Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Vicky Paschal Kamata (2 total)

MHE. VICKY P. KAMATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Nyamalembo, Nyamasagata, Semina na sehemu zote ambazo hawa wawekezaji wa GGM wamechukua maeneo yao ningependa kufahamu ni nini manufaa ya moja kwa moja wanayoyapata wananchi hao ambao waliruhusu maeneo yao yanatumiwa na GGM?
Swali la pili, kwa kuwa Serikali imekuwa ikiahidi mara kwa mara kuwapatia maeneo ya uhakika na ya kudumu wachimbaji wadogo na kwa kuwa mpaka sasa bado haijawapatia wachimbaji hawa. Je, Serikali inapanga nini kutatua tatizo hilo, ukizingatia hivi karibuni mwezi wa saba ile PML ya STAMICO ina expire ni kwa nini Serikali isitoe tamko hili sasa hivi hapa kwamba mara baada ya hii PML ku-expire basi lile eneo litapewa wachimbaji wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, manufaa ya wananchi wa Geita kulingana na mgodi huu ni kweli kabisa Watanzania wengi na wananchi wa Geita hasa wa maeneo yanayozunguka mgodi huu wamekuwa wakitarajia manufaa makubwa sana. Lakini hata hivyo mambo ambayo wananchi wa maeneo hayo wamenufaika ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mgodi ulipoanza mwaka 1999 wananchi wanaozunguka mgodi huo walifanyiwa fidia. Wananchi ambao waliofanyiwa fidia ni pamoja na maeneo ya Nyamalembo, wananchi wa Nyamalembo wapatao 346 walilipwa fidia jumla ya shilingi bilioni sita nukta nane, lakini wananchi wa Katoma ambao wanafikia karibu 732 walilipwa shilingi bilioni 2.7 kama fidia na wananchi wengine wa Nyakabale, Nyamatagata ambao wanafikia 700 walilipwa shilingi bilioni 732 hayo ni manufaa ambayo wananchi hao waliyapata.
Lakini hata hivyo, pamoja na manufaa hayo mgodi wa GGM umeendelea kutoa ushuru kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo ambayo ni service levy. Hadi sasa mgodi huo umeshatoa takribani shilingi bilioni 4.7 kama service levy lakini manufaa mengine wanayoyapata wananchi hawa ni pamoja na ajira. Mgodi wa GGM hivi sasa unaajiri Watanzania wanaofikia 1568 kama nilivyozungumza kwenye jibu langu la msingi wakati wa bajeti yetu. Lakini kadhalika bado mgodi GGM wananchi wanaozunguka maeneo ya Geita, Nyamatagata, Katoma, Nyakabale, pia wamezungumzia kujengewa hospitali, vituo vya afya pamoja na shule za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, kuhusu kuwapatia maeneo hasa ya Mgodi wa Bacliff ambao sasa hivi unamilikiwa na STAMICO pamoja na wabia wenzake. Niseme tu nitumie nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge Kamata ameendelea kupambana sana kwa wananchi wa Geita na mimi nimuombe aendelee kupambana. Lakini nimhakikishie tu sasa hivi Serikali inakamilisha mazungumzo kupitia STAMICO pamoja na wabia wake ili kuona sasa ni eneo gani kampuni yetu ya STAMICO pamoja na wabia wake kwenye Mgodi wa Bacliff maeneo yapi wanaachi kwa ajili ya wananchi wa Geita. Hata hivyo Serikali inaendelea kuwategea maeneo mengine mbadala karibu na mgodi huo. Maeneo ambayo Serikali itayatenga kama ambavyo tunasema kila siku pamoja na maeneo ya Mgusu pamoja na maeneo mengine machache sana ya kule Nyakabale pamoja na Nyamalembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumeshatenga maeneo mengine kule Kasubuya, Mheshimiwa Mbunge Kamata unajua ulikwishakuja tukazungumza sana tumewatengea hekta 432; kule Kasubuya. Lakini kule Matabe tumewatengea hekta 568; kule Chato kule kwangu kule tumewatengea hekta 1258; lakini pia bado tunawatengea maeneo mengine hekta 232 maeneo ya Geita.
Kwa hiyo, nimuomba sana Mheshimiwa Vicky Kamata bado tuko na wewe naomba uje ukae tena tuendelee kukaa tupange kama ambavyo huwa tunapanga siku zote kwa niaba ya wananchi wa Geita, ahsante.
MHE. VICKY P. KAMATA: Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Pamoja na majibu mazuri, nina swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa, GGM imekuwa ikitoa hili fungu la CSR kila mwezi kwa ajili ya kuhudumia hayo maeneo ambayo ameyataja katika maelezo yake ya msingi kwa maana ya elimu, afya, mazingira pamoja na wajasiriamali.
Mheshimiwa Spika, pia kwa kuwa, wamekuwa wakitoa kila mwezi hili fungu la CSR na kwa majibu haya inaonekana kwamba tangu Januari mpaka sasa GGM hawajatoa fungu hilo la CSR kwa maeneo hayo, nataka kujua kauli ya Serikali kwa wakati huu wa mpito kuhusiana na hawa waliokuwa wakisaidiwa na GGM kwa mfano, kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma wamekuwa wakisaidiwa pesa kila mwezi kwa ajili ya malazi ya wale watoto yatima, chakula, kuna mradi wa maji ambao kimsingi ni wa Serikali lakini GGM walikuwa bado wanaendelea kuutunza pamoja na ile hospitali inayotembea majini inayosaidia wanawake na watoto katika Visiwa kwa kuwa tangu Januari mpaka sasa pesa hazijatoka na imezoeleka kila mwezi huwa inatoka. Je, ni nini kauli ya Serikali katika kipindi hiki cha mpito?. Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baada ya marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017, tulisimamisha utoaji wa fedha hizi mpaka pale Baraza la Madiwani katika Halmashauri husika wakae, wakubaliane utekelezaji sawasawa wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo GGM, pia nimeongea na RAS wa Mkoa wa Geita, ule mpango wa kupitia kwa Madiwani umeshakamilika na kuanzia leo wanaanza kuzitumia zile fedha kutokana na jinsi walivyokubaliana na Halmashauri husika. (Makofi)