Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Suleiman Masoud Nchambi (4 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wabheja sana. Awali ya yote nakushukuru. Vile vile nakupongeza kama walivyosema, akinamama nanyi mnataka haki sawa, lakini waliimba hawa waimbaji, hata wakati wa kutembea, akinamama mbele, akinababa nyuma. Kwa hiyo, bado tunawaenzi. Akinamama wa Tanzania endeleeni kufarijika kwamba Serikali inayosimamiwa na Chama cha Mapinduzi...
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, usiyashangae haya, ukienda kusoma Biblia Luka 6:38 utayakuta. (Kicheko/Makofi)
Maana kile ambacho wanakipanda hapa, ndicho ambacho watakivuna. Niliwaambia shemeji zangu wa Kigoma, namshukuru sana Mheshimiwa Zitto, huwa anatumia knowledge yake kuleta mambo ambayo yana mashiko kwa Watanzania; lakini shemeji zangu wengine wote hawajarudi humu ndani. (Makofi)
Niliwaambia Luka 6:38, kile mnachokipanda humu ndani, ndicho mtakuja kukivuna 2015 Oktoba. Kwa hiyo, wamekivuna na hawa wengine, wala usiwe na mashaka, maana katika safari ya mamba na kenge na mijusi wamo, wala usitie mashaka juu ya hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndicho ambacho kimetokea hapa kabla ya kuanza michango yangu kwa Mheshimiwa Lwakatare. Amemaliza dakika zake zote, hakusemea Manispaa ya Bukoba. Mimi ni Mbunge wa Jimbo Kishapu, nimetokana na watu shapu, Wilaya yangu ni Shapu, mimi mwenyewe ni shapu. Naleta mambo yangu humu kwa ushapu kwa ajili ya wananchi wa Jimbo…
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Shapu! (Makofi)
Kwa hiyo, Wabunge wengine humu wanasimama wanapoteza muda wao wanaongelea mambo ambayo hayahusu. Mheshimiwa Lwakatare amesema sana, lakini hajatetea wananchi wake. (Kelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nataka niwaeleze ndugu zangu Wabunge kidogo, kazi ambayo huanza juu kwenda chini, ni kazi ya kuchimba kaburi peke yake. Kaburi huanza kuchimbwa juu kwenda chini. Kazi nyingine zote huanzia chini kwenda juu. Kwa hiyo, hata sisi hapa, kama Bunge ambalo Watanzania hawawezi kuenea humu ndani, wametutuma Wawakilishi wachache, tuje tuwasemee kuhusu mambo yanayohusu jamii na Taifa letu. Kwa hiyo, kazi tutakayoifanya hapa, ni ile wanayosema Wazungu a journey of thousand miles starts with a single step to a thousand steps. Tunaanza na hatua moja, mbili mpaka tunafika 1000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wanaobeza, lakini Mungu ameleta Mitume wengi sana, hakuleta Mtume au Nabii mmoja. Lazima, we still keep on learning through history. Mungu hakuleta Mtume mmoja, alileta mitume wengi na alikuwa na makusudi maalum. Nasi hapa Mabunge yatapita mengi, Wabunge watakwenda wengi, kwa sababu kazi za kibinadamu zinaendelea siku hadi siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, nataka niwaambie, maneno machache sana; mpango huu umeletwa humu Bungeni, kwa mujibu wa kanuni ya Kibunge ya kwetu ya 94; lakini yapo mambo yaliyosemwa hapa ni kwamba siyo sahihi jambo hili kuletwa kwa wakati huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwakumbushe, ukisoma kitabu chetu cha Sheria za Bajeti, 2015, Kifungu cha 20 naomba ninukuu: “The Minister responsible for planning commission shall prepare and lay before the National Assembly and the National Development Plan which shall be the basis for the preparation of the National Budget.” Kifungu hiki kinapelekea maandalizi katika sheria yetu ya 2015 ya kitabu chetu cha bajeti Kifungu na 26.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tuwekane sawa. Hapa hatukuja kutekeleza jambo, tumekuja kuandaa Mpango. Waheshimiwa Wabunge tusimamame hapa kwa Utaifa wetu, tusimame hapa kwa vitabu vyetu vya kikanuni, sheria na kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu. Hata dini, ninaposimama mimi Muislam nasoma the Holy Quran nina-refer; Wakristo wanasoma Biblia na kwa sisi wengine tunaamini Taurati na Injili. Hivi vitabu tuvipitie sana. Tuko kwa ajili ya Watanzania walio wengi nje, tuko kwa ajili ya Utaifa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu Na. 26, ni lazima tuliweke jambo hili sawa ili Watanzania walioko nje wasione tu tunawaburuza, tunakwenda hatua kwa hatua. Naomba ninukuu:
“The National Assembly shall on or before 30th June each year and after debating the National Assembly, approve the Annually National Budget of the Government for the next financial year, by the way of open vote and call of the name of each Member of Parliament.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge watashirikishwa mmoja baada ya mwingine katika Mpango. Hapa sisi tunatoa mapendekezo ya mpango. Nawaomba sana, wote tunatoka katika Majimbo hata wenzetu wa Viti Maalum, Majimbo yanaunganishwa, yanaletwa. Ni imani yangu, Chama changu, Chama cha CHADEMA na wengine, wanawaleta Viti Maalum pia ambao wanajua watasaidia wananchi wote na hasa akina mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nielekeze sasa michango yangu kwenye maeneo, kama ilivyo kawaida ya Mbunge sharp. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote haiwezi kupiga hatua, ni lazima iwe na mipango ya kiuchumi, tena mipango na mikakati mathubuti. Katika maeneo ya mipango ambayo itatekeleza uchumi, maana suala lote hapa, wanasema Mheshimiwa Magufuli ameahidi wanafunzi bure; tunataka watu watibiwe bure, fedha zitatoka wapi?
Mheshimiwa Magufuli amekuwa mstari wa mbele kutaka kuibadilisha Tanzania hii iende katika uchumi wa kati. Mambo yafuatayo ningeomba sana Waheshiwa Wabunge tuyasemee sana. Jambo la kwanza ambalo Mungu ametujalia Watanzania ni rasilimali watu. Tuna rasilimali watu, tena Watanzania wenye nguvu na sifa ya kuchapa kazi.
Jambo la pili ambalo nikikumbuka sana Mheshimiwa Muhongo alikuwa akipigwa madongo sana siku za nyuma; leo sote mashahidi, Wabunge tunapishana Ofisi za REA na maeneo mengine kuomba umeme na mambo mengine ambayo yatasaidia kututoa sisi katika uchumi wetu huu wa kimasikini kutupeleka katika uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ulinzi ni suala muhimu sana. Lazima mtu yeyote anapotaka kuwekeza awe ana uhakika, yuko salama, ana imani anapowekeza mambo yake yatakwenda vizuri. Ujenzi wa barabara zetu; wakulima wetu wanapolima wanasafirishaje? Katika gharama zipi? Ujenzi wa reli; eneo hili ni muhimu sana ndugu zangu naomba niwaambie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako mimi nimekuwa dereva wa bus; kwanza nimekuwa mpiga debe stand, nimebeba abiria mgongoni, nimekuwa dereva wa bus, nimekuwa dereva wa malori; najua gharama za kusafirisha mizigo; na sasa ni mwekezaji, tena mfanyabiashara mzuri tu, wala sina matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kuendelea katika nchi yetu, lazima tuwekeze katika miundombinu. Moja, reli itatusaidia sana. Lazima reli yetu iboreshwe katika level ya standard gauge, wananchi wetu wasafiri on and off. Unaweza ukatoka Kigoma kwa shemeji zangu kule amagambo bukebuke wakaja Dar es Salaam, asubuhi akanunua bidhaa akarudi. Mambo ni meeza, sivyo shemeji zangu, Mheshimiwa Zitto! Mambo yamekwenda! Wale wa Mwanza unaweza ukatoka jioni Mwanza ukaenda Dar es Salaam na ukarudi kesho, bila kulala guest. Ile fedha itasaidia kusomesha watoto na kuanzisha ujenzi wa nyumba zako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba katika mipango yetu, Waheshimiwa Wabunge tuungane, tuhakikishe tunapata reli ili kupunguza gharama za maisha ya Watanzania; lakini tusafirishe bidhaa zetu kwa urahisi. Atakayelima matunda leo; nenda South Africa ukaangalie reli walivyojenga; nenda Uingereza uone mambo yalivyokwenda. Mwalimu wangu hapa Mheshimiwa Ndassa, anajua. Mimi leo…
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa!
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI Nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti, wabheja wabheja, naunga mkono hoja. Kwa pamoja naomba… (Makofi)
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nikushukuru sana na nikupongeze kwa moyo wako wa kijasiri wakati kina mama wenzako walipokuwa wakijaribu kukuzomea. Nikutie moyo kwani hata Yesu Kristo wakati akiitangaza injili alipokuwa akipita katika mitaa wengi walimbeza, wengi walimuuliza eti wewe ni mwana wa Mungu, eti wewe ni mtakatifu na yeye aliwajibu ninyi mwasema. (Makofi)
Kwa hiyo, hicho wanachokisema wao ni wao wanakisema. Mimi nikutie moyo mama yangu umeanza vizuri, ongeza kasi na sisi Wabunge shapu tutaendelea kukunoa uwe shapu, mambo yako yaende kwa ushapu na Bunge hili lifanye kazi ya kutekeleza mipango mizuri ambayo wananchi wameingia mkataba na Chama cha Mapinduzi wakati wa uchaguzi na Chama cha Mapinduzi kimekabidhi Ilani ambayo inatekelezwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maandiko matakatifu yanasema na wala msifanane na hao kwa kuwa baba yenu anayajua mahitaji yenu kabla ninyi hamjamuomba. Kwa hiyo, sisi tunayo imani Watanzania lipo jambo waliliomba na kupitia Serikali ya Chama cha Mapinduzi Mungu amekabidhi usukani wakiwa na imani wakati wanaomba kama maandiko yanavyosema, niombeni na mkiamini mtapata, Bwana Asifiwe.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa niwape hesabu rahisi sana Waheshimiwa Wabunge. Mbunge mmoja wa Upinzani amesifu sana hotuba yao ya Upinzani, kitabu hiki kilichowasilishwa na kambi ya wenzetu kina kurasa 28 wakati kitabu cha Mheshimiwa Mwijage kina kurasa 217. Katika kurasa 28 zilizowasilishwa na Kambi ya Upinzani, ukurasa wa kwanza, mwasilishaji amewashukuru wapiga kura wake, ukurasa wa pili ametukana, ukurasa wa nne ametoa lawama tu, ukurasa wa nane imetukana na kukisema Chama cha Mapinduzi, ukurasa wa 27 na 28 ni kama viambatanisho. Kwa hiyo, ni dhahiri katika kurasa hizi sita zimebaki 22 ambazo asilimia 70 ya mistari iliyopo katika kitabu hiki kinachowasilishwa na wenzetu wa upinzani ni lawama, kejeli, matusi na mengineyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukipiga hesabu rahisi kurasa 217 ukigawanya kwa kurasa 22 ni kwamba wapinzani hawayajui matatizo ya Watanzania na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Waziri mchapakazi, hodari Mheshimiwa Mwijage amekwenda mara kumi zaidi ya matatizo wao wanavyoyajua, hiyo ni hesabu rahisi.
Kwa hiyo, ndugu zangu Wabunge mimi niwatie moyo kazi wanayoifanya wenzetu kwa sisi wafugaji tunapokwenda na ng‟ombe zetu kwenye mabwawa ama malambo, huwa wanaangalia saa hiyo sauti ya vyura ipo wapi ili wajue maji pale ndiyo yana kina kirefu wanakwenda wanakunywa. Kwa hiyo, wao wanapiga kelele kama vyura sisi tunanywesha ng‟ombe zetu, Watanzania wanapata maziwa, wanapata nyama ambazo sasa ndizo shughuli za maendeleo na matatizo na kero zao. Hawa ndiyo kazi iliyowaleta Bungeni wala msiwalaumu, wataendelea kupiga kelele kama vyura na ninyi Mawaziri chapeni kazi sisi Wabunge tutawasaidia na Wabunge wa CCM tufanye kazi ya kuishauri na kuikosoa na kuielekeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Magufuli amekuja na mkakati wa mabadiliko. Nilikuwa napitapita mtaani naongea na wenzangu kule wanasema kazi anayoifanya Mheshimiwa Magufuli ndiyo haswa ilikuwa kazi yetu sisi UKAWA, tena wengine wenzangu wa Zanzibar maana kuna Wabunge wenzangu kule Zanzibar wanakalia Dole, wengine wanakalia Mkanyageni, wengine wapo Mwembemchomeke, ni rafiki zangu huwa nakwenda kuwatembelea wakati mwingine katika maeneo yao hayo niliyoyataja wana Kiswahili ambacho kinazingatia misingi ya neno waliloliongea wanasema haswa anachokifanya Mheshimiwa Magufuli ndiyo ilikuwa hoja ya UKAWA kutekeleza mambo anayoyafanya yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka niwaambie ndugu zangu wakati fulani niliwahi kumwambia Waziri fulani wa CCM humu ndani nisingependa kumtaja, muda mwingine mtu akisoma sana akafika mwisho huwa nahisi mimi akili inarudi reverse. Sasa inategemea, inarudi reverse pengine dhamira yake ama ubongo wake umepata frustration fulani maana shetani huwa haonekani, unaona matendo unasema huyu matendo yake yanafanana na shetani. Maneno yake na matamshi yake yanafanana na shetani lakini mimi sijawahi kumuona na sina reference ya kitabu chochote cha Mungu ambacho kiliwahi kumuona shetani kupitia binadamu hapa duniani, lakini matendo ya mtu ndio yanamfanya aonekane ni mtakatifu ama shetani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu zipo lugha zinatumika ambazo Wabunge hao hao wanaotumia lugha hizo wanakuja na madai ya wao kuheshimika katika Taifa hili na Bunge hili, haiwezekani! Waziri anayechukua dhamana ya Wizara katika Wizara yake leo anaitwa muhuni, tapeli na maneno mengine.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Wacha muda uishe lakini nataka niwaeleze ukweli, kwa sababu kazi zenu ninyi ndizo hizo mnazozifanya. Lugha hizi hazipendezi sana…
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Nitachangia kwa maandishi msiwe na haraka, mbona sindano zikiwa zinawaingia upande wenu mnapiga kelele, quinine huwasha baadaye masikioni, tulieni kwanza tuwape vidonge vyenu maana mmekuja kufanya kazi ambayo mnaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi hawa kelele zao wala hazinipi shida mimi ni Mbunge shapu wala sina matatizo na wao.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo tatizo la baadhi ya majimbo kuruhusu watu ambao hawakuwa na sifa na wala hawakujiandaa kuja kutetea wananchi wao kuingia ndani ya nyumba hii lakini angekuwa amejiandaa, amejipanga na anajua wajibu wake wa kibunge ndani ya jumba hili takatifu asingekuwa anaropoka kama mwendawazimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie Watanzania wanaona na wanasikia. Nakuapia Mungu niliwahi kuwaambia wenzenu, shemeji zangu wa Kigoma akina Kafulila, niliwaambia kasomeni Luka 6:38, mtalipwa kwa kile mnachokifanya ndani ya jumba hili leo wako wapi? Akina Machali, Kafulila na Mkosamali wako wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, huyu anayeropoka maneno haya wapiga kura wake watamuona, watamsikia, mwaka 2020 tutaagana naye kwa sababu kazi aliyoifanya ndiyo hiyo ya kuzomea na kutukana, hatarudi humu wala asiwape shida yoyote. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwaeleza wenzangu na kuwakumbusha misingi na wajibu wao ndani ya Bunge nieleze machache.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko tatizo kubwa juu ya wakulima wetu, wakulima wetu wanapata tabu sana. Nikuombe Mheshimiwa Mwijage katika maeneo machache kulingana na muda na mengine nitachangia kwa maandishi. Mkitaka wakulima wa pamba waendelee ni lazima Serikali ijiandae kudhibiti bidhaa zote zinazotokana na mazao ya pamba zinazoingia nchini. Wako Wabunge humu walipiga kampeni tukatoa ushuru wa mazao mengi ya pamba kuingia katika Taifa hili tumewakandamiza Wasukuma wenzangu. Nataka nikuhakikishie zao la pamba nenda ka-review ili viwanda viwepo kutokana na zao la pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ubarikiwe sana.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu wa Spika, wabheja sana. Awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kuipongeza sana nchi yetu kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya na hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri. Jeshi hili zuri limetokana na matunda yetu sisi Watanzania. Ni mti mzuri umezaa Amiri Jeshi mzuri, umezaa Mkuu wa Majeshi mzuri na Wanajeshi wazuri, watiifu, hodari na wavumilivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme jambo moja la msingi sana. Unaweza ukawa na sikio halisikii, unaweza ukawa na macho, hayaoni na unaweza ukawa na mikono, miguu, viungo vya mwili wako usijue neema hiyo aliyokupa Mungu ni neema ya aina gani. Maana katika Quran tunasema, fa‟amma bini‟imati rabbika fahaddith (na tuzisimulie neema ambazo ametupa Mwenyezi Mungu). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo Wabunge hapa leo nimeshangazwa sana, sisi wengine kwa bahati nzuri treni ya siasa hatukuidandia tumeanza chipukizi darasa la tatu lakini nashangazwa sana na Bunge hili, Mbunge anasimama pengine hajui aelimishwe, this is not vocational training centre, hili ni Bunge. Watu wamekutuma hapa siyo kuja kufundishwa. Wamekutuma kuja kufanya kazi wakiamini wewe ni mwakilishi wao, unaomba kufundishwa Bungeni, haya ni mambo ya ajabu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka hata Mungu mbinguni ana jeshi lake, malaika na vimetaja vitabu vya Mungu. Jeshi letu naomba sana Mheshimiwa Mwamunyange liheshimike. Nilitegemea sana Wabunge wote tumuunge mkono Rais, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuvaa combat ya jeshi na kuanza kukimbia. Nchi zote duniani zinakimbia sisi hapa Wabunge, Bunge lililopita na Mabunge yaliyopita tulikuwa tunalalamika tunatambaa leo Magufuli anaikimbiza nchi watu wamekazana kuleta mambo ya u-baby hapa hatutakubali. Watu wamekazana kuleta mzaha hatutakubali. Watu wanataka kuleta kejeli na jeshi letu hatutakubali. Sisi wengine bado vijana, tunahitaji kuona matunda ya Taifa letu na wajukuu wetu wakute amani ya Taifa hili, jeshi halina siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Mwamunyange kwamba yamesemwa mengi sana lakini mimi nataka kumwambia yeye, Maafisa na Wanajeshi haya yaacheni humu humu, tuchukue mazuri yaliyosemwa. Jeshi sehemu yoyote duniani linalo heshima ya juu sana. Wamesema baadhi ya Wabunge hapa, hawa wote wanaopiga kelele humu wakisikia risasi moja tu wanabanana mlangoni…
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Hawatakwenda ulipotokea mlipuko wakaangalie lakini jeshi linakimbilia…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nchambi naomba ukae.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Wabheja sana.
NAIBU SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Msigwa...
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri sana huyu ni kama Mchungaji mwenzangu kwa sababu na mimi Vitabu vya Mungu navijua, namheshimu sana. Naomba nisipokee taarifa yake niendelee kutiririka na mtiririko ambao naona una maslahi kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa yamesemwa mambo, silaha feki zilikuja, haya ni mambo very serious. Kama mtu anaweza akajua taarifa za ndani za jeshi, unayo Kamati ya Maadili imuite Mbunge aliyetoa kauli hiyo kwa sababu tunaporopoka hapa ziko nchi jirani zinajua…
MHE. HALIMA J. MDEE: Kuhusu utaratibu.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Kumbe jeshi letu linazo silaha feki, linaweza likafanya manunuzi ya silaha feki jambo ambalo litahatarisha…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nchambi naomba ukae, kuhusu utaratibu....
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, wabheja sana lakini naomba muda wangu uulinde, dakika sita zimepotea kwa taarifa.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Halima Mdee wakati nikitoa taarifa alisema mimi siyo size yake ni kweli, wala mimi sikatai kwa sababu amemchukua dada yetu amekwenda naye kule ametushinda. Mimi wala siwezi kuona kwamba yeye hajashinda ni kweli ameshinda na mimi upande wao sijachukua mtu wa aina yangu nikamleta huku. Kwa hiyo, yeye ni mshindi, namkubalia kabisa, sawasawa aendelee na dada yetu hatuna shida.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nirejee katika hoja. Ninachotaka kusema, Ndugu zangu Wanajeshi, Maafisa wa Jeshi na Mkuu wa Majeshi, Wabunge ndiyo wenye uwezo wa kuongeza fedha ama kupunguza. Wengi wamekuwa hapa wakilalamika kwamba haiwezekani jeshi likose fedha, Bunge hili Afande Mwamunyange ndilo lenye mamlaka ya kuielekeza na kuishauri Serikali itoe fedha. Sasa hawa wenzetu wanaoendelea kubeza na kudharau jeshi, jambo la silaha ambalo lilitolewa taarifa nimesema ni serious sana, naomba sana suala hili lichukuliwe na ofisi yako kuhusiana na Mheshimiwa Kubenea aliyetoa taarifa hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili hatuwezi kukubali kuliingiza jeshi letu katika kashfa kwamba mpaka silaha zimekuja, zimeonekana feki, siri za Kamati ya Ulinzi na Usalama awe nazo mtu mmoja hili ni jambo la hatari sana kwa jeshi letu. Ni jambo ambalo linaweza likahatarisha hata usalama. Sehemu yoyote duniani jeshi ndicho chombo makini kinacholinda Taifa lolote. Tunao uhuru wa aina tatu. Tunao uhuru wa bendera, wa mawazo na kiuchumi lakini yote haya ni bure kama hatuna vyombo vinavyoweza kusimamia uhuru wa mawazo yetu, uhuru wa kiuchumi na hata bendera yetu kusimama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unyenyekevu mkubwa sana niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tusiweke kejeli kwa jeshi letu. Jeshi letu linafanya kazi nzuri, tusilete jambo lolote linaloashiria kulibeza jeshi letu. Jeshi letu linafanya kazi nzuri. Tena niwaombe sana maana katika Maandiko Matakatifu ukienda katika Mhubiri 9:10 inasema, lolote unaloweza kulifanya lifanye kwa mkono wako sasa maana hakuna hekima, maarifa, busara wala shauri unaloweza kulifanya huko kuzimu uendako. Waheshimiwa Wabunge, mikono yetu ifanye mambo sasa wakati sisi ni Waheshimiwa Wabunge. Tulitengeneze jeshi letu, tulitie moyo, tulisaidie lakini tusiendelee kuwa tunazomea huku tunapuliza kwa utaratibu wa panya. Mimi nishukuru sana kwa sababu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nchambi muda wako umekwisha.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, wabheja sana. Naunga mkono hoja na Mungu awabariki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti nipo kwenye orodha ya kuchangia, samahani unajua, kwanza kabisa nataka niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge wala msishangae, wajinga wameendelea kuwepo ili wafanye wenye akili waendelee. (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, baada ya kusema kauli hiyo ili kumrekebisha mwenzangu naomba sasa nichangie kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii inayosemwa haifuati utaratibu, sheria ama Katiba, jambo hili ni la kushangaza sana. Yapo mambo ya msingi ambayo Rais wa Awamu Tano ameyaainisha kama dira katika Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja mwaka huu na mwaka jana na awamu hii ya Rais John Pombe Magufuli ni awamu ya kazi. Mimi nashindwa kuelewa, mambo mengine ni ya kushangaza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mzee wao, mshauri wao wa chama chao amekwenda Ikulu kumpongeza Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Kama Mzee Lowassa amekwenda Ikulu kumpongeza John Pombe Joseph Magufuli, jambo la kwanza ana ainisha bayana kuwa Katiba ya nchi hii inafuatwa ndiyo maana anampongeza, lakini ana hakika sheria za nchi hii zinafuatwa ndiyo maana anampongeza. Utekelezaji wa Ilani, kwa maana ya kuwasaidia wanyonge na maskini wa Taifa hili kazi hiyo inafanyika. (Makofi)

Msheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya hata kanga yapo na mimi niwashukuru sana akina mama wana hekima na busara, maneno haya huwa wanayavaa katika kanga zao tena nyuma kwa chini kabisa, kwa hiyo ndiyo maneno anayoleta mheshimiwa hapa wala tusishangae.

Mheshimiwa Mwenyekiti…

T A A R I F A . . .
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba niendelee na michango yangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taifa hili lilipokuwa limefika na kufikishwa na watu wachache waliokuwa wakishawishi miradi mizuri na mikubwa, mfano mradi wa reli, kwa kipindi kirefu Serikali ya Chama cha Mapinduzi, ilitaka kutekeleza miradi mikubwa lakini watu wachache walikuwa wakishawishi watu juu ya mambo madogo sana, awamu hii wamefeli. Reli inajengwa, waliobomolewa ni watu ambao walikuwa wanakaa katika maeneo inayotakiwa kupita reli kisheria.

Leo hii hawa hawa baada ya muda watakuja kuwaambia wananchi 2019/2020 kwamba wao ndio waliopiga kelele standard gauge imejengwa hao ni wadandiaji wa treni, na wanaidandia treni kwa mbele wala tusiwe na mashaka nao safari hawatafika wanakokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo na mimi nilikuwa na michango michache sana.

Jambo la kwanza, naomba tutumie fursa, dada yetu Leah amesema ya maduhuli, Halmashauri zetu hizi zina minada mizuri kule katika Halmashauri, kwa mfano, Halmashauri yangu ya Kishapu, mimi ninaomba sana Mheshimiwa Waziri Jafo nikushauri ndugu yangu, tuna mpango mzuri sana Kishapu wa kutanua ile minada yetu na kuifanya minada ya kimataifa, tunakutana na kikwazo cha minada iliyoko sasa, iko chini ya Wizara ya Mifugo, tukienda kuomba minada ile tunaambiwa kuna madeni machache yanalipwa. Kishapu tuko tayari kulipia deni letu kama wanadaiwa ili tuachiwe ile minada na sisi tutanue own source zetu za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri, hoja hii ni yenu TAMISEMI ongeeni na Wizara ya Mifungo mtupatie mnada wa Muhunze na minada mingine. Sisi watu sharp tuitanue ile miradi iwe sharp na iweze kuingizia mapato makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefanya kazi kubwa sana na kwa kweli katika dini yetu sisi waislamu tunasema Faa-mma biniimati rabbika fahaddith na tuzisimulie neema za Mungu zilizoko juu ya ardhi. Neema iliyoko Tanzania kwa Serikali ya John Pombe Joseph Magufuli sio ndogo. Serikali hii imeleta miradi ya ndege zetu wenyewe tunajenga reli ya kisasa, tunapanua bandari, tunajenga barabara, tumeleta Makao Makuu Dodoma ili Watanzania wote wanapohitaji huduma za Serikali waweze ku-connect… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)