Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Stella Martin Manyanya (38 total)

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na shukrani nyingi kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kufahamu juu ya Chuo cha VETA ambacho kimejengwa Wilayani Nyasa. Nafahamu kimeshafikia zaidi ya asilimia 95, ni nini mpango wa Serikali kuanza kutoa mafunzo ili vijana waweze kunufaika na chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tunafahamu kwamba vyuo hivi ambavyo tayari ujenzi wake umekamilika, tuko katika mpango wa kuanza kutoa mafunzo mara moja. Suala lililokuweko mbele yetu sasa ni kuhakikisha kwamba tuna vifaa kwa ajili ya kufundishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuko kwenye mchakato wa manunuzi ya vifaa hivyo na pindi tu manunuzi hayo yatakapokamilika, program zile za ufundishaji katika maeneo haya zitaanza mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, jitihada ambayo inatumika na Wizara hii katika kukamata wale wanaotumia nyavu ambazo hazifai au katika masuala mengine yanayohusu kukusanya mapato ni kubwa sana kuliko zinazotumika katika kuwawezesha hawa wavuvi na ndiyo maana kuna wakati nilisema kwa nini wavuvi wameendelea kuwa maskini kuliko sekta nyingine. Nauliza swali hili kwa sababu Wizara yenyewe iliamua kutoa ruzuku ya injini za boti, lakini kwa kuwafanya hawa wananchi lazima wakae kwenye kikundi ni sawa na kuwafunga miguu yule mwenye ari ya kufanya kazi akimbie anamsubiri mwenzake ambaye anatakiwa mpaka achangie. Je, ni lini Serikali itaangalia upya suala hili ili kuwawezesha wavuvi hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Ziwa Nyasa lina mawimbi makubwa sana kiasi kwamba kuvulia ile mitumbwi midogo midogo ambayo haina injini inakuwa ni changamoto kubwa kwa hawa wavuvi, kiasi kwamba sasa inafikia mtu mwenye injini moja ya boti inabidi avute mitumbwi mitatu mpaka minne kwenda kilindini na kurudi, jambo ambalo ni hatari na wale wanaoenda kuvua wanazama kila wakati hata juzi kuna mvuvi amepotea. Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha, kuwezesha na kutoa mafunzo kamilifu kwa wavuvi hawa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Stella Manyanya kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele kuwapigania jamii ya wavuvi wa Ziwa Nyasa. Naomba nimhakikishie kwamba Serikali imejipanga vyema katika kuhakikisha wavuvi wote nchi wanapata suluhu ya changamoto zinazowakabili wakiwemo wavuvi wa Ziwa Nyasa na ndiyo maana katika wakati huu tulionao Serikali imejipanga kwenda kuhakikisha tunajenga soko la kisasa katika eneo la Mwambao wa Ziwa Nyasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni lini Serikali itaangalia upya suala la kuwezesha wavuvi mmoja mmoja. Sera yetu ya Vyama vya Ushirika ukiitazama vyema na lengo letu ni katika kuhakikisha kwamba wavuvi hawa wanakuwa na sauti ya pamoja. Ni kweli tunaweza tukawasaidia na tuko katika kuwasaidia kuhakikisha kila mmoja mwenye nia njema aweze kufikia lengo la kuwa na mashine na ikiwezekana awaajiri na wenziwe. Hata hivyo, wanapokuwa pamoja ni kwa ajili ya kuwawezesha kuwa na sauti ya pamoja kulifikia soko, ili kuwarahisishia kutokubanwa na kulaliwa na wateja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Waheshimiwa Wabunge tuliunge mkono jambo hili na sisi Serikali tumekubaliana kuhakikisha tunaongeza jitihada kwenye kupeleka mikopo kama vile ya VICOBA, mikopo kupitia Benki ya Kilimo na madirisha mbalimbali ya benki za kibiashara ili yaweze kuwasaidia hata mvuvi mmoja mmoja ambaye atakwenda kuajiri wavuvi walio wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya suala la kutoa elimu; utoaji wa elimu ni jambo endelevu. Nimpe pole sana Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya kwa ajali zinazowapata wavuvi katika eneo la Ziwa Nyasa na maeneo mengine ya wavuvi wote na sisi tumejipanga sana kupitia Chuo chetu cha FETA cha Utaalam wa Uvuvi kuhakikisha tunapeleka elimu ya kutosha katika maeneo yote ya wavuvi ili waweze kushindana na kuhakikisha kwamba wanakuwa tayari kuendana na hali halisi hasa za kimazingira na ili kuondoa uwezekano kupatikana kwa hizi ajali ambazo zinawapata wavuvi wa kule Nyasa.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mahakama ya Mwanzo ya Liuli ilijengwa toka kipindi cha mkoloni na ikawa imeharibika sana na kilichotokea ni Mahakama kuhama kabisa eneo hilo na kwamba shughuli za Mahakama haziendelei:-

Je, ni lini Mahakama hiyo itarejeshwa katika nafasi yake kama ilivyokuwa mwanzo hapo Liuli?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunakiri kwamba Mahakama nyingi zimechakaa. Kama nilivyoeleza katika maelezo yangu ni kwamba, mkakati wa kukarabati na kujenga majengo mapya kwenye maeneo ambayo hayana Mahakama, ukomo wake ni 2025 ambapo namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo la Liuli tunalichukua na katika kipindi kijacho cha fedha tutahakikisha tunawasogezea hii huduma ya ukarabati wa Mahakama yao. Ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali langu ni kwamba, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Daraja la Mto Luhuhu linalounganisha Wilaya ya Nyasa na Ludewa linakamilika? Kwa sababu kwa sasa hata ile Pantoni iliyokuwa inatumika nayo imeharibika.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mhandisi Stella Manyanya Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja analolisema linaunganisha Wilaya ya Nyasa na Wilaya ya Ludewa. Katika bajeti yetu ni kati ya madaraja ambayo yamepangiwa fedha kwa ajili ya kujengwa katika bajeti inayokuja. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara bajeti itakapoanza kutekelezwa daraja hili litaendelezwa kujengwa ili liweze kukamilika. Ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa imethibitika kwamba Wilaya ambazo ziko mpakani zinanufaika sana kupitia biashara na majirani zao wa nje, na kwa kuwa katika Wilaya ya Nyasa, kwanza kuna uasilia wa kindugu lakini vilevile kuna changamoto kubwa za kukuza biashara na Malawi ingekuwa ni mkombozi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameonesha kuwa na uwezo mkubwa wa kidiplomasia kwa jinsi ambavyo amenijibu swali langu, namshukuru sana, je, Waziri una mpango gani wa kwenda kuongeza nguvu ya kupeleka ushawishi katika nchi ya Malawi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa…

SPIKA: Ushawishi wa nini?

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ushawishi wa kuhakikisha kwamba suala hilo ambalo tumelizungumzia la kibiashara linafanyika kwa kutumia meli na nyenzo nyingine.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ninapenda pia kumualika Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri kuja Wilaya ya Nyasa ili kuwafahamu wananchi wa kule na shughuli wanazozifanya na kuona namna bora zaidi ya kukamilisha kushughulikia suala hili la kibiashara. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itafanya kila jitihada kwa kushirikiana na mamlaka husika nchini Malawi ili kuwezesha meli ya MV Mbeya II ianze safari zake kati ya Malawi na Tanzania pale taratibu zote zitakapokamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili ambao ni mwaliko, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba nitakuwa tayari, kwa idhini yako, kufanya safari hiyo ili kuona fursa mbalimbali ambazo ziko katika Wilaya ya Nyasa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kuishukuru sana Serikali kwa jitihada kubwa ambazo zimeshaanza katika kuboresha Mji huu wa Mbamba Bay. Lakini pamoja na shukrani hizo, ninapenda kupata majibu kutoka Serikalini, Mji huu wa Mbamba Bay ni mji ambao ni wa muda mrefu sana takribani miaka mia moja, lakini vilevile ni kitovu cha utalii katika Mkoa wa Ruvuma, lakini hiki kiasi cha kilometa moja, moja na nusu kinachotengwa ni kidogo kulinganisha na mahitaji yaliyopo kwa sababu mji huu umedumaa kwa muda mrefu.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba katika bajeti inayofuata angalau tupate hata kilometa mbili ili kuendana na kasi ya kukuza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Jimbo la Nyasa ni kubwa sana kwa ukubwa wake na jiografia milima mikali kiasi kwamba hawa TARURA ambao wanasimamia hizi barabara wanapata shida sana katika usimamizi kutokana na kuwa na gari bovu ambalo kila wakati linaendea matengenezo kutokana na hali halisi ya mazingira.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza gari jipya moja angalau kuwawezesha hawa watumishi wa TARURA waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya Mbunge wa Jimbo la Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mji wa Mbamba Bay ni Mji mkongwe na Mheshimiwa Mbunge kama alivyozungumza nafahamu jitihada kubwa ambazo anazifanya katika Jimbo lake na anahitaji tuongeze bajeti kuhakikisha ule mji unaongezewa lami.

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza katika swali letu la msingi kwamba tutaendelea kutenga fedha na katika mwaka wa fedha unaokuja kwa maana ya 2022/2023 basi Mji wa Mbamba Bay tutauongezea bajeti kwa ajili ya ujenzi wa kilometa walau moja ya lami nyingine ili kuongeza mtandao wa lami katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili ameeleza kwamba Halmashauri ya Nyasa gari lake watu wa TARURA ni bovu na wanashindwa kufika katika maeneo korofi ni muhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini tumeshaagiza magari mia moja ambayo tutayagawa katika Halmashauri za Wilaya 100 nchini ikiwemo Halmashauri ya Nyasa.

Kwa hiyo, hilo tunauhakika nalo atapata gari jipy. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru leo kwa kuniona pamoja na ufupi wangu. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya, leo umesimama. (Makofi/Kicheko)

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa ninayoiona katika utengenezaji wa hizi skimu ni ukosefu wa wataalam. Kwa mfano, nimeshtuka sana kujua kwamba Skimu ya Sakalilo mpaka leo eti haijakamilika. Yaani toka kipindi hicho mimi nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, wataalam walikuwa wanatoka Mbeya miaka ya 2013 mpaka leo haijakamilika. Kuna tatizo kubwa sana katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, naomba nifahamishwe, Wizara imejipanga vipi kupata wataalam wa kutosha ili kusaidia hizo skimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Manyanya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hatua ya kwanza tuliyofanya kama Wizara, kama alivyosema kwamba wataalam walikuwa wanatoka Mbeya. Sasa hivi tumevunja ofisi za kanda na sasa kila Mkoa una Ofisi ya Tume ya Umwagiliaji na tumepeleka manpower, kwa maana ya ma-engineer na kila Mkoa sasa una engineer wa umwagiliaji. Hivi karibuni tumewaruhusu ma-engineer wetu wa Tume ya Umwagiliaji, kuajiri intense ambao ni graduates kutoka University ambao ni ma-engineer wa irrigation waweze kwenda ku-beef up Ofisi za Mikoa.

Mheshimiwa Spika, hatua ya pili ambayo tunajipanga nayo ni kuhakikisha katika kila Wilaya tunakuwa na engineer wa umwagiliaji tukishirikiana na waliopo katika TAMISEMI ili tuweze kuhakikisha kwamba shughuli za umwagiliaji zinasimamiwa. Kwa mwaka ujao wa fedha tutakuwa na ofisi katika kila Halmashauri inayosimamia suala la umwagiliaji ili kuwe kuna efficiency katika kufuatilia miradi ya umwagiliaji na ku-plan ili siku ya mwisho tusifanye kazi hizi nusu nusu.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na miradi mingi ya umwagiliaji ambayo iko chini ya kiwango ambacho kinachotarajiwa na hili ni suala la planning na resource. Nasi kama Wizara tumepeleka mapendekezo yetu Hazina. Tunaamini mwaka ujao wa fedha na Waziri wa Fedha alisema ndani ya Bunge lako wakati anahitimisha kwamba umwagiliaji utakuwa ni sehemu ya kipaumbel. Tunaamini itakuwa hivyo na Bunge lako litatupatia rasilimali.

Mheshimiwa Spika, hatuna tatizo la wataalamu, tuna tatizo la rasilimali fedha ambayo tumeshapeleka kwa wenzetu wa Wizara ya Fedha ili tuweze kutatua hili tatizo. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na jitihada kubwa ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais kupitia Wizara ya Nishati kusambaza umeme kwa kiwango kikubwa, lakini changamoto kubwa ni kwamba inaonekana fedha hazitoshi kwa ajili ya usambazaji wa umeme kwa line ndogo ndogo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inapata fedha ili wananchi hawa sasa wafaidi umeme kupitia line ambazo zimeshajengwa nchini Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Manyanya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mahitaji ni makubwa lakini pesa haitoshi. Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Sita tayari imetoa shilingi 1,250,000,000,000 kwa ajili ya upelekaji wa umeme katika vijiji. Hivyo, tunaamini pesa angalau ipo ya kutosheleza mahitaji kadhaa tuliyokuwa nayo.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema juzi Mheshimiwa Waziri wa Nishati, kwamba sisi Wizara ya Nishati tunao mkakati mkubwa ambao baadaye utakuja kuwasilishwa kwa Mheshimiwa Rais na kwenu, kwamba tunatafuta fedha kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji vyote nchini na makadirio yetu yanaonesha ni kama shilingi trilioni saba na nusu. Tunaamini kwa sababu tunakopesheka, tunaaminika kwa Mataifa mengine na tunahitaji kupeleka umeme kwa wananchi wetu, fedha hiyo tutaitafuta na tutaipata kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kila mwananchi anayehitaji umeme anaupata.

Mheshimwia Spika, Mheshimiwa Waziri alisema, angalau ifikapo 2025 jambo hilo liwe limekamilika, Mheshimiwa Rais akisimama basi kura zimwagike kwa ajili ya kushinda vizuri.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na shukrani kwa majibu hayo yenye matumaini, na ninaamini kwamba nitaweza kupatiwa orodha ya hao walioajiriwa na maeneo waliyoajiriwa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kufahamu, hiyo kanzidata inafanya vipi kazi yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa ameeleza kwamba wanaajiriwa kwa kufuata usawa kwa watu wote, lakini mtu mwenye changamoto ni tofauti na mtu mzima. Kwa nini Serikali sasa isifikirie kuweka utaratibu maalum unaolihusu kundi hili ili lisipate tatizo kama ambavyo tunasikia kuna matatizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameuliza kama kanzidata ipo. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge ambaye amekuwa mstari wa mbele vilevile kulifuatilia hili suala, kwamba kanzidata hiyo ipo na inaratibiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Na katika kuratibu huko Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikitoa elimu mbalimbali kwa watu wenye ulemavu kupitia vyama vya watu wenye ulemavu, kupitia taasisi za elimu ili kuwaonesha kwamba kanzidata hiyo ipo na taarifa zao zinachukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili, kwamba kwa nini kusiwe na utaratibu maalum; utaratibu maalum upo. Kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, kifungu Na. 5(1)(1) na kifungu Na. 5(1)(2) kimeeleza wazi hii sheria ya mwaka 2008, imeeleza wazi namna ya kuweza kupata ile asilimia tatu ya watu wenye ulemavu katika utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nirejee tena kutoa rai yangu kwa watu wenye ulemavu na kwa waajiri wote, kwamba watu wenye ulemavu kwanza waombe hizi nafasi zinapotangazwa. Kwa sababu kwa mujibu wa sheria asilimia ile tatu ipo lakini ni lazima wafikie sifa na vigezo vya kuajiriwa katika utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili, vilevile ni waajiri wenyewe kuwapa kipaumbele hawa watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha wakati wa interviews hizi kuwe kuna mazingira rafiki ya kuweza kuhakikisha wanahudhuria interviews hizi, wanafanya mitihani hii ambayo inawekwa ili kuweza kupata ujumuishaji zaidi wa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Hospitali ya Kanda ya Mtwara bado inaupungufu mkubwa katika kuikamilisha kiujenzi, lakini pia vifaa tiba. Lakini Kanda yote ya Kusini inaitegemea hospitali hiyo kwa muda mrefu.

Sasa ni lini hospitali hiyo itakamilika ili kuwaondolea adha wananchi wa Kusini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kwamba kwa kweli Hospitali ile ya Kanda ya Mtwara ni mojawapo ya hospitali nchini ambayo imejengwa kwa majengo ya kisasa mno. Lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pamoja na kazi kubwa ambayo imefanyika pale, mwaka huu wametengewa shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuendelea na ujenzi ili kukamilisha mambo ambayo Mheshimiwa Mbunge anasema hayajakamilika. Niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa namna anavyofatilia shughuli za Mkoa wake.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza napongeze jitihada zinazoendelea kwa upande wa Serikali, lakini changamoto mojawapo inayofanya matumizi ya gesi kuwa yapo chini zaidi ni kukosekana kwa vituo vya kuuzia gesi, hasa katika maeneo ya vijijini ambayo yapo mbali na yanasabababisha kuongeza gharama kubwa kwenye mitungi pomoja na gesi kwa ujumla.

Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha hali hiyo?

Jambo la pili, sambamba na gesi umezungumzia kuhusu kuwezesha nishati safi katika maeneo ya vijijini, bado maeneo ya vitongoji ambavyo ni vikubwa sana havijapata nishati safi ya umeme, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha kufikisha nishati hiyo, sambamba na hii ya gesi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Manyanya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la kwanza, wakati wa utekelezaji wa huu mradi wa kutoa ruzuku, tunaamini wigo wa wafanyaji biashara kwenye eneo hili wataongeza na hivyo watafika katika maeneo yote kwa sababu Serikali itajitahidi kuhakikisha shughuli hii inapata ruzuku na hivyo wawekezaji mbalimbali wanaweza kushiriki. Pia, mwongozo tunaoutengeneza utaangalia namna ya kufanya, kama wanavofanya wenzetu wanaosambaza mbolea na maeneo kama hayo, ili tuweze kufika katika maeneo yote husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini, kwenye swali la pili la umeme wa vitongoji, Serikali inaendelea katika mzunguko wa tatu awamu ya pili ya REA, viitongoji baadhi vinapatiwa umeme, lakini pia kuna miradi ya jazilizi inaendelea katika maeneo yetu na Serikali inaendelea kutafuta fedha kuhakikisha kwamba vitongoji vyote vinapatiwa umeme ili wananchi waweze kutumia nishati hiyo safi.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya kuwatambua watoto ambao wamezaliwa na ulemavu katika hatua za awali kutokana na uelewa usiokuwa wakutosha kwa wale ambao wanazalisha yaani Manesi.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza elimu hiyo kwa kasi hasa vijijini ili mtoto atambuliwe katika hatua za awali kabisa na kuweza kusaidiwa kwa mfano kwenye mtindio wa ubongo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anachokisema Mbunge, lakini nimuondoe wasiwasi, uelewa kwa manesi ni mkubwa, lakini kumekuwa kukitokea maeneo machache ambayo kweli watoto wanachelewa kutambuliwa hasa kwa mfano wa wenye autism na matatizo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tutaendelea kuhakikisha elimu inakwenda na utaona sasa hivi kuna taasisi ambazo zinahamasaisha hayo maeneo ambayo kwa kweli yamekuwa na changamoto. Ukiona Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan ametenganisha Wizara ya Afya na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, ni kwa sababu vile kuna masuala mengine ni ya kijamii na sasa kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii tutahakikisha kwenye eneo la jamii sasa hata wale ambao wanaoweza jamii ikashirikiana na sisi kuwatambua kwa sababu bado tuna tatizo vilevile, kuna watu wanaozalia majumbani na wakati mwingine wasifike kwenye vituo vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kushirikiana wote kwa pamoja ninahakika tutaweza kutatua hayo matatizo na Mbunge uwe mmojawapo wa balozi wetu kuhakikisha eneo hilo linafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ikumbukwe kwamba Halmashauri hizi za Geita ni miongoni mwa Halmashauri ambazo zinachangia mapatao makubwa sana Serikalini kutokana na masuala ya uchimbaji wa dhahabu. Kwa hiyo, barabara hizi zinapokuwa hazitengenezwi vizuri hazitoi taswira nzuri kwa wananchi wa maeneo hayo. Kwa hiyo, naomba kuisisitiza Serikali kuongeza jitihada katika kuikamilisha vizuri barabara hii.

Mheshimiwa mwenyekiti, swali la pili ni kwamba, inaonekana katika Halmashauri nyingi amabazo ziko Vijijini na zile ambazo zinaanza kuchipukia zisizo na mapato makubwa, ugawaji wa fedha inayopelekwa kwa ajili ya barabara hizi za TARURA ni mdogo sana kiasi kwamba barabara nyingi zinashindwa kufunguliwa.

Je, ni lini Serikali itaeweka utaratibu mzuri wa kuongeza jitihada za kufungua maeneo haya ya vijijini ili wananchi waweze kupata huduma inayostahili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Halmashauri ya Geita kutokana na shughuli za kiuchumi ambazo ziko pale na ndiyo maana ukiangalia kwenye jibu letu la msingi tumetenga fedha na tutakacho hakikisha ni kwamba fedha hizo zinakwenda na zile barabra zinarekebishika, kwa hiyo hilo halina shaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu ugawaji wa fedha za barabara ambazo zimekuwa zikionekana kuwa chache na kwa sababu ya ukubwa wa mtandao wa barabara tulionao nchini Serikali tunalipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na tutalizingatia kulingana na bajeti ambavyo tutakuwa tukizitenga, ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na jitihada kubwa ambayo Serikali imefanya ya kutupa mkandarasi Palemon kwa ajili ya maji katika Kijiji cha Puulu, Songambele na Ngee. Mkandarasi huyu ana zaidi ya miezi mitano toka alipoonyeshwa mradi hajaonekana kabisa, wananchi wanalalamika, nini kauli ya Serikali kuhusu mkandarasi huyu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia Bunge lako Tukufu kusema wakandarasi wote ambao hawajafika kwenye maeneo ya kazi wafike mara moja kadiri ya mikataba yao inavyowataka. Nje ya hapo sisi kama Wizara tutachukua nafasi yetu na wasije wakatulaumu.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kufanya upembuzi yakinifu Barabara ya kutoka Nyoni hadi Mipotopoto-Mitomoni kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo kwenye ilani hii barabara kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami na tunategemea katika bajeti ijayo iweze kuingia ili iweze kufanyiwa usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwanza nishukuru na niipongeze Serikali kwa jitihada inayofanyika kwa ajili ya kuendeleza hospitali hii.

Mheshimiwa Spika, hospitali hii ni tegemeo kubwa sana kwa watu wa Kanda ya Kusini ambao wanalazimika kutembea umbali wa kilometa 1,200 kwa mfano kutokea Mbamba Bay mpaka Dar es Salaam kufuata hizi huduma kutokana na pale kutokuwa na huduma kamilifu. Hospitali hii haina ambulance, haina gari ya Mkurugenzi, haina chumba cha kuhifadhia maiti, hospitali hii OC yake ni ndogo sana lakini ndiyo Hospitali ya Kanda.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka jicho la kipekee katika hospitali hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili; sambamba na hilo watumishi pia wako wachache, lakini tayari kumeshakuwa na msongamano na pia kupunguza msongamano ambao pia unaelekea katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.

Je, ni lini Serikali itaongeza idadi wa watumishi ili kuondoa hadha hii ambayo imeendelea huko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mbunge kwa namna ambavyo anafatilia masuala ya huduma kwenye kanda yake, lakini pia tumepokea barua yake kuhusu vifaa vinavyohitajika na Wilaya yake, pamoja na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, lakinio niseme kwamba moja kwanza ieleweke kwamba hospitali hii ya kanda ni hospitali ambayo sasa ndiyo inaenda kufikisha miaka miwili toka izinduliwe na Makamu wa Rais na kwa kibali cha mwaka huu tumepeleka kuomba kuajiri watumishi 111; lakini kwa sasa wako watumishi 166.

Mheshimiwa Spika, lakini pia amezungumzia suala la ambulance; kwa hospitali hii ya kwenu katika ambulance 727 ambazo Rais wetu ametoa fedha kwa ajili ya kununua ambulance iko kwa ajili ya hospitali hii ya kwenu.

Mheshimiwa Spika, lakini amezungumzia suala la mortuary na mengine; shilingi bilioni 4.4 ambazo ninazungumzia hapa tayari manunuzi yameanza kufanyika kwa ajili ya ujenzi wa mortuary, ujenzi wa nyumba za wanyafakazi, umaliziaji wa maabara lakini umaliziaji wa jengo la mama na mtoto.

Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hospitali hii itaenda kuwa ni nzuri na unajua we mwenyewe kwamba katika hospitali zote za kanda nchini hospitali hiyo ndiyo ina majengo mazuri kuliko hospitali yoyote, ahsante sana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Barabara kutoka Kitai-Rwanda-Litui mpaka Ndumbi itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii tayari iko kwenye hatua za awali na nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi tunakamilisha usanifu wa kina na baada ya kukamilika usanifu wa kina kwa barabara hii ya kutoka Litui kwenda hadi Ndumbi na mpaka Nyasa tutaanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nashukuru kwa majibu yenye matumaini kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni mtindo kabisa wa Wizara hii kuanzisha majengo na kutokumaliza kwa wakati kwa sababu ya kutokupata mgao unaotakiwa kutoka Serikali Kuu, kwa maana ya Wizara ya Fedha: Je, kwa mwaka huu wa 2022, hiyo shilingi milioni 100 iliyoahidiwa ni kweli itatolewa? Naomba commitment ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba, Wilaya ya Nyasa haina kabisa chuo chochote kinachotoa mafunzo kwa sasa hivi ikiwemo haya ya ujasiliaamali: Je, SIDO kwa kuwa jengo bado halijakamilika, mtaweza kwenda kutoa mafunzo hayo angalau kila mwezi mara moja wakati tukiendelea na huo ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Martini Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa maana ya kukamilisha vituo vingi vya mafunzo na uzalishaji ambavyo vimeanzishwa katika wilaya na mikoa mbalimbali. Ni nia ya Serikali na sasa tunaamini tutapata hizo fedha ili kukamilisha kituo hiki na vingine ambavyo bado havijakamilika.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, nachukuwa maombi ya Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya kwamba tuanze sasa kuona namna ya kuanza kutoa mafunzo ya uzalishaji katika maeneo ambapo kuna wajasiliamali wengi ikiwemo katika Jimbo hili la Nyasa ambapo wajasiliamali hawa watapata mafunzo kupitia SIDO.

Mheshimiwa Spika, nawaagiza SIDO waanze sasa kupitia utaratibu ambao siyo rasmi, badala ya kusubiria majengo, waanze kutumia majengo ambayo Halmashauri zinaweza zikatupa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wazalishaji katika maeneo yote ikiwemo katika Jimbo la Nyasa.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa, Serikali imewekeza sana katika hii miradi ya maji vijijini na changamoto ninayoiona katika vile Vyama vya Ushirika vya maji ni kukosa mfumo mzuri wa kukusanya mapato. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia kupata drilling system itakayosadia kukusanya maji kiurahisi?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ninathamini mchango mkubwa na jitihada kubwa za uwekezaji wa miradi ya maji vijijini. Serikali kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini katika kuhakikisha inatatua tatizo la maji vijijini. Tumeona tuna jumuiya zetu hizi za watumiaji maji, changamoto kubwa jumuiya za watumiaji maji ni katika suala zima la usimamizi. Moja tumetoa maelekezo kwamba katika kila mradi sasa kutakuwepo na Technician kupitia wananfunzi ambao wanatoka katika Chuo cha Maji. Pili, tunataka kila mradi lazima awepo Mhasibu ambaye ataweza kusimamia na kuhakikisha kwamba tunaweka mifumo.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tutatangaza mfumo rasmi wa kuhakikisha kwamba wanakuwa na bei rahisi hata vijijini ili katika kuhakikisha wanapata huduma ya maji bila ya usumbufu wowote.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa, Serikali inawekeza fedha nyingi sana katika kusambaza umeme hasa kwa njia ya nguzo katika maeneo yetu. Lakini unakuta kwamba hizo nguzi sasa badala ya kuishi miaka 15 angalau ndio iwe life span yake inaishi wakati mwingine ni miaka 4 nguzo inadondoka. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua kali au kuwafukuza kabisa hawa watengenezaji wa nguzo hizo hafifu ili kupunguza gharama ambazo zitajitokeza katika ku-maintain mfumo wa TANESCO?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Manyanya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama unafahamu wiki kadhaa zilizopita nilikuwa Mafinga kuzungumza na wadau wa nguzo nchini ambapo moja ya masuala tuliyozungumza kwa kina ni uhakika wa upatikanaji wa nguzo zenye ubora wa kutosha kwa ajili ya miradi ya TANESCO na REA.

Ni kweli ipo changamoto kwamba katika maeneo mengi nguzo zilizowekwa hazikidhi viwango na ubora. Changamoto hiyo siyo tu kwa wauzaji wa nguzo bali hata kwetu sisi TANESCO na REA kwa sababu mpaka nguzo inasimikwa maana yake tumeipokea na kuikubali.

Kwa hiyo, tumeweka utaratibu mpya wa kuhakikisha pamoja na kwamba nguzo tutazipata ndani ya nchi lakini mfumo wa udhiti wa ubora unaanzia kiwandani, unaanzia kwetu sisi, mnunuzi pia na taasisi zinazohusika na ubora ikiwemo TBS. Kwa hiyo upo mfumo mpya ambao umewekwa sasa hivi wa kudhibiti viwango na ubora kwa nguzo zinazohitajika.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika ahsante sana, kwanza napenda kushukuru kwa majibu ya mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kufuatia umuhimu wa barabara hii ya Nyoni – Mitomoni kiuchumi Serikali ina mpango gani wa kuanza kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma wamekuwa wakilia, wakipiga magoti humu Bungeni kufuatia changamoto kubwa ya kuvuka katika Mto Ruvuma ulioko Mitomoni ili kutuunganisha na barabara ya Likwilifusi – Mkenda. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kujenga daraja hili kufuatia kilio kikubwa cha wananchi hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Martin Manyanya Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nikweli daraja la Mitomoni ni muhimu sana kwa wananchi wa Jimbo la Nyasa nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeishapata mkandarasi na sasa hivi tuko kwenye hatua za mwisho za manunuzi ili mkandarasi aweze kuanza kazi hiyo kwenye kujenga hilo daraja ambalo litagharimu si chini ya bilioni 22. Kwa hiyo, tupo kwenye hatua za mwisho kabisaa za manunuzi kwahiyo daraja hilo litajengwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hiyo, Meneja wa Mkoa wa Ruvuma alishaagizwa aweze kufanya tathmini, kufanya makadirio ya gharama ambazo zinaweza kuwa kwa ajili ya kuifanyia hiyo barabara upembuzi na usanifu wa kina wa hiyo barabara, ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika ahsante sana, kwa kuwa matibabu ya watu wenye ulemavu ni ya ghali sana kwa namna ya kuwapeleka hospitali lakini na hata matibabu yenyewe.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ruzuku ya bima ya afya kwa ajili ya watu wenye ulemavu ili kuwapunguzia adha wazazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa
Spika, ahsante, moja ya jitihada za Serikali ni pamoja na kuandaa mwongozo huo wa mwaka 2020 ambao umekamilika katika kuona na kuratibu masuala ya changamoto, kwanza kutambua changamoto za watu wenye ulemavu lakini pili kuona namna gani tunaweza kuwahudumia zaidi. Kwa hiyo kuwepo kwa mfuko wa watu wenye ulemavu utatatua changamoto nyingi sana ambazo zitasaidia sana kuona namna gani tunaenda kutatuta changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la bima, kwa kuwa tuko kwenye utaratibu sasa wa kupata universal health care, mfuko wa bima ya afya kwa wote tutaona pia umaalum wake kwa sababu kundi hili ni muhimu kuweza kuliangalia kwa umaalum wake na kulifanya hilo. Kwa hiyo niseme tu nimepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na kwamba tutaufanyia kazi, ahsante sana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza ninashukuru sana Serikali kwa jitihada ambazo zimeshaanza kufanyika katika ukanda wa Ziwa Nyasa. Kwa kuwa, Jimbo hili lina pande kuu mbili za Umatengo na Ziwa Nyasa, katika eneo hili la Umatengo kuna Kata ya Lumeme Kijiji cha Luhindo, Uhuru na Mipotopoto lakini pia Kata ya Luhangalasi zina tatizo kubwa sana la maji.

Je, Wizara ina mpango gani wa kupeleka fedha za dharura kwa ajili ya kuvisaidia vijiji hivi angalau hata kama ni Shilingi Milioni Moja.

Swali la pili, katika ukanda wa mwambao uliozungumzia kuna Kijiji cha Mtupale na Chiwimbi hivi havijazungumzwa, Je, mpango wa Serikali ni nini ili kuhakikisha na wenyewe wanapata maji? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya, Wizara ya Maji pamoja na mpango mkakati wa kuhakikisha tunatumia rasilimali toshelevu, kwa maana ya mito na maziwa Wizara ya Maji imejipanga sasa hivi tuna mitambo katika kila Mkoa, moja ya maelekezo ambayo niyatoe na tunashirikiana na Mheshimiwa Mbunge eneo hilo ambapo kama kuna tuwezekano wa kupata maji ya kisima basi tutachimba kwa haraka kuhakikisha wananchi wake wanaanza kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa nataka nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, tarehe 10 Mei, bajeti yetu ya Wizara ya Maji tunawasilisha kwa hiyo moja ya mikakati mizuri ambavyo tumejipanga ni kuhakikisha tunakamilisha changamoto ya maji kwa kiwango kikubwa sana. Ahsante sana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Chuo cha VETA Nyasa kina course mojawapo ambayo ni ya udereva lakini chuo hicho hakina gari kabisa ikiwemo ya utawala.

Je, nini mpango wa Serikali kukisaidia chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Manyanya Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika bajeti yetu ya mwaka huu 2023 tuliweka azma ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia pamoja na samani kwa ajili ya vile vyuo 25 vya Wilaya vipya pamoja na vyuo vine vya mikoa. Nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Manyanya, katika bajeti yetu ijayo ya 2023/2024 tutaendelea kuweka bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa ikiwemo na magari ya kufundishia pamoja na vifaa mbalimbali vya kujifunzia kwa ajili ya vyuo vyetu vile vya zamani lakini pamoja na hivi vipya.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nashukuru kwa kuianzisha mahakama hiyo. Kwa kuwa Mahakama ya Wilaya ya Nyasa inatumia majengo ya watu binafsi ambao pia wanaweza kuvunja sheria na kutakiwa kushtakiwa katika Mahakama hii;

Je, Serikali haioni kuwa kwa kufanya hivyo inaweza kuwafanya wadau wengine kutokuwa na Imani na Mahakama katika kutoa haki?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mahakama za mwanzo za Tingi na Litui ni chakavu sana.

Je, ni nini mpango wa Serikali katika kuboresha Mahakama hizi?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru naomba sasa nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella kama alivyouliza. Swali lake la kwanza, anasema jengo hili la Mahakama ya Wilaya liko katika majengo ya watu binafsi, na anapata wasiwasi kama Mahakama inaweza ikatenda haki pale ambapo mtu huyu ambako tumepanga kwake ana jambo na Mahakama.

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie kwamba muhimili wetu wa Mahakama umeona jambo hili, ndiyo maana tumetenga fedha ili kuhakikisha mwaka huu wa fedha tunajenga Mahakama takribani 24 za Wilaya. Kwa hiyo sisi tutaipa kipaumbele Mahakama hii, na kwa kuwa kazi imeshaanza Mheshimiwa Manyanya awe na imani tu kwamba jengo hili litakamilika ili pasiwepo na wasiwasi wowote, japo Mahakama siku zote inatenda haki.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili amependa kufahamu, kwamba hizi Mahakama za kata ambazo zimetajwa zitajengwa lini na kwamba zimechakaa sana. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mahakama yetu ya Tanzania imeliona jambo hili, na ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha tumetenga ujenzi wa Mahakama 60 kote nchini. Mahakama inafanya tathmini kujua kata zipi zipo mbali, na mpango wa Mahakama ni kujenga Mahakama katika maeneo ya tarafa ili kuhakikisha kwamba tunatoa huduma. Na taratibu tutaendelea kufikia kama bajeti utaruhusu kwenye hizo kata ambazo uhitaji umeonekana. Ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kuna baadhi ya maeneo unakuta kwamba jiwe la TANROADS limewekwa zaidi ya mita 30 kama ambavyo umetuhabarisha hapo;

Je, katika mazingira hayo TANROADS watakuwa tayari kuondoa mawe hayo kwa gharama zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kama ni barabara ambayo imesanifiwa maana yake ni kwamba pale ilipo ndipo zinapoishia mita 30, na maana yake ni kwamba pale ilipo barabara ambayo ipo itasogea upande huo ili kufikisha mita 30. Hao watakuwa watafidiwa pia kwa sababu barabara itakuwa imehama kutoka ilipokuwa na kusogea upande huo wa kwenye kigingi, ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza ninaishukuru sana Wizara pamoja na Madaktari wote wa Wilaya ya Nyasa kwa huduma ambayo inatolewa.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza kwa kuwa hali ya kituo hiki mbali ya kukosa wodi kabisa hasa ya akina mama pia hawana ultrasound kiasi kwamba hata inapofikia kupasua mama labda kwa ajili ya mtoto mimi naona ni suala la kubahatisha, hiyo inapelekea pia kuleta changamoto.

Je, ni lini Serikali itafikiria sasa kupeleka mashine hiyo ya ultrasound ili hawa wakina mama wafanyiwe huduma iliyo kamilifu?

Swali la pili, Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais wakati wa kampeni alipita katika Kata ya Lituhi na baada ya wananchi kumuomba akaahidi wajengewe kituo cha afya. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais ikizingatiwa kwamba ni Kiongozi Mkuu wa nchi na wananchi wanayo matumaini makubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Manyanya kuhusu hali ya kituo cha afya hiki ambacho ameulizia kwenye swali lake la msingi, tutaangalia katika bajeti ambayo tunaanza kuitekeleza mwaka wa fedha 2023/2024 kuona ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa ili waweze kununua ultrasound mara moja ambayo itaenda kuhudumia akina mama wajawazito katika eneo hili la Kihangara.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kata ya Lituhi kuhusu kujengewa kituo cha afya. Naomba nitumie nafasi hii kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuweza kufika katika Kata ya Lituhi na kufanya tathmini, kuona uhitaji ambao upo, idadi ya watu waliopo katika eneo hili na kisha kuwasilisha taarifa hizi katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ili katika mipango yetu tunayoweka ya ujenzi wa vituo vya afya, tuweze kuweka ujenzi wa Kituo cha Afya Lituhi ili kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara ya kutoka Liweta mpaka Mpopoma ni barabara ambayo ni muhimu sana kiasi kwamba inatenga hicho kijiji kuwa katika mawasiliano na Wilaya ya Nyasa ambayo ndiyo wilaya yake.

Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kipekee kuisaidia barabara hii ambayo pia ina milima kama ilivyo barabara ya Wampembe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la Mheshimiwa Eng. Stella Martin Manyanya la barabara hii ambayo inapita Liweta – Mpopoma kule Wilayani Nyasa, nayo vilevile nichukue nafasi hii kumwelekeza Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Nyasa kwenda kwenye barabara hii aliyoitaja Mheshimiwa Engineer Manyanya na kuifanyia tathmini na kuona ni kiasi gani kitahitajika kwa ajili ya kuweza kujenga ili tuweze kutengea fedha katika miaka ya fedha ambayo inafuata.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Jacqueline ana maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku kwenye nishati mbadala ikiwemo majiko ya gesi pamoja na gesi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa maeneo yanayochimbwa madini kama makaa ya mawe pamoja na mchanga yanafukiwa au kurejeshwa katika hali yake ya asili kwa wakati na inavyostahili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishiriki kwenye mjadala mmoja muhimu sana wa kitaifa ambao ulikuwa unazungumzia masuala ya kupunguza nishati ya matumizi ya kuni. Katika mjadala ule kuna maelekezo yalitoka tulipewa sisi Wizara tunaohusika na masuala ya mazingira na Wizara nyingine:-

(i) Tuendeleze kutoa elimu kwa wananachi;

(ii) Tunatakiwa tusimamie sheria, zipo Sheria za Mazingira; na

(iii) Tunatakiwa tuhamasishe wananchi wapande miti kwa wingi ili tuirejeshe miti ambayo ilishakatwa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo alilolishauri la kuhakikisha kwamba tunaweka ruzuku kwenye matumizi haya ya nishati hasa gesi na nishati nyingine, tutalichukua tunakwenda kulifanya kazi kuona namna ambavyo tunakwenda kuhamasisha zaidi wananchi katika masuala ya kutumia nishati bora ya kupikia instead of kutumia kuni.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, tayari tulishatoa maelekeza kwa wachimbaji wote wa madini au wachimbaji wote wa makaa ya mawe kuhakikisha kwamba mashimo wanayoyabakisha baada ya kuchimba wayafukie. Pia tulishatoa maelekezo kwa Mameneja wetu wote wa NEMC wahakikishe kwamba wanawapa taaluma na taaluma wameshapewa wachimbaji wote wa makaa ya mawe ili kuweza kuepuka athari kubwa ya mazingira ambayo inaweza ikajitokeza hapo mbele.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, barabara ya kutoka Mbamba Bay hadi Lituhi imo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kujengwa kwa kiwango cha lami. Je, Serikali imefikia wapi katika suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, barabara aliyoitaja ina sifa mbili, kwanza ni barabara ya ulinzi lakini pia ni barabara ambayo inaambaa ambaa na ziwa kutoka Mbamba Bay kwenda Lituhi. Barabara hii tulishafanya usanifu na sasa kinachotafutwa ni fedha ili kuijenga kwa kiwango cha lami ambapo itaunganisha Bandari ya Mbamba Bay ambayo tayari kuna lami, lakini na Lituhi ambako sasa Mheshimiwa Mbunge anakubali tunajenga kuanzia Amani Makolo mpaka Bandari ya Ndumbi. Kwa hiyo, kipande kilichobaki hapo tukishaunganisha tutakuwa tumekamilisha barabara za lami na itakuwa ni rahisi sana kufanya ulinzi, lakini pia kufungua Wilaya ya Nyasa, ahsante.

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wazee wa Wilaya ya Nyasa walipokutana tarehe 5 Machi, 2023, waliniagiza na walisema kwamba wanaona Wilaya ya Nyasa inadharaulika kwa sababu miradi yake inachelewa kupatikana na ikianza haiishi kwa wakati na hata kama ikionesha dalili ya kuisha haipewi vifaa vinavyotakiwa.

Je, Serikali haioni haya mawazo ya wazee wa Wilaya ya Nyasa yana ukweli kiasi fulani? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa pia kulikuwa kumejengwa karakana kwa ajili ya kutengeneza boti toka mwaka 2015 mpaka leo karakana hiyo haifanyi kazi iliyokusudiwa. Je, ni lini sasa na hiyo karakana itaweza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Jambo la kwanza nitambue maoni ya Mheshimiwa Mbunge ambayo yametolewa na wazee wake na nimhakikishie tu kwamba Serikali haidharau wananchi wa Nyasa wala wananchi katika maeneo yoyote yale. Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiyo maana tumemuelezea kwanza katika jibu la msingi, kuhakikisha kwamba soko hilo linafunguliwa na ndiyo maana zabuni imeshafunguliwa. Tunamaliza tu mchakato atakwenda atajenga na baada ya kujenga tutalifungua soko hilo ili liweze kuhudumia wananchi wa Jimbo la Nyasa kupitia Ziwa Nyasa.

Mheshimiwa Spika, suala la karakana na lenyewe basi tumelipokea, mimi mwenyewe binafsi nitafanya hiyo jitihada binafsi ya kuhakikisha inafunguliwa kwa wakati. Ahsante sana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Uzoefu unaonesha kwamba taasisi nyingi ambazo ziko chini ya NDC hazifanyi vizuri kutokana na ukosefu wa fedha kwa mfano General Tyre, Kilimanjaro Machine Tools na kadhalika.

Swali langu katika bajeti ya mwaka huu 2022/2023 Wizara imeanza kutenga fedha zozote kwa ajili ya kuendeleza kiwanda hicho cha Mang’ula Machine Tools?

Kwa kuwa kiwanda kile kimenyofolewa maeneo muhimu karibu yote kwa mfano sehemu za foundry imenyofolewa kiasi kwamba ni ngumu kukirudishia kama kilivyo na kitahitaji gharama kubwa sana. Kwa nini kwa sababu kuna majengo ambayo yanawezesha kukaa wanafunzi eneo hilo lisitumike kwa ajili ya kuendeleza taasisi za kiufundi?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Manyanya, Mbunge kama ifuatavyo:-

Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Stella Manyanya kwa kazi kubwa anayoifanya kufuatilia maendeleo ya sekta ya viwanda kwa sababu na yeye amekuwepo kwenye sekta hiyo kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kweli Shirika letu la Maendeleo la Taifa (NDC) lina miradi mingi ambayo kidogo ina changamoto lakini tumeshaanza kuyafanyia kazi ikiwemo Kilimanjaro Machine Tools ambako tumepeleka fedha ya kutosha kwa ajili ya kuihuisha ili kutengeneza foundry ambayo inafanana fanana na ile iliyokuwepo kule Mang’ula.

Kwa hiyo tumeshaanza kutengea fedha, lakini kwenye hii mahsusi ya Mang’ula baada ya kuona uhitaji huu tunafanya utafiti wa kuona nini kitafanyika halafu baada ya hapo sasa ndiyo tutakuja na bajeti yenye uhalisia. Kwa hiyo, tuko kwenye hatua za awali za kufanya utafiti wa nini kitafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu mitambo iliyokuwepo ni kweli na ndiyo maana tunataka tukihuishe kwa maana tuone sasa nini kitafanyika kwa sababu mwekezaji aliyekuwa amepewa mara ya kwanza ni kweli aling’oa mitambo mingi ikiwemo ya foundry, ya forging na fabrication na kuuza. Kwa hiyo, kimsingi tutaanza kama upya lakini kwa sababu nia ya Serikali nia ya kuona tunahuisha viwanda hivi kwa hiyo Serikali imeweka mkazo na tutakifanyia kazi na kutenga bajeti ya kutosha ili tuhakikishe tunarudi kwenye uhalisia wake wa awali, nakushukuru.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri kuwa je, ni kweli bei ya umeme imepanda kwa sababu naona kuna mabishano kwenye mitandao? (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Manyanya, Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, si kweli kabisa kwamba bei ya umeme imepanda na Serikali inasikitishwa na wale wanaoeneza maneno hayo na uvumi huo kwenye mitandao. Tumeomba mamlaka husika zichukue hatua kwa udanganyifu na upotofu huo unaofanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchakato wa kupandisha bei ya umeme ni mrefu, unahusisha maombi ya TANESCO kwa EWURA na unahusisha public hearing kwamba wananchi lazima wahusishwe na washirikishwe katika kutoa maoni yao pale bei ya umeme inapopandishwa. Ni mchakato mrefu ambao hauwezi kufanyika kwa siri. Kwa hiyo, hizi taarifa kwamba Serikali imepandisha bei ya umeme si kweli na naomba zipuuzwe na hatua zitachukuliwa kwa wale ambao wanaeneza uvumi huo. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kuwa Chuo cha VETA Nyasa ni chuo malkia kwa sababu Wilaya nzima haina chuo kingine zaidi ya kile na kile bado hakijaanza shughuli zake. Ni lini shughuli hizo zitaanza kwa sababu wananchi wanakiulizia sana?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Manyanya kwa ufuatiliaji wa karibu, lakini nimuondoe wasiwasi katika kipindi cha mwaka huu wa fedha Serikali imetoa zaidi ya bilioni 8.8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa kwenye vyuo vinne ambavyo vilikuwa vya Wilaya vilivyokuwa vimekamilika ambavyo ujenzi wake ulikamilika, lakini vifaa kulikuwa hakuna ikiwemo na chuo hichi cha Nyasa, Chuo cha Ruangwa, Chuo cha Kasulu pamoja na Chuo hiki cha Kongwa. Kwa hiyo, vifaa hivi tayari vimeshanunuliwa na tunaamini mara tu vifaa vitakapofika katika eneo hili la Nyasa ufundishaji au ufunguzi wa chuo hiki utaanza kwa kozi fupi lakini ifikapo Januari mwakani tutaanza kwa zile kozi ndefu. Nakushukuru sana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri yenye kutia moyo. Pia, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nyasa na jirani zao tunapenda kushukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay. Baada ya hapo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Bandari ya Mbamba Bay itakuwa ni kubwa na ya kisasa na itahitaji mzigo mkubwa kwa ajili ya kuhudumia Tanzania pamoja na nchi za jirani. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha sasa reli ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay inajengwa ili kuhakikisha kwamba bandari hii inatumika kiukamilifu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Bandari ya Mbamba Bay inategemeana sana mizigo yake na bandari ndogondogo zilizopo Kando ya Ziwa Nyasa. Bandari kama Liuli, Njambe, Lipingu na kule Manda katika Wilaya ya Ludewa. Nini mpango wa Serikali kuboresha bandari hizi ili ziweze kusaidia na kuhakikisha kwamba mizigo yote inachukuliwa vizuri?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimwa Mwenyekiti, kwanza kwa niaba ya Serikali nipokee pongezi za dhati za Mheshimiwa Manyanya kwa sababu ni kwa muda mrefu Wananchi wa Ruvuma na mikoa ya jirani wamekuwa wakitamani kuona bandari hii inafanyiwa uboreshaji na tayari Serikali ya Awamu ya Sita imeshaanza utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake pili anauliza kuhusu bandari ndogondogo kama za Liuli, Njambe na maeneo mengine. Hizi bandari zote zimejumuishwa katika mpango kabambe ambao ni The Updated National Proposed Master Plan 2022/2023 mpaka 2026/2027 ambazo zipo kwenye mpango wa kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye swali la kwanza ambalo ndio swali kubwa linaulizwa na Wabunge karibu wote wa Nyanda za Juu Kusini pamoja na Kusini. Kwamba ni lini sasa reli ya SGR ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay itaanza kujengwa na pengine reli hii wengine wanakwenda mbele zaidi wanataka kufahamu kuunganisha mpaka Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine nieleze kwa ufupi tu kwamba, Serikali inao mpango kwamba inatambua umuhimu na ukubwa wa mradi huu wa SGR ya Southern Corridor ambao ndani yake una miradi zaidi ya sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja reli hii ikijengwa ya kilometa 1,000 kutoka Mtwara kwenda mpaka Mbamba Bay kwenda mpaka Liganga na Mchuchuma utawezesha kusafirisha makaa ya mawe ambapo Mungu ametujalia zaidi ya metric tons milioni 400 na yaligundulika zaidi ya miaka pengine mia moja iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili itatusaidia makaa ya mawe yale yakishatengenezwa yataanza kuzalisha umeme zaidi ya megawati 600; nusu yake yakayeyushe chuma pale Liganga, nusu yake yaingie kwenye Gridi ya Taifa lakini kama haitoshi meli hii pia inakwenda kutoa ajira na inakwenda kutoa pia chuma ambacho kinakwenda kutengenezea magari na vitu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi mnafahamu Watanzania kwamba kwa sehemu kubwa zaidi ya asilimia 100 tunaagiza chuma kutoka nje jambo ambalo linachukua fedha zetu nyingi zaidi. Hivyo basi, Serikali kwa kutumbua umuhimu huo mkubwa; moja, imeshaanza kutengeneza uboreshaji mkubwa wa Bandari ya Mtwara ili mzigo upatikane kwa wingi zaidi; lakini pili, inaongeza bandari nyingine ya pili ya kisiwa mgao ili bidhaa chafu zote kwa maana ya makaa ya mawe, simenti na kadhalika ipitie pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ipo kwenye mpango wa kuhuisha stadi iliyofanyika miaka ya nyuma kwa maana ya kutafuta mshauri mwelekezi kuhuisha ile reli ili tuweze kujua mahitaji yake ni yapi. Mara tu baada ya kukamiliisha tunategemea kuanza kuijenga kwa mfumo wa PPP na hatimaye tunaamini likikamilika hili ni moja kati ya mambo ambayo Mheshimiwa Rais wetu anayapigania na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu atakayakamilisha na hivyo kwenda kufufua uchumi wetu kwa kiasi kikubwa zaidi.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yenye matumaini makubwa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa chuo cha VETA, Nyasa wakati huo kilikuwa na changamoto kubwa ya ulipaji wa fidia na kwa sababu kipo maeneo ambayo ni ya kimkakati, kwa hiyo eneo lake ni dogo kiasi kwamba uendelezaji wa chuo hicho unakuwa mgumu kwa hatua zinazofuata. Hakuna kiwanja cha mpira, lakini pia kwa fani nyingine kama za utalii ni ngumu kuendeleza hapo. Je, serikali ina mpango gani wa kuweza kuongeza eneo la chuo hicho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; naomba kwa kuwa Wizara ni hiyo hiyo moja kupitia mradi wa EP4R, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilijenga jengo la utawala na maktaba ya ghorofa katika Shule ya Sekondari Mbamba Bay ambayo kila siku nalisemea hilo jengo.

Je, ni lini jengo hili litaweza kukamilika na ikibidi Mheshimiwa Waziri sasa ifikie mahali wakatembelee wakaone hali halisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la eneo la chuo chetu cha VETA kuwa dogo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mimi pamoja na timu yangu ya wataalam wa VETA tutafanya ziara katika chuo hicho ili kujiridhisha na ukubwa wa hilo eneo. Kama kutakuwa na uhitaji wa kuongeza eneo, nimwondoe hofu, tulishalifanya jambo hilo katika Chuo chetu cha Kipawa ambacho kilikuwa na eneo dogo, tumeweza kuongeza eneo, basi na hapa katika Chuo chetu hiki cha VETA tutafanya ziara lakini vilevile tutahakikisha kwamba kama kutakuwa na eneo linahitajika kuongeza, Serikali itaweza kuongeza eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili katika shule hiyo aliyoitaja ya Sekondari ya Mbambabay kwamba Serikali ilishapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. Pia, kuna hili jengo la utawala ambalo halijakamilika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Wizara yangu kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI, tutafanya ziara katika eneo hilo. Vilevile, tumuagize Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa kuweza kufanya tathmini ya jengo hilo, kuona ni kiasi gani cha fedha kinahitajika ili basi Serikali iweze kupata tathmini hiyo na kuweza kuifanyia kazi ili jengo hili liweze kukamilika, nakushukuru.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa vitongoji vinavyopewa umeme ni vile ambavyo line za umeme kubwa tayari zilishapita, lakini kwenye jimbo langu kuna Kitongoji kama Nindi na Songeapori ambavyo viko mpakani na kuna changamoto kubwa za kiusalama.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvisaidia vitongoji hivi viwili kwa jicho la kipekee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella Manyanya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, vitongoji hivi viwili kwa kweli, vimekaa kimkakati. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa awamu hii ya ujazilizi utaweka addition scope ili vitongoji hivi viweze kufikiwa na umeme kwa umahususi wake, ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri yenye kutia moyo. Pia, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nyasa na jirani zao tunapenda kushukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay. Baada ya hapo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Bandari ya Mbamba Bay itakuwa ni kubwa na ya kisasa na itahitaji mzigo mkubwa kwa ajili ya kuhudumia Tanzania pamoja na nchi za jirani. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha sasa reli ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay inajengwa ili kuhakikisha kwamba bandari hii inatumika kiukamilifu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Bandari ya Mbamba Bay inategemeana sana mizigo yake na bandari ndogondogo zilizopo Kando ya Ziwa Nyasa. Bandari kama Liuli, Njambe, Lipingu na kule Manda katika Wilaya ya Ludewa. Nini mpango wa Serikali kuboresha bandari hizi ili ziweze kusaidia na kuhakikisha kwamba mizigo yote inachukuliwa vizuri?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimwa Mwenyekiti, kwanza kwa niaba ya Serikali nipokee pongezi za dhati za Mheshimiwa Manyanya kwa sababu ni kwa muda mrefu Wananchi wa Ruvuma na mikoa ya jirani wamekuwa wakitamani kuona bandari hii inafanyiwa uboreshaji na tayari Serikali ya Awamu ya Sita imeshaanza utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake pili anauliza kuhusu bandari ndogondogo kama za Liuli, Njambe na maeneo mengine. Hizi bandari zote zimejumuishwa katika mpango kabambe ambao ni The Updated National Proposed Master Plan 2022/2023 mpaka 2026/2027 ambazo zipo kwenye mpango wa kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye swali la kwanza ambalo ndio swali kubwa linaulizwa na Wabunge karibu wote wa Nyanda za Juu Kusini pamoja na Kusini. Kwamba ni lini sasa reli ya SGR ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay itaanza kujengwa na pengine reli hii wengine wanakwenda mbele zaidi wanataka kufahamu kuunganisha mpaka Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine nieleze kwa ufupi tu kwamba, Serikali inao mpango kwamba inatambua umuhimu na ukubwa wa mradi huu wa SGR ya Southern Corridor ambao ndani yake una miradi zaidi ya sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja reli hii ikijengwa ya kilometa 1,000 kutoka Mtwara kwenda mpaka Mbamba Bay kwenda mpaka Liganga na Mchuchuma utawezesha kusafirisha makaa ya mawe ambapo Mungu ametujalia zaidi ya metric tons milioni 400 na yaligundulika zaidi ya miaka pengine mia moja iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili itatusaidia makaa ya mawe yale yakishatengenezwa yataanza kuzalisha umeme zaidi ya megawati 600; nusu yake yakayeyushe chuma pale Liganga, nusu yake yaingie kwenye Gridi ya Taifa lakini kama haitoshi meli hii pia inakwenda kutoa ajira na inakwenda kutoa pia chuma ambacho kinakwenda kutengenezea magari na vitu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi mnafahamu Watanzania kwamba kwa sehemu kubwa zaidi ya asilimia 100 tunaagiza chuma kutoka nje jambo ambalo linachukua fedha zetu nyingi zaidi. Hivyo basi, Serikali kwa kutumbua umuhimu huo mkubwa; moja, imeshaanza kutengeneza uboreshaji mkubwa wa Bandari ya Mtwara ili mzigo upatikane kwa wingi zaidi; lakini pili, inaongeza bandari nyingine ya pili ya kisiwa mgao ili bidhaa chafu zote kwa maana ya makaa ya mawe, simenti na kadhalika ipitie pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ipo kwenye mpango wa kuhuisha stadi iliyofanyika miaka ya nyuma kwa maana ya kutafuta mshauri mwelekezi kuhuisha ile reli ili tuweze kujua mahitaji yake ni yapi. Mara tu baada ya kukamiliisha tunategemea kuanza kuijenga kwa mfumo wa PPP na hatimaye tunaamini likikamilika hili ni moja kati ya mambo ambayo Mheshimiwa Rais wetu anayapigania na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu atakayakamilisha na hivyo kwenda kufufua uchumi wetu kwa kiasi kikubwa zaidi.