Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ezekiel Magolyo Maige (28 total)

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya kweli. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kumekuwepo na malalamiko mengi sana kutoka kwa wananchi wa Mwakata walioathirika na hiyo mvua ya tarehe 3 mwaka jana kwamba usimamizi wa misaada mbalimbali nje ya ile iliyotoka Serikalini umekuwa na harufu mbaya, umekuwa na dalili za ufisadi. Nataka kujua Serikali iko tayari kufanya uchunguzi maalum wa Kiwizara ili kujua misaada yote iliyokusanywa na jinsi ambavyo ilitumika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, maafa haya yalikuwa na madhara makubwa sana kwa wananchi wanaoishi kwenye nyumba za tope. Serikali katika Ilani yake inayoitekeleza sasa hivi moja ya mkakati ni kujenga nyumba bora kwa maana nyumba za saruji. Nataka kujua Serikali imefikia wapi katika kupunguza ushuru wa vifaa vya ujenzi hasa simenti na kuweka standardization ya bei ili wananchi wanaoishi upande wa Magharibi mwa nchi yetu ambako hakuna viwanda na huipata bidhaa hiyo kwa gharama kubwa waweze kuipata kwa bei rahisi ili waweze kujenga nyumba bora na kuepuka majanga kama haya ambayo yanaweza yakawa yanajirudia endapo nyumba zitaendelea kutokuwa na ubora?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni kwamba Serikali ipo tayari siyo tu kufanya uchunguzi, lakini kuhakikisha kwamba kuna usimamizi wa karibu wa misaada yote inayotolewa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali kupitia Wizara husika na nafikiri Waziri yupo, zinatekeleza mikakati maalum ya kuhakikisha kwamba Watanzania wana uwezo wa kujenga nyumba kwa gharama nafuu.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa kupeleka fedha hizi kwenye shule za bweni zilizoko kwenye Wilaya ya Hanang. Pamoja na hatua hiyo nzuri na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nilikuwa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa kushirikiana na Mbunge wao wamefanya kazi kubwa sana ya kujenga shule pamoja na hosteli kwenye shule za Isaka, Baloha, Mwalimu Nyerere, Lunguya pamoja na Busangi. Lakini shule hizi au hosteli hizi hazitambuliki kabisa na Serikali kwa maana ya kutolewa au kupewa msaada wa aina yoyote kama inavyofanyika kwa wenzao wa Hanang. Je, Serikali inaweza sasa ikaziingiza shule hizi kwenye mpango wa kupatiwa huduma ya chakula kama ilivyofanyika kwenye maeneo mengine nchini?
Swali la pili, kwa kuwa tatizo la mabweni kwenye shule nyingi za sekondari za kata ni kubwa sana hasa kwenye shule zilizoko kwenye maeneo ya wafugaji ambao wengi wao wanaishi kwenye maeneo ya pembezoni na yenye mazingira magumu, na kwa kutambua mazingira hayo wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa kushirikiana na Mbunge wao wameanza juhudi au wanaendelea na juhudi za kujenga hosteli kwenye shule ambazo bado hazijapata ikiwemo shule za sekondari za Isakajana, shule za sekondari za Ngaya pamoja na zingine.
Je, Serikali inaweza ikachangia namna gani au ikaunga mkono namna gani juhudi hizi nzuri za wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala pamoja na Mbunge wa eneo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mbunge huyu pamoja na wananchi wake kuhakikisha kwamba wamejenga hosteli katika shule hizo za kata, lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba vijana especially wa kike au wanafunzi wa kike waweze kusoma katika mazingira rafiki. Mheshimiwa Maige nakumbuka kwamba tulikuwa pamoja katika gari yangu tukisafiri kutoka Msalala pale Mjini tukaenda mpaka kule Bulyanhulu, kwa hiyo ninalijua vizuri jiografia ya eneo lako. Naomba nikupongeze katika harakati kubwa ulizofanya na wenzako wa kule Msalala.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lako katika eneo la kwanza ulikuwa unaomba kwamba ikiwezekana shule hizi sasa ziingizwe katika utaratibu mwingine wa Kiserikali sasa vijana wa maeneo haya waweze kupewa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchakato wetu mpana tulioufanya na hili nimezungumza katika vipindi tofauti kwamba lengo kubwa lilikuwa kwanza programu ya kwanza ni ujenzi wa shule za kata, lakini suala lingine la pili inaonekana kwamba vijana wengi wanaoenda shule za kata wanapata ushawishi mkubwa sana kurubuniwa katikati tumejikuta kwamba vijana wengi wanapata ujauzito.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeelekeza maeneo mbalimbali kwamba zile shule za Kata zilizojengwa angalau ikiwezekana wazazi waone kama kutakuwa na utaratibu wa ujenzi wa mabweni ili kuweza kuwa- accomodate vijana katika mazingira ya karibu zaidi na shule. Jambo hili naomba nishukuru karibu Tanzania nzima limefanyika kwa upana mkubwa zaidi, lakini kuna shule maalum za bweni ambazo zinatambuliwa na Serikali, lakini kuna zile zingine hosteli zimejengwa na wananchi wenyewe. Tunachokifanya sasa hivi Serikali ni kumebainisha zile shule ambazo ziko katika mkakati wa Kiserikali kama tunavyozijua zile shule za Kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hivi sasa siwezi kuzungumza wazi kwamba kusema kwamba shule zote ambazo mabweni yamejengwa kwamba zitapewa chakula jambo hilo litakuwa ni jambo la uongo. Isipokuwa Serikali tunaangalia jambo hili kwa uzito wake na kufanya tathmini ya kina basi hapo baadaye kama tulivyoenda na programu ya elimu bure katika analysis ya kutosha hapo baadaye kuzibainisha baadhi ya shule tuzi - upgrade ziwe special shule za hosteli jambo hili Serikali hatutosita kuliangalia lakini jambo kubwa hilo tutafanya analysis kwa nchi nzima tutafanyaje kazi kuhakikisha mazingira bora yanatengenezwa kwa vijana wetu wasichana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sehemu ya pili ni kwamba kuna baadhi shule zingine bado hazijapata hosteli, naomba nikuunge mkono tena kwamba endelea na juhudi ile ile. Lakini naomba nikuahidi kwamba katika mipango yenu ya Halmashauri ikiwezekana ninavyofanya mchakato wa bajeti za Halmashauri wekeni vipaumbele hivyo na Ofisi ya Rais, TAMISEMI nia yake itakuwa ni kuweza kusukuma juhudi hizi za wananchi ifike muda kwamba shule zote ambazo zina changamoto kubwa tuweze kusaidia zipate mabweni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali lengo kubwa ni kwamba vijana wetu hasa wasichana watakuwa wanakwepa hivi vishawishi ambavyo vimekuwa ni tatizo kubwa sana na likiwagharimu vijana wengi kupata ujauzito.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza:-
Swali la kwanza; tarehe 3 Machi, 2015 kulitokea maafa ya mvua kwenye eneo la Mwakata kwenye Jimbo langu na watu 47 wakafa na misaada mingi ilikusanywa. Kwa bahati mbaya sana kumekuwepo usimamizi usioridhisha wa matumizi ya misaada ile na wananchi wamekuwa wakiwatuhumu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Bwana Ali Nassoro Lufunga na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, lakini pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Bwana Benson Mpesya, aliyekuwa Mkuu wetu wa Wilaya kwamba, misaada ambayo ililenga kuwafikia waathirika wa Mwakata haikuwafikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua Serikali itasaidiaje kuhakikisha kwamba, taarifa sahihi ya fedha zilizokusanywa na misaada mingine kwa ajili ya maafa ya Mwakata inapatikana kutoka kwa watuhumiwa hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, Serikali inakiri kwamba, maafa ni jambo ambalo halitabiriki na pia inakiri kwamba Serikali ina wajibu wa kusaidia wananchi. Hatutaki Serikali ilipe fidia au kufanya chochote, lakini ni kwa nini isiangalie uwezekano wa kuwa na Mfuko, kama tulivyopendekeza kwenye swali la msingi, ambao unakuwa unachangiwa kwa njia endelevu ili likitokea janga hata mnapokwenda kusaidia angalau mna mahali pa kuanzia kuepuka aibu ambayo inajitokeza kwa sasa kwamba, zinafika mpaka nchi nyingine kuja kusaidia, sisi kama Serikali tunawaomba na kuitisha harambee sisi hata shilingi moja ya kuanzia hatuna. Hivi Serikali haioni kwamba, ni aibu katika mazingira ya namna hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na upatikanaji wa taarifa sahihi kutoka kwa watu wanaotuhumiwa. Niseme tu si kupata taarifa sahihi, Serikali itafanya yote yanayowezekana kwa mujibu wa Sheria ili kupata taarifa sahihi na kama hao watuhumiwa wamefanya makosa basi hatua mbalimbali zitachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Maige ashirikiane na sisi, ili kuhakikisha kwamba, kweli kama kuna mtu ametumia fedha hizo vibaya, basi afikishwe katika mikono ya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu Mfuko. Tayari Sheria imeanzisha Mfuko wa Maafa, ni tofauti na Sheria ile iliyotungwa mwaka 1990 ambayo Mfuko ulikuwa kwa ajili ya Kamati na haukuwa umeelezewa vizuri sana. Sheria hii imeanzisha Mfuko wa Maafa ambapo una vyanzo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala kwamba ni aibu kwa wananchi kuchangia, naomba niweke sawa; masuala kama ya tetemeko ni majanga makubwa sana na Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kuchangiwa. Nitoe tu mfano, Iran lilipotokea lile tetemeko kubwa nafikiri mwaka 2013, lililofikia magnitude 7.7, mashirika mbalimbali yalisaidia ikiwemo National Federation of the Red Cross.
Mwaka 2015, Nepal kwa mfano, tunaona Wafaransa, Norway na nchi kadhaa yalisaidia, sitaki kusema nini kilitokea Japan na Indonesia na maeneo mengine ambayo matetemeko yamekuwa yanatokea mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi pia tumesikia kwa mfano Italy, ilikuwa inaomba msaada European Union ili kuangalia ni namna gani itaweza kurejesha hali baada ya kupata matetemeko kati ya Agosti na Oktoba. Kwa hiyo, kutokana na ukubwa wa matetemeko haya ni vigumu nchi kuwa haisaidiwi na ndio maana hata Umoja wa Mataifa ina wakala maalum wa kusaidia maafa kwa majanga kama haya, matetemeko, mafuriko na majanga mengine ambayo hayatabiriki. Kwa hiyo, niseme si aibu ila ni hali ya kawaida na Mfuko huu umeanzishwa kwa Sheria. Kwa hiyo, swali la pili kuhusu Mfuko nadhani limejibiwa.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa
kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la uhaba wa vyuo vya ufundi
na ahadi imekuwa ni ya muda mrefu na tatizo ni la muda mrefu. Katika
Halmashauri ya Wilaya ya Msalala tumekwishaanza juhudi za kufanya au
kutekeleza jambo hili. Kwa bahati nzuri kwa mazingira yetu tuna mgodi wa
Bulyanhulu ambao vijana wengi sana wanakosa fursa za kufanya kazi pale kwa
sababu ya kukosa elimu fulani ya ufundi na mgodi umeonesha nia ya kushirikiana
na Serikali kuutekeleza mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumwomba au kumuuliza swali
Mheshimiwa Waziri kwamba anaonaje akitusaidia katika kutia chachu
mazungumzo kati ya Halmashauri ya mgodi ili kuweza kutekeleza mradi huu kwa
yeye mwenyewe kufika na kukaa na watu wa mgodi ili kuona namna gani
tunaweza tukatekeleza mradi ambao tayari eneo lilishapatikana muda mrefu
kwenye Kijiji cha Bugarama?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu
Spika, ahsante. Niseme tu kwamba kwanza nawapongeza hao wadau wa
madini kwenye migodi wanavyotu- support katika masuala ya elimu kwa Mkoa
wa Shinyanga na Msalala nadhani ikiwa ni wanufaika wamojawapo. Kwa hiyo,
kama kuna jitihada za aina hiyo Wizara pia tuko tayari. Hata hivyo, niseme tu
kwamba Msalala mtakuwa hamjapungukiwa sana kwa sababu tayari kuna chuo
cha VETA kiko Shinyanga ambacho pia kinajihusisha na masuala ya madini.
Vilevile tunategemea kujenga chuo ambacho kitakuwa ni cha Mkoa katika
Mkoa wa Geita ambapo pia ni jirani zenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hizo jitihada nitakuwa tayari kushirikiana
nanyi kuweza kuomba kama kuna huo uwezekano.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Serikali ilikamilisha mradi wa maji wa Ziwa Victoria mwaka 2008 na kwa bahati mbaya kuna baadhi ya vijiji ambavyo bomba limepita kwenye vijiji hivyo vikawa
vimesahaulika na toka mwaka 2014/2015 vijiji kama Kabondo, Mwakuzuka, Matinje, Buluma, Mwaningi ambavyo bomba limepita wala si kilometa 12 bomba limepita kabisa kwenye
vijiji hivyo viliwekwa kwenye mpango kwamba vingepatiwa maji lakini hadi sasa vijiji hivyo havijapata maji kwa sababu fedha hazijatoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusikia uhakikisho kutoka kwa Waziri kwamba ni lini sasa vijiji hivi vitapata maji kama ilivyokuwa imeahidiwa toka miaka yote niliyoisema?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ajenda inayozungumzia ni suala zima la mradi wa maji wa Ziwa Victoria ambayo hivi sasa hata ukiangalia mradi huu hata watu wa Tabora hujo watakuja kusimama mpaka Sikonge, lakini kuna mpango mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba maji haya yanafika mpaka Tabora mpaka Sikonge, lakini kuna changamoto ya baadhi ya vijiji vingine vilivyopitiwa lakini maji havikupata na Mheshimiwa Waziri wa maji alikuwa
akizungumza mara kadhaa hapa Bungeni kwamba lengo kubwa la Serikali ni kuangalia kwa sababu maji yanakwenda kwa utaratibu maalum, lazima yafike katika tanki halafu yaweze kurudi kwahiyo yote inatakiwa ku-design ili iweze kufanyika lakini Waziri hapa alizungumza mara kadhaa kwamba kuangalia jinsi gani watu wote waliopitiwa katika bomba la Ziwa Victoria wataweza kupata maji. Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie kwa commitment ya Serikali abayo inaiweka kwa wananchi wa Tanzania na hasa wale wanaopitiwa katika bomba kubwa la Ziwa Victoria
ni kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha ni jinsi gani maji sasa maji yaweze kuwafikia Wananchi wako na wewe mwisho wa siku ni kwamba tuweze kukuona hapa Bungeni kwa heshima kubwa ya Wasukuma wa kule.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Pamoja na hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vijiji hivi ambavyo vimewekwa kwenye kundi la vijiji vilivyoko katika kilometa 12, infact viko vijiji vingine ambavyo viko ndani kabisa ya kilometa moja kwa maana kwamba vilisahaulika wakati wa usanifu wa mradi mwanzo hasa vijiji kama Matinje na Izuga. Kwa mfano pale Izuga lile bomba limepita kabisa kwenye uwanja wa shule ya msingi Izuga.
Sasa katika mazingira haya ambapo jibu linasema vitaunganishwa kutegemea upatikanaji wa fedha. Hivi ni sawa katika mazingira hayo ambayo bomba limepita pale pale kijijini halafu wanaendelea kukaa bila kujua? Nilitaka kujua Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini hasa vijiji hivi ambavyo bomba limepita pale pale kijijini kama Izuga na Matinje vitafanyiwa angalau mpango wa dharura wa kuunganishwa badala ya kusubiri mpango au lugha ya kwamba fedha zitakapopatikana? Nilitaka kujua lini katika hali ya dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika maeneo haya ambapo bomba kuu la Ziwa Victoria kutoka Mwanza kwenda Kahama na Shinyanga limepita hapakuwepo utaratibu wa kutengeneza mabirika ya kunyweshea mifugo (water traps); na mwaka 2014 tulikubaliana kwamba uwepo mpango wa kutengeneza water traps kwa ajili ya mifugo. (Makofi)
Je, ni lini Serikali sasa itafanya mpango huo ili maeneo haya pia mifugo iweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, amesema ndani ya kilometa 12 kuna baadhi ya vijiji ambavyo vimesahaulika. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hatutaacha kijiji hata kimoja, tunachotaka ni ushirikiano na Halmashauri husika kama kuna kijiji ambacho kimesahaulika basi tunaomba tupeane taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia umependa kujua ni mpango gani wa haraka, kwa mfano kama kijiji cha Mitinje, kijiji cha Izuga ambacho kina kilometa moja tu kutoka kwenye bomba. Tushirikiane Mheshimiwa Mbunge, Wizara ya Maji na Umwagiliaji kila mwaka inatenga fedha kwa kila Halmashauri. Basi ningeomba Halmashauri husika ijaribu kuangalia uwezekano wa kuunganisha kutokana na fedha tuliyotenga Wizara ya Maji na kama wanaona hawawezi basi wawasiliane na Wizara ili tufanye hiyo kazi haraka kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu mabirika. Mimi tu niseme Mheshimiwa Mbunge kwamba haya Mabirika tumepokea hii tutalifanyia kazi ili kuona ni namna gani tunaweza tukatumia maji haya ili kuweza pia kusaidia mifugo iliyo karibu na hilo bomba.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Pamoja na majibu hayo mazuri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa wananchi
wa Jimbo la Solwa, wananchi wa Jimbo la Msalala nao wameitikia vizuri sana wito wa Serikali kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa kuchangia, hivi tunavyozungumza wameshakamilisha maboma 40 ya zahanati, maboma manne ya vituo vya afya na maboma zaidi ya 70 ya nyumba za walimu na vyumba vya madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maboma haya ni ya muda mrefu, fedha ambazo zimekuwa zikiletwa mara nyingi zinatosha asilimia 10 hadi 20 ya maboma haya. Nilitaka kujua kwa nini Serikali isiwe na mpango maalum wa kufanya tathmini ya maboma yote na kuleta fedha zinazoendana na maboma ambayo yamekwisha kukamilika ili yaweze kukamilishwa badala ya kuachwa yaanguke?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, moja ya tatizo kubwa ambalo Halmashauri zinapata ni ukosefu wa fedha hasa kutoka vyanzo vya ndani, Halmashauri nyingi za mikoani zimekuwa zikipata shida kupata ushuru wa huduma kutoka kwenye makampuni ya simu. Kwa mfano, Kampuni ya Airtel inalipa zaidi ya shilingi bilioni tano kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, wakati minara yake imetapakaa nchi nzima. Kwa nini Serikali isizisaidie Halmashauri kule ambako minara ipo, ushuru wa huduma ukalipwa kule ili Halmashauri ziweze kupata fedha za nyongeza kutekeleza miradi kama hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyosema tunapokea, lakini nilitaka nimshukuru Mheshimiwa Maige kwa sababu kwao kule wamejenga maboma mengi sana lakini kwa kushirikiana na ile Kampuni ya Madini, wameendelea kujenga vituo vya afya. Hata hivyo, kipindi kirefu fedha zilikuwa haziji sasa kuanzia mwaka huu Wizara yetu imesimamia upatikanaji wa fedha na ndio maana mkiangalia kuna maboma mengi sana tunaanza kurekebisha. Bajeti ya mwaka huu tena kama mnakumbuka wakati tunapitisha bajeti hapa tumetenga fedha nyingine kuhakikisha kwamba maboma mbalimbali tunaweza kuyakamilisha katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie kwamba katika mwaka wa fedha unaokuja kutakuwa na mabadiliko makubwa sana katika umaliziaji wa maboma haya, kwa sababu yote haya tumeshayafanya tathmini Wizara ya TAMISEMI.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Isaka toka miaka ya 1990 imekuwa inajulikana kwamba ni bandari ya nchi kavu, uwekezaji mkubwa sana unafanyika pale na nchi jirani na hivyo ardhi imekuwa ni kitu adimu na uvamizi ni mkubwa. Kwa zaidi ya mwaka sasa wananchi wa Isaka walishaomba eneo hilo liwe mji mdogo na maombi yalishawasilishwa Wizarani lakini kumekuwa na ukimya. Nataka kujua ni hatua gani iliyofikiwa kwa lengo ya kuitangaza Isaka kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia maswali mengi na karibu maswali yote yanaomba Miji Midogo. Tunazo Mamlaka za Halmashauri 185 kwa nchi nzima. Tunayo Miji Midogo mingi, mingine inafanya kazi na mingine imeshindikana hata kuanza; lakini pia ndiyo unasikia maswali haya mengi, Bwana Keissy, Mipata wanazungumzia Namanyere, ukimuuliza Mheshimiwa Kikwembe hapa, anazungumzia Majimoto, ukimuuliza Mheshimiwa Edwin Ngonyani anazungumzia kule kwake Namtumbo kule na Lusewa; wengine wanazungumzia Isaka. Kwa hiyo, hapa Waheshimiwa Wabunge wana maswali haya mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jibu lake ni hili; ili uweze kuanzisha Mji Mdogo, lazima uangalie kwanza uwezekano wa kuweza kuwa na mapato ya ndani ya kujiendesha. Huanzishi tu halafu Serikali unataka ilete fedha ya kuendesha. Hizi Mamlaka 185 tulizonazo zinashindikana kupata fedha Serikalini kuziendesha; tunapoanzisha mamlaka nyingine tunaleta contradiction, kwa sababu kimsingi hizi mamlaka zinazaliwa na mamlaka mama. Halmashauri mama ndiyo inayozaa Mji Mdogo. Unaposema unaanzisha Mji Mdogo ukapeleka setup ya watumishi pale, maana yake Halmashauri mama ianze kugawana mapato na Halmashauri hii ndogo unayoianzisha ya Mji Mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa jambo hili mwanzo wake (genesis) yake ni huko huko kwamba je, hivi tunao uwezo wa kuweza kuanzisha mamlaka hii na ikajiendesha?Je, vyanzo hivi vikichukuliwa na Mji Mdogo, haviathiri Halmashauri mama? Ukimaliza stage hiyo sasa ukaona umejiridhisha, sasa omba.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha msingi ninachoweza kushauri Waheshimiwa Wabunge, ili kuweza kwenda na hatua nzuri, hebu twende na stages kama inavyokwenda Lamadi. Kwamba Lamadi wameshafanya Mipango Mji wa ile sehemu; wameipima, lakini wameshajitosheleza katika huduma kama za maji, lakini wamekwenda mbali zaidi wanajenga mpaka barabara za lami; sasa ukifika mahali hapo; kwa mfano, nafahamu kwamba Lamadi sasa wawekezaji wanaojenga mpaka hoteli za kitalii maeneo yale; kwa hiyo, naamini haka kamji kanaweza kakajiendesha.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwasihi, hebu jambo hili twende nalo taratibu. Kama tuliahidi, hebu twende nalo taratibu kwa sababu uamuzi wake utazingatia sana tathmini ya tulikotoka, Miji Midogo tuliyoianzisha imefika wapi na hali ikoje? Ndiyo tufikie uamuzi wa kuamua ku-establish mamlaka hizi ndogo ndogo mpya.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri unisikilize vizuri. Msimu uliopita wa mwaka juzi, wakulima wa pamba wote wa Kanda ya Ziwa walilazimishwa kutumia dawa ya kuua wadudu inayoitwa Ninja. Dawa hiyo ilikuwa inasambazwa na Bodi ya Pamba na haikusaidia kabisa na pamba iliharibika kabisa kwa sababu haikuwa na ubora. Niliuliza swali hapa Bungeni nikaahidiwa na Serikali kwamba, na yenyewe imethibitisha kwamba suala hilo ni kosa la uhujumu uchumi, kwa hivyo, wahusika watapelekwa mahakamani na wakulima watalipwa fidia ya gharama waliyotumia kununua ile dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kujua kwamba Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa hilo jibu ambalo Serikali iliniambia hapa Bungeni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba iligundulika kwamba ilitokea matatizo makubwa kwa wakulima wa pamba waliotumia kiuatilifu ambacho kilikuwa kinatiliwa shaka kuhusu ubora wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na uchunguzi kubaini ni nini hasa kilitokea, kwa sababu tayari kuna mvutano kuhusu je, suala lilikuwa ni ubora wa dawa, namna ya matumizi, namna ya matunzo au ni suala la wakulima wenyewe walivyotumia ile dawa. Kwa hiyo, Serikali bado inaendelea na uchunguzi, lakini pale itakapobainika kwamba ni kweli kabisa kwamba suala ni kuhusu ubora sheria zitachukua mkondo wake. Kama nilivyosema, itakuwa ni pamoja na kuwafungia na kuwachukulia hatua wale wote ambao wamehusika. Vile vile ikibainika kwamba kampuni ambazo zili-supply hiyo dawa kwa Bodi ya Pamba wao watawajibika moja kwa moja katika kuhakikisha kwamba wakulima wanalipwa fidia. Hata hivyo kama nilivyosema suala hili bado linachunguzwa, tufahamu hasa kiini kwa sababu bado kuna mvutano kuhusu sababu hasa yenyewe iliyosababisha tatizo hilo.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba kwa sababu ndiyo nazungumza mara ya kwanza baada ya sakata la makinikia kuwa limepata mwelekeo, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa hatua alizochukua. Hatua ambazo zimekuwa ni kilio changu na kilio cha wananchi wa Msalala kwa miaka yote toka Mgodi wa Bulyanhulu ulipokuwepo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa sababu, wananchi kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema, wameitikia vizuri sana katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa huduma za afya katika Halmashauri na jimbo lao na kwa sababu, changamoto ambayo ipo ni upatikanaji wa fedha Serikalini na kwa bahati nzuri tayari tumeshapata uhakika kwamba, tutalipwa zaidi ya bilioni 700 kutika kwenye makinikia.
Je, Serikali inaweza sasa ikakubaliana na ombi langu kwamba ni vizuri tukapata angalao shilingi bilioni 3.4 ambazo zinatakiwa kuyakamilisha maboma yote haya, ili wananchi hawa wasione nguvu zao zikiharibika kwa sababu mengine yana zaidi ya miaka saba toka yalipoanzishwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa tayari tumeshaletewa shilingi milioni 400 kwa ajili ya uboreshaji wa Kituo cha Afya cha Chela, fedha ambazo pamoja na kwamba ni nyingi, lakini bado hazitoshi kwa sababu, malengo ni makubwa zaidi. Je, Serikali inaweza ikakubaliana na ushauri wangu kwamba, kwa sababu lengo nikupeleka huduma kwa wananchi wengi zaidi na kuna maboma tayari kwenye Vituo vya Afya vya Isaka, Mega na Lunguya ambavyo kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri kwamba viko kwenye hatua mbalimbali. Je, Waziri anaweza akatukubalia ombi letu kwamba fedha hizi tuzigawanye kwenye hivi vituo, ili angalao navyo viweze kufunguliwa halafu uboreshaji utakuwa unaendelea awamu kwa awamu kadri fedha zinavyopatikana kuliko kukaa na kituo kimoja na vingine vikaishia kwenye maboma kama ilivyo sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya ombi la uwezekano wa kutizama hii bilioni 3.4 zitumike ili kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya pamoja na zahanati; kimsingi hitaji ni kubwa sana, lakini si rahisi kabla ya kufanya hesabu kujua katika mahitaji mengine kiasi gani kiende upande wa afya, kwani vipaumbele ni vingi. Kwa hiyo, ni vizuri, ni wazo jema likachukuliwa likafikiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya shilingi milioni 400 ambazo zimepelekwa, Mheshimiwa Mbunge anaomba kwamba ziruhusiwe zihame kwenda kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ili tuweze kukamilisha kituo cha afya kwa mujibu wa standard, lazima tuwe na uhakika chumba cha upasuaji kipo, wodi ya wazazi kwa maana ya akina mama na watoto, wodi ya akina baba ipo, maabara, nyumba za watumishi za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachowaomba na niziagize halmashauri zote, pale ambapo pesa zimeletwa na Serikali si lazima, eti pesa hiyo iishie hapo, itumike busara kuhakikisha kwamba, kwa utaratibu wa Force Account tunatumia pesa ili ikibaki tukiwa na serving hakuna dhambi ya kuhakikisha kwamba, pesa hizo zinaweza zikahamia kwenda kumaliza matatizo mengine. (Makofi)
MHE. EZEKIEL G. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza:
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Msalala kama ambavyo umesikia maeneo mengine haya mawili ambayo yameuliziwa maswali Songea Mjini na Mbogwe, wao pia wana maboma ya zahanati na vituo vya afya na bahati nzuri wenyewe wamekwenda mbali zaidi, kuna maeneo ambapo kumetajwa kwamba maboma yako kwenye lenta. Wananchi wa Jimbo la Msalala wana vituo vya afya vinne ambavyo vimekwishakamilika maboma yake, zahanati 38 ambazo zimekwishakamilika maboma yake. Maboma haya yamejengwa zaidi ya miaka mitatu na sehemu vimeanza kubomoka. Imefika mahali sasa wananchi wanagomea michango mingine wakisema kamilisheni kwanza miradi tuliyokwishaianza.
Nataka tu kujua toka Serikalini ni lini sasa Serikali na yenyewe italeta nguvu yake ambayo wastani ni kama bilioni ili kukamilisha maboma haya 42, manne ya vituo vya afya na 38 ya zahanati, Msalala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa dhati kabisa nianze kwa kumpongeza kwa jitihada kubwa ambazo anafanya kwa wananchi wa Jimbo la Msalala, kwa ujenzi mkubwa ambao umefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiongea mara nyingi alichokuwa anaomba kwanza katika hizi pesa ambazo zimepatikana zikitumika zikakamilisha hayo majengo ambayo yanatakiwa kujengwa katika vituo vya afya, anataka hicho kiasi kinachobaki kipelekwe kwenye maeneo mengine. Jambo ambalo Serikalini wala hatuna ubishi nalo ni kuhakikisha kwamba jitihada za wananchi na tukibana vizuri pesa zikatumika maeneo mengine yaweze kujengwa kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunakamilisha ujenzi wa vituo vya kutolea afya 1,845 na hivi tutavikamilisha.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi naomba nimshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na naomba tu niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, vijiji hivi 100 kimsingi ni ahadi iliyotolewa na Serikali mwaka 2014 hapa Bungeni na ilitegemewa kufika mwaka 2015 vingekuwa vimepata huduma ya maji, lakini mpaka sasa hivi kama ambavyo jibu limeeleza kwamba fedha hazijapatikana.
Nilitaka nipate tu uhakikisho wa Mheshimiwa Waziri, kwamba kwa mwaka huu wa fedha tunaouanza 2018/2019 je, Serikali inaweza ikamaliza hii ahadi ya muda mrefu ili vijiji hivyo vipate maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hivi sasa Serikali inatekeleza miradi miwili mikubwa ya maji. Mmoja ni wa maji kutoka Kahama kwenda Isaka na mradi mwingine ni wa kutoka Mangu kwenda Ilogi. Miradi hii yote inatekelezwa kwa awamu ya kwanza kwa maana ya kupeleka bomba kuu peke yake bila usambazaji kwenye vijiji vilivyo jirani. Ahadi imekuwa kwamba awamu ya pili ambayo itaanza 2018/2019 itahusisisha usambazaji wa maji kwenye vijiji vilivyo jirani.
Je, Waziri anaweza akanihakikishia kwamba utekelezaji wa hii awamu ya pili ambayo itahusisha usambazaji wa maji kwenye vijiji vilivyo jirani katika miradi hiyomiwili utatekelezwa pia?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba awali ya kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anazozifanya katika jimbo lake na kuwatetea wananchi wake wa Msalala.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kabisa ahadi ni deni na hii ni ahadi ya Serikali. Nataka nimuhakikishie kwamba katika vile vijiji 100 sisi kama Wizara ya maji tulikuwa tukitoa fedha na tutaendelea kutoa katika kuhakikisha vijiji vinapatiwa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu katika vijiji ambavyo vipo katika awamu ya pili, tunatambua siku zote safari yoyote ni hatua. Tumeshaanza hatua ya kwanza katika kuhakikisha kwamba tunaliweka bomba kuu, na tutahakikisha kwamba baada ya kukamilika utandazaji wa bomba hili kuu vijiji vilivyokuwa jirani ya kilometa 12 vyote vitapatiwa maji; ahsante sana. (Makofi)
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Serikali kwa ujumla kwa hatua hii ambayo imefikiwa; na nikiri kwamba ni kweli fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi. Hata hivyo nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa fedha zilizotengwa bilioni kumi na mbili ni kidogo sana ukichukulia wastani wa ujenzi wa kilomita moja haipungua bilioni moja, kwa hiyo fedha zinazotakiwa ni karibu bilioni
140. Kwa kuwa fedha zilizotengwa bilioni kumi na mbili ni kidogo sana na kwa maana hiyo inaweza ikachukua muda mrefu sana barabara hii kuanza kujengwa, je, Serikali haioni kwamba kwa mazingira tuliyonayo hivi sasa, ambapo tayari tuna makontena 277 yenye zaidi ya thamani ya bilioni 600 ambayo ni dhahiri kwamba kuna ukwepaji kodi mkubwa; je, Serikali haiwezi ikaona namna ya kutumia kiasi cha fedha kitakachopatikana kutokana na kodi hiyo iliyokwepwa ili kuweza kupata fedha za kujenga mara moja barabara hii kwa mwaka huu wa fedha tunaouanza? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali pili; wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, pamoja na wenzao wa Wilaya ya Nyang’hwale walishiriki kwenye mkutano wa kampeni wa Mheshimiwa Makamu wa Rais pale Kalumwa, na Mheshimiwa Makamu wa Rais aliahidi kwamba barabara ya kutoka Kalumwa kwenda Mwanza iko kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami na Serikali iko katika mpango wa kuangalia uwezekano wa kuunganisha kutoka Kalumwa kuja hadi Kahama. Je, Serikali imefikia wapi, katika utaratibu huo au mpango huo, au utekelezaji wa hiyo ahadi ya Makamu wa Rais wa kujenga barabara ya kutoka Kahama kupita Busangi, Chela, Nyang’holongo, Kalumwa hadi Mwanza kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaomba Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige akumbuke kwamba suala la ukwepaji halina uhusiano sana na ukiangalia jibu la msingi nililolitoa. Maadam Kampuni ya Acacia Mining imeonesha nia ya kushirikiana na Serikali tuna uhakika tutaendelea kuwafuatilia ili tuongeze fedha za ujenzi wa barabara hii ili iweze kukamilika kwa haraka zaidi. Suala hili la kitaifa la ukwepaji naomba tumuachie Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alikamilishe kwa namna alivyolianzisha baada ya hapo ndipo tuweze kuliongelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili ni kweli Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan alitoa hiyo ahadi na mimi naomba tu nikuhakikishie kwamba ahadi hii aliyoitoa mbele yako Mheshimiwa Mbunge ukiwawakilisha watu wako wa Msalala sisi Serikali tumeambiwa na tunaanza kuingiza katika mchakato wa kuitekeleza ahadi hiyo kama ambavyo tunapanga kutekeleza ahadi zote ambazo viongozi wetu wakuu wamekuwa wakizitoa sehemu mbalimbali za nchi. (Makofi)
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jiografia ya Jimbo na Halmashauri ya Wilaya ya Msalala wewe unaifahamu lakini pia hata Mheshimiwa Kandege anaifahamu kwamba vituo vya afya vimejengwa sana na wananchi na hivi sasa tuna vituo vya afya vitatu, cha Isaka, Ngaya na Bugarama. Lakini vituo vyote hivi havina gari la wagonjwa na kwa Halmashauri nzima gari ambalo linafanya kazi ni gari moja tu. Wananchi wamefanya kazi kubwa na wanaamini Serikali yao pia inaweza ikawashika mkono.
Kwa hiyo, nilitaka kujua Mheshimiwa Waziri unawaahidi nini wananchi hawa angalau kuwapatia gari angalau kwenye kituo kimoja katika hivi vitatu nilivyovitaja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna Halmashauri za kupigiwa mfano na kama kuna Wabunge ambao wanatakiwa wapongezwe ni pamoja na Mheshimiwa Maige. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni katika Halmashauri ambazo wamejenga vituo vya afya vingi, hongereni sana. Pia nimuombe Mheshimiwa Maige kwa kushirikiana na Halmashauri yake, natambua uwezo mkubwa wa Halmashauri yake hakika wakiweka kipaumbele kama ni suala la kununua gari hawashindwi na wengine wataiga mfano mzuri ambao wao wanafanya na hasa katika own source zao ambao wanapata mapato mazuri ni vizuri katika vipaumbele wakahakikisha wananunua na gari la wagonjwa kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Msalala.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kabla sijauliza maswali ya nyongeza naomba nioneshe tu masikitiko yangu kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri kimsingi hajaenda kwenye thrust ya swali langu.
Swali langu nimeuliza je, ni hatua gani imefikiwa katika mazungumzo kati ya ACACIA na Serikali kuhusu ulipaji wa fidia na athari nyingine ambazo wananchi wa msalala wamezipata?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika majibu yake pia, amesema kwamba hakuna fidia inayodaiwa, jambo ambalo si kweli kwa sababu kwa miaka 22 Serikali inafahamu kwamba watu walioondolewa mwaka 1996 Bulyanhulu, hakuna shilingi moja iliyolipwa. Mbaya zaidi kwa hawa wagonjwa Serikali imesema wamepatikana wagonjwa 78, lakini haijasema hatua gani zinachukuliwa kuhakikisha wanatibiwa, kwa sababu tayari kuna watu 49 wameshafariki na hawajalipwa fidia yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa sababu uharibifu au wizi uliofanywa na ACACIA kwa Tanzania haujafanywa kwa Tanzania peke yake, umefanywa hasa kwa wananchi wa Bulyanhulu pia; na kwenye ripoti ya Profesa Ossoro ilionesha mabilioni mengi ambayo Tanzania ilipaswa kupata na mimi nilishasema kwamba wananchi wa Msalala wanastahili kulipwa shilingi bilioni 973 kama service levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilitaka kujua kwa sababu ACACIA walisha-concede hivyo na tayari walishatoa kishika uchumba kwa Serikali, kile cha dola milioni 300. Nilitaka kujua kwa wananchi wa Msalala wanaodai bilioni 973, je, Serikali inaweza ikawasaidia sasa ili angalau katika hii mitambo inayotaka kuuzwa na ACACIA ikabidhiwe kwa Halmashauri kama sehemu ya fidia ya service levy ambayo haijalipwa kwa miaka yote? Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili,...
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Swali la pili, katika uwasilishwaji wa taarifa ya mazungumzo Mheshimiwa Rais aliagiza kwamba uchunguzi ufanyike kwenye migodi mingine kuhusu utoroshwaji wa madini, ukiacha makinikia peke yake, utoroshwaji wa vitofali vya dhahabu na Wizara iliagizwa kwamba ifanye uchunguzi kwenye migodi mingine. Nilitaka kujua uchunguzi kwenye hilo eneo umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la msingi imeonesha kabisa Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusiana na masuala ya fidia. Kwa taarifa tulizonazo katika Wizara yetu ni kwamba Mgodi ule wa Bulyanhulu ulivyokuwa unaanzishwa na kuanza kufanya kazi zake mwaka 2000 hakukuwa na madeni yoyote ambayo mgodi unadaiwa. Isipokuwa kama Mbunge ana hao watu ambao anawafahamu wanadai fidia katika yale maeneo kwa sababu yale maeneo ya Mgodi wa Bulyanhulu waliyapata kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli kuna watu ambao wanadai fidia zao, basi tunamuomba Mheshimiwa Mbunge awalete hao watu na madai yao, sisi kama Wizara tuko tayari kuwasimamia na kuhakikisha kwamba hakuna mwananchi yeyote anayedhulumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile ni kwamba ile taarifa ya ACACIA ambayo waliji-committ kutoa kishika uchumba, Serikali inaendelea na mazungumzo na uchunguzi ambao uliweza kutolewa, kama vile yalivyoweza kutolewa yale maoni na zile kamati mbili teule za Mheshimiwa; Rais ni kwamba yale mashauriano au ushauri uliotolewa wa uchunguzi, uchunguzi unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama itaonekana katika vile vitofali kuna wizi wa dhahabu ulitokea kwa sababu, kulikuwa kuna under declaration. Kama kweli ilitokea ni kwamba wale wa ACACIA wako tayari kuweza kutoa au kulipa fidia zote ambazo wameji-committ na walitoa kishika uchumba cha dola milioni 300, kwa maana ya kwamba waliji-committ kwamba kama kutakuwa na pesa nyingine za kutoa basi wataendelea kufidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ni kwamba maongezi yanaendelea na uchunguzi unaendelea na kama kuna upungufu wowote au kama kuna fedha yoyote ambayo inatakiwa ilipwe katika Halmashauri, kama service levy, na wewe mwenyewe umetaja kwamba kuna bilioni 973 kama kweli ni haki ya Halmashauri haki hiyo italetwa katika halmashauri hiyo. Uchunguzi unaendelea na maongezi yanaendelea. Nashukuru sana.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Chifu Kwandikwa, Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo amerasimisha hapa kwa sababu tunayaongea sana haya hata jana tulikuwa tunaongea ofisini kwake. Lakini nilipenda tu angalau anisaidie kurasimisha pia mengine ambayo tuliyaongea lakini hayako kwenye jibu hili la msingi yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, barabara ya kutoka Kahama kwenda Mwanza kupitia Bulige imekatika kabisa kile kipande cha kutoka Bulige kwenda Mwakitolyo kwa sababu ya hizi mvua zinazoendelea, lakini vilevile hata ile ya kupita Busangi - Kharumwa hadi Busisi na yenyewe imeharibika kwa kiasi kwamba magari madogo hayawezi kabisa kupita. Wakati mipango hiyo ya kujenga kwa kiwango cha lami ikiendelea ni hatua gani Serikali inafanya kwa dharura ili kuzitengeneza barabara hizi ziweze kupitika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali ilishaahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Kahama kupitia Segese – Mgodi wa Bulyanhulu hadi Geita kwa kiwango cha lami. Kwa miaka miwili mfululizo mwaka wa fedha uliopita na huu mwaka tulionao sasa hivi, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami. Nilitaka tu Mheshimiwa Naibu Waziri kama ulivyonithibitishia mimi tulivyokuwa wenyewe, wathibitishie wananchi na watanzania ni lini hasa sasa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kahama - Geita utaanza. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza pongezi alizozitoa nazipokea. Lakini nitakuwa mchoyo kama sitakushukuru wewe binafsi wakati wa mjadala wa Bajeti ya Maji ulilisemea sana Jimbo la Ushetu, kwa hiyo nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, nimjibu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nakupongeza sana kwa kufuatilia barabara hizi ambazo zinaunganisha Mji wa Kahama ikiwepo hii barabara muhimu uliyoisema inayotoka Mji wa Kahama ikipitia maeneo ya Ntobo, maeneo ya Segese ikipitia pia katika Jimbo la Mheshimiwa Bukwimba ikielekea kule Geita na wewe mwenyewe unafahamu kwamba tumeanza ujenzi wa barabara hii kiwango cha lami.
Kwa hiyo, niwathibitishie tu wananchi wote maeneo hayo kwamba ujenzi umeanza ila juhudi zitaendelea kufanyika kuweka fedha za kutosha ili barabara muhimu hii iweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, niwape pole wananchi kote nchini kwamba tumepata mvua nyingi na Mheshimiwa Ezekiel unajua kwamba barabara hii unayoitaja inayopita maeneo haya ya Mwakitolyo kwenda Mwanangwa kumekuwa na shida kubwa kwamba barabara zimekatika lakini bado pia kuna wananchi ambao nyumba zao zilidondoshwa kutokana na kuwa na mvua nyingi.
Mheshimiwa Spika, sisi upande wa Serikali tumejipanga kwa hatua ya kwanza kwamba kwanza tunayo bajeti kwa ajili ya kutibu emergency kama hizi. Tutatumia fursa hiyo, lakini pia tunafanya uratibu maeneo yote nchini lakini pia ninazo taarifa kuwa Mkoa wa Shinyanga kwamba Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza amefanya survey kwenye barabara hii na kutambua mahitaji muhimu ya maboresho katika barabara hii. Kwa hiyo, nikuombe tu uvute subira na niwatoe hofu wananchi kwamba barabara hii tunaenda kuifanyia marekebisho na niwapongeze kwa kweli Mameneja wa TANROADS mikoa yote kwa kazi nzuri ya uratibu wanayoendelea kuifanya muda huu ambao tuko kwenye shida. (Makofi)
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maelekezo yako lakini kipekee nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri japo ni marefu kama ambavyo umesema.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu hayo mazuri, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, wananchi wa Halmashauri na Jimbo la Msalala kama walivyo ndugu zao wa Jimbo la Nyang’hwale na kwa kushirikiana na Mbunge wao hivyo hivyo nao wamefanya kazi kubwa sana ya kuanza kujenga shule mpya za sekondari, Shule za Mwazimba na Nundu ambazo miundombinu aliyoitaja Mheshimiwa Naibu Waziri karibia yote imekamilika, lakini shule hizi hazijapata kibali cha kufunguliwa.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua ni lini shule hizi mbili za Nundu na Mwazimba katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala zitafunguliwa kuanza kupokea wanafunzi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Msalala kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Msalala katika kipindi cha miaka minne iliyopita wamefanikiwa kujenga hosteli kwenye shule saba za sekondari za Kata, shule za Busangi, Baloha, Segese, Lubuya, Bulige, Ntobo…
Mheshimiwa Spika, samahani, naomba nimalizie tu swali langu fupi kwamba shule hizi zina watoto lakini hazitambuliwi na Serikali na hazipati ruzuku ya uendeshaji wa hosteli. Ni lini shule hizi zitatambuliwa na Serikali ili ziwe zinapata ruzuku ya gharama za uendeshaji wa hosteli hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimsihi Mheshimiwa Mbunge taratibu zifuatwe ili hizo shule ziweze kufunguliwa. Kwa sababu ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba pale ambapo miundombinu ya shule imekamilika zinaweza kufunguliwa ili wananchi wetu wapate huduma kwa karibu.
Mheshimiwa Spika, katika hilo la pili amesema kwamba hosteli zimejengwa sasa anataka Serikali ianze kuhudumia hosteli.
Mheshimiwa Spika, sina uhakika kama msingi wa swali ni juu ya kwamba hosteli ikishajengwa ianze kupata huduma, lakini kama nimemuelewa sawasawa kwamba anachomaanisha ni kwamba shule hiyo itambuliwe kwamba ni miongoni mwa shule za boarding, naomba tu tufuate taratibu ili wananchi na hasa vijana wetu ambao wana adha ya kutembea umbali mrefu hosteli pale inapokamilika huduma ziweze kutolewa.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na hasa hili la kukubali ombi la kutuletea angalau gari moja kwa ajili ya kusaidia shughuli za polisi. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kutambua kwamba Jeshi la Polisi lina idadi ndogo sana ya askari, wananchi wa Msalala pamoja na kanda nzima ya ziwa walishaanzisha utaratibu wa ulinzi wa jadi (Sungusungu) ambao ni askari wa kujitolea na husaidia sana shughuli za polisi kukabili matukio pale ambapo polisi wanakuwa hawajafika. Kwa bahati mbaya sana Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi limekuwa likitoa ushirikiano mdogo sana kwa watu hawa ambao wanafanya kazi kwa kujitolea na mara nyingi wamekuwa wakiwa-harass pale tukio linapotokea badala ya kuwatafuta wahalifu wanakwenda kukamata wale viongozi wa Sungusungu na kuwalazimisha au kuwataka kwamba wasaidie kutaja au kutoa taarifa ambazo zingeweza kusaidia Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua Serikali au Wizara inachukua au ina mkakati gani wa kushirikiana na Jeshi la Sungusungu ili kusaidia jitihada ambazo tayari zipo kwa sababu pia askari wenyewe wa polisi si wengi kama ambavyo jibu limejitokeza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwepo na matukio mengi ya askari polisi kubambikizia wananchi kesi mbalimbali jambo ambalo limekuwa likiwavunja moyo sana wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi, jambo hili limekuwa likijitokeza kwenye vituo mbalimbali hasa vilivyoko Kata ya Isaka , Kata ya Bulige na hata Kata ya Bulyanhulu. Je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri atakuja kukutana na wananchi wa maeneo hayo ili kuweza kusikia kero hii na kuweza kukemea askari hao wenye tabia mbaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba siku zote tumekuwa tukihamasisha na tunaona umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika kushirikiana na vyombo vya dola kukabiliana na uhalifu nchini na ndiyo maana kupitia Kamisheni yetu ya Polisi Jamii ambayo tunayo, tumekuwa tukiandaa utaratibu mzuri, ili utaratibu huo ambao umekuwa ukitumika wa kushirikisha wananchi, ikiwemo Polisi Jamii, ikiwemo Sungusungu, uweze kufuata misingi ya kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia Kamisheni yetu hii ya Polisi Jamii tumekuwa tukitoa miongozo mbalimbali, ili wananchi waweze kutekeleza majukumu yao bila kukinzana na sheria za nchi yetu. Kama kutakuwa kuna mambo yametokea ambayo yanaweza kuwa yamesababishwa aidha na kutokana na uelewa mdogo wa ufahamu wa sheria wa jinsi ya hawa ambao wanaisaidia Polisi kutekeleza hizi shughuli za Polisi Jamii ama itakuwa mengine yametokea labda kwa makosa mengine, labda Mheshimiwa Mbunge labda atuwasilishie tuweze kuyashughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili kuhusiana na ubambikaji kesi, binafsi nilifanya ziara katika Mkoa wa Shinyanga na moja katika mambo ambayo niliyakemea baada ya kutembelea baadhi ya vituo na magereza katika maeneo ya Mikoa ile ya Kanda ya Ziwa na kupata malalamiko ya baadhi ya wananchi ambao walikuwa wamesema wamebambikiwa kesi, moja ni jambo hili ambalo tulilichukulia kwa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ombi lake la kutaka nifanye ziara katika jimbo lak mahususi, kwa ajili ya kufanya kazi hii ambayo tumeshaifanya katika maeneo mengine ya Mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine nchini ambayo imesaidia sana kupunguza malalamiko haya kwa wananchi tutaifanya baada ya Bunge hili kumalizika tutaandaa hiyo ziara ya kwenda jimboni kwake kwa ajili ya kushughulikia jambo hili mahususi.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Wananchi wa Kata za Isaka, Mwalugulu, Isakajana pamoja na Mwakata walishakamilisha mchakato wa kuanzisha Halmashauri au Mamlaka ya Mji Mdogo wa Isaka na taratibu zote ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezielezea hata hapa hadi kufika hatua ya kufika kwenye ofisi ya Waziri mhusika wameshafikia. Nataka kujua tu ni lini sasa hatimaye Mamlaka ya Mji Mdogo wa Isaka itaanzishwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Ezekiel Maige kwamba maombi ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Isaka yameshapokelewa, yanafanyiwa kazi, lakini tunawaomba wananchi wasubiri pale ambapo tutakuwa tayari mara moja tutatangaza.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri naomba tu kuuliza tu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kumekuwepo malalamiko sehemu nyingi za Shinyanga na hata Kahama kwa baadhi ya wazee kutokukamilishiwa utaratibu wa kupata vitambulisho ili wapate huduma za tiba bure kama Serikali ilivyowaelekeza. Je, Serikali inachukua hatua gani kuweka maelekezo maalum kwa Watendaji wa Serikali wa Kata na hata Vijiji ili kukamilisha zoezi hili wazee wapate tiba baila usumbufu?


Mheshimiwa Spika, swali la pili wananchi pamoja na Serikali hasa katika maeneo ya Msalala wamefanya kazi kubwa ya kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya na hivi sasa kwa mfano Msalala tuna vituo vya afya vipya viwili, kituo cha Bugalama na Chela. Lakini vituo hivi havina vifaa tiba wala madawa ya kutosha pamoja na watumishi. Je, Serikali inachukua hatua gani kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba, dawa na watumishi kwenye kituo cha afya cha Chela pamoja na Bugalama ambavyo ni vituo vya afya vipya nashukuru?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kwa lengo la kutoa vitambulisho ambavyo vitawatambua wazee zaidi ya miaka 60 ili waweze kupata matibabu kwa mujibu wa sera tunatambua kwamba baadhi ya Halmashauri hazijatekeleza hilo na nitumie fursa hii kuzikumbusha hizo halmashauri kuzingatia hili agizo la Serikali kuhakikisha kwamba wazee wote ambao wako zaidi ya miaka 60 wanapata vitambulisho.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri alifanya uzinduzi wa mpango mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wazee na Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo kwamba Wizara iharakishe zoezi la kufanya mapitio ya sera ya wazee ya mwaka 2003. Lakini vilevile kuanzisha na sheria ya wazee ili sasa haya mahitaji ya wazee yawe kwa mujibu wa sheria na sisi kama Wizara tumeshaanza utekelezaji wa hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili kuhusiana na vituo vya afya ambavyo vimeboreshwa nimthibitishie tu kwamba Mheshimiwa Mbunge kwamba baada kazi ya kukamilika ya ujenzi wa maboma ya vituo vya afya. Serikali inaendelea na utaratibu wa kupata vifaa kwa ajili ya vituo vyote vya afya ambavyo vimeboreshwa, baadhi ya vifaa vimeshafika na vingine viko njiani vinakuja.

Nimthibitishie tu kwamba Mheshimiwa Mbunge vifaa hivyo vinakuja na tutaendelea kupatia watumishi wa kutosha kadri ya uwezo na Serikali itakapokuwa inaajiri. Lakini nimuhakikishie kwamba dawa tunazo za kutosha zaidi ya silimia 90 kwa hiyo, mgao wa dawa tutauongeza kulingana na mahitaji.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona na kunipa nafasi, lakini pia naomba nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Pamoja na majibu hayo, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza; Mheshimiwa Waziri Mkuu pia alifanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala na kwa kuona hali ilivyokuwa na hasa wananchi walivyojitolea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kukabiliana tatizo la afya, alikubali pia kutushika mkono kwa kutupatia shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Isaka. Nataka kufahamu ni hatua gani imefikiwa katika utekelezaji wa ahadi hiyo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu?

Swali la pili; kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba kuna Halmashauri 67 ambazo zimepatiwa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi kwa Hospitali za Wilaya, kwa bahati mbaya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala haina hospitali ya Wilaya na haiko katika hizi Halmashauri 67. Nataka kufahamu: Je, itawezekana sasa kwa awamu hii ambayo itakuwa ni ya pili mwaka 2019/2020 Halmashauri hii nayo ikatengewa hiyo fedha ili na yenyewe iweze kupata Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kipekee kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Maige na wananchi wake jinsi ambavyo wamekuwa wakijitolea katika suala zima la afya, wamejenga maboma mengi kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu ametembelea Msalala na akahaidi kwamba na Kituo cha Afya Isaka nacho kingeweza kupatiwa fedha; ni ukweli usiopingika kwamba Isaka ni miongoni mwa eneo ambalo lina watu wengi na iko haja ya kuhakikisha kwamba kunakuwa na Kituo cha Afya ili kupunguza adha ya wananchi wengi kupata huduma ya afya. Naomba aendelee kuiamini Serikali kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba kwa kadri fursa ya fedha inapopatikana ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba ahadi zote za viongozi wa Kitaifa tunazitekeleza. Nasi bado tunakumbuka hiyo ahadi, naomba Mheshimiwa Maige avute subira.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba katika Halmashauri 67, Halmashauri yake haikuwa miongoni mwa zile ambazo zilipata fursa ya kujengewa hospitali. Sina uhakika katika orodha ya hivi sasa hivi tuna jumla ya Halmashauri 27 ambazo katika bajeti, tutakapokuja kuomba fedha tutaenda kuongeza fedha katika Halmashauri nyingine 27. Tuombe Mungu katika hizo 27 na yake iwe miongoni mwake.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Wananchi wa Kahama wamekuwa wakiulizia usafiri wa ndege kwa Mkoa wa Shinyanga. Kwa sababu Uwanja wa Ndege wa Shinyanga bado unafanyiwa matengenezo, ni lini ATCL itaanza kutua Kahama?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Maige, Mbunge wa Kahama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalo ni eneo lingine ambalo Serikali inakiri kwamba kuna abiria wa kutosha hata ATCL inafahamu hivyo lakini bado kuna changamoto kidogo ya uwanja, tunaendelea kurekebisha runway iweze kukidhi mahitaji ambapo ndege zetu za ATCL zitaweza kushuka. Tayari tumeshamu-assign TANROADS kwa ajili ya kufanya BOQ ya kurekebisha uwanja huo. Ukisharekebishwa vizuri tutaanza kutua kwa sababu pale abiria na soko la kutosha lipo.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake pamoja na majibu hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati utafiti wa awali unafanyika kuhusu maeneo yanayofaa kwa ajili ya mradi huu waliokuwa wakifanya utafiti walifika pia Isaka na Igusule kama ambavyo jibu limesema na baada ya maamuzi kufanyika kwamba mradi huu unajengwa Igusule walisema bado kuna miundombinu muhimu ya Isaka ambayo itatumika ikiwa ni pamoja na Ofisi za TRA, Bandari ya Nchi Kavu, Reli, Umeme pamoja na ofisi zingine za Kiserikali.

Sasa nilitaka kufahamu kwa sababu pia walisema wataweka transit yard pale Isaka nilitaka kujua hatua gani imefikiwa kwa ajili ya upataji wa eneo hilo la transit yard na maandalizi ya wananchi wa Isaka kwa ajili ya kushiriki katika huo mradi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa mradi huu unatoa fursa za kibiashara na ajira kwa wananchi waliowengi sana wa maeneo hayo. Je, ni maandalizi gani ya kiujumla ambayo yamefanyika kwa ajili ya kuandaa wananchi hawa wa Isaka pamoja na Igusule ili waweze kushiriki katika kunufaika na mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia mradi huu wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima Uganda na namna gani wananchi wake hususan wa Jimbo la Msalala watakavyoweza kufaidika na maswali yake mazuri ya nyongeza na mara baada ya kukubali uamuzi wa wabia wa mradi huu wa eneo la kujenga kiwanda iwe Igusule.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa maswali yake ya nyongeza yamehusiana na miundombinu mingine ni kweli tafiti mbalimbali zimeendelea kufanyika kuhuisha miundombinu mbalimbali ikiwemo reli, ikiwemo ofisi mbalimbali za kiserikali itakavyotumika katika mradi huu na nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika eneo la Isaka hapo pia vitajengwa ofisi ya mradi huu ya EACOP na miundombinu mingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wananchi wake na yeye mwenyewe anajua eneo la Igusule ni kama kilometa 5 tu kutoka Isaka. Kwa hiyo, ni wazi kabisa wananchi wa maeneo ya Isaka na maeneo mengine ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na Mkoa wa Tabora watapata fursa mahususi kabisa katika mradi huu ikiwemo ajira na masuala mengine ya kibiashara na mpaka sasa mradi huu umeajiri takribani watanzania 229 kwa hizi hatua za awali lakini kuna makampuni nane yanatoa huduma mbalimbali katika mradi huu lakini pia faida zake mojawapo ni utoaji wa ajira utakapoanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikutaarifu tu kwa sasa mazungumzo yanaendelea na kwamba hatua ambayo imefikiwa sasa hivi ni tumefika mbali na tunatarajia mradi huu kuanza mwezi septemba 2019. Kwa hiyo, utakapoanza utaleta tija kubwa na faida kwa wananchi wa mikoa nane iliyopitiwa na bomba hili, wilaya 24, kata 134 na vijiji 280.

MHE. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana yaliyosemwa na Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niwadhibitishie Waheshimiwa Wabunge Serikali kwa kutambua umuhimu wa mradi wa bomba hilo la mafuta na jinsi litakavyoweza kukuza ajira na uchumi wa Taifa letu, Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa programu maalum ya local content na tumeanza mafunzo maalum katika mikoa hiyo yote nane ili kuwahabarisha wananchi katika mikoa hiyo ni namna gani wanaweza wakatumia fursa mbalimbali ambazo zitapatikana katika mradi huo muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa Wabunge wote ambao wanatoka katika mikoa ambayo inapitiwa na bomba hilo tuweze kuwasiliana ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwaweka pamoja wananchi wao waweze kufaidika na mradi wa bomba la mafuta katika fursa mbalimbali zitakazopatikana.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nimetoka kuongea na rafiki yangu, Mheshimiwa Dkt. Kalemani, hapa lakini nataka awatangazie wananchi wa Msalala. Halmashauri ya Msalala Makao Makuu yake yako Ntobo na wameshahamia, lakini shughuli zote inabidi zifanyikie mjini, kwenda kutoa photocopy, hata shughuli za kibenki au za kiuhasibu kwa sababu ya ukosefu wa umeme. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye Kijiji cha Ntobo yalipo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa dharura?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli, ni kama takribani nusu saa tumemaliza kuongea na Mheshimiwa Mbunge. Kazi ya kupeleka umeme katika Kijiji cha Ntobo ambacho kiko kilometa nane kutoka umeme unapoishia inaanza Jumatatu ijayo na tayari leo wakandarasi wamekwenda ku-survey. Niwape taarifa wananchi wa Msalala, hasa wa Ntobo, kwamba kuanzia wiki ijayo kazi ya kupeleka umeme kwenye kijiji kizima na vitongoji vya Ntobo inaanza Jumatatu wiki ijayo.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba pia nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, ndugu yangu Chifu Kwandikwa kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Pamoja na majibu hayo mazuri nilikuwa naomba niulize swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara kubwa tatu zinazopita Jimbo la Msalala kwa maana ya barabara hii ya Solwa - Kahama kupitia Bulige; Busisi, Nyang’hwale - Kahama na Kahama – Geita, zote upembuzi yakinifu ulishakamilika. Bajeti ya mwaka huu mwezi Juni, tulipitisha fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kahama - Geita. Barabara hii imekuwa ni kero kubwa, nilitaka kujua na wananchi wafahamu ni hatua gani sasa imefikiwa ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kahama - Geita kuanzia pale Manzese – Segese - Bukoli - Geita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Mbunge alivyozungumza ukiangalia kwenye ukanda ule barabara hizi zote zinahusiana. Sisi kama Serikali tumejipanga kufanya barabara hizi ziwe kwenye mnyororo mzuri. Mheshimiwa Maige anafahamu hatua nzuri tuliyofikia ya ujenzi wa barabara hii kutoka Kahama kupitia maeneo aliyoyataja ya Bulige, Jimbo la Mheshimiwa Bukwimba kwenda mpaka Geita Mjini. Tumejipanga na tupo kwenye hatua za mwisho kuanza ujenzi wa barabara hii muhimu. Hatua hii sasa itapunguza urefu wa barabara hii ambayo Mheshimiwa Nassor naye ameuliza hapa na nimejibu muda uliopita kwa maana itaunganisha barabara hiyo kwa maana ya kupita kwenye mji wa Nyang’hwale.

Mheshimiwa Spika, hata barabara hiyo niliyojibu kwenye swali la msingi inapita kwenye maeneo mengi, alijaribu kutaja maeneo machache. Kimsingi inagusa Jimbo la Misungwi, inapita kwenye eneo la Kwimba na inaunganisha pia Jimbo la Solwa, Msalala na Mji wa Kahama.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa wananchi wa Kahama kwa ujumla na wananchi wa Mkoa wa Geita na Mwanza kwamba tumejipanga vizuri, tutaenda kwa awamu hivyo hivyo. Barabara hii kubwa itaanza lakini pia barabara hizi zingine tuko kwenye mpango wa kuzishughulikia. Tukionana baadaye ataangalia pia kwenye mpango mkakati wetu kama Wizara tumejipangaje hatua kwa hatua kukamilisha barabara zote hizi. Nampongeza sana kwa umahiri mkubwa katika kuwahudumia wananchi wa Msalala.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa kwa nafasi nimesikia majibu ya Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, Kiwanda cha Nyama cha Shinyanga kwa muda mrefu kimekuwa kikitazamwa kama ni jibu la matatizo yote haya, kwa maana ya kuzuia wafugaji wa Shinyanga wasihame, kwa maana ya kuzuia usafirishaji wa Wanyama na utesaji wa Wanyama na Mheshimiwa Waziri alipofika Shinyanga aliwahakikishia kwamba tatizo la Kiwanda kile ni Mwekezaji na akasema Mwekezaji wa kwanza atakayepatikana kuja kuonyesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya nyama atamleta Shinyanga, kwa bahati mbaya tumesikia amempeleka Ruvu, wana-Shinyanga wamenituma tumuulize Waziri kwamba wana-Shinyanga tumemkwaza nini, hadi yule Mwekezaji wa kwanza apelekwe Ruvu badala ya Shinyanga kama alivyoahidi mwanzo? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana kaka yangu Maige kuliuliza hili swali muhimu sana la kuhusu viwanda hivi. Kiwanda cha Shinyanga ambacho kilikuwa chini ya Tanganyika Parkers na kiwanda cha Mbeya, ambacho na chenyewe kilikuwa chini ya Shirika la Tanganyika Packers, hivi viwanda katika uwekezaji wake si viwanda tu ambavyo vilikuwa huru kuwekezwa.

Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki kilikuwa kimebinafsishwa kwa mwekezaji ambaye alishindwa naye pia kukiendeleza. Mkataba wake tukauvunja na baada ya kuuvunja mkataba na baada ya yeye ku-surrender hati ile Serikalini, tayari utaratibu wa ukamilishaji wa Serikali unaendelea lakini wawekezaji walioomba kiwanda hicho wapo mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niendelee kuwahakikishia wananchi wa Shinyanga na maeneo mengine, mkakati wa kukifufua kiwanda cha nyama cha Shinyanga uko pale pale na wawekezaji wetu walioomba kuwekeza katika kiwanda hicho wapo. Kwa hiyo, taratibu za Serikali zitakapokamilika basi mwekezaji atapatikana, mwekezaji mahiri ambaye atakiongoza kiwanda hicho.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikijaribu kuondoa zile kasoro zilizokuwa zikijitokeza zamani. Unampa mtu uwekezaji kumbe mwisho wa siku anatafuta mambo mengine. Anatafuta labda ile hati akaende akaweke kupata mikopo kwa ajili ya shughuli zingine. Kwa hiyo, tunataka kweli mwekezaji aliyejipanga vizuri ili tukimpa kiwanda hicho aweze kukiendesha.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kwa kiasi kikubwa swali langu linafanana na Mheshimiwa Njeza kumekuwepo confusion ya kuongeza maeneo na kupandisha hadhi. Mkoa wa Shinyanga tulishamaliza mchakato wa kupendekeza mji wa Kahama uwe manispaa na sifa zote tunakidhi na kigezo kikubwa kimekuwa ni suala la mapato ambayo halmashauri ya Manispaa ya Kahama ina uwezo wa kujiendesha kwa hiyo si changamoto kwa Serikali. Pia Mji wa Isaka na tulishafikisha wizarani je, ni lini Wizara kwa mtazamo maalum inaweza ikaruhusu Halmashauri ya Mji wa Isaka pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama itaanza?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Naibu wangu kwa ufafanuzi mzuri sana. Katika swali hili lakini tunafahamu kwamba nishukuru Mheshimiwa Maige kwa concern yake; tuna maeneo makubwa matatu kwanza, kuna Halmashauri ya Mji wa Geita, Kahama, pamoja na Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambao sasa iko katika suala la kufanya tathmini ya kuhakikisha kuzipandisha katika hadhi ya manispaa. Kwa hiyo lakini kuna utaratibu sasa hivi ambao tunaendelea kuufanya kwanza kutoanzisha maeneo mapya lakini hilo suala zima la hadhi tutalifanyia kazi pale jambo litakapoiva vizuri mtapata mrejesho Waheshimiwa Wabunge.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ilielekeza wananchi waunde vikundi vya uchimbaji ili wasimamie rush wenyewe, je, ni kwa nini sasa Kamishna wa Madini Kahama anaweka wasimamizi ambao si wanavikundi na utaratibu gani unatumika kuwapata wasimamizi hao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa nini eneo la Wisolele limetolewa leseni kwa watu binafsi akiwemo mtu mmoja ambaye anajinasibu kuwa karibu na viongozi wa tume (jina nalihifadhi) aliyepata leseni zaidi ya 17 peke yake badala ya vikundi vya wachimbaji wadogo kama Waziri alivyojibu kwenye jibu la msingi?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la swali la msingi kuwa, Serikali kupitia Tume ya Madini ilitoa Waraka wa Ndani Na.3 ulioanza kutumika tarehe 15 Oktoba, 2019, wenye dhumuni la kutoa mwongozo kwa Maafisa Madini Wakazi na watumishi wengine katika kusimamia, kudhibiti shughuli za madini na mapato ya Serikali katika maeneo yenye rush. Kwa mujibu wa Waraka huo Afisa Madini Mkazi ni Mwenyeketi wa Kamati ya Uongozi unaofuatilia na kuimarisha usimamizi katika eneo la rush. Kamati hiyo inajumuisha DSO (Katibu), TAKUKURU (Mjumbe), OCD (Mjumbe), REMA (Mjumbe) na Halmashauri (Mjumbe).

Mheshimiwa Spika, utaratibu unaotumika kuwapata wasimamizi wa rush ni kupitia Kamati ya Uongozi unaofuatilia na kuimarisha usimamizi katika eneo la rush kama ilivyotajwa hapo juu. Kamati hiyo huteua Wasimamizi wa rush, ambapo Mwenyekiti wa rush anapaswa kuwa na sifa zifuatazo:-

Awe mchimbaji mzoefu hasa katika usimamizi wa maeneo ya aina hiyo; awe hana historia ya wizi wa fedha za Serikali na awe mwaminifu. Wajumbe wengine kwenye usimamizi wa rush ni pamoja na Katibu, Mweka Hazina, Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji, Mjumbe wa REMA, TAWOMA, mwakilishi wa eneo/shamba.

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika eneo la Wisolele zimetolewa leseni za uchimbaji mdogo 55 kwa watu binafsi na vikundi mbalimbali. Aidha, kuna jumla ya maombi ya leseni za uchimbaji mdogo 95. Kati ya maombi hayo, maombi sita ni ya vikundi vya Amani Gold Mine, Chapakazi, Domain Gold Group na Pamoja Mining Group.

Mheshimiwa Spika, utolewaji wa leseni hizo 55 ukijumuisha leseni 17 zilizotajwa na Mheshimiwa Mbunge zilitolewa kabla ya rush na vikundi kuundwa. Kwa mujibu wa Sheria ya Madini, 2010 pamoja na Marekebisho yake ya 2017 mchimbaji mdogo hazuiwi kumiliki leseni zaidi ya moja.