Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph Kizito Mhagama (36 total)

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuhitimisha Hoja ya Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya Wabunge 23 walipata nafasi ya kuzungumza. Iingie kwenye kumbukumbu za kudumu za Bunge kwamba hoja hii ni moja katika hoja chache sana ambazo ndani ya Bunge lako zimepata kibali toka pande zote za Wabunge bila kuyumba. Sababu ni kwamba Waheshimiwa Wabunge wote wanaamini kwamba mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, hayawezi kutenganishwa kamwe na mafanikio ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye alihudumu kama Makamu wa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo moja limezungumzwa kwa namna ambayo linahitaji kidogo tulifafanue; hoja ya demokrasia na uhuru wa Habari. Kwamba Mheshimiwa Khatib na baadhi ya Wabunge humu ndani kuweza kuhama kutoka kwenye Chama cha CUF na kwenda ACT Wazalendo na kuweza kushiriki katika Uchaguzi na kushinda na kuzungumza ndani ya Bunge hili ni demokrasia ya kiwango cha juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, demokrasia huanzia ndani ya vyama. Kitendo cha Chama Cha Mapinduzi kuendelea na utaratibu wa kubadilisha wenyeviti wao kila miaka kumi ni kielelezo cha kutosha cha ukomavu wa demokrasia ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeshauri vyama vingine vifuate utaratibu huo kwa sababu huwezi kuwa na legitimacy ya kupigania demekrasia nje kama hujaimarisha demokrasia ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, tafsiri sahihi ya demokrasia; na hapa namnukuu Balozi Dkt. Wilbrod Slaa; demokrasia ya kweli ni demokrasia ya kuwasikiliza na kuwahudumia watu wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wa Tano alifanya kazi hii kwa uaminifu mkubwa akishirikiana na Rais wetu wa sasa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Kote walikopita Watanzania wamelilia elimu, maji, huduma za afya, mahitaji ya mitaji kwenye biashara na yale yote yaliyowekwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na hayo yote ndiyo yaliyobebwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KIZITO M. JOSEPH: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia muda niliopewa niende moja kwa moja, kwanza kutoa salamu za shukurani kwa Waziri, Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, ambaye majira ya jioni kuelekea saa moja, mvua zinanyesha, amechoka, amefanya kazi kutwa nzima Ludewa, anarudi anakwenda Songea Mjini, alikubali kuendesha mkutano Madaba. Wananchi wa Jimbo la Madaba hawataisahau ile taswira.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku ile Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, alitoa majibu ya moja kwa moja ya tatizo kubwa la umeme la wananchi wa Madaba. Wananchi wa Madaba wanamshukuru na wapo pamoja naye katika safari hii ya kutekeleza majukumu aliyopewa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto katika utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Waziri, lakini changamoto hizi zinahusisha zaidi muundo wa utaratibu huo wa utekelezaji. Kwa utaratibu ambao Mheshimiwa Muhongo ameuweka, ni kwamba Madaba ifikapo Desemba tutapata umeme, lakini katika kipindi hiki cha miaka miwili Madaba Mjini patakuwa hub ya umeme unaotoka Makambako kuelekea Songea, lakini pia hub ya umeme unaotoka Mchuchuma na Liganga kulelekea maeneo mengine ya Taifa letu. Maana yake nini? Maana yake Madaba inakwenda kupitia transformation kubwa sana ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto inayotupata kwa sasa ni kwamba Serikali bado ina ugumu kidogo wa kuchangia gharama kuweza ku-meet gharama za wafadhili kwenye hilo jukumu na kikwazo kinaonekana kipo Hazina. Naomba watu wa Hazina wasikalie pesa kama zipo. Kama pesa zipo na zimepangwa kwa matumizi hayo, basi zitolewe zikafanye hizo kazi ili hizi Wizara husika ziweze kujibu matatizo ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye hili tu kwa sababu linanigusa na wananchi wa Madaba lina wagusa sana. Ndani ya Jimbo langu la Madaba ni kijiji kimoja tu cha Lilondo kina umeme na umeme huu ni wa wananchi. Nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Mwijage, ambao kwa namna moja au nyingine wamesaidia sana kupatikana ule umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yote ya Jimbo la Madaba, Vituo vyote vya Afya, saa hizi mimi Mbunge kwa kutegemea posho ninazopata hapa Bungeni, naweka solar. Hata ukiiangalia gari ninayoitembelea ni ya kawaida sana ili niweze kubana matumizi ya kupata solar kwa ajili ya Vituo vyote vya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana na wananchi wa Jimbo la Madaba wanaomba sana kwa Mheshimiwa Waziri Profesa Sospeter Muhongo, kwamba yale ambayo ameyapanga wanamwomba Mwenyezi Mungu amjalie nguvu ili ifikapo Desemba na kuendelea changamoto hii iwe imekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo miradi ya kielelezo ya kiuchumi. Ndugu yangu…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda nimshukuru sana Mwenyenzi Mungu aliyenijalia wakati huu kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia kwa unyenyekevu mkubwa sana niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Madaba ambao kwa umoja wao wamenituma nifanye kazi yao wakiamini kwamba nitawatendea haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kupongeza sana hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa kwa Bunge lako Tukufu. Hotuba hii imejaa hekima kubwa lakini pia imejaa matumaini makubwa sana kwa wananchi wa Tanzania na hasa kwa wananchi wa Jimbo langu la Madaba. Hotuba ya Mheshimiwa Rais kwa sehemu kubwa imetoa mwelekeo wa Taifa letu kwa kipindi cha miaka mitano. Kwa hakika hotuba yake imeshakwishaanza kutafsiriwa kwa vitendo kupitia utekelezaji wa kazi hizo, lakini pia kwa kupitia Baraza lake la Mawaziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Mawaziri wote wa Awamu ya Tano, wanafanya kazi kubwa kwa ajili ya Watanzania. Kwa namna ya pekee sana naomba sana niwashukuru sana Mawaziri ambao tayari wameshakuja kwenye Jimbo langu na tayari wameanza kufanya kazi na wananchi wa Jimbo langu. Kwa namna ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Ummy Mwalimu, tayari amekuja kuangalia changamoto za afya na sasa yupo kwenye mchakato wa kuhakikisha kwamba tunapata hospitali ya Wilaya, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa heshima kubwa nimshukuru sana Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini katika mazingira magumu na muda mgumu alifika katika Jimbo langu kuangalia changamoto ya umeme na kuipatia majibu pale pale. Namshukuru na kumpongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika uchangiaji wangu nitajikita katika maeneo machache muhimu yanayohusu maslahi ya Taifa letu. Moja ni eneo la viwanda. Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais toka ukurasa wa 13 – 16 anaeleza ni namna gani Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuifanya sekta ya viwanda iwe sekta mama itakayotoa ajira za uhakika kwa Watanzania. Mheshimiwa Rais anakwenda mbali zaidi na kueleza namna gani hiyo sekta ya viwanda inakwenda kujibu matatizo ya masoko ya mazao, mifugo pamoja na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii kwa uzito ambao Mheshimiwa Rais ameupa na kwa hali halisi ya Tanzania ni sekta muhimu sana. Nitumie nafasi hii kupongeza hatua ya Mheshimiwa Rais kuzingatia viwanda lakini naomba nitoe tahadhari kwa wale ambao wamepewa kusimamia utekelezaji wa jukumu hili. Moja, lazima tujue kwamba sekta ya viwanda ina mahusiano makubwa sana na sekta ya biashara lakini pia kwa sababu hivyo viwanda vinahusu kilimo, uvuvi na mifugo, sekta hizi zote zinafanya kazi kwa karibu sana. Sera ya kuimarisha viwanda ndani ya Tanzania siyo sera ngeni, kigeni katika Awamu hii ya Tano ni mikakati mipya ambayo Mheshimiwa Rais amekuja nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tujifunze ni nini kilisababisha viwanda vyetu vya miaka ya 1980 na 1990 na kuelekea mwaka 2000 vikafa. Mikakati ya ndani ni mizuri, mitaji ilipelekwa lakini naomba wanaohusika na maandalizi na usimamizi wa eneo hili wakubali kurudi tena kwenye kusoma uzoefu hasa unaogusa sera zetu za nje, mikataba yetu na makubaliano ya kibiashara na mataifa mbalimbali zikiwemo jumuiya mbalimbali zenye maslahi ya kibiashara na Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia kwa undani pamoja na jitihada za ndani za kuzalisha mazao ya viwandani, mazao yetu yameendelea kukosa soko kwa sababu tumefungulia kiholela mazao ya viwandani yanayotoka mataifa mengine. Ndani ya Mkoa wa Ruvuma nimepambana sana kwa miaka zaidi ya sita kuhakikisha kwamba sekta ya mazao ya mafuta yakiwemo alizeti inakuwa sekta tegemezi kwa uchumi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuhakikisha kwamba tunazalisha mafuta ya kula ya kutosha yatakayoweza kukidhi mahitaji ya mkoa. Hata hivyo, jitihada hizo zimeangamizwa na mafuta ya bei rahisi yanayoingizwa toka Malaysia na nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo eneo halitaangaliwa vizuri, Watanzania tutaenda kuwekeza kwenye viwanda na tutafilisika na tutabaki maskini wa kutupwa kwa sababu Tanzania mpaka sasa imeendelea kuwa soko kubwa la mazao ya viwandani yanayotoka nchi zingine. Kwa hiyo, nashauri sera yetu inayohusiana na maeneo hayo iangaliwe vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ni mama kwa uchumi wetu ni kilimo na mifugo. Niishukuru sana Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Waziri Mwigulu na timu yake wananchi wa Madaba kwa namna fulani wamefaidika sana na Wizara hii kwa asilimia 75 ya wakazi wake kufanikiwa kupata pembejeo za ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu wa ruzuku siyo endelevu. Msimu wa mwaka jana wananchi wa maeneo yale hawakupata pembejeo za ruzuku iliathiri sana uzalishaji wao. Najua mfumo huu umechukua uzoefu kutoka Malawi na maeneo mengine na hapa tunau-apply. Naomba Wizara inayohusika na kilimo na mifugo tuchukue hatua za makusudi kujifunza mifumo mingine inayopendekezwa na wadau mbalimbali wa kilimo. Najua kumekuwa na miradi mbalimbali ya wadau wa kilimo inayojaribu mifumo mbalimbali ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata pembejeo kwa namna endelevu. Naomba sana Wizara hii iandae utaratibu maalum wa kufanya utafiti wa mifumo inayofaa. Mfumo huu hauna uendelevu kwa sababu unategemea asilimia 100 ruzuku ya Serikali, ruzuku ambayo hatuna uhakika nayo. Kuna mifumo ya kuwaunganisha wasindikaji, wanunuzi wa mazao, wasambazaji pembejeo pamoja na vikundi vya wakulima kwa kupitia mfumo wa mikataba ambayo itawasaidia kupata mikopo ya pembejeo, uhakika wa masoko ya kilimo na uhakika wa uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mengi nyeti yanayowagusa wananchi wa Jimbo la Madaba, eneo la soko la mazao ni mgogoro sana kwa sababu mpaka sasa tunategemea Serikali pekee kununua mahindi kupitia NFRA. Nashukuru sana Wizara ya Kilimo wamefanya jitihada kubwa sana kukarabati maghala ya kuhifadhia mazao wakati wa mavuno. Hata hivyo, maghala yale yametengenezwa kwa pesa za wakandarasi, wakandarasi hawajalipwa, hawajamaliza na mwezi wa sita wananchi wanaanza kuvuna hawana mahali pa kuhifadhia mazao yao, tunaomba hilo nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo gumu sana kwetu Madaba ni maji. Wananchi wa Madaba hawana maji, Jimbo la Madaba ni jipya, Halmashauri ya Wilaya mpya, Makao Makuu maji ni mgogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nikushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Mpango huu wa Miaka Mitano unaeleweka vizuri iwapo utasomwa katika context yake ya kwamba Mpango huu unatokana na Mpango Elekezi wa Miaka 15. Ukishauweka katika context ya miaka 15 unaelewa kwamba kilicholetwa hapa kwa miaka hii mitano ni hatua ya pili ya utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Miaka 15. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukishaelewa hivyo, unaweza ukapunguza sana kejeli ambazo zinatolewa na baadhi ya Wabunge humu ndani. Hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu ilikuwa kutanzua vikwazo vya uchumi; ni hatua nzuri ambayo imefikiwa kwa kipindi cha miaka mitano tunachokimaliza msimu huu wa 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, tunapokuja na Mpango wa miaka mitano inayoanzia mwaka 2016/2017, tunazingatia pia uzoefu tulioupata miaka mitano iliyotangulia. Ukiangalia katika Mpango huu, miaka mitano iliyopita ilieleza bayana, pamoja na kutanzua vikwazo vya uchumi, pia kipindi hicho cha miaka mitano iliyotangulia kilienda sambamba na kubaini maeneo ya vipaumbele. Maeneo ya vipaumbele yaliyobainishwa ni pamoja na Miundombinu, Kilimo, Viwanda, Rasilimali Watu, Huduma za Kifedha, Utalii na Biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapotoka kwenye awamu ya kwanza na tunapokwenda kwenye awamu ya pili ambayo itachukua tena miaka mitano, tumechagua eneo la viwanda kama eneo mahususi la kulifanyia kazi. Mpango huu ukiusoma kwa umakini na ukaulewa, utaelewa ni kwa nini sasa tumechukua viwanda na kwa nini Mpango huu umeitwa kama kipaumbele kujenga misingi ya uchumi wa viwanda? Tunapoongelea viwanda, tunaenda sambamba na miundombinu ambayo itafanya viwanda viimarike lakini biashara iimarike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mpango huu umebainisha vizuri maeneo ya ujenzi wa barabara, reli, bandari, lakini pia umeeleza miradi mahususi ambayo itaifanya Tanzania yetu iwe Tanzania mpya, Tanzania ambayo inakwenda kujibu kero za vijana, akinababa na akinamama wa Taifa hili. Ukiusoma katika context hiyo, unakubaliana nami kwamba Mpango huu wa miaka mitano kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Miaka 15, Mpango huu umekaa vizuri kwenda kutatua matatizo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali nzima ya Awamu ya Tano kwa kujifunza kutokana na uzoefu wa miaka mitano iliyotangulia na kuja na Mpango madhubuti utakaolijenga Taifa letu vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninavyouangalia Mpango huu na namna ulivyokaa, nina maeneo machache ambayo ningependa nishauri. Ukiangalia Mkoa wa Ruvuma ambao lango lake lipo katika Jimbo ninaloliongoza, Jimbo la Madaba unaona kwamba Mkoa wa Ruvuma umejaa fursa nyingi sana ambazo kama zitatumiwa vizuri na Mpango huu, kwa hakika Tanzania itakuwa nchi ya neema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zipo barabara muhimu ambazo zitatakiwa zijengwe na ziimarishwe ili Mpango huu wa viwanda uweze kuwanufaisha wananchi wa Jimbo la Madaba na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla ambao kwa asilimia kubwa wanachangia sana pato la Taifa na wanachangia sana chakula kinacholisha Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Madaba linapakana na Wilaya ya Ulanga, lakini kufika Wilaya ya Ulanga nahitaji kufika mpaka Mikumi na baadaye niende Ifakara ndipo niende Ulanga. Wakati wananchi wangu wa Kijiji cha Matumbi wanatumia siku sita kwa mguu au nne kufika katika Wilaya ya ulanga, lakini wanatumia siku mbili kwa mguu kufika mpakani mwa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na upande wa pili wa Malinyi.
Mheshimiwa Spika, hicho tayari ni kikwazo kikubwa sana cha uchumi kwa maendeleo ya maeneo yote mawili. Pamoja na kwamba Mpango huu bado haujabainisha nini kitafanyika, haujafafanua, nafikiri kwa sababu Mpango huu una sifa ya kujifunza kwa Mipango iliyotangulia, basi tuendelee kuangalia lile eneo ambalo linapakana na Jimbo la Madaba kama sehemu moja muhimu ambayo itachangia sana uchumi wa wananchi wa maeneo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia imeelezwa vizuri sana kwamba Mkoa wa Lindi unapakana na Mkoa wa Ruvuma, nalo ni eneo muhimu sana kama tunataka kuimarisha uchumi wa wananchi wale kupitia viwanda kwa sababu tunazalisha malighafi ya kutosha, tunahitaji kusafirisha, lakini tutazalisha bidhaa nyingi za viwandani, tutahitaji ziende Lindi, Ifakara, Mahenge na maeneo mengine ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa miaka mingi sana Mbunge aliyemtangulia Waziri Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mbunge Profesa Simon Mbilinyi, aliyestaafu, alianza kuongea sana kuhusu miradi ya NDC, hususan mradi wa Mchuchuma na Liganga. Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Peramiho, ambaye sasa kipande cha Jimbo lile kimekuwa Jimbo la Madaba, ninaloliongoza sasa, kwa miaka kumi amesimamia ajenda hiyo ya mradi wa Mchuchuma na Liganga.
Mheshimiwa Spika, mradi ule kama utafanikiwa kwa kiwango hiki ambacho umeelezwa katika Mpango huu, kwa hakika utatukomboa sana wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, utawakomboa sana wananchi wa Madaba na Jimbo la Peramiho. (Makofi)
Mheshimwa Spika, ni vizuri sasa, kwa vile maandalizi ya kuanza ku-explore ule mradi wa Liganga Mchuchuma, ni vyema sasa barabara inayotoka Wilaya ya Ludewa kufika Madaba iimarishwe ili kwamba wananchi wa pale waweze kunufaika na ule uchumi, lakini pia ndiyo barabara inayokuja kuunganisha na barabara ya Makambako kuja Dar es Salaam, kwa ajili ya kusafirisha mali na bidhaa zitakazozalishwa katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, tuna usemi wa Kiswahili, Waswahili wanasema, “Siku ya kufa nyani, miti inateleza.” Wakati nipo nje ya Bunge hili, kuna wakati nilikuwa naona kuna baadhi ya hoja zenye mashiko kutoka upande wa pili wa upande wangu wa kulia, lakini kadri ninavyozidi kukaa ndani ya Bunge hili, katika hiki kipindi cha miezi kama sita hivi nimekaa hapa, nazidi kuona kwamba hoja zenye mashiko zinazidi kupungua. Naamini sasa kweli miti inateleza. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna wakati ambapo hoja ya ufisadi ndiyo ilikuwa mhimili mkubwa wa kushikilia. Leo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli alipoisimamia hoja ya kutumbua majipu na kuondoa mafisadi, wale wale ambao walikuwa wameshikilia hiyo nguzo, wanamlalamikia na wanamlaumu. Ama kweli Waheshimiwa Wabunge ni lazima tujipime wakati mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inanisikitisha sana ninapoona mtu anaji-contradict mwanzo hadi mwisho wa hotuba yake. Anaanza na kusema Baraza la Mawaziri halifanyi kazi, halifai. Baraza hili ni lile lile la Awamu ya Nne, wanabadilishana nafasi, halafu baadaye anasema Mheshimiwa Waziri fulani umenifaa sana, unafanya sana kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuishi kwa contradiction. Lazima tuwe na consistent katika hoja zetu. Leo nimependa sana…
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, lazima ni-declare interest, approach aliyoitumia Mheshimiwa Ally Saleh, imetujenga sana na imemsaidia sana Waziri wa Fedha kuweza kuboresha Mpango huu wa Miaka mitano wa Maendeleo. Napenda sana tutumie approach hiyo ili kuisaidia nchi yetu na kuwasaidia Mawaziri waweze kutuletea majibu yanayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunalo eneo lingine muhimu sana kwa Jimbo la Madaba…
TAARIFA
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa kanuni ya 68 (8)!
SPIKA: Mheshimiwa Joseph, naona kuna taarifa ambayo haivumiliki...
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika ahsante. Taarifa hiyo siipokei kwa sababu wale ambao walileta ushahidi ndani ya Bunge hili, mimi nikiwa nje ya Bunge hili, kwamba Mheshimiwa Lowassa ni mmoja katika mafisadi wakubwa, ndio hao hao waliomkumbatia na kwenda naye katika kampeni ya Awamu hii ya Tano. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)
MBUNGE FULANI: Wanafiki wakubwa!
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, kwa namna yoyote siwezi kuipokea hiyo taarifa. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mhagama, muda wako umekwisha. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nikushukuru wewe binafsi kwa kunifanya kuwa mchangiaji wa pili kwa hotuba hii iliyotukuka ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii ambayo imebeba maudhui ya Wizara zote, imesheheni mipango na mikakati madhubuti ambayo kama itatekelezwa hivi ambavyo imewekwa, kwa hakika itatutoa Watanzania hapa tulipo leo na kutufikisha kwenye maisha ya uchumi wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Wazari Mkuu kwa hotuba hii nzuri, pia niwapongeze sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili, ambao pia wameleta hotuba yao mbele ya Bunge lako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika tu kwamba kwa bahati mbaya nilitarajia nipate mawazo mbadala, lakini yameshindikana, hata hivi nadhani tutakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikubaliane na mipango pamoja na mikakati yote ambayo hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imebeba. Maeneo ambayo nilipeda nitoe ushauri na niiombe Ofisi ya Waziri Mkuu kuifanyia kazi, katika kipindi hiki cha mwaka 2016/2017, moja ni Kitengo cha Maafa.
Katika hiki Kitengo cha Maafa kwanza nimpongeze sana Mkurugenzi wa Kitengo hiki kwa kazi yake nzuri anayoifanya mpaka sasa, licha ya changamoto alizonazo zinazoendana na ukosefu wa nyenzo za kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupitia makabrasha ya kitengo hiki, nilibaini kwamba pamoja na nia nzuri ya kitengo hiki kukabiliana na maafa, pamoja na jitihada nyingi zilizofanyika kuwajengea uwezo wanaofanya kazi katika kitengo hiki, bado kitengo hiki hakijawa na nguvu ya kutosha kuweza kukabiliana na changamoto za maafa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe jitihada za makusudi zifanyike kuhakikisha kwamba kitengo hiki, pamoja na kujengewa uwezo wa kinadharia ambao kwa sasa wameendelea kujengewe kupitia miradi mbalimbali ingefaa pia kitengo hiki sasa kiwe na vituo maalumu vyenye nyenzo maalumu za kuweza kukabiliana na maafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ni kwamba wakati Dodoma na Kondoa wanalia kwelea kwelea responsiveness ya kitengo kinachohusu maafa ilikuwa ndogo sana, huu ni ushahidi kwamba bado tuna changamoto kubwa kwenye eneo hili, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie kuhakikisha kwamba tunafanyia kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nilipenda nichangie ni eneo la elimu. Wakati nachangia jana nilimueleza Mheshimiwa Spika kuhusu hali ya Jimbo langu la Madaba. Jimbo letu la Madaba ni Jimbo changa lina takribani miezi michache sana na Halmashauri ya Wilaya nayo ina miezi michache tu. Lakini upande wa elimu kama ilivyo katika maeneo mengine tuna changamoto nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao walimu zaidi ya 412 ndani ya Wilaya ya Songea, walimu hao Wilaya ya Songea inahusisha pia Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, walimu hawajapandishwa madaraja kwa muda mrefu pamoja na kwamba wana hizo sifa. Nimeomba Chama cha Walimu kiniwasilishie nyaraka mbalimbali ambazo nitaziwakilisha katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili mtusaidie kutanzua tatizo hili kwa sababu ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya elimu katika Halmashauri yetu na Wilaya ya Songea kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo ningependa nitoe mchango wa kina ni eneo la soko la mazao ya mahindi. Kama unavyojua Mkoa wa Ruvuma ni ghala la Taifa la chakula. Mkoa huu kwa miaka mingi umeendelea kuzalisha chakula cha kuwalisha Watanzania, katika Mkoa huu Halmashauri Wilaya ya Madaba, Jimbo la Madaba lina wakulima ambao wanazalisha sana mahindi ambayo yanachangia sana kwenye chakula cha Taifa letu. Kwa bahati mbaya mfumo wa manunuzi wa haya mahindi bado siyo rafiki kwa wananchi wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa bado tunategemea kituo kimoja cha Madaba, yapo maghala katika kila Kata yanajengwa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Chakula kwa kupitia mradi wa BRN. Maghala haya mpaka sasa hayajakamilika, na ujenzi wake umesimama kwa muda mrefuwakandarasi bado wanalalamika hawajalipwa.
Naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati tunaendelea na mchakato huu tuhakikishe kwamba ule mchakato ambao umesimama katika vijiji vyote vya Halmashauri ya Wilaya Madaba ya kujenga na kuimarisha maghala ukamilike kwa sababu wananchi wa Jimbo la Madaba wataanza kuvuna mwezi ujao na watahitaji kuhifadhi mazao yao. kama ambavyo ulisema mwenyewe Mheshimiwa Waziri Mkuu ulipotembelea Mkoa wa Ruvuma, ulishauri kwamba NFRA wanunue mahindi katika vituo vilivyoko vijijini ili kuwaondolea Wananchi adha ya kusafirisha mazao haya kuyapeleka katika vituo maalum vya mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri yetu ya Madaba pia inachangamoto kubwa sana ya maji. Mji wa Madaba pekee na Kijiji cha Mkongotema ndiyo wenye maji yanayotiririka, lakini wingi wa mabomba hauwiani na idadi ya wananchi waliopo. Ipo miradi iliyofadhiliwa na World Bank, miradi hii imetekelezwa katika vijiji vitatu vya Mkongotema, Lilondo na Maweso. Kwa bahati mbaya miradi ya Maweso na Lilondo imesimama kwa muda mrefu sana, kwa vyovyote vile jitihada zilizofanyika mpaka sasa kubwa na niishukuru sana Wizara husika kwa kutufikisha pale ambapo tumefika. Ninaomba sana tunapoendelea na mchakato huu zoezi hilo pia la kukamilisha hii miradi ya maji katika maeneo yaliyobaki liendelee, lakini pia niombe sana Mji wa Madaba una kilio sana cha maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu, pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo ambao wamekuja ndani ya Jimbo langu na kushirikiana na wananchi kutatua kero zinazowakabili kwenye eneo la afya na eneo la umeme. Hivi ninavyokuambia Mheshimiwa Sospeter Muhongo yupo kwenye mchakato wa kukamilisha umeme wa maeneo ya Mji wa Madaba na Mungu bariki Disemba tutakuwa na umeme, ninaniomba sana zoezi hili liendelee, wananchi wa Madaba wanatambua sana juhudi za Mheshimiwa Sospeter Muhongo, lakini pia wanatambua sana jitihada za Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu za kuhakikisha kwamba Madaba tunapata Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho na la muhimu sana ni kwamba tulipokuwa tunaelekea uchaguzi wa mwaka 2015 vipo vijiji vingi vilivyozaliwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kama ambavyo vilizaliwa katika maeneo mengine ya Songea Vijijini. Vijiji hivi bado havijapata usajili wa kuduma na kama vimepata havija…
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napongeza sana hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba Madelu. Hotuba hii imesheheni mipango na mikakati madhubuti ya kuliondoa kundi la Watanzania wafikiao asilimia 80 na kuwafikisha kwenye uchumi wa kati. Umadhubuti wa Mipango na Mikakati iliyopo katika hotuba hii ni kielelezo cha umadhubuti wa Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba. Napenda nimthibitishie kuwa wananchi ninaowawakilisha, Jimbo la Maduba wanatambua sana umahiri na umadhubuti wa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielekeze mchango wangu katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni matumizi ya mbegu bora za kilimo. Kadiri ya Utafiti wa Masalwala (2013), asilimia 93 ya mbegu zinazotumiwa na wakulima katika misimu mbalimbali ni recycled from previous crops. Hii inatokana na gharama za mbegu hizo, upatikanaji, ubora wa mbegu hizo na uelewa wa wakulima juu ya matumizi na umuhimu wa mbegu hizo. Napongeza kuwa Wizara imeliona hilo na tayari imejipanga kuongeza uzalishaji wa mbegu kutoka tani 10,270.86 hadi tani 40,000 ikiwa ni mara nne. Ni hatua kubwa sana. Naomba Wizara isimamie hili, tujipime kwa kiasi hiki na mwaka ujao twende mbali zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ni muhimu katika mikakati ya kufanikisha zoezi hili, makampuni ya ndani yapate kipaumbele kujengewa uwezo wa kuzalisha mbegu. Yapo makampuni yenye nia na yamethubutu kuanza. Ni vema yakapata ruzuku kuyawezesha kuzalisha mbegu za mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni mfumo wa upatikanaji wa pembejeo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba kwa kuamua sasa kupitia upya mfumo wa usambazaji wa pembejeo kwa kuzingatia malalamiko makubwa ya mfumo wa sasa wa ruzuku. Mkakati huu mpya ni mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu ni kuharakisha mapitio haya. Case studies ni nyingi, zipo Asasi na wadau wengi waliojaribisha models mbalimbali. Miongoni mwa wadau hao ni AGRA, SNV, RUCODIA, RUDI, BRTENS na kadhalika. Wadau hawa tayari wana models mbalimbali za usambazaji wa pembejeo. Jambo muhimu ni kwamba mfumo mzima wa usambazaji pembejeo uwe enterprise led. Ni vema Wizara ikakutana na wadau hao na kuchukua uzoefu wao katika suala zima la Agro-Dealers Development.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni mazingira wezeshi ya kilimo-biashara. Hotuba ya Mheshimiwa Mwigulu imefafanua vizuri mazingira wezeshi ya kilimo-biashara. Katika aliyosema Mheshimiwa Waziri, ningependa kuongeza yafuatayo:-
(i) Mafanikio ya kilimo yanategemea sana mafanikio ya miundombinu ya barabara vijijini, upatikanaji wa rasilimali fedha na elimu ya kilimo; na
(ii) Model ya mradi wa MIVARF uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni nzuri sana ya comprehensive approach ambayo kama Wizara itachukua model hizi, maendeleo ya kilimo chenye tija tutayapata kwa haraka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nne, Chuo cha Mafunzo ya Mifugo LITA (Madaba). Tunaomba chuo hiki kitoe pia mafunzo ya kilimo na kipandishwe hadhi na kuwa chuo kikuu kwani Mikoa ya Kusini mahitaji yetu katika eneo hilo ni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, kuhusu vikwazo vya kufikisha pembejeo (mbolea, viatilifu na mbegu bora) kwa wakulima wadogo vijijini na hivyo kupoteza tija; wakulima wengi wadogo wapo vijijini ambako ndiko pia shughuli za kilimo zinafanyika. Maduka ya pembejeo kwa sehemu kubwa yapo mijini. Tanzania mkulima mdogo apate pembejeo ni lazima asafiri hadi mjini kununua. Hili linaongeza gharama za uzalishaji kwa mkulima mdogo.

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza tija haina budi maduka ya pembejeo yasambae hadi vijijini ambako wakulima wapo. Katika maeneo mengi wajasiriamali vijijini wanafanya jitihada za kufungua maduka ya pembejeo ili kufikisha huduma karibu na wakulima. Jitihada hizi zinakwamishwa na gharama kubwa za vyeti vinavyotakiwa. Vyeti ni kama ifuatavyo:-

(1) TOSCI = 100,000.
(2) TPRI = 320,000.
(3) TFRA = gharama ya chakula wakati wa mafunzo. (4) TFDA = 100,000.
(5) Leseni = 71,000.

Jumla ni 591,000

Mheshimiwa Spika, gharama hizi ni kubwa sana, zinakatisha tamaa kwa wajasiriamali. Wapo wengi wameshindwa licha ya kushiriki mafunzo na kujengewa hamasa bado wameshindwa kufungua maduka. Mifano halisi ni, katika Mkoa wa Kagera wajasiriamali 461 walijengewa hamasa na kupata mafunzo ya biashara hiyo kupitia Shirika la AGRA matokeo yake ni kama ifuatavyo:-

Waliopata mafunzo na kujengewa hamasa ni 461, Cheti TOSCI (82), Cheti TFRA (108), Cheti TPRI (17), WALIOFUNGUA MADUKA (139)

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Kigoma, kati ya Wajasiriamali 704 waliojengewa hamasa na kupatiwa mafunzo ya biashara na Shirika la AGRA ni wajasiriamali 389 tu ndiyo wamefungua maduka. Aidha, wajasiriamali 159 walipata mafunzo na TFRA Mwezi Oktoba, 2018 lakini hadi leo hawajapata vyeti vya TFRA ili kuwezesha kuanzisha maduka ya pembejeo vijijini. Utaratibu huu kama hautabadilika, ukuaji wa sekta hii utaendelea kudorora.

Mheshimiwa Spika, ushauri; Serikali iangalie upya ada hizo (TOSCI, TFRA, TPRI, TFDA) ziangaliwe upya au Serikali ibebe huo mzigo ili kuwezesha ufikishaji mbolea, viatilifu, mbegu bora kwa wakulima wadogo.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nakushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi. Pili, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa uwasilishi wake mzuri. Pamoja na kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Waziri nina mambo mawili, matatu ya kuishauri hii Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, unajua habari ya viwanda Tanzania siyo habari ngeni. Tumekuwa na viwanda miaka ya 80 kuelekea miaka ya 90 na viwanda vingi vimekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, sehemu pekee au mkakati pekee ambao ameuweka ambao umeonekana wa namna ya kulinda viwanda vya ndani ni kuongeza kodi kwenye bidhaa zinazotoka nje, zile bidhaa ambazo tunaweza kuzizalisha ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maoni yangu huo ni mkakati mzuri, lakini mkakati huu pekee hautatosha kulinda viwanda vya mafuta ya kula, hautatosha kulinda viwanda vya sukari nchini, hautatosha kulinda viwanda vya nguo nchini. kwa sababu kikwazo cha viwanda vya Tanzania siyo tu ushindani wa bei za bidhaa zinazoingia, bali pia mikataba ambayo tunaingia na nchi marafiki ambao tunafanya nao biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyovyote vile, mikataba ile bado inatubana. Pengine hata kuweka hizo kodi kwenye hizo bidhaa huenda tukagomewa na wadau marafiki tunaofanya nao biashara kwa sababu na wao wanataka kulinda viwanda vyao. Kwa hiyo, naishauri Wizara ya Fedha ifanye kazi ya kina. Mwezi wa Pili nilitoa ushauri huu na sasa narudia tena kwa sababu mpaka sasa sijaona assessment ya kutosha ya ku-assess kwa nini tulifeli miaka ya 1980 na 1990 na kwa nini tunadhani tutafaulu katika kipindi hiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ni suala zima la maji. Sera ya Taifa inatutaka Watanzania wote popote walipo waweze kupata maji katika umbali usiozidi mita 400. Ukiiangalia sera hii na mpango mkakati uliowekwa na Wizara ya Fedha, havifanani kabisa. Kukata sh. 50/= kwenye mafuta ya petrol na diesel pekee, havitoshi. Kamati ya Bajeti imeshauri tuweke angalau sh. 100/= na baadhi ya Wabunge wameshauri tuweke angalau sh. 100/=. Nami naomba tuweke angalau sh. 100/= ili tuweze kusogea mbele kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Madaba ni moja katika Majimbo ambayo yana tabu sana ya maji. Hivi ninavyoongea, Kijiji cha Lilondo na Maweso toka miradi imeanza mwaka 2015, haijakamilika na Wakandarasi bado wanahangaika kulipwa. Naishukuru Wizara ya Maji, tunawasiliana kwa jambo hili, lakini huu ni ushahidi kwamba kuna matatizo ya kutosha kwenye hili eneo, tulitengee bajeti ya kutosha kwa kuzingatia ushauri wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni ombi kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango avae viatu vya Walimu wa Sekondari na Shule za Msingi ambao katika uhai wao wote wanalitumikia Taifa hili, mishahara yao inakatwa kodi na wanapomaliza kipindi cha utumishi wanalipwa kiinua mgongo na kinakatwa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri avae viatu vya watumishi wengine wa Serikali na Sekta ya Umma ambao mishahara yao ni ya chini, wanakatwa kodi, wanafanya kazi, lakini wanapomaliza utumishi wao, bado kiinua mgogo kinakatwa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lililopita lilienda hatua mbele, likaiomba Serikali iondoe kodi kwenye hivi viinua mgongo, yaani kwenye mafao ya wafanyakazi. Nilitegemea Wizara ya Fedha ije na mkakati huo sasa wa kuondoa hizo kodi kwenye mafao ya wafanyakazi na kupendekeza njia mbadala ya kupata fedha kwa ajili ya kuendeshea Serikali, kwa sababu hawa wafanyakazi wameendelea kukatwa kodi wakati wote. Kilichonishangaza, tunazidi kurudi nyuma. Tulishapiga hatua mbili mbele, tunarudi hatua nne nyuma, tunaanza sasa kufikiria kukata kodi kwenye mafao ya Wabunge. Tunakwenda wapi? Tutafika lini tunakotaka kwenda kuwatengenezea Watanzania maisha bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri avae viatu vya Wabunge wanaotoka katika Majimbo yenye changamoto kama Jimbo la Madaba. Mbunge wa Madaba akishapata posho humu Bungeni, anakwenda kununua solar kuweka kwenye Vituo vya Afya. Anakwenda kuchangia maji Matetereka ili wananchi wapate maji kwa sababu Serikali bado haijaweza kufikia wananchi hao.…
Nasikitika sana ninapoambiwa kwamba...
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Makatibu Wakuu wa Wizara hii wote wawili pamoja na Wakurugenzi kwenye Wizara hii. Mimi nimefanya kazi nao na nime-interact nao, watu hawa ni watu makini sana na iwapo Bunge lako litawashauri vizuri, tutapata mapinduzi makubwa sana kwenye sekta hii, hiyo ndiyo imani yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo sikupenda nichangie kwa sababu ya mazingira yalivyo na mfumo na muundo wa Wizara hii bado haunishawishi kwamba maoni yetu yanaweza kuzaa matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye mapori yote ya Mikoa ya Rukwa, Ruvuma, Tabora, Katavi, mikoa yote ambayo wewe unaifahamu ambayo haikuwa na mifugo, mapori yote yamejaa ng’ombe. Madhara yake ni nini?

Mheshimiwa Spika, madhara yake ni kwamba katika muda mfupi ambao unaweza ukaupima kabisa kwa miaka, Tanzania inakwenda kuwa jangwa; na kwa nini tumefikia hapo? Tumefikia hapo kwa sababu wafugaji wetu kwanza hawana ardhi ya kufugia; lakini pili, hakuna malisho. Kwa hiyo wanahama, wanasafiri, wanakwenda, wanajaribu kuhangaika; lakini la tatu; ubora wa mifugo yetu ni duni, tunafuga wanyama wengi lakini tija ndogo kwenye ufugaji. Hizo ni baadhi ya sababu ambazo nilitaka nizitaje.

Mheshimiwa Spika, nafasi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kumaliza tatizo hili ni ndogo kwa sababu tatizo la kuhama wafugaji halihusu Wizara ya Mifugo peke yake na ndiyo maana nilikuwa nachelea kushauri Bunge lako liishauri Serikali iunde tume au iunde coordination team ambayo itahusisha Wizara zisizopungua tano, wafanye pamoja kazi hii ya kuratibu ufugaji nchini.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wanahitaji ardhi, wanamuhitaji Waziri wa Ardhi, wanapotaka kuingia kwenye eneo kuna Maliasili, kuna Kilimo, kuna Mazingira, Wizara hizi zote kama hazitaamua kufanya kazi pamoja hatutakuwa na ufugaji bora nchini, tuta-fail tu. (Makofi)

SPIKA: Nakuongezea na Wizara ya Maji.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, na Wizara ya Maji, ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niombe na nashindwa kwenda zaidi, hatuwezi kutoka hapa tulipo. Leo nchi hii inakwenda kuwa jangwa. Mimi ni mfugaji na nina ranchi, ninafuga lakini nikienda Songea Vijijini kila pori wapo wafugaji na ukiwauliza wanasema hatuna pa kufugia, hatuna ardhi.

Mheshimiwa Spika, leo tunashauri kwamba wapewe ranchi za Serikali, well and good, lakini kama hatuwajengei uwezo wa kuzalisha chakula cha mifugo kwa maana ya pastures, uwezo wa kutengeneza visima vya maji, uwezo wa kuzalisha ng’ombe bora, hatutamaliza tatizo hili kwa sababu tutamaliza hizi ranchi za Serikali lakini bado zitakuwa hazitoshi kwa sababu ng’ombe ni wengi sana.

Mheshimiwa Spika, mimi nikuombe na nitashika shilingi baadaye; Serikali ianzishe coordination team ya kuratibu ufugaji nchini. Ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mpango kwa kuleta mwelekeo wa Mpango huu, ili ujadiliwe na Bunge lako na mimi kupata nafasi ya kutoa mawazo yangu, lakini nasikitika itabidi nitumie sehemu ya muda wangu mzuri kuweza kueleza maeneo ambayo pengine yalikuwa very obvious.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya michango yetu inaonesha kwamba baadhi ya Wabunge tume-panic na Wabunge wengi tulio-panic tunaufanya umma wa Watanzania u-panic. Na ukifuatilia vitu vinavyotufanya tu-panic vinakosa mantiki na leo mbele ya Bunge lako Tukufu nalazimika kuongea kwa kutumia analogia kwa sababu ndio namna pekee ambayo nadhani nitaeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka kadhaa iliyopita hapa Dodoma watu wote wakiwemo Wabunge walikuwa wanakutana pale Chako ni Chako wanakula kuku. Miaka mitatu/minne baadaye sehemu mbalimbali zinazotoa huduma kama za Chako ni Chako zimefunguliwa na wateja wanachagua sehemu za kwenda, it is very natural. Miaka kadhaa iliyopita, labda kabla sijafika huko, kama unaishi mtaani, nasema ninatumia analogia, lugha rahisi kabisa na mifano rahisi, kama unakaa mtaani na katika mtaa wako unapakana na mitaa mingine minne/mitano katika mitaa hiyo mitano hakuna baa, kuna baa moja tu katika mtaa wako watu wote wanaokunywa katika maeneo hayo watakunywa katika baa yako, lakini siku mtaa wa tatu wamefungua baa tabia ya walevi ni kwenda kujaribu katika baa nyingine pia. Lakini wakiwa kule wataweza kulinganisha na ubora wa huduma ya baa yako; hiyo ndio lugha ya analogia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaendesha Bandari yetu ya Dar es Salaam bandari nyingine zimefuata baadae na kwa kawaida kwa tabia ya watu hupenda kujaribu. Leo bandari nyingine zipo kwa vyovyote vile huwezi kubaki na wateja wale wale ambao ulikuwanao kwa kipindi chote. Hiyo ni lugha rahisi, Watanzania tusiyumbishwe na kauli za baadhi ya Wabunge kuonyesha kwamba sababu za kupungua mizigo bandarini zinahusiana moja kwa moja na mambo ya kodi, si kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, hilo haliondoi jukumu la Waziri wa Fedha kuendelea kuchunguza sababu mbalimbali za kupungua wateja, lakini sababu nyingine ndio hizo. Lazima kazi ya ziada ifanyike ili kuweza kuvuta wateja zaidi na kuweza kuimarisha bandari yetu ili iweze kuchangia mapato zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana kuona baadhi ya Wabunge tunawalilia wafanyabiashara makanjanja. Ni ajabu kuona kwamba katika bandari ile ile ambayo tunasema kwamba mizigo imepungua, mapato yameongezeka, mantiki yake ni nini? Mantiki yake ni rahisi tu, wale ambao walizoea ubabaishaji wameenda kubahatisha maeneo mengine labda wakabahatishe kubabaisha. Lakini wafanyabiashara makini wanaendela kutumia bandari yetu na hao ndio wanaotupa mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi kwenye eneo hilo ni upotoshwaji wa mantiki nzima ya kusimamia matumizi na kukusanya kodi. Humu ndani baadhi yetu wametafsiri kama kubana matumizi; sijaona mantiki, bajeti ya mwaka jana tunayoimaliza mwaka huu ni shilingi trilioni 29 na mpango huu unatupeleka kwenye shilingi trilioni 32. Hiyo sio kubana matumizi, Serikali ya Awamu ya Tano inachokifanya ni kusimamia matumizi, kuna utofauti kati ya kubana matumizi na kusimamia matumizi. Serikali inachokifanya ni kuhakikisha inaongeza efficiency katika matumizi ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale maeneo ambayo hayana tija Serikali imepunguza kupeleka pesa na badala yake imepeleka maeneo yenye tija zaidi. Kwa hiyo, Watanzania tuelewe kwamba hatujabana matumizi isipokuwa tunapeleka fedha maeneo yenye tija zaidi, maeneo ambayo yatakuza uchumi zaidi na ndio maana bajeti imetoka toka shilingi trilioni 29 kwenda shilingi trilioni 32, hiyo ndio mantiki, ni kusimamia matumizi. Sasa wale waliozoea fedha rahisi, wale waliozoea ubabaishaji hilo nalo linawaumiza. Niwaombe Watanzania makini, wanaolipenda Taifa hili wamuunge mkono Mheshimiwa Rais katika jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuhakikishia katikati ya giza nene ndipo inakaribia asubuhi, hapa tulipo ndipo wakati sahihi kunakaribia kucha. Mheshimiwa Zitto Kabwe alisema lazima kuwe na maumivu tunapotaka kufanya mabadiliko makubwa kama haya. Tukumbuke miongoni mwetu baadhi ya Watanzania walizoea fedha rahisi, walizoweza leo anaanzisha biashara ya shilingi milioni 10 na kila mwezi anapata faida ya shilingi milioni tano kwa sababu, alikuwa anakwepa kodi. Tumueleze mantiki ya kodi na tumueleze kwamba biashara zinakuwa steadly, hatua kwa hatua. Watanzania makini hawana tatizo na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Mpango atoe ushirikiano na Mawaziri wengine waendelee kuasimamia matumizi ya Serikali na kuelekeza pesa katika maeneo yenye tija zaidi kwa Watanzania. Hilo lilikuwa kuweka tu mazingira sawa kwa sababu niliona linapotoshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa ambalo leo nilitaka nichangie ni dhana nzima ya kukuza viwanda. Katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tumeweka bayana aina gani ya viwanda vitatutoa Tanzania kwa haraka zaidi. Tulisema tuwekeze kwenye viwanda vinavyosindika zaidi mazao ya kilimo kwa lengo kwanza la kumuwezesha mkulima mdogo apate soko la mazao yake, lakini pia kutoa ajira kubwa zaidi kwa Watanzania. Katika mpango tulioupata hilo halijawekwa bayana, tumeongelea viwanda vya General Tyre, tumeongelea viwanda vingine ambavyo kimsingi havigusi asilimia 80 ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosikitika kwenye mpango huu ni kwamba hatujaoanisha vizuri ile Ilani ya Chama cha Mapinduzi na huu mpango. Tunapowekeza nguvu nyingi kwenye kushughulikia viwanda tumesema ni jambo zuri, Magadi ya Soda - Bonde la Engaruka, tumeongea viwanda chini ya TEMCO na nini, lakini viwanda hivi katika ujumla wake haviendi kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu walio asilimia kubwa na wala haliendi kutatua tatizo la soko la mazao yetu ya kilimo. Kwa hiyo, niishauri sana Serikali kwenye hili lazima turudi tukafanye kazi upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine kwa haraka haraka, tunahangaika sana na soko la mahindi ni vema katika mpango huu sasa ikawekwa bayana. Kinachomfanya mkulima akalime ni bei ya mazao. Tunatoa ruzuku, lakini bado wakulima hawazalishi kwa tija kwa sababu hawapati faida katika uzalishaji wao. Ipo haja sasa ya kuja na sera madhubuti itakayomfanya mkulima mdogo wa Tanzania awe huru kuuza mazao yake kokote na wakati wowote. Leo ukienda kila mahali pikipiki zimejaa, Serikali imetoa ruzuku sana kwenye power tiller, lakini huzioni kokote kwa sababu hazina manufaa
kwenye kilimo chao, lakini watu wangapi wananunua yebo yebo kwa sababu hizo bodaboda kwa sababu wanajua zinawalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutajenga mazingira mazuri kwenye sekta ya kilimo hatutahitaji kugharamia mbolea za ruzuku tena. Tujenge mazingira yenye ushindani kwenye sekta ya kilimo, tuwaache wakulima wadogo wauze mazao yao wanakotaka, anayetaka kupeleka Malawi, anayetaka kwenda Zambia na kama Serikali inataka kununua iingie kwenye ushindani. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumemuwezesha sana mkulima mdogo na wala hatutahangaika habari za kutafuta pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia muda ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nikushukuru wewe lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2017/2018. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmoja kati ya Wabunge waliobahatika kuwa katika Kamati ya Katiba na Sheria, Kamati ambayo inafanya kazi kwa karibu sana na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara zote zilizopo chini yake. Tumebahatika kujua mambo mengi na kujifunza mengi na nikuthibitishie kabisa kwamba Ofisi hii na Wizara zake zote wapo vizuri sana katika kuwatumikia Watanzania. Nikuombe wewe na Bunge zima kuunga mkono jitihada za Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa kuzingatia muda naomba nijikite kwenye eneo moja muhimu sana ambalo linagusa asilimia 90 ya Watanzania ambalo liko katika ukurasa wa 21 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu kulimo. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2012 asilimia 85 - 90 ya Watanzania tunaishi kwa kutegemea kilimo au moja kwa moja, kibiashara au kwa namna nyingine lakini asilimia 90 ya Watanzania tunategemea kilimo. Kwa mujibu wa sensa ya kilimo na mifugo ya hivi karibuni inatupa takwimu hizo za asilimia 85 - 90 lakini sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inatueleza idadi ya Watanzania ambao tupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 21 kwa taarifa tulizonazo, uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2015/2016 ukijumuisha mazao ya nafaka na yasiyo ya nafaka tumezalisha jumla ya tani milioni 16. Tani hizi milioni 16 maana yake zimezalishwa na asilimia 85 ya Watanzania kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012. Kama hivyo ndivyo maana yake kila Mtanzania anayetegemea kilimo amezalisha tani 0.34 au sawa na gunia nne tu za mahindi kwa mwaka mzima wa 2015/2016. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunaambiwa ziada ya mazao ya nafaka na yasiyo ya nafaka ni tani milioni tatu. Tukizigawa kwa idadi ya Watanzania wanaotegemea kilimo ambao ni asilimia 85 tunapata ziada ya tani 0.07 ambayo sawa na gunia moja tu la ziada. Kwa hiyo, ukiangalia kwa takwimu hizi maana yake Watanzania tunaotegemea kilimo asilimia 85 - 90 kila kaya au kila mtu amezalisha gunia nne za
mahindi na ametumia gunia tatu kwa chakula na amebaki na ziada ya gunia moja. Tanzania ya viwanda hatutaweza kuifikia kwa kasi hiyo ndogo kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naelewa kwa nini asilimia kubwa ya Watanzania hatuna pesa mifukoni ni kwa sababu ziada yetu ni ndogo sana tani 0.07 kwa maana ya gunia moja tu la mahindi kwa mwaka mzima sawa na Sh.35,000 – Sh.50,000. Ziada hii ni ndogo maana yake kilimo katika Taifa letu kinakua taratibu mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tumefika hapo? Kwa nini uzalishaji wetu uwe mdogo kiasi hicho? Tani milioni 16 za chakula siyo jambo la kujivunia. Tumefika hapo kwa sababu kubwa mbili. Moja, kilimo chetu hakina dira. Watanzania na taifa hatujui kwenye sekta ya kilimo tunatafuta nini. Tuna maneno ya jumla ya kusema kwamba tunataka ku-address food security, very good. Kwenye food security tumefaulu, Tanzania hakuna njaa mgawanyo wa chakula ukiwa vizuri kila kaya ina uwezo wa kujilisha, kwa hiyo, kwenye hilo tumefaulu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini malengo yetu kwenye sekta ya kilimo siyo ku-address food security pekee. Sekta ya kilimo pamoja na kuwa inakwenda ku-address food security kwa maana ya uhakika wa chakula, sekta hii ya kilimo inawaajiri Watanzania asilimia 90. Kwa hiyo, lazima tutoke hapo kwenye food security twende sasa kukifanya kilimo chetu kiwe biashara na kiwe chanzo cha mapato kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Serikali tumefanya vizuri kwenye suala zima la uhakika wa chakula lakini bado tuna kazi sasa ya kuwafanya asilimia 85 - 90 ya Watanzania wanaotegemea kilimo waweze kujiajiri katika sekta hiyo. Kwa hiyo, ni vizuri sasa Wizara ya Kilimo itoe dira ni nini kama Taifa tunataka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ni kwamba kilimo chetu siyo demand driven, hatulimi kwa kuzingatia mahitaji ya soko. Kama tunataka kujitosheleza kwa chakula tulime mazao gani na kwa kiwango gani, uwezo wetu wa ndani wa ku-consume kile ambacho tunazalisha ni upi na
ziada tunaipeleka wapi. Tumeona sekta ya kilimo inayumba sana kwenye eneo la masoko. Mara tunafunga mipaka tusipeleke mazao nje, mara tunafungua mipaka, hatuna uwezo wa ku-forecast production zetu katika sekta hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo ni tatizo na napenda sana Wizara inayohusika ichukue muda wa kutosha kufanya consultation na wataalam mbalimbali lakini hasa na Wabunge wa Bunge hili kwa sababu Wabunge hawa ndiyo wanaoishi na wananchi, ndiyo wanaojua matatizo ya wananchi na sisi ndiyo tunaolima mahindi, maharage, mpunga, soya na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la pili kwenye sekta ya kilimo ni uwezeshaji katika sekta hii umekuwa mdogo sana na uwezeshaji huu wakati mwingine umekuwa holela usiozingatia mahitaji halisi. Serikali imebeba mzigo mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba Watanzania tunapata pembejeo zenye ubora ikiwemo mbolea na kadhalika na zinakwenda kusaidia kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kukushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi na nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu sana ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia katika maeneo makubwa mawili na iwapo muda utaniruhusu, nitaongeza sehemu ya tatu. Kwanza kabisa, niungane na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamempongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kupitia Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Nisingependa kurudia maneno mazuri ambayo Wabunge wengi wamesema kuhusu kazi nzuri zilizofanyika, Tanzania sasa imeunganishwa kwa barabara nyingi, inaunganishwa kwa reli, lakini inaunganishwa kwa anga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kutambua mchango mkubwa sana wa Mawaziri kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais na kesho sisi wadau wa Mkoa wa Ruvuma tutakuwa pale Songea tarehe 30 kupokea ndege aina ya Bombardier ikitua kwa mara ya kwanza katika Mji wa Songea. Kwa hiyo, ni kazi nzuri ya Wizara hii, nachukua nafasi hii kuipongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo matatu ambayo napenda niishauri Wizara au Serikali katika ujumla wake. Eneo la kwanza, hii miradi tunayowekeza ni mikubwa sana. Wizara ya Nishati inawekeza katika miradi mikubwa sana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nao wanawekeza katika miradi mikubwa sana. Wizara hizi mbili, ili miradi hii inayowekezwa iweze kuwa na tija, ni muhimu sana hizi Wizara mbili zikafanya kazi kwa ukaribu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua sisi Jimbo la Madaba tunapakana na eneo lenye mradi mkubwa sana, tunaita Flagship Projects pale Liganga na Mchuchuma. Huu ni mradi mkubwa sana na ni mradi ambao umezungumziwa kwanza kabisa na Mheshimiwa Profesa Simon Mbilinyi, baadaye akafuatia Mheshimiwa Waziri Jenister Mhagama. Mimi leo ni Mbunge wa tatu katika Bunge lako kuzungumzia mradi huu kutoka eneo hilo hilo la Jimbo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu umechukua muda mrefu sana, lakini sasa mradi huu una matumaini makubwa ya kuanza; na taratibu zote za kuanza zimekamilika na tutaisikia kwenye Wizara wa Nishati na Madini watakapowakilisha. Kinachosikitisha ni kwamba hakuna maandalizi ya kutosha kuhakikisha kwamba barabara zinazokwenda kwenye mradi huu mkubwa zinakamilika. Huwezi kuzungumzia Mradi wa Lingaganga na Mchuchuma bila kuzungumzia barabara inayotoka Madaba kwenda Mkiyu - Linganga. Utawezaje kusafirisha mitambo kwenda katika eneo la mradi? Utawezaje kuvuna makaa na chuma kutoka katika eneo la mradi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, yawezekana Wizara kwa sababu moja au nyingine na yawezekana ni sababu za msingi kwamba hawajaweka bajeti ya kutosha ya kukamilisha barabara hii kwa kiwango cha lami, nawaomba Wizara, kama kweli tupo serious na kama kweli Miradi ya Mchuchuma na Linganga inaanza, lazima barabara ya Madaba - Mkiyu ikamilike. La sivyo, tutaiingiza Serikali kwenye hasara kubwa sana. Mradi upo tayari kuanza lakini barabara ya kwenda kwenye mradi haipo. Hatuwezi kufanikiwa tusipoweza kuunganisha haya mambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili linahusu Mfuko wa Barabara Vijijini. TAMISEMI wanapata asilimia 30 ya fedha zote zinazokusanywa kwa ajili ya Mfuko wa Barabara na asilimia 60 inabaki kwa TANROADs kwa ajili ya kushughulikia barabara za mikoa na hii asilimia 30 inakwenda TAMISEMI na inakuwa translated kwenye kutekeleza miradi ya barabara ndani ya Halmashauri. TAMISEMI wanakuja na wazo kwamba tuwe na Rural Road Agency, hili wazo ukiliangalia kwa haraka, linaonekana kama ni zuri na lenye tija, lakini niliomba ni-draw attention ya TAMISEMI na Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano. Kwanza lazima tujue kwamba kama kumekuwa na ufanisi katika ngazi za Halmashauri zetu, ni kwa sababu wale wanaofanya kazi katika Halmashauri za Wilaya wapo accountable moja kwa moja kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hiyo sense of accountability ndiyo inayofanya Halmashauri zetu ziwe na tija (efficiency) kwa sababu anayesimamia miradi katika Halmashauri ni Diwani ambaye yupo karibu na wananchi, anajua matatizo ya wananchi na anawajibika kwa wananchi. So sense of accountability imeleta tija sana katika utekelezaji wa miradi katika ngazi ya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukilinganisha na taasisi au agency mbalimbali zinazoundwa zenye hadhi ya Kitaifa sense of accountability haiwezi kuwa sawa. Halmashauri sense ya accountability ni kubwa zaidi. Naomba sana, tusi-attempt kutengeza huu Mfuko wa Barabara Vijijini, isipokuwa fedha hizi zigawanywe kwa uwiano sawa katika Halmashauri na ziendelee kusimamiwa na Halmashauri za Wilaya zetu. Italeta tija zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine najua TANROADs hakuna urasimu sana, lakini taasisi yoyote yenye muundo ina urasimu. Halmashauri zina urasimu, TANROADs wana urasimu na Taasisi yoyote ina urasimu kwa sababu ya muundo wake. Sasa ukilinganisha level ya urasimu katika Taasisi za Kitaifa na Halmashauri, Halmashauri level ya urasimu ipo chini sana. Kwa hiyo, tutumie hiyo fursa sasa kupeleka hizi fedha zikafanye kazi kwa tija katika Halmashauri, tukiziacha kwenye ngazi hizo za juu hatutapata ufanisi. (Makofi)
Mheshimwa Naibu Spika, pia ningeweza kusema, kwangu mimi kufikiria kutengeneza hii tunayoita Mfuko wa Barabara Vijijini kwa maana ya Rural Road Agency, katika context ile ile na mfananisho ule ule wa TANROADs ni jaribio la kudhoofisha dhana ya ugatuzi wa madaraka. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ifanye study upya ya efficiency za Halmashauri zetu ukilinganisha na efficiency ya agency mbalimbali zenye hadhi ya Kitaifa ili kuleta tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kama muda unaniruhusu, nichangie tu kwamba ukisoma katika hiki kitabu unaona kumekuwa na shida kidogo katika allocations za projects. Ipo mikoa ambayo imepata miradi mingi zaidi kuliko mingine. Sababu zinaweza zikawa za msingi kwa maana ya mahitaji halisi, lakini ni vizuri sasa niiombe Serikali iangalie priorities nyingine pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tumewekeza fedha nyingi sana kujenga Jiji la Dar es Salaam ambalo lina wananchi milioni tatu na zaidi kidogo…
Wanakaribia milioni tano, lakini tukumbuke pia mahitaji katika maeneo mengine ni muhimu pia. Naiomba Serikali sasa iangalie, ifanye rationalization ya miradi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile muda hauniruhusu, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wote, wanaompongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana anayoifanya kwa Watanzania.

Pili, nipongeze sana Serikali kwa kuleta mpango huu na bajeti hii ya mwaka 2017/2018. Ni bajeti ya kipekee sana ambayo inagusa maeneo yote makubwa ambayo kama ya tatekelezwa vizuri, yatawatoa Watanzania na kuwafikisha kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maslahi ya muda, kwanza niishukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kuitazama kwa namna ya pekee sana Halmashauri yetu ya Wilaya ya Madaba na Jimbo la Madaba. Kimsingi kushukuru ni kuomba tena, wana Madaba katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, tumeona maendeleo makubwa sana katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya, maji, nishati na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri na Wizara zenu, lakini zaidi Mheshimiwa Rais ambaye amewakabidhi haya majukumu. Wana Madaba tunatambua mchango mkubwa wa Serikali kwa maendeleo yetu na ninaamini tutaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali hii kwa sababu tunaamini ndani ya kipindi cha miaka mitano wana Madaba tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana ya kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango mkubwa ambao nilitaka niutoe kwako na kwa Wabunge leo hasa kwa Serikali, ni mahusiano ya kilimo na Tanzania ya viwanda. Kwa Muktadha wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015/2020. Ukitazama katika Ilani yetu, kipaumbele cha Awamu ya Tano ni kuwa na viwanda Tanzania nzima ili kutoa ajira kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sehemu kubwa Serikali imeweka misingi imara ya kutengeneza au yakujenga Tanzania ya viwanda. Miaka miwili tu baada ya kuanza Serikali hii au mwaka mmoja na nusu, tayari tunaona viwanda vingi vinajengwa. Hata hivyo ninaomba niikumbushe Wizara na niikumbushe Serikali kwamba aina ya viwanda vinavyojengwa, pamoja na kwamba ni viwanda vizuri, lakini aina hii bado haiendi kujibu kwa namna inavyotakiwa mahitaji makubwa ya Watanzania wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi, inatutaka aina ya viwanda ambavyo vinatakiwa tuvijenge sana ni vile ambavyo vitaongeza thamani ya mazao yetu na hivi kutoa soko na kuongeza kipato kwa mwananchi mkulima.

Tukumbuke kwamba Watanzania asilimia 80 tunaishi kwa kutegemea kilimo, tunategemea masoko mazuri ya kilimo na masoko haya tutayapata tu iwapo tutafanikiwa katika Serikali ya viwanda. Tutajenga viwanda vya kusindika mahindi, pamba, ufuta, alizeti, tangawizi na kadhalika. Hilo ninaliona hatujalifanyia kazi kwa namna ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, unaona kwamba mahitaji ya mafuta ya kula peke yake ni lita 400,000, hizi ni sawa na alizeti tani milioni mbili tu. Na hizi tani milioni mbili wana uwezo wa kuzalisha wakulima 4,000 tu, wanaweza kuzalisha mafuta yote ya kula…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi hiki, hizi lita za mafuta laki nne wanaweza kuzalisha wakulima 4,000 tu iwapo watajengewa uwezo. Lakini inasikitisha kuona hadi leo asilimia 70 ya mafuta ya kula tunaagiza kutoka nje, wakati wakulima wengi hawana fursa ya kuzalisha na kuuza kwa bei nzuri mazao yao kilimo, kwa hilo ni tatizo. Tatizo hili linatoka wapi...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzunguzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa naomba niungene na wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na Watanzania kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kukurejesha salama na kuendelea na majukumu yako ya kulijenga Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, naomba kutumia nafasi hii kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo wametupa kipaumbele wananchi wa Madaba. Wizara ya Afya, Maji, Elimu, Miundombinu, Umeme na TAMISEMI hawajakauka katika Jimbo la Madaba. Kwa kweli, katika maeneo hayo tumepiga hatua kubwa sana na wananchi wa Madaba hawataridhi kama nitaanza hotuba yangu bila kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Wizara hizo pamoja na watumishi wote wa Wizara hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, sitawatendea haki Mashujaa wa Vita ya Majimaji ambao tunawakumbuka tarehe 27 Februari, kila mwaka kwa sababu nisiposema baadhi ya maneno yamepotoshwa ndani ya Bunge lako Tukufu. Wiki iliyopita Mheshimiwa Ngombale aliilalamikia Serikali kana kwamba makumbusho tunayoyafanya Majimaji ni upendeleo.

Mheshimiwa Spika, tutatafuta nafasi ya kulifafanua, lakini kwa kifupi tu ni kwamba, historia ya makumbusho ya Majimaji sisi wenyewe wakazi wa Mkoa wa Ruvuma tulianza kuchukua hatua kuwakumbuka mashujaa wale na Serikali imekuja kushirikiana na sisi karibu miaka 90 baadaye. Sheria na miongozo ya Serikali ipo, nimshauri tu Mheshimiwa Mbunge afuatilie hatua mbalimbali za kufikia huko na sisi Wanaruvuma tunaunga mkono sana jitihada za Watanzania wenzetu waliopigana vita kulinda heshima ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niende moja kwa moja kwenye hotuba yangu. Hotuba yangu nitaiweka kwenye eneo moja tu kubwa muhimu, juu ya namna gani Serikali ya Tanzania, Serikali ya Uchumi wa Viwanda inahitaji sana ushiriki kamili wa Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki kifupi Wizara hizi mbili, Wizara ya Viwanda na Wizara hii ya Nishati, wamepiga hatua kubwa sana, hatua ambayo Waheshimiwa Wabunge hatuwezi kuibeza. Upande wa viwanda na biashara idadi ya viwanda imeongezeka kutoka 454 ambayo ilikuwa mwaka 2015 na sasa tuna viwanda vipya tu katika kipindi hiki cha miaka mitatu, viwanda 3,306.

Mheshimiwa Spika, katika hili nitaweka nukta kidogo. Kuna watu wanaibeza Serikali wakisema kwamba, viwanda hivi 3,306 si viwanda vyenye hadhi ni mashine za kusaga, sijui mafundi chereheni. Watu wafanye kazi ya kutafuta takwimu. Idadi ya ajira katika kipindi hiki kifupi, kwenye sekta binafsi, sekta ambayo inatokana na viwanda, ilifika 137,054; ukigawanya kwa idadi ya viwanda unapata wastani wa kila kiwanda kimeajiri watu wasiopungua 40. Sasa watu 40,000 si kiwanda? Watu wafanye kazi ya kutafuta takwimu.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine kuhusu viwanda tumepiga hatua; mwaka 2015 sekta hii ilikuwa inakua kwa asilimia 7.9 na sasa inakua kwa asilimia 9.8. Huu ni ukuaji mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, sekta ya umeme nayo imepiga hatua ambazo hatuwezi kuzibeza. Moja, sekta hii imejiwekea malengo ya mwaka 2020 ya kuwa na megawatts 4,915 na 2025 megawatts 10,000. Kwa kipindi hiki kifupi kuanzia mwaka 2015 wakati Serikali ya Awamu ya Nne inamaliza kipindi chake cha madaraka, ilimaliza wakati Watanzania tuna umeme wa megawatts 1,308 tu; leo tuna megawatts zaidi ya 2,500. Katika kipindi hiki kifupi katika sekta ya umeme, umeme umeongezeka kwa asilimia 52, hili si jambo la kubeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, Wizara hii inayoshughulika na umeme imeweka mikakati madhubuti ya kufikia malengo ya kuwa na umeme wa megawatts 4,915. Ipo miradi mipya ambayo imeanzwa ikiwepo Stieglers Gorge, lakini unaona kwenye Kinyerezi I na Kinyerezi II tunaona kuna Kinyerezi I Extension ambayo itazalisha umeme wa megawatts karibu 250, lakini kuna Kinyerezi III ambayo itazalisha umeme megawatts 600. Hiyo ni mikakati mizuri itakayotupeleka kwenye malengo yetu ya mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, naona kuna watu wemesema jimboni kwangu. Nichukue nafasi hii, kwa vile nimekumbushwa niishukuru sana Wizara ya Nishati. Leo katika historia ya Madaba, mwaka huu uliokwisha tarehe 25 Desemba, 2017 wananchi wa Madaba wameanza kupata umeme, tangu kupata uhuru. Hili ni jambo la historia na ni jambo la kujivunia sana, naomba niishukuru Wizara katika kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, sipendi kusema kwamba, kila penye mafanikio hapakosi fitina, lakini nataka niseme kila panye mafanikio hapakosi changamoto. Malengo ya megawatts 4,915 tuliyojiwekea kwa mwaka 2020 na malengo ya megawatts 10,000 tuliyojiwekea ukilinganisha na Tanzania ya uchumi tunaoutaka ni kiwango kidogo sana cha umeme.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mifano kadhaa. Zipo nchi kadhaa ambazo zimepiga hatua ambayo sisi sasa tunaelekea, lakini huko nyuma zilifanana sana na sisi kiuchumi na kimikakati.

Mwaka 1970 nchi ya Afrika Kusini ilikuwa na umeme wa megawatts 14,000 sisi leo tuna megawatts 2,500 na tunakwenda kutengeneza Tanzania ya viwanda kwa mkakati wa kuwa na megawatts 4,915. Umeme huu hautoshi kabisa na haya malengo ni ya chini sana, hayatatupa Tanzania ya viwanda tunayoitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo mifano mingi. Mexico mwaka 1994 walikuwa na megawatts 35,000; lakini leo Afrika Kusini wanaongelea megawatts 44,000 wakati nchi nyingine kama za Korea Kusini wanaongelea megawatts 84,000 sisi tumejiwekea malengo ya megawatts 4,000. Pamoja na kupiga hatua kubwa katika hilo, lazima tukiri kwamba, mkakati wetu lazima tuubadilishe na lazima tutengeneze vipaumbele.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka niishauri Serikali kwenye eneo hili. Natambua mikakati mikubwa ambayo Serikali imejiwekea kwenye umeme, tuna mikakati hiyo ambayo nilikwishaitaja. Hata hivyo, kadri ya utafiti wa Benki ya Maendeleo ya Afrika vyanzo vya umeme wa Tanzania vinavyotokana na maji haviwezi kutupatia umeme unaozidi megawatts 4,000. Tunataka tutafute megawatts 10,000 na tunataka tufike megawatts zaidi ya 40,000 ili kupata Tanzania ya viwanda. Hiki kiwango ni kidogo, ni lazima Serikali iangalie vyanzo vingine.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba zilizotangulia tumeongelea kuhusu umeme wa gesi, nadhani kwa bahati mbaya Mheshimiwa Waziri Mkuu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo ya kuchangia sekta muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa. Kwanza kabisa, niwapongeze Wizara na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kusimamia vizuri sana sekta hii ya viwanda na biashara kiasi kwamba wadau tunapata matumaini kwamba tunaweza kuifikia Tanzania ya viwanda ndani ya kipindi chake cha miaka 10 ya uongozi wake mahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huwezi kupata Tanzania ya viwanda kama tutaendelea kupuuza mradi wa Liganga na Mchuchuma. Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma, nataka nitumie nafasi hii nieleze vizuri, ulianza kuzungumziwa na Mbunge mtangulizi wa Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mheshimiwa Prof. Simon Mbilinyi, lakini imekuja kuongelewa kwa zaidi ya miaka 10 na Mheshimiwa Jenista Mhagama (Waziri) na mimi ni Mbunge wa tatu kulizungumza hili lakini mpaka leo commitment ya Serikali imekuwa ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Liganga kuna chuma, tathmini inaonesha chuma iliyopo Liganga inaweza kuchimbwa kwa kiwango cha tani milioni moja kwa mwaka, hiyo ni tani ya chuma. Chuma hii pamoja na kuzalisha chuma, inazalisha mazao mengine yanayoambatana na chuma. Kuna madini ya vanadium pentoxide na kuna titanium dioxide, haya nayo ni madini yanayoambatana na chuma. Watanzania wote tunajua chuma ni malighafi ya msingi ya viwanda. Ujenzi wa viwanda unatumia sehemu kubwa chuma, mashine zote za viwandani kwa asilimia kubwa zinahitaji chuma, unaipataje Tanzania ya viwanda bila kuchimba chuma ya Liganga? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda jikoni utakuta kijiko, kisu, na uma, hivi vyote vinatengenezwa na chuma. Ukienda shambani utakuta jembe, panga, nyundo, vinatengenezwa na chuma. Ukipanda gari, asilimia 80 ya gari ni chuma, ni utajiri mkubwa sana Watanzania tumeauacha pale Liganga. Ipo mifano mingi, tukienda kwenye nyumba zetu tunazozijenga, bati ni product ya chuma, madirisha yetu, nondo na grill zote hizi ni product ya chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni viwanda vingapi vinaweza kuanzishwa kutokana na chuma ya Liganga? Tunaweza kutengeneza viwanda vya bati, viwanda vya nondo, viwanda vya magari na kila aina ya kiwanda tunachokitaka tutatengeneza na sisi wenyewe tutakuwa wateja namba moja wa hivyo viwanda. Hatuwezi kuipata Tanzania ya viwanda kama hatuweki makusudi kwenda kuchimba chuma ya Liganga.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1864, nchi ya Marekani iliahirisha ujenzi wa reli kwa sababu walitaka watumie chuma yao kujenga reli kwa sababu waliamini kiwango cha chuma ambacho kitahitajika kujenga reli iwapo kitachimbwa ndani ya nchi husika, kwanza kitaokoa pesa kubwa ya Serikali lakini kitachangia sana kwenye pato la Taifa. Mwaka ule 1864 wakati Marekani wanajenga reli chuma cha ndani kilikuwa na bei mara mbili ya chuma kilichokuwa kinatoka nje ya nchi ya Marekani, hata hivi kwa sababu ya uzalendo waliamua kutumia chuma iliyozalishwa ndani. Kwenye hili niombe sana Wizara iamue sasa kwenda kuchimba chuma cha Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chuma cha Liganga pamoja na kutoa malighafi ya tani milioni moja ya chuma kwa mwaka itatoa ajira takriban 4,000. Ajira 4,000 ni mchango mkubwa sana kwenye idadi ya ajira. Tumesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ni nzuri. Hata hivyo, ukifanya uchambuzi, ajira zilizozalishwa kati ya mwaka 2015 mpaka 2017 ni 26,113, ajira 4,000 zina mchango gani katika hiyo maana yake ni zaidi ya robo ya ajira zilizozalishwa katika kipindi hicho.

TAARIFA . . .

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili taarifa hii. Nikibaki hapo, ajira zitakazozalishwa kwenye mgodi huu wa chuma pamoja na spillover effect, maana yake ni zaidi ya ajira zilizozalishwa katika kipindi hiki chote cha utawala huu, kwa hiyo, si jambo la kulifanyia dhihaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nabaki hapo hapo kwenye Liganga na Mchuchuma, mradi wa Mchuchuma utakaozalisha kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe, umeme ambao utazalishia chuma cha Liganga, mtambo huu utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme megawatts 600, hiyo ni faida nyingine. Sasa megawatts 600 ni sawasawa na nusu ya umeme wote tuliokuwa nao mwaka 2015. Mheshimiwa Rais amekabidhiwa nchi hii ilikuwa na umeme wa megawatts 1,308 sasa Mchuchuma peke yake itazalisha umeme megawatts 600, si kitu kidogo wala siyo cha kukidharau. Umeme huu sawa na robo ya umeme wote utakaozalishwa kwenye Stiegler’s Gorge. Stiegler’s Gorge watazalisha umeme megawatts 2,100 na megawatts 600 ni robo ya huo umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisisitize kwa kusema umeme huu wa megawatts 600 utakaozalishwa Mchuchuma ni asilimia
12.2 ya malengo tuliyojiwekea ya umeme tunaohitaji mpaka ifikapo mwaka 2020. Sasa unajua huwezi kuipata Tanzania ya viwanda bila umeme. Katika michango yangu iliyotangulia nilisema, umeme tulionao Tanzania hauwezi kutupa Tanzania ya viwanda. Afrika Kusini mwaka 1970 walikuwa na megawatts 14,000, sisi leo tuna megawatts 1,500 mpaka 2,500, tunahitaji uzalishaji mkubwa wa umeme. Mradi wa Stiegler’s Gorge ni mradi muhimu sana kwa Taifa letu, lazima tuupe nguvu, lazima tuunge mkono lakini lazima tuongeze vyanzo, chanzo kingine ni huu wa Mchuchuma, megawatts 600, kwa kutumia makaa ya mawe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeongea kwa msisitizo mkubwa kwa sababu ninaamini hatuwezi kuipata Tanzania ya viwanda bila umeme wa kutosha na hatuwezi kuipata Tanzania ya viwanda bila kwenda Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, niongezee tu hapo, kwenye hili suala la umeme. Wenzetu nchi nyingine wanaongea megawatts 84,000 sisi tunaitafuta Tanzania ya viwanda bila kwenda kuchimba chuma, bila kwenda kushughulika na Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine nichangie tu kwamba, Tanzania tuna bahati, tumeendelea kuvutia wawekezaji na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri amefanya sana kazi tumeona wawekezaji toka nchi mbalimbali wanakuja kutoka Ujerumani, Ufaransa, ni initiative kubwa sana hii, watu wamebeza lakini wanabeza kwa sababu hawajui misingi ya uchumi. Hawa wanapokuja watatuongezea teknolojia na mtaji, tutahakikisha kwa kuwatumia hao tunavuka, tunafikia haya malengo yetu lakini eneo muhimu ni kulinda viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu muda haujanitosha, nichukue nafasi hii kukushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye hoja na mchango wangu utajikita kwenye eneo la soko la mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kupata mapinduzi ya kilimo Tanzania kama hakutakuwa na mfumo madhubuti wa soko la mazao. Kinachomfanya mwananchi wa Madaba, mwananchi wa Njombe, Songea Mkoa wa Ruvuma, mwananchi wa Katavi, mwananchi wa Rukwa, mwananchi wa Sumbawanga, Songwe na Mbeya aamke asubuhi, aweke jembe begani akalime ni kwa sababu anataka kupata pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima haendi kulima kwa ajili ya kutatua tatizo la food security ya nchi, ile ndiyo ofisi yake. Mwananchi wa Madaba, mwananchi wa Katavi anakwenda kulima mahindi kwa sababu anataka ajenge nyumba bora, kwa sababu anataka asomeshe mtoto wake katika shule zenye sifa, kwa sababu anataka amudu mahitaji ya afya katika hospitali zenye ubora, anataka kuishi maisha bora huyu Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaongelea asilimia 70 ya Watanzania ambao kipato chao kinatokana moja kwa moja na shughuli za kilimo, lakini tunaongelea asilimia karibu 90 ya Watanzania ambao kwa namna moja au nyingine wanategemea kilimo. Huwezi kupata mapinduzi ya kilimo bila mfumo madhubuti wa soko la mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Madaba wameumia sana na mfumo wa masoko, pia wananchi wa Mikoa yote niliyoitaja ukiwemo na Morogoro wameumia sana juu ya ukosefu wa soko la mahindi. Wakulima hawa kama ambavyo Wabunge tunataka tuwasomeshe watoto wetu katika shule zenye sifa, tujitibu vizuri, tujenge nyumba bora, tuvae nguo safi, nao pia wana ndoto hiyo. Hatuwezi kuipata Tanzania yenye mapinduzi ya kilimo kama hatutaki kuwekeza kwenye masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe ushahidi, ukuaji wa sekta ya kilimo mwaka 2014/2015 ulikuwa asilimia 3.4 na ukuaji wa sekta hiyo mwaka jana 2016/2017 ilikuwa asilimia 2.1, kwa nini? Kwa nini ukuaji umeshuka ni kwa sababu incentive ya mkulima ni soko. Hawezi kwenda kununua mbolea, hawezi kujikita kwenye mbegu bora, hawezi kutafuta mbinu bora za kilimo kama kilimo hakimlipi. Kwani ni nani ameenda kuwaambia vijana wanunue bodaboda, wafanye biashara Mjini, si kwa sababu inalipa? Hivi leo tunahitaji kuwambia wakulima wakalime? Tuwape soko wakulima watakwenda kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima yeyote akishajua tangawizi inamlipa, mahindi yanamlipa, kahawa inamlipa huhitaji kwenda kumfundisha kulima atakutafuta mwenyewe, atakuambia nifundishe namna ya kulima mahindi, atakutafuta mwenyewe atakuuliza umwambie mbolea iko wapi. Leo tunawaweka wananchi wetu wakulima katika mazingira magumu sana, Madaba na maeneo mengine masikitiko ni makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea na hoja yangu nimshukuru sana Waziri na Ofisi yake Wizara ya Kilimo wamenisaidia sana, mwaka huu nilikuwa napoteza Ubunge Mabada kama suala la mbolea lisingezingatiwa. Ucheleweshaji ulikuwa mkubwa, wananchi wamelalamika lakini nakushukuru Waziri ulinisaidia na timu yako ya Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la soko la mahindi Serikali inajaribu kulitatua lakini bado halijapatiwa ufumbuzi. Mwaka 2015/2016 tulikuwa na ziada ya tani milioni 2.6 Serikali ilinunua tani 22,000 tu, mwaka uliofuata tani milioni tatu ziada Serikali ilinumnua tani 62,000 tu za mahindi. Mkoa wa Ruvuma hapa nina taarifa aliyopewa Waziri Mkuu alipokuja, tulizalisha ziada ya mahindi/nafaka tani milioni 1.4, ilinunuliwa tani 10,000 tu, tunakwenda wapi? Wakulima hawa wote mahindi haya wameyapeleka wapi? yameharibika, wameendelea kuwa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya kuzingatia muda nitakwenda moja kwa moja kwenye ushauri. Mheshimiwa Waziri azingatie mambo yafuatayo:-

Moja, sera ya kilimo inataka mambo manne nchi yoyote, nenda Marekani, nenda nchi zozote za Kusini mwa Afrika, Kenya na kokote sera yoyote ya kilimo ina mambo manne ambayo ni safety, security, sufficiency na quality ya maisha ya mkulima. Mheshimiwa Dkt. Tizeba hili naamini unalizingatia na tunaomba sana ulizingatie. (Makofi)

Pili, sera yoyote ya agricultural trade, sheria zote za mipakani zilenge kulinda maslahi na maendeleo ya wakulima ndani ya nchi yako ndipo utapata haya yote unayotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda haraka haraka. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imetoa mapendekezo juu ya ufumbuzi wa tatizo la soko la mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja imesema katika ukurasa wa 12, tuanzishe soko la mazao sasa commodity exchange kwa maana ya kwamba wakulima wetu wanapoingia shambani wawe na uhakika wa soko. Leo Sudan hawana chakula, Uganda na Tanzania tunapishana misimu ya kulima, Kenya wanahitaji mahindi ya Tanzania leo tunasema tunawanyima mahindi wakati mahindi yanaoza Madaba. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imetoa muongozo kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili imependekeza NFRA iwe na kitengo cha kununua mahindi, inunue mahindi ya hifadhi lakini inunue mahindi ya kutosha kwa ajili ya kutafuta soko la nje. Kama tunataka ku-control inflation, kama tunataka tu-control food security basi NFRA apewe hayo majukumu, leo amepewa bilioni 15 badala ya kupewa shilingi bilioni 86, shilingi bilioni 15…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kukushukuru kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango ya Taifa 2019/2020. (Makofi)

Kwanza nimpongeze kwanza Mheshimiwa Waziri Mpango na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano, katika ujumla wake kwa kuwa consistency katika kipindi hiki chote cha miaka mitatu kwa sababu mpango huu ni sehemu ya mpango mzima wa miaka mitano 2015/2016 - 2020/2021 na katika utekelezaji wake Serikali imekuwa consistency sana.

Pia niipongeze Serikali kwa kuzingatia maoni ya Wabunge kwa miaka yote mitatu ambapo tumekuwa tunatekeleza mpano huu. Maeneo kadhaa ambayo tulikuwa tunashauri yakiwemo maeneo ya kuongeza nishati tumeona Stiegler’s Gorge imeendelea kupewa kipaumbele lazima tuipongeze lakini pia tumeona leo Liganga na Mchuchuma, inaanza kupata sura ya utekelezaji kwa maana kwenda sasa kujenga kiwanda cha kufua chuma Liganga. Sasa haya yote ni mapato ya kazi ya Bunge hili na nimatokeo ya kazi nzuri ya Awamu ya Tano, na lazima tuipongeze Serikali na kwa namna ya pekee Mheshimiwa Rais na Waziri Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la kukua kwa uchumi wote tumejiridhisha pasipo mashaka uchumi wetu unakua kwa kasi kubwa sana na ukilinganisha na uchumi unavyokuwa duniani na uchumi unavyokuwa katika Afrika na maeneo mengine tunayopakana nayo sisi tunakuwa kwa kasi kubwa sana, kasi ya asilimia 7.2.

Sasa hili kimsingi kuna eneo dogo linatupa shida kidogo sisi Wabunge lakini Watanzania katika ujumla wake kwamba uchumi unakua, lakini mapato ya kukuwa uchumi huu tunayaona kwenye maeneo ya afya, tunaona kwenye masuala ya elimu, tunaona kwenye masuala ya miundombinu. Kwa hiyo, kimsingi faida za kukua uchumi huu tunaziona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo mimi nilitaka nitoe mapendekezo, ya kuboresha wakati wa maandalizi ya huu mpango ni namna gani sasa kwa sababu mimi nina amini hatuwezi kupata mapinduzi ya uchumi kama hatutakuwa na mapinduzi ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilitaka nijaribu kushauri kwamba sasa Mheshimiwa Mpango akae na hizi line ministry zinazogusa sekta ya kilimo na uchumi kiujumla kuona namna gani sasa tunaweza ku-transform agricultural sector kwa namna ni significant. Waatalam wa kilimo wanapo taka kujua changamoto kwenye sekta ya kilimo wanafanya upembuzi wa mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo na ukifanya upembuzi wa mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo katika ujumla wake utagundua kwamba tatizo kubwa kwenye sekta ya kilimo ni soko, yaani huo ndiyo mtego tunao na Serikali sasa lazima ikubali kwamba huo ndiyo mtego ambao tunao na tukiweza kuutegua huo sekta ya kilimo itakuwa kwa kasi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye huu mpango nashukuru Serikali imeweka vizuri sana interventions nyingi kwenye sekta ya kilimo, lakini utaona kwenye interventions zilizopendekezwa na Serikali kwenye mpango huu hazioneshi kwa ufasaha namna gani tunaenda tunaenda kutatua tatizo la soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachomfanya mkulima aende shambani ni faida anayoipata kutokana na kilimo. Tumejiridhisha kwamba kwa namna yoyote ile kwa mazingira aliyopo mkulima huyu mdogo lazima achangie kwenye usalama wa chakula, lakini lazima atengeneze fedha kwa ajili ya kujikimu. Sasa strategy ya Serikali lazima izingatie ukweli kwamba kumsaidia huyu mkulima mdogo apunguze gharama za uzalishaji na gharama za uzalishaji kwanza zinatokana na bei kubwa ya mbolea, nashukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu jana alieleza namna gani tunajipanga kupunguza gharama ya mbolea kwa kuzalisha mbolea yetu ndani, hilo litamaliza tatizo lakini kwenye mpango huu alijafafanuliwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo la pili ni transaction cost kutoka eneo lile ulilozalisha mpaka kufika kwenye maghala ya kuhifadhia mazao, barabara zetu vijijini hazileti tija kwa mzalishaji, eneo dogo la usafirishaji analipa gharama kubwa sana za kusafirisha mazao yake,
anapofikisha zao lake kwenye eneo la soko tayari garama imeshakuwa kubwa. Kwa hiyo anapokutana na bei ndogo, profit margin inabaki kuwa ndogo sana au anaweza asiipate kabisa. Kwa hiyo, Serikali iwekeze kwenye kupunguza gharama za uzalishaji kwa kupitia pembejeo zetu, mbegu bora na mbolea, lakini pia miundombinu ya masoko, na miundombinu ya masoko ndiyo hizo barabara za vijijini zinatoka mashambani lakini madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine baya linalochangia upotevu mkubwa wa mazao tunasema post harvet losses ni haya hadhi na sura ya maghala yetu na gharama za usafirishaji (miundombinu ya usafirishaji) asilimia 30 ya mazao yetu tunayoyazalisha yanapotea kabla hayajafika kwenye soko, sasa hiki kiwango kinacho potea nacho ni hasara kwa mkulima. Kwa hiyo pamoja kwamba hatuwezi kumsaidia mkulima kupata bei nzuri kutokana na hali halisi ya soko la dunia tunaweza kama Serikali kumwezesha huyu kuzalisha kwa gharama za chini na hii profit margin yake ikabaki kubwa na akawa ana visenti vya kwenda shambani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba nimshauri Mheshimiwa Mpango na Serikali katika ujumla wake katika eneo hilo na ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Awali ya yote naomba nitumie nafasi hii kuwashuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Madaba kwa kuitikia wito wa Mheshimiwa Rais wa Hapa Kazi Tu kwa vitendo. Wameshiriki kikamilifu katika ujenzi wa miundombinu ya elimu yakiwemo madarasa, mabweni na mabwalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee niwapongeze wananchi wa vijiji vya Wino, Lilondo na Maweso ambao katika umoja wao wamechangia zaidi shilingi milioni 104 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba makazi yao yanapata maji lakini shule zote za sekondari na za msingi wanapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti niwapongeze wazazi wa shule zote za msingi za Madaba. Kwa namna ya pekee, wazazi wa Shule ya Msingi Njegea, Igawisenga, Turiani, Kifaguro, Mahahanje, Likalangilo na shule nyingine ambazo katika umoja wao katika kila mwaka wanachangishana zaidi ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya kupata walimu wa ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali na kwa namna ya pekee Wizara hii ya Elimu na TAMISEMI ambao wameunga mkono jitihada za wananchi wa Madaba kwa kuhakikisha kwamba ile miundombinu ambayo wazazi wameendela kuijenga, Serikali inaikamisha. Tumepata fedha nyingi kwa ajili kukamilisha, lakini kutokana wingi wa mahitaji yetu, bado hizo fedha hizo hazitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sikupata nafasi kuchangia kwenye Wizara ya TAMISEMI, nitumie nafasi hii hii pia kuiomba Wizara ya TAMISEMI watuongee bajeti na kuhakikisha kwamba madarasa, mabweni na mabwalo ya shule zetu za msingi na sekondari yanakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekti baada ya hizo shukrani kwa wananchi wa Madaba na kwa Wizara, nitumie nafasi hii kutoa wito kwa Wanamadaba kuhakikisha kwamba tunaendelea kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja kwa sababu tuna jukumu la pamoja kuhakikisha kwamba watoto wetu wanapata elimu bora na wanapata katika mazingira mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nitoe ushauri kwa Serikali. Tunayo changamoto kubwa sana ya walimu katika shule zetu. Hili siyo kwa Shule za Madaba pekee, ni shule za sekondari karibu taifa zima. Tatizo hili la walimu pengine tunaweza tukalichukua kama dogo, lakini madhara yake yanaonekana dhahiri katika maeneo tunayotoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna vijana waliohitimu kidato cha nne katika shule zetu mbalimbali. Kijana huyu tangu anaanza Form One mpaka anamaliza kidato cha nne, kwa sababu ya kukosa Walimu darasani, wametumia madarasa yetu kama vijiwe vya kujadili masuala ya siasa na kuijadili Serikali katika mambo wasiyoyataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawa wanapotoka mashuleni wanahamishia mijadala kwenye vijiwe na kwenye mitaa yetu. Kwa kadri tunavyoendelea, Taifa hili sasa linaelekea kupata wanung’unikaji na siyo watenda kazi katika Taifa hili. Jambo hili leo tunaweza kulichukulia mzaha mzaha, lakini kwa kadri siku zinavyokwenda, tunazalisha vijana wa kijiweni ambao hawana ajenda nyingine zaidi ya kulalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imeelezwa kuhusu sera yetu ya elimu. Nimeona Wizara imeweka mkakati wa ku- review hii sera sayansi, teknojia na ubunifu. Hili lisichukue muda. Mwaka 2018 tumeona huo mchakato ukiangalia kwenye hii taarifa ya Wizara ambayo ni nzuri sana, lakini unaona katika ukurasa wa tisa wanasema Wizara imeanda Rasimu ya Mapitio ya Sera ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu. Mwaka umeisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa bajeti Wizara inaendelea na mchakato na inasema itakamilisha Mapitio ya Sera ya Sayansi na Teknolojia ya Mwaka 1996 ili kuwa na Sera ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu inayoendana na mahitaji ya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa miaka miwili inakatika; hili haliakisi kabisa kasi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Naiomba Wizara Watanzania wanatambua umuhimu na wanaona jithada zinazofanyika na hawana tatizo, lakini tuongeze speed ya kufanya kazi. Tufanye review ya hii sera kwa wakati ili Watanzania waliopo mashuleni, waliopo kwenye vyuo vyetu za ufundi waweze kunufaika na hii sera. Tutaisubiri hadi lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini sera hii inayoenda kufanyiwa review itazingatia ukweli kwamba kila Halmashauri ya Wilaya tunahitaji kuwa na Vyuo vya Ufundi na siyo kimoja. Kwa sababu watoto wanaohitimu kidato cha nne ni wengi, wanaopata fursa ya kujiendeleza sekondari kwa maana ya kidato cha tano na cha sita na wanaokwenda Vyuo Vikuu ni wachache. Hawa wanaobaki tunawaachia ujuzi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hatutaki ku- capture? Kwa nini hatuataki ku-tap hii rasilimali muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu? Namna nzuri ya kutumia hii rasilimali watu ambayo ina ari ya kazi ni kuiongezea ujuzi kupitia vyuo vyetu vya elimu. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri tuwajengee uwezo vijana wetu wawe na uwezo wa kiufundi na kiujasiliamali ili tuondoe tabia yao ya kulalamika, tuwajenge uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, walimu wetu katika maeneo mbalimbali wana hali ngumu sana. Wengi hawajapandishwa madaraja kwa muda mrefu. Kwa hili sisi Wabunge tumetekeleza wajibu wetu wa kuja mpaka kwenye Wizara zinazohusika kuyaeleza, lakini hayafanyiwi kazi. Wengine madaraja yamekwama kwa miaka minne, mitano; wengine posho zao za miaka mingi tunakwenda kujenga Taifa la walimu wanaolalamika ambao watawazaa wanafunzi na vijana wanaolalamika na mwisho tutapata Taifa la walalamikaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu sana Wizara ya Maji, na nianze kwa kumshukuru sana kuishukuru sana Serikali hususani Mheshimiwa Prof. Mbarawa Makame pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa ushirikiano mkubwa sana ambao mmetupa wana Madaba kuhakikisha miradi yetu ya maji inafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Prof. Mbarawa na Mheshimiwa Jumaa Aweso mmekuja wenyewe mmetembelea miradi mbalimbali ya maji Madaba, mmeshirikiana na wananchi wa Lilondo kuhakikisha kwamba miradi yao ya jamii kupitia vikundi inafanikiwa kwa kuchangia pesa ninyi wenyewe, pia kwa kuwatia moyo ninawashukuruni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru miradi mingine ambayo inaendelea iliyokamilika Madaba ya maji na hii ambayo imetengewa bajeti ya zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya kuendelea kuitekeleza. Siku ya leo nilitamani sana nitume muda mrefu kuishauri Serikali juu ya mambo kadhaa ambayo ninadhani kama hayatachukuliwa umaanani Wizara hii itawaangusha watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza naomba tulijue kwamba kama vitu ambavyo vinambeba Mheshimiwa Rais ni uzalendo wake na upendo wake kwa watanzania. Amejitoa kwa hali na mali kufa na kupona Watanzania wapate unafuu katika Nyanja zote, amekusudia kwa kufa, kupona kuhakikisha wakina Mama tunawatua ndoo vichwani ili kuhakikisha hawapati tena usumbufu wa maji. Lakini Watumishi ndani ya Wizara ya Maji ni mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie kusema na hili limesemwa na Mheshimiwa Waziri mwenyewe kwenye ukurasa wa 108 wa hotuba yake. Amesema: “moja katika changamoto katika Wizara hii ni uwezo mdogo katika utekelezaji, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji” na kama ningepata fursa ya kurekebisha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ningeiandika kama ifuatavyo: “Dhamira ndogo ya Watumishi katika idara inayohusiana na masuala ya maji kutekeleza na kusimamia miradi vizuri”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa nyingi zimetengwa kwenda kwenye miradi, sisi Madaba pia tumetengewa na Mheshimiwa Waziri anahangaika sana kuhakikisha tunafanikiwa, lakini procedure ndogo tu ya kupata vibali vya kutekeleza miradi iliyotengewa fedha inachukua karne nzima. Mwaka mzima Mtumishi wa Madaba anaandika barua Wizarani, anasubiri majibu ya kibali cha kutekeleza mradi. Mradi umetengewa fedha, tupo ndani ya bajeti, mradi hauchukuliwi umaanani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshauri Mheshimiwa Waziri, watu kama hawa awaondoe, wanamchafua, wanaichafua Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Inawezekanaje wewe umeandikiwa barua Mwezi wa nane, Mtumishi umeipokea kutoka kwa mtaalam mwenzako, hata ku-acknowledge kwamba umeipata hiyo barua na hata baada ya kukumbushwa, inakaa miezi sita, saba mpaka Mbunge anakwenda kwa Waziri, Waziri anafuatlia ile barua, tutafika kweli na Awamu hii ya Tano? Inasikitisha sana kuona kasi ya Mheshimiwa Rais, kasi ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu Waziri wake inaangushwa na watu wadogo, watu walio katika utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tumebadilika sana, Watanzania tumeakisi falsafa, tumeiishi falsafa ya Mheshimiwa Rais ya “hapa kazi tu”, wananchi wanahangaika kila siku, wanapambana kuhakikisha kwamba tunaitekeleza lakini bado baadhi ya watumishi wa umma wanaishi maisha yale yale ya business as usual. Yamesemwa haya na Mheshimiwa Adadi humu humu ndani, yamesemwa na Mheshimiwa senator hapa, yamesemwa na Mheshimiwa Keissy na mimi nayasema na naamini Wabunge wengine watayasema, wanaotuangusha naomba Mheshimiwa Waziri wa Maji akafanye nao kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto ya certificate, siyo Madaba peke yake, sehemu nyingi tunalalamika sana, Wakandarasi wametekeleza wajibu wao, walipwe ili kazi ziende, lakini nalo hilo linamhitaji Mbunge aende mguu kwa mguu mpaka Wizarani, hawa watumishi wana kazi gani?. Hili kwa kweli limenisikitisha na nimeungana na Wabunge wenzangu kulisema na naamini Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo sisi tunamwamini na tunamtegemea, atakapopitisha Bajeti yake ambayo tutaiunga mkono, aende akasafishe huko chini wanatuangusha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, pamoja na michakato hii, vijiji saba vya Wilaya ya Madaba vimeendelea na utaratibu wa usanifu wa mradi. Mradi wa Vijiji Saba unakwenda kunufaisha wananchi 25,000. Mradi huu ngazi ya Halmashauri walishamaliza usanifu wa awali kabisa na wameomba kwa Mheshimiwa Waziri na amewakubalia, amewapa kibali lakini wameomba pia kwake kibali alichowapa ni kwa ajili ya kuweka maji ya muda mfupi kwa kutumia visima virefu. Tunamshukuru na tunaamini utaanza kutekelezwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo walilonalo ni kwamba wanashindwa kufanya usanifu wa kina kwa sababu zaidi ya miezi sita sasa wanasubiri majibu ya Wizara, waletewe wataalam kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina na pengine hili lingekuwa limeshafanyika leo tungeweza kuisoma Bajeti ya eneo hilo. Mheshimiwa Waziri tunamwomba sana, tunamwamini, tunamtegemea na tunaunga mkono hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. Kwanza kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Manaibu Waziri wote wawili kwa ushirikiano ambao wanatupa wananchi wa Madaba kwenye masuala yote ya barabara na mawasiliano na nitoe salam za pekee kutoka kwa wananchi wa Ifinga ambao tangu nchi hii ipate uhuru hawakuwa na mawasiliano kabisa, walikuwa wanasafiri zaidi ya kilomita 30 kwenda kupiga simu, lakini sasa tatizo hilo limekwisha, tunawashukuru sana. Pia watu wa Madaba wanamkumbuka sana Mheshimiwa Waziri, alianza utumishi Madaba na leo ameshirikiria Wizara muhimu sana katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiifuatilia historia ya Madaba utagundua kwa nini ina matatizo makubwa ya barabara, Madaba ilikuwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea miaka minne iliyopita. Katika kipindi hicho, barabara ambayo ilikuwa inahudumiwa na Serikali kwa kupitia fedha za halmashauri ilikuwa kilometa 48 tu na sasa Madaba ni Halmashauri ya Wilaya na ni Jimbo na kilometa zinazohitaji kuhudumiwa kwa maana ya mtandao wa barabara Madaba umefikia kilomita 642. Mpaka sasa bajeti tunayopata Madaba kwa kupitia TARURA ni ya kilometa 48 tu, haizidi shilingi milioni 400.16. Madhara yake barabara nyingi za Madaba ni mbovu hazifai na hazipitiki katika kipindi cha masika na hata kiangazi bado kuna makorongo mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo barabara za kimkakati ambazo naamini Mheshimiwa Waziri tumeanza kuzungumza kwenye vikao vyetu ambavyo siyo rasmi na yeye, lakini hapa naongea mbele ya Bunge hili Tukufu kumwomba akubali kupokea baadhi ya barabara zitoke TARURA ziende TANROADS. Moja katika barabara hizi ni hii barabara ya kutoka Wino kwenda Matumbi – Ifinga. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro na barabara hii ndiyo barabara ambayo itachangia sana kwenye kuipata Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza hekta za ardhi zimewekeza kule kwa ajili ya kilimo cha miti na muda si mrefu kama Mheshimiwa Waziri atatusaidia, hawa watani zangu wa Iringa tutawapita kiuchumi. Uchumi wetu utafafana na uchumi unaouona Mafinga leo kwa kutokana na miti, lakini kinachotuangusha ni hii barabara. Hii ni barabara ya kimkakati, ni barabara yenye uchumi mkubwa sana. Barabara hii ina urefu wa kilomita 57, pia inaunganisha na mbuga ya Selou ambako tayari kuna vitalu ambavyo wawekezaji wamewekeza kwenye kuwinda na kwenye utalii. Kwa hiyo ina mchango mkubwa sana kwenye uchumi na hatuwezi wana Madaba kushiriki kwenye uchumi wa viwanda kama barabara hii Mheshimiwa Waziri hatakubali kuipokea. Namwomba sana kwa niaba ya wananchi wa Ifinga akubali kuichukua barabara hii iende TANROADS ili ijengwe kwenye viwango tunavyovitaka na matokeo yake ni uchumi ambao utatokana na kazi kumbwa inayofanyika katika maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ukiangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri aghalabu utakuta mahali pameandikwa Madaba, najua kwa sababu labda Madaba barabara zake ni fupi na ni barabara ambazo wanadhani TARURA itazikamilisha, lakini kiuhalisia sivyo hivyo, TARURA hawana fedha za kuweza kumaliza zile barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo barabara nyingine ya kimkakati inayounganisha Madaba na Njombe kwa kupitia Kijiji cha Maweso na kama Mheshimiwa Waziri alifanya kazi Madaba wakati ule, ili uje Dar es Salaam ilikuwa unapita Maweso unaenda Mikongo unatokea Kifanya unakwenda Njombe, ile barabara ya zamani, barabara kubwa ya kutoka Dar es Salaam kwenda Madaba, kwa sasa unaweza kwenda mwisho Maweso, baada ya pale huwezi kuendelea na ile barabara. Namwomba Mheshimiwa Waziri barabara hii pia aichukuwe kwa maana ya Mfuko wa TANROADS aihudumie ili kukuza uchumi wa wananchi wa Madaba na wananchi wa Maweso, lakini wananchi wa Njombe kwa sababu hilo ndilo eneo kubwa ambalo lina ardhi kubwa ya uzalishaji, lakini pia lina matukio ya kihistoria. Barabara hii ina kumbukumbu za kudumu za mashujaa wa vita ya Uganda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mhagama muda wako umekwisha.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Kilimo. Kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri kwa kazi nzuri sana wanayoifanya kwenye sekta hii. Pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwa msaada mkubwa sana kwa wakulima wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kati ya maeneo muhimu sana ambayo nilitaka nichangie kwa maslahi ya muda ni uelewa ambao tunatakiwa wote tuwe nao. Moja, Mheshimiwa Waziri ujue kwamba hakutakuwa na Mapinduzi ya viwanda nchini kama hatutakuwa na Mapinduzi ya kilimo ni kwa sababu asilimia 65 ya malighafi yanayokwenda viwandani yanatoka kwenye kilimo. Pili, hatutakuwa na mapinduzi ya kilimo kama hatutakuwa na mapinduzi kwenye mfumo wa kufikisha pembejeo kwa wakulima wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anafahamu vizuri, wakulima wetu wengi wapo vijijini, na pembejeo za kilimo kwa maana ya mbolea, mbegu bora na viuatilifu vinapatikana mjini. Ili huyu mkulima aweze kuzalisha kwa tija ni lazima atumie mbolea nzuri, mbegu bora na atumie viuatilifu. Kama hivi vyote vinaendelea kupatikana mjini maana yake huyu mkulima mdogo ni lazima asafiri kupata hii huduma, na unamuongezea gharama za uzalishaji. Akishazalisha zao Lake, anakuja kuliuza kwa gharama kubwa kwa sababu anataka kufidia gharama.

Mheshimiwa Spika, mfumo ambao Serikali unaufanya ni mzuri, wa kuhakikisha kwamba vijijini kunakuwa na maduka madogo madogo ya wauza pembejeo. Maduka haya vijijini yatauza mbolea, mbegu bora na viuatilifu.

Mheshimiwa Spika, changamoto tunayoipata kwenye hii sekta ya kilimo ni gharama za kufungua haya maduka vijijini, wajasiliamali wengi vijijini wamejengewa uwezo na uelewa wa umuhimu wa kuuza pembejeo vijijini ili mkulima mdogo aweze kupata huduma kwa karibu.

Mheshimiwa Spika, sasa vyeti vinavyotokana na kupata hicho kibali ni gharama kubwa sana. TOSIC peke yake wanataka 100,000, TFRA wanataka pia fedha lakini TPRA wanataka 320,000, TFDA wanataka 100,000, kabla hujafungua duka la pembejeo kijijini, lazima uwe na shilingi zaidi ya 600,000; hapo hujaweka shelves dukani, hujanunua bidhaa. Sasa mjasiriamali gani wa kijijini atakuja kuwekeza kwenye hii biashara ili kumsaidia mkulima mdogo kupata huduma kwenye sekta hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, ili tupate mapinduzi ya kilimo, Mheshimiwa Waziri azipitie tena hizi tozo na gharama, ikiwezekana aziondoe, kama haiwezekani basi zipunguzwe kwa kiwango ambacho kitamsaidia mjasiliamali mdogo aweze kuwa msaada kwenye hii value chain ya inputs kwa maana ya pembejeo, tusipofanya hivi tutaendelea kuwatesa wakulima na hatutapata majibu. Ninayo mifano halisi, Kigoma peke yake zaidi ya wajasiriamali 159 wamejengewa uwezo lakini wameshindwa kufungua maduka kwa sababu hawajakidhi viwango vya kuwa na vyeti kwa sababu ya gharama.

Mheshimiwa Spika, ukienda Mkoa wa Kagera wakulima 461 wamejengewa uwezo kupitia Shirika la Agra, lakini ni wakulima 139 tu wameweza kulipia gharama hizi na kufungua maduka vijijini, tutapata wapi mapinduzi ya kilimo kama hatutaki kuwekeza kwenye mfumo wa pembejeo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Awali ya yote naomba nitoe salamu za pongezi sana kwa Serikali sikivu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya kwa ajili ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya salamu za shukrani zimfikie Mheshimiwa Luhaga Mpina, Mbunge, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, pamoja na timu yake yote Wizarani. Salamu hizi zinatoka kwa wananchi wa Hanga Ngadinda katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba. Wananchi hawa kwa muda mrefu wamehangaika sana kupata eneo la kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hekima kubwa na kwa uzalendo Mheshimiwa Waziri amekubali kuwapa hekta 1,800 ili kutatua tatizo la wananchi hawa. Tunamshukuru sana, sana, sana. Mheshimiwa Luhaga Mpina amekuwa mmoja katika Mawaziri ambao wapo tayari kuchukua maamuzi magumu yanayotatua matatizo ya wananchi. Tunaomba Serikali pia itambue mchango mkubwa wa Waziri huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba nijielekeze kwenye kuishauri Serikali katika mambo muhimu yanayohusu kukuza uchumi, hatutapata Tanzania ya viwanda kama hakuna uratibu wa pamoja wa sekta na Wizara zinazotegemeana. Hizi Wizara zinazotegemeana tunaziita Line Ministry. Ili upate Tanzania ya viwanda unahitaji uratibu wa pamoja wa Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Viwanda na Biashara pia kwa karibu sana na Wizara ya Ardhi.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, malighafi asilimia 65 inayohitajika viwandani au niseme viwanda kwa asilimia 65 vinategemea malighafi kutoka katika sekta hizi nilizozitaja ambazo ni sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, madini lakini ardhi ndiyo Mama katika haya yote ambayo nimeyataja. Kama hakuna uratibu wa pamoja wa hizi Wizara hatutaipata Tanzania ya viwanda.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na eneo la kilimo. Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye hotuba yake ameondoa vikwazo vingi sana vya biashara, tunamshukuru na tunampongeza sana, hatua aliyoichukua itatatua tatizo la kufanya biashara nchini na ufanyaji biashara utakuwa rahisi zaidi, lakini Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesahau sekta Mama ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, sekta ya kilimo. Kwenye mchango wangu wakati nachangia Wizara ya Kilimo nilisema, hatutaweza kupata mapinduzi ya kilimo kama hatutawekeza kwenye usambazaji wa pembejeo na usambazaji wa pembejeo vijijini unakwazwa na gharama kubwa za kufungua maduka ya pembejeo na gharama hizo zinachangiwa na TFRA, TPRI, TOSC na TFDA.

Mheshimiwa Naibu Spika, tozo hizi Mheshimiwa Wazri Mkuu alizijibia humu ndani. Mheshimiwa Waziri wa Fedha naomba urejee kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu hizi tozo zinazokwaza uendelezaji wa sekta ya kilimo. Huwezi kupata mapinduzi ya kilimo kama hautaki kuwekeza kwenye usambazaji wa pembejeo. Sasa mtu wa kijijini anayetaka kufungua duka la kusambaza pembejeo na ninaposema pembejeo maana yake mbegu bora, mbolea na viuatilifu, kama hivyo havipo huwezi kupata mapunduzi ya kilimo. Kwa hiyo Mhehsimiwa Waziri wa Fedha naomba rejea kwenye majibu ya Waziri Mkuu kaondoe hizi tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha ondoa tozo kwenye TFRA shilingi 100,000, ondoa tozo kwenye TPRI shilingi 320,000, ondoa tozo kwenye TOSC na TFDA ili mjasiriamali wa kijijini aweze kufikisha pembejeo kwa wakulima wadogo bila hivyo huwezi kupata mapinduzi ya kilimo na usipopata mapinduzi ya kilimo hakutakuwa na Tanzania ya viwanda. Hili ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na kama kutakuwa na fursa ya kushika shilingi Mheshimiwa Waziri wa Fedha, wote tunaoamini kwamba wakulima ndiyo mtaji mkubwa wa Watanzania na mtaji mkubwa wa CCM tutasimama na tutashika shilingi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema sekta hizi Mama zisipofanyakazi pamoja hatutapata mapinduzi ya viwanda. Ninaomba pia Waziri wa Fedha akubali kuziratibu hizi Wizara zote nilizozitaja. Ukisoma kwenye hotuba ya Waziri wa Kilimo ana vipaumbele vya mazao, atakuambia katika msimu huu kipaumbele changu ni mazao moja, mbili, tatu, nne huyo ni Waziri wa kilimo. Ukienda kwa Waziri wa Viwanda na Biashara ukisoma kwenye hotuba yake Waheshimiwa Wabunge mkasome mtaona baadhi ya mazao ambayo yamepewa kipaumbele na Wizara ya Viwanda na Biashara hayapo kwenye vipaumbele vya Wizara ya Kilimo sasa huyu anayeenda kuzalisha viwanda malighafi anazitoa wapi? Kwa hiyo, uone kwamba hapa ni kama hakuna coordination. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili upate mapinduzi ya viwanda unahitaji coordination. Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Nishati na Madini, Viwanda na Biashara na Wizara ya Ardhi mkubali sasa kukaa pamoja, kutengeneza mpango kazi wa pamoja, utaratibu wa joint planning, mfanye joint evaluation na monitoring ili tuweze kuipata Tanzania tunayoitaka.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maslahi ya muda, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari Dkt. John Pombe Magufuli na wasaidizi wake akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kufanya kazi iliyotukuka kwa Watanzania kwa miaka hii mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo kubwa ambalo limejitokeza ni dhana ya uchumi jumuishi (inclusive economy). Mfumo huu wa uchumi jumuishi ni uchumi ambao unatoa fursa kwa Watanzania wote, kwa wananchi wote kuweza kunufaika nao. Dhana hii inatofautiana na dhana ya uchumi ambao sio jumuishi (extractive economy) ambayo inawanyima fursa watu walio wengi kuweza kushiriki kwenye uchumi au kunufaika na uchumi. Unawakumbatia mabeberu wachache na mabepari, hautoi fursa kwa watu wengi na watu wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu kwa miaka hii mitano imekuwa inatekeleza dhana ya uchumi jumuishi na imekuwa inafanya hivyo kwanza kwa kujenga mazingira na miundombinu wezeshi inayomfanya kila Mtanzania aweze kushiriki na kunufaika na uchumi wa Taifa lake. Imefanya hivyo kwa kujenga miundombinu ya reli, sasa programu kubwa ya ujenzi wa reli za kisasa imeanza na hii ya SGR inayoendelea sasa ni hatua ya kwanza na naamini tutaendelea kujenga reli. Pia programu kubwa ya umeme. leo Serikali imefikia vijiji 9,001 kutoka vijiji 2,118; ni achievement kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kutafsiri hii dhana ya uchumi shirikishi, Serikali imewekeza kwenye usafiri wa anga ili Watanzania waweze kujenga uchumi wao kwa kusafiri kwa haraka na kufanya mambo mengine ikiwemo uchumi wa utalii, lakini pia dhana hii tunaitafsiri kwenye namna ambavyo Watanzania wananufaika na ukuaji wa uchumi. Tunaona uchumi wetu unakua kwa asilimia 6.9. Kwenye maisha ya Mtanzania ananufaika nao vipi? Serikali imefanya kazi za kutukuka kwenye eneo hili. Leo tuna huduma za afya kwa kupitia vituo vya zahanati zaidi ya 1,198, Watanzania kwa maelfu wanapata huduma huko. Lakini tuna vituo vya afya, hospitali 69 mpya na hospitali za rufaa kumi, hiyo ni sehemu tu ya tafsiri ya ukuaji wa uchumi ambao umejengwa na Awamu hii ya Tano.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo nina ushauri wa mambo ya nyongeza kwa Serikali; kazi iliyofanyika ni kubwa sana, tumeona uchumi unakuwa na miundombinu inakuwa na mazingira wezeshi ya kiuchumi yanajengwa na Watanzania wananufaika na uchumi wao. Hata hivyo kuna mambo ambayo Serikali inapaswa kwenda kuyatafakari.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia takwimu za ukuaji wa uchumi ambao tumesema unakuwa kwa asilimia 9.9, sekta zilizochangia ukuaji huo zinatofautiana kwa umuhimu lakini Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo inaajiri asilimia 64 ya Watanzania ukuaji wake ni asilimia 3.6 wakati sekta zingine ambazo zimechangia kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa letu kama ujenzi unakua kwa asilimia 14.8, mchango wake kwenye ajira ni asilimia 2.42.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia uchukuzi, unakua kwa asilimia 8.8 lakini mchango wake kwenye ajira za Watanzania ni asilimia 2.94; ukiangalia huduma za usambazaji maji vijijini mchango wake kwenye ajira ni 0.05. Tafsiri yake ni nini; tafsiri yake eneo ambalo linawagusa Watanzania wengi ambao ni asilimia 64 mchango wake wa ukuaji ni mdogo sana ambao ni asilimia 3.6. Niiombe sana Serikali; dhana ya uchumi shirikishi ni kuwafikia hawa Watanzania walio wengi ambao sehemu kubwa ya maisha yao wanategemea kilimo. Nikiri, Serikali imefanya kazi kubwa kwenye kilimo, lakini kazi bado haijakwisha. Niiombe Serikali tunavyoendelea na mchakato huu wa bajeti ifikirie sasa kwenda kuwekeza zaidi kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, pili, Watanzania wengi, asilimia 60 mpaka 70 wanaishi vijijini. Dhana ya uchumi shirikishi au uchumi jumuishi ni kuwawezesha Watanzania hawa kuweza kushiriki kwenye uchumi. Watashiriki vipi kama barabara zao hazipitiki? Leo maeneo mengi ya vijijini bado yana changamoto na mafuriko ya mwaka huu yatufumbue macho tuone kwamba yapo maeneo ambayo tunahitaji kwenda kuwekeza nguvu zaidi.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wengi wapo maeneo ya vijijini. Kule Madaba kuna Vijiji vya Ifinga, kilometa 48 hazipitiki msimu mzima wa mvua, lakini huko ndiko kwenye Mbuga ya Selous na huko ndiko kwenye Watanzania ambao wanahitaji kushiriki kwenye uchumi. Niiombe Serikali yangu Tukufu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuwekeza pia kwenye miundombinu ya barabara, miundombinu ya uchumi vijijini ili Watanzania walio wengi wanaoishi katika maeneo hayo waweze kunufaika zaidi na uchumi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, pia nimshukuru Mheshimiwa Rais na wananchi wa Madaba kwa kupata fursa ya kutumikia jimbo la Madaba kwa awamu ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja katika mambo makubwa ambayo yamejitokeza kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, ni hoja na haja ya kuwa na uwekezaji jumuishi katika kilimo. Hili Mheshimiwa Rais alilipa kipaumbele kwenye hotuba yake kwa sababu kubwa tatu.

Mheshimiwa Spika, sababu ya kwanza sekta hii imeajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, lakini sababu ya pili ni kwamba asilimia kumi au zaidi ya Watanzania ambao hawajishughulishi moja kwa moja na kilimo wamejiajiri kupitia sehemu ya mnyonyoro wa thamani wa shughuli za kilimo. Wapo waliojiajiri kwenye biashara ya mazao ya kilimo, wapo waliojiajiri kwenye usindikaji kwa maana ya agro-process, wapo ambao wamejiajiri kwenye kutoa huduma za kifedha yakiwemo mabenki, SACCOS, wapo waliojiajiri kwenye usambazaji wa pembejeo, lakini pia wapo wengi waliojiajiri kwenye huduma za ugani.

Mheshimiwa Spika, sababu ya tatu ni kwamba sekta hii ndiyo inayochangia asilimia mia moja ya chakula cha Watanzania wote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais alitoa kipaumbele kikubwa sana katika kueleza namna gani sekta hii ipewe kipaumbele na ipewe msukumo katika safari hii ya miaka mitano sehemu ya pili ya kipindi chake cha miaka kumi.

Mheshimiwa Spika, leo naomba nitoe ushauri wa namna nzuri sasa ya kutekeleza maelekezo haya, ndoto na matamanio ya Mheshimiwa Rais kwenye sekta hii ya kilimo. Vitu ambavyo au jambo pekee ambalo linamfanya Mtanzania, mkulima aende shambani akawekeze kwenye kilimo, kivutio au incentive ya mtu kwenda kulima ni upatikanaji wa soko la uhakika na tija kwenye kilimo. Mambo makubwa yanayomfanya Mwanamadaba, Mwanasongwe na Mtanzania mwingine aache shughuli zingine akalime ni soko na tija kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitoa kipaumbele miaka mitano iliyopita na kumekuwa na mafanikio, mipaka ilifunguliwa, masoko walau yalikuwa na unafuu. Hata hivyo, bado changamoto ni kubwa kwenye sekta hii upande wa tija kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, nina mambo mawili ya kushauri na kabla sijashauri nimpongeze Profesa Mkenda na Naibu Waziri Mheshimiwa Bashe wameanza vizuri sana katika kukabiliana na changamoto za sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo napenda Serikali iendelee kuweka msisitizo ni kuwa na mkakati madhubuti wa masoko ya kilimo, bado hatujafaulu. Wakulima wa Madaba na maeneo mengine hata msimu huu wamepata shida ya soko la mahindi. Kwa hiyo ipo kazi kubwa ya kufanya. Namshauri Mheshimiwa Waziri aangalie sana mkakati endelevu wa kuimarisha vyama vya ushirika ili vitumike kama sehemu ya kupambana na changamoto ya soko lakini mkakati wa uwekezaji kwenye usindikaji wa mazao, sekta hii ni sekta mama ambayo itatutoa.

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili ambalo nitatumia muda mrefu kulifafanua ni hili la kuwekeza kwenye kupunguza gharama za kilimo. Jitihada zilizofanyika miaka hii mitano zimeonekana za kuhakikisha kwamba wakulima wanapata masoko ya mazao lakini hata pamoja na masoko kupatikana faida ambayo mkulima anaipata kutokana na shughuli zake bado ni ndogo kwa sababu gharama za uwekezaji kwenye kilimo ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mambo mengi yanayochangia mambo matatu nataka niyaseme. Jambo la kwanza linalochangia gharama ya uzalishaji ni upatikanaji wa pembejeo kwa gharama nafuu. Jambo la pili ni gharama za usafirishaji wa mazao maeneo ya vijijini na jambo la tatu ni upotevu na uharibifu wa mazao baada ya mavuno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo mkulima yupo Madaba na maeneo mengine ya vijijini, huko ndiko alikojaa Watanzania, huko ndiko wanakokaa asilimia 80 ya Watanzania na wanajishughulisha na kilimo. Moja ya vikwazo ambavyo nimevisema ni upatikanaji wa pembejeo kwa gharama nafuu. Hili la upatikanaji wa pembejeo lina mawanda mapanda, lakini moja katika maeneo ambayo nataka nisaidie na kuishauri Serikali ni uwekezaji kwenye maduka madogo madogo ya kusambaza pembejeo vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pembejeo nyingi zinapatikana mijini na huko vijijini ambapo wakulima wapo hakuna maduka ya kusambaza pembejeo. Mkulima ili azalishe anasafiri kilometa nyingi kufuata pembejeo mijini. Suala hili nililisema katika Bunge lililopita. Sasa kinachokwaza upatikanaji wa maduka ya pembejeo vijijini ni gharama za uanzishaji wa maduka. Hapa ningeweza kwenda kwa details, lakini TPRI, TFRA na TOSCI peke yao ili upate kibali cha kuwekeza kwenye duka la usambazaji pembejeo kijijini lazima uwe na laki nane ambayo haihusishi kununua mali ghafi. Sasa hatuwezi kupata mapinduzi ya kilimo kama hatutaki kutoa hizi tozo. Hatuwezi kumsaidia mwananchi wa kijijini kupata pembejeo kwa gharama nafuu kama hatutaki kupunguza hizi tozo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili tutaenda nalo lakini naomba tulizingatie. Tuondoe hizi tozo ili tusaidie wajasiliamali wawekeze kwenye maduka madogo madogo ya pembejeo vijijini ili mkulima apunguziwe gharama za uzalishaji kilimo ili hata kama atakosa soko nzuri bado atauza kwa faida kwa sababu atakuwa amezalisha kwa gharama ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili ni gharama za usafirishaji wa mazao vijijini. Nashukuru Mheshimiwa mama Kilango amesema Watanzania wengi wamejaa vijijini, huko ndiko kwenye changamoto kubwa za miundombinu ya barabara na madaraja. Bajeti ya TARURA ni ndogo sana kuweza kukidhi mahitaji yaliyoko vijijini. Leo mkulima amelima mazao yake ili kusafirisha sehemu ambayo angesafirisha kwa shilingi laki moja anasafirisha kwa laki tano, hiyo inaongeza gharama za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa mama Kilango amesema ipo haya ya kuangalia uwezekano wa kuongeza bajeti TARURA ili barabara za vijijini zijengwe katika ubora, zipunguze gharama za uzalishaji kwa mkulima mdogo. Ndiyo maana nasema ni mkakati jumuishi wa sekta ya kilimo, sekta ya kilimo haiwezi kukua kama barabara za vijijini hazijaboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu nililotaka kuliongelea na kuishauri Serikali ni kwamba Serikali iangalie namna gani itapunguza upotevu na uharibifu wa mazao baada ya mavuno. Tafiti zinaonyesha asilimia 30 ya mazao ya mkulima yanaharibika baada ya mavuno. Sasa hii asilimia 30 kama ingeweza kufika sokoni ingempa faida huyu mkulima mdogo. Leo mkulima mdogo pamoja na gharama kubwa za uzalishaji inazotokana na kutopatikana pembejeo kwa wakati na karibu pamoja na gharama kubwa za usafirishaji bado…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, hoja yako ni ya msingi sana lakini muda hauko upande wako.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano. Mpango huu wa Tatu wa Miaka Mitano unajengeka toka kwenye Mpango wa Pili wa Miaka Mitano ambao tumeukamilisha utekelezaji wake mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja katika mambo makubwa ambayo yamebebwa na Mpango huu, ni dhana ya kujenga misingi ya uchumi wa viwanda. Na hapa nitaweka mkazo, kujenga msingi wa uchumi wa viwanda. Maana yake nini, tuliamua, kwenye ujenzi huu wa uchumi wa viwanda au ujenzi huu wa msingi wa uchumi wa viwanda uzingatie viwanda vyenye sifa kubwa mbili. Sifa ya kwanza, viwanda vinavyotumia malighali ya ndani. Lakini sifa ya pili, ni viwanda ambavyo vitatoa huduma au vitakuwa na impact kwa watu wengi, kwa maana ya critical mass. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunapoongea viwanda vinavyogusa au viwanda ambavyo vitatumia malighafi ya ndani, moja katika eneo muhimu sana ambalo lingetupa malighafi ambayo sio tu yanakwenda kutengeneza viwanda lakini nayo ni msingi wa viwanda ni chuma ya Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika huu ni karibu ni mwaka wa 20 au zaidi tunaongea kuhusu kwenda kuchimba chuma ya Liganga. Labda niseme mawili au matatu kuhusu hii Chuma ya Liganga. Kwanza inaambatana na uzalishaji wa umeme megawatts 600. Megawatts 600 ni robo ya umeme wote ambao tulikuwa nao mpaka mwaka 2015. Robo, yaani asilimia 25 sio mchango mdogo kwa uchumi wa Taifa letu. Kwa hiyo, ule mradi sio kitu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, mradi wa Liganga na Mchuchuma unaenda kuzalisha iron owl chuma ngumu, tani milioni moja kwa mwaka. Sio jambo dogo, lakini sasa manufaa ya malighafi ya chuma ni makubwa sana kwa uchumi wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chuma ya Liganga ingeweza kuzalisha viwanda vya nondo vya kutosha na vya kumwaga nchi hii, Chuma ya Liganga ingeweza kuzalisha viwanda vya mabati nchi hii, ingeweza kuzalisha viwanda vya baiskeli na vipuri vya magari vya kutosha kwa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jaribu kufikiria ni viwanda vingapi na vya aina ngapi vingeweza kuzaliwa kutokana na uchimbaji wa chuma ya Liganga na Mchuchuma ukiachilia mbali suala zima la ajira kwa watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo nyakati pia tujifunze kwenye mataifa mengine Marekani, waliamua kuchelewesha ujenzi wa reli ili kujenga uwezo wa ndani wa kuchimba chuma yao ili wajenge reli yao kwa kutumia chuma yao. Maana yake ndio soko la kwanza la chuma yao ilikuwa ujenzi wa reli yao. Sisi nasi tuna fursa kubwa kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwenye eneo hili nimuombe sana Waziri wa Fedha, Ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, arejee kwenye ajenda zetu tangu mwanzo huwezi kujenga uchumi wa viwanda Tanzania kama hutaki kwenda kuchimba chuma ya Liganga. Tutadanganyana, tutapiga kelele hapa, miaka itapita, nyakati zitabadilika na vizazi vijavyo vitatushangaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, tulivyosema tunataka tujenge viwanda ambavyo vitatumia malighafi ya ndani na vina critical mass tulisema viwanda ambavyo vita- absolved bidhaa na mazao ya wakulima kwa asilimia kubwa. Mambo niliyotarajia niyaone kwenye Mpango wa mwaka 2015/2016 – 2020/2021 moja nilitaka nione viwanda vingi vya kusindika mazao ya kilimo na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ametoa mifano ya viwanda lakini ukivipima kwa mizani, viwanda ambavyo vina critical mass effect ni vi chache sana ambavyo vinagusa mazao ya ngozi, vinagusa mazao ya kilimo. Mheshimiwa wa Wiziri wa Fedha ulikuwa kwenye Wizara ya Kilimo, unajua huwezi kukuza kilimo kama hutakuza viwanda vinavyosindika mazao ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nina aamini, wakati huu upele umempata mkunaji na mkunaji ndio Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ulikuwa kwenye sekta ya kilimo sasa upo kwenye Wizara ya Fedha peleka fedha kwenye kilimo, peleka fedha kwenye ku-facilitate kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kupata mapinduzi ya viwanda kama hutaki kuwekeza kwenye utafutaji wa masoko ndani na nje ya mipaka yetu ya Tanzania. Leo tunaongelea barabara za mipakani bado hazipitiki hazina lami, soko kubwa la Mazao ya mkoa wa Ruvuma tunategemea Msumbiji lakini tunatumia barabara ya vumbi. Hatuwezi kujenga uchumi kama hatutaki kutengeneza miundombinu ambayo itakuza biashara, itakuza viwanda. Na mimi naamini hii kengele ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninazo hoja tatu za haraka. Eneo la tatu, uwekezaji kwenye biashara unahitaji facilitation na hapa tuna mifano mingi sana leo, tunataka tuingie kwenye soko la Dunia lakini hatujaweka mechanism ya kutosha kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kuweza ku-meet vigezo kwa maana ya quality and quantity demands za soko la nje, hatutaweza! Hatutaweza kufika huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja zilizobaki nitazihifadhi lakini nilitaka niseme tunapotaka kubadilisha uchumi wa nchi yetu pia lazima tuwekeze kwenye diplomasia ya uchumi, lazima tuwe na mazuri na majirani zetu, lazima tuunganishe nguvu zetu za ndani na nje ili tulete mapinduzi ya uchumi kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nampongeza sana Waziri Mheshimiwa Aweso kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye Wizara hii. Mheshimiwa Aweso ni mmoja katika Mawaziri ambao wanawafahamu wananchi wa Madaba na anafahamika na wananchi wa Madaba. Ametutembelea na kuangalia changamoto zetu katika Kijiji cha Mtyangimbole, lakini pia amekuja Mdaba Mjini Lituta, ameenda pia Kijiji cha Mtepa, Wino na pia amechangia fedha zake kuwezesha miradi ya maji ya wananchi. Ni mmoja katika Mawaziri wa kupigiwa mfano. Kwa niaba ya wananchi wa Madaba namshukuru sana sana Waziri Aweso kwa ushirikiano mzuri anaowapa wananchi wa Madaba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa kupitia Wizara ya Maji kwa kufanikisha miradi ya Madaba Mjini, tumefaulu kwa kiwango kizuri lakini bado hatujamaliza ule mradi kwa asilimia mia moja. Nimwombe Mheshimiwa Aweso kwamba eneo la Mtepa, Lituta na Kipingo maeneo ambayo tayari amekwishatembelea yamepata maji kwa kiwango, lakini kwa sehemu kubwa bado hatujamaliza usambazaji. Tunaomba Waziri aendelee kutupa support kwa kupitia timu yake ya mkoa na wilaya ambao kwa sasa wamefanya kazi nzuri sana, tunaomba aendelee kuwatia nguvu wafanikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri yetu ya Madaba tunao mradi mmoja mkubwa sana wa vijiji nane na Mheshimiwa Waziri anavifahamu. Vijiji hivyo nane, ni Rutukira, Ndelenyuma, Bangamawe, Ngadinda, Ngumbiro, Mtyangimbole, Ruhimba na Likarangiro. Vijiji hivi havikuwa na maji kabisa, tulianza mchakato na Mheshimiwa Waziri kutafuta fedha bilioni sita kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa utakaotoa maji Mgombezi kupeleka kwenye vijiji hivi nane. Hata hivyo ilionekana hizi fedha ni nyingi na haziwezi kupatikana kwa mara moja. Ushauri wa Wizara na wataalam ulikuwa twende kwa vipande vipande.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Serikali imeshatenga fedha milioni 350 kwa ajili ya Mradi wa Maji Rutukila na Ndelenyuma, lakini tayari imetenga fedha milioni 300 kwa Kijiji cha Mbangamawe kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi, lakini pia Kijiji cha Mahanje milioni 250. Jumla ya fedha iliyotengwa ni bilioni moja na milioni mia moja na tisa (Sh.1,109,000,000) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa vijiji vinne; kati hivyo vijiji vitatu vinatoka katika vile vijiji nane nilivyokwishavitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapompongeza Waziri kwa kukubali kutenga fedha hii na Serikali kufanya hivyo, ninao ushauri wa kuhakikisha namna gani tunatekeleza miradi hii kikamilifu. Uzoefu unaonyesha mifumo ya utekelezaji ndio iliyoikwamisha Wizara hii kuwafikishia maji watanzania. Moja kati ya mambo ambayo napendekeza, eneo la kwanza utamaduni umekuwa kuunda kamati za utekelezaji wa miradi hii baada ya miradi kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kamati ziundwe kabla ya mradi haujaanza, kamati zishiriki kwenye utekelezaji wa mradi ili wanapokabidhiwa mradi wajue changamoto za mradi. RUWASA watekeleze miradi yote kwa kushirikiana na Kamati za Maji tangu day one hii itasaidia sustainability.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na ushauri wa maeneo mengine matatu, lakini nimesikia kengele imepiga, nataka niongeze umuhimu wa kuhakikisha kwamba mifumo ya kuingiza maji kwenye nyumba, pale Madaba tuna shida, tunawataka wanaotaka kuingiza maji kwenye nyumba waje wanunue mabomba RUWASA.

Mheshimiwa Naibu Spika, inatosha kutoa viwango vya ubora vya mabomba yanayotakiwa, mteja akanunue mwenyewe vifaa vyote, RUWASA wakague wamsaidie mteja. Mfumo tulioweka sasa Mheshimiwa Waziri wananchi wanaamini kwamba ni mfumo unaowezesha watu kupiga fedha, hatutaki kuwapa wananchi fursa ya kutafsiri vibaya nia njema ya Serikali ya kuwawezesha, tuwaachie wananchi wakanunue vifaa. RUWASA wakague vifaa hivi vimefikia viwango viwekwe, sio wananchi wanunue kupitia RUWASA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa RUWASA kununua vifaa vya miradi kwa kutumia mfumo ambao ni centralized unachelewesha sana utekelezaji wa miradi maeneo ya miradi, waandae utaratibu mpya utakaowawezesha wilaya, halmashauri au RUWASA katika ngazi ya wilaya na mkoa kununua vifaa wenyewe moja kwa moja kwa sababu hiyo centralized system ni nzuri lakini inachukua miezi sita mpaka saba kupata vifaa tunavyotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wanapata maji, Mheshimiwa Aweso amekuwa makini na Naibu wake Waziri, hawajatukatisha tamaa, nasi tunawatia moyo wanaweza, tuhakikishe kwamba Watanzania wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye hotuba hii muhimu inayowahusu asilimia 80 ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameweka vipaumbele vya majukumu ya Wizara katika bajeti ya mwaka huu na kipaumbele namba tano (5) ni soko la mazao ya kilimo. Ningepata fursa, ningeweza kurekebisha hotuba yake na kusema kipaumbele namba moja (1) kiwe soko la mazao ya mkulima. Nasema hivi kwa nini? Kwa sababu mwarobaini wa Sekta ya Kilimo ni soko. Msingi wa kilimo ni soko. Katika mnyororo wa kilimo kuna shughuli mbalimbali ikiwemo uzalishaji, usafirishaji, usindikaji, masoko, lakini soko ndiyo dereva anayeendesha Sekta ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale ambapo mkulima ana uhakika wa soko, pale ambapo mkulima atakuwa anauza zao lake kwa faida, hatahitaji kukusubiri wewe umletee Afisa Ugani, atamtafuta yeye mwenyewe, atamwajiri yeye mwenyewe kwa sababu kuna faida kwenye kilimo. Ili kilimo kiwe na faida lazima tuwekeze kwenye masoko. Ukishawekeza kwenye soko una-create incentive ya mkulima kuzalisha, akiona inamlipa atatafuta Maafisa Ugani, huko ndiko tupeleke fedha.

Mheshimiwa Spika, ili kilimo kiwe na faida lazima tuwekeze kwenye masoko. Ukishawekeza kwenye soko una- create incentive ya mkulima kuzalisha akiona inamlipa atatafuta maafisa ugani, huko ndiko tupeleke fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupa mfano, kwenye Bunge lako kwa miaka yangu yote sita sijawahi kumuona Mbunge anayehamasisha vijana wakanunue bodaboda, lakini vijana wanaenda kununua bodaboda kwa sababu, bodaboda zinawalipa, hiyo ndiyo essence ya kuwekeza kwenye kitu kinacholipa. Hatujafanya promotion ya bodaboda nchi hii, lakini Watanzania vijana wetu wanawekeza kwenye bodaboda na sio kwenye kilimo cha mahindi; hawawekezi kwenye maharage kwa sababu, maharage hayalipi kwa sababu hatujawekeza kwenye soko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri abadilishe vipaumbele vyake kipaumbele namba moja kufanya mapinduzi ya kilimo nenda kawekee kwenye soko. Soko ndio lita-create demand ya maafisa ugani, lita- create demand ya processing, n.k. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ya kwenye soko ni nini? Moja changamoto Mheshimiwa Waziri vitu ambavyo anatakiwa kuvijua ni vitatu; changamoto ya kwanza kwenye soko ni upatikanaji wa masoko yenyewe ya mazao. Mwaka jana wakulima wa Mkoa wa Ruvuma wameibiwa sana fedha zao, wamedhulumiwa sana mahindi kwa sababu, hatuna soko la uhakika la mazao ya mahindi. Wameenda kuuza kwa msanii mmoja pale Mkako mamilioni ya fedha yamepotea. Mheshimiwa Waziri ajue changamoto ya kwanza ni upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ya pili kuhusu masoko ya mazao ya kilimo ni miundombinu ya masoko ya mazao ya kilimo. Na tunapoongea miundombinu ni dhana pana na sitaweza kuifafanua kwa kina, lakini Profesa Mkenda na Ndugu yangu Mheshimiwa Bashe ni wabobezi kwenye eneo hili. Tukisema miundombinu ya kilimo tuangalie maghala na maeneo ya kuhifadhia mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, soko lina specifications zake. Soko la mahindi ya Kenya wanataka mahindi ambayo hayana sumu kuvu, ili uweze kukidhi hitaji hilo lazima uwe na uhifadhi ambao utasaidia mahindi yako yanapokwenda Kenya yawe hayana sumu kuvu. Hiyo ndio miundombinu ya masoko, tuwekeze kwenye maghala na vifaa vya kuhifadhi ubora wa mazao yetu ili yawe shindani kwenye masoko tunayoyataka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili kuhusu miundombinu ni miundombinu ya barabara. Hii imefafanuliwa na Mwenyekiti wa Bajeti amesema. Kwa maslahi ya muda nitaruka eneo moja muhimu sana la miundombinu ya masoko naomba niende kwenye mfumo wa masoko.

Mheshimiwa Spika, mifumo ambayo tunaitumia kuuza mazao yetu ipo mingi, lakini hapa nitaitaja mitatu; tuna mfumo wa kilimo mkataba, tuna mfumo wa stakabadhi za ghala (warehouse receipt system), tuna mfumo wa TMX ambao nadhani tutakuwa tumeuchukua Ethiopia. Hii mifumo mitatu ningepeta nafasi ningeifafanua kwa kina faida na hasara zake. Lakini namuomba Mheshimiwa Waziri, Profesa Mkenda, naomba nenda kafanye assignment kuhusu kilimo mkataba, faida zake ni zipi. Moja ya faida muhimu ya kilimo cha mkataba kinakusaidia ku-meet demand za soko in terms of quality na quantity. Lakini pia kinakusaidia kupata ku-raise capital ya kuzalisha. Wakulima wengi hawana mitaji na hatuna namna ya kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mfumo wa soko la stakabadhi ghalani hautekelezwi kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizowekwa kuhusu soko la stakabadhi ghalani. Stakabadhi ghalani ya Tanzania imekuwa soko la kukusanyia mazao, hakuna stakabadhi ya ghala pale. Mkulima hapati pembejeo, mkulima hapati mbegu bora, hapati mbolea, hapati mtaji wa kwenda kulima, tunaita stakabadhi za ghala sio stakabadhi ya ghala hiyo, hiyo ni aggregation center, hiyoni collection center ya mazao sio stakabadhi ya ghala kwa sababu, ai-add value ya kutosha kwa mkulima. Mheshimiwa Waziri naomba ukafanyie assignment kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini tatu kafanyie assignment kwenye suala la TMX. Je, tunatumia modal gani ya TMX? Je, TMX ni complimentary ya warehouse receipt system au ni kitu kinachosimama peke yake? Unawezaje ku-implement TMX katika mazingira yetu kama huna maghala yenye ubora? Kama huna mifumo ya teknolojia inayoweza kukusaidia kuweza kuingia kwenye masoko shidani?

Mheshimiwa Spika, muda ni mchache sana, agenda hii ni pana. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge kukushukuru kwa kupata fursa ya kuzungumza, lakini kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii kwa kazi kubwa na kwa ubunifu ambao wanao ili kuendeleza sekta ya uhifadhi na utalii nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee namshukuru Mheshimiwa Waziri baada ya kumweleza changamoto za wananchi wangu wa Jimbo la Madaba alikwenda mwenyewe, kwenda kuwasilikiza na kuanza mchakato wa kumaliza changamoto zao. Namshukuru sana Waziri na naomba aendelee na moyo huu huu. Nimemwona anakwenda Tunduru, nimeona anakwenda sehemu mbalimbali ndani ya nchi yetu kwenda kuwasikiliza Watanzania na kuona namna gani tunamaliza changamoto zao na naamini approach aliyonayo itatufikisha salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ina changamoto kubwa sana, tumeipa mzigo mkubwa sana. Nchi hii inawategemea wakulima, inawategemea wafugaji, inawategemea watalii na inawategemea wahifadhi. Sekta hizi zote zinategemeana na Watanzania wanaongezeka kwa idadi. Changamoto ya Mheshimiwa Waziri ni namna gani tunaweza ku-accommodate tuka-strike balance miongoni mwa wafugaji, wakulima na hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu Mheshimiwa Waziri azingatie ushauri uliotolewa na baadhi ya Wabunge hapa wa kurejea upya michoro ya nchi hii ili kuweka bayana maeneo ya mifugo, maeneo ya kilimo na maeneo ya hifadhi ili kuhakikisha kwamba kila kitu kinapewa kipaumbele na Watanzania wanaishi kwa utulivu na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri pia aendelee kuangalia mgogoro wa wananchi wa Madaba kwa eneo la Slow ambalo tayari ameanza kulifanyia kazi. Wananchi hawa pamoja na kazi nzuri aliyoifanya Waziri, bado hawaamini kwamba lile eneo ni mali ya maliasili, wanaamini kwamba wameporwa. Naomba jukumu la maliasili siyo kushambulia wale wananchi, jukumu la maliasili ni kukaa nao chini na kuelekezana kwenye michoro, ni wapi inaonyesha kwamba ni mali ya maliasili na wapi ni mali ya vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya maeneo kama alivyosema Mheshimiwa Ng’wasi, yanatumia michoro ya zamani sana na tayari haya maeneo yameshatangazwa kuwa vijiji, Kijiji cha Nderenyuma kimetangazwa kwenye ziara ya mwisho ya Mheshimiwa Rais Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli ameitanganza Nderenyuma kuwa Kijiji. Mbangamawe ni Kijiji cha muda mrefu, maeneo haya yote sasa maliasili wanasema kwamba ni kivuko cha wanyama kwa hiyo wananchi wasilime mazao ya chakula kama mahindi. Ni ushauri mzuri, lakini ukiwa participatory utatusaidia kumaliza mgogoro huu. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Neema Mgaya.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa kaka yangu Mheshimiwa Joseph Mhagama kwamba tatizo hili la migogoro hii kati ya mipaka ya mapori ya akiba na hifadhi na vijiji vingi ndani ya Tanzania imekuwa tatizo kubwa sana na Wabunge wengi wanalalamikia tatizo hili. Ifikie mahali sasa Mheshimiwa Waziri waweze kutatua migogoro hii, wakae waende kwa pamoja na Waziri wa Ardhi ili mkienda kumaliza tatizo mnamaliza moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kule Wanging’ombe, alikuja Naibu Waziri wa Ardhi mwaka 2018, lakini mpaka leo lile tatizo halijamalizika, hebu wakae kwa pamoja na Wizara ya Ardhi muweze kumaliza matatizo haya…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Neema ahsante kwa mchango wako. (Kicheko)

Mheshimiwa Joseph Mhagama.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea kwanza taarifa ya dada yangu Neema Mgaya kwa sababu ya muda…

NAIBU SPIKA: Naambiwa na kengele ilikuwa imeshagonga hapa mbele.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri basi tuendelee kushirikiana na wananchi wa Madaba kumaliza changamoto zao kwa njia ya kushauriana. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kukushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia. Pia nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na siha nzuri kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia Muswada muhimu sana, Muswada ambao kama utasimamiwa utageuka kuwa sheria na utasimamiwa vizuri, utatutoa Watanzania toka hapa tulipo na kutufikisha Tanzania bora zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kueleza na namna ambavyo Muswada huu wa haki ya kupata taarifa. Chimbuko la Muswada huu ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo wengi wameeleza, Ibara ya 18(d) kila mtu ana haki ya kupata taarifa. Kwa hiyo, Muswada huu misingi yake ni universal law na misingi yake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wale ambao wanabeza Muswada huu wanaikosea haki Katiba ya Tanzania na wanawakosea haki Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona vema pia nieleze kidogo historia ya Muswada wenyewe. Kama ambavyo tayari imeelezwa hapo awali, Muswada huu haujatunguliwa tu hewani, mpaka mwaka 2005 nchi 66 duniani zilishapitisha sheria hii, toka mwaka 2005 nchi 66 wana-practice sheria hii katika nchi zao. Sheria hizi katika nchi mbalimbali zinaweza zikawa zinatofautina kwa majina lakini maudhui ya sheria hii katika hizo nchi zote 66 ni ambayo kwa sehemu kubwa yanafanana na maudhuhi ya hii sheria ambayo tunataka tuipitishe. Hivyo, ni vizuri wale ambao tunabeza hii sheria hebu tujikite pia kwenye historia na tujaribu kuangalia comparative studies za hii sheria zinasemaje na practice za nchi zingine wamewezaje ku-practice.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii kwa hapa Tanzania imechelewa sana kufika. Nchi ya Sweden tayari walishaanza ku-practice sheria hii mwaka 1766, ni miaka mingi sana iliyopita. Leo Tanzania tunashangaa huu Muswada ni ajabu sana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza kidogo historia ili tuweke kumbukumbu zetu vizuri, napenda pia nileleze relevance; mantiki ya huu Muswada. Muswada huu kwa namna ulivyo una mahusiano ya kiutatu na mambo matatu; moja ni uwazi, pili ni uwajibikaji na tatu ni maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa taarifa, utoaji wa taarifa unaleta uwazi na panapokuwa na uwazi unazaa uwajibikaji. Mtumishi yeyote wa umma au mtumishi yoyote wa sekta binafsi, sekta ambayo ina maslahi ya umma pale atakapoona kwamba taarifa zake zinatakiwa ziwe wazi ataongeza sana uwajibikaji, pia kwa kuongeza uwajibikaji dhana nzima ya kuwaletea Watanzania maendeleo itakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naona relevance kubwa sana ya Muswada huu kufika wakati huu katika Bunge lako Tukufu na niwaombe Waheshimiwa Wabunge tukiulewa Muswada huu katika muktadha huo, kwa hakika tutawatendea haki Watanzania kwa kupitisha kwa kuunga mkono Muswada huu kwa asilimia mia moja. Kwa sababu kwanza unaenda kuleta uwazi, unaenda kuongeza uwajibikaji kwa taasisi zote za umma na binafsi zinazogusa maslahi ya umma, lakini pia kwa kuleta uwajibikaji tunakwenda kupata maendeleo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshangaa sana katika Serikali hii ya Awamu ya Tano ambapo tunataka kupiga hatua kubwa ya maendeleo kama tungeweza kwenda bila kupata sheria hii. Hata hivyo, nina mapendekezo ya maboresho kwenye Muswada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza la mapendekezo linajikita kwenye taarifa zilizozuiliwa Ibara ya 6(6) ya Muswada huu. Ibara ya 6(6) inasomeka kama ifuatavyo:-
“Mtu yeyote anayetoa taarifa iliyozuiliwa kinyume na mamlaka ya umma, kinyume cha sheria hii anatenda kosa na endapo atatiwa hatiani atatumikia kifungo kisichopungua miaka 15 na kisichozidi miaka 20.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia makosa yaliyoainishwa katika Ibara hii yanatofautiana sana. Naona kwamba yale makosa ambayo yana maslahi makubwa kwa usalama wa nchi yetu, yanagusa moja kwa moja eneo la usalama, makosa haya yasiwe na adhabu mbadala isipokuwa adhabu ambayo imependekezwa katika Ibara hiyo. Makosa ambayo hayana athari kubwa kwa usalama wa Taifa letu basi yatafutiwe adhabu mbadala au adhabu ipunguzwe. Kwa hiyo, napendekeza kwamba haya makosa yawekwe kwenye mafungu mawili kulingana na uzito wake na kutegemeana na athari ambayo itakuwa kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nahofia kupendekeza adhabu hii ipunguzwe kwenye Ibara ya 6(6) tena kwa sababu kuna tabia ya watu waovu wanaolitakia Taifa letu balaa wanafanya makosa haya na wakishahukumiwa Mahakamani kulipa faini ya pesa wanakwenda mtaani wanachangishana pesa wanaenda kulipa faini. Tusiruhusu jambo hili kwa jambo ambalo lina maslahi mapana kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ambayo napenda nichangie ni wajibu wa kutangaza taarifa, Ibara ya 9. Ibara ya 9 inasema kila mmiliki wa taarifa siyo zaidi ya miezi 36 baada ya kuanza kutumika kwa sheria hii, baada ya kuombwa atatoa kwenye gazeti, tovuti au gazeti linalopatikana kwa wingi likiwa na maelezo hayo mengi hapo chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufikia maendeleo kama nilivyosema katika utangulizi wangu tunahitaji Serikali yenye uwazi na uwajibikaji. Palipo na uwazi na uwajibikaji ndipo tutapata maendeleo. Iwapo tutaacha kipindi hiki cha miezi 36 maana yake miaka mitatu kutoka sasa ni muda mrefu sana. Tutashindwa kujipima katika kipindi hiki cha miaka mitano. Ushauri wangu eneo hilo nalo liboreshwe kwa kuweka kipindi kifupi inavyowezekana ili kukidhi haja ya kupata Serikali yenye uwazi, uwajibikaji na hatimaye kufikia malengo ya maendeleo tuliyojipangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo niliona nichangie ni Ibara ya 11(1) na Ibara zote zinazoendelea Ibara ya 12, 13, 14 mpaka 16. Ibara hii ya 11(1) inaeleza kuhusu notice pale ambapo ombi la kupewa taarifa linapowasilishwa. Ipo haja, tumeona na tunaishi katika jamii hii ya Kitanzania tumeona mara nyingi unakwenda katika ofisi zetu za Halmashauri, unakwenda kwenye Wizara na unakwenda ofisi za Kijiji kuomba taarifa kwa barua, lakini unazungushwa miezi mitatu, minne. Kipindi cha siku 30 kilichopendekezwa hapa ni kirefu sana kwa taarifa ambazo tayari zipo mikononi mwa wamiliki wa taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu yangu Ibara hii ya 11 mpaka Ibara ya 16 zifanyiwe maboresho ili kuakisi haja nzima ya kupata taarifa kwa muda mfupi inavyowezekana. Naamini nikileta barua katika Halmashauri ya Wilaya, nataka taarifa ya maendeleo ya mradi „A‟ haitakiwi ichukue zaidi ya siku mbili kunitaarifu kwamba barua hiyo wameipokea na sitegemei ichukue zaidi ya siku saba kunipa hizo taarifa. Zipo tayari good practices katika Serikali yetu. TAMISEMI nimeona wana service charter, ile service charter inaweza ikawa model kwa Wizara, lakini pia inaweza ikawa model kwa maeneo mengine yote ambayo yanatakiwa kutoa taarifa. Imeelezwa vizuri ni lini unataarifiwa kwamba barua yako ya kuomba taarifa imefika na ni lini unapewa taarifa. Kwa hiyo, kila kitu kimeelezwa hivi, hata anayeomba taarifa anapolalamika angalau anakuwa na kitendea kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anatunga Kanuni za utekelezaji wa sheria hii basi aangalie hicho kipengele ambacho kitaboresha na kitaharakisha utoaji wa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana lakini niweke tu tahadhari kwamba watu wasitudanganye na wasiwadanganye Watanzania kwamba sheria hii inakwenda kuondoa haki za Watanzania na kwenda kugandamiza haki za Watanzania. Ni makosa makubwa sana kuoanisha haki ya kupata taarifa na haki ya habari ni vitu viwili tofauti japo vinafanana. Haki ya kupata habari siyo synonym ya haki ya kupata taarifa. Ni vema wakajikita kwenye historia ya nchi mbalimbali wakajua nchi zinavyo-practice hii sheria na sisi namna ambavyo tuta-practice ni vizuri tukashauriana namna nzuri ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, 2017
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia Muswada huu muhimu sana kwa maslahi ya Watanzania. Lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu ukiuangalia ni Muswada ambao unatoa fursa pana kwa Serikali kuongeza ufanisi katika utendaji wake. Katika mfumo wa kawaida wa kiutendaji kwa Waheshimiwa Wabunge ambao mna uzoefu kidogo wa kufanya kazi na taasisi kubwa utagundua kwamba, kunakuwa na taarifa za aina mbili; kuna taarifa za menejimenti, lakini kuna taarifa za governance.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika level ya menejimenti ni taarifa ambazo zinatolewa katika ngazi ya taasisi husika katika muda wa miezi mitatu, ili kuiruhusu menejimenti iweze kujitathmini na iweze kuji-re-orient kufuatana na mahitaji na hali halisi ya wakati ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini unapokuja kwenye level ya governance taarifa ile inatakiwa kwa kweli iwe imeshiba kidogo na iwe imejitosheleza kwa maana ya kwamba hata menejimenti yenyewe imepata nafasi ya kujitathmini na kuji-orient ili kuendena na malengo yaliyokusudiwa.

Sasa sisi Waheshimiwa Wabunge ni level ya juu sana ya utendaji wa Taifa hili. Katika mfumo nilioueleza sisi Wabunge tungejiweka katika level ya governance. Sasa tunapotaka kupata ripoti kila miezi mitatu ni kama vile ambavyo tunajiweka kwenye level ya menejimenti on daily basis. Kwa hiyo, mimi nikubaliane kabisa na Serikali kwamba kwa Muswada huu sasa haya mapendekezo yanayoletwa kwenye hizi sheria yakubaliwe na Wabunge na yaweze kuboresha utendaji wa Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Sura ya 439, Ibara ya 4 mpaka ya 11 nimeshangazwa kidogo na Hotuba ya Kambi ya Upinzani inayotutaka sisi Wabunge au sisi kama Taifa tuwe sawa na mnyama anayeitwa nyumbu! Ukienda katika mbuga za wanyama kuna wanyama wawili, wale mtakaobahatika kwenda katika mbuga za wanyama kujifunza kidogo, kuna aina za wanyama wawili ambao wanaweza kukupa somo zuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mnyama anaitwa nyumbu na kuna mnyama anaitwa nyati. Ukikutana na nyati anasafiri, anasafiri na kundi, katika kundi wanakwenda, wanasimama, wanaangalia mbele, wanaangalia nyuma, wanajipima, wanatafakari, wanasahihisha makosa, wanapiga hatua wanasonga mbele. Lakini ukimkuta mnyama nyumbu ameamua kwenda, basi atakwenda hata kama kuna makorongo, hata kama kuna nini, atatumbukia ataendelea na safari.

Sasa sisi Wabunge sio nyumbu, tumetekelza mfumo huu wa zamani wa quarterly reports, tumejifunza changamoto zinazotokana na mfumo huu, kwa sehemu kubwa Serikali imetumia muda mwingi kukaa kuandika ripoti kuliko kutekeleza majukumu waliyotumwa na Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejifunza nini katika huo mfumo; ufanisi wetu ulikuwa mdogho sana. Leo tumekaa tumeona hilo tatizo tunaamua kuli-focus, tunapoli-focus tunabadilisha huo mfumo tuiache Serikali ifanye kazi na menejimenti, wajipime wao ndani ya taasisi zao kwa miezi mitatu, halafu waende tena miezi mitatu, baada ya miezi mitatu mingine watuletee hapa ripoti iliyoshiba na inayojitosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshangazwa kwa taarifa ya Upinzani wanasema mamlaka ya Bunge yamepunguzwa. Lazima tutofautishe kati ya mamlaka na ufanisi. Mamlaka yanakuwa na tija tu pale ambapo pana ufanisi mzuri wa kazi. Sasa kama mamlaka yako wewe kama Bunge yana-compromise ufanisi katika Serikali, mamlaka yako yanakuwa hayana tija, ya nini! Hatuwezi kubaki kwenye mamlaka kama mamlaka hayo hayaisaidii Serikali kutekeleza wajibu wake na kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini napenda niwakumbushe wenzangu Kambi ya Upinzani, marafiki zangu kwamba, kama kuna sababu za msingi Bunge hili linaweza kuitisha taarifa yoyote toka Wizara yoyote wakati wowote. Mamlaka hiyo ipo na itaendelea kuwepo na mabadiliko haya hayaendi kuondoa hayo mamlaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuu sana na ninaunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2017
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa hii nafasi. Pili nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuwa mmoja katika wachangiaji wa kwanza kabisa wa Muswada huu muhimu sana wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 5 wa mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia kwa makini sana mawasilisho yaliyofanywa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pia na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria. Pia nimebahatika kusoma mambo mbalimbali ili nione namna gani naweza nikaishauri Serikali kwenye jambo hili mahususi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niipongeze sana Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. Ukisoma Muswada huu unapata picha iliyo dhahiri kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri sana kurudisha rasilimali za Watanzania mikononi mwa Watanzania na kuwajenga Watanzania kiuchumi. Sheria ya Ardhi, Sura namba 113 marekebisho yaliyoletwa hapa yanalenga kwenda kulinda rasilimali ardhi ambayo kwa sehemu kubwa imetumika vibaya sana na watu wasioitakia mema Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Sheria hii sitachambua maeneo mengi kwa sababu nataka nijikite kwenye eneo lingine, lakini niwashawishi Waheshimiwa Wabunge tuipitishe kama ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo nataka kwa muda mfupi niliopewa nijikite zaidi ni kwenye hii Sheria ya
Utumishi wa Umma, Sura 298. Ukisikiliza mawasilisho yaliyofanywa unapata picha dhahiri kwamba katika kipindi fulani tulijisahau kidogo kuweka ajira za kutosha kwenye eneo hili mahususi kabisa linalogusa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu lakini na Madaktari. Matokeo yake leo tuna upungufu mkubwa sana wa kada hiyo. Kati ya mwaka 2012 mpaka 2015 watumishi katika kada hiyo waliofikia umri wa kustaafu walifika
395. Katika kipindi hicho hicho Serikali ililazimika kuingia mkataba na watumishi hao hao waliostaafu na kufikia idadi ya 324.

Sasa unapata picha kwamba waliofikia umri wa kustaafu 395 wanaoombwa kurudi kuendelea na majukumu 324 sawa sawa na asilimia 82. Sasa huu ni ushahidi kwamba kada hiyo ina upungufu mkubwa sana wa watu. Sasa Serikali imechukua hatua hiyo kwa muda mrefu, imeendelea kuwa- retain wale waliostaafu kwa asilimia 82.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara yake ni matumizi makubwa ya fedha za Serikali, hawa watumishi wanapostaafu wanalipwa mafao yao yote, wanapewa stahiki zao zote ikiwemo kiinua mgongo. Tunapowaomba sasa warudi kazini kuendelea na kazi tuna-negotiate upya mikataba na masharti yanakuwa mapya wakati mwingine, na gharama pengine zinakuwa kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi wanapomaliza kipindi, kila kipindi cha miaka miwili kinapoisha sasa Serikali inalazimika kuwalipa tena gratuity ambayo kimsingi ni kubwa sana. Ukisoma katika makabrasha mbalimbali katika kipindi cha miaka miwili tu Serikali imetumia zaidi ya bilioni 2.9. Sasa kimsingi hizo ndizo hoja za msingi ambazo binafsi naziona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine kubwa inahusu gharama ambazo Serikali inatumia kuwekeza kwenye kuijenga hiyo kada. Hawa Madaktari na Maprofesa, Wahadhiri na Madaktari Bingwa ni kada ambayo ni rare sana katika Taifa lolote. Fedha inayotumika kuwafikisha hapo ni kubwa sana, lakini pia muda tunaotumia kuwajenga na kuwaelimisha ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa wa kawaida wengi wanafikia nafasi hiyo wakiwa na miaka 35 hadi 50 na muda wa kulitumikia Taifa unabaki labda miaka mitano, kitu ambacho ni hasara kubwa kwa Watanzania lakini pia hasara kubwa sana kwa Taifa. Pia gharama za kumsomesha daktari bingwa mmoja tu na taaluma hizi hapa hatuna, tunawapeleka nje ya nchi, ambapo UK peke yake inagharimu milioni mia moja thelathini na tisa, ni kiasi kikubwa sana cha pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Wahadhiri wa vyuo vikuu, wale ambao tunataka waweze kuwapeleka vijana wetu kwenye soko la ushindani wa ajira kwa nchi ya Uingereza peke yake inagharimu milioni themanini na nane kumpata mtaalam mmoja mwenye hizo sifa. Kwa hiyo, unaona ni uwekezaji mkubwa sana ambao mtu binafsi anaufanya lakini pia Serikali inaufanya. Itakuwa si jambo la hekima na la busara kuifanya hii rasilimali watu ambayo tunaijenga kwa muda mrefu itumike katika muda mfupi tu kwa maslahi makubwa ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna maeneo ambayo tunaweza tukajifunza; sisi Watanzania si watu wa kwanza kufikia maamuzi kama hayo. Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria ameeleza bayana, ametupa mifano, kwamba Nigeria muda wa kustaafu miaka 70 kwa hiyari lakini anakwenda mpaka miaka 75, nchi jirani ya Kenya miaka 70 kwa kada kama hiyo. Nchi zingine ambazo zimeendelea zaidi Ujerumani hata Uingereza hawana kipindi cha kustaafu inategemea uwezo wa mhusika lakini pia mahitaji ya kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, hiyo ni kada ambayo tukiziondoa na kada zingine zote ambazo zina haki sawa katika Taifa, hii ni kada adimu sana kuipata katika historia ya nchi yetu na ndiyo maana unaona wanatoka, wanamaliza watu 395 wanarudishwa kazini watu 324 asilimia
82. Kwa hiyo, naunga mkono hoja kwamba huu Muswada upite ili taifa letu liweze kunufaika na rasilimali watu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kwa Serikali ni hii, tunakwenda, naamini Waheshimiwa Wabunge tutakubali kuipitisha na sasa itakuwa sheria, lakini ni vyema sasa Serikali tukaja na mkakati mahsusi kabisa wa kupunguza hili tatizo. Hii ni kwa sababu kuna Watanzania wengi wanakosa fursa kama hizo kwenye maeneo mbalimbali. Hatua ambayo Serikali inaichukua kwanza itajenga motisha kwa vijana kuwekeza katika elimu ili waweze kuwa madaktari bingwa lakini pia wafikie hadhi ya uprofesa katika shughuli zao, itawapa hiyo motisha. Pia Serikali sasa ije na succession plan ya eneo hilo la elimu na eneo la afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndio ulikuwa mchango wangu wa leo. Nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia muswada ambao ni muhimu sana kwa demokrasia, amani na utulivu wa Taifa letu. (Makofi).

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuleta muswada huu mahususi ambao unakwenda kulijenga Taifa lenye nidhamu, demokrasia, amani na utulivu; na sifa hizo zote zitabaki sifa za kudumu kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili naomba nieleze masikitiko yangu. Kambi ya Upinzani imetumia muda mrefu sana kwenye jukwaa lako na ndani ya Bunge hili tukufu kupotisha umma. Hotuba nzima ya Kambi ya Upinzani ukiisikiliza au wanapotosha kwa makusudi Watanzania au hawajauelewa huu muswada. Sasa mimi naomba nifanya assumption kwamba wenzetu Kambi ya Upinzani hawajauelewa huu muswada na nichukue jukumu la kizalendo kabisa la Mtanzania anayewajibika katika Taifa lake kuufafanua huu muswada, hasa maeneo yale muhimu ambayo nimeona yamepotoshwa kwa makusudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya manufaa makubwa ambayo muswada huu unayaleta kwetu na kwa Watanzania wote ni dhana ya uwazi na uwajibikaji, kwa lugha ya kigeni tungesema transparency and accountability. Hizi dhana nilizozizungumza hapa unaziona kwenye Ibara ya 21 ambayo inataka vyama vyote vya siasa vitoe tamko la mali na madeni ya taasisi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Ibara ya 22 kuhusu dhana ya uwazi na uwajibikaji kwa vyama vya siasa inavitaka vyama vya siasa viwe na Afisa Masuuli (Accounting Officer) na Ibara ya 23 katika hiyo dhana ya uwazi na uwajibikaji inavitaka vyama vya siasa viwe na akaunti maalum ambayo itatumika kwa ajili ya kuhifadhi fedha za ruzuku. Ibara ya 25 kwenye hiyo hiyo dhana ya uwazi na uwajibikaji inamtaka mkaguzi Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akague hesabu za vyama vyote vya siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya naomba niyafafanue, hii dhana ya uwazi na uwajibikaji na Watanzania wajue kwamba wenzetu ambao walikuwa wanaendesha vyama vya kisiasa kwa mfumo wa ukanjanja, kwa mfumo wa udanganyifu, wenzetu baadhi yao wamekuwa wanavitumia vyama vya siasa sio kama taasisi za kwenda kuijenga nchi isipokuwa kama SACCOS ili waweze kujinufaisha na fedha za ruzuku. Fedha hizi Serikali imetambua kwamba, ni fedha za Watanzania; fedha hizi zinapatikana kwa kupitia kodi. Hii ruzuku inayopelekwa kwenye vyama vya siasa lazima isimamiwe, na ndiyo mantiki ya kuleta muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tusiupotoshe umma kuhusu jambo hili. Hili linakwenda kuwasaidia Watanzania, fedha zao na kodi zao zinakwenda kusimamiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nimeliona linapotoshwa, lakini limebeba maudhui muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu ni Ibara ya 5(5)(A)(1). Ni kuhusu uratibu wa elimu ya uraia na programu za kujengea uwezo vyama vya siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe unajua vizuri kwamba hata shule zetu tunazipelekea curriculum, wanachofundishwa tunakijua, tumekisimamia. Vyama vya siasa ni matanuru ya kupika viongozi, hawa viongozi wakishaiva katika chama ndio wanaokwenda kuliendesha Taifa hili. Kwa hiyo, haki na wajibu wetu kama Watanzania ni kujiridhisha juu ya maudhui ya mambo yote ambayo yanakwenda kwenye vyama vya siasa ili yale yanayokwenda kufundishwa katika vyama vya siasa yaendane kwanza na utamaduni wetu, yalandane pamoja na mila na desturi zetu za Kitanzania. Dunia yetu imebadilika, values zetu hazifanani hata kama nchi zetu ni za kiafrika bado kuhusu tunu tunatofautiana, values zetu zinatofautina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika imani tunu zetu zinatofautiana. Mataifa haya tunu zao zinatofautiana, tunazo mila, tunazo tamaduni zetu na tunazo desturi zetu hizo lazima tuzisimamie kufa na kupona. Kwa hiyo, muswada huu unakuja na hiyo kwamba, mtu yeyote au taasisi yoyote, iwe ya ndani au iwe ya nje, itakayokwenda kutoa elimu ya uraia kwa chama cha siasa, itakayokwenda kufanya programu yoyote ya kuwezesha kujengea uwezo vyama vya siasa lazima itoe taarifa kwa Msajili na ipeleke maudhui. Iwapo Msajili wa Vyama vya siasa ataona kwamba maudhui yaliyokusudiwa hayalindi utamaduni wetu, mila na desturi zetu, hailijengi Taifa letu katika umoja, amani na maendeleo yake atazuia na huo ndio wajibu wake. Kwa hiyo, hilo mimi naomba tusilipotoshe na Watanzania wote walijue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni kupanua wigo wa Watanzania kushiriki katika masuala ya siasa bila kujali ukanda wala ukabila. Tunavyo vyama ambavyo ukivitazama vinatafsirika kama vyama vya ukanda, wakati mwingine vinatafsirika kama vyama vya kabila fulani. Sasa tukiendelea na utaratibu huu tutalimaliza Taifa letu, tutaliangamiza Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muswada huu umelitazama hilo, Ibara ya 13 ya muswada huu inamtaka yeyote anayesajili chama cha siasa, kwanza wanachama wapya wasipungue 200…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Spika alitahadharisha kuhusu muda mfupi tulionao. Kwa hiyo, taarifa na miongozo na kila kitu havitaruhusiwa isipokuwa utaratibu kama mtu anavunja kanuni.

Mheshimiwa Mhagama.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Katika kipengele hiki ambacho tunataka tulijenge Taifa lenye umoja, Taifa la Kitanzania, ambapo vyama vyote vya siasa viwe na uwiano sawa wa aina za wanachama waliopo katika vyama vyao ili Tanzania ibaki kuwa moja imetutaka Ibara ya 13 tuhakikishe kwamba wanachama wanatoka kwenye nusu ya mikoa ya Tanzania.

Vilevile pili imetutaka watoke walao kwa mikoa miwili ya Tanzania Zanzibar. Katika Tanzania Zanzibar walau Mkoa wa Pemba na Mkoa mmoja wa Zanzibar ya Unguja. Sasa tunataka nini Watanzania, tunataka kujenga Taifa moja na huu ndio uzuri mkubwa wa huu muswada na tusijikite kwenye vitu vidogo vidogo, tujikite kwenye mambo makubwa yanayokwenda kulijenga taifa la kujivunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ambalo ningependa kuchangia ni kuimarisha utawala bora ndani ya vyama vya siasa. Moja katika tatizo tunalolipata sisi Watanzania tulijisahau. Usipojenga dhana ya utawala bora kwenye chama huwezi kuupata utawala bora kwenye Serikali, kwa sababu yeyote anayekwenda kulitumikia hili kama Waziri, atakayeshika nafasi ya urais, atakayeshika nafasi ya Uwaziri Mkuu, ametoka kwenye chama. Sasa tukiwa na chama ambacho hakina utawala bora utajenga Taifa gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunavyo vyaa ambavyo Mwenyekiti ndiye Accounting Officer, ndiye huyo huyo Afisa Masuuli, ndiye huyo huyo katibu, ndiyo msemaji wa chama. Sasa huyo huyo akipata nafasi ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tutakuwa na taifa gani katika nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wito wangu ni kwamba, Watanzania tuuelewe muswada huu katika upana. Tusiende kwenye details ambazo hazina tija, tuangalie maudhui mapana ya taifa ambayo yanakwenda kulijenga Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.8) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 8). Kwa maslahi ya muda nitakwenda moja kwa moja kwenye hoja yangu, nataka kwanza nijikite kwenye hii Tasnia ya Maziwa, Sura ya 262.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya ajenda kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali ya Jemedari Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha kwamba tunaifikisha Tanzania yetu kwenye uchumi unaotegemea viwanda. Moja katika maeneo makubwa ambayo yatachangia safari ya kuipata Tanzania ya viwanda ni sekta ya mifugo hususan eneo la maziwa na nyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kuanzisha maabara ya maziwa, kifungu kipya cha 33A kinalenga kuipata Tanzania ya viwanda. Baadhi ya wadau wamechangia hapa hasa hotuba ya Kambi ya Upinzani wakati wanachangia ilionesha kuwa na maabara hii ni kama kupoteza rasilimali kwa sababu tuna maabara ya TBS. Ikumbukwe kwamba maabara ya TBS kazi yake ni kuangalia ubora na viwango katika ujumla wake, lakini tunapotaka kutengeneza bidhaa ambayo inataka kwenda kushindana kimataifa, tunataka kwenda kuuza kwenye ISO Standards ni lazima tuwe na maabara maalum ambazo zinajibu mahitaji ya masoko ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, tayari tunazo maabara kama hizo hapa nchi, tuna maabara ya samaki ambayo inaitwa Water Quality Lab. Hii inalenga kuhakikisha kwamba samaki wanaovuliwa Tanzania kokote wanakokwenda kuuzwa ndani na nje ya nchi ubora wao kwa maana ya maji yaliyotumika unafahamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limefungua sana soko letu la samaki nje ya nchi, samaki wetu wameaminiwa nje ya nchi kwa sababu aina ya maji yanayotumika kuwakuza hao samaki inafahamika na imekubalika kimataifa. Tuna maabara za maji zipo mbili, ambazo nazo zinatumia ISO Standards, kwa maana hiyo maji yanayozalishwa kwa viwango hivyo yanaweza kuuzwa kokote dunia. Sisi Tanzania tunapotaka kwenda kwenye masoko ya kimataifa lazima bidhaa zetu zipate sifa hizo za viwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika zao ambalo litatupeleka katika masoko ya kimataifa ni zao hili la maziwa, kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa Mheshimiwa Waziri kuleta marekebisho haya ameyaleta wakati muafaka kabisa na naomba Bunge lako tukufu liunge mkono kuanzisha maabara kwa kifungu cha 33A.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mfano wa maabara nyingine TFDA pamoja na majukumu mengine waliyonayo wana maabara ya food quality. Pamoja na TBS wapo lakini TFDA wana maabara, kwa hiyo, maabara hii isieleweke kwamba ni maabara mpya kabisa kwa maana ya kwamba hakuna practice hiyo nchini. Practice hiyo nchini ipo na inatusaidia kwenda kushindana kuzifanya bidhaa zetu zishindane kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili katika Sheria ya Tasnia ya Maziwa ni kuhusu Bodi ya Maziwa kifungu cha 9. Aina ya bodi iliyopendekezwa hapa ni Bodi ya Ushauri, Bodi hii ni tofauti na bodi ambayo ningesema ni executive. Ni bodi ambayo ina maamuzi na ni bodi ambayo inaweza kuchukua maamuzi. Bodi iliyopendekezwa hapa ni bodi ambayo kimsingi haiwezi kuchukua maamuzi zaidi ya kumshauri Mheshimiwa Waziri. Kwa vile tunataka kuijenga Tanzania ya viwango, kuipata Tanzania ya viwanda, naishauri Serikali kwanza ianzishe hii bodi, lakini bodi hii ibaki kuwa interim tu, tuendelee na mchakato sasa wa kuwa na bodi ambayo ni executive ambayo uteuzi wake utamhusu Mheshimiwa Rais na itakuwa na meno na itaweza kuisaidia sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama muda utaniruhusu naomba nichangie kidogo kwenye Sheria ya Chama cha Mawakili Tanganyika, Sura ya 307, kifungu cha 22 kinachoitaka tasnia hii mkutano mkuu ushiriki wake uzingatie uwakilishi. Chama cha Mawakili kinazidi kukua kwa idadi ya wanachama, kama kitaachwa hivi kilivyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naomba kuunga hoja mkono na ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2019
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nikushukuru sana kwa kupata hii nafasi muhimu kuweza kuchangia Muswada huu uliopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu na kusema na iingie kwenye records kwamba naunga mkono Muswada huu ugeuke kuwa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niondoe upotoshaji mdogo unaoendelea wa kwamba tunashughulika na sheria 9. Muswada ni mmoja na unafanya marekebisho kwenye Sura 8. Natambua wadau wengi humu ni wanasheria, watalichukua hili kama maelezo sahihi, hakuna sheria 9, Muswada huu ni mmoja una Sura 8 na hizo ndizo tunazozifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niendelee kukupa comfort…

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Niendelee kukupa comfort kwamba…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mhagama, kuna taarifa, Mheshimiwa Salome.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa mzungumzaji kuwa Muswada huu unajadili mabadiliko ya sheria 9 ambazo ni Sheria ya Makampuni, Sura 212; Sheria ya Hakimiliki, Sura 218; Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza, Sura 230; Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Sura 56; Sheria ya Vyama vya Kijamii, Sura 333; Sheria ya Takwimu, Sura 351; Sheria ya Uwakala wa Meli, Sura 415 na Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini, Sura 318. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mhagama, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nasikitika kwamba siwezi kuipokea hii taarifa…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Ni kwa sababu kama ambavyo yeye mwenyewe alishakiri kwamba Kamati imekaa weekend nzima kufanya kazi hii, ina uwezo wa kutofautisha katiya Sura 8 na sheria 9. Hatujadili sheria kamili, tunajadili Sura katika sheria hiyo. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maslahi ya Watanzania naomba nitumie muda wangu uliobaki kuishauri Serikali. Moja nianze na kuipongeza kwamba tunazo principle tatu ambazo mimi ninazitumia katika maisha. Principle ya kwanza ni ku-focus, ya pili ni ku-sustain efforts na tatu ni ku-concentrate resources. Kama taifa tumejikita kwenye kuijenga Tanzania ya viwanda na ili tuijenge Tanzania ya viwanda tunahitaji kujenga mazingira bora ya makampuni yanayoshiriki katika kukuza biashara nchini. Makampuni haya tukiyaacha yamekaa holela holela kiasi ambacho hatuwezi kutofautisha kati ya kampuni ambayo ni guaranteed na shareholding, hatuwezi kuona namna gani tunaweza tukaratibu biashara nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa Sheria hii ya Makampuni, Sura ya 212 ambayo Serikali inapendekeza marekebisho yake naiunga mkono kwa asilimia 100 kwa sababu inaenda kuisaidia Serikali kwanza kujua walipa kodi ni wangapi kama makampuni. Kwa sababu tuna makampuni yamesajiliwa kama makampuni lakini yanafanya kazi yenye malengo yasiyo ya faida. Sasa kwenye makampuni kama hayo hatuwezi kwenda kuchukua kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ieleweke kwamba lengo la kuyaratibu haya, yale makampuni ambayo yanakwenda kufanya shughuli ambazo siyo za kifaida/ kibiashara yabadilishe utaratibu yakajisajili chini ya Sheria ya NGO, Na. 56 itakuwa ni utaratibu mzuri, sasa tutajua nani analipa na nani halipi kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitajikita kwenye maeneo ambayo pengine wajumbe waliotangulia hawakuyagusa. La pili, hii ajenda ya NGO kwa maana ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali imeleta kelele nyingi sana na pengine imepeleka message ovu ambayo Serikali haikukusudia kwa wadau. Kwanza, ieleweke kwamba Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini ni wadau muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu. Mashirika haya yanatusaidia kufanya tafiti mbalimbali, yanachangia Serikali, Halmashauri zetu za Wilaya, yanashirikiana na wakulima na maendeleo makubwa ambayo tumeyapata mpaka sasa huwezi kuondoa mchango wa taasisi zisizo za Kiserikali na hii Serikali inalijua. Kwa hiyo, wenzetu wasipeleke message tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mashirika haya ya Kiserikali yametusaidia sana katika masuala ya sera. Zipo sera nyingi ambazo zimefikiwa na zimekubaliwa ambazo zinaongoza shughuli mbalimbali za nchi yetu, zina mchango mkubwa sana wa wadau ambao ni NGOs. Kwa hiyo, mchango wa NGO nchi hii ni mkubwa sana na baadhi ya wadau humu ndani tusiwapotoshe wananchi na wala tusiyakatishe tamaa Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayofanya kazi nzuri sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii inalenga kuziratibu hizi NGOs, kuzijengea mazingira rahisi ya kufanya kazi ili pale ambapo wanakutana na vikwazo kama NGOs waweze kusaidiwa. Sasa imechukuliwa tu upande mmoja kana kwamba Serikali inataka izifute, hakuna mahali ambapo katika Miswada hii yote tuliyopita pamekusudia kuifuta NGO inayotekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili, nilikuwa tu na ushauri. Moja, tunayoyaona katika NGOs, kama nilivyosema zipo NGOs zinafanya kazi nzuri sana lakini zipo NGOs kama vichaka vya wala fedha za wafadhili. Sasa Serikali ina wajibu wa kuona kwamba fedha zinazoingia nchini kwa malengo ya kusaidia iwe utafiti, masuala ya sera, wananchi, wakulima wadogowadogo, kwenye maeneo ya elimu, vyuo vikuu ili mradi kwamba fedha hii ni ya wafadhili na inalenga kuboresha maeneo hayo, ifanye kazi zilizokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu uliokuwa huko mwanzo, ulikuwa ni kila mwaka NGO hizi zina-submit financial reports zikiwa audited. Utaratibu wa sasa umeboresha tu kwamba tusisubiri baada ya mwaka mzima, tuwe na quarterly reports ambazo zinaonesha kwamba nini kimefanyika katika kipindi hiki cha miezi mitatu, nani wamenufaika, wamenufaikaje, fedha kiasi gani kimetumika, kuna ubaya gani katika jambo hili? Ni utaratibu wa kawaida ni transparency. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tunazitaka Halmashauri zetu za Wilaya zifanye kazi kwa kuzingatia transparency, kama ambavyo tunaitaka Serikali Kuu ifanye kazi kwa transparency na vyombo vyote vingine vinavyoisadia Serikali zikiwemo NGOs lazima kuwe na transparency. Mimi ninaamini wadau wengi wanajua umuhimu wa transparency, hili halitawasumbua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu alipokuja kwenye Kamati alifafanua aina gani ya reports zinatakiwa kila miezi mitatu na kama wadau watapata nafasi na mashaka, watumie nafasi hii kujielimisha kupitia mamlaka husika zitatusaidia kuelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maslahi ya muda nilikuwa na mchango mrefu kidogo lakini basi niishie hapo na naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.3 wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata fursa ya kuchangia Muswada huu, na ni niungane na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kuchangia kwamba Muswada huu ni Muswada muhimu sana kwa Maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iingie kwenye kumbukumbu zako za Bunge kwamba Bunge lako limepitisha Miswada mingi sana muhimu kuwa Sheria ambayo imechangia sana ukuaji wa Uchumi wa Taifa letu. Lakini Muswada huu wa leo, Muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali namba tatu wa mwaka 2021 ni Muswada wa kipekee sana, kwa sababu unaenda ku-trigger kwa namna ya pekee sana ukuaji wa Uchumi wa Taifa letu, Muswada huu unaenda kufungua milango kwa uwekezaji mkubwa sana ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, limetajwa hapa Bomba la Mafuta huu ni moja tu, katika miradi mikubwa ambayo itakuwa accommodated na mabadiliko au na maboresho ya sheria hii. Mheshimiwa Rais akiwa Mwanza aliongelea mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao unaenda kuzalisha chuma ya kutosha kwa Maendeleo ya Taifa letu, marekebisho ya sheria hii yana- accommodate miradi ya aina hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini juzi tu Mheshimiwa Rais ameongelea uwezekano na utayari wa Tanzania kukaa chini na wawekezaji kuona namna gani miradi ambayo ilisimama ianze, ikiwemo na mradi mkubwa wa bilioni 10 dola, dola bilioni 10 wa Bagamoyo, aina hii ya Miswaada inaenda ku-accommodate aina hiyo ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema utangulizi huo nitumie fursa hii kumpongeza sana sana Mhehimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia kuleta mabadiliko haya ya Sheria ili kuruhusu uwekezaji mkubwa na wenye maslahi makubwa kwa Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iingie kwenye record za siku 100 za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi haya mabadiliko ya kiuchumi yatakayotokana na mabadiliko ya sheria zilizopendekezwa yatakuwa ni ya kujivunia kwa kizazi hiki na kwa kizazi kijacho cha watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo ya utangulizi nirudi kwenye muktadha wa sheria hii. Muktadha wa sheria hii wa mapendekezo haya unahusu miradi siyo mradi, inahusu miradi ambayo mikataba yake itakuwa na masharti maalum na itaridhiwa na Mabaraza la Mawaziri. Kwa hiyo, siyo mikataba bora mikataba ni mikataba yenye masharti maalum. Na nini kinapendekezwa na Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapendekeza kwamba miradi hii ambayo ina masharti maalum ambayo pia itakuwa imeridhiwa na Baraza la Mawaziri vifungu vilivyotajwa hapa kwenye Sheria 14 visihusike utekelezaji wake, utekelezaji wa vifungu hivi vilivyotajwa hapa kwenye hizi sheria 14 utekelezaji wake usiathiri utekelezaji wa miradi au mikataba hii mikubwa iliyotajwa na hiyo ndiyo mantiki na hiyo ndiyo adhma ya mapendekezo haya ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu wa miradi ya aina hii likiwemo pamoja na Bomba la Mafuta kutoka Hoima, naunga mkono kwa asilimia 100 mapendekezo yote yaliyoletwa na Serikali pamoja na marekebisho ya Kamati. Kwa vile muda unaniruhusu nataka nitaje maeneo matatu ambayo nadhani yanaweza kuchangia kuongeza uelewa wa Bunge lako Tukufu na Wabunge kuweza kupitisha sheria hii bila kuyumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sehemu ya Tatu ya mapendekezo ya Sheria zinazopendekezwa inahusu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191. Sheria hii ya Mazingira ilikuwa inazuia kufanyika shughuli zozote za kibinadamu ndani ya mita 60 ambako kuna vyanzo vya maji, mito, mabwawa na kadhalika. Sheria hii kama ingebaki hivi kwa miradi mikubwa, ikiwemo kama hii ya Bomba la Mafuta ingetukwamisha. Kwa hiyo, mabadiliko na mapendekezo haya ni muhimu sana ili kufanikisha mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hii Sehemu ya Sita, Sheria ya Bima, Sura ya 394. Pamoja na kifungu cha 133 kutaka mkazi yeyote wa Tanzania au makampuni yote ya Tanzania yanapotaka kupata huduma ya bima lazima yapate bima kwa kupitia makampuni ya Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii ilikuwa inatukwamisha kwa sababu mradi huu pamoja na miradi ya aina hii ina masharti makubwa na ina gharama kubwa za bima, makampuni yetu ya ndani yanaweza yakakosa uwezo huo. Sheria hii inaruhusu kwa makampuni ambayo yatakuwa na sifa na masharti yaliyoelezwa hapa, tuweze kutumia hata bima za makampuni ambayo sio ya Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maslahi ya muda, nakushukuru sana na naunga mkono hoja na naomba Watanzania na Wabunge wote tuunge mkono hoja hii ya Serikali. Ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) wa Mwaka 2021
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kukupongeza wewe kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nature na Muswada huu, nitaomba niwe specific kwenye mchango wangu na nitajikita moja kwa moja kwenye Sehemu ya Nne ya Muswada unaopendekezwa. Sehemu ya Nne ya Muswada huu inafanya marekebisho ya Kifungu cha 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambapo madhumuni ni kuzuia kukamatwa tena kwa mtuhumiwa ambaye ameachiwa huru kwa utaratibu wa nolle prosequi.

Mheshimiwa Spika, ili kuelewa vizuri haya mapendekezo ya Serikali, naomba nisome kifungu hicho cha 91 nikinukuu kwa sehemu. Kifungu cha 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Kifungu Kidogo cha Kwanza kinasema: “Katika kesi yoyote ya jinai na katika hatua yoyote ile, kabla ya hukumu au uamuzi, kama itakavyokuwa Mkurugenzi wa Mashtaka anaweza kuweka nolle prosequi, aidha, kwa kueleza Mahakama au kwa kuiambia Mahakama kuhusika kwa maandishi kwa niaba ya Jamhuri kuwa Mwenendo hautaendelea…”

Mheshimiwa Spika, ni ibara ndefu kidogo, lakini nitaenda kwenye hitimisho la Ibara hiyo ambapo anasema: “…lakini kuachiwa huko kwa Mtuhumiwa hakutachukuliwa kama kizuizi kwa mashtaka mengine ya baadaye dhidi yake na kwa kutumia maelekezo hayo hayo.”

Mheshimiwa Spika, practice imekuwaje? Kumekuwa na practice ambayo moja inaleta mzigo kwa Serikali, lakini pili, inaleta upendeleo. Katika mienendo ya kesi za namna hiyo, katika kutekeleza hicho kifungu cha 91 wapo watuhumiwa walioachiwa kwa utaratibu huo wa nolle prosequi, lakini utekelezaji wake siyo tu umeongeza mlundikano wa mahabusu Magerezani, lakini pia imeuletea mzigo mkubwa sana Serikali. Wengi wanaachiwa kwa utaratibu huu, lakini akishatoka tu getini, anakamatwa na anashtakiwa upya. Anaachiwa kwa utaratibu huu, anakamatwa anawekwa tena mahabusu. Kwa hiyo, utaratibu huu ni kama haujatusaidia kutatua tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia utekelezaji wa kifungu hiki cha 91, pamoja na kuwanufaisha Watanzania kwa baadhi, lakini wengi walionufaika ni watu wenye hadhi ya juu. Masikini wengi; watuhumiwa wengi ambao uchumi wao ni wa chini na hali yao ni ya chini, hawajanufaika vizuri na utaratibu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mapendekezo haya ya Serikali ambayo ningependa niyanukuu, yapo kwenye Ibara ya 25 ya Muswada na Fasili mpya ya (3). Naomba niyasome kama yalivyoandikwa:

“Where the accused is discharged under subsection one, he shall not be rearrested and charged on the same facts unless there is sufficient evidence and that the hearing of the case shall proceed immediately upon the rearrest of the accused person subject to section 131(a).”

Mheshimiwa Spika, ni kwa mara ya kwanza katika kipindi hiki kifupi cha Awamu ya Sita Serikali inaleta marekebisho ya Sheria ambayo ni very inclusive. Marekebisho haya yanaenda kuwafuta machozi Watanzania wengi; mamia kwa maelfu ambao wamewekwa Magerezani kwa muda mrefu, wameshitakiwa bila vielelezo na bila ushahidi. Kifungu hiki cha 131 (a) kinataka tusipeleke, tusikamate au kuwaweka watu vizuizini kabla hatujakamilisha ushahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vyombo vinavyohusika na ushahidi, vikamilishe Ushahidi. Mtu anapokamatwa, day two apandishwe kizimbani, ushahidi upelekwe, kesi iendeshwe na apewe haki yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili ni la kipekee na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono Muswada huu kwa sababu unakwenda kutatua tatizo kubwa, siyo tu la mlundikano wa mahabusu magerezani au siyo tu gharama kubwa za uendeshaji wa Magereza yetu lakini unaenda kutoa haki kwa Watanzania wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naliomba tena Bunge lako kuunga mkono Muswada huu kwa maslahi mapana ya Watanzania hasa wanyonge.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)