Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Elias John Kwandikwa (12 total)

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Napenda niulize maswali madogo mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kuna ng‟ombe 320 waliotaifishwa tarehe 08/2/2016 na kwa kuwa haieleweki hao ng‟ombe wameuzwa kwa nani, kiasi cha pesa kilichopatikana na kiko wapi.
Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatilia kwa kina ili na mimi niweze kujua hao ng‟ombe wameuzwa kwa nani na hicho kiasi kilichopatikana kimepelekwa wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa kwenye ziara yake Bukombe tarehe 2 mwezi wa nne alipofuatana na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo ili kuondoa changamoto hii ya suala la mifugo kuingia kwenye hifadhi alitoa agizo kwamba wafugaji watengewe maeneo kabla ya tarehe 15/06/2016. Je, utaratibu huo na zoezi hilo limefikia wapi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Elias Kwandikwa kwa kufuatilia kwa ukaribu suala hili na kwa kweli anastahili kuchaguliwa kuwa Mbunge wa eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na swali lake la pili la utaratibu ule, tumepanga kukutana na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili katika kipindi cha mwisho wa wiki hii kujadiliana utaratibu ambao tutaufuata kuhusu mambo haya ya ardhi. Tunategemea pia kumshirikisha Waziri wa Ardhi kwa sababu utengaji wa maeneo mengine ya malisho unaanzia kwenye Kamati za Vijiji za Matumizi Bora ya Ardhi ambapo jambo hilo halifanywi na Waziri wa Maliasili wala Waziri wa Kilimo. Kwa hiyo, kwenye utaratibu ule wa makundi ya mifugo ambayo yanatokana na vijiji yatatengwa maeneo ya vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu swali la kwanza, nimekuwa nikifuatilia hata mimi baada ya kuwa nimeambiwa na tuliongea pia na Waziri wa Maliasili, ni kweli sheria inakataza mifugo kuingia kwenye hifadhi na sisi Wabunge tuendelee kutoa elimu hiyo ya kuwaambia wananchi wasiingize mifugo kwenye hifadhi ama kwenye Mapori ya Akiba. Vilevile kumekuwepo na ukiukwaji wa sheria ya baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu kutumia fursa hiyo kama sehemu ya wao kujipatia kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata hizo taarifa kwamba baadhi ya mifugo ambayo imekuwa ikitaifishwa imekuwa ile ambayo wamiliki wake hawakuweza kuwapa fedha wale watu. Kwa hiyo, kwa wale ambao wanamalizana nao, kwa maana ya kutoa fedha wanaachiwa wanaondoka na mifugo. Hilo ni jambo ambalo liko kinyume cha sheria na taasisi zetu za Kiserikali ziendelee kufuatilia na iwachukulie hatua watu ambao wanapindisha sheria kwa manufaa yao binafsi kwa sababu wanaipaka matope Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wengine wamekuwa wakitaifisha mifugo kwa sababu tu wanaenda kuinunua wao wenyewe kwa bei ya kutupa. Hilo na lenyewe liko kinyume cha taratibu za kisheria. Sheria inatakiwa ifuatwe ili kuweza kuendesha nchi kwa utawala bora na wale wananchi wajione hawajaonewa bali wamekiuka sheria na sheria imechukua mkondo wake.
Kwa hiyo, sisi kama Wizara pamoja na Wizara ya Maliasili tutaendelea kutoa elimu lakini na kusimamia sheria ili haki iweze kutendeka.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu lakini nashukuru pia Serikali kwa msukumo wa kuimarisha mawasiliano. Nina swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa, iko minara ambayo imeshindikana kuihudumia muda wote kutokana na tatizo la barabara, katika Kata za Ulowa, Ushetu, Ubagwe, Bulumbwa, Ulewe, Nyankende wameshindwa kupeleka mafuta wakati wa mvua. Je, Serikali iko tayari kututengenezea madaraja ya katika maeneo ya Kasheshe na Karo ili mawasiliano yaweze kuimarika na huduma zingine kuendelea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara ni wajibu wetu vilevile pamoja na mawasiliano. Ninachoomba ni kumhakikishia matatizo ya barabara na hasa madaraja hayo mawili, daraja ya Karo na daraja la Kasheshe yatafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo na kwa nafasi hii namtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga afuatilie madaraja hayo mawili ili wajibu wetu kama Wizara wakutoa huduma ya mawasiliano pamoja na barabara uweze kutekelezwa kikamilifu katika eneo hilo la Ushetu.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa yapo mazungumzo yanayoendelea kwa ajili ya ujirani mwema kati ya mgodi na vijiji vinavyozunguka ikiwemo Kijiji cha Bugarama na kwa kuwa kijiji hiki kina shida ya maji na wana mpango wa kupata maji kupitia mgodi huu. Je, Serikali iko tayari kuratibu mazungumzao haya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kwamba Mgodi wa Bulyankulu umekuwa ukitoa pia huduma za jamii katika maeneo ya Ilogi, Kakora, Runguya na maeneo mengine lakini hivi karibuni mgodi umekuwa ukifanya mazungumzo na vijiji vya jirani na tumekuwa tukiendelea kuratibu shughuli za migodi pamoja na wananchi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari, itaendelea kuratibu mazungumzo mpaka suluhisho la wananchi kunufaika na mgodi huo zipatikane kama kawaida.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa Askari wa Wanyamapori ni wachache na kwa kuwa hifadhi zimekuwa zikiwatumia Askari wa Wanyamapori wa kujitolea kwa kufanya doria na kwa kuwa askari hawa wanapofanya kazi kama maeneo ya Kigosi kwenye mipaka ya Jimboni kwangu wamekuwa na utaratibu wa kufanya doria na kujilipa. Haoni sasa wakati umefika Serikali ichukue hatua kukomesha tatizo hili ili kuondoa migogoro kwa wafugaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Sheria ya Uhifadhi inatoa fursa ya wananchi kushiriki katika uhifadhi kwa kutumia vikundi vya kijamii pamoja na vikundi ambavyo vipo vijijini. Je, Serikali iko tayari kuweka msukumo wa aina yake ili kuhakikisha kwamba vikundi vya jamii ikiwepo sungusungu wanahusika katika uhifadhi ili kupunguza migogoro?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Askari wa Wanyamapori ni wachache lakini pia malipo yao na mishahara yao ni midogo sana. Kuanzia mwaka 2016/2017, Serikali italigeuza jeshi au askari hawa wa wanyamapori kuwa jeshi usu au paramilitary force ili kushughulikia ujuzi na uwezo wao, lakini pia kuangalia kwa undani mafao na mishahara yao ili wawe walinzi thabiti katika kulinda maliasili zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pia kwamba vikundi vya wananchi hata vikundi vya sungusungu vinaweza kulisaidia sana Jeshi la Wanayamapori katika kulinda na kuhifadhi maliasili zetu. Serikali imechukua wazo hili zuri na tutalifanyia kazi ili tuone ni jinsi gani vikundi hivi vinaweza kusaidiana na askari katika kuhifadhi mali zetu.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara hii inaunganisha Mikoa ya Katavi - Tabora na Mkoa wa Shinyanga ikianzia Mpanda – Ugala – Kaliua - Ulyankulu katika Jimbo langu la Ushetu na hadi Kahama Mjini; na kwa kuwa ipo katika mpango na kwa mwaka wa fedha 2016/2017 imetengewa fedha kwa ajili ya feasibility study na detailed design; na kwa kuwa barabara hii katika hatua za awali…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa fupisha swali lako tafadhali.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Kwa kuwa inasimamiwa na Meneja wa TANROAD, Mkoa wa Katavi; je, kwa nini Mameneja wa Mikoa mingine hawahusiki katika usimamizi na utaratibu huu ukatumika katika hatua za ujenzi wa lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Kwandikwa tukutane ofisini tulijadili kwa undani ili majibu ambayo tutampa yawe na uhakika na yatakayotekelezeka.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri sana nina swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, yapo maeneo machache viongozi hawa hawashirikishwi kikamilifu kutoa ushauri wa vifungu sahihi kwa matumizi kama ilivyoanishwa kwenye bajeti na kuathiri taarifa za fedha na kutekeleza hoja za ukaguzi. Je, Serikali iko tayari kutoa waraka, kusisitiza ushirikishwaji wa viongozi hawa wanaosimamia rasilimali fedha ili kuleta tija katika matumizi ya vifungu vya bajeti na kuboresha hesabu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia matumizi mbalimbali ya rasilimali fedha, lakini niendelee kukumbusha tu kwamba mamlaka za ajira pamoja na menejimenti katika taasisi zote za umma, zinatakiwa kuhakikisha kwamba zinatumia fedha za Serikali kwa mujibu wa taratibu pamoja na sheria mbalimbali za kifedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kusisitiza kwamba ni lazima waweze kushirikisha wakuu wote wa Vitengo, Wakuu wote wa Idara, katika menejimenti na vikao ili na wenyewe waweze kupata uelewa katika namna ambavyo mipango kazi ya taasisi inavyotekelezwa, pia waweze kutoa ushauri wao ni namna gani wanaweza kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao bila kuathiri taratibu mbalimbali za kifedha na sheria zinginezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Kwandikwa kwamba, kweli tuko tayari na baada ya kutoka tu hapa tutashauriana na Waziri wa Fedha ili kuona ni kwa namna gani sasa waraka unaweza ukaandaliwa, vilevile kwa upande wa utumishi kuweza kukumbushwa masuala haya.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana kwa kuniona ili na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mahitaji ya Jimbo la Msalala yanafanana kabisa na mahitaji ya Jimbo la Ushetu, na kwa kuwa maji haya ya Ziwa Victoria yamefikishwa Kahama Mjini na hayajawafikia kabisa wananchi wa Jimbo la Ushetu, je, Serikali inawaambia nini wananchi hawa ambao wanayasubiria maji haya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tuna bomba, na juzi tumesaini mkataba tarehe 22 Aprili kwa ajili ya kufikisha maji Nzega, Igunga na Tabora. Kama bomba limeshapita karibu na eneo lako, tutaendelea, na kama topography inaruhusu tutaendelea kuweka fedha ili kuhakikisha kwamba na maeneo kama haya ya Ushetu na nikuhakikishie tu kwamba bado capacity ipo kubwa, yapo maji ya kutosha, tutaendelea kutenga fedha kuhakikisha kwamba na hili eneno la Ushetu tuhakikishe tunalipatia maji. Na nikuombe Mheshimiwa Mbunge kwamba naomba tuwasiliane ili tuweze kupanga tuone namna gani tunaweza tukahakikisha kwamba maji yanafika haraka Ushetu.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona ili nami niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa hitaji la Mufindi Kaskazini linafanana na Ushetu na kwa kuwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliahidi kupandisha hadhi barabara hii inayounganisha mikoa mitatu; Mkoa wa Geita, Shinyanga na Tabora kwa kupitia maeneo ya Mbogwe, Mwabomba, Nyankende, Ubagwe, Uloa hadi Kaliua. Je, Serikali itaipandisha hadhi lini barabara hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizo ni barabara tatu tofauti lakini zinazoungana na kwa hiyo nadhani tufuate tu utaratibu. Kwa hapa itabidi mikoa yote mitatu kwa vipande vyake ifuate taratibu za kuomba kupandisha hadhi hizo barabara. Kama tayari zimefuata taratibu hizo basi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maombi yake yatashughulikiwa kama ambavyo tumeongelea kwa barabara ambayo inaanzia Mtili – Ifwagi – Mdaburo na kuendelea. Utaratibu huo tutaufuata na maombi hayo tutayapitia kwa pamoja na zile zitakazotangazwa tutakuja kuwajulisha rasmi baada ya kutokea kwenye Gazeti la Serikali.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali.
Kwa kuwa tuna kituo cha polisi chenye hadhi ya Wilaya, hiki ni kituo kipya na bado kina changamoto, tunao askari wachache 38 tu, lakini askari hawa wanafanya kazi nzuri kwa kushirikiana na wananchi, Madiwani na Halmashauri.
Pia kwa kuwa hakuna vifaa/vitendea kazi yakiwemo magari, kwa sasa Halmashauri ya Ushetu tumewapa Polisi jengo pamoja na gari. Tunahitaji kuwa na vituo vidogo kandokando kwa sababu Jimbo la Ushetu ni kubwa, linapakana na majimbo nane na tumedhamiria kutokomeza kabisa mauaji ya wazee na walemavu.
Je, ni lini Serikali itatupatia vifaa ikiwemo magari pamoja na askari ili angalau tufikishe askari 100. Hii itasaidia sana pia kupunguza makosa katika majimbo nane ambayo napakana nayo. Ni lini sasa Serikali itatusaidia?
Swali la pili, kwa kuwa tunazo jitihada za kujenga vituo vidogo kando kando katika maeneo ya Kata ya Chambo, Kata ya Ulowa, Kata ya Ubagwe na kata Idahina na kwa kuanzia katika Kata ya Idahina tuna jengo ambalo tumetumia nguvu za wananchi, Mbunge pamoja na wachimbaji wadogo, na litaweza kuwa accommodate ofisi pamoja na askari wapatao watano.
Je, Serikali iko tayari sasa kutusaidia kukamilisha jengo hili ili tuweze kupata askari tuweze kuimarisha masuala ya usalama katika eneo hili ambalo linakuwa kwa kasi?Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake kubwa alizonazo za kuhakikisha kwamba hali ya usalama katika Jimbo lake inaimarika, amekuwa akifuatilia kwa karibu sana maendeleo ya vyombo vyetu vya usalama katika Jimbo lake naomba nimpongeze sana kwa niaba ya wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kuongeza idadi ya askari na vitendea kazi vingine ikiwemo magari, naomba nilichukue hilo nikitambua kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha tuna matarajio ya kuongeza na kuajiri vijana wapya japokuwa ni kweli tuna uchache wa askari siyo tu katika Jimbo lake, ni katika maeneo mengi nchi nzima. Kwa hiyo, tutazingatia kulingana na mahitaji ya nchi nzima ili tuone jinsi gani tunaweza kufanya kusaidia jitihada za askari wetu pale katika Jimbo lake pamoja na usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na jengo lake ambalo amezungumzia vilevile kama nilivyokuwa nikijibu mara nyingi hapa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba majengo ya hivi vituo vyetu vya vyombo vya usalama vyote ni malengo ya Serikali kuhakikisha kwamba vinaimarika, tuna upungufu huo vilevile katika maeneo mengi nchini. Nichukue fursa hii kumhakikishia kwamba jitihada zinafanyika hata nje ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tumekuwa na utaratibu wa kutumia taasisi yetu ya Jeshi la Magereza kuweza kuanza ujenzi kwa kutumia rasilimali za maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutoa wito kwa Mheshimiwa Mbunge kulitumia Jeshi la Magereza katika eneo lake kwa ajili ya kuanza harakati za ujenzi wa kituo hicho na baadaye pale itakapofikia katika hatua nzuri tunaweza kulikamilisha kwani katika mwaka huu wa fedha tumetenga bajeti fedha za kutosha kuhakikisha kwamba tunamaliza maboma yote ambayo yamejengwea kwa nguvu za wananchi pamoja na nguvu na vyombo vyetu vya usalama kwa kutumia rasilimali za maeneo yale.(Makofi)
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na pia nimshukuru kwa kutupa Kituo cha Wilaya cha Polisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Sheria Na.23 ya mwaka 2002 inatoa fursa kwa msajili kwa ajili ya kusimamia hawa waganga wa tiba asili na tiba mbadala lakini kwa kuwa kamatakamata hii imesababishwa na wale waganga wasio waadilifu na hawajasajiliwa ambao kimsingi wamesababisha kuwa na mgongano na kusababisha mauaji ya vikongwe. Kwa mfano, katika Halmashauri ya Ushetu kuna watu 25 wameuawa katika kipindi cha mwaka 2012 na 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa kuwa, kamatakamata hii inaleta usumbufu kwa waganga wanaofanya shughuli hii kihalali, je, Serikali imejipangaje kuliimarisha Baraza hili la Tiba Asili au Tiba Mbadala ili lishirikiane na vyombo vingine kama polisi na kuwaondoa kabisa waganga wanaowachonganisha wananchi na kuwalinda vikongwe hawa dhidi ya mauaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Serikali itafungua vituo vya usajili mikoani ili kurahisisha usajili na kudhibiti waganga hawa na kuweza kushughulikia kabisa wasiokuwa na sifa na kuboresha huduma hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli utaratibu wa kusajili waganga wa kienyeji ambao kimsingi wanasajiliwa na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, baada ya mganga kuthibitishwa na Baraza hilo ndipo anapatiwa usajili, kwa hiyo, ni utaratibu mzuri tu. Kupitia utaratibu huu na mabaraza haya, nishauri waganga wote ambao wanajishughulisha na tiba asili kujisajili kisheria ili waweze kutambulika kihalali. Nina hakika watakapofanya hivyo hata kazi ya Jeshi la Polisi kuwabaini waganga wachochezi wanaopiga ramla chonganishi itakuwa ni nyepesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja ya kupeleka vituo hivi vya usajili mikoani, nadhani ni wazo zuri na kama Serikali tutalichukua na tutalifanyia kazi.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Naipongeza sana Serikali kwa hatua inayochukua ili kuweza kuboresha usimamiaji wa rasilimali zetu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa uwepo wa Kamati za Ukaguzi ni muhimu sana katika kuimarisha mfumo wa udhibiti katika taasisi hususan katika Halmashauri zetu. Kwa kuwa Kamati imara husaidia Maafisa Masuuli kutimiza wajibu wao na hii Kamati ni muhimu kwa ajili ya kusimamia pia mpango kazi wa Wakaguzi wa Ndani na Wakaguzi wa Nje. Kwa kuwa Serikali imetoa mwongozo wa mwaka 2013 na haujatekelezwa vizuri katika Halmashauri zetu.
Je, Serikali iko tayari kuzielekeza upya Halmashauri zetu kutekeleza mwongozo huu mzuri kikamilifu ili kuleta tija zaidi katika usimamiaji wa rasilimali zetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake katika kuhakikisha rasilimali za Taifa letu zinatumika ipasavyo na kama ailivyouliza, sisi kama Wizara tupo tayari na tumekuwa tukihakikisha Kamati hizi zinatekeleza maelekezo na miongozo yote inayotolewa na Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, sasa kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba tunaendelea kushughulikia sheria hii pamoja na kanuni zake ili tuje na sheria itakayohakikisha rasilimali za Taifa letu zinasimamiwa ipasavyo.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali.
Kwa kuwa tuna kituo cha polisi chenye hadhi ya Wilaya, hiki ni kituo kipya na bado kina changamoto, tunao askari wachache 38 tu, lakini askari hawa wanafanya kazi nzuri kwa kushirikiana na wananchi, Madiwani na Halmashauri.
Pia kwa kuwa hakuna vifaa/vitendea kazi yakiwemo magari, kwa sasa Halmashauri ya Ushetu tumewapa Polisi jengo pamoja na gari. Tunahitaji kuwa na vituo vidogo kandokando kwa sababu Jimbo la Ushetu ni kubwa, linapakana na majimbo nane na tumedhamiria kutokomeza kabisa mauaji ya wazee na walemavu.
Je, ni lini Serikali itatupatia vifaa ikiwemo magari pamoja na askari ili angalau tufikishe askari 100. Hii itasaidia sana pia kupunguza makosa katika majimbo nane ambayo napakana nayo. Ni lini sasa Serikali itatusaidia?
Swali la pili, kwa kuwa tunazo jitihada za kujenga vituo vidogo kando kando katika maeneo ya Kata ya Chambo, Kata ya Ulowa, Kata ya Ubagwe na kata Idahina na kwa kuanzia katika Kata ya Idahina tuna jengo ambalo tumetumia nguvu za wananchi, Mbunge pamoja na wachimbaji wadogo, na litaweza kuwa accommodate ofisi pamoja na askari wapatao watano.
Je, Serikali iko tayari sasa kutusaidia kukamilisha jengo hili ili tuweze kupata askari tuweze kuimarisha masuala ya usalama katika eneo hili ambalo linakuwa kwa kasi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake kubwa alizonazo za kuhakikisha kwamba hali ya usalama katika Jimbo lake inaimarika, amekuwa akifuatilia kwa karibu sana maendeleo ya vyombo vyetu vya usalama katika Jimbo lake naomba nimpongeze sana kwa niaba ya wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kuongeza idadi ya askari na vitendea kazi vingine ikiwemo magari, naomba nilichukue hilo nikitambua kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha tuna matarajio ya kuongeza na kuajiri vijana wapya japokuwa ni kweli tuna uchache wa askari siyo tu katika Jimbo lake, ni katika maeneo mengi nchi nzima. Kwa hiyo, tutazingatia kulingana na mahitaji ya nchi nzima ili tuone jinsi gani tunaweza kufanya kusaidia jitihada za askari wetu pale katika Jimbo lake pamoja na usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na jengo lake ambalo amezungumzia vilevile kama nilivyokuwa nikijibu mara nyingi hapa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba majengo ya hivi vituo vyetu vya vyombo vya usalama vyote ni malengo ya Serikali kuhakikisha kwamba vinaimarika, tuna upungufu huo vilevile katika maeneo mengi nchini. Nichukue fursa hii kumhakikishia kwamba jitihada zinafanyika hata nje ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tumekuwa na utaratibu wa kutumia taasisi yetu ya Jeshi la Magereza kuweza kuanza ujenzi kwa kutumia rasilimali za maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutoa wito kwa Mheshimiwa Mbunge kulitumia Jeshi la Magereza katika eneo lake kwa ajili ya kuanza harakati za ujenzi wa kituo hicho na baadaye pale itakapofikia katika hatua nzuri tunaweza kulikamilisha kwani katika mwaka huu wa fedha tumetenga bajeti fedha za kutosha kuhakikisha kwamba tunamaliza maboma yote ambayo yamejengwea kwa nguvu za wananchi pamoja na nguvu na vyombo vyetu vya usalama kwa kutumia rasilimali za maeneo yale.(Makofi)