Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. George Boniface Simbachawene (19 total)

MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:-
Kifungu cha 3 cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, na Kifungu cha 1(26) cha Kanuni za Kudumu za mwaka 2009 vinatoa tafsiri ya neno mwajiri kuwa ni mtu au taasisi ambayo mtumishi wa umma anaingia naye mkataba wa ajira na kumlipa mshahara.
Je, kwa kuzingatia tafsiri hiyo, mwalimu ambaye ni mtumishi wa umma, mwajiri wake ni nani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kujibu swali la Mheshimiwa Mwalimu Kasuku Samson Bilago Mbunge wa Jimbo la Buyungu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mwajiri wa watumishi wote wa umma wakiwemo walimu ni Serikali ambayo ndiyo inakusanya mapato na kulipa mishahara ya watumishi wake. Hata hivyo, Serikali imekasimu madaraka kwa mamlaka mbali mbali kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 6(1) cha sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kutungwa kwa sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu, sheria namba 25 ya mwaka 2015, Idara ya Utumishi wa Walimu ndiyo ilikuwa Mamlaka ya Ajira na nidhamu kwa walimu wote walio kwenye Utumishi wa Umma. Baada ya kutungwa kwa sheria hiyo ya Tume ya Utumishi wa Walimu namba 25 ya mwaka 2015, iliyoanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu.
Tume hii sasa ya Watumishi wa Walimu pamoja na majukumu mengine itakuwa Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu wa shule za msingi na sekondari walioajiriwa na Serikali.
WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika samahani.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza jukumu la kuwa mwajiri, Serikali huingia Mikataba ya Ajira na kulipa mishahara ya Walimu kupitia mamlaka za Serikali za Mitaa wanakofanyia kazi.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Malengo ya TASAF III ni kunusuru kaya maskini hapa nchini na kutengeneza miundombinu kutokana na mahitaji na uibuaji wa kaya maskini unaofanywa na wananchi kwenye mikutano ya hadhara:-
(a) Je, ni vigezo gani vinatumika kuondoa kaya zilizopendekezwa kwenye mradi na kubakiza kaya chache wakati malengo ya kaya zinazohitajika, wananchi wameshapewa tangu awali?
(b) Katika Wilaya ya Kaliua, vijiji vilivyoingia kwenye miradi ni 54 tu, wakati katika vijiji vyote kuna kaya maskini sana. Je, ni lini Serikali itapeleka Mpango wa TASAF III kwenye vijiji vilivyobakia kwenye Wilaya hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kujibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Magdalena Hamisi Sakaya, Mbunge wa Jimbo la Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utambuzi wa Kaya za walengwa unapitia mchakato wenye hatua zifuatazo:-
Hatua ya kwanza ni Mpango wa kunusuru kaya maskini kutambulishwa kijijini na wataalam wanaotoka katika Halmashauri husika kwa kusimamiwa na Uongozi wa kijiji na kisha kuweka vigezo vya kaya maskini.
Pili, wakusanya taarifa wanachaguliwa kutoka miongoni mwa vijana wanaoishi kijijini hapo na kupitia nyumba kwa nyumba ili kuorodhesha kaya ambazo zinakidhi vigezo vilivyoainishwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Tatu, orodha ya kaya zilizoorodheshwa na timu ya wakusanya taarifa kusomwa mbele ya Mkutano wa Kijiji na baada ya hapo jamii hujadili majina yaliyoorodheshwa na kufikia muafaka. Kaya ambazo jamii inaona hazistahili, huondolewa kwenye orodha na Kaya ambazo hazikuwa zimeorodheshwa, huingizwa kwenye orodha.
Nne, kutokana na orodha hiyo ambayo imeandaliwa, kaya hizo hujaziwa dodoso maalum linaloandaliwa na TASAF Makao Makuu kwa lengo la kupata taarifa zaidi za kaya.
Tano, dodoso hilo lililojazwa huchambuliwa kupitia mfumo maalum wa kompyuta ili kupata kaya maskini sana ambazo zinakidhi vigezo kulingana na taratibu za mpango huo.
Mwisho, baadhi ya kaya ambazo hazifikii kiwango cha alama zinazotakiwa huondolewa katika orodha.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya kaya maskini zilizotambuliwa na kupitishwa kwenye Mkutano wa Kijiji mara nyingine zimejikuta zimetolewa wakati wa kuchambua taarifa kutokana na taarifa ambazo mwanakaya aliyedodoswa anakuwa amezitoa wakati wa kujaziwa dodoso.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Kaliua, vijiji 54 vilivyoingizwa kwenye mpango huu wa TASAF ni asilimia 70 ya vijiji vyote ndani ya Wilaya hiyo. Hii ni kwa mujibu wa taratibu za mpango ambapo kila Halmashauri iliyomo ndani ya mpango, siyo Kaliua pekee, imeingiza wastani wa asilimia 70 tu ya vijiji au mitaa iliyomo ndani ya Halmashauri. Asilimia 30 ya vijiji na mitaa iliyosalia katika Halmashauri zote imepangwa kufikiwa katika mwaka 2016.
Serikali ilitoa maagizo hayo ili kuweza kufikia Vijiji, Mitaa, Shehia zote zilizobakia; na kwa upande wa Vijiji, Mitaa na Shehia zilizoanza ndizo zilizokuwa na hali mbaya zaidi. Kabla ya kuanza utekelezaji, takwimu za umasikini zilichukuliwa katika Vijiji, Mitaa na Shehia zote na kuorodheshwa kuanzia ambazo ni masikini sana mpaka zenye unafuu.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ndiyo pekee inayotoa huduma za Mkoa katika Mkoa wa Katavi, kwa kutumia bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda;
Je, ni lini Hospitali ya Mkoa itajengwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Suleiman Kakoso Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za awali za ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Katavi zimeshaanza ambapo eneo la ekari 243 limepatikana. Katika bajeti ya mwaka 2014/2015, Mkoa ulipokea shilingi milioni 750, kati ya hizo shilingi milioni 468 zilitumika kulipa fidia kwa wananchi walioachia maeneo yao kupisha ujenzi wa hospitali. Hadi sasa Mkoa upo katika hatua za mwisho kusaini mkataba na kampuni ya Y and P Consultant ikiwa ni hatua muhimu ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.4 ili kuendelea na ujenzi wa hospitali ya Mkoa katika Mkoa mpya wa Katavi.
MHE. HUSSEIN M. BASHE aliuliza:-
Wakati wa kampeni za uchaguzi Mheshimiwa Rais aliahidi ujenzi wa daraja la Nhobola na daraja la Butandula pamoja na barabara inayounganisha Kijiji hicho na Kijiji cha Mbogwe:-
Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa madaraja hayo pamoja na barabara zake?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimwia Hussein Mohamed Bashe, Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua za awali za ujenzi wa daraja la Nhobola na Butandula zimeshafanyika kufuatia kukamilia kwa upembuzi yakinifu (feasibility study), usanifu wa awali (preliminary design) na usanifu wa kina yaani (detailed design) ili kujua gharama za ujenzi wa madaraja yote mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa usanifu huo daraja la Nhobola linatarajiwa kugharimu shilingi milioni 589.8 ambazo zitahusisha ujenzi wa barabara yenye kilomita 5.1 kuunganisha kati ya Mbogwe na Nhobola. Ujenzi wa daraja la Butandula utagharimu shilingi milioni 245.57 na utahusisha matengenezo ya sehemu zote korofi zenye urefu wa kilomita 16.2 katika vipande vya barabara ya Ijanija-Butandula, Butandula-Izegwa, Mwangoye na Butandula-Uchama. Kwa kuwa hatua hiyo imekamilika, Halmashauri itaweka katika mpango wa bajeti yake ili kupata fedha hizo na kuanza ujenzi wa madaraja hayo yote mawili.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa/Vijiji wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu sana, hali wakiwa ndiyo viungo wa shughuli za maendeleo katika jamii:
(a) Je, ni lini Serikali itaaanza kuwalipa mshahara au posho Wenyeviti wa Mitaa au Vijiji?
(b) Je, kwa nini Madiwani wasiwe na ofisi zao kama ambavyo Wabunge hupewa ofisi zao?
(c) Je, ni lini Ofisi za Wenyeviti wa Mitaa au Vijiji zitajengwa ili kuepusha kuwa na ofisi majumbani kwako?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko Mbunge wa Tarime Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua wazi kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa katika kusimamia shughuli za maendeleo nchini. Serikali imeweka utaratibu wa kuwalipa posho Viongozi hao kila mwezi ambapo kwa Madiwani posho hiyo imeongezeka kutoka 120,000 mwaka 2010/2011 hadi shilingi 350,000 mwaka 2015 kwa mwezi. Kwa upande wa Wenyeviti wa Vijii na Mitaa posho hizo zinalipwa na Halmashauri kupitia asilimia 20 ya mapato ya ndani inayojumuisha ruzuku ya fidia ya vyanzo vilivyofutwa. Tunafahamu ziko changamoto kwa baadhi ya Halmashauri kutolipa posho hizo kutokana na makusanyo madogo. Mkakati uliowekwa na Serikali ni kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani kwa kubadili mifumo ya ukusanyaji pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kujenga uwezo wa kulipa posho hizo.
(b) Serikali inatambua umuhimu wa Madiwani kuwa na ofisi kutokana na majukumu makubwa waliyonayo. Ofisi ya Diwani inatakiwa kuwemo ndani ya ofisi ya Kata, ambayo ndani yake inajumuisha ukumbi wa mikutano ya Kamati ya Maendeleo ya Kata, Ofisi ya Mtendaji wa Kata na Ofisi za Maafisa Wataalam ngazi ya Kata. Ujenzi wa ofisi hizo unafanyika kupitia bajeti za Halmashauri kwa kuzingiatia vipaumbele vinavyopitishwa na Mabaraza ya Madiwani.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa ofisi za Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa unafanyika kupitia bajeti za kila Halmashauri. Hivyo kila Halmashauri inapaswa kuhakikisha inaweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizo kwa awamu.
MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y. MHE. DKT. ELLY M. MACHA) aliuliza:-
Kufuatia Mpango wa Serikali wa utoaji wa elimu bure kuanzia Elimu ya Msingi hadi Sekondari na kwamba, watu wenye Ulemavu wanakabiliwa na umasikini uliokithiri na hivyo kushindwa kumudu gharama za elimu:-
(a) Je, Serikali iko tayari kutoa elimu bure kwa wanafunzi wenye ulemavu kwa ngazi ya Kidato cha Tano na Sita?
(b) Je, Serikali inaweza kulihakikishia Bunge hili kwamba itaweka utaratibu mzuri wa usafiri na huduma nyingine muhimu za kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kupata elimu katika shule wanazopangiwa?
(c) Je, Serikali inaweza kulithibitishia Bunge hili kwamba wanafunzi wenye ulemavu wanaoingia Vyuo Vikuu watapewa kipaumbele katika kupata mikopo bila usumbufu wowote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Elly Marco Macha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia Mpango wa Serikali wa Utoaji Elimu Bure kuanzia Elimu ya Msingi hadi Sekondari na kwamba, watu wenye ulemavu wanakabiliwa na umasikini, Ofisi ya TAMISEMI imeandaa Mpango wa Utoaji wa Elimu ya Msingi bila malipo ili kutekeleza Sera ya Elimu ya Mwaka 2014. Sera hiyo inaelekeza kwamba wanafunzi wote wa madarasa ya Awali, Msingi na Kidato cha Kwanza hadi cha Nne wanatakiwa kusoma bila kulipia ada wala michango ya aina yoyote. Lengo ni kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Kitanzania mwenye umri wa kwenda shule, anapata fursa ya kupata elimu. Aidha, Sera ya Elimu Msingi Bila Malipo haijumuishi wanafunzi wa Kidato cha Tano na cha Sita. (Makofi)
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekuwa zikiingilia kati kwa kutoa misaada kwa watoto wenye mahitaji maalum pale inapojitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Jamii kwa ujumla kuhakikisha kwamba jukumu la kuwatunza na kuwalea wanafunzi wenye ulemavu ni la kwetu sote.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria Na. 9 iliyoanzisha Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, inatamka bayana kuwa waombaji wanaotakiwa kupewa kipaumbele katika kupewa mikopo ni pamoja na wanafunzi wenye ulemavu. Aidha miongozo ya ukopeshaji ambayo hutolewa na Serikali kila mwaka imeendelea kutamka wazi kuwa wanafunzi wenye ulemavu ni kundi linalotakiwa kupewa kipaumbele katika mikopo.
MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y. MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la mgawanyo wa fedha za TASAF ambapo wananchi wengi wasio na uwezo, wamekuwa hawapati fedha hizo.
Je, Serikali imejipangaje kutatua kero hii kwa wananchi ambao hawapati fedha hizo hususan katika Mkoa wa Kigoma?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utambuzi wa kaya za walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, ulianza mwezi Novemba, 2013 na hadi sasa umeshaandikisha kaya 1,100,000 katika Halmashauri 159 za Tanzania Bara, pamoja na Wilaya zote za Unguja na Pemba. Kaya hizi zinapata ruzuku kwa utaratibu wa uhaulishaji fedha baada ya kutimiza masharti ya kupeleka watoto shule na kliniki na pia kushiriki katika kazi za kutoa ajira ya muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaanza ulipanga kufikia asilimia 70 ya Miji, Mitaa na Shehia za Halmashauri ambavyo ndivyo vilivyofikiwa kutokana na mchakato wa kuvipanga, kutokana na viwango vya umaskini katika kila Halmashauri. Baada ya jamii kutambua kaya maskini na kuzipitisha kwenye mikutano ya hadhara iliyosimamiwa na viongozi wa Vijiji, Mitaa na Shehia. Kaya zilizotambuliwa zilijaziwa dodoso ili kukusanya taarifa zaidi za kaya na hatimaye Kaya hizo ziliandikishwa kwenye daftari la walengwa na kuanza kupokea ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa TASAF kwa kushirikiana na Halmashauri ilifanya kila jitihada kuhakikisha kwamba kaya zinatambuliwa na kuandikishwa kwenye mpango ni kaya maskini sana kwenye baadhi ya maeneo Kigoma ikiwa ni mojawapo, baadhi ya jamii na viongozi walifanya udanganyifu na kuingiza majina ya kaya ambazo siyo maskini sana na kuziacha kaya zinazostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuona changamoto hizo, TASAF imefanya mapitio ya orodha ya kaya zilizoandikishwa na kufanya ukaguzi wa nyumba kwa nyumba na kuziondoa kwenye mpango wa kaya zote ambazo siyo maskini. Zoezi hili ni endelevu na ni la kudumu. Kaya zote ambazo siyo maskini na ziliingizwa kwa makosa au kwa makusudi katika orodha ya kaya maskini zitaondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka kufikia tarehe 30 Mei, 2016 maeneo yote 161 ya utekelezaji ambayo ni Halmashauri 159 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba, zimeshaondoa Kaya ambazo hazistahili kuwemo kwenye orodha ya walengwa. Jumla ya kaya 25,446 zimeshaondolewa kwenye mpango kwa sababu mbalimbali ikiwemo vifo, kukosa vigezo vya kaya maskini na kuondolewa kwa Wajumbe wa Kamati za Mpango na viongozi wa Vijiji na Mtaa na Shehia katika orodha ya kaya maskini.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:-
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) upo katika Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili ziweze kumudu mahitaji ya chakula, elimu, afya na lishe bora kwa watoto:-
(a) Je, Serikali haioni ipo haja ya kuongeza viwango vya ulipaji kwa kaya maskini hasa ukizingatia upandaji wa bei za mahitaji ya kila siku na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yetu?
(b) Je, ni vigezo gani vya uhakika vinatumika ili kupata kaya maskini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Jimbo la Mtambwe, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni wa miaka kumi na utatekelezwa kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano kuanzia mwaka 2013 – 2023. Madhumuni ya Mpango huu ni kuwezesha kaya maskini kuongeza kipato na fursa na kuinua kiwango cha matumizi yao.
Mheshimiwa Spika, kiwango kinachotolewa kwa walengwa ni ruzuku ambayo ni kichocheo cha kuifanya kaya iweze kujikimu hasa katika kupata mahitaji muhimu huku ikiendelea kujiimarisha kiuchumi kwa kuweka akiba na kutekeleza miradi ya ujasiriamali ili iweze kusimama yenyewe na kujitegemea baada ya kutoka kwenye umaskini uliokithiri.
Mheshimiwa Spika, ruzuku inayotolewa kwa walengwa imeongezwa baada ya kufanyiwa mapitio kwa kuangalia hali halisi. Hata hivyo, ieleweke kwamba viwango vinavyotolewa vilipangwa hivyo ili kaya maskini iendelee kujishughulisha na kazi nyingine za kuongeza kipato na
isitegemee ruzuku peke yake. Kwa uzoefu uliopatikana, umeonesha kwamba kwa kiwango hicho walengwa wameweza kuboresha maisha yao kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, ujasiriamali na ujenzi wa nyumba bora, hivyo viwango hivyo vya ruzuku sio kidogo kama wengi wetu tunavyodhani.

(b) Mheshimiwa Spika, vigezo vya kupata kaya maskini huainishwa na jamii katika mkutano wa hadhara unaoendeshwa na wawezeshaji kutoka Halmashauri za Wilaya na kusimamiwa na viongozi wa vijiji/mitaa/shehia. Jamii huweka vigezo vya kaya maskini sana katika maeneo
yao. Hata hivyo, vigezo vikuu katika maeneo mengi ni kaya kukosa/kushindwa kugharamia mlo mmoja kwa siku, kaya kuwa na watoto ambao hawapati huduma za msingi kama elimu na afya kutokana na kuishi katika hali duni, wazee, wagonjwa wa muda mrefu na watoto yatima wanaoishi katika mazingira magumu na pia kukosa makazi ya kudumu au nyumba na mavazi muhimu.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA Aliuliza:-
Je, ni lini Mfumo wa Taarifa za Watumishi LAWSON utaboreshwa na kuondoa dosari zilizopo sasa hivi kama vile watumishi wa Umma kuondolewa kwenye makato ya mikopo wakati hawajakamilisha malipo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (Human Capital Management Informaton System) au kwa version nyingine ya LAWSON Version 9 unaotumika sasa kwa ajili ya kukusanya taarifa za kiutumishi na malipo ya mishahara ulianza kutumika mwaka 2012.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mfumo huu una changamoto ambazo zinasababisha watumiaji wasio waadilifu kuutumia vibaya kinyume na utaratibu ikiwemo kusitisha makato ya mkopo kabla mkopo wote haujamalizika kulipwa. Hii ilibainika kutokana na kaguzi za mara kwa mara zinazofanywa na Serikali ambapo hadi sasa watumishi wa aina hiyo wapatao 65 kutoka katika mamlaka za ajira 32 wamechukuliwa hatua mbalimbali baada ya kugundulika kuwa wametumia vibaya dhamana walizokabidhiwa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hii, Serikali inaendelea na hatua za kuhamia kwenye toleo jipya la mfumo huu (LAWSON Version 11) ambao unatarajia kuwekwa mifumo zaidi ya udhibiti ili kuhakikisha kwamba maafisa wenye dhamana ya usimamizi wake hawafanyi
mabadiliko yoyote bila kugundulika.
Mheshimiwa Spika, usanifu wa mfumo huu ili kuweza kuhamia katika toleo jipya la LAWSON Version 11 unaendelea ambapo wataalam wetu wa Wakala wa Serikali Mtandao (EGA) ndio wamepewa jukumu la kusimamia usanifu na usimikaji wake. Baada ya maboresho haya miundombinu madhubuti ya kuzuia matumizi mabaya ya mfumo itaimarishwa.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaamua kurudisha fedha zilizokusanywa na Halmashauri kupitia vyanzo vyake vya ndani ili ziweze kutekeleza majukumu yake na mikakati iliyopangwa kwa ufanisi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinakusanya mapato kupitia vyanzo vyake vya ndani kwa mujibu wa Sheria na Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, kifungu cha 6, 7, 8 na 9. Ukusanyaji wa mapato hayo unasimamiwa na Sheria Ndogo zinazofafanua sheria mbalimbali za kodi zinazopaswa kukusanywa na mamlaka hizo.
Mheshimiwa Spika, mapato ya ndani yanayokusanywa na Halmashauri hutumika kwa shughuli za maendeleo na uendeshaji wa Halmashauri kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa na Halmashauri zenyewe kwa kuainishwa katika mipango na bajeti zao za kila mwaka. Jukumu la Serikali Kuu ni kuidhinisha mapato na matumizi ya fedha hizo, kusimamia na kudhibiti matumizi ili kuhakikisha yanazingatia sheria na taratibu za fedha zilizowekwa na kuhakikisha zinatumika kwa madhumuni ya kuwaletea maendeleo wananchi katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kukusanya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwasilisha Serikali Kuu na kisha kuzirejesha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa haupo.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y. MHE. DOTO M. BITEKO) aliuliza:-
Je, ni kwa nini Serikali ilihamisha madaktari saba kwa mara moja kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bukombe huku ikijua Wilaya ya Bukombe ina upungufu mkubwa wa madaktari?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilihamisha madaktari sita katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa. Ili kuziba nafasi za waliohamishwa kwa lengo la kutoathiri utoaji wa huduma za afya hospitalini hapo, Halmashauri hiyo ilipelekewa madaktari wapya watano na badaye Serikali ilipeleka madaktari wengine watatu na kufanya jumla ya madaktari waliopelekwa Bukombe kuwa nane. Lengo lilikuwa ni kuboresha utoaji wa huduma katika hospitali hiyo.
MHE. MAULID S. MTULIA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Mto Msimbazi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Said Mtulia, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) inatekeleza mradi wa Tanzania Urban Resilience Program ambao unalenga kuzisaidia Halmashauri na Serikali Kuu katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko mya tabianchi. Mradi huu unalenga kutatua changamoto zinazolikabili Bonde la Mto Msimbazi lililopo katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ulibuniwa kupitia mchakato shirikishi uitwao Charrette ambao umewashirikisha wadau wote katika ngazi zote kuanzia mwezi Januari hadi Agosti, 2018. Mradi huu unatekelezwa na utaleta manufaa makubwa katika Jiji la Dar es Salaam ambapo utaongoa maeneo yaliyo hatari kwa mafuriko na kuyafanya salama kwa maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam, utapendezesha Jiji kwa kuweka maeneo mazuri ya maegesho ya magari (Dar Central Park, First of its Kind in Tanzania and East Africa), maeneo kwa ajili ya shughuli za Umma kama mikutano na matamasha na kubadilisha eneo la Mto Msimbazi linalokumbwa na mafuriko kuwa eneo linalofaa kwa ajili ya michezo na lenye manufaa ya kiikolojia kwa Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, andiko la mradi linaonesha gharama za utekelezaji mradi huu ni kiasi cha Dola za Marekani milioni 120 na tayari DFID kupitia Mradi wa TURP imeonesha nia ya kutoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 20 kwa ajili ya Bonde la Mto Msimbazi na vilevile Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Dar es Salaam Metropolitan Development Project (DMDP) imeonesha nia ya kutoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za Bonde la Mto Msimbazi.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-

Zanzibar inategemea sana biashara katika kuendeleza uchumi wake na uvuvi wa Bahari Kuu unaweza kukwamua uchumi wa Zanzibar na kwa sababu suala la Bahari Kuu ni jambo la Muungano:-

Je, Serikali haioni ni busara sasa kuondoa suala hilo kwenye orodha ya mambo ya Muungano ili kuisaidia Zanzibar kujiendesha yenyewe na kuweza kusaidia uchumi wa Zanzibar?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Territorial Sea and Exclusive Economic Zone Act, 1989 iliyoanzisha maeneo ya Bahari yaitwayo Bahari ya Ndani (Inner Sea), Bahari ya Kitaifa (Territorial Sea) na Eneo la Uchumi la Bahari (Exclusive Economic Zone – EEZ). Chimbuko la Sheria hii ni Sheria ya Kimataifa ya Bahari (The United Nations Convention on the Law of the Sea) ya mwaka 1982 inayotoa fursa sawa kwa nchi duniani kugawana rasilimali za bahari zilizopo kwenye maji (water column) na pia kwenye sakafu ya bahari (sea bed).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania iliridhia na kuanza kuitekeleza Sheria hii mwaka 1985. Hivyo, jukumu la kusimamia shughuli za uvuvi kwenye maji yaliyo katika Bahari ya Ndani (inner sea) na Bahari ya Kitaifa (Territorial Sea) ya Tanzania Bara hutekelezwa kupitia Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003, na upande wa Zanzibar Sheria ya Uvuvi (Na. 7) ya mwaka 2010. Ili kutekeleza sheria ya mwaka 1989 hususan katika kusimamia rasilimali za uvuvi zilizopo kwenye eneo la ukanda wa uchumi wa bahari ya Tanzania lenye ukubwa wa kilomita za mraba 223,000, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zilikubaliana kwa pamoja kuunda Taasisi Mamlaka ya Muungano yenye wajibu wa kusimamia uvuvi wa eneo hilo la Uchumi la bahari na pia Bahari Kuu kwa meli zenye kupeperusha bendera ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhitimisha suala hili, ninapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, uvuvi wa Bahari Kuu unatambulika Kimataifa kupitia Sheria ya Kimataifa ya Bahari ya mwaka 1982 hata katika mikutano mbalimbali ya Kimataifa Tanzania huwakilishwa kama nchi.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa kulisaidia kwa kulijengea uwezo Jeshi la Kujenga Uchumi la Zanzibar (JKU)?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chake Chake kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mashirikiano kati ya JKT na JKU yalianza mwaka 1975, kuanzishwa kwa JKU kutoka mfumo wa kambi za vijana ulioanzishwa tarehe 3 Machi, 1965 kwa sehemu kubwa kulitokana na mashirikiano hayo. Tangu wakati huo JKT na JKU wameendelea kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ya kiutawala na uzalishaji mali na ndiyo maana JKU ina sura ya JKT. Mwaka 2001 iliundwa Kamati ya Mashirikiano yaliyopelekea kuwa na Katiba ya Mashirikiano ya mwaka 2007. Katiba hiyo pamoja na mambo mengine imeainisha vikao mbalimbali vya mashirikiano ikiwa ni pamoja na ratiba za vikao vya wakuu wa vyombo hivyo.
MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Uhamiaji katika Kijiji cha Chikongo kilichopo Kata ya Moreha Wilayani Tandahimba ambacho huduma ya Visa kwa Watanzania waendao Msumbiji hutolewa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chikongo ni eneo lilioko pembezoni mwa Mto Ruvuma katika Wilaya ya Tandahimba ambayo kwa upande wa Msumbiji inapakana na Wilaya ya Nangale. Kwa sasa huduma za uhamiaji katika Kijiji cha Chikongo zinapatikana kupitia ofisi ya Uhamiaji ya Wilaya ya Tandahimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji itafanya mashauriano na nchi ya Msumbiji kuanzisha kituo cha uhamiaji katika eneo la Kijiji cha Chikongo kilichopo katika Wilaya ya Tandahimba ili kuendelea kutoa huduma kwa Watanzania waendao nchini Msumbiji.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza: -

Je, ni lini Kituo cha Polisi cha Chwaka kitapatiwa gari ili kutimiza majukumu yake kwa ufanisi zaidi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linatambua uhitaji wa magari katika Kituo cha Polisi cha Chwaka kama nyenzo ya kutendea kazi. Kupitia mkataba wake na Kampuni ya Ashok Leyland Jeshi la Polisi linategemea kupokea magari 369 toka Serikalini. Pindi magari hayo yatakapofika, kipaumbele kitatolewa kwa maeneo yote ya vituo vya polisi ambavyo havina magari kikiwemo pia Kituo cha Polisi Chwaka.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza: -

Je, nini kauli ya Serikali juu ya mapunjo ya fidia kwa wananchi walioathirika na mlipuko wa mabomu Mbagala?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa mkono wa pole na siyo fidia, kwa wananchi 12,647 waliothirika na milipuko ya mabomu iliyotokea tarehe 29 Aprili, 2009 katika Kambi ya JWTZ Mbagala. Malipo hayo, yalitolewa kwa awamu sita kuanzia mwaka 2009 hadi 2020. Vile vile, Serikali ilitoa kifuta machozi pamoja na kugharamia huduma za mazishi kwa familia 29 zilizopoteza wapendwa wao kutokana na milipuko hiyo ya mabomu ya Mbagala.

Mheshimiwa Spika, zoezi la kutoa mkono wa pole kwa waathirika lilisitishwa rasmi na Serikali mnamo mwezi Machi, 2020 baada ya walengwa wote waliokusudiwa kujitokeza na kulipwa.
MHE. ISSA J MTEMVU aliuliza: -

Je, nini mkakati wa kushughulikia malalamiko ya ajira za Kada ya Afya na Elimu kutolewa kwa waombaji wanaotoka baadhi ya maeneo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 2.1. 2 cha Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la mwaka 2008 na Kanuni D.6 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 ikisomwa kwa pamoja na Kanuni 12(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, ajira kwa nafasi zilizo wazi katika Utumishi wa Umma hujazwa kwa ushindani wa wazi kwa kufanya usaili na kupata washindi katika nafasi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliarifu Bunge lako kuwa, Serikali haitoi ajira kwa kuzingatia maeneo. Waombaji wote wa kazi Serikalini huchukuliwa kuwa na haki sawa na hivyo wote hupimwa na kuchujwa kwa vigezo vinavyofanana bila upendeleo wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahimize Watanzania wote wenye sifa stahiki kutoka maeneo yote nchini wajitokeze kuomba nafasi za kazi pindi zitakapotangazwa na Mamlaka zinazoshughulikia ajira nchini ili waweze kushindana na waombaji wengine.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID K.n.y. MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya uhakiki ili kuwarejesha walengwa 2,500 waliosimamishwa kupokea ruzuku ya TASAF?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuanza utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF, mwaka 2019 na 2021 Serikali iliagiza kufanyika uhakiki wa walengwa wote wa TASAF ili kupata taarifa sahihi ya walengwa wote waliomo katika kanzidata. Zoezi la uhakiki lilifanyika katika maeneo yote nchini na baadhi ya kaya zilibainika kukosa vigezo vya kuwa kwenye orodha ya walengwa na hivyo kusimamishwa kupokea ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaya ambazo zilithibitika kuwa na vigezo zimepewa nafasi ya kukata rufaa kwa mujibu wa sheria na taratibu na zilizobainika kuwa ni kweli zilikuwa na vigezo vya kuendelea kuwa kwenye mpango zilirejeshwa.