Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Anthony Peter Mavunde (23 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja za Kamati zote mbili. Pia nichukue fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa Kamati zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijielekeze moja kwa moja kwenye hoja kama ambavyo zimewasilishwa na Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na eneo la kwanza ambalo limegusiwa na wachangiaji ikiwemo mapendekezo ya Kamati, imezungumzwa hoja ya kuhusu uanzishwaji wa Baraza la Watu wenye Ulemavu na litangazwe mapema.

Ni kweli kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 inayozungumzia watu wenye ulemavu, imeweka bayana kwamba kutakuwepo kuna Baraza la Watu wenye Ulemavu. Hivi sasa navyozungumzia tayari Serikali imeshakamilisha zoezi la kutoa mapendekezo la kumpata Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza la Ushauri la Taifa la Watu wenye Ulemavu. Kwa hiyo, muda sio mrefu uteuzi huu utafanyika na litazinduliwa rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia imezungumzwa hoja ya kwamba kuanzishwe kifungu maalumu kwa maana ya kasma ya masuala ya watu wenye ulemavu. Wizara tayari imeshafanyia kazi eneo hili na kifungu hiki kimepatikana. Kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 kifungu hiki kitaonekana na kitatengewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imezungumzwa hoja ya kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu. Kama Wizara, kwa maana Ofisi ya Waziri Mkuu, tumeshandaa rasimu ya mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu na tumeshawashirikisha wadau, tumefanya kikao cha Dar es Salaam na eneo hili, Mheshimiwa Ikupa analisimamia kwa ukamilifu sana. Kwa hiyo, muda siyo mrefu baada ya sehemu hii kukamilika basi tutaona namna bora ya uanzishwaji wa Mfuko huu wa Watu wenye Ulemavu kwa ajili ya maendeleo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ilizungumzwa hoja ya kuweka usimamizi mzuri wa fedha kwa ajili ya watu wenye ulemavu kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatengwa na Halmashauri. Ni dhahiri kwamba Serikali imeelekeza kila Halmashauri nchini kutenga asilimia 2 ya mapato yake ya ndani ili kuwawezesha watu wenye ulemavu. Katika eneo hili pia, tumeandaa rasimu ya mwongozo mzuri wa utoaji wa fedha hizi za asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu ili ziweze kuwafikia kirahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ilizungumzwa hoja ya namna ya kuwashirikisha watu wenye ulemavu kwenye shughuli za michezo. Niseme tu kwamba kama Wizara tumekuwa tukifanya hivyo pale yanapotokea maombi. Mwaka 2009 tuliwahi kuisaidia Timu ya Watu wenye Ulemavu wa Akili ambao walikwenda katika Bara la Asia kushiriki mashindano ya mpira wa miguu na mbio. Halikadhalika kwa sababu BASATA na Baraza la Michezo Tanzania ziko chini ya Wizara, tutahakikisha kwamba tunafanya ushirikiano wa kutosha ili kundi hili pia liweze kuangaliwa katika masuala ya michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa pia hoja kuhusu Mfuko wa Maendeleo wa Vijana. Eneo hili limezungumziwa sana na moja kati jambo ambalo limezungumzwa ni usimamizi na udhibiti ili kuhakikisha kwamba fedha za mfuko huu zinawafikia walengwa ambao ni vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zote ambazo zinadaiwa fedha ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambapo vijana wamekopa na fedha hizi zinatakiwa zirudishwe, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tumeanza kuchukua hatua kuzifuatilia fedha hizi ili ziweze kurudishwa. Wale ambao tumeshawapa taarifa ya kurejesha fedha hizi bado hawajafanya kwa wakati, taratibu za kisheria zitachukuliwa kuhakikisha kwamba fedha hizi zinarudi ili vijana wengi zaidi waweze kukopeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa tu, fedha za Mfuko wa Maendeleo wa Vijana zimelengwa kwa ajili ya vikundi vya vijana ambapo utaratibu wake ni kwamba kila Halmashauri nchi nzima inaandaa SACCOS ya vijana yenyewe ndiyo inayokopa kupitia Halmashauri na ndiyo inayokwenda kukopesha vikundi vya vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza hoja ya Mheshimiwa Bobali, kwa kweli nimeshindwa kuelewa vizuri Mheshimiwa Bobali na nilitamani angekuwepo hapa Mbunge mwenzangu kijana kabisa anasema kwamba haujui Mfuko wa Maendeleo wa Vijana na vijana wake hawajanufaika. Nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa Bobali kwamba mwaka 2016 nilikwenda mwenyewe katika Wilaya ya Lindi Vijijini ambako nilikuwa na Programu ya Kuwawezesha Vijana Kiuchumi. Katika programu ile walikuwepo vijana 683 wakitoka katika majimbo mawili, la Mchinga na Mtama na Mheshimiwa Nape alikuwepo Mheshimiwa Bobali hakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hilo vijana hawa waliwezeshwa kiuchumi lakini pia baada ya kuhitimu mafunzo yao ya kuwezeshwa kiuchumi tulitenga utaratibu mzuri wa kuwakopesha kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Ninavyozungumza hivi sana, kwenye Wilaya ambayo anatoka Mheshimiwa Bobali, tumeshakopesha vikundi na moja ya kikundi ambacho kimekopeshwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 ni kikundi ambacho kinaitwa Juhudi kilichokopa Sh.3,500,000 na kingine kinaitwa Kitongamano walikopa Sh.6,000,000 na kikundi cha Mshikamano. Nikimsikia Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba haujui mfuko huu na vijana wake hawajanufaika jambo hili si la kweli, mfuko huu unawafikia vijana wengi nchi nzima na vijana wengi wamenufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia yalikuja mapendekezo hapa ya kutaka kuwe na namna bora ya mfuko huu kuwafikia watu nje ya mfumo wa SACCOS. Sheria ya kuratibu mfuko huu ilitungwa mwaka 1994. Sisi kama Wizara tukaona ni miaka mingi imepita, kwa sababu masharti ya mwongozo wa mfuko huu inataka SACCOS ndiyo ikopeshwe, tumeenda mbali zaidi, hivi sasa tumeanza kupitia mwongozo wetu ili baadaye kuruhusu vikundi vya vijana kwa maana ya makampuni na vikundi tofauti tofauti, nje ya SACCOS na wenyewe waweze kukopa. Kwa hiyo, naamini kabisa kwamba mfuko huu utawafikia vijana wengi zaidi na wengi watakopa kwa ajili ya kupata fursa hii ya kiuwezeshaji kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Ofisi ya Waziri Mkuu tunaendesha Programun ya Ukuzaji Ujuzi Nchini ambayo ina lengo la kuwafikia vijana takribani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami napenda nichukue fursa hii kwanza kabisa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa heshima kubwa aliyonipa kuendelea kuhudumu katika eneo hili na imani kubwa aliyonionesha katika eneo hili ambalo mpaka hivi sasa nalihudumu kama Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru sana Makamu wa Rais, pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa miongozo yao, lakini kipekee kabisa niwashukuru sana Mawaziri, mama zangu wapendwa kabisa, mama Jenista Mhagama na dada Angella Kairuki kwa namna ambavyo wameendelea kunipa ushauri na kuniongoza na upendo wao wa dhati kwangu. Mwenyezi Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu Mheshimiwa Ikupa Stella Alex kwa ushirikiano mkubwa anaonipa katika kutimiza majukumu yangu kama Naibu Waziri. Tunafanya kazi kwa ushirikiano na upendo mkubwa sana, nakushukuru sana dada Ikupa. Niwashukuru vile vile Makatibu Wakuu wote, ambao siwezi kuwataja lakini nawashukuru wote chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, niwashukuru Watendaji wa Wizara, lakini mwisho niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini ambao walinionesha imani ya kuwa Mbunge wao, nawashukuru sana kwa upendo wao na naendelea kuwafanyia kazi ya kuwatumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sasa naomba nijielekeze katika kujibu na kufafanua hoja ambazo zimeletwa na Waheshimiwa Wabunge. Hoja ya kwanza ambayo nitaanza nayo, ni hoja ya ujumla juu ya miradi ya kukuza ujuzi ambayo inatekelezwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Waheshimiwa Wabunge wanaonesha namna ambavyo pia Serikali tuwashirikishe katika utekelezaji wa miradi hii ili wapate uelewa, lakini vilevile, wawe wanai-own wenyewe kwa maana ya nafasi zao za uwakilishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli; chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu tunatekeleza miradi ya ukuzaji ujuzi hasa kwa vijana na ambao katika mradi mmoja tulioanza nao hivi sasa mkubwa kabisa, ni mradi wa kitalunyumba ambao utakwenda kuwagusa vijana 18,800 nchi nzima. Mradi huu wa ukuzaji ujuzi, ni mradi ambao utakwenda kuifikia kila halmashauri vijana 100, ambapo vijana 80 watafundishwa kulima kupitia kitalunyumba, na vijana 20 watafundishwa kutengeneza kitalunyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika awamu ya kwanza tunafarijika kusema kwamba, wale vijana walioanza katika awamu ya kwanza hivi sasa wameshapata ujuzi wa kutengeneza vitalunyumba na wameanza kuaminiwa na kupata ajira katika baadhi ya makampuni hapa nchini. Katika utekelezaji wa mradi huu, kama Waheshimiwa Wabunge walivyosema, utaratibu ni kwamba, Ofisi ya Waziri Mkuu iliandika mkoani na baadaye, mkoani walitoa taarifa katika wilaya, lakini kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambao pia alielekeza kwa Waziri wetu, ambaye pia ameshusha kwetu, Mheshimiwa Jenista Mhagama, kwamba hivi sasa miradi hii yote katika awamu ya pili ya utekelezaji tunaandaa utaratibu maalum wa kuhakikisha kwamba kila Mbunge katika eneo lake anafahamu mradi unavyotekelezwa na atapewa taarifa za awali. Tumeanza katika kutoa semina na kuelimisha Waheshimiwa Wabunge juu ya utekelezaji wa mradi huu, ambao naamini kabisa utakwenda kukidhi mahitaji katika kutatua changamoto za ukosefu wa ajira na ukosefu wa ujuzi kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ambayo ilizungumzwa hapa, ni hoja ya mkakati wa kusaidia ajira kwa vijana hasa vijijini. Ni hoja ambayo Wabunge wengi wameisema na wanataka kusikia mkakati wa Serikali. Mkakati wa kwanza wa Serikali katika kuhakikisha tunatatua changamoto ya ajira hasa kwa vijana. Eneo la kwanza tunalolifanya ni katika kutoa elimu hasa katika kundi hili kubwa la vijana, kwanza kabisa kwenye tafsiri ya neno ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sera ya Ajira, ya mwaka 2008, ajira ni shughuli yoyote halali inayomuingizia mtu kipato. Kwa hiyo, tunaanzia hapo kwanza kuwafanya vijana wetu na wananchi wote kwa ujumla kuelewa nini maana ya ajira kwa sababu kumekuwepo na dhana kwamba, ili mtu aonekane ameajiriwa lazima awepo ofisini tu. Kwa hiyo tumeanza na eneo hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, tunafahamu haiwezekani na katika hali ya kawaida watu wote kuweza kupata ajira katika mfumo rasmi. Kwa hiyo katika hili pia tunachokifanya ni kuelezea fursa zilizopo katika sekta isiyo rasmi ambayo pia itawezesha watu wengi zaidi waweze kupata ajira. Kwa hiyo, katika eneo hili, mkakati wetu ni kwamba hivi sasa kama Serikali kupitia azimio la mwaka 2014, ambalo lilikuwa ni chini ya aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, ilifanyikia Dodoma la Wakuu wa Mikoa wote kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali kwa ajili ya vijana. Mpaka ninavyozungumza hivi sasa, tayari yametengwa maeneo ya takribani ekari laki mbili kumi na saba elfu, mia nane na themanini na mbili nchi nzima kwa ajili ya shughuli za vijana za uzalishaji mali. Kwa hiyo lilikuwa ni eneo la kwanza katika mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni eneo la uwezeshaji, uwezeshaji wetu unafanyika kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Vijana ambao mpaka hivi sasa tayari tumeshavifikia vikundi takribani 755 na tayari bilioni 4.5 zimetoka kwa ajili ya kuwawezesha vijana. Katika eneo hili fedha zinazotumika ni zile asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ambazo pia zinatumika kama sehemu ya kuwawezesha vijana kwa ajili ya kupata mitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambayo ipo zaidi ya 19 ambayo ukiiunganisha kwa pamoja ina ukwasi wa kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kwa pamoja yake, pamoja na benki ya kilimo ambayo ipo maalum kwa ajili ya kuwawezesha vijana na makundi mengine katika jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika eneo hilo la uwezeshaji pia, tunaendelea kuhakikisha kwamba vijana wengi zaidi wanapata fedha za mikopo ili wafanye shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetambua moja ya mkakati mwingine wa kusaidia na kutatua changamoto ya ukosefu wa ajiri ni kwenye eneo la ujuzi. Kwa mujibu wa tafiti ya mwaka 2014, ambayo inaitwa, Intergrated Labour Force Survey inasema nchi yetu ya Tanzania ina takribani watu wenye uwezo wa kufanya kazi milioni 22.3. Changamoto kubwa iliyokuwepo ni katika eneo la ujuzi, ambapo watu wenye ujuzi wa juu kabisa ni asilimia 3.6, watu wenye ujuzi wa kati ni asilimia 16.5 na watu wenye ujuzi wa chini ni asilimia 79.9. Ili kwenda kuwa nchi ya kipato cha kati, ifikapo mwaka 2025 viko vigezo vimewekwa na moja ya kigezo kilichowekwa, ni katika eneo la nguvu kazi, lazima uwe una nguvu kazi yenye ujuzi wa juu kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nchi yetu ya Tanzania hivi sasa, tunatekeleza mradi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambao lengo lake ni kuwajengea ujuzi vijana wetu wapate nafasi ya kuweza kujiajiri wenyewe kupitia ujuzi wao. Ninavyozungumza hivi sasa, tuna mradi ambao unaitwa ni Mradi wa Kurasimisha Ujuzi kwa Vijana, ambao wana ujuzi lakini hawajapitia mfumo rasmi wa mafunzo. Hivi sasa wataalam wetu na wakufunzi wa VETA, wanawapitia vijana hawa mtaani, ukienda leo mtaani, kuna kijana anajua kuchonga vitanda vizuri, anajua kupaka rangi vizuri, ni fundi mzuri wa magari, hajawahi kusoma VETA, hajawahi kusoma Don Bosco.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inachokifanya ni kurasimisha ujuzi wake, tunakwenda mtaani na wakufunzi wa VETA wanakaa nae, wana-address upungufu alionao then tunampatia cheti cha VETA cha ufundi pasipo yeye kwenda kusoma VETA. Mradi huo kwa mwaka huu utawafikia takribani vijana elfu kumi. Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yao wajiandae tutawafikia kwa ajili ya kuwawezesha vijana wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunao mradi wa mafunzo ya ufundi stadi ambao tunautekeleza chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu inagharamikia mafunzo na fedha ya kujikimu kwa vijana hawa wa Kitanzania ambao tunawafundisha ufundi mbalimbali; kujenga, umeme, ushonaji, masuala ya kompyuta na fani zinginezo. Katika eneo hili tumepiga hatua kubwa sana, tumeshawasomesha vijana zaidi ya 2,278 katika awamu ya kwanza na itaendelea, lakini asilimia kubwa tayari wameshapata kazi na wengine wamejiajiri wenyewe. Kwa hiyo, ni dhahiri kuonesha kwamba program hizi za ukuzaji ujuzi zitasaidia sana katika kutatua changamoto katika eneo hili la vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ilisemwa hapa, ni kuhusu mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri lakini vile vile na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana namna ambavyo inachelewa kurejeshwa katika kundi hili kubwa la vijana.

Ni kweli kulikuwa kuna changamoto hiyo lakini Serikali hivi sasa kwa kushirikiana na halmashauri tumeendelea kufanya ufuatiliaji ili fedha hizi za mikopo katika makundi haya ya vijana, zirudishwe kwa maana ya Mfuko ule ambao ni revolving ili vijana wengine waweze kukopeshwa. Mpaka hivi sasa takribani shilingi milioni 356 zimerejeshwa kama sehemu ya marejesho ya mkopo ambapo vijana wengine pia watapata fursa ya kupata mkopo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imejitokeza hoja nyingine hapa kuhusu vibali vya kazi na imezungumzwa na Wabunge wengi sana. Mwaka 2015 Bunge hili tukufu lilitunga Sheria Na.1 ya Uratibu wa Ajira kwa wageni hapa nchini. Kwa mujibu wa sheria ile, kifungu 11 kinatamka bayana mtu mwenye mamlaka ya kutoa kibali cha kazi ni Kamishna wa Kazi ambapo mpaka atoe kibali lazima ajiridhishe kwamba kazi inayoombwa hatuna ujuzi wa namna hiyo ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ndivyo sheria inavyosema iliyotungwa na Bunge. Kamishna anachokifanya ni kusimamia sheria. Kamishna huyu tuliyenaye hivi sasa, Wakili Msomi Gabriel Malata anafanya kazi yake vizuri sana, ameonesha usimamizi uliotukuka na si kweli kwamba ni Mungu mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria hii, mtu akipeleka maombi ya kibali cha kazi inapaswa apewe ndani ya siku 14. Hivi sasa vibali vya kazi vinatoka ndani ya siku saba. Sisi tunaamini kabisa kwamba Tanzania siyo kisiwa, hatuwezi kuishi wenyewe. Tunapenda pia kupata wageni kwa ajili ya watu wetu kupata ujuzi lakini tunachokisema pamoja na hayo yote sheria yetu pia na yenyewe ichukue nafasi yake kwa maana ya vile vigezo vilivyowekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili najua kumekuwa na kelele nyingi sana ya baadhi ya wadau ambao wengi pia hawasemi ukweli. Kamishna anachokifanya ni kuangalia vigezo mbalimbali katika utoaji wa vibali lakini hajiongozi mwenyewe kwa mapenzi yake na nafsi yake, ni sheria ndiyo inamtaka afanye hivyo. Kuna baadhi ya maeneo kuna udanganyifu kiasi kwamba Kamishna akiachia tu kila mtu aje afanye kazi hapa, vijana wetu pia na wenyewe watakosa fursa ya ajira kama ambavyo Ibara ya 173 ya Chama cha Mapinduzi imeeleza katika Ilani ya Uchaguzi, kinachofanyika hapa ni utekelezaji wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sisi Ofisi ya Waziri Mkuu siyo robot kwamba hatuwezi kuangalia mazingira ya dunia ya leo, tunahitaji na tunawapenda wawekezaji. Hivyo, nitoe rai kwa wawekezaji wote nchini, kumekuwepo na tatizo la wawekezaji hawa katika ufuatiliaji wa vibali kuwatumia watu wa kati ambao wamekuwa wakileta shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi yetu hivi sasa tumeunganishwa katika mfumo ambapo sasa tutatoa vibali vya electronic ambavyo vitapunguza urasimu. Mimi nataka mwekezaji mmoja aje anitolee mfano kwamba amewahi kuleta maombi yamekaa miezi sita hajawahi kujibiwa. Hivi sasa jambo hilo hakuna katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Mtu akileta maombi leo, kama yamekamilika ndani ya siku saba anapata kibali chake, provided awe amekidhi matakwa yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunakwenda katika mfumo mzuri zaidi, kibali kitatoka chini ya siku saba kama mtu akikamilisha nyaraka zake. Tunaunganisha sasa mfumo wa vibali vya kazi na residency permit. Hivi sasa ndiyo tunakwenda katika utekelezaji wa programu hiyo, mtu akiomba kibali Kamishna wa Kazi atakiona na Uhamiaji wataona katika mfumo hapo hapo, Kamishna akimkubalia dakika hiyo hiyo Uhamiaji kule wataona wata-issue residency permit. Kwa hiyo, tunatoka kwenye mfumo wa siku saba mpaka siku moja ikiwezekana katika utoaji wa vibali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumekwenda mbali zaidi, kwenye eneo la rufaa, mimi ndiyo nashughulikia rufaa zote za vibali vya kazi. Hivi sasa rufaa zinazotoka TIC kwa mfumo tuliouweka hata nikikaa hapa ndani ya Bunge najibu rufaa zingine kupitia simu. Ni utaratibu ambao tumeuweka kwamba rufaa yoyote itakayoingia ili tusiwacheleweshe wawekezaji naiona moja kwa moja naijibia hapa hapa na kutoa maamuzi kama imekubaliwa au amekataliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kwenye eneo hili. Eneo hili lina changamoto kubwa sana na maneno huwa yanakuwa mengi sana. Katika eneo hili nataka niwaambie ndugu zangu Watanzania na Waheshimiwa Wabunge ambao mko hapa, hatufanyi kazi kwa kumuonea mtu, hatufanyi kazi kuwafukuza wawekezaji, mimi nasimamia tena eneo la ajira nafahamu maana ya uwekezaji. Mwekezaji mmoja akija hapa akiwekeza tunapata fursa za ajira, vijana wengi zaidi watapata ajira. Nitakuwa mtu wa ajabu kuwa mtu wa kwanza kuwafukuza wawekezaji kupitia sharia. Nachokisema taratibu pia zifuatwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli Waheshimiwa Wabunge, atoke mtu Pakistan aje kuunga nyaya hapa na mimi nitoe kibali cha kazi? Tuwaache vijana wa VETA, Don Bosco, tumchukue mtu wa Pakistan aje kuunga nyaya Tanzania? Haiwezekani!

Kwa hiyo, tunachokifanya ni kusimamia sheria, naomba mtuunge mkono na mumpe moyo Kamishna huyu, anafanya kazi kubwa sana. Mkianza kumzonga na maneno hapa ndugu zangu mtamfifisha moyo, mpeni moyo, kazi yake ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii; la kwanza ambalo ninataka nianze nalo naiomba Serikali sasa ni wakati muafaka kwa kuanza kutenga bajeti kuzisaidia timu zetu za Taifa. Ukienda duniani kote Serikali inazibeba timu za Taifa, ni Tanzania peke yake kwa sisi hapa Afrika ambapo timu ya Taifa inakwenda kwenye mashindano makubwa pasipokuwa na utaratibu maalum wa kuwasaidia kufika huko, wanakwenda kwa kuunga unga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo ninaiomba Serikali ione haja ya kuanza kutenga bajeti kubwa wafanye uwekezaji mkubwa msiishie kuwapa bendera tu wakati wanaondoka lakini msimamie pia na maandalizi yao. Nchi nyingi zinasaidia timu zao, Mheshimiwa Waziri nikuombe katika hili kama kweli tunataka Taifa Star na timu nyingine zifanya vizuri lazima tuwekeze, wakienda hivi wanavyoenda kila siku tutakuwa tunawaita kichwa cha mwendawazimu na vilevile tutakuwa hatuwatendei haki kwa sababu maandalizi yao hayaendani na kile ambacho sisi tunakitarajia. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri katika hili mjitahidi sana kuhakikisha kwamba tunatenga fedha kwa ajili ya timu zetu mbalimbali za Taifa, hii itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili naomba niungane na hoja ya Mheshimiwa Sanga na Wabunge wengine wote waliochangia juu ya miundombinu ya viwanja vyetu. Ninaanza kwa kuwapongeza kwanza Azam kwa uwekezaji mkubwa sana ambao wameufanya, Azam hivi sasa ukiangalia mpira ukioneshwa Azam kwenye HD ni kama unaangalia ligi ya Uingereza kwa namna ambavyo kamera wanazozitumia na uwekezaji mkubwa ambao wameufanya ni uwekezaji mkubwa sana, lakini ukienda katika aina za viwanja vyetu ukiondoa uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam; ukiondoa uwanja wa Kaitaba, Kagera, hivyo ndivyo viwanja ambavyo mpira unaweza ukachezwa watu wakauona vingine vyote mpira una kuwa unpredictable kwa sababu mchezaji huwa anajua mpira ukidunda hapa unadondokea pale, lakini kwa aina ya viwanja tulivyonavyo huwezi kujua mpira unadondokea wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na muda mwingine unaweza ukawalaumu watu wa viwango vibovu kwa sababu ya aina ya miundombinu ya viwanja tulivyonavyo. Haiwezekani tukawa tunaonesha ligi ambayo viwanja vyake vina vumbi hatueleweki, niiombe Serikali la kwanza kabisa kama Mheshimiwa Sanga alivyochangia tuiombe Wizara mkae na Chama cha Mapinduzi ambao ndio wanamiliki viwanja hivi mzungumze kwa pamoja ili tuone namna nzuri ya ujenzi wa viwanja hivi kupitia nyasi za bandia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivi sasa hakuna mtu anaweza kuleta nyasi za bandia hapa nchini isipokuwa Azam, Mo Dewji na watu wengine wenye uwezo mkubwa kwa sababu ya gharama kubwa. Kodi ya nyasi za bandia zinawavunja watu moyo na ukiangalia katika vyanzo vya mapato, mapato ya kodi ya nyasi bandia siyo ni chanzo kikuu sana kwa Serikali, hata leo mkiondoa haina athari hasi katika mapato ya Taifa letu, kwa sababu katika miaka mitano anaweza akaingiza mtu mmoja nyasi bandia, lakini leo mtu akiingiza nyasi bandia hapa nchini Tanzania za shilingi 200,000,000 ikiwa gharama yake hiyo maana yake lazima alipe asilimia 42 ya tozo ikiwemo excise duty na VAT.

Mheshimiwa Spika, excise duty ni asilimia 25 ya manunuzi ya ile bidhaa, lakini na VAT ni asilimia 18, kwa hiyo, mtu akitaka kuingiza leo majani ya nyasi bandia kwa ajili ya uwanja maana yake ni lazima akiwa na shilingi milioni 200 atafute shilingi milioni 84 nyingine kwa ajili ya kodi tu, hakuna mtu anayeweza kufanya hii.

Niiombe Serikali na bahati nzuri Wizara ya Fedha ipo chini ya Mheshimiwa Mwigulu mwana michezo, Naibu Waziri vilevile Masauni ni mwana michezo kaeni mliangalie hili, twendeni tukatoe kodi kwenye nyasi bandia. (Makofi)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Sanga.

T A A R I F A

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kumpa taarifa mzungumzaji anachokizungumza ni kitu sahihi na bahati nzuri ni kwamba kwenye sera ya michezo ukurasa namba 43 unasema vifaa vya michezo pamoja na malighafi za kutengenezea michezo zitozwe kodi nafuu, kwa hiyo, ninampa taarifa kwamba hili linawezekana Wizara ya Michezo na Wizara ya Fedha zikiamua.

SPIKA: Taarifa hiyo unaipokea Mheshimiwa Anthony.

MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Spika, ninaipokea kwa mikono miwili niiombe sana Serikali iliangalie hili ili tuboreshe viwanja vyetu vya michezo hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, la tatu ni sports arena Mheshimiwa Waziri na mimi nilitegemea ningeona kwenye hotuba yako, dunia ya leo ndio imekwenda huko Mheshimiwa Waziri na
bahati nzuri Mheshimiwa Innocent wewe una exposure kubwa sana umekaa Marekani unafahamu hizi vitu, duniani kote ndio tunaelekea huko hivi sasa, leo Kigali arena yenye uwezo wa kuingiza watu 10,000 tu leo ndio mashinano ya ligi ya basketball ya Afrika yanafanyikia pale Rwanda ambayo yameitangaza Rwanda dunia nzima inaijua Rwanda kwa sababu ya arena tu ya watu 10,000 pale Amahoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rwanda wamejenga kwa kutumia kampuni kutoka Uturuki, ni PPP, ni Shirika la Nyumba la Rwanda Wizara na ile kampuni wamejenga arena hiyo leo Rwanda inafahamika dunia nzima kwa sababu ya basketball na NBA wale wanaoandaa mashindano kule Marekani wametia mkono wao, kwa hiyo, hivi sasa zaidi ya viewers milioni 450 wanafuatilia mashindano ya basketball pale Rwanda. Hii ni sehemu yetu pia na sisi kujitangaza kama tunalipa fedha nyingi kwa ajili ya kujitangaza kwenye utalii huu ndio utalii wenyewe. Nikuombe Mheshimiwa Waziri tuone namna sasa ya kwenda huko na sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amesema Mheshimiwa Babu Tale hapa, matamasha yetu mengi yanafanyikia katika viwanda vya wazi na Mheshimiwa Waziri bahati nzuri tulikuwa wote siku zile katika Urithi Festival, mvua ilitunyeshea Uwanja wa Jamhuri tukakimbia wote, tulijibanza wote Mheshimiwa Waziri kwenye vibanda vya maonesho kwa sababu ya mvua, tutoke huko tuingie katika sposts arena na mimi nitafurahi kuona katika bajeti hii…

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Pokea taarifa Mheshimiwa Anthony.

T A A R I F A

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, mdogo wangu Mheshimiwa Anthony Mavunde ninasema kwamba lile eneo la kujenga sports arena liko Temeke pale Mwembe Yanga, lipo tayari, karibuni sana.

SPIKA: Mheshimiwa Anthony taarifa hiyo.

MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Spika, nimepokea taarifa niiombe Serikali kwa ajili ya utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupitia hivi vitu ndio tunaitangaza nchi yetu hata kwenye utalii leo nataka niwapongeze sana timu ya Simba Sports Club kwa kuvaa tu visit Tanzania, Afrika wameiona Tanzania. (Makofi)

Kwa hiyo, Serikali mnayo nafasi kubwa sana mkikaa pamoja katika kuhakikisha kwamba hata kwenye utalii tutumie michezo pia na wasanii wetu leo Diamond ana followers milioni 12 kwenye instagram, Diamond ndio msanii pekee Tanzania amefanya Tamasha Ouagadougou, Burkina Faso ya kuzaja watu 100,000 akarudia mara mbili ndani ya masaa 24; huyu akienda pale na nembo ya Tanzania. Tanzania inajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri naomba mliangalie hili, mkae pamoja katika kuhakikisha kwamba pia michezo inakuwa sehemu ya utalii. ouagadougou

Lakini Mheshimiwa Waziri nimeangalia katika hotuba yako ukurasa wa 46 umesema kwa uchache sana kuhusu uwanja wa mpira wa miguu Dodoma pale Nzuguni. Mheshimiwa Waziri ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, lakini pia mambo yote ya michoro yamekamilika, ujenzi wa uwanja mkubwa wa mpira wa miguu pale Nzuguni, uwanja huu ukijengwa utakuwa mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki na Kati, kwa hivi sasa ni viwanja viwili tu vinauwezo wa kubeba watu 60,000 kwa wakati mmoja ni uwanja wa Moi Kasarani pale Kenya na Uwanja wa Benjamin Mkapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini uwanja wa Dodoma ukijengwa utakuwa una uwezo wa kuwakalisha watu 80,000 kwa wakati mmoja. Nikuombe Mheshimiwa Waziri sijaona namna yoyote ambapo jambo hili linakwenda kutekeleza isipokuwa tu mmesema mnaratibu katika ukurasa 46 wa hotuba yako. Wananchi wa Dodoma wana hamu sana kusikia hatua ya uwanja huu imefikia wapi, nitakuomba ukija ku-windup utuambie sisi wananchi wa Dodoma tujue uwanja huu wa mpira wa miguu umefikia wapi ili tupunguze adha ya uwanja wa Jamhuri ambao hivi sasa tunavyozungumza hivi sasa kuna maonesho pale ya NACTE na TPSF. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, majukwaa yamekaa mpaka katika pitch ya kuchezea mpira ambayo ni changamoto kubwa sana kwa sisi kwetu ambao tunaosimamia uwanja ule. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri uwanja huu ukijengwa mwingine utakuwa na manufaa makubwa sana, lakini vilevile itafanya nchi nyingine zije zicheze hapa kufanya mazoezi; Brazil walishakuja kucheza katika uwanja wa Benjamin Mkapa mkiwa mna viwanja vizuri maana yake pia ni sehemu ya kutangaza nchi yetu ya Tanzania na watu wakaja kutumia viwanja hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nataka nichukue fursa hii kuendelea kutoa rai kwa watu wengi zaidi kuwekeza kwenye michezo, uwekezaji wa kwenye michezo ndio utakaotutoa hapa kutupeleka mbele, ni ukweli ambao upo dhahiri kabisa kwamba hatuwezi kuendelea pasipo uwekezaji mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nataka nichukue fursa hii niwashukuru wafuatao ambao wameleta chachu kwenye uwekezaji hapa nchini, wa kwanza nataka niwashukuru sana kampuni ya Azam kupitia Said Salim Bakhresa kwa uwekezaji mkubwa sana ambao ameufanya, lakini la pili nataka nimpongeze sana Mohamed Dewji kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya kupitia Klabu ya Simba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nataka nimpongeze sana Ghalib Said Mohamed wa GSM kwa uwekezaji mkubwa sana alioufanya katika Klabu ya Yanga, lakini pia nataka niipongeze jiji la Dodoma kwa uwekezaji mkubwa sana walioufanya katika timu ya Jiji la Dodoma ambalo leo ninaiona timu yetu inacheza vizuri sana na kwa kweli katika timu ambazo zinakuwa hivi sasa katika kandanda safi ni Dodoma Jiji na hata mechi yetu ya mwisho kule uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam mnaweza mkaona Simba walipata taabu kidogo ingawa walituzidi mbinu tu, lakini timu ipo vizuri ni kwasababu ya uwekezaji mkubwa ambao unafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa nguvu kubwa aliyoweka pale Namungo, ingawa juzi mlitupa furaha mpaka dakika 78 kuendelea mbele ikawa majanga. (Makofi/Kicheko)[Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, lakini pia niwapongeze sana KMC kwa uwekezaji mkubwa sana ambao wameufanya lakini vile vile nimpongeze Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Alexander Mnyeti kijana mdogo amefanya jambo kubwa sana pale Gwambina pale Misungwi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeyasema haya makusudi kwamba ili michezo iendelee lazima tufanye uwekezaji leo ligi yetu imebadilika, mimi ni mshabiki wa Yanga, lakini nitakuwa sijitendei haki kama sitasema ukweli, uwekezaji wa Mo Dewji umeibadilisha Simba, unaiona Simba leo jinsi ilivyo wanajitahidi wanacheza vizuri, lakini na sisi pia kupitia GSM tunakuja. Tunakuja na lengo letu ni kuleta ushindani mkubwa kwa sababu michezo haiwezi kuendelea bila uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niyaomba makampuni mengine pia izibebe hizi timu, hizi timu hizi ukiacha tu fedha wanazopata kutoka Azam kuendesha timu ni gharama kweli kweli, mimi kipindi fulani nilikuwa ninaimiliki hapa nilikuwa ninaisimamia Dodoma jiji hapa niliwahi kuweka reheni nyumba yangu kwa ajili ya kulipa mishahara, ni jambo gumu kweli kweli mpaka Mheshimiwa Kunambi amekuja kunisaidia kupita Jiji la Dodoma. Lakini tunaomba wawekezaji waje wengi zaidi ligi iwe ya ushindani, Simba akienda kucheza na Gwambina watu wasiyajue matokeo, uwe mchezo ambao hautabiriki, lakini leo ni gumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nianze kwanza kwa kuipongeza Wizara, hasa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, kwa kazi nzuri ambayo mmeendelea kuifanya.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipomshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo amejitoa sana kwenye sekta hii. Na kazi nzuri aliyoifanya tunaona hivi sasa; vijiji takribani 10,312 vimeshafikiwa. Na ninaamini kabisa azma ile ya kufikia vijiji vyote itafikiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, hapa Mkoa wa Dodoma ametuletea watendaji wazuri kwa TANESCO. Alikuwepo meneja wetu hapa Frank Chambua, amefanya kazi nzuri, umem-promote amekuwa Meneja wa Kanda. Lakini hivi sasa ametuletea Boimanda, na yeye anafanya kazi nzuri sana; tunamshukuru sana kwa kuona umuhimu wa kuwaleta watendaji hawa katika Mkoa wetu wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nianze kuzungumzia masuala ya utekelezaji wa miradi ya nishati ya umeme katika Jimbo la Dodoma Mjini, na hasa katika miradi hii mikubwa miwili ya densification na peri urban. Mheshimiwa Waziri, nataka nikushukuru sana na niishukuru sana Serikali kwa kutenga zaidi ya shilingi bilioni 100 ya utekelezaji wa miradi ya umeme katika Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii tafsiri yake ni kwamba itakwenda kuiwasha Dodoma nzima, na hapo sasa tutakuwa tumefikia malengo ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya kweli ya Nchi ambayo umeme utawaka maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, kwenye mradi densification tunashukuru kwamba mkandarasi aliyepo anafanya kazi yake vizuri sana, ameyafikia maeneo mengi yale ambayo yalikuwa hayajafikiwa na umeme. Na nimpongeze sana kwa kweli Mkandarasi Derm Electrics kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, na hivi sasa karibia maeneo yote ambayo yalirukwa kwenye umeme wa REA Awamu ya Kwanza na ya Pili, yanatekelezewa mradi huu wa densification. Kwa imani yangu ni kwamba yatakamilika yote na Dodoma yote itaendelea kuwaka.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri, jana nimepigiwa simu na nimekutana na mkandarasi wa CILEX ambaye ndiyo atakwenda kutekeleza mradi wa peri urban ambao kwa mara ya kwanza utakwenda kuwasha umeme kwenye Kata za Chihanga na Mbalawala ambazo hazijawahi kuona nguzo hata moja tangu kuumbwa kwa ulimwengu huu. Lakini pia utafika mpaka maeneo ya Mkoyo. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ombi langu; hivi sasa Jiji la Dodoma linakua kwa kasi sana, maeneo ni mengi sana ambayo yanaendelezwa. Niwaombe watendaji wako waongeze kasi na hasa katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, tuna maeneo yametengwa kwa ajili ya viwanda; eneo la Nala na eneo la Mpunguzi. Wawekezaji wengi wanashindwa kuja kuanza kuwekeza kwa sababu hakuna miundombinu ya nishati ya umeme.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana, ulitoa msisitizo mkubwa sana kwa mkuu wa mkoa na mkuu wa mkoa amelibeba suala la kiwanda cha mbolea pale Nala. Walishindwa kuanza kwa sababu hakukuwa na miundombinu ya umeme. Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Anthony Mtaka, ameshinda pale Nala siku mbili na watu wa TANESCO na Jumamosi umeme unawaka na mwekezaji ataanza kujenga kiwanda kile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Wizara, Dodoma maeneo haya mawili yanafahamika, ya Mpunguzi na Nala; nikuombe Mheshimiwa Waziri, twendeni tukawekeze kule tuweke miundombinu ili wawekezaji wengi zaidi waje. Kwa sababu hivi sasa tunamtegemea mwekezaji mkubwa wa SBL na TBL lakini wao wakifika itakuwa pia kichocheo kwa wawekezaji wengi kuja kuwekeza Dodoma.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, nikuombe katika mipango yako angalia sana maeneo ya industrial park ili tukaweke umeme kuwavutia wawekezaji wengi zaidi. Akija TBL hapa Dodoma, akija SBL, atawavutia wawekezaji wengine na viwanda vingi vitajengwa. Hivyo nikuombe Mheshimiwa Waziri uliangalie hili kwa macho mawili.

Mheshimiwa Spika, suala la mradi wa bomba la mafuta (EACOP); kwanza kabisa nataka nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo ameharakisha na ameshiriki katika mchakato wa kusaini mikataba hii muhimu sana kwa ajili ya bomba hili.

Mheshimiwa Spika, bomba hili lina urefu wa kilometa 1,443. Bomba hili ni refu sana na eneo kubwa liko eneo la Tanzania. Inapotoka kule Kabahale, Hoima, mpaka Chongoleani, maana yake ni kwamba katikati kote hapa bomba hili litaacha athari chanya.

Mheshimiwa Spika, sasa mchango wangu ni kuomba Serikali kwamba pamoja na uwepo wa bomba hili, lakini bomba hili lazima lilete manufaa kwa wananchi wetu wa Tanzania na hasa jumuiya ya wafanyabiashara na wajasiriamali katika Nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba kwenye bomba hili ajira takribani 15,000 zitatengenezwa. Lakini nawaomba Wizara kupitia EWURA najua mmewasajili wale watoa huduma takribani 570, lakini twende mbele zaidi. Uganda kwenye bomba hili hili Mheshimiwa Waziri, wame- ring fence baadhi ya categories ambazo lazima zifanywe na wazawa. Mheshimiwa Waziri, na hapa Tanzania mme-ring fence categories nyingi sana ambazo zitafanywa na wazawa isipokuwa hamjazitangaza. Mheshimiwa Waziri, tunaomba msiwa-take by surprise business community; mtangaze tujue maeneo gani Watanzania watafanya. Mkiwa-take by surprise watashindwa kujiandaa vizuri, watakuja wageni watazichukua hizi nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, kama tayari tunafahamu maeneo gani ambako huduma zitatolewa na bidhaa zitahitajika, naomba mtangaze mapema ili watu wajiandae. Kwa hivi sasa hamjatoa tangazo lolote Mheshimiwa Waziri, watu wanajua tu kwamba kuna fursa lakini hawajui fursa gani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningeomba EWURA, kama mmeshawasajili hawa watoa huduma toeni matangazo kila mtu ajue ili kama kuna masuala ya mafundi wa kuchomelea watu wajue, kama kuna masuala ya kuleta crane watu wajue; hayo yote lazima yaainishwe na Watanzania wajiandae katika hilo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, lakini kwenye Watanzania kujiandaa katika hili, naomba pia msiwasahau wajasiriamali wadogowadogo. Nimeona Wizara mmejielekeza sana kwa wafanyabiashara wakubwa wenye makampuni, lakini tunawasahau wale wajasiriamali wadogowadogo ambako bomba hili linapita.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, naomba upitie kufanya vikao pamoja na mikoa yote ambako bomba hili linapita ili tuwaandae akinamama, vijana na watu wenye ulemavu pia kushiriki kwenye mradi huu mkubwa. Najua mama lishe watahitajika, najua vijana nguvukazi itahitajika, lakini tuwaandae mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho katika hili niiombe Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Nishati na Madini mkae pamoja muwasaidie wafanyabiashara ambao wamekuwa listed pale EWURA ili waweze kufanya kazi hii vizuri. Kwa sababu najua moja kati ya changamoto kubwa ni changamoto ya mitaji.

Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara hawa ambao watashiriki kwenye bomba la mafuta wakienda kwa aina ya mikopo ya asilimia 21 katika commercial rate, hakuna mtu ataweza kufanya. Lakini Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Baraza la Taifa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Wizara ya Nishati pamoja na Wizara ya Fedha, naomba mkae na taasisi za benki, taasisi za kifedha, mkubaliane kwamba kwa sababu bomba hili mahitaji yake yanafahamika, wale wote ambao wamekuwa listed, yale makampuni 570, wakienda kuomba mkopo basi riba yao iwe tofauti na riba iliyoko hivi sasa katika soko la biashara ya kibenki kwa sababu asilimia 21 hawataweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana Wachina wanafanikiwa sana kwa sababu Serikali yao inaingia katikati na mikopo yao ni asilimia tatu mpaka nne. Asilimia 21 hakuna Mtanzania ataweza kufanya kazi hiyo, lakini mnao uwezo wa kukaa pamoja na benki.

Mheshimiwa Spika, hoja ya benki ni kwamba wakitoa mikopo mingi risk yake ni kubwa kwenye repayment. Lakini mkikaa nao kwa pamoja uko mfumo unaitwa contract cash flow discounting; unachukua mkataba aliyopewa huyu mtoa huduma unaupeleka benki, benki anafungua akaunti ya huyu mtoa huduma, mtoa huduma huyu akilipwa malipo yapitie katika benki iliyomkopesha, benki wakate hela yake iwe sehemu ya malipo ya deni halafui naye abaki na kile cha ziada. Tukifanya hivyo tutakuwa tumewasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa trend ambayo tunakwenda nayo hivi sasa, asilimia kubwa ya Watanzania hawataweza, watashindwa kwa sababu mikopo yetu iko juu sana.

Mheshimiwa Spika, niiombe Wizara ya Fedha; mnaweza mkaenda mpaka ikafikia asilimia nane katika riba. Hili linawezekana sana kwa sababu benki atakuwa na uhakika wa repayment ya mkopo wake. Lakini vinginevyo wazawa, wafanyabiashara wa Kitanzania wataishia kuuona mradi huu kwa mbali, watakuja Wachina na Wazungu hapa watachukua shughuli zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tutafurahi tukiona Watanzania wananeemeka na huu mradi, lakini Serikali lazima muweke mkono wenu. Muwawezeshe kama ambavyo mataifa mengine yanafanya. Mkiwaacha waende wenyewe blindly tu, naona hatari kwamba mwisho wa siku Watanzania wengi hawatanufaika.

Mheshimiwa Spika, hivyo, niwaombe Wizara ya Fedha, mnao uwezo wa kukaa pamoja na hizi taasisi za kifedha mkaweka huu utaratibu mzuri. Riba ishuke kutoka asilimia 21 iende asilimia nane mpaka kwenda chini huko ili Watanzania wengi zaidi waweze kushiriki kwenye mradi huu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii nami kipekee kabisa kuipongeza Serikali chini ya Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo wamekuja na bajeti inayogusa maisha na maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii kwa kiwango kikubwa kabisa imeweka mkazo mkubwa kwenye maji, barabara, na naamini kabisa wananchi wangu wa kule Mkoyo, Ntyuka, Michese TARURA wakiongezewa fedha hapa maana yake watakwenda kuwagusa pia na wao kwenye utatuzi wa changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba nijikite katika maeneo makubwa matatu tu, na ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu na Engineer Masauni, Katibu Mkuu Tutuba na Ndugu Alphayo Kidata Kamishna Mkuu wa TRA ninyi wanne nimewataja kwa majina mnao uwezo wa kuacha historia katika nchi yetu, mnao uwezo wa kuifanya nchi hii ipige hatua kwenda mbele, kama tu tutafuatilia ushauri wa Wabunge na kuufanyia kazi hasa katika maeneo ambayo nitayasema hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuamini sana, Mheshimiwa Naibu Waziri nakuamini sana, mnayo nafasi kubwa ya kuacha legacy kwenye nchi yetu. Uchumi wa nchi yetu, maendeleo ya nchi yetu yapo mikononi mwenu ni ninyi sasa muamue kuipeleka nchi hii mbele na kwa umri wenu naamini kabisa mnayo nguvu ya kutosha kulipeleka gurudumu hili mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri la kwanza ambalo nataka nianze nalo Sera ya Fedha – fiscal policy, Mheshimiwa Waziri lazima mipango yetu na mikakati tuliyojiwekea iendane sawa na sera zetu zinavyosema. Ilani ya Uchaguzi ya CCM inasema kuhusu ajira milioni nane, Mheshimiwa Waziri ajira milioni nane hizi zinatokea mikononi mwenu kupitia kanuni, kupitia sera na sheria katika usimamizi wa masuala ya fedha. Hakuna uchawi mwingine wowote isipokuwa hapo Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tuangalie namna nzuri ya kukuza uwekezaji na kuvutia wawekezaji waje nchini, hiyo ndiyo itakuwa namna nzuri zaidi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kwenye kupatikana ajira hizo milioni nane kwa sababu ajira hizi zitatokana na kazi kubwa ambazo zitafanywa na wawekezaji wa kuja kuwekeza hapa nchini. Mheshimiwa Waziri vipo vitu ambavyo lazima tuviangalie kwa haraka na kuvifanyia kazi mapema sana, lazima tuondoe tozo na kodi zote ambazo zinawatisha wawekezaji. Zipo kodi, zipo tozo ambazo ukiziondoa leo impact yake siyo kubwa sana na ikaathiri mapato ya nchi, lakini ukiziondoa zina mchango mkubwa kuwavutia watu, watu wakiona makodi yamejazana wanakimbia na zipo kodi ambazo hazina mchango mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe tuipitie tena sera yetu ya fedha tuziondoe kodi hizi. Kwa mfano, kwenye sekta ya utalii, Mheshimiwa Waziri hatuna haja tena ya kuendelea kuongeza tozo, wenzetu wote washindani wetu hakuna mtu kaongeza tozo. Kenya na Rwanda na nchi zingine ambazo zipo karibu nasi wanafikiri kupunguza sisi Mheshimiwa Waziri tunaongeza hii haiwezi kutusaidia ongezeko la tozo hasa katika park fees, land base rent itatuletea changamoto kubwa sana. Nikuombe Mheshimiwa Waziri uliangalie eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pia nashauri na kupendekeza tufanye mabadiliko ya corporate tax, Mheshimiwa Waziri hivi sasa kodi ya makampuni ni asilimia 30 ya mapato yanayotozwa kodi, Mheshimiwa Waziri ukiangalia Kenya ni asilimia 30, Rwanda asilimia 30, Uganda asilimia 30 nchi nyingi za Afrika ni asilimia 30, Mheshimiwa Waziri kwa nini Tanzania leo tusiishushe kodi ya makampuni kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 25 ili kuanza kuwavutia watu wengi zaidi kuja kuwekeza Tanzania, hatupotezi kitu Mheshimiwa Waziri kwa sababu hata ukiiacha mwisho wa siku haumpati mtu anayekuja nchini, umebaki na asilimia 30, lakini ukiipunguza unawavutia wengi na ile deficit utaipata kutoka kwenye pay as you earn, tax ambayo italipwa na kodi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nashauri pia sheria itungwe kuhusiana na masuala corporate tax kwamba mwekezaji yeyote atakayekuja kuwekeza Tanzania akiwekeza Dar es Salaam na Pwani atozwe asilimia 25, akitoka nje ya Pwani na Dar es Salaam ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi atozwe asilimia 12.5 ili watu waende Mbinga, watu waende Njombe, watu waende Ifakara na maeneo mengine, vinginevyo viwanda vitajaa Dar es Salaam tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mheshimiwa Waziri ukienda Ghana, Ghana amefanikiwa kupitia hivi. Ghana wanayp programu inaitwa one district, one factory kila wilaya na kiwanda chake, wametoza asilimia 12.5 ya corporate tax ndiyo dunia inapoelekea huko Mheshimiwa Waziri, nikuombe Mheshimiwa naamini hili unaliweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikupe mfano mwingine rahisi sana, tukiweka asilimia 25 utawavutia wawekezaji kwa nini aende Kenya kwenye asilimia 30, kwa nini aende Uganda, kwa nini aende Rwanda atakuja Tanzania na kwetu tutakuwa na manufaa makubwa sana. Mheshimiwa Waziri hivi sasa kwa Ulaya nchi ya Ireland ndiyo nchi ambayo inatoza corporate tax asilimia ya chini sana, asilimia 12.5, hivi sasa Facebook makao yake makuu wamepeleka Ireland kwa sababu tu wamevutiwa na corporate tax, nakuomba sana hili eneo uliangalie vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tunao uwezo wa kufanya jambo kubwa sana na mimi nakuamini sana Mheshimiwa kwa sababu yapo mabadiliko yaliyofanyika hapa, tumeona yalifanyika mabadiliko ya kodi hapa, tulishusha corporate tax katika viwanda vinavyoanzishwa vipya vya masuala ya madawa na ngozi mpaka asilimia 20, lakini viwanda vya kuanzisha vya kuunda magari mpaka asilimia 10 kwa nini hili pia lisiwezekane Mheshimiwa Waziri naomba uliangalie hilo na ninaamini kabisa lipo ndani ya uwezo wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili naomba sasa tutunge sera ya kuchukua michango ya kuchukua remittance kutoka katika diaspora. Mheshimiwa Waziri wapo Watanzania wenzetu wapo nje ya nchi ambao wana uwezo wa kuchangia maendeleo ya nchi yetu tusiziachie hizi fedha Mheshimiwa Waziri. Kwa hivi sasa kuna takribani Watanzania 1,300,000 wapo nje ya Tanzania. Mheshimiwa Waziri hawa wana uwezo wakawa wana mchango mkubwa kwenye nchi yetu na maendeleo yetu, niwaombe Serikali mtunge sera maalum ya kusaidia kuwawezesha hawa diaspora kuchangia nchi yao. Mheshimiwa Waziri ukienda Nigeria, Nigeria mwaka 2018/2019 diaspora wa Nigeria wamechangia dola bilioni 25 katika uchumi wa maendeleo ya nchi yao ambayo ni sawasawa na asilimia 83 ya bajeti ya Federal Government of Nigeria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Kenya diaspora wanachangia dola bilioni 2.2, Tanzania ni dola milioni 430. Mheshimiwa Waziri tuwajengee miundombinu rafiki waweze kuchangia katika nchi yetu pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho….

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Lugangira.

T A A R I F A

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru ningependa kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge Anthony Mavunde kwamba Kenya wameweka mazingira wezeshi zaidi kwa diaspora wetu wa Tanzania kuwekeza kwa hiyo hivi sasa diaspora wa Tanzania wanawekeza Kenya kuliko wanavyowekeza hapa Tanzania. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anthony Mavunde taarifa hiyo unaipokea.

MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa na nimuombe Mheshimiwa Waziri aliangalie hili ili tuweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu riba. Mheshimiwa Waziri jana Mheshimiwa Rais katoa maelekezo pale Mwanza maana yake najua maneno yake ni maelekezo juu ya riba, kaeni na BOT tunawatesa watanzania kwa riba kubwa, riba ya Tanzania ni kubwa sana, asilimia 21, asilimia 22, nani anaweza akakopa akaweza kufanya biashara hapa Tanzania kwa asilimia hizi. Mheshimiwa Waziri kaeni na BOT nendeni mkaangalie hati fungani, mkakae huko asilimia kule zishuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tuna CRB - Credit Reference Bureau hivi mimi nikikopa mwaka wa kwanza nimelipa, mwaka wa pili nimelipa mabenki tofauti, tofauti hivi kwa nini nikijakukopa kwa mara ya nne riba yangu iwe ile ile tena huku mmeshaona kuwa mimi ni mlipaji mzuri? Mheshimiwa Waziri hili naomba mlifanyie kazi kwa sababu vinginevyo hata makampuni yetu hayawezi kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kushindana na mchina anayetoka China kuja kuwekeza Tanzania anayelipa riba ya asilimia 4 vis-a-vis riba asilimia 21, Watanzania hawataweza kuwa washindani kwenye soko lolote la kibiashara na hasa kwenye ujenzi. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana kaeni na BOT, tafuteni namna bora ya kupunguza riba, riba yetu ni kubwa inawaumiza sana watanzania na hasa wafanyakazi wa Serikali, hasa Walimu ukiwaangalia, walimu wengi sana makochi yao na TV zao zipo kwenye taasisi za fedha. Anakopa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anthony kuna taarifa huku. Taarifa Mheshimiwa Munde, nenda kwenye mic sasa.

T A A R I F A

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kuhusu suala zima la riba hasa kwa vijana wetu wa bodaboda, Mama lishe ambao wanakopa Brac, Pride zile taasisi ndogondogo wanapata riba mpaka ya asilimia 30, kwa hiyo jambo hili ni jema tuwaombe BOT wahakikishe wanashusha riba kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge na Mheshimiwa Rais.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anthony Mavunde.

MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili ni muda muafaka sasa Serikali muone namna nzuri ya kuweza kurekebisha hili vinginevyo tunawatesa sana wafanyabiashara wa Tanzania, tunawatesa sana Watanzania kwa sababu wengi wana changamoto nyingi. Wakienda kuchukua mkopo mwisho wa siku mikopo yenyewe hii hailipiki, lakini vilevile hata wakienda kuchukua mikopo hii kama issue kubwa ni ya risk ambayo na mabenki wanaiogopa zipo namna, wapo watalaam wengi wa uchumi, yupo hata Dkt. Kimei hapa na watalaam wengine kaeni nao wawashauri vizuri namna ya kuweza kufanya, mimi naamini haya mambo yanawezekana kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku kwenye riba huku. Naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU – SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kwa sababu, ni mara yangu ya kwanza kuchangia na kusimama kutetea hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nichukue fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuniteuwa na kunipa dhamana ya kuhudumu katika nafasi ya Naibu Waziri Kazi, Vijana na Ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa ushirikiano mkubwa na miongozo mbalimbali ambayo amekuwa akitupa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt. Abdallah Possi, kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakinipa katika utekelezaji wa majukumu yetu, lakini pia na Mawaziri wengine wote wanaounda Baraza la Mawaziri kwa miongozo yenu na ushauri wenu katika utekelezaji wa majukumu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii pia, kipekee kabisa kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa kunichagua kuwa Mwakilishi wao kwa kura nyingi sana. Nataka niwaahidi tu kwamba, kwa yale ambayo waliyatazamia kutoka kwangu nitajitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu niweze kuwatumikia vyema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya 99(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 naomba sasa uniruhusu nitoe ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo ziliwasilishwa na Waheshimiwa Wabunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge walichangia, moja ya mambo yaliyojitokeza wakati wa uchangiaji, lilijitokeza suala la ukaguzi wa Sera ya Uwekezaji katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) pamoja na Benki Kuu ya Tanzania ilitoa Mwongozo wa Uwekezaji wa mwaka 2015 ambao kwa mujibu wa mwongozo huo SSRA na BOT imekuwa ikifanya special inspection kwenye miradi yote ya uwekezaji ambayo inahusisha Mifuko ya Hifadhi ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, lengo kubwa sana la kaguzi hizi ni kuhakikisha kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inawekeza katika miradi ambayo itakuwa ina tija na manufaa kwa Watanzania. Pia, kupitia SSRA zimekuwa zikifanyika kaguzi za mara mbili kwa mwaka ambapo lengo lake kubwa ni kuweza kuangalia miradi hii ambayo inawekezwa na kuona namna ambavyo inaweza kuleta tija hasa katika maeneo ambayo yanawagusa Watanzania moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ilijitokeza hoja ya kuhusu Mikataba ya Wafanyakazi na vilevile wageni wasiokuwa na vibali vya kazi. Serikali imeendelea kufanya kaguzi mbalimbali kwa kutumia Maafisa Kazi waliopo nchini ili kuweza kubaini Waajiri wote ambao hawatoi mikataba kwa Wafanyakazi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie tu fursa hii kutoa agizo kwa waajiri wote nchi nzima kuhakikisha kwamba wanatoa mikataba kwa wafanyakazi wao na Serikali haitasita kuendelea kuchukua hatua itakapobainika kwamba Waajiri hawatoi mikataba kwa Waajiriwa wao, jambo ambalo kwa mujibu wa Sheria zetu tutawachukulia hatua ili kuona ni namna gani sasa wata-comply na masharti ya Sheria zetu za Kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye suala la vibali vya ajira kwa wageni, tumeendelea kufanya kaguzi mbalimbali katika maeneo ya kazi kuweza kuwabaini wale wageni wanaofanya kazi pasipokuwa na vibali au ambao wanakiuka vibali vya kazi na hatua stahiki zimekuwa zikichukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, mtakuwa mashahidi, mmeona ziara mbalimbali ambazo zilifanywa na Mheshimiwa Waziri pamoja na mimi Naibu wake, kupitia katika maeneo tofauti tofauti ya kazi na tumekuwa tukichukua hatua stahiki kuhakikisha kwamba wale wageni wote waliokuja kufanya kazi nchini, kwa mujibu wa Sheria Na. 1 ya Mwaka 2015, wanafuata masharti ya Sheria na tunahakikisha kwamba vibali vya kazi walivyopewa wanavifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu ambazo wameziomba. Kwa hiyo, ikibainika tofauti, tumekuwa hatusiti kuchukua hatua na wako wageni wengi ambao tumewafutia vibali na wengine kusafirishwa nje ya nchi kwa kukiuka masharti ya Sheria hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilijitokeza pia, hoja nyingine ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Vijana katika Halmashauri na Viongozi wa SACCOS. Hoja hii ilijitokeza kama ushauri na kwa niaba tu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, niseme kwamba ushauri huu tumeupokea, tutaufanyia kazi kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini. Hata hivyo, tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imeshaanza kuwajengea uwezo Viongozi wa SACCOS na vikundi mbalimbali vya vijana na kufikia Machi mwaka huu, tayari vikundi 2,552 vilikwishakupatiwa Semina mbalimbali kuhusiana na masuala ya ujasiriamali, kilimo na masuala ya uongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja nyingine iliyojitokeza wakati Waheshimiwa Wabunge wakichangia, ilijitokeza hoja ya kuwa na idadi ndogo ya Watanzania wanaoajiriwa katika Sekta ya Viwanda. Katika hoja hii pia, ilizungumzwa kwamba asilimia kubwa ya watu wengi ambao ni wageni ambao wanafanya kazi katika maeneo haya, wamekuwa wakichukua kazi za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi kama Serikali, kama nilivyosema pale awali, tumeendelea kuisimamia na kuitekeleza Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 ambayo imeweka utaratibu wa kuwaajiri wageni ndani ya nchi yetu, hasa katika maeneo ambayo yana upungufu wa wataalam. Ili kuhakikisha kwamba idadi kubwa ya vijana wanaajiriwa katika viwanda vyetu, tumeendelea kufanya kaguzi mbalimbali na lengo lake ni kuweza kubaini wale wafanyakazi wageni ambao hawakidhi masharti ya Sheria Na.1 ya mwaka 2015 kwa kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimwondolee hofu Mheshimiwa Mbunge, mama yangu Mheshimiwa Mama Vullu, ambaye katika hoja yake alisisitiza pia, kwamba ikiwezekana, basi tuongozane naye katika eneo lile la Mkuranga ambako kumekuwa kuna changamoto kubwa kwamba viwanda vingi ambavyo viko pale, wanaofanya kazi, wengi ni wageni ambao hawana sifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwahidi tu Mheshimiwa Vullu kwamba kwa sababu tumedhamiria kuwatumikia Watanzania, niko tayari muda wowote kushirikiana naye kwenda kuhakikisha kwamba tunafanya kaguzi ili kuwabaini wale wote ambao ni wageni wanaofanya kazi pasipokuwa na vibali vya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, ilizungumzwa hoja kuhusu masuala ya afya na usalama mahali pa kazi. Ni kweli nataka nikiri kwamba kumekuwepo na changamoto kubwa sana, lakini Serikali imeendelea kufuatilia kupitia OSHA na imesajili na kukagua maeneo takriban 39 katika eneo la Mkuranga na hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kwa mujibu wa Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za kwanza ambazo zimekuwa zikichukuliwa tunapokwenda kufanya kaguzi na kukuta kwamba katika baadhi ya maeneo Sheria haijafuatwa kwa maana ya masuala ya afya na usalama mahali pa kazi, hatua ya kwanza imekuwa ni kutoa hati ya kumtaka Mwajiri afanye marekebisho, lakini pale inapoonekana kwamba hali hairidhishi na bado hakujafanyika hatua zozote za marekebisho, basi tumekuwa tukichukua sheria za kuwatoza fine na kuwapeleka Mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilizungumzwa pia hoja ya utengaji wa maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana na hii ilitokana na kuwa kumekuwepo na tafrani hasa baada ya Mheshimiwa Rais kuzungumza, kuwataka vijana waache kucheza pool na kwenda kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kulizingatia hilo, Serikali kupitia Wakuu wa Mikoa yote Tanzania imeelekeza Halmashauri za Wilaya na Serikali za Mikoa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za kiuchumi za vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya, lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba vijana wanapata maeneo ya kufanya shughuli za uzalishaji mali. Kwa hiyo, nachukua fursa hii kuendelea kuwasisitiza viongozi wote wa Halmashauri za Wilaya na viongozi wa Mikoa kuendelea kutenga maeneo maalum kwa ajili ya vijana ili wapate shughuli za kufanya; kilimo na shughuli za ujasiriamali kama ambavyo imekuwa maagizo yakitolewa mara kwa mara na Mheshimiwa Rais alivyoagiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ilizungumzwa hoja ya fedha za mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya makundi ya akinamama na vijana. Ushauri huu umepokelewa na Ofisi ya Waziri Mkuu imeweka mkakati kuhakikisha kwamba fedha hizi zinawafikia walengwa kuhakikisha kwamba mapato ya ndani ya Halmashauri, zile 5% kwa makundi ya vijana na akinamama zinayafikia makundi haya. Pia, tumeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba Halmashauri zinatoa taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo la Mheshimiwa Rais kila baada ya miezi mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kutoa rai kwa vijana nchi nzima kuhakikisha kwamba wanaendelea kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kupata fursa ya kuweza kuwezeshwa kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili, kwa kutambua kwamba tuna changamoto kubwa sana ya ukosefu wa ajira kwa vijana, tumekuwa tuna mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba vijana hawa kwanza kabisa tunawatambua; pili, tunawarasimisha na hatua ya tatu tuone namna gani tunaweza tukawawezesha kiuchumi ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nachukua tu fursa hii kuwaomba vijana wote nchi nzima waendelee kukaa katika vikundi vya uzalishaji mali ili sisi kama Serikali sasa, tuwe katika sehemu ya kuweza kuwasaidia katika kuwawezesha kiuchumi ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nichukue fursa hii kipekee kabisa kuwahimiza vijana wote nchi nzima kuendelea kufanya kazi kwa bidii hasa tukizingatia kwamba vijana ndiyo nguvukazi ya nchi hii. Nasi kama Serikali tutaendelea kuandaa mazingira wezeshi ya kuwafanya vijana washiriki katika uchumi wao na watumie muda wao mwingi katika kuujenga uchumi wa nchi yetu, badala ya kufanya shughuli ambazo hazina tija na zisizokuwa za uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili, nataka tu nisisitize ya kwamba takwimu zimeonesha nguvu kubwa hii ya vijana imekuwa ikitumia muda mwingi kufanya shughuli ambazo hazizalishi na zisizokuwa na tija kutokana na tafiti mbalimbali ambazo zimeelekeza. Kwa hiyo, ni vema sasa vijana wetu na sisi tukabadilisha mtazamo katika nchi yetu hii tukajielekeza katika kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kiuchumi ili na sisi kama nguvu kazi ya Taifa tuwe sehemu ya ujenzi wa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe vijana wote nchi nzima kuchukulia agizo la Mheshimiwa Rais la kufanya kazi kama ni sehemu ya kutekeleza wajibu wetu kama wananchi wema katika nchi yetu, lakini na sisi tuoneshe mchango wetu katika kuhakikisha kwamba tunatoa mchango katika nchi yetu katika kujenga uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie tu kwa kufanya nukuu kutoka Kitabu cha Virgil’s Georgecs katika mashairi haya, mstari namba 146; yalisomeka pale maneno ya Kilatini ambayo yanasema, “Labor omnia vincit” ambayo tafsiri yake ni kwamba, Work conquers all, ambayo inashabihiana kabisa na falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu, ikituhimiza kwamba kila mmoja kwa nafasi yetu hasa vijana, tuhakikishe kwamba tunatenga muda wetu kwa ajili ya kufanya shughuli za kuzalisha, tusaidie kujenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kujibu hoja hizo ambazo Waheshimiwa Wabunge, walizizungumza nichukue tu fursa hii kipekee kabisa nami niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia, lakini ambao wametushauri katika namna bora ya utekelezaji wa majukumu yetu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nasi kama Wizara tutaendelea kuhakikisha kwamba, tunatatua kero, changamoto na matatizo mbalimbali ambayo yanawakabili kundi kubwa hili la vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu wa rehema kwa kutujalia Waheshimiwa Wabunge wote uzima na afya njema. Pia nichukue fursa hii kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili kuchangia hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nikiwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, ninayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu, naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge na Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kwa ushirikiano mkubwa na miongozo wanayonipa inayoniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa ufasaha.
Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa naomba kutumia fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa kuendelea kuniunga mkono na kushirikiana na mimi katika utekelezaji wa majukumu haya ya kila siku.
Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima naomba sasa uniruhusu nichangie hoja hii kwa kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge walichangia na kutaka ufafanuzi. Nitatoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja na hoja nyingine zitajibiwa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, hoja ambayo ilijotekeza ya kwanza kabisa ilikuwa ni masuala ya Usalama na Afya Pahala Pa Kazi (OSHA). Waheshimiwa Wabunge walitamani kusikia kwamba tunaendelea kusimamia afya na usalama wa wafanyakazi pahala pa kazi na hasa wafanyakazi ambao
wanafanya kazi katika maeneo ya migodini na viwandani, na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wale wote ambao hawazingatii masuala ya afya na usalama wa wafanyakazi wao.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapokea ushauri wa Kamati wa kuendelea kusimamia afya na usalama pahala pa kazi hususan migodini na Serikali itaendelea kutoa elimu na kuchukua hatua kwa waajiri wote ambao hawatazingatia masuala ya afya na usalama kwa wafanyakazi wao kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, kila mtu anafahamu na ni dhahiri kwamba falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ni ya uchumi wa viwanda ambayo itakwenda kuwaajiri Watanzania wengi sana wengi wao wakiwa ni vijana, kwa hiyo, sheria hii sasa itakuwa ni sehemu ya kuweza kui-protect nguvukazi ya nchi kutokana na haya ambayo yanaweza kutokea katika migodi na viwandani.
Mheshimiwa Spika, aidha katika kipindi cha mwaka 2016/2017 Wakala wa Afya na Usalama Pahala Pa Kazi (OSHA) umewachukulia hatua waajiri 701 waliokiuka matakwa ya Sheria ya Afya, Usalama Pahala Pa Kazi ikiwemo wamiliki wa migodi mikubwa iliyopo nchini.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ilizungumzwa ni Serikali itoe elimu bora kwa watu wenye ulemavu ili wajiondoe katika hali ya utegemezi. Suala la kushughulikia changamoto za watu wenye ulemavu, ikiwemo kuwawezesha kujiondoa katika utegemezi ni moja kati ya vipaumbele ambavyo vimeainishwa kwenye Ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015, Ibara ya 166; hivyo, Serikali itaendelea kutoa elimu bora kwa watoto wote nchini, wakiwemo watoto wenye ulemavu kwa kutoa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi sasa Serikali inasambaza vifaa hivyo kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza ni kwa wanafunzi wasioona na viziwi, awamu ya pili vifaa vitasambazwa kwa watoto wenye ulemavu wa akili na wenye usonji na hatimaye kwa wenye ulemavu wa viungo. Hadi sasa vifaa vilivyosambazwa katika awamu ya kwanza katika shule za msingi na sekondari ni kama ifuatavyo; mashine za nukta nundu (brail machine) 932, shime sikio (hearing aids) 1,110, karatasi za kuandikia maandishi ya nukta nundu - rimu 2,548, karatasi za kudurufu maandishi ya nukta nundu - rimu 1,000, universal brail kits yenye vifaa mchanganyiko 1,495.
Mheshimiwa Spika, katika hoja zilizojitokeza pia hapa, Wabunge walizungumza kuhusu Mfuko wa Watu wenye Ulemavu kwamba haukutengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2016/2017 hivyo Serikali ijitahidi kutenga fedha kwa ajili ya mfuko huu ambao utawezesha Baraza la Watu wenye Ulemavu kutekeleza majukumu yake ya kisheria.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 50 ambazo zitatumika kuandaa mfumo na uratibu wa uendeshaji wa mfuko wa watu wenye ulemavu. Aidha, watu wenye ulemavu wanaendelea kupata huduma mbalimbali, hususan
kuwawezesha kiuchumi kupitia mifuko, ikiwa ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ngazi ya Halmashauri pamoja na programu ya kukuza stadi za kazi.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili pamoja na kuwa na programu nyingi sana za uwezeshaji katika kundi hili, lakini pia kila programu ya Wizara hasa katika ukuzaji ujuzi tumekuwa tukitenga asilimia kadhaa kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Mfano wa programu mojawapo ni Programu ya
Youth Economic Empowerment ambayo iliwahusisha takribani vijana 9,100 katika mikoa mitano ya Mtwara, Lindi, Morogoro, Dar es Salaam na Pwani ambapo walijitokeza watu wengi wenye ulemavu na walipata fursa kushiriki katika mafunzo haya na walikuwa ni kati ya watu ambao walifanya vizuri sana. Kwa hiyo, kama Serikali imekuwa ni sehemu ya msisitizo pia, kuona namna ya kutoa fursa katika kundi hili.
Mheshimiwa Spika, pia nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyekiti wa SHIVYAWATA, Dada Ummy Nderiananga, ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa sana pamoja na Serikali katika kuhakikisha kwamba tunaongeza uelewa katika kundi hili la watu wenye ulemavu ili wengi zaidi wajitokeze kushiriki katika programu mbalimbali ambazo ziko chini ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, ilijitokeza pia, hoja ya kwamba watoto wenye ulemavu wa macho kutokuwa na uwezo wa kurejea nyumbani nyakati za likizo kutokana na kutokuwa na wasindikizaji. Niliarifu tu Bunge lako kwamba Serikali tumeliona hili na tunalichukua na tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine iliyojitokeza ni kuitaka Serikali iwasilishe takwimu za hukumu zilizotolewa kwenye kesi zinazowahusu waliohukumiwa kwa makosa ya jinai, kuhusiana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, takribani kesi 28 za ukatili wa jinai kwa watu wenye ulemavu zimetolewa hukumu na kesi 37 ziko Mahakamani. Nichukue fursa hii kuwashukuru sana mhimili wa Mahakama kwa kuendelea kutoa msisitizo mkubwa wa usikilizaji na umalizaji kesi hizi kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, ilikuja pia hoja nyingine ya Wabunge walichangia uanzishwaji wa kambi za kilimo kwa ajili ya vijana ili iwasaidie vijana kuweza kujiajiri. Serikali kupitia Programu za Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi inalenga kuwawezesha vijana kujiajiri katika sekta za uzalishaji mali,
ikiwemo kilimo. Aidha, wadau mbalimbali wakiwemo FAO, Techno Serve, World Vision Tanzania, Heifer International, Swiss Contact, Planning International na ILO, wameendelea kutekeleza programu mbalimbali kuwawezesha vijana kujiajiri katika sekta ya kilimo pamoja na mnyororo wake wa thamani. Serikali pia kupitia Vituo vya Vijana vya Ilonga na Sasanda inaendesha programu za kilimo katika mfumo wa mashamba darasa ambapo vijana wanaojishughulisha na kilimo kutoka maeneo mbalimbali wanafika na kupata mafunzo hayo.
Mheshimiwa Spika, mafunzo yanayotolewa ni pamoja na kitalu nyumba kwa mazao ya mbogamboga, mazao ya biashara kama vile kahawa, mazao ya chakula, ufugaji wa ng’ombe, samaki na nyuki. Aidha, Serikali imezindua mkakati wa kuwawezesha vijana kujiajiri kwenye sekta ya kilimo pamoja na mnyororo wa thamani.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu tunaufanya pamoja na Wizara ya Kilimo ambapo tuna mkakati wa Kitaifa wa kuwaingiza vijana kwenye kilimo, moja kati ya maeneo ambayo tunaanza nayo ni katika eneo la Morogoro - Mkulazi, ambapo kitajengwa kiwanda cha sukari chini ya mifuko ya
PPF na NSSf. Katika eneo lile zimetengwa takribani ekari elfu 63. moja kati ya eneo ambalo tulilichukua kubwa tutapatengeneza blocks za mashamba kwa ajili ya vikundi vya vijana na tunategemea kutoa ajira kupitia mashamba haya, ajira takribani 100,000.
Mheshimiwa Spika, vilevile siyo kwa wananchi wa Morogoro tu mashamba haya yanaweza pia yakatawanywa pembezoni mwa Morogoro, hasa katika Mkoa ambao miwa ile ikilimwa inaweza kufika kiwandani ndani ya saa 24. Kwa hiyo, vijana wote waliopo nje ya Morogoro lakini wenye uwezo wa kufanya shughuli ya kilimo, wana uwezo wa kulima mua huu na soko lake liko assured kwamba viwanda hivi vitachukua miwa hii. Kwa hiyo, naendelea kutoa wito kwa vijana wote nchi nzima kuona fursa hii na kujitokeza.
Mheshimiwa Spika, ilijitokeza pia hoja ya pongezi, Wabunge walipongeza kwa programu mbalimbali ikiwemo ya ukuzaji ujuzi, hasa kupitia viwanda vya Tooku Garments cha Dar es Salaam na Mazava Fabrics Morogoro. Vilevile walishauri kwamba programu hizi zipanuliwe na ziweze
kuwafikia vijana wengi zaidi. Pongezi zimepokelewa na Serikali itaendelea kupanua wigo wa utekelezaji wa programu ya kukuza ujuzi na stadi za kazi ili kuwafikia vijana wengi zaidi nchini. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 vijana zaidi ya 17,350 watanufaika na mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi yatakayotolewa sehemu mbalimbali nchini, ukilinganisha na vijana zaidi ya 9,120 ambao watanufaika mwaka 2016/2017.
Aidha, mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi yatakayotolewa na Taasisi ya Ufundi Dar es Salaam (DIT) Mjini Mwanza mwishoni mwa mwaka huu wa fedha yatawanufaisha pia vijana kutoka Shinyanga walioomba kujiunga na mafunzo hayo.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ilijitokeza ni ya mkakati wa uwezeshaji wa vijana na akinamama kiuchumi uendane sambamba na kuwapatia elimu ya kitaalamu katika nyanja za ujasiriamali. Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendesha programu mbalimbali za mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana. Programu hizo zinaendelea kuongeza ujuzi kwenye maeneo mbalimbali. Mfano wa programu hizo ni pamoja na ufundi wa stadi za kazi kwa vijana wa Vyuo Vikuu, JKT, wafanyabiashara na waendesha bodaboda. Serikali imeanzisha utaratibu maalum wa majukwaa ya wanawake kwenye Mikoa na Halmashauri zote nchini. Katika majukwaa hayo wanawake wanapata fursa ya kupata elimu ya ujasiriamali, taarifa za mitaji na masuala mengine ya kuboresha shughuli zao za kiuchumi. Serikali pia inaendelea kuzisimamia kwa karibu Halmashauri zote nchini kulenga na kutoa fursa za mikopo kwa wanawake na vijana kwa asilimia tano kama ilivyoelekezwa.
Mheshimiwa Spika, ilizungumzwa pia hoja ya mikataba kwa wafanyakazi. Wabunge waliishauri Serikali kuendelea kusimamia sheria ili wafanyakazi wengi zaidi waweze kupata mikataba.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili ninataka nikiri kwamba, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kufanya kaguzi mbalimbali kuhakikisha kwamba Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004, inafuatwa kwa waajiri wote kutoa mikataba, kama ambavyo kifungu Namba 14
kinavyosema. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya kaguzi mbalimbali ili basi kuweza kuwabaini wale waajiri wote ambao wanakiuka Sheria hii na tunaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa nchi hii wanapata mikataba yao na wafanye kazi wakiwa na mikataba.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia katika hoja ambazo zimesemwa, baadhi ya wachangiaji walikuwa wanahoji mipango ya Serikali kama kweli ina nia thabiti ya kuwasaidia vijana wa nchi hii. Nataka niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge ya kwamba hata ukiangalia trend, katika kipindi hiki cha muda wa mwaka mmoja kazi nyingi sana za vijana zimefanyika, mafunzo mengi sana yamefanyika na kwa kweli, ukiangalia kazi ambazo zimefanyika zimewagusa vijana moja kwa moja na imewasaidia sana kuwafanya vijana hawa waondokane na utegemezi. Sasa tunawatengenezea utaratibu ili vijana wengi zaidi waweze kujiajiri kupitia katika programu zetu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika kushughulikia masuala ya vijana jambo la kwanza kabisa ambalo tunalifanya ni kuwatambua kwanza vijana, tunafanya identification ya vijana kwa makundi yao. Tuna vijana wa aina tofauti, tuna graduates, lakini tuna vijana
ambao hawakupata fursa ya kupata elimu ya juu. Vilevile hatua ya pili tunayoifanya ni ya kuwarasimisha (formalization), hapa tunawaweka vijana katika vikundi kupitia SACCOS na kampuni vilevile.
Mheshimiwa Spika, ninao huu mfano wa vijana ambao wanafanya vizuri sana, ambao ni vijana kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine ambao wao walihitimu pale chuoni na baadaye wakatengenezewa utaratibu na wakapewa mikopo. Vijana hawa wanaitwa SUGECO ambao wanafanya
shughuli za kilimo na hivi sasa ni kati ya vijana ambao wanafanya vizuri sana na wameanza kuwasaidia vijana wenzao nchini kwa kuwasaidia mitaji, vilevile na kuwapa mafunzo mbalimbali hasa katika maeneo ya kilimo. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanahoji namna ya uwezeshaji wa vijana. Katika Ofisi ya Waziri Mkuu tunayo mifuko mingi sana, lakini mifuko hii pia tunaratibu pamoja na Wizara zingine. Lakini huu mfuko mkubwa ambao tunautumia ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao mpaka ninavyozungumza hivi sasa tayari umeshakopesha takribani vikundi 297 kiasi cha shilingi bilioni 1.5 na vijana wamenufaika na tumeanza kuona matokeo na mabadiliko miongoni mwa vijana. Siyo hivyo tu, tuna Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Mfuko wa Rais wa Kujitegemea, vilevile tunao Mfuko wa Nishati ya Umeme Vijijini. Katika hili pia tunao mfuko wa kutoka BOT (SME) unaitwa Small and Medium Enterprises Credit Guarantee Scheme, hii yote inafanya kazi za kusaidia kuwawezesha vijana.
Mheshimiwa Spika, ilikuja hoja hapa ya kwamba kama Serikali tumejiandaaje? Inavyoonekana katika takwimu vijana wanaokwenda katika soko la ajira kila mwaka ni takribani vijana 800,000 mpaka 1,600,000, lakini nafasi za ajira zinazotengenezwa ni chache sana. Serikali tuliona jambo la kwanza la kufanya ili kumfanya kijana wa Kitanzania ajitegemee cha kwanza kabisa ilikuwa ni kuanza kuwabadilisha mtizamo, kuwabadilisha mtizamo vijana ilianza katika kuwapa elimu na kufafanua kwamba ajira maana yake ni nini. Kwa sababu mtazamo uliopo hivi sasa ni kwamba ili mtu aonekane ana ajira ni lazima awe tu ana ofisi yake, anavaa shati jeupe, ana tai, ana kiti cha kuzunguka, hiyo ndiyo ajira. Kwa mujibu wa Sera ya Ajira ya Taifa, inasema ajira ni shughuli yoyote halali ambayo inampatia mtu kipato. Kwa hiyo, tumeanza kuwaondoa vijana kimtazamo kuamini kwamba siyo wote lazima waajiriwe, kuna shughuli za kilimo, kuna shughuli za ufugaji, shughuli za ujasiriamali.
Ninavyozungumza hivi sasa tumetenga takribani ekari 85,000 nchi nzima kwa ajili ya shughuli hizi za vijana.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo nashukuru sana. Naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
NAIBU WAZIRI , OFISI YA WAZIRI MKUU (VIJANA, KAZI NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nitajielekeza katika kupambana na kudhibiti dawa za kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo napenda kulizungumza ni suala la bajeti kama ilivyoshauriwa na Kamati. Ni kweli ukiangalia bajeti ya mwaka 2017 na mwaka 2018, bajeti hii ililenga hasa katika muundo wa iliyokuwa Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. Baada ya mabadiliko ya sheria na hivi sasa kuwa na mamlaka na kufahamu majukumu ya mamlaka, Serikali katika kipindi cha fedha cha mwaka 2018/2019, tutaangalia namna ya kuweza kuongeza bajeti ili iendane na kazi ambazo zinafanywa na mamlaka hasa kwa kuwa tumeshapata uzoefu wa kazi ya mwaka mmoja ambayo mamlaka imefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja ya kuhusu Sera ya Taifa ya Dawa za Kulevya. Serikali inatambua umuhimu wa sera ya Taifa ya Dawa za Kulevya na utungwaji wa sera unapitia hasa katika kupata maoni ya wadau na mpaka ninapozungumza hivi sasa, tumeanza na Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo tayari Mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Kigoma na Geita wamekwishatoa maoni yao. Tunategemea kwamba katika bajeti ya mwaka 2018/2019 fedha zitaongezwa zaidi kuharakisha ukamilishaji utungwaji wa sera hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imekuwepo hoja ya kuwepo chombo cha kisheria kushughulikia udhibiti wa biashara na matumizi ya dawa za kulevya katika ngazi ya Halmashauri kama ilivyo kwa zile Kamati za UKIMWI katika ngazi ya Halmashauri. Kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sheria Na. 5 ya mwaka 2015 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2017, sheria hii imeipa mamlaka Tume kufanya kazi na chombo chochote katika kushughulikia matatizo ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tayari tumeanza mazungumzo chini ya uratibu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, sisi pamoja na TACAIDS kuona namna bora ya kufanya suala hili la uratibu ili Kamati zile zile za UKIMWI katika ngazi ya Halmashauri pia zifanye kazi ya Kamati ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ilikuwepo hoja hapa ya changamoto za upatikanaji wa tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya, kwa hivi sasa tunavyo vituo vitano ambavyo vinatoa tiba kwa waraibu wa madawa ya kulevya lakini mpango wetu ni kuongeza vituo vingine vitano mwaka huu wa fedha pale fedha itakapopatikana ili kuwafikia waraibu wengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hivi sasa tunakamilisha kituo cha Itega hapa Dodoma na Mwanza ambapo kwa Dodoma tayari tumeshapokea dola milioni 2.5 kutoka Global Fund ambayo lengo lake ni ukamilishaji wa kituo hiki ili tuweze kuwafikia vijana wengi zaidi ambao ni waathirika wa dawa za kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali imeongeza ukomo wa uagizaji wa dawa ya methadone kutoka kilo 120 mpaka kilo 300 na hii inatokana na mikakati tuliyonayo kama Serikali, hasa katika eneo la supply reduction, hali inayosababisha kunakuwa na upungufu mkubwa sana wa dawa za kulevya mtaani na hivyo kuwalazimu waraibu hawa kukimbia katika vituo vya tiba. Hivyo, tumeongeza ukomo wa uagizaji wa dawa ya methadone na hivi sasa ninavyozungumza muda wowote dawa hii itaingia kwa ajili ya kuweza kuwashughulikia watu walioathirika na dawa za kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, katika sehemu ya hoja ambazo zilisemwa hapa ni kuwepo kwa unyanyapaa kwa waraibu wa dawa za kulevya. Kwa kulitambua hili, ni kweli wako vijana na watu wazima ambao wameathirika na madawa ya kulevya ambao wakirudi mtaani wanapata
unyanyapaa mkubwa sana na vilevile hali hii inawasababisha pia kurudia kufanya matumizi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumeona hatua ya kwanza ni kuanzisha kituo ambacho tunakiita occupational therapy ambacho kitajengwa katika eneo la Itega Dodoma, lengo lake ni kuwapa elimu ya stadi za kazi ya fundi uashi, ufundi seremala, ili akiacha matumizi ya dawa za kulevya akirudi mtaani awe ana shughuli ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia limezungumzwa hapa jambo la nyumba za upataji nafuu (sober houses), Serikali inaendelea na ujenzi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kukushukuru kwa nafasi. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na afya Waheshimiwa Wabunge wote. Pia nichukue fursa hii kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu ili kuchangia hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa Naibu Waziri ninayeshughulikia masuala ya kazi, vijana na ajira, naomba nitumie fursa hii kwanza kabisa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa; Waziri wangu Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa ushirikiano na miongozo ambayo wamekuwa wakinipa kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu lakini pia nisimsahau Mheshimiwa Naibu Stella Ikupa kwa ushirikiano anaonipa katika utekelezaji wa majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue fursa hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa azma yake ya kutekeleza kwa vitendo Serikali kuhamia Dodoma ambako hivi sasa tumeshuhudia maendeleo mengi sana katika Jimbo la Dodoma Mjini ambayo yanatokana na uamuzi huo mkubwa wa Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kutokana na uamuzi huo wa Mheshimiwa Rais, kwa sababu asilimia kubwa hapa ya Waheshimiwa Wabunge mnaishi Dodoma na mimi ni Mbunge wenu kwa namna moja ama nyingine, nataka tu nitoe ufafanuzi katika baadhi ya mambo ambayo mmekuwa mkikutana nayo huko mtaani mojawapo ikiwa ni katika zile barabara ambazo zinawaletea tabu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ujio huu wa makao makuu hapa Dodoma tayari hata wahisani wenyewe wameanza kuona namna ya kuboresha mji wetu. Tumepata fedha za ziada na hivi sasa kuanzia Julai barabara nyingi sana za kwetu zitakuwa na lami. Pia tuna mradi mkubwa wa Storm Water Drainage katika eneo la Ilazo ambalo limekuwa kikwazo kikubwa sana kwa watu kufika kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kutokana na azma hii ya Serikali Dodoma sasa inakwenda kujengwa soko kubwa la kisasa ambalo litakuwa ni kubwa na lenye ubora kuliko mengi sana Afrika Mashariki na Kati. Vilevile tunakwenda kujenga stendi kubwa ya kisasa ambayo itakuwa ina maegesho ya zaidi magari 600 kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia utakwenda kujengwa uwanja mkubwa wa kimataifa wa mpira wa miguu ambao utatoa fursa nyingi katika Jimbo letu la Dodoma Mjini. Haya yote yanatokana na kazi kubwa ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais ya kuhamishia Dodoma kama sehemu ya makao makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo kama maneno ya utangulizi, kwa heshima na taadhima naomba sasa nijibu hoja ambazo zimewasilishwa na Waheshimiwa Wabunge waliokuwa wakichangia katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza kubwa lililojitokeza hapa ni kuhusiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ambapo Waheshimiwa Wabunge wamechangia kwa kuiomba Serikali kuhakikisha kwamba elimu ya kutosha inatolewa kwa wafanyakazi na waajiri na kuhakikisha kwamba sheria hii inazingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi umeanzishwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2008 ambayo lengo lake ni kuhakikisha kwamba wale wafanyakazi wote wanaopata matatizo yanayotokana na kazi zao waweze kufidiwa na mfuko huo. Sheria hii ilipita
hapa Bungeni na ndani ya sheria imetaka waajiri wote nchini wajisajili katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ili mfanyakazi yeyote anayepata matatizo akiwa kazini, mwajiri tumuachie kazi yake ya kimsingi ya shughuli anayoifanya na kazi ya kumhudumia mfanyakazi aliyeumia ifanywe na Mfuko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii ilitungwa hapa na kuwataka waajiri wote wajisajili na kabla ya kuanza kufuatilia waajiri wangapi wamejisajili, Mfuko ulifanya kazi ya kutoa elimu ya kutosha kwa kwenda katika kanda mbalimbali kuwaelimisha waajiri juu ya umuhimu wa huu Mfuko. Baadaye Mheshimiwa Waziri wa Nchi alitoa maelekezo kwamba sasa ufanyike utaratibu kuhakikisha kwamba waajiri wote wanasajiliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo imefanyika na hata baada ya kikao cha juzi cha Baraza la Biashara la Taifa ambalo lilikuwa chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Rais, maelekezo yalitoka kwamba zile kero ndogo ndogo ambazo zinawakabili waajiri Serikali tukae nao na tuweze kutafuta namna nzuri ya kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba tayari sisi katika Ofisi ya Waziri Mkuu maelekezo hayo tumeshayafanyia kazi na elimu inaendelea katika baadhi ya kanda tunakutana na waajiri ili kuwaambia umuhimu wa Mfuko huu wa Fidia kwa Wafanyakazi ambao ni mkombozi kwa wafanyakazi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine iliyojitokeza katika michango ya Wabunge ni kwamba tuhakikishe wafanyakazi wetu wengi wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya viwanda na maeneo mengine wanapatiwa vifaa kinga kwa mujibu wa sheria. Sisi kama Wizara kupitia Wakala wa Afya na Usalama Pahala pa Kazi (OSHA), tumekuwa tukifanya kaguzi mbalimbali kuhakikisha kwamba wafanyakazi wote wanapatiwa vifaa kinga ili itusaidie pia kuwakinga na madhara mbalimbali ambayo yanatokana na kazi na mwisho wa siku kumfanya mfanyakazi wa Kitanzania afanye kazi katika mazingira ambayo ni rafiki na kulinda na afya yake pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii inafanyika na niwashukuru sana na kuwapongeza OSHA kwa kufanya kazi hii kwa weledi mkubwa. Naamini kabisa kwamba tutaendelea kufanya kazi hii ya ukaguzi ili kulinda nguvu kazi ya Taifa hili isipate madhara au maonjwa kutokana na kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ilizungumzwa hoja na Waheshimiwa Wabunge hapa ya kuitaka Serikali kuboresha kilimo ili kuongeza ajira kwa vijana na vilevile kuwapatia mikopo washiriki katika shughuli za kilimo. Sisi kama Wizara tuliona kwamba ni kweli, ukisoma katika tafiti ya Integrated Labour Force Survey ya mwaka 2014 inazungumza kuhusu idadi kubwa ya vijana wanaoshiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu sana shughuli ya kilimo haikuwa inapewa kipaumbele sana kwa miaka ya nyuma. Sisi kama Serikali tukaona kwamba moja kati ya eneo ambalo linaweza likaajiri vijana wengi kwa wakati mmoja ni katika kilimo hasa kilimo biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulianza kwanza kwa kujaribu kubadilisha mitizamo (mindset) ya vijana juu ya suala zima la kilimo. Asilimia kubwa ya vijana walikuwa wanachukulia kilimo kama ni shughuli ya kufanya baada ya kukosa shughuli ya kufanya ni kama ni last resort. Kwa hiyo, sisi kama Wizara tukaitafsiri tukasema kwamba kwa mujibu wa Sera yetu ya Ajira inasema ajira ni shughuli yoyote halali inayompatia mtu kipato ikiwemo kilimo. Kwa hiyo, tukaanza kuhamasisha vijana kushiriki katika kilimo. Hii tunaifanya pamoja na Wizara ya Kilimo tukiwa tuna mpango mkakati wa kitaifa wa kuwahusisha vijana katika kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao vijana wa kwanza wa mfano ambao tumekuwa tukiwatumia ambao ni vijana waliotoka Chuo Kikuu cha Sokoine wanaoitwa SUGECO. Vijana hawa wali-graduate Chuo Kikuu cha Sokoine wakaziweka degree zao pembeni kwa kile walichokisomea, wakakaa sawasawa katika kilimo, leo hivi navyozungumza wale vijana wanatoa mafunzo kwa vijana wenzao lakini vilevile kilimo hiki sasa kimewafanya wasifikirie ajira nyingine. Hivi ninavyozungumza wameingia kwenye mipango mikubwa ya kidunia ikiwemo mpango wa Bill and Melinda Gates ambao kwa nchi za Afrika ni Tanzania na Nigeria tu ndiyo tumepata nafasi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu, katika mpango wa kukuza ujuzi wa miaka mitano wenye lengo la kuwafikia vijana takribani milioni 4.4, moja ya programu tuliyonayo ni Programu ya Kitalu Shamba. Katika mwaka ujao wa fedha tumeshaagiza mamlaka za mikoa waombe kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu maombi ya vitalu shamba, tutawafundisha vijana wa Kitanzania kutengeneza vitalu shamba na tutatoa vitalu shamba ili wafanye kilimo biashara cha kisasa. Lengo ni kuhakikisha kwamba vijana wengi zaidi wanafanya shughuli ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, pale Morogoro tuna shamba la miwa la Mkulazi kwenye kiwanda cha sukari, asilimia kubwa ya tuliowachukua kushiriki katika uchumi ule ni vijana ambao ndiyo out growers na pale kuna hekari 63,000. Vijana wa Morogoro na maeneo ya karibu watapata fursa kushiriki katika uchumi huu wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilijitokeza hoja nyingine hapa kwamba Serikali ihakikishe ajira hizi katika miradi hii mikubwa kama ya bomba la mafuta, mradi wa reli huu mkubwa inawagusa na kuwanufaisha Watanzania. Sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu tuliliona jambo hili, tulichokifanya awali ni kuhakikisha kwamba wataalam wetu wanakaa na kuona ni nafasi na ujuzi gani unaohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshafanya coordination ndani na hivi sasa ninavyozungumza Wakala wetu wa Huduma za Ajira anafanya kazi hiyo kuhakikisha kwamba Watanzania wengi zaidi hasa vijana wanapata fursa ya kushiriki katika uchumi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano katika hili bomba la mafuta, mpaka hivi sasa maombi ya vijana yaliyokuja ni takribani 23,650 ambapo uhakiki unaendelea ili kuwa-link na zile fursa. Lengo letu vijana wengi zaidi wapate nafasi za ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilijitokeza hoja moja hapa ya kwamba Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unatoa mikopo kwa ubaguzi wa itikadi ya vyama vya siasa. Naomba niliweke hili sawasawa, Mfuko wa Maendeleo wa Vijana (YDF) upo kwa mujibu wa sheria na una mwongozo wa nani anatakiwa kupewa mkopo akikidhi masharti gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mle hakuna sharti linalosema uambatanishe na kadi yako ya chama za siasa, hakuna. Sharti ni kwamba lazima kila Halmashauri iunde SACCOS ya vijana ndiyo itakopesha vikundi katika eneo husika. Kwa hiyo, niondoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba mikopo hii ni kwa ajili ya vijana wote wa Kitanzania wanaokidhi masharti ya mwongozo ambao umewekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilijitokeza pia hoja ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambapo Wabunge wali-raise concern tu kwamba yale maeneo yao wanayotumia especially kule Dar es Salaam hawana vyumba vya kutosha na wanafanya kazi katika mazingira magumu. Nichukue fursa hii kulitangazia Bunge lako Tukufu kwamba tumefanya mawasiliano na zile Wizara ambazo zinatoka kule Dar es Salaam ambazo zimeacha Ofisi wazi, hivi sasa Tume hii ipo katika hatua za mwisho za kupata majengo mengine ambayo yatawafanya wafanye kazi kwa uhuru na ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya mwisho ni kuhusu Nembo ya Taifa na ilisemwa kwamba nembo ile jinsi ilivyo haiakisi mazingira ya Tanzania na kwamba mtu akiiona anaweza akapata picha tofauti kwa sababu kuna mwanamke anaonekana pale ana kama nywele ambazo sio za Kitanzania kwa maana ya wig. Naomba niliweke wazi tu kabisa suala hili, Nembo ya Taifa imeanzishwa kwa mujibu wa National Emblems Act, Sura ya 10 na ukiangalia siyo kweli kwamba haiakisi mazingira yetu kama inavyoonekana hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nembo hii ni moja kati ya alama za Taifa na ukiangalia hapo, huyo anayeonekana kama kavaa wig, kile ni kilemba cha kuonesha kwamba huyu ni mwanamke wa Kitanzania na ndiyo mazingira yetu. Pia kuna Mlima Kilimanjaro ambao upo peke yake Tanzania, hakuna mlima mwingine wowote Afrika na duniani, hicho ni kielelezo kingine pekee. Pia kuna mawimbi pale kuonesha bahari, mito na maziwa yetu lakini pale chini ukiwaangalia wamekanyaga karafuu na pamba kuonyesha kwamba haya ni mazao makuu yaliyopo katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaondolee hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba siyo kweli nembo hii haiakisi mazingira ya Taifa letu la Tanzania. Ukiona yenyewe inasema jinsi ilivyo, wanasheria wana lugha moja wanasema res ipsa loquitur, kwamba mambo yanaongea yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya sasa, naomba nitamke rasmi naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetuwezesha kufika siku ya leo na kwa baraka zake tele tuko hapa siku ya leo. Pia kipekee kabisa nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa miongozo yao na maelekezo yao katika kutekeleza majukumu ndani ya Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kipekee kabisa naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri Hussein Mohamed Bashe, Waziri wa Kilimo pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakinipatia katika kutekeleza majukumu katika Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa mbele ya Bunge hili naomba niseme namshukuru sana Mheshimiwa Waziri amekuwa kaka, amekuwa rafiki, amekuwa kiongozi, lakini amekuwa Mwalimu mzuri. Nimejifunza kilimo kupitia yeye na mimi kila siku asubuhi nikiamka saa 12 lazima nisikilize kwenye YouTube jambo lolote la Hussein Bashe kwenye kilimo imenifanya nimekielewa vizuri kilimo hivi sasa. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na hoja ya kwanza, hoja ya BBT kwamba ni kwa nini hatujaenda Mikoa yote? Tulitoa utaratibu mzuri kabisa ambapo tuliandika barua kwa Mamlaka za Mikoa za kuwataka kutenga maeneo maalum kwa ajili ya program hii kubwa ya vijana na wakina mama. Ipo mikoa ambayo ilifanya kwa uharaka na iliandaa maeneo na ikawa rahisi katika sehemu ya kwanza ya utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kutoa rai kwa Mikoa mingine yote ambayo maeneo yapo kwa ajili ya kilimo kwenda kutekeleza program hii ya BBT, Wizara tuko tayari kuja kuyaangalia maeneo hayo, tutatuma wataalam wetu na tuko tayari kuanzisha program hizi katika maeneo hayo. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha tumeifikia nchi nzima kutokana na ikolojia ya kila eneo na hiyo ndiyo maksudi mazima ya program hii.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Shinyanga kwa mfano, ukiangalia hapa katika vitabu vyetu haimo lakini Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga namshukuru sana pamoja na Mheshimiwa Mbunge Katambi hapo walishirikiana kwa pamoja na Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga, tulizungumza na Mwekezaji pale Jambo ambaye yeye anazalisha juice na ana mahitaji makubwa sana ya maembe, Mkoa wa Shinyanga wanaweza kulima maembe. Ninavyozungumza hivi sasa wameshaandaa eneo na tumeshamuelekeza mtaalam wetu kwenda kupima afya ya udongo, tutakwenda kufanya BBT katika Mkoa wa Shinyanga na off taker tayari yuko pale ni Jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Geita wameonesha utayari. Mkoa wa Geita kwenye kilimo cha mananasi na wenyewe wako tayari kwa ushirikiano wa Mkuu wa Mkoa na kwenyewe pia kule tutakwenda, bahati nzuri mananasi ya Geita Jambo ameshayapima na ana uwezo wa kuyatumia kutengeneza juice, kwa hiyo soko la uhakika lipo na pale tutakwenda kuweka mradi mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza hoja za Waheshimiwa Wabunge, wamechangia vizuri sana na kutoa ushauri mzuri sana, liko jambo nataka niliweke vizuri ili lieleweke vizuri. Hapa kuna hoja mbili, kuna hoja ya program ya BBT na kuna hoja ya mashamba makubwa ya pamoja (block farms) haya ni mambo mawili tofauti. Ni sawasawa na kwamba kila Wakili ni Mwanasheria lakini siyo kila Mwanasheria ni Wakili. Maana yake ni hivi katika haya mashamba. Mashamba makubwa ya pamoja siyo lazima yote kuwemo kuna BBT. BBT ni program ya uwezeshaji wa vijana na wakina mama ambao siyo lazima iwekwe katika mashamba makubwa yote ya Pamoja, lakini BBT ni mkusanyiko wa eneo kubwa kwa hiyo ni shamba moja au mashamba ya pamoja lakini siyo lazima ya kwamba kila kwenye block farm kuna BBT, na hapa ndiyo dhana ile ambayo nataka niiseme kwamba watu wanafikiri tumewasahau wakulima wengine na tumewalenga vijana peke yao na wakulima wengine tumewaacha kabisa, hapana.

Mheshimiwa Spika, katika mashamba haya makubwa watakwenda kulima wakina mama, wakina baba, wenye umri ambao siyo umri wa vijana na vijana pia watakuwemo. Kwa hiyo, hoja ya kwamba tumewaacha kabisa hapana. Kwa hiyo nataka niliweke sawa sawa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni suala la umwagiliaji. Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi imetuelekeza kwamba ikifika mwaka 2025 tuwe tuna eneo linalomwagiliwa la hekta milioni 1.2, Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Wabunge mwaka jana mkatoa hoja na ushauri kwamba nchi yetu imejaliwa mabonde, maeneo mazuri, kwa nini hatuongezi eneo la umwagiliaji?

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita ni Serikali sikivu, Mheshimiwa Rais alisikia hoja ya Wabunge juu ya maeneo makubwa ya kimkakati ya kufanya kilimo cha umwagiliaji na Tarehe 20 mwezi Machi, 2023 mbele ya Mheshimiwa Rais, tumesaini mikataba ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika mabonde 22 ya kimkakati ambayo tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba tunakwenda kuimwagilia nchi nzima. Mabonde haya ya kimkakati inaanzia katika Bonde la Ziwa Victoria, zaidi ya hekta 20,000. Tunakwenda Bonde la Bugwema, Bonde la Suguti, tunakwenda Bonde la Mto Manonga Wembele, tunakwenda Bonde la Ruhuhu, Bonde la Tumbandiosi, Bonde la Makondeko, Bonde la Lukuledi, Bonde la Mto Songwe, Ifakara Idete, Kilombero, Mkomazi, Rufiji Basin, inakwenda mpaka Kasinde, Ngomai. Mabonde haya yote yanakwenda kutengeneza hekta 306,631 za umwagiliaji, ni nchi nzima tunakwenda kuigusa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hiyo tuliona kutokana na mabadiliko ya tabianchi lazima tuhakikishe tunafanya kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji maana yake nini? Lazima uwe una skimu zinazokusaidia kufanya kilimo mwaka mzima zaidi ya mara moja. Ili uweze kufanya hivyo lazima uwe na chanzo cha uhakika cha maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha huu 2022/2023 ambao unaishia, tumekwenda na Wakandarasi wako site tunachimba mabwawa 14 ya awali ambayo yatatupa mita za ujazo ya maji 131,535,000 ambazo ukizibadilisha ni sawa na maji lita bilioni 131. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyafanya hayo, kwenye bajeti hii ya mwaka huu ambayo Wabunge mtaipitisha hapa, tunakwenda kuchimba mabwawa mapya 100 ambayo yatakuwa yana mita za ujazo milioni 906 sawa na lita za maji bilioni 900. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuishii hapo, tunakwenda kuchimba visima 150 katika Halmashauri 184. Wako wakulima ambao kwao wanahitaji visima tu kuweza kuongeza uzalishaji, tutafanya Wizara ya Kilimo. Tumejifunza kwa Wabunge wametuambia hapa ya kwamba yako baadhi ya maeneo hatuhitaji visima, hatuhitaji mifereji mikubwa. Tutapeleka pia na pampu katika maeneo ambayo ni karibu na vyanzo vya maji ili wakulima wetu waweze kumwagilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ilizungumzwa hoja hapa kwanini hatuweki nguvu nyingi kwenye mazao ambayo yatatuletea pia fedha za kigeni? Sasa nafikiri tu kuna baadhi ya Waheshimiwa hasa aliyeongea hoja hii Mheshimiwa Halima Mdee nafikiri hakuangalia vizuri humu ndani. Nitampa mfano wa mazao mawili tu, mchele na parachichi ambayo aliisema yeye. Kwenye mpunga, maeneo ambayo tunayategemea sana ni Mkoa wa Mbeya, Wilaya ya Mbarali. Pale Wilaya ya Mbarali tumefanya uwekezaji mkubwa wa miradi ya umwagiliaji. Mheshimiwa Mtega yuko hapa ni shahidi.

Mheshimiwa Spika, pale tuna mradi wa Bonokuva Gigolo, tuna mradi wa Herman Chosi, tuna mradi wa Ipolo Isenyela, tuna mradi wa Matebete, ambayo ni miradi ya fedha nyingi na hii yote itakwenda kusaidia upatikanaji wa mpunga wa uhakika kwa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili kwenye parachichi ambayo aliisema. Kwenye parachichi tunafanyaje? Tumetafuta masoko ya uhakika ya parachichi. Tarehe 25 Novemba, 2021, Mamlaka ya Afya ya Mimea ya India walituruhusu kuingiza parachichi. Tunapeleka parachichi India, tutapeleka parachichi Hispania, tutapeleka parachichi China, Marekani tunamalizia hoja ya phytosanitary ili tupeleke kule nako parachichi. Serikali inafanyaje katika kuliandaa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zao hili linahitaji pia requirement ya kimataifa, mojawapo ni usafi wa mazao. Ukienda Arusha, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu tumepata ithibati ya kimataifa ya usafi wa mazao ambayo itasaidia kupeleka mazao yetu nje ya nchi, pale pia tumefunga mtambo mkubwa tunauita micro plasma atomic emission spectroscopy ambao unasaidia kupima usafi wa mazao na zamani mkulima wa Tanzania alikuwa analipa zaidi ya dola 10,000 kwa ajili ya kipimo hicho leo analipa dola 300 kwa ajili ya kupata hati ya usafi wa mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nataka niseme hapa haraka haraka ni kwenye mkonge. Wabunge mmesema hapa kuhusu mkonge, Wabunge wa Mkoa wa Tanga mmesema vizuri sana, tumesikia hoja zenu. Hoja kubwa ya mkonge ambayo inapelekea mkonge wetu kupata changamoto kubwa ni mkonge mwingi unaoza kwa sababu ya kukosa makorona. Wabunge wa Mkoa wa Tanga mwaka huu mtayaona makorona katika Mkoa wenu wa Tanga kuanza kuchakata mkonge. Tumeshaagiza na procurement process inaendelea, korona zile zitakuja na Wabunge wetu wa Mkoa wa Tanga mtatembea kifuambele, wakulima wenu watapata sehemu ya kwenda kuchakata mkonge wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunataka mkulima wa mkonge wa Tanga aache kuuza UG, aache kuuza SSUG, aache kuuza UF. Tunataka mkulima wa mkonge wa Tanga auze SL na 3S. Hii ndiyo mkonge wa daraja la juu kabisa ambao utampatia fedha nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa michango yenu ambayo kwa namna moja ama nyingine imekuwa ni sehemu ya kuboresha muswada huu wa sheria ambao umewasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyosema asubuhi, hata sisi ambao tulikuwa tunasikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge, unasikia kabisa ni michango ambayo inakwenda kuongeza thamani, ni michango ambayo iko very positive; na tunaamini kabisa kama Serikali iko michango ambayo tumeona ina umuhimu na sisi tutaichukua kwa ajili ya kuona namna bora ya utekelezaji wa sheria hii hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na jambo ambalo siyo muhimu sana lakini ni kwa sababu ya kumbukumbu. Nataka niweke kumbukumbu sawa. Wakati Msemaji wa Kambi ya Upinzani hajaanza kusoma hotuba yake, alizungumza ya kwamba ikumbukwe kwamba hoja hii ya kuunganisha mifuko ni hoja ambayo imeletwa na upinzani na akawataja baadhi ya Wabunge ambao waliianzisha hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumbukumbu tu ili Bunge lako liweke kumbukumbu sawa, nimepata mkanganyiko mkubwa sana wakati nasoma taarifa hii na mkanganyiko wenyewe ni kwamba sehemu moja inakubali, sehemu nyingine inakataa. Wakati maelezo ya msemaji anasema kwamba hoja hii imeanzia kwao, lakini ukisoma ukurasa wa pili, aya ya pili, naomba ninukuu kidogo tu kwa ajili ya kuweka kumbukumbu sawa. Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani anasema; “Kambi Rasmi ya Upinzani ina mtazamo kwamba badala ya Serikali kung’ang’ana kuweka

sheria za kupunguza na kuibana mifuko ya jamii, ingepanua fursa za ajira kwa Watanzania na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuajiri kwa wingi ili kupunguza umasikini wa kipato kwa Watanzania.”

“Pili, ni kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanawekewa akiba itakayowasaidia pindi umri wao wa kufanya kazi utakapokoma.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona kabisa contradiction hapa kwamba mwanzoni anasema hoja hii imetokea Upinzani, lakini ukisoma katika ripoti hii wanashangaa kwa nini tunaendelea kung’ang’ana kupunguza idadi ya mifuko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kumbukumbu hii ibaki sawa ni kwamba hoja hii kama walivyosema wachangiaji waliopita, ni hoja ambayo imeletwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na sisi kama Serikali tuliona ina umuhimu mkubwa ndiyo maana tumeichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuweka hiyo kumbukumbu sawa, niko katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Moja ya jambo ambalo limesemwa katika taarifa hii, limezungumzwa vyema kabisa kwamba tusiunganishe mifuko hii na badala yake tupanue fursa za ajira na kuweka mazingira wezeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mtoa hoja alielezea umuhimu wa kuunganisha mifuko hii na namna ambavyo itakwenda kuboresha mazingira ya wafanyakazi katika nchi yetu ikiwemo pamoja na mafao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja inayozungumzwa hapo na Kambi Rasmi ya Upinzani ni kutuambia kwamba badala ya kuunganisha mifuko, ni afadhali mtengeneze fursa zaidi za ajira kuliko kufanya jambo hili, ambayo inapingana na hoja ambayo aliitoa Mheshimiwa Zitto Kabwe ya kuongeza wigo wa sekta ya hifadhi ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tunaamini kabisa uunganishaji wa mifuko hii inakwenda kuongeza tija kubwa sana kwa wafayakazi wa nchi hii, lakini unapozungumzia suala la kuweka mazingira wezeshi na kuongeza fursa za ajira, mipango ya Serikali iko dhahiri, inafahamika. Tunayo miradi mikubwa katika nchi yetu ambayo itakwenda kutengeneza ajira nyingi sana ikiwemo ujenzi wa reli ya kati (standard gauge), likiwemo bomba la mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukienda katika falsafa ya uchumi wa viwanda ambayo inakwenda na ufungamanisho na maendeleo ya watu moja kati ya mambo ambayo tunayapigia kelele sana katika uchumi wa viwanda ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa ajira hasa katika kundi kubwa hili la vijana. Kwa hiyo, sioni kabisa kwamba ile hoja iliyoletwa hapa ya kusema kwamba, tuendelee kutengeneza nafasi tu za ajira na mifuko hii isiunganishwe, sikuona kama ina umuhimu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jambo lingine ambalo katika ripoti hii katika Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani wamesema ni msemaji anazungumza kwamba lazima mwanachama huyu anayechangia basi anufaike na michango yake kwa sababu kuna wengine unakuta hata michango hii hawajaitumia na tayari ameshafariki na hajaona utamu wa michango yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Msemaji leo wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Dada yangu Mheshimiwa Ester, kidogo alipitiwa leo na kama hakupitiwa basi hakuusoma vizuri muswada huu wa sheria. (Makof)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu wa sheria ambao tunaupendekeza katika kifungu cha 29, imeainishwa bayana mafao ambayo yatakwenda kutolewa. Hata katika previous position, kwa sheria zilizopo hivi sasa mwanachama ananufaika na mafao mbalimbali ambayo muda mwingine tunayasema ni mafao ambayo hata kabla hajafikia muda wake wa kustaafu, lakini anayapata kuanzia hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mafao ya uzazi, mafao ya kuumia kazini, ugonjwa na mikopo. Kwa hiyo, unapozungumza hoja ya kwamba, michango yake imsaidie ndio inavyomsaidia katika namna hii na ndio maana katika muswada wa sheria ambayo tunaipendekeza kifungu namba 29 kimeeleza bayana aina ya mafao ambayo sheria hii inayapendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini alikwenda mbali zaidi akazungumza kuhusu suala la life expectancy ya miaka 61.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, hoja yangu ni kwamba, katika Taarifa hii ya Kambi Rasmi ya Upinzani imezungumzwa hoja ya kwamba umri wa kuishi Mtanzania hivi sasa unakadiriwa kuwa ni miaka 61 kwa hiyo, na ndio maana ilikuja hoja kwamba ni afhadhali mtu anufaike na mafao yake haya kabla kwa sababu sio wote ambao wanakuwepo katika mda huo ambao aliusema hapa Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimpe tu taarifa kidogo kwamba, najua alikwenda kuchukua takwimu hii katika Taarifa ya NBS ambayo inazungumzia General Life Expectancy ambayo hii inamhusisha mpaka mtoto wa umri wa chini ya mwaka mmoja. Lakini nataka nimsaidie taarifa nyingine ambayo itamsaidia pia katika taarifa nyingine ambazo zinakuja. Ni kwamba kwa mujibu wa Acturial Valuation Report ambayo ilifanywa na ILO ambayo inazungumzia kuhusu wastani wa kuishi wa mstaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wastani wa kuishi wa mstaafu kwa mujibu wa taarifa ile inasema, mstaafu wa kiume ana uwezo wa kuishi miaka 20.9, lakini wa kike kwa miaka 22.3. Lakini kubwa zaidi kuliko yote tukichukulia kwa mfano tu wa PSPF ambao mpaka hivi sasa una takribani ya wastaafu 72,000 ni wastaafu asilimia nne tu waliofariki mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa pia katika taarifa hii kwamba hoja ya kwa nini tunamuingiza Mwanasheria Mkuu pindi pale Bodi inaposhitakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sera ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003 inamtamka Serikali kama ndiye guarantor. Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaingia kwa sababu ya kulinda maslahi ya Serikali. Ndio maana kwa mujibu wa sheria inayopendekezwa kifungu cha 60 kinatoa wajibu wa Serikali kama sehemu ya guarantee kwa mfuko huu, maana yake ni nini; maana yake ni kwamba Serikali lazima ilinde maslahi yake katika mfuko huu. Ikitokea jambo lolote limetokea mfuko huu una-colapse mwisho wa siku mzigo mzito inabeba Serikali na ndio maana Mwanasheria Mkuu wa Serikali likitokea jambo lolote la kushitakiwa kwa Bodi hii anaingia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kifungu hiki cha 60, inakwenda mbali zaidi ikitokea kwamba, kuna jambo ambalo linasababisha insufficience katika fund kwenye mfuko huu, Mfuko Mkuu wa Serikali unaguswa kwa namna moja, kwa hiyo, ndio maana nafasi ya Mwanasheria Mkuu inakuwepo katika Sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa pia, hoja hapa na Waheshimiwa Wabunge ambayo na sisi kama Serikali tunaikubali ya kuongeza wigo wa ku-cover mpaka informal sector na hoja hii, ukiifuatilia katika ripoti iliyotolewa
mwaka 2014 inaitwa Intergrated Labour Force Survey inasema, nchi yetu ya Tanzania tuna takribani ya nguvu kazi ya watu milioni 22.3. Watu milioni 22.3 maana yake ni watu kuanzia miaka 15 na kuendelea mbele ambao ndio the working age population (watu wenye uwezo wa kufanya kazi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mujibu wa takwimu zilizofanyika, utafiti uliofanyika inaonyesha kwamba, ni asilimia 10 tu ya nguvu kazi yetu ndio wapo katika hifadhi ya jamii. Ndio maana na sisi tunakubaliana na hoja hii kwamba, ni lazima, kama Serikali, tuje na mipango madhubuti ya kuhakikisha kwamba, tunaendelea kuwa-cover watu wengi zaidi kuingia katika mfumo wa hifadhi ya jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo yamefanyika pia katika marekebisho ya kifungu cha 30 cha Sheria ya SSRA ambayo imekwenda kutambua wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi kama wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii. Lakini vilevile kwa sheria hii ambayo leo tunaijadili hapa ndani na ikipitishwa inakwenda kupeleka mabadiliko katika Sheria ya NSSF ambapo NSSF sasa inapewa jukumu mahususi la kushughulika na private sector na informal sector.

Kwa hiyo, katika mpango na mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba, kupitia NSSF tunaifikia informal sector kwa eneo kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini na sera yetu imezungumza jambo hilo. Ukisoma sera yetu, Sera ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003, kifungu cha 3(2)(b) na chenyewe kinaelezea umuhimu wa kuwepo na informal sector katika coverage ya social security hasa katika maeneo ya kilimo, uvuvi, madini na biashara ndogondogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 95 cha Muswada kinakwenda kurekebisha kifungu cha 6 cha Sheria ya NSSF kuongeza maneno ya mtu aliyeajiriwa katika sekta binafsi na mtu ambaye amejiajiri ikiwa ni sehemu ya kwenda kutekeleza takwa hili la kusaidia coverage ya informal sector kwenye hifadhi ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa pia hoja hapa ambayo imewagusa Waheshimiwa Wabunge wengi sana kuhusiana na Fao la Bima ya Matibabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu wa fao hili tumeshuhudia Wabunge wengi wamkisimama wakilisema jambo hili. Niseme tu kama Serikali kwa kufahamu umuhimu wa jambo hili, tusingekuwa tayari kuliondoa kwa sababu ni jambo ambalo kwa kiwango kikubwa sana linagusa maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ilikuwa tu ni makosa ya kiuchapaji na ndio maana tumerekebisha. Fao hili la Bima ya Matibabu lipo palepale na marekebisho yetu ya Jedwali ambalo linakuja na Serikali lengo lake ni kupitia kifungu cha 97 kwenda kufuta kifungu cha 21(f) cha Sheria ya NSSF na kuingiza badala yake unemployment benefit, lakini kukiacha kifungu 21(g) cha sheria ile ambacho kinazungumzia masuala ya Bima ya Afya ya Matibabu. Kwa hiyo, jambo hili halijaondoka lipo palepale na kwa kweli, tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa concern yenu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilizungumzwa pia, hoja na Mheshimiwa Mtolea, Mheshimiwa Mtolea alikwenda specific kwenye kifungu namba 57 na akawa anastaajabishwa na matumizi ya neno shall ambalo kwa tafsiri yake anasema ni kama inatoa discretion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nafikiri rafiki yangu mwanasheria msomi Mheshimiwa Mtolea hakujielekeza vyema katika kifungu hicho. Kifungu hiki cha 57 kipo wazi kinasema, neno alilolisema yeye la shall katika kifungu hiki cha 57 neno hili linalenga kuweka sharti la lazima kwa bodi kuandaa ripoti ya uthamini kila baada ya miaka mitatu. (Makofi)

Kwa hiyo, ukisoma vizuri pale utaona imezungumzwa shall, lakini kwenye zile koma zile imekwenda kutoa jukumu kule mbele kwa hiyo, Mheshimiwa Mtolea ukikisoma vizuri bado hakijaharibu maana. Na uzuri katika Kifungu cha 57(2) imekwenda kueleza pia, kwamba, iwapo itatokea kwamba, kuna sababu za msingi za Bodi kutokuandaa ripoti ya Uthamini inaweza kuomba waiver kwa mujibu wa kifungu hicho kwa hiyo, nafikiri kabisa hapa Mheshimiwa Mwanasheria Msomi Mheshimiwa Mtolea hakujielekeza vyema katika kifungu hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimebakiza hoja moja ya mwisho, hoja hii imesemwa na Kambi Rasmi ya Upinzani na baadhi ya Wabunge kwamba, hawaoni tena umuhimu wa SSRA kwa sababu mifuko hii inakwenda kuunganishwa, itakuwa miwili, kutakuwa hakuna ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera yetu ya Hifadhi ya Jamii inajielekeza katika taa ya tatu ambazo naomba nizitaje kwa ufupi, taa ya kwanza inazungumzia kuhusu social assistance, taa ya pili inazungumzia kuhusu mandatory schemes na taa ya tatu inazungumzia kuhusu voluntary schemes. Sasa sisi kwa hoja inayosemwa hapa ni kwamba tayari tuna mifuko mwili SSRA anabaki kufanya kazi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niweke vyema kabisa hapa, hii mifuko miwili ambayo tunaizungumzia ipo kwenye taa ya pili ya mandatory scheme, lakini tunayo taa ya tatu ambayo ni ya voluntary scheme. Iko mifuko midogomidogo mingi sana, hauwezi leo kumuondoa SSRA ukaacha mifuko hii ikajiendesha yenyewe, hapo ndipo hasa umuhimu wa SSRA unaingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hivyo tu ukiacha mifuko hii miwili hapa kinachozungumzwa inazungumzwa Sera ya Hifadhi ya Jamii ambayo ndani yake pia inajumuisha mifuko mingine ikiwemo Mfuko wa CHF, ukiwemo Mfuko wa NHIF, ukiwepo Mfuko wa WCF. Hii yote pia inahitaji kuwa regulated kwa hiyo, hayo hasa ndio yanafanya na kuleta relevancy ya kwa nini SSRA iwepo. Lakini pia bado chombo hiki ni muhimu kuwepo katika kushughulikia malalmiko ya wanachama hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, hata uzoefu wa nchi za jirani Kenya wana mifuko mikubwa miwili, kama kazi ambayo tutakwenda kuifanya hapa, lakini Kenya wana kitu kinaitwa Retirement Benefit Authority ambayo kazi yake kubwa ni kama kazi inayofanywa na SSRA. Sasa kwa Kenya mifuko iko miwili, lakini Kenya wana voluntary schemes zaidi ya 10,000 ndio maana wenyewe wakaona umuhimu kwamba pamoja na mifuko hii mikubwa miwili, lakini bado mifuko hii midogo lazima iwe ina mtu wa kui-regulate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nichukue fursa hii tena kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao. Na kwa kweli, Muswada huu unakwenda kutibu matatizo mengi sana yaliyokuwa yanakabili wananchi wafanyakazi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi tu niseme naunga mkono hoja. Asante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii, kwanza kabisa napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyeniwezesha kusimama siku ya leo.

Mheshimiwa pia, nachukua fursa hii kipekee kabisa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa imani na heshima kubwa aliyonipa ya kuendelea kuhudumu katika eneo hili kama Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa miongozo yao ambayo imetusaidia sana katika utendaji kazi katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisingependa sana kurejea maneno ya Waheshimiwa Wabunge waliotangulia lakini niseme tu kwa kipekee kabisa tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa upendo wake, uvumilivu na namna ambavyo ametuongoza katika ofisi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kumshukuru kipekee sana Mama yangu mpendwa, Mheshimiwa Mama Jenista Mhagama pamoja na Dada yangu Mheshimiwa Angela Kairuki kwa namna ambavyo mmendelea kutulea katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kutupa ushauri lakini na upendo wenu wa dhati ambao umefanya kazi hii iwe nyepesi sana kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nichukue fursa hii kuwashukuru sana Makatibu Wakuu wote chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Watendani wote kwa ushirikiano mkubwa sana walionipatia lakini bila kumsahau Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu dada yangu Ikupa Stella Alex kwa namna tulivyoshirikiana kwa pamoja kutekeleza majukumu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nichukue fursa hii kukupongeza sana wewe mwenyewe kwa namna ambavyo umeleta mapinduzi makubwa ya kiteknolojia ndani ya Bunge letu. Hii ni kuonesha kwamba kuna uhusiano mkubwa sana kati ya maendeleo na teknolojia na watu wenye asili ya Mkoa wa Dodoma. Hongera sana kwa kazi kubwa ambayo umeifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, niwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa heshima kubwa waliyonipa. Niwaambie tu kwamba mwili wangu bado una nguvu na akili yangu ina nguvu ya kufanya kazi ikiwapendeza niko tayari kuendelea kuwatumikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, sasa naomba nijielekeze katika hoja za msingi ambazo zimewasilishwa. Hoja ya kwanza ilikuwa ni ushauri ambao ulitolewa kwa WCF (Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi), namna bora ya kuendelea kutoa elimu kwa waajiri ili waendelee kujiandikisha na kutimiza wajibu wao kisheria. Tumepokea ushauri huu na WCF wanaendelea kutoa elimu kwa waajiri, wafanyakazi na wadau wote kuhakikisha kwamba takwa hili la kisheria linafanyiwa kazi kwa sababu ni jambo ambalo linawasaidia sana wafanyakazi wanaopata madhara wakiwa kazini kupata fidia.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo lilizungumzwa ni Serikali kuendelea kuwapa mafunzo ya ujuzi waraibu wa madawa ya kulevya ambao wameachana na madawa ya kulevya na hivyo kukosa shughuli ya kufanya. Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Fungu 65 tumeendelea kutekeleza ushauri huu kwa kuwahusisha waraibu wa madawa ya kulevya katika shughuli mbalimbali za ukuzaji ujuzi. Hivi sasa tunavyozungumza katika Programu ya Kukuza Ujuzi ambayo inaendeshwa chini Fungu 65 - Ofisi ya Waziri Mkuu, tumewaingiza pia watu ambao walikuwa wanatumia madawa ya kulevya kama sehemu ya kuwajengea ujuzi na kuwafanya wapate shughuli ya kufanya na waache kuendelea kutumia madawa ya kulevya.

Mheshimiwa Spika, nchi nzima tuna takribani watu 5,875 ambao wameshaingia katika Program ya Kukuza Ujuzi katika eneo la ufundi stadi. Kati yao watu 1,020 ni waraibu wa madawa ya kulevya. Hii ni kuonyesha kwamba ni kwa namna gani kama Serikali tuliona kwamba lazima tuwashirikishe pia na wenyewe ili waweze kupata ujuzi.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ilizungumzwa ni kuhusiana na vikundi vya vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambapo ilitolewa rai na Waheshimiwa Wabunge kwamba idadi ya vijana kukusanyika kuunda kikundi ni kubwa sana na wakashauri pia twenda katika hatua hata ya kumfanya kijana mmoja aweze kukopeshwa. Kama Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana tuliliona hilo na kupitia Mwongozo wa mwaka 2013 ambao tumeufanyia marekebisho, hivi sasa tunakamilisha taratibu za kumfanya hata kama ni kijana mmoja ambaye anaweza kuleta tija na kuajiri vijana wengine pia anaweza kukopesheka pasipokuwa kwenye kikundi ili kuweza kuwasaidia vijana waweze kupata fursa hiyo ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ilijitokeza hoja ya kuboresha Programu ya Kukuza Ujuzi. Ofisi ya Waziri Mkuu inaendesha Programu ya Kukuza Ujuzi yenye lengo la kumjengea ujuzi kijana wa Kitanzania ili kupitia ujuzi huo aweze kujiajiri na kuajiri vijana wengine. Kazi hiyo tumeifanya mwaka huu lakini pia katika mwaka ujao wa fedha tutaifanya kazi hii kwa ukamilifu. Tutaendelea na Programu ya Kitalu Nyumba ambayo itafikia vijana wengi zaidi mikoa yote 14 ambayo imebaki katika awamu ya pili. Tutaendelea pia na Programu ya Kurasimisha Ujuzi kwa Vijana wenye ujuzi ambao hawajapitia mafunzo rasmi ya ufundi. Programu hii tunafanya na VETA na vijana wengi wamenufaika.

Mheshimiwa Spika, pia tunaendelea na Programu ya Mafunzo ya Vitendo Kazini (Internship) ambapo hivi sasa kwa kushirikiana na sekta binafsi tunawachukua vijana wahitimu wa vyuo vikuu tunawapeleka katika taasisi mbalimbali za kibiashara, iwe ni viwanda au makampuni wanakaa kwa miezi 6 - 12 wakipata uzoefu kwa fani waliyoisoma na baadaye wanapewa Hati ya Utambulisho kwa maana ya Certificate of Recognition. Ikitokea siku anakwenda kuomba kazi akiulizwa uzoefu basi anaweza akatoa ile Hati kuonyesha kwamba amewahi kufanya kazi kwa vitendo kwa muda wa miezi 6 - 12 ili tuwe tumeondoa changamoto hiyo ya uzoefu.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa katika eneo langu ilikuwa ni hoja ambayo ilisemwa na Waheshimiwa Wabunge ya ushiriki wa vijana katika kilimo. Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tunatekeleza mpango mkakati wa pamoja wa kuwahusisha vijana kwenye kilimo ambapo tunaanza na hatua ya kwanza ya kuwapa elimu na kuwaondolea fikra hasi kwamba kilimo ni shughuli ya mwisho ya kufanya mtu akikosa shughuli zote. Kwa hiyo, tumeanza na awamu hii ya kwanza ya kutoa elimu, tumezunguka karibuni kanda zote za nchi nzima kuwaelimisha vijana. Hatua ya pili tumeendelea kuwaweka vijana hawa katika makundi ilhali tukiendelea kusisitiza maelekezo ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyatoa ya kila mkoa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za kilimo na uzalishaji mali. Baada ya hapo hatua ya tatu ni kwenda kuwaunganisha na Benki ya Kilimo ili waweze kupata fursa ya mikopo na mitaji ili waendeshe shughuli hizo za kilimo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya, naunga mkono hoja nashukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyeniwezesha kusimama siku ya leo. La pili, nakishukuru sana Chama changu Cha Mapinduzi, chini ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniteua kupeperusha bendera ya CCM katika Jimbo la Dodoma Mjini na Wanadodoma wakaniamini na kunichagua tena. Jimbo hili watu wanakwenda msimu mmoja mmoja, mimi nimerudia namshukuru sana Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hotuba ya Rais, Mheshimiwa Magufuli ya mwaka 2015 na mwaka 2020, inakupa dira, inakupa dhamira na upendo mkubwa ambao Rais wetu anao katika kuipeleka Tanzania kwenye maendeleo. Ni dhahiri kabisa kupitia hotuba hizi, mtu yoyote anaweza akaona Tanzania ilipotoka na inapokwenda, tunakwenda pazuri sana, tumuunge mkono Rais wetu mpendwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza maeneo mawili ya kipaumbele ambayo Mheshimiwa Rais ameyagusia katika hotuba. La kwanza ni la uunganishaji wa Mifuko ya Uwezeshwaji Wananchi Kiuchumi. Hoja hii ni muhimu sana katika kuwasaidia wajasiriamali wa Tanzania kwa sababu Mifuko hii ilikuwa ni mingi, kila mmoja anatowa mikopo na ruzuku kwa wakati wake, lakini kwa kuunganishwa Mifuko hii maana yake ni kwamba itatoa wigo mkubwa zaidi kwa watu wengi kuweza kupata fursa ya mikopo hii. Imani yangu ni kwamba katika zile ajira milioni nane, ni rahisi sana kuzifikia kupitia katika Mifuko hii na naamini kabisa kwamba, Mifuko hii ikiunganishwa itasaidia pia katika mfumo wa ukopeshwaji, badala ya vikundi iende kwa mtu mmoja mmoja ili Watanzania wengi zaidi waweze kupata fursa hii ya mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nashauri Serikali kwamba Mifuko hii iende sambamba na program za kukuza ujuzi. Ofisi ya Waziri Mkuu wana programu nzuri sana ya kukuza ujuzi kwa vijana ambayo inaitwa RPL. RPL ni Recognition of Prior Learning, ni mfumo wa urasimishaji ujuzi kwa vijana wenye ujuzi ambao hawajapitia mfumo rasmi na mafunzo ya ufundi yaani wako vijana mtaani wanajua kuchonga vitanda, wanajua kuchomelea, hajawahi kusoma VETA, hajawahi kusoma Don Bosco, Serikali inachokifanya inakwenda kuwajengea uwezo na kuwapa uwezo na kuwapa vyeti vya kuwatambua. Programu hii iendelee na naamini itawagusa vijana wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashauri pamoja na kuunganisha hii Mifuko tusimamie pia ile program ya ODOP (One District One Product) itatusaidia sana kwenye kuimarisha na kukuza shughuli za vijana na akinamama na watu wenye ulemavu katika maeneo tofauti tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili na la mwisho, mimi ni Mbunge wa Dodoma Mjini na sisi tumepata heshima ya Dodoma kuwa Makao Makuu. Mwanzoni wakati wakati inasemwa watu walijua ni maneno ya utani, lakini Rais Magufuli amefanya kwa vitendo. Nachukua fursa hii pia kulishukuru sana Bunge letu kwa kutunga Sheria Maalum ya Dodoma Capital City Declaration Act ya mwaka 2018 ambayo haiwezi kubadilisha maamuzi ya Makao Makuu mpaka pale itakapoletwa tena Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia maendeleo makubwa ndani ya muda mfupi, Dodoma imechangamka, uchumi umeongezeka, maisha ya watu yamebadilika. Tunategemea mradi mkubwa wa uwanja mkubwa wa ndege wa Msalato, lakini barabara za mzunguko ambao zitaondoa msongamano katika Jiji la Dodoma. Hii ni kazi kubwa ambayo imefanywa na Rais Magufuli katika eneo la Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, mwaka 1989 ilitungwa sheria ya Dodoma Special Investment Area ambayo ilikuwa inatoa unafuu kwa wawekezaji wanaokuja kuwekeza Dodoma. Naomba sheria hii ipewe extension kwa sababu ime-expire mwaka 2019 ili kila mtu anayekuja kuwekeza Dodoma, apate unafuu na Dodoma iendelee kujengeka. Naamini kupitia sheria hii Dodoma itakua zaidi na zaidi na ile azma ya Mheshimiwa Rais kuwa Dodoma kuwa ni kati ya majiji bora Afrika itatimia kupitia sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya, naunga mkono hoja na nashukuru sana kwa nafasi, tuendelee kumsaidia Rais wetu. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa zawadi ya maisha ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye kupitia uongozi wake ametuachia mbegu ya ujasiri, mbegu ya kuipenda nchi yetu, mbegu ya uzalendo, mbegu ya kujiamini na mbegu ya kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika uongozi wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, nchi yetu imeshuhudia maendeleo makubwa na miradi mingi mikubwa ikitekelezwa ambayo tunaamini kabisa kwamba itakwenda kuleta tija kwa Mtanzania na kulifanya Taifa letu liendee kusonga mbele. Mheshimiwa Hayati Rais Dkt. Magufuli alifanya kazi yake kwa kumtanguliza Mungu na ametuachia hilo kama funzo sisi viongozi katika kazi zote ambazo tunazifanya, tumweke Mungu mbele ili tuweze kufikia malengo na mafanikio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamkumbuka sana Hayati Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika nchi yetu ya Tanzania na kwa sisi hapa Dodoma kama ambavyo ilikuwa ada ya Azimio la mwaka 1973 la Makao Makuu, Hayati Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alitekeleza kwa vitendo. Katika viongozi wote waliopita kila mmoja alifanya kwa sehemu yake, lakini tumeshuhudia chini ya uongozi wake, Makao Makuu ya Serikali yakiwa hapa Dodoma na Dodoma imebadilika hivi sasa, maendeleo yanakuja kwa kasi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashuhudia miundombinu mingi sana ikikamilika ndani ya Dodoma na kuifanya Dodoma kuendelea kuwa kati ya sehemu ambazo zinakua kwa kasi sana hapa nchini. Hii ni kazi kubwa na alama ambayo Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli ametuachia na tutaendelea kumkumbuka katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa kazi ambayo ameifanya katika nchi yetu ya Tanzania na hasa katika kuwaamini vijana, ametujengea heshima kubwa sana vijana wengi wa Kitanzania kuamini kwamba wana uwezo wa kufanya kazi na kazi ambayo inaweza kuonekana na watu ambayo inaweza kuonekana na watu kuithamini. Ni kiongozi ambaye aliamini katika vijana akawapa nafasi na kwa asilimia kubwa vijana hao wamelitendea vyema Taifa hili, hivyo tunamshukuru sana kwa heshima hiyo kubwa. (Makofi)

Mheshimwia Naibu Spika, pia kazi hii kubwa yote iliyofanywa na Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, tumempata mama yetu ambaye anakwenda kuiendeleza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye tunaamini kabisa atakwenda kuyasimamia yale ambayo Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli aliyaanzisha na kuyaendeleza kwa kasi kubwa zaidi. Imani yetu ni kwamba nchi yetu iko katika mikono salama. Wale wote waliokuwa wanadhani kwamba sasa mpira umerudi kwa goal keeper, hivi sasa kazi inaendelea pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kazi ambayo ameianza siku chache zilizopita, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan inaonyesha ni namna gani Tanzania ile ile ambayo kila mmoja alikuwa anaiota inaendelea. Nitoe rai kwa Watanzania nasi Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika kazi hii ngumu kabisa na tunaamini kabisa Mwenyezi Mungu atamsimamia ili tuipeleke Tanzania kule ambako kila mmoja anataka Tanzania yetu iende. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mmoja anaamini katika uadilifu na uchapaji kazi wa mama yetu Mheshimiwa Suluhu Hasssan. Ni Imani yetu kwamba nchi yetu ya Tanzania kupitia uongozi wake itaendelea kung’ara na basi yale yote ambayo yalifanywa akiwa na Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli, huu ndiyo mwendelezo wake mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, imani kubwa sana ambayo tunayo kwa akina mama naye akiwa Makamu wa Rais ambaye alipita kwenye kipindi kilichopita, tunaamini ataifanya kazi hii vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naunga mkono maazimio yote mawili. Ahsante sana.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia. Kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma aliyetuwezesha kufika siku ya leo na kuniruhusu mimi kusimama hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwama utekelezaji wa Mpango unahitaji fedha, na viko vyanzo vingi ambavyo vimeainishwa lakini moja kati ya chanzo ni mapato yetu ya ndani. Hivyo kwasababu dhima ya mpango inasema vyema kabisa, ni kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu. Kwa hiyo imani hapa ni kwamba fedha zikipatikana za kutosha za kutekeleza mpango huu tutakwenda kuifikia dhima hii. Nataka nichukue fursa hii kipekee kabisa kuuenzi mchango mzuri sana wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwenye suala zima la upatikanaji wa mapato ambayo naamini pia Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan pia atauendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika kuishauri Serikali kuongeza wigo wa kodi (tax base). Duniani kote hivi sasa nchi nyingi zinaelekea katika mfumo wa kodi ya huduma za kidigitali, wanaita DST ni Digital Service Tax. Kwa mujibu wa Jarida la Statista la mwaka 2019 hivi sasa duniani kuna watumiaji wa mitandao ya kijamii zaidi ya bilioni 3.6 ambao katika nchi zinazoendelea kule Ulaya wameanza na utaratibu huu, wameanza kuweka miundombinu ya kuwafanya walipe kodi na kodi hii imeanza kuchangia kwa kiasi kikubwa sana katika uchumi wa nchi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ninavyozungumza hivi sasa nchi ya Ufaransa wameshakamilisha taratibu zote na sheria ya kutoza 3% halikadhalika Hispania na yenyewe wanatoza 3% na Uingereza 2%, huu ni utaratibu ambapo kama nchi pia lazima tuangalie hili eneo halijaguswa kabisa. Kwa Afrika nchi ambayo imeanza kulifanyia kazi jambo hili ni nchi ya Afrika ya Kusini. Afrika ya Kusini wameunda mpaka Tume chini ya PBO (Parliamentary Budget Office) ya Bunge la Afrika ya Kusini ya kuhakikisha kwamba wanapitia na kuona namna ambavyo watawatoza kodi hasa hawa main players wa kwenye social networks. Hapa nazungumzia search engines kama Google, Amazon, Spotify, huku kuna hela nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kifungu cha 47 kimetoa ruhusa ya nchi yetu pia kutengeneza mifumo ya kukusanya kodi kupitia utaratibu huu. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Mwigulu Nchemba twendeni tukaliangalie eneo hili, lina hela nyingi sana, badala ya kuendelea kuhangaika na bodaboda na vyanzo vingine twendeni huku kuna hela nyingi ambayo imelala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni maeneo mawili; la kwanza, tutengeneze payment platform ambayo itaifanya TRA iweze kutoza kodi. Hivi sasa tukinunua vitu kupitia kadi yetu ya Visa, Mastercard au PayPal pale TRA wana uwezo wa ku-capture tax wakifanya integration. Kwa hiyo, mfumo huu uwekwe vizuri na naamini kabisa ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu una uwezo wa kulisimamia hili likaongeza wigo wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo nataka niwapongeze wameanza kulifanya, tukae na main players hawa Facebook, YouTube. Najua mmeanza na Facebook na Facebook kwa takwimu za mwezi Februari wana watumiaji zaidi ya bilioni 3.1 ulimwengu mzima na sisi Tanzania pia tukiwemo humo ndani. Mimi naamini kabisa hili liko ndani ya uwezo na tukilisimamia vizuri tutaongeza mapato kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye kilimo, bado naendelea kuamini kwamba sekta hii ina mchango mkubwa sana kwenye uchumi wetu hasa katika kilimo cha umwagiliaji. Hivi kwa nini tusiwe tuna miradi ya mkakati kwenye kilimo pia kama ilivyo katika maeneo ya miundombinu na uchukuzi, twendeni tukafanye haya kwa sababu naamini kabisa kilimo kina uwezo wa kutupeleka mbele zaidi kama sekta kiongozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ameyavalia njuga sana yale mazao ya kimkakati lakini tumuongezee nguvu pia katika eneo hili. Rai yangu ni kumuomba kaka yangu Mheshimiwa Prof. Kitila na rafiki yangu Mheshimiwa Mwambe mkae pamoja na sekta binafsi ili tutengeneze soko la uhakika la wakulima wetu, kuwepo na backward and forward linkage, mkulima anayelima nyanya aunganishwe na kiwanda moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Hussein Bashe amewahi kufanya kikao na Bakhresa nafahamu lakini tulikaa naye pamoja pia kwenye suala la ukwaju tu kwa sababu Bakhresa hivi sasa anaingiza mtambo wa kiasi cha shilingi bilioni 20 kwa ajili ya ukwaju tu lakini ukwaju huu ni wa kuutafuta. Sasa Serikali ndiyo sehemu ya ku-take advantage hapa kwa wakulima wetu, twendeni tukaweke mkazo hapo kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze kuhusu zabibu, zabibu ndiyo dhahabu yetu Dodoma. Zabibu ya Dodoma nitaomba Wizara ya Kilimo itusaidie kufanya utafiti lakini inasemekana hakuna nchi yoyote duniani yenye uwezo wa kuvuna zabibu mara mbili isipokuwa Tanzania na yenyewe ni Dodoma tu. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo iweke mpango mkakati madhubuti kulisaidia zao hili la zabibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatamani kuwatua akina mama wa Dodoma mabeseni yao ya zabibu ambayo wanauzia stendi wakatengeneze mchuzi wa zabibu badala ya kuhangaika kukaa kwenye jua Serikali ikawasaidia wakatengeneze mchuzi wa zabibu. Tunaishukuru sana Serikali imeshusha tozo ya mchuzi wa zabibu kutoka Sh.3,655 kwa lita mpaka Sh.450 hali ambayo imechochea sana ulimaji wa zao la zabibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikuombe Mheshimiwa Bashe, najua unafanya kazi nzuri sana, umeshaunda Kamati ya watu 12 kuhusiana na zao hili la zabibu twendeni mbele Zaidi. Natamani kuiona Tanzania inasifika kwa zabibu maana ndiyo zao pekee linavunwa mara mbili duniani unalikuta Dodoma. Nikuombe Mheshimiwa Naibu Waziri kazi ambayo umeianza naomba tuimalizie tuwatue mzigo wakulima wa Dodoma tupate soko la uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa najua tayari wanaendelea na masuala ya tafiti na mnakuja na mbegu mpya, mbegu ya Beauty, Georgina na Alphonse Lavalleé ambazo naamini kabisa zitaongeza tija. Nikuombe sana ndugu yangu na kaka yangu Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Waziri katika eneo hili tuwasaidie wakulima wa zabibu wa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu sisi tunataka tuanze sasa kuifanya Afrika Mashariki na Kati hasa Watanzania hapa tuache kuagiza St. Anne na wine zingine kutoka nje ya nchi, zabibu yetu ya Dodoma ndiyo zabibu nzuri na tamu kuliko zote pia ukiacha Italia. Hivyo niwaombe sana Wizara katika eneo hili twendeni tukawasaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini twende mbele Zaidi, Afrika Kusini hivi sasa kupitia zabibu inafanya utalii na imetengeneza ajira zaidi ya 450,000 kupitia mashamba ya zabibu. Mashamba ya zabibu hivi sasa ni utalii na uzuri katika Jiji la Dodoma kwenye masterplan yetu tumetenga maeneo ya kilimo cha mijini (urban farming), tunaomba msukumo wa Serikali. Tunataka tuifanye zabibu iwe sehemu ya kivutio cha utalii, watu waje washangae mashamba ya zabibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu akija Dodoma hapa akutane na kaulimbiu ile ya maneno makubwa kabisa ya Kilatini wanasema: “In vino veritas”, kwamba kwenye wine/mvinyo kuna ukweli, waje waukutie ukweli huo Dodoma. Naamini kabisa ndugu yangu Mheshimiwa Hussein Bashe na Prof. Mkenda mna uwezo wa kulisukuma hili. Tukifanya hili tutakuwa tumewasaidia sana wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, Mheshimiwa Waziri Mkuu alizungumza kuhusu mamlaka ya kilimo bustani (horticulture), alitoa maelekezo hayo. Wizara ya Kilimo anzisheni mamlaka hii, horticulture inakuwa kwa kasi sana hivi sasa, mamlaka ikiwepo itatusaidia sana. Wakulima wa kilimo cha bustani amebaki mtu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nami nianze kwanza kuwapongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Manaibu Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya na ninaamini wataendelea kuifanya katika kuimarisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika kuishauri Serikali katika namna bora ya kuendelea kutafuta fedha ya kuifanya TARURA iweze kufanya kazi vizuri. Nakubaliana na michango iliyotolewa na Mheshimiwa Mussa Zungu na Mheshimiwa Moshi Kakoso ya namna bora ya kuweza kupata fedha za kuifanya TARURA ifanye kazi. Kifungu cha 8(1) cha Government Notice No. 211 ya mwaka 2017 ilitengeneza utaratibu wa namna ambavyo TARURA watapata fedha (source of funds).

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika jambo ambalo halijasemwa humu lakini naamini linaweza litakaleta tija. Kabla ya TARURA, Halmashauri za Miji, Manispaa na Wilaya zilikuwa zikitenga bajeti ya barabara kupitia Idara ya Ujenzi. Sioni ni kwa nini zisiendelea kufanya hivyo kwa sababu tunamhudumia Mtanzania mmoja. Kama waliweza kuzitenga hapo awali, kwa nini wasiendelee tena kutenga? Ndiyo maana namwomba Mheshimiwa Waziri waende kulisimamia jambo hili na inawezekana kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wakati anawaapisha Mawaziri, alisema hili pia. Waende wakafanye coordination nzuri ndani, Halmashauri zitenge fedha, vilevile na fedha ya TARURA itaendelea kutumika. Lengo hapa ni kuhakikisha mfuko huu unaendelea kuwa na fedha za kutosha. Naamini Mheshimiwa Waziri atakuwa ameshakutana na hii nyaraka, ukienda ofisini, uko waraka ambao aliutoa aliyekuwa Katibu Mkuu, Iyombe ya kuzitaka Halmashauri za Majiji, Manispaa na Wilaya kutenga hizi fedha. Mheshimiwa Waziri naomba isiwe hiyari, iwe lazima fedha hizi zikatengwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nataka niishauri Serikali ni katika eneo la mapato ya malipo ya mbele kwenye ardhi (premium). Katika miji yetu yote zoezi la upimaji wa viwanja na urasmishaji linaendelea, lakini ndani ya zoezi hilo wananchi huwa wanalipa fedha ya premium ambayo imeelekezwa katika kuboresha huduma za kijamii na hasa miundombinu. Kwa nini fedha hii isitengewe utaratibu mzuri ikaingia TARURA kwa ajili ya kuweza kusaidia kwenye majukumu ya TARURA? Kwa sababu hivi sasa inabaki katika Halmashauri na kupangiwa matumizi mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa, kwa sababu katika upimaji wa viwanja vipya inatozwa asilimia 2.5 malipo ya premium na katika urasmishaji ni 1%, hizi ni fedha nyingi sana. Tuna uwezo pia wa kutumia chanzo hiki kwa ajili ya kuifanya TARURA iwe na mfuko ambao utafanya kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri una uwezo wa kukaa na Waziri wa Ardhi mkakubaliana tu, vizuri kabisa namna ya utaratibu huu kwa sababu mwenye mamlaka kwa mujibu wa Kifungu cha 31(1) cha Sheria ya Ardhi ni Waziri wa Ardhi. Mkukubaliane kwa pamoja ukawekwa utaratibu mzuri ili fedha hizi ziingie katika TARURA na wafanye kazi ya kutuhudumia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka nilichangie hapa, Dodoma hivi sasa ni kati ya majiji ambayo yanakuwa kwa kasi sana. Kwa mtandao wa barabara za lami, Dodoma ndiyo inaongoza kuliko jiji lolote Tanzania nzima kwa kuwa na mtandao mrefu wa barabara za lami. Huu tuliupata kupitia mradi wa TSCP.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi mwingine ambao unakuja, baada ya kuona mafanikio ya TSCP kuna mradi wa TACTIC hatujui umekwamia wapi? Tunaiomba Serikali, wakati Mheshimiwa Waziri anakuja kujibu hoja, atueleza jambo hili kwa sababu lina manufaa makubwa sana. Miradi hii ikitekelezeka, inaboresha miundombinu, inachochea uchumi katika eneo husika, inakuza na ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiliona leo soko la Ndugai, ukiona stendi ya ma-bus pale ni mradi wa TSCP, una mchango mkubwa sana. Kwa hiyo, nitaomba Mheshimiwa Waziri akija atuambie umefikia hatua gani kwa sababu tumesubiri muda mrefu katika jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mradi ukikamilika, unakugusa wewe pale kwenye Jiji la Mbeya, unamgusa Naibu Waziri Tanga, unanigusa mimi hapa Jiji la Dodoma, unakwenda Arusha, Mwanza na matokeo yake ni makubwa sana. Pia tuna jambo ambalo linaendelea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naanza kwa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri na kubwa ambayo wanaifanya. Lakini pia nampongeza sana Katibu Mkuu, Engineer Anthony Sanga, pamoja na Naibu Katibu Mkuu, mama Nadhifa Sadiki Kemikimba ambao kwa pamoja wanafanya kazi hii vizuri sana ndani ya Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jiji la Dodoma ni kati ya majiji ambayo yanaongoza kwa ukuaji wa kasi sana hivi sasa. Hali ambayo inasababisha kuwaleta watu wengi sana Dodoma wakiwemo wawekezaji wakubwa. Kwa hivi sasa lita za ujazo wa maji ambazo zinahitajika kwa Jiji la Dodoma kwa siku ni lita milioni 103, lakini uwezo uliopo hivi sasa ni lita milioni 66 kwa siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na mikakati ya Serikali kwenye kutatua changamoto hii. Mikakati hii miwili, wa muda mfupi na muda mrefu, nakubaliana nayo. Isipokuwa, naiomba Serikali katika mkakati huu wa muda mfupi, tuendelee kuongeza nguvu zaidi ili wananchi wengi wapate maji mengi na kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tunayo changamoto hapa ambapo maeneo mengi yanapata maji kwa mgao, na hivyo kuwasababisha wananchi wengi kupata adha. Niwaombe Wizara kuongeza kasi. Najua mmetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.4 cha kuyatoa maji kutoka pale Ihumwa mpaka Njedengwa ambayo itawagusa wananchi wa Kisasa, Nzuguni na maeneo mengine. Lakini vilevile ninafahamu pia kwamba kupitia mtandao huohuo tutagusa maeneo mengi ya katikati ya Jiji la Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Waziri, na bahati nzuri umetoa ushirikiano mkubwa sana, tumetembea mimi na wewe kwa pamoja tumeangalia maeneo yote hayo. Niombe tuongeze kasi ya uchimbaji wa visima vya pembeni ili maji mengi zaidi yaongezeke. Najua kule Mzakwe mnafanya, lakini tuongeze kasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumshukuru sana Waziri, ameniletea mtaalam pale DUWASA, Eng. Aaron; umeniletea mtu sahihi sana, anajitahidi sana, anafanya kazi nzuri sana. Ni mtu ambaye hakai ofisini, ukimwambia tatizo anakwenda site moja kwa moja. Mheshimiwa Waziri nikuombe katika hili utusaidie kutatua changamoto hii ya maji katika Jiji la Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mkakati wa muda mrefu umezungumza kuhusu Ziwa Victoria, nakubaliana nayo, lakini mmetenga kiasi cha fedha cha takribani shilingi bilioni moja. Lakini Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 19 wa hotuba yako umezungumza Farkwa kwa udogo sana, tunaomba ukija ku-wind up hapo utuambie mradi wa Farkwa inakuaje kwasababu sisi tunaamini mradi wa Farkwa na wenyewe utasaidia sana kuongeza vyanzo vya maji na kuondoa changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nikushukuru sana kwenye bajeti hii mmetutengea fedha za kutosha za miradi mikubwa ya maji ambayo pia itagusa maeneo mengi ya pembezoni kuazia Mzakwe yenyewe, Mbalawala, Veyula, Mpunguzi mnagusa mpaka Chololo, maeneo ya Kikombo yote mmeyagusa, tunashukuru sana kwa kuliona hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niishukuru Serikali kwa mkopo huu wa euro milioni 71 kutoka Korea kwa ajili ya mfumo wa maji taka kwenye Jiji la Dodoma. Hii ni changamoto kubwa hivi sasa lakini naamini kwa fedha hizi za mkopo kutoka Korea, maana yake tuta-address changamoto ya maji taka katika maeneo ya Swawa, Chamwino, Area C na Ipagala ambayo hivi sasa yana changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naiomba Wizara iangalie upya matumizi ya force account. Iko miradi mingi ambayo hivi sasa imekwama kwasababu Wizara inaitegemea DDCA. Mheshimiwa Waziri, ni ukweli ulio wazi kwamba DDCA haina capacity ya kuweza kuisimamia hii miradi yote kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, naomba ukija ku-wind up hapa utuambie kwa nini Serikali sasa msione haja ya kuruhusu contractors wengine wafanye kazi hizi za maji. Kwasababu DDCA tunamsubiri sana. Wananchi wanasubiri maji kwa muda mrefu lakini DDCA capacity yake ni ndogo, tunawakwamisha Watanzania kwasababu ya force account. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kuna miradi takribani 2,610 katika bajeti iliyopita ambayo ilipaswa kutekelezwa lakini capacity ya DDCA ni ndogo, mashine zake ni outdated, chache, ukimpa leo kisima kimoja hapo Ihumwa anakaa miezi miwili; hii miradi 2,000 anaifikia lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, naomba ukija ku-wind up utuambie namna ambavyo Serikali imejipanga kwenye hili la force account kwasababu wananchi wetu wanapata taabu kusubiri DDCA, na DDCA capacity yake ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naelewa sana dhana ya force account, lakini kwa miradi ya maji tuiangalie katika jicho tufauti Mheshimiwa Waziri. Kwenye miradi ya maji tuiangalie kwa jicho tofauti kwa sababu wananchi wengi wanakwama. Fedha zipo, tuna miradi ya PbR, tuna P4R; yote imekwama kwasababu ya utekelezaji mdogo wa DDCA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, nikuombe sana ili tuwakwamue wananchi wetu wa Tanzania kwa adha hii ya maji. Na hizi fedha za hii miradi ambayo iko chini ya DFDA na World Bank zipo. Nikuombe utoe tamko hap oleo kuziruhusu sasa hizi mamlaka ambazo zina miradi hii waweze kutoka nje ya mipaka ya force account kwa sababu DDCA wanatuchelewesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maneno ambayo nimeyasema hapa nakuamini sana Mheshimiwa Aweso kwa kasi uliyonayo, Waziri kijana, una uwezo wa kuyasimamia haya. Na sisi tunakuombea heri kwa sababu tunajua una nia njema; endelea kuwazingua sana ili maji yatoke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Awali ya yote, napenda niishukuru sana Serikali kwa namna ambavyo imetekeleza miradi mingi na mikubwa kwenye Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru sana Wizara kwa ulipaji wa fidia wa kupisha Uwanja wa Ndege wa Msalato, ambapo wananchi wameanza kulipwa fidia zao. Vilevile, naishukuru sana Serikali kwa sababu wameanza maandalizi ya malipo ya fidia kwa wananchi ambao wanapisha Outer Ring Road. Nashukuru sana kwa hatua hiyo. Pia naishukuru sana Serikali kwa kuwa hivi sasa ile barabara korofi ya kuanzia Ntyuka - Mvumi kuzunguka Kikombo ya kilometa 76 muda wowote zabuni itatangazwa ianze kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukrani hizi, hapa Dodoma panajengwa barabara ambayo ni Outer Ring Road, Middle Ring Road na Inner Ring Road. Kwenye Inner Ring Road, wananchi wangu wamesimamishwa kuendeleza maeneo yao kwa muda wa takribani miaka miwili hivi sasa; wananchi wa maeneo ya Nzuguni, Mbuyuni, Chidachi na Nkonze. Wananchi hawa wote wanashindwa kuyaendeleza maeneo yao kwa sababu wanaambiwa kuna mradi unakuja wa Inner Ring Road.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, kama mradi huu haupo tayari au hautekelezwi tunaomba wananchi wale wapewe taarifa kwa sababu ni muda mrefu umepita. Katika baadhi ya maeneo zoezi la urasimishaji makazi limeanza lakini wananchi hawa wanashindwa kurasimishiwa kwa sababu ya mradi huu ambao tunautengemea na bado haujafika. Hivyo, namuomba Mheshimiwa Waziri kwenye hii Inner Ring Road atuambie kama barabara hizi zipo au hazipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati anaweka jiwe la msingi pale SGR Ihumwa aliahidi zile kilomita kadhaa kutoka barabarani pale Ihumwa kwenda mpaka kwenye stesheni kule. Namwomba Mheshimiwa Waziri pia aliangalie hili kwa sababu ni sehemu ya ahadi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikumbushie barabara ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri alinijibu juzi ya Ihumwa - Hombolo - Mayamaya zaidi ya kilomita 57 ambayo na yenyewe pia ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi. Naomba Serikali iangalie kwa sababu mnaweza mkashughulikia hizi Outer Ring Road na mkahisi kwamba Dodoma ina barabara nyingi sana. Outer Ring Road lengo lake kubwa ni kupunguza msongamano wa magari makubwa hapa jijini lakini siyo barabara ambayo inakwenda kuwagusa wananchi moja kwa moja. Kwa hiyo, ziko barabara ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja ikiwemo hii ya Hombolo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri katika mipango ya Serikali muiangalie barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu wananchi wanapata shida kubwa sana na gharama za usafiri zimekuwa kubwa sana kutoka Hombolo kuja hapa mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia iko barabara ambayo wenzangu Mheshimiwa Dkt. Chaya na Mheshimiwa Nollo wameizungumzia; barabara ya kutoka Manyoni - Bahi inatokea Mbabala na kuikuta Outer Ring Road. Barabara hii ina mchango mkubwa sana kwa wananchi wetu wanaotokea pembezoni, ikijengwa kwa kiwango cha lami itakuwa imesaidia sana kwa sababu inakuja pia kuungana na barabara ya Outer Ring Road ili tuweze kuwarahisishia wananchi wetu usafiri na hasa kwa kuwa inagusa takribani majimbo zaidi ya mawili kwa maana ya Jimbo la Manyoni lakini vilevile Jimbo la Bahi na Jimbo la Dodoma Mjini. Ni barabara muhimu sana tunaomba Serikali iweze kuiangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa kuna changamoto wananchi wengi wakikutwa kwenye barabara ambao wanapaswa kusubiri utekelezaji wa miradi ya barabara, wenyewe wanapaswa wasubiri mpaka Serikali ikiwa tayari kujenga barabara lakini tunawatesa sana wananchi kama hawa ambao nimewasema wameacha kuendeleza maeneo yao wanasubiri mpaka Serikali ikiwa tayari kutekeleza miradi hii. Hii siyo Dodoma tu ni nchi nzima, naomba Serikali iweke utaratibu ambao hautamuumiza mwananchi wa kawaida, kama bado hatuko tayari tusiwasimamishie wananchi hawa uendelezaji wa maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Ili kukiboresha kilimo cha zao la zabibu hapa Dodoma ni lazima Wizara sasa iweke nguvu kwenye kituo cha utafiti cha TARI Makutupora ili kuboresha huduma za ugani na kuwafanya wakulima waweze kuzalisha kwa tija.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa kwa Dodoma wakulima wetu wanatumia gharama kubwa kulima kwenye shamba la hekari moja lakini wanachokipata ni tofauti na gharama waliyoitumia na hivyo kusababisha gharama kuwa kubwa sana. Ekari moja ya mkulima aliyelima vizuri zabibu Dodoma inaweza ikmapa mpaka tani tatu. Huyu ndiye aliyelima vizuri. Lakini ukienda Afrika Kusini, Western Cape mkulima anapata tani 12 kwa ekari moja.

Mheshimiwa Spika, niiombe Wizara, pamoja na kwamba tuna kituo pale cha Makutupora, tunaomba mafunzo yaendelee na ikiwezekana maafisa ugani hawa muwapeleke wakajifunze Afrika ya Kusini. Mheshimiwa Waziri, wasindikaji wa zabibu wa Dodoma walikuwa wako tayari kuwalipia maafisa ugani kwenda Afrika Kusini kujifunza. Itakuwa ni jambo la ajabu sana kama private sector wenyewe wakiwalipia maafisa ugani wa Serikali na Serikali ipo. Mheshimiwa waziri, nikuombe waende wakajifunze Afrika ya Kusini ili tuongeze tija ya mkulima wa zabibu wa hapa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hii ndiyo inasababisha St. Anna ya Afrika Kusini inauzwa shilingi 8,000 hapa Dodoma na Dompo ya Dodoma inauzwa shilingi 12,000 kwa sababu ya gharama za uzalishaji ni kubwa sana niiombe Serikali katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Hivi sasa Rwanda wame-take advantage, hivi sasa wanawakaribisha Wajerumani, muda sio mrefu wataanza kuwa wazalishaji wa bulk wine wakubwa hapa East and Central Africa. Wanyarwanda walikuwa wanakuja Mpunguzi, Mvumi na Chamwino kununua zabibu sasa hivi hawaji. Wameanza kulima wenyewe. Wakenya walikuwa wanakuja, sasa hivi hawaji, wanalima Mount Meru kule.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa Afrika, ukiondoa Afrika Kusini nchi nyingine hapa ya Kiafrika kama sisi kwetu hapa ni Tanzania peke yake ndiyo tunazalisha wine kwa kiwango kikubwa sana. Afrika ya Kusini wanazalisha tani lita bilioni 1 za wine kwa maana. Dodoma kwa maana ya Tanzania hatujawahi kuzidi lita milioni 15. Kuna kazi ya kufanywa hapa na niombe Serikali itusaidie katika hili. Wawapeleke wataalam wakajifunze, vinginevyo zabibu yetu itaendelea kulala na itaoza mashambani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo nataka nilichangie; Ilani yetu ya Uchaguzi inasema kuhusu ajira na naona ajira nyingi zinatengenezwa kwenye Sekta ya Kilimo. Nimesoma jarida the global employment trend, inasema sekta mbili zitachangia sana kwenye kutatua changamoto ya ukosefu wa waajira hasa kwa vijana, viwanda na kilimo. Hapa kuna mpango mkakati wa Wizara wa kuwahusisha vijana kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, iko fursa kubwa sana ambayo hatuitumii vizuri. Katika viwanda vya usindikaji wa matunda hivi sasa, hasa kutumia Mzee Bakhresa kwa viwanda vyake. Wana mahitaji ya tani za matunda 120,000 za maembe kusindika lakini capacity iliyoko hivi sasa ni takriban tani 25,000 kwa hiyo iliyobaki yote wana-import pulp kutoka nchi za nje.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Bashe unafahamu mzee Bakhresa alikuwa tayari kuisaidia Serikali kwenye kuandaa mashamba na kuweka miundombinu ya umwagiliaji ili vijana wengi zaidi wapewe mashamba ya kutosha tuanze kuuza matunda hayo kwenye viwanda vya Bakhresa na Sayona ambapo mahitaji yao ni tani 120,000 lakini hivi sasa wanapata tani 25,000 tu. Serikali ione jitihada sasa, ione ulazima wa kutayarisha mashamba makubwa soko la uhakika lipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye ukwaju Bakhresa anahitaji tani 15,000 za ukwaju kwa mwaka. Sisi tuna uwezo wa tani 4,000, anaingiza pulp kutoka nje ya nchi. Hili ni eneo ambalo pia tunaweza tukalifanyia kazi vizuri. Mananasi yetu, mengi yaliyoko hayafai kutengeneza juisi na mananasi pekee ambayo yanafaa kwa Afrika ni MD2 ambayo yaliingizwa miaka 42 iliyopita nchini Ghana kutokea Costa Rica ambayo ndiyo hata akina Bakhresa na Sayona wanayahitaji. Sasa tuna vijana hapa ambao wengi wangeweza kufanya kazi ya kilimo. Serikali, nawaomba kazi yenu nendeni mkatayarishe mashamba ya kutosha, wekeni miundombinu, soko lipo. Tukifanya hivyo tutakuwa tumewasaidia vijana wa Tanzania. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kipekee kabisa nichukue fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye sekta hii ya maji, ambao unakwenda kuleta mapinduzi makubwa.

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote katika Wizara ya Maji kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika kuhakikisha kwamba wanatatua changamoto za maji kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Juma Aweso ni kijana ambaye pia anatoa somo kwa vijana wengine wanaopewa dhamana namna ya kutekeleza majukumu yao. Anajitahidi sana kufanya kazi vizuri na tunamwombea kila la kheri kwa Mwenyezi Mungu akamilishe kazi hii kubwa ambayo anaendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Wizara ya Kilimo tunafanya kazi kwa ukaribu sana na Wizara ya Maji. Tumeshuhudia hivi karibuni mapinduzi makubwa kabisa kwenye sekta hii ya maji juu ya uingizaji wa mitambo zaidi ya 25 ambayo itasaidia katika uchimbaji wa visima na mabwawa. Mabwawa haya yatakwenda kuongeza vyanzo vya maji ambayo yatatumika pia kwa ajili ya matumizi ya binadamu, na katika maeneo mengine pia wanufaika watakuwa wakulima wadogo wadogo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kazi inayofanywa na Wizara ya Maji inakwenda sambamba na ile inayofanywa na Wizara ya Kilimo ya uchimbaji wa mabwawa 100 katika bajeti kama tulivyoyasema ambayo yatagusa maeneo mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania. Hii inatupa uhakika katika ku-address changamoto za mabadiliko ya tabianchi ambapo moja kati ya jambo kubwa ambalo limekuwa na athari kubwa ni la ukame. Sasa tutapata nafasi ya kuweza kuyavuna maji na pia kuyatumia kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, tunaingia katika historia katika kipindi hiki cha bajeti hizi mbili; ya kilimo na ya maji, zikitekelezwa ipasavyo, maana yake tutakuwa na uhakika wa vyanzo vingi sana vya maji kupitia mabwawa haya na visima ambavyo vitachimbwa.

Mheshimiwa Spika, sisi Wizara ya Kilimo pamoja na TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Wizara ya Mifugo, mbele ya Mheshimiwa Makamu wa Rais tuliweka makubaliano ya kuhakikisha kwamba tunatunza vyanzo vya maji ili tuwe tuna uhakika wa vyanzo vyetu vya maji na kuhifadhi mazingira katika vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, katika miradi ambayo tutaitekeleza katika Wizara ya Kilimo hivi sasa, tutahakikisha mifereji tutakayoijenga katika miradi yote ya umwagiliaji, ambayo itakuwa inatumia vyanzo vya maji ya mito na maziwa, tutahakikisha kwamba, maji yale yakishatumika kwenye kilimo yawe na uwezo wa kurudi katika mito na yatumike katika shughuli nyingine. Hivyo, sisi pamoja na wenzetu wa Wizara ya Maji katika eneo hilo, tutahakikisha kwamba mifereji ambayo tutaijenga safari hii kwenye miradi mikubwa hii ambayo inaendelea, itakuwa ni ile ambayo haitakuwa na upotevu mkubwa wa maji tofauti na ilivyo hivi sasa.

Mheshimiwa Spika, mifereji mingi ya hivi sasa inapoteza maji zaidi ya asilimia 40 kwa sababu ya kukosa ile miundombinu rafiki ya kuweza kurudisha maji katika chanzo chake cha awali. Kwa hiyo, sisi kwa pamoja tutaifanya kazi hiyo. Sambamba na hilo, tutahakikisha tunatumia mabomba katika baadhi ya maeneo ili maji yatumike katika ufasaha wake mzuri pasipo kuleta changamoto yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja kubwa hapa ni kuzuia upotevu mkubwa wa maji, na bahati nzuri sana tunao wakulima wetu ambao wanafanya kilimo pembezoni mwa vyanzo vya maji, tumeshakaa pamoja na Wizara kwa ajili ya kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya maji lakini na kilimo cha kisasa ambacho hakitaharibu mazingira. Hiyo ndiyo kazi kubwa ambayo tutaifanya kwa pamoja na wenzetu wa Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, katika mikakati ambayo ukiiangalia katika Wizara ya Maji wamezungumza jambo zuri sana la namna pia ya kuondoa changamoto kubwa ya huduma ya usafi wa mazingira katika maeneo mengi. Kwa sababu mimi pia nipo katika eneo hili, nataka nitoe ushuhuda wa kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Maji katika eneo letu la hapa hapa Dodoma ambapo tumeshuhudia juzi tu Mheshimiwa Waziri Aweso amesimamia uingiaji wa mikataba mkubwa kabisa wa zaidi ya Shilingi bilioni 164 ambayo inakwenda kutatua changamoto kubwa ya usafi wa mazingira katika jiji la Dodoma na hasa katika kuhakikisha kwamba sehemu zenye changamoto ya huduma ya majitaka, hivi sasa zinakwenda kuwekewa mfumo mzuri ili kutatua changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili, umefanya katika maeneo mengi nchi nzima, lakini nataka nitoe ushuhuda kwamba, katika eneo hili la Dodoma, ambapo pia Wabunge wengi sana mnaishi na mmesema katika sehemu ya hoja zenu, kwamba Serikali inakwenda kuweka mradi mkubwa ambao utagusa kata 14 na bomba refu la kilometa 117 kwa ajili ya kuondoa majitaka katika maeneo mbalimbali ambayo imekuwa ni changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hoja ambazo zimesemwa hapa ambazo nataka nizitolee ushuhuda kuonesha kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima ni suala la maji katika eneo letu la hapa Dodoma Jiji, na nikiwa kama sehemu ya Serikali na vile vile kama kiongozi katika eneo hili, nataka nipongeze kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Waziri ameifanya, juu ya changamoto mbalimbali ya maji kwa kutumia mfumo wa uchimbaji wa visima. Tumeona katika maeneo mengi hivi sasa huduma ya maji imeanza kupatikana hasa baada ya Mheshimiwa Waziri kuweka nguvu kubwa ya uchimbaji wa visima vya pembezoni. Tumeshuhudia mradi mkubwa wa Nzuguni ambao unakwenda kutatua changamoto kubwa katika maeneo ya Ilazo, Swaswa, Mlimwa C, pamoja na Kisasa. Vile vile na uchimbaji wa visima vingine virefu katika maeneo ya Makulu, Nala, Zuzu, Iyumbu na Chang’ombe. Haya maeneo yote yanakwenda kutatua changamoto kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ilikuwa ni kutoa tu ushuhuda wa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya Mheshimiwa Waziri katika eneo letu la hapa Dodoma, lakini kikubwa na katika kumalizia hoja yangu, nataka tu nimhakikishie kwamba sisi Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Kilimo tutafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha tunatatua changamoto za msingi na hasa katika kilimo ambacho hakitaharibu mazingira ili kwa pamoja basi, wakulima wanufaike na vyanzo vya maji, lakini na vile vile tuweze kuyatunza maji kwa ajili ya mazingira.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza ni shukurani kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma aliyetuwezesha kufika siku ya leo. Pili ni kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyonipa ya kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara hii ya Kilimo; na pia kuwashukuru wananchi wangu wa Dodoma Mjini kwa heshima kubwa waliyonipa kuwa Mbunge wao; na la tatu, ni kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Hussein Mohamed Bashe ambaye amekuwa kaka, rafiki, mwalimu, Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana. Pia nichukue fursa hii kuwashukuru sana watendaji wote wa Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu Andrew Masawe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ambalo nilikuwa nataka nizungumzie ni suala la program ya vijana kushiriki kwenye kilimo. Tunatambua kwamba vijana wetu wa nchini Tanzania si kwamba hawapendi kilimo lakini mazingira ya kuwafanya wafanye kilimo hayakuwa rafiki sana. Walikuwa na changamoto ya maeneo, mbiundombinu, pembejeo, masoko na mitaji. Tumekuja na program maalum ambayo inaitwa, jenga kesho bora ya vijana, ambayo lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba tunawapatia vijana maeneo, ambayo tutapima afya ya udongo. Pia tutawapatia pembejeo, tutawatafutia masoko na hatimaye lengo letu ni kuwa na kitu kinaitwa Kijiji cha Vijana cha Kilimo. Tunaamini kabisa hii itakuwa sehemu nzuri ya kuweza kuwavutia vijana wengi kufanya kilimo. Kwa kuanzia tutaanzia hapa Dodoma ndiyo itakuwa sehemu ya pilot zaidi ya ekari 20,000 zitatengwa kwa ajili ya block farms ambazo vijana wengi watahusishwa kushiriki katika kilimo hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni la zabibu. Tumejipanga kuendelea kuhamasisha wakulima wa zabibu kulima kwa tija ili hatimaye zao hili liwaletee mafanikio. Mwezi ujao tutakamilisha uanzishwaji wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Zabibu ili wawe na sauti moja. Lakini vilevile tumekwenda mbali zaidi, tunakwenda kuanzisha viwanda vitatu vikubwa vya uchakataji na uhifadhi wa mchuzi wa zabibu ili wakulima wetu waache kuuza zabibu wauze mchuzi wa zabibu na uwaletee tija kwenye kilimo chao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeongeza utafiti kwenye eneo hilo la zabibu na hivi sana ndugu zetu wa pale TARI Makutupora wametuongezea mbegu zingine. Tunataka wakulima wetu pia waanze kuuza zabibu za mezani; na hivi sasa tumeshagundua mbegu ya ruby seedless ambayo itakuwa ni zabibu za mezani. Lakini vile vile na zabibu za viungo (raisins), hizi zote zitafanyika katika kukuza zao letu hili zabibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeingia makubaliano na wenzetu wa TBL kwa ajili ya kilimo cha mkataba cha wakulima wa zabibu ili wapate uhakika wa masoko yao ya zabibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni masuala la mboga mboga na matunda. Tumeingia makubaliano na wenzetu wa TAHA chini ya Dkt. Jacquline Mkindi ambaye ametenga muda wake mwingi kuikuza tasnia hii ya mboga mboga na matunda. Makubaliano hayo ambayo tumeingia yatakuwa ni katika mfumo mzima wa usafirishaji wa mazao ya mboga mboga na matunda (cold chain management) ambayo itasaidia katika kulinda ubora wa mazao yetu. Hapa pia tunakuja na kitu kinaitwa green channel ambacho kitasaidia katika kusafirisha matunda hayo pasipo kikwazo chochote mpaka kufikia katika destination yake, kwa maana ya Airport au Bandarini. Tunafanya haya kwa ajili ya kulinda ubora wa mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na vilevile ndugu zetu wa TARI tumekubaliana nao katika eneo lingine kubwa kabisa ambalo ni la kusaidiana kuanzisha miongozo maalum kwa ajili ya kuratibu zoezi la mazao ya mboga mboga na matunda ili tupate mwelekeo mmoja ndani ya nchi yetu ya Tanzania. Pia tunakwenda kujenga common use facility tatu ambazo zitajengwa katika Mikoa ya Kilimanjaro, Iringa na Dar es Salaam. Lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba tunakuwa tuna collection center moja yakupokea parachichi au na matunda mengine kuya-grade na kuya-sort na mwisho wa siku ni kuhakikisha tunafikia lengo tulilojiwekea, la kwamba ifikapo mwaka 2030 tuwe tunauza mazao yetu ya matunda yenye thamani ya kufikia Dola bilioni mbili kutoka Dola milioni 750 ilivyo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la mkonge tunajua kuna changamoto kubwa, na mimi nilikwenda mwenyewe nimetembelea kule Korogwe. Changamoto kubwa ya mkonge ni kwamba wakulima wa mkonge wanashindwa kuvuna mara mbili mkonge wao na unaoza shambani kwa sababu ya ukosefu ya korona. Nilitangazie Bunge lako, tumeshamuelekeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge kuhakikisha anatangaza zabuni ya kununua korona tatu kwa ajili ya wakulima wa mkonge kule Korogwe. Korona hizi zitasaidia pia kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava juu ya ubora, tunatambua ya kwamba hivi sasa daraja la ubora wa Mkonge wetu wakulima wengi wanapata ile inayoitwa UG; lakini lengo letu ni wakulima waende katika 3L na 3S, watoke kwenye UG. Ukipata desiccator ambayo ni ya kisasa na bora itamsaidia pia mkulima kupata mkonge ambao unakidhi matakwa ya soko na ambao mkonge wa 3L and 3S una soko kubwa na bei yake ni kubwa zaidi kuliko ile ya UG na ile nyingine ya UF. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine pia ambalo tunalifanyia kazi ni la kuhakikisha kwamba tuna-diversify matumizi ya mkonge wetu, badala ya kujielekeza tu katika kutengeneza nyuzi na magunia, tumekaa na wenzetu Chama cha SAT na tumekubaliana waongeze pia wigo mpana wa matumizi haya ili kutafuta soko la uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkonge una uwezo wa kutengeneza dashboard za magari, cabin za ndege, milango na mkonge ukiuchakata vizuri una uwezo wa kutengeneza pombe kali ile aina ya Tequila. Kwa hiyo, tumezungumza nao kwa ajili ya ku-diversify kwenda katika eneo hilo pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoa maelekezo kama Wizara ya kwamba mazao yote ambayo yako chini ya Bodi zinazoshughulikia mazao, waanze kutumia magunia yatokanayo na mkonge. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunaongeza soko kwa ajili ya mkonge wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine katika mkonge hapa ambalo nataka niligusie kwa haraka haraka ni eneo la nyuzi za nailoni za kufungia magunia ya mkonge. Tumekubaliana na wenzetu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwamba sisi tumetoa maelekezo mazao yote ya kilimo, yatafungwa kwa kamba zitokanazo na mkonge na sio nailoni ili tuongeze soko la mkonge wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejipanga pia kuja na Sheria ya Kilimo na Sheria ya Ushirika tunataka tuwalinde wakulima wetu tulinde maeneo yetu, tupate maeneo ya kilimo ambayo pia tutayapima na tutaya-gazette ili mwisho wa siku tuondoe migogoro ya wakulima na wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeboresha eneo la maabara yetu iliyopo Arusha ambayo inatusaidia kwa ajili ya mazao yanayokwenda nje ya nchi. Maabara yetu imetambulika, imepata ithibati na tumefunga mitambo ya kisasa. Hivi sasa mazao yanayotoka Tanzania yakitua pale Arusha hakuna mtu yeyote atayatilia mashaka. Kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya na investment kubwa ya mashine za kisasa na hivi sasa mazao yetu yanatoka pasipo changamoto yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kazi kubwa ambayo imefanyika na tunaamini Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono kwenye safari hii. Safari hii ndio tunaianza, tunaomba twende pamoja, mtuunge mkono, tunajua matokeo yatakuja baadaye, lakini kazi ndio tumeianza, mtuunge mkono, tuko tayari kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania, kuifikisha Tanzania katika nchi ya ahadi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana, Mwenyezi Mungu awabariki, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nachukua fursa hii kwanza kabisa kuwashukuru Wabunge wote ambao mmechangia katika muswada huu kwa namna ambavyo mmeguswa na ukubwa wa jambo hili na kuona umuhimu
wa sheria ambayo ipo mbele yetu hasa katika kukabiliana na changamoto hiyo kubwa ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kabisa kwamba changamoto hii inagusa kundi kubwa sana hasa la vijana ambao ndio nguvukazi ya Taifa hili. Hivyo, kwa hiki ambacho kinafanyika hivi sasa, kwa maana ya sheria hii itasaidia sana katika kupambana na udhibiti na lengo la kuiondoa jamii yetu katika changamoto hii kubwa.


Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda moja kwa moja katika hoja ambazo zimekuwa raised na Waheshimiwa Wabunge hapa na nikianza na ya kwanza, Waheshimiwa Wabunge katika michango yao wamzungumza kuhusu matumizi ya baadhi ya maneno na moja wapo ilikuwa ni neno control, mapendekezo yalikuwa ni kulifuta neno control.

Mheshimiwa Naibu Spika, neno hili control ambalo kwa mujibu wa marekebisho haya tuliyonayo, neno hili limeongezwa kati ya maneno drug na council ili liendane na jina lenyewe ambalo ni tunasema ni Baraza la Kudhibiti Dawa za Kulevya (National Drug Control Council), ndiyo maana hii control haina namna kuiepuka, na lazima liwepo ili kwenda kukamilisha hasa jina lenyewe la Baraza la Kudhibiti Dawa za Kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine ambayo ilikuwa raised pia hapa ya masuala ya kuondoa neno institution na badala ya kusema tu taasisi, lakini taasisi hizi zitajwe kwenye sheria. Neno taasisi kama lilivyosemwa hapa kwenye sheria ukiliondoa na ukaanza kuzitaja moja moja, katika utekelezaji wa sheria italeta ugumu mkubwa sana, hii ni kwa sababu katika zile techniques za kwenda kutafsiri sheria iko rule moja ambayo inasema kwa lugha ya kilatini expressio unius est exclusio alterius maana yake ni kwamba the express mention of one thing is the exclusion of the other.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizitamka leo zile taasisi pale specifically, ikija kutokea jambo limefanyika katika taasisi moja ambayo haijatajwa na sheria then maana yake pale umeshajishindishwa mwenyewe sheria inajishinda yenyewe. Ndio maana tunaendelea kuona kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa neno institution liendelee kubaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Waheshimiwa Wabunge walichangia katika hoja ya kusema kwamba lazima tutoe elimu kwanza na badala yake tuibadilishe hii sheria isiwe ya adhabu sana lakini pia tufanye na masuala ya elimu. Ni dhahiri kwamba na ninyi Waheshimiwa Wabunge mnafahamu, mamlaka hii imefanya kazi kubwa sana kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali katika kutoa elimu na kuwafanya watanzania kuelewa madhara makubwa ya matumizi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo si kweli tu kwamba tunafanya kazi ya kukamata tu lakini pia tunaelimisha umma wa Watanzania ili wafahamu madhara makubwa ya matumizi ya dawa za kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia imezungumzwa hoja hapa ya kwamba kuna mianya ya kuingiza dawa za kulevya na sheria hii sasa iangalie namna bora ya kuweza kudhibiti. Ukiangalia katika marekebisho ambayo yamefanyika hapa, zamani katika namna ya kupambana na dawa za kulevya, kwa maana ya udhibiti wake tulikuwa tunaainisha njia kadhaa especially katika maeneo ya bahari, kwa maana ya majini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika mapendekezo ambayo yanakuja hapa sasa tumefanya mabadiliko. Tumetumia maneno conveyance ambayo sasa it’s a broader term ambayo ina-cover zaidi ya yale ambayo tulikuwa tukiyasoma pale awali, kwa maana ya masuala ya majini peke yake. Kwa hiyo, hivi sasa tunazungumzia pia katika viwanja vya ndege ambavyo vilisemwa hapa kama sehemu ya mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia imezungumzwa hapa hoja na Mheshimiwa Ruth Mollel, alitamani kufahamu na kupata ufafanuzi wa Serikali kuhusu matumizi ya maneno Government Chemist na analyst. Kwa nini tumekwenda katika Government Analyst; tumekwenda huko kwa sababu tumefanya hivi ili yaendane na sheria nyinginezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ilikuwa ni katika kuonesha utofauti wa kwa nini tunaendelea kusema litumike neno analyst.

Mheshimiwa Naibu Spika, neno analyst ndilo neno ambalo linatumika kwenye baadhi ya sheria ambazo zinafanya azi pamoja na sheria hii. Moja kati ya sheria ambayo neno hili la analyst linatumika ni pamoja na The Criminal Procedure Act, lakini vilevile katika kifungu namba 13(1) cha Sheria ya The Government Chemistry Laboratory Act ya mwaka 2016, maneno yaliyotumika ni analyst.

Kwa hiyo, neno analyst ndilo neno sahihi hasa katika muktadha wa sheria hii, na ndiyo maana tuliona kwamba bado kuna umuhimu wa kuendelea kutumia neno analyst ili iendane na sheria nyinginezo ikiwemo hiyo CPA ambayo

nimeitaja, na Sheria ya The Government Chemistry Laboratory Act ya mwaka 2016.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nakushukuru sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Awali ya yote napenda nichukue fursa hii kwanza kabisa kuipongeza sana Serikali yangu ya CCM kwa Awamu zote kuanzia wakati wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati wa Rais Mstaafu Mwinyi, wakati wa Mzee Mkapa na wakati wa Mzee Kikwete. Wote hawa kwa pamoja waliendelea kuyaishi na kutekeleza kwa vitendo yale maamuzi ya mwaka 1973 ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu ukiangalia kwa mujibu wa historia ya Dodoma inavyosema, katika mwaka 1912 mpaka mwaka 1915 eneo la Dodoma hapa katikati lilikuwa lina majengo 26 tu ambapo wakati wa ukoloni Wajerumani waliona umuhimu wa kuifanya Dodoma kuwa sehemu ya Makao Makuu yao ya shughuli mbalimbali na wakachagua eneo la katikati kuwa sehemu ya Makao Makuu ya shughuli zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1932 Waingereza pia na wenyewe waliona umuhimu wa kuifanya Dodoma kuwa sehemu ya Makao Makuu yao kwa shughuli mbalimbali. Kwa hiyo, suala hili la Makao Makuu ya Dodoma halijaanza leo, limeanza tangu wakati wa ukoloni, waliiangalia Dodoma, wakaona umuhimu wake wakaipa sifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1973, kama wenzangu walivyosema, yalifanyika maamuzi makubwa sana ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi. Tunashukuru kwamba baada ya miaka mingi tangu uamuzi huo, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imefanya mambo makubwa sana kwa maamuzi sasa ya kuhamishia kivitendo kabisa Serikali yote kuwa hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba uamuzi huu ni sahihi na umekuja kwa wakati muafaka. Nasi kama wananchi wa Dodoma tunamuunga mkono sana Mheshimiwa Rais na tuko tayari na tumeshaupokea ujio huu wa Makao Makuu na tunatoa ushirikiano wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanatokana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Ibara ya 151(a); mimi nilipata bahati ya kuwa mmoja kati ya watu walioandika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Moja kati ya eneo ambalo tulilisema kwamba lazima tulifanyie kazi ni kuitambua Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi kwa mujibu wa sheria hasa baada ya kuwa kuna tamko la mwaka 1973, lakini tukasema sasa iwe kwa mujibu wa sheria. Leo nasimama hapa kwa furaha kubwa kwamba Chama changu kimetekeleza Ilani yake ya Uchaguzi kwa leo kuleta Muswada wa sheria wa kuitambua Dodoma kama Makao Makuu ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye sheria yenyewe. Sheria hii ambayo leo tunaijadili, kwa kweli inaleta jambo lenye tija sana kwa wananchi wa Dodoma kwa kiu yao kubwa ya kutaka kuwepo na utaratibu maalum wa kuitambua Dodoma kama Makao Makuu. Kwa ujio wa sheria hii maana yake ni kwamba, tunakwenda kutengeneza utaratibu sasa wa kisheria wa kuitambua Dodoma na kwa mujibu wa Kifungu cha 4(1) cha Muswada huu kimetamka rasmi sasa kwamba Dodoma inatambuliwa kama Makao Makuu ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu 4(2) cha sheria hii kimeweka pia utaratibu mzuri kwamba, hakutakuwa na mabadiliko mengine yoyote yatakayofanyika katika maamuzi haya pasipo kupitishwa na two third ya Wabunge wote katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii inatupa assurance kwamba, uamuzi huu wa Serikali utaendelea kulindwa kwa sheria hii ambayo tunaitunga na ni jambo ambalo sasa linafanya Dodoma kwa utambuzi wake huu na sisi tupate amani kwamba Dodoma itaendelea kuwa Mkao Makuu ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hoja pia hapa kuhusu kuupanga Mji wa Dodoma na miundombinu ya Dodoma. Katika hili naomba niwambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu, kama watu hawana taarifa sahihi siyo vyema kuzungumza mambo ambayo hawana uhakika nayo. Katika Jiji la Dodoma kati ya miji ambayo imepangwa vizuri Tanzania Dodoma ni mmojawapo. Hili halina ubishani. Dodoma ni kati ya miji iliyopangika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha miezi sita tangu mwezi wa Tatu mwaka huu mpaka mwezi wa Tisa vimepimwa zaidi ya viwanja 20,000 ambavyo lengo lake ni kuufanya mji huu sasa uwe umepangika na kuondoa ujenzi holela. Hivi sasa ninavyozungumza mpango ule wa Master Plan ya Dodoma ambapo kuna baadhi ya watu, hasa Mheshimiwa aliyetoka kuchangia hivi sasa alikuwa anabeza kwamba hata shughuli za Kitaifa tunategemea Uwanja wa Jamhuri, hatuna sehemu ya kufanyia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Master Plan ya Dodoma ambayo itakwenda kuzinduliwa rasmi nafikiri Desemba mwaka huu, utaona katika maeneo ambayo yamepangwa vizuri, eneo la Mtumba ambako ndiyo
kutakuwa kuna Mji wa Serikali na Mabalozi wote wako pale, pale inakwenda kujengwa park kubwa ya Kitaifa ambayo Mheshimiwa Rais, Viongozi wa Kitaifa wote wakitaka kuhutubia Taifa watakuwa na eneo maalum, kama ilivyo Marekani vile, atakaa sehemu, eneo maalum, atahutubia Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, eneo hilo la Mtumba ambako tumewapa viwanja Mabalozi na Mji wa Serikali umeshapangwa vizuri. Ninavyozungumza hivi sasa, miundombinu yote imeenda ya maji na umeme, imebaki ya barabara tu. Tukumbuke haya mambo huwa hayawezekani over night tu, miji yote imejengwa kwa utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hoja hapa kuhusu barabara kwamba Dodoma hakuna barabara za kutosha, barabara nyingi za vumbi. Narudia tena kwa wale wote ambao hawana takwimu sahihi, wasizungumze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dodoma ndio Jiji la pili ukichukua Halmashauri zote nchi nzima, Manispaa za Wilaya na Majiji yote, Dodoma ndiyo ya pili kwa mtandao wa barabara za lami. Kwanza ni Kinondoni, ina kilomita 136 na ya pili ni Dodoma ina kilomita 130.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wa fedha tumetenga kiasi cha shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuongeza barabara za lami, lakini tuna mradi wa TSP wa shilingi bilioni
40.9 ambao utaongeza kilomita 26 za barabara za lami. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba mwakani Dodoma ndiyo itakayoongoza nchi nzima kwa mtandao wa barabara za lami. Hakuna Jiji lolote, Manispaa yoyote wala Halmashauri yoyote ya Wilaya itakayofikia Dodoma kwa mtandao wa barabara za lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza pia hoja ya kwamba hakuna miundombinu, masoko na vivutio mbalimbali. Wiki tatu zilizopita na Mheshimiwa Jafo alikuwepo kwenye kushuhudia, umesainiwa mkataba wa shilingi bilioni 78. Mkataba huo unakwenda kujenga miundombinu ya Dodoma likiwemo soko ambalo limezungumzwa hapa hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kujenga soko la kisasa nafikiri kuliko mengi ya Afrika Mashariki na Kati; tunakwenda kujenga stendi kubwa ya mabasi ambayo itakuwa ina uwezo wa kuegesha mabasi, magari madogo, bajaji na bodaboda 600 kwa wakati mmoja. Hali kadhalika zinakwenda kujengwa barabara ambazo ni outer na inner ring roads za kuondoa msongamano katika eneo letu hili la Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napata mashaka nikiona watu wanazungumza mambo ambayo hawayafahamu. Uamuzi wa huu ni sahihi na Serikali ilichokifanya ni sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kwa kumalizia hoja yangu, Waheshimiwa Wabunge wengi wa Upinzani wamesimama hapa wanasema, sisi tuna hoja moja tu kwamba Dodoma ni katikati ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.