Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Stanslaus Haroon Nyongo (59 total)

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri, nilikuwa naomba kupata ufafanuzi katika maeneo mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, ni takribani miezi minne sasa imepita toka Mkataba wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu usainiwe pale Chinongwe, lakini mpaka leo nazungumza, pamoja na majibu aliyoyatoa, kazi kubwa iliyofanyika ni kuweka tu vijiti. Sasa nilikuwa nataka kujua Serikali imekwama wapi kutoa fedha mpaka sasa hivi kwa ajili ya kuanza kazi hii ya kusambaza umeme vijijini?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nilikuwa naomba nimuulize Naibu Waziri, pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme pale Mahumbika ambacho tuliamini kingekuwa ni tiba kwa tatizo la kukatika umeme kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara. Ni jitihada gani za makusudi au za dharura ambazo Serikali itakwenda kuchukua, ili kuwaondoa wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara gizani, ukizingatia maagizo ya kufunga mashine yalishatolewa na Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara Mkoani Mtwara na aliwapa siku kumi, mpaka leo bado hakuna kilichotekelezwa, naomba kufahamu nini kinaendelea?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, mpaka sasa ni kweli wakandarasi wa REA walishaanza kazi kama anavyosema miezi minne iliyopita na ninaomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge pamoja n Bunge lako Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA) wameshalipa kiasi cha takribani bilioni 28 kwa wakandarasi wote kama advance. Nimeongea pia na Mkandarasi wa Mkoa wa Lindi ambaye ni State Grid, yupo anafanya kazi na alikuwa katika Wilaya ya Ruangwa na kati ya vijiji 34 alikuwa amevifikia vijiji 19 mpaka jana na akitoka Ruangwa ataelekea Wilaya ya Nachingwea. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kweli Serikali imedhamiria kabisa kwamba vijiji vyote vilivyosalia na kwa awamu hii ya kwanza ni vijiji 3,559 mpaka 2019 umeme vitakuwa vimepeta.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili aliuliza namna gani Serikali inachukua jitihada kumaliza tatizo la umeme Mikoa ya Mtwara na Lindi. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, mkandarasi anayefanya matengenezo ya mashine tisa za kuzalisha umeme Mkoa wa Mtwara ameanza hizo kazi. Vipuri vimewasili kama ambavyo Mheshimiwa Waziri alielekeza na kazi inaendelea. Na mpaka jana mashine sita zenye uwezo wa kuzalisha megawati 12 zilikuwa zinafanya kazi, lakini pia Serikali imechukua hatua imeagiza mashine mbili mpya kwa ajili ya kuzalisha megawati nne kwa thamani ya bilioni nane ambazo zitafika mwakani mwezi wa tatu na zitakuwa zimefungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia Serikali kupitia TANESCO inafanya matengenezo ya mtambo wa kuzalisha umeme Somangafungu ambao unazalisha megawati 7.5. Tuna uhakika, naomba niwathibitishie wakazi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi itakapofika Disemba, 31 hali ya upatikanaji umeme Mtwara na Lindi itaboreka. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunijibu swali langu kiufasaha kabisa, lakini vilevile nina maswali mawili madogo.
Je, Serikali inaweza kutuambia nini uchorongaji utafanyika wa kazi hiyo?
Swali langu la pili, je, nje ya Mkoa wa Rukwa kuna Mkoa mwingine wowote umeweza kugundulika kwa gesi hii?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya uchorongaji itaanza pale taarifa za kijiolojia zikishakamilika na kwa mujibu wa taratibu zilivyokuwa zimepangwa katika Kampuni hii ya Hellium One Tanzania Ltd. wamepanga kuanza shughuli ya uchorongaji kuanzia mwaka 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile swali la pili, ni sehemu gani ambapo hii hellium inapatikana. Kwa kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge ni kwamba gesi ya hellium vilevile inapatikana katika Ziwa Eyasi lililoko Mkoa wa Manyara na sehemu nyongine ni sehemu ya Singida ambapo na penyewe inapatikana hii gesi ya hellium. Ahsante sana.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali.
Kwa kuwa Serikali imekiri kufuta leseni 423 yenye eneo la hekta 69,652.88; je, Serikali iko tayari kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo eneo hili ambalo limefanyiwa utafiti ili waweze kujiajiri na kujipatia ajira na waweze kulipa kodi stahiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, Serikali iko tayari kuwanunulia vifaa vinavyohusiana na wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kukodisha kuliko ilivyo sasa wanachimba bila utaalam na vifaa vinavyostahili?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kwamba Serikali iko tayari kuwasaidia wachimbaji wadogo. Imekwisha kutenga maeneo 11 ambayo yana jumla ya hekari 38.9 kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo. Kwa hiyo, kwa maeneo haya ambayo yamesharudishwa Serikalini, Serikali itaendelea kufanya mpango wa kuweza kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kuchimba na wao waweze kupata faida na waweze kunufaika na madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wachimbaji wadogo kupitia ruzuku iliyokuwa inapitia SMMRP ambayo ilikuwa inatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo na wadau wengine wa uchimbaji iliweza kutoa fedha ili kuweza kuwasaidia wadau waweze kununua vifaa kwa ajili ya uchorongaji, kufanya utafiti na kuweza kusaidia wale wachimbaji wengine wadogo wadogo kwa kukodisha. Lakini vilevile STAMICO ambayo iko chini ya Wizara ya Madini pamoja na GST na yenyewe ina juhudi za dhati kabisa kununua vifaa ambavyo wachimbaji wadogo watakuwa wanakodisha ili waweze kujua mashapu yaliyopo ni mashapu ambayo yana faida ambayo wanaweza wakachimba na wakapata uchimbaji wa tija ili kujiondoa katika ule uchimbaji ambao wanachimba kwa kubahatisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo Serikali iko pamoja na wachimbaji wadogo. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba uniruhusu nimshukuru sana na kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuamua kujenga ukuta katika eneo lote ambalo Tanzanite inachimbwa katika Mkoa wa Manyara hususan eneo la Simanjiro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niruhusu nimshukuru na kumpongeza sana Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Job Ndugai ambaye alimua kwa dhati kabisa kuunda Kamati Maalum kwa ajili ya kuchunguza upotevu wa fedha kupitia madini hayo ya Tanzanite yanayopatikana peke yake duniani eneo la Simanjiro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu unaonesha kumekuwa na upotevu wa pesa kwa sababu wageni wanaotoka nje wanaokuja kununua Tanzanite hawalipi VAT, lakini wazawa waliopo pale eneo la Simanjiro, ama Arusha na Manyara wao ndio wanaolipa VAT. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu jambo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro unaohusiana na mitobozano hususan kwa wachimbaji wadogo wadogo katika eneo hilo la Mererani, ni nini sasa kauli ya Serikali ili kuzuia migogoro hiyo isiyo ya lazima? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linalohusiana na VAT, kwa kawaida VAT huwa hatozwi mtu mgeni. Vilevile ni kweli kabisa kwamba katika mnada huu, wageni walikuwa wanunua Tanzanite kwenye mnada bila kutozwa VAT, lakini kwa wale wenyeji walikuwa wanatozwa VAT. Mfano ukienda sehemu nyingine ni kwamba VAT unatozwa kule unakonunua bidhaa, kisha unaenda kurudishiwa kwenye kituo cha ndege (airport).
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi kama Serikali tunaangalia namna mpya ya kuhakikisha kwamba katika mnada ule, watu wote wanaonunua Tanzanite, sasa hivi tutaanza kuwatoza kodi ya VAT halafu mgeni aende akarudishiwe kule airport. Huo ndiyo msimamo wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la pili, kuhusu mitobozano. Ni kwamba mitobozano ni mgogoro wa muda mrefu pale Mererani na kuna kamati nyingi zimeundwa kuhakikisha kwamba wanakwenda wanatatua tatizo la mitobozano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba sasa hivi Umoja wa Wachimbaji wa Tanzanite pale pale Mererani wameweka mkakati wa namna wa kutatua mgogoro wa mitobozano. Kuna mkakati wameutengeneza na wamekubaliana kwa pamoja. Kwa hiyo, mkakati huo, ambao tuna hakika kwamba tukiufuata na utataribu ambao wameuweka mgogoro wa mitobozano utakwisha. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mbali na madini ya Tanzanite kuwa chanzo cha mapato kikubwa kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara, lakini pia kuna madini ya aina ya Rubi yanapatikana katika Kijiji cha Mundarara, Wilayani Longido Mkoani Arusha.
Ningependa kujua Serikali, inajipanga vipi ili madini haya aina ya Rubi iweze kuwanufaisha wananchi wa Longido? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru na ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kutetea wachimbaji wadogo wadogo Mkoani Arusha na kazi nzuri anayoifanya na wananchi wa Arusha wanaiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madini ya Rubi yanapatikana katika Kijiji cha Mundarara katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha. Madini hayo yanapatikana na eneo hilo kwa pembeni yake kuna leseni ya mtu anayeitwa Mheshimiwa Mareale. Sasa hivi ni kwamba kuna wachimbaji wadogo wanavamia eneo lile. Sisi kama Serikali tunawapenda wachimbaji wadogo, lakini tunataka wafuate taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokitizama sasa hivi ni kwamba lile eneo ambalo ni la mtu ambaye anayelimiliki na haliendelezi, tutaangalia namna bora ambayo tunaweza tukawatafutia wale wachimbaji wadogo waweze kuchimba na tuwatambue na wachimbe katika vikundi ili tuweze kuwatambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wanapochimba, basi tuweze kama Serikali kupata kodi zetu pale, tupate mrahaba pale, Halmashauri ya Longido ineemeke na Serikali kwa ujumla ineemeke na zile fedha tupeleke kwa wananchi wengine ambao wako nje na maeneo ya uchimbaji, waweze kuneemeka kupata huduma za maji, barabara na huduma za afya. (Makofi)
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kabla sijauliza maswali ya nyongeza naomba nioneshe tu masikitiko yangu kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri kimsingi hajaenda kwenye thrust ya swali langu.
Swali langu nimeuliza je, ni hatua gani imefikiwa katika mazungumzo kati ya ACACIA na Serikali kuhusu ulipaji wa fidia na athari nyingine ambazo wananchi wa msalala wamezipata?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika majibu yake pia, amesema kwamba hakuna fidia inayodaiwa, jambo ambalo si kweli kwa sababu kwa miaka 22 Serikali inafahamu kwamba watu walioondolewa mwaka 1996 Bulyanhulu, hakuna shilingi moja iliyolipwa. Mbaya zaidi kwa hawa wagonjwa Serikali imesema wamepatikana wagonjwa 78, lakini haijasema hatua gani zinachukuliwa kuhakikisha wanatibiwa, kwa sababu tayari kuna watu 49 wameshafariki na hawajalipwa fidia yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa sababu uharibifu au wizi uliofanywa na ACACIA kwa Tanzania haujafanywa kwa Tanzania peke yake, umefanywa hasa kwa wananchi wa Bulyanhulu pia; na kwenye ripoti ya Profesa Ossoro ilionesha mabilioni mengi ambayo Tanzania ilipaswa kupata na mimi nilishasema kwamba wananchi wa Msalala wanastahili kulipwa shilingi bilioni 973 kama service levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilitaka kujua kwa sababu ACACIA walisha-concede hivyo na tayari walishatoa kishika uchumba kwa Serikali, kile cha dola milioni 300. Nilitaka kujua kwa wananchi wa Msalala wanaodai bilioni 973, je, Serikali inaweza ikawasaidia sasa ili angalau katika hii mitambo inayotaka kuuzwa na ACACIA ikabidhiwe kwa Halmashauri kama sehemu ya fidia ya service levy ambayo haijalipwa kwa miaka yote? Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili,...
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Swali la pili, katika uwasilishwaji wa taarifa ya mazungumzo Mheshimiwa Rais aliagiza kwamba uchunguzi ufanyike kwenye migodi mingine kuhusu utoroshwaji wa madini, ukiacha makinikia peke yake, utoroshwaji wa vitofali vya dhahabu na Wizara iliagizwa kwamba ifanye uchunguzi kwenye migodi mingine. Nilitaka kujua uchunguzi kwenye hilo eneo umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la msingi imeonesha kabisa Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusiana na masuala ya fidia. Kwa taarifa tulizonazo katika Wizara yetu ni kwamba Mgodi ule wa Bulyanhulu ulivyokuwa unaanzishwa na kuanza kufanya kazi zake mwaka 2000 hakukuwa na madeni yoyote ambayo mgodi unadaiwa. Isipokuwa kama Mbunge ana hao watu ambao anawafahamu wanadai fidia katika yale maeneo kwa sababu yale maeneo ya Mgodi wa Bulyanhulu waliyapata kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli kuna watu ambao wanadai fidia zao, basi tunamuomba Mheshimiwa Mbunge awalete hao watu na madai yao, sisi kama Wizara tuko tayari kuwasimamia na kuhakikisha kwamba hakuna mwananchi yeyote anayedhulumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile ni kwamba ile taarifa ya ACACIA ambayo waliji-committ kutoa kishika uchumba, Serikali inaendelea na mazungumzo na uchunguzi ambao uliweza kutolewa, kama vile yalivyoweza kutolewa yale maoni na zile kamati mbili teule za Mheshimiwa; Rais ni kwamba yale mashauriano au ushauri uliotolewa wa uchunguzi, uchunguzi unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama itaonekana katika vile vitofali kuna wizi wa dhahabu ulitokea kwa sababu, kulikuwa kuna under declaration. Kama kweli ilitokea ni kwamba wale wa ACACIA wako tayari kuweza kutoa au kulipa fidia zote ambazo wameji-committ na walitoa kishika uchumba cha dola milioni 300, kwa maana ya kwamba waliji-committ kwamba kama kutakuwa na pesa nyingine za kutoa basi wataendelea kufidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ni kwamba maongezi yanaendelea na uchunguzi unaendelea na kama kuna upungufu wowote au kama kuna fedha yoyote ambayo inatakiwa ilipwe katika Halmashauri, kama service levy, na wewe mwenyewe umetaja kwamba kuna bilioni 973 kama kweli ni haki ya Halmashauri haki hiyo italetwa katika halmashauri hiyo. Uchunguzi unaendelea na maongezi yanaendelea. Nashukuru sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali dogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili sekta hii ya madini kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wachimbaji wa Jimbo la Mbulu Mjini, ni kwamba wanakosa mitaji, lakini pia uchimbaji wao ni wa kubahatisha. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia fursa za uwezeshaji, lakini pia na vifaa vya kubaini madini yako wapi na njia rahisi ya uchimbaji?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kwamba, wachimbaji wadogo wanakumbana na tatizo kubwa la kuwa na mitaji midogo. Sisi kama Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba, wachimbaji wadogo tunakwenda kuwasaidia, ili waweze kupata mitaji ya kuweza kuchimba na waweze kuchimba kwa kupata faida, na sisi kama Serikali tuweze kupata maduhuli na kodi kutokana na uchimbaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wachimbaji wadogo wengi wanachimba kwa kubahatisha. Sisi kama Wizara kwa kushirikiana na Geological Survey of Tanzania taasisi ambayo chini ya Wizara ya Madini, tuna mkakati kabambe wa kuhakikisha tunafanya tafiti mbalimbali. Tafiti ambazo zitaonesha ni wapi kuna madini ya kutosha na kuweza kuwapa ushauri wachimbaji wadogo kuchimba maeneo ambayo yana madini ili kuepukana na tatizo la kuchimba kwa kubahatisha. Wanatumia fedha zao za mfukoni, wengine wanauza hadi mali zao, ili waende wakachimbe maeneo ambayo hayajafanyiwa utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tumejipanga vizuri, tunafanya tafiti za kutosha na tutaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo, ili waweze kuchimba maeneo ambayo yana madini na waweze kuchimba kwa teknolojia nzuri ya kisasa na nyepesi, ili waweze kupata tija na waweze kuendesha maisha yao vizuri zaidi, ahsante.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na swali la kwanza la msingi mazingira hayo pia yanafanana na kule kwetu Geita ambako wananchi wa Geita wamekuwa wakiathirika kwa kiasi kikubwa na shughuli za Mgodi wa Geita Gold. Serikali kipindi cha Waziri Muhongo na Naibu Waziri Kalemani waliunda tume kwenda kuchunguza matatizo hayo kule Geita na kubaini nyumba ambazo zimeathirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa suala hili litaisha? Kwa sababu, wananchi wanaishi katika maeneo yenye mitetemo, wanaathirika na vumbi, wanapata hata madhara ya kiafya. Ni lini sasa Serikali itasimamia huo Mgodi wa Geita Gold Mine kuhakikisha ya kwamba, inawaondoa wananchi katika maeneo ya Compound na maeneo ya Katoma ili kupisha shughuli za mgodi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kuna watu ambao wanaishi ndani ya maeneo ambayo ni square kilometer 290,000 ambazo zinamilikiwa na GGM. Kwa mujibu wa sheria ilivyo ni kwamba kuna watu ambao bado wanamiliki zile surface area, yaani kwa maana ya eneo la juu la ardhi, na maeneo ambayo ni ya chini yanamilikiwa na mgodi wa GGM, kwa hiyo, kuna wananchi ambao bado wanaishi maeneo ambayo yako ndani ya leseni ya GGM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kufika pale mwezi wa pili na nilitoa tamko kwamba kuna Kamati ziliundwa na Waheshimiwa Mawaziri waliotangulia na ilionesha kabisa kwamba kuna watu ambao wameathirika katika maeneo yale. Nikatoa tamko kwamba wale ambao wako ndani ya maeneo ya GGM, GGM kama kampuni ikae nao iwalipe fidia iwaondoe yale maeneo ambayo wale wananchi wanaathirika na mgodi huo.
Vilevile kuna watu ambao wako maeneo ya Katoma, wameathirika na matetemeko kutokana na milipuko inayofanywa na GGM. Kulikuwa kuna taarifa mbili ambazo zilikuwa zimetolewa moja ikiwa ya GST kuangalia ni namna gani yale matetemeko yalikuwa yanaathiri zile nyumba. Majibu yaliyokuwa yanatoka yalikuwa yanakizanzana kwamba kuna wengine walisema milipuko ilisababisha nyufa katika nyumba zile na kuna taarifa nyingine inasema kwamba ile mitetemeko haikusababisha zile nyufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeamua kwa pamoja kwamba wakae waangalie tena upya na vile vile wafanye tathmini ya kutosha kwenye zile nyumba zilizoathirika wawalipe wale wananchi. Ikiwezekana wale wananchi walimo ndani ya hiyo leseni ya GGM waondolewe, wawalipe fidia, ikiwemo na watu wa Nyakabare, walipwe fidia waondoke yale maeneo ya uchimbaji. Kwa hiyo, hiyo tumeshawapa GGM na tunaendelea na maongezi na tunaendele na mikakati kuangalia namna gani ya kuweza kuwalipa fidia wananchi hawa. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa Halmashauri ya Geita inaudai mgodi wa GGM zaidi ya dola milioni 12; tumekaa tukakubaliana watulipe kwa awamu. Awamu ya kwanza ilikuwa itekelezwe mwezi wa pili, lakini utekelezaji huo haujafanyika na Halmashauri haina nguvu tena ya kuudai Mgodi wa GGM. Je, Wizara inaisaidiaje Halmashauri ya Geita ili tuweze kulipwa pesa hizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Halmashauri ya Geita inaudai GGM service levy. Tulitoa ushauri kama Wizara kwamba wakae kwa pamoja na waangalie ni namna gani Kampuni ya GGM inaweza ikawalipa wale Halmashauri ya Geita, yaani wakae kwa pamoja waelewane ili wangalie namna bora ya kuweza kulipa kidogo kidogo deni hilo na wameshakaa na nilipokwenda mara ya mwisho mwezi wa pili walisema kwamba wanakwenda kukaa na Halmashauri, ili waweze kusaini memorandum of understanding, namna ya kuweza kulipa deni hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hawajalipwa mpaka sasahivi, naomba nishirikiane na Mbunge kwamba nifuatilie. Sisi kama Wizara tuko pamoja tutahakikisha kwamba haki ya Halmashauri ya Geita italipwa kama inavyostahili. Ahsante sana.
MHE. VICKY P. KAMATA: Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Pamoja na majibu mazuri, nina swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa, GGM imekuwa ikitoa hili fungu la CSR kila mwezi kwa ajili ya kuhudumia hayo maeneo ambayo ameyataja katika maelezo yake ya msingi kwa maana ya elimu, afya, mazingira pamoja na wajasiriamali.
Mheshimiwa Spika, pia kwa kuwa, wamekuwa wakitoa kila mwezi hili fungu la CSR na kwa majibu haya inaonekana kwamba tangu Januari mpaka sasa GGM hawajatoa fungu hilo la CSR kwa maeneo hayo, nataka kujua kauli ya Serikali kwa wakati huu wa mpito kuhusiana na hawa waliokuwa wakisaidiwa na GGM kwa mfano, kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma wamekuwa wakisaidiwa pesa kila mwezi kwa ajili ya malazi ya wale watoto yatima, chakula, kuna mradi wa maji ambao kimsingi ni wa Serikali lakini GGM walikuwa bado wanaendelea kuutunza pamoja na ile hospitali inayotembea majini inayosaidia wanawake na watoto katika Visiwa kwa kuwa tangu Januari mpaka sasa pesa hazijatoka na imezoeleka kila mwezi huwa inatoka. Je, ni nini kauli ya Serikali katika kipindi hiki cha mpito?. Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baada ya marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017, tulisimamisha utoaji wa fedha hizi mpaka pale Baraza la Madiwani katika Halmashauri husika wakae, wakubaliane utekelezaji sawasawa wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo GGM, pia nimeongea na RAS wa Mkoa wa Geita, ule mpango wa kupitia kwa Madiwani umeshakamilika na kuanzia leo wanaanza kuzitumia zile fedha kutokana na jinsi walivyokubaliana na Halmashauri husika. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona. CSR ipo kwa mujibu wa sheria, lakini hii migodi wamekuwa wakionyesha kama ni hisani fulani wanawapatia wananchi. Kwa nini sasa Serikali isiwaagize hizi pesa zipelekwe moja kwa moja kwenye Halmashauri na zisimamiwe na Madiwani wetu katika kutekeleza miradi hii, kwa sababu unaona gharama zinazoandikwa ni kubwa kweli ukilinganisha na kazi halisi ambazo zinakuwa zinafanyika, yaani ziende kama vile kodi zingine zinavyoenda lakini zikiwa specific kama CSR ili zisimamiwe na Baraza la Madiwani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba hesabu zinazoonekana ni hesabu kubwa sana zilizotumika kuliko miradi yenyewe ilivyo, hilo tunakubaliana kabisa. Nimepita baadhi ya maeneo kwa mfano, GGM na North Mara tumewaagiza kwanza watupe taarifa ya utekelezaji wa zile fedha zilizotengwa kwa miaka miwili iliyopita ili tujiridhishe tuone zile fedha zilizotengwa na wamepeleka wapi na nini kimefanyika. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa sababu hizi fedha za corporate social responsibility huwa zinatolewa kutokana na jinsi wao wanavyotengeneza faida na kwa sasa hivi ni sheria lazima watoe zile fedha. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Madiwani husika wakakae na zile Kampuni waamue kwamba watekeleze miradi ile kwa jinsi wao walivyoweka kipaumbele chao.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna fedha ambayo inakwenda moja kwa moja kwenye Halmashauri, fedha hiyo ni service levy ambayo ni asilimia 0.3 ya mauzo ya madini wanayoyapata. Kwa hiyo, nadhani tu kwamba tuendelee kutoa ushirikiano na sisi kama Wizara ambayo tunasimamia Sheria ya Madini tutahakikisha kwamba zile fedha zinazotengwa zinakwenda zinavyostahili na Madiwani wasimamie utekelezaji wa miradi ambayo wamejipangia. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kuongezea majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini. Napenda kusema kwamba sheria ya sasa na kanuni kuhusiana na uwajibikaji kwa jamii ziko wazi.
Mheshimiwa Spika, niombe tu ushirikiano Waheshimiwa Wabunge pamoja na Halmashauri zetu za Wilaya na Miji waweze kutoa ushirikiano na kutupatia taarifa endapo wanaona kuna miradi imetekelezwa ipo chini ya viwango, lakini kiwango ambacho kimekuwa-declared ni kidogo kuliko fedha halisi ambayo inatamkwa kwamba imetumika.
Mheshimiwa Spika, pili; pamoja na maelezo aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba tumewataka GGM waweze kutoa maelezo na taarifa zao za miaka miwili, tutaenda kwa migodi yote ambayo imekuwa ikifanya uwajibikaji kwa jamii na tutapitia na kukagua na yeyote ambaye ataonekana alifanya udanganyifu, hatua kazi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ni hivi juzi tu siku mbili, tatu zilizopita Wabunge wa Geita tumeletewa barua inayoonesha CSR iliyotolewa na GGM 2017/2018 dola 9,600,000 lakini katika majibu ya Waziri amesema ni dola milioni 6.5 na hizi barua ambazo tumeletewa tayari ziko kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na baadhi ya wananchi wameshazipata, lakini kwa majibu ya Wizara ina maana tunachanganyikiwa tujue ipi ni sahihi na ipi siyo sahihi.
Mheshimiwa Spika, sasa ni nini kauli ya Wizara kuweza kuisaidia Halmashauri angalau kufanya auditing kujua uongo uko Wizarani au uongo uko mgodini. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ni kwamba GGM tuliwaeleza tarehe 27 Februari, 2018 watuandikie breakdown ya kuonesha ni jinsi gani wametumia fedha za CSR na majibu waliyonipa ni kwamba kwa mwaka 2017 wametumia kama nilivyosema katika jibu la msingi dola 6,358,000. Mheshimiwa Musukuma anachosema dola milioni 9.7 ni jumla ya miaka miwili yaani mwaka 2016 na 2017 kajumlisha kapata 9.7 lakini swali la msingi limeuliza mwaka 2017 jibu ni milioni 6.358. Mheshimiwa Spika, ahsante.
Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na Wizara ya Maliasili na Utalii. Swali linaulizwa na Mheshimiwa Hawa Mchafu.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo ambapo shughuli nyingi za uvuvi zinafanyika kunapatikana athari za kijamii za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Kama ilivyo kwenye maeneo zinapofanyika shughuli za uchimbaji wa madini ambapo maeneo yanayozunguka migodi hii yanapata mrahaba kama sehemu fulani ya ku-recover athari hizi.
Je, Serikali haioni sababu sasa sheria hii iweze kutumika kwenye maeneo ambako shughuli za uvuvi zinafanyika na kusababisha athari mbalimbali za kijamii kwa ajili ya ku-recover sehemu ya athari hizi? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameulizia suala la kupata service levy kutokana na uvuvi katika Ziwa Victoria. Naomba niseme tu suala la uvuvi haliko katika Sheria ya Madini ambayo tunaisimamia sisi. Nadhani ni vema Mheshimiwa Mbunge akaifuatilia Sheria ya Serikali za Mitaa kuona kama kuna stahiki ambayo unaweza ukaipata kutokana na masuala ya uvuvi. Ahsante.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilileta swali hapa Bungeni ili kujua maeneo yenye madini katika Wilaya ya Kakonko. Maeneo yaliyoanishwa na Serikali katika majibu yake ni pamoja na chokaa iliyoko eneo la Nkogongwa, dhahabu iliyoko Ruhuru Nyakayenzi na Nyamwilonge. Baada ya kuwa maeneo hayo yametambulika wananchi walichangamkia wakataka kuchimba madini lakini ghafla Serikali ikasitisha leseni za uchimbaji.
Ninachotaka kujua ni lini Serikali itafungua utoaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Kakonko ili waweze kuanza uchimbaji? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na mabadiliko yake ya mwaka 2017 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2018, ni kwamba sasa hivi Tume ya Madini ambayo imeundwa ndiyo itakuwa na wajibu wa kutoa leseni kwa wachimbaji wakubwa, wadogo na wachimbaji wote wa kati. Ni juzi tu Mheshimiwa Rais ndiyo ameteua Mwenyekiti wa Tume ya Madini ambayo sasa ndiyo inaendelea na michakato ya kuchakata kwa maana ya kutoa leseni kwa watu wote walioomba leseni za kuchimba madini. Kwa hiyo, nimueleze Mheshimiwa Mbunge aendelee kuhamasisha wachimbaji wake waombe leseni na sasa Tume imeanza kufanya kazi, watapata leseni walizoomba na wataendelea na uchimbaji. Ahsante sana.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pamoja na majibu ya Serikali jambo hili Mheshimiwa Tundu Lisu Mbunge wa Singida Mashariki amekuwa akilifuatia kwa muda mrefu sana, Serikali imeeleza kwamba leseni ya Shanta ni ya toka mwaka 2004...
lakini mpaka mwaka 2012 miaka nane Shanta walikuwa hawajajenga mgodi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo ubaguzi nilishakuandikia muda kwamba nauliza hili swali kwa niaba…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali; la kwanza toka 2004 mpaka sasa kampuni ya Shanta haijajenga mgodi wala haijaanza kuchimba. Ni kwa nini leseni yote wasinyang’anywe wakapewa wachimbaji wadogo wakaenda kuchimba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wakati Mheshimiwa Rais anapokea ripoti ya makinikia Mheshimiwa Rais…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Kishoa nina haki ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, naomba niendelee…
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais anapokea ripoti ya makinikia mwaka jana 2017 ilielezwa kwamba kampuni ya Acacia haipo kisheria…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza ni kwa nini Serikali ilipofuta leseni siku chache zilipopita haikuifutia leseni kampuni ya Acacia, kampuni ya Pangea, kampuni ya Barrick na kampuni ya Bulyanhulu kwa sababu zinadaiwa mabilioni hazijalipa na zinavunja sheria na pesa hatujapewa toka, Serikali itoe ripoti ya makinikia?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Shanta umepewa leseni siku za nyuma toka mwaka 2002 walipewa leseni ambayo ni prospect license yaani leseni ya utafiti. Baada ya pale miaka minne iyopita kampuni ya Shata ilipewa leseni ya uchimbaji yaani mining license. Walipewa mining license namba 455, 456 na 457. Leseni hizo wamepewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na leseni hizo zinadumu kwa muda wa miaka kumi; mwekezaji anatakiwa ndani ya miaka kumi aweze kujenga mgodi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi Shanta walikuwa wamekwama kutokana na kwamba kuna baadhi ya wamiliki wa ardhi yaani wenye surface areas walikuwa wamegoma kutoka, mmojawapo alikuwa ni Diwani Emili wa eneo lile. Hata hivyo, mpaka sasa hivi diwani yule na bwana mwingine ambaye alikuwa lile eneo wamekwishakubali kupewa fidia na sasa wako tayari kuondoka na wengine wako tayari kuachiwa maeneo kwa ajili ya kuwajengea wale wakazi wa maeneo yale kuwajengea nyumba za kudumu, kwa maana ya kuwaondoa lile eneo la uchimbaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mwezi Novemba Shanta wataanza kujenga processing plant na vilevile wataanza kujenga TSF na vilevile wataanza kufungua lile eneo la kufanyia uchimbaji wa mgodi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu Acacia na makinikia na kuhusu kutoa zile leseni au leseni zilizofutwa. Leseni za juzi zimefutwa na Tume ya Madini na leseni zilizofutwa siyo mining license wala siyo leseni za utafiti, zilifutwa leseni ambazo ni za kusubiria land detention license, mwekezaji anaweza akaomba leseni ya kusubiri uzalishaji kwa muda fulani. Sasa Serikali imegundua kwamba kuna watu wengine wanakaa muda mrefu na zile leseni bila kuzitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sheria ya mwaka 2010 na marekebisho yake mwaka 2017 zile sheria baada ya kufanya marekebisho leseni za retention license zimeamua kuondolewa na zinarudishwa Serikalini na Serikali itaangalia namna bora ya kuwapa tena wawekezaji wengine ambao wako serious ili waweze kuwekeza na waweze kuzalisha ili Serikali ipate kipato na wananchi waweze kupata ajira na faida zingine Serikali, nashukuru sana.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nipende tu kuongezea maana yake kumekuwa na mkanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na wengine wanaofuatilia, wafuatilie kifungu cha (16) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na marekebisho yake mwaka 2017 na wasome pia na kanuni ya 21(1) na (2) ya kanuni zetu za madini ya mwaka 2018 kuhusiana na mineral rights ataweza kuona ndiyo maana detention license zile 11 zimeweza kufutwa kutokana na sababu hizo. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba hili swali la wananchi niseme ifuatavyo wa Singida. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokuja Itigi kufungua barabara ya Chaya-Tabora, aliwahaidi wachimbaji wote wadogo atamsimamia Shanta aweze kuwalipa fidia na nashukuru wamelipwa kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipeleka maombi kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili wapatiwe leseni, wachimbaji hao walijiunga kwa makundi matatu ambao 1,000 wa Wilaya nzima ya Ikungi, ambao ni Dhahabu ni Mali, lakini Mang’oni Mining pamoja na Aminika na Serikali ilishapokea maombi hayo. Hivyo naomba kupatiwa majibu ya Kamati ya Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mheshimiwa Mtaturu ambaye ni DC wa Ikungi. Ni lini leseni zitapelekwa na wachimbaji hawa wakapewa maeneo yao, ahsate sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi vilivyoomba hivyo vitatu alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tayari wamekwishapewa maeneo ya kuchimba, mojawapo wakiwa ni Imarika, ni kikundi chenye watu 193 walipewa dola za kimarekani milioni 25 na waliweza kununua vifaa na walianza kazi za uchimbaji. Tatizo lililotokea ni kwamba sasa hivi waliingia kwenye madeni kwa sababu walikosa yaani utaratibu mzuri wa kuweza manage pesa zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tunataka sasa hivi wachimbaji wote wadogo tumejipanga tutawapa maeneo mengi kwa mfano pale Muhintili tutawapa leseni zaidi ya mia moja na sabini na kitu. Hizo leseni tutawapa, lakini vilevile kama Wizara tunataka kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo waweze kuchimba kwa faida waweze kuchimba vizuri na waweze ku-manage fedha zao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafanya hivi kwa sababu tumegundua kuna tatizo kubwa la wachimbaji wanapopata fedha nyingi wanakosa ule ujuzi wa kuweza kumiliki zile fedha. Hiyo inawafanya waende kutumia vibaya na waweze kuingia kwenye umaskini tena. Hivyo tumejipanga tutatoa elimu vizuri na tutahakikisha kwamba wachimbaji wetu wanachimba kwa tija.
MHE. MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri; lakini naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Wilaya ya Newala na Masasi hatuna mgogoro wa kimpaka ila migogoro ya mipaka watasababaisha watu wa madini. Kitendo cha viongozi wa Wilaya nyingine kwenda kufanya tathmini na kusema wao watalipa fidia kwenye wilaya nyingine wakati viongozi wapo kinavunja heshima kwa viongozi wa wilaya nyingine. Kwa hiyo inaonekana kabisda kwamba viongozi wa wilaya nyingine hawafanyi kazi. Je, Serikali ipo tayari kuacha kuwadhalilisha viongozi wa Wilaya ya Newala kuonekana hawafanyikazi na wanaofanyakazi ni Wilaya ya Masasi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, itakapotokea mrabaha, kama hawa wananchi wa Newala wanakwenda kufanyiwa tathmini Masasi italipwaje na Wilaya ya Newala itapataje haki zake? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro kati ya wilaya moja hadi nyingine, kwa maana ya mgogoro wa viongozi, nadhani ni kwamba ni vizuri tu viongozi hao wakakaa chini wakaelewana kwa sababu hakuna haja ya kugombana katika hatua hii wakati Kampuni ya Natural Resources inafanya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu mrabaha; hatua za utafiti ni hatua za mwanzo za uchimbaji. Pale madini yatakapogundulika kwamba Kampuni hii imefanya utafiti ikagundua madini yaani katika wilaya zote mbili kwa maana ya Newala na Masasi, basi sisi kama Wizara tutakaa chini na tutaangalia namna ya halmashauri hizi mbili kuweza kuneemeka katika kupata service levy na wala si mrabaha kwa sababu mrabaha wenyewe unakusanywa na Wizara moja kwa moja, kwa hiyo hakutakuwa na ugomvi, lakini katika service levy kwa sababu ni ushuru ambao unakwenda katika halmashauri, tutaangalia na tutakaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo siyo suala jipya, kuna maeneo mengine unakuta halmashauri mbili zinaweza zikaneemeka katika service levy kwa maana katika mradi mmoja. Kwa hiyo tutaangalia namna ya service levy zitakavyogawanywa kwenda katika wilaya hizo mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, utafiti utakapokwisha tutajua kwa sababu inawezekana ile leseni ya utafiti iko wilaya mbili lakini baadaye utafiti ukaonesha kwamba madini haya yapo wilaya moja, kwa hiyo wilaya hiyo ndiyo itakayoneemeka na ushuru wa service levy. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana. Kwanza kabisa wananchi wa Busokelo Kata ya Lufilyo wanakupongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri na kukushukuru sana kwa utendaji wako. Ulienda Kata ya Lufilyo ukiwa Naibu Waziri wa Elimu, ulisaidia sana katika uanzishwaji wa ujenzi wa Kituo cha VETA pale kwenye kata hiyo. Wanakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza; la kwanza; madini ya granite ni mazito sana na ndiyo maana katika kuyabeba kutoka Lufilyo kwenda mpaka Mbeya inaharibu miundombinu hasa hasa ya barabara sababu ya uzito.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wawekezaji waweze kuweka mtambo wa kutengeneza madini hayo hapo hapo sehemu ya Lufilyo ili tusiharibu miundombinu? La kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, uwekezaji katika Kata ya Lufilyo na Jimbo la Busokelo unafanana kabisa na uwekezaji katika Wilaya ya Chunya. Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara Chunya mwanzoni mwa mwaka huu na alishuhudia uchenjuaji wa tailings (makinikia) kwa wazawa na wageni na alifurahishwa sana na uchenjuaji huo uko Chunya. Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kwamba sasa hivi Serikali iko kwenye mchakato wa kuweza kuweka mtambo wa kuchenjua makinikia hapa nchini na akapendekeza kwamba Chunya inaweza kuwa sehemu mojawapo ya kuweka mtambo huu wa kuchenjua makinikia (smelter). Je, mchakato huo wa kuweka smelters nchini hasa Chunya umefikia wapi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Kwanza kabisa nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba kweli granite zina uzito mkubwa, lakini katika hatua za ku- process ni mwekezaji mwenyewe ndiye ana jukumu la kuangalia ni sehemu gani anaweza akaweka mtambo wa ku-process ili uweze kumtengenezea faida. Kwa hiyo, anatakiwa afanye cost benefit analysis kusafirisha na ku- process katika eneo husika na sisi kama Wizara ya Madini tunapendekeza mtu a-process madini katika eneo la uchimbaji ili atengeneze ajira katika eneo lile, hiyo moja.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika uchenjuaji wa tailings kwa manufaa ya Wabunge wote kufahamu kwanza tailings na makinikia ni vitu viwili tofauti. Tailings ni mabaki ya dhahabu katika udongo ambao umechenjuliwa katika hatua za awali yaani unapochenjua kwa kutumia mercury zinabaki tailings kwa ajili ya ku-process katika CAP yaani katika process ya aina nyingine. Sasa kutengeneza mtambo wa makinikia ni kweli kabisa Wizara ya Madini inashirikiana na makampuni makubwa kutoka nje kuweza kuwekeza katika mitambo mikubwa ya kuweza kufanya smelting. Mpaka sasa hivi tuna kampuni 27 ambazo zimekuja kuonesha nia za kuwekeza, kuanzisha smelters pamoja na refineries na mpaka sasa hivi tayari tuna kampuni 10 zime-qualify, kwa hiyo, Serikali kwa kushirikiana na hizo kampuni za nje muda si mrefu tutaanzisha zile smelters hapa nchini. Ahsante.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Menyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu. Inaonesha kwamba amefuatilia kweli katika Halmashauri ya Wilaya jinsi ambavyo imefanya kazi imekaa na GGM. Lakini vilevile niishukuru GGM kwa kuanza kutekeleza uwajibikaji wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 katika kipengele cha 105.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa kuna baadhi ya makampuni ya uwekezaji katika sekta ya madini ambayo mpaka sasa hayajaanza kufanya utekelezaji wa sheria hii. Kwa mfano Mgodi ule wa Bacliff pale hawajaanza kufanya utekelezaji. Je, Serikai inasemaje sasa kwa makampuni ambayo hayajaanza kufanya utekelezaji wa sheria hii mpaka sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mgodi wa Bulyanhulu ambao uko Kahama umepakana sana na Halmashauri ya Wilaya ya Geita, hasa katika Jimbo la Busanda katika Kata ya Butobela kule Nyakagwe pamoja na Kata ya Bukoli na wananchi walioko jirani na maeneo haya wananufaika, hasa wale wa Kahama, lakini wale wa upande wa Geita sasa ambao nimewataja wa Nyakagwe na Bukoli ni kilometa mbili tu kutoka kwenye mgodi ule lakini hawanufaiki chochote.
Je, Serikali inasemaje sasa kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Busanda pia, hasa wa maeneo ya Bukoli pamoja na Nyakago wanafaidika na mgodi uliopo Bulyanhulu ambao uko jirani sana na sisi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kwamba Mgodi wa Bacliff ni kweli kabisa haujatoa CSR Plan yao kutokana na mujibu wa sheria inavyosema. Lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Mgodi ule wa Bacliff mpaka sasa hivi hawajaanza uzalishaji. Kwa hiyo watakapokwenda katika uzalishaji ni lazima watupe CSR Plan yao na CSR Plan yao lazima iwe shirikishi kwa kushirikiana na Halmashauri husika waangalie namna gani wataweza kui- finance miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya au Halmamshauri hiyo.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba asiwe na wasiwasi, mradi huu wa Bacliff utakapoanza kufanya kazi basi lazima sisi kama Wizara tutahakikisha kwamba wamekuja na CSR Plan yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kwa kampuni yoyote, nipende kutoa wito kwa makampuni yoyote ya uwekezaji, makampuni yote ambayo yanawekeza katika sekta ya madini ni lazima yatii sheria na taratibu zilizowekwa. Sheria ya mwaka 2017 na Kanuni zake za mwaka 2018 zinahitaji kila kampuni ilete CSR Plan yao kuhakikisha kwamba wanashirikiana na jamii au Halmshauri husika katika kuratibu na kuhakikisha kuwa wanatoa fedha katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kanuni za mwaka 2018 zinasema kuna masuala ya local content plan pamoja na kile kiapo cha uaminifu. Ni lazima kila kampuni ikamilishe yale mambo ambayo yameainishwa katika kanuni za mwaka 2018, bila kufanya hivyo sisi kama Wizara hatutasita kuchukua hatua katika kampuni zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, kuhusiana na wale watu ambao wamepakana na Wilaya ya Kahama na hasa ambao wapo karibu na Mgodi wa Bulyankulu, sisi tunafuata sheria. Sheria ndiyo zinazosema kwamba halmashauri husika iweze kufaidika kwa maana ya kupata service levy. Lakini vilevile nitoe tu wito kwa Mgodi wa Bulyankulu, kama inawezekana kata ambazo ziko karibu na mgodi huo basi waweze kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo kwa kuwapa ajira kupitia ile kanuni yetu sisi ya local content kwa maana ya kuwajali Watanzania wanaoishi karibu na maeneo yale kwa kuwapa ajira lakini vilevile kuwapa fursa ya kuweza kuuza bidhaa na kuuza huduma mbalimbali katika mgodi huo. Ahsante.

MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, kwa kuwa mradi huu ni mradi ambao unatambulika kuwa ni mradi wa kimkakati na kwa kiasi mpaka 2013 ulikuwa unatengewa fedha ya maendeleo lakini kuanzia mwaka wa fedha 2014/2015 hadi sasa hivi hakuna fedha yoyote ambayo imekuwa ikitengewa mradi huu ilhali sasa hivi mradi huu umeanza kufanya kazi na tayari mbia amepatikana na wiki hii ameshaweka saini pamoja na STAMICO ya kuanza kuchimba makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo.
Je, Serikali imeuondoa mradi huu katika miradi ya kimkakati? Na kama ni hivyo, je, hiyo fedha ya kuendeleza hasa ukarabati wa Mgodi wa Kiwira wenyewe inayohitajika sasa hivi kwa sababu tayari mbia ameshapatikana itapatikana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa mradi huu ambao umekuwa kwa muda mrefu ukinufaisha Wilaya nyingine ya jirani sasa hivi umeanza kutambulika rasmi kuwa ni mradi wa Ileje na kwa urahisi wa kuufikia mradi huu kuna daraja katika Mto Mwalisi ambalo liliharibika kwa muda mrefu la kilometa karibu saba na barabara yake, imesababisha mradi huu sasa kuwa unatumia njia ndefu ya kupitia Kyela ambayo ni karibu kilometa 36 na kuleta gharama kubwa na kuongeza gharama kubwa kwa mradi huu.
Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kuwa hii barabara pamoja na Daraja la Mwalisi ambalo ndilo linalounganisha Wilaya ya Ileje na Mradi wa Kiwira na Kabulo inatengenezwa haraka sana ili mwekezaji huyu sasa hivi aanze kufanya kazi bila matatizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya. Ni mama ambaye yuko makini, anafuatilia sana majukumu yake ya kuwawakilisha wananchi wa Ileje kama Mbunge. Ni kweli mama huyu amejitosheleza sana katika jimbo hilo, Mungu ambariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kwamba je, Mradi huu wa Kiwira tumeuondoa katika miradi ya kimkakati? Jibu jepesi kabisa na la haraka ni kwamba bado mradi huu tunautambua kwamba ni mradi wa kimkakati ikiwa ni pamoja na miradi mingine mikubwa ambayo kwa kweli tunafahamu kama Serikali kwamba miradi ya kimkakati ni ile miradi mikubwa ambayo inawezesha miradi mingine au sekta nyingine kufanya kazi. Na kwa sababu sasa hivi tunataka nchi yetu iende katika kuwa nchi ya viwanda, makaa ya mawe ni kitu muhimu sana katika uendelezaji wa viwanda vyetu na hasa viwanda vya simenti. Kwa hiyo, mradi huu bado ni mradi wa kimkakati tunautambua kama miradi mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini sasa Serikali tutaiwezesha kujenga barabara hii ya Kiwira – Kabulo. Sisi kwa kushirikiana na TARURA, Wizara ya Madini tumekwishawaandikia TARURA barua ya kuhakikisha kwamba kilometa zile saba zinajengwa katika mradi huu ili kupunguza kilometa 36 ambapo mwekezaji huyu anatumia kwa maana ya kupeleka kusafirisha makaa ya mawe, inaingiza gharama kubwa kwa sababu tunatambua kuwa makaa ya mawe ni bulky mineral, ni mzigo mkubwa. Kwa hiyo unapoweka katika hali ya kusafirisha mwendo mrefu gharama inakuwa ni kubwa na mtumiaji wa mwisho analipa gharama kubwa kiasi kwamba inamfanya huyu mwekezaji apate shida katika kuendeleza mradi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumelitambua hilo na imetengwa shilingi bilioni 2.5 ya kujenga kilometa saba na vilevile imetengwa bilioni 1.5 ya kujenga daraja ambalo liko pale.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, sisi tunaendelea kulisimamia na sisi kama Wizara ya Madini tunahakikisha kwamba tuko pamoja na Serikali kuwawezesha wawekezaji wote katika sekta ya madini wafanye kazi kwa faida na wasifanye kazi kwa hasara. Ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pia namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake. Hata hivyo, niseme tu kwamba swali langu la msingi ni nini kimesababisha kupungua kwa shughuli za utafutaji wa madini, mafuta na gesi kwenye nchi yetu halijajibiwa na hilo ndilo swali langu la kwanza la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza ni kwamba, mwaka jana tulitunga sheria nzuri za kulinda rasilimali za uziduaji, yaani madini, gesi na mafuta ambazo ni “The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act, 2017”; The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act, 2017; na ile Sheria ya Madini ilirekebishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu; sheria hizi ni nzuri sana, lakini zimesababisha changamoto kadhaa ambazo zimefanya kupungua kwa shughuli za uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuwekwa kwa asilimia 25 ya retention kwa wachimbaji wadogo wanapotaka kuuza madini. Kodi hiyo inawafanya wachimbaji wadogo washindwe kufanya biashara ya wazi. Je, ni lini Serikali itachukua hatua kurekebisha changamoto hizi ili kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini na Mafuta? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi nimejaribu kuelezea ni jinsi gani wawekezaji wanavyozidi kuongezeka kuomba leseni za kufanya tafiti pamoja na leseni za uchimbaji mkubwa na uchimbaji wa kati, vile vile wakiwepo wachimbaji wadogo. Ongezeko hili limezidi na hii inaonesha dhahiri kwamba bado wawekezaji wanazidi kuja kutaka kuwekeza kwenye nchi yetu. Hii ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya sheria ambayo tuliyopitisha katika Bunge lako Tukufu mwaka jana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile mabadiliko yale ya sheria yalikuwa ni kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi yetu. Hata hivyo, tunaendelea kuboresha na kuna kanuni ambazo tumezitoa mwaka huu wa 2018 ambazo kwa kweli wawekezaji wengi walisubiri kuangalia zile kanuni zinakwendaje. Baada ya kuzitoa zile kanuni wengi wamezipitia, wameziona na wengi wameona kwamba wana uwezo wa ku-comply, yaani wana uwezo wa kuendana na zile kanuni na sheria kadri tulivyoweza kuibadilisha. Kwa hiyo wawekezaji wanaendelea kuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunaendelea kuwawezesha GST waweze kufanya tafiti za kina, waweze kufanya tafiti hadi kufanya zile resource estimation, kwa maana ya kuangalia resources tulizonazo ili baadaye tuwe na uwezo wa kuifanya GST iweze kuuza leseni kwa njia ya mnada. Ili wawekezaji wanapokuja wawe wanakuja kwa nia ya kuchimba tu, ili tuwaondoe katika ile nia ya kutaka kuja kukwekeza kwa maana ya utafutaji wa madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule utafutaji wengine unawafanya wasite kuja. Hata ukiangalia dunia nzima siyo Tanzania tu uwekezaji katika kutafuta madini umepungua kidogo. Kwa hiyo sisi kama Serikali inabidi tujiongeze kuangalia namna ya kufanya resource estimation, kuangalia kwa kina ili mwekezaji anapokuja aje kuwekeza kwa maana ya kuchimba tu si kutafuta. (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza ambalo linaelekezwa kwenye Wizara ya Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Naibu Waziri mtakumbuka kwamba miaka ya karibuni pamefanyika ugunduzi wa madini ya aina ya graphite kwenye Wilaya ya Masasi, Kijiji cha Chiwata, Kata ya Chiwata, vile vile Wilaya ya Ruangwa na vijiji vyake; ikiwemo baadhi ya maeneo ya Jimbo la Mtama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu, Kampuni ya Nachi Resources ndiyo ambao ilionesha nia ya kutaka kuwekeza, lakini mawasiliano ya mwisho tuliyoyafanya na wao yalionyesha kwamba hawawezi kuwekeza kwenye hayo maeneo kwa sababu pamekuwa na ucheleweshaji wa upatikanaji wa ripoti ya environmental assessment. Sasa Mheshimiwa Waziri, haoni haja ya kuwasaidia Nachi ili kuweza kukamilisha huu utaratibu ili waweze kuchimba hayo madini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Nachi Resources ni kwamba wanasubiri kupata ripoti kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) ambayo iko chini ya Mheshimiwa Makamu wa Rais. Sisi hatuna shida kwa upande wa Wizara ya Madini, ni kwamba wale tunaendelea kuwasaidia ili waweze kuwekeza, kwa sababu tunafahamu uchimbaji wa graphite sasa hivi duniani ndiyo unahitajika kwa sababu madini ya graphite sasa hivi ndiyo yanayohitajika zaidi duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi kama Wizara ya Madini tunashirikiana nao kuhakikisha kwamba baada ya muda waweze kuanza kuwekeza na kuanza kuchimba. Kwa hiyo, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba tunashirikiana nao na tunaendelea kuwasiliana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) ili iwawezeshe kupata environment impact assessment report ili kusudi waweze kuwekeza na waweze kuendeleza shughuli zao za uchimbaji kama kawaida. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE.SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Mkoani Kilimanjaro, Wilaya ya Same, Kata ya Makanya yanapatikana madini ya gypsum, madini hayo Tanzania nzima yanapatikana Manyoni, Pindilo na Makanya kwenyewe. Hata hivyo, miundombinu ya hapa ni mibaya sana na wachimbaji hao ni wachimbaji wakiwemo akinamama na akinababa. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia wachimbaji hao wakati tunapoelekea kwenye Sera ya Viwanda na Biashara?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kama Serikali tunazidi kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo tunawawezesha kimiundombinu, kimitaji na kuwasaidia kiteknolojia ili waweze kuchimba na waweze kujipatia kipato chao. Ni kweli kabisa hayo madini ya gypsum ni madini ambayo ni muhimu na yahahitajika katika soko la dunia na baadhi ya nchi za jirani wanahitaji madini hayo na kwa ajili ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali pamoja na kupitisha sheria ile ya mwaka jana ya Marekebisho ya Sheria ya Madini tumetaka kwamba madini yote ya gypsum tuweze kuwasaidia wachimbaji waweze kuchimba na kuya-process ili kusudi wapeleke kwenye soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi pamoja na Wizara nyingine tunasaidiana kupeleka miundombinu kwa maana ya maji, umeme, barabara kwa wachimbaji wadogo dogo ili waweze kuchimba vizuri na kwa gharama ndogo ili waweze kupata faida. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa maeneo ya uchimbaji madini (mining sites) katika Mkoa wa Dodoma yako zaidi ya 700 na kuna baadhi ya maeneo hayajaanza kuchimbwa kabisa madini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutangaza kwa wawekezaji ili kusudi waweze kuja kuchimba katika Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, tuna maombi mengi sana ambayo wachimbaji wadogo na wakubwa wameomba katika Wizara yetu kupitia Tume ya Madini. Hapa Dodoma kuna wachimbaji wadogo wadogo wengi wameomba leseni hizo, kwa maana ya kwamba wanataka au wameonesha nia ya kuchimba. Sisi kama Serikali hivi karibuni ile Tume imeshaanza kufanya kazi na zile leseni tutazitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema toka mwanzo kwamba tunataka tuwawezeshe wachimbaji wadogo. Mradi katika Wizara yetu ambao ni mradi unaopata fedha kutoka Word Bank, yaani Mradi wa SMRP; mradi huu tunaangalia namna bora sasa ya kuwawezesha wachimbaji wadogo, kwa maana ya kuwasaidia kuwapa teknolojia, elimu na mitaji ili waweze kuchimba. Pia wachimbaji wa Mkoa wa Dodoma na wao wamo kwa sababu sisi tunafanya kazi nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa wachimbaji wadogo ambao wako katika Mkoa wa Dodoma, nipende tu kusema, walioonesha nia au walioomba maombi ya leseni, leseni zitatoka na wachimbaji ambao wanataka kuomba leseni sasa hivi Tume imeanza kufanya kazi walete maombi hayo katika Wizara yetu, tuweze kuwapa leseni, na tuangalie namna ya kuwasaidia ili waweze kuchimba na Wizara iko tayari na tunaendelea na kazi hiyo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa mgodi wa Kiwira, umesimama kwa muda mrefu, je Serikali ina mpango gani ya kutafuta Wawekezaji ambao wanaweza kufufua mgodi ule ambao miundombinu yake inakufa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, Mgodi wa Kiwira sisi kama Serikali tumejipanga kuangalia ni namna gani ya kuwezesha mgodi huo uweze kufanya kazi. Niseme tu kwamba tunashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuangalia namna sasa ya kuzuia au kuangalia namna ya kuweza kuondoa zile changamoto zilizopo katika mradi wa Kiwira, ili uchimbaji ule wa Makaa uweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wengi wameonesha nia ya kutaka kushiriki katika kuchimba Mgodi huo wa Kiwira. Sisi kama Wizara, kwa kweli hatuna shida yoyote, tunahakikisha kwamba ikiwezekana mwaka huu, mgodi huo upate fedha na watu waweze kuchimba na vile vile tutafute wawekezaji wengine ambao wanaonesha nia ya kuwekeza pale, tushirikiane nao kuhakikisha kwamba Mgodi wa Kiwira unaanza kufanya kazi. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Madini ya rubi yanayopatikana katika Wilaya ya Longido kule Mundarara, biashara yake imedorora kwa sababu mpaka sasa Serikali haikutoa utaratibu wa kuendesha biashara ya madini hayo. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuleta mchakato mzima wa kusimamia na kuendesha biashara ya madini yale?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli madini ya rubi yanapatikana kule Mundarara, Mkoani Arusha. Madini yale ni pamoja na madini mengine. Baada ya mabadiliko ya Sheria 2010, tulizuia kutoa madini ghafi nchini. Tunataka madini yote yapitie kwenye uongezwaji wa thamani ili yaongezwe thamani kwa ajili ya kutengeneza ajira kwa wananchi lakini na vile vile kuisaidia nchi kupata kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi ni kwamba madini yale, baada ya zuio hilo, imeonekana kwamba imeshindikana kwa wale waliokuwa wanatoa madini ghafi. Sasa hivi sisi kama Serikali tunaangalia utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunawakaribisha wawekezaji, na wako wawekezaji ambao wameonesha nia, ya kuja kuyaongezea thamani madini ya rubi ili kusudi sasa yawe yanauzwa katika hali ambayo yameshaongezwa thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itawasaidia watu wa Mundarara na wachimbaji wote wengine kwa maana kwamba watakuwa sasa wanapata soko la uhakika kuuza ndani lakini vile vile madini hayo tutayatoa nje, yakiwa tayari yameshaongezewa thamani. Hii itasaidia kwa wawekezaji wa ndani wenyewe, lakini vile vile kama Serikali, itazidi kupata kipato kwa maana kwamba tutapata kodi na mrabaha katika madini ambayo yameongezewa thamani. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge kuwa tayari tu kwamba tunaendelea …
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kuna malalamiko makubwa kutoka kwa utatu wa uwekezaji katika maeneo yote ya uwekezaji, kwa maana ya jamii, Serikali, pamoja na mwekezaji mwenyewe, kila mmoja akilalamikia kwamba hapati stahiki zake. Je, ni lini Serikali itakaa pamoja sasa kuuweka utatu huu, kwa maana ya Serikali, jamii na mwekezaji na kuweka mazingira sawia ambayo kila mmoja atampa haki yake kuwe hakuna malalamiko katika uwekezaji kabla ya mwekezaji hajapewa kibali cha kuwekeza?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais mwaka jana alivyoanzisha Wizara Maalum kwa ajili ya Madini, kwa sababu zamani ilikuwa ni Wizara ya Nishati na Madini, lakini mwaka jana mwezi wa Kumi Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alianzisha Wizara Maalum inayoshughulikia Madini baada ya kuona umuhimu wa kuanzishwa Wizara hii. Kwa kweli tangu Wizara imeanzishwa, sisi tumeanza pale, tumeanza kukaa na wawekezaji, wawekezaji wa kati, wawekezaji wadogo na wawekezaji wakubwa, kuangalia changamoto walizonazo, kuangalia namna bora ya kuweka mazingira ya uwekezaji ili kila mwekezaji aondoke katika kulalamika kutokana na vikwazo anavyovipata katika kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi kama Wizara tuna mikakati mizuri katika kuhakikisha kwamba wawekezaji wanaokuja wanawekeza vizuri na wanawekeza bila vikwazo. Sasa hivi kuna wengine wamelalamikia kuhusu kodi, nao tumewaambia walete malalamiko yao tuyaangalie. Kwa mfano wawekezaji wa chumvi, kulikuwa kuna kodi 16, katika Bajeti hii zimeondolewa kodi 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni moja au kiashiria kimoja cha kuona kwamba Wizara inafanya kazi ya kuwasikiliza wawekezaji na wachimbaji kwa nchi nzima na kuangalia namna bora ya kuwaondolea vikwazo ili waweze kuwekeza na waweze kuchimba kwa faida. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nimpongeze Waziri kwa majibu mazuri, lakini naona majibu yake hayajitoshelezi.
Mheshimiwa Spika, kwa kifungu cha 105(3) kama alivyoainisha Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kwamba mgodi utapokea maelekezo kutoka kwenye mabaraza mawili maana yake Geita Mjini na Vijijini, na mgodi utatulipa kama shilingi bilioni 9.1. Lakini kwa mchanganuo wa Halmashauri zetu, Halmashauri ya Geita Vijijini inapata asilimia 46, asilimia 54 zinabaki Geita Mjini. Sasa kwa maelezo na mchanganuo aliyoutoa Waziri CSR ya Halmashauri ya Geita inaingiaje kwenye Chato, Bukombe na Mbogwe? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Geita Vijijini na Mjini tuna mgogoro na Mgodi wa GGM, tunawadai dola bilioni 12 wewe mwenyewe unafahamu na mlishauri watulipe kwanza dola laki nane mwezi wa kwanza, leo ni mwezi wa tano hatuoni majibu na hawatusikilizi, tumeshapeleka demand, sasa tunataka kupelekana mahakamani na Mgodi wa Geita unazidi kusafirisha dhahabu Jumanne na Ijumaa, na ili kibali cha kusafirisha dhahabu kitoke lazima walipe kodi za Serikali ninyi Wizara ndio mtoe kibali cha kusafirisha.
Mheshimiwa Spika, kwa nini Wizara isichukue action ya kutusaidia kuwanyima kibali ili waweze kutulipa hata kesho hizo dola laki nane? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Spika, katika swali la kwanza, ni kwamba mgawanyo wa fedha katika Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Geita Vijijini, haya ni makubaliano ambayo wao wenyewe walifikia na Baraza la Madiwani na Mheshimiwa Mbunge naye ni Mjumbe, kwa hiyo, walifikia maamuzi haya na huu ndiyo msimamo wa Halmashauri na hivyo ndivyo mgawanyo utakavyokuwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu shilingi hizo bilioni alizozitaja ambazo ni sawasawa na dola laki nane ambazo walisema kwamba wanatakiwa wapewe na Mgodi wa GGM, ni kwamba mpaka sasa hivi GGM wako tayari kutoa hizo fedha. Mgogoro uliokuwepo ilikuwa ni Halmashauri ipi au akaunti ya Halmashauri ipi ipewe fedha hizo, na mpaka hapa ninapozungumza ni kwamba tayari Mkuu wa Mkoa kesho kutwa, siku ya tarehe 10 Mei, anakaa na hizi Halmashauri mbili, anakaa na hiyo GGM waelewane kwa pamoja ni Halmashauri ipi akaunti yake iweze kupewa fedha hizo na wao waweze kutafuta utaratibu wa kuweza kugawana fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, la mwisho kwa kuongezea, suala la Halmashauri ya Mbogwe na halmashauri nyingine, Chato na maeneo mengine, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba waendelee kushiriki vile vikao vya Halmashauri ili waweze kuelewana vizuri kupitia Sekretarieti ya Mkoa waangalie ni namna gani ya kugawanya hizo fedha, sisi kama Wizara tutasimamia tu kuhakikisha GGM wameweza kutoa fedha za CSR. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maelezo mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Wilaya yetu ya Mbogwe kuna madini ya dhahabu na kumekuwa na mgogoro kati ya wananchi wa Nyakafuru pamoja na wawekezaji ambao wamekuja hapo. Sasa ninataka kujua msimamo wa Wizara uko vipi katika kuhakikisha kwamba leseni inatolewa kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wanaochimba Nyakafuru wanachimba chini ya leseni ya mtu mwingine, wanachimba bila kuwa na leseni, ni kama vile wachimbaji waliovamia leseni ya mtu mwingine. Sisi kama Wizara hatuchochei wachimbaji wadogo kwenda kuvamia leseni ya mtu mwingine, huo siyo utaratibu. Lakini sisi kama Wizara ya Madini tuna mpango na mkakati wa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, tuna maeneo zaidi ya 44, tuna heka zaidi ya 238,000 kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tunaomba ushirikiane na wananchi wako kwa kuwapa elimu ya kutosha kwamba tunakwenda kuwagawia maeneo ambayo ni halali, wachimbaji wadogo wachimbe kwa uhalali ili waweze kujipatia kipato chao, lakini wasiendelee kuvamia leseni za watu wengine. Ahsante.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wachimbaji wadogo wadogo wanachangia sana pato la Taifa kwa kulipa kodi na Wizara ya Madini kwa kuongeza kukusanya maduhuli. Je, Serikali ina mikakati gani kurudisha maduhuli haya katika Wizara ya Madini ili kutatua changamoto hasa hizi za wachimbaji wadogo wadogo kupata zana za kisasa za uchimbaji ili waweze kuliingizia tena Serikali pato la Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wale ambao walikopeshwa ruzuku kwenye sekta ya madini kama mikopo na wakaitumia sivyo. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha wale waliochukua mikopo ile wanachukuliwa hatua na mikopo ile kurudishwa tena kwa wachimbaji wale wadogo wadogo ili waweze kuendeleza sekta hizo za madini za wachimbaji wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Msabaha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wachimbaji wadogo tunawategemea sana katika kukusanya maduhuli. Wachimbaji wakubwa walikuwa wanachangia zaidi ya asilimia 95 za michango yote ambayo ilikuwa inakwenda Serikalini na wachimbaji wadogo walikuwa wanachangia asilimia 4 mpaka 5. Sisi kama Serikali tunatambua umuhimu wa wachimbaji wadogo, tukiwawezesha tutapata maduhuli mengi ya kutosha. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tulikuta katika Wizara ya Madini walikuwa tayari wachimbaji wadogo wanapewa ruzuku kutoka Serikalini. Ruzuku ile walipewa wanaostahili na wasiostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara ya Madini tumewafuatilia wale maafisa wote waliokuwa wanawawezesha wachimbaji wadogo wasiostahili kupata ruzuku zile. Tumeshawafuatilia na wengine tumeshawaondoa katika nafasi zao za kazi. Vilevile kwa wale wachimbaji wa madini waliopewa fedha kinyume na taratibu na hawana sifa ya kupewa fedha hizo tumewafikisha katika vyombo vya sheria na sasa hivi kuna kesi zinaendelea ziko chini ya PCCB na zingine zimepelekwa Mahakamani. Tunachotaka ni kwamba warudishe fedha hizo na tuangalie namna bora ya kuwawezesha wachimbaji wadogo. Nia yetu kama Serikali tunataka wachimbaji wadogo tuwawezeshe, wawe wengi kwa sababu tunatambua kabisa kwamba tukiwawezesha tutaweza kupata kipato kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais tarehe 22 alikaa na wachimbaji wadogo na walizungumza changamoto zao. Changamoto nyingine ilikuwa ni za kodi ambazo tunawatoza katika uchimbaji huo. Kwa hiyo, hatua tunachukua kuangalia namna ya kuwasaidia wachimbaji hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili ni kwamba changamoto za wachimbaji zipo na sisi kama Serikali tunaendelea kutoa elimu kuhakikisha kwamba wachimbaji hao wadogo wanapata elimu ya kutosha katika uchimbaji huo na wanatunza kumbukumbu ili wawe na sifa za kupata mikopo katika benki na vyombo mbalimbali ambavyo vinakopesha (financial institutions) na sisi kama Serikali tutashawishi vyombo hivyo kuwakopesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeze tu Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali kwa jinsi wanavyoshughulikia suala hili katika Mgodi ule wa ACACIA Nyamongo kule. Nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la fidia katika eneo la Nyamongo limekuwa la muda mrefu; na ni miaka mingi kila siku watu wanadai na wengine wanadai malipo hewa na wengine malipo halali: Ni lini sasa Serikali itamaliza hili tatizo kwa muda muafaka ili kutufa kabisa tatizo la kudai madai ya Nyamongo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, matatizo yanayotokea Nyamongo, yanafanana sana na matatizo yanayotokea katika kijiji changu cha Nyabuzume Jimbo la Bunda Kata ya Nyamang’uta; na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri wewe ulifika kenye kile kijiji, kuna wachimbaji wako pale, wanapiga yowe za muda mrefu, wanasumbua wananchi na hawawezi kushirikiana nao katika kupeana zile kazi za kijiji; nawe uliahidi kumaliza hilo tatizo. Ni lini tatizo la Nyabuzume wale wachimbaji wasio halali au walio halali ambao hawatekelezi suala la kuondoa matatizo ya wanakijiji katika kijiji kile?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza Mheshimiwa Getere, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa madai ya Nyamongo kule North Mara katika ile kampuni ya Acacia yamechukua muda mrefu. Yamechukua muda mrefu kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza ni kampuni yenyewe ya Acacia ilichelewa kulipa malipo kwa muda uliostahili. Sababu ya pili ni kwa wananchi wenyewe ambao baada ya evaluation ya kwanza ku-expire, evaluation ya pili kuna watu walifanya speculation, yaani walifanya kutegesha, kwa maana waliongeza majengo, wakaongeza mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli limetupa shida sana suala hili kwa sababu evaluation ya mwanzo ilikuwa inaonekana ni ndogo, kuja kufanya evaluation ya pili imeonekana ni kubwa sana. Mfano kuna sehemu ya Nyabichele. Wao walithaminishiwa kwenye mazao yao; gharama ilikuwa ni shilingi bilioni 1.6, lakini baada ya evaluation ya pili kuja kufanyika, gharama yake ikaonekana ni shilingi bilioni 12. Hili limefanya kampuni kusita kuweza kulipa fedha hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi nilisema kwamba hili suala lipo kwa Chief Valuer na leo nimeongea na Chief Valuer amefanya evaluation na ameandika barua kwa North Mara kwa maana ya Kampuni ya Acacia, ile evaluation ambayo wameandikiwa na Chief Valuer wailipe immediately. Wailipe mara moja, wasipoteze
muda ili kuondoa manung’uniko. Vilevile kupitia Serikali ya Mkoa wa Mara, tumeelewana na Kampuni ya Acacia kwa maana ya North Mara, walipe fidia kwa wale wananchi wanaodai wanaona kabisa kwamba wananchi hawa wana madai yao ya haki, hawana dispute yoyote, hawana mgogoro wowote, hao walipwe mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna wananchi wengine ambao ni 138 toka mwaka 2016 kuna cheque ya thamani ya shilingi bilioni 3.2 wamegoma kwenda kuchukua kwa sababu wanalishana maneno, wanasema kwamba wanacholipwa ni kidogo. Nawaasa na ninawaomba, wananchi ambao cheque zao ziko tayari, waende wakachukue cheque zao mara moja ndani ya wiki hii. Wasipochukua ina maana sasa Serikali ya Mkoa itachukua hatua nyingine na itakuwa vinginevyo. Kwa hiyo, itazidi kuwacheleweshea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nawaomba wananchi wa Mkoa wa Mara na maeneo ya North Mara tusilishane maneno. Watu ambao wana haki, wanatakiwa kulipwa na cheque zao ziko kihalali, waende wakachukue cheque zao mara moja. Kampuni ya North Mara, ndani ya wiki hii tumeshawaambia, yale maeneo ambayo hakuna dispute, walipe mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusiana na suala la Bunda kule ambako Mheshimiwa Mbunge amelielezea, kwa wale watu wanaomiliki PLs na hawazitumii, nimezungumza hapa hata jana, kwamba kwa wamiliki wa PLs wasiozitumia, hawafanyi tafiti, sisi tunapitia PL moja baada ya nyingine. Tunakwenda kufuta hizo PL na tunakwenda kuwapa wachimbaji wadogo wachimbe ili waweze kujipatia kipato na Serikali iweze kupata mapato kupitia uchimbaji mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza nawapongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Waziri wake kwa namna ambavyo wanafanya kazi kwenye Wizara hii. Hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa eneo lile na Tarafa nzima ya Mkwayungu limegundulika kuwa na madini mengi sana ya gypsum na dhahabu kwa upande


wa Mafulungu na ninyi Serikali mlikuwa mmeona kabisa watu wanachimba na wanapata fedha na nyie mnapata kodi lakini baadaye mlisimamisha uchimbaji wa madini ya gypsum. Je, ni lini Serikali itawafungulia wale wachimbaji wengine ili waendelee kuchimba na nyie muendelee kupata mapato na wananchi waendelee kufanya kazi zao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana nami ili twende tukajionee hali halisi ya watu wanaochimba dhahabu Mafulungu na wale wanaopata tabu ya kuchimba madini ya gypsum pale Manda ili tukaone na tukatatue matatizo yao kwa macho huku akishuhudia? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Livingstone Lusinde, Mbunge wa Mtera, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu nimpongeza Mheshimiwa Livingstone Lusinde kwa kuweza kufuatilia mambo ya wapiga kura wake na hasa wachimbaji wa maeneo ya pale Manda. Kwa kweli Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba wachimbaji wa gypsum eneo la Manda na Mafulungu ni kweli walikuwa wamesimamishwa kwa sababu hawakufuata taratibu ambazo zilikuwa zimewekwa na Tume ya Madini katika uchimbaji huo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda na watafunguliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwataarifu wachimbaji wote wa gypsum na wachimbaji wengine wote Tanzania, madini ya gypsum tuliyazuia kwa maana ya madini ghafi kuyapeleka nje ya nchi, naomba wapitie GN Na.60 ambayo tumeitoa siku ya tarehe 25 Januari, waangalie ile GN ambayo imetoa mwongozo wa madini yote,
wanachenjua katika kiwango gani na kiwango kipi ambacho kinaruhusiwa kutoa nje ya nchi. Wakishapitia mwongozo huo wachimbaji watakuwa hawapati shida tena katika kufanya biashara hii ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Mbunge ameomba niongozane naye kwenda katika eneo la Manda kuangalia changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo. Nimhakikishie baada ya Bunge hili niko tayari kuongozana naye twende tukaangalie changamoto zinazowakabili wachimbaji wa Manda tuangalie namna ya kutatua changamoto hizo vilevile tuwawezeshe wachimbaji hawa waweze kuchimba wapate faida na waweze kufanya biashara hiyo ya madini. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Kijiji cha Kwahemu, Kata ya Haneti, kuna vikundi 16 ambavyo vina wachimbaji zaidi ya 200 lakini havina maeneo ya kuchimba madini licha ya kupeleka maombi Tume ya Madini. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu kuwapa maeneo wachimbaji hawa wadogo ili waweze kujikimu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Fatma Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maeneo ya Kwahemu (Haneti), kuna uchimbaji mdogo mdogo wa madini ya vito. Katika eneo lile kuna leseni moja inamilikiwa na Bwana Dimitri, raia mmoja wa kigeni lakini kuna maeneo mengine ambayo yako katika utafiti kwa maana ya PL. Kama nilivyosema siku zilizopita ni kwamba tunafuatilia zile PL zote ambazo hazifanyiwi kazi tutazichukua na tutazifuta na tutawapa wachimbaji wadogo wadogo waweze kuchimba na waweze kujipatia riziki kama tulivyojipangia katika Serikali yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge watu wa Kwahemu maeneo ya Haneti tuna mpango kabambe wa kuwapa maeneo ya kuchimba. Wale wachimbaji walioko pale nilishafika na wakatoa kero zao na mimi kwa kweli naendelea kuzifuatilia kwa maana ya kuzitatua na tunahakikisha kwamba hawa watu wa Kwahemu watapata leseni na wataweza kupata nafasi ya kuchimba.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu yanaleta matumaini. Nina swali moja tu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri Bunge lililopita aliniahidi yeye mwenyewe jua linawaka kwamba angefuatana na mimi kwenda kuwasaidia wananchi hawa ambao tayari wameanza kuchimba madini haya, lakini bahati mbaya mambo yakawa mengi.

Sasa kwa kuwa wananchi hawa wameanza kuchimba madini kwa kutumia nyenzo duni, utaalam duni na wakati mwingine hata hawajui uzito wala purity ya madini; je, sasa anawaahidi nini wananchi hawa ambao wameanza kuchimba madini ili waweze kutumia sasa fursa hii na fursa za masoko ya madini ambayo yamefunguliwa kama lile la Geita ambalo amezindua Waziri Mkuu juzi, anawaahidi nini hasa katika uwezeshaji waweze kufanya shughuli hii kwa ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Chiza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na yeye kwamba nilimuahidi kweli nitakwenda Kigoma, hasa maeneo ya jimbo lake. Mimi tu nipende kusema kwamba nitashiriki naye, nitakwenda, tutakwenda hadi kwa wachimbaji, tutakwenda kufanya kazi na tutakwenda kuwaelimisha na kuwapa maelekezo ya Serikali yanavyostahili. Kwa hiyo kwa hilo mimi sina tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusiana na suala la wachimbaji wadogo. Kweli tuna matatizo makubwa sana ya kimitaji, teknolojia, maeneo, tafiti kwa wachimbaji wadogowadogo. Sisi kama Wizara ya Madini tumejipanga vizuri na tumeamua sasa hivi kupitia Geological Survey of Tanzania pamoja na STAMICO tutaendelea kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitawasaidia wachimbaji wadogowadogo ili tuweze kuwapa yale maeneo ambayo tukiwapa tunakuwa na uhakika kwamba wataweza kupata madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninapozungumza STAMICO tayari tumekwisha kununua rig machine ambayo inaweza kufanya kazi ya drilling kwa wachimbaji wadogo kwa gharama ndogo. Kwa hiyo tunawaomba wachimbaji wadogowadogo waje waombe maombi yao katika Wizara yetu tuwafanyie tafiti mbalimbali kwa gharama ndogo kwa sababu kufanya tafiti ni gharama kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunaendelea kutoa elimu ya uchimbaji, uchenjuaji, na uwepo wa masoko haya ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu amelifungua kule Geita na lingine juzi nimekwenda kufungua pale Kahama na maeneo mengine, tunaendelea na mikoa yote ambayo inakwenda kufungua masoko ya madini. Tunakwenda kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanapata ile tija ambayo wanadhamiria kuipata tofauti na sasa hivi walikuwa wanakwenda kuuza katika masoko ya pembeni wanadhulumiwa, wanauza kwa bei ndogo, vilevile wanaibiwa. Sisi kama Wizara ya Madini tumejipanga kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo kwa kuhakikisha kwamba wanapata tija. Ahsante sana.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Madini kwa uamuzi wake wa kuyagawa au kutoa leseni za wachimbaji wadogo kwenye maeneo ambayo awali yalikuwa yana leseni za utafiti za wachimbaji wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu ni kwamba kwa kuwa maeneo haya ambayo yalikuwa na leseni za utafiti za wachimbaji wakubwa yameshafanyiwa utafiti na Serikali ina taarifa za utafiti zinazoonesha wapi kuna madini, yako kiasi gani, yako umbali gani na kadhalika. Je, ili kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo waliopewa maeneo haya wasichimbe kwa kubahatisha na hatimaye kuingia hasara, Serikali iko tayari ku-share, kuwapatia wachimbaji hawa hizo taarifa za utafiti wa haya maeneo ili wachimbaji wadogo wawe wanachimba kwa uhakika wakijua hapa kuna madini na kuondokana na hali iliyopo sasa hivi ambapo wanachimba kwa kubahatisha na hatimaye wanapata hasara?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Zedi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kampuni kubwa na za kati ambazo zinamiliki maeneo ambayo ni ya utafiti sisi sasa hivi kama Serikali tumeamua kuyarudisha, kwa yale maeneo ambayo yalikuwa hayafanyiwi kazi, tumewarudishia wachimbaji wadogo waweze kuchimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amehoji kwa nini tusiwape data zile wachimbaji wadogo kwa ajili ya kuzitumia kwa maana ya kuchimba bila kubahatisha. Ni kwamba Geological Survey of Tanzania (GST) ambayo iko chini ya Wizara yetu ina ripoti nyingi za maeneo mbalimbali ya uchimbaji. Tunawaomba wale ambao walikuwa tayari wameshaanza kufanya utafiti watupe zile data walizozipata katika maeneo waliyofanyia utafiti. Kwa kweli data tunazo, kwa wachimbaji wanaotaka kupata geological data au report kutoka GST waje wafuate taratibu na watapewa data hizo na waweze kuchimba bila kubahatisha waweze kujipatia tija katika uchimbaji.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa wachimbaji wa Msalala kero zao zinafanana kabisa na kero ya Wilaya ya Nyang’hwale; nataka kujua ni lini Serikali itatoa leseni kwa wachimbaji wadogo wa maeneo ya Bululu, Ifugandi, Kasubuya, Isonda, Nyamalapa, Lyulu, Lubando na Iyenze ili hao wachimbaji waweze kupata hizo leseni na kuchimba ili waweze kuwa na uhakika wa uchimbaji wao na waweze kupata mikopo kutoka benki waweze kuchimba kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumetenga maeneo mengi na tumetenga maeneo makubwa, zaidi ya maeneo matano katika maeneo hayo.

Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyozungumza katika majibu ya swali la msingi, nimewaomba wananchi wa maeneo hayo wachangamkie hii fursa, waje waombe tuwagawie maeneo haya. Mpaka sasa hivi tuna maombi mengi ambayo tayari yamekwishatolewa na sisi sasa hivi tuko katika mchakato wa kuwagawia wachimbaji wadogo na ni maeneo ambayo ni mazuri, yana reserve ya kutosha na wataweza kuchimba kwa faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo bado tunaendelea kuweka mchakato mzuri wa kuweza kufanya resource estimation katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji ili tupate uhakika wa reserve na benki ziweze kuwaamini hawa kutokana na data ambazo tunaweza kuzitoa katika geological reports zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa fursa au kuwaeleza wananchi wa maeneo haya kwamba, wachangamkie fursa tuweze kuwagawia maeneo ya uchimbaji.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti ilishafanya utafiti Wilayani Biharamulo ikiwemo eneo la Busiri na ripoti ipo; na kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema STAMICO imenunua mtambo utakaosaidia wachimbaji kuongeza uzalishaji, je, Serikali iko tayari sasa kupeleka mtambo huo sambamba na kwenda na Waziri ili tukaweke mipango vizuri pale ili tuanze shughuli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Waziri amesema Vituo vya Umahiri vinaanzishwa na kwenye Mkoa wa Kagera ni mmojawapo lakini bahati mbaya siyo Biharamuro ambapo ndiko reserved kubwa ya madini ya dhahabu ipo. Je, Serikali inaweza ikatuambia ni kwa nini Kituo hicho cha Umahiri hakikuwekwa Biharamulo? Kwa sababu kuweka kiwanda cha korosho Bukoba au kiwanda cha kupaki senene Mtwara ni jambo ambalo linaweza lisiwe na tija.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na STAMICO tuko tayari kabisa kupeleka mtambo huo katika maeneo hayo kwa ajili ya utafiti. Walete maombi na sisi tupo tayari kupeleka mtambo huo kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa amehoji kwa nini Kituo cha Umahiri tumekiweka sehemu nyingine na wala si Biharamuro. Kwa kweli kituo hicho tumekiweka katika Mji wa Bukoba na kitaendesha mafunzo yake katika Mji wa Bukoba kwa sababu tumeangalia sehemu ambayo ni center.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera ni mkubwa, tuna uchimbaji mwingine mfano wa tin kutoka Kyerwa, dhahabu kutoka Biharamuro na maeneo mengine. Kwa hiyo, pale ni center ambapo wachimbaji watakutana na ni rahisi kufika Bukoba. Kama ilivyokuwa katika huduma zingine za kimkoa kutoka wilaya mbalimbali wanakusanyika pale Bukoba. Kwa hiyo, tuliamua hivyo kwa sababu pale ni center.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nimhakikishie tu Mheshimiwa Oscar kwamba tupo pamoja na yeye na tutakwenda na tutashirikiana naye na tufanya kazi pamoja kuwasaidia wapigakura wake. Ahsante sana.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri sana ya swali hili; na kwa kweli ni majibu sahihi. Napenda tu niulize maswali madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, yapo maeneo ambayo hayakutajwa hapa ambayo ni Dutumi Bwakila Chini, wana dhahabu na ruby; Konde wana dhahabu na gemstone, hiyo spinels; pia Singisa wana ruby ya kutosha. Sasa swali langu la msingi kwa maana ya yale yaliyojibiwa yajumuishwe na maeneo haya mapya ili sasa tuweze kupata uhalisi wa sehemu ambazo madini haya yanapatikana. Hili ni ombi tu.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Je, Serikali ina utaratibu gani kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo kifedha pamoja na vifaa kwa ajili ya kuboresha uchimbaji wao?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna maeneo ambayo hayajatajwa. Maeneo ambayo tumeyataja ni yale maeneo ambayo tumeona ni potential kwa uchimbaji. Vile vile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yote ya Morogoro tunayafahamu na tumetengeneza ile Quarter Degree Sheet ambayo inaonesha ramani zote za uwepo wa madini.

Mheshimiwa Spika, vile vile uwepo wa madini ni kitu kimoja, lakini madini yanayolipa automatically tu utaona kwamba wachimbaji wanaelekea katika maeneo yale. Ni kama vile inzi anavyofuata kidonda; wachimbaji wakishaona kuna potential maeneo ya uchimbaji, wenyewe unaona wameshasogea pale.

Mheshimiwa Spika, kwa uchambaji ule mkubwa inabidi utafiti wa kina ufanyike na pawe na ile hali ya kuonesha kwamba kuna madini ya kutosha na hata uwekezaji mkubwa unaweza ukawekezwa pale. Kwa wachimbaji wadogo wana uwezo wa kusogea na tuko tayari kuwasaidia kuendelea kuwapa taarifa za kijiolojia.

Mheshimiwa Spika, napenda tu kusema kuhusiana na kuwawezesha wachimbaji wadogo; Wizara imekuwa bado inasaidia kuwawezesha wachimbaji wadogo. Hapo nyumba tulikuwa katika huo mradi wa SMMRP, tulikuwa tunatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo, lakini ruzuku hiyo ilikuwa inatumika vibaya.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi tumesimamisha utoaji wa ruzuku hiyo, sasa tunaangalia namna bora ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ambapo tukiwapa fedha zile, basi waweze kununua vifaa, wafanye tafiti mbalimbali na kuwawezesha kuchimba. hapo awali, walikuwa wanapewa hata wasiyokuwa na sifa, na kweli mpaka sasa tunafuatilia na kuhakikisha kwamba tunakwenda kuwasaidia wachimbaji wadogo tunapokuja na modality nzuri.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kuna tatizo kubwa upande wa watumishi wa Madini na TMA. Kumekuwa na ucheleweshwaji sana wa ushushaji wa mashine upande wa elution na kusababisha hasara kwa wenye elution na pia kwa wachimbaji:-

Je, Serikali imejipanga vipi kuongeza watumishi upande wa TMA na Madini ili ushushaji wa mashine zile za elution iwe wa kila siku ili kupunguza zile hasara wanazozipata watu wenye elution?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna tatizo kidogo kwa wafanyakazi ambao wapo katika Tume ya Madini. Kwa sababu baada ya mabadiliko ya Sheria TMA ilikufa, imeanzishwa Tume ya Madini. Kwa hiyo, sasa hivi wafanyakazi wote, walioko Mikoani wako chini ya Tume ya Madini. Tuna tatizo kidogo kwa wafanyakazi, lakini sasa hivi tuna kwenda kuongeza wafanyakazi wengi zaidi ili waweze kutoa huduma kwenye zile elution.

Mheshimiwa Spika, bado naendelea kusisitiza, watu wote wenye elution tumeona kuna matatizo makubwa sana yanayofanyika, watu wengine wanaenda kule wanafanya mambo ambayo hayaeleweki. Tunaendelea kudhibiti na tunaendelea kutoa tamko kwamba wanapo-load carbon kushusha dhahabu wasijaribu kushusha bila uwepo wa wafanyakazi wa Tume ya Madini. Tunakwenda kuongeza, lakini sasa hivi tunajitahidi kuhakikisha kwamba kila siku waendelee kutoa huduma hiyo.

Mheshimiwa Spika, namhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, tunaendelea kurekebisha.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nipongeze majibu mazuri ya Serikali kutoka kwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu mazuri hayo, basi nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, ripoti hii ya utafiti wa awali sisi kama watu wa Ausia na kule Kondoa hatuna, kwa hiyo hata kuweza kujua kuna kiwango cha chokaa kiasi gani imekuwa ni mtihani na ukizingatia kwamba madini haya ni muhimu sana katika kazi za ujenzi, sasa tunataka kujua, ni hatua gani na wao kama Serikali watatusaidia ili twende kwenye utafiti wa kina tuweze kujua madini kiasi gani yapo kule tuendelee na hatua ya pili ya kupata mwekezaji na hatimaye kuanza kunufaika na uwepo wa madini hayo? Hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ili Mheshimiwa Naibu Waziri akajiridhishe na hali halisi iliyoko pale akifika site, je, anaonaje sasa mimi na yeye pamoja na wataalam wake wa Wizara tukaongozana tukaenda site tuweze kuharakisha mchakato huu wa wananchi wa Kondoa Mjini waweze kunufaika na madini haya ambayo yanaonekana yako kwa wingi.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edwin , Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Sannda kwa kazi nzuri anayoifanya kwa wananchi wa Kondoa, wananchi wa Kondoa nadhani watamtazama tena hapo mwakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu ni kwamba, alichokisema na majibu yangu ya msingi nilivyosema ni sawa, Wizara yetu kupitia GST tunafanya tafiti za kina kupitia zile QDS yaani Quarter degree sheets, tunafanya kitu wanaita Geophysical Survey ambayo inatambua uwepo wa madini katika maeneo hayo na kwa kweli kwa nchi nzima tuna ramani inayoonyesha uwepo wa madini na kila sehemu ni madini gani yako katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utafiti wa kina ambayo ni geochemistry ambayo inafanywa mara nyingi na mwekezaji mwenyewe. Anakwenda anafanya utafiti wa kina kujua deposit iliyopo pale na kama deposit hiyo anaona yeye inaweza ikamlipa, ikawa economical, sasa hatua ya pili ya kuomba leseni ya uchimbaji, anakuja kuomba kwetu na tunampatia kwa ajili ya uchimbaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba utafiti wa kina umeshaonesha madini katika maeneo niliyoyataja na sasa hivi tunakaribisha wawekezaji wengi waje wawekeze kwa sababu utafiti wa kina unahitaji fedha nyingi.

Kwa hiyo sasa hivi tunaweka mahusiano mazuri na maeneo mbalimbali kwa mfano jana nimepokea ugeni kutoka China, wao wanataka kutusaidia kufanya tafiti za kina kuweza kutambua maeneo na deposit zilizopo katika maeneo mbalimbali ili kuweza kuwasaidia wachimbaji kuwapa taarifa za kijiolojia na waweze kwenda kuwekeza maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ameuliza kwamba niko tayari kwenda Kondoa na wataalam, mimi nimweleze tu ni kwamba niko tayari, tunaweza tukaenda Kondoa na niko tayari muda wote na wataalam wapo, lakini pale panapohitajika tutaweza kubeba timu ya wataalam kwenda nayo, lakini kwa kufika pale na kujionea niko tayari wakati wowote.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niishukuru Serikali sana kwa kazi nzuri inayofanya ya kufanya utafiti wa awali ili kuchora ramani za kijiolojia. Hata hivyo, napenda niikumbushe Serikali kwamba iliahidi kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwafanyia utafiti wa kina maana yake minor exploration kwa kupitia STAMICO. Ni lini basi Serikali itafanya kwa sababu wachimbaji wadogo hawana huo mtaji wa kufanya huo utafiti wa kina kwa ajili ya uchimbaji wakiwemo hao wachimbaji na wanaotafuta madini ya chokaa kule Kondoa. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, Serikali ilitoa ahadi kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya tafiti mbalimbali na hasa tafiti za kina, kuweza kujua kuna kiasi gani cha madini katika maeneo mbalimbali na madini tofauti mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza tu STAMICO tayari imekwishanunua mtambo wa ku-drill yaani drilling machine kwa ajili ya kuweza kufanya tafiti za kina. Mtambo huo kwa kweli tayari upo na tumekwishaanza kufanya tafiti mbalimbali maeneo mbalimbali na niwaase tu wale wachimbaji wadogo ambao wanahitaji huduma hiyo wanaweza sasa hivi wakaleta mahitaji yao au maombi yao katika Shirika letu la Taifa, yaani STAMICO kwa ajili ya kufanyiwa hizo exploration.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tutaendelea kununua mashine mbalimbali ambapo tunaweza sasa tukaendelea kufanya tafiti za kina na kuweza kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa sababu tunatambua uchimbaji wao wa kubahatisha ambao unawatia hasara, wengine wanapoteza fedha nyingi kwa sababu ya kwenda kubahatisha. Uchimbaji wa kubahatisha unasababisha umaskini mkubwa. Ahsante sana.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kutokana na majibu hayo, inaonyesha kuwa mgodi huu utakuwa ni neema sana kwa nchi yetu kwa sababu ya uzalishaji wa hayo madini ya Ferro-Niobium ambayo ni muhimu sana kwa ujenzi wa madaraja, Reli ya Standard Gauge pamoja na mabomba ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu huo, napenda kuuliza maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, ni kwa kiasi gani hayo madini ya Ferro-Niobium pamoja na Niobium yenyewe yataongezewa madini ya chuma? Ni kwa kiasi gani haya madini ya chuma tutatumia madini yanayochimbwa hapahapa nchini kwetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, vilevile imeonyeshwa kuwa kuna fidia kwa ajili ya Gereza la Songwe. Je, mwekezaji au wawekezaji wana mkakati gani badala ya kutoa fidia tu lakini waboreshe miundombinu ya gereza hilo ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, vituo vya afya na huduma zingine za elimu hasa kwa wananchi wa Kata ya Bonde la Songwe ambapo kiwanda hicho na mgodi huo upo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Oran Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Ferro- Niobium ni matokeo ya uchakataji wa madini hayo utakaofanyika. Pale Mbeya uchimbaji utakuwa ni wa Niobium peke yake lakini Niobium haiwezi kutumika peke yake ni mpaka pale utakapoichanganya na iron, ndiyo maana tunaita Ferro-Niobium kwa maana ya kutengeneza high strength low-alloy, kwa maana ya material ya kuunganisha vyuma. Ndiyo maana Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba itatumika kwenye madaraja na kwenye pipes, ni kweli madini haya yakishakuwa Ferro-Niobium yanatumika katika kuunganisha vyuma vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge analitambua hilo na sisi kama Serikali tunalitambua hili. Kwa umuhimu wa material haya ndiyo maana katika jibu la msingi nimesema kwamba hii kampuni ikishaweka pale kiwanda, kwa maana ikishachimba Niobium itachanganywa na hiyo Ferro kwa maana ya iron kisha itauzwa nchi za nje. Kwa mfano, Amerika Kaskazini wanahitaji sana bidhaa hii kwa ajili ya utengenezaji au uunganishaji wa vyuma vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni material ambayo yanahitajika sana duniani na sisi kama Serikali tunatambua. Tunasema kabisa kwamba tukishaweka kiwanda hiki pale, wakishachimba Niobium yetu haitatosha mahitaji kwa sababu itakuwa ni kiwanda peke yake Afrika ambacho kitakuwa kimejengwa pale Songwe na Niobium itakayohitajika, itahitajika hata ile ambayo ni nje ya Tanzania, ina maana Congo na Zambia wataleta Niobium yao hapa. Kwa hiyo, tutatumia Niobium karibu ya Afrika nzima katika kiwanda hiki ambacho kitajengwa Songwe. Kwa hiyo, tunatambua umuhimu wa kiwanda hiki na sisi kama Serikali tumeshikamana kihakikisha kwamba sasa tunakwenda kuhakikisha machimbo haya yanaanza na utengenezaji wa kiwanda kwa maana ya kuongeza thamani kinaanzishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, tunatambua kweli machimbo au mgodi huu, yako chini ya Gereza la Songwe. Tunapenda kusema kwamba ile ziara ya Mheshimiwa Rais aliyokuwa amekwanda Mbeya imekuwa ni chachu kubwa sana kuhakikisha kwamba zile mamlaka husika kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Uwekezaji tunakweda kukaa pamoja kuangalia ni namna gani sasa mwekezaji huyu atalipa fidia na kuweza kuhamisha gereza lile kulipeleka pembeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua yuko tayari kulipa kiasi cha dola milioni saba kujenga gereza jipya ambalo litabeba wafungwa 500 na kujenga nyumba mpya kwa ajili ya wafanyakazi zaidi ya 120 na ataweka miundombinu ya umwagiliaji pamoja na barabara kuhakikisha kwamba anaboresha maisha na mazingira ya gereza lile ambalo litajengwa pale pembeni. Kwa hiyo, mamlaka husika zinafanya kazi kuhakikisha kwamba tunamsaidia mwekezaji huyu na masuala yote ya kodi tumeshayaweka sawa, tuna hakika kabisa tutakwenda kuanza mradi huu muhimu kwa Tanzania. Ahsante sana.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, napongeza viongozi wote wa Wizara hii ya Madini, Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya na matokeo yake tunayaona.

Mheshimiwa Spika, nashukuru pia kwamba tayari katika mchakato huu na katika ombi hili wameshatekeleza kwa sehemu kwa kuwapa kibali wachimbaji hawa kwa kuanza na tani 500, nashukuru na kuipongeza Serikali kupitia Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, Maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa lipo soko kubwa la madini haya ya manganese nje ya nchi; Uturuki, India, Afrika Kusini na tayari wachimbaji hawa wadogo wameunganishwa kwenye masoko hayo lakini uchimbaji wa madini hayo unahitaji mtaji mkubwa kwa maana mitambo pia ya kisasa, Serikali iko tayari kuwawezesha wachimbaji hawa wadogo wadogo ili waweze kupata mitambo kama excavator, tipping trucks ili waweze ku-meet uhitaji wa soko na kuongeza kipato kwa Serikali yetu na kwao binafsi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa vile miongoni mwa madini yanayopatikana katika Jimbo la Ngara ni pamoja na Nickel na kwa muda mrefu tumekuwa tukisubiria kuona mradi huu wa Kabanga Nickel unaanza ili kutoa ajira, kuongeza kipato kwa wananchi wa Jimbo la Ngara na Watanzania kwa ujumla, ni lini mgodi huu utaanza ili kuweza kuleta tija kwa wananchi na kwa Taifa pia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli soko la Manganese lipo ndani ya nchi na lipo nje ya nchi, na wachimbaji wadogo wamekutana sana na changamoto ya kuwa na upungufu wa mitaji kwa maana ya kununua vifaa vya uchimbaji, Serikali kupitia ule mradi wa SMRP ambao ulikuwa unafadhiliwa na World Bank kupitia katika Wizara yetu ya Madini ilikuwa inatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo, lakini ruzuku hizo hazikutumika vema inavyostahili ndipo tuliposimamisha utoaji wa ruzuku hizo na sasa hivi tunatoa elimu kwa wachimbaji, tunatoa taarifa za uchimbaji kwa maana ya geological information na hizi taarifa tunazipendekeza kuzipeleka, au tunazipeleka na kuwashauri watu wa mabenki mbalimbali waweze kuzitambua taarifa hizi na kuweza kuwapatia mikopo wachimbaji wadogo ili wachimbaji hao waweze kukopa na kununua vifaa mbalimbali ambavyo vinaweza vikatumika katika uchimbaji na kuongeza tija katika uchimbaji huo.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusiana na mgodi wa Kabanga Nickel ni kweli kabisa nickel hapo kipindi cha nyuma katika soko la dunia ilikuwa na bei ya chini sana ambapo uchimbaji wake ulikuwa hauna tija, kwa sababu bei ya nickel katika soko la Dunia ilikuwa chini ya dola 3.5 kwa pawn moja, lakini sasa hivi, bei ya pawn moja ya nickel imepanda kwenda hadi dola Sita katika soko la Dunia ambapo Wawekezaji sasa wameanza kuona kwamba wakiwekeza kwenye nickel itaweza kuwa na faida, katika ule mradi wa Kabanga moja ya leseni ambayo ilikuwa ni retention license ilifutwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, baada ya kufanya mabadiliko ya sheria mwaka 2017 hapa tulipo ni kwamba ile retention license ipo na sasa hivi tunaifanyia mchakato wa kutafuta Mwekezaji ambaye tunaona yuko serious anaweza akawekeza, sasa hivi tuko tayari kutoa leseni hiyo kwa mtu yeyote ambaye tunaona anaweza akafanya shughuli hiyo, mpaka sasa hivi tuna mchakato unaoendelea ndani ya Wizara yetu kuona namna ya kuweza kumpa Mwekezaji ambaye tunaona anaweza akawekeza kwa faida na mradi huo uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni wakati wowote watu wa Kabanga wataona mradi huo unaanza na ninapongeza Serikali kwa juhudi zake za kupeleka umeme eneo hilo pamoja na miundombinu ya reli na barabara ambayo sasa itakuwa ni miundombinu muhimu katika utekelezaji wa mradi huu wa Kabanga Nickel.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi. Vijiji vya Katani, Malongwe, Sintaling, Kana na vinginevyo viko katika Awamu ya III ya kupewa umeme mzunguko wa pili lakini mpaka sasa hatujapata. Je, ni lini mradi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu spika, nishukuru sana majibu yaliyotolewa upande wa Wizara ya Nishati lakini kwa kusisitiza kwa jinsi alivyouliza Mheshimiwa Atu sisi Wizara ya Madini kwa kushirikiana na TOL…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malizia kabisa jina lake kwa sababu kule ukikatisha kule kwao anaweza ikajulikana kuna Mbunge mpya humu ndani. Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu spika, ahsante sana Mheshimiwa Atupele Mwakibete. Ni kwamba Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Kampuni ya Oxygen Limited katika lile eneo ambalo linatoa ile hewa ya carbondioxide kampuni ya TOL wameweka sensa maalumu kwa ajili ya ku-detect hewa ile inapojitokeza kutambua mapema, na hewa hiyo inapojitokeza zile sensa zinatoa taarifa kwamba kuna hewa chafu inakuja na kwa kweli wanatoa taarifa katika maeneo yale kwa watu wanaozunguka maeneo yale kuweza kukaa mbali na lile eneo na kuhakikisha kwamba hapatokei tena vifo vinavyotokana na watu kupumua hewa hii ya ukaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuna zile hatua za awali zimeshachukuliwa na kwa kweli Tanzania Oxygen kupitia leseni yao namba 139 ambayo imetolewa mwaka 2002 wako tayari sasa kuhakikisha kwamba wanakwenda katika uwekezaji na kuhakikisha kwamba wanakwenda kuitumia ile hewa ya carbon dioxide katika matumizi mbalimbali ambao yamepangwa ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge yako katika mpango wa pili wa utekelezaji wa mradi wa REA, na kwa kweli katika eneo la Katani na Malongwe imeshaingia kwenye mpango huo na utekelezaji wake unaanza Februari mwaka huu kuanzia tarehe 28. Lakini kuna suala moja ambalo Mheshimiwa hajauliza kule Wampembe umbali takribani wa kilometa 68 kutoka Mjini ni eneo ambalo ni tengefu sana, eneo hili lilikuwa nalo liingie kwenye mpango wa round ya pili lakini badala yake tumeanza kuitekeleza kuanzia wiki iliyopita. Nimeomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge ili awape taarifa wananchi wake wananchi wa Wampembe ambao wanahitaji umeme kwa haraka sana ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Waziri na Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kutoa leseni 22 kwa wachimbaji wadogo wa Wilaya ya Nyang‟hwale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali kwa kuwa Wachimbaji wengi bado wako maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Nyang‟hwale kama vile Isekeli, Isonda, Lyulu, Nyamalapa, Ifungandi, Shibalanga pamoja na Kasubuya, Je, Wizara imejipanga vipi kuwapa tena maeneo hayo wale Wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imeshatoa leseni kwa Wachimbaji wadogo eneo la Bululu hivi karibuni uzalishaji wa dhahabu nyingi zitaanza kutoka lakini kuna jengo ambalo liko tayari kwa ajili ya ununuzi wa dhahabu. Je Serikali iko tayari sasa kukamilisha vibali vyote ili kufungua Jengo hilo la ununuzi wa dhahabu Wilaya ya Nyang'hwale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa katika majibu ya swali la msingi sisi kama Wizara ya Madini kwa kupitia Tume ya Madini tunaendelea kuhakikisha kwamba yale maeneo yote tunayoyaona kwamba yana madini ambayo wachimbaji wadogo wanaweza wakachimba basi sisi hatuhusiki kabisa kuwapa wachimbaji wadogo na kuchimba na hata katika majibu yangu ya msingi nimetoa wito kwa wale Wamiliki wote wanaomiliki maeneo makubwa ya utafiti na hawayaendelezi yale maeneo na utafiti hauendelei.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tuko tayari kuyafuta maeneo hayo, kufuta leseni hizo za utafiti na kuwapa wachimbaji wadogo ili waweze kuchimba, waweze kulipa Kodi na wao wenyewe waweze kujikimu katika maisha yao. Vilevile niendelee kumshukuru sana Mbunge kwa jinsi anavyofatilia na jinsi anavyokuwa karibu na wachimbaji wadogo katika Jimbo lake kwa sababu tunatambua Jimbo lake lina wachimbaji wadogo wengi sana.

Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie katika swali lake la pili ameuliza utayari wa sisi Wizara na Tume ya Madini kuanzisha soko kwa ajili ya kuuza madini katika Jengo ambalo liko tayari nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge sisi tuko tayari na sasa hivi nawaagiza Tume ya Madini waende katika Jengo hilo wakague kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa eneo hilo au wa Wilaya ya Nyang‟hwale walione kama linatimiza vigezo mara moja soko hilo lifunguliwe na madini yaanze kuuzwa katika soko hilo. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu ingawa ningefurahi zaidi yangekuwa siyo ya kijumla kiasi hicho kwa sababu ningependa japo nisikie tu kuwa kama wapo tayari kuja kufanya hata mafunzo tu kwa ajili ya vijana wetu ambao wanajishughulisha na shughuli hizi. Hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza:

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni kuhusiana na ule Mgodi wa Kiwira ule waunderground. Mgodi ule umesimama kwa muda mrefu sana na hivi sasa tunavyozungumza hatuna hakika yaani kuna sintofahamu ya kujua ni nani mwekezaji na lini ataanza kufanya kazi ili tuweze kuona mafanikio ya mgodi ule?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kuwa mwaka 2010 Kamati ya Kudumu ya Bunge ilishauri kuwa mgodi ule uwekwe chini ya STAMICO na TANESCO kwa sababu madhumuni ya mgodi ule ilikuwa ni kuzalisha umeme, lakini mpaka sasa hivi tunaona uko chini ya STAMICO lakini hatuoni ule ubia na TANESCO ambao ungesaidia sasa katika kuhakikisha kuwa umeme unapatikana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba ule Mgodi wa Kiwira umesimama kwa muda mrefu sasa na tatizo lilikuwa ni moja tu, baada ya ile kampuni ya TAN Power Resources kutoka pale ilitakiwa kwamba wahamishe zile share zao ili ziweze kuchukuliwa na Serikali na share hizo tungeweza kuzipeleka STAMICO kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza mradi ule.

Sasa wale TAN Power Resources walikuwa na deni ambalo walitakiwa walipe (capital gain tax)ambayo ilikuwa ni deni la bilioni 2.9 hawajalipa lile deni na Serikali kupitia TRAni kwamba wanafatilia kuweza kuwabana wale wahusika waweze kulipa deni hilo ili tuweze kupata tax clearance na kuhamisha zile share ziweze kwenda Serikalini au STAMICO ili kuweza kuanzisha mradi ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi TRA wanaendelea kufatilia hawa TAN Power Resources na inasemekana hawapo na watu hawa ambao hawapo sasa hivi kuna hatua inayofuata ya kufatilia kuwajua ma-director wa ile TAN Power Resources na kuweza kuwabana ikiwezekana kwenda kuchukua passport zao binafsi ili waweze kulipa lile deni la 2.9 bilioni. Baada ya kufanya hivyo STAMICO wakishachukua mradi huo mara moja mradi ule utaanza na uchimbaji utaendelea. Ahsante sana.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza, wachimbaji wadogo wadogo katika taifa hili wamekuwa ndiyo wagunduzi wa kwanza wa maeneo ya machimbo, hususan katika mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutokana na ukiritimba unaoendelea kwa baadhi ya matajiri, especially katika Mkoa wa Katavi, wamekuwa wanapora maeneo ya wananchi baada ya kugundua kwamba kuna madini, wanawapora lakini wanakwenda kufanya mazingira ya rushwa kwenye ofisi za madini wanahakikisha wanapata leseni za uchimbaji na huku wakiwaacha wachimbaji hawa wakiendelea kutapatapa na kukosa maeneo ya kuweza kuchimba.

Nini sasa Serikali ifanye ili kuhakikisha inatatua janga hili ambalo linaleta umaskini mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mkononi hapa nina malalamiko ya wachimbaji wadogowadogo ambao wameajiriwa sasa kwenye haya machimbo, wamekuwa wanasainishwa mikataba ambayo ni feki, wananyanyaswa na wanapokuwa wanadai mafao yao au wanadai mishahara yao wamekuwa wakifukuzwa na kupigwa, wengine na kufunguliwa mashitaka. Migodi hiyo iko katika Kata za Idindi, Isulamilomo, Magula, Kasakalawe pamoja na Society ambako ni katika Kata ya Magama.

Niambie Mheshimiwa Waziri ni lini utakuja sasa kuwasikiliza wachimbaji hao wadogo na kero na unyanyasaji ambao wanafanyiwa katika migodi hii ambayo nimeitaja?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimhakikishie, katika swali la pili kwamba niko tayari kuja Katavi, kuja kutembelea na kusikiliza kero za wachimbaji wadogo na tumekuwa tukifanya hivyo na nilikwenda Katavi, lakini vilevile niko tayari kwenda tena kama kweli kuna specific issue ambayo ninaweza kwenda kusikiliza na kuweza kuitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile, labda nimweleza tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba kama kuna matatizo ya waajiriwa, kwa sababu kwenye wachimbaji wadogo kuna waliojiajiri na walioajiriwa, kama kuna matatizo ya walioajiriwa na migodi, tunaomba hizo taarifa mtuletee. Yetote aliyeajiri na ananyanyasa wafanyakazi, sisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inashughulika na masuala ya ajira ambao wanashikilia Sheria ya Kazi, tuko nao kushirikiana nao kuhakikisha kwamba tunatatua kero za wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika swali lake la msingi Mheshimiwa Mbunge ameuliza katika masuala ya ushirika, ni kweli. Kuna vikundi vya ushirika, acha ushirika wa mazao, ushirika wa madini, tumewapa watu leseni mbalimbali kuchimba kwa ushirika, lakini unakuta wale wafanyakazi wanaochimba au wanachama wa vikundi vile, wananyanyaswa na viongozi wa vikundi hivyo. Tunaomba kutoa wito na tunatoa onyo, kwa wale ambao ni viongozi wa vikundi, wanawanyanyasa wenzao, waache mtindo huo mara moja kwa sabahu sasa hivi tunawashughulikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hatusiti kuwanyang’anya leseni vikundi ambavyo havifanyo mikutano ya mwaka, havitoi taarifa ya mapato na matumizi, tuko tayari kuvifuta na kuwapa watu wengine kuchimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, vilevile, katika alipozungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba, wachimbaji wadogo ndiyo wagunduzi wakubwa wa machimbo. Nikubaliane na yeye, kuna baadhi ya maeneo wachimbaji wadogo kweli unakuta ndiyo wamevumbua wachimbaji na wamekuwa wakinyanyasika, sasa hivi mtindo huu tumeukomesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kuna maeneo mengine watafiti wanakuwa wanagundua, wanapofanya kazi zao wa utafiti, wachimbaji wadogo wanavamia maeneo yale, kwa sababu wanaona kwamba kuna hali na dalili ya uchimbaji. Kwa hiyo, kunakuwa ni maeneo ambayo unaweza kukuta wachimbaj wadogo wametangulia au watafiti wametangulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini, tunayaangalia hayo na tunatatua kero mbalimbali zinazotokana na migogoro hiyo.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kwenye migodi yetu kuna watu ambao wamejiajiri kwa ajili ya kugonga kokoto zile zinazodhaniwa zina dhahabu, vibarua hawa wamekuwa wakilazimishwa kununua vitambulisho vya ujasiriamali na jana kumetokea sintofahamu, kuhusu hao vibarua na Mtendaji wa Kata ya Nyugwa na kusababisha wale vibarua kuondoka kwenye maeneo yao ya kazi kwa kulazimishwa kununua vile vitambulisho.

Je, Waziri, uko tayari kumwambia Mtendaji huyo aahirishe hilo zoezi? Kwa sababu hawa wanajiajiri wao kwa kugongagonga kokoto kwa mchanga mchana kutwa shilingi 2000, leo unakwenda kumlazimisha mgongaji kokoto huyu kitambulisho cha elfu 20. Je, Waziri uko tayari kusitisha hilo zoezi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mgogoro mkubwa ambao pengine ni kutokutambua au kutokuelewa. Tunasema wajasiriamali, tamko la Mheshimiwa Rais amesema, wajasiriamali wote walipe elfu 20, ambao hawazidi shilingi milioni nne kwa mwaka, yaani mapato yao, hilo ni tamko na tayari kutekelezaji umeanza. Sasa katika masuala ya uchimbaji wa madini, kuna kodi za upande wa uchimbaji wa madini, ambazo kweli tunazitoza, mtu anapopata dhahabu kwa mfano, analipa asilimia sita mrabaha analipa asilimia moja kwa ajili ya clearance, hizo kodi zinaeleweka, lakini hao ni wachimbaji ambao tunawatambua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale wachimbaji wadogo, maeneo mengi, ma-DC wamekuwa wakienda kule na kuhakikisha kwamba, wale kwa sababu wanatambulika na wenyewe kama wajasiriamali, waliojiajiri. Nimshauri tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba, ukichukua elfu 20, ukaigawanya kwa siku 365 ni shilingi 54 tu kwa siku, haiwezekani mtu anafanya biashara, asilipe chochote kabisa. Kwa sababu ile ile biashara ya mawe inaishia huko tu, tunayem-charge kodi kwenye upande wa migodi ni yule ambaye anapata dhahabu, hao wengine tunawapata vipi. Kwa hiyo, wapewe vile vitambulisho, kwanza tuwafahamu, lakini cha pili na wao wachangie kidogo pato la Taifa kwa kulipa shilingi 54 kwa siku, ambayo ni sawasawa na shilingi 20 kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Mji wa Tarime tuna Migodi midogo ya Buguti na Kibaga, tumekuwa tukishuhudia migogoro kwa wachimbaji wadogo kwenye mgodi wa Kibaga na Mgodi ule wa Kibaga leseni yake iko na Barrick kwa muda mrefu na nimeshawahi kuuliza hapa, Serikali ikasema kwamba ina- revoke leseni ya Barrick. Na kwa sababu leo Naibu Waziri imekiri kwamba zile leseni zote ambazo hazifanyiwi kazi mtaenda kuzifuta na kuwapa wachimbaji wadogo. Ningetaka kujua specifically, kwa wachimbaji wadogowadogo wale wa Kibaga, ni lini sasa ile leseni itaondolewa kwa Barrick ili waweze kupewa wachimbaji wadogowadogo wa Kibaga waweze kufanya kazi zao kwa ufasaha zaidi na bila kubughudhiwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tumekwishakutoa tamko, kwa leseni zote ambazo hazifanyiwi kazi, na hasa ambazo ziko kwenye utafiti na hazifanyiwi kazi, zirejeshwe, zirudishwe na sisi tuweze kutafuta namna ya kuwagawia wachimbaji wadogo na tunawagawia katika vikundi. Mheshimiwa Mbunge ameniuliza swali hilo lakini hakunipa specific namba ipi, naomba tu nilichukue suala hili, tuone ni leseni ipi, aidha ni ya uchimbaji, au ni leseni ya utafiti. Kama leseni ni ya utafiti na haifanyiwi kazi, sisi tutazirudisha, lakini nimhakikishie tu kwamba kuna leseni nne ambazo zilisharudishwa na watu wa Barrick maeneo hayo na wameshaturudishia sisi na walishaandika barua, tutaangalia namna ya kuangalia kuwagawia wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona, ili niulize swali la nyongeza kuhusu madini. Sisi katika Wilaya ya Longido tuna madini ya aina ya Ruby, na kuna mgodi wa miaka mingi, unaoitwa Mundarara Ruby Mine na sasa hivi wachimbaji wadogowadogo wameibuka wametokeza baada ya kujua madini haya yana thamani na ninaamini Serikali itakuja kuwajengea uwezo.

Lakini swali langu ni kwamba, huu mgodi ambao ulianzishwa tangu kabla ya uhuru, ni wa nani, na kama ni wa Serikali, Serikali inafaidikaje na huu mgodi na ni asilimia ngapi kama kuna ownership ya joint venture na mwekezaji?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, pale Mundarara, kuna mgodi ambao ni mgodi wa uchimbaji wa Ruby. Mgodi ule kabla, miaka ya 60, ni kwamba mgodi ule ulikuwa ni mali ya Serikali, na sisi tumeweza kufuatilia na tuliunda Tume ili kuona ni namna gani mgodi ule uliweza kuporwa. Nipende tu kusema kwamba tumelifuatilia na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mgodi ule unamilikiwa sehemu na Serikali na kuna kampuni nyingine ambayo ilikuwa inamiliki, lakini mgodi ule mpaka sasa hivi, asilimia 50 tunaumiliki sisi yaani Wizara ya Madini kupitia Shirika la Madini yaani la STAMICO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mgodi huu ulikuwa na mikiki mingi, ambako Tume tumeituma, tumetuma Tume ya watu maalumu, wafuatilie, watushauri tuone namna gani ya mgodi ule kuurudisha Serikalini au kutafuta namna ya kuweza kuungana na mchimbaji mwingine au mwekezaji mwingine na Serikali iweze kupata mapato yake kupitia shirika la madini la STAMICO.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa bahati mbaya swali langu lilinukuliwa tofauti na nilivyowasilisha. Lakini kwa faida ya wananchi wa Nyakabale ninaomba kujua kwamba sehemu ya Nyakabale ni eneo limekuwa likipata shida kubwa kutokana na mgodi wa Geita Gold Mine kwa maana ya kimatatizo ya kimazingira lakini hata wananchi wenyewe kuzuia kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ya kwamba itabidi wapishe shughuli za mgodi.

Mheshimiwa Spika, lakini ni miaka sasa hawawaondoi katika eneo hilo. Sasa ninaomba kujua tuliahidiwa na Mheshimiwa Waziri Kalemani kwamba wale wananchi wangeondolewa lakini mpaka leo hawajaondolewa. Je, Serikali inatupa leo kauli gani wananchi wa Geita hasa wananchi wa Nyakabale kuhusu kulipwa fidia ama kuruhusiwa kwamba waendelee na shughuli zao za kimaendeleo katika eneo hilo la Nyakabale?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili linahusu katika upande huo wa ulipwaji fidia, sheria yetu imeruhusu haya makampuni kuweza kutumia wathamini binafsi kwenda kuhesabu mali za wananchi na hatimaye kuweza kulipwa na hili limeleta malalamiko kwa maana ya wananchi wengine kuona kwamba wanapunjwa na kampuni hizo kutetea maslahi zaidi za makampuni hayo ya uwekezaji. Sasa Je, Serikali leo inatoa kauli gani kuhakikisha ya kwamba maslahi ya wananchi katika maeneo husika yanalindwa ahsante? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba maeneo ya Nyakabale yako ndani ya leseni ya uchimbaji yaani leseni ambayo ni special mining license ya mgodi huu wa GGM ndani ya zile kilomita 290 za mgodi huo.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba sheria inasema kwamba ni lazima mtu ambaye anataka kuwekeza kuchimba maeneo yale watu wanaoishi maeneo yale ni lazima awalipe fidia waondoke ili aweze kufanya operation zake.

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la Nyakabale liko nyuma ya mgodi huo na kweli kuna wakati fulani mimi mwenyewe niliweza kutembelea pale nikakuta kuna maeneo mengine ambayo wananchi walizuiliwa wasiendeleze yale maeneo yao au wasiendelee kujenga kwa sababu wako ndani ya leseni na mimi niliweza kuwapa nilitoa tamko kwa mgodi kwamba wawalipe wananchi hao na kuondoka kama wananchi hao wanaathirika na uchimbaji huo. Lakini vilevile ni kwamba mgodi walisema wako tayari wataweza kuwaondoa wale wote ambao wanaonekana wanaathirika na shughuli za mgodi.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika swali la pili kuhusu fidia ya yale maeneo ambayo yanazunguka mgodi ambayo yapo karibu na Mji wa Geita hapa tunavyozungumza ni kwamba uthaminishaji ulikuwa unaendelea na uthaminishaji ule ulikuwa unafanywa na kampuni binafsi lakini chini ya usimamizi wa Chef Valuer wa Serikali ambapo mpaka sasa hivi tumekwishakuona kwamba ni watu wangapi ambao wanatakiwa walipwe uthaminishaji umeshakubaliana waliothaminiwa na wathaminishaji wote wameshakubaliana na toka Jumatatu tayari fidia hizo zimeanza kulipwa na kampuni ahsante sana. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante wananchi wangu wa Epanko tangu wafanyiwe tathimini ni miaka miwili mpaka sasa hivi hawajalipwa, na Mheshimiwa Waziri alishafika huko na anajua shida, sasa sheria inasema mtu akifanyiwa uthamini baada ya miezi sita anatakiwa alipwe na ikizidi hapo analipwa fidia na uthamini ukizidi miaka miwili unakuwa cancelled unafanywa upya, nataka kusikia kauli Serikali. Je, hawa wananchi waliofanyiwa uthamini wao lini watalipwa ni miaka miwili imeshapita?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli uzuri kwenye sheria ya uthaminishaji na kulipa fidia iko wazi tunataka makampuni yote yakishafanya uthamini walipe ndani ya muda uliokubaliwa, mtu ambaye hatalipa ndani ya miezi sita sheria inasema atalipa lakini atalipa na interest yaani kwa maana ya usumbufu na asipolipa ndani ya miaka miwili, sheria inasema kwamba tayari ule uthaminishaji una- expire kwa mujibu wa sheria kwa hiyo ni lazima mrudi mfanye uthaminishaji upya.

Mheshimiwa Spika, nipende kutoa tu wito kwa makampuni yote walipe kwa muda ambao umepangwa wasipofanya hivyo inaleta mtafaruku, mfano mzuri uko kule Mara Tarime, kuna watu ambao hawakulipwa ndani ya muda matokeo yalivyokuja kuonekana ni kwamba sasa wale wenye zile nyumba waliona kwamba baadaye wataonekana watakuja kuondolewa wakawa wanajenga nyumba za kutegesha, nyumba za gharama nafuu ili waje walipwe fedha nyingi. Sasa hii imetokea maeneo mengi, kwa hiyo tunaomba sana makampuni yote tunawahasa mkishafanya uthaminishaji lipeni kadri ya sheria inavyosema usipofanya hivyo inaleta mtafaruku. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niipongeze Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya ya kuhakikisha inaboresha huduma za afya kwa ajili ya kupunguza vifo vya wanawake wanaojifungua. Pamoja na pongezi hizi nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza; moja ya sababu inayofanya wanawake wengi wanafariki kwa kujifungua ni kutokana na kutokwa damu nyingi wakati wakijifungua, lakini lipo tatizo kubwa sana la ile Benki ya Damu katika Hospitali za Mikoa. Kwa mfano, Kanda ya Ziwa Mikoa yote sita tunategemea Bugando. Damu inatolewa Serengeti, Bunda, Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga mpaka Tabora na Kigoma lakini inatakiwa iletwe Bugando kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Mheshimiwa Spika, wakati huo huo damu ikishatolewa kwenye mwili wa Mwanadamu inatakiwa ikae siku 30 baadaye ina-expire. Kwa hiyo, unakuta kutokana na tatizo na ule msongamano ulioko Bugando, damu inachelewa kurudi kule kwenye Vituo vya Afya na kwenye Hospitali za Mkoa na kwenye Hospitali za Wilaya. Ningependa kujua sasa, Serikali ina mkakati gani wa kujenga vituo vya Benki ya Damu katika Hospitali za Rufaa zote nchini pamoja na Hospitali za Wilaya na ikiwezekana hata Vituo vya Afya? Hilo swali la kwanza.

Mheshjimiwa Spika, swali la pili; moja ya sababu ya wanawake wanaofariki kwa kujifungua ni pamoja na kutoa mimba au mimba kutoka. Siku hizi humu mitaani kwenye maduka ya pharmacy kuna dawa zinaitwa misoprostol, Madakrati mtanisaidia kuijua vizuri maana mimi siyo Daktari. Vijana wa kike na wanawake huko mtaani wanafundishana siku hizi ndiyo wanazotolea mimba na hasa zile mimba ambazo hazikutarajiwa.

Mheshimiwa Spika, napenda kujua, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti hali hiyo? Kwa sababu wanapokunywa zile dawa, mimba inatoka lakini wakati mwingine kile kiumbe kinabaki ndani kinasababisha maambukizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa kujua Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti hali hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, naomba nimjibu Mheshimiwa Mama yangu Mheshimiwa Amina Makilagi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kwamba kweli akina mama wanapojifungua wakati mwingine damu nyingi hutoka na kuweza kupoteza maisha yao. Ushauri wangu tu ni kwamba akina mama wafuate masharti wanapokwenda kwenye kliniki wakati wa ujauzito, kuna elimu wanapewa wakati huo. Vilevile wakati wa kujifungua na hasa mimba ya kwanza ni kwamba akina mama ni vizuri wakajifungua kwenye Vituo vya Afya. Wakati mwingine wanapokuwa wanajifungua nje ya Vituo vya Afya au hospitalini hasa kwa ule ujauzito wa kwanza, inakuwa ni hatari sana, kwa sababu huwa wanafanyiwa kitu kinaitwa Episiotomy ambayo ni kuongeza njia wakati wa kujifungua. Sasa ile inafanya damu zinatoka nyingi, usipo-repair vizuri kwa wakati, mama huyu anaweza kupoteza maisha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kuwa na blood bank ni kwamba huu ni mkakati ambao kila hospitali inatakiwa iwe na blood bank hata kama ni kiasi kidogo, wanahifadhi damu kwa ajili ya matumizi, pale inapotokea kuna dharura, basi waweze kumpa mgonjwa waweze kuokoa maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuhusiana na suala la hizi dawa ambazo ni Misoprostol, hizi dawa huwa zinatumika katika kuondoa au kutoa mimba. Dawa hizi huwa zinatakiwa zitolewe chini ya usimamizi wa daktari, yaani daktari ndiye anayetakiwa aandike dawa hiyo. Mgonjwa anapokwenda pharmacy, basi aende na cheti cha kuweza kupewa dawa hiyo. Hizi dawa huwa zina matumizi mengine.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna dawa hizo zimeanza kuzunguka ziko kwenye ma-pharmacy na dawa hizi ni za kazi maalum kwa kuzuia damu zisitoke, lakini wanazitumia vibaya kwa sababu side effect ya hiyo dawa ni kuweza kutoa mimba. Kwa hiyo, tunawashauri watu wote wenye pharmacy wasitoe dawa hizi bila prescription. Lazima dawa hii daktari athibitishe, aandike cheti, ampeleke kwenye pharmacy na mgonjwa aweze kupewa dawa hiyo. Kwa maana tunafahamu kabisa madaktari wanapotoa dawa hizo wanazitoa kwa sababu maalum.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Vifo vingine vya akina mama vinatokana na akina mama wenyewe. Juzi tu Kirando katika Jimbo langu la Nkasi Kaskazini, mama mmoja, tena zao lake la nane, kachelewa mwenyewe makusudi, Kirando kuna kituo kizuri cha afya kikubwa na kizuri kinafanya na operesheni, ni kizuri sana. Kajifanyia operesheni mwenyewe kwa kutumia nyembe na katoa mtoto. Hivi sasa yuko hospitali katika Kituo cha Afya cha Kirando, hali yake siyo nzuri, ila hali ya mtoto ni nzuri. Vifo vingine vinasababishwa na akina mama wenyewe kuchelewa kwenda kwenye Vituo vya Afya. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO):
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, naomba nijibu hoja ya Mheshimiwa Keissy kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyozungumza katika majibu ya nyongeza ni kwamba akina mama wote nchini unapokuwa mjamzito, pale anapojitambua tu kwamba sasa hivi amekuwa mjamzito ni vyema ukaenda kliniki kwa ajili ya kwanza unaenda kupimwa, wanaangalia development ya mtoto, lakini vilevile wanaangalia afya yako wewe mama kama inakwenda vizuri na kama kuna tatizo watakwambia na nini ufanye.

Mheshimiwa Spika, vilevile ni kwamba kwa kipindi hicho wanakupa elimu ya uzazi salama. Kwa hiyo, ni vizuri wakina mama wote wakati wa kujifungua hili suala usichukulie kama zamani, tulikuwa na ma-tradition healers wale wanaitwa Wakunga wa Jadi, wasiende tena kule. Wengine pengine alivyosema Mheshimiwa Keissy, huyu mama ana uzao mwingi, kwa hiyo, ameshakuwa na experience, anaona kwamba kuzaa ni kitu rahisi, lakini kumbe kila kizazi ni special. Ni vizuri ukaenda kwenye Kituo cha aAya ukapewa huduma na Manesi ambao ni professional.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Kwa kuwa vifo vingi vya wamama wakati wa kujifungua hutokana na kukosa huduma na ufuatiliaji katika hatua mbalimbali za ujauzito, sasa basi Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kurasimisha hao Community Health Workers au watoa huduma katika jamii kwa mambo ya afya ili waweze kupewa mori, kuelimishwa na ili kuwawezesha wanajamii hususan akina mama wajawazito ili kupunguza vifo vya wamama wajawazito? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MADINI (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Semesi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Community Health Workers wanapewa elimu pana. Tumeanza kwenye masuala ya UKIMWI, lakini vilevile kwenye masuala ya afya ya uzazi na afya ya lishe kwa watoto. Hii elimu inatolewa kwa hawa Community Health Workers ili waweze kutoa elimu kwa wananchi, watoe elimu kwa wanavijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile ni kwamba sasa hivi mkakati mkubwa ambao tunafanya katika Wizara hii ya Afya ni kuhakikisha kwamba hata wale ambao ni Waganga wa Jadi na wenyewe wanapewa elimu waelezwe vihatarishi, wapewe elimu kuweza kutambua hali ya hatari ambayo inaweza kusababisha mtu kupata kifo kutokana na uzembe fulani, kwa mfano, kupungukiwa na damu, masuala hayo ya ujauzito, wanapewa ile elimu ambayo ni kujua kabisa hali hatarishi kwamba katika hali kama hii mgonjwa huyu anatakiwa apewe huduma fulani, lakini hali fulani ikizidi, basi mgonjwa huyu apelekwe hospitali aweze kupata huduma zaidi. (Makofi)
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu suala hili, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, namshukuru sana Waziri wa Madini, Mheshimiwa Doto ambaye alifika kabisa Sakale kwenye kijiji hiki na kujionea hali halisi ya pale na pili, nawashukuru sana Wizara ya Madini pamoja Mazingira, kwa kuweza kupeleka wataalam kwa haraka sana kwenda kuangalia mazingira ya eneo lile na nawashukuru sana wananchi wa Sakale na Mbomole kwa nidhamu ambayo wanaionesha kuweza kutunza chazo cha maji cha Mto Zigi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu la kwanza, ni ukweli kwamba pale dhahabu ipo kwenye Milima ya Sakale ambayo ipo karibu na Mto Zigi na dhahabu ambayo ipo pale ni ya kiwango cha juu. Sasa dhahabu ipo ndani ya mto na kwenye Milima ya Sakale. Sasa Serikali itakubaliana na mimi kwamba kuna umuhimu wa kutuma wataalam wa juu waliobobea kuweza kwenda kuangalia tena namna gani dhahabu ile inaweza kuchimbwa kutoka kwenye milima ambayo iko karibu na Mto Zigi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba kila wananchi wa Sakale, Mbomole wakitembea kwenye ardhi ile, wanahisia wanakanyaga dhahabu sasa na wanasikitika kwamba wanakanyaga mali ambayo ipo chini ya ardhi lakini Serikali haioni umuhimu wa kuwasaidia kutoa ile mali pale nje.

Sasa Serikali inaona umuhimu gani wa kuchukua hatua za haraka kupeleka wale wataalam na kuhakikisha kwamba wananchi wa Sakale, Mbomole na Muheza wanafaidika na dhahabu hiyo ambayo iko kwenye Milima ya Sakale? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika milima hiyo kuna dhahabu nyingi na milima hiyo kwenda hadi kwenye Mto Zigi kuna dhahabu nyingi tu ya kutosha, lakini kwa uchimbaji mdogo kwa sababu wachimbaji wadogo wanatumia kemikali ya zebaki ambayo ni hatari sana kwa afya ya binadamu, Wizara pamoja na wataalam wameshauri kwamba uchimbaji mdogo usifanyike pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa uchimbaji wa kati na uchimbaji mkubwa hilo linawezekana, lakini cha msingi tu ni kwamba ni lazima tupate mwekezaji ambaye anaweza akafanya utafiti wa kina kuweza kujua mashapo yamekaa vipi katika milima hiyo hadi kwenye mto na vilevile aweze kuchimba na uchimbaji wa maeneo hayo inabidi uchimbe katika style ya underground badala ya open cast mining. Ni kwamba wachimbe kwa kwenda chini na wahakikishe kwamba uchimbaji ule hautaathiri vyanzo vya maji kwa sababu vyanzo vya maji vya Mto Zigi vinategemewa katika Jiji la Tanga, Wilaya ya Korogwe na Wilaya ya Muheza yenyewe. Kwa hiyo, vyanzo hivi ni muhimu sana, ukiweka uchimbaji pale, ukawa unatiririsha kemikali kwenye vyanzo vya maji, ni hatari kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama uchimbaji wa kati au wa hali ya juu kwa sababu wale wanaweza wakachimba kwenda underground na vilevile ile processing plant inabidi iwekwe mbali na eneo hilo. Kwa hiyo, kusafirisha zile rocks za dhahabu kupeleka maeneo ambayo ni ya processing plant inabidi iwe ni distance kubwa, kwa hiyo, ni lazima uwekezaji uwe ni wa hali ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimshauri Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuwasiliana, tutafute wawekezaji ambao wanaweza wakafanya detailed exploration kwa maana ya kujua mashapo yamekaa vipi na wakaweza kuja na plan nzuri ya uchimbaji ambao hautaathiri mazingira, vyanzo vya maji, hilo linawezekana. Kwa hiyo, tushirikiane tu na Mheshimiwa Mbunge kwa hilo nadhani tunaweza tukafikia pazuri. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa maonesho ya madini yaliyokuwa yanajulikana kama Arusha Gem Fair yalikuwa yanafanyika kuanzia mwaka 1992 na mwaka 2017 maonesho haya yalisimamishwa. Maonyesho haya yalikuwa muhimu kwa kuwa yalikuwa yanaitangaza Tanzania na kuonesha Tanzania ina madini yenye ubora wa hali ya juu ya kuweza kuitangaza Tanzania katika soko la kimataifa na kuingiza Tanzania katika ushindani wa soko la kimataifa. Je, ni lini Serikali itarudisha maonesho haya ya madini ya Arusha Gem Fair? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kuwapigania wachimbaji wa madini wa Arusha, anafanya kazi kubwa sana na kwa kweli tunampongeza kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kusema kwamba baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini tuliyoifanya hapa Bungeni, ile Sheria ya Madini ya mwaka 2010, tukafanya mabadiliko mwaka 2017 ni kwamba tuliweza kuzuia utoaji wa madini ghafi (raw minerals) ni kwamba mpaka yaongezewe thamani ndiyo tuweze kuyatoa. Vilevile, ni kwamba maonesho haya mara nyingi yalikuwa yanafanyika pamoja na uuzaji wa madini hayo, kwa hiyo, wale organizer wa maonesho haya walikuwa wanatuomba kwamba kipindi cha maonesho haya waweze ku-export au kuweza kutoa nje madini ghafi na sheria ilikuwa inazuia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa hivi tumekwenda vizuri, nadhani kufikia mwaka huu mwezi Julai mpaka wa Septemba tutakuwa tumefika sasa mahala pazuri tumekwisha kuelewana na hawa organizer wa haya maonesho na uzuri wa maonesho haya huwa yana kalenda ya kidunia.

Kwa hiyo, kalenda yetu ya mwaka ambao ukifika kwa maana ya Tanzania kupata zamu ya kuweza ku-organize maonesho haya, basi tunaweza tukaanza kukaribisha wawekezaji, waoneshaji na waoneshaji wakatoka katika maeneo/nchi zingine lakini vilevile kuweza kuonesha madini yetu ya Tanzanite ambayo kwa kweli sasa hivi wadau wengi wamekubali kuyaongezea thamani kwa maana ya kukata na sasa wapo tayari kwa ajili ya kuweza kupeleka kwenye maonesho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tupo tayari sasa kuyaridisha maonesho hayo wakati wowote ratiba ikishakuwa sawasawa, basi tutaweza kuyarudisha maonesho hayo na wananchi waweze kushiriki, ahsante sana.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali katika sekta hii ya madini kuhakikisha kwamba tunapata faida. Je, Serikali sasa iko tayari kukaa kwa Wizara nne; Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuweza kutoa kikwazo cha dola 300 za viza ya biashara kwa wafanyabiashara wa Congo ambayo imekuwa ni kikwazo kikubwa cha kusababisha nchi yetu kukosa dhahabu licha ya kufungua biashara ya dhahabu hapa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika,ni kwamba sisi tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na kweli hata sisi tunaona kwamba ni vizuri sasa kutoa viza kwa watu wanaotoka Congo. Vilevile tumeanzisha masoko katika mikoa yote ikiwa ni pamoja na mikoa ambayo ipo mipakani mwa nchi yetu pamoja na Kigoma ambapo ni karibu na Congo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa tulipo sasa hivi ni kwamba tumetoa zile tozo ambazo zilikuwa zinakuwa charged katika Wizara yetu ya Madini kwamba mtu anapoingiza madini ni lazima alipe kiasi fulani, tumekwishakutoa hiyo ni moja ya hatua lakini vilevile tupo tayari kushirikiana na hizi Wizara kama alivyosema

Mheshimiwa Mbunge alivyotoa ushauri, basi tuangalie namna ya kuweza kurahisisha biashara kufanyika katika masoko haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi unaweza ukaleta madini katika masoko yetu na hatuulizi madini unayatoa wapi, wewe leta katika masoko yetu tutaangalia pale, tuta-charge sisi mrabaha wetu pamoja na clearance fee, utafanya biashara, wanunuzi utawakuta pale utaweza kufanya biashara yako vizuri na tumeweka mazingira mazuri.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika,asante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa mujibu wa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba leseni ya utafiti ya hao watu wa Mabangu imeisha muda wake na imerudishwa Serikalini. Sasa je, Serikali ipo tayari kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Mbogwe ili kusudi na wao waweze kufaidika na madini yanayopatikana katika eneo lao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, endapo Serikali itakuwa tayari kugawa hayo maeneo, je, Serikali itakuwa tayari pia kuwapatia vifaa na utaalam ili wananchi waweze kuchimba kwa kufuata kanuni na taratibu za uchimbaji wa kisasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunavyoongea sasa hivi ni kwamba tayari kuna wachimbaji wadogo wapo katika leseni hiyo wanachimba na Mheshimiwa Mbunge hilo unalifahamu. Lakini tu nipende kusema kwamba kampuni hii iliomba leseni ya kufanya utafiti na wamefanya utafiti na kawaida mtu ukimpa leseni ya kufanya utafiti, hatua inayofuata kama ameridhika na utafiti huo na akaona kwamba anaweza akafanya biashara au kwa maana anaweza akachimba kibiashara, katika hali ya kawaida ni kwamba akishafanya upembuzi yakinifu, anaomba tunampatia leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu leseni hiyo imesharudishwa Serikalini na tunadhani kwamba huyu mwekezaji atakuja na maombi yake sasa baada ya kufanya upembuzi yakinifu, hatuoni haja ya kumnyima leseni hiyo kwa sababu tayari ameshaingia gharama ya kufanya upembuzi yakinifu. Lakini kama atasema kwamba hakuna biashara, haiwezekani akachimba kibiashara, basi sisi Serikali hatusiti na tumekwishakuanza kuwapatia wachimbaji wadogo maeneo mbalimbali ili waweze kuendesha shughuli zao na hilo tunalifanya kwa kweli na wachimbaji wengi wamepata maeneo mengi ya kuchimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, Mbunge ametaka kujua kama Serikali tukishawapa hilo eneo basi na vifaa tutawapa? Mimi nipende tu kusema kwamba Wizara yetu hapo awali ilikuwa inatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo ili waweze kununua vifaa, kufanya tafiti, lakini vilevile katika ruzuku hiyo tuliona kabisa kulikuwa kuna ubadhilifu unafanyika, watu walikuwa wakipewa fedha hizo wanazitumia katika matumizi mengine, tumesitisha na sasa hivi tunaangalia namna bora ya kuwasaidia wachimbaji wadogo, lakini ikiwa ni pamoja na kuwafanyia tafiti ndogo ndogo kwa maana ya kufanya drilling kwenye maeneo ambayo yanaashiria uwepo wa dhahabu. Tumeshanunua rig machine kupitia STAMICO imekwisha kuanza kutoa huduma hiyo kwa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kama ana wachimbaji wadogo ambao wanataka kupata huduma ya hiyo rig machine basi aje STAMICO anaweza akapata huduma hiyo.