Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Daimu Iddi Mpakate (31 total)

MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini katika miradi miwili aliyosema imekamilika, mradi wa Nandembo na Nalasi tarehe 22 Julai, 2014, Rais wa Awamu ya Nne alifungua miradi ile, lakini cha kusikitisha hadi leo maji hayatoki katika miradi yote miwili. Je, yuko tayari kufuatana na mimi kwenda kuangalia miradi ile kama alivyosema imekamilika wakati maji hayatoki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mradi wa Mbesa umesimama kwa takribani kwa mwaka mmoja na nusu na vifaa viko pale, vina-hang hovyo bila usimamizi wowote. Je, ni lini Serikali itapeleka mkandarasi mwingine ili aweze kumalizia mradi ule?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, miradi miwili niliyoitaja amesema kwamba miradi hiyo haitoi maji. Nitafanya mawasiliano na Mkurugenzi wa Halmashauri husika ili aweze kutupatia maelezo kwa nini miradi hiyo haitoi maji ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakamilisha pale ambapo pamepungua kuhakikisha hiyo miradi inatoa maji. Pia kwa ridhaa yako, ridhaa ya Mheshimiwa Spika na Waziri wangu wa Maji na Umwagiliaji, hatuna matatizo kabisa, tukimaliza Bunge tunaweza tukaambatana naye ili kwenda kuangalia utekelezaji wa hii miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza kuhusu mradi wa Mbeso. Mradi huu ulikosa chanzo cha maji lakini kama mnavyofahamu Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tumeanza Programu ya Pili ya Maendeleo ya Maji ambayo imeanza Januari, 2016, baada ya kukamilisha programu ya kwanza. Ile miradi yote tuliyoi-earmark kwenye Programu ya Kwanza ambayo ilianza mwaka 2007 na haikukamilika ndiyo tutaanza nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika bajeti ambayo itasomwa na Mheshimiwa Waziri mwezi huu kwanza tunalenga kukamilisha miradi ambayo tulianza na haikukamilika na miradi ambayo pengine haikuanza lakini ilikuwa imependekezwa itekelezwe katika Programu ya Kwaza tutahakikisha kwamba miradi hii tunaikamilisha kabla hatujaenda kwenye miradi mipya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii miradi yote 11 katika Programu ya Pili tutahakikisha kwamba inakamilika kabla hatujaingia kwenye miradi mingine.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa mazingira ya Mchinga yanafanana kabisa na Wilaya ya Tunduru yenye kilometa za mraba 18,776; na kwa kuwa tayari kuna majimbo mawili na taratibu zote za kuigawa Wilaya ile zilishafanyika siku za nyuma; na kwa kuwa zilitolewa ahadi za viongozi wa Awamu ya Nne kuigawa Wilaya ile na Mkoa kwa ujumla. Je, ni lini taratibu za kuigawa Wilaya ile na Mkoa mpya wa Selous zitafanyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kumbukumbu zangu nilizokuwanazo ni kwamba eneo analozungumzia Mheshimiwa Mpakate ni kweli jambo hili liko ofisini, lakini nadhani kuna baadhi ya vitu vingi zaidi ya hapo hata kuna suggestion ya kugawa kupata Mkoa mpya wa Selous, kama sikosei katika eneo hilo! Na Mheshimiwa Ngonyani alikuwa akizungumza jambo hilo na hata Mheshimiwa Ramo Makani alikuwa katika mchakato huo wa pamoja kuhakikisha kwamba maeneo hayo, kutokana na jiografia yake, tunapata Mkoa mpya wa Selous.
Kwa hiyo, sasa kama Ofisi ya TAMISEMI itafanya uhakiki jinsi gani, aidha hizo Wilaya, Halmashauri au Mkoa mpya, mwisho wa siku tutakuja na majibu sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni kwamba kupeleka utawala katika eneo hilo kwa sababu, ni kweli, kuna wananchi wengine saa nyingine ukitoka huku Tunduru kwenda hata kule Ruvuma kuna changamoto, lakini uko karibu hapa karibu na Masasi. Kwa hiyo, walikuwa na maombi mengi kwa pamoja na viongozi waliopita walitoa ahadi mbalimbali.Ofisi ya TAMISEMI italifanyia kazi na mwisho wa siku ni kwamba, eneo hilo ki-jiografia litagawanywa vizuri kwa suala zima la kiutawala ilimradi wananchi wapate huduma ya karibu katika maeneo yao
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa matatizo ya ushirika yameenea katika maeneo yote ya nchi yetu ya Tanzania, na kwa kuwa Sheria Na. 6 ya Mwaka 2013 ilianzisha rasmi Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania. Je, ni lini Serikali itaifanya Tume hii iwe na uongozi wa kudumu kwa kuteua Mwenyekiti wa Tume pamoja na Makamishna wa Tume ili ushirika usimamiwe vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa anavyosema kwamba Tume ya Ushirika bado inakabiliwa na changamoto ya uongozi, nimhakikishie tu kwamba mapendekezo kuhusu uongozi tayari yapo mezani kwa Waziri, kwa hiyo muda mfupi tutasikia kukamilika kwa uteuzi wa viongozi wote wa Tume ya Ushirika.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Makambako - Njombe - Songea, ilijengwa tangu mwaka 1984, na sasa ina hali mbaya sana kila siku inawekwa viraka lakini hali imekuwa ni mbaya sana.
Je, ni lini Serikali itajenga barabara ile upya ili kuwahudumia watu wa Mkoa wa Ruvuma na Njombe kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Makambako hadi Songea na hususani Njombe hadi Songea imetengewa bajeti ya kufanyiwa ukarabati katika mwaka huu wa fedha. Na mimi nimhakikishie ukarabati huo utakaofanyika tutahakikisha ile kampuni itakayopewa kazi hiyo ya kufanya ukarabati inafanya kwa kiwango ambacho barabara hiyo inakuwa imara na kutumika kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mpakate na Wabunge wote wanahusika katika barabara hii, ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Leonidas Gama ambaye alinisumbua sana ofisini kuhakikisha kwamba hili eneo linakaa vizuri ili anapopita kule asipate matatizo anayoyapata sasa. Namhakikishia na wengine wote kwamba tutahakikisha mkandarasi atakayepata kazi hii ya ujenzi ambayo bajeti mmeshaipitisha anajenga kwa kiwango kinachotakiwa.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Tunduru Kusini kama alivyozungumza, kuna kata 15 kati ya hizo ni vijiji vinne tu vya Kata ya Chiwana na Kata ya Mbesa ndivyo vimepata umeme. Je, kati ya kata hizi zifuatazo ni lini watapatiwa umeme wa REA, Kata za Mtina, Nalasi, Mchoteka, Malumba, Mbati, Ligoma, Namasakata, Mchesi, Lukumbule, Chiwana na Msechela?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na tabia ya mkandarasi anayejenga laini ya Mbesa kuwadai wananchi wetu Sh.200,000/- mpaka Sh.300,000/- kwa ajili ya kupelekewa nguzo na kuunganishiwa umeme katika nyumba zao. Je, ni hatua gani imechukuliwa ili mkandarasi huyu asiendelee na tabia hiyo kwani umeme huu ni haki yao wananchi kupewa bure kwa kulipa Sh.27,000/-? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mpakate kwamba kwa kweli ni vijiji vinne tu ambavyo vimepata umeme kwenye jimbo lake lakini vijiji vingine vilivyosalia ambavyo jumla yake kwa kweli ni 67, vikiwemo Vijiji vya Semeni, Angalia, Jiungeni na vijiji vingine vya Mwenge vyote vitapata umeme kwenye REA Awamu ya III inayoanza mwezi Julai, 2016. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mpakate pamoja na wananchi wa Tunduru Kusini kwamba vijiji vyote vilivyosalia vitapata umeme kuanzia mwezi Julai 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na gharama ya nguzo ambayo wananchi wanatozwa, napenda kutumia fursa hii kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge na kuwahakikishia wananchi kama ifuatavyo: Kwanza kabisa, katika Mradi wa REA mteja yeyote hatakiwi kutozwa gharama ya nguzo, si Sh.200,000/- wala Sh.300,000/-. Naomba niwahakikishie wananchi wa Tunduru Kusini na Watanzania wengine, gharama za nguzo kwenye miradi ya REA Serikali imeshagharamia, kwa hiyo, mwananchi hatakiwi kutozwa gharama yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niendelee tu kusema kwamba kwenye miradi mingine ya TANESCO, gharama za nguzo ni kama ifuatavyo: Kwa mteja ambaye yuko umbali wa mita 30 -70, gharama yake ni Sh.177,000/- tu kwa vijijini na kwa mijini ni Sh.272,000/- tu. Kwa hiyo, napenda kutoa kabisa hili angalizo kwa wananchi, wasitozwe gharama zaidi ya hiyo kwa umbali ambao nimeutaja hata kwa miradi ya TANESCO.
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini katika vivuko vilivyotajwa; Kivuko cha Chaulesi kilichopo Makande na Chamba kilichopo Wenje kinaunganishwa na barabara mbili za mkoa ambazo zipo chini ya barabara ya ulinzi: Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitengeneza barabara hizi kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika muda wote wa mwaka kwa ajili ya kutoa huduma hiyo ambapo watu wa Msumbiji na Tanzania wanatembeleana kwa ajili ya kupata huduma kutoka Tunduru Mjini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa eneo la Chaulesi na Chamba watu wengi wanapita sana kutoka Msumbiji kuja Tanzania kufuata huduma za mahitaji ya muhimu kutoka Tunduru Mjini: Je, Serikali haioni haja ya kuweka Kituo cha Uhamiaji katika maeneo hayo mawili ili kuondoa kero ya Watanzania ambao wanapata tabu wanapovuka Msumbiji kwa ajili ya kukosa hati na kusumbuliwa na askari wa Msumbiji?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa barabara zote za mkoa tunazitengeneza kwa kiwango kizuri ili ziweze kupitika wakati wote wa mwaka. Kwa hiyo, nitaongea na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba tutaona mpango gani barabara hii tutaweza kuishughulikia, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusu utaratibu wa kuweka Kituo cha Uhamiaji, tutaongea na Wizara ya Mambo ya Ndani kuona kama kuna uwezekano wa kuweka kituo hicho ambacho kitapunguza matatizo kwa wananchi wetu wanaovuka sehemu hizo mbili.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira ya Tarime yanafanana kabisa na mazingira ya barabara zilizopo katika Jimbo la Tunduru Kusini kutoka Mtwara Pachani, Msewa na Rasi mpaka Tunduru Mjini iliahidiwa na Makamu wa Rais wakati wa kampeni kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini mchakato wa ujenzi wa barabara hii utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni ngumu sana unapokaa hapa kujibu swali linalohusu barabara yako, kwa hiyo, naomba nijibu kwa niaba ya Waziri wangu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Mtwara Pachani, Lusewa, Lingusenguse hadi Lalasi ni barabara ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais wakati wa uchaguzi, ndiyo kiongozi pekee aliyepita barabara hii. Kwa kweli baada ya kuiona na kuona idadi ya watu walivyo katika maeneo hayo akaahidi kwamba ataijenga kwa kiwango cha lami alipokuwa Lusewa na aliahidi vilevile barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami alipokuwa na Lalasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mpakate na wananchi wake wote wa Jimbo la Tunduru Kusini pamoja na wananchi wa Jimbo la Namtumbo na hasa Sasawala kwamba barabara hii kama ilivyoahidiwa tutaijenga, lakini naomba tu wananchi wetu waelewe kwamba ahadi tulizonazo za viongozi ni nyingi, zote tunazo tunazitekeleza kwa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka ujao wa fedha barabara hii imetengewa milioni 100 kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika nia ya kutekeleza ahadi ya Makamu wa Rais. Naomba nimhakikishie kazi hii itakapokamilika nitaweza kuwa na jibu sahihi lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa chuo kile hakikukidhi haja ya kukikarabati na kwa kuwa katika majibu ya msingi yamesema kwamba eneo la chuo lilikuwa dogo. Je, Serikali haioni haja ya kujenga chuo kipya kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina maeneo mengi ambayo yangeweza kujengwa chuo hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina upungufu mkubwa sana wa wafanyakazi katika Idara ya Afya kwa zaidi ya 70%. Ni kwa nini sasa Serikali isitoe upendeleo maalum kwa ajili ya Wilaya ya Tunduru na kwa vijana wa Tunduru ili waweze kuhudhuria mafunzo hayo katika vyuo ambavyo vimefufuliwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inayo haja ya kujenga vyuo vipya kwa ajili ya kutoa mafunzo ya watumishi kwenye sekta ya afya, si tu kwa Tunduru lakini ni kwa nchi nzima. Bahati mbaya sana Mpango wa MCH Aider Training ulipoanzishwa mwaka 1973 ulilenga kuzalisha wataalam wa kutoa huduma za uzazi kwa akinamama vijijini kwenye zahanati ambazo zilikuwa zinaanzishwa kwenye mpango ule kutokana na Azimio la Alma-Ata miaka hiyo na Azimio la Afya kwa Wote enzi za miaka ya 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango ule umebadilika na hatuwezi kujenga tena chuo kwenye kila mkoa kwa sababu mpango wa kujenga Vyuo vya MCH Serikali iliazimia kujenga chuo kwenye kila mkoa ili kuwazalisha hawa MCH Aider kwa kuwapa kozi ya mwaka mmoja na nusu kwa haraka ili tuwapate kwa wingi zaidi waweze kuwahi kwenda kuokoa maisha ya akinamama wajawazito na watoto. Mpango ule haupo tena na kwa maana hiyo vyuo vya afya sasa hivi haviwezi kuwa ni vyuo vya afya kwa kila mkoa bali vinakuwa ni vyuo vya afya vya kitaifa na utaratibu sasa hivi tunashirikisha pia sekta binafsi ambao nao wanaanzisha vyuo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya taaluma mbalimbali za kwenye sekta ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kwamba Tunduru wapate watumishi kwenye sekta ya afya, hili ni katika mipango ya Serikali ambayo ni endelevu. Kadri ambavyo tutapewa vibali vya kuajiri watumishi kwenye sekta hii ndivyo ambavyo tutaendelea kuajiri watumishi wapya na kuwatawanya si Tunduru peke yake bali ni kwenye wilaya zote hapa nchini.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mazingira ya barabara ya Mtwara yanafanana kabisa na mazingira ya barabara ya kutoka Masasi – Mangaka – Tunduru - Songea - Mbinga kutokana na machimbo yanayoendelea ya makaa ya mawe pale Ngaka, Mbinga. Makaa yale yanasafirishwa kwa malori makubwa yenye zaidi ya tani 30 kupitia barabara ya Tunduru – Mtwara
- Lindi - Dar es Salaam. Je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kujenga reli ili makaa yale yaweze kusafirishwa kwa njia ya reli kwa sababu magari yale yanahatarisha usalama wa barabara yetu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hiyo inasafirisha mzigo mkubwa lakini kila kwenye barabara tumeweka mizani ambayo kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba magari hayo hayazidishi mzigo ili kuhakikisha kwamba barabara hizo zinadumu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuitumia barabara hiyo lakini tutahakikisha kwamba magari hayo hayazidishi mzigo ili kulinda barabara yetu.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Serikali imetambua urefu mkubwa uliopo kutoka Ofisi ya Uhamiaji ilipo mpaka Wenje, Makande na Kazamoyo; na kwa kuwa wananchi hawa wa maeneo haya hawana uwezo mkubwa wa kuweza kufuata huduma hii ya uhamiaji zaidi ya kilometa 90 ziliko ofisi; na kwa kuwa Serikali inakosa mapato kutokana na tozo zinazotolewa kwenye hati hizi ya kusafiria; je, kwa nini Serikali haioni umuhimu kwa sasa wa kuweza kutoa huduma hii kwa njia ya mobile ili wananchi hawa waweze kupata huduma hii kwa haraka?
Swali la pili, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru
Ofisi ya Uhamiaji ina gari ambalo kwa muda mrefu ni bovu halina huduma yoyote katika maeno yote yaliyopo. Je, Serikali ni lini itatoa gari kwa ajili ya kurahisisha huduma hii ili wananchi wale wahudumiwe kwa urahisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukosa mapato Serikali si hoja ya kukosekana kituo karibu na mpaka. Kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiji namba 54 pamoja na Kanuni zake mwaka 2015, inaeleza kabisa kwamba ili mtu aweze kuvuka kutoka nchi yetu na kwenda nchi nyingine anahitaji kuwa na nyaraka za aina tatu.
Nyaraka hizo aidha ni passport ama hati ya dharula ya kusafiria ama kibali maalum. Kwa hiyo, kwa mwananchi yoyote anahitaji kuvuka lazima apitie katika njia hizo whether ofisi ipo katika mpaka, ofisi ipo katika Wilaya ama ofisi iko katika Mkoa, kwa hiyo hiyo naona ni hoja ambayo siyo sahihi, ninaomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwasisitiza wananchi wake juu ya umuhimu wa kuweza kutii sheria za nchi yetu ili kuepusha uvukaji wa mipaka kiholela na kuikosesha Serikali mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na gari, hili naomba Mheshimiwa Mbunge atuachie tulichukue, kwa sasa hivi hatuna gari za kutosha kwa Uhamiaji, pale ambapo gari zitapatikana tutaangalia na changamoto zingine za maeneo mengine na vipaumbele vilivyopo ili tuzingatie na kuchukua hatua stahiki.
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo. Tatizo la Manyoni linafanana kabisa na mazingira ya tatizo la barabara ya Mtwaro - Pachani - Lusewa - Mchoteka - Nalasi - Mbesa - Tunduru Mjini ambayo iliwekewa alama za ‘X’ zaidi ya miaka saba iliyopita. Je, ni lini ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Mheshimiwa Mbunge ameanza kutaja maeneo ambayo yako katika Jimbo langu katika kuongeza umuhimu wa swali lake. Naomba tu niseme masuala ya fidia ni ya Kitaifa na wakati ambapo tutaanza kujenga na sasa hivi siwezi kusema tunaanza lini kwa sababu fedha zilizotengwa kwa sasa ni za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sababu kazi hiyo bado haijakamilika. Naomba kwanza tuikamilishe kazi upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kabla hatujaanza kutafuta fedha za kujenga hiyo barabara.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Makaimu Watendaji wa Vijiji karibu maeneo mengi ya Tanzania hawapewi posho. Je, Serikali haioni haja ya kuwapa posho Makaimu Watendaji wa Vijiji ili waweze kufanya kazi zao vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, anachosema Mheshimiwa Mpakate ni kwamba katika maeneo mbalimbali ya vijiji vyetu watu wengi wanakaimu na kuna maeneo mengine walimu ndiyo walikuwa wanakaimu kama Watendaji wa Vijiji na tumetoa maelekezo katika Kurugenzi zetu kuacha kukaimisha Watendaji wa Vijiji hasa wale walimu kwa sababu wanaondoa nguvu kubwa sana ya ufundishaji. Katika jambo hili, kila Halmashauri tumeipa maelekezo na kila Mkurugenzi anajua ana watu wangapi wanakaimu sasa kupitia own source zao wataangalia utaratibu gani wa kufanya lakini lengo kubwa tunataka katika kila kijiji kazi ziweze kufanyika.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu aliyotoa Naibu Waziri, lakini Jimbo langu la Tunduru Kusini vituo vyake vya afya vimechakaa na vina hali mbaya na vina matatizo lukuki pamoja na uhaba wa wafanyakazi,hakuna gari, wala chumba cha upasuaji.
Swali langu, ni lini Serikali itahakikisha vituo hivi vya afya vinapata watumishi wa kutosha ili viweze kuhudumia wananchi wa Tunduru?
Swali la pili, katika kampeni ya uchaguzi mwaka 2010, Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya katika Mji wa Nalasi ambao una zaidi ya watu 25,000. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii ya kujenga kituo cha afya pale Nalasi ili kuweza kuwahudumia wananchi wale ambao wako katika vijiji sita katika Mji ule wa Nalasi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, katika suala zima la kuongeza watumishi, Serikali hivi sasa iko katika mchakato wa kuajiri watumishi mbalimbali. Katika hilo Jimbo la Tunduru tutalipa kipaumbele katika suala zima la mgawo wa watumishi kwa sababu Tunduru ina changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili nashukuru Mheshimiwa Mpakate alini-accompany vizuri sana wakati nimeenda katika Jimbo lake. Ni kweli watu wasioijua Tunduru, ukitoka barabarani mpaka Jimbo la Mheshimiwa Mpakate kuna changamoto kubwa sana. Ndiyo maana Mheshimiwa Mbunge alipoleta request, tukaamua kipaumbele cha kwanza twende tukamjengee kurekebisha Kituo cha Afya cha Mkasare.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba leo ninavyozungumza tayari tumeshaingiza shilingi milioni 500 kwa ajili ya kituo kile. Katika kituo kile tutajenga jengo la upasuaji, mortuary, wodi ya wazazi na tutafanya ukarabati mwingine halafu tutawawekea vifaa. Vilevile eneo hili la pili tutaliangalia kwa sababu lengo letu kubwa ni wananchi wa Tunduru waweze kupata huduma nzuri ya afya kwa sababu tunafahamu Wilaya ya Tunduru kwa jiografia yake, changamoto ya afya ni kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mpakate kwamba ahadi na maombi yake tulipokuwa katika mkutano, tumeyatekeleza na tunaendelea kuyafanyia kazi kwa kadri iwezekanavyo.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante na Mheshimiwa Naibu Waziri asante kwa majibu mazuri. Kwa kuwa kituo hiki kinahudumia zaidi ya Kata Tano, Kata ya Mtina, Lukumbulem Mchesi, Masakata na Tuwemacho.
Je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kuboresha kituo hiki ili kiweze kutoa huduma za upasuaji kwa wakina mama na wajawazito?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kampeni ya mwaka 2010 Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya katika Kata mbili za Nalase ambazo zipo katika Mji mmoja na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imekuwa inatenga kila mwaka na mpaka sasa imeishia kujenga msingi tu. Je, ni lini Serikali itaona haja ya kutimiza ahadi ile ya Rais wa Awamu ya Nne ili wapate kituo cha afya pale Nalasi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu nimpongeze kwa dhati jinsi ambavyo Mheshimiwa Mpakate anapigania kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata huduma ya afya iliyo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la kwanza ameuliza lini, na unaweza ukaona nia njema ya Serikali jinsi ambavyo inahakikisha huduma ya afya inapatikana na hasa katika ujenzi wa vituo vya afya katika kata husika. Hii ndio maana katika Halmashauri yake tumeanza na hiyo Kata ya kwanza na hiyo kata nyingine kwa kadri pesa itakavyopatikana. Nia njema ya Serikali ni kuhakikisha vituo vya afya vinajengwa katika kata zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, ni kweli kwamba kuna ahadi iliyotolewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne kwamba vingejengwa vituo vya afya katika kata mbili alizozitaja na yeye mwenyewe amekiri kwamba katika hizo kata mbili kazi ambayo imefanyika mpaka sasa hivi ni ujenzi wa msingi. Naomba nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na wananchi aendelee kuwahimiza ujenzi sio msingi tu, hebu waendelee kujenga mpaka kufikia usawa wa lenta na Serikali itaenda kumalizia ujenzi huo.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naitwa Mheshimiwa Mpakate. Napenda kuuliza swali la nyongeza. Katika maeneo yanayozalisha korosho, mfumo wa stakabadhi ghalani umesaidia sana wakulima kuongeza kipato, lakini moja ya changamoto inayokumbana nayo ni matatizo ya maghala katika vijiji vyetu katika maeneo yote ambayo yanalimwa korosho. Mradi wa MIVARF ungeweza kusaidia kujenga maghala kila Kata angalau ghala moja moja ili kuwapunguzia wakulima gharama ya kusafirishia korosho. Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa kujenga angalau ghala moja kila kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili kuwapunguzia wakulima wa Tunduru gharama ya kusafirisha korosho.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika mradi huu jambo kubwa ambalo linaangaliwa ni miundombinu ya masoko, barabara, lakini vile vile na huduma za kifedha kijijini. Katika eneo la miundombinu ya masoko jambo ambalo linaangaliwa pia ni suala la ujenzi wa maghala. Sasa katika programu hii yako maeneo ambayo tayari maghala yamejengwa lakini siwezi kutoa ahadi ya Serikali hapa kwamba tutajenga katika kila Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikoa ile ambayo inazalisha zao la korosho, kwa mfano, Ruvuma na Mtwara tayari maghala haya yapo, lakini kutoa ahadi ya kwamba tutajenga kila Kata Mheshimiwa Mbunge hii inategemeana pia na bajeti na programu jinsi tulivyojiwekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia katika ile mikoa ambayo tuliona umuhimu huo na ndiyo maana katika Mikoa ya Ruvuma na Mtwara tayari maghala haya yamekwishajengwa. Kwa hiyo, tunaamini kabisa labda baadaye fedha ya ziada ikipatikana hiyo inaweza ikawa sehemu ya consideration, lakini kwa sasa kama Serikali na kupitia programu hiyo hayo ndiyo maeneo hasa ambayo tumeanzia.

WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya msingi kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema hapa, Waheshimiwa Wabunge waielewe programu hii ya MIVARF, programu hii ni shirikishi, Mheshimiwa Mbunge anaomba ni kwa nini programu hii isiwe inajenga maghala tu. Tunachokifanya sisi Ofisi ya Waziri Mkuu, tunatafuta fedha na tunatengeneza plan ya nini kitafanyika kwenye fedha hiyo. Jukumu la kuamua aina ya mradi utakaotekelezwa kwenye Halmashauri husika ni jukumu la Halmashauri yenyewe na sio jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachokifanya sisi, tunapeleka aina za miradi, Halmashauri kupitia vikao halali vya kikanuni inaamua aina ya miradi katika Halmashari yao. Kwa hiyo, tunachotaka kusema hapa kama fedha hii itapatikana tena kwa sababu ni mradi ambao unaenda kwa phases, kama fedha itapatikana tena, Halmashauri zikishapelekewa miradi hii basi waamue aina ya miradi kwa kuzingatia hali halisi ya mazingira waliyonayo na shughuli wanazozifanya na Ofisi ya Waziri Mkuu tutakubaliana nao lakini sio wajibu wetu kuwaamulia wao nini kikafanyike kwenye mradi katika Halmashauri yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, katika maeneo ambayo miradi imefanyika wametupa ushirikiano wa kutosha. Nawapongeza sana na kama kuna tatizo lolote tunaomba tuendelee kuwasiliana ili miradi hii itekelezwe kwa viwango vinavyotakiwa huku ikisimamiwa na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, naishukuru Serikali kwa kutenga eneo la Mbesa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Je, Serikali ina mpango gani ya kuwasaidia wale wachimbaji wadogo kwa maana ya kuwawezesha kimtaji na kuwajengea mtambo wa kuchenjulia madini ya shaba ili waweze kusafirisha yakiwa yamechenjuliwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Tunduru kama alivyojibu kwenye swali la msingi ina mabango mengi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mtaalam wa kufanya valuation ya madini haya ya sapphire ili Halmashauri ipate takwimu sahihi za usafirishaji wa madini? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wachimbaji wengi wa madini wanahitaji kusaidiwa kimtaji kama alivyosema na hasa kwenye mnyororo mzima wa uongezaji thamani wa madini (value addition). Nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii Serikali inaifanya kwa umakini kwa sababu tuna historia mbaya hapo nyuma.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo walivyopatiwa mitaji kupitia ruzuku fedha nyingi sana hazikutumika kwa malengo yaliyokuwa yamekusudiwa. Kwa hiyo tunaangalia utaratibu mzuri zaidi kupitia mradi wetu wa SMRP kuona kwamba tunawasaidia wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wachimbaji wa Tunduru.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba tupeleke Mtaalam wa valuation Tunduru kwa ajili ya kufanya uthamini wa madini ya vito, tunalichukua jambo hili na tunalifanyia kazi. Vile vile tutaandaa watu baada ya Tume ikishakuwa imekamilisha kazi zake za kuchukua watalaam ili tuweze ku-station mtu mmoja kwa ajili ya kufanya valuation pale Tunduru.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa Serikali imekiri kwamba mgogoro upo katika eneo hili, je, haioni haja ya kuharakisha kufuta eneo hili ili wananchi wale wapate maeneo ya kulima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wananchi wale wana mahitaji makubwa ya ardhi, Serikali haioni haja sasa kupitia mipaka ya eneo lile ili kuongeza eneo la kijiji?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mpakate, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi atakubaliana na mimi kwamba hukumu ndiyo imepatikana Februari, 2018 na bado kuna tetesi kwamba huyu ambaye ameshindwa ni kama vile tayari ametuma application kwa ajili ya kukata rufaa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wale ambao wanahitaji eneo wanapatiwa lakini kwa kufuata sheria. Naomba tuvute subira taratibu zote zifuatwe ili wananchi wapate haki lakini na yule mwingine ambaye alikuwa anamiliki asije akasema kwamba haki yake imeporwa.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri aliyotoa Naibu Waziri, nina maswali mwili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada hizo za kuimarisha maeneo yaliyokuwepo sasa kuna tatizo la Watendaji Kata maeneo mengi katika Jimbo la Tunduru Kusini na Tunduru kwa ujumla walio wengi wanakaimu.
Je, Serikali itapeleka lini watendaji wa kudumu ambao wameajiriwa katika nafasi ya Kata, Vijiji na Katibu Tarafa?
Swali la pili, kwa kuwa majukumu mengi yaliyopo kwa sasa Vijijini yanafanywa na Watendaji wa Vijiji wakishirikiana pamoja na Wenyeviti wa Vijiji; na kwa kuwa Halmashauri nyingi zimeshindwa kutoa posho kwa maana ya asilimia 20 kwenye Vijiji husika.
Je, Serikali haioni haja kwa sasa kutoa posho kwa viongozi wa vijiji kwa maana ya Wenyeviti wa Vijiji ili waweze kufanya majukumu yao vizuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika nchi tunao upungufu mkubwa wa Watendaji wa Kata, kwa kweli siyo Watendaji wa Kata peke yake bali kada nyingi na Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha kwamba tunamaliza au tunapunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa watendaji wetu katika kada mbalimbali. Kwa upande wa Watendaji wa Kata, mwaka jana tuliajiri nafasi chache lakini mwaka huu tunao mpango wa kuajiri Watendaji wa Kata 1,000 nchi nzima. Ninaamini watakapoajiriwa hao watapunguza sana upungufu wa uwepo wa Watendaji Kata katika Kata nyingi hapa nchini ikiwemo Kata za Wilaya ya Tunduru.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kwamba Watendaji wa Vijiji na Wenyeviti wa Vijiji ndiyo wanaofanya kazi kubwa huko kwenye vijiji vyetu. Napenda nikubaliane sana na Mheshimiwa Daimu Mpakate kwamba ni kweli Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Vitongoji wanafanya kazi kubwa kwa kuwaongoza vizuri watendaji wa vijiji walioko huko kufanya kazi za Serikali kwa niaba ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, amesema kwamba posho hawapati, natoa hapa agizo ambalo lilishatolewa na Serikali tayari kwamba suala la kushusha asilimia 20 ya mapato ya ndani kupeleka kwenye Kata, Vijiji na Vitongoji kwa ajili ya posho za Waheshimiwa Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji, hilo ni suala la kikanuni na kisheria.
Kwa hiyo Wakurugenzi wa Halmashauri ni lazima watekeleze agizo hilo kikamilifu. Pale ambapo tutagundua kwamba mtu hatekelezi kwa sababu tu ya ujeuri au ukaidi itabidi tuchukue hatua za kiutawala na kiutumishi. Kuna wale ambao ni Wakurugenzi wanapata shida kidogo kutokana na makusanyo hafifu, tunawaomba sana Mabaraza ya Madiwani waridhie mapendekezo ya wataalam kuhusu kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ya ndani ambavyo vitasaidia kuweza kupatikana fedha ambazo hatimaye zitapelekwa kwa viongozi hawa kwa ajili ya posho.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Tatizo la Handeni linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Jimbo la Tunduru Kusini, kwamba wananchi wanapata shida kubwa ya maji, visima vilivyopo havitoshi. Je, ni lini Serikali itachimba visima katika Jimbo la Tunduru Kusini hasa katika Kata ya Mchoteka, Malumba, Tuwemacho, Lukumbule na Mchesi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kabisa kwamba eneo lake sijafika na baada ya bajeti hii mwezi wa Saba ndio eneo litakalokuwa la kwanza. Pia ninayo taarifa kwamba, utekelezaj wa baadhi ya miradi haukutekelezwa vizuri, haukusimamiwa vizuri na halmashauri ambapo waliuchelewesha mradi na kufanya wananchi wasipate hiyo huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaambatana na Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili, ili twende tukatatue changamoto zote zilizoko kule. Kwa sababu, kuanzia sasa utekelezaji wa miradi utasimamiwa moja kwa moja na Wizara yangu mpaka ngazi ya halmashauri. Nimhakikishie kwamba, tutachimba visima vya kutosha, tutatafuta vyanzo vya kutosha ili wananchi wetu waweze kupata huduma ya maji kama walivyoahidiwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa TAMISEMI, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa eneo la Sasawala ndiyo eneo ambalo linategemewa kuanzisha Wilaya Mpya na Makao Makuu yake kuwa Lusewa; je, ni kwa nini Serikali isianzishe Jimbo jipya la Uchaguzi katika eneo hilo la Sasawala?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilifuata utaratibu wote wa kuanzisha Wilaya mbili, kwa maana Wilaya ya Tunduru Kusini na Tunduru iliyopo sasa na kwa kuwa Halmashauri hiyo iliendesha vikao vya kuanzisha miji midogo miwili, katika Vijiji vya Nalasi na Mchoteka; je, Serikali haioni haja kwa sasa kuanzisha miji midogo katika eneo la Nalasi na Mchoteka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu yangu katika maswali yake mawili ya nyongeza, hayawezi kutofautiana sana na jibu langu la swali la msingi. Kuhusu kuanzisha Jimbo jipya, utaratibu wake uko tofauti kidogo na utaratibu wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuanzisha Jimbo jipya linahusisha sana Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi kabla ya michakato yoyote ya mikutano haijaanza, inatakiwa itangaze nia ya kuanzisha Jimbo jipya katika eneo fulani, baada ya hapo ndiyo vikao viridhie na baadae Mheshimiwa Rais aridhie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kwamba michakato ya kuanzisha Wilaya mbili kutoka katika Wilaya moja ya Tunduru, kwa maana Tunduru na Tunduru Kusini na miji aliyoitaja kwamba iwe miji midogo, utaratibu wake ni sawasawa na jibu langu kwenye swali la msingi kwamba hii miji midogo ni maeneo mapya ya utawala, kwa maana kwamba ukishakuwa na mji mdogo utakuwa na Halmashauri ya Mji, Mkurugenzi na utakuwa na vikao vinavyohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maeneo hayo yote ya utawala yamesitishiwa kuanzishwa hadi hapo tutakapoimarisha zaidi maeneo tuliyonayo sasa hivi. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, mwaka 2014 alipotembelea Jimbo la Tunduru Kusini alitembelea katika Kijiji cha Mbesa ambapo kuna Hospitali ya Mission pale. Hospitali ile inatoa huduma kubwa kuliko Hospitali ya Wilaya na Mheshimiwa Rais aliahidi kuipandisha daraja hospitali ile kuwa Hospitali Teule. Je, ni lini hospitali ile itapewa hadhi ya kuwa Hospitali Teule ili iweze kuendelea kutoa huduma vizuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Hospitali ya Mission ya Mbesa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekuwa nikijibu na ambavyo nimejibu leo, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo ambayo hakuna Hospitali za Wilaya zinakwenda kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni azma ya Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Dini na Mashirika mengine pale ambapo sasa hivi hatuna Hospitali Teule, tunatumia zile ambazo zipo ili zifanye kazi kwa muda tu kama Hospitali Teule. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunakuwa na hospitali zetu za Serikali na zile za Mashirika ya Dini pale ambapo tutakuwa tumejenga za Serikali wabaki wakiendesha kwao na sisi Serikali tuwe na za kwetu tukifanya kazi kama Serikali. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu kumshauri Mheshimiwa Mpakate, ili hospitali binafsi au ya Shirika la Dini ifanywe kuwa DDH sasa hivi tumeshusha madaraka haya kwenye Halmashauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Halmashauri ndiyo itafanya majadiliano na makubaliano na hospitali ile na tumeelekeza kuwe na mkataba wa muda maalum, kwamba Halmashauri ya Tunduru inaamua kuingia makubaliano na hospitali hii ili iwe Hospitali Teule ya Halmashauri na mkishakubaliana ndiyo mnaleta taarifa hizi TAMISEMI na Wizara ya Afya. Kwa hiyo, tutazitambua rasmi sasa kuwa ni Hospitali Teule ya Halmashauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, niseme tunatoka kwenye Hospitali za Wilaya, tunakwenda kwenye Hospitali ya Halmashauri. Kwa hiyo, sasa hivi kila Halmashauri itakuwa na Hospitali badala ya kuwa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna Wilaya zina Halmashauri mbili, zote zinapaswa kuwa na Hospitali ya Halmashauri ambayo ni ngazi ya kwanza ya Hospitali. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa ujenzi wa kituo kile cha afya ulitokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea katika Kata zile mbili za Nalasi zilizoko katika kijiji kimoja na kuagiza kwamba kipatikane Kituo cha Afya; na kwa kuwa Halmashauri imekuwa ikipanga kila mwaka bajeti ya kujenga kituo kile kwa shilingi milioni 80 na shilingi milioni 75, lakini mpaka leo hii bado wameshindwa kujenga kituo kile. Je, Serikali haioni haja sasa ya kutimiza ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne kwa kutoa fedha kwa ajili ya kujenga kituo kile cha afya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina gari moja ambalo ni bovu tangu 2007, mpaka leo ni zaidi ya miaka 11; na kwa kuwa eneo la Tunduru ni kubwa sana, lina Majimbo mawili (Kusini na Kaskazini), je, Serikali haioni umuhimu sasa kutoa gari mbili za wagonjwa upande wa Kaskazini na Kusini ili kuweza kuhudumia wananchi wa Wilaya ya Tunduru ambao eneo lao ni zaidi ya square kilometer 18,000? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mpakate, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza anaulizia Serikali kutoa nguvu ili kumalizia hicho kituo cha afya. Pesa ambayo imepelekwa, shilingi milioni 400 na shilingi milioni 500 inaashiria dhamira njema ya Serikali ya kuhakikisha kwamba vituo vya afya vinajengwa hususan katika Halmashauri ya Tunduru. Halmashauri nayo ina vyanzo vyake, kwa bajeti ambayo inaisha mwaka 2017/2018 wameweza kukusanya wastani wa shilingi bilioni 2.78 na katika bajeti inayokuja, wanatarajia kukusanya shilingi bilioni 3.1, ni wazi kabisa hakika wakiweka kipaumbele cha kumalizia hicho kituo cha afya na kwa sababu wamesaidiwa na Serikali, wanaweza kumaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kuhusu kupeleka ambulance, ni kweli tangu mwaka 2007 ile gari itakuwa imeshakuwa chakavu kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi. Ni vizuri tukashirikiana na Halmashauri kwa kutumia vyanzo vyao wakati Serikali Kuu tunahangaikia, tukipata, tutakuwa tayari kuwafikiria lakini siyo vizuri nao wakabweteka kwa sababu wana chanzo kizuri na wanakusanya vizuri. Ni vizuri kiasi hicho ambacho kinapatikana wakatenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kununua ambulance, sidhani kama itaathiri sana Halmashauri. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, ila nina maswali mawili ya nyongeza. moja ya Kampuni zilizoomba kujenga mtambo wa kuchenjua shaba pale Mbesa ni Metalicca Commodities Corporation ya Marekani ikishirikiana na Minerals Access System Tanzania (MAST) lakini ni muda mrefu toka wameomba na majibu hayatolewi kutokana na kuchelewa kwa mwongozo. Je, Serikali mpaka sasa imefikia wapi kutengeneza mwongozo mzuri ukizingatia shaba ina tabia tofauti na madini mengine ili kuwezesha wawekezaji hao walioomba kupata kibali cha kuweza kujenga mitambo yao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kumekuwa na leseni nyingi sana za utafiti zilizotolewa na Serikali kwa kampuni tofauti mbalimbali kwa muda mrefu na wamekuwa wanakaa kwa muda mrefu bila kuweza kuendeleza maeneo hayo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanyang’anya au kufuta leseni zile za utafiti kwa yale makampuni ambayo yamekaa muda mrefu na badala yake maeneo yale kupewa wachimbaji wadogo ili waweze kujikimu na kujitafutia riziki kwa njia ya kuchimba madini katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba Serikali imetoa mwongozo na mwongozo wenyewe umetoka tarehe 25, Januari, unaoonesha aina zote za madini yanaweza yakachenjuliwa katika kiwango gani na baada ya kuchenjuliwa yanapewa sasa ruhusa (permit) kwa ajili ya kusafirisha kupeleka nje ya nchi. Kwa hiyo, kwa kila aina ya madini tumetoa mwongozo huo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge afuatilie tu na aone kwamba sasa wale wawekezaji wanaokuja ambapo sisi tumejipanga kutafuta mwekezaji ambaye kweli yuko serious na kampuni zimekuja zaidi 11 wameonesha nia ya kuwekeza kwenye smelter, tunataka tuwawekee kampuni ambazo tuna uhakika nazo kwamba zinaweza kuwekeza kwenye kuchenjua au kuyeyusha zile shaba kwa maana ya smelter.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu hizi leseni za utafiti za makampuni mbalimbali, ni kwamba mpaka sasa hivi, katika meza zetu tunapitia leseni zote ambazo zinaonesha ni leseni zilizotolewa mwaka gani. Tunataka kuangalia status zake zikoje? Tunapitia leseni ambazo zinafanyiwa kazi; lakini zile leseni ambazo ni za PL walipewa makampuni mbalimbali, wengi tumeona wameshikilia maeneo na hawafanyi kazi yoyote. Sasa hivi Wizara yetu tunapitia leseni zote. Kwa kampuni ambayo haifanyi chochote katika leseni ambazo tumewapatia, tunakwenda kuzifuta.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa leseni ambazo tumewapa watu kwa ajili ya uchimbaji kwa maana ya Primary Mining License, Mining License, Special Mining License na zenyewe tunaangalia kwa mujibu wa sheria na taratibu. Kama umekuwa na leseni huwezi kuifanyia kazi, sisi Wizara ya Madini muda siyo mrefu tutawapa default notice na tunakwenda kuzifuta leseni zote.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri kutoka kwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba itatoa mafunzo kwa wafugaji na Maafisa Ugani katika Halmashauri zetu, je, ni lini itatoa mafunzo hayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambayo wafugaji wanaongezeka kwa kasi kubwa sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imetenga maeneo kwa maana ya vitalu vya wafugaji mbalimbali vinavyofikia 100; na kwa kuwa wakulima wengi wameshapewa maeneo hayo lakini mpaka sasa hawajaenda. Nini kauli ya Serikali kuhusu hawa wafugaji ambao wameshindwa kwenda kwenye maeneo yale ya wafugaji na kuendeleza migogoro na wakulima mbalimbali kwa mifugo yao kula mazao ya wakulima? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mpakate, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni lini tutakwenda kupeleka mafunzo haya Wilayani Tunduru? Naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba timu yetu iliyoko Kaliua ikitoka huko itakwenda Tunduru na Halmashauri zingine katika nchi yetu kwa ajili ya kutoa elimu hii kwa wafugaji na Maafisa Ugani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili analotaka kujua ni namna gani na tunatoa kauli gani kwa wale waliopata vitalu. Kwanza nataka niwapongeze sana viongozi wote wa kule Wilayani Tunduru kwa kazi kubwa waliyoifanya ya mfano ya kuandaa vitalu wao wenyewe Halmashauri na kuvigawa kwa wafugaji kwa ajili ya kufanya kazi ya ufugaji iliyo na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kauli ya Serikali ni kama ifuatvyo: Wafugaji wote waliopewa vitalu hivi na wakaacha kuvitumia kwa wakati, tunawapa tahadhari kwamba watanyang’anywa na watapewa wafugaji wengine walio tayari kufanya kazi hii kwa ufanisi.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika Vijiji alivyovitaja kuwa vilipata umeme awamu ya kwanza na ya pili vya Azimio, Chiwana, Mkandu na Mbesa umeme ulipita barabarani ndani ya mita 100 kutoka barabara kuu ilikopita nguzo kubwa. Je, ni lini mradi wa kujazilizia mitaa iliyobaki katika Vijiji hivyo vya Azimio, Chwana, Mkandu na Kijiji cha Airport itaanza?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwaka 2017 nilipeleka maombi maalum kuongeza vijiji katika Mradi wa REA katika Vijiji vya Tuwemacho, Chemchem, Ligoma, Makoteni, Nasia, Semeni, Mtina, Angalia, Nalasi, Mchoteka, Kitani, Mkolola pamoja na Masakata. Nini kauli ya Serikali kuhusu uwekaji wa awamu ya tatu ya umeme katika Vijiji hivyo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Mpakate, lakini vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mpakate jinsi anavyofuatilia umeme katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, ni kweli vijiji vingi tuliviweka kwenye round II ya awamu ya tatu inayoendelea, lakini baada ya kuona changamoto kubwa sana katika Jimbo la Tunduru Kusini tulifanya mapitio mapya na vijiji 13 tuliviingiza kwenye round inayoendelea. Kwa hiyo katika utaratibu tunaojenga line kwa sasa kutoka Tunduru Mjini mpaka Msingi umbali wa kilometa 20 tumechukua vijiji vingine 13 vikiwemo vijiji ambavyo anavisema vya Angalia, Semeni ambako Mheshimiwa Mbunge anatoka lakini mpaka Tuwemacho, Chemchem mpaka Chilundundu kwa vijiji vyote hivyo viko kwenye mpango. Pia Wakandarasi kupitia TANESCO sasa wanavifanyia kazi, kwa hiyo nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge pamoja na kumpongeza, vijiji 13 vya nyongeza tayari vimeshaanza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu nyongeza ya vijiji vya ujazilizi; mradi umeshaanza na utekelezaji wa maeneo ya kujaziliza, maeneo ya vitongoji unaanza mwezi huu utachukua miezi 12, lakini maeneo ya Azimio pamoja na Mbesa ambako tayari umeme upo kwenye Vitongoji 17, tayari pia TANESCO wameanza kuvifanyia kazi.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo lililopo kwenye Tarafa ya Mgeta linafanana kabisa na tatizo lililopo kwenye katika Tarafa ya Namasakata, katika Jimbo la Tunduru Kusini. Barabara ya Chemchem - Ligoma inazaidi ya miaka 10 tangu 2007 haijawahi kutengenezwa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza barabara ile ili wananchi waweze kufaidika na Uongozi wa Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda kwamba tangu tulivyoanzisha chombo chetu kwa maana ya TARURA, wengi wamekuwa wakipongeza ufanisi ambao umetokana na chombo hiki. Kwa hiyo, ni vizuri sasa tusiishi kwa historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwmaba ni vizuri tukawasiliana na Meneja wa TARURA ili atupe uhalisia katika barabara hii ambayo anaongelea na hiyo miaka 10 ambayo iliahidiwa, hakika kwa Serikali ya Awamu ya Tano tunaahidi na kutekeleza.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Na ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutembelea katika kijiji cha Mbesa aliahidi kisima kirefu amechimba, amekwenda kuangalia na sasa ameahidi kutoa milioni 200 kwa ajili ya kufanya ule mradi kukamilike vizuri. Vilevile tunawashukuru wafadhili wetu waliojenga visima 72 na wengine wamejenga visima 90 katika Jimbo la Tunduru Kusini. Na nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa mradi wa Mbesa, mradi wa Lukumbuli ambao ulikamika miaka mitatu iliyopita na mradi wa wanalasa ambao ulikamilika zaidi miaka 9 iliyopita haufanyi kazi kutokana na tatizo la kutumia mafuta ya diesel ambayo wananchi wameshindwa kutumia.

Je, Serikali ina mpango gani wa kufunga solar ili wananchi waweze kutumia kwa ukamilivu?

Kwa kuwa katika mradi wa Kijiji cha Mtina uliokamika mwaka moja uliopita umeshindwa kufanya kazi vizuri kutokana na panel solar zilizopo pale kutokutosheleza kusukuma maji kwa ajili ya kupeleka kwa wananchi.

Je, Serikali haioni haja yakuongeza solar panel katika mradi ule ili uweze kuhudumia wananchi wa Mtina ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kiukweli ni miongoni mwa Wabunge wanafanya kazi kubwa sana, na niseme hili ni baba lao kwa eneo la Tunduru Mungu akubariki sana. Lakini kikubwa ninachotaka kukisema watalamu wetu kwa maana ya WARUSA pamoja na wizara hawana kisingizio tena, utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na fedha, tumepata fedha kwa mikoa 17 zaidi ya bilioni 119. Hata katika Jimbo lako la Tunduru tumeshapeleka bilioni 1.3 hizi fedha ni kwa ajili ya kwenda kutatua changamoto za miradi ya maji. Ni mtake mhandishi wa maji wa Tunduru Kusini katika kuhakikisha anatumia changamoto hizi ili kukarabati na wananchi wako waweze kupata huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza. Ahsante sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza Kijiji cha Misiaje kilichopo katika Kata ya Malumba na Kijiji cha Imani na Kaza moyo kilichopo Kata ya Lukumbule havina mawasiliano. Je, ni lini Serikali itajenga minara katika vijiji hivyo ili kuwapa mawasiliano wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naompongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nilivyofanya ziara Mkoani Ruvuma tulikuwa na mawasiliano mazuri sana kulikuwa na changamoto nyingi sana na hasa hasa maeneo haya ambayo yapo mpakani. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira kama nilivyosema tunaorodha ndefu sana, aje tu tupitie kwa pamoja halafu tutakapoweka minara hii katika maeneo ambayo yameainishwa tutaangalia tena tuone kama kuna maeneo bado yanachangamoto Serikali itakuwa ipo tayari kuendelea kupunguza tatizo ambalo lipo katika maeneo yetu.

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Katika Jimbo langu la Nkasi Kusini kuna Vijiji sita vya Kisambala, Ng’undwe, Mlalambo, Kasapa na Izinga, mara nyingi nimepeleka orodha Wizarani ili vipatiwe mawasiliano. Je, ni lini Serikali itavipatia mawasiliano vijiji hivi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu changamoto zilizoko katika maeneo haya sababu ya jiografia yake, naona ndiyo maana amekaa na jirani yake pale Mheshimiwa Malocha. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo hili ambalo analizungumzia tutaweka msukumo wa kipekee ili tuone changamoto hizi zinakaa vizuri kwa sababu nafahamu kwamba kuna changamoto nyingi sana kwenye eneo lake, kwa hiyo, avute subira. Pia, naomba tuonane na Mheshimiwa Mbunge ili aweze kuona kwenye orodha namna ambavyo tumejipanga ili aweze kwenda kusema kwa wananchi kwamba Serikali hii imejipanga kuhakikisha kweli mawasiliano yanakuwa mawasiliano kwa wote.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Barabara ya Mitema Upinde kwenda Msinji iliyopo upande wa Tunduru ni sehemu ya barabara hiyo ya ulinzi katika upande wa mto Ruvuma. Barabara hiyo ilitolewa madaraja yake wakati wa vita vya Nduli Iddi Amin, na tangu yametolewa madaraja yale mpaka leo bado hayajaweza kurudishwa. Ni lini Serikali itarudisha madaraja yale ili barabara hiyo iweze kupitika kwa urahisi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Barabara ya Tunduru na Masakata Liwanga mpaka Misechela ni barabara ya ulinzi ambayo inaunganisha Msumbiji na Tanzania kupitia katika Kijiji cha Misechela. Je, Serikali haioni haja ya kukichukua kipande hicho kiwe Barabara ya Mkoa kwa sababu mchakato wote wa kufanya barabara hiyo ichukuliwe na TANROADS ulishafanyika kwa ngazi ya Mkoa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, anafuatilia sana hususani mtandao wa barabara katika maeneo yake. Niseme tu kwamba hii barabara ya Itema Msinji ilitolea madaraja. Utaratibu wa kwetu kawaida ni kwamba madaraja yaliyowekwa kwa wakati wa dharura huwa tunayatoa na kuyahifadhi kama asset; pale ambapo itahitajika sasa kuyaweka madaraja haya sehemu zingine tutaenda kuyaweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge nielekeze tu wataalamu waangalie maeneo haya kama yanastahili kurudishia madaraja haya yaliyotolewa tutafanya utaratibu huo, lakini kama tutakuwa na mahitaji ya kujenga upya maeneo hayo ili kutoa huduma nzuri kwa wananchi pia tutafanya hivyo. Kwa hiyo nielekeze tu TANROADS Mkoa wa Ruvuma waangalie sehemu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu kwamba tunafanya upembuzi yakinifu wa barabara hii kutoka Mtwara – Pachani – Lusewa – Ligusenguse kwenda Nalasi (km 211), na tumetenga fedha za kutosha. Kwa hiyo wakati wa zoezi hili la kutambua changamoto zilizoko katika maeneo haya pia tutatazama kwa macho mawili maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu barabara hii ya Misechela kuwa Barabara ya Mkoa tumeanzisha chombo hiki cha TARURA. Sisi juhudi zetu ni kuhakikisha TARURA inapata fedha za kutosha, lakini kama kutakuwa na mahitaji mahsusi ya kupandisha Barabara hii tutaiangalia kwa nia hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge umeomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini chanzo cha kituo kile kuchomwa ni mgogoro wa ugomvi wa usalama barabarani kati ya Askari pamoja na bodaboda, hii ndiyo imekuwa tabia ya Askari wasiokuwa wa usalama barabarani kuwakamata bodaboda na kuwapiga bila kuwaeleza makosa yao.

Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na tabia hiyo ya Askari wasiokuwa wa usalama barabarani kuwakamata bodaboda na kuwapiga bila kuwaeleza makosa yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na Msumbiji likiwa na Tarafa tatu. Tarafa ya Namasakata tangu imeundwa haijawahi kuwa na Kituo cha Polisi. Je, Serikali haioni haja sasa ya kupeleka Kituo cha Polisi Misechela na Namasakate yenyewe kwa kituo cha polisi ili kuwahudumia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini na Tarafa ya Namasakata kwa ujumla.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hatuwezi kuhalalisha jambo lolote na vitendo vya uchomaji vituo vya Polisi, kwa hiyo hata kama kulikuwa kuna matatizo kati ya bodaboda iwe na Askari wa Usalama barabarani ama awe Askari yeyote basi haihalalishi uchomaji wa kituo cha polisi, hilo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja yake kwamba kuna watu ambao siyo Askari wa Usalama Barabarani wanawapiga bodaboda. Niliwahi kujibu swali hili siku chache zilizopita na nilieleza kwamba hatujapata taarifa ya kuona Askari Polisi wakipiga bodaboda na kama kuna taarifa hizo basi ni vema tukapatiwa ili tuzifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amekiri kwamba wanaofanya hivyo siyo Askari wa Usalama Barabarani, kwa sababu tunaamini askari wa usalama barabarani wamepata mafunzo na weledi wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao, Askari wa aina nyingine yoyote ama watu wa aina nyingine yoyote ambao wanafanya vitendo kama hivyo kama wapo kauli ya Serikali ni kwamba ni kinyume na utaratibu hivyo watumie weledi katika kuhakikisha kwamba wanawakamata wanaovunja sheria ikiwemo hawa waendesha bodaboda.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu maeneo hayo mawili aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge ambapo anataka kujua ni lini tutajenga kituo cha polisi. Jibu ni kwamba katika maeneo yote nchini tutajenga kuanzia kwenye wilaya hata ngazi ya kata ikiwemo maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge pale ambapo hali ya kifedha itaruhusu.