Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Daimu Iddi Mpakate (41 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa, naomba nitoe shukurani kwa kuniteua leo kuwa mchangiaji katika bajeti ya kilimo.
Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo nikiwa salama kuongea katika Bunge lako kwa mara ya kwanza. Pia napenda niwashukuru wapiga kura wangu wa Tunduru Kusini na Tunduru kwa ujumla walioniwezesha leo kuwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kukosa fadhila, nakishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua kuwa mgombea wa Jimbo la Tunduru Kusini na hatimaye kuhakikisha kwamba ninashinda na leo niko ndani ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, napenda kumpongeza Waziri wa Kilimo kwa hotuba yake nzuri ambayo ameiwasilisha leo. Nami napenda sehemu ya hotuba hiyo nichangie mambo mawili matatu ambayo najua yakirekebishwa, basi utendaji wetu utaendelea vizuri na wakulima wetu watapata manufaa mazuri na kulima zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ni suala la pembejeo. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri amelieleza vizuri. Kero ya voucher imekuwa ni donda ndugu, kwa kweli lilikuwa linatugombanisha na wakulima wetu; mahali penye kaya 2000, kaya 30 zinapata voucher, matokeo yake inaleta migongano katika vijiji vyetu.
Nashukuru sana kwa kuliona hili, lakini pamoja na kuahidi kwamba pembejeo zitauzwa kama soda, ni vyema Mheshimiwa Waziri uhakikishe kwamba unaweka bei dira, bei elekezi ya hizo pembejeo kama wanavyofanya EWURA ili kila mkulima ajue kwamba katika eneo lake pembejeo itapatikana kwa bei fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kufanya hivyo, wafanyabiashara ambao ni mawakala watakaosambaza pembejeo zile, watatumia mwanya ule ule kuendelea kuuza bei juu kuliko vile ilivyokusudiwa na Wizara. Naomba sana jambo hili litiliwe mkazo ili kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanapata fursa nzuri ya kupata pembejeo kwa bei nzuri na mahali walipo ili kuendeleza kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la muhimu ni suala la umwagiliaji. Ninachojua mimi katika dhana ya umwagiliaji ni kuhakikisha kwamba kilimo kinaendelea through out the year, kwamba mkulima anakuwa analima kifuku na kiangazi, lakini umwagiliaji uliopo sasa katika maeneo mengi, kilimo kile kinakuwa ni kilimo cha umwagiliaji wakati wa kifuku tofauti na kusudio lile la kulima through out the year. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wataalam wetu wanatakiwa waende mbali zaidi kuhakikisha kwamba ile mifereji inayotengenezwa kwa ajili ya kifuku peke yake, tuone namna nyingine ya kutengeneza mifereji kwa ajili ya kulima kipindi cha kiangazi. Maeneo mengi yaliyotengenezwa kwa ajili ya kilimo hiki yanatumika kifuku badala ya kiangazi kama inavyokusudiwa na dhana yenyewe ya umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naomba nielezee suala mtambuka la ushirika. Kwanza naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mmojawapo wa watumishi wa ushirika ndani ya miaka nane katika sekta ya korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri amesema kuhusu kuanzisha commission ya ushirika. Ni kweli ushirika umedorora lakini tunasahau wapi tulipojikwaa, tunaangalia tulipoangukia. Kamisheni hii kwa kweli haina nguvu kwa mujibu wa taratibu za kikazi. Utakuta kamisheni haina watumishi mikoani; kamisheni haina watumishi Wilayani, inategemea watumishi kutoka Halmashauri za Wilaya ambao katika utendaji wa kazi wanawajibika kwa Wakurugenzi wa Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hili ni tatizo, utendaji hauendi sawasawa kama kamisheni ilivyokusudia kwa ajili ya kufufua ushirika. Mbaya zaidi, hata hao watumishi waliokuwepo katika Halmashauri, hawatoshi kusimamia ushirika. Ni hali ya hatari, utakuta Wilaya ina vyama 20, 40, SACCOS pamoja na Vyama vya Wakulima, lakini Afisa Ushirika utamkuta mmoja au wawili. Inakuwa ni ngumu! Ni kazi kubwa kwa Maafisa Ushirika kuhakikisha kwamba vyama vile vinakwenda kama inavyokusudiwa na kama sheria inavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, commission ipewe nguvu, iwe na watumishi wa kutosha mpaka Wilayani ili waweze kusimamia Vyama vya Ushirika vizuri viweze kuwasaidia wakulima wao. Tunajua bila ushirika maeneo mengi kwa kweli inakuwa ni tatizo kubwa ingawa wenzangu wameeleza, ushirika ni jumuiya ya hiari, kwa hiyo, wanaushirika wenyewe wafanye yale yanayotakiwa ili kuhakikisha ushirika unaboreshwa kama inavyoeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo jambo la ushirika, kuna jambo la mikopo. Nashukuru ndugu yangu ameeleza kuomba kupeleka Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ruvuma ni eneo mojawapo ambayo wanazalisha sana mahindi, lakini tukiangalia suala la mikopo hali siyo nzuri kwenye Benki zetu za kawaida. Riba inakuwa kubwa haimwezeshi mkulima kukopa na kupata return ya kuweza kurudisha faida na yeye mwenyewe kupata chakula kwa ajili ya maisha yake na familia yake ilivyo.
Tunaomba sana suala la benki lifanyiwe hima kuhakikisha kwamba Benki za Kilimo zinakwenda mikoani ili kuweza kuwasaidia wakulima walio wengi kwa kupata mikopo iliyokuwa nafuu ili waweze kuendeleza kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni suala la uhifadhi wa chakula, ni aibu! Nimesema nimekuwa kwenye sekta ya kilimo kwa muda wa miaka nane. Ukienda vijijini maghala ya kuhifadhia mazao hakuna na ndiyo maana utakuta sehemu kubwa iliyopo tunazalisha vizuri lakini uhifadhi wa mazao unakuwa ni tatizo. (Makofi)
Kuhusu ile programu ambayo ilikuwepo miaka ya nyuma ya kuhakikisha kwamba kila kijiji kinapata ghala la kisasa, basi naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja, atuhakikishie angalau vijiji vile ambavyo vinaonekana uzalishaji wa mazao ni mkubwa waanzishiwe miradi ya kujenga maghala kwa ajili ya kuhifadhi mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, kwa hayo machache, nashukuru sana kwa kuniruhusu kuchangia mawili, matatu, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa siku ya leo kuchangia katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, napenda kupongeza hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini napenda kupongeza kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi, ikiongonzwa na Rais wetu John Pombe Magufuli. Pamoja na pongezi hizo ningependa kutoa mapendekezo mawili, matatu, naomba sana kwenye hili Waziri wa Fedha anisikilize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2009 Serikali iliamua kuanzisha export levy kwenye zao la korosho, katika hili kulikuwa na utaratibu na sheria ilieleza matumizi halisi ya ile export levy. Katika matumizi hayo mojawapo asilimia 65 itarudi kwa wananchi wenyewe na asilimia 35 itaenda Hazina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana naishukuru Serikali ilifanya vizuri ilitoa pembejeo za sulphur bure kwa wakulima wetu, ilitoa magunia kwa wakulima wetu bure. Lakini kisayansi tunaweza kusema kwamba siyo bure kwa sababu hakuna zao lolote la biashara ambalo linatoza export
levy. Lengo la export levy ilikuwa ni ku-discourage exportation of cashew na ku-incourage uzalishaji ubanguliwa wa korosho hapa nchini, hili lengo bado halijafa lipo kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hiki ni kizungumkuti mpaka leo hii dalili ya sulphur hakuna wala magunia na ile pesa tukitaka tuzungumze ukweli, kila mkulima katika kilo moja ya korosho anachangia zaidi ya shilingi 500 jambo ambalo ni kubwa na kwa kila mkulima ukipiga hesabu mwaka huu uliopita tumepata zaidi ya bilioni 160. Ukipiga hesabu ya asilimia 65 ya bilioni 160 inatakiwa zaidi ya bilioni 100 irudi kwenye sekta ya korosho na huko kwenye sekta ya korosho tayari kuna sheria imesema matumizi ya ile pesa inaenda kwenye utafiti, inaenda kwenye ubanguaji, inaenda kuendeleza zao lenye na hata hizi korosho wanazopanda Singida, sijui wapi, Mbeya inatokana na pesa hii ambayo inazalisha mbegu wanapelekewa wenzetu ili kuzalisha korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa hili wenzetu na wenzangu tulioko kwenye Kanda ile tunayozalisha korosho ni kilio kikubwa na usione ajabu mwaka 2020 nusu ya hao wasirudi kwa sababu wakulima wanajua kwamba asilimia 15 au dola 160 kwa tani moja inakuwa charged kama export levy. Leo tunataka kuwanyima haki yao ya kuwapa pembejeo aidha kwa ruzuku au kama tulivyofanya mwaka jana kupewa bure. Naomba sana sheria ifuate mkondo wake, export levy imeeleza kwa urahisi, vizuri namna ya kutumia ile pesa kwenye zao la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa ile siyo ya Serikali, pesa ile ni ya wakulima wa korosho. Kama nilivyosema mwanzo zaidi ya shilingi 500 kwa kilo moja imekuwa-charged kama export levy. Naomba sana jambo hili msitutwishe mzigo, wenzenu tutakuwa kwenye hali ngumu, biashara ya mwaka 2020 inataka kufia hapa kwa sababu jambo hili hakuna asiyelifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nitaweza kuongelea pamoja na hilo kwenye kilimo ni suala la ushirika. Mwaka jana nililiongea sana hapa nashukuru Serikali ni sikivu tayari imeunda Tume ya Ushirika kwa upande wa Mwenyekiti na Makamishna, lakini Tume hii inaishia mikoani, kwenye Wilaya ambako ndiko usimamizi wa ushirika upo hatuna watendaji, tunategemea watendaji ambao wameajiriwa na Halmashauri na wale wanapewa kazi kubwa ya kukusanya mapato tu ya Halmashauri, kazi ya ushirika hii hawafanyi ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa kuwa Serikali imedhamiria kufufua ushirika, basi ni vema Serikali iendeleze mtandao wa wafanyakazi mpaka maeneo ya Wilayani ili matatizo madogo yaliyotokana na mfumo wa stakabadhi ghalani inatokana na mfumo wetu mbovu wa kusimamia wanaushirika ndiyo maana tumefika hapo tulipo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nimeisifu sana hotuba ya Waziri Mkuu, imesema ina dhamira ya dhati kwenye mazao makuu ya biashara kuweka mfumo wa stakabadhi ghalani. Hakuna asiyejua ndani humu leo tunazungumza vizuri Mtwara, tunazungumza vizuri Lindi, Tunduru kwa sababu ya mfumo wa stakabadhi ghalani. Wakulima wananeemeka sana kwa bei nzuri kwa sababu ya mfumo wa stakabadhi ghalani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri Mkuu usikate tamaa pamoja na Waziri wa Kilimo. Mtwara haikuwa kazi rahisi watu kuwageuza kufika kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani. Utapata vijembe kwa sababu inakata mirija ya wale wote ambao walikuwa wanafaidika na mfumo ule holela. Naomba sana ili kumsaidia mkulima wa kahawa, tumbaku, pamba kama ilivyofanywa kule Mtwara basi mazao hayo kama dhamira ilivyo yaingie kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kuliongelea ni suala la afya. Naishukuru Serikali nimepata kituo kimoja cha afya kinaendelea kujengwa, naishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Lakini pamoja na hayo nina kata 15, katika kata 15 nina zahanati 21 na katika hizo kata 15 nina vituo vya afya vitano tu, mtu anatembea zaidi ya kilometa 15 kufuata huduma ya afya. Naomba sana hii mikoa ya pembezoni hebu tuangalieni tuna hali ngumu sana kwenye afya. Tunapakana na Msumbiji wateja wengi wanaohudumiwa na zahanati zile wanatoka Msumbiji. Kwa hiyo tunaomba sana jitihada ziendelee kufanyika kuhakikisha kwamba haya maeneo ambayo yako pembezoni yanapewa huduma za afya ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo vituo vyangu hivyo 22 kila kituo au zahanati ina watumishi wawili au mmoja. Kwa hiyo, mmoja akiugua anaenda hospitali maana yake kituo kinafungwa, mmoja akifuata mshahara mjini maana yake kituo kinafungwa. Mwaka jana alikuja Naibu Waziri ambaye sasa hivi ni Waziri kamili wa TAMISEMI Mheshimiwa Selemani Jafo aliona matatizo ya upungufu wa wafanyakazi Tunduru na alituahidi akasema mko miongoni mwa wale sita ambao mna tatizo kubwa la wafanyakazi. Ukweli afya ya Tunduru inalegalega kwa sababu hatuna wahudumu, tuna ukosefu zaidi ya wafanyakazi 700 wa afya. Sasa hili jambo ni tatizo kubwa na halileti afya kwenye utawala wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo suala la elimu, nitaendelea kushukuru elimu bure lakini nitaeleza mapungufu ambayo yamejitokeza na elimu bure. Tumesajili watoto wengi, wako madarasani, ukitembea huko vijijini utakuta darasa moja kuna madarasa mawili huku 120 huku mi120 wameweka pazia katikati. Huku wanafundisha darasa la kwanza huku wanafundisha darasa la pili, kwa kweli majengo ni tatizo. Hata hayo yaliyokuwepo yamejengwa miaka ya 1975/1970 utawala wa Nyerere, mpaka leo yanauliza tuue lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na majengo hayo vyoo ndiyo kabisa hakuna. Nyumba za walimu ni mtihani, katika hili nashukuru Mkuu wa Mkoa aliyepita alihamasisha sana ufyatuaji wa tofali katika kila kijiji kuwa na tofali laki moja. Lakini tuliwaahidi kwamba mkiwa na tofali Halmashauri itatoa fedha kununua vile vitu vya madukani, lakini kwa kuwa Halmashauri ile ni kubwa ina jumla ya kata 39 Halmashauri inashindwa. Yale matofali yanageuka kuwa kichuguu, hivi inakuwa mbogo kwetu hata unavyoenda kwenye mikutano ya hadhara swali la kwanza unaulizwa matofali haya yatatumika lini.

Kwa hiyo, naomba sana kwa kuthamini ule mchango wa wananchi wale waliofyatua tofali zile nyingi basi Serikali ione namna ya kusaidia wananchi hawa waweze kupata fedha ili madarasa, vyoo na nyumba za walimu ziweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho katika hili ni suala la afya ni suala la wagonjwa wa UKIMWI. Kama nilivyozungumza mwanzo zahanati ziko chache, vituo vya afya viko vichache hata vituo vyenyewe vinavyotoa huduma ya wagonjwa wa UKIMWI ni tatizo. Mgonjwa anatembea zaidi ya kilomita ishirini, kumi na tano kufuata dawa. Nadhani imefika mahala pamoja na kwamba misaada inapungua basi tufikirie nilisikia jana hapa kuna marekebisho ambayo yanaweza kufanyika kwenye masharti inayoonesha namna ya kutumia asilimia kumi, basi naomba katika hilo hata angalau mtakapoweka walemavu asilimia mbili au moja basi na hawa wagonjwa wa UKIMWI muwatengee asilimia moja au mbili waweze kujikimu ili waweze kufanya kazi zao vizuri, wapunguze stress za maisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii kuchangia hoja mahususi, naomba kwanza niunge mkono hoja hii. Pili, naomba niishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutimiza dhamira ya kuunganisha Mtwara na Mkoa wa Ruvuma kwa maana ya Mtwara Corridor kuhakikisha kipande kile cha Mbinga kwenda Nyasa kimeanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba jambo hili haliwezi kukamilika kama hatutaweza kuzungumzia suala la reli ya kusini ambayo inaunganisha kati ya Mtwara na Mbambabay. Ukweli uzalishaji wa makaa ya mawe Ngaka, tunapozungumzia Mchuchuma na Liganga jambo hili haliwezi kwenda sawasawa bila kuzungumzia suala la reli ya kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali, nimeona kwenye maelezo ya Mheshimiwa Waziri lakini hayaleti matumaini kwa sababu wameendelea kutafuta wawekezaji wa reli hii lakini bado tunaona speed ya kuweza kuwekeza katika reli hii bado ni ndogo. Tunaomba, tunapofikiria suala la kujenga kiwanda cha Mchuchuma na Liganga iende sambamba na ujenzi wa reli ya kutoka Mtwara mpaka Mbambabay ili kusukuma maendeleo katika ukanda wa kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zetu kwa sasa hivi kwa kweli zinaharibika sana, kwa mfano kuna malori makubwa sana yanayobeba makaa ya mawe kutoka Ngaka kwenda Dar es Salaam yanapita Songea – Tunduru –Lindi na kufika Dar es Salaam, lakini bado mengine yanapita Songea – Njombe mpaka Arusha. Jambo hili kidogo kama tungekuwa tuna reli basi barabara hizi zingeweza kudumu kwa muda mrefu, ukiona barabara ya Songea – Njombe ina hali mbaya sana, kama ni mgeni unaendesha barabara ile basi utegemee kupata ajali wakati wowote kwa sababu barabara ile ina hali mbaya, inatokana na kwamba inabeba mizigo mizito ya makaa ya mawe kutoka Ngaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nilidhani katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri angeweza angalau kuingiza suala la ujenzi wa meli katika mwambao wa bahari. Kwa kweli barabara ya Mtwara – Lindi mpaka Dar es Salaam imeharibika sana; Dangote peke yake ana magari 600 ambayo kila siku yanabeba simenti kupeleka Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, solution ya jambo hili ilikuwa ni Serikali angalau kuweka msisitizo wa kuwa na meli ya mizigo kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam ambayo ingeweza kupunguza adha hii. Naomba Mheshimiwa Waziri aende kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam ataona barabara ile jinsi ilivyoharibika kwa hali ya juu, kitu ambacho kingeweza kupunguzwa na usafirishaji wa simenti kwa kutumia meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kulizungumzia ni suala la umeme vijijini. Naipongeza Serikali kwa jitihada kubwa inayoifanya. Pamoja na pongezi hizi, umeme vijijini una dosari kidogo; baadhi ya maeneo vijiji kwa kweli vina hali mbaya, umeme haujafika. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu mpaka sasa nina vijiji vitano tu kati ya vijiji 65, kwenye awamu hii nilipewa vijiji 23 lakini mkandarasi bado hajaweza kufikisha hata vijiji nne, ukimuulizia ni suala la nguzo ambalo linasumbua. Jambo lingine ambalo linasumbua wanadai mkandarasi hajalipwa kwa muda mrefu anafanya kazi, invoice ime- raise lakini pesa bado hajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, suala la umeme kwenye Halmashauri ambayo ina majimbo mawili ina shida kidogo, utakuta Halmashauri hiyo hiyo mwenzako ana vijiji 20 wewe una vijiji viwili. Jambo hili watu wa REA wanavyopanga mipango yao ya kupeleka umeme vijijini basi waangalie maeneo ambayo yana Majimbo mawili, basi waangalie maeneo hayo wawe wanagawa vijiji kadiri inavyowezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tunapiga kelele sana kwamba vijiji na vitongoji vyote vitakuwa na umeme lakini shida iliyokuwepo wakandarasi wanapewa scope ndogo sana, ukiangalia high tension inaenda kilometa 30 mpaka 40, katikati anavyopita kuna vitongoji ambavyo havijatajwa kwenye hiyo scope. Kwa hiyo, naomba sana kwa awamu ijayo basi waangalie scope wanayopewa wakandarasi kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji mbalimbali basi iongezwe angalau vile vitongoji vilivyo katika line ile viweze kupata umeme kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuliongelea ni suala la kilimo, kama wenzangu walivyoongea, kilimo ni uti wa mgongo lakini kilimo kwa upande wa kusini (upande wa korosho) tunategemea sana mfumo wa stakabadhi ghalani. Mfumo wa stakabadhi ghalani hauwezi kufanyika bila maghala, kuna maghala ya Bodi ya Korosho yana muda mrefu sasa hivi ni mwaka wa tatu yalianza kujengwa lakini mpaka leo yale maghala hayajaweza kukamilika. Naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa jicho la huruma, tuna shida sana ya maghala katika maeneo yetu hasa upande wa Tunduru hatuna ghala la kudumu ambalo lina uwezo wa kuhifadhi korosho kwa wakati mmoja ili biashara ya mfumo wa stakabadhi ghalani iweze kufanyika kama inavyofanyika kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la maghala hata ukiangalia kwenye vyama vya msingi kwa maana ya vijijini, maghala yao mengi ni mabovu, yanavuja, yanahatarisha usalama na ubora wa mazao hasa korosho pamoja na mazao mengine mpunga, mahindi, ufuta na kadhalika. Kwa hiyo, naomba sana bajeti ijayo iangalie namna ya kusaidia angalau ujenzi wa maghala katika vijiji mbalimbali ili kupunguza adha hii ambayo inawakumba wakulima wetu kukosa mahali pa kuhifadhi mazao yetu ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda nilizungumzie ni suala la maji; maji ni uhai. Kuna siku moja nilicheka kidogo, Mheshimiwa Diwani mmoja alisema hivi tusipooga wote hapa wiki nzima tutakuwaje?

Jambo hili ni zito sana kwa sababu vijijini maeneo mengi ukame umeathiri maji, maji yamekuwa ni tatizo. Naomba angalau tuweze kuhakikisha kwamba tunapata fedha nyingi zinazoweza kuchimba visima angalau kila kijiji kipate visima vitano ama vinne, tujinyime kwa maana ya aina yoyote ile kwa sababu bila maji maisha kwa kweli yanakuwa ni magumu kwa sababu wote tunaishi kwa kutegemea maji na magonjwa mengi yanapungua kama maji yatakuwepo ya uhakika na usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana pamoja na Waziri anayehusika basi waliangalie suala la maji katika maeneo mbalimbali ya vijiji vyetu kutilia mkazo ili kuhakikisha kwamba angalau asilimia ile ya maji iongezeke ili wananchi waweze kupata maji salama ambayo ni ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo napenda nilizungumzie ni suala la TARURA. TARURA kwa kweli wana kazi kubwa lakini kazi yao inakwamishwa kwa sababu pesa wanayopewa ni kidogo ambayo haikidhi barabara ambazo tunazo/TARURA wanazimiliki. Ukichukulia mfano Wilaya ya Tunduru, ina kilometa 1,200 za barabara za vijijini ambazo zinamilikiwa na TARURA, lakini pesa wanayopewa inaweza kutengeneza kilometa 100 mpaka 200 tu, sasa sijui tutachukua miaka mingapi kuzipitia barabara hizi mpaka kumaliza maeneo yote. Kwa hiyo, naomba sana Serikali waangalie namna ambavyo wanaweza kuwaongezea pesa TARURA waweze kufanya kazi yao vizuri na waweze kuwahudumia wananchi kwa ajili ya kutengeneza barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa ni suala la afya. Naishukuru Serikali imefanya jambo jema la kuongeza vituo vya afya ambavyo vimeleta tija na matumaini kwa wananchi wetu. Jambo hili linaenda sambamba na idadi ya watumishi, mimi Jimboni kwangu tuna vituo vya afya viwili lakini kila kituo kina wafanyakazi sita/saba, jambo ambalo linakwamisha juhudi hizi za kujenga vituo vya afya vipya na vizuri na utoaji wa huduma haulingani na hadhi ya vituo vya afya ambavyo vipo kwa sasa. Kwa hiyo, naomba Serikali ifikirie suala la ajira la watumishi wa afya kuongeza ili kuhakikisha kwamba tunapunguza kero ya watumishi wa afya katika zahanati zetu, vituo vya afya pamoja na hospitali zetu za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa ni suala la watumishi upande wa elimu. Halmashauri yetu ya Wilaya ya Tunduru ina zaidi ya shule 157, ina upungufu wa Walimu zaidi ya asilimia 40 ambayo ni zaidi ya Walimu 600. Naomba Serikali iangalie namna pekee ya kuongeza idadi ya Walimu hasa kwenye shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha kwamba watoto wetu wanapata elimu iliyo bora na ambayo inaweza kuwafanya waweze kuendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuongea. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kuchangia hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu bure ukweli kabisa sera hii imezibagua shule za Kata za kutwa na zile shule za Serikali ambazo zinahudumiwa kwa chakula kwa mabweni yaliyojengwa na wananchi na watoto/wanafunzi kukaa bweni wakati shule hizo bado zinaitwa za kutwa na hawapewi fedha za kununuliwa chakula kutoka nyumbani.
Hivyo ni vema suala hili likaangaliwa upya namna ya kusaidia shule hizo zenye mabweni zipewe chakula kama nyingine za Serikali. Wapiga kura wetu wanapiga kelele juu ya ubaguzi huo wa shule za bweni za wananchi hivyo kuongeza mzigo wa michango ya chakula. Shule hizo ni nyingi sana zilizopo kwenye Kata mbalimbali nchini kuliko shule za Serikali za bweni mfano Semeni, Likumbule, Wamasakata, Walasi, Malumba na Mbega Mchiteka Wilayani Tunduru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo ya posho za likizo za Walimu na madai ya zabuni mbalimbali. Kuna madai mengi hawajalipwa walimu katika shule mbalimbali kutokana na posho za likizo, uhamisho na posho nyingine mbalimbali. Kuna chuo cha maendeleo Nandembo watumishi wanadai 7,164,000 na wazabuni wanadai 5,447,000 na wametishia kusitisha kutoa huduma zao na kuna mtumishi mmoja Saidi Salanje alifariki mwaka 2011 lakini warithi wale hawajapata mafao yao ya kiinua mgongo mpaka leo hii. Ni vema madai hayo yakashughulikiwa mapema ili kuondoa malalamiko na kero zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukarabati shule za sekondari za Serikali, majengo ya shule za sekondari Tunduru, masonya na Frank Wiston zilijengwa muda mrefu zaidi ya miaka 30 iliyopita lakini hakuna ukarabati wowote uliofanyika katika majengo na yanatishia usalama wa wanafunzi na walimu wao. Hivyo, tunaomba majengo hayo yafanyiwe ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari; Kuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa sekondari hasa wa sayansi karibu shule zote za sekondari zilizopo Tunduru na walimu wa shule za misingi takribani mia tano jambo ambalo linashusha kiwango cha ufaulu wa watoto wetu katika masomo ya sayansi. Tunaomba tupewe kipaumbele cha kupewa walimu katika ajira ya mwaka 2016/2017 ili kupunguza pengo hilo na mwaka 2015/2016 hatukupewa hata mwalimu mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa vya kufundishia tunaomba Serikali kuliingilia kati suala la vifaa vya maabara ili watoto/wanafunzi wajifundishe kwa vitendo badala ya kuwaachia Halmashauri zetu, kwa sababu uwezo wa Halmashauri nyingi kupata vifaa hivyo kwa kutumia mapato ya ndani ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuboresha walimu kimasomo. Tunaomba Serikali itoe fursa kwa walimu wa vijijini kujiendesha kielimu ili kuwapa motisha wa kazi zao za kila siku. Ni vema kuimarisha vyuo vya Ualimu ili kupewa elimu na ujuzi wa kufundishia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba ya Viwanda na Biashara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani inatakiwa ifanyiwe marekebisho kutokana na upungufu, kwani ilishindwa kumfidia mkulima pindi mzigo wake ulivyopotea katika maghala makuu. Mzigo ukipotea ghala kuu sheria inamtaka mtunza ghala amfidie mweka mali, lakini sheria haimlazimishi kulipa, matokeo yake mweka mali anakuwa anadai mali zake bila mafanikio. Hivyo ninaomba sheria hii irekebishwe ili itoe msisitizo wa mtunza ghala kulipa mara moja pindi akipoteza mzigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tozo nyingi sana zinazotolewa na Serikali pamoja na Halmashauri bila kumfahamisha tozo hizo wakati mfanyabiashara anapata leseni ya biashara. Ni vyema mfanyabishara apewe orodha ya tozo zote anazopaswa kulipa wakati anapewa leseni ya biashara. Kuna ule ushuru wa vipimo, kodi ya majengo, ushuru wa mazingira, tozo mbalimbali kama EWURA, Halmashauri na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna ukiritimba wa kupata vibali mbalimbali. Ni vyema mfanyabiashara akahudumia sehemu moja ili kuharakisha uwekezaji wa wafanyabiashara. Kwa mfano, vibali vya ujenzi, vibali vya mazingira, vibali vya Taasisi mbalimbali kama EWURA na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingi vimebinafsishwa, lakini wafanyabiashara wamebadili matumizi ya viwanda hivyo bila kujali kuwa viwanda hivyo vilijengwa kwa madhumuni fulani ili kuwezesha mazao yetu kuongeza thamani. Ni vyema viwanda hivyo vifufuliwe kama ilivyokusudiwa ili kuongeza ajira kwa vijana wetu. Tuna malighafi nyingi sana tunazalisha, lakini tunauza ghafi badala ya kuongeza thamani ya mazao hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna ucheleweshaji wa huduma mbalimbali katika vitengo vilivyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwa ni pamoja na kufumbia macho sekta ndogo ya biashara ndogo ndogo (Wamachinga) ambao wanaendesha biashara bila utaratibu maalum ambao ungewezesha kundi ili kuwa na leseni za biashara na kuiongezea mapato Serikali kupitia leseni hizo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia hoja ya Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Walemavu, Wazee pamoja na Watoto. Kwanza kabisa, napenda niwapongeze Mawaziri hawa wote wawili kwa ku-translate Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika hotuba yao iliyofanya kila mmoja asisimke. Nasi ni wajibu wetu kuchangia kuongeza nyama ili pale ambapo pamepungua waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, naungana na wasemaji wenzangu waliozungumza awali kuhusu suala la wazee; tumezungumza bima, tumezungumza suala la dirisha maalum la wazee, lakini tunaleta msisitizo mkubwa kwa sababu Ilani ya Chama cha Mapinduzi tumeinadi sana vijijini kuhusu pensheni ya wazee zaidi ya miaka 65. Katika maelezo yake au hotuba yake haijaonyeshwa vizuri ni lini program hii itaanza au ikoje ili Waziri atakapokuja atueleze hawa wazee wataanza lini kufikiriwa suala hili la pensheni ya wazee wenye umri zaidi ya miaka 65.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nitazungumzia suala la Hospitali ya Wilaya ya Tunduru. Hospitali hii ni ya muda mrefu, tangu miaka ya 1990 huko, lakini hadi hivi sasa ina majengo yaliyochakaa na mbaya zaidi hakuna wodi ya upasuaji. Wagonjwa wakipasuliwa, wakitoka theater wanachanganywa na watu wengine pamoja na madonda yao waliyokuwa nayo. Hii ni hatari, inahatarisha zaidi afya ya wale wagonjwa ambao wanafanyiwa upasuaji. Kwa hiyo, naomba Serikali ifikirie namna ya kuweza kusaidia hospitali ile kupata wodi kwa ajili ya wagonjwa ambao wamefanyiwa upasuaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru kulikuwa na chuo pale ambacho kilikuwa kinafundisha Manesi mbalimbali ambao walikuwa wanatoka vijijini, lakini chuo kile kiliungua moto zaidi ya miaka kumi iliyopita na mpaka leo majengo yale hayajafanyiwa renovation na kile chuo kimekufa moja kwa moja. Ile nafasi ambayo walikuwa wanapata vijana wa Tunduru kusoma pale na baadaye walikuwa wanaajiriwa na zahanati zetu zilizoko vijijini kwa mikataba na vijiji wakisubiri ajira ya Serikali Kuu, sasa imekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atupe majibu halisi, chuo kile ni lini kitakarabatiwa ili kiweze kuwafundisha vijana wetu ambao wanaweza kusaidia jamii zetu kwa sababu tunalalamika sana kwamba wahudumu ni wachache katika zahanati zetu na mbaya zaidi Wilaya ya Tunduru, pamoja na kuwa na zaidi ya vijiji 150, lakini kuna zahanati 49 tu, vituo vya afya vitano na gari ni moja tu ambalo lipo kwenye Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, akinamama wanatembea umbali wa zaidi ya kilometa 30 kufuata huduma ya afya, ni mbaya sana. Naomba sana, pamoja na kwamba Wizara ya Afya inatekeleza sera, naamini pacha wake ambaye ni Serikali za Mitaa, analijua hili na naomba alifahamu na ikiwezekana baadaye waweze kufika kule waangalie hali mbaya ya Wilaya ile; kwa sababu Wilaya ile ni kubwa ukilinganisha na Mkoa wa Mtwara. Wilaya ya Tunduru ni kubwa na Mkoa wa Mtwara una Wilaya tano. Naomba sana hili tufikiriwe kwa sababu tuko katika hali mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia katika hotuba hii ni suala la wafanyakazi wa ustawi wa jamii. Ni kweli ni tatizo, kama nilivyochangia katika Idara ya Kilimo, suala la ushirika linafanana sambamba na ustawi wa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara hii tumeisahau sana; watumishi ni wachache, huduma hakuna, usafiri hakuna, incentives hawapewi; sasa tunategemea vikundi vya akinamama vya maendeleo vyote vipate huduma kutoka kwa hawa watumishi wa ustawi wa jamii, lakini bahati mbaya nao wako katika hali mbaya, hoi, huduma hawapewi. Naomba sana wathaminiwe ili waweze kufanya kazi yao nzuri ya kuwasaidia ndugu zetu huko vijijini waweze kujikwamua kiuchumi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho naomba nichangie suala la upungufu wa madawa. MSD ni tatizo. Mara nyingi sana dawa nyingi zinazofika katika Hospitali, Zahanati zetu na Vituo vya Afya, zinakuwa zimepitwa na wakati. Sijajua ni kwa nini muda mwingi dawa zile zinakuwa zimepitwa na wakati. Mbaya zaidi wananchi wanasikia namna MSD wanavyoteketeza dawa ambazo zimepitwa na wakati, huku vijijini hakuna dawa. Naomba sana suala la MSD kupata dawa na kusambaza kwa wakati liwe la muhimu sana ili watu wetu wapate huduma ya dawa kwa wakati ili kufufua matumaini ya watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba sana Vyuo vya Maendeleo ya Jamii. Tunduru tuna Chuo cha Maendeleo ya Jamii, kipo pale Nandembo, lakini hakina huduma. Kwa mwaka kinafundisha chini ya watu 200. Sasa sijui maendeleo haya tunayoyataka kwa wananchi wetu wakati chuo kile hakiwezi kuchukua watu zaidi ya 200 kwa mwaka! Kwa kweli ni hatari! Tunaomba sana Serikali itilie mkazo chuo kile iweze kuwapeleka wataalam wazuri, iwapelekee fedha waendeshe program zao za kila siku ili watu wa Tunduru nao waweze kufaidika na jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba sana Serikali iangalie suala la usafiri katika zahanati zetu zilizoko na vituo vya afya ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, upungufu wa Maafisa Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ni mkubwa sana kiasi kwamba inasababisha maeneo mengi kutokupimwa kwa wakati na watu kujenga holela. Hata hivyo, wafanyakazi waliokuwepo wanashiriki kwa namna moja au nyingine na kujihusisha na rushwa kwa kupima maeneo ya wazi hata maeneo ya hifadhi ya barabara kama ilivyojitokeza kwa mwekezaji mmoja anayeitwa Cross Road Petrol Station kujenga petrol station eneo la barabara. Kwa mujibu wa mchoro wa awali sehemu hiyo iliwekwa kwa ajili ya kutengeneza junction ya barabara kuu ya Masasi - Tunduru - Songea na barabara ya Bomani jambo ambalo limesababisha mgogoro mkubwa na mkandarasi anayejenga kwa lami barabara ya Tunduru - Matemanga ambapo mwekezaji huyo anadai fidia kwa vile ana hati miliki ya eneo hilo ingawa ni sehemu ya hifadhi ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ucheleweshaji wa michoro/ramani za viwanja vilivyopimwa ni kero kubwa sana. Tangu mwaka 2012 mchoro wa viwanja vilivyopimwa bado haujarudi kutoka Wizarani ili walionunua viwanja waanze kutafuta hati ya viwanja vyao. Kwa hiyo, ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Tunduru. Mimi nikiwa mmojawapo nimeshindwa kupata mkopo kwa kukosa hati ya nyumba yangu kwa vile mchoro bado haujapitishwa na Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, tatizo la viwanja vilivyopimwa kupewa watumishi badala ya wananchi wa kawaida. Watumishi hao baadaye huviuza viwanja hivyo kwa bei ya juu kwa wananchi wa kawaida wakati wao wamevinunua kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, mipaka ya vijiji inavunjwa sana na watumishi wa ardhi kwa kusogeza na kutoa beacon zilizowekwa wakati vijiji hivyo vimeanzishwa na kusababisha migogoro ya kijiji na kijiji. Kwa mfano kijiji cha Namasalau na Kitando, Semli na Chikomo/Mchesi/Muungano suala hili limeleta ugomvi wa wakulima kwa wakulima kutokana na Ofisi ya Ardhi kutotoa ramani za awali za vijiji hivyo. Hivyo, ni vyema Ofisi ya Ardhi wakatoa ramani ya Wilaya ya Tunduru kwa kila kijiji ili wajue mipaka yao ya awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, mikopo ya nyumba kwa wafanyakazi. Mikopo mingi ya mabenki kwa wafanyakazi inatolewa kwa walio Dar es Salaam tu, wa mikoani ni wachache sana ambao wanafanikiwa kupata mikopo hiyo. Hivyo ni vyema Serikali ikasimamia mabenki waweze kukopesha wafanyakazi waliopo mikoani na wilayani ili waweze kujenga sehemu za kuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, Shirika la Nyumba ya Taifa lijielekeze kujenga nyumba wilayani na mikoani ambako mahitaji ya makazi kwa ajili ya wafanyakazi ni makubwa sana. Shirika lijielekeze huko badala ya kuendelea kujenga nyumba Dar es Salaam na miji mikuu ya majiji na manispaa pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, nashauri Wizara iondoe wafanyakazi wasio waadilifu wanaotoa hati mbili katika kiwanja kimoja; wanaopima maeneo ya wazi na kubadilisha matumizi bila utaratibu; wanaodai rushwa ili kuwapa huduma wananchi ya kupatiwa hati ya viwanja vyao kwa mkoani na wilayani. Pia kupata hati ya kiwanja ni gharama kubwa sana na inachukua muda mrefu sana, naomba nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nane, maeneo yanayochukuliwa na Halmashauri wananchi walipwe kutokana na thamani ya ardhi kwa wakati huo badala ya kuangalia mazao pekee yaliyoko kwenye kiwanja hicho.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kuchangia hoja katika hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika eneo la environmental assessment katika miradi mbalimbali ya uwekezaji wa viwanda na hasa vituo vya mafuta ya petrol (petrol stations). Kuna tatizo kubwa sana juu ya upatikanaji wa vyeti vya mazingira katika miradi mbalimbali ya uwekezaji kutokana na mlolongo mrefu unaotokana na upungufu mkubwa wa wataalam wa mazingira katika halmashauri zetu za wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mlolongo mrefu wa masharti ya kutimiza katika kuandaa andiko la mazingira kwenye mradi unaofanywa hutengeneza mazingira ya rushwa kubwa kwa wafanyakazi wa Idara ya Mazingira ili vyeti vya mazingira vipatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo nyingi na faini kubwa zinazotolewa bila kufuata sheria za mazingira, wakati mwingine vitisho vingi na vikubwa vinavyotolewa na watumishi/wanaohusika na mazingira katika kuhalalisha rushwa inayoambatana na gharama kubwa ya kulipia ili kupata certificate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bureaucracy katika kupatikana kwa vyeti vya mazingira inayochukua muda mrefu, jambo ambalo linakatisha tamaa wawekezaji na hatimaye kuacha kabisa kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ufanyike kila halmashauri kuwa na wataalam wa mazingira ili kurahisisha tathmini za mazingira kwenye halmashauri zetu. Ni vyema kuwa na kiwango cha mradi kinachotakiwa kusainiwa na Waziri ili kuruhusu vyeti vingine viweze kutolewa katika ofisi za mikoa badala ya kutegemea kila cheti kusainiwa na Waziri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu itolewe kwa wadau mbalimbali wa mazingira kabla ya kuwapa adhabu/faini ili kutoa fursa kwa wadau kutekeleza miradi yao kwa mujibu wa mahitaji ya masharti ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoa masharti ya jumla ya mazingira katika kuanzisha miradi ya uwekezaji hasa petrol stations katika ofisi ya halmashauri, ili kuondoa usumbufu kwa wadau wa mazingira pindi wanapoanzisha miradi ya uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama/faini za mazingira ziangaliwe upya ili kurahisisha wadau wengi wa mazingira kuweza kuzilipa bila kikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali umekuwa ni wa kutisha sana, hivyo ni vyema kuimarisha Kitengo cha Mazingira katika Halmashauri mbalimbali za Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, semina mbalimbali zitolewe mpaka vijijini ambapo uharibifu wa mazingira umekuwa mkubwa kutokana na shughuli za uchumi kama ufugaji, kilimo na uwindaji. Semina hizi zitasaidia wananchi kuona umuhimu wa kuhifadhi mazingira ili kuzuia tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Mazingira yaimarishwe katika kata ili kuepusha na kusimamia vyema uharibifu wa mazingira usiendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya magogo imekuwa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira kwa kushirikiana na TFS, biashara hii ipigwe marufuku kwa kuwa inaathiri sana mazingira.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia bajeti hii ya Serikali. Katika mchango wangu kwanza naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, nitaongea maneno mawili matatu kuhusiana na kilimo, ushirika pamoja na tozo za zao la korosho katika maeneo yale ambayo yanalima korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kuzungumzia suala la ushirika ninaamini Sheria Na. 6 ya mwaka 2013 ilianzisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika, lakini katika bajeti yetu ya kilimo ipo chini ya asilimia tano, sidhani kama Tume hii ya Maendeleo ya Ushirika imepewa kipaumbele kwa ajili ya kuendeleza wakulima wetu, kwa sababu wakulima walio wengi vijijini wanategemea sana ushirika ili kupata masoko ya mazao yao pamoja na pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutegemea huko, jambo kubwa lililopo kwenye Tume ya Ushirika, ninaomba Serikali tangu sheria hii imeanza huu ni mwaka wa tatu Tume ile haina Mwenyekiti wa Tume imekuwa ni jina peke yake, Makamishna hawapo. Naomba sana katika bajeti hii iangalie namna ya kuiwezesha Tume hii iweze kufanya kazi kwa kuteua Mwenyekiti wa Tume ya Ushirika na kupata Makamishna wake ili waweze kusimamia ushirika usimame vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna matatizo mengi sana ya ushirika, lakini yanatokana na uongozi kukosa viongozi walio imara katika Idara ya Maendeleo ya Ushirika. Pamoja na hilo watumishi waliopo kwenye ushirika ni wachache, ninaomba sana kwa sababu tunapitisha bajeti hii basi waliangalie namna ya kuongeza watumishi kwenye Idara hii ya Tume ya Ushirika ili waweze kusimamia Vyama vyetu vya Ushirika viweze kufanya kazi vizuri. Kwa mfano, vyama vya Mkoa wa Mtwara, Lindi, Pwani Ruvuma ambavyo vinajihusisha na shughuli za biashara ya korosho vinatumia zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya biashara ya korosho, usimamizi haupo makini kwa kuwa Maafisa Ushirika wamekuwa ni wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba wanaongeza watumishi walio na elimu ya ushirika pamoja na uwezo wa kufanya na kusimamia ukaguzi wa vyama vya ushirika mara kwa mara, kwa sababu vyama hivi vina-transact fedha nyingi sana kinyume na Sheria ya Fedha inavyotaka. Vyama vyetu vya Msingi viongozi walio wengi ni darasa la saba, mtu wa darasa la saba anafanya transaction ya shilingi bilioni mbili, bilioni tatu! Kwa kuwa Maafisa Ushirika ndiyo wasimamizi tunaomba Maafisa Ushirika wenye taaluma ya kusimamia na kukagua vyama hivi vya msingi waajiriwe waweze kuendelea kusimamia vyama hivi ili tupunguze malalamiko ya watu na wakulima wengi huko vijijini hasa kwenye Mikoa ya inayozalisha korosho na Mikoa inayozalisha tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja naomba niende kwenye tozo ya zao la korosho kama ilivyopendekezwa katika bajeti hii. Nakubaliana kwenye mchakato wa kutoa tozo katika unyaufu. Nimekuwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani zaidi ya miaka nane, mfumo ulivyoanza kulikuwa na tozo 17, taratibu namna utendaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani ulivyoendelea zimepunguza zile tozo mpaka zikafikia saba kwa umuhimu wake ili kuweze kumsaidia mkulima aweze kupata hela yake. Kwa mapendekezo yaliyojitokeza naomba nieleze yale ambayo ninayaona mbele ya safari yataleta mkanganyiko katika kutekeleza mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni suala la ushuru wa kusafirisha korosho wa shilingi 50. Mfumo wa stakabadhi ghalani unataka ghala lolote lenye uwezo wa kuhifadhi kwa wakati mmoja tani 200 uweze kupewa kibali cha kuhifadhi korosho. Maghala yetu yaliyopo vijijini mengi yapo chini ya uwezo huo. Mbaya zaidi ubora wa yale maghala hauruhusu kuifadhi korosho kwa muda mrefu; mbaya zaidi maghala yale hayana umeme, ni vumbi tu, hakuna chochote ambacho kinaweze kustahili kuweka korosho kwa muda mrefu ili mfumo wa stakabadhi ghalani uweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo tunalalamika wataalam wa ugani hawapo katika maeneo mengi, kwa kuhakiki ubora kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani tunahitaji Maafisa Ugani katika kila Chama cha Msingi. Katika sekta ya korosho kuna vyama 739 ambavyo vinajihusisha na biashara ya korosho, kwa hiyo, tunahitaji Maafisa Ugani 739 ili kuhakikisha kila chama kinakuwa na Mhakiki Ubora ambao utasadia kuhakikisha zao linakwenda v izuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi tunahitaji kipimo kinachotumika kupima ubora wa korosho kwa content ya moisture na nut counting pamoja na ubora wenyewe wa korosho kama ilivyo kile kipimo kinauzwa shilingi milioni sita kwa bei ya mwaka 2014/2015 tulinunua shilingi milioni sita, tunahitaji vipimo 739 kwa kila chama cha msingi ili viweze kuhakiki huu ubora. Kwa matatizo haya naamini kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani ukihamia kwenye maghala ya chama cha msingi moja kwa moja tayari tutawakaribisha Wahindi waende moja kwa moja kwenye maghala ya vyama vya msingi wawe wanatembea na moisture meter yao na watakuwa tayari kuwadanyanya wakulima wetu matokeo yake bei ya korosho itakuwa imeshuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kuondoa tozo hii maana yake tunaondoa wakulima kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani. Sambamba na hilo usimamizi wote unaofanyika kwenye vyama vya msingi unafanywa na Chama Kikuu kwa sababu Chama Kikuu ndicho chenye wahasibu…
Mheshimiwa Naibu Spika, ooh! Ahsante, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuchangia hotuba hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Tunduru kuna hifadhi kadhaa za misitu ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Selous iliyopo Jimbo la Tunduru Kaskazini pamoja na Hifadhi ya Misitu ya Mwambesi, Muhesi na kadhalika. Mwaka huu tembo wamekuwa wakipita katika hifadhi hizo na kuzagaa katika vijiji mbalimbali kama Mtina, Angalia, Mchesi, Kazamoyo na Kalulu na kuharibu mazao ya wananchi na wanadai malipo ya uharibifu huo wa tembo bila mafanikio. Kumekuwa na malalamiko mengi ya wakulima ambayo hayajafanyiwa kazi na Idara ya Wanyamapori, wanyama hao wanasumbua sana hivyo kuna uhitaji mkubwa wa watumishi wa Idara ya Wanyamapori ili kusaidia kufukuza wanyama hao waharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Tunduru Kusini kumekuwa na kero kubwa ya fisi kuua watu. Mpaka sasa watu wawili wameuawa na fisi na watu wawili wameuawa na mamba katika Mto Ruvuma na wawili wamejeruhiwa lakini utaratibu wa kulipwa fidia unachukua muda mrefu. Mpaka sasa wahanga hao hawajalipwa, mbaya zaidi majibu wanayopewa yanawakatisha tamaa. Ni vyema utaratibu wa kuwalipa wahanga hawa wa wanyamapori ukafanyiwa marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TFS inashirikiana na Watendaji wa Vijiji kukata miti/magogo bila kufuata utaratibu wa kisheria na wanashirikiana na wafanyabiashara kukata miti hovyo bila kufuata utaratibu. Kwa mfano, katika Kijiji cha Semeni na Muungano, mfanyabiashara mmoja amekata magogo bila ridhaa ya mikutano mikuu ya vijiji hivyo na hata ushuru wa vijiji hivyo haujalipwa na kuna mgogoro mkubwa unafukuta na wanataka viongozi wa Halmashauri wa Kijiji na Mtendaji kupelekwa mahakamani. Hivyo, TFS inamaliza misitu ya Tunduru kwa kuruhusu magogo na mbao kukatwa hovyo bila kufuata utaratibu wa kisheria na sasa wanakata magogo Kijiji cha Machemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya hifadhi za misitu na wakulima. Ni vyema mipaka ya hifadhi hizo ikaangaliwa upya ili kutoa maeneo kwa wakulima kutokana na ongezeko la watu mfano Muhesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wa hifadhi na wanyamapori kutumia nguvu kubwa kuwanyanyasa watu kwa kuwapiga, kuharibu mazao yao, kuwanyang‟anya vitu vyao bila makosa. Ni vyema wakatumia ustaarabu katika kuwaelimisha wakulima badala ya kutumia nguvu. Ni vyema sheria ikatumika zaidi badala ya nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Operesheni Tokomeza. Jambo hili limekuwa mradi wa watu kwani kila mwaka wanaokamatwa ni watu walewale, wanateswa, wanapigwa, wanatoa rushwa ili waachiwe bila kupelekwa mahakamani. Ni vyema basi watuhumiwa wote wapelekwe mahakamani wakachukuliwe hatua badala ya kila mwaka wanakamatwa, wanateswa, wanawekwa ndani, wanatoa rushwa, wanaachiwa bila kuwapeleka mahakamani. Jambo hili linasababisha wananchi kuichukia Serikali yao bila sababu. Inaonekana kuwa umekuwa mradi wa watu fulani badala ya kufuata utaratibu. Ni vyema utaratibu wa kisheria ukafuatwa na haki za binadamu zikazingatiwa zaidi. Hakuna anayependa uharibifu unaofanywa, bila kuwachukulia hatua makundi mengine yanajitokeza, ila wakifungwa watu wataogopa kujishirikisha na biashara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kutenga maeneo ya hifadhi ni vyema elimu na mikutano ikafanyika katika vijiji husika ili kuondoa migongano na migogoro ya kutoelewa manufaa ya misitu. Naamini wananchi wakipewa elimu migogoro hii itapungua kwa kiasi kikubwa na hifadhi zisaidie vijiji vinavyopakana ili kutoa imani na nguvu ya watu wa maeneo hayo kulinda hifadhi hizo. Hifadhi zikisaidia vijiji jirani vijiji vingine vitahamasika katika kuanzisha hifadhi zao ili kupata manufaa wanayopata wenzao.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kama ifuatavyo:-

(i) Katika hospitali ya Wilaya ya Tunduru kuna tatizo la chumba cha kuhifadhi maiti cha kisasa na katika hospitali ile hamna wodi ya kulaza wagonjwa waliofanyiwa upasuaji, wagonjwa hao hulazwa katika wodi ya magojwa mchanganyiko kitu ambacho kina hatarisha afya ya wagonjwa hao.

(ii) Katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina kata 39 lakini kuna vituo ya afya vitano tu jambo ambalo linasababisha wananchi wanapata shida kutembea kilometa ndefu kufuata huduma za afya.

(iii) Katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna Hospitali ya Mission ya Mbesa ambayo inahudumia wananchi zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wa Tunduru na Wilaya jirani ya Namtumbo. Hospitali hii ina madaktari wanne tu, kati yao wawili ni wazungu ambao mkataba wao unaisha mwezi Juni, 2017. Hivyo naomba Serikali ipeleke madaktari kulingana na mkataba wa Serikali na hospitali hiyo.

(iv) Katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru tuna upungufu mkubwa wa wafanyakazi katika sekta ya afya. Zaidi ya wafanyakazi 700 wanahitajika ili kukidhi mahitaji ya zahanati zilizopo. Tunaomba sana ajira zitakapotangazwa tuangaliwe kwa jicho la huruma ili kututengea wafanyakazi katika sekta hii ili kunusuru wananchi wa Wilaya ya Tunduru.

(v) Kuna upungufu mkubwa wa dawa katika zahanati, vituo vya afya kwa ajili ya kuhudumia wananchi wetu, sambamba na upungufu wa vifaa tiba ikiwa ni pamoja na kukosekana kabisa kwa ambulance katika vituo vyetu vya afya ukizingatia Wilaya ya Tunduru ni eneo kubwa sana, wananchi wanatembea zaidi ya kilometa 100 kufuata Hospitali ya Wilaya, watu wanabebana kwenye matenga, akina mama wajawazito wanabebwa kwenye matenga kufuata huduma za afya.

(vi) Serikali ya Awamu ya Nne iliahidi Hospitali ya Mission Mbesa kuwa Hospitali Teule kwa vile inahudumia wananchi wengi sana hasa wa hali ya chini wa Tunduru na Namtumbo. Ninaomba basi ahadi ile itekelezwe ili kupandisha hadhi hospitali ile kuwa Hospitali Teule kama ilivyoahidiwa na Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

(vii) Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 tumeahidi kutoa posho kwa wazee wenye umri zaidi ya miaka 65, mpango huu utaanza lini ili kusaidia wazee hawa kupambana na hali ngumu ya maisha inayokabili wananchi?

(viii) Uboreshaji wa vituo vya afya katika kituo cha Mtina, Mchoteka, Nkade ili viweze kufanya upasuaji wa kawaida, mpaka leo vituo hivyo havina vyumba vya upasuaji, wananchi wanapata huduma hiyo Hospitali ya Mbesa au Hospitali ya Wilaya. Hivyo tunaomba tupatiwe vyumba vya upasuaji katika vituo vyetu vya afya na kuongeza vituo vingine vya afya kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naunga mkono hoja ya mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018. Pili, napenda kutoa mapendekezo au ushauri wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo liangaliwe kwa upana zaidi ili kumsaidia mkulima kupitia vyama vya ushirika waweze kusaidiwa kwa urahisi zaidi kwani takribani asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima. Hivyo, ili kuwahudumia vizuri inapaswa kuangalia chombo chao kinachowaunganisha kupitia vyama vyao vya ushirika vya mazao ili aweze kupata huduma kwa urahisi zaidi wakiwa pamoja kama elimu ya kilimo biashara, matumizi bora ya mbegu za mazao yao, kupata mikopo kupitia mabenki kwa kutumia vyama vya ushirika na mashamba yao kama dhamana ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia pembejeo za kilimo zipatikane kwa urahisi na kwa wakati ili wakulima waweze kuendana na msimu wa kilimo ulivyo katika maeneo mbalimbali. Vilevile aina ya pembejeo kwa kila eneo izingatiwe zaidi kulingana na udongo wa maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ujenzi wa maghala bora ya kuhifadhia mazao ni muhimu katika maeneo ya vijijini na Hifadhi ya Taifa ya Chakula kwa kuwa baada ya kuvuna vyakula hivyo ni vyema vikahifadhiwa vizuri kwa matumizi ya kipindi kijacho ambapo uzalishaji hamna. Ni vyema basi Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2017/2018 ukazingatia ujenzi wa maghala haya kwani kwa mfano maghala ya Hifadhi ya Taifa ya Songea mahindi mengi yapo nje ambapo yana hatari ya kuharibika katika kipindi cha mvua, asilimia 50 ya mahindi yamehifadhiwa nje maghala yamejaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuimarisha ushirika na mazao ni vyema basi Mpango wa Maendeleo wa Taifa ukatilia mkazo wa kuimarisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kuiwezesha kifedha. Ni vyema Tume hii ikaimarishwa kiutaalam katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Halmashauri za Wilaya kwa kuongeza watumishi wenye uwezo wa kusimamia ushirika na kurudisha imani ya wakulima kuamini vyama vyao vya ushirika. Ni vyema Makamishna wa Tume ya Ushirika wakateuliwa ili kuipa nguvu Tume hii kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kuimarisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika, ni vyema kuimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kwa kukiongezea uwezo kifedha na watumishi ili wapate muda wa kukagua vyama vya ushirika kila mwaka kwa maendeleo ya ushirika na wakulima wetu. Karibu wakulima wote wa Tanzania kwa njia moja au nyingine wanahudumiwa na ushirika wa mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu soko la mazao yetu, ni vyema Serikali ikasisitiza kuuza mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kama inavyofanyika katika mikoa inayolima korosho ambapo mafanikio makubwa yanaonekana kwa wakulima wa Mkoa wa Lindi na Mtwara na imehakikishia Halmashauri zetu kuwa na uhakika wa kupata ushuru wa mazao kupitia mfumo huu. Mkulima anakuwa na uhakika wa kupata malipo yake ya mazao kupitia mfumo rasmi wa kiuchumi. Naiomba Serikali kuangalia uwezekano wa mazao yote ya biashara na chakula kuingia katika mfumo huu kwani unaruhusu wanunuzi kushindana katika bei.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naunga mkono hoja ya mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ni kuhusu fidia ya watu wanaouawa na kujeruhiwa na wanyama wakali kama mamba katika kijiji cha Makaule na Kazamoyo Tunduru. Watu waliouawa na fisi katika kijiji cha Jiungeni na Mchesi Wilaya ya Tunduru bado hawajalipwa fidia hadi leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia kwa watu walioharibiwa mazao yao na wanyama wakali hasa tembo katika kijiji vya Mchoteka, Wenje, Likweso, Walasi, Nasomba, Kazamoyo, Lukumbule, Makande, Mtina, Angalia, Malumba, Misyaji na maeneo mengine ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru hadi leo hawajalipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro wa mipaka na hifadhi katika kijiji cha Misyale na Ukala, ambapo askari walizoa vyakula vya wananchi wanaolima katika maeneo ya hifadhi na kuuza bila kuwachukulia hatua za kisheria. Maeneo mengine yenye migogoro ni Hifadhi ya Misitu Misedula na kijiji cha Msinji katika kata ya Ligoma. Ni vyema baadhi ya maeneo yakagawiwa kwa ajili ya kilimo na huduma za jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kuna vivutio vingi sana ambavyo vinaweza vikatangazwa na kutembelewa na watalii na kuliingizia Taifa pato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TFS wanamaliza misitu kwa kutoa vibali ovyo vya mbao na uvunaji wa magogo bila kujali athari za mazingira. TFS wana mahusiano mabaya na wananchi waliopo karibu na hifadhi za misitu. TFS wameshiriki kuhujumu misitu karibu maeneo yote yenye hifadhi za misitu. Misitu ya asili inaisha kama TFS hawataacha kulinda vizuri misitu yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. DAIMU I. MPAKATE Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi siku ya leo kuchangia hoja ya hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza naunga mkono kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuunga mkono nataka nianzie kwenye jambo la vijana, Serikali imeagiza Halmashauri zetu kutoa asilimia tano kwa vijana na asilimia tano kwa akinamama, jambo hili kiutekelezaji bado linaendelea kuwa gumu, maeneo mengi Halmashauri zetu hawatekelezi ipasavyo kwa hiyo, inasababisha kudumaa kwa maendeleo katika maeneo yetu ambayo tunatoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wazee kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi tulihubiri sana. Suala la posho ya wazee zaidi ya miaka 65, lakini mpaka leo utekelezaji wake bado haujaonesha dalili kwamba jambo hili litafuatiliwa na wazee wetu kuanza kupewa posho kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la elimu katika maeneo mengi tunashukuru kiasi ambacho kinatolewa na Serikali kwa ajili ya kuwapinguzia mzigo wazazi, lakini changamoto kubwa tunayopambana nayo katika maeneo yaliyokuwa mengi, hasa Jimboni kwangu, ni juu ya uchakavu wa majengo ya madarasa ya shule za msingi na sekondari katika maeneo karibu yote yaliyopo katika maeneo ya Jimbo langu. Shule hizi zilijengwa miaka ya 1975, 1970, 1980, zilizo nyingi zina umri mkubwa, pengine Wabunge wengine humu ndani walikuwa bado hawajazaliwa, kama ilivyo mdogo wangu Mheshimiwa Goodluck.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa majengo yale yamechakaa, yanapaswa tena kutokana na ongezeko la wanafunzi lilivyo, tuongeze mapya na haya ya zamani yaweze kukarabatiwa ili yawe na hadhi ya kuweza kusomesha watoto wetu katika madarasa yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna upungufu mkubwa sana wa walimu, hasa katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Tunduru tuna upungufu mkubwa wa zaidi ya walimu 650 ambao wanapaswa kuwepo katika madarasa kwa sababu maeneo mengi katika shule zangu za msingi walimu hawazidi wanne, watatu, shule chache zina walimu watano mpaka sita. Jambo hili linairudisha sana Halmashauri yetu ya Tunduru kielimu kwa kuwa watoto wamekuwa wengi
lakini kuna upungufu wa walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, walimu wa awali kwa ajili ya madarasa ya awali hakuna kabisa, anachukuliwa mtu ambaye ana idea kidogo anaenda kufundisha, naomba Serikali ione umuhimu wa kuwafanya walimu wa awali waweze kupata mafunzo, waweze
kuwafundisha watoto wetu ili waweze kuwahudumia ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuliongelea zaidi ni suala la afya katika maeneo yetu. Kwa kweli kuna upungufu mkubwa wa zahanati katika Jimbo la Tunduru Kusini na Jimbo la Tunduru kwa ujumla. Jimboni kwangu kuna vijiji 67, lakini ni vijiji 24 tu ambavyo vina zahanati. Pamoja na kuwepo zahanati hizo 24 bado watumishi katika zahanati hizo ni wachache sana. Kuna watumishi wasiozidi wawili kila zahanati jambo hili linatia doa sana kwa wananchi wetu kwa sababu wanashindwa kupata huduma ile kwa uhahika zaidi kwa sababu idadi ya watumishi katika zahanati hizo imekuwa ni ndogo kwa hiyo, hawapati ile huduma inayotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru tuna Hospitali moja ya Mbesa ambayo miaka ya nyuma, wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, Rais aliahidi hospitali hiyo kuwa hospitali teule kwa niaba ya watu wa Tunduru Kusini. Hospitali ile
inahudumia asilimia 80 ya wakazi wa Wilaya ya Tunduru na Halmshauri yake, lakini idadi ya waganga wako watatu tu.
Naomba Serikali kulingana na mikataba iliyokuwepo na Hospitali ile ya mission basi itekelezwe kuongeza ikama ya idadi ya wafanyakazi wanaotakiwa katika hospitali ile ili waweze kuhudumia watu wetu wa Tunduru kwa ujumla na Wilaya ya jirani ambayo inategemea hospitali ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuliongelea, ni suala la kilimo. Tumepiga kelele sana ndani humu, jambo la pembejeo, katika hotuba ya Waziri wa kilimo mwaka jana, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alizungumzia suala la pembejeo kuuzwa madukani kama soda, ninaomba Serikali ituambie imekwama wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa ruzuku unatugombanisha wakulima na Serikali yao, inagombanisha wakulima na Wabunge, Unagombanisha wakulima na Madiwani, kwa sababu wale wanaochaguliwa kupewa zile ruzuku wanakuwa ni wachache kulingana na idadi ya kaya
zilizopo katika kila kijiji. Naomba sana, mpango ule ulikuwa ni mzuri, kila mtu atakayekuwa na uwezo ataenda kununua pembejeo ile dukani kulingana na hali ilivyo. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikafikiria namna ya kutoa ruzuku katika viwanda vyetu vinavyozalisha pembejeo ili viweze kutoa asilimia 100 kwa pembejeo zote zinazozalishwa katika viwanda vile na kusambazwa kwa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukazungumzia wakulima ukaacha kuzungumza suala la ushirika. Ushirika huko vijijini ndiyo unaosaidia sana wakulima wetu katika maeneo yaliyokuwa mengi. Hata walio wengi, Wabunge na Madiwani, wametokea katika sekta hii ya ushirika, lakini bado kuna jambo ambalo linafanywa, Serikali bado haijaweza kuiimarisha Tume ya Ushirika ili iweze kufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba Serikali ihakikishe Tume hii inapewa meno kwa kuipa viongozi wanaotakiwa kwa maana ya Mwenyekiti wa Tume na Wajumbe wake ili waweze kusimamia ushirika huu uweze kufanya kazi vizuri. Mbili, naomba Serikali ihakikishe kwamba,
watumishi wa Tume wanaenea kutoka Mikoani mpaka Wilayani ili kuhakikisha kwamba wanasimamia ushirika ipasavyo, wakulima waweze kupata tija katika mazao yao wanayozalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta kwamba kwa mfano sekta ya korosho wanaushirika wengi wanajiendesha bila usimamizi wowote, hata kama ni mtoto wako umempa ndizi kila siku anaanza kuuza sokoni, anakaa mwezi mzima hujamtembelea ukajua amepata shilingi ngapi, siku ukimuuliza atakupa majibu ambayo hayataendana na wazo lako amepata kiasi gani kwa muda huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili linaendana pamoja na ushirika, tunawatumia hawa kwa muda wote, lakini kwa sababu wamekosa usimamizi wa biashara yao kwa muda wa miezi mitatu, minne tunaporudi kuwahakiki tunakuta kuna matatizo mengi, wakulima wanakosa malipo yao bila maelezo ya kutosha kwa sababu Maafisa Ushirika wa kusimamia zao hili la korosho wanakuwa ni wachache kwa kipindi kile cha msimu wa korosho wanashindwa
kuwasimamia kuhakikisha kwamba pesa wanayopelekewa inanunua korosho kama ambavyo imekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo ningependa sana niliongelee ni mgawo wa maeneo ya utawala. Tunduru ni kubwa sana, inalingana katika eneo la ukubwa na Mkoa wa Mtwara na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imeanza tangu 1905. Mkoa wa Ruvuma naamini
ndiyo Halmashauri ya kwanza, lakini kuna Halmashauri tano, saba zimezaliwa Tunduru iko palepale. Kutoka eneo moja mpaka lingine naamini Naibu Waziri wa TAMISEMI amefika pale ameona. Kutoka mwanzo mpaka mwisho kilometa 200 unatembea mtu anatafuta huduma kwa ajili ya Halmashauri yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba maombi yetu yafikiriwe tuhakikishe kwamba, Majimbo yote mawili yanakuwa na Halmashauri zinazojitegemea ili tuweze kuwahudumia watu wetu kwa haraka. Kwa sababu tunavyozungumza zahanati kama nilivyozungumza mwanzo ziko 24, mtu anatembea zaidi ya kilometa 30 hadi 40 kufuata huduma za afya. Utapozungumza hospitali ya Wilaya iko zaidi ya kilometa 80 hadi 100 ili kuipata hospitali hii. Mkitugawia maeneo haya mambo mengine haya zahanati, hospitali ya Wilaya itakuwa rahisi zaidi kuwahudumia wananchi wetu. Naomba sana Serikali iweze kufikiria mgawo huu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili tuweze kuwahudumia wananchi wetu kwa uzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho kabisa suala la barabara. (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa maelezo yangu ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kuna uwanja wa ndege ambao kwa sasa umezuiliwa kutumika kwa kuwa upo katika Kata ya Mji. Halmashauri imetenga eneo lingine la kujenga uwanja wa ndege. Hivyo tunaomba uwanja ule wa zamani upewe Halmashauri ili kujenga majengo ya huduma za jamii. Kwa kuwa eneo la Hospitali ya Wilaya limebana sana, hilo eneo linaweza kutumika kuongezea eneo la Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo ya Halmashauri ya Wilaya limebana, hivyo sehemu ya uwanja huo inaweza kusaidia Halmashauri ya Wilaya kuongeza majengo kwa ajili ya kutolea huduma. Magereza nao eneo limebana sana kiasi kwamba hawana uwezo wa kujenga chochote. Hivyo eneo hili litasaidia Magereza kupata eneo la kuongeza majengo hasa nyumba za Askari wa Magereza na nyumba za Askari Polisi. Hivyo, tunaliomba sana eneo hili likabidhiwe kwa Halmashauri ili litumike kuongeza majengo mbalimbali ya Halmashauri na Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tunduru Kusini imepakana na Msumbiji kupitia Mto Ruvuma, maeneo mengi ya Vijiji hayana huduma ya simu. Maeneo hayo ni Makade, Msinji, Semei, Chikomo, Lukala, Misyaje, Mbati, Nasumba na Likweso. Naomba sana maeneo hayo yajengewe minara ya simu ili iwe rahisi kuwasiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la usikivu wa redio katika Wilaya ya Tunduru TBC, haipatikani kabisa. Hivyo tunaomba mdau aliyejitokeza kuweka Kituo cha Redio Tunduru, apewe frequency haraka ili wananchi wa Tunduru wapate huduma ya redio, kwani ni muda mrefu sana anapeleka maombi lakini hajapewa kibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara, Jimbo la Tunduru Kusini lina barabara kuu inaunganisha na Wilaya ya Namtumbo kutokea Mtwaro – Pachani – Lusewa – Lingusenguse – Nalasi mpaka Tunduru Mjini. Nashukuru kwa kipande cha Mtwaro – Pachani mpaka Nalasi, kipo katika mchakato wa upembuzi yakinifu. Hivyo naomba kipande kilichobaki cha Nalasi – Mbesa Tunduru chenye urefu wa kilomita 64 nacho kiingie kwenye mpango huu wa kufanya upembuzi yakinifu, tayari kwa kujengwa kwa kiwango cha lami kwani kipande hiki ni korofi na kinasumbua sana wakati wa kifuku na Tarafa hii ndiyo yenye idadi kubwa ya watu ambao wanatumia barabara kufuata huduma za kijamii Tunduru Mjini. Barabara hii ndiyo inayotumiwa na wananchi wa Tunduru kwenda kwenye Hospitali ya Mission Mbesa ambayo inahudumia zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wa Wilaya ya Tunduru pamoja na Wilaya jirani ya Namtumbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Njombe – Songea ina umri wa zaidi ya miaka 30 tangu ianze kutumika na sasa imechakaa sana, ina viraka vingi ambavyo vinaweza kusababisha magari kupata ajali. Barabara hii inapaswa ijengwe upya kwa kuwa ni muda mrefu sana na imechoka sana na sasa magari yanaumia sana kutokana na ubovu wa barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mji wa Tunduru kuna eneo la makutano ya barabara inayotoka Masasi na Songea (cross road). Mahali hapa panatakiwa kujenga round about, lakini kuna sheli imejengwa hapo kimakosa, kwa sababu ipo ndani ya eneo la barabara. Hivyo tunaomba sheli ile ibomolewe na ijengwe round about, kwa sababu eneo hili limejengwa vibaya na linasababisha ajali za mara kwa mara na kusababisha vifo kutokana na makutano haya kujengwa bila mpangilio wa kiusalama kwa watumiaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, washauri wa mgambo hawatendi haki katika kuchukua vijana wanaojiunga na JKT na wengi wao wanatuhumiwa kuchukua rushwa kwa kuwapa vijana nje ya eneo la Wilaya husika. Jambo hili linachafua jeshi letu. Hatua ichukuliwe kuchunguza mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tunduru Kusini inapakana na Mto Ruvuma na Msumbiji lakini eneo lote la mpaka huu hakuna ulinzi wowote wa jeshi na wala hamna mawasiliano yoyote ya simu jambo ambalo ni hatari kwa nchi. Hata ile barabara ya mpaka ambayo ilikuwepo miaka 1970 na 1980 haipo kabisa, barabara hiyo imekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tunduru kulikuwa na Kambi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania maeneo yale yamebaki kuwa mapori. Hivyo tunaomba Serikali iyakabidhi maeneo yale kwa Halmashauri ya Wilaya ili yatumike kwa shughuli zingine za wananchi ikiwa ni pamoja na makazi ya wananchi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tunduru Kusini lipo pembezoni mwa mpaka katika Mto Ruvuma hivyo wananchi wengi wa Tunduru wanaenda Msumbiji kupitia Mto Ruvuma, ninaomba kijengwe kivuko katika Mto Ruvuma sehemu ya Chamba au Makade ili wananchi waweze kutumia badala ya kutumia mitumbwi ambayo inahatarisha maisha ya wananchi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara za ulinzi, miaka ya 1970 mpaka 1980 kulikuwa na barabara ya ulinzi ilitoka Mtwara mpaka Mbamba bay, barabara hii ilikuwa inasaidia kufanya patrol kwa Wanajeshi wa JWTZ kwa ajili ya kulinda mipaka yetu. Barabara hii imekufa kabisa haionekani kabisa, barabara hii ilisaidia sana hasa wananchi wanaoishi kandokando ya Mto Ruvuma. Barabara hii ilitumika sana na askari wetu pamoja na wananchi kusafirisha mazao kwenda kwenye masoko. Sasa hivi wananchi wanazunguka sana kutoka kijiji kimoja kwenda kingine kwa kuwa barabara hii imekufa kabisa na imesababisha ongezeko la magendo sana kutokana na njia maalum inayounganisha vijiji vilivyo kando kando na Mto Ruvuma. Hivyo basi, ninaomba barabara ile ifufuliwe ili kuongeza ulinzi wa mipaka yetu kwa kuwa Watanzania wa vijiji hivyo wanaingiliana sana na wananchi wa Msumbiji na wamepata mahitaji yao ya kila siku kutoka Tanzania hasa Tunduru Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, matengenezo ya barabara ya Tunduru – Nalasi - Chamba na Nalasi – Mtwara Pachani; barabara hizi ni za vumbi na zina milima ambayo kila mwaka ukitengeneza kwa kifusi cha kawaida zinatumika miezi sita. Kwa hiyo, tunaomba barabara hizi zitengenezwe kwa kiwango cha changarawe hasa barabara ya Tunduru – Chamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mawasiliano ya simu, tunaomba mitandao ya simu katika vijiji vya Misyaje, Nasomba, Lukala, Makande, Msinji, Semeni na Azimio upatikanaji wa mawasiliano umekuwa wa shida, hivyo tunaomba minara ya simu ijengwe katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa reli ya Mtwara Corridor, reli hii ni muhimu sana katika Kanda ya Kusini kwa vile kuna makaa ya mawe na chuma kitasafirishwa katika reli hii pamoja na mazao ya korosho, kahawa, tumbaku, mahindi na maharage jambo ambalo litakuza bandari ya Mtwara na Bandari ya Mbamba bay. Hivyo naomba sana ujenzi huu kwa maana ya upembuzi yakinifu ufanyike kwa kina ili ujenzi uanze muda mfupi ujao kwa sababu barabara za Kusini zinaharibika haraka kwa sababu ya kupitisha malori makubwa ya makaa ya mawe, korosho na mahindi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi siku ya leo kuchangia katika hotuba hii muhimu ya Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo kusimama katika Bunge letu kuchangia hoja hii. Pili, niishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kile kilichokifanya katika Wilaya ya Tunduru kwa kukamilisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, ambao umewezesha wananchi wa Tunduru kupata fursa kubwa ya kusafirisha mazao yao kwa wakati na kwa muda mfupi kuelekea kwenye masoko ya Dar es Salaam na maeneo mengine. Ninaishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nitakuja kwenye hoja ya Hotuba ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. La kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuunda mbinu nzuri ya usambazaji wa pembejeo, pembejeo ilikuwa ni kero kubwa sana hasa kwa wakulima wa Tunduru na maeneo mengine kwa sababu mfumo wa ruzuku ulikuwa unagombanisha wakulima pamoja na viongozi wao. Hata hivyo naomba sana jambo hili lichukuliwe maanani sana na lifanyike haraka kwa sababu wale wenzetu, wafanyabiashara ambao walikuwa wanafanya biashara hii hawatapenda mfumo huu uweze kufanikiwa. Kufanikiwa kwa mfumo huu inatakiwa mbolea ije mapema na kwa wakati na isambazwe katika maeneo yote ili wakulima waweze kununua mapema ili waweze kufanikisha malengo ya kilimo chao.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo huwezi kuliongelea bila kuliongelea suala la ushirika. Mimi ni mwana ushirika, nimekuwa mtumishi wa ushirika miaka minane, kwa hiyo kuna jambo ambalo ni muhimu Serikali ilitilie maanani sana; na a hii mara ya pili naliongelea suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Tume ya Maendeleo ya Ushirika. Tume hii tangu imeundwa mwaka 2013 bado haijawa na uongozi kwa maana ya Mwenyekiti na Makamishna wake, jambo ambalo linafanya utendaji wa kazi kuwa hafifu zaidi kwa sababu wanafanya bila kuwa na uongozi kamili unaosimamia ushirika.

Pamoja na hayo hata watumishi wa Tume ya Ushirika walio wengi wanakaimu. Unajua mtu akikaimu muda mwingi maamuzi yanakuwa ya mashaka mashaka kutokana na kutokuwa na title kamili ya nafasi yake anayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara ifanye juu chini ili wale wanaokaimu wapewe nafasi ya kuweza kuwahudumia Watanzania na kama hawafai basi wateuliwe wengine ili kuhakikisha kwamba Tume hii inaenda vizuri. Pamoja na hilo, watumishi wa Tume wapo katika ngazi mbili tu, ngazi ya Taifa na Mkoa, huko Wilayani hakuna mwakilishi wa Tume. Walio wengi wanategemea Maafisa Ushirika ambao wapo chini ya Mkurugenzi wa Halmashauri. Hawa wote wanafanya kazi ya ushirika, lakini wanakuwa chini ya Mkurugenzi, Mkurugenzi ana Mamlaka ya kumpa kazi nyingine nje ya ushirika ili aweze kutimiza malengo yake kama Mkurugenzi wa Halmashauri. Kwa hiyo naomba suala la watumishi kutoka Makao Makuu Mkoani basi wafike mpaka Wilayani ili kazi ya Tume iende sawa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizungumzia suala la Tume huwezi kuacha shirika hili la COASCO. COASCO ndio wasimamizi wakubwa, ndio wanaokagua vyama vya ushirika vyote nchini. COASCO hawana watumishi wa kutosha, vyama vyetu vinachukua muda mrefu bila kukaguliwa. Na nilizungumza mara ya mwisho, hata kama ni mtoto wangu umempa ndizi auze mwezi mzima hujamkagua, siku ukienda kumkagua mambo hayataenda vizuri. Hilo ndilo linajitokeza kwenye vyama vyetu vya ushirika. Vyama vyetu vya ushirika vinakaa muda mrefu bila kukaguliwa, naomba sana muimarishe kitengo hiki cha COASCO kwa maana ya fedha na watumishi ili kuhakikisha kwamba kila mwaka chama cha ushirika kinakaguliwa ili kujua hesabu zake zinaenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la korosho. Mfumo wa Stakabadhi Ghalani Tunduru ulikwama kwa muda mrefu, mwaka 2011/2012 wakulima hawakupata mafao yao kwa kuwa Mfumo wa Stakabadhi ulileta hitilafu na wakulima wa Tunduru walikosa zaidi ya milioni mia sita themani kutokana na bei ya mazao yalivyouzwa kuwa nje na matarajio ambayo yalikuwepo. Kutokana na hili mwaka jana tumejitahidi tukawahamasisha wakulima wakakubali na sasa mfumo umeenda vizuri, bei imekwenda vizuri, nashukuru tena kwa barabara zile, imeleta wanunuzi wengi Tunduru.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo bado kuna wakulima mpaka leo wanadai korosho zao ambazo ziliuzwa chini ya mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada tulizozifanya mwaka jana kuwalazimisha wale wakulima waingie kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani.

Kwa hiyo, naomba Wizara kupitia Tume ya Ushirika iende ikakague vyama vile, tuone ni wangapi wamekosa na tuone namna gani hatua gani inachukuliwa kwa wale ambao wamehusika katika kutumia pesa zile za wakulima na wao kusababisha kukosa hela halali kwa ajili ya korosho zao ambazo waliziuza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado ninaenda huko huko kwenye korosho kwenye suala la export levy. Export levy tangu imeanzishwa ilikuwa na lengo kubwa la kuzuia usafirishaji wa korosho nje zikiwa ghafi, na ku-encourage kubangua korosho tukiwa ndani ya Tanzania. Hata hivyo lengo hili bado halijakamilika mpaka leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, export levy asilimia 65 inaenda Bodi ya Korosho, katika asilimia 65 kuna kiasi cha fedha kinachotakiwa kitumike katika kuendeleza ubanguaji; lakini tangu imeanzishwa export levy hakuna kiwanda chochote kilichojengwa hadi leo. Naomba sana Mheshimiwa Wizara kupitia Bodi ya Korosho wafikirie namna ya kuitumia export levy kubangua korosho kwa wananchi wetu na kutumia export levy kuwakopesha wale walioonesha nia ya kuweza kubangua korosho ili kuongeza kipato cha mkulima wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, ningepena sana Serikali iliangalie suala la kuainisha pembejeo kwa wakulima ili uzalishaji uende sambamba na kalenda ya kilimo kama inavyoeleweka kila mara ambapo kilimo kinatumika. Tunduru na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla ni wakulima wazuri, tuna mahindi mengi, Mpunga Tunduru tunalisha takribani asilimia nusu ya Mkoa wa Lindi na Mtwara wanapata mazao ya mpunga kutoka Tunduru. Mkituletea mbolea mapema naamini wananchi wetu watanunua mbolea hiyo mapema ili waweze kuzalisha zaidi na kuweza kuepukana na njaa kwa maeneo mengine ambayo hayazalishi kwa wingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuongea siku ya leo kuchangia Hotuba hii ya Waziri wa Fedha. Jambo la kwanza napenda nitoe pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo amejitahidi kukusanya mapato ya Serikali, mpaka kufikia Aprili amesema amefikisha asilimia 74.3. Kwa kweli amejitahidi sana kwa sababu nyingi ambazo tunaziona na nitazieleza mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo kuna mambo mawili, matatu ambayo inabidi tuyaongelee ili kuweka sawa na kumpa nguvu ili aweze kukusanya zaidi.

Mheshimiwa Spika, ukweli uliokuwepo kama msemaji aliyetangulia alivyosema, vyanzo vingi vya mapato havikusanywi ipasavyo. Kwa mfano mdogo ambao upo kwa kila mmoja, kuna sekta moja ya kodi ambayo kwa asilimia kubwa haikusanywi, kodi hii ni ya withholding tax.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia wakazi wengi wa mijini zaidi ya asilimia 80 pamoja na sisi Wabunge tuliopo humu ndani tunapanga nyumba ambazo tunaishi kwa sasa, lakini ukiangalia kiasi ambacho kinakusanywa kwenye kodi hizi kama withholding tax kwa kweli ni kiasi kidogo sana. Hata wafanyabiashara walio wengi maeneo ya mijini, vibanda vyote vilivyopo mjini vinapangishwa na wafanyabiashara nao bado hawalipi withholding tax.

Mheshimiwa Spika, kwa jambo hili kama kweli TRA wangekuwa very serious wakiwa wana watumishi wengi wa kuwafuatilia kwa kila nyumba ambapo wapangaji wapo, kodi hii ikapatikana, naamini gap kubwa la kodi au mapato lingeweza kuzibwa kutokana na kodi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hiyo, tukiangalia taarifa yake, halmashauri zimeweza kukusanya mapato yake hadi Aprili kwa asilimia 64. Hapa kuna tatizo na tatizo hili ni kwamba usimamizi wa makusanyo ya Halmashauri umekuwa ni mdogo sana. Kwa kuwa makisio ya mapato ya Halmashauri yanatolewa na wao wenyewe, kwa hiyo vyanzo vile ambavyo wanavitoa wana uhakika wa kukusanya, ni kwa nini hawafikii kiwango cha kuridhisha ili kuleta mchango mzuri wa maendeleo katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, jambo hili nilisikia mwaka jana Waziri mmoja alisema kwamba kuanzia mwaka wa fedha ujao halmashauri yoyote ambayo itashindwa kukusanya angalau kwa asilimia 80 ya makisio yake basi halmashauri hizo zijiandae kuondolewa. Je, mpaka sasa mpango huo ukoje, kwa inaonekana wanakisia kitu ambacho wanashindwa kukikusanya?

Mheshimiwa Spika, naomba sana Halmashauri nazo ziangalie wale wanaoshindwa kukusanya basi hatua ile ichukuliwe ili nafasi wapewe halmashauri nyingine zilizo kubwa kama Tunduru ambayo inaweza kukusanya zaidi ya asilimia 100 kutokana na makisio yake.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nitaliongelea kwa uchungu mkubwa sana ni suala lililopo kwenye ukurasa wa 69 wa hotuba yake ambayo naona inahusiana na sheria zinazosimamia bodi za mazao. Naomba kwa ruhusa yako nisome kwa sababu ni mistari michache ili niweze kutoa mchango mzuri wa kuweza kumshauri Mheshimiwa Waziri namna ya kufanya. Amesema:-

“Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye sheria zote zinazosimamia Bodi za Mazao mbalimbali kwa lengo la kuwezesha ushuru wote unaokusanywa na bodi hizo kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kwamba mapato yatokanayo na ushuru unaotozwa kwenye mazao mbalimbali yanasimamiwa ipasavyo na kutumika kwa ajili ya shughuli zilizokusudiwa. Aidha, shughuli za kuendeleza pamoja na gharama za uendeshaji wa bodi zitagharamiwa kupitia bajeti ya Serikali.”

Mheshimiwa Spika, walivyoanzisha bodi hizi na mazao ilitokana na changamoto za uendeshaji wa kuendeleza mazao mbalimbali likiwemo zao la korosho na ndiyo maana zikaanzishwa bodi ili kusimamia mazao haya yaweze kuzalishwa kwa wingi na baadaye tuweze kupata fedha za kigeni kwa ajili ya kuendeleza Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, nitaenda kwenye zao la korosho; mwaka 2008 wadau wa zao la korosho walikubaliana kuanzisha export levy ambayo katika makubaliano ikaundwa sheria mwaka 2009 na katika sheria ile kama tulivyoeleza siku za nyuma, tulikubaliana kwamba asilimia 35 ya mapato yaende Mfuko Mkuu wa Serikali na asilimia 65 irudi kuendeleza zao la korosho.

Mheshimiwa Spika, huu ndio ulikuwa mkakati wa wakulima wenyewe baada ya kuona kwamba korosho zimekuwa zikiyumba na uzalishaji umepungua na tunamshukuru Mwenyezi Mungu tangu mwaka 2009 tulivyoanza kutumia sheria hii, uzalishaji umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka mpaka msimu uliopita tukapata zaidi ya tani 300,000. Katika tani hizo 300,000 Serikali ilikusanya zaidi ya bilioni mia moja hamsini na nne. Kati ya hizo, bilioni mia moja na kumi zilitakiwa zirudi kwenye sekta; nina mashaka na mapendekezo haya.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali imeshindwa kurudisha kwa muda wa miaka miwili pesa hii ambayo tayari imezungumzwa kwa sheria kwamba asilimia 65 irudi kuendeleza zao husika la korosho, leo tunachukua pesa hii na tunabadilisha kwamba ziende moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu, nina mashaka kwamba yale yaliyotokea miaka miwili hii ambayo mpaka leo wakulima wa korosho tunalia yataendelea kujitokeza na hatimaye zao la korosho na mazao mengine yatauawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu dhamira na nia ya kuanzisha bodi hizi ilikuwa ni kulisaidia zao lenyewe ili liweze kujiendeleza baada ya kuonekana Serikali kupitia bajeti ya Serikali yenyewe imeshindwa kuendeleza haya mazao. Njia mbadala ilikuwa ni wakulima wenyewe kujinasua kwa kuanzisha hizi bodi na mifuko mbalimbali ambazo walianzisha tozo na ada mbalimbali zilizokubaliana na wakulima wenyewe ili kuendeleza mazao haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki kilio alichokizungumza Mbunge wa Kilwa ni kikubwa sana maeneo mengi ya Tunduru ambako wanategemea uzalishaji wa korosho kulingana na hii fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba, kwa kuwa haya ni mapendekezo, mapendekezo haya hayana tija kwenye bodi zetu za mazao kwa sababu zinaenda moja kwa moja kuua uzalishaji wa mazao na kama tulivyosema asilimia 20 ya export ya nje, pesa ya kigeni inategemea na mazao yetu.

Mheshimiwa Spika, tukiangalia mwaka jana zao la korosho peke yake liliingiza zaidi ya trilioni 1.2, pesa za Kitanzania kwa ajili ya mauzo yake. Kwa maana hiyo, kama pesa zile hazitaenda kuhudumia zao kwa maana kwamba uzalishaji utapungua na hili lengo linalosema Serikali inaweza kupata fedha nyingi kutokana na hii pesa kupelekwa kwenye Mfuko Mkuu maana yake itashuka.

Mheshimiwa Spika, naomba sana, kwa kuwa dhamira ni nzuri basi haya madeni ya nyuma yaende kuhudumia wakulima ili na sisi wanasiasa twende tukawaeleze wananchi wetu kwamba kuanzia mwaka wa fedha ujao tarehe 1 Julai mfumo utabadilika pesa hii itakuwa inapelekwa moja kwa moja Serikalini na kuamuliwa matumizi kwa njia ambayo amependekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana jambo hilo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo kuchangia hoja ya TAMISEMI pamoja na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza nitaenda moja kwa moja kwenye suala la mgao wa wilaya. Halmashauri yetu ya Wilaya ya Tunduru ni kubwa sana na kilio chetu kimekuwa cha muda mrefu. Pamoja na kwamba Rais amesema hatutakuwa na mgao lakini hali yetu ya kiutawala ni ngumu kutokana na ukubwa wa eneo letu tulilokuwa nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tunduru imeanzishwa tangu mwaka 1905 lakini mpaka leo haijawa na wilaya nyingine na ukubwa wake ni zaidi ya Mkoa wa Mtwara ambao sasa una wilaya zaidi ya sita (6). Kwa hiyo, utakuta kimaendeleo kuhudumia wananchi wetu inakuwa ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba kulingana na idadi ya watu tuliokuwa nao, ukubwa wa eneo uliokuwepo na umbali wa makao makuu kuhudumia maeneo mengine yaliyokuwepo tunaomba sana mtufikirie kwa hali na mali ili tuweze kupata wilaya nyingine kwa ajili ya kuwahudumia watu wetu vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nitalizungumzia ni suala la elimu. Kama nilivyozungumza juzi tunashukuru sana elimu bure lakini tuna changamoto nyingi sana upande wa Tunduru ambazo kwa kweli ni aibu, mpaka leo tuna madarasa ya nyasi katika maeneo mengi ya shule zetu za msingi. Pamoja na madarasa ya nyasi lakini bado hata vyoo hatuna. Kulingana na idadi ya watoto ilivyokuwa utakuta shule ina watoto 840 matundu ya vyoo ni saba, kumi ambayo hayaendani na hali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi kwenye nyumba za Walimu ndiyo usiseme, walimu ni wachache kupita kiasi hata nyumba zao hazipo. Kwenye eneo langu nimetembea karibu jimbo zima na shule zote za msingi nimezitembelea, shule ina watoto 840, Walimu watano, sita au watatu. Asilimia 60 ya shule za msingi zilizopo kwenye jimbo langu zina Walimu chini ya watatu, jambo ambalo ni gumu hata tukifikiria namna wanavyofundisha na kufaulisha Walimu wale wanastahili pongezi kubwa sana kwa sababu Walimu ni wachache na madarasa yamekuwa mengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nimeliona miaka hii kunakuwa na session katika madarasa ya kwanza mpaka darasa la saba. Kwa kweli wale watu wanastahili kupewa hata overtime kwa sababu wanafunzi ni wengi, madarasa ni mengi lakini wanafundisha Walimu wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nitazungumzia juu ya ujenzi wa vituo vya afya. Naishukuru kwa mara nyingine Serikali kwa kutupatia Kituo cha Afya Nkasale lakini eneo la Tunduru kwa maana ya halmashauri yote tuna kata 35. Katika kata 35 tuna vituo vya afya vitano (5) tu na hivyo kwenye jimbo langu kuna vituo vya afya vitatu (3).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kituo cha Afya Nalasi, Rais wa Awamu ya Nne Rais Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa ahadi ya kujenga kituo hiki. Nalasi ni mji mkubwa una zaidi ya wakazi 30,000 ambao wako kwenye kata mbili katika kijiji hicho hicho kimoja. Kwa hiyo, alivyokuja kwa mara ya mwisho aliahidi kwamba angeweza kujenga kituo cha afya katika kata ile na aliahidi kutoa gari la wagonjwa lakini ile ahadi mpaka leo haijatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013/2014 kwenye bajeti waliweka shilingi milioni 80, wananchi walifyatua tofali za kujenga boma. Bahati nzuri shilingi milioni 80 ilipatikana wakaanza ujenzi ule lakini tofali zile sasa zimekuwa kichuguu, tangu umejengwa huo msingi kwa maana ya foundation mpaka leo ahadi ile haijatekelezeka na halmashauri imejitahidi kila mwaka kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa halmashauri yetu ni kubwa kama nilivyozungumza tuna kata 35, tuna Madiwani 52, tukijumlisha sisi Madiwani kwa maana Wabunge halmashauri yetu ina Madiwani 55 yaani ni darasa kubwa ambalo hata kusikilizana inakuwa ni ngumu. Kwa hiyo, bajeti ya afya haitoshi na ya elimu inakuwa haitoshi kwa sababu mapato yetu hayawezi kukidhi kuweza kuhudumia vituo vya afya vyote kwa maana ya kupata fedha za majengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni suala la maji. Tuna miradi mingi sana ambayo inasimamiwa na halmashauri yetu kwa maana ya maji. Tunayo miradi ya muda mrefu, Mradi wa Mtina mpaka leo haujakwisha. Juzi bahati mbaya halmashauri imesitisha mkataba na mkandarasi yule lakini naomba waende wakaangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetembelea ule mradi kwa macho yangu na kwa scope ya kazi niliyoona inaonekana mradi ule umefikia zaidi ya asilimia 80, lakini kwa matakwa ya watendaji wetu naweza kusema kwa maslahi binafsi wameweza kusitisha ule mkataba tangu Desemba mwaka jana mpaka leo mkandarasi mwingine hajapatikana, wakati wangeweza kumuachia ndani ya mwezi mmoja kama alivyoomba mradi ule ungekuwa umeweza kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tabia nchi ya ukame katika maeneo mengi, Tunduru tulikuwa na mito mingi lakini bahati mbaya mito hii imeendelea kukauka. Kwa hiyo, tunahitaji miradi ya maji mingi kwenye vijiji vyetu kwa ajili ya visima vifupi na virefu ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ningependa kuchangia juu ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru. Halmashauri yetu kama nilivyozungumza ni kongwe na ni imezeeka lakini ina watumishi wachache sana. Watumishi waliokuwepo ni wachache mno ukizingatia na namna ambavyo kazi zile zinafanyika. Mbaya zaidi kuna watumishi wanazeeka na halmashauri ile, wana zaidi ya umri wa miaka 20 kwenye halmashauri moja, kwa hiyo, wanafanya kazi kwa mazoea kiasi kwamba kila wanachokifanya wanafanya kwa namna ambavyo wao wanaona siyo kwa matakwa ya masharti ya kazi kama ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba basi ikiwezekana watusaidie angalau kufanya internal transfer kwa maana ya kutoka halmashauri moja au nyingine ili wale waliokaa muda mrefu ambao sasa imekuwa ni mazoea kufanya kazi zao ikiwezekana na wao waweze kupelekwa sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna jambo linanisikitisha kwenye halmashauri yetu. Tumekuwa na tabia sisi ya kusomesha wataalam wetu katika halmashauri...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo wa kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Nitaenda moja kwa moja kwenye hoja ya msingi. Kwanza napenda kuunga mkono kwa asilimia mia moja hoja zote mbili na nitaanzia kwenye TAMISEMI kwa upande wa vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali yetu kwa kutupatia Jimbo letu la Tunduru Kusini vituo viwili vya afya ambavyo vimejengwa pale Mchoteka na kingine kimejengwa Rukasale. Nasikitika kwa kile kituo cha kwanza cha Rukasale kama Mheshimiwa Waziri alikuwa hana taarifa, bado hakijakamilika mpaka leo kutokana na matumizi mabaya ya fedha yaliyotokana na usimamizi mbovu wa Watendaji wetu. Hii imetokana na kwamba Halmashauri ya Tunduru haina mhandisi ambaye angeweza kusimamia vizuri katika ujenzi wa zile zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukurani hizo, Jimbo la Tunduru Kusini lina Kata 15 na katika Kata 15 tuna vituo vya afya vitatu tu na tuna ahadi ya muda mrefu ya Kituo cha Afya Narasi iliyotokana na Rais wa Awamu ya Nne ambaye aliahidi kujenga kituo cha afya katika eneo lile. Nimeleta swali hili mara tatu katika Bunge lako Tukufu, nimeahidiwa kupewa pesa lakini hadi leo kile kituo bado hakijajengwa na watu zaidi ya 30,000 wako katika Kata zile mbili ambazo zinakitegemea sana na wapo mbali zaidi ya kilometa 70 kutoka Mjini Tunduru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuchangia katika hilo hilo, kulikuwa na ahadi vile vile ya Rais wa Awamu ya Nne ya kutoa gari kwa ajili ya Kituo cha Afya Mchoteka. Jambo hili bado nalo ni tatizo na Halmashauri yetu ina gari chakavu, ukizingatia kwamba Hamashauri ya Wilaya ya Tunduru ina eneo kubwa sana kuliko hata Mkoa wa Mtwara kwa ujumla wake. Kwa hiyo, tuna gari bovu la miaka ya 1980 mpaka leo hii, hatuna gari yoyote ambayo inaweza kusaidia wagonjwa wetu kutoka katika sehemu moja kwenda sehemu ya pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda kuzungumzia ni suala la elimu. Katika suala la elimu tuishukuru Serikali kwa kutoa elimu ya msingi bila malipo, lakini kuna changamoto kubwa ambayo imejitokeza katika maeneo yetu hasa katika Jimbo la Tunduru Kusini kwamba watoto wamekuwa wengi, madarasa yamekuwa kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imesababisha watoto wengi kusoma katika darasa moja zaidi ya 100 mpaka 200. Nikichukua mfano katika Shule ya Msingi Tuwe Macho ina zaidi ya watoto 800; Shule ya Msingi Semeni ina zaidi ya watoto 900; Shule ya Msingi Mtina ina watoto zaidi ya 1,000, lakini madarasa yaliyokuwepo hayazidi saba au matano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba katika miundombinu ya shule za msingi iongezwe bajeti ili kuhakikisha kwamba majengo yanajengwa ili watoto wale waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la watumishi. Kwa kweli tatizo la watumishi limekuwa ni kubwa sana katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru. Tuna upungufu wa wafanyakazi katika Sekta ya Afya zaidi ya asilimia 65. Katika Sekta ya Elimu zaidi ya asilimia 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule nyingi za msingi katika jimbo langu zina walimu ambao hawazidi watano na minimum ni watatu; na shule hizo ziko kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la saba. Kwa kweli kwa walimu wale imekuwa ni mzigo mkubwa sana kufundisha madarasa saba wakiwa walimu watatu, wanne au watano. Naomba sana kwa kuwa tuko ndani ya bajeti tunaomba sana watumishi wa Sekta ya Elimu waongezwe ili kuhakikisha kwamba wanaweza kufanya kazi vizuri kwa ajili ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna tatizo la walimu waliostaafu katika kipindi hiki ambacho kikokotoo kipya kimetengenezwa. Walilipwa kwa hesabu ile ya kikokotoo cha zamani. Wamekuja ofisini kwangu mara mbili mpaka mara tatu, wanasema itakuwaje? Tumelipwa kwa kupunjwa na Rais amesema kikokotoo kitumike kile cha zamani. Walimu hawa wanaulizia watapewa lini mapunjo yao ili waweze kujikimu katika maisha yao ya kustaafu kama ilivyo sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni suala la Makatibu Tarafa. Naishukuru Serikali katika Jimbo kangu la Tunduru Kusini kuna Tarafa tatu, mwaka 2018 tumepata watumishi wote, Maafisa Tarafa watatu. Changamoto waliyokuwanayo, hawana ofisi kabisa. Ofisi za Maafisa Tarafa hakuna kwenye Tarafa zetu. Halmashauri yote ina ofisi moja tu katika Tarafa saba. Kwa hiyo, hawana ofisi, hawana nyumba za kuishi, tunabanana nao humo humo kwenye maeneo yetu ambayo tunaishi. Tunaomba sana, mtengeneze angalau bajeti kwa kuwajali hao Maafisa Tarafa ili waweze kupata Ofisi na nyumba za kuishi waweze kufanya kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano ambalo napenda nizungumzie ni suala la TARURA. Kwa kweli TARURA pamoja na kazi nzuri wanayoifanya, tatizo fedha inakuwa ni kidogo. Kwenye upande wa Jimbo langu la Tunduru Kusini, kuna barabara zina zaidi ya miaka 10 hazijawahi kutengenezwa. Tulitegemea TARURA atakuwa ni mkombozi katika kutengenezea barabara zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Lukumbule – Imani – Kazamoyo, kuna barabara ya Mlingoti – Tuwemacho – Ligoma, kuna barabara ya Chemchemi – Namasakata – Liwanga mpaka Msechela, kuna barabara ya Namasakata – Amani – Msechela, kuna barabara ya Nandembo – Mpanji mpaka Njenga, kuna barabara ya Mchoteka – Masuguru – Malumba. Barabara hizi zina zaidi ya miaka saba hazijafanyiwa kazi yoyote. TARURA kwa kweli kila unapoona hesabu yao, ukiangalia kwa sasa wamepewa 1.3 billion na hizi barabara zina zaidi ya kilometa 455. Kwa hela ile waliyopewa kwa matengenezo ya kawaida tu kwa kweli haitaweza kukidhi haja ya kutengeneza barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana TARURA waongezewe pesa ili waweze kufanyia matengenezo barabara zetu ambazo zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo napenda kulizungumza ni suala la mapato ya Halmashauri zetu. Hapa kuna shida, hasa kwenye mikoa ya kusini; mwaka jana na mwaka juzi tulikuwa tunaenda vizuri, mapato yetu mengi tunapata kutokana na ushuru wa korosho. Bahati mbaya mwaka huu biashara ilivyokwenda, hatukuweza kupata ushuru wa korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, kwa kutambua kwamba walikuwa na mipango na bajeti zao kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ambayo ilikuwepo kwenye mahesabu, basi Serikali ifanye huruma kuwasaidia angalau ruzuku Halmashauri zile ziweze kukidhi haja ya kuweza kutekeleza ile miradi ambayo ilikuwa imepangwa mwaka 2018/2019. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mbunge.

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi jioni hii kuchangia hoja ya Wizara ya Maji. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kusimama, lakini nitakuwa sina fadhila niwashukuru wadau walionisaidia Jimbo la Tunduru Kusini kwa kuwataja kuchimba vya maji, nikianzia na Help for Under Reserved Community ambao wamechimba visima 74 vya maji virefu kwa gharama ya kila kisima shilingi 650,000 kitu ambacho ni kikubwa kwetu gharama ya visima vinaeleweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba niwashukuru Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Masasi, kwa kupitia Mradi wa CHIP wao wamechimba visima virefu vya maji 24 ambavyo vinawasaidia wananchi wangu kuweza kupata maji salama. Tatu, nawashukuru Taasisi za Kidini za Firdaus na Istiqama wao wamechimba visima 60 kwenye Jimbo langu bure bila hata senti tano. Kwa hiyo nawashukuru sana wamesaidia kuondoa kero ya maji kwa asilimia kubwa katika maeneo yangu. Kwa hiyo ukiangalia katika Jimbo langu, hawa wadau wamechimba visima zaidi ya 200 ambavyo vimesaidia kupunguza kero ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda moja kwa moja kwenye hoja, naomba nimshukuru sana Waziri. Waziri pekee aliyekanyaga kwenye Jimbo langu, kaenda kwenye Mradi wa Mtina na kwenye mradi wa Mbesa. Mradi wa Mtina alitoa maagizo, mradi ule unaendelea vizuri kidogo, lakini kuna matatizo mawili, matatu ambayo yametokana na kutokuelewana kati ya Mkandarasi na Mhandisi wa Maji. Katika mchoro wa ule mradi ulionesha kwamba watatumia solar panel 16 na kutumia battery 32. Ushauri wa Mkandarasi alishauri kwamba tutoe battery 32, wanunue panel 16 jumla ziwe 32 ambazo zitakuwa na uwezo sawa na kuwa na battery 32 ili waweze kusukuma maji. Matokeo yake Mhandisi alivyokataa imeonekana maji hayapandi ipasavyo kwa hiyo wakati wa kifuku kama sasa wananchi wale hawapati maji. Kwa hiyo tunaomba Wizara iingilie kati ili yule Mkandarasi aruhusiwe kununua panel zingine 16 ili maji yaweze kupatikana kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Waziri alivyokuja Mbesa alitoa ahadi ya kuchimba kisima kirefu kimoja, kile kisima mpaka leo hakijachimbwa. Naomba sana afuatilie ile ahadi yake iweze kutekelezeka wananchi wa Mbesa pamoja na kuwa watu wengi sana lakini wana shida kubwa ya maji. Maji Mbesa ni tatizo kubwa sana, Waziri mwenyewe amefika, Mradi ule wa Benki ya Dunia mpaka leo maji hayafiki kwenye lile tenki kubwa, limekuwa ni tatizo kubwa sana. Hata feasibility study iliyofanyika maji yanaishia kwenye tenki na pesa kwa ajili ya kugawanya maji kwenye vijiji bado haijaweza kupatikana. Kwa hiyo naomba Waziri afuatilie ile ahadi yake bado haijatekelezwa na wananchi wanaendelea kupata shida kubwa ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine amblo napenda nilizungumzie ni suala la wafanyakazi wa Idara ya Maji, kwa upande wa Tunduru ina shida kubwa sana. Mwaka jana mwaka wa fedha 2017/2018, tulipata fedha kwa ajili ya kukarabati visima vya DANIDA. Vile visima vya DANIDA vingi vimejengwa miaka ya 80 na 90 na ndivyo vinavyowasaidia karibu maeneo mengi ya Jimbo la Tunduru Kusini, lakini kutokana na ongezeko la watu vile visima vimeshindwa kutosheleza mahitaji ya watu na vimezeeka. Mwaka jana tulipata fedha kwa ajili ya kukarabati visima 25, kwa milioni tatu kila kisima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya tatizo la wataalam mpaka leo vile visima vyote, walinunua vifaa lakini havifanyi kazi. Vifaa vimenunuliwa, wamekwenda kuvifunga, naamini kutokana na ujuzi na namna fulani ilivyofanyika vile visima mpaka leo havitoi maji pesa imeondoka. Kwa hiyo tuna tatizo kubwa la watumishi katika idara yetu hasa Mhandisi nina mashaka naye kwa sababu miradi mingi ameshindwa kuisimamia. Hata hawa wahisani niliokuwa nawashukuru walikuwa na mkataba na halmashauri kwa ajili ya kusimamia, watoe gari, watoe mafuta, watoe mfanyakazi, lakini wameshindwa kufanya hivyo, tumekaa vikao mara chungu nzima, lakini imeshindikana. Mpaka leo bado anaendelea kufanya kazi halmashauri kwa upande wa Idara ya Maji wameshindwa kusimamia. Kwa hiyo naomba kwa kuwa Idara ya Maji sasa iko chini ya Mheshimiwa Waziri, awasiliane na huyu Mhandisi, kwa kweli ni kero, ni shida, ameshindwa kusimamia kutekeleza miradi ya maji katika Jimbo la Tunduru Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda sana kuliongelea ni suala la maji kwa vile vijiji vilivyopo kandokando ya Mto Ruvuma. Kuna vijiji takriban 10, kuna Vijiji vya Amani, Mkalachani, Misechela, Liwanga, Mkapunda na Makande, vyote hivi vipo pembezeni mwa Mto Ruvuma, lakini hawa watu wana shida kubwa sana ya maji, maji yako kilomita nne, tatu, tano. Kwa hiyo hawana visima vya maji, wanategemea kuchota maji mtoni, mara nyingi watu wanapata shida sana wanakumbana na mamba kule watoto wanakwenda na maji, wanakufa na maji kutokana na shida ya maji. Naomba kama Serikali yetu inajali watu wetu kama tunavyozungumza kila siku basi tuanzishe mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kwa ajili ya hivi vijiji vilivyopo pembezoni mwa Mto Ruvuma ili hili kero ya maji iweze kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, sio kwa umuhimu, naomba kwenye vile vijiji vilivyokuwa kwenye miradi ya Benki ya Dunia kwa mfano Mchoteka na Namasakata. Vile vijiji vilionekana havina vyanzo vizuri vya maji kulingana na utafiti, lakini lakini ukweli vyanzo vipo. Tunaomba basi ule mradi urudi tena ili vile vijiji viweze kupata maji ya kutosha kwa sababu Mchoteka peke yake ina vijiji vine, umati ulioko pale ni zaidi ya watu 8,000, wanategemea visima vinne tu ambavyo kila kijiji ina kisima kimoja. Naomba sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwa tulikuwa na nia nzuri ya kuweka Mradi pale wa Benki ya Dunia, lakini utafiti ulifanywa shaghalabaghala, haukuweza kutosheleza mahitaji yale, naamini kuna andiko lilipelekwa Ofisini kwa Mheshimiwa Waziri tangu 2017 kutokana na utafiti uliofanyika na Mhandisi wa Maji aliyekuwepo kipindi kile, lakini mpaka leo lile andiko halijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na andiko hilo kuna andiko la Namasakata, nacho Namasakata ni kijiji kikubwa sana, nacho tulikuwa na andiko ambalo thamani yake ilikuwa ni milioni 180 tu ambavyo ingeweza kusaidia kupata maji ya uhakika kutokana na utafiti ambao ulifanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa kuna mradi wa Amani. Naishukuru sana Serikali ule mradi umeweza kusaidia vijiji vitatu, lakini maji yale ni mengi, mabomba yanapasuka kila siku nilipeleka Ofisini kwa Mheshimiwa Waziri andiko la kuongezea vijiji vitatu ili kuweza kuondoa tatizo hili la kupasuka mabomba kila siku kutokana na presha kubwa ya chanzo cha maji ambayo yanakuwa supplied katika mradi ule. Lile andiko liko ofisini kwa Mheshimiwa Waziri, lina thamani ya milioni 300 tu ambalo lingeweza kusaidia kuondoa hilo tatizo la kupasuka mabomba yale kila siku ili kuweza kuwahudumia wananchi wengine wa Misechela, pamoja na Liwanga ambao wanateseka na wanashida kubwa sana ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi ya maji ya Benki ya Dunia katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru miradi iliyokamilika ni minne, miradi mitatu inasuasua kwa kuchelewa fedha na mitatu mingine haijaanza kabisa kutokana na matatizo mbalimbali. Hivyo, tunaomba miradi ile mitatu inayoendelea ya Mbesa, Mtina na Matemanga ipelekewe fedha ili ikamilike kwa sababu ni muda mrefu wakandarasi wanasuasua kukamilisha miradi hiyo. Vilevile miradi mitatu ya Mchoteka, Matemanga na Namasakata ianze kwa vile wananchi walishachangia sehemu ya fedha kama masharti ya miradi ile iliyohitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Tunduru vyanzo vya maji ni vingi sana lakini miundombinu ni michache sana. Maji yanapatikana ndani ya mita 100 za urefu ardhini, hivyo tunahitaji gari la kuchimbia visima vifupi na virefu ili kupunguza gharama za upatikanaji wa maji. Nadhani kama Halmashauri yetu ingekuwa na gari la kuchimbia visima tungeweza kusaidia kupata maji kwa wepesi zaidi kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maji inayotumia generator wananchi wameshindwa kuendesha hivyo Serikali iangalie upya katika miradi ya jamii kuweka solar badala ya kutumia generator ambazo wananchi wameshindwa kununua diesel kuendesha mashine za maji. Hivyo, ninaomba miradi iliyobaki ni vema mashine na pump zinunuliwe zote zinazotumia solar badala ya generator ya diesel.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi ya umwagiliaji Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imebahatika kuwa na maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na maeneo kadhaa tayari yana miradi ya umwagiliaji, lakini tatizo wataalamu wetu wanatuangusha sana, miradi ile inatumika wakati wa kifuku tu, kiangazi miradi hii haifanyi kazi kutokana na upungufu mkubwa wa maji katika mito na mabwawa yanayotumika, ubovu wa miundombinu ya mifereji kutokana na mapungufu makubwa ya kitaalamu. Miradi hii inatumia fedha nyingi sana lakini haifanyi kazi
iliyokusudiwa. Ninaomba wataalam wetu kutumia utalaam wao kwa uangalifu sana ili kufanya miradi hiyo iwe endelevu, miradi ya umwagiliaji hailingani na kiasi cha pesa kinachotumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Tunduru bado tuna maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni vema basi tukafikiria kutumia maji ya kuchimba visima virefu na vifupi na kutumia mabomba ya kawaida badala ya kutumia mabanio ya kujenga mifereji inayotegemea maji ya mito au mabwawa ambayo kwa sasa yanakosa maji kipindi cha kiangazi, hivyo kutokuwa na uzalishaji kwa sababu maji yanapungua sana hayawezi kupanda kwenye mifereji na mitaro iliyojengwa na mifereji mingi inabomolewa wakati wa kipupwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa maji ndiyo kila kitu katika maisha ya binadamu, basi ni vema tozo ya maji kwenye mafuta ingeweza kuongezwa kutoka 100 ili kuongeza fedha za miradi ya maji vijijini na ni vema ukaanzishwa Mfuko wa Maji Vijijini ili kuharakisha maendeleo ya miradi ya maji vijijini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna kata 15 na kuna shule za sekondari za kata nane tu ambazo zote ni za kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne. Ninaomba angalau shule ya kidato cha tano na sita, moja au mbili ili kuwachukua wanaomaliza katika shule hizo. Kwani wengi wanaomaliza kidato cha nne wanabaki vijijini bila kuendelea mbele kidato cha tano wala vyuo. Hivyo kukatisha tamaa wanafunzi na wazazi wao kuonekana kuwa watoto walimaliza kidato cha nne wanaishia kuishi kijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu mkubwa wa madarasa, nyumba za walimu, maabara, mabweni na miundombinu ya library. Shule zote nane hazina library, hazina mabwalo ya chakula wala majiko ya kupikia chakula. Kutokana na tabia ya wananchi wa kusini, tunalazimika watoto wakae mashuleni kwenye shule zote za kata ili kupunguza utoro na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Mhesimiwa Mwenyekiti, ipo idadi kubwa ya wanafunzi wanaopelekwa mashuleni kuliko miundombinu iliyopo. Mwaka 2016 na 2017 baada ya Sera ya Elimu bila malipo, watoto wengi wamekuwa wanafaulu kupelekwa kidato cha kwanza bila kuangalia miundombinu iliyopo katika shule hizo.

Hivyo Serikali iangalie namna ya kuwapeleka mashuleni kulingana na miundombinu ya mabweni, madawati, madarasa hata vyoo katika shule hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi. Shule zote zilizopo kwenye Jimbo langu, kuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi, hivyo kufanya watoto wachukue masomo ya sayansi na wote kusoma masomo ya arts.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tunaomba Serikali kuajiri walimu wengi wa sayansi hasa hesabu, physics, chemistry na biology. Somo la kilimo (agriculture) lipewe kipaumbele kwa sababu ajira hamna, vyuo ni vichache, havitoshi ili watu tu wajifunze kilimo chenye tija zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu, kuna Shule za Msingi ambazo mpaka leo zimeezekwa kwa nyasi pamoja na nyumba za Walimu. Ninaomba Serikali ione namna ya kuzisaidia shule hizo ambazo ni Mbati ya leo Mkambala, Mchangani, Mrusha, Tupendane, Tukaewote na Mchangamoto.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hotuba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na upungufu wa vituo vya afya; Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina jumla ya kata 39 lakini tuna vituo vya afya vitano tu na zahanati 57 kati ya vijiji 167. Hali hii inadhoofisha utoaji wa huduma ya afya kwa akina mama na watoto. Akina mama wajawazito wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 10 kufuata huduma za afya. Hivyo, tunaomba Serikali itupie jicho Wilaya hii ya Tunduru kutokana na uchache wa vituo vya afya na zahanati. Jitihada za Halmashauri ya Wilaya zinagonga mwamba kutokana na ukubwa wa eneo pamoja na makusanyo madogo ya mapato ya ndani. Hata hivyo, kuna upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta ya afya; zahanati nyingi zina wahudumu si zaidi ya wawili, nyingine zina mhudumu mmoja tu, jambo ambalo linadhoofisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ya muda mrefu ya Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2014 alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya katika Kijiji cha Nalasi chenye wakazi zaidi ya 50,000 katika mgawanyo wa vijiji vinne. Jambo hili limekuwa ni kero kubwa sana, wananchi walijitolea kufyatua tofali na Halmashauri ilitoa shilingi 80,000,000 mwaka 2015 lakini fedha hizo ziliishia kujenga foundation tu, pamoja na uwepo wa matofali yale mpaka leo hakuna kilichoendelea. Halmashauri imejitahidi kutenga shilingi milioni 100 kila mwaka lakini upatikanaji wa fedha umekuwa mgumu sana. Hivyo ninaiomba Serikali kutekeleza ahadi hii ya muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi ya muda mrefu ya gari la wagonjwa; Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kutoa gari katika Kituo cha Afya Mchoteka mwaka 2014 lakini hadi hivi leo ahadi hiyo haijatekelezwa. Ninaomba Serikali kuona umuhimu wa kutekeleza ahadi hii kwani kituo hiki cha afya kipo umbali wa kilometa 80 kutoka ilipo Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Mtina kimejengwa mwaka 1970, majengo yake ni machakavu na hakuna wodi ya akina mama na watoto; haina maabara wala theater (chumba cha upasuaji) na kituo hiki kinahudumia Kata nne; Lukumbule, Mchesi, Tumemado na Kata ya Mtina yenyewe; zaidi ya wananchi 80,000 wanahudumiwa katika kituo hiki. Hivyo, ninaiomba Serikali kutoa fedha kuongeza huduma za afya kama ilivyo katika vituo vingine vilivyoongezewa majengo ili kutoa huduma ya malazi, upasuaji na huduma ya maabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna Hospitali ya Mission ya Mbesa ambayo inategemewa takribani na wananchi zaidi ya 200,000. Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kuifanya hospitali hii kuwa Hospitali Teule ya Wilaya lakini mpaka leo ahadi hiyo haijatekelezwa pamoja na kwamba Halmashauri inapeleka watumishi katika hospitali ile ili kusaidia kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyo katika hospitali nyingine teule zilizopo maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya ina gari bovu sana la wagonjwa na ukizingatia Wilaya ile ni kubwa sana, hivyo, tunaomba gari la wagonjwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na tatizo la tabianchi, maeneo mengi ya Jimbo la Tunduru Kusini yameathirika kwa kiasi kikubwa kwa kukauka kwa mito mingi, hivyo kufanya kuongezeka kwa kukosekana kwa maji katika vijiji vingi sana. Kuna uhitaji mkubwa wa visima vya maji vifupi na virefu ili kupunguza kero ya maji hasa katika vijiji vyenye mkusanyiko mkubwa wa watu. Vijiji hivyo ni Azimio, Seveni, Mgalia, Mwaji, Jiungeni, Mrusha, Lukala, Mahande, Mitwana, Kazamoyo, Imani, Nasya, Tuwemecho, Namesaku, Mdingula, Chemchemi, Namasakata, Ligoma, Makate, Chiwana, Mkadu, Mbesa, Chikomo, Chinunje, Umoja, Misyaje, Mchuba, Meladi, Wenji, Njenga, Likwaso, Mcheteko na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Kijiji cha Mtina ni wa muda mrefu sana, tangu mwaka 2012 katika Miradi ya World Bank. Halmashauri imesitisha mkataba na mkandarasi tangu Desemba, 2017 na mradi umesimama. Tunaomba mradi ule ukamilishwe haraka iwezekanavyo ili kuondoa kero za wananchi wa eneo la Mtina.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji katika Kijiji cha Mbesa bado unasuasua. Tunaomba Serikali kuweka mkazo mradi huo ukamilike kwa wakati ili kuondoa kero za maji katika Kijiji cha Mbesa ambacho kina idadi kubwa ya wakazi kutokana na uwepo wa Hospitali ya Mbesa ya Mission. Mradi wa Umwagiliaji wa Misyaje ni wa muda mrefu sana. Umetumia zaidi ya shilingi milioni 800, lakini mpaka leo mradi huo haufanyi kazi kabisa. Hivyo fedha zinakwenda bure na upo kwenye kiwango cha chini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umwagiliaji Madaba nao umegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja, lakini haupo katika kiwango kizuri kwa maana na hufanyi kazi ipasavyo. Hivyo unahitaji marekebisho makubwa sana ili uweze kufanya kazi vizuri. Vilevile kuna miradi mipya miwili katika vijiji vya Wenje na Mkapunda. Tunaomba miradi hiyo ifanyiwe kazi ili kuongeza uzalishaji wa mpunga ambao unaonekana kuwa na tija kwa wakulima wa Tunduru Kusini.

Mhesjhimiwa Naibu Spika, miradi ya maji Lukumbule na Nalasi wananchi wanashindwa kuiendesha kwa kwa kuwa na gharama kubwa sana kutokana na kutumia dizeli. Tunaomba miradi hii ya wananchi itumie umeme wa solar ili kupunguza gharama za dizeli ambapo zaidi ya lita 60 kwa siku zinatumika kuendesha mitambo ya kusukuma maji. Kuna miradi mitatu iliandika andiko la miradi, tulileta Ofisi ya Wizara ya Maji ili kututafutia pesa kwa ajili ya kuchimba visima na kusambaza maji katika vijiji vya Namasakata, Tuwemacho na Malumba/Molandi pamoja na Kijiji cha Mchoteka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba miradi hiyo ipewe umuhimu wa kuifanyia kazi ili wananchi wa maeneo hayo wapate maji kuondoa adha inayowakumba.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hoja ya hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za askari na vituo vya polisi, Jimbo la Tunduru Kusini ina tarafa tatu katika tarafa hizo ni moja tu Tarafa ya Nalasi ina vituo vya polisi lakini Tarafa ya Lukumbule na Tarafa ya Namasakata haina kituo cha polisi hivyo wananchi wanalazimika kufuata huduma hiyo Tunduru Mjini, zaidi ya kilometa 60 mpaka 80. Tunaomba angalau kila Makao Makuu ya Tarafa kuwa na kituo cha polisi ukizingatia kuwa tarafa hizo zinapakana na Msumbiji hivyo kuna mwingiliano wa watu kutoka Msumbiji na Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya uhamiaji; Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na Mto Ruvuma kwa maana ya Msumbiji kuanzia mwanzo mpaka mwisho, lakini hamna kituo chochote cha uhamiaji jambo ambalo linaleta kero kwa wananchi wa Tunduru mara wanaposafiri kwenda Msumbiji kwa sababu tunaingilia sana kati ya Msumbiji na Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Msumbiji kuna askari wengi sana wa Uhamiaji na polisi wanawanyanyasa sana wananchi wanaovuka mpaka kwenda Msumbiji wakati wao wakija kwetu hamna mtu anayebugudhiwa. Hivyo naomba angalau Kituo cha Uhamiaji katika Kijiji cha Lukumbule ili kuhudumia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Boma la Polisi Lukumbule, wananchi pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilianzisha ujenzi wa kituo cha polisi Lukumbule tangu 2011, mpaka leo kituo hicho hakijakwisha, limejengwa boma tu halijaezekwa mpaka leo. Hivyo tunaomba Serikali itusaidie kumalizia kituo hicho ili kiwasaidie wananchi wa Kata za Lukumbule na Mchasi ambao wapo zaidi ya umbali wa kilomita 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makazi ya polisi Tunduru; katika Halmashauri ya Tunduru ilikuwa na makazi ya polisi lakini yaliungua na moto zaidi ya miaka mitano iliyopita lakini nyumba zile mpaka leo hazijajengwa tena na askari wale sasa wanakaa uraiani. Hivyo tunaomba askari wetu wapatiwe makazi ya kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa askari polisi pamoja na vifaa vya kufanyia kazi, Tunduru hatuna polisi wa kutosha kuhimili eneo kubwa la Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru. Hivyo, tunaomba tuongezewe askari ili waweze kuhudumia wananchi wetu pamoja na mali zao. Vilevile kuna tatizo kubwa sana la usafiri, pindi matukio ya uhalifu yanapotokea, askari hawafiki kwa wakati kutokana na tatizo la usafiri. Wakati mwingine hata mafuta ya kuweka kwenye gari wanakuwa hawana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la fedha za uendeshaji wa ofisi; polisi wamekuwa ombaomba wa mafuta kwa ajili ya magari yao kutokana na ukosefu wa fedha za kununulia mafuta ya magari. Hivyo, tunaomba Serikali ipeleke fedha za OC ili polisi wafanye kazi zao kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la rushwa, wananchi wengi sana wanalalamikia Jeshi la Polisi kutokana na rushwa inayoendelea, wananchi kwao limekuwa kawaida kuombwa rushwa mshtaki na mshtakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanasema kuingia polisi bure ila kutoka polisi lazima uwe na pesa. Jambo hili linalichafua jeshi la polisi. Vilevile bado kuna malalamiko ya rushwa kwenye Jeshi la Polisi la Usalama Barabarani kwani kuna askari wa usalama barabarani wamefanya kazi hiyo kama mradi wao wakujipatia kipato kisicho halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linachafua sana Jeshi la Polisi la Usalama Barabarani; kwa mfano kila basi linalotokea Ubungo linatozwa zaidi ya Sh.20,000 la sivyo gari/ basi halitoki. Vilevile vituo vyote vya ukaguzi vya mabasi kila basi linatozwa Sh.5,000 mpaka Sh.10,000, la sivyo basi linacheleweshwa kwa visingizio mbalimbali. Tunaomba jambo hili likomeshwe. Vitendo hivyo vipo kwenye vituo vyote vya mabasi yanayosafiri kwenda sehemu mbalimbali ya Mikoani na Wilayani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kuchangia hoja ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la migogoro ya ardhi katika Baraza la Ardhi kuchelewa kusikilizwa kutokana na tatizo la kukosa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi. Tunduru hatuna Mwenyekiti na Baraza la Ardhi ili kusikiliza kesi za migogoro ya ardhi hivyo tunaomba tupatiwe Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi ili kuondoa kero hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kuchelewa kupitishwa ramani/michoro ya Mji wa Tunduru kwa muda mrefu jambo ambalo linasababisha ucheleweshaji na wananchi kuendelea na mchakato wa kupata hati. Kwa mfano, Halmashauri ilitoa offer ya baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru (Nakayaya) tangu 2011 mpaka 2018, bado wananchi wanaambiwa mchoro haujarudi Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linawakwaza wananchi wanaotaka kuendeleza maeneo yao kwa kutumia hati zao. Kukopa pesa benki tunaomba Wizara iangalie upya namna ya kutoa/kupitisha michoro ya Halmashauri mapema ili maeneo yaliyopimwa yapate hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya vifaa vya kupimia ardhi pamoja na wafanyakazi wenye ujuzi katika kupima ardhi. Kumekuwa na tatizo la wafanyakazi katika Kitengo cha Ardhi jambo ambalo linachelewesha upimaji wa ardhi na utoaji wa hati kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna tatizo la baadhi ya wafanyakazi kuendelea na tabia za kupokea rushwa ili watekeleze majukumu yao ya kila siku. Vilevile Watumishi wa Halmashauri Kitengo cha Ardhi bado wanafanya kazi kwa mazoea bila kufuata maadili ya kazi. Vilevile kuna upungufu mkubwa wa Watumishi katika Kitengo cha Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la fedha. Kitengo cha Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kinakumbwa kwa kiasi kikubwa na tatizo la fedha ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo linawalazimisha kuwachangisha wananchi wanaotaka huduma ya kupimiwa ardhi na hatimaye kupata hati ili kutekeleza majukumu yao. Hali hii inalazimisha wafanyakazi kutotekeleza majukumu yao na hatimaye kuingia kwenye mtego wa kuomba rushwa ili huduma itolewe kwa wananchi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama ifuatavyo:-

Kwanza ni mgao wa Wilaya. Wilaya ya Tunduru ina eneo kubwa sana la utawala ambalo linalingana na eneo la Mkoa wa Mtwara wenye Wilaya Sita. Tunaomba Serikali ifikirie suala la kugawa Wilaya ya Tunduru ili kurahisisha shughuli za kuhudumia wananchi kwa kuleta huduma karibu na wananchi. Kila eneo la Jimbo liwe Wilaya kamili inayojitegemea kutokana na wingi wa watu na umbali kutoka Makao Makuu ya Wilaya ilipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tatizo la watumishi wa Halmashauri. Tuna upungufu mkubwa wa watumishi wa Halmashauri katika sekta zote za afya, elimu na kada zingine za kilimo. Tuna upungufu wa Walimu wa Shule za Msingi zaidi ya 1,000 na Walimu wa Sayansi wa Shule za Sekondari zaidi ya 100 na kuna upungufu wa watumishi wa afya zaidi ya 700, tuna watumishi asilimia 26 tu katika Sekta ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watumishi wa Halmashauri wamekuwa na muda mrefu katika Halmashauri ya Tunduru na wanasababisha kudumaa kwa kazi za Halmashauri na wanafanya kazi kwa mazoea. Hivyo, tunaomba watumishi waliokaa muda mrefu wahamishwe, wapelekwe Halmashauri zingine ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vituo vya afya. Halmashauri ya Tunduru ina Kata 35 ina vituo vya afya vitano tu. Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya Nalasi lakini mpaka leo kuna msingi tu. Wananchi walifyatua tofali za udongo lakini tangu 2014 mpaka leo hamna kinachoendelea. Halmashauri inatenga fedha kila mwaka lakini hazipatikani kabisa, hivyo naomba Kituo hicho cha Afya Nalasi ambacho kitahudumia Kata mbili za Nalasi Magharibi na Nalasi Mashariki zenye wakazi zaidi ya 30,000 kijengwe na Serikali ili kuheshimu ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kituo hicho naomba Serikali isaidie Halmashauri kujenga vituo vya afya angalau vinne zaidi kupunguza adha ya huduma kwa akinamama na watoto. Kata hizo ni Malumba, Lukumbule, Ligoma, Misechela na Tuwemacho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ni maji. Kuna tatizo kubwa la maji katika maeneo mengi ya Jimbo la Tunduru Kusini, kutokana na mabadiliko ya tabianchi mito mingi imekauka kabisa hasa katika Vijiji vya Mchoteka, Likweso, Mnemasi, Molandi, Mdumba, Misyaje, Mbesa, Uliwana, Chukano, Nasumba, Wenje, Mkapande, Nuwemecho, Nasya, Namasadau, Miseula, Ligoma, Chemchem, Makade, Kozango, Likada, Senei, Azimio, Angalia na kadhalika. Tunaiomba Serikali kutuchimbia visima virefu na vifupi ili kutoa huduma ya maji safi kwa wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya maji miwili ya Mbesi na Mtina ni ya muda mrefu bado inasuasua katika ukamilishaji wake na mradi wa Mtina Mkataba wa ujenzi Halmashauri umekatishwa wakati mradi umefikiwa zaidi ya asilimia 60, kufanya mradi ule uendelee kuchelewa zaidi kukamilika. Vile vile tunaomba miradi mipya ya maji ili kupunguza adha ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu. Upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa na vyoo pamoja na nyumba za Walimu. Kuna tatizo kubwa sana la vyumba vya madarasa kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule za msingi, hivyo tunaomba Serikali isaidie kutoa fedha kuongeza jitihada zilizofanywa na wananchi ambao wanaweza kufyatua tofali 100,000 kwa ajili ya madarasa na nyumba za Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Tunduru Kusini halina high school hata moja, tumeomba angalau shule mbili za Kata zipandishwe hadhi ili ziwe high school.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia hoja ya hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgao wa Wilaya, Wilaya ya Tunduru ina eneo kubwa sana la utawala kulinganisha na eneo la Mkoa wa Mtwara wenye Wilaya sita. Tunaomba Serikali ifikirie suala la kugawa Wilaya ya Tunduru ili kurahisisha shughuli za kuhudumia wananchi kwa kuleta huduma karibu na wananchi. Kila eneo la jimbo liwe Wilaya kamili inayojitegemea kutokana na wingi wa watu na umbali kutoka Makao Makuu ya Wilaya ilipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la watumishi wa halmashauri; tuna upungufu mkubwa wa watumishi wa halmashauri katika sekta zote za afya, elimu na kada zingine za kilimo. Tuna upungufu wa Walimu wa shule za msingi zaidi ya 1,000 na Walimu wa sayansi shule za sekondari zaidi ya 100 na kuna upungufu wa watumishi wa afya zaidi ya 700, tuna watumishi asilimia 26 tu katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watumishi wa halmashauri wamekaa muda mrefu katika Halmashauri ya Tunduru na wanasababisha kudumaa kwa kazi za halmashauri na wanafanya kazi kwa mazoea. Hivyo, tunaomba watumishi waliokaa muda mrefu wahamishwe wapelekwe halmashauri zingine ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vituo vya afya, halmashauri ya Tunduru ina kata 35 ina vituo vya afya vitano tu. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga Kituo cha Afya Nalasi lakini mpaka leo kuna msingi tu. Wananchi walifyatua tofali za udongo lakini tangu 2014 mpaka leo hamna kinachoendelea. Halmashauri imetenga fedha kila mwaka lakini hazipatikani kabisa, hivyo naomba Kituo hicho cha Afya Nalasi ambacho kitahudumia Kata za Nalasi Magharibi na Nalasi Mashariki zenye wakazi zaidi ya 30,000 kujengwa na Serikali ili kuheshimu ahadi ya Rais Awamu ya Nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba na kituo hicho naomba Serikali isaidie halmashauri kujenga vituo vya afya angalau vinne zaidi kupunguza adha ya huduma kwa akinamama na watoto. Kata hizo ni Malumba, Lukumbule, Ligoma, Msechela na Tuwemacho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa la maji katika maeneo mengi ya Jimbo la Tunduru Kusini. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi mito mingi imekauka kabisa hasa katika Vijiji vya Mchoteka, Likweso, Mnemasi, Molandi, Machemba, Misyaje, Mbesa, Chiwana, Chikomo, Nasomba, Wenje, Mkapunda, Tuwemacho, Nasya, Namasalau, Misechela, Ligoma Chemchem, Mkandu, Kazamoyo, Lukala, Semeni, Azimio, Angalia na kadhalika. Tunaiomba Serikali kutuchimbia visima virefu na vifupi ili kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya maji miwili ya Mbesa na Mtina ni ya muda mrefu bado inasuasua katika ukamilishaji wake. Mradi wa Mtina mkataba wa ujenzi halmashauri umekatishwa wakati mradi umefikia zaidi ya asilimia 60 na kufanya mradi ule kuchelewa zaidi kukamilika. Vilevile tunaomba miradi mipya ya maji ili kupunguza adha ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la elimu, kuna upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa na vyoo pamoja na nyumba za Walimu. Kuna tatizo kubwa sana la vyumba vya madarasa kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule za msingi, hivyo, tunaomba Serikali isaidie kutoa fedha kuongeza jitihada zilizofanywa na wananchi ambao wameweza kufyatua matofali 100,000 katika kila kijiji kwa ajili ya kujenga vyoo, madarasa na nyumba za Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Jimbo la Tunduru Kusini hamna shule ya high school hata moja. Tunaomba angalau shule mbili za kata zipandishwe hadhi ili ziwe high school.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hoja ya Waziri wa Katiba na Sheria kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru; kumekuwa na ucheleweshwaji wa kazi za ardhi na migogoro kutokana na kutokuwepo kwa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi. Tunaomba Tunduru tupatiwe Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi ili kupunguza migogoro ya ardhi inayozidi kuongezeka siku hadi siku katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa majengo ya Mahakama; kuna upungufu mkubwa wa majengo ya Mahakama. Katika Jimbo la Tunduru Kusini, hivyo shughuli nyingi za Mahakama kufanyika katika maeneo yaliyofanana na Mahakama. Pamoja na kutokuwepo kwa nyumba za Mahakimu wengi na Mahakimu wanakaa katika nyumba za kukodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Mahakama; kumekuwa na upungufu mkubwa wa Mahakama. Jimbo la Tunduru Kusini lina Tarafa tatu, Nalasi, Hukumbule na Namasakata na Kata 15, lakini Mahakama zinazofanya kazi hazizidi tatu, moja kila Tarafa, hivyo tunaomba angalau kila Kata kungekuwa na Mahakama ya mwanzo ili kupunguza migogoro ya wananchi wetu huko vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu mkubwa wa Mahakimu; Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina upungufu mkubwa wa watumishi wa Mahakama (Mahakimu) pamoja na Makarani wa Mahakama, hivyo tunaomba tuongezewe Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo ili kurahisisha kusikiliza kesi mbalimbali. Mahakama zilizopo hazina Mahakimu na kufanya Mahakimu waliokuwepo kuwa na mzigo mkubwa wa kusikiliza madai mbalimbali ya wateja hivyo kufanya Mahakimu kufanya mzunguko kupita kusikiliza kesi katika Mahakama zilizopo vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa vitendeakazi; Mahakama zilizopo Tunduru zina changamoto kubwa ya vitendeakazi hasa magari na pikipiki. Mahakimu waliopo hawana hata vyombo vya kusafiria ili kwenda kusikiliza kesi vijijini, hivyo kufanya kesi kuahirishwa mara kwa mara kutokana na kutokufika kwa Hakimu kusikiliza kesi hizo kwa kukosekana usafiri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna Tarafa tatu, Kata 15, vituo vya Polisi vinavyofanya kazi ni viwili tu. Kwa kuzingatia kuwa Tunduru Kusini inapakana na Mto Ruvuma katika mpaka wa Msumbiji. Hivyo, tunaomba Kituo cha Polisi katika Kata ya Lukumbule, katika eneo la Lukumbule pamoja na Kituo cha Uhamiaji ili kudhibiti watu wa Msumbiji wanaoingia Tanzania bila kufuata utaratibu na sheria za nchi. Vilevile tunaomba Kituo cha Polisi katika Kata ya Misechela, Kijiji cha Misechela na katika Kata ya Namasakata katika Kijiji cha Namasakata ili kuwarahisishia katika Kata ya Mchateka ambayo ina idadi kubwa ya wakazi. Tunaomba kituo cha Polisi katika Kijiji cha Mchateka Kati ili kuhudumia wananchi wa Kata hiyo. Lengo la kuomba Vituo hivi vya Polisi ni kupunguza kero kubwa kwa wananchi kutembea mwendo mrefu kufuata huduma ya Kipolisi.

Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Namasakata hamna hata kituo kimoja cha Polisi. Tarafa hiyo ina Kata tano yaani Ligoma, Misechela, Tuwemacho, Mchuruka na Namasakata na hamna kituo cha Polisi hata kimoja. Huduma ya Kipolisi wataipata Makao Makuu ya Wilaya ya Tunduru Mjini.

Mheshimiwa Spika, sambamba na vituo vya Polisi, tunaomba vituo vya Uhamiaji ili kupata huduma za visa kwani maeneo niliyotaja yamepakana na Msumbiji hivyo kuna mwingiliano wa wananchi wa Msumbiji na Tanzania, lakini wananchi wa Tanzania wakienda Msumbiji wanapata shida sana kwa vile Askari wa Msumbiji wananyanyasa sana Watanzania kwa kuwapiga hatimaye kuwafunga na kuwanyang’anya mali zao wakati wao wakija Tanzania hawanyanyaswi hivyo. Kwa hiyo, tunaomba vituo vya Uhamiaji ili wananchi wa Tanzania wapate visa za kwenda Msumbiji kwa ukaribu zaidi badala ya kufuata Tunduru Mjini ambapo ni zaidi ya kilometa 80 kutoka mpakani.

Mheshimiwa Spika, pamoja na vituo vya Polisi, tunaomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga nyumba za Askari katika Kituo cha Polisi Walasi na Kituo cha Polisi Masuguru ambao karibu wote wanakaa uraiani na hata Askari waliopo Makao Makuu ya Polisi Wilaya hawana makazi ya kudumu. Kuna nyumba 300 za Polisi ziliungua moto miaka mitano iliyopita lakini hadi hivi leo nyumba hizo hazijajengwa. Tunaomba nyumba zile zijengwe ili kupunguza adha ya makazi kwa Askari wetu wanaofanya kazi katika mazingira magumu sana ya makazi kwa kuchanganyika na wananchi ambapo ni hatari kwa maisha yao.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, Serikali iongeze bajeti ya fedha kwa ajili ya kununua mafuta kwa ajili ya magari ya Polisi. Ni aibu kubwa sana kwa Jeshi la Polisi na Uhamiaji kuwa ombaomba wa mafuta kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kila siku na ndiyo maana Polisi wakiitwa mahali kuna uhalifu hawafiki kwa wakati kwa sababu ya kukosa mafuta ya kufika eneo la tukio. Wakati mwingine wanalazimika kuomba mafuta kutoka kwa mtoa taarifa ili waweze kufika eneo la tukio.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyeiti, ninapenda kuchangia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kama ifauatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Tunduru Kusini kuna shule za Kata nane na tunategemea kuongeza shule mbili za sekondari ya Misechela na Tuwemacho jumla 10 katika kata 15. Changamoto kubwa ya shule hizo ni za kutwa tunalazimika wanafunzi kuwalaza madarasani kutokana na umbali wa vijiji wanavyotoka watoto hai hivyo madarasa haya mchana na usiku mabweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tunaomba Serikali kutusaidia kujenga mabweni katika shule hizo ili kupunguza kero za wanafunzi hao kutembea kilomita nyingi kufuata shule na uwezo mdogo wa wazazi kuwapangia watoto wao nyumba za kuishi. Changamoto nyingine ni upungufu wa madarasa kutokana na idadi kubwa ya watoto wanaofaulu kwenda kidato cha kwanza kipindi cha sera ya elimu bila malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni upungufu wa maabara ya sayansi. Tunashukuru Serikali na wananchi kwa kujitolea kujenga maabara ya masomo ya sayansi. Lakini pamoja na jitihada hizo bado majengo hayo hayajakamilika kwa kupewa vifaa vya maabara. Kwa hiyo tunaomba Serikali kutoa vifaa vya maabara ili kuzifanya maabara zile zifanye kazi ipasavyo sambamba na upungufu wa maabara kuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi kwa masomo ya fizikia, kemia, biolojia na hesabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali iendelee na jitihada za kuajiri walimu wa sayansi angalau kila somo apatikane mwalimu mmoja ili kuweza kuwafundisha watoto wetu katika teknolojia mpya ya sayansi na teknolojia. Changamoto nyingine ni kwamba katika shule hizo zote hamna shule yoyote ya high school jambo ambalo linalozimisha wanafunzi wengi kukosa kuendelea na masomo ya high school. Hivyo ninaomba angalau tupate high school mbili kwa kuanzia shule ya sekondari Semeni na shule za sekondari Mchoteka ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaokwenda high school.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changanoto nyingine ni kutokuwa na chuo cha ufundi kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya wanafunzi. Hivyo ninaomba fursa itakayopatikana chuo cha ufundi kijengwe katika Jimbo la Tunduru Kusini hususani katika Kata ya Mtina ambako mahitaji makubwa muhimu na ya kutosha yapo, kama vile ardhi, maji safi na barabara inayopatikana wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, VETA ni muhimu sana ili kuendeleza vijana wetu wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne na cha sita ambao wanakosa nafasi za kuendelea mbele kimasomo. Changamoto nyingine ni la nyumba za walimu ambapo walimu wengi wanakaa kwenye nyumba za kupanga vijijini. Tukumbuke kwamba shule zote hizi zipo vijini ambapo huduma ya nyumba za kupanga si nzuri sana wanalazimika kupanga ili waishi. Ni vyema Serikali kuona umuhimu wa kujenga nyumba za walimu ili kupunguza kero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni mikopo kwa walimu. Kwa kuwa kipato cha walimu ni kidogo ninaomba Serikali kuona namna ya kuwakopesha usafiri hasa pikipiki ili waweze kujikimu pindi wanapotaka kusafiri kwenda mjini kufuata mahitaji pamoja na mishahara. Walimu wengi wana madai mengi kwenye mabeuli SACCOS jambo ambalo linawafanya waishi katika mazingira magumu sana na kushindwa kufanya kazi vizuri. Hivyo ninaomba mishahara ya walimu iongezwe pamoja na kupewa fursa ya kukopeshwa na Serikali kwa riba nafuu kama zile za vijana akinamama na walemavu ili kuwapunguzia mzigo wa kukopa kwa riba kubwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia hotuba hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mradi wa REA katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna vijiji vitano tu kati ya vijiji 65, hivyo naomba vijiji vya nyongeza nilivyoomba viingizwe kwenye REA lll, awamu ya kwanza, Vijiji hivyo ni Semeni, Mtina, Angalia, Nasya, Tuwemacho, Chemchem, Ligoma, Mkoteni, Namasakata, Luwingu, Nalasi, Chilundundu, Lipepo, Mchoteka na kadhalika ili kupunguza idadi kubwa ya vijiji visivyokuwa na umeme.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo naomba Serikali inapopanga vijiji waangalie sana Halmashauri zenye majimbo zaidi ya moja kuchukua vijiji kila upande wa jimbo ili kupunguza malalamiko.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umeme unawekwa kwenye vijiji vingi ni vizuri TANESCO wakafikiria ofisi ndogo katika tarafa ili kutoa huduma kwa haraka kwa wateja wake.

Mheshimiwa Spika, katika miradi ya REA kuna changamoto ya mafundi wanaoweka nyaya (wiring) kwenye nyumba za wananchi kuwa na gharama za juu kuliko uhalisia wa kazi, ni vizuri TANESCO wangetoa mwongozo kwa wakandarasi na mafundi wanaofanya wiring katika majumba ya wananchi juu ya bei na gharama za kufanya wiring.

Mheshimiwa Spika, viongozi/management ya TPDC wateuliwe viongozi wa kudumu badala ya kuwa na makaimu kila siku ambapo wanakosa ujasiri wa kutoa maamuzi kwa kuhofia vyeo vyao kuyeyuka na kwa kuwa mpango kazi uliopo unaonyesha matumaini ya Shirika/TPDC kukua ni vyema basi management ya kudumu ikawekwa badala ya kuweka makaimu katika kila idara ya TPDC.

Mheshimiwa Spika, gharama ya bomba la gesi ichukuliwe na Serikali badala ya kuwatwisha mizigo TPDC ili kupunguza bei ya gesi kama inavyolalamikiwa na wawekezaji wengi. Hii itasaidia kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutumia gesi katika kuendesha viwanda vyao na kwa matumizi ya majumbani.

Mheshimiwa Spika, TPDC iharakishe usambazaji wa gesi majumbani ili kuongeza kiwango cha gesi kinachotumika na kuongeza pato la TPDC na Serikali kwa ujumla.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuchangia mchana huu. Kwanza kabia naomba niweke record sawa. Naona kuna baadhi ya wenzetu hawaelewi hii certificate of original inatolewaje? Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, cerificate of original anapewa exporter. Akishapewa exporter, yeye anaweza akawa anapeleka sehemu tatu tofauti. Kwa hiyo, sehemu zinazokwenda, zinaenda nakala, certificate of original anabakinayo exporter. Kwa hiyo, ninaungana mkono na wenzangu waliotangulia, hasa Mheshimiwa Turky kwamba, siyo sahihi TRA kudai certificate of original kwa sababu certificate of original ni mali ya exporter. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo nilikuwa napenda nichangie sehemu mbili ambazo nilikuwa nimejipanga nichangie. Suala la kwanza ni suala la wakala wa vipimo. Wote tunajua tatizo la vipimo lilivyo. Kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba anategemea kuajiri watu 153. Katika kero ambayo inaendelea katika maeneo mengi hasa ya nchi yetu ni suala la vipimo. Vipimo vinatumika kwa wakulima, madukani na kila mahali, hata barabarani magari yanapimwa kwa kutumia vipimo. Vile vipimo vimetengenezwa na vyuma na ofisi za vipimo ziko mikoani tu. Kwa hiyo, wanakagua maeneo mengi hivyo vipimo kwa mwaka mara moja. Kwa hiyo, utakuta mara nyingi wanaotumia vipimo wanakuwa wanawapunja wateja wao kwa ajili ya vipimo ambavyo wanavitumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Wizara mjipange kufungua ofisi kwenye wilaya ili wale watumishi wa vipimo upande wa wilayani waende kukagua mizani ile mara kwa mara. Kwa sasa watu wanaotumia vipimo wanapata tabu sana, wakitaka huduma ya watumishi wa vipimo lazima mtu aende mikoani, hasa watu wa mafuta shida hiyo wanayo, mizani mingi shida hiyo wanayo ndiyo maana wakulima wengi wanalalamika kwamba wanapunjwa katika vipimo vyao ambavyo wanavitumia wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo napenda nilichangie ni suala la mfumo wa stakabadhi ghalani. Mfumo huu upo kwa mujibu wa sharia, lakini kanuni zimeleta matatizo mengi ambayo yamesababisha watumiaji wa mfumo ule kuwa tofauti. Kwa mfano, sasa hivi limezuka janga, hawa wanaotumia mfumo wa stakabadhi ghalani hasa wakulima na vyama vya ushirika kupunjwa mazao yao yanapopotea kwenye maghala makuu, lakini hatua yoyote inayochukuliwa kutoka kwenye Serikali au kwa mfumo wa stakabadhi ghalani. Kwa hiyo, naomba Sheria ya mfumo wa Stakabadhi Ghalani irekebishwe ili kuhakikisha kwamba inaweza kumlinda mkulima au mtumiaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani aweze kupata haki yake ya mapunjo ambayo yanatokana na matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia mfano halisi uliopo kwenye Sekta ya Korosho, sasa hivi korosho zipo maghalani na tunategemea kwenye mazao mengine tutumie mfumo wa stakabadhi ghalani, sehemu ya kuhifadhi yale mazao hakuna. Naomba, nadhani Serikali jambo la kwanza kulitilia maanani lingekuwa ni suala la kuongeza maghala katika maeneo yetu ambayo yanazalisha mazao, bila kuwa na maghala, mfumo wa stakabadhi ghalani hauwezi kufanya kazi kama wanavyosema wenyewe mfumo wa stakabadhi ghalani. Kwa hiyo, naomba sana Serikali kwa ku-rescue situation iliyopo sasa kwa upande wa maeneo ya kusini, basi ichukue hatua za haraka ili kuongeza maghala katika maeneo mbalimbali ili korosho au mazao yaweze kuhifadhiwa kama yanavyotarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hiyo, kuna risk kubwa kwa upande wa ma-warehouse operator ambao wanafanya shughuli zile, wanaingiliwa sana na Serikali tofauti na sheria inavyohitaji kuhusu huu mfumo wa stakabadhi ghalani. Sasa hivi wengi ma-warehouse operator wanaogopa kufanya kazi ile kwa sababu muda/wakati wowote wanaweza kuwekwa ndani bila ya utaratibu, jambo ambalo linakatisha tamaa watumiaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani. Hii inapoteza haki yao ya msingi ambayo ipo katika mfumo wa stakabadhi ghalani. Naomba sana Serikali iangalie hii sheria, iangalie upungufu wote uliopo kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani urekebishwe ili wadau wa mfumo wa stakabadhi ghalani uweze kupata haki yao kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ndiyo nilikuwa napenda nichangie. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo na mimi kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza niipongeze Serikali yetu kwa mambo makubwa ambayo imeyafanya, lakini nitatoa pongezi za kipekee kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Tunduru kwa ujumla kwa Serikali pamoja na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutuokoa katika janga la korosho. Nitashukuru kwa sababu wakulima karibu asilimia 80 wamelipwa wamebaki asilimia 20; lakini nilitegemea katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wakati amekuja angalau angezungumza jambo kidogo kuhusu suala la korosho, lakini bahati mbaya sikuiona, naomba nimkumbushe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, korosho ni zao la biashara upande wa Kanda ya Kusini, lakini ndio tegemeo kubwa kwa wananchi wa Kusini, nilikuwa naomba kati ya tozo ambazo umeziona zitolewe ningeomba na export levy kwenye korosho nayo iondolewe ili iweze kusaidia wakulima kwa sababu kwa sasa imeonekana export levy ni gharama kwa mnunuzi halafu ni mzigo kwa mkulima ambapo bei yake ya korosho inapungua. Tukiangalia kwa sasa hali tuliyokuwa nayo korosho kuwepo maghalani madhara ya kuwepo maghalani hapo mbele itakuwa ni makubwa, lakini kama tungeweza kutoa export levy ninaamini kuna wanunuzi ambao wangeweza kujitokeza kuweza kununua korosho zile kwa bei ambayo ingeweza kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kuwa gharama zetu ni kubwa ukiongeza mzigo wa export levy korosho zile mpaka sasa hivi wanunuzi waliokuwa wengi wanaziogopa na athari zake zitakuwa ni kubwa kwa sababu msimu ujao wa korosho unakaribia kuanza hapo mwezi wa nane jambo ambalo kutakuwa na madhara makuu mawili. La kwanza tutakosa mahala pa kuhifadhia korosho kwa sababu korosho nyingi zimejaa kwenye maghala ambayo ndio tunayoyategemea, kwa hiyo nilidhani katika mkakati wa Serikali wa awamu ijayo, moja ya mkakati ingekuwa ni kuongeza maghala katika maeneo ambayo yanazalisha korosho; lakini madhara ya pili wanunuzi wetu ni wale wa kila siku ambao ni Wahindi wa Vietnam ukweli wanajua tuna tani 224,000 kwenye maghala yetu, kwa hiyo, wataogopa kuja katika msimu ujao kununua korosho zetu kwa sababu wanajua kwamba korosho zikikaa zaidi ya miezi sita ubora unaendelea kushuka siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba naongea hili kwa uzoefu nimekuwa General Manager zaidi ya miaka nane kwenye sekta ya korosho. Ninaijua korosho, naombeni sana Serikali kwa kuangalia hali ilivyo sasa basi tukubali bei itakayojitokeza tuuze zile korosho isije yakatokea yaliyotokea mwaka 2013/2014; jambo hili lilijitokeza na korosho tuliuza nusu bei, naomba sana Serikali iliangalie hili kwa kuangalia gharama zake ambazo zitasaidia korosho zile ziuzwe ili kunusuru msimu ujao korosho ziuzike kwa urahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nilikuwa ninaomba kuna wananchi ambao wanadai mpaka leo, waliobaki walio wengi ni wale ambao ni wakulima wakubwa vijijini kwetu, hawana namna ya kuhudumia mikorosho, hawana namna ya kupulizia, basi kwa kuwa wanadai na Bodi ya Korosho wana pembejeo ambazo zipo kwenye maghala basi uwekwe utaratibu wa kuwakopesha wale wananchi pembejeo pindi Serikali itakapopata fedha basi waje kupunguza kwenye hayo mapato yao ili na wao waweze kuhudumia mashamba yao ili angalau mwakani nao waweze kuvuna zaidi. Jambo hili ni muhimu sana kwa sababu hawana namna kilio kimekuwa ni kikubwa sana, naomba sana Mheshimiwa Waziri uliangalie hili kwa upande wa huruma sana wale wakulima hawana namna yoyote ya kuweza kuwasaidia zaidi ya kuwakopesha pembejeo ili waweze kupalilia na kupulizia mikorosho yao.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine napenda niishukuru sana Serikali na kuipongeza kwa sheria ile ya mwaka 2005 ya mfumo wa stakabadhi gharani na ndio iliyoifanya korosho iongezeke uzalishaji mpaka mwaka 2017/ 2018 ukafikisha tani 3,13,000; lakini bahati mbaya yale yaliyojitokeza mwaka jana ambayo tuliyayalalamikia kwa muda mrefu uzalishaji umeshuka mpaka tani 224,000 na hii ilitokana na namna ambavyo tuli-handle pembejeo kwa wakulima wetu ambazo jambo tulilokuwa tumelilalamikia kwa muda mrefu, lakini halikutilia maanani.

Kwa hiyo, ninaomba sana ili kuongeza uzalishaji basi tupunguze gharama na miaka ya nyuma Serikali ilikuwa inatoa ruzuku kwenye pembejeo, nimesema nimekuwa kwenye korosho miaka nane, miaka ile Serikali ilikuwa inatoa ruzuku kwenye sulphur, ilikuwa inatoa ruzuku kwenye mbolea, lakini jambo lile limesitishwa naomba ile ruzuku irudie tena kwa wakulima ili waweze kununua pembejeo kwa bei rahisi na waweze kununua kwa wingi waweze kuzalisha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mfumo ule wa Stakabadhi gharani tulisema tunaanza kwa mfano katika kanda ya korosho mafanikio yameonekana na hata sasa hivi upande ule tumeamua ufutwe kutumia mfumo wa stakabadhi gharani. Matokeo yake yamekuwa mazuri, bei imekuwa nzuri. naomba Serikali kwa kuwahurumia wakulima wa Tanzania ule mfumo ni mzuri uendelee kwenye maeneo mengine ya kahawa, pamba na tumbaku ili wakulima waweze kufaidika kama wenzao wa ufuta na korosho walivyoweza kufaidika miaka miwili, mitatu iliyopita. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imegonga Mheshimiwa.

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa siku hii ya leo kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Mwaka Mmoja. Kwanza napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kurudi tena kwa awamu ya pili, lakini nawashukuru wapiga kura wangu ambao hawakufanya ajizi, wameona yale niliyoyafanya wakaamua kunichagua tena. Pia nitakuwa ni mchoyo wa fadhila bila kukishukuru Chama Cha Mapinduzi. Nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango nitachangia mambo mawili, jambo la kwanza ni suala la elimu. Kwanza niipongeze Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ikiongozwa na Rais wetu, jemedari, Mheshimiwa Dkt. Pombe Joseph Magufuli, kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye Sekta ya Elimu. Naamini wengi tumeona mafanikio yaliyotokana na Sekta ya Elimu, tumetoka kwenye kuongeza shule za sekondari, kuongeza wanafunzi katika shule za msingi, vyuo pamoja na majengo na ukarabati wa miundombinu katika shule za sekondari na vyuo vikuu vilivyopo hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hili la elimu bure napenda tuone namna mpango unavyoweza kusaidia shule za kata. Naamini wengi tuliotoka kwenye majimbo ya vijijini wanafunzi wengi wanasoma kwenye shule za kata. Ongezeko la wanafunzi kwenye shule za msingi limesababisha shule za kata ziwe na watoto wengi. Sasa miundombinu iliyopo kwenye shule hizi si rafiki sana ukilinganisha na shule zile ambazo zinahudumiwa na Wizara ya Elimu kama shule zile 89 ambazo zinafanyiwa ukarabati. Ndiyo maana hata ufaulu wake umekuwa wa kiasi kidogo sana ingawa zinajitahidi na watoto walio wengi kutoka vijijini wanasoma kwenye shule hizi. Naomba mpango ungeweka badala ya sasa kuendelea kukarabati naamini shule katika miaka mitano zimekarabatiwa zile kongwe, basi Serikali iangalie shule hizi za kata kuweza kuziongezea miundombinu ili zilingane na shule nyingine ambazo ziko katika mazingira mazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia shule hizi nyingi wanasoma watoto wa maskini ambao wamejitahidi kujenga mabweni lakini watoto wanakwenda na vyakula shuleni. Naomba Serikali kupitia Mpango wa Miaka Mitano ijayo ijitahidi kuongeza ruzuku kwenye shule za kata ili watoto wanaosoma kwenye maeneo yale ambao wanatoka katika mazingira magumu kwenye kata zetu waweze angalau na wao kupata chakula kwenye shule hizi za kata ili kuwafanya watoto hawa waweze kufaulu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini watoto hawa kwa mazingira tunayoyaona wanafaulu katika mazingira magumu sana na ndiyo maana utakuta private school wanafaulu vizuri zaidi kwa sababu wako kwenye mazingira mazuri, wanalala mahali pazuri, Walimu wengi wa sayansi, Walimu wa masomo mengine wako wengi na maabara za kutosha. Naomba mpango uangalie namna ya kuimarisha shule zetu za sekondari za kata ili miundombinu ya maabara, madarasa, mabweni, hata chakula Serikali iweze kutoa ruzuku kwenye shule hizi za kata waweze watoto wetu kusoma katika mazingira mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, napenda nichangie sana suala la barabara. Ukizungumzia barabara ukweli tunaishukuru Serikali, Mtwara Corridor, barabara kutoka Mtwara sasa imefika mpaka Nyasa. Tunaishukuru sana Serikali kwa kitendo hiki cha kutujali watu wa kusini kuhakikisha barabara hizi zimekamilika na sasa unapiga lami kutoka Mtwara mpaka unafika Ziwa Nyasa na baadaye unapanda meli kwenda Malawi unakwenda Mbeya, unakwenda wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizi, tunaomba tukumbukwe Mtwara Corridor kwa maana ya Reli ya Kusini. Reli ya Kusini ndiyo solution itakayosaidia kuleta maendeleo Mtwara, Lindi na Mkoa wa Ruvuma. Leo Ruvuma kunapatikana makaa ya mawe Ngaka, yote yanasafirishwa kwa njia ya barabara. Utengenezaji au ukarabati wa Bandari ya Mtwara utakuwa na maana kama Reli ya Kusini itajengwa mpaka kufika Mbambabay ambako makaa ya mawe kutoka Ngaka yatatembea kwa njia ya treni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango kazi ambao unajengwa pale Mchuchuma na Liganga hauna maana kama hatutaweza kujenga Reli ya Kusini ili kusaidia uchukuaji wa mawe pamoja na chuma kutoka kwenye machimbo kwenda Bandarini Mtwara ambako bandari yake sasa inakuzwa kwa kiasi kikubwa ili kuhakikisha kwamba inahudumia huku mikoa ya kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na barabara hii ya kutoka Mtwara mpaka Nyasa, kwa kweli kwa upande wa Kusini kupitia Mkoa wa Ruvuma hakuna barabara ya lami kwenda Msumbiji. Tunaomba barabara ya Songea kwenda Ngaka iwe ya lami na barabara hii ya Songea – Mokuru – Mkenda ijengwe kwa lami kwa sababu ndiyo njia pekee itakayosaidia kukuza biashara kutoka Msumbiji kuja Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara moja ya kutoka Mtwara Pachani – Nalasi mpaka Tunduru Mjini, tumeona iko kwenye ilani, tunaomba Serikali ndani ya miaka mitano hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu ndiyo njia pekee ya kuokoa mikoa hii ya kusini, hasa Wilaya ya Namtumbo pamoja na Wilaya ya Tunduru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna barabara moja ambayo ninadhani nayo iingizwe kwenye ilani na iingizwe kwenye mpango ili isaidie watu wa Msumbiji kwa sababu watu wa Tunduru mambo yao mengi yanakwenda na watu wa Msumbiji kwa sababu tunafahamiana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Tunduru Azimio mpaka Lukumbule mpaka Makande ambayo inamilikiwa na TANROADS nayo ingeweza kuingizwa kwenye mpango kuhakikisha kwamba barabara ile inajengwa kwa kiwango cha lami ili kuwahudumia wananchi wa Tarafa ya Lukumbule na wa Jimbo la Tunduru Kusini kwa ujumla kwa ajili ya kwenda Msumbiji kupeleka mali na kuchukua mali kutoka Msumbiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia ili niweze kutoa mawazo yangu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya TAMISEMI kwanza niwashukuru Serikali kwa yote yaliyofanywa katika Jimbo la Tunduru kusini. Kwasababu ya hotuba iliyotolewa na Waziri naomba nichangie katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni suala la Utawala bora na sehemu ya pili ni Afya na sehemu ya tatu itakuwa ni suala la Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na suala la Utawala bora kama ulivyoeleza kwenye hotuba yako umeeleza vizuri namna ambavyo Utawala Bora inatakiwa viongozi wetu wa Serikali waweze kuwasikiliza wananchi ili kupata kero zao. Lakini kwenye Wilaya yetu ya Tunduru, halmashauri yetu ina vijiji 157 na ina vitongoji zaidi 1,100 tuna Mkurugenzi mmoja, tuna DC mmoja akitaka kupita maeneo yote kusikiliza kero vijijini maana yake kwa mwaka atabidi atumie zaidi ya siku 157 ili kupita kusikiliza kero katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni tatizo kubwa kwasababu linasababisha viongozi wetu wa wilaya wasiweze kufika maeneo ya vijijini kusikiliza kero za wananchi. Naomba sana tumewahi na tumepitisha mara nyingi maombi ya kugawa Wilaya ya Tunduru pamoja na kuwa na halmashauri mbili na Wilaya peke yake ziwe mbili, hii itarahisisha kupata Mkurugenzi, kupata Wakuu wa Wilaya wawili ambao watasaidia kuhakikisha kwamba wanasikiliza kero za wananchi kwa urahisi zaidi kuliko ilivyokuwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali iangalie Wilaya ya Tunduru halmashauri hii ilipata Wilaya tangu mwaka 1905 Mkoloni, walio wengi humu ndani tulikuwa hatujazaliwa, tunaomba sana Wilaya hii muifikirie, halmashauri hii iweze kugawika katika sehemu mbili ili kurahisishia wananchi wapate huduma hizi na kero zao wazieleze kwa urahisi zaidi kwasababu Mkurugenzi, Wakuu wa Wilaya watafanya kazi hii ya kuwasikiliza wananchi kwa wakati mmoja ili waweze kutoa kero zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili suala la Afya ukiangalia kama Halmashauri ya Tunduru ina kata 39, ina zahanati 52 tu kati ya vijiji 157. Kwa hiyo, kwasababu ya ukubwa wake ulivyo utakuta kituo cha afya kimoja kinahudumia kata tatu mpaka nne, tuchukulie mfano kituo cha Afya Mtina kuna kata tano zinahudumia kituo kimoja, kaini bado kuna matatizo ya miundombinu ya maeneo yale kwasababu hakuna Wodi ya akinamama hakuna Maternity ward kama nilivyozungumza hakuna chochote, hakuna chumba cha upasuaji, kwa hiyo watu wanatembea mwendo mrefu sana kwenda kufuata huduma za Afya Mtina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mara nyingi kutokana na hali mbaya ya barabara zetu zilivyo wananchi wale wanabebwa kwenye matenga, matenga yanabebwa kwenye baiskeli au pikipiki kwenda Hospitali. Akinamama wajawazito wanabebwa kwenye matenga kwenda kwenye kituo cha Afya kwa ajili ya kuwahudumia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kama sera inavyosema kila Kata iwe na kituo cha Afya, naomba tuboreshe kituo cha Afya Mtina ili kiweze kutoa huduma ile ambayo inatakiwa na ikiwezekana tuongeze kituo cha Afya kingine kwenye Kata ya Lukumbure, Nchesi Tuwemacho pamoja na Namasakata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuna ahadi ya muda mrefu sana ya Rais wa Awamu ya Nne ya kujenga kituo cha Afya Nalasi jambo hili tangu mwaka 2014 nimeuliza Bungeni term iliyopita Bunge la Kumi na Moja zaidi ya mara tatu. Halmashauri imejitahidi imepeleka zaidi ya milioni 80 pale kuanza kujenga, lakini kila mwaka kwenye bajeti yetu tunatenga shilingi 100,000,000 kwa ajili ya kuendeleza kile kituo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kutokana na ukubwa wa Halmashauri yetu na mapato yetu pamoja na kwamba tunapata zaidi ya Bilioni tatu kwa mwaka lakini hazitoshi kwasababu eneo letu ni kubwa kata ni nyingi mgao unakuwa hautoshelezi kuweza kujenga kituo cha afya maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kwasababu nimeuliza mara chungu nzima nimeenda kwa Mheshimiwa Waziri Jafo kipindi kile hadi kwa Katibu mkuu kuhusiana na ahadi hii naomba muiangalie namna ambavyo Nalasi inaweza kuingia kwenye bajeti hii kituo kile kiweze kujengwa ili kuondoa hii dhana ambayo Serikali imeshindwa kutekeleza ahadi ya viongozi wetu wa Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo suala la Elimu kwa kweli kwa Wilaya ya Tunduru tuna shule ya Msingi 152 kati ya hizo zina upungufu wa walimu zaidi ya 1,000 tunahitaji walimu 220 tunao 991. Shule nyingine zina walimu watatu hadi wanne, asilimia 60 zina walimu watano, maana walimu wengi wapo mjini hapa vijijini kwangu hakuna walimu. Naomba sana suala la walimu litakapokuja kufanyiwa ufumbuzi wa kuajiri walimu wengine tuone sisi wenye Majimbo ya vijijini kuhakikisha kwamba wanapata walimu wa kutosha ili kuhakikisha kwamba wanatoa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana shule zetu za Serikali ufaulu unakuwa ni mdogo kwasababu walimu hawapo, hawatoshelezi nichukulie mfano shule ambayo ninatoka shule ya Semeni ina zaidi ya wanafunzi 900 walimu wapo saba, madarasa yapo sita wanaelewaje hawa watu, wanafundishaje? Wanafauluje hawa Watoto? Naomba sana kwenye miudombinu ya madarasa tujitahidi kama walivyozungumza wenzangu kwenye mgao huu wa majengo ya zahanati, majengo ya shule za msingi muangalie maeneo au Majimbo ambayo yana vijiji vingi yapewe kipaumbele ili mgao uwe wa kutosha kuhakikisha kwanza tunapunguza tatizo la madarasa tunapunguza matatizo ya zahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ningependa kuongelea suala la TARURA, kwa kweli TARURA naungana mkono na wenzangu Bunge lililopita tuliomba tuongeze shilingi hamsini kutoka kwenye mafuta ili wapewe TARURA kuhakikisha kwamba barabara zetu wanatengeneza vizuri, naona wenzangu wamesahau tunaomba sana jambo hili tuliongea kwa uchungu miaka mitano iliyopita, kama mmeshindwa kwenye mafuta basi chukueni hata kwenye simu, ili tupate fungu la kuhakikisha kwamba tunajenga barabara zetu ziwe nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukulia mfano Tunduru Wilaya nzima ya Halmashauri ina kilometa 1,200 bajeti iliyopita tulipewa bilioni moja na Milioni 250 ambayo kwa hesabu ya kawaida ambayo wanatumia TARURA wana uwezo wa kukarabati barabara ambayo ina urefu wa kilometa 103 kwa maana hiyo Kilometa 1,100 zote hazina fedha, kwa maana hazijatengewa fedha, na kwa hali ilivyokuwa mbaya kama tutaendelea na mtindo huu wa TARURA kupewa fedha zilizopo bila kutenga fedha nyingine hizi barabara zitakuwa bado zina shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwenye Jimbo langu kuna barabara ambazo zina zaidi ya miaka 20 hazijawahi kupitiwa na greda, greda yao ni miguu ya watu na baiskeli, kwa hiyo inaonekana hapa kuna barabara kwasababu miguu ya watu inapita pale, baiskeli zinapita pikipiki zinapita unajua kwamba hii barabara inakwenda kijiji fulani. Kuna barabara ya Chemchem kwenda Ligoma mpaka Msinji ina zaidi ya miaka 15 haijawahi kufanyiwa ukarabati, kuna barabara ya Ipanje, Ndishyaje mpaka Marumba ina zaidi ya kilometa 40 haijawahi kufanyiwa chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya Marumba - Masugulu nayo haijawahi kufanyiwa chochote kuna barabara ya Mchina Lashya Chemacho hamna kitu, barabara Amani kiungo mpaka Misechela, nayo haijawahi kutengenezwa kwa muda mrefu sana. Naomba sana jambo hili mliangalie TARURA wapewe fedha za kutosha ili waweze kuhakikisha kwamba barabara zetu zinapitika kwa wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante mchana huu kuchangia bajeti ya kilimo kwanza naunga mkono hoja pamoja na kuunga mkono hoja naomba nichangie katika maeneo mawili jambo la kwanza ni suala la mfumo wa stakabadhi ghalani na jambo la pili ni suala la export levy kwenye zao la korosho.

Mheshimiwa Spika, tujiulize ni kwa nini mfumo wa stakabadhi ghalani uliletwa na Serikali naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tupitie sheria ya mwaka 2005 iliyeanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani na sheria ile iliyeanzisha export levy kwenye zao la korosho kwa nini tulianzisha hivi vitu viwili.

Mheshimiwa Spika, stakabadhi ghalani ilianzishwa kwa ajili ya kutatua changamoto ya masoko kwenye zao la korosho na mazao ya biashara mwaka 2005, baada ya kuanzisha na kweli mwaka 2006/2007 korosho zilikuwa zinauzwa 150 mpaka shilingi 200 kwa kilo moja baada ya mfumo wa stakabadhi ghalani kuanzishwa korosho ikawa inauzwa shilingi 600 mpaka 800 kwa kilo moja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ndugu zangu naomba sana Wabunge wezangu tuende tukaangalie sheria hii na hapa ninaomba wanaye husika bodi ya leseni za maghala, Wizara ya Kilimo pamoja na viwanda na biashara kuna haja ya kutoa elimu ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa wakulima na hasa ukianzia kwa Wabunge wenyewe tuliokuwa humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mkoa wa Mtwara Lindi Tunduru ukimwambia habari ya mfumo wa stakabadhi ghalani haufai kwenye korosho haufai kwenye ufuta utapigwa mawe. Lakini tunapoanza na jambo hili changamoto lazima ziwepo kwa sababu mfumo wa stakabadhi ghalani unakata mirija ya watu waliokuwa wanafaidika na mnyororo wa biashara hii ya ufuta, mnyororo wa biashara ya korosho mnyororo wa biashara ya kahawa na mazao mengine ambayo yako kwenye sheria ya mfumo wa stakabadhi ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mtwara tulipoanza mfumo wa stakabadhi ghalani wakati huo nakumbuka Tyson ndiye aliyekuwa waziri alitukanwa hadharani kwenye mkutano wa hadhara, viongozi wa shirika waliathirika mazao yao mikorosho ilikatwa nyumba zilichomwa moto kwa sababu ya watu wa kati ambao walikuwa wafaidika katika mfumo wa kawaida ili kujua kwamba...

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Mpakate.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nampa taarifa mbali na mchango wake mzuri kwa sababu imeingia kwenye hansard aliyekuwa waziri wa kilimo aitwe Tyson anaitwa Stephen Wasira. (Makofi)

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika naipokea taarifa kwa mikono miwili.

SPIKA: Mheshimiwa Mpakate anayekupa taarifa anamjua vizuri Mheshimiwa Stephen Wasira kwa hiyo yuko sahihi. (Makofi/Kicheko)

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, yuko sahihi naipokea taarifa yake wakati huo vurugu zilikuwa ni kubwa kuliko hizi unazoziona leo hapa kwenye korosho kwa sababu wafaidika wa mfumo wa zamani ndio waliokuwa wanawaambia wakulima wagome kufuata mfumo wa stakabadhi ghalani na haya ndio yanayotokea maeneo mengine kwenye mazao mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Naomba turejee kwenye sheria ya mfumo wa stakabadhi ghalani na kwa nini Serikali iliamua kuanzisha huo mfumo stakabadhi ghalani. Na bahati nzuri zaidi ni sheria iliyopitishwa kwenye Bunge hili la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, walianza na mazao makuu ya uzalishaji 2009 wakaongeza kwenye mazao mchanganyiko sikatai kuna changamoto ambazo Serikali inatakiwa izifanyie kazi, naomba changamoto zote zilizojitokeza kwenye mfumo wa stakabadhi gharali pamoja na ucheleweshaji wa wakulima kupata siwezi kufanya. (Makofi)

MHE: DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa unapewa Mheshimiwa Mpakate endelea Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa rafiki yangu mtani wangu Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate kwamba kila mfumo ambao utawekwa kwa ajili ya kununua mazao ya biashara ama ya chakula utakuwa na losers na winners.

Mheshimiwa Spika, mfumo uliokuwepo awali una losers na winners’ wake, na huu mfumo wa stakabadhi ghalani nao una losers na winners wake miongoni mwa watu ambao ni winners ama wafaidika mfumo huu mpya ni watu ambao wanakaa kwenye kikao kuzigungua zile zabuni wakishaona killichowekwa mle ndani utoka nje kwenda kwa wale wanunuzi ambao wame-submit zile zabuni na kuzungumza kuhusu asilimia 10 ambayo inawekwa over and above bei ambayo alikuwa ameiweka pale ambayo ulipwa pembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hao wanafaidika na hiyo ten percent hao ni winners, kwa hiyo hata ule mfumo wa zamani nao ulikuwa na watu ambao walikuwa wanafaidika na watu ambao walikuwa wanaonewa na huu mpya pia una watu ambao wanafaidika na watu wanaoonewa kwa hivyo Serikali ifanyie kazi hayo mapungufu ya hiyo ten percent ambayo huwa ilikuwa inawekwa juu ya bei ambayo mtu ame-bid kwenye karatasi nashukuru. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Daimu unapokea taarifa hiyo?

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, kwanza nikubaliane kwamba kila mfumo una winners na losers na ndio maana nimesema hata mfumo huu unachangamoto ambazo zinatakiwa zifanyiwe kazi na Serikali kwa hiyonakubaliana na maelezo yake kwamba wanatakiwa wafanyie changamoto zote zilizojitokea katika utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani hili wakulima waendelee kunufaika kuliko vile ambavyo vilikuwa mwanzo. Naamini mfumo huu unawasaidia sana wakulima kufaidika ingawa kuna changamoto hizo ambazo mwezangu amezieleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye export levy mwaka 2018 Serikali ilivyoamua kubadilisha sheria ya export levy iliahidi mambo yote ambayo yalitokana na maamuzi ya wadau wa zao la korosho kukubaliana export levy waanzishe yatayafanya. Miaka mitatu iliyopita Serikali imekusanya zaidi ya bilioni 210 kutoka kwenye sekta ya korosho kama export levy mwaka wa fedha 1920/2021/2018/ 2019 lakini Serikali haijapeleka hata shilingi moja.

SPIKA: Mheshimiwa Mpakate bahati mbaya muda ndio huo.

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii na mimi nichangie kwenye Wizara hii ya Nishati. Naungana na wenzangu waliowapongeza Mawaziri pamoja na watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, mimi nitaongelea point mbili ambazo ni muhimu kwa Wilaya ya Tunduru na Jimbo la Kusini kwa ujumla. Moja, nashukuru kwa kuletewa mkandarasi, Wilaya ya Tunduru ina vijiji 157 lakini kati ya hivyo 83 havina umeme. Kwa kuwa mkandarasi amekuja basi tunaomba ajitahidi kazi hii ianze mapema, maana ilitakiwa ianze mwezi wa tatu huu ni mwezi wa sita naamini ndani ya mwezi ujao ataanza kazi ili kukamilisha hivyo vijiji 83 ambavyo havina umeme kabisa.

Mheshimiwa Spika, katika hivyo vijiji 83 Jimbo la Tunduru Kusini kuna Kata 10 ambazo hazina umeme kabisa, ziko gizani. Kuna Kata ya Nalasi Mashariki na Magharibi, Mchoteka, Marumba, Mbati, Mtina, Mchesi, Lukumbule na Masakata pamoja na Misechela. Kata hizo zote hazina kabisa umeme, kwa hiyo tunaomba mkandarasi afanye chini juu aweze kuwahi kufanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili nitazungumzia suala la kukatika kwa umeme Wilaya ya Tunduru. Sisi tuna majibu, kwa hiyo, namuomba Waziri ayafanyie kazi majibu ambayo tumeyaona. Tunashukuru Serikali imeleta umeme Gridi ya Taifa lakini umeme ule kutoka Songea mpaka Tunduru ni kilometa 265 Kv 33, kwa hiyo, umeshindwa kuhimili vishindo. Umeme huo huo unaenda mpaka Mang’aka, Masasi mpaka Nachingwea kilometa 600 Kv 33. Kwa hiyo, majibu tuliyoyapata ni kwamba tunatakiwa tuweke substation pale Tunduru na Masasi ili ku-boost umeme uweze kufika kwa kiwango kili ambacho kinatakiwa, lakini bado mnatakiwa muongeze ile nguvu kwa maana kutoka Kv 33 mpaka kufika Kv 132. Jambo hili limekuwa ni kero kubwa sana Tunduru, umeme unakatika kila siku na kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Tunduru inapita Namtumbo, Namtumbo ina barabara mbili; ina barabara inayopita Namtumbo Mjini na ina barabara inayopita Lusewa ambako nako umeme umekwenda basi ikiwezekana mfanye utaratibu wa kuweka line mbili za kupeleka umeme Tunduru ambao unaenda moja kwa moja mpaka Masasi na Nachingwea. Mkatumia line ya Lusewa, Nalasi, Mbesa mpaka Tunduru Mjini ili iweze kufanya kazi ile ambayo imekusudiwa. Kwa hiyo, naomba sana suala hili mliangalie, mtuwekee extention nyingine ya line ambayo itaenda Tunduru kupitia Nalasi ili ihakikishe kwamba inaleta umeme ule na usumbufu unapungua kwa asilimia kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni suala la gesi. Kwa kweli kwa taarifa ya Wizara magari 700 yanayotumia gesi ndani ya miaka mitatu ni madogo sana. Naomba tuweke mkakati mahsusi, hasa sisi Wabunge walete wale wataalam watufungie yale matanki ya gesi ili magari yetu yatumie gesi kwa sababu ni gharama nafuu sana.

Nawashauri TPDC waweke kituo cha gesi hapa kwa ajili ya kujanza kwenye magari ya Wabunge pamoja na wananchi waliopo Dodoma ili kupunguza adha hii ya kutumia mafuta ya diesel na petrol. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii itatusaidia moja, kuongeza mauzo ya gesi na pili itawapunguzia watumiaji gharama ya kutumia mafuta ya petrol pamoja na diesel, haya yatatusaidia sana. Wenzetu Dangote kama ulivyozungumza wale wana magari 600, mpaka sasa magari 250 tu tena maroli ndiyo yanatumia gesi. Hili ni jambo nzuri sana na ni funzo kwa Serikali kutumia magari yanayotumia gesi ili kuhakikisha tunatumia gesi kwa uadilifu zaidi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa napenda tuliangalie ni suala la LNG pale Lindi. Kwa kweli suala la LNG ni kizungumkuti na ni la muda mrefu, naomba sasa mhakikishe ila kazi inaanza kwa maendeleo ya watu wa Kusini ili watu wa Mtwara na Lindi waone kwamba gesi yao inathaminiwa na ule mradi unaanza kwa sababu utatupatia fedha nyingi sana kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataala aliyeniwezesha kusimama leo hii na kuwa Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, nimshukuru kipekee Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kukubali hisia za Wabunge wengi ambacho ndicho kilikuwa kilio cha muda mrefu kuanzia Bunge la Kumi na Moja na Bunge hili la Kumi na Mbili kuhusu suala la maji pamoja na TARURA nashurkuru sana, naamini ametoa heshima kwa Wabunge leo tunajisikia furaha sana, kuona namana ambavyo Rais ameyachukua yale yote ambayo tulikuwa tulikuwa tunayazungumzia katika kipindi chote na kuyaweka katika bajeti na katika utekelezaji halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuchambua bajeti hii kwa makusanyo yaliyopita ya Mwaka 2020/ 2021niwapongeze sana Wizara ya Fedha na wale wote waliohusika kukusanya fedha kwa kutumia mipango mbalimbali na kufikia asilimia 86 ya makusanyo yetu ya bajeti iliyopita. Kwa kweli hili jambo ni likubwa tunatakiwa tuwape pongezi hasa Wizara ya Fedha na wengine wote kwenye idara mbalimbali waliohakikisha kwamba fedha hizi asilimia 86 ya makisio ya Mwaka wa Fedha 2020/2021 yamefikiwa naomba sana Jambo hili tuliangalie na tuwape moyo hawa watu waendelee kufanya vuzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo nikirejea kwenye bajeti zilizopita za kisekta za Wizara mbalimbali sioni reflation hii ya asilimia 86 kwenye shughuli za maendeleo katika Wizara zingine, inaonekana kwamba kuna Wizara ambazo zimepata fedha za maendeleo chini ya asilimia 30 ambacho kwa kweli kwa hali ya kawaida hawasemi lakini inaonekana kama kuna Wizara zimekuwa ni muhimu zaidi kuliko Wizara zingine kwa kupewa fedha ya maendeleo ambayo iko chini ya asilimia 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama makusanyo yamekua asilimia 86 kwa tuliosoma hesabu tulitegemea na shughuli za maendeleo kwenye Wizara mbalimbali zifikie zaidi ya asilimia 50 lakini haikuwa hivyo, ina maana kwamba kuna Wizara ambazo zimependelewa zaidi kwa makisio yake kutekelezwa ya maendeleo zaidi kuliko vile ambavyo vimekisiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa hali ilivyokuwa kwa miezi miwili iliyobaki makusanyo yanaweza yakafika asilimia 90 au 92 kwa mwenendo huu, kwa hiyo naomba zile Wizara ambazo hazijafikia angalau asilimia 50 nazo ziangaliwe zipewe fedha za maendeleo ili haja ile ya mipango yao iweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia na hili kuna jambo lingine naomba Wizara nalo uliangalie kwenye miradi hii ya maendeleo nashukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa milioni 500 kwa kila Jimbo. Siku zote huwa tunazungumza majimbo yetu yanatofautiana wote tuna furaha kila Jimbo limepata milioni 500, lakini kwa maeneo mengine ni kilio! Kwa sababu hiyo milioni 500 namna ya kuitumia na kilometa tulizo nazo ni kizungumkuti, tunaona kwamba hili jambo mlione mbele ya safari mnavyogawa hivi vipaumbele vya maendeleo angalieni na ukubwa wa Majimbo kama tunavyolia siku zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ugawaji wa fedha za majengo, majengo ya zahanati, shule za msingi na sekondari ni vizuri basi muangalie na ukubwa wa majimbo, wingi wa shule na Kata jinsi ilivyo kubwa ratio ni muhimu sana. Kwa sababu inaonekana mwisho wa siku kuna Majimbo yataenda mbele Zaidi kuliko Majimbo mengine kutokana na ukubwa wa Majimbo ulivyo. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati unagawa mipango hii ya miradi muangalie na ukubwa wa Majimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano; Tunduru tuna Kata 39 Jimbo langu lina Kata 15 napata shule moja, mwingine ana Kata Nane anapata shule moja, hayo majengo kila mmoja anapata matano matano ina maana mwenye kata nane atamaliza mapema kujenga majengo kuliko wenye Kata 15 na 39. Kwa maana hiyo tunaomba ratios iangaliwe wakati wa kugawa miradi ya maendeleo ili kila mmoja afikie ile standard ambayo inatkiwa kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana kulizungumza suala la kilimo, kwa watu wa Kusini, kilimo cha Korosho ni uti wa mgongo. Mkutano wa 18 uliona sakata la korosho lilivyokuwa, natamani sana ile sheria ya export levy iangaliwe upya ili kuhakikisha kwamba aidha ifutwe ili kile kiwango kinachotozwa kwenye export levy ambacho ni sehemu ya gharama ya nunuzi kirudi kwa mkulima au irudishwe yale yote yaliyokubaliwa na wadau na kuanzisha export levy basi yafuatiliwe ili sekta ya korosho iweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili mwaka 2018 lilipotokea uzalishaji wa korosho umeshuka kwa asilimia kubwa. Mara ya mwisho tumezalisha tani 330,000, lakini msimu uliopita tumepata tani 206,000 ni kwa sababu kwamba yale yote ambayo yalikuweko kwenye export levy yalitakiwa yarudi kwenye kutekeleza sera ile ya Bodi ya Korosho na makubaliano ya wakulima pamoja na wadau wa korosho hayakuweza kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ahadi ya Serikali kwamba yote yale Serikali itatekeleza lakini kwa masikitiko makubwa napenda kusema ndani ya miaka mitatu misimu mitatu, Serikali imetoa bilioni tatu kwenye kituo cha Naliendele na bilioni 10 kwa ajili ya kununua sulphur, yale mengine yote hayakuweza kutekelezeka.

Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie kwa namna moja aidha wafute export levy kwenye korosho kwa sababu hakuna zao lingine lolote la biashara ambalo linatozwa export levy, hii tulianzisha wenyewe kwa ajili ya kuona namna ambavyo zao letu la korosho linadumaa na tukaanzisha ili kutafuta fedha la kusaida zao liweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeikiti, jambo hili kwa kweli Serikali inahangaika sana inatafuta kila aina, nawaonea huruma Wizara ya Kilimo wanatafuta kila aina na sasa hivi kuna mgogoro wa sulphur huko kwa sababu wakulima wetu wameshindwa kupata sulphur ili waweze kuhudumia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa nizungumzie ni suala la hili property tax. Niishukuru Serikali na niipongeze Serikali kwa kubuni jambo hili, lakini kuna changamoto ambazo mnatakiwa mzifanyie kazi hasa tunaotoka Majimbo ya Vijijini, Naibu Waziri wetu wa Nishati anasema wekeni umeme hata kwenye nyumba za matembe. Leo nyumba nyingi za matembe zina umeme, zina Luku tuna zi-charge shilingi 1,000 maana yake tunaongeza gharama kwenye zile nyumba za tembe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wakati wa utekelezaji muangalie hizi nyumba ambazo kwa kweli hadhi yake hazistahili kulipa hii property tax kwa kutumia LUKU na hasa zile nyumba za ibada. Nyumba za ibada ni kweli vijijini zina umeme lakini hizo ni nyumba za ibada kwa hiyo mfanye chini juu muweze kutambua nyumba hizi za ibada mtambue nyumba hizi za matembe ambazo hazistahili kulipa hii property tax ili kuleta maendeleo kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka kuzungumza suala la Linganga na Mchuchuma. Namshukuru Rais ametoa mwanga wa kuendelea na mradi huu wa Linganga na Mchuchuma. Kwenye Linganga kwa maana ya makaa ya mawe kuna matatizo, naomba turejee mkataba ule, turejee sheria mpya ya Madini, Ngaka pale tunachima madini ya makaa ya mawe, lakini Serikali haipati chochote, hata NDC yenyewe hawapati chochote kutokana jinsi mikataba ilivyokaa na hawa wawekezaji ambao tumeingia nao mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili Serikali ifanyie kazi ipitie ile mikataba yote Ngaka, ipitie mikataba ya Kiwira, ipitie mikataba ya Mchuchuma ili kuhakikisha kwamba Serikali inapata mapato kutokana na makaa ya mawe ili kuendeleza nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, napenda kutoa mchango wangu kama ifuatavyo; kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wake pamoja na Waziri Mkuu pamoja na Naibu wote wawili kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020.

Mheshimiwa Spika, pamoja na utekelezaji huo mzuri naomba kutoa mchango wangu kama ifuatavyo; kwanza ni usambaji wa umeme vijijini. Nipongeze dhamira ya dhati ya Serikali ya kusambaza umeme na kufikia zaidi ya vijiji 9000, ombi langu kwenye usambazaji umeme kuangalia yale maeneo ambayo bado usambazaji wa umeme kama ilivyo kwenye Jimbo la Tunduru Kusini ambapo kati ya vijiji 65 ni vijiji vitano ndio vina umeme tena kwa mitaa michache sana kama kijiji cha Mchuruka, Azimio,Umoja,Chiwana na Airport pamoja na kijjiji cha Mbesa. Hivyo ninaomba Serikali kupitia mradi wa REA III sehemu ya pili kutoa kipaumbele maeneo ambayo yapo nyuma kama ilivyo Jimbo la Tunduru Kusini.

Pili ni usambazaji wa maji vijijini; ninaishukuru Serikali kutupatia miradi ya maji mitano katika vijiji vya Amani, Mtina, Mbesa, Lukumbule na miradi midogo midogo ya Namasakata, Nalasi, Chiwana, Semeni.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali ni kuongeza kiwango cha fedha kwenye maji vijijini kwani vijiji vingi havina maji kutokana na tabianchi, mito mingi imekauka hivyo kuna mahitaji ya visima vifupi na visima virefu. Kutokana na uwezo mdogo wa wananchi wetu kulipia maji huko vijijini ni vyema miradi hiyo iwekewe umeme wa jua kupunguza gharama za uendeshaji, hasa kwenye mradi wa Nalasi, Lukumbule na Mtina. Serikali imetumia fedha nyingi sana lakini haifanyi kazi kama ilivyotarajiwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, tatu ni kuhusu barabara za vijijini na mijini. Kutokana na hali ya mvua nyingi zilizonyesha mwaka 2019/2020 ninaiomba Serikali kuangalia uwezekaji wa kuongeza fedha TARURA ili iweze kukarabati barabara na madaraja zilizoharibika na mvua. Kuna haja ya kuongezea TARURA fedha kutoka Mfuko wa Barabara kutoka 30% mpaka 40% ili kutengeneza barabara nyingi zaidi kwani mazao mengi ya chakula na biashara yanatoka huko vijijini.

Mheshimiwa Spika, nne ni suala la elimu ya msingi na sekondari. Ninaomba Serikali kutenga fedha nyingi za kujenga madarasa ya shule ya msingi na sekondari kukabiliana na wingi wa wanafunzi ili kuondokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika darasa moja.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Tunduru Kusini wananchi walifyatua tofali zaidi ya laki moja kwa ajili ya kujenga miundombinu za shule za msingi na sekondari lakini Halmashauri imekosa fedha za kujenga miundombinu hiyo. Hivyo ninaiomba Serikali kutoa fedha kuunga mkono juhudi hizo za wananchi ili kupunguza adha ya madarasa na vyoo pamoja na nyumba za walimu. Vilevile shule nyingi za kata hazina maabara ya sayansi pamoja na upungufu wa walimu wa sayansi. Ni vyema Serikali ikaitupia jicho.

Katika Jimbo la Tunduru Kusini hakuna sekondari ya high school, hivyo ninaiomba Serikali kuweka high school katika kila tarafa ili kuongeza usihofu wa watoto kwenda high school.

Mheshimiwa Spika, tano, ujenzi wa vituo vya afya na zahanati. Nipongeze Serikali kwa kutupa vituo vitatu katika Halmashauri ya Tunduru, pamoja na pongezi ninaomba Serikali iongeze kukarabati Kituo cha Afya Mtina ambacho hazikupata majengo ya ziada ya kuboresha kama ilivyo Nkasale na Mchoteka. Vilevile ninaiomba Serikali kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga Kituo cha Afya Nalasi, Mbeya ambapo kuna vijiji sita na kata mbili na wakazi zaidi 30,000.

Vilevile ninaomba ongezeko la kasi ya ujenzi ya zahanati kwani bado idadi ya zahanati na vituo vya afya ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watu.