Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Daimu Iddi Mpakate (15 total)

MHE. MPAKATE D. IDDI aliuliza:-
Katika Wilaya ya Tunduru kuna miradi mingi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ambayo imesimama kwa muda mrefu bila kukamilishwa na wakandarasi kwa sababu ya ukosefu wa fedha:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kumalizia miradi hiyo ambayo wananchi wanajua kuwa fedha zilitolewa na Benki ya Dunia lakini hazijulikani zilikwenda wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mpakate Daimu Iddi, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambapo ugharamiaji wa maji chini ya programu hii hutokana na fedha za Serikali na wadau wengine ikiwemo Benki ya Dunia. Hivyo, upelekaji wa fedha kwenye halmashauri hutegemea upatikanaji wa fedha kutokana na bajeti ya Serikali na fedha za wadau wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa programu hii, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilipanga kutekeleza jumla ya miradi 11. Hadi sasa jumla ya miradi miwili katika Vijiji vya Nandembo na Nalasi imekamilika na inahudumia wananchi 21,224. Miradi minne ya Vijiji vya Lukumbule, Amani, Mtina na Matemanga ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Mradi wa maji katika Kijiji cha Mbesa umesimama kutokana na mkandarasi kukiuka masharti ya mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika, mpaka kufikia Februari 2016, Wizara imeshatuma kiasi cha shilingi milioni 537.2 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa ajili ya kuendelea kukamilisha miradi hiyo. Aidha, miradi minne katika Vijiji vya Majimaji, Muhuwesi, Nakapanya na Mchoteka haijaanza kutekelezwa kutokana na kukosa vyanzo vyenye maji ya kutosheleza. Miradi hii itatafutiwa vyanzo mbadala katika utekelezaji wa awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Maji.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Wilaya ya Tunduru iko miradi mingi ya REA ambayo kampuni mbili zimepewa kazi hiyo lakini wakandarasi wanasuasua kukamilisha miradi hiyo na muda wake umeisha kwa kigezo cha kutolipwa:-
Je, ni lini Serikali itatoa pesa kukamilisha miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi kabambe wa REA Awamu ya II katika Wilaya ya Tunduru na kazi hii imeshaanza na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, mwaka 2016. Kazi ya kupeleka umeme katika Wilaya ya Tunduru inaunganisha pia kazi ya ujenzi wa njia ya umeme Msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 293.2, ujenzi wa njia ya umeme Msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 77.1 lakini pia ufungaji wa transfoma 38 zenye ukubwa mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi hizo, kazi nyingine inayofanyika ni kuwaunganishia umeme wateja wa awali 3,330 lakini pia mradi umekamilika kwa asilimia 79 ambapo ujenzi wa laini kubwa umekamilika kwa asilimia 83, laini ndogo asilimia 74, transfoma saba zimeshafungwa na wateja 182 wameshaunganishiwa umeme. Gharama ya mradi wa Mkoa wa Ruvuma ikiwemo Wilaya ya Tunduru ni shilingi bilioni 32.56. Kiasi ambacho mkandarasi hadi sasa ameshalipwa ni shilingi bilioni 27.22 ambayo ni sawa na asilimia 83.6. REA wanasubiri kupata uthibitisho kutoka kwa mkandarasi kuhusu madai ya shilingi bilioni 3.19 ili aweze kulipwa mara tu baada ya uthibitisho huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Tunduru vijiji vinne vya Jimbo la Tunduru Kusini ambavyo ni Azimio, Chiwana, Mbesa na Mkandu, vimeunganishiwa miundombinu ya umeme ambayo inafanyiwa marekebisho na matayarisho kwa ajili ya kuwashwa. Hivi sasa mkandarasi anaendelea kufunga transfoma na mita za Luku katika vijiji vingine 34 ambavyo vimesalia katika Wilaya ya Tunduru ili viweze kupatiwa umeme ifikapo tarehe 30 Juni, 2016.
MHE. MPAKATE D. IDDI aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Jimbo la Tunduru Kusini imepakana na Mto Ruvuma na vijiji vingi vipo pembezoni mwa mto huo, hivyo wananchi wake hupata baadhi ya bidhaa kutoka Msumbiji kwa kutumia mitumbwi ambayo siyo salama kwa maisha yao wanapovuka mto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia kivuko wananchi wa Wenje na Makande ili waweze kuvuka Mto kwenda Msumbiji kwa usalama?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupata mahitaji halisi ya kivuko kwa wananchi wa Wenje na Makande Wilayani Tunduru, Wizara yangu itatuma mtaalam kutafiti uwezekano wa kuweka kivuko eneo hilo. Utafiti huo utajumuisha upatikanaji wa eneo lenye kina cha maji cha kutosha kuwezesha kivuko kuelea wakati wowote wa mwaka, wakati wa masika na wakati wa kiangazi pamoja na kupata kibali cha kuweka maegesho ya kivuko upande wa Msumbiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo ya utafiti huo yatawezesha Wizara kuweka mpango wa kuweka kivuko hicho kwenye bajeti yake.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru kulikuwa na Chuo cha MCH kilichokuwa kikitoa mafunzo ya taaluma mbalimbali za afya kwa vijana wengi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru lakini mwaka 1980 chuo hicho kiliungua moto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukikarabati chuo hicho ili kiweze kuendelea kutoa wataalam wa afya kama hapo awali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Tunduru ni mojawapo wa vyuo vilivyokuwa vimefungwa baada ya kusitisha mafunzo ya Martenal and Child Health Aider mwaka 1998. Chuo hiki ambacho kipo katika eneo la Hospitali ya Tunduru kiliungua moto sehemu ya bweni na bwalo la chakula. Katika utekelezaji wa mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) vyuo vinne vya aina hii ambavyo vilikuwa vimefungwa vilifanyiwa tathmini mwezi Agosti 2008 kwa nia ya kuvifufua kuanza kutoa mafunzo kwa wauguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika tathmini hiyo ilipendekezwa Vyuo vya Nzega, Nachingwea na Kibondo vifufuliwe na kuanza kutoa mafunzo ili kuchangia kuongeza idadi ya wataalam kutokana na mahitaji ya Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya Chuo cha Tunduru hakikukidhi vigezo vya kufufuliwa kutokana na gharama kubwa iliyohitajika kufanya ukarabati. Aidha, nafasi ya upanuzi wa chuo ilikuwa ndogo hivyo kupendekeza sehemu hiyo ya chuo kujumuishwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Tunduru.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika upande wa kusini mwa Jimbo la Tunduru Kusini wananchi takribani 200 wa Tanzania na Msumbiji huvuka Mto Ruvuma kila siku kutafuta mahitaji yao ya kila siku, upande wa Msumbiji wameweka Askari wa Uhamiaji ambao huwanyanyasa sana Watanzania kwa kuwapiga na kuwanyang’anya mali zao kwa kukosa hati ya kusafiria.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka Kituo cha Uhamiaji katika kijiji cha Makande Kazamoyo na Wenje ili kuwapatia Watanzania huduma ya uhamiaji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha kuwa inasogeza huduma karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na huduma za Uhamiaji. Katika kutekeleza hilo Wilaya zilizo nyingi ikiwemo Tunduru zina Ofisi za Uhamiaji. Aidha, Serikali inatambua umbali mrefu wa takribani kilometa 90 uliopo kutoka vijiji vya Makando, Kazamoyo na Wenje kutoka Mjini Tunduru zilipo ofisi za Uhamiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo na uhitaji
wa huduma za uhamiaji katika vijiji hivyo ili kuwawezesha wanakijiji kuingia na kwenda nchini Msumbiji kihalali, tunafanya ufuatiliaji ili kujua gharama za kufungua ofisi za Uhamiaji katika kijiji cha Makando. Kwa kuanzia Ofisi hiyo itahudumia vijiji vya Kazamoyo na Wenje ili kuwawezesha kuvuka mpaka Kihalali. Tunawaomba wananchi na Mheshimiwa Mbunge kuwa na subira kwa kuzingatia kuwa suala hili linahitaji kutengewa fedha katika bajeti.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna vituo vitatu vya afya. Kituo cha Afya Mtina kina zaidi ya miaka 30 hakijafanyiwa ukarabati na pia hakuna wodi ya wazazi.
Je, ni lini Serikali itajenga wodi ya wazazi katika kituo hicho na kufanya ukarabati ili kiweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa vijiji vya Nasya, Semeni, Nyerere, Angalia na wakazi wa kata ya Mchesi na Lukumbule?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na nguvu za wananchi imekamilisha ujenzi wa zahanati sita za Njengi, Mwenge, Tuwemacho, Nasumba, Semeni na Kazamoyo ambazo zimeanza kutoa huduma.
Aidha, nampongeza Mbunge wa Jimbo kwa kuweka kipaumbele na kutumia shilingi milioni 6.2 kwa ajili ya ukarabati wa chumba cha kujifungulia na chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya Mtina.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaweka kipaumbele na kuhakikisha fedha zinatengwa kupitia Halmashauri katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha afya Mtina kinakamilika. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna vituo vitatu vya afya ambapo Kituo cha Afya Mtina kina zaidi ya miaka 30 hakijafanyiwa ukarabati na pia hakuna wodi ya wazazi.
Je, ni lini Serikali itajenga wodi ya wazazi katika kituo hicho na kufanya ukarabati ili kiweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa Kata za Nasya, Semeni, Nyerere, Angalia na wakazi wa Kata ya Mchesi, Vijiji vya Likumbula, Tuwemacho na Namasakata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina vituo vitano ambapo vituo vya afya viwili vipo katika Jimbo la Tunduru Kusini na vitatu katika Jimbo la Tunduru Kaskazini. Kituo cha Afya Mtina kilianzishwa mnamo mwaka 1970 na kimekuwa kikiendelea kutoa huduma za kujifungua na huduma za matibabu ya kawaida kwa kipindi chote. Kwa sasa chumba cha kupumzikia akina mama baada ya kujifungua kimetengwa ndani ya wodi ya kawaida ya wanawake. Serikali kupitia wadau wa maendeleo (Walter Reed Program) waliweza kufanya ukarabati wa jengo la tiba na matunzo (CTC) kwa wagonjwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa msingi wa wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Mtina unaendelea kupitia fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo la Tunduru Kusini ambapo kiasi cha shilingi milioni nne zilitolewa. Aidha, Halmashauri katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/ 2019 imetenga kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ukarabati na kuboresha Kituo cha Afya Mtina.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Tunduru, Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Afya Mkasale kilichopo katika Jimbo la Tunduru Kusini. Aidha, Halmashauri inajenga wodi mbili za upasuaji katika Hospitali ya Wilaya, nyumba ya mganga katika zahanati ya Naikula, ukarabati wa nyumba mbili za watumishi katika Kituo cha Afya Mchoteka na kuendeleza ujenzi wa zahanati ya Legezamwendo kupitia mapato yake ya ndani. Serikali itaendelea kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya kwa kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Mji wa Tunduru yako mabango mengi yanayoelezea ununuzi wa madini jambo linaloashiria upatikanaji mkubwa wa madini kutoka kwa Wachimbaji wadogo wadogo ambao hawatambuliwi kwa mujibu wa sheria:-
Je, ni lini Serikali itawatengea maeneo ya kuchimba madini na kuwatambua Kisheria Wachimbaji hao wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini na kabla sijajibu swali hili naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Profesa Idris Kikula kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume mpya ya Madini.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2017 inawatambua wachimbaji wadogo. Kwa kutumia sheria hiyo Serikali inatoa leseni za uchimbaji za madini (Primary Mining Licenses) kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kuna mabango na maduka mengi yanayotangaza uwepo wa madini ya vito katikati ya Mji wa Tunduru huko Mkoani Ruvuma. Baadhi ya madini ya vito hayo yaliyopo Wilaya ya Tunduru ni pamoja na Sapphire, Ruby, Garnet na kadhalika. Maduka ya madini yenye mabango ni ya wafanyabiashara wakubwa wenye leseni kubwa (Dealers License) ambazo huhuishwa kila mwaka kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2013 Serikali ilitenga eneo la Mbesa, Wilaya ya Tunduru, lenye ukubwa wa hekta 15,605.3 kwa tangazo la Serikali Namba tano la tarehe 22 Februari, 2013, kwa ajili ya uchimbaji mdogo wa madini ya shaba. Hadi Aprili, 2018 jumla ya leseni hai 649 za wachimbaji wadogo wa madini yaani (PML) zimetolewa Wilaya ya Tunduru.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadri taarifa za utafiti katika maeneo hayo zitakavyoandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ili wachimbaji wadogo hao waweze kuchimba madini siyo kwa kubahatisha.
Mheshimiwa Spika, aidha, wachimbaji wadogo wanahimizwa kuomba leseni ili wafanye shughuli za utafutaji wa madini kwa mujibu wa sheria za nchi ili kuinua vipato vyao kutoa ajira kwa Watanzania, kuchangia pato la Taifa kupitia tozo mbalimbali zinazotokana na shughuli za madini.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina jumla ya kata 39 na vijiji 157. Halmashauri iliomba kuigawa Wilaya hiyo ambayo ina ukubwa zaidi ya Mkoa wa Mtwara wenye Wilaya sita:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuigawa Wilaya ya Tunduru ili iwe rahisi kutoa huduma karibu zaidi na wananchi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzigawa Kata za Mchoteka, Mtina, Namasakala, Lukumbule, Mchasi, Tuwemacho na Misechela ambazo zina wakazi zaidi ya 30,000 kila Kata?
(c) Je, Serikali itaidhinisha lini mgao wa vijiji uliopendekezwa na Halmashauri mwaka 2015 ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, taratibu za kuanzisha au kugawanya maeneo ya kiutawala zimeainishwa kwenye Sheria ya Serikali za Mitaa Sura ya 287, pamoja na Mwongozo wa Serikali wa mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, maombi ya kugawa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na kuanzisha Halmashauri ya Wilaya ya Nalasi na kuzigawa Kata za Mchoteka, Mtina, Namasakala, Lukumbule, Mchasi, Tuwemacho na Msecheke yaliwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI yakiwa pamoja na ombi la kuanzisha mkoa mpya wa Selous. Serikali imetafakari maombi haya na kuyaona kuwa ni ya msingi, hata hivyo, kutokana na changamoto ya kuimarisha kwanza miundombinu kama majengo ya ofisi na nyumba za watumishi na mahitaji mengine kama vifaa vya ofisi, watumishi wa kutosha na vyombo vya usafiri kwenye maeneo mapya ya utawala yaliyoanzishwa tangu mwaka 2010 na 2012, Serikali imesitisha uanzishwaji ya maeneo mapya ya utawala hadi yaliyopo yaimarishwe kikamilifu.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika kampeni za uchaguzi mwaka 2010 Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga Kituo cha Afya katika Mji wa Nalasi na kutoa gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya
Mchoteka:-
(a) Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nalasi?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Mchoteka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Afya - Nalasi ulianza Oktoba, 2013 kwa gharama ya shilingi milioni 80 ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa msingi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD). Katika mwaka wa fedha 2017/2018, kiasi cha shilingi milioni 75 zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hicho kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka kipaumbele na kutoa shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya nane katika Mkoa wa Ruvuma ambapo kati ya hivyo, vituo vya afya viwili vinajengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambavyo ni Msakale kilichogharimu shilingi milioni 400 na Kituo cha Afya Matemanga kilichogharimu shilingi milioni 500.
(b) Mheshimwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina gari moja ambalo linahudumia vituo vyote vya afya kikiwemo Kituo cha Afya Mchoteka. Hata hivyo, gari hiyo kwa sasa ni chakavu kwa kuwa ilinunuliwa tangu mwaka 2007. Halmashauri inashauriwa kuweka kipaumbele na kutenga fedha katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya ununuzi wa gari lingine la wagonjwa.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-

Serikali imeweka zuio la kusafirisha shaba ghafi kabla ya kuchakatwa, jambo ambalo limesababisha uchimbaji mdogo wa Mbesa wa Shaba usimame na wachimbaji wadogo kukosa kazi za kufanya:-

Je, ni lini Serikali itajenga mtambo wa kuchenjua shaba katika Kijiji cha Mbesa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa tarehe 3 Machi, 2017, Serikali iliweka zuio la kusafirisha nje ya nchi madini ghafi na kuelekeza madini yote yanayoongezewa thamani yaongezewe thamani hapa nchini. Zuio hilo lilikuwa na nia njema ya kutaka shughuli zote za uongezaji thamani madini zifanyike hapa nchini ili kuongeza manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kutokana na rasilimali ya madini.

Mheshimiwa Spika, kutokana na zuio hilo, kuna GN Na. 60 ya mwaka huu, yaani tarehe 25, Januari, 2019, Serikali imetoa mwongozo wa kuhakiki uongezaji thamani madini au miamba nchini kabla ya madini hayo kupata kibali cha kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, madini ya shaba yanapatikana katika maeneo mbalimbali nchini. Hivyo, kwa kuzingatia hilo, Serikali imepokea maombi ya kampuni 11 zenye nia ya kujenga vinu vya kuyeyusha madini hayo (smelters) baada ya kutangaza uwepo wa fursa hiyo. Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuteua kampuni zitakazojenga smelters hizo ili kuwaondolea adha ya soko la madini hayo wachimbaji wadogo na wakubwa.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-

Jimbo la Tunduru Kusini lina jumla ya vijiji 65, kati ya hivyo ni vijiji vinne tu ndiyo vimefikiwa na umeme wa REA Awamu ya I na ya II:-

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA katika vijiji 61 vilivyobaki?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Idd Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi ya kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini. Jimbo la Tunduru Kusini lina vijiji 65, kati ya vijiji hivyo Vijiji vinne vya Azimio, Chiwana, Mkandu na Mbesa ndivyo vimekwishapata umeme kupitia mradi wa REA II na Vijiji vingine vinne vya Mchuluka, Umoja, Masalau na Msinji vinatarajiwa kupatiwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea na unaotegemea kukamilika mwezi Juni, 2020.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme katika Jimbo la Tunduru Kusini inahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolt 33 yenye urefu wa kilometa 9.4, ujenzi wa njia ya msongo wa umeme wa kilovolts 0.4 yenye urefu wa kilometa nane, ufungaji wa transfoma nne za KVA 50 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 275. Gharama za kupeleka umeme katika vijiji hivyo ni shilingi milioni 644.

Mheshimiwa Spoika, vijiji 57 vya Kata za Chiwana, Mchuluka, Mtina, Nalasi, Mchoteka, Ligoma, Tuwemacho na Lukumbulu vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya III, mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021. ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-

Jimbo la Tunduru Kusini lina changamoto ya maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima virefu na vifupi katika kata ya Tuwemacho, Mchuluka, Mchoteka, Mbati, Marumba, Wenje, Nasomba, Namasakata na Lukumbule.
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa maji naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate Mbunge wa Tunduru Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Jimbo la Tunduru Kusini lina jumla ya miradi mitano ya maji ya bomba kwenye vijiji 11. Miradi hiyo ipo kwenye Kata za Mbati, Nalasi, Namasakata, Misechela, Mtina, Ligoma, Mchesi na Lukumbule. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Maji Help for Underserved Communities imechimba visima 72 katika Kata za Tuwemacho, Marumba, Lukumbule Mbesa na Mtina. Visima hivyo vimefungwa pampu za mkono. Vilevile Wilaya ya Tunduru kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Maji All Mother and Child Count imechimba visima virefu katika kata za Mchuluka, Namasakata, Chiwana na Lukumbule. Visima hivyo vitatumika kujenga miradi ya maji ya bomba katika maeneo hayo. Tayari utekelezaji umeanza kwa kata ya Chiwana na Namasakata

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha huduma ya maji inakuwa ya uhakika katika Wilaya ya Tunduru, Serikali kupitia Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini imetenga na kutoa fedha katika bajeti ya mwaka 2019/2020 kiasi cha shilingi milioni 974 kwa ajili ya kujenga, kukarabati na kufanya upanuzi wa miradi ya maji katika vijiji mbalimbali vilivyopo wilaya hiyo vikiwemo vijiji vya Jimbo la Tundurru Kusini. Vijiji hivyo ni Mbesa, Airport, Nasomba, Namasakata, Chiwana, Semeni, Nalasi, Misechela, Angalia, Ligoma na Mchekeni. Aidha, Serikali imepanga kuchimba visima Virefu viwili katika vijiji vya Wenje na Likweso vilivyopo Jimbo la Tunduru Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga na kutoa fedha kadri zinavyopatikana ili kuweza kujenga na kukarabati miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Jimbo la Tunduru Kusini ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya majisafi na usafi wa mazingira.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-

Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na Msumbiji kupitia Mto Ruvuma kuanzia mpaka wa Wilaya ya Nanyumbu na Wilaya ya Namtumbo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua barabara ya ulinzi inayounganisha mikoa yote ya Kusini yaani Mtwara na Ruvuma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate Mbunge wa Tunduru Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara anazozungumzia Mheshimiwa Mbunge ni barabara ya Mahangamba, Madimba, Tangazo, Kitaya, Mnongodi, Mapili, Mitemaupinde yenye urefu wa km 351 na barabara ya Mtwara pachani Lusewa, Tunduru yenye urefu wa km 300 zinazohudumiwa na Wakala wa barabara Tanzania TANROADS Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa kutambua umuhimu wa barabara hizi, hasa kwenye ulinzi wa mipaka ya nchi yetu Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mtwara tayari imefungua sehemu ya barabara kuanzia Mahangamba, Madimba, Tangazo, Kitaya na Mnongodi – Mapili yenye urefu km 216 kwa kiwango cha changarawe. Katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 jumla ya shilingi bilioni mbili na milioni mia nane sabini na nane zimetengwa kwa ajili ya kuendelea kufungua km 90.4 za barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma inaendelea kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka zabuni kwa sehemu ya barabara ya Mtwara - Pachani, Lusewa – Tunduru ambapo kazi hiyo imefikia asilimia 65.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pamoja na Serikali kuendelea kufungua barabara hizo Serikali inaendelea kuzifanyia matengenezo mbalimbali sehemu ya barabara iliyofunguliwa ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-

Kituo cha Polisi Lukumbule kiliungua moto miaka iliyopita na mpaka sasa kituo hicho hakina Askari kimefungwa:-

(a) Je, ni lini Serikali itakirejesha kituo hicho hasa ikizingatiwa kuwa kipo mpakani mwa nchi ya Msumbiji?

(b) Je, ni lini Serikali itaweka kituo cha Uhamiaji katika kituo hicho cha Lukumbule?

(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Lukumbule ambacho kimeishia kwenye lenta baada ya Halmashauri kushindwa kumalizia ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Idd Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi Lukumbule kilichomwa moto mwaka 2013 na baadhi ya wananchi wasiotaka kutii sheria katika eneo hilo. Baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi kwa kutambua kwamba eneo husika ni la mpakani na nchi ya Msumbiji limekuwa likifanya doria za mara kwa mara na pia kushirikisha taasisi nyingine za Serikali ambazo ni wadau wa ulinzi na usalama katika kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa wananchi wa eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa kufungua Kituo cha Uhamiaji Kata ya Lukumbule upo kwenye hatua za mwisho na inatarajiwa kufanguliwa wakati wowote mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuupongeza uongozi wa Halmashauri ya Tunduru kwa ujenzi wa kituo cha Polisi cha Lukumbule ingawa bado ujenzi wake haujakamilika. Hata hivyo, Serikali inatambua umuhimu na uhitaji wa kituo cha Polisi katika eneo hilo. Aidha Serikali kupitia Jeshi la Polisi itafanya tathmini ili kubaini gharama halisi za kukamilisha sehemu ya ujenzi uliobakia na kuona uwezekano wa kukamilisha ujenzi huo.