Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jenista Joackim Mhagama (33 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, nami naanza kwa kushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nachukua nafasi hii pia kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kunipa kazi ya kumsaidia na hasa kumsadia Waziri Mkuu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba nimhakikishie nitakuwa mtumishi mwema.
Vilevile nawashukuru pia wapigakura wa Jimbo la Peramiho, nawaambia Hapa ni Kazi Tu, wasibabaishwe na kelele za mpangaji wakati sisi wenye nyumba tupo, tunaendelea kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Rais wetu ametupa kazi kadhaa za kufanya. Naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu na hasa kwa kuonyesha kwa vitendo anajali makundi maalum na hasa ya walemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu amelidhihirisha hilo kwa matendo. Chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Rais amemteua Naibu Waziri anayeonyesha kama ni kielelezo cha watu wenye ulemavu katika nchi yetu ya Tanzania wanaweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kwanza kuwapongeza Wabunge wote kutoka katika kundi hilo na Watanzania wote kutoka katika kundi hilo ambao wameonyesha umahiri mkubwa katika kutoa mchango wao kwenye maendeleo ya Taifa letu bila kusita na kuonyesha kwamba kundi hili ni kundi muhimu katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2010 tumetunga Sheria Na.1 ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kusimama katika maneno ya Mkataba wa Kimataifa ambao unatoa haki za binadamu na hasa kwa kundi la watu wenye ulemavu. Mkataba huo tuliuridhia mwaka 2008, mwaka 2010 tumetunga sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hotuba ya Rais inatukumbusha, watu wenye ulemevu wana haki sawa na Watanzania wote. Kwa niaba ya Serikali na kwa maagizo ya hotuba ya Rais, tutakwenda kusimamia wapate haki sawa kwenye elimu, wapate haki sawa kwenye afya, wapate haki sawa kwenye ajira, wapate haki sawa kwenye masuala yote ya uchumi. Hiyo ni kazi tumepewa katika hotuba hii ya Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kuondoa kila dhana ya unyanyapaa. Kumekuwa na tabia imezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge kwamba wapo watoto wenye ulemavu wanafungiwa na hata jamii zetu zimekuwa zikiwachukulia watoto wenye ulemavu, kwa mfano wenzetu wenye ulemavu wa u-albino wafungiwe mahali fulani kwa ajili ya ulinzi na usalama. Katika mipango tulionayo sasa, tumeanza kuona ni namna gani watu hawa walindwe lakini watolewe nje wakawe na wao ni part ya jamii ya Watanzania katika kuleta maendeleo na kupatiwa maendeleo endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nyingine kubwa ambayo tumepewa pamoja na kusimamia sera, maafa na mambo mengine yote, matatizo ya dawa za kulevya na UKIMWI, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kazi hiyo tunaifanya sawia. Tutapambana na dawa za kulevya, hakuna kurudi nyuma, tutaendelea kupambana na ugonjwa wa UKIMWI hakuna kurudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge lililopita tulishatunga sheria, tutazisimamia na ole wao watakaoendeleza biashara ya dawa za kulevya, sheria ile itafanya kazi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepewa kazi nyingine kubwa ya kuhakikisha kwamba tunaongeza ajira katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, katika hotuba yake ametuagiza, katika kuhakikisha Watanzania wanaondokana na tatizo la ajira mpango huu wa kuwezesha sekta ya viwanda, ifanye kazi ya kutosha kati ya Wizara yetu lakini na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha huu mpango wa sekta kubwa ya viwanda vidogo, vya kati na viwanda vikubwa, iweze kuchukua asilimia 40 ya nguvu kazi ya Taifa. Waheshimiwa Wabunge, tutafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kuimarisha mifuko tuliyonayo sasa. Waheshimiwa Wabunge mmesema vijana wetu wanamaliza vyuo, hawana mikopo, vijana wana uwezo wa kuongeza stadi walizonazo ili kuchangia pato la Taifa na kujiajiri, wanashindwa kupata uwezo wa kufanya hivyo. Tumejipanga kuimarisha mifuko hiyo, iwape vijana wetu mikopo yenye riba nafuu na Waheshimiwa Wabunge tunaendelea kuwasiliana, tutaleta mipango hapa Bungeni muiunge mkono, tunataka kuonyesha mwaka 2020 haya yanawezakana; na tuwawezeshe vijana wetu kuweza kuajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutatekeleza mikakati mingine ambayo tayari iko ndani ya Wizara, kwa mfano kukuza ajira kwa vitendo na tutashirikiana na Halmashauri zetu kuhakikisha tunafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tutakapopata muda, tutatoa maelezo ya kina. Nachukua nafasi hii kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais na ninampongeza sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia Waheshimiwa Wabunge wote uzima na afya njema kiasi cha kutuwezesha kukutana tena leo katika ukumbi huu kwa majukumu yetu ya Kibunge lakini kwa manufaa ya Watanzania wote ambao tunawawakilisha ndani ya Bunge hili kwa ujumla wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Meza na Kiti chako ili kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge zinazohusiana na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu toka nilipoteuliwa na Mheshimiwa Rais wetu kwa wadhifa huu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia mambo ya Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kunipa dhamana hii kubwa. Naamini kabisa kwamba sote tunafahamu uzito wa majukumu ya kuwatumikia wananchi na umma mzima wa Watanzania. Naahidi kwamba nitajitahidi kutenda kazi zangu zote kwa moyo wote ili kuleta maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kwa dhati kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa na miongozo mbalimbali anayonipa katika kutekeleza majukumu yangu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika kipindi hiki kifupi cha Serikali ya Awamu ya Tano. Toka nimeingia madarakani nimeona kwa kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu amesheheni umakini mkubwa wa uongozi na uongozi usioyumba katika kusimamia, kufuatilia masuala ya msingi yanayohusu maslahi ya umma. Ni mchapakazi na ni muadilifu katika uongozi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kwa dhati niwashukuru sana Manaibu Waziri wawili, Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Dkt. Possi kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Nimeamini hawa Naibu Mawaziri wawili kwa kweli ni vijana ambao ni ma-caterpillar wenye uwezo mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru pia Makatibu Wakuu wote, Wakurugenzi na viongozi wa taasisi mbalimbali ambazo ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na ushirikiano ambao wamekuwa wakinipa katika kutekeleza majukumu yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati pia niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Peramiho kwa kunichagua lakini kwa kuendelea kuniunga mkono katika utekelezaji wangu wa majukumu haya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii ambayo inanifanya leo kuja kuhitimisha hoja hii mbele yako isingeweza kufikia mahali hapa kama si Wajumbe wa Kamati mbili za Kudumu za Bunge ambao walifanya kazi ya umakini katika kupitia mapendekezo ya bajeti yetu na kuifanya bajeti hii iweze kuja hapa mbele yako.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa na Naibu wake dada yangu Mheshimiwa Giga na Wajumbe wote wa Kamati ya Katiba na Sheria kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia wakati wa kuchambua bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya UKIMWI wakiongozwa na Mheshimiwa Mwenyekiti Hasna Mwilima na Makamu wake Mheshimiwa Kanyasu na Wajumbe wote kwa kazi kubwa waliyoifanya na ushirikiano mkubwa waliotupatia katika kuhakikisha kwamba tunafanikiwa katika kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mwenyewe umejidhihirisha kwamba umekuwa kiongozi mahiri wa kuliongoza Bunge letu pamoja na Wenyeviti wa Bunge na Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge. Kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, napenda niwapongeze, niwashukuru na niwatakie kila la kheri katika kutekeleza majukumu haya mazito wakiwemo Makatibu wanaotuhudumu katika Kamati mbalimbali za Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 99(2) ya Kanuni za kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 inayohusu kujadili utekelezaji wa bajeti za Wizara, naomba sasa kwa heshima na taadhima uniruhusu nitoe ufafanuzi katika maeneo mbalimbali ambayo Waheshimiwa Wabunge waliyachangia na kutaka kupata ufafanuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachukua maeneo machache na maeneo mengine Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuja mbele hapa leo wakati wa kuhitimisha hoja hii basi atayatolea ufafanuzi wa kina.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapokwenda kutoa ufafanuzi wa maeneo haya, nawashukuru sana Wabunge wote waliochangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na hasa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ambao walishiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika kuchangia mapendekezo ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka wa huu wa fedha wa 2016/2017. Niwahakikishie tulikuwa wasikivu na tumeyachukua maoni na ushauri wenu na kama yote hayatajibiwa ipasavyo hapa basi Ofisi yangu itafanya utaratibu wa kuyajibu kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge mtaweza kuyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kujibu hoja hizi pia kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nitoe pole sana kwa maeneo mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania waliokumbwa na maafa ya mafuriko. Tumekuwa tukishuhudia katika Bunge letu na sehemu nyingine, maeneo mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania yamekumbwa na mafuriko makubwa na Watanzania wengi wamejikuta wakihangaika na hii yote ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na mvua zilivyonyesha kwa wingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kushirikiana na Kamati zetu za Maafa, lakini tuendelee kuwaagiza viongozi wote katika maeneo mbalimbali wahakikishe wanaendelea kuchukua tahadhari na hasa kuwahamisha wananchi katika maeneo hatarishi ili kuweza kuepusha majanga ya maafa katika kipindi hiki ambacho utabiri unaonyesha tutakuwa na mvua nyingi sana zinazoweza kupelekea kupatikana kwa maafa mengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujibu hoja hizi, nianze na hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati zote mbili, nikianza na hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria alituagiza Serikali kufanya uchambuzi wa kina wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kubaini tuhuma zilizotolewa katika miradi ya NSSF na kuchukua hatua za kisheria za kuwawajibisha watu wote waliohusika katika kadhia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakubaliana na ushauri huo wa Kamati, ripoti ya hesabu za Serikali imeshatolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ndani ya Bunge. Kwa hiyo, kwa kufuata taratibu zile zile za kikanuni lakini taratibu za Serikali za kufuatilia ripoti hiyo, Serikali inaahidi kwamba italifanyia kazi suala hilo kwa namna yoyote ile itakayowezekana ili kuendana na agizo la Kamati kama lilivyowekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia SSRA kwa kushirikiana na Benki Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 39 kikisomwa pamoja na kifungu cha 40 na 48 cha Sheria Na.8 ya mwaka 2008, Sheria ya SSRA itaendelea kufanya ukaguzi maalum kwa maana ya special inspection kwenye vitega uchumi vyote ndani ya Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Sheria Na. 8 ya mwaka 2010 ilianza kutumika mwezi Septemba 2010. Sheria hiyo iliyomuunda Mdhibiti Mkuu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ililetwa kwa maana halisi ya kuondoa migongano ya kisheria katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, lakini vilevile ilitaka kuweka sera jumuishi za uwekezaji ndani ya mifuko hiyo na ilitaka pia kusimamia suala zima la kuongeza wigo na ufinyu wa hifadhi ya jamii katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya pekee, naomba nimpongeze sana Mkurugenzi Mkuu wa SSRA dada Irene kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika kusimamia sekta yetu ya hifadhi ya jamii nchini. Na sisi kama Serikali tutaendelea kumpa ushirikiano na niwaombe Waheshimiwa Wabunge mnaweza kumtembelea na kupata ushauri mara zote bado anaendelea kusimamia sekta hii vizuri na kwa uadilifu wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, agizo lingine lilikuwa ni SSRA iendelee kusimamia na kuchukua hatua kali kwa waajiri ambao hushindwa kuwasilisha michango ya wanachama wakiwemo waajiri wa sekta binafsi na taasisi za Serikali. Kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria Na. 8 ya mwaka 2008, SSRA ina wajibu wa kutekeleza na kulinda maslahi ya wanachama wote katika mifuko yetu.
Hata hivyo, SSRA imekuwa ikijikuta wakati mwingine ikipata shida katika kusimamia suala zima la kuwalazimisha waajiri kuhakikisha kwamba wanapeleka michango yao kwa wakati katika mifuko hii ya hifadhi ya jamii. Hivyo basi, SSRA kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu tumeandaa rasimu ya mabadiliko ya Sheria Na. 8 ya mwaka 2008 kwa lengo la kuipa nguvu SSRA ipate meno ya kuhakikisha kwamba waajiri wote wanakusanya michango na kuifikisha kwenye Mfuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati na kuondoa usumbufu kwa wanachama wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati iliiagiza Serikali ichukue hatua za dhati na za makusudi kuboresha mitambo na mazingira ya Idara ya Mpiga chapa Mkuu wa Serikali ili kuiwezesha idara hiyo kufanya shughuli zake kwa ufanisi na kibiashara. Tunayo mipango ya muda mrefu na muda mfupi katika kuhakikisha kwamba tunaboresha Idara hiyo ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali. Kwa sasa tumeamua kabisa kuyatambua mazingira hayo magumu ya Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na tumeamua kwa haraka kuanza kuchukua hatua za dharura za kukarabati mitambo yote ambayo ilikuwa imenunuliwa na bado inaweza kufanya kazi nzuri ya kuweza kurahisisha kazi katika kiwanda hiki. Tumejipanga kwa mpango wa muda wa kati na muda mrefu ili kuhakikisha tunaendelea kuboresha mazingira na majengo ya kiwanda hicho. Vilevile kwa kushirikiana na taasisi za Serikali ikiwemo Benki ya TIB na taasisi nyingine tumeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kuboresha kiwanda hicho. Pia tuna mpango wa kujenga kiwanda kingine katika Makao Makuu ya nchi hapa Dodoma ambacho kitakuwa cha kisasa na kinaweza kukidhi mahitaji ya Taifa na tayari Serikali imepata ekari tano za kuweza kujenga kiwanda hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliagizwa pia kwamba Serikali ijitahidi kadiri inavyowezekana kuboresha huduma za maafa ili kuiwezesha Serikali kutoa misaada ya haraka pindi maafa yanapotokea katika nchi yetu ya Tanzania mahali popote. Serikali imeanza kuchukua hatua za dhati kabisa kuhakikisha tunaboresha huduma za Idara ya Maafa katika nchi yetu ya Tanzania. Hii ni pamoja na kupitishwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 7 ya mwaka 2015.
Pamoja na kazi hizi tunazozifanya, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mkurugenzi anayesimamia Idara ya Maafa nchini kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha kwamba kwa resources hizo ndogo tulizonazo lakini shughuli hii imeendelea kufanyika kwa ufanisi na Waheshimiwa Wabunge wengi walisema na kumpongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo sheria hiyo inaweka maagizo mbalimbali ya kisheria yanayotakiwa kufuatwa ikiwemo kuanzishwa kwa Kamati za Maafa katika ngazi ya Kata, Wilaya, Mikoa. Kamati hizo zinaweza kutoa mchango mkubwa wa awali katika kusimamia suala zima la maafa pale yanapotokea na kutambua pia viashiria hatashiri ili kuchukua hatua kama vile kuwahamisha watu katika maeneo yanayoonekana ni hatarishi na hasa wakati wa masika kama inavyotokea sasa.
Waheshimiwa Wabunge, niwaombe sana tuendelee kushirikiana na viongozi wenzetu na hasa wale viongozi wa Kamati za Maafa katika maeneo yetu ili kusaidiana kuhakikisha kwamba ama tunatoa taarifa mapema majanga haya yanapotokea ama tunachukua nafasi ya kushauri kuchukua tahadhari katika maeneo mbalimbali ili kupunguza maafa katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Kamati na Waheshimiwa Wabunge wengine waliomba Serikali iongeze fungu kwa ajili ya Idara hii ya Maafa. Serikali imeendelea kuweka fedha kwa Idara hii ya Maafa kwa kuzingatia ukomo wa bajeti. Vilevile tumeendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na Wizara na taasisi nyingine ili kuhakikisha vifaa vya misaada ya maafa katika nchi nzima vinapatikana. Serikali imeweka maghala mbalimbali kwa ajili ya huduma hii katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuzingatia kanda. Serikali pia imejiandaa na inaendelea kufanya tathmini ya majanga yaliyokwisha kutokea, imeendelea kuwafundisha wataalam mbalimbali mbinu na namna bora za kukabiliana na maafa na majanga mengine nchini ili majukumu haya yaweze kusimamiwa vema na Serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuliagizwa pia na baadhi ya Wabunge waliochangia na vilevile Kamati ya Katiba na Sheria ya kwamba Serikali ichukue hatua za makusudi kukamilisha haraka ujenzi wa jengo la makazi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa Dodoma. Naomba kulihakikisha Bunge lako Tukufu kwamba awamu ya kwanza ya ujenzi wa makazi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, yanayojumuisha nyumba na makazi ya Waziri Mkuu, ofisi binafsi na nyumba ya wageni imekwishakamilika na kukabidhiwa Serikalini tarehe 19 Februari 2016. Awamu ya pili ambayo itajumuisha ujenzi wa uzio, barabara, mandhari, nyumba za walinzi, wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu na uwekaji wa samani ikiwemo ujenzi wa barabara. Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.5 kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ulitolewa wito na Wabunge kadhaa ndani ya Bunge lako ya kwamba Serikali iboreshe huduma za malipo kwa wastaafu wakati wa kustaafu na kusiwe na mapungufu na kadhia nyingine kwa wastaafu wanapomaliza muda wao wa kazi. Hadi kufikia Juni 2015, idadi ya wastaafu wote kwa kila mfuko wa pensheni katika nchi yetu ya Tanzania wale ambao walikuwa wamekwishalipwa kupitia Hazina ilikuwa ni wastaafu 89,532. Aidha, utaratibu wa kuhakiki wastaafu kwa mifuko yote hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubaini mahali walipo na kama tayari mafao yao ya kustaafu wamekwishayapata. Serikali inaahidi kuendelea kusimamia zoezi la malipo ya pensheni kwa wastaafu kwa utaratibu unaotakikana mara kwa mara ili kupunguza kadhia ya hii kubwa wanayoipata wastaafu wetu katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, agizo lingine lilikuwa Serikali iweke utaratibu wa pensheni ya wazee wote hata wale ambao hawakuwa wakifanya kazi katika sekta rasmi. Agizo hili Serikali imelipokea na agizo hili limewekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika mwaka wa 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, rasimu ya andiko la Mpango wa Pensheni kwa Wazee wote na Watu Wenye Ulemavu imekwisha kukamilika. Hatua inayofuata kwa sasa ni ushirikishwaji wa wadau na taasisi zinazohusika na utekelezaji wa mpango huu ili mara tutakapokuwa tumekubaliana na wadau wote tuanze sasa kujipanga ndani ya Serikali na kulipa pensheni hii kwa wazee wetu kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi pia walishauri elimu ya hifadhi ya jamii itolewe ili watu wengi zaidi wajiunge na mifuko hiyo. Naomba niwahakikishe Waheshimiwa Wabunge kwamba wigo wa hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania umeendelea kupanuka ingawa siyo kwa speed kubwa. Mpaka sasa takribani asilimia 8.8 ya nguvu kazi ya Taifa imeshajiunga katika Hifadhi ya Jamii ingawa asilimia hiyo bado ni ndogo. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya mwaka 2008 ya SSRA kazi kubwa nyingine ambayo imekuwa sasa ikifanywa na SSRA ni kuhakikisha inachukua jukumu hilo la kuanza kutekeleza mpango mkakati wa kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii nchini yaaani Social Security Extention Strategy. Hii ni pamoja na kuweka mkakati wa mawasiliano yaani Social Security Communication Strategy kwa makundi mbalimbali kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili kufikia lengo hilo. Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba Watanzania wengi na hasa vijana waliopo katika sekta isiyo rasmi wanaingia katika mfumo huu wa pensheni ili kuweza kuwaandalia maisha yao ya baadaye kwa namna moja au nyingine.
Serikali iliwezesha Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi kushughulikia masuala ya wafanyabiashara wadogowadogo wakiwemo bodaboda, akina mama lishe na wajasiriamali. Sheria ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi ilitungwa mwaka 2004 na Sera ya Baraza hilo ilitolewa mwaka 2004. Kwa sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshazindua mpango mkakati wa utekelezaji wa kazi za Baraza hili lakini vilevile ameshazindua uanzaji wa utekelezaji wa shughuli hizi za Baraza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi Baraza limeshaanza kutengeneza programu kupitia NSSF na Baraza lenyewe na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa waendesha bodaboda katika SACCOS 16 za bodaboda katika Mikoa ya Dae es Salaam, Arusha, Mbeya, Dodoma, Kigoma, Tanga, Rukwa, Mara na Geita lakini kazi hii itaendelea katika mikoa mingine. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi anayesimamia sekta hii Dada Beng‟i Issa kwa kazi nzuri anayoifanya na jinsi alivyojipanga kuhakikisha anatusaidia kujibu tatizo la ajira kwa vijana kupitia mpango huu wa uwezeshaji wananchi kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kukuarifu kwamba kwa sasa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Tanzania, limeanza pia kutoa mafunzo maalum kabisa kwa vijana wetu wanaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa. Tunafahamu vijana wetu wengi pia wanajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa na wanapomaliza mafunzo yao wengi wamekuwa wakikosa kuajiriwa. Baraza limeshaanza kuwafundisha viongozi katika makambi mbalimbali ya Majeshi yetu ya Kujenga Taifai ili wanapowafundisha vijana wetu katika mafunzo ya kijeshi wawafundishe jinsi ya kuunda vikundi na kupatiwa mikopo ili waweze kujiajiri wao wenyewe. Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana viongozi wote wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini kwa ushirikiano mkubwa na jinsi walivyopokea wito huu wa kuwasaidia vijana wetu Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Baraza pia linasimamia mpango wa akiba na mikopo kupitia VICOBA na SACCOSS. Niendelee kuwaomba vijana wengi wajiunge kwenye mipango hiyo ya akiba na mikopo lakini na VICOBA ili tuanze kuwaweka katika mifumo ya kukopesheka na kuwasaidia kujiajiri na kuwaajiri wenzao pale wanapoanza kufanikiwa katika mipango tuliyojiwekea. (Makofi)
Mchango mwingine ulihusu miradi ya MIVARAF katika nchi yetu ya Tanzania. Mchango huu uliletwa na Mheshimiwa Edwin Ngonyani na Wabunge wengine. Naomba niwathibitishie kwamba mradi wa MIVARAF utafika katika maeneo yote ambayo yamekwishapangwa. Naomba niahidi mbele ya Bunge lako Tukufu tutawashirikisha Wabunge wote wanaohusika na mradi huu ili wajue miradi inayofanyika katika maeneo yao na watupe ushirikiano wa kuifuatilia na kuitizama inavyoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni hoja iliyotolewa na Kamati ya Mapambano dhidi ya UKIMWI, ikiomba Serikali kutenga fedha ya kutosha kwa Tume ya Kudhibiti UKIMWI na Dawa za Kulevya. Agizo hilo limezingatiwa na kama mlivyoona Serikali imeanza sasa kuweka fedha kwenye Mfuko Maalum wa kisheria katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Takribani Watanzania 670,000 kwa sasa wanaishi kwa kutumia dawa lakini waliopimwa na kugundulika wanaishi na Virusi vya UKIMWI, ni takribani Watanzania 1,500,000. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba tunafanya kazi ya kutosha katika eneo hilo. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa pia ni Wajumbe wa Kamati za UKIMWI katika Halmashauri zetu basi tushirikiane kuangalia fedha zinazotengwa katika eneo hilo zinatumika ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine iliyotolewa ni kuhusu tatizo la dawa za kulevya nchini, lilitolewa pia na Kamati hiyo hiyo ya UKIMWI. Kamati ilitutaka tuhakikishe kwamba tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunapambana na tatizo hili la dawa za kulevya nchini. Naomba niwathibitishie sheria tuliyoitunga mwaka 2015 imeanza kuchukua mkondo wake na tayari adhabu kali zimeanza kutolewa kwa wale wote ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania. Sheria imetoa adhabu kali sana kwa makosa ya kujihusisha na matumizi ya biashara hiyo ambayo ni kifungo cha maisha. Sheria hiyo pia imetoa adhabu kali kwa wale wote wanaowahusisha watoto katika suala zima la matumizi ya dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni kuhakikishia Serikali inahamishia Makao Makuu Dodoma na hasa kwa kutunga sheria. Naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kwamba sheria ya kuhamishia Makao Makuu ya nchi Dodoma imeshaandaliwa na imeshaanza kupita katika vikao vya kisheria vya kiutaratibu ili hatimaye tuilete katika Bunge lako Tukufu iweze kujadiliwa na kupitishwa. Tutashirikiana na Wabunge kuhakikisha kwamba zile kero ambazo zimekuwa zikitokea Dodoma kwa namna moja ama nyingine zinazohusu sheria basi zitarekebishwa kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Manaibu Waziri wangu wakijibu maswali, walizungumzia mambo mengi yanayohusu wafanyakazi, lakini vilevile yanayohusu walemavu, naomba niwathibitishie tumejipanga vizuri kukabiliana na changamoto zote za wafanyakazi katika nchi yetu ya Tanzania, kuboresha maisha yao, kuangalia sheria zile ambazo zimekuwa zikitumika kuwakandamiza katika maeneo ya kazi, tutazisimamia ili kuhakikisha sheria za kazi zinatekelezwa. Tumejipanga kuhakikisha kwamba suala zima la walemavu tunalipa kipaumbele katika Ofisi ya Waziri Mkuu, tutalisimamia na kutoa ushirikiano na hivyo kuhakikisha dhamira njema ya Serikali katika kuwajali na kuwahudumia walemavu katika nchi yetu ya Tanzania inafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamaliza kutoa majibu haya ya awali na kumpisha Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kumalizia majibu mengine yaliyobakia, nitumie nafasi hii kuwatakia wafanyakazi wote maandalizi mema ya sherehe za Mei Mosi ambazo zitafanyika Kitaifa katika Mkoa wa Dodoma. Sisi kama Serikali tunawahakikishia kwamba tupo pamoja nao, tutashirikiana nao na tutaendelea kufanya kazi nao kwa kuzingatia sheria na taratibu ili kuongeza tija na kukuza uchumi wa nchi yetu kama vile tunavyofahamu wafanyakazi ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, naomba kwa heshima na taadhima nichukue nafasi hii tena kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nikirudia kuanza na Wabunge Wajumbe wa Kamati zote mbili lakini na Wabunge wote waliochangia hapa ndani ya Ukumbi wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote na mimi naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuweza kutufikisha tena siku hii ya leo tukiwa wazima na salama. Ninakushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili niweze kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge kuhusu utendaji kazi wa Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa ni kiongozi mahiri, imara na shujaa katika kusimamia maendeleo ya nchi yetu. Naomba nichukue nafasi hii pia nimpongeze Makamu
wa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya na vilevile kwa nafasi ya pekee kabisa, nimpongeze sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwangu binafsi naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi anavyoniongoza, kwa jinsi anavyonisaidia kumsaidia kazi katika Ofisi yake. Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba nikushukuru sana. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mchapakazi, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni jembe hasa linalotosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwapongeza Viongozi Wakuu hao niliowataja, nichukue nafasi ya pekee nimpongeze sana Mheshimiwa Antony Peter Mavunde, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Mheshimiwa Antony Mavunde amekuwa ni msaada mkubwa sana katika kazi zangu, naomba nimshukuru sana. Kwa nafasi ya pekee nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Antony Mavunde kwa sababu leo amepata baby girl, first born wake, Mungu ampe maisha marefu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumkumbuka pia Balozi Dkt. Abdallah Possi ambaye alifanya kazi nzuri ya kunisaidia. Nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amekuwa ni mshirika wangu mkubwa katika kuhakikisha shughuli za Bunge na shughuli za Serikali zinakwenda vizuri. Siwezi kuendelea na majibu ya hoja za Waheshimiwa Wabunge bila kutambua mchango
mkubwa wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania linaloongozwa na Rais wao Ndugu Tumaini Nyamhokya na Katibu Mkuu, Dkt. Yahaya Msigwa, pamoja na Shirikisho la Waajiri Tanzania linaloongozwa na Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Almasi Maige na Mtendaji Mkuu Ndugu Aggrey Mlimuka, wamekuwa wakitupa ushirikiano mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini sio kwa umuhimu nawashukuru sana wapiga kura wa Jimbo la Peramiho, Hapa Kazi Tu, tutaendelea na mwaka 2020 ni mambo vilevile, Hapa Kazi Tu, ushindi kwa Chama cha Mapinduzi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu hoja hizi za Kamati nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Ndugu yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na Makamu wake, ndugu yetu Mheshimiwa Najma Giga, lakini na Wajumbe wa Kamati hiyo kwa ushurikiano mkubwa. Niwashukuru pia, Wajumbe wa Kamati ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile na Makamu wake Mheshimiwa Dkt. Tiisekwa na Wajumbe wote. Nichukue nafasi ya pekee kumshukuru sana dada yangu Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Ndugu yangu Mheshimiwa Josephat Kandege na Wajumbe wote kwa
ushirikiano mkubwa waliotupa.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee niwashukuru sana Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu Tanzania, vikingozwa na dada Ummy. Naomba nitambue mchango wa pekee wa Wabunge wawili ndani ya Bunge hili wenye ulemavu, dada yangu Mheshimiwa Stella Ikupa Alex na dada yangu Mheshimiwa Amina Mollel, wanafanya kazi nzuri sana na tunashirikiana nao vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge, Katibu wa Bunge na wafanyakazi wote wa Bunge kwa jinsi wanavyotusaidia ndani ya Serikali kutekeleza majukumu yetu hapa Bungeni sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 99(2) naomba sasa kwa heshima kubwa nitoe majumuisho ya hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Ninaomba kwanza hotuba yangu hii iingie yote kwenye Hansard, vilevile tutaleta kitabu cha majibu ya maswali ya
Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu muda ni mfupi hatutaweza kuyajibu yote. Kabla ya kujibu hoja naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Nsanzugwanko alisema sana hapa, tuendelee kama waratibu wa Serikali kuangalia kuleta maendeleo kwa kuzingatia uwiano wa mikoa yetu na jinsi maendeleo yalivyo ndani ya mikoa yetu. Kwa hiyo, ndani ya Serikali tutaangalia kwa sababu, lengo letu ni kuhakikisha Watanzania nchi nzima wanaendelea bila kujali ukabila wala ukanda wala nini, lakini ni lazima wote wapate maendeleo.
Mheshimiwa Spika, nitaanza na hoja ya Makao Makuu Dodoma. Kulikuwa na hoja nyingi zinazohusu Serikali kuhamia hapa Dodoma. Hii ilikuwa ni ndoto ya Marehemu Baba wa Taifa, lazima niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge. Tarehe 30 Agosti, 1973 mpaka tarehe 9 Septemba, 1973 Halmashauri Kuu ya chama cha TANU ambacho ni baba ni Chama cha Mapinduzi, iliketi Dar es Salaam na kuridhia kwamba Makao Makuu ya nchi yatakuwa Dodoma na mwaka1973 Chama cha TANU kiliamua na kupitisha maazimio hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa uhamiaji tunaohamia nao kwenye Serikali ya Awamu ya Tano, wote tunakumbuka kwamba, tarehe 23 Julai, 2016 Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa anahutubia kwa mara ya kwanza kwenye Mkutano wa CCM kama Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, aliwatangazia Watanzania kupitia Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Serikali ya Awamu ya Tano itahamia Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, Serikali hii imeshakwishakuhamia hapa Dodoma na tumehamia hapa watendaji wakuu wote, Mheshimiwa Waziri Mkuu akituongoza, Mawaziri, Naibu Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wote, Naibu Makatibu Wakuu wote na baadhi ya Watumishi ambao tumehamia nao hapa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wengi walifikiri hili ni suala la kisiasa na kuna watu wamechangia wanasema Serikali haina dhamira ya dhati. Naomba niwakumbushe huu ni utekelezaji wa Ibara ya 151 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, faida za kuhamia Dodoma, Wabunge wamechangia kuuliza ni zipi? Pamoja na kutusaidia kwamba Makao Makuu kuwa katikati ya nchi yetu, lakini tunaona kabisa kwamba Serikali itapunguza gharama kubwa sana za matumizi ya uendeshaji wa Serikali na hasa
inapokuwa vipindi vya Bunge, kuhamisha Serikali kutoka Dar es Salaam kuja kushughulika na shughuli za Bunge. Vilevile tutaenda kuchachua uchumi wa nchi kwa kuhakikisha kwamba tunatoa nafasi ya maeneo mengine kuendelea.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya kuleta Bungeni Sheria ya Makao Makuu, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kwamba mchakato wa maandalizi ya sheria hiyo uko tayari na mara tu tutakapokuwa tumefikia hatua ya mwisho tutaomba ridhaa yako na wewe
umetuagiza sana na umetuambia hapa hakieleweki mpaka sheria mwaka huu iingie Bungeni. Tupo tayari tutawasiliana na Ofisi yako na tutaleta sheria hii humu ndani. Mpaka sasa tunaendelea kuhamia Dodoma kwa kutumia GN Na. 230 ya mwaka 1973 na hiyo nayo ni tamko la kisheria la Serikali.
Mheshimiwa Spika, tulipokea hoja nyingine ya kuhakikisha kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza katika ujenzi wa viwanda kama ni tija na inaweza ikawa na faida gani. Kwanza niseme kabisa kwamba uwekezaji katika sera hii ya viwanda unatokana pia na mpango wetu wa
maendeleo wa miaka mitano. Hivyo basi, Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii imeamua kuwekeza kwenye miradi ya viwanda 25 yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 153 mpaka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulichokifanya kama Serikali ni kuhakikisha kwamba uwekezaji huo unakuwa na tija na tija ya kwanza utakwenda kuzalisha ajira za watoto wa Kitanzania 310,000 kwenye viwanda hivyo 25. Kwa hiyo, ni jambo la kupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vipo baadhi ya viwanda vimeshaanza kufanyakazi tutatoa orodha kwa Wabunge muda ni mfupi tungeweza kuvisoma hapa, Mheshimiwa Naibu Waziri ameweza kutaja baadhi ya viwanda hivyo. Tumesema pia viwanda hivyo vitasaidia pia kutengeneza soko la mazao yetu na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa pia na hoja kuhusu mradi wa MIVARF, huu ni mradi wa miundombinu ya masoko na uongezaji wa thamani na huduma za fedha vijijini. Mradi huu Waheshimiwa Wabunge pamoja na Kamati walitaka kujua maendeleo ya ujenzi wa ukarabati wa barabara na ukarabati wa masoko Pemba na Unguja. Mradi huu ulianza kufanyiwa kazi mwaka 2014 na ulikamilika katika maeneo kadhaa na hasa kwenye eneo la barabara mwaka 2015 kule Pemba na Unguja. Kwa sasa tunaendelea na mradi wa kukamilisha maeneo ya masoko. Jumla ya kilometa za barabara 148.5 zimejengwa na masoko manne makubwa yameweza kujengwa kule Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema mradi huu unazo faida nyingi na umekuwa ni mradi shirikishi, mradi huu umekuwa ni kichocheo kikubwa cha muonekano wa mashirikiano yetu ya Muungano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Ninaomba tu niseme kwamba pamoja na mafunzo yanayotolewa kwa wananchi, jamii kushirikishwa kuweza kubadilisha mfumo mzima wa uzalishaji mazao na masoko yao, nawapongeza Wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria na hasa Mheshimiwa Ally Saleh. Mheshimiwa Ally Saleh alikiri kabisa kwamba mradi huu ni kiashirio kizuri cha Muungano kati ya Tanzania Bara na Visiwani.
Mheshimiwa Spika, ninaomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono na mawazo ya Mheshimiwa Ally Saleh, lakini tujue kabisa kwamba Muungano wetu una faida kubwa na ni lazima tuendelee kuuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja iliyohusu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi. Mfuko huu umeanzishwa kwa Sheria Namba 20 ya mwaka 2008. Mfuko huu umeweka mfumo mzuri ambao ni wa kidijitali wa kuhakikisha kwamba taarifa zote zinazotokana na watu ama wafanyakazi
wanaopata ajali kazini zinapatikana kwa haraka na malipo kwa watu hao wanaopata ajali kazini yanafanyika kwa haraka. Sheria hii iliyoanzisha huu mfuko imeweza kuwakomboa wafanyakazi wengi sana katika nchi yetu ya Tanzania na tunategemea itafanya kazi nzuri ya kutoa fidia
kwa magonjwa, vifo na ajali zinazotokea maeneo ya kazi.
Mheshimiwa Spika, Wabunge walitaka kujua kazi zilizofanywa mpaka sasa. Mpaka sasa tumeshafundisha madaktari kama 359 nchini ambao wamepewa uwezo wa kubaini magonjwa na namna ya kutathmini athari na ulemavu unaotokana na ajali kazini. Kwa hiyo, naomba
niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa kazi za mfuko huu kwa kuwa sasa zimeshaanza basi malalamiko ya wafanyakazi katika sekta ambazo zimeainishwa kwenye mfuko na Sheria ya Mfuko hatutakuwa tena matatizo ya kutoa fidia kwa wafanyakazi wote nchini. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge mtusaidie kuwaeleza taasisi mbalimbali ambazo zinawaajiri katika maeneo yenu ili watambue sasa tuna mfuko huu wa fidia kwa wafanyakazi ambao umeshaanza kutoa fidia kwa wafanyakazi na wajisajili waajiri wote.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja pia mfuko wa fidia kwa wafanyazi uzingatie sera na miongozo ya uwekezaji. Naomba nilihakikishie Bunge lako kwamba agizo hilo linasimamiwa vizuri na Serikali, vilevile linasimamiwa vizuri na SSRA ambaye ni mdhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii pamoja na Benki Kuu ambao ndio wamepewa kazi ya kusimamia uendeshaji na uwekezaji unaofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja pia mfuko huu wa fidia kwa wafanyakazi uchukue jitihada za kutosha katika kupambana na kudhibiti mianya yote ya rushwa. Naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba mfuko unazingatia maagizo ya Serikali na umeweza kuweka miongozo ambayo inaongozwa na sheria iliyoanzishwa ya mapambano dhidi ya rushwa katika nchi yetu ya Tanzania hivyo, mfuko
unaendelea kutekeleza agizo hilo vizuri.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni kuboresha kiwanda cha Mpigachapa Mkuu wa Serikali na Waheshimiwa Wabunge na Kamati walituagiza tuhakikishe kwamba tunaboresha mazingira ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kazi hiyo tuliianza kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 na tulitenga fedha za Kitanzania milioni 150 za kuanza mchakato wa zoezi hilo. Fedha hizo zimetumika mpaka sasa kumuweka Mshauri Elekezi ambayo ni Taasisi ya Viwanda na Ujenzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wao wameshaanza utafiti wa awali wa kuweza kuboresha Ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali na Kiwanda chetu cha Uchapaji cha Serikali. Tayari taarifa ya awali tumeshaipokea na mwishoni mwa mwezi Aprili tutapokea taarifa kamili ya jinsi tunavyoweza kufanya kazi hiyo vizuri.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshafanya mazungumzo na Benki ya Rasilimali (TIB) kuona ni namna gani wanaweza kutusaidia fedha sasa za kuweza kujenga kiwanda kipya kizuri, kikubwa hapa Dodoma ili kuweza kusaidia shughuli hizo za Mpigachapa Mkuu wa Serikali. Tayari tumeshapata kiwanja na tumeshakilipia na umiliki wa kiwanja hicho umeshahamia kwenye Serikali tayari kwa kuanza kazi hiyo mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala Sheria ya Maafa, tuliagizwa Serikali kupitia Sheria ya Maafa nchini, naomba niwaambie na niliarifu Bunge lako tukufu kwamba tayari Bunge lilishatunga Sheria ya Usimamizi wa Maafa Namba 7 ya mwaka 2015. Aidha, Kanuni za utekelezaji wa sheria hii zimeshakamilishwa na zinangoja tu muda ufike ili ziweze kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali na ziweze kutumika inavyotikiwa.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya kutoka Kambi ya Upinzani kwamba kumekuwa na ukimya kuhusu matumizi ya fedha zilizokusanywa wakati wa tetemeko la ardhi na pendekezo la kumwagiza CAG kufanya ukaguzi maalum wa matumizi ya fedha hizo. Ofisi ya Waziri Mkuu ilishaunda kikosi kazi maalum ili kufanya ukaguzi kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa alipofanya ziara Mkoani Kagera tarehe 2 Januari, 2017. Jambo hili lilishaagizwa na Rais na tulishaanza kulitekeleza, kwa hiyo nadhani tutaendelea na maagizo yale Mheshimiwa Rais aliyokwishakuyatoa na tutaendelea kuyatekeleza. Hata hivyo, zipo kazi nzuri ambazo zimeshafanywa katika kurudisha miundombinu na hasa ya taasisi za Serikali kule Kagera.
Mfano mzuri ni ujenzi wa shule ya Ihungo, pia tumeboresha kwa kiasi kikubwa zahanati ya Ishozi na imeboreshwa vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeboresha sana makazi ya wazee ya Kilima na vilevile tumeshatoa fedha za Kitanzania zisizopungua bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule ya sekondari ya Nyakato. Kwa hiyo, nimuombe sana na kumshawishi tu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni aliyetoa hoja hii atembelee shule hizo na maeneo hayo ataona kazi nzuri iliyokwisha kufanyika mpaka sasa.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya Serikali kudhibiti Wabunge wa Upinzani wawapo Bungeni. Naomba niseme kwamba Serikali haina uwezo wa kufanya udhibiti wowote wa Wabunge wa Upinzani wawapo Bungeni ama hata Wabunge wa Kambi ya Chama Tawala. Majukumu ya Bunge yametajwa katika Ibara ya 84 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Uendeshwaji wa shughuli za Bunge unaongozwa na Kanuni za Bunge na pale maamuzi yanapokuwa hayamridhishi Mbunge yeyote, Kanuni za Bunge zinamruhusu Mbunge huyo kuchukua hatua zaidi kwa mujibu wa Kanuni. Kwa hiyo, ninaomba nilithibitishie Bunge lako kuwa Serikali haina mkono wowote wa kumkandamiza Mbunge yeyote.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja Serikali kutimiza ahadi ya milioni 50 nadhani Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameijibu vizuri sana leo hapa ndani asubuhi. Ofisi ya Waziri Mkuu tunaendelea na maandalizi ya pensheni kwa wazee, tumeshakamilisha documents zote na taratibu sasa za kuwasilisha maandiko yetu katika vikao vya maamuzi Serikalini yanaendelea ili hatimaye tuweze kutekeleza Ilani ya Uchaguzi Ibara ya 165(e) kuhusu pensheni kwa wazee.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya kutuuliza tumefikia wapi kuunganisha mifuko ya pensheni. Tumeshafika hatua nzuri, tathmini imefanyika, andiko la mapendekezo ya kuunganisha mifuko limeshaboreshwa na tunasubiri maamuzi ya Serikali. Tutaendelea kutoa fedha kwenye Mfuko wa UKIMWI lakini vilevile tutaendelea kutoa fedha za kutosha ili Mamlaka ya Kupambana Dawa za Kulevya nchini iweze
kufanya kazi zake vizuri. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge mapambano dhidi ya UKIMWI na dawa za kulevya ni ya kwetu wote pamoja na ninaomba tushirikiane kwa pamoja kama Watanzania ili kupiga vita dawa za kulevya na UKIMWI.
Mheshimiwa Spika, pia tulipewa ushauri kuhusu kuboresha mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa ahadi za Serikali za viongozi na Ilani ya Uchaguzi. Tumepokea ushauri huo na mfumo huu siku moja tutakuja kuwaonesha watatuunga mkono na watatusaidia ili kazi hii ifanyike sawa
sawa.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa pia na hoja ya kuhakikisha kwamba Serikali inashughulikia tatizo la fao la kujitoa. Naomba tu niwambie Waheshimiwa Wabunge katika mafao ambayo yanaorodheshwa kama ni mafao yatolewayo kwenye sekta ya hifadhi ya jamii fao la kujitoa
halipo. Ibara ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatueleza na inatupa mwongozo wa jinsi ya kuwakinga Watanzania na hasa siku za uzee na majanga yoyote yanayoweza kuwapata. Hata hivyo, kulingana na mabadiliko ya uchumi na Sera ya Hifadhi ya Jamii ibara ya 3(8) inatupa mwongozo wa kushughulikia namna nzuri ya kuona ni namna gani tunaweza kuwakinga Watanzania wanaokosa kazi ili waweze kumudu maisha yao. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tumeanza mazungumzo na Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi nchini na hivyo basi tunataka tumalize mzizi wa fitna wa fao la kujitoa ili wafanyakazi waweze kufanya kazi zao wakiwa na amani na suala la fao la kujitoa isijekuwa ni ajenda tena ya kuwasumbua katika shughuli na mifumo yao mbalimbali ya ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kusema kwamba kwa sababu muda wangu umepita, ninaiunga mkono sana hoja hii na ninaomba Waheshimiwa Wabunge tuiunge mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa sababu mafanikio haya yote ambayo yamekuwa yakionekana dhahiri ni mafanikio ambayo yamekuwa yakiratibiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu na ndugu yetu Kassim Majaliwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba niwahakikishie Wabunge tutaendelea kuheshimu michango na ushauri wao na Serikali tupo tayari kufanya kazi kwa weledi mkubwa na uaminifu mkubwa kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele kwa maendeleo, Hapa Kazi Tu, hatutalala na hivyo basi tunaamini baada ya miaka mitano tutakuwa tumepiga hatua ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naona kengele karibu inagonga, naomba niunge mkono hoja hii, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, na mimi naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini mimi pamoja na Naibu wangu, Mheshimiwa Antony Mavunde lakini vilevile kwa kututeulia Mheshimiwa Stella Ikupa, jembe la nguvu kushirikiana na sisi katika kuhakikisha kwamba tunamsaidia Mheshimiwa Rais katika majukumu aliyotupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa ni kielelezo cha utendaji bora wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kusimamia majukumu makubwa ambayo hayataki mtu aambiwe aone kazi inayofanywa na Serikali hii. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pia kwa kutulea vizuri sisi Mawaziri ambao tupo katika Ofisi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu nakutakia kila la kheri na hasa pale unaposhughulika na maswali ya Waziri Mkuu hapa Bungeni umeonyesha kabisa kwamba wewe ni kiongozi wetu Mawaziri wote. Nakushukuru na nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Dkt. Mpango. Dkt. Mpango naomba nikuthibitishie usikate tamaa. Wanaouponda Mpango wako wana ajenda binafsi. Dkt. Mpango chukua mawazo mazuri ya Wabunge waliotushauri sisi kwa pamoja kama Serikali, Mawaziri wote pamoja na wewe lakini yale mawazo ambayo kwa dhahiri unaona yanaponda Mpango wako kwa nia ovu achana nayo. Hasa Wabunge wa CCM wamechangia mawazo mazuri sana kwenye Mpango wa Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji hapa wanasema Serikali yetu inakurupuka tu, inakuja hapa haijajipanga, haifanyi utafiti na inapanga mipango tu ambayo haieleweki. Naomba niwaambie hao wanaosema hivyo hawajasoma Mpango wala hawajaangalia mwongozo ulioletwa pamoja Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye sekta moja tu ya ajira, hivi unafikiaje mahali pa kujua hitaji la ajira katika nchi yetu ya Tanzania bila kufanya utafiti na kutengeneza mpango. Leo nitawaambia, Serikali yetu inafanya utafiti na ndio inakuja na mwongozo na inakuja mpango. Kwa mfano, sisi tumeshafanya utafiti wa kujua nguvu kazi iliyopo katika nchi yetu ya Tanzania ni idadi gani ya Watanzania na fedha za utafiti zimetolewa na Mheshimiwa Dkt. Mpango ili awe na mpango mzuri wa ajira katika nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utafiti huo tumegundua Watanzania milioni 25 ndiyo nguvu kazi ya nchi yetu ya Tanzania na tunapozungumzia viwanda hawa milioni 25 ndiyo watakaokwenda kuchukua ajira kwenye viwanda hivyo ambavyo vitajengwa kwenye nchi yetu ya Tanzania. Nani anasema Serikali hii inakuja na mipango bila kufanya utafiti, tunafanya utafiti. Katika hiyo milioni 25 tumegundua asilimia 56 ni vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumefanya utafiti mwingine, sasa kama tunataka kushughulikia tatizo la ajira, hivi ukosefu wa ajira kwa vijana katika nchi yetu ya Tanzania ukoje. Tumegundua kwamba ukosefu wa ajira kwa vijana kwenye nchi yetu ya Tanzania unazidi kupungua, ulikuwa asilimia 11.7 sasa hivi ni asilimia 10.3 na ni kwa sababu ya mipango mizuri ya Serikali na sekta nyingi za uzalishaji zinavyoongezeka na upungufu wa ajira unazidi kupungua. Hiyo ndiyo mipango inayogharamiwa na Waziri wa Fedha na Mipango katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumegundua sekta ya kilimo ndiyo inayoongeza katika kutoa ajira nyingi kwenye nchi yetu ya Tanzania na tumegundua asilimia 60.7 kilimo kinaongoza katika kutoa ajira. Sasa tunapofanya hivi ndipo tunapowaambia Watanzania baada ya utafiti huo tumemwagiza Mheshimiwa Mwijage aanzishe viwanda lakini viwanda vitakavyotumia malighafi ya kilimo inayolimwa ndani ya nchi ya Tanzania ili tutatue tatizo la ajira kwa vijana wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema Mheshimiwa Mwijage kwa kushirikiana na sekta hizo nyingine zote za umeme, maji na kadhalika atusaidie kutengeneza sera za viwanda unazozizungumza wewe Mheshimiwa Mwenyekiti iwe ni hospitali, gereji au kitu chochote, hivyo vyote ni viwanda vinatofautiana ukubwa na mazingira. Akifanya hivyo viwanda hivi vitazalisha bidhaa ambazo ndizo zinazohitajika zaidi katika soko la Watanzania hapa nchini na hivyo mwisho wa siku tutakuwa tumeweza kutatua tatizo la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tumeshafanya nini? Ili kuhakikisha vijana wa Tanzania wanaajiriwa, tumetengeneza programu maalum ya kukuza ujuzi katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitasema mafanikio yaliyopatikana, kwa kutumia Mpango huu wanaouponda wa Mheshimiwa Mpango tumefanya yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, tumetambua na kurasimisha ujuzi wa vijana wa Tanzania mpaka sasa 3,900 wameshamaliza mafunzo ya ujuzi katika nchi yetu, 3,440 wanaendelea na mafunzo na vijana 13,432 tumeshawatambua wanasubiri tuwafundishe. Sasa nani anayesimama hapa na anasema eti huu mpango fake wakati unajibu mahitaji ya Watanzania. Hawa vijana ambao tumewapa ujuzi wengine wanatoka mpaka kwenye Majimbo ya wapinzani, watawashangaa Wabunge wao kama hawaungi mkono Mpango huu ambao umewapa ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao graduates wengi katika nchi yetu ya Tanzania lakini wamekosa mafunzo ya vitendo ya kukuza ujuzi wao. Tumeshatengeneza programu ya internship ya kuwasaidia vijana wa Kitanzania wakapate uzoefu na inalipiwa na Serikali kwa fedha za Mheshimiwa Mpango Waziri wa Fedha. Vijana 2,122 wameshaomba na Serikali inawapangia utaratibu wa kwenda kwenye mafunzo ya vitendo, hela yote inatolewa na Mpango na iko kwenye Mpango wetu. Nataka kuwaambia Watanzania kwamba tunafanya kazi na Serikali yetu inafanya kazi sana tena kwa kupitia Mpango ambao unaletwa na Mheshimiwa Mpango ndani ya Bunge la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni machache tu ningeweza kusema mengi, lakini muda tu hauniruhusu. Napenda sana nizungumze jambo lingine hapa kuhusu mwenendo wa shughuli za Bunge. Wabunge hapa na hasa Wabunge wa Upinzani wamelidhalilisha sana Bunge lako eti Bunge hili halifanyi kazi yake sawa sawa, linaingiliwa na Serikali na halina tija yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, Ibara ya 62 na nakupongeza sana wewe, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge, ndiyo iliyokuweka wewe na Bunge lako hili Tukufu na sio mtu. Hata hivyo, unapimaje tija ya Bunge, hupimi tija ya Bunge kwa kelele nyingi ndani ya Bunge, hupimi tija ya Bunge kwa kuleta fujo na kupambana na askari ndani ya Bunge, hapana. Hupimi tija ya Bunge eti kwa kufunga midomo ndani ya Bunge kwa plasta na kuvaa nguo nyeusi, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri nakuongezea muda, kwa hiyo, endelea vizuri, endelea Mheshimiwa Waziri. (Makofi/ Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba niseme unapima tija ya Bunge kwa namna Bunge linavyoongoza shughuli za Bunge na shughuli zinazojadiliwa ndani ya Bunge zina manufaa kwa kiasi gani kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nani Mbunge hapa atakayesimama ambaye hatashukuru na kupongeza kazi kubwa iliyofanywa na Wabunge wa Bunge la Kumi na Moja? Niwaombe Wabunge wenzangu na hasa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, bebeni ajenda ya mafanikio makubwa ya Bunge letu ndiyo itakayotuvusha mwaka 2020. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mifano, wewe mwenyewe umedhihirisha kwa mifano dhahiri kabisa kwamba Bunge hili limefanya kazi itakayokumbukwa na vizazi vyote katika nchi ya Tanzania. Umeunda Kamati hapa kwenye Bunge hilihili la Kumi na Moja ambayo imeweza kuisaidia Serikali kuweka mfumo wa kupata faida ya nchi kwenye madini ya vito katika nchi yetu ya Tanzania. Leo hii Mbunge anapata wapi courage na kusema Bunge hili halifai, halijawa na mvuto, halifanyi kazi zake linavyotakiwa! Mbunge gani huyo? Leo nitawaeleza Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako hili limeweka historia ya kutunga sheria ya kuhifadhi maliasili za nchi yetu ya Tanzania, ni Bunge hili la Kumi na Moja chini ya uongozi wako Mheshimiwa Job Ndugai na siyo mtu mwingine yeyote. Leo hii Wabunge wanapata wapi courage ya kulibeza Bunge hili badala ya kujisifia na kwamba ni kazi nzuri tuliyoifanya ambayo pia inaendana mipango mizuri ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili limetunga sheria ya Msaada wa Sheria kwa Watanzania watakaohitaji kusaidiwa kwenye masuala ya sheria hata wanyonge kwenye maeneo ya vijijini, ni Bunge hili la Kumi na Moja. Nimesema Waheshimiwa Wabunge wenzangu tabia ya kulibeza Bunge letu na mwenendo mzima wa Bunge siyo tabia njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitamalizia la mwisho kwa ufupi sana, wakati tunachangia humu ndani na hasa Kiongozi wa Upinzani alipokuwa anachangia humu ndani alitaka kupotosha umma na kutaka kuyajadili madaraka ya Mheshimiwa Rais ya uteuzi wa viongozi eti kwamba anafanya uteuzi huo kwa upendeleo, hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 36(1), (2), (3) na (4) inatoa mamlaka kwa Rais kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara hiyo haisemi Rais atakapokuwa anafanya uteuzi eti aangalie ukanda, haisemi hivyo Ibara yetu kwenye Katiba. Ibara hiyo haisemi Rais anavyoandaa na kufanya uteuzi aangalie makabila mbalimbali kwenye nchi ya Tanzania, haisemi hivyo hiyo Ibara. Ibara hii haisemi Rais atakapokuwa anafanya uteuzi eti aangalie rangi ya Mtanzania, haisemi hivyo. Unasimamaje ndani ya Bunge kuhoji uteuzi wa Mheshimiwa Rais wa nafasi ambazo amepewa Kikatiba, ni upotoshaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme unaona wateule wa Mheshimiwa Rais wanafanya kazi vizuri. Ameteuliwa hapa Mheshimiwa Mwanri kutoka Siha na ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, anafanya kazi nzuri sana. Ameteuliwa Mheshimiwa Mnyeti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, anafanya kazi vizuri sana. Ameteuliwa hapa Mama yetu, Mama Anne Kilango jembe la nguvu kutoka Same anafanya kazi nzuri sana. Nina orodha ndefu nikiisema hapa ni ndefu kweli, lakini uteuzi huo unafuata madaraka ya kikatiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana Wabunge wenzangu tusiingilie madaraka ya Rais aliyopewa kwa mujibu wa katiba. Anayafanya kwa utashi wa hali ya juu na ukiangalia Ibara ya 34 inamtaka ateue watu watakaowajibika kumsaidia kubeba dhamana kwa niaba yake yeye mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniongezea muda na baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja iliyopo mbele yetu asilimia mia moja, nakushukuru sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JENISTA J. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hoja. Pili, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri, nazidi kuwaombea mafanikio katika utekelzaji wa majukumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbusha Mheshimiwa Waziri Halmashauri ya Wilaya Songea imeleta muda mrefu sana maombi ya gari la chanjo. Tafadhali sana Serikali itusaidie.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Ubaharia wa Shirika la Kazi Duniani na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Vitambulisho vya Mabaharia Na. 185 wa Mwaka 2003 wa Shirika la Kazi Duniani
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu
Spika, naomba kwanza kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, niwashukuru sana Wabunge wote waliochangia, wote wameunga mkono hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuunga mkono hoja yetu ya leo humu ndani Bunge tunaendana pia na kilio cha Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), lakini na Vyama vya Wafanyakazi ambavyo vimekuwa vikisimamia sekta ya mabaharia nchini, wamekuwa wakililia sana jambo hili Bunge letu Tukufu liweze kuridhia na hivyo leo wanavyotusikia kwa pamoja, ninaposema kwa pamoja , ukisikiliza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni leo wameunga mkono Maazimio yote haya mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nichukue nafasi hii kumpongeza sana Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa sababu si kwamba kila jambo jema linalofanywa na Serikali ni lazima kupinga, mambo yanayofanywa na Serikali kama ni jambo jema lina faida kwa Watanzania, Kambi Rasmi ya Upinzani inapounga mkono huu ndio uungwana na huu ndio mwenendo mzuri wa uwakilishi wetu ndani ya Bunge kwa kuhakikisha kwamba tunawawakilisha Watanzania wote. Namshukuru sana Mheshimiwa Mtolea kwa kuliona jambo hili ni la msingi kwa manufaa ya Watanzania wote na kuunga mkono hoja yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria na Kamati nzima. Wamefanya kazi kubwa sana, Kamati hii na kwa namna ya ajabu kamati ilianza kukutana na wadau mbalimbali, iliamua kuchukua hatua ya kujielimisha kwa kina namna nzuri ya kuendana na hoja ambayo Serikali ilikuwa imeipeleka kwenye Kamati, kwa kweli naomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu niishukuru sana Kamati na maoni yao yote tunayachukua na tutayazingatia katika kutekeleza mkataba wenyewe baada ya kuridhiwa na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nizungumze kidogo kuhusu maoni ya Kambi ya Upinzani; Kambi ya Upinzani wao wamesema kwamba ni kwa nini tunachelewa kuleta mikataba ndani ya Bunge ili iweze kuridhiwa. Kama Serikali ni lazima baada ya kusainiwa kwa mikataba ni lazima Serikali tufanye kwanza tafiti za kina tujiridhishe kabla ya kuridhia kweli mikataba hiyo inaendana na hali halisi ya mazingira katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tujiridhishe, tufanye tafiti za kutosha, tuangalie sera tulizonazo katika nchi yetu, tuangalie uzoefu wa Mataifa ambayo wamekwisha kuridhia, tuone changamoto ambazo wenzetu wanazipata, kusudi sisi tunapokuja kufanya kazi ya uridhiaji angalau tuone tuko kwenye position ya kujihakikishia kwamba hatutakuwa na shida ya utekelezaji wa mkataba wenyewe ndani ya nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimtoe hofu Mheshimiwa Mtolea kwamba, tunafanya hiyo kwa nia njema na sio kwamba tunachelewesha kwa makusudi hapana. Tumekuwa tuna uzoefu baadhi ya mikataba ukiangalia unakuta inakinzana kwa namna moja ama nyingine na mazingira halisi ya utendaji wa kazi na usimamizi wa shughuli mbalimbali za kisheria na za kisera ndani ya nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, tutakuwa tunajitahidi kufanya tafiti za kutosha na tunapokwenda kuridhia mikataba tunaridhia tukiwa na uhakika Watanzania watanufaika na kila kila kitu tutakachokiridhia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kaka yangu Salum Rehani, Mheshimiwa Mbunge amezungumza sana masuala ya leseni kwenye vyombo vyetu vya majini na namna gani pia mabaharia wetu wanaofanya kazi kwenye vyombo vya majini wanavyokosa mikataba ya ajira na mambo mengine ambayo yangeweza kuwapa haki stahiki kama wafanyakazi katika vyombo vya majini. Naomba nimhakikishie kwamba kwa kuridhia mkataba huu kwanza tutakwenda kuweka mfumo mzuri ambao utawasaidia sana Mabaharia kutambulika ndani na nje ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mabaharia wetu wengi ambao walikuwa wanapata ajira kwenye vyombo vya usafiri na hasa vyombo vya nje walikuwa wanadharauriwa sana, hawakuwa wakipata haki, walikuwa hawatambuliki Kimataifa, kwa hiyo, walikuwa wanapata shida sana. Hata hivyo, mkataba huu sasa unatupa sisi nafasi ya kuzitazama sheria tulizonazo ili kuwafanya Mabaharia wetu wanapopata vile vitambulisho sasa waweze kutambulika hata kwenye medani za Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wale Mabaharia wanaofanya kazi ndani ya nchi yetu ya Tanzania kwa kutumia vyombo tulivyonavyo ndani ya nchi yetu ya Tanzania na sheria tulizonazo, tutaendelea kusimamia. Namhakikishia Mheshimiwa Salum Rehani kwamba, sasa tumepata nguvu mpya ya kuhakikisha kuwa tasnia hii ya kazi ya Mabaharia inakuwa ni kazi yenye staha, yenye heshima na inayotoa fursa kwa vijana wa Tanzania kujiajiri na kuajiriwa na kupata haki na stahiki sawa ndani na nje ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana umeunga mkono na wewe na umeona jambo lenyewe lina msingi kwa hiyo naomba nimshukuru kwa kuliona hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kaka Mheshimiwa Machano ametukumbusha IMO ni muhimu na hasa sisi upande wa Bara, tuwe tunashiriki, namhakikishia kwamba tutaendelea kufuatilia vikao hivyo na kushiriki kwa manufaa ya nchi yetu. Hata hivyo, ametukumbusha pia kwamba kumekuwa na shida ya usajili wa meli na tozo ambazo zimekuwa zikitolewa wakati wa usajili wa meli na amefurahi sana mkataba huu sasa utakwenda kutatua matatizo mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kwamba baada ya kuridhia tutakwenda kukaa ndani ya Serikali, chombo kimoja na kingine kinachohusika na mkataba huu ni lazima huko mbele tutakwenda kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali ili kuhakikisha kwamba mkataba unaendana na sheria tulizonazo ndani ya nchi yetu ya Tanzania. Nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge, tutatoa fursa nyingi kwa vijana wa Tanzania na kupata ajira za ubaharia katika vyombo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Pia nakubaliana na yeye, kwamba tunavyo vyuo vinavyofundisha tasnia ya ubaharia bara na visiwani katika nchi yetu na ni vyuo vizuri, vinatoa Mabaharia wazuri na wamekuwa wakitambulika ndani na nje ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba huu unatuimarisha kwa sababu unatoa fursa ya kupata utaalam kutoka nje ukaletwa tena na kwenye vyuo vyetu vya ndani na kuwafanya mabaharia wetu waweze kubobea katika medani za ndani na nje ya Tanzania. Kwa hiyo, mkataba huu kwa kweli ni mzuri sana na utatoa fursa nzuri sana kwa Mabaharia wetu na vijana wetu wa Tanzania wanaotaka kufanya kazi kwenye tasnia hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa dada Taska amepongeza vijana wengi sasa angalau ajira zao zitakuwa za staha na zitaweza kutambulika vizuri, nakubaliana na yeye. Ametoa hapa rai kwamba ni lazima tuangalie sheria za usajili wa meli na vitu vya namna hiyo. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Taska kwamba, Serikali inalichukua kwa sababu ni suala ambalo litabidi lifanyiwe mazungumzo ya pande zote mbili za Muungano. Tutaendelea kujadiliana na kuona namna nzuri ya kurekebisha utaratibu na mifumo yetu ili pande zote mbili za Muungano ziweze kufaidika na mkataba huu, lakini na sheria zote ambazo zinasimamia masuala yote ya usajili wa meli lakini na masuala ya ajira kwa vijana wetu kwenye tasnia hii ya ubaharia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Shangazi amezungumza hapa kwa urefu na amesema tumechelewa. Ni kweli tumechelewa lakini tumechelewa kwa makusudi maalum nimesema hapo mwanzo na lengo letu lilikuwa ni kujiridhisha kile tunachoenda kufanya kama kweli kitaendana na hali halisi ya mazingira katika nchi yetu ya Tanzania lakini kitakuwa na tija kwa Watanzania ambao wameingia kwenye tasnia hiyo ya ubaharia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ametukumbusha hapa kwamba ni lazima tuangalie tunalinda mipaka yetu kwa sababu kuna vyombo ambavyo vingine vimesajiliwa na vitatakiwa kuendeshwa na mabaharia lakini viko katika maji ya maziwa kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, ametukumbusha ni lazima tuhakikishe vinasajiliwa kwa sheria tulizonazo kuepusha ajali na usalama wa abiria, vilevile mabaharia wanaoendesha vyombo hivyo waweze kuwa na viwango vinavyotambulika. Naomba nimwambie Mheshimiwa Shangazi kwamba, tunalichukua hilo na tutalizingatia kwa sababu hata mkataba wenyewe ndio unatutaka tufanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Shangazi ametuambia kwamba ni lazima tuangalie fursa nzuri za kuwatambua Mabaharia tulionao katika nchi yetu Kitaifa na Kimataifa na tuwe na data maalum ya kufanya hivyo, mkataba unatuagiza kuandaa database ya kuwatambua Mabaharia wetu. Kwa hiyo, tutafanya hivyo na tutaweka mfumo na mkataba umetuelekeza Nchi Mwanachama atakayeridhia ni lazima afungue database ya kuwatambua Mabaharia wote. Hiyo pia itatusaidia kuondoa nafasi za kuwepo na Mabaharia ambao watajiingiza katika masuala mengine kama ya uharamia na vitu vingine vya ugaidi na kahdalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo namwambia Mheshimiwa Shangazi tutayazingatia hayo maoni aliyoyasema. Nakumbuka aliyazungumza sana wakati wa Kamati nikiwa pale na naomba tu kumhakikishia kwamba tunayachukua na tutayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mtolea amezungumza kwamba tuangalie ni namna gani tunawasaidia wavuvi katika kupata hivi vitambulisho. Naomba tu niliambie Bunge lako Tukufu kwamba, vitambulisho hivi kwanza ni kwa ajili ya Mabaharia lakini wavuvi nao hawakatazwi kusomea ubaharia katika vyuo vyetu na wao wakapata vitambulisho hivi na wakaweza kufaidika na mkataba huu lakini tasnia ya ubaharia katika nchi yetu. Vile vile ametuagiza na ametuomba tuharakishe sana kuona sheria zetu tulizonazo zinaweza kuendana sambamba vipi na mikataba hii tuliyoridhia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu, kama nilivyosema mwanzo wakati nawasilisha, tayari tunazo sheria kwa pande zote mbili Bara na Visiwani. Vilevile tunayo nafasi nyingine nzuri baada ya uridhiaji na kuwasilisha hati ILO tukaangalia pia je, sheria hizi sasa zinaendelea kuwa rafiki kwenye mikataba hii? Kama hazionyeshi kuwa rafiki basi Bunge hili tutakuja kwenu tutashirikiana na nyie. Lengo letu siku ya mwisho ni kuwafanya Watanzania waweze kunufaika na kufaidi fursa hii muhimu ya kazi za staha kwenye tasnia hii ya ubaharia ndani na nje ya nchi ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Baada ya kusema hivyo, naomba sasa kutoa hoja Maazimio haya ya Bunge yote mawili kwa pamoja yaweze kuridhiwa na Bunge lako Tukufu ili yaweze kuendelea na hatua nyingine zinazostahiki kwa manufaa ya nchi yetu na kwa manufaa ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuweza kutufikisha siku hii ya leo ambapo tunapata nafasi ya kuhitimisha hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya bajeti ya Ofisi yake lakini vilevile na Mfuko wa Bunge kwa bajeti ya mwaka 2018/2019 na baada ya kupitia pia utendaji kazi wa Serikali katika ofisi hii kwa mwaka wa fedha uliopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nasema hivyo kwa sababu Watanzania wamempambanua Mheshimiwa Rais wetu kama kiongozi mahiri, imara, shupavu na ni mzalendo wa kweli kabisa ambaye amedhamiria kusimamia maendeleo ya nchi yetu na kufanya mageuzi ya kisasa katika kuleta maendeleo ya Taifa la Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja naye nimpongeze sana Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na vilevile nimpongeze sana Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ally Mohamed Shein. Hawa wote wanafanya kazi nzuri sana katika kujenga Taifa letu, kudumisha Muungano na kuhakikisha kwamba misingi iliyojengwa na Waasisi wa Taifa hili inaendelea kufuatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya pekee nimshukuru sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo na maelekezo ambayo amekuwa akinipatia mimi pamoja na watendaji wote wa Ofisi yake ili kuhakikisha kwamba tunachapa kazi na tunatekeleza maagizo ambayo tumekuwa tukiyapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu ni mchapa kazi na kiongozi mahiri na hiyo ameweza kujipambanua kabisa katika shughuli zake za Serikali ndani na nje ya Bunge. Tumwombee kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kumjalia afya njema ya kutekeleza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwapongeza hao niliowasema lakini kwa dhati nimpongeze sana Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde na Mheshimiwa Stella Alex Ikupa, Naibu Mawaziri katika Ofisi yangu. Hawa wamekuwa ni wasaidizi wangu wa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niwashukuru sana Bi. Maimuna Tarishi, Bw. Erick Shitindi, Profesa Faustine Kamuzora pamoja na Wakuu wa Taasisi zote, Wakurugenzi na wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo tumepeana ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sina fadhila kama sitamshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu Spika, Katibu wa Bunge, wafanyakazi wote wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi nzuri ambazo wamekuwa wakizifanya katika Bunge hili na hasa kutusaidia sisi Ofisi ya Waziri Mkuu kama waratibu wa shughuli za Bunge kuweza kutekeleza majukumu ya Serikali ipasavyo ndani ya Bunge lako. Shukrani zangu za dhati pia ziwaendee Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge ndani ya Bunge letu na Wabunge wote kwa ujumla kwa kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee niwashukuru sana Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ndugu yangu Mheshimiwa Jitu Soni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa na dada yangu Mheshimiwa Najma Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI ndugu yangu Mheshimiwa Oscar na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Dkt. Tisekwa na wajumbe wote kwa jinsi ambavyo wametusaidia sana kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee niwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Peramiho kwa kuendelea kuniamini, kuniunga mkono na kunipa ushirikiano mkubwa kutekeleza majukumu katika Jimbo letu na tunaona na kushuhudia maendeleo makubwa ya Jimbo la Peramiho. Naendelea kuwaeleza kwamba tupo pamoja na hasa kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu Hakuna Kulala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze katika hoja ambazo zimebakia, lakini kwa muda muafaka Mheshimiwa Waziri Mkuu atakuja kujibu hoja nyingine ili kuhitimisha hotuba yake. Hoja nitakazoanza kuzijibu ni hoja zinazomhusu Msajili wa Vyama vya Siasa na Ofisi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza ilikuwa ni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ifanye jitihada za kutosha kusuluhisha mgogoro katika Chama cha Wananchi (CUF) ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza katika Muungano na katika mgogoro huo. Naomba nichukue nafasi hii kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba mgogoro huu wa Chama cha CUF kwa sasa upo Mahakamani, kwa hiyo sitachukua nafasi hii kuujibu mgogoro huo ama kumuagiza Msajili wa Vyama kushughulika na mgogoro huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ninachotaka kusema hapa ni hiki kifuatacho. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya siku zote wakati akiratibu na akitekeleza majukumu yake kama Msajili wa Vyama vya Siasa. Amekuwa akifanya kazi nzuri sana na sisi wote ni mashahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Msajili wa Vyama vya Siasa anafanya kazi hii kwa kuzingatia Sheria Na. 5 ya Vyama Vya Siasa ambayo ndiyo inayosimamia vyama vya siasa katika nchi yetu ya Tanzania. Sisi wote tumekuwa ni mashahidi, Msajili wa Vyama vya Siasa mpaka sasa amefanikiwa kusajili vyama vya siasa 19 ndani ya nchi yetu ya Tanzania ambavyo vimepata usajili wa kudumu lakini Msajili wa Vyama vya Siasa
ameendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni mbalimbali za vyama vya siasa katika nchi yetu ya Tanzania kwa weledi mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba tu niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na kutakiwa kusuluhisha migogoro hiyo ambayo nimeisema katika Chama cha Wananchi CUF, naomba niwashauri wenzetu wanaohusika na mgogoro ndani ya chama cha siasa cha CUF, ili mgogoro huu Mheshimiwa Msajili wa Vyama vya Siasa aweze kuushughulikia vizuri, uko utaratibu wa kisheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali anajua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunamtaka Msajili wa Vyama awe mediator katika mgogoro huo basi niwashawishi na kuwaomba waondoe mgogoro huu katika Mahakama ulikopelekwa mgogoro huo na Msajili wa Vyama anaweza akafanya kazi yake. Vinginevyo Msajili wa Vyama hawezi kuingia katika mgogoro huu kwa sababu mgogoro huo tayari umeshasajiliwa na upo katika Mahakama zetu na hivyo tumwache Msajili wa Vyama aendelee na shughuli nyingine ambazo hafungwi nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee na hoja nyingine. Waheshimiwa Wabunge na hasa Wabunge wa Upinzani wamelalamika sana na kusema kwamba suala la maandamano ni suala la Kikatiba na wamesema kwa sababu suala la maandamano ni haki ya Kikatiba wanafikiri upo msingi wa vyama vya siasa kuachiwa waendelee na maandamano bila kuzingatia sheria, hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba suala la maandamano katika nchi yetu ya Tanzania linaratibiwa na sheria za usalama ndani ya nchi yetu chini ya vyombo vya usalama na hasa polisi na Katiba haiwezi kuchukuliwa kwamba ndicho kigezo cha kuviruhusu vyama kufanya maandamano bila kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa. Naomba sana kwa heshima yote niwaombe Watanzania wote, niviombe vyama vyote vya siasa katika nchi yetu ya Tanzania wahakikishe wanazingatia sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba yetu imeruhusu maandamano lakini maandamano yameratibiwa kisheria na kama yameratibiwa kisheria ni lazima tuhakikishe kwamba tunazingatia sheria katika kuratibu maandamano kwenye nchi yetu. Labda niulize kitu kimoja, tukiamka hapa siku moja asubuhi na kila mtu ameamua kuandamana; wakulima au wafanyakazi au kila mtu aamue tu kuandamana kwa sababu Katiba imesema, nadhani itakuwa siyo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuviomba vyama vyote katika nchi yetu kuheshimu Katiba na sheria katika kutekeleza wajibu wao na siyo kuvunja sheria za nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo ilikuwa imetolewa na Waheshimiwa Wabunge ni kwamba chaguzi ndogo ambazo zimekuwa zikiendelea kwa sasa, zimekuwa zikigharimu sana fedha za Serikali. Baadhi ya Wabunge wakajaribu kulinganisha pia gharama ambazo zimekuwa zikitumika katika chaguzi hizi ndogo na utekelezaji wa majukumu ya Serikali na miradi mingine ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme demokrasia ni gharama. Hakuna demokrasia yoyote mahali popote ambayo haina gharama yoyote. Nasema hivi kwa sababu kama Jimbo la Uchaguzi kwa mujibu wa sheria na Katiba yetu liko wazi, hakuna jinsi, ni lazima tufanye uchaguzi. Kama ni Jimbo la Uchaguzi la Ubunge ama la Udiwani ni lazima kwa mujibu wa sheria na Katiba apatikane mwakilishi wa kuwawakilisha wale wananchi kwenye jimbo husika. Hatuwezi kufanya uchaguzi bila kutumia gharama, kwa hiyo, hiyo ni demokrasia ndiyo maana nasema ni gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, niseme neno moja, nina mfano tu mdogo. Jimbo la Songea Mjini baada ya kuwa wazi na uchaguzi kufanyika, Mbunge ambaye sasa hivi anawakilisha Jimbo la Songea Mjini, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, ameniambia kwa muda huu mfupi kwa sababu nafasi iliyokuwa wazi imejazwa ameweza kufanikiwa kupata fedha za Kitanzania zisizopungua bilioni sita kwa ajili ya ujenzi wa barabara na miundombinu ya stendi katika jimbo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, gharama tulizozitumia kwenye uchaguzi ni bilioni nne, lakini zimewawezesha wananchi wa Jimbo la Songea kupata bilioni sita kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Kwa hiyo, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba ni ukweli usiopingika kwamba demokrasia ni gharama na kama demokrasia ni gharamani ni lazima tuendelee kufanya uchaguzi kujaza nafasi wazi kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo hoja nyingine iliyozungumzwa, imesema kwamba kuna kila dalili ya Msajili wa Vyama kukusudia kuua Upinzani katika nchi yetu ya Tanzania. Naomba niseme yafuatayo:-

Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Ali Hassan Mwinyi, mwaka 1991 alimteua Jaji Nyalali kukusanya maoni ya Watanzania kuamua kama nchi yetu iende katika mfumo wa vyama vingi au ibaki katika mfumo wa chama kimoja. Watanzania asilimia 80 walisema hawataki mfumo wa vyama vingi, Watanzania asilimia 20 walisema wanataka mfumo wa vyama vingi, lakini ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi iliyofanya maamuzi magumu tuingie katika mfumo wa vyama vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu za kuingia katika mfumo wa vyama vingi zilikuwa wazi tu, ni kuwafanya Watanzania waone kwanza Chama cha Mapinduzi hakiogopi mageuzi na hakiogopi mfumo wa vyama vingi. Vilevile ilikuwa ni kuhakikisha kwamba demokrasia ya wachache waliochagua mfumo wa vyama vingi inaheshimiwa na wengi waliokataa mfumo wa vyama vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya niliyoyasema inajidhihirisha kabisa kwamba Serikali ya chama chetu ilifanya maamuzi ya kuingia katika Mfumo wa Vyama Vingi ili kufuata demokrasia, kwa hiyo hakuna sheria yoyote inayomruhusu Msajili wa Vyama kuvunja demokrasia na kufuta Mfumo wa Vyama Vingi katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Msajili wa Vyama aendelee kuchukua hatua stahiki kama Kamati ya Bunge ilivyotushauri kwa vyama vyote ambavyo havitaki kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria na taratibu tulizoweka ili kusaidia Mfumo wa Vyama Vingi katika nchi yetu uweze kuwa ni mfumo halisia ambao unaendana na matakwa ya kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nizungumze machache kuhusu Tume ya Uchaguzi. Kwenye Tume ya Uchaguzi imetokea hoja kwamba Tume hiyo imekuwa haina weledi, haizingatii sheria na taratibu katika kuendesha shughuli za uchaguzi na wakati mwingine imekuwa pia ikisimamia uchaguzi huo bila kuzingatia sheria na taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Tanzania. Tume ya Uchaguzi imeanza kufanya kazi ya kusimamia uchaguzi mwaka 1995 tulipoingia katika mfumo wa vyama vingi. Mwaka 1995 tumemaliza uchaguzi salama na Serikali imeingia madarakani na tumeendelea kufanya kazi. Vilevile mwaka 2000, 2005, 2010, 2015, Tume hii ya Uchaguzi ndiyo imesimamia uchaguzi wetu na hata sisi Wabunge ambao tuko ndani ya Bunge lako Tukufu tumesimamiwa uchaguzi wetu na Tume hiyohiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kushangaa sisi tuliposhinda, Tume hii ya Uchaguzi ilikuwa imefanya vizuri, hatukusema lolote na hatukuwa na malalamiko yoyote lakini leo tunasimama na kusema Tume hii haina weledi na haifuati utaratibu wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kukuhakikishia sisi kama Serikali tumeendelea kuisimamia na kuiratibu Tume ya Uchaguzi kwa kuzingatia Katiba kwa sababu Katiba inasema wazi Tume ya Uchaguzi ni huru na inafanya kazi zake kwa uhuru ulio kamili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa Katiba pale ambapo uchaguzi umekwishafanyika na kama chama chochote kinaona kwamba misingi ya kisheria haijafuatwa, chama hicho kimeruhusiwa kwenda mahakamani na kule mahakamani ndipo kutakapopatikana haki ya kisheria kwa chama chochote kinacholalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu, kwa chaguzi hizi ndogo zote zilizopita kesi zilizofunguliwa kwenye kata hizo takribani kama arobaini na kitu mpaka 50, kesi za uchaguzi zimefunguliwa kwa kata mbili tu. Kwa hiyo, naomba tuone kama kweli Tume hii ilikuwa haisimamii uchaguzi huo kwa haki naamini kabisa kata nyingi kesi za uchaguzi zingekuwa zimefunguliwa. Kwa majimbo yote ambayo Tume ya Uchaguzi imeshaendesha uchaguzi hakuna jimbo hata moja ina kesi ya kupinga uchaguzi katika jimbo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niseme kwamba Tume hii ya Uchaguzi inafuata utaratibu katika uendeshaji wa shughuli zake na kama mtu yeyote, chama chochote kina malalamiko naomba sana kifuate sheria na kiende Mahakamani. Niviombe vyama vyetu vya siasa visikimbilie kulalamika kwenye vyombo vya habari, ni vyema vyama vya siasa vizingatie sheria za nchi tulizonazo katika kuendesha chaguzi zetu tunazoendelea nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine kwa Tume hii ya Uchaguzi ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunaboresha daftari la wapigakura kwa wakati. Naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba shughuli ya kuboresha daftari la wapigakura tumeshaianza ndani ya Serikali kwa mujibu wa sheria na taratibu tulizonazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaanza kuhuisha kanzidata ya daftari la wapigakura katika nchi yetu ya Tanzania, tumeshaanza kutoa elimu na tumeshaanza kufanya shughuli zote ambazo zinatakiwa ili daftari la wapigakura katika nchi yetu liwe limeboreshwa na liendane na wakati kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliambiwa pia tuhakikishe kadiri iwezekanavyo watendaji wote wa Tume ya Uchaguzi ambao watakiuka maadili ya kisheria kama watendaji ndani ya Tume basi wachukuliwe hatua na ikiwezekana wapewe adhabu zinazostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kazi hiyo inafanyika vizuri wa sababu tunazo sheria, tunayo miongozo na tunazo taratibu ambazo zimewekwa bayana. Kwa hiyo, watendaji wote ambao wataonekana wanakiuka taratibu za kisheria katika kufanya kazi ndani ya Tume yetu ya Uchaguzi basi watachukuliwa hatua stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambazo zilikuwa zimejitokeza zilikuwa zinahusu mapambano dhidi ya UKIMWI katika nchi yetu ya Tanzania. Katika eneo hili mambo yafuatayo yaliongelewa kwa kiasi cha kutosha.

La kwanza, ilikuwa ni bajeti kuendelea kutolewa kwa wakati; la pili ilikuwa ni tozo ndani ya Serikali ili kutunisha Mfuko wa ATF (AIDS Trust Fund); la tatu ilikuwa ni kuhakikisha kwamba asilimia 10 ambayo iko kwenye own source ambayo inatumika kwa akinamama na vijana inatumika pia kwa ajili ya kuwahudumia wanaoishi na VVU lakini ya nne ilikuwa kuhakikisha kwamba upatikanaji wa dawa kwa ajili ya wenzetu wanaoishi na VVU unaendelea kuwa wa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako kwamba tumefanya kazi ya kutosha na Wizara zinazohusika. Bajeti ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania kwa mwaka huu wa fedha imeongezeka. Suala la tozo kwa ajili ya Mfuko wa Kudhibiti UKIMWI katika nchi yetu, tumeshapeleka mapendekezo yetu kwenye Ofisi ya Waziri wa Fedha na tunaamini kabisa wenzetu watatushauri njia gani ya kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwamba mfuko wenyewe kupitia bodi umeshaanza kufanya kazi ya kutosha ya kukusanya fedha ili kuhakikisha kwamba unakuwa na fedha na hiyo ni kujihami na upungufu wa fedha za wafadhili.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la asilimia 10, naomba mtuachie, tunachukua pendekezo hilo, tutalifanyia kazi kwa pamoja na wenzetu wa TAMISEMI. Tutakuja kutoa majibu tuone kama hiyo asilimia kumi tunaweza tukagawana hiyohiyo ama tunaweza kutumia Mifuko kama TASAF ama mifuko mingine kuhakikisha hawa wenzetu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI na wao wanaweza kusaidiwa ili kuweza kukidhi mahitaji yao na kuwafanya waweze kutumia dawa vizuri, lakini kuwasaidia waweze kuendelea kuishi wakiwa na afya njema. Naomba niseme hilo nalichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine lilikuwa ni suala la kuwezesha wananchi kiuchumi. Tuliambiwa kwamba kwenye miradi inayoendelea kwa sasa tujitahidi kuhakikisha kwamba Watanzania wazawa na wao wanapata nafasi za kazi ama wanakuwa ni wakandarasi washiriki katika miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie, kupitia mpango wetu wa local content ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tumeweza kuanzisha mpango mkakati mahsusi wa kuzungumza ndani ya Serikali kuhusu suala la local content kuhakikisha kabisa kwamba Watanzania katika miradi mikubwa ya kitaifa, lakini vilevile katika shughuli zinazoendelea katika halmashauri zetu na wao wanapata nafasi ya kushiriki kama washiriki wa uchumi katika nchi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka pia tulifanya hata marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ambayo inatupelekea kuwafanya Watanzania waweze na wao kuwa ni washiriki kwenye suala zima la maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya sekta ya hifadhi ya jamii, Waheshimiwa Wabunge wametushauri kwamba tutoe elimu kwa Watanzania kuhusu sekta hii. Naomba kukuhakikishia kwamba kazi hiyo inafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, walitaka tuhakikishe sheria mpya inaanza kutumika kwa haraka kwa kuwa na kanuni zake, naomba niwahakikishie kanuni ziko tayari na zinakamilishwa kwa hatua ya mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Wabunge walituagiza tupanue wigo wa hifadhi ya jamii ifike mpaka kwenye sekta isiyo rasmi. Naomba niwahakikishie kwa mabadiliko ya sheria tuliyoyafanya Bunge lililopita sasa sekta isiyo rasmi inatambulika rasmi katika suala zima la hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la BAKWATA, kwa nini wamefanya mkutano wao hapa Bungeni. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, Serikali yetu haina dini, Serikali yetu inafanya kazi na taasisi zote za dini bila kujali ni aina gani ya taasisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, wala isiwe tabu kwa BAKWATA kufanya mkutano wao hapa, kama kuna taasisi nyingine inataka kufanya mkutano hapa Bungeni na wao walete maombi ili mradi tu wafuate taratibu na sheria. Vilevile mkutano wanaotaka kuja kuufanya hapa uwe ni mkutano ambao tutakuwa tumejiridhisha kwamba mkutano huo hauna madhara ndani ya Bunge na nje ya Bunge letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hakuna haja ya kuhangaika ni kwa sababu gani BAKWATA wamefanya mkutano hapa, ninachosisitiza ni suala la misingi ya kisheria na aina ya mkutano unaotakiwa kufanyika hapa, kama ni vitu ambavyo vinaelezeka na havina madhara kila mtu anaweza akafanya mkutano mahali popote ambapo pana ukumbi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala ambalo pia nataka nilizungumze kwa ufupi ni suala la dawa za kulevya. Nianze kwa kuipongeza Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya katika nchi yetu ya Tanzania kwa kazi nzuri. Imefanya kazi nzuri sana katika maeneo matatu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la supply (kudhibiti upatikanaji wa dawa); kwenye suala la demand (kudhibiti uhitaji) na katika kupunguza madhara (kwenye masuala ya harm reduction). Kwa hiyo, Tume imefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tukubaliane hapa kwamba suala la uhalifu katika nchi yetu ya Tanzania si la Muungano na wala suala la Mahakama si suala la Muungano, lakini suala la ulinzi wa Taifa ndilo suala la Muungano katika nchi yetu. Kwa hiyo, mamlaka hii kwa sheria tuliyonayo inafanya kazi upande wetu huku Bara lakini kwa sababu uhalifu hauna mipaka ndiyo maana tunasema ni lazima mamlaka hii ifanye kazi ya kutosha na mamlaka katika upande wa pili wa Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ni hali ya kawaida tu, kama upande mmoja ukifanya kazi, upande mwingine usipofanya kazi ni shida ama pande zote mbili tusipofanya kazi kwa pamoja itakuwa shida. Naomba niwahakikishie sisi wenyewe ndani ya Serikali jambo hili tunalifanyia kazi kwa pamoja pande zote mbili za Muungano kuhakikisha dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania zinakoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa nafasi uliyonipa, hoja bado ziko nyingi kiasi, tutazijibu kwa maandishi. Nichukue nafasi hii kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kuheshimu sheria na hasa katika kushughulika na shughuli ya vyama vya siasa katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kujibu hoja ambazo zimewekwa mbele yetu katika siku hii ya leo. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia sisi Wabunge wote afya njema na kuweza kukutana jioni hii ya leo, tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nikupongeze sana wewe mwenyewe binafsi kwa kweli unaongoza Bunge hili kwa umahiri mkubwa sana sana na ni mfano mzuri wa viongozi wanawake katika Taifa letu, hongera sana. Pia upeleke salamu zangu za shukrani kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mheshimiwa Spika kwa kazi nzuri anayoifanya kuliongoza Bunge letu akisaidiana na Wenyeviti wa Bunge, mnafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi kuanza kuhitimisha hoja hii bila kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge Mheshimiwa Rais huyu kwa kweli amejipambanua kuwa Rais shupavu anayeaminiwa na kutumainiwa na Watanzania wengi na hasa wanyonge. Kwa kweli nchi yetu imepata jembe, imepata Mheshimiwa Rais mahiri kabisa; na tumeshuhudia kwa muda mfupi maendeleo yamekuwa makubwa sana. Kwa pamoja naye nimpongeze sana Makamu wa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan, lakini ninaomba kwa dhati ya moyo wangu nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wangu na watendaji wote ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tunamwona Mheshimiwa Waziri Mkuu kama kioo na kiongozi mahiri anayeweza kutuongoza vyema ndani ya Taasisi yetu. Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba upokee shukrani zangu za dhati kwa uongozi wako ambao umetufanikisha, umenifanikisha mimi na wenzangu kufika katika hatua hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli mwenye macho haambiwi tazama, hawa viongozi wetu wakubwa niliowataja hapo juu wameweza kulipatia Taifa hili maendeleo makubwa sana kwa kipindi kifupi cha takriban miaka mitatu. Tumeona maendeleo makubwa kwenye Sekta ya Ujenzi, barabara, madaraja, meli, reli, miundombinu ya maji, afya, elimu na mambo mengine mengi kadha wa kadha. Serikali ya Awamu ya Tano chini ya usimamizi wa viongozi hawa imefanya mabadiliko makubwa na jitihada hizi tuziunge mkono Watanzania wote pamoja na sisi Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi ya pekee kumkaribisha ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, dada yangu mpenzi Mheshimiwa Angella Jasmine Mbelwa Kairuki, Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji, nina imani naye kubwa, tutashirikiana sana, ni Waziri mchapakazi, mwanamke wa mfano, Mheshimiwa Angellah karibu sana.

Vilevile naomba nichukue nafasi hii kuwatambua na kuwashukuru sana Manaibu wangu wawili; Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde na Mheshimiwa Stella Ikupa, vijana hawa wasomi, wenye weledi, wazalendo, waaminifu na wachapakazi, kwa kweli wamekuwa ni nguzo kubwa sana sana katika kazi zangu na ni mhimili mkubwa kwangu. Nawashukuru sana sana Makatibu Wakuu wote watatu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi na watendaji mbalimbali ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisisahau kabla sijaenda mbele niwashukuru wapigakura wa Jimbo la Peramiho, Mwenyezi Mungu awape baraka kwa kuendelea kunijali na kunipa imani. Nawashukuru pia watoto wangu, vilevile niombe tu kuwaomba Ndugu zangu wana Peramiho, mwezi Novemba mwaka huu habari ni ileile, hakuna kulala na mwakani mwaka 2020 matokeo ni yaleyale hakuna kupunguza. Kwa hiyo nawashukuru sana wapigakura wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusingeweza kufika hatua hii sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu bila juhudi za Kamati ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mwenyekiti Ndugu yangu Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa na Mheshimiwa Najma Murtaza Giga na Wajumbe wa Kamati wamefanya kazi kubwa; pia Kamati ya UKIMWI inayoongozwa na kaka yangu Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa na dada yangu Mheshimiwa Jasmine Tisekwa na Wajumbe wa Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Jimbo uko pia ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hivyo basi, nimshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mheshimiwa George Simbachawene na Ndugu yangu Mashimba Mashauri Ndaki na Wajumbe wote wa Kamati kwa kazi kubwa na miongozo na ushauri walionipatia. Kazi hii inafanyika kwa kutumia kanuni ya 99(2) ambacho kinaniruhusu sasa kukaa hapa mbele ya meza yako ili mwisho wa hotuba yangu lakini, mwisho wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuombe fedha za kutekeleza majukumu mbalimbali ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Hivyo basi, nitaanza kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge na zile ambazo tutashindwa kuzijibu kwa siku hii ya leo tutazijibu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mambo mahususi ambayo pia ni mambo ya jumla, Waheshimiwa Wabunge wengi wameunga mkono na kupongeza sana bajeti yetu, lakini wakimpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, hata hivyo, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wametilia shaka Ofisi ya Waziri Mkuu na utendaji kazi wake kama kweli umetekeleza majukumu yake sawasawa. Kwanza, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge uwepo wa Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 52 mpaka Ibara ya 57 ya mwaka 1977; Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiye mratibu na msimamizi mkuu wa utekelezaji wa shughuli na mipango yote ya Serikali, Wizara na Taasisi zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwanza ni lazima tujue Mheshimiwa Waziri Mkuu hajajiweka mwenyewe, amewekwa kwa mujibu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, wote tumeshuhudia ni kwa kiasi gani Mheshimiwa Waziri Mkuu huyu amekuwa mchapakazi na ametekeleza majukumu yake kisawa sawa kweli kweli. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameweza kufanya ziara takriban katika mikoa yote nchi nzima ya Tanzania kwenye wilaya zote, kwenye halmashauri zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, suala la msingi hapa siyo idadi ya ziara zilizofanywa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, ziwe ziara fupi ama ziara ndefu ama ziara zilizofanywa na viongozi wa kitaifa; suala la msingi hapa ni yale matokeo ya ziara hizo zilizofanywa na viongozi wakubwa wa kitaifa na Mawaziri na Viongozi wengine wote ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano. Jambo la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu ziara zake na viongozi wengine wa kitaifa zimeweza kurudisha nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika nchi nzima ya Tanzania, lakini ziara hizo zimezaa matunda ya kuongezeka kwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya huduma za jamii, ikiwemo, elimu, afya, maji, miundombinu ya barabara, umeme na kadhalika na sisi ni mashahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziara hizi na Mheshimiwa Waziri Mkuu halali na ziara hizo, zimeweza kuongeza tija kwenye mazao ya kilimo na hasa mazao ya biashara ya kimkakati, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakupongeza sana. Ziara hizo zimeweza kuimarisha ukusanyaji wa mapato ndani ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu. Nitoe tu wito kwetu sisi Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote tuanze kulipa kodi kwa hiari bila shuruti. Pia ziara hizi zimeimarisha hali ya usalama, amani na utulivu nchini na kuongeza mshikamano wa kitaifa na umoja wa kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kwa ushahidi mkubwa, juzi nilikuwa Mkoa wa Songwe kwenye shughuli za Mwenge wa Uhuru na shughuli za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zilifanyika kwenye eneo la Mloo ambalo pale Mheshimiwa Mbunge wake ni wa CHADEMA, lakini wananchi wote walionesha ushirikiano bila kujali chama, bila kujali itikadi za vyama, dini zao wala makabila. Sasa unaona tu ni kwa namna gani nchi hii amani na utulivu viko sawasawa na wananchi wanaendelea kushikamana pamoja na kujenga umoja wa kitaifa. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuwe mawakala wa amani na utulivu katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako masuala yamezungumzwa hapa kuhusu Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wabunge wengine wanatia shaka na wanalalamika kwamba Bunge hili limeshindwa kutekeleza majukumu yake sawasawa na yako maneno mengi ambayo yamekuwa yakitafsiri kazi na mwenendo mzima wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bunge hili la Kumi na Moja. Hata hivyo, nitaeleza mifano michache ya kuonesha ni kwa kiasi gani Bunge hili limefanya kazi ya kutukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka leo ninaposimama mbele yako Waheshimiwa Wabunge hawa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameshaiuliza Serikali yao maswali yasiyopungua 2,653, lakini wameshauliza maswali ya nyongeza yasiyopungua 8,202, ni kazi nzuri imefanywa na Waheshimiwa Wabunge hawa. Maswali hayo yalikuwa yanataka kuwa na uhakika wa uwakilishi wa wananchi katika kufuatilia Mpango wa Taifa wa Maendeleo, bajeti za Serikali, ahadi za viongozi wetu na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka kusema kitu kidogo ukiangalia maswali hayo yote yasiyopungua 10,000 na kitu, ukijumlisha maswali ya nyongeza na maswali ya msingi, yanaonesha hawa Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi wametumwa nini na wananchi wao kuja kuliuliza Bunge na kuiuliza Serikali. Maswali haya kipaumbele kiliwekwa kwenye Sekta ya Maji, Umeme, Afya, Elimu na Miundombinu. Imeletwa hoja ndani ya Bunge hili katika bajeti hii kwamba, kipaumbele cha wananchi wa Tanzania ni Katiba pendekezwa, Katiba iliyopendekezwa ambayo inatarajia kubadilisha Katiba tuliyonayo sasa, Waheshimiwa Wabunge wengi wamesisitiza kwamba hicho ndiyo kipaumbele cha wananchi kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuliarifu Bunge lako Tukufu maswali yaliyoulizwa humu ndani ambayo yanatokana na kero za Watanzania, yameletwa na wawakilishi wa Watanzania, Wabunge nimesema hapa yanafika kama maswali 10,000 na kitu, lakini katika maswali hayo 10,000 na kitu maswali yaliyoletwa na Waheshimiwa Wabunge hawa wakiwakilisha mahitaji ya Watanzania yaliyokuwa yanadai Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi ni maswali mawili tu kati ya maswali hayo 10,000 na kitu. Hapa nataka kusema nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu hapa, naendelea kusisitiza kama kweli sisi ni wawakilishi wa wananchi, maswali tunayoyaleta Bungeni yanaashiria mahitaji ya Watanzania, basi mahitaji ya Watanzania kwa sasa ni maji, umeme, afya, elimu, miundombinu, utawala bora, masuala ya wafanyakazi na mambo mengine yanayohusiana na maeneo niliyoyasema hapa. Hivyo basi, suala la Katiba mpya, suala la Katiba pendekezwa, suala la Tume ya Uchaguzi kwamba haitendi haki, kwa maswali yetu sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge, hayo siyo maeneo ya kipaumbele kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili limefanya kazi kubwa, limetunga Sheria mbalimbali, limeridhia mikataba, limetengeneza maazimio mbalimbali mpaka tunapofika siku hii ya leo Bunge letu Tukufu limeshatunga Sheria mpya zisizopungua 44, lakini zimefanya mabadiliko ya Sheria mbalimbali takribani kama zizopungua 95. Nirudi pale pale, haitoshi kusema tumetunga, tumefanya mabadiliko ya Sheria hizo zote nyingi, tumetunga Sheria hizo zote mpya, hizo Sheria zinaakisi nini katika mahitaji ya Watanzania na nchi nzima ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitasema Sheria chache kama mfano tu wa kazi nzuri iliyofanywa na Bunge letu Tukufu. Moja kwa mfano tumefanya marekebisho ya Sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Na.5 ya mwaka 2015 (The Drugs Control Enforcement Act)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya uwepo wa Sheria hii; uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania kwa kazi nzuri iliyofanywa na Waheshimiwa Wabunge imekwenda mpaka asilimia 90, udhibiti na uingizaji wa dawa umedhibitiwa kwa asilimia 90 ndani ya Taifa letu. Nashangaa kama kazi hizi nzuri hatutazisema na kujisemea sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge na Bunge letu, basi kwa kweli hatujitendei haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili pia limetunga Sheria ya kutambua kwa mfano, Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi ya Tanzania, kitu ambacho kilikuwa kinaliliwa na Watanzania wengi. Vilevile tumefanya marekebisho ya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura Na. 200 na Sheria hii imetusaidia sana kudhibiti ufisadi katika Taifa hili, kwa hiyo ni lazima tujipongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria nyingine nzuri ambayo lazima niiseme ni marekebisho ya Sheria ya ununuzi wa umma ambayo imesaidia sana kutengeneza mfumo wa kielektroniki wa kufanya procurement (The Tanzania National Electronic Procurement System). Hiyo imepunguza ubadhirifu kwenye manunuzi ya umma, kwa hiyo tunajipongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili limetunga Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi Na.9 ya mwaka 2018 na Sheria hiyo imezaa nini? Inakwenda kuzaa mradi muhimu sana wa ujenzi wa reli, Mtwara - Mbamba Bay
- Mchuchuma na Liganga. Sheria hii mpya ya PPP inakwenda kuzaa ujenzi wa reli ya Tanga Mwambani, Arusha, Musoma, ujenzi wa kipande cha barabara ya treni cha Tanga - Arusha, lakini na barabara nyingine kutoka Dar es Salam – Chalinze - Morogoro. Kwa hiyo unaona ni kwa kiasi gani hili Bunge ambalo wengine wanabeza kwamba haliwezi, halijafanya kazi nzuri limewezaji kufanya kazi nzuri kwa kiasi hicho?

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengine mazuri tu kwa mfano Azimio la Mkataba wa Kuanzisha Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe ambalo baadaye litatuletea kuwa na bwawa kubwa la maji la ubia ambalo litazalisha umeme, huduma za viwandani na mahitaji ya nyumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Bunge hili nimeridhia mkataba wa eGA mkataba kati ya Serikali ya Uganda na Tanzania kuhusu bomba la mafuta, ni Bunge hilihili. Mkataba huo tija yake unaenda kuzaa ajira zisizopungua 10,000 kwa vijana wa Tanzania wakati wa ujenzi, lakini baada ya hapo ajira takriban 1,000 zitapatikana katika kuendesha mradi huo. Mikoa nane, Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara, Tanga itanufaika na mradi huo, Wilaya 24 na Vijiji 134 vyote vinanufaika na mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niseme kwa kweli Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge ukiacha hapo Ofisi ya Waziri Mkuu imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Vitambulisho vya Mabaharia Na. 185 wa mwaka 2003 na imeridhia pia Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Ubaharia wa Shirika la Kazi Duniani (Maritime Labour Convention) ya mwaka 2016. Mikataba hii imeweza kuongeza fursa za ajira kwa Mabaharia wa Kitanzania kwenye meli za ndani na meli za nje ya nchi, imeweza kuleta mafunzo fursa za mafunzo ya kitaalam, lakini imeongoza viwango vya kazi za staha kwa Mabaharia wetu. Kwa hiyo, kazi hizo zote zimefanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu uratibu na usimamizi na zimetufikisha mahali pazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo lilizungumzwa na Waheshimiwa Wabunge, ni suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi. Jambo hili lilizungumzwa sana eneo la local content kwa maana ya ushiriki wa Watanzania katika kumiliki uchumi wa Taifa lao. Ofisi ya Waziri Mkuu imekamilisha kazi ya msingi sana ya kutengeneza Mwongozo na tunaamini Mwongozo huu utawezesha wadau kutambua wajibu na majukumu yao katika kushiriki kwenye suala zima la kuhakikisha Watanzania na wao wanapata ajira katika miradi yote inayozalishwa katika Taifa letu, lakini vilevile masuala ya ununuzi kama wa bidhaa, ununuzi wa huduma na mambo mengine watanzania pia wanaweza kushiriki.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupitisha Mwongozo huo, mwamko ni mkubwa kweli kweli, naomba nitoe mifano michache, wakati tulipomaliza kuandaa Mwongozo huu wa local content tumefanya utafiti na tumegundua yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwenye mradi mkubwa wa uwekezaji wa daraja ya Mfugale, daraja la Mfugale lilitoa ajira 616, Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge kwa sababu ya Mwongozo huo kati ya ajira 616 ajira 589 zilichukuliwa na Watanzania na ilikuwa ni asilimia 95 ya ajira zote. Hiyo haitoshi, lakini ununuzi wa bidhaa mbalimbali ambazo zilitumika katika ujenzi wa huo mradi ulitaka makampuni 28 ndiyo yaende yakafanye ununuzi wa hizo bidhaa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kati ya makampuni hayo 28, makampuni 24 yote yalikuwa ni makampuni ya Watanzania, makampuni ya wazawa na ilikuwa ni asilimia 85 ya makampuni yote. Makampuni matatu tu ndiyo yalikuja kutoka nje na kampuni moja ilikuwa ni ya ubia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hilo linaendelea kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ni hivyo hivyo hata kwenye barabara za juu za Ubungo, mpaka sasa ajira ya Watanzania ni asilimia 89, kwenye mradi wa SGR, asilimia ya Watanzania kwenye ajira katika mradi huo ni asilimia 93, mradi huo wa SGR kuna sub-project ndani ya mradi huo na ndani ya mradi hiyo sub-project imetoa ajira 1,129 za Watanzania na wageni ni 152 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni mifano michache, tunayo mifano mingi sana ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu inafuatilia na tukipata muda tutaiweka hapa. Naomba niwaambie Ofisi ya Waziri Mkuu inafanya kazi kukuza ajira kwa kutumia miradi ya kimkakati ambayo inaendeshwa na Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli na msimamizi wake akiwa ni Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Miradi hiyo ni pamoja na Salender Bridge na umeme Rufiji. Kwa hiyo, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge hatutakiwi kubeza mambo haya yanayofanywa na Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine lilizungumzwa sana hapa na Wabunge wachache ilikuwa ni Ofisi ya Msajili wa Vyma vya Siasa. Kumekuwa na hali ya upotoshaji na ninaomba niseme ya upotoshaji kwamba hali ya kisiasa ni tete na ni mbaya na demokrasia inaminywa. Mimi naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba hali ya demokrasia katika nchi yetu ni shwari na ni tulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kabisa kufananisha hali ya siasa na demokrasia katika nchi yetu na mataifa yanayotuzunguka ambayo tumekuwa tukiona na kushuhudia hali jinsi ilivyo huko. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa kama mnaona kuna tatizo hebu tujaribu kusaidiana, kushauriana na kukaa kwenye meza moja kujadiliana na kutatua matatizo yetu kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu gani? Hapa tumeshuhudia viongozi wa vyama wakihama kutoka chama kimoja kwenda chama kingine. Kama hali ya kidemokrasia na siasa ingekuwa siyo nzuri, unapata wapi raha ya kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine? Hiyo ni dalili tosha kwamba hali yetu kisiasa hapa ni nzuri. Hiyo ni sababu tosha inamfanya mtu awe huru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waitara aligombea mwaka 2015 kupitia CHADEMA leo Mbunge wa Chama cha Mapinduzi ni kwa sababu ya utulivu wa kisiasa na demokrasia. Mheshimiwa Nyalandu alishinda Chama cha Mapinduzi leo amehamia CHADEMA ndiyo mambo hayo hayo ya utulivu. Mheshimiwa Lowassa aligombea Urais kupitia CHADEMA leo amerudi CCM, utulivu huo wa demokrasia. Ndugu yetu Maalim Seif alikuwa CUF kindakindaki lakini leo yuko ACT-Wazalendo, huu ndiyo uhuru. Waheshimiwa Wabunge tuko shwari, anayetaka kuhama ahame, anayetaka kubaki abaki, safari ya siasa na demokrasia inaendelea, taratibu na sheria zifuatwe tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme kama ni masuala ya uchaguzi hakuna chama ambacho kilikataliwa kuweka mgombea na kushiriki kwenye uchaguzi. Hatukuwahi kusema hivyo na tumeendelea kusimamia kuona kwamba kila chama kinaendelea kupata haki. Nirudie kusema kama haki haipatikani vipo vyombo vya sheria vitatusaidia kupata haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mifano, wako watu ambao walihisi kwamba haki zao zimepotea. Nitatoa mifano miwili na mifano hiyo inatupelekea kuthibitisha kwamba ukiona kwenye demokrasia na hali ya siasa nchini haiko sawa nenda Mahakamani utapata haki tu. Mfano wa kwanza, tarehe 22 Februari, 2019 Mheshimiwa Ally Saleh alishinda kesi dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chama cha CUF kwenye Mahakama Kuu, iliamuliwa na jopo la Majaji na alishida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 18 Machi, 2019, Mheshimiwa Lipumba alishinda na akatambulika yeye ni Mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi (CUF). Haki hii haikupatikana Bungeni wala mahali popote ilipatikana Mahakamani. Leo nimemsikia hapa Mheshimiwa Bwege nampongeza sana amesema sisi CUF sasa ni chama kimoja, wamoja, ni kitu kimoja hatutaki mgogoro lakini kama watu wasingekwenda Mahakamani mgogoro wa Chama cha Wananchi CUF usingekwisha na mpaka leo ungeendelea kuwa ni mgogoro mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niviombe vyama vya siasa kuendelea kutii Sheria ya Vyama vya Siasa. Lengo la sheria yetu ni kufanya hivi vyama viwe ni taasisi. Kwa mfano, leo Maalim Seif alivyohama kama chama chake cha CUF kisingekuwa taasisi ingekuwa shida lakini kwa sababu ni taasisi ndiyo maana na leo Mheshimiwa Bwege amesema sisi ni CUF moja kwa sababu chama ni taasisi. Sheria hii inataka vyama viwe taasisi na visiwe vyama vya mtu mmoja kwamba mtu mmoja ndiye anakiendesha chama yeye peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunataka vyama hivi kupitia Sheria yetu ya Vyama vya Siasa tuendelee kuondoa chuki, ubaguzi wa dini, vitendo vya vurugu, kulinda amani na utulivu na ustawi wa Taifa hili, sisi wote ni Watanzania. Niendelee tu kutoa wito kwa wenzangu wote na viongozi wote wa vyama kutii sheria bila shuruti. Hilo ni jambo zuri na litaendelea kudumisha umoja wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja Tume ya Taifa ya Uchaguzi siyo huru, watendaji wake siyo huru, muundo wake siyo huru, jambo hili limesemwa sana. Mimi hapa leo ni Yohana Mbatizaji tu naandaa mapito ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mwenye Wizara yake atakuja kusema zaidi hapa. Nataka niseme jambo moja, Tume ya Uchaguzi imewekwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 74(1) na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 na kifungu cha 4(1) kinaeleza sifa ya Wajumbe wa Tume ya Taifa ya uchaguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa sifa za Wajumbe wawili tu kwanza kwenye Bunge hili kwa siku ya leo. Mjumbe wa kwanza ni Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi, sifa yake, anatakiwa awe Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufaa, tena amefanya kazi hiyo ya Ujaji kwa miaka isiyopoungua 15 na Makamu Mwenyekiti wa Tume hivyo hivyo. Wajumbe wa Tume sifa zao zinatokana na kifungu cha 4(1) kwenye Sheria, Sura 343.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijiulize kidogo, kwa namna hiyo ya aina na sifa za Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi na hasa hao Viongozi Wakuu (Majaji) na jinsi wanavyopatikana na Majaji hawa nimetoa mfano hapo mbele ndiyo hao hao wamehusika kutoa haki hata kwa vyama ambavyo ni vya upinzani, leo hii tunasemaje kwamba Tume hii ya Uchaguzi siyo Tume halali, haitendi haki? Naomba kwa kweli hebu tujaribu kujiuliza zaidi na tuendelee kuiunga mkono Tume yetu ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko hoja hapa zimesemwa kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri wanatuhumiwa wao ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi, walikuwa ni wagombea wa Ubunge kwenye Majimbo kupitia Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo Halmashauri 185 lakini humu ndani kuna Wabunge 392. Ukichukua Wabunge 392 ukasema hawa Wakurugenzi wote ndiyo waligombea ukagawa kwa hiyo 185 ina maana kila Halmashauri ina Wakurugenzi wawili na 1.18, sasa huo uhalali sijui unapatikana wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine kubwa, suala la uumini wa chama kwa kiongozi yoyote liko katika moyo wake na linatawaliwa na Sheria za Utumishi wa Umma. Naomba niseme kidogo, humu ndani ya Bunge letu wako Wabunge walikuwa ni wafanyakazi katika taasisi mbalimbali za Serikali lakini leo ni Wabunge kupitia vyama vya upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iko mifano tu wengine walikuwa mpaka Viongozi Waandamizi, Makatibu wakuu wa Wizara lakini wametoka na leo ni Wabunge wakiwakilisha vyama vingine. Tuna uhakika gani kwa tuhuma hii kwamba hawa Wakurugenzi wote niliowasema 185 eti ni waumini wakubwa wa Chama cha Mapinduzi? Naomba tukubali kwamba Tume ya Uchaguzi inaongozwa na Katiba, Ibara ya 74 na naomba muamini kwamba uchaguzi utakuwa huru na wa haki kama tulivyoingia, tutaendelea kuingia na Tume itaendelea kutusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Uchaguzi imeshafanya kazi kubwa, imeshafanya uhakiki wa vituo vya kupiga kura 37,814, kati ya vituo hivyo 407 viko Zanzibar. Imeshafanya majaribio ya vifaa vya kuboresha daftari kwenye Wilaya mbili Kisarawe na Morogoro. Imeshafanya maandalizi ya kuhakikisha kwamba kanzidata ya Daftari la Kudumu la Wapiga kura iko tayari na mifumo mingine yote iko tayari. Serikali imeshatenga bajeti kwenye MFUKO MKUU wa Serikali kwa ajili ya kuboresha Daftari vilevile kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge tuko salama, maandalizi yako salama, uchaguzi utafanyika kwa amani, tusiwe na wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja moja ililetwa na Mheshimiwa Bulembo kuhusu suala la kibali cha ajira ya wageni kwa mwekezaji mmoja. Naomba hii hoja nisiijibu kwa sababu mwaka jana hoja hii ilivyotolewa, eneo ambalo lilitakiwa lifanyiwe kazi na Ofisi ya Waziri Mkuu tumeshalikamilisha. Ombi la kibali cha mwekezaji huyu kuwa raia wa Tanzania limekwenda Uhamiaji, mwenye mamlaka ya kuzungumza jambo hili ni Waziri wa Mambo ya Ndani. Kwa hiyo, naomba niliache nisitolee ufafanuzi suala hili, Waziri wa Mmabo ya Ndani ndiye mwenye mamlaka ya kupitia sheria na kujua huyu mwekezaji kama atapewa uraia ama hawezi kupewa uraia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kuhusu namna gani Serikali yetu imeshirikiana na taasisi nyingine kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia programu mbalimbali. Nikuhakikishie kwamba tumekuwa na miradi ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa mfano, Mradi wa Miundombinu ya Masoko na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) umefanyakzi nzuri sana Bara na Visiwani. Mradi huu umewafikia wakulima wadogo wakiwemo wafugaji, wavuvi, wafanyakazi na umetoa mikopo kwa watu mbalimabli, umewawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wadogo vijijini, asasi za kifedha, vyama vya msingi vya ushirika na asasi zinazojishughulisha na usindikaji wa mazao.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo machache nitayasema hapa kama ni matunda ya mradi huu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambao umeongeza nguvu kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo. Kazi nyingine zilizofanywa na mradi huu ni pamoja na ukarabati wa barabara. Jumla ya kilomita 1,076.6 zimekarabatiwa pande zote mbili za Muungano na zimeweza kurahisisha sana usafirishaji wa mazao ya wakulima. Mradi huu umejenga na kukarabati maghala 35 ambayo yamekwishakukamilika na maghala sita yanaendelea kukarabatiwa. Vilevile wakulima wameweza kuunganishwa na huduma za fedha, zaidi ya shilingi milioni 300 zimekopeshwa kwa wakulima hao kupitia mpango wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili la ukarabati na ujenzi wa maghala, asilimia 40 ya wanawake katika maeneo hayo wameweza kunufaika na kuweka mazao yao katika maghala hayo. Mradi umejenga masoko 16 na matokeo yake programu hii ya ujenzi wa masoko imerahisisha wakulima kuwaunganisha na wafanyabiashara na kuuza mazao yao na Halmashauri zimeweza kuongeza mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mradi huu umeweza kutoa ruzuku za mashine na mitambo ya usindikaji wa mazao ili kuongeza thamani ya mazao. Kazi hiyo imefanyika vizuri, mashine takribani 34 zimeweza kusimikwa kwenye maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu ya Tanzania Bara na Visiwani. Kwa hiyo, kazi hiyo pia imefanyika kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi umeweza kuwajengea uwezo wazalishaji katika kuzalisha na kutafuta masoko na kuwaunganisha na masoko. Vilevile mradi umeweza kuongeza Mfuko wa Huduma za Fedha Vijijini kupitia asasi za kifedha. Pia mradi kabla haujafungwa umeanzisha Mfuko wa Dhamana yaani Guarantee Fund kwa ajili ya ubunifu kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Shughuli hii Mheshimiwa Waziri Mkuu ataizundua muda siyo mrefu. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge baada ya uzinduzi wa jambo hili tuungane pamoja ili kuhakikisha kwamba tunaitendea haki programu hii iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kwamba baadhi ya wanachama wa Chama cha CUF wamehamia ACT-Wazalendo na kuonekana kwamba Serikali inatumia nguvu kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa ili kukikandamiza Chama cha ACT. Waheshimiwa Wabunge, naomba tu niwaambie, Msajili haangalii chama hiki kikubwa, kidogo, kikoje yeye anafuata sheria na utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee tu kusema Waheshimiwa Wabunge, nguvu ya chama pia inapimwa pia na idadi ya Wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania. Sasa sisi wote tutajiuliza kama ACT- Wazalendo inaweza ikamtikisa Msajili ama kuitikisa Serikali nzima kwa sababu kiongozi mmoja ama wanachama fulani wamejiunga na Chama cha ACT-Wazalendo. Sisi wote nadhani tunaweza tukatafakari na tukapata majibu labda nisiendelee kusema zaidi ya hapo na jambo hili liko tu wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zimetolewa hoja kuhusu utendaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Naomba kukubaliana na Waheshimiwa Wabunge liko eneo bado halijakaa vizuri kwenye mifuko hii. Naomba kuwahakikishia kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tutajitahidi, tunachotaka ni kuhakikisha michango inafika kwenye mifuko kwa wakati, wastaafu wanafanyiwa uhakiki, ulipaji wa mafao unafanyika kwa wakati, usumbufu kwa wastaafu unaondolewa haraka sana. Wakurugenzi mko hapa naomba mnisikilize vizuri na kwa kweli tutaendelea kuchukua hatua kama haya tunayoendelea kuyaagiza hayatekelezwi na sisi kama Serikali hatutakuwa tayari kubeba dhamana yenu na ninyi ndiyo wenye wajibu wa kuyasimamia haya yote na kuhakikisha kwamba wastaafu hawaendelei kupata shida, wanaendelea kupata maisha mazuri hata baada ya kustaafu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Serikali kutumia nguvu nyingi kama Polisi wakati wa kusimamia uchaguzi. Najua iko sheria inasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani atakapokuja Waziri atatoa maelezo. Naamini kabsia suala la msingi hapa ni kufuata sheria bila shuruti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hizi ni nyingi kweli kweli lakini kwa sababu muda unapingana nami, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge maswali yaliyobakia tutayajibu kwa maandishi, nawashukuru sana kwa michango yenu. Naomba kuunga mkono hoja, ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi/ Vigelegele)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wote watatu wa Kamati zote tatu kwa ripoti nzuri ambayo ameweka hapa mezani. Pia nawapongeza Wajumbe wa Kamati hizo.

Kamati ya Sheria Ndogo ninawapongeza sana kwani wamekuwa ni msaada mkubwa sana katika maboresho na marekebisho ya makosa ya namna moja ama nyingine ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye sheria ndogo ambazo zimekuwa zikitungwa kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa lakini vilevile kwenye Serikali Kuu, Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mwenyekiti Andrew Chenge kwamba tutaendelea kushauriana na Kamati yake na Wajumbe ili tuweze kuboresha. Kama walivyosema, kwa kweli tumeanza kwenda vizuri ndani ya Serikali, wametupongeza, tunapokea pongezi hizo tutajitahidi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Kamati ya Tawala za Mikoa, Waheshimiwa Wabunge wamesema mengi, ninawashukuru pia. Kipekee nampongeza ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa na Kamati ya Katiba na Sheria. Kamati hiyo nayo imekuwa ni msaada mkubwa sana kwetu kwenye maeneo mbalimbali na hasa Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kweli wametusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisiti kusema, hata wewe uliyekalia kiti kama Makamu Mwenyekiti mmesaidiana sana na Kamati katika kuhakikisha tunafanya kazi zetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Wajumbe wote ama Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja hizi, lakini hasa niungane na wale Wabunge ambao wameanza kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri zinazofanywa na Serikali yetu. Vilevile nami bila kusita, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi anazozifanya. Niwathibitishie tu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote, Mheshimiwa Rais wetu amedhamiria kuleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu nasi wote tunayashuhudia kwa macho. Tumemshuhudia Mheshimiwa Rais pamoja na utendaji mbalimbali wa kazi ndani ya Serikali na Taasisi amefanya ziara za kikazi katika mikoa yote bila kubagua hata kwenye Majimbo ya Upinzani Mheshimwa Rais amefika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesikiliza kero za Watanzania, amezitafutia ufumbuzi, amefanya hivyo kwa mapenzi makubwa na dhamira ya dhati kabisa, tuna kila sababu ya kumpongeza na kumshukuru Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Makamu wa Rais na hata Waziri Mkuu mmeona, sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu tunaratibu kazi za Mheshimiwa Waziri Mkuu, mmemwona Waziri Mkuu kwa kweli naye amefanya kazi nyingi na kubwa katika mikoa yote na katika nchi nzima ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye baadhi ya hoja. Nawashukuru Wajumbe wa Kamati na Taarifa za Kamati nikiacha ile ya Sheria Ndogo nimeshasema, lakini Kamati ya Katiba na Sheria tunawashukuru, mmeendelea kuboresha katika maeneo ya Mfuko wa Vijana; naomba niwahakikishie kwamba mmetupongeza, tunataendelea kuongeza bidii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeamua Mfuko wa Vijana sasa hivi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu ubadilishe mwelekeo, kutoka katika kutoa mikoa midogo midogo kwa wajasiriamali wadogo wadogo, ile tutaicha TAMISEMI. Sisi sasa tunataka ku-concentrate na vijana ambao ni graduates, wana certificate, walioanzisha makampuni ili wakopeshwe fedha hizo, wafungue makapuni na miradi mikubwa ambayo itatoa ajira kwa vijana wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tumeli-present kwenye Kamati na Kamati mmeshuhudia, tumeshafanya mageuzi makubwa sana kupitia Mfuko wa Vijana; tunawahakikisha vijana na Waheshimiwa Wabunge, tunataka kuutumia mfuko huu tofauti na 10% ya Halmashauri twende sasa kwenye mitazamo ya ajira ambazo zinahusika na miradi mikubwa itakayofanywa kupitia kwenye mifuko wa vijana. Tutafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, tunajitahidi sasa hivi ili kuondoa gap ya ujuzi nchini. Tunazo program na mkakati wa Taifa wa kukuza ujuzi, kuhakikisha kwamba tunaondoa tatizo la ujuzi katika uwekezaji ndani ya Taifa letu. Kwa hiyo, tayari kazi hiyo inafanyika vizuri, Kamati mmeona na mmsema, nasi tutaendelea kufanya hivyo. Ili kutatua tatizo la ajira kwa vijana, tumekuja na program ya internship ambayo sasa tunawachukua vijana wetu graduates tunawapeleka kwenye private sector, wanakwenda kufanya mafunzo ya uzoefu na wengi wamekuwa sasa wakiajiriwa huko kwenye private sector. Kwa hiyo, Kamati imetushauri mambo mengi na tunaipongeza tunawashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa sana pia ndani ya Bunge na hasa Wabunge wa Upinzani kwamba Serikali hii haijali Wizara ya Kilimo na sekta ya kilimo. Naomba tu niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, kwenye utaratibu wa kupitia bajeti; bajeti za Serikali ni bajeti zinazochukua sura ya kisekta. Ukichukua bajeti ya Wizara ya Kilimo utaikuta kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara, utaikuta kwenye Wizara Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekuwa budgeted huko na kwenye Wizara nyingine. Hata kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu hata sisi pia tuna bajeti ya kilimo ambayo inaenda kutekeleza miradi ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawapa mfano, tulikuwa na programu ya MIVARAF ya kuongeza thamani ya mazao na miundombinu ya masoko. Mradi huo peke yake kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda kwenye sekta ya kilimo tumetumia bilioni 282.16 na hizo zote zimetoka tena programu hii imewanufaisha Bara na Visiwani pande zote mbili za Muungano. Tumeweza kujenga masoko mapya, masoko mapya peke yake 16 na nyie Wajumbe wa Kamati ni mashahidi, tumekarabati masoko matano, tumejenga maghala mapya 29 katika hiyo programu.

Lakini tumeweza kujenga miundombinu ya barabara na mpaka sasa programu hiyo imeweza kusaidia sana usafirishaji wa mazao kutoka shambani kwa sababu ya kuboresha miundombinu ya barabara kwa sasa tani za usafirishaji wa mazao kwenye programu hii zimetoka tani 230 mpaka 808 kwa sababu ya programu hiyo.

Sasa tunashangaa kama kuna wenzetu wanasimama hapa ndani halafu wanabeza kazi nzuri hii inayofanywa na Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli. Haiwezekani. (Makofi)

Ninaomba tunapokuwa tunachangia humu ndani tupingane kwa facts sasa mtu anaenda anachukua kipande kidogo tu, akichukua hicho kipande kidogo ndiyo anatangaza kama ni jambo zito kweli kweli. Naomba niwaambie Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mpango wa bajeti za kiwizara tunao mpango na mfumo wa bajeti za kisekta, bajeti ya maafa haiwekwi kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu peke yake, itawekwa miundombinu barabara watawekewa, madarasa wataweka TAMISEMI, wataweka Wizara ya Elimu, vituo vya afya watapeleka Wizara ya Afya huo ndiyo utaratibu tunaenda kileo zaidi na tunawaambia kwamba Serikali hii imejipanga kweli kweli mtatutafuta hamtatupata, lakini sisi tunasonga mbele na vitu vyetu vinaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaendelea programu hii pia imepunguza muda wa kusafirisha mazao. Kusafirisha mazao kabla ya programu hii ni ya kilimo tumebeza sana hapa fedha za kilimo, wakulima walikuwa wanatumia masaa matatu sasa wanatumia chini ya nusu saa moja na nusu kusafirisha mazao yao.

Kwa hiyo naona kwamba tumeboresha sana sana. Lakini naomba nikubaliane na ninyi yako maeneo mengine bado tunatakiwa kuyafanyia kazi zaidi, kwa mfano kwenye suala la uwekezaji na biashara tunalo Baraza la Biashara la Taifa wanafanya kazi nzuri lakini sisi sasa ndani ya Serikali tumeamua kutengeneza mifumo, mfumo wa ki-TEHAMA wa utoaji wa vibali vya ajira kwa wageni ili mfumo uwe wazi, usiwe na usumbufu wa kusababisha kero na mlolongo mkubwa kwa wawekezaji wanapotaka kupata vibali vya wageni kama ni TIC ama kwenye sekta nyingine kazi hiyo tunaifanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa masuala ya local content na local content ipo pia ndani ya ofisi yetu na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, ambalo linasimamia sheria ya mwaka 2004 na sera ya mwaka 2004 imeendelea kufanya kazi zake vizuri. Tulichokifanya Waziri Mkuu amezindua Mkakati wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile tumezindua muongozo wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na baada ya kuyafanya hayo matokeo chanya yamepatikana, kwa mfano wakati wa ujenzi wa Daraja la Mfugale, Daraja la Mfugale lilikuwa linahitaji wafanyakazi 616 lakini wafanyakazi waliofanyakazi katika ujenzi wa daraja la Mfugale, 589 ni Watanzania na 27 ndiyo walikuwa wafanyakazi wa kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, manunuzi kwenye sekta ya manunuzi tulikuwa tunataka makampuni 15 lakini kwenye manunuzi makampuni 14 yalikuwa ya Kitanzania na kampuni moja tu ndiyo lilikuwa kutoka nje ya nchi ya Tanzania. Kwa hiyo, miradi hii ya kimkakati inafanyakazi vizuri sana kwenye dhana ya local content, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge muendelee kutuunga mkono, tutayasimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kwenye suala la mwisho na lenyewe ni kuhusu uchaguzi sasa hapa naomba Waheshimiwa Wabunge mnisikilize vizuri. Kwenye suala la uchaguzi tumeshaanza kuboresha daftari la mpiga kura awamu ya kwanza na kwenye kuboresha daftari la mpiga kura awamu ya kwanza, umeshafanya route 13 kati ya route 14 imebakia route moja tu mikoa miwili Pwani na Dar es Salaam, na tukishamaliza route ya 14 tunaanza uboreshaji awamu ya pili kwa mujibu wa sheria, kwa hiyo siyo kweli kwamba eti hatujajipanga, tumejipanga vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namuomba tu Halima atulie, ninachotaka kusema tulikadiria kuandikisha, kuboresha daftari kama ni kuandikisha wapiga kura wapya, kama nikubadilisha maeneo ya kupigia kura, kama ni jambo lolote linalohusiana na uboreshaji, tulitarajia uboreshaji huo uwe wa asilimia 17 lakini ajabu wananchi wamejitokeza wengi wamekuja kuboresha, wengi wamekuja kujiandikisha uboreshaji mpaka sasa umefika 29% ya wapiga kura wa mwaka 2015. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba wanaimani na Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli, na wanajiandaa kuhakikisha kwamba wanaingia kwenye uchaguzi. Sasa tunaambiwa kwamba hapa hii tume sijui ya uchaguzi siyo huru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-quote tu Katiba ya Jamhuri ya Muungano kifungu cha 74 (7) kifungu hicho cha 7 kinasema, kwa madhumuni ...

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu jamani.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima naomba tumwachie amalize

MHE. HALIMA J. MDEE: Sasa hizi hoja ni za Wenyeviti sasa huyu hoja siyo yake anajibu kama hoja ya kwake?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jenista naomba umalizie endelea, naomba uendelee.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaanza upya eneo hili. (Makofi/Kicheko)

Kwa utaratibu wa shughuli zetu za Bunge...

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, naomba mtulie amalizie, Mheshimiwa Jenista naomba umalize.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo heshima sana ya kiti chako na ninaomba niendelee kusema, Ibara ya 74(7), (11) na (12) labda nisome ile ya 11 katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii Tume ya Uchaguzi haitalazimika kufuata amri ama maagizo ya mtu yeyote, au idara yoyote ya Serikali au maoni ya chama chochote cha siasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mifano dhahiri tu na ninaomba Waheshimiwa Wabunge Tume hii imefanya kazi toka ilipoundwa kwa mujibu wa sheria na mfano mzuri mwaka 2010 tulipofanya uchaguzi kwa sababu Tume hii ni huru hata kama kunatokea mashtaka ya matokeo ya uchaguzi, tulijifunza kwa mfano wananchi wa Jimbo la Arusha walikwenda kupinga ushindi wa Godbless Lema mahakamani, lakini Tume ya Uchaguzi kwa sababu ni huru ilisimama na ilimpasa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aungane na Tume kumtetea Godbless Lema na akabaki kuwa Mbunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine mwaka 2015 Mheshimiwa Mbunge Chief Whip Ester Bulaya, Mheshimiwa Wasira alipinga matokeo ya Ester Bulaya, lakini kwa sababu Tume hii ni huru Mwanasheria wa Serikali alisimama na Tume ya Uchaguzi na walimtetea Ester Bulaya na leo ni Mbunge mpaka leo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Ninataka kusema nini, nataka kusema hivi kifungu cha 74(7), (11), (12) kimeeleza kabisa tume yetu ni tume huru labda tu kama tunataka kuibadilisha jina, lakini kwa mujibu wa Katiba tume hii ni huru na inafanyakazi zake kwa uhuru bila kuagizwa na chama chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuingie kwenye uchaguzi tukapambane kwa hoja chama ambacho kitakuwa na hoja za msingi kitashinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nitoe shukrani na pongezi za dhati sana kwa Waziri mwenye dhamana ya Fedha na Mipango. Tunamshukuru sana na tunampongeza kwa kweli kwa Mpango mzuri, Mpango utakaotuvusha nchi yetu katika kutupeleka kwenye Taifa na hali ile tunayoitaka, Taifa la kipato cha kati. Mheshimiwa Waziri wa Mipango tunakushukuru na tunakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kusema mambo machache sana. Nafurahi kuona kwamba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Fedha na Mipango sasa ametuletea dira inayotupeleka kujibu hoja kubwa sana ya ajira kwa vijana wa Tanzania Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo yote Mheshimiwa Rais wetu wakati akiwa kwenye kampeni za uchaguzi, hoja iliyotawala kwa vijana wa Tanzania ni namna gani wanaweza kutengenezewa mazingira ya kupata ajira kwa utaratibu wa aina tofauti na kwa misingi ya ajira za aina tofauti.
Kwa hiyo, Mpango huu ukiutazama na hasa mtazamo huu wa kulifanya Taifa letu sasa liende kuwa Taifa la viwanda na viwanda vile vikiwa katika level mbalimbali, naomba niwahakikishie vijana wa Tanzania tatizo la ajira sasa litakwenda kutatuliwa kwa kiasi cha kutosha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wanahitaji sasa watambuliwe. Mchango wao kwenye maendeleo ya Taifa hili ueleweke wazi, lakini wanahitaji kuwezeshwa, kutengenezewa miundombinu ambayo itawasaidia kushiriki katika uchumi wao wa Taifa. Mpango huu unatuelekeza huko na Mpango huu unatuambia kama tunakwenda kufungua viwanda kazi yetu sisi sasa, kama Wizara ya Kazi, ni kuhakikisha tunaanza kuwa na programu maalum, moja; ya kuwafanya vijana waweze kupata mitaji na mifumo itakayowafanya waweze kupata fedha za kujiingiza katika Mpango huo wa Maendeleo.
La pili, ni lazima sasa kupitia Wizara hii tujipange kuona vijana hawa sasa wanapata ujuzi, zile skills zinazohitajika ili waweze kujiajiri na kuajirika katika kujenga uchumi huu na kukamata uchumi wa nchi yao. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge muunge mkono mapendekezo haya ya Mpango ili tatizo la ajira katika nchi yetu ya Tanzania tuweze kulitatua kwa kiasi cha kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme; Mpango huu pia, unakwenda kujibu hoja nyingi sana za muda mrefu za kundi maalum kabisa la wenye ulemavu katika nchi yetu ya Tanzania. Mpango huu sasa pia, utakwenda kutafsiri sheria na mikakati mbalimbali ambayo itakwenda kuwaruhusu watu wenye makundi ya ulemavu katika hatua mbalimbali na wao washirikishwe katika mipango ya maendeleo. Waweze kushiriki katika uchumi, waweze kushiriki katika uzalishaji, waweze kushiriki katika shughuli zote ambazo zitajitokeza kwa kuzingatia Mpango tulionao.
Kwa hiyo, naomba niwaambie Watanzania, Mpango ulioletwa na Serikali unakwenda kujibu matatizo mengi katika nchi yetu ya Tanzania na kama tulivyoona tutakapokuja kuunganisha Mpango huu sasa na bajeti, utajibu mambo mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana ambao wamesoma, vijana ambao wako kwenye elimu za kati, vijana ambao wako vijijini, unaona kabisa Mpango huu sasa tutakwenda kujipanganao na hayo matatizo yote ya makundi hayo yatakwenda kupatiwa majibu. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tutaendelea kuyashughulikia yale mnayotuambia ili tuweze kupata majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa hapa mambo mbalimbali, kero za dawa za kulevya; naomba niwaombe Watanzania wote tushirikiane kwa pamoja. Kama tunazungumzia maendeleo ya uchumi, tusipopambana na dawa za kulevya vijana hawa tutashindwa kuwashirikisha katika kujenga uchumi wa nchi yetu ya Tanzania. Sheria na mikakati yote itakayoletwa na Serikali tuiunge mkono, ili …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii na naomba Serikali iende mbele.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani nitatumia dakika chache tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba kama ni kwa muktadha ya taarifa ya PAC ambayo tunayo hapa mezani leo na hasa katika suala la Mradi wa Dege; taarifa ya PAC imejipambanua wazi imesema ukienda ukurasa wa 18 kwamba PAC ilishafanya kazi yake na tarehe 13 Februari, 2017 imewasilisha taarifa ya kamati ndogo ilyoundwa ndani ya PAC kwa Mheshimiwa Spika ili utekelezaji wa yale yaliyopendekezwa na kamati kuhusu Mradi wa Dege yaweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda ukurasa wa 44 wa Taarifa ya PAC inasema unaiagiza na kuipendekeza kwa Serikali kwamba Serikali itekeleze mapendekezo ya kamati yanayohusu Mradi wa Dege mapema iwezekanavyo ili kuokoa fedha za umma zilizowekwa katika mradi huu. Ndiyo maana nimekwambia hapa mimi nasimama wala siwezi kutumia dakika nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tunaagizwa kutekeleza maagizo ya kamati tunasubiri basi Bunge tuleteeni kwasababu bado hatujapokea taarifa hiyo ili sisi tuweze kutekelezwa hayo yaliyoagizwa na Kamati ya PAC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mara mtakapokuwa mmetuletea tutafanya wajibu wa kutekeleza lakini wakati huo tunaposubiri tumeshafanya kikao na bodi yetu ya NSSF, Bodi yetu ya NSSF tulicho waagiza ni kuhakikisha wana hakikisha ile fedha bilioni 219 ambazo ni fedha za wanachama, kama kuna mazungumzo, kama kuna jambo lolote, jambo la kwanza ni kuhakikisha bilioni 219 hazipotei ambazo ni fedha za wanachama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuisema hapa ni kwamba PAC tunawapongeza, mnaendelea kufanya kazi zenu kwa utaratibu unaotakiwa. Kwa hiyo, mara mtakapotukamilishia, mkatuletea ripoti na mkaona ripoti hiyo inatakiwa ije Serikalini ili Serikali tutekeleze yale mliyoagiza sisi kama Serikali tuko tayari na tunawasubiri; tuleteeni tuweze kuchukua hatua mtakazozisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, jana tumetunga sheria ya kuunganisha mifuko na nilishawaambia kwamba kwenye suala la madeni ya Serikali kwenye mifuko na hasa fedha ambazo zinahusu michango ya wanachama Serikali tayari imeshalipa trilioni 1.3 ili kuhakikisha kwamba michango ya wanachama inakuwa salama. Masuala mengine tunamwachia Mheshimiwa Waziri wetu wa fedha ataendelea kuyafanyia kazi kwa utaratibu unaotakiwa

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niokoe dakika zako, kwa sababu haya ndiyo yaliyojiri kwenye sekta ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ninakushukuru kwa kunipa muda.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
kwa kudra za Mwenyezi Mungu, naomba kwanza nichukue nafasi hii na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha kwenye mkutano huu wa Kumi na Tisa. Huu ni mkutano wetu wa mwisho katika kipindi cha miaka mitano. Inshallah Mwenyezi Mungu ametupa uhai tumeweza kufika siku hii ya leo. Kwa vile tunakwenda kwenye uchaguzi, naomba nianze kwa kukutakia wewe binafsi kila la kheri katika uchaguzi mkuu ujao. Tunaamini utapita kwa kishindo na dua za kupita bila kupingwa zikaanguke juu yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nimtakie Mheshimiwa Waziri Mkuu kila la kheri. Bosi wetu, kiongozi wetu mkuu na yeye akapite bila kupingwa ili kuonyesha ni namna gani tunaweza kufanya kazi nzuri. Siwezi kuacha kusema nakitakia kila la kheri Chama changu cha Mapinduzi kikashinde kwa kishindo. Hizo lugha za kushindwa zinazotoka upande mwingine zishindwe na zilegee na tutakwenda kushinda kwa kishindo kabisa. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuweza kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Sambamba na kukushukuru kwa kunipa nafasi kwa dhati ya moyo wangu nakupongeza sana, wewe umeunganisha sifa za Maspika wote. Kama ni standard wewe umekuwa na standard iliyopitiliza, kama ni kutumia utaratibu na mifumo wewe umepitiliza, kwa kweli unastahili sifa zote na pongezi. Vilevile nipongeze timu ambayo imekusaidia sana Naibu Spika, tumemwona hapa amefanya kazi nzuri, Wenyeviti wa Bunge na viongozi wote wakiongozwa na Katibu wa Bunge kama Mtendaji Mkuu ndani ya Bunge. Kwa kweli tunawashukuru mmefanya kazi vizuri, mmetusaidia sana Serikali kuweza kutekeleza majukumu yetu na hasa yale yanayohusiana na shughuli za kibunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niungane na Mawaziri wenzangu na Wabunge wote ambao wamempongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Wamempongeza sana inajieleza wazi hotuba ya Waziri Mkuu kwa nini Rais huyu anastahili hizo pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upande wangu naomba niongeze mambo machache kwa nini tunampongeza Rais huyu. Rais huyu ni Rais mwenye msimamo thabiti pale yanapokuja maslahi ya Taifa la Tanzania. Rais wetu huyu ana sifa nyingine ya kutokuyumba wala kuyumbishwa kwenye maamuzi ambayo yanakwenda kuleta maendeleo kwa Watanzania na nchi yetu. Tumeshuhudia Rais wetu ni shujaa na jasiri kweli kweli na mmeona katika mambo magumu ambayo Taifa hili lilitakiwa lipite Rais wetu amesimama kuwa jasiri na shujaa hakutetereka anastahili pongezi sana. Rais huyu anasifa ya kuwa mwenye kujali, mmeona katika ziara zake anavyojali maisha ya Watanzania na anavyoumizwa na maendeleo ya nchi hii nani Rais kama Magufuli? (Makofi)

WABUNGE FULANI: Hakuna. (Makofi/Vigelegele)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, Rais wetu ni namba moja na anastahili sifa zote kwa kweli.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema Rais huyu amejipambanua kuwa ni Rais mnyenyekevu lakini ni msikivu na mstahimivu. Haya yote unayaona, hasemi mwenyewe matendo yake ndiyo yanajidhihirisha. Ukimkuta Kanisani anadhihirisha hayo matendo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ni kwa nini amekuwa msikivu na mnyenyekevu, amebezwa na watu ambao yeye ndiyo anawaletea maendeleo. Rais wetu Mwenyezi Mungu akubariki na akuongezee miaka mingi. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, nadiriki kwa kumaliza eneo hili la Rais wetu kwa kusema, tumepata Rais bora mwenye maono ya dhati kabisa, msimamo thabiti, mkweli, anayewajali wananchi wake na aliyekubali kuwa tayari kufia Taifa letu la Tanzania, Mwenyezi Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kunipa fursa na nafasi ya kuweza kutumikia katika Serikali yake na leo tunaingia kwenye bajeti ya tano tukiwa tunamaliza miaka mitano. Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani uliyonipa mpaka kufika hatua hii ya siku ya leo. Pia nimshukuru sana Makamu wa Rais, mama yetu Mama Samia, kwa kazi nzuri, na hasa kumsaidia Rais wetu. Tumemuona amekuwa msaada mkubwa kwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa dhati niungane na Waheshimiwa Wabunge kumshukuru sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa. Kwangu Mheshimiwa Waziri Mkuu alitumia taaluma yake ya ualimu kunifundisha mwalimu mdogo Jenista, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli amejidhihirisha katika kutusaidia kutenda kazi zetu ndani ya Serikali kwa sababu amefanya kazi kwa weledi mkubwa sana.

Naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu; tunakushukuru, tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu kila la heri katika maisha yako yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siwezi kuacha kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Angellah, pacha wangu, mdogo wangu, Waziri mwenzangu, lakini nawashukuru sana wadogo zangu, vijana shupavu; Mheshimiwa Antony Mavunde na Mheshimiwa Stella Ikupa. Hawa kwa kweli kama ni uteuzi ulipata mahali pake, ni vijana wachapakazi kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwashukuru sana washirika wangu katika kazi ya utatu, Vyama vya Wafanyakazi, Vyama vya Waajiri na tasisi zote zinazosimamia masuala ya kazi. Mambo haya yasingewezekana kama sio Makatibu Wakuu watatu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambao walikuwa ni mhimili mkubwa sana wakiwaongoza watendaji wote, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na Taasisi zote ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tumefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niwaambie Wanaperamiho, nawapenda na nawashukuru sana. Wameendelea kuniamini, naomba waendelee kuniamini, wembe ni uleule na mwaka huu wa 2020 kitaeleweka tu. Nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Peramiho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shukrani zangu za dhati katika kipindi hiki cha miaka mitano zimuendee Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, kaka yangu, Mheshimiwa Omary Mchengerwa na Makamu Mwenyekiti, dada yangu Mheshimiwa Najma Giga, Wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria wamesoma hotuba yao hapa, wameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya kazi vizuri sana, ni kwa sababu wao walitushauri vizuri, nawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana kaka yangu, Mheshimiwa Oscar Mukasa na Mheshimiwa Dkt. Tisekwa na Kamati nzima ya UKIMWI, tumefanya kazi kubwa sana kwa pamoja, nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Kamati ya Bajeti ikiongozwa na kaka yangu, Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki na hasa kwenye Mfuko wa Bunge. Kamati hii iliisaidia kuiambia Serikali mahitaji ya Bunge ili Bunge liweze kutekeleza kazi zake za Kibunge; nawashukuru sana Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Spika, siwezi kumaliza shukrani zangu bila kumtaja Mheshimiwa Mtemi Chenge na ndugu yangu, Mheshimiwa Ngeleja, Kamati ya Sheria Ndogo na Wajumbe wa Kamati hiyo tumefanya nao kazi sana sisi ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ninawashukuru sana Wajumbe hao wote.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pia shukrani za dhati kwa Wabunge wote. Kazi hii ya kuwa Chief Whip hapa mbele isingewezekana kama Wabunge wote upande wa Upinzani na Chama Tawala wasingenipa ushirikiano. Nawashukuru sana na Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kutoa msisitizo kwamba pongezi zetu na shukrani hizi tunazozitoa zinatoa fursa kwetu sisi kama Serikali kuweza kujifunza mambo mengi, lakini katika kipindi hiki pia tumepata taarifa za misiba, majanga ya mafuriko na vitu mbalimbali ambavyo vimepoteza baadhi ya wenzetu. Nitoe pole kwa Chama cha CUF kwa kupotelewa na kiongozi wa chama; nitoe pole kwa TBC kwa kumpoteza mtangazaji mahiri aliyesaidia kuihamishia Serikali hapa Dodoma, tunawapa pole sana. Vile vile tunawapa pole na wengine waliokumbwa na majanga ya namna moja ama nyingine.

Mheshimiwa Spika, naomba nimalize eneo hilo la kwanza kwa kusema yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, tunaingia kwenye Uchaguzi Mkuu, tunapoingia kwenye Uchaguzi Mkuu watu wamekuwa wakitafakari na kuomba uchaguzi huu uwe huru na uwe uchaguzi wa haki. Naomba kuwaomba sana Vyama vya Siasa vyote nchini, wadau wa demokrasia na wadau wengine wote, ili uchaguzi huu uishe salama, naomba sana tufuate sheria bila kushurutishwa, tutii kanuni na taratibu na miongozo itakayotolewa na Tume ya Uchaguzi. Kwa kufanya hivyo ndiyo tutakuwa na uchaguzi huru na uchaguzi wa haki na sio vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa mujibu wa Kanuni ya 99(2) nitaendelea kujibu hoja kadhaa na zile ambazo sitapata nafasi ya kuzijibu naomba tutazileta kwa maandishi na zitaingia kwenye Hansard ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza kutoka Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, kama nilivyosema pale mwanzo walitupongeza sana kwa kazi nzuri ambayo imefanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu na hasa katika kukusanya maduhuli. Idara moja tu ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali kwa muda mfupi sana waliweza kuvuka lengo la maduhuli ambayo walikuwa wamepangiwa na tukaweza kufikia zaidi ya asilimia 80 kabla mwaka haujaisha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge Ofisi ya Waziri Mkuu ni Ofisi Kiongozi, ndiyo inayotakiwa kuonesha njia. Tutajitahidi kuhakikisha hii standard ambayo tuko nayo tunailinda ili tusimwangushe Waziri Mkuu na tusiiangushe Serikali kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ilizungumzwa sana na Wabunge wa Upinzani, alizungumza sana Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mheshimiwa Mwakajoka, Mheshimiwa Susan, Mheshimiwa Bungara, Mheshimiwa Sophia Mwakagenda na hii ilikuwa inahusu Tume Huru ya Uchaguzi; hoja hii imezungumzwa sana. Tumekuwa tukijibu hoja hii mara kadhaa hapa Bungeni na tumekuwa tukiendelea kueleza ipasavyo kwamba Tume hii ya Uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukienda Ibara ya 74(7) imetamkwa kabisa kwamba taasisi hii ya Tume ya Uchaguzi ni taasisi huru; imetamkwa kabisa. Pia ukienda Ibara ya 11 inaonesha kabisa Tume ya Uchaguzi haitaingiliwa na mtu yeyote, hata vyama vya siasa, katika kufanya maamuzi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kujua ni jambo moja; ninao hapa mfano wa tume hizo ambazo zina jina la tume huru ambazo ziko katika nchi mbalimbali kwenye regions ambazo na sisi ni wanachama, lakini tume hizi zote zinazoitwa ni tume huru ni lazima tujiulize misingi yake kwanza ya tume yoyote ya uchaguzi ni ipi ambayo inatakiwa kuangaliwa ili kuweza kuipima tume hiyo?

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa la kwanza ni kuangalia muundo wa tume hiyo. Tume hizi zote zimewekwa kwa mujibu wa Katiba ya kila nchi, hata tume yetu sisi imewekwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi yetu ya Tanzania. Lakini tume hizi zinapimwa kwa utendaji wake katika misingi ya kufuata sheria na kanuni; Tume yetu hii pia imewekwa kwa mujibu wa sheria na inafuata sheria na kuweka utaratibu wa kikanuni wa kuendesha mambo yake; huo ni msingi mwingine.

Mheshimiwa Spika, Tume yetu imeendelea kupimwa kwa mwenendo wake unaoakisi weledi wake katika kufanya na kusimamia chaguzi. Hili linapimwa namna gani; tunaipima tume ndani ya nchi lakini viko vyombo vya kimataifa vinaipima Tume yetu ya Uchaguzi kama inafuata weledi na inazingatia sheria. Hao wote wamefanya hiyo kazi na hakuna hata mara moja waangalizi wa kimataifa wamesema Tume hii sio tume bora na haifai kuendelea kusimamia uchaguzi katika Nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nilisema pale mwanzo; tume hii imeundwa kwa mujibu wa Katiba na tume hizo nyingine zilizopewa majina ya huru zinakuja kujifunza kwenye tume yetu. Sasa nimesema kama imewekwa kwa mujibu wa Katiba ina maana hii ni tume inayowawakilisha Watanzania na imewekwa na Watanzania wenyewe kwa sababu Katiba ni document ya Watanzania wenyewe.

Mheshimiwa Spika, nimeendelea kujiuliza; ninayo hapa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bunge la Jamhuri ya Muungano linawekwa na Sura ya Tatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia, naomba nisome kifungu cha 63(2) kwamba; 63.-(2) Sehemu ya Pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.

Kwa hiyo sisi hapa Wabunge tuna madaraka kwa niaba ya wananchi, lakini tunatekelezaji majukumu yetu kwa madhumuni ya madaraka hayo tuliyopewa? Kifungu cha 63(3)(a) kinasema tunaweza kutekeleza majukumu yetu kwa niaba ya wananchi kwa kuuliza maswali kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yako katika wajibu wetu wa kila siku.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Chief Whip katika Bunge lako hili, nimefanya utafiti mdogo; mpaka hapa tulipofika tumeuliza maswali ya msingi 3,545; tumeuliza maswali ya nyongeza 9,317. Maswali hayo na naomba niendelee kusema nimefanya utafiti mdogo ambao wewe ndio unaweza ukasema vizuri zaidi kwa sababu ni utafiti wa Bunge; Mbunge wa Upinzani ambaye ameongoza kwa kuwa na maswali mengi ya msingi na ya nyongeza ana maswali 52; na Mbunge wa Chama cha Mapinduzi ambaye ameongoza kwa kuwa na maswali mengi, huu ni utafiti wangu mdogo, unaweza kufanya zaidi – ana maswali 103.

Mheshimiwa Spika, nimefuatilia, kati ya maswali hayo yote 9,317 yaliyoulizwa kwa mujibu wa Katiba iliyotupa madaraka ni maswali mangapi yameulizwa kuhusu Tume huru ya Uchaguzi, maswali hayo hayafiki hata asilimia moja ya maswali yote yaliyoulizwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya hapo nimejiuliza ajenda ya Tume Huru ya Uchaguzi ni agenda ya Watanzania ama ni ajenda ya watu wachache? Kwa hiyo hayo mambo ni lazima tuyaangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeendelea kufuatilia, hotuba zinazosomwa wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu kutoka upande wa Upinzani, nimeendelea kufanya huo utafiti; mwaka 2014 hotuba wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu ndani ya Bunge hili ilibeba hoja ya Katiba Mpya; 2015 hotuba ya Kiongozi wa Upinzani wakati wa Hotuba ya Waziri Mkuu ilibeba ajenda ya Katiba Mpya; mwaka 2016 hotuba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ilibeba hati idhini ya Mawaziri kufanya kazi kutoka kwa Rais; hotuba ya mwaka 2017 ilibeba dhana ya kesi za Wabunge wa Upinzani. Sasa najiuliza hivi kipaumbele cha wale ambao wanasema sasa ni lazima tupambane kwa ajili ya Tume huru ya Uchaguzi badala ya yale ambayo ni matakwa ya wananchi; wananchi wanataka maji, barabara, kilimo, elimu, afya, na hayo tumeyafanya vizuri sana katika kipindi chetu chote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ilikuwa tuhakikishe kwamba uchaguzi wa mwezi Oktoba, 2020 usibague vyama vya siasa, wote twende tukiwa na haki sawa. Tunapokea ushauri wao lakini tunataka tukumbushe kidogo; vyama vingi vya siasa vilianza toka mwaka 1992 katika Nchi yetu ya Tanzania. Tume ya Uchaguzi hii ambayo ni tume huru kwa mujibu wa Katiba imeanza toka mwaka 1993 ikaanza kusimamia uchaguzi wa mwaka 1995.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1995 wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu walikuwa wanne, Vyama vya Upinzani na Chama cha Mapinduzi, kwa hiyo tume haikujali nani anagombea ilitekeleza wajibu wake. Wabunge 186 walishinda wa Chama cha Mapinduzi na Wabunge 46 wa Upinzani. Mwaka 2000 wagombea urais walikuwa wanne, mchanganyiko wa vyama, Wabunge walioshinda 202 CCM, 29 Upinzani.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2005 wagombea urais walikuwa 10, wapinzani tisa CCM mmoja, wote waligombea na Tume hiyo ya Uchaguzi haikujali misingi ya vyama. Wabunge walioshinda walikuwa 206 CCM, 26 walikuwa kutoka Upinzani. 2015 wagombea urais pia walikuwepo, Wabunge walioshinda 195 walikuwa wa Chama cha Mapinduzi, 65 walikuwa wa Upinzani. Hao ni Wabunge kwenye Majimbo.

Mheshimiwa Spika, kama hivyo ndivyo, naomba kuwahakikishia Watanzania uchaguzi huu utasimamiwa vizuri, vyama vyote vitapata haki sawa, vitashiriki ipasavyo, lengo letu liwe moja; kulinda amani na utulivu wa nchi yetu ili uchaguzi uweze kuisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni kuhusu UKIMWI. Kwenye suala la mapambano dhidi ya UKIMWI ilikuwa ni Mfuko wa ATF. Tulikuwa tumeulizwa kuhusu fedha za wafadhili, tuliulizwa kuhusu masuala ya ukusanyaji wa data na uwezo wetu wa ndani katika kukabiliana na tatizo hili la UKIMWI. Tunamshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya UKIMWI, Makamu wake na Wajumbe, walitushauri vizuri sana na sisi tumeanza kutekeleza

Mheshimiwa Spika, kwanza, ili kuifanya ATF ijitegemee bodi imekamilisha mpango mkakati wa kuhakikisha tunakusanya rasilimali za kutosha za ndani lakini Bodi ya Mfuko huo pia imeshafanya kazi ya kumwajiri Resource Mobilization Manager ili aweze kukusanya uwezo wa kuhakikisha Mfuko huu unakuwa na kazi. Tumepata Mshauri Elekezi wa kutusaidia kuhakikisha fedha za mfuko huu zinakusanywa. Hata hivyo, tunaishukuru Kamati na tunaendelea na majadiliano kati ya Kamati na Serikali kuwa na vyanzo vya uhakika vya Mfuko wa UKIMWI Tanzania.

Mheshimiwa Spika, vilevile tunawashukuru wafadhili, wameendelea kutoa commitment yao. PEPFAR kwa mwaka 2020/2021 wameongeza bajeti ya UKIMWI katika nchi yetu kwa asilimia nane, kwa hiyo tunawashukuru sana. Kwa hiyo tutaendelea kufanya hizo kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, tumeanza mradi Serikali, TACAIDS na shirika ambalo linatusaidia katika mapambano dhidi ya UKIMWI nchini la Umoja wa Mataifa UNAIDS, tumeamua kutengeneza mradi wa pamoja wa ku-train utaratibu na mfumo mzuri wa ku-collect data kutoka katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na UKIMWI. Kwa hiyo tunayafanyia kazi hayo yote.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kuhusu Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Nchini. Hoja ya kwanza ilikuwa ni kwa nini hakuna mradi wa maendeleo; tumepokea ushauri huo, lakini kwa kuanzia tumeamua kutumia Fungu 65 kwenye Mradi wa Skills Development kuanza kuwafundisha wale wote wanaoacha kutumia dawa kuwapa mafunzo ya ufundi ili waweze kujiajiri. Nadhani jambo hili litawasaidia sana vijana wetu na wataondokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, tuliagizwa tukamilishe maabara ya kitaifa ya kuhakikisha tunakuwa na maabara ya kupima sampuli za dawa za kulevya, hasa kesi zinavyotokea na ukamataji. Hiyo maabara tumeanza kuifanyia kazi, vifaa vyote tumekwishanunua, tunachosubiri sasa hivi ni kupata miongozo ya TBA ili jengo letu liweze kutengenezwa vizuri na hayo yote yaweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, wametusaidia kutushauri Kituo chetu cha Itega kiwe ni kituo cha kitaifa kitakachokuwa na combination ya kazi kuhusu waraibu. Kwa hiyo pale itakuwa ni medication center, itakuwa ni vocation center lakini itakuwa ni counseling center. Tunataka kukigeuza Itega iwe ni model ya vituo vyote vitakavyoanza kujengwa katika Nchi ya Tanzania. Kwa hiyo tunazingatia jambo hilo na tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, tumeweza kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya nchini kwa asilimia 90 na sasa hivi bei ya dawa ya kulevya Tanzania kwa kilo moja imefika Dola za Kimarekani 12,000, lakini kwa nchi nyingine ambazo udhibiti bado haujawa mkubwa bado kilo moja inauzwa kwa 4,000 tu. Kwa hiyo hiyo ni kazi nzuri iliyofanywa na nadhani tuwapigie makofi sana na tuwapongeze wenzetu kwa kazi nzuri waliyoifanya.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na hoja za Bunge. Bunge limepewa pongezi sana kwa kazi nzuri uliyoifanya wewe mwenyewe na hasa kuanzisha Bunge Mtandao. Sisi Serikalini tunakushukuru, umeokoa fedha za Kitanzania zisizopungua shilingi bilioni mbili kwa makaratasi yaliyokuwa yanazunguka hapa Bungeni. Tunakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya Ofisi za Wabunge, unafahamu kwamba mjadala huu tunao ndani ya Tume ya Huduma za Bunge, kwa hiyo, inshallah Mwenyezi Mungu akituridisha, basi jambo hili litazungumzwa ili lipatiwe muafaka ndani ya Tume. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya michezo ya Wabunge kwa mwaka huu wa 2020. Bado tunashawishika kuendelea kutii utaratibu na sheria. Nchi ambayo inakuwa na uchaguzi, haishiriki mashindano hayo. Kwa hiyo, tunaomba mtukubalie tuendelee kuzingatia hiyo sheria na tusishiriki mashindano hayo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na maswali kuhusu OSHA, tutaendelea kufanya ukaguzi wa afya na usalama mahali pa kazi. Tumeshatengeneza mfumo wa work place inspection management, kaguzi za kisekta na kupunguza tozo ili kuwavutia waajiri wengi wajisajili. Hiyo yote tunafanya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Maige aliuliza kuhusu Workers Compensation Fund kuona ni namna gani tunaweza kuhakikisha kwamba tunafanya kazi ya kupunguza tozo kwenye private sector. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Maige kwamba tumefanya acturial mwaka 2018, mfuko unaendelea vizuri. Wataalam wametushauri tufanye acturial nyingine mwaka 2021, matokeo yake sasa ndiyo yatupeleke kwenye kubadilisha viwango vya tozo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na ushauri mwingine kwamba mifuko ya hifadhi ya jamii iwekeze kwenye miradi ya kimkakati. Tumeshaanza kufanya hivyo. PSSSF muda siyo mrefu watafungua kiwanda kikubwa sana cha bidhaa za ngozi pale Karanga Moshi. Kwa hiyo, ni kazi ambayo tumeamua kujikita nayo. Mfuko wa NSSF umebadilisha matumizi ya nyumba zake kuwa ni hostel za vijana wetu wa Vyuo Vikuu na wanafunzi wapatao karibu elfu nane na kitu wamepata nafasi na fursa ya kupata makazi bora katika nyumba za NSSF na tumegeuza mradi huo umekuwa ni mradi wa kimkakati.

Mheshimiwa Spika, tulisikia malalamiko ya Mheshimiwa Goodluck:-

Mheshimiwa Spika, nitaomba tukutane naye ili tujue kule PSSF tunaweza tukafanya nini kuondoa hilo tatizo. Kama Mkurugenzi ananisikia hapa, basi aanze kujipanga ili tuendelee kufanya kazi kwa weledi, tuwasaidie wastaafu wetu wasipate matatizo katika masuala yote ya pension.

Mheshimiwa Spika, maswali ni mengi, lakini ninaona kwa muda ambao umenipatia, haya yanaweza kutosha kujibiwa kwa siku hii ya leo, lakini tutaendelea kuyajibu yote kwa maandishi na tutayaleta katika ofisi yako. Ninawahakikishia Wabunge, Serikali imejipanga, Tume ya Uchaguzi itasimamia uchaguzi vizuri na tutakuwa na uchaguzi wenye matokeo ambayo ni halali kwa mshindi na ni halali kwa yule ambaye atakuwa ameshindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, ninamshukuru kila mtu kwa kunisikiliza na ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nimesimama hapa kwanza kabisa kuwapa moyo Wanajeshi wote wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya kuwapa moyo, naomba nichukue nafasi hii kuwathibitishia Wanajeshi wetu wote wa jeshi letu, Serikali iliyopo madarakani ya Chama cha Mapinduzi itaendelea kuwajali na kuwaheshimu siku zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kusema, tunaendelea kuthamini kazi na michango yao mizuri katika kulinda amani ya nchi yetu ya Tanzania bila kujali chama chochote cha siasa katika nchi yetu ya Tanzania.
Sisi kama Serikali tutaendelea kufanya nao kazi, wasisikilize propaganda ya mtu yeyote. Sisi kama Serikali tunaendelea kufanya nao kazi na tunatambua mchango wao muhimu katika Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati leo tukizungumza kwenye Bunge hili na tunajua kwamba 61% ya nguvu kazi ya nchi yetu ya Tanzania ni vijana kati ya umri wa miaka 15 na 35 na Jeshi hili la Wananchi wa Tanzania kupitia JKT wamekubali kushirikiana na Serikali na kuamua kuwachukua vijana wa Tanzania kutoka Jimbo la Iringa na majimbo mengine yote katika nchi hii ya Tanzania na wamekwenda kufanya mafunzo ya JKT. Pamoja na mafunzo hayo ya JKT, Serikali imeona umuhimu wa wale vijana wanaokwenda pale kwa kujitolea na imeona wanatakiwa wafanyiwe maandalizi ya kutosha ili tutatue tatizo la ajira nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, yamezungumzwa maneno hapa, Serikali haina mpango na hao vijana. Leo nataka kuliambia Bunge hili tayari Serikali imeingia mkataba na Jeshi la Kujenga Taifa, tayari Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Tanzania limeanza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wote wanaochukuliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwenye JKT kwa kujitolea ili wanapomaliza mafunzo yale waweze kuunganishwa na vyombo mbalimbali vya mikopo na kujiajiri kutokana na skills wanazozipata wakiwa jeshini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo jeshi hili ambalo linaenda kutatua matatizo ya ajira kwa wapiga kura wetu, ilitupasa humu ndani leo tulipongeze na kulipa heshima kubwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na si vinginevyo. Ndiyo maana imenipasa hapa kusema nawashukuru na kuwapongeza Makamanda wote wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na kulinda amani ya nchi ya Tanzania bado wamejitolea kuhakikisha malengo ya Jeshi la Kujenga Taifa kama hawafahamu hapa Wabunge ambao wanadharau uwepo wa Jeshi hili, ni haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi hili lina kazi ya
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
180
kutoa malezi bora kwa vijana, jeshi hili lina kazi ya kutoa mafunzo ya ujasiriamali na jeshi hili lina kazi ya kufundishwa kuwa jeshi la akiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maneno haya na umuhimu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania tutasimama imara kulilinda na kulitetea daima. Tutasimama imara kuliheshimu na kuwapa heshima Wanajeshi wote wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali tunasema tunawaomba waendelee kulinda amani ya nchi ya Tanzania kila siku. Waendelee kukuza maadili ya vijana wetu wa Tanzania kwa namna zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumaliza mchango wangu kwa kumpongeza sana Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Sisi kama Wabunge tunamtia moyo aendelee kuliongoza jeshi letu sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri mwenye dhamana ya kusimamia Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Nakushukuru Mheshimiwa Dkt. Mwinyi, endelea kutusaidia kulipa moyo Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JENISTA J. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nina maombi maalum kama ifuatavyo:-
(i) Mgao wa madawati ufike Peramiho, kwa kuwa corridor hiyo inafika Muhukuru kutokea Tunduru kuvuka kuelekea Msumbiji;
(ii) Suala la upatikanaji wa teknolojia maalum kwa kuwezesha uwepo wa system ya vyoo Mlima Kilimanjaro ni muhimu sana kwa sasa;
(iii) Kwa kuwa sasa Serikali imeamua kukuza utalii kwenye sekta ya hoteli na huduma, ili kukuza ujuzi wahudumu wa sekta hiyo, kuna kila haja Wizara hii na Idara ya Kazi na Ajira zishirikiane kukuza ujuzi na kuondoa tatizo hilo haraka. Ofisi ya Waziri Mkuu imezindua mpango mkakati wa kukuza ajira; na
(iv) Kwa kuwa kuna malalamiko makubwa ya sekta ya upagazi katika kupandisha mizigo ya utalii Mlima Kilimanjaro, naomba masuala ya viwango vya kazi na ajira vilivyopo kisheria vizingatiwe katika kusimamia sekta hiyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuunga mkono hoja ambayo iko mbele yetu. Pamoja na kuunga mkono hoja hii, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Lameck Mwigulu, Doctor kwa kazi nzuri anayoifanya katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Doctor nakupongeza sana. Pia nampongeza sana Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Masauni.

Waheshimiwa Wabunge, mara nyingi jambo ama kiatu usichokivaa huwezi kujua maumivu yake. Nasema hivi kwa sababu gani? Kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani na kuhakikisha kwamba misingi ile ya usalama wa raia inasimamiwa mahali ambapo unawasimamia binadamu wenye hulka na tabia tofauti, kwa kweli ni kazi ngumu na ndiyo maana nasema ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu na Naibu wake wanapaswa kupongezwa kwa kazi hii wanayoifanya katika Taifa letu; na sio wao tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, kwa dhati ya moyo wangu, nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Kamanda Sirro na timu yake ya Jeshi la Polisi katika nchi yetu ya Tanzania. Ninaposema hivyo, sitaki kumaanisha kwamba askari wetu wote labda ni wazuri, hapana. Ni lazima Waheshimiwa Wabunge tukubaliane, naomba niseme na wala ninaposema haya sitaki kumaanisha kwamba Serikali yetu eti inafurahia askari labda mmoja kwa kutokufuata utaratibu na sheria, akasababisha matatizo makubwa kwenye nchi yetu, hapana. Serikali haisemi hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka wote tukubaliane, kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi kwa namna yoyote ile ni lazima tuwapongeze, tuwaunge mkono na tuhakikishe kwamba tunawatia moyo katika kazi hii ngumu waliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa Kabudi amesema hapa, wameapa kuilinda nchi na wawe tayari hata kufa kwa ajili yetu. Jambo hili siyo dogo, ni jambo zito sana. Kwa hiyo, hata sisi kama Wawakilishi wa Wananchi, tuna kila namna na sababu ya kuwapongeza askari wetu kwa kazi nzuri ya ulinzi na usalama wa raia katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitasema maneno kidogo tu, labda huko mbele nitaomba mwongozo wako baadaye kidogo kwa sababu Mheshimiwa dada yangu Mheshimiwa Mary Muro wakati anachangia amesisitiza sana kwamba kila jambo baya linalotokea kwa Jeshi la Polisi, kila akifuatilia anaambiwa kwamba ni maagizo kutoka juu. Hatupendi kuwe na watu wanaharibu halafu wanasingizia ni maagizo kutoka juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani ili tuweze kushughulika na hao watu wanaoharibu taswira ya Taifa letu, tutaomba angalau tuambiwe tu mmoja ama wawili wanaosema hayo maagizo kutoka juu ili watupe tu ushahidi wa mtu mmoja au wawili kusudi tusichafue taswira ya Jeshi letu la Polisi katika nchi yetu ya Tanzania. Nadhani huko mbele kwa kweli tuondoe jambo hili. Tukiliondoa nadhani tutaweza kulifanya jeshi letu libaki katika misingi ya heshima yake. Hivyo, baadaye tutaomba tu mwongozo Mheshimiwa Dada Mary atusaidie tu ili tuweze kuwa kwenye nafasi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza sana hapa masuala ya Vyama vya Siasa na nampongeza sana mdogo wangu Mheshimiwa Upendo Peneza, alizungumza Ibara ya tati (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na alitusomea kwamba Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa isiyokuwa na dini yenye kufuata Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa. Ni kweli kabisa Ibara ya tatu (3) inasema hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda Ibara ya 3(2) inasema:-

“Mambo yote yanayohusu uandikishaji na uendeshaji wa Vyama vya Siasa nchini yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo sheria iliyotungwa na Bunge Cap 258 ambayo ndiYo inasimamia uhuru huo wa Vyama vya Siasa vyote vilivyosajiliwa katika nchi yetu ya Tanzania. Ukienda kwenye kifungu cha 11 cha hiyo Sheria ya Vyama vya Siasa kwenye suala la mikutano ya hadhara, limetolewa maelezo mazuri sana tu. Maelezo haya kama vyama vyote vya siasa vingekuwa vinayafuata, tusingefika katika hii migogoro na kuwasababishia Polisi kama ndio vyanzo vya kuharibu amani katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakubaliana na ushauri wako uliousema asubuhi, Waheshimiwa Wabunge tukiweza kuisoma katiba kwa ujumla wake, lakini tukaweza kusoma na sheria zilizotungwa kwa mujibu wa Katiba, ninaamini kabisa hakuna mtu ambaye ataingia kwenye mgogoro na Jeshi la Polisi kwenye nchi yetu ya Tanzania. Kwa mfano, kifungu cha (5) cha Katiba, kinaeleza kabisa haki ya kupiga kura na uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utaratibu wa kisheria wa uchaguzi uliowekwa, baada ya uchaguzi Jenista anakuwa amechaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho na mwingine, kila mtu anakuwa tayari ni mwakilishi kwenye Jimbo lake husika. Inapendeza; na kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea na hasa kwenye sheria hii, nimesema kifungu cha 11 ukikisoma, kila Mbunge awajibike kwenye Jimbo lake kwa wananchi waliomchagua. Ukishachaguliwa kwenye Jimbo husika, yapo mambo mengi ambayo wananchi wako wanatarajia utawawakilisha inavyopasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukisoma kifungu hicho cha 11 nenda kwenye kifungu kidogo cha (2) utapata maelekezo kabisa hapa, wajibu wa Polisi kutumia sheria walizonazo katika kusimamia masuala yote ya mikutano ya hadhara; iko wazi kabisa na wala haihitaji ugomvi wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe rai kwetu sisi Wanasiasa wote kutambua haki za Kikatiba lakini kwenda kwenye wajibu wa Kikatiba kama Ibara ya 25 ya Katiba inavyosema, kila mtu ana haki lakini ana wajibu katika nchi yetu kuhakikisha anazingatia sheria za nchi zilizowekwa kwa misingi ya Katiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, naomba sana Vyama vya Siasa vifanye yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, vijielimishe zaidi kuhusu katiba tuliyonayo katika nchi yetu ya Tanzania; pili, vijielimishe kuhusu maana na muktadha wa sheria ambazo zimetungwa kwa kuzingatia Katiba tuliyonayo; na tatu, Vyama vya Siasa vijifunze utii wa sheria bila kushurutishwa. Tukifanya hivi nadhani tutaweza kuwa tunaenda vizuri na hatutakuwa na migongano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyama vya Siasa vikubali kuwa sheria kwa kweli ni msumeno na itakata kila chama; iwe ni Chama cha Mapinduzi, CHADEMA, CUF, ni kila mahali. Ni lazima tunapofika kwenye suala la kuheshimu sheria, kila kiongozi na kila chama kijue kwamba kina wajibu wa kuheshimu sheria kwa mujibu wa Ibara ya 25 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujitafakari sisi kama viongozi, tumepewa dhamana, tuna kila namna ya kuheshimu dhamana tulizopewa na wananchi katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeaminiwa, lakini tunategemewa na Watanzania. Tunapokiuka miiko ya kisheria na dhamana tulizopewa, hatutendei haki dhamana tulizopewa wala hatutendei haki Katiba wala sheria ambazo tumezitunga wenyewe Wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, navipongeza vyama vile ambavyo kwa kweli vimeonyesha ukomavu wa kisiasa. Ukiangalia kama kaka yangu Mheshimiwa Mbatia na chama chake huwezi kukuta kwamba kimekuwa na migogoro; na vyama vingine vingi. Kwa hiyo, unaona kabisa kwamba viko vyama unavipima tu na unaona kwamba vimetambua hii mipaka ya demokrasia ilivyo, sheria tulizonazo na Katiba ya nchi yetu ya Tanzania. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuvihimiza vyama kwa mujibu wa sheria tulizonazo na kwa mujibu wa Katiba, hakika tunapaswa kuheshimu sheria, tunapaswa kuheshimu Katiba tuliyonayo. Tukifanya hivyo, tutawawakilisha wananchi wetu vizuri sana na hakutakuwa na haja ya kugongana na vyombo vyovyote vinavyosimamia usalama wa raia katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, IGP na timu nzima ambayo inasimamia usalama katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kwanza kabisa naomba nikushukuru wewe kwa kuongoza vizuri kikao hiki leo. Kikao hiki leo ni kikao cha kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania, kwa hiyo nakushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja hii, lakini kwa dhati ya moyo wangu niwashukuru wale wote ambao wametupa marekebisho na wameiunga mkono hoja hii, ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nitakwenda moja kwa moja kwenye hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na maoni ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia Masuala ya UKIMWI na inayoshughulikia pia masuala ya dawa za kulevya. Kamati ilitupa maoni mengi na iliomba Serikali ifanye marekebisho katika ibara mbalimbali. Naomba kulihakikishia Bunge lako kuwa tulichukua ushauri wa Kamati na tumeleta jedwali la marekebisho la Serikali, kwa hiyo tunaunga mkono maoni ya Kamati katika kufanya marekebisho ya Muswada wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati pia ilitushauri kwamba kuna umuhimu wa kuongeza nguvu kama Serikali katika kuhakikisha tunapambana na biashara hii haramu ya dawa za kulevya kwa upande wa pili wa Zanzibar. Naomba niliarifu Bunge lako tukufu kwamba tumeanza utaratibu huo vizuri; mimi mwenyewe nimeshafanya kikao cha kwanza na Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar katika kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu za pamoja kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, niliagiza Mamlaka yetu ikutane na Mamlaka ya Zanzibar ili itengeneze mpango mkakati ambao sasa utatumia nguvu za Bara na Visiwani kwa pamoja katika kuhakikisha kwamba jambo hili linafanyiwa kazi ipasavyo. Ninaomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, na mimi kama Waziri mwenye dhamana nitafuatilia mkakati, huo na ninawahakikishia Wazanzibari kwamba tutafanya kazi sambamba, bega kwa bega mpaka tuhakikishe kwamba vita hii inatokomezwa sio Bara tu, hata upande wa pili wa Visiwani, kwa sababu lengo ni kuwaokoa watoto wetu wote wa pande zote mbili za nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilisema kwamba hii sheria si sheria rafiki, Sheria hii inaweka adhabu kali na kwa kuweka adhabu kali itapandisha thamani ya biashara ya dawa za kulevya na hivyo basi hakutakuwa na manufaa makubwa kwa sheria hii katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba niseme yafuatayo; kwanza, kama biashara hii itakuwa imepanda thamani kwa maana itakuwa ni biashara aghali, ina maana wale wafanyabiashara wanaojihusisha na dawa za kulevya wao ndio watakaoingia kwenye matatizo kwa sababu biashara itakuwa ni ghali kuliko ilivyo nyepesi kwa sasa, na kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewaondoa Watanzania wengi sana katika kufanya biashara hii ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa jinsi sheria ilivyo, kama biashara itakuwa aghali ina maana hata wale wamiliki wa biashara itabidi wawe na bidhaa nyingi na wazinunue kwa wingi ndipo waweze kufanya biashara hii. Sheria yetu sasa imeweka sasa masharti; kadiri utakavyokamatwa na mzigo mkubwa, ndivyo adhabu itakavyoendelea kuwa kubwa na itakushughulikia kweli kweli. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwa mabadiliko haya ya sheria itatusaidia sana kupunguza matumizi na biashara ya dawa za kulevya katika nchi yetu, lakini kwa kufanya hivi itaondoa upatikanaji wa dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania na hivyo tutaweza kuleta ustawi wa watoto wetu na ustawi wa uchumi wetu na wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kabisa matumizi ya dawa yanavyoongezeka ni kiashiria pia cha kuongezeka kwa tatizo la UKIMWI katika nchi yetu ya Tanzania, na hasa kwa wale wanaojidunga sindano za dawa za kulevya. Kwa hiyo naomba Waheshimiwa Wabunge tuungane kwa pamoja tupitishe sheria hii leo tukapambane na dawa za kulevya na matumizi yake katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Upinzani wamesema hapa kwamba Sheria hii imejaa sana kusisitiza katika kuwadhibiti wafanyabiashara wadogo wadogo badala ya kutoa tiba, lakini vile vile kutoa elimu. Naibu Waziri amejibu kwenye suala la elimu, na mimi naongezea kwamba kifungu cha 4(1)(e) kinaipa kazi kabisa Mamlaka yetu kutoa elimu kuhusu suala hili la dawa za kulevya nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi kwenye suala la tiba, ninaomba kwa dhati niipongeze Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini; kwa sababu kifungu cha sheria mama, kifungu cha 63, kimeagiza kabisa mamlaka ishughulikie pia suala la kuanzisha vituo vya tiba katika nchi yetu ya Tanzania vya kupunguza uraibu. Na ninaomba niliarifu Bunge lako Tukufu, toka mamlaka hii imeanza kufanya kazi tayari vituo hivi vya tiba vimeshaanza kuongezwa katika nchi yetu ya Tanzania, tunafungua kituo kingine hapa Dodoma kwa sababu hapa tatizo ni kubwa sana, na hizo ni juhudi za Mamlaka, na ninaomba kwa kweli tuwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunakwenda kufungua kituo kingine cha tiba kule Mwanza, kitakuwa ni kituo kikubwa na chenyewe kitatoa sana msaada wa tiba, tuwapongeze kweli mamlaka. Vile vile tutafungua kituo kingine cha tiba ya methadone kule Mbeya, na hivyo unaona kabisa kwamba tumekwenda kusambaa katika majiji makubwa, ukiacha vituo vitatu vikubwa ambavyo tunavyo mpaka sasa pale Dar es Salaam. Kwa hiyo, kama ni suala la tiba tunafanya. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge, kutokupitishwa kwa sheria hii sababu isiwe ni tiba, tiba tunafanya na tunawahudumia vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema hii sheria ingegharamia sana kwenye suala hilo la tiba, naomba niwaarifu Waheshimiwa Wabunge yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, makadirio kwa mfano kwa mwaka 2016 kwenye tiba ya methadone ilikuwa ni kilo 120 kwa mwaka na kwa mwaka 2017 ilikuwa ni kilo 300 na kilo moja ya kuweza kutoa tiba kwa wagonjwa hawa inauzwa dola kwa chini kabisa ni dola 650 lakini kwa bei ya juu ni dola 1,500, kilo moja. Sasa kwa mwaka 2016 peke yake tumetumia takribani dola 180,000 na kwa mwaka 2017 tunakadiria kutumia dola takribani 450,000 kwa ajili ya kununua dawa hii na kutoa tiba kwa vijana wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni juhudi zimefanywa na malaka na sasa hivi mamlaka wameamua kununua dawa hii moja kwa moja kutoka India na tukifanikiwa kufanya hivyo tutapata dawa nyingi. Lengo ni kuongeza vituo vingi zaidi kwenye nchi nzima ya Tanzania na tiba iwakute vijana wengi na Watanzania wengi, tuweze kuondoa uraibu kwa Watanzania ambao wameshaathirika na dawa za kulevya. (Makofi)

Kwa hiyo, naomba niwapongeze sana tume kwa kazi hii nzuri ambayo wameendelea kuifanya na wanaifanya vizuri sana na hata Kamati imeshawahi kwenda kuangalia wanavyofanya shughuli hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 29, Waheshimiwa Wabunge wanasema kwa nini tumekiweka; kifungu hicho cha 29 tunapendekeza kufanya marekebisho kwa lengo la kuongeza makosa yasiyostahili dhamana ambayo yatajumuishwa katika makosa ya kumiliki mitambo na kutengeneza dawa za kulevya, kufadhili biashara ya dawa za kulevya na kuwaingiza watoto kwenye biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule mwanzo makosa haya yalikuwa hayajaingizwa kisheria kama ni makosa ambayo hayastahili dhamana. Unaweza ukaenda ukakuta mtu ana mtambo wa kutengeneza dawa za kulevya kutokana na kemikali bashirifu, na anapopatwa hatia mahakamani kwa sababu sheria haijamfunga kupata dhamana alikuwa anaashiwa mahakamani anapata dhamana na anaweza kwenda kucheza na kesi yake kwa namna moja ama nyingine.

Waheshimiwa Wabunge, tumegundua mwanya huu umetumika vibaya sasa tunafunga dhamana kwa watu hawa wote. Kwa hiyo ukikutwa tu na kosa la kumiliki mitambo inayotengeneza dawa za kulevya hakuna dhamana mpaka kieleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukikutwa pia unawashirikisha watoto kwenye biashara ya matumizi ya dawa za kulevya, kosa hili halina dhamana. Kwa hiyo, tunataka tuwalinde watoto wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 4(2) kama nilivyosema, tunakirekebisha ili kuipa mamlaka nguvu ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, si kushughulikia tu makosa ya dawa za kulevya bali tunataka pia mamlaka ishughulikie na makosa mengine yanayohusiana na dawa za kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, mamlaka inapokwenda kufanya kazi zake labda za operesheni huko maeneo mbalimbali, inaweza ikafika mahali ina taarifa kwamba pana dawa za kelevya, na hiyo experience wameshaipata, lakini wanapofika pale wanagundua kwamba pamoja na kuwa pale mahali pana dawa za kulevya, lakini inawezekana pana dhahabu fake ambazo zimewekwa hapo, maana wafanyabiashara wanaofanya biashara ya dawa za kulevya wanafanya pia na biashara nyingine haramu.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukafika hapo ukawakuta pia wana pembe za ndovu ziko hapo, ukakuta na vitu vingine tu ambavyo vinamilikiwa kinyume cha sheria hata kama ni silaha na vitu vingine. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono, tunaipa mamlaka sasa nguvu, ikikuta hakuna dawa za kulevya lakini kuna pembe za ndovu watachukua hatua kwa kushirikiana na vyombo vinavyohusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano wakati wanafanya operesheni zao, walifika mahali wakakuta dawa za kulevya zimetoroshwa lakini wale watu wanamiliki dhahabu feki ambayo walitaka kuiuza kwa siku hiyo hiyo mamlaka ilipokwenda hapo; na biashara nyingine tu za hovyo, hata bidhaa ambazo ni mbovu ambazo hazina viwango. Kwa hiyo tumewapa mamlaka sasa watafanya kazi hiyo yote, wapeni hilo rungu wakafanye kazi, watatusaidia sana katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeongelea pia katika kifungu cha 51(a) tunataka kumpa uwezo Kamishna Jenerali kushikilia akaunti za watuhumiwa kwenye benki mbalimbali. Unapomkamata mtuhumiwa lakini hujamuwekea utaratibu wa Kamishna wa kuweza kuzuia fedha ya mtuhumiwa kwa muda fulani wakati anafanya upelelezi, tulichogundua ni kwamba watuhumiwa wengi wamekuwa wakihamisha zile fedha kutoka akaunti moja kwenda nyingine. Na wanapozihamisha, wanazitakatisha fedha zile kwa matumizi mengine. Kwa hiyo sheria inakwenda kubana mianya hiyo yote, na sasa kwa kweli tunataka tuwe na nidhamu ya kutosha katika nchi yetu ya Tanzania, na hasa kwenye suala zima hili la biashara ya dawa za kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeulizwa hapa kwa nini mnawapa mamlaka makubwa sana mamlaka hii mpaka wanafikia hatua ya kumiliki silaha. Mimi naomba Waheshimiwa Wabunge kwanza tukumbuke sheria mama ya mwaka 2015 ilipokuwa inatungwa iliweka kazi za mamlaka katika kifungu cha saba cha sheria mama, lakini ika-define pia kazi za Kamishna Jenerali wa Mamlaka hii ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanapokwenda kwenye shughuli za mapambano dhidi ya dawa za kulevya mahali popote, hebu wote tujiulize tu; hawa wanaofanya biashara ya dawa za kulevya wanajikinga na silaha kubwa, wakati mwingine usiku mnapata taarifa na mnataka mkafanye operation na uvamizi mahali, mnakwenda kukutana na mtu mwenye silaha kubwa, lakini kwa sababu mamlaka haina mamlaka ya kisheria kumiliki silaha, wakati mwingine watumishi wa mamlaka wamekuwa wakijitosa kwenda bila kuwa na silaha hata moja na kuhatarisha maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoweka kifungu hiki sasa tunataka mamlaka iweze kumiliki silaha zake na itakapokuwa inakwenda kwenye mapambano iende ikiwa imejitosheleza Waheshimiwa Wabunge na wala lengo sio kwamba mamlaka itatumia silaha hizi vibaya, hapana, sheria inawaruhusu makampuni ya ulinzi kumiliki silaha na kulinda kwa kutumia silaha, kwa nini tusiruhusu chombo kikubwa kama hiki na chenyewe kikawa kinamiliki silaha kiende kikatusaidie katika mapambano haya dhidi ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, naomba mtuunge mkono, mapambano haya ni makubwa yanahitaji weledi, lakini yanahitaji kujitoa na usalama wa kutosha kwa watumishi ambao wanafanya kazi hiyo kwenye mamlaka yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, imeelezwa hapa ni kwa nini sasa Sheria yetu sisi inapingana na mikataba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Msemaji wa Kambi ya Upinzani amesema ukienda kule Kenya mirungi inaruhusiwa ukija huku kwetu hairuhusiwi. Nataka tu niwape uzoefu wa nchi za Afrika Mashariki. Nchi ambayo inaruhusu matumizi ya mirungi nadhani ni moja tu, ni Kenya, Uganda hawaruhusu na nchi nyingine kadhaa ikiwemo Tanzania hawaruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi niwaulize Waheshimiwa Wabunge, kwa kuwa Kenya wanaruhusu mirungi, ambayo sisi tunajua ni aina ya dawa za kulevya, itumike kwao isiwe ni kigezo na sisi Tanzania turuhusu wakati tunajua inaweza kuwaathiri watoto wetu kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, sisi tutaendelea na utaratibu wetu, tutaendelea kushauriana na nchi za jirani waone umuhimu wa kuwakinga vijana wote wa Afrika Mashariki waondokane na janga hili kubwa la dawa za kulevya. Serikali zetu zitaendelea kuongea, lakini kwetu bado tunaamini kwamba jambo hili haliwezekani na tutaendelea kulisimamia kama jambo ambalo haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imeulizwa hapa, pamoja na kudhibiti aina hizo zote za dawa za kulevya, lakini zipo kemikali na dawa nyingine zinaweza zikawa zinatumiwa kama dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania. Sheria hii inampa sasa mamlaka Waziri mwenye dhamana kuendelea kuorodesha majina ya dawa na kemikali zozote zile ambazo tunaona kwamba zinaweza kutumika kama dawa za kulevya nchini na zenyewe zikawekwa katika jedwali na zikaelezwa kama ni dawa ambazo hazitatakiwa kutumika bila utaratibu katika nchi yetu ya Tanzania zikiwa chini ya jedwali ambalo linaorodhesha kemikali ama dawa ambazo zinaeleweka kama ni dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Lucy Mayenga, ametupa ushauri mzuri pia naye, na kwa kweli ametueleza hapa kwa kina ni kwa kiasi gani tunatakiwa kupambana kwa nguvu zote, na amewapongeza sana mamlaka kwa kazi nzuri wanayoifanya, na mimi nakushukuru sana Mheshimiwa Lucy, na tunayachukua yote uliyoyasema kama ni kumbukumbu sahihi ya kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dada yangu Lucia Mlowe amesema tumechelewa kuleta sheria hii. Naomba nimwambie hatujachelewa, imepitishwa mwaka 2015 na mamlaka imeundwa hivi karibuni tu; lakini umeona mamlaka ilivyoanza kufanya kazi na baada ya kugundua kwamba yako maeneo ambayo si rafiki kwa mamlaka kufanya kazi leo tumeleta kufanya marekebisho na ninaamini baada ya marekebisho haya kazi itakuwa nzuri zaidi Mheshimiwa Lucia tutakuja mpaka kule Njombe na unajua tatizo la Njombe lilivyo; tutakuja kushirikiana na ninyi huko ili tuweze kusaidiana. Kwa sababu UKIMWI unaenda sambamba sana na matumizi ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameeleza suala la RC wa Dar es Salaam kujishughulisha na ukamataji. Waheshimiwa Wabunge naomba niwaambie kwamba jamani vita hii ya dawa za kulevya ni ya kila Mtanzania, kila Mtanzania afanye kazi hii. Tusioneane wivu wala tusipambane wakati tunajenga nyumba moja kwa kutumia fito zinazofanana. Cha msingi kila anayefanya kazi hii aheshimu sheria inayotuongoza katika kupambana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania wote, kazi ya kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania ni ya Watanzania wote; haibagui wala haichagui nani afanye nani asifanye.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea ushauri wa Mheshimiwa Adadi na nadhani kuna vifungu ambavyo tumeelewana na vifungu vingine tunafikiri tutaviacha kama vilivyo, lakini umezungumza sana sana kifungu cha (15) na una hofu ukubwa wa mzigo na hasa katika matumizi ya biashara ya bangi na mirungi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge ninaomba tu niwaambie jambo moja kwamba hawa wafanyabiashara walipoona kwamba sheria haiwabani kuwa na kiasi kidogo kidogo cha dawa walichoamua kufanya mtu analima shamba la bangi labda magunia 1000, lakini anajua ilimawe salama asikamatwe anagawa yale magunia 1000 katika viwango vidogo vidogo na anaviweka kwa watu mbalimbali. Kwa hiyo, hiyo sasa ilikuwa inatoa hamasa ya mtu kuwa na mmiliki wa dawa za kulevya nyingi lakini anazigawa katika mafungu madogo madogo, akikamatwa ana dhamana lakini sheria inayomkamata haina makali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tumesema kamata mtu huyo zaidi ya hizo kilogram tulizosema tunafunga huko maisha. Kwa hiyo kila mtu aone kwamba matumizi na biashara ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzaniaa hatuna mchezo nayo na sheria tumeiweka kuwa kali na sheria hii kwakweli tunataka ishughulike na kila mtu anayetaka kuharibu maisha ya kizazi cha Watanzania uchumi wa nchi yetu na mafanikio na mwelekeo wa maadili katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yaliyoulizwa ni mengi, kwa hiyo mengine tutaendelea kuyajibu kwa maandishi lakini nimalizie kwa kusema tunawaomba sana, sana, sana Waheshimiwa Wabunge mpitishe Sheria hii leo muwape mamlaka ya kudhibiti ya kudhibiti dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania wafanye kazi ya kuokoa kizazi cha Tanzania leo na kesho.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba nichukue nafasi hii niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamepata nafasi ya kuchangia muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge waliopata nafasi ya kuchangia muswada huu ni pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, lakini pamoja na Maoni ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile Wabunge walioweza kuchangia kwa kuzungumza hapa Bungeni ni Waheshimiwa Wabunge 17 na waliochangia kwa maandishi ni Wabunge watano. Naomba niwashukuru sana Wabunge kwa michango yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze kwa kusema kwamba, nichukue nafasi ya pekee kwa niaba ya Serikali kuwahakikishia wafanyakazi wote wa Tanzania kwamba, Serikali yao inawapenda sana na niwaombe sana wafanyakazi wa Tanzania wasifikiri kuletwa kwa muswada huu wakayasikiliza maneno ya uchonganishi kutoka mahali kokote kwamba muswada huu una lengo la Serikali kudhulumu maslahi ya wafanyakazi, si kweli, kwa sababu wafanyakazi wanajua chanzo cha muswada huu ni nini. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie tuko pamoja wafanyakazi wote na tunaendelea kuwaheshimu na tutaendelea kufanya kazi nao kwa maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa kilichonifurahisha katika majadiliano ya muswada huu ni kwamba Wabunge waliochangia wengi wamedhihirisha kabisa kwamba, wanaunga mkono muswada wetu ikiwa ni pamoja na Msemaji wa Kambi ya Upinzani na yeye anasema hoja hii hata wao waliitafakari tafakari hivi. Kwa hiyo, hiyo inadhihirisha kabisa kwamba kwa kweli, Waheshimiwa Wabunge wa Kambi zote mbili wanaunga mkono hoja hii, ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema toka asubuhi kwamba, haki ya hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania imwekwa katika misingi ifuatayo; msingi wa kwanza ni Mkataba wa ILO Namba 102, lakini msingi wa pili ni Pendekezo Namba 202 la mwaka 2012 ambalo linaweka utaratibu na mfumo wa ulipaji wa mafao katika nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa. Pendekezo namba 202 linatoa nafasi kwa kila nchi mwanachama kuangalia mafao yale ambayo yametajwa na ILO katika muongozo na mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi inao uwezo wa kuamua kutengeneza aina ya mifumo na sheria ambazo zitatafsiri mahitaji ya hifadhi ya jamii katika nchi husika na ndio maana sisi katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 11(1) kimejieleza wazi mamlaka ya nchi yetu haina budi sasa kwa kutafsiri miongozo hiyo, lakini vilevile kwa kutafsiri mikataba tunao uwezo wa kutunga sheria mbalimbali zitakazowahifadhi Watanzania watakapokutana na majanga yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada wa leo ni utekelezaji wa mikataba, lakini ni utekelezaji wa mapendekezo ya Shirika la Kazi Ulimwenguni. Kwa hiyo, wale Wabunge waliounga mkono ninawashukuru sana kwa sababu tunaendana na Umoja wa Mataifa unavyotaka na hasa Shirika la Kazi Ulimwenguni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo tunapoendelea kuyatekeleza matakwa haya wote tunaona kwamba sekta ya hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania imeendelea kuwa na mabadiliko makubwa na imeendelea kuchangia katika kukua kwa Taifa letu ukiachia mbali suala zima la kuwahifadhi wananchi wa Tanzania wakiwemo wafanyakazi kwa kutumia misingi ambayo tumejiwekea kisheria lakini kwa kuzingatia sera ambayo tumeiunda ya hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania. Na hivyo hivyo imetupelekea tukakutana leo kwenye Bunge lako tukufu, tukaja kuangalia umuhimu wa kuunganisha mifuko na mifuko hii tunapoiunganisha leo ziko sababu za kimsingi za kuunganisha mifuko hii nitarejea kwa ufupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Kazi Ulimwenguni lilishatuagiza baada ya kufanya utathimini wa mifuko lilishatoa mapendekezo ya kuishauri nchi yetu ya Tanzania toka mwaka 2013 kufikiria namna bora ya kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii kwa kuiunganisha mifuko hii ya hifadhi ya jamii ambayo nchi yetu ya Tanzania ilionekana ina mifuko mingi kulinganisha na nchi nyingine. Shirika la Kazi Ulimwenguni kama mdau mkubwa anayesimamia vigezo vya hifadhi ya jamii katika mataifa mbalimbali na yeye alitushauri hivyo. Lakini na sisi kupitia mdhibiti wa sekta katika nchi yetu ya Tanzania tuliona kwamba iko hoja ya msingi ya kuhakikisha kwamba mifuko hii tunaiunganisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo ya utangulizi sasa nitajikita katika kujibu hoja za
Waheshimiwa Wabunge lakini ambazo zimezungumzwa kwa ujumla. Labda nianze na hoja ambayo ni hoja kubwa sana. Ninaona Bilago mwalimu mwenzangu na jirani yake Haonga Kambi Rasmi ya Upinzani wameizunguza kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hoja yao kubwa kikokotoo ambacho kinatakiwa kielekeze mfumo wa malipo ya pensheni kiingizwe kwenye sheria. Hiyo ndiyo hoja kubwa, na Mheshimiwa kaka yangu Bilago mwalimu mwenzangu amekwenda mbali zaidi akasema ni lazima kikokotoo cha moja chini ya mia tano arobaini (1/540) kijionyeshe pale dhahiri. Lakini alipokuja kuchangia jirani yake ndugu yangu Haonga akasema tena hiyo moja chini ya mia tano arobaini (1/540) haitoshi twende moja chini ya mia tano ishirini (1/520). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kusema mambo yafuatayo; ningeomba sana wafanyakazi tusiwapotoshe, wafanyakazi tusiwajengee mtazamo kwamba Bunge hili ndilo Bunge linaloweza kuwahurumia sana katika suala la mafao yao. Ninasema hivyo kwa sababu gani ninazo sababu za msingi. Kabla hatujafikia kuunganisha hii mifuko nimesema pale mwanzo ILO walifanya tathimini wa sekta ya hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania. Wamefanya utathimini mwaka 2010; wamefanya utathimini mwaka 2016 nilitegemea kaka yangu Haonga anapokuja kuleta hilo pendekezo na kaka yangu Bilago na Kambi Rasmi ya Upinzani wasingeishia kwenye eneo la kikokotoo peke yake, wangeenda mbele kwenye zile findings zote ambazo zililetwa baada ya kufanya utathimini wa mifuko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu yafuatayo; baada ya kufanya utathimini wa mifuko mwaka 2010 na 2016 yafuatayo ndiyo yaliyojitokeza; la kwanza, ni funding level ya mifuko yote katika nchi ya Tanzania. Mfuko wa NSSF ambao kikokotoo chake ni moja chini ya mia tano themanini(1/580); mwaka 2010 funding level yake ilikuwa asilimia 75.8 mwaka 2016 funding level ikaendelea kupanda. Mfuko wa PPF walipofanya utathimini wa mfuko mwaka 2010 funding level ya PPF ilikuwa asilimia 47.1 mwaka 2016 ikawa 49.6. LAPF ambayo inatumia kikokotoo cha moja kwa mia tano arobaini (1/540) funding level ilikuwa asilimia 46.7 mwaka 2010 ilipofika mwaka 2016 kwa sababu ya kikokotoo cha moja chini ya mia tano arobaini funding level ya LAPF ikaanza kushuka na ikafika asilimia 27.7. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, PSPF mwaka 2010 funding level ilikuwa asilimia 10.1 ilipofika mwaka 2016 funding level ikawa asilimia 6.2. Lakini hatukuishia hapo matokeo ya utathimini baada ya kupata hizi findings wakatoa ushauri, ushauri wa wazi kabisa tukitaka kuendelea na kikokotoo cha moja chini ya mita tano arobaini (1/540) kwa mfuko wa LAPF na mfuko wa PSPF ni lazima contribution rate itoke asilimia 20 iende asilimia 30.

Sasa ninataka kumuuliza kaka yangu Bilago anapopendekeza kikokotoo cha moja chini ya mia tano arobaini achotaka kuwaambia wafanyakazi wa Tanzania anakubaliana na mapendekezo ya ILO yaliyofanywa mwaka 2010 na 2016 kwamba sasa kikokotoo kiondoke asilimia 20 kiende asilimia 30. (Makofi)

Ninaomba nitoe ufafanuzi wa maana ya asilimia 30. Mfanyakazi huyo sasa akipelekwa asilimia 30 ina maana mwajiri atachangia asilimia 15 mfanyakazi atachangia asilimia 15 na mwenye kalamu aanze kushika karamu yake aorodheshe. Mfanyakazi atachangia asilimia 15 ya Mfuko wa Pensheni, atachangia asilimia 15 ya Bodi ya Mikopo, atachangia asilimia tatu ya Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa atachangia mbili, Chama cha Wafanyakazi, achangie asilimia tisa ya Kodi ya Mapato, achangie asilimia tano labda ya mkopo ambao ameukopa labda binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli kwa asilimia 15 kwa funding level ya moja chini ya mia tano arobaini (1/540) ambayo itampelekea mfanyakazi huyu kukatwa makato ambayo yanazidi Sheria ya Utumishi wa Umma vigezo vilivyowekwa. Mfanyakazi huyu mshahara wake utabaki takribani kama asilimia 23 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuliona hilo lakini pia kwa kuyatazama na mengine ambayo nitayasema TUCTA (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi) ambao hoja hii ndiyo hoja yao pamoja na Kamati walikuja Serikalini na ushahidi wao ninao hapa, wakaomba Bunge lisiwaamulie kikokotoo, hayo ndiyo maoni ya TUCTA na TUCTA ndiyo wenye sheria yao na ndiyo waliyoiomba Serikali na ndiyo wadau namba moja. Kikokotoo hiki turudi kwenye kanuni na kwa kuzingatia sheria za kazi tulizo nazo na utaratibu wetu wa collective bargaining katika dhana ya Utatu tuende tukatafakari jambo hili kwa pamoja na mwisho wa siku tukubaliane sisi kule na wadau wa mfuko huu kikokotoo kiwe ni kikokotoo kipi.

Waheshimiwa Wabunge, ninawaomba sana kama tutaamua sisi kuwapangia wafanyakazi tutakuwa tumewapangia wafanyakazi na contribution rate ambayo itakuwa ama inawaumiza ama haitawasaidia. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo tutakuwa hatujawatendea haki wafanyakazi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba sana ndugu zangu wa upinzani muelewe kabisa hoja hii kwa msingi huo ambao nimeusema. Sheria yetu sisi tumeamua kuweka bayana kikokotoo ili tusiwaumize wafanyakazi kibakie kuwa asilimia 20 mfanyakazi achangie asilimia tano, Serikali inachangie asilimia 15. (Makofi)

Sasa kaka yangu Bilago unapotaka kung’ang’ania twende katika mfumo huo kabla hatujarudi kukaa pamoja na kutafakari na kuwabebesha hao wafanyakazi mzigo wakuchangia asilimia 30 unawasaidia ama unawaingiza kwenye matatizo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba sana Waheshimiwa Wabunge jambo hili ni jambo zito wala siyo jambo la kuliamua tuhumu ndani wenye Maulid yao ni wafanyakazi wa Tanzania watakaokutana na Waziri wa Kazi. Na Maulid kaka Bilago siyo ya kwako usiyavalie kanzu, acha wenye maulid wayafanyie kazi, tutarudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge mmesema hapa kwamba hamumwamini Waziri wenye dhamana kurudi kukaa na wadau katika kutengeneza vikokotooo. Waziri wa Kazi haongozwi na sheria moja katika nchi ya Tanzania. Uzoefu wa Kimataifa na mikataba niliyoisema Waziri wa Kazi anaongozwa na sheria nyingi, mimi ninaongozwa na Sheria Namba 7 ya mwaka 2014. Sheria hiyo inaunda Baraza la LESCO na Baraza la LESCO kazi yake ni kumshauri Waziri kama kubadilisha sheria lazima nitarudi kwenye Baraza la LESCO na Baraza la LESCO lina Wajumbe ambao ni wafanyakazi, mwajiri lakini na Serikali tunakuwa mle ndani kwa pamoja na hiyo niwaondoe tu shaka kwamba jambo hilo tutalifanya kwa pamoja na wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niongeze pia katika kufanya pia utathimini wa mifuko tulichogundua hii mifuko ambayo inatumia kikokotoo cha moja kwa mia tano arobaini (1/540) imeendelea kushuka hata kwa uwiano na uwiano wa walipwaji wa pensheni. Standard za kimataifa inatakiwa katika mfuko mwanachama mmoja aliyesitaafu achangiwe fedha ya kustaafu na wanachama 25, lakini tukirudi kwa sababu ya kikokotoo kile kile, mifuko ambayo kikokotoo chake ni hicho ambacho Kaka Bilago unasema twende tu hata bila kufanya utathimini tuamue tu unaona kwamba wameshindwa kufikia standard hizi za Kimataifa. Mfuko wa PSPF uwiano ni mwanachama mmoja kwa wanachama watano tu. Lakini ukienda kwenye mfuko wa LAPF ni mwanachama mmoja kwa wanachama 19. Lakini ukienda kwenye mfuko wa NSSF ni mwanachama mmoja kwa wanachama 32.

Kwa hiyo, unaona kabisa hali ya sekta ilitakiwa tufanye maamuzi haya, ninarudia kusema Waheshimiwa Wabunge tupitisheni sheria tutakwenda kufanya actuarial mpya. Kwa sababu hata hapa tunapoongea wako wanachama ambao mpaka sasa wanaendelea kujiunga na mifuko hii na wako wanachama wanaostaafu. Sasa niulize hivi tukiamua tu hapa ndani hawa wanachama wanaojiunga leo. Wanachama wanaoendelea kustaafu wakati sisi tuko na huo muswada, hao nao tutafanya nini.

Kwa hiyo, ndiyo maana tunasema tumalize sheria hii, turudi tukafanya actuarial yetu tutapata picha nzuri tutatengeneza regulation kwa taratibu wa sheria za kazi tulizonazo, tuna Sheria Namba 6 na Sheria Namba 7 na hizi zote zitatusaidia kutuhakikishia kwamba jambo hili tunalifikisha salama na wafanyakazi. Wafanyakazi nieleweni Waziri wenu nipo hakuna kitakachoharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa fao la kukosa ajira, kwanza niwashukuru Wabunge wote ambao wameunga mkono fao hili ninawashukuru sana. Fao hili nisema labda maneno machache ya utangulizi, kwenye mafao ambayo yanatambulika na Umoja a Mataifa hakuna fao la kujitoa. Fao hili la kujitoa liliingizwa na mifuko yetu mingi kwa kulazimishwa ama sheria ama kulitoa fao bila kuwa na mandate za kisheria kwa sababu ya ushindani kwenye sekta. Lakini hakuna fao la kujitoa katika mafao duniani halipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali sikivu ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli baada ya kusikiliza kilio cha wafanyakazi kwa muda mrefu na hasa wafanyakazi wa kwenye migodi ndiyo maana tumekuja na fao hili sasa unemployment benefit ili tutibu tatizo la wafanyakazi hao. Nilitegemea Wabunge leo mngeshangilia sana fao hili kwa sababu linaenda kusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema hivi fao hili kwenye sheria tumelipa masharti, baada ya kulipa masharti kaka yangu Mtolea alisema kitu kizuri sana hapa ni lazima wakati wa kuliangalia hili fao la kujitoa tukajue aina za wafanyakazi walioko katika sekta mbalimbali na tujue watalipwa je hayo mafao yao kwenye hili fao la kukosa ajira kama mbadala wa fao la kujitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili utaweza kulifanya tu kama utarudi kwenye regulation ukamaliza utathimini wako wa mfuko ukaangalia mahitaji halisi ya wafanyakazi kwenye fao hili la kosefu waajira na baada ya hapo ukalitengenezea mfumo wa malipo mzuri ambao utakuwa endelevu.

Ninaomba Waheshimwa Wabunge muamini hapa tulipofika tumefika kwa sababu tumefanya kazi kwa pamoja na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini na hii siyo hoja ya Serikali peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hofu ya hatima ya wafanyakazi ambao wako kwenye mifuko yetu mpaka sasa. Kifungu cha 87 kiko wazi kabisa na sisi tumesema kwamba hatuwezi kuwaacha Watanzania wenzetu ambao wamehudumia kwenye sekta ya hifadhi ya jamii kwa miaka hii yote eti kwa sababu ya kuunganisha mifuko tukawaacha wapotee tu hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya wafanyakazi waliopo kwenye sekta mpaka sasa mpaka Septemba mwaka jana ni wafanyakazi 2,147. Lakini idadi ya wanachama hai na wanachama wastaafu mpaka mwezi Septemba, 2017 ilikuwa ni 1,448,861. Baada ya kuunganisha hii mifuko kwa takwimu sahihi ambazo tunazo idadi ya wafanyakazi kwenye mfuko wa umma watakuwa 988 na idadi ya wafanyakazi kwenye mfuko binafsi watakuwa 1,159. Sasa ili uweze kujua wafanyakazi hawa unawachukua ama huwachukui ni lazima uzingatie uwiano wa wafanyakazi na uwiano wa wanachama na wastaafu katika kila mfuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya hiyo kazi kwa kiasi cha kutosha na naomba niwaombe wenzetu Wabunge wa Upinzani hatujaja hapa tumekurupuka, jamani tumefanya kazi kwa ajili ya wafanyakazi wa nchi hii ya Tanzania. Ni tofauti na mtu aliyekutana tu na muswada huu bila kujua kazi iliyofanyika. SSRA baada ya kuangalia sekta itakavyokuwa huko mbele tunapokwenda tumegundua uwiano unaonatakiwa kwa mfuko wa umma utakuwa ni 1:675 na kwa hali hiyo wafanyakazi wote 988 watahitajika na tutahitaji ziada ya wafanyakazi 114. (Makofi)

Kwa hiyo, hiyo tu inatosha kabisa kukuambia kwamba pamoja na kifungu cha 87 lakini bado sekta itahitaji wafanyakazi wa ziada na hivyo basi ninaomba niwahakikishie wafanyakazi, ambao wako kwenye sekta ya jamii mpaka sasa tumeshafanya hesabu yao, tunajua waliko, tunajua wanafanya nini, na sisi tumejipanga kuwachukua ili waimarishe sekta ya hifadhi ya jamii.

Lakini hata hivyo kwenye sekta ya hifadhi ya jamii bado tunayo mifuko mingine tunao Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa unahitaji wafanyakazi, tunao Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi wanapoumia kazini tunahitaji wafanyakazi na mfuko huo wa private wa NSSF tuliouanzisha unahitaji wafanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kifungu cha 87 ninaomba niwahakikishie kabisa kabisa ndugu zangu Wabunge wafanyakazi wako salama. Labda kutokee jambo ambalo kati ya hao wafanyakazi lazima utakuta kuna wengine labda maadili yao hayafanani na sekta yetu na inawezekana tu lazima watakuwa wapo, ama aina moja au nyingine ya mfanyakazi ambaye hatakuwa anaendana na sekta tunayokwenda kuijenga. Sheria za utumishi wa umma zimeweka ufafanuzi wa kila jambo na kwa namna hiyo basi tutaweza kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitolewa hoja hapa kwamba hii mifuko wakati mwingine imekuwa inakufa kwa sababu ya madeni.

Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani tulikuwa na madeni ya aina tatu kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Deni la kwanza kubwa ambalo ni la msingi lilikuwa ni malimbikizo ya michango ya wanachama yenye thamani shilingi za kitanzania trilioni 1.3, naomba kuwaarifu Wabunge fedha hiyo yote imekwisha kulipwa kwenye mifuko, fedha yote trilioni 1.3 tumekwisha kuilipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumebakiza madeni mengine ambayo ni lazima yahakikiwe lakini vilevile yatengenezewe mfumo wa kuyalipa. Lakini wakati tunafanya utathimini wa mfuko tulijiuliza swali lingine moja la msingi, je, madeni haya ni sababu ya mfuko kama wa PSPF kutokufanya vizuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo hapa taarifa ya utathimini ambayo imejionyesha wazi. Ukiacha hata hayo madeni mengine kwa mfano ukauacha mfuko wa PSPF kama vile una kila kitu, mfuko huo maisha yake ni mafupi sana na Mfuko wa PSPF ulitakiwa uwe umekwisha kufa mwaka 2018 hata kama madeni yangekuwa yamelipwa yote. Lakini vilevile Mfuko wa LAPF na Mfuko wa GEPF ulikuwa unakufa mwaka 2049 na mifuko hiyo ndiyo ile mifuko ambayo pendekezo lake ilikuwa ichangiwe sasa kiwango cha uchangiaji kifike asilimia 30. Lakini Mfuko wa PPF maisha yake yalikuwa yanakwenda mpaka mwaka 2075 kwa kikokotoo cha moja chini ya mia tano na themanini (1/580). Mfuko wa NSSF uhai wake ni miaka 75 mpaka 85.

Sasa Waheshimiwa Wabunge ukishapata data kama hizi utabebaje hoja ambayo haina uchambuzi wa kitafiti kama uchambuzi ninaoutoa hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikwenda mbali zaidi tukajiuliza hivi kwenye Mfuko wa PSPF wale wanachama ambao wako kwenye mfuko huo, kwa mwezi wanachangia shilingi ngapi na malipo ya pensheni zao kwa mwezi ni shilingi ngapi, tulilolikuta michango yao kwa mwezi ni shilingi bilioni 44 lakini mafao wanayolipwa ni shilingi bilioni 77. Sasa Waheshimiwa Wabunge hebu fanya huo ulinganishi na kwa sababu kikokotoo kilikuwa kimewekwa kwenye sheria unapokuja na matokeo sasa ya utathimini wa mfuko hali ilikuwa ni tete ya kutokuelewana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka sasa hivi turudi kama nilivyosema tukakae kwa pamoja, tujue mwenendo mzima wa namna tutakavyofanya kwa kukubaliana na wafanyakazi wenyewe na hiyo itatusaidia kutuweka mahali pazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kwamba suala zima la deni la malimbikizo la michango ambalo lilikuwa kwa Serikali na baada ya kulipwa, inakupa nafasi ya kutathimini sekta na mifuko ilivyo hali yake ilivyo na nini cha kufanya, lakini sasa kwa kutumia sheria ulizonazo za kazi ni lazima urudi ukakae na wafanyakazi wenyewe na mkishafanya utathimini mtakaa mtakubaliana, mtaelewaa na safari itakuwa salama zaidi. Ninaamini kwa maneno haya hata Mheshimiwa Bilago sasa ananielewa vizuri na nitamshukuru kama ataelewa hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo tumepata pendekezo toka kwa Mheshimiwa Bashe linalohusu kuangalia kifungu cha 40 na 41 na kuona ni namna gani tunaweza kufanya ili kuona Makatibu Wakuu nao wanakuwa considered kwenye mfuko wetu na kwenye sheria ambazo zinaenda kueleza mfumo wa mafao yao. Jambo hili Waheshimiwa Wabunge naomba mtuachie ili turudi na tukalitafakari na tuone ni watu wengine wa aina gani ambao watashiriki na wao watahitaji kushirikishwa katika kufanya utathimini na kuja na pendekezo ambalo litabeba dhana zima ya mahitaji halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimalizie na fao la elimu tumewasikia Waheshimiwa Wabunge. Tutakachokifanya kwa sababu kifungu cha 29(3) kinatuelekeza kuangalia namna nzuri ya kuendelea kulipa mafao, kwanza niwahakikishie watoto wote ambao wanalipiwa fao la elimu hakuna mtoto atakayeacha kuendelea kulipiwa fao la elimu, hiyo tutaendelea kuwalipia na kama tutaona fao hili baada ya utathimini ni fao ambalo ni zuri ambalo linaweza kuwasaidia wanachama kwa kutumia kifungu cha 29(3) tutafanya hivyo na ninaomba sana Waheshimiwa Wabunge muwe na imani na sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango iliyoletwa na Wabunge ni mingi niseme tu labda tutaijibu ile ambayo tutashindwa kuijibu, tutaijibu kwa kutumia maandishi.

Nimalizie kwa kusema Waheshimiwa Wabunge Muswada huu ni muswada unaowahusu wafanyakazi wa nchi Tanzania na kwa kuwa muswada huo toka tulipoanza tumefanya kazi ya kutosha kwa kushirikiana na wafanyakazi wenyewe kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania yaani TUCTA. Na kwa kuwa TUCTA wenyewe kwenye barua niliyonayo na maoni haya wameridhia vipengele ambavyo vipo kwenye muswada huu. Ninawaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa shughuli hii ina wenyewe na wenyewe ni wafanyakazi wa Tanzania, yale tuliyomesema tunakwenda kujadiliana na wafanyakazi, mridhie mtuache tukajadiliane na wafanyakazi na tutayarudisha ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba sana tusije tukatumia nafasi hii kuwaamulia wafanyakazi mambo ambayo ama hawatoyapenda ama yatakiuka misingi na taratibu zetu za kisheria za kutekeleza matakwa ya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo niwashukuru sana sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa mara nyingine ninawaomba sana muunge mkono muswada huu. Muswada huu umefanyiwa kazi nzuri sana na Kamati, muswada huu unahitajika sana na wafanyakazi wa Tanzania, muswada umeweka mafao mengine mapya mengi ambayo wafanyakazi walikuwa wanayahitaji, muswada huu hatma yake ni makubaliano kati wafanyakazi na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya, sasa naomba kutoa hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU:
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nyingine ili niweze kuja kuhitimisha hoja ambazo zimetolewa na
makundi mbalimbali katika mjadala huu mkubwa ambao utatupelekea leo kutengeneza historia ya kufanya mabadiliko ya nane ya sheria inayosimamia demokrasia ya vyama vingi katika nchi yetu ya Tanzania nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru wewe binafsi kwa kuongoza mjadala huu vizuri lakini nimshukuru sana Naibu Spika kwa kukusaidia pia kuongoza mjadala huu vizuri katika siku hii ya leo. Lakini kwa kweli kwa dhati nishukuru sana wachangiaji wote nikianza na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba ya Sheria kwa kazi kubwa waliyoifanya. Umeshuhudia hapa Serikali ikiwa imekubaliana na ushauri tuliopokea kwa Kamati yako ya Katiba na Sheria, ninaweza kusema kwa kiasi cha 100% katika masuala makubwa yote ambayo Kamati ilkuwa imetushauri. Naishukuru sana Kamati yako namshukuru Mwenyekiti, nawashukuru na wajumbe wote.

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno haya ya shukurani labda kwanza nianze moja kwa moja kwenye jambo kwenye hoja ambayo Mheshimiwa Zitto aliisema hapa wakati anachangia na alinipa tahadhali mimi na Serikali lakini na wale wote wanaounga mkono Muswada huu leo upitishwe kuwa sheria. Kwamba sheria hii itakwenda kuanza kushugulika na Chama cha Mapinduzi kwa sababu Chama cha Mapinduzi bado hakijapata usajili. Ninaomba nimwambie tu Mheshimiwa Zitto aende akafungue sheria mama ya vyama vya siasa na akasome kifungu cha 7 kinasema nini na kile kitaenda kumpa kumhakikishia usalama wa Chama cha Mapinduzi mpaka sasa na si tatizo lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini labda pia nizungumzia kidogo tu kwanza suala la Mheshimiwa Kubenea amesema hapa kwamba Muswada huu hauna uhalali wa kuendelea kwa sababu ushiriki wa Baraza la Vyama vya Siasa katika kutoa maoni ya Muswada huu ulikuwa ni hafifu. Sitaki kurudia sana wadau walisema nini. Nikushukuru umelizungumza jambo hili kwa kiasi chake lakini naomba tu nikuthibitishie sheria mama ya vyama vya siasa namba 258 inasema Baraza la Vyama vya Siasa ni mshauri wa msajili lakini Baraza kazi yake siyo kutunga sheria lakini itashauri maoni ambayo yanaweza kuchukuliwa kwenye kutunga sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Na kazi hiyo waliifanya vizuri tu na ninaomba nikukuhakikishie kwamba utaratibu ulioweka wa kukialika chama kimoja kimoja ulikuwa ni ushauri mzuri na maamuzi mazuri sana kwa sababu Kamati ilipata kukisikia chama kimoja, kimoja katika ya vyama vyote 19. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wakati wa mchakato wa maandalizi ya kupokea maoni ya Muswada huu sisi wote Waheshimiwa Waabunge tutakumbuka vyama hivi 19 baada tu ya Muswada kuwa umesomwa mara ya kwanza hapa Bungeni viko vyama vilikwenda mahakamani kupinga Muswada huu usiletwe Bungeni. Viko vyama vilikuja hadharani vikasema Muswada huu haufai usije Bungeni. Lakini viko vyama kati hivyo vyama 19 vikasema kwamba Muswada huu unafaa na ni lazima upitishwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa hali tu ya kawaida kama vyama vilishakuwa na maoni tofauti, vingine vimeenda Mahakamani, vingine vimeita muswada huu tena vikauita majina tofauti ambayo wala siwezi kuyarudia, unavikusanyaje hivyo vyama tena vikae pamoja halafu vilete maoni ya pamoja?

Mheshimiwa Spika, halikuwa ni jambo la busara, jambo la busara ni lile ulilolisema kila chama kije kueleza mbele ya Kamati na walifanya hivyo. Niishukuru sana Kamati yako, walikuwa watulivu, walivisikiliza vyama vyote 19, na vile vyama 19 viko vyama viwili vilipokuja mbele ya Kamati ama Mwenyekiti wa Kamati alipinga muswada, Katibu wa Kamati akaunga mkono muswada. Vyama hivyo vilikuwa viwili na vyama vingine ulikuta kwamba chama kizima viongozi wote waliunga mkono muswada wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niwahakikishie Wabunge ushiriki wa vyama katika kutoa maoni kwenye muswada huu kwa kweli nafasi ilikuwa kubwa na vyama vinafanya kazi yao vizuri na mimi ninaomba kuvishukuru vyama. Wakati wote kila mtu anapopata nafasi ya kutoa maoni yake basi, wakati mwingine maoni ya wachache yatasikilizwa na maoni ya wengi yatachukuliwa na leo tunahitimisha shughuli hii, naishukuru sana Kamati yako.

Mheshimiwa Spika, michango ya Waheshimiwa Wabunge, lakini na hasa Taarifa ya Kambi ya Upinzani imezungumza sana kifungu hiki cha 5(5)(A)(1), ambacho kinaweka masharti ya utoaji wa elimu ya uraia. Nataka niwatoe hofu tu Wabunge na hasa wale wanaoogopa kwa nini kifungu hiki kiletwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme jambo moja, kwa sasa ndani ya Serikali yetu tunayo Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inaipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi mamlaka ya kuratibu elimu ya mpiga kura inayotolewa kwa mpiga kura. Sasa kama tayari tunayo sheria ya namna hiyo tunaogopa nini kumpa Msajili madaraka ya kuratibu aina ya elimu ya uraia itakayotolewa kwa vyama vya siasa? Tunaogopa nini na ni kitu gani kigeni hapo?

Mheshimiwa Spika, hakuna jambo geni na hakuna hofu yoyote. Mwenyekiti wa Kamati ametuambia ziko sheria katika nchi nyingine tena ndani ya Bara la Afrika, sheria hizo pia zinaweka masharti magumu sana ya kuratibu elimu ya uraia ndani ya nchi zao. Kwa hiyo, jambo hilo wala sio geni kwa nchi yetu tu, limeshafanywa kwenye nchi nyingine na sisi tunaenda kufanya jambo hilo, tunaulizwa hapa tumeona kuna ombwe gani mpaka tunaleta kifungu hiki?

Mheshimiwa Spika, hakuna mtu asiyejua kwamba dunia na ulimwengu mzima umebadilika. Hali ya usalama katika dunia hii imebadilika na kila jambo katika dunia hii kila nchi inajifunza kutoka kwa jirani yake ama kwa Taifa lingine. Ni wakati muafaka sasa elimu ya uraia katika nchi yetu ya Tanzania inayoingia katika vyama vyetu ni lazima iratibiwe na ikiratibiwa itatusaidia kudumisha umoja na usalama wa Taifa letu, pamoja na kuendelea kuangalia mwenendo wa
shughuli za demokrasia na uendeshaji wa shughuli za vyama katika Taifa letu.

Kwa hiyo, niwaombe tu Wabunge wasiwe na hofu na wale wenzetu wenye hofu itabidi tuanze kuwashangaa kwa nini wanakuwa na hofu? Kulikuwa na nini katika kutokuratibu elimu hiyo ya uraia kwenye vyama vyao? Hilo ni jambo ambalo tunatakiwa kujiuliza, unapokataa sana kuratibu jambo ambalo linaleta tija ulikuwa unaficha nini kabla ya sheria hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niliambie Bunge lako tukufu kwamba wakati tunapokea maoni ya wadau yuko kiongozi wa chama kimoja cha siasa alituambia wakati wa kupokea maoni anasema yeye aliwahi kugombea Urais mwaka fulani katika Taifa letu, na akatuambia alikuwa hana fedha yoyote, hakuwa hata na senti tano, lakini alipata fedha, akaletewa kila kitu na taasisi mbalimbali kutoka nje ya nchi, lakini vilevile akatengenezewa uratibu wa kuratibu elimu ya uraia kupitia kwenye chama chake na taasisi mbalimbali. Sasa tushukuru Mungu tu labda huyo mgombea hakuwa na lengo baya kwenye Taifa letu, angekuwa na lengo baya tungepata shida. Kwa hiyo, wenye mapenzi mema watulie, wale ambao hawakuwa na mapenzi mema ni lazima wakubali sasa nchi yetu ni lazima mambo haya yaratibiwe ili tuwe na usalama na uhakika wetu.

Mheshimiwa Spika, muswada umelenga kudhibiti vyama vya siasa. Iko hoja hapa imeletwa na tumeambiwa kwamba kwa nini muswada huu unataka kudhibiti vyama vya siasa?

Mheshimiwa Spika, mimi naomba tu niseme, kwamba muswada huu unalenga kwa kweli kukuza demokrasia na hasa kukabiliana na changamoto ambazo tulikuwanazo. Kifungu cha 6C(5); kifungu hiki kinaenda kuweka utaratibu sasa wa kuvikataza vyama kukasimu shughuli muhimu sana ambazo zitaleta umoja na demokrasia kwenye vyama vyao.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano tumeshuhudia hapa ndani ya mienendo ya vyama vyetu vya siasa kwamba mgombea wa Urais anaweza akapatikana tu labda kwa watu kumi ama 20 kukaa mahali na wanaamua huyu atakuwa mgombea wetu wa Urais bila ridhaa ya chama. Maamuzi hayo yanayofanywa na watu wachache yamekuwa yakileta mpasuko na migogoro mingi na migogoro mikubwa sana ndani ya chama, wote ni mashahidi. Sheria hii inapokuja kuweka mfumo na uratibu, kwa mfano mgombea Urais apatikane kupitia mikutano mikubwa ya vyama, mtu anasema sheria hii inabana vyama, haileti demokrasia.

Mheshimiwa Spika, ni lazima hapa ujiulize kinachotakiwa ni nini? Kwa hiyo, utaratibu wa mtu kuamua kukaa ndani ya ofisi na kuteua mgombea ndio demokrasia kuliko Mkutano Mkuu wa chama kuteuwa mgombea wa Urais?

Mheshimiwa Spika, haya ni mambo ya kujiuliza. Sheria inakuja kuweka utaratibu Mwenyekiti wa Chama wa Taifa achaguliwe na Mkutano Mkuu wa Taifa na Mkutano Mkuu huo wa taifa uwe umeshaonekana kwenye mfumo wa kiuratibu wa katiba ya chama. Viko vyama hapa Wenyeviti wao wa Taifa hawachaguliwi na Mikutano yao Mikuu ya Taifa, vipo.

Mheshimiwa Spika, na ninakwambia kwamba sheria hii sasa inakwenda kutibu hayo na ukiona watu hawataki ujue ajenda hizi zilikuwa zinaendelea kwenye vyama vyao, kwa hiyo acheni tupate sheria ambayo itatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linadhihirisha kabisa kwamba sheria hii inaenda kukuza demokrasia. Kabla ya sheria hii chama kilikuwa kinaweza kuadhibiwa kwa makosa ya mwanachama, lakini katika sheria hii sasa tumekubaliana kwamba akifanya makosa mwanachama ataadhibiwa mwanachama mwenyewe na si chama chake, lakini watu nashangaa kwamba wanakataa wanasema huu sio mfumo mzuri.

Mheshimiwa Spika, ili kukuza demokrasia viko vyama vilikuwa vinabadilisha Katiba za vyama vyao ndani ya ofisi na wanachama hawana habari. Mtu akitaka kuongeza madaraka ya kukiongoza chama alikuwa na uwezo wa kuibadilisha Katiba mahali popote, sheria hii sasa inaenda kuweka utaratibu. Kwa hiyo, kama tunaweka utaratibu huo hiyo ni demokrasia na si kwamba tunenda kuminya demokrasia. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge muukubali muswada huu, ili haya matatizo yaweze kuondoka.

Mheshimiwa Spika, na mimi nikuhakikishie Ofisi ya Msajili wa Vyama ina malalamiko mengi kutoka kwa wanachama wa vyama mbalimbali wakilalamikia mienendo ya kunyimwa demokrasia ndani ya vyama vyao kwa aina moja ama nyingine. Sasa hapa tunaenda kutoa dawa na ninadhani sheria hii itatusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, hapa imezungumzwa kwamba muswada una nia ya kumpa Msajili nguvu kubwa na hiyo nguvu si sawa kwa muktadha wa siasa na demokrasia ya nchi yetu tuliyonayo kwa sasa hivi. Ukiangalia mwenendo mzima wa shughuli za siasa zilivyokuwa zinafanywa ndani ya vyama vyetu, leo tunapoamua kumpa Msajili, kwa mfano, madaraka ya kufuatilia matumizi ya fedha ndani ya vyama ni jambo la msingi sana. Tumepokea hapa ripoti ya CAG na umeona ni kwa kiasi gani vyama vimekuwa vikifanya matumizi mabaya ya fedha na hakuna sheria ambayo ilikuwa inavibana vyama hivyo katika kudhibiti matumizi ya fedha ambayo ni fedha za walipa kodi wa Tanzania na hasa vile vyama ambavyo vilikuwa vinapata ruzuku.

Mheshimiwa Spika, tuliona hapa na tuna malalamiko kwamba kuna baadhi ya vyama kwa viongozi wa vyama wanavikopesha vyama vyao fedha na wanapovikopesha hakuna kumbukumbu zozote za aina ya mikopo inayopelekwa kwenye vyama kutoka kwa viongozi na wala haielezi matumizi ya mikopo hiyo ni kwa ajili ya shughuli gani? Na Serikali inapotoa fedha za ruzuku baadhi ya viongozi wa vyama wamekuwa wakichukua fedha za ruzuku kujilipa mikopo ambayo haina maelezo ilipelekwa kwa sababu gani?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukiangalia haya yote yanayoenda kufanywa na huu muswada unagundua kabisa kwamba muswada huu sasa unaenda kutibu matatizo mengi katika uwanda wa demokrasia, lakini uwanda wa uendeshaji wa shughuli za kisiasa ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, limesemwa jambo hapa kwamba, kwa nini kile kifungu kidogo cha 6A(5) kinaweka hii misingi na alama muhimu za taifa letu. Watu wamebeza mwenge wa uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar kwamba hivi si vitu ambavyo vinastahili kukaa katika kifungu hiki.

Mheshimiwa Spika, mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba tuendelee kushangaana. Hawa hawa leo wanaoyakataa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar wakitoka hapa wanaenda tena kuwashawishi Wazanzibar kwamba
wanapenda sana kuwatetea kwenye hoja zao. Lakini tujiulize kuhusu historia ya muungano wa taifa letu, kwamba utawezaje kuzungumza muungano wa taifa hili bila kuzungumzia mapinduzi matukufu ya Zanzibar? Haiwezekani!

Mheshimiwa Spika, huwezi kuzungumza uhuru wa taifa letu la Tanzania bila kuuzungumzia mwenge wa uhuru, haiwezekani. Tunayo Sheria ya Nembo ya Taifa na Sheria ya Nembo ya Taifa inaweka mwenge kama alama mojawapo kwenye Nembo ya Taifa letu. Vilevile kinaenda kusisitiza kwamba vyama vyote wakati wa kutengeneza sera za vyama vyao ni lazima watambue hiyo misingi mikubwa na alama muhimu za Taifa letu zinazoonesha utaifa wetu pamoja na utawala bora, mambo ya amani na kukimbia rushwa. Leo tunasema tunaongeza na masuala ya jinsia kama ni masuala ya msingi sana katika uendeshaji wa vyama vya siasa, lakini watu wanaona jambo hili si jema pia.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hilo tumeona kabisa kwamba sasa tunakokwenda vyama vitakapoteuwa wagombea wake, kama mgombea atayakataa mapinduzi yetu ya Zanzibar hatoshi kuwa kiongozi katika chama cha siasa. Kama mgombea katika uongozi wa chama cha siasa hatazungumzia masuala ya jinsia, masuala ya mapambano dhidi ya rushwa, masuala ya wenye ulemavu na masuala yote yanayozingatia utamaduni na uhuru wa Taifa letu, kiongozi huyo hatoshi, acheni tuweke hapa. Lakini niseme kama sera za vyama hivi vyote katika Taifa letu havitathamini mwenge wa uhuru kama alama ya uhuru wa Taifa letu ni lazima chama hicho tukishangae na tutajua chama hicho hakina nia njema ya kulinda uhuru wa Taifa la Watanzania, kwa hiyo jambo hili lazima lieleweke vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaona watu wamezungumza sana kuhusu kifungu cha 8E, kwa nini tunaondoa hivi vikundi vya ulinzi?

Mheshimiwa Spika, mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge labda msome vizuri kwanza hicho kifungu kinasema nini. Kifungu hicho kinaenda sambamba na kifungu cha Katiba ambacho tumekieleza cha 147 kwa sababu gani! Kifungu hicho cha 8E(1) kimesema; “kiongozi au mwanachama asije akaandikisha wala kuunda vikundi vinavyofanana na vikundi vya kijeshi”, kifungu ndicho kimesema hivyo. Kama wewe unaona kwamba unataka kulindwa nenda huko kachukue hizo taasisi zilizoanzisha vikundi vya ulinzi na usalama watakulinda, lakini tunasema wewe kama chama, kiongozi, usianzishe kikundi kinachofanana na kikundi cha kijeshi ndani ya chama chako, hilo jambo limepigwa vita hapa wazi kabisa ama usianzishe hicho kikundi kitakachofanya kazi zinazofanana na taasisi ambazo zinashughulika na ulinzi na usalama katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sasa umeshaambiwa usifanye, usianzishe vikundi ambavyo vinafanana na taasisi za ulinzi na usalama nchini, sasa wewe unataka kuanzisha kikundi kinafanana na polisi, kinafanana na wanajeshi, kinafanana na kikundi cha makomandoo. Kuna Mbunge mmoja alisema wao hawachukui silaha wanapigana kwa mikono, sasa kama wanapigana kwa mikono, lakini wanafanana na vikundi vya kijeshi, nduguzanguni machafuko yote katika nchi za wenzetu yalianzishwa kwa sababu ya kutokuzingatia kifungu hiki ambacho kiliruhusu vikundi vya namna hiyo kwenye vyama vya siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba niwathibitishie wanasiasa wenzangu, tumeona mfano dhahiri wakati wa uchaguzi, kila mgombea Urais katika nchi hii anakuwa analindwa na polisi tena ni polisi wa Serikali hii hii, hakuna mgombea wa Urais hata mmoja wakati wa uchaguzi amelindwa na green guard ama amelindwa na red brigade ama amelindwa na blue brigade. Wagombea wote wa Urais, Makamu wa Rais wakati wa uchaguzi wote wamelindwa na polisi hawa hawa wa Tanzania na hakuna aliyepata matatizo hata mmoja. Leo tunasema kwamba, hatuna imani na Polisi wa Tanzania katika kuwalinda wanasiasa tunaanzia wapi?

Mheshimiwa Spika, ninaomba ndugu zangu tuendelee kukipitisha kifungu hiki. Tuondoe vikundi hivyo ambavyo mwisho wa siku vinaweza kuleta matatizo makubwa ya usalama, amani katika nchi yetu ya Tanzania. Ndugu zangu kama tunaendelea kung’ang’ania hivi vikundi kila mtu atatuuliza tuna ajenda gani ya kuwatumia hawa?

Mheshimiwa Spika, na Mjumbe mmoja amesema tunawapa mafunzo kweli kweli. Sasa hayo mafunzo mwisho wa mafunzo inaweza kuwa ni shida kubwa kuliko kuendeleza amani na utulivu kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 17 tumetoa maelezo sasa hivi kuhusu vyama kuweka mashirikiano. Ninaomba sana Waheshimiwa Wabunge muunge mkono kifungu hiki. Tumeshuhudia vyama vikishirikiana bila kuwa na utaratibu na matokeo ya kufanya mashirikiano bila kuwa na utaratibu yameleta migogoro mikubwa sana ndani ya vyama vya siasa nchini.

Mheshimiwa Spika, ilifikia hatua, vyama vya siasa vinafanya ushirikiano halafu vinatumia ushirikiano huo ambao siyo rasmi kurasimisha shughuli ambazo zinaenda kinyume na sheria tulizonazo nchini. Jambo hili halipaswi kufumbiwa macho. Sheria sasa inasema, kila chama kitakachotaka kufanya ushirikiano, kitamtaarifu Msajili, kwani shida ipo wapi? Nendeni tu mkatoe taarifa kwa Msajili kwamba mnataka kufanya ushirikiano na lengo la ushirikiano wenu. Sasa shida ipo wapi? Kutoa tu taarifa kwamba tunataka kushirikiana, shida haipo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani sasa kifungu hiki kitatusaidia kuratibu ushirikiano huo, kila chama kifanye ushirikiano katika malengo wanayoyataka lakini kitatusaidia pia kuondoa migogoro. Sasa sheria inataka hao wanaotaka kufanya ushirikiano, ni lazima kwanza ushirikiano huo upitie kwenye Mikutano yao Mikuu ya Taifa na siyo watu wanakutana wapi au wapi wanashirikiana, hapana. Hiyo itasaidia sana kuondoa migogoro kwenye vyama vya siasa.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, labda kwa kumalizia kwa sababu ya muda, ni huu utaratibu ambao umewekwa na Kifungu cha 21(e), nilisema pale mwanzo, haya ni Mamlaka ya Msajili kushungulikia Mwanachama anayekiuka Katiba ya chama chake lakini pia anakiuka sheria za nchi na hasa Sheria za Vyama vya Siasa. Huko mwanzo nilisema, mwanachama huyu akikiuka Sheria ya Vyama vya Siasa chama chake ndiyo kilikuwa kinapata taabu na kuadhibiwa.

Mheshimiwa Spika, kifungu hiki sasa kimeweka vizuri sana, kinamfanya Msajili, akigundua Mwanachama amekiuka sheria, Msajili atakiandikia chama chake, jamani mtu wenu huyu amefanya mambo ambayo siyo sawa sawa, ni kinyume cha sheria na atakiagiza chama chake kichukue hatua. Kisipochukua hatua, Msajili sasa apate nguvu na yeye ya kumchukulia hatua huyo Mwanachama na kukiacha chama kibaki salama. Hapo kuna tatizo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie kwamba kwa kukiweka kifungu hiki, vyama vingi vitakuwa salama, ninyi mmekuwa ni mashahidi, wanachama wa vyama vyetu wamekuwa wakileta fujo bila kutumwa na vyama vyao na mwisho wa siku chama kilikuwa kinaadhibiwa na mwanachama anajificha ndani ya chama. Kwa hiyo, Kifungu cha 21(e) sasa kinaweka utaratibu mzuri, chama kitakuwa salama, mwanachama atakayeshughulika kuvunja sheria, yeye ndiye atakayebeba dhamana ya kushughulikiwa na chama chama chake kwanza, lakini baadaye atakuja kushughulikiwa na Msajili kwa utaratibu mzuri kabisa ambao umewekwa na sheria hii ambayo leo mkiipitisha itatusaidia sana kuweka utaratibu huo wa kutoa nidhamu kwa vyama vyetu.

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kusema yafuatayo: watu wamechangia na wamesema kwamba sisi wote tunatakiwa wote tunatakiwa kusimama kwenye misingi ya demokrasia, lakini hakuna demokrasia yenye uhuru ambayo hauna mipaka. Demokrasia nchini imeendelea kukua, haya mabadiliko tunayoyafanya ni mabadiliko ya nane na Sheria hii ya Vyama vya Siasa wala haijafanyiwa mabadiliko mara ya kwanza kwenye mwaka huu, lakini mwisho wa siku tunaamini baada ya sheria hii, haki usawa na uendeshaji wa shughuli wa vyama vya siasa na shughuli za siasa katika nchi yetu zitaratibiwa vizuri. Wenye nia njema wataonekana na wasio na nia njema wataonekana. Mwisho wa siku Taifa hili ni la kwetu sisi wote. Kama Taifa hili ni letu wote, kama tutafanikiwa kuweka mfumo na utaratibu mzuri wa uendeshaji wa demokrasia, uratibu wa shughuli za siasa nchini, sisi wote ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tutakuwa salama. Tusipofanya hivyo, tutapata shida.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niwashawishi sana Waheshimiwa Wabunge waunge mkono hoja hii, tupitishe hii sheria ikatusaidie kusimamaia masuala ya demokrasia na utaratibu na uratibu wa vyama vya siasa katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja yangu lakini naomba kutoa hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 – Wizara ya Fedha na Mipango
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa dhati kabisa nianze kwa kukupongeza wewe mwenyewe kwa umahiri mkubwa na umakini mkubwa unaoonesha katika kusimamia shughuli za Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli umejipambanua kama ni mtaalam na mwanamke unayeweza kuhimili mikiki ndani ya Bunge, lakini unao weledi wa hali ya juu wa kuhakikisha kwamba Bunge hili linaongozwa kwa kufuata Kanuni ambazo zimewekwa na sisi Wabunge wenyewe. Naomba nikutie moyo, katika safari yoyote kuna magumu, lakini yastahimili kwa sababu Umma wa Watanzania unaamini kabisa kwamba unao uwezo wa kutusaidia kuliongoza Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi ya pekee pia kuwapongeza sana Wabunge wa Chama cha Mapinduzi. Nawapongeza sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi walikuwa wanadhani kwamba Wabunge hawa wa Chama cha Mapinduzi uwezo wao katika kuyachambua mambo, kuchangia michango yenye kuwawakilisha Watanzania ni mdogo, lakini katika Bunge la Bajeti la mwaka huu, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wameonesha wanao uwezo mkubwa sana wa kujenga hoja; wa kuwakilisha matatizo mbalimbali na mahitaji ya wananchi waliowachagua na kuamua kuwaweka wawakilishe katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge hawa wa Chama cha Mapinduzi wamefanya kazi kubwa ya kihistoria katika Bunge hili kwa mwaka huu na katika bajeti ya mwaka huu. Kwa hiyo, kwa kweli, naomba niwapongeze. Wameishauri Serikali, wametoa michango ambayo Serikali ikiifanyia kazi, inaweza ikatimiza vizuri Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote ambao wameshiriki kikamilifu katika mchango wa Hotuba ya Bajeti ya kwamba michango yao ambayo wameotoa, kwanza kupitia Kamati za Bunge, lakini na michango ambayo wameitoa na ushauri walioutoa kupitia Kamati ya Bajeti, sisi kama Serikali tutaichukua na kuifanyia kazi ipasavyo. Nasema hivyo kwa sababu gani?
Katika bajeti ambayo tumekuwa tukiijadili ili tuipitishe leo, ingawa watu wengi wanasema kwamba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wamejiandaa kutokupitisha bajeti yao, jambo ambalo siyo kweli na leo watashuhudia tutakapopitisha bajeti hii! Nasema hayo kwa sababu sitaki Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wachonganishwe na Rais wao na Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti hii ni ya kwetu sisi kama Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi na inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na tunaamini kabisa kama Serikali, haya ambayo yamechangiwa, tena na Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, ndiyo wananchi waliyotutuma kuyafanya ndani ya Bunge la Hamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli wa jambo hili unajidhirisha katika Kanuni yako ya 94 ya Kanuni za Bunge. Kanuni hiyo ya 94 kwa faida ya Watanzania nitaisoma tu kidogo. Kanuni ya 94 inasema, “Katika Mkutano wake wa Mwezi Oktoba na Novemba kwa kila mwaka Bunge kwa siku zisizopungua tano litakaa kama Kamati ya Mipango, ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 63(3)(c) ya Katiba kwa kujadili na kuishauri Serikali kuhusu mapendekezo ya Utekelezaji wa Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha unaofuata.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kanuni hiyo ya 94, kazi ya Mkutano huo, Mkutano ambao ni Mkutano wa Kuishauri Serikali, itapokea na kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali.
Kwa hiyo, sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuna miaka mitano ya kuishauri Serikali yetu na kuhakikisha tunatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatuna shaka na tutayafanya hayo yote bila wasiwasi wowote na Serikali yetu itaendelea kutekeleza matakwa ya Watanzania, bajeti moja hadi nyingine kwa kipindi chote cha miaka mitano na Watanzania wawe na amani Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuko imara na Serikali iko imara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi wamezungumza matatizo ya Sekta ya wafanyakazi na hasa katika sekta binafsi. Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa Sheria za Kazi, kumekuwa na tatizo kubwa la wageni kufanya kazi bila vibali katika nchi yetu ya Tanzania, lakini vilevile kumekuwa na wageni ambao wanatumia ujanja ujanja tu katika kupata ajira katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote, yako marekebisho ya Kisheria tutayaleta hapa katika Bunge hili yataipa meno Serikali kupambana na waajiri wote wanaokiuka Sheria za Kazi katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Wabunge wamechangia sana kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii kwa maana ya Social Protection. Tunajua, tunajipanga kupitia upya Sheria zetu zinazosimamia mifuko ya hifadhi ya jamii ili kero ambazo zinawapata Watanzania katika sekta hiyo ziweze kushughulikiwa inavyotakiwa, lakini kubwa zaidi ni kuhakikisha tunaongeza wigo wa kuwafanya Watanzania wengi wafikiwe na suala zima la hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Munde na Wabunge wengine wameomba sana tuongeze fao la bodaboda katika mafao ambayo yatakuwa yanatolewa katika sekta hii ya hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshakubaliana na mifuko yote kuona ni namna gani sekta binafsi, hawa vijana wetu wa bodaboda nao waingizwe katika suala zima la social protection ili waweze kupata faida ya mafao yanayotolewa na mifuko.
Mhshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, mimi na Naibu Waziri wangu, Mheshimiwa Mavunde, tumejipanga na tutapita katika Mkoa mmoja baada ya mwingine ili kuona namna gani tunashirikiana na nyie katika suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine tutayajibu kimaandishi, lakini naunga mkono bajeti hii na ninampongeza sana Waziri wa Fedha na Naibu wake. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya masuala haya ya ardhi, ndugu yangu Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, kwa kazi yake nzuri anayoifanya pamoja na Naibu Waziri wake. Niseme tu kwamba sisi kama Serikali tutaendelea kushirikiana nao ili haya yote yanayojiri kwenye migogoro ya ardhi yaweze kupatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kusema kwamba yale yote ambayo yanafikiriwa kwamba Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ingeyachukua na kuyashughulikia kwa uzito, Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali hapa Bungeni yupo na ameya-note vizuri. Mimi pia kama Waziri mwenye dhamana chini ya ofisi hiyo basi niseme kwamba tunayachukua yote. Waheshimiwa Wabunge tuwahakikishie kwamba tutayafuatilia na tutayatekeleza na tutashauriana na ninyi ili kuboresha haya yote yaliyojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza sana Wabunge wa Mkoa wa Dodoma na hapa leo wamewakilishwa vizuri sana na Mheshimiwa Felister Bura, amezungumza vizuri sana habari ya CDA na Mheshimiwa Kunti naye amezungumza vizuri sana habari ya CDA. Niseme Wabunge hawa wawili wamewawakilisha Wabunge wenzao wa Mkoa wa Dodoma lakini naamini kabisa Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde naye amekuwa mstari wa mbele sana kushughulikia masuala haya yanayohusiana na CDA. Wote kwa ujumla wao mara nyingi wamekuwa wakinieleza habari moja ama nyingine kuhusiana na CDA. Kwa hiyo, naomba tu niwahakikishie Wabunge wa Mkoa wa Dodoma na Wabunge wengine wote na Watanzania kwa interest ya kuhamishia makao makuu yetu ya nchi hapa Dodoma tuko pamoja na tutashirikiana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Wabunge wote wa Mkoa wa Dodoma na hasa Mbunge mwenyeji wa Jimbo la Dodoma Mjini, nadhani itapendeza sana kama tutapata nafasi kabla Bunge hili halijaisha tungekutana ili tutizame haya yote ambayo yamekuwa yakijiri kwa CDA hapa Dodoma. Pia tutathmini kwa pamoja umuhimu wa kuhamishia makao makuu ya nchi hapa Dodoma na hii itakuwa pia kwa faida ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma.
Kwa hiyo, naomba tu nichukue nafasi hii kuwahakikishia Wabunge wa Mkoa wa Dodoma kwamba tuko tayari sisi kama Serikali na mimi Waziri niko tayari kukutana nao na tukatathmini haya matatizo ambayo wanafikiri kwamba yamekuwa yakijitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ili kuwapa matumaini vizuri naomba niwathibitishie kwamba tumeanza kujipanga na CDA na hasa baada ya Mkurugenzi wa CDA kuthibitishwa rasmi na Mheshimiwa Rais, mwezi Februari, 2016, kuona kwamba tunarudisha mahusiano mazuri kati ya CDA na wananchi wa Mji wa Dodoma na kumaliza ile migogoro yote ambayo ilikuwa ikijitokeza kwa namna moja ama nyingine. Ijumaa nilianza kwa kufanya kikao na wafanyakazi wote wa CDA, tumekutana kwa pamoja, tumejitathmini kwa pamoja na tumejenga mkakati wa pamoja wa kuhakikisha kwamba tunapohamia hapa Dodoma kwa kweli wao wana wajibu mkubwa wa kusimamia mambo na mipango yote itakayowekwa. Kwa hiyo, naomba tu niwathibitishie kwamba tuko pamoja na tutaifanya kazi hii kwa uadilifu mkubwa.
Mheshimiwa mwenyekiti, lakini jambo lingine naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba ili kuondoa kutokuelewana kwenye masuala haya kati ya CDA na wananchi wa hapa Dodoma tumefikiri ni lazima tuharakishe sana kuleta ile sheria ambayo itaitambulisha vizuri Dodoma kama capital city. Kwa hiyo, sheria ile tumeanza kuitengeneza na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba sheria ile iko mbioni kabisa kuletwa na niwaombe tutakapoileta ndani ya Bunge basi mtusaidie kuipitisha. Tukiipitisha sheria hiyo itasaidia sana kupunguza migongano na migogoro mingi ambayo inajionyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ile pia itasaidia kusimamia azma ya Serikali ya kuhamia hapa Dodoma. Niwathibitishie tu kwamba ni lengo hasa la Serikali kuhamia Dodoma na iko pia kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, ni lazima tuone kwamba katika kipindi hiki tunajitahidi kuhamisha makao makuu na kuyaleta hapa Dodoma na hilo tutalisimamia na sheria itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini sheria hii pia itaondoa migongano ya kisheria kati ya taasisi mbalimbali ambazo pia zinasimamia matumizi ya ardhi katika makao makuu haya yanayotarajiwa kwenye mji huu wa Dodoma. Vilevile itaondoa pia migongano ya kisheria kwa sababu pia zipo sheria nyingine mbalimbali kwa mfano Sheria ya Local Government Authority na sheria nyingine. Tutakapoileta sheria hii itakuwa ni mwarobaini, itatusaidia sasa ku-define mipaka ya CDA lakini kutoa tafsiri halisi ya majukumu ya kila chombo ili migongano hii yote iweze kuondoka na azma hii ya Serikali ambayo ni njema iweze kutekelezeka ikiwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niendelee kutoa rai kwa wananchi wote wa Dodoma waamini Serikali yao inafuatilia kwa karibu sana kwanza kuhakikisha azma hii inatekelezeka lakini vilevile kuona kwamba migogoro inaisha kwa kufuata sheria na taratibu tulizojiwekea. Niwaombe wananchi wa Dodoma pale wanapoona kuna matatizo waamini kwamba sisi kwa kushirikiana nao tunaweza tukafanya vizuri sana na siyo vinginevyo. Sisi tuko tayari na tumeanza kufanyia kazi changamoto zilizopo na juzijuzi tu tumemaliza migogoro kadhaa ambayo ilikuwa inawakabili wananchi wa Dodoma. Kwa hiyo, waamini ile migogoro iliyobaki tutaendelea kuumaliza mmoja baada ya mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile waelewe kwamba na wao wanatakiwa kufuata sheria na kuzingatia sheria, kila jambo ni lazima litaenda kwa kuzingatia sheria. Pale ambapo tutaona kwamba wana haki watapewa haki yao na pale ambapo wao wanaona kabisa sheria inawataka watekeleze majukumu mengine naomba watupe ushirikiano. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ameamua kabisa kufanya kazi na sisi ili kuhakikisha kwamba tunamaliza matatizo haya yanayojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kabisa sheria hii pia itatufanya tuweze kuwa na mji wa kisasa, makao makuu ya nchi ambayo yatafanana na hii azma ya Serikali yetu tuliyonayo. Waheshimiwa wengi wamezungumza hapa, Mheshimiwa Shally ametuuliza mnakwenda kutembea huko hamuoni miji ya wenzenu ilivyo? Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Shally tumeona, tumejifunza miji mingi jinsi ilivyo mizuri na hivyo tunataka kuujenga Mji wa Dodoma uwe nao una picha ambayo itaweza kupeleka ujumbe wa namna nchi yetu ya Tanzania ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi mkiangalia jinsi Mheshimiwa Rais wetu sasa hivi hata ukienda kwenye mataifa mengine amekuwa akitambulika kwa sifa na heshima kubwa sana. Kwa hiyo, tutakapoujenga mji huu katika kipindi hiki cha kwake pia itabidi uendane na hadhi ya nchi yetu na vilevile uendane na kile tunachokifikiri kitakuwa ni sura ya Taifa letu katika mataifa mengine katika ulimwengu mzima. Naomba tu niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge tumeanza kufanya kazi ya kutosha ya kujenga miundombinu na tutaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo naomba niwahikikishie tuko tayari tutafanya kazi pamoja na ninyi na CDA kujenga makao makuu ya nchi hapa Dodoma. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa dhati kabisa nianze kwa kukupongeza wewe mwenyewe kwa umahiri mkubwa na umakini mkubwa unaoonesha katika kusimamia shughuli za Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli umejipambanua kama ni mtaalam na mwanamke unayeweza kuhimili mikiki ndani ya Bunge, lakini unao weledi wa hali ya juu wa kuhakikisha kwamba Bunge hili linaongozwa kwa kufuata Kanuni ambazo zimewekwa na sisi Wabunge wenyewe. Naomba nikutie moyo, katika safari yoyote kuna magumu, lakini yastahimili kwa sababu Umma wa Watanzania unaamini kabisa kwamba unao uwezo wa kutusaidia kuliongoza Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi ya pekee pia kuwapongeza sana Wabunge wa Chama cha Mapinduzi. Nawapongeza sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi walikuwa wanadhani kwamba Wabunge hawa wa Chama cha Mapinduzi uwezo wao katika kuyachambua mambo, kuchangia michango yenye kuwawakilisha Watanzania ni mdogo, lakini katika Bunge la Bajeti la mwaka huu, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wameonesha wanao uwezo mkubwa sana wa kujenga hoja; wa kuwakilisha matatizo mbalimbali na mahitaji ya wananchi waliowachagua na kuamua kuwaweka wawakilishe katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge hawa wa Chama cha Mapinduzi wamefanya kazi kubwa ya kihistoria katika Bunge hili kwa mwaka huu na katika bajeti ya mwaka huu. Kwa hiyo, kwa kweli, naomba niwapongeze. Wameishauri Serikali, wametoa michango ambayo Serikali ikiifanyia kazi, inaweza ikatimiza vizuri Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote ambao wameshiriki kikamilifu katika mchango wa Hotuba ya Bajeti ya kwamba michango yao ambayo wameotoa, kwanza kupitia Kamati za Bunge, lakini na michango ambayo wameitoa na ushauri walioutoa kupitia Kamati ya Bajeti, sisi kama Serikali tutaichukua na kuifanyia kazi ipasavyo. Nasema hivyo kwa sababu gani?
Katika bajeti ambayo tumekuwa tukiijadili ili tuipitishe leo, ingawa watu wengi wanasema kwamba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wamejiandaa kutokupitisha bajeti yao, jambo ambalo siyo kweli na leo watashuhudia tutakapopitisha bajeti hii! Nasema hayo kwa sababu sitaki Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wachonganishwe na Rais wao na Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti hii ni ya kwetu sisi kama Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi na inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na tunaamini kabisa kama Serikali, haya ambayo yamechangiwa, tena na Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, ndiyo wananchi waliyotutuma kuyafanya ndani ya Bunge la Hamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli wa jambo hili unajidhirisha katika Kanuni yako ya 94 ya Kanuni za Bunge. Kanuni hiyo ya 94 kwa faida ya Watanzania nitaisoma tu kidogo. Kanuni ya 94 inasema, “Katika Mkutano wake wa Mwezi Oktoba na Novemba kwa kila mwaka Bunge kwa siku zisizopungua tano litakaa kama Kamati ya Mipango, ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 63(3)(c) ya Katiba kwa kujadili na kuishauri Serikali kuhusu mapendekezo ya Utekelezaji wa Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha unaofuata.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kanuni hiyo ya 94, kazi ya Mkutano huo, Mkutano ambao ni Mkutano wa Kuishauri Serikali, itapokea na kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali.
Kwa hiyo, sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuna miaka mitano ya kuishauri Serikali yetu na kuhakikisha tunatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatuna shaka na tutayafanya hayo yote bila wasiwasi wowote na Serikali yetu itaendelea kutekeleza matakwa ya Watanzania, bajeti moja hadi nyingine kwa kipindi chote cha miaka mitano na Watanzania wawe na amani Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuko imara na Serikali iko imara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi wamezungumza matatizo ya Sekta ya wafanyakazi na hasa katika sekta binafsi. Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa Sheria za Kazi, kumekuwa na tatizo kubwa la wageni kufanya kazi bila vibali katika nchi yetu ya Tanzania, lakini vilevile kumekuwa na wageni ambao wanatumia ujanja ujanja tu katika kupata ajira katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote, yako marekebisho ya Kisheria tutayaleta hapa katika Bunge hili yataipa meno Serikali kupambana na waajiri wote wanaokiuka Sheria za Kazi katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Wabunge wamechangia sana kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii kwa maana ya Social Protection. Tunajua, tunajipanga kupitia upya Sheria zetu zinazosimamia mifuko ya hifadhi ya jamii ili kero ambazo zinawapata Watanzania katika sekta hiyo ziweze kushughulikiwa inavyotakiwa, lakini kubwa zaidi ni kuhakikisha tunaongeza wigo wa kuwafanya Watanzania wengi wafikiwe na suala zima la hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Munde na Wabunge wengine wameomba sana tuongeze fao la bodaboda katika mafao ambayo yatakuwa yanatolewa katika sekta hii ya hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshakubaliana na mifuko yote kuona ni namna gani sekta binafsi, hawa vijana wetu wa bodaboda nao waingizwe katika suala zima la social protection ili waweze kupata faida ya mafao yanayotolewa na mifuko.
Mhshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, mimi na Naibu Waziri wangu, Mheshimiwa Mavunde, tumejipanga na tutapita katika Mkoa mmoja baada ya mwingine ili kuona namna gani tunashirikiana na nyie katika suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine tutayajibu kimaandishi, lakini naunga mkono bajeti hii na ninampongeza sana Waziri wa Fedha na Naibu wake. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nichukue nafasi hii kwanza niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hizi, lakini kwa namna ya pekee niwapongeze Wajumbe wa Kamati zote mbili kwa ushauri wao kwa Serikali. Niendelee tu kusema kwamba Serikali hii sikivu itaendelea kusikia na hakuna shaka lolote na wale wenye wasiwasi naomba waondoe tu wasiwasi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu kwanza na la Mheshimiwa Paresso kuhusu kuunganisha Mifuko. Ningependa tu kusema suala hili Mheshimiwa Paresso wala asifikiri kwamba yeye ndio analianzisha leo hapa Bungeni. Kama alikuwa anasikia vizuri Mheshimiwa Paresso tukubaliane kwamba Mheshimiwa Rais alishatuagiza siku ya Mei Mosi akatuambia ni lazima tufikirie sasa kuunganisha hii Mifuko, kwa hiyo ushauri wake ni mzuri sana unaendana pia na agizo la Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Paresso tuko pamoja na Mheshimiwa Rais alishaagiza suala hili, kwa hiyo, tutalitekeleza tu na tunaendelea na mchakato huo wa kutekeleza agizo hili la Rais pia la kuunganisha Mifuko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumzwa hapa suala la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kukopesha Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo. Waheshimiwa Wabunge, naomba niseme hivi, Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii inaongozwa na sheria. Kwanza Mifuko yenyewe ina sheria zake, lakini pia inasimamiwa na Mdhibiti wa Sekta hii ya Hifadhi ya Jamii, na mdhibiti anaongozwa na sheria ambayo tuliitunga mwaka 2008, tukaifanyia marekebisho mwaka 2012 na tukaifanyia marekebisho mwaka 2013. Kifungu cha 9 cha miongozo ya uwekezaji kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kinaruhusu Mifuko hii kukopesha Vyama vya Akiba na Mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama miongozo inaruhusu, kwa hiyo, Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii inapokopesha SACCOS haifanyi makosa, labda makosa yawe mengine, lakini haifanyi makosa. Naomba Waheshimiwa Wabunge muelewe kwamba mahali pekee ambapo wanachama wanaweza kufaidika na Mifuko hii kupata mikopo yenye riba nafuu ni kupitia kwenye vyama vyao vya akiba na mikopo na watakapokopa fedha kwenye vyama hivi vya akiba na mikopo ndipo wanachama wanaweza kwenda kufanya shughuli nyingine za uzalishaji na uchumi na kuwafanya waendelee kuwa wanachama sustainable kwenye Mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba suala la Mifuko kukopesha Vyama vya Akiba na Mikopo tusilipotoshe. Tuzungumze sekta nyingine kama walivyozungumza kwenye Kamati, lakini Mifuko hii inaruhusiwa kufanya hivyo. Tumeona kwamba sasa hivi tunataka kupanua wigo wa wanachama, hivi tunapopanua wigo wa wanachama kwenda kwenye sekta binafsi, vijana wetu waliopo katika sekta isiyo rasmi watafaidikaje na hifadhi ya jamii kama hawatapatiwa dirisha la kukopa kwenye Mifuko hii? Kwa hiyo, naomba tuunge mkono juhudi za mifuko kukopesha wanachama wake wakajenge nyumba, wakafanye nini na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme, kama kuna tatizo katika utekelezaji wa jambo hili, hilo ndilo suala ambalo sasa Serikali ni lazima ikasimamie kuhakikisha kwamba vigezo vinafuatwa, lakini kuikataza Mifuko hapana, mwongozo uko hapa…
TAARIFA...
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, namheshimu sana mdogo wangu Mheshimiwa Ester, lakini angefuatilia ninachotaka kusema ni kitu gani na naomba ulinde muda wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kumwambia Mheshimiwa Esther, akifuatilia Hansard leo wapo baadhi ya Wabunge wachangiaji wamesema Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii isikopeshe fedha kwa wanachama kupitia mfumo wa akiba na mikopo. Sasa nataka kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge kwamba Mifuko ile haifanyi nje ya utaratibu na mwongozo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeendelea kusema hapa na naomba Mheshimiwa Esther anisikilize vizuri; kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha kwamba mikopo hiyo sasa itolewe kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na zisigeuze utaratibu wowote. Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Esther, asichukulie udhaifu wa mtu mmoja kuwakosesha haki wanachama wengine wa mifuko, haitakubalika, sisi tutasimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Manji liko mahakamani, Serikali kupitia mfumo tumeshaanza kuchukua hatua na ni lazima tutaendelea kuchukua hatua hata kwa wakopaji wengine. Ninyi Waheshimiwa Wabunge mnajua, hata Mheshimiwa Ester anajua, mimi nina taarifa za NSSF hapa, kuna viongozi, hata kiongozi mmoja mkubwa wa chama fulani hapa ndani na yeye amekopa mkopo chechefu, hajarudisha! Kwa hiyo, tunapozungumza haya tuyaweke yote wazi, bayana, tusifichefiche vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme hivi, kifungu cha tisa (9) kama nilivyosema, kinaweka mfumo wa kukopesha Vyama vya Akiba na Ushirika lakini tunasema hivi, asilimia 10 ya rasilimali za uwekezaji kwenye Mifuko ndicho kigezo kinachowapa ruhusa ya kukopesha Vyama vya Akiba na Mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa vyama hivyo vimeshakopesha kwenye vyama hivyo vya akiba na mikopo, mikopo isiyozidi hiyo asilimia 10 ya assets zilizopo. Sisi kama Serikali tutaendelea kusimamia na nina kuhakikishia watu wote waliokopa ni lazima warudishe hela kwenye Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, menejimenti zote ambazo zinafanya kazi kwenye Mifuko hii bila kufuata utaratibu Waheshimiwa Wabunge nawahakikishia Serikali tutaendelea kuchukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema kwamba, Waheshimiwa Wabunge sisi kama Serikali tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushauri mliotupa, tutafanya kazi na Bunge, lakini tutahakikisha kwamba sekta ya hifadhi ya jamii haitaweza kuhujumiwa na mtu yoyote na tutakuwa makini katika jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie muda huu ambao umenipa kupata nafasi ya kuchangia hoja ambazo zimeletwa mbele yetu na Kamati mbili za Kudumu za Bunge. Nami nianze kwa kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala. Yeye pamoja na Makamu Mwenyekiti lakini na Wajumbe wa Kamati hiyo ya Katiba, Sheria na Utawala kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi cha mwaka mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwe mkweli, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kamati hii imefanya kazi kubwa sana ya kutushauri Serikalini katika mambo ambayo yanahusu utendaji kazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba niseme kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naishukuru sana Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitumie pia nafasi hii nimpongeze sana Rais wetu, Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli; Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, ndugu yetu Mheshimiwa Kassim Majaliwa na Serikali nzima kwa maana ya watendaji wote ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano. Nasema hivi kwa sababu, kwa kweli mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Mheshimiwa Rais wetu na Serikali nzima wamejipambanua kwa nia njema ya kuleta maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania. Watanzania wanalifahamu hili na sifanyi vibaya kusema kwamba ndiyo maana hata uchaguzi huu mdogo uliopita Watanzania wameonesha imani kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa mchango mzuri walioutoa katika taarifa hizi mbili za Kamati. Nasi kama Serikali, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwa yale ambayo ni mambo yanayohusu Wizara moja na nyingine, Ofisi ya Waziri Mkuu itachukua nafasi ya kuyaratibu ili kuona mawazo mazuri haya yaliyosemwa na Wabunge na Kamati hizi mbili yanafanyiwa kazi kwa maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja zilizotolewa, jambo ambalo lilichukua nafasi kubwa hapa ilikuwa ni suala zima la ajira kwa vijana. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kazi hii ya kutambua ni namna gani Serikali ya Awamu ya Tano itajikita katika kupunguza tatizo la ajira nchini imeshaanza kwa kiasi cha kutosha. Naomba niwahikikishie Waheshimiwa Wabunge tunaposhughulikia tatizo hili la ajira tutaangalia Watanzania wote bila kujali itikadi zao za vyama, bila kujali dini, bila kujali kitu chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliamua kwa kuanza kufanya utafiti wa kutambua nguvu kazi iliyoko katika nchi yetu ya Tanzania. Hilo ndilo lilikuwa jambo la msingi ili tuweze kushughulikia ajira. Baada ya utafiti wa mwaka 2014 tulitambua viwango mbalimbali vya nguvu kazi iliyopo katika nchi yetu ambavyo vinaweza kusaidia na kutupeleka kwenye maendeleo tunayoyataka. Tuliona ni muhimu pia tuzitambue sekta kiongozi ambazo zina uwezo wa kutoa ajira za kutosha kwa vijana wa Tanzania. Tulibainisha sekta tano ambazo zinaweza kuwa ndizo sekta hasa za kutoa ajira nchini kilimo ikiwa ni sekta mojawapo, mawasiliano na teknolojia, utalii, ujenzi na sekta nyingine ambazo ndizo tuliona tuanze kuzifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kufanya utafiti wa mwaka 2014 tulichokigundua ni kwamba tunayo kazi kubwa ya kufanya kama Serikali. Tuligundua kwamba kiwango cha nguvu kazi ya juu kilichopo katika nchi yetu ya Tanzania ni asilimia 3.6 na tunatakiwa kukipandisha kiwango hicho cha nguvu kazi mpaka asilimia 12 ndipo tuweze kutengeneza ajira. Pia tuligundua kiwango cha nguvu kazi tulichonacho katika nchi yetu ya Tanzania ili kuweza kutatua tatizo la ajira ni asilimia 16.6 na tunatakiwa kukipandisha mpaka asilimia 14. Tuligundua kiwango cha nguvu kazi tuliyo nayo nchini ya ujuzi wa hali ya chini ni asilimia 79 hadi 80. Ukiwa na ujuzi mkubwa wa kiasi kidogo, ukiwa na ujuzi wa hali ya juu wa kiasi cha kawaida huwezi kutoa ajira wala kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilishukuru sana Bunge lako Tukufu katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ili kuinua viwango vya ujuzi na nguvu kazi katika nchi yetu, mlitutengea fedha na sisi sasa tumeweza kutengeneza progamu nne muhimu sana za kuweza kutengeneza ajira kwa wananchi wa Tanzania. Ili kuinua ujuzi na kuwafanya vijana wa Tanzania waajirike tumeamua kufanya mambo yafuatayo:-
(i) Tumetengeneza ajira ya kukuza ujuzi kupitia mfumo wa uanangezi; (ii) Tumetengeneza programu ya kukuza ujuzi kwa kurasimisha ujuzi katika mfumo usio rasmi wa mafunzo;
(iii) Tumetengeneza programu ya mafunzo kwa vitendo (internship) kwa wanafunzi wetu ili waweze kuajirika na kujiajiri; na
(iv) Tumetengeneza programu ya kukuza ujuzi kwa Watanzania waliopo makazini waweze kuendana na soko la ajira na teknolojia tuliyonayo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini hayo yakifanyika kwa mwaka mmoja tumejiwekea lengo la kukuza ujuzi na kuwafanya vijana wa Kitanzania wajiajiri ama waajirike wasiopungua 27,000. Kwa hiyo, kazi hiyo inaendelea vizuri. Nataka kusema hapa kazi hiyo imekuwa nzuri kwa sababu Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala imetushauri vizuri sana na tumefanya nao kazi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea yote yaliyozungumzwa kuhusu NSSF na ni kweli tunaendelea kufanya kazi nzuri. Nichukue nafasi hii kuipongeza sekta ya hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania kwa kazi nzuri wanazozifanya. Sekta ya hifadhi ya jamii imeendelea kukua na mpaka sasa rasilimali zilizopo kwenye sekta hii ya hifadhi ya jamii zimefikia thamani ya shilingi trilioni 10.2 katika nchi yetu ya Tanzania, ni mtaji mkubwa sana. Uwekezaji katika sekta hii tu ya hifadhi ya jamii umefikia thamani ya shilingi trilioni 9.2 katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, unaona kwamba sekta hii ina mchango pia mkubwa sana wa uchumi wa nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kama Serikali tutaendelea kusimamia sekta ya hifadhi ya jamii vizuri kwa kuzingatia miongozo na sheria tulizonazo pamoja na kuboresha mafao ya wastaafu katika sekta ya hifadhi ya jamii lakini tutaitumia pia sekta hii kukuza uchumi wa Tanzania na kutengeneza ajira kwa Watanzania wote katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya pekee sana kuwashukuru sana Wabunge lakini kulishukuru sana Bunge lako Tukufu kwa jinsi ambavyo mmekuwa mstari wa mbele kuishauri Serikali katika mambo yale ambayo mnaona kwamba yanaweza kuendeleza maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania. Naomba niwahakikishie Serikali ya Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli ni Serikali sikivu, ina nia njema ya kuleta maendeleo ya nchi yetu na tutaendelea kufanya hivyo bila kusita. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wote kwa pamoja tufanye kazi na wote lengo letu liwe ni kuleta maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi kwa haraka haraka lakini siyo kwa umuhimu, nianze kwa kuipongeza sana Kamati inayosimamia masuala ya UKIMWI na masuala ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile na Makamu Mwenyekiti Dkt. Tiisekwa na Wabunge wote Wajumbe wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hii kwa kweli imeanza kazi vizuri na ninaomba niseme kwamba inatushauri vizuri sana. Kwa hiyo, naomba niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati hiyo. Sitakuwa nimejitendea haki kama sitakumbuka mchango mkubwa uliotolewa na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile na Mheshimiwa Ester Bulaya wakati wa kutungwa kwa Sheria Namba 5 ya mwaka 2015 ambayo imetupelekea katika azma ya Serikali ya kupambana na dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nichukue nafasi pia ya pekee kabisa kuwapongeza sana Wabunge wote ambao tulikuwa wote pamoja katika Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nakumbuka sheria hiyo ilikuwa ni sheria yangu ya kwanza nilipoteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini Waheshimiwa Wabunge waliniunga mkono sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli sheria hii mpya ni sheria nzuri na imeweka adhabu za kutosha kabisa za kupambana na tatizo la dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa labda niseme yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania lina historia. Historia ya ongezeko la tatizo hili ilianza toka miaka ya 1990 na miaka ya 1990 Serikali imekuwa ikihangaika sana kuona ni namna gani itaweka mifumo ya kisheria na taratibu za kupambana na dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1995 Serikali kupitia Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitunga Sheria Namba 9 ya mwaka 1995 lakini sheria ile ilikuwa na kazi ya kuratibu tu masuala haya ya tatizo la dawa za kulevya nchini na ilionekana kwamba sheria ile haina nguvu yoyote. Watu wakikamatwa, sheria ilikuwa haiipi Tume ya Dawa za Kulevya nguvu ya kupekua, kupeleleza na kushitaki. Kwa hiyo, tulikuwa tunaona kulikuwa na upungufu mkubwa sana katika Sheria ya mwaka 1995. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ilianza kujionesha mwaka 2014. Mwaka 2014 tulifanya utafiti wa nguvu kazi katika nchi yetu ya Tanzania na tukagundua kwamba nguvu kazi ya vijana kwa miaka 14 mpaka 35 ni asilimia 56. Hiyo asilimia 56 ya nguvu kazi ya vijana ndio hao ambao wanaathiriwa na madawa ya kulevya katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa dhamira ya dhati, mwaka 2015 ndipo tukaamua kuja na Sheria Namba 5 ya mwaka 2015; lakini sheria hiyo sasa ikaweka nguvu nyingine ya ziada; hiyo sasa ikawa na ajenda ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo hapa, mchakato sasa wa kuunda hii mamlaka ambayo itafanya kazi yake vizuri ambayo inategemewa na Watanzania wengi, mchakato huu umefika mahali pazuri sana. Mwaka 2015 Serikali ya Awamu ya Nne, kazi kubwa Serikali hiyo ilifanya ni kutunga sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, jamani mapambano haya ya dawa za kulevya ni ya kwetu Watanzania wote, yasichague mtu yeyote. Na mimi kwa dhati ya moyo wangu, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, kila atakayeamua kupambana na jambo hili tuungane mkono pamoja kwani ni ajenda ya kitaifa inayotuhusu Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaoneshwa hapa ni kama vile Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake hawana nia ya dhati ya jambo hili, hapana. Mheshimiwa dada yangu Mheshimiwa Halima, namheshimu, amesema hapa kitu ambacho siyo sahihi.
Waheshimiwa Wabunge, bajeti kwa ajili ya kutengeneza mamlaka hii mmeipitisha. Tumepitisha bajeti ya shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kwenda kuunda mamlaka hii itakayopambana na dawa za kulevya nchini. Bajeti hiyo hatujaweka fedha ya maendeleo, kwa sababu unawapaje hawa watu fedha ya maendeleo? Unataka wakatekeleze nini…
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: ...badala ya kuwapa OC ya kwenda kufanya kazi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo bajeti, hiyo tumeitenga na tunategemea bajeti hiyo itaenda kufanya kazi.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuambie kwamba chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli tayari kanuni za sheria hizi tumeshazikamilisha na zipo tayari. Chini ya Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli, muundo wa mamlaka hii ya kupambana na dawa za kulevya iko tayari. Muundo umeshakamilika. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosubiri ni uteuzi wa Kamishna ambaye ataongoza mamlaka hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleweke, kuteua Kamishna ambaye atashughulika na jambo hili siyo jambo la lelemama. Ni lazima atafutwe mtu mwenye maadili anayeweza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme. Narudia kusema, ni lazima atafutwe kiongozi anayeweza kuwa na maadili ya kutosha ya kupambana na tatizo hili…
T A A R I F A....
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu ulinde dakika zangu. Ninachokisema hapa sitaki kusema kwamba Mheshimiwa Halima Mdee haja-quote taarifa ya Kamati. Nilichokuwa nalieleza Bunge hili, sisi kama Serikali, wakati tunaelekea kuunda mamlaka mpya yenye nguvu ya kudhibiti, hatukuona haja ya kuweka fedha ya mradi wa maendeleo. Tunaipaje Tume fedha za maendeleo ambapo sisi tumeweka shilingi bilioni mbili kwa ajili ya OC ya kuratibu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusema, taarifa ya Kamati hiyo anayoi-quote Mheshimiwa Halima, lakini mimi kama Waziri mwenye dhamana, najua Tume hii wakati inajibadilisha kwenda Mamlaka, tumeitengea shilingi bilioni 2.5 ili iweze kutengeneza Mamlaka na kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waheshimiwa Wabunge tuelewane. Narudia kusema, ninampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuonesha nia ya dhati…
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alisema wakati anafungua Bunge hili, alionesha nia ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema ndiyo maana hii Sheria ya Namba 5 ya mwaka 2015, yale yote ambayo yanatakiwa yafanyike kwa mujibu wa sheria yameshatekelezwa yote. Bajeti kwa ajili ya mamlaka hii mpya itapangwa katika bajeti ya mwaka 2017/2018 na hiyo ndio nia ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi/Kelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni ya Watanzania wote na sisi wote tuungane pamoja, tuhakikishe kwamba vita hii tunakwenda nayo pamoja. (Makofi/Kelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye tatizo la UKIMWI katika nchi yetu ya Tanzania. Tumejipanga. Tumegundua kwamba ufadhili wa fedha za UKIMWI unazidi kwenda chini. Tumepitisha sheria mwaka 2016 ya kuanzisha Mfuko wa UKIMWI; na mfuko ule Serikali tumeutengengea shilingi bilioni 1.5 mpaka sasa. Naomba Waheshimiwa Wabunge mwamini Serikali ina nia ya dhati ya kuwakomboa Watanzania dhidi ya mapambano pia ya tatizo la UKIMWI katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa za kulevya hazikubaliki na tutaendelea kuratibu na kupambana na dawa hizi tukiongozwa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru, na mimi nianze kwa kuwapongeza sana hasa Kamati mbili, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, lakini vilevile kwenye muktadha wa mjadala wetu wa leo niwapongeze pia Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza sana Wajumbe wa Kamati hizi mbili kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana katika kuishauri Serikali na wametekeleza majukumu yao sawasawa. Kwa hiyo kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko hoja kadhaa zimejitokeza katika Kamati hizi zote ambazo zimesoma taarifa na mimi nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja ya Kamati hizo zote mbili ambazo zinairuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo la kwanza limezungumzwa suala kuhusu Baraza la Vijana. Ninaomba nichukue nafasi hii nitoe taarifa kwenye Bunge lako Tukufu, wote tunakumbuka mwaka 2015 tulipitisha Sheria ya Kuunda Baraza la Taifa la Vijana katika nchi yetu ya Tanzania. Lengo letu kubwa lilikuwa ni kuwaunganisha vijana wote wawe pamoja, kuondoa itikadi zao za kisiasa na kuwafanya wawe wazalendo kwa nchi yao ya Tanzania. Vilevile kuwafanya vijana wa Taifa hili la Tanzania waelewe umuhimu wao wa kuwepo katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, baada ya sheria ile kupita, tayari kanuni za kuanzisha Baraza hili zimeshakamilika. Hata wewe Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kikao cha leo nakumbuka Ofisi ya Waziri Mkuu ilishakuja mbele ya Kamati yako ili kupitia kanuni zile na kuziweka sawa sawa na sasa muda si mrefu, uundwajiwa wa Baraza la Taifa la Vijana utaanza kupitia ngazi mbalimbali kama sheria inavyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge vijana wote, tutakapofika nafasi hiyo sasa ya uundaji wa Baraza la Vijana la Taifa watoe ushirikiano kwa Serikali kusudi kazi hii iweze kufanyika vizuri. Kwa hiyo, katika suala hilo tunakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Sheria Ndogo imetuelekeza Serikali na kwa kweli tumekuwa Ofisi ya Waziri Mkuu tukitekeleza jukumu la kisheria la kuweka mezani sheria ndogo zote ambazo zimekuwa zikiandaliwa na kupitishwa na mamlaka mbalimbali za Serikali ikiwemo Wizara mbalimbali. Tumekuwa tukipokea maoni ya jumla yanayohusiana na sheria hizo ndogo zote katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Sheria Ndogo imefanya kazi kubwa, imepitia sheria nyingi sana ndogo katika nchi yetu ya Tanzania. Mimi niseme kama Serikali na taasisi zake itaendelea kufanya vizuri katika kutunga sheria ndogo katika nchi yetu ya Tanzania, ni kwa sababu Kamati ya Sheria Ndogo imebaini makosa na imeturekebisha katika maeneo mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nichukue nafasi hii kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba tutazingatia maoni na ushauri wa Kamati ya Sheria Ndogo katika kuhakikisha kwamba sheria ndogo zitakazokuwa zinatumika katika nchi yetu ya Tanzania zinaendana na sheria mama na zitakwenda kutenda haki katika kusimamia sheria mama katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, maagizo ya Kamati ya Sheria Ndogo tumeyapokea na tutayapeleka Serikalini kwa ajili ya utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lilizungumzwa suala lingine kuhusu NSSF. Waheshimiwa Wabunge ninaomba niwaambie, sisi kama Serikali hatujafumba macho kuhusu suala la NSSF. Kamati ya PAC ilishasoma taarifa yake hapa ndani ya Bunge, na mimi niliwaamba kwamba pamoja na shughuli inayoendelea ndani ya Serikali ya kuimarisha NSSF, tumeimarisha Bodi na hivi juzi tumeunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, lakini tumesema NSSF itabakia kuwa mfuko kwa ajili ya private sector na kwa ajili ya sekta isiyo rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moja kwa moja Serikali inaona jukumu kubwa la NSSF. Ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tunaendelea kuyatupia macho yale yote yaliyojiri kwenye NSSF na tumeiagiza Bodi kuhakikisha kwamba inasimamia ipasavyo na inatenda haki katika kushughulikia masuala yote yaliyojitokeza kwenye NSSF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge, jambo hili sisi tunalishughulikia vizuri na msiwe na hofu. Lengo letu ni kuhakikisha fedha za wanachama zinabaki kuwa salama, na vilevile Mfuko wa NSSF ambao uhai wake unafika mpaka mwaka 2085 uendelee kuwa mfuko ambao una maisha marefu ya kuhudumia Watanzania. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge niwahakikishie kwamba tupo imara na tutafanya kazi hiyo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa suala la ajira katika nchi yetu ya Tanzania na hasa kwa ajili ya vijana. Mwaka 2014 tulifanya utafiti wa hali ya nguvukazi katika nchi yetu ya Tanzania, na tuligundua kwamba Watanzania takribani milioni 25 ndio nguvukazi ya taifa katika nchi yetu. Lakini asilimia 56 ya hao Watanzania milioni 25 ni vijana. Tulijitahidi pia kuangalia ujuzi wa hawa vijana je, unaendana na soko la ajira katika nchi yetu ya Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inafahamu tulipokwenda kwenye Kamati tuliwaeleza baada ya utafiti huu, Ofisi ya Waziri Mkuu iliandaa programu tano za kuhakikisha tunakuza ujuzi wa vijana ili waweze kuajirika katika miradi mbalimbali kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafurahi kukuambia kwamba kwa taarifa tulizonazo sasa mwaka 2015/2016 katika nchi yetu ya Tanzania ajira ambazo zilikuwa zimetengenezwa nchini zilikuwa ni ajira 390,676. Mwaka 2016/2017 ajira zilizotengenezwa katika nchi yetu ya Tanzania zimeendelea kuongezeka mpaka kufikia ajira 421,803.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta inayoongoza kwa kutoa ajira kwa wingi ni sekta binafsi, sekta inayofatia ya kutoa ajira kwa wingi ni sekta ya miradi ya maendeleo. Kwa hiyo, tunajitahidi kusimamia miradi ya maendeleo ili kukuza ajira katika nchi yetu ya Tanzania. Ahsante sana.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. JENISTA J. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Naipongeza sana Ofisi ya Makamu wa Rais, Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Kizuka kimeanzisha mradi wa kutunza mazingira kwa kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kuweka mradi wa maji. Tungeomba kufahamu Ofisi ya Makamu ya Rais inatusaidiaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vikundi vingi vya hifadhi ya mazingira vikiwa na miradi ya upandaji miti na ufugaji wa nyuki. Tunaomba msaada wa ushauri na teknolojia rahisi katika suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuokoa mazingira akinamama wameanzisha mpango wa majiko yenye utunzaji wa mazingira, tunaomba usimamizi wa kuwasaidia akinamama hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JENISTA J. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wenzangu kuunga mkono hoja. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na timu nzima ya Uongozi wa Wizara. Napongeza uamuzi wa Serikali wa kuanzisha safari za ndege Songea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi ya Jimbo la Peramiho:
(i) Kupandisha hadhi barabara ya Tulila-Chipole- Matomonda kuwa ya Mkoa kwa sababu inaunganisha Wilaya mbili lakini ni barabara inayotupeleka katika mradi mkubwa sana wa umeme wa maji unaotumika Songea.
(ii) Barabara ya Mkenda-Likuyufusi. Barabara hii inatajwa katika Ilani ya Uchaguzi, ni barabara inayotuunganisha na Nchi ya Msumbiji, ni barabara ya Taifa. Upembuzi yakinifu umekamilika, usanifu tayari japo ni muda mrefu sana sasa, naomba sana tuanze kuweka lami japo kilomita 15 tu kuanzia ulipo mpaka wa Tanzania na Msumbiji.
(iii) Barabara ya Mpitimbi-Ndongosi ni ya mpakani na inahudumiwa na Mfuko wa Barabara Mkoa. Tunaomba tutengewe fedha.
(iv) Barabara ya Mkoa ya Mletewe-Matimila- Mkongo ya Mkoa haijatengewa fedha muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua anazochukua kukabiliana na Upotevu wa Mapato ya Serikali katika Sekta ya Madini
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba niungane na Wabunge wote wazalendo wa nchi hii ya Tanzania ambao wanampongeza Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, kumekuwa na maneno mengi katika jambo hili. Tukitizama hoja ambayo ipo hapa ndani ya Bunge letu Tukufu, hoja yenyewe kimsingi inatutaka sisi Wabunge kwa pamoja tuungane na Watanzania wenzetu ambao kwa mara ya kwanza wameshuhudia uzalendo, ujasiri na hekima na busara iliyotumiwa na Rais wetu katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na mwenendo mzima wa utendaji kazi wa Serikali katika kulinda rasilimali za Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika historia ya nchi yetu ya Tanzania, nashukuru leo Mheshimiwa Tundu Lissu amezungumza vizuri sana, ameona kuna umuhimu tunapompongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli tuwapongeze na Marais waliotangulia pia. Ingawa jana Tundu Lissu huyo huyo aliwadhalilisha pia Marais waliotangulia katika hoja hii hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachojifunza hapa ni kwamba hata dhamira ya mioyo ya wenzetu kumbe wanakubaliana na kazi nzuri aliyoifanya Rais pamoja na watangulizi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa nini? Marais waliotangulia walianzisha hoja hii kwa namna moja ama nyingine kwa kuunda Kamati zile zinazojulikana, lakini kazi iliyokuja kuendelezwa ambayo pia tunaipongeza vizuri leo, ni kitendo cha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wetu, kuziweka kwanza ripoti hizo zote mbili hadharani na zikasikika na Watanzania wote. Pili, ni kuanza kuchukua hatua kwa ripoti ile ya kwanza. Tatu, ni kutoa maagizo makubwa kwenye ripoti hii. Kwa hiyo, Watanzania wote… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mujibu wa kanuni ina jukumu na kwa mujibu wa sheria tulizonazo inajukumu la kuleta mbele ya meza yako sheria ndogo zote ambazo zimekwisha kutangawa kwenye Gazeti la Serikali na inawekwa mbele ya meza yako tukufu na baada ya Kamati ndogo Kamati ya Sheria Ndogo kumaliza kazi yake hii yote nzuri kama ilivyofanywa leo. Ofisi ya Waziri Mkuu inajukumu la kupokea maoni yaliyotolewa na Kamati ndogo na ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wawe watulivu wajue tunachotaka kusema. Na wakati mwingine utaratibu wa kelele kelele siyo wa Kibunge.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu ina jukumu la kupokea maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Sheria Ndogo na kuyawasilisha kwa Wizara zote husika kwa jinsi yalivyochambuliwa na Kamati ya Sheria Ndogo. Hata Mheshimiwa Halima anajua, nimekuwa nikienda mpaka kwenye Kamati kupokea majedwali hayo kwa niaba ya Wizara zote.

Ninasimama hapa kusema yafuatayo, kwanza ninampongeza Mwenyekiti kwa kazi yake nzuri; pili, ninawapongeza Wajumbe kwa kazi yao nzuri; na tatu ninatambua yale yaliyojiri kwenye taarifa ya Kamati ndogo na yamewekwa vizuri sana na summary ya Mheshimiwa Mwenyekiti wakati akihitimisha hoja yake. Ni yapi? (Makofi)

Kwa mujibu wa sehemu ya tatu ya Kamati za Kisekta Mtambuka ambayo kifungu kidogo cha (c) kinaitambua Kamati yetu ya sheria na kifungu cha 11 kimeelezwa vizuri na Mwenyekiti wakati akihitimisha hoja yake, wajibu wa Kamati Ndogo wameutekeleza Kamati inayoshughulikia Sheria Ndogo wametekeleza vizuri mambo makubwa yaliyojiri ambayo ninatokanayo na nitayawasilisha kwenye Wizara husika kama yalivyowekwa mezani na Mwenyekiti wa Kamati Sheria Ndogo ni pamoja na hayo mawili aliyoyazungumza kuhusu majedwali yanayoenda na sheria mama. Lakini vilevile makosa madogo madogo ambayo yamekuwa yakijitokeza na kujirudia katika sheria ndogo zina zotungwa yanayoendana kinyume na sheria mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo limejitokeza suala la Watendaji wetu wanaosimamia ama wanaoshughulikia sheria hizi ndogo kutokuwa na umakini katika kufanya kazi yao. Jambo hilo ninaomba nilichukue pia na liweze kufanyiwa kazi ya kutosha na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile amesema ziko Wizara ambazo zimejitokeza kwa nguvu kidogo kwenye taarifa ambazo zimekuwa zikichambuliwa na Kamati yetu Kamati ya sheria ndogo, nazo tutazifikishia majedwali hayo ili yaweze kufanyiwa kazi sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu kadri tunavyofanya kazi na Kamati ya Sheria Ndogo tumekuwa na mabadiliko makubwa na tunaishukuru sana Kamati ya Sheria Ndogo imekuwa ni msaada mkubwa sana kwa uandishi wa sheria ndogo ndani ya Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo na sisi kama Serikali tutaendelea kufanya nao kazi kwa karibu ni kwa maslahi ya Taifa na nchi yetu na si kwa maslahi ya mtu mwingine yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa niaba ya Serikali tutayatekeleza hayo yote.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kabla sijaendelea, nachukua nafasi hii kuunga mkono Azimio lililoletwa na Mheshimiwa George Simbachawene. Ninaunga mkono Azimio hilo na niseme tu kwamba ukweli ni kwamba jambo hili wala siyo jambo la kukurupuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 151 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi iliielekeza Serikali ndani ya miaka mitano ihakikishe kwamba Serikali imehamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma. Ibara hiyo ya 151 iliweka bayana mambo ambayo hata azimio hili limeyaelekeza. Ilani ilisema la kwanza; Serikali ihakikishe kwamba majengo yote ya Serikali yaanze kujengwa Dodoma kitu ambacho tumeanza kukifanya. Ilani imeelekeza, viwanja vipimwe katika Mji wa Dodoma Makao Makuu kwa ajili ya shughuli za Serikali na wananchi wa Tanzania. Mheshimiwa Jafo, amesema na ndivyo tunavyofanya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ilani imeelekeza itungwe sheria ya kutambua Dodoma kuwa Makao Makuu, ndiyo azimio ambalo linaletwa leo. Kwa hiyo, tuna kila haja ya kuunga mkono Azimio hili lililoletwa na Mheshimiwa George Simbachawene. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme yafuatayo: sisi kama Serikali tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Serikali zote zilizotangulia nakubaliana sana na Mheshimiwa Komu zilitengeneza mazingira wezeshi, lakini maamuzi ya kuhamia Dodoma kulifanya Dodoma kuwa Jiji, kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu yamefanywa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na anastahili kupewa pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kusema tunapohamia hapa Dodoma sasa, tumeweza kutekeleza, tumetekeleza kwa vitendo na tunapotekeleza kwa vitendo na kumuenzi Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, maneno haya aliyatamka Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na sisi tumeyatekeleza mpaka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliarifu Bunge hili, mnaposema kwamba kuna mgongano wa wafanyakazi kuhamia hapa Dodoma, ninaomba niwaambie kati ya wafanyakazi 7,440 wa Wizara zote wanaotakiwa kuhamia hapa Dodoma tumebakiza wafanyakazi 909 tu, wengine wote wameshahamia hapa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya wafanyakazi hawa kuhamia hapa Dodoma, Waheshimiwa Wabunge wanafikiri kutakuwa na migongano ya miundombinu, lakini mpaka sasa mmeona Dodoma ni shwari na shughuli za Serikali zinatekelezwa kama inavyotakiwa na hakuna tatizo lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuthibitishie, kama Serikali tutaendelea kulisimamia agizo hili la Mheshimiwa Rais, kutekeleza matakwa ya Marehemu Baba wa Taifa na azma ya Ilani ya Uchaguzi Ibara ya 151. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona adui yako anakusifia, ujue umeharibu, lakini ukiona adui hasifii unachokifanya, ujue umefanikiwa. Kwa hiyo, sisi tutaendelea kuifanyia kazi azma hii njema ya kuhamia hapa Dodoma. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii nimpongeze sana sana Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwakweli tunampongeza sana Dkt. Mwinyi kwa kazi nzuri anayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mkuu wetu wa Majeshi nchini, mmeona kabisa kwa siku hizi zote za karibuni nilisema hapa asubuhi, Sera yetu ya Ulinzi na Usalama imejikita katika maeneo kadhaa kama manne hivi. Ukiangalia la kwanza ni ulinzi wa mipaka yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Waheshimiwa Wabunge hatutakuwa na moyo wa shukrani kama siku hii ya leo hatutalipongeza Jeshi letu la Ulinzi kwa ulinzi mkubwa unaofanywa kwenye mipaka ya nchi hii na hiyo imesababisha nchi yetu kuendelea kubaki ni nchi pekee sisemi kwenye mataifa mengine, sijui kinachoendelea huko, lakini mmeona ulinzi wa Taifa letu kwenye mipaka yetu ni imara kweli kweli na tuko salama kweli kweli. (Makofi)

Kwa hiyo, ni lazima kwakweli siku hii ya leo ilikuwa ni siku yetu sisi Wabunge wote kwa pamoja kuungana kwanza kulishukuru Jeshi letu la Ulinzi na kulipongeza kwa kiasi kikubwa na kiasi cha kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera yetu ya Ulinzi na Usalama inasema Jeshi hili la Ulinzi na Usalama katika hali moja ama nyingine litashirikiana na raia katika masuala mbalimbali. Mmeshuhudia Jeshi hili, tulipopata m aafa kwenye kivuko, Jeshi letu la Ulinzi na Usalama na Jeshi la Polisi walifanya kazi kubwa kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mmeona nilisema hapa asubuhi sitaki kurudia yale yaliyokuwa yanasemwa lakini pale ilipotokea kuna umuhimu wa Jeshi letu la Ulinzi na Usalama na Jeshi letu la Polisi kufanya kazi kwa pamoja wamefanya kazi nzuri Njombe, wamefanya kazi nzuri kule Kibiti na maeneo mengi tu wamefanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwakweli nasimama hapa kulipongeza Jeshi letu la Ulinzi na Usalama, lakini tumeona kabisa kwamba Jeshi hili lina kazi na limeendelea kurithi maono na maoteo mazuri ya Baba wa Taifa kudumisha ushirikiano na mahusiano mema na nchi nyingine na hasa katika Bara la Afrika. Mmeshuhudia Wanajeshi wetu wakijitoa kweli kweli kwenye ulinzi na usalama hata kwenye mataifa mengine nje ya Taifa letu na hiyo ndiyo Sera yetu ya Ulinzi na Usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunachokisema hapa tunampongeza kwanza Amiri Jeshi Mkuu, Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu kama leo wote sisi Wabunge tunakubaliana na kuungana mkono kwamba kazi nzuri inafanywa na Jeshi letu la Ulinzi na Usalama ina maana Amiri Jeshi Mkuu anafanya kazi yake sawa sawa kulisimamia Jeshi letu. Kwa hiyo ni lazima na yeye tumpongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa sisi tunachokichukua kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge ni ushauri ambao, ushauri mwema, ushauri wenye msingi ambao Bunge linatushauri Serikali namna nzuri ya kuliboresha Jeshi letu, ya kuhakikisha Jeshi letu linaendelea kufanya kazi yake vizuri tena kwa weledi mkubwa na hiyo hatuna shaka, tumekuwa tukishuhudia lakini tunaendelea kupokea ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wa kuhakikisha kwamba Watanzania wanaungana mkono na Jeshi letu na wanaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi letu ili liendelee kuwa Jeshi la mfano na liendelee kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya ambayo hata ungeniamsha kwenye usingizi ningeyasema tu, ninaomba nichukue nafasi hii kuunga mkono hoja, kumpongeza Waziri, kulipongeza Jeshi letu na kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuwapongeza sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili kwa ripoti nzuri. Nawapongeza sana Wajumbe ambao ni washiriki wa Kamati hizo kwa ripoti ambazo wametuletea. Nami naomba nikiri kwamba ndani ya Serikali tunawashukuru kwa sababu wanaendelea kutushauri mambo mema na ninaomba kuwahakikishia kwamba tupo pamoja na tutaendelea kuyazingatia ili kujenga ustawi wa Taifa na wa Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kabla sijaendelea nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Ni ukweli usiopingika, Rais wetu toka ameingia kwenye Serikali hii ya Awamu ya Tano amefanya kazi kubwa za utekelezaji wa Ilani lakini utekelezaji huo unaowagusa Watanzania wengi. Kwa sasa maendeleo ya Taifa letu yamekuwa ni mtambuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia miradi ya maendeleo ambayo imetekelezwa ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano unaiona kabisa mgawanyo wake unawagusa Watanzania kwenye mikoa yote kwa kuzingatia mahitaji na vipaumbele walivyonavyo. Ukisema masuala ya elimu bure, miundombinu ya maji, miundombinu ya barabara, ujenzi wa hospitali mpya, ujenzi wa vituo vya afya, ukarabati wa shule, kabisa Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana name kwamba Rais wetu na Serikali wamefanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo basi, kama tunatekeleza Ilani ya Uchaguzi, Rais wetu na Serikali wanatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Hata kuhamia hapa Dodoma haikuwa kukurupuka, ilikuwa ni utekelezaji wa Ilani. Kuhamia hapa Dodoma wote tumekuwa ni mashahidi, hakuna mji wowote ama nchi yoyote ambayo inaweza kukua kiuchumi kama haipanui shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wala isingetusaidia, ukiachia mbali kurithi mawazo mazuri ya Baba wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni mwasisi wa Serikali kuhamia Dodoma, lakini Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na maamuzi dhahiri ya Rais wetu ya kuhamishia Serikali Dodoma yamekuwa na effect ambayo ni positive kwenye kukua kwa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa nini? Baada ya Serikali kuhamia hapa Dodoma, tumeona kabisa miji inayozunguka hapa Dodoma imeanza kukua. Ukienda Singida inakua, Manyara - Babati kunakua, Iringa inakua na Morogoro inaendelea kukua. Kwa hiyo, kwa kuhamia tu hapa Dodoma unaona ile multiplier effect ya kuhamia Dodoma imeambukiza na Miji mingine ambayo ipo karibu na hapa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini maana yake? Mwisho wa siku tutakuwa tumekuza uchumi katika maeneo mengi ya nchi ya Tanzania, tutaongeza mapato, tutaboresha huduma za jamii, vile vile ukuaji wa uchumi huo utatatua na matatizo mengine ambatanishi kama matatizo ya ajira na mambo mengine kama miundombinu na huduma za jamii. Hapa Dodoma sasa hivi tuna hospitali kubwa ya Benjamin Mkapa, ukiacha mbali ile ya Muhimbili ambayo ilikuwa Dar es Salaam kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema tumehamia Dodoma, hatujaiacha Dar es Salaam. Dar es Salaam nayo imeendelea kufanyiwa mambo makubwa. Waheshimiwa Wabunge nyie ni mashahidi, katika historia ya nchi hii, miundombinu ya barabara inayojengwa kwa sasa kwenye Jiji la Dar es Salaam ni miundombinu ya hali ya juu. Huo ni ushahidi kabisa. Miundombinu inayowekezwa pale Dar es Salaam itafanya Jiji la Dar es Salaam kuwa ni Jiji la kibiashara na likiwa Jiji la kibiashara litasaidia sana kukuza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niseme Waheshimiwa Wabunge, ninadhani sisi kama Wabunge tukihesabu yale yanayofanyika Dar es Salaam na katika Mikoa mingine yote Tanzania, hakika tunayo kila sababu ya kumpongeza sana Rais wetu kwa maamuzi aliyoyafanya katika kipindi chake pamoja na Serikali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimtoe hofu dada yangu Mheshimiwa Halima, Mwenyekiti mpya wa Wanawake wa CHADEMA na kumwomba tu aunge mkono juhudi za Rais wetu na hasa pale Dar es Salaam katika kuleta maendeleo. Namwomba afikishe salamu hizi za upendo wa kazi znuri ya Rais wetu kwa wanawake wa CHADEMA nchi nzima na hasa pale Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa hapa suala la Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Ninaomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, nakubali NSSF huko nyuma baada ya Serikali yetu kuingia, tumegundua kulikuwa na matatizo makubwa. Sasa tulichokifanya ni kuendelea kuhangaika kuona kwamba ule uwekezaji ambao ulifanyika huko nyuma usiokuwa na tija unarekebishwa haraka ili kuwe na manufaa na tija kwa wanachama na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hivi juzi tu, tunayo majengo ya muda mrefu Mtoni Kijichi, nimeyakabidhi wa Waziri wa Elimu yatumike kama hosteli za wanafunzi wa elimu ya juu, wanaosoma katika Vyuo Vikuu pale Dar es Salaam. Tumekabidhi hosteli zile mpaka kufika mwezi wa Tatu wanafunzi wasiopungua 4,000 na kitu watapata makazi kwenye zile hosteli mpya. Tutakwenda mpaka nafasi zisizopungua 8,000 na kitu. Kwa hiyo, hiyo ni kazi kubwa, ni lazima muone Serikali inafanya kazi na inajaribu kurekebisha kila ambapo hapakuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa imetolewa hoja kwamba hili shirika linakufa. Ninachokwenda kufanya sasa hivi ni utathmini wa mfuko (actuarial), hii ndio itatuambia. Hatuwezi kusema kitu kingine chochote, mfuko unakufa bila actuarial.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua facts za kawaida kwa sasa, makusanyo ya shirika mwaka 2018 kwa mwezi yalikuwa shilingi bilioni 60 tu. Kufika mwaka 2019 yameongezeka mpaka shilingi bilioni 96 kwa mwezi. Hilo ni ongezeko na tunaona kumbe shirika linakua. Uwekezaji kwenye dhamana za Serikali ilikuwa ni negative mwaka 2018, lakini baadaye ikaja kuongezeka mpaka 8%. Leo ninaposimama hapa, imefika asilimia 20 kwenye dhamana za Serikali. Kwa hiyo, hilo ni ongezeko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na malimbikizo ya wastaafu yenye thamani ya fedha za Kitanzania shilingi bilioni 109, mpaka kufika 2019 toka hiyo 2018 fedha hizo za malimbikizo na malipo mengine tumeshalipa shilingi bilioni 409. Kwa hiyo, unaona kwamba shirika linaendelea kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, daraja la Kigamboni ambalo ndiyo mradi umesemwa hapa, ni kweli una matatizo na tunaufanyia kazi kuyaondoa. Tumeweza kuongeza makusanyo kwenye Daraja la Kigamboni kutoka shilingi bilioni 697 mwaka 2018 mpaka shilingi bilioni 950 mwaka 2019. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, Serikali imejipanga, tunajua miradi hii ya uwekezaji kwenye Mashirika yetu ya Hifadhi ya Jamii ni fedha za wanachama. Tunachokifanya sasa hivi ni kutembelea mradi mmoja baada ya mwingine, kutafuta namna ya kuhakikisha uwekezaji huo unakuwa na tija kwa wanachama na Watanzania kwa ujumla.

Kwa hiyo, nakubaliana na ushauri walioutoa Waheshimiwa Wabunge, pale ambapo hapajafanyika vizuri, tutafanya vizuri, lakini kama shirika linafanya vizuri, tutaendelea kuwapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ahsante sana kwa hoja zilizotolewa. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU,SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Kwanza kwa dhati kabisa jukumu hili la kupokea majedwali mbalimbali ya marekebisho ya sheria ambayo yamekuwa yakichambuliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo limekuwa likifanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu, na sisi pia tumekuwa na wajibu wa kuweka Mezani Magazeti yote ya Serikali yanayohusiana na sheria ndogo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli sisi tumekuwa ndio tukienda kupokea mapungufu yote yanayojitokeza kwenye sheria ndogo ambazo zimekuwa zikitungwa chini ya taasisi, mamlaka mbalimbali za Serikali na Wizara mbalimbali. Na kifupi niseme Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo imekuwa na nafasi kubwa ya kukutana ana kwa ana na Kamati ya Sheria Ndogo na kuyajua na kuyafahamu yote yanayojiri katika mfumo mzima na mlolongo wa utungaji wa sheria ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nasema hivyo kwa nini; nataka nianze kwa kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati hii ya Sheria Ndogo kwa kazi nzuri anayoifanya ndugu yetu, mzee wetu, Mheshimiwa Chenge amekuwa akifanya kazi nzuri sana siyo kwa niaba ya Kamati tu lakini kwa Serikali nzima. Lakini anashirikiana bega kwa bega na Makamu Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Ngeleja na Wajumbe wa Kamati hii ni wabobezi na ni Wajumbe mahiri kwelikweli katika kuishauri Serikali kwenye eneo hili la kusimamia na kuendelea kuzipitia sheria hizi ndogo zinazoletwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanafanyika kwa kuzingatia Kanuni ya 37(2) ambayo inatutaka sisi Serikali baada ya utungwaji wa sheria zote ndogo kuziwasilisha hapa Mezani, na tumekuwa tukifanya hivyo katika kila mkutano na baada ya hapo Kamati ya Sheria Ndogo inapata nafasi ya kuzifanyia uchambuzi. Niungane na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, jambo hilo sisi kama Serikali tumekuwa tukilishughulikia vizuri. Mwanasheria Mkuu wa Serikali amejibu hoja mbili na mimi nitajibu hoja kama mbili zilizobakia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tuliagizwa na Kamati ya Sheria Ndogo kwamba kila wanapotoa jedwali kama hili lililotolewa leo, taasisi, Wizara na mamlaka nyingine zote ndani ya Serikali zihakikishe kwamba katika yale maeneo ambayo tumekubaliana kati ya Kamati na Serikali yanakuka misingi ya utungaji wa sheria mama katika utekelezaji wake kwa kutunga hizo sheria ndogo haraka sana zifanyiwe mabadiliko ili ziweze kuendana na sheria mama na ziweze kuwafaa wananchi katika matumizi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba lilihakikishie Bunge lako hili Tukufu katika Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge agizo hilo limeanza kutekelezwa.

Nitatoa mfano wa sheria ndogo mbili tu lakini nyingi zimeshafanyiwa kazi; mfano Sheria Ndogo ya Ushuru wa Stendi Halmashauri ya Chalinze ya mwaka 2018 kifungu cha 9(6) kimekwisha kurekebishwa na kimetangazwa upya baada ya marekebisho katika Gazeti la Serikali Na. 604 la tarehe 16, Agosti, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine ni Sheria Ndogo za Ushuru wa Maegesho Halmashauri ya Mji wa Bunda ya Mwaka 2018 kifungu cha 4(2), na yenyewe imetangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 606 la tarehe 16, Agosti, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hizi ndogo mbili tu lakini zile zote ambazo tulishaletewa. Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tumeshaandika kwenye wizara mbalimbali, na wizara zimeshafanya marekebisho na zimeshatangaza kwenye kwenye Gazeti la Serikali kama tulivyoagizwa na Kamati ya Sheria Ndogo. Tayari tumeshawasilisha nakala za magazeti hayo kwenye Ofisi ya Katibu wa Bunge. Kwa hiyo Kamati ya Sheria Ndogo tunaomba kuwahakikishia kwamba tunatekeleza maagizo yenu. Mlitushauri pia kwamba mamlaka zote zilizokasimiwa na Bunge madaraka ya kutunga sheria ziwashirikishe wadau katika utungaji wa sheria hizo ndogo; tunafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa kwa mfano nina Sheria Ndogo za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Mlimsikia Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, alitoa ushahidi pia hapa wakati wa kutungwa kwa sheria hizo ndogo zitakazosimamia pia uchaguzi ambapo wadau wote walishirikishwa. Kwa hiyo mawaziri wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa kuzingatia maagizo ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, agizo lingine lilikuwa kwanza, kuimarisha Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kazi hiyo imefanyika vizuri. Tumeshaanza kununua mitambo na tumeshaanza kuiondoa ile mitambo ambayo ilikuwa imepitwa na wakati na mingine iliyoharibika tumeanza kuitengeneza ili kuiimarisha ifanya kazi yake vizuri. Vilevile mmetuambia ofisi ile ishughulike kufanya uhariri kwa kushirikiana na mamlaka zote ambazo zimetunga hizo sheria ndogo. Kazi hiyo tumeanza kuifanya, na matokeo chanya ya kuanza kufanyika kwa kazi hiyo ni kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkutano wa Kumi na Nne wa Bunge, Serikali iliwasilisha sheria ndogo kama 196, na baada ya uchambuzi kupitia kwenye kamati ndogo tuliona kwamba, kama nitakuwa nina kumbukumbu sahihi, sheria ndogo 14 ndiyo zilizoonekana na kasoro. Kwa hiyo unaona kwamba tayari Serikali inazidi kupunguza mapungufu ambayo yanajitokeza kwenye utungaji wa sheria wa sheria ndogo. Hii yote ni kazi nzuri inayofanywa na Kamati yetu ya Sheria Ndogo ambayo sisi Serikali inatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, labda mfano mwingine mdogo wa mwisho, Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge Serikali iliwasilisha mezani sheria ndogo kama 174, na baada ya uchambuzi wa Kamati ya Sheria Ndogo tuliona sheria kama 22 zilikuwa na matatizo. Kwa hiyo unaona kwamba kuna trend pia ya kazi nzuri ambayo inaibuliwa na Kamati ya Sheria Ndogo inayotufanya sisi ndani ya Serikali kujipanga sawasawa na kuhakikisha sasa zile sheria ndogo tunazozileta ziwe ni sheria ambazo zinafuata mfumo wa uandishi wa sheria kwa kuzingatia sheria mama, na vile vile ziwe zinakidhi matakwa halisi ya watumiaji wa sheria hizo ambao ni wananchi wa Tanzania. Tumesema sisi na tumekubaliana ndani ya Serikali, tumeweka mpango mkakati wa kujitathmini wenyewe ndani ya taasisi na wizara mbalimbali kuhakikisha kwamba jambo hili halijirudiirudii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli wakati mwingine ninaomba nikubaliane na Kamati ya Sheria Ndogo, wakati mwingine makosa tunayoyafanya ni makosa ambayo kwa kweli yangeweza kurekebishwa mapema kabla hata sheria haijaanza kutumika wala haijafika Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwa ushauri miongozi ambayo tumekuwa tukiipata kutoka kwenye Kamati ya Sheria Ndogo tutaendelea kuizingatia. Nia ni njema, na hatima yake ni Tanzania yetu, kwa manufaa ya Watanzania wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Kamati ya Sheria Ndogo, na kwa kweli kazi yenu ni kazi nzuri, kazi njema iliyotukuka. Waheshimiwa Mawaziri wote tutaendelea kuwaunga mkono, tutakuwa pamoja na ninyi kwa sababu tunasaidiana kwa ajili ya ustawi wa taifa la Watanzania na sisi wote ni Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)