Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni (1 total)

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake na kama alivyosema kwamba nafuatilia, ni kweli nimefuatilia hii fedha imeshafika huko Busega na imeshafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri kasema kwamba, makusanyo yanazidi kuimarika na kwa kuwa, Busega ni moja ya Wilaya ambazo ni mpya na miundombinu bado ina matatizo hususan barabara. Barabara ya Mwamanyiri kwenda Badugu, Barabara ya Kisamba – Nyaruhande – Nyangiri na Barabara ya Mkula – Kijereshi – Lamadi. Je, kwa kuwa, makusanyo yanaimarika; Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa barabara hizi sasa zinaboreshwa ili ziende sambamba na bajeti jinsi inavyoimarika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, Mikoa Mipya ikiwemo Simiyu, Katavi, Geita, Njombe na Mkoa mpya wa Songwe, ina matatizo sana ya miundombinu na kwa kuwa, bajeti ambazo zimekuwa zikitengwa za Mikoa mama ni kubwa kuliko bajeti za mikoa mipya. Je, Serikali haioni kuna haja sasa kwa mikoa mipya hii na wilaya nyingine mpya zipewe kipaumbele cha kibajeti ili zipate mafungu ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri kwamba, hivi sasa kwa dhamira tuliyonayo kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano, nafurahi sana kufanya kazi katika Wizara hii. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, lazima tuimarishe barabara zote, hizi ambazo amezisema Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni na nyingine zote za wilaya zote na halmashauri zote Tanzania nzima. Tuna dhamira hiyo na naamini tutafikia malengo haya kwa namna tulivyodhamiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la Mikoa mipya, naomba nichukue nafasi hii kuielekeza Bodi ya Barabara Nchini pamoja na TANROAD kuangalia kwa makini sana wanavyoweka migawo ya fedha za matengenezo. Wazingatie mahitaji mahsusi yaliyoko katika mikoa hii ambayo Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni, Mbunge wa Busega, ameitaja pamoja na mikoa mingine ambayo nayo ina mazingira mahsusi kwa maana ya mazingira magumu ya usafiri.