Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Eng. Edwin Amandus Ngonyani (176 total)

MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Ujenzi wa barabara ya Sumbawanga hadi Mpanda bado haujakamilika.

Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utakamilika?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Lupembe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya kutoka Sumbawanga hadi Mpanda umegawanyika katika sehemu nne ambazo ni Sumbawanga – Kanazi km 75, Kanazi – Kizi – Kibaoni km 76.6, Kibaoni – Sitalike km 72 na Sitalike – Mpanda km 36.

Mheshimiwa Spika, maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya Sumbawanga – Kanazi umefikia asilimia 68.6 na mpaka sasa km 43.47 za lami zimekamilika, maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya Kanazi hadi Kibaoni kupitia Kizi ujenzi umekamilika kwa asilimia 50.3 na mpaka sasa km 23.43 za lami zimekamilika. Maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya barabara ya Sitalike – Mpanda ni asilimia 76 na mpaka sasa km 20 za lami zimekamilika. Ujenzi wa sehemu hizo tatu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2016.

Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu iliyobaki ya Kibaoni hadi Sitalike ambayo ni km 7.2 umekamilika na Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI aliuliza:-
Wilaya ya Kilombero ni moja kati ya Wilaya zinazozalisha kwa wingi mazao mbalimbali ya kilimo hususan zao la mpunga:-
(a) Je, ni nini kauli rasmi ya Serikali juu ya kuanza na kumalizika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kidatu - Ifakara na Ifakara - Mlimba?
(b) Je, ni lini Daraja la Mto Kilombero linalounganisha Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga litaanza kujengwa na kuanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa kilometa 73.26 ni sehemu ya barabara kuu ya Mikumi – Kidatu – Ifakara – Mahenge yenye urefu wa kilometa 178.08 na barabara ya Ifakara – Mlimba ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Ifakara – Taveta – Madeke yenye urefu wa kilometa 231.53
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara kwa kiwango cha lami umekuwa ukitekelezwa kwa awamu kati ya Ifakara na Kidatu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika awamu ya kwanza na ya pili, ujumla ya kilometa 16.17 zilijengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami kuanzia Kijiji cha Kiberege hadi kijiji cha Ziginali na kutoka eneo la Kibaoni (Ifakara) hadi Ifakara Mjini.
Awamu ya tatu ya utekelezaji ilihusisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya barabara kutoka Kibaoni (Ifakara) hadi Ziginali kilometa 16.8; na sehemu ya barabara ya Mikumi – Kidatu – Ifakara kilometa103.3 ambao umekamilika. Usanifu wa barabara umegharamiwa na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na Umoja wa nchi za Ulaya (EU) umeonesha nia ya kutoa fedha za ujenzi. Zabuni za kuanza ujenzi zinasubiri uthibitisho wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) kuhusu uwepo wa fedha za kutosha kugharamia mradi huo.
Aidha, upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara ya Ifakara – Taveta – Madeke kupitia Mlimba upo katika hatua za mwisho na ujenzi wake utaanza baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika na fedha za ujenzi kupatikana.
Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Daraja la Kilombero ulianza kutekelezwa mwezi Januari, 2013 chini ya Mkandarasi M/S China Railway 15 Bureau Group Corpration wa kutoka China kwa gharama ya Shilingi bilioni 53.214. Mradi huu unasimamiwa na Mhandisi Mshauri M/S AARVE Assiociate Architects Engineering and Consultants Pvt kutoka India akishirikiana na Advanced Engineering Solutions (T) LTD wa Tanzania kwa gharama ya Shilingi milioni 2,759.225.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huu unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na maendeleo ya jumla ya mradi huu yamefika asilimia 42. Ujenzi wa daraja la Kilombero unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2016.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:-
Kwa muda mrefu wananchi wa Busokelo wamekuwa wakikumbana na adha kubwa ya ubovu wa barabara ya Katumba - Mbando - Tukuyu yenye urefu wa kilometa 82 inayoanzia Katumba (RDC) kupitia Mpombo, Kandete, Isange, Lwangwa, Mbwambo (BDC) hadi Tukuyu (RDC) na barabara hii imekuwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami kwa muda mrefu na Mkandarasi yuko eneo la ujenzi wa kipande cha kilometa kumi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha barabara hiyo kwa kujenga sehemu iliyobaki yenye kilomita 72?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Fredy Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Katumba - Mbwambo - Tukuyu yenye urefu wa kilometa 82 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mbeya. Barabara hii ni ya changarawe na ipo kwenye hali nzuri kwani inapitika vizuri isipokuwa maeneo machache yenye miteremko mikali inayoteleza wakati wa mvua. Serikali imekuwa ikifanya matengenezo ya aina mbalimbali ili barabara hii iendelee kupitika wakati wote bila matatizo.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, katika mwaka wa fedha 2009/2010, Serikali kupitia Wakala wa Barabara ilianza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami ambapo upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulikamilika mwezi Februari, 2012.
Baada ya usanifu wa kina kukamilika katika mwaka 2013/2014 kiasi cha shilingi milioni 1,270 kilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kilomita 2.5 kwa kiwango cha lami. Aidha, baadaye Serikali iliamua kujenga kilimeta 10 ambapo mwezi Aprili, 2014 Wakala wa Barabara uliingia mkataba na kampuni ya CICO kujenga kilometa 10 kuanzia Lupaso hadi Bujesi kipande kilichopo
Wilayani Busokelo kwa gharama ya shilingi milioni 8,929.724. Ujenzi wa Kipande hicho unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2016.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na ujenzi wa kilometa 72 zilizobaki kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:-
Je, ni lini barabara ya Magu - Bukwimba - Ngudu - Hungumalwa itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kuchukua nafasi hii kujibu swali la Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2010/2011 na 2011/2012, Wizara kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) ilitenga jumla ya shilingi milioni 1200 ambazo zilitumika kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Magu - Ngudu - Jojiro sehemu ya Ngudu Mjini yenye urefu wa kilometa 1.9
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 na 2015/2016, Serikali ilitenga jumla ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 70 na taratibu za kumtafuta Mhandisi Mshauri zinaendelea. Baada ya kukamilika kwa usanifu na gharama za mradi huo kujulikana, Serikali itatafuta fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Wakati akiwa Makao Makuu ya Jimbo la Nkasi Kusini, Makamu wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, aliwaahidi wananchi wa Jimbo hili mawasiliano ya simu za mkononi kwa Kata nne za mwambao wa Ziwa Tanganyika ambazo ni Ninde, Wampembe, Kizumbi na Kala; je, ni lini utekelezaji wa ahadi hiyo utafanyika
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata wa Nkasi Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza sera ya kuzipatia huduma ya mawasiliano ya simu Kata zenye uhitaji ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi, wakiwemo wa Jimbo la Nkasi Kusini. Katika mwaka wa fedha wa 2015/16 Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) imetenga jumla ya dola za Kimarekani 199,850 kwa ajili ya upelekaji wa mawasiliano katika Kata ya Ninde katika Awamu ya Pili A ya mradi huo. Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania ndiyo iliyopewa zabuni ya kupeleka mawasiliano katika Kata hiyo. Mradi ulianza kutekelezwa kuanzia mwezi Aprili, 2015 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata za Wampembe, Kizumbi na Kala, zimejumuishwa katika mradi wa mawasiliano vijijini Awamu ya Kwanza A (Phase I A) wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na maandalizi ya ujenzi wa mnara yanaendelea chini ya kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania. Kwa sasa Vodacom wanawaandaa wakandarasi wa kutekeleza mradi huo ambao ujenzi wake umepangwa kukamilika mwezi Juni, 2016.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-
Kufuatia upanuzi wa barabara ya Kilwa mwaka 2002 wapo wananchi 80 waliolipwa maeneo ya Kongowe mwaka 2008 na wengine 111 walilipwa baada ya hukumu ya shauri lililofunguliwa na ndugu Mtumwa.
Je, Serikali itakamilisha lini malipo ya fidia ya nyumba zote zilizobomolewa kupisha upanuzi wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili linaulizwa mara saba na Wabunge mbalimbali wa Temeke ikiwa ni pamoja na Wabunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Dar es Salaam. Ninawaombeni Waheshimiwa Wabunge tunapotoa majibu ni muhimu tukawaeleza wananchi majibu hayo na tukienda nje ya hapo tutakuwa tunarudia rudia na sisi wengine hatujisikii vizuri tunaporudia kutoa majibu .
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa wananchi wanaodai fidia kutokana na nyumba zao zilizokuwa zimejengwa ndani ya eneo la hifadhi ya barabara ya Kilwa ambayo ilibomolewa mwaka 2002 kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 167 ya mwaka 1967.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nyumba hizo zilijengwa ndani ya eneo la hifadhi ya barabara na hivyo kukiuka Sheria ya Barabara namba 167 ya mwaka 1967, Serikali haina mpango wa kuwalipa fidia wamiliki wa nyumba hizo kwa kuwa hawastahili kulipwa fidia.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-
Kata za Semembela, Isagenhe na Kahama ya Nhalanga hazina kabisa mawasiliano ya simu za mkononi:-
Je, ni lini Kata hizi zitapatiwa huduma hii muhimu ya mawasiliano ya simu za mkononi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seleman Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia zabuni zinazotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Kata ya Kahama ya Nhalanga ilijumuishwa katika Zabuni ya Awamu ya Kwanza B (Phase 1B) ya mradi chini ya Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya Airtel kwa ruzuku ya Dola za Kimarekani 32,000. Utekelezaji wa mradi ulianza rasmi Aprili, 2014. Kazi ya ujenzi wa mnara imeanza na inatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Zabuni ya Awamu ya Pili A (Phase 2A), Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya MIC kwa maana ya Tigo imepewa jukumu la kupeleka huduma za mawasiliano ya simu za mkononi katika Kata ya Isagenhe kwa ruzuku ya Dola za Kimarekani 66,309. Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Aprili, 2015. Survey ya mradi imefanyika na utekelezaji upo katika hatua ya manunuzi ya vifaa vya mnara. Aidha, ujenzi wa mnara unatarajiwa kukamilika kabla ya kwisha mwaka huu wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Semembela imejumuishwa katika mchakato wa awamu ya tatu ya mradi wa mawasiliano vijijini ambapo zabuni yake inatarajia kutangazwa ndani ya mwaka huu wa fedha 2015/2016. Pia kampuni ya Viettel kwa maana ya Halotel itaanza kujenga mnara wa mawasiliano ya simu mapema mwezi Mei, 2016.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuza:-
Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Rukwa ilishaomba juu ya barabara za Kitosi – Wampembe na Nkana – Kala kuchukuliwa na Mkoa na Serikali imeendelea kuzifanyia matengenezo ya dharura ili zipitike na kilio cha barabara hizo kilifikishwa kwa Rais pamoja na Makamu wa Rais wa Awamu ya Tano na wote walitoa ahadi ya kuboresha barabara hizo:-
(i) Je, Serikali ina mpango wowote wa kuzipandisha hadhi barabara hizo?
(ii) Je, ni lini Serikali itaitikia kilio hiki cha wananchi wanaopata shida kwa barabara hizo kutopitika katika kipindi chote cha mwaka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kitosi – Wampembe ina urefu wa kilometa 67 na barabara ya Nkana – Kala ina urefu wa kilometa 68 na barabara zote hizo zipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imepokea maombi ya kuzipandisha hadhi barabara ya Kitosi – Wampembe na Nkana – Kala kutoka Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Rukwa na baada ya kupokea maombi hayo, timu ya wataalam ilitembea barabara hizi ili kubaini iwapo zinakidhi zigezo vya kupandishwa hadhi. Maombi hayo ya kuzipandisha hadhi barabara tajwa yanafanyiwa kazi na Wizara yangu sambamba na maombi kutoka mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imesikia kilio cha wananchi wa Wilaya ya Nkasi na inaendelea kutoa fedha za matengenezo ya barabara ya Kitosi – Wampembe. Katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 500 na katika mwaka wa fedha 2015/2016, shilingi milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) ili kuifanya barabara hiyo iweze kupitia katika kipindi chote cha mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali ilitenga shilingi milioni 45 na shilingi milioni 60 zimetengwa katika mwaka wa fedha 2015/2016, kwa ajili ya matengenezo ya aina mbalimbali ya barabara ya Nkana – Kala kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ili kuhakikisha inapitika kwa kipindi chote cha mwaka.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Ujenzi wa Barabara ya Tabora – Ndono – Urambo ulikuwa unaendelea vizuri kabla ya shughuli hizo za ujenzi kusimamishwa ghafla kilomita tano nje ya mji wa Urambo kwa karibu mwaka sasa.
Je, ni lini ahadi ya Serikali ya kujenga kilomita nane kupitia katikati ya mji wa Urambo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara ya Tabora – Urambo kwa kiwango cha lami umegawanyika katika sehemu mbili. Kuna Tabora - Ndomo ambayo ni kilometa 42 na Ndomo - Urambo kilometa 52. Ujenzi wa sehemu ya Tabora – Ndomo ulikamilika Februari, 2014 na barabara kukabidhiwa rasmi Februari 2015. Ujenzi wa sehemu ya Ndomo - Urambo unaendelea.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa sehemu ya Ndomo - Urambo unaendelea na utekelezaji umefikia asilimia 88.7 ambapo kilometa 46 zimekamilika kwa kiwango cha lami na mradi unategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya barabara inayopita katikati ya mji wa Urambo, kilometa 6.3 haikuwa katika mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Ndomo – Urambo. Sehemu hiyo itajengwa kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Tabora katika mwaka wa fedha wa 2016/2017. Usanifu wa barabara na makisio ya gharama za ujenzi wa sehemu hiyo umefanyika. Hivyo baada ya kupata fedha, ujenzi wa kiwango cha lami wa sehemu hiyo utaanza.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliahidi kujenga barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa kwa kiwango cha lami; na barabara hiyo tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu.
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa yenye urefu wa kilometa 55 umeanza kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Ujenzi wa kiwango cha lami wa sehemu ya barabara hii ulianza katika mwaka wa fedha 2013/2014 ambapo jumla ya kilometa sita zilianza kujengwa na kukamilika kutoka Kongwa Junction hadi Kongwa, kilometa tano, pamoja na Mpwapwa mjini kilometa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya pili ya ujenzi wa barabara hii uliendelea katika mwaka wa fedha 2014/2015 ambapo kilometa moja ilijengwa kutoka Kongwa Mjini hadi Ugogoni; na kilometa moja inaendelea kujengwa Mjini Mpwapwa katika mwaka wa fedha 2015/2016.
Ujenzi wa barabara hii utaendelea kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 kulingana na upatikanaji wa fedha. Lengo likiwa ni kuikamilisha barabara ya Mbande - Kongwa Junction hadi Kongwa na Kongwa Junction – Mpwapwa – Gulwe hadi Kibakwe ambapo pana jumla ya kilometa 102.17 kwa kiwango cha lami.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Barabara ya Mbulu – Hydom – Babati – Dongobeshi, imekuwa na miundombinu mibovu na haipitiki muda wote wa mwaka na kumekuwepo ahadi ya kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Je, Serikali itatekeleza lini ahadi hiyo ambayo pia imetolewa na Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mbulu – Hydom ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Kilimapunda – Mbulu – Hydom – Kidarafa yenye urefu wa kilometa 114. Aidha, barabara ya Dareda – Dongobesh yenye urefu wa kilometa 60, ni barabara ya Mkoa na inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) na barabara zote hizi mbili ni muhimu sana kwa shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara, na hasa wa Jimbo la Mbulu Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya Mbulu – Hydom – Kidarafa imejumuishwa kwenye mradi wa upembuzi yakinifu wa barabara inayopita kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Seringeti (Southern Bypass) ya Mbulu Route unaojumuisha barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom - Kidarafa hadi Sibiti. Mradi huu upo kwenye hatua ya ununuzi ili kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu na usanifu chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) ambapo kazi ya kuchambua Zabuni inaendelea.
Aidha kuhusu barabara ya Dareda kwa maana ya Babati hadi Dongobeshi yenye urefu wa Kilomita 60, imejumuishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 katika Mradi wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na itaweka katika mpango wa utekelezaji kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kwa kutambua umuhimu wa barabara hizo, Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa miaka minne mfululizo kwa ajili ya matengenezo ya aina mbalimbali ili kuhakikisha barabara hizo zinapitika kwa muda wote wa mwaka wakati maandalizi ya kuzijengwa kwa kiwango cha lami yanaendelea. Mathalani, fedha zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 zilikuwa ni shilingi milioni 1,254.163; mwaka 2013/2014 zilitengwa shilingi milioni 1,425.163; mwaka 2014/2015 zilitengwa shilingi 1,258.876 na mwaka huu wa 2015/2016 zimetengwa shilingi milioni 1,655.504.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Barabara ya Mbeya – Chunya - Makongorosi imejengwa kwa kiwango cha lami kwa asilimia 80. Je, ni lini Serikali itaweka mizani katika barabara hiyo ya lami ili kuilinda iweze kudumu muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo:-
Barabara ya Mbeya – Chunya – hadi Makongorosi yenye urefu wa kilometa 117 ni barabara kuu inayohudumiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Mkoa wa Mbeya. Barabara hii imejengwa kwa kiwango cha lami, sehemu ya barabara kati ya Mbeya hadi Chunya ambayo ni kilometa 72 na imekamilika hivi karibuni. Aidha, Serikali inafanya maandalizi ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya Chunya hadi Makongorosi ambayo ni kilometa 45.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inatambua kuwa katika Wilaya ya Chunya kuna shughuli nyingi za kiuchumi kama vile uchimbaji wa madini, kilimo na mazao ya misitu ambayo huchangia kwa kiwango kikubwa upitishaji wa magari yenye mizigo mizito na hivyo kuna umuhimu wa kuweka mizani kwenye barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itajenga mizani katika barabara ya Mbeya - Chunya hadi Makongorosi wakati wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Chunya - Makongorosi. Aidha, katika kipindi hiki ambacho ujenzi wa mizani ya kudumu haujafanyika, Serikali kupitia TANROADS itaendelea kudhibiti uzito wa magari katika barabara hiyo kwa kutumia mizani ya kuhamishika (mobile weighbridge).
MHE. DUA W. NKURUA aliuliza:-
Katika ujenzi wa barabara ya Mangaka - Mtambaswala na Mangaka - Nakapanya, wapo wananchi ambao walishafanyiwa tathmini ya fidia ya kupisha ujenzi huo hawajalipwa na wengine wamepunjwa.
Je, Serikali italeta lini wataalamu wa kuhakiki fidia hizo ili kila mwananchi apate haki yake?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dua William Nkurua, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ujenzi wa barabara ya Mangaka – Mtambaswala na Mangaka - Nakapanya, Serikali ilitenga fedha shilingi milioni 3,023.528 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi waliokwisha fanyiwa tathmini ya mazao yao kati ya mwaka 2009 na 2012. Aidha, baada ya uthamini kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali mwaka 2013, fidia ililipwa mwaka 2014 kwa kufuata taratibu na sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya wananchi ambao mali zao hazikufanyiwa tathmini katika kipindi hicho hawakulipwa fidia. Tathmini ya fidia kwa mali za wananchi hao imefanyika mwezi Oktoba 2015 na taarifa ya uthamini imekamilika na imewasilishwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa hatua ya kuidhinishwa ili malipo yaweze kufanyika.
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-
Mkoa wa Shinyanga na Simiyu inaunganishwa kwa barabara ya vumbi, tofauti na mikoa mingine ambayo imeunganishwa kwa barabara za lami.
(a) Je, Serikali itaunganisha lini mikoa hiyo kwa barabara ya kiwango cha lami kwa kumalizia kilometa 102 zilizobaki katika barabara ya Lamadi - Mwigumbi kupitia Bariadi?
(b) Je, Serikali itaona umuhimu wa kuunganisha makao makuu ya Wilaya za Mkoa wa Simiyu kuunganishwa kwa barabara za kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gimbo Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mweshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mwigumbi - Maswa - Bariadi - Lamadi yenye urefu wa kilometa 171.8 kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ikiwa na lengo la kuunganisha Mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Mwanza na kwa barabara ya lami. Sehemu ya barabara hii kuanzia Bariadi - Lamadi yenye urefu wa kliometa 71.8 tayari imejengwa kwa kiwango cha lami na imekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016, TANROADS ilitia saini mkataba wa ujenzi na mkandarasi CHICO kutoka China kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya pili ya barabara hiyo kuanzia Mwigumbi - Maswa ambazo ni kilometa 50.3 kwa gharama ya shilingi bilioni 61.462. Hadi sasa mkandarasi yuko katika eneo la mradi na anaendelea na kazi za kujenga kambi, kuleta mitambo na wataalam kwa ajili ya kutelekeza mradi huo. Aidha, kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami wa sehemu ya Maswa - Bariadi ambazo ni kilometa 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kuwa kukamilika kwa barabara hii inayoendelea kujengwa kutawezesha Makao Makuu ya Wilaya za Busega, Bariadi na Maswa zilizoko katika Mkoa wa Simiyu kuunganishwa kwa barabara za lami. Wilaya nyingine zilizobaki zitaungwanishwa kwa barabara za lami kwa awamu kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-
Serikali inatambua umuhimu wa barabara; na barabara inayounganisha Mtwara Mjini, Nanyamba, Tandahimba, Newala hadi Masasi haipitiki vizuri wakati wote na hivyo kuwafanya wananchi waone kama wametengwa na Serikali yao.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) ilisaini mkataba na Mkandarasi Mshauri Multi Tech Consult (pty) Ltd. kutoka Botswana akishirikiana na Unitec Civil Consultants Ltd ya hapa nchini tarehe 15 Mei, 2014 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mtwara Mjini – Nanyamba – Tandahimba – Newala na hadi Masasi yenye urefu wa kilometa 210 kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi milioni 1,280,832. Usanifu wa kina wa barabara hii ulikamilika mwezi Aprili, 2015.
Taratibu za kumpata Mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami sehemu ya Mtwara hadi Mnivata ambapo ni kilometa 50, zipo katika hatua za mwisho ambapo ujenzi utaanza mara baada ya mkataba kusainiwa. Aidha, ujenzi wa sehemu iliyobaki kati ya Mnivata na Masasi, utafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na kwa kuzingatia kwamba barabara hii imeahidiwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 hadi 2020 na wakati huo huo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne na wa Awamu ya Tano. Kwahiyo, tutaijenga.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, tunaomba utusomee tena hicho kiasi ulichosoma kwenye majibu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni shilingi 1,280.832 au shilingi bilioni 1.280.832.
MHE. RASHID M. CHUACHUA (K.n.y. MHE. JEROME D. BWANAUSI) aliuliza:-
Kulikuwa na ahadi ya Serikali ya kujenga minara ya mawasiliano katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji (a) Je, ni lini wananchi wa Kata ya Mchauro, Mkundi na Sindano watajengewa minara ili kurahisisha mawasiliano?
(b) Je, ni utaratibu gani unaotumika ili waliotoa maeneo yao na kijiji husika wapate ushuru kutoka kwenye Kampuni iliyojenga mnara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Rivango kutoka katika Kata ya Mchauro, pamoja na Kijiji cha Luatala kutoka katika Kata ya Sindano na Vijiji vya Chipango, Mkoropola, Nakachindu na Kijiji cha Nakalola kutoka katika Kata ya Mikundi vimeshapata huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa Awamu ya kwanza ya mradi wa Kampuni ya Simu ya Viettel.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Lichehe, Sindano kutoka katika Kata ya Sindano na vijiji vya Maparawe, Mkowo Mwitika na Nangomwa kutoka katika Kata ya Mchauro vipo katika orodha ya miradi ya Viettel inayotegemewa kutekelezwa katika Awamu ya Pili na ya Tatu iliyoanza Novemba, 2015 na kutarajiwa kukamilika Novemba, 2017. (Kicheko/Makofi)
Aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imevijumuisha Vijiji vya Mchauro, Mhata, Mirewe na Namwombe katika orodha ya miradi ya siku za usoni itakayotekelezwa na mfuko katika mwaka wa fedha 2016/2017 kulingana na upatikanaji wa fedha. (Kicheko/Makofi)
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kiutaratibu kampuni inayotaka kujenga mnara huingia mkataba na mwananchi mwenye eneo husika na hukubaliana kiasi cha malipo kwa mwezi kwa muda wa mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna wananchi walitoa maeneo yao kwa makubaliano ya kulipwa, basi wafatilie utekelezaji wa mkataba wao na kampuni husika.
Ujenzi wa Barabara ya Kidahwe - Kasulu - Nyakanazi
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Je, ni lini barabara ya Kidahwe – Kasulu – Nyakanazi itakamilika kwa lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kigoma - Kidahwe - Kasulu hadi Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 330 unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo sehemu ya barabara hii kutoka Kigoma hadi Kidahwe yenye urefu wa kilometa 28.2 imejengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika, sehemu ya Kidahwe - Kasulu yenye urefu wa kilometa 50 na sehemu Kibondo - Kakonko mpaka Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 50 zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha, kazi ya kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu zilizobaki kati ya Nyakanazi na Kasulu, pamoja na barabara ya Kasulu hadi Manyovu zenye jumla ya kilometa 250 inatarajiwa kuanza Aprili, 2016 kwa kutumia fedha za NEPAD kupitia Benki ya maendeleo ya Afrika chini ya utaratibu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hii inatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI (K.n.y MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-
Serikali chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ilitangaza Jimbo la Rorya kuwa Wilaya mpya na sasa ina miaka saba tangu kutangazwa na hitaji kubwa la kwanza ni kutekeleza ahadi ya Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na kurudiwa tena kuahidiwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano za kujenga kwa lami barabara ya kutoka Mika - Utegi - Shirati - Kirongwe yenye urefu wa kilometa 58, kwa kuzingatia umuhimu wake kwamba ni kiungo kati ya Tanzania na Kenya kupitia Rorya, itainua pato la Halmashauri kupitia ushuru wa mpakani na tarafa tatu kati ya nne kupata urahisi kuingia nchi jirani ya Kenya kwa ukaribu zaidi kuliko kutumia barabara ya kwenda Sirari:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hii ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Wilaya ya Rorya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mika – Utegi – Shirati – Ruariport/Kirongwe, yenye urefu wa kilometa 58 ni muhimu kwa Wilaya ya Rorya kiuchumi na kijamii, kwani inaunganisha Wilaya ya Rorya na Wilaya nyingine za Mkoa wa Mara pamoja na nchi jirani ya Kenya. Kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii, Serikali ilianza kuijenga kwa awamu kwa kiwango cha lami barabara kutoka Mika – Ruariport au Kirongwe tangu mwaka wa fedha wa 2009 - 2010. Hadi sasa kipande cha barabara chenye urefu wa kilometa 7.5 kwenye barabara hii kimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, sehemu iliyobaki itaendelea kujengwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Licha ya Jimbo la Mlimba kuwa na uzalishaji wa mazao ya kilimo, linakumbwa na ukosefu mkubwa wa miundombinu ya barabara zinazopitika na madaraja, jambo linalosababisha wakulima kushindwa kusafirisha mazao yao kwenda kwenye masoko na hivyo kuendelea kuwa maskini licha ya kuwa na utajiri wa mazao ya kilimo:-
(a) Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Ifakara - Mlimba, Mlimba - Madeke na Mlimba - Uchindile?
(b) Je, ni lini Serikali itajenga madaraja ya kudumu katika Mito ya Mtunji, Chiwachiwa, Mngeta na Londo kwa kuwa yaliyopo sasa ni ya miti?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Ifakara - Mlimba - Madeke yenye urefu wa kilometa 231.53 inahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) na barabara ya Mlimba - Uchindile inahudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero. Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Ifakara - Mlimba kwa kuanza na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu ya barabara ya kutoka Ifakara – Kihansi yenye urefu wa kilometa 126 kwa lengo la kuunganisha kipande cha barabara ya lami chenye urefu wa kilometa 24 kati ya Kihansi – Mlimba. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa ujenzi wa madaraja ya kudumu katika Mito ya Mtunji, Chiwachiwa na Londo utatekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Aidha, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa daraja la Mngeta. Hadi sasa ukaguzi wa eneo la kujenga daraja umefanyika na taratibu za ununuzi ili kumpata mkandarasi wa kujenga daraja hilo ziko katika hatua za mwisho.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Wilaya ya Serengeti ni Wilaya yenye mbuga kubwa ya wanyama inayotambulika duniani na kupokea watalii wengi, lakini imekuwa kama kisiwa kwa kusahaulika kuunganishwa na barabara ya lami itokayo Makutano ya Musoma mpaka Mto wa Mbu:-
Je, ni lini barabara ya lami ya Musoma – Mugumu mpaka Mto wa Mbu itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ta Makutano – Nata – Mugumu – Loliondo hadi Mto wa Mbu ina jumla ya kilometa 452. Kati ya hizo kilometa 192 zipo upande wa Mkoa wa Mara na kilometa 260 upande wa Mkoa wa Arusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, barabara ya kuanzia Makutano – Nata – Mugumu – Loliondo hadi Mto wa Mbu kilometa 452 umekamilika. Aidha, ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami unatekelezwa kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii, ulianza kutekelezwa kuanzia Makutano hadi Sanzate kilometa 50, mwezi Oktoba, 2013 na unaendelea. Aidha, ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya barabara iliyobaki ya Sanzate – Nata – Mugumu kilometa 75 na Loliondo hadi Mto wa Mbu kilometa 213 utatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani juu ya barabara ya Handeni – Mzika – Dumila na ile ya Handeni – Kiberashi, hasa ikizingatiwa kuwa upembuzi yakinifu umeshafanyika tangu kipindi cha uongozi wa Awamu ya Nne?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Abdallah Kigoda, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Handeni hadi Mzika yenye urefu wa kilometa 70 ni sehemu ya barabara ya Handeni – Magole – Turiani – Dumila, yenye urefu wa kilometa 154.6. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii ulishakamilika. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii unafanywa kwa awamu kwa kuanza na sehemu ya Magole hadi Turiani yenye kilometa 48.8 ambapo ujenzi wake unaendelea na umefikia asilimia 69. Ujenzi wa sehemu ya Turiani – Mzika hadi Handeni wenye urefu wa kilometa 105.8 utaanza baada ya kukamilika sehemu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Handeni hadi Kiberashi yenye kilometa 80 ni sehemu ya barabara ya Handeni – Kiberashi – Kijungu – Chemba – Kwamtoro hadi Singida yenye urefu wa kilometa 461 ambayo iko katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Upembuzi yakinifu wa barabara hii umekamilika na usanifu wa kina na utayarishaji wa nyaraka za zabuni uko katika hatua ya mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa barabara hizi zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kuunganisha Mikoa ya Tanga, Morogoro na Manyara na kuinua uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Fedha za Mfuko wa Barabara zimekuwa zikisuasua sana:-
Je, Wilaya ya Busega imetengewa kiasi gani kwa mwaka huu wa fedha ili zitumike kutengeneza miundombinu ya barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Mwaka wa Fedha 2014/2015, Fedha za Mfuko wa Barabara zilikuwa hazitolewi kama ilivyotarajiwa kutokana na hali ya makusanyo kutoka vyanzo mbalimbali vya Mfuko kutokuwa vya kuridhisha, lakini hali hiyo imebadilika na kuimarika katika mwaka wa fedha wa 2015/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi mwisho wa mwezi Machi, 2016 kiasi cha shilingi bilioni 462.789 sawa na asilimia 53.4 ya Bajeti ya Mfuko wa Barabara ya shilingi bilioni 866.63 ilikuwa imeshapokelewa na Bodi ya Mfuko wa Barabara na kupelekwa kwa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Halmashauri zote nchini. Tunatarajia kwamba, hadi kufikia Juni, 2016 fedha zote za Mfuko wa Barabara zilizopangwa kugharamia kazi za matengenezo na ukarabati wa barabara katika bajeti ya mwaka 2015/2016, zitakuwa zimepokelewa na kupelekwa Wakala wa Barabara na Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2015/2016, Halmashauri ya Wilaya ya Busega imetengewa jumla ya shilingi milioni 570.38 na hadi mwisho wa mwezi Machi, 2016 kiasi cha shilingi milioni 432.63 sawa na asilimia 75.9 ya bajeti hiyo, ilikuwa imeshapelekwa Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Chegeni kwa kufuatilia kwa karibu masuala ya barabara katika Jimbo lake na kumwomba aendelee kufuatilia ili kujiridhisha kwamba fedha za Mfuko wa Barabara zinatumika vizuri na kwa malengo yaliyopangwa na Halmashauri ya Busega.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Chegeni, swali la nyongeza.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAWA A. GHASIA) aliuliza:-
Je, ni lini barabara ya uchumi kutoka Mtwara – Nanyamba – Tandahimba - Newala – Masasi, itaanza kujengwa baada ya upembuzi yakinifu kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahmani Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala hadi Masasi, yenye urefu wa kilometa 210 pamoja na Daraja la Mwiti ulikamilika mwezi Aprili, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala hadi Masasi utaanza kwa sehemu ya Mtwara hadi Mnivata, yenye urefu wa kilometa 50. Taratibu za kumpata Mkandarasi wa kujenga sehemu hii ya barabara zimekamilika. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu hii ya Barabara ya Mtwara hadi Mnivata umepangwa kuanza katika Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. HUSSEIN M. BASHE aliuliza:-
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Jimbo la Nzega Mjini tarehe 14/10/2015, Mheshimiwa Rais aliahidi kuwa majengo yanayotumiwa na mkandarasi wa barabara ya Nzega – Tabora na majengo ya TANROADS yatakabidhiwa kwa Halmashauri ya Mji wa Nzega ili yaweze kutumika kwa ajili ya Chuo cha VETA:-
(a) Je, Serikali imefikia hatua gani kutekeleza ahadi hiyo ili majengo hayo yakabidhiwe katika Halmashauri ya Nzega?
(b) Je, Serikali ipo tayari kuwaambia wananchi wa Nzega lini chuo hicho kitaanzishwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Nzega na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora zimeandaa na kuwasilisha Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano maombi ya majengo ya kambi iliyokuwa inatumika wakati wa ujenzi wa barabara ya Nzega - Puge kwa ajili ya kutumia kambi hiyo kama chuo cha VETA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na mkataba wa ujenzi wa barabara, majengo ya mkandarasi ni mali yake na hayarejeshwi Serikalini. Majengo aliyokuwa anatumia Mhandisi Mshauri ndiyo yaliyorejeshwa kwa mwajiri, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Wizara bado inayafanyia kazi maombi ya kuyakabidhi majengo hayo kwa Halmashauri ya Mji wa Nzega kwa kuzingatia taratibu za uhamisho wa mali za Serikali kutoka taasisi moja kwenda taasisi nyingine. Aidha, uamuzi wa lini Chuo cha VETA kitaanzishwa, utategemea upatikanaji wa majengo hayo na uamuzi wa mamlaka inayohusika na kutoa vibali vya kuanzishwa kwa Vyuo vya VETA.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Mwaka 2012 Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya China, Railway Bureau 15 Group Corporation, waliingia mkataba wa miaka miwili wa ujenzi wa Daraja la Kilombero na barabara zake za maingiliano kwa gharama ya Sh.53.2 bilioni lakini mpaka sasa ujenzi huo bado haujakamilika:-
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kimetengwa na kutolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo tangu mkataba huo uanze?
(b) Je, ni lini daraja hilo litakamilika na kuanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, jirani yangu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2010/2011 hadi mwaka huu wa fedha 2015/2016, Serikali imekwishatenga jumla ya shilingi bilioni 25.59913 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Kilombero na gharama za Mhandisi Msimamizi anayesimamia ujenzi wa daraja hilo ni shilingi bilioni 2.75 bila ya Kodi ya Ongezeko la Thamani.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ulipangwa kukamilika tarehe 20 Januari, 2015. Hata hivyo, haukuweza kukamilika katika muda uliopangwa kutokana na ufinyu wa fedha uliosababisha kuchelewa kulipwa kwa madai ya malipo ya mkandarasi kwa kazi zilizofanyika. Kutokana na tatizo hilo, mkandarasi alikosa mtiririko mzuri wa fedha za kufanya kazi na hivyo kupunguza kasi ya utekelezaji wa mradi.
Hata hivyo, hadi Februari, 2016 Serikali imeweza kulipa madeni yote ya mkandarasi aliyokuwa anadai. Aidha, Serikali itaendelea kumlipa mkandarasi kulingana na kazi atakazozifanya. Kwa sasa kazi ya ujenzi wa daraja imesimama kutokana na Bonde la Mto kilombero kujaa maji. Kazi ya ujenzi wa daraja itaanza mara maji yatakapopungua katika Bonde la Mto Kilombero.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Eneo la Msalato lenye kilometa tisa katika ujenzi wa barabara ya Dodoma – Kondoa – Babati kwa kiwango cha lami bado halijakamilika.
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kipande hicho kilichobaki cha Dodoma – Manyara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kipande cha barabara chenye urefu wa kilometa 8.65 cha eneo la Msalato ni sehemu ya barabara ya Dodoma – Kondoa hadi Babati yenye urefu wa kilometa 251. Barabara hii inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na imegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni barabara ya kutoka Dodoma mpaka Mayamaya yenye urefu wa kilometa 43.65; sehemu ya pili, ni barabara ya kutoka Mayamaya mpaka Mela yenye urefu wa kilometa 99.35 na sehemu ya tatu, ni barabara ya kutoka Mela mpaka Bonga yenye urefu wa kilometa 88.8. Aidha, barabara ya kutoka Bonga hadi Babati yenye urefu wa kilometa 19.6 ilishajengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa sehemu ya Dodoma hadi Mayamaya yenye urefu wa kilometa 43.65 unaendelea. Utekelezaji umefikia asilimia 80 ambapo jumla ya kilometa 35 zimeshawekwa lami na zimebakia kilometa 8.65 katika eneo la Msalato.
Mheshimiwa Spika, ujenzi ulikuwa umesimama kwa muda kutokana na Mkandarasi kutokulipwa kwa wakati. Kwa sasa Serikali inaendelea kulipa madai ya Wakandarasi akiwemo Mkandarasi anayejenga barabara hii ya Dodoma hadi Mayamaya.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea malipo, Mkandarasi anayejenga barabara hii sasa yuko kwenye maandalizi ya kuanza ujenzi na kazi inatarajia kukamilika mwezi Desemba, 2016.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA (K.n.y. MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:-
Ili kurahisisha msukumo wa kimaendeleo na kukuza uchumi katika Bonde la Ziwa Rukwa, Serikali iliahidi kujenga daraja linalopita katika Mto Momba kati ya Kata ya Kamsamba (Jimbo la Momba) na Kata ya Kipera (Jimbo la Kwela) mwaka 2009. Je, ni lini ahadi hiyo ya Serikali itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jitihada za Serikali kuhusiana na ujenzi wa daraja la Momba lililoko kwenye barabara ya Sitalike hadi Kilyamatundu, Mkoa wa Rukwa katika Jimbo la Kwela na vile vile Kamsamba hadi Mlowa, Mkoa wa Songwe, zinaendelea, ambapo kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni pamoja na kuandaa na nyaraka za zabuni imekamilika mwaka 2015. Kazi ya Ujenzi wa daraja la Momba imepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017 kama ambavyo Waziri wangu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alivyomwahidi Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela.
MHE. RIZIKI SHAHARI MNGWALI aliuliza:-
Serikali ilijenga Gati kubwa la Kilindoni katika Wilaya ya Mafia kwa mabilioni ya fedha ili kuwezesha meli kubwa kutia nanga na hivyo kutatua tatizo sugu la usafiri wa majini Wilaya ya Mafia, licha ya Gati hilo kukamilika na kuzinduliwa na Rais aliyepita Mheshimiwa Jakaya Kikwete tangu mwaka 2013, bado Gati hilo halijaanza kutumika jambo ambalo limesababisha wananchi kuendelea kupata adha kubwa ya usafiri kwa kutumia bahari.
Je, Serikali itaelekeza meli kubwa na boti zenye viwango na bima kuanza kuwahudumia wananchi wa Mafia kwa kutumia Gati la Kilindoni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, majukumu makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ni pamoja na kujenga miundombinu ya kibandari na kuendesha shughuli za Bandari. Katika utekelezaji wa majukumu yake, Mamlaka ilikamilisha Ujenzi wa Gati la Kilindoni-Mafia lililofunguliwa rasmi tarehe 2/10/2013 na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Ujenzi wa Gati hili uligharimu kiasi cha shilingi bilioni 27. Aidha, katika kuboresha matumizi ya Gati hili, mamlaka ilikamilisha kazi zifuatazo:-
(i) Landing barge kwa ajili ya kuegesha majahazi,
(ii) Shed kwa ajili ya mizigo, na
(iii) Uzio kwa ajili ya usalama wa waendao kwa miguu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza awali, Gati hili lilikamilika na liko tayari kwa ajili ya matumizi. Hata hivyo, pamoja na utayari huo kama tunavyofahamu, wadau wakubwa wanaoendesha shughuli za usafiri wa majini katika mwambao wa bahari ni sekta binafsi. Kwa kutambua hilo, Wizara yangu itaendelea kuwashawishi na kuwashauri wadau hao wawekeze katika usafiri wa kwenda Mafia kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Bunge ambazo zinasimamiwa na SUMATRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya usafiri wa majini ni kama ilivyo biashara nyingine yoyote. Hivyo, milango iko wazi kwa makampuni yanayotoa huduma hii, pia kuwekeza katika Mwambao wa Mafia. Hata hivyo, tunamuomba Mheshimiwa Mbunge aendelee vilevile kuwashawishi wananchi kwa ujumla kujitokeza na kuwekeza katika Mji wa Mafia ili ukue kibiashara zaidi ya ulivyo sasa ili kuwavutia watu na watoa huduma kushawishika na kuwekeza katika Mwambao wa Mafia.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:-
Kata za Uyogo, Igwamanoni, Ushetu na Chena katika Jimbo la Ushetu hazina mawasiliano ya simu za mkononi ya uhakika. Je, ni lini maeneo hayo yatapatiwa mawasiliano ya simu za mkononi yenye uhakika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Elias John Kwandikwa, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa naibu Spika, vijiji vya Manungu na Uyogo katika Kata ya Uyogo pamoja na vijiji vya Iramba, Luhaga, Mwamanyili kutoka katika Kata ya Igwamanoni na vijiji vya Mwazimba na Nundu kutoka katika Kata ya Chela vimekwishapata huduma ya mawasiliano kupitia utelekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa Kampuni ya simu ya Vietel.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Jomu na Buchambaga vya Kata ya Chela, vijiji vya Mhuge na Ibambala, Kata ya Ushetu na Kipangu na Igwamanoni Kata ya Igwamanoni vipo katika utekelezaji wa awamu ya pili na awamu ya tatu ya miradi ya kampuni ya simu ya Vietel ulioanza Novemba 2015 na kutarajiwa kukamilika Novemba 2017.
Aidha, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, vijiji vya Kata ya Ushetu, vijiji vya Bugoshi na Kalama kutoka katika Kata ya Uyogo na vijiji vya Chela, Mhandu kutoka katika Kata ya Chela, vitaingizwa katika awamu zijazo za mradi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Serikali iliwaahidi wananchi wa Jimbo la Kawe kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba na barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill – Madale:-
Je, ni lini ujenzi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba pamoja na barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill - Madale Goba ni kati ya barabara ambazo zimo kwenye mpango wa Serikali wa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ambao utekelezaji wake ulianza mwaka 2010 na unagharamiwa na Serikali za Tanzania kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo ujenzi wa kiwango cha lami umekamilika ni Ubungo Bus Terminal - Kigogo Roundabout ambayo ni kilomita 6.4, Ubungo Maziwa - Mabibo External kilomita 0.65 na Jet Corner - Vituka - Davis Corner ambayo ni kilomita10.3. Aidha, barabara zinazoendelea kujengwa ni pamoja na Tangibovu - Goba kilomita 9, Kimara Baruti - Msewe - Changanyikeni kilomita 2.6, Kimara - Kilungule - External kilomita 9 na Tabata Dampo - Kigogo kilomita 2.25.
Mheshimiwa Naibu Spika, usanifu wa kina wa barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill -Madale - Goba na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi umekamilika. Aidha, usanifu wa kina wa barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba utafanyika sambamba na ujenzi wa barabara hiyo yaani design and build.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara za Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba na Tegeta Kibaoni - Wazo Hill - Madale - Goba umepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-
Ili Watanzania wanufaike katika ajira zinazotokana na shughuli za uchimbaji wa gesi na mafuta wanatakiwa kuwa na cheti cha Basic Off Shore Safety Certificate ambacho kwa sasa hakipatikani katika vyuo vya hapa nchini:-
Je, ni lini Serikali itakiwezesha Chuo cha DMI (Dar es Salaam Marine Institute) kianze kutoa kozi hizi ili wananchi wote waweze kupata cheti hiki ili waweze kuajiriwa katika shughuli za gesi na mafuta?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Bandari kinachosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mafuta na gesi kutoka hapa nchini kikiwemo Chuo cha DMI yaani Dar es Salaam Marine Institute na Norway, kinakamilisha maandalizi ya kuanza kutoa mafunzo na kujenga miundombinu inayotakiwa ili kuendesha mafunzo ya usalama katika sekta ya mafuta na gesi. Kutolewa kwa mafunzo hayo hapa nchini kutaongeza fursa ya ajira kwa wahitimu wetu kufanya kazi katika sekta ya mafuta na gesi lakini pia kupata wanafunzi kutoka nchi jirani zenye viwanda vya mafuta na gesi kama Uganda, Sudan na Kenya. Tunategemea ifikapo Disemba, 2016 mafunzo hayo yatakuwa yameanza kutolewa na Chuo cha Usimamizi wa Bandari. Mafunzo yatatolewa kwa kufuata mitaala ya kimataifa na hivyo wahitimu watapewa vyeti vinavyotambuliwa Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Chuo cha DMI (Dar es Salaam Maritime Institute) kitaendelea kufanya maandalizi muhimu ya kumpata mtaalamu wa kufanya tathmini ya vifaa vya kufundisha kama vile helikopta dunker, bwawa la kuogelea, smoke house na kadhalika ili kuanzisha mafunzo hayo.
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:-
Ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani - Saadani yenye kilometa 178 kwa kiwango cha lami ni ahadi ya muda mrefu ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa Awamu ya Tano:-
Je, ni lini sasa ujenzi huo utaanza hasa ikizingatiwa kuwa ahadi hiyo ni ya muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara wa Tanga - Pangani - Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 178 ni sehemu ya Mradi wa Kikanda wa barabara ya Malindi – Mombasa - Lunga Lunga/Tanga - Bagamoyo. Mradi huu wa Kikanda unaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Bagamoyo kwa kiwango cha lami ilianza Januari, 2011 na kukamilika Novemba, 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Benki ya Maendeleo ya Afrika tayari imeonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii. Taratibu za kumpata mkandarasi zitaanza baada ya kupatikana kwa fedha za ujenzi.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Barabara ya Oldeani Junction - Mang‟ola – Matala - Manuzi ni kiungo muhimu sana kwa kuunganisha Kanda ya Kaskazini (Mkoa wa Arusha) na Mikoa ya Kanda ya Ziwa (Simiyu):-
Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili iweze kupitika muda wote?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na maandalizi ya nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Oldeani Junction - Mang‟ola - Matala - Manuzi ambayo pia hujulikana kama Kolandoto - Oldeani Junction yenye urefu wa kilometa 328 umeanza na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami zitaanza baada ya kukamilika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unaoendelea na kupatikana kwa fedha za ujenzi.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA aliuliza:-
Hali ya kipande cha barabara ya kutoka Chaya - Tabora ni sehemu ya barabara ya kutoka Urambo – Kaliua:-
Je, ni lini ujenzi wa barabra hizo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanne Ismail Mchemba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Chaya – Nyahua na Urambo – Kaliua ni sehemu ya barabara ya Manyoni – Tabora – Urambo – Kaliua – Malagarasi – Uvinza - Kigoma yenye jumla ya kilometa 843.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuunganisha Mkoa wa Singida, Tabora na Kigoma kwa barabara ya kiwango cha lami. Katika kutimiza azma hiyo, tayari ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu za Manyoni – Itigi – Chaya yenye urefu wa kilometa 89.3 pamoja na Tabora – Ndono yenye kilometa 42, Kigoma – Kidahwe yenye kilometa 28, Kidahwe – Uvinza yenye kilometa 76.6 pamoja na daraja la Malagarasi na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 48 umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ujenzi kwa kiwango cha lami unaendelea kwa sehemu ya barabara zifuatazo na utekelezaji umefikia asilimia kama nitakavyoieleza. Sehemu za Tabora - Nyahua yenye urefu wa kilometa 85.4 ujenzi umefikia 90%. Sehemu ya Ndono - Urambo yenye urefu wa kilometa 52 ujenzi umefikia 87%. Sehemu ya Kaliua - Kazilambwa yenye kilometa 56 ujenzi umefikia 63%.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya Nyahau - Chanya yenye urefu wa kilometa 85.5 na Urambo - Kaliua yenye urefu wa kilometa 28 utaanza katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kufuatia kukamilika kwa usanifu wa kina wa barabara hizo.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Barabara ya kutoka Mlalo kupitia Ngwelo – Mlalo – Makanya – Mlingano – Mashewa ni ya muda mrefu sana na ipo chini ya halmashauri licha ya kwamba barabara hiyo ni kichocheo cha uchumi kwa Majimbo manne:-
Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kupandisha hadhi barabara hiyo na kuwa chini ya TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya kupandishwa hadhi barabara ya Mlalo – Ngwelo – Makanya – Mlingano hadi Mashewa kuwa barabara ya mkoa yanaendelea kufanyiwa kazi na Wizara yetu sambamba na maombi kutoka mikoa mingine. Aidha, kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hiyo kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Barabara ya kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Chamwino kuelekea Kaskazini ni vumbi na ina madaraja mawili makorofi yaliyoko kati ya Chilonwa na Uzali na lingine kati ya Dabalo A na Dabalo B. Daraja lililopo kati ya Chilonwa na Nzali limewahi kuua watu mwaka 2014 na mifugo mingi pia imekufa kwenye daraja hilo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuyajenga madaraja hayo mawili ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya ya Chilonwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, madaraja aliyotaja Mheshimiwa Mbunge yote yapo katika barabara ya Chamwino Ikulu Junction, kuelekea Chamwino Ikulu - Dabalo hadi Itiso yenye urefu wa kilometa 80.43 ambayo ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Spika, kati ya Chilonwa na Nzali kuna daraja la mfuto (vented drift) lililojengwa mwaka wa fedha 2013/2014 ambalo linatumika ingawa linakabiliwa na changamoto ya kuziba yaani siltation. Aidha, kati ya Dabalo A na Dabalo B pia kuna daraja la mfuto ni solid drift lililojengwa mwaka wa fedha 2014/2015 ili sehemu hiyo iweze kupitika.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) itaendelea kuyafanyia matengenezo madaraja hayo mawili yaliyopo ili yaweze kupitisha maji na barabara hiyo iweze kupitika majira yote ya mwaka. Aidha, Wakala wa Barabara utaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii ili kuhakikisha inatumika kwa usalama wa watumiaji na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii wananchi wa Chilonwa.
MHE. ALI SALIM KHAMIS aliuliza:-
(a) Je, Shirika la Ndege Tanzania ni Shirika la pamoja kati ya Tanganyika na Zanzibar?
(b) Kama ndiyo je, Zanzibar ina asilimia ngapi katika Shirika la ATCL?
(c) Je, ni lini ATCL italipa deni la kodi ya kutua (landing fee) kwa Mamlaka ya Ndege Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ali Salim Khamis, Mbunge wa Mwanakwerekwe, lenye vipengele (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Ndege ya Tanzania, Air Tanzania Company Limited ilianzishwa mwaka 2002 chini ya Sheria ya Makampuni (The Companies Act). ATCL ilichukua majukumu ya lililokuwa Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania Corporation) ambalo lilibinafsishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 16 ya 2002 (Air Tanzania Corporation Reorganisation and Vesting of Assets and Liabilities Act, 2002).
(b) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria nilizozitaja hapo juu ATCL inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Umiliki wa ATCL haujatenganishwa kuonyesha asilimia za hisa zinazomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(c) Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Kiwanja cha Ndege cha Zanzibar inaidai ATCL kiasi cha shilingi 230,767,986.00 kama deni la tozo za kutua (landing fee). Madai haya ni sehemu ya orodha ya madeni ya siku nyingi ya ATCL ambayo yamewasilishwa Serikalini. Deni hili ni moja ya madeni ambayo yanahakikiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Serikali italipa deni hili mara baada ya kupokea taarifa ya uhakiki ambayo itathibitisha kuwa ni deni halali.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA) aliuliza:-
Kumekuwepo na ahadi nyingi wakati wa kampeni kutoka kwa Marais wa Awamu ya Nne na ya Tano kuwa barabara ya kutoka Mkomazi kupitia Bendera, Kihurio, Ndungu, Maore, Kisiwani hadi Same Mjini itajengwa kwa kiwango cha Lami.
Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu ahadi hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mkomazi - Kihurio - Ndungu – Kisiwani hadi Same ni barabara ya mkoa yenye urefu wa kilometa 96 inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS). Ili kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika katika majira yote ya mwaka, Serikali imeendelea kutenga fedha za kufanyia matengenezo ya aina mbalimbali. Aidha, julma ya kilometa 19.2 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami katika maeneo yenye watu wengi ya Kisiwani, Gonja, Maore na Ndungu.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza ahadi za Serikali kuhusu barabara hii, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imepanga kufanya usanifu wa kina kuanzia Same- Kisiwani- Gonja- Bendera hadi Mkomazi ambapo ni kilometa 96 katika mwaka wa fedha 2016/2017 ikiwa ni maandalizi ya kujenga barabara yote kwa kiwango cha lami kama viongozi wetu wakuu walivyokuwa wameahidi. Mara usanifu wa kina utakapokamilika Serikali itatafuta fedha ili kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Barabara kutoka Gulwe - Berege - Chitemo- Mima- Sazima - Igoji Kaskazini - Iwondo - Fufu inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ni mbaya sana na inapitika kwa shida sana hasa wakati wa mvua/masika.
Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba ipo haja kubwa ya barabara hiyo kuhudumiwa na Serikali Kuu (TANROADS) badala ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambayo uwezo wake kifedha ni mdogo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, baba yangu na Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kumshauri Mheshimiwa Mbunge na kama ambavyo tumeongea kwamba maombi hayo yaanzie katika Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dodoma na ninamhakikishia Mheshimiwa Lubeleje na kama ambavyo tumewasiliana maombi haya yatakapofika Wizarani tutayafikiria pamoja na maombi yale mengine yote na nina uhakika yatafika mahali pale ambapo yanatakiwa. Hayo yote ni kwa mujibu au matakwa ya Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na Kanuni ya 43(1) ya Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009.
Aidha, ninatoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara zinazotengwa kupitia bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ili iweze kupitika majira yote ya mwaka na kwa kweli tusiendelee kumpa kazi kubwa Mheshimiwa Lubeleje ya kuja Wizarani kwetu kama ambavyo anaifanya ili tuweze kuikamilisha hii barabara iweze kupitika na kusiwe tena na malalamiko makubwa kama yalivyo kwa sasa, kwa mujibu wa Mheshimiwa Lubeleje kadri anavyoyaleta Wizarani kwetu.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni akiwa Mkoani Mwanza aliahidi kuifanya Mwanza kuwa Geneva; lakini Mwanza Mjini kuna barabara zenye urefu wa kilometa 546.1 ambapo kilometa 43.67 zina lami na kilometa 3.556 zimejengwa na mawe:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza barabara zenye kiwango cha lami?
(b) Je, Serikali itashirikiana vipi na Halmashauri za Ilemela na Nyamagana ili kuboresha barabara zilizopo chini ya halmashauri hizo kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaboresha barabara za Jiji la Mwanza kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 jumla ya shilingi milioni 500 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 1 ya barabara ya Nyakato - Buswelu -Mhonze kwa kiwango cha lami na taratibu za kumpata mkandarasi atakayejenga barabara hizo ziko katika hatua za mwisho. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.16 kwa ajili ya kujenga kilometa 1.4 kwa kiwango cha lami katika barabara hiyo hiyo ya Nyakato - Buswelu - Mhonze yenye urefu wa kilometa 18.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga pia kujenga barabara ya Sabasaba –Kiseke- Buswelu yenye jumla ya kilometa 9.7 kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais. Aidha, Serikali inaendelea na upanuzi wa barabara ya Airport - Pansiasi na kujenga daraja la Furahisha, huu ukiwa ni mpango wa kuboresha barabara za Jiji la Mwanza na kupunguza msongamano wa magari uliopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu ndiyo yenye dhamana ya barabara zote nchini. Hivyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Halmashauri za Ilemela na Nyamagana itaendelea kuhakikisha kuwa fedha zinatengwa mwaka hadi mwaka ili kuhakikisha barabara za Jiji la Mwanza zinajengwa kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA Aliuliza:-
Jimbo la Rufiji ni miongoni mwa majimbo yasiyo na barabara hata nusu kilometa.
Je, ni lini Serikali itafikiria kujenga barabara kuelekea Makao Makuu ya Wilaya yaani kutoka Nyamwage – Utete yenye urefu
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa Mbunge wa Rufiji kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya kilometa 717.5 za barabara kuu ya Dar es Salaam Kibiti hadi Lindi kutoka Jaribu Mpakani hadi Malendego zimejengwa kwa lami na ziko katika Wilaya ya Rufiji na Wilaya mpya ya Kibiti; hivyo Wilaya ya Rufiji inayo barabara ya lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Nyamwage – Utete yenye urefu wa kilometa 33.8 ni barabara Mkoa na inahudumiwa na Wakala wa Barabara kupitia ofisi ya meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Pwani. Barabara hii imekuwa ikitengewa fedha na kufanyiwa matengenezo ya aina mbalimbali kila mwaka na inapitika vizuri katika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 barabara hii imetengewa shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika mwaka 2016/2017 barabara hii imetengewa shilingi milioni 579.147 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali na shilingi milioni 85 kwa ajili ya ukarabati. Aidha, Wizara kupitia Wakala wa Barabara itafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Miaka kadhaa iliyopita Serikali iliahidi kuwa itajenga barabara ya kutoka Kitai Wilayani Mbinga hadi Lituhi Wilayani Nyasa kwa kiwango cha lami, lakini hadi sasa wananchi hawaelewi kinachoendelea juu ya ujenzi huo:-
Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Mbinga na Nyasa juu ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martin Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kitai - Lituhi yenye urefu wa kilometa 84.5 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Ruvuma. Ili kuhakikisha kuwa barabara hii inapitika muda wote, Wizara inaendelea kutenga fedha za kufanyia matengenezo mbalimbali ambapo mwaka 2013/2014 ilitenga shilingi milioni 440 na mwaka 2014/2015 ilitenga shilingi 682.99. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, jumla ya shilingi milioni 1015.123 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii ili iendelee kupitika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maandalizi ya ujenzi wa barabara za Kitai - Lituhi kwa kiwango cha lami, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imekamilisha taratibu za ununuzi za kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hiyo.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Mji wa Lindi imezungukwa na bahari, ambapo wananchi wa Kijiji cha Kitunda wanajishughulisha na shughuli za kilimo na kuishi huko kutumia usafiri ambao sio salama wa mitumbwi midogo midogo kutoka kijijini hapo kwenda Lindi Mjini kwa ajili ya mahitaji muhimu ya kibinadamu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka kivuko kwa ajili ya kuvusha wananchi hao ambao maisha yao yapo hatarini kwa kutumia mitumbwi midogo midogo kutoka Lindi Mjini kwenda Kata ya Kitumbikwela?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyao:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuweka kivuko kati ya Lindi Mjini na Kijiji cha Kitunda. Mradi huu pia utahusisha ujenzi wa maegesho ya kivuko na barabara za maingilio. Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi huu.
MHE. ZAYNAB M. VULU – (K.n.y. MHE. GIBSON B. MEISEYEKI) aliuliza:-
Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Simanjiro ni maeneo yanayotegemeana sana kiuchumi lakini hayana barabara ya kuwaunganisha kiuchumi:-
Je, ni lini Serikali itayaunganisha maeneo haya ya Arusha, Simanjiro, Naberera, Kibaya – Kongwa kwa barabara ili kuimarisha maendeleo ya kiuchumi katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gibson Ole Meiseyeki, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa barabara ya Arusha – Simanjiro – Kibaya hadi Kongwa yenye urefu wa Kilomita 434 ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi, kwani inapita katika maeneo muhimu ya uzalishaji wa kilimo, madini, ufugaji na utalii na pia inaunganisha mikoa mitatu ya Arusha, Manyara na Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo, Serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Arusha – Simajiro – Kibaya hadi Kongwa yenye urefu wa Kilomita 434 ili hatimaye iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha, shilingi milioni 521.3 tayari zimetengwa na kiasi cha shilingi milioni 350 zimeombwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kuanza taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mhandisi mshauri wa kufanya kazi hiyo ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, Serikali itatenga fedha za kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mipango hiyo na kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali imekuwa ikitenga fedha za matengenezo kila mwaka ili kuhakikisha inapitika majira yote ya mwaka. Kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2015/2016, jumla ya shilingi 4,383,895,000/= zilitengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa Bandari ya Karema na ina mikakati gani na Bandari hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa awali wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ulikuwa wa kujenga gati dogo kwa ajili ya kuhudumia abiria wanaozunguka eneo la Karema. Hata hivyo, kutokana na mpango wa Serikali wa kuboresha Reli ya Kati ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kaliua – Mpanda – Karema yenye urefu wa kilometa 360 ambayo kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inaendelea, TPA imelazimika kuboresha mpango wake kwa kujenga bandari badala ya gati ili kukidhi matarajio ya shehena ya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itakayopitia Bandari hiyo ya Karema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kumpata Mshauri Mwelekezi atakayefanya upembuzi yakinifu wa mradi huu ambaye anatarajiwa kuanza kazi ifikapo Juni, 2016 na kukamilika mwezi Desemba, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee kusema kwamba, hiyo kazi imeshaanza. Aidha, baada ya kupokea taarifa ya upembuzi yakinifu, TPA itatangaza zabuni kwa ajili ya kuwapata wajenzi ambapo kazi ya ujenzi wa Bandari ya Karema unatarajiwa kuanza katika mwaka fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Karema wavute subira, kwani Serikali yao imedhamiria kujenga bandari hiyo ambayo itakuwa ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Karema na Taifa kwa ujumla.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo yaliyopo Matai kwenda Kasesya ni ahadi ya muda mrefu ya Serikali na Ilani ya CCM tangu mwaka 2010:-
(a) Je, Serikali itaanza lini kukamilisha ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?
(b) Je, ni lini ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Sumbawanga hadi Kasanga Port utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshmiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Matai hadi Kasesya yenye urefu wa Kilometa 50 ni sehemu ya Barabara Kuu inayounganisha nchi za Tanzania na Zambia katika mpaka wa Kasesya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali ya Tanzania imekwishaanza kutekeleza mpango wa kuijenga kwa lami. Kazi ya usanifu wa kina na maandalizi ya zabuni ilianza mwezi Julai, 2014 na kukamilika Januari, 2015. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 11.614 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Matai – Kasesya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Sumbawanga – Matai hadi Kasanga Port yenye urefu wa Kilometa 112 imekamilika kwa takriban asilimia 53 ambapo kilometa 56 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 32.01 ili kukamilisha ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Matai hadi Kasanga Port ambapo ujenzi unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2017.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Barabara ya kutoka Maswa Mjini kupitia Kijiji cha Njiapanda mpaka Mwigumbi inajengwa kwa kiwango cha lami na barabara hii inaendelea kutoka Kijiji cha Njiapanda kupitia Mji Mdogo wa Malampaka mpaka Mwabuki. Barabara hii ni ya muhimu sana kwa shughuli za kibiashara, kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Maswa Mjini, Mji Mdogo wa Malampaka na Wilaya ya Maswa kwa ujumla na inaunganisha Mkoa wa Simiyu na Mwanza kwa upande wa Wilaya ya Kwimba:-
Je, Serikali ina mpango wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Njiapanda mpaka Mwabuki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya kutoka Kijiji cha Njiapanda – Malampaka - Mwabuki na imeendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali kwa kiwango cha changarawe ambapo katika mwaka wa fedha 2014/2015 barabara hii ilitengewa kiasi cha shilingi milioni 561.225 kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum, matengenezo ya kawaida pamoja na ujenzi wa madaraja matatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, matengenezo hayo yalihusisha eneo la kutoka Jojiro - Nyamilama na Kijiji cha Mwankulwe ambacho kina jumla ya kilometa 20 na madaraja matatu. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 barabara hii imetengewa jumla ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida na matengenezo ya muda maalum ambapo TANROADS Mkoa wa Mwanza imefanya ukarabati kutoka Mwabuki - Jojiro pamoja na kipande cha kutoka Kijiji cha Mwankulwe hadi Malampaka ambacho kina jumla ya kilometa 120. Mpango wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Njiapanda - Mwawabuki utategemea upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafufua barabara ya Mkoa wa Mbeya kwenda Kasanga Port pamoja na kivuko cha Mto Kalambo ambayo pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoizungumzia Mheshimiwa Mbunge ni barabara iliyokuwa inatumika zamani enzi za Wajerumani inayoanzia Wilayani Momba katika Mkoa wa Songwe hadi Kasanga Port. Barabara hiyo ilikuwa inapita katika Vijiji vya Kapele – Kakosi - Ilonga, ambapo jumla ni kilometa 55, ambayo kwa sasa ni sehemu ya barabara ya wilaya inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Momba. Aidha, katika Mkoa wa Rukwa barabara hiyo ilikuwa inapita katika Vijiji vya Mambwenkoswe – Kalepula - Mwimbi - Kasanga Port.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya maeneo katika barabara hiyo ya zamani, kati ya Mwimbi - Kasanga Port hayapitiki kabisa hasa wakati wa masika na katika maeneo mengine barabara inapitika kwa shida hususan katika eneo la Mto Kalambo kwa kuwa hakuna barabara rasmi. Serikali inawaasa wananchi wanaosafiri kutoka Momba na Mbeya kwenda Kasanga Port kutumia barabara ya lami ya Mbeya – Tunduma - Sumbawanga na kuunganisha katika barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumiaji barabara wanaweza pia kutumia barabara ya Wilaya ya Kapele – Kakosi - Ilonga Mkoani Mbeya, barabara ya Mkoa ya Mwambwenkoswe – Kalepula - Mwimbi - Matai na kuunganisha katika barabara kuu ya Sumbawanga – Matai - Kasanga Port Mkoani Rukwa.
MHE. SAUMU H. SAKALA (K.n.y. MHE. MUSSA B. MBAROUK) aliuliza:-
Awamu zote za Serikali zilizopita Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne ziliahidi kujenga barabara ya Tanga – Pangani – Saadani hadi Bagamoyo kwa kiwango cha lami:-
(a) Je, ni lini Serikali itaamua kujenga barabara ya Tanga – Pangani kwa kiwango cha lami?
(b) Kupitia Bunge la Kumi na Moja, je, Serikali inaahidi nini kuhusu ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, lenge kipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Tanga – Pangani – Saadani hadi Bagamoyo, yenye urefu wa kilometa 178 ni sehemu ya mradi wa Kikanda wa barabara ya Malindi – Mombasa – Lungalunga – Tanga hadi Bagamoyo. Mradi huu wa Kikanda unaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Bagamoyo kwa kiwango cha lami ilianza mwezi Januari, 2011 na kukamilika mwezi Novemba, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kutoka kwa washirika wa maendeleo. Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), tayari imeonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa barabara hii. Taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa barabara hii ya Tanga – Pangani – Saadani hadi Bagamoyo zitaanza baada ya kupatikana kwa fedha za ujenzi. Aidha, zoezi la uhakiki wa taarifa za uthamini wa mali za wananchi watakaoathirika na ujenzi wa barabara hii linaendela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imedhamiria kuijenga barabara hii ya Tanga – Pangani – Saadani hadi Bagamoyo kwa kiwango cha lami.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. DKT. NORMAN A. SIGALLA KING) aliuliza:-
Je, ni lini Mkoa wa Njombe utaunganishwa na Mkoa wa Mbeya kilomita 205 kutoka Njombe – Makete – Isionje - Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla King, Mbunge wa Makete kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Njombe – Makete – Kikondo - Isionje (Mbeya) yenye urefu wa kilometa 205.6 ni barabara inayosimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Njombe kwa sehemu ya kilometa 183.4 kutoka Njombe hadi Kikondo na sehemu iliyobaki ya kilometa 22.2 kutoka Kikondo hadi Isionje inasimamiwa na TANROADS Mkoa wa Mbeya. Ili kutekeleza azma ya kuunganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Mbeya, Serikali itatekeleza ujenzi wa mradi wa barabara ya Njombe – Makete – Isionje - Mbeya kwa awamu.
Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo kwa sehemu ya Njombe – Ndulamo - Makete, yenye urefu wa kilometa 109.4 umefanyika na kukamilika mwezi Machi, 2014. Aidha, Serikali inafanya maandalizi ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya Makete – Kikondo - Isionje yenye urefu wa kilometa 96.2.
Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njombe – Ndulamo - Makete, yenye urefu wa kilometa 109.4 unatarajiwa kuanza katika Mwaka wa Fedha 2016/17.
MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:-
Shirika la Reli Kigoma linawahudumia wakazi wa Kigoma, Burundi, Congo, Zambia na kadhalika na inawalazimu wakazi hao kulala stesheni au waamke alfajiri ili kuwahi tiketi na wakati mwingine hukosa tiketi hizo:-
Je, ni kwa nini Shirika la Reli Tanzania (TRL) wasianzishe mfumo wa uwakala wa tiketi ili kupunguza adha hiyo wanayopata wakazi hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri wa treni katika Mkoa wa Kigoma, uuzaji wa tiketi katika Stesheni ya Reli ya Kigoma umekuwa na changamoto kubwa kutokana na ubaguzi na ulanguzi wa tiketi. Ili kudhibiti ulanguzi huo, Kampuni ya Reli Tanzania iliamua kubadilisha utaratibu wa kuuza tiketi siku za safari na kwa kutumia vitambulisho, jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ulanguzi wa tiketi. Hata hivyo, utaratibu huo umekuwa na changamoto zake kwa kusababisha wasafiri kulala Stesheni au kuwalazimu kuamka alfajiri ili kuwahi tiketi hizo.
Mheshimiwa Spika, ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo siyo kuanzisha mfumo wa wakala ambao utaiongezea Tanzania Railway Limited gharama za uendeshaji. Tatizo kubwa lililopo ni idadi ndogo ya safari za treni ambapo huduma inayotolewa hivi sasa haikidhi mahitaji halisi ya wananchi na hivyo kuwa na uhaba wa tiketi kwa abiria. Hivyo ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatarajia kuongeza idadi ya treni za abiria kwa njia ya Kigoma ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa mkoa huo.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Ilani ya CCM iliahidi kutengeneza barabara ya kutoka Njombe - Lupembe - Madeke - Morogoro - kwa lami katika mwaka 2015/2016:-
Je, ni lini barabara hiyo itaanza kutengenezwa hasa ikizingatiwa kuwa imebaki miezi mitano katika mwaka wa fedha 2015/2016?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika ni kweli kuwa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 imeweka katika mpango wa ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kibena – Lupembe - Madeke.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara TANROADS, imeshaanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Njombe (Kibena) – Lupembe - Madeke yenye urefu wa kilometa 126.2 kwa kiwango cha lami. Maandalizi haya yalianza kwa kusaini mkataba kati ya TANROADS na Mhandisi Mshauri M/S Howard Humphreys (T) Limited kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo. Kazi ya usanifu ilikamilika mwezi Machi 2014 kwa gharama ya shilingi milioni 503.55, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njombe – Lupembe - Madeke unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-
Barabara ya Ipole - Mpanda yenye urefu wa kilometa 359 iliyoko kwenye mpango wa kujengwa kwa lami iko kwenye hali mbaya sana kutokana na kuharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha, maji maji yamejaa kuvuka barabara na maeneo mengine yanatitia kiasi kwamba mabasi ya abiria na magari ya mizigo yanapata shida kupita na wananchi wa Tabora, Sikonge na Katavi nao wanataabika sana na barabara hiyo.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani za dharura za muda mfupi kuwasaidia wananchi wa Tabora, Sikonge, Katavi na maeneo mengine wanaoathirika na tatizo hilo?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya mapitio ya haraka ya usanifu wa barabara hiyo ili kunyanyua zaidi tuta na kuongeza madaraja na makalvati ili kudhibiti maji ya mvua yasiharibu barabara mpya itakayojengwa?
(c) Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa lami na kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, lenye sehemu (a), (b) na (c), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mwezi Januari hadi Machi mwaka 2016 Mikoa ya Tabora na Katavi ilipata mvua nyingi na sehemu ya barabara ya Tabora, Ipole, Koga hadi Mpanda kuharibika, hususan Mto Koga kujaa maji na kupita juu ya daraja la Koga. Hali hii ilisababisha barabara ya Tabora - Mpanda, sehemu ya Ipole hadi Nyonga, kufungwa kwa muda Serikali ilichukua hatua za haraka za kuifanyia matengenezo ya dharura barabara hii baada ya mafuriko kupungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, barabara mbadala ya Tabora - Uvinza hadi Mpanda, ilipatiwa pia matengenezo ya dharura ili Mkoa wa Katavi usijifunge kabisa. Kwa kuwa maji yamepungua, hatua nyingine ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kuruhusu magari madogo na mepesi kuanza kutumia barabara ya Tabora hadi Mpanda. Serikali itafanya mapitio ya usanifu wa kina, wakati wa utekelezaji wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Tabora hadi Mpanda. Ujenzi wa barabara hii unategemea kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017 chini ya ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
MHE. SUSAN L. KIWANGA (K.n.y. MHE PETER A. LIJUALIKALI) aliuliza:-
Wilaya ya Kilombero ni moja kati ya Wilaya zinazozalisha kwa wingi mazao ya chakula lakini barabara zake nyingi ni mbovu na hivyo kushindwa kusafirisha mazao kwa urahisi.
(a) Je, ni lini barabra ya Kidatu - Ifakara na Ifakara - Mlimba zitajengwa kwa kiwango cha lami?
(b) Je, ni lini daraja la Mto Kilombero linalounganisha Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga litamalizika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara kwa kiwango cha lami umekuwa ukitekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika awamu ya kwanza Serikali ilijenga kilometa 10 kutoka Kijiji cha Kiberege hadi Ziginali ambapo kazi hii ilikamilika mwaka 2006. Katika awamu ya pili, Serikali ilijenga kilometa 6.17 kutoka Kibaoni hadi Ifakara Mjini ambapo kazi ilikamilika mwaka 2008.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali ilipata msaada kutoka Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa la USAID kwa ajili ya kugharamia kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara yote. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imekamilika. Kazi ya kuandaa nyaraka za zabuni na kutafuta Mhandisi Mshauri atakayesimamia ujenzi wa barabara inaendelea. Kazi ya ujenzi wa barabara ya Mikumi - Kidatu -Ifakara itaanza mara baada ya kukamilika taratibu za ununuzi ili kumpata mkandarasi wa kujenga barabara hii.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Ifakara - Mlimba kwa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu ya barabara kutoka Ifakara hadi Kihansi kilometa 126 ili kuunganisha na sehemu ya barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 24 iliyojengwa hapo awali kati ya Kihansi na Mlimba. Kazi ya upembuzi yakinifu ipo katika hatua za mwisho na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2016. Kazi ya usanifu wa kina inatarajiwa kuanza mara baada ya upembuzi yakinifu kukamilika.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa daraja la Kilombero ulianza tarehe 21 Januari, 2013 ambapo gharama za ujenzi ni shilingi bilioni 55.97. Utekelezaji wa kazi ya ujenzi wa daraja la Kilombero umefikia 50% ambapo kazi inaendelea vizuri na inategemewa kukamilika mwezi Disemba, 2016.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Mkandarasi katika barabara ya kutoka Mwegusi - Maswa tayari ameshapatikana na yuko eneo la kazi.
Je, ni lini barabara ya kutoka Maswa - Itilima - Bariadi itapatiwa mkandarasi kwa ajili ya kuunganisha kipande hicho cha barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Maswa – Itilima hadi Bariadi ni sehemu ya mradi wa barabara kuu ya Mwigumbi - Maswa - Bariadi hadi Lamadi yenye urefu wa kilometa 171. Mradi huu umegawanywa katika sehemu kuu tatu; sehemu ya Mwigumbi hadi Maswa - kilometa 50.3, sehemu ya Maswa hadi Bariadi - kilometa 48.9; na sehemu ya Bariadi hadi Lamadi - kilometa 71.8. Mradi huu wa barabara ya kutoka Mwigumbi - Maswa - Bariadi hadi Lamadi unatekelezwa kwa awamu kwa kugharamiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Bariadi hadi Lamadi - kilometa 71.8 umekamilika. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Mwigumbi hadi Maswa - kilometa 50.3 unaendelea kutekelezwa. Aidha, kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Maswa hadi Bariadi yenye urefu kilometa 48.9 ambapo ujenzi utaanza baada ya fedha kupatikana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Kila Mtanzania ana haki ya kupata habari wakiwamo wananchi wa Itigi.
Je, kwa nini wananchi wa Itigi na maeneo ya jirani wananyimwa haki ya msingi kutokana na Kituo cha Redio Mwangaza kuzuia masafa ya redio nyingine ikiwemo Redio ya Taifa TBC na TBC FM?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inatambua kuwa kila Mtanzania ana haki ya kupata habari wakiwemo wananchi wa Itigi. Upatikanaji wa matangazo yanayotolewa katika masafa ya mawasiliano ya FM hutegemea na ukaribu wa mahali kilipo kituo cha utangazaji husika. Itigi iko umbali mkubwa kutoka vituo vya utangazaji vinavyoweza kusikika katika eneo hilo. Kwa sasa Itigi ni moja ya maeneo ambayo mawasiliano ya vituo vya utangazaji vilivyo mbali hayapatikani vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Itigi ni Wilaya iliyoko Mkoa wa Singida takribani umbali wa kilometa zaidi 150 kutoka mji wa Dodoma na kama kilometa 100 toka Singida Mjini ambako vituo vingi vya redio vinarushia matangazo yake. Hii inafanya redio nyingi kutosikia vizuri eneo kubwa la Wilaya ya Itigi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, uwekezaji wa redio za FM ikiwemo TBC umefanyika katika miji ya Singida na Dodoma ambapo kitaalam mawimbi ya redio hufifia na kusababisha kutokuwepo na usikivu mzuri wa redio katika eneo la Itigi toka miji hiyo. Vilevile Redio Mwangaza imesimika mitambo ya kurusha matangazo (booster stations) Itigi katika kujikwamua na tatizo la usikivu usio wa uhakika toka Dodoma kwa kuzingatia masharti ya leseni katika eneo la Itigi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhimiza TBC kusimika mitambo ya kurusha matangazo kwa ajili ya wakazi wa Itigi ili waweze kupata haki yao ya kupata habari.
MHE KHALIFA MOHAMMED ISSA aliuliza:-
Imekuwa ni kawaida kwa ndege ndogo zenye uwezo wa kubeba abiria kumi hadi kumi na sita kuendeshwa na rubani mmoja bila ya kuwa na msaidizi na rubani kama binadamu anaweza kukumbwa na hitilafu yoyote kiafya na kushindwa kumudu kuongoza ndege:-
(a) Je, Serikali haioni kuwa kuruhusu ndege kuongozwa na rubani mmoja ni sawa na kuyaweka rehani maisha ya abiria?
(b) Je, sheria za nchi yetu na zile za Kimataifa zinasemaje juu ya ndege ya abiria kurushwa na rubani mmoja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Mtambwe, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu zinazoongoza fani ya kuendesha ndege hapa nchini huongozwa na miongozo inayokubalika Kimataifa na ambayo imeridhiwa hapa nchini na Bunge. Katika taratibu hizo kuna matakwa ya kisheria na kiufundi ambayo yakifuatwa yanawezesha kuwa na uwezekano mdogo sana wa marubani kukumbwa na athari ya kiafya na kushindwa kumudu kuendesha ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, marubani hupimwa afya zao na Madaktari Bingwa kila muda maalum kulingana na umri kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 140 mpaka 177 ya The Civil Aviation Personnel Licensing Regulations, 2012. Hivyo basi, Serikali inaruhusu ndege kuendeshwa na rubani mmoja kwa kuzingatia taratibu hizo. Aidha, Kanuni ya 32(5) inasema kwamba ndege iliyoandikishwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuruka kwa shughuli za kibiashara yenye uzito unaozidi kilo 5,700 itakuwa na marubani wasiopungua wawili.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za usalama wa anga nchini zinaongozwa na Sheria Namba 80 (Civil Aviation Act) na Kanuni zilizotengenezwa chini yake. Aidha, urushaji wa ndege yenye abiria tisa au zaidi unaongozwa na Kanuni ziitwazo The Civil Aviation Operation of Aircrafts Regulations, 2012 ambapo ndege inayotimiza vigezo vilivyowekwa kwenye vifungu Namba (2), (3) na (4) vya Kanuni ya 32 kuwa na uzito wa chini ya kilogramu 5,700 inaruhusiwa kuendeshwa na rubani mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika viwango vinavyotolewa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) kwenye kiambatisho Namba 19 chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga wa Chicago, hakuna kiwango chochote kinachobainisha wazi kuwa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 10 au zaidi ni sharti iendeshwe na marubani wawili. Pia, hakuna hata mapendekezo ya kiutekelezaji (recommended practice) kwenye suala hilo. Aidha, kiambatisho cha sita chenye sehemu tatu kinachohusisha uendeshaji wa ndege (operations of aircrafts) ambacho ndicho kinachozungumzia idadi ya marubani katika uendeshaji wa ndege hakuna katazo hilo.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Upembuzi yakinifu wa barabara ya kutoka Nyololo hadi Mtwango yenye urefu wa kilomita 40 umefanyika mwaka 2013/2014:-
Je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa barabara ya Nyololo - Igowole hadi Kibao ilikamilika mwaka 2014 yakiwa ni maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara TANROADS, itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii kwa kiwango cha changarawe ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka wakati taratibu za kutafuta fedha za kuijenga kwa kiwango cha lami zinaendelea na ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo imeelekeza hii barabara katika ukurasa wake wa 61.
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Ulyankulu kwa muda mrefu wamekuwa wakipata tabu ya usafiri kutokana na barabara zake kuwa mbovu kwa muda wote:-
(a) Je, ni lini barabara ya kutoka Tabora hadi Ulyankulu itajengwa kwa kiwango cha lami ili kuondoa kero hiyo?
(b) Je, ni lini barabara ya kutoka Ulyankulu hadi mpakani mwa Kahama itaimarishwa zaidi hata kwa kiwango cha moramu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Tabora – Ulyankulu yenye urefu wa kilometa 79 ni barabara ya Mkoa na inahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS). Kwa sasa kipaumbele ni kuunganisha Mkoa wa Tabora na Mikoa ya Mwanza, Kigoma, Singida na Katavi kwa barabara za lami. Hatua hii ikikamilika Serikali itaanza kujenga barabara za mikoa kwa kiwango cha lami kwa vipaumbele kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Ulyankulu – Kashihi - Nyandeka hadi Kahama yenye urefu wa kilometa 344 ni sehemu ya barabara ya mkoa kutoka Mpanda – Ugala – Lumbe – Kaliua - Ulyankulu hadi Kahama yenye urefu wa kilometa 428 ambayo ipo katika mpango wa kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utakapokamilika, barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji na fedha. Ujenzi huo utajumuisha madaraja yaliyopo katika barabara hii. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha katika bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara hii kwa kiwango cha changarawe.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-
Wapo baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa wakitumia bandari „bubu‟ ili kukwepa kodi na kusababisha Serikali kukosa mapato:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti wafanyabiashara hao wanaotumia bandari bubu?
(b) Je, ni wafanyabiashara wangapi waliokamatwa katika bandari bubu na kufikishwa Mahakamani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu(a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa wafanyabiashara wasio waaminifu, wanaotumia bandari zisizo rasmi, yaani bandari bubu kupitisha biashara za magendo, madawa ya kulevya, maliasili, uhamiaji haramu, uvuvi haramu na matumizi ya vyombo vya majini visivyo salama ili kukwepa kodi na pia kuhatarisha usalama wa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kulipatia ufumbuzi suala hili, Serikali imeanzisha utaratibu wa kufanya vikao vya Wakuu wa Mikoa ya Mwambao wa Bahari ya Hindi na Zanzibar, Kamati za Ulinzi na Usalama na kushirikisha Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Taasisi zinazoshughulikia usafiri majini ambayo ni Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Mheshimiwa Naibu Spika, vikao hufanyika kila robo mwaka. Lengo la vikao hivyo ni kutambua na kurasimisha bandari bubu ambazo kulingana na vigezo vya wingi wa biashara inayopita katika bandari hizo na umuhimu wa bandari hizo kijamii, zinastahili kuendelea kuwepo na kusimamiwa na Halmashauri za maeneo husika. Bandari ambazo hazikidhi vigezo hivyo zinatakiwa kufungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bandari bubu zilizoamuliwa kurasimishwa katika mwambao wa Bahari ya Hindi kwa upande wa Tanzania Bara ni hizi zifuatazo:-
Mkoa wa Dar es Salaam ni Mbweni, Pwani ni Mlingotini, Kisiju na Nyamisati. Kwa Mkoa wa Tanga ni Jasini, Kigombe, Kipumbwi, Mkwaja na Pangani. Kwa Mkoa wa Mtwara ni Kilambo na kwa Mkoa wa Lindi ni Rushungi na Kilwa Kivinje.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, utaratibu wa kurasimisha bandari binafsi umefanyika katika Ziwa Victoria, Halmashauri ya Ilemela na Nyamagana. Bandari tisa binafsi zimetambuliwa na kurasimishwa. Utaratibu huo utaendelea pia katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wema wamekuwa wakiisaidia Serikali kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo yenye bandari bubu kutoa taarifa kwa vyombo vya doria kuhusu kuwepo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu katika bandari bubu na hivyo kuwezesha kukamatwa.
Katika mwaka wa 2015 walikamatwa wafanyabiashara 81 na kuanzia mwezi Januari hadi Machi, 2016 wafanyabiashara 17 wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani. Aidha, kuna bidhaa nyingi zilikamatwa ambazo wamiliki hawakufahamika, hivyo kuzitaifisha moja kwa moja.
Viwanja vya ndege nchini ukiondoa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere - Dar es Salaam havina miundombinu au huduma ya kubebea abiria wasiojiweza ikiwemo wagonjwa, wazee pamoja na watu wenye ulemavu.
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa huduma hii katika viwanja vingine nchini?
(b) Huduma hii imekuwa ikifanya kazi na wakati mwingine kuharibika katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere - Dar es Salaam, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha huduma hii inapatikana muda wote kwenye uwanja huu wa Mwalimu Nyerere?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, (a) Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwa na huduma kwa ajili ya wasiojiweza, wagonjwa, wazee pamoja na watu wenye ulemavu imeweka vifaa vya kubebea wagonjwa (wheel chairs na stretchers) katika viwanja vya ndege vya Mwanza, Mafia, Arusha, Tanga, Songwe na Mtwara; pamoja na lift kwa kiwanja cha ndege cha Bukoba. Juhudi za kuboresha miundiombinu au huduma hiyo katika viwanja vingine zinaendelea kadiri ya upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania imetenga fedha za ndani kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege ikiwemo huduma ya wasiojiweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, (b) naomba nishukuru kuwa Mheshimiwa Stella Ikupa Alex anatambua uwepo wa miundombinu au huduma kwa ajili ya wagonjwa, wazee pamoja na watu wenye ulemavu katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere. Aidha, naomba nimfahamishe kuwa huduma hizo zipo za aina mbalimbali kulingana na mahitaji. Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na huduma zitolewazo katika lift, gari la wagonjwa (ambulance), viti vya magurudumu (wheel chairs) na gari lenye lift (ambulift). Aidha, haijawahi kutokea kuwa nyenzo zinazotumika kutoa aina hizo za huduma zimeshindwa kufanya kazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere una chumba maalum cha maulizo ambapo mtu yeyote mwenye msafiri anayehitaji huduma maalum akifika katika chumba hicho atapata maelezo ya namna atakavyopata huduma anayoihitaji.
Tunatambua uwepo wa baadhi ya watu ambao hufika katika uwanja huo bila kusoma maelezo na hivyo, kushindwa kutambua wapi watapata huduma hiyo. Naomba kuwajulisha kuwa wafanyakazi wa mamlaka ya viwanja vya ndege mara wanapotambua uwepo wa mhitaji wa huduma malaam humsaidia.
MHE. EDWARD F. MWALONGO (K.n.y. MHE. LUCY M. MLOWE) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Njombe - Makete kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina iliyofanywa na Mhandisi Mshauri, Crown Tech Consult Ltd. kwa barabara yote ya Njombe – Ndulamo hadi Makete yenye urefu wa kilometa 109.4 yakiwa ni maandalizi ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga shilingi bilioni 19 kupitia bajeti ya maendeleo kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Njombe - Ndulamo - Makete, na ninaomba kulishukuru Bunge lako, kiwango hiki mmekipitisha.
MHE. LOSESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa gati la Bukondo katika Halmashari ya Wilaya ya Geita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini ninajibu swali namba 405 na naomba kujibu swali namba 405 la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari katika mwaka wa fedha 2016/2017, itafanya tafiti za eneo la gati (Geotechnical Survey na Bathymetric Survey) pamoja na usanifu wa kina (detailed design) kwa kutumia wataalam wa Mamlaka wa Usimamizi wa Bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imepanga kuanza taratibu za kumilikishwa eneo na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya matumizi ya bandari ikiwemo ujenzi wa Gati la Bukondo. Baada ya kukamilika kwa maandalizi ya ujenzi Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi ya Bandari itatenga fedha za ujenzi wa gati hili katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Ujenzi wa barabara ya kutoka Bigwa - Kisaki upo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na fedha za ujenzi zitatoka kwenye mpango wa MCC II au Serikalini na nyumba zote zilizomo ndani ya mita 60 zimewekwa alama „X’ tayari kubomolewa katika maeneo ya Ruvu, Kibangile, Kisemu, Mtamba, Nzasa, Kangazi, Kisanzela, Tambau, Mvuha na Magazi hadi Kisaki:-
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kuwawekea wananchi hao utaratibu wa kuwajengea nyumba bora ili kuachana na utaratibu wa kuwalipa fidia kidogo isiyolingana na mali zao wanazoziacha?
(b) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza ili wananchi waliowekewa alama ya kubomolewa nyumba zao waanze maandalizi ya maeneo ya kuhamia?
(c) Je, ni lini Serikali itatengeneza upya madaraja ya Ruvu, Mvuha na Dutuni yaliyomo kwenye barabara hiyo hasa ikizingatiwa kuwa madaraja hayo ni mabovu sana na yamedidimia na yanaweza kusababisha ajali kwa wanaopita hapo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi huu wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Bigwa hadi Kisaki kwa kuanza na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya barabara ya Bigwa hadi Mvuha ambapo ni kilomita 78 uliokwishaanza baada ya kusaini mkataba wa Mhandisi Mshauri, Unitec Civil Consultants Ltd. wa Dar es Salaam akishirikiana na Mult-Tech Consultant (Pty) Ltd. wa Gaberone Botswana kwa gharama ya Sh. 713,471,140,000/=. Mkataba wa kazi hii ulisainiwa tarehe 9 Septemba, 2014 na utatarajia kukamilika tarehe 30 Juni, 2016. Aidha, upembuzi yakinifu na usanifu huo utajumuisha pia madaraja ya Ruvu, Mvuha na madaraja mengine yote yaliyoko kwenye sehemu ya barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, ujenzi wa sehemu ya barabara ukijumuisha madaraja ya Ruvu na Mvuha yaliyoko katika sehemu ya barabara hii yatajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, usanifu wa daraja la Dutuni ulikishwafanyika na kukamilika mnamo Septemba, 2014. Hata hivyo, ujenzi wa daraja jipya haujaanza kutokana na ufinyu wa bajeti. Wakala wa Barabara Mkoa wa Morogoro utaendelea kuyafanyia matengenezo stahiki madaraja haya ili yaendelee kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia, Serikali haina mpango wa kuwajengea nyumba wananchi waliowekewa alama ya „X’ na ambao nyumba zao zitahitajika kubomolewa ili kupisha ujenzi wa barabara mpya. Fidia ya fedha italipwa moja kwa moja kwa kila mwananchi anayestahili fidia kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na.13 ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009.
Barabara ya Masasi – Nanganga – Nachingwea

(a) Je, Serikali ina mpango gani juu ya ujenzi wa barabara ya Masasi – Nanganga – Nachingwea, yenye urefu wa kilometa 91 kwa kiwango cha lami?
(b) Je, ni lini Serikali italipa fidia wananchi wanaotakiwa kupisha ujenzi wa barabara hiyo hasa ikizingatiwa kuwa tathmini imeshafanyika muda mrefu?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekwishakamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 91 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Kazi za usanifu zimekamilika mwezi Septemba, 2015. Aidha, kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Nanganga.
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la tathmini kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaoathirika na kazi ya ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea – Nanganga limekamilika na ulipaji wa fidia kwa wananchi hao ili kupisha ujenzi utaanza mara baada ya fedha kupatikana.
MHE. BONNAH M. KALUWA aliuliza:-
Mwaka 1995 Serikali ilifanya uthamini wa wananchi wa Kata ya Kipawa ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege Dar es Salaam ambapo baadhi ya wananchi hao walilipwa fidia lakini kuna baadhi ambao mpaka sasa bado hawajalipwa fidia hiyo na hawajui ni lini watalipwa:-
Je, Serikali imejipanga vipi kuwalipa wananchi hao ambao hawajalipwa ili waweze kupisha upanuzi wa uwanja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonna Mosses Kaluwa, Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilifanya uthamini wa mali za wananchi ili kupisha upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Dar es Salaam mwishoni mwa miaka ya 90. Maeneo yaliyoainishwa kwa ajili ya upanuzi huo ni Kipawa, Kigilagila na Kipunguni. Kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali imekuwa ikilipa fidia wakazi hao kwa awamu kama ifuatavyo:-
(a) Mwaka 2009/2010: Kaya/wakazi wapatao 1,500 wa eneo la Kipawa walilipwa fidia zilizofikia shilingi za Kitanzania bilioni 18. Zoezi hili lilikamilika Januari, 2010.
(b) Katika mwaka wa fedha 2010/2011, Serikali ililipa shilingi za Kitanzania bilioni 12 za fidia kwa wakazi 864 wa eneo la Kigilagila na malipo yalikamilika Januari 2011.
(c) Mwaka 2013/2014 Serikali ililipa shilingi za Kitanzania bilioni 1.2 ikiwa ni fidia kwa wakazi 59 kati ya wakazi 801 wa eneo la Kipunguni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, hadi sasa ni wakazi wapato 742 wa Kipunguni ndio ambao hawajalipwa fidia zao yenye thamani ya takriban shilingi bilioni 19. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha fidia za wakazi hao waliosalia.
MHE. MBONI M. MHITA (K.n.y. MHE. MUSSA B. MBAROUK) aliuliza:-
Daraja la Mto Wami ni miongoni mwa daraja la muda mrefu na jembamba (single way). Aidha, daraja hilo limesababisha ajali za mara kwa mara na kusababisha wasafiri kupoteza maisha na mali zao:-
Je, ni lini Serikali itajenga daraja jipya katika Mto Wami hasa ikizingatiwa kuwa daraja hilo ni kiunganishi kati ya Dar es Salaam na Mikoa ya Kanda ya Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbaruok, Mbunge wa Tanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbarouk kuwa daraja la Mto Wami ni miongoni mwa madaraja ya muda mrefu ambayo yamejengwa kwa muundo ambao hupitisha magari kwa mstari mmoja yaani (single lane).
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga upya daraja hili ili kukidhi ongezeko la magari yanayopita katika eneo hilo. Kwa hivi sasa kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina zinaendelea ambapo tayari ripoti ya awali ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imeshakamilishwa na inafanyiwa mapitio kabla ya kukamilisha ripoti ya mwisho. Baada ya kukamilisha kazi ya usanifu wa kina wa daraja la Wami, Serikali itatafuta fedha za ujenzi wa daraja hilo.
MHE. DEOGATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Serikali ilitoa ahadi ya kutengeneza barabara ya lami toka Itoni – Njombe – Manda na upembuzi yakinifu tayari umeshafanyika.
Je, ni lini ujenzi huo utaanza hasa ikizingatiwa kuwa barabara hiyo imekuwa kero kubwa hasa kipindi cha masika lakini pia ni muhimu kwa sababu ya ujiio wa miradi ya makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deogratias Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya Itoni – Ludewa hadi Manda yenye urefu wa kilometa 211.4 kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa barabara yameshaanza ambapo kwa sasa barabara inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, usanifu wa kina kwa sehemu ya barabara yenye urefu wa kilometa 50 kuanzia Kijiji cha Lusitu hadi Kijiji cha Mawengi umekamilika na taratibu za kumpata mkandarasi wa kujenga sehemu hii ya barabara zipo katika hatua za mwisho. Ujenzi wa kiwango cha zege wa sehemu ya Lusitu hadi Mawengi umepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usanifu wa kina wa sehemu ya barabara iliyobaki, unatarajiwa kukamilika Julai, 2016. Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO (K.n.y. MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA) aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga barabara ya Geita – Bukoli - Kahama kwa kiwango cha lami.
Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremia Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imeanza maandalizi ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Geita – Bukoli – Kahama yenye urefu wa kilometa 139, kwa kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo. Ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, TANROADS itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali ili barabara hii iweze kupitika majira yote ya mwaka
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAWA A. GHASIA) aliuliza:-
Uwanja wa Ndege wa Mtwara ulijengwa mwaka 1965.
(a) Je, ni lini uwanja huo utafanyiwa ukarabati mkubwa ili kuwezesha ndege kuruka na kutua bila matatizo?
(b) Je, ni lini uwanja huo utawekewa taa ili ndege ziweze kutua wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imeendelea kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya Kiwanja cha Ndege cha Mtwara. Ikiwa ni mpango wa muda mfupi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania inafanya tathmini ya uchakavu wa matabaka ya lami ya njia ya kuruka na kutua ndege ili kubaini ukarabati stahiki unatakiwa na mahitaji ya fedha ya kufanya ukarabati huo. Katika kutekeleza jukumu hili, shilingi milioni 290 zimetengwa na mamlaka katika mwaka 2015/2016 na kazi hiyo ya tathmini inatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2016. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imetenga shilingi bilioni kumikwa ajili ya ukarabati wa kiwanja hiki.
Katika mpango wa muda mrefu, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege katika mwaka wa fedha 2015/2016 ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuandaa mpango kabambe kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho kutoka Daraja III(C) la sasa kwenda daraja IV(E) ili kiweze kuhudumia ndege kubwa zaidi na hivyo kuwa kitovu cha usafiri wa anga kwa Ukanda wa Kusini. Ukarabati na upanuzi wa kiwanja utahusisha miundombinu yote ya kiwanja ikiwemo taa na mitambo ya kuongozea ndege pamoja na majengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo ya uandaaji wa mpango kabambe wa usanifu wa awali inatarajiwa kukamilika Julai, 2016. Kukamilika kwa mpango huu kutaiwezesha Serikali kutafuta fedha za kukarabati na upanuzi wa kiwanja ikiwemo ufungaji wa taa za kuongoza ndege wakati wa kutua na kuruka nyakati za usiku.
(b) Ikiwa ni mpango wa muda mfupi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imeingia makubaliano na Kampuni ya British Gas (BG) kwa ajili ya kutumia taa zake ambazo ni za kuhamisha (portable airfield ground lighting) kwa ajili ya kuongozea ndege pale ambapo ndege itatakiwa kutua usiku.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Barabara ya ulinzi kati ya Tanzania na Msumbiji ni muhimu sana kwa ulinzi na kiuchumi.
Je, ni lini barabara hiyo itajengwa hasa ikizingatiwa kuwa imekuwa ikiahidiwa kwa miaka mitano sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mangamba – Madimba – Tangazo – Kitaya – Mnongodi – Mapili hadi Mitemaupinde ni barabara ya ulinzi inayounganisha Wilaya za Mtwara Vijijini, Newala na Nanyumbu. Barabara hii inayoambaa na mpaka wa Tanzania na Msumbiji ilikuwa inatumiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya ulinzi wa mpakani. Kipande cha barabara hii kati ya Mangamba – Madimba – Tangazo – Kitaya hadi Mnongodi chenye urefu wa kilometa 108 kinahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Sehemu inayobaki yenye urefu wa kilometa 250 haiko chini ya milki ya mamlaka yoyote, hivyo imekuwa pori baada ya kukosa matengenezo kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania, imefanya na kukamilisha usanifu wa kipande cha barabara chenye urefu wa kilometa 120 kati ya Mapili na Mtemaupinde pamoja na daraja la Lukwamba na usanifu kukamilika mwaka 2007. Kwa kuanzia Serikali ilianza kazi ya ujenzi wa daraja hili mwaka 2013 na kazi zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ufunguzi wa sehemu Mapili hadi Mitemaupinde na hadi sasa jumla ya kilometa 25 zimefunguliwa. Aidha, Wizara yangu imetenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kuendelea kuifungua barabara hii na barabara nyingine za ulinzi zilizopo katika Mkoa jirani wa Ruvuma.
MHE. GODFREY W. MGIMWA aliuliza:-
Tatizo la mawasiliano ya simu katika Jimbo la Kalenga bado ni kubwa.
Je, ni lini Serikali itapeleka minara ya simu kwenye vijiji vya Kaning‟ombe, Ikungwe, Lyamgungwe, Igunda na Ikuvilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua ukubwa wa tatizo la mawasiliano ya simu katika Jimbo la Kalenga. Kwa kulitambua hilo Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iliainisha vijiiji vya Kata ya Wasa kikiwemo kijiji cha Ikungwe na kuviingiza katika Mradi wa Awamu ya Kwanza (A). Mradi huu unatekelezwa na Kampuni ya Simu ya TTCL kwa ruzuku ya dola za Kimarekani 107,968 ambapo mpaka sasa mnara tayari umeshajengwa. TTCL itaanza kutoa huduma za mawasiliano huko Kalenga mwishoni mwa mwezi Juni, 2016 baada ya kukamilisha ufungaji wa vifaa vya mawasiliano katika mnara uliojengwa.
Aidha, vijiji vya Igunda na Lyamgungwe kutoka katika Kata ya Lyamgungwe vimeingizwa katika utekelezaji wa miradi ya mawasialiano ya Viettel katika awamu ya pili na awamu ya tatu iliyoanza Novemba, 2015 na kutarajiwa kukamilika Novemba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kijiji cha Kaning‟ombe katika kata ya Mseke na kijiji cha Ikuvilo katika kata ya Luhota vitaingizwa katika miradi ya mwaka wa fedha 2016/2017 kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote UCSAF kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI (K. n. y. MHE. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Ni zaidi ya miaka mitano sasa tangu Meli ya MV Butiama isitishe huduma zake katika Ziwa Victoria kati ya Mwanza na Nansio (Ukerewe) hali inayosababisha shida na usumbufu mkubwa wa usafiri kwa wakazi wa Ukerewe.
(a) Je, ni lini meli hiyo ya MV Butiama itatengenezwa na kuendelea kutoa huduma kati ya Mwanza na Nansio?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta meli mpya sasa ikizingatiwa kuwa meli ya MV Clarius imechakaa sana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, meli ya MV Butiama ambayo ilikuwa inatoa huduma ya usafiri majini kati ya bandari ya Mwanza na bandari ya Nansio - Ukerewe ilisitisha huduma hiyo mwaka 2010 baada ya engine yake kupata uharibifu mkubwa na kukatika muhimili wake (crankshaft). Kufuatia uharibifu huo tathmini ilifanyika na kubaini kuwa injini hiyo isingefaa tena kutumika kwa ajili ya usafirishaji wa aibiria na mizigo na kwamba inabidi iununuliwe engine mpya pamoja na gear box yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni ya huduma za meli MSCL ilikamilisha mchakato wa kupata engine stahiki kwa ajili ya meli hiyo na gharama elekezi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli imetenga kiasi cha fedha za Kitanzania shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya matengenezo ya meli ya MV Butiama. Aidha, kulingana na tathmini iliyofanyika matengenezo ya meli hiyo yanategemewa kukamilika ndani ya miezi wa kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mipango thabiti ya kujenga meli mpya zitakazotoa huduma ya usafiri na usafirishaji katika Ziwa Victoria na maziwa mengine makuu ya Tanganyika na Nyasa. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha fedha za Kitanzania shilingi bilioni 21.0 ikiwa malipo ya awali ya asilimia 50 kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Serikali imeweka alama ya “X” ya kijani na nyekundu katika nyumba za wakazi wa Jimbo la Njombe Mjini kikiwemo na Kituo cha Polisi cha Njombe.
Je, Serikali inasema nini juu ya tafsiri sahihi ya alama hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na Sheria ya zamani ya Barabara ya mwaka 1932 ambayo ilirekebishwa mwaka 1967 (The Highway Ordinance CAP. 167) upana wa eneo la hifadhi ya barabara kuu na barabara za mikoa ulikuwa ni mita 45 yaani mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kila upande.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii naenda taratibu kwa sababu najua watu wengi sana wana-interest nalo na wananchi wasikie. Sheria mpya ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 (The Road Act, No. 13 of 2007) na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009 (The Road Management Regulations of 2009) ziliongeza upana wa eneo la hifadhi ya barabara kuu na barabara za Mikoa kuwa mita 60, yaani mita 30 kutoka katikati ya barabara kila upande, hivyo kuna ongezeko la mita 7.5 kila upande wa barabara kulingana na Sheria mpya ya Barabara ya mwaka 2007.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na maelezo ya utangulizi napenda kutoa ufafanuzi kwamba, nyumba zilizo ndani ya eneo la mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kila upande zipo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara kinyume cha sheria, hivyo zimewekewe alama ya “X” nyekundu na zinatakiwa kubomolewa bila malipo yeyote ya fidia.
Aidha, nyumba zilizojengwa katika eneo la kutoka mita 22.5 hadi mita 30 kutoka katikati ya barabara kila upande kabla ya Sheria mpya ya Barabara ya mwaka 2007 zimewekewa alama ya “X” ya kijani katika baadhi ya Mikoa kwa ajili ya utambuzi ili maeneo hayo yakihitajika kwa ajili ya ujenzi au upanuzi wa barabara wamiliki walipwe fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wananchi kutofanya uendelezaji mpya wa nyumba kwenye eneo la hifadhi ya barabara ili kuepuka hasara ya kuvunjiwa nyumba zao bila kulipwa fidia.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA aliuliza:-
Je ni lini Serikali itawasaidia wananchi wa Wilaya ya Mkuranga kwa kuwaunganisha kwa barabara ya moja kwa moja kutoka Mkuranga - Kisarawe - Kibaha bila ya kupitia Mkoa wa Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasialiano napenda kujibu swali la Mheshimwia Abdallaha Hamis Ulega, Mbunge wa Mkuranga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya za Mkuranga, Kisarawe na Kibaha zimeunganishwa na barabara za lami kupitia Dar es Salaam kutokana na sababu za kijiografia. Aidha, Wilaya za Kibaha na Kisarawe zinaunganishwa na barabara ya Kiluvya - Mpuyani yenye urefu wa kilometa 22, na Wilaya za Kisarawe na Mkuranga zinaunganishwa na barabara ya lami kupitia Mbagala - Charambe yenye urefu wa kilometa 29.
Mheshimiwa Naibu Spika, Makao Makuu ya Wilaya za Mkuranga na Kibaha yapo kwenye barabara kuu za Dar es Salaam – Kibiti – Lindi; na Dar es Salaam - Chalinze - Mbeya hadi Tunduma na barabara hizi zinapitika na zipo kwenye hali nzuri. Aidha, barabara ya moja kwa moja ya Mkuranga - Kisarawe -Kibaha, itawekwa katika mipango ya baadae ya Serikali kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE (K.n.y. MHE. JOHN W. HECHE) aliuliza:-
Barabara ya Tarime - Nyamwaga - Serengeti inapita kwenye Mgodi wa Nyamongo na pia ndiyo tegemeo kuu la uchumi wa Wilaya ya Serengeti na Tarime kwa kutoa mazao kwa wakulima na kuyasafirisha hadi sokoni Musoma Mjini:-
Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Wegessa Heche, Mbunge wa TarimeVijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Tarime – Nyamwaga – Mugumu - Serengeti ni barabara ya Mkoa yenye urefu wa kilometa 85 na ni kiungo muhimu sana kiuchumi na kijamii kwa Wilaya za Tarime na Serengeti. Barabara hiyo pia ni kiungo muhimu kwa watalii wanaotokea nchi ya Kenya kupitia Sirari kuelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hiyo, Serikali imeanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu kutoka Tarime kuelekea Mugumu Serengeti. Hadi sasa jumla ya kilometa sita za barabara hiyo zimekamilika kwa kiwango cha lami katika eneo la Mji wa Tarime. Pia ujenzi wa kilometa mbili unaendelea na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi 430 milioni kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Tarime, Nyamwaga hadi Mugumu yakiwa ni maandalizi ya kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mara katika barabara ya Tarime, Nyamwaga hadi Mugumu.
MHE. DUSTAN L. KITANDULA (K.n.y. MHE. OMAR A. KIGODA) aliuliza:-
Kufuatia kukamilika kwa barabara za Handeni – Korogwe na Handeni – Mkata:-
Je, ni lini Serikali itafungua Vituo vya Mizani katika barabara hizo ili kuokoa barabara hizo na kukusanya mapato hasa ikizingatiwa kuwa miundombinu hiyo imeshatengenezwa lakini inaendelea kuharibika na haijawahi kutumika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kulinda barabara ya Handeni - Korogwe pamoja na Handeni - Mkata zisiharibiwe Serikali imeshafungua vituo vya mizani vya Kwachaga kilichopo barabara ya Handeni hadi Mkata na Misima kilichopo barabara Handeni hadi Korogwe. Mizani zote zimefunguliwa na kuanza kazi mwezi Desemba, 2015.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano katika kampeni zake za uchaguzi alipokuwa Itigi aliombwa na wananchi wa Itigi kuwajengea barabara ya kuingia Mji wa Itigi yenye urefu wa kilometa 8.3 na akakubali.
Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kama ilivyoahidiwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kuingia Mji wa Itigi (Itigi access road) yenye urefu wa kilometa 8.3 iko chini ya Halmashauri ya Mji wa Itigi. Hata hivyo, ujenzi wa barabara hii utatekelezwa wakati wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara kuu ya Makongorosi - Rungwa - Itigi hadi Mkiwa yenye urefu wa kilometa 413.
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Makongolosi -Rungwa - Itigi hadi Mkiwa umekamilika na kwa sasa Serikali inatafuta fedha za kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu ya mkononi kwenye Kata za Mbembaleo, Nyuundo, Mnima na Kiyanga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Mbambakofi, Mwamko na Mwang’anga kutoka katika Kata ya Mbembaleo, vijiji vya Namahukula, Namambi na Namgogoli kutoka katika Kata ya Mnima na vijiji vya Mkahara, Mnongodi, Mwamko na Tulia kutoka katika Kata ya Kiyanga vimo katika orodha ya vijiji vitakavyopata huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa awamu ya pili na awamu ya tatu ya mradi wa mawasiliano ya Viettel (Halotel).
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa awamu ya pili na awamu ya tatu ulioanza Novemba, 2015 na unategemewa kukamilika Novemba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Kata ya Nyuundo vimeainishwa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na vitaingizwa katika miradi ya siku za usoni kwa kadri ya upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi zitakavyopatikana.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea Jimbo la Mtera katika Kijiji cha Mvumi-Misheni aliahidi kutujengea barabara ya lami kutoka Mlowa Barabarani hadi Mvumi-Misheni kwenye Hospitali Teule ya Wilaya ya Chamwino. Pia Rais wa Awamu ya Tano katika kampeni zake alipofika Mvumi-Misheni alisisitiza kuwa barabara hiyo itajengwa haraka iwezekanavyo. Je, ujenzi huo utaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Joseph Lusinde, Mbunge wa Mtera, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea Jimbo la Mtera katika Kijiji cha Mvumi – Misheni aliahidi kujenga barabara ya lami kutoka Mlowa Barabarani hadi Mvumi- Misheni kwenye Hospitali Teule ya Wilaya ya Chamwino. Aidha, ni kweli kuwa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Rais wa Awamu ya Tano, naye aliahidi kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii kwa jamii na hususan katika kusaidia wagonjwa wanaoenda kupata huduma ya matibabu katika Hospitali ya Mvumi Misheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu huo, azma ya Serikali ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami iko pale pale na itatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa sasa barabara hiyo itaendelea kuhudumiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kufanya matengenezo ya aina mbalimbali kwa kiwango cha changarawe kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Kata ya Kizara tangu uhuru haijawahi kuwa na mawasiliano ya simu:-
Je, ni lini Kata hiyo itapatiwa mawasiliano ya simu?
NAIBU WIZARA WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kuwa Kata ya Kizara haina mawasailiano ya uhakika ya simu. Kwa kulitambua hilo, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ilikiingiza Kijiji cha Bombo-Majimoto kutoka katika Kata ya Kizara katika utekelezaji wa Mradi wa Mawasiliano Vijijini wa Awamu ya Pili ‘B’.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unaotekelezwa na Kampuni ya Simu ya TIGO kwa ruzuku ya Dola za Kimarekani 105,920, ulianza kutekelezwa tarehe 23 Mei, 2015. Hadi sasa TIGO wameshafanya technical surveys ya eneo la kujenga mnara na manunuzi ya eneo hilo ambapo mradi unategemewa kukamilika ifikapo tarehe 30 Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Vijiji vya Kilangangua, Kizara Kwemkole na Kwenkeyu vimo katika utekelezaji wa Awamu ya Pili na Awamu ya Tatu ya miradi ya Viettel kwa maana ya Hallotel ambapo vijiji vinavyobaki vya Foroforo, Kiuzani na Mangunga-Mziya vitaingizwa katika miradi ya mawasiliano itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 kutegemeana na upatikanaji wa fedha za mradi.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE (K.n.y MHE. KHATIB SAID HAJI) aliuliza:-
Kutokana na Sheria ya Makosa ya Kimtandao (Cyber Crime Act) kuanza kutumika hapa nchini:-
Je, ni mafanikio gani yamepatikana na kuanza kutumika kwa sheria hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatibu Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 13 ya mwaka 2015 iliyoanza kutumika Septemba, 2015 ililenga kuainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na teknolojia ya habari na mawasiliano, kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki. Kupungua kwa makosa ya mtandao, kuchukua hatua stahiki pindi makosa yanapotendeka na kuimarika kwa matumizi salama ya mtandao katika shughuli mtambuka ikiwemo fedha, biashara, elimu na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwepo kwa Sheria ya Mtandao kumesaidia kupungua kwa usambazaji wa ujumbe wa uchochezi ambazo zingepelekea uvunjifu wa amani, kupungua kwa uwekaji wa picha za ngono kwenye mitandao ya kijamii ambapo zingepelekea uporomokaji wa maadili, kupungua kwa makosa ya udhalilishwaji kwa njia ya mtandao na kupungua kwa usambazwaji wa nyaraka za siri za Serikali kwenye mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia Agosti 2014 hadi Septemba 2015, kabla ya Sheria kuanza kutumika uwekaji wa picha za ngono mtandaoni, matukio yalikuwa 459 yalitolewa taarifa Polisi, usambazaji wa ujumbe wa uchochezi matukio yalikuwa sita, matumizi mabaya ya mtandao matukio yalikuwa 117 na usambazaji wa nyaraka za siri za Serikali matukio yalikuwa tisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonesha kuwa kuanzia Oktoba, 2015 sheria hii ilipoanza kutumika hadi Mei 2016 tukio moja lilitolewa taarifa Polisi kuhusu uwekaji wa picha za ngono. Usambazaji wa ujumbe wa uchochezi hakukuwa na tukio lolote, matumizi mabaya ya mtandao hakukuwa na tukio lolote na usambazaji wa Nyaraka za siri za Serikali matukio mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutumika kwa sheria hii, baadhi ya makosa ya mtandao yameshafikishwa mahakamani ikiwa ni pamoja na kesi nne za uchochezi kwa kutumia mtandao, kesi moja ya kutoa taarifa ya Uchaguzi wa 2015 bila kibali cha Tume ya Uchaguzi, kesi moja ya kutengeneza na kusambaza Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 yasiyo sahihi kwenye mtandao na kesi moja ya kutoa taarifa zisizo sahihi kwa njia ya mtandao.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Barabara ya Murushaka ni kiungo muhimu kwa Karagwe na Kyerwa na ni barabara muhimu sana kiuchumi, lakini barabara hiyo ni mbovu sana wala haipitiki kabisa:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutengeneza barabara hiyo ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Kyerwa?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kwa lami barabara hiyo kwa sababu zaidi ya magari asilimia 90 yanayotoka Uganda na Kyerwa hutumia barabara hiyo iliyosahaulika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara inayozungumziwa ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Kagera inayoitwa Bugene au Omurushaka hadi Kaisho hadi Murongo, na ni ya changarawe, yenye jumla ya kilometa 112 na inapitika wakati wote licha ya sehemu chache korofi wakati wa mvua nyingi. Barabara hii inaunganisha Wilaya za Karagwe na Kyerwa na nchi jirani ya Uganda eneo la Murongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii imekuwa ikitenga fedha kila mwaka ili kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali pamoja na kuimarisha mlima mkali wa Rwabunuka ili uweze kupitika wakati wote, ambapo hadi sasa jumla ya kilometa 10 zimeshawekwa lami na kupunguza usumbufu kwa magari ya mizigo na abiria yanayopita katika mlima huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2015/2016, matengenezo ya barabara yanayojumuisha kuchonga barabara, kuweka changarawe sehemu korofi na kuimarisha mifereji yamefanyika ambapo tayari kilometa 40 zimeshawekwa katika hali nzuri na kilometa moja zaidi ya lami itajengwa katika mlima Rwabunuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna magari mengi katika barabara hii ya Bugene – Kaisho hadi Murongo. Serikali kulingana na vipaumbele vyake na umuhimu wa kila barabara inaendelea kutafuta fedha ili kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hii ili hatimaye iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, Barabara Kuu ya Omugakorongo – Kigarama – Murongo yenye urefu wa kilometa 105 nayo imepewa kipaumbele, kwani hivi sasa inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa barabara hii utarahisisha usafiri wa bidhaa, mazao na abiria kati ya nchi ya Uganda na Wilaya za Kyerwa, Karagwe na pia kupunguza wingi wa magari katika barabara ya Bugene yaani Omurushaka – Kaisho hadi Murongo.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Katika karne hii ya sayansi na teknolojia, mawasiliano ya simu za mkononi ni muhimu sana katika kurahisisha na kuharakisha huduma mbalimbali kwa watumiaji wakiwemo wavuvi, wakulima, wafanyabiashara, wafanyakazi, wasanii na kadhalika:-
Je, ni lini Serikali itaboresha ujenzi wa minara ya huduma ya mawasiliano ya simu katika Vijiji vya Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa mawasiliano ya simu za mikononi ni muhimu katika kurahisisha na kuharakisha maendeleo na ndiyo maana Serikali imeweka sera madhubuti za kuhakikisha wananchi katika maeneo yote ya nchi wanapata huduma hiyo. Kwa kutambua hilo, Serikali ilianzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili kutekeleza sera hiyo kwa kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo yote ya nchi yenye uhitaji wa huduma husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imetenga jumla ya dola za Marekani 2,186,061 kwa ajili ya kupeleka mawasiliano katika jumla ya kata 25 za Mkoa wa Lindi zilizokuwa ama na huduma duni au kutokuwa na huduma kabisa za mawasiliano ya simu za mikononi. Kati ya Kata hizo, Kata ya Kiegi Wilaya ya Nachingwea imeshapata mawasiliano ya simu za mkononi kupita kampuni ya TTCL wakati kata nyingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote itaendelea kuyaainisha maeneo mengine ya Mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla wa kadri ya uhitaji na upatikanaji wa fedha katika kufanikisha malengo ya uanzishwaji wa Mfuko ambayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa kila mwananchi wa Tanzania bila kujali mahali alipo anapata huduma za mawasiliano ili kurahisisha na kuhakikisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kimaendeleo.
MHE. JOHN W. HECHE (K.n.y. MHE. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Ni miaka mitatu sasa tangu barabara ya Bunda – Kisorya - Nansio iwekwe katika mpango wa ujenzi kwa kiwango cha lami lakini ujenzi huo unasuasua tu.
(a) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utakamilika?
(b) Je, Serikali ina kauli gani juu ya ujenzi wa daraja kati ya Kisorya (Bunda) na Lugezi (Ukerewe)?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nyamuswa (Bunda) - Kisorya - Nansio yenye urefu wa kilometa121.9 inaunganisha Mikoa ya Mara na Mwanza.
Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imeanza kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami katika awamu ya tatu; Nyamuswa - Bunda - Bulamba (kilometa 55); Bulamba – Kisorya (kilometa 51) na Kosorya - Nansio (kilometa 15.9) ikihusisha pia ujenzi wa daraja kubwa kati ya Kisorya na Lugezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara hii umekamilika isipokuwa sehemu ya Kisorya - Nansio (kilometa 15.9). Ujenzi wa kiwango cha lami umeanza kutekelezwa Disemba 2013 kwa sehemu ya Bulamba - Kisorya (kilometa 51) na unaendelea. Hadi sasa ujenzi wa sehemu hii ya barabara umekamilika kwa asilimia 14. Hata hivyo, ujenzi wake umekuwa ukisuasua kutokana na kucheleweshwa kwa malipo ya mkandarasi. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha ili kukamilisha ujenzi wa barabara hii.Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imeanza mipango ya ujenzi wa daraja kati ya Kisorya na Lugezi linalounganisha Mikoa ya Mara na Mwanza ambayo imekamilisha upembuzi yakinifu na kwa sasa usanifu wa kina unaendelea.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, ni lini Ujenzi wa barabara ya Kibaha - Mapinga, km 23 kwa kiwango cha lami utaanza na kukamilika kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2015?
NAIBU WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibaha (TAMCO) - Mapinga yenye urefu wa kilometa 23 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara kupitia Ofisi ya Meneja wa Mkoa wa Pwani. Ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami, Serikali imefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao umekamilika. Pamoja na juhudi hizo hadi sasa tayari ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa moja kuanzia njia panda ya TAMCO umekamilika kwa kuwa eneo hilo halikuwa na tatizo la ulipaji wa fidia.
Eneo lote lililobaki katika barabara hii linahitaji kulipa fidia kwa wananchi watakaoathirika na ujenzi wa barabara hiyo. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha za kulipa fidia kabla ya kuendelea na ujenzi wa sehemu iliyobaki.
MHE. MIZA B. HAJI aliuliza:-
Kumekuwepo na kutoridhishwa kwa wananchi kutokana na barabara zetu kutengenezwa chini ya kiwango hali ambayo inapelekea barabara hizo kufanyiwa matengenezo mara kwa mara.
(a) Je, Serikali inaweza kugundua ni barabara ngapi nchini zilizotengenezwa chini ya kiwango?
(b) Je, ni hatua gani zilizochukuliwa kwa waliosababisha tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Miza Bakari Haji Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimwa Spika, Serikali inaweza kugundua kama barabara imejengwa chini ya kiwango kwani ukaguzi wa ujenzi wa miradi ya barabara unatekelezwa wakati wote wa ujenzi na hata baada ya mradi kukamilika kabla ya muda wa ukaguzi wa mwisho kupita. Aidha, ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara nne za Mbagala Rangi Tatu - Bendera Tatu, Sekenke - Shelui, Kyamyorwa - Buzirayombo na Nangurukuru – Mbwemkulu ulipokamilika yalijitokeza matatizo mbalimbali kabla ya muda uliotarajiwa yalijitokana na mapungufu kwenye ubora kama mashimo madogo madogo katika maeneo kadhaa ya barabara na kuharibika kwa tabaka mbili za juu.
Mheshimiwa Spika, kwa kawaida ujenzi wa barabara hutekelezwa kwa kuzingatia mikataba kati ya TANROADS na mkandarasi, na kati ya TANROADS na mhandisi msimamizi. Viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara vimetajwa katika mikataba husika. Endapo kunatokea tatizo lolote kuhusu ubora wa kazi, kwa mfano barabara kujengwa chini ya kiwango, vipengele vya mikataba husika hutumika kabaini nani aliyesababisha mapungufu hayo kati ya mkandarasi, mhandisi msimamizi au mwajiri na hatimaye kuwajibika. Kutokana na mapungufu hayo niliyoyataja juu katika barabara hizo nne, hatua zilichukuliwa kulinganana vipengele vya mikataba husika na makandarasi wa miradi hiyo walirekebisha mapungufu hayo kwa gharama zao wenyewe.
Mheshimiwa Spika, sababu nyingine inayosababisha uharibifu wa barabara ni wingi wa magari makubwa ya mizigo hususan magari makubwa ya mizigo yanayotumia excel zenye tairi moja yaani super single tyre. Hivyo kwa kuwa Sheria ya Uthibiti wa Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki imeweka kiwango kidogo cha uzito wa tani 8.5 kwenye excel zenye tairi moja (super single), Wizara inafanya utaratibu wa kuona ni jinsi gani itafanya mabadiliko ya Kanuni za Usalama Barabarani za mwaka 2001 ziweze kuona na sheria hiyo kwenye kipengele cha super single.
MHE. WILLIAM D. NKURUA aliuliza:-
Ujenzi wa barabara za lami hufuata Ilani ya Chama Tawala na matamko ya viongozi. Katika ziara yake Wilayani Nanyumbu, Rais wa Awamu ya Nne aliahidi ujenzi wa barabara ya Nangomba hadi Nanyumbu kwa kiwango cha lami.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa William Dua Nkurua, Mbunge wa Nanyumbu, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Nangomba – Nanyumbu uliofanywa na Kampuni za UWP – Consulting PTY kutoka Afrika Kusini na UWP Consulting Company Limited ya Tanzania ili kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha ili kuanza ujenzi wa barabara hii. Aidha, TANROADS Mkoa wa Mtwara inaendelea na itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Gharama za usafiri wa vyombo vya baharini na angani kwa safari za Zanzibar na Dar es Salaam ni za juu sana licha ya bei ya mafuta kupungua.
Je, Serikali inachukua hatua gani kusaidia wananchi hao kudhibiti nauli hizi za meli na ndege kwa kushirikiana na mamlaka husika toka pande zote mbili za Muungano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kuunguza nauli Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ina jukumu la kujenga ushindani katika sekta ndogo ya usafiri wa ndege na hi ni kwa mujibu wa Ibara ya 25 ya Sheria ya Usafiri wa Anga (Civil Aviation Act [Revised Edition 2006]). Panapokuwa na ushindani katika njia moja nauli hutokana na soko. Aidha, mamlaka huingilia kati kisheria kuweka kiwango kikomo pale tu inapotokea kuna ukiritimba na wananchi wanaumia.
Mheshimiwa Spika, mamlaka imejitahidi kuhusu ushindani kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ambapo zaidi ya makampuni kumi ya ndege yanatoa huduma katika njia hiyo kwa nauli kati ya shilingi 140,000 na shilingi 278,000 kwenda na kurudi pamoja na kodi endapo msafiri atanunua tiketi mapema zaidi kabla ya safari. Kwa mfano, tarehe 4 Aprili, 2016 nauli ya juu kwa kampuni kumi za ndege zilizokuwa zinatoa huduma katika njia hiyo ilikuwa shilingi 139,000 na ya chini ilikuwa shilingi 75,000 ambapo wastani wa nauli kwa makampuni yote kumi kwenda tu pamoja na kodi ilikuwa shilingi 88,700.
Mheshimiwa Spika, utaona kuwa wastani wa bei ya nauli ya kwenda Zanzibar pamoja na kodi ni wa chini na unaendana na gharama halisi za uendeshaji na faida kidogo kwa mtoa huduma ukilinganisha na sehemu ambazo hakuna ushindani kabisa au hakuna ushindani mkubwa kama ilivyo Songwe na Mwanza. Hivyo, nashauri kwa mtu anayehitaji kusafiri afanye mipango ya safari yake mapema ili kupata unafuu wa nauli, maana kadri anavyonunua tiketi yake mapema kabla ya safari, ndivyo nauli inavyokuwa chini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu vyombo vya usafiri wa bahari kwa safari za Zanzibar na Dar es Salaam, kwa sasa kuna jumla ya vyombo sita vya majini vinavyotoa huduma hiyo. Vyombo hivyo vyote vimesajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Bahari Zanzibar (Zanzibar Maritime Authority). Hivyo, Wizara yangu kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imekwishafanya mawasiliano na ZMA ili viwango hivyo vya nauli za vyombo vya majini baina ya Dar es Salaam na Zanzibar vitathiminiwe kwa kuzingatia taratibu za mamlaka ya usajili wa vyombo hivyo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Kumekuwa na ahadi za viongozi wa juu hususan Marais za kujenga daraja la Magara pamoja na barabara ya Mbuyu wa Mjerumani kwa kiwango cha lami na usanifu wa daraja na lami ya zege sehemu ya mlimani hasa ikizingatiwa kuwa ukosefu wa daraja na jiografia ya Mlima Magara kuwa hatarishi sana hasa kipindi cha mvua.
(a) Je, ni lini ahadi hiyo ya viongozi wetu wa Kitaifa itatekelezwa?
(b) Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilometa tano katika Mji wa Mbulu itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuunganisha Mji wa Mbulu na barabara Kuu ya Babati – Arusha katika eneo la Mbuyu wa Mjerumani. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja la Magara lenye urefu wa mita 84. Taratibu za kumpata mhandisi mshauri wa kusimamia ujenzi wa daraja hili zinaendelea. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), inafanya maandalizi ya kutangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Magara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017, jumla ya shilingi milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja la Magara na shilingi milioni 455 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha zege (rigid pavement) kwenye Mlima Magara katika barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itaendelea kutekeleza ahadi za viongozi wa Serikali kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ikiwemo ahadi ya ujenzi wa barabara ya lami katika Mji wa Mbulu yenye urefu wa kilometa tano.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Barabara ya Mkiwa – Rungwa - Makongorosi ni ya udongo na nyakati za mvua barabara hiyo inaharibika sana kiasi cha kutopitika kabisa:-
Je, Serikali ina Mpango gani wa kuitengeneza barabara hiyo kwa lami ili kuwaondelea kero wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi hususan wa Kata za Mwamagembe, Rungwa na Kijiji cha Kitanula.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mkiwa - Rungwa - Makongorosi ni sehemu ya barabara kuu ya kutoka Mbeya – Chunya – Makongorosi - Rungwa - Itigi hadi Mkiwa yenye urefu wa kilomita 413. Kati ya hizo kilometa 219 zimo katika mtandao wa barabara Mkoa wa Singida na sehemu kubwa ikiwa katika Jimbo la Manyoni Magharibi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu ya Mbeya hadi Chunya kilometa 72 umekamilika. Barabara ya Mkiwa - Rungwa hadi Makongorosi ni ya changarawe na hupitika kipindi chote cha mwaka isipokuwa sehemu korofi katika maeneo ya Kintanula na Mwamalugu katika Mkoa wa Singida ambazo husumbua wakati wa kipindi cha mvua nyingi kutokana na hali ya kijiografia na udongo unaoteleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini TANROADS imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami barabara hiyo. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 5.848 kwa ajili ya kuanza sehemu ya barabara sehemu ya Mkiwa – Itigi - Noranga ambazo ni kilometa 57. Tumetenga shilingi bilioni 8.848 kwa ajili ya kuanza ujenzi sehemu ya Chunya -Makongorosi ambayo ni kilometa 43. Aidha, zabuni kwa ajili ya kazi hizi zinatarajiwa kuitishwa mwezi huu Novemba, 2016.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Hivi karibuni tumeshuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizindua Daraja la Kisasa la Kigamboni ambalo limepewa jina la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye hakuwahi kuishi Kigamboni;
Kwa nini daraja hili halikupewa jina na Rais Mstaafu wa Zanzibar na Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Muungano, Mheshimiwa Aboud Jumbe ambaye ana historia kubwa katika Mji huo kwa kuishi karibu miaka 32.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Kigamboni una historia ndefu kwa viongozi mbalimbail wa Taifa letu wakiwemo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Hayati Rashid Mfaume Kawawa na Hayati Aboud Jumbe na wengine wengi. Daraja la Kigamboni lilipewa jina la daraja la Nyerere kwa heshima ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutokana na mchango wake mkubwa kwa maendaeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba wazo la ujenzi wa daraja la Kigamboni lilianza wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza ambapo katika mipango ya maendeleo ya miaka 60, Serikali chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilianza mikakati ya ujenzi wa madaraja makubwa matano ya Kigamboni, Rufiji, Malagarasi, Kirumi na Kilombero.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna barabara, madaraja na miundombinu mbalimbali ya umma iliyopo na inayoendelea kujengwa. Mheshimiwa Mbunge anaweza kupeleka mapendekezo katika mamlaka zinazohusika ili moja ya barabara, daraja au miundombinu iliyopo au itakayojengwa iweze kuitwa kwa jina la Aboud Jumbe kadri itakayoonekana inafaa.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI aliuliza:-
Tangu awamu zilizopita hadi Serikali ya Awamu ya Tano, wananchi wa Kilombero wamekuwa wanapewa ahadi za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kidatu hadi Ifakara na kutoka Ifakara hadi Mlimba:-
(a) Je, Serikali haitambui mchango wa Wilaya ya Kilombero katika nchi wa kulisha Taifa?
(b) Kitendo cha Serikali ya awamu hii kuahidi ujenzi wa viwanda wakati eneo muhimu kwa uchumi wa nchi kama Kilombero likiachwa bila barabara inayosafirisha wakulima na mazao; je, maana yake ni nini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mchango wa Wilaya ya Kilombero katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwa wingi kwa ajili ya matumizi yao na Taifa kwa ujumla hivyo kulifanya eneo hilo kuwa miongoni mwa maeneo ya ghala la Taifa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano, pamoja na kuahidi ujenzi wa viwanda imeweka pia katika kuimarisha miundombinu ya barabara kuelekea kwenye maeneo yenye umuhimu wa kiuchumi kama Kilombero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza azma hiyo, Serikali katika eneo la Kilombero, pamoja na ujenzi wa Daraja la Kilombero unaoendelea, imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami kilometa 16.17 katika Barabara ya Kidatu hadi Ifakara kati ya Kiberege na Ziginali na Kibaoni hadi Ifakara. Aidha, katika barabara ya Ifakara hadi Mlimba zimejengwa kwa kiwango cha lami kilometa 24 kati ya Mlimba hadi Kihansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutimiza ahadi ya Serikali ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mikumi – Kidatu – Ifakari, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mikumi – Kidatu – Ifakara (kilometa 103.3) umekamilika. Usanifu huo umejumuisha upanuzi na ukarabati wa barabara ya lami iliyopo na madaraja sehemu ya Mikumi hadi Kidatu kilometa 35.2 na Kidatu hadi Ifakara kilometa 74.4. Ujenzi wa kiwango cha lami wa sehemu ya Kidatu hadi Ifakara pamoja na madaraja umepangwa kuanza katika robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Serikali ya Marekani kupitia USAID na Serikali ya Uingereza kupitia DFID.
Usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara kutoka Ifakara hadi Kihansi (kilometa 126) ili kuunganisha na kipande cha barabara ya lami (kilometa 24) kilichojengwa awali kati ya Ifakara na Mlimba unaendelea na umepangwa kukamilika mwishoni mwa Oktoba, 2016.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Serikali kupitia Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ililihakikishia Bunge kuwa madaraja ya Mto Mresi katika barabara ya Ulinzi na Shaurimoyo na Nachalolo katika Mto Mwiti yalizolewa na mafuriko na yatajengwa kwa dharura:-
(a) Je, ni maandalizi gani yamefanyika ili madaraja hayo yajengwe kwa haraka?
(b) Je, madaraja hayo yataanza kujengwa lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ulinzi ya kutoka Mangamba – Madimba – Tangazo – Kitaya – Mnongodi – Mapili hadi Mitema Upinde inaunganisha Wilaya za Mtwara Vijijini, Newala na Nanyumbu. Sehemu ya barabara hii, yaani Mangamba – Madimba – Tangazo – Kitaya - Mnongodi hadi Namikupa yenye urefu wa kilomita 108 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANROADS imekamilisha usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha changarawe wa sehemu ya barabara hii yenye urefu wa kilomita 120 unaojumuisha madaraja ya Mbangara, Miesi na Kigwe yaliyopo katika barabara hii ya Ulinzi. Serikali kwa sasa inatafuta fedha ili kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, madaraja ya Shaurimoyo na Nakalola yaliyopo katika barabara za Mpindimbi hadi Shaurimoyo na Mpindimbi hadi Nakalola zinahudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ambapo fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja hayo bado zinatafutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali itaendelea kuifanyia barabara hii matengenezo ya kawaida, matengenezo ya muda maalum na matengenezo ya sehemu korofi. Aidha, kuhusu sehemu ya barabara ya Ulinzi iliyobaki kuanzia Mapili hadi Mitema Upinde yenye urefu wa kilomita 250, Serikali imetenga shilingi milioni 140 kwa ajili ya kuifungua.
MHE. MARIA N. KANGOYE (K.n.y. MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA) aliuliza:-
Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuanza ujenzi wa daraja la Kilombero na utakamilika lini na kuanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa daraja la Kilombero ulianza tarehe 21 Januari, 2013, nao unaendelea vizuri. Ujenzi wa daraja hili haukuweza kukamilika kwa wakati uliopangwa ambao ni Septemba, 2016 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo mvua nyingi za masika zilizosababisha Mto Kilombero kufurika na kupunguza kasi ya utekelezaji wa ujenzi. Kwa sasa ujenzi wa daraja hili umefikia asilimia 75 na ujenzi unatarajiwa kukamilika mwishoni wa mwezi Desemba, 2016 na daraja kuanza kutumika.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Halmashauri ya Busokelo ina changamoto za miundombinu ya barabara ambayo hairidhishi, na ukizingatia kuwa wananchi wake wanategemea zaidi shughuli za kilimo na usafirishaji wa gesi asilia ya carbondioxide.
(a) Je, ni lini Serikali itajenga barabara inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Njombe kupitia Mwakaleli, kata za Kandete na Luteba?
(b) Je, ni lini Serikali itajenga barabara inayounganisha Jimbo la Busekelo (kijiji cha Kilimansanga) na Jimbo la Rungwe (kijiji cha Suma)?
(c) Vyanzo vya Halmashauri haviwezi kujenga barabara zote na hivyo kulazimika kuomba msaada TANROADS; je, ni lini maombi ya Halmashauri ya Busekelo, kuhusu kupandishwa hadhi ya barabara zaidi ya tano tulizoomba ili ziwe chini ya TANROADS yatajibiwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Jimbo la Busokelo lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Njombe kupitia Mwakaleli, kata ya Kandete na Luteba inapitia Katumba – Lusanje – Kandete – Ikubo hadi Luteba. Sehemu ya barabara ya Katumba - Lusanje – Kandete – Ikuba ambayo ni kilometa 34 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na TANROADS, na sehemu ya Ikuba hadi Luteba inahudumiwa na Halmashauri ya Busokelo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANROADS inaendelea kufanyia matengenezo kwa kiwango cha changarawe ili iendelee kupitika ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 271.805 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Katumba - Lwangwa hadi Mbambo na shilingi milioni 38.086 zimetengewa kwa ajili ya barabara ya Lusanje - Kandete hadi Ikubo. Mpango wa Serikali kwa sasa ni kuendelea kuzifanyia mategenezo barabara hizi ili zipitike wakati wote wa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na milima yenye miinuko mikali kwa sasa hakuna barabara inayounganisha Jimbo la Busokelo na Jimbo la Rungwe kupitia vijiji vya Kilimansanga na Suma. Serikali haifikirii kufungua barabara ya kuunganisha maeneo hayo kutokana na milima hiyo mikali, hivyo barabara zilizopo tunaomba ziendelee kutumika kuhudumia maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, maombi ya Halmashauri ya Busokelo kuhusu kupandishwa hadhi barabara zaidi ya tano zilizoombwa ili ziwe chini ya TANROADS yanafanyiwa uchambuzi pamoja na maombi mengine yaliyopokelewa kutoka nchi nzima kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kwenye Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009. Mara taratibu za uchambuzi zikikamilika barabara ambazo zina kipaumbele kiuchumi na kijamii zitapandishwa madaraja kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA aliuliza:-
Mji wa Newala tangu utawala wa kikoloni ulikuwa na Uwanja wa Ndege mdogo uliowezesha kutua ndege ndogo. Uwanja huo kwa sasa umejengwa nyumba za kuishi. Kwa vile Mji wa Newala unapanuka sana na una hadhi ya Halmashauri ya Mji na Uongozi wa Wilaya umetenga eneo la kujenga uwanja mpya wa ndege:-
Je, Serikali imefikia hatua gani katika maandalizi ya kujenga Uwanja Mpya wa Ndege katika Halmashauri ya Mji wa Newala?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikifunga Kiwanja cha Ndege cha Newala mwaka 1998 kutokana na uwepo wa mazingira yasiyo salama ya uendeshaji wa ndege, uliosababishwa na makazi ya watu kusonga katika maeneo yanayozunguka kiwanja hicho. Aidha, ukatizaji wa watu kiwanjani na mmomonyoko wa ardhi uliopo eneo la kiwanja ulionekana kuhatarisha usalama wa ndege na watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Halmashauri ya Mji wa Newala kutenga eneo jipya kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, ilipeleka wataalamu wake kukagua eneo hilo na ikaonekana kukidhi vigezo vya kiwanja cha ndege kulingana na viwango vya Kimataifa vinavyotolewa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO Standards).
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia kukamilika kwa ukaguzi huo, utaratibu unaofuata ni kwa Halmashauri husika kutekeleza jukumu lao muhimu ambalo ni kukamilisha upimaji na uthamini wa mali zilizomo ndani ya eneo hilo. Hadi sasa hatua hizo za kulitwaa eneo husika hazijafanyika. Hivyo, kupitia Bunge lako Tukufu, Wizara yangu inawataka Halmashauri ya Mji wa Newala kukamilisha hatua za utwaaji wa eneo hilo na kulikabidhi kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ili waweze kuanza hatua ya upembuzi na usanifu wa Kiwanja Kipya cha Ndege cha Newala.
MHE. PETER J. SERUKAMBA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye kampeni Jimbo la Kigoma Kaskazini aliahidi kuwalipa fidia wahanga wa Barabara ya Mwandiga – Manyovu.
Je, ni lini jambo hilo litatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mwandiga - Manyovu, yenye urefu wa kilometa 56.26 ulianza mwaka 2009 na kukamilika mwaka 2011.
Mheshimiwa Spika, wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa barabara hii wananchi wa Mwandiga hadi Manyovu walilalamika kwa kuvunja nyumba zao wenyewe bila kulipwa fidia kwa agizo la Serikali. Mwaka 2010 Serikali iliunda tume ya kuchunguza malalamiko hayo na kugundua kuwa wananchi hao walivunja nyumba hizo kwa kuwa zilikuwa ndani ya eneo la hifadhi ya barabara kinyume na Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 pamoja na kanuni zake, hivyo wananchi hao hawakusatahili kulipwa fidia.
MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga viwanda mahali zinapopatikana malighafi.
(a)Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Tumbaku Mkoani Tabora?
(b)Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Kusindika Asali Mkoani Tabora?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-
(a)Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Tabora huzalisha tumbaku nyingi hapa nchini. Kwa mwaka 2015, Mkoa wa Tabora ulizalisha tumbaku tani 39,502. Pamoja na uzalishaji wa tumbaku hiyo, Mkoa wa Tabora hupokea tumbaku inayozalishwa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kigoma. Kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inalipa kipaumbele suala la ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani tumbaku mkoani Tabora. Serikali imefanya mawasiliano ya awali na wawekezaji nchini Vietnam na China ili kuvutia nchi hizi kuwekeza hapa nchini. Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kimepewa maelekezo maalum kunadi fursa hii kwa wawekezaji katika sekta ya tumbaku na sigara hapa nchini.
(b)Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Tabora unazalisha asali takribani lita 11,461,500 sawa na tani 11,500 kwa mwaka. Asali hiyo husindikwa na wajasiriamali wadogo kwa njia ya asili bila kutumia mitambo yenye teknolojia ya kisasa. Wajasiriamali hao wanasindika lita 4,126,140 sawa na tani 4,126 ikiwa ni wastani wa asilimia 36 kwa mwaka. Kiasi cha lita 7,335,360 kinabaki bila kusindikwa.
Mheshimiwa Spika, kulingana na maelezo hayo, Mkoa wa Tabora una fursa kubwa ya uwekezaji wa malighafi hiyo muhimu ambayo pia ina soko la kutosha ndani na nje ya nchi. Kinachotakiwa ni wananchi kutumia fursa hii kuanzisha viwanda vidogo na vya kati hapa nchini. Natoa wito kwa Halmashauri za Wilaya zitenge maeneo ya viwanda vidogo na vya kati na kuyajengea miundombinu wezeshi kisha kuchangamkia fursa kwa kufungua viwanda Tabora na maeneo yote inakopatikana asali kwa wingi.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-
Serikali inatakiwa kuweka mkakati wa kuhakikisha mazao yanauzwa katika vituo maalum vinavyotambuliwa ili kuzuia walanguzi kufuata mazao shambani na kununua kwa bei ndogo:-
Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kutunga sheria kuzuia walanguzi kwenda kununua mazao shambani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa kuna umuhimu wa kutungwa Sheria ya Kuzuia Walanguzi kwenda kununua mazao ya wakulima mashambani. Aidha, kutokana na umuhimu huo, Serikali imeweka sheria ya kuzuia kununua mazao yakiwa mashambani kwa mazao yote yanayosimamiwa na Bodi za Mazao. Mazao hayo ni kahawa, chai, pareto, pamba, korosho, mkonge na tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri za Wilaya zimepewa mamlaka kamili ya kutunga sheria ndogo (bylaws) au kuweka kanuni na taratibu zinazofaa za kuuza mazao ya wakulima katika vituo vilivyowekwa na Halmashauri hizo. Vituo hivyo ni pamoja na magulio na minada, ambapo mazao mbalimbali ya wakulima na wafugaji huuzwa kwa ushindani na kwa kutumia vipimo rasmi. Vituo Maalum vya kununua mazao vinawezesha kusimamia ubora na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imefanya marekebisho ya Sheria ya Vipimo kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa mwaka 2016 (The Written Laws Miscellaneous Amendments)(No. 3) uliopitishwa na Bunge hili mwezi Novemba, 2016. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine, itawezesha Halmashauri kutunga sheria ndogo za usimamizi wa vipimo kwa kuhakikisha kila kijiji kinaaanzisha vituo vya kuuza mazao na kusimamia matumizi ya vipimo rasmi.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Serikali inajitahidi kujenga na kuimarisha madaraja ili kuondoa kero na kupunguza maafa; Daraja la Mto Wami lililopo barabara ya Tanga ni jembamba sana kiasi kwamba magari mawili hayawezi kupishana kwa wakati mmoja:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kulipanua daraja hilo la Mto Wami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa Daraja la Wami katika barabara ya Chalinze – Segera ni kiungo muhimu kati ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania. Daraja lililopo sasa ambalo ni jembamba lilijengwa miaka mingi, hivyo halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwenye barabara hiyo kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa daraja hili katika kukuza uchumi wa nchi, Serikali kupitia TANROADS imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na maandalizi ya nyaraka za zabuni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hili. Zabuni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja jipya la Mto Wami zitaitishwa mwezi Februari, mwaka 2017. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo.
MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Barabara ya TAMCO hadi Mapinga katika Mji wa Kibaha, Mkoani Pwani imekuwa kwenye maandalizi ya kujengwa kwa kiwango cha lami kwa takriban miaka kumi (10) sasa:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hiyo kwa lami.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya TAMCO hadi Mapinga yenye urefu wa kilometa 23 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania kupitia Ofisi ya Meneja wa Mkoa wa Pwani. Ili kujenga kwa kiwango cha lami, barabara ya TAMCO hadi Mapinga kupitia Vikawe kuunganisha na barabara ya Bagamoyo, Serikali imefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao umekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi hizo, hadi sasa tayari ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa moja kuanzia njia panda ya TAMCO umekamilika kwa kuwa eneo hili halikuwa na tatizo la ulipaji wa fidia. Eneo lote lililobaki katika barabara hii linahitaji kulipa fidia kwa wananchi watakaoathirika na ujenzi wa barabara hiyo. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha za kulipa fidia kabla ya kuendelea na ujenzi wa barabara sehemu iliyobaki yenye urefu wa kilometa 22.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Mitambo wameahidi kuhamishia kivuko cha MV Kilombero II kwenda katika kivuko cha Kikove katika Mto Kilombero Juu (Mnyera) baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Kilombero.
Je, ni lini matayarisho ya uhamisho wa Kivuko hicho yataanza rasmi kwa kuwa ujenzi huo wa daraja la Kilombero unatarajia kukamilika hivi karibuni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), imeanza maandalizi ya kuhamisha vivuko vya MV Kilombero I na MV Kilombero II kuvipeleka eneo la Kikove katika Mto Kilombero kwenye barabara inayounganisha Mlimba na Malinyi. Wakala wa Barabara kwa kushirikiana na Wakala wa Ufundi na Umeme umefanya ukaguzi wa barabara ya Mlimba hadi Malinyi ili kubaini mahitaji ya miundombinu itakayowezesha kivuko hicho kufanya kazi katika eneo hilo la Kikove. Miundombinu hiyo ni pamoja na maegesho na barabara unganishi katika kila upande wa mto.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuhamisha vivuko vilivyopo eneo la Ifakara kwenda eneo la Kikove katika barabara ya Mlimba – Malinyi mara tu baada ya mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Kilombero na barabara za maingilio kukamilika. Hivi sasa ujenzi wa daraja la Mto Kilombero umekamilika na Mkandarasi anakamilisha ujenzi wa barabara za maingilio ili daraja lianze kutumika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Ni zaidi ya miaka mitano sasa tangu Meli ya MV Butiama isitishe huduma zake katika Ziwa Victoria kati ya Mwanza na Nansio (Ukerewe) hali inayosababisha shida na usumbufu mkubwa wa usafiri kwa wakazi wa Ukerewe.
(a) Je, ni lini meli hiyo ya MV Butiama itatengenezwa na kuendelea kutoa huduma kati ya Mwanza na Nansio?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta meli mpya hasa ikizingatiwa kuwa meli ya MV Clarius imechakaa sana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.6 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ili kufanya matengenezo makubwa ya meli ya MV Butiama iliyositisha kutoa huduma zake tangu mwaka 2010 kutokana na hitilafu kubwa ya injini zake. Zabuni kwa ajili ya kupata mkandarasi wa kufanya kazi hiyo zilikwishatangazwa na sasa kazi ya uchambuzi wa kina inaendelea. Matarajio yetu ni mkandarasi kuanza ukarabati huo mwezi Machi, 2017 na kumaliza mwezi Novemba, 2017 (b) Kuhusu mpango wa kujenga meli mpya kwa ajili ya kutoa huduma kati ya Mwanza na Nansio, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuimarisha huduma ya usafiri wa majini katika eneo hilo.
MHE. DUA W. NKURUA aliuliza:-
Kuna tatizo la usikivu wa simu za mkononi katika Kata za Napacho na
baadhi ya maeneo ya Kata ya Maratani na Kata ya Mnauje:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti na hatimaye kuweka
minara ya simu katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dua William Nkurua, Mbunge
wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-
Vijiji vyote katika Kata za Napacho, Maratani na Mnauje viliiingizwa katika
awamu ya pili na awamu ya tatu ya utekelezaji wa mradi wa mawasiliano vijijini
wa kampuni ya simu ya Vietel(Halotel). Mpaka sasa Vijiji vya Kazamoyo na
Nakopi Kata ya Napacho na Kijiji cha Mchangani Kata ya Maratani
vimekwishapatiwa huduma ya mawasiliano kupitia kampuni ya Vietel(Halotel).
Aidha, vijiji vilivyobaki vitafikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa
mradi awamu ya tatu ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2017.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Serikali ilipanga kujenga na kupanua Uwanja wa Ndege wa
Sumbawanga Mjini.
Je, ni lini ujenzi huo utakamilika pamoja na kuwalipa fidia wananchi
wanaozunguka uwanja huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata,
Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kujenga Kiwanja cha Ndege
cha Sumbawanga kwa kiwango cha lami pamoja na jengo jipya la abiria
(Terminal Building). Kiwanja hiki ni miongoni mwa viwanja vinne ambavyo
vitajengwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Rasilimali ya Ulaya (European
Investment Bank). Viwanja vingine vitakavyojengwa kwa mkopo kutoka
European Investment Bank katika kundi hili ni Viwanja vya Shinyanga, Kigoma na
Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi
zilitangazwa mwezi Agosti, 2016 na kufunguliwa mwezi Oktoba, 2016 ambapo
Mkataba na Mkandarasi wa kujenga kiwanja hiki utasainiwa baada ya kupata
idhini (no objection) kuhusu taarifa ya uchambuzi wa zabuni ambayo watu wa
EIB (European Investiment Bank) tunatarajia kuipata. Aidha, napenda
kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa zoezi la uhakiki wa mali za wananchi
ambao wataathirika na mradi huo lipo katika hatua za mwisho.
MHE. KHATIB SAID HAJI (K.n.y. MHE. MUSSA BAKARI MBAROUK) aliuliza:-
Kwa muda mrefu hakuna usafiri wa uhakika kati ya Pemba na Tanga hali inayopelekea vyombo vya usafiri vya kienyeji kupata ajali mara kwa mara na kupoteza maisha ya watu na mali zao:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kununua meli ya kisasa na ya uhakika ili kuokoa wasafiri wa Tanga – Pemba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa kuanzia tarehe 29 Januari, 2017 Kampuni ya Azam Marine imeanza kutoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kati ya Pemba na Tanga kwa kutumia meli ya Sealink 2 yenye uwezo wa kubeba abiria 1,650 na mizigo tani 717.
Mheshimiwa Spika, tarehe 31Januari 2017 Meli ya Sealink 2 ilizindua safari ya kutoka Tanga saa 3.00 asubuhi kwenda Mkoani Pemba hadi Unguja. Sealink 2 itafanya safari zake mara moja kwa wiki baina ya Pemba na Tanga hadi pale idadi ya abiria na mizigo itakapolazimu kuongeza safari nyingine.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu inapenda kutumia fursa hii kuipongeza kampuni ya Azam Marine kwa kuitikia wito wa kuanzisha huduma ya usafiri majini baina ya Tanga, unguja na Pemba na kuendelea kutoa wito kwa wawekezaji wengine kuleta vyombo vya usafiri majini vya kisasa ili kuongeza huduma ya usafiri katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto hiyo.
Mheshimiwa Spika, pia tunaomba wananchi wanaosafiri kati ya Pemba na Tanga kutumia huduma za meli salama na kuachana na vyombo visivyo salama vinavyohatarisha maisha na mali zao. Aidha, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Tanga na Pemba kuendelea kuhamasisha wananchi kuachana na vyombo visivyo salama ili kulinda maisha na mali zao.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:- Uwanja wa ndege wa Moshi ni muhimu sana kwa kukuza masuala ya utalii kwani unatumiwa na watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro lakini uwanja huo unahitaji kufanyiwa ukarabati ili uweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa. Je, ni lini Serikali itaufanyia ukarabati uwanja huo ili uweze kufanya kazi yake kwa ufanisi hasa kuendeleza sekta ya utalii na uchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuhusu umuhimu wa kiwanja cha ndege cha Moshi kwa sekta ya usafiri wa anga na mchango wake katika uendelezaji wa sekta ya utalii na uchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na nchi kwa ujumla. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu huo wa kiwanja cha ndege cha Moshi, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia. Kazi hii ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inahusisha pia viwanja vya ndege vya Iringa, Njombe, Songea, Lindi, Kilwa Masoko, Tanga, Lake Manyara, Singida, Musoma na kiwanja kipya katika Mkoa wa Simiyu na inatarajiwa kukamilika ifikapo Machi, 2017. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ifikapo Machi, 2017 Serikali itaendelea na hatua inayofuata ya kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati wa kiwanja hicho. Aidha, mamlaka ya viwanja vya ndege imekuwa ikifanya matengenezo ya miundombinu ya kiwanja mara kwa mara ili kiweze kutoa huduma katika kipindi chote cha mwaka. Vilevile katika mwaka 2016/2017, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imetenga shilingi milioni 350 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya kiungio na maegesho ya ndege.
MHE. DANIEL E. MTUKA (K.n.y. OMARY A. BADWEL) aliuliza:- Rais wa Awamu ya Nne aliahidi barabara ya kijiji cha Nondwa - Sanza, Wilaya ya Bahi itachukuliwa na TANROADS Mkoa wa Dodoma, hata hivyo ahadi ya Mheshimiwa Rais haijatejelezwa mpaka sasa. Kwa kuwa kipande hicho kinahusisha TANROADS Dodoma na Singida. Je, Serikali ipo tayari kuiagiza TANROADS Dodoma na TANROADS Singida kukiingiza kipande hicho cha barabara katika mpango wa matengenezo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Badwel, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Chidilo - Zegere hadi Nondwa yenye urefu wa kilometa 31 ni barabara ya Wilaya inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Barabara hii inaungana na barabara ya Mkoa ya Igongo, ambapo ni mpakani mwa Dodoma na Singida kuelekea Chipanga - Chidilo hadi Bihawana Junction, yenye urefu wa kilometa 69 ambayo mwaka 2010 ilipandishwa hadhi kutoka barabara ya Wilaya na kuwa barabara ya Mkoa. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kuwa hadi sasa maombi ya kupandisha hadhi barabara ya Chidilo - Zegere hadi Nondwa hayajawasilishwa rasmi Wizarani kwangu. Ili Wizara yangu iweze kuyafanyia kazi maombi ya kuipandisha hadhi barabara hii kuwa barabara ya Mkoa, ninamshauri Mheshimiwa Mbunge afuate utaratibu uliobainishwa kwenye Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009 kwa kupitisha maombi hayo kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa.
MHE. LUCY F. OWENYA aliuliza:-
Barabara ya Old Moshi - Kiboriloni - Kikarara - Tsuduni - Kidia yenye urefu wa kilometa10.8 ni muhimu kwa uchumi wa wakazi wa Kata ya Old Moshi Mashariki na Taifa kwa ujumla hasa ikizingatiwa kuwa ni njia mojawapo ya kupanda Mlima Kilimanjaro.
Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kuzingatia ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Old Moshi hadi Kidia yenye urefu wa kilometa 10.8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Old Moshi - Kiboriloni - Kikarara - Tsuduni hadi Kidia ni barabara ya Wilaya inayohudumiwa na Halmashauri ya Moshi. Hata hivyo, ujenzi kwa kiwango cha lami utatekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kwa sasa kazi ya usanifu wa kina wa barabara hii upo katika hatua za mwisho kwa kuwa Mhandisi Mshauri tayari alishawasilisha rasimu ya usanifu ambayo tayari imepitiwa na TANROADS. Kwa sasa Mhandisi Mshauri anafanyia marekebisho ya rasimu ya usanifu ili kuzingatia maoni yaliyotolewa na TANROADS. Hatua itakayofuata baada ya kukamilika kwa marekebisho hayo ni kutangaza zabuni ili kumpata mkandarasi atakayetekeleza kazi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga jumla ya Shilingi milioni 2,583 ili kuanza ujenzi. Aidha, matengenezo mbalimbali ya barabara hii yanafanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete ya ujenzi wa daraja la Kamsamba–Kilyamatundu bado haijatekelezwa tangu mwaka 2009.
Je, ni upi mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano kukamilisha ujenzi wa daraja hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Momba lililopangwa kujengwa katika barabara ya Mkoa ya Kibaoni - Muze - Ilemba - Kilyamatundu na barabara ya Mkoa ya Kamsamba hadi Mlowo ni kiunganishi muhimu cha Mkoa wa Rukwa katika eneo la Kilyamatundu na Mkoa wa Songwe katika eneo la Kamsamba. Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kuimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi katika Bonde la Ziwa Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azma hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano imepanga kuanza ujenzi wa daraja hilo katika mwaka huu wa fedha 2016/2017. Zabuni za ujenzi wa daraja la Momba ziliitishwa tarehe 11 Januari, 2017 kwa ajili ya kumpata Mkandarasi. Mara baada ya hatua hii ya zabuni na tathmini kukamilika, mkataba kwa ajili ya kuanza ujenzi utasainiwa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017 kiasi cha shilingi bilioni 2.935 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea Jimbo la Mtera katika kijiji cha Mvumi Misheni aliahidi kutujengea barabara ya lami kutoka Mlowa barabarani hadi Mvumi Misheni kwenye Hospital Teule ya Wilaya ya Chamwino. Pia Rais wa Awamu ya Tano katika kampeni zake alipofika Mvumi Misheni alisisitiza kuwa barabara hiyo itajengwa haraka iwezekanavyo.
Je, ujenzi huo utaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimwa Livingstone Joseph Lusinde, Mbunge wa Mtera kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea Jimbo la Mtera katika Kijiji cha Mvumi Misheni aliahidi kujenga barabara ya lami kutoka Mlowa barabarani hadi Mvumi Misheni kwenye Hospitali Teule ya Wilaya ya Chamwino. Aidha, ni kweli kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Rais wa Awamu ya Tano naye aliahidi kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumfahamisha Mheshimwa Mbunge kuwa Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii kwa jamii na hususan katika kusaidia wagonjwa wanaoenda kupata huduma ya matibabu katika hospitali ya Mvumi Misheni. Kwa kuzingatia umuhimu huo, azma ya Serikali ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami iko pale pale na itatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, kwa sasa barabara hiyo itaendelea kuhudumiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa kufanya matengenezo ya aina mbalimbali kwa kiwango cha changarawe kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:-
Kwa muda wa miaka tisa sasa baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kakonko nyumba zao zimewekwa ‘X’ kwa lengo la kuvunjwa ili kupisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami:-
(a) Je, ni wananchi wangapi kati ya hao wenye alama ya ‘X’ kwenye nyumba zao wanakidhi vigezo vya kulipwa na sababu ni zipi kwa wasiolipwa?
(b) Je, ni kiasi gani cha fedha kitatumika kulipa fidia nyumba hizo?
(c) Je, fidia hiyo itazingatia gharama ya nyumba kwa sasa au gharama ya zamani ya nyumba zilizowekwa ‘X’ na ni lini watalipwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, eneo la Kakonko ni mojawapo ya maeneo yanayopitiwa na barabara kuu inayopitia Tunduma – Sumbawanga – Mpanda – Kanyani – Kasulu – Kibondo – Kakonko hadi Nyakanazi. Alama za ‘X’ ziliwekwa ili kubainisha wananchi waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara ambayo ina upana wa mita 30 kutoka katikati ya barabara kila upande.
Mheshimiwa Spika, hakuna mwananchi anayekidhi vigezo vya kulipwa nyumba iliyowekwa ‘X’ kwani nyumba hizo ziko ndani ya hifadhi ya barabara yaani ndani ya mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya mwaka 1967 na nyongeza ya hifadhi ya
barabara ya mita 15 yaani mita 7.5 kila upande kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hakuna nyumba iliyofuatwa na barabara, hakuna fedha ya fidia kwa ajili ya nyumba hizo. Aidha, kuna mashamba 99 ambayo yamo ndani ya hifadhi ya barabara iliyoongezwa ya mita 7.5 ambayo yatalipwa fidia kulingana na sheria zilizopo.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Barabara ya kutoka Tarime kwenda Serengeti ni barabara muhimu sana kwa wakazi wa Wilaya hizo na kwa maisha yao ya kila siku:-
Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Tarime – Serengeti ni barabara inayojulikana kwa jina la Tarime – Nyamwaga - Mugumu yenye urefu wa kilometa 87.14 ambayo inaunganisha Wilaya za Tarime na Serengeti.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Tarime – Nyamwaga – Mugumu (Serengeti) ni barabara inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara. Kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii, Wizara kupitia TANROADS imekuwa ikijenga kwa kiwango cha lami kwa awamu kutokea Tarime Mjini hadi Kibumayi ambapo kilometa saba zimekamilika. Vilevile, katika mteremko wa Nyamwaga kuelekea mgodi wa Nyamongo kilometa 0.6 zimekamilika.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2016/2017, ujenzi wa kilometa 2.2 unaendelea katika maeneo ya Kibumayi na mteremko wa Nyamwaga. Aidha, ujenzi wa daraja la Mto Mara lenye urefu wa mita 94 na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara unganishi ya kilometa 1.8 unakaribia kuanza kwa sababu mkandarasi amekwishapatikana na yupo katika maandalizi ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi huo unaoendelea, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara yote yenye urefu wa kilometa 87.14 unaendelea na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2018. Hivyo, ujenzi wa barabara hii yote kwa kiwango cha lami unatarajiwa kuanza pindi kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina zitakapokamilika.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB Aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko makubwa kwa wafanyabiashara wa Zanzibar wanaotumia Bandari ya Dar hulipishwa fedha nyingi na mizigo kupimwa kwa CBM tofauti na ilivyokuwa kabla; huku baadhi ya wafanyabiashara wengine wanachajiwa kwa tani ambapo ni nafuu kutokana
na hali halisi ya mizigo yenyewe. (a) Je, ni sawa kwa vyakula (local goods) kama vile viazi mbatata, dagaa, mahindi, dawa zinazopelekwa hospitalini, vitunguu kuchajiwa kwa CBM; na je, ni kweli kunasaidia wafanyabiashara au kuwakandamiza kiuchumi hasa ikizingatiwa kuwa bidhaa zenyewe ni vyakula?
(b) Je, nia ya Serikali ni kuwakwamua wananchi kiuchumi au kuwakandamiza hasa ikizingatiwa kuwa baadhi yao ni wafanyabiashara wadogo wadogo?
(c) Je, ni sababu gani za msingi kwa bandari hiyo kuchukua fedha wakati huduma nyingine hawazipati kwa miaka yote?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Tozo zote bandarini huzingatia uzito yaani tonnage au ujazo wa shehena (CBM) kwa mujibu wa kitabu cha Tozo cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA). Viwango vya tozo vilivyopo vimelenga katika kuwasaidia wafanyabiashara kupata huduma bora na pia kuhakikisha kuwa bandari inajiendesha na gharama za uendeshaji zinarudishwa (cost recovery). Aidha, hufanyika mashauriano ya wadau kabla ya viwango vilivyopo kuridhiwa.
(b) Serikali siku zote imekuwa na nia njema ya kuwakwamua wananchi kiuchumi kwa kuweka mazingira mazuri kwa wananchi kufanya biashara kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utoaji huduma za bandari. Aidha, Serikali kupitia mamlaka ya usimamizi wa bandari imenunua vifaa vya ukaguzi wa mizigo, vifaa vya kuhudumia shehena na kuboresha maeneo ya kupumzikia abiria. Serikali itaendelea kuboresha huduma za bandari na kuangalia tozo ambazo ni stahiki kwa wadau wa bandari.
(c) Sababu za msingi kwa TPA kutoza tozo kisheria ni kurejesha gharama za utoaji wa huduma za bandari ili kufanya huduma hizo kuwa endelevu na kuendelea kuwekeza katika mifumo ya usimamizi ambayo itaongeza ufanisi na hatimaye kupunguza gharama za utoaji wa huduma za bandari.
MHE. MUSSA R. SIMA Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uwanja wa ndege katika eneo lililotengwa katika Kijiji cha Manga kwa msaada wa Benki ya Dunia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipata mkopo kutoka Benki ya Dunia ambapo sehemu ya mkopo huo imetumika kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa viwanja 11 vya ndege vya Iringa, Njombe, Songea, Lindi, Kilwa Msoko, Tanga, Moshi, Lake Manyara, Musoma, kiwanja kipya katika Mkoa wa Simiyu na Singida kwa ajili ya ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja hivyo kwa kiwango cha lami.
Ninapenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kiwanja cha Singida unafanyika katika eneo la kiwanja cha sasa na si katika eneo jipya la Manga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafutaji wa fedha za kazi za ukarabati, upanuzi na ujenzi kutoka vyanzo mbalimbali utaanza baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao kwa sasa upo katika hatua za mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kazi hii ya usanifu ikiendelea, Wizara yangu ilipata maombi ya Mkoa wa Singida ya kutaka wataalam kwenda kufanya tathmini ya awali ya eneo jipya linalopendekezwa katika eneo la Uhamaka karibu na kijiji cha Manga kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo la Uhamaka limependekezwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha Mkoa wa Singida katika mpango kabambe wa uendelezaji wa Manispaa ya Singida kwa mwaka 2015 – 2035. Tathmini ya awali iliyofanywa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mnamo Februari, 2016 kuhusu eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2400 (kilometa sita kwa kilometa nne) imeonesha kuwa eneo pendekezwa linafaa kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia matokeo ya tathmini, hatua zitakazofuata ni utwaaji rasmi wa eneo hilo unaohusisha ulipaji fidia ya mali za wananchi waliomo ndani upimaji wa eneo kwa ajili ya hatimiliki, usanifu wa miundombinu ya kiwanja, utafutaji wa fedha za ujenzi wa kiwanja na hatimaye ujenzi wenyewe.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI aliuliza:-
Nyumba nyingi katika barabara kuu ya Zambia Jijini Mbeya kuanzia maeneo ya Uyole mpaka Lwambi ziliwekwa alama ya “X” kuashiria kuvunjwa ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo muhimu na wapo wananchi waliowekewa alama nyekundu walivunja nyumba zao wenyewe na
wananchi waliowekewa alama ya “X” za kijani bado wanasubiri fidia.
(a) Je, mradi huo umefikia wapi na ni lini upanuzi huo utaanza?
(b) Je, upanuzi huo umezingatia ushauri wangu wa kuweka njia nne (four lines) toka Uyole mpaka Songwe Airport ili kuondoa kabisa tatizo la foleni ambalo linakua siku hadi siku Jijini Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Osmund Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekaji wa alama za ‘X’ katika majengo yaliyopo ndani ya hifadhi ya barabara kuu ya TANZAM Jijini Mbeya pamoja na maeneo mengine mengi nchini ni utekelezaji wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 na kanuni zake za mwaka 2013. Kutokana na sheria hiyo, mapendekezo yote yaliyopo ndani ya mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kwenda kila upande yanapaswa kuondolewa bila fidia, hivyo wamiliki wote wa mali zilizokuwepo ndani ya eneo hilo waliwekewa alama za ‘X’ nyekundu na kupewa notice za kubomoa nyumba zao bila fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wote waliokuwa na maendelezo kati ya mita 22.5 na mita 30 kutoka katikati ya barabara kila upande wa barabara, kabla Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 haijaanza kutumika waliwekewa alama za ‘X’ za kijani na kupewa notice za kutofanya
maendelezo mapya kwa kuwa maendelezo yaliyopo yatalipwa fidia wakati eneo hilo litakapohitajika kwa ajili ya upanuzi wa barabara ili kujiweka tayari na kuzuia ucheleweshaji wa kuanza kazi za ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upanuzi wa barabara ya kutoka Mbeya kwenda Zambia hususan kuanzia Uyole kwenda Songwe utaanza pale upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utakapokamilika na kuonesha viwango vya upanuzi vinavyohitajika na Serikali tutakapopata fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inakusudia kujenga barabara ya mchepuo wa Mbeya (Mbeya Bypass) yenye urefu wa kilometa 40 inayoanzia Uyole hadi Songwe ambapo mradi huu upo kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na unatekelezwa chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua sahihi ya kuondoa msongamano na magari kwenye Jiji la Mbeya itatokana na mapendekezo yatakayotolewa baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unaoendelea.
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-
Ujenzi wa barabara ya Kilindoni - Utende (Airport Access Road) yenye urefu wa kilometa 14 umekamilika, lakini mkandarasi CHICO ameijenga barabara hiyo chini ya viwango kwani ina viraka vingi.
Je, ni lini Serikali itaitaka kampuni hiyo kufanya marekebisho makubwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, barabara ya Kilindoni – Utende ni barabara inayounganisha kiwanja cha ndege cha Mafia na sehemu muhimu za kiuchumi, yakiwemo maeneo ya kitalii ya Fukwe za Utende na Gati la Kilindoni.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kilindoni – Utende yenye urefu wa kilometa 14 ilijengwa kwa kiwango cha lami na Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Limited (CHICO) na kukamilika tarehe 1 Januari, 2015 na kufuatiwa na kipindi cha uangalizi cha mwaka mmoja hadi tarehe 1 Januari, 2016.
Hata hivyo, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilikataa kuipokea barabara hiyo kutokana na kasoro zilizojitokeza wakati wa kipindi cha uangalizi na iliamuliwa ufanyike uchunguzi, ili kubaini kiwango cha mapungufu ya ubora katika ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya uchunguzi yalionesha kuwa baadhi ya sehemu za barabara ya Kilindoni – Utende hazikujengwa katika ubora unaotakiwa, hivyo mkandarasi ameelekezwa kurudia kwa gharama zake mwenyewe maeneo yote yaliyoonekana kuwa na mapungufu kulingana na matakwa ya mkataba; kazi hiyo itaanza mara baada ya kipindi cha mvua kumalizika.
Aidha, uangalizi wa karibu wa maeneo mengine unaendelea kufanywa na TANROADS ili kuhakikisha kuwa barabara hiyo inakabidhiwa Serikalini ikiwa na viwango vya ubora vinavyokubalika kimkataba.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) walipewa kandarasi ya kujenga Ofisi na Makazi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe lakini ujenzi huo umesimama.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza tena ujenzi huo na kuukamilisha kupitia TBA?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilitenga fedha kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa nyumba 149 za viongozi katika maeneo mapya ya utawala katika mikoa 20 ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, mradi ulihusisha ujenzi wa nyumba za Wakuu wa Mikoa nne, Wakuu wa Wilaya 21, Makatibu Tawala wa Mikoa nyumba nne, Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa nyumba 40, Makatibu Tawala wa Wilaya nyumba 38 na Maafisa Waandamizi nyumba 42.
Mheshimiwa Spika, mkataba wa ujenzi wa nyumba 149 za TAMISEMI ulitiwa saini tarehe 3 Mei, 2014 kati ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa gharama ya shilingi 17,988,016,924.56. Hadi mradi unasimama kiasi cha shilingi 4,169,477,121.62 sawa na asilimia 23.2 kilikuwa kimetolewa kwa ajili ya ujenzi kwa gharama hizo. Kiasi hicho cha fedha kiliwezesha kuanza ujenzi wa nyumba 84 kati ya nyumba 149 za miradi. Katika Wilaya ya Mbogwe mradi ulihusisha ujenzi wa nyumba nne, zikiwemo nyumba moja ya Mkuu wa Wilaya, nyumba moja ya Katibu Tawala na nyumba mbili za Maafisa Waandamizi kwa gharama ya jumla ya shilingi 500,585,277.70.
Ujenzi wa nyumba hizi kama zilivyo nyumba nyingine chini ya mradi huu umesimama kutokana na ukosefu wa fedha. Mradi huu umepangwa kuendelea kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. MOSHI S. KAKOSO Aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga Barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mpanda hadi Uvinza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mpanda hadi Uvinza yenye urefu wa kilometa 194. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mpanda – Uvinza – Kanyani yenye urefu wa kilometa 256. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania imesaini mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami mwezi Julai, 2016 kwa sehemu ya Mpanda hadi Usimbili (Vikonge) yenye urefu wa kilometa 35 na Mkandarasi, Kampuni ya China Railway Seventh Group kutoka China ameanza kazi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha za kuendelea na ujenzi wa sehemu iliyobaki ya kutoka Usimbili hadi Uvinza yenye urefu wa kilometa 159.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. SILAFU J. MAUFI) Aliuliza:- Rukwa ni miongoni mwa Mikoa inayozalisha mazao ya chakula hasa mahindi na mpunga kwa wingi na hivyo kusaidia upatikanaji wa chakula kwa Taifa. Maeneo mengi ya kilimo katika mkoa huo ikiwemo Bonde la Rukwa yanakabiliwa na changamoto ya barabara mbovu na hivyo wakulima kushindwa kusafirisha mazao yao kwa wakati:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za Kibaoni (Katavi) – Muze (Rukwa) – Kilyamatundu – Kamsamba (Songwe) hadi Mlowo, Sumbawanga – Muze, Kalambazite – Chambe (Ilemba) na Miangalua – Kilyamatundu (Kipeta) kwa kiwango cha lami ili wakulima wasafirishe mazao yao kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge Viti Maalum wa Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibaoni – Kasansa – Kilyamatundu – Kamsamba hadi Mlowo ni miongoni mwa barabara zinazounganisha Mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe. Barabara hii ni muhimu katika uchumi wa nchi kwa kuwa inapita katika Bonde la Ziwa Rukwa ambalo ni maarufu sana kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Aidha, barabara za Ntendo hadi Muze, Kalambazite hadi Ilemba na Miangalua hadi Chombe hadi Kipeta ni muhimu katika usafirishaji wa mazao ya kilimo katika Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutambua umuhimu wa barabara hizi imeanza kuchukua hatua za dhati za kuhakikisha kuwa barabara hizi zinapitika katika majira yote ya mwaka. Katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017, Serikali ilitenga jumla ya Sh.3,989,030,000 kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya aina mbalimbali ya barabara hizo pamoja na madaraja yake.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imedhamiria kuanza ujenzi wa Daraja la Momba ambalo linaunganisha barabara ya Sitalike – Kibaoni – Muze – Ilemba hadi Kilyamatundu na Kamsamba hadi Mlowo ambayo ni kiungo muhimu kwa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe. Daraja hili limetengewa jumla ya Sh. 2,935,000,000 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 na limeombewa Sh. 3,000,000,000 katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe kuwa Serikali inatambua umuhimu wa barabara hizi kiuchumi na kijamii na inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hizo ili hatimaye zijengwe kwa kiwango cha lami.
MHE. SUBIRA K. MGALU Aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi wa barabara ya kutoka Kisarawe - Mwanerumango kilometa 64 itajengwa kwa lami na kukamilika kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kisarawe - Mpuyani - Maneromango yenye urefu wa kilometa 54 ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Pugu - Kisarawe - Maneromango - Vikumburu ambayo jumla yake ni kilometa 97.7 inayohudumiwa na Wakala ya Barabara wa Mkoa wa Pwani. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii umekamilika. Aidha, mpaka sasa kilometa 7.67 zimeshajengwa kwa kiwango cha lami. Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa kipande kingine cha mita 800.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu iliyobaki ya barabara hii ni ya changarawe na hufanyiwa matengenezo ya kawaida na ya muda maalum kila mwaka ili ipitike muda wote. Ujenzi kwa kiwango cha lami utaendelea hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 3,157 zimependekezwa kwa ajili ya kuendelea kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hii.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA (K.n.y. MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI) Aliuliza:-
Kumekuwa na ahadi ya kujenga upya Gati la Nyamikoma – Busega ili kuboresha usafirishaji wa mizigo na mazao ya samaki katika Ziwa Victoria:-
Je, ni lini utengenezaji huo utaanza na kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Gati la Nyamikoma utaanza mara tu baada ya ramani zitakazotoa taarifa za kijiografia (Geographical Information System - GIS) kwa bandari na magati katika mwambao wote wa Maziwa Makuu kukamilika na kuthibitika kuwa eneo hilo la Nyamikoma linafaa kujengwa gati. Ramani hizo zinatarajiwa kukamilika Oktoba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wataalam wanaoendelea na ukusanyaji wa taarifa za kijiografia.
MHE. HASSAN E. MASALA Aliuliza:-
Barabara ya Nanganga – Nachingwea – Masasi imeshafanyiwa upembuzi yakinifu toka mwaka wa 2015/2016.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MWASILIANO
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ilikamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Nanganga. Aidha, katika mwaka wa 2017/2018 Wizara imeomba kutengewa shilingi bilioni 3.515 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami baraba Mnanila – Manyovu – Kasulu ili kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilometa 48.7 ni barabara ya kiwango cha changarawe na inahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kasulu hadi Manyovu ni sehemu ya mradi wa kikanda wa Barabara ya Kibondo - Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilometa 250 inayofanyiwa mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kupitia mpango wa NEPAD yaani New Partnership for Africa’s Development kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika chini ya uratibu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii unatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA Aliuliza:-
Majanga ni mambo yasiyotarajiwa ila huwa yanatokea tu, majanga kama ajali za baharini, ziwani, barabarani, matetemeko, vimbunga, majanga ya njaa na kadhalika yamekuwa yakitokea:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha na kuimarisha nyenzo na ujuzi kwa Kikosi cha Uokoaji wa Majini kinachojulikana kama Coast Guard kwa ajili ya uokoaji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina utaratibu wa namna ya kushughulikia masuala ya utafutaji na uokoaji majini. Kituo maalum kijulikanacho kama Dar es Salaam Maritime Rescue Coordination Center (MRCC) kimeanzishwa na kimekuwa kikitoa huduma kwa saa 24 kila siku. Kituo hiki kinasimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA). Aidha, kwa kuzingatia ukubwa wa shughuli za usafiri, uvuvi na nyinginezo katika maziwa, kituo kidogo cha Uratibu wa Utafutaji na Uokoaji (MRCC) kimeanzishwa Jijini Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuimarisha utaratibu wa utafutaji na uokoaji, Wizara yangu imeandaa rasimu ya sheria ya utafutaji na uokoaji (search and rescue) inayozingatia miongozo ya Kimataifa ya Utafutaji na Uokoaji (International Air and Maritime Search and Rescue Guidelines) na wadau mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu rasimu hiyo na sasa kazi ya kurekebisha rasimu ya sheria hiyo ili kuzingatia maoni ya wataalam mbalimbali inaendelea ili kuruhusu hatua zaidi za kupitisha sheria hiyo kuendelea.
MHE. GODFREY W. MGIMWA Aliuliza:-
Tatizo la mawasiliano ya simu katika Jimbo la Kalenga bado ni kubwa:-
Je, ni lini Serikali itapeleka minara ya simu kwenye vijiji vya Kaning’ombe, Ikungwe, Lyamgungwe, Igunda na Ikuvilo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote iliainisha maeneo mbalimbali katika Jimbo la Kalenga na kuyaingiza katika miradi mbalimbali ya utekelezaji. Vijiji vya Igunda na Lyamgungwe kutoka katika Kata ya Lyamgungwe vimo katika utekelezaji wa mradi wa Viettel. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 2017. Aidha, Vijiji vya Ikungwe na Kaning’ombe vimeingizwa katika orodha ya miradi inayosubiri fedha ili kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Serikali imesema ina mkakati wa kujenga viwanda katika Mkoa wa Mtwara, lakini njia ya usafirishaji wa mizigo inayotumika ni barabara tu hali inayosababisha barabara hiyo kuwa na uwezekano wa kuharibika kwa haraka:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha meli ya mizigo itakayotoka Dar es Salaam kwenda Mtwara ili kuinusuru barabara hiyo isiharibike?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa uwepo wa huduma mbadala za meli za mizigo na abiria kati ya Dar es Salaam na Mtwara na maeneo mengine ya mwambao ni jambo muhimu kwa maendeleo na kuzifanya barabara zidumu kwa muda mrefu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa mahitaji ya huduma za usafiri wa majini katika mwambao wa bahari yetu ni fursa kwa sekta binafsi nchini. Serikali kwa upande wake inaendelea kujenga mazingira wezeshi na kuhamasisha sekta binafsi kutumia fursa hii kutoa huduma za usafiri wa majini katika mwambao kwa kutumia meli za kisasa. Hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuchochea sekta binafsi nchini kufanya uwekezaji katika huduma hii. Moja ya hatua hizo ni kuzuia meli za kigeni kujiingiza katika usafirishaji wa shehena katika maeneo ya mwambao yaani cabbotage restriction ambapo lengo la zuio hili ni kuwalinda wawekezaji wa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuendelea kutoa wito kwa wawekezaji kuwekeza katika vyombo vya kisasa vya usafiri wa majini ili kutoa huduma ya usafiri katika maeneo ya mwambao wa Tanzania ikiwemo Mtwara.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Je, ni lini Kampuni ya Simu iliyofunga mnara wake katika kijiji cha Kwamatuku itauwasha ili wananchi wapate huduma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote uliikabidhi Kampuni ya Simu ya MIC (Tigo) kazi ya kujenga mnara katika kata ya Kwamutuku yenye vijiji vya Komsala, Kwamatuku, Kweingoma na Nkale. Ujenzi huo ulikamilika mwishoni mwa mwaka 2015 na kuanza kutoa huduma katika kata hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa za Kampuni ya Simu ya Tigo, mnara huu wa Kwamatuku uliwashwa na upo hewani ukitoa huduma za mawasiliano tangu tarehe 4 Desemba, 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tumetuma wataalamu wetu waende na vifaa vya kupima mawasiliano ili kuhakikisha kwamba taarifa hii ya Tigo iko sahihi.
MHE. DOTO M. BITEKO aliuliza:-
Wakati wa Kampeni za Mwaka 2015, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania aliahidi kilometa tano kwenye Mji wa Ushirombo:-
Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko, Mbunge wa Bukombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za Mji wa Ushirombo zinahudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imekusanya ahadi zote za viongozi na kuweka utaratibu wa jinsi ya kuzitekeleza, ikiwemo ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa tano zilizoahidiwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2015, Mjini Ushirombo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msimamo wa Serikali ya Awamu hii ya Tano ni kuhakikisha kuwa inatekeleza ahadi zake zote katika kipindi cha miaka mitano.
MHE. DAVID E. SILINDE (K.n.y. MHE. CECIL D. MWAMBE) aliuliza:-
Barabara ya Masasi – Nachingwea imekuwa na matatizo kwa muda mrefu ya kupitika kwa shida:-
Je, barabara hiyo itajengwa lini kwa kiwango cha
lami ili kufanya wananchi wa Jimbo la Ndanda waondoe imani kuwa wametengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 91 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, mradi huu umeombewa fedha za jumla ya sh. 3,515,394,000/= kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya barabara ya Masasi – Nachingwea yenye urefu wa kilometa 45 imekuwa ikifanyiwa matengenezo ya kawaida na matengenezo ya muda maalum kila mwaka na inapitika vizuri katika kipindi cha mwaka mzima. Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hiyo ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka wakati barabara hii inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Barabara ya kutoka Mgakorongo, Kigarama mpaka Murongo iliwekwa kwenye ilani kuwa itajengwa kwa kiwango cha lami na wananchi waliokuwa ndani ya mradi waliowekewa alama ya ‘X’ wanashindwa kuendeleza maeneo yao wakisubiri fidia zaidi ya miaka mitano sasa:-
(a) Je, ni lini wananchi hawa watapewa fidia ili waendelee na mambo ya kimaendeleo?
(b) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba, Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Omugakorongo – Kigarama hadi Murongo ni barabara kuu inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Kagera na ina jumla ya kilometa 111. Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii ndiyo maana imeiweka kwenye mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami. Hivi sasa upembuzi yakinifu wa barabara hii umekamilika, kazi inayoendelea ni usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania inaendelea na uhakiki wa fidia ya mali zitakazoathiriwa na mradi kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Wananchi wote wanaostahili kulipwa fidia kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 watalipa fidia mara zoezi la uhakiki litakapokamilika na Wizara yangu itahakikisha kuwa taratibu zote za malipo ya fidia na sheria zinafuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kazi za ujenzi wa barabara ya Omugakorongo – Kigarama hadi Murongo zitaanza mara baada ya usanifu wa kina kukamilika na fedha za ujenzi kupatikana.
MHE. ALMAS A. MAIGE (K.n.y. MHE. MUSA R. NTIMIZI) aliuliza:-
Eneo la kilometa 89 la kipande cha Barabara ya Chaya – Nyahua katika Barabara ya Itigi – Chaya – Nyahua -Tabora bado halijaanzwa kutengenezwa:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kujenga kipande hicho kwa sababu kwa sasa hakipitiki kabisa?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kipande hicho kinapitika wakati wote wakati mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo ukiendelea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Chaya hadi Nyahua yenye urefu wa kilometa 85.4 ni sehemu ya barabara kutoka Manyoni – Itigi – Chaya – Nyahua hadi Tabora yenye urefu wa kilometa 259.7. Zabuni za kumpata Mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara hii zilitangazwa tarehe 2, Februari, 2017 na ufunguzi ulifanyika tarehe 3, Aprili, 2017. Kwa sasa tathmini ya zabuni zilizopokelewa inaendelea. Mradi huu utagharamiwa kwa fedha za mkopo nafuu kutoka Kuwait Fund.
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018, jumla ya shilingi bilioni 15.73625 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Chaya – Nyahua kilometa 85.4. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka wakati kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami zikiendelea.
MHE. BONNAH M. KALUWA aliuliza:-
Mwaka 1995 Serikali ilifanya uthamini wa wananchi wa Kata ya Kipawa ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam ambapo baadhi ya wananchi hao walilipwa fidia lakini kuna baadhi ambao mpaka sasa bado hawajalipwa fidia hiyo na hawajui ni lini watalipwa.
Je, Serikali imejipanga vipi kuwalipa wananchi hao ambao hawajalipwa ili waweze kupisha upanuzi wa uwanja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Moses Kaluwa, Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ilifanya uthamini wa mali za wananchi ili kupisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Dar es Salaam mwishoni mwa miaka ya 1990. Maeneo yaliyoainishwa kwa ajili ya upanuzi huo ni Kipawa, Kigilagila na Kipunguni. Kutokana na gharama za fidia na uhaba wa fedha, Serikali imekuwa ikilipa fidia kwa wakazi hao kwa awamu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza ililipwa mwaka 2009/2010 kwa wakazi wapatao 1,500 wa eneo la Kipawa ambao walilipwa fidia zilizofikia shilingi bilioni 18 na zoezi hili lilikamilika Januari, 2010. Katika mwaka wa fedha 2010/2011, Serikali ililipa shilingi bilioni 12 za fidia kwa wakazi 864 wa eneo la Kigilagila na malipo yalikamilika Januari, 2011. Mwaka 2013/2014 Serikali ililipa shilingi bilioni 1.2 ikiwa ni fidia kwa wakazi 59 kati ya wakazi 801 wa eneo la Kipunguni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa ni wakazi 742 wa Kipunguni ndio ambao hawajalipwa fidia zao zenye thamani ya takriban shilingi bilioni 19. Katika mwaka wa fedha 2016/ 2017, Serikali ilitenga shilingi bilioni tano kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa Kipunguni. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi bilioni 30 ili kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi hao.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJABU aliuliza:-
Reli ya Tanga inategemewa sana kiuchumi kwa usafirishaji wa abiria na mizigo. Aidha, ni kiunganishi hadi Bandari ya Tanga:-
Je, ni lini Serikali itaboresha na kuijenga kisasa kwa kiwango cha Standard Gauge ili iongeze uchumi na kuleta maendeleo?
NAIBU WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa reli ya Tanga katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini Tanzania. Mpango wa Serikali uliopo ni kuunganisha Bandari ya Tanga na Bandari mpya ya Mwambani kwenye reli ya Standard Gauge ya Ukanda wa Kati (Central corridor) kupitia reli ya njia panda ya Ruvu hadi njia panda ya Mruazi ambayo inaunganisha reli ya kati na reli ya Tanga hadi Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usanifu wa kina (detailed engineering design) wa reli ya kutoka Tanga hadi Arusha (kilometa 438) umekamilika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kuanza ujenzi wa reli ya Tanga hadi Arusha kwa kiwango cha Kimataifa. Aidha, Mhandisi Mshauri, Kampuni ya HP Gauff ya Ujerumani inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa awali, yaani feasibility study and preliminary engineering design kati ya Arusha na Musoma pamoja na matawi ya kwenda Engaruka na Minjingu.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Kukua kwa soko huria katika utoaji wa huduma za anga nchini kumevutia na hivyo kuimarisha Sekta ya Usafirishaji wa abiria na mizigo. Baadhi ya Mashirika ya Ndege yamekuwa yakitoza nauli kubwa na hivyo kuongeza mzigo kwa watumiaji:-
Je, Serikali inatoa kauli gani dhidi ya ongezeko la nauli lisiloendana na uhalisia inayotozwa na baadhi ya Mashirika ya Ndege?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na sekta nyingine, nauli za ndege hutozwa kutegemeana na nguvu ya soko katika njia husika. Mpango uliopo ni kuongeza ushindani katika njia husika ili kupunguza nauli. Wizara yangu kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga imeendelea kutoa leseni kwa watoa huduma za usafiri wa anga ili kuleta ushindani kwa kutoa huduma zilizo bora na kutoza nauli ambazo abiria wanazimudu. Aidha, mamlaka huingilia kati kisheria kuweka kiwango kikomo pale tu inapoonekana kuna ukiritimba na wananchi wanaumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunakubaliana kuwa nauli kwa baadhi ya njia zilikuwa juu kutokana na kuwa na mtoa huduma mmoja. Baada ya Kampuni ya Ndege ATCL kuanza kutoa huduma katika njia hizo, nauli za ndege zimeshuka kutokana na ushindani. Kwa mujibu wa Ibara ya 25 ya Sheria ya Usafiri wa Anga (Civil Aviation Act, Revised Edition of 2006), Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) itaendelea kufuatilia kuchukua hatua pale inapobainika kuwa hakuna ushindani wa kutosha na wananchi wanatozwa nauli kubwa.
MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. MAHMOUD H. MGIMWA) aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa Waziri wa Miundombinu aliahidi kupandisha hadhi barabara ya kutoka Mtiri – Ifwagi – Mdaburo, Ihanu, Isipi –Mpangatazara – Mpalla Mlimba ambayo inaunganisha Wilaya ya Mufindi na Wilaya ya Kilombero pia Mkoa wa Iringa na Morogoro.
Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi barabara hiyo muhimu kwa uchumi wa Wilaya ya Mufindi na Taifa kwa ujumla ambayo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imeshindwa kuihudumia wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mtili – Ifwagi –Mdaburo, Ihanu, Isipi – Mpangatazara – Mlimba ni barabara ya Wilaya inayohudumiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inaifanyia kazi ahadi hiyo ya Serikali ya kuipandisha hadhi barabara hii na barabara nyingine nchini kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa kwenye Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009. Baada ya taratibu za kisheria kukamilika, Wizara yangu itamjulisha Mbunge pamoja na kutangaza barabara zilizopandishwa hadhi kwenye Gazeti la Serikali.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Barabara ya kutoka Kibaoni – Kasansa – Muze – Ilemba – Kilyamatundu – Kamsamba hadi Mlowo Mkoani Songwe inaunganisha Mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe; wananchi wa mikoa hiyo wamekuwa na maombi ya muda mrefu kutaka barabara hiyo itengenezwe kwa kiwango cha lami ili kuboresha maisha na kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla:-
Je, ni lini barabara hiyo itatengenezwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibaoni –Kasansa ambayo ni kilometa 60.57 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Katavi. Barabara ya Kasansa – Kilyamatundu ambayo ina urefu wa kilomita 178.48 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Rukwa; na barabara ya Kamsamba – Mlowo ambayo ina urefu wa kilomita 130 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni kiungo sana kati ya mikoa hii mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe kwani inapita katika Bonde la Ziwa Rukwa ambalo ni maarufu sana kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Hali ya barabara hii ni nzuri kwa wastani ila inapitika kwa shida wakati wa masika katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kufahamu umuhimu huo itaanza ujenzi wa Daraja la Momba ambalo ni kiungo muhimu katika barabara hiyo na katika mwaka wa fedha 2016/2017 ndiyo tuaanza ujenzi huo wa barabara ya Momba. Kwa sasa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) upo katika hatua za mwisho za kupata mkandarasi wa kujenga daraja hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga sh. 2,935,000,000 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kuanza ujenzi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa sh. 3,000,000,000 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Daraja la Momba kwenye barabara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kazi za kuifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hiyo uanze na hatimaye ujenzi kwa kiwango cha lami ufanyike.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Serikali iliahidi kuweka minara katika Kata ya Sindano, Mchauru, Lipumbiru na Lupaso.
Je, ni lini minara hiyo itajengwa ili kuondoa tatizo la kutokuwa na mawasiliano katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iliingia mkataba na Kampuni ya TTCL kufikisha huduma ya mawasiliano katika Kata za Lupaso na Lipumbiru kwa ruzuku ya dola za Kimarekani 94,000. Ujenzi wa mnara huo ulikamilika tangu mwezi Machi, 2015 na kuanza kutoa huduma. Hata hivyo, baada ya mnara huo kuwaka Kampuni ya TTCL inaendelea na taratibu a kubadilisha masafa kutoka teknolojia ya CDMA 800 Mhz kwa lengo la kukabiliana na changamoto iliyopo katika teknolojia hiyo ya CDMA katika kutoa huduma za ziada kwa wateja, ikiwa ni pamoja na huduma za mobile money, mobile banking, na kadhalika. Kampuni ya TTCL inaendelea kuboresha upatikanaji wa mawasiliano kwenye eneo la Lipumbiru na Lupaso na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Simu za Mkononi
ya Viettel itafikisha huduma ya mawasiliano katika kata za Sindano na Mchauru, kwa mujibu wa makubaliano baina ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Kampuni hiyo. Kwa upande wa kata ya Mchauru yenye vijiji vya Mchauru, Mhata, Mirewe na Namombwe iliingizwa katika zabubi ya mfuko ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ya mipaka iliyofunguliwa tarehe 27 Aprili, 2017 ambapo kampuni itakayopewa jukumu la kufikisha mwasiliano kwenye kata hiyo ya Mchauru itajulikana mara tu baada ya taratibu za tathmini kukamilika.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Kuna maeneo ambayo hayana kabisa mitandao ya mawasiliano huko Mpanda Vijijini hususan kata ya Katuma, Sibwesa, Mwese na maeneo ya Bujumbo, Kapanda pamoja na Wilaya ya Mlele kata ya Ilunde.
Je, ni lini Serikali itawapelekea mawasiliano wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote uliviainisha vijiji vya Kata za Katuma na Sibwesa na kuviingiza katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mawasiliano vijijini.
Kata ya Katuma imekwishafikishiwa huduma ya mawasiliano na Kampuni ya Simu ya Vodacom ambapo shughuli za ujenzi wa mnara zilikamilika mwezi Septemba kwa ruzuku ya dola za Kimarekani 236,700.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kijiji cha Sibwesa katika kata ya Sibwesa tayari kimefikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia kampuni ya simu ya Vodacom kwa rukuzu ya dola za Kimarekani 90,411 ambapo utekelezaji wa mradi ulikamilika tarehe 23 Mei, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vijiji vya Ligonesi, Lwesa katika kata ya Mwese vimeshafikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia mtandao wa Viettel (Halotel). Ujenzi wa mnara kwa ajili ya vijiji vya Nkungwi na Kabage vilivyoko katika kata ya Sibwesa uko katika hatua za mwisho kukamilika. Kata ya Ilunde yenye vijiji vya Ilunde na Isengenezya pamojana vijiji vya Kasekese vitaingizwa katika orodha ya utekelezaji wa mradi ya siku za usoni.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Barabara ya Mishamo imeombewa kibali ili ipandishwe hadhi na kuwa barabara ya Mkoa lakini hadi sasa hatujui kinachoendelea.
Je, ni lini barabara hiyo itapandishwa hadhi na kuwa chini ya TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Seleman Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishwaji hadhi wa barabara hufanywa kulingana na Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009 ambapo maombi yanatakiwa kuwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana na Wizara ya Ujenzi kupitia kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano haijapokea maombi ya kupandishwa hadhi barabara ya Mishamo. Hata hivyo, Wizara yangu itaifanyia tathmini barabara hii iwapo inakidhi vigezo vya kupandishwa daraja na kuchukua hatua stahiki kulingana na matakwa ya sheria.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Wananchi wa Mbulu Vijijini hawana mawasiliano ya simu wala minara katika Kata za Tumati, Yaeda, Ampa, Gidhim na Gorati:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka minara katika Kata hizo ili kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, iliainisha maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Mbulu likiwemo Jimbo la Mbulu Vijijini na kuyaingiza maeneo hayo katika miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa. Kijiji cha Yaeda Ampa kutoka Kata ya Yaeda Ampa kimeingizwa katika zabuni ya mradi wa kufikisha huduma ya mawasiliano kwa maeneo ya mipakani na kanda maalum. Zabuni hii ilifunguliwa tarehe 27, Aprili, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yetu kuwa Kijiji cha Yaeda Ampa kitapata kampuni ya kufikisha huduma ya mawasiliano na kuondoa kabisa tatizo la mawasiliano katika kata hiyo. Aidha, Kata za Tumati, Gidhim na Gorati zimeingizwa katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kutegemeana na upatikanaji wa fedha kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. ALLY K. MOHAMED aliuliza:-
Kutokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa alipokuwa Waziri wa Ujenzi na sasa ahadi aliyoitoa akiwa Rais wakati wa kampeni zake za uchaguzi kwamba barabara ya Kirando – Kazovu –Korongwe yenye urefu wa kilometa 35.6 ingejengwa kwa sababu Halmashauri haina uwezo wa kuijenga.
Je, ni lini Serikali itaanza kuijenga barabara hiyo ili iwasaidie wananchi wa vijiji vya Katete, Chongo, Isaba na Kazovu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Keissy Mohamed, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kirando -Kazovu - Korongwe (kilometa 35.6) inahudumiwa na Halmashauri ya Wiaya ya Nkasi na haijawahi kuhudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Hata hivyo, Serikali kupitia TANROADS Mkoa wa Rukwa ilifanya tathmini ya awali ya barabara hii ili kuweza kujua hatua za kuchukua kwa nia ya kuifungua. Katika tathmini hiyo zilionekana changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na barabara kupita kwenye milima, mabonde, mbunga, mapori na milima yenye miamba. Barabara hii inahitaji kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili iweze kujengwa kikamilifu. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha ili kukamilisha kazi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuiwezesha barabara hii kupitika, katika mwaka wa fedha katika mwaka wa fedha 2016/2017, kiasi cha shilingi 705,000,000 zimetengwa zikiwa ni fedha za maendeleo kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya kuanza kujenga kilometa 15 za mwanzo za barabara hii kwa kiwango cha changarawe. Zabuni kwa ajili ya matengenezo ilitangazwa tarehe 15/02/2017 na kufunguliwa tarehe 07/03/2017 ambapo mkataba wa kazi ya matengenezo unatarajiwa kusainiwa tarehe 18/05/2017 yaani kesho.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza:- Wakati akiwa kwenye Kampeni ya Uchaguzi wa Mwaka 2010 Wilayani Singida Vijijini, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa. Dkt. Jakaya Kikwete aliahidi kuwa Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Njuki –Ilongero – Hydom lakini ni miaka saba imepita bila utekelezaji wa ahadi hiyo; na Mji wa Ilongero ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Singida Vijijini unakua kwa kasi sana na suala la ujenzi na uboreshaji wa miundombinu yake ni suala la msingi sana kwa sasa:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo iliyotolewa kwa wananchi wa Singida Vijijini ambao wanatarajia barabara hiyo kuwa mkombozi mkubwa wa maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe ,Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Singida kutoka Njuki kuelekea Ilongero hadi Haydom yenye urefu wa kilometa 96.4 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia TANROADS. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Manyara. Serikali inaendelea kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2013/2014, Sh.2,851,585,000 zilitumika kujenga kwa kiwango cha lami, jumla ya kilometa 5.6 kuanzia Singida Mjini kuelekea Ilongero. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Sh.1,297.377 zimetumika kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa jumla ya kilomita 2.1.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika katika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga fedha kwa ajili yakuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya Njuki – Ilongero hadi Ngamu tumetenga shilingi milioni 2,043.53 na hizo utazikuta katika ukurasa wa kitabu cha bajeti wa 326 na 345, 365 na 376 Kitabu cha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Sehemu ya Ilongero kupitia Mtinko hadi Nduguti, shilingi milioni 169.76 zimetengwa, rejea ukurasa wa 345 na 376 wa kitabu cha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-
Ujenzi wa barabara kutoka Kilindoni – Mafia – Rasi Mkumbi kwa lami ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Ilani ya CCM 2015 – 2020. Je, ni lini ujenzi huo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kilindoni -Mafia hadi Rasi Mkumbi yenye urefu wa kilometa 51 ni barabara ya Mkoa na inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kuhusu ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kilindoni - Mafia hadi Rasi Mkumbi kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Serikali inaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika katika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 359.52 kwa ajili ya kuendelea na matengenezo ya aina mbalimbali ya barabara hii.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-
Eneo la Muhalala katika Wilaya ya Manyoni ni moja ya maeneo matatu yaliyoteuliwa na Serikali kujenga vituo vya ukaguzi wa mizigo katika barabara ya kati; maeneo mengine ni Vigwaza Pwani na maeneo mawili yameshajengwa kimebaki kituo cha Muhalala tu:-
(a) Je, ni lini wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa tangu mwaka 2012 watalipwa fidia?
(b) Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Ukaguzi wa Mizigo Muhalala baada ya kituo cha Vigwaza kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali imeamua kujenga vituo vya pamoja vya ukaguzi wa mizigo inayokwenda nje ya nchi katika barabara ya Ukanda wa Kati na Ukanda wa Dar es Salaam. Katika Ukanda wa Kati vituo vitajengwa Muhalala, Mkoani Singida na Nyakanazi Mkoani Kagera chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya. Aidha, katika Ukanda wa Dar-es Salaam, vituo vitajengwa Vigwaza, Mkoani Pwani, Ruaha-Mbuyuni, Mkoani Morogoro, Makambako, Mkoani Njombe na Iboya - Mpemba Mkoani Mbeya chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 5.86 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa watu watakaoathirika na ujenzi wa vituo hivyo. Tathmini ya maeneo ya watu walioathirika na ujenzi huo katika Ukanda wa Kati yaani (Muhalala - Manyoni na Nyakanazi - Kagera) imefanyika na malipo kwa waadhirika wa ujenzi wa vituo hivyo yamefanyika na kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mkataba wa ujenzi wa vituo vilivyopo Ukanda wa Kati ulisainiwa tarehe 16 Disemba, 2016 kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mkandarasi M/s IMPRESA DI CONSTRUZIONI ING E. MANTOVANI wa Italia. Mpaka sasa mkandarasi yupo katika eneo la kazi na yupo katika hatua za awali za ujenzi wa vituo hivyo. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Septemba, 2018.
MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:-
Bandari ya Tanga siku hadi siku inafanya kazi chini ya kiwango:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kina, kuipanua na kuifanya bandari ya kisasa ili kuvutia wafanyabiashara kushusha mizigo yao na wasikimbilie Mombasa Kenya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuvutia wafanyabiashara kushusha mizigo yao na kutokukimbilia bandari ya nchi jirani, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ina mpango wa muda mfupi na wa kati wa kuboresha bandari ya Tanga kwa kutekeleza mradi wa kuimarisha gati namba mbili (2).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kuboresha Bandari ya Tanga ulianza Februari, 2016 na unatarajiwa kukamilika Juni, 2017. Mradi huu unatekelezwa na Kampuni ya Ukandarasi ya COMARCO kutoka Kenya. Maboresho ya bandari yanayofanyika katika mradi huu ni pamoja na kuongeza kina cha gati kwa kuchimba (dredging) kiasi cha mita 1 na kufanya kina cha gati kufikia mita 4.5; kuimarisha gati na kuweka mfumo wa kuzuia kutu katika nguzo (cathodic protection).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ukikamilika utasaidia kuongeza uwezo wa bandari kuhudumia meli zenye wastani wa ukubwa wa tani 1,200 kuingia bandarini. Aidha, Serikali kupitia TPA ina mpango wa muda mrefu wa kujenga bandari katika eneo la Mwambani ambayo ina kina kirefu na uwezo wa kuhudumia meli kubwa. TPA tayari inamiliki ardhi yenye ukubwa wa hekta 92 katika eneo la Mwambani.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE) aliuza:-
Katika Kamati ya Bunge la Kumi Serikali iliahidi kufunga mtambo kwa lengo la kudhibiti takwimu za simu za nje na ndani ili kudhibiti mapato ya Serikali:-
(a) Je, utekelezaji wa suala hilo umefikia wapi?
(b) Je, ni kiasi gani Serikali imekusanya tangu utaratibu huo uanze na kabla yake mapato yalikuwaje?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania iliweza kusimika mtambo wa kuhakiki na kusimamia huduma za mawasiliano yaani TTMS hapa nchini mwishoni mwa mwaka 2013. Mtambo huu umeisaidia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuongeza ufanisi katika kusimamia sekta ya mawasiliano pamoja na kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko yanayotokea katika sekta ya mawasiliano duniani kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mtambo wa TTMS umeiwezesha TCRA kuwa na uwezo wa kusimamia mawasiliano ya simu za kimataifa na zile za mwingiliano; kudhibiti mawasiliano ya simu za ulaghai za kimataifa; kusimamia ubora wa mitandao katika kutoa huduma bora kwa wananchi; kudhibiti namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano nchini pamoja na usimamiaji wa miamala ya fedha inayopita katika mitandao ya simu hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo, jitihada za kuboresha zaidi mfumo huu ili kuweza kubaini na kujiridhisha juu ya mapato yote yaani revenue assurance yatokanayo na huduma za mawasiliano kwa maana ya simu za sauti, data na SMS yanakidhi mahitaji ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na TCRA yanaendelea. Kwa vile vifungu vya mkataba wa TTMS vinamtaka mkandarasi kuweka mfumo wa kubaini na kujiridhisha juu ya mapato yote (Revenue Assurance System), Serikali kupitia TCRA imemwagiza mkandarasi aweke mfumo huo bila gharama za ziada kwa Serikali. Mkandarasi hatimaye amekubali kuweka mfumo wa Telecom Revenue Assurance ambapo unategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Oktoba, 2013 hadi Februari, 2017 kiasi cha sh.63,015,450,230.40 zilipatikana na katika hizo Sh.56,987,368,631.08 zimewasilishwa Hazina na Sh.6,028,081,599.41 zimewasilishwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa ajili ya kugharamia tafiti mbalimbali zenye manufaa kwa nchi yetu. Kabla ya mfumo huu, mapato haya hayakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuwajengea uwezo wataalam wa TCRA ili waweze kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano hususan katika eneo hili la kuchakata taarifa mbalimbali za huduma za mawasiliano zinazopatikana kutoka kwa watoa huduma ili kuweza kubaini na kujiridhisha juu ya mapato yote.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA (K.n.y. MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:-
Ili kurahisisha mfumo wa kimaendeleo na kukuza uchumi katika Bonde la Ziwa Rukwa, Serikali iliahidi kujenga daraja linalopita katika Mto Momba kati ya Kata ya Kamsamba (Jimbo la Momba) na Kata ya Kipeta (Jimbo la Kwela) mwaka 2009.
Je, ni lini ahadi hiyo ya Serikali itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la Momba ni kiungo muhimu katika barabara ya Kibaoni - Kasansa - Muze - Ilemba - Kilyamatundu - Kamsamba hadi Mlowo ambayo inaunganisha mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe. Barabara hii ni kiungo muhimu sana kati ya mikoa hii mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe kwani inapita katika Bonde la Ziwa Rukwa ambalo ni maarufu sana kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Hali ya barabara ni nzuri kwa wastani ila inapitika kwa shida wakati wa masika katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kufahamu umuhimu huo itaanza ujenzi wa daraja la Momba ambalo ni kiungo muhimu katika barabara hiyo katika mwaka wa fedha 2016/2017. Serikali imetenga shilingi milioni 2,935 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 na kwa sasa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) upo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 3,000 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa daraja hilo.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA (K.n.y. MHE. JACQUELINE
N. MSONGOZI) aliuliza:-
Barabara ya Makambako - Songea yenye urefu wa kilometa 295 imeharibika sana na inahitaji kufanyiwa matengenezo.
Je, ni lini Serikali itakarabati barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuifanyia ukarabati kwa kiwango cha lami barabara ya Makambako hadi Songea yenye urefu wa kilometa 295 ili kupunguza gharama na muda wa kusafiri kwa watumiaji wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania –TANROADS, tayari imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na utayarishaji wa nyaraka za zabuni. Lengo la kazi hiyo ni kuikarabati barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kazi hii imefanyika kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati kwa kiwango cha lami barabara ya Makambako hadi Songea. Aidha, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania inaendelea kuifanyia matengenezo barabara hii kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ili iendelee kupitika wakati Serikali inatafuta fedha za kuifanyia ukarabati kamili.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA aliuliza:-
Je, Serikali ipo tayari kuwalipa fidia wananchi waliowekewa alama za ‘X’ kwenye nyumba zao katika Barabara ya Mkuranga kwenda Kisiju?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega, Mbunge wa Mkuranga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu, eneo la hifadhi ya barabara kwa barabara kuu na barabara za mikoa limeongezeka kutoka mita 22.5 zilizotajwa katika Sheria ya Barabara ya mwaka 1967 hadi mita 30 kila upande kutoka katikati ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mkuranga hadi Kisiju yenye urefu wa kilometa 46 ni miongoni mwa barabara za mikoa zilizopo chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Katika kutimiza matakwa ya Sheria ya Barabaa ya mwaka 2007 Wakala wa Barabara Tanzania ulifanya zoezi la utambuzi wa mali zilizopo ndani ya hifadhi ya barabara kuu na barabara za mikoa nchini nzima ikiwemo Barabara ya Mkuranga hadi Kisiju. Lengo la kuweka alama ya ‘X’ ni kuwajulisha na kuwatahadharisha wananchi juu ya ongezeko la eneo la hifadhi ya barabara ili wasifanye maendeleo mapya kwenye maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya nyumba zilizowekwa alama ‘X’ kuna ambazo zimo katika hifadhi ya barabara ya mita 22.5 kila upande wa barabara ambapo wamiliki wake walipewa notice ya kuziondoa bila kulipwa fidia kwa kuwa walivamia eneo la hifadhi ya barabara. Kwa zile ambazo zimo kati ya mita 22.5 hadi 30 kila upande wamiliki wake wanastahili kulipwa fidia. Kwa sasa wananchi hawa hawatakiwi kufanya maendelezo yoyote katika maeneo hayo ingawa hawalazimiki kuomba wala kuondoa mali zao mpaka hapo Serikali itakapolihitaji eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Aidha, kabla Serikali haijatwaa eneo hilo uthamini utafanyika na wananchi wanaostahili kulipwa fidia watalipwa.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Wananchi wa Chilonwa wanaishukuru Serikali kwa kuendelea kukarabati daraja lililoko kati ya kijiji cha Mahampha na Nzali kwa kiwango cha mkeka, korongo hili hupitisha maji mengi sana wakati wa masika toka Bwawa la Hombolo kiasi cha kukosa mawasiliano kabisa kati ya Kaskazini na Kusini mwa Jimbo la Wilaya ya Chamwino kwa ujumla wake.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kulijenga daraja hili kwa kiwango cha daraja la kupitika juu na sio ya mkeka ili kuondoa kero hii ya kukatika kwa mawasiliano kabisa wakati wa masika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikilifanyia ukarabati daraja la Mfuto yaani drift liitwalo Chilonwa lililopo kati ya kijiji cha Mahampha na Nzali ili kuhakikisha kuwa daraja hilo pamoja na barabara ya Chamwino Ikulu - Dabalo junction hadi Itiso yenye urefu wa kilometa 75 inapitika majira yote ya mwaka. Kwa kawaida daraja la mfuto (drift) hujengwa katika eneo lenye kina kifupi ambalo maji hukatisha barabara yaani shallow water crossing. Hali hii ndio iliyosababisha daraja la mfuto kujengwa kati ya kijiji cha Mahampha na Nzali. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kufanya uangalizi wa karibu wa eneo hili ikiwa ni pamoja na kuangalia mapungufu yaliyopo na kupendekeza aina ya daraja ambalo litakuwa suluhisho la kudumu katika eneo hilo.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, ni lini ukarabati wa barabara ya Mlandizi – Chalinze utaanza kama ilivyoahidiwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mlandizi – Chalinze yenye urefu wa kilometa 44 ni sehemu ya barabara kuu itokayo Dar es Salaam kwenda Tunduma kupitia Morogoro. Kwa mara ya mwisho sehemu hii ya barabara ilifanyiwa ukarabati mkubwa kati ya mwaka 1990 hadi 1992. Kulingana na umri huo barabara hii inatakiwa ijengwe upya hata hivyo kutokana na uhaba wa fedha Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbli za kuwezesha barabara hii kupitika wakati inatafuta fedha za kuijenga upya.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Marabara Mkoa wa Pwani pamoja na maabara kuu ya vifaa vya ujenzi yaani Central Materials Laboratory, imefanya utafiti wa kina ili kutathimini uwezo wa barabara ya Mlandizi – Chalinze kuhimili ongezeko kubwa la magari na uzito. Matokeo ya utafiti huo yalipendekeza zichukuliwe hatua za muda mfupi ambazo zinahusisha kuondoa tabaka la lami ya sasa katika maeneo yenye mawimbi na yaliyodidimia na kuweka tabaka ya lami nzito iliyoimarishwa. Kazi hii ya ukarabati itaanza mara tu msimu wa mvua utakapoisha.
Mheshimiwa Spika, aidha, hatua za muda mrefu zitahusisha kuijenga upya barabara hii mara fedha zitakapopatikana.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 na 2015/2016 jumla ya kilometa 15 zilifanyiwa ukarabati kwa gharama ya shilingi bilioni 9.072. Aidha, katika mwaka huu wa fedha wa 2016/2017 shilingi 3,000,000,000 zilitengwa kwa ajili ya ukarabati na mkandarasi ataanza ukarabati mara tu msimu wa mvua utakapoisha ambapo jumla ya kilometa 12.55 zitafanyiwa ukarabati. Vilevile Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.175 kwa ajili ya kuendelea na ukarabati wa barabara hii katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Katika miaka ya 1950 Lindi kulikuwa na reli inayotoka Nachingwea kupitia Mtama, Mnazi Mmoja, Mingoyo hadi Bandari ya Mtwara na ilikuwa ikisafirisha korosho, mbao, magogo na watu. Kwa sasa Lindi kuna viwanda vingi na vingine vinatarajiwa kujengwa, barabara ya Kibiti – Lindi ambayo hupitisha mizigo mizito huenda ikaharibika mapema, hivyo reli ni muhimu sana.
Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka wa kuifufua reli ya Kusini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara inaunganishwa kwa reli ili kutumia Bandari kubwa ya Mtwara katika kusafirisha mizigo mbalimbali, Serikali imeshafanya upembuzi yakinifu wa reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay ambapo inatarajiwa reli hiyo ijengwe kwa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP). Baada ya kukamilika kwa reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay utaratibu wa kuunganisha Lindi na Mtwara kwenye reli utafuata.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kumwajiri Mshauri wa Uwekezaji (Transaction Advisor) atakayekuwa na jukumu la kuunadi mradi kwa ajili ya wawekezaji mbalimbali na hatimaye kujenga reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay na matawi ya kwenda Liganga na Mchuchuma yenye jumla ya urefu wa kilometa 1,000. (Makofi)
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Kata ya Kula ipo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika umbali wa takribani kilometa 50 kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi huku kukiwa hakuna barabara ya kuunganisha kata hiyo yenye mawe mengi na miteremko mikali kufika huko.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuzichukua barabara zenye kuelekea Bonde la Ziwa Tanganyika na kuwa chini ya TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuna barabara tatu zinazoelekea katika mwambao wa Ziwa Tanganyika ambazo zinaunganisha Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi. Barabara hizo ni Nkana – Kala ambazo urefu wake ni kilometa 67, Kitosi - Wampembe yenye urefu wa kilometa 68 na Namanyere hadi Ninde yenye urefu wa kilometa 60 ambazo pia zinaunganisha Makao Makuu ya Kata za Kala, Wampembe na Ninde. Barabara zote hizi zinasimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Mheshimiwa Spika, maombi ya kupandisha hadhi barabara mbili kati ya tatu nilizozitaja, tayari yamewasilishwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Tathmini ya Wizara baada ya kuyapitia maombi hayo ilibainisha kuwa Barabara za Nkana hadi Kala yenye urefu wa kilometa 72 na Kitosi hadi Wampembe yenye kilometa 68 hazikidhi vigezo vya kupandishwa hadhi kuwa barabara ya mkoa. Hivyo ilipendekezwa zibaki katika hadhi ya sasa. Kwa upande wa barabara ya Namanyere hadi Ninde yenye kilometa 60, kumbukumbu za Wizara zinaonesha haijawahi kuombewa kupandishwa hadhi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na Serikali kuanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), barabara zote zitaendelea kuhudumiwa na TARURA chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Mwaka 2014 Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Kilindi hadi Wilaya ya Gairo.
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kilindi kuanzia Songe kuelekea Gairo ina urefu wa kilometa 111.29. Sehemu ya barabara hii kutoka Songe hadi Kwekivu Junction na mpaka Iyogwe yenye urefu wa kilometa 69.5 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Tanga na sehemu ya barabara ya Iyogwe hadi Chakwale mpaka Ngilori yenye urefu wa kilometa 41.79 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Spika, barabara hii imekuwa ikitengewa fedha kila mwaka na kufanyiwa matengenezo ya kawaida, matengenezo ya muda maalum, matengenezo ya sehemu korofi, ujenzi wa madaraja na matengenezo makubwa ya madaraja. Matengenezo haya yameifanya barabara hii iweze kupitika majira yote ya mwaka. Aidha, mwaka 2014 Mheshimiwa Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami kwa barabara hii.
Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa barabara hii ya kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Kilindi inayoanzia Mji wa Songe hadi Kwekivu Junction - Iyogwe - Chakwale hadi Ngilori, Wilaya ya Gairo yenye urefu wa kilometa 111.29 inaingizwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii, Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. AJALI R. AKBAR) aliuliza:-
Wakati wa kampeni za uchaguzi, Makamu wa Rais alipokuja katika Mji Mdogo wa Kitangari miongoni mwa matatizo aliyoelezwa ni tatizo la barabara kati ya Newala na Jimbo la Mtama, Mkoani Lindi yenye urefu wa kilometa 50, naye aliahidi kusaidia ujenzi pindi fedha zitakapopatikana:-
Je, ni lini sasa barabara hiyo itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ajali Rashid Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Newala hadi Mtama ina urefu wa kilometa 74.23. Kati ya hizo, kilometa 17.03 ni za lami na kilometa 57.2 ni za changarawe. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Mtwara huifanyia matengenezo ya kawaida, matengenezo ya muda maalum na matengenezo ya sehemu korofi kila mwaka ili ipitike muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/20118 jumla ya shilingi milioni 783.815 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii. Aidha, maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hii yataanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, napenda kutoa tamko kwamba barabara hii tutaipa umuhimu unaostahili.
MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza:-
Sayansi na teknolojia imeleta mapinduzi makubwa sana kwa maendeleo ya mwanadamu, ikiwa ni pamoja na simu za mkononi ambazo zimerahisisha sana mawasiliano na huduma za kifedha; pamoja na mazuri hayo baadhi ya vijana na makundi rika mengine husikiliza simu kwa kutumia headphones na hatimaye hupoteza uwezo wa kusikia (uziwi):-
(a) Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka kutoa tamko kwa vijana hao kuacha matumizi yasiyokuwa na tija?
(b) Je, Serikali haioni ni vema simu zinazoingizwa nchini ziingizwe bila headphones kwa ajili ya kuwanusuru na uziwi vijana hao ambao ni tegemeo la Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Kuteuliwa, Mama yangu, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kitaalam hakuna taarifa za kitabibu kuhusu madhara ya utumiaji wa mara kwa mara wa headphones kwa muda mrefu. Aidha, vifaa vyote vya mawasiliano zikiwemo headphones huwekewa viwango na Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano Duniani (International Telecommunication Union – ITU) kwa ajili ya matumizi salama, hivyo, hakuna madhara ya utumiaji wa vifaa hivyo kwa kuwa vimethibitishwa Kimataifa. Kwa hapa nchini Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wana jukumu la kuhakiki viwango vya vifaa vya mawasiliano kabla havijaanza kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kutoa tamko kuwaasa vijana wanaotumia muda mwingi kwenye matumizi ya headphones waache na watumie muda mwingi katika ujenzi wa Taifa kwa kufanya kazi kwa ufanisi ili kuwa na maisha bora. Wizara yangu kwa kushirikiana na taasisi husika itaendelea kutoa elimu katika masuala mbalimbali ya matumizi ya TEHAMA ili kuleta tija na uelewa sahihi wa matumizi ya TEHAMA pamoja vifaa vyake.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, headphones ni sehemu ya kifaa ambatanishi (accessory) cha simu ambacho humpa mtumiaji husika uhuru wa kusikiliza sauti inayotoka kwenye simu yake kutegemea na kitu anachosikiliza bila kusababisha uchafuzi wa mazingira wa sauti (sound pollution) au usumbufu usio wa lazima kwa watu wengine. Aidha, vifaa vya mawasiliano vina nyenzo nyingine zikiwemo vipaza sauti (speakers) ambazo humwezesha mtu kusikia pasipo kuweka kifaa masikioni.
Mheshimia Naibu Spika, kwa misingi hiyo na kwa kuwa Serikali haijapokea malalamiko ya kuwepo kwa changamoto iliyotajwa, sio wakati muafaka kuzuia kuingia kwa headphones nchini.
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:-
Ujenzi wa barabara ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na hata ajira na mawasiliano. Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani –Saadani hadi Bagamoyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Tanga – Pangani – Saadani - Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 246 unajumuisha madaraja makubwa ya Pangani na Wami Chini, barabara za mchepuo katika Jiji la Tanga na Mji wa Pangani pamoja na barabara zinazoingia kwenye hoteli za kitalii za ufukwe wa Bahari ya Hindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni sehemu ya Mradi wa Kikanda wa Barabara ya Malindi – Mombasa – Lungalunga – Tanga – Pangani - Saadani haadi Bagamoyo na unaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ilikamilika mwezi Juni, 2015 chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank). Aidha, kutokana na gharama za mradi huu kuwa kubwa, taratibu za kupata fedha kutoka African Development Bank na washirika wa maendeleo wengine zimechukua muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi milioni 4,435 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Tanga – Pangani – Saadani - Bagamoyo wakati taratibu za kupata fedha zaidi kutoka African Development Bank na washirika wa maendeleo zinaendelea.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Serikali iliahidi kutoa kipaumbele kwa barabara zinazounganisha mikoa.
Je, ni lini barabara ya Handeni – Kiberashi – Kiteto –Nchemba na Singida itaanza kujwengwa ili kuunganisha mikoa minne ambayo ni ya kiuchumi hususan kilimo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa Barabara ya Handeni – Kiberashi –Kijungu – Chemba – Kwamtoro hadi Singida yenye urefu wa kilometa 461 umekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii, Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii unatekelezwa ili kuunganisha mikoa inakopita na maeneo mengine hasa ukizingatia hivi sasa tuna mradi wa kujenga bomba la mafuta linalotoka Uganda kwa maana ya Hoima hadi Tanzania kwa maana ya Tanga.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara ya kilometa 40 ya kutoka Nyololo - Igowole - Mtwango kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nyololo- Igowole hadi Mtwango au hadi Kibao yenye urefu wa kilometa 40.4 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami yanaendelea ambapo upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii yamekamilika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika katika majira yote ya mwaka wakati ikiendelea kutafuta fedha kwa ajilii ya ujenzi wa kiwango cha lami. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 450.077 na katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 160.511 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii.
MHE. MWITA M. WAITARA (K.n.y. MHE. ANATROPIA L. THEONEST) aliuliza:-
Kuna mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa Kipunguni ‘A’ na Kipunguni Mashariki dhidi ya Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Jijini Dar es Salaam. Wananchi hao wanapinga uthamini uliofanywa na fidia kidogo kwa kikundi cha watu wachache huku wengine wakizuiwa kuendeleza maeneo yao.
(a) Je, ni lini Serikali itaenda kumaliza mgogoro huo uliodumu tangu mwaka 2007?
(b) Je, Serikali ipo tayari kuwapa fidia ya kiwango cha soko wananchi waliozuiwa kuendeleza maeneo yao na kuendelea kubaki maskini kwa muda wote huo?
NAIBU WAZIRI WA WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, aah samahani naona Mzee Waitara ameniroga hapa.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a ) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya uthamini wa ardhi katika maeneo ya Kipunguni ‘A’ na Kipunguni Mashariki ikiwa ni pamoja na maeneo ya Kigilagila na Kipawa mwaka 1997 kwa kuwashirikisha wakazi wa maeneo husika kwa mujibu wa Sheria ya Utwaaji Ardhi (Land Acquisition Act) ya mwaka 1967 ambayo inaainisha mambo ya kuzingatia ikiwa ni thamani ya mazao na majengo yaliyopo kwenye maeneo husika, kumpatia mkazi wa eneo linalotwaliwa kiwanja na vilevile kulipa riba ya asilimia sita kwa mwaka pale ambapo malipo yanacheleweshwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali haikuwa na fedha za kutosha kuwalipa wakazi wote kwa pamoja, malipo yalifanyika kwa awamu tatu kadri fedha zilivyokuwa zinapatikana. Awamu ya kwanza na ya pili ya mwaka 2009 - 2011 ilihusu malipo ya wakazi wa Kipawa na Kigilagila na katika awamu ya tatu ambayo ilitolewa mwaka 2014 ililipa baadhi ya wakazi wa Kipunguni ambao idadi yao ilikuwa 59.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa sasa Serikali imekusudia kumaliza kulipa fidia wananchi waliobaki katika maeneo hayo kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba viwango vya ulipaji fidia huzingatia sheria iliyotumika kufanya uthamini husika. Hivyo kwa kuwa uthamini wa maeneo ya Kipunguni ‘A’ na Kipunguni Mashariki ulifanyika mwaka 1997 kwa mujibu wa Sheria ya Utwaaji Ardhi ya mwaka 1967 malipo au fidia kwa wakazi wa maeneo husika yatazingatia matakwa ya sheria hiyo.
MHE. KASUKU S. BILAGO (K.n.y. MHE. ZITTO Z. R. KABWE) aliuliza:-
Mamlaka ya Usimamizi wa Usafirishaji wa Ardhini na Majini (SUMATRA) hutoa vibali vya usafiri kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika.
(a) Je, ni kifungu gani cha sheria kinaipa mamlaka SUMATRA kutoza ushuru kwa wavuvi na wakati huo huo haifanyi hivyo kwa matrekta kwenye kilimo?
(b) Je, Serikali haioni kuwa inadidimiza wavuvi kwa kuwarundikia tozo nyingi na kuwafanya waendelee kuwa maskini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zitto Zuberi Ruyagwa Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(i) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) haitoi vibali wala haitozi ushuru kwa vyombo vya usafiri majini nchini ikiwa ni pamoja na wavuvi wa Ziwa Tanganyika, ila kwa mujibu wa Sehemu ya III, Kanuni ya 18 ya Kanuni za Sheria, zinazoitwa: The Merchant Shipping (Small Ships, Local Cargo Ship Safety, Small Ships Safety, Survey and Inspection for Vessels engaged on Local and Coastal Voyages Inland Waters) Regulations 2006, GN. 106, SUMATRA inalo jukumu la kukagua ubora wa vyombo vya usafiri majini kwa pamoja na vya uvuvi na kutoa Cheti cha Ubora (Seaworthness Certificate) na usajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya majukumu ya msingi ya SUMATRA katika vyombo vya usafiri majini na vya uvuvi ni kuhakikisha kuwa vyombo hivyo ni salama kabla havijaanza kutoa huduma au kufanya shughuli za majini.
(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, SUMATRA inapokagua vyombo vya usafiri majini kwa mujibu wa Sehemu ya II, Kanuni ya 9 ya Kanuni za Sheria, zinazoitwa: (The Merchant Shipping (Fees) Regulations, 2005), wenye vyombo vya usafiri majini ikiwa ni pamoja na vya uvuvi hutakiwa kulipa ada ya ukaguzi kwa SUMATRA kwa ajili ya ukaguzi uliofanyika. Hivyo, Serikali haikusudii kudidimiza wavuvi wala haijawarundikia tozo nyingi ambazo zitawafanya wawe masikini bali inawahakikishia wavuvi hao mazingira salama kwa ajili ya kufanya shughuli zao za uvuvi.
MHE. SAUMU H. SAKALA aliuliza:-
Kando kando mwa Bahari ya Hindi Mkoani Tanga, pameibuka bandari bubu ambazo nyingine zinakuwa kubwa na kuhudumia watu wengi zaidi na askari wasio waaminifu hufanya bandari bubu hizo kuwa vyanzo vyao vya mapato kwa kuchukua rushwa kwa watu wanaopitisha mizigo yao katika bandari hizo.
Je, ni lini Serikali itazirasimisha bandari hizo na kuzifanya zitambulike ili wafanyabiashara wanaozitumia wawe huru?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saumu Heri Sakala, Mbunge wa Viti Maalum, swali lake kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina taarifa ya uwepo wa bandari bubu katika mwambao wa Pwani ikiwa ni pamoja na maeneo ya Tanga. Aidha, kuibuka kwa bandari hizi bubu kumeleta changamoto za kiusalama, kiulinzi na kiuchumi. Hivyo, ili kudhibiti matumizi ya maeneo haya mamkala zinazohusika za pande zote mbili za Serikali ya Muungano zinashirikiana na kudhibiti hali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mikakati ya pamoja na vikao vya kiutendaji ambavyo vimekuwa vikifanyika kwa kuwahusisha Wakuu wa Mikoa yote ya mwambao na visiwani, Wizara zinazohusika kutoka Bara na Visiwani, Mamlaka ya Usafiri Baharini ya Zanzibar (ZMA) Mamlaka ya Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Shirika la Bandari la Zanzibar (ZPC), Mamkala ya Usimamizi wa Bahari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Uhamiaji, Halmashauri na vyombo vyote vya ulinzi na usalama nchini. Mikakati ya pamoja iliyowekwa ni pamoja na:-
(a) Kutambua bandari zenye umuhimu kwa wananchi kiuchumi na kijamii ili kuzirasimisha kwa kuziweka chini ya uangalizi wa vijiji vilivyo kwenye maeneo husika;
(b) Kuimarisha ushirikiano na Serikali za Mitaa kwa kutumia Kamati za Ulinzi na Usalama ili zihusike katika kudhibiti matumizi mabaya ya bandari bubu katika maeneo ambayo mamlaka husika hazina uwakilishi wa moja kwa moja;
(c) Kuwa na kaguzi za mapoja kwa lengo la kuongeza ufanisi katika matumizi ya vifaa kama vile boti za ukaguzi na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa suala hili, Serikali kupitia mamlaka nilizokwishazitaja, inasimamia kuhakikisha mikakati hii iliyowekwa inatekelezwa kwa wakati ili bandari bubu hizi zikiwemo za mwambao wa Mkoa wa Tanga zirasimishwe na kuwekwa chini ya uangalizi wa mamlaka husika.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Serikali iliunda Bodi ya Kusajili Wakandarasi (CRB) ambayo ina jukumu la kusajili, kuratibu na kusimamia mwenendo wa makandarasi nchini.
• Je, tangu kuanzishwa kwa CRB ni wakandarasi wangapi Watanzania wamesajiliwa na taasisi hiyo?
• Je, Serikali Kuu na Halmashauri za Wilaya zinatumia vigezo gani kutoa kazi kwa wakandarasi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ka niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Usajili wa Makandarasi tangu ilipoanzishwa mwaka 1997 imesajili jumla ya makandarasi wa Kitanzania 13,523. Kati ya makandarasi hao, makandarasi 8,935 usajili wao uko hai na makandarasi 4,578 wamefutiwa usajili kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kushindwa kulipia ada ya mwaka na kukiuka taratibu nyingine zinazoongoza shughuli za ukandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotumiwa na Serikali katika utoaji wa zabuni kwa makandarasi vinazaingatia matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 na Kanuni zake za mwaka 2013. Vigezo hivyo ni pamoja na kampuni kusajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi, ukomo wa ukubwa wa kazi kulingana na daraja la usajili, mahitaji maalum ya mradi husika, wataalam, vitendea kazi, uzoefu wa utekelezaji wa miradi ya aina hiyo na uwezo wa ampuni kifedha wa kutekeleza mradi husika. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-
Upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Ipole - Lungwa ulianza miaka mingi iliyopita na hii ni sehemu ya barabara kuu (trunk road) inayounganisha makao makuu ya Mkoa wa Mbeya. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 barabara hiyo imetengewa shilingi 350,000,000 kwa ajili ya kumalizia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni pamoja na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa barabara ya Ipole hadi Lungwa yenye urefu wa kilometa 172 inaendelea. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya shilingi milioni 1,211 zimetengwa na katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, tunashukuru mmezipitisha shilingi milioni 435 kwa ajili ya kukamilisha kazi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu, usanifu wa kina pamoja na maandalizi ya nyaraka za zabuni na gharama za mradi kujulikana, Serikali itaanza kutafuta fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Ipole hadi Lungwa.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Ilani ya CCM 2015 - 2020 imeelekeza kwamba Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara inayounganisha Mji wa Kahama (Manzese) hadi Geita kupitia Mgodi wa Bulyanhulu na upembuzi yakinifu ulishakamilika na Mheshimiwa Rais katika ziara yake aliahidi ujenzi huo kuanza mwaka 2017/2018.
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kinahitajika ili kutekeleza mradi huo?
(b) Je, Serikali imejiandaaje kuanza ujenzi huo mwaka 2017?
(c) Kwa kuwa mara zote miradi ya Serikali huchelewa kutokana na ukosefu wa fedha, je, Serikali imewashirikisha wawekezaji wa Migodi ya Buzwagi, Bulyanhulu na Geita ili washiriki katika ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kahama hadi Geita yenye urefu wa kilometa 139 imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na Wizara imefanya mazungumzo ya awali na wawekezaji wa mgodi wa Bulyanhulu, Kampuni ya Acacia Mining, ili kuona uwezekano wa kushirikiana katika ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami baada ya Kampuni hiyo kuonesha nia ya kushirikiana na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambazo ni hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hizi zimekamilika, sasa ujenzi ndiyo hatua inayofuata. Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi 12,403,000,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, barabara ya Kahama - Geita.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
Kwa kipindi kirefu sasa Bandari za Tanga na Mkokotoni zimekuwa zikitumika na kusababisha maafa makubwa kwa watumiaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha usalama wa wasafiri hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa wakazi wa maeneo ya Tanga, Visiwa vya Unguja na Pemba wanapata huduma bora na salama na hivyo kuwaepusha na usafiri wa vyombo vya majini visivyokidhi matakwa katika kubeba abiria na mizigo. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na:-
(a) Kuhakikisha kuwa vyombo hivyo ni salama kabla havijaanza kutoa huduma. Kwa sababu hiyo SUMATRA hufanya ukaguzi wa lazima (Statutory Inspection) wa vyombo kila baada ya mwaka ili kubaini kwamba vyombo hivyo vinaendelea kukidhi ubora na usalama wa kuelea majini. Aidha, SUMATRA hufanya kaguzi za kushtukiza ili kuhakikisha kuwa vyombo vya majini vinaendelea kuwa salama wakati wote.
(b) Kuweka na kutekeleza mikakati ya namna ya kudhibiti uibukaji na matumizi ya bandari bubu katika mwambao wa Pwani kwa kuwa vyombo vingi vinavyoanza safari zake katika bandari zisizo rasmi siyo rahisi kufuata masharti ya ubora na usalama wa kuelea majini. SUMATRA inashirikisha uongozi wa Serikali za Vijiji na Kata, vikundi vya kudhibiti uvuvi haramu na usimamizi wa mazingira ya mialo ambao husaidia kusimamia utaratibu wa uondokaji wa vyombo katika mialo ili kuhakikisha vyombo vinavyotumika vinatambulika na kuacha taarifa ya orodha ya abiria na mizigo.
(c) Kuhimiza sekta binafsi kuwekeza katika utoaji wa huduma za usafiri kwa kutumia meli za kisasa kati ya Tanga, Unguja na Pemba ili wananchi wapate huduma bora na za kutosha kupitia bandari rasmi hivyo kuondoa mazingira yanayolazimisha kutumia bandari bubu.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Je, ni nini Sera ya Magari ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Magari ya Serikali, kama ilivyo kwa mali zingine za Serikali samani, ardhi na majengo, madini, misitu, uoto wa asili na kadhalika husimamiwa na sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha menejimenti ya mali za Serikali, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imeanza kuandaa Sera ya Menejimenti ya Mali za Serikali (Government Asset Management Policy). Sera hiyo ambayo inaandaliwa chini ya uratibu wa Wizara ya Fedha na Mipango itasimamia menejimenti ya mali zote za Serikali yakiwemo magari. Sera hiyo pamoja na mambo mengine itaelekeza utaratibu mzima wa ununuzi, utunzaji na ufutaji/uondoshaji wa mali za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali inaendelea kukamilisha Sera hiyo, ununuzi, utumiaji na uondoshaji wa magari ya Serikali utaendelea kusimamiwa na Sheria ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Sura ya 410 na kanuni zake, Sheria ya Fedha na kanuni zake pamoja na miongozo inayotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma pamoja na Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa magari yote ya Serikali hununuliwa kwa pamoja (bulk procurement) ili kuipunguzia Serikali gharama za ununuzi. Kwa mujibu wa sheria ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, Sura 410, Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi wa Serikali (GPSA), ndiyo yenye dhamana ya ununuzi baada ya kupata kibali cha ununuzi wa magari hayo toka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuzingatia viwango (specifications) vinavyotolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma pamoja na kanuni zake, matengenezo na usimamizi wa matengenezo ya magari yote ya Serikali hufanywa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA). Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Fedha, miongozo inayotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma uondoshaji (disposal) wa magari ya Serikali katika matumizi ya umma hufanywa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikisha Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA (K.n.y MHE. ORAN NJEZA) aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini wanaipongeza Serikali kwa kuanzisha Wilaya ya Kipolisi Mbalizi.
• Je, ni lini Ofisi ya Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi itajengwa zikiwemo nyumba za kuishi askari?
• Je, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari mangapi na Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya vituo vya polisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua ukosefu wa Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya na ukosefu wa nyumba za kuishi askari Wilaya ya Kipolisi Mbalizi. Ni lengo la Serikali kukamilisha ujenzi wa vituo vya polisi kwenye wilaya 65 zilizosalia na ujenzi wa nyumba za makazi. Ujenzi huu utatekelezwa kwa awamu kutegemeana na upatikanaji wa fedha zitakazotengwa katika bajeti kila mwaka na kutumia rasilimali zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari mawili, moja liko Mbalizi na lingine lipo kituo kidogo cha Inyara. Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya Vituo vya Polisi katika Halmashauri ya Mbeya na kwingineko kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyoongezeka.
MHE. PETER J. SERUKAMBA aliuliza:-
Jimbo la Kigoma Kaskazini katika Kata ya Ziwani kuna tatizo kubwa la mawasiliano ya simu hasa katika vijiji vya Kalalangobo, Rubabara, Kigalye, Mtanga, Nyantole na Kazinga. Je, ni lini wananchi watapatiwa mawasiliano hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeviainisha vijiji vya Kata ya Ziwani vikiwemo vijiji vya Kalalangobo, Kigalye, Manga, Rubabara, Nyantole na Kazinga na kuviingiza katika miradi ya kufikisha huduma ya mawasiliano vijijini kwa kadri ya upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Bandari ya Mtwara ni Bandari yenye kina kirefu Afrika Mashariki na Kati na Serikali kwa makusudi imeamua kuitupa na kujenga Bandari katika maeneo mengine ya nchi tena kwa gharama kubwa sana:-
Je, Serikali ipo tayari kukiri makosa na kuiboresha Bandari ya Mtwara ili korosho zote zisafirishwe kupitia Bandari hiyo kwa lengo la kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuendeleza bandari zote nchini kadri uwezo utakavyoruhusu ili kuchochea ukuaji haraka wa uchumi. Hii inatokana na ukweli kwamba bandari ndiyo njia kuu ya kuchochea uchumi katika Taifa lolote lililobahatika kuwa na bahari.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mtwara Mjini na Mtwara yote kwa ujumla kuwa Serikali haijawahi na haina nia ya kuitupa Bandari ya Mtwara kwani inafahamu fursa zilizopo katika ukanda wa maendeleo wa Mtwara yaani Mtwara Development Corridor.
Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza azma yake, katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017 Serikali ilitenga shilingi bilioni 59.32 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa gati moja lenye urefu wa mita 350 la kuhudumia shehena mchanganyiko ikiwemo ya korosho. Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania imetenga shilingi bilioni 87.044 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa gati hilo. Gati hili linasanifiwa na kujengwa na Mkandarasi China Railway Construction Company (CRCC Group) kwa kushirikiana na China Railway Major Bridge Engineering Company Limited kwa gharama ya shilingi bilioni 137.39 pamoja na VAT. Mkataba wa ujenzi kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari na kampuni hiyo ulisainiwa tarehe 4 Machi, 2017 na ujenzi wa gati hilo utakamilika ndani ya miezi 21.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Tarafa ya Mwambao katika Wilaya ya Ludewa yenye Kata za Lupingu, Lifuma, Makonde, Kilindo na Lumbila hazina mtandao wa mawasiliano ya simu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea wananchi wa maeneo hayo mtandao wa mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deogratias Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote inatambua tatizo la huduma ya mawasiliano katika maeneo ya Tarafa ya Mwambao. Kwa kulitambua hilo, Serikali kupitia Mfuko huo wa Mawasiliano kwa Wote imeainisha maeneo ya Vijiji vya Kata za Lumbila, Kilindo, Makonde na Lupingu na kuyaingiza katika zabuni iliyotangazwa tarehe 20 Februari, 2017. Zabuni hiyo ilifunguliwa tarehe 27 Aprili, 2017. Aidha, baada ya tathmini ya zabuni kukamilika Kata za Lumbila, Kilindo, Makonde na Lupingu zimepata mtoa huduma wa kufikisha huduma ya mawasiliano.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Ujenzi wa barabara kutoka Bigwa - Kisaki iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli alitoa ahadi ya kujenga barabara hiyo alipohutubia wananchi wa Morogoro na kwamba fedha za ujenzi zitatoka Serikalini, nyumba zote zilizomo ndani ya mita 60 zimewekwa alama ya ‘X’ tayari kubomolewa katika maeneo ya Ruvu Kibangile, Kisemu, Mtamba, Nzasa, Kangazi, Kisanzala, Tambuu, Mvuha, Mngazi hadi Kisaki:-
• Je, Serikali itakuwa tayari kuwawekea wananchi hao utaratibu wa kuwajengea nyumba bora kwa wanaopenda badala ya kuwalipa fidia kidogo isiyolingana na mali zao wanazoziacha?
• Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza ili wananchi waliowekewa alama ya kubomolewa nyumba zao waanze maandalizi kwenye maeneo watakayohamia?
• Je, ni lini Serikali itatengeneza upya madaraja ya Ruvu, Mvuha na Dutumi yaliyomo kwenye barabara hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa madaraja hayo ni mabovu sana na yanaweza kusababisha ajali kwa wanaopita hapo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Jimbo la Morogoro lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Bigwa hadi Kisaki kwa kuanza na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya barabara ya Bigwa hadi Mvuha yenye urefu wa kilometa 78, pamoja na madaraja ya Ruvu na Mvuha kwa gharama ya Sh.713,471,140/=. Usanifu wa barabara ya Bigwa hadi Mvuha unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2017. Aidha, usanifu wa daraja la Dutumi ulishakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina sehemu ya Bigwa hadi Mvuha, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara pamoja na madaraja yaliyopo kwenye barabara hii. Serikali inaendelea kufanya matengenezo ya aina mbalimbali kwa barabara yote ya Bigwa hadi Kisaki ili iendelee kupitika katika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa jumla ya shilingi milioni 807.84 na katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa jumla ya shilingi milioni 1,126.36.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wote ambao nyumba zao zipo kwenye eneo la hifadhi ya barabara kati ya mita 22.5 na mita 30 kutoka katikati ya barabara kwenda kila upande watalipwa fidia wakati Serikali itakapohitaji kuyatumia maeneo hayo kwa ajili ya upanuzi wa barabara. Aidha, wale wote waliopo kwenye eneo la hifadhi ya barabara ndani ya mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kwenda kila upande wanatakiwa kuondoa mali zao kwa mujibu wa sheria ya barabara Na. 13 ya mwaka 2017 na hawatalipwa fidia.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. MUSSA B. MBAROUK) aliuliza:-
Kwa kuwa usafiri wa majini, mizigo na watu havifanyi usajili na vipimo.
Je, kwa nini Serikali isianzishe utaratibu wa kupima mizigo na usajili wa abiria katika vyombo vyote kama wanavyofanya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCCAA) ili kuepusha ajali za mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuna utaratibu wa aina mbili unaotumika kupima mizigo na usajili wa abiria katika vyombo vinaavyotumika majini. Kwanza usajili na uorodheshaji wa mizigo wakati wa ukataji wa tiketi za abiria na upakiaji wa mizigo kama inavyoainishwa katika passenger or Cargo Manifests and Crew List. Pili, uhakiki wa upakiaji kabla ya chombo kuruhusiwa kuanza safari, kwa kuhesabu abiria wakati wa kuingia kwenye chombo na kuhakiki kuwa alama ya Loading Mark haivukwi. Aidha, matumizi ya Port Clearance Forms huwezesha kudhibiti kiwango cha upakiaji abiria na mizigo kwenye chombo na kuacha taarifa za safari.
Mheshimiwa Spika, Serikali hufanya udhibiti huo, kupitia mamlaka ya udhibiti usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA) na mamlaka ya usimamizi wa bandari TPA ambazo husimamia utaratibu wa upakiaji bandarini na kudhibiti usalama wa vyombo vya usafiri majini. Taratibu hizi hufanywa au hatakiwa kufanywa kwenye bandari na mialo yote iliyosajiliwa.
MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza:-
Tanzania tuna ushindani mkubwa wa Kampuni za Simu na katika Jimbo la Manonga maeneo kama ya Kata ya Mwashiku, Ngulu, Kitangari, Sungwizi, Mwamala, Uswaya, Tambarale na Igoweko hayana minara ya mawasiliano.
Je, ni lini Serikali itazielekeza Kampuni za Simu kusimamia minara yao kwenye maeneo ambayo hayana mtandao wa mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kuwa maeneo ya Kata za, Mwashiku, Ngulu, Ntobo, Kitangiri, Sungwizi, Mwamala, Uswaya, Tambarale na Igoweko hayana minara ya mawasiliano. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote uliyaanisha maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Igunga, hususan Jimboni Manonga na kuyaingiza kaitka utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, vijiji vya Matinje na Mwashiku kutoka kata ya Mwashiku, vijiji vya Imalilo na Mwasung’ho kutoka katika kata ya Ngulu, kijiji cha Mwamloli kutoka katika kata ya Ntobo na vijiji vya Igoweko na Uswaya kutoka kata ya Igoweko vitafikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi wa Viettel unaotarajiwa kukamilika Novemba, 2017. Aidha, vijiji ya Kitangiri kutoka Kata ya Ndembezi na vijiji vya Sungwizi na Mwamala kutoka Kata ya Sungwizi vimeingizwa katika orodha ya miradi inayosubiri upatikanaji wa fedha ili kutekelezwe, kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018.