Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Andrew John Chenge (3 total)

MHE. ANDREW J. CHENGE aliuliza:-
Sera ya Serikali ni kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa kwa barabara za kiwango cha lami. Mkoa wa Simiyu haujaunganishwa na mikoa jirani ya Singida na Arusha.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara ya Bariadi – Kisesa – Mwanhuzi hadi Daraja la Mto Sibiti na hatimaye ijengwe kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshaanza juhudi za kuunganisha Mkoa wa Simiyu na Mikoa jirani ya Singida na Arusha kwa kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mchepuo wa kusini wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Serengeti Southern Bypass). Upembuzi yakinifu unajumuisha barabara ya Karatu – Sibiti kupitia Mbulu na Karatu kupitia Ziwa Eyasi hadi Sibiti – Mwanhuzi – Lalago hadi Maswa. Matokeo ya mapendekezo ya njia ipi ya kupita yatapatikana kazi hii itakapokamilika katika mwaka wa 2018. Kazi hii inafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo (KfW).
Aidha, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara ya Kolandoto Junction – Lalago – Mwanhuzi – Sibiti
– Oldean Junction (kilometa 328) umekamilika ikiwemo sehemu ya barabara kuu ya Ng’oboko – Mwanhuzi hadi daraja la Sibiti. Kazi hii imegharamiwa na Serikali ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Bariadi – Kisesa Mwanhuzi hadi daraja la Sibiti imegawanyika katika sehemu mbili kama ifuatavyo: sehemu ya kwanza ni barabara ya Mkoa wa Baliadi - Kisesa – Mwandoya hadi Ng’oboko yenye urefu wa kilometa 100.71 inavyoungana na barabara kuu ya Kolandoto – Lalago – Mwanhuzi hadi Daraja la Sibiti. Sehemu ya pili ni sehemu ya barabara kuu kuanzia Ng’oboko – Mwanhuzi hadi daraja la Sibiti yenye urefu wa kilometa 79.1.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa ujenzi wa daraja la mto Sibiti lenye urefu wa mita 82 pamoja na barabara unganishi (kilometa 25) unaendelea na unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Bariadi – Kisesa - Mwandoya – Ng’oboko (kilometa 105) pamoja na Sibiti – Mkalama – Nduguti – Iguguno hadi Singida (kilometa 103.54) ziko kwenye mpango mkakati wa miaka mitano kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hizo tajwa za usanifu zikikamilika, Serikali itatafuta fedha za kujenga barabara zote kwa kiwango cha lami kwa awamu na kulingana na upatikanaji wa fedha. Hivyo, Makao Makuu ya Mikoa ya Simiyu, Arusha na Singida yatakuwa yameunganishwa.
MHE. ANDREW J. CHENGE aliuliza:-
Katika miaka ya 1980 wanakijiji wa Kijiji cha Mwanchumu, Salaliya na Matongo walitoa maeneo yao kwa Serikali ili yatumike kwa shughuli za kilimo zilizokusudiwa na Gereza la Matongo lakini kwa sasa maeneo hayo hayatumiwi na Magereza kikamilifu.
Je, Serikali ipo tayari kurejesha eneo hilo ambalo halitumiki kikamilifu kwa wananchi wa vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Gereza la Matongo liko Mkoani Simiyu katika Wilaya ya Bariadi na lina ukubwa wa hekari 2472.62. Gereza hili lilianzishwa mwaka 1975 kwa kuchukua eneo lililokuwa la Mbunge wa zamani wa eneo hilo, Marehemu Edward Ng’wani ambapo alifidiwa eneo hilo kwa kupewa eneo lingine na Serikali. Aidha, wananchi wa Vijiji vya Mwanchumu, Salaliya kwa asili ni wahamiaji kutoka maeneo mengine na siyo wenyeji wa Matongo.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa Serikali iko kwenye mpango wa kuboresha kilimo kupitia Jeshi la Magereza kwa kuliwezesha kuzalisha chakula cha kutosheleza kulisha wafungwa na mahabusu. Eneo la Gereza la Matongo lipo kwenye orodha ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika kilimo cha mahindi, alizeti, pamba, ufugaji wa nyuki na mifugo pamoja na upandaji wa miti na uhifadhi wa mazingira.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitwa eneo hilo ili kuwezesha Magereza kuendeleza shughuli za urekebishaji wafungwa kwa kutumia kilimo cha ufugaji ambapo mazao mbalimbali ya kilimo hustawi. Kwa sasa eneo hilo limeshapimwa na taratibu za kufuatilia upatikanaji wa hati unaendelea.
Mheshimiwa Spika, kutokana na eneo hilo kuwa kwenye mpango mkakati wa Jeshi la Magereza wa kujitosheleza kwa chakula na shughuli nyingine, Serikali haina mpango wa kulirejesha eneo hilo kwa vijiji tajwa.
MHE. ANDREW J. CHENGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi yake ya kujenga barabara za Mji wa Bariadi kwa Kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa barabara katika Mji wa Bariadi kwa kiwango cha lami kwa kujenga barabara zenye urefuwa kilometa 7.76 kwa kiwango cha lami, njia za waenda kwa miguu kilometa 9.4, mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 10.11 na uwekaji wa taa 302 chini ya mradi wa uendelezaji miundombinu katika miji (Urban Local Governments Strengthening Project-ULGSP).

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara na madaraja katika Mji wa Bariadi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.