Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Stephen Julius Masele (7 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo anafanya ya kujenga nidhamu ya nchi yetu na kurejesha nidhamu ya Utumishi wa Umma na nidhamu ya wananchi kutii sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimpongeze Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo kwa kazi nzuri ambayo anaifanya ya kusukuma mbele Sekta ya Nishati na Madini nchini.
Mheshimiwa Spika, wote sisi ni mashahidi, Wizara hii ina changamoto nyingi sana kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamezieleza, lakini wizara hii haihitaji malaika wa kwenda kufanya kazi pale. Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo ameonesha ubora na anastahili kupewa support, anastahili kuungwa mkono na Waheshimiwa Wabunge na tutakuwa tumelitendea haki Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimefanya kazi na Mheshimiwa Muhongo, namwelewa, tunapozungumzia moja ya Mawaziri makini nchi hii ni mmojawapo. Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Leo Mheshimiwa Rais ameeleza wazi anataka Tanzania iwe nchi ya viwanda, Mheshimiwa Rais ameeleza wazi, anataka asilimia 30 ya ajira za vijana zitokane na viwanda. Sasa Wizara hii na Hotuba ya Mheshimiwa Muhongo ndiyo ambayo itatupeleka kwenye kuwa na Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Spika, leo Waziri wa Viwanda na Biashara hata aseme ataleta viwanda elfu ngapi, kama hakuna nishati ya umeme ni sawa na kazi bure na Waziri ameonyesha kwa vitendo kwa kutenga asilimia 94 ya bajeti yake kwenye maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na niseme tu kwamba kwenye REA kila mtu anafahamu kazi inayofanywa ni nzuri, lakini changamoto zipo, najua ataendelea kuzitatua. Nimpongeze pia kwa kuteremsha gharama za umeme, Watanzania wengi wanalia gharama za umeme ziko juu na nakumbuka aliahidi kwamba atalifanyia kazi atapunguza gharama za umeme leo ametekeleza.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwenye viwanda nchini moja ya changamoto kubwa ambayo wanahangaika nayo ni bill zisizoeleweka ambazo wanapelekewa na TANESCO kwenye maeneo husika. Ziko charge nyingi ambazo viwanda vinapelekewa ambazo zinakatisha tamaa uwekezaji wa viwanda vilivyopo na hata hivyo vinavyokuja. Nina hakika kama bili hizi zitaendelea kuwa hivyo, basi kutakuwa na changamoto kubwa ya bidhaa zinazozalishwa nchini kushindana na bidhaa za masoko za kutoka nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliahidi kwa Watanzania kwamba atafanya mahesabu na atahakikisha hata nguzo za umeme itafika mahali atatutangazia atazigawa bure, tunasubiri ahadi hiyo na nina uhakika anaweza.
Mheshimiwa Spika, leo Tanzania, Mheshimiwa ameeleza kwenye hotuba yake, inazalisha megawati 1,400. Ili tuweze kuwa nchi kweli ya kipato cha kati, ili tuweze kuwa Taifa la Viwanda ni lazima tuongeze speed ya uzalishaji wa umeme. Speed ya uzalishaji wa umeme ni kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji hasa kupitia gesi asilia. Leo Tanzania tunazalisha gesi yetu wenyewe na Mungu ametusaidia, tusingekuwa na hii gesi na tusingekuwa na uimara wa Mheshimiwa Profesa Muhongo kusimamia bomba la gesi likamilike kwa kutegemea mvua haya malengo yote tusingeweza kuyafikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie, Taifa la Uturuki leo linaongoza kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwenye soko la Ulaya, ni kwa sababu wana umeme wa kutosha na hata hiyo gesi yenyewe hawana, wanaagiza kutoka kwenye Mataifa yenye gesi. Uturuki peke yake inazalisha megawatt 60,000 za umeme. Afrika Kusini inazalisha megawati 80,000 za umeme. Unapokwenda kule kama Waziri unamwambia mwekezaji kama Toyota njoo uwekeze kiwanda cha ku-assemble magari Tanzania atakuomba megawati 5,000 peke yake, huna, safari yako haina maana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Bunge hili litatenda haki kwa Watanzania endapo tutafikiri kimkakati namna gani Tanzania itazalisha umeme wa kutosha ili kuweza kukidhi mahitaji ya majumbani lakini pia tuweze kukidhi maendeleo ya viwanda tunayoyazungumza.
Mheshimiwa Spika, umeme tulionao huu vikiunganishwa migodi mitano tu Tanzania tutaingia kwenye mgao. Leo iko migodi hapa inazalisha yenyewe umeme. Tukiunganisha viwanda vikubwa tutaingia kwenye mgao. Kwa hiyo, bado tuna kazi ya kufanya, bado tuna kazi ya kumpa ushirikiano Waziri kwa jitihada ambazo amezionyesha kwenye bajeti hii ili tuweze kufikia hayo malengo tunayoyataka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa leo Tanzania tunazalisha kupitia TANESCO, malengo yetu kama nilivyosikia kwenye hotuba tunatakiwa tuwe na megawatt 2,500, tunatakiwa tuwe na megawatt 10,000 ifikapo 2025. Tutafikishaje megawatt 10,000 kama hatuvutii uwekezaji binafsi kuja kuwekeza katika Sekta ya Umeme? Serikali peke yake kuzalisha megawatt 100 za umeme ni zaidi ya Dola za Marekani milioni mia moja na! Tukitaka megawatt 10,000 leo tunahitaji zaidi ya dola bilioni 10 za Marekani labda ni bajeti yetu hii ya miaka 10 ijayo tusifanye jambo lingine lolote. Kwa hiyo, lazima Serikali tuwe na mikakati ya kuhakikisha kwamba tunawekeza katika umeme sawa, lakini tuvutie pia sekta binafsi kuwekeza katika miradi hii.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie kwenye Sekta ya Madini, zipo jitihada kubwa Wizara inafanya, niwapongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuendeleza jitihada za kuwainua wachimbaji wadogo Tanzania, nimpongeze Naibu Waziri kwa kazi kubwa ya kusuluhisha migogoro ya Nyamongo, lakini bado ziko changamoto ambazo tunatakiwa kuzishughulikia na bado katika uwekezaji mkubwa pia tunahitaji kuwa na migodi mipya.
Mheshimiwa Spika, tulipitisha miaka miwili iliyopita hapa sheria inayotoza kodi kwenye vifaa vya utafiti. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri ni mjiolojia bingwa duniani, tunapoweka sheria hizi za fedha za kutoza kodi kwenye vifaa vya utafiti ni sawasawa unasema tunataka kilimo cha kisasa halafu tunakwenda kuweka kodi kwenye matrekta, tunakwenda kuweka kodi kwenye mbegu.
Mheshimiwa Spika, kwenye uzalishaji wa migodi mipya haiwezi kutokea migodi mipya Tanzania endapo utafiti utakufa, endapo makampuni yanayofanya utafiti yatapunguza bajeti ya kufanya utafiti. Mheshimiwa Waziri naomba hili alifanyie kazi tupitie upya hizi sheria hasa kwenye eneo hili la utafiti ili kuweka unafuu wa utafiti na hatimaye nchi yetu iweze kupata viwanda vipya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuiwezesha Tanzania kupata mradi mkubwa wa kujenga bomba la mafuta kutoka Uganda. Nafahamu jitihada zako, nafahamu jitihada za Serikali. Miradi hii itasaidia sana kukuza uchumi wa Taifa letu. Nimwombe aendelee na jitihada, natambua Uganda imetuomba Tanzania tupeleke bomba la gesi, natambua Kenya tume-sign makubaliano nao ya kuwauzia megawatt 1,000. Leo wapo Watanzania wanajiuliza kwa nini shilingi haina nguvu? Wachumi wanasema unapoingiza zaidi kuliko kupeleka nje zaidi maana yake unadhoofisha shilingi yetu. Tukiweza kuuza megawatt 1,000 za umeme Kenya tutaingiza mapato ya kigeni mengi ambayo yatasaidia hata kuimarisha shilingi yetu.
Mheshimiwa Spika, miaka mingi tangu uhuru tumetegemea mazao ya mashambani; pamba, tumbaku, madini kidogo bei imeshuka, uzalishaji umeshuka; lakini tuna bidhaa, tuna zao jipya la gesi ambayo tunaweza tukazalisha megawati 1,000 ambazo Kenya wanazihitaji na tuka- export megawatt 1,000 tukapata mapato mengi ya kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja hii ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo imetoa dira ya nchi yetu inakoelekea hasa kwenye siasa za Kimataifa na diplomasia ya uchumi. Nitumie nafasi hii kumpongeza Naibu Waiziri Mheshimiwa Dkt. Susan Kolimba, Katibu Mkuu Dkt. Aziz na watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kuitangaza nchi yetu na kuvutia uwekezaji katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina historia na ina historia kubwa hasa kwenye siasa za kimataifa. Tangu tupate uhuru chini ya uongozi wa Baba wa Taifa alijenga misingi imara ya kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na sauti kwenye ukanda wa Kusini mwa Afrika na hasa kwenye masuala ya ukombozi wa Bara letu la Afirika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, misingi ile ilijengwa na msingi imara na unatakiwa kuendelezwa kwa kukifanya Tanzania kuwa nchi yenye sauti kubwa na ushawishi wa kisiasa na kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Kusini mwa Bara la Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kupongeza uongozi mzima wa Wizara pamoja na Serikali kwa kushiriki kikamilifu kusuluhisha mgogoro wa Kongo (DRC). Wote hapa tunafahamu umuhimu wa Kongo (DRC), mahusiano yetu ya kindugu, ya kijamii na kiuchumi. Kwa hiyo, uhusiano na ushiriki wa Tanzania kuhakikisha kwamba nchi ya Kongo inapata amani ya kudumu ni jambo la kipaumbele kwa Tanzania na kwa Serikali yetu. Lakini hivyo hivyo niipongeze Serikali kwa kuhakisha kwamba Burundi inaendelea kuwa salama na Baba wa Taifa alieleza kabisa kwamba huwezi kuwa salama kama majirani zako wote hawako salama, na wote tunatambua umuhimu wa kiuchumi wa nchi hizi zinazotuzunguka kwa maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita zaidi kwenye diplomasia ya uchumi ambayo mwelekeo wa Wizara na Serikali kwa sasa imeweka mkazo mkubwa kwenye diplomasia ya kiuchumi.
Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba zako zinazofuata ni vyema ukaja na takwimu uoneshe Watanzania mipango na safari na mikutano ya nje ambayo nchi yetu inashiriki imeleta faida gani kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa taarifa na Ripoti ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa Tanzania kwa mwaka 2014 imeongoza kwa kuwa ni Taifa la kwanza kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuingiza mapato mengi ya uwekezaji wa fedha za kigeni kwa maana ya Foreign Direct Investments. Leo kwa ripoti ile Tanzania iliingiza zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.14 ukilinganisha na Taifa ambalo lina uchumi mkubwa kwenye ukanda wetu la Kenya ambalo liliingiza dola milioni 900. Uganda ilifuatiwa ya pili nyuma ya Tanzania kwa kuingiza zaidi ya dola bilioni 1.1. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mafanikio Mheshimiwa Waziri, kwa sababu haya ndio majukumu ya Wizara yako kwa shughuli zote zinazohusiana na uchumi wa Taifa hili na hasa uwekezaji kutoka nje na ukitazama katika uwekezaji huu unaona kabisa ni Sekta ya Gesi, Sekta ya Madini kwa Tanzania ndio imeongeza kwa kuingiza mapato mengi ya uwekezaji baada ya kugundua gesi asilia, Taifa letu limeingiza mapato mengi ya kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ni vyema sasa kuangalia ushiriki wetu kwenye majukwaa mbalimbali ya kiuchumi kwa mfano tunaposhiriki kwenye Jukwaa la Kiuchumi la TICAD kwa mahusiano ya Japani na Afrika ama India na Afrika, ama Marekani na Afrika, na block zingine za kiuchumi kwa mfano block ya BRICS lazima tuoneshe kwa takwimu tunapata faida gani. Taifa linapata mapato kiasi gani kutoka nje kwa maana ya uwekezaji unaotoka nje. Hiyo itaweza kuonesha uhalali wa safari ambazo tunakuombeeni fedha mnazokwenda nje na huwezi kuwa mwana diplomasia ambaye unaishia kwenda Shinyanga badala ya kwenda nje kutafuta uwekezaji kwa faida ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niseme kwamba ukitazama kama nilivyoeleza awali, Sekta ya Nishati kwa maana ya utafiti na gunduzi za gesi na madini ndio zimeongeza mapato mengi ya kigeni hasa katika uwekezaji. Je, Wizara inajipangaje sasa kuhakikisha kwamba sekta zingine kama Sekta ya Kilimo na Viwanda inafanya vizuri kuwekeza, kuingiza fedha nyingi za kigeni.
Ukitazama kama Ethiopia imefanikwa sana kwenye viwanda hasa kwenye maeneo ya kilimo, imefanikiwa sana kuvutia uwekezaji kwenye kilimo na viwanda ambayo imechangia mapato makubwa ya Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kama Afrika Kusini ambayo ndio inaongoza kwa Afrika kwa zaidi ya dola bilioni 145 za uwekezaji ambazo imepokea, imewekeza zaidi kwenye Sekta ya Viwanda, Biashara pamoja na Madini. Sasa Sekta zingine zinasubiri nini! Je, wizara yako inawezaje kusaidia kutafuta wawekezaji zaidi wa kuongeza mapato na uwekezaji katika sekata za Kilimo, biashara pamoja na viwanda katika nchi yetu.
Mheshimiwa Rais amesema anataka Tanzania iwekeze zaidi kwenye viwanda. Je, Wizara yako inafanya nini na hawa wawekezaji wanaokuja kuwekeza hapa baada ya kuwekeza je, Wizara yako inafuatilia kuona wanaendeleaje? Maana wawekezaji wengine wanakuja kwenye sekta hizi mbalimbali lakini wanaishia kuchanganyikiwa, wanaishia kuwa frustrated na mazingira mengine ya uwekezaji. Je, Wizara hii inafuatilia kujua wanaendeleaje? Na kama kuna changamoto ambazo zinawakabili mnafanya nini kuhakikisha kwamba mnashirikiana na sekta zingine kuhakikisha changamoto hizi mnazitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa kwamba Taifa lolote duniani haliwezi kuendelea bila uwekezaji, hasa uwekezaji wa fedha zinazotoka nje. Marekani yenyewe inashika nafasi ya tatu kwa kupokea fedha nyingi za uwekezaji kutoka mataifa mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, China imeendelea kwa sababu imepokea fedha nyingi za uwekezaji kutoka mataifa mengine, na kutoka ndani ya China wenyewe. Lakini Tanzania tunapovutia wawekezaji lakini tunatumia muda mwingine kuwa-frustrate wawekezaji na kuona kama ni maadui ama wezi wa mali za asili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wetu kuwa na sheria nzuri, ni wajibu wetu kusimamia vizuri rasilimali zetu, lakini taifa hili linahitaji kuendelea, Taifa hili linahitaji kuwa Taifa la uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Hatuwezi kuwa na uchumi wa kati mwaka 2025 kama dira ya Taifa ya uchumi ya maendeleo inavyoelekeza kama hatutoweza kuvutia uwekezaji kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri, badala ya kufanya siasa, badala ya maelezo mengi, next time uje na data, uje na figures uoneshe faida, ya kushiriki kwenye mikutano hii yote, Taifa linapata nini. Uoneshe fedha tunazozipokea kutoka Asia, Marekani, Uingereza katika uwekezaji, wala sio fedha za misaada, nazungumzia fedha za uwekezaji ambazo zinaongeza mzunguko wa uchumi katika Taifa letu. Leo katika mradi wa bombo la gesi tu, tulipokea zaidi ya dola bilioni 1.2, dola bilioni 1.2 imetumika hapa Tanzania, na makampuni ya kitanzania yamepata fedha, na mzunguko wa fedha umemfikia kila mwananchi wa Tanzania.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja, na nampongeza Waziri na Wizara yake. Yeye ni mzoefu nina uhakika kwamba atalisaidia Taifa hili, kuhakikisha heshima ya Tanzania, kwenye nyanja za kimataifa inaendelea kuwepo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi pia ya kuchangia bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ambayo inatoa dira ya mipango ya maendeleo ya Serikali. Nitumie nafasi hii pia kuwapongeza Mawaziri, Mheshimiwa Jenista Mhagama, kwa kazi nzuri na anaonesha kweli akinamama wanaweza. Nimpongeze pia Naibu Waziri kijana, Mheshimiwa Anthony Mavunde kwanza kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kuwaunganisha vijana wa Tanzania lakini pia kwa programu ile ya mafunzo ya vijana ambayo anaifanya. Nimwombe tu programu hiyo pia ifike Shinyanga kwa sababu kuna vijana wengi wanahitaji programu kama hiyo na kusema kweli kama vijana wenzako hujatuangusha.
Mheshimiwa Spika, kipekee sana kwa niaba ya wananchi wa Shinyanga nataka nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. Alipofanya ziara Shinyanga alitoa maelekezo kwa Mamlaka na Wizara ya Maji kushughulikia tatizo la bei ya maji Shinyanga. Kama Mheshimiwa Shabiby
alivyosema, leo nazungumzia kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu bado hatujaona jitihada za Waziri wa Maji kushughulikia tatizo la uendeshaji wa Mamlaka ya Maji Shinyanga.
Mheshimiwa Spika, maji ni huduma ya msingi, maji sio anasa. Shinyanga na mikoa ya Kanda ya Ziwa ni mikoa michache ambayo ina chanzo cha maji cha uhakika cha Ziwa Victoria. Serikali imetumia shilingi bilioni 250 kujenga Mradi wa Maji wa Ihelele, kodi za Watanzania, leo Wizara
haiweki msisitizo wa kutunza mitambo ile. Shilingi bilioni 250 hazijamaliza hata miaka 10, Serikali haipeleki pesa za kutunza mitambo ile. Ni asilimia 25 tu ya mitambo ile ndiyo inafanya kazi, asilimia 75 haifanyi kazi. Ipo mikoa mingine kama Arusha wanahangaika vyanzo vya maji, Gairo huku amezungumza Mheshimiwa Shabiby wanahangaika na vyanzo vya maji, lakini sisi tuna chanzo cha maji cha uhakika lakini hatukitunzi, tumeweka shilingi bilioni 250 hatutunzi.
Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita Shinyanga, Kahama, Ngudu, Igunga ambayo yote yapo kwenye Mradi huu wa Ihelele yanatakiwa yapelekewe maji lakini hayajapelekwa. Mradi ule umekatiwa umeme, siku nne wakazi wa Shinyanga hawana maji kwa sababu Serikali haijapeleka mchango wake wa asilimia 60 wa kuendesha mradi ule. Sasa wananchi wanapata adhabu ambapo wamelipia bili zao za maji wanastahili wapate huduma wanaikosa huduma kwa uzembe wa watu wengine, hii inasikitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mradi ule hauwezi kuharibika kwa uzembe wa watu wachache. Nimwombe Waziri, namheshimu, ni rafiki yangu, akae na Wabunge wa Kanda ya Ziwa ambao wanahusika na ule mradi wa maji tushauri namna bora ya uendeshaji wa mradi ule. Mradi ule ukiweza
kuwafikia watumiaji wengi, kwa mfano wa Ngudu, Kwimba, Igunga, Nzega, Tabora, Sikonge na kwa capacity ya mradi ule unaweza kuleta maji mpaka Mkoa wa Dodoma. Pampu zile nane zikifunguliwa zote Dodoma inaweza kupata maji ya Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, andiko la mradi ule linaweza kuhudumia watu milioni 10. Leo ni wakazi wa Manispaa ya Shinyanga ambao hawafiki 200,000 na wakazi wa Mji Mdogo wa Kahama ambao hawafiki 200,000 ndiyo wanahudumia gharama za uendeshaji za mradi wa shilingi bilioni 250. Naomba Serikali iangalie kwa upana mradi huu. Naomba pia Serikali iongeze bidii za kusambaza haya maji kwenye vijiji vile vinavyohusika, zile kilometa tano vijiji vile vipate maji.
Mheshimiwa Spika, lakini yapo mambo ambayo tunaweza kumshauri Waziri, kwa mfano, mamlaka hizo zote mfano SHUWASA na mamlaka nyingine, kwenye vifaa vya mabomba kwa mfano vya kuunganisha maji, vimewekewa kodi, kuna SDL iko pale, kuna VAT iko pale. Vitu kama hivi vikiondolewa kwa sababu maji ni huduma, gharama za uendeshaji wa mamlaka hizi zitakuwa chini na hatimaye wananchi watapata huduma ya maji kwa gharama nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia madeni hayalipwi. Sasa taasisi muhimu kama Mamlaka za Maji zinakatiwa huduma, nilikuwa naangalia television, Kigoma pale wananchi wanagombania maji kwa sababu mamlaka imekatiwa maji. Shinyanga pale tumekatiwa maji siku nne, tuna viwanda pale vya maji, kuna viwanda vya soda, wananchi wanakosa maji eti kwa sababu bili ya KASHUWASA haijalipwa na huyo KASHUWASA hiyo pesa anayotakiwa atoe inatakiwa itolewe upande wa Serikali. Sasa sisi wananchi tumelipa bili tunataka huduma tu. Tunapata adhabu kwa sababu ya watu wengine. Hospitali haina maji, imagine hospitali ya mkoa inayopokea wagonjwa zaidi ya 200 inakatiwa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimezungumza hili kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu kule nyumbani wananchi wamenituma wamesema tunataka nizungumzie suala la maji. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu suala hili ulisimamie kwa karibu kwa sababu pale tumeweka pesa nyingi za walipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Shinyanga imejengewa mtandao wa maji safi lakini hakuna mtandao wa majitaka, majitaka yote yanayonyonywa hakuna pa kuyapeleka. Naomba Serikali itenge fedha kwenye bajeti hasa ya Waziri wa Maji, tujenge mtandao wa maji taka kwa sababu ulikuwepo kwenye andiko la mradi huu kwamba lazima na mitandao ya majitaka pia ijengwe. Leo majitaka pale Shinyanga hakuna pa kuyapeleka, mbaya zaidi hata vifaa vinavyokuja vyote ikiwemo na mita zinakuja mita feki, bili za wananchi zinachakachuliwa, wananchi wanapigwa bili kubwa kwa mita feki zinazokuja.
Mheshimiwa Spika, naomba Waziri asimamie hizi mamlaka kwa karibu, aangalie hata hizo mita zinazoagizwa, huyo mtu aliyepewa tenda ya kuagiza mita ziwe zina ubora unaostahili sio kuwaibia wananchi kwa kuleta mita ambazo ni feki, zinaongeza gharama za uendeshaji, zinaongeza bili ya maji kwa wananchi. Wananchi wangu bado hawana uwezo mkubwa wa kubeba mzigo wa gharama za kuhudumia maji ambayo kimsingi Serikali ilitakiwa isaidie ruzuku ili kuweza kuhakikisha mradi huu unawafikia watumiaji wengi.
Mheshimiwa Spika, tukiongeza foot print ya mradi huu gharama zile tutagawana wote, maji yale yafike mpaka Tabora, Sikonge, Ngudu, Sumve, Igunga, Singida na Malya, wote wapate yale maji ili tuweze kugawana gharama za uendeshaji. Tusipofanya hivyo tutaendelea kubeba msalaba huu sisi peke yetu na mradi ule utakufa kwa sababu hatuna uwezo wa kuuhudumia. Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Itifaki ya Nagoya ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo Sahihi wa Faida zitokanazo na Matumizi ya Rasilimali za Kijenetiki.
MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja hii na nizungumze mambo mawili. Kwanza ni kwenye eneo la utafiti, lakini la pili ni kwenye usimamizi na utekelezaji wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itifaki hii ni muhimu sana kwa Taifa letu na itaweka ulinzi wa rasilimali zetu hasa za baharini na tafiti zinazoendelea kufanyika zinaonesha kwamba kwenye bahari zetu tuna rasilimali zenye thamani kubwa sana inawezekana kuzidi rasilimali zilizopo nchi kavu. Kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali ni kuongeza uwezo wa vyombo vyetu vya utafiti hasa kupitia vyuo vikuu vyetu ili tuwe na uwezo mkubwa wa kibajeti na kitaalam na sisi tuweze kufanya tafiti hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kushirikiana na vyombo vya utafiti va Kimataifa ili kujua kinachoendelea kwenye tafiti ambazo zinafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo tafiti nyingi zinaendelea hapa nchini wakati mwingine unaweza kukuta hata kwenye Wizara Serikali haitambui kama tafiti hizi zinafanyika. Kwa mfano, kuna taifiti moja inafanyika na Chuo Kikuu cha Florida cha Marekani wa kutafiti maji ya mito yetu kwa mfano Mto Wami, Mto Mara, Mto Morogoro na Mito mingine miwili hapa Tanzania lakini unakuta wale wanaotafiti hawana coordination kabisa na Serikali, kwa hiyo mimi ombi langu kwa Serikali kwamba baada ya kupitisha ikawa sheria basi tusimamie na tuhakikishe tunasimamia na tunashiriki katika tafiti zinazofanywa ndani na Mashirika ama makampuni ya Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutimize wajibu wetu kama Wabunge wa kutunga Sheria na Serikali itimize wajibu wake wa kutekeleza haya ambayo tunayapitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii ya Serikali. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Dokta Mpango, ama kweli ameonesha uwezo wake kwamba yeye ni mchumi aliyebobea kwa kutuletea bajeti ambayo kwa kweli imeandaliwa kisayansi sana. Pia nipongeze sana timu yake yote ya watendaji, ikiongozwa na Katibu Mkuu Ndugu Dotto James na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri ya kutengeneza bajeti ambayo inatoa majawabu ya matatizo ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasiasa na watu mbalimbali wamekuwa wakisema Serikali haisikilizi ushauri, Serikali haishauriwi, lakini nimesoma bajeti hii mambo mengi ambayo wananchi na Wabunge wamekuwa wakishauri yamezingatiwa. Kwa kweli, naomba sasa Mheshimiwa Mpango na timu yake waharakishe utekelezaji wa maamuzi ya kisera waliyoyafanya. Wamepunguza ushuru kwenye baadhi ya maeneo hasa kwenye mazao kwenye Halmashauri na wametoa maelekezo kwa TRA ifanye kazi bila kubughudhi wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Shinyanga, Shinyanga tuna wafanyabiashara wadogowadogo na wakubwa, wafanyabiashara wanasumbuliwa, wanafuatwa na Polisi, wanafuatwa na PCCB. Maelekezo aheshimiwa Mpango naomba ayapeleke kule chini na ayasimamie kuhakikisha wafanyabiashara wanapewa mazingira wezeshi ili waweze kuzalisha na hatimaye Serikali iweze kupata kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia huu ushuru wa mama-ntilie, mama-lishe, wakulima wadogo wadogo wa bustani, yote ambayo wamepunguza maelekezo yaende kwenye Halmashauri zetu. Hatuwezi kujenga Taifa hili kwa kutegemea ushuru wa mama-lishe au wa mama anayeuza mboga. Kwa hiyo, nina imani na kazi yake, nina imani na uwezo wake, naamini atayazingatia haya na atapeleka maelekezo kwenye ngazi za chini za wananchi ili wasiweze kusumbuliwa na wananchi wangu wa Soko la Nguzo Nane kule Kambarage, Soko Kuu la Shinyanga waweze kufanya biashara zao bila kusumbuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wiki nzima hii nchi yetu imekuwa inazungumzia suala la mchanga wa dhahabu. Mimi nimewahi kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge kama kuna vita yoyote duniani hivi leo ni vita ya uchumi. Yale yote mnayoyaona yanatokea Syria, watu wengi hawaelewi Syria ni nini kinatokea, pale kuna gesi ya Qatar inazalishwa na Wamarekani wanataka kusafirisha kwenda Ulaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Urusi ndiye muuzaji wa gesi mkubwa Ulaya, Marekani na Qatar wanataka wajenge bomba la gesi lipite Syria liende Ulaya, Urusi hataki lijengwe litaharibu soko lake, anamwambia Assad weka ngumu, hakuna bomba kupita mimi nitakusaidia. Marekani na yenyewe inaingiza nguvu zake kumng’oa Assad. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuwaambia Waheshimiwa Wabunge, tunapozungumzia masuala ya uchumi ni mazito na yanaingilia hadi na Mataifa. Leo hii Tanzania tumetoa maamuzi haya, Mataifa ya kibeberu na kibepari yatataka kutuingilia ndani. Nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa maamuzi aliyoyafanya kwa sababu atakumbana na vikwazo mbalimbali vingi na ili Taifa letu liendelee ni lazima tuwe na utulivu wa kisiasa, lazima wananchi tutulie na tuelewe nini tunataka kupata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine unapata tabu Watanzania wanalalamika tunanyonywa, tunaibiwa, unapochukua maamuzi ya kudhibiti kunyonywa na kuibiwa ndipo watu wanaanza kugeuka tena. Mtu anaanza kusema ooh, kwa nini mnafanya hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiwa Naibu Waziri niliwahi kutoa tamko hapa Bungeni, nilitegemea Watanzania wenzangu na Wabunge wenzangu asilimia kubwa waunge mkono unyonyaji na unyanyasaji tuliokuwa tunafanyiwa na Mataifa ya kibeberu, lakini Wabunge wengine humu wakasimama kuanza kutetea mabeberu. Tulikuwa tunajenga bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar-es-Salaam kuongeza uwezo…

TAARIFA . . .

MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimsaidie rafiki yangu Mheshimiwa Heche. Cha kwanza jana kuna mtu amesema hapa ripoti ile ni rubbish.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hauwezi ukapinga ripoti ya kitaalam na ya kisayansi kwa maneno, unaipinga ripoti ya kisayansi kwa kuja na ripoti ku- counter ripoti iliyotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wengine humu tumeshakuwa wakongwe. Nataka nimwambie mimi nikiwa Naibu Waziri, Halmashauri zote zenye migodi Tanzania zilikuwa zinalipwa dola laki moja, dola laki mbili. Nilisimamia kuhakikisha kwamba tunafuata sheria za nchi ambapo Halmashauri zetu zinapata asilimia 0.3 ya turn over ya migodi hii, leo Halmashauri ya Geita inapata zaidi ya bilioni tatu kwa mwaka, ilikuwa inapata dola laki mbili tu. Haya mambo yanawezekana, tukiwabana wawekezaji wanaonyonya kwa mikataba nyonyaji tunaweza kufanikiwa kupata mapato zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tufanye radical decisions, hatuwezi tukakaa mezani tunachekeana tukitaka kupata mapato zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Kongo pale thamani ya madini ya Kongo kwa takwimu inaonesha ina thamani zaidi ya GDP ya European Union lakini Kongo inaibiwa, watu wamekaa, wananchi wana shida. Leo Tanzania tumeweka mfano, Tanzania tume- set standard na wote tunatakiwa tumuunge mkono Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetoka kwenye Vikao vya Bunge la Afrika, nchi nyingine za Afrika zinatuuliza, zinatusifia, zinamsifia Rais wetu na zina hamu aende akashiriki kwenye mikutano ya kimataifa ili waweze kujifunza nini anafanya Tanzania. Kwa hiyo, ndugu zangu nataka niwaambie muda wa kunyosheana vidole huyu kafanya nini, kafanya nini, utatupotezea muda kama Waheshimiwa Wabunge, ni vyema Waheshimiwa Wabunge tuanze kufikiria mapendekezo, maoni ambayo yataboresha ile task force iliyoundwa na Mheshimiwa Rais ya kuboresha mikataba hii. Kama una maoni mazuri yaandike yapeleke kwa Mheshimiwa Profesa Kabudi ili aweze kuyaingiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mikoa yote yenye rasilimali haipati chochote, pelekeni mapendekezo angalau asilimia moja kinachovunwa kibaki kwenye mikoa husika ili maisha ya wananchi yafanane na rasilimali zao. Leo ukienda Geita maisha ya wananchi hayafanani na rasilimali zao. Ukienda Shinyanga almasi ile, maisha ya watu wa Kishapu na Shinyanga hayafanani. Ni lazima Serikali iamue kwa makusudi asilimia moja ama asilimia yoyote ambayo itaonekana kitaalam ibaki kwenye maeneo ya wananchi ili kuboresha maisha yao yafanane na rasilimali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na nimshukuru Mheshimiwa Rais amelianzisha jambo, amelisimamia, amelifikisha mwisho. Kitendo cha watu wa ACACIA kuja kukaa naye mezani maana yake sasa tunapata muafaka wa matatizo tuliyokuwanayo. Unaweza ukalianzisha jambo na usiweze kulisimamia, unaweza ukalianzisha jambo na usiweze kulifikisha mwisho, lakini tuna Rais ambaye ni mtendaji, mtekelezaji, analianzisha jambo, analisimamia na analifikisha mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote tumuunge mkono na tusimamie na tutambue kwamba hii vita tunayopigana siyo vita ndogo. Siyo vita ndogo kuanzia kwa makampuni, siyo vita ndogo kuanzia kwa Mataifa ya kibeberu kwa sababu kazi yao iliyobakia ni kunyonya rasilimali za Afrika. Wanakuja na mbinu mbalimbali lakini Waafrika lazima tusimame tuoneshe mfano na Tanzania imeonesha mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikushukuru kwa nafasi hii na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maamuzi yake ya makusudi ya kudhibiti na kusimamia rasilimali za nchi, kwa kuagiza kuletwa Muswada huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Waziri wa Katiba na Sheria kwa kazi kubwa ambayo ameifanya usiku na mchana na niwapongeze watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Madini kwa michango yao mbalimbali ya mawazo na maarifa kuboresha Muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka sekta ya madini naomba nitoe tu mfano wa nchi nne. Nchi ya Canada ina uzoefu wa sekta ya madini kwa miaka 440, ilianza tangu huko nyuma chini ya utawala wa Waingereza. Australia ina uzoefu wa zaidi ya miaka 176, Afrika Kusini ina uzoefu wa miaka 150, Ghana tangu enzi za triangle trade ina uzoefu wa miaka zaidi ya 167. Sisi kwa uwekezaji mkubwa ukiachilia mbali kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na hasa enzi ya Waarabu tuna uzoefu wa miaka 25.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachotaka kusema tunapozungumza kwamba muda hautoshi; katika utawala wa Mzee Mkapa, katika utawala wa Mzee Kikwete wameunda Tume tatu muhimu ambazo zimefanya kazi ya kitaalam, zimetafiti, zimefanya fact finding mission kwenye nchi mbalimbali zenye uzoefu na ndiyo zimekuja na mapungufu ya sheria zetu za madini, kuanzia sheria ya Mwaka 1979, sheria ya mwaka 1998, sheria ya 2010 ambayo ilikuwa na maboresho mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hapa tuna muda wa kuchambua mapendekezo na maoni ya kitaalam yaliyoundwa na Tume zilizotumia pesa za walipa kodi kutuletea taarifa hizi za kitaalam. Unaweza ukasema tu unaibiwa lakini mwisho wa siku usiainishe wapi unaibiwa. Kwa hiyo, ninachotaka kusema, taarifa kwa maana ya literature ziko za kutosha, ipo Tume ya Kipokole, iko Tume ya Bomani, Tume ya Masha – zote zimetupa taarifa za kutosha. Hata hao wadau waliokuja hapa hawakuandika overnight, taarifa zile wanazo wamechukua tu kwenye archives zao wametuletea. Wajibu wetu sisi ni kuziweka pamoja kuzichambua na kutengeneza sheria iliyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri wa Katiba na Sheria kwanza kwa usikivu, anapokea ushauri. Tumemshauri mambo mengi ameyazingatia kwenye Muswada lakini amezingatia katika Majedwali aliyoleta. Kwa mfano, kwenye local content tunataka kutunga sheria hapa ambayo itawawezesha wazawa kushiriki katika biashara ya ku-supply kwenye migodi na makampuni ya uwekezaji. Hata hivyo, ukiangalia kwenye Sheria za Kodi, capital goods ambazo zimeainishwa na sheria, wazawa wanapopata mikataba ya ku-supply bidhaa zile, wakija upande wa TRA wanaambiwa mikataba ile ni baina ya mwekezaji pamoja na TRA siyo kwa yule mzawa aliyepewa tender ya ku-supply bidhaa zile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo gharama za bidhaa zile zinakuwa ghali na kusababisha kwamba migodi sasa iamue kuagiza yenyewe direct. Kwa hiyo, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla, Sheria hizi lazima zitamke na zitambue mkataba wa ku-supply ambao amepewa mzalendo, Sheria ya Kodi itambue kwamba bidhaa zilizoorodheshwa na capital goods ziwe ni sehemu ya msamaha wa kodi ambao yule mzalendo amepewa apeleke. (Makofi)

Mheshimiwa Nabu Spika, pia nataka kuishauri Serikali; kwenye ubia wa kampuni ni sahihi kabisa, asilimia 16 sahihi kabisa, lakini tuendelee kuongeza kwamba Serikali imiliki, iwe na ubia kwenye kumiliki leseni. Kwa kufanya hivyo tutaweza kudhibiti kuanzia utafiti, kwa sababu iko biashara kubwa ya utafiti. Yako makampuni kazi yao ni kutafiti na kuuza leseni kwenye makampuni ya uchimbaji. Kwa hiyo, kama Serikali haishiriki pale, tafsiri yake kwamba kuna mapato yatatupita na kuna mambo mengi yatafanyika pale bila sisi kutambua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la uthamini sheria imeweka vizuri sana, imedhibiti vizuri uthamini nami nisisitize tu Serikali pia tuwe na laboratory zetu ili tuweze kujua thamani halisi ya madini tunayozalisha. ….…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuleta Muswada huu. Kipekee kabisa, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake ya Manaibu Waziri, kwa kuwa wasikivu na kupokea ushauri ambao sisi Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukiutoa kwa Serikali kupitia Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza mambo mawili; la kwanza, maamuzi ya Serikali ya kuiacha NSSF ku-deal na
private sector pamoja na informal sector. Utafahamu kwamba kwa population ya Tanzania, Watanzania wengi wako kwenye informal sector na wengi hawaratibiwi na mfuko wowote. Kwa hiyo, maamuzi haya yanaifanya sasa Watanzania walio wengi ambao wako kwenye informal sector kupata fursa ya kuratibiwa na mifuko hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama kabisa NSSF iki- deal na informal sector itaweza kutoa mafao ambayo yatawanufaisha Watanzania wengi ambao ni wanyonge na ambao hawana uwezo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sheria hii, wale watumishi ambao ni wa Serikali na walioko kwenye mifuko hii ambayo tunaiunganisha kupitia Muswada huu ambao tutatunga sheria, watafaidika na mafao mengi ambayo yako kwenye minimum requirements za ILO. Mimi nitajielekeza sehemu moja hasa kwenye section number 29 ambapo kuna orodha ya mafao ambayo yapo kwenye Muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama orodha hii, kuna fao la matibabu halipo. Vilevile ukitazama kwenye sheria iliyoanzisha NSSF, tukiichukulia kama ni standard, fao lile lipo. Sasa nilikuwa naomba kushauri Serikali…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Masele, samahani niko hapo kwenye section 29.

MHE. STEPHEN J. MASELE: Section 29, ukiangalia pale subsection (1)(a) “retirement benefits, survivors benefits, invalidity benefits, maternity benefits, unemployment benefits, sickness benefits and death gratuity.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napendekeza Serikali ilete amendments iongeze medical benefits ama health insurance benefits ili watumishi wa umma ambao watakuwa wakichangia kwenye mfuko huu mpya tutakaouanzisha waweze kunufaika na fao hili moja kwa moja bila kuchangia tena kwenye NHIF. Ziko hoja zinazungumzwa kwamba Watumishi Umma wote watakuwa wananufaika na health Insurance kupitia NHIF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizama kwa makini, unaona kwamba watumishi hawa wa Umma watakuwa wanachangia mara mbili; wanakatwa kwenye NHIF ili waweze kupata huduma, lakini kwa kuwa wao wako chini ya mfuko huu, pia watakatwa huku ambapo wakikatwa huku, moja kwa moja wana-qualify kupata huduma ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa naishauri Serikali, ilete mabadiliko hapa, iongeze medical insurance; na kupitia kukatwa huko kwa watumishi wa umma, huu mfuko sasa upeleke hizo fedha kule NHIF ili ukagharamie matibabu ya wanachama ama members ambao watakuwa ni wanachama wapya wa mfuko huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewaondolea wanachama ama Watumishi wa Serikali ama watumishi wa umma kuchangia mara mbili. Hivi ilivyo, watakaochangia kwenye mfuko huu watakuwa wanakatwa na upande wa NHIF ili wale members pia watakatwa. Kwa hiyo, mtumishi huyu atakuwa anakatwa mara mbili kwa jambo lile lile ambalo anaweza kulipata kwa kuchangia katika mfuko huu ambao tunatunga sheria leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naishauri Serikali na ninaamini Mheshimwa Waziri na Mwanasheria Mkuu, watalizingatia hili, walete mabadiliko ili tuweze kuwaondolea michango ya mara mbili watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ulikuwa umeegemea hapo. Naomba niunge mkono muswada huu, naomba Serikali izingatie maoni haya ili kuwaondolewa mzigo watumishi wa umma. Nashukuru sana.