Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni (14 total)

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Fedha za Mfuko wa Barabara zimekuwa zikisuasua sana:-
Je, Wilaya ya Busega imetengewa kiasi gani kwa mwaka huu wa fedha ili zitumike kutengeneza miundombinu ya barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Mwaka wa Fedha 2014/2015, Fedha za Mfuko wa Barabara zilikuwa hazitolewi kama ilivyotarajiwa kutokana na hali ya makusanyo kutoka vyanzo mbalimbali vya Mfuko kutokuwa vya kuridhisha, lakini hali hiyo imebadilika na kuimarika katika mwaka wa fedha wa 2015/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi mwisho wa mwezi Machi, 2016 kiasi cha shilingi bilioni 462.789 sawa na asilimia 53.4 ya Bajeti ya Mfuko wa Barabara ya shilingi bilioni 866.63 ilikuwa imeshapokelewa na Bodi ya Mfuko wa Barabara na kupelekwa kwa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Halmashauri zote nchini. Tunatarajia kwamba, hadi kufikia Juni, 2016 fedha zote za Mfuko wa Barabara zilizopangwa kugharamia kazi za matengenezo na ukarabati wa barabara katika bajeti ya mwaka 2015/2016, zitakuwa zimepokelewa na kupelekwa Wakala wa Barabara na Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2015/2016, Halmashauri ya Wilaya ya Busega imetengewa jumla ya shilingi milioni 570.38 na hadi mwisho wa mwezi Machi, 2016 kiasi cha shilingi milioni 432.63 sawa na asilimia 75.9 ya bajeti hiyo, ilikuwa imeshapelekwa Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Chegeni kwa kufuatilia kwa karibu masuala ya barabara katika Jimbo lake na kumwomba aendelee kufuatilia ili kujiridhisha kwamba fedha za Mfuko wa Barabara zinatumika vizuri na kwa malengo yaliyopangwa na Halmashauri ya Busega.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Chegeni, swali la nyongeza.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Mradi wa REA II ulitarajia kuvipatia umeme vijiji vyote vya Jimbo la Busega na kumekuwepo na kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo jimboni humo:-
(a) Je, mpaka sasa ni vijiji vingapi vimepatiwa umeme kupitia mradi huo?
(b) Je, ni lini vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya vijiji 13 vimepatiwa umeme katika Jimbo la Busega kupitia mradi kabambe wa REA Awamu ya II unaoendelea kutekelezwa hivi sasa. Mradi huu utakamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016 ambapo vijiji vyote 18 vitapatiwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme Wilaya ya Busega inayotekelezwa na Mkandarasi Sengerema Engineering Group inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 91.6; ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 52; ufungaji wa transfoma 33 za ukubwa mbalimbali pamoja na kuwaunganishia umeme wateja 932.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi umekamilika kwa asilimia 94 ambapo ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 umekamilika kwa asilimia 97; ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 0.4 umekamilika kwa asilimia 93 na transfoma 18 zimefungwa. Wateja 420 wameunganishiwa umeme. Kazi hii itagharimu jumla ya shilingi bilioni 4.88.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji ambavyo havikujumuishwa katika mradi kabambe wa REA Awamu ya II vitapatiwa umeme katika Mradi wa REA Awamu ya III utakaoanza mwezi Julai, 2016. Kazi ya kupeleka umeme katika maeneo hayo itajumuisha ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 68; ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 198; na ufungaji wa transfoma 19 za ukubwa mbalimbali. Pamoja na kazi hizo pia wateja 6,096 wataunganishiwa umeme. Kazi hii itagharimu shilingi bilioni 8.6.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Wilaya za Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu unaanzia Wilaya ya Busega na tayari mipango pamoja na fedha ya kuanza kutekeleza mradi imeshapatikana:-
Je, lini Serikali itaanza kutekeleza mradi huo muhimu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa maji safi kutoka Ziwa Victoria kwenda Mkoa wa Simiyu katika Miji Mikuu ya Wilaya za Bariadi, Maswa, Meatu, Itilima na Busega pamoja na vijiji vilivyopo umbali wa kilomita 12, kando ya bomba kuu. Tayari Mtaalam Mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu na uandaaji wa mkabrasha ya zabuni ameajiriwa. Gharama za utekelezaji wa mradi mzima zinakadiriwa kuwa kiasi cha Euro milioni 313 na mradi huu utatekelezwa katika awamu mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza itagharimu kiasi cha Euro milioni 105 na itahusisha kufikisha maji katika miji mikuu ya Wilaya za Bariadi, Itilima na Busega pamoja na vijiji vilivyo kando ya bomba kuu. Hadi hivi sasa Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya KFW imechangia kiasi cha Euro milioni 25 na kiasi kilichobaki cha Euro milioni 80 kinatarajiwa kupatikana kutoka Mfuko wa Green Climate Fund.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka 2016/2017 na utachukua miaka miwili hadi kukamilika. Kwa sasa mtaalam mshauri anaendelea kufanya usanifu wa tathmini ya athari za kimazingira na kijamii katika maeneo ya mradi huo. Kazi hiyo itakamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya pili ya mradi itafikisha maji katika Miji ya Mwanhuzi na Maswa kwa gharama ya Euro milioni 208. Fedha hizi pia zinatarajiwa kutoka Green Climate Fund. Miradi hii ikikamilika, inatarajiwa kunufaisha watu zaidi ya 834,204.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Kuendelea kuwepo kwa uvuvi haramu kunatokana na Serikali kutochukua hatua stahiki kwa wanaofanya vitendo hivyo, hasa watengenezaji na wauzaji wa nyavu haramu, badala yake wanabebeshwa lawama wavuvi peke yao:-
Je, Serikali itakomesha lini tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa lipo tatizo kubwa la uvuvi haramu hapa nchini. Katika kudhibiti uvuvi haramu hapa nchini, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hili kwa kutoa elimu kwa wadau wanaochangia kuendelea kuwepo kwa uvuvi haramu wakiwemo wenye maduka yanayouza nyavu na zana haramu, wasuka nyavu zenye macho madogo na makokoro, wauzaji wa mabomu , ndoano na zana nyingine zinazozuiliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeendelea kufanya doria za kudhibiti uvuvi haramu na kaguzi kwenye maduka yanayouza zana za uvuvi ili kubaini uwezo wa zana haramu kupitia vituo 25 vya doria vilivyoanzishwa Kwenye maziwa makubwa, mwambao wa Bahari ya Hindi na mipaka ya nchi.
Vile vile kwa kushirikiana na Halmashauri, elimu kuhusu madhara ya uvuvi haramu imeendelea kutolewa kwa wadau mbalimbali wakiwemo wavuvi, watendaji wanaohusika na Ushuru wa Forodha mipakani ili kuwa na juhudi za pamoja za kudhibiti biashara ya zana haramu na kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi kupitia vyombo vya habari na maonesho ya Kitaifa yakiwemo Siku ya Wakulima (Nane Nane) na Siku ya Mvuvi Duniani ambayo hufanyika tarehe 21 Novemba kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ushirikishwaji wa jamii za wavuvi katika kusimamia rasilimali za uvuvi unafanyika kupitia vikundi vya usimamizi wa rasilimali za uvuvi (Beach Management Units) 754 vilivyoanzishwa katika maeneo mbalimbali. Pia vipindi mbalimbali vya televisheni na redio vimeandaliwa ili kuonesha madhara ya uvuvi haramu na vitaanza kurushwa hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hatua hizo, Serikali ikishirikiana na Idara ya Mahakama inaendesha zoezi la Mobile Court ili kuharakisha mashauri ya wavuvi haramu mara wanapokamatwa. Utaratibu huu umeelekezwa uanze kutumika kwenye maeneo yote yenye kukithiri katika uvuvi haramu na vyombo vyote vya dola vinapaswa kutoa ushirikiano stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu nawaomba Waheshimiwa Wabunge ambao ni Wajumbe katika Mabaraza ya Madiwani wazielekeze Halmashauri, Kata, Vijiji na Mitaa kudhibiti uvuvi haramu kwenye maeneo yao na wananchi kutoa taarifa za wavuvi haramu kwa vyombo vya dola ili hatua stahiki zichukuliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Halmashauri zote nchini zielimishe jamii za wavuvi na wadau wengine kuhusu madhara ya uvuvi haramu ili kusimamia rasilimali za uvuvi na kuwa na uvuvi endelevu kwa ajili ya kuwapatia wananchi ajira, chakula, kipato na mapato kwa Taifa kwa ujumla. Ni kwa njia hii Taifa litaweza kudhibiti uvuvi haramu hapa nchini.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA (K.n.y. MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI) Aliuliza:-
Kumekuwa na ahadi ya kujenga upya Gati la Nyamikoma – Busega ili kuboresha usafirishaji wa mizigo na mazao ya samaki katika Ziwa Victoria:-
Je, ni lini utengenezaji huo utaanza na kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Gati la Nyamikoma utaanza mara tu baada ya ramani zitakazotoa taarifa za kijiografia (Geographical Information System - GIS) kwa bandari na magati katika mwambao wote wa Maziwa Makuu kukamilika na kuthibitika kuwa eneo hilo la Nyamikoma linafaa kujengwa gati. Ramani hizo zinatarajiwa kukamilika Oktoba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wataalam wanaoendelea na ukusanyaji wa taarifa za kijiografia.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Mji mdogo wa Lamadi kwa muda mrefu umeidhinishwa kuwa Halmashauri ya Mji Mdogo:- Je, lini sasa utekelezaji wake utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mwaka 2016 Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilipokea maombi ya kupandisha hadhi Mji wa Lamadi kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lamadi. Mwezi Agosti, 2016, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilifanya uhakiki wa vigezo na taratibu zilizopo kwa mujibu wa sheria zoezi ambalo lilifanyika sambamba na maeneo mengine hapa nchini. Tathmini imeonesha kwamba kuna mambo ya msingi yanayotakiwa kukamilishwa yakiwemo kuwa na mpango wa uendelezaji wa mji huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna miji midogo mingi inayochipua, Serikali inaendelea na mazungumzo na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) ambalo limeonesha nia ya kusaidia utekelezaji wa mpango huo ambao utawezesha kupima na kuweka miundombinu ya barabara na maji katika miji inayochipua ikiwemo Lamadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pindi baadhi ya vigezo vikikamilika, Serikali haitasita kuupandisha hadhi Mji Mdogo wa Lamadi kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lamadi.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja ya kurekebisha Road Licence au ifutwe ili ukusanyaji wa kodi hii uendane na matumizi halisi ya vyombo vya moto vya barabarani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphel Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ada ya mwaka ya magari inatozwa kwa wamiliki wa vyombo vya moto kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ambapo mmiliki wa chombo cha moto hutakiwa kulipa ada ya kila mwaka kuanzia tarehe ya mwezi ya kwanza ambao chombo kilisajiliwa. Ada hii inatozwa kulingana na ukubwa wa injini ya chombo husika. Msingi wa tozo hii ni umiliki wa chombo na siyo matumizi ya chombo barabarani. Hivyo basi, mmiliki wa chombo hutakiwa kulipa ada hiyo bila kujali kama chombo kimetumika katika mwaka husika au hakijatumika.
Mheshimiwa Spika, ada ya mwaka ya umiliki wa chombo cha moto inaweza kusitishwa kulipwa endapo mmiliki wa chombo cha moto atatoa taarifa kwa Kamishna wa Kodi na kuthibitishwa kuwa chombo hicho cha moto hakitumiki tena kutokana na sababu mbalimbali kama ajali ya barabarani, moto au uchakavu. Taarifa hizo za chombo husika zitawezesha chombo kufutwa (deregistered) kwenye kumbukumbu za mamalaka na ada hiyo itasitishwa kutozwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea mapendekezo na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Chegeni wakitaka ada hii ifutwe au ilipwe kulingana na matumizi ya chombo cha moto.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itafanya mapitio ya sheria na kanuni ya umiliki na matumizi ya vyombo vya moto ili kupata njia bora zaidi ya kukusanya ada hii, hivyo basi ada hii kwa sasa itaendelea kulipwa kwa utaratibu uliopo.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Mafao ya wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mashirika mengi ya Hifadhi ya Jamii yamekuwa na utata kuhusu fao la kujitoa. Je, Serikali inatoa tamko gani ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuunganisha mifuko hiyo na kuondoa mkanganyiko kwa wanachama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 102 wa mwaka 1952, fao la kujitoa sio miongoni mwa mafao yaliyoainishwa katika mkataba huo. Kwa hapa Tanzania fao la kujitoa ni utaratibu wa wanachama kujitoa na kuchukua mafao yako katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inayotoa mafao ya pensheni kabla ya kufikisha umri wa kustaafu. Utaratibu huu umezoeleka miongoni mwa wanachama wa mifuko hiyo na hata kuonekana ni mojawapo ya mafao ya hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua changamoto ya kipato inayowakabili wafanyakazi wale wanaopoteza ajira, Serikali itawasilisha Bungeni mapendekezo ya marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii yatakayoanzisha fao la upotevu wa ajira (unemployment benefit) kwa wafanyakazi watakaokuwa wanapoteza ajira kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kazi. Fao hili litakuwa linatolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inayotoa mafao ya pensheni.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya wingi wa mifuko inayoikabili Sekta ya Hifadhi ya Jamii. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, mwaka 2015 Serikali ilifanya tathmini ya mifuko yote ya pensheni kwa lengo la kuangalia uwezekano na namna bora ya kuiunganisha. Matokeo ya tathmini hiyo yalionesha kuwa inawezekana kuunganisha mifuko hiyo na kubaki na michache kwa kuzingatia hali halisi ya mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na matokeo ya tathmini hiyo, Serikali imeandaa mapendekezo ya kuunganisha mifuko mitano inayotoa mafao ya pensheni na kubaki na michache iliyo imara. Mapendekezo hayo yameshajadiliwa na wadau wa kukubaliwa. Hatua inayoendelea hivi sasa ni kuwasilisha mapendekezo hayo katika vikao maalum vya Serikali ili Serikali itoe kibali. Matokeo ya kuunganisha mifuko hiyo ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji, kuboresha mafao na kuifanya mifuko kufanya kazi kwa ufanisi na kwa uendelevu katika kipindi cha muda mrefu ujao.
MHE.DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Migogoro ya ardhi na mipaka ya vijiji na hifadhi bado imeendelea kuwa tatizo sugu licha ya kuwepo kwa ahadi na kauli mbalimbali na Serikali.
Je, mgogoro wa Pori la Akiba Kijereshi na Sayanka katika Wilaya ya Busega utatatuliwa lini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba la Kijereshi lenye ukubwa wa kilometa za mraba 65.7 ililtangazwa rasmi na tangazo la Serikali Na. 215 la mwaka 1994. Pori hilo lilikabidhiwa rasmi kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori mwaka 2005 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Pori la Akiba la Kijereshi limepakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa upande wa Kaskazini na Kijiji cha Lukungu upande wa Mashariki, Mwamalole, Mwakiroba, Kijilishi, Igwata na Muungano upande wa Kusini Mashariki mwa pori hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, uvamizi wa mapori haya ya akiba kwa kilimo, makazi na ufugaji umesababisha ongezeko la matukio ya wanyamapori kuharibu mazao na kudhuru wananchi. Aidha, hali hii imesababisha migogoro baina ya wananchi na mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua migogoro kati ya wakulima, wafugaji na maeneo ya hifadhi nchini Serikali imechukua hatua mbalimbali. Wizara kwa kushirikiana na wananchi imetambua na kuweka mipaka kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo Pori la Akiba la Kijereshi na Hifadhi ya Msitu wa Sayanka. Hadi mwisho wa Januari, 2018 jumla ya vigingi 74 vimesimikwa katika pori la Akiba Kijereshi, Aidha, katika Hifadhi ya Msitu wa Sayanka jumla ya vigingi 67 vimesimikwa, hatua hii imesaidia kupunguza migogoro ya mipaka kati ya wananchi na hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tatizo lililobaki kwa sasa ni baadhi ya wananchi kutaka kulima na kuanzisha makazi ndani ya Hifadhi ya Misitu ya Sayanka na wengine kutaka kulima ndani ya mita 500 kutoka mpaka wa Pori la Akiba la Kijereshi kinyume cha Sheria ya Misitu na Wanyamapori.
Wizara kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega na Halmashauri ya Wilaya ya Busega inaendelea kutoa elimu na kufanya vikao na mikutano na wananchi wanaozunguka Pori la Akiba Kijereshi. Mikutano hiyo inalenga kuwakumbusha wananchi umuhimu wa uhifadhi na kuepusha kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 500 kutoka mpaka wa pori la Akiba. Katazo hilo ni kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009. Aidha, Serikali inatoa wito kwa wananchi kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi ili kudumisha uwepo wa bioanuai kwa faida yetu ya sasa na vizazi vijavyo. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Vijiji vya Nyakaboja, Kabita, Chumve, Kalemela, Kalago, Badugu na Nyaluhande vimepitiwa na nguzo na nyaya za umeme, lakini wananchi hao hawana huduma ya umeme:-
Je, ni lini Serikali itawapatia umeme wananchi wa maeneo hayo ili wasiendelee kuwa walinzi wa nguzo za TANESCO?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Busega ina Vijiji 59, kati ya vijiji hivyo vijiji 18 vimepatiwa umeme kupitia miradi ya Electricity V na REA Awamu ya II. Kijiji cha Kalemela kilipatiwa umeme kupitia REA Awamu ya Kwanza. Kijiji cha Badugu kimepatiwa umeme kupitia mradi wa Electricity V na baadhi ya maeneo ya Kijiji cha Nyaluhande vimepitiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Kabita, Nyakaboja na Kalago vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza ambao utekelezaji wake umekwishaanza kupitia Mkandarasi White City Guangdong JV Limited. Kazi za mradi wa kupeleka umeme katika Wilaya ya Busega zinajumuisha ujenzi wa kilometa 49.7 za njia ya umeme, msongo wa kilovoti 33, kilometa 116 za njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4, ufungaji wa transforma 58 na kuunganisha wateja wa awali 1,783. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 5.5. Mradi unatarajiwa kukamilika Julai, 2019.
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Chumve pamoja na vijiji vingine vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DKT. RAPHAEL M.CHEGENI aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwepo na migogoro mingi kati ya Hifadhi za Taifa na wananchi ambao ni wakulima na wafugaji hali inayosababisha uvunjifu wa amani:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa tatizo hili linapata ufumbuzi endelevu hasa maeneo ya Lamadi, Makiloba, Kijereshi na Nyamikoma katika Wilaya ya Busega?
(b) Baadhi ya wanyama kama tembo wamekuwa wakifanya uharibifu wa mali na mazao ya wananchi wanaoishi maeneo hayo. Je, Serikali inatoa tamko gani la kuzuia tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Lamadi, Mwakiloba, Nyamikoma na Kigereshi yanapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la Akiba la Kijereshi, hivyo kuna muingiliano kati ya wanyama pori na binadamu jambo linalosababisha migogoro. Aidha, maeneo yaliyohifadhiwa yanakabiliwa na changomoto nyingi ikiwemo uvamizi unaotokana na shughuli za kibinadamu kama kilimo na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kumaliza tatizo la migogoro ya mipaka, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wananchi na wadau wengine, inayo nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba migogoro kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi inatatuliwa. Kazi hii inahusisha kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi, kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi, kuimarisha miradi ya ujirani mwema na kupitia upya mipaka iliyopo katika maeneo yenye migogoro. Kazi ya kupitia mipaka na kuweka vigingi kwa sasa itaendelea kwa ushirikishwaji wa wadau wote muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na madhara yanayosababishwa na wanyamapori hususan tembo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kunusuru maisha na mali za wananchi waishio kando ya Hifadhi ya Serengeti na Pori la Akiba la Kijereshi kama vile kuimarisha Timu ya Udhibiti wa Wanyamapori Hatari na Waharibifu ambao inajumuisha watumishi kutoka Kikosi dhidi ya Ujangili Bunda, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba Kigereshi na Halmashauri ya Wilaya, pia kwa kutumia ndege zisizo kuwa na rubani kwa ajili ya kufukuza tembo. Lengo ni kuhakikisha kwamba tukio lolote la uvamizi wa tembo linashughulikiwa kwa haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea kusizitiza kuhusu umuhimu wa kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu kwenye shoroba za wanyamapori na maeneo ya mipaka ya hifadhi ya vijiji. Aidha, Wizara imeandaa kanuni za kutenga na kuhifadhi shoroba na maeneo ya mtawanyiko ili kuruhusu mwingiliano wa kiikolojia kati ya wanyamapori utakaoimarisha utofauti wa vinasaba pamoja na kuboresha ustawi endelevu wa bioanuai.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI) aliuliza:-

Kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na kuongeza uwekezaji kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa vikwazo vinavyoathiri dhana hiyo vinaondolewa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Jimbo la Busega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Dira ya Taifa ya mwaka 2025 ni kuifanya Tanzania kuwa Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ili kutimiza dhamira hiyo tunatekeleza mipango mitatu ya maendeleo ya miaka mitano mitano ambayo imeainisha vipaumbele vya Taifa kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Kwa sasa Serikali inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa kipindi cha 2016/2017 hadi kufikia mwaka 2020/ 2021 ambao kipaumbele chake ni ujenzi wa uchumi wa viwanda. Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha vikwazo vinavyoathiri uwekezaji na biashara nchini vinaondolewa kwa kuweka miundombinu muhimu na mazingira ya kisera, kisheria, kanuni na kiutendaji ambao ni wezeshi kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha miundombinu wezeshi kama vile ujenzi wa reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari, umeme na maji hatua ambayo inapunguza gharama za uendeshaji wa biashara na uwekezaji na kuleta wepesi katika uwekezaji na biashara. Aidha, Serikali imeimarisha upatikanaji wa ardhi ambapo Mamlaka za Upangaji Miji zimeelekezwa kuzingatia utengaji wa asilimia 10 ya kila aneo la Mpango Kabambe wa Mji kwa ajili ya uwekezaji wa biashara na viwanda. Vilevile Serikali inaendelea kuendeleza Maeneo Maalum ya Uwekezaji au Special Economic Zones ili kuwezesha upatikanaji wa maeneo ya uzalishaji yenye miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imeendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira bora ya uwekezaji kwa kutekeleza programu za kuboresha mazingira ya uwekezaji na hii ni pamoja na mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa mazingira ya biashara nchini au Blueprint. Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano na majadiliano na Sekta binafsi kupitia Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) pamoja na mikutano ya wadau wa Sekta mbalimbali kwa ngazi za Kitaifa, Mikoa na Wilaya ambapo changamoto zinazobainishwa zinapatiwa ufumbuzi.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-

Je ni nini maana ya dhana ya uchumi kukua ukioanisha na maisha ya wananchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali Ia Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, dhana ya uchumi kukua ikioanishwa na maisha ya wananchi inaweza kutafsiriwa katika dhana kuu mbili. Dhana ya kwanza ni kwa kuangalia upatikanaji, ubora na gharama ya huduma za jamii zinazotolewa na Serikali. Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na elimu, afya, maji, umeme na miundombinu ya usafiri na usafirishaji. Mathalani, kutokana na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, muda na gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa zimepungua, sambamba na gharama za matengenezo ya vyombo vya usafiri na usafirishaji. Aidha, upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi umepunguza kwa kiasi kikubwa adha na gharama ya matibabu kwa wananchi. Pia, ugharamiaji wa elimu msingi bila malipo na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ni miongoni mwa matokeo ya kukua kwa uchumi. Kwa muktadha huu, ni muhimu kutafsiri dhana ya ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi kwa kuangalia kiwango cha upatikanaji, ubora na gharama za huduma muhimu za jamii zinazotolewa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, dhana ya pili ya kutafsiri ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi ni ushiriki wa wananchi wenyewe katika shughuli za kiuchumi. Ukuaji wa uchumi ni matokeo ya wananchi kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za uzalishaji mali na huduma. Wananchi wanaoshiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kiuchumi hufikiwa moja kwa moja na matokeo chanya ya ukuaji wa uchumi ikilinganishwa na wale ambao wapo nje ya mfumo wa uzalishaji. Aidha, wananchi wanaoshiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kiuchumi wananufaika kwa tafsiri ya dhana zote mbili; yaani kupitia huduma za jamii zinazotolewa na Serikali yao pamoja na matokeo ya moja kwa moja ya shughuli wanazofanya.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kufanya jitihada za dhati kabisa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara, ili kila Mtanzania aweze kutumia kikamilifu fursa zilizopo kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na huduma. Miongoni mwa hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara Nchini. Lengo ni kuhakikisha kwamba, tunapunguza kwa sehemu kubwa gharama za uwekezaji na kufanya biashara ili kuvutia wawekezaji mahiri katika sekta mbalimbali, hususan viwanda vinavyotumia malighafi za ndani. Ni matarajio ya Serikali yetu kuwa, uwekezaji katika viwanda utaongeza ajira na uzalishaji katika Sekta ya Kilimo, sekta ambayo huajiri idadi kubwa ya watu hapa nchini, lakini imekuwa ikikua kwa kasi ndogo na hivyo kuwa na mchango mdogo katika kupunguza umaskini wa wananchi walio wengi, hususan wakulima.
MHE. LEAH J. KOMANYA (K.n.y. MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI) aliuliza:-

Ongezeko la tembo na wanyama waharibifu imekuwa kero kubwa sana kwa wananchi wanaoishi maeneo ya kando kando ya hifadhi na ziwa.

Je, Seikali ina mkakati wa kudhibiti tatizo linalosabishwa na kadhia hiyo?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali Mheshmiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni Mbunge wa Busega kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kanuni za wanyamapori wakali na waharibifu za mwaka 2011 zimeanisha aina wanyamapori ambao wanapaswa kushughulikiwa kama wanyamapori wakali na waharibifu. Kwa mujibu wa kanuni hizo, jedwali la tatu limeorodhesha wanayapori hao ambao ni tembo, kiboko, mamba, nyati, chui na simba.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati ifuatayo katika kunusuru maisha na mali za wananchi kutokana na madhara yanayosababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu:-

Mheshimiwa Spika, moja kufanya doria za udhibiti wa wanyamapori hatari na waharibifu, kupitia askari wa wanyamapori Tanzania, TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Halmashauri za Wilaya na Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro na wadau wengine. Lengo ni kuhakikisha kwamba tukio lolote la uvamizi wa wanyamapori wakali na waharibifu linashughulikiwa kwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, mbili kutumia mbinu na teknojia mbalimbali mfano kupanda pilipili na kutundika mizinga ya nyuki pembezoni mwa mashamba, kufunga vitambaa vyenye vilainishi vya magari yaani oil kuzungushia mashambani na kutumia ndege zisizokuwa na rubani kwa ajili ya kudhibiti tembo.

Mheshimiwa Spika, tatu kuendelea kutoa elimu za uhifadhi kwa jamii ili wananchi waepuke kulima kwenye maeneo ya shoraba.

Mheshimiwa Spika, wapo wanyamapori waharibifu ambao wanaweza kushughulikiwa na mkulima mmoja mmoja pamoja na Wizara ya Kilimo. Wanyamapori hao ni pamoja na nyani, ngedere, tumbili, nguruwepori na ndege aina ya kwelea kwelea na wengine. Aidha, Wizara intoa rai kwa Maafisa Ugani wa kilimo kushirikikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na wanyamapori jamii.