Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Edwin Amandus Ngonyani (10 total)

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza swali la nyongeza, naomba kuchukua fursa hii kukushukuru sana wewe kwa ushiriki wako mkubwa kutafuta fedha za kujenga Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo kupitia Selous Marathon na hivi karibuni tutakuwa na chakula cha jioni kule Dar es Salaam, nakushukuru sana. Wananchi wa Namtumbo wataenzi sana kazi hiyo unayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, hivi Serikali hususani Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na TAMISEMI haioni umuhimu wa kuongeza bajeti ya kuendeleza ujenzi wa jengo la upasuaji kutoka milioni 100 zilizotajwa kwa mwaka ujao wa fedha hadi walau bilioni moja ili kweli ujenzi ufanyike?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla alishafika Lusewa, Makao Makuu ya Mji Mdogo wa Sasawala na kujionea umbali ulivyo kutoka pale Lusewa hadi maeneo ambayo yanaweza yakapatikana huduma za upasuaji na hivyo akajionea kabisa hatari ambayo akina mama wajawazito wanaipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi Waziri wa TAMISEMI atatusaidiaje kuteleleza ahadi ambayo Naibu Waziri huyo aliitoa ya kuhakikisha Kituo hiki cha Afya cha Lusewa kinakamilika na kuanza kutoa huduma ndani ya mwezi mmoja wakati akijua kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo haina fedha kabisa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ngonyani kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwalilia wananchi wake. Bahati nzuri mimi nimeweza kufika kule Namtumbo na Naibu Waziri wakati huo sasa hivi Waziri wa Maliasili, ni kweli changamoto ni kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwa ujumla wake na ndiyo maana kutokana na changamoto ya eneo hili ukiachia kile Kituo cha Afya cha Namtumbo tulichopeleka takribani shilingi milioni 400 mwezi Desemba na kazi tume-target mpaka tarehe 30 Aprili, zote ziwe zimekamilika lakini tumeanza juhudi tena kubwa zingine kuhakikisha tunaongeza vituo vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Msindo na Mkongo ambapo tunaenda kuweka thearter maalum kwa ajili ya upasuaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tumesikia kilio chake, tutafanya kila liwezekanalo na timu yangu hapa chini ya Naibu Mawaziri wangu kuhakikisha kwamba mambo haya yanaenda kwa kasi na ndiyo maana kutokana na jiografia ya Wilaya ile jinsi ilivyo leo hii tuna zoezi tena la vituo vya afya viwili. Ahsante.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa. Na mimi nilitaka niulize kuhusu barabara ya kutoka Mtwara – Pachani - Mkongo – Gulioni – Ligera - Lusewa inaenda Magazine - Likusenguse hadi Tunduru ambayo ina urefu wa kilometa 300 iliyoahidiwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Awamu ya Nne, ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kipande hicho cha barabara kimekuwa kikisumbua kwa muda mrefu na kwa kweli tumekuwa tukipata mawasiliano mazuri sana na Mbunge akiwa anatetea kipande hicho cha barabara. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo suala tunalo na tunalifanyia kazi; tunawasiliana mara kwa mara na Meneja wa TANROADS wa Mkoa kuhakikisha kwamba inaingizwa kwenye utaratibu ambapo tutaanza kuifanyia matengenezo makubwa. Ahsante.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Katika vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, ni pamoja na vijiji vya Wilaya ya Namtumbo. Nampongeza sana kwa safari yake na mambo makubwa tuliyoyafanya katika Wilaya ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka tu nifahamu, kwa kasi ile aliyoitumia kutatua miradi mitano ambayo ni ya World Bank, atatumia kasi ile ile kutatua miradi mitano mingine ili tutimize ile miradi kumi ya World Bank?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kasi hiyo hiyo ambayo tumeitumia kukamilisha miradi inayoendelea, tutaendelea nayo kwa sababu bado tuna miradi 376 ambayo haijakamilika kutoka kwenye miradi 1,810. Kwa hiyo, kasi ni hiyo hiyo. Tunachosisitiza ni kwamba Halmashauri ziendelee kusimamia vizuri wakandarasi watekeleze miradi na sisi wakati wowote kutoka kwenye Mfuko wa Maji ukileta certificate tunalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji aliyomjibu Mheshimiwa Chikambo, Mheshimiwa Chikambo katika swali lake aliomba aletewe orodha ya miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge wote, nilitaka tu nizungumze kwamba Wizara ya Maji inatenga fedha na inapeleka katika Halmashauri. Watekelezaji ni Halmashuri. Wao ndio wanaoweka mpango kazi kuona ni vijii gani watatekeleza. Kazi yetu sisi kuweka ni miongozo na wakishatekeleza, wanaleta hati, sisi tunalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pia hilo ni jukumu la Waheshimiwa Wabunge wao wenyewe kwa sababu ni Madiwani kwenye maeneo yao kujua ni miradi ipi inatekelezwa ni miradi mingapi.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Tatizo la Mtera halina tofauti kabisa na tatizo la kata nzima ya Likuyu Sekamaganga na hususan Kijiji cha Mandela. Walioathirika walishafanyiwa tathmini muda mrefu na hakuna dalili ya kuwalipa hicho kifuta jasho na kifuta machozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itatoa hicho kifuta jasho na kifuta machozi kwa wale walioathirika katika Vijiji vya Mandela, Likuyu Sekamaganga, Mtonya pamoja na majirani zao wa Mgombasi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kumekuwa na matukio mengi katika lile Jimbo la Tunduru na maeneo mengine pamoja na kile Kijiji cha Mandela. Naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba matukio haya ya wanyama waharibifu ni mengi sana katika nchi yetu kwa sasa hivi. Hili inatokana na kwamba uhifadhi umeimarika na wanyama wameongezeka lakini pia kuna changamoto nilizozisema nilipokuwa najibu swali la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kuna matukio zaidi ya 3,509 ambapo wananchi wamepatwa na matatizo mbalimbali. Jumla ya fedha ambazo zinadaiwa mpaka sasa hivi katika maeneo na wilaya mbalimbali ni zaidi shilingi milioni 828. Kwa hiyo, kazi tunayoifanya sasa hivi ni kutafuta hizi fedha ili kuhakikisha kwamba hao wananchi wote walioathirika na wanyamapori na wanyama waharibifu basi waweze kupata kifuta jasho na kifuta machozi kinachostahili. Baada ya kupata fedha hizo tutafanya hivyo mara moja. (Makofi)
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, pamoja na kusahisha jina la eneo la Kitungule badala ya Kitungule isomeke Kilungule.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ali Mangungu anaishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa iliyoifanya katika kipindi hiki cha mwaka mmoja na kwa kweli wanaomba yale maeneo yaliyobakia yakamilishwe, kwa hiyo, eneo la kwanza ni ombi.
Mheshimiwa Spika, pili, ndugu zao wa Namtumbo wanaomba kuna vijiji 70 na miji midogo miwili. Katika miji midogo miwili mji mdogo mmoja tu mitaa yake ina umeme, vinginevyo vijiji vyote 70 pamoja na mitaa ya Mji Mdogo wa Lusewa havina umeme. Pamoja na kwamba dalili zinaonekana lakini muda unapita na hakuna dalili ya umeme kupatikana katika Wilaya hiyo nzima ya Namtumbo.
Ni lini Serikali itawasha umeme katika Wilaya ya Namtumbo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza tumepokea pongezi za Mheshimiwa Mbunge Mheshimiwa Issa Ali Mangungu na Serikali tunampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia maendeleo ya nishati katika Jimbo lake la Mbagala na ombi lake tumelipokea katika maeneo yaliyosalia kama nilivyosema mradi umekamilika kwa asilimia 90 basi asilimia 10 ndani ya muda mfupi itakamilika.
Swali lake la pili la ndugu wa kutoka Jimbo la Namtumbo. Kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu na niwapongeze Wabunge wote wa Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe kwa kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa line ya kusafirisha umeme Makambako - Songea yenye urefu kilometa 250. Napenda nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge tarehe 01 na tarehe 02 tulifanya ziara kukagua mradi huo na kimsingi mradi umekamilika.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa substation tatu Madaba, Songea - Makambako umekamilika, ujenzi wa line umekamilika, kinachoendelea sasa hivi ni usambazaji umeme katika maeneo ya vijiji 122, vijiji 60 ni Mkoa wa Ruvuma, na vilivyosalia ni Mkoa wa Njombe. Katika Jimbo lake la Namtumbo takribani vijiji 35 vitapata umeme kupitia mradi huu mkubwa wa ujenzi wa line ya Makambako - Songea.
Mheshimiwa Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako mwezi huu Septemba tarehe 25 au 26 mradi huu utazindua rasmi na sasa hivi kinachoendelea ni test mbalimbali zinazoendelea katika line hii. Kuanzia tarehe 15 Septemba tutasafirisha umeme kwa mara ya kwanza kwenye Gridi ya Taifa kuelekea Songea Mkoa wa Ruvuma. Nawashukuru sana wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kutuunga mkono na kwa kweli mambo mazuri. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wananamtumbo hawafahamu ni majengo gani yanayojengwa na wapo wanaosema kwamba linajengwa jengo la bwalo la chakula, nyumba za wakufunzi, nyumba za kulala wanafunzi, kwa hiyo wanahisi tu hawajui. Je, Serikali iko tayari kuwaeleza wananchi wa Namtumbo kwanza, hizo hisia zao kama ni sahihi na kama sio sahihi ni majengo gani yanayojengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Profesa Ndalichako alipofika Namtumbo watu walikuja kupata taarifa baada ya yeye kuondoka na walipobeba ngoma zao kwenda kumshangilia wakakuta hayupo, je, yupo tayari hicho chuo kitakapokamilika ama yeye, kwa sababu wakimwona yeye ni sawa wamemwona Mheshimiwa Rais au kiongozi yeyote wa ngazi ya juu aje akifungue kile chuo ili wale wananchi waondoe kiu yao ya kutaka kuwaona viongozi wao wanaowapenda?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ni majengo gani yanajengwa katika ujenzi unaoendelea, naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa majengo ambayo yanajengwa ni jengo la utawala, karakana za ufundi seremala, uashi, bomba, umeme wa majumbani na maabara ya komputa. Majengo mengine ni pamoja na madarasa, maktaba na stoo ya generator lakini katika awamu zitakazokuja tutajenga majengo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili kama Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kwenda wakati wa ufunguzi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa namna Serikali inavyotilia mkazo suala la ufundi na namna ninavyomfahamu Mheshimiwa Waziri anavyosisitiza masuala hayo Wizarani, nina hakika kwamba atakuwa tayari kwenda katika ufunguzi lakini hata baada ya kusikia kuna ngoma hata mimi nafikiri nitaungana naye. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa. Niipongeze Serikali kwa hatua inazozichukua kuimarisha soko la tumbaku nchini. Njia mojawapo ya kuimarisha soko la tumbaku kwa upande wa sisi Wanaruvuma ni kufufua Kiwanda cha Kuchakata Tumbaku kilichoko Songea ambacho kinamilikiwa na SONAMKU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SONAMKU kwa kushirikiana na mnunuzi wanakwamishwa na Serikali kwa kutoilipa VAT return ya jumla ya shilingi bilioni 12 Kampuni hiyo ya Premium Active Tanzania Limited na hivyo kampuni hiyo kushindwa kushirikiana na SONAMKU kuanzisha au kufufua kile kiwanda.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha hizi fedha zinalipwa ili sisi Wananamtumbo tuwe na uhakika na soko la tumbaku kwa kufufua hicho kiwanda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wananamtumbo tunajihusisha vilevile na kilimo cha Korosho na Mazao mchanganyiko ya mahindi mbaazi, ufuta, alizeti na soya. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha masoko ya mazao haya ili Wananamatumbo tuendelee kupata nafuu lakini na suala la mbolea au pembejeo kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Edwin Ngonyani kwa namna alivyoshirikiana na Serikali kupata soko la tumbaku kwa kampuni ya Premium Active Tanzania Limited. Nampongeza sana Mheshimiwa Ngonyani na kwa namna anavyohangaikia Wananamtumbo katika kuhakikisha wananufaika na sekta ya kilimo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ni kufufua viwanda vikiwemo viwanda ambavyo vinachakata mazao yanayotokana na kilimo likiwemo zao la tumbaku. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya Kilimo tutakaa na wenzetu upande wa Wizara ya Fedha kuangalia hili suala la VAT ambalo Mheshimiwa Ngonyani ameliuliza kama swali lake la nyongeza namba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali lake la pili ni kuhusu mkakati wa Serikali katika uhakikisha tunapata masoko ya uhakika ya mazao mchanganyiko pamoja na zao la tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya Serikali ya kuhakikisha tunapata masoko ya uhakika kwa wakulima wetu kwanza tumeanza na mikakati ya kupata institutional buyers na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, walishuhudia Serikali ikisaini mkataba na World Food Programme kwa upande wa zao la mahindi kwa wakulima wetu na tunaendelea kuongea na institutional buyers wengine ambao watasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara kwa kushirikiana na Balozi zetu nje ya nchi tunaendelea kuwasiliana nao na kuangalia mikakati ya kushirikiana ili tuweze kupata masoko zaidi katika mazao mchanganyiko na mazao ya kimkakati. Kwa mfano, mwezi Mei, kuna timu inaenda China hususan kwa ajili ya kutafuta soko la tumbaku pamoja na parachichi, karanga na mazao mengine.

Kwa hiyo napenda kumhakikishia Mheshimiwa Ngonyani pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inaendelea kujipanga na tayari tumefanikiwa katika maeneo ya kupata masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Waheshimiwa Wabunge kama Mheshimiwa Ngonyani alivyoshirikiana na Serikali kupata soko la tumbaku kuptia kampuni ya Premium Active Tanzania Limited, basi na wao waendelee kushirikiana na sisi Wizara ya Kilimo kuwasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika. Ahsante.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nitoe shukurani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa makubwa aliyoyafanya katika Wilaya ya Namtumbo. Alipofika tarehe 5 Aprili, 2019 katika Kijiji cha Nchomoro katika mambo ambayo wananchi walimlalamikia ni pamoja na kutaka maeneo ya kulima mpunga katika maeneo ambayo wamezoea kuyalima. Maeneo hayo ni Luvele, Bomalili, Nahimba, Makangaga na Mpigamiti katika Kijiji cha Nchomoro na Nangunguve, Namayani na Mkuti katika Vijiji vya Mteramwai na Songambele pamoja na eneo la Nandonga la Kijiji cha Likuyu Sekamaganga. Jibu ambalo Mheshimiwa Rais alilitoa linafanana kabisa na kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, nashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, tatizo langu tu katika utekelezaji, Halmashauri pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya bado hawajapata fedha za kupitia upya hayo maeneo ili kupata maeneo ya kilimo, ufugaji pamoja na hifadhi na hivyo kuondoa mgogoro huo moja kwa moja lakini fedha za kufanya doria kila wakati zinapatikana. Sijui suala hili la fedha kama Wizara inaweza kutusaidia zipatikane ili tatizo hili liondoke moja kwa moja? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mimi kama Mbunge wao katika maeneo hayo kila napopita changamoto hii ya kukosa ardhi ya kilimo hasa kilimo cha mpunga katika maeneo yote yanayozunguka hifadhi za Mbalang’andu, Kimbanda na Kisungule ndiyo kubwa. Dawa pekee ni kupitia upya mipaka ya maeneo hayo na kupata maeneo rasmi ya kilimo, uhifadhi na mifugo. Je, ni lini Serikali itatusaidia kuondoa hili tatizo moja kwa moja kwa kufanya hayo mapitio haraka inavyowezekana kama makubaliano yalivyokuwepo toka awali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuwasemea na kuwatetea watu wake ili kupunguza migogoro kati ya wafugaji na wakulima katika Jimbo lake na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la msingi anataka kujua kwa nini ahadi ya Mheshimiwa Rais haijatekelezwa lakini pia kazi ya kupitia na kutenga maeneo haijafanyika kwa maana ya Halmashauri na Mkuu wa Wilaya labda kama kuna upungufu wa fedha. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mambo ambayo hatuwezi kufanya mchezo nayo ni pamoja na kuchezea ahadi za Mheshimiwa Rais kama amepita mahali na kuahidi. Kwa hiyo, naomba nimuelekeze Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo na Mkurugenzi wakae pamoja wajadiliane, watuambie changamoto iliyopo ili tuweze kusaidiana kwa pamoja na Wizara kuondoa changamoto hii lakini pamoja na kuondoa kero kwa wananchi wale na magomvi yasiyokuwa na lazima lakini kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais katika eneo hilo la Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge anauliza namna ambavyo tuliweza kusaidia kupima maeneo haya kuondoa changamoto mbalimbali katika mazingira ambayo ameyazungumza. Mheshimiwa Mbunge tumeshazungumza juzi na jana na Mheshimiwa Waziri ameshalipokea hili, tumetoa maelekezo maeneo yote ambayo kuna migogoro hii ya ardhi kama kuna changamoto ya fedha, mambo ya mipaka na vitu mbalimbali viangaliwe. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais amechukua hatua hata maeneo ya hifadhi zile za Taifa (National Parks) ametoa maelekezo Mawaziri wamepita kuchukua changamoto mbalimbali. Mheshimiwa Rais angependa wananchi wakulima na wafugaji wapate maeneo yao, mipaka itambuliwe na waishi kwa amani bila magomvi ili waweze kujiletea maendeleo. Mheshimiwa Mbunge naomba utupe fursa tuifanyie kazi, viongozi wa eneo hili watoe taarifa, tushirikiane pamoja na tuondoe changamoto katika maeneo haya ya mipaka. (Makofi)
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Serikali yetu kwa ujumla kwa jibu hilo zuri.

Hata hivyo ili tuwe na uelewa wa pamoja kati ya Serikali na wakulima wa tumbuku wa Namtumbo; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuzifafanua changamoto hizo za mnunuzi wa tumbaku zinavyotakiwa kutatuliwa na Serikali kwa ujumla wake? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali dogo la pili, wakulima wa Namtumbo wanalishukuru sana Bunge lako tukufu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa kwa umahiri mkubwa na Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, Rais wetu kwa kuwawezesha wakulima wa Namtumbo hadi sasa katika minada mitatu tu wamepata shilingi bilioni 5.5 la zao la ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. (Makofi)

Je, Serikali iko tayari kuendelea kutatua changamoto za wakulima wa Namtumbo hususan katika mazao ya korosho, soya, mbaazi na mengineyo na hasa katika korosho wale wakulima wachache ambao mpaka sasa hawajalipwa, wameuza korosho zao mwezi wa kumi hususan wa Tarafa wa Sasawala, lini watalipwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Ngonyani angependa kupata commitment ya Serikali kama tunaweza tukakaa pamoja na Mheshimiwa Mbunge, pamoja na wakulima wake ili kuweza kutatua changamoto ambazo anakabiliana nazo huyu mwekezaji PATL. Kwa sababu ya muda na kwa vile Mheshimiwa Ngonyani ni mfuatiliaji mzuri, hili ni swali la pili katika kikao hiki basi nimuahidi kwamba nitakaa naye na tutafute muda kuweza kukaa pamoja na kuainisha hizi changamoto ambazo tayari Wizara tunazifahamu na kuzijadili na kuangalia namna bora ya kuzitatua haraka iwezekanavyo ili mwekezaji huyo aweze kuendelea na uwekezaji, wakulima wetu waweze kupata mahali pa kuchakata tumbaku yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Ngonyani anauliza kama Serikali iko tayari kufanya maboresho na kuongeza jitihada za kuhakikisha mazao ya korosho, soya, mbaazi na mazao mengineyo yanamsadia mkulima Mtanzania na jibu ni ndiyo. Azma ya Serikali ni kuhakikisha mazao yote haya na mengine tunaongeza uzalishaji na tunawasaidia wakulima wetu kuwa na kilimo cha tija na sambamba na hilo tunawasaidia wakulima wetu kuwaunganisha na masoko. Suala la malipo ya korosho nimhakikishie Mbunge kuwa Serikali inaendelea kufanya kila iwezekanavyo kuhakikisha waliobaki ambao hawajalipwa na ambao ni wachache waweze kulipwa malipo yao, ahsante.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa huyu mwekezaji amefanya jitihada kabisa kuhakikisha kwamba anawekeza katika kile kiwanda na amewekeza anadai zaidi ya dola za Marekani milioni tatu na hivi sasa alikuwa amesimama kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikimkabili. Lakini Serikali tumepanga kabisa kwamba ndani ya wiki mbili hizi tutakaa naye ili tuweze kuzungumza pamoja ikiwa ni pamoja na kuangalia suala lile la madai ya VAT ambayo yalikuwa yamekaa muda mrefu ambayo anasema kwamba yamemuathiri katika kuendeleza hiki kiwanda. Kwa hiyo, tutakaa naye pamoja na makampuni mengine yale ambayo nayo yana changamoto hiyo hiyo ili tuweze kuhakikisha kwamba hili suala linafikia mwisho na kusudi waendelee kununua zao letu la tumbaku. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona, naomba nirudi tena pale kwenye Kiwanda cha SONAMCU, nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu kwamba changamoto iliyopo kwa kutotekeleza ule mkataba, ni kwa Serikali kutowarudishia wale wanunuzi haki yao ambayo ni VAT return na kama mnakumbuka Mheshimiwa Rais aliliongelea hilo juzi kwamba inaonekana Wizara ya Viwanda haifanyi jitihada yoyote ya kuwasaidia wawekezaji kuondokana na changamoto zao.

Je, sasa Wizara ya Viwanda na Biashara imejifunza na iweze kutatua changamoto hiyo ya VAT return kwa kampuni inayonunua tumbaku Songea ili iweze kujenga kile kiwanda?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kama nilivyosema hapo awali, hizi VAT return haidaiwi na kiwanda cha SONAMCU peke yake, kuna wadau wengi ambao walidai, wengine wamerejeshewa, wengine bado wapo katika mchakato wa uhakiki.

Nipende tu kusema kwamba, kimsingi Serikali ina dhamira njema ya kurejesha VAT returns lakini, baadhi ya waliodai, wengine hawakutoa taarifa ambazo ni sahihi, na hiyo imepelekea kufanya zoezi hili kuwa kubwa kwa kuhakiki wale wote ambao walikuwa wanadai VAT returns zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Wizara inao wajibu wa kuendelea kujifunza lakini kuendelea kutatua changamoto ambazo wote tunaona kwamba ni za msingi. Tunayo dhamira njema na niseme tu kwamba katika maeneo ambayo tutafuatilia ni pamoja na Kiwanda hiki cha SONAMCU Songea.