Serikali ina jukumu la kulinda Rasilimali na Maliasili za Taifa, ikiwa ni pamoja na kuzuia uharibifu unaosababishwa na uvamizi wa mifugo ndani ya maeneo ya Hifadhi.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wanapokamatwa na mifugo ndani ya hifadhi kesi zao hupelekwa Mahakamani ambapo hukumu hutegemea na maamuzi ya Mahakama. Hukumu inaweza kuwa kulipa faini na kurejeshewa mifugo au kutaifishwa. Endapo kuna wananchi ambao mifugo yao ilikamatwa na Mahakama kuamuru kurejeshewa mifugo yao na hawajarejeshewa, wawasilishe malalamiko yao Wizarani ili yashughulikiwe.

Mheshimiwa Spika, ili kuepukana na migogoro ya wafugaji, Serikali inawaomba wananchi hususani wafugaji kujiepusha kuingiza mifugo kwenye maeneo ya Hifadhi.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, ni Vijana wangapi hawana ajira nchini na Serikali imewaandaaje kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2021 unaonesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15-35 ambao wana ukosefu wa ajira ni 1,732,509. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 12.2 ya nguvu kazi, maana ya vijana walio katika umri huo na wapo katika mfunzo au hawana ulemavu unaosababisha wasijishughulishe na shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika kuhakikisha kwamba Vijana wanaendelezwa ipasavyo kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeweka mkakati wa kitaifa wa kukuza ujuzi wa miaka 10 mwaka 2016/2017 – mwaka 2025/2026. Kupitia mkakati huu, Serikali imefanya maboresho ya miundombinu ya mitaala katika ngazi za Elimu ya Juu, Elimu ya Kati, na Mafunzo Stadi ya Ufundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, sambamba na maboresho hayo, Serikali imetoa mafunzo ya kuwezesha vijana walio nje ya mafunzo rasmi ili kumudu ushindani katika soko la ajira, yakiwemo mafunzo ya uanagenzi, mafunzo ya uzoefu wa kazi (internship) kwa wahitimu, mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu (RPL), na mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya vitalu nyumba. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA K.n.y. MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, nini kimesababisha mbolea kuadimika na kuleta hasara kwa Wakulima na Wawekezaji nchini katika msimu wa mwaka 2022/2023?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nchi katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 hatukuwa na uhaba wowote wa mbolea. Vilevile Serikali haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wakulima na wawekezaji yanayohusu kupata hasara kutokana na kuadimika kwa mbolea. Changamoto pekee ilijitokeza ilikuwa ni mwamko mkubwa wa wakulima kuhitaji kununua mbolea kuliko uwezo wa mtandao wa mawakala, ambapo Serikali imeendelea kuipatia ufumbuzi na kuongeza idadi ya mawakala kutoka 1,392 mwezi Agosti, 2022 hadi 3,265 mwezi Machi, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makadirio ya mahitaji ya mbolea kwa msimu wa 2022/2023 yalikuwa ni tani tani 667,730 na hali ya upatikanaji wa mbolea hadi kufikia mwezi Machi, 2023 umefikia tani 748,890 sawa na asilimia 112 ya mahitaji ya mbolea ndani ya nchi, ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, kwa nini ilitumika njia ya single source kumpata Mkandarasi wa SGR Lot No. 6 Tabora – Kigoma na kusababisha hasara ya trilioni mbili?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Manunuzi ya Umma imeainisha njia mbalimbali za manunuzi ya mkandarasi zinazoweza kutumiwa na Serikali ikiwa ni pamoja na njia ya single source. Aidha, Manunuzi ya Mkandarasi kwa kipande cha Tabora - Kigoma yalifuata Sheria za Manunuzi ya Umma Na. 7 ya Mwaka 2011 na Kanuni zake Na. 161 (1) (a) mpaka (c) (Single source Procurement for works) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2013 na Marekebisho yake ya mwaka 2016.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa hakuna hasara yoyote iliyosababishwa na ununuzi wa mkandarasi wa ujenzi wa njia ya reli ya Tabora – Kigoma, bali ununuzi wa mkandarasi ulifuata taratibu zote za manunuzi ikiwemo majadiliano kwa lengo la kuhakikisha gharama sahihi za mradi zinapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, makadirio ya gharama za kihandisi (Engineering Estimates) yalikuwa dola za Marekani bilioni 3.066 sawa na shilingi trilioni 7.2 ikilinganishwa na gharama halisi za bei ya Mkandarasi (base price) baada ya majadiliano ambayo ni dola za Marekani bilioni 2.216 sawa na shilingi trilioni 5.2. Hii ni baada ya majadiliano yaliyookoa dola za Marekani milioni 273,913,703.25 sawa na shilingi bilioni 632.74 kutoka kwenye zabuni ya awali ya dola za Marekani 2,490,124,575.00 sawa na shilingi trilioni 5.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuwa utaratibu wa manunuzi kwa njia ya Single source ndiyo uliotumika kumpata Mkandarasi YAPI MERKEZI wa Ujenzi wa kipande cha tatu kutoka Makutupora kwenda Tabora, na Kipande cha nne, yaani Tabora - Isaka, ambapo gharama zake ni dola za Marekani bilioni 2.213 sawa na Shilingi za Kitanzania trilioni 5.19, ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, upi mkakati wa kutokomeza wizi wa dawa na vifa vya afya, hatua zilizochukuliwa kwa wahusika na fedha zinazopotea kwa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Suala la kupambana na wizi na ubadhirifu wa bidhaa za afya si la Serikali pekee bali ni suala letu sisi wote, hasa wawakilishi wa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali katika kutatua tatizo la wizi wa dawa na vifaa tiba kama ifuatavyo: -

a) Kufanya agenda ya ulinzi wa bidhaa za afya kuwa agenda ya kudumu katika vikao vya kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya.

b) Kujenga uwazi wakati wa kupeleka bidhaa za afya na kuwapa wakuu wa wilaya na Wabunge nyaraka za makabidhiano ya dawa na vifaa tiba kwa ajili ya rejea.

c) Kuimarisha mifumo ya usimamizi wa bidhaa za afya ikiwemo kufunga mifumo ya kielektroniki pamoja na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara.

d) Kuimarisha kamati za usimamizi za vituo kwa kuzijengea uwezo kuhusu majukumu yao katika usimamizi wa bidhaa za dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilifanya uchunguzi wa ubadhilifu wa bidhaa za afya na taarifa kuwasilishwa kwenye semina ya wabunge, na kupelekwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kufanya thamani halisi ya bidhaa zilizopotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza:-

Je, Serikali imejiimarisha vipi kukagua miamala ya uhamishaji bei ya mauziano ya bidhaa/huduma za makampuni ya Kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia vihatarishi vilivyopo kwenye miamala husika, Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali zinazolenga kuimarisha udhibiti na kuzuia upotevu wa mapato. Hatua hizo ni pamoja na:-

a) Kuanzisha Kitengo Maalum cha Usimamizi wa Kodi za Kimataifa ndani ya Mamlaka ya Mapato ya Tanzania kuanzia 2011.

b) Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa kanuni na miongozo kuhusu ukaguzi wa kodi kwenye kampuni zenye mahusiano.

c) TRA imenunua Kanzidata ya Orbis kwa ajili ya kupata taarifa za kusaidia kufananisha bei za Miamala ya Kimataifa ili zisaidie kujenga hoja wakati wa ukaguzi unaofanywa kwenye Kampuni za hapa nchini.

d) Tanzania imejiunga na Jukwaa la Kimataifa la Ubadilishaji wa Taarifa za kikodi kwa lengo la kuhakikisha nchi yetu inajenga uwezo wa kubadilishana taarifa za kikodi na nchi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatarajia kusaini Mkataba ujulikanao kama “Multilateral Convention on Mutual Administrative Assistance in Tax Matters” ambao utaiwezesha TRA kupata taarifa mbalimbali kutoka katika nchi 146 duniani ambazo zitasaidia katika kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa Miamala ya Kimataifa. Ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza:-

Je, ni vijana wangapi hawana ajira nchini na Serikali imewaandaaje kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali namba 216 lililoulizwa na Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2021 unaonesha kuwa vijana wa umri wa miaka 15 – 35 ni 17, 712,831 ambapo kati yao, vijana 14,219,191 wana uwezo wa kufanya kazi na vijana 3,493,640 hawana uwezo wa kufanya kazi kutokana na sababu mbalimbali kama vile masomo, ugonjwa na kadhalika. Kati ya vijana wenye uwezo wa kufanya kazi, vijana 12,486,682 sawa na asilimia 87.8 wana ajira na vijana 1,732,509 sawa na asilimia 12.2 hawana ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha vijana wanaandaliwa ipasavyo kushindana katika soko la ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maana ya Serikali imekuwa ikiandaa programu mbalimbali za kuweza kuhakikisha kwamba kunakuwa na mikakati ya kuwapatia vijana fursa za ajira na kuwaandaa kuweza kupata fursa ikiwemo mafunzo mbalimbali kwa maana ya uzoefu kazini, internship kwa hitimu wa vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo imekuwa na scheme mbalimbali ya kuweza kuwapatia mikopo, mafunzo, ya utarajali na mafunzo ya kilimo cha kisasa kutumia teknolojia ya vitalu nyumba kupitia mafunzo haya, zaidi ya vijana 84,245 wamenufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Elimu pia Wizara ya Kilimo, kuweza kuhakikisha zinatolewa program mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikopo, mafunzo na kutengeneza fursa mbalimbali zaa jira kutokana na Wizara hiyo.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza:-

Je, ni kwa kiwango gani Serikali imejiimarisha kukagua miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya makampuni ya Kimataifa.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRA imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kiukaguzi wa miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya makampuni ya Kimataifa kwa lengo la kuzuia upotevu wa mapato. Hatua hizo ni pamoja na:-

(i) Kuendelea kuboresha mifumo ya ndani ya ukusanyaji kodi kama vile Mfumo wa Usimamizi wa Mashine za Utoaji wa Risiti za Kielektroniki na Mfumo wa Kuwasilisha return Kielektroniki;

(ii) Kutoa mafunzo ya vitendo kwa watumishi katika nchi mbalimbali zenye uzoefu wa kushughulikia miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya makampuni ya Kimataifa;

(iii) Kuimarisha utekelezaji wa mkataba wa kubadilishana taarifa kati ya Serikali ya Tanzania na nchi nyingine;

(iv) Kuendelea kufanya majadiliano na wadau mbalimbali ili kuona uwezekano wa kujiunga na Global Forum on Tax Transparency na ubadilishanaji wa taarifa kwa lengo la kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa. Ahsante.