Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama (11 total)

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-
Miradi ya maji inayojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia katika vijiji vya Lilondo na Maweso imekwama kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, licha ya miradi hiyo kutumia fedha nyingi na nguvu kubwa za wananchi:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha miradi hiyo?
(b) Je, ni lini miradi hiyo itakamilika ili kutatua kero za maji kwa wananchi wa vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji ya Maweso na Lilondo katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ni kati ya miradi iliyoibuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Songea katika mpango wa vijiji kumi kwa kila Halmashauri chini ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini. Aidha, utekelezaji wa miradi hii imekuwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea kutokana na kuwa illibuliwa na kuanza kutekelezwa wakati Madaba ikiwa ni sehemu ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa Maweso kwa mujibu wa mkataba una gharama ya shilingi 546,792,163.2. Jumla ya shilingi 109,771,259 zimetumika kumlipa mkandarasi. Vilevile, mradi wa Lilondo kwa mujibu wa mkataba una gharama ya shilingi 1,048,875,254 na jumla ya shilingi 224, 491,637.25 zimetumika kumlipa mkandarasi. Hivi karibuni Halmashauri ya Wilaya ya Songea imewasilisha hati ya madai ya wakandarasi wa miradi hiyo na Wizara imetuma jumla ya shilingi 101,444,072 ili kuwalipa wakandarasi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima kuu ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Hivyo, Serikali kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa itahakikisha inapeleka fedha kwa kadri zinavyopatikana katika miradi hii kulingana na hati za madai zilizohakikiwa na Halmashauri, Sekretarieti ya Mkoa na Wizara ili iweze kukamilika ifikapo mwezi Julai, 2017.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-
Zaidi ya wananchi 181 wa kijiji cha Ngadinda Halmashauri ya Madaba wanalima ndani ya Wilaya ya Namtumbo kwa sababu ya kukosa eneo katika kijiji chao. Baraza la Madiwani lilishauri sehemu ya shamba la hekta 6,000 la Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lililopo ndani ya kijiji hicho ambalo lilikabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ili litumike kwa shughuli za kilimo na sehemu ibaki kwa ajili ya mifugo. Hivi sasa wafugaji toka maeneo mbalimbali nchini wapo katika shamba hilo lakini wakulima hawajatengewa eneo.
(a) Je, Serikali haioni kwamba kitendo hicho ni ubaguzi na kinaweza kuchochea migogoro kati ya wafugaji na wakulima?
(b) Je, ni lini Serikali itasikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Ngadinda cha kutengewa eneo la kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Songea mwaka 2014 iliunda Tume ya kuchunguza matumizi ya shamba hilo ambalo lilikuwa linamilikiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kubaini kuwa shamba hilo halitumiki vizuri kwa shughuli za ufugaji. Kwa msingi huo Tume ilipendekeza hekta 4000 wapewe wananchi wa Kijiji cha Ngadinda na eneo linalobaki la hekta 2000 libaki kwa shughuli za uwekezaji na ufugaji. Hata hivyo, baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya ya Songea kugawanywa na kupata Halmashauri mpya ya Wilaya ya Mababa uamuzi huo haukutekelezwa. Hivyo, Halmashauri ya Madaba inatakiwa kujadili suala hili katika vikao vya Halmashauri na kufanya uamuzi kuhusu matumizi ya shamba hilo kwa kuzingatia maslahi ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoelezwa katika sehemu (a) ya jibula msingi, Halmashauri ndiyo yenye jukumu la kujadili na kukubaliana kuhusu matumizi ya shamba hilo lililokuwa linatumika kwa shughuli za ufugaji. Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha maslahi ya wakulima na wafugaji yanazingatiwa kuhusu matumizi ya shamba hilo.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-
Idadi ya watu nchini inazidi kuongezeka, ongezeko hili linaenda sambamba na ongezeko la mahitaji ikiwemo ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji ili waendeshe shughuli zao katika maeneo madogo lakini kwa tija kubwa na kuwaondolea adha wanazozipata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Madaba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali huwajengea uwezo wakulima na wafugaji nchini kupitia elimu na ushauri wa kitaalam ambao hutolewa na Maafisa Ugani walioko kwenye Kata na Vijiji vya Halmashauri zote nchini. Hadi Desemba, 2017 tunao Maafisa Ugani 13,532. Kati ya hao Maafisa Ugani 8,232 ni wa kilimo cha mazao, 4,283 ni wa mifugo, 493 ni wa uvuvi na 524 ni wa ushirika.
Elimu ya kilimo na ufugaji bora hutolewa kupitia mashamba darasa 11,213 nchi nzima kwa wakulima na wafugaji wakubwa na wadogo, vikundi vya ushirika vya miradi ya umwagiliaji kwa njia ya mitaro na njia ya matone (drip irrigation) na vikundi vya ushirika vya ufugaji wa kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo itakayoanza kutekelezwa mwaka ujao 2018/2019 Serikali inaandaa mradi wa kilimo cha kutumia vitalu nyumba (green house) utakaotekelezwa kwa kila halmashauri kujenga vitalu nyumba visivyopungua viwili ili kusambaza teknolojia mpya ya kilimo yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha shehena ya mazao mengi katika eneo dogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingine ni pamoja na kufanya sensa mahsusi ya kuwatambua wakulima wadogo na wakubwa, kuwasajili, kujua uwezo wao na kujua mahitaji yao ya mbegu, mbolea na madawa. Zoezi hilo limeanza na mazao ya kahawa, tumbaku, korosho, chai na pamba kwa mazao ya biashara; pamoja na mazao ya mahindi, mpunga, ngano na muhogo kwa upande wa mazao ya chakula. Takwimu hizo zitasaidia utekelezaji wa mikakati ya kuongeza uzalishaji kwa kuhakikisha pembejeo za kilimo zinawafikia wakulima mapema ili zitumike kwa wakati stahiki wa kilimo kwa lengo la kuongeza tija.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-

Moja kati ya maombi yaliyowasilishwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati wa ziara yake Mkoani Ruvuma, katika Wilaya ya Songea ni zahanati za Mbangamawe na Magingo zilizoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba zitakapokamilika zipandishwe hadhi kuwa Vituo vya Afya kutokana na ukubwa wake na mahitaji kwa Wananchi:-

Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza jukumu hilo muhimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama Mbunge wa Madaba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa akiwa ziarani Mkoani Ruvuma tarehe 05 Januari, 2017 katika Halmashauri ya Madaba alipokea maombi kutoka kwa wananchi ya kuiomba Serikali kuzipandisha hadhi Zahanati za Magingo na Mbangamawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini iliyofanyika imebaini kuwa ujenzi wa Zahanati zote mbili umefikia asilimia 45 kila zahanati ina jengo moja kubwa lenye vyumba 21 kwa kufuata ramani zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kabla ya mwaka 2010 kwa kuzingatia mpango wa MMAM. Vyumba 5 kati ya 21 kwa kila zahanati vimekamilika. Tathmini inaonyesha kuwa ili kukamilisha ujenzi kiasi cha shilingi milioni120 kinahitajika kwa zahanati ya Mbangamawe na milioni 100 kwa zahanati ya Magingo. Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha ili kukamilisha na kufuata taratibu zote zinazotakiwa ili kuzipandisha hadhi zahanati hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendelea kuboresha huduma za afya Madaba katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepatia Halmashauri ya Madaba kiasi cha shilingi milioni 900 kwa ajili ya ukarabati, ujenzi na upanuzi wa vituo vya afya vya Madaba, Mtyangimbole. Vilevile katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Madaba. Serikali inaendelea na jitihada za kujenga, kukarabati, kupanua na kuboresha miundombinu ya afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO (K.n.y. MHE. JOSEPH K. MHAGAMA) aliuliza:-

Miongoni mwa mambo yanayokwamisha ukuaji wa sekta ya kilimo nchini ni pamoja na kukosekana kwa maduka ya pembejeo za kutosha maeneo ya vijijini ambako ndiko walipo wakulima wengi. Miongoni mwa sababu za kukosekana maduka hayo ni gharama kubwa ya kufuzu (certifications) kama vile TOSC 1 – Sh. 100,000; TPRI – Sh.320,000; TFDA - Sh.100,000; leseni na kadhalika na hivyo kufanya gharama kuwa zaidi ya Sh.600,000:-

Je, ni kwa nini Serikali isiondoe gharama hizi ili kutoa hamasa kwa wajasiriamali kupata mafunzo, kufuzu na kuwekeza maduka ya pembejeo ili kusogeza huduma kwa wakulima wadogo na kuharakisha kasi ya ukuaji wa kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo katika hatua za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kutatua changamoto zinazokabili sekta ya kilimo zikiwemo za biashara ya pembejeo kama zilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara (Blue print). Aidha, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa, pembejeo zenye ubora zinapatikana kwa wakulima kwa urahisi na kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutoa hamasa kwa wajasiriamali wanaohitaji kufungua maduka ya pembejeo vijijini, mwaka 2017/2018, Serikali ilifanya mapitio na kufuta jumla ya tozo tano katika biashara ya mbegu ambazo ni Sh.100,000 ya Cheti cha Usajili na Utambuzi wa Muuzaji; Sh.50,000 Cheti kwa ajili ya aina ya mbegu; Sh.5,000 Cheti cha Majaribio ya Mbegu; Sh.2,500 ada ya nakala ya cheti na Sh. 5,000 ada kwa ajili ya Cheti cha Majaribio.

Mheshimiwa Naibu Spika, viuatilifu ni sumu ambayo huweza kuhatarisha maisha ya binadamu, mifugo na mazingira kama havitatumiwa kwa usahihi. Hivyo muuzaji lazima awe na taaluma maalum ya viuatilifu kwa mujibu wa Sheria Na. 13 ya mwaka 1997 ya Udhibiti wa Visumbufu vya Mimea kama ilivyo kwa maduka ya dawa za binadamu. Aidha, mfanyabiashara anapotaka kufungua duka la viuatilifu hupatiwa mafunzo maalum ya siku sita kwa gharama ya Sh.320,000 kwa mujibu wa Kanuni Na.31, kifungu cha 3 cha Kanuni za Huduma za Afya ya Mimea, hivyo, gharama za mafunzo ya viuatilifu haziwezi kukwepeka.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA Aliuliza: -

Je ni lini Serikali itachukua hatua kudhibiti watu wanaodanganya kupeleka ng’ombe katika mnada wa Mtyangimbole kisha kuwatorosha na kuwaingiza katika maeneo mbalimbali ya Madaba, Namtumbo na Songea ilihali Madaba haina uwezo wa kuhimili wingi wa mifugo hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Madaba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na matumizi mabaya ya vibali vya kusafirisha mifugo kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine ambapo baadhi ya wafugaji wanakata vibali vya kusafirisha mifugo kwenda mnadani kwa ajili ya biashara lakini kinyume chake inahamishwa kuelekea maeneo mengine ya mikoa ukiwemo Mkoa wa Ruvuma, Halmashauri ya Madaba.

Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kwa kipindi cha kuanzia Aprili 2020 hadi Aprili 2021 idadi ya idadi ya mifugo iliyosajiliwa katika Halmashauri ya Madaba yenye vibali kuelekea mnada wa upili wa Mtyangimbole ni ng’ombe 8,925 ilhali walioingia mnadani ni ng’ombe 5,753, sawa na tofauti ya ng’ombe 3,172 wanaosadikika kuingia katika maeneo mbalimbali na kusababisha migogoro.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tazizo hili, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Madaba itaimarisha ufuatiliaji wa vibali vya mifugo ili kuhakikisha mifugo iliyoandikiwa vibali kwenda Mnada wa Mtyangimbole imefika. Vilevile katika kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa malisho na maji kwa mifugo katika maeneo ya wafugaji, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 193.28 kwa ajili ya utatuzi wa migogoro na utengaji wa maeneo ya malisho.

Mheshimiwa Spika, pia shilingi bilioni 1.586 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa mabwawa/malambo na visima virefu, ambapo katika Mkoa wa Ruvuma, Halmashauri ya Songea, kisima kimoja kitachimbwa kwa lengo la kuwapatia mifugo maji.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuwahamasisha wadau wengine wakiwemo wafugaji kujiunga kwenye vikundi na kushiriki kwenye ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya maji na uendelezaji wa malisho katika maeneo yaliyotengwa ili kuzuia uhamaji usio wa lazima unaosababisha migogoro.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapunguza gharama za vibali vya kuanzisha biashara ya kuuza pembejeo za kilimo Vijijini ambapo TFRA, TOSCI na TPRI huchukua takribani shilingi 600,000 kabla mfanyabishara hajaingiza mtaji dukani?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Madaba, kama ifuatavyo: -

Mhashimiwa Mwenyekiti, watoa huduma wa pembejeo ikiwemo mbegu, viuatilifu na mbolea katika ngazi zote, wanatakiwa wawe na uelewa mpana wa huduma wanazozitoa. Gharama za kuanzisha biashara ya pembejeo hizo hutokana na mafunzo maalum yanayotolewa na taasisi husika kwa lengo la kujenga uwezo kwa Mawakala na Kampuni za pembejeo ili kutoa huduma stahiki kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu Na. 18 ya mwaka 2003 na marekebisho yake ya mwaka 2014 pamoja na Kanuni za mwaka 2007 na marekebisho ya mwaka 2017; hakuna tozo za kuanzisha biashara ya mbegu, isipokuwa kuna ada ya mafunzo ambayo ni shilingi 150,000 kwa kampuni na wazalishaji/ mawakala wasambazaji wa mbegu bora. Aidha, kwa wazalishaji wa mbegu za kuazima (Quality Declared Seed) hutozwa shilingi 50,000 kwa ajili ya mafunzo maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa viuatilifu na ukaguzi wa eneo la duka linalofunguliwa ni kiasi cha shilingi 172,500 na shilingi 350,000 hutozwa kwa ajli ya mafunzo. Malipo haya ni kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Mimea ya mwaka, 2020. Kwa upande wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania - TFRA hakuna tozo kwa mfanyabiashara anayetaka kuanzisha duka la kuuza mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuboresha mazingira ya wazalishaji na wasambazaji wa pembejeo ilifuta tozo na ada mbalimbali kwa upande wa mbegu jumla ya tozo 12 zilizokuwa zikigharimu jumla ya shilingi 180,500 zilifutwa. Vilevile Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea ilifuta tozo nne zilizokuwa na shilingi 2,240,000. Hivyo, nitoe wito kwa wafanyabishara wenye nia ya kuanzisha maduka ya pembejeo kujitokeza na kuanzisha maduka hayo ili kusogeza huduma hiyo karibu na wakulima. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza: -

Je, ni kwa nini Mfumo wa Stakabadhi Ghalani hautekelezwi kikamilifu kiasi cha kuwawezesha Wakulima kupata fedha wanapohitaji?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya ushindani, wanunuzi kupata mzigo wenye ubora pamoja na Halmashauri kupata takwimu halisi za mauzo na mapato. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba zao la kahawa, ufuta na korosho ni baadhi ya mazao ambayo huuzwa kupitia mfumo huo. Mfumo huo, umekuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo baadhi ya wanunuzi kuchelewesha malipo kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hiyo Serikali itaimarisha usimamizi wa mwongozo unaoainisha muda maalumu wa kuwalipa wakulima kwa kuchukua hatua za kisheria kwa wanaokiuka taratibu.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasaidia ujenzi wa Stendi ya Madaba ikizingatiwa kwamba stendi hiyo ipo kwenye eneo la kimkakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kuwa na stendi ya mabasi katika Mji wa Madaba ili kuboresha upatikanaji wa huduma na kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba katika mwaka wa fedha 2018/2019 iliandaa na kuwasilisha Serikali Kuu andiko la Mradi wa Kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya mabasi ambalo halikukidhi vigezo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba imepanga kutumia Shilingi Milioni Tano, kwa ajili ya kukamilisha upembuzi yakinifu (feasibility study) kwa ajili maandalizi ya andiko la mradi wa ujenzi wa stendi litakalowasilishwa Serikali Kuu ili iweze kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza: -

Je, kwa nini hoja za ukaguzi hutokea pale fedha za Mfuko wa Jimbo zinapotumika kwa wajasiriamali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa Sheria Na. 16 ya mwaka 2009 na unaelekeza miradi ya kutekelezwa kupitia Kamati ya Mfuko ambayo Mbunge ni mwenyekiti na afisa mipango wa halmashauri ni katibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo mahususi la kuanzishwa kwa Mfuko huu wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo ni kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoibuliwa katika ngazi ya jamii na kupitishwa kwenye vikao mbalimbali vya kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya halmashauri zimekuwa zikitumia fedha za Mfuko wa Jimbo kutoa mitaji kwa wananchi, hususan wanawake, watu wenye ulemavu na vijana, hali inayosababisha ugumu wakati wa kufanya ufuatiliaji na tathmini na kusababisha hoja za ukaguzi.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara ya Wino hadi Ifinga ambayo wakati wa masika haipitiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini kwa maana ya TARURA, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuboresha barabara ya Wino – Ifinga yenye urefu wa kilomita 57 ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 barabara ya Wino – Ifinga ilitengenezwa jumla ya kilomita 21 kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya Shilingi Milioni 398.00 na katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya kilomita 15 zimejengwa kwa kiwango cha changarawe kwa gharama Shilingi Milioni 360.46.

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga Shilingi Milioni 380.00 kwa ajili ya kujenga kilomita 10.5 kwa kiwango cha changarawe na ujenzi wa maboksi kalavati matatu. Serikali itaendelea kuboresha Miundombinu ya barabara za Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.