Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Luhaga Joelson Mpina (52 total)

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa hizi dakika tano ulizonipa, lakini pia nichukue nafasi hii kuipongeza sana Kamati. Kamati imetoa taarifa nzuri sana na imenikumbusha enzi hizo nikiwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Kamati kwa kweli taarifa yenu ni nzuri na mmetushauri vizuri sana Serikali. Sasa kwasababu ni dakika tano nilizopewa, niseme kwa kifupi haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la jinsi ambavyo Serikali ilishughulikia suala la magwangala hasa upande wetu wa mazingira kwa taasisi yetu ya NEMC. Tulichokihakikisha sisi kimefanyika ni kwamba NEMC walishiriki kutoa mwongozo, kwa maana ya kuhakikisha kwamba mahali ambapo yataondoshwa haya magwangala kuna mtaalam na kuhakikisha kwamba wanawapa masharti na vigezo vya kuzingatia kadri ya magwangala hayo yatakapohamishwa kutoka eneo fulani kwenda mahali fulani, na kuhakikisha kwamba kwa namna yoyote ile hakutakuwa na uharibifu wowote ule wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, limezungumzwa suala la ujenzi wa mradi huu wa climate change adaptation program.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema na kuliambia Bunge lako kwamba mradi huu tayari mkandarasi yupo kwa ajili ya miradi yote ya Ocean Road, Pangani, Kilimani pamoja na ya Kisiwa Panza, yote hii mkandarasi ni huyu isipokuwa kwa sasa hivi ndiyo yupo hapo Dar es Salaam pale Ocean Road ndiyo ameanza. Maeneo mengine haya yote ana mobilise resources ili kuweza kupeleka kwenye maeneo hayo ili miradi hii iweze kuanza. Kwa kifupi sana unaweza kuona kwamba huyu contractor anaitwa DEZO Contractor Limited na alianza toka mwezi wa kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za kutekeleza miradi hii tunazo. Fedha za kutekeleza miradi hii ninayozungumza, mkandarasi yuko site na ataenda kujenga kuta zote zinazotakiwa, sehemu za kujenga mitaro na yenyewe tayari inajengwa kama maeneo yale ya Kigamboni kule kwa Mwalimu Nyerere, Buguruni, mitaro ile inaendelea kujenga; na sehemu zingine tayari tumeshatekeleza kwa mfano Rufiji tayari tumeshapanda mikoko iliyokuwa itakiwa zaidi ya hekta 792 tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Wabunge wote wa maeneo mengine ambayo mradi huu unajumuisha kama Pangani, Kilimani, Kisiwa Panza ambako tayari na kwenyewe mikoko tumekwisha kupanda wakae wakijua kwamba mkandarasi yupo na muda wowote ataanza kazi ya ujenzi mara moja. Kama nilivyosema mkandarasi yupo na fedha tunazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu suala la Mfuko wa Mazingira. Suala la Mfuko wa Mazingira, hali iliyopo mpaka sasa hivi ni kwamba tayari tumeshapeleka maombi yetu Hazina tena kwa ajili ya kupitisha zile tozo ambazo zinatakiwa zitozwe, lakini vile vile tayari Waziri ameshateua ile Bodi ya Wadhamini ya kusimamia mfuko huu na tayari kikao cha kwanza kimekaa. Kwa hiyo, tunachoomba tu ni kuendelea kuungwa mkono ili tuweze kutekeleza mambo makubwa ya kimazingira kama ambavyo Wabunge mlivyoyazungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitake kuwahakikishia kwamba kwa kweli tunajua tatizo la mabadiliko ya tabianchi na nchi hii ya Tanzania inavyosakamwa sasa hivi na mabadliko ya tabia nchi. Tunajua uharibifu wa mazingira unaoendelea, tunahitaji support ya Bunge hili ili tuweze kufanya kazi hiyo ya kuhakikisha kwamba tunayarejesha mazingira kwenye hali yake, tunayazuia mazingira kwenye uharibifu wake na mimi na Waziri wangu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii hatuwezi kulala hadi pale mazingira ya Tanzania yatakapokuwa yamerekebishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Leah pale amezungumzia suala la mradi ule wa maji wa Ziwa Victoria ambao unakuja mpaka Jimboni kwangu na mpaka Meatu. Niseme kwamba mradi huo wa umwagiliaji ukweli ni kwamba katika dunia hii ya mabadiliko ya tabianchi, bila wakulima wetu kuwaelekeza katika miradi ya umwagiliaji, bila wakulima wetu kuwaelekeza katika matumizi ya mbegu zinazovumilia ukame na mbegu ambao zinakomaa kwa muda mfupi hatuwezi kufanikiwa katika mapambano haya ya kilimo. Nimhakikishie kwamba mradi huu unaotekelezwa ambao unasimamiwa na Wizara ya Maji na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu ya Rais,….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu ni mfupi na naomba nianze kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Kisesa kwa kuendelea kuniamini na baadhi yao mko hapa kuja kushuhudia. Niendelee kuwaambia tu kwamba, kama ni Mbunge mlikwishapata na nitaendelea kuwawakilisha kikamilifu hapa Bungeni na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kujibu hoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; kuna suala lililoelezwa na Kamati hapa kuhusu suala la Kamati ya Katiba na Sheria imetupongeza sana kwa hatua tulizozichukua katika suala la upungufu la Jengo la Luthuli Two katika Ofisi ya Makamu wa Rais na hatua tulizozichukua. Sasa hivi nataka niwahakikishie kwamba hatua tunaendelea kuzichukua, moja ni hayo marekebisho ambayo sasa hivi yanafanyika. Pili, baada ya marekebisho hayo kukamilika ambayo yanafanywa kwa sasa hivi tutam-engage PPRA ili aweze kufanya ile value for money ili kuhakikisha kwamba, fedha za Watanzania zilizotumika zimetumika sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa zimekuja hoja za Kiongozi au Msemaji wa Kambi ya Upinzani wakati anawasilisha, alizungumza sana suala la Muungano na kuonesha kwamba, Muungano huu wakati mwingine labda anaona yeye kwamba, hauna faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna faida kubwa sana za Muungano na Tanzania tunatakiwa kujivunia sana Muungano huu. Moja, tuna Kifungu kile cha GBS ambayo kila mwaka tunatoa zaidi kati ya bilioni 20 mpaka bilioni 50 kwa ajili ya GBS, pia pay as you earn haikuwepo, leo tunatoa pay as you earn ya bilioni 1.75 kila mwezi na kwa mwaka tunatoa bilioni 21 za pay as you earn(PAYE) na hazina utata wowote katika kutoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dividend ya BOT ambayo nayo inatolewa kati ya bilioni mbili mpaka bilioni nane kila mwaka na haina utata katika kutolewa. BOT bado inazikopesha hizi Serikali mbili, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kuziba pengo la mapato na matumizi. Kwa mfano, Zanzibar katika mwaka huu wa fedha ilikuwa na kiwango ambacho kinafikia mpaka bilioni 45.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msemaji wa Kambi ya Upinzani alisema hapa kwamba, Muungano huu umeshindwa kuchochea maendeleo na umeshindwa kuchochea mabenki kwenda Zanzibar. Tumeshuhudia wote mwaka 1990 benki Zanzibar zilikuwa mbili tu, lakini sasa benki Zanzibar zimefikia 12. Tafiti nyingi zinafanywa, anasema kwamba, hakuna uchocheaji wa maendeleo, Benki Kuu tu yenyewe imeshafanya tafiti zaidi ya 13 Zanzibar na tafiti hizi ni kwa ajili ya maendeleo na kwa ajili ya uchumi na zimekuwa zikiwa incorporated katika maendeleo ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema pia makampuni mengi hayaendi Zanzibar, tukitolea mfano Makampuni haya ya Simu, hakuna Kampuni ya Simu ambayo ipo Bara hapa haipo Zanzibar. tiGO, Voda, Zain, wote wameanzisha branch kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo hii Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu. Uvuvi wa Bahari Kuu ambao unatoa faida kubwa tu, mpaka sasa hivi toka uanzishwe tunatoa zaidi ya billion nne. Mfuko wa Jimbo kila mwaka, fedha hizi hazina utata, Mheshimiwa Ngwali alikuwa anasema zina utata, hazina utata wowote, tunapeleka 1.24 billion kila mwaka na hazina utata wowote. TASAF toka tuanze tumepeleka shilingi bilioni 31.5 na miradi mikubwa imefanyika ya ujenzi wa barabara na miundombinu mikubwa ya kiuchumi bilioni 31. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, MIVARF tumepeleka zaidi ya bilioni 13.49 na miradi mikubwa imefanyika Zanzibar, barabara zaidi ya kilometa 83. Tumejenga masoko ya kisasa ambayo mpaka yana cold room Unguja na Pemba, yamejengwa zaidi ya bilioni 13.49 zote zimekwenda, halafu mtu anasema kwamba, haoni shughuli ambayo imefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, COSTECH; tumefanya miradi mikubwa ya COSTECH, miradi mikubwa ya utafiti imefanyika zaidi ya shilingi bilioni tatu zimekwenda katika shughuli hii na tafiti zinafanyika na Zanzibar wananufaika sana na tafiti zinazofanywa na COSTECH katika uzalishaji wa mpunga, uzalishaji wa muhogo na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo makampuni yetu yanafanya vizuri sana. Nani asiyejua kwamba, Bodi ya Mikopo inatoa mikopo bila kubagua watu wa kutoka pande zote mbili za Muungano? Nani asiyejua kwamba leo TRA inakusanya kodi pande zote za Muungano tena kwa usahihi na kwa ufanisi mkubwa na pande mbili zote zinanufaika. Taasisi za Muungano 39 tulizonazo, taasisi 30 zote zina ofisi Zanzibar, isipokuwa Taasisi tisa tu ambazo na zenyewe tayari tumeshatoa maelekezo lazima ziwe na ofisi Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa suala kwamba Taasisi hizi za Muungano hazishirikiani, ushirikiano ni mkubwa. Mmeona ushirikiano uliozungumzwa hata na Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini kuhusu mapato ya ZESCO na TANESCO. Pia Wizara ya Nishati na Madini kubeba mzigo wa asilimia 31 kwa ajili ya kupunguza gharama zinazolipwa Zanzibar yote hayo unasema kwamba Muungano huu hauna manufaa! Tendeeni haki Muungano, mengi yamefanyika, tutaendelea kuyaboresha na sisi tuko hapa, tunatembea kila siku kwenda Zanzibar, kwenda Unguja na kwenda Pemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Pemba hata ukimuuliza tu mtoto mdogo, ukiuliza Mpina, wewe sema Mpina tu, yeye atasema Naibu Waziri Muungano atamalizia. Tunafanya kazi, endeleeni sasa kutuunga mkono, ili tuweze kufanya kazi vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya mambo makubwa katika upande wa mazingira. Nani asiyejua hali ya mazingira ilivyokuwa Novemba mwaka 2015, Serikali ya Awamu ya Tano inapoingia madarakani? Nani asiyejua takataka zilivyokuwa zikizagaa kila mahali? Nani asiyejua majitaka yalivyokuwa yakitiririka kila mahali na kuleta athari kubwa kwa wananchi? Nani asiyejua migodi na viwanda vilivyokuwa vikichafua mazingira? Nani asiyejua? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya mabadiliko makubwa, leo utashuhudia na kuona jinsi maboresho tulivyofanya. Wakati tunaingia mwaka 2016 wagonjwa wa kipindupindu mwaka 2016 walikuwa 11,000 na watu waliofariki mwaka huo walikuwa 163. Leo mwaka 2017 kwa
jitihada tulizozifanya ofisi hii pamoja na Wizara ya Afya wagonjwa wa kipindupindu mwaka huu walikuwa 1,146 tu waliofariki 19. Kwa hiyo, utaona jinsi ambavyo tunafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa wanatokea baadhi ya Wabunge wanataka kuwabeba wahalifu, watu wanaopigwa faini, watu tunaowatoza, lazima mjue kuna suala la utiririshaji wa majitaka kwenye viwanda, nenda kaangalie, wagonjwa wa saratani walivyoongezeka sasa hivi. Mwaka 2006 wagonjwa wa saratani walikuwa 2,416, kila mwaka wamekuwa wakiongezeka wagonjwa wa saratani. Sasa hivi tuna wagonjwa wa saratani toka 2,416 hadi wagonjwa wa saratani 47,415. Kwa hiyo, huwezi ukakinga kifua kwa wahalifu hawa. Wahalifu hao waambiwe kufuata na kuzingatia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyoingia kwenye ofisi ile tumeongeza kasi ya ukaguzi wa mazingira kuhakikisha kwamba hakuna mtu anachafua mazingira, hakuna mtu anaharibu mazingira. Wakati tunaingia uwezo wa kukagua mazingira kufikia taasisi 425, leo tumefikia taasisi 1,548 hadi kufikia hii Juni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya mapinduzi makubwa katika ukusanyaji wa mapato, mapato NEMC sasa yamepanda. Tulikuta wana uwezo wa kukusanya mapato ya bilioni tano, katika muda mfupi tuliokaa tumeweza kuchochea ukusanyaji wa mapato NEMC hadi wamefikia bilioni 12, ongezeko la bilioni saba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengine wanakaa hapa wanasema ooh! hili Baraza la Mawaziri halina Mawaziri wa kumshauri Mheshimiwa Rais. Hivi mnataka Mawaziri wa aina gani wa kumshauri Mheshimiwa Rais? Tunayafanya haya tulitakiwa kupongezwa tu. Tumefanya transformation hizi kuhakikisha kwamba, maendeleo yanaweza kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya operations nyingi mbalimbali na tozo nyingi na faini mbalimbali watu wameweza kutozwa kwa ajili ya kuhakikisha tunarejesha mazingira yetu, tutaendelea kufanya hivyo. Ukitaka uepukane na utozwaji wa faini wewe zingatia sheria hakuna mtu ambaye atakugusa, Mpina hutamuona wala NEMC hutawaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya mapinduzi makubwa ya kuleta usafi katika nchi hii. Leo Dar-es-Salaam (DAWASCO) mifumo yao mibovu ilikuwa ikitiririsha taka kila leo, miundombinu imeimarika na leo taka hizo hazitiririshwi tena kwa kiwango kile kilichokuwa kinatiririshwa. Tulikwenda Kahama, tukawakuta wanatiririsha majitaka tena mbugani na kuharibu vyanzo vya maji, leo nenda, wana mfumo mzuri wa ku-contain majitaka hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, SBL, Mbunge wa Temeke atanishuhudia, SBL walivyokuwa wanatiririsha majitaka. Tumedhibiti tatizo hilo halipo tena, wananchi hawapati shida tena. Wananchi wa Keko waliokuwa wanakumbwa na mafuriko, leo hayapo tena, tumetatua tumemaliza. Mgodi wa Dhahabu wa North Mara walivyokuwa wakitiririsha maji yenye kemikali, tumepiga marufuku na hali ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya mapinduzi makubwa sana, watu walikuwa wanashuhudia uchafuzi wa mazingira barabarani, mabasi yanatupa taka ovyo, leo tumeweka utaratibu mzuri, mnaona tangazo hilo la SUMATRA ambalo linamtaka kila abiria kuhakikisha kwamba anatunza mazingira, hakuna utupaji taka ovyo. Kwa hiyo, ukiona mazingira yako safi barabarani sasa hivi ujue Vyombo vya Serikali ya Awamu ya Tano viko kazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchafuzi uliokuwa unafanywa na meli za mafuta na za mizigo katika bahari yetu, leo tumeweka mfumo mzuri wa uchukuaji taka, uzoaji taka na wa utupaji taka ambao unafanywa majini. Tumeweka mfumo mzuri ambao sasa hatuwezi tena kurejea kwenye uchafuzi huo uliokuwa unafanyika. Operesheni za mara kwa mara zinafanyika na hivyo hakuna uchafuzi tena uliokuwa ukiendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uimara huu na kazi hii kubwa ambayo tumeifanya tumeweza kuaminiwa. Leo hii wawekezaji na wafadhili wengi ambao wanaidhinisha fedha zao kwa ajili ya kuisaidia Tanzania katika kutengeneza miundombinu ya uondoshaji wa taka na utunzaji wa maji taka wengi wamejitokeza. Hapa ninavyozungumza katika mwaka huu wa fedha kwa mara ya kwanza eneo la majitaka lilikuwa halipewi fedha. Leo kwa DAWASA tu peke yake wafadhili wengi wamejitokeza na tunategemea zaidi ya shilingi bilioni 800 kutoka kwenye taasisi tu moja ya DAWASA. Sasa mtu akisimama hapa na mbwembwe kusema kwamba eti Serikali ya Awamu ya Tano haiaminiki kwa wafadhali, wafadhili gani unaowa-refer wewe kama majitaka tu peke yake mfadhili tu kwa DAWASA peke yake ni zaidi ya shilingi bilioni 800? Tumeaminiwa na miradi inaendelea kujengwa katika majiji na miji kwa ajili ya kuboresha hali ya usafi wa mazingira katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ali King alikuwa anazungumza kuhusu ahadi yangu niliyoitoa nilipokuwa Zanzibar ya kufanya tathmini katika eneo lililodidimia. Nataka nimwambie asome randama nimeshaweka, lile eneo tumekubaliana Wizarani tutalifanyia tathmini katika mwaka huu ujao wa fedha wa 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani ilitushauri kwamba tufanye audit eneo la Bagamoyo, Pangani, Rufiji na Zanzibar ile miradi ya mabadiliko ya tabianchi. Wakati tunaagizwa bajeti ya mwaka 2016/2017 sehemu kubwa ya miradi hii ilikuwa haijaanza, sisi tulienda kukagua miradi hii yote ilikuwa …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kifupi niseme kwamba sasa hivi ndiyo tunaipia miradi hii. Mradi mmoja tu ndio umefikiwa kuhakikiwa ni mradi wa Rufiji, tumeukagua na tumeugundua una kasoro na tumemwagiza Mkaguzi wa Ndani kufanya ukaguzi huo. Mkaguzi wa Ndani atakapotuletea taarifa tutawasilisha kwenye Kamati kuona status ya mradi huo ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na naunga mkono hoja na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano tuko kazini, tuungwe mkono tufanye kazi ili tuonyeshe uwezo na tuibadilishe Tanzania yetu. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii. Na mimi ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kunipa dhamana hii ya kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na kumuahidi kabisa kwamba nitaitumikia nafasi hii na kuwahakikishia Watanzania wenzangu kwamba nitawatumikia kupitia nafasi hii kwa nguvu zangu zote na kipaji chote nilichopewa na Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni Mapendekezo ya Mpango wetu wa Maendeleo. Waheshimiwa Wabunge wetu wamezungumza mambo mengi sana, lakini ninachotaka kusema kwa sababu haya ni mapendekezo ya mpango, zile inputs zao walizozisema tumezichukua ili sasa tuje na Mpango wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hatujibu sana kihivyo kwa sababu tumepewa ushauri na Waheshimiwa Wabunge ili tukaandae Mpango wenyewe. Hata katika mapitio hapa nimeona kwenye Wizara yangu na wamependekeza mambo mengi, wamezungumzia suala la bandari ya uvuvi, meli ya uvuvi, umuhimu wa kuwa na viwanda vya kuchakata samaki, umuhimu wa kuwa na viwanda vya nyama, umuhimu wa kuwa na viwanda vya maziwa, haya yote ni inputs wametupa ili tukaandae Mpango wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kabisa kwamba kwa moyo mmoja, michango yote ambayo imehusu sekta yangu nimeichukua ili kwenda kutengeneza Mpango wenyewe ambao ndiyo baadae muda utakapofika tutauwasilisha hapa Bungeni na hapo ndipo mtakapoona kwamba tumefanya kufikia wapi zile inputs ambazo ninyi mmetuwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo na kwa sababu muda unakuwa hautoshi sana nitoe ufafanuzi wa baadhi ya mambo machache.

Moja, limezungumza sana suala hili la uchomaji wa vifaranga vya kuku 6,400 ambavyo vilikuwa vinasafirishwa kuingia nchini mwetu kutoka Kenya. Tukajaribiwa kulaumiwa sana kama Wizara na kama nchi wakati mwingine kwa kitendo hicho tulichokifanya. Jambo moja tu niseme, hapa tuko Mawaziri pamoja na Wizara yangu tumeapishwa kusimamia sheria na tunatekeleza kwa misingi ya sheria iliyowekwa katika kutekeleza majukumu yetu na kwamba hatuwezi kufanya vinginevyo kwa sababu tukifanya vinginevyo Bunge hili litatuuliza kwa nini tumefanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria yetu ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya mwaka 2003 inatoa utaratibu wa namna ya kuingiza kuku pamoja na mazao yake ndani ya nchi. Vilevile kuna mazuio ambayo yalitolewa kulingana na jambo hili. Tarehe 29 Oktoba, 2017 tulipowakamata hao vifaranga, tuliwachoma moto kwa sababu kubwa kwamba tulikuwa na zuio ambalo tulishaliweka toka tarehe 7 Juni, 2006 kwamba kutokana na tishio la ugonjwa wa mafua ya ndege lililokuwepo duniani tulilazimika kuzuia uingizaji wa kuku pamoja na mazao yake na tukawa tumezuia mtu yeyote kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu ndugu aliyeingiza hawa vifaranga kwanza aliingiza kinyume cha utaratibu bila kibali chochote ilikuwa ni illegal importation, pili, alitaka kuingiza wale kuku wakiwa hawajakaguliwa. Kwa namna yoyote ile kuingia ndani ya nchi ambako kungesababisha kero kubwa. Kwa mfano, kuku wale wangekuwa wana ugonjwa huo wa mafua ya ndege maana yake tungeua ndege wetu wote walioko hapa nchini, vilevile mafua haya ya ndege yanambukizwa mpaka kwa binadamu tungeweza kuua binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuzungumza kwa urahisi jambo la vifaranga hivi kuwateketeza ukawa unazungumza tu kiurahisi kwamba unajua, sijui mambo gani! Ni lazima tuchukue hatua hizi kali kwanza kwa yule aliyefanya hivyo kuhakikisha kwamba hakuna mtu mwingine ambae atafanya jambo kama hilo, mtaji wake tumeuteketeza maana yake kama ana njia zingine ambazo alikuwa anatumia kuingiza vifaranga nchini hawezi kurudia tena, Watanznaia watuelewe kwamba tunasimamia maslahi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuku wakifa, biashara Tanzania imekufa ya kuku, Watanzania watakufa kwa mafua ya ndege na kama Watanzania watakufa kwa mafua ya ndege kutokana na uzembe wa Wizara yangu na wale askari au watu waliokuwa wanafanya inspection kama wasingewachoma kuku siku ile, ningewafukuza kazi wote siku hiyo.

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwamba Bunge hili ndilo ambalo linatunga sheria. Utekelezaji wa sheria hauwezi ukafanyika kama Mheshimiwa Mbunge anavyopendekeza. Sheria ya Magonjwa ya Mifugo, Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2013, Kifungu cha 8(2) kinasema “ni kukamata na kuteketeza” na siyo anavyozungumza yeye. Tumekamata na tunateketeza na tunapelaka salamu Afrika na duniani kwamba lazima wanapotaka kufanya hivyo waangalie sheria za nchi yetu zinasema nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tunafanya operation ya mifugo kutoka nje ya nchi. Ni takribani asilimia 30 ya malisho ya nchi hii yanalishwa na mifugo ya kutoka nje, napo tunalalamikiwa, tumekatana ng’ombe, tumekamata, tumetaifisha na tumepiga mnada. Napenda niwambie watu ambao wanatetea mambo haya, kuna jambo moja tu wanalotaka kufanya…

TAARIFA . . .

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya operation ya kuondoa mifugo kutoka nje ya nchi ambao wameingia nchini kinyume cha sheria. Hili pia limelalamikiwa na wakati mwingine wanaolalamika ni watunga sheria za nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria hiyo niliyoitaja Sheria ya Magonjwa ya Mifugo Namba 17 ya mwaka 2013 imeonesha utaratibu wa kuingiza mifugo ndani ya nchi kutoka nchi nyingine. Ukieda kinyume na huo utaratibu umevunja sheria. Sheria hiyo pia inakataza kuingiza mifugo kwa ajili ya malisho. Watanzania wetu sasa ukiruhusu mifugo ile kuingia hapa nchini madhara yake ni nini? Madhara yake unaweza kuleta ugonjwa wa kutoka nchi jirani kuingia hapa nchini. Kwa hiyo, tumekamata ng’ombe wale 1,325 wa kutoka Kenya na sasa hivi tunashikilia ng’ombe wengine zaidi ya 10,000 kutoka Rwanda na Uganda ambao tutawapiga mnada hivi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya hivyo kwa sababu gani, moja, kuhakikisha kwamba tunalinda mifugo ya Watanzania isipate magonjwa, mbili, tunalinda Watanzania wasipate magonjwa kupitia mifugo hiyo,tatu; tunalinda pia malisho ya Tanzania, Tanzania haiwezi ikawa malisho ya nchi za kutoka nje, nne, tunahakikisha kwamba migogoro ya wakulima na wafugaji inayochochewa na mifugo ya kutoka nje inakwisha, tano, kuhakikisha kwamba tunalinda mazingira pamoja na vyanzo vyetu vya maji ambavyo vinaharibiwa na makundi makubwa haya ya mifugo. (Makofi)

Kwa hiyo basi, watu wanaojaribu kuhusisha mahusiano yetu na Kenya pamoja na nchi zingine za jirani wanatakiwa wazingatie mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna ushirika wa uhalifu. Watu wanaoingiza mifugo kutoka nje ya nchi ni wahalifu kwa sababu wamevunja sheria na wale wanaozungumza hivyo ni kwa sababu Waziri wa Mifugo ametangaza. Je, ni Watanzania wangapi wamekamatwa Kenya leo wako lockup, wapo wamefungwa kwa kuvunja sheria nani anajua idadi? Nani anajua Watanzania ambao wako Uganda kwa kuvunja sheria leo wako mahabusu, leo wamefungwa nani anajua kuwa Rwanda, Burundi. Hivyo hivyo, mhalifu akija hapa hawezi kutetewa kwa sababu ya ushirika, ushirika wetu siyo wa uhalifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashirikiano yetu yanayoendelea katika nchi za Afrika Mashariki ni mazuri mno, ecellent. Mahusiano tuliyonayo na Kenya ni mazuri mno kwa sababu mashirikiano yetu ni ya kisheria, mashirikiano na Uganda yapo kwa sababu ni ya kisheria. Kukamatwa kwa ng’ombe hawa ni wavunja sheria haiwezi kuhusishwa na ushirika wetu, wanashauriwa wahusika kufuata sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nilipotangaza operation hii ya siku saba, Waziri wa Mambo ya Nje alichukua hatua ya kuzijulisha nchi zote kwamba wawaambie watu wao kuondosha mifugo Tanzania kulingana na sheria yao. Ng’ombe wengi waliondolewa, sasa hivi nimesema tuna ng’ombe 10,000 tunawashikilia ambao tutawapiga mnada hivi karibuni lakini mifugo mingi imeondolewa, wale ambao wamekaidi ukweli tutapiga mnada ng’ombe zao bila huruma, operation inaendelea na tunaendelea kuwashauri ambao hatujawakata waondoe mifugo yao kwa hiari yao.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, kwa nafasi ambayo umenipatia, na nianze kwa kuwapongeza sana Kamati yangu hii Kamati ya Kilimo, Maji na Mifugo ambayo inaendeshwa na akina mama, nawapongeza sana kwa uendeshaji wa Kamati hiyo vizuri sana Mheshimiwa Mwenyekiti wetu Dkt. Mary Nagu pamoja na Mheshimiwa Dkt. Ishengoma ambaye ni Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati kwa weledi wao mkubwa sana katika kutusimamia na kutuongoza kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, najua zipo changamoto nyingi sana ambazo zimezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge na kwa dakika 10 haitatosha sana kuzijibu, lakini nijaribu kusema kwa kifupi kwamba Kamati hii yangu ambayo imewasilisha taarifa hapa chini ya Mwenyekiti wake, imezungumizia juu ya kushughulikia changamoto ambayo zinahusu viwanda vyetu vya maziwa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu changamoto ya maziwa hapa nchini tunafahamu tatizo la uingizaji maziwa ambao leo imefikia zaidi ya kilogramu milioni 88 ya uingizaji wa maziwa kutoka nje ya nchi na kusababisha ushindani usio sawa katika Taifa. Tunafanya tathmini na tutapata majawabu. Lakini vilevile wamezungumza suala la Ranchi za Taifa (NARCO) kwamba tufanye tathmini tujue uwekezaji uliopo, tujue changamoto zilizopo ili tuweze kuja na mapendekezo sahihi ya namna bora ya kuwekeza katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeunda Kamati hiyo tayari chini ya maagizo hayo hayo ya Kamati hii ilivyotuelekeza tukaunde Kamati na kamati hii imeshamaliza kufanya tathmini, kesho napokea ripoti ikiongozwa na Mheshimiwa Archad Mutalemwa DG Mstaafu wa DAWASA na kesho napokea taarifa hiyo na tutakapoipokea hiyo taarifa tutaenda mbele ya Kamati yetu kushauriana nayo au kama kuna input zingine ili tuweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi haramu, nishukuru sana Kamati yetu imetupa msukumo mkubwa katika ukurasa wa 32 ya kwamba tuongeze bidii katika kupambana na uvuvi haramu, lakini tuongeze bidii katika kuhakikisha kwamba wale wanaotorosha samaki wetu mazao ya samaki, tunawadhibiti ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niihakikishe Kamati kwamba na Wizara yangu, tutahikisha hili tunalisimamia kwa nguvu zote, hizi ni rasilimali za Taifa, na rasilimali hizi haziwezi kuwa shared kwa ukanda. Rasilimali hizi zinakuwa shared kwa nchi nzima kwa hiyo kama Wizara, inayosimamia sheria ambayo zimepitishwa na Bunge hili, tutahakikisha kwamba hakuna kabisa uvuvi haramu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tutahakikisha hakuna mfanyabiashara atakayejihusisha na kuuza wala kusambaza zana haramu, hakuna kiwanda kitakachochakata samaki wasioruhusiwa, hakuna mtu yeyote atakayevua kwa kutumia nyavu haramu, lazima mali zetu tuzilinde kwa nguvu zote, na bila kumumunya maneno labda nitoe takwimu zilizopo kwa sasa hivi, tuko wapi katika rasilimali hizi za uvuvi, ukizungumzia Ziwa Victoria…

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi natoa majibu hapa kwa maelekezo yake yeye au natoa majibu kwa mpangilio ambao ulioko hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndio naanza kujibu tu sijafika hata mbali, anisubiri asikilize vizuri ninavyozungumza hili ni Bunge, mimi ni Mbunge na yeye mwenzangu huyu ni Mbunge, anisikilize vizuri. Sasa sijamaliza hata kuzungumza sijamaliza hata sentesi.

Mhesimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kusema kwamba takwimu kwa sasa hivi katika Ziwa Victoria, linasema hivi, samaki ambao wanaruhusiwa kuvuliwa, sangara, ambao ni sentimita 50 mpaka sentimita 85 wamebakia asilimia tatu tu, kwa hiyo hata uvuvi huo tunaouzungumza hauwezi kuwepo kama uvuvi haramu huu tutauruhusu. Samaki wazazi katika Ziwa Victoria wamebaki asilimia 0.4 huna wazazi, huna ziwa, huwezi kuvua samaki ambao leo sasa ambao ni wachanga na ndio wanaovuliwa, wachanga wasioruhusiwa, chini ya sentimita 50, ni asilimia 96.6.

Kwa hiyo, kwa mantiki hiyo hatuna samaki wanaofaa kuvuliwa katika Ziwa Victoria, Kamati imezungumza juu ya viwanda kufungwa tulikuwa na viwanda 13 hapa viwanda 13 vilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 1,065 leo tumebakiza viwanda nane na viwanda nane hivyo vina uwezo wa kuzalisha tani 171 tu. Sababu ya kukosekana kwa rasilimali hizi za uvuvi, samaki hawapo wamekwisha kutoweka kwa sababu ya uvuvi haramu, watu wanavua mpaka mayai, watu wanavua mpaka wachanga wale, utapata wapi samaki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira zilikuwa 4000 na kitu leo ni 2000 tu katika ziwa letu hilo la Victoria, lakini nataka niseme hii operation ambayo inayoendelea na kama Waziri niliyeapishwa kusimamia rasilimali hizi kwanza niweke kabisa wazi msimamo wa Serikali kuwa wananchi wanaojishughulisha na wafanyabiashara wanaojishughulisha na uvuvi haramu waache, kwa sababu wakiendelea kufanya hivyo, rasilimali hizi zitatoweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpina hapa ni mlinzi tu, kibarua sitaenda kuvua Ziwa Victoria wataenda kuvua wananchi wa Geita, wataenda kuvua wananchi wa Chato, wataenda kuvua wananchi wa Mara, wataenda kuvua wananchi wa Mwanza, mimi sitabeba nyavu, nazuia wale samaki na Wizara yangu kazi yetu ni kuhakikisha rasilimali zile zinakuwepo wananchi wetu wafanye biashara vizuri, wavue vizuri, wale samaki wazuri, ndio kazi ya Serikali. (Makofi)

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, utunze muda tu muda wangu ili usiingie ndani ya miongozo ambayo inaulizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika operation hii, niliyoiunda ya operation katika Ziwa Victoria, operation sangara mwaka 2008, operation hii ina wataalam hafanyi maamuzi mtu mmoja, timu hii ina wavuvi, ina NEMC, ina TISS toka Ofisi ya Rais, ina TAMISEMI na ina Polisi.

Kwa hiyo, watu hawa wanafanya assessment mambo ya vipimo vya ngazi mbili, ngazi tatu hayo ni kwa mujibu wa wataalam wetu, wataalam wetu wapo wanaofanya maamuzi na kutushauri kama Serikali, sisi tunasimamia maamuzi hayo. Katika operation hii tuliyoyaona yanatisha, ziko gari za Waheshimiwa Wabunge tumezikamata na samaki haramu, wapo Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri, wapo wenyeviti wa vijiji tumefukuza watu tumesimamisha kazi watendaji wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa katika kufanya opetation hiyo, tulipokagua viwanda vyote, hakuna kiwanda hata kimoja tulichokikuta kinachakata samaki ambao wanaruhusiwa, vyote vilikuwa vinachakata samaki ambao wasioruhusiwa.
Tumekamata viwanda, tumekamata viwanda vya nyavu, viwanda vya nyavu ....

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya awamu ya kwanza ya operation sangara mwaka 2018 inayoendelea iko karibuni mbioni hatua ya kwanza kumalizika na mimi mbele ya Kamati yangu, nilishaiahidi kwamba baada ya taarifa hii kutoka nita-share na Kamati na niki-share na Kamati itaaingia kwenye Bunge lako, hilo wala halina tatizo. Ninachotaka niseme sasa ni haya yafuatayo; katika operation tuliyoifanya…

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niruidie kusema katika operation hii tumesimamisha watendaji wa Serikali waliokuwa wanajihusisha na uvuvi haramu, tumekamata baadhi ya magari ya Waheshimiwa Wabunge ambao wako humu humu Bungeni, tumekamata baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri, tumekamata na hata kuwaweka ndani baadhi ya Madiwani, na nasema hivyo sasa kwa mantiki hiyo, kama nilivyosema kwamba tunakamilisha taarifa, operation hii inafanyika katika mikoa mitano. (Makofi)

T A A R I F A . . .

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekamata zaidi ya kilo 133,000 zikitoroshwa kwenda nje ya nchi, za samaki aina ya kayabo na dagaa, 133,000 zikitoroshwa kwenda Rwanda, zikitoroshwa kwenda Burundi, zikitorosha kwenda Kongo na Sirari, zaidi ya tani 133,000. Tumekamata samaki wachanga zaidi ya kilo 73,000 rasilimali hizi zote zinachezewa kwa kiwango hicho. Tumekamata mpaka wageni walikuwa wanaingia mpaka kwenye visiwa vyetu wanashiriki uvuvi, wanunua samaki mpaka kwenye visiwa ambayo ni kinyume cha sheria wageni kutoka Rwanda, wageni kutoka kutoka kutoka Kenya, wageni kutoka kutoka Burudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumekamata viwanda, vilikuwepo hapa viwanda vya mabondo 22 vinafanya biashara ya mabondo lakini vilivyokuwa na leseni halali vilikuwa viwili tu. Kwa hiyo, tukisema tunapambana na uvuvi haramu, tunapambana nao kweli kweli na hii operation yangu hii haina mwisho hadi uvuvi haramu utakapomalizika hapa nchini mwetu na kwamba uvuvi wa wa bahari kuu na kwenyewe tumeshapata ya kufanya doria katika uvuvi wa bahari kuu walikuwa wamezoea wanavua wanaondoka Taifa letu linaachwa halina chochote. Tunashindwa kukusanya chochote na ndio maana mara ya kwanza tu nimeenda kukamata meli ile ambayo tumeikamata na tumepiga faini shilingi milioni 770.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea Bunge hili litapongeza jitihada hizi kubwa za Wizara ambazo zinalinda rasimiali hizi, leo hii mkakati wa kulinda uvuvi wa bahari kuu tutazikagua meli zikiwa zinaendelea kuvua huko huko, hakuna mtu atakayeondoka kwenye maji ya Tanzania akiwa amebeba rasilimali ya Watanzania na tutaongeza meli zingine mbili za doria, tunahikisha kwamba uvuvi wa baharini kuu pamoja na bahari nzima, coastal nzima yetu inalindwa kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba rasilimali hizi nchini mwetu, Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zote rasilimali hizi zinanufaisha Watanzania, hatarusiwa mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeki, niseme nasema kabisa hapa kama mtu atajishirikisha na uvuvi haramu hata mimi Mpina hata Mzee Mpina mwenyewe ninyi doria mkamateni kama anajishughulisha na uvuvi haramu wa Taifa hili. Hatuwezi kuongelea kwa maneno mapesi katika rasilimali za Taifa, sisi kama Serikali ni walinzi tu, makolokoloni, kolokoloni ukikuta mlango wa tajiri umevunjwa una shida kubwa, mimi ni kibarua wenu, kazi yangu ni kuhakikisha katika wizara mliyonipa rasilimali zinalindwa kwa nguvu zote na kazi hiyo na wizara yangu tutaifanya usiku na mchana. Lakini nasema kama kuna hoja ya msingi Wabunge wasituhumu kwa jumla, yawezekana kuna mtendaji akakosea katika kuchukua hatua unasema katika eneo fulani, katika kijiji fulani, kuna jambo hili na hili limefanyika Mpina - Waziri lishughulikie hata sasa hivi ukiniletea nitafanyia kazi na kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rasilimali hizi za Taifa zimetoroshwa kiasi cha kutosha na ninyi hapa Bunge hili muda wote limekuwa likilia makusanyo ambayo tunakusanya Halmashauri na Wizara kuhusu uvuvi ukijumlisha sisi sote ni takribani shilingi bilioni 20 ukiwaondoa wenzetu labda wa TRA. Kwa hiyo, makusanyo ni hafifu licha ya bahari kubwa tuliyonayo, licha ya maziwa tuliyonayo, licha mito tuliyonayo kwa hiyo ni wakati sasa wa Bunge hili kuisaidia hii Wizara, vijana hawa wanaofanya doria wanafanya kazi ya kujitolea sana, wangekuwa wepesi wasingeweza kufanya hatua kubwa hizi ambazo wanazozichukua sasa hivi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, na mimi nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ili niweze kuhitimisha hoja yangu kwa kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja za Wabunge zipo nyingi, zipo ambazo nitafanikiwa kuzieleza hapa na zipo nyingine ambazo utaturuhusu tuzilete kwa maandishi ili Wabunge wetu waweze kupata hoja mbalimbali walizoziuliza na ziweze kusaidia katika kusukuma hatua hii ya shughuli nzima ya sekta yetu ambayo ni ya mifugo na uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikianza moja kwa moja na eneo ambalo limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge zaidi ya nane ambao wapo hapa ilikuwa ni eneo la malisho ya mifugo ambalo wameliongea kwa hisia kubwa. Wewe mwenyewe najua ni mfugaji pia umeliongea kwa hisia kubwa sana. Pia imezungumzwa kuna migogoro mingi ya wakulima na wafugaji ambayo nayo imo mle, kuna migogoro kati ya wakulima na watumiaji wengine wa ardhi, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu aliwahi pia kuunda Tume ya watalaam ya kufuatilia suala la migogoro hii kati ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu kuwa katika mwaka 2017/2018 Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi imetenga jumla ya hekta 10,378.53 kwa ajili ya maeneo ya ufugaji kwenye vijiji 13 katika Wilaya za Makete, Kilolo, Tanganyika, Mpanda na Kalambo. Hadi sasa hekta milioni 2.545 katika vijiji 741 zimetengwa kwa ajili ya malisho.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu katika kuangalia hili suala la malisho ya wafugaji imefanya mambo yafuatayo; moja, katika ranchi zote za taifa (ranchi mama) hekta 2,000 zimetengwa kwa ajili ya wafugaji hasa wakati wa ukame na zitasimamiwa na NARCO yenyewe lakini unapofika muda wa ukame, wafugaji waliopo kwenye maeneo hayo watakuwa wanalishia mifugo yao, haya ni mageuzi makubwa hayakuwepo. Jumla ya hekta 7,000 tayari zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo. Pia hata hapo Kongwa tumetenga hizo hizo hekta 2,000 kwa ajili ya wananchi waweze kupata maeneo ya malisho. Kwa hiyo, katika Wilaya mbalimbali hizi za Kongwa, Longido, Siha, Arumeru na Karagwe kote kule tumetenga hekari hizo. Kwa hiyo, NARCO pamoja na TALIRI yote tunatoa hekta hizo kwa ajili ya malisho.

Mheshimiwa Spika, lingine tuliloamua ni kwamba katika maeneo ya ranchi zetu ambazo kuna watu wamewekeza, wale wawekezaji wote wababaishaji ambao na Waheshimiwa Wabunge mmewazungumza hapa kwa hisia kubwa, tumefanya tathmini wengine hawajawekeza kabisa na wengine hawalipi kodi ya Serikali, wote wale tunawaondoa. Taratibu zimeshakamilika kilichobaki ni kwamba kufikia tarehe 1 Julai, tutakuwa tumeshamaliza kuwaondoa wawekezaji wote wababaishaji na tutabaki na maeneo yetu ambayo tutaweza pia kuwapa baadhi ya wafugaji kwa ajili ya kulishia mifugo yao kwa utaratibu ambao utakuwa umewekwa.

Mheshimiwa Spika, vilevile tukaweka utaratibu mwingine kwamba kutakuwepo na ardhi ambayo haitakodiwa na mwekezaji wa kudumu. Itakuwa standby kwa ajili ya ku-accommodate kama kunatokea changamoto katika eneo hilo la malisho ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, tukaenda mbali zaidi kwamba wenzetu Wizara ya Maliasili na Utalii walishakuja hapa kutokana na timu hiyo iliyoundwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo Wabunge wengine wanauliza kwamba matokeo yake yapo wapi, lakini matokeo tayari tulishayaleta Bungeni. Hizi hekta nilizozitaja za watu ambao tunawaondolea ni zaidi ya hekta 65,000. Vilevile Maliasili na Utalii wamekubali kuyaondoa maeneo tengefu ambayo hayana sifa na wanakamilisha tu, wametuambia hapa watakamilisha hivi karibuni ili maeneo hayo yaweze kutolewa kwa wafugaji. Zaidi ya hekta 96,000 nazo zitatolewa ili kwenda kumaliza migogoro ya wafugaji wetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kubwa ambalo limefanyika hapa leo, nadhani watu wote wamesikia maamuzi ya Serikali dhidi ya malalamiko ya wafugaji ambao mifugo yao ilikuwa imeshikiliwa na hifadhi. Waziri wa Katiba na Sheria hapa ametoa matokeo ambayo ni zaidi ya ng’ombe 500 kesho zitaondoka. Hii inatokana na kikao ambacho nilikutana na wafugaji juzi kabla ya kuwasilisha bajeti yangu hapa. Tukazungumza wakanipa malalamiko yao nikachukua hatua ya kumuomba Waziri Mkuu baadhi ya Wizara tukutane. Tukakutana Wizara yangu, Wizara ya Katiba na Sheria, Mwanasheia Mkuu wa Serikali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali na Wizara ya Mambo ya Ndani tukazungumza tukakubaliana na hatua zinaendelea kuchukuliwa kwa ajili ya kupunguza haya malalamiko ya wafugaji hasa wanapokuwa wamekamatwa kwa makosa mbalimbali katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kabla ya hapo nilichokifanya ilikuwa kuwakumbusha pia wenzangu wa Wizara zingine umuhimu wa kuzingatia sheria unapokuwa umekamata mifugo ili kupunguza malalamiko ya mifugo kukamatwa na kufa na kukosa mahitaji muhimu kama ya maji na malisho. Nikaandika Waraka kwa wenzangu wote na unafanya kazi, naamini kabisa kwamba malalamiko ya namna hiyo sasa yameanza kupungua. Nataka niwahakikishie wafugaji wa nchi hii wapo kwenye mikono salama na tutahakikisha kwamba haki zao zinalindwa kwa nguvu zote ili waweze kuzalisha kwa maslahi ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni kuitaka Wizara kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwekezaji mkubwa katika viwanda vya nyama, maziwa na kadhalika. Nataka niwahakikishie kwa muda huu mfupi ambao nimekuwepo mimi na Naibu wangu kwenye ofisi ile tumefanya mambo makubwa. Tumefanya tathmini ya mikataba yote na mikataba mingi tumevunja ambayo haina tija kwa Taifa na mingine ambayo haijakamilika tupo kwenye hatua za kuikamilisha hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano Kiwanda cha Shinyanga kilichukuliwa na kikauzwa kinyemela na hati haikupatikana. Tumesimamia mpaka ile hati imepatikana kwa muda mfupi na sasa Kiwanda cha Shinyanga tathmini imeshakamilika na niwahakikishie kwamba mwezi huu wa sita tunatangaza tender ya kumpata mwekezaji mahiri kwa ajili ya kiwanda hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeenda Kiwanda cha Mbeya kiko vizuri kina ranchi safi. Kiwanda hiki na chenyewe tumehakikisha kwamba kinafanyiwa tathmini sasa ili mwezi huu wa sita na chenyewe kitangazwe ili tuweze kupata mwekezaji mahiri. Kiwanda cha Ngozi cha Mwanza ambacho Wabunge hapa wamekizungumza sana na chenyewe tayari Msajili wa Hazina anaenda kufanya tathmini ya kujua thamani yake ili na chenyewe tuweze kukitangaza ili tuweze kupata mwekezaji mahiri katika kiwanda hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mnaweza kuona kasi ya Wizara katika kuhakikisha kwamba viwanda vinajengwa Tanzania na vinaimarika kwa ajili ya ku-support hili soko la mifugo kwa sababu mifugo yetu tusipohakikisha viwanda hivi vinaanzishwa basi faida yake itakuwa ngumu sana. Kwa hiyo, viwanda hivyo vinaanzishwa na kile cha Utegi, lakini tuna kiwanda kingine kinajengwa Longido cha mtu binafsi, tuna kiwanda kingine kinajengwa Chato, Geita cha mtu binafsi. Kwa hiyo, mtaona kwa muda mfupi mageuzi makubwa ya mifugo yanakuja.

Mheshimiwa Spika, mmezunguzia juu ya uwekezaji katika Ranchi za Taifa (NARCO) na kuna wachangiaji zaidi ya 12. Kuna migogoro ya mipaka imezungumzwa huko na kuna mikataba imevunjwa ambayo haina. Ni kweli kabisa, mkisoma kwenye ripoti yangu mtaona mikataba ambayo tumeamua kuivunja ambayo haina tija. Moja, ni mkataba wa TMC, kiwanda chetu cha nyama hapo ambapo toka tukibinafsishe mpaka leo Serikali haijapata gawio, leo miaka kumi. Tumefanya tathmini katika kiwanda hicho, tukaona madhaifu yalipo na tukakuta kwamba miaka kumi hiyo hawajaweza kufanya malipo ya gawio lolote la kwetu.

Kwa hiyo, tunakamilisha hatua na mkataba huo tutauvunja. Tulipotishia tu kuvunja mkataba wakaja kwetu wakituambia kwamba tayari wana karibu shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya kutoa gawio. Kwa hiyo, mnaweza kuona mambo ambayo yalikuwa yanafanyika, ni mambo ambayo yalikuwa yanahitaji tathmini nyingi ili uweze kufikia maamuzi. Ndiyo maana mtaona kwenye ripoti hii kuna tathmini na operesheni, mambo hayapo sawa ukiona hali imekaa namna ile.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Diodorus Kamala, kaka yangu na kwa kweli nilikuwa mbeba mikoba hata alipokuwa Waziri. Yeye amezungumza suala la mgogoro wa mpaka alionao kati ya wananchi wake na NARCO. Mambo ya mipaka ni ngumu sana kiongozi kuyaamulia mezani, inahitaji nipate muda niende huko nikaone huo mgogoro kati ya NARCO na wananchi wale ukoje, tutatatua hakuna
ambalo litatushinda kwa sababu sheria ipo na nyaraka zipo, tutazipitia tutaona nani yupo sawa na kuna kasoro wapi. Nilishamuahidi Mheshimiwa Diodorus Kamala kwamba nitakwenda huko kwa ajili ya kushughulikia suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa suala la Operation Nzagamba. Operation Nzagamba imekuja baada ya kuona rasilimali zetu zinatoroshwa. Waheshimiwa Wabunge nataka niwaambie, tupo hapa tumekula kiapo kwa ajili ya Taifa hili na kulinda rasilimali hizi za Taifa. Hakuna mtu yeyote mwenye nia yoyote mbaya na Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania hawa wafugaji na wavuvi, mimi kama Waziri mwenye dhamana ya mifugo ningependa wapate mafanikio makubwa sana na lazima wapate mafanikio makubwa. Rasilimali hizi zinaibiwa, kila mtu anabeba anavyoweza. Kwa mwaka mmoja ng’ombe 1,600,000 wamebebwa, kondoo na mbuzi zaidi ya 1,500,000 wametoroshwa kwenda kuuzwa nje ya nchi bila kulipa chochote. Wanapoenda kuuzwa nje ya nchi sisi hatupati kitu chochote. Ngozi, nyambi, ajira na mapato ya Serikali yanaenda nje, tutaendeshaje? Yaani tuchunge sisi halafu wafaidike watu wengine? Hatukatai rasilimali zetu kwenda nchi jirani hata kidogo na isichukuliwe kwamba kuna Waziri au mtu yeyote anakataa, tunachokataa ni lazima Taifa hili linufaike kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.

Mheshimiwa Spika, gharama ya mtu akitaka kuuza ng’ombe nje ya nchi analipia shilingi 20,000 kwa mujibu wa sheria kwa ng’ombe mmoja na kwa mbuzi analipia shilingi 5,000. Haiwezekani ng’ombe wetu wakaenda bila kuzilipa hizo tozo na mimi Waziri nipo hapo kwenye Wizara, haiwezekani. Lazima tuweke utaratibu ambao utalifanya Taifa hili linufaike. Tulikuwa tunakusanya shilingi bilioni 1.1 kwa mwezi kwa maana ya sekta ya mifugo, leo niwaambieni kutoka shilingi bilioni 1.1 hizi operesheni ambazo mmezihoji tunakusanya shilingi bilioni 3.5 kwa kudhibiti fedha ambazo zinaibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaamini wamekuja Mawaziri hapa wa Afya mmewapigia makofi kwa sababu wanajenga vituo vya afya lakini si ndiyo hela zenyewe lazima tusimamie vyanzo vyetu ili tuweze kulijenga Taifa letu. Sasa wewe una mifugo, unatangaza una mifugo milioni 30; mbuzi milioni 18 na kondoo milioni 50, uchunge wewe asubuhi mpaka jioni halafu wakanufaike watu wengine hata kodi kidogo usitoze, halafu ukitoza kidogo iwe lawama tena? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nakubali yapo mambo ambayo tunaweza kushauriana kwa namna ya kuyaweka yawe vizuri zaidi, lakini nataka niwaambie tunaibiwa mno na ndiyo maana nikawapa na hiyo tathmini ya shilingi bilioni 263 zinatoroshwa. Mifugo iliyopo kwenye Taifa hili, Wizara ya Mifugo kwa kodi tunayokusanya haiwezi hata kulipa mishahara ya Wizara labda niwaambieni sasa ndiyo muone wingi wa utoshaji ulivyo. Hata Wizara ya Mifugo yenyewe mapato yanayopatikana hayawezi kulipa mishahara, hatuwezi kukubali ikawa hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanya operation hapa, watu wanaingiza maziwa na nyama ambazo hazijalipiwa. Wazalishaji wa nchi hii wanakula hasara kubwa, wenye viwanda vya nyama na maziwa wanapata hasara. Sisi ndiyo Wabunge na ninyi ndiyo muda wote mmetulalamikia kushindwa kusimamia unregulated importation. Sasa unataka Waziri afanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitegemea na naomba mnipe nguvu zaidi ya kuhakikisha kwamba tunazilinda hizi rasilimali. Katika miezi sita niliyokaa kwenye Wizara hii makusanyo ambayo tumekusanya pamoja na kodi mwaka jana mlioziondoa nyingi sana Waheshimiwa Wabunge katika Wizara hii lakini tumekusanya mpaka sasa hivi tuna shilingi bilioni 37; zaidi ya shilingi bilioni kumi za mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu walisema Wizara hii wanatoza watu kodi kwa ajili ya kubaki na hela, hakuna fedha yoyote inayobaki Wizarani. Fedha hizi zote zipo Hazina na ndizo hizo zinazoenda kwenye miradi yenu ya maji, zahanati na kila kitu. Mimi Mpina na Wizara yangu tunapata mshahara tu uliowekwa, ndiyo tunachopata lakini hakuna maslahi mengine yoyote yale katika kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Taifa hili ni la kwetu, mmetuapisha kwa katiba na kwa sheria tunazisimamia sheria ili Taifa linufaike. Mtaona makusanyo haya, tulikuwa tunakusanya kama shilingi bilioni 32 tu Wizara yote yaani sekta yote ya mifugo na uvuvi unayoijua. Nawaambieni tupo hapa leo mwaka unaokuja wa fedha katika Wizara hii tutavunja rekodi ya kukusanya karibu shilingi bilioni 100. Yote haya ni ili Watanzania wapate fedha wanufaike na rasilimali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapiga kura wangu wa Kisesa wako hapa wananisikiliza, mimi siyo mnafiki na mpaka naingia kaburini sitakuwa mnafiki. Sekta hii tutaisimamia kwa weledi mkubwa kuhakikisha kwamba Taifa hili linaendelea maana tumechezewa mno. Kama tunachezewa halafu hatujui tunachezewaje tutaingia kwenye mgogoro mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie sekta ya uvuvi. Tumefanya maamuzi, Waheshimiwa Wabunge mmekuwa mkituomba muda wote mnataka Shirika la TAFICO lifufuliwe, nimefanya maamuzi Shirika la TAFICO sasa linafufuliwa tarehe 1 Julai na watendaji watakuwa ofisini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mmezungumzia kuhusu ujenzi wa bandari, ujenzi wa bandari tayari na tumeshapata mpaka na mtu wa kufanya huo upembuzi yakinifu. Miezi nane anakamilisha, Tanzania tunaanza kujenga bandari ya uvuvi. Mungu awape nini kama siyo Mawaziri wenye kuthubutu kama mimi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanya maamuzi, wafanyabiashara wetu wengi wanalalamika juu ya importation ya samaki wengi sana. Tuna maziwa haya lakini samaki wanaoingizwa hapa mpaka sato ambao tunaweza tukazalisha sisi, vibua ambao wako wengi tu, kwenda kuvua katika katika Ziwa Victoria, watu wanaingiza. Kuna watu wangependa sisi hapa tusivue hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi hali ya uvuvi haramu ilivyo na nitawapa documents ninazo hapa, nataka niwape taarifa. Kuna Wabunge wengine hapa waliongea mpaka wakalia lakini nadhani kama kweli ni wazalendo, hizo taarifa nitakazozitoa hapa zitawaliza machozi kwa ajili ya Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaibiwa kila sehemu, kwenye uvuvi hapa nimeendesha hiyo Operation Sangara inaitwa Operation Sangara 2018. Operation Sangara 2018 ninavyoiendesha mimi na Wizara yangu, kwanza, utaratibu wa muundo wake, tumeunda operation ambayo sio ya wavuvi tu, tulijua hili na mimi najua operation hizi, kila mtu aliyefanya operation, Waziri yeyote aliyefanya operesheni alipata tatizo katika Bunge hili na nilijua toka mwanzo kwamba haya yatajitokeza. Ndiyo nikasema tunapounda operation hii, nikasema Wavuvi, Mazingira, Polisi, Usalama wa Taifa wote wawemo ili tunapokwenda, tunakwenda kama task force kwa ajili ya kwenda kung’oa huu mzizi wa uvuvi haramu ulioshamiri ambapo Taifa linakosa mapato yake. Watanzania wanakula vifaranga, hii nchi siyo ya kula vifaranga, yenye maziwa na bahari kubwa. Halafu Watanzania wanakula vifaranga na wanakula samaki wa kutoka nje na wana furaha kubwa kufanya hivyo wakati samaki wao wanavuliwa kwa shuka, wanavuliwa kwa nyavu zisizoruhusiwa. Kwa hiyo, tukawa tunafanya hivyo.

Vilevile kulikuwa na timu ambayo inaratibu zoezi hili ambayo nayo ilishirikisha Wizara hizo ninazozisema. Tulifanya tathmini za mara kwa mara kuangalia hizi operation zinavyokwenda.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme na Wabunge wanisaidie. Nimeingia kwenye Kamati yangu, ikanieleza kuhusu uvuvi haramu, wakanipongeza kwa kazi nzuri na wakasema niendelee. Nilipokuja kwenye Bunge lako nililieleza kwamba kama kuna changamoto yoyote kuhusu uvuvi haramu, naomba basi hiyo document mimi niishughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo Wabunge ambao walikuja ofisini kwangu na malalamiko ya wananchi wao. Mengine yalikuwa ya kutaka tu Waziri aone huruma dhidi yao na nilifanya hivyo na wako wengi. Mimi niliomba nipewe hizo nyaraka lakini mpaka leo ninavyozungumza hakuna nyaraka hata moja niliyoletewa na Mbunge hata mmoja ambayo Wizara yangu ilishindwa kushughulikia. Ndugu zangu uvuvi haramu unaliangusha Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nitoe matokeo, tumefanya operation mara tatu, katika operation ya awali watuhumiwa walikuwa 1,200, tulipokwenda kipindi cha mpito wakafika 610 na tumekwenda kipindi cha pili wakawa 1,474; kwa hiyo wanaongezeka. Zana haramu, kokoro, tulivyoanza zilikuwa 2,661 tulizoziondoa majini, tulipokwenda kipindi cha mpito ikawa 335 na baadae awamu ya pili zikawa 8,007.

Mheshimiwa Spika, kuhusu nyavu haramu awamu ya kwanza ilikuwa 410,213, ya pili 63,757, ya tatu 81,461. Jumla ya nyavu haramu tulizozitoa Ziwa Victoria ni pieces 555,431 ukizidisha mara mita 80 unakuta karibia kilometa 40,000. Kilometa 40,000 ni sawa na kwenda Afrika Kusini karibu mara tano, unaenda unarudi, unaenda unarudi, ndiyo nyavu zilizokuwepo Ziwa Victoria.

Sasa kama una nyavu hizo katika ziwa lako, utafanya nini? Nyavu hizi zote tumeziondoa na sasa kama mnavyoyaona matokeo ni makubwa, samaki wameongezeka katika ziwa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tumekamata samaki wakitoroshwa kwenda nje ambao Taifa lisingenufaika kwa chochote zaidi ya kilo 181,217. Maana yake ni magari 18 ya tani 10 zilikuwa zinatoroshwa tu kwenda Congo, Malawi, Kenya na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, mabondo ambayo yana thamani kubwa, zaidi ya kilo 5,147. Kuhusu pikipiki zinazokamatwa zikibeba samaki wachanga zaidi ya pikipiki 269 zimekamatwa wakibeba samaki wachanga na kwenda kufanya biashara usiku. Magari zaidi ya 564 yakiwa yamebeba samaki wachanga na wasioruhusiwa kwa mujibu wa sheria yalikamatwa.

Mheshimiwa Spika, sasa Ziwa Victoria kama mlivyopata kwenye taarifa katika rasilimali ya tani milioni 2.7 ambazo Taifa hili ndiyo stock yetu ya samaki, tani milioni 2.1 zinatoka Ziwa Victoria. Kwa hiyo, usipo-manage uvuvi haramu kwenye Ziwa Victoria, maana yake sekta au Taifa haliwezi kunufaika kabisa na uchumi wa nchi yake.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na mambo yafuatayo; hii taasisi yetu ya TAFA walikuja ofisini na walikuwa na mambo mawili makubwa waliyoyawasilisha. Moja, ilikuwa ni suala la nyavu za kuunganisha, ndilo lililokuwa tatizo lao kubwa. Walipokuja kwangu nikawaambia nitalifanyia kazi na nikawaagiza TAFIRI kufanya utafiti huo ili tuweze kuja na majawabu ya nini tufanye katika uvuvi huu wa nyavu za kuunganisha.

Mheshimiwa Spika, lakini hata tulipoenda kwenye kikao chetu cha Lake Victoria Fisheries Organization, ndiyo matokeo haya yanatarajiwa yapatikane ili sisi wote kwa pamoja tuweze kuunga lile zoezi la kwamba kama East Africa tutaamua kuvua kwa nyavu za aina gani. Kwa sheria zilizopo zinakataza kufanya uvuvi kwa nyavu zilizoungwa, ndiyo sheria zilizopo na sio Mpina.

Mheshimiwa Spika, vilevile wavuvi hao walivyokuja kwangu baada ya kuachana nao na kuwasihi kwamba waache uvuvi haramu, jioni tu wote walikamatwa, sehemu kubwa wanahusika na uvuvi haramu. Mambo mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge walikuwa wakipigiwa simu na wananchi wakiwa kule walikuwa wakiniwasilishia mimi malalamiko. Wanaponiwasilishia malalamiko anaambiwa amekamatwa tu akiwa hana koleo la plastiki, amepigwa faini shilingi milioni tano. Ukienda kufuatilia, ukweli siyo huo na Mbunge mwenyewe mhusika anathibitisha kweli nilidanganywa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hapa nataka niweke hivi, cha kwanza lazima mfahamu, kukamatwa tu kwenyewe ni changamoto, ama umeonewa au umekamatwa kwa haki. Kwa hiyo, taarifa zinaweza zikaletwa zikawa sivyo.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na huyu Mbunge wa Ukerewe Jimboni kwake, tulikuwa na Waziri Mkuu, tumefanya ziara katika eneo la Ukerewe, mabango yote ya Waziri Mkuu yalionesha wanaomba maji na vitu vingine, lilitoka bango moja tu la kulalamikia kuhusu nyavu. Waziri Mkuu ameweza kufanya ziara kule na mimi akaniita. Hakuna mahali ambapo Wizara ililalamikiwa kwa malalamiko ambayo yanazungumzwa hapa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana mimi muda wote niwapo hapa nimekuwa nikiwaomba Waheshimiwa Wabunge kwamba kama kuna tatizo, Mbunge umepewa muda wa kuongea na Mheshimiwa Spika, umepewa dakika 10 zote za kuongea, mpaka unamaliza kuzungumza unasema tu operation hii imejaa uonevu mkubwa, watu wetu wameonewa sana, watu wetu wamedhulumiwa sana lakini kwa nini mimi sijawahi kuambiwa ni wapi, licha ya kuliomba Bunge hili mara kwa mara lituambie ni wapi ambapo wananchi wameonewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Musoma nimekwenda mara nyingi mimi, amezungumza kaka yangu hapa, Mheshimiwa Mathayo kuhusu yale magari ya wafanyabiashara. Amekaguliwa akakutwa na maboksi matatu ya samaki wasioruhusiwa, unataka watendaji wafanye nini? Una samaki maboksi matatu katika gari lako na wanafanya sampling, wakishayapata yale lazima wakukague, wafanye nini sasa, njia mbadala wafanyaje? Unajua kabisa wewe huruhusiwi kununua wala kuuza samaki wasioruhusiwa, alitaka Mheshimiwa Mbunge wafanye nini?

Mheshimiwa Spika, lile gari lingine lililokuwa limekamatwa akanipigia mimi simu, mimi na yeye tunapigiwa simu tu. Yakakutwa maboksi 27 ambayo yana samaki wasioruhusiwa. Sasa ukisharuhusu sheria ya namna hiyo huyu mwenye pikipiki asikamatwe hata akiwa na samaki wasioruhusiwa, huyu mtu wa class hii asiruhusiwe, mtaisimamiaje sheria na hawa watendaji wangu watasimamiaje sheria?

Kwa hiyo, mimi niseme Wizara yangu tuko committed, tuko tayari kuchukua maelekezo ya Waheshimiwa Wabunge, watushauri katika maeneo yote ambayo wao wanaona kwamba hapa kuna kasoro na sisi tunayafanyia kazi. Aliwahi kuja Mheshimiwa Ngeleja ofisini kwangu saa tano usiku akakuta Wizara nzima tuko ofisini. Tunakesha kufanya tathmini hizi lakini kwa shabaha moja tu kuhakikisha kwamba rasilimali za Taifa letu tunazikomboa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kwamba hawana nia mbaya na operation lakini tunalalamikia kasoro. Sasa mimi kwenye Kamati niliomba kasoro, nikaja hapa Bungeni mwezi Februari nikaomba kasoro na bahati nzuri kuna Wabunge wengine wanasema kabisa tuna ushahidi, huo ushahidi kwa nini hautolewi au kuna tatizo gani? Kwa nini mtu aseme tu nina ushahidi lakini usitolewe? Naweka mezani kwamba sijawahi kuletewa tatizo lolote na Mheshimiwa Mbunge nikashindwa kulitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaeleze jinsi mambo yanavyokuwa na niwape mfano mmoja wa Kisiwa cha Lubili, Bukoba ambapo tulikuta wamevuliwa samaki wachanga kilo 65,000, wameanikwa mpaka hakuna hata pa kukanyaga na yule mtu ni Mkongo ambaye ndiyo anavua. Wanakuja Wacongo na Waganda wanalipa fedha hapa, wana- facilitate uvuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, ukienda Uganda, Mheshimiwa Yoweri Museveni ameamua kupeleka jeshi kabisa ziwani kwa ajili ya kupambana na uvuvi haramu. Sisi tunatumia multi-agency yeye anatumia jeshi. Uganda sasa hivi wamepiga hatua kubwa sana katika rasilimali za uvuvi katika Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kueleza kwamba tuliwapa rekodi ya kupungua kwa samaki kutoka tani 50,000 mpaka tani 25,000/26,000 kwa maana ya karibia nusu ya rasilimali zetu zote zilizoko katika Ziwa Victoria zimepungua.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala ambalo limeletwa hapa la uwekezaji wa viwanda katika Ukanda wa Pwani. Tunaomba tuwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba katika Ukanda wa Pwani mipango tuliyonayo sasa uwekezaji utafanyika tu na ndiyo maana nimeamua kwamba TAFICO iwepo pale ili sasa iweze ku-coordinate uwekezaji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge hapa, kaka yangu sana, Mheshimiwa Alhaji Bulembo, amelalamikia juu ya kumualika mwekezaji mmoja kuja hapa Bungeni na akasema kwamba yule mwekezaji ana tuhuma. Ninachoweza kukisema huyu mwekezaji kwa sasa hapa kwetu katika sekta ya uvuvi, Mafia ana shamba lake ambalo sasa hivi anavuna kwa mwaka tani 300 hadi 400 na ameajiri Watanzania 1,700. Mimi hapa Mpina kumualika kuja Bungeni kama ana tuhuma haimuondoshi kwenye tuhuma zake na wala Mpina hawezi kuingia kwenye mtego huo ambao unazungumzwa, mtego upi sasa? Mimi nimemualika tu kama mwekezaji aje hapa, kama ana matatizo vyombo vya dola si vipo, vitachukua nafasi. Kwa nini nalo hili liletwe liwe kama lawama kwa Waziri kualika mtu kuja hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hebu tupendane, tulijenge Taifa letu kikamilifu. Tulishachelewa mno, ni lazima tuungane sasa kulijenga kwa nguvu zote ili tuweze kufikia mahali ambapo kutaleta matumaini makubwa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza dhidi ya nyavu na amefafanua vizuri kwamba tatizo la nyavu tumefanya hivyo baada ya kufanya operation, umekamata kila mtu ana nyavu haramu, isingewezekana muda huohuo tena ukasema kwamba unaweza kuruhusu watu kuingiza nyavu. Sheria inamtaka yule anayetaka kuingiza nyavu ahakikishe kwamba anapata kibali kwanza ndiyo anaagiza nyavu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi katika kipindi hiki tulichokuwa tunafanya tathmini na tumemaliza kufanya tathmini, tumeona, kama ni nyavu tutaruhusu za kutoka nje tunataka turuhusu kiasi gani? Si ndiyo Bunge hilihili mnalotaka tuvilinde viwanda vya ndani? Tumetathmini tumeona viwanda vyetu vina uwezo wa kuzalisha karibia asilimia 50 ya nyavu zinazohitajika lakini tumeona bado hawana uwezo wa kumaliza kabisa gap. Kwa hiyo, sasa hivi tutaruhusu kiasi fulani cha nyavu kuingia ili kuweza kuziba gap ambalo watu wetu wanalilalamikia.

Mheshimiwa Spika, nimalizie na hoja nyingine mbili ambazo na zenyewe zimekuwa zikijirudia sana na zimezungumzwa katika maeneo mbalimbali. Wizara iwasaidie wavuvi kupata samaki wengi baharini, hilo Waheshimiwa Wabunge tunalifanya vizuri sana na miradi mingi sana tunapata kwa ajili ya kuwasaidia wavuvi wetu.

Sasa hivi NMB wamekuja na mpango mzuri sana wa kuwatafuta wavuvi wote na kuwaingiza kwenye usajili na kuwafungulia akaunti ili tuanze kuwafahamu wavuvi wetu wako wapi na wanafanya nini. Hili tumelisimamia vizuri sana pale Wizarani na sasa hivi karibu akaunti 20,000 za wavuvi zimefunguliwa nchini na NMB katika maeneo mbalimbali. Tutakwenda kuwafikia wavuvi wote ambao wako takribani 200,000 ili waweze kuingia kwenye mfumo rasmi wa uzalishaji waweze kukopesheka. Kwa sababu watakapokuwa na mikakati hii wavuvi wetu wataweza kukopesheka.

Mheshimiwa Spika, lakini limezungumzwa sana suala la BMUs kwamba zitumike katika kusimamia mambo haya. Katika operation inayoendelea, watendaji na viongozi wengi wa BMUs tumewakamata kwa uvuvi haramu. Kwa hiyo, lazima utathmini kidogo uone mambo ya namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, kaka yangu, Mheshimiwa Kanyasu, yeye kila siku akisimama anazungumzia suala la furu, nembe na gogogo; anazungumzia suala la nyavu ambazo ni double. Nimesema haya mambo jamani ukizungumzia mifugo na samaki, unazungumza sayansi. Waziri au Naibu Waziri hatuwezi kujifungia tu tukasema leo tunaruhusu single, utafiti unakamilika na TAFIRI tumempa fedha alikuwa na upungufu wa shilingi milioni kumi tu kufanya na kuimaliza kazi hiyo ya utafiti. Tutakuja na majibu, Waheshimiwa Wabunge mtuvumilie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hata hawa tuliowapa kazi ya utafiti hawajamaliza swali linaulizwa kila siku lile lile. Suala la nembe na gogogo sheria zilizopo zinakataza kuwavua wale kwa maana ya nyavu zitakazotumika zitakuwa ni haramu Ziwa Victoria. Tayari tumesha mua-sign TAFIRI kufanya hiyo kazi na fedha tumempa; mambo haya yatakamilika tupeni nafasi tunauwezo wa kuleta mageuzi makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninajua, kwamba leo makofi yanaweza kuwa machache sana kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, lakini nitakapokuja mwakani tarehe kama ya leo Bunge lako lote hili watageuka kuwa washangiliaji kutokana na mageuzi ambayo tunaenda kuyafanya. Tumejipanga, hatutashindwa, tupeni imani hiyo ili tuendelee kuwatumikia.

Mheshimiwa Spika, najua ilishagonga ya kwanza, lakini nimalizie tena kwa kuwashukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kunipa imani kubwa ya kuisimamami sekta hii, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Baraza zima la Mawaziri. Pia niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Kisesa ambao wanaendelea kunivumilia katika hii kazi ngumu ninayoendelea nao ya kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mhehimiwa Spika, na mwisho Waheshimiwa Wabunge niwaombe, niliwasikia Waheshimiwa Wabunge wakisema kwamba hii bajeti itakuwa ni bajeti ngumu sana kupitishwa na Bunge hili. Mimi naomba iwe bajeti rahisi sana kupitishwa na Bunge kwa pongezi ya kazi kubwa tulizozifanya
kwa mageuzi kama hayo. Mmeona vitu vilivyokamatwa, hawa watu kama wangekuwa sehemu kubwa yao si waaminifu haya mambo tusingeyafanya. Kukusanya bilioni 7.5 katika muda huu za kuuza samaki wanaotoroshwa na faini ambazo zilizokuwa zikipigwa, shilingi bilioni 7.5 si kazi ndogo, wangekuwa wala rushwa hapa tusingefikia kukusanya hayo makokoro yote 555,000 kama wangekuwa watu si waaminifu tusingefikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi ningewaomba kwanza tuwatie moyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambao wanasimamiwa kikamilifu ili waendelee kufanya kazi hiyo nzuri ya kulinda rasilimali na ili waweze kulinda Ziwa Victoria na maeneo mengine na maziwa yote na baharini kote. Tumefanya operesheni kule mmeona fani zaidi shilingi bilioni 20, tumekamata ile meli ipo mahakamani tunarajia tutashinda kesi hiyo, tunataifisha hiyo meli. Watu wamegeuza shamba la bibi hapa, wanavuna wao zaidi ya bilioni mia nne na hamsini, sisi tunakusanya kodi shilingi bilioni 3.2; jamani mmekubali haya yaendelee kutokea?

Mheshimiwa Spika, huko kwenye operation Mati nimezungumza suala la yule mwananchi ambaye alikufa. Jambo hili liko kwenye vyombo vya dola kuona mambo yalienda vipi na ndiyo maana Waziri wa Mambo ya Ndani hapa alishatoa majibu ya jambo hilo, linachunguzwa, watendaji hawa wa Serikali wana sheria zinazowaongoza, kama kuna kosa lilifanyika mhusika atachukuliwa hatua.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwaomba tena Waheshimiwa Wabunge waunge mkono bajeti hii ili waiwezeshe Serikali kutekeleza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ninawaomba tena; mimi Mpina na Wizara yangu ni vibarua tu, tuleteeni mapungufu ya maeneo mbalimba hapa hata leo, hata sasa hivi tutaenda kwenye maeneo hayo, kwenye vijiji hivyo kukutana na wananchi hao ili tuweze kumaliza mzizi wa fitina na kuondoa kasoro hizo ambazo wananchi wametendewa isivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba sasa kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nami nishukuru sana kwa nafasi hii ambayo umenipatia ili niweze kuchangia kuhusiana na mapendekezo na maazimio ya Kamati hizi zote mbili. Niipongeze sana Kamati yangu, Kamati ya Kilimo, Mifugo, Maji na Uvuvi kwa kazi nzuri sana waliyoifanya ikiongozwa na Mheshimiwa Mahmood Hassan Mgimwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakubaliana na mimi kwamba hata ukisoma tu ripoti yao utajua kwamba hii Kamati ina Mwenyekiti makini na Wabunge makini sana wanaofanya kazi vizuri sana. Niwapongeze sana kwa pongezi walizotupa ukurasa wa 42 kwa kuanzisha Dawati la sekta binafsi kwenye Wizara, tunazipokea pongezi hizo. Dawati hilo limekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi wetu, wazalishaji, wenye viwanda na wafanyabiashara wote na wawekezaji hapa nchini. Pia wamealika vijana wa vyuo vikuu wakiongozwa na Ndugu Peter Nibonye, Rais wa Vyuo Vikuu (TAHLISO) ni mambo mazuri vijana hawa nao waweze kujifunza na kuona jinsi tunavyofanya shughuli zetu humu.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri sana. Kwa kuanzia nianze kusema kwamba yale mapendekezo na Maazimio ya Kamati yaliyowekwa nakubaliana nayo asilimia 100 na sisi kama Serikali tutayasimamia kuhakikisha kwamba utekelezaji wake unafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi walipochangia waliniomba na waliniagiza kwenda kutembelea na kukutana na wavuvi hasa katika Ukanda wa Pwani. Napenda tu kusema kwamba nimekubali, nimeandaa ratiba ambayo nitatembelea eneo lote kuanzia Moa hadi Msimbati; kuhakikisha kwamba nakutana na wavuvi wote na kuzungumza nao na kuona changamoto zao na kuzitafutia majawabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati na Waheshimiwa Wabunge wengi na kwa muda mrefu wamezungumzia sana suala la kufufuliwa kwa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO). Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali ya Awamu ya Tano iko kwenye hatua nzuri sana za kulifufua hili Shirika. Moja, tayari mpaka sasa hivi, kama Kamati ilivyozungumza menejimenti tumeiweka, uhakiki wa mali unaendelea ambapo mpaka sasa hivi zaidi ya shilingi bilioni 141, samani, viwanja, maghala, ofisi na nyumba ambazo zilikuwa zinamilikiwa na watu kinyemela na nyingine walikuwa wamejimilikisha tumeshazitaifisha na sasa zimerudi mikononi mwa TAFICO, vitu vyenye thamani ya shilingi bilioni
118. Tunaendelea kwenye maeneo mengine kuhakikisha kwamba assets zote za shirika hili zinarejea.

Mheshimiwa Spika, vilevile tunakwenda kwa kasi kuandaa mipango ya biashara, nayo tunaenda vizuri. Mpaka sasa hivi tayari tumeshapata shilingi bilioni 4.3 kutoka Serikali ya Japan kwa ajili ya kufufua ile miundombinu yetu, kwa maana ya majokofu ya kuhifadhi samaki, gari la barafu, meli moja ya uvuvi na kujenga gati la kuegesha meli za TAFICO, kwa hiyo, tunaenda vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, katika huo mpango wetu wa biashara tunaoufanya tunajiandaa kununua meli mbili kubwa ambazo tutaingia kwenye uvuvi wa bahari kuu. Wabunge kwa muda mrefu na mingi sana wamekuwa na kilio kikubwa sana, ya sisi kuingia kwenye maji ya bahari, nataka niwahakikishie Serikali ya Awamu ya Tano tunaingia kuvua katika uvuvi wa bahari kuu na mipango iko vizuri na ndio maana unaona sasa hivi kwa muda mfupi tu tumezipata hizi bilioni 4.3 ambazo zinaturahisishia sana safari yetu kuendelea.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa bandari kama nilivyosema tayari Mtaalam Mwelekezi sasa hivi anafanya anaendelea na zoezi ambalo ni miezi minane tu atakuwa amemaliza suala la upembuzi yakinifu ili tuanze ujenzi wa bandari. Hili nalo limezungumzwa miaka mingi, lakini sasa tunaenda kuanza, rasmi ujenzi wa bandari yetu ya uvuvi.

Mheshimiwa Spika, la nne, Wabunge wengi wamelalamika na nakubaliana nao kabisa, malalamiko yao ni ya haki juu ya viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo, viwanda hivyo vingi havipo, ni kweli kabisa nakubaliana nao. Hata hivyo, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge habari njema za Serikali ya Awamu ya Tano, mipango tuliyonayo, viwanda vingi, tunaenda kuvifufua na sasa hivi ninavyozungumza tunaenda kujenga kiwanda kikubwa sana pale Ruvu. Kiwanda ambacho kitakuwa na machinjio, kiwanda ambacho kitakuwa na uchakataji wa kusindika nyama, kiwanda ambacho kitasindika ngozi, kiwanda ambacho kitasindika mazao ya ngozi, maana yake ukiingiza ngozi mpaka unaenda kutoka na kiatu. Pia tutajenga mnada mkubwa sana wa Kimataifa pale Ruvu na hii mchana Bunge lilipoahirishwa Waziri mwenzangu kwa sababu kiwanda hiki kinajengwa baina ya Kampuni ya NARCO Tanzania na Kampuni ya Misri na fedha zipo. Tunatajia kwamba kuanzia Machi, ujenzi wa kiwanda hiki utaanza, matatizo ya wafugaji wa nchi hii yamefika mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiwanda hicho kinajengwa na fedha tunazo. Leo kama ninavyozungumza Waziri mwenzangu wa Mifugo na Uvuvi kutoka Misri tumekutana na tumeazimia kwamba sasa ujenzi uanze kuanzia Machi na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna viwanda vingi vinajengwa, kipo Kiwanda kikubwa sana kinajengwa Longido, chenye uwezo wa kuchakata mifugo mingi kwa siku, tuna Tan Choice Kibaha, kinajengwa chenye uwezo wa kuchinja ng’ombe zaidi 1,000 mbuzi zaidi 4,000 na kiko kwenye hatua ya mwisho kukamilishwa, lakini kule Kahama, Chato tunajenga kiwanda kingine.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge napenda niwaambie, Serikali ya Awamu ya Tano, iko kazini, matatizo ya wananchi kukosa soko sasa yamefika mwisho na viwanda hivi, ni tegemeo kubwa sana la uchumi wa nchi yetu ambalo litawawezesha wananchi wetu kuwa na soko la uhakika litawawezesha wananchi wetu kupata manufaa ya mazao haya ya mifugo ambayo muda mrefu wameshindwa kunufaika nayo.

Mheshimiwa Spika, tumeenda tumefanya makubwa ambayo yalikuwa yamesimama kwa muda mrefu, kama uogeshaji wa mifugo, sasa hivi tunaogesha mifugo kila kona, mahali ambapo hawaogeshi mifugo ni mahali tu ambapo hawana josho lakini maeneo yote tumegawa dawa kwenye maeneo yote yenye majosho kwa ajili ya kuweza kuogesha. Kwenye majosho 1,409 yote ninavyozungumza hivi sasa wanaogesha mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeazimia kwamba uogeshaji wa mifugo utakuwa ni wa kila siku na Wizara itaendelea kutoa madawa kwa ajili ya uogeshaji. Wafugaji walikuwa wanateswa kuogesha ng’ombe mmoja unadumbukiza unalipa Sh.1,000, Sh.500, Sh.2000 tumesema hapana, watakuwa wanachangia gharama ndogondogo tu ya kujaza maji na kununua zile dawa ndogo ndogo na ng’ombe akiingia majini analipa Sh.50 tu na tutaweka mpaka kwenye Kanuni kwa sababu wafugaji wamedhulumiwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na hili tatizo kubwa hapa la muda ambalo ninalohangaika nalo, sasa nizungumzie hoja za Waheshimiwa Wabunge, wamezungumza mambo mengi mazuri na hasa pia wakazungumzia suala la doria na wakazungumzia suala la operesheni. Waheshimiwa Wabunge hapa tuelewane, tunazungumza uwekezaji leo, hivi nani anayeweza kuja kwenye uwekezaji kwenye nchi ambayo haiwezi kulinda raslimali zake, hakuna. Nani atakayejenga Kiwanda leo hapa, cha Kusindika Samaki wakati samaki wakati samaki wote wanatoroshwa kwenda nje, bila hata kufata utaratibu unaokubalika, ni nani? Nani atakayekubali kuwekeza kuzalisha vifaranga kuzalisha kuku, kuzalisha ng’ombe wa maziwa katika nchi ambayo maziwa yanatoka nje ya nchi hayana vibali, hayajalipiwa kodi yoyote hayajapimwa ubora na yanauzwa na yanashindana na viwanda vya ndani, nani atakayejenga viwanda hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, pia nani atakayejenga viwanda katika nchi ambayo inaruhusu mpaka vitu vilivyokwisha muda wa matumizi, kuuzwa hapa nchini na kushindana na wazalishaji wa ndani, nani atakubali? Ni lazima tukubali, doria zinazoendelea, doria zinazoendelea hapa nchini zinalenga kuwalinda wazalishaji wa ndani ili waweze kuzalisha vizuri. Leo nenda kawaulize wazalishaji wa Viwanda vya maziwa, wameji-commit hata kuongeza uzalishaji kwa sababu kuna ulinzi madhubuti, hakuna mtu anaingiza leo mzaha kutoka nje, mzaha mzaha hapa nchini hakuna.

Mheshimiwa Spika, katika vitu ambavyo nilichukia kuliko vyote, ulikuwa Naibu Spika, lakini wewe ni kiongozi wangu wa muda mrefu nikiwa Mbunge wa kawaida, kitu kilichokuwa kinaniuzi na kupita vyote ni suala hili, watu wanaleta vitu hapa nchini vilivyokwisha muda wa matumizi wamepita njia za panya, halafu Waziri mhusika anakuja kuwasilisha naye analalamika juu ya mambo hayo, wakati yeye ndiyo ana uwezo wa kuwashika. Tutawashika na sisi hatutakubali raslimali zetu kuvuruga wawekezaji wetu hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, naomba tuungane pamoja tuzilinde hizi rasilimali kwa ajili ya wananchi wetu kwa sababu zikitoweka hata wao hawawezi kunufanika, samaki wakitoweka majini yakabaki maji tu, nani anayewahurumia wavuvi? Mtu ambaye anaruhusu watu wakavue kwa nyavu haramu, halafu baadaye mvuvi anayeenda kuvua kwenye ziwa, anaenda na mafuta yake na gharama kubwa, halafu anarudi bila samaki, nani anayetetea wavuvi, ni yule ambaye analinda mwisho wavuvi wakienda kuvua wakarudi na samaki wengi ili wawe matajiri, ndiyo msingi hasa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachokitaka nikiseme leo hii kwa Wabunge wenzangu, ni kitu kimoja, zipo baadhi ya changamoto mmezizungumza kwenye sharia nimeziona mimi na wenzangu, ndiyo maana tukaamua kuifumua Sheria ya Uvuvi, Na. 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 ili kukaribisha mwanya wa wananchi wetu wachangie waone mambo yaliyopitwa na wakati tuyaondoe na mimi niko tayari.

Mheshimiwa Spika, nimesema tena kwenye Kanuni kwa sababu uwezo ni wa Waziri wakimaliza kunishauri mambo, nitatengeneza hata task team ya kutengeneza Kanuni haraka ili mambo yanayotukwaza kusonga mbele tuyafute, ili wananchi wetu waweze kunufaika na Sheria zingine ambazo nimeamua tuzifumue ni Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Sheria Na. 29 ya mwaka 1994 ili na yenyewe mambo ambayo yanakwaza wazalishaji, wavuvi wetu, wafanyabiashara wetu na wawekezaji wetu, tuyaondoe pamoja na Sheria za Bahari zote hizi ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu tumewaweka vizuri, wanafanya biashara vizuri sana katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kwenye mifugo nako wameshauri hapa shabaha ya kuwa na tozo za rasilimali za nchi, huwezi ukawa na rasilimali zako hapa zinavunwa, zinaenda nchi nyingine halafu Taifa linaachwa halina chochote, lazima tuweke tozo zinazolingana na thamani ya rasilimali zetu ili zinapozouzwa nje, Taifa linufaike, lakini inapotokea labda tumezidisha sana, ikawa maumivu kwa wafugaji wetu au kwa wafanyabiashara wetu, au kwa wawekezaji wetu, sisi hatuna tatizo, tunakaribisha mawazo yenu, tutafanya review; kama kuna tozo zimezidi upande wa uvuvi au mifugo tutazi-regulate. Lengo letu, ni kuhakikisha kwamba hawa wafugaji wetu wanafuga vizuri, lakini na hawa wavuvi wanavua vizuri na wafanyabiashara na wawekezaji katika eneo hili wanafanya biashara vizuri, lakini bila kuyasahau maslahi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nimesoma hotuba yako vizuri sana, lakini nasikitika miradi ya Jimbo na mkoa wangu hazipo. Mradi wa lami Makao Makuu ya Jimbo la kisasa (Mwandoya); kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa barabara ya lami kutoka Bariadi – Kisesa Mwandoya – Mwanhunzi, Bukundi (Sibiti) - Egiguno.

Mheshimiwa Spika, mradi huu ni wa kimkakati hasa baada ya ujenzi wa daraja la Sibiti kukamilika. Mradi huu utafungua uchumi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa Mara, Kagera, Mwanza, Simiyu na Shinyanga pamoja na nchi jirani za Kenya na Uganda.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa nafasi uliyonipa tena, lakini pia nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wa Kilimo Mifugo na Maji, lakini na Msemaji wa Kambi ya Upinzani anayesimamia masuala ya Mifugo na Uvuvi wa hotuba zao nzuri sana walizozihutubia hapa Bungeni na vile vile michango ya Waheshimiwa Wabunge wote. Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa mchango ambayo mliyoitoa na sisi tumenufaika sana na michango yenu mliyoitoa.

Mheshimiwa Spika, Azimio letu hii la PSMA, bahati nzuri sana Wabunge wote waliopata nafasi wameunga mkono na wametoa ushauri. Kwa ujumla kwa masaa na dakika ulizonipa, ni ngumu sana kupitia maswali ya Waheshimiwa Wabunge, lakini pia na ushauri walioutoa, lakini itoshe kusema kwamba ushauri wote ambao Waheshimiwa Wabunge wametupatia tumeuzingatia na utatusaidia sana katika utekelezaji wa majukumu yetu ya maeneo haya ya uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, labda ambalo Wabunge wameliongelea sana na limezungumzwa miaka mingi suala la Bandari ya Uvuvi, nataka niwaambie Wabunge kwamba hii Serikali ya Awamu ya Tano inaenda kutanzua huu mtego wa miaka mingi ambao umekuwa kilio kikubwa kwa Taifa. Bandari hatua ambayo tumefikia mpaka sasa hivi tuliliambia Bunge lako wakati wa Bajeti kwamba, tunafanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga bandari ya uvuvi hapa nchini. Nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Mshauri Mtaalam Mwelekezi wa kampuni ya Italy amekamilisha report yake ya upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi maeneo yaliyopendekezwa kwa ajili ya kuijenga hiyo bandari ni Bagamoyo, Kilwa Masoko na Lindi. Kwa hiyo, kati ya hayo maeneo hayo tutachagua sasa eneo imebaki sasa kwenye maamuzi ya ku-decide kama Serikali kwamba tutajenga bandari ya uvuvi kati ya maeneo haya mawili. Kama hiyo haitoshi Serikali tayari iko kwenye hatua za mwisho kabisa na Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bandari ya uvuvi hapa nchini. Kwa hiyo ninachotaka kusema kwa sasa ni kwamba kilichobaki kwa sasa hivi ni maamuzi ya bandari ijengwe wapi na baada ya hapo katika mwezi huu jambo hili litaamuliwa na mwezi unaofuata wa Desemba ni matarajio kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Korea zitasaini makubaliano tayari kwa kuanza bandari ya uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili lililoulizwa, ni bandari zinazotambuliwa ni bandari zipi zinazotambuliwa sasa ambazo zitahusika huu Mkataba wa PSMA. Bandari zinazotambuliwa na ambazo zimeingia na ambazo zitahusika na PSMA ni Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa, Bandari ya Zanzibar, Bandari ya Mtwara na Bandari ya Tanga, hizi ndizo zitakazohusika katika utekelezaji wa makubaliano yetu na Mkataba wetu huu wa PSMA.

Mheshimiwa Spika, suala lingine lililozungumzwa hapa na Waheshimiwa Wabunge ni suala la udhibiti wa uvuvi haramu kwenye eneo la high seas kwamba hivi sasa hakuna udhibiti na hata hii PSMA tunayoazimia haifiki katika eneo hilo la high seas. Nataka nitoe taarifa kwamba tayari UN wameanza kuandaa legal instruments za usimamizi za resource katika high seas, yaani biodiversity beyond national jurisdiction, tayari inaandaliwa na mara hii instrument itakapokuwa imekamilika, sasa mfumo huu wa PSMA utaenda mpaka high seas. Kwa hiyo, huu ulinzi wa rasilimali wale waliokuwa wanafanya uvuvi haramu kwenye maeneo hayo hawatapata excuse tena.

Mheshimiwa Spika, suala la marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya mwaka 1968 pamoja na kanuni zake za mwaka 2007 ambazo zilifanyiwa marekebisho mwaka 2016, hivi sasa tuko kwenye marekebisho ya Sheria yenyewe pamoja na kanuni zenyewe. Katika marekebisho hayo eneo hili la PSMA ambalo tunalozungumza litaingizwa, lakini pia tutazingatia maombi mbalimbali ambayo yatawezesha ruhusa ya uvuvi yaani authorization to fish kwa meli zenye bendera ya Tanzania kuweza kuvua katika maeneo ya high seas na EEZ za nchi nyingine. Kwa hiyo katika hizi kanuni ambazo kanuni na sheria ambazo tunazifanyia mapitio kwa sasa na zingine zitaingia Januari kwenye Bunge lako Tukufu, tunawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba maboresho mengi yatakayohusika na Kanuni ya uvuvi wa bahari kuu yatazingatiwa katika haya marekebisho ambayo tunafanya kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambao Waheshimiwa Wabunge wamelizungumza ni suala la eneo la kitutia Mafia kwamba ni muhimu sana kwa mazalia ya samaki, lakini halilindwi ipasavyo, nataka nitoe taarifa kwamba hili eneo linalindwa ipasavyo na liko chini la MPRU, linalindwa uvuvi hauruhusiwi eneo hilo kwa sababu ni eneo ambalo lina mazalia ya samaki, kwa hiyo eneo letu hili tunalilinda na tunatambua umuhimu wake kwamba ni eneo mahususi sana kwa ajili ya mazalia ya samaki.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge hapa walizungumza sana na wakaomba sana kwamba hii kuondolewa kwa tozo ya dola za Kimarekani 0.4 kwa kilo ya samaki inayovuliwa na kusafirishwa nje ya nchi hasa na meli hizi za foreign vehicles kutoka nje ya nchi zinazofanya uvuvi katika ukanda wetu wa uchumi wa uvuvi wa bahari kuu. Waheshimiwa Wabunge walisema na waliomba sana Serikali kwa muda iondoe tozo hii ili kuwezesha uvuvi uweze kufanyika kwa sababu meli zilizokuwa zinakuja kuvua zilishindwa kabisa kuvua baada ya kuweka hii tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba na kama wewenyewe walivyosema ni kweli kabisa sisi Serikali tumeridhia kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja wakati tunatafakari njia bora ya kunufaika na rasilimali zetu zilizoko katika ukanda wa bahari kuu ili tuweze kunufaika kwa hiyo, hii tozo tumeiondoa na Waheshimiwa Wabunge tayari tumeshasaini nadhani GN itatoka muda wowote, lakini wavuvi wetu wako ni rurksa sasa hivi kuvua na kwamba 0.4 haitatozwa ila watatozwa zile gharama zingine ikiwemo kulipia leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ilikuwa ni suala la kuwekeza kikamilifu katika utafiti; ni kweli kabisa kwamba hakuna mtu anayeweza kukubali ku-risk investment yake katika eneo ambalo halina utafiti. Hakuna Taifa ambalo linaweza kuwa na mipango mizuri kama hakuna taarifa za kiutafiti za kutosha kwenye eneo husika na sisi kama Serikali tunakubaliana na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na wamekuwa wakitushauri mara kwa mara na kwa sasa tumeanza. Kwa mfano sasa hivi hii Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), tumeshaipatia fedha kupitia Mradi wa SWIOFISH. Jumla ya shilingi milioni 457.7 ambazo hizi tunaanza sasa kufanya utafiti wa kujua rasilimali zetu zilizoko katika eneo la uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Spika, tutafanya hivyo kuhakikisha kwamba zipatikane taarifa zote za uhakika ambazo wananchi wetu wanazitaka, wawekezaji wetu wanazitaka ili sasa tuweze kuhakikisha tunaweka mipango madhubuti yenye taarifa za uhakika za kiutafiti juu yake na sisi tunaamini kwamba tunazo resources katika eneo letu la EEZ ambazo haziko maeneo mengine yote na kwamba pia sisi katika usimamizi wa rasilimali na katika mapambano juu ya uchafuzi wa bahari, pamoja na usimamizi wa uvuvi haramu tunafanya vizuri Waheshimiwa Wabunge, sisi kimataifa eneo letu linatambulika kuwa eneo ambalo bado ni clean, maeneo mengi katika sehemu nyingi duniani watu wameshachafua sana mazingira, lakini maendeleo haya …

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naongeza nusu saa ili tuweze kumaliza mambo yetu. Haya Mheshimiwa Waziri malizia.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nataka kusema kwamba nchi yetu inazidi kupata sifa kubwa kimataifa katika usimamizi wa rasilimali hizi na tulivunja rekodi kubwa sana tulipokamata ile meli maarufu inaitwa meli ya Magufuli, lakini baadaye majuzi, tukaja kukakamata meli ya Buhanaga One, sisemi ya Mpina, lakini hiyo ni ya Buhanaga One. Ile meli tulipoikamata tumepata sifa kubwa sana duniani katika kuhakikisha kutuma message kubwa sana ya ulinzi wa rasilimali hizi za Taifa.

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie Waheshimiwa tuko vizuri sana tunapongezwa kila kona kwa jinsi ambavyo tumesimama kidedea katika kuhakikisha kwamba hizi rasilimali zinalindwa sana. Hivi majuzi kuna baadhi ya viongozi tuliwaambia wanaotaka kutumia rasilimali hizi za Taifa kujipa sifa za ziada katika kuchaguliwa, kiongozi anashindwa kutaja sifa zake za kuchaguliwa anaanza kuwaambia wananchi wakafanye uvuvi haramu au anaanza kusitisha zoezi la doria linalolinda rasilimali kwamba kwa sababu hiki ni kipindi cha uchaguzi. Tunazidi kusisitiza Watanzania wasimamie sheria rasilimali hizi za uvuvi zitalindwa muda wote, bila kuzingatia majira ya mvua au ya jua, uchaguzi hauwezi kuwa na mahusiano na ulinzi wa rasilimali hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kusema kwamba viongozi wote wanaohusika wahakikishe kwamba na leo tunaunga mkono hili Azimio hii kubwa la dunia ambalo litaleta mchango mkubwa katika kusimamia kwa dhati hizi rasilimali tulizonazo ili tuendelee kuzivua kwa uendelevu kwa leo na siku zijazo.

Mheshimiwa Spika, sitaki niende nje sana ya muda huu ulionipa, lakini nizungumzie suala la by-catch, suala hili tunaangalia changamoto zake katika haya marekebisho ya kanuni ambayo tunayazungumza ili kuweka utulivu na kuondoa malalamiko yaliyoko hivi sasa ya by-catch.

Mheshimiwa Spika, mwisho suala la ku-extend ile continental shelf ambayo imezungumzwa hapa, nimshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ametoa ufafanuzi mzuri, lakini na Mheshimiwa aliyezungumzia hoja hii naye alizungumza vizuri. Sisi kama Serikali tunaendelea kufuatilia kwa karibu kuhakikisha kwamba tunafikia haya malengo yetu.

Mheshimiwa Spika, nalishukuru sana tena Bunge lako katika kuunga mkono hii hoja iliyoko mbele yetu kwa sasa baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi uliyonipa. Ninazo hoja chache ambazo nataka kuchangia. Moja, ni ile hoja ya kemikali zenye sumu zinazotumika mashambani ambazo zinazagaa kwenye mazingira na kuathiri vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla. Hoja hii iliulizwa na Waheshimiwa Wabunge katika michango yao na Mheshimiwa Vullu ndio aliuliza. Ni kweli kwamba kwanza tunazo taasisi nyingi sana ambazo zinasimamia kemikali hapa nchini; uingizaji, usambazaji, uzalishaji na utumiaji wa kemikali hapa nchini. Taasisi zote hizo kwa pamoja kila moja inalo eneo lake la kusimamia. Sasa eneo hili la kemikali za mashamba linasimamiwa na TPRI na NEMC.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema hapa, tutakachokifanya kule ambako Mheshimiwa anakulalamikia ni kwamba hizi sumu zimekuwa na shida kubwa na zinaathiri wananchi, tutawatuma TPRI pamoja na NEMC waende wakafanye kazi hiyo ili kujua hatua sahihi za kuchukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa maana ya kemikali nchini, tumegundua pia kwamba kulikuwa pia na usimamizi dhaifu kule nyuma. Tumeimarisha mfumo mzima wa kuhakikisha kwamba kemikali hapa nchini zinasimamiwa vizuri ili zisiweze kuleta athari kwa wananchi. Moja ya hatua kubwa ambayo tumeichukua ni kuanza maandalizi ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na incinerator kwa ajili ya kuteketeza mabakio ya vifungashio vya hizo kemikali lakini pamoja na kemikali ambazo zimesha-expire.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia sana juu ya Jiji la Dar es Salaam kwamba linazidi kuongezeka ukubwa, watu wanazidi kuongezeka na shughuli za kiuchumi zinazidi kuongezeka, lakini miundombinu ya majitaka haiongezeki. Nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge, ni kweli kwa muda mrefu Jiji la Dar es Salaam ni asilimia 10 tu ya miundombinu ya majitaka. Miundombinu ya majisafi imekuwa ikiendelea kujengwa lakini miundombinu ya majitaka ilikuwa ni asilimia 10 tu toka miaka ya 1970 na kusababisha madhara makubwa sana ya kutapakaa kwa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumechukua hatua kubwa na mkisoma katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 74, ndiyo utaona hatua tulizozichukua kupitia Shirika la Serikali za DAWASA ambapo leo tunazungumzia zaidi ya shilingi bilioni 342 ambazo zimetolewa na Serikali ya Korea pamoja na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tunajenga miundombinu ya kuimarisha Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia DAWASA hiyo hiyo, kuna commitment kubwa ya fedha nyingine za kutoka DANIDA pamoja na IFD kwa maana ya Serikali ya Ufaransa ambayo itakuwa na zaidi ya karibu shilingi bilioni 914. Katika hii Serikali ya Awamu wa Tano tunaenda kumaliza kabisa tatizo la majitaka ambalo linazungumziwa na Waheshimiwa Wabunge katika Jiji la Dar es Salaam. Nami nawapongeza DAWASA kwa kazi nzuri hiyo waliyoifanya ambapo ujenzi unaanza mwaka huu tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatutaishia hapo, suala la kutoa vibali kwa ajili ya majengo makubwa pamoja na shughuli nyingine ambazo zinapelekea majitaka kutapakaa, tutazidhibiti kwa karibu zaidi ili kuhakikisha kwamba utapakaaji huo wa majitaka hauwezi kutokea tena. Kwa kwa mipango hii tuliyonayo tu hii ya hivi karibuni kwa maana ya kupitia DAWASA ni kwamba miundombinu hii ikijengwa, asilimia 10 mpaka asilimia 30 tutakuwa tumefikia katika uondoaji wa majitaka katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuishii hapo tu, hata ukiangalia pia Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alizungumza kuhusu miundombinu ambayo imejengwa na miradi mbalimbali katika Majiji saba pamoja na Halmashauri 18, yote hayo ni kuhakikisha kwamba tunadhibiti utapakaaji wa majitaka na hivyo tunaongeza ubora wa maji yetu tunapouepusha na hizi taka ambazo zinazagaa kila mahali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tutakalohakikisha kabisa ni kwamba hakuna namna yoyote ambayo watu wataendelea kuchafua maji yetu ambayo watu wataendelea kuharibu maji kwa namna yoyote au kwa shughuli zozote zile za kiuchumi ambazo zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo Waheshimiwa Wabunge walilizungumza ni kwamba Serikali kuchukua hatua gani katika suala la vyanzo vya maji? Katika suala la vyanzo vya maji, kuhusu kuvilinda vyanzo hivyo pamoja na madakio yake, sheria mbili zote tunazo; Sheria ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Na. 12 ya mwaka 2009 pamoja na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, zote hizi zinatoa nafasi nzuri sana ya kusimamia hivi vyanzo vya maji. Kwa hiyo, la kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba sheria hizi tunazisimamia vizuri ili tuhakikishe kwamba maji yetu yako salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, lazima tuvilinde vyanzo hivyo vya maji na Serikali kwa kuanzia tumehakikisha kwamba TFS imeenda kila Wilaya. Kwa sasa hivi TFS iko kila Wilaya na tunahakikisha kwamba wanachangia angalau miche 150,000 mpaka 500,000 kwa kila Halmashauri na kwa kila Wilaya. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, waoneni TFS kule kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mnapeleka msukumo mkubwa katika upandaji wa miti hasa katika maeneo ya vyanzo vya maji ili kulinda vyanzo hivyo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala hili la mabadiliko ya tabianchi. Suala la mabadiliko ya tabianchi ni tatizo kubwa sana hapa nchini sasa. Ni takriban zaidi ya shilingi bilioni 180 Taifa hili linapata hasara kwa mwaka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Sasa tuamue kuchukua hatua. Tumeingia mikataba na dunia sasa hivi inahangaika makubaliano na mkataba wa Paris tumekubaliana kwamba tusiruhusu gesi joto iongezeke zaidi ya nyuzijoto mbili na kwa sasa hivi ongezeko la nyuzijoto limefikia 0.85.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati wetu sasa ni lazima tukubaliane kama Taifa kuhakikisha kwamba tunafanya kwa nguvu zetu zote; moja ni kupanda miti kama wendawazimu katika Taifa hili ili kuweza kumudu haya madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhakikisha kwamba tunabuni miradi mizuri ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi sasa. Kama sasa hivi inavyoripotiwa mvua nyingi, maporomoko, mafuriko, wananchi wana matatizo makubwa. Kwa hiyo, sasa kama Taifa, tuamue kuhakikisha kwamba njia bora zitakazotuwezesha kwa ajili ya kuondosha hili tatizo la mabadiliko ya tabianchi tuweze kulihimili, ni kuhakikisha kwamba miradi hiyo tunayoibuni ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi tunaifanya kwa nguvu zetu zote. Sasa hivi sekta zote za kiuchumi zimeathirika.
Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tunachopaswa kufanya ni kuhakikisha kwamba tunao mkakati wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2012, kwa hoja za Waheshimiwa Wabunge ambao wamezizungumza hapa; huu mkakati tumeuandaa toka mwaka 2012.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona ni vyema basi, tutaomba kwa nafasi yako ikiwezekana tuendeshe Semina na Wabunge ili tuweze kuwasilisha mkakati wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2012 mbele ya Bunge hili. Vile vile tuweze kuwasilisha hali ya mazingira ya Taifa hili ya mwaka 2014. Pia tuweze kuwasilisha mkakati wa kuhifadhi mazingira na ardhi na vyanzo vya maji ya mwaka 2006 pamoja na mkakati wa hatua za haraka za kuhifadhi mazingira ya bahari ukanda wa Pwani; maziwa, mito na mabwawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo, nadhani sasa tutakuwa tumepata mwanzo mzuri wa kwenda pamoja na Bunge hili katika kushughulikia mambo haya ambayo ni makubwa na kuweka mipango ya pamoja ambayo itatuhakikishia kwamba tunatoka hapa tulipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kunipa dhamana hii. Nimshukuru sana Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa miongozo yao wanayonipa katika utekelezaji wa majukumu yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru na nimpongeze sana Waziri wangu, nilimsikia kwa makini hapa wakati alipokuwa akijaribu kunishukuru na kunipongeza kwa jinsi ambavyo nashiriki katika shughuli nzima za Wizara tuliyokabidhiwa na Mheshimiwa Rais. Aliongea maneno mengi ambayo hata mengine hayajaandikwa kwenye vitabu na mimi namshukuru sana. Namshukuru sana pia kwa weledi wake kwa jinsi ambavyo anaiongoza Wizara. Pia niwapongeze Wenyeviti wa Kamati zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababau muda ni mfupi na hoja za Waheshimiwa Wabunge ni nyingi mno, basi nianze moja kwa moja na hoja za Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, hoja yao ya kwanza ilikuwa ni kwamba kutokana na Serikali kujenga jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais chini ya kiwango, Kamati inashauri Serikali kuwa makini wakati wa uteuzi wa wakandarasi ili kuhakikisha kuwa wanaopewa tender ya ujenzi wa ofisi kama ya Makamu wa Rais wanakuwa na uadilifu, uwezo, ujuzi, weledi wa hali ya juu.
Aidha, Wakala wa Majengo wa Serikali (Tanzania Building Agency - TBA) wawe makini wakati wote kukagua na kuhakikisha kuwa majengo ya Serikali yanajengwa kwa ubora wa kiwango stahiki. Pia wakala ahakikishe kwamba Serikali kwa namna yoyote ile haikabidhiwi jengo lililojengwa chini ya kiwango ili kuepusha kupata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua nafasi hii kuwapongeza sana Kamati hii chini ya Mwenyekiti mahiri Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa kwa kuliona hili. Naomba tu niweke kumbukumbu sawasawa kwamba wakati Wizara yangu ina-appear kwa Mwenyekiti tayari ilikuwa imeshamuandikia barua CAG kuchunguza uhalali wa jengo hili, uhalali wa gharama zilizotumika pamoja na upungufu uliojitokeza. Sasa hilo ndilo ninalotaka kuliweka sawasawa. Sasa hivi naliarifu Bunge lako Tukufu kwamba hatua zinaendelea vizuri ili CAG aweze kufanya tathmini ya kujua thamani halisi ya jengo hilo na tulishamuandikia barua mapema na sasa hivi anaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Ofisi yangu ilikuwa tayari imeshazuia malipo. Tulikuwa tumeshaandika kuzuia kwamba malipo yoyote yale hayawezi kufanyika hadi pale tutakapokuwa tumejiridhisha kwamba gharama zilizotumika katika jengo hili ni halali ndipo hapo tutakapotoa tena ruhusa ya kutoa malipo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ya Kamati ilikuwa Serikali iendelee kuchukua jitihada za dhati katika kutatua kero za Muungano ili kuongeza tija katika shughuli mbalimbali za biashara na maendeleo kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Ushauri huu umepokelewa, Serikali zetu mbili zitaendelea kuhakikisha kuwa mambo yote yanayokwamisha utekelezaji wa masuala ya Muungano yanapatiwa ufumbuzi wa haraka. Nataka nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba tutakachokifanya katika Awamu hii ya Tano, vikao vyote kwa mujibu wa ratiba za Serikali hizi mbili vya mazungumzo na maridhiano vitafanyika kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa, hiyo kazi tutakahakikisha tunaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lazima ifahamike kwamba sisi na Mheshimiwa Waziri wangu hatuna uwezo, kwa sababu maamuzi haya yanatokana na vikao viwili vya maridhiano kati ya pande zote mbili. Sisi ni kuhakikisha kwamba tunaratibu vizuri, ni kuhakikisha kwamba vikao vinafanyika salama, lakini mimi na Waziri wangu hatuna uwezo wa kuamua hata jambo moja katika mambo haya ya changamoto za Muungano zilizopo, tukasema kwamba hili tunataka tuamue hivi, haya yote yatatokana na maridhiano ya pande zote mbili. Kwa hiyo, tutakachohakikisha ni kwamba vikao vyote vilivyopangwa vinafanyika kwa mujibu wa ratiba kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine lililozungumzwa na Kamati ilikuwa ni suala la Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa faida zitokanazo na Muungano kwa pande zote mbili. Ushauri tunaupokea, jitihada zaidi zitaongezwa ili kuelimisha umma kuhusu muungano kadri rasilimali fedha zinavyopatikana. Ndivyo tutakavyofanya na mkisoma vizuri hotuba yetu tumeeleza mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda basi niende tena hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira chini ya Mwenyekiti hodari Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu.
Hoja ya kwanza, Serikali iendelee kuwaelimisha wananchi juu ya udhibiti wa taka za plastiki, kukuza matumizi ya mifuko mbadala na pia mpango wa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako linafahamu tulikuwa na Kanuni za mwaka 2006 baadaye zikaondolewa na Kanuni za mwaka 2015 ambazo zinazuia matumizi ya plastiki yanayozdi macron 50. Kamati imesema ni tarehe 01 Julai, 2017 lakini tulishalitangazia Bunge lako Tukufu kwamba tumetoa huu muda wa kutosha wa wenye viwanda na wahitaji wengine wa matumizi ya plastiki ya kwamba ifikapo tarehe 01 Julai, 2017 itakuwa mwisho wa matumzi ya plastiki hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ilikuwa ni vyanzo vya fedha kwa ajili ya Mfuko wa Taifa wa Mazingira vitokane pia na tozo zitakazotozwa na Wizara zingine, zitambuliwe na zihamishiwe katika mfuko. Tumeainisha shughuli muhimu za Mfuko wa Taifa wa Mazingira na Waheshimiwa Wabunge hapa kila mmoja amezungumza kwa hisia kubwa kuhusiana na mambo muhimu yanayohusu suala la mazingira. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza jinsi athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi ambazo Taifa sasa hivi linasakamwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unazungumzia kuta za Pangani ambapo sasa Pangani inakuwa kwenye hatari ya kudidimia kutokana na hiyo mikondo ya maji ya bahari ambayo imeuandama Mji huo. Mimi mwenyewe nilifika na kujionea. Ukizungumza kuhusu Kisiwa Panza - Pemba, kisiwa kile kimeandamwa na maji ya bahari ambayo sasa hivi mikondo yake inaingia mpaka kwenye mji ule. Kisiwa kile kiko kwenye hatari kubwa ya kuzama.
Vilevile unazungumzia Kilimani lakini unazungumzia Wabunge ambao leo wanalalamika kuhusu mafuriko makubwa yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi. Mabonde yamejaa, hakuna mifereji, hakuna mabwawa ya kutunza yale maji ili kuweza kuyaondosha kwenye makazi ya watu. Unazungumzia suala zima la uharibifu mkubwa wa mazingira na suala la jinsi misitu ilivyoandamwa na kukatwa kulingana na shughuli mbalimbali za kiuchumi za wananchi ambapo Taifa linalazimika lipande miti kwa nguvu zote. Unazungumzia uchafu wa mazingira, lazima uzungumzie ujenzi mkubwa wa madampo na ujenzi mkubwa wa machinjio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yote haya ndiyo Mfuko huu wa Mazingira ambao tunaupigania kwamba lazima upate fedha za kutosha walau shilingi bilioni 100 kwa kila mwaka wa fedha. Bunge hili tunaliomba na kama Mwenyekiti alivyoshauri na sisi tunapokea ushauri wake, ni lazima tujipange kwa nguvu zote tuhakikishe tunapata fedha za kutosha kupambana na mambo yanayotukabili ya mazingira na tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wabunge wengine walifikia mahali wakajaribu kusema kwamba suala la mazingira hivi ni kufagia tu au kuondosha taka tu au ni kufanya ukaguzi wa viwanda. Tumekwenda zaidi ya hapo labda kwa mtu ambaye hajasoma hotuba yetu. Ukisoma hotuba yetu imesheheni mambo mazito kuhusu mazingira ya nchi hii, imesheheni mambo mazito kuhusu mabadiliko ya nchi hii, yamechambuliwa kisayansi na kwa ufasaha mkubwa.
Waheshimiwa Wabunge, mkisoma mtaiona nia ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha kwamba mazingira yetu yanakuwa salama, katika kuhakikisha kwamba hali ya mabadiliko ya tabianchi iko salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jitu Soni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mheshimiwa Hawa Ghasia wameliongelea vizuri sana suala la mita 60 na kutuomba kwamba hizo mita 60 tujaribu kuangalia upya matumizi yake. Serikali inapokea kwa heshima zote wazo hili na sasa hivi tuko kwenye mapitio ya Sera na Sheria ya Mazingira ya 2004 ili kuangalia vifungu vya sheria ambavyo vina dosara katika utekelezaji ambavyo havina tija kwa wananchi, tunavifanyia marekebisho ili viweze kuleta tija na faida kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu walisema Serikali hii inafungia viwanda, inapiga faini wenye viwanda na kwamba kwa kufanya hivyo inakuwa haiwatendei haki na inadhulumu ajira pamoja na uchumi wa nchi. Nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, sisi ndiyo mmetupa dhamana ya kusimamia jukumu hilo. Kwanza haya mambo tunayafanya kwa mujibu wa sheria lakini hivi mnazungumzia mtu gani aliyefungiwa na kwa faida ipi? Yaani mnamzungumzia mwenye kiwanda ambaye anatiririsha maji ya kemikali watu wanakunywa sumu kwamba huyo ndiyo anatoa ajira kwenye Taifa? Ndiyo mnamzungumzia kwamba eti huyo analipa kodi na anatoa faida katika uchumi wa Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kama kile cha Rhino Tanga tulikifunga kwa sababu kinatoa vumbi na limeenea mji mzima, wanafunzi hawawezi kusoma wala walimu hawawezi kufundisha, ndiyo viwanda hivyo mnavyovitetea? Mnazungumzia Kiwanda cha Ngozi cha Shinyanga ambacho kinatoa harufu mji mzima kiasi kwamba watu wanaugua maradhi makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia inatutahadharisha inatuambia sasa hivi zaidi ya watu milioni tano katika nchi maskini wanakufa kwa magonjwa ya saratani za mapafu kwa maana ya kushindwa kupumua, wanavuta hewa ambayo hairuhusiwi, wanavuta hewa chafu, leo Wabunge ndiyo mnazungumzia hilo? Mnazungumzia migodi ambayo inatiririsha kemikali kwa wananchi, wananchi wanakunywa sumu, wananchi wanababuka, wananchi wanakufa, mifugo inakufa, leo Mbunge ndio unazungumzia migodi hiyo kwamba tunahujumu, tuna-frustrate ajira, tuna-frustrate uchumi wa nchi! Tutaendelea kuchukua hatua na tutazingatia sheria katika kutekeleza majukumu yetu haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, NEMC, nataka niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kwamba NEMC itafanya kazi. Pamoja na changamoto zake zote za ukosefu wa rasilimali, tunaomba rasilimali ziongezwe lakini kabla ya hapo tutaendelea kuhakikisha kwamba mapinduzi ya viwanda hapa nchini yanakwenda sambamba na utoaji wa huduma ya kufanya tathmini kwa athari ya mazingira. Tumeshatoa maelekezo NEMC kwamba Sheria ya Mazingira ya 2004 inatupasa kutoa cheti cha mazingira ndani ya siku 90.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilihakikishie Bunge hili, pamoja na changamoto tulizonazo tutaendelea kuhakikisha kwamba tunatoa cheti cha mazingira kwa muda wa siku 90. Tumeshawaelekeza NEMC hakuna namna yoyote ile ya kuchelewa ndani ya siku 90. Wale consultants waliokuwa wanahusika na uchambuzi wa miradi, wale wavivu wale, tulimuagiza Mkurugenzi wa NEMC kuwaondoa mara moja kwenye orodha na wameshaondolewa. Vilevile tulimuelekeza ndani ya idara yake inayosimamia uchambuzi wa tathmini ya mazingira inaweka watu ambao ni competent, wenye uwezo wa kuchambua tathmini ya mazingira kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Nsanzugwanko ameongea kwa hisia kubwa sana kuhusu suala la wakimbizi kwamba halimo kwenye taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeomba fedha za Mfuko wa Mazingira shilingi bilioni 100, tusaidiane Wabunge tutafute fedha hizi za kutosha ili Mfuko huu uweze kutunishwa. Tusingeweza kuainisha mambo yote hapa lakini tumesema Mfuko huu wa Mazingira ukiimarishwa tutatatua mambo makubwa yaliyoliathiri Taifa hili katika mazingira, tutatatua mambo makubwa ambayo yamelisababisha Taifa hili kuwa na mabadiliko ya tabianchi. Tuungeni mkono hapa ili tufanye kazi hizi kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nataka niseme tu kwamba mpango huu ambao tunauzungumza wa mwaka 2017/2018 suala la mazingira na mabadilio ya tabia ya nchi limezingatiwa vizuri sana katika kipengele cha 6.6 (a), (b), (c). Kwa hiyo, mkisoma pale Waheshimiwa Wabunge mtaona jinsi ambavyo suala la mazingira limezingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Mpango huu wa Maendeleo jambo kubwa lilikuwa ni kuanzisha Mfuko wa Mazingira ambao tayari Serikali imekubali na tayari tumeshaanzisha mfuko huo, kwa hiyo tunaamini kabisa kwamba mambo ya mazingira sasa yatakuwa sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo nilitaka pia kuyaweka sawasawa. Moja ni suala hili la Mawaziri kutokumshauri Rais na kusababisha mambo mengine kutokwenda sawa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya mambo mengi, sasa hivi Serikali tumeweza kuongeza mapato toka tulivyoingia kila mwezi, wastani wa mapato yetu yameenda shilingi bilioni 400; lilikuwa ni jambo la kupongezwa na Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii toka ilivyoiingia madarakani hivi sasa tumeweza kuanzisha kanuni zile ambazo zilikuwa hazijasainiwa muda mrefu, kanuni zinazowalazimisha wamiliki wa madini kusajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam. Sasa hivi kanuni hizo zimeanzishwa na Mawaziri hao hao ambao leo wanaambiwa kwamba hawana uwezo wa kumshauri Mheshimiwa Rais. Vilevile Mawaziri hawa hawa, leo tumeweza kufuta mashamba sita yenye zaidi ya hekta 89,388 ambapo baadhi ya mashamba haya wamepewa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo baadhi ya Wabunge wanasema Mawaziri hawa tumeshindwa kumshauri Mheshimiwa Rais, leo Wabunge wote wanapongeza jitihanda za Serikali upande wa kilimo, leo wakulima wa pamba wanajivunia bei imeenda mpaka shilingi 1,200 kwa mara ya kwanza, korosho imeenda mpaka zaidi ya shilingi 3,000 kwa mara ya kwanza, Wabunge hawa hawa ambao wanaambiwa kwamba hawana uwezo wa kumshauri Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mambo mengine ya kusema serikali imefilisika, haiwezi kumudu majukumu yake kwa sababu haina pesa na kwamba hata fedha unazokusanya ni za arrears, si kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatakiwa tupongezwe na bunge hili tumeweza kukusanya mapato zaidi ya shilingi bilioni 400 kila mwezi, na kwamba mpaka sasa hivi tumeweza kulipa madeni ya wakandarasi na wazabuni zaidi ya shilingi bilioni 878, tumeweza kulipa miradi mipya ya barabara shilingi bilioni 604, tumeweza kulipia miradi ya umeme shilingi bilioni 305, tumeweza kulipa mikopo ya wanafunzi shilingi bilioni 371, tumeweza kununua ndege kwa shilingi bilioni 103, tumeweza kulipa ndege kubwa advance kwa shilingi bilioni 21 na pointi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya yote tumeweza kufanya katika muda mfupi, Bunge hili lilikuwa linatakiwa kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwa muda mfupi uliopo napenda niongelee suala la vinyungu ambalo limezungumziwa sana na Waheshimiwa Wabunge hapa ndani lakini vilevile wakati tunazungumzia hotuba ya Maji na Umwagiliaji nilitolea ufafanuzi jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba, suala hili ni la kisheria ambapo linalindwa na Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999, Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 pamoja na Sheria ya Matumizi Bora ya Ardhi ya mwaka 2007, vyote hivi ni katika kulinda vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema kwa Waheshimiwa Wabunge ni kwamba sisi kama Serikali hatujazuia vinyungu nje ya mita 60 lakini kama nilivyosema kwamba tutakwenda kuyaona maeneo hayo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyazungumza ili tuone yameguswa vipi na tuone hatua za kuchukua. Kwa hiyo, ahadi itabaki ile ile ya kwenda kuyaona maeneo hayo ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wameyalalamikia na Serikali itachukua hatua katika jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala limezungumzwa dhidi ya Taasisi za Muungano yaani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokushirikiana katika kufanya utafiti. Nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba Taasisi zetu za Muungano na zisizokuwa za Muungano zinashirikiana vizuri sana hasa katika hili suala la utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Benki Kuu imefanya utafiti mwingi sana Zanzibar, zaidi ya tafiti 13 katika mazao mbalimbali mazao ya mpunga, mchele, minazi, karafuu na ripoti yake kukabidhiwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na inayafanyia kazi na inanufaika vizuri sana na tafiti hizi ambazo zinafanywa na Benki Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, COSTECH ndiyo mratibu mkubwa wa tafiti za kisayansi pamoja na hizi za kilimo na imekuwa ikitoa fedha katika Taasisi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na zile za Zanzibar kwa mfano SUZA pamoja na IMS kwa maana ya Institute of Marine Science na tafiti zake zimekuwa zikileta tija kubwa sana. COSTECH wameweza kutoa zaidi ya bilioni tatu kwa ajili ya ku-facilitate tafiti nyingi ambazo zimefanyika Zanzibar na zimeleta tija kubwa sana katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa nafasi na vile kwa muda mfupi huu kuweza kuchangia na mimi kidogo katika taarifa ya hao Wenyeviti wawili; Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Mwenyekiti wa Kilimo, Mifugo na Maji.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti hawa wote wawili, hoja zao ni nzuri. Niwapongeze Kamati yangu ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa muendelezo wao uleule wakuendelea kutusimamia vizuri sana sisi kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kuwezesha kutekeleza majukumu yetu vizuri sana hapa Bungeni lakini na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, kwa nafasi hii ya muda mfupi napenda kusemea baadhi ya maeneo machache kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wametupongeza sana kwa jitihada tulizozifanya za uwekezaji wa viwanda hapa nchini lakini wakaona kwamba kama vile tunaenda kwa spidi ndogo sana katika kuboresha mifugo yenyewe na katika kuhakikisha kwamba mifugo hii ipo salama na inazalishwa na inakua vizuri.

Mheshimiwa Spika, tumefanya mambo makubwa pia ya kuhakikisha kwamba tunapambana na magonjwa. Sasa hivi utakubaliana na mimi kwamba nchi nzima sasa hivi katika kipindi tu hiki cha nusu mwaka tayari tunakamilisha ukarabati wa majosho 449. Kama hiyo haitoshi tumepeleka dawa za kuogesha kwenye Wilaya zote kwenye majosho yote 1,725 ambayo tayari nchi nzima wanaogesha mifugo kwa ruzuku ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi tumefanya mambo mengi kama ambavyo yamezungumzwa hapa na Waheshimiwa Wabunge. Kwa mfano, kuongezeka kwa maeneo ya malisho, leo maeneo yetu yameongezeka kutoka 1,400,000 mpaka leo tumefikia maeneo yaliyotengwa hekta 2,800,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na bado Serikali ikaenda mbali zaidi ikamega mpaka mashamba yake ya Serikali kwa ajili ya kuwagawia wafugaji na wakulima kwenye vijini 920 na imeelezwa kwenye kumega misitu na mapori ya akiba, imeelezwa kwenye kumega mashamba mpaka ya Serikali ya NARCO na mashamba mengine ya taasisi zetu. Hizi zote ni jitihada za kuhakikisha kwamba wafugaji wa nchi hii wanapata maeneo mazuri ya kufugia na wanafuga vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la uvuvi wa bahari kuu. Waheshimiwa Wabunge katika hili msiwe na mashaka, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri kufanya kazi hiyo na ndiyo maana Shirika la TAFICO tayari limeshafufuliwa, mpango wa biashara umeshaandaliwa wa kununua meli na kuanza shughuli za uvuvi wa bahari kuu. Na kama hiyo haitoshi bandari ya uvuvi tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unaendelea na tupo kwenye hatua za mwisho na tayari tuende kwenye hatua za kujenga.

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, tayari Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi Na. 1 ya Mwaka 1998 tumeifuta ili kuleta na kuwavutia watu mbalimbali waliokua wanakwazwa na sheria kuja kuwekeza katika uvuvi wa Bahari Kuu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kuna mambo ya makokoro yataisha lini. Kuna changamoto, bidhaa za nyuzi hizi zinapoingia nchini zinakuwa ni halali lakini zinapokuja kutengenezwa, wavuvi wetu wanapokuja kusuka nyavu sasa wanaweza kusuka kokoro; lakini nyavu inapoingia nchini ni halali kama nyavu tu (raw material kwa ajili ya kutengeneza bidhaa. Kwa hiyo, hiyo ni tatizo kubwa na hili limetusababisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukaa na wenzetu wa TBS pamoja watafiti wetu wa TAFIRI ili kutafuta namna bora ya kusimamia hili eneo. Kwa hiyo, tuna imani hivyo tutafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo lingine la hizi nyavu ni kwamba kila maeneo yana nyavu tofauti ya kuvulia kulingana na aina ya samaki waliopo kwenye eneo hilo. Samaki waliopo Bahari ya Hindi ni tofauti na samaki waliopo Ziwa Tanganyika, ni tofauti na samaki waliopo Ziwa Victoria, kwa hiyo hata nyavu zake nazo pia ni tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa kuna maneno mengine yalizungumzwa ya kwamba wananchi wanahitaji maji, hawahitaji ndege. Waheshimiwa Wabunge hivi hayo maji mnaenda kuyajenga bila ya kuwa na fedha? Miundombinu ya ndege inaponunuliwa nchini inawezesha uchumi kukua, mazao yetu ya samaki leo, samaki atavuliwa saa 2 Ziwa Victoria anaenda kuliwa saa 4 Zimbabwe. Samaki atavuliwa hapa Dar es Salaam saa 12 asubuhi kufikia jioni analiwa India; huu ndio uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa unapozungumza kwa ajili ya kujifurahisha kwamba eti wananchi wanahitaji maji hawahitaji ndege, huwezi ukaondoa mahitaji muhimu ya wananchi katika kupatikana kwa ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii Ziwa Victoria tunavua kila siku tani 250, kwa hiyo unahitaji ndege za kubeba samaki tani 250 kila siku. Leo samaki wetu hao wanabebwa Uganda, samaki wetu hao wanabebwa Kenya, tungekuwa na ndege zetu – na ndiyo maana Waziri wa Uchukuzi nimemwambia piga, garagaza, ua lazima tununue ndege zetu za kusafirisha mazao yetu. Tani 250 kwa maji moja, hujaenda Tanganyika, hujaenda Bahari ya Hindi.

Mheshimiwa Spika, lakini kama hiyo haitoshi, la mwisho labda ni hili Mawaziri, kwa sababu yanazungumzwa maneno hapa mengine ni vizuri kutolewa clarification. Mtu anasema tu hapa Mawaziri ambao ni wasimamizi wa sera wanafanya mambo ya operation, nadhani alikuwa anazungumza kutofautisha operational na oversight. Lakini tangu lini wewe mtu wa oversight utafanya shughuli zako za oversight bila kwenda kwenye maeneo unayoyasimamia. Ni tangu lini wewe msimamizi utafanya ukiwa ndani mambo ya kisera, unasema nafanya mambo ya kisera unajifungia chumbani, utashindwa kwenda kwenye maeneo ya uvuvi, utashindwa kuonana na wavuvi, utashindwa kwenda kuwaona wafugaji, utashindwa kwenda kwenye maeneo eti wewe unatunga sera. Sera hizi utazitungia ukiwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, ni vizuri kama ukiwa huna la kuchangia unaacha tu, sio kusimama hapa na kupoteza muda wa nafasi na muda wako. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri nakuongeza dakika tano. (MakofiVigelegele)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa ongezeko hilo. Mheshimiwa Spika nataka niweke mambo vizuri hapa; kuna suala la oversight function, kuna suala la operation function. Kama wewe ni oversight utawezaje kuwa oversight bila kukaa na hawa operational? Kama wewe ni oversight utawezaje kufanya kazi yako ya oversight function bila kwenda kwenye operational sight? Haiwezekani! Ni mambo ambayo unazungumza kama huyajui au kama umeambiwa nje unakuja nayo hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachotaka niwaambie, Serikali ya Awamu ya Tano kama mtu yeyote anatafuta eti kutupotezea uelekeo…

SPIKA: Mheshimiwa Mchungaji Msigwa hoi kabisa.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Kama mtu yeyote anatafuta kutupoteza uelekeo, kama mtu yeyote anatafuta eti kutukatisha tamaa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilishakataa katakata kukatishwa tamaa na mtu yeyote yule. Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilishakataa katakata kukatishwa tamaa na mtu yeyote. (Makofi/Vigelegele)

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WABUNGE FULANI: Aaaaa!

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, endelea.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ninachotaka kukieleza hapa ni kwamba watu wajue katika taarifa hii ya Kamati kuna mambo makubwa yaliyoelezwa hapa. Nilitegemea Wabunge wakayaona hayo. Leo mapato ya uvuvi…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane, naomba tusikilizane; mlipokuwa mnawapiga Mawaziri hapa wala hawakusema kitu…

WABUNGE FULANI: Ndiooo!

SPIKA: Sasa wanapojibu naomba na ninyi mtulie, ndiyo kuwa na ngozi ngumu, tulieni. Mheshimiwa Waziri, endelea.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Kamati hii imeongea mambo mazuri sana ambayo leo wastani wa makusanyo ya Wizara ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi yalikuwa bilioni 21, leo yamefika bilioni 72. Fedha hizi zimeenda kwenye elimu, fedha hizi zimeenda kwenye maji, fedha hizi zimeenda kujenga miundombinu ya maji ya wananchi. Mauzo yetu ya samaki nje ya nchi yameongezeka kutoka bilioni 379 hadi bilioni 691; hiyo ni Serikali ya Dkt. Magufuli imeyafanya hayo. Tulitegemea Mbunge badala ya kwenda kwenye vitu vidogovidogo hivi angesema mambo haya makubwa yaliyofanyika ya kitaifa.

Mheshimiwa Spika, tumepunguza manunuzi ya samaki nje ya nchi. tulikuwa tunanunua samaki nje ya nchi kwa thamani ya bilioni 56 kwa mwaka. Leo tunafika hapa mwaka mzima manunuzi yetu ya samaki nje ya nchi ni milioni 37, fedha hizo ziko hapa kwa Watanzania, bilioni 56 zinaliwa na Watanzania leo, zinaliwa na wavuvi hawa, ni Serikali ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, nataka niwathibitishie Watanzania wote na Wabunge kwamba Serikali ya Awamu ya Tano tumejipanga na tutahakikisha kwamba kero zote za Watanzania tunazishughulikia. Tutaenda site moja baada ya nyingine, tutaenda maeneo yote kuhakikisha Tanzania na matatizo ya Watanzania yanaokolewa, kuhakikisha kwamba tunafuta, kuhakikisha kwamba Watanzania ambao wamelia muda mrefu tunafuta machozi yao, tunakwenda kupangusa machozi ya Watanzania wote walioteseka na kunyanyaswa muda mrefu, na tupo kwa ajili ya kufanya hiyo kazi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimshukuru sana Mwenyenzi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele hapa ili niweze kuhitimisha hoja yangu.

Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru sana wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa uwezo na umahili mkubwa mnaounesha katika kuliendesha Bunge letu Tukufu. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana kwa dhati Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa umakini wake wa kusimamia shughuli za Serikali hapa Bungeni. Aidha, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliopata nafasi ya kuchangia hoja yangu niliyoiwasilisha hapa Bungeni kwa michango yao mizuri na ya kina yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wizara yangu.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingi zimetolewa, na hii ni dalili ya dhati kwamba upo mwamko mkubwa sana upande wa kuendeleza sekta ya mifugo na uvuvi ili ziweze kupiga hatua zaidi katika maendeleo. Aidha, katika michango hiyo imedhihilisha wazi kuwa kuna mahitaji makubwa ya kusimamia sekta ya mifugo na uvuvi kupitia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayoongoza Wizara yangu. Ni dhahili kuwa masuala ya kuendeleza utafiti wa mifugo na malisho ikiwa ni pamoja na kuendeleza kosafu bora za mifugo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa, nyama, mayai na ngozi kuendana na mnyonyoro wa thamani wa uchumi na viwanda. Aidha, tafiti mbalimbali zinahitaji kuendelea kufanyika kwa nyakati tofauti zenye lengo la kujua rasilimali za uvuvi ikiwa ni tafiti katika ukanda wa bahari kuu.

Mheshimiwa Spika, napenda kutambua Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja mbalimbali katika Wizara yangu ambapo wapo jumla 46. Sitawaja majina yao lakini walichangia kwa kusimama 29 na ambao wamechangia kwa maandishi ni 17. Michango ya Waheshimiwa Wabunge wote niliowataja ilikuwa mizuri sana na iliyosheheni busara na heshima na hekima na changamoto. Aidha, si rahisi kujibu kwa kina na kutosheleza hoja zote za Waheshimiwa Wabunge kwa muda huu mfupi. Naahidi kwamba hoja zote tutazijibu kwa maandihsi na Waheshimiwa Wabunge wote watapewa.

Mheshimiwa Spika, ushauri na maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji umezingatiwa.

Pia maombi ya Kambi ya Upinzani vilevile yamezingatiwa isipokuwa moja tu. Mchango wa kambi ya upinzani safari hii ulikuwa mzuri sana, isipokuwa pendekezo moja tu lililosema kwamba Wizara itumie sera za CHADEMA. Wizara haitatumia sera za CHADEMA kwa sababu sera za CCM ni nzuri na hazina mfano kwa hiyo hakuna sababu yoyote ya kutumia sera za CHADEMA, zinajitoshereza. Kwa hiyo sera hapa ni za CCM na ilani hapa itatumika ya CCM.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nizungumze kuhusu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Hoja zilizozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge ni nyingi mno, kama nilivyosema. Kwa hiyo nitajaribu ambazo nitaweza kuzifikia ili kuweza kutoa ufafanuzi huo kwa Wabunge. Moja ni hili la Mheshimiwa Mzee wangu Lubeleje Mbunge wa Mpwapwa la kuhusu kituo cha tariri. Kilichofanyika pale hatuja hamisha kituo cha utafiti cha tariri tulichohamisha ni Makao Makuu. Makao makuu ni Mkurugenzi ni mambo ya utawala si mambo ya kiutafiti tena. Kwa maana ya kituo cha utafiti bado kipo pale, kwa hiyo mzee wangu Lubeleje hana sababu yoyote ile ya kukamata shilingi kwa hoja hiyo, kwa sababu kama wananchi wa mpwapwa kituo chao hatujakiondoa cha utafiti. Walioondoka ni hao wakurugenzi ambao wanawajibika kwa mambo ya kiutawala ndio tuliowaleta hapa.

Mheshimiwa Spika, la pili Waheshimiwa Wabunge mmezungumzia hoja mbalimbali za uvuvi na mifugo. Sasa katika hoja za uvuvi baadhi yake ikiwa mmesisitiza sana kwamba sheria kuharakisha mchakato wa kuboresha sera na sheria za uvuvi. Awali niliwaambia kwenye hotuba kwamba tumeamua kwa dhati kuhakikisha kwamba sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009 tumekubaliana kama wizara tumezifumua na tumetembea kwa wadau kanda zote kutaka mawazo yao. Tayari sasa hivi mchakato Serikalini unaendelea.

Mheshimiwa Spika, na kama tulivyowaahidi Waheshimiwa Wabunge sheria hizi zitafika mikononi mwenu Ili muweze kutushauri kadri matakavyoweza ili tuweze kutengeza kanuni au sheria zitakazoendana wakati wa sasa na kuondoa changamoto zilizopo. Sasa sioni tatizo tena la lawama juu ya Wizara kwa sababu maamuzi ya Wizara ni maamuzi makubwa, kuamua kufumua sheria yote ili tuweze kupata maoni mengi. Lakini vilevile kuamua kufumua mpaka kanuni ili tuweze kupata maoni mengi. Kakini vilevele hata katika kufumua kanuni hiyo ndiyo maana tukaamua kwamba yapo mambo ya dharura ambayo inapaswa yafanyike sasa hivi kwa haraka sana kwa sababu yalikuwa yanakwaza sana wavuvi. Kwa hiyo nilitegemea kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi mngeyashangilia.

Mheshimiwa Spika, Moja uvuvi wa ukanda wa bahari kuu ambao unalazimisha watu kuvua kwa kutumia nyavu za mm 10 ilikwepo kwa mijibu wa sharia; kuvua kwa tumia mm 10. Wananchi wakalalamika, Waheshimiwa Wabunge mkalalamika, Serikali ikakubali kurekebisha sheria na kanuni zimesainiwa na GN ipo tayari na leo mnondoka na GN hiyo. Wananchi wa ukanda wa pwani hawawezi tena kukamtwa kuzuiwa kuvua kwa kutumia mm nane. Sasa hizo ni achievement zenu wala si za Wizara, mliishauri Wizara, Wizara hii ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo ni nyenyekevu sana na sikivu imetekeleza.

Mheshimiwa Spika, lakini ukanda wa Ziwa Victoria, ukomo wa kuvua samaki wa sentimita 85; kwamba huruhusi kuvua samaki wa sentimita 85 napo Serikali imesikia. Katika kufanya hiyo tumekubali tumerekebisha, tumeondoa ukomo huo ambapo sasa wananchi wa ukanda wa ziwa victoria watavua bila ukomo. Tunahakikisha kwamba hairuhusiwi kuvua chini ya sentimita 50. Lakini huku na kuendelea kwa maana ya samaki sangara mtaendelea kuvua samaki wa urefu wowote ule. Hii ni mileage kubwa upande wetu kwa sababu viwanda vingi vitapata malighafi nyingi lakini vilevile uzalishaji wa bidhaa kama mabondo utazalishwa kwa wingi sana. Hata hivyo hili nalo ni la kwenu Wabunge mlilalamikia na kuomba Serikali ifanye na tumetekeleza, tatizo nini tena?

Mheshimiwa Spika, mmesema kwamba wananchi wanahangaika kupata leseni kila wilaya; na ninataka niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja hii mmsifikie mahala mkajisahau kwamba maji yalipo kwenye eneo lako kama ni ziwa lipo pale Sengerema eti lile ziwa ni la Sengerema, msijisahau hivyo. Kama bahari ipo rufiji usijisahau ukasema hiyo bahari ni ya rufiji, hiyo bahari ni rasilimali ya taifa, ya wananchi wote, mkatushauri kama Serikali kwamba kwa nini mwananchi akate leseni kila wilaya?Wakati mwingine uko ndani ya maji, unavua hujui kama umefika chato, hujui kama umefika Sengerema. Unavua, unavua tu unaenda. Hujui kama umefika Tanga hujui kama umefika Bagamoyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kila unafika unakamatwa unaambiwa kata leseni nyingine, tukakubali tuka-amend sheria. Sasa mnataka Serikali yenye usikivu wa aina gani? Tume-amend, tumekubali tumrekebisha sheria wananchi sasa hivi watavua maji yote. Uikata leseni ya Bahari ya Hindi ukanda wa pwani utavua kote. Ukikata leseni ya kuvua ziwa victoria utavua ziwa lote. Ukikata leseni ziwa Tanganyika utavua ziwa lote; sasa hiyo ndio Serikali sikivu.

Mheshimiwa Spika, na Waheshimiwa Wabunge sisi tuko vizuri kuwasiliza sana tu. Mmezungumzia wala kukosekana wa uwiano wa sheria za uvuvi katika nchi za Afrika Mashariki. Mimi nataka kwanza Waheshimiwa Wabunge mjivunie sana na haya mafanikio, kwa sababu haya mafanikio sisi tungewafuata wenzetu. Tulipokwenda kufanya Oparesheni Sangara Ukanda wa Ziwa Victoria watu wote walisema kwamba Kenya wenyewe hawana masharti hayo na hawana sheria hizo Tanzania sisi tuna sheria hizo; sasa kama tunakwenda maana yake sisi tutakuwa looser. Nataka niwahakikishie, sisi ndio tuna maji mengi, kama ni looser sisi tungekuwa ni looser namba moja. Ziwa victoria sisi tuna asilimia 51. Hatuweze tukawa tunawafuata watu, kwamba Kenya wapo hivi lazima na sisi tuwe hivyo. Wakibadilisha leo, wanabadilisha kesho tunabalisha tena kwa sababu Kenya wamebadilisha?

Mheshimiwa Spika, lakini sisi tuka-stick tukasema lazima oparesheni ziendelee. Leo baada ya taasisi za kiutafiti za nchi zote tatu wote wanaipongeza Tanzania. Tatifi ambazo zimefanywa na TAFIRI pamoja na taasisi zingine za kitafiti za Kenya na Uganda baada ya samaki kuongezeka kwa muda mfupi sana katika Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, ongezeko hilo mwaka 2016/2017 kwa samaki waliokuwepo Ziwa Victoria; uvunaji wa samaki katika ziwa victoria ulikuwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati tunaanza oparasheni samaki wachanga ziwa victoria walikuwa asilimia 96.6 samaki wachanga, yaani lile ziwa lilikuwa na samaki wachanga wote. Baada ya oparasheni asilimia ya samaki wachanga imefikia asilimia 62.8, imeshuka. Vilevile samaki waliofaa kuvuliwa wakati tunaanza oparesheni Ziwa Victoria ilikuwa ni asilimia 3.3. Sasa kama ni asilimia 3.3 ndio samaki wanaofaa kuvuliwa; leo samaki wanaofaa kuliwa ziwa wamefikia asilimia 32. Sasa walikuwa wanazidi asilimia 85 ambao ndio samaki wazazi Ziwa victoria walikuwa 0.4, na leo wapo asilimia 5.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, urefu wa samaki sangara wastani ulikuwa 16 leo urefu umefikia urefu umefikia wastani wa sentimita 25.2; haya ni mafanikio makubwa. Nchi zote zinajivuni kwa hatua ambazo zimechukuliwa na Tanzania, na wanaendelea kuwekeza viwanda mbalimbali na sisi tutaenda kuwekeza viwanda, na ndiyo maana tukakubali kurekebisha hata kuruhusu kuvua samaki wa zaidi wa sentimita 85 kwa sababu moja kwamba samaki wazazi sasa hivi tunaona wengi. Sasa una 0.4 Waheshimiwa Wabunge unataka uvue kwa utaratibu unataka, una samaki wazazi 0.4 lile ziwa victoria tungefunga uvuvi isingewezekana uvuvi kufanyika, 0.4 za samaki wazazi tulikuwa tunaenda kumaliza lile ziwa. Sasa tuna asilimia 5.2, ni samaki wengi. Kwa hiyo sasahivi tunafunga uvuvi hii viwanda vingi vitajengwa na wananchi wengi watanufaika sana na uwekezaji huu.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Kuwepo kwa Faini ya Gandamizi Sisizozinga Sheria. Waheshimiwa Wabunge hakuna namna yoyote Serikali hii ya Awamu ya Tano na Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi ninayoingoza ambayo inaweza kuwavamia wananchi kwenda kwaongea bila sababu; hakuna namna yoyote ile na hatuwezi kufanya hivyo na hatuna sababu ya kufanya hivyo. Waheshimiwa Wabunge hili jambo ni vizuri likaeenda case by case. Kwa sababu mnapolileta hapa kwa ujumla wamepigwa wananchi wameumizwa bila hata kueleza ni wapi walipoumizwa na wapi walipopigwa imekuwa ikituleta changamoto sana. Mara nyingine tumekuwa tukifuatilia ukweli tunaokuta kule sio ule. Sheria za Serikali zilizopo Serikali ndizo itakazo zifuata. Sheria hizi zimetungwa na Mbunge, hili hakuna namna yoyote ya Bunge hili kuzikana hizi sheria.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya Mwaka 2003 imetungwa na Bunge hili. Kanuni za mwaka 2009 ziliinidhishwa kutumika kulingana na sheria iliyokuwepo; kwahiyo hakuna namna yoyote ya Bunge kujitoa katika utungaji wa sheria. Kwa hiyo tunafika kwenye jambo hili, na bahati nzuri mnaweza mkawa mnatuona Naibu Waziri yupo, Makatibu wa Wakuu wapo kuchambua case by case. Sasa hivi imeripotiwa (be reported) hoja ya Tunduma, ya kwamba watu hawana leseni tu wamepigwa faini milioni mbilimbili. Lakini ukweli si huo, tumefuatilia kwa kina, wale watu wana under declaration. Mtu ana tani 20 anaandika tani tano, anaandika tani 10. Sisi mnapotuambia internally tutafuatilia kwa kina kujua kama tatizo ni la mtumishi tutamshughulikia yule mtumishi. Kama tatizo ni mambo mengine tutashughulika nayo. Kwa hiyo nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tuwe pamoja katika ulinzi wa hizi rasilimali.

Mheshimiwa Spika, na operesheni hizi, tumesema mudawote, zimekuwa zikifanyika kwa nia njema, na katika hili hakuna atakayepona, yoyote atakamatwa kuhusu zoezi hili la watu kujishughulisha na uvuvi haramu. Sasa uvuvi haramu huu wakati mwingine nyingine hata Wabunge wengine hapa tunageukana. Akisha kamatwa ndugu yako au mtu wako wa karibu tayari unaigeuka Wizara, tayari unawageuka watumishi wa Wizara hiyo. Kwamba ni watumishi wabovu, amezungumza hapa Mheshimiwa Tizeba. Tizeba alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi; amezungumza hapa, mambo mengine nitayasema baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hili la vijana kusema wanaonea watu kwenye jimbo lake si kweli. Mheshimiwa Tizeba akiwa waziri amekuwa akipigia simu vijana wa mifugo na uvuvi kuwa-harass na kuwaambiwa hataki watu wake wakamatwe kwa ajili ya uvuvi haramu. Mheshimiwa Tizeba amekuwa akiwa-harass vijana wa uvuvi, hata sasa hivi akiwa mbunge, akisema kwamba hataki mtu wake akamtwe kwenye eneo la lake la uvuvi. Sasa ukifika hapa unabadilika inakuwa hawa vijana kwa sababu hawapo ndani ya Bunge hili wanashutumia kwa kiwango hivyo, si vizuri.

Mheshimiwa Spika, wapo vijana wetu ambao wanafanya kazi vibaya, tuletee tu tutawshughulikia. Hata hivyo vijana hawa wamefanya kazi nzuri sana. Leo tunajivunia kama taifa kupambana na uvuvi haramu, tunajivunia kama taifa kupamba na uvuvi haramu. Sasa wamefanya kazi nzuri hivyo hasa sisi vingozi wenyewe tuliozitunga sheria wenyewe, tumepewa mpaka na mamlaka kwa sababu wameguswa tu watu wako, kwa sababu limeguswa tu jimbo lako maafisa hawa wote wanakuwa ni wabaya. Twendeni case by case.

Mheshimiwa Spika, nalizungumzia hili suala la oparesheni, hizi operesheni zote, Oparesheni Sangara pamoja, Oparesheni MATT na Operesheni Jodari zimeleta mageuzi makubwa, lazima tujivunie. Uzalishaji wetu wa samaki umeongezeka, uzalishaji wetu wa mazao mbalimbali umeongezeka kwa kiwango kikubwa sana hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, mambo tuliyoyafanya baada ya oparesheni hizi; mauzo yetu ya nje ya samaki yameongezeka sana. Uzalishaji wetu wa ndani wa samaki umeongeza sana. Nilikuwa nasikiliza kwenye tv mama mmoja anahojiwa anasema mimi jambo ambalo namkumbuka Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na kumpongeza ni moja; tulikuwa tunanunua samaki sato kwa shilingi 14,000 leo tunanunua kwa shilingi 7,000/ Tulikuwa tunanunua samaki sangara kwa kilo shilingi 9,000 leo tunanunua kwa shilingi 6,000. Samaki wapo kila sehemu wameongezeka. Ilitokea Watanzania walianza kula vifaranga; hatusahau jinsi rasilimali hii ya uvuvi ilivyovurugwa na uvuvi haramu, hatuja sahau.

Mheshimiwa Spika, Watanzania leo wanakula samaki wazuri, bora na wenye viwango, tena kwa bie ndogo, na wanapatikana kila sehemu na mauzo yetu ya nje yanazidi kuongezeka. Mlikuwa mnazungumzia mauzo kwamba mauzo yetu yanapungua; hivi unawezaje kuongeza mauzo ya samaki ilhali samaki wazazi waliobaki; kwa sababu uzalishaji wetu wa samaki takriban asilimia 90 wote ni Ziwa Victoria. Sasa samaki wazazi umabakiza 0.4, samaki wa kuvua umebakiza asilimia 3.3; utawezaje wewe kuleta mauzo makubwa nje ya nchi? Haiwezekani! Hata hivyo vilevile watu walitorosha, watu wanavua samaki wetu hapa, watu wanakuja hapa kutoka nchi mbalimbali wanapakia samaki wetu wanaondoka nao. Warwanda walikuja hapa wakapakia samaki wetu wakaondoka nao, Wakenya walikuja wakachukua samaki wetu, Warwanda walikuja hapa wakachukua samaki wetu, Waganda hivyo hivyo na nchi nyingine bila kulipa chochote; lakini leo tumewabana wanalipa; hatukatazi kuchukua rasilimali lakini tunawabana wanalipa, tatizo liko wapo?

Mheshimiwa Spika, nilitegemea Waheshimiwa Wabunge kwa makofi makubwa mngewapongeza sana vijana wangu kwa jinsi wanavyochapa kazi nzuri ya ujenzi wa taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Mabomu; hatujasahau watu walivyokufa Ukanda wa Pwani kwa kulipuliwa na mabomu, hatujasahau, watu wamepoteza maisha sana, Serikali ya Awamu ya Tano ikasema hapana tutakomesha mabomu. Watu wanavua kwa sumu, watu wanavua kwa mabomu, tuwachekelee tu, tuseme sawa tu vueni, ninyi ni wapiga kura wetu haturuhusiwi kuwakataza, hapana, hatuwezi kuwa nchi ya namna hiyo, haya lazima tuyakatae. Mwaka 2016 nchi hii mpaka wageni walianza kuikimbia wakikaa kwenye mahoteli mabomu yanalipuka, watu maskini wanaenda kuvua kwa ratiba zao kwa utaratibu wao wanalipukiwa na mabomu wanakufa.

Mheshimiwa Spika, leo mpaka tunavyozungumza uvuvi umeendelea kushuka 2017, 2018 na leo 2019, uvuvi wa kutumia mabomu wameenda ku-test sifuri, hakuna mtu anafanya uvuvi wa mabomu, lakini Waheshimiwa Wabunge, leo kwa nini hatutaki kujivunia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, meli za uvuvi kutoka nje zilikuja hapa kuvua, zimekuja hapa kuvua meli za kigeni kutoka nje ya nchi, zikavua samaki na wakaondoka. Wamefanya uvuvi haramu uliopitiliza kwenye maji yetu, tumekamata meli ya Buhanaga One, tumekamata meli, tumesimamia kesi ile, walizoea mpaka na kesi wanafanya maneuver inakuwaje sijui, sijui inakuwa vipi, tumeshinda kesi Mahakamani, kwa nini isiwe suala la kujivunia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, meli za Kigeni zimekuja hapa nchini, Meli ya Buhanaga One, ambayo tuliipiga faini ya shilingi milioni sabini na saba, kama to compound now, milioni sabini na saba, wakasema tumewaonea. Wameenda Mahakamani wamepigwa faini ya bilioni moja au kifungo cha miaka ishirini, hivi sasa tunavyozungumza, Meli tuliyoikamata ya Buhanaga One, ipo Tanzania, samaki waliyokuwemo mle tani thelathini na mbili, wako ndani ya meli wanashikiliwa, wako Tanzania na yale mapezi ya papa na yenyewe yapo na Mmiliki wa meli amefungwa, Wakala amefungwa na Nahodha amefungwa miaka ishirini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanatakiwa either walipe bilioni moja au wafungwe miaka ishirini, kulipa bilioni moja au kufungwa miaka ishirini, kwa nini isiwe suala la kujivunia hili? Jambo kubwa namna hii, kwa nini Taifa mnalisoma kwenye kitabu hiki Waheshimiwa Wabunge mnaliona la kawaida, ni rekodi ambayo haijawahi kufanyika toka nchi hii ipate uhuru na hata Mungu aumbe dunia na akaiumba Tanzania, haijawahi kuitokea. Kwa nini mnalisoma na hamsemi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanzania sasa hivi imeheshimika Kimataifa kwamba tunasimamia rasilimali zetu na tunapongezwa. Juzi hapa nchi mbalimbali zilikuwa zinachukua vijana kwenda kusoma mafunzo nje ya nchi, tulikuwa tunachukua vijana wanne, watatu, wawili, sasa hivi nimepeleka zaidi ya kumi na wanaombwa wengine watafika zaidi ya ishirini kwa sababu ya hatua Tanzania inazozichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukija hata kwenye hili suala la 0.4, Waheshimiwa Wabunge walitendee haki Bunge. 0.4 kwa samaki wanaovuliwa Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu, kulipia mrabaha wa dola 0.4, hili jambo halijaanzwa na Serikali, hili jambo limeanzia kwa Wabunge wenyewe na tukaweka maazimio humu ndani ya Bunge. Tukasema kwamba ni lazima Taifa linufaike, watu walikuja na meli zenye ukubwa wa mpaka tani 300. Wanalipa leseni ya dola 65,000 peke yake ni kama shilingi milioni 150 tu, anaingia na meli yenye uwezo wa kuchakata mpaka wa kubeba mzigo wa tani 300 za tuna.

Mheshimiwa Spika, mbona hawajajiuliza tuna akivuliwa hapa anauzwa kwa bei gani, kabla hawajaishauri Serikali kuondoa 0.4 mbona hawajajiuliza hilo swali,? Leo mbona hawajajiuliza swali, watu wanavua dagaa, dagaa ambao wanauzwa kilo moja Sh.10,000 au Sh.15,000, tunatoza ushuru wa 0.3 na wanalipa, leo kwa nini lizungumziwe Kampuni la Kigeni linalokuja kuvua hapa matani kwa matani ya rasilimali za Watanzania na kwenda nazo, halafu tuachwe watupu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Bunge ndiyo liliiambia Serikali kwamba tumechoka kudhulumiwa, tumechoka kuonewa na hizi meli za uvuvi zinazotoka nje ya nchi. Serikali ya Awamu ya Tano ilipokuja ikatekeleza mara moja, ikaweka kile Kifungu kile cha 0.4 kwa mabadiliko ya Kanuni za mwaka ule wa 2009 zikabadilishwa mwaka 2016, tukaweka tozo ya 0.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge hapa ni mashahidi, Waziri aliyekuwepo, Mheshimiwa Tizeba, alitoa holiday ya miezi sita ya kutokulipa hii 0.4. Alipotoa ile holiday ya 0.4, Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Spika ikabaini kuna dosari na Tanzania imepoteza bilioni tano kwa holiday ile na Serikali tukalaumiwa kwa nini tumetoa holiday, tukapoteza rasilimali hizo. Sasa Bunge linalalamika, kwa kutoa holiday tu ya miezi sita, Bunge hili hili na Wajumbe hao hao na wengine walichangia jana, ambao wameilalamikia Serikali kwa holiday ya miezi sita, leo wanageukaje ghafla kwamba 0.4 ni makosa, Serikali ilifanya njama za kuhujumu uvuvi wa Bahari Kuu. Waitendee haki Serikali yao. Hii Serikali ni ya kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakiwa mnazungumza Mheshimiwa Waziri mwenzangu Tizeba ndiye aliyeiweka na hakuiondoa, Mheshimiwa aliiweka tozo ya shilingi 0.4 na jana ananilaumu mimi tena kwamba sijaiondoa hii 0.4.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, facts are facts, naomba mtulie msikilize majibu, Watanzania hatupendagi facts, sijui tukoje. Ninyi msikilizeni Waziri aseme, angekuwa anasemwa mtu ambaye yuko nje ya Bunge hilo ni sawa kwa sababu hana nafasi ya kurekebisha. Kama Selasini umefanya jambo nakwambia Selasini umefanya hivi, usiseme usinitaje, hapana, wewe si uko hapa, (Makofi)

Endelea Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mbona hata mimi nimetajwa tu vizuri tu, mpaka wengine wakaenda mbali wakasema Waziri hasalimii watu, mbona nimetajwa tu, mbona hakuna Mbunge aliyekataa.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Ongea bwana.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema, Waziri aliyekuwepo aliweka hii Kanuni na yeye jana amegeuka kuwa mlalamikaji ya kwamba mimi nime-frustrate uwekezaji kwa kuweka 0.4. Kwa hiyo ninachotaka kusema Waheshimiwa Wabunge waitendee haki Serikali yao, 0.4 wameiweka wenyewe kwa nia njema ili kuweza kulifanya Taifa letu linufaike, ndiyo maana akaunda na Kamati ya kutushauri juu ya jambo hili tufanyaje ili uvuvi wa Bahari Kuu tuweze kunufaika zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wanapozungumza kuhusu kutoza shilingi 0.4 Waheshimiwa Wabunge lazima tutafakari vizuri, 0.4 tunaiondoa, lakini mbadala wake ni nini, Taifa litanufaika na nini, twende kwa utaratibu gani, kama kuna issue yoyote ile ya kuhusu 0.4 kwa wavuvi wetu ndiyo wameshindwa kuja kuvua kwenye maji yetu, tutaitafutia majawabu, lakini nataka niwakumbushe, tulipoanza kufanya Operation MAT, Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu, meli ishirini na nne zote zilizokuwa zinavua, ndani ya EZ yetu tulizikamata kwa kujihusisha na uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo lazima watu wajue, Tanzania, siyo Tanzania ile ya zamani, hatuwezi kuendelea kukubali kuruhusu watu wanakuja, eti kwa sababu tu lazima waje kwenye maji yetu kuvua, watufanyie wafanye uvuvi haramu, wahujumu raslimali zetu, halafu sisi tuendelee kuwaacha, tutaendelea kuwadhibiti. Hata hivyo, niseme, wako watu sasa hivi wanashindwa kuja kuvua, kwa sababu yawezekana bado wana hiyo kesi ya kutoroka kutokana na jinsi tulivyowatuhumu juu ya uvuvi wa Bahari Kuu, walivyotoroka kwa sababu ya uvuvi haramu au kwa sababu zingine. Sasa hili, hatuwezi kuliamua hapa, watupe muda Serikali, tufanye uchambuzi wa kina, tulinganishe wapi na wapi kwa sababu hiyo 0.4 iliwekwa kwa mazungumzo mapana ya Serikali ili nchi yetu kuiwezesha iweze kukusanya mapato makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niongelee suala la mapato na lenyewe limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengine wakaenda mbali sana, wakasema hii Wizara yenyewe inajivunia leo mapato haya, kwa sababu ya faini, Waheshimiwa Wabunge watendeeni haki basi hawa vijana wanaofanya hizi kazi. Hizi fedha wanazokusanya hawaweki mifukoni mwao, hizi fedha zote zinazokusanywa zinaingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na sisi hao hao, ndiyo ambao tuna oiomba maji Serikali tunaomba Zahanati, barabara, umeme na huduma mbalimbali za Serikali. Fedha hizi, hakuna Afisa hata mmoja ambaye anachukua yeye anaweka mfukoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa wamesema, suala la faini, Wizara kwa mfano, katika Sekta ya Mifugo katika para ya 23, mapato ya mwaka 2018/2019 ni bilioni 33.9, lakini mapato hayo faini kati ya fedha hizo ni bilioni tatu, ambayo ni sawa na asilimia tisa. Kwa hiyo siyo kweli kwamba mapato haya ni ya faini tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika upande wa Sekta ya Uvuvi, para ya 124 katika mapato ya mwaka 2018/ 2019 ni bilioni 30.3 na hii ni kuishia tarehe 15 Mei, mwaka haujaisha. Faini ni bilioni 6.5 ambayo ni sawa na asilimia 21.3.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kwamba, jitihada hizi zilizofanywa na Wizara ni suala la kudhibiti, tumefanya usimamizi vizuri, wa kuhakikisha kwamba kila eneo linalotakiwa kutoza, linatozwa, wale watu waliokuwa wanatorosha mapato, waliokuwa wanatorosha mifugo yetu tumewadhibiti, waliokuwa wanatorosha rasilimali za uvuvi watu kama nilivyosema, walipakia samaki zetu hapa wakaenda bila kulipa chochote, tumehakikisha wanalipa. Wale watu waliokuwa wanakwepa kodi, tumewasimamia wanalipa kodi, lakini vilevile hata wahalifu lazima waendelee kulipa faini na hizi faini zitaendelea hadi pale wahalifu watakapoisha. Kwa sababu hakuna namna nyingine, sheria zimesema ukifanya hivi utapigwa faini hii.

Mheshimiwa Spika, pia kutoza faini sio dhambi kama kuna mhalifu, kwa hiyo wahalifu wakimalizika na faini hazitakuwepo zitaendelea kushuka kadri watu watakavyokuwa wana-comply. Sasa Waheshimiwa Wabunge, leo nikizungumza trend ya mapato ya uvuvi, mwaka 2009/2010 yalikuwa bilioni 6.6 tu, mwaka 2010/2011 ilikuwa bilioni 8.2, mwaka 2011/2012 ilikuwa bilioni 8.9, mwaka 2012/2013 ilikuwa bilioni 8.3; mwaka 2013/2014 ilikuwa bilioni 10.8; mwaka 2014/2015 ilikuwa bilioni 15.5; mwaka 2015/2016 bilioni 17.87; mwaka 2016/2017 ilikuwa bilioni 18.58; mwaka 2017/2018 ilikuwa bilioni 26.9; na mwaka huu kuishia Mei tarehe 15 ilikuwa bilioni 30.3. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye mifugo mwaka 2009/2010 ilikuwa bilioni 2.7; mwaka 2011/2012 ilikuwa bilioni 8.7; mwaka 2012/2013 ilikuwa bilioni 5.6; mwaka 2013/2014 ilikuwa bilioni 6.8; mwaka 2014/2015 ilikuwa bilioni 6.4; mwaka 2015/2016 ilikuwa bilioni 14.1; mwaka 2016/2017 ilikuwa bilioni 12.5; mwaka 2017/2018 ilikuwa 21.7; na leo tarehe ya leo 23 Mei, 2019 ni bilioni 33.85 na ni kuishia tarehe 15 Mei. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukija na mtiririko huo, ukija na mtiririko huo mwaka wa 2000 kwa jumla yake, mwaka 2017/2018 ilikuwa bilioni 17.3 na leo 2018/2019 tuna makusanyo mpaka sasa hivi ya bilioni 64.15 na tutafika bilioni 70 ifikapo tarehe 30 Juni, kwa malengo tuliyopewa ya bilioni 40. Makusanyo zaidi ya bilioni 30 na haya makusanyo ya bilioni 30 ambayo yamekusanywa na Wizara hii, yote yako kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, yanaendelea kutekeleza Mipango mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa mmempongeza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, amejenga Zahanati ndiyo hizo fedha, mmempongeza Waziri wa Maji, ndiyo hizo fedha. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Rudia, MBUNGE FULANI: Rudia tu. MBUNGE FULANI: Arudie.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, sisi tunatafuta hizi hela, lakini wanawapongeza, wamempongeza sana Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa amepata pongeza nyingi sana, amejenga zahanati nchi nzima, ni fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamepongeza miradi ya maji imejengwa, tunaishukuru Serikali na wakawa wanaomba hata tozo ziongezeka, sisi tumetoa mchango wa ziada siyo ile tuliyopewa na Serikali, wa ziada ya bilioni 30. Nataka niwaulize bilioni 30 kama hawa watumishi wangu na mimi Waziri ni mla rushwa, kama sisi ni wala rushwa hizi fedha tungezifikishaje Hazina,? Wapongezeni Vijana hawa, kwa sababu kama wangekula rushwa hizi fedha zisingepatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nawaomba, tuwe wakweli tukiwa hapa, hata Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatueleza kutekeleza Ilani hii, hata hiyo ya CHADEMA au ya Chama kingine, sijaona Ilani ambayo itatekelezwa bila pesa, hakuna Ilani ya Chama chochote duniani ambayo inaweza kutekelezwa bila fedha. Kwa hiyo kama kuna njia zozote za kupinga ukusanyaji wa mapato ni kuzipinga hata Ilani za vyama vyenu, kwa sababu hakuna Ilani duniani ambayo unaweza kuitekeleza bila kukusanya kodi, lakini tutaendelea kukusanya kodi hizo na hatutawaonea wananchi kama inavyozungumzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yamezungumzwa mambo mengi, migogoro ya wafugaji; utatuzi wa migogoro, Wizara yetu imefanya mambo makubwa katika historia ya utatuzi wa migogoro na hata dada yangu yule aliyeanza kusema, Mheshimiwa Gimbi, aliyesema kwamba Mpina ameonea wafugaji, Mpina amewasaliti Wasukuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza moja, nikubali kabisa kwamba mimi siyo Waziri wa Wasukuma, mimi ni Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. La pili, hatutawa- favor watu kwa ukabila wao, wakivunja sheria watashughulikiwa. Niliwahi kusema hapa, kwenye uvuvi haramu hata Mzee Mpina mwenyewe tukimkuta ameshiriki uvuvi haramu tutamkamata. Leo nazungumza Mzee Mpina yuko pale, kama atashiriki uvuvi haramu, tutamkamata, kwa sababu hakuna, hatuwezi kutengeneza mazingira ya ukabila ukienda huku unafanya hivi, lakini nataka nimhakikishie hakuna kipindi kingine ambacho migogoro ya wafugaji imetatuliwa kama kipindi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Timu zimeenda maeneo mbalimbali, Wabunge wengine wamezungumza vizuri, kuna watu wengine walikamatwa, ng’ombe 540, Naibu Waziri wangu akaenda tukawaomba watu wa Maliasili na Utalii, ni kweli ng’ombe walikuwa ndani ya hifadhi, tukawaomba wawasamehe, wakasamehewa, ng’ombe 500 wakatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Katibu Mkuu nikamtuma siku ya Pasaka, kwenda Simiyu ambako ng’ombe zilikuwa zimekamatwa zaidi ya 200, siku ya Pasaka, akaenda kuomba na kwenyewe tukawaomba wenzetu wa Maliasili na Utalii watusaidie kutokana na mazingira yaliyokuwepo, mifugo ile ikatoka. Vilevile tumehangaika nchi nzima, kutafuta malisho ya wafugaji ambako leo, Wizara yetu imetenga hekta 373,000 za kuwapangisha wafugaji katika hatua hii wakati tunawatafutia maeneo mbalimbali kwa ajili ya malisho. Maeneo ya Serikali. haijawahi kutolewa offer hiyo katika kipindi kingine chochote kile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo, Halmashauri tumezifuata moja baada ya nyingine kwenye migogoro mikubwa ya mifugo, tumepata mpaka sasa hivi hekta 199,000 ambazo na zenyewe tutaweka mifugo. Mambo haya hayajawahi kufanyika migogoro ya wafugaji kupigana mapanga na kufanya nini, leo imepungua, ilikuwa dhahama kubwa nchi hii, mbona haipongezwi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, migogoro ya mifugo tuliyoibua mikoa hiyo michache (mitano) tuliyokwenda ni migogoro 43. Katika migogoro hiyo 43 tuka-solve migogoro 27, sawa n a asilimia 63 ya migogoro. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye na mimi naungana sana na Watanzania wengine wote wanaoendelea kumpongeza aliamua kuunda timu ya Mawaziri wanane kwenda kushughulika na migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Tumetembea nchi nzima na tumetoa mapendekezo mengi juu ya kutatua migogoro hii. Ninaamini baada ya hatua hizi kufikiwa tatizo la migogoro la wananchi kukosa malisho litakuwa limepungua.

Mheshimiwa Spika, nawakumbuka wapiga kura wa Kongwa. Tayari tumetenga hekta 13,500 kwa ajili ya wananchi katika Ranch ya Kongwa ili kuweza kuwanufaisha wananchi wa kongwa ambao wamekaa na Ranch hii kubwa sana na kwa muda mrefu lakini hawana mahali pa kuchungia. Kwa hiyo tumekwenda maeneo mbalimbali kutatua changamoto hizi. Mmeona hata juzi hapa Mawaziri tunazunguka nchi nzima kutatua migogoro tukiwa pamoja kama timu moja ya Serikali, kutatua migogoro ya wafugaji. Kwa hiyo mambo haya Waheshimiwa Wabunge Serikali hii tuko kazini na tunaendelea kuyapigania kwa nguvu zetu zote.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, suala la magonjwa ya wanyama. Tumefanya kazi kubwa sana kwenye suala la magonjwa ya mifugo ambapo kwa mara ya kwanza Serikali imeweza kuogesha ng’ombe nchi nzima baada ya kutoa dawa 8,823, tumeogesha nchi nzima. Katika bajeti hii mnayoipitisha tumetenga zaidi ya milioni 500 ambazo tutaogesha tena mwaka unaofuata; kwa hiyo tumejipanga vizuri. Kituo chetu kile cha TVI kinaendelea kuongeza uzalishaji wa chanjo. Tulikuwa tunazalisha chanjo nne tu hapa nchini, sasahivi tumeendelea kuzalisha chanjo, hata hii ya homa ya mapafu ya ng’ombe tayari tumeshaanza na tunaendelea, na tunategemea kwamba baada ya muda mfupi tutafikia chanjo zote 11 ambazo leo tunatumia mabilioni ya fedha za Watanzania kuagiza chanjo kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, naomba muendelee kutuunga mkono. Mama mmoja akanipigia simu akaniambia Mpina Waziri wa Mifugo hivi Nyerere amefufuka? Nikamuuliza kwanini mama? Mama mtu mzima mwenye umri wa karibia miaka 100 na kitu; Nyerere amefufuka? Nikamuuliza kwanini? Yaani Serikali imeanza kuogesha mifugo! Tunaona kila sehemu Serikali inaogesha mifugo! Nikamwambia mama Nyerere hajafufuka ila kuna kijana wake anait wa Magufuli, kijana wa Nyerere ndiye anayeyafanya haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, operesheni Nzagamba. Operesheni Nzagamba imefanyika kwa nia njema sana. Waheshimiwa Wabunge tukumbuke, lazima tujiulize hili swali; kwa nini viwanda vyetu vimekufa? Watanzania wengi wamejiuliza swali hili lakini ukweli ni kwamba viwanda hivi havikupata ulinzi wa kutosha ndiyo maana vilikufa. Tumeendesha operesheni hapa na matokeo ya operesheni Waheshimiwa Wabunge mmeyaona. Tumeendesha Operesheni Nzagamba, tumekamata watu mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali wakijaribu kufanya utoroshaji mkubwa wa rasilimali zetu.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, hakuna mtu atakayekwenda kuwekeza kwenye nchi ambayo hailindi wawekezaji wa ndani. Yaani leo hii unamwambia mtu ajenge kiwanda, kesho watu wanaingiza maziwa hapa nchini, hayana vibali, hayajalipa chochote hayajapimwa hata ubora yanaingia hapa nchini yanauzwa kwa bei ya chini kiasi kwamba huyu hawezi kushindana. Unamwambia mtu ajenge kiwanda cha nyama wakati hoteli zote zinakula nyama kutoka nje, Watanzania wote wanakula nyama kutoka nje na zinauzwa kwa bei ndogo kumbe zingine zimeingizwa hapa zingine zikiwa zime-expire, Watanzania wamekula. Usipowalinda namna hiyo watakula chakula ambacho hakina ubora na hakina viwango. Tufanye nini?

Ukiwakamata tayari una-frustrate wawekezaji. Nani anaye-frustrate wawekezaji? Viwanda vyote nchi hii ilishindikana kuendelea. Wawekezaji wakawa wanapiga danadana wanakimbia. Leo tumeleta hapa mpango, viwanda vipya vinajengwa, uwekezaji wa takriban bilioni 200 kwa muda mfupi wa hatua ambazo Seri kali sisi tumezichukua katika kupambana na watu waliokuwa wanaharibu soko la Watanzania ili kuwepo na ushindani ulio sawa.

Mheshimiwa Spika, huwezi kuupata ushindani ulio sawa kama haya mambo utayaendeleza. Leo tunajenga kiwanda cha chanjo chenye uwezo wa ku-supply chanjo 27, Tanzania, haitaagiza chanjo tena. Mnataka Serikali hii ifanye nini? Viwanda vikubwa vya nyama vinavyojengwa havijawahi kuwepo. Watu wengine walisema wingi wa viwanda si tija, tija ni ufanisi. Sasa hata hivyo viwanda vingi vya aina hiyo hatukuwa navyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima wawekezaji wetu wa ndani tuwalinde na ndiyo maana operesheni hizi zimekuwa zikifanyika. Wafugaji wetu hakuna namna yoyote ile ambayo tunaweza tukawaona kwa namna yoyote ile. Tozo tunazoziweka ni tozo ambazo zinalifanya walau Taifa nalo linufaike. Huwezi ukawa na mifugo nchi hii halafu hupati chochote. Mifugo hii, Tanzania kuwa ya pili Afrika kuwa na mifugo; na ninataka nisahihishe hizo takwimu, watu wamesema kwamba Tanzania ni nchi ya tatu, hapana Tanzania ni nchi ya pili baada ya Ethiopia kuwa na mifugo mingi. Sisi tunashikilia asilimia 1.4 ya mifugo yote iiyoko duniani; tunashikilia asilimia 11 ya mifugo yote iliyoko Bara la Afrika, halafu unakusanya mapato ya bilioni 12, hatuwezi kuruhusu hilo.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, mtuamini, nia ni njema ya kujenga uchumi wa nchi yetu. Tuzalishe mifugo yetu, tupate malighafi ya viwanda, tuzalishe nyama, tuuze nje ya nchi, tuuze maziwa nje ya nchi, tutosheleze soko la ndani. Hivyo hivyo na kwenye samaki. Leo samaki tulikuwa tunaagiza kwa mabilioni ya fedha, uagizaji wa samaki sasahivi umeshuka kwa asilimia 67 tangu tuanze kuchukua hatua hii na mambo yanaenda vizuri. Leo kiwanda chetu cha Chobo kila wiki kinabeba tani 45 kutoka mwanza kuja Dar es Salaam kwa kutumia ndege zetu wenyewe za ATCL. Leo mageuzi haya yanafanyika, sasa tutapata kiwanda cha kuchinja ng’ombe 1,000 cha Chobo kule Mwanza. Tuna minofu ya samaki inayotakiwa kusafiri kila leo. Uvunaji wetu wa samaki sasahivi uko tani 180 mpaka 200 kwa siku; kwa hiyo tuna mzigo mkubwa wa kusafirisha kwenda nje ya nchi. Viwanda hivi vyote vya nyama tunavyovijenga vitatuwezesha kuzisafirisha nyama kwenda nje ya nchi, tutapata fedha za kigeni. Tumetengeneza ajira nyingi za Watanzania, tumetengeneza soko la Watanzania, tumetengeneza bei ya Watanzania katika rasilimali za mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo niwaombe endeleeni kuunga mkono jitihada za Serikali ambazo zina nia njema kabisa ya dhati katika kuhakikisha kwamba mageuzi ya kweli yanapatikana na taifa linanufaika na rasilimali zake na kuhakikisha kwamba mtu yeyote yule hatachezea soko la nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, tumetengeneza dawati la sekta Binafsi, dawati hili limeleta mageuzi makubwa sana hapa nchini. Sekta ya mifugo na uvuvi ilikuwa hata haikopesheki. Mpaka leo hii tunavyozungumza kupitia dawati hili tayari mikopo ya bilioni 17 imetolewa kwa wawekezaji wa sekta ya uvuvi na kwa wawekezaji wa sekta ya mifugo. Hivi tunavyozungumza mikopo ambayo inategemewa kutolewa hivi sasahivi kupitia dawati hili ni bilioni 55 ambayo nayo itatolewa muda wowote kupitia hili dawati ambalo limekuwa kiungo kikubwa sana kati ya Wizara na Serikali na kati ya wadau na wawekezaji wote na wafugaji wote, na wavuvi wote nchini. Leo tunavyozungumza mambo yanaendelea, wanaenda mbali zaidi hata kusaidia mpaka kuandika business plans ili kuwezesha tu mambo haya yaweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, wengine mmezungumzia kuhusu Kiwanda cha Azam. Nataka nizungumzie Kiwanda cha Azam, kiwanda cha Azam kiko Zanzibar, ni cha maziwa, ambapo wana-import maziwa ya unga kutoka nje na baadaye wanayachakata wanazalisha maziwa hapa nchini. Kiwanda hiki cha Azam cha Zanzibar baada ya Kanuni mpya ambazo ziliwataka kila wanapo-supply maziwa kutoka Zanzibar kuingia nchini wanatakiwa walipe shilingi 2,000 kiwanda kilifungwa, wakashindwa kufanya hivyo. Kilipofungwa kiwanda, kukawa hakuna tena ajira zilizopo pale za Watanzania, zikawa zimesimama hakuna kitu kinaendelea. Tukaamua kwa dhati kabisa kwamba tuwape unafuu.

Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba hatukuwapa punguzo lolote ila tuliwapa unafuu wa tozo. Kwa maana ya kwamba maziwa ya unga yanapoingizwa hapa nchini tunatoza 2,000, yanapoingizwa ya maji tunatoza 2,000. Sasa huyu anayeingiza ya unga akichakata anapata lita 8, anapoingiza Tanzania Bara anatakiwa alipe shilingi 16,000 kwa lita moja aliyoichakata.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tulichoona kwamba hapa Zanzibar wameajiriwa Watanzania wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na hoja ilitoka kwa Wabunge hawahawa humu humu ndani, mkituomba kwamba hiki kianda tukiwezeshe kifanye kazi. Tulichokifanya sisi tunamtoza yule kwa equivalent. Tunamtoza kwa uwiano; kwa maana ya kwamba tunamtoza kwa equivalent ya kilo ya unga ambayo ni shilingi 2,000. Kwa hiyo unachukua shilingi 2,000 ukigawa kwa nane unakuta shilingi 250. Ndicho tulichokifanya ili kiwanda kile kiweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, lingine tulilofanya, sheria inasema maziwa yakitoka Zanzibar yakiingia huku yametoka nje ya nchi yanatakiwa kulipa import levy na maziwa yakitoka hapa low milk inayozalishwa hapa ikitaka kupelekwa Zanzibar kwa ajili ya kuchakatwa na yenyewe inatakiwa ilipe export levy. Tukasema sasa hii kwa sababu maziwa haya yamezalishwa na Watanzania, maziwa ya Watanzania hapa bara hayana soko, maziwa ya Watanzania yanayozalishwa Zanzibar hayana soko, tukasema hii tuiondoe kabisa, wakitaka kuingiza maziwa yaliyochakatwa kutoka Zanzibar ya Wanzanzibari wenyewe waliyoyazalisha, yakiingizwa hapa Bara wasilipe chochote.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile maziwa yatakayochukuliwa hapa kwenda kiwanda cha Azam yaliyozalishwa na Watanzania hapa yakienda kule wasilipe chochote, ndiyo concept ya Serikali. Hakuna favour yoyote tuliyompa, na ndiyo maana tunaendelea kumtoza kwa sababu tu ya yale maziwa anayoyaagia kutoka nje ya nchi. Baada ya hapo, akiacha kuagiza kabisa ya nje ya nchi atatozwa asilimia sifuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya haya niliyoyazungumza ninataka sasa nimalizie na baadhi ya hoja chache ambazo Waheshimiwa Wabunge wengine mbalimbali waliweza kuziuliza hapa. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri alivyojibu baadhi ya hoja mbalimbali hapa ile asubuhi alipopata fursa ya kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge; na akajaribu kutoa clarification nyingi sana juu ya hoja mbalimbali zilizotolewa za baadhi ya Waheshimiwa Wabunge, akiwemo Mheshimiwa Zitto Kabwe.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, mlizungumzia sana suala hili kwamba Serikali ya Awamu ya Tano hakuna jambo lolote ambalo imelifanya; Ilani yote haijatekelezwa; kama Mheshimiwa Naibu Waziri ambavyo aliweza kuzungumza ile asubuhi. Lakini hoja hii ameizungumza kwa nguvu sana Mheshimiwa Zitto Kabwe, akasema na Wizara inajivunia tu faini n.k. hakuna kinachofanyika, Serikali ya Awamu ya Tano hakuna jambo lolote iliyofanya katika Ilani ya Uchaguzi. Nilikuwa nataka Mheshimiwa Zitto Kabwe angekuwepo hapa; kwa sababu kwa muda mrefu sana amekuwa hata akitoa takwimu za uongo juu ya ukweli na uhalisia wa utekelezaji wa shughuliza Serikali ya Awamu ya Tano, lakini wakati mwingine na kuonekana chuki dhahiri juu ya Serikali hii ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, anawadanganya watu kwamba mapato yalipanda mwaka ule wa 2014 na leo yameshuka, yamekuwaje, Serikali hii hakuna hatua yoyote nyingine ambayo imeichukua juu ya mambo haya.

Mheshimiwa Spika, sisi tunakwenda vizuri. Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi juu ya ujenzi wa bandari tumejipanga vizuri. Sasa hivi upembuzi yakinifu unafanyika na mkandarasi wetu yuko kazini anafanya kazi hiyo na Serikali imeshatenga na imeshaanza kumlipa na hivi karibuni atatoa ripoti ambayo itatuonesha tukajenge wapi bandari. Tayari mazungumzo tumeshayafanya na Serikali ya Korea na tuko vizuri katika kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, TAFICO imeanzishwa na tayari tumepata billion 4.2 kutoka Japan kwa ajili ya kuboresha baadhi ya miundombinu iliyoko pale. TAFICO Business plan imeshaandaliwa kwa kulitekeleza jambo hili. Sasa unaposimama hata kama una chuki namna gani, hata kama una chuki namna gani na Serikali hii ya Awamu ya Tano ni bora hata ukawa mvumilivu tu; kwa sababu hakuna namna yoyote ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inaweza ikashindwa kutekeleza majukumu yake eti kwa sababu ya watu wawili watatu ambao wana chuki nayo.

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuhakikisha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza majukumu yake, Ilani ya Uchaguzi inatekelezwa kwa kiwnago kikubwa. Ni vizuri sana Mheshimiwa Zitto Kabwe asiiharibu ile rekodi tuliyoiweka naye enzi hizo. Tuliweka rekodi nzuri ya michango mizuri hapa Bungeni ambayo imelisaidia taifa hili lakini ameanza na kuku- attack mpaka wewe Mheshimiwa Spika ambaye ndiye muasisi wa mageuzi, sio uchonganishi!

Mheshimiwa Spika, ninachosema, siku ya ESCROW, Mheshimiwa Spika, akiwa Naibu Spika wa wakati huo ndiye aliyeamua Mpina aingie kwenye Kamati ya ESCROW, Kangi Lugola, Hamis Kigwangalla aingie kwenye Kamati ya ESCROW na maombi hayo yaliombwa na Filikunjombe pamoja na Zitto Kabwe. leo hii Zitto Kabwe anasimama katika Bunge hili, na maeneo mbalimbali kuzungumza hata maneno ya uongo dhidi ya Mheshimiwa Spika ambaye mimi nasema kati ya watu ambao wametengeneza viongozi humu Bungeni kwa watu ambao hamuijui historia ni Mheshimiwa Job Ndugai Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na watu waliomtengeneza hata Mpina Mheshimiwa Job Ndugai yumo, sio mtu mwepesi wa kusimama na kumnyooshea kidole, sio mtu mwepesi kihivyo unless ni kwa watu ambao wasioijua historia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Job Ndugai amefanya mambo makubwa ya nchi hii. Sasa ukiendesha kwa chuki zako, Rais John Pombe Magufuli ni kwa sababu watu tu hawamjui, laiti wangekuwa wanaijua siri ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli hata wale ambao wanaongea haya na yale kule wasingepoteza huo muda. Hakuna mtu atakayemkwamisha Mheshimiwa John Pombe Magufuli kutekeleza majukumu yake, kwa chuki, kwa hila, kwa namna yoyote na wala wanaotegemea kwamba anaweza akayumba wala kuyumbishwa kwa maneno ya hapa na pale wasitegemee hilo.

Mheshimiwa Spika, Rais huyu ni Rais ambaye ameshavuka mipaka mingi ya viongozi, na historia ya Tanzania itaandika, sisemi haya mimi Mpina kwa sababu ni Waziri hapa, niwe mwananchi wa kawaida kabisa kwetu nyumbani Meatu Mwamuge nitasema haya, kwamba Rais Magufuli ni wa mfano na wa kuigwa mfano katika taifa hili. Niwe Mbunge wa kawaida nitayasema haya, niwe Waziri hivi nitayasema haya. Ni mara chache kupata viongozi wako committed namna hii, anatakiwa aungwe mkono na Watanzania wote katika mageuzi anayoyafanya ya ukombozi wa nchi yetu. Ni mara chache sana kumpata Rais ambaye akiamua kupasua hapa anapasua, na mnalijua tatizo la kupasua bila kuangalia. (Makofi/Kigelegele)

Mheshimiwa Spika, ukipasua bila kuangalia, utapasua mjomba wako, unapasua shangazi yako, utapasua mali za watu ambao hawakamatiki, utapasua mali za watu ambao huwezi kuwagusa nchi hii. Kwa hiyo ni mara chache sana ndiyo maana viongozi wengi wanayumba kwa sababu ya kukosa misimamo hiyo. Mimi nataka kama taifa tumuunge mkono Rais huyu tutafika mbali katika ukombozi wa nchi yetu, tuijenge nchi yetu, tuache hizi siasa nyepesi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, someni! Ooh! Nimejisahau.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana, lakini nimalizie kwa kusema kwamba, safari ya mageuzi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza, tena iko hatua nzuri. Nami na wasaidizi wangu kama tulivyoahidi na tunaendelea kuwaahidi Wabunge, tutatumika sisi kwa nguvu zote, watendaji wangu hawa, waoneni hawa, wana mateso makubwa, kuwa mtumishi halafu chini ya Wizara ya Mpina, wana mateso makubwa. Pale Wizarani tumeshakubaliana kwamba muda ni namba tu, kwa hiyo hatujali muda gani, hatujali sasa hivi ni usiku katika kufanya majukumu yetu na tunaendelea kuwahakikishia, sisi tutakuwa vibarua hivyo, mpaka tutakapomaliza hili jukumu na tumejitoa hivyo mimi na wasaidizi wangu kuhakikisha kwamba mageuzi haya yanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi na Naibu Waziri wangu hapa, tunafanya hivyo, hakuna gain yoyote, hakuna any personal gain tunayoipata zadi ya maslahi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kusema kwamba, sasa baada ya kuwa nimemaliza kutoa maelezo yangu hayo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wasitucheleweshe, waipitishe hii bajeti tu mara moja, tusifike hata hiyo saa kumi na mbili ili tuwahi kwenda kutekeleza, kwa sababu, majukumu ya wafugaji na wavuvi yanatusubiri sana na wengine wadau wako hapahapa wanamhitaji Waziri, kwa hiyo, kuendelea kuchelewesha kupitisha bajeti itachelewesha utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuzungumza baada ya uchaguzi wa mwaka 2020, nikishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi na wapiga kura wangu wa Jimbo la Kisesa, kwa kunirejesha tena Bungeni kwa mara ya nne. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru wewe na Naibu Spika mnavyoliendesha Bunge vizuri sana. Sasa kwa sababu ya muda naomba niongelee Jimbo la Kisesa; jimbo hili lina changamoto nyingi sana; moja ni uvamizi wa tembo ambao umekuwa ni wa muda mrefu. Wananchi wanavamiwa na tembo, mazao yao yanaliwa yakiwa shambani na hata yakiwa nyumbani. Chakula kinaliwa mashamba yote yanakanyagwa, watu wamepoteza Maisha, wengine wamepata vilema vya kudumu. Tumelalamika sana na tumeomba sana Serikalini kulitatua hili tatizo, lakini leo miaka miwili, mitatu sasa wananchi hao bado wanaendelea kwenye dhiki kubwa sana ya uvamizi wa tembo, lakini huu uvamizi wa wanyama wakali pia upo kwenye maeneo mengine ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni muda mrefu sana na tumekuwa tukipeleka haya malalamiko Serikalini na haijatatulia mpaka sasa hivi ambao imepelekea umaskini mkubwa sana kwa wananchi, tunaomba sasa kwa mara hii tatizo hili lifike mwisho. Tunajua Serikali ya Awamu ya Tano na Awamu ya Sita imetatua mambo mengi yaliyokuwa yameshindikana, imeweza kutatua mambo makubwa, haiwezi kushindwa kuwazuia tembo. Tumeweza kumaliza mambo ya rushwa na ufisadi, tumeweza kumaliza madawa ya kulevya, tumeweza kumaliza ujambazi na ujangili, tumeweza kumaliza uvuvi haramu, tuje tushindwe na tembo; hapa kuna mtu mmoja tu ambaye hajawajibika sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunataka safari hii wananchi waishi kwa amani katika maeneo yao na tatizo hili tembo Mheshimiwa Waziri Mkuu, aagize likomeshwe mara moja. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mpina, Waheshimiwa Wabunge wa Zanzibar wanashangaa kwamba jimbo limevamiwa na tembo, endelea kuchangia Mheshimiwa.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, tunalo tatizo pia kubwa sana la wananchi wafugaji ambao walikuwa wanafuga wakakamatwa na wahifadhi kwamba wanachungia ndani ya hifadhi na baada ya hapo wakakatiwa rufaa wakaenda kushinda kesi mahakamani, zaidi ya wafugaji 30 wenye ng’ombe wasiopungua 5,000, ng’ombe wao mpaka sasa hivi wanashikiriwa na Serikali, licha ya kushinda kesi mahakamani. Wamefuatilia Serikalini kurudishiwa mifugo yao kwa sababu wameshapewa haki hiyo na mahakama kwamba warudishiwe mifugo yao, lakini mpaka sasa hivi tunavyozungumza ng’ombe hao hawajarudishwa.

Mheshimiwa Spika, sababu za kutorudishwa hazijulikani, mtu ameshinda kesi mahakamani, kwa nini uendelee kuzuia mifugo yake? wafugaji ukichukulia wa sehemu zingine mbalimbali lakini wa jimboni kwangu tu peke yake ni ng’ombe zaidi ya hizo 5,000 wa Jimbo la Kisesa ni zaidi ya 1,000 ambao mpaka sasa hivi zinashikiliwa licha ya wananchi hao kushinda kesi mahakamani. Wananchi akina Malimi Sendama na wenzake Ndatulu Malolo, Kwandu Malaba, Masunga Muhamali, Subi Maduhu na wengine ng’ombe 5,000 wanashikiliwa.

Mheshimiwa Spika, tunataka tuambiwe huko Serikalini aliyekataa hawa ng’ombe wasitolewe ni nani? Kama mahamaka imesha-grant haki ya hawa wafugaji, aliyekataa huko Serikalini ni nani? Namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu aliingilie kati suala hili, tukatende haki kwa hawa wananchi wanyonge ambao mifugo yao imeshikiliwa na Serikali licha ya wao kushinda kesi mahakamani. Tukitoka kwenye hili Bunge niende na hao ng’ombe wa wananchi hao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hili suala limezungumzwa hapa, nataka nishauri, suala la ukusanyaji wa mapato. Wabunge wengi wamezungumza hapa mianya mbalimbali, fursa mbalimbali ya ukusanyaji wa mapato ambayo bado hatujakusanya sawasawa, nami nakubaliana nnalo. Naomba hapa tufanye upya tathmini ya mapato yetu, zile Wizara pamoja na taasisi ambazo zinakusanya mapato na zina vyanzo vingi vya mapato ziende kwenye Kamati ya Bajeti ili tuweze kuyaona maeneo ambayo tunaweza tukakusanya mapato kwa wingi. Hatima yetu na maendeleo yetu yanategemea upatikanaji wa fedha ili tuweze kutekeleza miradi hii ya maendeleo, hatuna njia nyingine ya mkato zaidi ya kutafuta fedha.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi kilichopita cha Serikali ya Awamu ya Tano iliyoongozwa na mbabe wa vita, Rais wa wanyonge, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, tulipiga hatua kubwa sana katika ukusanyaji wa mapato. Ndio maana tukaweza kutoka kwenye kuanzia ukusanyaji wa mapato wa bilioni 850 kwa mwezi mpaka leo tumefikia trilioni mbili kwa mwezi. Tukaenda kwenye maduhuli kutoka bilioni 697 mpaka trilioni 2.4.

Mheshimiwa Spika, ukusanyaji wa mapato haya umeiwezesha nchi yetu kuweza kugharamia miradi mingi sana, tumeweza kuzuia maeneo ambayo mapato yetu yalikuwa yanapotea. Tumetunga sheria, tumefanya marekebisho ya sheria, tumezuia hata ile transfer pricing ambayo ilikuwa inabeba mapato yetu mengi sana, tumedhibiti hata e-risk financial flow ambayo nayo inachukua fedha zetu nyingi sana tumeweza hata kufuta mikataba iliyokuwa inanyonya Taifa letu mikataba ya IPTL, Aggreko lakini Symbion iliyokuwa inachukua 719,000,000,000 kwa mwaka, leo tumeweza kufuta mikataba hiyo na Watanzania wanaendelea kupata fedha.

Mheshimiwa Spika, kwenye madini ndio maana hapa imezungumzwa, madini, tulikuwa tunakusanya 194,000,000,000; tumefika 500, 000,000,000; kule Mererani baada ya kujenga ukuta, tulikuwa tunakusanya 70, 000,000kwa mwezi leo tunakusanya 3,000,000,000 kwa mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Mifugo na Uvuvi tulikuwa tunakusanya 21,000,000,000 tu kwa mwaka, leo tunakusanya 74, 000,000,000 kwa mwaka. Sasa katika kuyafanya haya tumeweza kupiga hatua kubwa sana kwa maendeleo. Nataka niseme na nirudie kusema tena, nawahurumia hata wale ambao wanajaribu kubeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano iliyoongozwa na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo aliweza kujipambanua na kupata haya mapato, wengine wanasema alikuwa fisadi.

Mheshimiwa Spika, hivi wewe fisadi, ukusanye fedha hizi, ununue ndege za Watanzania wote, huo ni ufisadi! Wewe fisadi, ukusanye hizi, ujenge barabara nchi nzima, ukarabati meli zilizokuwa hazitembei leo zinatembea, Watanzania wanaenda kote wanakotaka, ufufue reli iliyokuwa imelala miaka nenda rudi ya kutoka Dar es Salaam mpaka Arusha! Huyo ni fisadi! Kwa hiyo nawahurumia watu wa namna hiyo kwa sababu fikra zao ni fupi na uelewa wao wa kupambanua mambo ni mdogo sana. Tutaendelea kumuenzi Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kazi kubwa ya maendeleo aliyopigania kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda unakimbia sana, nataka niongelee kidogo tu kwenye taarifa ya ukaguzi. Nizi-alert hizi kamati zinazoenda kufanya uchambuzi wa mambo yaliyopo kwenye taarifa yenyewe. Kuna mambo yalivyoandikwa kwa jinsi yalivyoandikwa si ya kawaida, kwa mfano ukienda kule maliasili, walipokuwa wanajaribu kuandika fedha zilizoibiwa na adhabu za watu wanapaswa kuchukuliwa hatua. Ukienda kule wanasema kuna matumizi ya fedha zinazotoka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Utalii, bilioni 34, mwanzo wakasema sehemu ya fedha hizo bilioni 5.7 kama sikosei na bilioni 2.8 na milioni 100, zilihamishwa kupelekwa kwenye taasisi nyingine bila Afisa Masuhuli kujua. Halafu adhabu inayopendekezwa inasema Mkurugenzi wa Utalii pamoja na Mhasibu wake wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Spika, Afisa Masuhuli ambaye hakujua fedha zinahamishwa amekingiwa kifua cha nini? Kwa nini taarifa ya CAG iwe na kinga kwa wahalifu wengine, ukienda huku kwingine, upande mwingine utakutana na fedha 171,000,000 zimetumika kwa ajili ya bonanza, halafu milioni zingine kama 148,000,000 zilihamishwa na zenyewe zikatumika bila Afisa Masuhuli kujua, lakini adhabu inayopendekezwa, Waziri wa Maliasili wa kipindi kile, tena akatajwa kwa jina Mheshimiwa Dkt. Kigwangala na Katibu wake wachukuliwe hatua. Katibu Mkuu ambaye ndiye Afisa Masuhuli ambaye huyu Waziri aliandika dokezo, lakini waliyoidhinisha fedha na kutoka ni Katibu Mkuu na Ma-CEO hawa, kwa nini taarifa hii inawakingia kifua?

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Taarifa Mheshimiwa Spika.

SPIKA: Mheshimiwa Mpina pokea taarifa ya Mheshimiwa Kingu.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa anayezungumza, kwanza hatujaanza bado kujadili ripoti ya CAG. Bunge hili ni Bunge la utaratibu, ni Bunge linaloongozwa kwa misingi ya utaratibu, lakini hata sivyo, tusubiri hoja za Serikali zitakapokuwa zimejibiwa, tutakuja kuanza kuteteana humu, lakini si sasa hivi. (Makofi)

SPIKA: Pokea taarifa hiyo Mheshimiwa Mpina.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, sipokei taarifa yake na najua ninachokizungumza. Sasa hivi Kamati zetu za PAC na LAAC zimeipokea hii taarifa, zinaenda kufanya uchambuzi juu ya hizi taarifa. Zinapoenda kufanya uchambuzi sisi Wabunge hatujazuiwa kuzi-alert mambo yaliyomo humu, ziende zikayaangalie. Wewe jana ulikuwa unazungumza ATLC na unazungumza taarifa ya CAG, ulikuwa unazungumzia taarifa gani? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niongeze muda kidogo niongeze nimalizie.

SPIKA: Tunaendelea, Mheshimiwa Mpina inatosha, muda hauko upande wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa ili niweze kutoa mchango wangu katika hii sekta muhimu sana kama ambavyo umeshaeleza hapa kwamba huu ndiyo moyo wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza vizuri sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nimesikiliza vizuri sana taarifa ya Mwenyekiti wetu wa Kamati ambayo maeneo mengi mbalimbali wameyagusa, lakini nataka tu kujikita katika mambo haya yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, yapo maeneo mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka ili kuwezesha utoaji wa elimu katika sekta shule zetu za sekondari na msingi ili kwenda vizuri zaidi. Kwa mfano, tunalo tatizo kubwa sana sasa hivi la vyoo vya kisasa katika shule zetu za msingi na sekondari ambavyo maeneo mengi kutokana na ukosefu wa hivi vyoo vya kisasa, vinajaa kila siku. Kwa sababu vinajaa na vyoo vile siyo vya kisasa, inabidi kila kinapojaa mbomoe miundombinu ile mjenge mingine.

Mheshimiwa Spika, kuna shule moja eneo lililochimbwa vyoo sasa hivi limefikia ekari tatu. Kwa hiyo, itafika mahali eneo la shule lote litachimbwa vyoo kila sehemu. Kwa hiyo, ni lazima Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI kuja na mkakati wa haraka sana wa kujenga vyoo vya kisasa, lakini pamoja na kuandaa madampo ya kisasa kwa ajili ya kumwaga zile taka. Hilo ndio litakalotuwezesha kuwa salama zaidi, ili vijana wetu katika shule za msingi na sekondari wasome vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii kampeni lazima tuende nayo kwa speed kubwa sana ya ukamilishaji wa magofu ambayo wananchi wameyaanzisha. Tuna upungufu mkubwa wa madarasa, magofu yapo wananchi walishajenga wamefikia ile hatua, lakini bado hayajamaliziwa. Tuna maabara, bado hazijakamilika, nyingine zimejengwa zimekamilika, lakini vifaa hamna, tuna mahitaji makubwa sana ya hostels.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi kubwa sana iliyofanywa katika Serikali ya Awamu ya Tano, lakini bado kuna mahitaji makubwa ambayo tunatakiwa kuhakikisha kwamba, tumeyakamilisha kikamilifu ili vijana wetu waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ni muhimu sana, limezungumzwa na kila tukizungumza suala la ajira, tunazungumza suala la ujuzi. Mambo haya ni makubwa sana na wewe umekuwa uki-comment hapa Bungeni, lakini nataka niseme hivi tunataka kupata vijana wenye ujuzi, vijana ambao wameandaliwa. Tunawapataje…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge nawaomba sana, kama kawaida yetu tumpe nafasi anayezungumza, tumsikilize vizuri.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, tunawapataje vijana wenye ujuzi wakati masomo ambayo yangeweza kuwawezesha vijana hawa kupata ujuzi hayapo, yameondolewa. Kwa mfano, leo hii vijana wanaoenda internship ni wale tu wanaosoma masomo ya udaktari wa binadamu, lakini wale wanaosoma masomo ya udaktari wa mifugo hawaendi intern. Wale wanaoenda kusoma mafunzo mengine ya uvuvi, mafunzo mengine ya kilimo, ili tuweze kuandaliwa wataalam ambao wamepitishwa kwenye tanuru na wakaiva, lakini hawaendi intern. Sasa mwisho wa siku unategemea unawapata wapi vijana wenye ujuzi wanaoweza kutumika sawasawa?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo unakuta kwa upande wa Madaktari kwa sasa hivi wanafanya vizuri sana kwa sababu, wanapata mwaka mmoja kwa ajili ya intern na wanalipiwa na Serikali. Sasa shida iko wapi kwa vijana wengine hawa? Tunahitaji Maafisa wa Mifugo na Madaktari wa Mifugo walioandaliwa vizuri, wanafundishwaje? Tunahitaji wataalam wa uvuvi walioandaliwa vizuri, wamefundishwaje? Tunahitaji wataalam wa kilimo walioandaliwa vizuri, wanafundishwaje na mtaala wetu unasemaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulifika mahali hapa masomo kwa mfano ya kilimo yaliondolewa shuleni; shule ya msingi yakaondolewa, sekondari yakaondolewa, lakini unafundisha vijana shule ya msingi, unafundisha vijana sekondari ambao unatarajia baada ya kumaliza masomo yao asilimia 70 waende kulima, halafu somo lenyewe la kilimo halifundishwi na liliondolewa shuleni. Sasa tunategemea mabadiliko gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, somo la ujasiriamali nalo kwa nini halijawekwa kuwa la lazima? Kwa sababu, hata ukisoma udaktari si lazima ujifunze kutunza hizo fedha na huo mshahara ili uweze kukutosheleza? Si lazima ujifunze ku-debit na ku-credit ili ujue matumizi yako unasimamiaje mwisho wa mwezi? Kuna shida gani somo la ujasiriamali kufundishwa kwa kada zote kuanzia shule za msingi, vijana wakafundishwa vizuri ujasiriamali, wanafika sekondari wanafundishwa vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa unafundisha watu waende kulima, wakienda kule hawajui hata kufungua tractor, hawajui hata kuwasha tractor, hawajui hata kuswaga plough, hawajui hata kushika jembe, halafu Taifa lenyewe ni la wakulima hili. Sasa Taifa la wakulima, somo la kilimo limehujumiwa, halifundishwi, sasa sababu za kuhujumiwa somo la kilimo ni nini? Sababu za kuhujumiwa somo la ujasiriamali ni nini? Naona ni kuifanya Tanzania hii itengeneze watu ambao hawana uwezo wa kwenda kutumika sawasawa katika kulitumikia Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la utafiti. Limeelezwa ukisoma vizuri sana wanaongea hapa, lakini niseme suala la utafiti katika nchi yetu halijapewa kipaumbele kinachotakiwa. Hili suala tusipolipa kipaumbele kama inavyotakiwa tutaendelea tu kuanguka kila mwaka kwa sababu, leo hii tunazungumzia udahili wa wanafunzi na tunasema udahili umeongezeka, chuo kikuu umeongezeka, vyuo vya ufundi umeongezeka, lakini nani anayefanya trace study ya kuwajua hawa watoto baada ya kumaliza masomo yao wanaenda wapi? Wanaenda kufanya nini? Wako wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nikiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi tulifanya utafiti wa kufuatilia vijana wanaomaliza, waliosoma masomo ya mifugo baada ya kumaliza masomo hayo wanaenda wapi. Katika vijana 8,000 vijana mia saba na kitu tu ndio walioonekana kupata ajira na vijana asilimia 90.5 hawajulikani wako wapi na wanafanya nini. Sasa kama tafiti hizi haziwezi kufanywa mtakuwa mnasema tu tunadahili wanafunzi, udahili umeongezeka. Sasa udahili umeongezeka, umeongezeka kwenye jambo gani?

Mheshimiwa Spika, bado tuna vijana leo anataka sasa achague kozi yake anataka kwenda kusoma mchepuo gani. Anataka kwenda kusoma kilimo, anataka kwenda kusoma uvuvi, anataka kwenda kusoma uhasibu, anataka kwenda kusoma biashara, lakini utafiti uliofanyika wale waliosoma masomo hayo leo wako wapi? Atachaguaje sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pengine unaenda kuchagua unataka kwenda kusoma biashara, vijana toka mwaka 2005 waliosoma biashara graduates hawajapata kazi. Sasa wewe leo unachagua kwenda kusoma biashara ili uajiriwe na nani? Soko la ajira linasema nini? Linahitaji nini? Linahitaji kijana gani aliyeandaliwa wapi? Takwimu hizi na utafiti huu kwa nini haufanywi?

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu kwa nini utafiti huu haufanyiki, ili vijana wakapata base ya kuchagua kwamba, sasa hivi nataka mimi kwenda kusoma mifugo. Sasa nataka nijue vijana waliosoma mifugo ajira katika sekta binafsi ajira zipo? Hamna, ingeoneshwa percent kwamba, leo hii ajira katika sekta ya mifugo ni asilimia mbili. Leo hii ajira katika uvuvi ni asilimia kadhaa, leo hii katika kilimo ni kadhaa, vijana wetu wangeweza kuchagua kulingana na mahitaji ya ajira kwa wakati huo. Hivyo, hata udahili wa wanafunzi sasa hata vyuo vyetu vinavyoweza kupanua udahili vipanue udahili kulingana na madai na mahitaji ya soko yaliyopo kwa sasa, sio tu mtu anachagua tu kwa hiyari mimi naenda kusoma accounts, mimi naenda kusoma business administration; unaenda ku-administer wapi? Mahitaji yako wapi?

Mheshimiwa Spika, lakini hata training pia ya Maprofesa wetu na Madokta wetu tunaowapeleka chuoni kwa sasa bado kuna shida kubwa kwa sababu kijana anayebakishwa shuleni kwa ajili ya kuwa lecturer ni yule aliyepata “A” nyingi, lakini si yule aliye-practice katika lile eneo. Kwa hiyo, unafundishwa biashara na mwalimu ambaye amepata “A” nyingi, lakini hajawahi kufanya biashara yoyote na wala hajawahi ku-practice eneo lolote. Kwa hiyo, mwisho wa siku utatengeneza vijana gani wa namna hiyo? Kwa nini mfumo huu usibadilishwe?

Mheshimiwa Spika, leo hii tunafanya vizuri sana na nataka nipongeze kabisa, kwa sababu, mara nyingi wanaowafundisha madaktari wetu ni wale ambao wanatibu binadamu, kwa hiyo, wanakuwa na experience ya kutosha katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunayo safari kubwa ya kufanya mageuzi kwenye nchi yetu na mageuzi ya kweli yatafanyika kwa kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu. Tukishajipanga vizuri kwenye sekta ya elimu, leo hii tunazo taasisi ambazo zinafanya shughuli ya utafiti, kwa mfano kwenye uvuvi tuna TAFIRI, kwenye mifugo tuna TARIRI, kwenye kilimo tuna TARI, kwenye misitu tuna TAFORI, tuna COSTECH, tuna NBS. Hizi taasisi zinakutana wapi? Nani anaandaa zile agenda za utafiti? Ile database ya tafiti zinazofanyika nchini tutaiona wapi? Hizo tafiti zinazoandaliwa zinawafikiaje watu? Kanuni zilizopo kwa ajili ya tafiti hizo, kuzilinda zile tafiti zipo wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu saa nyingine hata taasisi zetu za utafiti zinafanya hata mambo ya nje ambayo wakati mwingine hayana manufaa kwenye Taifa letu. Tufanye mageuzi ya kweli katika sekta hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana Wizara ambayo inatunza rasilimali za Watanzania na niseme tu nampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoendelea kwamba mpaka sasa hivi hatuna mradi wowote ule ambao una sua sua miradi yetu ya kimkakati yote inaendelea vizuri certificate zote zinalipwa kwa wakati kwa hiyo ni pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wetu, lakini zaidi pia kwa kutenga fedha bilioni 372.6 kwa ajili ya kipande cha Isaka Mwanza cha SGR, na kama hiyo haitoshi kwa kutoa fedha bilioni 187 kwa ku-support TARURA kupata miradi ambapo kila Jimbo limepelekewa Milioni 500 na mimi za Jimbo langu nimeshataarifiwa zimeshafika na mipango kule inaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tukitoka hapo tunazungumza suala leo la Wizara ambayo inakusanya mapato ya nchi yetu na changamoto zake tumepokea changamoto nyingi hapa wakati tukipokea taarifa za kila Wizara, baadhi ya Taasisi kushindwa kufikia malengo sababu wanaeleza ni Corona, na mimi niseme kwamba ni kweli kabisa Corona inaweza kuwa imechangia kupunguza mapato yetu. Lakini haiwezi kulingana na maeneo pengine ambazo waliweka lockdown wakazuia kila kitu hali zao ni mbaya zaidi. Na kwa hili ninataka nimpongeze sana Hayati tinga tinga Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alivyotusimamia vizuri sana katika hili eneo madhara ya Corona sisi hatujadhulika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ninachotaka nitahadharishe hapa pia isije ikawa kinga watu wamekuwa wazembe kule kukusanya mapato ya Serikali alafu wanakuja hapa wanasema Corona, na Wizara ya fedha mnafuatilia namna gani kwenda kujiridhisha kweli sababu hizi zinazotolewa ni za kweli mnajiridhishaje mnafuatilia mkiambiwa Corona tu mnasema ni Corona kweli au kuna sababu zingine? Kwa mfano, tumeelezwa anguko kubwa sana la Taasisi za TANAPA, NCAA pamoja na TAWA ambao walipanga kukusanya bilioni 584 wameweza kukusanya bilioni 89 tu katika kipindi cha kufikia mwezi wanne, sasa kweli sababu ni hizo tu sababu ni Corona au zipo sababu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamepata anguko la bilioni 12.5 ikilinganishwa na mwaka jana kwa kipindi kama hiki Je, sababu ni hiyo Corona kweli au kuna sababu nyingine mnaenda kufuatilia na ndio maana Mwenyekiti wa Kamati hapa akasema ile monitoring and evaluation inayofanya na Wizara ya fedha inausahihi gani, katika kuhakikisha kwamba inakwenda kubaini chanzo cha matatizo kinachosababisha kodi yetu kushuka.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la pili ambalo ni Bandari bubu, tuna bandari bubu 693 hizi bandari bubu zote zinatumika kuingiza shehena ya mizigo zinatumika kuingiza shehena za mizigo bila kuhakikiwa, bila kukaguliwa ubora na kama kama hazihakikiwi wala kukaguliwa ubora tunategeema kwamba watu wanaingiza mizigo hiyo bila kulipa kodi, watu wanaingiza bidhaa fake na bandia na kama wanaingiza bidhaa feki na bandia usalama wa viwanda vyetu uko wapi, lazima viwanda vyetu vitakufa ni lazima ajira zetu zitakufa, zitapotea sasa hili jambo linashughulikiwaje.

Mheshimiwa Spika, mbona hizi bandari bubu zimekuwa muda mrefu sana na zinaleta madhara makubwa sana kwenye Taifa letu kodi zinapotea. Bandari bubu kila leo zinaripotiwa. Bunge lako hili lingetarajia leo kuambiwa ya kwamba;

(i) Bandari bubu zote zimerasimishwa na vimekuwa bandari rasmi.

(ii) Tungetarajia bandari bubu zote zimepigwa pini hazipo tena lakini kuendelea kuwa na Bandari bubu ambazo zinahatarisha uchumi wetu wa Taifa hili tatizo ni nini na kwenyewe mtasema tatizo ni Corona?

(iii) Kushindwa kufunga Bandari bubu tatizo ni Corona kushindwa kurasimisha hizi bandari tatizo ni Corona? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lipo tatizo jingine la nne ambalo shehena za nguo zinapoingia hapa nchini zinapimwa kwa kutumia urefu tunakokotoa kodi kwa kutumia urefu mfumo huu wa kukokotoa kodi kwa kutumia urefu kwanza, hauwezi kuhakiki inabidi ukubaliane na kile kilichoandikwa na yule aliyeingiza mzigo. Sasa kama ndio tunatoza kodi kwa kutumia urefu uwezekano ni mkubwa sana wa kufanya under declaration kwa wale watu ambao wanaingiza mizigo mizigo hiyo ya nguo hapa nchini. Na wanapofanya under declaration maana yake ni nini, maana yake tutakosa kodi kwa sababu hatuwezi kupata kodi sahihi katika eneo sahihi.

Mheshimiwa Spika, na vile vile maana yake watakapoingiza nguo hapa viwanda vyetu vya nguo haviwezi ku-survivor viwanda vyetu vya nguo vitakufa Serikali imekosa mapato, ajira za watanzania zimeuwawa, lakini pia hata mapato ya Serikali na yenyewe hayawezi kupatikana na ajira zenyewe zitaendele kufungwa. Na hili jambo limelalamikiwa muda mrefu kwanini halishughulikiwi na kwenyewe tutasema tumeshindwa kukusanya mapato kwasababu ya Corona. (Makofi)

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Spika, Taarifa!

SPIKA:Taarifa, endelea.

T A A R I F A

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimwa Spika, napenda kumpa taarifa mzungumzaji ndugu yangu kwamba anachokisema kuhusu sababu zinazopelekea kuanguka kwa makusanyo tuhoji kama ni Corona tu ama kuna lingine kwa sababu mwaka jana mpaka mwisho wa mwaka Tanzania ndio nchi pekee ambayo ilikuwa ina uchumi chanya kati ya nchi zote nane zinazoizunguka, kwa hiyo, lazima kipo kitu kingine zaidi ya Corona, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Unaipokea hiyo taarifa?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ninaipokea vizuri kabisa, na niseme katika hili suala hili ninalolizungumzia hili la shehena za mizigo kwamba tunaweza tu kupima hizi shehena kwanini zisipimwe kwa uzito ambapo hakuna namna yeyote ile ya kukwepa sasa huwezi ukachukua zile kanga ukaanza kupima zile mita kujiridhisha matokeo yake tunaibiwa sana, tunapigwa sana kwenye eneo hili? Marekebisho haya kwanini hayafanyiki? Kwanini Wizara ya Fedha haibadilishi utaratibu huu kwanini TRA hawabadilishi utaratibu huu.

Mheshimiwa Spika, marekebisho haya kwanini hayafanyiki? Kwanini Wizara ya Fedha haibadilishi utaratibu huu, kwanini TRA hawabadilishi utaratibu huu?

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni baadhi ya taasisi zetu zinazokusanya mapato kuna mashirika ambayo yanakusanya mapato mengi sana sasa hivi, kwa mfano, wanapokusanya mapato wanapata mpaka mapato ya ziada mapato ya ziada haya maana yake nini? Mapato ya ziada ni kwamba umefanya matumizi yako yote lakini ukabakiwa na fedha hayo ndiyo mapato ya ziada ninayoyazungumza, baadhi ya taasisi zinakusanya fedha nyingi sana. Kwa mfano, TASAC katika kipindi cha mwaka 2017/2018 mpaka 2019/2020 walikusanya mapato ya ziada zaidi ya bilioni 119.48 lakini kilichoenda Serikalini ni bilioni 50.48, bilioni 69 zilienda wapi? TPA na wenyewe hivyo hivyo wlaikusanya mapato ya ziada bilioni 36, sasa haya ni mapato ya ziada kwamba matumizi yote umeshafanya, kila kitu ulichokipanga kwenye mwaka huo, hizi fedha ambazo hazikuwasilishwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali zilienda wapi na kwa nini Wizara ya Fedha inaruhusu haya mambo kutokea? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Msajili wa Hazina anasimamiaje hili eneo katika Taifa ambalo lina changamoto nyingi, tuna changamoto kubwa za maji, tuna changamoto kubwa za elimu, changamoto za afya madawa hamna fedha zinakusanywa zinaenda wapi, kwa nini haizendi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ziende kupangiwa matumizi Watanzania wakanufaika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ni tathmini ya matumizi ya OC, hivi tunapo bajeti kila mwaka matumizi ya OC siku zote yamekuwa kwa mwendo wa ukomo wa bajeti, mwendo wa ukomo wa bajeti wanazungumzia tu ukomo wa bajeti, kwamba mwaka huu bajeti yako imeongezeka kwa asilimia Tano imepungua kwa asilimia ngapi. Lakini huu mwenendo tutaenda nao mpaka lini? Kwa nini OC zisitolewe kwa umuhimu wa mahitaji ya kila Wizara? Matokeo yake katika hili eneo tumekuwa tukipoteza fedha nyingi sana, wizi mwingi unaandaliwa kwenye bajeti, pesa zinaandaliwa zinawekwa fungu mahsusi kwa ajili ya kuchotwa baadaye, mfano wake ndiyo hili sakata ambalo ameliibua Waziri Mkuu katika Wizara ya Fedha bilioni 1.6 zimepigwa pale na huu ni mkakati ambao umeandaliwa kuanzia kwenye bajeti hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kuliibua hili Sakata. Sakata hili mwanzo wake ni mipango ambayo imeandaliwa kutoka kwenye bajeti, fedha zimelundikwa kwenye kazi fulani, kazi ambayo haina umuhimu na mwisho wa siku ni lazima zile fedha zitumike kugawana kwa sababu njama zimefanyika kuanzia kwenye mpango wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Taifa kama hili tutaendelea kuwa na mipango ya namna hiyo mpaka lini? Kwa nini hizi OC zisipangwe kwa umuhimu wa matumizi, kwa Wizara inahitaji matumizi hayo kwa ajili ya jambo gani tunajiridhisha nacho kuliko ilivyo sasa hivi, kwamba tunazungumza tu ukomo wa bajeti basi fedha zinaidhinishwa. Tukienda kwa namna hiyo kwa Taifa changa lenye mapato madogo kama haya, tutapata matatizo makubwa sana. Wizara ya Fedha follow up yenu iko wapi? Wasimamizi wa mambo haya mko wapi katika kusimamia mambo haya mpaka yaendelee kutokea katika Taifa hili changa ambalo tunamahitaji makubwa ya kitaifa lakini fedha zinagawanwa tu?(Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine la mwisho ni kwamba hata taarifa zetu za mapato zinapowasilishwa kwa nini taarifa zinazowasilishwa za mapato kila zikiwasilishwa zinawasilishwa za TRA tu. Kwa nini taasisi zingine mapato yake haya wasilishwi kwa mwezi? Kwa nini taasisi zingine na Wizara zinazokusanya mapato yake kwa nini hatuletewi mkeka wote wa wahusika wote wanaokusanya mapato yetu, tukaletewa ili kama Taifa tukawa tunajua mwenendo wetu na safari yetu tunayoenda nayo ya ukusanyaji wa mapato na hasa tukijua kwamba hakuna matumizi bila mapato na nchi haiwezi kuendeshwa bila mapato? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo eneo la ukusanyaji wa mapato ni eneo muhimu sana ambalo Taifa linatakiwa kuwekeza na kuweka kipaumbele. Wizara ya Fedha mipango yenu katika kuweka mikakati ya kuhakikisha mapato yanakusanywa iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Itifaki ya Nagoya ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo Sahihi wa Faida zitokanazo na Matumizi ya Rasilimali za Kijenetiki.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunawashukuru sana Wabunge wote waliopata nafasi ya kuchangia ambao wamechangia vizuri sana kuhusu hoja hii na bahati nzuri wote Mkataba pamoja Itifaki zote mbili zimeungwa mkono na Bunge hili na kwamba hakuna upande wowote ambao umepinga, tunaahidi kwamba yale mapendekezo waliyoyatoa Waheshimiwa Wabunge tutayazingatia katika kuhakikisha kwamba tuna usimamizi bora wa mkataba pamoja na itifaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme moja la nyongeza katika hayo kwamba Serikali hapa imelaumiwa katika kuleta nyaraka. Serikali inaonewa kwa vipi katika jambo hilo? Siyo kazi ya Serikali kugawa nyaraka Bungeni. Kazi ya Serikali tulipoingiza kazi za Serikali katika Mkutano huu wa Saba tuliainisha kazi zote na nyaraka zote tuliwasilisha.

Kwa hiyo, siyo kazi ya Serikali tena kulaumiwa kuhusu nyaraka na kwa Wabunge wanaojua kufuatilia nyaraka kama rafiki yangu hapa amekuwa akilalamika na ni mkongwe kabisa anajua, Serikali ikishaorodhesha kazi zake document zipo kwa Katibu wa Bunge. Hivyo, Serikali haihusiki tena katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoleta mikataba hii na itifaki hizi, haimaanishi kwamba Serikali haijafanya lolote katika utekelezaji wa majukumu yake. Serikali tumefanya mambo mengi katika usimamizi wa Bahari Kuu pamoja na Ukanda wa Pwani, hilo lazima lifahamike. Sheria na kanuni nyingi zimetungwa na usimamizi wa usiku na mchana kuhakikisha kwamba Ukanda wa Pwani unalindwa katika uchafuzi, unalindwa katika uharibifu wa mazingira ambayo yanaweza yakafanyika Ukanda wa Pwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi pia iongelee kuhusu baadhi ya hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge. Tumeshauriwa kwamba mali zetu zimekuwa zikiibiwa kwa utaratibu huu, wizi wa rasilimali za kijenetiki kwa mfumo wa watu wanajifanya ni watafiti na wafanyabiashara na tukaombwa kwamba tuweke mwongozo mahsusi ambao utalinda rasilimali zetu zisiweze kuporwa tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwaambia kwamba Kambi zote bahati nzuri imezungumzwa na Kamati yenyewe ya Viwanda, Biashara na Mazingira na imezungumzwa na Kambi ya Upinzani na Serikali haina tatizo katika hili. Tutaandaa mkakati mahsusi ambao unadhibiti wizi wa aina yoyote katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maisha ya Pwani yamekuwa bora vipi toka mwaka tulivyoridhia. Amezungumza Makamu Mwenyekiti wangu enzi hizo wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara kwamba wamenufaika vipi Pwani pamoja kuridhia mwaka 1996. Wamenufaika kwa mengi, moja ni kwamba miradi mingi sana inayojengwa sasa hivi tuna ujenzi wa kuta katika Pwani kwa maana ya Pangani, Rufiji, Zanzibar, Pemba na Kilimani zinajengwa. Tunapanda mikoko katika maeneo yaliyoharibiwa ya pwani, tunaanda mikoko Rufiji, Zanzibar na maeneo mengine ili kuhakikisha kwamba tunanusuru. Pia tunajenga mifereji maene ambayo yanaathiriwa na kuongezeka kwa kina cha bahari ili kuweza kuhimili pia maji ya mvua ambayo yanaleta mafuriko makubwa kwa wananchi, kama kwa rafiki yangu hapa Mheshimiwa Mtolea kule miradi mbalimbali inaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hatujakaa, tunacho chuo kikubwa sana ambacho wamekisifu sana Kamati hapa, hiki chuo chetu cha Taasisi ya Sayansi ya Bahari ambacho kinafanya kazi kubwa na kimejengwa Zanzibar kwa maana hiyo hiyo ya kuhakikisha kwamba ukanda wa pwani unalindwa kwa nguvu zote na tafiti zinapatikana kwa wakati na kutumika kwa wakati. Sio hivyo tu, tumeanzisha sheria mbalimbali nyingi za kulinda mazingira yetu katika ukanda wa bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi za tafiti zinafanya vizuri tu, COSTECH na IMS katika kuhakikisha kwamba Ukanda wa Pwani unanufaika hasa katika maeneo ya ufugaji wa samaki, mwani pamoja na mazao mengine ya bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji mmoja alisema kwamba Tanzania imegeuzwa kuwa dampo na sisi hatusimamii. Ni kweli tuna haja tu ya kuongeza usimamizi, lakini ni kweli kabisa mipaka yetu yote tunailinda, ndani ya eneo la bahari yetu tunalilinda kwa nguvu zote na taasisi za Serikali zipo kazini. NEMC, SUMATRA na TPA wapo kazini kuhakikisha kwamba kwa namna yoyote meli zinapongia ndani katika eneo letu hili udhibiti wa uchafuzi wa mazingira hauruhusiwi kwa aina yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata upande wa kemikali tupo vizuri, sawa zinaweza zikatokea kesi mbalimbali ambazo zipo hapa nchini za umwagaji wa sumu katika bahari yetu na katika kingo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa na wa kweli ni dakika saba muda mfupi. Niseme tu kwamba maelezo zaidi ya kina yatapatikana wakati wa hotuba yangu nitakayowasilisha hapa Bungeni. Sasa kwa muda huo mfupi niongelee mambo machache ambayo yanawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lililozungumzwa kubwa hasa lilihusu migogoro ya watumiaji ardhi ikiwemo mifugo pamoja na upatikanaji wa malisho kwa ajili ya wafugaji. Ilifikia hatua Waheshimiwa Wabunge wakamshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba aweze kuliingilia kati suala hili kwa sababu ni suala kubwa, wafugaji wanahangaika huku na kule kutafuta malisho, wafugaji wameingia kwenye migogoro mikubwa na watumiaji wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, narejea kusema kwamba kumekuwa na tatizo kubwa la wafugaji mahali pote ambapo wamekuwa wakilalamikiwa suala la kuingilia kwa wafugaji katika maeneo mbalimbali ya watumiaji wengine wa ardhi na kuleta adha kubwa sana kwa wafugaji katika kitendo hicho cha kukosa malisho na kutafuta maji huku na kule. Ikafika mahali Waheshimiwa Wabunge wakamuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kuingilia kati suala hili ili kuweza kutafuta suluhisho lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu tayari ameshalishughulikia suala hili kwa kiwango kikubwa. Wizara tano zilipewa jukumu la kuhakikisha kwamba zinapitia maeneo mbalimbali kuona kwamba suluhisho la migogoro, kukomesha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi kama kilimo, hifadhi na maeneo mengine na tayari Kamati hiyo imeshamaliza kazi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba mambo yaliyopendekezwa kwenye hii Kamati yatakuwa ni suluhisho kubwa la migogoro kwa wafugaji wetu; litakuwa suluhisho kubwa la migogoro ya wafugaji pamoja na watumiaji wengine wa ardhi. Upande wangu mimi yale yaliyoshauriwa kwenye Wizara yangu kuyatekeleza niseme tu hapa kwamba haitafika mwezi Desemba, 2018, nitakuwa nimemaliza mapendekezo yote ya Kamati yaliyowasilishwa kwangu kuyatekeleza, ili wafugaji hawa waweze kupata ahueni katika nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine ambalo linazungumzia sana suala la Ranchi zetu za Taifa ambazo zinamilikiwa na Shirika letu la NARCO. Ugawaji wake, jinsi ulivyogawiwa na wafugaji wengi kuendelea kukosa maeneo ya malisho.

Mheshimiwa Naibu Spika niombe tu kutoa taarifa kwamba nililiambia Bunge lako kwamba, tunafanya tathmini; tayari tathmini tumeshamaliza ya mashamba yote ya kwetu tuliyonayo, Ranchi za Taifa zote, holding grounds zote na hata LMUs zote. Tumemaliza kufanya tathmini na sasa tunaingia kwenye kupanga matumizi sahihi ya mashamba haya. Nikuhakikishie kwamba, baadhi ya wafugaji wetu wanaotangatanga huku na kule watapata maeneo ya kulishia mifugo yao katika maeneo haya katika mashamba haya ya taifa ambapo tutawaondoa wale wawekezaji ambao wamekuwa matapeli katika mashamba haya na kuweka wafugaji ambao wanahangaika huku na kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika tathmini hiyo bado tuna mashamba mengine ambayo yapo yanamilikiwa na Serikali ambayo nayo tunafikiria kwamba baadhi ya wafugaji wengi tutawaondoa katika maeneo mbalimbali na kuwaweka kwenye mashamba haya. Hivyo tatizo la malisho kwa kiwango kikubwa, tukitekeleza haya tuliyoshauriwa na Kamati, lakini na taasisi nyingine zinazohusika, kama mwenzangu wa maliasili na utalii akitekeleza na yeye yale aliyoshauriwa na Kamati tatizo la malisho kwa wafugaji wetu litapungua kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hili tatizo ambalo linani-face hapa, la muda labda nizungumzie suala lingine lilizungumzwa suala la upigaji chapa, kwamba je, katika hotuba ya Waziri Mkuu limeoekana tu suala la upigaji chapa. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wasubiri kwa sababu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi itakuja na hotuba yake hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na labda nimalizie hili suala lililozungumzwa, linalohusu, naona kengele ya kwanza, suala la uvuvi haramu. Suala la uvuvi haramu niombe jambo moja kwa Bunge hili, jambo hili ni kubwa, tunaendesha operation zaidi ya tatu za uvuvi haramu. Kuna Operation Sangara 2018, kuna Operation MAT na una Operation Jodari.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni mambo makubwa ambayo yamefanyika katika hatua za utekelezaji wa mambo haya. Kwa sababu Wabunge wengi wameonesha nia ya kutaka kuelewa jambo hili na kwa sababu Wabunge wengi wameuliza maswali mengi sana katika eneo hili, ilinilazimisha/ nililazimika; na Kamati yangu ya Maji, Kilimo na Mifugo iliniagiza kwamba nifanye semina kwa Wabunge wote ili tuweze kuelezana kwa kina nini kinachotokea katika suala la uvuvi hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu maelekezo yao waliponipa tayari nimeshaomba kibali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimeomba kibali kwa Mheshimiwa Spika, ili akubali tarehe ya 21 Aprili 2018 tuweze kutoa semina ili tuwaambie Waheshimiwa Wabunge ili tuwaambie Watanzania jinsi gani rasilimali za taifa ambavyo zimekuwa zikifujwa na watu mbalimbali wasiolitakia mema taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme yapo mambo ambayo yameshauriwa na Wabunge ambayo ni madogo ya uboreshaji. Mimi yale sina tatizo katika uboreshaji na ndiyo maana hata katika lile Bunge nilisema kwamba Mbunge yeyote mwenye hoja yoyote, mwenye ushahidi wowote atuletee sisi ili tuweze kuchukua hatua.

Naomba kutoa taarifa kwamba tayari tumeshasimamisha kazi watumishi tisa ambao walihusika kwa namna ile au nyingine katika kuhujumu zoezi hili, katika kujinufaisha binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile kuna mambo yalijitokeza ikafikia wananchi kwamba, hata wanapotaka kubeba samaki wao tu wa kula nyumbani, ka-box kake ka samaki 10, samaki watano wanazuiliwa kwamba hairuhusiwi kisheria, hapana. Nimekataa na nimetoa maelekezo kwa watendaji wote wa Serikali lazima wajue kwamba samaki hawa lazima watasafirishwa kwa njia ya usafiri kuwafikia walaji. Na hili haliwezi kuendelea kutokea.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kamba, tayari tumeshatoa maelekezo mambo haya yanafanyika, sasa hakuna tena kuzuiliwa wananchi kusafirisha samaki kwa ajili ya kitoweo. Hata hivyo hii isigeuzwe tena ikawa loop hole ya watu kutumia mabasi ya abiria kwa ajili ya kufanya biashara.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa nami nijumuike katika kuchangia hii hotuba ya Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nami nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anayoifanya kwa Watanzania. Jana tumeona alivyoenda kuzindua kile Kiwanda cha Kusafisha Madini kule Mwanza. Tumeona jinsi anavyoenda kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya kile kipande cha Mwanza – Isaka. Kwa hiyo, hii ni kazi nzuri sana ambayo Mheshimiwa Rais wetu ameendelea kuifanya na kuendelea kufuata nyayo vizuri sana za mtangulizi wake bulldozer, Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri pia kwa kutuwasilishia hotuba hii nzuri ya bajeti ambayo tutaendelea kuijadili hapa na kushauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na neo la mapato. Mapato unaweza kuyaongeza kwa njia tatu au zaidi ya hizo. Moja, kwa kutumia ukuaji wa uchumi wa Taifa mapato yanaweza kuongezeka; pili, kwa kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato pamoja na kuimarisha zile njia zako unazotumia kukusanya mapato; na tatu, kutunga vyanzo vipya vya mapato. Hivi vyote kwa pamoja vinaweza kuongeza mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na hili moja ambalo nadhani Mheshimiwa Mwakagenda alilizungumza hapa kwamba, kwa nini tunajiuliza kuhusu ile Mahakama ya Rufaa pamoja na Baraza la Rufaa la Kodi pamoja na Bodi ya Rufaa za Kodi, hizi zote zimeshikilia kesi zaidi ya 1,097 ambazo zinaendelea kule na zina hiyo shilingi trilioni 360 na Dola za Marekani milioni 181.4. Mheshimiwa Waziri, kuna shida gani kuimarisha Mahakama zetu za Rufaa, kuimarisha Bodi ya Rufaa ya Kodi, kuimarisha Baraza la Kodi la Rufaa ili hizi kesi zote ziende zikaamuliwe?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kwenye bajeti yako umesema kwamba kuna kesi mpya zilizoingia 653 zenye thamani ya shilingi trilioni 2.7. Kwa nini tusiimarishe hizi kesi zikawa zinaamuliwa kwa wakati tukapata mapato? Hapa tunaweza tukakusanya mapato mengi sana ya Serikali. Hatuhitaji kwenda hata kwenye kodi mpya, hizi tu zenyewe katika hili eneo Mheshimiwa Waziri kama tunaweza tukawezesha haya Mabaraza na hizi Bodi kuamua hizi kesi kwa wakati. Kwa sababu yawezekana tu tukawa na upungufu wa Majaji, upungufu wa watendaji, upungufu wa rasilimali fedha. Kwa nini tusipeleke fedha nyingi pale ili hizi kesi zikaamuliwa kwa wakati na mapato haya yaweze kupatikana Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni ukaguzi dhaifu unaofanywa kwenye miamala ya transfer pricing. Miamala hii ya transfer pricing katika nchi yetu tuna kampuni kubwa za Kimataifa 504. MNCE’s ziko 504. Katika 504 tunakagua makampuni matano tu kwa mwaka average ya makampuni matano na miamala sita na haya makampuni yana fedha nyingi sana ambapo nyingine zinapopitia katika utaratibu wa miamala ya transfer pricing, Serikali yetu inapoteza mapato mengi sana. Kwa mfano, katika makampuni 20 tu yaliyokaguliwa yalikuwa na mzunguko wa fedha wa shilingi trilioni 4.2 na kodi iliyokaguliwa ni shilingi bilioni 152 katika lile eneo. Just makampuni 20 yaliyofanyiwa ukaguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukienda namna hiyo, kwa mantiki hiyo hiyo, maana yake sasa, kama tutayakagua makampuni yote 504 kwa mwaka, tunategemea kwamba tutapata mzunguko wa fedha zaidi ya shilingi trilioni 105 na tunategemea kodi zaidi ya shilingi trilioni nne katika lile eneo. Tatizo ni kwamba watu wetu wa TRA na hicho kitengo chetu cha ITU, (International Tax Unit) hakijawezeshwa kikamilifu kufanya haya majukumu na matokeo yake hili eneo la transfer pricing tunaendelea kupigwa katika hili eneo. Taifa linaendelea kupoteza mabilioni ya fedha katika hili eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, akiwekeza nguvu zake katika hili eneo, tutakusanya matrilioni ya fedha. Hapa tunaweza kukusanya shilingi trilioni nne na zaidi katika hili eneo, lakini ni fedha ambazo hatuzikusanyi na tunapigwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tunaweza kukusanya mapato ni maeneo tu hayo mengine kama kuziba mianya hiyo kama ya Bandari bubu, ukokotoaji sahihi wa kodi tunaoweza kuufanya katika maeneo; na katika eneo hili peke yake kama tunaweza kufanya vizuri sana, tunaweza kuongeza mapato mpaka shilingi trilioni 4.71.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mkataba wa ETS ambao unatumika kukusanya kodi za ushuru wa bidhaa. Mkataba huu umeingiwa tofauti na mikataba mingine. Kwanza, ni mkataba wenye bei kubwa sana, una gharama kubwa sana. Wananchi wanaingia gharama kubwa sana lakini hautoi gawio lolote lile kwa Serikali. Huyu anakusanya fedha zake anakwenda; na sasa hivi haijaelezwa uwekezaji wake ni shilingi ngapi? Haijaelezwa pia hata yeye analipwa shilingi ngapi kwa mwaka? Sasa kutokana na utata huu, kwanza mkataba huu ni lazima uchunguzwe vizuri ili kuona na kuweka uwazi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili mapato yanayopatikana tugawane kama tunavyogawana kwenye mtambo wa TTMS, kwa nini TTMS, kule TCRA tunagawana asilimia 50 kwa 50? Mwekezaji anapata 50 na Serikali inapata
50. Katika huu mtambo wa ETS ambao ni ubia kati ya TRA na kampuni ya CISPA hatupati chochote kama Serikali; na tukigawana hapa tunaweza kupata mapato ya karibia shilingi bilioni 150 kwa fedha anazozipata sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Msajili wa Hazina tunaweza kufanya maboresho madogo tu tukapata fedha nyingi sana. Tuna kampuni nyingi na mashirika mengi sasa hivi ambayo yamekuwa parasite kwenye Taifa ambayo tunalazimika kuyawezesha fedha kila leo badala ya yenyewe kutoa fedha kwa Serikali. Mashirika haya, yanahitaji mtaji tu. Yakipewa mtaji na Serikali yanaweza kutoa gawio kubwa sana kwa Serikali. Sasa hivi tunakusanya mapato kidogo sana na mwaka huu yameshuka kwa zaidi ya shilingi bilioni 81. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa ardhi hivyo hivyo. Ardhi tuna fedha nyingi kule. Sasa hivi kwa mujibu wa Taarifa ya CAG ana malimbikizo ya shilingi bilioni 61, hatujajua tatizo ni nini kule kwenye ukusanyaji? Huyu naye akiwezeshwa fedha, tunaweza kuongeza mapato. Haya maeneo tunaweza kuongeza mapato hata tukafikia mpaka shilingi bilioni mpya kutoka kwenye kiwango Mheshimiwa Waziri alivyokisia, shilingi bilioni 260 tunaweza tukafikia mpaka hata kwenye shilingi bilioni 300 na zaidi kwenye hili eneo tu la ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye madini na kwenyewe kuna shida kwa sababu masoko yale 39 tuliyoyafungua na vituo vya kuuzia madini 50 vinafanya kazi siku za kazi tu, lakini siku za weekend hazifanyi kazi na kutusababishia kupoteza mapato mengi. Hili eneo pia tunaweza kuongeza mapato mengi. Katika hili eneo tu kwa hesabu zangu nimepata shilingi trilioni 7.1 ambazo zinaweza zikapatikana nje ya bajeti ya Serikali iliyotengwa. Shilingi trilioni 7.1 tunaweza kuzipata tukienda kuimarisha haya maeneo ambayo nimejaribu kuyataja katika huu muda mfupi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la kufanya marekebisho ya Kanuni Na. 15 ya ukokotoaji wa kodi za Kimataifa (transfer pricing) ambapo Waziri anapendekeza kuondoa faini ya asilimia 100 katika miamala ya transfer pricing. Mheshimiwa Waziri, ukifanya hili kosa la kuondoa hiyo faini, nchi yetu utakuwa umeiingiza kwenye mtego wa kupigwa kila siku. Ni bora ukasema unataka upunguze adhabu ili kuongeza compliance, lakini ukisema hawa ma- tycoon hawa ambao wanafanya biashara kubwa na ziko organized na wanahamisha faida kutoka nchini na kuzihamisha kupeleka nchini kwao, unasema wakifanya miamala yao hiyo ya wizi halafu then fine yao ikaondolewa, tutapigwa na hakuna duniani kote ambako sasa hivi wanaweza kuikubali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata best practice duniani kote, kwa sababu upigaji mkubwa na wizi mkubwa wa kodi sasa hivi uko kwenye eneo la transfer pricing. Ni lazima tukawekeza vizuri kuhakikisha kwamba tunawabana ili kila mtu alipe katika hii miamala. Tuhakikishe kwamba ukaguzi wa kampuni zote 504 unafanyika ili Serikali yetu iendelee kupata fedha zinazostahili. Tukifanya hivyo, mapato ya Serikali tutakuwa tumeyaongeza kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa. Nami nijumuike na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Tulimwona alipokuwa kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, tumemwona alipokuwa kwenye Mkutano wa Mazingira wa Mabadiliko ya Tabianchi huko Duniani na hotuba alizozitoa ambazo kwa kweli zilikuwa na mvuto mkubwa na msisimko mkubwa. Hakika analitendea haki Taifa lake na aendelee kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango hii kama ingekuwa tunafika mahali tunaweza tu kuwa kwenye mipango muda wote; na hata yale tunayoyazungumza wakati mwingine yasipate muda wa kufanyiwa kazi; tulizungumza mengi sana wakati tunapitisha bajeti ya mwaka huu. Nami naamini kama yale tuliyoyazungumza wakati huo kama kuishauri Serikali yangezingatiwa kwenye huu Mpango tuliowasilishiwa, leo hii tusingekuwa na maneno mengi hivi ya kusema. Hayo tuliyoyazungumza na ushauri wote tuliousema, hatuyaoni kwenye Mpango, sasa tutashauri mpaka lini ili tuweze kusikilizwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauri mengi sana kuhusu ajira za vijana wetu, zinapatikanaje? Tulishauri mengi sana kuhusu sekta binafsi, kuhusu mapato ya Serikali na kuhusu kuumaliza umasikini Tanzania. Vile vile ukipitia Mpango huoni ni wapi sasa ambapo maoni yetu yamezingatiwa. Nami nianze moja kwa moja na hili eneo la ugharamiaji wa Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Hotuba ya Mapendekezo ya Mpango wa Bajeti uliowasilishwa na Waziri, sehemu kubwa inazungumzia tu matumizi, lakini ni namna gani haya mapato tutayapata kwa ajili ya kugharamia Mpango wenyewe? Huoni wapi yameelezwa. Unaona jitihada tu zilizozungumzwa, tutahamasisha matumizi ya Tehama, tutahamasisha hiki, tutahamasisha hiki. Ni mambo ambayo yamekuwa yakirudiwa kila mwaka na ni ya ku-copy na ku-paste.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo changamoto kubwa sana kwenye ukusanyaji wa mapato ambazo zingeweza kufanyiwa utaratibu na tukatoka hapa tulipo. Kwa mfano, hivi ni utafiti gani tunaoufanya? Kila mwaka huwa tunafanya utafiti kweli? Kwa nini huu Mpango usituambie tunafanya utafiti gani kufikia ukusanyaji wa mapato yetu? Vyanzo vyetu vya mapato tunavifanyia utafiti? Hao TRA wanapofanya ukusanyaji wa mapato, tunawachunguza namna gani uwezo wao wa kuweza kukusanya mapato yetu na tunachukua hatua gani? Sasa unakuta mwisho wa siku mnaingia kwenye bajeti mnasema tu, hili limesamehewa, hiki kimetozwa, hii tozo tumeongeza; na mfano upo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka 2020 hapa kwa sababu ya sisi wenyewe kutokuwa na utafiti wa kutosha katika mapato yetu, tumekuwa tukiingia kwenye mgogoro mkubwa sana. Tumeingia kwenye mgogoro mkubwa kwenye tozo za simu. Tumebishana hapa, tukatoka tulivyotoka, tumefika mahali tumerekebisha wenyewe viwango vya tozo vya miamala ya simu vilivyokuwa vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda na withholding tax tukawaambia watu kwamba tunataka kuweka withholding tax kwenye mazao ya 2%, halafu tukaenda kusamehe wanywa bia kwamba wasilipe kodi ili zao la shayiri liweze kuzaishwa. Wakati huo unamsamehe mnywa bia ili kilimo kiongezeke, halafu unaenda kumtoza anayelima shayiri yenyewe. Sasa unaenda kutoza withholding tax 2% huku ukijua kuna Service Levy 3%. Huyo mkulima atalimaje? Matokeo yake najua, watakuja kufanya marekebisho hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda kwenye mafuta, nako hivyo hivyo, tulisema yanaweza kua-attract inflation, hata kama tuna nia hiyo njema, Serikali imefanya marekebisho katikati ya safari. Hii yote ni uthibitisho kwamba tunaibuka na mabadiliko ya kodi bila ya kufanya utafiri wowote. Kwa nini hatufanyi utafiti? Kwa nini hatuwekezi? Kwa nini suala hili la mapato limekuwa la siri siri tu, halafu linakuja kuibuka hivi, hakuna mafanikio ambayo tunaweza kufika nayo popote? Hata hivyo Mpango hauzungumzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema hapa Wabunge, tunazo shilingi trilioni 360 zimeshikiliwa na Mahakama, uamuzi haujatoka. Nilitegemea kwenye Mpango hapa isemwe kwamba hizo shilingi trilioni zetu 360 ziko wapi? Leo hapa Bunge zima linapiga makofi kwa shilingi trilioni 1.3 tulizopewa na IMF. Fedha ndogo shilingi trilioni 1.3 tunapiga makofi mpaka mikono inauma; na kwa kweli tunashukuru kwa hilo, lakini tuna shilingi bilioni 360 za kwetu, hata kama ni asilimia 10 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 10 ya shilingi trilioni 360 ni shilingi trilioni 3.6. Bado hilo kwetu halijatuuma, Bunge halijaumia, Serikali haijaumia. Fedha zimeshikiliwa tu kwa maamuzi tu ya Mahakama. Kama tatizo ni hizo bodi zetu za rufaa za kodi zina shida na wataalamu, si tuajiri wataalamu hata wa kutoka mpaka nje kama ni wataalamu? Ni nini kinachosababisha? Mpango haujazungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la transfer pricing nalo tulilisema. Tunayo makampuni 504 yenye miamala zaidi ya shilingi trilioni 105 kwa mwaka. Uwezo wa TRA kuyakagua makampuni haya ni asilimia moja. Hawana wataalamu, hawana fedha na hawawezi kukagua na hivyo hatuwezi kupata kodi katika maeneo hayo. Fedha nyingi za Watanzania zinapotea, matrilioni ya fedha. Makampuni 504 unakagua asilimia moja kwa mwaka, unapata nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote kwetu sisi, mipango yetu hatuoni kama ni shida, lakini tukiletewa hata shilingi bilioni tano hapa tunafurahi kweli kweli, lakini fedha zetu zimeshikiliwa na watu, hatupati hasira katika hili. Nilitegemea hata mikataba mibovu ya akina SICPA na TRA ingezungumzwa humu kwamba tunaenda kuifuta mara moja. Mikataba ya kinyonyaji ambayo inanyonya fedha za Watanzania tungeweza kuifuta tukapata mapato mengi tu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaye TR, anasimamia Mashirika ya Umma 237, makampuni haya yamekuwa mzigo mkubwa kwa Serikali, yanategemea ruzuku kutoka kwa Serikalini. Tumeshindwa kuyawezesha kuyapa fedha, hayana mtaji, yapo tu, hayatekelezi majukumu yake sawa sawa. Kwa nini Mpango hauzungumzi juu ya Mashirika yetu ya Umma, kuyapatia mtaji yaweze kufanya biashara tuweze kupata gawio kubwa la Serikali na hela tunazozipeleka kwa ajili ya ruzuku zifanye mambo mengine? Ila kwetu sisi tunaona hii ni sawa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu TR leo, Msajili wetu wa Hazina ana uwezo wa kuyasimamia makampuni haya kwa asilimia 13 tu. Hana fedha, hana wataalamu, lakini kwetu sisi tunaona kukaa na kupanga tu ni sawa, lakini upembuzi wa matatizo haya yanayotukabili hatuyafanyii kazi. Tatizo letu lipo wapi?

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Amos Bulaya.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwa mchango wake mzuri kwamba, ni kweli Serikali mbali ya kutoa ruzuku, inashindwa kutoa mtaji kwa mashirika yake ili yaweze kufanya vizuri. Mfano Shirika la TTCL, linahitaji mtaji wa shilingi bilion 300 ili liweze ku-compete na Voda na Airtel, lakini mpaka sasa hivi wameshindwa na shirika haliko kwenye hali nzuri kama ilivyo mwanzo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, unapokea taarifa hiyo?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea sana taarifa ya dada yangu na ninamkubali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna maeneo mengi, kuna utoroshaji mkubwa tu wa fedha, utoroshaji mkubwa sana. Ukienda mipakani mle madini yetu bado yanatoroshwa, mazao yetu ya uvuvi bado yanatoroshwa, mifugo yetu bado inatoroshwa, misitu na hata wanyamapori bado wanatoroshwa. Mpango unatueleza nini? Unaenda kudhibiti namna gani maeneo haya ili tuweze kupata mapato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuangalia hapa sasa hivi, tunazungumza kwenye Mpango huu, kwa mwaka unaokuja wa fedha, mapato yetu tunayotegemea kuongezeka ni shilingi trilioni 1.16 peke yake. Ila ukiangalia hiyo shilingi trilioni 1.1 wanaipata wapi? Hilo ongezeko wanalipata wapi? Wanaserma mapato yataongezeka kwa asilimia 7.6, lakini 7.6 wameipataje wakati uchumi utakua kwa 5.2%, mfumuko wa bei utaifikia kwenye 4%, tayari ni 9.2%, bado kuna kuongezeka kwa tozo, tunakuja na kodi mpya ambayo ni walau 1%, tunapata 10.2%, bado kuna uthibiti wa upotevu wa mapato kama huu atunaouzungumza. Kukishaweka mikakati kama hiyo, nayo kuna asilimia kama moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaweza ukakuta mapato yetu yakaweza kukua hata kwa 12%, kama tungekuwa tunafanya utafiti wa kutosha kuhusu mapato yetu; lakini hapa tunafika tu tunasema mapato yataongezeka kwa shilingi trilioni 1.2, halafu yanatokana na nini? Kwa hiyo, wakusanyaji nao wanaenda kiuzembe kukusanya, wanashindwa hata kushughulikia fedha hizi ambazo zipo, ni za kuchukua tu kwa sababu sisi Bunge tumewaidhinishia makadirio madogo. Sasa tutabaki hapa mpaka lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kuhusu ushiriki wa sekta binafsi. Hatuwezi kukua kama ushiriki wa sekta binafsi tunaenda nao namna hii na kama sekta binafsi itaendelea kudhulumiwa namna hii. Sekta binafasi, kwa mfano taarifa zetu za madeni, watu wa sekta binafasi walikuwa wanatudai shilingi trilioni 3.8 tulipoanza uhakiki mwaka 2015/2016, lakini ikaja kugundulika kwamba shilingi trilioni 1.16 ni malipo ambayo siyo halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kuhusu ushiriki wa sekta binafsi. Hatuwezi kukua kama ushiriki wa sekta binafsi tunaenda nao namna hii, kama sekta binafsi itaendelea kudhulumiwa namna hii. Sekta binafsi ambapo kwa mfano taarifa zetu za madeni, watu wa sekta binafsi walikuwa wanatudai trilioni 3.8 tulipoanza uhakiki mwaka 2015/2016, ikaja kugundulika kwamba trilioni 1.16 ni malipo ambayo siyo halali. Kwa hiyo, karibia asilimia 30 ya malipo hayo siyo halali. Inayosema siyo halali ni Serikali siyo wananchi waliokopwa. Hii ni dhuluma kwa sababu wewe unakuja kuhakiki huku deni langu nilishakupa service, ukapata service hiyo halafu unakuja kusema hili deni asilimia 30 walioingia madeni hao ni akina nani, waliruhusiwa na nani na wamechukuliwa hatua gani waliodanganya hilo? Mnaenda kuwaadhibu hawa wananchi ambao ni haki yao, kumdhulumu mtu kwa fedha au kwa mali ulioichukua ni sawasawa na ujambazi mwingine tu. Kwanini, Serikali ijihusishe kwenye ujambazi wa namna hiyo? (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mpina.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii ambayo umenipatia na mimi niweze kuchangia hii taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo na mwanzo kabisa nimeshindwa kujizuia kuwapongeza sana Kamati hii ya Sheria Ndogo kwa uchambuzi wao mzuri sana wa hizi sheria na kasoro zilizokuwepo pamoja na mapendekezo ambayo wameyapendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo imeelezwa hapa na Kamati kwamba hili suala la sheria ndogo ni suala ambalo ni muhimu sana, ni suala ambalo kama lisiposimamiwa vizuri linaweza kwenda kupoteza hata maana ya sheria zenyewe ambazo zilitungwa na kupitishwa na Bunge hili tukufu. Sasa tusipoliwekea maanani na msimamo mzuri kuanzia kwenye mfumo wa utungaji wake na mpaka utekelezaji wake, tunaweza tukawa tunapiga mark time kila wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri sana kamati hapa imefanya uchambuzi na imefanya uchumbuzi wa sheria wa kanuni kama 14 lakini ukweli ni kwamba sheria ambazo zina changamoto nyingi, ni nyingi sana kwa hiyo hizo ni 14 ni sehemu ndogo sana ya kanuni ambazo zina kasoro na zinazohitaji marekebisho. Kwa hiyo, ina maana kwamba hii Kamati ya Sheria Ndogo pamoja na kazi nzuri sana ya kufanya uchambuzi wa kanuni 14 katika taarifa hii lakini bado wana kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba zile kanuni zote zenye changamoto ambazo zinaleta mkanganyiko mkubwa kwa wananchi katika utekelezaji wake zinashughulikiwa na zenyewe zinafanyiwa uchambuzi na kuletwa hapa Bungeni kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nakubaliana nao, kwa mfano wametolea mfano kukinzana na masharti ya sheria inayotoa mamlaka ya kutunga sheria ndogo na sheria nyingine za nchi. Hizi tunazo nyingi sana na bahati mbaya sana Kamati wao wamezungumzia suala la sheria ndogo tu lakini kuna waraka nao ambao ukiandikwa na Katibu Mkuu, kuna waraka nao ukiandikwa na Waziri unaenda kutumika na wenyewe kama sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hizi sheria ndogo pamoja na waraka zinapoenda kule zinaenda kwenda ku-distort au kuharibu kabisa hata mifumo ya sheria ambayo ilishawekwa na zingine zimekuwa zikienda hata tofauti kabisa na sheria zenyewe zilizopo sasa kwa mfano kipindi cha UVIKO - 19 tunatekeleza miradi ya UVIKO-19 kuna baadhi ya taasisi hapa ziliandikia taasisi nunuzi barua za kuwataka wakafanye manunuzi kwenye viwanda fulani kwa kuvitaja kwa jina na hayo yalifanyika huku wakijua Sheria ya Manunuzi hairuhusu hilo hayo yalifanyika huku wakijua Sheria ya Ushindani Na. 8 ya mwaka 2003 hairuhusu hilo, lakini yalifanyika na sheria zipo, kuja huku kwenye waraka wakaandikiwa barua ya waraka wahusika wafanye manunuzi katika maeneo hayo, kuja huku ikatekelezwa hivyo hivyo ilivyotekelezwa kinyume cha sheria na kinyume cha utaratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pale Mvomero kuna kijiji kimoja katika Wilaya ya Mvomero wametunga sheria kwamba mifugo hairuhusiwi kuwepo kwenye kijiji hicho huku wakijua wananchi wanayo ruksa kwa mujibu wa Katiba ya nchi kufanya shughuli za kiuchumi zozote wanazozitaka. Sasa unatunga sheria inasema kwenye kijiji husika hakuna mfugaji kuingia, inatungwa, kanuni inafanya kazi ya muda mrefu na watu wamekuwa wakipigwa faini ya mamilioni ya fedha wakiingiza mifugo kwenye eneo hilo, jambo ambalo linakiuka Katiba, jambo ambalo ni uonevu na manyanyaso kwa wananchi wasiokuwa na hatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kanuni hizi ndogo ndio zimetufikisha kwenye kasoro nyingi, mrundikano wa tozo na kodi nyingi katika eneo moja zinatungwa kila taasisi inatunga, TBS anatunga, TMDA anatunga na taasisi zingine zenyewe zinatunga kwenda kusimamia jambo moja, kijiji kina kodi eneo husika, halmashauri ina kodi kwenye eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka zingine zinazosimamia NEMC mlolongo huu wote umetufikisha hapa katika mfumo mzima wa utungwaji wa hizi kanuni na sheria zetu ndogo.

Sasa nasema nini; mfumo wa utungaji wa hizi sheria ni bora tuanzie pale, mfumo wa utungaji wa kanuni za hizi sheria ndogo ukoje utaratibu wa sasa sheria hizi kanuni ndogo hizi zinatungwa na taasisi kwa mfano Serikali ya Kijiji, Halmashauri ya Kijiji, lakini na Waziri kutunga sheria ya utekelezaji wa baadhi wa sheria, na anapomaliza kutunga na ana-gazette kwenye Gazeti la Serikali na baada ya kuwa gazetted kwenye Gazeti ya Serikali ndio Kamati yetu ndogo inarudi kuzipitia na kubaini kasoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nauliza leo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bunge hili na wewe mwenyewe Naibu Spika, kwani kuna shida gani hizi kanuni ndogo zikafanyiwa mapitio na Kamati yetu ndogo ya Sheria Ndogo kabla hazijaenda kuwa gazetted kwenye Gazeti la Serikali ili changamoto leo tunazojiuliza leo ziwe zimeshapata oversight mapema kabla hazijaenda kwenye utekelezaji wa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hapa imezungumza na sisi wote ni mashahidi kwamba hizi sheria ndogo zimeenda ku-distort hata sheria yenyewe iliyotungwa, zimeenda kufifisha sheria yenyewe, nguvu ya sheria imeenda kufifishwa kwa kutunga sheria ndogo, lakini pia zimeenda kutungwa hata sheria ndogo ambazo ni kinzani na hata ile sheria mama, na kwa kufanya hivyo wananchi wengi wamepata mateso makubwa kwa sababu wameenda kuadhibiwa kwa kosa ambalo hata linakinzana na sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia inazuia hata utekelezaji wa sheria yenyewe lakini Serikali tumekuwa tukishindwa kesi nyingi sana Mahakamani kutokana na haya, ukienda kutafsiriwa sheria Mahakamani vs hatua iliyochukuliwa kwa kanuni kwa sheria ndogo Serikali inatangazwa kushindwa wakati mwingine tunafidia mabilioni ya fedha kwa hizo technical zilizofanyika katika utungaji na uchukuaji wa hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hiyo lakini pia tumeelezwa hapa hata inapotekea kasoro kurekebishwa hazirekebishwi kwa wakati, sheria ndogo ina kasoro, Kamati imeita mamlaka husika, wamekaa nayo, wamezungumza na wamekubaliana, lakini miezi minne tunaambiwa na Kamati hakuna marekebisho, hayafanyiki, inachukua muda mrefu kufanya marekebisho. Sasa kama haya yote yanafanyika na tunaenda kuwaadhibu wananchi wasiokuwa na hatia na tunaenda kuiingiza Serikali hasara kubwa kwa nini hizi sheria ndogo Bunge hili likakasimu madaraka, kwa hiyo Kamati ya Sheria Ndogo kushughulika na hizi sheria ndogo kabla hazijaenda kwenye utekelezaji ili kuweza kuepuka hizi hasara ambazo tunawezakuwa tunazipitia za kunyika haki watu, lakini pia za kuleta mkanganyiko hata tafsiri ya sheria Mahakamani na kusababisha wakati mwingine watu wengine kukosa haki na kusababisha hata Serikali yenyewe kushindwa baadhi ya kesi mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili tusipofanya maamuzi ya namna hiyo ninajua kwamba sheria ndogo hizi hata wakati mwingine kwa mfano kuna mambo tunapitisha humu kama Bunge na mnayapitisha mpaka kwenye bajeti, mnayaweka mpaka kwenye bajeti, halafu baadaye inaamuriwa kwamba kuna maeneo ya sheria ambayo yanarusu Waziri ataenda kutunga sheria ndogo kule, mwisho wa siku Waziri huyo huyo anaenda kufuta baadhi ya hata ya tozo ambazo mlikubaliana humu Bungeni kwa mamlaka hayo aliyonayo kupitia hiyo sheria ndogo bila hata consultation ya Bunge mambo ambayo yanaenda hata kuathiri bajeti yenyewe iliyopitishwa na Bunge, mambo ambayo yanaenda kuleta hasara kubwa kwenye Taifa na mkanganyiko mkubwa wa mhimili wa Bunge pamoja na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ambalo ninaomba Kamati ya Sheria Ndogo ikaliangalie ni utekelezaji wa force account. Suala hili la utekelezaji wa force account sasa hivi lina changamoto kubwa, leo hii mradi unapelekwa kwenye shule husika wa madarasa, mwalimu mkuu wa shule hiyo na mwalimu mwingine kila leo mguu na njia kwenda kufanya manunuzi, hawafundishi watoto wapo safari na njia kwenda kufanya manunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kwa madaktari zahanati ni moja, mnajenga pale nyumba ya mtumishi, daktari wa eneo hilo kila siku anaenda kwenye manunuzi, akileta mbao leo anaambiwa rangi imeisha, akimaliza kuleta rangi anaambiwa cement imeisha, kila leo yuko safari. Madaktari wetu wagonjwa wetu awatibiwi kwa sababu madaktari wameshapewa kazi nyingine ya manunuzi, kazi nyingine ya kusimamia ujenzi badala ya kazi ambazo husika walizopewa kuzisimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kanuni ya sheria ya manunuzi ambayo ndio ina utekelezaji wa force account ni muhimu sana iende ikatizamwe upya, lakini hili suala la force account linatuletea hasara nyingi. Leo hii mradi ukiwa unatekelezwa kwa sababu unasimamiwa na watumishi wa umma maana yake kama ni kwenye halmashauri Mkurugenzi mguu na njia anaenda kuukagua mradi huo, engineer mguu na njia anaenda kukagua mradi huo, Afisa Elimu kama ni wa elimu mguu na njia kila siku anaenda kukuagua mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo watumishi karibu halmashauri nzima yote wako barabarani na jana Waziri wa Fedha ametuthibitishia hapa kwamba sasa hivi kuna gharama kubwa sana ya matumizi ya force account kwa sababu ina involve usimamizi wa watu wengi mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninyi mnasema mmepunguza gharama, lakini ukweli kwamba hakuna miradi yenye gharama kubwa kama ya force account na inakwepa vitu vingi kwenye force account tunajinyima sisi wenyewe kwa sababu hata VAT hatulipi, kama angekuwa contractor pale hata kama ni mdogo namna gani angelipa VAT. Lakini sisi tunajidanganya, mradi umetekelezwa kwa fedha ndogo kwa sababu tumekwepa kulipa kodi sisi tunajidanganya mradi umetekelezwa kwa fedha ndogo lakini ukichukulia fedha ya mafuta, ya madiwani kwenda kukagua mradi huo, Mkurugenzi Injinia, Afisa Elimu sijui nani gharama zake ni kubwa mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini na hasara nyingine pale inapotokea sasa mradi umejengwa chini ya viwango, nani anakamatwa sasa, nani analipia kama ni mkandarasi tungeweza kumwambia mkandarasi kwamba mradi huu aurudie, abomoe na ajenge upya. Sasa leo umejengwa kwa force account, baada ya mwaka mmoja jengo limebomoka, tunaenda kumkamata nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, tukamkamate Mkurugenzi Mtendaji, tukamkamate Mganga, tukamkamate nani inahusisha mlolongo mkubwa wa watumishi wa Serikali inahusisha mlolongo mkubwa wa wananchi katika jamii husika. Tunaenda kumkamata nani?

Sasa mimi niombe sana hizi kanuni zilianzishwa kwanza Kamati yetu ya Sheria Ndogo ikajiridhishe na matakwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa ili niweze kuchangia katika hotuba hii iliyo mbele yetu ya Bajeti Kuu ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Mpango pamoja na Naibu wake.

Mheshimiwa Spika, kwanza niungane kwa dhati kabisa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa hili katika kupigania maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nifunguke tu kwamba Bunge lako hili kabla ya mimi sijawa Waziri hapa nimepitia maeneo mengi sana na Bunge hili limenipeleka kwenye Taasisi mbalimbali kwenye Mabunge ya Afrika, nimeenda kwenye Mikutano mingi ya kikanda na ya Kimataifa sijawahi kuona Kiongozi ambaye committed kama Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Nampongeza sana kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu hii ya Tanzania katika kupigania maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nikupongeze wewe sana, moja ya sifa ya Kiongozi ni kutengeneza viongozi. Toka ulivyokuwa Mwenyekiti wa Bunge hili, baadaye ukawa Naibu Spika, baadaye ukawa Spika umetengeneza viongozi wengi sana kwenye Bunge hili. Kwa hiyo, uwezo wako siyo wa kutiliwa mashaka yoyote na mtu yeyote anayejua historia na mimi pia tu nikuombe kwamba kwa baadhi ya wale Wabunge wageni ambao hawaijui historia wasiwe wanakurupuka kushambulia watu wasiowajua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo na nirudie pia kumpongeza sana Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na Naibu wake Ashatu Kijaji kwa kazi kubwa sana ambayo wanayoifanya katika kulinda uchumi wa nchi yetu. Katika kipindi hiki kifupi cha Utawala huu wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali hii ya Awamu Tano mambo mengi yamefanyika sana, mageuzi makubwa yamefanyika ya kiuchumi ambapo Mheshimiwa Dkt. Mpango tunampongeza sana kwa kazi hiyo kubwa kwa kuendesha hilo gudurumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtakumbuka na Wabunge watakumbuka hapa na wengine wameni-refer kwenye michango yao niliwahi kulia mbele ya Bunge hili na kukataa Bajeti ya Serikali, kipindi ambacho kilikuwa kigumu sana kwangu pia kwa chama changu, lakini yalikuwa ni baadhi ya mambo ambayo leo hii yamefanyiwa marekebisho makubwa na mageuzi makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yapo mambo makubwa nsihukuru, nimpongeze hapa Mheshimiwa Stanslaus Mabula ambaye alipata nafasi hapa ya kuchangia kuna mambo makubwa katika Taifa hili ambayo tulikuwa tukiingia hasara kubwa na tulirekodiwa kati ya nchi ambayo ina-facilitate zoezi la Illicit Financial Flow kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, mapambano yaliyowekwa, mechanism zilizowekwa, kupiga vita suala la Illicit Financial Flow katika nchi yetu, huwezi kuamini leo akina nanii ambao wanafanya tathmini ya Illicit Financial Flow, tunawakaribisha Tanzania waje watu- access.

Mheshimiwa Spika, watakuja kuona jinsi udhibiti mkubwa uliyofanyika na sasa zoezi hili linafanyika kwa kiwango cha chini sana hapa nchini kwetu. Pia mambo ya transfer pricing vilevile, mambo ya dollarization vilevile na suala gumu hili lilishindikana siku zingine suala la credit rating na lenyewe katika kipindi hiki limeweza kufanyika. Kwa hiyo, viongozi wetu ambao wanaongoza jukumu hili, Waziri wa Fedha na msaidizi wake, pamoja na Katibu Mkuu wake na wengine wote wanaohusika katika usimamizi wa uchumi wetu tunawapa heko na tunawapongeza sana kwa bidii hizo za kazi.

Mheshimiwa Spika, basi baada ya kusema hayo, niweze kuzungumza kidogo kuhusu baadhi ya mambo ambayo yamezungumzwa ambayo yanatekelezwa katika Wizara yangu:-

Mheshimiwa Spika, moja ni jambo la chanjo na uogeshaji wa mifugo kwamba, tunayo shida kubwa. Ni kweli kabisa nakubali kwamba, suala la chanjo na uogeshaji wa mifugo ambapo mifugo mingi inakufa kila mwaka kwa kukosa chanjo na mifugo mingi inakufa kila mwaka kutokana na kupe na kwa kutokana na kutokuogeshwa. Sasa tunafanya kila aina kuhakikisha kwamba, jambo hili tunalifanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, Chuo chetu cha Utafiti cha Uzalishaji wa Chanjo cha Kibaha kinaendelea vizuri kuzalisha chanjo hapa nchini. Vilevile tumepata bahati ya kupata mwekezaji mpya kutoka India ambaye naye anakuja kujenga kiwanda hapa kwa ajili ya kuzalisha chanjo kwa wingi. Kwa kufanya hivyo, tutaweza kuwahakikishia wananchi wetu na kuwa-guarantee kupatikana kwa chanjo kwa muda na kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kama hiyo haitoshi pia, kwamba, Wizara yangu inatengeneza sasa mpango ambao utawezesha chanjo kupatikana kiurahisi, lakini vilevile uogeshaji wa mifugo kuwezekana kwa urahisi na vilevile kwa bei ambazo wafugaji wetu watazimudu. Kwa hiyo, jukumu hilo linafanyika na mpango huo tutahakikisha kwamba, wafugaji wote, halmashauri zote zinashirikishwa katika kuutekeleza.

Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine la pili liliwahi kuzungumzwa hapa Bungeni kuwa ni suala la uzalishaji wa maziwa hapa nchini na hasa ikilinganishwa nchi yetu na nchi ya Kenya kwamba, sisi tunazalisha mpaka sasa hivi lita za maziwa bilioni 2.4 wakati Kenya wanazalisha bilioni 5.2.

Mheshimiwa Spika, katika ulinganifu huo ni kweli kabisa, lakini nataka kuwa-assure Waheshimiwa Wabunge kwamba, kutangulia si kufika, tumejipanga vizuri katika kuhakikisha kwamba, tunakuja na uzalishaji mkubwa wa maziwa hapa nchini. Sisi hatuwezi kushindana na Kenya, hatuwezi kushindana na nchi yeyote ile ya Afrika kwa sababu, sisi kama ninavyosema, ni nchi ya pili tu kuwa na mifugo mingi hapa Afrika ikiwa nchi ya kwanza inayoongoza mpaka sasa hivi ni Ethiopia.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, sisi tuna malisho mazuri kuliko mtu yeyote, tuna maji bora kuliko mtu yeyote pamoja na kwamba, ng’ombe wa maziwa sasa hivi ni 789,000 tu, lakini mpango tulioanzisha sasa hivi wa kuhimilisha mifugo yetu ambao tunaita this is a massive artificial insemination ambapo tutahimilisha kila mwaka kutafuta mitamba milioni moja kwa mwaka, kwa miaka mitatu tutakuwa na mitamba milioni tatu na tutaweza ku-compete na yeyote na tutaweza kuzalisha maziwa mengi kuliko mtu yeyote. Tuna mifugo, tuna maeneo mazuri na swali hili limenifurahisha na liliulizwa na Mheshimiwa Jesca. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niseme kwamba, Kituo chetu cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) tumekifanyia ukarabati mkubwa sana ambao utawezeasha kuzalisha mbegu nyingi za kutosha. Tumenunua madume bora 11, kuna mtu mmoja aliwahi kuchangia hapa Bungeni akasema kwamba, madume hayo 11 hayawezi kutosheleza na kwamba, ni kidogo mno na kwamba, Serikali haiko serious.

Mheshimiwa Spika, niwaambieni kwamba, haya madume 11 yanaweza kuhimilisha ng’ombe zote wa Afrika Mashariki. Mbegu zinazozalishwa na madume 11 zinaweza kuhimilisha mahitaji yote ya uhimilishaji katika nchi za Afrika Mashariki. Kwa hiyo, tumejipanga vizuri na tutakuwa na maziwa mengi ya kutosha katika nchi yetu.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii uliyonipa niweze kuchangia hizi taarifa za Kamati ya PAC, LAAC na PIC ambazo zimeripoti juu ya taarifa ya CAG.

Mheshimiwa Spika, kwa ajili tu ya kumbukumbu Mheshimiwa Getere alikuwa WEO, naona tumefuatana Ma- WEO hapa na mimi nilikuwa WEO wa Kata ya Ngoboko, kwa hiyo tuko hapa.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana na kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati zote hizi tatu, hoja zao walizoziwasilisha hapa Bungeni zimesheheni mambo mengi zimesheheni uchambuzi mkubwa juu ya taarifa na juu ya matumizi ya fedha za nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nikianza na taarifa ya PAC labda kwa sababu nimepitia haraka. Kuna mambo makuu matatu ambayo sijayaona na nilitarajia niyaone kwenye taarifa hii. Deni la Serikali, Kamati ya PAC wanajua kwamba deni la Serikali kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa kipindi kile zilionesha kwamba Serikali imekopa zaidi ya kile kilichoruhusiwa na Bunge. Kwa hiyo tulitarajia kwamba kama sehemu hii ya deni la Taifa ingewasilishwa, wangeweza kuwa wameeleza vizuri juu ya mkanganyiko huo.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, jambo ambalo nilitarajia kwamba wangeweza kulieleza vizuri kwenye taarifa hii Kamati ya PAC ni suala la malimbikizo ya kodi za makinikia shilingi trilioni 360, ambazo maelezo yanatolewa kwamba fedha hizi zimeshasamehewa zote, lakini maelezo mengine yanatolewa fedha hizi hazijasamehewa. Hili nalo nilitarajia kwenye taarifa ya PAC lingekuwa limeandikwa vizuri, lingelielekeza hili Bunge kujua hatma ya hili eneo.

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu nililotegemea lielezwe vizuri ni eneo la uhamishaji wa bei ya mauziano ya bidhaa na huduma baina ya makampuni yenye mahusiano ya kimataifa, transfer enterprising ambako katika taarifa ya CAG ya mwaka 2019/2020 na mwaka 2020/2021 ilionesha kwamba katika hili eneo hatukusanyi mapato yanayostahili. Kwa hiyo nilitarajia Kamati hii ingeweza kushughulika na haya maeneo, lakini bahati mbaya sana sikuweza kuyaona kwenye taarifa yao.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo nataka kuchangia hapa ni suala la malipo yaliyofanywa na Serikali kwa Kampuni ya Symbion Power LCC. Serikali imelipa bilioni 360 kwa hii kampuni kwa maana ya dola milioni 153.43. Mkaguzi anatueleza na Kamati imetueleza kwamba makubaliano haya yalifanyika bila kujumuisha kodi wala gharama zingine. Sasa maswali ya kujiuliza ni kwa nini Serikali illipe bilioni 350 kwa Kampuni ya Symbion Power bila kuangalia Symbion Power inadaiwa kodi kiasi gani na Serikali, bila kuangalia gharama ambazo Symbion Power anahusika kuilipa Serikali na je, kulikuwa na udharura gani haraka tu baada ya makubaliano Mei, 2021 ya kulipa hizi fedha, kwa nini zililipwa haraka palepale na kama zililipwa kwa dharura namna hiyo, nani aliidhinisha fedha hizi? Kwa maana Bunge hili lilikuwa tayari limeshaidhinisha bajeti ya mwaka 2020/2021, sasa ilipofika Mei zimelipwa bilioni 350 na Serikali kwa Kampuni ya Symbion Power. Hizi fedha zilitoka wapi? Nani aliziruhusu wakati Bunge hili lilikuwa limeshapitisha bajeti tayari?

Mheshimiwa Spika, katika huo mwaka wa fedha tulikuwa na miradi mingi ya maendeleo iliyokuwa inatakiwa kutekelezwa. Serikali iliwezaje kulipa fedha hizo wakati bajeti ya Serikali ilikuwa imeshapitishwa? Hata hivyo, Mkaguzi hapa anatuambia kwamba hapa kulikuwa na usimamizi mbaya wa mkataba. Hawa waliosimamia mkataba vibaya mpaka nchi yetu wameisababishia kulipa bilioni 350 ni akina nani? Mbona hawajatajwa? Waliosababisha mpaka tukala hasara hii kwa Serikali hii ya wananchi maskini, bilioni 350 imesababishwa na mtu kusimamia mkataba mbaya, aliyeusimamia huu mkataba mbaya ni nani mpaka tukalipa shilingi bilioni 350 na kwa nini huyo mtu hatajwi? Aliusimamamia vipi huo mkataba vibaya?

Mheshimiwa Spika, Mkataba huu ulikuwa unaisha tarehe tarehe 18/09/2015, lakini ulikuja kuuhishwa na makubaliano ya tarehe 15/9/2015, siku tatu kabla ya mkataba kufika mwisho. Mkataba huu ulihuishwa kwa dharura namna hiyo kulikuwa na shida gani kwa sababu Bunge la wakati huo lilikuwa limeshaambiwa kwamba huu mkataba umefika mwisho na hautaendelea.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani shilingi za Watanzania bilioni 350 kulipwa bila kufanyika uhakiki wa kutosha. Najiuliza hizi kodi za Serikali, yaani huyu Symbion Power analipwaje kwa sababu cha kwanza kama yeye alikuwa anatudai shilingi bilioni 350, sisi tulikuwa tunamdai kodi, kodi zetu ni shilingi ngapi tunazomdai? Leo anakuja kulipwa shilingi bilioni 350, nchi hii ya maskini, kweli kabisa?

Mheshimiwa Spika, suala la Tatu, ni malimbikizo ya kodi ambazo zilikuwa zinashikiliwa na Mamlaka ya Rufani za Kodi (TRAB na TRAT) yapatayo Trilioni 360. Serikali ilituambia hapa Tarehe 24 Januari, 2020, Serikali ilifuta madai haya, kwa maana Serikali tukawa hatudai tena. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG ya Mwaka 2019/2020 inatambua kuwa Serikali inadai Shilingi Trilioni 360, ilipofikia taarifa ya CAG ya mwaka 2020/2021 CAG anasema: ‘‘inaonesha kuwa kesi za makinikia zipatazo 45 zenye thamani ya Shilingi Triloni 5.595 ziliamuliwa na Mamlaka za Rufani za Kodi, TRAB na TRAT’’. Kodi hizo zilipoamuliwa, Serikali ikaagizwa kufafanya majadiliano na makampuni hayo yaliyotakiwa kulipa hizo kodi. Kwa hiyo, inaonekana kwamba katika Mahakama hizi, ziliamua kati ya Trilioni 360 ziliona nchi yetu inastahili kulipwa, kwa maana ya Mahakama Trilioni 5.595.

Mheshimiwa Spika, Serikali ikafanya majadiliano na makampuni hayo yanayotakiwa kulipa ili wakubaliane namna ya kulipa. Kampuni la kwanza ambalo linatajwa kwenye Taarifa ya CAG ni Kampuni la North Mara Gold Mine; Kampuni ya Pili ni Pangea Mineral Limited; Tatu ni Bulyanhulu Gold Mine na Nne ni ABG Exploration. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya Mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, nikafuatilia ripoti za viongozi waliokuwepo kama waliweza kulisamehe hili deni. Nikafuatilia taarifa ya vikao vyote ambavyo Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliwahi kukaa na Barrick juu ya jambo hili. Nikafuatilia taarifa za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kama aliwahi kuzungumza jambo lolote kuhusiana na kusamehewa kwa kodi hizi.

Mheshimiwa Spika, hotuba zote za Viongozi hawa nimezisikiliza, hakuna mahali popote ambako wamesema fedha hizi zimefutwa. Mahakama iliagiza kampuni ya madini pamoja na Serikali yajadiliane namna ya kulipa Trilioni 5.595. Aliyeenda kufuta kodi za Watanzania hizo ni nani? Serikali lazima ituambie ukweli juu wa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu suala hili lipo kwenye taarifa ta CAG ukurasa wa 60 mpaka 63, Mheshimiwa CAG alete taarifa juu ya jambo hili ili Watanzania wajue hitimisho na ukweli wake juu ya fedha zao. Nchi hii maskini haiwezi kuingia kwenye makubaliano ya kwenda kusamehe kodi kubwa zote hizo, halafu tukaendelea kwenda kutoza kodi kwa wananchi, kodi ndogondogo tunaendela kutoza, halafu wafanyabiashara wakubwa kama hao wanasamehewa na nani? Kwa ajili ya nini? Tulishaelezwa kule mwanzo hizi kodi zilipatikanaje! Watu walikuwa wanatengeneza mahesabu ya aina mbili, mahesabu ya kulipia kodi na mengine ya kukwepea kodi na kuonyesha uhalisia kule kwao wanaporipoti, tuliona ukweli huo! Sasa aliyeenda kusamehe alisema nini? Kwamba mlifanya vizuri tu kutupunja, tumewasemehe. Alienda kusamehe akisema nini katika nchi maskini kama hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umesema vizuri sana leo, kwamba sisi tunaisimamia Serikali na Serikali leo itoe kauli juu jambo hili, tulimalize. CAG akachukue documents zote, kama kweli Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alisamehe hili deni, kama kweli Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alisamehe hili deni. Tuletewe hapa ili tuweze kufanya maamuzi zaidi kama Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la Nne ni kuhusu TRA, Kamati hapa imetueleza, inasema kwenye eneo la malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi. Amesema vizuri hapa Mtendaji wa Kata mwenzangu ameeleza vizuri sana, kwamba hivi tutasemaje sasa, tuna Taasisi yetu inayohusika na ukusanyaji wa mapato ya Serikali, inafika mahali kwa mwaka mmoja kodi ambayo haijakusanywa na hazina kesi Mahakama ni Trilioni 3.87. Katika Taasisi inayokusanya hata Trilioni 20 haifikishi. Trilioni 3.87 hazijakusanywa na hazina Mahakamani, sasa hii Taasisi yetu inachangamoto gani? Wanaeleza kwamba malimbikizo haya yameongezeka kwa asilimia 95 ya madai ya kodi.

Mheshimiwa Spika, hii taasisi yetu ina shida gani, kwa sababu hata tungeongea namna gani, hatuwezi kuyaleta maendeleo ya Watanzania kama hii taasisi haiwezi ikafanya kazi sawasawa. Trilioni 3.87, hizi ni zile kodi ambazo hazina kesi Mahakamani, kuna kodi ambazo zina kesi Mahakamani, ukizijumlisha zote hizo karibia asilimia 30 ya mapato hatuyakusanyi! Sasa kama hatuyakusanyi, tuta-survive namna gani? Maendeleo tuliyoyaahidi na kwenye Ilani ya Uchaguzi na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, tutaujenga na tutalipa na nini? Madeni tunayokopa leo tutayalipa na nini? Kama hatuwezi kukusanya kodi, tukaweza kulipa madeni, tukaweza kujenga, tukaweza kuhudumia Serikali.

Mheshimiwa Spika, ifike mahali sasa tuwe tunaambiwa ukweli, eneo hili la Taasisi yetu ya TRA kama inalo tatizo ambalo lenyewe lipo juu ya uwezo wake kwa nini tusiambiwe kama Bunge tuamue? Kuna mambo mengine tu wanalalamika, mara watumishi wachache, hivi kweli kabisa anayepanga watumishi unaweza ukaamua Taasisi inayolipa watu mishahara yote na yenyewe ikawa na upungufu wa watumishi kabisa kabisa ukawa na nia njema na Watanzania hawa?

Mheshimiwa Spika, TRA ikose fedha ambaye analipa mishahara ya watu wote, TRA anapeleka fedha za maendeleo kote, ambaye anatulipia Deni la Taifa, huyo naye awe na upungufu wa watumishi? Kama kuna matatizo yaliyojificha kwa TRA, kama ni udhaifu wa TRA uwekwe wazi, kama kuna udhaifu wa TRA ambao upo juu ya uwezo wao, Bunge hili linahitaji kufanya maamuzi, tufanye maamuzi leo, tuiwezeshe Taasisi hii na tuchukue hatua kwa wale ambao wanaturudisha nyuma.

Mheshimiwa Spika, leo tunazungumza malimbikizo ya kodi yasiyokuwa na kesi yamefikia trilioni 7.54 jumla…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mpina, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Simbachawene.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba Mheshimiwa Mbunge anayechangia Mheshimiwa Mpina, ameshalizungumza hili jambo hili Bungeni mara kadhaa. Pengine Mheshimiwa Mpina ili aweze kutenda haki na kwa sababu yeye ni Mwanataaluma wa eneo hili ni vizuri akaelezea vizuri kinachotokea katika masuala ya rufaa za kodi. Kunapokuwa na mgogoro, kodi ikawa inabishaniwa kati ya Mlipa Kodi na TRA kile kiasi ambacho hakibishaniwi mfanyabiashara anayetakiwa kulipa huwa kinalipwa na Serikali inachukuwa kiasi chake. Kinachobaki ambacho kina-dispute kinaingia kwenye mgogoro, kwa hiyo ni kwa sababu ni maisha ya shughuli mbalimbali zinazoendelea na wafanyabiashara, kuna uwekezaji, kuna mambo mbalimbali, huendelea kwa sababu ni suala la mgogoro na ni suala la haki.

Mheshimiwa Spika, katika kundi la hao wanaodaiwa wengine waloshafunga makampuni, wameshindwa kufanya biashara, hapa mnasema tuvutie wawekezaji, hapa mnasema tuhakikishe kwamba wawekezaji wanapata mazingira mazuri, ni katika mazingira hayo ambayo yamepelekea hata baadhi ya wawekezaji kuondoka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali makini kama hii ambayo tunatafuta pesa kila siku, hatuwezi tukaacha kudai kodi, hatuwezi tukaacha kudai mapato ambayo Serikali inataka kuyapata, lakini sasa tunapokutana na mgogoro ambao kile kiasi kinachobishaniwa kinabaki katika mgogoro lakini kile cha msingi kinakuwa kimelipwa. Kwa hiyo, hakuna hakuna fedha iliyoachwa makusudi ila kuna kesi. Kesi ni suala la haki jamani, hauwezi kusema leo hii kwa sababu ni Serikali mmeacha. Isionekane hivyo, kwa hiyo ielezwe vizuri. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mpina unaipokea taarifa hiyo?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, taarifa yake siipokei na sababu ya kutokuipokea ingekuwa haya maelezo yake yanakubalika angeyapeleka kwa CAG, CAG angetuandikia hapa Kamati inasema malimbikizo haya yanatokana na kutokushughulikiwa ipasavyo kwa madeni ya kodi mathalani mwaka 2020/2021. Hawa Mawaziri wetu wasome taarifa, wasiwe wanapoteza muda wetu hapa tunapochangia hapa Bungeni. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naendelea kusisitiza malimbikizo ya Trilioni 7.54 na hizi hazina kesi Mahakamani, TRA walitakiwa kukusanya, nikaeleza kwamba kwa mwaka mmoja wamefeli kukusanya malimbikizo ya Trilioni 3.87, mwaka mmoja wa 2020/2021. Kama tutaenda namna hiyo, utakusanya kodi ya nani, kama tutaenda hivyo, tutaijenga nchi yetu kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba mambo makubwa kama haya yakiletwa hapa Bungeni, yakielezwa kwa ufasaha, Bunge lako litaelewa na litajua hata lichukue hatua gani.

Mheshimiwa Spika, kama muda unaniruhusu nimalizie suala la mwisho. Suala la mwisho ni suala la utoaji mikopo asilimia 10 ya akina mama, vijana na Wenye Ulemavu. Wenzangu hapa wamechangia na bahati nzuri Kamati ya LAAC imelizungumza suala hili, ninachotaka kushauri ni kwamba sasa hivi tunavyoenda hili eneo ni kubwa, Taasisi inayosimimia ambayo siku hizi inaitwa Division ya Maendeleo ya Jamii, haina uwezo wa kulisimamia jambo hili. Idara Zetu za Maendeleo ya Jamii hazina watu competent wa mambo ya fedha, hazina watu competent wa kusimamia mikopo, unaenda kumchukua Afisa wa Maendeleo ya Jamii asambaze mkopo wa Bilioni Mbili, asambaze mkopo wa Bilioni Kumi, asisimamie, azikusanye, azilitele, akaunde vikundi na akopeshe tena.

Mheshimiwa Spika, jambo hili tulianzisha vizuri lakini kadri tunavyoenda zipo halmashauri mapato yao kwa mwaka ya own source yanafikia hata Bilioni Ishirini. Kwa maana hiyo, ukichukua asilimia kumi yake kwa mwaka wanapata bilioni Mbili, ukichukua kwa miaka Saba tu, wanafikia kile kimo cha kuanzisha benki cha Bilioni 15. Sasa kama ndivyo ilivyo, kwa nini tusianzishe utaratibu wa hizi fedha zikakusanywa, tukaingia na benki ambazo zinapatikana maeneo ya karibu, NMB na CRDB, tukaweka masharti ambayo hayaathiri malengo na maksudi yaliyowekwa na Serikali. Mikopo hii ikaanza kupitia kwenye Benki, lakini mchakato wake wa awali utakanywa na hii Idara yetu ya Maendeleo ya Jamii na fedha hizo zikaanza kutolewa kwenye Benki, ambako kuna competent personnel waliosomea mambo ya utoaji wa mikopo, kule kuna watu wanaoweza kuifuatilia mikopo hii.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunashuhudia changamoto nyingi, sehemu zingine upendeleo mkubwa, wanapewa kundi la watu hela yote ya Halmashauri inachukuliwa na watu wawili watatu inaisha, sehemu nyingine fedha hawakusanyi, unakuta asilimia 20 tu ya marejesho leo miaka mitatu, miaka mingapi. Kwa hiyo, kwa changamoto hizi za upendeleo na uwezo wa kusimamia kodi zenyewe na idara zetu na upungufu wa watumishi tulionao, hili eneo hatuna uwezo wa kulisimamia vizuri. Ningeshauri tuende kwenye MOU na benki zinazoweza kuhudumia suala hili, najua linaweza kufanyika vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, zipo taasisi kama PASS ziliweza ku-guarantee watu wetu kwenye kilimo, wanafunzi vijana na kadhalika zina-guarantee, sasa Serikali na yenyewe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi ili nami niweze kuchangia hii hoja iliyoko mbele yetu kwa kujadili hali ya uchumi pamoja na mpango wa maendeleo. Nianze kwa kupongeza sana Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na timu nzima kwa kazi nzuri walioifanya ya kutayarisha hii bajeti ya nchi na kufikia hii hatua.

Mheshimiwa Spika, kwa muda huu mfupi nianze moja kwa moja kuchangia baadhi ya maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge walisimama hapa. Wengine walijaribu kuzungumza suala la kwamba tozo nyingi sana kuhusu uvuvi na imeonekana tozo za mifugo peke yake ndizo ambazo zimeweza kushughulikiwa na Serikali lakini tozo za uvuvi hazijaweza kushughulikiwa.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme hivi kwa kifupi kwamba, moja tuliamua baada ya kuona changamoto za wavuvi tukaamua kufanya marekebisho ya Sheria ya Kanuni ya Uvuvi ya mwaka 2009 kwa Tangazo la Serikali 383, tukaweza kuondoa kigezo kilichokuwa kinalazimisha Ukanda wa Pwani kuvua dagaa kwa kutumia milimita 10 na badala yake ikiwa ni milimita nane, jambo ambalo lilikuwa ni kilio kikubwa sana kwa wananchi wa maeneo ya Pwani. Hili lilifanyika na tayari kila kitu kiko sawasawa, sasa wanavua kwa milimita nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija kwenye hili eneo hili la kwa nini tozo, ukweli ni kwamba hotuba ya Waziri wa Fedha isingeweza kuchukua mambo yote tuliyoyashughulikia mwaka huu kuyaonesha kwenye taarifa. Nataka niseme kwamba ni kweli kabisa kwamba dagaa walikuwa wanatozwa dola 1.5. Sasa nataka niwaambie hivi, tumerekebisha, Serikali imekubali kilio cha wavuvi na imekubali pia ushauri wa Wabunge, tumepunguza kutoka 0.5 mpaka 0.3 dola za Kimarekani, lakini Ukanda wa Ziwa Nyasa vilevile tumepunguza kutoka 0.5 dola za Kimarekani mpaka 1.3 dola za Kimarekani na Ziwa Tanganyika tumepunguza kutoka dola 1.5 mpaka dola moja.

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine ni kwamba kwa nini hizi tozo zinatozwa tofauti tofauti kila eneo; tunatoza tofauti kila eneo kwa sababu Waheshimiwa Wabunge tozo hizi zinapangwa kulingana na thamani ya zao hilo la uvuvi linalozungumziwa. Kwa hiyo dagaa wa Ziwa Tanganyika huwezi kuwalinganisha na dagaa wa Ziwa Victoria, huwezi kuwalinganisha na dagaa wa Pwani.

Mheshimiwa Spika, la pili, ni suala hili la mauzo ya nje; kwamba mauzo ya nje yanaporomoka sana katika sekta hii ya uvuvi kwamba tunauza kidogo. Nataka niseme kwamba ni kweli takwimu zinaonesha na hali ya uchumi katika ukurasa wa kama sikosei wa 72 imeonesha kwamba mauzo yetu ya nje mwaka 2018 yalikuwa dola za Kimarekani milioni 158, lakini mwaka 2017 ilikuwa milioni 193 dola za Kimarekani. Miaka mingine yote kule inacheza kwenye milioni 160, milioni 195, lakini nataka niwaambie Wabunge tumefanya kazi kubwa mambo haya yalisababishwa na vitu vingi. Moja, uvuvi haramu wa kutumia mabomu, wa kutumia nyavu harama ambao tumeushughulikia kwa kiwango kikubwa lakini pia na mambo mengine.

Niwaambie mpaka sasa hivi tunavyozungumza mwaka huu wa fedha 2019, mauzo yetu ya nje mpaka leo hii tunavyozungumza yamefikia milioni 284.7, sawa na bilioni 654, haijawahi kutokea katika awamu nyingine yoyote ile katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala hapa Wabunge wamesisitiza sana la uvuvi wa bahari kuu kwamba tuwekeze kwenye bahari kuu. Nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya. Moja, mpaka sasa hivi tunavyozungumza consultant wetu anayefanya feasibility study anakabidhi ripoti tarehe 30 Juni, 2019 ya kukamilisha kuanza ujenzi wa bandari yetu ya uvuvi na baada ya tarehe 30 Juni tutaendelea na hatua zinazofuata.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi mazungumzo kati ya Tanzania ya nchi ya Korea kuhusu kujenga hii bandari ya uvuvi yako kwenye hatua nzuri. Kwa hiyo, tunategemea baada tu ya kupata hiyo taarifa ya consultant tutaingia sasa kwenye hatua za ujenzi wa bandari hii ya uvuvi ambayo nayo kwa miaka mingi haikuweza kufanikiwa lakini Serikali hii ya Awamu ya Tano imeweza na hatimaye tunaenda kuwa na bandari yetu ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Wabunge wameshauri Serikali ikubali kununua meli na kuvua majini. Nataka niwape taarifa nzuri kwamba mpaka sasa hivi tumejipanga vizuri kwamba maandalizi mazuri sana yanafanyika ya kununua meli zetu na kuingia kuvua katika ukanda wetu wa bahari kuu. Mwaka huu wa fedha matarajio yetu makubwa tutakuwa tumenunua meli na tumeingia majini. Taasisi zetu zote mbili, TAFICO na ZAFICO ziko kwenye maandalizi mazuri ya kuingia uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata Wabunge walipochangia wanasema Serikali hii inaenda kutoza wig na kadhalika, Waziri wa Fedha amesema bayana kwa mara ya kwanza tunaenda kuingia kwenye uvuvi wa bahari kuu na mipango yote ile imekaa vizuri na tumejipanga vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la 0.4 zinazotozwa watu wanapovua katika ukanda wetu wa bahari kuu limelalamikiwa na Wabunge, imeonekana ni changamoto. Kesho tunakutana mimi na Waziri mwenzangu wa Zanzibar anayeshughulikia mambo ya uvuvi tuweze kuliamua jambo hili. Kwa hiyo, maamuzi yatakayotoka katika kikao kile yatakuwa ndiyo maamuzi ya Serikali juu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la ngozi limezungumza na Wabunge, kwanza wakiomba asilimia 10 ya export levy kwa ngozi ya wet blue nje ya nchi iondolewe au ipunguzwe. Pia wakaomba asilimia 80 inayotozwa malighafi yetu kuiuza nje ya nchi na yenyewe iondolewe au ipunguzwe.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kifupi kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, malizia.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, namalizia kwa kusema kwamba jambo hili Serikali imeshindwa kulifikisha mwisho katika kipindi hiki kwa sababu changamoto za sekta hii ya uvuvi ni nyingi.

Kwa hiyo, nachotaka kuliahidi Bunge lako Tukufu ni kwamba watuachie Serikali tushughulikie hizi changamoto za ngozi hapa nchini kwa kuangalia parameters zote ambazo zinakwamisha biashara hii ambapo tumeshakubaliana Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Fedha na mimi mwenyewe kuhakikisha kwamba hili jambo linafika mwisho sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, utangulizi; ninayo heshima kubwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka wa fedha 2023/2024, pamoja na Mapendekezo ya mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapitia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa tukiwa na takwimu sahihi ya idadi ya watu na majengo kutokana na Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika tarehe 23 Agosti, 2022 ambapo idadi ya watu imefikia 61,741,120. Takwimu hizi zinatuwezesha kuandaa mpango jumuishi na unaotekelezeka. Maendeleo ni takwimu, hongera sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kusimamia vyema zoezi la sensa mpaka takwimu zimepatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze kwa dhati Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara Mheshimiwa Mama Anne Semamba Makinda na Kamisaa wa Sensa Tanzania Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Mohamed Haji Hamza. Hongera timu ya watakwimu wote walioshiriki, Makarani wa Sensa, Wenyeviti wa Vitongoji na wananchi wote kwa moyo wa kizalendo walioonesha katika kukamilisha zoezi hili muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchambuzi wa utekelezaji na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2023/2024. Deni la Serikali; takwimu zinaonesha kwamba deni la Serikali limeongezeka kutoka shilingi trilioni 60.72 kipindi cha Aprili, 2021 hadi shilingi trilioni 69.44 Aprili, 2022 hili ni ongezeko la shilingi trilioni
8.72 katika kipindi hicho ambalo ni ongezeko la 14.4%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwendendo wa ukuaji wa deni la Serikali; deni la Serikali lilikuwa kwa asilimia saba (2019/2020), asilimia 13.7 (2020/2021), asilimia 11(2021/2022) lakini pia takwimu zinaonesha kuwa Serikali ilipokea mikopo mipya kipindi cha miezi miwili, Mei na Juni, 2021 kiasi cha shilingi trilioni 3.799.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu hizi zinazua maswali mengi yasiyo na majibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kujiuliza kwa nini deni la Serikali liongezeke kwa shilingi trilioni 8.72 wakati katika mwaka husika wa fedha wa kuishia Aprili, 2022 deni lililipwa kwa zaidi ya shilingi trilioni 7.2 na wakati huo huo shilingi ya Tanzania iliimarika kwa wastani wa 0.03%. (sababu ya riba haiwezi kupandisha deni kwa kiwango hicho).

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tafsiri yake Serikali ilichukua mikopo mipya yenye thamani ya shilingi trilioni 15.92 kinyume na kiwango kilichoruhusiwa na kupitishwa na Bunge cha wastani wa shilingi trilioni 10.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, deni la Serikali lilikuwa linakua kwa wastani wa asilimia nne lakini ghafla miaka ya 2020/2021 na 2021/2022 deni la Serikali limekua kwa wastani wa asilimia 12.33. Wakati deni la Serikali likiongezeka kwa kasi hiyo ukusanyaji wetu wa mapato ya ndani sio wa kuridhisha ambapo Tanzania inakusanya asilimia 11.40 ya pato la Taifa ikiachwa nyuma na nchi jirani za Kenya asilimia 13.70 na Rwanda asilimia 15.90 ya pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha Taarifa ya Kamati ya Bajeti ukurasa wa tano na sita kipengele cha 2.5 imeshtushwa na kasi ya ukopaji unaoendelea, nanukuu; ”Aidha imekuwa ni rai ya Kamati ya muda mrefu kuweka na kutumia kiashiria cha ukumo wa ulipaji wa deni la Serikali kwa mapato ya ndani (Debt Service to Domestic Revunue Ratio) ili kuhakikisha kwamba mapato ya ndani yana uwezo wa kugharamia shughuli zote za Serikali pamoja na deni la Serikali.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa kasi wa deni la Serikali wa namna hii ambao pia hauzingatii uwezo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani usipodhibitiwa kuna hatari nchi yetu kuingia kwenye mgogoro mkubwa wa kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina tatizo na Serikali kukopa, lakini ni lazima mikopo inayochukuliwa na Serikali izingatie uwezo wa nchi kulipa madeni hayo na ukomo wa kukopa uliopitishwa na Bunge katika bajeti ya mwaka husika, na hii ni kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Katiba na Sheria za nchi (Sheria ya Fedha, Sheria ya Bajeti na Sheria ya Mikopo) zinaeleza bayana utaratibu wa namna ya kukopa na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma, kwa nini Serikali ikope zaidi ya kiwango kilichoruhusiwa na Bunge?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama miradi yote iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 ilitengewa fedha na kuidhinishwa na Bunge, je, mikopo ya ziada iliyokopwa na Serikali imetekeleza miradi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba ufafanuzi katika kipindi cha kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023, bahati mbaya sana Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba hakutoa maelezo yoyote juu ya hoja hii. Ninaomba kushauri tena kama ifuatavyo; kwanza, Waziri wa Fedha na Mipango atoe maelezo ya kina kuhusu ziada ya mikopo ya Serikali katika mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 ili Bunge liweze kuchukua nafasi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, CAG afanye ukaguzi maalum wa deni la Serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 ili kuweka uwazi na kuondoa mkanganyiko kwa Watanzania kuhusu hali ya deni la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu mikopo iliyochukuliwa na Serikali izingatie uwezo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani badala ya kung’ang’ana na vigezo vya kimataifa ambavyo vinaweka rehani mustakabali wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo; hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango ukurasa wa 28 kipengele cha 35 ameainisha kuwa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unatarajiwa kutekelezwa kwa kushirikisha sekta binafsi, lakini pia hotuba ya Kamati ya Bunge ya Bajeti ukurasa wa 13 kipengele 3.1.4.1 (c) naomba kunukuu; ”Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri Serikali kutafuta njia nzuri ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambayo itazingatia manufaa mapana ya Taifa kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo ili kutekeleza mradi huo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushauri huo wa Kamati ya Bajeti yapo maswali mengi ya kujiuliza kabla ya kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; kama Taifa tumeshafanya tathmini ya kina na kujiridhisha kuwa mradi wa Bandari ya Bagamoyo unaweza kutekelezwa kwa njia ya ubia na bila kuathiri uchumi wa ustawi wa nchi yetu, tutawezaje kulinda mifumo ya kiusalama ya nchi, mwekezaji binafsi anaweza kuamua kupandisha gharama za usafirishaji na uchukuzi wa mizigo bandarini wakati wowote tutawezaje kudhibiti mfumuko wa bei, tutawezaje kuwalinda wafanyabiasha na wawekezaji wetu wa ndani, tutawezaje kudhibiti mifumo ya ukusanyaji wa mapato nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili; Taifa hivi sasa tuna miradi mikubwa ya kimkakati ambayo iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na yenye mahitaji makubwa ya fedha, miradi hiyo ni pamoja na Reli ya SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere, Bwawa la Kidunda, ujenzi na ufufuaji wa meli, uboreshaji wa bandari zilizopo, ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato, ununuzi wa ndege mpya na kadhalika. Je, kama Taifa tunao uwezo wa kiuchumi na kimapato kwa sasa kuweza kubeba gharama za mradi mpya wa Bandari ya Bagamoyo wakati tuna miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea maeneo mbalimbali nchini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; tumejiandaaje kulinda haki za Watanzania katika mkataba huo kwani uzoefu unaonesha mikataba mingi ya ubia tuliyoingia kama Taifa ni ya upigaji na mifano dhahiri ipo na wote tunakumbuka kama Symbion, Richmond, IPTL, TRL, City Water, Aggreko na kadhalika, mikataba ambayo imelitia hasara kubwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne; Kamati ya Bajeti imeonesha mashaka yake kwa chanzo cha fedha kilichopendekezwa na Serikali cha ubia na ndio maana ikashauri itafutwe njia nzuri ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambayo itazingatia manufaa mapana ya Taifa kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu mimi Mradi wa Bandari ya Bagamoyo ni mradi mzuri na una manufaa makubwa kwa Taifa letu, lakini tujipe muda kukamilisha miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa maeneo mbalimbali nchini na pia kujipa nafasi ya kutafuta fedha za kugharamia mradi huo bila kuathiri uchumi na ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP – MW 2,115); kuhusu utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP – MW 2,115) kama ilivyotolewa taarifa kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2023/2024 kipengele (b) ukurasa wa 19 na Taarifa ya Kamati ya Bajeti kipengele 3.1.3.1 ukurasa wa 9 na 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikushauri hapa Bungeni kuunda Kamati Teule ya Bunge na nikasema utanishukuru. Leo hii unashuhudia mkanganyiko mkubwa uliobainishwa na Kamati yako ya Bajeti ambayo imeshindwa kupata taarifa za uhakika juu ya kinachoendelea katika utekelezaji wa bwawa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Arab Contractors ya Misri umeongezwa na Serikali bila sababu za msingi, bila kufanya tathmini na bila kubainisha gharama za ongezeko la muda wa mkataba (variations cost) zitabebwa na nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, muda ulioongezwa katika mkataba baina ya TANESCO na Mkandarasi Arab Contractors haujulikani hadi sasa kwamba ni miezi 12 au miezi 24, TANESCO inaonesha kwamba mkandarasi ameongezewa muda wa miezi 12 yaani hadi tarehe 15 Juni, 2023 lakini mkandarasi na Wizara ya Nishati wanasema muda ulioongezwa ni miezi 24 hadi Julai, 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, huku tunaelezwa mradi umefikia 75% ya utekelezaji, lakini mkandarasi ameongezewa muda mrefu wa miaka miwili kumalizia mradi ulibakiza 25% tu ya utekelezaji hali inayoleta mashaka makubwa juu ya ukweli wa hatua za utekelezaji zinazowasilishwa na Serikali Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, mara tunaletewa maelezo hapa Bungeni kuwa TANESCO na mkandarasi wanavutana bila Bunge kuelezwa wanabishania nini. Ni hatari sana kuingia kwenye mabishano huku mradi ukiwa umefikia 75% ya utekelezaji na malipo yakiwa yamefanyika zaidi ya 70%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, sababu hazitolewi za kwa nini malipo halali ya kimkataba ya CSR kiasi cha shilingi bilioni 260 haijatolewa licha ya Serikali kuendelea kufanya malipo kwa mkandarasi yaliyofikia zaidi ya 70% ya madai yote ya mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, Kampuni ya Arab Contranctors inapaswa kulipa gharama za ucheleweshaji wa mradi (variations cost) kwa muda wa miaka miwili kiasi
cha shilingi trilioni 1.3 kwa mujibu wa mkataba ambayo ni 10% ya gharama za mradi kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti,si Wizara ya Nishati wala TANESCO iliyodai fedha hizo kwa mkandarasi ambaye hivi sasa ameshalipwa madai yake kwa zaidi ya 70%. Kwa nini Serikali iendelee kumlipa mkandarasi bila kukata fedha za CSR na faini ya ucheleweshaji? Madai haya ni haki ya Watanzania kwa mujibu wa mkataba na sio hisani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuchelewa kwa mradi huu wa Bwawa la Julius Nyerere kumeliingiza Taifa kwenye hasara kubwa ikiwemo kuwepo migao na katakata ya umeme isiyoisha, migao ya maji, Mradi wa SGR kutokufanya kazi baada ya kukamilika, kukosa wawekezaji kutokana na nchi kutojitosheleza kwa umeme, hasara na ajira kuyeyuka kwa shughuli za uzalishaji zinazotegemea umeme, nchi kushindwa kuuza umeme nje ya nchi na Taifa kukosa mapato na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha Wizara ya Nishati kuendelea kuwasilisha taarifa zenye mkanganyiko Bungeni kuhusu utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, kuongeza muda wa mkataba kiholela na kushindwa kudai madai halali ya kimkataba ya shilingi trilioni 1.56 yanaleta mashaka makubwa na kuashiria kuwepo kwa mianya ya rushwa, uwezo mdogo wa Wizara ya Nishati kusimamia utekelezaji wa mkataba na ni dharau kubwa kwa Bunge lako tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka mwanzo nilishauri kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge ili kuchunguza ukweli wa jambo hili na leo ninashauri mambo mawili yafanyike ili kuunusuru Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere na kuepuka hasara inayoweza kutokea mbeleni ya kupoteza matrilioni ya fedha za Watanzania na mradi kuishia njiani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, iundwe Kamati Teule ya Bunge kubaini ukweli na chanzo cha mkanganyiko wa taarifa zinazotolewa na Wizara ya Nishati na kupendekeza hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Bunge liiagize Wizara ya Nishati na TANESCO kukata fedha zote za CSR na gharama za ucheleweshaji wa mradi kwa Kampuni ya Arab Contractors kiasi cha shilingi trilioni 1.56 katika malipo yatakayoendelea kutolewa kuanzia sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maeneo ya kupewa kipaumbele; Serikali imeweka vipaumbele vingi ambavyo ni ngumu kuvitekeleza kwa ufanisi na ikumbukwe kuwa kupanga ni kuchagua. Ni vyema utekelezaji wa miradi mbalimbali ukafanyika kwa awamu kulingana na uwezo wa rasilimali zilizopo. Nimepitia maeneo mbalimbali ya mapendekezo ya mpango na naomba kushauri kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naipongeza Serikali kwa hatua ya kupata mkandarasi na kusaini mkataba wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda hali itakayopelekea kumaliza tatizo la maji la muda mrefu linaloikabili Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu, Serikali itekeleze kwa vitendo mradi ulioahidiwa kwa muda mrefu wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Mkoa wa Simiyu ambao maji yatasambazwa katika Wilaya za Busega, Bariadi, Itilima, Meatu na Maswa. Wananchi wa Jimbo langu la Kisesa wanausubiri mradi huu kwa hamu kubwa ili kutatua matatizo ya maji ya kunywa, kilimo, mifugo na shughuli nyingine za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwenye mipango ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji, msitusahau wakulima wa Jimbo la Kisesa na Mkoa mzima wa Simiyu kwa kuwa tunayo maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya mpunga, pamba, mahindi, mbogamboga na kadhalika na Serikali itenge fedha za kutosha katika kilimo, mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Serikali itenge fedha za kutosha kuwezesha utafiti kufanyika nchini katika taasisi zake za kama COSTECH, TARI, TALIRI, TAFIRI, TAWIRI na kadhalika ili kuwezesha kupata taarifa muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ujenzi wa madaraja ya Mwamhuge katika Mto Sanga (mpakani mwa Meatu na Maswa), ujenzi wa daraja la Sanjo (mpakani mwa Meatu na Itilima), ujenzi wa Daraja la Mwabuzo (linalounganisha Meatu, Kishapu na Igunga) pamoja na maombi haya naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TARURA na TANROADS kwa utekelezaji mzuri wa ujenzi wa barabara na madaraja jimboni kwangu Kisesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu; uUjenzi wa zahanati kila kijiji na ununuzi wa vifaa muhimu vya kitabibu, madaktari na wauguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, Serikali itenge fedha za kutosha kwa uboreshaji wa bandari zote katika Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kutafuta masoko ya mazao nje ya nchi hongera sana. Tumeshuhudia mkiwezesha kupata masoko makubwa ya mazao kama korosho, soya, parachichi, pamba, choroko, dengu, mabondo, samaki, nyama na mazao ya mbogamboga, lakini kupata masoko ya nje ni suala moja na kumudu mahitaji ya soko ni kitu kingine. Kama Taifa tunapaswa kuwekeza vya kutosha katika kuhudumia masoko ya kimataifa ili kuhakikisha tunazalisha kwa wingi na kwa viwango vinavyohitajika na masoko husika. Hongera sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri unayoifanya ya kuiunganisha Tanzania na dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikishwaji wa Watanzania na upatikanji wa ajira; mpango lazima uzingatie ushirikishwaji wa Watanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini, lakini yapo mambo yanayoendelea ambayo yanakinzana na hii dhamira njema ya Serikali, mifano; moja, wafugaji wa mifugo ya asili wa kijiji cha Ilunde B, Kibondo Mkoani Kigoma kila leo wanafukuzwa kwenye maeneo yao ikidaiwa kuwa ni eneo la Hifadhi la Pori la Akiba la Kigosi Muyowosi. Wananchi hawa wameiomba Serikali kufika na kuhakiki mipaka ili kubaini ukweli bila mafanikio badala yake operation za kuwafukuza zinaendelea kila uchao kufukuzwa, kuchomewa moto makazi, kutaifishwa mifugo, kupigwa faini na kupigwa na kuumizwa kinyume na haki na misingi ya utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kusitisha operation zinazoendelea katika Kijiji cha Ilunde B, Wilayani Kibondo Mkoa wa Kigoma na badala yake ufanyike uhakiki wa mipaka ambao utashirikisha wananchi wote na Serikali ya eneo husika ili kuondoa utata wa mipaka uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wananchi wa vijiji 33 vya Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kufukuzwa kwenye maeneo ya makazi na kilimo kwa kisingizio kwamba wako ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula amepiga marufuku shughuli za kilimo kuendelea katika maeneo hayo ambayo kwa muda mrefu wamekuwa wakiyatumia kwa shughuli za kilimo cha mpunga ambapo mchele huo umekuwa ukiuzwa ndani na nchi jirani za Uganda, Malawi, DRC, Zambia, Visiwa vya Komoro, Sudani Kusini, Kenya na Rwanda ambapo linapunguza tatizo la upungufu wa chakula nchini, kuingiza kipato kwa wananchi na kupata fedha nyingi za kigeni kutokana na mauzo ya mchele nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu wameiomba Serikali kufika eneo hilo ili kupitia na kuhakiki mipaka baina yao na hifadhi lakini badala yake limetolewa tamko la kuondolewa bila kusikilizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi ya Waziri ambayo yanalenga GN No. 28 inayolalamikiwa na wananchi kila sehemu ambapo imetanua mpaka bila ushirikishwaji wa wananchi na kwa sehemu kubwa haina uhalisia kwa kuwa ramani haijafanyiwa uhakiki wa mipaka na kutoa tafsiri ya ramani chini ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wananchi hawa waachwe waendelee na shughuli zao za kilimo na Serikali iende ikakae na wananchi hao ili kufanya uhakiki wa mipaka na pande zote kujiridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, TANESCO kuingia mkataba na kampuni binafsi ya kutoa huduma ya kuendesha kituo cha huduma kwa wateja (callcenter) ambapo TANESCO ina otusource uendeshaji wa kituo chake cha huduma kwa wateja kwa kampuni binafsi kazi iliyokuwa ikifanywa na vijana wa Kitanzania 279 waliokuwa na mkataba na TANESCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu za kukasimu shughuli za uendeshaji wa kituo cha huduma kwa wateja kwa kampuni binafsi hazijawekwa wazi. Vijana 279 wanaachishwa kazi kumpisha mtu binafsi kuendesha huduma hiyo, haya ni mawasiliano nyeti yanayofanywa na wateja kupitia callcenter ya TANESCO inakuwaje yaendeshwe na mtu binafsi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu TANESCO isitishe uamuzi wake wa kubinafsisha vituo vya kutoa huduma kwa wateja (callcenter) na badala yake iimarishe kitengo hicho na kiendelee kuendeshwa na shirika hilo huku ajira za vijana 279 zikilindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, wafugaji walioshinda kesi Mahakamani zaidi ya ng’ombe 6,000 lakini Serikali imekaidi kurejesha mifugo yao, licha ya wananchi hawa kushinda kesi Mahakamani miaka zaidi ya mitatu iliyopita mifugo yao haijarejeshwa na Serikali hali inayopelekea familia hizo kuingia kwenye lindi kubwa la umasikini. Sababu za kutorejesha mifugo hiyo hazitolewi na hili sio jambo zuri kwa nchi inayofuata misingi ya sheria ya utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iwarudishie wananchi mifugo yao au kiasi cha fedha kinacholingana na thamani ya mifugo iliyoshikiliwa kama Mahakama zilivyoamua. Nawasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii ili niweze kuchangia kwa hizi Kamati zote mbili Kamati ya Bajeti na Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na nianze kwa kuwapongeza sana Wenyeviti wa Kamati hizi kwa taarifa zao nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nivipongeze sana Vyombo vya Dola na Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri sana ambavyo vinaendelea kufanya hapa nchini. Pia niwapongeze kwa hili, ajira zinazotolewa sasa hivi za Polisi, Magereza, Zimamoto pamoja na Uhamiaji ambazo zimetolewa ajira nyingi kwa wingi, vijana wetu wengi waliokosa ajira sasa watapata ajira. Kwa hiyo, tunawapongeza sana Serikali katika hili na najua sharti kubwa lilikuwa la vijana wale wa JKT na wengine wapo kwenye vikosi kule tunawatakia kila la kheri sana kwa ajili ya kwenda kulijenga Taifa lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba niunge mkono sana pendekezo la Kamati la kurejesha Tume ya Mipango ili tuwe na think tank ya Taifa katika kugakikisha kwamba mipango yetu inakuwa iko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la ukusanyaji wa mapato, nilipokea taarifa za mapato ya TRA ya mwezi wa kumi na mbili, naamini kama sikosei takwimu zangu yalikuwa yamefikia shilingi trilioni 2.5. Nawapongeza sana kwa hatua hiyo. Moja ya sababu ilizungumzwa hapa kwamba ni baada ya wao kuwa wameajiri watumishi 1,500 wakaenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge tulishauri hapa, Serikali imeenda kutimiza. Tulihoji, kwa nini watu waliokabidhiwa jukumu kubwa la ku-service deni la Taifa, waliokabidhiwa jukumu kubwa la kulipa mishahara halafu wawe na tatizo la upungufu wa watumishi? Tunawataka sasa waendelee hivyo hivyo, hata ule ushauri uliotolewa kwamba waajiri hata vijana wa mkataba, vijana wetu wengi waliosemea kodi na pia tunao vijana wengi wa JKT kwenye vikosi vya kijeshi ambao wanaweza kuungana na hizi timu kwenda kuhakikisha maeneo yote ambao tunaweza tukapoteza mapato kwenye mipaka yetu, kwenye maeneo ya maji, bandari bubu na maeneo yote ambayo kuna ukwepaji mkubwa wa kodi, waweze kwenda kudhibiti maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu akiba ya fedha za kigeni, wenzangu wamezungumza hapa. Ukweli ni kwamba fedha za kigeni zimeshuka kutoka Shilingi milioni 5,209.8 hadi Shilingi milioni 5,110.3. Hili ni anguko la mwaka mmoja. Kama tusipoziba ufa, tutajenga ukuta. Uchumi wetu hauwezi kuimarika kama fedha za kigeni zinadondoka kwa kiwango hicho. Tutahimili vipi kulipa deni la Taifa? Tutahimili vipi kuagiza bidhaa kutoka nje? Kama unavyosikia sasa hivi wafanyabiashara wameanza kulalamika hawapati Dola; lakini tutahimili vipi uwekezaji hapa nchini? Kama mikataba mingine tumeingia ya Dola, tutahimili vipi kuweza ku-manage mikataba hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama fedha hizi za kigeni zitaendelea kupotea, maana yake Tanzanian Shilling itaendelea kupoteza thamani, itaadimika. Kama Tanzanian Shilling itaendelea kuadimika, lazima tutakuwa tumechochea mfumuko wa bei kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu zipo mbili tu katika hili eneo. Moja, usimamizi hafifu wa Sera za Fedha na Bajeti ambayo ni Monentary and Fiscal Policy lakini pia na ile Balance of Payment. Sasa tuliposema hapa, Waziri wa Fedha akazungumza kwamba labda kazi tunayoiweza ni Uganga wa Kienyeji, lakini hizi ndizo takwaimu ambazo zimezalishwa na taasisi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuchukue hizo hatua sasa za kuhakikisha kwamba tunaweka pendekezo lingine kali sana hapa kwa ajili ya ulinzi wa hizo fedha zetu za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi ya Serikali nje ya bajeti, Waziri wa Fedha siku hiyo alizungumza hapa kwamba Shilingi bilioni 246 zimetumika nje ya bajeti, lakini pia ruzuku ya mafuta, Shilingi bilioni 700, hizo fedha hazimo kwenye bajeti. Pia, akazungumza kwamba Shilingi bilioni 360 alizolipwa SYMBION kama CAG alivyosema siyo hizo, lakini pia hakutaja ni shilingi ngapi yeye anazozijua? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea fedha hizi zote ambazo Serikali imetumia nje ya bajeti, ingekuwa imezipeleka kwenye Kamati ya Bajeti kwa ajili ya kwenda kuangalia uhalali wake ili Kamati ya Bajeti ikubaliane nazo na kuzipitisha, lakini sasa hivi taarifa ya Kamati ya Bajeti haya yote hayamo. Maana yake Serikali imetumia fedha nje ya bajeti kinyume cha sheria, kinyume cha utaratibu na utaratibu unaofuata pale unajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Kamati ya bajeti wanatakiwa watusaidie. Kwanza tuweke azimio la kuitaka Serikali ilete matumizi yote ambayo yamefanyika nje ya bajeti halafu sasa kuanzia hapo Bunge lako Tukufu hili liweze kuchukua hatua zinazostahili kwa Waziri wa Fedha aliyesabibisha mkwamo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu deni la Serikali, ukweli kabisa nilitegemea Kamati ya Bajeti wangetuondoa kwenye mkwamo huu. Tulilalamika kwamba Deni la Serikali kwanini limeongezeka kwa kasi? Swali la pili, kwanini deni la Serikali inaonekana kwamba kuna madeni ambayo Serikali imeingia zaidi ya kiwango ambacho kimeidhinishwa na Bunge? Sasa tulitegemea leo Kamati ya Bajeti wangekuja na madeni yote. Wangekuja na jedwali linaloonesha Serikali imekopa fedha kiasi gani na kwa ajili ya miradi gani katika kipindi hiki tunachokizungumza, lakini kwa ulinganifu na zile takwimu zilizowasilishwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Aprili, 2021 mpaka Juni, 2022 ongezeko la deni la Taifa limekua kwa Shilingi trilioni 10.83, lakini kipindi cha Mei na Juni, 2021 Serikali ilikopa zaidi ya Shilingi trilioni 3.9. Katika kipindi cha mwaka 2020/2021 na 2021/2022, deni la Taifa lilikuwa linakua kwa wastani wa 4% lakini kwa sasa hivi deni la Serikali linakua katika miaka hiyo miaka miwili,...

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina, subiri taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Christopher Ole-Sendeka.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelezo mazuri ya Mheshimiwa Mpina, na kwa kuwa taarifa iliyoko hapa ni ya Kamati ya Bajeti ambayo pamoja na mambo mengine inashughulikia masuala haya ya fedha; kama unavyojua Kamati yetu ilikuwa inashughulikia masuala ya Kero za Muungano na mpaka sasa taarifa yake haijawekwa hadharani na baadhi ya maeneo mengine yalikuwa yanahusiana na fedha na mpaka sasa nchi na Bunge halijatoa taarifa juu ya masuala yanayohusiana na fedha ambayo imeridhiwa katika Kamati ya Kero za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwanini Kamati hii ambayo ingetumia fursa hii kutupa picha halisi na Serikali iweze kutupa na kanuni zinazotumika katika kugawanya fedha nyingine za Muungano katika pande zote mbili zikiwemo fedha za UVIKO ambazo tulizipata hivi karibuni tujue kanuni ambayo inatumika ili tuweze kuishauri Serikali vizuri katika masuala haya ambayo ni lazima yalindwe kwa wivu wa hali ya juu na pande zote mbili za Muungano ziweze kuridhika maana ndiyo msingi wa umoja na mshikamano wa dhati katika nchi yetu? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina, unaipokea taarifa?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilindie muda wangu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina unaipokea taarifa au hupokei?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa. Naomba unilindie muda wangu. Nimesema deni la Taifa lilikuwa likikua kwa wastani wa 4% lakini kwa mwaka 2020/2021 na 2021/2022 sasa linakua kwa 12.33.

Mheshimiwa Mwenyekiti, deni la Taifa, Kamati imesema katika jedwali Na. 2 lililowasilishwa na Kamati ya Bajeti, ukifanya hesabu pale inaonekana kwamba Serikali imekopa zaidi ya Shilingi bilioni 322 nje ya kiwango kilichoruhusiwa na Bunge. Ukiangalia pale kwenye jedwali, ni zaidi ya Shilingi bilioni 322. Pia Serikali imeenda kukopa, iliidhinishiwa hapa na Bunge kwenda kukopa mikopo ya ndani kwa ajili ya uwekezaji wa miradi ya maendeleo Shilingi trilioni 1.84, lakini Serikali ikaenda kukopa Shilingi trilioni 2.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni zaidi ya Shilingi trilioni moja. Maamuzi hayo yanasababisha sekta zetu za fedha za ndani zisiweze kupata mikopo. Pia inachochea kuongezeka kwa riba. Kama inasababisha kuongezeka kwa riba, lazima utegemee kuna mfumuko mkubwa wa bei tunaouandaa. Ndiyo maana nasema, usimamizi hafifu wa Sera za Fedha na Bajeti (Monetary and Fiscal Policy) katika nchi yetu sasa hivi umetamalaki sana. Naamini kwamba kuna shida katika utekelezaji wa Wizara ya Fedha kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana tunaposimama hapa Bungeni na mbele ya Bunge lako Tukufu, Mbunge unaambiwa kwamba wewe hujui uchumi, Mbunge eti wewe unaweza kuchangia tu kuhusu uganga wa kienyeji na kwamba mchumi ni mmoja tu katika nchi hii. Aliyesoma uchumi ni Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba peke yake ndio anayeujua uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yanasemwa kwenye Bunge lako. Ni muhimu sana kusikiliza haya ambayo tunachangia.

Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye mfumuko wa bei...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina muda wako umeisha.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja.

MWENYEKITI: Nakuongeza dakika moja kwa ajili ya kuhitimisha hoja yako.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe dakika moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbolea, katakata ya umeme na ruzuku ya mafuta. Maeneo haya ni nyeti sana ambayo yame-attract sana mfumuko wa bei hapa nchini. Naomba jambo moja, wafanyabiashara wetu wote ambao wanadai leo malimbikizo ya mbolea ni Shilingi ngapi? Mbolea ya ruzuku iliyosambazwa mpaka sasa hivi kwa wananchi wetu ni tani ngapi? Kwanini Serikali imeshindwa kulipa fedha hizo na kusababisha wananchi wetu waendelee kuteseka na suala la mbolea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini kilichopelekea usumbufu mkubwa huu wa mbolea nchini ilhali Waziri wa Kilimo aliahidi hapa Bungeni kwamba he is ready to bear any cost. Akasema ruzuku inayokuja sasa hivi haitaibiwa, ruzuku inayokuja sasa hivi haitachakachuliwa, ruzuku inayokuja sasa hivi hatuwezi kuuziwa mbolea bandia, wananchi wetu mbolea yao haiwezi ikatoroshwa na wananchi watapata mbolea kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake leo wananchi wanapata mbolea kwa shida kubwa, wengine wanafia kwenye foleni, wengine wameshindwa kulima ambako tunategemea pia kilimo kitaanguza kutokana na maamuzi hayo tuliyoyafanya. Sasa Serikali ifanye jambo moja, suala hili la mbolea liletwe hapa Bungeni kwa ukubwa wake tulijadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la katakata ya umeme ambayo haina utaratibu liletwe hapa Bungeni tulijadili kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi uliyonipa. Kwa sababu ya changamoto ya muda, niende moja kwa moja kwamba kuna baadhi ya Halmashauri zetu ambazo zina wazabuni na wakandarasi ambao walishatoa huduma muda mrefu, mpaka leo hii hawajalipwa fedha zao. Hii ni kutokana na zile Halmashauri kuelemewa na changamoto za kimapato. Kwa hiyo, wameshindwa kuwalipa wakandarasi na wazabuni ambao walishatoa huduma. Matokeo yake wananchi hawa wanateseka sana, wanauza nyumba zao, wanakimbia miji yao, wamefilisika na wana mateso makubwa. Watu walishatujengea shule tayari zinafanya kazi, barabara zinafanya kazi, miradi ya maji inafanya kazi lakini hawajalipwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu, Waziri aratibu madeni yote ya Halmashauri zilizoelemewa kulipa madeni ya wananchi hawa ili wazabuni na wakandarasi wapate haki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, tunao Waheshimiwa Madiwani, Waheshimiwa Wenyeviti wa Vijiji na Waheshimiwa Wenyeviti wa Vitongoji. Tunakubaliana sote hapa umuhimu wa hawa viongozi. Hata hivyo, viongozi hawa ambao ni Madiwani wetu ambapo leo tunaidhinisha shilingi trilioni 7.68 waende kuzisimamia, hawalipwi. Malipo ya Waheshimiwa Madiwani ni madogo mno kiasi kwamba hawawezi kuhimili na usimamizi huo wala kukidhi mahitaji ya shughuli zao wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wenyeviti wetu wa Vitongoji na Vijiji hawalipwi kabisa. Tatizo ni nini? Viongozi hawa wame- sacrifice muda wao wote kwa ajili ya kuitumikia Serikali, wanachangisha michango; tukitaka madarasa, wao ndio wanaochangisha, tukitaka zahanati wao ndio wanaofanya; tukitaka mkutano wa hadhara, wao ndio wanaofanya; kwa nini hawalipwi viongozi hawa? Sababu za kutokulipwa ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mtendaji wa Kijiji analipwa, Watendaji wengine wote kwenye Kijiji hata 30 wanalipwa, lakini Mwenyekiti wa Kijiji mshahara wake unakosekana. Ni nani huko Serikalini ambaye alishakataa hawa viongozi wasilipwe mishahara yao inayostahili kulingana na kazi wanazozifanya? Nashauri Serikali ifanye maamuzi ya kuwalipa hawa viongozi ili nao waweze kutoa huduma sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, tumezungumzia kuhusu kupeleka shilingi trilioni 7.68 kwenye Halmashauri zetu. Kwanza nikubaliane kwamba hizi fedha ni ndogo kulingana na mahitaji tuliyonayo; mahitaji ya barabara, maji, zahanati na huduma mbalimbali kwenye maeneo yetu ya Serikali za Mitaa na kwamba hili ndiyo eneo muhimu sana ambalo wananchi wetu wanapata huduma moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tunapeleka fedha katika eneo ambalo tayari lina changamoto nyingi. Kama tulivyoona taarifa ya CAG kwamba, hati safi zinazidi kuporomoka, hati zenye mashaka zinazidi kuporomoka na kwenda kwenye hati mbaya. Maana yake tunapeleka fedha eneo ambalo lina changamoto kubwa sana ya usimamizi.

Mheshimiwa Spika, sasa hizi changamoto kwa nini zimekuwa za kudumu? Nadhani hapa kuna kazi ambayo haijafanyika sawasawa. Hii kazi tukitaka tuifanye sawasawa lazima tuzifanye kikamilifu zile activities zote ambazo zinazohusika ili tuweze kukomesha. Haiwezekani Bunge hili kila likikutana linazungumzia watu kutosimamia fedha vizuri na watu kupata hati chafu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, leo tunaweza tukazungumza Halmashauri zilizopata hati mbaya na chafu, lakini unakuta watumishi wanaohusika hata na kuandaa hizi hawapo. Unakuta hakuna wahasibu, hakuna wakaguzi, unapataje hati safi katika mazingira haya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkaguzi hapa anasema, nafasi 510 zinakaimiwa. Kwa nini nafasi 510 zikaimiwe? Kwa nini tuwe na upungufu mpaka wa watumishi Wakuu wa Idara, Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo; tunakuwaje na upungufu na watu hawa? Kwa nini hizi nafasi zisizibwe mara moja? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, hivi kwa nini tuendelee na utaratibu wa vetting na mambo ya seniority katika kuajiri? Hivi kuna shida gani Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na Wakuu wa Vitengo wakapatikana kwa njia ya ushindani tu? Tunavijana wengi competent sasa hivi. Sasa unafanya vetting, miaka mitatu unampata mtu uliyemfanyia vetting miaka mitatu, halafu miezi sita unamtumbua kwa kutokuwa na uwezo. Kwa nini tusifanye ushindani? Wakafanya oral, wakafanya written, tukapata competent? Vijana tunao wa sekta zote, competent kabisa. Kwa nini twende na mambo haya?

Mheshimiwa Spika, nafasi hizi zijazwe na tusikubali kuwa na upungufu mpaka wa watalaamu? Mtu wa kusoma X-Ray ni mmoja, halafu unakuwa upungufu wa huyo huyo, kweli! Meatu pale leo miaka mitatu X-Ray haifanyi kazi. Ipo pale, haifanyi kazi, hakuna mtaalam wa kusoma.

Mheshimiwa Spika, la pili, tunao hawa wakaguzi wetu, hivi tunapate hati chafu? TAMISEMI mnapataje hati chafu wakati una Kitengo cha Ukaguzi ambacho kinatoa taarifa kila robo mwaka? Mnazisimamiaje hizo taarifa? Mnazi- coordinate vipi zile taarifa za ukaguzi mpaka mwingie kwenye hati chafu? Hapa kuna tatizo kubwa la usimamizi.

Mheshimiwa Spika,...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Luhaga.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia Taarifa ya hizi Kamati mbili; Kamati ya Katiba na Sheria, Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla hoja zote za Kamati naziunga mkono japo kuna baadhi ya maeneo taongezea ushauri wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni madai na usuluhishi; Serikali yetu imekuwa ikiendesha kesi mbalimbali za madai na usuluhishi Kitaifa na Kimataifa na tulipewa taarifa kwamba na labda kwa kuanzia mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria na tulipewa taarifa kwamba Serikali imeweza kuokoa shilingi trilioni 13.33 katika haya mashahuri ya madai na usuluhishi yaliyokuwa yakiendeshwa Kitaifa na Kimataifa. Lakini kiwango hicho ni kikubwa, lakini pia ni cha kupongezwa kwa Serikali kuweza kuokoa matrilioni hayo ya shilingi ya Watanzania katika madai na usuluhishi yaliyokuwa yakiendeshwa sehemu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto moja tu; kiwango tu ni cha fedha, lakini bango kitita sasa linaloeleza kwa kina ni kesi gani, zilifunguliwa mwaka gani, kwa mkataba gani, juu ya nani, tulishtakiwa na kampuni gani mpaka tukaokoa hizi fedha ili tuweze kujua kwanza tuliingiaje kwenye mikataba hiyo na mpaka leo tumeendesha mashauri ya madai na mashauri ya usuluhishi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili; Serikali haijatuambia katika kipindi hiki cha ripoti hii wakati inawasilishwa ni mashauri mangapi ya madai na usuluhishi ambayo Serikali imeshindwa? Na yalikuwa kwenye maeneo gani? Tulikuwa tunashtakiwa kwenye nini? Ni fedha kiasi gani tulicholipa mpaka sasa hivi? Hii itatuwezesha Wabunge kufahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Bunge hili likawa linaletewa tu tumeshindwa kesi Mahakamani, mmeshindwa kesi hiyo juu ya nini? Mmeshindwaje shindwaje na lazima uwepo utaratibu mzuri wakuwa wanawasilisha haya mashauri kama sasa hivi tunavyozungumza wewe unajua kwamba ndege yetu moja ya Airbus imekamatwa juu ya mkataba mbovu, imeshikiliwa kwa sababu tunadaiwa. Sasa hilo nalo tunapaswa tuelezwe hatima ya hiyo ndege yetu mpaka sasa hivi ikoje?

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Kuhusu Utaratibu, nimekuona Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

KUHUSU UTARATIBU

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa kwa mujibu wa Kanuni ya 71; shauri analoliongelea Mheshimiwa Luhaga Mpina kuhusu kukamatwa kwa ndege bado lipo Mahakamani kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kiuwekezaji. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Kanuni ya 71 ni shauri ambalo haliwezi kuwa na sifa ya kujadiliwa kwa sasa.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti unilindie muda wangu. Sijadili, lakini Bunge hili linalo haki ya kupewa taarifa kama alivyoisema sasa hivi ambayo haina siri yoyote, tujue, unaambiwa tu ndege imekatwa, ndege imekamatwa kwa jambo gani? (Makofi)

Kwa hiyo, taarifa ni muhimu sana na yeye kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitakiwa kuleta kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ikaelewa nini kinachoendelea juu ya mambo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na usiri huu utakuja kushtukia mambo yanatokea mengine ndege imetaifishwa, ndege imefanya nini? Tuwe tunapeana taarifa juu ya mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tatizo na changamoto hapa ya muda ninachoweza kusema tu kuanzia sasa hivi tuongeze azimio moja la kuitaka Serikali mashauri yote ambayo Serikali imeshindwa Mahakamani wayalete kwenye Kamati husika, tujue wameshindwa kwenye jambo gani, kabla ya kulipa hizo fedha za Watanzania. Hatuwezi kuendelea kulipa fedha za Watanzania katika mchezo, mchezo tu ambao baadhi ya watumishi wa umma wanaenda kunufaika na hizo kesi na ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais amelalamikia sana juu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, marekebisho ya Katiba na upatikanaji wa Katiba mpya; Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa mwongozo kuanzia Juni, 2022 kuhusiana na kuanza mchakato wa maandalizi ya marekebisho ya Katiba tuliyonayo, lakini pia hata mapendekezo ya Katiba mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo mpaka sasa hivi Wizara ya Katiba na Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hakuna mwongozo wowote, hakuna deadline yoyote, hakuna utafiti wowote, hakuna jambo hili mpaka sasa hivi toka kiongozi wa nchi atoe maelekezo leo ni miezi saba halijawekwa mahala popote kwa hiyo huwezi hata kuona linafanyika kazi kwa namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninafikiri na ninaungana kabisa na Mheshimiwa Rais kwamba muda muafaka wa kuangalia Katiba yetu na moja ya eneo ambalo ni muhimu sana ni kwamba Katiba tuliyonayo haina nguvu za kutosha kulinda na kusimamia fedha na rasilimali za umma kwa sasa na ndiyo maana sasa hivi Wabunge wote hapa walivyokuwa wakichangia Kamati hizi za kifedha wote wamelalamika fedha zimeibiwa, fedha zimeliwa, kila mtu Taarifa za CAG, Taarifa ya TAKUKURU, Taarifa ya PPRA zote watu wanalalamikia juu ya wizi wa fedha lakini wizi wa fedha ambao hauna dawa inawezekana kabisa tobo kubwa lipo kwenye Katiba ndiyo maana hatujaweza kutatua tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matobo unaweza kuyaona, Taarifa ya CAG hapa Bungeni, Taarifa ya PPRA na Taarifa ya TAKUKURU hazipati muda wa kutosha kujadiliwa na Wabunge juu ya hatua mahususi zinazochukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia usiri wa mikataba; kuna usiri mkubwa sana wa mikataba, matokeo yake usiri huu wa mikataba ndiyo imekuwa tobo la kusababisha fedha za Watanzania kupotea. Hapa kuna mkataba ule wa SGR kipande cha Tabora – Kigoma ambao tayari una mashaka ya shilingi trilioni 1.7 malipo ambayo yanatarajiwa kwenda kulipwa yenye mashaka, lakini tuna Mkataba wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao mpaka sasa hivi haujulikani mradi huu utaisha lini, tarehe haijulikani, lakini hata hatma ya Watanzania fine ya shilingi trilioni 1.3 anayotakiwa kuilipa mkandarasi haijulikani na CSR ya shilingi bilioni 260 na yenyewe haijulikani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mikataba kama ya TRAT na TRAB, CAG amesema tulipwe, Waziri wa Fedha anasema tusilipwe. (Makofi)

Sasa mpaka nayo haina hukumu hiyo na mikataba mingine yote ambayo inaingiwa na Serikali kwa siri. Tukatae mambo haya kwa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kuziba hili tobo kwenye Katiba mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa Bungeni Waziri wa Fedha…

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, nani anatoa Taarifa?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, unitunzie muda wangu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Ndumbaro, Taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba TRAB na TRAT sio mikataba bali ni vyombo vya utatuzi wa migogoro ya kodi. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina, unapokea taarifa?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake. Ni hukumu ya TRAT na TRAB. Nilimaanisha hukumu ya TRAT na TRAB ambayo CAG ameshathibitisha Watanzania tunaweza kulipwa shilingi trilioni 5.595, lakini mpaka sasa hivi hakuna hatima yake na hata tukihoji Wabunge mnakaliwa kimya, hamjibiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba mingine iliyoingiwa na Serikali mingine inaingiwa kwa usiri, mingine hatujui hata tumeingia mkataba ambao una madhara gani kwa Watanzania. Hili tobo hili ni lazima tulizibe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katika Bunge usimamizi dhaifu wa sheria, Waziri wa Fedha alisimama hapa akasema, nimalizie lingine nimeongea tena na ndugu yangu jirani kwamba mwaka juzi reserve zimeshuka kutoka dola bilioni 6,000 zimeshuka zikawa bilioni 4,500. Jamani masomo ya uchumi ni sayansi, narudi tena twendeni tufuatilie kwa makini reserve zina-build vipi. Reserve zilizoongezeka zilikuwa ni trilioni 1.3 tumetoa IMF na ndio zikaongezeka reserve.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, toka nchi hii ianze hatujawahi kuwa na akiba ya fedha za kigeni bilioni 6,000 wala hatujawahi kuwa na akiba ya fedha za kigeni reserve bilioni 4,500. Kwa hiyo, haya ni maneno ya uongo, hatujawahi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii ambayo umenipa ili nami niweze kuchangia hii Hotuba muhimu sana ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimepitia Hotuba, nimesoma hotuba yote ya Mheshimiwa Waziri ambayo ina kurasa zipatazo 201. Napenda nikiri kabisa kwamba taarifa hii ya Mheshimiwa Waziri imesheheni mambo mengi muhimu sana katika ujenzi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimeangalia Taasisi zetu zinavyofanya kazi vizuri. Taasisi ya CAMARTEC, TIRDO, TIMDO na SIDO. Kazi nzuri waliyoifanya ya taknolojia ya kisasa ya kuandaa mashine ambazo zinaongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa kwa ajili ya usindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Hii ni kazi nzuri sana ambayo inafanywa na taasisi zetu hizi na mimi nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Ma-CEO wa taasisi hizo pamoja na watumishi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kazi kubwa hapa ni kuzisaidia hizi taasisi sasa ziweze kufanya kazi vizuri zaidi. Utakuta taasisi kama hizi zinafanya kazi kubwa kama hiyo, lakini nenda kaangalie bajeti zao, utasikitika sana. Serikali itenge fedha nzuri, nyingi za kutosha kuziwezesha hizi Taasisi. Tuna vijana wetu waliobobea vizuri na ndio wanaoyafanya haya mambo makubwa. Kwa hiyo, ni muhimu sana wakaweza kupewa fursa ya kuweza kufanya kazi vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu uwekezaji wa Serikali pamoja na sekta binafsi. Waheshiwa Wabunge hili suala la uwekezaji wa Serikali na sekta binafsi linahitaji kuangaliwa kwa makini sana. Mikataba mingi tuliyoingia inanyonya mapato ya nchi. Mikataba mingi tuliyoingia katika uwekezaji wa Serikali na sekta binafsi inanyonya uchumi wa nchi, inahamisha rasilimali za nchi na inahamisha ajira za Watanzania. Lakini vilevile katika mikabata hii mingi tunayoingia inapora ajira za Watanzania, kwa hiyo unajikuta kwamba mkataba unaingiwa wa Watanzania hawa ambazo fedha za Watanzania zinaenda kulipa ajira kwa watu wengine wakati tunao vijana ambao wanaweza kufanya kazi nzuri sana hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mikataba mingi ambayo tunayoingia ambayo ni questionable na mingine imetuletea madhara makubwa sana. Tunayo mikataba, sasa hivi TPA naye ameanza kutafuta mdau, ameanza kutafuta mbia. Mikataba ya namna hii; lakini ipo mikataba inayotusumbua mpaka sasa hivi ya TRA na SISPA Company ambayo nayo inahamisha fedha za Watanzania. Lakini ipo mikataba mingine tumeingia majuzi hapa ya India Tech Mahindra na TANESCO ya ziadi ya bilioni 70 kwa ajili ya kuendeleza mifumo ya TEHAMA wakati wataalam wa TEHAMA tunao hapa wa kila aina wanaoweza ku-develop mifumo ya TEMAHA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu wameandaa mifumo mizuri kama GePG, POS na hata MaxMalipo, mifumo mizuri tu. Leo unaenda kutafuta mfumo India kwa ajili ya kufanya nini? Sasa mikataba ya namna hii imekuwa ikituletea madhara makubwa sana. Na hivi sasa hivi nasikia Symbion inapigiwa chapua hapa tuilipe bilioni 356, bilioni 356 lakini inapigiwa hili chapuo wakati huo huo hatuambiwi aliyeingia mkataba huo na kutusababisha tuwe na mkataba ambao hatuwezi ku-exit hata kama mkataba ule unatuingizia hasara, amechukuliwa hatua gani? Tunaambiwa na chapuo hilo linapigwa bila kuambiwa kwamba huyu Symbion malimbikizo yake ya kodi ni shilingi ngani na anapaswa kutulipa shilingi ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, linapigwa hilo chapuo hatuambiwi ukaguzi gani uliofanyika juu ya mambo yaliyojificha nyuma ya pazia hili. Wabunge tukataeni mikataba ya namna hii lakini tukataeni hata kulipa hizi fedha. Uchunguzi ufanyike, ukaguzi wa kina ufanyike kilichojificha nyuma ya Symbion tuweze kuyajua yote mazagazaga yaliyopo na tuweze kuzijua haki zetu zilizopo katika hilo eneo. Lakini mikataba yote ambayo tunaitambulisha kwamba ni mikataba mibovu iitishwe hapa Bungeni tuweze kuifuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hili suala la mfumuko wa bei. Suala la mfumuko wa bei. Ni kweli imeelezwa hapa kwamba mfumuko wa bei umesababishwa na UVIKO 19 pamoja na vita vya Urusi na Ukraine, tumeelezwa hapa. Ni kweli sababu hizi zinachangia mfumuko wa bei, lakini zipo sababu zingine ambazo zimechangiwa na ukosefu wa uadilifu wa viongozi wetu na watendaji wetu. Ziko sababu zilizosababishwa na uzembe na usimamizi dhaifu wa maeneo mbalimbali ambao tunaufanya sisi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachosema na kuliambia Bunge lako hili ni kwamba mfumuko wa bei huu unaoendeelea hivi sasa umesababishwa na umetengenezwa na tumeutengeneza sisi wenyewe tuliomo humu ndani. Mateso haya ya mfumuko wa bei ambayo wanayapata wananchi sasa hivi tumeyatengeneza hapa kwa kukosekana kwa uadilifu, kwa kukosekana kwa usimamizi makini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la upangaji holela wa bei. Upangaji holela wa bei sisi wote tunashuhudia hapa, bidhaa zote zimepanda bei, kila siku zinatangazwa bidhaa kupanda bei. Lakini ukweli ni kwamba pamoja na sababu zingine, sababu ya upangaji holela wa bei, mtu anaamua tu kupandisha bei hili suala limekuwa likiturudisha nyuma sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri hapa ametueleza kwamba kuna upandaji holela wa bei lakini tunachoshangaa ni kwamba kama kuna upandaji holela wa bei, na yeye Waziri anajua na anayo mamlaka yake ya FCC inayosimamia ushindani, na Sheria ya Ushindani Namba Nane ya Mwaka 2003, hawa watu wanaopandisha bei kiholela kwa nini hawajachukuliwa hatua? Kwa nini hawajachukuliwa hatua? Waziri anawajua waagizaji wa mafuta nje ya nchi, anawajua waagizaji wa ngano nje ya nchi, anawajua wazalishaji wa ndani na amefanya tathmini na akagundua watu wamepandisha bei kiholela. Hao waliopandisha bei kiholela kwa nini hawajarudishwa kwenye mstari ili wananchi waweze kupata bei nafuu? Waziri kwa nini anawaogopa hawa? Au anataka kutuambia kwamba watu hawa wana nguvu zaidi kuliko Serikali? Au Waziri anaubia nao? Na kuwaacha Watanzania waendelee kuteseka na mfumuko huu mkubwa wa bei wa kuamuliwa na watu waliokaa na kukubaliana tu tupandishe bei? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la uhaba wa nishati ya umeme. Kuhusu suala la uhaba wa nishati ya umeme, Kamati imetueleza hapa imesema ilipotembelea viwanda viwili ikaenda kugundua kwamba kuna viwanda umeme ulikuwa unakatika mara 10 ndani ya masaa manne. Ni maneno ya Kamati siyo maneno ya Mpina. Umeme ulikuwa unakatika zaidi ya mara 10 ndani ya masaa manne. Pale unategemea kuna uzalishaji gani? Uzalishaji viwandani unashuka na kama uzalishaji viwandani ukishuka wafanyabiashara wataamua kupandisha bei, kwasababu uzalishaji wao utakauwa umeshuka, ili waweze kufidia gharama ya uzalishaji na kupata faida, na ndiyo lazima upate mfumuko wa bei.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja.

MWENYEKITI: Haya malizia.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni mafuta. Mafuta, Mbunge mwenzetu hapa Mheshimiwa Hamis Tabasam, Mbunge wa Sengerema alitueleza kuna wizi mkubwa unaofanywa kwenye Petroleum Bulk Procurement Agency kuna wizi mkubwa unafanyika kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa hivi hoja ya wizi unaofanyika kule kwenye agency ya kununua mafuta tulitegemea ingeweza kuwekewa ukaguzi wa haraka, CAG na PCCB wakavamia wakafanya ukaguzi na kuujua ukweli kama Watanzania wamepandishiwa bei na mafisadi wachache na wezi wachache tukaujua ukweli lakini sasa hivi hoja inaondolewa kwenye wezi waliofanya wizi inapelekwa kwenye tozo ambazo hizi tunapata shughuli za maendeleo nyingi kutokana na hizo tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi seriousness yetu iko wapi? Watanzania wanalia, wanapandishiwa bei za mafuta, watu wanatangazwa kufanya njama za manunuzi, wanafanya wizi kwenye manunuzi, wanapandisha bei makusudi, tunaletewa taarifa hapa Bungeni ukaguzi haufanyiki na uchunguzi haufanyiki. Ni lazima mambo haya tuyakatae na lazima tuwahurumie Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi uliyonipa na nianze kabisa mwanzo niwaombe kabisa Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Naibu Spika kwamba Bunge hili tusikubali kutumika kama mahali pa kuhalalisha wahalifu na wabadhirifu wa fedha za umma, na kwamba la kuvunda halina ubani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana na kuwapongeza sana mamlaka za ukaguzi pamoja na za uchunguzi, CAG, CPA Charles Kichere pamoja na CP Salum Hamdun, Mkurugenzi wa TAKUKURU, kwa kazi nzuri sana waliyoifanya ya ukaguzi wa fedha za umma mwaka huu. Taarifa zao walizozitoa pamoja na watendaji wao kule ofisini ni kielekezo kikubwa sana cha uzalendo wa Taifa lao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana kipekee Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukataa katakata nchi yake kugeuzwa kuwa shamba la bibi. Na mimi nasema Mawaziri waliohusika, watendaji wote wa Serikali waliohusika mapema iwezekanavyo wakamatwe, washtakiwe na wafunguliwe makosa ya uhujumu uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii tunajadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna mambo mawili tu ya kiujumla ninayotaka kuyasema; moja bajeti ya maendeleo tuliyopanga mwaka huu wa fedha, katika mpango wetu wa miaka mitano tulipanga iwe asilimia 37.1 lakini mpango wa maendeleo uliowasilishwa na Serikali, fedha za maendeleo ni asilimia 34.1 tu; nini kilichosababisha mpango wetu kushuka, nini kilichosababisha fedha za maendeleo kushuka tofauti na mpango wa maendeleo tuliouweka wa miaka mitano?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala zima la Katiba; nimesoma mpango wa maendeleo na ukomo wa bajeti sijaliona suala hili; nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu sijaliona suala hili, na suala hili Mheshimiwa Rais amelisisitiza sana, sikutegemea nilikose kwenye hotuba kubwa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu au kwenye taarifa kubwa ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ikija Serikali hapa itueleze hili suala likoje, licha ya Mheshimiwa Rais wetu kulisema kwa msisitizo mkubwa kwamba ni lazima tufanye mabadiliko katika Katiba yetu na ikiwezekana tupate Katiba mpya inayohitajika kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu ni suala la vihatarishi au changamoto mahususi katika utekelezaji wa bajeti tunayoizungumza leo. Ukipitisha bajeti kukiwa na vihatarishi vingi ambavyo vinaashiria kwamba mpango wa bajeti tunaoupitisha unakwenda kukwamba tu, ni lazima ujishirikishe, ufanye tathmini ya kutosha juu ya tahadhari hizo, juu ya changamoto hizo, ufanye tathmini ya kina, uone ni namna gani unakwenda kuzitatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Serikali kupitia mpango wa maendeleo ukurasa wa 89 kipengele cha 2.4.2 inakiri wazi kwamba kuna vihatarishi vingi vinavyopinga utekelezaji wa bajeti. Kwa kifupi tu kwamba kuna upungufu mkubwa wa rasilimali watu, kuchelewa kukamilisha taratibu za utoaji cheti cha msamaha wa kodi, usanifu duni, usimamizi usioridhisha katika utekelezaji wa miradi kwa mujibu wa mikataba na mipango kazi kwa baadhi ya watekelezaji wa miradi, kucheleshwa kwa malipo ya wakandarasi na sababu nyingine nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi sababu inasema Serikali yenyewe kwamba hizi ni changamoto. Moja, maana yake Waziri Mkuu atuambie kwamba Serikali imeshindwa kuzidhibiti hizi sababu? Lakini la pili; tunashindwaje kutoka pale? Na ukienda sasa kuzichambua hizi hoja ndizo hizi ambazo zinaturudisha nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakaa hapa, tutaidhinisha bajeti ambayo mwisho wa siku inakwenda kutafunwa na watu wachache. Tunarudi hapa tena unatupa tena jukumu la kupitia bajeti inakwenda kuliwa na watu wachache. Ni lazima hizi nyufa tuzizibe leo. Tunapopitisha bajeti na nyufa zenyewe tumeziziba ili fedha za wananchi zisiende kuliwa tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, kushindwa kutekeleza mpango wa manunuzi ni jambo ambalo kwenye mpango wa maendeleo wamesema wao wenyewe Serikali na hapa imetokea, na CAG amelisema. Jumla ya trilioni 3.14 hazikutumika, zikiwemo fedha tulizozituma kwenda TANROADS.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania mwaka 2021/2022 waliahidiwa kujengewa barabara zao zaidi ya trilioni 2.9 za TANROADS hazikwenda kufanya kazi, hakuna mradi ulikuwa implemented. Leo tena tunarudi hapa kupitisha bajeti halafu pesa zikawekwe, Watanzania waendelee kuteseka bila kupata maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kutokufuata Sheria ya Manunuzi. Tunajua tunapitisha bajeti hapa, mwisho wa siku hizi pesa zinakwenda kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia Sheria ya Manunuzi, halafu sheria hiyo inakiukwa kila leo, halafu tunaletewa tena bajeti inakiukwa na fedha za wananchi ziliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisimama hapa kwenye Bunge lako tukufu nikazungumzia juu la Lot No. 6, mradi wa SGR kutoka Tabora kwenda Kigoma kwamba TRC imeacha bei ya ushindani kwa kilometa moja ya standard gauge ya bilioni 9.1 imekwenda kumpa mkandarasi CCECC kwa bilioni 12.5, zaidi ya bilioni 3.4 kwa kilometa na kuisababisha Serikali hasara ya trilioni 1.7. Mkataba huu bado unaendelea, tusipofanya intervention utaendelea. Nchi imekula hasara ya bilioni 1.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lot 3 na Lot 4 mkaguzi ame- confirm kwamba tumepunjwa trilioni 1.7; lakini pia na ununuzi wa mabehewa bilioni 503; jumla trilioni nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi fedha ni za Watanzania, Waziri wa Fedha alikwenda kukopa hizi fedha kwa sharti la kuvunja Sheria ya Manunuzi ambayo hana uwezo huo, hana uwezo huo mkubwa wa kisheria, hana uwezo mkubwa huo wa Kikatiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi Waziri wa Fedha, Waziri wa Uchukuzi na Mkurugenzi wa TRC kwa nini hawajakamatwa na kufunguliwa makosa ya uhujumu uchumi mpaka sasa hivi wako hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, tusicheke, shilingi trilioni nne za Watanzania zinakwenda kupotea kwenye mradi huu. Hata kama tungeenda kukopa mkopo sijui wa riba ngapi, tunalipa fedha kidogo sana katika mambo mengine haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hizo dakika tatu zilizobaki, nizungumzie mambo mawili ya mwisho; kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere hapa na kwenyewe tulisema sana hapa Bungeni ikiwemo mimi, kwamba jamani hawa watu tunawadai fedha zetu, kwa nini hawalipi? Majibu ambayo yanatolewa na Waziri wa Nishati hayaeleweki, kila leo tukiuliza hapa Bungeni. Mkaguzi amekwenda ku-confirm tunawadai bilioni 327 kwa mwaka mmoja wa 2022. Mwaka 2023 tunadai zingine, kwa hiyo ni jumla ya bilioni 655. Ukijumlisha na zile za CSR ni bilioni 270; jumla ni bilioni 926 tunazowadai. Na mkataba unakaribia kwenda mwisho, lakini fedha hizi hazidaiwi na hawa watu, Waziri wa Nishati yupo, Mkurugenzi wa TANESCO yupo, hawadai fedha hizi na bado wapo kwenye ofisi za Serikali. Mamlaka zinazotakiwa kuchukua hatua ziko wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho; leo tulikuwa tunalalamika hapa sisi tunawezaje kupitisha Bajeti, halafu mtu mwingine anakwenda kutumia matumizi nje ya bajeti, mtu mwingine anakwenda kukopa mikopo zaidi ya fedha tulizoidhinisha hapa. Kwa hiyo, fedha alizokopa hatujaidhinisha, matumizi ya hizo fedha zinakwenda kutumika kwenye nini, hatujaidhinisha. Leo mkaguzi amekwenda ku- confirm, mwaka wa 2021/2022 Waziri wa Fedha amekwenda kukopa trilioni 1.285 bila ridhaa ya Bunge, bila ridhaa ya mtu yeyote, fedha za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatujui hizo trilioni 1.285 zimekwenda kufanya nini, hatujui alizikopa akazipeleka wapi, mpaka sasa hivi na jambo hili linaendelea kutunzwa kwa usiri mkubwa. Mambo haya inawezekanaje yakafanyika hivyo yanavyofanyika?

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunawadai IPTL bilioni 342, fedha hizi tulishashinda kesi kihalali toka tarehe 1 Machi, 2021; kazi ni TANESCO na Waziri wa Nishati kwenda kuzidai, imeshindikana. Wanashindwa nini kwenda kudai; wana ubia gani na huyu IPTL, wananufaika nini na huyu IPTL fedha za Watanzania? Na kama jambo hilo limewashibda si wawaachie Watanzania wengine wazalendo ambao wanaweza kuzipigania fedha za Watanzania. Watanzania wanyonge hawa ambao wanateseka kwa kodi zinazowaumiza kila leo, fedha zao wanazoweza kuzichukua, ambazo zipo kwa mujibu wa sheria hazidaiwi na watu ambao walishapewa dhamana ya kuziomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa summary tu hapa, ubadhirifu wote huu wa CAG ambao mimi nimeainisha na bado naendelea kuainisha ni zaidi ya trilioni 30. Sasa ukishakuwa na ubadhirifu wa trilioni 30 unakaa kwenye bajeti kufanya nini? Yaani unazipitisha hela zote zikagawanywe? Na hapa lazima tuchukue hatua kali dhidi ya watu hawa wanaofanya haya mambo. Kama Bunge lako litashindwa kuchukua hatua katika hili, basi hili Bunge liwajibike… [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, utangulizi; na kabla sijaanza kuchangia, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Spika tusikubali Bunge hili tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutumika kama sehemu ya kusafisha wahalifu na wabadhirifu wa mali za umma kwani la kuvunda halina ubani. Na hapa nichukue nafasi hii, kuzipongeza sana Mamlaka za Ukaguzi na Uchunguzi kwa kazi nzuri walizofanya katika hesabu zinazoishia mwaka 2021/2022 kwa kuibua wizi, ubadhirifu na ufisadi pamoja na matumizi mabaya ya madaraka katika taasisi mbalimbali za Serikali nchini.

Mheshimiwa Spika, hongera sana kwa CAG, CPA – Charles Kichere na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP – Salum Hamduni, hongereni pamoja na maafisa wote wa Ofisi zenu. Uchunguzi na ukaguzi mlioufanya ni kielelezo kikubwa cha uzalendo mlionao kwa Taifa letu, Mungu awabariki sana; na kipekee nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukataa kata kata nchi yetu kugeuzwa shamba la bibi. Na hapa naweka msisitizo Mawaziri na watendaji wote waliohusika wakamatwe na washtakiwe kwa makosa ya uhujumu uchumi.

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024, lakini pia nimesoma Mpango wa Maendeleo na ukomo wa bajeti ya mwaka 2023/2024 pamoja na taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 ili kuona hatua za utekelezaji wa majukumu na changamoto za Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla. Baadhi ya masuala ya kiujumla ni kama ifuatavyo: -

(i) Bajeti ya maendeleo kushuka na kufikia 34.1% mwaka wa fedha 2023/2024 ni kinyume na Mpango wa Maendeleo III wa miaka mitano ambapo walau fedha za maendeleo zisipungue chini ya 37.1% ya bajeti nzima. Nini kimesababisha bajeti ya maendeleo kushuka?

(ii) Katiba Mpya, licha ya maelekezo ya muda mrefu ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuanza kwa mchakato wa marekebisho ya Katiba na upatikanaji wa Katiba Mpya, hotuba ya Waziri Mkuu na mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/2024 hazijaeleza chochote kuhusu maandalizi ya suala hili muhimu. Waziri Mkuu aeleze hatua zilizofikiwa katika mchakato wa Katiba Mpya.

Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto mahsusi ya utekelezaji wa bajeti; mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/2024, ukurasa wa 89 kipengele cha 2:4:2 Serikali inakiri kuwepo kwa changamoto mahsusi zinazokwaza utekelezaji wa miradi nanukuu kama ifuatavyo: -

(a) Upungufu wa rasilimali watu hususan wahandisi wa kusimamia utekelezaji wa miradi pamoja na wataalamu wa uendeshaji wa mitambo na vifaa vinavyotumia teknolojia ya kisasa;

(b) Watekelezaji wa miradi kuchelewa kukamilisha taratibu za utoaji wa cheti cha msamaha wa kodi hali inayosababisha kuongezeka kwa gharama za mradi (madai ya riba) na kuchelewa kwa kutekeleza mradi;

(c) Usanifu duni wa mradi hali inayosababisha kuongezeka kwa mawanda, gharama na muda wa utekelezaji wa miradi;

(d) Usimamizi usioridhisha katika utekelezaji wa miradi kwa mujibu wa mikataba na mipango kazi kwa baadhi ya watekelezaji wa miradi;

(e) Kuchelewa kwa malipo ya makandarasi kunakosababishwa na kutowasilishwa kwa nyaraka muhimu za kuwezesha kufanyika kwa malipo kwa wakati hali inayosababisha malimbikizo ya riba na ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi;

(f) Usimamizi na uratibu kwa baadhi ya taasisi kufanyika katika ngazi ya makao makuu bila kushirikisha wasimamizi waliopo katika eneo la mradi hali inayosababisha miradi kuchelewa, kuongeza gharama na kupunguza ufanisi katika malengo ya mradi;

(g) Ushirikishwaji mdogo wa wadau muhimu wa mradi katika kipindi cha maandalizi hali inayosababisha kubadilika kwa mawanda ya kazi wakati wa utekelezaji; na

(h) Kuchelewa kwa malipo ya fidia kwa wananchi wanaopisha miradi.

Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu wewe ndio msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali na haya yote yanatokea chini ya usimamizi wako, nini kilichoifanya Serikali ishindwe kuchukua hatua stahiki na kuondoa dosari hizo? Kama Wabunge tulitegemea Serikali ingekuwa imetatua changamoto hizo badala ya kulalamika kwa wananchi huku Taifa likiendelea kupata hasara kubwa.

Mheshimiwa Spika, usimamizi wa bajeti na fedha za umma; leo tunajadili hotuba ya bajeti ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 kukiwa na wizi, rushwa, ubadhirifu na ufisadi wa fedha na rasilimali za umma umetamalaki kila sehemu, fedha nyingi zinazoidhinishwa na Bunge zinaishia mikononi mwa wezi wachache ndani ya Serikali kutokana na mikataba mibovu, usimamizi dhaifu wa mikataba, malipo yasiyo na tija, matumizi na mikopo nje ya bajeti, manunuzi yasiyozingatia sheria, kuongeza bei katika hati za malipo (over invoicing), kutokutekeleza mipango ya manunuzi kama ilivyoidhinishwa na Bunge na kukosekana uwajibikaji Serikalini.

Mheshimiwa Spika, leo ni siku mbaya ambayo tunakwenda kuidhinisha fedha za umma zikagawanwe tena na wachache. Katika kufanya hivyo ni muhimu sana kupitia na kufanya tahmini ya kina juu ya vihatarishi vitakavyopelekea bajeti hii kutotekelezwa ipasavyo, ipo mifano michache kupitia taarifa za utekelezaji na Ripoti ya CAG inayoonesha kuwa kuna vihatarishi vikubwa vinavyoweza kufanya bajeti hii isitekelezeke kwa tija kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kushindwa kutekeleza mpango wa manunuzi; mapitio ya utekelezaji wa mpango wa manunuzi mwaka 2021/2022 imeonesha taasisi 22 zilishindwa kutekeleza mpango wa manunuzi wenye thamani ya kiasi cha shilingi trilioni 3.14 kati ya fedha hizo TANROADS ni shilingi trilioni 2.9 ambazo taasisi hiyo ilishindwa kukamilisha mchakato wa manunuzi kutokana na kuchelewa kupata kibali cha kutangaza zabuni za miradi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (CAG).

Mheshimiwa Spika, Bunge liliidhinisha fedha hizi katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi mbalimbali kwa maslahi ya Taifa na badala yake fedha hizo hazikutumika na hazijulikani zilipo. Katika mwaka huo wa fedha mapato ya Serikali yalipatikana kwa 97.2% na mikopo ilipatikana kwa 106%; iweje zabuni zisitolewe kwa mwaka mzima, wananchi wanaendelea kuteseka kwa kukosa huduma muhimu ikiwemo barabara, Wabunge wanalia Bungeni, wengine wanapiga magoti Bungeni, wengine wanapiga sarakasi Bungeni kutokana na kukosa fedha za kugharamia miradi ya majimbo yao.

Mheshimiwa Spika, ushauri; CAG na TAKUKURU wafanye uchunguzi na ukaguzi maalum ili kujua sababu zilizopelekea Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, TANROADS na taasisi zingine kukaa na fedha mwaka mzima bila matumizi na pia kujua fedha hizo ziko wapi.

Mheshimiwa Spika, hatua kali za kiutawala na za kisheria zichukuliwe ikiwemo kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi kwa wote waliohusika kwa uzembe na ufisadi huu.

Mheshimiwa Spika, kutokufuata Sheria ya Manunuzi wakati wa kutoa zabuni ya Mradi wa SGR, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 inaonesha kuwa gharama ya ujenzi wa SGR Lot. No. 3 na Lot No. 4 ziliongezeka dola za Marekani milioni 1.3 na milioni 1.6 kwa kilometa moja ya SGR baada ya TRC kuacha njia ya ushindani na kutumia njia ya single source na kusababisha hasara ya jumala ya shilingi trilioni 1.7 kwa mchanganuo ufuatao: -

Mheshimiwa Spika, Lot No. 3 Mkataba wa TRC na Kampuni ya Yapi Markenz wa ujenzi wa SGR kipande cha Makutupora – Tabora urefu wa kilometa 368 uliosainiwa Disemba 2021 ambapo TRC iliacha bei ya ushindani ya kiasi cha shilingi bilioni 9 kwa kilometa ya SGR na kutoa zabuni kwa njia ya single source kwa Kampuni ya Yapi Markenz kwa shilingi bilioni 11.97 kwa kilometa ya SGR ambao kumeisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi trilioni 1.09.

Mheshimiwa Spika, Lot No. 4 Mkataba wa TRC na Kampuni ya Yapi Markenz wa ujenzi wa SGR kipande cha Tabora – Isaka urefu wa kilometa 165 uliosainiwa Julai, 2022 ambapo TRC iliacha bei ya ushindani ya kiasi cha shilingi bilioni tisa kwa kilometa ya SGR na kutoa zabuni kwa njia ya single source kwa Kampuni ya Yapi Markenz kwa shilingi bilioni 12.69 kwa kilometa ya SGR ambao kumeisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 608.8.

Mheshimiwa Spika, licha ya PPRA na Bodi ya Zabuni ya TRC kukataa sharti la kutumia mzabuni mmoja, lakini TRC ilitoa zabuni hiyo kwa njia ya single source kwa Kampuni ya Yapi Markenz. Maamuzi haya yalitokana na maelekezo ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa barua yenye Kumb. Na. PST/GEN/2021/01/55. Ili kukidhi matakwa ya kupata mkopo kutoka Benki ya Standard Charted na kusababisha hasara kwa Serikali ya shilingi trilioni 1.7.

Mheshimiwa Spika, TRC ilimkataa mzabuni wa shilingi bilioni 616.4 na kumpa mzabuni wa shilingi trilioni 1.119 kwa ajili ya ununuzi wa vichwa vya treni vya umeme na makochi bila sababu za msingi na kuisababishia Serikali hasara ya shilingi bilioni 503 hii ni kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, dosari alizoziona CAG katika Lot No. 3 na Lot No. 4 zipo pia katika Lot No. 6, Mkataba wa TRC na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) wa ujenzi wa SGR kipande cha Tabora – Kigoma yenye urefu wa kilometa 506 ambapo TRC iliacha bei ya ushindani ya kiasi cha shilingi bilioni 9.1 kwa kilometa ya SGR na kutoa zabuni kwa njia ya single source kwa Kampuni ya CCECC kwa shilingi bilioni 12.5 kwa kilometa ya SGR hii ni zaidi ya bilioni 3.4 kwa kilometa ya SGR katika mkataba uliosainiwa mwaka 2022, gharama hiyo imeongezeka wakati idadi ya vifaa na ukubwa wa miundombinu umepunguzwa na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya trilioni 1.7.

Mheshimiwa Spika, malipo ya ununuzi wa vichwa vya treni na makochi na ujenzi wa SGR Lot. No. 3, Lot. No. 4 na Lot No. 6 ambapo TRC iliacha bei ya ushindani na kutumia njia ya single source na kusababisha upotevu wa fedha kiasi cha takribani shilingi trilioni 4 huku sheria na kanuni za manunuzi ya umma zikiwa zimevunjwa. Ufisadi huu wa fedha za umma umepata baraka zote za Waziri wa Fedha, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TRC na bahati mbaya bado wako kwenye Ofisi za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kama Mbunge hapa Bungeni nilihoji Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi sababu za kukiuka sheria ya manunuzi na kutoa zabuni bila ushindani na kuisababishia hasara Serikali, lakini Wizara haikuweza kutoa majibu yanayojitosheleza (Hansard za Bunge zipo). Leo CAG ameweka wazi suala hili pamoja na PPRA na Bodi ya Zabuni ya TRC kutoa ushauri wa zabuni kutolewa kwa mujibu wa sheria, lakini Waziri wa Fedha na Mipango na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi waliridhia zabuni hizo kutolewa kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma Na. 7 mwaka 2011 na marekebisho yake ya mwaka 2016 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2013 na marekebisho yake ya mwaka 2016 kwa sababu wanazozijua wao na kuliingizia Taifa hasara ya takribani shilingi trilioni 4. Huu ni uhujumu uchumi wa nchi kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi (The Economic and Organized Crime and Control Act).

Mheshimiwa Spika, utakumbuka pia kuwa baada ya kuchangia suala hili hapa Bungeni mara kwa mara na kukosa majibu fasaha kuhusu ukiukwaji mkubwa wa sheria, niliamua kumuandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi yenye Kumb. Na. MB/KSS2023/21 ya tarehe 13 Machi, 2023 ambapo na wewe nilikupa nakala nikionesha ukiukwaji mkubwa wa sheria na hasara kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, hivyo badala ya kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya mradi huu hatua za haraka zifuatazo zichukuliwe: -

Mheshimiwa Spika, kwanza; hatua kali za kiutawala na kisheria zichuliwe ikiwemo kukamatwa na kufunguliwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu wa TRC na wengine wanaohusika.

Mheshimiwa Spika, pili; kuvunja mikataba au kufanya makubaliano mapya kwa mikataba ya Lot 3, Lot 4 na Lot 6 ili kuondoa dosari zote zinazosababisha Serikali hasara.

Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi na mikopo nje ya bajeti; kama Mbunge nimeuliza mara kwa mara hapa Bungeni Serikali kukopa nje ya bajeti, lakini Waziri wa Fedha alishindwa kutoa majibu ya kina kueleza imekopa kiasi gani nje ya bajeti, amekopa mikopo ya ziada kwa shughuli gani na sababu za kulikwepa Bunge ni zipi (Hansard ya Bunge inajieleza). Leo CAG ameweka wazi ukweli uliokuwa unafichwa. Kama fedha hizi zilikopwa kwa nia njema na kwa maslahi ya Taifa kwa nini zipokelewe na kutumika kwa siri? Huku ni kupoka madaraka ya Bunge na kuna harufu ya ufisadi wa kutisha.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya CAG 2021/2022 Serikali Kuu jedwali na 17 linaonesha kuwa Serikali imekopa nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge na bila ridhaa ya Bunge kiasi cha shilingi trilioni 1.285. Waziri wa Fedha alikopa fedha hizi kwa ajili ya shughuli gani na kwa ridhaa ya nani? Fedha na kazi zilizopangwa katika bajeti 2021/2022 zilipitishwa na kuidhinishwa na Bunge tena kwa kupigiwa kura ya ndiyo, fedha za ziada alizokopa Waziri wa Fedha ni kwa ajili ya shughuli gani na kwa ridhaa ya nani?

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo (Government Loans, Guarantees and Grants Act) ambapo mamlaka ya kukopa mikopo amepewa Waziri wa Fedha kwa niaba ya Serikali na atafanya hivyo kwa kuzingatia ukomo uliowekwa na Bunge kupitia bajeti iliyoidhinishwa na endapo katika utekelezaji wa bajeti kutakuwa na mahitaji mapya atapata kibali cha Bunge.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilipotokea ongezeko la mikopo la shilingi trilioni 1.31 kutoka IMF kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kukabiliana na hali ya uchumi baada ya kupungua kwa ugonjwa wa Covid-19 bajeti ilifanyiwa marekebisho kupitia Bunge kutoka trilioni 36.68 hadi trilioni 37.99. Hapa Waziri wa Fedha alizingatia matakwa ya sheria ya mikopo inavyotaka ambapo Bunge liliridhia kwa kauli moja na hakukuwepo malalamiko.

Mheshimiwa Spika, swali kubwa wanalojiuliza Watanzania kwa nini ongezeko la mikopo ya ziada la kiasi cha shilingi trilioni 1.285 aliyokopa Waziri wa Fedha haikuwekwa wazi na hakupata ridhaa ya Bunge? Fedha hizi Bunge ni vigumu kuzisimamia kwani halijui ziko wapi na kwa matumizi gani hali inayoweza kusababisha matumizi mabaya na ufisadi. Maamuzi ya Waziri wa Fedha yamekwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Bajeti, Sheria ya Fedha na Sheria ya Mikopo lakini pia ni matumizi mabaya ya Ofisi kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Mheshimiwa Spika, ushauri; CAG na TAKUKURU wafanye uchunguzi na ukaguzi maalum ili kubaini sababu zilizomsukuma Waziri wa Fedha kukopa na kutumia fedha za mikopo nje ya bajeti iliyopitishwa na Bunge pamoja na uhalali wa matumizi yaliyofanywa.

Mheshimiwa Spika, hatua kali za kiutawala na kisheria zichukuliwe kwa Waziri wa Fedha na wahusika wengine wote ikiwemo kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi ambao umepelekea kuliingiza Taifa kwenye hasara na mzigo mkubwa wa madeni.

Mheshimiwa Spika, kushindwa kusimamia mikataba kikamilifu (JHNPP – 2115); kama Mbunge nilihoji mara kwa mara suala hili hapa Bungeni kuhusu Kampuni ya Arab Contractors kutakiwa kulipa faini ya ucheleweshaji na CSR lakini Waziri wa Nishati muda wote amekuwa mtetezi wa mkandarasi Arab Contractors na kumkingia kifua asilipe malipo hayo halali kwa mujibu wa mkataba (Hansard za Bunge zipo).

Mheshimiwa Spika, CAG ameuweka wazi ukweli wa jambo hili kuwa TANESCO wameshindwa kutoza faini ya fidia ya ucheleweshaji kwa mwaka kiasi cha shilingi bilioni 327.93 sawa na kiasi cha shilingi bilioni 655.86 kwa miaka miwili. Pia wameshindwa kutoza CSR ya kiasi cha shilingi bilioni 270.67 kwa mujibu wa mkataba wa mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP – 2115) na kusababishia jumla ya upotevu wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 926.53.

Mheshimiwa Spika, kwa nini Waziri wa Nishati amekuwa akitumia nguvu nyingi kiasi hicho kumkwepesha mkandarasi kulipa faini iliyowekwa kwa mujibu wa mkataba? Mkataba unakaribia kufika mwisho na fedha anazodai Kampuni ya Arab Contractors zimepungua, je, ni wakati gani Serikali itaanza kukata madai hayo? Huu ni uhujumu uchumi lakini pia ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Mheshimiwa Spika, ushauri; hatua kali za kiutawala na za kisheria zichukuliwe ikiwemo kukamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi kwa Waziri wa Nishati, Mkurugenzi wa TANESCO na wahusika wengine kwa kuisababishia Serikali hasara ya shilingi bilioni 926.53.

Mheshimiwa Spika, Serikali ianze kukata malipo ya faini ya fidia ya ucheleweshaji na mchango wa CSR kwa kila hati ya malipo inayowasilishwa na kulipwa na kuhakikisha kuwa fedha zote za umma zinazodaiwa zimelipwa kabla ya mkataba kumalizika.

Mheshimiwa Spika, suala la TANESCO kushindwa kuidai IPTL; kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022, TANESCO kushindwa kudai malipo ya shilingi bilioni 342 kutoka Kampuni ya IPTL baada ya Serikali kushinda kesi Machi, 2021 fedha hizi zinatakiwa kupatikana ili kulipa deni Benki ya Standard Chartered, Hong Kong dola za Marekani milioni 148.4 pamoja na riba kama ilivyoamuriwa na Kituo cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro ya Uwekezaji. Kitendo cha kushindwa kukusanya fedha hizi kutafanya Serikali ilipe mkopo pamoja na riba kwa Benki ya Standard Chartered Hong Kong. Nini kilichofanya Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na TANESCO washindwe kudai IPTL madai hayo halali kwa amri ya Mahakama?

Mheshimiwa Spika, CAG hakuona hatua yoyote iliyochukuliwa na Wizara ya Nishati na TANESCO tangu hukumu hiyo itolewe Machi, 2021 na hivyo kuleta sintofahamu kubwa lakini ilikuwa rahisi kwa Wizara kulipa malipo ya kiasi cha shilingi bilioni 350 katika Kampuni ya Symbion Power LCC.

Mheshimiwa Spika, ushauri; hatua kali za kiutawala na za kisheria zichukuliwe ikiwemo kukamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi kwa Waziri wa Nishati, Mkurugenzi wa TANESCO na wote waliohusika na kuisababishia Serikali hasara ya shilingi bilioni 342.

Mheshimiwa Spika, Serikali iitake IPTL kwa haraka kulipa fedha kiasi cha dola za Marekani milioni 148.4 pamoja na riba kama Mahakama ilivyoamuru.

Mheshimiwa Spika, kuhusu malipo ya tozo za riba bila sababu za msingi; malipo ya tozo na riba kutokana na kuchelewesha malipo ya wazabuni, wakandarasi, bima na mifuko ya jamii katika Serikali Kuu, mashirika ya umma na Serikali za Mitaa na kuipelekea Serikali hasara ya kiasi cha shilingi bilioni 418.5. ucheleweshaji huu ni kinyume cha sheria na pengine unafanywa kwa maslahi binafsi na Wizara ya Fedha na taasisi zingine za Serikali. Fedha hizi zingeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo badala ya kulipa faini. Wahusika wote wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya fedha za umma nje ya bajeti; taarifa ya CAG 2021/2022 inaonesha kuwa matumizi ya fedha za umma nje ya bajeti iliyoidhinishwa katika maeneo mbalimbali ya Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa ambapo kwa ukokotoaji wangu ni kiasi cha shilingi bilioni 502.87 ambapo kati ya hizo shilingi bilioni 104.21 ni za TANESCO hii ni kinyume na sheria ya bajeti na sheria ya manunuzi; hatua zichukuliwe kwa wahusika.

Mheshimiwa Spika, fedha kupelekwa moja kwa moja TARURA; taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 inaonesha Wizara ya Fedha kupeleka moja kwa moja TARURA fedha za ongezeko la tozo ya mafuta kiasi cha shilingi 100 kwa lita ya dizeli na petroli badala ya kupeleka kwenye Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) kama sheria zinavyosema kiasi cha shilingi bilioni 330.33 huu ni ukiukwaji mkubwa wa sheria ya ushuru wa barabara na mafuta Sura ya 220. Sababu za kuikwepa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) hazifahamiki na pengine fedha hizi zimetumika vibaya.

Mheshimiwa Spika, ushauri; TAKUKURU ifanye uchunguzi ili kubaini sababu za Wizara ya Fedha kukiuka sheria na kama fedha hizo zimefika na kutumika kihalali TARURA.

Mheshimiwa Spika, hatua za kiutawala na kisheria zichukuliwe kwa wahusika wote.

Mheshimiwa Spika, ucheleweshaji wa maamuzi katika Mahakama za Rufani za Kodi; Mahakama za Rufani za Kodi za TRAB, TRAT na CAT kuchelewa kutoa uamuzi katika mashauri ya malimbikizo ya kodi hali inayopelekea kushindwa kukusanya mapato ya Serikali katika mwaka husika na kukosesha Serikali mapato. Mara nyingi CAG amekuwa akijibiwa sababu za ucheleweshaji ni upungufu wa rasilimali fedha na watu. Hizi sababu sio za msingi kwani eneo nyeti kama hili kuacha kupewa kipaumbele na kutumika kama kichaka cha kukwepa kulipa kodi. Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 mashauri ya malimbilikizo ya kodi yamefikia kiasi cha shilingi trilioni 4.84.

Mheshimiwa Spika, ucheleweshaji wa maamuzi unaonekana kwenye malimbikizo ya kodi pekee, lakini upande wa mashauri ya kesi za manunuzi chini ya Mamlaka ya Rufani za Manunuzi ya Umma (Public Procurement Appeals Authority – PPAA) maamuzi yamekuwa yakifanyika kwa wakati na kusifiwa na wadau.

Mheshimiwa Spika, ushauri; Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza chanzo cha ucheleweshaji huo na kupendekeza hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Spika, malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi Mahakamani; taarifa ya CAG ya mwaka wa fedha 2020/2021 ilionesha TRA kushindwa kukusanya malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani kiasi cha shilingi trilioni 7.54 bila sababu za msingi, kitendo cha TRA kushindwa kukusanya kodi hizi kwa wakati kuikosesha Serikali mapato ambapo CAG alilalamikia kasi ndogo ya ukusanyaji wa malimbikizo hayo ambayo ilikuwa ni 10% tu. Taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 haijatoa taarifa ya hatua iliyofikiwa katika ukusanyaji wa malimbikizo hayo lakini pia haijaeleza malimbikizo ya kodi ya mwaka husika.

Mheshimiwa Spika, eneo hili la malimbikizo ya kodi lisipotazamwa upya na kubaini sababu zinazosababisha TRA ishindwe kukusanya mapato ambayo imeshayafanyia assessment na hakuna pingamizi yoyote itapelekea taasisi hii kuendelea kupoteza uwezo wa kukusanya mapato na eneo hili kutumika kama uchochoro na kichaka cha kukwepa kodi na kuikosesha mapato Serikali.

Mheshimiwa Spika, CAG aweke wazi malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani yaliyopo kufikia mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, ushauri; Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza chanzo cha ucheleweshaji huo na kupendekeza hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Spika, kufuta madai ya malimbikizo ya kodi; taarifa ya CAG ya mwaka 2020/2021 inaonesha miongoni mwa kesi za rufani zilizoisha ni kesi 45 zenye thamani ya shilingi 5,594,675,387,242.40 ambazo zipo katika mazungumzo kati ya Serikali na kampuni ya madini ambayo ni North Mara Gold Mine, Pangea Minerals Limitied, Bulyanhulu Gold Mine na ABG Exploration, kati ya jumla ya deni la shilingi trilioni 343.5. kesi hii imetolewa kutoka Mahakama za Rufani za kikodi na kurejeshwa kusikilizwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mheshimiwa Spika, kama Mbunge nimekuwa nikilihoji suala hili mara kwa mara hapa Bungeni kuitaka Serikali kueleza hatua iliyofikia ya kulipwa kiasi cha shilingi trilioni
5.595 za malimbikizo ya kodi kwa makampuni ya madini maarufu makinikia, lakini majibu ya Waziri wa Fedha yalikuwa tofauti na ripoti ya CAG ambapo alidai kuwa madai hayo hayapo na kwamba yalishafutwa na sherehe ya kufuta ilifanyika Ikulu. Ingawa kila nilipomuomba kutoa ushahidi kuhusu uamuzi wa kufutwa madai hayo hakufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 haijaonesha suala hili limehitimishwa vipi na Serikali, lakini pia malimbikizo ya kodi ya kiasi cha shilingi trilioni 5.595 ambazo zilikuwa kwenye mazungumzo na kiasi cha shilingi trilioni 343.5 ambazo zilirejeshwa TRA hazipo tena kwenye vitabu vya TRA. Nani aliyetoa maamuzi ya kufutwa madai halali ya kiasi cha shilingi trilioni 5.595 na kufutwa kwenye vitabu madai ya kiasi cha shilingi trilioni 360 bila ridhaa ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, ushauri; Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza sababu za kufutwa madai halali ya malimbikizo ya kodi kiasi cha shilingi trilioni 5.595 na kuondolewa kwa madai ya shilingi trilioni 360 kwenye vitabu vya TRA na kama yamefutwa kwa mujibu wa sheria na kupendekeza hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mashirika ya Umma yaliyopata faida kupata hasara; Mashirika ya Umma 16 yamepata hasara ya shilingi bilioni 34.5 mwaka 2021/2022 wakati mashirika hayo yalipata faida ya shilingi bilioni 56.57 mwaka 2020/2021 na kupelekea jumla ya hasara shilingi bilioni 91.07 ikiwemo Kampuni ya Mawasiliano (TTCL) ambayo imepata hasara ya shilingi bilioni 15.56 mwaka 2021/2022 wakati mwaka 2020/2021 TTCL ilipata faida ya shilingi milioni 517. Hatua zichukuliwe kwa wahusika wote.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mashirika ya umma ambayo yameongeza hasara; mashirika na taasisi zingine za umma 45 CAG alipofanya ukaguzi wa utendaji wa fedha alibaini kuwa hasara katika mashirika hayo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 281.76 mwaka 2020/2021 hadi kufikia shilingi bilioni 416.37 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la shilingi bilioni 134.61 ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao hasara yake imeongezeka kutoka shilingi bilioni 109.7 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 204.65 mwaka 2021/2022. Hatua zichukuliwe kwa wahusika wote.

Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi yasiyostahili katika Mashirika ya Umma; CAG alibaini mashirika 21 ambayo yamefanya matumizi yasiyostahili ya jumla shilingi bilioni 77.75 ambayo yalitokana na malipo ya posho kwa watumishi wasiostahili, malipo yasiyokuwa na uthibitisho na vielelezo vya matumizi husika. Ikiwemo Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambayo ilitumia kiasi cha shilingi bilioni 65.33. Hatua kali zichukuliwe kwa wahusika.

Mheshimiwa Spika, DPP kushindwa kukusanya malipo ya ahadi ya washtakiwa chini ya makubaliano ya mikataba ya kukiri makosa (plea bargain) na hukumu za mahakama kiasi cha shilingi bilioni 179.61 bila sababu za msingi. Hatua zichukuliwe kwa wahusika na Serikali ikusanye fedha hizo haraka.

Mheshimiwa Spika, ubadhirifu wa fedha za umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma uliosababishwa ukiukwaji wa mikataba, matumizi mabaya ya fedha za umma, marejesho ya fedha ya mifuko ya kina mama, vijana na wenye ulemavu, ukiukwaji wa sheria ya manunuzi na upotevu wa mapato, katika Serikali za Mitaa na Sekretarieti za Mikoa Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 inaonesha ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Fedha, Sheria ya Manunuzi na Sheria ya Bajeti ambako kumesababisha wizi, ubadhirifu, ufisadi na hasara ambapo kwa ukokotoaji wangu ni kiasi cha shilingi bilioni 637.55. Hatua zichukuliwe kwa wahusika wote.

Mheshimiwa Spika, haya yote yamefanyika Waziri Mkuu yupo, Waziri wa Fedha yupo, Mawaziri wa Wizara husika wapo, Mwanasheria Mkuu yupo, Mlipaji Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu wapo, PPRA ipo na PPAA ipo hadi kufikia ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma kiasi hicho.

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa mwezi Novemba, 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitoa maazimio kuhusu taarifa ya CAG ya mwaka 2020/2021 kwa watu wote waliotajwa kuhusika na ubadhirifu wachukuliwe hatua, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji uliofanyika kuarifiwa Bunge hili.

[MANENO YAMEONDOLEWA KWA MAELEKEZO YA KITI]

Jedwali la Ubadhirifu na Upotevu wa Fedha za Umma

Mheshimiwa Spika, hatua za dharura na za haraka zichukuliwe ili kulinusuru Taifa kupata hasara kubwa na kudidimia kiuchumi na kushindwa kutoa huduma kwa wananchi wake kikamilifu kutokana na ufisadi unaofanywa na baadhi ya Mawaziri na watendaji wengine wa Serikali. Nikipongeze sana chama changu, Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa msimamo thabiti wa kupiga vita wizi, rushwa, ubadhirifu na ufisadi wa fedha na mali za umma.

Mheshimiwa Spika, kipekee pia nipongeze sana maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi katika kikao chake cha tarehe 1 Aprili, 2023 chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuazimia na kutoa maelekezo ya kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi walizoaminiwa kutumikia watu, badala yake wanaweka maslahi binafsi.

Mheshimiwa Spika, aidha Kamati Kuu imeielekeza Serikali kuchukua hatua thabiti kwa wahusika waliobainika kuhusika katika ukiukaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi. Agizo la Kamati Kuu litekelezwe kikamilifu.

Nawasilisha, Kazi iendelee.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi ili nami niweze kuchangia hii hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana na kuwapongeza wananchi wangu wa Jimbo la Kisesa kwa namna ambavyo wanavyoendelea kuchapa kazi kule, nami nipo hapa Bungeni kuhakikisha kwamba nawawakilisha kikamilifu kwa mujibu wa Ibara ya 63(2) na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wananchi wa Jimbo la Kisesa kama tulivyokubaliana kwamba masaa ni namba, na hakuna kupumzika mpaka kazi ikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, suala la mambo ya kiujumla. Moja, Serikali imeshindwa kurudisha mifugo ya wafugaji 6,000 ambao wameshashinda kesi Mahakamani. Mheshimiwa Waziri suala hili ni la muda mrefu sana. Kwa sababu ni la muda mrefu, sasa Serikali itekeleze. Wapiga kura wangu mimi wa Jimbo la Kisesa ambao wanadai mifugo hii zaidi ya ng’ombe 400, sasa hivi wapo njiani kuja kuchukua mifugo yao. Akina Sai Maduhu, Masunga Muhamari, Ndaturu Muhororo, Zengo Kusekelwa, Dandika Kamasaga, Sambai Deke, hata akina Mzee Rerina kule kwa ndugu yangu hapa Mbunge, nao wote wako njiani kuja kuchukua mifugo yao. Sasa ni muhimu Serikali ikabidhi hao mifugo kwa hao wananchi ambao wameshinda kesi kihalali Mahakamani, warudishiwe mifugo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwa haraka haraka…

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Rais ya Haki za Binadamu…

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Mpina.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa tu mzungumzaji, mimi pia Ushetu nina wananchi wangu walishinda kesi mwaka 2019, wako watatu, ng’ombe 500 na documents zote nimeshawapelekea. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake na kwamba hawa wafugaji wote wa ng’ombe 6,000 wapo njiani kuja kuchukua mifugo yao hapa Dodoma kwa Waziri wa Katiba na Sheria. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Tume ya Rais ya Haki za Jinai, mimi ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake haya makubwa ya kuamua kuangalia kasoro na dosari zilizopo katika suala la ukamataji, upelelezi, uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka na kuinda hii Tume. Pia naipongeza Tume sasa hivi inavyoendelea. Changamoto moja tu ni kwamba wanapopata maoni hadharani ya watu wanaowapa maoni: Moja, wanasababisha watu wengine ule uhuru wa kutoa mawazo unapungua, lakini pia inaweza ikafanyika kampeni ya upotoshaji ili mwisho wa siku wakatoka na results ambazo hazikutarajiwa, ambazo Mheshimiwa Rais hakuzitarajia wala wananchi hawakuzitarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ni Maazimio ya Bunge kuhusu kufuta hasara na upotevu wa fedha na vifaa vya Serikali. Imesema, taarifa ya Mheshimiwa ya Waziri Kiambitisho B, ukurasa wa 146 anasema, Bunge liliazimia kuridhia kufuta hasara ya upotevu wa fedha na vifaa vya Serikali kwa kipindi kinachoishia tarehe 30 Juni, 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo hapa, taarifa hii ililetwa hapa Bungeni kwa Order Paper tarehe 19 Septemba, 2022 lakini haikujadiliwa hapa Bungeni na madai yaliyokuwa ya Waziri wa Fedha yalikuwa ni shilingi bilioni 19.75 zisamehewe, zifutwe kwenye vitabu vya Serikali, lakini Bunge hili halikujadili taarifa hiyo. Bunge liliahirishwa siku hiyo saa 4.39, hatukujadili wala hatukuridhia. Sasa haya mambo ya kuridhia, Waziri wa Katiba na Sheria ameyatoa wapi? Nani amemletea taarifa za kuridhia? Kwa nini anataka kulidanganya Bunge? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele cha pili, eneo hilo hilo la Azimio la Bunge, ni kufutwa kwa madai ya malimbikizo ya kodi. Nilisema kipindi kile; nililalamika sana huko nyuma kuhusu kufutwa kwa madai ya Shilingi trilioni 5.59, na kama maelezo ya Waziri ya Fedha alivyokuwa akiyatoa hapa, lakini Taarifa za Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mwaka 2021/2022 zinasema kwamba haya mahesabu hayajaoneshwa kwenye vitabu hivyo, na hivyo inamaanisha kwamba yamefutwa. Kama yamefutwa, basi itakuwa amekiuka sheria Waziri wa Fedha anayehusika, na TRA watakuwa wamekiuka sheria kwa sababu hawana mamlaka hiyo kwa mujibu wa sheria, kifungu cha 34(1) ambacho kinataka lazima yapite hapa Bungeni na tuamue kwa njia ya azimio. Kwa hiyo, ukifuta tu kienyeji, maana yake unaingia kwenye makosa ya uhujumu uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni uendeshaji wa mashtaka. Hapa, DPP ameshindwa kukusanya Shilingi bilioni 170.61 ambazo tayari Mahakama imehukumu kwamba Washitakiwa wanatakiwa kutoa, hizi ni fedha za plea bargaining. Sasa ameshindwa kukusanya hizo fedha bila sababu zozote za msingi, na alikuwa na uwezo wa kukata rufaa upya, alikuwa na uwezo wa kutaifisha mali za washitakiwa wanaodaiwa, lakini mpaka sasa hivi DPP wetu ameshindwa kukusanya fedha hizo, na sababu za kutokukusanya hazieleweki. Namwelewa vizuri sana uwezo wake Sylvester Mwakitalu, huyu DPP wetu, ni Mwanasheria mzuri, nini kilichomkwazwa ashindwe kukusanya mapato halali ya Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa zinaletwa mbwembwe nyingi, mara unajua walionewa, mara unajua hawa... Kama ulinionewa, maamuzi haya hayakufanywa kwa DPP wakati huo. Maamuzi haya yalifanywa na Mahakama. Kama ulionewa, ulikata rufaa? Kwa nini hizi fedha hazijakusanywa? Suala la kutokukusanya fedha hizi limefanyika, Waziri wa Katiba na Sheria yupo, Waziri wa Fedha yupo, lakini naye DPP yupo. Kama DPP anashindwa kukusanya mpaka fedha ambazo zipo kwa mujibu wa sheria: Je, anapopokea mashtaka mengine kutoka kwa DCI, anapopokea mashauri mengine kutoka kwa TAKUKURU, anayafanyaje? Kama hawezi kukusanya, hata yale haya ambayo yako kwa mujibu wa sheria, Shilingi bilioni 170 Watanzania wanateseka fedha zao zipo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hili suala la usimamizi wa mikataba. Tumeelezwa kwenye hotuba ya Waziri kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameweza kufanya upekuzi mikataba 1,304 na katika mikataba hiyo, mikataba 567 ina thamani ya Shilingi trilioni 91. Maana yake kuna mikataba 737 nayo haijafanyiwa uthamini katika mwaka mmoja wa fedha. Sasa kama Serikali imeenda kuingia mikataba ya trilioni moja, Bajeti ya maendeleo tulinayoipitisha iko around Shilingi trilioni 15. Sasa hii mikataba ni ipi? Kwa nini haijawekwa kwenye majedwali? Ukienda kwenye viambatisho vyake kule, ameweka vitu vingine tu. Kilichoshindikana nini kuweka jedwali linaloonesha mikataba hii ya trilioni 91 ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, tusipofanya hivyo, Serikali inaweza ikaingia mikataba ambayo haimo kwenye bajeti, haipo kwenye mpango wa maendeleo na sisi kama wasimamizi wa rasilimali za Taifa tukawa hatujalitendea haki Taifa hili kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa nini Waziri ameshindwa kuweka kiambatisho hapa kama Wabunge tujue mikataba hiyo ni ya nini? Miradi hiyo ni ya jambo gani? Sasa hivi tumeona mikataba 737 haijafanyiwa uthaminishwaji; na kwa nini haijafanyiwa uthaminishwaji? Mingine imefanyiwa uthamanishwaji, kwa nini hii haijafanyiwa? Hii ambayo imefanyiwa uthamanishwaji ni 567 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tutende haki. Waziri huyu, hakuna kupitisha bajeti yake, nanyi Wabunge nawaomba mpaka alete hili jedwali ili tujiridhishe na hicho ambacho kilichomo kwenye Hotuba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la karibia mwisho, ni mashauri na madai ya usuluhishi; mashauri na madai ya usuluhishi hapa, jambo zuri hapa limetajwa kwamba tumeokoa hasa kwenye usuluhishi kwenye madai tumeokoa kama shilingi bilioni 165. Kwenye usuluhishi ni shilingi trilioni 13.33 na nasema; dakika moja tu namalizia.

MWENYEKITI: Malizia.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi trilioni 13.33 wanasheria wetu wameshinda kesi mahakamani na tukaokoa shilingi trilioni 13.33 ni jambo zuri. Mwezi wa 12 niliomba hapa jedwali lile liletwe tumeshinda kwenye mambo gani? Ni kesi zilihusu nini? Kwanini unatuletea tu idadi ya kesi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho kama tusipofanya hivyo, tutaendelea kuingia kwenye matatizo. Hapa Waziri amesema tu kesi tulizoshinda lakini tulizoshindwa ameshindwa kusema na ndiyo maana hapa tuna ile kesi….

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina muda wako umeisha.

MHE. LUHAGA J. MPINA:… ya Standard Chartered Bank ya Hong Kong shilingi bilioni 342 ambayo nayo tulishindwa. Sasa haya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa ili na mimi niweze kuchangia hii Wizara muhimu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hii ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni-declare interest kwamba niliwahi kuwa Waziri wa Wizara hii tangu mwaka 2017 mpaka 2020, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Abdallah Hamis Ulega kwa uteuzi na kwamba mimi namwamini kwa sababu wakati ule alikuwa Msaidizi wangu, najua uwezo wake na najua kwamba atafanya kazi nzuri kwenye Wizara hii. Nakumbuka mambo mengi tuliyofanya pamoja lakini pia nawakumbuka Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Upande wa sekta ya mifugo namkumbuka Dkt. Asimwe, Dkt. Furaha Mramba, Dkt. Mwambene, Dkt. Mlawa, Dkt. Shirima, Ndugu Stephen Michael pamoja na Iman Sichalwe na Ndugu Noel.

Mheshimiwa Spika, upande wa uvuvi pia nawakumbuka vizuri sana Ndugu Chama Marwa, Ndugu Madaha, Ndugu Komakoma ambaye alipima samaki hapa Bungeni, ninamkumbuka Ndugu West Mbembati, Ndugu Romani Mkenda, Ndugu Ruhasile, Ndugu Judith Mgaya, Dkt. Sweke na Dkt. Mgalila, tulifanya kazi nzuri pamoja na watumishi wengine wote wa Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi ambao tulifanya kazi nzuri, kuzunguka nchi hii karibu kila sehemu, pia tulifanya kazi hadi Saa Saba usiku wakati mwingine hata wakati mwingine tulikesha ofisini katika slogan ya masaa ni namba. Nawashukuru sana bado nakumbuka mchango wenu mkubwa katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipongeze sana hatua za Wizara ambazo sasa hivi wanaendelea na ujenzi wa bandari, hili ni jambo ambalo nililitamani sana lakini uwekezaji unaoendelea NARCO sasa hivi, napongeza sana ni jambo zuri, tofauti na mawazo ambayo tuliletewa mwanzo kwamba sasa inabadilishwa tena inakuwa shamba la alizeti. Hii mipango ndiyo tunayoitaka na Waziri aendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri utakumbuka kwamba Wizara iliahidi ujenzi wa mnada wa Kimataifa Mwambea na eneo lilishapatikana wataalam walishalikagua, sasa tunachokitaka ni huu mnada ujengwe, tunataka utuambie utakapokuwa una-wind up, sasa mnada huu wa Kimataifa ulioahidiwa na Serikali toka mwaka 2020 wa Mwambea unaenda kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni wapangaji katika Ranchi ya Mabale, kuna wananchi waliopanga zaidi ya vitalu 23 na walishasaini mikataba yao muda mrefu, zaidi sasa ya mwaka mzima, lakini nakala ya mikataba hiyo hadi sasa kampuni la Ranchi za Taifa (NARCO) haijawarejeshea mikataba yao tatizo ni nini? Waziri kamilisha maliza hili tatizo la migogoro ya hawa wafugaji ili waweze kupata haki yao kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ni ukamataji holela wa mifugo. Kumekuwa na tatizo kubwa sana la ukamataji holela wa mifugo, sheria ziko wazi, Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2003 (The Animal Disease Act No. 2003) lakini pia na Sheria ya Ustawi wa Wanyama Na. 19 ya mwaka 2008 na Kanuni ya The Animal Welfare Impounded Animal Regulation 2020.

Mheshimiwa Spika, hizi kanuni ziko vizuri sana juu ya ukamataji wa mifugo lakini bahati mbaya sana watendaji wengi wa Serikali wamekuwa wakizivunja kanuni hizi, mambo haya yamekuwa yakijirudia. Kikubwa ni kwamba kuna maslahi makubwa juu ya ukamataji huo wa kiholela, tunasikitika kwamba kila tunapozungumza hapa Bungeni hakuna hatua zinazochukuliwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, mfano ni ukamataji holela ambao unapelekea Wanyama wanayimwa malisho, wananyimwa maji, wanayimwa dawa, wananyimwa chanjo, matokeo yake mifugo imekuwa ikifa tu ikiwa imeshikiliwa na Serikali. Tunazungumza wafugaji wa mwisho wa mwaka 2020 waliokamatiwa mifugo yao ikafa zaidi ya 6,000 mpaka leo hii wanakuja kudai hapa mifugo, wafugaji zaidi ya 12 kutoka Jimbo la Kisesa wamekuja na fimbo zao kufuata ng’ombe zao hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni ukamataji bila kushirikisha viongozi. Mifugo inakamatwa viongozi hawashirikishwi, wafugaji hawaitwi kuhakikisha mifugo yao, matokeo yake mifugo inaibiwa, mifugo inapotezwa, mifugo inauzwa kiholela. Sasa hivi tunavyozungumza kule Kilombero, DC wa Kilombero amekamata mifugo zaidi ya siku 10 sasa. Mifugo hawakuwa kwenye hifadhi zaidi ya ng’ombe 2,082, hawakuwa kwenye hifadhi lakini wameshikiliwa tu, maelezo hayatolewi, ushirikishwaji haukutolewa, mifugo wanaendelea kufa na wengine wanazidi kupotea na wengine wanazidi kuibiwa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni mifugo kuuzwa kiholela. Mifigo inakamatwa baadae inauzwa kuholela tu kwa sababu haijahesabiwa haijulikani inauzwa kuholela. Sheria zinasema mifugo hii lazima iuzwe kwenye minada kwa bei ya ushindani na kwa uwazi, matokeo yake mifugo hii imekuwa ikiuzwa porini na Serikali inaruhusu hilo jambo kuendelaa.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilituletea hapa kuishia Disemba Serikali iliuza mifugo ng’ombe 3,828, hawa ng’ombe baada ya hapo Serikali ikauza kwa milioni 685, kwa maana ya kwamba kila ng’ombe aliuzwa kwa shilingi 180,000 wakati average ya mifugo ng’ombe mmoja ni 750,000 maana yake zinaibiwa karibu 570,000 kwa kila ng’ombe. Katika transaction hiyo tayari wale watumishi walijinufaisha zaidi ya bilioni 2.18, haya yanafanyika na Wabunge tuko hapa na Serikali iko hapa (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile wafugaji wanatozwa faini ya Shilingi 100,000 ambayo haimo kwenye Sheria ya Wanyamapori, haimo kwenye Sheria ya Misitu lakini wanaendelea kutozwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa tamko hapa la kuzuia hayo mambo kutokea, lakini mambo hayo yamekuwa yakiendelea, mimi siamini kama wale watumishi wana uwezo wa kuzuia maelekezo ya Waziri Mkuu, isipokuwa Waziri Mkuu mwenyewe anaruhusu haya mambo yafanyike na yanafanyika kwa ridhaa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la hereni Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa tamko hapa la kuzuia suala …

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mpina kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro Waziri wa Katiba na Sheria.

TAARIFA

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mpina kwamba hakuna uthibitisho huo kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa ridhaa, huko ni kutumia vibaya jina la Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo ambalo kauli ambayo siyo nzuri na siyo ya kiungwana. Jambo la pili nimpe taarifa pia kwamba….

SPIKA: Taarifa ni moja Mheshimiwa.

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Luhaga Mpina unapokea taarifa hiyo?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, sipokei taarifa yake na ninaomba niendelee. Suala la ufungaji wa hereni mifugo, Mheshimiwa Waziri Mkuu..

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ananimalizia muda wangu naomba usipokee taarifa yoyote. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Mpina kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, kati ya watu mahiri sana wanaosaidia wafugaji katika kutatua matatizo yao ni Waziri Mkuu, kwa hiyo naomba hilo jambo asiliingize kwenye mchango. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Luhaga.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee na unilindie muda wangu, naweza nikaendelea pamoja na makofi haya yakiendelea.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naombeni mkae kimya.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, suala la ufungaji wa hereni linaloendelea hivi sasa, Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa taarifa hapa……

(Hapa Waheshimiwa Wabunge waliendelea kupiga makofi ambayo yalisababisha Mheshimiwa Luhaga J. Mpina kushindwa kuendelea kuchangia)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge,…

MHE. LUHAGA J. MPINA: Hizo ni fujo, Mbunge huwezi kufanya mambo hayo, hizo ni fujo, waniachie muda ambao..

(Waheshimiwa Wabunge waliendelea kupiga makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mpina subiri kwanza, umepewa taarifa na Mheshimiwa Getere unaipokea taarifa hiyo?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, siipokei taarifa naomba niendelee.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya mambo yanayolalamikiwa katika Wizara hii, yapo mambo yanayolalamikiwa katika Wizara hii, wananchi na Wabunge lakini Wizara imekaa kimya. Mambo ambayo wakati mwingine yanaenda kupelekwa mpaka kwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, mambo ambayo yalitekelezwa kwa mujibu wa sheria, mambo hayo mfano uchomaji wa vifaranga…..

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utaratibu.

SPIKA: Mheshimiwa Mpina kuna Kanuni inavunjwa inaonekana. Mheshimiwa Waziri wa Nchi Kanuni inayovunjwa.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utaratibu Kanuni ya 71(1)(a) na Kanuni ya 75 kama nilivyoanza nayo, kinasema: “Mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli.” Katika ku-support Kanuni hiyo, inanipasa mimi kuthibitisha ni kwa namna gani Mbunge huyo anatoa taarifa ndani ya Bunge ambazo hazina ukweli.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mpina anamtuhumu Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba ni chanzo cha kutotekelezwa kwa utendaji bora kwenye masuala hayo ya kutetea wafugaji na kusimamia haki za wafugaji.

Mheshimiwa Spika, naomba kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba taarifa zinazotolewa na Mheshimiwa Mbunge hapa ndani hazina ukweli kwa sababu, ni juzi tu Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa kauli hapa ndani mbele ya Bunge lako kuonesha ni kwa kiasi gani Serikali, na yeye akisimamia na kutoa maelekezo kwa Serikali, namna bora ambayo Serikali itafanya kushughulikia migogoro ya wafugaji, kushughulikia migogoro ya hifadhi na kuhakikisha pia malalamiko ya Wabunge, malalamiko ya Watanzania na Maazimio ya Bunge yanafanyiwa kazi ipasavyo, ili kulinda heshima ya Serikali na heshima ya Wabunge na vile vile kujali hali na malalamiko ya Watanzania katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba utaratibu wako kama jambo hili analoendelea nalo Mheshimiwa Mbunge pamoja ya kupewa taarifa mbili amezikataa, kama ni jambo sahihi na linakubalika ndani ya Bunge lako. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, amesimama Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, akionesha kwamba kuna kanuni inavunjwa wakati Mheshimiwa Mpina akichangia na ametupeleka kwenye Kanuni ya 75 ambayo inampa fursa ya yeye kusimama na kueleza ni Kanuni gani inayovunjwa na ametupeleka kwenye Kanuni ya 71(1)(a), akieleza kwamba, kanuni hiyo inakataza Wabunge kutoa taarifa ambazo hazina ukweli. Pia ameeleza kuhusu mchango wa Mheshimiwa Mpina ambao kwa yeye Mheshimiwa Jenista ameona ametoa taarifa ambazo hazina ukweli.

Waheshimiwa Wabunge, mimi nimemsikiliza Mheshimiwa Mpina, ameeleza maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri Mkuu huko nyuma, na kwamba hayo maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri Mkuu hayafuatwi katika hili eneo analochangia yeye. (Makofi)

Kwa muktadha huo, ndiyo anasema, ikiwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maelekezo na hayafuatwi na wale wanaopaswa kuyafuata, basi maana yake mtoa maelekezo, yeye mwenyewe pia anaona sawa. Ndiyo mchango wake ulipo. Kwa sababu mimi nimemsikiliza kwa maneno aliyoyasema. Sasa Mheshimiwa Jenista ameomba utaratibu kwamba taarifa alizozisema hazina ukweli.

Sana sana hapo mimi nitataka kujua katika yale maelekezo ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyasema, ni kweli aliyasema hayo maelekezo ama hayapo? Kama yapo, je, yamefanyiwa kazi au Hapana? Kama hayajafanyiwa kazi, hoja ya Mheshimiwa Mpina ni kwamba, kama hayafanyiwi kazi, na yapo maelekezo, maana yake mtoa maelekezo ameona kwamba yale maelekezo yake yanaweza yakafuatwa, ama yasifuatwe. Ndiyo hoja ilipo ya kisheria kabisa kuhusu utaratibu. (Makofi)

Kwa hiyo, ndivyo mimi nilivyomsikia Mheshimiwa Mpina. Sasa kama amesikika vinginevyo, Mheshimiwa Jenista mimi nitakupa nafasi nyingine. Hicho ndicho nilichokisikia ili niweze kutoa maamuzi kuhusu utaratibu huu ulioombwa. Kama maelezo yapo tofauti na hayo niliyotoa, Mheshimiwa Jenista nakupa tena fursa, na kama sio haya, basi nitaenda kufuatilia kwenye Hansard halafu nitakuja kutoa uamuzi hapa.

Mheshimiwa Jenista nakupa nafasi nyingine.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Spika, nadhani wote tumemsikia Mheshimiwa Mpina maelezo aliyoyatoa Bungeni. Maeneo yote ambayo Mheshimiwa Mpina anayazungumzia kwa muktadha wake yanahusu migogoro ambayo inawahusu wafugaji. Nimesimama kusema kwamba, Serikali haitekelezi ama hakuna hatua ambazo zimechukuliwa kwa namna moja ama nyingine.

Mheshimiwa Spika, nilichotaka kulithibitishia Bunge lako ni kwamba, mfano halisi ambao Serikali tunao, huku ndani na hasa katika michango ya Bunge la Bajeti lililopita na michango mingine ya Wabunge ambayo ilikuwa inazungumzwa kuhusu migogoro hii, Bunge liliiomba Serikali iunde Timu za Uchunguzi, itafute njia za kufanya na kusuluhisha migogoro yote ambayo imekuwa ikijitokeza. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ujumla wa hayo yote, yakiwemo hayo ambayo anayazungumza Mheshimiwa Mpina, aliyajumisha utekelezaji wake katika taarifa aliyoitoa akionesha yaliyofanywa na Serikali na maelekezo ya ziada kwa Mawaziri na Serikali kuhakikisha mambo hayo yote yanafanyiwa kazi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaposema kwamba ama Waziri Mkuu hajasimamia, ama Serikali haijachukua hatua, ndiyo inawezekana yapo maeneo machache, lakini kwa ujumla wa maagizo ya Serikali na mwongozo ambao umekuwa ukitolewa na aliyeutoa Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa ndani, unadhihirisha kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu mwenyewe, Serikali kwa ujumla na sekta zinazohusika zimechukulia uzito suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe taarifa kwako, tayari tumeshaelekezwa na shughuli zimeshaanza na ratiba za kushughulikia masuala hayo zilishaanza na zinaendelea. Hata weekend hii zipo ratiba ambazo zitaendelea. (Makofi)

SPIKA: Haya. Mheshimiwa Mpina maeneo mahususi ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyatolea maelekezo ili usiwe umeeleza kwa ujumla hayo mambo ili tushughulike na hayo, nitoe maamuzi juu ya jambo hili.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika,…

SPIKA: Ni maelekezo gani Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyatoa na hayajafanyiwa kazi?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nilifurahi sana uliposema kwamba tutaenda kwenye Hansard ili kwenda kuthibitisha kile nilichokizungumza mimi. Nilisema hapa, Wabunge hapa wamezungumza wengi, nami nina ushahidi. Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema, sasa hivi kamata kamata ya bila kushirikisha wananchi ni marufuku. Toka Agizo la Waziri Mkuu la kamata kamata ya mifugo bila kuzingatia sheria; na hii kanuni ninayoizungumza, mimi ndio nilikuwa Waziri, niliisaini mimi ya kuzuia ukamataji ovyo ovyo; watu wanakamatwa.

Mheshimiwa Spika, toka Waziri Mkuu alipotoa tamko, watu wameendelea kukamatwa, na ushahidi upo. Sasa Waheshimiwa Wabunge, Waziri Mkuu ni Mtendaji wa Shughuli za Serikali hapa Bungeni, na sisi ndio tunamthibitisha. Sasa unapotokea upungufu kama huu hatuwezi kuufumbia macho kuusema.

Mheshimiwa Spika, hata kama anavyotaka yeye kuleta, ushaidi wa matukio…

SPIKA: Mheshimiwa Mpina, tuelewane vizuri. Maelekezo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa siku ya Alhamisi wiki iliyopita, ndiyo unayosema? Kati ya ile Alhamisi alipoyatoa mpaka sasa, kamata kamata imeendelea?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Hilo eneo ndilo ambalo wewe una ushahidi nalo?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Sawa.

Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu, jambo hili limefika mahali ambapo linahitaji ushahidi. Sasa ili niweze kutoa huu mwongozo, kwamba yale aliyoyasema Mheshimiwa Waziri Mkuu yanafanyiwa kazi, Mheshimiwa Mpina anasema yeye anao ushahidi kwamba yale aliyoyasema Mheshimiwa Waziri Mkuu hayafanyiwi kazi.

Mheshimiwa Mpina utaniletea huo ushahidi. Kwa hiyo, hiyo hoja unaiacha ili uendelee na nyingine mpaka nitakapopata ushahidi ili nitoe mwongozo kwenye hoja hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mpina, malizia mchango wako.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, najua umenitunzia muda wangu. Sasa nilikuwa…

SPIKA: Ngoja, ngoja, tuelewane vizuri. Muda wako uliotunzwa vizuri ni ule unaohusu Utaratibu, siyo unaohusu taarifa. Kwa hiyo, usije ukaanza kudai dakika zako za Mheshimiwa Getere na za Mheshimiwa Waziri hapa. Dakika pekee unazonidai ni zile za kuhusu utaratibu ambazo nilikuwa namsikiliza Mheshimiwa Jenista hapa.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, utaniongeza kidogo tu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nazungumzia suala la utekelezaji wa mambo yaliyotekelezwa kwa mujibu wa sheria, halafu mwisho wa siku anakuja kulaumiwa mpaka wanalaumiwa viongozi wetu wakuu. Analaumiwa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu wa Tano wa Nchi hii, mambo ambayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyatekeleza kwa mujibu wa sheria, halafu Wizara iko kimya. Waziri yuko kimya, na watendaji wa Serikali wako kimya.

Mheshimiwa Spika, suala la uchomaji wa vifaranga. Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilichoma vifaranga 6,550 kwa mujibu wa sheria. Tunalo zuio la kuingiza mazao yote ya ndege kutoka nchi yoyote ile kutokana na nchi yetu kuwa suspected na kuenea kwa magonjwa ya mafua makali ya ndege. Tuna zuio la toka mwaka 2006, hairuhusiwi. Kosa lingine, ni kwamba huyu aliyekuwa anaingiza, hakuwa na kibali chochote kinyume cha Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya Mwaka 2003. Hana kibali chochote na haijulikani hao vifaranga wametoka wapi?

Mheshimiwa Spika, la pili, hakukuwa na cheti cha afya. Ukaguzi wowote wa kujua hao mifugo walikuwa wamechanjwa wana magonjwa gani? Hakuna kibali chochote. Sasa katika mantinki hiyo, sheria inasema, ukikutana na bidhaa za namna hiyo uzichome. Serikali ingefanya nini? Utawapeleka wapi? Hawajulikani walipotoka, hakuna kibali cha afya, hawajachanjwa, yaani Waziri au Serikali ikubali kuridhia Watanzania waje kufa na magonjwa ya mafua ya ndege hapa! Serikali ikubali kuridhia wafugaji wa Tanzania zaidi ya kuku 76,000,000 wa Watanzania, Waziri uliyeapishwa kwa mujibu wa sheria, uje uruhusu wafugaji hawa wote kuku wao wafe kwa magonjwa ya ndege kwa kumbeba mfanyabiashara mmoja, ili mfanyabiashara tu huyo wa vifaranga 6,000 aingize vifaranga vyake hapa nchini! Hayo mambo kwa nini hayazungumzwi na Wizara?

Mheshimiwa Spika, la tatu, suala la kupima samaki kwa rula Bungeni. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini kinachomfanya Waziri wa Mifugo na Uvuvi kutamka kwa sauti kwamba samaki anapimwa kwa urefu, na kwa urefu huo anapimwa kwa kutumia rula? Waziri wa Uvuvi anashindwa nini kusema nini kwa sauti kwamba ili uweze kukidhi matakwa ya Kanuni Namba 58 ya Kanuni ya Uvuvi ya Mwaka 2009, ni lazima umpime kwa rula ili uthibitishe vipimo kama ni sangara au sato? Anashindwa nini kufanya hivyo? (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Spika, mambo haya wanazidi kutapakazwa viongozi, walipima kwa rula, walifanya hiki na kile!

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Mpina, muda wako umekwisha, ahsante sana.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, dakika moja, dakika moja tu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja tu. (Makofi)

SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, dakika moja.

SPIKA: Hiyo dakika ilikuwa nikupe, lakini nachelea unatukumbusha mtu anapima na rula samaki ambaye ameshapikwa, yuko tayari kwa ajili ya kuliwa! (Kicheko/Makofi)

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nusu sekunde. Nusu dakika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, utangulizi; nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa nafasi hii uliyonipa nami niweze kuchangia hotuba hii muhimu ya Makadirio ya Mapato na Matumzi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Awali ya yote naomba nipongeze hatua zinazochukuliwa na Serikali kuendelea kuongeza bajeti ya kilimo na suala la kilimo cha umwagiliaji kupewa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, nipongeze kwa uamuzi wa Serikali wa kujenga Bwawa na Skimu za Umwagiliaji katika Kijiji cha Mwakasumbi na Mwaukoli katika Jimbo la Kisesa. Suala hili nimekuwa nikilipigia kelele humu Bungeni kwa muda mrefu sana na ninaomba maeneo mengine yaliyobaki ya Mwandu Itinje, Mwasengela, Sakasaka, Tidabuligi na Mwabusalu nako maeneo hayo wananchi wanazisubiri kwa hamu kubwa skimu na mabwawa kwa kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kushindwa kukusanya maduhuli ya Serikali ambapo imeweza kukusanya kiasi cha shilingi milioni 679.57 sawa na asilimia 0.5 ya lengo la shilingi bilioni 126.1 zilizokadiriwa mwaka 2022/2023 hata mwaka wa fedha 2021/2022 mchezo ulikuwa ule ule Tume ilishindwa kukusanya mapato. Kitendo cha Wizara kutochukua hatua stahiki kwa uongozi wa Tume hii maana yake imebariki uzembe na ubadhirifu unaoendelea, hali hii inanipa mashaka makubwa juu ya uwezo wa Tume kusimamia majukumu na miradi mikubwa ya umwagiliaji ambayo tunaitengea mabilioni ya fedha kila mwaka. Hatua stahiki zichukuliwe ikiwemo kuwajibika kwa uongozi na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa bajeti ya maendeleo; hapa kuna mkanganyiko mkubwa, fedha za maendeleo zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 ni shilingi bilioni 569.97; hadi kufikia Aprili, 2023 fedha zilizokuwa zimetolewa ni shilingi bilioni 470.75 sawa na asilimia 82.6 ya bajeti nzima ya maendeleo. Fedha hizo zimetolewa na zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi, kuimarisha utafiti na uzalishaji wa mbegu bora, kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja na kugharamia ruzuku ya mbolea.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya maendeleo ya shilingi bilioni 569.97 fedha kwa ajili ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ni shilingi bilioni 361.5 sawa na asilimia 63.4 ya bajeti nzima ya maendeleo. Kiasi kilichokuwa kimelipwa hadi Aprili, 2023 kwa ajili ya miundombinu ya umwagiliaji ni shilingi bilioni 85.15 sawa na asilimia 23.5 tu ya bajeti ya umwagiliaji. Fedha zilizopokelewa na kutumika zilifikiaje kiasi cha shilingi bilioni 470.75 wakati fedha zilizotolewa kwa ajili ya miundombinu ya umwagiliaji ni shilingi bilioni 85.15 tu kati ya shilingi bilioni 361.5?

Mheshimiwa Spika, hata tafsiri yake ni kwamba fedha kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji imeshabadilishiwa matumizi na hapa kwa hesabu zangu ni takribani shilingi bilioni 200 hazijulikani zilipo na matumizi yake hayafahamiki. Waziri hana mamlaka kisheria kubadilisha matumizi ya vifungu na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Waziri atueleze fedha ziko wapi na zimebadilishiwa matumizi kwa ridhaa ya nani?

Mheshimiwa Spika, kuhusu Tume ya Taifa ya Ushirika; Serikali iliahidi kwa muda mrefu kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Ushirika lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua, mwaka jana Waziri wa Kilimo aliahidi hapa Bungeni kuwa benki hii ingekuwa imeanza katika mwaka huu wa fedha unaomalizika. Taarifa iliyowasilishwa inaonesha mtaji umefikia shilingi bilioni 5.2 tu kati ya mtaji wa shilingi bilioni 15 unaohitajika ili kukidhi vigezo vya kuanzisha benki kama vilivyowekwa na BOT na hatujaelezwa benki hiyo itaanzishwa lini.

Mheshimiwa Spika, aidha, ukaguzi uliofanywa na COASCO katika Vyama vya Ushirika 6,005 matokeo ya ukaguzi huo yameonesha kuwa hati safi ni 5.65% huku hati zenye mashaka, mbaya na kushindwa kutoa maoni zikiwa 94.35% na mwaka jana hali ilikuwa vilevile na kwa maana hiyo hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika na hii ni ishara ya kuota mizizi kwa ubadhirifu wa mali za umma na udhaifu wa mifumo ya udhibiti ya ndani hata Tume ya Maendeleo ya Ushirika ilipofanya ukaguzi ilibaini vyama vingi vya ushirika vinakabiliwa na madeni makubwa.

Mheshimiwa Spika, nimshauri mwaka jana na leo namshauri tena, Waziri aachane na mpango wa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Ushirika na badala yake aimarishe mifumo ya usimamizi ya vyama hivi na kuondoa mianya ya upotevu wa fedha za wanachama na fedha za umma na kadhalika. Pia ili kuwezesha kupata mikopo kwa wingi na kwa urahisi lianzishwe dirisha la Vyama vya Ushirika katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

Mheshimiwa Spika, kuhusu utoaji wa mbolea ya ruzuku; huu utaratibu wa utoaji wa mbolea za ruzuku ulianzishwa na Serikali katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 kwa lengo la kuongeza upatikanaji na kuwapunguzia gharama wakulima baada ya mtikisiko wa kiuchumi uliosababishwa na Covid-19 na vita ya Ukraine na Urusi. Utaratibu huu ulitarajiwa kuondoa kasoro na dosari zilizokuwepo lakini badala yake hali imekuwa mbaya zaidi, mbolea kuadimika na kusababisha wakulima kukosa mbolea, wakulima kuuziwa mbolea fake ambayo imeenda kuua mazao na kuharibu afya ya udongo, mbolea kuchelewa kufika kwa wakulima, utoroshaji wa mbolea nje ya nchi, kuuziwa michanga badala ya mbolea, wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata mbolea, kupoteza muda na wengine kupoteza maisha wakiwa kwenye foleni wakihangaika kutafuta mbolea.

Mheshimiwa Spika, utoaji wa mbolea ya ruzuku umekuwa na changamoto nyingi kama ifuatavyo: -

(i) Takwimu zilizotolewa na Waziri zina mkanganyiko mkubwa ambapo anasema hadi kufikia Aprili, 2023 mbolea za ruzuku zilizokuwa zimepokelewa na kusambazwa kwa wakulima ni tani 449,795 na wakulima walionufaika ni 801,776 lakini kiambatisho Na. 8 kinaonesha kuwa mbolea ya ruzuku iliyosambazwa ni tani 342,729 na wakulima walionufaika ni 782,553. Nini chanzo cha mkanganyiko huo wa takwimu au hizi takwimu ni za kupika? Waziri afafanue.

(ii) Wakulima waliosajiliwa ni 3,050,621 lakini wakulima walionufaika na mbolea ya ruzuku ni 801,776, nini kilichosababisha wakulima zaidi ya milioni 2.2 waliosajiliwa na kuahidiwa kupewa mbolea ya ruzuku wakose mbolea wakati nchini tuna ziada ya mbolea ya ruzuku tani 369,647?

(iii) Serikali ilifahamu kuwa haitawafikia na kuwasajili wakulima wote kwa mara moja, kwa nini ilianzisha mfumo wa utoaji wa mbolea ambao unalazimisha kupata lazima upitie mfumo wa mbolea ya ruzuku?

(iv) Mfumo wa kimtandao wa mbolea za ruzuku, hapa najiuliza kwa nini Wizara ya Kilimo ilianza kutumia mfumo huu ukiwa na changamoto nyingi kiasi hiki, na siamini kuwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) inaweza kutoa kibali (clearance) kuruhusu mfumo huu kutumika nchini. Mfano mfumo huu unaruhusu: -

(a) Mfumo hauna usalama wala ukomo (Security and Limit). Imewezekana kufanyika mikwaruzo ya kivunge cha mwitikio wa haraka (QR code scanning) zaidi ya mara moja (double scanning) or multiple scanning) kwa mauzo ya mfuko mmoja wa mbolea ambayo ingeweza kufanywa na waagizaji, mawakala, muundaji wa mfumo au haramia yeyote wa mfumo na kupelekea mauzo hewa ya mbolea kwa wakulima na madai hewa ya fedha kwa Serikali. Hapa ushahidi upo TFRA ilifutia leseni za mawakala 721 kwa makosa ya double scanning tarehe 17 Aprili, 2023.

(b) Mfumo huu hauwezi kung’amua kama mbolea imetumika kwenye shamba husika (traceability). Hivyo mtu anaweza kuja kuchukua tu mbolea kwa namba ya mkulima halafu akaenda kuiuza nchi jirani kwa magendo ambao wanampa bei kubwa zaidi kuliko bei ya ruzuku. Hali hii imepelekea utoroshaji mkubwa wa mbolea nje ya nchi. Kesi za utoroshaji wa mbolea nje ya nchi zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara. Hata Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alipofanya ziara Nyanda za Juu Kusini alikuta kesi za utoroshaji wa mbolea za ruzuku zimefurika kwenye Mahakama za Mikoa iliyo mipakani kama Songwe.

(c) Mfumo ulianzishwa bila kuzingatia kwamba huko mashambani mitandao ya simu inasumbua na inabidi wakulima wasafiri umbali mrefu kuitafuta mbolea sehemu zenye mitandao ya simu hali ambayo imekuwa ikiwaingiza hasara kubwa wakulima ya pesa za nauli, kulala guest house na gharama ya chakula.

(d) Mzabuni wa aliyeunda mfumo hatujaelezwa uwezo wake namna alivyopatikana, au alipatikana kwa kupewa mkataba bila kushindanishwa na wengine kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma (Public Procurement Act).

(e) Mfumo huu unachelewa ku-left na hivyo unamwezesha mkulima ku-draw zaidi ya kiwango alichonacho mfano anaweza kuchukua mbolea zaidi ya kituo kimoja na hivyo kupelekea hasara kwa mawakala.

(f) QR Codes zinaingiliana na kampuni nyingine mfano QR Codes za Kampuni X na Kampuni Y zinaingiliana na hivyo kusababisha mawakala kushindwa kutofautisha na hivyo kusababisha hasara na kudaiwa upande mwingine.

(g) Mfumo na matumizi ya Agrodealer Too/ hauruhusu kufanya Branch au Sub–Agent na hivyo kulazimisha wakulima kuja mjini sehemu moja kufuata mbolea na hautambui gharama nje ya eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha Wizara ya Kilimo kuanzisha na kutumia mfumo bila kupata kibali (clearance) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), ni kwenda kinyume cha sheria ya Serikali Mtandao (Electronic Government Act of 2019) na wahusika wanapaswa wawe wanatumikia kifungo hadi sasa. Mfumo huu umeleta hasara kubwa kwa wakulima, mawakala na Serikali ikiwemo. Madai hewa ya fedha za ruzuku za mbolea, mazao kudumaa na kukosa mavuno na madeni makubwa ya mawakala na waagizaji wa mbolea makampuni, kutumia fedha zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge cha shilingi bilioni 150. Nani atafidia hasara hii, huu ni uhujumu uchumi, ni lazima tupate maelezo ya kutosha ili Bunge lichukue nafasi yake.

(v) Kufuta leseni za mawakala wa usambazi wa mbolea 721, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) iliwafutia leseni mawakala 721 wa usambazaji wa mbolea ya ruzuku kupitia matangazo ya magazeti ya Mwananchi na The Guardian ya tarehe 17 Aprili, 2023 ambapo pia maamuzi hayo yalipata kibali cha Waziri wa Kilimo alipoongea na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Bunge Dodoma kupitia Kituo cha Televisheni cha Azam (UTV). Tarehe 19 Aprili, 2023 TFRA iliwaandikia barua mawakala hao wajieleze kwa nini wasifutiwe leseni ya biashara ya mbolea kwa kosa la kuvunja sheria kwa kufanya udanganyifu wa ku-scan QR Codes zaidi ya mara moja (multiple scanning). Jambo hili linaleta mkanganyiko mkubwa sana.

(a) Serikali kwa nini iandae mfumo unaoruhusu kufanya udanganyifu yaani double scanning or multiple scanning?

(b) Kwa nini TFRA iwafutie leseni mawakala 721 na kuwatangaza nchi nzima kuwa sio waadilifu halafu iwaandikie barua ya kuwataka wajieleze; kwa nini wasifutiwe leseni huku ikiwa tayari imeshawahukumu?

(c) Kwa nini TFRA imekiuka Sheria ya Mbolea ya mwaka 2009 ambayo inataka kutoa notisi ya siku 30 na kupata maelezo ya mawakala hao kabla ya kuwaondoa? Hapa kuna nia ovu iliyokusudiwa na Wizara dhidi ya hawa mawakala.

(d) TFRA ilijuaje kama double scanning imefanywa na mawakala wakati mfumo ulioandaliwa hauna usalama (security) kiasi kwamba multiple scanning inaweza kufanywa na waagizaji, muundaji wa mfumo au haramia mwingine yeyote wa mifumo ya mitandao.

(e) TFRA hakufahamu changamoto hizo, multiple scanning anasubiri imebaki miezi miwili kuisha msimu wa kilimo ndio anaanza kuchukua hatua?

Mheshimiwa Spika, nani atawafuta machozi mawakala 721 ambao wamevunjiwa heshima kwenye umma na mitaji yao kuwekwa rehani? Uvunjifu wa sheria ukiruhusiwa uendelee namna hii utaleta matatizo makubwa kwenye Taifa, watu wote waliohusika kufanya dhuluma hii wawajibishwe na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

(vi) Kutokufanyika uhakiki wa bei kabla ya kuanza kutoa mbolea ya ruzuku, Wizara ya Kilimo iliandaa mfumo wa kuanza kutoa mbolea za ruzuku bila kufanya uhakiki wa bei katika viwanda vinavyozalisha mbolea na matokeo yake pamoja na kushuka sana kwa bei za mbolea katika soko la dunia bado wakulima wanaumizwa kwa bei kubwa huku Serikali ikidaiwa pesa nyingi na makampuni yanayoingiza mbolea nchini ambazo zingeepukika kama ufuatiliaji wa bei za mbolea viwandani ungeendelea kufanyika mara kwa mara kama ilivyokuwa wakati wa BPS. Mfano, TFRA ilitangaza bei elekezi ya mbolea ya Urea kwa mfuko wa kilo 50 mwezi Agosti, 2022 kwa wastani wa shilingi 124,734, mwezi Novemba, 2022 wastani wa shilingi 116,687 na mwezi Machi, 2023 wastani shilingi 72,911. Mbolea katika soko la dunia ilikuwa inashuka bei kila mwezi kwa nini TFRA haikutangaza bei elekezi?

Kwa nini bei imeporomoka ghafla baada ya msimu wa kilimo kukaribia kufika mwisho na mahitaji ya mbolea kupungua? Lakini pia bei haina tabia ya kushuka ghafla inashuka kwa slope ni price elasticity or price volatility.

Mheshimiwa Spika, bei elekezi iliyotolewa na TFRA ilitokana na matamko ya wafanyabiashara na hakuna uhakiki wa kiuchunguzi (due diligence) uliofanywa na Serikali kupitia TFRA kama sheria inavyoelekeza. Pamoja na bei ya soko la dunia kuendelea kushuka, lakini ziliendelea kutumika bei zilezile za juu mpaka msimu wa matumizi makubwa ya mbolea ulipomalizika Machi, 2023 ndipo TFRA ikatangza bei ndogo zaidi (wastani wa shilingi 76,421 na hivyo kufanya wastani wa ruzuku ambayo Serikali ilitakiwa kuwalipa mawakala kuwa shilingi 6,421 kwa mfuko wa kilo 50). Hiki kitendo cha kuacha kufuatilia bei za soko la dunia kama sheria inavyoelekeza kumeifanya Serikali kulipa na kudaiwa na makampuni madai na malipo hewa.

(vii) Kiasi cha fedha kilicholipwa hadi sasa kugharamia mbolea ya ruzuku hakijatajwa mahali popote na Waziri wala madai ya waagizaji wa mbolea, kwa nini Waziri anatumia nguvu kubwa sana kuficha taarifa hizo.

Mheshimiwa Spika, ushauri; CAG afanye ukaguzi maalum kuhusu utekelezaji wa utoaji wa mbolea ya ruzuku kwa haraka kabla ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2023/2024 ili kubaini mapungufu yaliyopo na Bunge kuchukua nafasi yake.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa niweze kuchangia kuhusu hii Itifaki ya Biashara ya Huduma ya SADC. Awali ya yote niwapongeze sana Wabunge wenzetu na baadhi ya Mawaziri ambao wameteuliwa na wengine wamebadilishiwa nafasi zao. Tunawatakia kila la kheri wakati wa kula kiapo chao ili waje hapa Bungeni tufanye kazi za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia soko la SADC tunazungumzia soko ambalo nchi yetu inauza bidhaa na huduma takriban zaidi ya shilingi trilioni 4.5 kwa mwaka. Kwa mfano, mwaka 2022, mauzo yetu katika nchi za SADC tumeuza zaidi ya shilingi trilioni 4.5. Kwa hiyo, unapoliendea soko la SADC unaliendea soko ambalo ni kubwa, soko ambalo tunalitegemea na ni soko ambalo ni la pili kwa ukubwa katika masoko ambayo tunayauzia bidhaa zetu ikitanguliwa na Asia na masoko mengine kama la East Africa, Europe, AGOA na masoko mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, soko la SADC ni soko kubwa ambalo tunapofikiria kufanya jambo lolote ni lazima tulifikirie kwa umakini mkubwa na tuhakikishe kwamba tuko vizuri. Tunapozungumzia hii Itifaki ya Biashara ya Huduma (Protocol on Trade in Service, 2012), kabla hatujakubaliana kuridhia ni lazima tupewe majawabu kwenye mambo fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni lazima tujiulize kwa nini Azimio hili tangu lisainiwe na Wakuu wa nchi mwaka 2012, leo ni miaka 11 halijawahi kuridhiwa? Sababu zilizosababisha lisiridhiwe kwa miaka yote hiyo 11 ni nini? Mazingira gani yalikuwepo, Azimio hili linazaliwa tarehe 18/08/2012, sasa mpaka leo miaka 11 ndiyo linaletwa hapa Bungeni, kwa nini? Kwa nini halikuletwa kabla?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua Dkt. Stergomena Lawrence Tax ambaye anatoka Tanzania ndiye aliyekuwa Katibu Mtendaji wa SADC toka mwaka 2013 mpaka 2022 na leo ni mwaka 2023. Wakati akiwa kule Azimio hili halikuwahi kuletwa Bungeni wala halikuwahi kuidhinishwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais mstaafu wa Tanzania ambaye alisaini hii Itifaki mwaka 2012, amekaa madarakani miaka minne zaidi mpaka mwaka 2015, lakini hakuwahi kuleta hili Azimio ndani ya Bunge liridhiwe. Aliyelisaini hakuwahi kulileta hapa Bungeni liridhiwe, leo kwa nini linaletwa? Sababu za kuchelewa muda wote huo ni nini? Kama kulikuwa na kasoro za kurekebishwa mbona hatujaambiwa kama zimerekebishwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaletewa hili Azimio kuridhia lakini tuna SADC Protocol for Finance and Investment, tuna SADC Protocol on Trade, hizi protokali zote zipo. Hii protocal tunayotaka kuiridhia leo inaenda kutibu nini? Inaenda kuziba changamoto gani ambayo haipo katika protocol au katika Itifaki ambazo tumeshaziridhia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ile Ibara ya 16(2) imezungumzia kwamba tunataka huduma ya biashara kwenye hizi sekta sita. Je, tunaenda kunufaika katika muktadha gani? Tunaenda kufanyaje, kwa mfano kwenye TEHAMA tunaenda kufanya nini na TEHAMA? Kwenye ujenzi tunaenda kufanya nini na ujenzi? Haijaelezwa kwa kina. Ukisoma taarifa ya Waziri mwenyewe anayewasilisha Itifaki hii, hata taarifa ya Kamati yenyewe huoni ni kwa muktadha gani na kwa namna gani tunakwenda kufanya hizi biashara ambazo sasa hivi tunashindwa kuzifanya kwa sababu hii Itifaki haipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haijaelezwa nchi tano ambazo mpaka sasa hivi hazijaridhia hili Azimio. Haijaelezwa kwa nini nchi tano kwa muda wa miaka 11 hazijaridhia hili Azimio. Lazima kuna tatizo, kwa nini halisemwi? Kama kulikuwa na tatizo na tuliliona kwamba ni tatizo, tumefanya marekebisho gani na kwa nini leo tunataka Bunge hili lishiriki kuridhia hili Azimio bila kuelezwa matatizo yaliyopo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 6(4) inazungumzia suala la CMT, Committee of Ministers Responsible for Trade, kuanzisha utaratibu wa kinidhamu. Mawaziri wanaoshughulika na viwanda na biashara wanapewa mamlaka ya kuweka utaratibu wa kinidhamu huku tukijua chini ya WTO utaratibu wa kinidhamu wa kibiashara wa pamoja umeshawekwa katika General Agreements on Trade and Service (GATS).

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu ulishawekwa, sasa hii duplication ya kuweka utaratibu mwingine inatoka wapi? Kama Mawaziri wakiruhusiwa wakaenda kutengeneza mkanganyiko, hatuoni kwamba tunaweza kusababisha Nchi za SADC kuwa kwenye migogoro muda wote, kusuluhisha matatizo kila leo? Kwa nini tusitumie zile general rules, zile general disciplines zilizowekwa kwenye GATS badala ya hao Mawaziri kupewa fursa ya kwenda kuandaa na kutengeneza utaratibu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 8(2) imeweka sharti la mabadiliko yote ya sheria, kanuni na miongozo inayoathiri biashara ya huduma ya Nchi Wanachama kupeleka taarifa TNF Services yaani Trade Negotiation Forum Services. Takwa hili linaweza kutuletea matatizo makubwa, tunapotunga sheria zetu hasa zile domestic physical legislations ambazo katika nchi yetu hazitabiriki, mara nyingi tumekuwa tukianzisha tozo, faini, ada na ushuru mpya kila mwaka. Unaanzisha baadaye unafuta, baadaye unapunguza, baadaye unaondoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukifanya hivyo kila Mwaka wa Fedha ukifika, tunabadilisha sheria, tunaongeza tozo hii, tunapunguza tozo hii, tunasamehe ipi? Haya yote yamekuwa yanafanyika bila utafiti wowote na bila tathmini yoyote. Sasa kama kila mwaka tunaripoti kwa nchi zetu wanachama ambazo tunategemea soko kubwa sana kutoka kule SADC, tukiwa tunafanya hayo marekebisho kila mwaka, tunaweza kutengeneza mkanganyiko mkubwa sana na nchi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 16(2), tunaposema tunaenda kuingia kwenye huduma katika maeneo ya mawasiliano, fedha, ujenzi na usafirishaji tumejiandaaje ndani ya nchi? Mbona miradi mingi tuliyonayo sasa hivi hatuwapi wenzetu wa SADC? Hata miradi ambayo inaweza ikatekelezwa na wenzetu wa SADC mbona hatuwapi? Miradi ya TEHAMA mingapi tumeingia hapa na mikataba ya nchi za nje? Kwa mfano, Mradi wa CISCA ambao tungeweza kuutekeleza ndani ya Nchi zetu za SADC, Mradi wa TEHEMA wa TANESCO unatekelezwa na Mahindra Tech kazi ambayo ingeweza kufanywa na vijana wetu wa e-GA waka-develop huo mfumo, lakini tumewapa watu wa nje ya ukanda wa SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo tunapozungumza, tunaji-limit kabisa, tunaandika hapa, tunaruhusu mpaka kanuni za nidhamu ziwekwe. Mpaka tunaenda kuweka namna ya utatuzi wa migogoro kwa maana ya ile Annex one iliyowekwa katika Itifaki hii. Hivi tuna maandalizi gani wakati hata shughuli tulizonazo hivi sasa zote tunawapa watu wa nje ya ukanda? Tunafanya hivi kumfurahisha nani? Mbona hata maandalizi ya ndani ya kuridhia Itifaki hii hayapo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye ujenzi na uchukuzi, hata barabara fupi tu, za hela ndogo consultant anatoka Ulaya, consultant anatoka Asia. Hata kwa mambo ambayo tungeyafanya sisi ndani ya ukanda. Leo tunajifurahisha nini kusema kwamba tunaingia mkataba huu wakati hata miradi ambayo naizungumza tumefunga mikataba nje ya ukanda, wakati Itifaki hii Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alisaini toka mwaka 2012, kuna marekebisho gani toka kusainiwa kwa Itifaki hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia ushirikiano wa fedha wa sekta ya fedha. Sekta ya fedha nchini hapa na hata SADC wote tunategemea Dola. Sasa hivi Dola hakuna, Dola zimeadimika, wafanyabiashara hawapati Dola, hivyo hawawezi kuagiza mizigo, tunafanyaje? Maelezo yanayotolewa na Serikali, uwekezaji umeongezeka ndani ya nchi maradufu, watalii wameongezeka nchini maradufu, Dola zimeenda wapi kama uwekezaji, utalii na mauzo ya nje yameongezeka?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Luhaga Mpina, malizia sentensi moja ya mwisho.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimisha kwa kusema kwamba, Serikali ni lazima itatue tatizo la kuadimika kwa dola na hasa ninavyoona sababu ambayo haizungumzwi ni suala la ufisadi mkubwa ulioripotiwa na FIU kwa kuonyesha miamala shuku ya zaidi ya shilingi trilioni 280. Inawekana dola zetu zimetoroshwa kupitia mipakani na kwenye benki na leo nchi haina dola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kwa maelezo haya niliyoyatoa ambayo sikuweza kuyasema yote, nasema kwamba siwezi kuridhia Azimio hili na nalishauri Bunge kwamba lisiridhie hii Itifaki kwanza unless tupate maelezo ya kina ya Waziri nini kilichosababisha miaka 11 Itifaki hii haikuridhiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa ili nami niweze kuchangia hii Wizara muhimu sana. Nami niungane na wenzangu kuwapongeza sana watoa huduma wote wa afya hapa nchini kwa kazi nzuri sana wanayoifanya ya kutibu watu wetu na kuwapatia maisha mapya. Pia naipongeza Serikali kwa hatua nzuri ilizozichukua kuongeza idadi ya madaktari na kuhakikisha kwamba vifaa tiba pamoja na vitendanishi vinapatikana katika maeneo mbalimbali nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo shida kubwa kweli kweli hapa nchini ya upungufu mkubwa sana wa zahanati. Kama tunavyofahamu, zahanati hizi ndiyo huko huko kabisa kwenye msingi wa afya ya mwanzo, lakini hapa nchini kwa takwimu tulizonazo toka uhuru, tumeweza kujenga zahanati 6,120. Maana yake mpaka sasa hivi tuna upungufu wa zahanati 6,197. Kwa hiyo, tuna vijiji 6,197 havina zahanati. Kwa hiyo, asilimia 50.3 ya wananchi hawana huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hii hali, inaendelea kusababisha adha kubwa sana kwa wananchi wetu, akina mama wajawazito hawawezi kujifungua, mpaka watembee kilometa 10 mpaka 20 kupata huduma hiyo. Watoto wadogo wanapoteza maisha kwa kuchelewa kufika kwenye huduma kutokana na hizo kilometa ndefu za kufuata huduma hiyo kwenye vijiji jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili limekuwa likileta shida kubwa, hata sasa hivi tumepiga hatua kubwa, kwa mfano, kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano ambapo sasa hivi tunazungumza kwamba katika vizazi hai 1,000 watoto wanaopoteza maisha ni 50.3. Pia katika wajawazito 100,000 tunapoteza akina mama 321. Sasa hizi takwimu pamoja na safari ndefu tuliyotoka kule tumeweza kuzipunguza, lakini bado idadi hii ni kubwa na idadi hii sababu yake kubwa ni upungufu wa hizi zahanati katika vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu huu; na tunajua magonjwa hayana likizo na wala hayana week-end, lakini utaratibu wa Serikali tulionao sasa hivi na sisi wote ni kwamba zahanati mpaka tujenge jengo kwanza, likimalizika, mjenge nyumba ya mganga kwanza iishe, halafu mkimaliza, ndiyo sasa mfikirie kupeleka waganga, mfikirie kupeleka dawa. Hivi kuna shida gani leo hii tukiamua vijiji 6,197 ambavyo havina huduma ya afya, tukapeleka daktari, tukapeleka muuguzi, tukapeleka na dawa, watu wakaanza kutibiwa leo hii, badala ya kusubiri jengo lijengwe mpaka likamilike ndiyo tupeleke huduma. Kwa nini miundombinu itangulie badala ya huduma kutangulia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati hizi kwa awali zinaweza tu zikaanzishwa hata kwenye nyumba ya kupanga tu, wananchi wakaanza kupata huduma badala ya kusubiri majengo. Sasa leo tuna miaka 61 ya Uhuru, wananchi wanasubiri jengo likamilike ndiyo wapate huduma. Miaka 61 hakuna huduma ya msingi kwenye kijiji husika, tunasubiri mpaka tujenge zahanati, tunasubiri nyumba ya mganga ikamilike, tunasubiri jengo la zahanati likamilike: Kwa nini haya tunayaruhusu yafanyike?

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi ni pale ambapo hawa wananchi wameshamaliza kujenga majengo, daktari hakuna, huduma hakuna. Mimi ninayo mifano ya vijiji nadhani karibia nane, ambayo zahanati imejengwa na imekamilika, ina nyumba ya mganga, kuna zahanati imekamilika, lakini hakuna huduma, leo miaka nane. Ukienda Kijiji cha Semu, Ukienda Mwageni, ukienda Mwagai, Mwanduitinje, Igigijo, Tindobuligi na Malwilo, zahanati zimejengwa zimekamilika, lakini hakuna huduma. Sasa haya mambo kwa nini tunayaruhusu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri strongly kwa Serikali, Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI tuamue sasa wananchi hawa kuwamalizia tatizo lao. Vijiji 6,197 vipelekewe madaktari, vipelekewe dawa, vipelekewe wauguzi, zianze kutoa huduma mara moja. Vile vile mahali ambapo zahanati zimejengwa na kukamilika, watumishi waende mara moja, vifaa viende mara moja, huduma zianze kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni wizi wa dawa. Nimesoma hotuba ya Waziri kuhusu suala hili. Nadhani ipo ukurasa wa 61. Suala hili la wizi wa dawa linavyoripotiwa, ni kubwa sana, lakini nimeona kwenye hotuba ya Waziri pale imeandikwa kama para moja tu. Nataka niseme kwa ufupi kwamba, tatizo hili ni kubwa, dawa zinaibiwa. Songwe mlitangaza, nadhani Waziri mwenyewe alisema ni dawa karibia za shilingi milioni 13.5 ziliibiwa. Pia Ukerewe dawa za shilingi milioni 200 ziliibiwa; na kwenye taarifa yake huku ya tathmini anakiri kwamba wizi huu unasababisha huduma za dawa zisiwafikie wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kweli leo hii Serikali imeshindwa kabisa kudhibiti hawa wezi wa dawa? Mpaka leo hii wanaendelea kuiba dawa? Nani anayeiba dawa hizi? Anafanikiwaje kuiba dawa katika Serikali ambayo imejipanga kuanzia kwenye Kitongoji, kwenye Kijiji, kwenye Kata, kwenye Tarafa, kwenye Wilaya na ina vyombo vya dola kila sehemu, hawa wezi wa dawa ni akina nani ambao hawawezi kukamatwa na kuadhibiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Waziri hapa angetuambia amekamata wezi wangapi toka ianze vita dhidi ya wezi wa dawa? Hakuna, nani ameiba dawa? Anafanikiwaje kuiba dawa? Dawa hizi zinaibiwa zinaenda kuuzwa wapi? Nani ananunua dawa hizi? Mtandao wa wizi huo nani anaufadhili kiasi kwamba tushindwe kukomesha suala hili? Sasa watu wanaiba dawa, leo tunaenda kuidhinisha bajeti ya dawa zikaibiwe. Ni shida sana kupitisha bajeti ya Waziri huyu ambaye yeye mwenyewe anakiri kwamba kutokana na wizi huu, dawa haziwafikii wagonjwa. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama dawa haziwafikii wagonjwa, Bunge hili lijishirikishe kikamilifu kuhakikisha kwamba kwanza tunamaliza tatizo la wizi wa dawa, halafu ndiyo tupitishe bajeti, kwa sababu kinyume cha hapo tutakuwa tunawaongopea Watanzania. Ukisoma kiambatisho cha sita ambacho Waziri amekisema yeye mwenyewe, ukisoma yale matukio, ukiukwaji mkubwa wa manunuzi, watu wananunua dawa wanavyotaka wenyewe, watu wameiba dawa, watu wamefanya kila aina ya hujuma, hatua kwa nini hazichukuliwi? Kwa nini hatuambiwi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulitegemea kwamba wezi wa dawa hawa tungekutana nao kila siku wana pingu mkononi kila kunapokucha. Serikali hii haiwezi kushindwa kudhibiti wezi wa dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweza ufisadi, tumeweza uvuvi haramu, tumeweza madawa ya kulevya, leo hii tunakuja kushindwaje suala la wizi wa dawa? Kuna mtu hapa hajawajibika sawa sawa. (Makofi)

(Hapa kengele ililila kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa ili na mimi niweze kuchangia hii Taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo kama ambavyo imewasilishwa na Mwenyekiti na ni-declare kabisa mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya utungaji wa sheria ndogo kama ambavyo Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati imezungumza na jinsi alivyobainisha, changamoto ya utungaji wa sheria ndogo katika Halmashauri; changamoto ya kwanza, zinatungwa sheria ambazo zinatofautiana, kwa mfano, viwango vya tozo na ushuru vinatofautiana kutoka Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ya sekta kama za mifugo, uvuvi, kilimo, zinatofautiana na kusababisha malalamiko makubwa kwa wananchi wanapoona kwamba wenzao wanatozwa kidogo na wao wanatozwa pakubwa. Kwa mfano katika katika uvuvi, ushuru wa samaki, maeneo mengine wanatoza ushuru wa shilingi 100 kwa kilo sehemu nyingine wanatoza shilingi 300 kwa kilo. Suala hili limekuwa likileta usumbufu mkubwa sana na kuwasababishia wananchi manung’uniko kila sehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la pili ni kuwepo kwa utitiri wa sheria ndogo nyingi mno. Kutokana na kuruhusiwa kila Halmashauri moja inatunga sheria zake, kila kijiji kimeruhusiwa kutunga sheria zake, kila manispaa imeruhusiwa kutunga sheria zake, matokeo yake tumekuwa na sheria nyingi kiasi kwamba tumeshindwa hata kuzisimamia. Tumekuwa na sheria ndogo nyingi mno kiasi kwamba hatuwezi kuzisimamia sheria hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa mujibu wa Taarifa ya Auda’s Index pamoja na Taarifa ya JUTA Index of Subsidiary Legislations inaonesha kwamba tangu mwaka 1920 tumeshatunga sheria ndogo 41,051 ambapo sheria ndogo zinazofanya kazi mpaka sasa hivi ni 25,000, na kila mwaka tunatunga sheria ndogo zaidi ya 500. Sasa ukishakuwa na sheria ndogo nyingi namna hii huwezi tena kuzisimamia na zitaendelea kuleta madhara tu kwa wananchi kwa sababu haziwezi kuwa kwenye scope nzuri ya usimamizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la tatu kwenye Halmashauri ni kuwepo kwa upungufu mkubwa wa wataalam, jambo ambalo linasababisha sasa zinatungwa sheria ambazo zina mapungufu makubwa, zinatungwa sheria ambazo zinaweka adhabu na faini kubwa kuliko hata zile zilizoko kwenye sheria mama, zinatungwa sheria ambazo zina masharti na makatazo ambayo ni kinyume na sera, makatazo ambayo ni kinyume na Katiba ya nchi yetu, zinatungwa sheria ambazo zinapeleka dhuluma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukishakuwa na utaratibu huu wa utungaji wa sheria unatuletea madhara makubwa sana katika Serikali yetu na malalamiko makubwa sana ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napendekeza kufanyike nini; kwa nini tusiachane na huu utaratibu wa kila halmashauri inatunga sheria yake, kila kijiji kinatunga sheria zake, kila halmashauri ya mji inatunga sheria yake, kila manispaa tukawa na sheria moja tu kwamba halmashauri zote ziongozwe na sheria ndogo itakayotungwa na Waziri na itumike kwa halmashauri zote, yaani uniform by-laws, kwa kuzingatia makundi yote manne ya halmashauri ambayo ni mamlaka za mji, mamlaka za wilaya, mamlaka za miji midogo, mamlaka za halmshauri za vijiji, tunaweza tukafanya hivyo na tukafanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa bahati nzuri sheria inaturuhusu, Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura 287 na Sura 288 zinampa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutunga kanuni ndogo ambazo zitakuwa ni uniform kwa maeneo yote ambayo niliyoyataja na kwa kufanya hivyo ni rahisi tu kwa sababu itatulazimisha kufanya amendment kwenye vifungu vya sheria hiyo ya Serikali za Mitaa, Sura ya 287 na Sura ya 288 katika vifungu vinavyozipa mamlaka hizo, Mamlaka za Miji, Mamlaka za Wilaya, Mamlaka za Miji Midogo na Mamlaka za Halmashauri za Vijiji kuziondolea yale mamlaka zilizopewa kwa mujibu wa sheria, kutunga sheria na badala yake akatunga tu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kutungwa kwa sheria ndogo nyingi zenye dosari, lakini zinaanza kutumika kabla hazijahakikiwa na Bunge, kabla Bunge halijafanya sehemu yake ya oversight function tayari hizi sheria zinaenda kutumika. Madhara yake ni nini zinapoenda kutumika?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyekiti wa Kamati amezungumza na mimi ninazungumza kwamba moja, wananchi wanaadhibiwa kwa makosa ambayo si yao. Sheria imetungwa na Serikali, inaenda kutekelezwa ikiwa na dosari, wananchi wanaonewa kwa mambo ambayo ni kinyume cha sera ya nchi, kwa mambo ambayo ni kinyume na sheria za nchi, kwa mambo ambayo ni kinyume na Katiba ya nchi, lakini yameruhusiwa. Imeenda kutungwa kule sheria na kwenda kuleta madhara makubwa sana kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa bahati mbaya hata inapokuja kutokea kwamba sheria ile ilikosewa, kinachofanyika ni sheria ndogo tu inarekebishwa, halafu madhara waliyoyapata wananchi hakuna anayefidia; mtu aliyesababisha kuingia kwenye matatizo hayo hawajibiki na wala hachukuliwi hatua yoyote. Jambo hili limekuwa likituletea matatizo makubwa sana, lakini pia ni kinyume pia hata ya Ibara ya 8(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inazungumzia ustawi wa watu.

Kwa hiyo, Serikali na Bunge haziwezi kuruhusu mambo yanayokinzana na ustawi wa nchi yanaenda kutungwa na kwenda kwa wananchi wakati yanakatazwa kwa mujibu wa Katiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tatu katika hili eneo ni Bunge kunyang’anywa mamlaka yake; kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 97(5) ambayo imetupa mamlaka ya kukasimu utungaji wa hizi sheria ndogo, umekuwa ukivunjwa mno sasa hivi na mamlaka tulizozikasimiwa kufanya hilo jukumu. Sasa kama zinavunjwa na wananchi wanaenda kutengenezewa mgogoro mkubwa na matatizo makubwa ni lazima kama Bunge hili tuone kwamba tusikubali tena mamlaka yetu hayo yakatumika vibaya. Wananchi wanajua Katiba imelipa mamlaka Bunge la Jamhuri ya Muungano kutunga sheria na hivyo mtu yeyote atakayetunga sheria ya aina yoyote ikaenda kutumika kwa wananchi, moja kwa moja limetunga Bunge. Sasa Bunge hili lijitoe katika hilo, lisikubali tena hizi sheria ndogo kutungwa na kuanza kutumika bila kufanyiwa uhakiki kwanza na Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, kuchelewa kufanyiwa marekebisho ya dosari; hata dosari hizo tunapozibaini tunakuja hapa tunaagiza zikafanyiwe marekebisho, zimekuwa zikichelewa mno na wananchi wanaendelea kupata matatizo makubwa katika kanuni hizo. Marekebisho hayafanywi, kwa mfano, tulifanya maamuzi katika kipindi cha Februari, 2023 ambapo mpaka sasa hivi dosari 19 katika kanuni 10 bado hazijafanyiwa marekebisho na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kutoka katika jambo hili, nashauri kwamba tuziondoe changamoto nilizozitaja (a), (b) na (c); sasa napendekeza kila sheria ndogo inapotungwa na kutangazwa katika Gazeti la Serikali, isitumike kwanza hadi hapo Bunge hili litakapokuwa limefanya uhakiki wa sheria hizo na Bunge hili litafanya uhakiki wa sheria hizo kupitia Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ninalotaka kuzungumza, Mwenyekiti wa Kamati amempongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali nami nampongeza na jambo moja ninalompongeza, hata ukimpigia simu saa saba za usiku anapokea na anakujibu. (Makofi)

Sasa suala la kujiuliza ni kwa nini Sheria Ndogo hizi zinatungwa, zinafanyiwa vetting na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini zinaendelea kuwa na dosari kiasi hiki? Tatizo ni nini katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali? Tatizo ni sheria hizi zimekuwa nyingi wameshindwa kuzi-manage? Tatizo ni kwamba kuna upungufu wa fedha au wana upungufu wa watumishi au ni nini katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali? Mwanasheria Mkuu wa Serikali lazima atuambie ukweli juu ya jambo hili ili nchi hii isiendelee kupata matatizo inayoyapata hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu isikubali haya mambo yakaendelea kutokea na wananchi wetu wakaendelea kupata madhara makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba Bunge hili sasa lisiruhusu hizi kasoro ziendelee kutokea, wananchi wetu wakaendelea kutozwa tozo kubwa kuliko uhalisia, wananchi wetu wakaendelea kutozwa faini kubwa kuliko uhalisia, wananchi wetu wakaendelea kufukuzwa kwenye makazi yao bila sababu za msingi, wananchi wetu wakaendelea kutaifishiwa mifugo yao kinyume cha sheria na sera za nchi, wananchi wetu wakaendelea kutozwa kodi kubwa na tozo kubwa za maji, simu na mambo mengine kama umeme, unashtukia tu ghafla tozo na ushuru wa umeme umepandishwa na wananchi wanalazimishwa kulipa.

Mheshimiwa, Naibu Spika, haya yote yanafanyika kwa sababu ya Bunge hili kukasimu madaraka ya utungaji wa Sheria Ndogo kama Ibara ya 97(5) inavyosema, lakini eneo hili linatumika vibaya.

Sasa kupitia Bunge hili leo tukatae hayo kwa kuhakikisha kwamba hizo Sheria Ndogo ambazo zinatumika kama uchochoro wa kufanya dhuluma, wa kufanya uonevu kwa wananchi wetu kwa kisingizio cha kutunga Sheria Ndogo, sasa tukatae rasmi kupitia uchochoro huu kwa kukataza hizo sheria zote kupitia kule na matokeo yake ziletwe kwenye Kamati zetu ili tuzifanyie uhakiki kabla hazijenda kuumiza wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa na leo nashukuru nimemaliza yale niliyoandaa kusema. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi. Naamini kabisa tunakubaliana kwamba Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni sekta muhimu sana kwa Taifa letu na ndiyo maana tunasema tunachangia asilimia 25 ya fedha za kigeni, lakini zinachangia asilimia 30 ya pato la Taifa, zinachangia asilimia 65 ya ajira na zinachangia asilimia 100 ya chakula.

Mheshimiwa Spika, tunakubaliana pia kwamba kwa mwaka tuna wastani sasa hivi wa kuagiza chakula cha thamani ya trilioni 1.3. Sasa tu niseme nimesikia hapa wadau wazalishaji wa mbogamboga, matunda, maua na viungo wako kwenye Bunge lako hili. Nachukua nafasi hii kuwapongeza sana kwa sababu kati ya sekta ambazo zimefanya vizuri katika miaka mitano iliyopita 2015 - 2020 ni hiyo sekta ya wazalishaji hao ambao nimesikia wapo hapa pamoja na CEO wao Jacqueline Mkindi ambao uzalishaji ulikuwa milioni 400 tuliweza kuuza maouzo yetu ya nje milioni mia nne kumi na mbili mwaka 2015 ilipofika mwaka 2020 tayari wameshafika milioni 779, karibu mara mbili. Kwa hiyo, ni moja ya eneo linaenda vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, tunazungumza hiki kilimo chetu cha wananchi wetu hawa ambacho kimekumbwa na mzigo mkubwa wa matatizo, kimebeba mzigo mkubwa wa matatizo. Hapa wenzangu wamezungumzia suala la watumishi, watumishi wamesema wako 6,000 na kitu hapa, lakini wengine wako wilayani, hawapo kwa wakulima kwa hiyo tuna vijiji karibu 7,000, havina Maafisa Ugani. Sasa kama huna Afisa Ugani, ni nani anawaongoza wananchi wako, nani anakagua magonjwa ya wananchi katika mimea yao, nani anayewaongoza wakulima kupata mbegu bora, nani anayetibu mimea yao na kama hakuna wa kutibu na sisi ndiyo tunasema hili eneo ndiyo uti wa mgongo, ni uti wa mgongo gani ambao hauangaliwi hata ukipata magonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tuna suala hili la mbegu bora. Mheshimiwa Waziri amezungumza mambo ya mbegu bora hapa. Kwanza mbegu zinazozalishwa ni chache na hazitoshi, lakini gharama yake ni kubwa sana, tatizo la gharama limetatuliwaje? Mbona hatujaelezwa kwenye hotuba yake kwa sababu wananchi wengi wanashindwa kununua mbegu kwa sababu ya gharama kubwa sana, kilo moja unaambiwa Sh.6,000/=, Sh.7,000/= au Sh.8,000/=, nani atanunua? Kamfuko kamoja ka kilo mbili unauziwa Sh.10,000/ na zaidi nani atanunua?

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ni kubwa sana, Wabunge wenzangu wamezungumza hapa, ni suala la bei na suala la masoko. Wananchi wetu wana tatizo kubwa sana la masoko na tatizo linalotupeleka kwenye masoko hapa ni kwa sababu tunauza malighafi nje ya nchi. Tutaacha lini kuuza malighafi katika masoko ya Ulaya, tutaacha lini kuuza malighafi masoko ya China, India na sehemu zingine za AGOA na kwingine na kwanini tuendelee kuuza malighafi? Ni lini tutajenga viwanda vyetu wenyewe na kwa nini tusiamue leo na kukataa kuuza malighafi nje ya nchi? Tukiuza malighafi nje ya nchi wananchi wetu wananyonywa bei, wananchi wetu hawapati kipato kinachostahili, ajira tunaziuza nje, Watanzania wanageuka kuwa manamba wa kufanyia kazi viwanda vya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kujenga viwanda vya kimkakati shida kubwa ni mitaji kwa baadhi ya watu. Nani atakuja akujengee kiwanda hapa cha pamba wakati pamba anaweza akaichukua kwa bei ya kutupa, akaipeleka China, aka-process, akakuletea nguo, pamba ya s Sh.3,000/= akaja kukuuzia shati la Sh.50,000/= au Sh.100,000/=, nani atakuja kujenga kiwanda hapa? Kwa nini tusifanye maamuzi kama tulivyofanya kwenye umeme au kama tunavyofanya kwenye miundombinu ya barabara? Tukajenga viwanda hapa, tunajenga kiwanda kikubwa cha nyuzi, tukajenga kiwanda cha nguo, tukajenga kikubwa kiwanda kikubwa cha korosho kwa kutenga fedha zetu wenyewe, hata kama sisi Serikali tusipoendesha Watanzania wako wa kuendesha./ Tunajenga kiwanda kama ni cha bilioni 100, tunawakabidhi Watanzania waendeshe.

Mheshimiwa Spika, pia tunaweza kuwapa mikopo ya masharti nafuu, hata ya miaka 30, tatizo liko wapi? Leo hii tungekuwa na viwanda vyetu tusingekuwa tunapata matatizo haya, wananchi wetu wangenufaika kwa bei nzuri, lakini Taifa lingepata kodi nzuri katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tu ya muda, niseme pia kwamba, viwanda hivi tunaweza kuvijenga, lakini tatizo tulilonalo lingine ni ulinzi wa viwanda vyenyewe, viwanda vingi vilikuwepo, vingine vimekufa, vingine vimefungwa na wawekezaji wengine hawatakuja. Moja linalofanya viwanda vyetu viwe na changamoto kubwa ni mfumo wa kodi mbaya, unsupportive taxation regime yetu haifanyiwi tathmini mara kwa mara. Unaweza kukuta wakati mwingine hata mazao ya kutoka nje ya nchi yanakuwa exempted, wazalishaji wa ndani wanapigwa kodi, wale wanaoingiza mazao hayo ndani ya nchi na bidhaa hizo ndani ya nchi wamesamehewa. Sasa atashindanaje mwenye kiwanda hapa ndani? Hawezi kushindana.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa huu mfumo nilitegemea Wizara ya Kilimo wangeleta tathmini hapa ya kodi ambazo zina changamoto kubwa, tuna changamoto kubwa sana kwa mfano kwenye maziwa, ngano na kadhalika. Wazalishaji wa ndani ya nchi wanapigwa kodi lakini wanaoingiza wanasamehewa kodi, sasa nani atawekeza viwanda ndani ya nchi yako. Matokeo yake tuna mfumo wa ku-favour watu wanaoingiza bidhaa ndani kuliko wale wanaozalisha wakauze ndani. Huwezi kupiga hatua kwa namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, lingine ni ulinzi wa viwanda vyenyewe, viwanda hivi vinalindwaje wakati bado kuna importation kubwa ya mazao mengine kutoka nje ambayo sambamba na haya yanayozalishwa hapa nchini, mengine yanaingia holela bila kufuata utaratibu, hawalipi kodi wala hawafanyi chochote, wanaingiza na kuuza mazao hapa. Ulinzi unafanywaje na Wizara ya Viwanda na Biashara, ulinzi unafanywaje na Wizara ya Kilimo, ulinzi unafanywaje na vyombo vyetu vya dola, hapa kuna viwanda vinakufa kwa sababu ya kukosekana kwa ulinzi wa kulindwa viwanda hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hata mipango yetu mingine tunaanza tena, wananchi wanahangaika kuuza hiyo malighafi, tunaleta ushirika wa kuua wanunuzi wengine, unatengeneza ushirika wa kwenda kuua wanunuzi wengine, matokeo yake wananchi wanakopwa mazao yao hawalipwi, wengine wanapoteza kabisa fedha zao na wengine wanacheleweshwa fedha zao halafu kwenye Kijiji kimoja wanakuwepo wanunuzi wapo kumi unaenda kuamua awe mnunuzi mmoja; unaua ajira zote, Na Waziri hapa kwenye hotuba yake anazungumza ana… (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. LUHAGA J. MPINA: …anazungumza mambo ya ajira ya vijana wakati umeenda kuua ajira za vijana kwa kuthamini ushirika peke yake na kuwaondoa vijana waliokuwa wamejiajiri; kwa nini usiweke ushirika wenye pesa na vijana wanaonunua kivyao wakanunua halafu wakashindwana kwenye bei, wananchi wakaenda kuuza kwenye bei nzuri iliyokubwa aidha ya ushirika au ya mtu wa kujitegemea, tatizo liko wapi? Sera zetu zinakinzana na tunachotaka kufanya. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa. Niipongeze sana Wizara ya Fedha, Waziri wa Fedha na timu yake yote kwa namna ambavyo wametuletea taarifa muhimu kutuwezesha kujadili hotuba hii, lakini pia Kamati yako, Kamati ya Bajeti ambayo pia imetupa taarifa muhimu sana na ofisi zingine wezeshi kama NBS pamoja na CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya vizuri tunaisoma taarifa na hatua mbalimbali ya utekelezaji wa miradi yetu tumetekeleza vizuri. Tunaona sasa hivi tunaanza na LNG ambao tuko kwenye hatua nzuri, lakini utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta ambao tayari mchango wetu tumeshalipa bilioni 354, nusu ya fedha zinazotakiwa, lakini pia Mradi wa SGR tuko vizuri na Mradi wa Mwalimu Nyerere tunaendelea vizuri, sasa tuko asilimia 87. Kwa hiyo, ni mambo ambayo ni mazuri na tumepiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa labda nianzie mambo ya masuala ya kiujumla. Kwanza, naunga mkono sana pendekezo la Kamati yako ya kuhakikisha kwamba Finance Bill inaletwa na kujadiliwa angalau katika kipindi cha mwezi mzima, kuacha ilivyo sasa leo umewekwa mezani ambayo ni siku saba tu itakuja kuamuliwa hapa Bungeni. Kwa hiyo, naunga mkono kabisa kwamba tupate mwezi mzima wa kujadili taarifa ya Finance Bill. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika mambo ya kiujumla, nashauri lile bango kitita waliloshauriana lenye hoja kumi na saba zilizoibuliwa zingine ndani ya Bunge, lakini zingine kwenye Kamati, wangeleta hapa jedwali lile kuona Serikali imejibu nini na wa wamesema nini, badala ya kusema huko huko tu Kamati ya Bajeti walielewana sasa walielewana nini? Sisi tutajua nini hapa Bungeni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, katika yale maeneo ya kiujumla ni katika hotuba ya Waziri, katika hotuba ya Waziri wa Fedha, ibara nadhani ya 9, anapozungumzia Ibara ya 9 Mheshimiwa Waziri wa Fedha anazungumzia mwaka 2008 ambako Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, ukiweka ibara ya namna hiyo kwa maelezo waliyoyaweka pale inakuwa ni kama matumizi mabaya ya jina la Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne, katika haya mambo ya kiujumla ni pale ambapo katika Ibara ya 126 ambako Waziri anasema kupiga marufuku ufungaji wa biashara kwa sababu zozote zile. Ukiweka Ibara ya namna hiyo, unaweza kuleta mkanganyiko mkubwa, moja; kwanza mambo haya ni ya kisheria, yanafanyika kisheria, lakini la pili, kuna mambo ambayo yanalazimika biashara ifungwe. Kwa mfano, unakuta kiwanda au unakuta mgodi unatiririsha sumu kwenye makazi ya watu, unatiririsha sumu kwenye vyanzo vya maji, hizi Mamlaka za Usimamizi zifanye nini? NEMC wafanye nini katika mazingira ya namna hiyo kama siyo kufunga ili kuhakikisha kwamba wana–rescue maisha ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine unaweza kukuta mtu anafanya biashara hana leseni, hana kibali chochote, anauza bidhaa bandia, anauza bidhaa fake, unamfanya nini? Kwa hiyo, tukiweka vifungu kama hivyo vinaleta mkanganyiko kwa wasimamizi wa sheria ambao tumetunga sheria sisi wenyewe na kuwaagiza katika maeneo hayo wafanye nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ibara za namna hiyo aidha ziondolewe au Waziri azitolee ufafanuzi na mamlaka hizi zinazohusika na hizi kazi tujue kwamba zinafanya pia kazi nzuri sana ya ulinzi wa biashara. Kwa hiyo tusizikatishe tamaa kwa kuweka mistari mikubwa hivi kwenye hotuba ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda siwezi kuendelea kuzi–mention, lakini nadhani zinafanya kazi nzuri na zinahitaji kupongezwa, lakini pale ambapo mtumishi anaonekana ame–violate sheria za nchi ashughulikiwe na natamani watu wa namna hiyo atuambie kuwa amewachukulia hatua wangapi, lakini siyo kuzituhumu hizi taasisi za usimamizi na udhibiti ambazo zinafanya kazi nzuri sana hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la tatu ni ukusanyaji wa mapato. Nataka nizungumzie suala la ukusanyaji wa mapato na namna ambavyo hatujakusanya zaidi ya trilioni 15, kwa sababu ya usimamizi mbovu wa ukusanyaji wa mapato hapa nchini. Moja, imeripotiwa hapa kufikia Aprili, 2023 hatujakusanya fedha ambazo ziko kwenye malimbikizo ambazo zimeshikiliwa za kikodi zaidi ya trilioni 7.35. Trilioni 7.35 hatujazikusanya. Kesi hizo ziko kwenye mahakama hizi za rufaa za kodi TRAB na TRAT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unajiuliza mwaka mzima umeisha tumeshindwaje kuzikusanya fedha hizi? TRAB na TRAT hizi mamlaka zetu zina changamoto gani kiasi cha kushindwa kukusanya hizi fedha na ukiangalia uwezo wa TRA kushinda kesi katika haya mashauri ni asilimia 81, ina maana kwamba kwenye malimbikizo ya trilioni 7.35 tuna uwezo wa kukusnaya trilioni sita. Kwa hiyo, katika kipindi hiki tunaweza kukusanya trilioni sita kupitia hiki chanzo. Lakini tatizo ni nini tunashinda kuyakusanya hapa mapato? Nini kinachotukwaza kufanya hivyo? Tunaingia kwenye mikopo, tunaingia kwenda kuwa-harass wananchi wetu kuwawekea kodi ambazo hazina sababu za msingi, mapato yapo hayakusanywi kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili hapa kwenye suala la ukusanyaji wa mapato ni utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi. Taarifa ya FIU inaonesha miamala ya fedha taslimu na fedha zilizopitia katika miamala, zaidi ya trilioni 280 kuishia Aprili, 2023. Hivi utawezaje kukusanya kodi katika nchi ambayo ina miamala ya fedha haramu trilioni 280, halafu hauoni mikakati ya kushughulika na hizi fedha, hauoni mikakati iliyowekwa ya FIU kushughulika na hizi kesi na katika kipindi hicho kesi zilizosikilizwa au miamala iliyochambuliwa na FIU ni miamala 769 tu, kati ya miamala 16,035 iliyochambuliwa ni 769 peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo huoni mkakati wowote huwezi ukakusanya fedha, kodi katika eneo hili kwa sababu ukikuta miamala mingi namna hiyo maana yake ni kuna ukwepaji wa kodi uliopitiliza, maana yake kuna a list financial flow iliyopitiliza, maana yake kuna utoroshaji wa fedha nyingi nje ya nchi uliopitiliza, kuna transfer pricing illegal zinazofanyika zilizopitiliza. Utakusanyaje kodi katika mazingira haya? FIU ni kitengo tu mpaka leo, hakuna mechanism huioni, DCI anashughulikaje? PCCB anashughulikaje? DPP anashughulikaje kuhakikisha kwamba hii miamala tunapata fedha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili eneo tu ni fedha nyingi sana zilizopotea, lakini bado Tanzania iko kwenye financial action tax force na nini na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni magendo, magendo katika mipaka na katika maeneo ya bandari. Tunazo bandari bubu 693. Tunashindwaje kuwa-engage vijana wetu wa JKT tukaweka fence kila mahala tukaweza kukusanya fedha nyingi tu katika hili eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu una changamoto nyingi na mambo ni mengi niende kwenye mikopo, matumizi ya mikopo ya ECF na LTP. Kamati imetueleza bayana kwamba matumizi haya ya hizi fedha ni mikopo imeingiwa na Serikali. Serikali zaidi ya mikopo hii iliyoko kwenye hili eneo la ECF na LTP ni trilioni 2.75 na Kamati ya Bajeti inatueleza dhahiri kwamba hapa fedha hizi hazikwenda kwenye matumizi yenye tija, zaidi ya trilioni 2.75. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiambiwa hapa tunakopa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, inaenda kwenye miradi ya maendeleo. Leo Kamati yako ya Bajeti ina-prove kwamba fedha nyingi hizi zimekopwa, trilioni mbili zitakopwa na kuelekezwa kwenye maeneo ya matumizi ambayo hayana tija, trilioni 2.75. Fedha hizi tumekuwa tukikopa tunasema tunapeleka kwenye miradi ya maendeleo. Leo deni letu la Taifa limekuwa kwa asilimia 13.9 it is almost asilimia 14.9 kutoka mwaka mmoja kwenda mwaka mwingine. Ni mikopo ambayo hatujawahi kukopa kwa kiwango hicho, lakini tumekuwa tukiambiwa fedha zinaenda kwenye miradi ya kimkakati, lakini tumekuwa tukiambiwa kwamba fedha hizo tumekopa kwa sababu tuna miradi mingi ya maendeleo na mpaka sasa hivi tuna hiyo hoja ya Mkaguzi kwamba zaidi ya trilioni 1.285 zimekopwa nje ya kibali cha Bunge hili lilivyoidhinisha kukopa katika mwaka husika wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mikopo kama hii ikiendelea kuruhusiwa, Bunge hili likiendelea kuruhusu mambo kama haya yafanyike na mikopo hii ya ECF pamoja na LTP ambayo hata Bunge hili liliagiza ikajadiliwe kule na nimeona majadiliano mliyoyafanya inaonekana mmeshindana. Liletwe jedwali zima la fedha hizi trilioni 2.75 zinaenda kwenye maeneo gani na Waziri wa Fedha amepata wapi kibali cha kwenda kuidhinisha mikopo ya matumizi ya kawaida wakati msimamo wa nchi fedha zote zinakopwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Waziri wa Fedha yeye amepata wapi mamlaka ya kuruhusu fedha ya kwenda ku–negotiate mkopo ambao unaenda kwenye matumizi ya kawaida badala ya matumizi ya maendeleo? Lakini fedha nyingine nazungumza EPC+F. Hii EPC+F ni mfadhili anakuja na hela, anaajiri Wakandarasi yeye, anasimamia mradi yeye, anafanya design yeye, ananunua yeye. Mbona hatupewi maelezo ya kina Taifa linapata faida gani? Tutasimamiaje gharama? Tutasimamiaje ubora kwa Wakandarasi ambao hatuwalipi sisi? Lakini pia mikopo hii ni ndani ya mikopo yetu ile tunayokopa hapa nchini au ni mikopo mingine? (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Luhaga, muda wako umeisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nakupongeza sana kwa wadhifa huo. Pia nawapongeza sana Wizara ya Maliasili na Utalii; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote kwa kazi nzuri mliyoifanya hasa kudhibiti ujangili kwa asilimia 90. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza pia kwa kutuhakikishia kwamba mnaenda kuanzisha vituo vya askari wa kudumu katika maeneo hatarishi ya wanyama wakali na waharibu kwa maana ya tembo. Sasa hili nendeni mkalitekeleze, nasi tunawapongeza sana kwa kazi hiyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni suala la wafugaji walioshinda kesi Mahakamani, lakini Serikali imekaidi kurudisha mifugo yao. La kwanza, katika Pori la Maswa na WMA ya Makao, ng’ombe walikamatwa 1,739, walipoenda kwenye Mahakama Kuu Shinyanga wafugaji hawa walishinda, wakaenda kwenye Mahakama ya Rufaa Tabora, wakashinda. Ng’ombe jumla 1,739 mpaka leo hawajarejeshwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Kanda Dodoma kwa kesi ya jinai ya 136 ya mwaka 2017 ng’ombe 466 zilikamatwa katika Pori la Akiba la Swagaswaga ambapo ni ng’ombe 113 tu walirudishwa, lakini wengine wote katika 400 na kitu hawajarudishwa mpaka sasa. Pori la Akiba la Moyowosi ambapo ng’ombe 216 walikamatwa mpaka leo hawajarudishwa na Serikali. Katika ile hesabu ya ng’ombe 6,000 hii ni mifano tu ya wafugaji wetu ambao wameshashinda kesi Mahakamani, lakini Serikali haijarudisha mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza wakati nachangia hotuba ya Mheshimiwa Rais hapa kwa uchungu mkubwa nikijua kwamba Serikali italichukulia hili maanani. Nimesoma hotuba ya Waziri, hakuna hata mstari mmoja alipozungumzia juu ya mifugo hii. Wewe unajua kwamba haki inatolewa na chombo gani? Nanukuu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 107 (a) (1) Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji wa haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama imeshaamua ng’ombe warudishwe, wahusika hawajarudisha mpaka leo hii hawa ng’ombe wa wafugaji. Waziri wa Maliasili na Utalii hajarudisha mifugo ya wananchi, Waziri wa Katiba na Sheria amekataa kurudisha mifugo ya wananchi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amekataa kurudisha mifugo ya wananchi, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP amekataa kurudisha mifugo ya wananchi. Hawa wote wamevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo wao wameapa kuitetea na kuilinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Mawaziri wote wanne na hawa watendaji wengine wamevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo wao wameahidi kuilinda. Kwanza ni wasimamizi wa haki na sheria, inakuwa vipi waivunje sheria hiyo? Kama sheria imevunjwa, kama Katiba ya Jamhuri imevunjwa, Bunge hili ambalo limeapa kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba imevunjwa…

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina, naomba tupokee taarifa.

T A A R I F A

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa kwamba mchangiaji wakati ule alikuwa Waziri wa Mifugo na hizi kesi zimetokea akiwa Waziri. Tunataka kujua ni kwa nini yeye hakurudisha? (Kicheko)

MWENYEKITI: Hilo ni swali au taarifa! Mheshimiwa Mpina endelea.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, acha niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Mawaziri wamevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 107 (a). Kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano imevunjwa na Mawaziri hawa, Bunge lako lichukue nafasi. Hatuwezi kukubali wananchi wakadhulumiwa kwa namna hiyo inayoendelea sasa. Ng’ombe 6,000 wamekamatwa, wananchi hawa wameshinda kesi Mahakamani halafu mifugo hii inaendelea kushikiliwa…

MHE. MUSUKUMA J. KASHEKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Musukuma.

T A A R I F A

MHE. MUSUKUMA J. KASHEKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumpa taarifa tu mzungumzaji kwamba maneno anayoyazungumza yananikumbusha Bunge lililopita wakati tukichangia kuhusu suala la uvuvi, lakini alishindwa kutusaidia kwa sababu alikuwa anatekeleza sheria. Sasa nadhani angejikita kushauri kama Bunge tubadilishe sheria kuliko kumu-attack Mheshimiwa Waziri. Akiendelea hivi, kuna watu tutalia humu, tumechomewa mitego, Mheshimiwa Mpina uliapiza humu.(Kicheko/Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina, unaipokea taarifa?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna taarifa pale ya kupokea, itanipotezea muda. (Kicheko)

MWENYEKITI: Haya endelea.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nitaomba adjourning motion nizungumze kidogo haya maeneo yanayochomekwa haya kwa sababu muda wote niliisimamia hiyo Sheria ya Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananchi hawa wameshinda kesi Mahakamani, Mahakama Kuu zimeamua mifugo irudishwe; Mahakama ya Rufaa imeamua mifugo irudishwe; nani tena mtoa haki mwingine ambaye anasubiriwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge lako liamue leo, azma ya mifugo ya wananchi hawa irudishwe kwa wananchi ambao wamepata mateso makubwa sana kwa muda mrefu na Serikali imeshindwa kurudisha mifugo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nilizungumze hapa ni suala la utanuzi wa maeneo. Maeneo ya malisho yaliyo mengi mipaka ya hifadhi ilitanuliwa, ikachukua maeneo mengi sana ya malisho. Baada ya kutanuliwa, kwa mfano, ukienda kule Nsumba kule Ushetu; msitu ule wa Nsumba umeingizwa GN juu ya GN. Waziri wa Maliasili akatangaza GN wakati ule ni msitu wa wananchi wa eneo hilo na ulikuwa ukitumika kulishia mifugo. Huo ni mfano tu mmojawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tujue katika nchi yetu, tumeanzisha WMA zaidi ya 22, nadhani kwenye hotuba ya Waziri inaonyesha ni 38; na hiyo 38 imechukua hekta 3,062,300. Vile vile kuna shida kubwa sana katika hayo maeneo ya WMA ambapo vijiji 37 wameomba kujitoa, lakini hawasikilizwi. Bado kuna vijiji vingine walitoa eneo la WMA la zaidi ya asilimia 78 ya maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Vilima Vitatu kule Manyara, ukaenda Ipona kwenye Pori la Akiba la Mara, asilimia 75 imechukuliwa. Wananchi wale wanaomba muda wote kwamba maeneo yao yaweze kuangaliwa kufanyiwa tathmini, lakini hawaendi. Waziri wa Maliasili kuna shida gani kwenda kuwasikiliza wananchi wenye malalamiko haya? Waziri wa Ardhi ambaye ndio refa wa ardhi nchini, unafanya nini kwenda kumaliza migogoro ya wananchi hawa tukaimaliza kabisa, mpaka mwishowe tuwe na malalamiko ya kudumu ya muda wote huo mrefu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamechukua maeneo, kama ninavyozungumza hekta 3,062,300, yote haya tujue kabla ya WMA yalikuwa ni maeneo ya kulishia mifugo. Kwa nini leo hii maeneo haya wananchi wanaomba kwenda kufanya tathmini yasiende kufanyiwa tathmini ili sehemu nyingine ya ardhi ambayo inaweza ikapatikana wafugaji hawa wapewe? Sasa wananchi hekta zao 3,062,300 zimechukuliwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na maarifa ambapo leo Waheshimiwa Wabunge ni zaidi ya miezi mitatu tuko hapa kujadili na kuamua bajeti iliyowasilishwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru wewe, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge, Katibu wa Bunge na timu yake kwa namna mlivyotuongoza vyema katika kipindi chote cha kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, pia nashukuru upande wa Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa namna walivyojibu maswali na kutolea ufafanuzi wa hoja zetu hapa Bungeni, asanteni sana.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambavyo ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Usalama wa Taifa kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda amani na usalama wa nchi yetu, kulinda mipaka, kulinda raia na mali zao kazi ambayo inafanywa na vyombo vyetu usiku na mchana kwa uzalendo na kwa kujitoa kwa kiwango cha juu na kuifanya nchi yetu iendelee kuwa kisiwa cha amani.

Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru na kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoingoza Serikali na kuhakikisha maendeleo kwa Watanzania yanapatikana ambapo tumeshuhudia miradi mingi ikikamilika na mingine mingi ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwemo miradi ya Ikulu ya Chamwino, ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, bomba la mafuta kutoka Uganda, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, reli ya SGR, mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia wa LNG, Daraja la Tanzanite, Daraja la JPM-Kigongo Busisi, ujenzi wa meli ya Mv Mwanza - Hapa Kazi Tu, ujenzi uwanja wa ndege wa Kimataifa Msalato, ununuzi wa ndege mpya ya mizigo na miradi mingine ya elimu, afya, maji, barabara pamoja na kuanzishwa kwa Tume ya Taifa Mipango na kadhalika haya sio mambo madogo kama Taifa tuna kila sababu ya kujivunia.

Pia niwapongeze Watanzania wote wakiwemo wapiga kura wangu wa Jimbo la Kisesa kwa namna mnavyojitoa kwa hali na mali kulijenga Taifa letu katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, nimepitia Mpango wa Maendeleo, Hali ya Uchumi na hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2023/2024, pia nimepitia Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti; kwa ujumla hotuba hizi zimetoa takwimu na taarifa muhimu kutuwezesha Wabunge kutoa michango yetu. Aidha, nampongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Naibu Waziri, Mheshimiwa Hamad Hamis Chande, Katibu Mkuu na timu yote ya watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi zake za BOT, TRA, NBS na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), PPRA na kadhalika, pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa kazi nzuri mliyofanya.

Mheshimiwa Spika, mambo ya kiujumla; baadhi ya ibara katika hotuba ya Waziri wa Fedha zinahitaji ufafanuzi wa kina au kuondolewa kabisa kwenye hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa kuwa zinakwenda kinyume na Kanuni za Bunge pamoja na Sheria za nchi. Naomba kupitia mambo ya kiujumla katika vipengele vinne kama ifuatavyo:-

(i) Naunga mkono pendekezo la Kamati ya Bajeti la kutoa muda wa kutosha kuwasilisha na kujadiliwa Muswada wa Sheria ya Fedha (Finance Bill) walau mwezi mmoja badala ya siku saba ilivyo sasa ili kutoa nafasi ya kutosha kwa wadau na Waheshimiwa Wabunge kupitia kwa makini kabla ya kuupitisha.

(ii) Kamati ya Bajeti kutokuwasilisha bango kitita linaloonesha hoja 17 zilizoibuliwa katika Kamati za Kisekta na majadiliano Bungeni, bango kitita hilo lingeeleza hoja, majibu ya Serikali na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti badala ya maelezo waliyoyatoa na Kamati kuwa walikubaliana na Serikali bila kueleza walikubaliana nini na kulifanya Bunge lisielewe hoja zake zimeshughulikiwaje.

(iii) Waziri wa Fedha, kutumia vibaya jina la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhihaka kinyume na Kanuni za Bunge kwa kumsingizia kuwa alianza Urais mwaka 2008, huku ni kutumia vibaya jina la Mheshimiwa Rais. Kauli hii inatolewa kwenye hotuba ya Serikali Ibara ya 9 ukurasa wa tano wa hotuba ya Waziri wa Fedha huku akijua fika kuwa wakati huo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa wakati huo mwaka 2008 alikuwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, imekuwaje Waziri aweke taarifa ya aina hii? Naomba kunukuu; “Mheshimiwa Spika, Serikali ya CCM chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilianza mchakato wa kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni (sovereign credit rating) mwaka 2008 ambapo zoezi hilo halikukamilika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mdororo wa uchumi pamoja na kuyumba kwa soko la fedha duniani” mwisho wa kunukuu.

(iv) Kupiga marufuku ufungaji wa biashara kwa sababu zozote zile Waziri wa Fedha katika Ibara ya 126 ya hotuba anapendekeza kutofunga biashara kwa sababu zozote zile kuanzia tarehe 1 Julai, 2023 huku akijua kuwa kufunga biashara ni sehemu ya takwa la kisheria inapobidi kufanya hivyo, mfano mgodi au kiwanda kinapokutwa kinatiririsha maji machafu na yenye kemikali za sumu kwenda kwenye makazi ya wananchi na kwenye vyanzo vya maji na kuhatarisha maisha ya watu na viumbe hai wengine.

Je, mamlaka za udhibiti zifanye nini, ziache watu wafe ili kulinda biashara? Mfanyabishara anakutwa hana vibali, hana leseni, hana nyaraka yoyote, anauza bidhaa fake/bandia na zilizokwisha muda wa matumizi zenye athari za kiuchumi na kiafya kwa binadamu na viumbe hai wengine, ashtakiwe yeye halafu bidhaa zake ziendelee kuuzwa kwa wananchi? Hata wafanyabishara wa dawa za kulevya, fedha haramu na biashara haramu zingine nao waachwe waendelee na biashara zao wasifungiwe?

Kauli hii ya Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba inaleta mkanganyiko mkubwa wa kisheria na mifumo ya udhibiti nchini, lakini pia inarudisha nyuma jitihada za Serikali zinazofanywa na Mamlaka za Udhibiti katika kusimamia ustawi wa Taifa na wananchi kwa upande mwingine wataelewa kwamba Serikali imekuwa ikiwaonea.

Aidha, ifahamike kuwa ada na tozo zinazotozwa na mamlaka za udhibiti zipo kwa mujibu wa sheria na zilikubalika kwa Waziri mwenye dhamana ya Fedha hivyo sio sahihi kusema kwamba usimamizi wao makini unasukumwa na kuongeza mapato ya taasisi husika. Lakini pia ni muhimu kuthamini kazi nzuri inayofanywa na mamlaka zetu za udhibiti katika kulinda biashara, usalama wa afya za walaji na uchumi wa nchi, taasisi kama TBS, NEMC, TMDA, TPRI, OSHA, Polisi, TRA, DCEA, LATRA, EWURA, BOT, TCRA, eGA, TCAA, FIU, WMA, NACTVET, FCC, BRELA, PPRA na kadhalika zinapaswa kupongeza kwa kazi nzuri wanazofanya.

Mheshimiwa Spika, Waziri alipaswa kulieleza Bunge hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini (blueprint), lakini pia Waziri angeeleza hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi wachache wasio waaminifu ambao wamekuwa wakikiuka sheria na taratibu na kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuwanyanyasa wafanyabishara badala ya kuzituhumu kiujumla taasisi za udhibiti ambazo zimekuwa zikifanya kazi nzuri kwa mujibu wa sheria na kwa ustawi wa Taifa letu.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali; mapato ya kodi, yasiyo ya kikodi na ya halmashauri yamekuwa yakiongezeka kila mwaka lakini ongezeko hilo haliendani na kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Wastani wa pato la Taifa kwa makusanyo ya kodi kwa mwaka 2022 ilikuwa ni asilimia 12.3; uwiano huu ni chini ya uwiano kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao ni asilimia 15. Zipo changamoto nyingi zinazotufanya tushindwe kukusanya kodi stahiki.

(i) Malimbikizo ya kodi yenye mapingamizi Mahakamani taarifa ya TRAB na TRAT kuishia Aprili, 2023 inaonesha kuwa mashauri 1,155 ya rufani za kodi yenye thamani ya shilingi trilioni 7.35 yalipokelewa na kusajiliwa katika Mahakama za Rufani za Kodi za TRAB na TRAT ambapo mashauri 423 yenye thamani ya shilingi bilioni 849.8 yaliamuliwa sawa na 11.5% ya mashauri yote. TRA ilishinda mashauri 344 yenye thamani ya shilingi bilioni 824 sawa na 81% na walipakodi walishinda mashauri 79 yenye thamani ya shilingi bilioni 25.7 sawa na 19%. Mtiririko unaonesha kuwa nafasi ya kushinda kesi kwa TRA ni wastani wa 81%, hii ina maanisha kuwa endapo kesi zote zingesikilizwa kwa wakati TRA ingekusanya takribani shilingi trilioni sita kwa kipindi husika na kuongeza mapato ya Serikali. Hapa unaona kuwa mapato mengi ya Serikali yameshikiliwa katika mapingamizi ya kikodi bila sababu za msingi.

Je, nini kinachoifanya Serikali ishindwe kuweka mikakati ya kuzifanya Mahakama za TRAB na TRAT kuamua mashauri haya kwa wakati? Tunaacha kukusanya mapato haya ya wazi na badala yake tunakimbilia kuweka tozo na kodi kwa kuwakamua watu maskini. Nashauri iundwe Tume ya Bunge ili kubaini ukweli uliojificha na kuwezesha kukusanya mapato ya Serikali pamoja na kuondoa usumbufu ambao wafanyabishara wanaupata kwa kukaa na kesi muda mrefu.

(ii) Utakasishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi; taarifa ya Waziri inaeleza kuwa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) kuishia Aprili, 2023 kimeripoti ongezeko kubwa la taarifa shuku, kutoka taarifa shuku za fedha taslimu na usafirishaji kwa njia ya kielektroniki 724; Aprili 2021 taarifa shuku 12,651 zenye thamani ya shilingi trilioni 122.85; Aprili, 2022 hadi kufikia taarifa shuku 16,035 zenye thamani ya shilingi trilioni 280; Aprili, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 130. Aidha, Kitengo kimechambua miamala shuku 769 na kuandaa taarifa fiche 314 sawa na asilimia 40 ya miamala shuku iliyofanyiwa kazi na kuwasilisha kwenye taasisi za utekelezaji wa sheria kwa hatua za uchunguzi Aprili, 2023.

Mheshimiwa Spika, ni vigumu kwa Serikali kukusanya mapato stahiki katika mazingira ya namna hii ambapo taarifa shuku za fedha taslimu na usafirishaji wa fedha kwa njia ya kielektoniki zimeongezeka na kufikia trilioni 280 sawa na asilimia 130, hii inatupa ishara kuwa kuna ukwepaji mkubwa wa kodi unaofadhiliwa na mbinu mbalimbali ikiwemo biashara za magendo, wizi, rushwa, ufisadi, utoroshaji wa fedha na rasilimali nje ya nchi (Illicit Financial Flows), Transfer Pricing, uhamishaji wa mitaji (Capital Flight) na kadhalika. Hapa kuna maswali mengi ya kujiuliza:-

a) Kwa nini FIU ifanye uchambuzi wa miamala shuku 769 tu kati ya miamala shuku 16,035 ambayo ni asilimia tano tu ya miamala yote kwa mwaka mzima?

b) Serikali inachukua hatua gani za dharura kushughulikia taarifa shuku za utakasishaji wa fedha haramu zilizofikia shilingi trilioni 280 ili kuzuia ukwepaji mkubwa wa kodi na utoroshaji wa fedha nje ya nchi unaondelea nchini.

c) Ni fedha kiasi gani zilizoshikiliwa na FIU kutokana na taarifa shuku za fedha taslimu na usafirishaji kwa njia ya kielektoniki hadi sasa?

d) Kwa nini FIU isiwe mamlaka kamili badala ya kuwa kitengo chini ya Wizara ya Fedha kama ilivyo sasa? Pamoja na taarifa hizi za FIU kutishia uchumi, mapato ya Serikali na usalama wa nchi yetu, lakini hakuna mkakati madhubuti uliowekwa na Serikali kupambana na matukio haya ya uhalifu, leo tunazungumzia taarifa shuku 16,035 zenye thamani ya shilingi trilioni 280 lakini zilizofanyiwa uchambuzi ni taarifa shuku 769 tu sawa na asilimia tano kwa mwaka mzima. Hivi sasa nchi yetu inatekeleza Mpango Kazi wa Kikosi Kazi cha Kifedha cha Kimataifa (Financial Action Task Force – FATF), matukio ya utakasishaji fedha haramu yanazidi kuongezeka kila mwaka licha ya mikakati na hatua zilizochukuliwa na Serikali kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 18 ya hotuba ya Waziri. Lakini pia sijaona mkakati wa uwezeshaji, uratibu na kufanya kazi kwa pamoja kwa taasisi zinazosimamia utekelezaji wa sheria katika hatua ya kukamata, kuchunguza na kuendesha mashtaka kwa mamlaka zinazohusika za FIU, DCI, PCCB, DCEA na DPP.

(iii) Biashara za magendo na utoroshaji wa rasilimali za Taifa nje ya nchi; tumeshuhudia matukio mengi ya kushamiri kwa biashara za magendo ambapo bidhaa nyingi za magendo zinaingia nchini lakini pia kuna utoroshaji mkubwa wa rasilimali kama madini, nyara za Serikali, mazao ya misitu, mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi hali ambayo inaathiri kwa kiwango kikubwa uchumi, ukusanyaji wa mapato ya Serikali, mfumuko wa bei na ugumu wa maisha. Magendo haya yameshamiri katika maeneo ya mipakani na kwenye bandari bubu zinazofikia 693. Licha ya Serikali kupoteza mapato mengi katika hili eneo hakuna mifumo madhubuti ya udhibiti iliyowekwa na kulifanya tatizo hili kuwa sugu. Tunao vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa na wengine wakiendelea kujitolea katika Kambi zetu JKT na Jeshi la Akiba (mgambo) waliandaliwa uzalendo na moyo wa kujituma tuwatumie kudhibiti maeneo yote tete na kuongeza mapato ya Serikali.

(iv) Mifumo ya TEHAMA; Taarifa ya Wizara ya Fedha imeonesha kuwa kuna kasi ndogo ya ujengaji na maboresho ya mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali ikilinganishwa na kasi ya mabadiliko ya TEHAMA duniani na hivyo kuhatarisha ufanisi na usalama wa mifumo ya usimamizi wa fedha za umma. Kifungu cha 24(1) na (2) cha Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019 (e-Government Act No. 10 of 2019) inazitaka taasisi za umma kutekeleza miradi ya TEHAMA kwa namna ambayo itahakikisha manufaa yanayotarajiwa kupatikana na hatari zinapunguzwa kwa kuzingatia viwango na miongozo ya kitalaamu kama ilivyoagizwa na mamlaka. Aidha, hairuhusiwi kuanzisha na kutumia mifumo ya TEHAMA bila kupata kibali (clearance) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Mheshimiwa Spika, matumizi ya mifumo ya TEHAMA yamesaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi ya Serikali kwa kiwango kikubwa, baadhi ya mifumo hiyo ni GePG, GIMIS, TTMS, TANCIS, ITAX, EFDMS, TAUSI, HCMIS, TANePS, MUSE, LUKU na kadhalika ingawa pia zipo changamoto zinazopunguza ufanisi kama ifuatavyo:-

(i) Miundombinu ya mifumo ya TEHAMA kuhujumiwa; baadhi ya watendaji wa Serikali kwa maslahi binafsi wamekuwa wakiharibu miundombinu ya TEHAMA ili kuficha ukweli unaowekwa wazi na mifumo katika kuzuia wizi na ubadhirifu wa fedha za umma. Mfano kuzima scanner bandarini, mifumo kutosomana, mtandao uko chini na kadhalika.

(ii) Baadhi ya Wizara na Taasisi za Umma zimeanzisha na kutumia mifumo ya TEHAMA bila kibali cha eGA mfano Wizara ya Kilimo (Mfumo wa Mbolea ya Ruzuku) na TANESCO (Mfumo wa Mipango wa Rasilimali za Biashara – ERP) na kadhalika.

(iii) Kukosekana kwa uunganishwaji wa mawasiliano (connectivity) kutokana na baadhi ya maeneo hawajafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, minara ya simu na umeme hivyo mifumo kutofanya kazi.

(iv) Kutokuzingatia viwango na miongozo iliyowekwa na eGA, kukosekana ushirikiano wa kitaasisi na baadhi ya taasisi kuamini zaidi wataalamu na mifumo ya kutoka nje ya nchi kupata suluhisho la changamoto za mifumo yao.

(v) Baadhi ya taasisi za Serikali kutokuwa na watalaamu wabobezi wa mifumo ya TEHAMA na hivyo kupelekea ufanisi mdogo wa mifumo na kadhalika. Serikali itatue changamoto zinazokabili ufanisi wa mifumo ya TEHAMA na kuwekeza kikamilifu katika wataalamu wabobezi wa TEHAMA, pamoja na changamoto nilizozitaja nchi yetu ya Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA kwa kushika nafasi ya 26 kidunia na ya pili Barani Afrika baada ya Mauritius kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) mwaka 2022 kuhusu ukomavu wa matumizi ya teknolojia duniani katika utoaji wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi (GovTech Maturity Index).

(vi) Kushindwa kukusanya mapato kwa mujibu wa mikataba na sheria; baadhi ya Wizara na Taasisi za Serikali zimeshindwa kukusanya mapato yatokanayo na faini, tozo na CSR katika utekelezaji wa mikataba na zingine zimeshindwa kukusanya malipo baada ya kushinda mashauri mahakamani. Mfano Wizara ya Nishati na TANESCO kushindwa kukusanya faini shilingi bilioni 655 na CSR shilingi bilioni 270 kutoka Kampuni ya Arab Contractors na malipo kutoka Kampuni ya IPTL kiasi cha shilingi bilioni 342 ambapo jumla ni kiasi cha shilingi trilioni 1.268, Wizara ya Katiba na Sheria na DPP kushindwa kukusanya shilingi bilioni 170 kutokana na malipo ya kesi za plea bargain. Kwa mifano hii michache hatujakusanya jumla ya shilingi trilioni 1.438 bila sababu za msingi, tulimsikia Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba eti kutokukusanya fedha hizo za umma alitumia hekima na busara, hizo hekima na busara tunazipimaje katika fedha za umma ambazo ziko kisheria na kwa mujibu wa mkataba. Mawaziri wetu wanageuka kuwa mawakili wa makampuni halafu leo tunaenda kuweka tozo ya ushuru wa barabara na mafuta ya shilingi 100 kwa mafuta ya petroli na dizeli ili zitumike kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ambapo itaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 381.8, tozo hii inakwenda kuwakamua wananchi masikini, inafikirisha sana, hapa nasema bila kumung’unya maneno Serikali haiwatendei haki wananchi katika hii tozo.

(vi) Malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani; malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani yalifikia kiasi cha shilingi trilioni 7.54 mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo ilionesha uwezo mdogo wa 10% wa TRA kukusanya mapato hayo. Taarifa ya Waziri wa Fedha haijaonesha malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani yalifikia kiasi gani mwaka wa fedha 2021/2022. Kama assessment ya kodi ilifanyika na hakuna mapingamizi nini kilichowafanya TRA washindwe kukusanya mapato hayo? Eneo hili hata tungeweza kukusanya 50% tu tungepata kiasi cha shilingi trilioni 3.77. Nashauri iundwe Tume ya Bunge ili kubaini ukweli uliojificha na kuwezesha kukusanya mapato ya Serikali.

(vii) Malimbikizo ya Kodi za Madini (Makinikia) mwaka wa fedha 2020/2021 inaonesha miongoni mwa kesi za rufani zilizoisha ni kesi 45 zenye thamani shilingi 5,594,675,387,242.40 ambazo zipo katika mazungumzo kati ya Serikali na kampuni za madini ambayo ni North Mara Gold Mine, Pangea Minerals Limited, Bulyanhulu Gold Mine na ABG Exploration. Kati ya kesi hizo jumla ya deni la shilingi trilioni 343.5 lilirejeshwa kusikilizwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Hotuba ya Waziri wa Fedha haijaeleza hitimisho ya suala hili la malimbikizo ya kodi ya kiasi cha shilingi trilioni 5.594 ambapo Mamlaka za Rufani za Kodi za TRAB na TRAT ziliona Serikali inastahili kulipwa madai hayo. Pamoja na maelezo ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa madai hayo yalifutwa na sherehe ikafanyika Ikulu hadi leo ameshindwa kuleta uthibitisho na sababu za msingi za kufutwa kwa madai hayo. Kwa mujibu wa kifungu cha 43(1) cha Sheria ya Fedha za Umma Bunge linaweza kwa Azimio la Bunge kutoa idhini kwa Waziri wa Fedha kufuta hasara na upotevu wa fedha na vifaa vya Serikali, madai ya kodi pamoja na riba itokanayo na malimbikizo ya kodi. Bunge halijawahi kupitisha Azimio hilo. Kwa msingi huo wa kisheria bado naamini hakuna mamlaka yoyote iliyofuta madai ya kodi ya malimbikizo ya kodi za Makinikia kutoka kwa makampuni ya madini kiasi cha shilingi trilioni 5.594 na inashangaza kuona kwa nini Serikali haijakusanya mapato hayo hadi sasa.

Nashauri iundwe Tume ya Bunge ili kubaini ukweli uliojificha na kuwezesha kukusanya mapato ya Serikali.

(viii) Kuweka misamaha ya kodi kwenye kundi la watu wachache kupitia Finance Bill ya mwaka 2022 tuliamua kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kumpa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha mamlaka ya kusamehe kodi hizo kwa wawekezaji mahiri maalum. Kuweka misamaha ya kodi kwenye kundi la watu wachache maarufu kama wawekezaji mahiri maalum, maamuzi haya yanainyima Serikali mapato pasipo sababu za msingi, kodi za namna hii ni za kibaguzi na zinaondoa ushindani wa haki, misamaha ya kodi sio kivutio pekee cha uwekezaji, kunufaisha kundi la wachache na kuwakamua wananchi masikini kwa kuwawabebesha mzigo wa tozo na kodi kubwa kufidia mapato ya Serikali yanayopotea mfano malalamiko ya wafanyabishara kule Kariakoo na maeneo mengine nchini, Waziri atuambie tangu kuanza utaratibu huo Serikali imevutia wawekezaji wangapi na imepoteza mapato kiasi gani?

Waheshimiwa Wabunge, tuamue leo kupitia Finance Bill ya mwaka 2023 kufuta utaratibu huu ili kuleta usawa katika ulipaji kodi na kuokoa mapato ya Serikali yanayopotea bila sababu za msingi. Ni hatari kwa Taifa kuwa na mfumo wa kodi wa aina hii hususan katika kipindi ambacho Taifa linavutia uwekezaji na kuingia mikataba mikubwa ya rasilimali za nchi mfano miradi ya kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG), madini, gesi, mafuta, makaa ya mawe na kadhalika na kuikosesha mapato Serikali.

(ix) Kuondoa faini kwenye miamala ya transfer pricing kupitia Finance Bill ya mwaka 2021, Waziri wa Fedha alifanya marekebisho ya Kanuni Na. 15 ya Ukokotoaji wa Kodi za Kimataifa (Transfer Pricing Regulations) kwa kufuta kifungu kinachoweka adhabu ya asilimia 100 kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya sheria. Lengo la hatua hii ni kuwaondolea walipakodi adhabu kubwa ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuvutia uwekezaji nchini. Uamuzi huo aliufanya Waziri wa Fedha huku akijua kuwa TRA ina uwezo mdogo wa kukagua miamala ya transfer pricing katika Makampuni ya Kimataifa (MNCs) na Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kupitia miamala ya Kimataifa (Transfer Pricing) uamuzi huu unahamasisha uvunjaji wa sheria yaani makosa yafanyike halafu hatua zilisichukuliwe kwa wahusika na kuikosesha Serikali mapato bila sababu za msingi.

Bunge limuagize Waziri wa Fedha kuirejesha kanuni hii ili kudhibiti ukwepaji wa kodi unaofanywa na MNCs. Jitihada za Serikali za kuimarisha udhibiti na kuzuia upotevu wa mapato katika vihatarishi vilivyopo katika miamala ya uhamishaji wa bei ya mauziano ya bidhaa na huduma baina ya makampuni ya kimataifa (transfer pricing) hazitazaa matunda kama sheria ndani ya nchi haina meno ya kudhibiti wahalifu. Hatua kubwa iliyopigwa na Serikali kupitia TRA ni pamoja na kununua kanzidata ya Orbis kwa ajili ya kupata taarifa za kusaidia kufananisha bei za miamala ya kimataifa ili zisaidie kujenga hoja wakati wa ukaguzi unaofanywa kwenye kampuni za hapa nchini. Pia Tanzania imejiunga na Jukwaa la Kimataifa la Ubadilishaji wa Taarifa za Kikodi kwa lengo la kuhakikisha nchi yetu inajenga uwezo wa kubadilishana taarifa za kikodi na nchi nyingine na Serikali inatarajia kusaini mkataba ujulikanao kama Multilateral Convention on Mutual Administrative Assistance in Tax Matters ambao utaiwezesha TRA kupata taarifa mbalimbali kutoka katika nchi 146 duniani ambazo zitasaidia katika kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa miamala ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, mwisho katika hili eneo la ukusanyaji wa mapato Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na taasisi zingine za Serikali zinazohusika na ukusanyaji wa mapato zinapaswa kujipanga vizuri kwa kuweka programu na mikakati madhubuti ili kuweza kukusanya mapato kwa ufanisi mkubwa na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali. Wigo mdogo na ulegevu wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali unapelekea kuanzisha kodi na tozo kubwa kwa wananchi masikini, kuchochea mfumuko wa bei na ugumu wa maisha. Mfano kwa uchambuzi wangu mdogo katika vipengele tisa nilivyovitaja Serikali ingekusanya mapato ziadi ya shilingi trilioni 15. Kiasi hiki cha fedha kingewezesha kugharamia miradi yote ya kimkakati na ya maendeleo bila kuchukua mkopo kokote.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya mikopo ya ECF na LTP kutoka IMF na WB; utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za mikopo katika kipindi cha miaka mitatu ambapo mkopo kutoka dirisha la Extended Credit Facility (ECF) kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wa miaka mitatu wenye jumla ya shilingi trilioni 2.4 na Mkopo wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki ya Ardhi (LTP) kutoka Benki ya Dunia wa dola za Marekani milioni 150 sawa na shilingi bilioni 350. 65 Kamati imeeleza kuwa mikopo ya ECF na LTP kiasi cha shilingi trilioni 2.75 kimeelekezwa katika shughuli ambazo hazina manufaa ya muda mrefu. Fedha hizo zimeelekezwa katika mafunzo, ununuzi wa vifaa vya ofisi, utekelezaji wa shughuli zisizo na tija na kutokuwa na mpango wa uendelevu wa miradi pindi mkopo utakapokoma.

Mheshimiwa Spika, msimamo wa nchi yetu ni kutochukua mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida bali mikopo yote iwe ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Waziri wa Fedha alipata wapi kibali cha kuchukua mikopo isiyo na tija na alifanya kwa manufaa ya nani? Katika siku za hivi karibuni deni la Serikali limekuwa likiongezeka kwa kasi kubwa mfano katika kipindi cha Aprili, 2022 hadi Aprili, 2023 deni la Serikali limeongezeka kwa shilingi trilioni 9.84 sawa na ongezeko la 14%; huu ni ukuaji mkubwa sana wa deni la Serikali. Kila tukiuliza tunajibiwa deni ni himilivu na kwamba linaongezeka kwa sababu ya kugharamia miradi ya kimkakati ya SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere, Daraja la Kigongo Busisi lakini leo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeweka wazi ukweli uliokuwa unafichwa kwa nguvu kubwa na Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amekwenda kufanya makubaliano na kukopa mikopo ya isiyo na tija ya zaidi ya shilingi trilioni 2.75, ni Waziri huyu huyu kwenye Taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 ambaye amekopa zaidi ya trilioni 1.285 nje ya bajeti na bila kibali cha Bunge, lakini pia ni Waziri huyu huyu amechukua misaada na mikopo ya nje yenye masharti nafuu ya shilingi trilioni 2.531 ambayo haikupitia Mfuko Mkuu wa Serikali kinyume cha sheria.

Mheshimiwa Spika, Bunge liitake Serikali kuwasilishwa mchanganuo wa mpango wa matumizi na mgao wa fedha hizi za mikopo ili Bunge liweze kuchukua nafasi yake.

Mheshimiwa Spika, ufadhili wa miradi kupitia utaratibu wa EPC+F; kupitia mpango wa maendeleo, hotuba ya Waziri wa Fedha na hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ilielezwa kuwa mwaka 2022/2023 Wizara ilianza taratibu za manunuzi kwa ajili ya kuwapata makandarasi wa kujenga barabara saba kwa kiwango cha lami kwa kutumia utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC + F). Hatua iliyofikiwa hadi sasa ni kuwa makandarasi wa miradi yote saba wamepatikana na mikataba ya kazi za ujenzi imesainiwa tarehe 16 Juni, 2023 ambapo makandarasi wanne wamepewa kazi hiyo ya barabara saba zenye urefu wa kilometa 2,035 kwa gharama ya shilingi trilioni 3.7.

Mheshimiwa Spika, uamuzi wa kujenga barabara zenye jumla ya kilometa 2,035 maeneo mbalimbali nchini ikiwemo barabara inayopita Jimbo la Kisesa ya kutoka Karatu-Mbulu-Sibiti-Meatu-Lalago-Maswa ni jambo la kupongezwa kwani mtandao huo wa barabara utaleta tija kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo na uchumi wa nchi kwa ujumla. Hapa unazungumzia nchi kuingia mkopo wa trilioni 3.7 lakini nimepitia taarifa zote za Serikali hakuna maelezo ya kina namna miradi hii itakavyotekelezwa na makampuni yaliyopewa zabuni ya ukandarasi wa ujenzi yatakavyorejesha fedha zake na fedha hizo zitarejeshwa kwa kipindi gani.

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa miongoni mwa Wabunge waliohudhuria hafla ya utiaji saini mikataba hiyo lakini hakuna ufafanuzi wa kina uliotolewa kuhusu suala hili na kuacha maswali mengi ya kujiuliza kama ifuatavyo:-

(i) Gharama za mradi (project costs) huandaliwa na mfadhili na baadaye shughuli za ujenzi na manunuzi hufanywa na mfadhili mwenyewe na hivyo si rahisi kwa Serikali kujiridhisha na thamani halisi ya mradi (value for money) kwani mzabuni haimzuii kufanya upandishaji wa bei na gharama. Je, nafasi ya Serikali itakuwa wapi katika usimamizi wa gharama na ubora wa miradi wakati mfadhili analipa moja kwa moja kwa Makampuni yake? Kwa nini haielezwi kilometa moja ya barabara inajengwa kwa shilingi ngapi ikilinganishwa na gharama ya kilometa moja tunazojenga barabara za lami nchini hivi sasa.

(ii) Fedha hizi haziingii kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwani mfadhili analipa moja kwa moja kwenye makampuni yake ya ujenzi. Je, nafasi ya CAG na Bunge katika usimamizi wa miradi ya aina hii itakuwaje? Na kuna hatari miradi hii ikatumika kama uchochoro wa ubadhirifu wa fedha za umma, mfano fedha trilioni 3.7 hazimo kwenye bajeti ya Wizara - sekta ya ujenzi Fungu la 98.

(iii) Tulishaweka ukomo wa mikopo katika bajeti ya Serikali mwaka 2023/2024 hizi fedha za EPC+F ziko kwenye fungu gani? Hii inaweza kuwa njia ya kutanua goli la kuchukua mikopo nje ya utaratibu maalum uliowekwa kisheria ambao unaweza kulipelekea Taifa letu kutumbukia kwenye mzigo mkubwa wa madeni yasiyolipika.

(iv) Hapa ulinzi wa ajira za Watanzania uko wapi? Kazi zote zitafanywa na mfadhili ku-design mradi, ununuzi wa vifaa vya ujenzi, kuajiri makandarasi na kadhalika. Miradi ya aina hii inavunja mnyororo wa thamani na ni hatari kwa Taifa ambalo lina vijana wengi wanaohitimu katika vyuo mbalimbali wakiwa na tatizo kubwa la ajira. Mwisho wa siku huu ni mkopo ambao kama Taifa tutalazimika kuulipa na hivyo ni lazima tujue ukweli wa masharti ya mikataba hii na Serikali iache kuweka siri katika jambo hili na iweke wazi faida itakayopatikana ya mradi huu ikilinganishwa na mikopo ya kawaida, huko nyuma tumekuwa tukikataa mikopo ya utaratibu wa EPC+F kutokana na masharti magumu na yasiyozingatia maslahi ya Taifa. Serikali ilete maelezo ya kina juu ya miradi hii ikibainisha masharti yote ya mikataba na mchanganuo wa gharama kwa kila mradi na muda wa kukamilisha miradi ili Bunge lichukue nafasi yake.

Mheshimiwa Spika, miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP); nimesoma mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2023/2024 na hotuba za Mawaziri kuhusu maeneo ya miradi itakayotekelezwa kwa utaratibu wa ubia na sekta za umma na sekta binafsi (PPP) baadhi ya miradi hiyo ni kama ifuatavyo; kuanza ujenzi wa barabara ya Kibaha – Chalinze - Morogoro hadi Dodoma yenye urefu wa kilometa 461 kwa utaratibu wa PPP na barabara ya tozo Mbeya Bypass (Uyole – Sogwe kilometa 48.9).

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Waziri kuhusu ujenzi wa barabara kwa kutumia utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi (Public Private Partnership - PPP), Wizara inaendelea na manunuzi ya makandarasi kwa ajili ya ujenzi wa expressway kutoka Kibaha – Chalinze – Morogoro yenye urefu wa kilometa 205. Hadi sasa kazi inayoendelea ni uchambuzi (evaluation) wa makandarasi watano walioonesha nia (expression of interest) ya kutekeleza mradi huu kwa sehemu ya kutoka Kibaha – Chalinze yenye urefu wa kilometa 78.9. Kwa sehemu ya Chalinze – Morogoro yenye urefu wa kilometa 126.1, Mshauri Elekezi anaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu. Utaratibu wa PPP ni mzuri katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika ujenzi wa barabara kwa kuwa mara nyingi huwa kuna njia mbadala (alternative roads/competing roads) ambayo sio ya kulipia, lakini hapa nina wasiwasi mkubwa juu ya masharti ya mkataba utakaoingiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inajenga reli ya SGR kutoka Dar es Salaam - Dodoma hadi Mwanza ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo na pia kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo lakini pia kuwepo kwa barabara shindani isiyo ya kulipia. Hii inanipa mashaka na maswali mengi kama ifuatavyo:-

(i) Barabara hii inakwenda kujengwa wapi kwenye eneo la hifadhi ya barabara iliyopo sasa (road reserves) au itakwenda kununua maeneo yake mengine mapya kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo? Hapa tunaambiwa mchakato wa manunuzi uko hatua za mwisho, lakini mambo muhimu yanayohusu ardhi za wananchi hayawekwi wazi kwenye taarifa zote za Serikali kuhusu mradi huu.

(ii) Je, mkataba unaoingiwa hauzuii ukarabati, maendelezo au upanuzi wa barabara iliyopo? Kwani mara nyingi mikataba ya aina hii imekuwa ikiweka mazuio, hatuwezi leo kufanya maamuzi makubwa kiasi hiki ya kuzuia uendelezaji wa barabara zetu kwa manufaa makubwa ya kiuchumi ya wananchi na Taifa letu kwa ajili ya kumnufaisha mwekezaji.

(iii) Nani atakayekuwa mwamuzi wa gharama za matumizi ya barabara hizo Serikali au mwekezaji? Mikataba ya PPP ya aina hii hupelekea barabara za bure zinazotumiwa na wananchi kutelekezwa na pengine eneo ambalo lingetumika kufanya upanuzi kuchukuliwa na wawekezaji na hivyo kupelekea ulazima wa kila mmoja kupita kwenye barabara ya kulipia hali itakayosababisha ugumu wa maisha, gharama kubwa za usafiri na usafirishaji, double taxation na anguko kubwa la uchumi.

Mheshimiwa Spika, Serikali wakati wa kuhitimisha hoja yake ilete maelezo ya kina juu ya masharti ya mikataba ya PPP ya ujenzi wa barabara, usiri mkubwa ulioko sasa utatuletea matatizo makubwa, upanuzi wa barabara za njia nane Kibaha hadi Kimara umepunguza kwa kiasi kikubwa foleni na Serikali inaweza kuendelea na upanuzi huo polepole kupunguza msongamano uliopo sasa.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali iwasilishe Bungeni masharti yote ili yapate ridhaa ya Bunge kabla ya mkataba kusainiwa.

Kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi, ada, tozo na hatua nyingine za mapato; kila mwaka tunaanzisha, tunafuta na kupunguza kodi, tozo na ada mbalimbali lakini Serikali imekuwa haileti tathmini ya utekelezaji wa maamuzi hayo kabla ya kupendekeza maboresho ya mwaka wa fedha unaofuata hali hii inawaweka Wabunge na wananchi kutokujua kama malengo na madhumuni ya uamuzi huo yamefikiwa. Tujiulize katika maeneo ambayo tulipunguza kodi, tozo, ushuru na ada bei za bidhaa zilipungua? Mapato ya Serikali yaliongezeka? Hivi tujiulize haya maamuzi huwa tunayafanya kumnufaisha nani? Na kwa nini Serikali haitaki kuleta tathmini ya mabadiliko ya kodi yanayofanyika kila mwaka ili iwe msingi wa maamuzi ya mwaka unaofuata, kuna uwezekano eneo hili la mabadiliko ya kodi limeingiliwa na baadhi ya maamuzi yanafanywa kwa maslahi binafsi kwani ukipima huoni tija yake.

Mheshimiwa Spika, pia napongeza hatua ya Serikali kuondoa ada kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kupangiwa na Serikali kujiunga na vyuo vya ufundi, kuongeza kima cha usajili kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani kinachotakiwa kwa mfanyabiashara kusajiliwa kutoka shilingi milioni 100 hadi shilingi milioni 200, kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa kutumia pamba na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ninapendekeza kufanya marekebisho katika baadhi ya maeneo kama ifuatavyo:-

(i) Serikali inapendekeza kufuta adhabu ya asilimia 15 ya thamani ya bidhaa inayotozwa na Shirika la Viwango Tanzania kwa bidhaa zinazoingia nchini bila ya kuwa na Cheti cha Uthibitisho wa Ukaguzi wa Ubora (Certificate of Conformity - CoC). Aidha, bidhaa hizo zisizo na Cheti cha Uthibitisho wa Ubora zitafanyiwa ukaguzi wa ubora zinapofika nchini na kulipiwa gharama za ukaguzi pekee. Nchi yetu ilianzisha mfumo wa ukaguzi wa bidhaa kabla hazijasafirishwa kuja nchini (Pre-shipment Verification of Conformity-PVoC) ambapo baada ya ukaguzi huo hupewa cheti cha ubora (Certificate of Conformity-CoC), utaratibu huu ulianzishwa ili kuhakikisha kuwa kuna ubora wa bidhaa na usalama wa afya za watumiaji, kuhifadhi mazingira na kukataa Tanzania kugeuzwa kuwa dampo la bidhaa fake na bandia, au zilizokwisha muda wa matumizi.

Mheshimiwa Spika, uamuzi wa Waziri wa Fedha wa kuondoa faini ya asilimia 15 kwa bidhaa zinazoingizwa nchini bila cheti cha CoC inamaanisha kuwa amefuta utaratibu wa PVoC ambapo sehemu mbalimbali duniani TBS imeweka watoa huduma (service provider). Waziri wa Fedha amefanya utafiti wa kutosha wa kuwa na mbadala wa PVoC ili kuhakikisha nchi yetu haigeuzwi kuwa dampo la bidhaa zisizo na ubora, fake, bandia au zilizokwisha muda wa matumizi ambazo ni hatari kwa afya na maisha ya Watanzania, kuua ushindani, kuua ajira na uchumi wa Watanzania, lakini pia nchi yetu inaweza kuingia kwenye migogoro ya kimataifa kwa kushindwa kuzingatia viwango.

Mheshimiwa Spika, uamuzi huu ulifikiwaje na Serikali? Kitendo cha Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba kuondoa faini ya cheti cha CoC na kuondoa PVoC bila kujiridhisha na uwezo wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kivifaa, kirasilimali watu na fedha ni kitendo cha usaliti kwa nchi ambacho kitalingiza Taifa kwenye matatizo makubwa ya kugeuzwa kuwa dampo la bidhaa zisizo na ubora. Pendekezo hili lisikubaliwe na Bunge, lakini itafutwe namna bora itakayorahisha na kuondoa kero wanazopata wafanyabiashara kwa sasa kupitia utaratibu huu.

(ii) Waziri wa Fedha anapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220 kwa kuongeza Ushuru wa Barabara na Mafuta kwa kiasi cha shilingi 100 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli ambayo itaiwezesha Serikali kukusanya shilingi bilioni 381.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, bei za nishati ya mafuta bado ziko juu sana nchini na tozo nyingi zimewekwa na Serikali, pendekezo hili linakwenda kuongeza gharama za usafiri na usafirishaji, kupanda kwa bei za bidhaa na kuchochea mfumuko wa bei na ugumu wa maisha kwa wananchi masikini. Yapo maeneo mengi ya kukusanya kodi na kufidia eneo hili. Pendekezo hili lisikubaliwe na Bunge.

(iii) Waziri wa Fedha kupendekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha shilingi 20 kwa kila kilo moja ya saruji inayotoka nje ya nchi na inayozalishwa ndani ya nchi ili kuongeza mapato ya Serikali kwa shilingi bilioni 147.549. Vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji bei zake ziko juu hivyo kuweka ushuru wa bidhaa wa shilingi 20 kwa kilo ni kuongeza gharama za ujenzi kwa wananchi, mapato haya yanaweza kufidiwa katika maeneo mengine. Pendekezo hili lisikubaliwe na Bunge.

(iv) Waziri wa Fedha anapendekeza kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri kwa mwaka mmoja kwenye mabasi ya abiria yanayotambulika kwa HS Codes 8702.10.99 na HS Codes 8702.20.99 yanayoingizwa nchini kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka. Hatua hii inalenga kupunguza gharama za uingizaji wa mabasi hayo ili kurahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi. Pendekezo hili linapunguza mapato ya Serikali bila sababu za msingi hivyo lisikubaliwe na Bunge.

(v) Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za Marekani 500 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho (refined), hatua hizi kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 1.258. Pendekezo la kushusha Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 hadi asilimia 25 linaondoa ulinzi wa viwanda na kuua bei na soko la wazalishaji wa ndani wa mazao ya mbegu ikiwemo alizeti, Bunge lisikubali pendekezo hili. Uchambuzi zaidi kwenye eneo hili utafanyika kipindi cha kuujadili na kupitisha Finance Bill.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuadimika kwa dola za Marekani; taarifa ya Waziri na ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeeleza sababu za kuadimika kwa dola za Marekani na hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali, lakini wananchi na wafanyabishara wanalalamika juu ya kuadimika kwa dola za Marekani, kupanda kwa viwango vya kubadilisha fedha za kigeni na kusababisha kushindwa kuhudumia mahitaji ya malipo ya uagizaji bidhaa nje ya nchi. Pamoja na sababu zilizotajwa lakini sababu kubwa ya kuadimika kwa dola za Marekani inalotokana na kukosekana kwa mifumo imara ya udhibiti na usimamizi hafifu wa Sera za Fedha na Bajeti (Fiscal and Monetary Policy) ambapo kumesababisha mahitaji na matumizi makubwa ya dola za Marekani nchini kama ifuatavyo:-

(i) Hakuna mkakati madhubuti uliowekwa na Serikali wa kuzuia uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi zinazozalishwa nchini hali inayosababisha uhitaji na matumizi ya dola pasipo na sababu za msingi. Mfano kuruhusu biashara holela ya kuuza na kuingiza mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi nje nchi. Pia bidhaa za misitu na kadhalika, ununuzi wa chanjo za mifugo nje ya nchi wakati nchi yetu ina kiwanda kinachozalisha chanjo cha Hester Biosciences Africa Limited na Kiwanda cha TVI Kibaha na kuagiza dawa za kuogesha mifugo nje ya nchi wakati ndani ya nchi tuna kiwanda cha Farm Base Ltd.

(ii) Serikali kuajiri wazabuni na wakandarasi kutoka nje ya nchi hata kwa miradi ambayo ingeweza kutekelezwa na Watanzania ambapo hulazimika kulipa dola za Marekani badala ya shilingi ya Tanzania. Mfano ukarabati wa Kivuko cha Mv Magogoni (shilingi bilioni 7.5), Mkataba wa Tech Mahindra na TANESCO (shilingi bilioni 70) kujenga mfumo wa TEHAMA, ujenzi wa barabara ya bypass huko Maswa (shilingi bilioni 12) na miradi mingine mingi ya barabara, umeme, TEHAMA, maji, madaraja na kadhalika.

(iii) Kukosekana kwa mikakati thabiti ya kudhibiti soko haramu la kubadilisha fedha za kigeni ambapo kumepelekea soko kubwa lisilo rasmi la kubadilisha fedha za kigeni nchini (black-market).

(iv) Utoroshaji wa fedha nyingi za kigeni kwenda nje ya nchi na utakasishaji wa fedha haramu hali inayopelekea matumizi na mahitaji makubwa ya dola nchini. Taarifa FIU ya kuishia Aprili, 2023 inaonesha taarifa shuku za fedha taslimu zenye thamani ya shilingi trilioni 56.65 na usafirishaji fedha kwa njia ya kielektroniki zenye thamani ya shilingi trilioni 222.81 ikijumuisha usafirishaji wa fedha taslimu na hati za malipo kupitia mipakani. Hii ni ishara kuwa kuna ukwepaji mkubwa wa kodi na utoroshaji wa fedha nje ya nchi. Hotuba ya Waziri wa Fedha haina suluhisho juu ya changamoto hizi, ninashauri Serikali kupitia bajeti hii iimarishe mifumo ya udhibiti na uzingatiaji wa sera za fedha na bajeti ili kuimarisha hali ya uchumi na upatikanaji wa dola nchini.

Mheshimiwa Spika, kuhusu usimamizi wa fedha za umma; usimamizi dhaifu wa fedha za umma ni kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa bajeti nchini, mamlaka za ukaguzi na uchunguzi za CAG, PPRA, FIU na PCCB na Mbio za Mwenge zimekuwa zikitoa taarifa za ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma hali inayoonesha kuwa hatuko vizuri katika usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma. Maeneo ambayo yanaripotiwa ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi, matumizi nje ya bajeti, ukopaji holela wa mikopo, matumizi yasiyo na vielelezo, kushindwa kukusanya mapato ya Serikali bila sababu za msingi na wizi na ubadhirifu wa fedha za umma. Mfano Wizara ya Kilimo ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 150 kwa ajili ya ununuzi wa mbolea ya ruzuku, lakini hadi kufikia Aprili, 2023 ilikuwa imetumia kiasi cha shilingi bilioni 218 zaidi ya shilingi bilioni 68 ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge. Lakini pia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na TRC kufanya manunuzi kwa kuacha bei ya ushindani na kutumia single source na kuisababishia hasara Serikali ya takribani shilingi trilioni nne.

Mheshimiwa Spika, licha ya matukio hayo ya ubadhirifu, wizi na ufisadi wa fedha za umma, hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa na badala yake wahusika kuendelea kuwa katika Ofisi za Serikali na wakiendelea kutumia nguvu kubwa kila leo kujisafisha mbele ya umma. Utekelezaji wa mapendekezo na maazimio ya Bunge kuhusu hoja za CAG nao umekuwa wa kusuasua ambapo hadi sasa taarifa ya utekelezaji ya hoja za mwaka 2020/2021 na mwaka 2021/2022 hazijawasilishwa. Mamlaka za kuchukua hatua zote zimekaa kimya juu ya ripoti ya CAG na zingine kurushiana mpira mfano Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba kupitia hotuba yake Ibara ya 63 anazilaumu mamlaka zingine kwa kujidogosha na kushindwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya watuhumiwa wa ubadhirifu na ufisadi wa fedha za umma. Haya ni maneno mazuri kutoka kwa Waziri kuona Mamlaka za DCI, TAKUKURU na DPP hazichukui hatua ingawa yeye binafsi akiwa mhusika mkuu hajaeleza amechukua hatua gani?

Aidha, awali wakati nikichangia Bungeni hotuba ya Waziri Mkuu nilieleza kuwa kwenye uchambuzi wangu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 nilibaini ubadhirifu wa zaidi ya trilioni 30 lakini hadi leo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa dhidi ya hatua zilizochukuliwa kwa wahusika. Lakini pia jambo lingine la kushangaza zaidi CAG ameshindwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 47(3) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008 (The Public Audit Act) kuwafikisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) watuhumiwa aliojiridhisha pasipo mashaka kuhusika na ubadhirifu na ufisadi wa fedha za umma kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani.

Kuhusu mikataba; (i) kwa nini Serikali inaendelea kuingia mikataba ya raslimali za Taifa kwa usiri mkubwa kinyume cha Sheria ya The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act, 2015 na Sheria ya The Natural Wealth and permanent Sovereignty Act No. 5 ya mwaka 2017 ambazo zinataka kuweka uwazi wa masharti ya mikataba kwenye hatua za awali na kupata kibali cha Bunge. Mfano Mkataba wa LNG, Mkataba wa IGA wa Bandari na Mkataba wa Mradi wa barabara wa PPP.

(ii) Je, kwa nini jedwali la mikataba yenye thamani ya trilioni 91 iliyofanyiwa upekuzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali halijawasilishwa ili lisomwe pamoja na Mpango wa Maendeleo na hotuba ya Bajeti ya Serikali?

Waheshimiwa Wabunge, eneo hili tusipoliangalia vizuri Serikali inaweza kuingia kwenye mikataba ambayo hatujakubaliana, haimo kwenye bajeti wala kwenye Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano. Pia Serikali inaweza kuingia kwenye mikataba ambayo nchi haina uwezo wa kiuchumi kuihudumia.

Mheshimiwa Spika, kuhusu sekta binafsi; (i) kuimarisha sekta za uzalishaji bidhaa za kuuza nje ya nchi ambapo Mfuko wa Dhamana kwa Wakopaji Wanaozalisha Bidhaa za Kuuza Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme - ECGS) na Mfuko wa Dhamana wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (Small and Medium Entreprises Credit Guarantee Scheme - SMECGS) kutengewa zaidi ya shilingi bilioni 600. Hii ni hatua nzuri na ya kupongezwa ingawa fedha zilizotengwa kwenye eneo husika ni kidogo na haziwezi kukidhi mahitaji, lakini pia lazima kujipanga na usimamizi wa fedha hizi ili ziwafikie walengwa na kuleta tija iliyokusudiwa, kwani uzoefu uliopo fedha za aina hii hutumika vibaya. Mfano mabilioni ya JK, fedha za kufidia hasara iliyosababishwa na mtikisiko wa uchumi duniani (financial crisis), na asilimia 10 ya Halmashauri kwa ajili ya makundi maalum.

(ii) Utoaji wa mikopo, riba na dhamana katika mabenki; viwango vya riba vimepungua kwa kasi ndogo kutoka asilimia 16.31 Aprili, 2022 hadi kufikia asilimia 15.91 Aprili, 2023 hali inayopelekea gharama za biashara na uwekezaji kuendelea kuwa juu ingawa hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) zinatia matumaini. Niipongeze Benki ya CRDB, NMB, TIB, TCB, AZANIA, TADB, BOA, PASS na kadhalika kwa namna zinavyoendelea kutoa mikopo nchini na kuwezesha upatikanaji wa mitaji na fedha za uwekezaji. Serikali ichukue hatua zaidi za kushusha viwango vya riba ili kupunguza gharama za biashara na uwekezaji na ugumu wa maisha, pia kuwezesha Watanzania kupata dhamana ya mikopo mikubwa ili waweze kushiriki katika zabuni na kandarasi kubwa za barabara, umeme, maji na kadhalika.

(iii) Malimbikizo ya VAT refunds imekuwa ni tatizo linalolamikiwa na walipa kodi wengi nchini hali inayosababisha kuua mitaji, ajira na kudhoofisha biashara na uwekezaji nchini. Kufikia Machi, 2023 Serikali ilikuwa imelipa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 836 hii ni hatua nzuri na ya kupongeza ingawa Waziri hajaeleza ni malimbikizo ya shilingi ngapi ya VAT refunds yanadaiwa na walipa kodi nchini. Nini mkakati wa Serikali kupitia bajeti hii wa kumaliza tatizo la madai ya marejesho ya kodi?

(iv) Malimbikizo ya madeni makubwa ya wakandarasi na wazabuni; eneo hili limekuwa na malalamiko ya muda mrefu hali inayosababisha kuua ajira, mitaji, kufisilika na wengine kupoteza maisha. Kufikia Aprili, 2023 Serikali ilikuwa imelipa kiasi cha shilingi trilioni 1.2 hii ni hatua nzuri ingawa Waziri hajaeleza hadi sasa Serikali inadaiwa madeni ya kiasi gani? Nini mkakati wa Serikali kupitia bajeti hii wa kumaliza tatizo hili la madeni ya muda mrefu? Kulimbikiza madeni ni kinyume cha kifungu cha 52(1) cha Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 pamoja na Waraka Namba 4 wa Mlipaji Mkuu wa Serikali wenye Kumb. CBA187/355/01/15 wa tarehe 31 Disemba, 2014.

Mheshimiwa Spika, taarifa ya kuishia tarehe 30 Juni, 2022 inaonesha madeni ya wazabuni na wakandarasi ya muda mrefu yalifikia trilioni 3.4. Ucheleweshaji wa malipo na uhakiki wa madeni usio na mwisho umekuwa ukikera sana wananchi huku upande wa wazabuni na wakandarasi wa kutoka nje ya nchi wakilipwa kwa wakati na hata wakicheleweshewa malipo yao wanalipwa pamoja na faini. Mwaka wa fedha 2021/2022 malipo ya tozo za riba ya ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi, wazabuni, bima na mifuko ya hifadhi ya jamii bila sababu za msingi ilikuwa shilingi bilioni 418.5. Nini kinachosababisha malimbikizo ya madeni hayo wakati fedha zimeidhinishwa katika mwaka husika?

(v) Katakata ya umeme na migao isiyoisha ya umeme imekuwa kikwazo kikubwa cha biashara na uwekezaji nchini pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika sekta ya nishati na kuongeza uzalishaji wa umeme katika Gridi ya Taifa bado tatizo la mgao wa umeme ni kubwa na linaathiri uzalishaji. Majibu yanayotolewa na Wizara ya Nishati yanakinzana na hayana ukweli, lakini pia Vituo vya Miito ya Simu (Unified Call Centre) kuunganishwa na kuendeshwa na kampuni binafsi umeshusha viwango vya utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Spika, hitimisho; bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha haitoi suluhisho la tatizo la mfumuko wa bei na ugumu wa maisha unaowakabili wananchi kwa sasa, udhibiti hafifu wa viwango vya riba na viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni. Bajeti imeshindwa kuimarisha mifumo ya usimamizi na udhibiti hali itakayopelekea kuimarika kwa biashara za magendo, biashara haramu na utoroshaji wa raslimali za taifa nje ya nchi. Bajeti haina mkakati madhubuti wa kudhibiti upotevu wa mapato na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma, lakini pia bajeti hii haitoi ulinzi wa ajira za Watanzania, viwanda na wawekezaji wa ndani. Hivyo bajeti hii kama itapita kama ilivyowasilishwa pamoja na Finance Bill italisababishia Taifa matatizo makubwa. Bajeti hii sio pro-poor budget.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi ambayo umenipa ili niweze kuchangia hizi hotuba mbili, Hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya PAC pamoja na Hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti. Kwa ujumla wenyeviti wote hawa wawili wametoa hotuba nzuri sana hapa Bungeni, na kwa kweli tunawapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nizungumzie Mashirika ya Umma ambayo Mwenyekiti pamoja na Kamati nzima ni vizuri kwenda kuisimamia Serikali kule ili kuhakikisha kwamba TR anajengewa uwezo mkubwa wa kifedha na rasilimali watu ili aweze kuyasimamia mashirika haya kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni kwamba hapa tunazungumzia mapato ya Serikali. Kwenye taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ukurasa wa 31 ameeleza performance ya ukusanyaji wetu wa mapato. Pale kwenye mapato yasiyo ya kodi tuna asilimia 36 tu, yaani hadi mwezi wa 12 tuna asilimia 36; kwa hiyo ni likely kwamba hatuwezi kufikia asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliomba tuletewe jedwali la wizara na taasisi zote zinazohusika na ukusanyaji ili tujue ni nani ambaye hakusanyi vizuri na sababu zake. Kwa bahati mbaya sana mpaka tunawasilisha hotuba hii hatukuweza kuletewa jedwali hilo. Lakini bado tunasisitiza kwamba jedwali la wakusanyaji wote wa kodi liletwe tulione na tuone ni nani ambaye anashindwa kukusanya mapato ya Serikali sawasawa, kwa sababu pale nyuma walikuwa wanasingizia Corona haipo, sasa kwa nini wameshindwa kukusanya mapato kama ilivyotakiwa kwenye Bajeti ya Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ninalotaka kulizungumzia, wengi wamezungia ajira za Watanzania hapa. Ni ukweli usiopingika kabisa kwamba tusipojipanga vizuri kuhakikisa kwamba tunalinda ajira za Watanzania, na Watanzania hawa milioni 60 wasiposhiriki kikamilifu katika uchumi wao hatuwezi kupata maendeleo, hata tungefanyaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo hujuma nyingi zinazofanywa, nyingine zinafanywa hata na Serikali yenyewe. Kwa mfano kwenye manunuzi, inakuwaje mpaka leo hii Serikali inaenda kununua bidhaa na huduma nje ya nchi ilhali ina viwanda hapa nchini ambavyo vinazalisha bidhaa hiyo? Mfano sasa hivi Serikali imeanza kununua dawa za kuogesha mifugo katika bajeti ya mwaka 2021/2022, wameanza kununa dawa za kuogesha mifugo kwa wazabuni wanaoingiza kutoka nje ya nchi ili hali hapa nchini tuna kiwanda kinachozalisha dawa nyingi za kutosha kuhudumia mifugo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, bado hadi leo hii Wizara ya Ujenzi inaajiri mkandarasi na mshauri mwelekezi kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kujenga barabara ya kilometa 11 za lami; ili hali kuna Watanzania wenye uwezo wa kujenga mradi huo na wana weledi wa kutekeleza mradi huo. hivi ni kwa nini tufikie hapo? Haya yote yamefanyika na Bunge hili lipo na Serikali ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni hili ambalo tumelizungumza sana, nalo hili ni sababu kubwa ya kukosesha Watanzania ajira, katakata ya umeme. Katakata ya umeme imeelezwa kwenye Bunge lako, na jana ilizungumzwa na Bunge lako Kamati husika ilipowasilisha, na majibu ya Serikali yaliyotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kushauri hapa, kwa majibu yaaliyotolewa na Serikali na taarifa ya Kamati ya Nishati iliyowasilishwa, na majibu yaliyotolewa zamani na Serikali kwenye Bunge hili, ninaomba jambo hili tulifikishe mwisho. Tulishawahi kuyafikisha mwisho mambo mengi magumu. Tuliwahi ufikisha Richmond, ESCROW; na hili kwa majibu ya mkanganyiko yanayotolewa na Serikali kuhusu katakata ya umeme na kuwasababishia Watanzania kuingia kwenye dhiki kubwa, viwanda vnafungwa, uzalishaji unashuka na inaleta mfumuko mkubwa wa bei…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Ningependa kumpa taarifa mzungumzaji kuhusiana na suala la katakata ya umeme. Nimpe taarifa tu kwamba Mheshimiwa ukiendelea kuliongelea suala hili na wewe utaambiwa kama nillivyojibiwa mimi, kwamba sikupenda Mama Samia awe Rais au yeye awe Waziri. Ni hiyo tu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mpina hiyo si taarifa, endelea.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan asiingizwe katika mambo haya, Rais wetu asiingizwe katika udhaifu wa utendaji wa baadhi ya Mawaziri, wamuache Rais wetu afanye kazi nzuri ya Watanzania. Udhaifu wa Waziri autetee mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuyasema haya, kwanini nataka tume teule ya Bunge iundwe? Kuchunguza suala hili la katika katika ya umeme na kuchelewa kwa mradi wa Mwalimu Nyerere, ziko sababu!

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 mapato ya TANESCO yalikuwa bilioni 72, tulisimamia yakapanda mpaka yakafikia bilioni 160 kwa mwezi, na sasa imewasilishwa mwaka 2021 mapato ya TANESCO yamefika trilioni 2.4. sababu za kushindwa kufanya ukarabati na matengenezo zinatoka wapi? Hawa hawa TANESCO walikuwa na madeni sugu yaliyofikia bilioni 272, yakasimamiwa yakapungua mpaka yakawa bilioni 49, sababu ya kushindwa kufanya matengenezo yanatoka wapi? TANESCO hawa wameweza kufanya kazi nzuri mpaka tukazima mitambo ya mafuta ya IPTL, AGRECO na Symbion ambayo yalikuwa yanagharimu bilioni 719 kwa mwaka; na sasa gharama hizo wameziokoa, sababu za kushindwa kufanya ukarabati wa mitambo inatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ilikuwa inafanyiwa ukarabati, tulikamilisha miradi mipya kutoka mwaka 2015 mpaka 2020, tumekamilisha miradi mipya iliyokuwa haijakamilishwa, tukaweza kupanua njia na kusafisha njia za usafirishaji wa umeme na mpaka tukasababisha vijiji ambavyo vilikuwa na umeme kutoka 2018 mpaka 10,312. Upanuzi huo wote umefanyika. Leo hii TANESCO sababu za katakata ya umeme zinatoka wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Bunge lako liambiwe ukweli, na kama miaka mitano, kama inavyozungumzwa, ni kama miaka sita kama inavyozungumzwa, kwamba ukarabati ulikuwa haufanyiki, kwa nini sasa umeme ulikuwa haukatiki? Kwa nini umeme ukatike leo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Watanzania waambiwe ukweli, majibu ya bla bla katika jambo hili hatuwezi kukubali katika Bunge hili. Ukikosa umeme kwenye Taifa; Mheshimiwa Rais wetu leo hii anahangaika sana kutafuta wawekezaji ndani na nje ya nchi, utamleta mwekezaji wa nani anayeambiwa kwamba Taifa halitakuwa na umeme mpaka uwe na trilioni mbili. Ina maana kwamba tusipopata umeme hauwezi kuwaka?...

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. LUHAGA J. MPINA: … na utaendelea kukatakata…

NAIBU SPIKA: Ahsante!

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili lisikubali, na tume teule ya Bunge iundwe, ichunguze jambo hili pamoja na lile…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 2) Act, 2022
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii uliyonipa nami niweze kuchangia kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya Mwaka 2022 ambayo inakwenda kufanya marekebisho ya Sheria Nne; Sheria ya Kuzuia Usafirishaji wa Binadamu Sura ya 432, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, Sheria ya Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura ya 398.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia hasa kwenye Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95. Jambo la kwanza kabisa nitumie nafasi hii kuipongeza sana hii Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kazi nzuri sana wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, tatizo la dawa za kulevya hapa nchini lilikuwa kubwa sana. Kabla hizi hatua madhubuti hazijaanza kuchukuliwa, tatizo hili lilikuwa ni kubwa, vijana wetu walipata matatizo makubwa, uingizaji wa dawa za kulevya kutoka nje ya nchi ulikuwa mkubwa, usambazaji wa dawa za kulevya ndani ya nchi ulikuwa mkubwa, matumizi ya dawa za kulevya ndani ya nchi ulikuwa mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mamlaka yetu hii imefanya kazi nzuri sana mpaka leo hii tumeingia kwenye rekodi ya dunia kati ya nchi ambazo zinapambana na dawa za kulevya kikamilifu. Hii ni hatua kubwa sana katika Taifa. Kwa hiyo, mpaka sasa hivi, pamoja na marekebisho haya yanayoletwa lakini ukweli ni kwamba tumepiga hatua kubwa na tumedhibiti kwa kiwango kikubwa suala la dawa za kulevya hapa nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, nikienda ile Ibara ya 13 katika Kifungu Kipya cha 32(4) na Kifungu Kipya cha 32(5) ambapo yanawekwa masharti ya kuanzisha mahabusu, mamlaka iwe na mahabusu zake lakini pia iwe na uwezo wa kuweka watuhumiwa kizuizini. Jambo hili ni muhimu sana likafanyika kwa umakini mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, moja, ulazima huu wa mamlaka kuwa na mahabusu zake, mimi sina tatizo na marekebisho mengine, wakamate, wachunguze, wafanye nini, sina tatizo, lakini unapotaka kuanzisha mahabusu zako, kwa ajili ya nini? Yaani ule ulazima wa kuanzisha mahabusu zako ni kwa ajili ya nini? Kwa sababu kama kuna kitu special tunakitaka kwenye mahabusu zilizopo sasa hivi ambazo zipo chini ya Polisi, mahabusu ambazo zipo sasa hivi chini ya magereza, tuna uwezo wa kufanya marekebisho zika-accommodate yale mahitaji ya mamlaka badala ya kujenga mahabusu nyingine.

Mheshimiwa Spika, suala hili la kutunza mahabusu limekabidhiwa Jeshi la Polisi, wamekabidhiwa Jeshi la Magereza, leo tena tunataka kuwakabidhi na watu wa Mamlaka na wenyewe wawe na jukumu tena la kutunza mahabusu. Na hawa mahabusu na wenyewe wanao utaratibu wake wa namna ya kuwekwa, wa namna ya kutunzwa. Sasa kama kila mtu atakuwa na jukumu la kutunza mahabusu itakuaje?

Mheshimiwa Spika, pia tunaweza kuingia kwenye mkanganyiko mkubwa hata namna ya kushughulika na hizi kesi, kwa maana ya DPP, DCI na Mahakama zenyewe, na maana ya ushahidi huo tunaouzungumza, na hata namna ya upelelezi tunaokwenda kuufanya, kama hawa tunakwenda kuwapa jukumu tena la kukaa na mahabusu badala ya kwenda kupeleka kwenye taasisi ambazo zilishapewa jukumu hilo kulifanya.

Mheshimiwa Spika, pia kuna abuses nyingi msimamizi anapopewa jukumu la kukaa na mtuhumiwa, abuse hiyo inaweza kufanyika kwa sababu checks and balances zitakosekana. Wako watu hapa watakwenda kushinikizwa, hata kulazimishwa kukiri, kwa sababu ni huyu msimamizi ndiye anayesimamia na ushahidi huu tunao.

Mheshimiwa Spika, zipo mamlaka ambazo tulizipa jukumu la kutunza tu vielelezo au ushahidi mahakamani, mfano ni TAWA, tuliwapa jukumu hapa la kutunza vielelezo, kutunza ushahidi Mahakamani, wakakaa na mifugo ya wafugaji, mifugo hao wote walikufa mikononi mwao kwa kutelekezwa bila kupewa dawa au malisho. Tatizo la msimamizi anapopewa atakapofanya abuse nani atamsimamia? Italeta changamoto kubwa.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2009 kama sikosei, wakati tunatunga Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009, kikawekwa Kifungu kile kinachomruhusu Afisa wa Wanyamapori kum-shoot raia yeyote anayepatikana kwenye eneo lililohifadhiwa, akiwa hata anakimbia kukamatwa, wakaruhusiwa kukamata. Ikapita hapa tukaambiwa haitakuwa hivyo, tumekwenda kwenye utekelezaji wananchi wengi wameuawa kwa kupigwa risasi. Tumekwenda kwenye utekelezaji wanyama wengi wameuawa, mifugo wameuawa kwa kupigwa risasi, abuse iliyopitiliza.

Mheshimiwa Spika, leo hili Bunge lako linataka tena kupelekwa kwenye sheria hizi, linataka kupelekwa kwenye sheria za aina hiyo, iende ikafanyike tena abuse hii. Watu wakamatwe unasingiziwa, unatajwa Mpina wewe unahusika na dawa za kulevya, unakwenda kushinikizwa kule unapigwa unalazimishwa usaini mahali. Abuse hiyo nani anakwenda kuisimamia? Na kwa nini kama Taifa tutunge sheria za namna hiyo?

Mheshimiwa Spika, lakini kama hiyo haitoshi, tunazo taasisi ngapi zinazohusika na usimamizi. Leo hii TAWA nao watakuja wanashughulika na majangili na majangili na yenyewe ni kesi za kupangwa zinahusisha watu wengi, na wenyewe waanzishe mahabusu zao. PCCB wanakamata watu wengi wa makosa mbalimbali na yenyewe yana mtandao mrefu sana kama rushwa, ufisadi na mambo mengine, na wenyewe waje watuombe hapa wanahitaji wajenge mahabusu.

Mheshimiwa Spika, pia tunao Uhamiaji, wana-deal na biashara mbaya sana ya binadamu, biashara haramu. Hawa nao watuombe tujenge mahabusu itakuaje? Wizara ya Uvuvi wanaohusika na mambo ya uvuvi haramu na wenyewe waje watuombe wakajenge mahabusu ya wavuvi haramu. Nchi hii patajengwa mahabusu kila sehemu. Itakuwa ni nchi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama leo Bunge linaikubalia Mamlaka ya Dawa za Kulevya kujenga mahabusu, mamlaka nyingine zikija kutuomba tutafanya nini? Kwa hiyo nchi hii itajengwa mahabusu kila sehemu, kila mtu atakuwa mtunzaji wa mahabusu, hatuwezi kupiga hatua kwa utaratibu huo.

Mheshimiwa Spika, jambo la nne ni suala la rasilimali fedha. Mpaka leo hii hatujakamilisha kujenga Magereza kila Wilaya. Kuna baadhi ya Wilaya wanabeba mahabusu kupeleka Wilaya nyingine. Mpaka leo hii kuna Wilaya ambazo mahabusu wanabebwa na kupelekwa Magereza za Wilaya jirani.

Mheshimiwa Spika, leo hii tunataka kwenda kuli-commit Taifa likajenge mahabusu za Mamlaka za Dawa za Kulevya ambazo sijui zitajengwa na zenyewe kila Wilaya? ambazo na zenyewe sijui zinakwenda kujengwa kila Mkoa hizo mahabusu? Kama leo hii tumeshindwa kukamilisha ujenzi wa Magereza kila Wilaya, fedha za ujenzi huu wa mahabusu wa Mamlaka ya Dawa za Kulevya zinatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna changamoto kubwa ya kupata fedha za kujenga hizo mahabusu lakini kama fedha hiyo ndogo tunayo, kwa nini tusiende kufanya ukarabati wa zile mahabusu zilizopo Magereza na zile zilizopo Polisi na hata kama tunataka kufanya marekebisho madogo…

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mpina kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa George Simbachawene.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi, lakini pia nimpongeze mchangiaji kwa maelezo anayoendelea kuyatoa na mawazo yake hayo. Hata hivyo, nataka nimpe taarifa tu kwamba mahabusu wa madawa ya kulevya ni tofauti kabisa na mahabusu wengine. Dawa za kulevya zinasafirishwa kwa njia nyingi sana, binadamu ana maarifa makubwa; lakini iko sayansi ya usafirishaji wa madawa ya kulevya ambayo unaweza ukute akayameza ndani ya tumbo na yakatakiwa kukaa kwenye tumbo lake mpaka baada ya muda fulani; katika mazingira hayo ndiyo maana chombo hiki kinakuja na mawazo kwamba tupate muda wa kukaa na huyu mtu katika maeneo mahsusi, kusubiria endapo kitatokea nini katika kuthibitisha kama anayo kweli tumboni au lah!

Mheshimiwa Spika, katika kufanya hivyo kuna facility maalum, kuna dawa maalum anazotakiwa kutumia na kuna utaalam maalum. Hayo mambo hayawezi kufanyika kwenye Vituo vyetu vya Polisi. Ndiyo maana Serikali inakuja na mawazo hayo baada ya research na changamoto kubwa. Ninayeongea hapa nilikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, najua yanayotokea. Kwa hiyo, kama tutakaa hapa kama Serikali tunatetea wasafirishaji wa madawa ya kulevya; nadhani basi hili Taifa linaingia kwenye matatizo. Kwa hiyo nataka kutoa taarifa tu kwamba, hizi ni special crimes lazima ziwe tackled kwa special means. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Luhaga Mpina, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, kwanza hiyo taarifa yake siipokei na yeye kama Waziri alikuwa na nafasi ya kuja kuchangia, angezungumza hayo anayoyasema na Serikali wajipange vizuri kusikiliza Wabunge wanasema nini.

Mheshimiwa Spika, narudia kusema, unaposema kwamba, Polisi hawawezi ku-handle haya mambo, leo hii tumepambana na madawa ya kulevya kwa muda gani? Hatua hizi tulizofikia tumezifikiaje leo, kama leo Polisi wanazungumzwa hawawezi ku-handle mtuhumiwa wa dawa za kulevya; na kama leo mamlaka ya Polisi inaonekana kwamba haina uwezo wa ku-handle watuhumiwa wa madawa ya kulevya. Kama unataka special facilities hizo special facilities kwa sababu fedha yote ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; hizo facilities haziwezi kujengwa polisi? hizo facilities haziwezi kujengwa magereza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri sana kuelewa hata tunachokizungumza na hawa watuhumiwa wa dawa za kulevya wanakamatwa leo kila sehemu ya nchi. Unakwenda kujenga leo wilaya nzima unakwenda kujenga mahabusu kila wilaya unazo hizo fedha? Kama zipo hizo fedha nimesema mpaka leo hii tunazo wilaya zetu hazina magereza, hizo fedha mbona hazikupatikana leo hii zimepatikana kutoka wapi?

SPIKA: Dakika moja malizia Mheshimiwa, kengele imeshagonga, dakika moja malizia.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, naomba nihitimishe kwa kusema yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, kifungu hiki cha Ibara hii ya 35 hasa kwenye kifungu cha 32(4) na 32(5) kifutwe. Kifungu hiki kifutwe na badala yake uwekwe utaratibu mzuri ambao utawezesha changamoto walizonazo hivi sasa mamlaka…

T A A R I F A

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mpina katika hiyo dakika yako moja ya kumalizia naona kuna Mheshimiwa Mbunge amesimama anataka kukupa taarifa.

Mheshimiwa Emanuel Mwakasaka.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, naomba unilindie muda wangu.

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Unajua Mheshimiwa Mpina ni shemeji yangu, sasa naomba nimpe taarifa, bahati mbaya hajashiriki kwenye Kamati yetu ya Katiba na Sheria ambayo yeye ni Mjumbe, tulishafanya mjadala wa kutosha kama Kamati kupitia hicho kifungu ambacho anataka kifutwe. Kwa hiyo, nampa taarifa kwamba angekuwepo kwenye Kamati pengine angeona uzito kwa nini hicho kifungu hatukukifuta. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mpina, unapokea taarifa hiyo?

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, kwanza sikubaliani na taarifa yake, Bunge ni Bunge, Kamati ni Kamati; na mimi Mjumbe wa Kamati nimeshiriki vikao vyote na haya maelezo yalitolewa mbele yangu na niliyakataa na hapa kwenye Bunge lako nayakataa na naliomba Bunge lako likubaliane hiki kifungu kiondolewe.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2023/2024 pamoja na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeze Serikali kwa hatua iliyofikia katika ujenzi wa Bwawa la Kidunda ambapo sasa wamepata Mkandarasi sasa tunaenda kupata majawabu ya tatizo la maji katika Mkoa wa Pwani, Morogoro pamoja na Dar es Salaam, lakini wahakikishe kwamba ule mradi wa Ziwa Viktoria kwa Mkoa wa Simiyu ambao karibia Wilaya zote za Busega, Bariadi, Itilima, Maswa, Meatu zote zinahusika na huu mradi na wananchi wanausubiri kwa hamu. Wananchi wa Jimbo langu la Kisesa wanausubiri kwa hamu sana mradi huu kumaliza tatizo la maji ya kunywa, maji ya mifugo, maji ya kilimo na maji ya shughuli mbalimbali zingine za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la scheme za umwagiliaji, Wizara inayohusika isisahau kwamba hata huko Simiyu na hata huko Kisesa kuna maeneo mazuri tu kwa ajili ya shughuli za kilimo cha umwagiliaji, hata pamba inawezekana kufanyiwa scheme za umwagiliaji.

Mheshimiwa mwenyekiti, ili tuweze kuwa na mipango mizuri na tuweze kupiga hatua za maendeleo, tunahitaji sana uwekezaji mkubwa kwenye eneo la utafiti. Tunatakiwa tupeleke fedha nyingi COSTECH, TARI, TAFIRI na TAWIRI ili tuweze kupata majawabu ya maendeleo yetu kwa wakati. Mpango huu pia usisahau kutenga fedha za daraja la Mwamhuge kule Jimboni kwangu mpakani mwa Meatu na Maswa ni daraja la muda mrefu na limeahidiwa na Serikali pia daraja la Mto Sanjo ambao ni mpakani mwa Itilima na Meatu, hilo ni daraja la muda mrefu sana kwa hiyo Wizara inayohusika itenge fedha kwa ajili ya hilo daraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna daraja la Mwambuzo mpakani mwa Meatu na Igunga na Kishapu, hili daraja nalo litengewe fedha ili kuweza kupiga hatua za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na wenzangu wamezungumza hapa, Serikali imepiga hatua kubwa sana katika kutafuta masoko ya mazao yetu na huu ndiyo uelekeo tunaoutaka. Mazao ya korosho, parachichi, pamba na mpunga. Kwa kweli katika hili eneo, ninaishukuru sana Serikali kwa sababu wananchi wetu watakapofanya uzalishaji kwa wingi wanapata soko la uhakika. Hili tunaendelea kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuifungua nchi yetu na kutafuta masoko makubwa Tanzania, kuitafutia nchi yetu masoko makubwa ili kuiunganisha na dunia ili wakulima wetu waweze kulima na kuuza, waweze kuzalisha na kuuza mazao ya samaki, mabondo, tumeona mikataba ya mazao ya mabondo, tumeona mikataba ya samaki na mikataba mingine ambayo ni makubaliano ya masoko mapya. Hiyo ni hatua kubwa sana kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Mpango umezungumza na Kamati imezungumza. Hapa kwenye Bunge lako nilipendekeza kwamba iundwe Kamati Teule ya Bunge ili kufuatilia ukweli juu ya jambo hili, kwa sababu mara nyingi tumekuwa tukiletewa taarifa ambazo zina mkanganyiko. Leo hii Kamati ya Bajeti imeenda kuthibitisha hilo kwamba taarifa zenye mkanganyiko zimewasilishwa. Mpaka sasa hivi mkataba baina ya TANESCO na Arab Contractors haujulikani kwamba huo muda uliyoongezwa ni muda gani. TANESCO wanasema ni mwaka mmoja (miezi 12) wameongeza. Maana yake kufukia Tarehe 15, Juni 2023 mradi huu utamalizika lakini Contractor pamoja na Wizara na hapa Bungeni tumeambiwa huu mradi utaisha Julai mwaka 2024, miaka miwili kwa maana ya miezi 24, sasa Bunge lako lishike taarifa gani ya kufanyia kazi juu ya hili jambo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeeleza kwamba, mkataba huu umeongezwa bila sababu za msingi, mkataba wa Bwawa la Mwalimu Nyerere baina ya Contractor umeongezwa bila sababu za msingi na bila kufanya tathmini, bila kubaini gharama za ongezeko pia gharama hizo za ongezeko la muda zitabebwa na nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiyauliza haya lakini mara inaelezwa kwamba wako kwenye mvutano, hivi wanavutana jambo gani? Mradi umeshafikia asilimia 75 mnavutana nini? Ni hatari sana kwa mradi uliofikia hatua hiyo halafu mkaingia kwenye mvutano. Tumeuliza hapa mara nyingi hatuelezwi na Kamati nayo imelalamika, mkataba wetu unasema lazima walipe CSR Shilingi Bilioni 260, ailimia Nne ya mkataba mpaka sasa hivi tunaendelea kuwalipa hawa zaidi ya asilimia 70 sasa, lakini hizi fedha hazikatwi na maelezo hayatolewi, tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Kamati zote zimeshasema, Kamati ya Nishati na Kamati ya Bajeti, kwamba sababu za ucheleweshaji zimesababishwa na Mkandarasi mwenyewe kwa uzembe wake. Sasa kama sababu ni hizo, mkataba wetu unasema, ucheleweshaji wa uzembe ni asilimia 10 ya thamani ya mradi. Asimilia 10 ya trilioni 6.4 ni shilingi bilioni 650, anachelewesha kwa miaka miwili ambayo ni trilioni 1.3, hizi fedha mbona haziombwi? Hakuna mahali popote ambapo Wizara utaiona hata hapa Bungeni ikizungumza kwamba tumeenda kumchaji hizo fedha hakuna hatuelezwi! Zaidi Wizara imekuja hapa inamtetea Mkandarasi, unajua zilikuwa ni sababu za UVIKO-19 lakini Kamati zote zimeshakataa kwamba sababu siyo UVIKO-19, huu ni uzembe wa Mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini huyu Mkandarasi anabebwa kwa kiwango hicho? Sababu za kubebwa huyu mkandarasi ni nini? Sasa hivi kama tumefikia 70%, hizi fedha tutakuja kuzi-recover na nini? Tunamdai shilingi trilioni 1.3 kwa ucheleweshaji wa mwaka mzima, tunamdai shilingi bilioni 260 kwa ucheleweshaji wa miaka miwili, tunamdai shilingi bilioni 260 za CSR, hizi fedha hazijalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza seriously kwamba hili jambo kama Serikali kila leo imekuwa ikipiga danadana kulifanya, basi iundwe Kamati Teule ya Bunge tuende tukaujue ukweli. Jambo la pili, Bunge liiagize Wizara ya Nishati ikazidai zile fedha, shilingi trilioni 1.56 tunazihitaji kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Deni la Taifa. Deni la Taifa takwimu zinaonesha hapa kutoka Aprili 2021 na kufikia Aprili 2022 limeongezeka kwa shilingi trilioni 8.7, hili ni ongezeko la asilimia 14.4. Hili ongezeko linaongezekaje kwa kiwango hicho wakati deni wakati huo tulili-service kwa shilingi trilioni 7.2, maana yake Serikali katika kipindi hicho imekopa shilingi trilioni 15.92. Hapa Bungeni tuliiruhusu Serikali ikakope shilingi trilioni 10.5, kwa nini Serikali imeenda kukopa zaidi ya kiwango kilichoruhusiwa na Bunge? Kama miradi iliyoidhinishwa na Bunge hapa kwa kasma ya kiwango kilichoruhusiwa kwenda kukopwa pamoja na mapato ya ndani, hizi fedha za ziada zilizokopwa na Serikali zilienda kutekeleza miradi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ukiangalia trend ya ongezeko la Deni la Taifa, Deni la Taifa lilikuwa linaongezeka kwa asilimia saba mwaka 2019/2020, lakini ilipofika mwaka 2020/2021, Deni la Taifa likaongezeka kwa wastani wa asilimia 13.7 na mwaka 2022 limeongezeka kwa asilimia 11. Ongezeko hili ni karibia mara mbili, sasa tumefikaje hapa na bahati mbaya sana niliuliza kipindi cha bajeti hili jambo sikupewa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hili la Deni la Taifa kwa speed kubwa, uwezo wetu wa kukusanya mapato kwa Pato la Taifa ni 11.4%, nchi jirani ya wenzetu wa Kenya ni asilimia 13.7 lakini nchi ya Rwanda ni asilimia 15.9, madeni haya tumefikia hapa. CAG afanye uchunguzi kwenye hili eneo na Serikali itoe maelezo ya kina kuhusu jambo hili. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hizi Kamati mbili, Kamati ya Miundombinu pamoja na Kamati ya Mifugo, Kilimo na Maji.

Mheshimiwa Spika, nikianzia na Kamati ya Kilimo, usimamizi wa rasilimali za uvuvi. Nimepokea kwa masikitiko makubwa sana juu ya taarifa ya kupungua kwa samaki katika maziwa, mabwawa na mito yetu. Maelezo ya kamati ni kwamba upungufu huu unatokana na usimamizi hafifu wa rasilimali, lakini wakaenda mbali wakasema samaki aina ya sangara kwenye Ziwa Victoria wamepungua kwa 50% na wakaenda mbali zaidi wakasema sasa hivi samaki wazazi wamebaki 0.4%. Sasa kama Ziwa Victoria samaki wazazi wamebaki 0.4%, maana yake ni kwamba ziwa letu hilo linaenda kuwa sawa tu na swimming pool kwa sababu huwezi ukawa na Samaki wazazi 0.4% na ukawezesha kuwepo kwa samaki majini.

Mheshimiwa Spika, kwa takwimu zinazoishia Desemba, 2020 samaki wazazi kwenye Ziwa Victoria walifikia 5.2% na kima cha chini kinatakiwa walau wasiwe chini ya 3%. Kwa hiyo hili ni jambo ambalo linahitaji kuchukuliwa hatua haraka sana na wameeleza mpaka madhara yake kwamba kwa vyovyote vile maana yake viwanda vyetu haviwezi kuzalisha tena inavyotakiwa, viwanda vingi vitafungwa, ajira zitakosekana katika hilo eneo, chakula kitakosekana hapa nchini, bei ya chakula cha samaki itakuwa ni kubwa, madhara ni mengi yanayoweza kupatikana.

Mheshimiwa Spika, sasa tufanye nini? Tatizo kubwa hapa na ninachojiuliza nini chanzo cha usimamizi hafifu, kwa sababu kamati inatueleza hapa inasema inaitaka Serikali idhibiti uvuvi haramu kwa kutumia njia sahihi ambazo hazitwezi utu. Nakubaliana nao lakini chanzo cha usimamizi hafifu ni nini mpaka maji yetu yamefikia hiyo hatua.

Mheshimiwa Spika, nina mapendekezo yafuatayo kuongeza kwenye pendekezo la Kkamati kwamba Bunge liitake Serikali kuwasilisha Bungeni chanzo cha usimamizi hafifu katika rasilimali za uvuvi ili Bunge liweze kuchukua nafasi yake. Pendekezo la pili, Bunge liitake Serikali kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi katika maeneo yote kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Mheshimiwa Spika, hii Wizara ukiiangalia mapato yanayotokana na uvuvi yameanguka vibaya sana, mapato yatokanayo na mifugo yameanguka vibaya sana. Sasa hili tatizo ni kubwa na moja ya mambo mengine nitaeleza huko kwenye mfumko wa bei kwamba huwezi ukau-control mfumko wa bei kama nchi haina chakula. Kama samaki wanauzwa kwa bei kubwa na hawapatikani, huwezi ku-control mfumko wa bei. Sasa suala hili ni lazima tulichukulie kwa ukubwa kama lilivyo kwa ukubwa kama Wawakilishi wa wananchi.

Mheshimiwa Spika, suala la pili limezungumzwa na Kamati ya Miundombinu, Kamati hii imelalamika sana juu ya uingiaji kwenye mikataba na Wakandarasi wasiokuwa na uwezo, juu ya miradi mingi ya maendeleo kutelekezwa na kukaa kwa muda mrefu bila kumalizika na juu ya miradi mingi kutekelezwa chini ya viwango.

Mheshimiwa Spika, ni lini Bunge lako linaanza usimamizi wa Serikali? Hapa tulilalamika, Wabunge walilalamika, Mkataba wa TRC na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation tukasema kwamba baada ya kupatikana kwamba tender yao kwenye mfumo wa TANePS tukasema unawezaje mradi mkubwa kama huu ukaupata kwa njia ya single source? Wabunge wakahoji hapa, mradi mkubwa wa trilioni 6.34 unatumiaje mfumo wa single source? Mfumo ambao hauruhusu competition, hauruhusu ushindani na ni mfumo ambao mtu anaweza akapendelea kampuni anayoitaka yeye, anaweza akaingia kwenye rushwa, huwezi kumkwamua katika mfumo wa single source, tukalalamika Wabunge hapa.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu kampuni hii iliyokuwa inaingia mkataba CCECC iliingia mkataba lot six, Tabora-Kigoma kilomita 506 kwa trilioni 6.34, lakini wakati huohuo imeshapewa Tenda ya Isaka-Mwanza kilomita 341 kwa trilioni 3.12, unawezaje kuipa mkataba mwingine wakati ina mkataba mbichi kabisa huo wa Isaka-Mwanza? La pili, kampuni haijawahi kujenga hata kilomita moja na mbaya zaidi kipande cha Kigoma-Tabora ndio sasa hivi ni kipande ambacho kina gharama kuliko vipande vyote.

Mheshimiwa Spika, average ya mradi huohuo ambao Kampuni ya CCECC ndio inautekeleza wa Isaka- Mwanza, wastani wa kilomita moja ya SGR ni bilioni 9.1, lakini wastani wa kilomita moja katika kipande cha Tabora - Kigoma bilioni 12.5, tafauti ya bilioni 3.4 kwa kilomita. Mbaya zaidi wakati huo wataalam wetu wanafanya usanifu wa kina wa kujenga barabara kipande cha Tabora - Kigoma walisema kipande hicho kingeweza kujengwa kwa trilioni 4.89, average ya shilingi bilioni 9.5 kwa kilomita, lakini tenda imekuja kutoka ya trilioni 6.4 tofauti ya trilioni 1.5. Sasa mkataba wa aina hii unakubaliwaje? Hivi juzi Serikali imesaini huo mkataba licha ya Bunge lako kutoa tahadhari zote lakini Serikali imesaini huo mkataba.

Mheshimiwa Spika, naomba kupendekeza mambo yafuatayo kuhusu mkataba huu: -

Mheshimiwa Spika, moja, Bunge liitake Serikali kuwasilisha taarifa ya mchakato wa manunuzi Bungeni kuanzia kutangaza zabuni ya tathmini ya utoaji wa zabuni ya SGR kipande cha Tabora - Kigoma kilomita 506. Mkataba huu uwasilishwe Bungeni na kazi hii inaweza ikafanywa vizuri sana na Kamati ya Miundombinu, lakini Kamati ya Katiba na Sheria wakawasilisha mchakato wote. Mkataba huu unaenda kuwa gharama zaidi ya ile inayotakiwa kwa trilioni 1.7, Taifa linakwenda kuingia na wataalam wetu wamesaini, Wabunge wamelalamika hapa viwango na nini na nini, mambo yote yanafanyika huko miundombinu, lakini hawakusikilizwa.

Mheshimiwa Spika, pili, ufanyike Ukaguzi Maalum, CAG na PPRA waunde timu ya pamoja na PCCB waukague mradi huu na kutoa taarifa za kiukaguzi juu ya kile kilichofanyika katika Mradi wa SGR kipande cha Tabora - Kigoma. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa ili nami niweze kuchangia katika hizi kamati mbili. Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukabiliana na wanyama wakali tembo. Suala hili ni suala kubwa, katika Wilaya yangu ya Meatu, wananchi waliouwawa na tembo kwenye Jimbo la Kisesa na Jimbo la Meatu kwa maana ya Wilaya ya Meatu. Wananchi waliouwawa na tembo ni 18, wananchi waliojeruhiwa ni tisa, mashamba yaliyoharibiwa ni 2,086 na nyumba zilizobomolewa ni 480. Mazao yaliyoliwa nyumbani ndani ya majumba ya wananchi ni tani 150.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili tunapolizungumza ni suala nyeti, suala ambalo lina tatizo kubwa la wananchi wetu na tunataka kwa kweli majibu sahihi ya Serikali namna ya kupambana na hawa wanyama wakali. Taarifa hapa imeandikwa, Serikali inapambana na wanyama, inafanya doria kupambana na hawa wanyama lakini inajenga vituo. Suala la kujenga vituo nilipongeze kwa sababu katika Jimbo langu la Kisesa, vituo viwili vimejengwa, Kituo cha Ng’anga pamoja na Kituo cha Marwiro. Vinajengwa na viko hatua ya kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu kubwa ni kwamba hizi doria zinazozungumzwa na Serikali zinaendeshwa wapi? Mbona mashambulizi ya wanyama hawa hasa tembo ni makubwa kiasi hicho? Je huyu TAWA ambaye kazi yake ni kupambana na hawa wanyama kuwadhibiti wasiingie kwa wananchi ametengewa bajeti kiasi gani? Fedha zilizotengwa katika hiyo doria kwa sababu doria lazima uwe na fedha, magari, mafuta na vifaa. Sasa hawa tembo tunakwenda kupambana nao kwa namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaitaka Wizara ituambie leo, lini itakomesha tatizo la tembo kwa wananchi ambao wanahangaika nalo kila siku? Watu wanauwawa kila leo, kipaumbele chetu ni nini? Lazima Wizara leo ituambie namna inavyoenda kushughulikia jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la migogoro ya ardhi. Migogoro ya ardhi hii kila mahali, wahifadhi, wakulima, wafugaji wanapigana kila leo. Kila leo wanapigana na baadhi ya watendaji wa Serikali wamegeuza mtaji wa haya mapigano na hawako tayari kuona haya mapigano yamekwisha kwa sababu wamegeuza kuwa mtaji unaowapatia fedha. Wamegeuza kuwa ATM. Kwa hiyo, migogoro hii hawako tayari migogoro iishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mmoja, suala la mipaka na alama zinazoonekana kwenye hifadhi zetu umekuwa ni wimbo wa miaka nenda rudi. Maeneo mengi hayajapimwa, alama hazijawekwa, mipaka inayotenganisha shughuli ya wananchi na shughuli za wakulima na wafugaji wataachaje kugombana na kupigana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni utanuzi holela wa hifadhi. Kumekuwa na utaratibu tu watu wanaweza kutanua tu unashtukia GN imetangazwa ambayo siyo shirikishi, maeneo yanatanuliwa, maeneo ya wafugaji yanachukuliwa, maeneo ya wakulima yanachukuliwa, migogoro itaisha lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni maeneo mengi ya wafugaji yanageuzwa kuwa hifadhi, yanageuzwa kuwa WMA, wafugaji kila leo maeneo yao yametaifishwa, migogoro itakwisha lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukamataji holela wa mifugo, mtu anakamata tu mifugo inakamatwa kiholela, inauzwa kiholela na wananchi wamelalamika muda wote mifugo mingine inafungiwa bila maji, bila malisho mpaka inakufa. Sheria za Mifugo zipo zinazozuia hayo lakini watu wanavunja sheria makusudi kwa kisingizio cha uhifadhi. Haya mambo yatamalizika lini na wananchi wakawa kwenye hali nzuri? Mahusiano yatapatikana lini kama wengine wanashinda kesi mahakamani kama wafugaji, zaidi ya ng’ombe 6,000 wameshinda kesi mahakamani lakini hazijarejeshwa mpaka leo. Mahusiano utayapata wapi ya wakulima na wafugaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, faini kubwa zinazotozwa hasa kwa wafugaji, ng’ombe mmoja kutozwa faini ya shilingi 100,000 ambayo hata kwenye sheria haipo. Leo Mwenyekiti wa Kamati atuambie hizi faini Wizara ya Maliasili wanaitoa wapi ya kutoza shilingi 100,000 kwa ng’ombe mmoja ambayo ni karibia 30% ya thamani ya ng’ombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gari likipata shida, basi la Milioni 300 likipata matatizo litatozwa faini ya Shilingi 30, ngo’mbe wa shilingi laki tano anatozwa faini ya shilingi laki tatu…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatutaki mifugo nchi hii si tuseme kuliko kuwanyanyasa wafugaji kiasi hicho, kuliko kuwaonea Wafugaji kiasi hicho? Sheria za mifugo ziko vizuri…

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Mpina.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, The Animal Welfare iko vizuri, Kanuni zinazozuia manyanyaso haya ya mifugo ziko vizuri, kwa nini sheria zinazoangaliwa ni Sheria za Uhifadhi tu na Sheria za Mifugo zikitelekezwa? Leo Mwenyekiti wa Kamati atuambie manyanyaso hayo yanafanywa chini ya misingi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wetu wamekuwa wakipata shida kubwa maeneo mbalimbali, nenda huko Ilunde kule Kigoma, Mwandubanu, Kisesa Jimboni kwangu kule mpakani mwa hifadhi, manyanyaso ni makubwa! Nenda huko Serengeti, nenda Tarime, nenda hata huko Mbarali majuzi hapa wakulima unafika msimu wa kilimo wanaambiwa ondokeni hapa, mambo haya hayakubaliki! Mwenyekiti atupe maelezo ya kina juu ya masuala haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mfumuko wa bei. Suala la mfumko wa bei tukiendelea kupokea taarifa za kwamba eti! mfumuko wa bei umesababishwa na COVID-19, eti! mfumuko wa bei umesababishwa na vita ya Ukraine na Russia tukakubaliana na hayo, mfumuko wa bei unaowatesa wananchi wetu hatuwezi kuutatua. Mfumuko wa bei kwa sehemu kubwa mimi nakubaliana na hizo sababu lakini sababu kubwa za mfumuko wa bei kama nilivyosema tumezitengeneza wenyewe. Kama tumezitengeneza sisi wenyewe tuondoe mfumuko wa bei sisi leo katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumuko wa bei wa nchi hii umesababishwa na mambo makubwa mawili; Moja, usimamizi dhaifu wa sheria; Pili, usimamizi hafifu wa sera za fedha mambo mawili tu. Nasema hayo kwa sababu gani? Huwezi uka-control mfumuko wa bei kama unaweza kufanya malipo, kama usimamizi wako wa bejeti hauko sawasawa. Unaweza kufanya malipo ambayo ni nje ya bajeti, Bilioni 350!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bilioni 350 tumemlipa Symbion fedha ambazo hazimo kwenye bajeti, huwezi kupata utulivu wa inflation katika mazingira ya namna hiyo. Pia kama huwezi kupeleka fedha zilizopangwa kwenye maeneo husika hasa kwenye sekta muhimu kama ya kilimo, jana tumeambiwa mpaka Februari hii ni asilimia 17 tu ya fedha zilizopelekwa uta-control vipi mfumuko wa bei?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuingia mikataba mibovu. Unaingia mkataba mbovu kama mkataba ulioingiwa wa TRC pamoja na CCECC wa Trilioni 6.34 mkataba ambao una mashaka, una malipo yenye mashaka ya zaidi ya Trilioni 1.7 halafu ukategemea kwamba utapata utulivu wa fedha nchini, halafu ukategemea kwamba uta-control inflation haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera za kodi, ukawa na sera za kodi hapa. Tumekuwa na sera za kodi za mpaka unaenda unawasamehe wawekezaji mahiri, unasema hawa ni wawekezaji mahiri ukawasamehe kodi zote, kodi ya VAT, corporate tax zote umewasamehe halafu maskini akaendelea kutozwa kodi zote zinazotakiwa kutozwa mpaka tozo, lakini Tajiri huyu ameambiwa kwamba amesamehewa kodi halafu ukafanikiwa kwa nchi yenye …

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi uka-control inflation katika mazingira hayo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii ambayo umenipa na kwa sababu ya changamoto ya muda pia mchango wangu nitaupeleka kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, kwa dakika hizi chache nilizozipata niseme kwamba tuko leo kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya sekta muhimu sana ya Wizara nyeti ya Katiba na Sheria ambako tunaenda kuwahakikishia wananchi wetu kwamba haki itaendelea kutolewa pia haki itaendelea kupatikana kwa wakati na rasilimali zao za umma zitaendelea kulindwa.

Mheshimiwa Spika, bado tuna changamoto nyingi sana kufikia haki hizi kutolewa sawasawa.

Moja, kuna baadhi ya Watendaji wa Serikali ambao wanavunja Katiba na wanavunja na Sheria wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Pili, bado kumekuwepo na usiri mkubwa sana kwa mikataba inayoingiwa na Serikali kwa niaba ya wananchi.

Tatu, bado kuna ucheleweshaji mkubwa wa maamuzi ya Mahakama na taasisi zingine ambazo zimepewa jukumu la kutoa haki.

Nne, maeneo mengi muhimu ya kiuchumi na kijamii hayajatungiwa sheria na hivyo kutumia matamko ya Viongozi katika kutoa uelekeo wa nini kifanyike katika eneo husika.

Tano, ni upendeleo na kukosekana kwa uwiano wa utoaji wa adhabu zinazotolewa katika baadhi maeneo ya kisheria.

Mheshimiwa Spika, haya yasipofanyiwa tathmini vizuri tutaendelea kupiga mark time kwa sababu yana madhara makubwa sana katika uchumi wetu tunaousimamia. Tunasema tu kirahisi kwamba Mahakama imechelewesha maamuzi au Taasisi iliyopewa dhamana ya kutoa haki imechelewesha maamuzi, lakini madhara yake ya maamuzi hayo kwenye Taifa ni yapi, madhara hayo ya kuchelewa kwa maamuzi kwa mtu aliyetakiwa kuipata hiyo haki ni yapi.

Mheshimiwa Spika, tunasema tu kiurahisi kwamba mikataba inaingiwa kwa usiri na inatunzwa kwa usiri, lakini madhara ya kutunza mikataba kwa usiri kama Taifa ni ipi. Tunakuwa kwenye changamoto kubwa za namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, niweze tu kutoa mfano wa madhara makubwa sana ambayo tunayapata kutokana na ucheleweshaji wa maamuzi wa kesi katika Mahakama. Hapa tunakumbuka kwamba tulikuwa na tatizo la pingamizi za kikodi la Shilingi Trilioni 360, hili jambo lililalamikiwa na Bunge hili, hili jambo lililalamikiwa na mimi mwenyewe binafsi hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa ya CAG ya mwaka 2020/2021 inasema kwamba Mahakama hizi zimehitimisha haya mashauri na katika hitimisho Trilioni 5.65 jumla ya kesi 54 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 5.65 zimeamuliwa na Mahakama, Serikali pamoja na wadau wa makampuni ya madini wamekabidhiwa kwenda kufanya mjadala wa namna ya kuhitimisha hili suala. Kesi zenye thamani ya Shilingi Trilioni 343.5 zenyewe zimerudishwa TRA kwa majadiliano, na kesi zenye thamani ya Shilingi Trilioni 5.19 zenyewe bado zinaendelea katika Bodi na Baraza la Rufani za Kodi.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa zilizopo hivi sasa ni kwamba tayari Serikali imehitimisha mjadala huu na imekubaliana kupokea Dola za Kimarekani Milioni 300 ambayo badala yake ukibadilisha nadhani ni kama Bilioni 692.61.

Mheshimiwa Spika, hiki kidogo kilichopatikana ni cha kupongeza, nami kabisa nataka nipongeze na Bunge lako hili Tukufu kwa kulisimamia hili jambo, tumeweza kupata hizo Bilioni 692.61 jambo ambalo hapa tuliambiwa hizi fedha ni za mchongo, haya makampuni ya madini madeni ya nyuma hatuwezi kulipwa kwa hiyo tunapoteza muda. Fedha hizi tumezipata leo Bilioni 692.61 ni suala la kujivunia sana.

Mheshimiwa Spika, hapa namkumbuka tingatinga Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alivyosimama kidete kuhakikisha kwamba hizi fedha za Watanzania zinapatikana, watu wakasema haziwezi kupatikana lakini dunia nzima aliiambia na akaihakikishia na leo Taifa limepata Bilioni 692.61.

Mheshimiwa Spika, nakubali kabisa kwamba ndiyo maana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alimteua Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais Awamu ya Kwanza na Awamu ya Pili, alimuona uwezo wake na ndiyo maana leo hii amekuja kulisimamia hili kwa kauli yake aliyoisema kazi iendelee.

Mheshimiwa Spika, jambo moja lingine pamoja na mafanikio haya tuliyoyapata lakini suala la kujiuliza hawa wenzetu walioenda kwenye negotiation Mahakama zilisema Trilioni 5.65 zinaweza kupatikana na Serikali iende ikajadiliane walikubalije kupokea Milioni 300 ambayo ni Bilioni 692 tu wakati Mahakama hizi za Bodi ya Rufaa za Kodi, Bodi pamoja na Baraza zilisema kwamba Trilioni 5.65 zinaweza kupatikana kama kodi, kwa nini tupate Bilioni 692.65.

Mheshimiwa Spika, ninaomba eneo hili lina changamoto kubwa na ninashauri na kulishawishi Bunge lako likubali tuunde Tume Teule ya Bunge ikachunguze suala hili, kwanza negotiation timu hiyo ilifikiaje maamuzi ya kupokea Bilioni 692.61, pia ikaangalie uhalali wa majadiliano hayo na kile ambacho kilichopatikana.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni hapo ambapo bado ukiondoa sasa hivi kesi za makinikia kwa sababu ni karibu zote zimeondolewa mahakamani. Ukiondoa hizo, bado tunabakiza kesi zenye thamani ya Shilingi Trilioni 5.19 za makosa tu mbalimbali, sasa hivi ukataji wa rufaa kwenye bodi hizi na Mabaraza ya Kodi za Rufaa yamefikia wastani wa Trilioni Mbili kwa mwaka, tukiruhusu hili likaendelea na tukaendelea kuchelewesha hizi kesi? Tutajikuta watu wote watatufungulia kesi au watatukatia rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kama leo imefikia Trilioni Mbili inakatiwa rufaa Mahakamani na wadau hawa wa kodi, ni lazima tuhakikishe kwamba kesi zinamalizika kwa wakati, sababu za kuchelewesha kesi eti Mabaraza hayana pesa, sababu za kuchelewesha kesi eti kwa sababu mabaraza haya hayana watumishi! Hili ni jambo ambalo haliingii akilini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo ambalo unaweza kwenda kukusanya mapato siku hiyo hiyo kesi zikiamuliwa, haki za wale waliokata rufaa zikasikilizwa, pia haki ya Serikali kupata kodi yake na yenyewe ikaweza kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho kutokana na changamoto hii ya muda ni usiri mkubwa wa mikataba ambayo Serikali inaingia. Mfano mmoja wa usiri wa mikataba unavyoliathiri Taifa letu ni utekelezaji wa bwawa la Mwalimu Nyerere, utekelezaji wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Spika, nizungumze hapa kwa kusema kabisa kwamba maeneo haya ya kimkataba yana changamoto nyingi na ndiyo maana taasisi zetu za kiuchunguzi CAG, PPRA pamoja na PCCB wote wamekuwa wakilalamikia maeneo haya ya kimkataba kuwa na changamoto nyingi sana za ubadhirifu wa fedha za umma, changamoto za wizi wa fedha za umma, changamoto za ufisadi wa fedha za umma.

Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na mkataba wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, hivi majuzi hapa tumetangaziwa kwamba mkataba huu utamalizika baada ya miaka miwili ijayo, lakini ndani ya mkataba iko clear kwamba kuna Bilioni 260 ambazo ni CSR lakini Mkandarasi akichelewesha mkataba wetu anapaswa kulipa asilimia Kumi. Kwa hiyo, kama amechelewesha Mkandarasi kwa miaka miwili anapaswa kutulipa shilingi trilioni 1.3.

Mheshimiwa Spika, kwa nini haya mambo hayajawekwa wazi katika hili jambo? Tunamdai bilioni 260 za CSR, tunamdai ucheleweshaji wa miaka miwili ambayo ni Trilioni 1.3. Kwa nini haya mambo yana usiri gani? Siri hizo zinawekwa kwa ajili ya kumlinda nani?

Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa nafasi.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii ili nami niweze kuchangia hii Wizara ya Kilimo katika makadirio yake ya mwaka 2023/2024. Niwapongeze sana Wizara kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea huu mradi wa upembuzi yakinifu katika Kijiji cha Mwakasumbi pamoja na Mwalukoli katika Jimbo la Kisesa, kazi nzuri sana lakini na namna bajeti inavyoongezwa ya kilimo ni jambo ambalo wakulima tunafurahia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba leo wafugaji ambao wamekwazwa na madhila yale ya wahifadhi wote leo wako hapa ambao Mheshimiwa Spika aliomba vielelezo hivyo viletwe wamekuja wenyewe na vielelezo. Kwa hiyo leo jioni tunakabidhi vielelezo hivyo vilivyoombwa na Mheshimiwa Spika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa bajeti. Katika utekelezaji wa bajeti hapa, bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Kilimo katika mwaka huu wa fedha ni shilingi bilioni 569.97. Fedha zilizotolewa mpaka sasa hivi na Serikali ni shilingi bilioni 470.75. lakini katika fedha hizo, shilingi bilioni 361.5 ni za umwagiliaji ambazo mpaka sasa hivi zilizotolewa ni shilingi bilioni 85 tu sawa na asilimia 23. Sasa unaipataje asilimia 40, unaipataje shilingi bilioni 470 wakati fedha za umwagiliaji shilingi bilioni 361 ambazo ni sawa na asilimia 63 ya fedha za maendeleo zimetolewa asilimia 23 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji mpaka sasa hivi imeshabadilishiwa matumizi. Zaidi ya shilingi bilioni 200 na kama imebadilishiwa matumizi, fedha za maendeleo, fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji zimebadilishiwa maendeleo, zimepelekwa wapi? Kwa idhini ya nani? Waziri ana uwezo wa kubadilisha fedha za maendeleo zilizoidhinishwa na hili Bunge akazipeleka kwenye shughuli zingine. Tuambiwe kwa umakini juu ya hizi takwimu zilivyokaa na Waziri atakapokuja hapa ili tuweze kujua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la utoaji wa mbolea ya ruzuku. Ukiangalia taarifa ilivyowasilishwa kwamba mpaka sasa hivi tayari mbolea tani 449,795 zimekwishatolewa na wanufaikaji 801,000 lakini ukienda kwenye ile jedwali alilosema jedwali la nane lina takwimu nyingine. Mbolea iliyopokelewa na kusambazwa mpaka sasa hivi ni tani 342,729 badala ya hiyo 400. Kwa hiyo kuna mkanganyiko mkubwa sana wa takwimu. Sasa hizi takwimu ni za kupika? Sasa kama zina uhalisia kwa nini zinatofautiana ukurasa hadi ukurasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kama tuliandikisha wakulima 3,050,000, wakulima walioenda kunufaika na mbolea ni 801,000 peke yake, hawa wakulima wengine 2,200,000 walipata wapi mbolea? Kama tulijua kwamba mfumo huu wa utoaji wa mbolea ya ruzuku hatuwezi kuwafikia wakulima wote kwa pamoja, kwa nini tulileta mfumo ambao unapelekea mbolea kuipata mpaka upitie mfumo wa ruzuku ya mbolea? Hawa wananchi wengine wamelimaje kama hawakufikiwa? Kama tulikuwa na lengo la kusajili wakulima milioni saba na leo tumesajili milioni tatu, hawa wakulima wengine wanaendeshaje kilimo chao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto nyingi sana katika zoezi hili la utoaji wa mbolea ya ruzuku. Moja, mfumo wa mtandao wa mbolea za ruzuku uliokuwa ukitumika una changamoto nyingi. Moja, unaruhusu double scanning mpaka multiple scanning. Pili, mtambo huu hauwezi kuruhusu sub-agent. Mfumo unachelewa ku-left na hivyo mkulima anaweza aka-draw zaidi ya mara moja. Sasa kama una mfumo umeandaliwa wa namna hii, unaweza kwenda kufanya mpaka double scanning waharamia wengine wa kimtandao wanaweza kuiba fedha yoyote ile wanayoitaka kwenye huu mfumo, Wizara inaandaje mfumo na kuuleta kwa wananchi wenye changamoto za namna hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo ambao unaweza ukaiba fedha za nchi tukaenda kulipa mbolea hewa, unawezaje kuingia mfumo huo? Sitaki kuamini kwamba Serikali Mtandao kwa maana ya e-GA kwamba hawana uwezo wa kuwasimamia Wizara ya Kilimo, lakini nataka kuamini kwamba Wizara ya Kilimo walianzisha mfumo huu wa utoaji wa mbolea ya ruzuku bila kuwashirikisha e-GA na yawezekana kabisa hawana clearance ya e-GA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendesha mfumo bila kupata clearance ya e-GA ni kosa kisheria na matatizo yake yanaenda kuzalisha matatizo makubwa ya uhujumu uchumi. Sasa Wizara inaweza namna gani kwanza huyu vendor alipatikanaje? Huyu vendor aliyetengeneza huu mfumo alipatikanaje? Alipitia zile procedure zinazotakiwa? Au alipatikana kwa kuteuliwa tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili huu mfumo uliwezaje kuingia kwenye operation bila kupata clearance ya e-GA na tukawa na mfumo ambao una matatizo namna hii? Umepeleka matatizo makubwa kwa wakulima wetu. Wakulima wetu huko wanaambiwa mbolea ipo, tunaambiwa mbolea ipo lakini mbolea hawakupata wakulima wetu. Wakulima wameteseka kupata mbolea, wengine wamefia kwenye foleni. Mbolea zingine zimeibiwa, wameenda hawa mawakala 721 wamekuja kuambiwa kwamba tunawafutia leseni kwa sababu eti kwamba wamefanya double scanning. Sasa double scanning unawezaje kuifanya katika mfumo proper? Unawezaje kufanya double scanning kwenye mfumo proper halafu unamwambia nimekufutia leseni, halafu unamwambia jieleze kwa nini nisikufutie leseni wakati umeshamfutia tayari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria inakwambia toa notisi ndiyo umfukuze, huu mkanganyiko wa kuvunja sheria za nchi unaruhusiwaje kufanyika kwenye Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bei elekezi. Wizara ilianza na bei elekezi ambayo haikufanyiwa uhakiki, hawakuhakiki bei elekezi inayotolewa kwa ununuzi wa mbolea na kusambaza mbolea, matokeo yake tumeenda kuwauzia wakulima kwa bei kubwa ambayo haina sababu yoyote kwa matamko tu ya wafanyabiashara. Wizara haikufanya uhakiki wa bei ya mbolea katika viwanda na katika masoko. TFRA haikufanya uhakiki huo matokeo yake leo mbolea eti ilipofika Machi baada ya kugundua kwamba sasa mahitaji ya mbolea yameisha nchini, yamepungua sana nchini, ilipofika Machi, TFRA inatoa bei elekezi ya shilingi 72,911 kwa mfuko wa urea wa kilo 50 kutoka shilingi 116,650 baada ya kuona mahitaji sasa hayapo. Wanashusha bei na price haiwezi ikashuka kama jiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, price volatility na price elasticity haiwezi kuruhusu mshuko wa namna hiyo, maana yake ni kwamba hapakuwa na usimamizi mzuri kwenye bei, matokeo yake pamoja na kutoa bei ya ruzuku, lakini ukweli ni kwamba tumeenda kutoa ruzuku kwenye bei fake. Sasa ukitoa ruzuku kwenye bei fake huwezi kupata value for money. Tumewachangia wananchi kulipia, tumetumia billions of money za fedha za Watanzania kwa bei ambazo hazina uhakiki, kwa bei ambazo hazina ukweli, matokeo yake tumepoteza fedha nyingi na hatuambiwi, bei mpaka sasa hivi wakandarasi wanatudai shilingi ngapi, mpaka sasa hivi tumetumia shilingi ngapi kwa ajili ya ruzuku ya mbolea na kwa nini tunafichwa vitabu vyoote havizungumzi gharama ya mbolea, mpaka sasa hivi ni shilingi ngapi Tanzania tumelipa? (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa. Nami nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri. Nimemsikiliza na nimesoma kurasa zote 277 za hotuba yake, zimesheheni mambo muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza wakulima kote nchini, nawapongeza wakulima wangu wa Jimbo la Kisesa kwa kazi nzuri sana wanayofanya ya uzalishaji mali. Katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri amezungumza suala la kuanzisha Benki ya Taifa ya Ushirika. Hili suala la kuanzisha Benki ya Ushirika ya Taifa halina tija yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, watu wa ushirika hawajakosa mahali pa kukopa. Tuna Taasisi nyingi sana za mikopo ambazo zinaweza zikatoa mikopo kwa washirika. Tunayo Benki ya Kilimo, unakwenda kuanzisha benki nyingine ya nini? Benki yenyewe hii ya Kilimo bado hatujaiimarisha, tunaenda tena kuanzisha benki nyingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, wanazungumzia urahisi wa kupata mikopo. Masharti na vigezo vinasimamiwa na Benki Kuu. Kwa hiyo, suala la kusema kwamba eti washirika wakianzisha benki watapata mikopo kiurahisi ni nadharia, kwa sababu vigezo na masharti yote yanasimamiwa na Benki Kuu na yatakuwa ni yale yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, majukumu ya Vyama vya Ushirika ni mengi sana. Tumewapa jukumu la kufufua viwanda vilivyotelekezwa, tumewapa jukumu la kuwasaidia wakulima kupata mbegu bora, kuwasaidia wakulima waweze kupata huduma ya afya ya udongo, kupambana na magonjwa. Wanaliacha hili jukumu la msingi, wanakimbilia kuanzisha benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mfano, kuna Benki hapa zilianzishwa kwa mbwembwe nyingi, matokeo yake benki hizo tumeenda kupata hasara kubwa, benki zikafungwa, fedha za Watanzania zimo humo ndani. Kwa mfano Bank (M) iko wapi? Twiga Bank iko wapi? Benki ya Wanawake iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa hayo hayo, leo tunaenda kuanzisha Benki tena za mfano huo huo. Hata kidonda hiki bado hakijapona, Benki Kuu bado wanalitatua hili tatizo, hatujamaliza kulitatua, leo Waziri unaenda kuruhusu kuanzisha Benki nyingine, kwa ajili ya jambo gani? Benki Kuu nanyi mmekubali kuanzisha hii Benki wakati tunayo Benki ya Kilimo? Duplication hizi ni za kazi gani? Mnataka kuzichukua fedha za wananchi ambazo zingeweza kuwasaidia wananchi, ziende zikagawanywe huko kujenga majengo na mambo mengine wakati wakulima wana shida kubwa hapa! (Makofi)

Benki Kuu na ninyi mmekubali kuanzisha hii benki ilhali tunayo ya kilimo, duplications hizi za kazi gani? Mnataka kuzichukua fedha za wananchi ambazo zingeweza kuwasaidia wananchi ziende zikagawanwe huko kujenga majengo na mambo mengine ilhali wakulima wana shida kubwa hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la mbolea. Wenzangu wanezungumza hapa, upandishaji wa bei za mbolea, narudia kusema mfumuko bei za mbolea zetu ni wa kutengenezwa. Waziri amekuja hapa ameshindwa kusema utatuzi wa bei za mbolea zilizotengenezwa. Moja, kwa wafanyabiashara wametengeneza, bei za mbolea zimepanda, urea hapa imetoka 50,000/= imeenda mpaka 110,000/= mpaka 150,000/= kwa maeneo mengine, lakini ukiangalia kwa undani hizi bei zimetengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninasema, na hasa takwimu ambazo wanazo Serikali waziangalie. Kwa mfano Waziri anaposema kwamba, bei za mbolea zimepanda katika soko la dunia, bei ya urea imepanda kutoka dola 251 mpaka dola 1,214; kwa maana hiyo katika soko la dunia unataka kutuambia kwamba, bei ya mbolea ya urea kwa kilo 50 imepanda kutoka 28,000 mpaka 139,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hizo ndizo takwimu mnazotuambia, kama katika soko la dunia mbolea ya urea ya kilo 50 inauzwa kwa bei ya 139,000/= utaiuza kwa bei gani hapa? Kwa hiyo, hizo takwimu zenyewe sijui ni source gani na sijui kama Serikali wanajiridhisha na takwimu hizo, zinatoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu ni Serikali na Wizara hii ya kilimo; waliamua kufuta utaratibu wa bulk procurement system. Badala ya kutatua matatizo yaliyokuwemo kwenye bulk procurement system wakaenda kuiondoa bulk procurement system ili kufanikisha njama za wafanyabiashara wachache waliokuwa wamepanga njama za kuja kuwaongezea wakulima bei za mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Waziri atuambie toka walivyoondoa mfumo wa bulk procurement system mwaka 2021, Juni, bei za mbolea zilianza kupanda palepale, hata kabla ya vita ya Ukraine ambayo ndiyo inayozungumzwa hapa bei za mbolea zilianza kupanda kwa kasi bila usimamizi. Kwa hiyo kuna usimamizi dhaifu katika jambo hili. Na kwa uthibitisho hata Mheshimiwa Waziri mwenyewe anakiri kwamba wale TFRA walipoenda kufanya ukaguzi walienda kukuta mambo ya ajabu, wakakuta mbolea zinauzwa zikiwa hazijasajiliwa, hazina vibali, ziko wazi na vilevile kulikuwa na zilizokuwa na uzito wa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanathibitisha kwamba, hakuna usimamizi thabiti katika hili eneo la mbolea na kusababisha wananchi kwenda kuuziwa mbolea kwa bei kubwa sana. Halafu sasa mfumo tumeutengeneza sisi wenyewe nab ado kuna nchi jirani zetu ambao wanauza mbolea chini. Wanatumia Bandari ya Dar-es-Salaam, wanasafirisha mbolea na bado wanaenda kuuza huko kwa bei ya chini; kwa nini sisi hapa bei yetu hapa iko juu? Na haya yote tunayokubali na tumeyatengeneza sisi wenyewe Wizara ya Kilimo halafu tunatoka tunasema kwamba, eti bei ya mbolea tunamfumuko wa bei ya mbolea kwa bei ambazo tumezitengeneza wenyewe? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umeisha Mheshimiwa, nilikupa umalizie tu.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kukisema hapa, ni majonzi makubwa sana kwa Taifa letu, tunatengeneza mfumuko wa bei sisi wenyewe. Leo hii tunatenga fedha trilioni 150 kwa ajili ya kwenda kuweka ruzuku, unaenda kuweka ruzuku kwenye bei iliyotengenezwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi za Watanzania bilioni 150 ziende kwenye bei ya halisi ya mbolea. Wizara ya Kilimo ihakikishe kwamba inaenda kuondoa makandokando yote yaliyosababisha bei za mbolea kupanda… (Makofi/kicheko)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 6) Bill, 2021
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa nafasi uliyonipa na mimi niweze kuchangia huu mswada wa marekebisho ya sheria namba 6 kama ambavyo umewasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali lakini pamoja na ushauri wa kamati wa bajeti kwa Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kusema kwamba tunashukuru sana Serikali sana sana kwa kukubaliana na kamati yetu kwa mapendekezo ambayo tuliyoshauriana nayo kwa muda mrefu na hadi tulipofikia hapo tulipofikia. Nataka nihakikishie Bunge lako kwamba Muswada huu umechambuliwa kikamilifu na utaleta tija kubwa sana kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, Bunge lako leo linatuma salamu za furaha kubwa na sherehe kubwa kwa wafugaji wa nchi hii, kwa wavuvi wa nchi hii lakini kwa wakulima wa nchi hii, ilikuwa mzigo hii withholding tax asilimia 2 ilienda kukwaza sana kilimo ambacho kinachangamoto tayari kubwa nyingi, mifugo ambayo ina changamoto nyingi, shughuli za uvuvi ambazo zina changamoto nyingi, sasa ilipoletwa hii ilikwaza sana wananchi wetu ambao wanafanya kazi katika hili eneo, lakini hatimaye wewe mwenywe uliliona mapema kamati iliona mapema, Bunge lako liliona mapema hatimae leo hii chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na mama yetu Samia Suluhu Hassan wameridhia na Bunge lako naamini litaridhia maamuzi haya kwa hiyo huu ni ushindi mkubwa na ni vizuri tukaenda namna hii hivi tunavyoenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasa vipengele vile vingine vitatu vyote tumekubaliana vizuri mno na wenzetu, na hatuoni sababu tena ya kuzungumza chochote lakini baada ya vipengele kwa mfano sura ya tatu kurekebishwa na sura ya nne kuondoshwa kabisa, sheria sasa ilivyo hapa inabaki haina changamoto.

Mheshimiwa Spika, sasa labda ushauri mdogo katika eneo hili ni amejaribu kugusia na Makamu Mwenyekiti wa kamati ya bajeti, kwamba ni vizuri sana sasa tuwe tunafanya utafiri wa kina katika kuanzisha kodi zetu kuanzisha tozo zetu, tunapo taka kuanzisha tozo mpya tunapotaka kuanzisha kodi mpya ni muhimu sana tukafanya utafiti wa kina kabla hatujafanya hivyo, ili kuepuka changamoto kama hizi. Kwamba mmemaliza kupitisha bajeti miezi mitano tu tayari leo mnagundua kasoro tena ni kasoro za kimapato ambapo wakati mwengine zinawalazimu kuzikagua ni mapato ambayo mlikuwa mmeyatabiria kuweza kuyakusanya katikati ya safari.

Mheshimiwa Spika, ushauri mdogo tu katika eneo hili amejaribu kugusia Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwamba ni vizuri sana sasa tuwe tunafanya utafiti wa kina katika kuanzisha kodi zetu, kuanzisha tozo zetu, tunapotaka kuanzisha tozo mpya, tunapotaka kuanzisha kodi mpya ni muhimu tukafanya utafiti wa kina kabla hatujafanya hivyo ili kuepuka changamoto kama hizi kwamba mmemaliza kupisha bajeti miezi mitano tu tayari leo mnagundua kasoro tena ni kasoro za kimapato ambapo wakati mwingine zinawalazima ku-foregone mapato ambayo mlikuwa mmeyakadiria kuweza kuyakusanya katikati ya safari, kumbe taasisi yetu ya utafiti iliyoko pale TRA kwa maana ya Kitengo cha Utafiti TRA kingekuwa kimeimarishwa vizuri kikawa na wataalam wengi wa kutosha na wakawa shirikishi, lakini pia hata pale Hazina, kile kitengo kinachoshughulika au idara inayoshughulika na mambo ya utafiti ingekuwa na yenyewe inafanya kwa kina, kwanza tusingekuwa tunabishana kirefu kwa sababu tungekuwa na ushahidi wa kila tunachotaka kukiamua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, ni muhimu sana kwanza kuimarisha hivi vitengo viimarishwe viwe vinafanya utafoti wa kina, lakini hii itatusaidia sana pia kwa sababu ni kwa muda mrefu sana mapato yetu hayaongezeki kwa kasi kama ambavyo tunakusudia. Mapato yetu hayaongezeki ukilinganisha na ukuaji wa uchumi, mapato yetu hayaongezeki ukilinganisha na mfumuko wa bei, mapato yetu hayaongezeki kulingana na sababu nyingine zile za kiuchumi tulizonazo. Kwa hiyo, kuna haja kubwa ya kufanya huu utafiti ambao utatuwezesha kuongeza mapato yetu kwa kiwango kikubwa pia, tutaepuka kuanzisha tozo na kodi ambazo zinapoanzishwa zinaleta mkanganyiko kwa wananchi wetu na kurudisha nyuma hata jitihada pia za kupiga maendeleo mbele.

Mheshimiwa Spika, pili ambalo naweza kushauri katika hili eneo ni suala la utafiti na tathmini ya misamaha inayotolewa. Kwanza ni kweli kabisa lazima tukubaliane kwamba, tunataka kupata misamaha katika maeneo mbalimbali, lakini pia tunataka kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuhakikisha kwamba, misamaha yetu isizidi asilimia moja ya Pato la Taifa, hapo itatuwezesha kwenda vizuri zaidi na misamaha inayotolewa pia ni lazima iwanufaishe walengwa.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani kwenye hotuba tu ya bajeti mnasema tumesamehe hili, tumesamehe hili, tumesamehe hili, lakini hakuna siku unaelezwa hiyo misamaha uliyoitoa imemnufaisha nani? Walengwa waliolengwa kwenye huo msamaha wamenufaika? Lakini Taifa pia limenufaika nini na msamaha unaotolewa? Kwa sababu, ni lazima tuwe na misamaha ambayo tunaweza kuipima na misamaha ambayo kweli tunathibitisha kwamba, huu msamaha tumeutoa kwa sababu hii. Sasa mwisho wa siku unaweza ukawa na misamaha ya kufurahisha watu tu, anapewa msamaha mwisho wa siku bidhaa mliyotegemea itashuka bei haikushuka bei, mnategemea kwamba, wananchi wale watanufaika kutokana na misamaha iliyotolewa na Bunge lao mwisho wa siku bei hazikushuka, sasa mnakuwa na misamaha ambayo ni ya kufurahisha kundi la watu, misamaha ambayo ni ya kufurahisha baadhi ya makampuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo mwaka jana katika bajeti hii ya mwaka 2021/2022 hapa tulipitisha tukasema kwamba, basi tukawatoze wale wakulima wa shairi Withholding Tax ya asilimia mbili, lakini wale wanywa pombe tuwasamehe kodi, matokeo yake hata wanywa pombe wenyewe pombe haikushuka bei pamoja na ile pombe inayotengenezwa kwa kutumia shairi na yenyewe haikushuka bei, kwa hiyo, unakuwa ni msamaha ambao umetolewa kufurahisha kundi la watu. Ni lazima kwamba, misamaha hii inayotolewa iwe focused na iwe kweli kwa manufaa ya Taifa. Tukiyazingatia haya na tukayafanya kwa usahihi na kwa ushirikiano mkubwa tunaweza kupiga hatua mbele sana katika Taifa letu tukakusanya mapato mengi ya kutosha lakini na kuliwezesha Taifa letu kupiga hatua.

Mheshimiwa Spika, nimalizie tena kwa kusema naishukuru sana Serikali, nashukuru sana Waziri wa Fedha kwa kuwa msikivu sana. Daktari wa Uchumi kijana ambaye anafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja na kuwahakikishia Wajumbe kwamba, Muswada tumeuchambua vizuri sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu wa Mwaka 2022
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa ili nami niweze kuchangia haya mabadiliko ya Sheria ya Anti-Money Laundering Amendment Act ya Mwaka 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangulie kuipongeza sana Serikali kwa ushirikiano mkubwa iliyotupa na kwa kukubali ushauri wa Wabunge, kwamba takriban maeneo yote tulikubaliana, na hizi pongezi zimfikie Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa Serikali yake ni sikivu na imewasikiliza sana Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Makamu Mwenyekiti amewasilisha hapa Taarifa ya Kamati, tulifanya mapitio. Kwa mfano ukiangalia ibara ya 12 ambayo ilifanya marekebisho katika sheria Ibara ya 15 ambako adhabu zilikuwa zimeainishwa kwamba zitatajwa tu kwenye kanuni, lakini tukasema hapana, hatuwezi kutunga sheria ambayo hahitaji adhabu na badala yake adhabu zimewekwa kwenye kanuni. Kwa hiyo Serikali ikakubali na wote tukakubaliana na sasa adhabu zimewekwa kwenye sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine ya pili ni hii Ibara ya 35 ya Muswada ambapo hapa hapakuwa na tofauti ya matendo makubwa na matendo madogo, ikaonekana kwamba huenda hata matendo madogo tu yakaingia kwenye ugaidi, kwa hiyo hii nchi ingekuwa kwenye shida kubwa kwa sababu tungeanza tu kutuhumiana ugaidi, mtu amefanya jambo dogo unamtisha tu basi gaidi. Kwa hiyo tukakubaliana na Serikali ikafanya marekebisho na marekebisho hayo sasa kwa jedwali ambalo limewasilishwa na Serikali kwa kuweka neno seriously, kwa hiyo tayari makosa yale madogo yote tutakuwa tumeyaondoa kwenye ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la pili ni hili suala la kutangazwa kuwa gaidi. Sheria ikampa Waziri kutangaza mtu yeyote anaweza kutangazwa kuwa gaidi. Hii nayo ilikuwa na changamoto kubwa kwa sababu ingefika mahali unatangazwa tu kuwa gaidi; lakini nchi yetu hatujawahi kuwa na gaidi ambaye yuko mitaani. Magaidi wote wanaoshukiwa kuwa magaidi wanatumikia jela na wengine wako chini ya vyombo vya dola. Kwa hiyo ndiyo maana tukakubaliana na Serikali ikakubaliana na ushauri wa Kamati kwamba sasa haya mambo mtu atakayetangazwa na Waziri ni yule tu ambaye atabainika kwamba anatafutwa (wanted) akamatwe ili afikishwe kwenye vyombo vya dola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni kwamba, yeye tayari anakwepa kukamatwa ili kufikishwa mahakamani na kwenye mikono ya dola. Kwa hiyo baada ya kufanya marekebisho hayo, hakuna tena wasiwasi wa mtu yeyote kutangazwa kuwa gaidi katika nchi yetu na nchi hii itaendelea kufanya shughuli za kimaendeleo bila tatizo lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Tanzania, pamoja na nchi yetu kuwa chini ya uangalizi wa Financial Action Task Force (FATF) na ESAAMLG kwamba sisi tumekuwa na mifumo ya fedha hatarishi, lakini changamoto kubwa iliyoko katika sheria hii ni Serikali kuleta marekebisho badala ya kuileta sheria yote. Ukweli ni kwamba sheria hii ya Anti- Money Laundering ilitakiwa iletwe yote ili tuweze kuijadili yote kwa pamoja, lakini badala yake sasa hivi imeletwa sehemu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuletwa sehemu ya Sheria hii kunasababisha baadhi ya vifungu ambavyo vilipaswa vifanyiwe marekebisho visiweze kufanyiwa marekebisho. Kwa mfano, ukienda Ibara ya Nne ya Sheria hii ambayo ni establishment of Financial Intelligence Unit (FIU), hii FIU iko chini ya Wizara ya Fedha mpaka sasa hivi tunavyozungumza, ni idara tu. Taasisi inayoshughulika na mambo makubwa haya ambayo leo tunaipa jukumu la kuhangaika na utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi, ufadhili wa silaha za maangamizi, lakini ni idara tu chini ya Wizara ya Fedha. Kitengo hiki kikiendelea kuwa hapo hakitakuwa na nguvu ya kiutendaji na ya kisheria ya kuweza kuchukua hatua stahiki katika mambo haya inayoyasimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa taasisi tunaweza kusema ni sawa na dawati tu, tunaweza kusema ni sawa tu na eneo la kupokelea taarifa, tunaweza tukasema kwamba haina nguvu yoyote ile ya kuiwezesha kusimamia majukumu yake ya kisheria, ni kama baraza la wazee. Sasa kama tutaendelea namna hii hatuwezi kuleta mageuzi tunayoyatarajia, hata haya mabadiliko ambayo tunayazungumza hapa hayawezi kuleta tija katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kinachoshauriwa, hii FIU inashauriwa iwe Wakala chini ya Wizara ya Fedha. Iwe na uwezo wa kushtaki na kushtakiwa, iwe na uwezo wa kuchukua hatua. Leo tunaenda kuwaweka watoa taarifa wengi tu, takriban ishirini na kitu; hao watoa taarifa watatoa taarifa wapi? Watatoa taaarifa kwenye mamlaka ambayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika mbili tu.

MWENYEKITI: Malizia dakika moja.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa na uwezo. Leo tunaiongezea mamlaka ya watoa taarifa ili iweze kuwawajibisha, walete taarifa ili iweze kuchukua hatua, lakini haina nguvu, ni idara tu. Sasa ikiendelea kuwa idara namna hii hatuwezi kupata tija. Idara hii tuifanye kuwa Wakala wa Serikali na wenzetu kama Wakenya wao wanaita Financial Reporting Center, ni mamlaka kamili, ina nguvu kubwa kisheria. Sasa na sisi hapa tuweke hayo maamuzi ili tupate hiyo nguvu ya kisheria na haya tunayoyatarajia tutaweza kuyapata. Ahsante sana. (Makofi)