Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sixtus Raphael Mapunda (31 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia mchana wa leo. Awali ya yote nachukua fursa hii kuwashukuru sana wananchi wapenda amani wa Jimbo la Mbinga Mjini kwa heshima kubwa waliyonipatia, nami
nawahakikishia tu kwamba sitawaangusha, nitawawakilisha kama wanavyotarajia. (Makofi)
Pia nachukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kwa kutoa hotuba nzuri, iliyosheheni weledi, iliyoangalia kila sekta na kwa maoni makubwa na mapana kwa maslahi ya Taifa hili la
Tanzania. Nawaomba tu Watanzania wote tuendelee kumwombea ili azma yake ya kuleta maendeleo ndani ya nchi hii ifanikiwe. Kusema ni rahisi, kutenda ni vigumu. Watapita wengi watakejeli, watapita wengi watasema lugha ambazo wanadhani zinastahili ili kuipunguza
thamani hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mimi niseme tu kwamba Mheshimiwa Rais ametenda, amesema, ameelekeza na utekelezaji tumeuona.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme neno moja tu kwa kifupi. Tunapozungumzia habari ya amani, umoja, mshikamano na utulivu wakati wa chaguzi, naomba niwakumbushe jambo moja.
Watanzania tunaofanya active-politics tuko milioni tisa tunaotokana na vyama vya siasa. Milioni 50 ya Watanzania wote wanaobaki hawako kwenye active politics. Inapofika wakati wa uchaguzi, sisi milioni kumi tunajiona ndio wababe, tunaoweza kufanya kila kitu, tukawaacha
Watanzania wengine, tunachoma matairi barabarani. Askari wakituzuia sisi wanasiasa, tunasema aaah, mnahatarisha amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tofauti kati ya kuhatarisha amani na kusimamia amani. Alichokieleza Mheshimiwa Rais katika hotuba yake, uchaguzi ulikwenda vizuri, zile rabsha rabsha mlizokuwa mnaziona za vyombo vya ulinzi na usalama vilikuwa ni kuhakikisha kwamba nchi hii
inakuwa hamna amani. Nawashukuru sana Jeshi la ulinzi pamoja na Polisi kwa kazi kubwa waliyoifanya. Sisi tutaendelea kuwatia moyo, fanyeni kazi kusimamia amani ili maendeleo yapatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye sekta moja; sekta ya kilimo ukiondoa sekta nyingi ambazo Mheshimiwa Rais alizielezea katika hotuba yake. Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais anakiri kwamba asilimia 95 ya chakula tunachokipata hapa nchini kinatokana na Sekta ya Kilimo, lakini anakubali kwamba asilimia 30 ya mapato ya kigeni yanatokana na sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee niseme tu mambo machache kuhusu takwimu ya mwaka 2014, sekta gani ziliongoza kwenye kuleta pato la kigeni? Ukiondoa dhahabu ambayo ilileta shilingi bilioni 2,705, sekta zote zilizofuatia kwenye zile sekta tisa, zilikuwa
ni sekta zenye uhusiano na kilimo. Korosho ilileta shilingi bilioni 647, Pamba ilileta shilingi bilioni 558, Tumbaku ilileta shilingi bilioni 319, Kahawa ilileta shilingi bilioni 204, Mkonge ulileta shilingi bilioni 111, Chai ilileta shilingi bilioni 72 na Karafuu ilileta shilingi bilioni 50. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? Ukiangalia zile top ten unakutana na sekta ya kilimo kwenye uchumi wa nchi wetu. Pamoja na mchango wa kilimo kwenye uchumi wa nchi yetu, bado wakulima wadogo wadogo wana changamoto nyingi sana ambazo
tunaiomba Serikali yetu itusaidie kwa haraka sana kuzitatua changamoto hizi. Changamoto ya kwanza ni ya pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru Serikali inatusaidia pembejeo kwenye kilimo cha mazao ya chakula, lakini ukifika kule kwangu Mbinga Mjini. Mbinga Mjini imegawanyika katika maeneo mawili. Kuna milimani ambako tunazalisha Kahawa na mabondeni tunalima mahindi,
lakini wote hawa ni Watanzania, wote hawa wana mchango kwenye uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwa watu wa kule Mondeki, Miyangayanga, Luwaita, Utili kwenye milima kule, wale watu wanalima Kahawa, hawawezi kulima mahindi. Kutokuwapatia ruzuku ni kuwafanya wadumae na mwisho wa siku kilimo kitakuwa mzigo baada
ya kilimo kuwa msaada kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni ukosefu wa centers za kufanya utafiti ambazo tunaweza tukajua eneo hili mbegu gani inaweza ikafaa, eneo hili aina gani ya mbolea inaweza ikafaa, mwisho wa siku tuweze kuleta kilimo chenye tija. Tukiulizana hapa sasa hivi ni maeneo
gani, kuna hizi research centers ziko kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa eneo husika, jibu utakalolipata litakuwa bado viko kwenye mchakato au vimekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ukosefu wa wataalamu, hawa tunaowaita Mabwana Shamba na mabwana mifugo. Tuzunguke kule vijijini tuulize lini Bwana Shamba alikwenda kumsaidia mkulima aweze kupanda kwa wakati, aweze kufanya palizi yake kwa
wakati na kumpatia ile elimu ya kilimo bora. Utakuta kwenye sekta hii, sehemu ya wataalamu, Mabwana Shamba na Mabwana Mifugo hatujafanya vizuri sana. (Makofi)
Lingine ni kushuka kwa bei ya mazao. Mkulima analima kwa nguvu zake mwenyewe. Inapofika masuala ya bei, haitabiriki. Pembejeo ziko juu, gharama za uzalishaji ziko juu. Matatizo haya yote yanasababisha kilimo kidumae na malengo tunayotaka ya kuajiri asilimia 75 ya Watanzania wote kutoka vijijini kwenye Sekta ya Kilimo, Mfugo na Uvuvi itapata tatizo kubwa. Changamoto nyingine inayotokana na hili eneo la kilimo ni kodi na tozo mbalimbali zinazowaumiza wakulima. Ukienda kwenye zao la kahawa, kodi na ushuru unaotozwa kwa wakulima unawatesa sana. Unakuta kuna kodi inaitwa Tanzania Coffee Research Institute ambayo ni 0.75, halafu kuna kodi nyingine inaitwa Tanzania Coffee Development Fund ambayo mkulima anatozwa 0.10 kwa kila kilo.
Lingine, kuna leseni ya TCB. Leseni ya TCB kabla ya mwaka juzi ilikuwa ni dola 24, sasa hivi imefika kuwa dola 24,000. Hivi mkulima wa kawaida atawezaje kwenda sambamba na ongezeko hili la dola kwenye TCB? Hali inakuwa ngumu sana. Naiomba Serikali, ili kumwongezea Mheshimiwa Rais nguvu ya kuleta maendeleo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mapunda, muda umekwisha!
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kuendelea bila kuwa na mambo manne yafuatayo:-
La kwanza, ni uwezo wake kukusanya kodi; la pili, nidhamu ya kutumia kile ilichokusanya; la tatu, kujenga mazingira ya kodi endelevu yaani kodi isiyo ya muda mfupi, kutengeneza mazingira wananchi waendelee kulipa kodi kwa wakati wote; na la nne ni kutengeneza mazingira mapya ya kupata kodi mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya Awamu ya Tano imeonesha nia ya dhati, imeonesha dhamira ya dhati kwenye haya niliyoyasema kwa kiwango kikubwa sana. Tumeona mikakati ya kubana mianya ya wakwepa kodi, lakini tumeona mikakakti inayopelekea kukusanya kodi kwa wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tumeiona Serikali hii katika mipango yake imeelekeza asilimia 40 kwenye shughuli za kimaendeleo, hii ndiyo inakuwa tafsiri sahihi ya kuelekeza kile ulichokikusanya kwenye eneo sahihi, yaani shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maamuzi haya ya Serikali ya Awamu ya Tano kwenye hii bajeti si madogo, ni kwa mara ya kwanza imewekeza pesa nyingi kwenye shughuli za kimaendeleo. Sisi Waheshimiwa Wabunge katika ujumla wetu ni wajibu wetu kuishauri Serikali na kwa wingi wetu tuna uhakika tukipeleka sauti yetu kwa Serikali watatusikiliza. Ndugu zangu Walatini wana methali yao, huwa wanasema quot capita, tot sententiae wakimaanisha kwenye wengi hapaharibiki neno. Huu wingi wetu wa Waheshimiwa Wabunge ndani ya Bunge lako Tukufu tukiipitia hii bajeti katika ujumla wake, tuna mawazo mazuri ambayo tunaamini Serikali wakiyabeba yatatufikisha kule tunakotaka kwenda kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeainisha mambo mengi, kwa asilimia kubwa ni mazuri sana, lakini kuna mengine machache inabidi tuyaboreshe kidogo na tuiombe Serikali iwe flexible kwenye kutusikiliza. Wasione ugumu kuyapokea yale tunayowaeleza, nia yetu ni njema kama wao walivyokuwa na nia njema, kama wenzetu wanavyosema quot capita, tot sententiae, palipo na wengi hapaharibiki neno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya mambo ambayo Mheshimiwa Waziri amekuja nayo mazuri, nimependa wameondoa tozo na ushuru kwenye Sekta ya Kilimo. Wameondoa kwenye korosho, pamba na kahawa, lakini nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwenye zao la kahawa, ameondoa kodi moja, leseni ya kusindika kahawa ya Dola 250, lakini siku zote tumekuwa tukisema na Mheshimiwa Rais amezunguka kwenye kampeni yake nchi nzima ameeleza wakulima wa kahawa wanasulubika sana, wana kodi na tozo 26.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ameiondoa moja tu Mheshimiwa Waziri, nimwombe, tulisema kuna ushuru wa halmashauri wa asilimia tano, tuliomba Serikali shusheni angalau uwe wa asilimia tatu ili wakulima wetu wapate ahueni. Kuna leseni ya kununua kahawa ya Sh. 300,000, kuna tozo ndogondogo, kama sisi kule kwetu Mbinga kuna tozo ya Sh. 20 kwa kila kilo kwa ajili ya wale wadudu vidung’ata, kuna leseni ya Bodi ya Kahawa ya Dola 1,024. Kuna tozo ya TACRI ya asilimia 0.75 kwa kila kilo ya kahawa, kuna mchango wa Tanzania Coffee Development Fund (TCDF) wa 0.10, kuna ushuru wa ulinzi zaidi ya 200,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hayo yote tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri ile Dola 250 waliyotoa ya usindikaji ni ndogo sana kwa wakulima wa kahawa, aziangalie zile kodi zote katika ujumla wake, akifanya hivi itampendeza Mungu na akifanya hivi maendeleo tutayapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tunatoa misamaha ya kodi, lengo la Serikali kutoa misamaha ya kodi si kupunguza mapato yake, ni kutengeneza mazingira yule mtu ambaye anasamehewa aende akawekeze au akafanye jambo lingine ambalo litaleta kodi nyingi kwa watu wengi kwa wakati mmoja, ndiyo maana Serikali imekuwa na utaratibu wa kutoa misamaha ya hizi kodi ili kutengeneza mazingira mazuri ya kukusanya hizo kwa mlango mwingine, hiyo ndiyo maana na dhamira ya dhati ya kuweka hiyo misamaha ambayo Serikali imeiweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mpango wa kwenda, tena kwa kiasi kikubwa kwenye maendeleo ya kiwango cha hali ya juu ya viwanda. Viwanda haviwezi kufika kama Serikali haitakusanya mapato, viwanda havitaweza kufika kama Watanzania hawatakuwa na uwezo wa kujiletea kipato na kuweza kujikwamua katika maisha yao ya kila siku. Kwa sababu viwanda vinahitaji kwanza mashine kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine viwanda vinahitaji raw material, hawa wakulima lazima wawe na uwezo wa kuzalisha sana pamba, wawe na uwezo wa kuzalisha kahawa, wawe na uwezo wa kuzalisha katani, wawe na uwezo wa kuzalisha tumbaku ili viwanda vyetu viendelee kujiendesha kwa muda wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya mambo yote ndiyo inakuja ile hoja ya tatu kwa Serikali makini ambayo inataka maendeleo; lazima itengeneze mazingira kwa wananchi wake waweze kulipa kodi kwa wakati wote. Hawawezi kulipa kodi kama wana mazingira magumu ya kuzalisha. Ndipo namwomba Mheshimiwa Waziri na timu yake, najua Serikali ya CCM ni sikivu, Serikali ya Awamu ya Tano ina maono, inatufikisha mbali, wakakae na timu yake akirudi aje atuelezee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo Mheshimiwa Waziri alilisema juzi kwenye hotuba yake, sasa anaingiza VAT kwenye utalii. Hili jambo ni jambo zuri sana, lakini nilipoisoma hotuba yake inasema reference kwanza tuliweka sheria mwaka jana, tulikuwa na mikataba tukasema mwaka huu tuimalize halafu tuendelee, lakini amei-refer Kenya wenzetu wameiondoa, ami-refer Rwanda, amei-refer South Africa; juzi wenzetu wa Kenya wameiondoa VAT.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, aende akaangalie kitu gani kilitufanya sisi tusiiweke, kitu gani kimewafanya Kenya juzi waiweke, ili aitazame katika mapana yake, siyo kwa sababu tu South Africa wanafanya, kwa sababu tu Rwanda na Kenya wananfanya, sidhani kama ilikuwa ni dhamira.
Mheshimiwa Naibu Spika, nahisi Mheshimiwa Waziri ana hoja za kutosha za kutushawishi sisi tuamini au tuelewe kwamba kuweka ile kodi ya VAT kwenye utalii itatuongezea mapato sio kutukimbizia. Tukumbuke kwa sasa utalii unatuletea Dola karibu bilioni 2.5 kwa mwaka jana, 2015. Nadhani hii ilitokana na sisi tulikuwa na mazingira mazuri ya kuwezesha watalii wakafanya kazi. Leo hii wenzetu Kenya, wanasema ile the last token tuliyokuwa nayo inayomzidi Kenya kwenye ushindani, mwenzetu ndiyo kaibana ile, ameondoa sisi tumeweka, naomba Mheshimiwa Waziri alitazame hili kwa mapana zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, Mheshimiwa Waziri alisema sasa tutakwenda kutengeneza sheria ambayo itaondoa misamaha kwa taasisi za kidini. Hii naomba niseme kidogo na nimuunge mkono ndugu yangu, Mheshimiwa Richard Ndassa aliyeongea juzi. Hili jambo Mheshimiwa Waziri tulitizame kwa mapana kidogo. Unajua haya madhehebu ya kidini huduma wanayotoa ni huduma, hawafanyi biashara. Wamewekeza kwenye hospitali, wamewekeza kwenye elimu, wamewekeza kwenye maji safi na salama, wamewekeza kwenye shule, ndiyo kazi wanayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kumwambia mtu leo, anataka alete mashine ya CT Scan kwenye hospitali ile ya mission au ile ya taasisi ya kidini, alipe kwanza ushuru wote halafu baadaye tufanye assessment arudishiwe, nina uhakika hawatanunua hizo mashine, kwa sababu kwao kazi yao ya kwanza si huduma za kijamii, wao kazi yao ya kwanza ni kumtumikia Mungu na kuleta injili na kupeleka aya ili wanadamu wamfikie Mungu, ile wanatusaidia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkizingatia haya maeneo yote ninayoyasema, nendeni mkaangalie zahanati zilikojengwa, hospitali zilikojengwa; mnaikuta Mvumi kule, utaikuta Hospitali ya Mvumi, nenda Lugarao utaikuta kule, nenda Ikonda, nenda utakuta Hospitali ya Peramiho, Hospitali ya Ndanda, Hospitali ya Lituhi, Hospitali ya Litembo, Hospitali ya Ifakara; hizi zote zinatoa huduma na nawaambia kabisa ukifika kule unajikongoja una shida, wanaweza wakakuhudumia hata bila kukutoza halafu uje uwalipe baadaye, hiki kitu hakipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali, kwenye suala la afya tuwape msamaha, kwenye suala la elimu tuwape msamaha na kwenye suala la maji safi na salama. Kwa mfano kwangu mimi kule Mbinga, toka dunia imeumbwa maji ya kwanza ya kunywa yalikuwa ya Buruda Otmar, (Brother Otmar) leo hii akitaka kubadilisha mabomba eti alipe kwanza ushuru sisi tupate maji safi na salama. Mheshimiwa Waziri, namwomba sana kwa dhati ya moyo wangu, alitazame hili jambo vizuri sana, sisi tulioko humu ndani nia yetu ni njema sana, hatutaki watu wakwepe kodi na tutashirikiana nao wasikwepe kodi, quot capita, tot sententiae. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia asubuhi hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sio muumini wa ushirikina ingawa kuna wengi wanaamini katika ushirikina. Kila nikiangalia mazingira rafiki yenye kuvutia, yenye uwezo wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kuanzia ukubwa wa ardhi yenye uwezo wa kustawisha mimea ya kila aina, aina ya mifugo tuliyokuwa nayo, idadi ya watu, kwa maana ya soko la ndani, malighafi muhimu kwa maana ya chuma, makaa ya mawe na madini utayataja kadri utakavyoweza, uwepo wa bandari kubwa tatu zenye uwezo wa kufanya kazi katika standard za kimataifa na bandari nyingine ndogo ndogo kwenye maziwa na bahari isiyokuwa na idadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi imekaa vizuri kimkakati, inazungukwa na nchi nane ambazo zote zinatutegemea. Tuna mtandao mzuri wa barabara za lami ambao nchi za Afrika Mashariki na Kati hakuna nchi hata moja iliyounganishwa vizuri kwa mikoa na wilaya kama nchi yetu, na bado tuna reli na tunaendelea kutengeneza reli ya kisasa ya standard gauge. Kwa hizi sifa zote nzuri tusipokuwa na viwanda vya uhakika napata shida na ndiyo maana ninasema huenda tumerogwa. Kama huyo aliyeturoga sijui ni nani na kama kuna mganga wa kutugangua huko tulikorogwa basi atusaidie. Haiwezekani tukawa na nchi nzuri kama hii, yenye haya mambo mazuri yote leo hii tunasua sua kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote zilizokua kiviwanda dunia nzima zilianza na mahitaji ambayo wananchi wake wanayahitaji sana. Nchi ya Ujerumani ilipoanza viwanda ilianza na makaa ya mawe na chuma; nchi ya Uswisi ilipotaka kukua kwa viwanda ikaanzisha viwanda vidogo vidogo vya jibini, maziwa pamoja na mboga mboga; nchi ya Uholanzi ilipotaka kukua kwa viwanda ilianza kwenye maua na mboga mboga; nchi za China na India zilipotaka kukua kiviwanda zilijielekeza kwenye viwanda vya nguo. Kila nchi inakuwa na ajenda mahsusi inapotaka kwenda kwenye viwanda kulingana na mahitaji halisi ya watu wake, lakini vilevile kwa soko linalowazunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina bahati ya kuwa na ajenda mahsusi ya viwanda. Tanzania ya viwanda ni national strategy ambayo wimbo huu ukipigwa unapaswa uchezwe na kila Mtanzania na katika tune ya ule muziki uliochezwa. Tunachokiona kwenye huu mkakati mkubwa wa kitaifa wa kuifanya Tanzania ya viwanda ni kana kwamba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inacheza muziki wake na wengine hao ambao inabidi waifanye hii Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji iende vizuri nao wanacheza muziki wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mwaka wa tatu sasa ta Tanzania ya viwanda. Sikilizeni bajeti zote hapa, tutaanza na Wizara ya Kilimo, wapi mtu wa kilimo ana-link mipango yake ya kilimo na viwanda tangu mwaka 2016 wapi ana- link, anakuja na mkakati wa kilimo unaoenda sambamba na Tanzania ya viwanda. Twende kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi yote watakayosema na hotuba zao watakazozitoa wapi wana-conclude kwa kufanya moja, mbili, tatu kwenye kilimo, mifugo na uvuvi. Hapa sasa ndipo dirisha la kutokea kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye Ardhi. Mikakati ya mashamba, mikakati ya kurasimisha maji, wapi tuna-link ardhi na viwanda. Twende kwenye elimu, tutakwenda kutengeneza viwanda nchi nzima, mafundi michundo wako wapi? Wapi tume–link VETA na Tanzania ya viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa haya yote hayawezi kwenda bila fedha. Ili twende kwenye Tanzania ya viwanda namba moja sasa mwezeshaji huyu fedha ndiye a-pump pesa kwenye haya maeneo manne niliyoyatoa ndipo hatimaye mtapata viwanda. Waziri wa Fedha asipoelekeza nguvu zake kwenye kilimo, asipoelekeza nguvu zake kwenye mifugo, asipoelekeza nguvu zake kwenye elimu hiyo Tanzania ya viwanda haiwezekani. Nilianza kwa kusema mwanzoni zile sifa nne/sita za Tanzania zina kila kitu kizuri, kwa nini hatuendi? Ndipo tunaishia kusema kwamba pengine tuanze kuamini na ushirikina, pengine tumerogwa na kama kuna mganga aje atugangue, sitaki kuamini hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchawi wa Mtanzania ni Mtanzania mwenyewe na mganga wa Mtanzania ni Mtanzania mwenyewe. Tunachohitaji sasa hivi ni kuthubutu kwa dhati, Watanzania wote tucheze tune moja, Watanzania wote tupate uelewa. Leo hii tunaongelea Tanzania ya viwanda, leo hii tunaangalia Tanzania ya viwanda yenye changamoto nyingi, lakini mahitaji yetu sisi hatukuwahi kujitosheleza kwa kila kitu. Tuanze tu na sembe, tunalima mahindi kule Kusini, tunalima Rukwa mahindi, mahindi yanafika yanatujalia hatuna uwezo hata wa kuyafanya yale mahindi angalau yasubiri misimu miwili kuangalia soko linakwendaje au tunasaga kwa kiasi gani kuwasaidia na majirani zetu. Kwa hiyo, tutakwenda kwa mwaka mmoja hatuna maghala, mahindi yataoza mwishowe tunaharibikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachotaka kukisema, sisi tuna changamoto nyingi lakini zote zinatibika. Tulivyotaka kutengeneza standard gauge hatukujadiliana na mtu tukaanza tu kwenda, hali kadhalika viwanda tunavyotaka kuweka. Tunapozungumzia Mchuchuma na Liganga hatuhitaji tena maneno kwa sababu tuna uhakika Tanzania ya viwanda inahitaji umeme wa kutosha, inahitaji chuma cha kutosha. Sasa Mchuchuma na Liganga tuna yote mawili kwa wakati mmoja. Una-caal hapo hapo na una-steel hapo hapo na ukienda kusoma kwenye historia za nchi zilizokuwa kwa viwanda unakuja kukuta Ujerumani walianzia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii huu ukanda wetu huu tunaongelea ile story ya mafuta, sijui mchikichi, sijui alizeti, hivi tunashindwaje leo kuwaambia jamani JKT hebu kaeni, Magereza kaeni, wataalamu wa SUA hebu fanyeni breeding nzuri ya mbegu ya alizeti au mbegu ya mchikichi tuiweke ndani ya miaka mitatu/minne tusiwe na tatizo la mafuta au tunaongelea mambo ya sukari? Sitaki kuyasema haya, yamesemwa sana. Tanzania ya viwanda ianze na yale mahitaji. Tunakwenda kwenye nyama Tanzania yetu ni nchi ya pili kwa kuwa na ng’ombe wengi Afrika, lakini tujiulize maeneo yote ambayo wanahitaji nyama kwenye mahoteli nyama zinatoka wapi? Sasa hivi tunaongelea suala la maziwa, hatuna sehemu ya ku-process maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tutakwenda kwenye msimu wa nyanya, Waheshimiwa Wabunge, ninyi ni mashahidi mnapita hii njia mnafika pale Dumila, mnakuta nyanya zimemwagwa pale chini, nyanya zinauzwa mpaka shilingi 200 na hakuna mnunuaji. Hivi kweli tumeshindwa hata kuwasaidia kuwapa mawazo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kitu kimoja, Mheshimiwa Mwijage usidhani kwamba Watanzania unaposema viwanda wanaelewa kama unavyoelewa wewe. Wenzako wanaelewa kwamba wewe ndiye mwenye ajenda ya viwanda, wewe utawapelekea mashine na si kwamba wao wafikiri kulingana na mazingira yao. Hata hivyo ukitoa tafsiri ya viwanda, kama ulivyotuwekea, kwamba viwanda vinatokana na ile hali halisi ya watu kuyaona mazingira yao, wakaziona fursa, wakatatua shida zao kulingana na mazingira yao jinsi walivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa hivi ukiondoa hizo efforts zako unazozifanya kwenye viwanda, tengeneza timu maalum ya kufanya industrial mapping. Hiyo industrial mapping itanguliwe na research. Uwe na kitengo maalum kifanye tafiti eneo gani yanastawi mazao gani, eneo gani tukiweka kiwanda cha aina gani kitakwenda vizuri. Tukifanya hivi mambo yetu yatakwenda vizuri, bila kufanya research sasa na kujua ajenda ya viwanda si ajenda ya hiari. Hii ajenda ya viwanda ni ajenda ya lazima kwa sababu ndiyo National Agenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi leo tunasema Awamu ya Tano tuna ajenda gani, ni Tanzania ya viwanda hatuna ajenda nyingine. Sasa Tanzania ya viwanda ambayo hatuna mkakati wa viwanda, hatuwezi kwenda, uwe ni wimbo wa nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikupe mfano tu Tanzania tuna uzoefu wa kuamua na kufanikiwa. Mimi nina mifano miwili ambayo naijua kabisa tuliwahi kuamua na tukaenda. Siku tulipoamua kuweka standard gauge hatukuulizana na mtu tukaweka ikaenda. Siku tulipoamua kuifanya UDOM iwe university tukaamua tukaenda. Mimi nina imani mambo haya yote yanachohitaji ni kitu kimoja tu kuamua, kutenda na kutekeleza.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nami nafasi ya kuchangia kwenye Muswada huu asubuhi ya leo. Kabla sijajikita kwenye vifungu, naomba niweke kumbukumbu sahihi kwenye Bunge lako Tukufu. Chama cha siasa ni taasisi kubwa sana. Chama cha siasa ndiyo taasisi inayotoa uelekeo wa nchi katika maana ya uongozi na kupanga mambo yote ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chama cha siasa ndiyo walezi wa viongozi. Kwa namna yoyote ile, chama cha siasa kinahitaji kuwa na wanachama. Siyo tu kuwa na wanachama, kuwa na wanachama wanaojulikana na wanaofahamika kwenye nyaraka zao za chama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa sana, nchi yetu ya Tanzani tupo milioni 50 na ushee. Tunaofanya kazi za kisiasa katika maana ya idadi ya wanachama wa vyama vyote 19 vilivyosajiliwa, hatufiki milioni 13.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa sana, katika nchi yetu ya Tanzania tuko milioni hamsini na ushee, tunaofanya kazi za kisiasa katika maana ya idadi ya wanachama wa vyama vyote 19 vilivyosajiliwa hatufiki milioni 13. Chama cha Mapinduzi kina zaidi ya milioni nane na hawa wote wapo kwenye register, Kanisa Katoliki duniani kina wafuasi wake dunia nzima na register ya Wakatoliki yote ipo Roma, ni ajabu sana, ni ajabu sana mwanasiasa anayetarajia kuwa kiongozi aseme kuwa na idadi, kuwa na majina ya wanachama wake ni jambo dogo. Hili jambo si dogo hata kidogo, tunataka tuongoze chama cha aina gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, waungwana wana sema historia ni Mwalimu, naomba hoja yangu niijenge ni kijikita kwenye historia ya chimbuko la demokrasia ya nchi yetu. Mnamo mwaka 1992, nchi yetu iliamua kwa makusudi kuanzisha mfumo wa vyama vingi uliotokana na sheria ya vyama vya siasa mwaka 1992 na imefanyiwa marekebisho mara saba na leo haya yataenda kuwa ya nne, miaka 26 ni mingi sana na inatosha kwa Taifa letu kufanya tathmini na kuona tunakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 92 nchi yetu ilipoamua kwenda kwenye mfumo wa vyama vingi ilikuwa na malengo makubwa matatu. Lengo la kwanza tulikwenda kwenye mfumo wa vyama katika vingi ili kupanua demokrasia ya nchi yetu. Jambo la pili, tulikwenda katika mfumo wa vyama kwa ajili ya kuimarisha umoja wetu kama Taifa na jambo la tatu tuliamua kwenda katika mfumo wa vyama vingi ili kuifanya nchi yetu iwe huru na iendeshwe kama Taifa huru linalojitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka 26 tafiti zimeonesha vyama vyetu vya siasa katika ujumla wake vingi havikuwahi kuendeshwa kidemokrasia ingawa lengo la msingi ilikuwa ni kuendeshwa kidemokrasia. Jambo la pili, watafiti wanakwambia umoja wa kitaifa wa nchi yetu katika kipindi hiki cha miaka 26 umekuwa unayumba ukilinganisha na tulipokuwa na mfumo wa chama kimoja. Katika hali ya kawaida kwa watu ambao wenye pumzi zenye uhai, lazima wajitafakari, nchi yetu imejitafakari imeona miaka 26 kuna hitilafu kwenye hii sheria, inahitaji iongezewe nguvu ili iende sambamba na matarajio tulioanzisha 1992, kuifanya nchi yetu ikue kidemokrasia, kuifanya nchi yetu iwe na umoja wa Kitaifa, kuifanya nchi yetu iwe huru na ilinde uhuru wake na isiingiliwe na mtu yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu unakuja kuvifanya vyama vya siasa viendeshe shughuli zake kwa ubora zaidi na kulinda demokrasia, kifungu cha Muswada cha 6(1) – (5) kinaweka mambo ambayo yatavifanya vyama vya siasa vifanye kazi yake vizuri kwa kulinda demokrasia ya nchi na demokrasia ya vyama vyao. Hivi nani asiyejua kulikuwa kuna utaratibu mtu akikaa akiona mwaka huu ni uchaguzi pengine nitaguswa guswa mimi kama Mwenyekiti basi hahitaji mkutano mkuu, wanakutana wahuni wachache wanabadili Katiba. Sheria hii inakwambia mamlaka ya kubadili katiba ni ya mkutano mkuu, , hii ni experience ya miaka 26 ya uholela. Uholela ukizoeleka sana unakuwa uholela halali na tusiifikishe nchi kwenye uholela halali.

Muswada huu unakwenda kuimarisha muungano na kuvifanya vyama vyetu viwe vyama vya kitaifa, nani asiyejua, nani asiyejua kuna utaratibu mpya anachukua kachama kake kwenye mkoa fulani akatafuata watu watatu akapata usajili. Kwa sheria hii sasa utatakiwa uwe na wanachama 200 nusu ya Tanzania Bara na sharti upate Mkoa mmoja wa Pemba na Mkoa mwingine wa Unguja. Hiyo ndio spirit behind, huu ndio moyo uliotufanya tuingie katika mfumo wa vyama vingi, tuwe chama cha kidemokrasi cha Kitaifa. Siyo unakuwa chama cha kidemokrasia Mwenyekiti baba, Katibu mama, Mtunza Fedha mtoto na mjomba ndio anakuwa pale Mwenezi; hatuwezi kwenda kwa style hiyo. Miaka 26 imetupa haya mafundisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu unatutengenezea utaratibu mzuri wa udhibiti wa rasilimali za chama na udhibiti wa rasilimali za umma zinazotokana na ruzuku. Hapa naomba tuelewane vizuri, hapa hatuongelei ruzuku ambayo Mheshimiwa Halima Mdee amesema, hapa tunakwenda zaidi ya hapo, kuna vyama Mwenyekiti ndiye
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Chama, anatoa hela kwenye mfuko A anapeleka kwenye mfuko B. Ikumbukwe meli ya chama ni wanachama na wanachama ni Watanzania tulivyoamua kujiweka ili tueleze mambo yetu yanayotugusa kwa kupitia vyama vya siasa haiondoi kwamba kile chama cha siasa kina hati miliki ya Mwenyekiti, wanachama wana haki na wangapi wamelalamika, wakilalamikia viongozi wao kwamba wanakula ruzuku na mengine, mara ngapi wamelalamika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara ngapi wamelalamika kwamba viongozi wao wanawakopesha hela zile zile za ruzuku halafu wanawalipa, mara ngapi? Mbona wanajitoa fahamu kwenye hili, Mheshimiwa Mwenyekiti huu mfumo ndio unatufanya sisi tuwe viongozi wanachi, tukaguliwe, tusimamie rasilimali zetu na tusimamie rasilimali za watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu unalinda maslahi mapana ya nchi, naomba nirudie, maslahi ya mapana ya nchi. Nchi yetu ni bado Taifa changa sana, linabidi kulelewa na kutunzwa, rasilimali zetu hizi zinapaswa kulindwa na kutunzwa na viongozi ambao tunawajua pasipo kuwa na shaka lolote ni Watanzania safi. Naomba ileweke kifungu cha 6B(a) hata kama wakikipotoshwa katika maana yoyote kinasimamia maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu, watasema lakini mwishoni tukitoka nje tutakubaliana ndio mwarobaini wa kuondoa uhasama unaotakokana baina ya vyama vya siasa. Kwa sisi ambao tumefanya hizi chaguzi nyingi na ndugu zangu mtakuwa mashahidi, ilifika hatua vijana wetu badala ya kutulinda wanageuka kuwa wanamgambo kama Al- qaida. Tunakwenda kwenye chaguzi vijana wanamwagiana tindikali, tunakwenda kwenye chaguzi vijana wanakatana masikio, wanakatana migongo for the extent of the party. Hii sheria inakwenda kuwaondoa hawa, si lugha nzuri, wahuni kama kiningiki vile, inaondoa hawa wahuni kukifanya chama kiwe chama cha kisiasa, maana yake uhuru tulioupata kwa kuongea tukiwatengeneza vijana wetu wawe wanamgambo, leo hawana silaha ila kuna siku wakiwa na skills silaha kwa kuipata watajua wao wenyewe. Nishukuru sana Muswada huu unatuweka sisi na wenzetu tuwe tunakaa vizuri bila kugombana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine Muswada huu unakwenda kutatua matatizo na migogoro inayoendeshwa na vyama vya siasa. Ninyi mtakuwa mashaidi, rafiki yangu Mheshimiwa Bobali atakuwa shahidi, Mheshimiwa Ally Saleh atakuwa shahidi, wote wanajua kilichotokea kwa CUF A na CUF B. Msajili alipowaambia nipeni nyaraka za kumfukuza kiongozi wetu, hakuna hata mmoja aliyeweza kutoa muhtasari. Leo Msajili anakuja kuwaambia jamani tunzeni nyaraka za vikao vyenu pamoja na maamuzi ili yakiwa magumu mkirudi kwangu niwaambie kuwa haya ni maamuzi yenu, leo hawaelewani, mbingu na dunia havikutani, CUF Lipumba na CUF Maalim ni vurugu tupu kwa sababu ya hiki kifungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuweka hiki kifungu tuna uhakika vyama hivi sasa vitakuwa na utaratibu mmoja. Nazidi kukumbusha hawa sio malaika ni binadamu kama sisi na sifa ya kuwa binadamu, binadamu wana sifa kubwa mbili; sifa ya kwanza ni furaha na sifa ya pili ni machungu. Mtu akibanwa katika machungu hutafuta njia yoyote kuwa na furaha. Tumethibitisha katika kuendesha vyama vyao, haviendeshi kidemokrasi ushahidi upo, tumeona wamekuwa na migogoro isiyoisha ushahidi upo. Hakuna hoja yoyote ile itakayoweza kuja kusimama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya mwisho, Muswada huu unatupeleka kuwa Taifa huru linalojitambua, linalojitegemea na lenye uhuru kamili usioingiliwa na mtu yeyote ndani na nje ya nchi. Tumepata mfano kutoka nchi nyingi, elimu ya uraia imekuwa ikitumika kufarakanisha watu. Kuna mataifa ya kutosha yaliyokuwa kama paradise leo kama yamekuwa kama Somalia, wote mnajua nini kilitokea Libya, wote manajua nini kilitokea Tunisia, wote mnajua nini lilitokea Egypty. Hii yote ilisababishwa kwenda sehemu ambapo sipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii ya leo. Awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza Waziri Mkuu kwa jinsi alivyoitoa hotuba yake kwa umahiri na ufundi mkubwa, iliyogusa kila sekta. Hakika hotuba hii ime-reflect katika maana ya utendaji, hotuba iliyotolewa na Mheshimiwa Rais siku analizindua Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri Mkuu imegusa mambo mengi ambayo kama hayo yote tutakwenda kuyafanyia kazi kama alivyoyawasilisha hapa, nina uhakika ndani ya miaka michache nchi yetu itakuwa katika kiwango cha hali ya juu sana cha maendeleo. Niwaombe Mawaziri wote, kadiri Waziri Mkuu alivyoeleza kwenye hizo sekta, tuziongezee nguvu ili maendeleo kwa Watanzania yapatikane kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya mambo yote mazuri ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameyaeleza, kuna maeneo machache naomba nijikite ili kuiomba Serikali iongeze nguvu sana ili tuweze kuendelea kwa wakati.
Jambo la kwanza ameelezea nishati ya umeme. Umeme ni jambo muhimu sana kwenye maendeleo ya Taifa lolote lile. Tuko kwenye mfumo wa gesi na aina nyingine zote za umeme ambazo zimewekwa katika programu ya mwaka 2016/2017. Niwaombe sana mtusaidie na sisi watu wa Songea katika maana ya Mkoa wa Ruvuma kama mlivyoeleza kuweka mfumo mpya wa umeme wa gridi ya Taifa kilowatt 220 kutoka Makambako Songea na nina imani hautaishia Songea utafika Mbinga utakwenda mpaka Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala la viwanda. Suala la viwanda ni zito na ni kubwa sana na ni moja kati ya sera ya Awamu hii ya Tano. Kama tutawekeza kwenye viwanda hasa vile viwanda ambavyo vilisinzia na vingine vilikufa au vingine vinafanya kazi chini ya kiwango, nina uhakika ajira itapatikana kwa vijana na maendeleo makubwa yatapatikana kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Mbinga tuna kiwanda cha kahawa. Niiombe Serikali ikitazame kile Kiwanda cha Kahawa Mbinga na kiende hatua ya pili sasa kuweka kiwanda kingine cha Instant Coffee ili kahawa ile ikishakobolewa siyo lazima tuipeleke Brazil, India au Ujerumani, tutengeneze pale pale kahawa na sasa tuwe na kahawa made from Mbinga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niliongelee ni suala la afya. Kati ya changamoto ambazo zinatukabili kule Mbinga ni Hospitali yetu ya Wilaya. Hospitali yetu ya Wilaya ilianzishwa kama kituo cha afya. Kwa bahati nzuri maendeleo ya Mji wa Mbinga yakapelekea kuwa na Wilaya ya Mbinga ambayo baadaye ikazaa Wilaya ya Nyasa. Hata hivyo, hizi wilaya zote mbili, Wilaya ya Mbinga na Nyasa zinategemea Hospitali ya Wilaya ya Mbinga, Hospitali ya Mbuyula ambayo kwa sasa inahudumia Halmashauri nne za Nyasa, Mbinga Vijijini, Mbinga Mjini na sehemu ya Halmashauri ya Songea Vijijini. Niombe sana Serikali iwekeze kwenye ile hospitali ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ninayoomba Serikali iongeze nguvu ni kwenye huduma ya maji safi na salama. Ule mji unakua kwa kasi sana lakini mpaka sasa hatuna mradi mkubwa wa maji wa kuweza kuwasaidia wananchi wa Mbinga wanaoongezeka siku mpaka siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza hotuba nzuri sana ya Waziri Mkuu, nimepata muda kidogo kuisoma hotuba ya Kambi ya Upinzani. Hii hotuba ya Waziri Mkuu ina page 82, imegusa kila maeneo, hii iliyowasilishwa na Mheshimiwa Freeman Mbowe ina vi-page kama tisa vile, font ni kubwa sana na double space, haiwezi hata kidogo ikajibu hoja ya page 82. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiondoa hayo, ameiwasilisha hoja hii na amepotosha watu hapa kana kwamba watu hawasomi au hawafikiri. Nimwombe Mheshimiwa Mbowe akasome mambo yafuatayo. Kwanza, akaisome vizuri Katiba aielewe, akishaielewa vizuri akasome Sheria ya Bajeti, halafu vile vile akasome na Appropriation Act ya mwaka 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoongelea kutengeneza bajeti lazima uweke sheria itakayosimamia utekelezaji wa bajeti ile na sheria hiyo inaitwa Appropriation Act. Kwa muktadha wa shughuli yetu ya leo ile Appropriation Act ilikuwa ya mwaka 2015 ambayo ina section sita au kwa lugha nyingine ina vifungu sita. Katika vile vifungu sita kuna kifungu cha 6 kinasema mamlaka ya Serikali kubadilisha matumizi kadiri itakavyoona inafaa kwa maslahi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Mbowe alinukuu vipengele vya Katiba sasa mimi nimuambie Katiba ni sheria mama, inatafsiriwa kwenye sheria na ukitoka kwenye sheria ukafika kwenye bajeti utekelezaji wa bajeti unakwenda kwenye Appropriation Act. Sasa mimi nampeleka kwenye Appropriation Act ya mwaka 2015, kifungu cha sita (6) kinachosema, power of the Minister to reallocate certain appropriated moneys. Imeelezea kifungu cha kwanza (1) mpaka cha tano (5) ila kwa faida ya kikao hiki mimi nakisoma vizuri kifungu kile cha tano (5), kinasema hivi, nanukuu:-
“The Minister may, by certificate under this hand, reallocate any sums arising from savings in the Consolidated Fund to any of the purposes specified in the second, third and fourth columns respectively of the Schedule to this Act, and where this occurs, the provisions of section 3 and 4 shall take effect as if the total sum granted out of the Consolidated Fund and the amounts appropriated for the purpose specified in such certificate were raised by the amount or amounts specified in the certificate”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anachotuambia hapa ni nini? Anachotaka kutukoroga hapa ni nini?
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbowe aliongea kwa Kiingereza, mimi najua alikuwa na maana ya kupotosha watu wasielewe Kiingereza. Kwa Kiswahili kisichokuwa rasmi, Waziri ana mamlaka kwenye hii Sheria ya Bajeti tuliyoipitisha kwa maslahi ya nchi anaweza akaondoa kifungu kimoja under certificate kwa matumizi mengine yenye muktadha ule ule unaofanana kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuchukua pesa ambayo ilibaki kwenye matumizi from July, August, September, October ambapo Bunge halikuwepo tukaenda kununua madawati kwa mujibu wa sheria aliyetunga yeye mwenyewe na alikuwa amekaa pale, leo anajidai kasahau, huku kujisahaulisha kunatokana na nini? Niwaombeni, watu kama hawa tuwaangalie vizuri wenye ndimi mbilimbili, huku unauma huku unapulizia…
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Unafikiri sisi wote hapa ni matutusa? Humu hakuna zero, watu tunafikiri kwa kutumia vichwa, hatufikirii kwa kutumia matumbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba iliyowasilishwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba niungane na wale waliochangia jana kumpongeza Waziri kwa jinsi anavyofanya kazi zake vizuri na tukijua kwamba Wizara hii ni kubwa na ndiyo iliyobeba uchumi wa nchi yetu. Kwa jinsi anavyofanya kazi zake, nimpongeze na nitakuwa miongoni mwa wale watakaokuwa wanakesha Makanisani kumwombea awe na nguvu hizo ili matumaini kwa Watanzania walio maskini yapate kufikia katika kiwango kinachostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye kuchangia hoja hii kwenye mambo matatu. Jambo la kwanza ni suala la ruzuku ya pembejeo. Waziri ameeleza vizuri na amefafanua changamoto zilizojitokeza. Nimwombe atakapofika kufanya majumuisho aweke mambo yafuatayo ili angalau wakulima wapate faraja na wapate ahueni waweze kuiona kesho yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuweka ruzuku ya pembejeo lakini kimsingi ile ruzuku ukiitazama vizuri kuna maeneo haiwasaidii wakulima ambao wanatarajiwa. Ruzuku ile ya pembejeo kuna asilimia mkulima anapaswa kulipa ili apate ile seti ya mbolea ya kupandia, mbolea ya kukuzia, pamoja na mbegu, anatakiwa atoe hela wakati yeye hana hela. Ukiangalia kwenye tathmini nani ana sifa ya kupata ile ruzuku unajikuta yule ambaye anapelekewa hana uwezo hata wa kununua huo mfuko au nusu mfuko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara ifanye mambo yafuatayo:-
Kwanza ipeleke ile ruzuku kama mkopo mapema, ipeleke mbolea ya kupandia, ya kukuzia na ipeleke mbegu. Baada ya mavuno sasa wale wakulima ndiyo walipe ile gharama ya pembejeo. Tukifanya hivi hali itakuwa nzuri sana kwa wakulima wangu wa mahindi kule Lipilipili, Luangai, Masimeli, Ruvuma Chini, Mpepai, Mzopai na Kikolo. Ukiyafanya haya Mheshimiwa Waziri utawafanya watoke kwenye mstari wa umaskini waende juu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mbinga na hususan Jimbo la Mbinga Mjini limegawanyika katika maeneo mawili. Eneo la kwanza ni milimani la wakulima wa kahawa na eneo la pili ni bondeni ambao ni wakulima wa mahindi. Hawa wote ni Watanzania ambao wanahitaji Serikali kwa namna yoyote ile iwasaidie. Huo mfumo wa ruzuku ya pembejeo umeelekezwa kwenye mazao ya kilimo cha mahindi tu hawajaelekeza kwenye zao la kahawa. Wale ndugu zangu wa milimani hawakupenda kuzaliwa kwenye maeneo ambayo hayastawishi mahindi, ni Mwenyezi Mungu aliwaumba wakakaa kule milimani ambako ukipanda mahindi hayawezi yakastawi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali itazame hili kwa jicho la upekee kidogo, itoe ruzuku vile vile ya dawa na mbolea kwenye mazao ya biashara hususan kahawa. Tukifanya hivi, ndugu zangu wa kule Miyangayanga, Mateka, Mundeki, Luwaita, Kagugu, Sepukira, Utiri, wataweza kupata ahueni ya maisha yao na wataiona kesho yao katika hali nzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye sehemu ya pili ambayo wenzangu waliongelea jana kuhusu tozo nyingi zinazowakumba wakulima wa kahawa na wakulima wa mazao mengine. Kuwa specific, niliongelee zao la kahawa. Mnunuzi wa kahawa huwa analipia leseni kwenye Bodi ya Kahawa, analipa Dola 1,024 lakini akitaka kwenda kununua kahawa aidha amekwenda Mbinga, Mbozi au Kagera, akifika kule atakutana tena na leseni nyingine ya ununuzi wa kahawa kwenye halmashauri husika. Hizi gharama ambazo unampelekea mnunuzi wa kahawa zikisambaa zinakwenda kumuumiza mkulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiondoa gharama hii, kuna makato mengine hata ukiyatazama unashindwa kuyaelewa. Kuna gharama ya kulipia Tanzania Coffee Research Institute – TACRI ambapo kwa kila mkulima aliyeuza kahawa kwa kilo moja ya kahawa unailipia 0.075 kwenda kwenye kitengo hiki cha research. Vile vile wanakatwa kuna kitu kinaitwa Tanzania Coffee Development Fund ambayo ni 0.10 wanalipa kwa kila kilo ya kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza haya makato yakishatokea na ikatokea labda sehemu fulani wakulima wamepata magonjwa ya mlipuko, sijawahi kuona sehemu yoyote pesa inatoka kwenye hii Mifuko kwenda kuwasaidia wakulima. Matokeo yake wakulima wanatafutiwa mfumo mwingine wa kulipwa, wanakuwa double charged! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, hebu aangalie huo Mfuko kwa ajili ya maboresho ya kilimo cha kahawa unafanya kazi gani? TCDF, ile 0.10 anayokatwa kila mkulima kwenye kilo yake ya kahawa inaenda kufanya nini? Sisi kule Mbinga tumepata ugonjwa wa vidung’ata, kule wanauita viporomba, ukashambulia kahawa matokeo yake wale wakulima wakakatwa kila mkulima kwenye kilo yake kulipia hiyo na wakati walikwishalipa wakijua kabisa kuna Mfuko ambao utawasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni ushuru. Kwa mujibu wa sheria mkulima atapaswa kulipa 0% - 5% kwa kila kilo kwa ajili ya ushuru wa halmashauri. Hii range ya 0% - 5% imewekwa kwa halmashauri kuamua waweke wapi. Nimejaribu kuuliza hata kwa wenzangu wa Mbozi nao kule ni 5% haishuki, imebaki kwenye 5% pale pale nao wanaumia kama tunavyoumia sisi Mbinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanasababishwa na hizo tozo nyingi ambazo huko juu wanazichukua. Wakizichukua hizi tozo huko juu wanasababisha halmashauri zishindwe kuendeshwa na kwa sababu watu wa karibu ni wale wakulima, watawabana tu wakulima, hali hii haitaweza kuondoka hata siku moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni uhakika wa masoko na bei kwa mazao yote, mazao ya kilimo na mazao ya biashara katika ujumla wake. Kuna jambo nadhani hatujalifanya vizuri katika kutazama. Hivi tatizo la mkulima ni bei, uzalishaji au gharama za uzalishaji? Maana haya mambo matatu usipoyaweka katika level zake unaweza ukatatua tatizo ambalo si tatizo. Ukitizama kila mkulima analalamika, tumelima soko hakuna. Sisi tunakwenda ku-address soko na wakati tatizo ni gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachomfanya mkulima alalamike na anung‟unike ni ile pesa ambayo inaitwa mtaji, kaenda kuichukua kwenye SACCOS, VICOBA, UPATU, akaiingiza kwenye matuta yake mawili, mwisho wa siku anapata kidogo kuliko kile alichokiweka. Niiombe Serikali ijaribu kuangalia namna nzuri itakayowezesha kupunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima ili azalishe katika hali nzuri. Hata kama soko likiyumba badaye maumivu yanakuwa madogo sana kwa sababu, gharama ya uzalishaji ilikuwa ni ndogo kuliko ile gharama ya kuuzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii tena kurudia kwanza kumshukuru na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri aliyoifanya na anayoendelea kuifanya. Pili, nimshukuru na kumpongeza Waziri Mkuu kwa hotuba yake iliyoonesha uelekeo na kuonesha Serikali ya Awamu ya Tano itakwenda kufanya nini. Mwisho kabisa, nimshukuru kaka yangu Comrade Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba kwa kazi anayoifanya. Nikuombe kaka yangu wewe pigana, pambana kweli kweli lakini katika kufanya shughuli zako usisahau kutenga siku kadhaa twende Mbinga ukaone jinsi gani wakulima wanavyosulubika kule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Nimezifuatilia hotuba zile mbili vizuri na michango michache ya waliotangulia, wamenilazimisha kufikiri baadhi ya mambo ambayo ningependa niyaseme jioni ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijiuliza hivi kwa nini kulikuwa na Serikali? Nikajiuliza kwa nini kulikuwa na Polisi, Magereza, Bunge na Mahakama? Ikanirudisha nyuma kwenye kumbukumbu yangu kipindi kile ulimwengu ulipokuwa hauna utawala kwenye state of nature na human nature. Nikawakumbuka akina Thomas Hobbes walivyokuwa wanaongelea; nikawakumbuka akina John Locke, Montesk, Jean-Jacques Rousseau na wengine wengi walivyokuwa wanaelezea dunia ilikuwaje kipindi kulikuwa hakuna utaratibu uliopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema hivi, kabla ya kuwa na huu mfumo tunaouona leo dunia ilikuwa nasty, ilikuwa brutal, ilikuwa inakatisha tamaa. Maisha yalikuwa mafupi, vita ilikuwa kwa kila mtu, kwa yeyote. Tena Thomas Hobbes anasema kwa lugha ya Kilatini, katika kipindi kile kulikuwa na bellum omnium contra omnes, maana yake war of all against all, yaani vita ya wote dhidi ya wote. Ndiyo tukatengeneza huu mfumo. Huu mfumo ulivyotengenezwa ulikuwa ni kwa ajili ya ku-control tabia za wanadamu na hulka yake. Usipom-control, atatumia mamlaka yake vibaya. Mwisho wa siku unapata kile kitu kinaitwa survival for the fittest. Wenye nguvu na wenye mabavu wataendelea kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? nasema hivi ku-respond yaliyosemwa hapa na waliotangulia. Askari wanatumia nguvu zilizopitiliza katika kipindi cha chaguzi na wakaelezea maeneo na maeneo. Niwaambie kitu kimoja, kama wako makini, wao ndiyo wamewafanya Askari wafikie hatua hiyo, kutokana na ile ile hulka ya mwanadamu, akishajua kwamba hakuna kitu kinachom-control anafanya vitu vya ziada, anapambana katika jinsi anavyoona yeye mwenyewe inamfaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichotokea kwenye uchaguzi uliopita ambao mwenzangu ameusema pale wote ni mashahidi, nani ambaye alikuwa hajui kulikuwa na watu wanaitwa red brigade wakavalishwa kininja wakapewa mazoezi ya kupambana? Sasa mlitaka Askari waangalie red brigade wakiwa wamevaa kininja wamepambana ili nchi iwe ya makambale, vita of all against all. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wanafanya kazi yao vizuri, ninyi mnakwenda mnasema yale yasiyowezekana. Nawaombeni ndugu zangu tuelewane. Tusipofika kwenye hatua hiyo, tunarudi kwenye state of nature, tunarudi kwenye human nature. Vitu hivi lazima viwe regulated! Lazima vitengenezewe utaratibu ili twende vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na utaratibu huu wa migawanyo ya majukumu, hawa ndugu zetu Askari nao lazima tuwaangalie ili wafanye kazi zao vizuri, watulinde vizuri, ili tufike siku wafanye ile kazi inayotarajwa kuifanya nchi hii iwe nchi ya wote yenye amani inayofuata sheria na utaratibu. Wana mambo ya msingi, inabidi lazima nao tuwaangalie. Waliosema Askari kwake kambini, walikuwa wana maana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani leo Askari akatoka nyumbani kwa baba John alikopanga, akaenda ofisini, halafu anarudi akamkamate baba John, hiyo haiwezekani. Turudi kwenye utaratibu wa zamani kuwaandalia Askari maeneo ya kukaa na kuwapatia facilities zitakazowasaidia wakafanye operations zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi dakika zilizobaki ataongea Mheshimiwa Kingu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia asubuhi ya leo. Awali ya yote, nichukue fursa hii kama walivyosema waliotangulia kumshukuru sana na kumpongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Comrade William Vangimembe Lukuvi. Kwa kweli ukiitazama Wizara yake, ukitazama majukumu yaliyopo katika Wizara hiyo na jinsi anavyofanya kazi na ile flexibility yake ya kwenda kwenye migogoro ya ardhi, kwenye masuala yanayohusu ardhi kila kona ya nchi yetu, kwa kweli inatupatia matumaini makubwa. Huenda mwarobaini wa migogoro ya ardhi ndani ya nchi yetu umeshapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya ya utangulizi, naomba nijielekeze kwa kifupi kwenye mambo matano ambayo naomba Serikali iyatazame kwa kiwango cha hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ya nchi yetu ipo vile vile ila inapungua kutokana na shughuli za bahari, size inapungua, lakini binadamu wanaongezeka kila kukicha. Kwa hiyo, watu wanazaliana, wanaongezeka, lakini ardhi bado ipo vile vile. Tusipokuwa na mpango mahususi wa kuitazama Tanzania ya leo, ya kesho na ya miaka 50 ijayo, tutakuja kuzalisha migogoro ya ardhi ambayo tutashindwa kabisa kuja kuituliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona miji inakua, sasa hivi Jiji la Dar es Salaam limekua katika kiwango cha hali ya juu, sasa linatusumbua jinsi ya kupanga. Wapi upitishe barabara, ni shughuli! Wapi upitishe maji safi, ni shughuli! Wapi upitishe maji taka, ni shughuli! Wapi upitishe nguzo ya umeme, ni shughuli! Hata sasa tunapotaka kwenda kwenye huo mpango wa gesi ambapo inapita kama mtandao wa maji, tutashindwa kwa sababu kila utakayemgusa, utalazimika kumlipa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea Dar es Salaam lingekuwa ni kosa letu la mwisho kufanya kwenye miji mikubwa na miji inayofuata yote isiwe na matatizo ambayo yametukuta Dar es Salaam. Sasa tunaona majiji yanayokuja tena, yanapita kwenye matatizo yale yale ya Dar es Salaam. Nenda kaangalie Tanga, matatizo ni yale yale; Arusha inakuja kwa kasi, matatizo ni yale yale; Mwanza ndiyo kabisa, tena itafungana kuliko Dar es Salaam; nenda kaangalie Mbeya, matatizo ni yale yale. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri na Serikali, hii miji inayokua na ambayo mingine tuna-predict baada ya miaka 10 itakuwa miji mikubwa, tumalize mpango wa ramani ya miji. Miji ijulikane itakuwa na sura hii, tusirudi tena kwenye migogoro iliyopita huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii unaenda kutatua mgogoro wa Kigamboni; Kigamboni imekuwa darasa zuri sana kwenye mipango miji. Tupange mji, barabara itapita wapi, nyumba itakuwa wapi, uwanja utakuwa wapi na ikiwezekana twende kwenye hatua ya pili; na ramani ya nyumba pale iweje? Sasa atakapofika mtu apate kiwanja chake ajenge nyumba kwa mujibu wa ramani jinsi ilivyo. Tunazunguka nchi za watu, tunaona haya mambo yapo, siyo mageni. Namwomba Mheshimiwa Waziri alipe kipaumbele hili suala, litaweza kuja kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, hii Wizara ina changamoto kutokana na centers nyingi za decision making kwenye ardhi. Kijiji kina mamlaka, Halmashauri ina mamlaka, Wizara ina mamlaka. Ukiondoka kwa upande mwingine, unakwenda kwenye Wizara nyingine, ina mamlaka vile vile kwa mujibu wa sheria kwenye ardhi hiyo hiyo. Sasa matatizo ya Wizara moja au matatizo ya sehemu moja yenye mamlaka kisheria, yanaweza yakapelekea madhara kwenye eneo lingine.
Kwa mfano, migogoro ya ardhi kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi, unakutana na Wizara tatu ziko kwenye sakata moja; unakutana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, unakutana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi; unakutana na Wizara ya Maliasili na Utalii; unakutana na TAMISEMI tena nao wapo humu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi Wizara nne zisipokaa zikajadili kwa kina, zikaona baadhi ya sheria nyingine ambazo tunaona zinaleta migongano ya kimaslahi, migongano ya kimadaraka zifutwe, hatutatoka hapa. Leo hii ninavyoongea, kule Mbinga tuna mgogoro wa ardhi. Halmashauri inamiliki ardhi ina mamlaka ya kupima kama kawaida kwa mujibu wa sheria; kijiji kimemkaribisha mwekezaji kwenye ardhi ambayo wapo pale wanakijiji. Baadhi ya wanakijiji wamekubali kumpokea mwekezaji, wengine hawataki. Imekuwa ni mivutano mikubwa. Sasa Wizara huku juu wanaweza wakadhani kule chini mambo yanakwenda sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kigonsera, Kijiji cha Mihango, Waziri anaweza akaja akapatiwa maafa ambayo kwa kweli yatakuwa hayawezi kuelezeka kwa sababu pale wanakijiji wapo juu wanakasirika kwa nini mwekezaji anakuja? Tunatambua kwamba wawekezaji ni muhimu sana katika Sekta ya Kilimo, nami na-encourage sana waendelee kuwepo kwa sababu kweli kuna mambo mengi tunayapata kupitia hawa watu, isipokuwa uelewa wa watu wetu, ukoje. Hii mifumo ya mamlaka katika ardhi inakuwa ni kikwazo kikubwa sana kuiwezesha Wizara yako kufanya kazi smoothly katika speed ya Mheshimiwa Waziri. Nawaomba wafanyeni watakaloweza kulifanya, hao wanne ambao ni wadau wakubwa wa ardhi, wakae, wapange mpango mzuri, tukitoka hapo mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, migogoro mingi ya ardhi ndani ya nchi yetu ina uhusiano na nani mmiliki? Nani kapima? Kapima wapi? Kwenye Halmashauri zetu, wana mamlaka ya kupima ardhi, lakini uwezo wao wa kupima ardhi ni mdogo. Naiomba Wizara itengeneze program maalum ya kutafuta vifaa vya upimaji kwa nchi nzima. Ikishapata hivyo vifaa vya upimaji kwa nchi nzima, kwa sababu kila Halmashauri tuna Maafisa wa Mipango Miji, waende wapime ardhi yote kusiwe na mgogoro, eneo la makazi mtu akitaka kununua kiwanja aende sehemu tayari kimeshapimwa, akalipie apate hati yake, ajenge aendelee na maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwangu pale maeneo ya Lusonga, Mji sasa unakua ardhi haijapimwa. Ukienda Lusewa, Mji wa Mbinga unakua, hakuna kupima. Ukienda Mateka, Kilimani, Tanga, Luwaita, haya maeneo yote ya miji hayajapimwa. Kesho mji utakuwa mkubwa, tutakuja kwenye migogoro mikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nadhani litakuwa la mwisho, nisemee kuhusu ujenzi wa hizi nyumba za bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naipongeza Serikali kwa kuifufua sasa National Housing Corporation i-operate katika kiwango cha hali ya juu. Tunaona nyumba zinajengwa lakini zile nyumba hazinunuliki. Mtu wa kawaida hawezi akanunua kabisa, ni ghali! Mbaya zaidi, tumeingia katika mortgage financing, mtu anakwenda kukopa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba akajisitiri, anaenda kwenye mkopo wa riba kwenye hiyo nyumba; yaani unanunua nyumba una riba, Nationa Housing Corporation wamechukua vifaa kwa ajili ya ujenzi wa ile nyumba, wanakatwa Value Added Tax kwenye yale mambo, ukiyaweka yale yote gharama zinakuwa kubwa sana. Hii siyo njia sahihi ya kumsaidia mtu kwenye ujenzi wa nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kitu kimoja kifanyike. Kama Serikali, tumeamua sasa tujenge nyumba za bei nafuu, twende kwenye mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tuiwezeshe National Housing Corporation ijenge kwa pesa zake, iuze na ipangishe. Zile nyumba zilizokuwepo miaka ya 1960 na 1970 mbona ilikuwa hakuna mambo kama haya tunayoyaona leo! Tuna flats zipo kila sehemu, ukiuliza wanasema hii ya National Housing Corporation, kila Mkoa zilikuwepo! Namwomba Mheshimiwa Waziri, najua haya mambo anayaweza. Kaa na National Housing Corporation, wasikilize changamoto zao, waweke vizuri wajenge nyumba za bei nafuu ili kila Mtanzania sehemu ya kulala isiwe tatizo tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara asubuhi ya leo. Wizara ya Maliasili na Utalii ni miongoni mwa Wizara mtambuka inapokuja mahusiano yake na wakulima, inapofika mahusiano yake na wafugaji. Nchi yetu ina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 947,300. Kati ya hizo ardhi ambayo tunaweza kutumia kwa ajili ya kufuga, kulima, kujenga na shughuli nyingine za miundombinu ya kijamii ni takribani kilomita za mraba 885,800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilomita za mraba 61,500 ni kwa ajili ya water bodies, kwa ajili ya bahari, mito na maziwa. Kwa maneno mengine shughuli zote tunazozitumia kwa ajili ya ustawi wa maisha yetu, tunategemea kilomita za mraba 885,800 ambazo wakulima wanazihitaji hizo hizo, wafugaji wanazihitaji hizo na hifadhi wanahitaji hizo hizo. Ukifuatilia hotuba ya Mheshimiwa Waziri unakuja kugundua asilimia 33 ya hizo kilomita za mraba nilizozitaja ndiyo mbuga na hifadhi za misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tunaendelea kuongezeka kwa idadi kila siku na ng‟ombe wanazidi kuzaliana na kuongezeka kila siku. Katika hiyo 885,800 kilomita za mraba, kuna ukame unaikuta hilo hilo eneo, kuna mafuriko, lakini kuna shughuli nyingine za volcano kwa mfano kule Oldoinyo Lengai ikipiga volcano pale huwezi kulima, huwezi kufuga. Kwa hiyo, ardhi bado inaendelea kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hapa watu wamesema wafugaji wanahitaji malisho na hizi sababu nilizozitaja ndizo zinazowafanya wahamehame. Tumesahau kwamba na wakulima nao wanahamahama kutafuta chakula, kutafuta sehemu nzuri ya kulima kwa hoja hizo hizo kama za wafugaji. Tukisema leo tuangalie tu mgogoro kati ya wakulima na wafugaji kwenye sehemu ya malisho ya wanyama, tukienda kutazama mgogoro kati ya hifadhi na wakulima kwenye yale maeneo ya buffer zone kama maeneo ya Mto Kilombero, eneo lina rutuba nzuri wakulima wanakuja eneo la hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukienda upande wa selous kule wakulima wamekata miti wanaingia eneo la hifadhi. Ukija Kilosa, Mikumi the same, kila sehemu utakuta mkulima anaongezeka kutafuta maeneo ya kilimo kwa sababu eneo analolima kwanza rutuba nayo inapungua, ikipungua rutuba aina yetu ya kilimo kwa sababu siyo kilimo cha kisasa tunakutana na matatizo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye upande wa mifugo, takwimu zinatuonesha tuna zaidi ya ng‟ombe milioni 25 na hawa ng‟ombe wanazaliana kila mwaka kwa zaidi ya milioni moja. Baada ya miaka 10 tutakuwa na ng‟ombe milioni 35. Nashangaa humu ndani tunasema tuna wafugaji, mniwie radhi humu ndani tuna wachungaji hatuna wafugaji. Huwezi ukajiita mfugaji unahama pori moja unakwenda pori lingine na huwezi ukajiita mkulima, hatuna wakulima, tuna wabangaizaji wanaotafua maeneo kwa ajili ya kulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri kitu kimoja, juzi nilisema hizi Wizara nne, tano zikae pamoja kwa ajili ya kupanga vizuri, tukisema leo tutenge maeneo kwa ajili ya ufugaji, ng‟ombe wanazidi kuongezeka, ardhi bado ni ndogo na aina yetu ya ufugaji tunaona kabisa hatuwezi kuja ku-solve hili tatizo. Baada ya miaka10 tuna ng‟ombe milioni 35 tutawatengea maeneo gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaondoa kule Ihefu tumewapeleka Lindi, yale maeneo Lindi yaliyopangwa kwa ajili ya wafugaji leo watu wanalima ufuta. Kwa tatizo lile lile wakulima wana matatizo, wafugaji wana matatizo. Sasa hili haliwezi likajibiwa kwa Waziri kuja kutuambia hili tatizo atalimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tujadiliane hivi, lakini baada ya bajeti mimi niiombe Serikali, ikae Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Maliasili na Utalii na Wizara ya Mazingira. Lazima haya tuangalie, tunakwenda tunamsahau wa mazingira huyo, ukame ukija, tunamsahau wa mazingira huyu, mafuriko yakija na haya maeneo yanayotengwa yanatengwa kwa hoja za ikolojia. Tukisema tulime kote, tufuge kote, mwisho wa siku mvua tutakosa, nchi nzima itakuwa jangwa. Kwa hiyo, hoja siyo hoja ya hisia, siyo hoja ya kusema mimi ni mkulima nataka wakulima wangu wakae vizuri, mimi ni mfugaji nataka ng‟ombe wangu akue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku tutalima wote, tutafuga wote, tutashindwa sehemu ya kufuga, ardhi itageuka jangwa na hata tunaohama hama wakulima kutafuta maeneo mazuri ya hifadhi yenye udongo wa rutuba kwa ajili ya kupata mahindi mazuri, kwa ajili ya kupata maharage mazuri, ufuta, itafika muda haya maeneo mvua haitafika, na hiyo mito tunayotegemea kumwagilia nayo mvua haitakuwepo, maji hayatakuwepo, samaki hawatakuwepo. Kwa hiyo, sekta moja ikikorofisha itapelekea sekta nyingine kuharibikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kwa nia njema kabisa, tutajadili kila kona kuhusu Maliasili na Utalii kwenye eneo la migogoro ya wafugaji, kwenye maeneo ya matumizi bora ya ardhi, lakini hatutafika mwishoni kama hakutakuwa na mpango mkakati wenye sura mbili. Kwanza mpango wa dharura, uitwe transformation strategy, kuwatoa wakulima wanaohama hama wawe centralized katika kilimo cha kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuwaondoa wachungaji wanaohama kuchunga chunga wawe centralized, wafuge ng‟ombe wao vizuri wazaliane na wawe na tija. tukienda hapo tutafika mbele kwa haraka na ardhi yetu tutaitunza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna kosa moja tunalifanya, tunapoongelea vyanzo vya mapato na nguvu kazi ya Taifa letu tunatazama wakulima, tunatazama wafanyakazi tunasahau kuwatazama wafugaji kama sekta rasmi ambayo ipangiwe mipango kama tunavyopanga mipango kwenye maeneo ya kilimo. Tunamwangalia mkulima, yaani mfugaji anakwenda kwenda tu, ndiyo kwa maana leo yuko Lindi, keshokutwa anatoka, hatuwezi kwenda kwa staili hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, wafugaji sasa kwa sababu sio wafugaji, tuwa-transform kwenda kuwa wafugaji, wawekwe kwenye utaratibu mzuri, tija tutaipata. Hatuwezi leo kusema tuna ng‟ombe milioni 25, halafu pato hatulioni. Baada ya miaka 10 tutakuwa milioni 35 halafu wao wanazunguka tu nchini, haiwezekani hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kwa nia njema kabisa hizi Wizara nne zikae pamoja, zije na mkakati mkubwa, hii migogoro haitakuwepo na wala tusitoe hapa maneno ya kuwafurahisha wakulima, kuwafurahisha wafanyakazi ili migogoro itulie, haitatulia. Ardhi ni ndogo sana, msijidanganye mnatoka hapa mpaka Dumila mnaona yale si mapori, yale ndiyo kwa ajili ya kuleta vertilization ni AC ile ya kuleta hali ya hewa nzuri. Sasa siku mki-clear ile miti, cha moto mtakiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niwapongeze kwa mpango mzuri waliotengeneza. Ukiusoma mwanzo mpaka mwisho hupati shaka kwa yanayoenda kutekelezwa na hasa walipogundua kuingia na mfumo wa program wa kibajeti ambao mimi naamini wakijielekeza kwenye program itawasaidia huu Mpango ukatekelezeka vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uzuri wa Mpango huu, nimeusoma kurasa zote lakini huu Mpango una changamoto moja, umekosa kitu kinachoitwa rejea. Tukipata nafasi ya kurejea mafanikio ya Mpango uliopita, unatupa nafasi nzuri ya kushauri Mpango huu tuutekeleze vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walatini wana msemo repetitio est mater studiorum wakimaanisha marejeo ni mama wa mafunzo. Tutakwenda na mpango huu, tusipopata fursa ya kurejea mwaka mmoja uliopita kwamba tulipanga nini, tumefanikiwa nini, tufanyeje ili tusirudi nyuma, hatutafika. Hilo ndilo jambo linalotia shaka mpango huo mzuri. Tusipopata marejeo ya mafanikio ili twende vizuri zaidi; ya upungufu ili turekebishe, hatutakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango aje angalau na summary ya tulikotoka, tulipo na tunakokwenda ili tuutendee haki huu mpango ili tufanye vizuri ndani ya mwaka ujao na baada ya miaka mitano tuseme Tanzania tuliikuta hapa, tumeitoa mwaka 2015, tunaiacha hapa 2020 kwa mpango unaoeleweka na unatabirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1981 Chama cha Mapinduzi kilitoa mwongozo. Kwenye ule mwongozo kuna maneno mimi napenda sana kuyatumia na huwa napenda sana yawe sehemu ya maisha ya viongozi wenye utu. Yale maneno yanasema hivi, “kujikosoa, kukosolewa na kujisahihisha siyo dalili ya kushindwa bali ni njia sahihi ya kujipanga na kufanikiwa vizuri zaidi.” Tukiona pale tulipokosea aidha kwa kuambiwa au kwa sisi wenyewe kuona maana yake tumejikosoa, siyo kwamba tumeshindwa, inatupa njia nzuri ya kutoka hapa tulipo, twende mbele zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Nasema hivi kwa sababu huu mpango umekuja na programs ambazo tunaamini tumezipa vipaumbele. Kuna miradi ya vielelezo. Unaposema miradi ya vielelezo tafsiri yake ni kwamba kwenye haya mambo baada ya mwaka mmoja tutasema hiki ndicho kielelezo kinachotuonesha kwamba tumefanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeelezea vizuri sana kuhusu viwanda, lakini nikiangalia sioni sehemu ambapo kuna mikakati itakayokuja kukabiliana na changamoto za viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifuatilia sana nchi zilizokuwa na viwanda, aidha zile za zamani za Ulaya zilizoanza na coal and steel industries, Wajerumani na Waingereza; au zile za Mashariki ya Mbali zilizoanza na textile industries baadaye zikaendelea, hawa wote walikuwa na misingi minne ambayo namwomba Mheshimiwa Waziri Mpango aiangalie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa kwanza wa viwanda ni power (energy) na gharama za energy; msingi wa pili wa ni qualified personnel (manpower); watu wenye uwezo wa kuviendesha hivyo viwanda; msingi wa tatu ni malighafi (raw materials). Utavilishaje hivyo viwanda? Msingi wa nne siyo katika maana ya udogo wake, is financing. Una uwezo gani wa kuviendesha, kuvi-finance, kuvigharamia hivyo viwanda aidha kwa mapato yako ya ndani au kwa kushirikiana na watu wengine wenye mitaji kuja kwenye mifumo ya kuwekeza kwa kushirikiana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiyaangalia haya yote, yananipa sababu za kutosha kumwomba Mheshimiwa Waziri ayaangalie maeneo mawili kwenye mkakati wake. Eneo la kwanza kubwa ni mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na mradi wa chuma wa Liganga. Kwa nini nilianza na kusema repetition est mater studiorum? Huu Mpango ulikuwa mwaka 2007, ndiyo kwa mara ya kwanza tunataka sasa Mchuchuma na Liganga ije iwekeze kutuletea chuma, ije ituwekee umeme wa kutosha na iongeze umeme mwingine kwenye gridi ya Taifa, it was 2007. Leo tunapoongea, we are approaching ten years.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo nasema marudio ndiyo mama wa mafunzo. Tusiporudia kutaka kujua tulipotoka, tutadhani tunakuja na kitu kipya kumbe kitu kipya kilipata changamoto nyingi sana na hizo changamoto hatukupata fursa ya kuzirekebisha. Kwenye huu mpango, Mchuchuma, mmesema itazalisha Megawatt 600. Kati ya Megawatt 600, Megawatt 250 ndiyo zitazalisha umeme kwa ajili ya chuma kile cha Liganga na 350 ndizo sasa watauziwa TANESCO kuingia kwenye grid ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa za wazi zinasema haya mambo yote yako sawasawa isipokuwa kuna mvutano mmoja kwenye power purchase agreement ambapo mbia anataka tununue umeme kwa 13% sisi tunataka tununue umeme kwa 7%; lakini tukumbuke agenda ya umeme ni ya mradi mmoja tu na agenda ya chuma ile siyo hoja pale ya sisi kujadiliana tumeuziana umeme kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa kuendelea na mradi wa chuma cha Mchuchuma kwa sababu tu ya bei ya umeme. Kwa nini kwenye zile Megawatt 250 ambazo ndiyo za mbia, azalishe 250, atuletee chuma sisi tuzalishe chuma, tuachane na 350 ambao tutaununua kwa sh. 7/= au sh.13/=. It is wastage of time! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Mpango, kwa dhati ya moyo wangu, hebu a-focus kwenye hili kwa sababu nalo lina maneno ya hujuma; hujuma zina sura mbili. Wanasema, bwana, kusikiliza maneno ya mtaani siyo jambo zuri, lakini yakisemwa kwa muda mrefu yanawafanya watu waamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema huu mradi unahujumiwa; kwanza unahujumiwa na mashirika makubwa na makampuni makubwa ya upande mwingine kwa sababu mradi kapewa Mchina, wanataka usuesue usifike kwa wakati, lakini wa pili wanasema, eh, kwa sababu Kusini siku zote ni Kusini, basi Kusini iwe ya mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya mambo hayatujengi sisi kama Wabunge, haya mambo yanatufarakanisha, yanatufanya sisi watu wa Kusini tuendelee kuwa maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie Kusini siyo Kusini kama mnavyofikiri, kama Kusini ingekuwa inamaanisha chini, Mto Nile usingetoka Ziwa Victoria kwenda Kaskazini. Nataka kukwambia Kusini ni juu na Kaskazini ni chini kwa lugha kama hiyo. Niombe kabisa, tusifike sehemu tukawafanya watu wa Kusini ionekane kwamba wanahujumiwa katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujipe muda wa kutosha kwenye hoja nzima ya Mchuchuma na Liganga. Kwa nini nasema hivi? Kanuni ni mbili tu; tukifanikiwa kwenye Mchuchuma katika maana ya kuleta chuma na chuma kile hakitafika peke yake, kitakuwa na madini mawili, tutapata vanadium na titanium. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku chuma sasa ndipo tutakapoongelea mataruma yale ya kwenda reli ya kati yapatikane pale; mtakapotaka sasa madaraja yenu, vitu vitoke pale. Ndiyo zile kanuni nne nilizozisema; angalia sehemu zote, angalia eneo la power; power tunayo. Sasa unafanyaje kukifanya kiwanda cha textile industry kiende vizuri? Power yetu ni ghali, tuangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utatengeneza kiwanda cha nguo, tuna soko kubwa la nguo, tutashindwa ku-compete kitakufa. Kwa sababu nguo ya Thailand, China na Uturuki itauzwa bei ya chini kwa sababu ya cost of production, haya mambo yote Mheshimiwa Mpango yaweke katika mizani yake, tutatue hili tatizo Watanzania tutoke hapa tulipo twende mbele zaidi. Watanzania wanataka viwanda, nami nataka viwanda, nawe unataka viwanda; lakini viwanda lazima tuvipange vizuri kwa kuangalia kila element, tusiache untouched stone, kila jiwe likanyagwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Mkataba huu wa ubia baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote niwapongeze waliotangulia kuupinga huu mkataba kwa nguvu kubwa na maneno mazuri yalio-base kwenye content nikianzia na mchangiaji wa mwisho Cosato Chumi aliyechangia kabla ya mimi, michango ya Mheshimiwa Kabwe Zitto, Mheshimiwa Azzan Zungu, Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mheshimiwa Hussein Bashe na wengine wote, wameenda vizuri sana kwenye content, na Mheshimiwa Hamidu Bobali na chama chake na Mheshimiwa Khatib Said Haji.
Mheshimiwa Spika, sitakwenda kwenye content nitagusa mambo ya jumla ambayo ninadhani jumba lako hili Tukufu ni vema likajua ili tuweze kwenda katika mtiririko mzuri. Kuna watu wamesema hapa, nakubaliana Tanzania siyo kisiwa na wengine wamesema tusiikimbie hii ndoa, hii ndoa ni muhimu ni nzuri ina mazuri yake ni vema tukayatafuta mazuri yaliyoko sirini yasiyoonekana ili tuone kuna nia njema ndani ya hili. Naomba niseme machache yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, nchi yoyote inapoamua kufanya urafiki na Taifa lingine lolote, kuna mambo inapoteza kama Taifa na kuna mambo inayapata kama Taifa, kwa maneno mepesi, mahusiano yoyote baina ya mataifa yanaunganishwa na principle ya statism, principle ya self-help na principle ya survival. Katika mazingira yoyote yale unapoingia kwenye makubaliano na Taifa lolote lile, kanuni ya kwanza inayopaswa kuku-guide, una interest gani kama Taifa kwenye ule mkataba.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, unalopaswa kuliangalia, utanufaika kwa kiwango gani katika ule mkataba? Lakini kuna mazingira mengine, unaweza usinufaike, ila ule mkataba ukakusaidia kuishi uione kesho yako, labda kuwakimbia maadui hiyo ndiyo inayoitwa national survival.
Mheshimiwa Spika, yawezekana kuna wengine wanayatafuta mazuri kwenye Mkataba huu kwa sababu tu ya ule woga katika makubaliano kuna mchawi asiyeonekana, yaani wanatafuta ku-survive sehemu ambayo hakuna survival. Niwaombe ndugu zangu Wabunge, historia ya nchi yetu tumeshirikiana na mataifa mengi katika nyakati tofauti. Kuanzia karne ya tano tuliposhirikiana na nchi za Mashariki ya Mbali na nchi za Uarabuni mpaka kipindi nchi za Ulaya zilipoingia, kipindi cha ukoloni na mahusiano baada ya uhuru. Wote mmeona kila Tanzania tulipojikwamua kutoka kwenye makucha ya kutaka kuendelea kumekuwa na uhusiano wa mjomba wa kuturudisha nyuma.
Mheshimiwa Spika, tumetoka kuanzia mwaka 1961 mpaka leo tunaongea mwaka 2016, kuna mikakati mingi sana tumeipanga kama Taifa, kuna mikakati mingi sana tumeipanga kama nchi na majirani zetu, kuna mikakati imefanikiwa na mikakati haikufanikiwa. Ni jukumu letu sasa kujiuliza kama Taifa, haya mahusiano tuliyowahi kuyafanya nyuma yalitusaidia kwa kiasi gani? Na haya mahusiano tunayotaka kuyafanya sasa yana tija kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, niwakumbusheni ndugu zangu Wabunge, tulishawahi kugawanywa katika block mbili, block ya East na block la West. Mnakumbuka kipindi cha cold war. Nchi yetu kama Taifa ilisimama ikasema hatutageuka kulia wala kushoto tutakwenda katika mfumo ambao tunaona nchi yetu ina maslahi nayo, hatukugombana na Wamarekani na Waingereza na wala hatukugombana na marafiki zetu wa Urusi.
Mheshimiwa Spika, leo tunavyokwenda kuujadili mkataba huu, ni mkataba wa kwanza ndani ya nchi yetu kuwekwa fungu moja as a bargaining block against European Union. Haikuwa kutokea huko nyuma na wala hatukuwahi na experience ya kundi zima tukawa na interest sawa, tukawa na historical background sawa, tukawa na matamanio sawa, tukawa na ndoto sawa, leo tukae kwenye meza ya majadiliano against a huge block - European Union.
Mheshimiwa Spika, ninaona kuna tatizo, kuna matatizo mawili; tatizo la kwanza si mahusiano yetu na Jumuiya ya Ulaya na wala siyo mahusiano yetu na majirani zetu wanaotuzunguka, tuna tatizo la kwanza la content, mambo yaliyopo ndani ya mkataba ambayo tunayapinga. Kwa bahati mbaya sana kwa hatua tuliyofikia, hatuna fursa ya kuchambua kifungu kimoja baada ya kingine, tuna fursa moja tu sasa hivi ya kuukataa, kwa sababu ya kukubali hatunayo. Baada ya kukataa hayo mazuri msiyoyaona hapa mnayodhani yapo, ndiyo yatakuja.
Mheshimiwa Spika, leo hii hapa tujadili nini, tu-suspend, uende halafu urudi, hapana. Hatuna fursa hiyo, tuna fursa leo ya kusema Serikali isaini mkataba au Serikali isisaini mkataba. Kutokana na hoja zote zilizotolewa ndani humu na Wabunge, nakubaliana na ninaiomba Serikali isisaini mkataba huu. Kwanza, haujatupa room ya kufanya marekebisho, kama kutaonekana huko mbele kuna haja ya kurekebisha vifungu tutakwenda.
Mheshimiwa Spika, tuna marafiki zetu wametangulia, ndugu zetu Walatini wana msemo amicorum omnia communia wakimaanisha between friends all is common au wakimaanisha for friends all things are shared. Sasa kwa style ya wenzetu wanavyokwenda tunaona ile principle ya amicorum omnia communia haipo, hatuoni kitu hapa kinachoenda in common. Walishakaa Wakuu wetu wa nchi wakasema tujipe muda wa miezi mitatu, wenzetu wamekwenda speed.
Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kusema machache yafuatayo; umefika wakati sasa kwa Watanzania kutoka kwenye giza nene la urafiki wa kinafiki wenye lengo la kudidimiza na kuua ndoto ya Tanzania kuwa na viwanda. Umefika wakati sasa kwa Tanzania kutoridhishwa na aina hii ya urafiki mpaka pale mishipa yetu ya fahamu itakapojiridhisha kwamba urafiki huu haufanani na ule urafiki wa paka na panya kukumbatiana na kubusiana ilhali shimo la panya la kutorokea liko mbali.
Mheshimiwa Spika, wakati sasa umefika kwa Watanzania kutokuwa na kiu ya kutaka kunywa maji ambayo yako kwenye kikombe cha mateso, uchungu na maumivu makubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa maneno haya, siungi mkono hoja na ninaiomba Serikali isipitishe na isisaini mkataba huu. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye taarifa ya Kamati. Awali ya yote niungane na walioipongeza Kamati kwa kazi nzuri walioifanya ya uchambuzi na kutupatia mwelekeo, huenda bajeti ijayo ikawa nzuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imefanya kazi kubwa ya kutuonesha maeneo gani tunapaswa kuyafanyia kazi kama nchi, Kamati imetusaidia kutuonesha hali halisi ya nchi yetu iko wapi katika masuala ya kiuchumi na vilevile kutuwekea mazingira mazuri ya kutuwezesha kufanya tathmini na kujipanga kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuipitia taarifa hii nimeona kuna mambo mawili, matatu tunapaswa kujifunza na wataalam wetu watusaidie. Sina hakika kama tumewahi kujiuliza swali kitu gani kinacho-run uchumi wa nchi yetu. Ukiangalia kwa umakini vipimo vinavyotumika kuielezea Tanzania inaendelea au haiendelei ukitafakari kwa makini unakuja kugundua tunaishi Kitanzania na tunafikiri Kiulaya. Mwisho wa siku tukitafsiri fikra za Ulaya kwenye maisha ya Kitanzania tunakuja na majibu kwamba uchumi unakua halafu tunaona idadi ya maskini inaongezeka. Kwa nini hili linatokea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya World Bank inaeleza itakapofikia mwezi August inflation rate itashuka, inaweza ikafika 4.5 kutoka kwenye 6.5. Hata hivyo, katika kipindi hiki uchumi wa nchi yetu unaonekana unaendelea kuimarika na wakatoa sababu kwa nini tunaendelea kuimarika. La kwanza wanalolisema ni kwamba Tanzania ina political stability nzuri yaani nchi yetu ina utulivu wa kisiasa kiasi kwamba tuna fursa zote za kufanya nchi yetu ikaendelea. La pili, nchi yetu ina fursa za kiuchumi nyingi za kutosha ambazo bado nyingine hazijatumiwa katika kiwango cha kusema hii nchi ni kuzimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaposema kiwango cha umaskini kimeshuka halafu taarifa hiyohiyo inakwambia maskini wanaongezeka unaweza ukasema hii hai-make sense, ni kwamba tumeshindwa kutafsiri maisha ya Watanzania. Hivi kuna utafiti gani umefanyika baada ya kujengwa kwa barabara ya Dodoma - Iringa kupitia Mtera ukafika katika vile vijiji vilivyojengwa baada ya ile barabara wanauza nyama za mbuzi pale, kuna mtu ameweza kujua pato lao kwa siku ni shilingi ngapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu amewahi kufika Mbinga akakuta matuta kumi ya viazi yanayomfanya mwananchi pale aishi akienda dukani anakwenda kununua tu sabuni, chumvi na mafuta ya taa, akakaa Januari mpaka Desemba akauza magunia yake mawili ya mahindi akampeleka mtoto wake shuleni akasoma halafu mwisho wa mwaka mnasema huyu kwa siku yuko chini ya dola, vipimo gani tunavyovitumia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wataalam wetu mtusaidie. Katika kipindi hiki nchi yetu imeendelea sana ndiyo maana wanasema uchumi wa nchi unakua. Anayesema maisha ya Watanzania hayakui ni kwamba hajakwenda into details, hajaenda kuangalia familia kwa familia tukoje. Hivi tuseme ule ukweli, kama kweli hapa ndani wote tuna familia na kuna watu tunawalea, kama tupo chini ya dola kweli tungeishi? Mnaelewa maana ya chini ya dola, maana yake tunaishi chini ya Sh. 2,000 kwa siku mtu ana familia ya watoto saba hakuna mtu anayekufa na njaa, does it make sense? Kuna vitu vingine mimi sivielewi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe wataalam, tukitaka tulingane na nchi nyingine zilizoendelea kama Asian Tigers, tukiwafuata tutapotea. Tukitaka tukajifunze Botswana kama wengine wanavyosema tutapotea. Mfumo wa Tanzania ni wa kipekee, unahitaji study yake ya kipekee utaleta matokeo tunayoyataka. Tukienda hivi, wachumi hawa wamesoma sana wamekuja na makabrasha na hawa si ndiyo walioshauri bajeti iliyopita, si ndiyo hawa wanaokuja na vyanzo vya mapato vilevile!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme kabisa, tunahitaji a serious discussion, we need serious research kuhusu uchumi wa kipekee wa Kitanzania unapoishi na watu wanaoishi chini ya dola wakati huohuo wakaweza kusomesha, wakaweza kula, wakaweza kujenga, hii hali sio ya kawaida. Tutadanganyana tu na haya makaratasi hapa, tunasema uchumi umepanda, uchumi umeshuka, tutapelekwa kulia, tutapelekwa kushoto hatutafika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nikasema, kinachotutesa sisi na narudia tena, ni kufikiri Kitanzania, kuishi Kitanzania lakini tunadhani kwamba mifumo ile ya Ulaya ya uchumi ndiyo inayofaa kutafsiri uchumi wetu. Mipango ya Ulaya ya kukuza uchumi na projection zao ndiyo tunadhani zinatufaa kwa Watanzania, zimefeli na hazikuwahi kufanikiwa kutuletea majibu yanayotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kaangalie hali ya maisha ya kawaida ya Mtanzania, sawa, kuna vitu kama nchi lazima tuvifanye, tukivifanya hivyo tuna uhakika ile gap inayoonekana watu kuongezeka kuwa maskini kwenye maandishi ikapotea ni kwenye suala la infrastructure. Bajeti zijazo zijielekeze kwenye infrastructure, reli ya kati iimarike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi reli ya kati ilipokuwa inafanya kazi mtu wa maisha ya chini alikuwa anakula wale dagaa wanaotoka Kigoma, walikuwa wakifika Dar es Salaam ndiyo chakula kinachokuwezesha kuishi, unanunua kilo moja kwa Sh. 200, 300 leo hii kilo moja ya dagaa wa Kigoma anayeweza kula ni from royal family, kwa nini? Kwa sababu reli ya kati imeshindwa kuleta ule mtiririko uliokuwa una-cover matatizo mengine. Sasa tukiimarisha reli ya kati haya mambo mengine yote yatakwenda vizuri. Tukifungua barabara, kama nilivyosema, leo mimi nikitoka Dar es Salaam kwenda Mbinga sihitaji kupita Iringa, nitapita Masasi nitaongea na Ndugu yangu Mheshimiwa Mwambe dakika mbili nasonga mbele naingia Mbinga haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali kama hii, leo inapasuliwa barabara hii ya Arusha kwa kupitia Msalato unapunguza kilometa nyingi ambazo tulikuwa tunazitumia kwenda Singida. Hali kadhalika ukatoboa barabara ya Kigoma – Mpanda – Sumbawanga na ukatoka Sikonge – Mpanda ukaja Tabora utaratibu unakuwa mzuri. Haya ndiyo maendeleo, tusiende kwenye hizi figures ambazo zinaonesha namba, hazina uhalisia katika hali ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nakubali maendeleo ni watu, hatuwezi kusema kuna maendeleo ya vitu tukayatofautisha na maendeleo ya watu. Tukawa na barabara, viwanda, watu wakawa wanasononeka hawana furaha wanaishi maisha ya hovyo, haya siyo maendeleo. Maendeleo ya nchi yetu ni maendeleo ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Naomba nichangie kwenye maeneo mawili, eneo la kwanza nitachangia eneo la michezo na eneo la pili nitachangia kwenye eneo la utamaduni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kuu inayoikabili Wizara hii katika kukuza sekta ya michezo, sekta ya habari, sanaa na Utamaduni nchini ni changamoto fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 161 cha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 kinasema yafuatayo:-

“Katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani hii, Serikali itaimarisha sekta ya michezo nchini kwa kuifanya sekta ya michezo kutoa fursa ya ajira hususan kwa vijana kwa kupanua wigo wa vyanzo endelevu vya fedha za uendeshaji na ugharimishaji wa maeneo ya michezo hapa nchini kwa kuanzisha bahati nasibu ya michezo.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo ilikuwa commitment ambayo tuliitarajia sasa, baada ya miaka miwili ya kuwa madarakani Wizara ingekuja na mkakati wa kuanzisha hicho chombo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri ufuatao; badala ya Serikali kwenda kuanzisha chombo kingine cha bahati nasibu, ni vyema sasa ingetumika hii Bodi ya Bahati Nasibu ya sasa, isipokuwa iboreshwe kidogo. Sasa inafanya kazi zake ikiwa chini ya Wizara ya Fedha na ukiangalia kwa ujumla wake, Wizara ya Fedha ina majukumu mengi, haiwezi ikafanya kazi vizuri na ikaifanya hii Bodi ya Bahati Nasibu ikaleta mapato yale tunayoyatarajia ukilinganisha na nchi nyingine waliyowahi kufanya mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ya Fedha na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, mkae mkubaliane ihame huku ije kwenye Wizara ya Michezo. Nasema hivyo kwa sababu nne zifuatazo:-

Kwanza, msingi mkuu wa kuhamisha majukumu kuyapeleka kwenye Wizara ya Habari ulishaainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi; la pili, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ina miundombinu inayojitosheleza ya kuifanya ikafanya kazi vizuri kuliko ikikaa kwenye Wizara ya Fedha. Kwa sababu ili bahati nasibu ilete mapato mazuri inahitaji hamasa. Wizara ya Fedha haina room ya hamasa, ila kwenye michezo kuna hamasa. Tukiiweka hii italeta picha nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya tatu, wanaocheza hii michezo wana uhusiano wa moja kwa moja na michezo, kwa hiyo, ukiiweka kule kwenye Wizara ya Fedha inakuwa ime-hang, umeweka kitu kama mtoto mkiwa hana baba wala mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne na la mwisho, the best practice kutoka nchi nyingine, kuna nchi zimefanikiwa kwa kuweka hii kwenye Wizara ya Michezo na wakapata pesa nyingi za kuendesha Wizara. Brazil wanafanya hivyo, Australia wanafanya hivyo, Uingereza wanafanya hivyo na hata majirani zetu Kenya wanafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiombe Serikali isipate kigugumizi, isianzishe Bodi nyingine ya Bahati Nasibu, isipokuwa hii iliopo iondoke Wizara ya Fedha ikasimamiwe chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka kulichangia ni kuhusu utamaduni. Taifa lolote duniani linatambulika kutokana na utamaduni wake na hata kama zile nchi zilizokuwa na utamaduni wa pamoja unaoeleweka kama nchi yetu Tanzania tukiongea kiswahili tunaeleweka kama Watanzania, nchi nyingine zina alama nyingine zinazotambulisha mataifa yao. Nchi yetu ukiondoa lugha ya kiswahili, ina mambo mengine ambayo yanalitambulisha Taifa letu.

Jambo la kwanza, ni Bendera ya Taifa; jambo la pili, Wimbo wa Taifa; jambo la tatu, Mwenge wa Uhuru na jambo la nne ni Ngao ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf alikwenda mbali sana katika kuchangia, alifika hatua ya kusema Mwenge wa Uhuru uondolewe upelekwe kwenye makumbusho. Naomba nichukue fursa hii kuyasema yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzito wa Mwenge wa Uhuru ni ule ule, sawa sawa na Wimbo wa Taifa; uzito wa Mwenge wa Uhuru ni ule ule sawa sawa na Ngao ya Taifa, uzito wa Mwenge wa Uhuru ni ule ule sawa sawa na wimbo wa Taifa. Kwa nini nasema haya? Hayo mambo yote ni package moja.

T A A R I F A...
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba unilindie muda wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa lolote duniani na mifumo yoyote ya sheria duniani inatokana na mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo sheria inayotungwa inaweza ikatokana na the best practice. Jambo hili limefanyika katika jamii kwa muda gani? Limekubalika katika jamii kwa muda gani? Hapo ndipo linapopelekea kwenye kutunga sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie kitu kimoja, mila na desturi za Taifa lolote lile zinatokana na historia yake. Huwezi ukauondoa Mwenge wa Uhuru kwenye historia ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe kidogo, mwaka 1961 tulipopata uhuru tulikuwa na ajenda mahususi, tulisema mambo yafuatayo: “Sisi tunataka kuuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimajaro umulike hata nje ya mipaka yetu ulete tumaini pale ambapo hapana matumaini, ulete upendo pale ambapo pana chuki na ulete heshima pale ambapo pana dharau.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu mniambie haya mambo yote mazuri, hivi kweli yapotee hewani! Huo ndiyo msingi wa historia ya utu wa Watanzania. Kwa hoja hiyo ninashangaa, kwa nini Mwenge wa Uhuru haukuwahi kutungiwa sheria! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo lilinikwaza jana, kuuita Mwenge wa Uhuru ni ibada. Kila jambo tukilifanyia ibada hatutafanya hata moja. Mwaka 2016 nilikuwa Jimboni, mwananchi mmoja akaniambia, Mheshimiwa Mbunge kwa nini mkiingia Bungeni mnafanya ibada? Nikamuuliza ibada gani? Akasema, ninyi mkifika si kwanza siwa mnaliinamia, hamfanyi kitu bila siwa na mkiondoka kama Bunge kwenda kwenye Kamati, siwa mnaifunika ndani, mkirudi wote mnasimama mnafanya ibada ya siwa. Jamani, wote tungesema hizi ni imani, tungefika? Kitu kimoja ninachotaka kusema, nchi yoyote unaitambua kwa vitu vingi; alama ni moja ya ishara ya kuitambua nchi. Ninamshangaa sana ndugu yangu, Mheshimiwa Tundu Lissu, amesema Ngao ya Taifa imetungiwa sheria, lakini hakujipa muda wa kutosha kuangalia Ngao ya Taifa imeundwa na nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambieni, kwenye Ngao ya Taifa ina mambo yafuatayo, kuna bibi na bwana, kuna pembe za ndovu mbili zikichunguliana, kuna mwenge wa uhuru umekaa katikati, chini yake kuna bendera, sasa sioni kipya hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo tunaweza tukafika sehemu tukaelewana, jambo ambalo tunaweza tuka-discuss tukaelewana kuhusu mwenge wa uhuru ni modality ya kuukimbiza mwenge wa uhuru. Hili liko open to discussion. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuupeleka mwenge wa uhuru kwenye makumbusho, ni kuipeleka historia ya Taifa la Tanzania kwenye makumbusho. Haya mambo anayeweza kuyafanya ni yule ambaye sio mzalendo wa Taifa hili, ni yule ambaye hajui mambo matatu yanayoongelewa katika moto wa mbio za Mwenge ndiyo unayotengeneza utu wetu? Nani anapenda dharau humu ndani? Nani anapenda chuki humu ndani na nani ambaye hapendi heshima humu ndani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaombe ndugu zangu, mwenge wa uhuru ni jambo jema sana, ni jambo ambalo inabidi tulienzi, tuliheshimu, tukiudharau mwenge tutapata shida. Mimi najua kwa nini wanadharau mwenge. Siku zote historia ni nzuri hata kama aliyeandika ile historia… (Makofi/ Vigelegele)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia mchana huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kwanza kumpongeza Waziri na Naibu Waziri wa Elimu. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri amekuwa msikivu, mkarimu, akipigiwa simu anapokea na tukimpelekea matatizo yetu ya elimu anatusikiliza kwa utii na uadilifu mkubwa. Nimwombee kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuwa na hilo hilo sikio la usikivu, liambatane vilevile na kusikia hoja ambazo tunaziwasilisha tunapochangia bajeti yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walatini wana msemo, non scholae sed vitae discimus, wakimaanisha we do not learn for school but we learn for life. Mfumo wetu wa elimu lazima utambue kwamba tunatengeneza maisha yetu, maisha ya watoto wetu, maisha ya wajukuu zetu na maisha ya kizazi kijacho. Mjadala unaoendelea ni uthibitisho tosha tumejikwaa kwenye kutengeneza kizazi chenye matumaini ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopata vitabu vinavyokinzana, tunapopata mifumo ya elimu inayotofautiana kwenye Taifa lilelile, inayonung’unikiwa upande mmoja na upande mwingine ni tafsiri tosha Mheshimiwa Waziri ana kazi kubwa ya kufanya kwenye hili. Nimwombe hoja zinazohusu hadhi, value, quality ya elimu yetu, azibebe vizuri na azifanyie kazi kwelikweli, tukifanya hivi tutatengeneza Taifa ambalo lina matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mifumo mizuri sana siku za nyuma na wote tumepitia kwenye mifumo. Mkono wa kulia na wa kushoto haufanani. Hata huohuo mkono wa kulia una vidole vitano vyenye urefu tofauti na Mwenyezi Mungu katuumba hivyohivyo tulivyotofautiana na yeye ana makusudi ili tutegemeane. Haiwezekani wanafunzi wote Tanzania nzima wakawa na upeo sawa, wakawa na fikra sawa, wakaenda sawasawa. Ndiyo kuna watu ambao Mwenyezi Mungu kawaumba wanafaa kuwa wanasayansi, madaktari, watu wa art, watu wa kilimo na wengine watu wa biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii iko wapi SHYCOM? Mtu toka akiwa mtoto mdogo anajua akipenda biashara basi kuna form five na form six iko SHYCOM. Ziko wapi zile Shule za Ufundi za Ifunda, Mbeya Tech, Dar Tech, Arusha Tech ziko wapi leo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo tunapokwenda kusema tunatoa elimu za ugoko, tusiangalie tulikodondokea tuangalie pale tulipojikwaa. Nimwombe Waziri, hata mnaposema university sijui zote ziko sawa, mimi namwambia hakuna kitu kama hicho, ni kanuni ya maisha. University ya Mzumbe lazima itakuwa tofauti na University ya Tumaini kwa hoja za kihistoria, kwa hoja za infrastructure, kwa hoja ya curriculum, kwa hoja zote utakazotaka kuziweka. Mimi nimwombeni sana, hili jambo ni lazima tuliweke vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kukaririshwa madarasa. Hili wala hatuhitaji kuweka utaratibu kwamba watu wote wapite kutoka darasa la kwanza mpaka la saba bila kukaririshwa darasa, sasa kuna haja gani ya kufanya mitihani na mitihani tunafanya kwa ajili ya nini? Mitihani hii imewekwa kwa ajili ya ku-control human behavior. Usipopata tishio huwezi ukafanya au uka-behave, it is human nature.

Mheshimiwa Mwenyekiti, human nature siku zote jinsi ilivyo lazima umwekee utaratibu wa kumfanya akae kwenye mstari. Moja kati ya vitu hivi ni pamoja na kuweka mitihani, lingine usipofikisha wastani tutakufukuza, ni kama tulivyoweka sheria na taratibu nyingine. Sasa huku mnasema waende tu kwa nini mkifika university kuna ku-carry over, kuna supplementary, this is contradiction! Tunaji-contradict sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema hii elimu tunaiburuzaburuza, sawa twendeni lakini mimi niwaambieni kama university mnasema kuna ku-supp, tafsiri yake ni kwamba tunataka tutengeneze a certain quality of education, the same i-apply kwenye ngazi zote. Walatini wanasema, repetitio est mater studiorum…

Mambo uliyoyafanya toka ukiwa darasa la kwanza ndiyo yanayokujenga wewe mpaka unapokuwa university. Sasa huku aende holela halafu akifika university ndiyo kwanza apate utaratibu, haya mambo hayawezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme lingine, hili naomba niseme kwa utaratibu kidogo, ni jambo ambalo limegusa hisia nyingi sana za watu, ni suala la mimba za utotoni, mimba za shuleni, yule anayepata mimba aendelee na mafunzo au arudi akajifungue na atafutiwe utaratibu mwingine wa masomo. The same spirit tunayoiweka kwenye kuitengeneza elimu ya nchi yetu izingatie mila na desturi, izingatie taratibu lakini vilevile izingatie mazingira mazuri yanayofanya kitu kinachoitwa social structure vis-a-vis social responsibilities, maana yake nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamii yetu hii imekaa katika makundi ya rika, tunatarajia mtoto wa darasa la kwanza mpaka darasa la saba atakuwa na behavior fulani inayoendana na jamii. Atakayekwenda university ata-behave tofauti na atakayetoka hapa akawa baba, mfanyakazi, mzee mpaka kikongwe, hiyo ni social structure imetengenezwa. Mwenyezi Mungu ameumba kuna muda wewe utasoma, kuna muda utapevuka utazaa, kuna muda utakuwa baba, kuna muda utakuwa kiongozi, kuna muda utakuwa mzee umezeeka baadaye una-rest in peace.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongea juzi, nashukuru waliosema hapa wengi tulikuwepo, wa kwanza Mheshimiwa Mama Sitta alikuwepo, wa pili Mheshimiwa Susan Lyimo alikuwepo, Mheshimiwa Ndassa alikuwepo, tuliongelea kuhusu wale watoto wa Shinyanga waliopata mimba wakiwa watoto, tulilia na kusikitika. Tukajipanga kule tukasema tuje hapa Bungeni tushinikize Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaruhusu mtoto wa kike aolewe akiwa na miaka 14 tuifute.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunataka watoto wazae warudi shuleni. Tunajichanganya wenyewe hatujui tunakotaka kwenda. Leo hii tuna ajenda kubwa sana ya kuhakikisha Sheria ya Ndoa inayomkandamiza mwanamke tuiondoe halafu huku wazae, hivi sisi tumelogwa, hatujui tunachokitaka. Basi niwaulize swali moja, kama tunaruhusu mimba mashuleni, kuna mechanism gani ambayo tumeiandaa kuhakikisha kwamba hawa watoto hawataoana mashuleni? This is a contradiction! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe mama zangu na mimi natokana na mama, naelewa…

TAARIFA...

HE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Ndiyo hapo unapopata tofauti kati ya kuelimika na elimu. Ukipata tofauti kati ya kuelimika na elimu hutapata shida. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani unaposema huyu mtu asiolewe akiwa chini ya miaka 18, tafsiri yake nini? Hata Sheria ya Ndoa wanakuambia ndoa haiwezi ikawa ndoa mpaka mke na mume waingiliane. Tafsiri yake kama wanaingiliana maana yake kuna mimba. Yaani vitu vingine jamani wala hatuhitaji kutafuta misamiati, hatuhitaji kutafuta maneno ya kupakana matope.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize na neno moja, naomba nilinde kwenye muda wangu. Najua hili jambo lina hisia, hasa kwa mama zetu hata kama mimi ningekuwa mama nisingependa mwanangu limkute baya. Kihistoria sisi tuliotoka kwa mama zetu tuna mapenzi ya dhati sana kati ya mama na mtoto, mama siku zote hupenda mwanaye yasimkute mabaya. Katika upendo huu wa mama kumpenda mwanae kuna maeneo upendo humletea madhara mtoto.

TAARIFA...

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Na iwe kama ulivyonena nani amewaroga. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali ya kawaida niwaombe sana jambo hili tulitazame katika mapana, ni jambo lililogusa hisia, hakuna mstari ulio-clear unaoweza kutofautisha mimba ya mtoto anayepata chini ya miaka18 na ndoa. Tukihalalisha hilo basi tukubaliane kimsingi tunataka ile Sheria ya mwaka 1971 iendelee kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya mwisho ya kufunga dimba kwenye siku hii ya leo. Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi kusema, Mheshimiwa Komu alitumia Ibara hii kutoa mawazo yake, yanaheshimika; akasema, Hotuba ya Waziri ni hewa, the same alichokifanya Mheshimiwa Kingu kutoa uhuru wake wa mawazo aliposema haina alternative. Katika mazingira kama haya tuvumiliane tu. Ukijua kucheka, lazima ujue na kulia. Sindano inapoingilia, ndiyo pale pale inapotoka. Kwa hiyo, tuvumiliane tu, tuendelee. Kwa hiyo, ili isinipotezee muda, niende kwenye hoja yangu ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, toka Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne na Awamu ya Tano, tuliona mkakati wa kukuza viwanda kwenye Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere. Ikaenda ikakuza viwanda ikatuachia viwanda vikubwa sana na viwanda vidogo vidogo. Katikati hapa viwanda vikafa na vingine vikauzwa. Hatukuwahi kupata matumaini mpaka ilipofika Awamu ya Tano. Ilipokuwa kwa kauli yake ya kusema sasa Tanzania inakwenda kwenye nchi ya viwanda ili twende sambamba na mpango wetu wa maendeleo ifikapo mwaka 2025 angalau tufike kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nayasema haya? Nayasema haya kwa sababu tunaona kabisa kuna dhamira ya dhati ya kwenda kule. Kusema ni neno moja na kutenda ni neno lingine. Tukumbuke tunakuja kwenye mkakati huu mkubwa. Kipindi tukiwa na miaka zaidi ya 20 ya kusuasua kwa viwanda, kwa namna yoyote ile ni lazima tuanze popote, aidha, tumeanza kwa usahihi sana au kwa kukosea, lakini tulipoanza tumeanza sehemu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hadithi moja inaitwa hadithi ya jongoo na mwana jongoo. Jongoo alizaa jongoo mwana, sasa alipomwona mama yake akitembea, jongoo mwana akamwuliza mama, nina miguu mingi sana nitatembeaje? Jongoo mama akamwambia mwana, anza na wowote. Jongoo mwana alipoanza na wowote akatembea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takribani miaka 20 tumekwama kwenye viwanda, tunauliza tutoke na mguu gani? Mheshimiwa Mwijage, aanze na mguu wowote, mwisho wa siku tutatembea. Tukisema tulie kwenye mkakati, tulie kianze kipi, in process tutajua jinsi ya kwenda, lakini ni lazima tuanze na tulipoanza tumeanza sehemu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema ni sehemu sahihi? Kwa hoja zote za kiuchumi zinafsirika. Hoja ya input, out put zinatafsirika vizuri tu. Ndani ya mwaka mmoja, Julai, 2016 mpaka Machi, 2017 vimesajiliwa viwanda 170. Kati ya hivyo, viwanda 54 vipo kwenye hatua ya ujenzi na viwanda 17 vimeanza kufanya kazi ndani ya mwaka mmoja. Huko ndiko tunakosema jongoo anza na mguu wowote, mbeleni huko tutapata njia ya kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, niseme mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kusema na nitarudia tena kusema. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, tunapotaka kutengeneza viwanda aidha vimekuwa viwanda vikubwa au vidogo, ni commitment kubwa ambayo tunaifanya kwenye uchumi wa nchi yetu. Factors nne hizi lazima siku zote zituongoze na zituelekeze kwenye kujenga Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni jambo la umeme (power), jambo la pili ni watu (manpower), jambo la tatu ni raw materials na la nne ni mtaji. Haya mambo yote ukiyaangalia ndiyo yanaweza yakatuhakikishia kwamba ndani ya miaka hii mitatu au minne tutakwenda kwenye Tanzania ya viwanda kwa kiasi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejiuliza ni kwa kiasi gani kwa viwanda hivi vidogo vidogo ambavyo nchi karibu zote zilizoendelea kama Malaysia, Ujerumani, China, walianza? Walianza na zile asilimia 89 mpaka asilimia 99 viwanda vidogo vidogo (small scale industry). Kule majumbani, mtu anaweza akakamua maziwa yake ya ng’ombe akatengeneza siagi, akaenda akauza, ndiko tunakoongelea. Hivi in process huko mbele ndivyo vitapelekea kukua kwa viwanda vingine vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanabeza hivi viwanda vidogo. Niseme, tumeanza sawa sawa, ila inabidi tufanye marekebisho kwenye vitu vifuatavyo: tuna viwanda vidogo vidogo vya SIDO ambavyo vinatengeneza mashine ambazo zinaweza zikawasaidia hawa watu wanaoendesha viwanda vidogo vidogo. Vile vile tuna Shule za VETA; naomba Serikali i-link hizi sekta mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anayesoma VETA akifuzu mafunzo yake aunganishwe na SIDO kwa kile alichokuwa amejifunza ili SIDO impatie vitendea kazi kwa mkopo. Anapozidi kuendeleza ile sekta ya ufundi wake ataleta tija na viwanda vidogo vidogo vitakua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tutaimba mpaka jua litakuchwa na kucha kama hatujaona agriculture ndiyo sehemu pekee itakayokuza viwanda, hatutatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuitengeneze ramani ya nchi yetu kwa zone. Sehemu wanayolima pamba, sasa tufikirie kuwa na kiwanda cha spinning kwenye maeneo ya pamba. Sehemu wanayolima mahindi, sasa tuwe na mills kubwa ya kutengeneza sembe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii watu wa Rukwa, watu wa Songea, watu wa Mbeya na Iringa wanauza gunia moja la mahindi kwa shilingi 40,000 mpaka shilingi 60,000. Likienda kwenye yale makampuni yanayonunua mahindi, pumba ili ulishe ng’ombe wako na mifugo yako, gunia moja la pumba ambalo tunaita makapi ni shilingi 200,000. Tukitengeneza hizi mills kwenye haya maeneo, tutakuwa tumewasaidia wakulima na Tanzania ya viwanda tutaiona bila shida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna maeneo wanalima alizeti. Leo hii mafuta ya Korie yanauzwa bei chini, lakini mafuta ya alizeti ya Singida, ya Dodoma mpaka Kibaigwa, unapata shilingi 18,000 mpaka shilingi 20,000 kwa ile galoni la lita tatu. Kwa nini tufike huko? Kuna gharama zinakwenda kwa yule mkulima mdogo ambazo Serikali iki-intervene; nilipoongea kwenye eneo la power, kwenye kuwakopesha mashine ili waweze kukamua, tutatoka. Ndiyo hiyo hoja tunayoiongea ya import na export kwa nini vinakuja? Kwa sababu tunavyozalisha kwanza havitutoshelezi na hata kama tunazalisha gharama yake inakuwa kubwa, automatic kutokana na hali yetu ya uchumi, tunalazimika kuingiza vitu vya nje kuja hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho niseme kuhusu Mchuchuma na Liganga; hapa ndipo kwenye moyo wetu. Ukiuangalia vizuri mradi wa Mchuchuma na Liganga, ndiyo mradi pekee unaoifanya Dar es Salaam na Mtwara, Mtwara na Ruvuma, Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya kuja Morogoro itoke katika maana ya reli ya uhakika, chuma cha uhakika na madini mengine. Tunaongelea mwaka huu wa 17, tatizo liko wapi? Kila tukifika tunaongelea Mchuchuma na Liganga, Mchuchuma na Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tunaomba, najua kuna sehemu ataweza kuijibia Mheshimiwa Waziri Mwijage, lakini nyingine atakuja kujibu Waziri mwenye dhamana. Nawaomba kabisa, suala la Mchuchuma na Liganga, mwaka huu tufunge huu mjadala au halipo; na kama lipo tujue tunatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho tena la mwisho kabisa, nimalizie na la matrekta. Ilikuwa SUMA JKT, ilikuja na vitu vinaitwa power tiller na wakulima wakakopeshwa matrekta kwamba sasa tutaondokana na jembe la mkono hatutainamisha tena viuno. Kilichotokea wote tunakijua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tufanikiwe vizuri, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwenye sekta hiyo ya merchanization, yaani ya kumtoa mkulima kwenye jembe la mkono...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi name nichangie kwenye uti wa mgongo wa Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Awali ya yote nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, muda wote nilipokuwa nauliza maswali ya msingi na ya nyongeza kuhusu kero zinazowakabili wakulima wa kahawa kwenye tozo nyingi zisizoeleweka, leo wamelijibu hili kwa kuondoa tozo 17. Tulipokuwa tunapigania zile tozo zitoke kwenye 26 na 27, tulitambua kwamba kati ya vitu vinavyomkwaza mkulima wa kahawa kule chini, ni bei ndogo iliyosababishwa na tozo nyingi zilizokuwa katikati ya mchakato, yaani kutoka kwa mkulima mpaka unafika juu kwa mnunuzi mnadani na nje ya mnada. Sasa mmelifanya hili jambo kubwa sana na kuna wachache watabeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba kwenye hili Serikali mmefanya jambo zuri na ongezeni moja lingine. Kwa sababu mmeziondoa zile 17, msiache hewani, wekeni na bei ya kiwango cha chini cha ununuzi wa kahawa. Kwa sababu



kwenye tafiti zetu tunajua, hizo dola zote zilizopungua zimeondoa gharama za uendeshaji, uzalishaji na gharama za usafiri na kitu kingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tumsaidie mkulima kule chini tufanye kama tulivyofanya kwa mahindi mwaka 2016, tukasema mtu asinunue mahindi ya mkulima mpaka awe na shilingi 500 kwa kilo ndiyo yanunuliwe. Kwenye kahawa, korosho, tumbaku na kwenye pamba tunaweza tukafanya hivyo hivyo. Tukifanya haya ninayoyasema, ule wasiwasi aliokuwa nao ndugu yangu Mheshimiwa Silinde utakuwa umeondoka. Kwa kweli tutakuwa tumemsaidia mkulima, ila tunafahamu gharama zilizokuwa katikati ya mchakato zilikuwa zina-trickle down zinafika zinamsumbua mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala lingine kuhusu ukuaji wa kilimo na Tanzania ya viwanda. Tutaongea hapa siku zote kuanzia asubuhi mpaka jioni, tusipo-link hizi sekta mbili; sekta ya kilimo na sekta ya viwanda, mambo yote mawili hayataweza kwenda. Kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema tunataka tumsaidie mkulima aliyelima nyanya zake zikaoza pale Dumila kabla hajafika kwenye soko, anahitaji katikati kitu kinaitwa processed Industry ili kwanza kuongeza value ya zile nyanya zake, lakini kuzitunza ili zisiweze kuharibika. Pale anahitaji awe na kiwanda. Utaongelea korosho, the same, utakwenda kwenye mahindi, tutazalisha mahindi ya kutosha, lakini tusipoyaongezea ubora wa kutosha tutapata tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hakuna maendeleo ya viwanda kwenye Taifa la Tanzania bila kuwa na maendeleo ya kilimo, vyote vinakwenda pamoja. Utakwenda kuongelea habari za ufugaji, utaongelea masuala ya ngozi hapa, mimi mpaka nashangaa. Hivi kweli tunashindwa ku-intervene tukapata kiwanda kimoja hata kwa mkopo kwa ajili ya ku-process bidhaa zinazotokana na ngozi, halafu wafugaji wetu wakawa na ahueni kwenye maisha yao? Kweli hili linashindikana.

T A A R I F A . . .

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Mheshimiwa Kanyasu. Kimsingi hiyo taarifa ana- compliment kwa ninachokiongea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachohitaji, we need a serious government intervetion kwenye vitu kama hivi. Kama kiwanda kilikuwepo, vilikuwepo vingi, sitaki kurudi nyuma. Nilichotaka nikiseme hapa kwa nia njema, tukitaka tutoke tuisaidie Sekta ya Kilimo, tunahitaji a serious intervetion kwenye kuwekeza kwenye kilimo. Kwenye mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, lazima tuichore tena ramani ya kilimo ya nchi yetu including watalaam wa research, wafanye tafiti. Ukiangalia Morogoro, ina sifa kubwa ya alluvial soil. Alluvial soil ni udongo wenye rutuba na Mkoa wa Morogoro tukiungalia unapata mvua bila matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiondoa mvua, bado una mito mikubwa inayoweza kufanya Morogoro peke yake ikafanya Tanzania isife njaa. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu Serikali hapa haija-invest kwa huyu mkulima, inadhani mkulima anajua. Mkulima hajui. Hapa lazima tumwambie mkulima cha kufanya, namna ya kufanya na namna gani tutatoka hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mvua zilizopita zimetuletea mafuriko lakini mafuriko yale kwa wenzetu ni neema. Hebu tujiulize tungeweka mabwawa ya kuyaelekeza yale maji ya mafuriko kipindi hiki ambacho wakulima hawawezi kulima na wakilima mvua zinazidi mazao yanaharibika, tungeyateka yale maji tungeweka katika maeneo ya mabwawa, kipindi cha mwezi wa Sita, wa Saba ambapo mvua hakuna, maji yale yale ambayo yalitukwaza sasa yatumike kwenye kilimo. Vitu kama hivi vinahitaji tu kuelekezwa, Serikali elekezeni tu kila kitu kitafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine mnaongea irrigation, irrigation, irrigation, kuna njia rahisi sana za kuifanya Tanzania iwe ya umwagiliaji. Tuna utaratibu tumeuweka hakuna shule ya sekondari, shule ya msingi itakayojengwa bila choo, tunashusha tu circular, hakuna shule yoyote ya msingi na sekondari itakayojengwa bila kuwa na miundombinu ya kuvuna maji ya mvua. Ukivuna maji ya mvua from day one mtoto akiwa shule ya msingi anajifunza umwagiliaji kutokana na maji ya mvua. Sasa sijui tumelogwa, hata sijui tufanyeje lakini ninachoweza kusema hapa kwa kweli Serikali inahitaji serious intervention kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine huwezi ukakuza sekta ya kilimo bila kuwa na uhakika wa matumizi bora ya ardhi. Douglass Jerrold katika andiko lake la “A land of Plenty” alitumia methali moja ya kilatini, alisema “Cujus est solum, ejus est usque ad coelum” akimaanisha “He who owns the soil or land owns up to the sky” kwamba matumizi bora ya ardhi ni utajiri mkubwa kuliko kitu kingine chochote. Nchi yetu tumebarikiwa kuwa na ardhi bora, kinachotusumbua sisi kila siku tunadhani tunaanza upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize swali moja Mheshimiwa Waziri anaikumbuka Kapunga Rice Project? Project ambayo ilikuwa kuwa ya irrigation scheme, iliandaliwa kwa ajili ya kuwasaidia watu, ukifika pale kwa sababu maji yapo, mkulima ana uhakika wa kuvuna. Nenda pale Morogoro kuna ile Dakawa Rice Project nayo ni irrigation system nzuri, kama Serikali ilishawekeza watu wananufaika pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuichore ramani ya Tanzania kwa maeneo sita au saba ya kuanzia kama tulivyofanya Dakawa, tufanye vilevile Kilombero, tufanye hivyo kwa Mheshimiwa Mwamoto kwenye lile Bonde la Mto Ruaha wanalima vitunguu vizuri sana kule, wawekewe utaratibu uleule wa irrigation haya mambo yote yatakwisha tutakuwa hatuna matatizo na twende maeneo ya Rungwe kule kuna mifumo mizuri ya kilimo kuanzia Januari mpaka Disemba. Tusipofanya a serious intervention kwenye kilimo hatutatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo naweza nikashauri ili twende vizuri, tunataka tuwasaidie wakulima, wakulima tukiwaacha na hekari moja moja hatutafanikiwa. Jambo la kufanya, wale wote ambao wanalima kwenye eneo linaloelekeana tufanye mechanization of agriculture. Kama mtu ana hekari mbili kijiji kizima mna jumla ya hekari 10,000, hizi hekari 10,000 zote zinakuwa communal tuna-inject pale trekta na taaluma, kwa hiyo, kila mwenye hekari yake moja ana-offer labour kwenye ardhi yake ili tupate tija kwa sababu hatuna uwezo wa kila mmoja kuwa na trekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ndivyo kilimo kilivyokuwa duniani kote, hatuwezi tukaendelea na hii asilimia 65 hapa tunajidanganya. Asilimia 65 ya hekari moja moja tunalima nini? Mimi hapa nimepata magunia mawili, mwingine matatu halafu tunajiita wakulima, we are not…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie bajeti hii ya kihistoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Comrade Senator Ndassa amesema kwa uzoefu wake wote aliokaa katika Bunge hili, hajawahi kuiona bajeti iliyoshiba na yenye matumaini kama hii. Na mimi pamoja na umri wangu huu mdogo, toka nimeanza kupata ule ufahamu kuweza kujua redio, tv na kuweza kusoma na kuandika sijawahi kuiona bajeti iliyosheheni matumaini kama hii. Bajeti hii ni bajeti ya wananchi, bajeti hii inawagusa wakulima wote, wafugaji, wafanyabiashara wa kada zote na bajeti hii inawagusa wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba bajeti hii ni bajeti ya pili ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejipambanua kwamba inakwenda kuitengeneza Tanzania ya viwanda na kumuondoa Mtanzania angalau ifikapo mwaka 2025 tufike katika level ya kati ya uchumi. Kwa namna yoyote ukitizama bajeti hii, imefanikiwa kutujibu swali la siku zote la tafsiri ya maendeleo, maendeleo ni nini? Bajeti hii imetujibu development should be people centered. Kwa namna yoyote utakapoingalia inakuonyesha bajeti hii ni bajeti ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi bajeti hii imejikita katika kuwasaidia watu wa uchumi wa chini, uchumi wa kati, wafugaji, wakulima, wafanyabiashara na wawekezaji. Ili twende vizuri na tuelewane katika hili kuwaambia kwamba bajeti hii ni bajeti ya kihistoria, naomba niwapeleke kwenye mambo kumi muhimu yaliyopo kwenye bajeti hii. Kwa lugha nyingine naweza kuyaita ten tenants. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, Taifa lolote unaweza kulipima kama lina matumaini kuhusu kesho baada ya miaka kumi na miaka 50 ijayo kwa namna gani inajikita kwenye miradi mizito ya vielelezo, miradi ya maendeleo. Bajeti hii imeanza pasipokuwa na shaka lolote kutekeleza miradi ya vielelezo zaidi ya saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kwanza ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Ni watu tu ambao hawafikiri dunia inakwendaje wanaweza wakahoji hili. Kwa miaka yote tumelalamika kwamba reli ya kati kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma kwamba bidhaa zinakwenda shida, maendeleo hayawezekaniki, tumetoka sasa tunakwenda kwenye standard gauge. Dola bilioni 300 zimekwishatengwa na tayari zimekwenda kwenye kuandaa karakana na kufanya upembuzi yakinifu ili ndani ya hii miaka michache, mtu anatoka Dar es Salaam mpaka anafika Kigoma akiwa amelala usingizi, anasoma gazeti lake kwa muda wa saa saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuboreshwa kwa Shirika la Ndege Tanzania. Hili kuna watu hawalielewi, wakiambiwa Serikali imenunua ndege huwa haelewi. Unaponunua ndege hatuangalii mapato yanayopatikana kwa wewe kupanda ndege kutoa hapa kwenda Kigoma, Songea na sehemu nyingine. Tunaangalia vitu vingine vinavyosababisha kukua kwa uchumi lakini kwa sababu umetumia saa chache sana barabarani, uchumi unakua. Hii ni hatua kubwa sana ya nchi yoyote inayotaka kwenda kwenye uchumi wa kati lazima iimarishe shirika lake la ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa tatu, tumezungumzia sana suala la Mchuchuma na Liganga, hii imewekwa katika mpango huu. Tushukuru sana Serikali tumeipigia kelele sasa tunakwenda ile hoja mliyokuwa mnalalamika chuma sasa kinatoka Liganga na makaa ya mawe yatatoka Liganga. Utaratibu wa reli sasa haitakuwa ya kati tu, kwa chuma cha Liganga tunao uwezo wa kuuza chuma nje, tunao uwezo wa kutandaza reli kwenye Wilaya zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa nne ni ununuzi na ukarabati wa meli kwenye maziwa makuu. Juzi tulipokuwa tunaongelea hapa Wizara ya Uvuvi, ndugu yangu Ulega alisema hatutumii vizuri ile bahari kuu kwa sababu hatuna meli za kisasa zenye uwezo wa kuvua, sasa Serikali imeiona hili na imeliweka. Sasa nashangaa watu wanaosema hawaoni basi yawezekana ni vipofu tuwasaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano ni ule wa gesi kimiminika (liquefied natural gas). Hili ni jambo kubwa ambalo sasa litakwenda kujibu matatizo mengi. Ile gesi ikishafika tunaiboresha sasa itakaa kwenye mitungi ni hatua ya baadae hata yule aliyekuwa anatia mashaka mafuta ya taa yamepanda bei, huko sisi tunataka kutoka, mafuta ya taa kwanza yanaleta air pollution, ni adha na ukipika na chakula nacho kinanuka, tunataka tumtoe mtu huyo huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mama yangu ulinifundisha siwezi kukusema sana ila ili kuweka tu kumbukumbu sahihi, siyo sawa unaposema kuhusu mafuta ya taa. Hesabu zote za kiuchumi zinatuonyesha tunatoka kwenye mafuta ya taa tunakwenda kwenye gesi. Mwalimu wangu wataalam wanasema you can not strengthen the weak by weakening the strong. Hoja ya msingi ni kumfanya yule weak awe strong siyo kwa kumdhoofisha yule ambaye ni strong. Kupeleka bei ya mafuta kwa wale watu wenye magari hakumaanishi kuwa tunamfanya huyu asiyekuwa na uwezo awe weak, tunajaribu kumuimarisha kwa njia nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika mambo yangu yale kumi, hili lilikuwa la kwanza tu, la pili ni Kodi ya Majengo. Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 ndiyo kwa mara ya kwanza iliyoipa mamlaka TRA kukusanya mapato kwenye majengo. Safari hii imefanya maboresho tu kwa sababu ilikuwa haieleweki watu wanakadiriwa vipi, Serikali imekuja sasa na ukomo, nyumba ya kawaida iwe shilingi 10,000, ya ghorofa shilingi 50,000, tatizo liko wapi hapa sasa? Unaona sasa tunataka tupate mapato katika njia inayoeleweka, kila nyumba itatoa Sh.10,000 kila ghorofa shilingi 50,000, Serikali inayotabirika katika maendeleo ndiyo inakuonyesha namna gani itatutoa hapa tulipo itupeleke sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wafugaji, Serikali imeondoa VAT kwenye mayai ya kutotolesha vifaranga (fertilized eggs for incubation), jambo hili ni kubwa sana.

Ndugu yangu Mwita pale atakuwa shahidi kule Kitunda, walishaacha sasa kuleta mayai pale mjini kwa sababu gharama za chakula na kutotolesha vifaranga ilikuwa kubwa kutokana na kodi hii. Kwa kuiondoa kodi hii sasa unamsaidia mtu wa kawaida wa chini, wale vijana na akina mama watakuwa wanafuga kuku na kutotolesha mayai. Hapa sasa ndiyo hatua ya kwanza ya kutengeneza viwanda vidogo vidogo vya kusindika nyama na ku-process mayai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni viwanda na uwekezaji. Serikali imeondoa VAT kwa uagizaji wa bidhaa za mitaji yaani capital goods, hili jambo linasaidia kwanza kuwa-encourage Watanzania wawe export oriented. Huwezi ukapata pesa za kigeni kama hau-export lakini vilevile tukumbuke Tanzania it’s a strategic area, tuna-control hizi land locked countries, tukiwa na mfumo mzuri wa kuondoa hizi kodi na kupeleka malighafi nje…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kuipongeza Wizara kwa hotuba nzuri ambayo kwa kweli ukiitizama kwa kina inatoa matumaini ya Taifa letu kwenda kwenye nchi ya viwanda hasa ukizingatia msingi mkuu wa Taifa la viwanda unatokana na Wizara hii ya Nishati na Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 kipindi cha kampeni, Rais wetu mpendwa wakati anajinadi alipofikia kuongelea suala la sekta ya madini alijipambanua pasipokuwa na kificho kwenye changamoto kubwa tano zinazoikabili Wizara ya Nishati na Madini au katika ujumla wake sekta ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu mpendwa alizunguka nchi nzima akasema, toka tumeingia ubia na wabinafsishaji na hawa wenzetu, tukawapa migodi wakashirikiana na sisi tumepita kwenye changamoto kubwa zifuatazo:-

(i) Kunyanyaswa kwa wachimbaji wadogo, sambamba na kulipwa fidia ndogo wawekezaji wanapotwaa maeneo. (Makofi)

(ii) Sekta ya madini ina usimamizi mbovu unaopelekea Serikali kukosa mapato. (Makofi)

(iii) Sekta ya madini inakutana na changamoto ya kutoroshwa kwa madini kwa njia mbalimbali kunakoipotezea Serikali mapato. (Makofi)

(iv) Sekta ya madini inakutana na changamoto ya mikataba mibovu inayoipunja Serikali mapato. (Makofi)

(v) Sekta ya madini inakutana na tatizo la matumizi mabaya ya misamaha ya kodi ambayo wawekezaji wamepewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais akamalizia kwa kusema mkinipa ridhaa ya kuongoza nchi hii, nitahakikisha haya mambo matano nakwenda kuyafanyia kazi. Watanzania wakamuamini wakampatia Urais, akaingia ofisini toka siku kwanza kipindi cha hotuba yake hapa Bungeni akasema nchi yetu tajiri, nchi yetu ina rasilimali nyingi, tukizitumia rasilimali zetu vizuri nchi yetu itakuwa donor country. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina uhakika aliyasema haya kwa sababu alikuwa anaijua Tanzania vizuri. Akajipa muda wa kutosha, akai-study hiyo sekta ya madini akaja kugundua kuna makinikia yanatoweka nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yote niliyoyasema yapo kwenye changamoto namba tatu niliyosema sekta ya madini inakutana na utoroshwaji wa madini, kwa namna yoyote ile iwe hoja ya kisheria, iwe hoja ya mahusiano, hoja ya kutoroshwa kwa madini yetu Watanzania Rais alikwishaisema na akafanyia kazi. Leo hii namshangaa Mtanzania yeyote yule anayehoji modality au namna Rais alivyoitengeneza Tume ya kwenda kuyakamata na kuyachunguza yale makontena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu mmoja anaitwa Edmund Burke na baadaye Abraham Lincoln na Martin Luther the King waliwahi kusema, evils will prevail if good people do nothing. Changamoto zote za madini tunazoziona zitaendelea kuwepo kama watu wazuri hawatafanya kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, alichokifanya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni ile segment ya watu wazuri wanapofanya jambo ambapo kuna uovu. Kinachonishangaza mnataka uovu tuutengenezee modality? Unavyokwenda kumkamata mwizi unataka umtaarifu mwizi kesho nitakuja kukukamata, ujiandae pamoja na mtu wa kukuwekea dhamana ili ukifika Mahakamani tukutoe, jamani! Hivi kweli sisi ni wazalendo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonikwaza zaidi hii ajenda kwa muda mrefu pioneers walikuwa wale pale. Pioneers wa ajenda hii kwa muda mrefu walikuwa wale pale, tutawataja kwa majina.

Mheshimiwa Naibu Spika, waliosema hizi changamoto tano wale kule, Mheshimiwa Mnyika umewahi kusema, Mheshimiwa Mwita Waitara umewahi kusema, Mheshimiwa Tundu Lissu amewahi kusema, hawa ndiyo waliosema hayo mambo matano. Tena wakasema mnakaa na hii mikataba ya nini si vunjeni, hawakusema wale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilichowafanya leo wabadili gia angani ni nini? Hawa watu wana tatizo la uzalendo, niwaombe ndugu zangu tuwe wazalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu yeyote anayeona shaka ambapo kuna evils and good people they are doing something halafu akawatilia mashaka, kwa kweli napata shida sana kuwaelewa. Nilichotarajia kutoka kwao, kwanza wangesema tunakushukuru Rais, tumesema kwa miaka mingi hakuna aliyewahi kutusikiliza wewe umetusikiliza halafu ndiyo twende yale mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mnyika amekuja hapa ana hoja ya mikataba it is true, mikataba ni tatizo hakuna mtu anayepinga na Rais alishasema mikataba ni tatizo. Nilichotegemea waseme makinikia ndiyo foundation ya mjadala ya mikataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakwenda kwenye kujadili mkataba ukiwa na evidence tunaibiwa kwa kiasi gani, ninyi wawekezaji rekebisheni hapa kwa sababu tumethibitisha pasipokuwa na shaka lolote mnatuibia. Sasa mnataka twende tujadili terms za mikataba hatuna kitu mikononi?

TAARIFA....

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Ahsante sana Mheshimiwa Bashe, kwanza naipokea taarifa yako kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna siku hapa niliwahi kusema story ya jongoo na mwana jongoo.Katika misingi ileile ya habari ya jongoo na mwanajongoo. Unapotaka kutatua matatizo katika sekta hii ya madini lazima uwe na sehemu ya kuanzia. Hivi mnataka tuanzie wapi kwenye hili?

TAARIFA ....

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba unilindie muda wangu wameuchezea sana. Hii taarifa ngoja niipe maelezo mazuri ili iwe taarifa iliyokamilika kwa sababu haijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wowote wa kisheria kuna mhimili unaitwa mhimili wa Bunge ndiyo unaotunga sheria na mfumo wowote wa kuongoza nchi katika namna yoyote ile chimbuko lake ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Upungufu wowote unaoonekana ninyi mlikuwepo na sisi tulikuwepo. Ajenda ya sheria zote zilizopitishwa humu ndani ninyi mlikuwepo sisi tulikuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, my concern is not about the past, my concern ni sasa tunapoanza kupiga hatua. Tumeliona tatizo, tunatatua tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napata shida sana kuwaelewa watu wa aina kama ya akina Mheshimiwa Mwita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna kichekesho cha mwaka kama kile ambapo mtu umeliona kosa, unalirekebisha halafu mtu anatokea anakuambia kwa nini ulikosea si uendawazimu huo? Yaani mimi napata shida kuelewa, kosa limetokea unalirekebisha, katika process ya kulitatua tatizo unasema eti kwa nini ulikosea, ni akili za chizi tu zenye uwezo wa kufanya mambo kama haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. SIXTUS R.MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi na mimi ili nichangie jioni ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, niseme kwa masikitiko makubwa kwamba natoa pole kwa familia ya Mzee wetu Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye ndiye alikuwa Mwalimu wetu sisi vijana wa siasa na amewahi kuwa Katibu Mkuu wa TANU Youth League na mwasisi wa Umoja wa Vijana wa CCM; kwa namna ya pekee sana natoa pole zangu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baada ya hizi pole naomba nijielekeze sasa kwenye kuchangia kwenye hotuba zilizowasilishwa leo hapa Bungeni. Umuhimu wa mashirika na taasisi za umma kwa nchi yetu ni mkubwa sana. Mashirika mengi yalianzishwa kwa lengo moja, kwa kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la pili ni kutoa gawio kwa Serikalil; huo ndiyo ulikuwa moyo wa sprit behind ya kuanzisha haya mashirika. Kwa bahati mbaya ufanisi wa mashirika hayo yote hauwezi ukapimika kwa faida wanazotoa au hauwezi ukapimika vizuri na ukaonekana kwa aina ya huduma wanazozitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hoja hiyo niiombe Serikali iyatazame haya mashirika na kuyasaidia kulingana na aina ya huduma au matokeo ambayo Serikali inatarajia. Huwezi ukalipima shirika linalotoa huduma kwa jamii kwa vigezo vya faida lakini huwezi ukalipima shirika ambalo unatarajia linaendeshwa kibiashara one hundred percent kwa vigezo vya huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujumla wake performance indicators ni kipimo muhimu kwa kupima ufanisi wake. Nimelitizama kwa kina sana shirika la ATCL niombe Serikali iitizame ATCL katika jicho la tatu. Ukilitizama kwa kiasi gani linaleta faida na kiasi gani liko efficient unaweza usipate jibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali sasa ingalie na kuisaidia ATCL kwenye kipimo kingine ambacho kinaitwa spillover effects indicator au positive externalities indicator au a third party effect indicator. Hiyo ikoje; unaweza ukawa na shirika kwa nature yake jinsi ilivyo mpaka Yesu anarudi ukipiga pale ulichokiweka naulichokipata ndani ya lile lile shirika moja kwa moja usione faida, lakini likawa na faida nyingi sana zisizoonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ATCL serikali msitegemee faida mtapata mwaka huu, mwakani au mwaka wa kesho kutwa, linaweza likanyumba katika nchi zozote itakazoelezeka lakini ATCL ina faida kubwa sana, kwanza ndiyo brand ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ATCL inasaidia sekta nyingine zikimbie, zikue na zilete faida kwa Taifa. Wanakwambia principal ya faida ya duniani kote inatokana na speed ya mtu anavyo-move kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfanyabiashara yeyote duniani asingependa kukaa masaa mengi barabarani, kwa jinsi anavyofika kwenye huduma kwa urahisi ndivyo faida inavyopatikana kwa hiyo niiombe Serikali iitizame ATCL na wala isiache kununua ndege kwa sababu tulishaona kwenye mashirika mengine kama Ethiopian Airline wamenyumba hawakupata faida, lakini hawakuacha kununua ndege na wamenunua ndege. Emirates hawajawahi kupata faida hawajaacha kununua ndege na wameongeza ndege nyingine kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Air Rwanda wameongeza Mabombadia (Bombadier) na mamboing (Boeing) haya yote wanayofanya KQ mwaka jana waliyumba kiasi kwamba watu wakafikiri shirika litafungwa hawajaacha kununua ndege na wameongeza kununua ndege; kwa nini hawa wanafanya hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafanya hivyo kwa sababu wanajua faida inayotokana na shirika hili siyo ya moja kwa moja ni ya huduma kwa upande mmoja, watu wata- move lakini kwa upande mwingine itasababisha sekta nyingine zikue hiyo ndicho wanachosema a third part effect indicator tunapaswa tuitazame katika lengo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Serikali imewekeza jumla ya shilingi trilioni 47.7 kwenye mashirika yote mpaka ilipofika Juni, 2017 lakini faida iliyopatikana kwenye investment ya shilingi bilioni 47.7 ilikuwa ni shilingi bilioni 8.2 tu ambayo ni sawasawa na asilimia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haya mashirika yangewekezwa vizuri na yakatengenezewa mazingira angalau yalete asilimia kumi tu ya investment ambayo tuliiweka, maana yake tungepata shilingi trilioni 4.7 kwa mwaka jana, sawasawa na asilimia kumi ya mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini haya yanatokea hivyo? Haya ni masuala ambayo Serikali/Wizara ya Fedha lazima myafikirie kwa kina. Vilevile Msajili wa Hazina aangalie kuna mashirika ya hovyo, ni mzigo kwa Serikali, hata ukiyapima kwa huduma, huduma yake haitapimika na hata ukiya-grade ukayalea kama unavyoilea ATCL yatatutia hasara mpaka Yesu anarudi na faida inayotokana kwa third party hutaweza kuipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali kupitia kwa Msajili wa Hazina, ndani ya Kamati tumetoa mapendekezo kwenye mashirika ya hovyo, ambayo yana mikataba ya hovyo, ambayo yana watendaji ambao hawana weledi, unakuwa na CEO, Wenyeviti wa Bodi na Board of Directors hawana idea hata moja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia jioni hii ya leo. Naomba tu nikwambie kwamba nimeongea na Mheshimiwa Mlinga ameniambia nitakapoishia, dakika zake tano nitaendelea kuongea mimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takriban miongo miwili na nusu, yaani miaka 25 Shirika letu la Ndege la Taifa lilikuwa linafanya vibaya sana. Watu wote tulikuwa tunalitazama kwa aibu na kuna baadhi yetu walilalamika na kusema tunazidiwa na kanchi kidogo kama Rwanda, tunazidiwa mpaka na Msumbiji ambao wana ndege yao kwa wiki inakuja Tanzania mara moja. Hayo yote yalitukwaza wengi sana ambao tulikuwa na nia ya kuiona Tanzania ikisonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee sana, nampongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuamua kwa makusudi kututoa kwenye msukosuko wa miaka 25 ambapo shirika letu la ndege la Taifa lilikuwa linayumba.

T A A R I F A . . .

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikuombe unitunzie muda wangu, halafu pili sitaijibu hiyo, inanipotezea muda wa kushusha yale ninayopaswa kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Ni ninyi ambao mlikuwa mnasema shirika hili halifai; ni ninyi mliokuwa mnasema kwamba hatuna ndege hata moja. Juzi tumenunua ndege, nyie mnakuwa tena wa kwanza kuturudisha nyuma kwa nini tumenunua ndege?

Haki yake mpeni! Ni Kiswahili safi. Hivi nani asiyejua kwamba Rais wetu amekuwa na ujasiri mkubwa wa kulifufua shirika la ndege?

Nani asiyejua humu ndani? Kinachowakwaza nini kulisema jina la Rais kwenye mambo yaliyo mema? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ni kawaida yao, wana macho lakini hawaoni; wana masikio lakini hawasikii; na wana roho zenye chuki zisizoweza kutenda jema lolote. Sasa tukisifia mambo mazuri wanataka tuseme nini? Ni wao walikuwa wanasema hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mchana Mheshimiwa Halima Mdee alilidanganya Bunge. Nataka nimpe taarifa mchana ule, lakini kwa sababu nilijua nitapata muda sasa hivi, nikasema niutumie muda huu kwanza kumpa hiyo taarifa na kuwapa taarifa watu wengine wote ambao wanaona lakini wanajifanya hawaoni; wanasikia na wanajifanya kuwa hawasikii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Halima Mdee mchana alisema ATCL haina strategic plan na haina business plan. Mwaka 2017 tukiwa kwenye Kamati ya PIC tuliliita Shirika la ATCL. Mimi nilikuwa Mjumbe na cha kushangaza wengine waliokuwa wanapiga makofi kwenye uongo huo nao walikuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba moja, Mheshimiwa Frank Mwakajoka tulikuwa naye; namba mbili, Mheshimiwa Esther Bulaya, tulikuwa naye; namba tatu, Mheshimiwa Maftaha, tulikuwa naye; namba nne, Mheshimiwa Kwandikwa tulikuwa naye; na namba tano, Mheshimiwa Edwin Sannda tulikuwa naye. Kwenye taarifa yao, sio yangu. Walisema mwezi Juni, 2016 Serikali iliamua kulifufua upya shirika la ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kulifufua Shirika la Ndege lilikuwa na mambo mawili ilibidi yote yafanyike kwa wakati mmoja. Jambo la kwanza kurudisha hadhi ya ATCL kipindi inaelekea kufa; na suala la pili kuifanya iendelee kwenda kwa muda mrefu ili tusirudi kwenye upungufu uliofanya shirika life. Katika kipindi cha mwaka mmoja kilikuwa mwezi Juni, 2016 na Julai, 2017 ATCL walikuwa wana mpango wa muda mfupi ulioitwa Turn Around Strategy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018 wakaja na mpango wa miaka mitano ambao ni Corporate Strategic Plan iliyokuwa na malengo yafuatayo:-

T A A R I F A . . .

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza anazidi kuongopa, anasema amepata Taarifa ya Msajili wa Hazina ya Mwaka 2007 na wakati mimi naongea strategic plan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango mkakati wa mwaka 2017 - 2022, shirika liliamua kwa makusudi kufanya mambo matatu. Jambo la kwanza, kuhakikisha wananunua ndege mpya ambayo wamefanya; jambo la pili, ilikuwa ni kuendeleza marubani ili itakapofika ndege zote tusipate anguko ambalo lilipatikana miaka 25 iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa Shirika la Ndege, kutokana na mikataba mipya ya kununua ndege mpya, inasomesha marubani 62. On top of that, inasomesha marubani 12 kutokana na makubaliano ya Shirika la Ndege la Taifa la Tanzania pamoja na Shirika la Ndege la Ethiopia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba niseme kuhusu faida zinazoweza zikapatikana na ATCL. Wengi wamesema wakiangalia hasara ya uendeshaji wa Shirika la Ndege kwa kuangalia ununuzi wa tiketi na huduma ambazo ndege inatoa ndani ya ndege kipindi abiria wanasafiri. Shirika la Ndege ukiondoa hizi faida zinazoonekana moja kwa moja ina faida tatu kubwa, faida ya kwanza ni ancillary services. Kuna muda ukimsafirisha abiria nchi inapata faida kwa huduma ambazo katika nchi husika zinatolewa. Naomba nitoe mifano ya mashirika ya ndege ambayo hayakuwahi kupata faida ya moja kwa moja ya tiketi, lakini yalipata faida kutokana na ancillary revenue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ya kwanza ni Shirika la Ndege la EasyJet la Uingereza mwaka 2006 walipata faida ya jumla ya Euro milioni 189; Shirika la pili ni Aer Lingus ya Ireland ilipata faida ya Euro milioni 63; Shirika la Tatu ni AirAsia ya Malaysia, lilipata faida ya Euro 22. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ni United Airlines la United States of America, mwaka 2009 lilipata faida ya bilioni 1.5 nje ya kuuza tiketi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, watu wasiojua hii industry, wakasome waijue, wasibishe vitu wasivyovijua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nami nafasi hii ya kuchangia asubuhi kwenye Wizara hii. Kwa sababu nina dakika tano, nitajitahidi niende haraka sana ili mambo yangu haya mtatu niweze kuyawasilisha vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naipongeza hii Wizara kwa hatua ya kupitia ile sera ya mwaka 1995 na kuja ile ya mwaka 2017 ili iboreshe Sekta ya Michezo. Namwomba Mheshimiwa Waziri aikimbize sana, kwa sababu kwa hali jinsi iliyo tukakaa kama tulivyo kwa muda mrefu, Sekta ya Michezo itazidi kushuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ambalo ningependa niliseme asubuhi ya leo ni kuhusu kuwawezesha wale ambao wana nia ya kujenga viwanja vya michezo au sports facilities mikoani ili waweze kuifanya kazi hii vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kuna taasisi nyingi zina nia ya kujenga viwanja hasa kwa kutumia nyasi bandia, lakini changamoto kubwa wanayokutana nayo ni gharama ya kuweza kulipia ushuru ili zile facilities zije.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara, ukienda pale Kidongo Chekundu, ukiangalie zile facilities zilizojengwa, tukipata vilabu vyenye uwezo wa kufanya hivyo, vikatengeneza, vikapewa msamaha wa zile nyasi bandia, nina uhakika viwanja vitakuwa bora zaidi na michezo itakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka niliseme, nchi yetu sisi hatuna Sports Academy, lakini ni wajibu wa Serikali sasa kuona namna gani tunatoka. Mimi nina ushauri, umefika wakati sasa Serikali ichague shule moja ya sekondari ya mkoa iipatie facilities na iwe na curriculum ya michezo tu, iwe na masomo saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masomo hayo saba, ziwe lugha zote ikiwepo Kiswahili, Kifaransa, Kiingereza na Kispaniola halafu na somo la Historia, Geografia na Uraia. Yanatosha kabisa. Halafu vyama vya soka vikishirikiana na Maafisa Utamaduni watafute wachezaji kupitia UMITASHUMTA na UMISETA, hao waingie kwenye ile shule maalum ya michezo ya Mkoa. Tukifanya hivi, nina imani baada ya muda siyo mrefu, mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, naomba niliseme kwa kifupi tu. Hii wiki kuna sintofahamu iliyokuwa ikiongelewa humu Bungeni kuhusu umiliki wa viwanja vya michezo vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi. Naomba nitumie fursa hii kuliambia Bunge lako Tukufu, sera ya TANU mwaka 1957 ilikuwa ni kuboresha michezo. Pamoja na hilo, katika harakati zetu za kupata uhuru, Chama cha TANU kiliishirikisha Yanga na Simba katika vuguvugu la kuleta uhuru mpaka uhuru ukapatikana mwaka 1961. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka ule mpaka leo Chama cha Mapinduzi kimekuwa na sera kila kwenye tawi lao au kwenye Ofisi ya Mkoa kutenga eneo kwa ajili ya michezo. Hiyo kazi hawakuwahi kuicha. Kwa kukuthibitishia hilo, mlezi wa Yanga kwa kipindi kile alikuwa ni Mzee Karume na mlezi wa Simba alikuwa Mzee Kawawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1961 Tanzania ilikuwa katika mfumo wa vyama vingi, wala hakikuwa chama kimoja. Katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi 1961 mpaka 1965 bado TANU iliendelee kuhimiza ukuaji wa michezo na maazimio ya kujenga viwanja vya mpira halikuwahi kuwa azimio la Serikali, bali lilikuwa ni azimio la Halmashauri Kuu ya TANU na baadaye Halmashauri Kuu ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuwaambia, mwaka 1992 tulipokwenda kwenye mfumo wa kurudisha vyama vingi kwa mara ya pili, waliotaka kwenda kwenye vyama vingine walikwenda kwa hiari yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilipata swali la kujiuliza, hebu tuulizane hapa Mheshimiwa Lwakatare alianza na CUF. Je, alipojenga zile Ofisi za CUF baada ya kuhamia CHADEMA anadai matofali ya Ofisi zake? Ni kitu ambacho hakiingii akilini. Ninachotaka kusema, sera ya michezo ni sera ya CCM.

T A A R I F A . . .

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, tatizo ni tafsiri tu. Kujenga au kununua ni wazi ilitokana na michango ya Wanachama. Hela za wanachama ndizo zilizojenga. Mchango wa mwanachama mmoja mmoja ndiyo uliojenga hizi facilities. Hii siyo hoja ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya msingi ni kwamba from day one, TANU ikiazishwa na CCM ilikuwa na sera mahususi ya michezo, ndiyo maana mpaka leo kila kwenye Ofisi ya CCM kuna kiwanja cha michezo. Hebu tuwaulize nyie wenzetu, kwenye Ofisi zenu mna hata yadi mbili za watoto kucheza kitenesi? Sasa kwa nini leo mnataka kudai viwanja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwaambieni kitu kimoja, kukuthibitishieni kwamba michezo ni sehemu ya Chama cha Mapinduzi mpaka mwaka 1998 kwenye Katiba ya Yanga na Simba, viongozi wao, Marais wao walikuwa wanateuliwa na Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Vijana wa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyokuwa nasikiliza michango dhidi ya utendaji wa Jeshi la Polisi, ilifika hatua nikajiuliza kwa hizi sifa kwa nini tunakuwa na Jeshi la Polisi? Wamepewa sifa mbaya ambazo kwa kweli hawastahili hata kuendelea kufanya kazi. Nikajiuliza, kwa nini bado wanaendelea kuwepo? Pamoja na hizi sifa zinazotolewa dhidi yao, kwa nini bado wapo? Ikabidi nijipe homework kidogo ya kusoma na kujua kwa nini kulikuwa na Jeshi la Polisi? Kabla ya kuwa na utaratibu huu rasmi wa kuwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama na kuwa na Serikali yenye mihimili mitatu inayojitegemea, dunia ilikuwa inaishi kama wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa wewe ukilima shamba lako, mtu anakuja anaswaga ng’ombe zako, anaondoka nao. Mbabe akikuona mtaani, akijisikia kukuchezesha makofi ya kutosha, anakupiga makofi ya nyota nyota, utaratibu ulikuwa hivyo. Baadaye dunia ikaamua kuja na Jeshi la Polisi likiwa na kazi tatu ambazo dunia nzima kazi za Polisi ni hizo. Kazi ya kwanza ni kulinda raia na mali zao; kazi ya pili, ni kuzuia uhalifu na uvunjaji wa sheria; na kazi ya tatu, ni kusimamia utekelezaji wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kazi tatu ukiziangalia katika mtitiriko, karibu wote hapa tunaipenda sana kazi ya kwanza. Kazi ile ya kwanza ambayo ni kulinda watu na mali zao, kila mmoja hapa anapenda kulindwa; na kila mmoja hapa anapenda mali yake ilindwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya pili na kazi ya tatu ni ile kazi ambayo uhuru wangu unapoisha ndipo unapoanza uhuru wa mtu mwingine. Hapo tunatofautiana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikajiuliza, hivi hawa Askari wetu ni kweli wachache wana mambo ya hovyo, hivi kweli wote tunawapa lugha mbaya namna hii za kuwachoma, hatutambui mema yao hata kidogo? Walichofanyiwa Askari leo huku ndani kwenye mjadala ni ule msemo wa samaki mmoja akioza, wote wameoza. Ule msemo umepitwa na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msemo wa siku hizi, samaki mmoja akioza, atolewe yule mmoja, waliobaki tunaweka ndimu, pili pili na chumvi tunawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Askari wote wakabebeshwa mzigo hapa ikaonekana ni watu wa ovyo kama hawafanyi kazi. Hivi leo, tukubaliane tu kimsingi hapa. Sirro aamue traffic wote leo Dar es Salaam ondokeni kwenye zile traffic lights. Kwa sababu kati ya kazi za msingi za Askari siyo ku-control zile robot, kuita magari. Taa zifanye kazi yake; lakini inafika kipindi, taa zinashindwa, Askari pale wanatusaidia. Siku ikitokea wote waondoke pale, kitakachotukuta, Mungu nisaidie. Au leo ondoa Askari wa doria wote, halafu Panya Road waingie barabarani, tutatafutana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kawaida sana ya kuwaona Askari ni wema pale wanapofanya yanayotupendeza, lakini pale wanapofanya kazi ya pili ambayo inawezekana imemgusa jamaa yako, imemgusa jirani yako; hata inawezekana hata mimi akaguswa mtu ambaye kanigusa sana, sitaweza kufurahi. Hiyo ndiyo hulka ya mwanadamu. Siyo kila mwanadamu hufurahia pale anapopata msukosuko wa kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba kwa Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na IGP afanye mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, anapojitokeza Askari akaenda kinyume na maadili na utendaji wa Askari, hatua zake anazopaswa kuchukuliwa ziwe tofauti sana na raia wa kawaida. Nafahamu kuna Askari wanachukuliwa hatua za kinidhamu kwenye Kambi zao, lakini inapofika mahali Askari anafanya uhalifu against raia, aina za hatua ziwe tofauti na umma ujulishwe kwamba nini yule Askari mkosefu alifanyiwa. Wakiendelea kuwapa adhabu za kule ndani, jamii haitawaelewa na ndiyo maana wanakuja kuambiwa samaki mmoja akioza, wote wameoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana RPC wa Mara alivyoi-handle issue ile, ni issue mbaya sana. Unapokutana na Askari anamuua raia aliyemkamata, ni jambo baya, hatupaswi kulifurahia, hatupaswi kulichekea. Ila hatua alizozifanya RPC akasema tumemkamata, tumemfanyia moja, mbili, tatu na kesi inaendelea hivi na tumethibitisha hili liko sahihi. Sasa Askari, IGP ukiwaeleza Ma- RPC wako wote na Ma-OCD wa-handle suala kwa design hii hatutapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, nchi yetu inapakana na nchi nane. Kati ya hizi nchi nane tunazopakana nao hakuna nchi hata moja ambayo iko salama. Tafsiri yetu, usalama wa nchi yetu ni tenge, una matege, hauna miguu iliyonyooka. Nchi zote nane zinazotuzunguka ukianzia Kenya mpaka unakuja kumalizia Mozambique, hakuna nchi ambayo iko stable. Nchi zote zina chokochoko, zina mambo yasiyokuwa sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingine zina population iliyozidi kiasi kwamba ardhi haiwatoshi, nyingine zina njaa kali ambazo zinahitaji chakula. Katika mazingira haya, mikoa yetu ya mipakani ina hali mbaya sana sasa hivi. Kwa taarifa nilizozipata rasmi, Idara ya Uhamiaji tafadhali, wafanye kazi sana mipakani kuhusu raia. Mara baada ya kuona nchi yetu ina ardhi ya kutosha ya kulima na chakula kiko cha kutosha, jirani zetu wengi wameingia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tulipo- introduce elimu bure, kuna watu wameingia kwa sababu tuna jamaa zetu; nchi zote za mipakani haya makabila, kuna Wamakonde kwa ndugu zangu akina Bobali kule wako wengine Msumbiji. Ukienda Masai kule ndugu zangu wa Tarime wanapakana kule na Migori ni ndugu, ni jamaa tu wale. Kwa hiyo watu ku-cross ni kitu cha kawaida. Naiomba Idara ya Uhamiaji, sasa hivi ifanye kazi yake ya kukagua Uraia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, tumeitumia demokrasia vibaya na tumeshindwa kuitafsiri demokrasia vizuri. Demokrasia kwa asili yake haikuwahi kuwa ya Kiafrika. Demokrasia kwa asili yake haikuwahi kuwa ya Kitanzania. Demokrasia inatokana na maneno mawili ya Kigiriki na ndiyo wenye asili ya demokrasia; “Demons” inayomaanisha “people” na “Cratos” inayomaanisha “Power.” Kwa tafsiri nzuri na fupi “The people holds power.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya wanaoitazama demokrasia juu juu wameshindwa kujua vitu gani vinapima demokrasia. Kuna sehemu tunapima demokrasia inayoendana na watu ili tuthibitishe kweli hii demokrasia ni ya watu, ni pale ambapo kila Mtanzania anapochagua. Kwa hiyo, kipimo namba moja cha demokrasia na kuisema nchi hii ina demokrasia, yaani ina nguvu zinazotokana na watu, lazima kuwepo na election.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa election zinatofautiana. Kuna wengine wanachangua mtu, wengine wanachagua vyama, wengine wanakwenda winner takes it all, wengine wanakwenda PR System; kuna mifumo mingi duniani kutokana na mila na desturi. Sasa ninyi ndio mnajiamulia kwamba kwa mazingira yetu mfumo huu ndio unaotufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa kampeni za uchaguzi kupita kila kijiji ni mila na desturi za watu husika. Leo mnaweza mkauona huu mfumo unawafaa, kesho mkaona hauwafai. Tukumbuke kwamba unapoishia uhuru wangu, ndipo unapoanza uhuru wa mtu mwingine. Demokrasia nzuri ni ile inayotetea the right of individual. Unaposema the right of individual ni pamoja na kutokunikwaza, kwa nini haki yako wewe iwe kunikwaza mimi? Wewe unakuja na mkutano wako, mimi nasali. Kwa nini haki yako ilindwe, yangu isilindwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwambieni ndugu zangu, nchi yetu anayefanya active politics hatujafika asilimia 10. The rest 90 percent hawana habari na siasa zetu hizi, active politics za Majimbo, hawana kabisa. Wao wanakwenda asubuhi kulima, wanakwenda kufanya kazi zao, wanarudi makwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili tukilichukua demokrasia kwa kisingizio cha upuuzi wetu na upumbavu wetu, hatupaswi kuwa watu wa namna hiyo. Tuisome demokrasia tuijue. Demokrasia nzuri ni ile inayoendana na mila na desturi za watu husika na ile inayolinda haki za mtu mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara ya Kilimo. Nianze mchango wangu kwa nukuu maarufu sana iliyopendwa kutumiwa na Marais wawili wa Marekani kwa nyakati tofauti, Ronald Reagan na Abraham Lincoln naomba niisome hiyo nukuu; “You can not strengthening the weak by weakening the strong.” Kwa Kiswahili kisichokuwa rasmi ni kwamba “hauwezi ukamuimarisha mtu aliye dhaifu kwa kumdhoofisha aliye imara.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo ndiyo sekta imara kuliko sekta zote kwenye nchi yetu. Ni sekta pekee inayoongoza kwenye pato la Taifa kwa ripoti sahihi na statistics zinatuambia inaongoza pato la Taifa kwa asilimia 26.1 ikifuatiwa na viwanda asilimia 7.3, sekta ya madini asilimia 4.1 na sekta ya utalii asilimia 3.1 kwenye kuzo la pato la Taifa. Pia sekta hii ndiyo sekta inayoongoza kwa kuajiri Watanzania wengi zaidi ya asilimia 70, sekta hii ndiyo inayoongoza kwa export zaidi ya asilimia 85, sekta hii ndiyo inayoongoza kwa kutuhakikishia chakula kinapatikana nchini kwa asilimia 100. Pamoja na uimara wa sekta hii, tukaiangalia report ya Waziri mwanzo mpaka mwisho hatuoni sekta hii ikiimairishwa zaidi tukiona ikidhoofishwa kwa expense ya sekta nyingine, hii haiwezi ikawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa Tanzania wanahitaji matumaini, wamefikishwa sehemu wamekata tamaa kabisa. Wamekata tamaa katika eneo la uzalishaji, wamekata tamaa katika bei, wamekata tamaa katika mfumo mzima wa kilimo kuanzia mazao ya chakula mpaka mazao ya biashara hakuna zao hata moja ambalo tunasema hili ni salama, kila zao lina tatizo. Tulitarajia leo hii angalau tupate njia ya kutokea, lakini hatuoni matumaini katika sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri inasema kwa makadirio mwaka huu tunaweza tukazalisha mahindi tani milioni nane, maana yake itakuwa imepanda kwa tani milioni mbili kutoka mwaka jana milioni sita sasa tunakwenda milioni nane lakini uwezo wa NRFA kununua mahindi, wana uwezo na wamepanga kutumia tani 28,200 tu. Tafsiri yake tutakuwa na tani zaidi ya milioni saba hazitanunuliwa na NRFA, maana yake ili kiwepo chakula wakulima wa mahindi, lakini sisi kule kwetu nenda ukaanzie Rukwa, Katavi, Iringa, Mbeya, Njombe na Ruvuma wote katika ujumla wetu hatulimi mahindi tu kama chakula, tunalima vilevile mpunga unakubali, viazi vinakubali, ndizi zinakubali na mihogo inakubali. Ukituambia tule mahindi tu tusiuze maana yake unataka tufe kwa kwashakoo, kitu ambacho si sawa! Lazima hii sehemu iliyobaki ya mahindi tani milioni saba Waziri uje hapa na mchanganuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati za hizi tani 2,220 zitakazonunuliwa na NFRA utuambie una mpango gani wa soko la nje, una mpango gani kwa kiwango gani pia kwa kiwango kitakachobaki kitumike kama chakula ndani ya nchi yetu.Vinginevyo mimi sitakuunga mkono kwenye hoja hii na wakulima hawatanielewa nikikuunga mkono kwenye huo mchanganuo uliouweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la kahawa bado tunaendelea kuumia, tunaumia katika maana ya uhakika wa soko, tunaumia kwa maana ya uhakika wa pembejeo, tumeomba kwa muda mrefu sana Serikali ijaribu kutazama pembejeo kwenye zao la kahawa, kwa sababu ni zao la muda mrefu lilikuwa linatuletea fedha za kigeni kwa kiwango kikubwa sana, lilipoanza kusuasua vyama vya ushirika vilivyokufa na Serikali ilipoondoa mikono na miguu ndipo tulipoharibikiwa. Leo hii tunashukuru sana Waziri Mkuu kwa ziara alizofanya kwenye maeneo ambayo tunalima kahawa kwa kweli tumeona dhamira ya dhati ya Waziri mkuu kurudisha vyama vya ushirika viende kwenye mazao ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliopo site, mashaka tunayoyaona kwenye vyama vya ushirika ni makubwa, leo hii hawa watendaji wa vyama vya ushirika ndiyo walioshiriki kuviua miaka hiyo ya nyuma. Tunakwenda mwezi ujao kwenye msimu ujao, wakulima wa pamba wanalalamika watalaam hawapo, wakulima wa kahawa tunalalamika wakulima wa korosho tunalalamika, watumbaku tunalalamika, tutakwendaje? Katika huu muda mfupi katika crash program tunaiomba Serikali ipeleke watalaam kama kweli tunataka tufufue ushirika. Vyama vya Ushirika haya mazao ambayo mwaka huu tumeyahamasisha tumezalisha kwa kiwango kikubwa tunayahifadhi wapi? Kwa mfano pamba, consumption ya pamba yetu ndani kabla ya uzalishaji ilikuwa only 20% viwanda vyetu vya ndani vinaweza kuchakata, asilimia 80 tulikuwa tuna-export tumehamasisha pamba imezalishwa kwa wingi, tutaiweka wapi? Lazima kuwe na mkakati wa dharura vinginevyo tutakuja mwakani hapa tena tutaanza kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho naomba niseme kuhusu pembejeo, tumelalamikiwa sana kuhusu mawakala wa pembejeo wametiwa umaskini, wametoa huduma lakini hakuna tamko la Serikali linaloelezea haki yao watapataje? Kama hawajafanya kitu kizuri basi ieleweke, nani kakosea na nani kapatia, kuwaweka jumla tu kwa muda mwaka wa miaka miwili wakazika hela yao tunatengeneza umaskini uliokithiri, umaskini uliopitiliza. Lakini niseme neno moja Serikali ikiimarisha bei nzuri ya haya mazao hatutahiji mbolea ya rukuzu kwa sababu mbolea ya rukuzu inakuja kwa kuchelewa lakini muda mwingine inakuja hailingani na udongo wa eneo husika. Tungekuwa na utaratibu wa kununua mazao ya wananchi vizuri kwa bei nzuri tusingepata shida...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu imebarikiwa sana kuwa na maeneo mazuri yenye uwezo wa kuifanya mifugo ikaneemeka na maziwa makubwa na bahari yenye uwezo wa kutuletea samaki wa kutosha. Baraka hizi zisipotumika vizuri hazitofautiani na mwanafunzi mwenye akili darasani halafu hana jitihada, mwisho wa siku lazima atafeli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi ya asilimia 36 ya familia za Kitanzania zinajihusisha na ufugaji. Nchi yetu ni nchi ya pili Barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe, inazidiwa na Ethiopia tu. Nchi yetu kwa sasa ina ng’ombe zaidi ya milioni 30. Takwimu zinatuonyesha kila mwaka kwa wastani wanaongezeka ng’ombe milioni moja. Kwa hiyo, ng’ombe milioni 30 ni fursa. Naiomba Wizara isitazame mifugo na uvuvi kama tatizo na kinachotupatia shida ni kuitazama kama tatizo, tunajinyima fursa ya kuitazama kama fursa na kuifanya ikaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwa utaratibu ukachanganua, kama nchi yetu ina ng’ombe milioni 30, tuchukulie ng’ombe wanaoweza wakauzika, yaani tukafanya strategic farming tunavuna ng’ombe kimkakati, tuwavune kimkakati ng’ombe milioni tano kwa mwaka, tafsiri yake, tutapata shilingi bilioni tano. Ukipata shilingi bilioni tano ukaenda kwenye upande wa maziwa, kila ng’ombe walete lita moja moja, katika hii hesabu utakuwa na lita bilioni sita. Ukizidisha kwa lita moja kwa shilingi 1,000 kwa upande wa maziwa tu nchi yetu inao uwezo wa kupata trilioni1.8 kwa mwaka. Kwa upande wa kuuza ng’ombe hujagusa ngozi, hujagusa kitu chochote, unaweza ukapata trilioni 2.8 kwa mwaka. Kwa hiyo, sekta ya ng’ombe peke yake tukiitengenezea mkakati mzuri tunaweza kupata kwa mwaka trilioni nne.

Mheshimiwa Spika, tatizo ninaloliona, ni kwamba hatujatazama hii fursa na tukaangalia zile changamoto zake vizuri tukaziweka pembeni. Tukienda hivi tutafanikiwa.

Mheshimiwa Spika, nina mfano mmoja. Kulikuwa na DC mmoja kama sikosei alikuwa wa Iramba, alipofika Iramba akatengeneza programu ya kuku mmoja, nyumba moja, familia za Iramba zikazalisha Kuku wa kienyeji wengi sana, ndani ya muda mfupi watu walijenga, mpaka kuku tunaokula hapa ni mchango wa Nawanda alipokuwa DC wa Iramba. Kwa nini tusifanye hivi kimkakati kwenye ng’ombe?

Mheshimiwa Spika, ng’ombe wengi siyo tatizo, uchache siyo tatizo; tatizo, tunawavuna vipi? Tukitengeneza utaratibu wa kuwavuna ng’ombe kimkakati, kila mwaka mnaondoa ng’ombe milioni tano, wanazaliwa milioni moja; automatic echo system itaji-set. Ni jinsi tu ya kupanga. Kupanga ni kuchagua, tukiacha kama inavyokwenda, hatutaweza. Ng’ombe watakuwa tatizo, kilimo kitakuwa tatizo na samaki watakuwa tatizo.

Mheshimiwa Waziri Mpina, hoja hapa ni ndogo tu. Mifugo kweli kuna maeneo ni matatizo. Kuna maeneo wanaingia kwenye hifadhi, kuna maeneo kule wanashambulia mahindi, kuna maeneo wanasababisha soil erosion, lakini lazima tutengeneze utaratibu. Mifugo imeshakuwa utamaduni. Kitu kikishakuwa utamaduni, jinsi ya kukiondoa lazima kitaleta resistance. Njia pekee ni kwenda nacho sambamba, automatic kitakuja kitapotea. Kama ng’ombe wanakulete trilioni nne kwa mwaka hakuna mtu ambaye ataacha kuuza ng’ombe wake, atauza tu kwa sababu wanamletea faida. Ni kutengeneza tu modality nzuri ya kuuza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni huu utaratibu wa kupiga chapa. Utaratibu wa kupiga chapa huu umepitwa na wakati. Sijui unamgonga ng’ombe kiunoni, anatoka na muhuri mkubwa, tunapoteza thamani ya ngozi. Wenzetu wana hereni (pin). Pin ina serial number anagongwa sikioni hapa anakuwa na data, anajua joshoni atakwenda lini, leo atapigwa sindano sijui ya kifaduro, yaani kila kitu, chanjo, wenzetu wanafanya hivi. Kumpiga ng’ombe muhuri, ngozi automatic inapoteza thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Wizara ijaribu kwenda kwenye teknolojia, tuweke serial number, anagongwa, inakwenda kwenye database ya Wizara, unajua kabisa ng’ombe “x” alipata chanjo siku fulani, data zinakuja. Hata ng’ombe aliyekufa unajua kabisa alitoka kwenye familia ya mtu fulani kwa sababu tayari tuna-database.

Mheshimiwa Spika, lingine, kama nilivyosema awali, zaidi ya asilimia 36 ya Watanzania wanajihusisha na ufugaji, ama mbuzi, au ng’ombe au kuku na kitu kingine chochote kile. Mazingira hutofautiana, kwa maeneo ya kwetu sisi kule Mbinga hatuwezi kuwa na ng’ombe tukawachunga, maeneo hayako. Lazima maeneo yetu sisi, twende kwenye mkakati sasa ninaousema ndugu yangu Keissy namuunga mkono kuhusu kufuga kisasa. Kwamba utafuga ng’ombe wachache, eneo dogo, tija kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo mengine ukienda kufuga ng’ombe wachache, eneo kubwa unapata hasara. Haya mambo lazima tuyaangalie. Hii Dunia haifanani, Tanzania siyo kisiwa, lazima tui-map hii nchi yetu kiufugaji. zone zile zenye ardhi ndogo, mfumo wa ufugaji lazima utakuwa tofauti.

Mheshimiwa Spika, mimi hapa nina hekari 2,000 zinanitazama mbele yangu, nina ng’ombe 300, nifuge ng’ombe wanne kwa ajili ya nini wakati ardhi ninayo? Tunatofautiana. Kuna maeneo lazima tubane, ardhi haitoshi, lakini kuna maeneo tunaweza tukafuga tu, haina tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, mifugo ina thamani kubwa sana na kuna muda nadhani tunakosea. Mimi ni mkulima wa mahindi, sisi wakulima wa mahindi adui yetu namba moja ni mfugo kwa sababu akiingia ng’ombe anamaliza.

Mheshimiwa Spika, kule kwenye familia zetu, mtu mwenye ng’ombe mmoja, mwenye mbuzi wawili, mwenye kuku ni biashara ambayo inatusaidia sana. Thamani ya ng’ombe mmoja inakuwa kubwa kuliko magunia 20 ya mahindi. Ukitaka sasa hivi kumpeleka mtoto shuleni, magunia 20 ya mahindi hayauziki, lakini ng’ombe mmoja, uchu wa nyama haujawahi kwisha, ng’ombe anauzika, mbuzi anauzika. Kwa nini tusiitazame hii kama fursa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja la mwisho niseme kidogo kwenye kusafirisha samaki. Mheshimiwa Mpina tusijisahau kuwajua Watanzania. Hulka ya Mtanzania akitoka kwenda kumtembelea jirani, kama ametoka shambani ana kawaida ya kubeba unga, akitoka ziwani ana kawaida ya kubeba dagaa na samaki ili anakokwenda asiende kumtia mzigo anayemtembelea. Mtu kabeba kwenye gari samaki wawili, anakwenda kumwona jirani yake, tatizo liko wapi? Sasa hivi kwenye mabasi huwezi ukabeba hata samaki wa mboga. Nikikaa hapa sasa hivi nikitaka samaki kutoka Mwanza, nitafute cooler box, nitaweza?

Mheshimiwa Spika, haya mambo hebu tuya- moderate, tuyaweke katika hali ambayo tunajua kabisa kusafirisha samaki wawili, dagaa ni utamaduni wa Mtanzania ili anakokwenda kule asiwe mzigo. Anatoka anakwenda Dar es Salaam, hakuna mboga; anabeba dagaa zake kutoka Mwanza au samaki wake watatu, unaweka kwenye basi, unamtoza mtu fine. Why? Kwa nini tunajisahau kuwa sisi hatujafika hiyo stage ya kuwa na cooler box na kuwa na yale malori yana-pack samaki yanasafirisha? Hata yakiwepo, yatakuwa mangapi? Watakula wangapi hao samaki watakaosafirishwa kwenye hayo magari? Tuwe wa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nichukue fursa hii kumpongeza sana, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiangalia hii sekta ya madini. Kuchimba madini katika status yetu ya sasa siyo jambo ambalo ni too early au too late, maana yake kuna wengine wanalalamika tumeibiwa au tumefanyiwa nini, ukiangalia Tanzania ilivyo na madini ya kila aina kuanzia Mto Ruvuma kupakana na Msumbiji, mpaka North Mara, kila mkoa utakaogusa vitu vilivyoko chini havijawahi kuguswa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukurupuka tu kwenda kuanza kwenda kuchimba leo bila kutengeneza mifumo mzuri ya kisheria na ya kiutendaji katika sekta ya madini, hatutafanikiwa. Nimshukuru Rais na naishukuru sana Wizara, nimpongeze Waziri anafanya kazi vizuri sana na Naibu Mawaziri wake wawili, kila siku unawaona wanasikiliza wachimbaji wadogowadogo, unaona wako na wachimbaji wakubwa, unaona kabisa kuna vitu wanakusudia kututoa hapa tulipo kutupelekea mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema hapo mwanzo tuko kwenye mpito, kutengeneza mfumo bora wa kujinufaisha na madini yetu lakini wakati huo Serikali lazima ipate mapato kwa ajili ya kuleta shughuli za maendeleo kuendeleza watu wake. Haya mambo yote yanahitaji utulivu wa akili, ushirikiano na kupeana moyo. Huu mfumo ni mpya, hakuna mtu asiyejua biashara ya dhahabu ni ya familia kubwa duniani, wote tunajua, jinsi ya kuingilia hili lazima utumie ubongo mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu walianza hii biashara wanasema Karne ya 5 baada ya Kristo mpaka leo wameendelea kuchukua dhahabu na ndiyo wenye stock kubwa ya dhahabu duniani, Uingereza na Marekani. Kwa hiyo, unapoingia kupambana na hawa watu, lazima uwe na mfumo mzuri wa kisheria vilevile uelewa wa watu wako.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa minajili hiyo, naishauri Serikali kwamba inapoendelea na kazi yake nzuri ya kutengeneza mifumo, kwa namna yoyote ile mikataba inayotengenezwa na hao waliokuwa wakitunyonya siku zote na ndiyo tunaowategemea wanunue madini yetu, kwa haraka hawa hawawezi wakakubali kiurahisi, lazima kuna maeneo watatuhujumu. Lazima tuende na mpango ‘B’ kipindi tunategemea wawekezaji kuja, Serikali kwa dhati kwa sababu dhahabu haiozi hata ikachimbwa ikahifadhiwa hapa hapa kuna siku thamani yake itakua, niiombe Serikali ijielekeze kwa wachimbaji wadogo wadogo kwenye yale maeneo ambayo tumekwisha kuyaainisha, kwa sababu tumekwisha kuthibitisha kwamba wachimbaji wadogowadogo ndiyo wale wanaoleta tafsiri ya maendeleo, maendeleo is a social centred. Kila sehemu wachimbaji wadogo wadogo walipofanya kazi zao vizuri maeneo yale yalithibitika kuonekana yakiendelea sana watu wakijenga nyumba vizuri na kadhalika. Tukii-paralyse hii sekta ya wachimbaji wadogowadogo hatutafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Wizara, inafanya vizuri katika kuwasaidia ruzuku lakini iwasaidie vilevile katika elimu, itoe elimu ya biashara ya madini lakini itoe elimu ya madini katika ujumla wake. Niliwahi kuongea na mtu mmoja anafanya kazi katika sekta ya madini huko China, akasema Tanzania mna bahati ya kuwa na maliasili za kutosha lakini hamjasomesha vya kutosha watu wakawa na uelewa wa madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali watu wale 20, 30 tunaowapeleka kila mwaka kusoma nje, kwa rasilimali tulizokuwa nazo ni wachache sana, tuongeze nguvu ya kutosha tuwapate wengi ili kila mkoa uwe na wataalam na tufanye assessment vizuri, hata kama mwekezaji akifika tunajua exactly anakwenda kwenye madini ya aina gani. Wakija kufanya assessment wao matokeo yake wanatupunja na kutuibia nchi yetu inaendelea kuwa shamba la bibi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa sehemu moja, nimepitia hotuba ya Waziri, kwenye sehemu ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania. Hii taasisi ni muhimu sana katika sekta ya madini. Nimeangalia hapa, maduhuli yao ni shilingi milioni 350, mwaka uliopita walikusanya shilingi milioni 294, tafsiri yake hiyo ndiyo watumie kwenda kufanya research nchi yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, wana majukumu tisa, yote ni mazito, ila niyaseme mawili tu. Jukumu la nne wanasema, kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo hasa katika kubaini umbile na aina ya mbale, kutambua aina na ubora wa madini, pamoja na namna bora ya uchenjuaji. Hili jambo ni kubwa, shilingi milioni 350 haiwezi ikatosha hawa wakaweza kuifanya kazi hii nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, wana kazi nyingine ya kisayansi very technical, ya tano, kuratibu majanga asilia ya jiolojia kama vile matetemeko ya ardhi, milipuko ya volcano, maporomoko ya ardhi na kutoa ushauri wa namna bora kujikinga. Kwa bajeti ya shilingi milioni 350 hawawezi wakaweza ku-predict leo Oldonyolengai lini ile volcano ita- erupt. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ijaribu kuwaangalia hawa ndiyo watakaotusaidia kujua nchi yetu tuna rasilimali kiasi gani, ziko wapi, zenye thamani gani na zichimbwe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia majukumu au kazi za Kamati hizi mbili zilizoko mbele yetu. Awali ya yote, nichukue fursa hii kuwashukuru sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili kwa jinsi walivyotuwasilishia kwa ufasaha sana kazi zao; lakini pili, kutuelezea changamoto na namna bora ya kuondokana na zile changamoto ili Bunge lako Tukufu lipate fursa nzuri ya kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mnajili wa kuchangia hoja yangu ya leo, itoshe tu kuongea mambo mawili ambayo yanatokana na mjadala wetu wa leo; lakini vile vile katika kuwekana sawa ili kama kuna jambo linapotosha humu ndani, wote tulielewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mijadala imeendelea huku ndani ikielezea separation of power, good governance, uhuru wa hii mihimili mitatu na majukumu ya hii mihimili mitatu. Sisi kama Bunge tunapata fursa ya kufanya kazi zetu kwa Ibara ya 62, 63 na kuendelea ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposema mgawanyo wa kimajukumu wa hii mihimili mitatu, kama msemaji aliyepita, Mheshimiwa Salome Makamba aliposema separations of power halafu akaiacha hewani; separation of power haimaanishi hii mihimili mitatu ifanye kazi kwa kujitegemea, ndiyo maana kuna kitu kinaongezeka. Separation of power, checks and balance ikimaanisha, the three pillars should work independently, lakini katika kufanya kazi kule pamoja, inategemeana. Ndiyo maana kunakuwa na checks and balance.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kidogo kwa manufaa ya watu ambao hawakuwahi kumsoma Montesquieu na Jean-Jacques Rousseau hebu tuwasaidie kidogo waweze kujua. Huu msingi wa separation of power, unatokana na maandikio aliyowahi kuyaandika Baron De Montesquieu, huyu ni mwanafalsafa wa Kifaransa kwenye kitabu chake cha The Spirit of Law cha mwaka 1748. Katika kuelezea alisema tunapaswa kuwa na mfumo ambao kila organ inajitegemea ili kuepusha fusions of power kwenda kwa entity moja. Maana yake alikuwa anapinga kipindi kile mifumo ya aristocracy, alikuwa anapinga mifumo ya ki-monarchy, alikuwa anapinga mifumo ya autocracy. Sasa katika kuweka hivi ndio sisi hapa tunakuwa tunatunga sheria, sasa nikamshangaa sana ukiunganisha hoja ya Mheshimiwa Salome na ya Mheshimiwa Kubenea zinakuja kukutana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kubenea anasema sisi tutunge sheria, tukishatunga sheria, hatuwezi tena sisi tukatafsiri sheria, hatuwezi sisi tena tuka-enforce law. Tuna maeneo yetu sisi lazima tuishie, ndio maana kuna msemo wa Kilatini unaosimamia hilo unasema trias politica principle ukimaanisha (The separation of power, checks and balances). Hii mifumo lazima ifanye kazi kwa kutegemeana, huwezi ukawa na Mahakama isiyokuwa na aliyeanzisha shtaka yaani Executive katika maana ya Polisi. Huwezi ukawa na mtafsiri wa sheria bila kuwa na mtu aliyetunga sheria. Hawa watu wote wanafanya kazi kwa kushirikiana. Kikubwa zaidi kinachonishangaza, sikutegemea kama hii ingekuwa kweli ajenda ya kujadiliwa kwenye nyumba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Siku ya Wanasheria. Mwanasheria amemwalika Polisi, Mwanasheria kwa hiari yake mwenyewe ameamua kumwalika mgeni rasmi awe Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya au mtu mwingine yeyote, tatizo liko wapi? Hivi kweli ukiweka red carpet pale ukawaweka Majaji, ukamweka na Mkuu wa Mkoa, maana yake kweli Mkuu wa Mkoa ni mkubwa kuliko Jaji au Jaji Mkuu kuliko Mkuu wa Mkoa? Ile ni context, ile ni shughuli kama shughuli nyingine ina taratibu zake haiingilii mamlaka ya Jaji kama Jaji na wala haiingilii mamlaka ya Mkuu wa Mkoa kama Mkuu wa Mkoa.

T A A R I F A

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichotaka kusema hapa kwa kuanza hii mifano ya nyuma, hii mihimili mitatu inafanya kazi kwa kutegemeana sana. Bunge lako tukufu lisiwe sehemu ya kufarakanisha kwa kuweka chuki, nani mkubwa, nani mdogo, hoja ambazo hazitusaidii, ni vyema tujielekeze kwenye kuifanya hii mihimili ifanye kazi zake ufasaha, Wenyeviti wa Kamati wameelezea hapa changamoto zao, tuwasaidie kwenye kutatua changamoto ili kazi zao ziwe nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba niongee kidogo kwenye mobile court. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria na Mheshimiwa Kubenea ni Mjumbe mwenzangu, wote tulikuwa kwenye kikao, sielewi amefanya kwa makusudi kwa kutaka kupotosha au hajui maana ya mobile court. Ukisoma Ripoti ya UNDP kuhusu Mahakama zinazotembea, ripoti iliyofanyia kazi Sierra Leone, Democratic Republic of Congo na Somalia inaeleza mobile court au Kiswahili (Mahakama inayotembea). Mobile Courts are defined as the formal courts that conduct proceedings in location other than their home Offices, usually in remote areas where no justice service are available.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa anachotaka kuongelea ni kwamba, mobile courts si lile gari, mobile court ni kwamba zile huduma zinatoka Mahakamani tulivyozoea kuziona, zinaenda sehemu nyingine, zinaweza zikawa kwenye bajaji, zikawafikisha Mahakimu na timu wakafanya kazi zao kule au wakatumia mfumo mwingine wowote wa kufika kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnakumbuka scenario kama hii iliwahi kutokea kipindi cha genocide Rwanda, walikuwa na court zao zilikuwa zinaitwa Gacaca ambao watu walikuwa wanatoka wanakwenda maeneo ambapo watu hawajapata huduma na kwa sababu Mahakama zilikuwa zina msongamano sana wa watu na cell zilikuwa zimejaa, wakalazimika kutafuta mechanism ya kutatua matatizo. Mobile courts labda kwa lugha tunaweza tu tukasema, kuna hizi mobile banks mnaziona eeh, au mobile clinic haimaanishi kuwa lile gari, unaweza ukatumia chombo chochote…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri, kengele ya pili, Mheshimiwa Mlinga.

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Wizara hii. Wamekuwa wasikivu sana na tunaona kazi zinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachina wana msemo usemao, ‘ukitaka mafanikio ndani ya mwaka mmoja panda mahindi, ukitaka mafanikio baada ya miaka kumi mpaka ishirini panda miti, ukitaka mafanikio yatakayodumu kizazi na kizazi basi wekeza kwenye elimu’. Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi sana kutengeneza miundombinu ya elimu kwa kuhakikisha kila mtu mwenye uwezo wa kwenda darasa la kwanza anakwenda na afike mpaka form four na kujitahidi kuweka maboma, madarasa na madawati ili wanafunzi waende shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miundombinu mizuri inayoendelea kuwekwa na Serikali tuna changamoto kubwa moja ambayo kama nchi lazima tuwe na tafakari. Changamoto ni ubora wa elimu ambayo tunaitoa nchini. Ukiangalia kwa umakini matatizo yote ambayo yapo kwenye sekta ya elimu yameshindwa kujibu swali tunatoa elimu kwa ajili ya nini? Baada ya kutoa elimu matokeo ya ile elimu nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwetu sisi mafanikio ya elimu tunayahesabu kwa viwango vya madarasa yaani tulikuwa na wanafunzi 2,000 wenye uwezo wa kwenda darasa la kwanza wote wakaenda darasa la kwanza, wote wakamaliza darasa la saba, wote wakaenda form four, wote wakaenda chuo kikuu ndiyo kipimo chetu cha elimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa upande mmoja tunatatua tatizo moja tu we call it delaying techniques kumpa mtu matumaini kwamba kuna promise land inaweza ikaja huku mbele, kuna maana na asali iko huko mbele lakini in reality hicho kitu hakipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wetu wa elimu ulipaswa umuandae mwanafunzi katika level atakayoishia yoyote ile imwezeshe kuishi. Kama nguvu zake ni kuishia darasa saba akimaliza darasa la saba awe na uwezo wa kuishi. Kama ana nguvu za kufika form four, hawezi kwenda form five na form six, elimu aliyoipata imsaidie akifikia pale aweze kuishi hali kadhalika mpaka university. That’s why today unakuwa na engineer ambaye hawezi hata kutengeneza barabara na unakuwa na daktari ambaye badala ya kupasua mguu anapasua kichwa. Hii ni tafsiri kwamba elimu yetu haijamtengeneza vizuri wanasema umepata elimu lakini haujaelimika, tunatengeneza watu wenye elimu lakini hawajaelimika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri kuna mambo mawili lazima uyaangalie ndiyo yatakayotusaidia. Jambo la kwanza ni Sera yetu ya Elimu. Sera yetu ya Elimu ya mwaka 2014 ina changamoto mpaka leo haitekelezeki kwa sababu yawezekana stadi haijafanyika vizuri au tu kuna mtu anaamua ku-roll a ball, sisi kwenye mpira tunasema unaamua tu kukokota mpira uwende basi ukifika golini likiwa goli sawa mipira ukipaishwa sawa, tuna changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine mnaitengeneza wenyewe kwa nyaraka na miongozo mnayoitoa. Kwa mfano, Waraka Na.5 wa mwaka 2011 unasema mwanafunzi katika mwaka atahudhuria vipindi siku 194 lakini kama kutakuwa na mtoro hatafukuzwa shule mpaka asihudhurie siku 90 mfululizo, unatengeneza nini hapa? Huu Waraka unatengeneza mazingira ya mwanafunzi kuwa mtoro kwa sababu hatahudhuria darasani siku 30 atakuja siku mbili, hatahudhuria tena 30 atakuja siku tatu ili tu zile siku 90 mfululizo ambazo kwa mujibu wa Waraka mlioutoa ndiyo unazipa mamlaka shule na vyombo vyake kumfukuza huyu shule matokeo yake tunatengeneza wazembe ndani ya shule. Niiombe sana Wizara iangalie Waraka Na.5 wa mwaka 2011 ambao unasema mwanafunzi atafukuzwa shule tu endapo hatahudhuria vipindi mfululizo kwa siku 90, hii si sawa iangaliwe tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine, kipimo chetu cha ufaulu ili mtu atoke kidato cha pili kwenda kidato cha tatu anapaswa kuwa na D mbili au awe na A moja au na B moja au C moja. Taafsiri ya D mbili ya form two ni zero au ‘F’ ya form four. Maana yake from day one unaiandaa zero na kuipalilia iende. Kwa nini mtu huyu kiwango chake cha kuvuka darasa kiwe D mbili ambacho tunajua ni kiwango cha chini kabisa cha kufaulu, tutarajie mbele aje afanye mambo mazuri, kitu hicho hakiwezekani na tukienda hivi tutatengeneza kizazi cha zero cha kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunaongelea sayansi na teknolojia (ICT). Mpaka leo ni ya ajabu nchi yetu haina combination ya kidato cha nne yenye somo la ICT. University tuna computer science, kidato cha tano na sita hakuna ICT. Niiombe Wizara, najua mmeshafanya kazi, mko katika hatua za mbali kwenye hili hakikisheni ICT iwepo kati ya combination za form five na form six. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kuna jambo ambalo sielewi Serikali mnalichukuliaje kati ya uhusiano wa Serikali kwenye upande wa elimu na private sector. Kwa sasa inavyoonekana uhusiano wa Serikali na private sector kwenye elimu siyo kama hawa equal partners wanaotoa huduma katika jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia historia private sector imetusaidia sana kutoa elimu sehemu Serikali haikuweza kutoa kwa miaka mingi. Nitoe tu mfano, kwa Mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma mpaka mwaka 1997 kulikuwa hakuna hata high school moja, waliokuwa wanataka kusoma high school za Serikali ilikuwa lazima watoke nje ya mikoa hii niliyoitaja na ikitokea hakuna nafasi basi waende wakasome private kidato cha tano na sita kipindi kile zilikuwa shule tatu tu Mbeya ama akasome Irambo, Sangu na Meta, hawa watu wamesaidia sana ku-cover gap ambayo Serikali haikuweza kufanya katika kipindi kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unakuta kama kuna aina ya upendeleo kwenye kutoa adhabu kati ya shule za Serikali na shule za private endapo zitakuwa zimekosea. Mwaka jana kulikuwa na uvujaji wa mitihani wote tulizisikia shule za Serikali kule Chemba mlisikia na shule nyingine, zile shule za private zote zimefungiwa, zile shule za Serikali hazijafungiwa.

Mheshimiwa Mwyekiti, sasa watu wanauliza, hivi kumbe ukiiba mtihani kwenye shule za Serikali adhabu yake ni ndogo tu mwalimu anaondoka, ukiiba mtihani kwenye shule ya private unafungiwa, matokeo yake private wataendelea kuwa makini …. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye bajeti hii. Nchi yetu bado ni Taifa changa linalo-struggle sana kwa wananchi wake kuwa na uhakika wa kupata chakula, kuwa na uhakika wa kupata sehemu ya kulala na vilevile wanahangaikia sehemu ya kujihifadhi katika maana ya nguo na mambo mengine elimu na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hali ya namna hiyo, ni ngumu sana mtu unapoyahitaji yote kwa wakati mmoja kwa aina ya uchumi wetu ukayapata yote kwa wakati mmoja na kutokana na hali hiyo hiyo mahitaji yote unayataka kwa wakati mmoja, vilevile ni ngumu kukiacha kimoja ndiyo maana naungana sana na Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa jitihada zake za kwenda na miradi mikubwa wakati huo huo ikirekebisha mambo madogo. Haya mambo yote ndani ya nchi yetu siyo mapya yana mifano, wote mtakumbuka tuliposema tuwe na shule za sekondari kwa kila kata na wengine hapa mtakuwa mashahidi watu humu ndani waliwahi kusema ni vema tukaanza kutengeneza walimu, halafu baadaye tukajenga shule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kutokana na hali jinsi ilivyo hatuwezi tukasubiri watu kuzaliana watoto wakakua wasubiri kwanza mwalimu atakayepatikana kwa muda wa miaka saba, badala ya kujenga boma moja utakalolimaliza baada ya miezi mitatu. The same here, leo tunaongelea kuhusu viwanda mwingine anasema hapana tusijenge kiwanda twende kwanza tuka-produce, tukishazalisha kiwango cha hali ya juu sasa twende kwenye viwanda hili linakuwa ni kosa la pili linafanana vilevile leo unataka kujenga shule kipindi huna mwalimu, ukizalisha sana kabla hujaenda kwenye viwanda crisis yake itakuwa ni kubwa zaidi ni vema ukaanza kiwanda ukakikuza kiwanda kulingana na mahitaji yake kuliko ukaenda kwenye kuzalisha sana bila kiwanda yale malighafi utapeleka wapi? Ndiyo kwa maana nikasema nchi yetu ni nchi changa, inahitaji yote kwa wakati mmoja na yote lazima yaende hatuna njia ya mkato, kila utakalolichagua halitakuwa sahihi zaidi kuliko lingine. Ukisema leo uwekeze kwenye kilimo huwezi ukaacha afya, ukisema leo uwekeze kwenye afya hutaacha elimu. Kwa nchi yetu jinsi ilivyo hakuna namna, kweli kupanga ni kuchagua we don’t have choice, we must choose all of them. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili naomba niseme kidogo kwa mambo ambayo yameongelewa kwa muda wa miaka hii mitatu/minne kwa mfululizo miradi mikubwa sana mradi wa reli ya Mtwara, Liganga na Mchuchuma katika upande wa chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapoenda kwenye maendeleo makubwa ya viwanda na Mheshimiwa Waziri wa Fedha nitakuomba sana ulitizame hili kama nilivyosema awali kupanga ni kuchagua mjadala wa Liganga na Mchuchuma umekuwa mrefu mno, tunaanza sasa hivi reli ya kati ya kisasa Liganga na Mchuchuma imejadiliwa miaka na miaka kwa nini tusimalize hilo? Lakini jambo la pili, siyo kila kitu lazima tukifanye wenyewe. Reli ya Mtwara itakwenda kuunganisha Liganga na Mchuchuma, itapita mpaka kwangu pale Mbinga, itakwenda mpaka Mbamba bay kwa nini tusianze kwa PPP kwa theory ile ile bila kuogopa miradi mikubwa kwenda nayo pamoja, kupanga ni kuchagua lakini hatuna choice lazima tuyachague yote kwa wakati mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine hili naomba niliseme kwa utulivu kidogo; Mungu alipotuumba wanadamu, kwanza zile siku zake tano za mwanzo akasema na liwe jua na uwe mwanga, ardhi na mimea vyote vikawepo. Ilipofika siku ya sita akasema na tufanye mtu kwa sura na mfano wetu. Baada tu ya kumuumba na kumwambia zaeni mkaongezeke akamwambia ukavitawale viumbe vyote vya ardhini na ndege wote wa angani; maana yake nini kila kitu kilicho juu ya sura ya ardhi ya Tanzania lazima kitawaliwe bila masharti yoyote kwa sababu tu kinatija kwa mwanadamu.

Mheshimiwa Spika, leo hii mnaongelea mambo ya umeme, reli ya kati mnasema mto Rufiji, Stiegler’s Gorge, nakupa hoja nyingi za kubeza mimi niseme kitu kimoja, moja ya biblia imesema tutawale, tuweke umeme kwa njia zozote zile lakini kwa hoja ya pili ni hoja ya kisayansi watu wamesema sijui maji, yataisha, sijui nini kitatokea, kuna kitu kimoja kwenye sayansi na wanasayansi wa anatomy watanisaidia. Ukisoma introduction to anatomy inakuambia sensitivity, irratibity na adaptation; kila kiumbe duniani ameumbwa kwa ajili ya kukabiliana na mazingira. Ukiona jambo linakusaidia leo kwa ajili ya kupiga hatua moja hata kama ina negative effect akili yako mwanadamu umeumbwa kukabiliana na mapungufu yanayotokana na maamuzi yako.

Mheshimiwa Spika, tukienda leo pale kuweka ule mradi kuna watu wanasema kuna baadhi sijui ya swala hawanywi maji wanakula ule mvuke unaotokana na maporomoko tutapoteza utalii, si kweli; kama binadamu anayekuwa kwenye baridi akitoka kule Mbeya anakuwa na vinyoleo akifika Dar es Salaam miezi miwili vinyoleo vinapuputika kwa ajili ya joto. Huyu swala atashindwa ku- adapt nature?

Jamani tusiogope kutoa maamuzi kwa ajili ya nature, Mwenyezi Mungu katuumba na hizi rasilimali tuzitumie, tukiziacha zitakuja kuwa laana kwetu, hatuwezi leo kwenda kulipa gharama kubwa sana ya umeme kwenye majenereta miaka nenda miaka rudi umeme wa maji uko pale hata kama utakuja kuchukua kinu cha kwanza kitatoa umeme mwaka 2029 is better ku-make decision leo. Ukiacha kutoa maamuzi leo, kesho aje atoe nani? Waliotengeneza reli ya kati walikuwa wanajua tutahitaji namna hii wali-make decision, we must make decision hata kama hata maamuzi yanatuumiza sana lazima tuyafanye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini moja la mwisho niseme kuhusu Watanzania. Watanzania inabidi si neno zuri sana kulisema lakini inabidi niliseme inabidi kidogo tuangalie akili zetu zikoje, kuna muda hatujui tunachokitaka, ukiambiwa reli isipokuwepo matatizo, ikiwepo mbona miradi yote mikubwa inaenda kwa wakati mmoja. Ndege isipokuwepo matatizo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa...

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Spika, ukiileta...

SPIKA: Mheshimiwa Sixtus malizia.

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa maneno mawili ya mwisho; Watanzania tujifunze kujua tunachokotaka lakini la pili ni afadhali tuwe na uwezo na udhubutu wa kutoa maamuzi yenye tija hata kama yatakuwa na hitilafu gari lililoanza safari ni rahisi kulirekebisha kuliko ambalo halijaanza kufanya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru na mimi kupata nafasi ya kuchangia muswada huu jioni ya leo.
Mheshimiwa Mwneyekiti, kwa muda mrefu sana tasnia ya habari haikuwahi kupata hadhi inayostahili ndani ya nchi yetu. Pamoja na kazi nzuri ya tasnia ya habari katika kuhabarisha, kufundisha, kukosoa, kuwasaidia watu wenye matatizo kwa kuvumbua changamoto mbalimbali hata kufikia hadhi ya kuitwa muhimili wa nne wa dola, bado tasnia hii haikuwahi kulindwa, haikuwahi kuenziwa, haikuwahi kupata heshima inayostahili; moja, kwa mwandishi wa habari mwenyewe; pili, kwa chombo cha habari; na tatu, kwa mmiliki wa chombo cha habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na tasnia nyingine kama uhandisi, madaktari, wahasibu, wanasheria ambao wana chombo chao maalum kinacho-govern their conduct na kinachowalinda waendelee kulinda ile profession yao, wakue na watoe huduma bora. Hii tasnia kubwa ya habari haikuwahi kupata heshima hii. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza ndani ya nchi hii, heshima ya tasnia ya habari inapatikana. Kwa takribani miaka 23 toka tumeanza kusema kupigania haki za waandishi wa habari, haki za vyombo vya habari, tumeongea from unseen morning to unseen night bila kupata ufumbuzi wa kudumu kwa hawa waandishi wa habari. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Walatini wana msemo; “verba volant, scripta manent” wakimaanisha spoken words fly away, but written remain. Kwa nini nasema hivi? Kwa miaka 23 mnasema kuhusu haki za waandishi wa habari, you don’t write, you don’t put down, you don’t put in laws na matokeo yake wanalalamika na hamuwasaidii. Leo Serikali kwa mara ya kwanza inakuja na kujibu hili. Maneno tunayoyaongea yanapepea hewani, lakini tukiyaweka katika maandishi yanadumu. Hiyo ndiyo njia sahihi ya kuisaidia tasnia hii ya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu tutakaoenda kuupitisha unatutatulia matatizo yote tuliyokuwa tukiyaongea kutokana na upungufu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976. Kwa muda mrefu tumelalamika hapa Waziri anaweza akaamka asubuhi akalifungia gazeti. Kwa kupitia muswada huu, kuna marekebisho yaliyofanyika kwa kuweka Bodi. Sasa hivi tuna Bodi ya Ithibati, Mfuko wa Mafunzo na tuna Baraza Huru la Habari. Haya yote ni mambo mapya yanapatikana kwenye sheria hii yaliyotokana na upungufu wa sheria zilizopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema sasa tofauti ya uelewa ambao ninao na ninaamini wanaelewa lakini wanafanya makusudi kuwa hawaelewi; ni kwamba tunachokifanya hapa ni kufanya a total transformation ya tasnia ya habari from occupation to profession. Kuna watu hapa wameongea maneno mengi mimi mpaka nikachoka, nikasema dah, hili mpaka kaka yangu Mheshimiwa Zitto kalisema? Kwa jinsi ninavyomfahamu kaka yangu Mheshimiwa Zitto siyo mvivu wa kufikiri, anakuja anasema time is standing still, ana-compare mwaka 1961 kipindi wasomi wanahesabika, leo hii turudi kule tulipotoka? No bwana hatuwezi kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zitto ametoka hapo amekwenda na mfano wa pili wa Mheshimiwa Harrison Mwakyembe aliyeanza na tasnia ya habari akaenda akafika akawa mwanasheria. Tafsiri yake ni nini? Harrison Mwakyembe angekuwa mwandishi wa habari na angeendelea kuwa na taaluma ya uandishi wa habari, leo asingekuwa lawyer. Tunachokifanya hapa leo, tunataka waandishi wa habari wote wawe…
Siyo tafsiri yake wawe ma-lawyer, wawe na hadhi inayofanana na ma-lawyer; wawe na hadhi inayofanana na madaktari; wawe na hadhi inayofanana na ma-engineer. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo tunasema…, aah my God! (Kicheko/Makofi)
Anasema uandishi wa habari is passion. Mimi nikusaidie kaka yangu, kila kitu ni passion. Passion ni wito. Mcheza mpira, ana passion; mwanasheria, ana passion; daktari ana passion; kila mtu ana passion. What we are doing here ni kuifanya ile passion iwe profession. Ndiyo maana tumekuja na muswada. Msituondoe kwenye mstari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa watu siyo kwamba hawajui, wanajua ila wanafanya kusudi. Hivi kweli hakuna tofauti kati ya journalist as a profession na mtu mwenye uwezo wa kuandika habari? Tofauti ipo clear.
Huyu journalist tunamfanya anakuwa na profession kutokana na taaluma yake. Hii haizuii mawazo yako Mheshimiwa Zitto kama mchumi, haizuii mtu mwingine yeyote mwenye mawazo yake ya kilimo akayaandika kama makala yakatumika kwenye vyombo vya habari. Sasa kwa nini mnapotosha mambo ambayo yapo wazi dhahiri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu nahisi mnataka uandishi wa habari uendelee kuwa kindergarten usifike university. Tunachokifanya leo ni kuvusha daraja kuwaondoa waandishi wa habari kutoka eneo moja ambao mnawachukualia wa kawaida, tena mpaka mnawaita majina ya hovyo makanjanja, sasa wanakuwa na taaluma inayoheshimika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tofauti kubwa sana nimeisema kati ya reporter, radio presenter na mwandishi wa habari. Mimi nikikaa kwenye tv ku-broadcast kuelezea kipindi fulani I am not a journalist, mimi ni presenter.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa sasa msitake kwa sababu kuna watu hawakusomea uandishi wa habari, kwa karama ambazo Mwenyezi Mungu aliwaumba, wakikaa kwenye tv wanaongea vizuri sana, wakikaa kwenye redio wanaeleweka, haimaanishi kwamba wale hawatafanya kazi zile. Hii ndiyo hali ambayo ukiangalia muswada kuanzia page ya kwanza mpaka mwisho haijakataza mambo hayo, haijakukataza Mheshimiwa Zitto na taaluma yako ya uchumi kutoa mawazo ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, umemtolea mfano Mbarak Islam, yule alietoa taarifa ile ya kwanza. Yule katika lugha ya kawaida ni source ya taarifa, source ya taarifa, siyo taaluma. Mimi naweza nikawa source ya taarifa, wewe unaweza ukawa source ya taarifa na mtu yeyote anaweza akawa source ya taarifa. Kwa hiyo, msichanganye haya mambo eti ionekane kwamba hii Serikali ina nia mbaya kwenye muswada. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niwaambie waandishi wa habari, mimi nawapenda sana na kwenye hili tunawaondoa hapa mlipo muwe kwenye taasisi inayotambulika kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ndugu yangu Mheshimiwa Kubenea umeongea kuhusu shares; unajua mambo mengine haya, kabla hujaongea soma soma kidogo. Shares za nani? Zile shares hazisemi kwamba mimi hapa nikifungua gazeti langu na mwenzangu hapa shares zisomeke. Shares zinazoongelewa hapa ni zile za mmiliki anayetoka nje ya nchi; mambo mawili tofauti. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hili linafanyika? Kwa nini tunasema siku zote; tena hawa wanaosema, wamekuwa wakisema mashirika ya nje yakiingia humu ndani yana-control each and everything. Kinachofanyika hapa ni kuwawezesha Watanzania wawe na sauti ya asilimia 51 dhidi ya 49 ya wale wageni wanapokuja kuanzisha chombo cha habari. Hii ni hali ya kawaida kabisa. Nilitegemea washangilie na kufurahi sasa Serikali inataka ku-empower Watanzania wawe na uwezo wa kumiliki vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno haya machache naomba niseme yafuatayo; huu muswada ni mzuri sana, nawaomba wote tuunge mkono akiwemo na dada yangu Mheshimiwa Esther naye aunge mkono.
La pili, lazima tutofautishe tunachokifanya hapa, is not a status quo, siyo hadithi ya miaka 40, tunataka tutoke hapa tulipo twende mbele zaidi. Kama kuna maswali yoyote yanayotokana na modality, piga hatua kwanza, time can’t stand still. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kuja na marekebisho haya makubwa ya sheria yakiwa na maslahi mapana ya nchi yetu. Kwa haraka sana niungane na hoja zote zilizotolewa na Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria, tulipata muda wa kutosha wa kuangalia maeneo yote na tuliwasikiliza wadau, kwa kweli majibu tuliyopewa na Serikali kwa umoja wetu yalituridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, naomba nichangie vitu vingine viwili ambavyo havikusemwa; moja, niseme kwa kifupi kwenye Sheria ya Kudhibiti Ugaidi na pili nitaongelea kidogo kwenye NIDA. Septemba, 2015 mpaka Desemba, 2016 nchi yetu ilifanya tathmini ya kuona uwezekano wa nchi yetu kufadhili vitendo vya kigaidi. Baada ya kufanya hiyo stadi kwa kina na ukienda kuisoma kwenye financial intelligence unit report inaeleza nchi yetu ilikuwa na maeneo kama manne ambayo yanaweza yakasababisha ufadhili wa ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza lilikuwa ni kwamba tumezungukwa na nchi ambazo usalama wake hauko sawasawa; Jambo la pili lilikuwa kuwepo kwa vikundi vya ugaidi majirani zetu kama Al-Shabaab; Jambo la tatu lilikuwa kuna baadhi ya nchi zina vita za wenyewe kwa wenyewe; Jambo la nne mfumo wa uchumi wetu wa kutumia cash, miamala ya fedha, inaweza ikasababisha nchi yetu ikawa katika level ya kufadhili ugaidi. Sasa nchi yetu ikawa katika rate ya moderate, haiko kwenye kubaya sana haiko kwenye kuzuri sana, ila tusipofanya management nzuri tunaweza tukadondokea kwenye ubaya. Sasa Serikali kuja na sheria hii kwa upande wangu naona inajibu kabisa hili tatizo ambalo lilikuwa linaisumbua kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninalotaka niliseme sasa kwenye maboresho ya hiyo sheria; mwaka 2015 kiongozi mmoja anayesadikika alikuwa ni wa kigaidi kutoka kwenye kikundi fulani cha ADF alishikwa na milipuko hapa nchini, kesi yake ikashindikana kwa sababu sheria ilikuwa na upungufu ikabidi apelekwe nchini kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali inapokuja kumwongezea Waziri nguvu ya kutunga kanuni ni jambo jema sana ila niiombe Serikali iangalie kitu kimoja; kwenye kifungu cha 20 kiongezwe kifungu cha 20A kitakachoeleza offence, kielezee ile offence, matendo gani yatakuwa yanaonekana kuwa ni matendo ya kufadhili ugaidi. Tukiyaacha kama yalivyo tutamkamata mtu kama yule tuliyemkamata, kwa sababu Sheria ya Ugaidi haijaelezea vitendo gani ni vya ugaidi, ingawa tuna Sheria ya Armament Act na Firearm na Ammunition Control Act ambazo zinaelezea yale matendo, kwenye Sheria ya Ugaidi hayapo. Sasa niombe Serikali waweke kifungu kimoja wakienda ku-craft kutoka kwenye zile sheria mbili watapata kabisa offence watakayoitengeza, kwa hiyo mtu atakapokamatwa mwingine hataweza kupelekwa kwao, atahukumiwa kwa sheria zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, wameongelea vizuri sana kumfanya NIDA awe custodian wa taarifa zote za watu waliojiandikisha. Hata hivyo, nadhani kuna kitu kimoja wamekiacha; waweke na exception kwenye ile sheria kwa vyombo vya uchunguzi wawe na uwezo wa kuzipata zile taarifa, wakimwacha NIDA peke yake akafanya kila kitu, vyombo vya uchunguzi havitaweza ku-access zile information kwa ajili ya maslahi na usalama mpana wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.8) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.8) wa mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufinyu wa muda naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye eneo ninalotaka kuchangia hususan mabadiliko ya sheria kwenye Chama cha Mawakili Tanzania (TLS).

Mheshimiwa Spika, hiki chama kiliundwa mwaka 1954 kikiwa na Mawakili 14 au chini au plus au minus. Katika kipindi kile iliwezekana kabisa hao watu wakakaa katika chumba kimoja wakajadiliana, wakamaliza kila kitu, nadhani ule ndiyo ulikuwa msingi wa aina ya demokrasia wanayoongelea na mimi naikubali kabisa. Ndiyo msingi wa historia ya demokrasia hata kule Athens, Ugiriki walipoanza kushiriki kidemokrasia walikuwa wanakutana pamoja, wanajadiliana pamoja na kutoa masuluhisho pamoja. Walipozidi kuongezeka na changamoto za wingi wao zilipokuwa kubwa wakalazimika kuwa na uwakilishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa kwenye Kamati, wadau walitueleza sasa wanafika 8,000 na watakwenda 10,000 ikifika mwishoni mwa mwaka huu. Kwa jinsi Vyuo vya Sheria vinavyoongezeka na performance inavyozidi kuendelea kuna uwezekano ndani ya miaka michache tukawa na wanachama zaidi ya 25,000. Kwa watu wote wenye busara na wanaoangalia mbali na wenye mtazamo mpana wanajua kabisa sheria ya mwaka 1954 iliyoweka pamoja wakikutana wakiwa 14, leo wakiwa 8,000 imethibitisha pasipokuwa na shaka lolote inatakiwa ifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yawezekana tu mazoea kama ilivyokuwa kawaida watu huyakimbia mabadiliko, lakini ukweli wa mambo wametudhibitishia kwenye kamati ingawa wako 8000 haijatokea mkutano hata mmoja wao waliwahi kufika 2000 attendance. Tafsiri yake ni nini, tafsiri ya kwanza hawa watu wanahitaji uwakilishi, kama walikuwa 8000 kwa sheria hii hii hawakuwahi hata siku moja kwenye mkutano wao mkuu kule Arusha waliwahi kufika 2000 tafsiri yake wanahitaji uwakilishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuna watu wanasema kutengeneza chapters katika uwakilishi aidha katika level ya mkoa au katika bar yoyote ile ipe tafsiri yoyote ile inasema watu wanasema unawapunguzia watu uhuru wao wa kushiriki na kuamua mambo. Mimi bado sielewi unaposema mimi nikiwakilishwa na watu wangu nikienda kusema mambo ya watu waliyonituma ni kwamba nimepunguza uwakilishi. Kama hiyo, ndio kesi basi tukubaliane humu ndani hatuwakilishi watu tumebana nafasi ya watu wa majimboni kwetu wangekuja wote wakae hapa Bungeni tujadiliane, lakini hii haiwezi ikawa hoja, tunajadili TLS ambao ni mdau mkubwa wa sheria nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mkutano wa watu 8,000 mtajadili nini? Mtakaa siku ngapi? Tuna experience hapa mikutano yote mikuu tuchukue tu chama cha siasa ambacho okay kuna mmoja hapa amesema sisi tuna historia ya grassroot tumepatikana tumechaguana kwenye shida ile sio hoja, hoja hapo ni uwakilishi, umepatikana vipi jinsi ya taasisi yako ilivyo ndivyo itakavyokutafsiri. Hoja ya msingi kwenye congress mnapokutana kwenye mkutano wenu mkuu wa CHADEMA au mkutano wetu mkuu wa CCM au mkutano mkuu wa CUF, mkakutana pale watu 2,000 mnajadili nini ndio kwa maana uwakilishi baada ya kujua taasisi yenu ina watu wengi sana ili mwakilishe vizuri, ili mjadiliane vizuri, ili m-digest kila kitu vizuri kama taasisi mahususi ya kisheria nchini lazima uwakilishi uwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi yangu hata ukaweka hizi hoja nyingine zote ukaweka pembeni mimi naitizama TLS katika ukubwa wake katika miaka kumi ijayo. Naitizama TLS ikiwa na wanachama 50,000 halafu muone ugumu wa kupata congress, watalazimika kukaa kwenye uwanja wa mpira watu 50,000 itakuwa ni shida huku mbele, lakini si hoja itasumbua vilevile hata kwenye akidi kama hii ya leo tu 8,000 hawakuwahi kufika 2,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali na niipongeze kwenye hili tunapo pa kuanzia watu wa TLS wameshatuthibitishia katika 8,000 hawakuwahi kufika 2,000 wanahitaji uwakilishi vilevile ni mfumo bora utakaofanya wajadiliane vizuri. (Makofi)

Kuhusu asilimia 70 ya mawakili wote kuwa Dar es Salaam ni hoja ya kawaida kabisa, inatafutiwa utaratibu unaowezekana ili uwakilishi wa Dar es Salaam uwe mkubwa zaidi. Haiwezekani watu wa Dar es Salaam wako asilimia 70 wakafanana na watu wa Songea, mimi ninaamini kanuni zitatupelekea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kw amuda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mapunda kwa ushauri wako.

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)